Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Mwanne Ismail Mchemba (33 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi nichangie hotuba iliyopo mbele yetu ya Mheshimiwa Rais wetu mpendwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe masikitiko yangu kidogo au nitoe angalizo, nisamehewe kwa sababu nina mafua, nina flu kali kwa hiyo sauti yangu inawezekana isisikike vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya Mheshimiwa Rais ni hotuba ambayo imekonga mioyo ya watu, ni hotuba ambayo mjadala wake ni wa kumsifia tu. Kwa nini nasema hivi? Hotuba ya Mheshimiwa Rais wakati anaitoa hiyo tarehe 20 Novemba alichokuwa anakazia ni yale aliyoyafanya wakati wa kampeni yake. Kampeni yake imezunguka Tanzania nzima na kila eneo, yale aliyoyasema alikuja kuwasilisha kwenye Bunge ili Serikali yake iweze kuyafanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais kwa kuwa alikuwa anakerwa sana na umaskini wa nchi hii aliona ni afadhali ajionee mwenyewe yale ambayo alikuwa anayasikia. Kila eneo alilokwenda wamempa malalamiko yake ambayo Kata, Wilaya au Jimbo lile linahusika, kwa hiyo, ni pongezi kubwa sana kwake. Lakini si hilo tu hotuba yake haikuchagua imegusa makundi yote. Wakati anaunda Baraza lake la Mawaziri ametambua hilo akaunganisha Wizara ili ufanisi wa ahadi zake uwe karibu na wananchi, kwa hiyo, nampongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuchangia kwa kuokoa muda, nianze na huduma ya afya. Nimpongeze sana Naibu Waziri wa Afya, alikuja katika hospitali yetu ya Kitete, akajionea hali halisi lakini baada ya hapo aliweza kuchukua majukumu mengine na akaweza kutoa ahadi. Hospitali ya Kitete ambayo iko Mkoa wa Tabora ina changamoto nyingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya kwanza, hospitali ile inaitwa ya Hospitali ya Rufaa lakini hivi navyoongea hatuna madaktari bingwa. Inawezekana tatizo hilo ni la Mkoa wa Tabora lakini pia inawezekana ni nchi nzima. Tuna upungufu wa Madaktari Bingwa hususani upande wa gynecologist, akina mama wengi wanateseka lakini madaktari bingwa wa mifupa hawapo. Mimi niombe, kwa kuwa Hospitali ya Kitete ya Rufaa kwa wilaya zake saba ambazo ziko katika mkoa ule, niiombe Serikali itekeleze au angalau basi tuwe na madaktari ambao wanaweza wakawa na fani hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo katika hospitali ile tuna tatizo kubwa la mashine za kufulia nguo yaani laundry. Tatizo hilo linatokana na ongezeko la wagonjwa linalofanya ongezeko la nguo au mashuka kuwa kubwa. Mashine ile ina miaka zaidi ya 30. Hatujaletewa mashine ya kisasa ya kufulia nguo za wagonjwa, ukienda pale ni taabani. Ukiangalia mashuka hata upeleke leo, kesho halitakuwa katika hali nzuri. Kwa hiyo, naomba Serikali ya Chama cha Mapinduzi iangalie sekta hiyo ya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna tatizo kubwa la madai ya wafanyakazi ingawa ni kidogo lakini ni mali yao. Niiombe Serikali, haya malimbikizo ya wafanyakazi inawavunja moyo ni lazima mtu alipwe kile ambacho amekifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vifaa tiba ni tatizo sana hasa kwa wodi ya akina mama. Kile kiwanda hakuna asiyekipitia hususani wanawake, ni kiwanda kigumu. Nashukuru Serikali angalau sasa hivi inapunguza vifo vya akina mama na watoto lakini huduma zingine bado zinalinganishwa na huduma za kawaida. Kwa hiyo, nashauri Serikali ya Chama cha Mapinduzi iangalie kwa jicho la huruma wodi za wanawake nchi nzima na hususani vijijini hakuna gloves, hakuna sindano, huyo mama unayemwambia gloves hazijui na wala maana yake pia haijui. Anachojua yeye ni kuongeza uzalishaji, tumeambiwa sisi tuongeze dunia. Kwa hiyo, niombe na nitoe angalizo kwa Wizara ya Afya iangalie ni jinsi gani inaweza kutusaidia kwa tatizo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, si hilo tu, nimpongeze Mheshimiwa Rais, kazi aliyofanya pale Muhimbili kupitia Kitengo cha MSD ni sifa kubwa, ni kazi nzuri, ameokoa mamilioni ya watu ambao wangekufa wasiokuwa na uwezo wa kwenda kununua dawa kwenye maduka ya watu binafsi. Kwa hiyo, niombe hospitali za Mikoa, Wilaya MSD wasogeze huduma pale ili angalau watu wa kawaida waweze kununua dawa kwa bei nafuu. Kwa hiyo, vifaa tiba, nadhani navyo viwe ni angalizo kwa kumsaidia Rais wetu kama mfano uliotolewa Muhimbili sasa hivi kila anayesimama pale anazungumzia habari hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni ahadi ya Mheshimiwa Rais ya shilingi milioni 50 kila kata au kila kijiji. Wakati wa mfuko wa Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete wapo wajanja walichakachua wakafanya ile miradi kama ni yao wakafungua SACCOS zao. Ombi langu kwenye pesa hizi, ifuate na iangalie vikundi vya akina mama lishe, vikundi vya kilimo, vikundi vya walemavu, vikundi vya wajane na vikundi vya VICOBA. Kwa kufanya hivyo, fedha alizosema Mheshimiwa Rais shilingi milioni 50 watafaidika wananchi wengi, nchi hii ina wajanja wengi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia ameelezea kuhusu ushuru mdogo mdogo, ni kero kwa akina mama, mtu anadaiwa Sh.200. Kwa hiyo, naomba hiyo nayo iwe angalizo kwa wale ambao watasimamia mfuko huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie habari ya barabara, ingawa Wabunge wote wa Tabora na mikoa mingine ya jirani wamezungumzia habari ya barabara. Barabara ya Chaya inaharibu utamu wa barabara yote na kazi zote zilizofanyika kutoka Itigi – Tabora, ni kilomita chache sana. Naomba Waziri mhusika atusaidie kwa hili. Tunazunguka tunahangaika, kilometa zinazozidi ni nyingi na walalahoi hawawezi kuzunguka kwa sababu bei inakuwa kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara ya Urambo – Kaliua, ni kilometa 32 tu kuunganisha. Watu wanapata taabu kutoka Kigoma wakifika Kaliua wanatumia saa nyingi wanaichukia na Serikali yao. Kwa hiyo, naomba sana hilo liangaliwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna barabara ya Sikonge. Naomba Waziri twende naye huko akaione barabara ya Sikonge inayokwenda Mpanda, kama atarudi amevaa hata koti, hawezi, wananchi wanateseka. Kwa hiyo, naomba barabara ya Tabora – Sikonge nayo ishughulikiwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara nyingine ambayo inaunganisha Majimbo mawili, barabara ya Puge – Ndala – Simbo – Nkinga - Ziba ambayo inakwenda kwenye barabara kuu inayokwenda Singida, hii nayo ni kilometa chache. Naomba nayo waiweke katika mipango yao ili ikiwezekana twende pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kufufua viwanda, wamepewa miezi sita, kiwanda cha kwanza nchi hii kinachowadhulumu wananchi ni Kiwanda cha Nyuzi cha Tabora, ni mateso. Kiwanda kile Mbunge aliyepita Mheshimiwa Mzee Msigalo alitoa shilingi ndani ya Bunge hili.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, basi baada ya hapo, naunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Rais, mengine nitaandika kwa mkono, ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi nichangie machache kuhusu mapendekezo ya Mpango kwa kazi tuliyokuwa nayo mbele yetu ya Kitaifa ya maendeleo.
Awali ya yote nichukue nafasi hii kwanza kabisa kuwashukuru wapiga kura wangu walionichagua baada ya kunipa likizo kwa miaka mitano tena. Kwa hiyo, nawashukuru mama zangu wameweza kunipa nafasi mbili nikiwa kama Mwenyekiti wao wa Mkoa, lakini si hilo tu wakanipa na nafasi ya Ubunge, nawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, kwa taarifa na Mapendekezo ya Mpango aliotuletea. Wakati nasoma nimeona amegusa sekta zote na hizi sekta kubwa ambalo tunamwombea ni utekelezaji, hilo ndilo kubwa, lakini Mpango, Maelekezo, itakavyokuwa, lakini kitabu hiki kinakidhi maeneo yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja bila kupoteza muda kwenye upande wa viwanda. Viwanda hapa nchini amezungumzia kwenye ukurasa wa 24, viwanda twende kwa kufuata jiografia. Viwanda vingi vimefungwa, maeneo mengine hayana viwanda kabisa na sehemu nyingine viwanda vilikufa. Kwa mfano Mkoa wa Tabora, Mkoa wa Kigoma, Mkoa wa Katavi, tunalima tumbaku, lakini mpaka sasa kiwanda kiko Morogoro. Kwa hiyo, tunaiomba Serikali katika Mpango huu iangalie ni jinsi gani ya kuweka kiwanda cha uchakataji katika Mkoa wa Tabora ile ni center Mheshimiwa Mwenyekiti, si hilo tu kulikuwa na Kiwanda cha Nyuzi, kiwanda hiki kilikuwa kinachakata nyuzi kama nyuzi, nyuzi hizo ni za pamba. Wazalishaji wa pamba wakuu ilikuwa ni Tabora, Shinyanga, Mwanza na Kigoma, lakini pamba hizi zinasafirishwa badala ya kuzalisha kwenye Kiwanda cha Nyuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe Serikali katika Mpango unaoletwa iangalie ni jinsi gani ya kuweka kiwanda kizito kama kile katika eneo hilo, kwa sababu lazima tutafute center, jiografia yetu inasemaje. Si hilo tu, kuna viwanda ambavyo vimefungwa na vinatarajiwa kufungwa kutokana na mafuta yanayokuja, kwa mfano, kutoka nje au viwanda ambavyo vinazalisha nchini kukosa malighafi. Pia kuna viwanda ambavyo mpaka hivi sasa, kwa mfano, Viwanda vya Mafuta, vingi vinategemea kufungwa kwa sababu mafuta yanaletwa kutoka nchi za nje. Hawa wanalipa kodi kubwa, lakini viwanda vinapofungwa ni athari kubwa kwa nchi yetu kwa sababu ajira inakuwa haipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Serikali kwa ujumla, watusaidie kuhakikisha kwamba wanalinda viwanda vyetu vya nchini ili kuweza kupata ajira ya kutosha. Pia kutoa elimu kwa vijana wetu ili waingie katika soko la ushindani. Kwa hiyo, tunaomba wenye viwanda pia waweze kutoa mafunzo kwa wale wafanyakazi wao ili tuweze kwenda nao pamoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka ya nyuma kulikuwa na viwanda vya SIDO. SIDO ni mkombozi mkubwa wa viwanda vidogo vidogo, hiyo nayo isisahaulike, SIDO ni mkombozi, akinamama wengi, vijana wengi wamejitokeza kupata mafunzo kwenye viwanda vidogo vidogo vya SIDO. Hata hivyo, si hilo tu, niombe Serikali yangu ni sikivu, haina wasiwasi, tena haya tunayoyazungumza asiwe na wasiwasi mtu yeyote kwamba hayatachukuliwa, yatachukuliwa na yatafanyiwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoathiri viwanda vya ndani na tusipoviwezesha viwanda vya ndani nchi yetu tunaikosesha mapato, kwa sababu asilimia kubwa ya mapato inategemea sana viwanda. Kwa hiyo, kubwa ambalo ningeishauri Serikali, walinganishe, waoanishe, sera ya viwanda na sera ya biashara. Hivi vitu viwili vinakinzana na kama vinakinzana vinatuathiri sana. Nimwombe Waziri wa Viwanda aliangalie hilo, ashirikiane pia na Baraza la Mawaziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende tena kwenye suala la reli, limezungumziwa kwenye ukurasa wa 53, lakini halikukaziwa, limewekwa juu, juu. Niombe kwa niaba ya wenzangu na wenyewe watachangia, tusilete mzaha kwenye suala la reli ya kati. Reli ya kati itatutenga sana. Hatuwezi tukaidharau kwanza kwa mambo mawili, wapiga kura wetu na wananchi wetu wa Tanzania wanategemea sana reli ya kati, wanategemea sana TAZARA, lakini si hilo, ubebaji wa mizigo barabara zote zinaharibika kwa sababu ya magari mazito.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakapoweza kuimarisha reli, ingawa wamesema latiri 80 kwa kipande, kwa mfano, wamesema kati ya Igalula, Tabora, Lolangulu, jamani tuizungumzie yote ili ifike Kigoma, ifike Mpanda, ifike Mwanza ili wabebe mizigo yote, hata hao nchi za nje wanategemea reli hii iwaunganishe kutoka Dar es Salaam kwenda huko. Unaposema kwamba nyingine ianzie huku kwa kweli niombe…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Bado dakika zangu.
MWENYEKITI: Kengele hiyo.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ukarabati… Bado ni ya kwanza.
MWENYEKITI: Ya pili.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Ya pili? Hapana Mwenyekiti ni ya kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nisibishane na wewe naunga mkono hoja, lakini ni ya kwanza, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ujenzi wa Chuo cha Uhazili Tabora, naomba Serikali ikamilishe majengo hayo kwa hatua iliyobaki, kwani Chuo hicho kina historia kubwa katika Mkoa wa Tabora.
Mheshimiwa Naibu Spika, Walimu/Wakufunzi hawatoshi, pia usafiri wa Wanachuo hakuna na computer hazitoshi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Zahanati ya Chuo haina hadhi ya Chuo. Tunaomba Serikali ilione hilo ili kuwapa moyo wanafunzi hao. Tunaomba ukarabati wa vyoo ufanyike kwa vile vyote vya zamani. Kwani afya ya wanafunzi ni hatarini, pia itawaepusha na magonjwa hatari ya kipindupindu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba elimu itolewe kwa jamii ili watambue umuhimu na madhumuni ya TASAF III. Kabla fedha hazijatolewa, watendaji wote wapewe elimu kuhusu walengwa; Watendaji wa Kata/Vitongoji, Vijiji, Wenyeviti wote, Wajumbe wa maeneo husika. Wale wote walipewa nafasi, ambao siyo wahusika waondolewe kwenye orodha ya malipo hayo. Mikutano ya hadhara ni muhimu kwenye jamii kwa kushirikisha Wanasiasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, pongezi kwa Waziri, Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba; Mheshimiwa Naibu Waziri, William Tate Ole-Nasha; Dkt. Florence Martin Turuka, Katibu Mkuu na Makatibu Wakuu wote wa Wizara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri ni kwamba, migogoro ya ardhi, wafugaji, wakulima ni vema Serikali sasa kuchambua sera mbalimbali zinazohusiana na matumizi makubwa kuchunguza mikakati ya utekelezaji wa sera hiyo. Mikakati yote ya Serikali ya kusuluhisha migogoro ya wakulima na wafugaji. Wananchi washirikishwe kutoa mapendekezo yatakayoondoa migogoro iliyopo ili kudumisha mahusiano mazuri kati yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wenyeviti wa Vitongoji na Vijiji wapewe elimu ya mahusiano, kutenga maeneo ya wafugaji na wakulima. Elimu kwa wafugaji kufuga kisasa kwa kupunguza mifugo. Majosho ni machache, Serikali ipange katika bajeti hii ongezeko la mabwawa na majosho, ni kero kwa wafugaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, matatizo na changamoto. Chuo cha Kilimo Tumbi hakijafanyiwa ukarabati wa miundombinu kwa muda mrefu. Wakufunzi katika Chuo cha Tumbi wachache, madai ya wafanyakazi yalipwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu tumbaku; tozo kwenye zao hili la tumbaku ni nyingi, Serikali ifuatilie ili kuwapunguzia wakulima mzigo. Soko la tumbaku ni kero, pamoja na pembejeo kufika kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, machinjio ya Tabora Manispaa yapo katika hali mbaya na hayafai kabisa kwa afya ya wanadamu, pia kuboreshwa kwa bwawa la Igombe ili kuweka mbegu ya samaki ya aina zote. Kutoa elimu ya kufuga samaki kwa wajasiriamali ambao wana vikundi vya ufugaji katika mikoa yetu hapa nchini. Kusambaza mbegu ya alizeti kwa wakulima wote kwenye wakulima wa zao hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vitendea kazi. Maafisa Ugani wapewe angalau pikipiki hata baiskeli, wapewe motisha ya kazi katika mazingira magumu. Serikali ijenge nyumba za Maafisa Kilimo na Mifugo Vijijini, wakopeshwe mikopo kwa ajili ya kuandaa mashamba darasa kwenye maeneo husika, hali za maisha yao ni mbaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi jioni hii na mimi niweze kuchangia kutoa machache ambayo niliiyokuwa nayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nianze kumpongeza Mheshimiwa Profesa Ndalichako, Naibu Waziri, Makatibu Wakuu, pamoja na watumishi wote wa Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba nimeipitia, sijasoma yote lakini nimeielewa. Pia nishukuru Mungu kwamba leo Mheshimiwa Simbachawene yupo, kwa hiyo, haya nitakayoyasema na yeye pia yatamgusa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Tabora una historia kubwa sana ya suala zima la elimu, ina historia kubwa mno, lakini Tabora inaongoza kwa kuwa na shule zenye vipaji maalum. Shule za vipaji maalum hazijawahi kushika nafasi kumi bora, kwa nini hazijawahi kushika? Shule hizi zimetelekezwa na Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini shule hizi hawasomi wakazi wa Tabora, wanafunzi wa Tabora, ni wanafunzi wa nchi nzima ambao wanapelekwa kusoma kama vipaji maalum lakini wakishuka pale getini vipaji maalum havipo. Kwa sababu Tabora Boys ina historia hata ya Baba wa Taifa, Milambo ina historia ya Baba wa Taifa, Tabora Girls ina historia kubwa mno, viongozi wengi wemetoka Tabora Girls hususani wanawake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mazingira yaliyopo katika shule hizi hayafai, watoto wanaokwenda pale wanateseka, miundombinu ni mibovu. Wanafunzi wanaokwenda pale hata kama walikuwa na shida ya kusoma hawawezi kusoma. Miundombinu ambayo naizungumzia hakuna maji, umeme na miundombinu ya shule zile hazijafanyiwa ukarabati miaka dahari na dahari. Kwa hiyo, wale wazazi wanaowapeleka watoto kwa sababu wako mbali anaambiwa tu mtoto amefaulu anampeleka lakini mazingira ni magumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali sasa iangalie kwa nini shule hizi hazipati nafasi ya kushika nafasi kumi bora, lakini kama tutakuwa tunawalaumu walimu hatuwatendei haki. Shule ya Tabora Girls ni ya wasichana, shule ile tumeomba kujenga uzio takribani sijui miaka 30 sasa, shule ile ni pana, wanafunzi wale mabweni ni mabovu, tunajitahidi sana kusema uzio ule ukamilike lakini wanafunzi wanaogopa kwa sababu panapokuwa hakuna uzio usalama wa watoto wa kike ni mdogo. Usalama wa wanafunzi wale kwa sababu ni wanawake wanaogopa na ni kweli wanateseka, kwa sababu ikifika usiku hawawezi kutoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niiombe Serikali yangu kwa sababu ni sikivu iangalie usalama wa wale wanafunzi wa shule ya sekondari ya wasichana, wanateseka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini si hilo tu, wanapokosa maji, wanafuzi wa kike, wanawake wote mliomo humu mnajua. Mnajua adha ya mtoto wa kike anapofika katika siku zake anavyoteseka kwenda kutafua maji. Wanawake wenzangumimi niombe Wizara hii ilete mpango mkakati wa kuhakikisha kwamba shule zote nchi nzima ambazo wasichana wanasoma wapewe kipaumbele za taulo. Kwa sababu kwa kweli aah, mimi siwezi kusema mengi lakini wanawake tunajua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika shule hizi kuna upungufu mkubwa wa walimu wa sayansi, hakuna unategemea nini, niombe madamu tunaita shule za vipaji maalum basi Serikali iwape kipaumbele ili walimu hawa wa sayansi waweze kufika huko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia madai ya wazabuni. Wazabuni hawa ndio wanaohudumia hawa watoto, shule hizi ni kama za watoto yatima, wanapokosa huduma chakula ni matatizo, hawana mahali pa kushika. Kwa mfano, kuna wadai wa zabuni wanadai tangu mwaka 2011 Mheshimiwa Ndalichako. Na ndio maana nimesema Mheshimiwa Simbachawene alipate hili, mwaka 2011 wazabuni wanadai, mwaka 2013 wanadai, mwaka 2014 wanadai, hawajapewa fedha zao. Hawa watu wengine wanakwenda kwenye mikopo lakini unategemea watawahudumia wanafunzi? Kwa hiyo mimi niombe hili wasipolitolea ufafanzu wa madai ya wazabuni patakuwa hapatoshi hapa, nitashika mshahara wa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tabora, pia tuna chuo cha elimu cha Walimu, nacho kimetelekezwa, miundombinu hovyo, hivi unategemea mwalimu anayejifunza kwa tabu atakwenda kufundisha huko mnakompeleka? Kwa hiyo ningeomba Chuo cha Ualimu Tabora kiangaliwe na kipewe nafasi ya kukarabati miundombinu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini si hilo tu nizungumzie habari ya Chuo cha VETA. Chuo cha VETA ni kikubwa mno na majengo mazuri sana kuliko Chuo cha Chang‟ombe. Lakini VETA Tabora haijatangazika, hakuna, hata ukisoma humu hutapata maelekezo ya Chuo cha VETA Tabora, hakipo. Chuo cha VETA Tabora au nchi nzima watu wengi wanafikiri chuo cha VETA ni wale walioshindwa darasa la saba, sio kweli. Tukiviendeleza vyuo vya VETA nchi nzima tutatoa wataalam wazuri kuliko wa chuo kikuu kwa sababu hawa ni watu ambao wanajituma na hawa watakuwa na uchungu wa maisha. Kwa hiyo, nilikuwa naomba Serikali yangu iangalie ni jinsi gani itaweza kuwasaidia wanafunzi wanaomaliza VETA kuwapa vitendea kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu tusipowapa vitendea kazi anamaliza kusoma akishamaliza kusoma unamwambia nenda kajiajiri, anaenda kujaajiri wapi. Wapewe mikopo, wakishapewa mikopo wanaweza wakafanya kazi nzuri ambayo itasaidia pia na wao kuwaendeleza katika maisha yao. Lakini nishukuru pia Serikali kuunganisha VETA na FDC. FDC nayo ilikuwa imekufa, ilikuwa haipo, lakini ndio ilikuwa inasaidia mpaka vijijini, kwa sababu vyuo vingi viko mjini, lakini FDC ililkuwa inakwenda mpaka vijijini watu wanapata elimu ambayo ilikuwa inawasaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi niombe Wizara ya Elimu na Wizara ya TAMISEMI washirikiane kikamilifu kuisaidia Wizara hii ya Elimu ambayo ndio inayotambuliwa ingawa ni mtambuka, lakini kuipeleka TAMISEMI Wizara ya Elimu ni kama kuionea. Kwa sababu kila mtu anayejua ukimwambia habari ya TAMISEMI haelewi, walimu wana madai yao, wana madai mengi kwa sababu TAMISEMI wameelemewa na mzigo mkubwa, afya imeenda huko, elimu imeenda uko, sijui nini wamepelekewa huko, mara wakusanye kodi huko huko, ardhi huko huko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa naomba kwa heshima na taadhima Wizara hizi zikae chini na zifanye mambo ambayo watanzania wataridhika, wataelewa, jamani msione hivi walimu wanapata taabu kubwa mno tena kuwe na fungu maalum la kuwakopesha walimu hata magari, hivi Serikali inashindwa kudhamini walimu wakopeshwe magari ambayo watakuwa wanakatwa kwenye mishahara yao, hiyo nayo itatusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nyumba za walimu, nyumba za walimu hata hizi shule nazosema za vipaji maalum ziko hovyo, haziko katika mazingira ya kumfanya mwalimu ambaye anastahili kufundisha shule zile. Ahsante nashukuru sana naunga mkono hoja asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi kwa Waziri wa Viwanda, Mheshimiwa Charles Mwijage, Mbunge na uongozi wote wa Wizara. Pongezi za pekee kwa Katibu Mkuu kwa hotuba nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na suala la kufufua viwanda. Naomba Serikali ifufue Kiwanda cha Nyuzi Tabora kwani kiwanda hicho ni cha zamani, pia ni mitambo ya kizamani ambayo imepitwa na wakati. Ni vema Serikali ikamshauri mwekezaji kuagiza mitambo mipya ya kisasa. Serikali ikajiridhishe kuona kama kweli mitambo ipo, isiwe wameihamisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukarabati wa majengo yaliyojengwa na Serikali ambayo alipewa mwekezaji ameshindwa hata kukarabati, ni vema apewe mwingine. Kukosekana kwa viwanda Mkoa wa Tabora ni kuongeza ugumu wa maisha kwa wakazi wa Mkoa wa Tabora, kusababisha ongezeko la uhalifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Kiwanda cha Maziwa, niiombe Serikali kuwawezesha wawekezaji wa ndani ambao uwezo wao ni mdogo kimtaji kama vile mwekezaji anayemiliki Kiwanda cha Nyamwezi. Kukosekana kwa mitaji hiyo, pia kumechangia kufungwa kwa kiwanda hicho mara kwa mara, pia kufanya wafugaji kukosa mahali pa kupeleka maziwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kutafuta wawekezaji ambao wanaweza kuweka kiwanda cha kusindika asali kwani Tabora ni centre ya mikoa jirani ambayo nayo wanayo asali kwa wingi kama vile Katavi, Singida na Kigoma. Hivyo basi, ni rahisi kwa mwekezaji kupata mahitaji ya kiwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Kiwanda cha Tumbaku, naishauri pia Serikali kuleta wawekezaji Mkoa wa Tabora ili zao la tumbaku lisindikwe kwa urahisi na kuondoa usumbufu kwa wakulima. Pia wananchi wa Mkoa wa Tabora kupata ajira na mikoa jirani kuliko ilivyo hivi sasa ambapo mazao yote hupelekwa Morogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iweke nguvu zote kwa kuwezesha bajeti ya viwanda vidogo vidogo (SIDO) kupewa fedha za kukuza uchumi kwa wajasiriamali, kwani SIDO imefanya kazi kubwa hapa nchini, imefanikisha kutoa elimu kwa wananchi wengi hapa nchini kwa kada mbalimbali hasa wanawake. Ofisi za SIDO zipewe vitendea kazi kama vile magari, vifungashio vya elimu ambavyo hujifunzia wajasiriamali hapa nchini.
Ombi langu kwa Serikali isaidie kiwanda cha SIDO ambacho hutengeneza sabuni, kusindika karanga, pia mikopo midogo midogo kilichopo Tabora; tumbaku ipewe kipaumbele kwa kutafuta wawekezaji kwani hulimwa Mkoa wa Tabora kwa 60%. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami kwa jioni hii ili niweze kutoa mawili, matatu, lakini ili kuweka record sawa jina langu sahihi naitwa Mwanne Ismail Mchemba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uwezo leo wa kuwa hapa na kuweza kupata nafasi ya kuchangia. Naanze na kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayofanya kuhusu suala zima la sukari. Nampongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la sukari tusiliangalie hivi hivi tu kwa lele mama, sukari inaathiri jamii nzima ya Kitanzania na ndiyo maana wanakamatwa sasa hivi kwa sababu ya laana ya Mwenyezi Mungu. Sukari hiyo inapofichwa inaathiri watoto, wagonjwa, wazee, wajawazito lakini siyo hilo tu kwamba eti kwa sababu ya mwezi wa Ramadhani, hawazidi kwa sababu ya mwezi wa Ramadhani; mpaka hivi leo ninavyokwambia kuna watu wanafunga. Kwa hiyo, inaathiri sehemu kubwa. Nampongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza Mawaziri; nampongeza Mheshimiwa Waziri Ummy na kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla kwa kazi nzuri wanayofanya. Imeonyesha tangu walivyoteuliwa kwamba hawa watu wanatosha. Ni tumaini langu kwamba Wizara waliyopewa ni sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuchangia. Maradhi ya wanawake yako mengi sana, ni vyema Wizara sasa ikaangalia kutoa kipaumbele kwa maradhi ya akinamama. Kwa mfano, kansa ya mfuko wa uzazi kwa wanawake ni tishio, ni balaa! Kuna kansa ya matiti nayo pia ni balaa! Kuna ugonjwa wa fistula, huo nao ni muziki! Watu wengi wanaachika kwa sababu hiyo. Bado elimu haijawafikia walengwa hususan vijijini. Vile vile kuna uvimbe kwenye tumbo la uzazi la wanawake; namwomba Mheshimiwa Waziri, magonjwa kama haya yapewe kipaumbele na kutoa elimu hususan vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza MEWATA. Mheshimiwa Waziri naomba Kitengo hiki cha akinamama walionesha ujasiri, MEWATA nadhani Serikali ingewapa support kubwa sana. Wamefika mpaka vijijini; ni Madaktari Bingwa ambao wamejiamini kuwasaidia wanawake. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri anaye Daktari, anajua umuhimu wa timu ya Madaktari wa MEWATA. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu, wodi za wazazi haziridhishi. Naomba wodi hizi ziangaliwe, zipewe kipaumbele, kwa sababu kuna matatizo makubwa, hususan vitanda vya kuzalia. Vitanda vya kuzalishia vijijini havipo? Anaambiwa tu kaa hapa, jipange na nini, wewe mama unajua, kwa sababu shule hii umeipitia, ni kiwanda nyeti. Kwa hiyo, naiomba Serikali kupitia mama yangu hapa iliangalia hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende moja kwa moja kwenye ukarabati wa majengo katika Hospitali ya Kitete, Tabora. Tuna matatizo! Kuna miradi ambayo ilishaanza, lakini haijakamilika. Naiomba Serikali ikamilishe miradi hiyo ili angalau sasa madhumuni ya kile chuo kuwepo yaonekane. Kuna wodi ambazo zipo hazijakamilika, nazo ni za akinamama, naomba Mheshimiwa Waziri, nilichangia kwa maandishi, lakini ziangaliwe pia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna tatizo kubwa la mashine ya kufulia nguo. Jamani, ile sasa hivi ni Hospitali ya Rufaa, hatuna mashine ya kufulia nguo na iliyopo ni ya zamani ukilinganisha na population ya watu sasa hivi, inahudumia Wilaya saba na wagonjwa wale wanakuwa referred kwenda pale, lakini mashine hakuna. Siyo hilo tu, pia uchakavu wa jiko, miundombinu yake ni ya tangu Ukoloni. Inawezekana hata mimi nilikuwa sijazaliwa bila shaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni vizuri Serikali ikaangalia, kwa sababu kuna watu wengine ambao wanatoka vijijini, hawana ndugu, lakini ameletwa pale kaachwa kwa sababu hakuna sehemu ya kuweza kusubiri wagonjwa. Kama chakula kitaandaliwa vizuri, basi hata wagonjwa wetu watapata nafuu. Kwa hiyo, uchakavu huo ni mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni uchakavu wa jengo la wagonjwa, sijui wanaitwa wagonjwa wa akili, sijui lugha gani nzuri…
Mheshimiwa Mwenyekiti, wale wenye matatizo ya akili, ile wodi ya miaka mingi! Miundombinu yake hovyo, hakuna vyoo, yaani wale tusiwa-dump, wale nao ni wagonjwa kama wagonjwa wengine. Magonjwa haya hayana kuchekwa, mtu unaweza kupata ugonjwa huo au akapata ndugu yako. Kwa hiyo, naomba nchi nzima kuwe na mradi maalum ambao unaweza kutembelea wodi hizo. Ni tatizo kwa kweli! Ukienda pale yaani mpaka utawaonea huruma, wale hawakupenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba na kusisitiza, wodi ya Kitete ya Kichaa, yaani ya wagonjwa wa akili, kwa kweli iangaliwe vizuri ili waweze kupata msaada, hawakupenda. Kwa hiyo, nilikuwa nataka nilisisitize hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nataka kuzungumzia makazi ya wazee. Makazi ya wazee, nachukulia ya kwangu Mkoa wa Tabora kwa sababu nimezungukia, hayafai jamani. Tunaita makazi ya wazee lakini yalikuwa ya aina mbili; kuna wale ambao walikuwa na ugonjwa wa ukoma, waliambiwa wasitiriwe wakae mahali pamoja kwa ajili ya matibabu. Kuna wazee ambao hawajiwezi, nao makambi yao yapo, lakini huduma yao hafifu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, huduma kwa wale wa makambi ya wenye ugonjwa wa ukoma, wale jamani vifaa vingine vinafanya kazi. Ni wazima! Wamezaa na wanazaana na kuna watoto na wajukuu. Kwa hiyo, kama mna hesabu ya wazee, basi wapo wengine kwa sababu kazi ile wanafanya bado. Kwa hiyo, wanazidi kuzaana. Ukienda Kambi ya pale Ipuli kuna watoto wadogo, kuna vijukuu vipo mle. Kwa hiyo, naomba wasihukumiwe kwamba ni wazee, lakini bado mambo mengine wanaendelea nayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie Sheria ya Ndoa. Tumeambiwa kwamba Sheria ya Ndoa inafanyiwa marekebisho, lakini mpaka ikifika kufanyiwa marekebisho, akinamama wameumia, kwa sababu sheria ile inasema unapodai fidia ya mtoto, unalipwa sh. 100/= kwa sheria ya zamani. Kwa hiyo, akinamama wanateseka. Sheria hiyo pia gharama za fidia kwa akinamama wajane napo kuna matatizo wanapokwenda Mahakamani. Kwa hiyo, naomba pia sheria hii iangalie pia na mazingira ya wajane na mazingira ya watoto, kwa sababu ndoa zinapovunjika watoto wa mitaani wanakuwa wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba suala hili la sheria hii ya mwaka 1971, Mheshimiwa Waziri ashirikiane na Mheshimiwa Waziri wa Sheria ili iweze kufanya kazi yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la Maafisa wa Ustawi wa Jamii. Kwa kweli naomba wapewe vitendea kazi; wanunuliwe basi hata pikipiki ili waweze kuzunguka vijijini. Kama tunasema bajeti finyu, lakini hawa watu hawawezi kufanya kazi inavyotakiwa, inakuwa ni ngumu sana kwa sababu hawa watu ndio tunaowategemea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nizungumzie kuhusu Benki ya Wanawake, nawapongeza. Benki ya Wanawake ni mwanzo, tuliianzisha mwaka 2009. Walioanzisha Benki ile kwa kusaidiana na Serikali walikuwa Wabunge wa wakati ule, walichangia sana. Nampongeza Mama Chacha kwa kazi nzuri anayofanya ila tuendelee kumwomba kwanza riba ipungue, lakini waende mikoa yote na ndiyo ilikuwa azma yake, kwamba wafungue madirisha kila mkoa ili angalau watu waende kwenye dirisha kwenye mabenki yale wafaidi, lakini sasa hivi wanafaidi upande mmoja tu na ndiyo ambao wanapata mkopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mikopo asilimia 10, naomba Mheshimiwa Waziri, kwa sababu nayo hiyo huduma ya wanawake iko kwake, hatupewi, asilimia 10 haifiki! Kwa sababu kinachotakiwa, kweli sisi ni Madiwani kwenye maeneo husika, lakini inapofika kwamba bajeti finyu…
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja asilimia mia kwa mia. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nitangulize shukurani za pekee kwa kupata nafasi hii kwa muda huu wa asubuhi. Pia nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kunifikisha siku hii ya leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie kwa kutanguliza pongezi lakini nitachangia kwa kuanza na TAMISEMI na badaye Utawala Bora. Tuliponadi sera mwaka 2015 tulikuwa na wasiwasi mkubwa sana kuhusu Mheshimiwa Rais wetu kwa sababu wakati anazunguka Tanzania nzima alinadi na alikuwa na uhakika bila uwoga. Kwa hiyo, nampongeza sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kumpongeza huko niseme alisema hivi, naomba Watanzania wenzangu mnipe nafasi niweze kuongoza nchi hii kwa uchungu niliokuwa nao na Watanzania kwa umaskini wao. Sasa hiyo ilitia mashaka kwamba watu wangemnyima kura kwa sababu alisema atapambana na mafisadi, bandari, rushwa na ubadhirifu wa aina yoyote katika nchi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa basi kwa sasa kiongozi huyo ametimiza matakwa yake kulikuwa na wasiwasi wakati ule kwamba angenyimwa kura lakini alisema itakavyo kuwa na iwe lakini niwatendee haki Watanzania wangu. Hivyo basi, nichukue nafasi hii kumpongeza sana, naomba aendelee hivyo hivyo, jina lake kubwa na Watanzania wana imani kubwa naye.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimpongeze Makamu wa Rais, mwanamke anaweza na amejipanga. Pamoja na kwamba ni mwanamke ameweza kuzunguka nchi nzima, nampongeza sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini si hilo tu, nawapongeza sana Mawaziri pamoja na Manaibu wote wasiogope, kazi wanayofanya wananchi wanaiona na wanamsaidia Rais ipasavyo. Mawaziri hawa wanafanya kazi kiasi ambacho hata sisi tunaona na tunawapenda na tunawaamini kwamba watafanya kazi hiyo hadi miaka mitano na 20 ijayo. Wasiogope kama mahali pa kutumbua majipu watumbue haiwezekani hata kwenye Halmashauri Rais akatumbue majipu wao ndiyo watumbue majipu hayo kama walivyoanza na watumishi hewa, walikuwepo kweli lakini Mheshimiwa Rais anawatumbua.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niwapongeze Marais waliotangulia wa Awamu zote Nne kazi waliyofanya imeonekana mpaka tumefika hapa leo. Kwa hiyo, nawapongeza sana Marais wote, Rais wa Awamu ya Nne kazi aliyofanya imeonekana na leo Mheshimiwa Rais ameipokea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuchangia kuhusu TAMISEMI. Kazi kubwa tumeifanya kwenye Kamati kwa sababu na mimi ni Mjumbe wa Kamati hii, kwa hiyo niwapongeze Waziri wa TAMISEMI na Naibu wake kwa ushirikiano waliotuonyesha lakini ninayo machache ya kuongezea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna miradi ya Awamu ya Kwanza na ya Pili ya TASAF ambayo haijakamilika. Kwa sababu iko chini yao naomba waikamilishe ipasavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia wenzangu wamezungumzia kuhusu posho ya Madiwani, kweli ni ndogo. Naomba yatolewe maelekezo kwa sababu posho anayolipwa Diwani hailingani na kazi anayofanya, pesa yao ni ndogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine, Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji, hawa nao waangaliwe kwa jicho la huruma. Watu hawa kazi wanazofanya wanatuwakilisha pia sisi Wabunge tuliomo humu ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, asilimia 10 inayotengwa na Halmashauri zetu na Manispaa haijatiliwa mkazo pamoja na kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu aliizungumzia alipokuwa Lindi. Asilimia 10 inatolewa kama zawadi wakati si kweli. Ningemuomba Waziri asichoke, asisitize, atoe waraka mgumu ili watu wajue kwamba ni haki ya Watanzania wote kupata asilimia 10 bila kujali itikadi za watu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika vikundi hivyo vinavyopata hiyo asilimia 10 ningeomba Serikali iangalie vikundi vya akina mama wajane. Fedha hii wanapewa tu vikundi vyote lakini kuna vikundi ambavyo vimesajiliwa vya akina mama wajane navyo viangaliwe kwani wanatia huruma kwa sababu wengine wamenyimwa haki zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, si hivyo tu, hata hii shilingi milioni 50 ilenge pia kwenye vikundi hivyohivyo ambavyo vipo lakini mkisema kwamba vianzishwe harakaharaka kuna vingine vitaanzishwa ambavyo havistahili kupewa. Ningeweza kuchanganua sana lakini kwa sababu ya muda naomba niseme asilimia 10 haitolewi kama inavyotakiwa. Mtu anatoa asilimia 2, asilimia 3 kama mfano tu. Kwa hiyo, naomba Wizara husika iweze kutia mkazo katika jambo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie kuhusu ukusanyaji wa mapato. Tulishazungumzia sana kuhusu masuala ya minara, mabango, ushuru huo umeachiwa tu wananchi, wao wamepata mwanya wa kwenda kukusanya kule kodi zao lakini wanapeana kienyeji mno, sheria ya Halmashauri ingeweza kutumika katika suala hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu bima ya afya, kuna vituo vingine vya afya na zahanati zake havina umeme na bado REA haijafika. Naomba katika maeneo hayo basi kuwe na utaratibu wa kuweka solar.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niende kwenye Menejimenti ya Utumishi wa Umma. Naomba Mheshimiwa Waziri azisaidie ofisi zote ambazo ziko chini yake, Tume ya Utumishi na kadhalika, kwa mfano, Idara ya Kumbukumbu za Nyara za Serikali, asipotimiza hili nalolisema nitaishika shilingi ya mshahara wake. Tulitembelea eneo hilo tukakuta wafanyakazi wako katika mazingira magumu sana, hakuna AC, kuna chombo ambacho kimeharibika takribani miaka miwili inahitajika shilingi milioni 26 tu lakini mpaka leo haijatolewa. Sehemu ile ni nyeti, ina kumbukumbu nzuri za Taifa hili ambazo ni za kizazi na kizazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tulitembelea masuala ya TASAF III, tumekwenda Kigoma, Mwanza, watu waliopewa sio walengwa na hawa wote wako chini ya TAMISEMI. Ofisi zao ziko chini ya TAMISEMI, watendaji wako chini ya TAMISEMI, wamepewa ambao sio walengwa. Kwa hiyo, nashauri pia hili nalo liangaliwe vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, Tume hizi za chini ya Ofisi ya Rais mpaka leo zinapanga na wanalipa kwa dola, ni hasara. Ni vyema Serikali ikajipanga wawe na majengo yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niiombe Serikali inapofanya marekebisho mbalimbali ya kupandisha vyeo, mishahara iende sambamba na kupewa pesa zao. Kuna watu wamepandishwa vyeo lakini mpaka wamekufa hawajapata hela zao na hao walioachiwa sio rahisi kufuatilia. Kwa hiyo, ucheleweshwaji wa ongezeko la mishahara nayo ni kero kwa Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kuhusu uhamisho. Uhamisho unapotolewa ni vyema basi uambatane na pesa inayokuwepo kwenye bajeti. Kama tusipofanya hivyo ina maana bado tutaendelea kuwa na madeni na malimbikizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine…
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa heshima na taadhima, naunga mkono hoja asilimia mia kwa mia. Ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsate kwa kunipa nafasi na mimi nichangie kidogo hotuba ya Waziri wa Fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama hapa siku hii ya leo. Lakini kubwa nimpongeze Waziri wa Fedha na timu zake zote kwa kazi nzuri waliyoifanya. Kwa kweli hotuba nzuri na mwelekeo wa bajeti hii ni mzuri, angalau unaweza ukapunguza makali ya umaskini wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Hotuba ya Waziri wa Fedha nimeona kuna asilimia tano ya mapato ya Halmashauri zetu nchini ambao huwa wanatenga asilimia 10 vijana asilimia tano na wanawake asilimia tano.
Mheshimiwa Waziri wa Fedha, mimi nikuombe, chonde chonde asilimia hii tano ni ya miaka dahari na dahari iko pale pale tunaondoaje umaskini na tunapunguzaje umaskini? Lakini kama tuna nia ya dhati ya kupunguza umaskini; katika hotuba yako umesema ongezeko la makusanyo ya mapato yetu limeongezeka kwa kutokana na haya yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza mianya ya rushwa imezuiliwa, wafanyakazi hewa mshahara wake upo umeingia kwenye mapato, wakwepaji kodi ambao walikuwa wanakwepa mpaka kuingiza makontena hela yake ipo, mapato ya gesi na cement viwanda vyake vipo. Mimi nikuombe Mheshimiwa kwa heshima na taadhima kubwa hebu muangalie sekta hii ya waakina mama na vijana ajira haipo, lakini tunapobana tu asilimia tano umekuwa wimbo wa Taifa na Halmashauri hizo asilimia kubwa hawakidhi viwango vya kupeleke hii asilimia 10. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi nimuombe Mheshimiwa Waziri, yeye kwa huruma yake atusaidie kwa hilo ili angalau sasa aongeze kwa njia moja au nyingine anavyoona yeye inafaa kwa mapato haya mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nizungumzie shilingi milioni 50. Kuna Mbunge mwenzangu hapa amezungumzia; kwa sababu tukiipeleka kwenye SACCOS moja kwa moja yatarudi yale ya Mfuko wa Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete, kwa sababu wajanja wote ndio wenye SACCOS, vijijini kule hawana SACCOS, sasa inakuwa ni masharti makubwa kiasi ambacho watanuafaika watu wachache. Mimi nadhani Serikali ina wataalamu wazuri wa maendeleo ifanye utaratibu isifanye haraka ya kusambaza hela kupitia SACCOS. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna Wenyeviti wa Mitaa, tuna Makatibu tarafa Wakuu wa Wilaya ndio wanaohodhi eneo la kijiji chote. Mimi ningeomba kabla hamjafanya maamuzi ya kupeleka kwenye SACCOS mimi naomba pesa hizi ziende kwa utaratibu wa vijiji, pia kila Jimbo wapewe maana ndiyo tupo shuleni sasa, ya kwanza ilipita free, sasa hii maadamu tunaipigia sasa; na kwa kuwa Rais hakutoa ahadi mijini, amepita kwenye kampeni yake vijijini kote pamoja na Mheshimiwa Makamu wa Rais; isiwe kwa kuwa wale wa mjini kwa sababu ndio wenye SACCOS nyingi wapate, vijijini ambapo hakuna wakose. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naomba hilo liangaliwe sana kwa sababu tuna mengi ya kuongea, lakini niombe hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine afya. Mheshimiwa Waziri wa Fedha mimi niombe katika fedha za mwaka huu Wizara ya Afya tuna miradi mingi ambayo haijakamilika, tuna zahanati nyingi zimejengwa na zina hospitali ambazo zimejengwa hazina theatre, kuna wafadhili wamekuja wameweka vifaa vyao hivi mnawaambiaje? kwa sababu kila mwaka watafuatilia pesa zao ziko pale lakini mnasema daktari wa usingizi hayupo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano kama Zahanati ya Bukene Mawaziri wote wamepita pale wameiona waakina mama wanakufa, hivi unapunguzaje vifo wakati ipo tayari vifaa vya kisasa ambavyo hata Muhimbili hawana, Bungando hawana vipo pale kwa ajili ya kuokoa maisha ya mama na mtoto. Kwa hiyo, mimi niombe kipaumbele Wizara ya Afya iangaliwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mimi nimeangalia kitabu hiki katika kupunguza kodi, kuondoa misamaha bado hujatoa misamaha kwa nguo za akina mama, kwa lugha nyingine mataulo yao bado sijaiona. Kuna wanafunzi wanashindwa hata kununua pedi, leo hakuna uondoaji wa kodi. Mimi ningeomba Serikali hata hii inapata kigugumizi gani kutoa iondoe kodi ili angalau viweze kuingia kwa urahisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nizungumzia tozo nyingi za tumbaku. Hivi unaweka tozo nyingi za tumbaku halafu unasema unamsaidia mkulima? Mheshimiwa Waziri wa Kilimo liangalieni hili mnapokaa kwenye Baraza la Mawaziri, tozo ni nyingi hazifai, wakulima wanazidi kuwa maskini, kilimo chenyewe cha mkono lakini hawapati msaada wowote kutoka Serikalini. Mimi naomba Serikali iangalie sana suala zima la tumbaku. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia pamoja na hayo sekta hii imetengwa haisaidiwi na Serikali, hawa wanunuaji wa tumbaku wanajipangia wenyewe bei, wanaamua juu ya soko wanavyotaka wenyewe. Waziri wa Fedha utapataje ongezeko la pesa ikiwa wakulima wa tumbaku wananyanyaswa ambao asilimia 60 ya tumbaku wanayolima inasaidia mapato ya Serikali? Kwa hiyo, hilo nalo ningeomba Serikali muangalie tuna hali ngumu sana huku wakulima wa chini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee habari ya maji. Ukigusa umegusa wanawake, akina baba wote humu mnafuliwa nguo na akina mama, mnapikiwa na akina mama, lakini wao ndiyo wanahangaika na maji. Leo hakuna bajeti inayoeleweka ikaambiwa kwamba hii ni bajeti ya maji. Mheshimiwa Waziri, mimi nimesikia sana hotuba zako, umesifia wanawake, umewaonea huruma wanawake, sasa huu Mfuko wa Maji Vijijini toka kwenye 50, weka kwenye 100 hili suala usisumbuke...
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi kwa Mheshimiwa Profesa Jumanne Maghembe, Waziri na Naibu Waziri Engineer Ramo Makani, Katibu Mkuu na watumishi wote kwa hotuba nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iangalie uharibifu wa misitu kwa uvamizi wa wafugaji kwani kila wanapofika sehemu hukata miti yote. Kwa mfano, Kizengi, Bukene, Urambo, Bukumbi, Kitundo na kadhalika. Pia ukataji miti kwa kuchoma mkaa ni tatizo hivyo Serikali iangalie upya sheria zilizopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ufugaji nyuki, elimu itolewe kwa wajasiriamali ili wafuge kisasa kwa kutumia mizinga ya kisasa. Wajasiriamali hasa wanawake wakopeshwe mizinga ya kisasa kwa bei nafuu. Kuanzisha kiwanda cha kusindika asali kama ilivyokuwa zamani kwani Tabora ina historia ya kurina asali. Pia kiwanda hicho kinaweza kutumika kama Kanda ya Magharibi, Singida, Tabora, Kigoma na kadhalika kwa kusafirisha nje ya nchi pia kusindika nta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Chuo cha Nyuki tuombe chuo hicho kitambuliwe rasmi ili wanafunzi hao wanapohitimu mafunzo haya wapewe ajira kwani mpaka sasa ajira zao ni za kujitegemea, ni vyema sasa ajira hizo zilingane na vyuo vingine. Wanachuo hao wapewe vitendea kazi kama vile mizinga ya kisasa ili wakatoe elimu darasa maeneo mengine. Ukarabati wa chuo hicho niombe uendelee kwani maeneo mengi ni machakavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya makumbusho; katika Mkoa wa Tabora katika Kata ya Kwihara kuna makumbusho ya kihistoria ya kumbukumbu za Dkt. Livingstone, Stanley, Said Ibin Batuta, waliokuwa watu maarufu kihistoria. Ni vyema eneo hilo pia likatangazwa kama utalii. Pia kuna majengo ya Ujerumani ambayo yana historia, ni ya maajabu. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MWANNE I. NCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi kwa Mheshimiwa Waziri, Balozi, Dkt. Augustine Philip Mahiga, Naibu Waziri Dkt. Susan Kolimba na Katibu Mkuu wa Wizara kwa hotuba nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara yetu iangalie sana mipaka yetu ambayo ina vichocheo vingi na ambavyo wahamiaji haramu hupenya hasa kwenye mipaka ya Kenya na Tanzania kwa kupitia njia za Arusha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu masoko ya ujirani mwema; elimu itolewe. Hapa nchini kuna wafanyabiashara wadogo ambao wanasafirisha bidhaa zao kama mahindi, mpunga, kahawa, chai ili wafanye biashara kwa weledi, kwani mikoani hakuna elimu ya kutosha. Waheshimiwa wetu ambao ni Wabunge wa Afrika Mashariki wapewe uwezo wa kuzunguka nchi nzima kutoa elimu hata mashuleni na vyuoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la utumishi; Wizara hii iwasiliane na Wizara ya Mambo ya Ndani kuongeza Watumishi wa Uhamiaji ili ajira iongezeke na kusaidia kulinda mipaka yetu kwani mpaka sasa bado watumishi hao ni wachache. Pia suala la utalii Waheshimiwa Mabalozi watangaze vivutio vyetu vilivyopo nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia maneno mawili, matatu hususani kuhusu viwanda na mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote mimi nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya, lakini nitoe masikitiko yangu makubwa, kama leo Baba wa Taifa ingekuwa kuna jambo la kusema anaweza akasimama akauliza, angeuliza habari ya Tabora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tabora tuna mateso sana, tulikuwa na viwanda vifuatavyo kwa sababu ni dakika tano lakini nilikuwa nimejipanga kwa dakika kumi ningeeleza nadhani leo Mheshimiwa Waziri yangemuingia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Tuna Kiwanda cha Nyuzi na Mheshimiwa Riziki amesema, kiwanda hiki kimehujumiwa na wawekezaji. Wamechukua kila kitu hata kama tunakwenda kwa science na teknolojia wameondoa vifaa vyote na wametapeli, mimi ninasema kwa lugha nyepesi, wametapeli. Tangu wamechukua hawajafanya chochote; kwa hiyo hata tukisema zao la pamba liweze kuimarishwa hakuna, tulikuwa tunatengeneza nyuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti lakini tuna Kiwanda cha kusikitisha sana cha Manonga, Mheshimiwa Waziri anajua kipo Igunga. Kiwanda hiki alikuwa amechukua Rajan. Mimi mwaka 2006 nikiwa Mbunge niliwahi kuuliza swali, lakini huyu mwekezaji Rajan amefariki, wamechukua watoto wake, bado kuna usumbufu mkubwa tangu mwaka 1999 kiwanda kile kimefungwa. Ni uchungu mkubwa sana wa unyanyasaji wa Mkoa wa Tabora. Lakini pamoja na hayo, Mheshimiwa Waziri anajua, tulimuomba awakutanishe Rajan pamoja na Igembe Nsabu, hajafanya hivyo na alitoa ahadi ya kwenda kuongea nao, nina uchungu sana, inasikitisha na inakatisha tamaa.
Mheshimiwa mwenyekiti, si hilo tu, Mheshimiwa Waziri alisema katika Bunge lako hili wakati tunauliza swali na alisema wawekezaji wa Kichina wameishia airport, sasa hivi mpaka leo bado wameishia airport? Inasikitisha, leo nipate majibu kama kweli wawekezaji hawa wapo au hawapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vigezo vya kutafuta wawekezaji Tabora inayo, jinsi ya kuiuza Tabora ipo. Tuna masuala ya tumbaku, tuna masuala ya urinaji wa asali. Hivi asali yote inayotoka nchi nzima hii inatoka Tabora bado hakuna uwezekano wa kuweka kweli? Mheshimiwa Waziri, namheshimu sana naomba aangalie hilo.
Mheshimiwa Mweyekiti, lakini nizungumzie habari ya mazingira. Tabora inalima tumbaku, lakini hawa wanunuzi hawana mpango wa kuhakikisha mazingira endelevu yapo katika Mkoa wa Tabora. Kwa nini nasema hivyo? Wanabeba mbegu za miche, wanatupa kuwapa…….
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru nami pia kwa kunipa nafasi nichangie hotuba ya Waziri Mkuu. Kwanza nianze na pongezi. Nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu kwa kazi nzuri anayoifanya, asirudi nyuma, ana uhakika na kitu anachokifanya nasi tunamuunga mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Waziri Mkuu kazi aliyoifanya katika nchi hii ni kubwa sana, siyo hilo tu uamuzi wake wa kuhamia Dodoma inataka ujasiri, ametekeleza jinsi Mheshimiwa Rais alivyosema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze tena ndugu yangu Mheshimiwa Jenista Mhagama, amesimamia vizuri sana uanzishwaji wa Makao Makuu na Serikali kwa ujumla akiambatana na Naibu wake Mheshimiwa Antony Mavunde.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sitatenda haki kama sitatoa pongezi kwa Mheshimiwa Spika, Naibu Spika, wewe Mwenyekiti na Viongozi wote ambao wameweza kufanya kazi ya Bunge hadi sasa tuko vizuri ingawa Bunge lilikuwa katika hali ngumu. Nimpongeze sana Mheshimiwa Katibu wa Bunge Dkt. Thomas Kashilillah amefanya kazi nzuri, tumetembea, tumefanya kazi kwenye miradi na Kamati zimekwenda vizuri, niwapongeze sana kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya ya kuisimamia Bunge. Pia nimpongeze tena AG kwa kazi nzuri ya kusimamia sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo, niwapongeze Mawaziri wote, wamezunguka Tanzania hii kuhakikisha Ilani ya Uchaguzi ya CCM inafanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie hoja sasa ya kuchangia Bajeti hii. Mimi nichangie moja kwa moja kuhusu viwanda, bahati nzuri au mbaya Waziri wa Viwanda hayupo. Tabora tuna matatizo makubwa sana ya viwanda, tulikuwa na kiwanda cha nyuzi hakipo, nimpongeze Waziri wa Viwanda amesema kwamba wako njiani na yule Mwekezaji anakuja kuzindua kiwanda hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda hicho kinasikitisha, kina historia kubwa sana katika Mkoa wa Tabora, kiliwezesha kuwapa ajira vijana wetu lakini sasa tumerudi kwenye umaskini. Tuna kiwanda kingine cha Manonga, kila siku nazungumza na sitachoka kuzungumza. Kiwanda cha
Manonga cha Rajan mpaka sasa kina matatizo ambacho kiko Wilaya ya Igunga. Naomba katika uwekezaji sasa iangalie suala zima la viwanda katika Mkoa wa Tabora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunasindika asali, tunarina asali nyingi sana katika Mkoa wa Tabora na zamani tulikuwa na kiwanda cha Kipalapala ambacho kilikuwa kinasindika mpaka tunauza nchi za nje lakini kimekufa, kwa hiyo natangaza soko na ombi la wawekezaji kama watakuja kuwekeza ardhi ipo na ipo ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kidogo suala zima la afya. Tuna tatizo sana la hospitali za Wilaya, Manispaa ya Tabora, Kaliua, Uyui mpaka sasa Hospitali za Wilaya hazipo. Niombe Serikali iangalie kwa jicho la huruma kwa sababu tabu wanayopata wananchi wa maeneo hayo Mheshimiwa Waziri Mkuu aiangalie. Wilaya ya Kaliua haina Hospitali ya Wilaya, wanakwenda Urambo kutibiwa lakini wazingatie pia
kwamba kuna huduma ambayo inatakiwa akinamama na mtoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Igunga kuna kituo cha Afya ambacho ni cha Jimbo la Manonga. Kimekamilika, kilikuwa kimefadhiliwa na ADB mpaka sasa hakifanyi kazi, hakuna vifaa vya kufanyia kazi, hakuna gari la wagonjwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala zima la maendeleo kwenye maeneo yetu. Serikali imefanya kazi kubwa sana kuondoa umaskini kwenye kaya maskini hususan TASAF, imefanya kazi nzuri sana. Imezunguka na imesaidia miradi ya awamu ya kwanza na ya pili ambayo haijakamilika tungeomba sasa awamu ya tatu Serikali iangalie na ikamilishe miradi yote hususan vituo vya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe sana Serikali kusimamia na kuhakikisha mradi wa MKURABITA unakwenda vizuri na wanapewa pesa za kutosha ili angalau wapunguze umaskini kwenye kaya ambazo ziko chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie asilimia 10 ya Wanawake na Vijana, Serikali imefanya vizuri. Niwapongeze Wakuu wa Mikoa, niwapongeze Halmashauri na Majiji nchi nzima, kwa sababu naomba nichangie kama Makamu Mwenyekiti, nina uhakika na ninachokizungumza kwa sababu wamekuja kwenye Kamati yetu, tumeona bajeti waliyopanga na mafanikio yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, karibu Halmashauri zote zimetenga asilimia 10 kwa sababu mwaka 2016/2017 tuliwapa masharti kama Kamati, wamefanya kazi nzuri, nawapongeza na kwenye bajeti wameonesha. Kwa hiyo, kazi wanaifanya, hatuwezi kusema hawafanyi, asilimia 10 ipo.
(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna baadhi ya Halmashauri imeweza kutenga katika asilimia 10 imesaidia makundi maalum. Kwa mfano, Tanga tumekuta wale wenzetu kwenye makundi maalum wasiosikia wametengewa fedha. Kwa hiyo, niiombe Serikali iangalie jinsi gani ya kutenga asilimia 10 angalau asilimia mbili waweze kupata wenye makundi maalum. Ukurasa wa kumi na sita Mheshimiwa Waziri Mkuu amesema, naungana naye na ni kweli hii fedha imetolewa, tuombe tu Serikali iangalie ni jinsi gani sasa ya kusaidia kuhakikisha fedha zile zinaongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni barabara niipongeze sana Serikali, barabara ya kutoka Itigi kwenda Tabora imetengewa fedha, lakini bado kazi ile inasuasua. Kwa hiyo niombe barabara ya kutoka Chaya kwenda Tabora ipewe kipaumbele. Niombe tena barabara ya kutoka Puge kwenda Ndala, Nkinga hatimaye Manonga, hii barabara tumeiombea sana iweze kutengenezwa, Nkinga kuna hospitali kubwa sana ambayo inasaidia wananchi wa Mkoa wa Tabora kwa ujumla. (Makofi). Kwa hiyo, niombe sana Serikali iangalie… (Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi kwa Mheshimiwa Ummy A. Mwalimu (Mb), Waziri, Mheshimiwa Dkt. Hamisi Kigwangalla (Mb), Naibu Waziri na ndugu Katibu Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto zilizopo ni pamoja na vituo vya wazee katika makambi; ni muhimu majengo yao yakarabatiwe, wazee wasiojiweza waingizwe kwenye mpango wa TASAF ili kuipunguzia mzigo Serikali, kuwe na huduma ndogo za upatikanaji wa dawa kwenye maeneo ya makambi angalau duka dogo, kwani uwezo wa kufuata dawa kwenye zahanati ni mdogo, Wizara ishirikiane na TAMISEMI kuhakikisha wanajenga x–reter (kuhifadhi kondo la uzazi) kwenye zahanati na vituo vya afya ni tatizo kwani kwenye vituo hivyo wakazi wengi wanalalamika kuwa mbwa wanachukua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa vyumba vya akina mama wanaokwenda kusubiria kujifungua vipewe kipaumbele kwa kutoa msisitizo, vifaa tiba kwa wazazi na watoto vipewe kipaumbele hasa gloves, dawa za kuzuia damu kutoka kwa wingi, kuwepo na wodi maalum ya kuwalaza wanawake wenye ugonjwa wa saratani mikoani na kupeleka dawa za kupunguza maumivu, elimu iendelee kutolewa kwa ugonjwa wa fistula hususan zahanati na vituo vya afya, ugonjwa wa tezi dume.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza kwa ukarabati wa ujenzi wa wodi ya wanawake ya upasuaji katia Hospitali ya Bombo – Tanga, iko vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Benki ya Wanawake, waandae utaratibu na kupelekwa mikoa yote kwani si Dar es Salaam peke yake au mikoa mikubwa yenye Majiji, hata Tabora tunao uwezo. Kwa kuwa mimi ni mwakilishi ambaye nilitoa shilingi 2,000,000 mpaka sasa sijaona faida yoyote, niombe maelezo ya hisa zangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi nichangie Wizara hii kwa uchungu kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara kwa mara nikisimama hapa huwa nasikitika, nasikitika sana kwa kuusahau Mkoa wa Tabora. Awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri anayofanya. Mheshimiwa Waziri mimi nina sababu ya kumpongeza. Mwaka 2006 alifanya kazi ambayo Tabora hawatamsahau, nataka nimkumbushe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Chuo cha Nyuki Tabora, chuo hiki kiliondolewa kikapelekwa Arusha. Mwaka 2006 nilimwomba sana Mheshimiwa Waziri na mimi nilikuwa Mbunge na yeye wakati ule alikuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, akakubali akakirudisha. Pamoja na kurudisha mimi nikawa Mwenyekiti wa Bodi, nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kushangaza, tangu 2006 hakuna mabadiliko. Niliomba sana ukarabati wa jengo la utawala ambalo lilikuwa na maabara ndani yake, jengo hilo limejengwa tangu 1949, kwa hiyo ujue umuhimu wa chuo hicho tangu Mkoloni. Mimi simlaumu, inawezekana wataalam nao wana matatizo na Tabora. Kupeleka Chuo cha Nyuki Tabora kulikuwa na sababu za msingi sio upendeleo, kule tunarina asali yaani sisi ni wafugaji kabisa wa nyuki na Tabora kuna miti ambayo inaitwa miombo ambayo ina maua mazuri, lakini nashangaa bado kinapigwa danadana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tabora kuna asali ya nyuki wadogo kwa hiyo wanapokitangaza Chuo cha Nyuki cha Tabora maana yake unatangaza na biashara ya asali lakini wameondoa, hakuna ukarabati wowote. Nimeangalia kwenye kitabu hapa. Mwaka jana ilitengwa shilingi milioni 500 lakini mwaka huu shilingi milioni 200 lakini ni pamoja na Chuo cha Misitu Arusha. Sasa hapo sijajua kama kweli Tabora watapata siyo rahisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la kusikitisha sana na ambalo linauma, tulikuwa na TAWIRI-Tabora, kituo cha wataalam wa utafiti kuhusu nyuki na mizinga ya kisasa yenye tija, nacho wamekiondoa wamekipeleka Arusha, hivi Waziri anajua hilo? Kwa hiyo, nimekuja mwaka huu nianze tena kumwomba kituo cha utafiti kirudi Tabora, hivi inawezekana? Nimwombe Mheshimiwa Waziri, namheshimu na najua kazi anayoifanya lakini kuionea Tabora nachukia sana, hiyo itasababisha na mimi nimchukie. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini siyo hilo tu mpaka gari imeondolewa imepelekwa Arusha, Waziri ana habari hiyo? Watafiti wa TAWIRI wako pale lakini wameondoa mpaka komputa. Mimi nilienda wakati ule kutembea nikakuta wanafunzi wa Arusha wanakuja kuchukua practical Tabora. Nikauliza swali humu ndani, hivi inakuwaje gharama hii, wanataka Arusha wanakuja Tabora? Wameacha kabisa na kukitangaza kwani miaka ile walikuwa wanakuja watu kutoka Ethiopia, Zimbabwe kujifunza sasa hivi wamewaondoa, sababu ni nini, hawaitaki Tabora? Leo nimwombe Waziri anisaidie kwa nini wanaidharau Tabora na kwa nini wanahamisha vitu vilivyowekwa Tabora kupeleka Arusha? Wote tuhamie Arusha? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika kitabu hiki hiki cha bajeti hela za ukarabati zimeenda Njiro lakini Tabora hakuna, ukisoma humu unaona kama ukarabati upo lakini haupo. Naomba Waziri akija kuhitimisha alizungumzie suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna wazabuni wanadai hebu aangalie hilo ni haki yao lazima walipwe. Wanadai madai yao ya 2016, Waziri akisimama hapa lazima aseme kitu chenye uhakika, naomba afuatilie hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nahamia Malikale kwenye suala zima la utalii. Watu wanaidharau Tabora lakini ina kumbukumbu nyingi. Ukizungumzia utalii Tabora kwamba haupo, zamani nilikuwa silalamiki sana kwa sababu miundombinu ilikuwa hakuna, leo Rais kaleta ndege kwa hiyo lazima niseme ili vile vivutio ambavyo wamevisema kwenye taarifa ya Kamati na yeye mwenyewe amesema kwamba tujitahidi ila sijui lugha ya kwenda kuongelea kutafuta watalii kwa sababu ingekuwa kama kuna sehemu ya kwenda kujifunza mimi ningeenda kutafuta watalii ili waende Tabora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tabora kuna kumbukumbu ya Livingstone na Stanley na ukiongelea Tabora unaongelea na Kigoma-Ujiji, hivi navyo siyo vivutio hivyo? Tabora kuna eneo ambalo alikaa Livingstone walipokutana na Stanley wakitokea Kigoma eneo la Kuyara, nayo ni kivutio cha utalii. Nimwombe Waziri atume delegation yake iende ikaone halafu baada waitangaze. Pia Livingstone alikaa Ujiji karibuni miaka 27, njia aliyopita ni Tabora na aliacha alama. Jamani naomba niwarudisheni shule ili mjue historia ya Tabora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tabora kuna majengo ya Wajerumani kama ilivyo Amboni (Tanga), kuna kumbukumbu ziko pale lakini nani atazisemea? Leo bajeti ya Wizara ya Maliasili imeanza leo na mimi naitangaza Tabora kama sehemu ya utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna njia ya watumwa kwa sababu ilikuwa watumwa wakitoka Kigoma wanakuja Tabora wanakwenda Bagamoyo. Juzi tulipokuwa kwenye semina, Tabora haimo kwenye hiyo kumbukumbu ya Malikale, sasa leo naitangaza Waziri aikumbuke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini siyo hilo tu, tuna kumbukumbu nzito sana katika dunia hii ya Hayati Baba wa Taifa. Wanafunzi wanasoma shuleni lakini hata utalii wa ndani unatosha kuwapeleka Tabora. Baba wa Taifa alisoma Tabora Boys, akafundisha Mirambo lakini wakati wa kupigania usalama wa nchi na uhuru umeanzia Tabora, jamani hii nayo inataka mtu kwenda shule kwa ajili ya kuitangaza tu Tabora? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini uhuru huo ulisaidia pia kuwa na karata tatu za kuunda Serikali pale Tabora… Mwaka 1958, wenzangu wananiunga mkono, hiyo historia inatakiwa isomeke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia pale Tabora kuna shule ya msingi inaitwa Town School, ndipo alipokuwa anakutana na Wanyamwezi wakarimu sana, wanamfundisha, anajificha… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto za Mkoa wa Tabora ni kama zifuatazo:-

(i) Ukarabati wa jengo la utawala na maabara katika Chuo cha Nyuki Tabora ili kiwe cha kisasa;

(ii) OC kwenda kwa wakati, pia malipo ya wazabuni yaangaliwe;

(iii) Kutangaza Chuo cha Nyuki, nchini na nje ya nchi ili kupata wanafunzi wa kutosha; na

(iv) Kuanzisha mafunzo mbalimbali ya ufugaji nyuki kisasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) kituo cha Tabora kwa miaka mingi hakifanyi kazi na kilianzishwa kwa ajili ya tafiti za nyuki, mazao ya nyuki na mizinga yenye tija na kusababisha wataalam na watumishi kukaa bila kazi. Kwani gari liliondolewa katika kituo hicho, pia mpaka computer zimetolewa, nini hatima ya Kituo hicho cha Utafiti Tabora?

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Mheshimiwa Waziri afike Tabora kujionea haLi halisi na Mkurugenzi husika ili kutatua changamoto hizo. Nakushukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hotuba iliyoko mbele yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya, amefanya kazi kubwa ya mfano. Nijenge hoja ya kumpongeza, maana yake wengine watasema kwa nini wanapongezana; mimi nampongeza Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa sana kwa mwaka huu kwa Mkoa wa Tabora; amefanya mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza ameamua kupeleka maji katika Mkoa wa Tabora kutoka lake Victoria, hiyo pongezi ya kwanza. La pili, ametengeneza barabara ambazo ziko kwenye mpango na ambazo zimekamilika tangu akiwa Waziri. Kubwa zaidi, amefanya kazi kubwa mno ya kuleta usafiri wa ndege katika Mkoa wa Tabora, hayo yote lazima nimpongeze. Si hilo tu, ameleta tena standard gauge ambayo itapita Tabora, mimi bado nitaendelea kumpongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri anayoifanya ya kutangaza viwanda na biashara kwa ajili ya kuondokana na umaskini kwenda kwenye lengo la uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo, naomba sasa niende kwenye hoja. Hoja yangu nzito kabisa nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri wa Viwanda kwamba mimi nilikuwa Mbunge mwaka 2000 mpaka 2010, hilo kwanza alielewe, kwa hiyo ninapochangia hapa kuzungumza haya ninayoyasema ayazingatie ayafuatilie.

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, Kiwanda cha Manonga cha Usindikaji wa Mbegu za Pamba, kiwanda hiki kina historia yake, hawa wawekezaji wanambabaisha wanamtapeli, aende kwa kina, Rajan alikuwa mbabaishaji. Tumeanza kuzungumza kuhusu kukifufua kiwanda hiki ajenda ni ubabaishaji tu. Nimwombe Mheshimiwa Waziri, nakuheshimu; wakati anajibu swali la Dkt. Kafumu alisema yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, alisema hivi huyu mwekezaji inaonekana hana nia ya kuja kuwekeza au kukifufua kile kiwanda, sasa kigugumizi cha nini? Kwa nini asiamue akawapa Igembensabo ambao wapo na wanaweza kufanya kazi hiyo? Haya nayo yanachangia kuwafanya wananchi wa Tabora, vijana pamoja wakulima kurudi nyuma. Kwa hiyo, naomba hilo Mheshimiwa Waziri, mimi nitamfuata mpaka Ofisini kwake ili ajue uchungu wa wananchi wa Tabora. Maana alilijibu kama vile suala hili kama lipo lipo tu, lakini nimwombe alifuatilie kwa kina, lina uchungu sana na wananchi wa Tabora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine Kiwanda cha Nyuzi cha Tabora kimepoteza ajira za vijana wa Mkoa wa Tabora wote na mikoa jirani kwa uzembe. Hivi hawa wawekezaji kwa nini mnawaogopa? Mpelekeeni Mheshimiwa Rais, atayatumbua haya ili angalau na sisi tuonekane katika nia ya Serikali ni kupeleka viwanda. Kiwanda cha Nyuzi cha Mkoa wa Tabora ambacho kiko Manispaa kina historia.

Mheshimiwa Naibu Spika, alikuwepo Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Misigalo alishika shilingi katika jengo hili miaka ile. Kwa hiyo, alipolipeleka hilo wananchi wakaona anafaa bora aendelee akakaa vipindi viwili. Kwa matokeo hayo mpaka leo hakuna Mbunge anayekaa vipindi viwili kwa Mkoa wa Tabora kwa sababu hakuna wanachokiona tunachofanya. Sasa na mimi ili niweze kurudi tena lazima tupambane mimi na wewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Mkoa wa Tabora kutokuleta wawekezaji ni makosa, tunazo fursa zifuatazo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, Tabora inaongoza katika nchi hii kwa ulinaji wa asali, hilo nalo alizingatie na lazima niseme fursa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kwamba kuna nta ya kutosha, tumbaku ya kutosha, pamba ya kutosha, maembe ya kutosha pamoja na karanga za kutosha; na maeneo ya kuwaweka hao wawekezaji yapo na alishakiri mwenyewe, alikuwa anatuletea wawekezaji, lakini juzi wakati anajibu swali alisema hivi, aah wale wawekezaji tena hawapo. Hivi akisema hawapo kwa mtu wa chini kabisa kule inaonekana Serikali haitendi haki, kwingine wanapeleka wawekezaji, kwingine hawapeleki wawekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba kiwanda cha nyama, mifugo ipo, zamani pale tulikuwa Kiwanda cha Maziwa, kwa hiyo ukileta Kiwanda cha Nyama kitahudumia Singida, Shinyanga, Mbeya na Kigoma, lazima watapita pale. Hata hivyo si hilo tu, Tabora iko kati; kwa nini nasema iko kati, ukiwatangazia wawekezaji ukasema Tabora kuna fursa zifuatazo, watauliza kuna nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nasema Tabora iko kati; ukiichukua Mbeya kuleta kutoka Zambia wapo pale watafika Tabora, ukitoka DRC lazima apite Tabora, ukitaka kwenda Burundi lazima apite Tabora, anapokwenda Rwanda lazima apite Tabora, anakwenda Uganda lazima apite Tabora.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, akiwekeza pale atakuwa na mfumuko wa kupata soko mpaka Afrika Kusini, kwa sababu hii ni center ambayo inafungua; kama anavyofanya Mheshimiwa Rais wetu anafungua barabara. Kwa hiyo hayo ndiyo nimesema nimfafanulie Mheshimiwa Waziri ili angalau aone uchungu tunaopata sisi Wanatabora na yeye aupate.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanda cha Tumbaku nilifikiri atakitaja leo humu, hakuna chochote alichokitaja ambacho nilimwomba mwaka 2016/2017, hakuna alichoweka humu. Leo ningepata majibu wala nisingechangia, sana sana ningefanya kumpongeza, anafanya kazi nzuri sana lakini si maeneo ya Tabora na Kigoma, majirani zangu wananiambia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine, hili ni la jumla, tuna tatizo sasa hivi la wawekezaji wa viwanda kuhusu sukari. Tuna tatizo la sukari tusijibu tu bla bla hapa; sukari sasa hivi ni tatizo kwa nchi nzima na kuna wenye viwanda ambao si waadilifu na si wazalendo. Sukari imekamatwa Kagera ambako anatoka Mheshimiwa Waziri, hivi imekamatwaje na imeuzwa na nani, ambayo ilikuwa inavuka wanaipaki kupeleka Kenya. Sasa hebu aniambie Tanzania tukoje?

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri, suala la sukari ajiulize kwa nini wanafanya vitu vya namna hii hususan unapoanza mwezi wa ramadhani? Maana ni keshokutwa tu, wanamchafua Rais wangu, hiyo ni hujuma ili wamsaliti lakini hawezi kusalitika, tunamuunga mkono hata yawe mapambano lakini sukari kwa nchi hii itapatikana na Mheshimiwa Waziri Mkuu alishasema. Kwa hiyo nimwombe afuatilie suala hili, nendeni kwenye ma- godown hawa watu mnawaogopa nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, nimwombe, mikataba ya ubinafsishaji wale waliobinafsishiwa, waliopewa wale wa Kiwanda cha Nyuzi cha Manonga anipe majibu. Kwa nchi nzima viwanda vyote vile vije hapa, kwani kuna tatizo gani kuwanyang’anya? Mheshimiwa Lukuvi hapa ananyang’anya hati na kadhalika kwa nini Wizara ya Viwanda isifanye hivyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe, nimesema kwa hisia na uchungu kwamba nchi hii tusipopambana, nchi hii tusipoielekeza watamlaumu Waziri wa viwanda lakini utekelezaji wake utakuwa haupo. Nimwombe Mheshimiwa Waziri hawa watu awanyanga’anye hizo nanii zao kwani lazima?

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo na Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. MWANNE J. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi nichangie hotuba zote mbili za kamati tatu, lakini nijikite kwanza kwenye Kamati yangu ya Utawala na Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa iliyotolewa na Kamati yangu ni sahihi na ninaipongeza na ninaunga mkono.

Kazi yangu leo sasa hivi hapa ni kuiboresha tu au kukazia yale ambayo yamo kwenye taarifa yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende haraka haraka, hivi karibuni Kamati yangu ilikwenda ziara Mkoa wa Iringa, lakini niiombe Serikali, miradi mingi ambayo ilianzishwa na Serikali kwa miaka iliyopita ikamilishwe kwa haraka iwezekanavyo. Kwa mfano tulipokwenda Iringa kwenye Wilaya ya Kilolo tulikuta kuna mradi mkubwa sana wa Serikali ambao pesa zake nyingi zimetumika, lakini kwa bahati mbaya pesa iliyobaki ni kidogo, lakini Serikali haijatoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nizungumzie tu hivi, Hospitali ile ya Wilaya Mheshimiwa Jafo anaijua jinsi ilivyoanza, ni hospitali ya mfano, ina maghorofa manne, inajengwa kwa shilingi bilioni 4.4; ndiyo gharama ya ujenzi na inasimamiwa na TBA, lakini ukiangalia jinsi inavyosuasua inasikitisha, kwa sababu sisi kama Kamati tulisema hivi, ile hopsitali iwe ya mfano kwa nchi nzima. Hii ni kwa sababu kuna makadirio mengine ambayo ni ya hospitali hizo za Wilaya zinatumia zaidi ya shilingi bilioni 10 na 15, lakini hawa niwapongeze sana Halmashauri ya Kilolo kwa kazi nzuri waliyoifanya. Kamati zote zimeenda, watu wa Hazina wameenda, Hazina Makao Makuu wameenda, Hazina Mkoa wameenda, wamethibitisha kwamba yale majengo yako vizuri na gharama yake inaridhisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niiombe Serikali na najua Serikali ina azma nzuri na ina matarajio mazuri ya kuhakikisha wananchi hawapati tabu kwenye huduma ya afya, lakini niombe Serikali ihakikishe inapeleka pesa haraka sana za wakandarasi, imeathiri. Eneo lile hospitali ile kama ingekamilika ingehudumia wananchi wengi sana ukizingatia na jiografia ya Iringa ilivyo kwa kweli, wananchi wanateseka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine ambalo tulikuwa tumeomba kwenye Kamati yetu ni kwamba Wizara ya TAMISEMI itusaidie kutoa waraka wa ujenzi ambao utazingatia mazingira magumu au utazingatia walemavu/ mahitaji maalum. Kwa sababu kuna maeneo mengi wanajenga majengo ya Serikali lakini kwa bahati mbaya hawazingatii mahitaji maalum. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine ambalo mimi nimeliona pia ni kwamba, wanapojenga nyumba, madarasa wanapojenga hawazingatii kutoa waraka wa sera ambayo itasaidia ujenzi wa matundu ya vyoo. Sasa hivi wanaongeza kujenga madarasa, lakini matundu ya vyoo hayapo, ujenzi wa nyumba za walimu haupo, ujenzi wa nyumba za madaktari haupo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa naomba sana, namuomba Mheshimiwa Jafo, ni msikivu na Serikali yangu ya Awamu ya Tano ni sikivu, itusaidie kwa hilo ili angalao tuweze kwenda sambamba na mahitaji ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nilikuwa nataka nimuombe Mheshimiwa Mkuchika Waziri wangu, samahani nakutaja jina lakini Waziri wa Utumishi, nafasi ambazo ziko wazi baada ya uhakiki wa vyeti fake kwa kweli Serikali ingeangalia upya, ili iangalie namna ya kujaza hizo nafasi upande wa madaktari, upande wa walimu, hakuna kinachofanyika kwa sasa hali ni ngumu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningeiomba Serikali iangalie jinsi ya kuweza kuhakikisha kwamba, EGA badala ya kuwa wakala awe na mamlaka kamili ili kuhakiki takwimu za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nataka kuomba pia kuhusu TARURA, kwa sababu tunaenda haraka haraka. TARURA sasa hivi inafanya kazi nzuri, lakini inafanya kazi kwa kusuasua.

Nilikuwa naishauri, kama walivyosema Kamati yangu, kwamba sasa ipewe 50 kwa 50, TANROADS wapate 50 na TARURA wapate 50 kwa sababu, barabara za vijijini zimeharibika sana na Kamati yangu inakwenda mpaka vijijini barabara hazifai, madaraja hayafai, masika hii hakuna njia…

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, hotuba zote.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nichangie hotuba ya bajeti ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi. Awali ya yote nianze kumpongeza Rais wangu kwa kazi nzuri anayofanya, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Profesa Mbarawa, Mheshimiwa Engineer Nditiye, Mheshimiwa Kwandikwa na wataalam wote kwa kazi nzuri wanayofanya kwa sababu, mwenye macho haambiwi tazama. Mheshimiwa Profesa kazi ameiweza pamoja na timu yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia, kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri wote wa Wizara zote kwa sababu, sitapata nafasi ya kuwashukuru kwa kazi nzuri wanayofanya na Manaibu wao. Kazi wanayofanya kwa nchi hii wanaitendea haki Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuchangia hoja hii ambayo iko mbele yetu kwa kusema haya yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote niiombe Wizara ichukue ushauri wa barabara wanazotoa Wabunge kwa sababu, Wabunge ndio wanaotembea kwenye maeneo hayo na ndio wanaoyafanyia kazi. kwa hiyo, la kwangu naomba nichangie kuhusu barabara inayotoka Puge
– Ndala – Simbo – Nkinga – Ndembezi – Ziba – Manonga na Shinyanga, sijaona kama imewekewa fedha yoyote kwa ajili ya usanifu, lakini naomba nijenge hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii kuna hospitali kubwa mbili. Kuna Hospitali ya Ndala Mission, kuna Hospitali ya Nkinga, lakini azma yetu ni kufungua barabara ya Mkoa na Mkoa, barabara hii inaenda mpaka Shinyanga. Kwa hiyo, ikipatikana nafasi, kwa mwaka huu najua haitawezekana kwa sababu, haimo kwenye vitabu, lakini niombe tu kwamba, kama kutakuwa na uwezekano 2018/2019, namwomba Mheshimiwa Waziri iingie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara nyingine nishukuru kwa ajili ya kuweka upembuzi yakinifu barabara ya Tabora – Mambali – Bukene – Itobo na Kahama. Hii barabara nayo ni kubwa sana, kwa hiyo, nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwamba, ameitengea fedha. Hata hivyo, barabara ya kutoka Tabora – Mambali – Bukumbi – Shitage – Kahama, hii haijaonekana, nimwombe Mheshimiwa Waziri hii barabara nayo aiangalie kwa jicho la huruma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejaribu sana kuongea na Mheshimiwa Kwandikwa, lakini majibu aliyokuwa ananipa naona kama Wizara yake haiitambui barabara hii. Kwa hiyo, niombe nayo pia iangaliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara nyingine ni barabara ya Sikonge – Ipole – Mpembampazi – Kitunda – Rungwa. Hii barabara ni muhimu sana. Barabara hii akiifungua ikatoka Sikonge, ikapita Ipole, ikaenda Rungwa maana yake inaenda kukutana na barabara ya Itigi inayokwenda Singida. Kwa utaalam huo pia, barabara hii akiifungua kwa kupitia Sikonge maana yake itaunganisha wageni kutoka Afrika Kusini, itaunganisha usafiri kutoka Malawi ambao wote wanaotaka kwenda Mwanza na kwenda Uganda, hii njia ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara nyingine ambayo naomba niichangie ni ujenzi wa Ipole – Koga. Njia hii inasuasua, ina mkandarasi na mpaka sasa hakuna mawasiliano ya aina yoyote, imekatika kwa ajili ya mvua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kuna Barabara nyingine ya Kaliua – Uvinza – Kigoma, sasa hivi hamna kitu kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri anapoiacha hii ya Kaliua maana yake anatenganisha Kigoma na Tabora ambayo ndio njia rahisi ambayo inaweza kuunganisha Watanzania wote kwa kwenda Dar-es-Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo pia, Mheshimiwa Waziri bajeti ya mwaka huu kwa TANROADS pamoja na TARURA imevurugika. Mwaka huu mvua imenyesha sana, sijui Serikali imejipangaje kwa sababu, fedha iliyomo kwenye vitabu haitoshi na haitatosha. Kwa hiyo, niiombe Serikali itenge fedha ya dharura kwa ajili ya matengenezo ya barabara kwa sababu, mvua hii hatukuitegemea kunyesha kiasi hicho, lakini imenyesha Tanzania nzima na Tanzania nzima kuna mafuriko ya kila aina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe waiangalie TARURA na TANROADS kwa sababu, TARURA pia ingawaje iko chini ya TAMISEMI, lakini haina fedha na kama haina fedha ina maana kwamba, hata TANROADS haina fedha. Kwa hiyo, niiombe Serikali iangalie kwa jicho la huruma kwa sababu, tutakuwa tunawalaumu kumbe fedha hazipo kwa hiyo, wapewe fedha ya uhakika, ili waweze kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna uharibifu mkubwa wa barabara, kuna mashimo makubwa ambayo hayazibiki kwenye barabara kuu. Haya nayo ni matatizo kwa sababu, hata juzi juzi ajali iliyotokea Singida ni madereva walikuwa wanakwepa mashimo. Kwa hiyo, niiombe Serikali iangalie jinsi gani ya kuziba mashimo ambayo ni marefu mno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nataka kuzungumzia kidogo kuhusu ununuzi wa ndege. Ununuzi wa ndege ni jambo zuri, naipongeza sana Serikali yangu na ikiwezekana iongeze tena na tena ili Watanzania tuwe kwenye neema tusiwe tunaziona tu ndege nyingine za Emirates zinaleta watalii, basi na za kwetu ziwe na wimbo mmoja, lakini niipongeze Serikali pia kwa standard gauge ambayo nina imani itafungua mambo mengi ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niongelee ukarabati wa majengo ya TBA hasa Site II, yako katika hali mbaya. Tunakaa kwa kusema hatuna mahali pa kukaa kwa sababu, sisi ni Wabunge, ni wageni, lakini tuko katika hali mbaya. Lingine uchafu uliokithiri. Kuna majumba yale yaliyowekwa sijui ni majumba, sijui manini ya taka, yamejaa mpaka yanatapika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe ushauri. Mitaani tunachangia usafi wa mazingira, kwa nini TBA wasijipange wakaleta waraka wa kuchangia angalau Sh.10,000/= kwa kuondoa uchafu wa taka mle? Kwa sababu, tukisema kila kitu bure ndio hayo; nimwombe Mheshimiwa Waziri, atume delegation yako ikakague usafi na uchafu uliopo katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe tu kwamba, kama atapata muda mzuri ni vizuri watuandikie waraka wapangaji, tuna uwezo ndio maana tukapanga. Kwa hiyo, lazima kuwe na utaratibu wa kuchangia tusifanye bure au kuogopana bure, itatoka wapi hela? Kwa sababu, usafi ni wa kwetu, kodi tunayolipa ni ndogo kiasi ambacho kuchangia Sh.10,000/= hatutashindwa. Kwa hiyo, niombe tuweke utaratibu, tutafute jinsi ya kukusanya angalau Sh.10,000/= kwa kila nyumba tutoe ule uchafu ambao upo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni miundombinu rafiki na maji. Barabara nyingi zinakatwa wakati wa kuingiza maji, hivi hakuna ramani? Inajengwa barabara ya lami kwa gharama kubwa sana, lakini ndani ya mwezi mmoja au miezi miwili miundombinu ya maji inapita pale inakata barabara, hivi sheria hatuna? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nataka nichangie hayo tu, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na naunga mkono kwa asilimia mia moja bajeti hii.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami nichangie machache kwenye bajeti hii ya Wizara ya Fedha, lakini pia nichukue nafasi hii pekee kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu kwa kazi nzuri anayoifanya. Uongozi wa Awamu ya Tano umejipanga na umejipanga kwa mambo mazuri matupu na yenye kufanikisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimpongeze pia Mheshimiwa Dkt. Mpango, nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri Dkt. Kijaji, nina sababu zangu. Nawapongeza kwa sababu muda hautoshi, lakini nampongeza na Katibu Mkuu wa Wizara hii kwa kazi nzuri waliyofanya kwenye Kamati ya Uongozi na Bajeti (Kamati ya Bajeti). Wamefanya kazi nzuri miongoni mwa kazi nzuri kwa sababu kwa mara yangu ya kwanza nimeweza kukaa nao meza moja na kuona wanafanya nini. Mheshimiwa Waziri amekuwa mtiifu na amekuwa kiongozi pekee kwa ufafanuzi wa Wizara yake; hiyo nafasi nampongeza sana na amekuwa mtiifu sana.

Mheshimiwa Spika, niombe yale yaliyokuwa yamezungumzwa na maombi yaliyotolewa kwenye Kamati Mheshimiwa Waziri wa Fedha ayazingatie kwa sababu ni Kamati ya Uongozi na Kamati ya Bajeti. Sasa Kamati ya Uongozi maana yake Mheshimiwa Spika alikaa kwenye kiti hicho na akabariki yale aliyokuwa ameyaahidi.

Mheshimiwa Spika, lakini la kwanza tulikuwa na ombi la Kamati ya Bajeti kwamba ajitahidi katika utaratibu wake na mipango yake kuhakikisha kwamba hii Sh.50 iongezwe kwenye petrol na diesel kwa ajili ya maji. Mfuko wa Maji ni muhimu sana, kero yote hii, mazunguzo yote haya, yanajitokeza na lawama kwake ni kwa sababu hiyo kwamba bajeti ya maji ni ndogo, kama hataongeza basi atafute vyanzo vingine vya kuhakikisha kwamba anaongeza kwenye bajeti ya maji ili tuondokane na matatizo la maji.

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo alikubali yeye mwenyewe kwenye Kamati ya Bajeti ni kupeleka fedha kwenye miradi ambayo wananchi wamejitokeza na wameifanyia kazi kubwa, miradi ya afya, maji, elimu ambayo haijakamilika. Kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Dkt. Mpango kwamba anapokuja sasa ahakikishe pesa zinapelekwa kwa wakati; hilo ndilo tatizo. Pesa zipo kidogo lakini haziendi kwa wakati. Kuna fedha ambazo zilitakiwa kukidhi bajeti iliyopita ya 2017/2018, lakini mpaka sasa kwa bahati mbaya au kwa makusudi au bahati mbaya hasa mimi nasema kutokana na makato kutokamilika kwa wakati basi amepeleka asilimia kidogo.

Mheshimiwa Spika, kuna suala zima la TARURA na TANROAD, ile asilimia 30 kwa 70 bado TARURA wana kazi kubwa sana. Kwa hiyo, niombe kama hatapunguza kwenye TANROAD, basi ni vizuri akaangalia jinsi gani ya kuibeba TARURA kutoka kwenye vyanzo vingine ili angalau wapate asilimia 40. Kwa sababu kwa mwaka huu mvua imeharibu asilimia kubwa ya miundombinu vijijini. Kwa hiyo barabara ambazo ni mbaya ni vijijini na barabara pia za mjini ambazo ni barabara kuu pia zimeharibika. Kwa hiyo, ingekuwa ni vizuri zaidi zote zikaangaliwa ili pesa ziende kwa usawa.

Mheshimiwa Spika, pia niombe pia kuhusu suala la kuongeza fedha kwenye Mifuko hii ifuatayo:-

Mheshimiwa Spika, kuna mfuko wa Rais wa Kujitegemea, TASAF na MKURABITA. Mheshimiwa Dkt. Mpango haya mambo sisi tumeyaona kwa sababu ni Kamati yangu ya Utawala na Serikali za Mitaa, mimi kama Makamu. Mifuko hii inafanya kazi vizuri sana. Mfuko wa Kujitegemea wa Rais unaweza ukasaidia ukaitoa hata ile milioni 50 ambayo inakwenda kila kijiji ingepitia kule. Tumejifunza mengi kwenye Mfuko wa JK ambao ulikwenda hovyo; sasa huu asikurupuke, asifanye haraka wala asikosee tena.

Mheshimiwa Spika, ziende kwenye TASAF na MKURABITA, kwa sababu uelewa sasa hivi wa wananchi kuhusu msaada wa Mfuko wa Rais wa Kujitegemea ni mkubwa na sasa hivi wameenea nchi nzima mpaka vijijini. Kwa hiyo hawa tukiwalea nadhani Mheshimiwa Mpango ataondokana na hii kadhia ya milioni 50; kwa hiyo awe na utaratibu wa kupeleka fedha kwenye Mifuko hiyo. Pia hata asilimia 10; akiiweka vizuri hii asilimia 10 ikapita mle, wananchi wengi sana watanufaika, kwa sababu sisi tumekwenda moja kwa moja na Kamati yangu kwenye maeneo hayo na tumeona nini wanachokifanya, kwa hiyo mafanikio ni makubwa sana.

Mheshimiwa Spika, lakini lingine ni suala zima la korosho, ila mimi sitaunga mkono kwa kuandamana, alishatupa ufafanuzi wa deni hilo la korosho. Niiombe Serikali, mimi naweka msisitizo tu, niiombe Serikali ione jinsi gani ya kusaidia hili zao la korosho kwa sababu imekuwa ni kero, kero hiyo itatuathiri. Mheshimiwa Mbunge aliyemaliza tunaona kama ana dhihaka lakini ana maana ya kulizungumzia ndani ya Chama cha Mapinduzi tatizo hili.

Kwa hiyo, hili tatizo ningeomba; kwenye Kamati alizungumzia kwamba kunatakiwa uhakiki, kuna mambo mengi wameyaona. Sasa yale ambayo wameshahakiki basi hizi pesa zipelekwe kwa wakati angalau surphur basi ipelekwe kwa wakati ili waweze kuokoa zao hilo.

Mheshimiwa Spika, lingine la mwisho, Mheshimiwa Dkt. Mpango, nimejitahidi sana pamoja na Naibu wake nimepeleka taarifa nyingi sana za kuhusu TRA na kuhusu jinsi makusanyo ya Serikali yanavyopotea. Nimempelekea na nashukuru ndiyo maana nimesema ni watiifu kwa sababu walitekeleza na waliona. Kwa hiyo, ningeshauri kuitegemea TRA peke yake si mbadala, ni vizuri tukajipanga tukaanzisha pia kitengo maalum cha kufuatilia hizi mashine za EFDs; kwa sababu watu kweli hawazitumii kwa neno la kusema kwamba mashine mbovu kwa sababu walishatangaza kwamba hizi mashine zinasumbua, kwa hiyo watu wengi wanachukulia advantage hiyo kwamba mashine ni mbovu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ni vizuri sasa ufuatiliji uwe ni wa makini na zile barua ambazo wanaandika baada ya mashine kuharibika, nadhani sasa atoe mkakati maalum, atoe agizo maalum kusiwe na zile barua ambazo wameweka kwenye lamination wanazungumzia tu kwamba tumeambiwa wanabadilisha tu.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi Tanzania hii tena wameelimika ujanja ni mwingi, matapeli ni wengi, kwa hiyo tunapokwenda kwenye maeneo ya biashara mtu anapiga magoti kuomba kwamba apunguziwe. Kwa hiyo niombe Wizara ya Fedha, niiombe kwa msisitizo mkubwa iendelee kutoa elimu ya maana ya ulipaji kodi kwa wananchi wote kwa kutumia local radios kutumia TV, vipindi maalum. Mheshimiwa Waziri asione ubahili wa kutumia vipindi maalum.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nataka kuishauri Serikali ijitahidi itoe elimu, Watanzania hatukuwa na tabia hiyo ya kulipa kodi. Kwa hiyo wengi watakwepa kwa lolote atakalotaka kwa ajili ya kuongeza mapato ya Serikali. Nichukue nafasi hii kumpongeza sana kwa kazi nzuri anayoifanya, ni wakati mgumu lazima atapata matatizo mengi, lakini lazima tujipange, tushirikiane katika ulipaji kodi na matumizi yake. Tukifanya hivyo vikaenda pamoja Serikali itakwenda juu na tutatoka hapa tulipo. Nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru na naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili nichangie japo machache kwa sababu ni Mjumbe wa Kamati hii, pia Makamu Mwenyekiti wa Kamati hii. Nimpongeze Mheshimiwa Mwenyekiti wangu kwa uwasilisho wake mzuri na pia kuipokea hii taarifa kwamba ni sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mchango wangu utaanza na shukrani kwa Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano kwa kazi nzuri anayoifanya ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM. Ndani ya miaka mitatu ameweza kufanya mambo ya ajabu mengi sana, sina sababu ya kuyataja, lakini miongoni mwa miradi hiyo ambayo anaifanya na sisi kama Kamati tumeona ina mafanikio ni suala la afya. Suala hili lilikuwa nyuma sana lakini Awamu ya Tano imepeleka pesa kwenye Wizara ya Afya au TAMISEMI kwa ajili ya ukarabati wa Hospitali za Mikoa, Vituo vya Afya, pia Hospitali za Wilaya. Mpaka sasa kitu ambacho tumethibitisha Hospitali za Wilaya 67 na Vituo vya Afya 350 vimeshapelekewa pesa. Kwa hiyo, hayo ni mafaniko makubwa sana ambayo tumeyaona baada ya ziara zetu. Si hilo tu bali kuna ongezeko kubwa la madawa, Mheshimiwa Rais wetu ameweza kuongeza bajeti ya madawa na mafanikio yake yanaonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata upande wa elimu, kwa ziara tulizotembelea sekta ya elimu kwa kweli kazi kubwa imefanyika. Nimpongeze sana Mheshimiwa Jafo amesimamia miradi yote pamoja na Naibu Mawaziri wake wanafanya kazi nzuri sana.

Mheshimiwa Spika, mambo haya yanaleta heshima kwa Serikali yetu, upo upungufu mdogo unaohitaji maboresho. Tuiombe Serikali itusaidie kwa mwaka wa fedha 2019/2020 bajeti iongezeke TASAF, Awamu ya III. Fedha inayotolewa na Serikali ni kiasi kidogo sana, wafadhili ndiyo wanaochangia kwa kiasi kikubwa, iwapo wale wafadhili watajiondoa ina maana TASAF itakufa. Kazi wanayofanya TASAF Awamu ya III ni nzuri sana kama itaendelezwa kwa kupatiwa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ni MKURABITA. Kwenye ziara za Mikoa yote tuliyokwenda MKURABITA imefanya kazi nzuri sana lakini wanachopungukiwa ni fedha kwani inayopelekwa ni kidogo sana. Kama MKURABITA itapewa fedha ya kutosha katika bajeti ina maana kazi itakayofanyika itawafafikia wananchi wote kwa sababu sasa hivi tayari wananchi wameshaelewa maana ya hatimiliki za kimila na kazi inafanyika vizuri, hata kwako Kongwa tuliwahi kupita na kuhakikisha kwamba Wagogo wote sasa wameshaelewa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, suala ligine ni TARURA. TARURA inafanya kazi nzuri sana kwenye maeneo yote ya Halmashauri lakini tatizo ni fedha, mahitaji ni mengi lakini fedha haitoshi. Kazi ya TARURA ni kufungua barabara za Wilaya, Vijiji na Mikoa hatimaye kuwa pamoja lakini hakuna fedha za kutosha.

Mheshimiwa Spika, niipongeze sana TAKUKURU kwa kazi nzuri inayoifanya. Sasa hivi heshima imerudi Wizara ya Afya, elimu na maofisini hakuna rushwa imepungua. Watu wanachukua rushwa lakini kwa uwoga, rushwa imepungua. Tatizo lao ni fedha ndogo wanayopewa, kwa hiyo, hawawezi kufika maeneo mengi kadri inavyotakiwa.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo napenda kulichangia, Mjumbe mwenzangu wa Kamati aliyemaliza kuzungumza sasa hivi amesema kuhusu asilimia kumi ya Halmashauri. Kazi kubwa imefanyika katika Awamu ya Tano kuhusiana na asilimia hii kumi. Kwa nini nasema hivyo? Sisi wenyewe Wabunge humu ndani ni Wajumbe wa Halmashauri zetu, hizi bajeti zinapita kwetu. Sasa kama zinapita kwetu kwa nini tusizuie bajeti zao wakati wa Mabaraza ya kupitisha bajeti ya kila mwaka? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tutailaumu Serikali kwamba asilimia kumi watendaji wanachukua si kweli kabisa, udhaifu upo lakini na sisi kama Wabunge tunachangia kwa sababu ni Wajumbe wa Mabaraza, hususani wanawake wenzangu, Waheshimiwa Wabunge wa Viti Maalum ni Wajumbe wa Mabaraza tupiganie tuhakikishe hii haki ambayo ni wanawake, vijana na walemavu bajeti zisipite pamoja na Wabunge wa Majimbo mtusaidie ninyi ni Wajumbe wa Kamati ya Fedha. Kama ni Wajumbe wa Kamati ya Fedha kwa nini msitambue kwamba asilimia kumi ni muhimu sana kwa maendeleo ya wanawake, vijana na walemavu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Rais…

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Spika, taarifa huku.

SPIKA: Naomba tuvumiliane tu aongee, maana hata wanaotoa taarifa siwaoni.

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Spika, kushoto kwako.

MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kuamua kutoa vitambulisho kwa wajasiriamali. Naomba kweli kabisa Waheshimiwa Wabunge tupambane kwani asilimia kubwa ni wanawake na ndiyo wanaopambana Mheshimiwa Rais ametuokoa. Kwa hiyo, niombe Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wawatambue wajasiriamali kwa sababu kutokutoa vitambulisho hivyo ni kumvunja moyo Mheshimiwa Rais. Kwa hiyo, niombe Wabunge tuchangie jinsi gani ya kusimamia kuhakikisha wajasiriamali wanapata huduma kama ilivyotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu muda unaniruhusu niombe, nimeona Serikali sasa hivi ina mabadiliko ya kuondoa Idara zingine TAMISEMI, kwa mfano, Serikali sasa hivi imeondoa masuala ya maji TAMISEMI, inategemea pia kuondoa Idara ya Kilimo, kwa nini nasema kilimo ibaki TAMISEMI? Wananchi wote wako TAMISEMI na TAMISEMI ni kwenye grass root, sasa unapomwondoa huyo Mkuu wa Idara aende Wizarani watu ambao anatakiwa kuwaongoza, kwa mfano Mkuu wa Mkoa wangu alitoa agizo kwamba Wakuu wote wa Idara wa Ugani hakuna kwenda likizo mwezi Novemba kwa sababu ya mvua na kilimo, alisema wote watakaokwenda atawasukuma ndani.

Mheshimiwa Spika, kitu ambacho ningeomba…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana, malizia hiyo sentensi.

MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hotuba ya Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa, yote yaliyoandikwa na maoni yao yachukuliwe. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi kwa siku hii ya leo nami niweze kuchangia Wizara ya Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nashukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uwezo wa kuamka leo salama na kunipa nafasi kama hii ya pekee kuweza kuchangia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na pongezi. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuleta Sera ya Viwanda nchini na kuisimamia yeye mwenyewe kikamilifu. Nampongeza sana kwa sababu siyo hilo tu ameyafanya Mheshimiwa Rais wetu, lakini ana mengi ameyafanya katika nchi hii kwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015/2020. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza pia Makamu wa Rais, anafanya kazi nzuri ya kumsaidia Mheshimiwa Rais, wamejipanga. Nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu na timu yake, wanafanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuchangia. Nimeanza kwanza kwa pongezi, sasa nakwenda kwenye jukumu kubwa ambalo ninalo moyoni mwangu. Mheshimiwa Waziri naomba Mwenyekiti alipokee hili na alisikilize kwa makini. Nataka nizungumzie habari ya kiwanda cha Tabora cha Nyuzi (TABOTEX). Kiwanda hiki kimeanza muda mrefu, tangu mwaka 1978 kama sikosei au 1975. Baada ya kubinafsishwa, kiwanda hicho kimesuasua na mpaka leo hakifanyi kazi. Malighafi yote imeondolewa. Nilishamwomba hapa ndani Mheshimiwa Naibu Waziri twende mimi na yeye akaangalie hali halisi ilivyo kwa sababu hatuwezi kukubali kutafuta wawekezaji ambao ni wababaishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiwanda hiki kilikuwa kinasaidia sana ajira kwa watu wa Mkoa wa Tabora, lakini mpaka sasa hakuna ajira, vijana wanahangaika, lakini mwekezaji hakuna chochote alichokifanya. Nilitegemea basi, kwamba angalau Mheshimiwa Waziri angeweza kuiweka mle TABOTEX. Nimeangalia ukurasa wa nane hamna kitu, nimeangalia ukurasa wa 20 hamna kitu, labda mimi sijui kusoma. Kama sijui kusoma leo Mheshimiwa Waziri ataniambia kwamba ameiweka wapi? Kiwanda cha Nyuzi ambacho ni tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda hiki historia yake ni kwamba kulikuwa na Mbunge anaitwa Marehemu Mzee Misigalo. Miaka ya nyuma ili kuweza kufanikisha alimwomba Baba wa Taifa kwamba kiwanda hiki kiwepo Tabora baada ya kuonekana kwamba hakuna kiwanda chochote ambacho kinaweza kikawa kinatengeneza nyuzi kwa Kanda ile ambayo wanalima pamba. Kwa hiyo, akaitoa shilingi, nami leo naitoa kwako. Aliitoa Shilingi, Baba wa Taifa akampa hicho kiwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati nzuri mwaka uliofuata anaomba kura, wakampa tena akatawala vipindi viwili. Alivyotawala vipindi viwili, hakuna tena aliyevunja ile historia kwa sababu ya kile kiwanda. Sasa nami kwako Mheshimiwa Waziri shilingi hii nitaondoka nayo, naenda nayo Tabora mpaka wewe uje ujieleze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni ujenzi wa Kiwanda cha Tumbaku. Ujenzi wa Kiwanda cha Tumbaku tulitegemea pia tungekiona humu kwenye kitabu hiki, hamna. Tumbaku inalimwa Tabora asilimia 60 na tuliomba kwamba kuwepo na kiwanda cha kutengeneza, kusindika Tumbaku Mkoa wa Tabora lakini hakimo. Mheshimiwa Waziri ana ajenda gani? Ana ajenda gani wakati Tumbaku tunailima sisi wenyewe? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda hiki gharama zake ni kubwa ambazo wanatoa tumbaku kupeleka Morogoro. Wakipeleka Morogoro, gharama yote inakwenda kwa mkulima na wakulima wa tumbaku wanalima katika mazingira magumu, hawana afya nzuri kutokana na usumbufu wa zao la tumbaku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu aliweka mazingira mazuri ya suala zima la bei ya tumbaku, lakini nilitegemea sasa leo Waziri mhusika mwenye dhamana angeweza pia akaliongelea hili suala la kiwanda cha tumbaku kwa ajili ya Mkoa wa Tabora na nchi nzima, kwa sababu Kanda ile yote Kigoma, wapi wanalima tumbaku, lakini hakuna kitu chochote alichoweza kuandika. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri aliangalie hili kwa upana, ni jinsi gani atakavyojipanga aliweke hili jambo la kiwanda cha nyuzi aweke pia na suala zima la kiwanda cha tumbaku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la SIDO. SIDO ni mkombozi mkubwa sana, watu wanadharau; SIDO imeweza kulea wanawake, imewatoa wanawake na vijana kwenye ujasiriamali sasa wamekuwa wawekezaji wakubwa, lakini hakuna fedha yoyote ambayo inakwenda kwenye mikopo. Kwa hiyo, bado nina wasiwasi, tunawasaidiaje vijana na wanawake kwa kuidharau SIDO? SIDO ilitakiwa ipewe fedha nyingi ili waweze kukopesha wanawake na vijana na walemavu, watu wote ambao ni wajasiriamali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia vifungashio. SIDO imewaelimisha wananchi, wajasiriamali wote wamepita mafunzo ya SIDO na ndiyo maana wanajua maana ya vifungashio. Sasa hivi wanafnyakai nzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni Maonyesho ya Saba Saba. Wajasiriamali wanateuliwa wachache sana tena kwa kupitia vikao ambavyo havihusiki na SIDO. SIDO wanaleta tu mwelekeo, wanatoa waraka, lakini nani anayeweza kudhibiti wajasiriamali ili waende kwenye Masoko ya Maonyesho ya Kimataifa na Maonyesho ya Saba Saba? Ni lazima SIDO iingize mkono wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ili SIDO iweze kufanya kazi nzuri, mimi siafiki kutokuwapa pesa SIDO. SIDO hawapati fedha zozote. Kwa hiyo, hata mimi ningeweza kuishauri Serikali, kama kuna fedha nyingine zozote ambazo wanaona ni rahisi kuwafikia walengwa, wananchi ambao ni wa chini, lazima ipitie SIDO. Tangu imeanza SIDO haina mgogoro wowote wa kazi kubwa ambayo inafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, ukiisoma kwenye taarifa ya SIDO, urejeshaji wa mikopo ni tofauti na asilimia 10 ambayo inatolewa na Manispaa au Halmashauri. Wao wameweza kukusanya marejesho asilimia 91.5. Hata ukitaka kusoma lile jedwali lake liko ukurasa namba 16. Ni watu ambao wanaweza wakasaidia nchi hii kuondokana na figisu figisu ya mikopo midogo midogo kwa sababu mikopo yao ni ya riba nafuu. Kwa hiyo, nilikuwa nataka nizingatie hayo ambayo ni ya muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho mimi sikutaka kuchangia mengi. Nakuomba sana Mheshimiwa Waziri, sitaki kuichafua Serikali yangu, lakini utakapokuja hapa unipe majibu ya mambo mawili; la kwanza Kiwanda cha Nyuzi, kwa nini wanaondoa vifaa wanapeleka Manonga? Vingi wamepeleka Manonga. Kwa hiyo, nataka majibu hayo, kwa sababu sasa hivi asilimia 100 ya wakulima wa pamba wanatoka Igunga. Kwa hiyo, bila hilo, sitaki kukosana, nimesharudia mara tatu, mara nne; nitakosana na wewe kwa ajili ya Kiwanda cha TABOTEX, nitakosana na wewe bila kupata majibu. Sitaki kujua kama unatoka Tabora au unatoka wapi! Mimi sitambui. (Makofi)

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mimi najua wewe ni Waziri, kwa hiyo, siitambui. Yeye ni Waziri lakini sitaki kujua huko nyuma kama anatoka Tabora. Mimi na wewe humu ndani ama kesho patakuwa hapatoshi. Nipate majibu mawili ya Kiwanda cha Nyuzi na Kiwanda cha Tumbaku, lini kitaanza mchakato? Hayo ndiyo ya kwangu ambayo nataka wewe Mheshimiwa Waziri sasa, nakuomba, nam-address yeye kwa sababu haijalishi kama anatoka wapi? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja asilimia mia kwa mia. Ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge na Utawala na Serikali za Mitaa pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi jioni hii kuwa mchangiaji wa kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwweza siku hii ya leo kuwa na afya njema na kupata muda wa kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Makamu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa. Kwanza naunga mkono maoni ya Kamati na nimpongeze Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati hii kwa uwasilishaji wake mzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuchangia, pia nianze na pongezi. Nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayofanya lakini pia kuzilea ofisi hizi mbili za TAMISEMI na Utumishi na Utawala bora. Wizara hizi mbili kuwa chini ya Mhehsimiwa Rais kuna mafanikio makubwa, pia wateule wake, Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI na Waziri wa Utumishi, kazi wanazofanya kwa kweli wanamuwakilisha vizuri sana Mheshimiwa Rais. Pia Manaibu Waziri wa Wizara zote mbili wanafanya kazi nzuri za kusaidia kwenye Wizara hizi, vilevile Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, niwapongeze sana kwa kazi nzuri wanayofanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo pia kuna mambo ambayo sisi kama Kamati tulikuwa tumeridhika na Wizara zote mbili kwa wao kukubali maoni ya Kamati. Asilimia kubwa ya mafanikio haya yametokana na maoni ya Kamati yetu. Tuwapongeze Wizara chini ya Mawaziri hawa kukubali ushauri wa Kamati, kwa kweli niwapongeze sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, nichukue nafasi ya pekee kumpongeza Mheshimiwa Waziri Jafo; hivi karibuni tu, siku mbili zilizopita TAMISEMI walikuwa na kongamano au taarifa ya utekelezaji wa miradi ambayo Serikai ilitoa fedha na miradi hiyo imefanikiwa kwa asilimia 88 mpaka hivi sasa. Kwa hiyo ni imani yangu kwamba ifikapo Juni, kwa fedha hizi zitakazotengwa na zile zilizotengwa nina imani kubwa sana miradi yote itakuwa imekamilika, na sina shaka usimamizi ambao tunao kwenye Wizara hii mambo yote yatakwenda kama tulikusudia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nimpongeze Waziri wa Fedha na Wizara yake na Naibu wake kwa kupeleka fedha TAMISEMI kwa asilimia zaidi ya asilimia 75. Kwanini ninasema hivyo; ni kwamba miradi mingi ya afya imetekelezwa vizuri sana, yote hii ni kutokana na usimamizi mzuri pamoja na umakini katika makusanyo ya fedha ambayo yameweza kuweka rekodi ya pekee kwa maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa tukizungumzia vifo vya mama na mtoto vimepungua kwa sababu zahanati na vituo vya afya vimesogea kartibu. Jana nilikuwa nasikia Mheshimiwa Kiula anasema kwake tayari wameshafanya oparetions za mama mjamzito na wakaokoa mtoto. Sasa kwa hilo nimeona nisisitize kwamba TAMISEMI sasa siyo TAMISEMI ile, TAMISEMI inapaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine nilitaka kusisitiza kwenye Kamati ni kwamba tuna mabasi ya mwendokasi, na kuna wakala ambaye anatarajia kupewa, au tender kutangazwa. Ningeshauri TAMISEMI wajitahidi kwanza Sheria iwepo kabla ya kuplewa mkataba, kwa sababu bila sheria tutarudi tena kusema mikataba mibovu na kadhalika. Kwa hiyo la kwanza niishauri TAMISEMI ihakikishe kwamba sheria inaletwa hapa na inapitishwa ili mambo yaweze kuwa mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano sasahivi wanasema kwamba mabasi mengi yako pale, wakati wamvua wanapata shida. Hata hivyo, baada ya sisi kufuatilia kwa sababu tayari Kamati yetu ilitembelea kwenye maeneo; si kweli yale mabasi ni mabasi ambayo yalishaharibika. Hata hivyo Kamati yetu iliwashauri kwamba ni vizuri yakaondolewa kwenye eneo ili watu wasijue na wasielewe kwamba ni kila siku mabasi yanjaa maji; si kweli. Ni mabasi ambayo kweli wakati ule maji yalikuwa yanajaa, lakini sasahivi yaliyobaki ni yale ambayo huwezi kuyatengeneza na huwezi kuyafanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, niende harakaharaka, ni suala zima la miundombinu. Kwakweli niipongeze sana TARURA inafanya kazi katika mazingira magumu kwa sababu haina fedha na haina tegemeo. Hizi Wizara mbili zote zina malalamiko Wizara ya Miundombinu wanasema kwamba fedha hiyo haiwatoshi na TARURA wanasema haiwatoshi. Mimi ningeshauri, hizi Wizara zingekaa pamoja, zikae pamoja zituletee nini kinachoweza kufanyika ili Sheria ya TANROADS ibadilishwe ya na TARURA waweze kupata fedha. Kama TARURA wangepata asilimia 40 kazi nzuri wangefanya kwa sababu tumetembelea miradi, wanajitahidi sana pamoja na kwamba hawana fedha. Tatizo kubwa ni kwamba kwa hali ya mvua ya sasahivi kuna matatizo makubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, niende harakaharaka kwa sababu nina Wizara mbili; Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI tukuombe sana kwa bajeti hii; madeni ya Madiwani ambayo wanadaiwa hatutaki tena kwenye bajeti yetu tuje tukutane nayo. tunataka ikifika wakati wa bajeti ya mwaka huu madeni yote kama ulivyoagiza yale yamekwisha kwa sababu Madiwani wanafanya kazi ngumu, wanakopwa vikao hawalipwi na wana madeni. Kwa hiyo hili suala kwenye Kamati hatutaki tena lirudiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini si hilo tu, niombe pia kuhusu Shirika la Kariakoo Sheria ile imepitwa na wakati, ni ya tangu mwaka 1974. Wakati ule kulikuwa na watu wachache, sasa Kariakoo si ile ya mwaka 74 iletwe Sheria ifanyiwe marekebisho, lakini kwa upande wa TASAF mpaka hivi leo karibuni walengwa kwa asilimia 30 hawajapatiwa fedha. Sasa, kwa kuwa tunaingia wkenye awamu nyingine ni vizuri asilimia 30 ikamilishwe ili walengwa wote waweze kupata haki yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, niende harakaharaka, ni kuhusu suala la MKURABITA. Suala la MKURABITA ni tatizo kubwa tumetembelea kwenye Ofisi zao, lakini kwa bahati mbaya hati mpaka leo hazijachukuliwa. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge hawa Wabunge wawahamasishe wananchi ambao hati zao ziko kwenye Ofisi wakachukue ili wajue maana ya kwenda kukopea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ningeomba kwa ridhaa yako kwamba wakala wa mafunzo kwa njia ya mtandao TAGLA, lengo la TAGLA kuanzishwa ni kuwawezesha watumishi wa Serikali au watumishi wa umma kwenda kujifunza na hatimaye kutumia mfumo huu wa mtandao ambao sasahivi upo. Kwa hiyo nimwombe Waziri mwenye dhamana ya utumishi ahakikishe kwamba anatoa waraka kwenye halmashauri kuhakikisha watumishi wanapata haki zao na wanakwenda kujifunza haya mafunzo ili kutumia posi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono.(Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nichangie hoja hii iliyopo mbele yetu. Nianze na pongezi; kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rais wetu kwa kazi kubwa anayofanya ya kuutambua utalii.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Order ndani ya Bunge, order!

MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, shida kubwa iliyopo sasa hivi ni jinsi gani Rais alivyojipanga na kuhakikisha kwamba sasa utalii unakuwa katika nchi yetu, ndani ya miaka mitano amefanya kazi kubwa sana. La kwanza, amenunua ndege, hizi ndege kununuliwa kwake maana yake zinaporuka nje ya nchi zinatangaza tayari Tanzania ni kitu gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Dkt. Hamisi Kigwangalla kwa kazi nzuri anayoifanya, wakati huo huo nimpe pole kubwa sana kwa sababu kipindi kile baada ya kumaliza bajeti ya mwaka jana, 2018, alipata ajali mbaya sana. Hatukutegemea tena kwamba leo atasimama na kuisoma tena hotuba yake ya bajeti; yote hayo ni kwa sababu ya uwezo wa Mwenyezi Mungu, leo kamrejesha tena ndani ya Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yote hiyo inatokana na jinsi anavyojituma kwa Watanzania. Amesema Mheshimiwa Catherine Magige, amezunguka Tanzania nzima kuona kero ambazo zilikuwepo kwa muda mrefu na miaka mingi ambazo zilikuwa zinawagusa Watanzania; nimpongeze sana na nimpe pole sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze Naibu Waziri, Mheshimiwa Kanyasu, kwa kazi nzuri anayofanya, akimsaidia Waziri. Hata alipokuwa anaumwa alifanya kazi nzuri, lakini pia ushirikiano wake ni mzuri. Vile vile nimpongeze Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanayofanya na ushirikiano wanaompa Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Bodi ya Utalii; bodi hii kwa sasa inafanya kazi, sasa imesimama. Niwapongeze sana kwa sababu Mheshimiwa Jaji na timu yake yote wanafanya kazi nzuri sana ya kuutangaza na kuusimamia utalii kwa ujumla. Hivi karibuni tumeona watalii ambao walifika kutoka China, lakini tumeona mambo makubwa waliyoyafanya. Kwa hiyo, niendelee kuwapongeza kwamba Tanzania sasa inapaa kwa hali ya juu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo, ninze sasa kuchangia Mkoa wangu wa Tabora. Wakati nachangia Wizara ya Viwanda na Biashara nilitoa tahadhari na leo natoa tahadhari kwa sababu haya ninayoyachangia nachangia kwa Waziri, sichangii kama Mheshimiwa Dkt. Hamisi Kigwangalla, nachangia kama Waziri wa Maliasili na Utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tabora kuna vivutio vingi sana vya utalii ambavyo nchi hii ya Tanzania ikitaka kufuatilia vivutio vya Tabora na sababu yake, ni kubwa sana. Tabora kuna njia kubwa ya utumwa ambayo ilikuwa inatoka Tabora kwenda Kigoma, watumwa wale walikuwa wanapita njia ile, nimeomba katika miaka yote hii kwamba hii njia ifanyiwe utafiti ili iweze kuboreshwa na watalii wapite waone jinsi gani watumwa walivyokuwa wanasafirishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile Tabora kuna njia ya watumwa ambayo ilikuwa inapita chini kwa chini kupitia boma kubwa inakwenda railway station ili wasiwatoroke. Kwa hiyo bado vivutio vikubwa sana viko pale. Wabunge wote wa Tabora kila mtu anayesimama ni lazima azungumzie habari ya utalii wa Tabora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna boma kubwa la Ujerumani ambalo liko pale, kwa hiyo hakuna sababu ya kutokuwaleta Wajerumani Tabora ili waone vizazi vyao karne zilizopita walifanya nini, kwa hiyo ni history ambayo itatembea. Hata hivyo, pia kuna maboma makubwa ambayo yaliachwa na Machifu. Tabora ilikuwa inaongoza kwa Machifu, Tabora ndiyo kazi ambayo walikuwa wanafanya na mpaka wakasaidia kusitisha suala zima la utumwa. Kwa hiyo historia ambayo iko pale, nimwombe Waziri aione. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri mimi nikuombe lakini si hilo tu, pia tuna Ugala Reserve ambayo iko pale inasaidia pia, ukiwatoa watalii kwenye mambo ya historia unawapeleka sasa kwenye utalii ambapo wanaenda kupumzika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati napitia vitabu hivi, nimeangalia kwenye ukurasa 69 na 70; nishukuru kwamba Wizara imetambua kwamba kweli kuna vitu vya namna hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado nina ombi, hakuna barabara zinazo unganisha kutoka pale Kwihala kwenda kwenye maboma ambayo yapo, njia za watemi, hakuna. Kwahiyo niombe basi Wizara yako itusaidie kuhakikisha kwamba kuna barabara za lami zinajengwa kutoka Urambo kwenda Ugala, lakini pia ijengwe barabara hata kama kwa changarawe kutoka pale kwihala kwenda kwenye maboma yale ambayo watumwa waliweza kufikia pale, lakini pia Warabu, Stanlety na Livingston walikutana pale. Kwahiyo kuna historia kubwa sana kama wataboresha; lakini pia hata katika ukarabati nimeona pale haipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna historia ya uhuru. Wakati nauliza swali langu namba mia ngapi huko wiki iliyopita walisema kwamba hii historia ya uhuru inakwenda Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo. Hata hivyo ni vizuri pia hata Wizara ya Maliasili na Utalii ikaeleza historia ya Baba wa Taifa, ikaeleza tarata tatu zilipatikanaje, ikaeleza uhuru, kwasababu kuna utalii wa ndani. Watu wengine wanasoma tu kwenye vitabu lakini Tabora bado ipo, kuna watu ambao wamesoma Tabora, Tabora Waingereza waliitambua na ikawa ina shule nzuri, Kuna watu waliosoma Tabora Boys na Tabora Girls. Kwahiyo historia yake bado ikipangwa vizuri utalii unaweza ukafanikisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini si hilo tu kuna suala zima ambalo nilitaka niliongelee, la TAWA. Wakati nimeuliza swali langu hapa nilimuuliza Naibu Waziri kuhusu Bodi ya TAWA, haijakabidhiwa mpaka hivi leo, tangu ya Naibu Waziri alivyotoa kauli, kwamba sasa mkoa iwakabidhi. Sasa hivi TAWA ina mipango mizuri lakini haiwezi kufanya kazi, haina meno. Siku ile niliomba sana kwa Mheshimiwa Naibu Waziri, kwamba kwa nini utaratibu huu haufuatwi? Kama Wizara imetoa amri, maelekezo au waraka, kwamba sasa Bodi ile ianze kufanya kazi; hakuna kazi inayofanyika kwenye game reserve, hakuna kazi inayofanyika kwenye Zoo ya Tabora Manispaa; hakuna chochote kinachofanyika kwa sasa kwasababu hawana meno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka nipate majibu vinginevyo hapa tena ndiyo itakuwa tabu. Nipate majibu kwanini mpaka sasa Bodi hiyo haijapewa nafasi ya kufanya kazi, na kwanini hawajahamisha kuwapa madaraka kutoka Mkoani kwenda kwenye Bodi hiyo ambayo ni ya TAWA? Mpaka sasa hawajapewa kitu chochote na bado makabidhiano hayajafanyika, hii figisufigisu inatoka wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine nililotaka kuchangia ni kuhusu Chuo cha Nyuki; hapa sasa leo napongeza. Niipongeze sana Wizara hii na hasa niwapongeze kwa kazi nzuri wanayofanya kwasababu sasa kuna mabadiliko ya Chuo cha Nyuki. Yale mahitaji ambayo yalikuwa yanahitajika kwa kweli angalau Serikali imefanya kazi nzuri na imetambua. Sasa kwa kuwa kitakuwa chuo rasmi sasa cha kufuga malkia wa nyuki ni vyema sasa niiombe Serikali iongeze fedha na fedha zipelekwe kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ombi langu kwa Chuo cha Nyuki, kuna uzio ambao walitoa ahadi kwamba utajengwa; niombe sasa fedha ziende kwa wakati ili ule uzio ujengwe kwasababu wananchi wanasogea na wakisogea wananchi kuwatoa ni gharama kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwahiyo mimi niiombe Wizara ya Maliasili na Utalii, nikuombe sana Mheshimiwa Kigwangala, hebu iangalie hii mipaka, kwa sababu kuna Chuo cha Ardhi ambacho kiko pembeni na kuna shule ya Msingi. Kwahiyo tusipoziba uzio na tusipoweka mipaka ya uhakika tutakuja kuwaondoa wale kwa gharama kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwahiyo mimi msisitizo wangu ni huo, kwamba Bodi ipewe meno ya kufanyakazi, kwasababu hata kama ina mipango ya kufanya kazi haitafanyika kwasababu tunakwenda kwa utaratibu na tunakwenda kwa sheria. Sasa kama ni sheria basi utakapokuja hapa kumalizia kutoa majibu nipate jibu sahihi lini Bodi ya TAWA itapewa meno ya kufanyia kazi au itakabidhiwa rasmi ili waweze kufanya kazi hiyo lakini…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono asilimia 100.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi kwa Waziri, Mheshimiwa Profesa Joyce Ndalichako, Naibu Waziri, Mheshimiwa Injinia Stella Manyanya na Katibu Mkuu wa Wizara kwa kazi nzuri na hotuba iliyosheheni utaalam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule kongwe zenye historia kubwa hapa nchini ni pamoja na Tabora Girls ambayo imetoa viongozi wengi lakini ina hali mbaya hasa kukosa uzio. Pamoja na hayo, watu wamevamia na kujenga kwenye eneo la shule. Hivyo, niiombe Serikali inapotoa fedha za ukarabati iangalie shule hiyo. Bwalo la chakula kwa wanafunzi hao ni la muda mrefu na miundombinu yake haifai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule kongwe nyingine ni Tabora Boys na Milambo. Shule hizi ni muhimu sana katika historia ya nchi hii. Ni shule zenye kumbukumbu na historia kubwa ya Baba wa Taifa, lakini hazina uzio, majengo ni machakavu sana pia hata miundombinu ya maji ni hatari kwa afya zao na matundu ya vyoo ni machakavu. Nashauri pamoja na uhaba wa fedha ni vema wakaanza ukarabati huo kwani wanafunzi wanateseka sana. Ningeomba sana mchango wangu uangalie kwa jicho la huruma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu madai ya walimu naomba yazingatiwe na yalipwe kwa wakati. Vilevile ukarabati wa shule ni vema uende sambamba na ukarabati wa nyumba za walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto ya wazabuni kutolipwa madai yao. Wazabuni hawa wanaolisha shule wanadai fedha nyingi na kusitisha huduma kimya kimya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hotuba hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Tabora una Kambi ya muda mrefu ambayo inaitwa Milambo Barracks. Kumekuwa na changamoto za uchakavu wa miundombinu ya barabara zinazozunguka kambi hiyo ya muda mrefu. Niombe Serikali iangalie mambo yafuatayo:-

Kwanza, ukarabati wa barabara, pili, ukarabati wa nyumba zao na tatu, ukarabati wa jengo la geti lililoko kabla ya kuingia ndani ya kambi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha niiombe Serikali kupeleka vifaa vya kisasa kwa ajili ya Hospitali ya Jeshi, ipeleke Madaktari Bingwa hususani wa magonjwa ya wanawake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuomba msaada huo kunatokana na kutokuwa na Hospitali ya Manispaa ya Wilaya na hivyo kusababisha watu wengi kwenda Jeshini kupata huduma hiyo. Miundombinu ya maji ikarabatiwe kwani ni michakavu sana.

Vilevile Serikali ilipe madeni ya maji/TANESCO ili kusitokee ukataji wa huduma hizo kwenye majeshi kwani kukatiwa huduma hizo ni aibu kubwa. Fedha za matumizi hayo zipelekwe kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali kupeleka fedha zilizoombwa bila kupunguza, pia kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hotuba hii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo cha Tumbi kimesahaulika kwa ukarabati wa majengo, upungufu wa wakufunzi, mashamba darasa kutengewa fedha za kutosha. Mashamba darasa hayo yanatumika kwa kufundishia kwa vitendo; madai ya watumishi yalipwe kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu zao la tumbaku, natoa pongezi kwa kutatua tatizo la wakulima wa zao hilo kutoka Chama Kikuu cha Ushirika cha WETCU. Niombe Serikali kuhakikisha madai ya wakulima ambao walipunjwa na wanunuzi ili walipwe haki zao. Pembejeo zipelekwe kwa wakati, watumishi wanaodai haki zao WETCU walipwe kwani ni ya muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Benki ya Kilimo, nashauri benki hiyo tufunguliwe dirisha Tabora ili wakulima waweze kukopeshwa. Wakulima wakopeshwe matrekta ili wapunguze umaskini kwa kulima kilimo cha kisasa. Wakulima watafutiwe masoko ya uhakika kwa mazao yao. Tuombe benki iweze kusaidia wakulima wadogo wadogo hasa wanawake, wafugaji pamoja na wavuna asali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kupunguza zaidi idadi za tozo hususani kwenye zao la tumbaku ili bei ya uuzaji ipande. Kiongozi wa Ushirika angalau awe kidato cha nne, kwani kukosa elimu kwa viongozi kunachangia kuibiwa kwa fedha za wakulima. Pia mizani ya kupimia tumbaku (uzito wa kilo) iwe inakaguliwa mara kwa mara, masoko ya tumbaku yasicheleweshwe kwani kuchelewa kununua kunapunguza uzito, ndio ujanja wa wanunuzi na mawakala wao. Tuwasaidie wakulima wetu kama azma ya Serikali ya Awamu ya Tano.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono taarifa ya Kamati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niipongeze MVIWATA kwa kazi kubwa wanayoifanya kutoa ushauri, elimu kwa wakulima hapa nchini. Pamoja na hayo, niombe Halmashauri zetu kuunga mkono kazi wanayofanya kama vile kuunda vikundi vya umoja, kujenga masoko ya kuuzia mazao yao. Hivyo, nishauri Serikali kuunga mkono juhudi za MVIWATA kwa kutatua changamoto zilizopo hivi sasa kama ifuatavyo:-

(i) Kurejesha kwa wakati gawio la ushuru wa asilimia 35 wa kuendesha shughuli za masoko kwani Halmashauri nyingi hazirejeshi;

(ii) Kukarabati barabara za vijijini zinazokwenda kwenye masoko;

(iii) Kuzuia wakulima kuuza mazao yakiwa shambani;

(iv) Kuzuia mazao yanayozidi kilo 100 kama vile rumbesa;

(v) Kupunguza kodi ambazo ni utitiri kwenye vikundi vya SACCOS ambavyo vinaendesha masoko;

(vi) Kuweka ulinzi kwenye njia za panya wanazotorosha mazao bila kulipa ushuru.

(vii) Kupeleka mbolea kwa wakati;

(viii) Serikali itoe elimu kwa vikundi vya MVIWATA;
na

(ix) Kujenga viwanda vya kuchakata mazao.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na Sera ya Viwanda na Biashara, nashauri Serikali ifufue na kuimarisha Vyuo vya VETA katika mambo yafuatayo:-

(i) Ifundishe mafundi mchundo ili kukidhi mahitaji ya viwanda vitakavyoanza;

(ii) Mafunzo maalum ya ujasiriamali yatolewe; ma

(iii) Chuo cha VETA Tabora kipelekewe vifaa vya kisasa kwani ni chuo kikubwa; kipelekewe walimu wa kutosha na gari la mafunzo ya driving na wanafunzi wanaomaliza mafunzo wapewe mitaji ili wajikwamue kimaisha na kuendeleza ujuzi wao (cherehani, vifaa vya ujenzi na kadhalika).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu rushwa, nashauri mitaala ianzie kidato cha kwanza mpaka cha nne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu upungufu wa walimu, nashauri Serikali iangalie kujaza nafasi kwenye shule zenye upungufu mkubwa hasa vijijini wa walimu wa masomo ya sayansi na hesabu, kukamilisha maabara nchini na kuwapa mikataba walimu wa masomo ya sayansi na hesabu waliostaafu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ukarabati wa shule kongwe, niipongeze Serikali kwa kukarabati shule kongwe hapa nchini. Naishukuru kwa kuona umuhimu wake kama vile Shule ya Wasichana Tabora lakini bado kuna kero kubwa ya uzio kwenye shule zote za Mkoa wa Tabora ambazo ni Tabora Girls, Tabora Boys, Milambo na Kazima. Niiombe Serikali kuongeza bajeti kwenye shule hizo ili tukamilishe maana ya ukarabati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, madeni ya watu mbalimbali wanaoidai Serikali. Niiombe Serikali tulipe madai ya wazabuni, walimu na wakufunzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule ya wasiojiweza/ wasioona. Niombe wapewe walimu wa kutosha katika ngazi ya shule za sekondari na vyuo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na nianze na suala la elimu ya uvuvi. Kwa kuwa wavuvi wadogo hawana uelewa wa nyavu zinazofaa na zisizofaa, ningeshauri Serikali iendelee kutoa elimu kwa njia mbalimbali kama vile tv, local radio pamoja na vipeperushi vya lugha rahisi. Pia kutoa elimu mbalimbali ya madhara ya uvuvi huo, viongozi mbalimbali na vikundi wapewe semina kwenye eneo husika na Serikali iwasaidie wavuvi wadogo wadogo wenye vikundi mitaji yenye mikopo ya riba nafuu.

Mheshimiwa Spika, kuhusu upungufu wa ajira, Serikali iajiri Maafisa Mifugo kwenye maeneo mengi kwani upungufu ni mkubwa. Wafanyakazi wa Idara hizo hasa ngazi ya chini wapewe vitendea kazi kama vile pikipiki na kadhalika na madai ya watumishi wa ngazi zote yalipwe kwa wakati, kupandishwa madaraja kwa wakati kutokana na elimu zao, kusiwe na watumishi wanao kaimu kwa muda mrefu na maafisa samaki waongezwe.

Mheshimiwa Spika, wafugaji wapewe elimu ya ufugaji bora, kupunguza mifugo, kufuga kisasa, kuchungia eneo moja na kuondoa migogoro ya ardhi. Pia viwanda vya maziwa (usindikaji) vijengwe kwenye mikoa yenye mifugo mingi.

Mheshimiwa Spika, niiombe Wizara ije Mkoani Tabora kutoa elimu kwenye kiwanda cha maziwa ili kiboreshwe, ikiwezekana kuingia ubia na wawekezaji, kutafuta masoko ya mafuta ya samli, kutafuta wawekezaji wa viwanda vya nyama kwenye maeneo ya mifugo.

Mheshimiwa Spika, pia kukagua machinjio mara kwa mara, usafi, upimaji mifugo inayoingia machinjioni, idadi ya ng’ombe wanaotoka safari na kuingia minadani.

Mheshimiwa Spika, madawa ya mifugo yapelekwe kwa wafugaji ili wasisumbuliwe na mawakala, kutengwe maeneo kwa ajili ya malisho, kujengwe mabwawa kwa maeneo yenye mifugo mingi na ukarabati wa mabwawa.

Mheshimiwa Spika, Serikali ione umuhimu wa kuongeza bajeti ya mifugo ili sekta hii iweze kuwa rafiki na wavuvi, wafugaji ili iweze kuboresha miundombinu. Bajeti ikiongezwa itasaidia ufuatiliaji na kero mbalimbali. Wafanyakazi kazi wapate mafunzo ya kisasa ili waboreshe elimu zao.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, pongezi kwa Mheshimiwa George Mkuchika, pia Mheshimiwa Dkt. Mary Mwanjelwa kwa hotuba nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, natoa pongezi kwa Mkurugenzi wa TASAF kwa kazi nzuri ya kusaidia kupunguza makali kwa wananchi walio masikini, angalau kwa sasa wanakula milo mitatu, watoto wanaenda shule na wanawake wengi wamepeleka watoto Clinic.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo wa awamu ya tatu isaidie walengwa ambao wamefanikiwa kujikwamua kwa maendeleo ili wale ambao hawakuingia awamu ya kwanza na ya pili, kutoa nafasi nao wawezeshwe. Pongezi kwa kutafuta wafadhili wenye mikopo nafuu ili kusaidia maendeleo kutokana na bajeti kuwa finyu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni MKURABITA. Serikali iongeze bajeti ya maendeleo ili kupunguza migogoro ya ardhi, pia wananchi waweze kupata hati za kimila na kuweza kukopa. Serikali iendelee kufuatilia fedha za maendeleo za mwaka 2018/2019 ili zitolewe kabla ya Juni, 2019 zifanye kazi iliyokusudiwa. Hata hivyo, naomba MKURABITA ibuni jinsi ya kupata wafadhili kwa kuandika michangonuo ya mikopo yenye riba nafuu kama walivyofanya TASAF kwa kutegemea Serikali hawajafikia malengo waliyokususidiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara iangalie jinsi ya kumaliza suala zima la watumishi wanaokaimu kwenye ofisi mbalimbali, kupandisha madaraja kwa wale wanaostahili, uhakiki na madeni ya watumishi yafanyike haraka, vibali vya ajira vitoke haraka kwenye Wizara mbalimbali kutokana na wahitaji ili watumishi waajiriwe hasa katika huduma ya afya na elimu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mheshimiwa Ummy Mwalimu, Waziri wa Wizara hii, Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote kwa hotuba nzuri yenye uelewa, pia kwa kazi nzuri wanayofanya kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru sana kwa ongezeko la madawa na vifaa tiba. Ushauri; kwa kuwa Hospitali ya Rufaa Kitete ina majengo ambayo hayajakamilika, niombe Serikali ikamilishe ili yaweze kutumika hasa Chuo cha Uuguzi. Nishauri pia katika majengo yanayojengwa sasa ni vema yakazingatia ujenzi na jengo la mama Ngojea, ili wanawake wengi waweze kupumzika wanaposubiri kujifungua, ishirikiane na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wizara kutenga sehemu maalum katika kila Kituo cha Afya kwa ajili ya kutunzia watoto Njiti.

Mheshimiwa Naibu Spika, magonjwa; niombe elimu iendelee kutolewa kwa ajili ya ugonjwa wa dengue, Ini, ili wananchi wengi waweze kujua tiba yake, tahadhari pia. Kwa nini ugonjwa huu wa dengue haupo kwenye Bima za Afya? Kwani wananchi wengi wanasumbuka.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile naomba Serikali ipeleke mashine za kupimia sukari katika Vituo vya Afya na Zahanati ili kuokoa maisha ya wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Benki ya Wanawake; kwa kuwa benki hii tangu ianze haijatoa gawio lolote mpaka sasa na mimi nikiwa ni mhanga wa kutoa hisa (hisa Milioni mbili) nini hatima yangu? Kwa kuwa fedha yangu imekaa muda mrefu, je, naruhusiwa kuuza hisa zangu, ili niipate fedha yangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Benki ya Wanawake lini itafika Mkoa wa Tabora ili wanawake waweze kukopa. Niombe Serikali iweke Dirisha la ukopaji kwenye Benki ya TPB.

Mheshimiwa Naibu Spika, usafi wa mazingira, kwa kuwa maeneo mengi hususan Hospitali ya Rufaa Kitete kuna vifaa chakavu kama vile vitanda, meza na magari, je, hakuna utaratibu wa kuuza au kuviondoa kwenye eneo la hospitali na kupeleka eneo lingine? Kwa kuwa vinawekwa eneo la nje na kusababisha mazalia ya mbu. Niombe Wizara itembelee hospitali yangu na kuona hali halisi (Kitete Tabora).

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971; niishauri Serikali kuleta haraka Sheria ya Mabadiliko ya Sheria Ndoa ili wanawake na watoto wapewe haki zao. Ukatili wa kijinsia unaongezeka hapa nchini, kunyimwa haki wajane na kudhulumiwa mali zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono.
Muswada wa Sheria ya Serikali Mtandao wa Mwaka 2019
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza ni Mjumbe wa Kamati hii, lakini pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati hii. Nichukue nafasi hii kwanza kabisa kuwapongeza Mheshimiwa Waziri George Mkuchika, Naibu Waziri Dkt. Mwanjelwa na Mheshimiwa Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee nimpongeze Mheshimiwa Kairuki, kwanini nasema hivyo? Kwa sababu wakati tunaanza mchakato huu yeye alikuwa Waziri, mchakato huu ulianza kwenye Kamati yetu baada ya kutembelea sehemu zote ambazo wakala alikuwa anasimamia. Dkt, Jabir amefanya kazi nzuri sana. Baada ya kuzunguka sasa baadaye kwa sababu ofisi haihami na documents hazihami, walipofika Mheshimiwa Mkuchika pamoja na Mheshimiwa Dkt. Mwanjelwa wakafuata yale na kukamilisha yale mahitaji ya Kamati. Kwa hiyo, niipongeze sana Wizara kwa kukubali mapendekezo yote ya Kamati tangu mwanzo na hatimaye leo Muswada ule umeletwa mbele ya Bunge lako tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo baada ya pongezi hizo nimeona yafuatayo lazima niyaseme. Wakati tumeanza akiwa wakala mtandao upande wa TEHAMA tulipata shida sana kwa sababu mambo mengine walikuwa hawana mamlaka tena kwa hiyo walikuwa wanafanya mambo sivyo ndivyo lakini sasa wakipata mamlaka kamili nina imani tutakwenda mbali na mtandao hautachezewa tena. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia hii sheria ikipitishwa leo humu ndani niwashawishi Wabunge wenzangu tuikubali kwa sababu sisi tumepata uelewa kwa niaba ya Bunge na tumehakikisha kwamba yale ambayo yanastahili kurekebishwa tuliyapeleka kwenye Wizara na matokeo yake Kamati imekubali mambo yote, lakini nitoe angalizo, baada ya kupatikana na kutungwa kwa sheria hii sasa, niwaombe mamlaka waliyopewa sasa wasimamie mambo mengi sana. Wasimamie kwenye mtandao hususan wa simu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi utapeli ni mwingi, wanatumia mtandao kwa sababu kulikuwa hakuna sheria wanatapeli, hususan vijijini kwa hiyo wanafanya mambo ambayo hayapo hususan kwenye haya mambo ya kampuni ya Tigo, Voda, Airtel na Halotel. Nina ndugu yangu ambaye alitapeliwa. Nimetuma pesa dakika hiyo hiyo akaulizwa wewe ni fulani akajibu ndiyo. Umepokea shilingi fulani akasema ndiyo. Wakamwambia hiyo hela imekosewa inatakiwa irudishwe. Kwa hiyo, tuangalie na mchezo ambao uko ndani ya mitandao kwenye sehemu husika, watu wamelia hususan vijijini hawajui chochote. Kwa hiyo, niombe inapoanza kazi sasa na meno haya tuliyowapa kama mamlaka ichukue hatu kwa vyombo hivyo na hasa makampuni ambayo yanazembea na kuendeleza utapeli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine niombe kwa kuwa tunawapa meno leo usajili wa simu usimamiwe ukamilike. Kwa sababu uharibifu huu unatokea kwa sababu chip nyingi zinauzwa mitaani, ukitaka laini unanunua mtaani. Kwa hiyo, sasa hivi kwa udhibiti na meno haya mimi nina imani kazi kubwa ataifanya ambayo itatuletea heshima na Serikali Mtandao sasa itakuwa inafanya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo ningeliomba Wizara ni kwamba isimamie taasisi zote ambazo ziko chini ya Serikali kuhakikisha zinaingia kwenye mfumo huo kwa ajili ya kuboresha mapato. Zamani walikuwa wanasuasua kwa sababu hawakuwa na meno sasa kwa sababu wana meno basi tuhakikishe kila fedha ya Serikali ipite kwenye mtandao huu, kusiwe na pesa ambazo zinatoka nje ya mfumo huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika kanuni, tuhakikishe inaweka adhabu kali kwa wale ambao watakiuka sheria ambayo leo tunaipitisha. Kwa hiyo, wale watu wapate adhabu kali na sheria isimamie sawasawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Serikali mtandao itatusaidia pia, zamani mafaili yalikuwa yanapotea, kumbukumbu na nyaraka zote zilikuwa zinapotea lakini kwa hili hata wastaafu hawatapata shida, kwa sababu itakuwa zimeingia kwenye data kiasi ambacho kazi yake itakuwa ni rahisi kwa Serikali pia hata mtu anapostaafu anapata haki yake sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niombe sheria hii isaidie kudhibiti udukuzi ambao upo sasa hivi kwenye mitandao, kwa sababu mamlaka ukishapewa sasa hukaimu wala siyo wakala, kwa hiyo, utafanya kazi ambayo ni ya uhakika kiasi ambacho itatusaidia. Kwa mfano, sasa hivi usajili wa ajira, usajili wa wanafunzi imekuwa rahisi hata kijijini sisi tulipata uelewa huo. Hata kijijini watu wamesajili kwenda chuo kikuu, kupata ajira na kwenda JKT. Kwa hiyo, sheria hii ikisimamiwa vizuri na mamlaka waliopewa nina imani sasa tutasonga mbele na tutakwenda sawasawa, hatujachelewa. Mambo mengi yamechelewa lakini ni kwa sababu walikuwa wakala lakini sasa kuna mamlaka kazi kubwa itafanyika kiasi ambacho Serikali itakuwa imetendea haki wananchi wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, niipongeze sana Serikali kwa kukubali kuuleta Muswada huu. Nimpongeze AG pia kwa kukubali yale masahihisho ambayo tumeyapeleka sisi Wabunge lakini ameyafanyia kazi na yamepita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja asilimia 100. Ahsanteni sana. (Makofi)