Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Munde Abdallah Tambwe (32 total)

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii niweze kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, nianze kuipongeza Serikali kwa kutupelekea madaktari wawili kwenda kusoma waje kuwa Madaktari Bingwa kwa sababu hiyo ndiyo njia pekee ya kutusaidia sisi ambao tuko mikoa ya pembezoni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile nimhakikishie Mheshimiwa Waziri wale ma-volunteer wa Kichina watano anaosema ni Madaktari Bingwa, wanaingia hospitali saa 5.00 na kutoka saa 7.00. Kwa maana hiyo, hawatusaidii ile ni Hospitali ya Rufaa, wagonjwa wanaingia ndani ya masaa 24. Kwa hiyo, wale Madaktari wa Kichina watano anaowasema hawatusaidii ipasavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimekuwa nikisema Bungeni hapa toka 2011 nikidai Madaktari Bingwa wa Mkoa wa Tabora, akina mama wanapata vifo vingi vya uzazi, watoto wetu wanakufa kwa sababu hatuna Madaktari Bingwa, vijana wetu madereva wa bodaboda wanavunjika miguu, hatuna Madaktari Bingwa wa Mifupa. Hii imekuwa kero kubwa kwetu sisi Wabunge ndani ya Mkoa wa Tabora na nimekuwa nikilisemea hilo kwa muda mrefu toka 2011 naingia hapa Bungeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri hajanijibu vizuri, ana mkakati gani wa kutuletea Madaktari Bingwa ndani ya Mkoa wa Tabora?
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeomba vibali miaka 10 iliyopita lakini hatujapewa kibali cha kuajiri Madaktari hao. Naomba anijibu ana mkakati gani wa kutuletea Madaktari Bingwa katika Mkoa wa Tabora kwa sababu watu wanakufa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kuhusiana na vifaa. Niipongeze Serikali kwa mkakati wake mzuri wa kusema kwamba Bima ya Afya itatukopesha na tupate vifaa ndani ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora. Hospitali ni ya siku nyingi, haina vifaa vyovyote, watu wanaendelea kufa. Hata hivyo, nimesema hatuna huduma ya ICU pale Tabora…
Mheshimiwa Naibu Waziri, yuko tayari kufuatana nami kwenda Tabora kuangalia changamoto zilizopo katika Hospitali ya Rufaa?
NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, usimuone Mheshimiwa Munde ana-rap sana ni kwamba ameguswa na jambo hilo na ndiyo maana nimesema kwamba Serikali imepeleka madaktari kwa ajili ya kwenda kubobea katika maeneo hayo na lengo kubwa na mahsusi ni kwa ajili ya Mkoa wa Tabora, hili ni jambo moja kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nafahamu fika, wiki chache zilizopita nilifika Mkoani Tabora pale. Nilienda katika Kituo cha Afya cha Bukene na Itobo, kote kuna vifaa vya upasuaji vinataka wataalam. Hata katika kipaumbele chetu tumesema suala la Mkoa wa Tabora lazima liwe kipaumbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe sana wataalam wetu, mara nyingi sana hospitali zilizoko pembeni madaktari wanaona ni tabu sana kwenda kwenye maeneo hayo. Sisi sasa hivi tumejipanga, lengo letu ni kuelekeza wataalam kwenye maeneo yote ya pembezoni na kuhakikisha kwamba wataalam wanaosomeshwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanaenda kuwahudumia Watanzania.
Suala la vifaa nimesema pale mwanzo na Waziri wa Afya na yeye analizungumza mara nyingi sana kwamba suala la vifaa kuna utaratibu maalum. Naomba niwaambie, kuna mchakato mkubwa sana wa hivi vifaa mwisho wa siku Hospitali zote za Kanda na Mikoa zifungiwe vifaa maalum ili mradi akina mama na wagonjwa mbalimbali waweze kuhudumiwa. Huu ni mpango mkakati wa Serikali na unaanza mwaka huu. Kwa hiyo, dada yangu Munde usihofu, mimi mtani wako umesema tuongozane, nitaongozana na wewe Mungu akijalia. (Makofi/Kicheko)


WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi (TAMISEMI), napenda kuongeza kidogo ufafanuzi katika suala la uhaba wa watumishi especially Madaktari Bingwa, nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuwathibitishia Waheshimiwa Wabunge kwamba tumefanya tathmini ya uhaba wa watumishi katika sekta ya afya, especially Madaktari na Madaktari Bingwa. Tumebaini mikoa tisa ina uhaba mkubwa ikiwemo Tabora, Simiyu, Katavi, Geita, Shinyanga, Rukwa na Singida.
Kwa hiyo, kipaumbele cha ajira za Madaktari Bingwa katika mwaka huu tunatoa katika mikoa hiyo tisa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Munde na Waheshimiwa Wabunge wengine wote ambao mnatoka katika hiyo mikoa tisa tutawapa kipaumbele kwa sababu mnao uhaba wa wataalam chini ya 52%. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumekusudia kufanya zoezi moja kugumu sana. Tunataka kuondoa tatizo la Madaktari Bingwa wataalam kurundikana katika mkoa mmoja na kuiacha mikoa ya pembezoni, kwa hiyo, tunataka kuangalia mgawanyo.
Waheshimiwa Wabunge mtuvumilie tutakapoendesha zoezi hili gumu mkasema huyu naomba umbakize, mwanamke wa Rukwa, Katavi, Njombe, Simiyu, ana haki ya kupata huduma za Daktari Bingwa kama mwanamke wa Dar es Salaam. Kwa hiyo, tunataka kuendesha zoezi la redistribution, tuwatawanye madaktari waende mikoani wakatoe huduma ili wanawake wa huko wapate huduma nzuri kama wanawake wa Dar es Salaam, Arusha na Kilimanjaro.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. (Makofi)
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nami nimuulize swali dogo Mheshimiwa Naibu Waziri.
Kwa kuwa, toka Bunge lililopita niliiomba Serikali itufungulie dirisha dogo la Benki ya Wanawake katika Mkoa wa Tabora na kwa kuwa, Mkoa wetu uchumi wake ni duni sana, yeye anafahamu, je, yuko tayari yeye au Waziri wake kwenda Tabora na mimi au kuja Tabora kuongea na wanawake wa Tabora, kuwapa ahadi ya ukweli yeye mwenyewe, kwa sababu mimi nilishaahidiwa hapa Bungeni litafunguliwa dirisha dogo mpaka leo halijafunguliwa, ili uwaambie ni lini sasa Serikali itakuwa tayari na benki hiyo, kuwafungulia dirisha dogo wanawake wa Mkoa wa Tabora ili nao waweze kufaidika na keki hii ya Taifa letu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Munde Tambwe Abdallah kwa swali lake la nyongeza na hapo naona ananitega tu kwa sababu mimi mwenyewe natokea Tabora. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ni ahadi ya Serikali toka awamu iliyopita kufungua matawi Mkoani Tabora kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge anasema, naomba nitoe maelekezo kwa Mkurugenzi wa Benki ya Wanawake Tanzania, afanye haraka sana kwenda kufungua madirisha hayo Mkoani Tabora ili kutekeleza ahadi za Mawaziri waliokuwepo kabla yetu sisi hapa Bungeni, kwa sababu Serikali inaendelea kuwepo hata kama Mawaziri wanabadilika.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Kwanza kabisa nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini pia, niipongeze Serikali kwa kuonesha baadhi ya mikakati yao inayoendelea nayo na ninayo maswali mawili ya nyongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, je, Serikali kupitia diplomasia yake ya kiuchumi nchini ina mkakati gani wa kuwashawishi wakulima wakubwa wa tumbaku nchini China waje kuingia ubia na wakulima wadogo wa tumbaku Mkoani Tabora, ili wakulima wa tumbaku Mkoani Tabora waweze kupata faida kubwa na yenye tija na kuona kilimo cha tumbaku sasa kinawasaidia, tofauti na hali ilivyo sasa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa vijana wengi nchini wamejiajiri kwenye biashara ya bodaboda, hususan Mkoa wangu wa Tabora ambao vijana wengi wanaoendesha bodaboda hizo zisizo zao, je, Serikali kupitia diplomasia yake ya uchumi nchini inaweza leo kunihakikishia hapa kwamba, itafanya kila liwezekanalo kuhakikisha Mkoa wa Tabora unapata kiwanda cha pikipiki kutoka kwenye viwanda vikubwa kama SanLG, labda Boxer na viwanda vingine vyovyote vilivyopo China, ili kuweza kuwapatia vijana hawa pikipiki kwa bei nzuri, ili na sisi watu wa Mikoa ya Tabora, Katavi, Sumbawanga, Kanda ya Ziwa, tuweze kujikomboa kiuchumi kwa kupitia diplomasia hii? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Munde kwa kufanya kazi kubwa ya kuwatetea wananchi wa Tabora. Naomba niende kujibu maswali yake mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ambalo linahusu jinsi Wizara yangu inaweza kufanya mkakati gani wa kuweza kuwezesha wakulima wakubwa wa China kujakuwekeza na kufanya kazi pamoja na wakulima wadogo wa Tabora.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Munde kwamba Wizara yangu ilifanya mkakati huo, sisi kama Wizara ni Wizara kiunganishi, tumefanya mkakati na mkakati huo ni kuwahakikishia kwamba watu wa China wanaweza wakawekeza katika zao la tumbaku na nimwambie tu kwa hali sasahivi ilivyo ni kwamba Balozi wa China nchini Tanzania pamoja na Wizara ya Kilimo wako katika mkakati wa majadiliano wa kuweza kufikia makubaliano ya kujua zao la tumbaku na bei ya tumbaku itakuwaje na sisi tumeaachia wao kama Wizara kwasababu sisi kazi yetu ni kuhakikisha kujenga mahusiano mazuri. Tukishawaleta, wakifika nchini tunawapeleka katika Wizara husika. Mheshimiwa Spika, kwahiyo, nikuhakikishie kwamba wakulima wa Tabora pamoja na wale wakulima wa China watafanya biashara hiyo ya tumbaku lakini baada ya mazungumzo na majadiliano yatakapokwisha kati ya Wizara ya Kilimo na Balozi wa China nchini Tanzania.
Mheshimiwa Spika, lakini la pili la kuhusu bodaboda na kuhusu vijana wa bodaboda waliopo Tabora na Kanda ya Ziwa, nikuhakikishie si tu Tabora na Kanda ya Ziwa lakini kwa Tanzania. Nafikiri umeshawahi kusikia ndani ya Bunge hili Waziri wa Viwanda na Biashara amezungumzia kuhusu suala la watu wa china kuwekeza katika viwanda vya kutengeneza bodaboda hapa Tanzania.
Kwa hiyo, biashara hiyo itakuwepo na watawezeshwa katika namna hiyo na kufundishwa pia jinsi ya kuendesha biashara ndogo ndogo kama ujasiriamali ili kusudi wasiwe tegemezi na waweze kutoka katika utegemezi na kufanya kazi yao vizuri.
Mheshimiwa Spika, niendelee kumhakikishia Mheshimiwa Munde kwamba sisi kama Wizara kwa kutumia diplomasia ya kiuchumi tutaendelea kupambania Tanzania iende katika kuhakikisha kwamba inatimiza ahadi yake ya kuhakikisha kwamba Tanzania inatoka katika hali ya kawaida na inakwenda katika uchumi wa viwanda.
Mheshimiwa Spika, tutatumia diplomasia hiyo kwa kutumia Mabalozi wetu wote waliopo nje na wale waliopo Tanzania na kutumia vijana wetu na watumishi wetu wenye ujuzi na weledi uliostahiki katika kuhakikisha kwamba miradi hii na projects zote ambazo tunazikuta katika mikutano na sehemu mbalimbali zinaletwa Tanzania na kuwafaidisha na kunufaisha Watanzania kwa ujumla wake, ahsante. (Makofi)
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa swali la msingi linaongelea suala la visima; na kwa kuwa Tabora Manispaa wananchi walichangia pesa kwa ajili ya uchimbaji wa visima kwa masharti ya mradi lazima kila Kata ichangie pesa ndiyo wachimbiwe. Visima hivyo vilichimbwa maji hayakupatikana.
Je, Mheshimiwa Waziri anaweza kutuambia na kwa sababu Serikali ilifanya research Mheshimiwa Waziri anaweza kutuambia yule mtu aliyefanya research na kutupotosha wananchi pamoja na mradi, tuchimbe visima virefu wakati hakuna maji, Serikali ilimchukulia hatua gani? Ili tuweze kujua kwa sababu pesa za Watanzania zimepotea na pesa za mradi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi walichangishwa pesa, utafiti ulifanyika, lakini visima vikachimbwa na havikutoa maji! Kwa bahati nzuri Mkoa wa Tabora ni miongoni mwa mikoa ambayo imepata bahati ya kupata msaada wa Wajapani, Wajapani wana teknolojia ya hali ya juu sana ambayo wao wanaweza wakabaini kama kweli chini kuna maji. Kwa bahati mbaya pamoja na tafiti walizozifanya bado na wao kuna maeneo ambayo wamekosa maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge, kwa kweli teknolojia ya maji chini, bado dunia haijawa nayo. Kwa hiyo, bado tunakwenda kwa kubahatisha. Unaweza ukapima ukakuta maji yapo lakini unakwenda kuchimba unakuta maji hakuna. Vilevile ameuliza kwamba huyu mtu anachukuliwa hatua gani? Huu ni utafiti ulifanyika na kwa bahati mbaya kwamba maji yale hayakupatikana na kimikataba kwa sababu tunafanya kazi kwa kutumia mikataba kama hatukuweka kifungu kwenye mkataba kwamba kama utakosa maji tutakuchukulia hatua fulani basi huwezi kuchukua adhabu yoyote.

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, siyo kwamba tunafanya kwa kubahatisha ila nasema kwamba tunapofanya tunakuwa tumelenga kwamba tutapata maji. Lakini trend au historia inaonyesha kwamba mara nyingi unaweza ukafanya utafiti wa visima kumi lakini ukachimba ukapata visima saba, vitatu vikakosa maji ndiyo maana nikatumia hilo neno kubahatisha. Lakini siyo kwamba tunapofanya utafiti tunafanya kwa kubahatisha hapana tunakuwa tumedhamiria kwamba tunafanya utafiti ili tuweze kupata maji, lakini kwa bahati mbaya kutokana na mabadiliko ya miamba kule chini inatokea wakati mwingine unataka kuchimba visima 100 unachimba visima 80 vinapata maji, visima 20 vinakosa, kwa hiyo hatufanyi kwa kubahatisha.

WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba niongezee kipengele kidogo, ni kwamba tulivyoanza huu mradi wa vijiji kumi, aliyekuwa anafanya utafiti alikuwa ni Mhandisi Mshauri na aliyekuwa anachimba kisima alikuwa ni Mkandarasi. Sasa tumeunganisha kwamba Mkandarasi atapewa mkataba utakaofanya kazi zote za kufanya utafiti na kuchimba. Kwa hiyo, akikosa maji sasa itakuwa ni gharama kwake kutafuta eneo lingine ili kusudi isiwe hasara kwa Serikali.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niulize swali dogo la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize swali dogo la nyongeza. Kwa sababu suala hili limekuwa ni kero ya muda mrefu toka naingia Bungeni humu 2010, watu wanaongelea kuhusu kujazwa kwa magereza na Serikali imekuwa ikitujibu kwamba itafanya upanuzi na itapeleka pesa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, je, Serikali ina mpango mkakati gani wa kutuletea sheria humu Bungeni ili tubadilishe makosa madogomadogo yalipiwe faini polisi; kama yale aliyosema Mheshimiwa Waziri, mtu kanywa soda anawekwa ndani mwezi mmoja, dada amekutwa barabarani akaambiwa anajiuza anawekwa ndani miezi mitatu, mtu amegombana kisimani na mwenzake anawekwa ndani miezi mitatu. Je, Mheshimiwa Waziri, anaweza kuleta sheria sasa tukabadilisha humu Bungeni makosa mengine yakalipiwa faini polisi kama yalivyo ya trafiki?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Munde kwa hoja aliyoitoa na kwa jinsi alivyoleta mapendekezo kwa umakini. Sisi kama Wizara tumepokea na tutaliangalia kwa ujumla wake hili alilolisema na kabla ya hapa, njiani alinishauri tulifanyie kazi na suala la parole kwa kupanua wigo kwa wanaonufaika na parole, wale ambao wamesharekebika waweze kufanya kazi wakiwa nje. Kwa hiyo, tumelipokea na tutakapokuwa tuna fursa ya mabadiliko ya sheria tutazingatia mapendekezo ya Mheshimiwa Mbunge ili kuweza kupunguza msongamano kwa njia hiyo na kuendelea kuwarekebisha watu kwa kadri sheria inavyosema.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa swali la msingi kipengele (b) linafanana kabisa na tatizo tulilonalo Mkoa wa Tabora. Mkoa wa Tabora tulipata mamilioni ya pesa tukajenga chuo cha nursing na theatre ya kisasa, mpaka sasa tumekamilisha kwa asilimia 90 sasa hivi tuna miaka minne bado asilimia 10 tu jengo lile na theatre ya kisasa vianze kufanya kazi.
Mheshimiwa Spika, nilikuja hapa Bungeni nikamuuliza Naibu Waziri Mheshimiwa Kigwangalla akaniambia ataleta wataalam na yeye atakuja na atalifuatilia kwa sababu ni kama milioni 40 na kidogo tu ndiyo zinasababisha lile jengo liharibike na lishindwe kufanya kazi na theatre ya kisasa ishindwe kufanya kazi.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri kwa mara ya pili leo, anawaeleza nini wananchi wa Mkoa wa Tabora kuhusu chuo chao nursing na theatre yao ya kisasa? Na atupe majibu ya ukweli.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Mheshimiwa Spika, nimepokea concern yake nitafika pale Tabora wakati natoka kumzika mzee wetu Mzee Sitta, nitapita pale kukagua na kuona progress imekuwa ni nini kwa sababu tayari suala hili nilikwishaanza kulishughulikia na ninaamini kwamba lingekuwa limepatiwa ufumbuzi kufikia sasa. Kwa kuwa anasema bado naomba nitumie fursa hii ya kwenda mazishi ya Mzee Sitta kupita pale ili niweze kuona hali halisi.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa, zao la pamba linafanana kabisa na matatizo ya zao kubwa la tumbaku la Mkoa wa Tabora; na
kwa kuwa, Mkoa wetu wa Tabora unategemea sana zao la tumbaku. Zao la tumbaku limekuwa na tozo kuanzia 19 mpaka 38 zinazomuumiza mkulima wa tumbaku na kusababisha mkulima huyu faida yake yote kwenda kwenye matozo 38. Je, Serikali ina mpango mkakati gani wa kuhakikisha inapunguza tozo hizi ili mkulima wa tumbaku apate faida kama ilivyopunguza tozo kwenye kilimo cha korosho?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba, kati ya changamoto ambazo wakulima wa mazao hapa nchini wanapata ni tozo nyingi ambazo zinaendelea kuongeza changamoto kubwa
katika uendeshaji wa kilimo. Namwomba Mheshimiwa Mbunge asubiri kusikia hotuba ya bajeti yetu kwa sababu mwaka huu wa fedha unaokuja, Wizara imeamua kuondoa karibu nusu ya tozo zote ambazo ziko kwenye mazao.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, sitaki kuwahi kuanza kueleza yaliyoko kwenye hotuba yetu ya bajeti, lakini nimweleze tu kwamba Serikali tayari ilishatambua changamoto hiyo; viongozi wetu wakuu, Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Makamu wa Rais na Mheshimiwa Waziri Mkuu kila wakati wamesisitiza kwamba tuondoe tozo hizo. Kwa
sasa Wizara imeondoa tozo kwa 50% lakini kama
ninavyosema tukija na maelezo yetu ya bajeti ataona ni tozo gani zimepungua.
Mheshimiwa Spika, vilevile Mheshimiwa Mbunge
atakumbuka kwamba, hivi karibuni katika jitihada za kuondoa changamoto zilizopo kwenye zao la tumbaku (Tabora), Mheshimiwa Waziri Mkuu alienda kule na anajua yaliyotokea kule. Sasa changamoto ya chama kikubwa cha WETCU kuweza kuhudumia vizuri wakulima tayari
inashughulikiwa pamoja na mambo mengine kwa kugawa iwe ni vyama viwili lakini vilevile ubadhirifu ambao umefanyika tayari wahusika wameshachukuliwa hatua.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kimsingi kuna mikakati mingi ambayo inaendelea ya kuhakikisha kwamba tunaboresha zao la tumbaku. Vilevile nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba Jumamosi hii tumeitisha Mkutano wa Wadau wa Tumbaku na nachukua nafasi hii kumkaribisha tarehe 7 kwenye huo mkutano ili aangalie ni
mikakati gani mbayo tumeweka. Nashukuru sana.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kuuliza swali.
Kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba pesa zile za Jimbo huwa zinakwenda kutumika kwa wananchi; na kwa kuwa Wabunge wa Viti Maalum wanafanya kazi na wananchi hao hao; na kwa kuwa tumelisema suala hili kuanzia mwaka 2011 mpaka leo hii na Serikali bado ina kigugumizi, bado inaona ugumu kuwapa pesa Wabunge wa Viti Maalum, huenda bajeti ya Serikali haiko vizuri.
Je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari sasa kwa nia njema kabisa ya kusaidia Wabunge hawa wa Viti Maalum, walau kila Mbunge wa Jimbo husika kwa mfano kwangu mimi nina Majimbo 11, kila Mbunge wa Jimbo husika walau akakatwa asilimia 10 ya Mfuko wa Jimbo ikakaa kwa Mkurugenzi, amount ya pesa zile wakagaiwa Wabunge wa Majimbo siyo kugaiwa cash, zikakaa kwa Mkurugenzi labla mimi nikawa na milioni nne tu, nikaenda eneo fulani nikakuta hamna gloves nikawaambia zile milioni nne Mkurugenzi m-deposit kwa ajili ya kina mama? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima kubwa naomba kujibu swali ambalo nadhani litakuwa swali maarufu la mwaka na limeulizwa kwa staili ambayo haijawahi kufanyika, ninakupongeza Mwenyekiti kwa utaalamu wa kujua Kanuni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali hili linahusu Mfuko wa Jimbo na Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Ester Mmasi, Mheshimiwa Munde Abdallah na wengine wengi Wabunge wa Viti Maalum wanataka na wao wapate mgao wa fedha za Mfuko wa Jimbo. Swali hili siyo kwamba linaulizwa kwa mara ya mwanzo leo, limekuwa likiulizwa na mara nyingi tumekuwa tukitoa majawabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu maarufu ambayo tumeyatoa kwamba tutakwenda kushughulikia tuone utaratibu wake, lakini kila tunaposhughulikia tunapata ugumu kwa sababu mfuko huu umezaliwa kwa mujibu wa sheria, sheria yenyewe inaitekeleza Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mfuko wenyewe unaitwa Mfuko wa Jimbo na kwa hiyo, kuupa jina linguine lolote lile ni kazi ngumu kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, humu ndani kuna Wabunge
wa Majimbo, kuna Wabunge wa Viti Maalum, kuna Wabunge wa Mikoa, kuna Wabunge wanaoteuliwa na Mheshimiwa Rais. Bunge hili likitambua kwamba Wabunge wa aina hizi zote wapo, lilitunga Sheria ya Mfuko wa Jimbo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kwenye instrument yangu kwa mujibu wa sheria nilizopewa kuzisimamia nina sheria inayosema nitasimamia Mfuko wa Jimbo, haisemi vinginevyo. Ndiyo maana kwenye jibu letu la msingi nimesema kama Bunge litaona vinginevyo suala hilo linakuja kwa utaratibu mwingine, lakini kwa sasa mimi ninasimamia Mfuko wa Jimbo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata wale Wabunge waliokuwa wanadai sana mfuko huu, waliokuwa wa Viti Maalum, walipopata majimbo na wenyewe msimamo wao umebadilika, ni kwa sababu ya majukumu anayoyapata Mbunge wa Jimbo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali mengine yameulizwa na Mheshimiwa Masoud Abdallah Salim ambaye ameuliza suala la fedha kuchelewa Zanzibar, hili tumelichukua, tunawasiliana na Ofisi ya Makamu wa Rais tuone utaratibu bora zaidi wa kuweza kufanya fedha hizo ziwafikie Wabunge wa Zanzibar, hasa tunatambua yapo mapendekezo ya kwamba bora zikapita katika Ofisi ya Bunge Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine dogo limeulizwa na Mheshimiwa Paresso kwamba Wabunge wa Viti Maalum hawaingii kwenye Kamati za Fedha. Kamati za Fedha zinatambua uwepo wa Madiwani na Mbunge unapoingia kwenye Halmashauri huwi Mbunge unakuwa Diwani, kule kwenye Kamati ya Fedha wanaoteuliwa kuingia kwenye Kamati ya Fedha huwa ni Madiwani. Sasa nadhani ni utaratibu wa Halmashauri zenu, kama wewe Mbunge kuteuliwa kuna baadhi ya Wabunge ambao wanaingia kwenye Kamati ya Fedha, lakini kule wameingia kwa tiketi ya Udiwani wao kwenye Halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa napata shida hapa
kwa sababu la kwanza, kwamba kwa Majimbo ambayo yana Wabunge wengi wa Viti Maalum, na mfahamu kikao kile kina utaratibu wa gharama zake na mambo mengine. Ingawa gharama siyo hoja kubwa, lakini kwa Jimbo ambalo lina Wabunge wa Viti Maalum nane, 10, sijui hali itakuwaje kwa sababu gharama za uendeshaji wa Halmashauri zitakuwa kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili ingelikuwa Wabunge labda ni mmoja au wawili pengine unaweza kuichukulia hili jambo likawezekana, lakini kwa hali ilivyo kuna tatizo kubwa sana na ninadhani ni vema hili jambo likabaki kama ilivyo na ndio utaratibu ulivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa tiketi ya Udiwani, Mbunge anaweza akateuliwa na Mwenyekiti kwa utaratibu ule akawa Mjumbe wa Kamati ya Fedha.(Makofi)
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ambayo hayaridhishi kabisa, naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; Mheshimiwa Waziri haoni Serikali kushindwa kumalizia majengo haya na kutoa majibu haya ni kuwavunja moyo wafadhili tuliowabembeleza na kuwaomba watujengee majengo haya? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; wafadhili kujenga majengo na kuyamalizia au kutoyamalizia ni jambo la kawaida kabisa kwenye nchi yetu; na kwa kuwa Serikali imesema kwamba haiukufuata sheria wakati majengo yale yamesimamiwa na Engineer wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga. Je, Mheshimiwa Waziri haoni anawanyima haki wananchi wa Igunga kwa kukosa kuwa na VETA yao ambayo wameihangaikia kutafuta wafadhili, bado tu kumalizia lakini wanasema kwamba sheria haikufuatwa wakati Engineer wa halmashauri ndiye aliyesimamia majengo haya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, nadhani hakunisikia vizuri katika jibu langu. Nimesema kwamba shirika linaweza likajenga chuo na kuikabidhi Serikali, lakini kwa sababu katika swali la msingi haikuzungumzwa kwamba chuo hicho kimeshakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachosisitiza ni kwamba, kwa sababu mwisho wa yote hicho chuo itabidi kiendeshwe kwa mujibu wa taratibu na sheria zilizopo, ndiyo maana tunasisitiza kabla ya wadau wetu wa maendeleo kuanza kufanya shughuli ya ujenzi, ni vema kuwasiliana na taasisi husika ili kile wanachokifanya kiendane na viwango na kiweze kuwa na tija kwa maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, sijasema kwamba wao wamejenga bila kufuata sheria. Katika jibu langu la msingi nilisema kwamba ni vema kabla ya kujenga yawe yanafanyika mawasialiano kupitia halmashauri na VETA ili kwa pamoja kuweza kuzingatia masuala ya kisheria. Kwa misingi hiyo, ninachosema ni kwamba, kwanza hicho chuo hatujakitembelea na hatuwezi kukiamuru kama ilivyo, lakini niseme tu kwamba nazidi kuwaomba wadau wa maendeleo, wanapofanya shughuli yoyote ya kimaendeleo kuhusiana na Wizara fulani, ni vema kushirikisha Wizara husika ili kile kinachofanyika kiwe na tija ili fedha zao zisipotee bila utaratibu ambao pengine usingekuwa wa lazima.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii niweze kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Waziri, lakini nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Mheshimiwa Waziri pale manonga tuna Kiwanda cha kuchambua pamba cha siku nyingi ambacho kina utata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuja tukaongea na Mheshimiwa Waziri, akatuahidi kumwita Rajan na Igembensabo ili kuja kutatua tatizo hili na hatimaye kiwanda hicho kiweze kufanya kazi ili wananchi wa Igunda waweze kupata ajira na sehemu rahisi ya kuuza pamba zao. Je, Mheshimiwa Waziri amefikia wapi kuwaita watu hao ambao alituahidi kuwaita hapa Dodoma ili kuja kupatanao mwongozo ili tuweze kujua tunaanzaje kuhusu kiwanda kile cha Manonga Ginnery? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Mkoa
wa Tabora umekuwa na adha kubwa ya ukosefu wa viwanda; na kwa kuwa Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara alituahidi kwamba amepata mwekezaji Mchina wa kiwanda cha kujenga Tumbaku Tabora; na lilitokea tatizo pale Airport hatimaye yule mwekezaji hakuweza kuja Tabora kuongea na sisi ili kuweza kujenga Kiwanda hicho cha Tumbaku. Je, Mheshimiwa Waziri, mpaka sasa status ya mwekezaji huyo ambaye alikuwa anakuja Tabora akapata matatizo Airport imefikia wapi? (Makofi)
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kujadiliana na Rajan juu ya Manonga Ginnery. Tatizo ninalolipata kuhusu Rajan, aliyerithi kiwanda yuko nje ya nchi. Kwa hiyo, nawasiliana naye kupitia mtu wa kati, lakini naomba mwendelee kunikumbusha, mwendelee kunishinikiza kusudi tuweze kufikia suluhu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inaonekana hawa Rajan hawana interest tena na kiwanda na hawako tayari kununua na mwendelee kuwapa shime watu wa Igembensabo waendelee na nia hiyo, tutafikia muafaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la tumbaku; sina mpango tena na yule Mchina ila natafuta wawekezaji wengine wa kuweza kuwekeza kwenye zao la Tumbaku kwa kujenga Kiwanda. (Makofi)
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa na mimi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa sisi wadau wa reli tuna imani kubwa na Wizara lakini tuna imani kubwa na Mkurugunzi wa TRL, Bwana Masanja lakini tumekuwa na kero kubwa ya kutokukata tiketi bila kuwa na kitambulisho huku tukijua mazingira ya stesheni za vijiji zilivyo, tukijua watu wetu wanaoishi vijijini walivyo. Mtu akiwa mgonjwa mahuhuti hana kitambulisho anataka kwenda stesheni yenye zahanati anakataliwa kupewa tiketi. Je, Wizara pamoja na Shirika inakubaliana na mimi kufuta hilo sharti la vitambulisho ili mtu aweze kupata tiketi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimia Naibu Spika, ni kweli kuna adha katika suala la uhitaji wa tiketi na tumeliona hilo, lakini kuna ukweli vilevile wapo watu wengi wamekuwa wakitumia fursa hiyo ya kutotumia kitambulisho kurusha tiketi, wanakusanya tiketi nyingi wanakuja kuwauzia watu wengine. Kwa upande wa pili vilevile suala la kiusalama, watu wengi sana ambao siyo Watanzania wamekuwa wakitumia safari zetu za reli na hivyo kuonekana kwamba TRL inashiriki katika kusafirisha wasafiri haramu. Kwa hiyo, tutaangalia katika hasara na faida ya suala hilo, kwa sasa naomba atuvumilie tutaendelea kufuata huo utaratibu hadi hapo tutakapoona kwamba changamoto hizi mbili kubwa zitafutiwe namna nyingine ya kuzishughulikia.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tabora Manispaa mara mbili tulitenga pesa kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya, tulianza majengo hayo miaka mitatu iliyopita, lakini na mwaka huu wa fedha tumetenga tena bajeti hiyo ya shilingi milioni 120 kwa ajili ya kuendeleza majengo hayo.
Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kutupa pesa ili tuweze kumalizia Hospitali hiyo ya Wilaya ili tuweze kutatua kero kubwa inayoikabili Hospitali yetu ya Rufaa kwa population kubwa iliyopo Tabora Manispaa ili wananchi waanzie kwenye Hospitali yao ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimhakikishie Mheshimiwa Munde kwa sababu muda mwingi sana amekuwa ukipigia kelele Mkoa wake wa Tabora na ndiyo maana kwa mapenzi makubwa mpaka Mheshimiwa Rais akaona amkabidhi ambulance kwa ajili ya wananchi wake wa Tabora katika sekta ya afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hili, naomba nimhakikishie kwamba mwaka wa fedha bado haujaisha, japokuwa tumepeleka fedha za Local Government Development Grants katika Halmashauri mbalimbali waweke vipaumbele tutaangalia kwa Tabora nini kimewekezwa. Naomba nimhakikishie kwa sababu mwaka haujaisha tutajitahidi kwa kadiri iwezekanavyo bajeti ile iweze kufika ili mpango wa bajeti wa Manispaa ya Tabora uweze kukamilika kama ulivyokusudiwa katika ujenzi wa Hospitali ya Wilaya.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize maswali madogo mawili ya nyongeza. Pamoja majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Viwanda napenda kuuliza maswali kama ifuatavyo.
Swali la kwanza; kiwanda cha Nyuzi cha Tabora kinazalisha vifa tiba ambavyo vinatangenezwa na pamba yetu inayolimwa hapa hapa nchini. Inazalisha vifaa kama pamba, bandage na nyuzi. Je, kwa nini Serikali kupitia MSD isimuunge mkono Mheshimiwa Rais maneno yake aliyotamka Mwanza na kununua vifaa tiba kwenye viwanda vyetu vya ndani hususan Tabora badala ya kuagiza nje ya nchi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kiwanda hicho kina uwezo wa kutengeneza sare za wanafunzi (uniform). Kwa nini sasa Serikali isitoe agizo, badala ya kununua sare za shule sehemu tofauti, sare za shule zinunuliwe kwenye viwanda vilivyopo nchini? Kwanza, ili kuchochea uchumi pia kupanua ajira hususan katika Mkoa wetu wa Tabora ambao kwa kweli hauna viwanda vya kutosha. Naamini vijana wetu wa Tabora watapa ajira za kutosha kama sare zitanunuliwa katika kiwanda hicho cha nyuzi cha Tabora.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Ni kweli kabisa iko haja ya kuunga mkono jitihada zinazofanywa na viwanda vyetu nchini ikiwemo vifaa tiba. Kimsingi viwanda hivi wakati vinaanzishwa vilikuwa na lengo la kusaidia kutoa malighafi katika viwanda vingine, lakini baada ya kuanza biashara huria na mikataba mbalimbali tuliyosaini Kimataifa, tumejikuta kwamba baadhi ya viwanda vyetu vinashindwa kuzalisha kutokana na wadau waliokuwa wanunue vifaa hivyo kutoka kwetu wanaamua kuagiza kutoka nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, hilo ni suala ambalo Wizara tayari tumeshaliona na tunalifanyia kazi. Vilevile kuimarisha masoko ya ndani na nje kwa hiyo kitengo chetu kitaendelea kufanyia kazi eneo hilo na hivyo niwaombe MSD waweze pia kufuatilia na kuweza kununua pamba na bandage zinazozalishwa katika kiwanda hiki nasi tutafutilia.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kuhusu uniform; naomba vilevile kuwashawishi wadau mbalimbali ambao wanatumia uniform zinazofanana na zile zinazozalishwa katika kiwanda hiki waweze kukipatia kipaumbele pamoja na viwanda vingine ambavyo viko humu nchini. Niwaombe pia Watanzania wote kupenda bidhaa zetu kwanza. Tufahamu kwamba viwanda hivi vinapokufa vinakosesha ajira kwa watu wetu na kwa kweli uzalendo ni kutumia mali zetu za ndani. (Makofi)

WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nichukue fursa hii kumshukuru na kumkaribisha Naibu wangu mpya. Napenda nitoe jibu la nyongeza kuhusu bidhaa tiba za Tabora Textile.
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Mbunge Munde Tambwe kwa jinsi alivyopigana kufufua kiwanda hiki, watu wa Tabora watamkumbuka. Nataka nisisitize tamko la Mheshimiwa Rais, Wawekezaji wa Tabora Textile na wote mnaozalisha vifaa tiba nendeni sasa hivi MSD, msisubiri MSD iwafuate. Ni agizo la Rais kwamba MSD kwanza inunue vifaa vinavyotengenezwa hapa ndiyo maana ya kutenga bilioni 269 kwa ajili ya tiba. Kwa hiyo wote nendeni mkanunuae vifaa pale, mkauze vifaa vyenu pale kwa kufuata taratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu hili la uniform, hili wazo la uniform namshukuru Mheshimiwa Tambwe, maamuzi yetu sasa tutaleta mapendekezo kwenu na watu wasituletee mambo ya WTO. Tukiweza kununua uniform kutoka kwenye viwanda vyetu vya nguo, tutaweza kuchochea viwanda vyetu kufanya kazi na kutumia pamba yetu badala ya kununua nguo zisizofaa zinazotoka nje ya nchi. Hiyo italeta kelele tunategemea ninyi Wabunge mtusaidie kutetea viwanda vyenu vya ndani. Ahsante. (Makofi)
MHE. MUNDE A. TAMBWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa swali la msingi linafanana kabisa na matatizo yaliyopo katika Wilaya ya Urambo na Kaliua na Serikali imekuwa ikituambia kwamba imekamilisha mchakato wote wa kutoa maji Mto Malagarasi kupeleka Kaliua na Urambo, fedha tu ndiyo bado hazijapatikana toka mwaka jana walituambia fedha hizo zitapatikana.
Je, status ya kupata pesa kupeleka maji katika Wilaya ya Urambo na Kaliua ikoje mpaka sasa kwa sababu hali ni mbaya sana kwa wananchi hao? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tunao mradi wa usanifu unakamilika wa kutoa maji Malagarasi kupitia Kaliua kuja Urambo hadi Tabora, pia Mheshimiwa Rais ametuagiza kwamba huu mradi unaotoa maji Solwa kutoka Ziwa Victoria kupeleka Tabora wakati unaendelea tayari tumeshaagiza Mamlaka yetu ya Maji ya Tabora iangalie uwezekano wa kuweka mabomba mengine kutoka matanki ya Tabora kupeleka Urambo na ikiwezekana yafike mpaka Kaliua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie Mheshimiwa Munde kwamba Serikali inafanya kazi kuhakikisha Kaliua na Urambo wanapata maji safi na salama. (Makofi).
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami niulize swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa swali la msingi limeongelea vigezo na kwa kuwa Rais aliyepo madarakani wakati akiwa Waziri wa Ujenzi, aliweka kigezo kwamba kazi zinapotangazwa walau kampuni moja ya mwanamke ipate kazi ili kuwainua wanawake na jambo hilo kwa sasa linafifia.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anaweza kutuambia ana mkakati gani wa kutoa walau waraka TANROADS na Halmashauri kwamba wanawake wanapopata kazi wame- qualify wapewe kazi hizo ili kuwainua wanawake? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninamshukuru sana Mheshimiwa Munde kwa swali hili la nyongeza kwa sababu ananipa fursa ya kuelezea nini Wizara yangu inafanya katika kuwainua wakandarasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu tuna mradi maalum wa kuhakikisha kwamba wakandarasi wanawake kwanza wanapatikana kwa sababu ili wapatikane kwanza lazima wajisajili na Bodi ya Usajili wa Wahandisi. Ndani ya Bodi ya Usajili wa Wahandisi tuna programu maalum kwa ajili ya wanawake tu na nashukuru wenzetu wa NORAD wanatusaidia fedha kwa ajili ya kuhakikisha hawa wahandisi wanawake wanasajiliwa, wakishasajiliwa wanaanzisha kampuni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kawaida kampuni hizo zinazoanzishwa na akina mama tunazilea kama nilivyosema, kila wanapopata kazi na wamekuwa wakipata kazi mbalimbali ingawa kwa sasa bado ni kampuni chache zilizoanzishwa kupitia njia hiyo na tutaendelea kuzihamasisha nyingi zaidi zianzishwe. Kila wanapopata kazi wanalipwa malipo yao yote wanayostahili ili waweze kuendelea kukua, huwa hatuwaachii deni la aina yoyote katika wakandarasi hawa wazalendo na hasa hawa wakandarasi akina mama. (Makofi)
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa kuwa Mkoa wa Tabora ni Mkoa ambao uko katikati ya Mikoa ya Singida, Shinyanga, Kigoma na Katavi; na kwa kuwa Mikoa hii haina Vyuo Vikuu vya Serikali ambavyo mwanafunzi anaweza akapata mkopo wa Serikali tofauti na Open aliyoisema Mheshimiwa Waziri, ni lini sasa Serikali itaweka mkakati wa kukipandisha hadhi Chuo cha Uhazili Tabora ambacho ni kikubwa na ni kizuri kama ilivyofanya katika Chuo cha Chang’ombe cha Dar es Salaam na katika Chuo cha Ushirika Moshi, walivipandisha hadhi, sasa wana mpango gani wa kupandisha hadhi Chuo cha Utumishi wa Umma cha Uhazili cha Tabora? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kiwe Chuo Kikuu cha Serikali ambacho kitaweza kutoa degree ambayo sasa hivi haitoki.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, ahsante na nashukuru kwa maswali yake ya nyongeza; nikianzia na umuhimu wa Mikoa ya Tabora pamoja na jirani zake kuwa na Chuo eneo hili, kimsingi Vyuo Vikuu ni Vyuo vya Kitaifa na kwa sasa hivi tuna Vyuo ambavyo bado havijaweza kudahili kwa idadi ambayo ni ya kutosha kwa mfano Chuo Kikuu cha UDOM bado kina nafasi nyingi na hata vyuo vingine, kwa hiyo tutakuwa tunaanzisha Vyuo kulingana na uhitaji.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Chuo cha Uhazili Tabora ambacho kimsingi kipo chini ya Wizara ya Utumishi, naomba tu niseme kwamba hiyo sasa itategemeana na hali halisi ya Mazingira na uainishwaji wa kozi husika kulingana na mitaala iliyoboreshwa, ikitokea hivyo nadhani Mheshimiwa Waziri atakubaliana na mimi kwamba wataona namna gani kinavyoweza kufanyika.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na namshukuru pia Mheshimiwa Naibu Waziri wa Elimu kwa majibu mazuri nipende tu kusema yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika, Chuo hiki ni mahususi kabisa kwa kuwaendeleza watumishi wa umma na kitaendelea kubaki hivyo na kama alivyoeleza kwa masuala ya Vyuo Vikuu kwa kuwa yako chini ya Wizara ya Elimu endapo wataona kuna haja ya kufungua Vyuo Vikuu vingine hayo yako chini yao, lakini kwa Chuo hicho cha Uhazili ni Chuo cha Watumishi wa Umma na tuna mipango ya kuviendeleza zaidi ili kuhakikisha kwamba wanatoa kozi nyingi kuwahudumia Watumishi wa Umma. Ni mafunzo maalum kwa watumishi wa umma.
MHE. MUNDE A. TAMBWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize maswali madogo mawili ya nyongeza. Kwanza kabisa nianze kwa kuishukuru Serikali kwa kutuletea pesa kwenye Wilaya ya Sikonge, Nzega na Uyui kwa ajili ya ujenzi wa hospitali za wilaya, naishukuru sana Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza swali langu la kwanza la nyongeza. Ukizingatia population ya Wilaya ya Tabora Manispaa, ukizingatia Sera ya Serikali yetu kwamba mnatakiwa muanze ninyi wenyewe na Serikali iwa-support kitu ambacho wananchi wa Tabora Manispaa wameshakifanya. Kinachotushangaza zaidi ni pale Wilaya mpya zilizoanza mwaka jana zinavyopelekewa pesa ya kujenga Hospitali ya Wilaya na kuacha kupeleka katika Wilaya za zamani…
MHE. MUNDE A. TAMBWE: zenye watu wengi na…
MHE. MUNDE A. TAMBWE: ...kuacha kupeleka kwenye Wilaya ya Tabora Manispaa. Je, Serikali inanipa commitment gani sasa ya kuleta pesa kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Tabora Manispaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Jimbo la Igalula halina hata zahanati moja wala kituo cha afya kimoja; hii inasababisha wananchi wote wa Jimbo hilo kwenda kwenye hospitali kubwa ya Mkoa wa Tabora ambayo ni Kitete na kuongeza msongamano mkubwa. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuhakikisha inaleta pesa kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya na kumalizia zahanati ambazo zilianzishwa na wananchi wa Jimbo la Igalula pamoja na Mbunge wao na mimi Mbunge wao wa Viti Maalum? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika tangu nimeingia Bunge hili na Mheshimiwa Munde akiwa ndani ya Bunge hili amekuwa ni mpiganaji kuhusiana na suala zima la afya kwa Mkoa wake wa Tabora, nampongeza sana kwa jitihada zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maswali yake mawili, swali la kwanza anauliza commitment ya Serikali katika kuhakikisha kwamba tunakamilisha ujenzi wa hospitali ya Manispaa ya Tabora kwa maana ya hospitali ya wilaya. Katika jibu langu la msingi nimemweleza commitment ya Serikali kwamba katika awamu ya pili, fedha zitakazopatikana kwa ajili ya ujenzi wa hospitali za wilaya hatutaisahau Manispaa ya Tabora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili anaongelea kuhusiana na Igalula ambayo hawana kituo cha afya na Hospitali ya Wilaya. Kwanza naomba niwaase na niwaombe wananchi wa Igalula, wao waanzishe ujenzi kama ambavyo Manispaa ya Tabora wamefanya na pesa ikipatikana awamu itakayofuata na sisi kama Serikali tutahakikisha kwamba tunaunga mkono juhudi za wananchi. (Makofi)
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa niulize swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa Tabora Manispaa mpaka leo hii kuna baadhi ya Kata hazina umeme na Serikali ilituahidi hapa Bungeni kuanzia mwaka 2013 itatuletea umeme wa REA, lakini cha kushangaza Makao Makuu ya Kata hizo yote yamewekewa umeme wa REA ambapo vijiji vyake mpaka leo hii havijawekewa umeme wa REA. Umeme wa REA umewekwa Itonjala, Ifucha, Kalunde, Ntalikwe, Tetemia, Misha, Kakola na baadhi ya Makao Makuu ya Kata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimuulize Mheshimiwa Waziri, ni lini sasa Serikali itatuletea umeme wa REA kwenye baadhi ya vijiji ambavyo mpaka leo hii havijawekewa umeme wa REA ukizingatia ile ni Manispaa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Munde Abdallah Tambwe swali lake la msingi linahusu maeneo ambayo tulipeleka umeme kwenye Makao Makuu ya Kata na bado vijiji. Naomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kama ambavyo alipata kuja ofisi akaelezea na ninampongeza kwamba vitongoji na vijiji vya Kata zile vitapata umeme kupitia mradi wa densification awamu ya pili. Mkoa wa Tabora ni miongoni mwa mikoa 11 ambapo mradi huu utaanza mwaka 2018/2019.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama nilivyoomba Wabunge wote wa Viti Maalum kwa sababu ni wahanga, ni wafaidika wa umeme kwa kuwa wanawake wakipata umeme wamefaidika wote, waendelee kufuatilia ili umeme upatikane katika maeneo yote. Ahsante. (Makofi)
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Kwanza kabisa niishukuru Serikali kwa Mradi wa Ziwa Victoria ambao unaendelea katika Wilaya ya Nzega, Igunga na Tabora Manispaa. Naomba niulize swali, kwa kuwa hali ya upatikanaji wa maji katika Jimbo la Kaliua, Uliyakhulu na Urambo ni mbaya kwa sasa na Serikali iliahidi kutuletea maji kutoka Mto Malagarasi au Ziwa Victoria; je, Serikali ina mkakati gani sasa wa kuhakikisha maji yanakwenda katika hayo Majimbo matatu ili wananchi wa huko waweze kuondokana na tabu kubwa waliyonayo upatikanaji wa maji? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana, ndiyo uzuri wa kuwa Mbunge wa Viti Maalum kwa sababu Mkoa wote ni wa kwako. Nimjibu tu kwamba baada ya kuanza utekelezaji wa Mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kupeleka Tabora, tayari kupitia ile shilingi milioni mia tano kutoka Serikali ya India ambayo mkataba wake wa kifedha umesainiwa tunapeleka maji Sikonge, Urambo na Kaliua na utekelezaji utaanza mwaka ujao wa fedha. Kuhusiana na eneo la Uliyankhulu la Mheshimiwa Kadutu nalo tunalifanyia kazi kutafuta fedha nyingine ili tuweze kupeleka maji katika hilo eneo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na Mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria, ule Mradi tumeona kwamba bado unafanyiwa kazi. Mhandisi Mshauri hajakamilisha usanifu, lakini kwa sababu Tabora sasa tutakuwa na maji mengi, tutakuwa hatuna haja ya kuwekeza tena hela nyingi kwenda kutoa Malagarasi. Kwa baadaye tunaweza tukatumia chanzo cha Mto Malagarasi, lakini kwa sasa maji ya Ziwa Victoria yatakuwa yanatosheleza kupeleka maeneo mengine.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa na mimi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kuuliza swali, naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kugawa tablets kwa walimu wakuu wa shule za msingi ili kuboresha elimu na ufundishaji. Mheshimiwa Rais aliahidi na ameanza kutekeleza, angalau ni kawaida yake kuahidi na kutekeleza, tunampongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa taratibu zote za kuugawa Mkoa wa Tabora zilishakamilika na Serikali iliahidi kutimiza kuugawa mkoa huo ambao una Wilaya saba na una wakazi wengi na kuwasababishia wakazi wa mkoa huo kukosa huduma za msingi kama inavyostahili.
Je, ni lini sasa Serikali itaugawa Mkoa Tabora kama ilivyogawa Mkoa wa Mbeya kuwa Songwe na kama ilivyogawa Shinyanga na Simiyu ili wananchi wa Tabora nao waweze kupata haki zao za msingi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitoe maelezo kwamba sisi katika Mkoa wa Tabora tunajivunia sana utendaji kazi wa Mheshimiwa Munde Tambwe Abdallah kwa jinsi ambavyo anafuatilia masuala mbalimbali kwenye Mkoa wa Tabora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimkumbushe kwamba Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alipotembelea Mkoa wa Tabora mwaka 2017 na kufanya mkutano wa hadhara pale Nzega lilijitokeza swali hili la ombi la kuugawa Mkoa wa Tabora kwamba tuwe na Mkoa mpya wa Nzega.
Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu yake katika mkutano ule ndiyo ambayo yamejenga mwongozo wa kitaifa kwa sasa kwamba kuna haja kwanza kuimairisha miundombinu na mahitaji mengine katika Mikoa, Wilaya na Halmashauri mpya ambazo zilishaanzishwa tangu zamani ili tukikamilisha uimarishaji huo ndiyo tuje kwenye mikoa mpya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Mkoa wa Nzega limeshajadiliwa RCC na vikao vyote vimekamilika, tutakapokuwa tumeimarisha maeneo haya mapya yaliyopo, Mkoa huo mpya wa Nzega, naomba sana watu wa Nzega wasiendelee kubishana tena, utatangazwa mara moja na utapewa kipaumbele.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa, katika Mkoa wa Tabora kumekuwa na kero kubwa ya kuwapiga, kuwanyang’anya baiskeli zao, kuwajeruhi, kuwanyang’anya simu zao na pesa walizonazo mfukoni wanaobeba mkaa kutoa vijijini kuleta mjini. Je, Mheshimiwa Waziri ni haki mtu anapofanya kosa kuchukuliwa hatua kupigwa hapo hapo bila kupelekwa kwenye vyombo vya sheria? (Makofi)
NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kumekuwa na changamoto hizo, katika maeneo mengi nchini, watu wamekuwa wakinunua mkaa na wamekuwa wakisafirisha kwa baiskeli, wamekuwa wakisafirisha kwenye bodaboda na vyombo vingine ambavyo kwa mujibu wa sheria za usalama barabarani haviruhusiwi kufanya hivyo. Pale ambapo wanakuwa wamekiuka hizo taratibu wanatakiwa wakamatwe, wapelekwe katika vituo, wapelekwe katika mikondo ya sheria siyo kuwapiga. Wale ambao wanaowapiga wananchi bila ya kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria, ni ukiukaji wa taratibu na ukiukaji wa sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwaombe watendaji wote kokote waliko nchini wahakikishe wanazingatia sheria na kanuni na miongozo iliyopo na wahakikishe wanawatendea haki wananchi ili kusudi wasinyanyaswe na kupigwa. (Makofi)
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na Mheshimiwa Mbunge aliyeuliza swali la msingi kumpongeza Rais kwa kupigania kupunguza riba kwenye benki, lakini kwenye taasisi ndogo ndogo, kwa mfano PRIDE, FINCA, Tunakopesha mpaka navyoongea sasa hivi riba inafika asilimia 33. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwadhibiti hawa watu wanaofikisha riba mpaka asilimia 33 na kusababisha akina mama kunyang’anywa vitu vyao kila siku? Maana yake pesa ile sasa inakuwa haizai kazi yake ni kurudisha riba inapofikia miezi sita mama yule anaanza kunyang’anywa vitu vya ndani. Mheshimiwa Waziri ana mkakati gani wa kukomesha tabia ya kufikisha riba asilimia 33?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali moja la nyongeza la dada yangu, Mheshimiwa Munde, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya msingi, tumepitisha Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo ya Fedha na moja ya malengo yake ni kuhakikisha kunakuwa na uzingatiaji wa kanuni za utawala bora kwenye taasisi zinazotoa huduma kwenye sekta ndogo ya fedha. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Sheria ya Huduma Ndogo ya Fedha iko katika hatua za mwisho na ni imani yangu ndani ya mwaka huu sheria hii itapitishwa ili kuwalinda wakopaji wadogo katika sekta ndogo ya fedha. Naamini itakuwa ndiyo mkakati wetu na suluhisho la kuwalinda watu wetu.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, hospitali nyingi zinatoza wanawake wajawazito wanapokwenda kujifungua. Hospitali ya Kitete ni moja kati ya Hospitali ambazo zinatoka akina mama; anapojifungua mtoto wa kiumbe analipa Sh.50,000 na anapojifungua mtoto wa kike, analipa Sh.40,000. Je, Serikali imeweka tozo hii kwa ajili ya nini? (Kicheko/Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, utoaji wa huduma za afya nchini unatolewa kwa mujibu wa sheria, sera na miongozo ikiwemo utoaji wa huduma za afya kwa wajawazito wakati wa kujifungua. Serikali imeelekeza bayana kwamba huduma za wajawazito na watoto wa chini ya umri wa miaka mitano zinatolewa bila malipo yoyote na Serikali inaendelea kusimamia utekelezaji wa sera na miongozo hiyo.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba baadhi ya maeneo, kwa baadhi ya watumishi wasio waaminifu, kwa namna moja ama nyingine wamekuwa wanatekeleza kinyume na sera na mwongozo huo. Kazi ya Serikali ni pamoja na kupokea maoni ya Waheshimiwa Wabunge na kuyafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niyachukue mawazo ya Mheshimiwa Mbunge na niwahikikishie kwamba tutaenda kuyafanyia kazi ili kuondokana na changamoto hiyo. (Makofi)
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii nami niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa, Mkoa wa Tabora ulifanikiwa kupata maji ya Ziwa Victoria; na kwa kuwa, Mheshimiwa Rais alipokuja kwenye Kampeni alisema kwamba, sasa maji ya Ziwa Victoria yapelekwe Urambo, Kaliua na Ulyankulu:-

Je, Mheshimiwa Naibu Waziri ni lini sasa mnatarajia kuyatoa maji hayo Tabora Mjini na kuyapeleka Urambo, Kaliua, Ulyankulu pamoja na Sikonge? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Maeneo ya Urambo, Kaliua, Ulyankulu na Sikonge, yote haya tumeendelea kuyaweka katika mikakati ya Wizara kuona namna ambavyo tutaendelea kupata fedha ili maeneo haya yote maji yaweze kufika. Tutafanya jitihada za makusudi kuona kwamba tunapeleka fedha mapema na hii itakuja kuingia mwaka ujao wa fedha.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii niulize swali la nyongeza. Barabara ya Tabora – Ulyankulu imekuwa sasa ni muda mrefu zaidi ya takribani miaka kumi imejengwa kilometa mbili tu za lami. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri ana mkakati gani sasa wa kuhakikisha barabara hiyo ya muda mrefu inakwisha? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge Munde, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kuwa Serikali imeshaonyesha nia na kama nilivyosema kwenye baadhi ya majibu yangu kwamba dhamira ya Serikali ni kuzijenga hizi barabara na tumeshaanza, lakini kuikamilisha barabara hii kwa kweli lazima tuseme itategemea na upatikanaji wa fedha. Pale fedha itakapopatikana basi Mheshimiwa Mbunge hii barabara tutaikamilisha kwa kiwango cha lami kama tulivyoahidi na kama tulivyoanza kujenga hizo kilometa za awali. Ahsante.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa Tabora Manispaa ina population kubwa ya watu zaidi ya 600,000; na pale Tabora Mjini kuna zahanati ambayo inazalisha watu 10 mpaka 20 kwa siku: Je, ni lini Serikali sasa itakuwa tayari ku-upgrade ile zahanati na kuwa kituo cha afya na kuiwekea wodi wa wazazi pamoja na theatre? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa
Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Munde, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inafanya tathmini ya maeneo ambayo yana zahanati, lakini yana idadi kubwa ya wananchi na yana umbali mkubwa kutoka kituo cha afya au hospitali. Tutafanya tathmini kwenye zahanati hii aliyoisema ili tuone kama inakidhi vigezo iweze kupandishwa hadhi kuwa kituo cha afya.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa nimeshawahi kuongea na Mheshimiwa Naibu Waziri mara kadhaa kuhusu kituo cha afya cha Une-Clinic Tabora, kwamba tunahitaji majengo ya upasuaji, theater na maabara ili kiweze kuwa kituo cha afya, kwa sasabu akina mama wajawazito wanazaa pale, kama akina mama 200 kwa mwezi.

Je, Serikali ni lini sasa itatuletea hizo fedha ili tuweze kukamilisha Kituo cha Afya cha Kaoni Clinic?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Munde, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Mheshimiwa Munde amefuatlia suala Kituo cha Afya cha Town pale Tabora Manispaa; na alikuja pamoja na Mkurugenzi wa Manispaa, tulikubaliana wafanye tathmini ya ukubwa wa eneo lililopo ili tuweze ku-design michoro inayoweza kukaa pale ili tujenge jengo la ghorofa ili wananchi wa Tabora Manispaa wapate huduma.

Mhesimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie kwamba zoezi hilo linaendelea litafanyiwa kazi na Serikali.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa zahanati ya Town Clinic ya Tabora Manispaa ambayo Naibu Waziri anaifahamu vizuri ina wagonjwa wengi na haina gari la wagonjwa; ni lini sasa Serikali itatuletea gari la wagonjwa kwa ajili ya kusaidia kata hizo 30 ambazo inaitumia?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza Mheshimiwa Munde Abdallah, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba zahanati hii inahudumia wananchi wengi, lakini kigezo cha gari ya gari la wagonjwa ni kuwa kituo cha afya au hospitali ya halmashauri, lakini kwa sababu ya upekee wa zahanati hii tutafanya tathimini na kuona uwezekano wa kupeleka gari baada ya kujiridhisha na vigezo ambavyo vinatakiwa, ahsante.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi nami niulize swali dogo la nyongeza. Ni lini sasa Serikali itatoa commitment ya kuibadilisha Zahanati ya Town Clinic Tabora Mjini na kuwa kituo cha afya kwa sababu inazalisha watu wengi kwa mwezi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Town Clinic katika Manispaa ya Tabora ni zahanati ya muda mrefu na inahudumia wananchi wengi sana. Serikali ilishatoa maelekezo kwa Mkurugenzi, walishaelekezwa kuandaa michoro ya ghorofa kwa sababu eneo lile ni dogo ili fedha ziweze kutengwa kwa ajili ya kujenga ile zahanati na kupandisha hadhi kuwa kituo cha afya.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, natumia fursa hii kumkumbusha Mkurugenzi na Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, kutekeleza maelekezo ya Serikali mapema ili tathmini ifanyike, fedha zitafutwe kwa ajili ya kupandisha hadhi zahanati hii kuwa kituo cha afya. Ahsante. (Makofi)
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante, niungane na wenzangu tatizo lililopo kwenye mikoa yao, hususani katika Mkoa wetu wa Tabora hasa kwenye zahanati za pembezoni kwenye wilaya pamoja na kwenye manispaa, watumishi wa afya ni wachache sana.

Mheshimia Spika, ni lini Serikali itatuletea watumishi wa afya wa kutosha kwenye zahanati na vituo vyetu vya afya katika Mkoa mzima wa Tabora?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa hakika Waheshimiwa Wabunge lakini na Wananchi wa Tanzania kwa ujumla ni mashahidi kwamba Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha miaka hii mitatu, ameajri watumishi wengi sana wa Kada za Afya na kuwapeleka kwenye vituo vyetu vya huduma za afya.

Mheshiwa Spika, zoezi hili ni endelevu, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Munde kwamba, mara ajira za Kada mbalimbali za afya zitakapojitokeza, tutahakikisha pia tunatoa kipaumbele katika Mkoa wa Tabora lakini hasa katika vituo ambavyo viko pembezoni na vina upungufu mkubwa wa watumishi.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante; nimekuwa nikiuliza kila siku kuhusu Zahanati ya Town Clinic ambayo ina msongamano mkubwa wa watu kufikia kuzalisha wanawake 200 kwa mwezi, na Mheshimiwa Naibu Waziri amekuwa akinijibu Mkurugenzi alete michoro; je, Mheshimiwa Naibu Waziri ana mkakati gani wa kumwandikia sasa Mkurugenzi kwa maandishi ili aweze kuleta huo mchoro na Zahanati ya Town Clinic iwe Kituo cha Afya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Munde, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Munde, alikuja, tulimwita Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, tulikaa naye mimi, Mheshimiwa Mbunge na Mkurugenzi, tukampa mkakati wa kwenda kuandaa michoro hiyo aweze kuiwasilisha. Si kwa barua, bali tulimwita na tukakutana. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari tuna taarifa zote za hatua ambazo zinaendelea kwa ajili ya kupandisha hadhi Zahanati ile ya Town kuwa Kituo cha Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasisitiza kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora kuleta michoro ile haraka iwezekanavyo Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili tuweze kuona namna gani tunaanza ujenzi wa Kituo cha Afya cha Town. Ahsante. (Makofi)
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante; nimekuwa nikiuliza kila siku kuhusu Zahanati ya Town Clinic ambayo ina msongamano mkubwa wa watu kufikia kuzalisha wanawake 200 kwa mwezi, na Mheshimiwa Naibu Waziri amekuwa akinijibu Mkurugenzi alete michoro; je, Mheshimiwa Naibu Waziri ana mkakati gani wa kumwandikia sasa Mkurugenzi kwa maandishi ili aweze kuleta huo mchoro na Zahanati ya Town Clinic iwe Kituo cha Afya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Munde, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Munde, alikuja, tulimwita Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, tulikaa naye mimi, Mheshimiwa Mbunge na Mkurugenzi, tukampa mkakati wa kwenda kuandaa michoro hiyo aweze kuiwasilisha. Si kwa barua, bali tulimwita na tukakutana. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari tuna taarifa zote za hatua ambazo zinaendelea kwa ajili ya kupandisha hadhi Zahanati ile ya Town kuwa Kituo cha Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasisitiza kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora kuleta michoro ile haraka iwezekanavyo Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili tuweze kuona namna gani tunaanza ujenzi wa Kituo cha Afya cha Town. Ahsante. (Makofi