Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Munde Abdallah Tambwe (25 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia Wizara ya Viwanda na Biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nianze kuipongeza hotuba ya Mheshimiwa Waziri iliyojitosheleza. Namfahamu sana Mheshimiwa Mwijage, nilijua na niliamini ataleta hotuba nzuri ambayo imejitosheleza kama alivyoisoma hapa. Pia Waziri huyu ni msikivu na ni mfuatiliaji sana na Wizara hii inamfaa kwa sababu amekuwa akitushauri, amekuwa akitufuatilia kwenye mikoa yetu kuona kipi kinafaa ili tuweze kufanikiwa. Tunakushukuru sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa azma yake ya kufanya Awamu ya Tano kuwa ya viwanda. Hii analenga kutubadilishia uchumi tulionao wa chini na kutupeleka kwenye uchumi wa kati. Hivyo tuungane sisi Waheshimiwa Wabunge kumwombea Mheshimiwa Rais na Serikali yetu ili tufikie hapo tunapokwenda na tusiwe watu wa kukatisha tamaa, tuwe watu wa kuwapongeza na kuwashauri ili tuweze kufikia pale tulipokuwa tumejipanga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa hotuba ya Waziri Mkuu niliongelea kuhusu suala la tumbaku lakini kwa umakini wa suala hili, naomba niongee tena. Nimkumbushe pia Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Tabora tunalima tumbaku kwa asilimia 60 lakini Serikali imewekeza pesa nyingi sana kwenye reli na barabara, hii pia inasaidia sisi Mkoa wa Tabora kupata viwanda kwa sababu sasa tutakuwa na reli na barabara nzuri, tumbaku tunalima asilimia 60, sioni sababu gani inayoweza kufanya sisi Tabora tusiwe na viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumepiga kelele sana kuhusu viwanda vya tumbaku Tabora, lakini hata kiwanda cha ku-process hatuna. Wakati nachangia hotuba ya Waziri Mkuu niliongea, namshukuru sana Mheshimiwa Mwijage, alinifuata na akaniambia kwamba amepata mwekezaji wa Kichina na atakuja hapa sisi Wabunge wa Mkoa wa Tabora tutaongozana naye kwenda Tabora. Nimwombe sana Mheshimiwa Mwijage atutimizie hilo neno alilotuambia ili sisi Wabunge wa Tabora angalau tuonekane sasa tunajali wananchi wetu maana hawatuelewi na wana Wabunge humu ndani zaidi ya 12. (Makofi)
Wabunge wa Tabora sasa tuna mkakati mkubwa wa kuhakikisha Tabora tunapata kiwanda cha tumbaku, wote tumekubaliana tuhakikishe Serikali inatupa kiwanda cha tumbaku au hata cha ku-process tumbaku. Nimshukuru Waziri Mwijage ametuahidi kwamba atatuletea Mchina. Mheshimiwa Waziri hali ya ajira Tabora ni mbaya, vijana wetu hawana ajira wakati sisi ni wakulima wakubwa wa tumbaku, naomba tupate kiwanda. Sijui nani alitoa wazo nchi hii la kupeleka kiwanda cha tumbaku Morogoro wakati tumbaku inalimwa Tabora!
Kwa kweli huwa najiuliza hata sipati jibu, sioni sababu. Kibaya zaidi juzi tena kimejengwa kiwanda kingine cha sigara Morogoro, kwa kweli hii inatuumiza sana kama wananchi wa Mkoa wa Tabora. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niongee kuhusu Kiwanda cha Nyuzi. Pale Tabora kuna Kiwanda cha Nyuzi cha muda mrefu, lakini kiwanda hiki kimekufa muda mrefu. Naiomba Serikali yangu, kama kweli inaheshimu wakulima wa pamba, wahakikishe kiwanda hiki kinafufuliwa na kinaanza kufanya kazi. Naomba sana!
Mheshimiwa Naibu Spika, pia namwomba Mheshimiwa Waziri atuambie, nini hatima ya kiwanda hiki? Kiwanda hiki kimeanza kupigiwa kelele na Wabunge wengi waliotutangulia ambao leo hii hawamo humu; nasi pia toka mwaka 2011 mpaka leo tunakipigia kelele, lakini hatupati hatima yake ni nini, hakitengenezwi, hakifunguliwi!
Mheshimiwa Naibu Spika, leo namwomba Mheshimiwa Waziri wakati ana-windup atuambie ana mkakati gani kuhusu Kiwanda cha Nyuzi cha Mkoa wa Tabora? Nasi pia vijana wetu wanahitaji ajira, hawana ajira, hali ya uchumi inakuwa mbaya kila siku, mpaka kuna baadhi ya watu wanatucheka kwamba Tabora hakuna maendeleo. Ni Serikali haijatuletea hayo maendeleo, tunalima tumbaku lakini hatuna viwanda, lakini pia tuna Kiwanda cha Nyuzi ambacho kimefungwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba tena Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara ageuze sasa zao la asali liwe zao la biashara. Watanzania wengi humu ndani ya nchi yetu wameshajua nini maana ya kutumia asali na naamini watu wengi sasa hivi wanatumia asali. Pia zao hili lina soko kubwa nje ya nchi yetu. Namwomba sasa Mheshimiwa Waziri aliboreshe zao hili, awe na mkakati maalum wa kuboresha zao la asali ili liwe zao la kibiashara; lakini pia tupate viwanda vya ku-process asali ili vijana wetu wafaidike na zao la asali na pia wapate ajira ili na sisi kama watu wa Tabora tupunguze huo umaskini. Naomba sana Mheshimiwa Waziri akija ku-windup atuambie pia mkakati wake alionao katika kiwanda cha ku-process asali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kutuletea EPZ ndani ya Mkoa wa Tabora. Sisi kama watu wa Tabora tumeipa Serikali heka 200 ili kujenga viwanda vinavyotokana na mazao ya kilimo, ikiwemo tumbaku, asali pamoja na viwanda vya ufugaji. Naiomba sana Serikali, ile ardhi tumewapa bila kulipa fidia, bila gharama yoyote ile ili waweze kutusaidia kutafuta wawekezaji tupate viwanda. Nia yetu ni kupata viwanda ili tuweze kupata ajira za vijana wetu na hatimaye na sisi tuweze kuondoa umaskini.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa tukipiga kelele sana Wabunge wa Mkoa wa Tabora, kwa kweli Mkoa ule ni wa siku nyingi, lakini cha kushangaza na cha kutia masikitiko makubwa, Mkoa ule hauna kiwanda hata kimoja. Malighafi zinazopatikana, Tabora zinapelekwa mikoa mingine kuwekewa viwanda na watu wa kule ndio wanaofaidika. Kitu hiki kinatuumiza sana sisi Wabunge wa Mkoa wa Tabora na kuonekana kama vile hatuji kuwasemea na kuwasaidia waliotuweka madarakani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kusema kwamba tumtie moyo Mheshimiwa Waziri, tuitie moyo Serikali yetu ya Awamu ya Tano, iendelee na mkakati wake wa kuhakikisha Awamu ya Tano inakuwa Awamu ya Viwanda, hatimaye tutoke kwenye uchumi wa chini na kuingia kwenye uchumi wa kati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wale wenzetu wanaosema kwamba huu Mpango hauna maana yoyote, hatuko kwenye dhana ya viwanda…
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Washindwe na walegee. Naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ili na mimi niweze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nianze kuipongeza hotuba nzuri ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha na niseme tu Serikali makini ni ile inayokusanya kodi. Kwa hiyo, nampongeza sana Waziri, hakuna nchi yoyote iliyoendelea bila kukusanya kodi. Serikali ya Awamu ya Tano imekwenda mbali zaidi, imepanua wigo wa kukusanya kodi ili iweze kuhudumia wananchi wake, tunaipongeza sana Serikali kwa kupanua wigo na kupeleka huduma kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa zaidi, Serikali imepeleka asilimia 40 ya mapato yake kwenye miradi ya maendeleo, imepeleka pesa za walipa kodi kwa wananchi moja kwa moja. Pesa hizi zitajenga zahanati, barabara, madaraja, shule na kadhalika. Naipongeza sana Serikali na imeonesha dhamira ya Mheshimiwa Rais Magufuli ambapo katika kila hotuba yake amekuwa akiongelea masuala ya wanyonge, leo kwenye bajeti yake ametuonesha dhamira yake kwamba amedhamiria kusaidia wanyonge kwa pesa za walipa kodi, tunamtia moyo kwamba aendelee kukusanya kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee kuhusu CAG kama walivyoongelea wenzangu. Naomba pesa za CAG ziongezwe kwa sababu yeye ndiye Mkaguzi Mkuu wa vitabu vya Serikali, CAG ndiye anakagua kitaalamu. Tusidanganyane anaweza kuja mtu mwingine kukagua, akakagua juu juu tu asiingie in deep. Mhasibu anakaguliwa na Mhasibu? Mhasibu anakaguliwa na External Auditor ambaye ana uelewa wa kumkagua, ukimkagua juu juu akifika Mahakamani, wewe ni Mwanasheria, huwezi kumthibitisha kwa asilimia 100 atakukimbia tu na atashinda kesi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe sana Serikali impe hela CAG akatimize dhamira ya Mheshimiwa Rais ya kutumbua majipu na kuhakikisha fedha za Serikali haziliwi hovyo. Kwa mfano, kwenye Halmashauri au system nzima ya Serikali sasa hivi wanatumia EPICAR System, walianza kutumia Platinum System wakatumia EPICAR 7, sasa hivi wanatumia EPICAR 9.5 ambayo External Auditor wamesomea. Huwezi kumpeleka PCCB akafungue EPICAR 9.5, hawezi kufungua na kuingia ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii External Auditor akienda kumkagua Mhasibu anapewa cash book nzima akiona kuna longo longo anamwambia Chief Accountant nipe password yako anaingia moja kwa moja kwenye system ya EPICAR 9.5 kwa sababu wamefundishwa. Hivi ni nani mwingine anaweza akaingia kwenye system ya EPICAR? Ni nani mwingine anayeweza kumkagua Mhasibu mtaalam anayeiba kwa kalamu, anayeiba kisomi zaidi ya External Auditor? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mnawapa pesa za mishahara na pesa za matumizi ya ofisi, watu hawa wanafanya kazi mpaka saa nane ya usiku kwa macho yangu nimeona. Unakuta kuna risiti feki, anaenda kuchukua vitabu vya revenue anahakikisha kitabu kwa kitabu kuona kwamba ni sawa, anachukua password ya Revenue Accountant anaingia kwenye system anakagua mpaka saa saba ya usiku, mnawavunja moyo watu hawa, hamuwatendei haki. Niiombe Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, mpeni CAG pesa afanye kazi ya kubana pesa za Watanzania zinazoliwa na watu wachache. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi ni vitu vya kitaalam jamani, vinakwenda kwa utaalamu. Haiwezekani mtu tu akaja akakagua mkasema eti huyu mtu Mahakamani mtamtia hatiani asilimia 100, siyo rahisi, ndiyo maana wanashinda kesi kila siku, niombe kabisa CAG akague. Leo ameokoa shilingi bilioni 20 kwa mwezi pesa za mishahara hewa angekuwa siyo CAG tungeokoa hizi shilingi bilioni 20 ambazo zimeenda kulipa watumishi hewa? Siyo CAG ndiye ametuletea shilingi bilioni 20 ambazo tumeziokoa? Naomba sana Serikali iangalie hili kwa makini, mpeni pesa aendelee kuwabana watumishi wasio waaminifu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ningeweza kuliongelea kwa upana ila muda wangu ni mchache niende moja kwa moja katika Mkoa wangu wa Tabora. Kitu kinachoumiza zaidi RC wa Mkoa wa Tabora hana gari, leo utamkuta kwenye Pick up, kesho utamkuta kwenye gari ya mradi, ukimkuta kwenye gari ya RC yupo njiani nimemuona kwa macho yangu anasukumwa gari imekufa. Naiomba Serikali, Mkoa wa Tabora ni mkubwa, jinsi ya kuutembelea kwa gari bovu hauwezi, anahangaika kuomba magari mpaka kwa Wakurugenzi, ni jambo la aibu sana. Naiomba Serikali impe Mkuu wa Mkoa gari. Mkuu wetu wa Mkoa mnamjua siyo jembe ni katapila, nani ambaye hamjui Mheshimiwa Mwanry hapa? Anafanya kazi sana mpeni gari afanye kazi aliyopewa na Rais. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, nije sasa kwenye suala zima la kodi, mimi sipingani na Serikali kulipa kodi, hakuna Serikali ambayo inaweza kuendelea bila kulipa kodi lakini boda boda wa Tabora wanalipaje sawa na boda boda wa Mwanza wakati population ya Mwanza ni kubwa, mzunguko wa pesa wa Mwanza ni mkubwa, unamwambia boda boda wa Tabora alipe kodi sawa na boda boda wa Mwanza! Jamani acheni watoto walipe kodi kwa haki zao na ili waweze kujikomboa na waendelee, msiwape kodi kubwa tofauti na uwezo wao wa kulipa. Naiomba sana Serikali iliangalie hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niliongea na kaka yangu Mheshimiwa Mavunde, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Vijana, nikamuambia aje Tabora tukae na boda boda wa Tabora tuone jinsi ya kuwasaidia kuwapa mikopo ili waweze kujikomboa kiuchumi. Mikoa yetu bado maskini sana, nimuombe kaka yangu Mheshimiwa Mavunde alitafutie siku maalumu aje Tabora nimuitie vijana wa boda boda akae nao ili tuweze kuona ni jinsi gani tutainua mikoa ile ya pembezoni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee kuhusu suala la mkopo. Naibu Spika wewe ni mwanamke, wanawake wengi wanashindwa kwenda kukopa benki kwenye riba ndogo kwa sababu hawana hati za nyumba, hawana hati za magari, wanaenda Pride, Finca ambapo riba ni asilimia 30 kuendelea. Mikopo hii wanashindwa kulipa wananyang‟anywa makochi yao, mafriji, waume zao wanawageuka wanawafukuza hatimaye tunazalisha watoto wa mitaani kila siku, Serikali ipo tu! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siku hizi habari ya mjini imekuwa ni microfinance, kila mtu akipata pesa anafungua microfinance, ndiyo unatajirika kwa haraka kwa sababu wanatoza riba kubwa, Serikali imekaa kimya tu! Nani anatoa leseni za hizi riba, wanamkopesa mtu kwa riba mpaka ya thelathini na huyu mtu atatajirika saa ngapi, atatoaje huo umaskini? Niiombe sana Serikali, nimuombe Waziri anayeshughulika na wanawake, Mheshimiwa Ummy Mwalimu, nilimsikia siku ya Sikukuu ya Wanawake akimwambia Mkurugenzi wa Benki ya Wanawake kwamba anakopeshaje kwa riba ya asilimia 18 wakati anapewa ruzuku ya Serikali lakini benki hizi mikoani kwetu hazipo. Mimi sijui maana ya Benki ya Wanawake kwa sababu mkoani kwangu haipo! Wanawake wa Mkoa wa Tabora hawapati hiyo huduma ya Benki ya Wanawake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe sasa Mheshimiwa Ummy Mwalimu ambaye tuna imani naye, ana uwezo mkubwa wa kufanya kazi, aniambie lini atakuja Tabora kuongea na akina mama na awape ahadi lini atafungua deski la Benki ya Wanawake kwenye Mkoa wa Tabora. Wanawake hawa wamekuwa waaminifu kwa Serikali hii, lazima muwatendee haki na hii benki ni ya wanawake wote siyo benki ya wanawake wa Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Mbeya hata sisi kwetu kuna wanawake na wanahitaji huduma hii na ni haki yao wanastahili kwa sababu ni haki ya Serikali kuwapelekea huduma hii. Naomba sana Mheshimiwa Ummy aniambie atakuwa tayari lini kuja Tabora kuongea na wanawake wa Tabora awaahidi suala la hata deski tu kama siyo benki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee suala la chuo cha manesi. Tabora tumejengewa chuo cha manesi na Serikali wakisaidiana na ADB. Chuo kile ujenzi umefikia asilimia 90 bado asilimia 10 tu kumalizia lakini miaka miwili hatujapata fedha ya kumalizia. Majengo yale yameanza kupasuka, majengo yale yameanza kushuka kwa maana value ya majengo yale imeanza kupotea. Kwa kuweka maji na umeme asilimia 10 tu tutakuwa tumekamilisha. Mradi huu pia ulikuwa unajumuisha jengo la operesheni ambalo na lenyewe limesimama, pesa ni ndogo sana. Nimuombe Mheshimiwa Waziri aangalie jinsi ya kutupa hii pesa ndogo iliyobakia kwa sababu ya jengo la manesi ambalo litazalisha manesi wengi, wataweza kusaidia wananchi wa Mkoa wa Tabora.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
HE. MUNDE A. TAMBWE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia bajeti ya Serikali. Kwanza kabisa nianze kumpongeza Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Waziri na Naibu wake, lakini niwapongeze Menejimenti nzima ya Wizara ya Fedha kwa kutuletea bajeti nzuri, bajeti ya kihistoria, bajeti ya Watanzania, bajeti ambayo Wabunge wengi walipigia kelele vitu vyao, leo tumeviona kwenye bajeti hii. Tunaipongeza sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niongelee kuhusu Motor Vehicle. Sisi Wabunge kwenye bajeti ya fedha tulisema kwamba tunaomba Motor Vehicle iondolewe, Serikali imetusikia. Napata taabu kuwaona Waheshimiwa Wabunge leo hapa wanalaumu kwa nini Serikali imeondoa Motor Vehicle na imeweka Sh.40/= kwenye lita ya mafuta kama tozo kwa ajili ya Road License. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jana dada yangu Mheshimiwa Susan Lyimo aliongea hapa kwamba tunawaonea watu wa vijijini wanaowasha vibatari, kwa nini tunawawekea tozo ya mafuta? Mheshimiwa Msigwa pia aliongea, kaka yangu Mheshimiwa Heche ameongea hapa. Niwaulize tu, tunalipa tozo ya Railway Development Levy, Arusha kuna treni?

Mheshimiwa Spika, mimi nimezaliwa Tabora tena Mjini. Toka nimezaliwa umeme unawaka kwetu, lakini natozwa tozo ya REA. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunalipa tozo ya maji, mimi kwetu mjini, kuna maji toka nimezaliwa, lakini nalipa tozo ya maji. Waache kutuchonganisha na Watanzania.

TAARIFA .....

MHE. MUNDE A. TAMBWE: Mheshimiwa Spika, nimemsikia Mheshimiwa Msigwa.

Mheshimiwa Spika, wamesema kuna mtu ana generator, kuna mtu ana mashine ya unga, kwa nini anatozwa Sh.40/= kwa ajili ya Road License? Wamesahau tunalipia reli, tunalipia maji, tunalipia umeme wa REA na sisi tunakaa mijini. Kwa hiyo, mimi wa mjini ningesema sitaki kutozwa tozo ya REA kwa sababu mimi sikai kijijini. Baba yangu alishakufa, mama yangu alishakufa, bibi yangu alishakufa; sina ndugu kijijini.

Mheshimiwa Spika, mimi ni Mtanzania, tumejengwa kwenye umoja, ndiyo utamaduni wetu, tumejengwa kusaidiana. Leo napata taabu anaposimama hapa Mbunge anatubagua, anasema kwamba hawa watu wa vijijini tunawatoza Sh.40/= wakati hawatumii barabara. Nani asiyetumia barabara? Nani ambaye hatumii barabara? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, waache kutuchanganya, waache kutuchonganisha. Sisi ni wamoja na tutaendelea kuwa wamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hawa watu waache kuichanganya Serikali. Hawa watu wamwache Rais Dkt. Magufuli afanye kazi! Niliwahi kusema humu ndani tumwache Rais afanye kazi na anafanya kazi. Kazi yetu sisi ni kumwombea na kumuunga mkono; lakini wenzetu hawa mimi napata shida kweli, sijui wanamaanisha kitu gani? Wanakuja kuleta sababu ambazo hazina msingi kabisa hapa. Uzalendo wao ni mdogo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais leo anapambana kuhusu rasilimali za Taifa. Mgogoro huu ukikaa mezani, mambo haya yakiwekwa vizuri tutapata zahanati, tutapata maji, tutapara barabara. Mheshimiwa Rais ambaye anafanya kitu ambacho ni cha ukombozi kwa Tanzania, tumeibiwa muda mrefu, tumeonewa muda mrefu, anapambana, badala ya sisi tumuunge mkono, mtu anakuja kulalamika. Halafu mtu huyo huyo anasema sina maji kwenye Jimbo langu, sina zahanati kwenye Jimbo langu, rasilimali zinaibiwa. Mheshimiwa Rais leo amejua, anapambana tuzirudishe, lakini mtu huyu hataki, anasema tunawaonea Wazungu, tunavunja mikataba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakupongeza, jana umesema kama nimenukuu vizuri: “Hata kama mikataba imeingia miaka 50 iliyopita, lakini kama ni mikataba ya hovyo tutaikataa.” Amesema kipande chake cha Bunge kitatenda haki ikiwa ni pamoja na kubadilisha sheria hizo haraka sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakupongeza kwa uzalendo wako, nasi Wabunge wako tuko nyuma yako tunakuunga mkono, tunazubiri sheria hizo zije tuanze kuzibadilisha haraka iwezekanavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lazima Watanzania waelewe kwamba huyu mzee wetu Mheshimiwa Dkt. Magufuli anafanya nini? Jana kuna statement aliitoa mpaka nilitamani kutao machozi. Alisema: “Jamani na mimi nina damu, nami ni binadamu, lakini naumia kwa sababu yenu ninyi.”

Hivi Mheshimiwa Dkt. Magufuli angetaka kupokea mabilioni, angetaka kupokea mahati ya nyumba ya Marekani ili akae kimya tu, tungemfanya nini?

Mbona tunaibiwa siku zote hivi vitu? Ameonesha uzalendo wake. Mimi sitaki kuamini kwamba hakufuatwa kupewa hela, lakini amekataa chochote, anataka Watanzania wote wafaidi.

Anainuka Mbunge anakutaja kupingana na jambo hili ambalo ni kwa faida yetu sisi zote.
Mheshimiwa Spika, kwa kweli tumpongeze Mheshimiwa Rais, tumuunge mkono na tuendelee kumwombea Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anazozifanya…

TAARIFA......

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, naomba unitunzie muda wangu. Naomba nimwambie dada yangu Mheshimiwa Sophia, mabadiliko hayana wakati. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kutuletea Rais jembe, Rais mpambania wanyonge, Rais mpambania maskini, Rais ambaye hana tamaa yake binafsi na familia yake. Leo hii Rais Magufuli angekuwa na tamaa yake na familia yake angekomba mahela yote akaenda kuweka Uswiss huko na yeye na tungeendelea kuibiwa hapa na wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwaambie hawa watu ambao hawajui madini; siku ile Mheshimiwa Musukuma aliwaambia, mimi nimetoka Tabora Nzega, ukiona mashimo yaliyopo kule utalia. Kodi iliyolipwa kwa muda wote na Resolute haizidi shilingi bilioni 30. Wametuibia vibaya sana, wameondoka Halmashauri ya Nzega tunawadai Development Levy ambayo walitakiwa walipe shilingi bilioni 10 mpaka leo hawajalipa, Serikali inajua. Toka wameingia mpaka wanaondoka pale wamelipa shilingi bilioni mbili tu ya levy ya Halmashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna mtu mwingine anaongea tu, hajui chochote anachokiongea. Mimi nampongeza Rais, Mheshimiwa Dkt. Magufuli na nimefunga na sala zangu zote namwombea kwa Mwenyezi Mungu. Maadui wengine wa Rais Magufuli tunao humu ndani, sijui wanataka nini hawa watu. Mtu anapambana kwa sababu yetu na watoto wetu, hivi vyama kuna vipindi tuweke itikadi pembeni tuangalie Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniongezea dakika kumi. Kwa kweli kuna vitu ambavyo tunashangaza sana kwetu sisi. Nikitoka kuongea mambo ya makinikia ambayo ni mambo yamegusa Tanzania nzima; kule Tabora kuna Mwenyekiti wa UKAWA, jana amenipigia simu ameniambia Mheshimiwa Munde nimeenyoosha mikono kwa Mheshimiwa Dkt. Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kutaka kuwadhibitishia hilo, nikimaliza Bunge nitafanya mkutano wa hadhara Tabora nitamkabidhi kadi ya CCM ili wajue kwamba Watanzania wamemkubali Mheshimiwa Dkt. Magufuli kwa asilimia 100. Nilisema humu Bungeni kwamba wataelewa tu na wameelewa. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, naendelea kuwaambia Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwamba kazi tuliyonayo mbele yetu ni kui-support Serikali yetu ya Awamu ya Tano, Inafanya kazi vizuri sana. Nimekaa Bungeni, nimepita bajeti saba za Bunge, sijawahi kuona bajeti kama hii.

Mheshimiwa Spika, tusisahau kwamba Mheshimiwa Dkt. Magufuli ndiyo bajeti yake ya pili. Ana miaka miwili tu. Hata sisi Majimboni tuna mambo mengi hatujayafanya ya kwetu peke yetu. Leo kuna mtu anafanya kana kwamba Mheshimiwa Rais Magufuli leo ana mwaka wa kumi. Sijui kwa sababu amefanya mambo mengi, wanajisahau kwamba huyu mtu ameanza juzi tu. Sijui wamechanganyikiwa! Mimi hata sielewi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nawaonea huruma na kuwapa pole na kuwaambia bado nafasi tunazo mpaka 18 Juni tunafunga kupokea watu wa kutoka Upinzani. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Spika, bajeti imekuwa nzuri, nimpongeze kaka yangu Mheshimiwa Mpango, lakini niwaambie Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwamba bajeti haiwezi kumaliza matatizo ya nchi nzima, hii bajeti ya pili tu. Tuendelee kuipongeza bajeti hii, watufanyie kazi kama walivyotuahidi kwa kasi yao ya Awamu ya Tano, lakini kila mwaka tutaongea watatukubalia kama walivyotukubalia safari hii.

Mheshimiwa Spika, tumeongea motor vehicle wamekubali, tumeongea sana kuhusu kurasimisha Wamachinga na Mama Lishe. Leo hii wamekuja kutuambia kwamba wanarasimisha sasa. Watajulikana sasa. Wamachinga na Mama Lishe watakuwa wanajulikana na sekta rasmi.

Mheshimiwa Spika, mimi kama Mbunge wa Tabora tuliongea sana kuhusu reli, leo tunaenda kwenye standard gauge. Naomba niongelee sasa kuhusu suala zima la viwanda. Mheshimiwa Dkt. Magufuli wakati anajinadi, akiomba kura alisema anataka Tanzania ya viwanda. Bajeti hii imetuonesha mwelekeo mzuri wa Tanzania ya viwanda. Hivi jamani tunataka nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hii wamefuta capital goods, wameifuta kabisa imebakia zero, wamefuta VAT kwenye vifaa vya uwekezaji, wamepunguza kodi ya mboga mboga na matunda, wameondoa kodi kwa mtu anatayekwenda kuuza mjini tani moja ya mazao na ndiyo wengi mama zetu hawa, ndiyo wengi baba zetu hawa; anajilimia ekari zake kumi anaenda kuuza mjini kila siku kidogo kidogo. Walikuwa
wanapambana na watu wa kuwadai kodi, sasa hivi hakuna. Jamani Mheshimiwa Rais afanye nini? Serikali ifanye nini? Hii ni bajeti yake ya pili tu, wamejitahidi sana jamani. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kuchangia bajeti ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa mimi nianze kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa makusudi na dhati kubwa anayoifanya ya kuendeleza viwanda vya ndani. Anapambana kwa nguvu zake zote, na kweli Rais wetu ni mzalendo; na mimi niwaambie tu wale wanaobeza wanaosema hovyo, viwanda hivi siku vikija ku-achieve Magufuli atakuwa kamaliza muda wake, tutafaidika sisi, watoto na wajukuu zetu.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Rais anafanya kazi hii kwa ajili ya watanzania, ni wajibu wetu kumuunga mkono Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niungane na Wabunge waliotangulia kusema, lazima Serikali hii iwe na mkakati maalum. Tumechoka sasa kuagiza mara mafuta mara sukari, kama Mheshimiwa Rais anavyotaka viwanda vya ndani vifanye kazi basi na Waziri na viongozi wote wa Serikali waungane na Mheshimiwa Rais kwa vitendo. Tujiwekee labda miaka miwili au mitatu tusiagize tena mafuta wala sukari nje ya nchi, tunaweza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano sasa hivi NSSF wana shamba kubwa la miwa, ni kuhakikisha tunaongeza uwezo mkubwa kwa wafanyabiashara wengine wa viwanda, lakini NSSF tuweke nguvu zetu zote, wafanye bonde lingine na bonde lingine, tuwaongezee nguvu hatimaye miaka miwili tusinunue sukari nje ya nchi. Tuna uwezo mkubwa wa kufanya hivi kama tutaamua. Tuna Mkurugenzi mzuri sana pale NSSF mkimpa nguvu anaweza kufanya hili jambo, lazima tuwe na mikakati, lazima tuamue. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Waziri Mkuu kwa kauli yake nzuri aliyoitoa juzi kuhusu sukari na mafuta, kwamba ndani ya siku tatu vitu hivyo viwe vimetoka. Nasema hivyo kwa sababu mahitaji ya mafuta ni tani 28 hadi 30 kwa mwezi, Januari, Februari na Machi tumeingiza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Aprili mafuta hayo waliyoleta nyaraka hazitimii, Serikali haiwezi kukuingizia bila nyaraka, hivi vitu ni mafuta/ni chakula, hauna TBS ya Malaysia tukuingizie kama, kuna sumu. Hakuna code iliyoonesha mafuta ghafi yamelipiwa Malaysia, Malaysia hawatoi mafuta ghafi bila kulipia kodi, nyaraka hazitoshelezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii isiwe sababu ya kuwaadhibu Watanzania kwa kuficha mafuta haya. Nasema hivi nina maana yangu, haya mafuta waliyoingiza wanaita wameingiza crude oil (mafuta ghafi). Haya mafuta ghafi ya mwezi wa nne kwa mfano yangeingia mpaka process kila kitu labda tarehe nne au tano yangekuwa yameingia, lakini mafuta haya ni lazima waende kuya-refine kuyasafisha ili yaje kuingia sokoni. Mpaka waya-refine ina maana sokoni mafuta haya yangeingia kwenye tarehe 12, 13 na 14; leo vipi mafuta hakuna nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, watu hawa wameficha mafuta ku-demand bei ipande na kuikomesha Serikali. Nakupongeza sana Waziri Mkuu kwa kauli yako ya watoe mafuta, kwa sababu mafuta ya Aprili hata kama yangekuwa yameingia wangekuwa hawajamaliza kuya- refine, kuyasafisha na kuyaingiza sokoni, iwaje leo mafuta yapotee kabisa ndani ya soko la Tanzania. Mheshimiwa Waziri Mkuu mafuta yapo, Serikali iweke nguvu mafuta yatoke na Watanzania wauziwe kwa bei inayostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa tuamue kabisa, tuna asilimia 30 ya mafuta tunayolima mbegu hapa Tanzania, tuamue kuwekeza. Serikali juzi iliamua kuwekeza nguvu zake zote kwenye pamba, TAMISEMI, Waziri wa Viwanda, Waziri wa Kilimo, Mkuu wa Mkoa, Wakuu wa Wilaya hatimaye mwaka huu pamba imekuwa nyingi sana Mwanza. Tuamue kwenye alizeti, michikichi. Hatuwezi kuamua kwenye vitu vyote kwa wakati mmoja, tuchague mazao yetu ambayo tuamue, kwa mfano uchukue Dodoma, Singida, Tabora useme ni zone ya alizeti, hii ni zone ya alizeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mwijage nimepitia hotuba yako kuna sehemu umesema una matrekta 148 unauza, nikwambie kwa hali ya sasa hivi kununua cash yale matrekta watu wengi hawatamudu. Sasa lazima Serikali itusaidie. Mimi niombe tuanzie Mkoa wangu wa Tabora, nina wilaya saba, kila Halmashauri moja mtupelekee matrekta matatu mtukopeshe, mdhamini atakuwa Halmashauri, Mkuu wa Mkoa, DC na mimi Mbunge wa Viti Maalum pamoja na Wabunge wa Majimbo yangu ya Mkoa wa Tabora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapewe matrekta matatu matatu, haya matrekta yawe mali ya Halmashauri, mtu akienda Halmashauri aandikiwe mkataba utajaza mafuta, utalipa posho, ukiimbua utalipa pesa za gharama ya kulimia. Zile pesa zitakuja kulipwa kwako Mwijage, lakini hutapata cash lakini utakuwa umesaidia Watanzania. Wakati huo huo mtafute mbegu za kisasa za alizeti, zilizopo hazitoi mafuta mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mwijage hata mchikichi pia tufanye vivyo hivyo. Mchikichi unaweza kupeleka Kigoma, Mbeya kwa maana ya Kyela pamoja na Katavi na ukaita mchikichi zone na akili zote, viongozi wote wakaelekezea kwenye haya mambo, inawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumechoka kunyanyasika Mheshimiwa Mwijage, watu wanaficha mafuta demand inapanda, Serikali nzima inapata stress mnashindwa kufanya vikao na vitu vingine, mnakaa kwenye vikao mpaka saa saba za usiku, hivi vitu tunaviweza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbona Rais ameamua tutajenga standard gauge, Afrika nzima hakuna anayejenga standard gauge kwa hela yake, mbona ameweza? Mbona ameamua kununua ndege na kusomesha elimu bure ameweza; watu wamepiga kelele haiwezekani, imewezakana. Nina amini tukifanya hii alizeti zone na mchikichi zone tukawekeza tunaweza Mheshimiwa Mwijage. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi trekta zikipelekwa Halmashauri wakabidhiwe wakurugenzi ma-DC, RC na Wabunge watu wakakope pale kwa mikataba wakalime baadae watalipa kwenye Halmashauri, tutaenda mbali sana. Pia mtusaidie viwanda vidogo vya kukamulia hizi alizeti, kila Halmashauri ikopeshwe. Serikali bado ina uwezo huo, Halmashauri zetu zina uwezo wa kununua viwanda vidogo, ni maelekezo tu. Kama kweli tumeamua kumsaidia na kumuunga mkono Mheshimiwa Rais naamini hivi vitu vinawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee sasa kuhusu suala zima la viwanda, nianze na Kiwanda cha Tabora. Tabora kule tuna kiwanda cha nyuzi, kiwanda cha nyuzi cha Tabora kinazalisha pamba, tumekuja kuomba mara kadhaa pamoja na mwenye kiwanda tuiombe Serikali inunue pamba za hospitali kutoka kwenye kiwanda cha nyuzi cha Tabora; tuwasaidie wenye viwanda vyetu, kwa mfano mtu ana kiwanda cha kutengeneza kitu ambacho kinawezekana Serikali kinaitaka, Serikali inunue kwake kumpa support. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais kila siku amekuwa akisema jamani tengenezeni hata syringe za hospitali tutanunua kwenu, kwa hiyo tum-support. Kule Tabora hamji kununua pamba kwa ajili ya matumizi ya hospitali, mnaagiza nje ya nchi. Tunaomba Mheshimiwa Mwijage mje mnunue kule kwetu Tabora. (Makofi/kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niendelee kuongelea viwanda vidogo, kumekuwa na kebehi zinafanyika hapa Bungeni kwamba cherehani si viwanda, hakuna viwanda 3000; mimi naomba ni-declare kuhusu cherehani, nitoe ushuhuda. Kuna ndugu yangu ni fundi cherehani, alishindwa
kusoma akaishia form three akajisomesha cherehani akaendelea akanunua cherehani nne, huyu akaenda kukopa benki, wakamwambia huwezi kukopeshwa bila leseni wala TIN, akapata. Baadae akapata tender ya kutengeneza mashati ya taasisi X, siwezi kuitaja hapa, wakamlipa shilingi milioni 70; sasa hivi amenunua cherehani 45. Mheshimiwa Mwijage nifuate nitakuonyesha na amenifuata mimi, dada nitafutie eti tenda ya kushona nguo za jeshi nikamwambia eeh umefikia huko mwenzetu? Kwa hiyo, wale wanaodharau hizi cherehani nawaambieni hivi watu wanatoka kwa hizi cherehani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe sasa Serikali kwa sababu Serikali mmekubali cherehani ni viwanda vidogo hakikisheni taasisi zenu, wenye viwanda hivi vya cherehani wapeni kazi. Kwa mfano uniform za TPA, TANAPA na uniform sijui za nini wapeni washone, wapeni uwezo, watu wasiende kushona hizi uniform nje, Serikali hii inaweza ni kiasi cha kujipanga tu. Kwa hiyo, mimi bado naitia moyo Serikali kwamba tunaweza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, A to Z ya Arusha ni kiwanda kikubwa sana, Kamati tuliwahi kwenda kutembelea mwaka 2013. Historia yake mwenye A to Z alikuwa na cherehani moja, alianza na cherehani moja, mwenye A to Z ya Arusha, anayebisha akamuulize. Leo hii ni kiwanda kikubwa duniani, hata huu mchakato wa malaria amepata tender viwanda vitano duniani na yeye amepata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, anatengeneza mashuka, uniform na kila kitu. Kwa hiyo, tusidharau hizi cherehani watu wanaponda viwanda gani kama cherehani, mimi nasema hivi ni viwanda na vinafanya kazi na watu wananufaika kutokana na hizi cherehani.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii nami niweze kuchangia. Nilikuwa na mambo mengi ya kuchangia kuhusu Tabora, lakini nimeona muda wangu kidogo nichukue kumjibu kaka yangu Mheshimiwa Mnyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mnyika amesema Mheshimiwa Rais kwa sababu ana nafasi ya kufanya uzinduzi wa miradi, angechukua nafasi ile akafanya Sala ya Kitaifa kuiombea nchi hii. Mimi nadhani Mheshimiwa Rais anafanya kazi kubwa na ndiyo maana kuna miradi mingi ya kuzindua. Hiyo ni kazi, tena kubwa ya kuwaonesha Watanzania ni nini Serikali yao inafanya? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii ina dini; ina Wakristo, Waislam na dini tofauti tofauti. Kila siku tunasali kumwomba Mwenyezi Mungu. Hapa leo ni Ijumaa, nikitoka hapa naende Msikitini kusali, kumwomba Mwenyezi Mungu kwa ajili yangu na familia na nchi yangu. Nadhani watu wote wanafanya hivyo.

Mheshimiwa Rais ameweza kuita viongozi wa dini mara kadhaa, anaongea nao kutaka maoni yao na kuwaomba waendelee kuiombea nchi yao. Mimi nadhani Mheshimiwa Mnyika labda ana stress. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mnyika ameongea kuhusu Katiba mpya. Ni hao walijiunga UKAWA mara ya kwanza kwa ajili ya kwenda kuipinga Katiba iliyopendekezwa. Namshangaa leo anaidai Katiba hiyo ambayo wao kwa mara ya kwanza waliungana kwenda kupinga nchi nzima watu wasiiunge mkono Katiba iliyopendekezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa leo namshangaa ndiyo niseme ndimi mbili, ndiyo niseme mna stress kwamba hamtapata Ubunge tena, yaani nachanganyikiwa kwa kweli. Mliikataa Katiba, leo mnaitaka Katiba. Yote hiyo ni kui- frustrate Serikali ishindwe kufanya kazi yake, tukae na Katiba tushindwe kuendeleza miradi iliyopo ili pesa yetu tuimalizie kwenye Katiba mje mseme kwamba Mheshimiwa Rais aliahidi maendeleo, ameshindwa kufanya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudie kusema tena Mheshimiwa Rais fanya kazi yako kama inavyostahili, achana na mambo ya Katiba, hukuwaahidi Watanzania Katiba, uliwaahidi maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongee tena kidogo kwamba wamekuwa wanasema sana kwamba Wakurugenzi, Ma-DC, ni wana CCM ni nani anaweza kufanya kazi na mtu ambaye hamwamini. Hata leo nikifungua duka, nitamweka ndugu yangu, nitamweka mtu ninayemwamini aliye karibu name. Ni nani anaweza kuwa Rais kati yao wao akachukua Mbunge wa CCM Munde akampa Ukuu wa Mkoa? Hatuwezi kufanya hivyo. Mheshimiwa Rais angalia watu unaowaamini, uliowachuja, wakakuridhisha kufanya kazi na wewe kama vile wao ambavyo wanabebana, wanasaidiana wao kwa wao kwenye nafasi zao chungu nzima ikiwepo Ubunge. (Makofi/Kicheko)

MBUNGE FULANI: Wape dozi. (Kicheko)

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee na Bajeti Wizara. Naipongeza Wizara ya TAMISEMI kwa kazi nzuri wanayoifanya. TAMISEMI wamefanya kitu kizuri sana, wameboresha ukusanyaji wa mapato. Leo hii ukiwa popote, viongozi wa TAMISEMI wanaweza kuangalia Halmashauri gani imekusanya shilingi ngapi, imetumia shilingi ngapi na imefanya nini? Hii ni hatua kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza sana kaka yangu Mheshimiwa Jafo na Manaibu Waziri pamoja na Menejimenti nzima ya TAMISEMI. Vile vile naipongeza Wizara ya Utawala Bora, mzee wetu Mheshimiwa Mkuchika, mpenzi wetu Naibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Mary Mwanjelwa tunakupongeza sana, mnafanya kazi kubwa mno tunawaona. Tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu mwendelee kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii system waliyoiweka ni nzuri sana. Kwa kweli mimi nimefanya kazi Halmashauri, naomba ni-declare. Hakuna tena mtu atakayeweza kuiba revenue ya Halmashauri. Watu wataiba kwenye matumizi hewa, kwenye ten percent, kuagiza vitu ambavyo siyo vya kweli. Kwenye revenue kwa kweli mmedhibiti na mtaacha legacy, hii kazi mmeifanya ni kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongee kuhusu vitambulisho. Wenzetu hawa wamekuwa wanaongea sana kuhusu vitambulisho vya 20,000 wakiviponda na kuvibeza. Kama nilivyosema, nimefanya kazi Halmashauri. Zamani akina Mama Lishe, Wamachinga walikuwa wanatozwa shilingi 500 kwa siku. Anapewa risiti ya shilingi 500/=, kesho anapewa risiti ya shilingi 500, analipia shilingi 500.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya wiki mbili anaenda kufurumuliwa, masufuria ya wali yanamwagwa, maharagwe yanamwagwa, mboga zao zinatupwa. Leo Mheshimiwa Rais amewatambua kwenye Sekta Rasmi ya Wamachinga kwa kuwapa vitambulisho wa shilingi 20,000. Nilidhani tutafurahi, tutaridhika wamama hawa, Wamachinga, vijana wetu hawatanyang’anywa tena vitu vyao, watafanya kazi wakiwa na confidence zao na wameambiwa wasiguswe wafanye kazi popote. Mnaka nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zamani shilingi 500/= ukiizidisha mara siku 365 za mwaka walikuwa wanalipa shilingi 182,000/=. Leo shilingi 20,000/= ukiigawa kwa siku 365, wanalipa shilingi 55/= kwa siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimetoka Tabora. Sisi ni maarufu sana wa kupika vitumbua. Mama anayepika vitumbua; kitumbua kimoja shilingi 500/=, akiuza vitumbua 40 ana shilingi 20,000/=. Mwaka mmoja una wiki 52. Kila wiki mama huyu aweke hela ya kitumbua kimoja tu 500, ndani ya wiki 40 amefikisha 20,000/=. Hivi mnataka nini jamani? Au mmezoea kupinga tu? Mlipinga reli, mmepinga Stiegler’s, mnapinga ndege. Tumewazoea! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwaambie Serikali, nimwambie Mheshimiwa Jafo, vitambulisho hivi viendelee, ni kitu kizuri sana, kinawatambua Wamachinga wetu, Mama Lishe wetu, hawafukuzwi tena, hawamwagiwi vitu vyao, lakini 20,000 ni reasonable price. Wale watu ilikuwa vikishachukuliwa vile vitu vikamwagwa na Mgambo wao wanawachukua wanawatumia kwenye maandamano. Safari hii mmewakosa. Safari hii mtoto wake ambaye yuko India, yuko Marekani, amlete aandamane. Wamachinga tena hamwapati. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie haraka haraka. Niseme tu, ni lazima kila Mtanzania achangie pato la Taifa. Tuache kujidanganya. Hamna nchi yoyote duniani watu hawalipi kodi; hamna nchi yoyote duniani watu wanafanya kazi bila kulipa ushuru; tusidanganyane. Hawa watu wenye sekta ambazo siyo rasmi, ndogo ndogo ndio walio wengi. Kwani wanapita barabara zipi? Hospitali wanatibiwa ipi? Kwa nini wasichangie pato la Taifa? Kwa hiyo, tusitake kuivuga Serikali na kuitoa kwenye msimamo wake thabiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie kuhusu Jimbo la Ulyankulu. Jimbo hili lina wakimbizi wengi sana. Wakimbizi hao wamekubaliwa kupiga kura ya Mbunge na kura ya Mheshimiwa Rais. Wakimbizi hawa wamekataliwa kuchagua Diwani kwenye maeneo yao, hawachagui viongozi wa Serikali za Mitaa, jambo linalotushangaza kabisa. Kwa sababu huu ni uadui mkubwa. Huwezi kukaa na mtoto wa ndugu yako ukambagua, hiki fanya, hiki usifanye. Kama walikuwa hawatakiwi, wasingepewa uraia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu hawa wameshakuwa raia sasa, Watanzania, kwa nini mnawazuia wasichague Madiwani? Kwa nini mnawazuia wasifanye uchaguzi wa Serikali za Mitaa? Ukiangalia ni double standard. Kwa sababu kwa yangu Mheshimiwa Kakoso kule kuna wakimbizi, lakini wanachagua Madiwani, wanachagua Serikali za Mitaa, wanachagua Wabunge, wanachagua Rais. Sasa huku ninyi mmetuwekea wachague Wabunge na Rais tu. Sasa kama anamchagua Rais, anamchagua Mbunge, kwa nini unamkatilia asichague Diwani na umeshampa urai? Huyu ni raia. Kwa hiyo, naomba mwatendee haki, wapate nafasi, wapate fursa nao wachague na wajichague. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, imeenda mbali zaidi, hawapati chochote cha Kiserikali wakati tumeshawapa urai. Juzi nilikuwa kule Kaliua, wamana hawo wanakataliwa kupata mikopo ya Halmashauri na wakati vikundi vyao na wakati tumeshawapa uraia: Je hii ni sahihi jamani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunatengeza bomu ndani ya nchi yetu. Hawa tumekuwa kama tumewapa uraia, lakini tunawabagua. Basi kama ni hivyo, tuwanyime uraia, tuwanyang’anye. Kwa sababu tumeshawapa, naomba pia wakubaliwe kufanya kila kama wanavyofanya wengine. Kule kwa Mheshimiwa Kakoso, kwa kaka yangu Mbogo kuna wakimbizi, lakini wanafanya kila tu. Kwa nini isiwepo na Ulyankulu hivyo hivyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni lini Kambi za wakimbizi zitafungwa? (Makofi)

(Hapa kengele ya pili ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na kuwapongeza Mawaziri wote, Mawaziri wa Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya, wasitishwe na watu wanaowaambia wanavamia vamia. Wafanye kazi kwa kujiamini, ni Serikali yao, wawatumikie
Watanzania kama Mheshimiwa Rais John Pombe alivyowaaamini kuwapa Uwaziri huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kidogo kuhusu uchaguzi wa Zanzibar tarehe imetangazwa. Niwaombe Wazanzibari wote wasubiri siku ya uchaguzi iliyotangazwa wakapige kura. Acheni kuwatisha Watanzania, acheni kuwatisha wananchi na kuwajaza jazba ambazo hazina msingi wowote na baadaye mtatuhatarishia amani ya nchi yetu, tunaomba sana.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kuipongeza hotuba ya Mheshimiwa Rais, kwa kweli hotuba ya Mheshimiwa Rais imesheheni mikakati ya kuijenga Tanzania mpya, imesheheni mikakati ya kuijenga Serikali ya Awamu ya Tano. Nampongeza sana Rais John Pombe Magufuli kwa hotuba yake nzuri kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nisisite kusema tu, kwa kweli Mheshimiwa Magufuli amewashangaza Watanzania, kwa muda mfupi tu ameanza kutekeleza ahadi zake alizozitoa Novemba hapa Bungeni. Ni vyepesi sana kukosoa na kulaumu, lakini kwa muda alioanza kutekeleza ahadi, ahadi zenyewe ni kubwa sana, zinahitaji utaalamu, zinahitaji pesa, ameanza kuzitekeleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mtu amesema kwamba, mambo elimu bure ni double standard, siyo kweli, mwanzo ni mgumu. Mheshimiwa Simbachawene ametuambia, wamepata hesabu vibaya ya wanafunzi, lakini wanaamini watakwenda vizuri huko mbele. Tuwatakie kila la heri kwenye mipango yenu, tuwatie moyo, tumsaidie Rais wetu, tuwasaidie Mawaziri kuhakikisha Watanzania wanapata huduma alizozisema Rais wetu. Tunawatakieni kila la heri na Mwenyezi Mungu atawasaidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, niongee kidogo kuhusu maji. Niipongeze Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, ilituahidi maji ya Ziwa Victoria watu wa Tabora, iko kazini inafanya kazi vizuri na imeahidi kuanzia mwezi wa sita itaanza kukarabati maji kutoka Ziwa Victoria kuleta Tabora, tutafaidika sana. Nzega mpaka Tabora Manispaa vijiji 86 vitapitiwa, vitapata maji ya Ziwa Victoria. Niiombe Serikali yangu, iende na action plan yake isije katikati ikakatiza.
Tunaambiwa kufika 2019, Tabora tutapata maji ya Ziwa Victoria. Naiomba sana Serikali ya Awamu ya Tano ambayo tunaiamini, Serikali ya hapa kazi tu, 2019 itupatie maji ya Ziwa Victoria.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pale Tabora kwenye maji ya Igombe, tulikuwa na shida ya pampu, tulikuwa na shida ya machujio, Serikali ya Chama cha Mapinduzi imeshatuletea sasa na tunategemea kupata lita milioni 30 za maji badala ya lita milioni ishirini nne ambazo
tunazihitaji. Tunaipongeza sana Serikali kwa kazi nzuri inayoifanya na tunaomba wananchi wa Mkoa wa Tabora mwendelee kutuunga mkono.
Mheshimiwa Naibu Spika, juzi kati hapa maji yalikatika tulipigiwa simu kama Wabunge, lakini tatizo kubwa ni umeme, umeme kwa kweli Tabora umekuwa na mgao mkubwa sana, lakini niwaombe wananchi wa Tabora mtulie. Tumepata mwarobaini wa umeme ambae ni Profesa Muhongo. Profesa Muhongo yuko kazini, ameingia juzi, atafanya kazi, tunamwamini sana na tunaamini baada ya muda mgao huu utapotea. Tunamwamini na tunamwombea kwa Mwenyezi Mungu afanye kazi yake kama tulivyomzoea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara, kuna kilometa 80 ambazo tunaziombea lami, Mheshimiwa Rais ametuahidi kutuwekea lami. Tunamwomba Waziri husika aiwekee lami hiyo katika hizo kilometa 80. Sasa hivi barabara ya Itigi-Tabora hakuna mawasiliano, imekatika,
tunaomba pesa za dharura, magari yamekwama pale, watu wanazunguka Singida, hali ni mbaya, nauli ni kubwa, watu wanashindwa kusafiri kupeleka wagonjwa wao na kuwahudumia.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Serikali, namwomba Waziri wa Ujenzi, tunaomba pesa ya dharura, tutengeneze madaraja hayo yaliyokatika Itigi-Tabora na pia tunaomba ufuatilie hiyo lami ya kilometa 80. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naongelea sasa suala la zima la reli. Hakuna Mtanzania wala Mbunge asiyejua reli ni uchumi, reli inaleta maendeleo, reli inapunguza bei ya bidhaa.
Tunashangaa kwa nini kila tukipanga masuala ya reli yanaishia njiani. Nashindwa kuelewa, naiomba sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, ihakikishe tunaboresha reli, ihakikishe reli hii inakuwa kama ni kitega uchumi cha Tanzania. Tukiboresha reli tutasafirisha mizigo ya Congo, Rwanda na Burundi. Nashangaa tatizo ni nini? Tunapata habari za mitaani kwamba kuna watu wenye malori wanatufanyia vitu fulani kiasi kwamba reli yetu isiendelee. Naomba sana kama hilo suala lipo basi liangaliwe na lichukuliwe hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna vitu vinavyoudhi sana kwenye suala zima la reli. Reli ni mbovu kwa muda mrefu, matengenezo yaliyofanyika ni Dodoma mpaka Igalula tu, lakini Kaliua-Mpanda haijatengenezwa, Tabora-Mwanza, Tabora-Kigoma, Igalula-Tabora reli hii haijatengenezwa. Kuna kilometa 35 kutoka Igalula kwenda Tabora Manispaa, hali ni mbaya sana, tunaiomba sana Serikali iangalie suala zima la reli.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwenye reli kuna majipu ya kutumbuliwa, hii ndiyo kazi ya Mheshimiwa Magufuli na Mawaziri wake. Tunaomba sana, kuna watu wamepewa miradi ya kukarabati reli. Kwa mfano, kuna mradi wa kukarabati reli kuanzia Kaliua-Mpanda, kuna watu
wapo pale wanaikarabati hii reli, lakini reli hii toka imeanza kurabatiwa na watu wanaojiita ni Wahandisi waliostaafu, wana Kampuni yao inaitwa ARN, wanaikarabati bila kokoto bila chochote na mabehewa yanaendelea kuanguka na hakuna chochote kinachokarabatika.
Tunaomba sana hili ni jipu na Serikali yangu sasa hivi ina mpango mzima wa kutatua matatizo haya basi ikafanye.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mradi wa kukarabati reli ya Godegode. Godegode pale kuna watu wanakarabati reli kila mwaka, lakini ndiyo kuna ajali kila mwaka za treni, kwa hiyo, nashindwa kuelewa watu wanalipwa pesa za nini wakati ajali zinaendelea. Kuna Wamalaysia
walikuja kututengenezea injini zetu, injini zetu za muda mrefu zilikuwa mbovu, wametutengenezea injini, ni jambo jema, tunawashukuru kwa kututengenezea injini zetu, lakini kinachonishangaza, tuna mafundi wa railway, lakini bado hawaa Wamalaysia wanakuja kila mwezi eti kufanya service za zile injini. Kwa nini service hizi zisifanywe na mafundi wetu wa railway ambao wanalipwa mishahara na Serikali ya Chama cha Mapinduzi? Leo Wamalaysia wanakuja kufanya service kila mwezi, hili ni j pu Mheshimiwa Waziri tunakuomba sana uliangalie.
Kuna Injini 9010 mpya imenunuliwa kwa mamilioni ya shilingi. Juzi tu imeanguka Zuzu kwa sababu reli ni mbovu. Naumia sana kukwambia kwamba katika mabehewa mapya yaliyonunuliwa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa gharama kubwa, mabehewa 70
yameshaanguka katika mapya na yako porini mpaka leo hayajanyanyuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri afuatilie mabehewa haya mapya yaliyoanguka huko porini na yarudishwe, yakarabatiwe ili yaendelee kufanya kazi. Mheshimiwa Naibu Spika, naongelea suala zima la wafanyakazi, wafanyakazi hawa
wanakatwa mishahara yao ya kwenda kwenye Mifuko ya Jamii mfano NSSF, lakini wanakatwa kupelekwa kwenye SACCOS zao, wanakatwa wale waliokopa NMB. Hata hivyo, makato haya hayapelekwi NSSF, hayapelekwi kwenye SACCOS zao, tunashindwa kuelewa pesa hizi
zimekatwa kwenye mishahara yao zinakwenda wapi. Naomba sana Serikali ifuatilie suala hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna afisa amezuka anaitwa afisa wa kumsindikiza dereva, afisa huyu anapanda pamoja na dereva wa treni, analipwa laki moja na nusu kwa trip, dereva halipwi hata senti tano, eti yeye anaangalia treni isikimbie. Treni isikimbie wakati tuna vituo?
Mheshimiwa Naibu Spika, inajulikana kutoka Dodoma mpaka Zuzu ni dakika fulani, akiwahi ataulizwa? Kwa nini awekwe mtu ambaye analipiwa pesa nyingi? Kwa hiyo, huu ni mpango wa wakubwa, tunaomba ukomeshwe mara moja na pesa hizi walipwe madereva.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kumezuka utaratibu ambao siuungi mkono, anayekwenda kukata tiketi ya kuondokea treni anaambiwa aende na kitambulisho. Sisi wote hapa asilimia kubwa tumetoka vijijini, tunajua ndugu zetu wa vijijini hawana utaratibu wa kutembea na vitambulisho. Unakuta mtu amemleta stesheni moja ya Kintinku siku moja, anaumwa, wanamkatalia kumpa tiketi eti hana kitambulisho au anaambiwa aende na picha.
Mheshimiwa Naibu Spika, mambo mengine nitaandika kwa maandishi.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Munde, muda wako umekwisha.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MUNDE A. TAMBWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa ninaipongeza hotuba nzuri ya Waziri Mkuu, lakini nimpongeze Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nimpongeze Waziri Mkuu na nipongeze Baraza zima la Mawaziri kwa kazi nzuri wanayoifanya, kazi yao inatutia moyo sana na inafanya sisi kama wana CCM tutembee kifua mbele. Tunawapongeza sana, tunaomba muendelee kufanya kazi kwa juhudi kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze moja kwa moja kuchangia kuhusu mambo ya Tabora. Naomba nianze na suala zima la tumbaku, maana tumbaku ndiyo Tabora, bila tumbaku Tabora haipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, zao hili la tumbaku limekuwa ni zao linalochangia kodi kubwa, pato kubwa la Taifa, lakini wakulima wa tumbaku wanatozwa tozo 19 za tumbaku, hili suala linadhoofisha sana wakulima wa tumbaku. Mkulima wa tumbaku ukimkuta leo hana maendeleo yoyote, tozo ni nyingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaiomba Serikali yangu, ninamuomba Waziri Mkuu na Serikali ya Awamu ya Tano, kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu mziangalie hizi tozo, muweke mkakati maalum wa kupambana na hizi tozo kuzipunguza ili wakulima wa tumbaku waweze kufaidika na kilimo wanacholima, najua Serikali ya Awamu ya Tano ni Serikali ya kusaidia wanyonge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Tabora tunalima tumbaku kwa asilimia 60 lakini huwezi kuamini hatuna kiwanda cha ku-process tumbaku, hatuna kiwanda cha kutengeneza sigara, inaumiza sana nasema kwa uchungu mkubwa, juzi amekuja mwekezaji wa kujenga kiwanda cha sigara, kiwanda hicho kimewekwa Morogoro, Morogoro hawalimi tumbaku, ajira zetu watapata watu wa Morogoro kule sisi tunaumia, miti inakwisha, watu wetu wanakonda na moto wa tumbaku, hatuna faida yoyote na hiyo tumbaku. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaiomba Serikali ya Awamu ya Tano iliangalie hili suala kwa makini sana, ninamuomba Waziri Mwijage ninamuamini, ana uwezo mkubwa wa kufanya kazi. Tumehangaika naye kutafuta mwekezaji wa tumbaku mara nyingi, lakini Mheshimiwa Waziri Mwijage nikuombe sana hata kama tumekosa kiwanda cha sigara atusaidie tupate hata kiwanda cha ku-process tumbaku hali ya Tabora kwa kweli siyo nzuri, hatuna kiwanda chochote, ajira ni shida. Ninaiomba sana Serikali ya Awamu ya Tano itusaidie, ituonee huruma, tumbaku yote inapatikana Tabora. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumbaku imeliingizia Taifa dola milioni 3 lakini pia inachagia pato la Taifa asilimia 27 ya GDP ya Taifa. Kwa hiyo, tunaomba sana mtuangalie watu wa Tabora.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kuhusu suala la hospitali, Tabora Manispaa hatuna hospitali ya Wilaya, tumeliweka hili suala kwenye bajeti toka 2012, tumepata shilingi 150,000,000 tumeanza, lakini tunaiomba Serikali kupitia kwa Waziri Mkuu iangalie jinsi ya kutuwekea hospitali ya Wilaya, pale ni Makao Makuu ya Mkoa population ni kubwa sana, mtu akiumwa malaria moja anaenda hospitali ya Mkoa, msongamano unakuwa mkubwa, matokeo yake tunawalaumu madaktari kila siku lakini kwa kweli msongamano ni mkubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Uyui ambayo iko Tabora Manispaa haina hospitali ya Wilaya, ninaiomba Tabora Manispaa na Uyui tupate pesa za kuweka hospitali za Wilaya ili kupunguza population kubwa ya wagonjwa kwenye hospitali ya Mkoa wa Tabora. Leo siongelei Madaktari Bingwa, Mheshimiwa Ummy aliwahi kuniahidi hapa kwamba analishughulikia suala la Madaktari Bingwa na ninamwamini sana Mheshimiwa Ummy, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kwa kazi anazozifanya ninaamini atatuletea Madaktari Bingwa ndani ya Mkoa wa Tabora. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee kuhusu kupata Mkoa mpya wa Tabora. Katika Mikoa mikongwe ya nchi hii, Mikoa ya kwanza toka tunapata uhuru ni Mkoa wa Tabora. Kwa kweli Mkoa ule umepanuka jiografia yake ni kubwa, Mheshimiwa Waziri Mkuu amefanya kazi Tabora, anaijua kabisa jiografia ya Mkoa wa Tabora, tunaomba atusaidie kuugawa huu Mkoa, RCC imeshakaa zaidi ya mara tatu, mara nne tukitoa mapendekezo ya kuugawa Mkoa wa Tabora, tunaomba atusaidie sana, tupate Mkoa wa Tabora na Mkoa mpya wa Nzega. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Tabora Manispaa lina population kubwa sana, lina Kata zaidi ya 30 watu ni wengi sana, leo ukiangalia watu wa Jimbo la Pangani ni kama watu 45,000 tu, lakini angalia watu wa Jimbo la Tabora Manisipaa, tuko kwenye 300,000 na kidogo uwajibikaji unakuwa mgumu, kuwafikia wananchi inakuwa kazi sana. Ninamwomba Waziri Simbachawene ni lini sasa atagawa hii Wilaya ya Tabora Manispaa na kuwa Majimbo mawili. Tunamwomba sana atusaidie hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Wilaya ya Uyui tuliomba Halmashauri ya Wilaya ya Mji Mdogo muda mrefu, tunaiomba Serikali ikija ku-wind up ije na majibu kwa ajili ya Halmashauri ya Wilaya ya Uyui. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu milioni 50 ya kila Kijiji na kila Mtaa. Kwanza nianze kwa kukipogenza Chama changu cha Mapinduzi, viongozi wangu wa Chama cha Mapinduzi kwa kuweka kwenye Ilani yao ya Chama cha Mapinduzi, kwamba kila Mtaa watu wapate milioni 50 na Kijiji ili kusaidia watu wanyonge, watu wa chini, vijana na sisi kina mama. Niwapongeza sana Chama cha Mapinduzi na niseme hiki ni kitu kikubwa sana walichofanya it is not a joke. Kwa hiyo, mimi nawambie tu wale wanaosubiri kukitoa hiki chama madarakini watasubili sana!
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Watasubiri sana hiki chama kutoka madarakani siyo rahisi, jambo hili ni kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nitoe pongezi zangu za dhati kwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Sikudhani kabisa kwamba bajeti hii ya mara ya kwanza Rais Magufuli na Serikali yake watakuja na mpango wa hizi milioni 50, nilijua wana mambo mengi, wana elimu bure, wana elimu bure kwa vyuo, mimi ninaiita elimu bure kwa vyuo kwa sababu revolving ya vyuo vikuu hatuanza kuiona, pesa zinazoenda kukopesha watoto wetu wa vyuo mimi niseme ni bure tu, Serikali ya Chama cha Mapinduzi inafanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais na Waziri Mkuu kwa kuanzisha bajeti yao ya kwanza tu kuweka hizi milioni 50. Mimi nilikuwa nadhania kwamba shilingi milioni 50 labda zitakuja 2018, niliwahi kwenda Tabora kwenye kikao cha akina mama wakaniuliza, nikasema jamani tumeingia juzi tu madarakani hebu tumpe Rais na Waziri Mkuu nafasi ya kufanya kazi. Mimi nilidhani labda itakuwa bajeti ya 2017 au 2018 lakini kwa mshangao mkubwa wameleta bajeti hii 2016 big up sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nazidi kuipongeza Serikali yangu.
MHE. MUNDE A. TAMBWE: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali hii imekuwa ikituahidi toka 2011 kutuletea maji ya Ziwa Victoria na leo hii nimesoma kwenye randama kuna maji ya Ziwa Victoria yanaonekana lakini sijaona pesa za maji ya Ziwa Victoria. Ninaiomba sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, ikija hapa Wizara ya Maji ituambie imetutengea shilingi ngapi kwa ajili ya Ziwa Victoria na mkandarasi anaanza lini kazi ili tuweze kumjua ni mkandarasi yupi na yupi, tunaiomba sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kuipongeza Serikali hii, imeleta nidhani kubwa kwenye ofisi za Serikali, imeinua ari ya Watanzania na ari ya wafanyakazi. Leo hii mtu akienda Polisi anahudumiwa, mtu akienda ofisi ya Serikali anahudumiwa, mtu akienda hospitali anahudumiwa, yote hii ni juhudi ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mawaziri wako endeleeni kufanya kazi, tuko nyuma yenu tunawapongeza, tunawaunga mkono na tunawasaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi vyama vya siasa haviwezi kutumbuliwa majipu! Naomba niulize kwa sababu kuna vyama hapa ni SACCOS, kuna vyama ni NGO’s kuna vyama vinapata hati chafu. Hivi vyama mwanachama wa chama hicho akiuliza anaitwa msaliti, anafukuzwa. Lakini nimeona Chama cha Mapinduzi kwenye Ilani yake kimeweka milioni 50 kila Mtaa, lakini kuna watu wanaruzuku za Wabunge wao hawajawahi kuweka kwenye Ilani yao hata madawati kumi kila Wilaya. Leo hii wanakuja hapa wanalaumu na kusema kwamba, Serikali ya Chama cha Mapinduzi haifai. Serikali ya Chama cha Mapinduzi inafaa na inawaona wananchi wake.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa!
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika….
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Munde kuna Taarifa....
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba unitunzie dakika zangu siwezi kuipokea hiyo taarifa kwa sababu haina msingi wowote. Serikali hii ni ya Chama cha Mapinduzi na Chama cha Mapinduzi ndiyo kimeweka kwenye Ilani yake mambo yote haya yanayoendelea kufanyika, wao kwenye Ilani yao na wao wanapata pesa za walipa kodi za ruzuku wameweka nini kwa ajili ya wananchi wa Watanzania? (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Naibu Spika, wao katika pesa za ruzuku ambazo ni za walipa kodi wamefanyia nini wananchi wa Tanzania, hawajawahi hata kujenga choo cha shule kwa ajili ya hela ya ruzuku ya walipa kodi. Pesa hizo wanageuza ni NGOs zao ni SACCOS zao kwa manufaa yao wao binafsi na familia zao, tunataka sasa Serikali ya Chama cha Mapinduzi, sisi ndiyo Wabunge tunatunga sheria, tutunge sheria Waziri Mkuu akatumbue majipu kwenye vyama vya siasa, hivi Vyama siyo kwa ajili ya NGOs. Ahsante sana, nashukuru.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii niweze kuchangia. Dakika tano ni chache yaani leo nitaacha hata kukisifia chama changu na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nichangie moja kwa moja matatizo yangu ya Mkoa wa Tabora. Mkoa wa Tabora tuna Chuo cha Waaguzi pamoja na Madaktari, nimeongea hapa Bungeni mara kadhaa. Mheshimiwa Naibu Waziri amekwenda Tabora kufuatilia, akatoa maagizo kwamba Katibu Mkuu atakuja, Katibu Mkuu hakwenda Tabora, wakaenda Maafisa watatu tarehe 27 Januari, wakasema watarudi lakini mpaka leo hii hawajarudi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pesa za walipa kodi zimefanya kazi kubwa, mpaka napoongea hapa chuo kimefikia stage ya magodoro na vitanda, theatre imekamilika kwa mashine zote, kasoro mitungi ya hewa tu lakini mkandarasi amefunga, ufunguo anao yeye, hata Naibu Waziri alivyokwenda amechungulia dirishani hakuweza kuingia. Ni asilimia kumi tu zimebaki, kwenye chuo ni tape za mabomba na kwenye theatre ni mitungi ya hewa lakini hela ya walipa kodi inapotea bure, jengo lile limegeuka kuwa gofu, linaharibika, value for money imepotea.

Mheshimiwa Waziri utakapokuja hapa uje uniambie kuhusu status ya Chuo cha Manesi na Madaktari wa Tabora. Kwa kweli hizi hela za walipa kodi zinapotea hivi hivi huku mkiziangalia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka haraka naomba niongelee Hospitali ya Wilaya ya Tabora Manispaa. Tabora Manispaa tumeanzisha jengo la Hospitali ya Wilaya miaka mitatu sasa, tulitenga shilingi milioni 150, tukatenga shilingi milioni 120 lakini Serikali Kuu haijatuunga mkono. Tunamuomba sana Mheshimiwa Simbachawene, Mheshimiwa Ummy, najua hizi Wizara zinaingiliana mtusaidie kuhusu Hospitali ya Wilaya ya Tabora Manispaa. Msongamano katika Hospitali ya Mkoa ni mkubwa sana, Wilaya ya Tabora Manispaa ina population ya watu zaidi ya 400,000 bila kuwa na Hospitali ya Wilaya hatutaweza kabisa kumudu hali hii. Tutabaki tunailaumu Serikali kila siku lazima tuwe na Hospitali ya Wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya Uyui pia wameanza kujenga jengo lao la ghorofa lakini wameshindwa kumalizia tu. Tunaomba muwa-support nao wapate Hospitali ya Wilaya ili kuondoa msongamano mkubwa kwenye Hospitali ya Mkoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Ummy bajeti iliyopita alituahidi mikoa yote ya pembezoni atapeleka Madaktari Bingwa. Ninavyoongea hapa Hospitali ya Mkoa wa Tabora kuna Madaktari Bingwa wawili tu badala ya 34. Kuna daktari wa mifupa na daktari wa wanawake alioazimwa kwenye Manispaa. Tunaomba mtupelekee Madaktari Bingwa sisi tulioko pembezoni kwani nako pia kuna Watanzania wanaohitaji huduma za hospitali. Muhimbili madaktari wamejaa tele, lakini huku kwenye hospitali zetu hakuna. Mheshimiwa Waziri alituahidi naomba anapokuja kutujibu atuambie kuhusu suala hili la upatikanaji wa Madaktari Bingwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Nursing Officer tunahitaji 37 lakini tunao watatu tu, tunahitaji Assistant Nurse 131 tunao 82, wauguzi wenye certificate tunahitaji 147 tunao 44, hatimaye wodi kubwa wenye watu 80 analala nurse mmoja atahudumiaje watu, tutakuwa tunalaumu ma-nurse lakini tatizo kwa kweli lipo. Haiwezekani nurse mmoja akahudumia watu 80, mmoja drip imeisha, mwingine anataka kujisaidia, mwingine muda wa sindano umefika, matokeo yake wanaona kama ma-nurse hawawasaidii watu, lakini kwa kweli ma-nurse ni wachache wagonjwa ni wengi sana. Mheshimiwa Ummy tunakuamini naomba na sisi uendelee kutunza imani yako kwetu, hili jambo ni kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee tena suala la x- ray ya Nzega, Wabunge wote wa Nzega wameongea. Mimi niseme tu Phillips anadai hela zake Mheshimiwa Ummy tuambie unamlipa lini hela zake atengeneze x-ray ya Nzega, tusipindishe maneno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee Benki ya Wanawake. Mheshimiwa Ummy uliahidi utakuja…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja.
Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Uamuzi wake wa Kuendeleza Mji wa Dodoma na Kuupa Hadhi ya Jiji
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii nami niweze kuchangia hoja iliyopo mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi niungane na Waheshimiwa Wabunge wote waliompongeza Mheshimiwa Rais kwa wazo hili, lakini naungana na Waheshimiwa Wabunge wote waliompongeza Mheshimiwa Rais kwa maamuzi magumu aliyoyafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukumbuke Rais huyu ana muda wa miaka miwili na nusu au mitatu, hajatimiza mitatu kamili, lakini amefanya mambo makubwa sana ikiwepo kuamua maamuzi magumu ya kufanya Mji wa Dodoma uwe Makao Makuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata mimi mwanzo nilipata shock alivyoamua kipindi kile mwanzo tu anaanza. Kwa sababu wakati anaamua ndiyo alikuwa ameamua elimu bure, ndiyo alikuwa ameamua kujenga reli, kununua ndege, kujenga flyover, ndiyo alikuwa mambo chungu mzima katika nchi hii. Nikasema jamani yatawezekana?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mshangao mkubwa, leo hii Mji Mkuu wa Dodoma unaendelea kwa kasi kubwa sana, mambo yote mengine ya reli yanaendelea, ndege zimeendelea kuja na karibu zitafika saba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naunga mkono hoja hii aliyoitoa Mheshimiwa Simbachawene.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naitakia Serikali yangu kila la heri pamoja na Mheshimiwa Rais ili waweze kutimiza jambo hili na wale wote waliyokuwa wanaona kwamba haiwezekani, basi waje waone aibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti juzi tu wametekeleza kugawa tablets kwa shule zote za msingi jambo ambalo huwezi kuliamini kwa haraka haraka ukizingatia Rais huyu ana muda wa miaka miwili na nusu tu. Amegawa tablets ili walimu wetu wa shule za msingi wazidi kufundisa vizuri. Angalau Mheshimiwa kaka yangu Sugu alisema ile ni ahadi hewa, lakini nimpe taarifa tu kwamba Mheshimiwa Rais ameshaitekeleza, sasa hivi walimu wa shule za msingi wanatumia tablets. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais, naendelea kumwombea kila la heri ili aweze kufanya yale yote aliyokuwa ameyakusudia na tutaendelea kumuunga mkono na kumtia moyo pale panapostahili. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa fursa hii.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii ili na mimi niweze kuchangia mpango wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuchangia Mpango huu leo Siku ya Ijumaa nikiwa mtu wa kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kutoa pongezi zangu za dhati kwa Serikali yangu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais, Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa kutekeleza mpango kwa asilimia karibia 80. Wamefanya kazi kubwa sana ambayo Watanzania wote wanaiona. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri, kaka yangu, Mheshimiwa Dkt. Mpango, Naibu Waziri, Katibu Mkuu pamoja na management nzima ya Wizara ya Fedha kwa kuratibu mpango huu na hatimaye kutekelezeka kwa kiwango kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mafaniko haya yamedhihirika wazi kwa kazi kubwa inayofanywa na Rais wetu pamoja na viongozi wote. Kwanza kabisa kwa kuongeza ukusanyaji wa mapato kwa kiwango kikubwa lakini pili Serikali hii imedhibiti matumizi mabaya ya fedha ambapo ilikuwa inasababisha fedha za Serikali zinazopatikana kutoonekana lakini leo hii Watanzania wote wanaona fedha yao inakwenda wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuweka nidhamu ya watumishi ya Serikali hatimaye kuzilinda hizi fedha na kuzifikisha mahali husika. Miaka iliyopita fedha hizi zilikuwa zinakusanywa lakini kiwango kikubwa zilikuwa zinaliwa na watu wachache lakini katika Serikali hii ya Awamu ya Tano hilo limedhibitiwa, maendeleo tunayaona, kazi inaonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongee kuhusu miradi mikubwa iliyofanywa na Serikali kwa kutumia mpango huu wa Serikali. Serikali hii imeweza kujenga reli, wenzetu walikuwa wanabeza kwamba haiwezekani, leo Dar es Salaam – Morogoro reli imekamilika, inakuja Morogoro – Makutupora na kwenda Tabora – Kigoma – Mwanza – Uvinza – Kaliua – Kalema mpaka Rwanda. Pongezi kubwa kwa Serikali. Hiki kitu kitaacha legacy kubwa kwa Serikali ya Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, hakitasahaulika milele na milele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Dkt. Mpango katika mpango wake ni vyema akaweka bandari kavu pale Tabora kwa sababu Tabora ndiyo njiapanda ya safari zote hizi tunazozitaja hapa. Mabehewa yakitoka 20 au 30 Dar es Salaam yakafika Tabora yanakatwa
10 yanayokwenda Mwanza, yanakatwa matano yanayokwenda Kigoma, yanakatwa mangapi yanayokwenda Mpanda lakini pia tuna karakana kubwa ya ukarabati wa reli pamoja na vichwa vya treni. Kwa hiyo, nikuombe sana kaka yangu, Mheshimiwa Dkt. Mpango, pale Tabora kunafaa kabisa kwa bandari kavu kwa sababu ni njiapanda ya nchi zetu jirani za Maziwa Makuu za Kongo, Rwanda na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali yangu kwa ununuzi wa ndege, imefanya kazi kubwa sana. Nilikuwa napitia taarifa miaka 30 iliyopita kabla Rais, Dkt. John Pombe Magufuli hajaingia madarakani hatukuweza kununua hata ndege moja leo ndani ya miaka minne tumenunua ndege saba na ndege ya nane inakuja. Hii ni pongezi kubwa na histora kubwa ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeweza kuanzisha mradi mkubwa wa umeme ambao una megawati 2,100. Mradi huu ukikamilika naiona Tanzania imekuwa Malaysia, imekuwa Uturuki, naona maendeleo yatakayokuja kwa kasi kwa kupata umeme wa uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze elimu bure; watoto wetu kule vijijini sasa wanasoma, hata ukitafuta house girl kumpata ni shida. Yote haya ni matunda mazuri ya udhibiti wa pesa za Serikali, ukusanyaji wa pesa za Serikali hatimaye imeweza kuwasomesha bure watoto wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maji yametapakaa, hata kama kero bado ipo lakini kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano inaonekana. Watu wakumbuke tu historia kwamba ndani ya miaka 50 ilikuwa vipi na ndani ya miaka minne imekuwa vipi. Tumefanya kazi kubwa sana, tunastahili kumuunga mkono Rais, kumpongeza na kumtia moyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miundombinu, tumeunganisha mikoa, wilaya lakini sasa tunakwenda kwenye vijiji na mitaa. Vilevile viwanja vya ndege vimepanuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wakati tunachangia jana mpango hapa, Mheshimiwa Silinde, leo hayupo, alisema kuna mambo mengi hayajatekelezwa akasema hasa Bandari ya Bagamoyo haijajengwa na ipo kwenye Mpango. Mimi nimwambie, hatuwezi kutekeleza mradi ambao una masharti ya ajabu ajabu na ya hovyo. Masharti yanayosema tukianza kujenga Bandari ya Bagamoyo, Tanga isijengwe, Dar es Salaam isipanuliwe, Mtwara isijengwe, leo tukubali tu kwa sababu ni kwamba kipo kwenye Mpango; kwani Mpango ni Msaafu au ni Biblia, si kitu ambacho kinaweza kurekebishika? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimtoe wasiwasi, miaka mitano bado, hii ni miaka minne. Hii nchi ni ya kwetu wote, Mheshimiwa Silinde ni mzalendo, ni Mtanzania, alete mwekezaji ambaye hana masharti Bandari ya Bagamoyo itajengwa. Hatuwezi kujenga bandari kwa masharti ya aina hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii ya Awamu ya Tano imefanya kazi kubwa sana wote tumeona lakini na mimi niongelee kidogo tu suala zima la Serikali za Mitaa. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge, kazi tunayoifanya hapa ni kazi kubwa sana, tunajadili Mpango wa Serikali utakaotupeleka kwenye bajeti yetu, itakayowasaidia Watanzania kupata dawa, kusomesha watoto wetu, kujenga vituo vya afya, kujenga barabara na kadhalika. Leo anainuka Mbunge anaanza kuongelea vyeo tu, yaani hapa ni vyeo tu, watu wanawaza vyeo hawawazi Watanzania. Mimi niwaombe sana tujadili Mpango wa Serikali tuisaidie ili iweze kutuletea bajeti nzuri itakayosaidia wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua sheria na taratibu zipo, sisi hapa ni Wabunge; kama kuna mtu kaonewa, kadhulumiwa aende kwenye vyombo vya sheria akatoe malalamiko yake na sheria itafuata mkondo wake na sio kuja kwenye Mapendekezo ya Mpango kuanza kuongea habari za vyeo tu. Tukae tukifikiria Watanzania na tusifikirie hivyo vyeo kwa muda wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe mapendekezo yangu kidogo kwenye Mpango wa Maendeleo. Niiombe Serikali kama inawezekana kipindi kijacho uchaguzi wa vitongoji, vijiji, Madiwani, Wabunge na Rais hebu ufanyike siku moja. Mimi nadhani itakuwa ni vizuri zaidi kuliko kupanga baada ya miaka minne uchaguzi huu, baada ya miaka mitano uchaguzi huu. Kwanza inaigharimu Serikali kwa sababu tunapitia uchaguzi mara mbili, tunaweka mawakala mara mbili na tunatoa semina mara mbili. Kwa hiyo, mimi naona hakuna haja ya kumaliza pesa za Serikali, ni vyema uchaguzi wote ukafanyika siku moja na mambo yakaisha na tutakuwa tume-save pesa ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wenzetu wameitwa na Mheshimiwa Jafo kupewa kanuni za uchaguzi waende wakazitangaze kwa watu wao wakawaeleweshe kanuni hizi zinataka kufanya nini hawakufanya hivyo kwa sababu pesa zao zote za ruzuku zimeshapigwa, hawawezi kusaifiri Tanzania nzima kwa wanachama wao kwenda kuwaelimisha kwamba uchaguzi unataka moja, mbili, tatu. Naibu Katibu Mkuu alikuwepo pale kwa Mheshimiwa Jafo wakati anatoa hizo kanuni, hawakuzifuata kanuni hizo. Sasa kama wameonewa basi niwaombe waende mahakamani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongee suala zima la tumbaku. Tumbaku ni zao linaloingizia Serikali Pato kubwa la Taifa kwa sababu linauzwa kwa fedha za kigeni. Niiombe sana Serikali iweke mkakati maalum na wa makusudi wa kuhakikisha inalikomboa zao hili la tumbaku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imejitahidi, Waziri Mkuu binafsi ameonesha jitihada kubwa sana katika suala hili lakini Wizara ya Kilimo na yenyewe pia imefanya kazi kubwa sana. Hatimaye tumepata mnunuzi anaitwa BAT (British American Tobacco). Nimwombe sana Waziri wa Kilimo mnunuzi huyu aje kwa muda husika ili tumbaku ile isikae muda mrefu na kuanza kuharibika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna kesi nyingi za FCC. Niiombe Serikali kumaliza kesi hizi ili sekta hii ya tumbaku iweze kufikia malengo iliyojiwekea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kidogo pamba na sisi Tabora tunalima pamba. Niishukuru Serikali kwa kuweka bei elekezi. Safari hii Serikali isingeweka bei elekezi naamini kuna wakulima wangeuza pamba mpaka 400, 500 na 600 lakini Serikali ikaingilia kati ikaweka bei elekezi pamoja na kwamba bei elekezi pia ina changamoto kidogo. Kwa hiyo, niiombe Wizara husika ianze kukaa na wadau wa pamba mapema kujadili mfumo bora na safi wa kuweza kununua pamba yao. Niombe hiki kikao cha wadau kisiwe mara moja kwa mwaka kiwe mara kwa mara ili kupata mawazo na ushauri mpya ili kuweza kuboresha zao hili la pamba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mpango niiombe Serikali tuna Shirika letu la TTCL. Shirika hili kwa kweli haliendi vizuri kutokana na ukosefu wa fedha, shirika hili linadai Serikali madeni mengi, zaidi ya…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Tambwe kwa ushauri wako mzuri.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kuchangia Wizara ya Maji, nimshukuru pia Mwenyezi Mungu kwa kuniweka hapa salama na kuweza kuchangia hotuba hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Maji kwa hotuba yake nzuri iliyosheheni mambo mengi sana hasa kwenye Mkoa wangu wa Tabora, safari hii kwa kweli kama yatatimia yote haya watakuwa wametutendea haki sana. Wametutengea pesa za Halmashauri karibu shilingi bilioni tano na milioni mia nane za maji. Lakini pia kuna miradi tofauti ya skimu za umwagiliaji, hekta nyingi sana zimechukuliwa Nzega, Igunga na Urambo. Ukiangalia ukurasa 134, 65, 154, 166 na 167 nimesoma sana na nimeona kwamba kwa kweli Serikali imejitahidi sana, tunaomba tu kwa Mwenyezi Mungu mambo haya yote yatekelezwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na mradi wa Ziwa Victoria. Naipongeze Serikali kwa kutupa mradi mkubwa wa Ziwa Victoria, mradi huu utaanzia Shinyanga - Nzega, Nzega - Tabora, Nzega – Igunga - Tabora kwa baadaye utaenda Sikonge lakini mradi huu utapita kwenye vijiji 100 ambavyo vitafaidika na maji ya Ziwa Victoria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu tuliahidiwa toka mwaka 2008 mpaka leo mradi huu haujatimia, tumekuwa tukiambiwa upembuzi yakinifu, upembuzi wa kina lakini mchakato wa kuwapata wakandarasi unaendelea. Tulikuja hapa Bungeni mwaka 2011 tukaiomba sana Serikali wakatuahidi mwaka 2013 watakuwa mradi huu umekamilika wa maji wa Ziwa Victoria. Mpaka sasa mradi huu haujakamilika baadaye tukaja kuambiwa utakamilika mwaka wa fedha 2014/2015 haujakamilika tukaambiwa mwaka 2015/2016 Juni mradi huu utakamilika lakini haujakamilika (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nachangia hotuba ya Waziri Mkuu niliongelea suala hili lakini Waziri hakupata nafasi ya kunijibu, nikakutana nae mwenyewe nikamuuliza akaniambia Munde mchakato wa kuwapata wakandarasi unaenda kumalizika na mradi huu utakuwepo.
Mheshimiwa Waziri nikuombe sana tumesubiri kwa muda mrefu kuhusu mradi wa Ziwa Victoria tunaiomba sasa Serikali ya Awamu ya Tano ambayo tunaiamini sana ije na majibu. Mheshimiwa Waziri ukisimama hapa leo hii uje na majibu ya maji ya Ziwa Victoria nimeona kwenye bajeti yako umeweka, lakini naomba unipe action plan, uniambie huo mchakato wa Wakandarasi unaisha lini, Wakandarasi wanaingia lini site na kazi inaanza lini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nahemewa sana kumwambia Waziri kwamba nitatoa shilingi, kwa sababu Serikalini hii ni mpya imeanza kazi ndiyo bajeti yao ya kwanza na wameanza kazi kwa ari mpya, wamefanya kazi kwa nguvu sana na kwa kasi kubwa na hii ndiyo bajeti yao ya kwanza, mimi nasema nawapa muda nikiamini ahadi atakayoitoa hapa Waziri na action plan atakayoitoa hapa Waziri itakuwa ni ya ukweli kwa asilimia mia moja. Tunaiamini sana Serikali ya Awamu ya Tano na tunaamini kwa sababu ni bajeti yao ya kwanza tuwape muda watuambie hizo ahadi zao na tunaamini watazitekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongee kuhusu bwawa la Igombe, pale Tabora Manispaa tuna Bwawa la Igombe tuna ipongeza sana Serikali, mwaka 2011 wakati nimeingia humu Bungeni tulikuwa tunapata maji lita milioni 15 na sisi tulikuwa tunahitaji maji lita milioni 25. Serikali ya Chama cha Mapinduzi imefanya kazi na sasa hivi tunapata maji lita milioni 30. Napata taabu sana mtu anaposema Serikali hii haifanyi kazi yoyote, sasa tunapata maji lita milioni 30 pale Tabora Manispaa, lakini changamoto tuliyonayo hatuna mtandao wa mabomba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli ni jambo la aibu ule ni Mkoa wa siku nyingi sana ni mji wa zamani toka tunapata uhuru kukosa mtandao wa mabomba pale katikati ya Mji Manispaa kwa kweli ni jambo ambalo linasikitisha. Niiombe Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi Mheshimiwa Waziri utupe sasa hivi pesa za mtandao wa mabomba, tuliomba mkatuahidi mwaka 2013 mtatupa pesa za mtandao wa mabomba tupate mabomba pale mjini. Pale mjini kuna kata hazina mabomba Kata ya Mtendeni, Kata ya Kibutu, Kata ya Simbachawene, Kata ya Uledi na Kata ya Mawiti. Kata hizi hazina mtandao wa mabomba, tunakuomba sana.
Mheshimiwa Waziri, mliwaahidi TUWASA mwaka 2013 mtawapa hizi pesa kwenye mradi wa pili wa WSDP mpaka sasa pesa hizo TUWASA hawajazipata. Ninaiomba Serikali ijue kwamba TUWASA inajitegemea, inalipa mishahara, inalipa posho lakini kubwa zaidi inanunua madawa kwa ajili ya kutibu maji wanayokunywa wananchi wa Mkoa wa Tabora. Serikali tunaidai pesa nyingi sana, niombe kupitia Bunge lako Tukufu tunadai shilingi bilioni 2.3 TUWASA ili kuhudumia maji ya wananchi wa Tabora hasa kuya-treat ili tuweze kunywa maji safi. Watu hawa wanapokopwa, hawapewi hizi pesa haya maji wataya-treat vipi? Ndiyo maana siku nyingine ukiamka asubuhi ukifungua maji kwenye bomba maji ni meusi hayakuwekwa dawa Serikali inadaiwa pesa nyingi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalidai Jeshi la Wananchi shilingi bilioni 1.9, naomba Jeshi la Wananchi wahusika mpo humu Waziri Mkuu upo unasikia, watulipe kama kupitia Hazina kama ni kupitia kwao shilingi bilioni 1.9 ili TUWASA iweze kujiendesha yenyewe. Tusiwafanye hawa watu wakashindwa kujiendesha, watu watakufa, milipuko ya magonjwa inapotokea kipindupindu Serikali ina gharamia pesa nyingi sana. Sasa wapeni pesa zao ili waweze kufanya kazi, Polisi tuna wadai shilingi milioni 230 na Hospitali ya Mkoa shilingi milioni 136 na Magereza shilingi milioni 76. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe tu uongozi wa TUWASA ujaribu kuongea na wafanyakazi wake wa chini, wafanyakazi hawa wamekuwa wakibugudhi sana wapiga kura wetu wa Chama cha Mapinduzi. Wamekuwa wakienda kudai pesa kwa kutaka rushwa, wamekuwa wakidai pesa kwa manyanyaso makubwa, niombe sana baadhi ya wafanyakazi wachache wanaichafua TUWASA Tabora. Wanakwenda kumwambia mtu unadaiwa maji ya shilingi ngapi, shilingi 18,000 nakukatika unipe shilingi 10,000, sasa jamani hiyo shilingi 10,000 unayochukua ya huyo bibi kizee ambayo angeongeza 8,000 akalipa maji unataka rushwa wewe nikuombe sana Mkurugenzi wa TUWASA naamini umo humu ndani unanisikia, tunaomba sana ulifanyie kazi hili suala. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mradi wa Inala, Inala tuna bwawa kubwa la shilingi bilioni 1.9 tumepata msada wa JICA lakini bwawa lile limepasuka mbele linamwaga maji, Serikali imetoa pesa nyingi sana zaidi ya shilingi bilioni (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mambo mengi ya kuongea lakini nitaandika mengine kwa maandishi, naomba nipate muda wa kumjibu Waziri Kivuli wa Upinzani, amesema Serikali ya Chama cha Mapinduzi itaingia kwenye kitabu cha maajabu na mimi nakubaliana na yeye tutaingia kwenye kitabu cha maajabu, tumepata Rais jembe anasifika dunia nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukifungua BBC utamsikia Magufuli tutaingia kwenye kitabu cha maajabu, lakini tukishaingia kwenye kitabu cha ajabu mwaka 2020 tutapofuta Upinzani wote, kwa sababu Serikali inafayakazi, Serikali imedhibiti rushwa, inasimamia wafanyakazi wake na miradi hii itaendelea kwa sababu imedhibiti wizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaingia kwenye kitabu cha maajabu CCM sasa hivi haina makapi ya kupeleka mgombea Urais, kwa hiyo, sasa hivi tumejipanga kwa hiyo tutaingia kwenye kitabu cha maajabu kwa sababu tunafanya kazi. Museveni ameomba kura Uganda kwa kutumia Jina la Magufuli anasema nipeni kura ili nifanye kazi kama Magufuli. Kwa hiyo, anavyosema Serikali hii itaingia kwenye kitabu cha maajabu mimi namuunga mkono tutaingia kwenye kitabu cha maajabu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu muda wangu unaendelea naomba nichangie kuhusu bwawa la Manonga, Kule Manonga kuna bwawa kubwa Mheshimiwa Naibu Waziri amekuja, tunaomba sana Serikali itupe pesa kwa ajili ya kujenga tuta, bwawa lile litatusaidia kilimo cha mboga mboga, lakini litasaidia wakulima wetu kutokuhama hama kwa ajili ya kunywesha mifugo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu.
Kwanza kabisa niapongeza Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, nampongeza Waziri Mkuu pamoja na Mawaziri wake, Mheshimiwa Jenista, Mheshimiwa Mavunde pamoja na Baraza zima la Mawaziri kwa kazi nzuri wanayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na Wabunge wenzangu wa Tabora kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anayoifanya ya kutatua kero ya tumbaku Mkoani Tabora. Mheshimiwa Waziri Mkuu tunakuombea kila la heri, Mwenyezi Mungu akuwezeshe ili umalize kero hii ya tumbaku ambayo imetukabili kwa miaka mingi sana. Tunakuamini, tunajua utaimaliza na umedhamiria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kazi kubwa wanayoifanya, wameanzisha programu maalum ya kuhakikisha wanafuatilia Ilani ya Chama cha Mapinduzi itekelezeke, lakini kufuatilia ahadi zote za viongozi wakuu. Nawapongeza pia kwa kuhamia Dodoma, wamefanya kazi kubwa. Tulikuwa tunasikia toka tukiwa wadogo kwamba Serikali inaenda Dodoma, lakini imeenda Dodoma leo hii. Tunaipongeza sana Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza Kitengo cha Baraza la Uwezeshaji ambacho kipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Baraza la Uwezeshaji limefanya kazi kubwa ya kuwatambua, kuwabaini wajasiriamali wadogo ambao kwa Mkoa wa Tabora wameianza kazi hiyo na kuwawezesha
kuwapa mitaji ili waweze kusonga mbele na huu ndiyo uchumi wa kati ambao tunautaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri tu Serikali yangu, naishauri Ofisi ya Waziri Mkuu kwamba hili Baraza la Uwezeshaji lingeungana na watu wa SIDO likaungana na Wizara ya Viwanda ili kuwawezesha hawa wajasiriamali wadogo sasa waweze kuingia kwenye viwanda vidogo
vidogo, mkiungana nadhani itakuwa vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongee kuhusu bajeti. Nimesikia wenzangu wanasema kwamba kulikuwa na bajeti hewa, nimesikia jana kuna neno linaitwa bajeti hewa ambapo mimi kama Mbunge wa Tabora sikubaliani na hiki kitu cha bajeti hewa na sababu ninazo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ukiniambia bajeti hewa, mimi nimeingia hapa Bungeni mwaka 2011, nilikuwa nahangaika kila siku kugombana kuhusu maji ya mradi wa Ziwa Victoria, leo hii mkandarasi yuko site toka mwaka 2016. Kwa hiyo, ukiniambia bajeti hewa, siwezi
kukuelewa. Tulikuwa tunahangaika na barabara ya lami ya Chaya – Tula ambayo inaunganisha kutoka Dar es Salaam - Tabora mpaka Urambo kwa lami, leo hii mkandarasi yuko site. Pia tulikuwa tunahangaika kwamba uwanja wetu wa ndege unatua ndege ndogo tu, leo hii mkandarasi yuko site anafanya matengeneza ya kupanua uwanja wa Tabora.
Kwa hiyo, sikubaliani kabisa na kuniambia kwamba kuna bajeti hewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, punda hasifiwi kwa rangi zake, anasifiwa kwa kazi anazozifanya na mzigo anaobeba. Hii Serikali ya Hapa Kazi Tu inafanya kazi sana, Rais wangu Mheshimwia Dkt. Magufuli anafanya kazi sana. Wamwache Mheshimiwa Rais afanye kazi! Toka nikiwa mdogo nikiwa Tabora nasikia Waheshimiwa Wabunge wa Tabora wanalalamika kuhusu reli ya kisasa, lakini leo hii minara ya reli ya umeme imeanza kutengenezwa. Reli ya standard gauge inajengwa. Leo mtu ananiambia kuna bajeti hewa, sitakaa nikubali. Huu ni uongo na niwaombe Wabunge wenzangu, tuseme Serikali inapofanya mambo mazuri, tusinyamaze, tusiogope, tuseme. Nimetoka kifua mbele, nasema Serikali yangu imefanya mambo makubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa humu Bungeni kipindi kilichopita, kaka yangu Mheshimiwa Zitto kama yupo atasema. Tulikuwa tukisimama tukiungana kulilia ndege, wanasema nchi gani hii, inashindwa hata na Rwanda, haina hata ndege moja. Leo tuna ndege, watu wanasema kwa
nini tumenunua ndege? Wamwache Mheshimiwa Rais afanye kazi, waiache Serikali ifanye kazi. Tukifanya kazi, mnasema, tusipofanya kazi, mnasema. Tunajua binadamu hata ufanye nini, hawezi kukusifia kwa asilimia 100, tufanye kazi kama tulivyojipangia. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaongelea elimu bure.
Kuna mtu labda ana hela watoto wake hawasomi shule hizi anaona utani. Leo hii shule zimejaa, madarasa yamejaa, watoto wanasoma, hakuna ma-house girl vijijini. Yote hii ni juhudi ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi na Mheshimiwa Rais, Waziri Mkuu na Serikali yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tumeona juzi, mwaka 2016 hii bajeti hewa UDSM, leo hii watoto 4,000 watakaa kwenye mabweni UDSM, yamejengwa kwa muda wa haraka sana. Leo unaniambia Serikali haijafanya chochote, sitakubali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, REA, tumemwona Mheshimiwa Muhongo huko, umeme unawaka vijijini. Leo hii tunashindwa kusifia Serikali yetu. Nawaomba Wabunge wenzangu, tusiingie baridi, tutoke tuseme mema yaliyofanywa na Serikali yetu. Watu wanasema viwanda, viwanda gani? Vitajengwa lini? Viwanda hewa. Mpaka hapa ninapoongea, tunajenga viwanda 2,160 na hii issue ya viwanda tumeanza juzi mwaka 2016, Magufuli kaingia mwaka mmoja. Mimi niwaulize Wabunge wenzangu, ninyi kwenye Majimbo yenu mwaka mmoja mmefanya mangapi?
Mbona mnaisema Serikali tu! Kuna watu hapa hawajawahi kufanya chochote.
Akimwona DC ameenda kwenye mkutano wa DC, naye anakwenda kama Mbunge. Lako wewe kama Mbunge liko wapi? Tuoneshe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru sana Serikali yangu, nampongeze Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mawaziri wake, wanafanya kazi. Hii nchi ni kubwa jamani, kazi ni ngumu. Ni rahisi sana kukosoa, lakini ukiambiwa kafanye wewe, hiki kitu ni kigumu
jamani, tuwatie moyo, tuwaombee kwa Mwenyezi Mungu waweze kutekeleza walioyaahidi. Ni faida yetu sisi wote.
(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunajisifu Tanzania ni kisiwa cha amani, Tanzania ina amani, Tanzania ina utulivu, nani aliyetuletea utulivu? Ni Usalama wa Taifa. Leo tumo humu, tuna amani tu. Leo tukitoka tutaenda Club, tunaenda tunarudi hata saa 9.00 usiku, tuna amani. Kama kuna madoa madogo madogo, basi yatashughulikiwa, lakini tusiseme Usalama wote hawafanyi kazi. Hiki kitu nakataa na nitaendelea kukataa. Tuko hapa kwa sababu ya amani.
Tunajisifu, tuna sifa dunia nzima, kisiwa cha amani. Amani inatengenezwa, kuna watu hawalali kwa ajili ya amani hii tuliyonayo, ni lazima tuwatie moyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukifuga mbwa ukiona habweki, bweka mwenyewe. Leo nimeamua kusema mwenyewe. Wenzetu hawa kama hawayaoni haya, leo nimeamua kuyasema mimi niliyeyaona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongezee kidogo kuhusu Msajili wa Vyama vya Siasa (Registrar), amekuwa akishambuliwa sana. Nasema vyama vingi ni tatizo, ni kazi kubwa. Sheria zake anazozisimamia, ndiyo maana leo tumekaa Wabunge wa CUF, wa CCM, wa CHADEMA
tunaongea kwa sababu wa usimamizi mzuri wa Registrar.
Tulishuhudia watu walitaka kupigana viti kule Ubungo kwenye mikutano yao, lakini Registrar kwa kazi yake kubwa aliyoifanya, ndiyo leo CUF kuna amani na utulivu. Ndiyo leo wameweza kukaa pale wote wakiwa pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napata shida sana tunapokuwa tunawashambulia wataalam, tuwatie moyo kwa kazi wanazozifanya. Pale kwenye upungufu tusiache kusema; tuseme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirudie kusema, naipongeza sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, nampongeza sana Rais, Mheshimiwa Dkt. Magufuli na sisi tumwambie tupo, tutasema. Sisi ni wanasiasa, kazi yetu ni kusema. Tutasema na tunamuunga mkono kwa asilimia mia moja kwa kazi anazozifanya. CCM oyee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunisikiliza.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji
MHE. MUNDE A. TAMBWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia Wizara hii nyeti, Wizara ya Maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa mimi binafsi nianze kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, niwashukuru Mawaziri wote, lakini hususan Waziri wa Maji. Sisi kwa Mkoa wa Tabora kwa kweli tunawashukuru sana. Mheshimiwa Rais alivyokuja Tabora kwenye kampeni alituahidi atatuwekea maji ya Ziwa Victoria. Lakini mpaka ninavyosema hivi tumeshazindua na mkataba umeshafanyika wa maji Ziwa Victoria na maji haya yataenda karibia eneo kubwa sana la Mkoa wa Tabora. Kwa hiyo, tunaishukuru sana Serikali, tunaishukuru Wizara na nimeongea na Mheshimiwa Waziri amesema muda mfupi watakuja kufanya uzinduzi Tabora tayari kwa kuanza kujengwa kwa mradi huu mkubwa ambao utamtua mwanamke ndoo ya maji kwa asilimia 90. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile niishukuru Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa kutuletea mradi mkubwa wa JICA wa bilioni 29. Mradi huu umetusaidia Mkoa mzima, niweke tu sawa tu Hansard siwezi ku-attack Mbunge mwenzangu. Jana Mheshimiwa Sakaya alisema mradi huu umegusa Wilaya moja ya Uyui, si kweli; mradi huu umegusa Mkoa mzima wa Tabora. Mradi huu Wilaya ya Tabora Manispaa umeenda Kakolo kwa maana ya bomba, umeenda Mabama - Uyui, Kizengi - Uyui, Nzega kwa maana ya mabomba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile mradi huu umechimba visima 101 Kaliua kwake Mheshimiwa Magdalena Sakaya visima vipo, Urambo, Sikonge na Mkoa mzima wa Tabora. Kwa hiyo, niweke Hansard sawa Mradi wa JICA umepita Mkoa mzima wa Tabora na si tu Wilaya moja kama ilivyosemwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kusema hayo machache naendelea kuipongeza Serikali, lakini changamoto hazikosi. Tunaiomba Serikali sasa wakati ikituletea maji ndani ya Tabora Manispaa maji haya sasa yatoke Tabora Manispaa kwenda Sikonge awamu ya pili. Vilevile hatukuwa na mpango wa kuyatoa maji haya ya Ziwa Victoria Tabora kuyapeleka Urambo, mimi nadhani tuweke mpango huu wa kupeleka Urambo. Najua Urambo kuna mkakati mkubwa wa Malagarasi kwa kupitia Kaliua na kwenda Urambo. Hata hivyo Mheshimiwa Waziri hili jambo ni kubwa, Malagarasi ipo mbali sana na Urambo na Kaliua, litachukua muda mrefu. Nikuombe Mheshimiwa Waziri kwenye mipango yako uweke maji ya Ziwa Victoria yaende Urambo, ni kilometa 90 tu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama mtayapeleka Igalula baadaye mkija kuyapeleka Urambo nadhani ni rahisi zaidi kuliko kupigana na Malagarasi kwa sasa. Ila mradi wa Malagarasi uendelee kama mlivyokuwa mmeupanga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto nyingine kubwa ambayo tunayo watu wa Tabora Manispaa ni water table ambayo iko juu. Serikali imetuletea maji mengi sasa, kwa hiyo niwaombe Serikali itupatie pesa tulizoomba shilingi bilioni 14 kwa ajili ya mabomba ya maji taka. Tumeomba shilingi bilioni 14 tupate mabomba ya maji taka ili tuweze kupitisha maji taka, maji yasiwe mengi ili kuepuka magonjwa ya milipuko yatakayokuja baada ya kupata hayo maji mengi ya Ziwa Victoria.

Sasa hivi tuna mtandao wa mabomba ya maji taka kwenye kata mbili tu Ngongoni na Bachu Kidogo, huko kote hakuna mtandao wa maji taka. Kwa hiyo, tunaomba Serikali itupatie mtandao wa maji taka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto nyingine ni madeni, Idara ya Maji inadai madeni makubwa sana. juzi nikiwa Tabora tarehe 28 mpaka tarehe 3 tulikatiwa maji, nikaenda Mamlaka ya Maji kuuliza tatizo ni nini? Wakaniambia tumekatiwa umeme tunadaiwa shilingi milioni 500 za umeme na TANESCO. Lakini TUWASA Tabora inadai shilingi bilioni tatu; ambapo Jeshi linadaiwa shilingi bilioni mbili, Kitete Hospitali ya Mkoa na inadai Polisi na Magereza hawawalipi pesa zao. Sasa hii taasisi itaendeshwaje kama taasisi hii ya TUWASA tu Tabora inadai shilingi bilioni tatu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Serikali ije na mpango mkakati mwingine. Mimi nimefanya kazi Halmashauri, tulikuwa tunakatwa LAPF na nini, lakini hela haziendi sehemu husika. Serikali ikaamua madeni yote yale yatoke Hazina moja kwa moja yapelekwe sehemu husika. Kwa hiyo, mimi naomba Serikali yangu iamue sasa madeni yote ya hizi Mamlaka za Maji, ya Jeshi na nini bajeti zao za maji zikatwe moja kwa moja na Hazina zipelekwe zikalipe maji ili na wananchi wengine waweze kufaidika na haya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tumekatiwa maji Tabora nzima kwa sababu tu kuna taasisi za Serikali zinagaiwa. TANESCO wakakata umeme wao, kwa hiyo, sisi watu wa Tabora wote tukakosa maji kwa sababu watu wanadaiwa madeni makubwa ambao ni Taasisi za Serikali. Naomba Serikali ije na mpango mkakati otherwise watu watakosa maji wakati Serikali imeshayaleta maji mpaka sehemu husika. Nawaombeni sana Serikali mliangalie hili suala. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naenda moja kwa moja kwenye bajeti. Naungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kuhusu suala suala la tozo na mimi naiomba Serikali yangu iongeze shilingi 50 kwenye Mfuko wa Maji ili kupata shilingi 100. Lakini napingana na watu wanaosema kwamba tuikatae bajeti au tuibadilishe bajeti kwa sababu ukiangalia Kanuni ya 105 kwa kuokoa muda sitaisoma inasema kwamba sisi Wabunge kwa ushauri wetu Kamati hii inaweza ikarudi kwenye Budget Committee, ikakaa upya na ikaangalia taratibu je, hizi tozo tukiongeza kuna tatizo gani? Kama kuna tatizo basi labda tupunguze REA au tupunguze kwenye Mfuko wa Barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tuwape muda Serikali wakakae kwenye Budget Committee wafanye hii kazi, lakini tukisema humu ndani tunaikataa bajeti hakuna tutakachokuwa tumekifanya ndugu zangu. Tusikubali kabisa kukataa bajeti, kanuni inatuelekeza kwamba tuna uwezo wa kuirudisha Serikali ikakaa tena upya na wakaja kwenye Kamati ya Bajeti wakati wa hotuba ya bajeti wakatuletea wameonaje na wamefikiriaje. Nawaomba sana ndugu zangu bajeti hii isirudishwe, isipokuwa warudi kwenye Budget Committee wakakae upya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu naomba niongelee kidogo, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya PAC, nilipata bahati ya kwenda kukagua DAWASCO Dar es salaam. Nilikuta vitu vya ajabu kweli na vikashangaza na nikaona kweli Serikali yangu sasa iko kazini na inafanya kazi na inadhibiti hizi taasisi za Serikali. Wakati tumekwenda tumesomewa ile taarifa wakati huyu CEO aliyepo sasa hivi anaingia alikuta DAWASCO haina chochote hata senti tano, lakini alikuta deni la shilingi bilioni 28 la PPF, shilingi bilioni 16 la TRA, watumishi shilingi bilioni tano na alikuta upotevu wa maji asilimia 56 lakini alijitahidi kufanya kazi mpaka sasa hawadaiwi hata senti tano.

Mheshimiwa Naibu Spika, fikiria hii ni mwaka 2017 ameingia mwaka 2015 mwishoni, hakuna deni hata moja; tunajiuliza kipindi kile hizi hela zilikuwa zinakwenda wapi mpaka madeni yakawa makubwa kiasi hiki? Kwa hiyo, naamini kabisa Mheshimiwa Waziri wa Maji hii kazi unaifanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Mheshimiwa Waziri nilikuwa na ushauri mmoja; DAWASCO inakusanya shilingi bilioni tisa kwa mwezi lakini inatoa asilimia 23 sawa na bilioni mbili inapeleka DUWASA.

Sasa mimi najiuliza hizi bilioni mbili DUWASA za nini? Wakasema sijui kwa sababu maji yanalipiwa umeme na umeme unalipwa na DAWASCO, service ya mitambo inafanywa na DAWASCO, lakini DUWASA ina watumishi 68 na hawa watumishi 68 wanapelekewa shilingi bilioni mbili kila mwezi, kwanini DUWASA na DAWASCO visiunganishwe kama tulivyofanya TRL na RAHCO? (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. MUNDE A. TAMBWE: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. MUNDE A. TAMBWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa hii niweze kuchangia hotuba ya CAG na PAC na hotuba ya LAAC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kuipongeza ofisi ya CAG kazi nzuri walioifanya, lakini niipongeze Kamati yangu ya PAC kwa kazi kubwa walioifanya katika kupitia vitu hivi. Nianze moja kwa moja na mambo ya TANESCO, kwa sababu nchi yetu iko kwenye Sera ya Viwanda, hatuwezi kuwa na viwanda bila kuwa na umeme wa uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, taasisi za Serikali zinadaiwa pesa nyingi, ukiangalia ukurasa wa 21 mwaka 2016 tulikuwa tunadaiwa shilingi bilioni mia moja ishirini na tisa. Kufikia sasa ukiangalia ukurasa wa 22 tunadaiwa shilingi bilioni mia moja themanini na tisa. Niiombe sasa Ofisi ya ya Waziri wa Fedha, Hazina, ifanye mkakati wa makusudi mazima, kuzikata fedha taasisi hizi zinazodaiwa, kutokana na bajeti zao za umeme kila wanapoleta bajeti zao, huwa kuna bajeti za umeme, tunaomba bajeti hizi za umeme zikatwe moja kwa moja na zipelekwe TANESCO ili tuweze kuwa na umeme wa uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili linawezekana, Local Government walikuwa wanakatwa hela za LAPF, hazipelekwi kwenye mifuko yao, lakini Serikali ikaamua kukata moja kwa moja kupitia Hazina na kupeleka kwenye mifuko yao na sasa hivi pesa zinakwenda. Tunaomba sasa kwa umuhimu wa TANESCO, ili tuweze kuenda na sera ya viwanda, Serikali ikate pesa hizo za Taasisi moja kwa moja na kuzipeleka kwenye sehemu husika ambayo ni TANESCO. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumuunge mkono mkono Rais katika suala hili la umeme, Rais amehangaika sana, kwanza kabisa, ameanza kuvunja mikataba mibovu ya umeme, amevunja mikataba ya Symbion, lakini, amevunja mkataba mkubwa wa kifisadi wa IPTL ambao ulikuwa unachukua karibu milioni thelathini, kila mwezi, kuwapa kununua mafuta mazito ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais anafanya kazi sana, anastahili pongezi na anastahili kuungwa mkono kwa vitendo. Niwaombe sana Hazina wahakikishe fedha hizi zinarudi TANESCO kupitia Taasisi zinazohusika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais, ameweka nguvu kubwa Kinyerezi one (I), lakini ameweka nguvu kubwa Kinyerezi II. Yote hiyo ni kuhakikisha umeme unapatikana. Kuna watu waliokuwa na wasiwasi sana na Stieglers Gorge, kwamba haiwezi kufanikiwa, lakini kwa jambo la kushangaza Mheshimiwa Rais na Serikali yake wameshatangaza tenda, kwa ajili ya kujenga huo mgodi wa umeme na umeme huo nadhani muda sio mrefu mwaka 2021 tutaanza kupata megawatts 2000 kutoka huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli Mheshimiwa Rais anapojituma niwaombe Mawaziri wanaohusika nao wajitume, tuone tunamuunga mkono kiasi gani, ili kupata umeme wa kutosha na viwanda vyetu tunavyovijenga kwa kasi viweze kufanya kazi kutokana na umeme huo tutakaoupata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli nampongeza sana Mheshimiwa Rais na nimwambie tu kwamba hizi ni legacy anazoziacha, hatutakaa tumsahau kwa kazi kubwa anazozifanya na ataweza tu, ameweza standard gauge, barabara, Flyovers, ameweza elimu bure, naamini ataweza na Stieglers Gorge itajengwa na itatoa umeme na watu tutafaidika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende sasa nikachangie kuhusu NSSF, kwanza nianze kupongeza, miradi mizuri ya majengo ya NSSF, mradi mzuri wa Twangoma tumeenda kukagua zile nyumba ni nzuri, tumekagua nyumba za Kijichi ni nzuri, lakini naamini na nyumba za Dege zitakapokwisha zitakuwa nzuri. (Makofi)

TAARIFA. . .

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti kwanza naomba unitunzie muda, lakini nisimlaumu sana Mheshimiwa Sophia ni njuka, haelewi chochote, sijawahi kuwa Mjumbe wa Bodi ya TANESCO. Kama ana uhakika alete uthibitisho Bungeni kwamba niliwahi kuwa Mjumbe wa Bodi ya TANESCO, mwambie atulie, huo unjuka usimsumbue sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti naomba kuendelea. NSSF, ina mradi wa Dege ambao tumeenda kuutembelea mradi ule umechukua pesa nyingi za umma karibu bilioni mia mbili na point. Tunaiomba sana Serikali aidha iongeze mbia mwingine mradi ule uishe au itumie mbinu mbadala yoyote kuhakikisha mradi ule unakwisha ili mradi ule ufanye kazi pesa za umma zirejee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuiombe pia Serikali, miundombinu ya barabara ya kwenda Kijichi na Tuangoma, kwa kweli hairidhishi hata mtu anakwenda kupanga akianza kupelekwa anaweza kuona huko anapokwenda hapafai. Kwa hiyo, tunaomba sana mradi wa miundo ya barabara itengenezwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii Watanzania hizi nyumba za NSSF, zinakopesheka, kwa sababu ukienda leo kununua nyumba ya milioni themanini, unaambiwa ulipe asilimia 10. Ukilipa asilimia 10 zinazobaki zinagawiwa kwa miaka 15. Unaingia ndani na unalipa polepole, tofauti na mashirika mengine unatakiwa ulipe hela cash ndiyo uingie ndani. Aidha, ukakope Benki na Benki tunajua kwamba watu wengi hawakopesheki hasa sisi wanawake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawapongeza sana NSSF kwa kazi nzuri wanaifanya. Napongeza pia uongozi mpya kwa Mkurugenzi wa NSSF, naye ni Mkurugenzi mzuri sana anajitahidi tunamwombea kila la kheri aweze kupata mwekezaji mwingine amalizane na huu mradi uliopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongee sasa kuhusu Mlimani City, ulipata bahati ya kwenda kutembelea mradi wa Mlimani City, kwa kweli tunaomba Serikali ifuatilie mradi huu kwa makini zaidi. Inasikitisha sana mkataba huu ni mbovu kupita kiasi, watu hawa kwenye mkataba walikubaliana walipe 10 percent ya gross ya mapato ya Milimani City, lakini mpaka leo hii, watu wao wanalipa net ya ten percent sio gross.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipouliza Mlimani City Uongozi wa Chuo cha UDSM kwa nini watu wao hawalipwi gross wanalipwa net, wanasema mgogoro unaendelea. Sasa hivi wana miaka 13, ni jambo la kushangaza kusikia bado mgogoro unaendelea, haujatatuka kwa maiaka 13, tunamnufaisha mwekezaji ambaye alikuja bila mtaji na dola 75 kama shilingi laki moja na nusu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kuamini, sasa hivi pale Dar es Salaam wameanzisha Milimani City mradi wa parking za magari, hakuna mfumo wowote, unawaonyesha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwamba parking zile zinaingiza shilingi ngapi kwa siku, kwa wiki, wala kwa mwezi. Ni mwekezaji anakuja ku-declare kwamba kwa mwezi huu, nimeingiza milioni tatu wanakubali bila kujua chochote, ni vitu vinasikitisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti kuna ukumbi pale Mlimani City, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, hawajui ukiwauliza ukumbi ule unaingiza shilingi ngapi kwa mwezi au kwa wiki, ni mwekezaji anakuja ku-declare. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkaguzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, haruhusiwi kwenda kukagua Mlimani City, anakatiliwa na mwekezaji, hivi ni vitu ambayo nimwombe sana Waziri wa Fedha, aunde Tume ya haraka iwezekanavyo na Waziri Mkuu, wakakague upya ule mradi ufanyiwe uchunguzi wa kina. Mtu huyu amepewa mkataba wa miaka 85, inatia shaka. Niiombe sana Serikali yangu ifanye pale kazi mpya iende ikaague, tukae tena mezani Mkataba ufumuliwe na uwekwe mkataba vizuri. Kuna vitu vinasikitisha sana huwezi kuona majengo yote haya yale hatuingizi pesa yoyote kwenye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kidogo kuhusu Pride, kwa sababu ni mama, sisi akinamama ndiyo tunaokopa Pride ni jambo linalosikitisha sana kuona kwamba kuna watu wamezihodhi pesa za Pride, niiombe Serikali sasa ichukue hatua za makusudi mazima kuhakikisha wale wote waliohusika kwenye masuala mazima ya Pride, wanachukuliwa hatua za kisheria. Tunaamini Serikali ya Awamu ya Tano ina uwezo huo mkubwa na tunaamini watajulikana na pesa zetu zitapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MUNDE A. TAMBWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii nami niweze kuchangia katika Wizara ya Afya. Kwanza nianze kuipongeza Serikali yote kwa ujumla wake, nimpongeze Rais kwa kuweka nguvu za makusudi kabisa kuboresha Wizara ya Afya. Nampongeza Mheshimiwa Waziri Ummy kwa kazi nzuri anayoifanya pamoja na Naibu wake, tunaona matunda yao wanayoyafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na mambo yangu ya Mkoa wa Tabora kwanza. Kule Tabora tulikuwa tumejengewa Chuo cha Madaktari. Chuo kile kilikuwa kimekamilika kwa asilimia 90 kuanzia mwaka 2014 mpaka magodoro yamo ndani ya chuo hicho, lakini mpaka sasa chuo hicho kimebakiza asilimia 10 tu kumaliziwa toka mwaka 2014 mpaka sasa hakijamaliziwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri kwa sababu kitu hiki sasa kinaenda chini ya Wizara yake, jengo lile linaharibika, pesa haionekani thamani yake kwa sababu jengo limeanza kupasuka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tumejengewa jengo la kisasa la upasuaji, jengo lile limekamilika kila kitu ndani toka mwaka 2014, mkandarasi hajalipwa pesa yake, amelifunga na kufuli jengo lile halitumiki, ukizingatia Hospitali ya Kitete ni Hospitali ya Rufaa, jengo letu la upasuaji ni la kizamani, halina vifaa vya kisasa. Jengo la kisasa tunalo, mkandarasi amelifunga.

Nawaomba Wizara wakae na mkandarasi waongee naye wampe ahadi, lifunguliwe jengo lile lianze kutumika, lina kila kitu ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa kuhusu madaktari; Tabora hatuna Madaktari Bingwa. Ikama yetu ya Mkoa wa Tabora, tunatakiwa tuwe na Madaktari Bingwa 21, lakini sasa tuna Madaktari Bingwa watano tu. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri atusaidie. Pia tuna madaktari watatu wa kujitolea, wanafanya kazi nzuri sana. Namwomba Mheshimiwa Waziri wakati wa kuajiri asisahau kutupa nafasi hawa madaktari wanaojitolea mpaka leo hii, wanatufanyia kazi kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wauguzi tunatakiwa tuwe nao 185, tunao 120. Tunaomba sana wakati wa kuajiri wauguzi watukumbuke. Tunasomesha Madaktari Bingwa watano, tunaiomba Wizara, madaktari hawa wakitoka kusoma, msije tena mkawahamisha mkawapeleka sehemu nyingine. Tunaomba mtuachie na sisi waweze kutusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba pia kuongeza majengo kwenye Hospitali yetu ya Rufaa ya Mkoa, majengo yake ni machache, population ya mkoa imeshakuwa kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi tena kuipongeza Wizara ya Afya kwa kazi kubwa wanayofanya. Nashangaa tu mtu anaposema kwamba sisi tunajifanya kusaidia wanyonge, Serikali inajifanya ya wanyonge, lakini siyo kweli ya wanyonge. Hii Serikali ni ya wanyonge. Niwakumbushe kidogo tu, tulikuwa tuna bajeti ya shilingi bilioni 30 mwaka 2015; leo tuna bajeti ya shilingi bilioni 270 kwa ajili ya madawa. Yote hii ni juhudi za Mheshimiwa Rais kuhakikisha watu wake wanapata tiba za uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunatibu watu bure. Wagonjwa wa UKIMWI wanatibiwa bure, wagonjwa wa TB wanatibiwa bure, wazee wanatibiwa bure, akina mama wajawazito wanatibiwa bure, watoto chini ya miaka mitano wanatibiwa bure. Zote hizi ni gharama kubwa zinazobebwa na Serikali ya Awamu ya Tano, watu wanasahau hivi vitu. Kila siku wanakuwa wanapenda kulaumu tu, hawapendi kuona mambo mazuri yanayofanywa na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii siyo kazi ndogo, tuna wagonjwa wa UKIMWI wangapi? Leo Serikali ikisema wagonjwa wote wa UKIMWI wanunue dawa, ndugu zetu wangapi wataangamia? Naomba sana kuipongeza Serikali na kuitia moyo iendelee kufanya kazi kama inavyoendelea kutufanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimjibu Mheshimiwa Ruge alivyokuwa anasema kwamba vifo vya wajawazito takwimu zake ni za mwaka 2015/2016.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii imewekeza sana kwenye zahanati na vituo vya afya. Ninaamini taarifa itakayokuja haitakuja na vifo hivyo vya akina mama wajawazito na watoto, naamini taarifa itakuwa imeboreshwa. Tumesikia taarifa ya Mheshimiwa Waziri, tumesikia taarifa ya Mwenyekiti wa Kamati jinsi Serikali ilivyowekeza kwenye Wizara ya Afya.

Kwa hiyo, nataka niwaambie kwamba hiki kitu hakitaendelea kuwa hivi, kazi iliyofanyika ni kubwa.

T A A R I F A . . .

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo taarifa siikubali kwa sababu mimi kwenye Mkoa wangu wa Tabora akina mama wanatibiwa bure. Mheshimiwa Waziri alisema yeyote anayetaka kujiboresha zaidi ile kit ilikuwa ni kubwa, ina vitu vingi, anaweza akachukua kwa shilingi 21,000 lakini siyo kusema kwamba watu hawatibiwi bure. Wajawazito wakienda Kitete Hospitali wanazaa bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sikubaliani na alilolisema Mheshimiwa Owenya. Kama yeye Kilimanjaro wanazaa kwa pesa na watoto wanatibiwa kwa pesa, basi ni kwake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Ruge aliongelea kuhusu Azimio la Abuja akisema kwamba pesa tulizozitenga ni chache. Nasema hivi ameangalia kwenye Fungu 52, lakini pesa za matibabu ziko pia kwenye fungu la TAMISEMI.

Ukichukua TAMISEMI, ukichukua na Wizara ya Afya ukajumlisha utapata pesa nyingi zilizotengwa kwa ajili ya Wizara ya Afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiona makelele, ujue jua limewapiga kichwani. Kwa hiyo, hata huwa hainisumbui kwanza.

T A A R I F A . . .

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Esther nakusheshimu na unajua nakuheshimu, tafadhali. Nimesema kwamba takwimu alizozitoa Mheshimiwa Ruge asilimia tatu siyo sawa. Ukichukua TAMISEMI, Afya, ukichukua na Fungu 52 huwezi kupata asilimia tatu, utapata zaidi ya asilimia tatu, ndicho nilichokisema, siyo kwamba nilichokisema sikijui. Nakijua na ninakifahamu. Narudia kusema, nakusheshimu sana Mheshimiwa Esther. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee tena jambo moja ambalo limekuwa sana kwenye mjadala. Binafsi kama Munde na ni Mbunge wa wanawake siliungi mkono, naomba niseme wazi. Kumekuwa na mjadala wa kuiomba Serikali igawe taulo za kike bure, mimi siungi mkono na sababu ninazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais anafanya kazi kubwa, Mheshimiwa Rais anajenga barabara, anasomesha watoto bure, madawati bure, kila kitu bure, tunataka tupelekewe na pads bure! Kwa sasa bado nchi yetu haijafikia, tuache Serikali ijikite kwenye kazi inazozifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi nitaunga mkono kama mkisema tupunguze kodi kwenye hizi taulo ili watu wazinunue kwa bei rahisi. Bado hatujafikia kugawa taulo hizi bure, uwezo huo hatuna. Tusitake kuijazia Serikali mambo mengi, kesho na kesho kutwa tukaanza kuja kuwahoji mbona hili hamjalitimiza?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana wale wote wenye kuwa na hiyo azma ya kupewa taulo bure, mimi nasema sitaunga mkono, naendelea kupinga na nitaendelea kupinga siku hadi siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ameshatusomeshea watoto wetu bure, nasi kama wazazi tuwajibike; tuna sababu ya kuwajibika. Hatuwezi kutegemea kila kitu kiwe bure kwa Serikali. Hata Uingereza hawatoi hizo taulo bure. Kwa nini sisi kila kitu tunataka bure? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naendelea kusema, naendelea kuipongeza Serikali.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekitti, ahsante kwa kunipa fursa hii niweze kuchangia Bajeti ya Serikali. Nimeisoma vizuri bajeti hii, jambo moja ambalo naweza kuwaambia Watanzania pamoja na Waheshimiwa Wabunge kwamba Tanzania tuna bahati kubwa sana. Tumepata Rais msikivu amesikia vilio vya Wabunge, amekaa na Mawaziri wake, vitu vyao vingi wametuwekea kwenye bajeti yetu, tunawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze pia Mawaziri, nimpongeze Mheshimiwa Mwigulu Nchemba kaka yangu Waziri wa Fedha pamoja na Naibu wake kaka yangu Masauni, kwa kweli wamekuwa ni wasikivu na wanyenyekevu. Wamechukua mambo yetu humu Bungeni wameenda kukaa na Amiri Jeshi Mkuu, Rais mwanamke mwenye kuandika historia ya kwanza Tanzania kwamba ni Rais mwanamke na kuleta bajeti nzuri ambayo mimi mwenyewe ikiwa ni bajeti yangu ya 11 toka nikiwa Mbunge nimeiona ni bajeti ya kipekee, nawapongeza sana sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii imepanua wigo wa kodi, lakini imetuletea kodi za kisayansi, kodi ambazo hazimuumizi moja kwa moja mwananchi, kodi ambazo mwananchi anazilipa bila kuzisikia. Yote hii ni dhamira ya Rais wetu mwanamke ya kuleta mageuzi ya maendeleo ndani ya nchi yetu ya Tanzania. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna nchi isiyolipa kodi, dunia nzima tunalipa kodi ila inategemea ni kodi za aina gani ambazo wananchi wako watazimudu. Nitoe mfano kama kodi iliyoandikwa kwenye bajeti yetu ya property tax, nimesikia kuna watu wanaiongelea kodi hii, wakisema kwamba kodi hii italeta mkanganyiko baina ya mwenye nyumba na mpangaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii ina watalaam, nyumba zetu zina hati za nyumba, kwa mfano nyumba imeandikwa Munde ndiyo mwenye nyumba, kwa hiyo watalaam hawa wataenda kufanya katika zile LUKU kama kuna LUKU tatu au nne, wataangalia nyumba hii hati ya nyumba ni ya nani, kama ni ya Munde house rent ya huyo property tax rent itafidiwa kwenye LUKU ya mwenye nyumba. Kwa hiyo niwatoe wasiwasi Watanzania pamoja na Waheshimiwa Wabunge waliokuwa wanadhania kwamba huu ni mkanganyiko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kama ikitokea kwa bahati mbaya mpangaji amekatwa property tax rent risiti itaandikwa kuna property tax rent ya Sh.3000 au Sh.2000, siku wana-renew mkataba wao wataiweka mezani kwamba nilichangia LUKU Sh.20,000, kwa hiyo wakati una-renew mkataba nitakatwa hiyo 20,000 kwenye mkataba wangu. Kwa hiyo niwaombe Watanzania na Waheshimiwa Wabunge tuzipokee kodi za kisayansi za Amiri Jeshi Mkuu mama yetu Samia Suluhu, hazitamuumiza mwananchi, unakatwa elfu moja moja, hutaisikia kama kuna kodi, lakini Serikali itakusanya mapato mengi na hatimaye kutekeleza yale mambo yote tuliyokuwa tunayataka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji trilioni 36 ili kutekeleza mambo yetu. Ni lazima tulipe kodi Watanzania, hatuwezi kuwa na nchi ambayo hailipi kodi, lakini kodi hizi ni nzuri na za kisayansi. Tuache propaganda ya kuzalisha maneno kwamba ukiamka asubuhi simu yako inakatwa Sh.200, simu yako inakatwa shilingi 50 siyo kweli, ukiweka voucher, ukiweka muda wa maongezo wapo watakaokatwa shilingi 10 ambayo kwa mwezi ni shilingi 300 kwa kuweka muda wa wapo watakaokatwa shilingi 20 ambayo kwa mwezi ni Sh.600 kwa kuweka muda wa maongezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wale watumiaji wakubwa wa juu wanaotumia shilingi 100,000 mpaka shilingi 200,000 labda Wakuu wa Taasisi ndiyo watakatwa shilingi 200 kwa siku watakayoweka muda wa maongezi. Akiweka muda shilingi 800 tu. Kwa hiyo jamani kodi hii haina tatizo twendeni tukalipe kodi, tukahamasishe Watanzania, Mheshimiwa Rais apate pesa aweze kuleta maendeleo kwenye nchi yetu, twendeni tukamuunge mkono Amiri Jeshi Mkuu wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais amejipambanua kwamba yeye ni Rais mpenda haki na mimi nawathibitishia Watanzania na Wabunge, Mheshimiwa Rais ni mpenda haki, mimi najua Mheshimiwa Rais ni mpenda haki. Pia amekuwa na slogan zake, anapenda kusema kwamba kazi iendelee na zege hailali, twendeni tukakusanye kodi, Mheshimiwa Rais afanye kazi iendelee na zege hailali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata Amiri Jeshi msikivu, mchapakazi, mwanamama wa kwanza Tanzania, naamini ndani ya miaka yake kumi ya uongozi wake wa urais mpaka 2030 atakuwa kafanya kazi kubwa na ataacha legacy kubwa ya maendeleo kwa jinsi hapa alivyotuonyesha ukusanyaji wake wa kodi, najua pesa zitapatikana na malengo yake yatakwenda kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema bajeti hii ni ya wananchi na bajeti hii imegusa watu, Mheshimiwa Rais ameenda kugusa watu wa chini kabisa kama bodaboda, walikuwa wanalalamika muda wote bodaboda, wanalalamika wapunguziwe faini muda wote, lakini Mheshimiwa Rais Samia ameenda kuwapunguzia kodi bodaboda wetu, faini kutoka shilingi 30,000 mpaka shilingi 10,000 kwa kweli vijana hawa walikuwa wanaumia sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais amesikia kilio cha muda mrefu cha Madiwani wetu kulipwa na central government posho zao. Leo tunaenda kuwalipa Madiwani wetu kutokea central government. Malipo kwa Serikali za Mitaa, mimi Madiwani wangu wamekaa miezi sita hawajalipwa posho zao, naamini sasa watakuwa wanapata kwa wakati muafaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, toka tupate uhuru, hakuna awamu iliyowahi kulipa posho ya madaraka ya Mtendaji wa Kata na Katibu Tarafa, ni awamu hii ya Rais mwanamke Mheshimiwa Mama Samia Suluhu. Nani kama mama?

MBUGE FULANI: Hakuna!

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa watu ndio wanaosimamia maendeleo yetu, wanasimamia utekelezaji wa ilani kule chini, Mheshimiwa Rais amewaona na ninaamini kazi itakuwa nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Rais ameenda kumaliza kero ya ukamilishaji wa maboma ambayo ilikuwa inakera kwenye majimbo yetu. Tuliwahamasisha wananchi wakajenga maboma, lakini yalikuwa yamebakia wazi na wakaona kama nguvu zao zimekwenda bure. Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu amekwenda kumaliza kero ya maboma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais amekwenda kuandika historia kwa kujenga shule za watoto wa kike za mabweni kila mkoa, tena za sayansi ili kupata wanasayansi wazuri wanawake. Vile vile Mheshimiwa Rais ametuwekea pesa za TARURA. Ameongeza Mfuko wa TARURA kwa shilingi mia mia kwenye lita ya mafuta ili tutokane na kero kubwa ya barabara kwenye vijiji vyetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisikia kuna Mbunge mmoja analalamika kwamba tukipandishwa shilingi 100 vitu vitapanda bei. Hivi kero ya barabara inayoua magari yetu, inayoshindwa kusafirisha na shilingi 100, kipi bora? Tuache kuwa walalamishi. Naipongeza sana Wizara ya Fedha, nampongeza sana Waziri aliyepo madarakani na Naibu Waziri wake kwa kazi nzuri, lakini Mheshimiwa Mama Samia Suluhu amefanya mambo mengi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nirudi kwa Mheshimiwa Waziri wa Fedha, namwomba sana, watakapokuwa wanakusanya hizi fedha, hizi fedha ni kwa ajili ya maendeleo. Tunaomba azi-ringfence ziwe kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania, zisiwe kwa ajili ya kulipana posho. Kazi maalum shilingi milioni 400 kwenye pesa hizi za kodi ya Watanzania.

Namuomba sana Mheshimiwa Waziri na Wizara yake ya Fedha, pesa hizi wazipeleke zikafanye kazi ya kuwakomboa Watanzania kama Mheshimiwa Rais Samia alivyodhamiria na siyo kwa ajili ya kulipana posho kwa kazi maalum. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli tunamwomba sana Mheshimiwa Waziri sana na Naibu Waziri wasimamie hilo kwa watendaji wao. Pamoja na Katibu Mkuu kama yupo humu, hizi sio pesa za posho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza tena na tena Mheshimiwa Rais wetu Mheshimiwa Mama Samia Suluhu, kwa kweli...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naunga mkono hoja. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Munde bado dakika zako.

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa suala zima la TARURA. TARURA kulikuwa na kero kubwa. Waheshimiwa Wabunge humu walikuwa wanalalamika wakiisema TARURA, lakini ilikuwa haina fedha za kuweza kufanya kazi kukidhi mahitaji yaliyopo kwenye majimbo yetu.

Hata hivyo, kwa maono makubwa ya Mheshimiwa Rais pamoja na Wizara yake ya fedha nikimaanisha Waziri, Naibu Waziri na Katibu Mkuu wa Wizara hii, wameliona hili, wameamua kuongeza pesa kwa ajili ya kuongezea mfuko huu. Wameanza kwa kupeleka shilingi milioni 500 kila jimbo hili kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami niwahakikishie Watanzania, tumepata Rais mzoefu, mchapakazi, tunakwenda kufanya kazi kwa bidii, tunakwenda kuandika historia, mpaka ikifika mwaka 2030 ambapo Mheshimiwa Mama Samia anakabidhi kijiti, ninaamini atakuwa ameacha legacy kubwa sana ndani ya nchi ya Tanzania. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili mimi niweze kuchangia Wizara ya Ujenzi. Kwanza kabisa nimpongeze Waziri, Naibu Mawaziri wote wawili, Katibu Mkuu wa Wizara na wataalam wote wa Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja kwenye Mkoa wangu wa Tabora, nianze kuongelea suala zima la fidia. Kule Tabora tumepata pesa ya kujenga barabara ya Chaya - Nyahua ambayo ni barabara yetu kubwa tunayoitegemea kututoa Tabora mpaka Dar es Salaam na sehemu zingine lakini tunasumbuliwa sana na suala zima la fidia. Mkandarasi anapata shida sasa, anafanya kazi kipande hiki anaruka anaenda kufanya kazi kipande kingine anaruka. Uthamini ulishafanyika lakini bado fidia haijalipwa. Tunamwomba Mheshimiwa Waziri sana anapokuja hapa kujibu atupe commitment ya fidia hii italipwa lini. Vilevile kuna fidia ya Urambo - Kaliua bado haijalipwa, matokeo yake mkandarasi pia anasuasua lakini fedha zimeshapatikana bado fidia tu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna barabara ya Kaliua – Kazilambwa - Chagu ambayo ina kilometa 41 tu ili tutoke na lami kutoka Tabora mpaka Kigoma. Mheshimiwa Waziri, tunaomba mtupe pesa ya kilometa 41 ili tuweze kutoa hiki kipande kidogo sana kinachotuwekea doa. Kwa mfano, sasa hivi hii kilometa 41 haipitiki, kwa hiyo, lami yote mliyotuwekea inakosa maana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Tabora kuna barabara zimejengwa na TANROADS vizuri, lakini kuna tatizo la taa eneo la Isevya Tabora, usalama ni mdogo sana. Namuomba Mheshimiwa Waziri amuagize Meneja wa TANROADS wa Tabora atuwekee taa eneo lile kwa ajili ya usalama.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee barabara ya Ndala – Ziba, hii ni ahadi ya Mheshimiwa Rais, tunaomba Mheshimiwa Waziri aiwekee lami.

Naomba niongelee reli ya kati ambayo sasa hivi inajengwa standard gauge, kule ambako standard gauge bado haijafika hali ni mbaya. Tunaomba itengenezwe wananchi wanakaa mpaka saa tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kuongea sasa maajabu ya miaka miwili na nusu ya Rais John Pombe Magufuli. Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli amejenga reli ya standard gauge kwa muda wa miaka miwili na nusu kitu ambacho huwezi ukakiamini. Ameanza Dar es Salaam- Morogoro na sasa hivi ameanza Morogoro-Makutopora, haijawahi kutokea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais amenunua ndege ambazo zinawatoa sana mapovu upande wa pili. Haya ni maajabu ya Rais John Pombe Magufuli ndani ya miaka miwili na nusu ameweza kutuletea ndege tatu na kwa taarifa yao kuna Boeing zingine ziko njiani zinakuja. Naonge haraka haraka siingii ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maajabu ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, flyover tumefika asilimia 72. Waambie waangalie ukurasa wa 22 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maajabu ya Mheshimiwa John Pombe Magufuli, barabara line sita Morogoro Road, haijawahi kutokea Tanzania tukawa na highway …

T A A R I FA . . .

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, siwezi kujibishana na bwege, mimi siyo bwege. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee kutaja maajabu ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli katika Wizara ya Ujenzi. Amenunua vivuko vinne: MV Kazi, MV Magogoni na MV Kivukoni kwa muda wa miaka miwili na nusu. Mimi najiuliza amewezaje ndani ya miaka miwili na nusu? Mbona sisi Wabunge kwenye majimbo yetu hatujaweza kufanya haya mengi kwa miaka miwili na nusu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea na maajabu ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli; nawapongeza TCAA na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa ajili ya ununuzi wa rada. Nawapongeza TPA, Mkurugenzi Kakoko anafanya kazi kubwa sana waongezewe tu kina cha bahari pamoja na pesa za ujenzi wa Gati Namba 7 mpaka 13 ili waweze kufanya mambo yao vizuri. (Makofi)

KUHUSU UTARATIBU . . .

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nilikuwa pia napenda kuiambia Serikali iwasaidie TTCL ili waweze kuendana na ushindani kwa kuhakikisha wanalipwa madeni wanayodai kwenye taasisi za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maajabu mengine ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, ndani ya miaka miwili amepanua viwanja kadhaa vya ndege kikiwemo Kiwanja cha Tabora. Sisi tulikuwa tumekata tamaa, tulikuwa hatuna barabara ya lami tunayo, tulikuwa hatuna uwanja wa ndege upo, tulikuwa hatuna standard gauge inakuja, Mungu atupe nini, mambo ni fire. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niwaambie tu ndugu zangu hawa wanaopenda kulalamika kila siku tusilalamike, tufanye kazi. Kila siku Serikali inaiba, inaiba haya mambo mazuri yamefanyikaje? Kama huu wizi unaotendeka kila siku na mambo haya mazuri yanafanyikaje? Wao ruzuku wanaiba hatusemi mpaka michango ya wagonjwa wameiba hatusemi. Wameenda kuomba msaada Ubalozi wa Ujerumani mgonjwa atibiwe wakati wametuchangisha humu mapesa, wamechangisha kwa mitandao, wamechangisha watu chungu mzima hela zote wameiba, sisi mbona hatusemi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naomba tu kuwaambia waache kusemasema sana, wafanye kazi ili Taifa liwe na maendeleo. Mbona Rais kila siku anaongea yeye ni Rais wa CHADEMA, wa CCM na wa Watanzania wote na analeta maendeleo ya Watanzania wote. Sijawahi kuona tukaambiwa madarasa yanajengwa kwenye majimbo ya CCM, majimbo ya upinzani hayajengewi madarasa, mimi sijawahi kuona lakini nashangaa ni kila siku shutumu Serikali inaiba, kushutumu Chato imejengewa kiwanja cha ndege. Jamani yule ni Rais wa nchi hii muwe mnaelewa, yule ni mamlaka hata vitabu vya dini vinatamka kutakuwa na mamlaka na ile ni mamlaka. Mkitaka msitake Mwenyezi Mungu ameiweka pale na itaendelea kuwepo pale mpaka muda wake utakapokwisha. Rudisheni hela za mgonjwa.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii nami niweze kuchangia Mpango wa Serikali.

Kwanza kabisa ni pongeze Serikali ni mpongeze Rais wangu John Pombe Magufuli, kwa kazi kubwa anayoifanya, lakini kwa kweli kwa dhamira ya dhati kabisa nimpongeze Waziri Dkt. Mpango hakika Dkt. Mpango amekuwa mvumilivu, amekuwa kiongozi wa mfano, amevumialia mno matusi maneno lakini amefanya kazi kubwa ndani ya miaka mitatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano Waziri Mpango amefanya kazi kubwa ya kuleta nidhamu ya kuleta pesa za umma, wote tunajua, mmejenga mfumo sahihi ya ukusanyaji wa kodi hakuna asiyejua, kila mwaka mapato yetu ya ndani ya kodi na yasiyo ya kodi yanakuwa yakiongezeka hii yote ni kazi ya Dkt. Mpango, Naibu wake, na Wizara nzima ya Fedha mimi binafsi kwa dhati yangu nawapongezeni sana. Maana kila siku tunawasema kwa mabaya yale mema wanayoyafanya tunashindwa hata kuwatia moyo. Kwa kweli Uwaziri wa Fedha ni kazi kubwa sana lazima tuwapokengeze. (Makofi)

Nimesikia wapinzani wanasema utekelezaji wa bajeti hauridhishi, lakini hawasemi bajeti hii imekuwa ikiongezeka kila mwaka, hawasemi wanasema tu kwamba hairidhishi, kwa sababu tulianza na asilimia arobaini na kidogo tukafata na asilimia hamsini na kidogo sasa hivi tupo na asilimia 57 lakini hivi asilimia 57 zinaonekana kazi inayofanyika inaonekana unaweza ukasema tumetekeleza kwa asilimia 80 lakini ukiangalia kazi haionekani hakika Serikali inafanya kazi kubwa na inastahili kupongezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Nimesikia kuna Mheshimiwa Mbunge amesema Mheshimiwa Rais atamaiza kumi hakuna kilichofanyika amenishangaza sana, mimi niwaambieni niwaombe mchukue kalamu na karatasi, niwaambie Rais Magufuli ikifika mwaka 2020/2025 ataacha legacy kubwa hata sahaulika katika nchi hii ya Tanzania, naomba niwaambie Rais Magufuli ataacha amejenga reli andikeni? Msinitizame Rais Magufuli atajenga Stiegler’s Gorge na umeme huo mtautumia kwa bei rahisi. Rais Magufuli ataacha amejenga zahanati za kutosha, amejenga vituo vya afya vya kutosha mpaka sasa hivi vituo vya afya ni zaidi 300 ndani ya mikaka mitatu, lakini toka tumepata Uhuru tumejenga vituo vya afya 500 Rais Magufuli miaka mitatu amejenga 300 leo unaniambia Rais Magufuli ataacha amefanya chochote ndani ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mimi nasema viongozi wetu labda akili zao zimezidi maana wanafanya mambo makubwa ambayo hatukuyategemea, hatukutegemea kabisa kwamba Rais anaweza kutujengea reli ya kisasa, hatukutegemea kama watoto wetu watasoma elimu bure, lakini leo watoto wetu pamoja na wakwenu wanasoma elimu bure.

Hatukutegemea kama mikopo ya vyuo vikuu kuongezeka kwa kiwango hiki, lakini leo watoto wetu wanapata mikopo na wanasoma. Hatukutegema upanuzi mkubwa unaoendelea wa viwanja ndege, upanuzi wa bandari, ujenzi wa flyover, ununuzi wa ndege ambao na wao wanapanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu anayesema mpango huu haufai mimi nasema mpango huu unafaa na unaendelea vizuri. Nimesikia Mheshimiwa Mbunge anaongelea kwamba hakuna ajira tangu Rais Magufuli ameingia, jamani tuone aibu, tumuongope Mwenyezi Mungu sisi wote tuna dini humu ndani, tumeapa kwa bible na wengine tumeapa kwa misahafu tumuongope Mwenyezi Mungu, tumeajiri walimu 13,000, tumeajiri watu wa afya 8,447 na tumeajiri watendaji wa kata, lakini kila siku ukifungua website ya Wizara ya Utumishi wanatangaza nafasi za kazi juzi tu nilifungua namtafutia mwanangu nimeona UTT wametangaza, nimeona SUMATRA wametangaza, nimeona TANESCO wametangaza, nimeona Bandari wametangaza, leo hii mnakuja mnasema hakuna ajira muogopeni Mwenyezi Mungu, pale tunapofanya kazi nzuri semeni mmefanya kazi nzuri, pale tunapokosea sio mseme jumla kwa chuki zenu binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikia wenzetu hawa sana wanaongea kuhusu swala zima la Katiba, kwamba Katiba imeachwa, Katiba imefanya nini mimi niwaambie ndugu zangu hawa waache kutafuta kiki za kisiasa, tulivyokuwa kwenye Bunge la Katiba walitoka nje, Katiba ilipitishwa na watu wachache kwa busara ya viongozi cha Chama cha Mapinduzi wakasema mapendekezo ya wachache yatachukuliwa na yatakwenda kuwaambia wananchi kupendekeza Katiba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mara ya kwanza walijiunga kama UKAWA wakatembea nchi nzimaya Tanzania kwamba Katiba isiungwe mkono iliyopendekezwa leo nawashangaa watu hawa yametoka wapi leo nawashangaa watu hawa wanaililia Katiba ninyi si mlikwenda nchi nzima kusema Katiba inayopendekezwa isichukuliwe?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu hawa walienda nchi nzima wakajiunga UKAWA wakaanza kusema Katiba iliyopendekezwa isiungwe mkono leo nashangaa wanasema Rais anakataa Katiba Mpya, mimi naomba nimuombe Rais wangu asitoke kwenye reli, Rais Magufuli wakati anaomba kura aliwaahidi Watanzania maendeleo, hakuwaahidi Watanzania Katiba, wananchi wanataka maendeleo, wananchi wana taka reli, wanataka zahanati, wanataka maji wanataka dawa, wananchi awataki Katiba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kuna mkakati, wa kumtoa Rais Magufuli achukuwe mamilioni aweke kwenye Katiba tushindwe kutimiza malengo waje watuhoji, mimi niwaambie hatutakubali. Mhe.Rais usikubali ujinga huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Katiba limeeleweka naomba sasa kuhusu suala zima la usalama. Kumekuwa na masuala ya usalama yanaongelewa kwamba nchi hii haina usalama, nchi hii watu wanatekwa, nchi hii watu wanauwawa, suala la usalama ni suala la janga la dunia, Marekani wanalindwa kwa mitandao kwa mitambo kwa satellite lakini nikwambie kwa siku wanatekwa zaidi 240 kwa siku. Mimi nadhani imefika wakati sisi Wabunge tupige kelele tuiambie Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi iongeze pesa kwenye vyombo vyetu vya usalama, iongeze training za vijana wetu wa usalama, training za polisi, training za jeshi letu ili kukabiliana na janga kubwa lililopo la uwalifu katika nchi yetu linalotaka kuingia hili ni janga la dunia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesikia juzi mwandishi wa habari kule ametekwa, ameuwawa mpaka leo wenzetu wale wamesonga mbele kiteknolojia bado hawajapata uhakika nani kafanya. Lakini leo likitokea Tanzania imefanya Serikali, mimi napata taabu Mwenyekiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natoka Tabora kutoka nikiwa mdogo kule kwetu mauwaji ya vikongwe yanaendelea, mauaji ya kimapenzi yanaendelea, wanauwaga polisi kila siku? Mbona yapo na Serikali zote zipo zimepita na Serikali zinapambana na hayo mambo.

Kwa hiyo, mimi nitoe rai yangu Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu unanisikia upo humu ndani, niombe sana Serikali iongeze pesa kwenye vyombo vya usalama, wakawasomeshi watu waweze kukabiliana na teknolojia za hawa watu wahalifu wao na teknolojia za kisasa na sisi tupate teknolojia za kisasa ili tuweze kukabiliana nao ili ndiyo naweza kulisema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kidogo Tume Huru ya Uchaguzi watu hawa wamekuwa wakiongea kwamba tunataka tume huru Katiba mpya ibadilike mimi naomba niwaulize humu ndani wapo zaidi ya asilimia 30 waliingiaje kama hakuna Tume Huru waliingiaje ndani watu hawa, wamezidi zaidi ya 100 tupo Wabunge 300 na kidogo wenzetu hawa wako zaidi ya 100 walifikaje humu ndani kama wako zaidi 100 kama hakuna Tume Huru ya Uchaguzi wasitake kututoa barabarani, wasitake kututoa kwenye reli tunataka maendeleo kama anavyosema Rais wetu John Pombe Magufuli. Tunamuombea kila heri Rais wetu amkinge na mapala na manuksi ya maneno yenu ya ajabu ajabu inshallah. Ahsante kwa kunipa nafasi hii.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii ya kuchangia. Kwanza kabisa nianze kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa ambayo anaifanya, wote tunaiona lakini nimpongeze kaka yangu Waziri Mpango, Naibu Waziri na menejimenti nzima ya Wizara ya Fedha kwa kazi kubwa wanayoifanya ya usimamizi mzuri wa bajeti ambayo waliileta hapa Bungeni. Tunaamini bajeti hiyo inasimamiwa vizuri na ndio maana mambo yote yanakwenda kwa sababu ya usimamizi na udhibiti wao mzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja kwenye mjadala, nimesikia wanasema kwamba tusipokuwa makini Waziri na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha baada ya utawala huu wanaweza kufungwa. Niwaambie hafungwi mtu hapa, kwa sababu kazi zote zinaonekana zinavyofanyika. Serikali iliyopita tulikuwa hapa Bungeni walikuwa wanasema Serikali hii haidhibiti rasilimali za nchi, Serikali hii ni dhaifu, leo tumepata Serikali inayodhibiti maliasili ya nchi yao, utafikiri maliasili zile ni za kwao wao binafsi, lakini leo hii wanakuja tena kuwaambia watu hawa watafungwa kwa kushindwa kudhibiti rasilimali za nchi yetu. Niseme hiki kitu siyo kweli, tumeona Mheshimiwa Rais amepambana kwenye madini, ameleta sheria tumebadilisha, yote hiyo ni kudhibiti rasilimali za nchi yetu ili Watanzania waweze kunufaika na rasilimali hizo. Tumeona Rais amepambana kwenye rushwa kwenye uwajibikaji, kwenye nidhamu ya watumishi na mambo yanaenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii wanamwambia mtu atafungwa, unabaki unashangaa, atafungwa kwa kutoa bajeti ya afya bilioni 30 mpaka bilioni 260, atafungwa kwa kusimamia ujenzi wa reli ya kisasa kwa kutumia pesa zetu za ndani, atafungwa kwa ujenzi wa barabara, atafungwa kwa kusomesha watoto wetu elimu bure, atafungwa kwa ndege sita zilizonunuliwa kwa mpigo. Nimuombe Waziri wa Fedha na Katibu Mkuu wasikate tamaa, waendelee kuwafanyia kazi Watanzania kama wnavyowafanyia. Tumeona kabisa ndani ya miaka mitatu kazi kubwa iliyofanywa na Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeonekana. Leo kule kwetu sisi Tabora, Mkuu wetu yule wa Mkoa, watu wanaona kama vichekesho lakini anaongea ukweli, anasema Tabora imekuwa kama Toronto, sio utani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukifika saa 12 mitaa yote inawaka taa, mitaa yote ina lami, kule tulipozaliwa sisi Uswahilini kulikuwa hakuna lami toka tumezaliwa mpaka sasa ndio tumekuja kuiona lami. Nasema Serikali inafanya kazi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu hawa hawaeleweki, wasipofanya kazi wanawaita dhaifu, wakifanya kazi wanawaita madikteta, tabia zao sio za kiume wala sio za kike, hawa watu sijui ni wa aina gani, nashindwa kabisa kuwaelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Rais kwenye suala zima la korosho, tulikuja hapa Bungeni tukajadili sana kuhusu korosho, tukapata wanunuzi wanataka kununua kwa shilingi elfu mbili na kidogo. Rais wa wanyonge akakataa, akasema korosho hizo atazinunua yeye mwenyewe, lakini tunashuhudia amepatikana mnunuzi, amezinunua kwa shilingi 4,480, tunampongeza sana Rais amepambania wanyonge wake kwa vitendo. Ajabu leo unakuta mtu analaumu tu, anaona haya mambo ni mepesi, anaona haya mambo ni rahisi, huu ni uthubutu wa hali ya juu aliouonesha Rais. Rais wetu ni jasiri Rais ana maamuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napata tabu sana, hawa watu kila siku wanatuambia hawauoni utawala bora, wanaona udiktekta tu. Mimi nashindwa kuelewa hawa watu wako huru, wanaita vyombo vya habari, wanaongea na vyombo vya habari, wanafanya wanavyovitaka, wanaisema Serikali, wanamsema Rais lakini bado wanasema hakuna utawala bora. Utawala bora kwao ni maandamano tu ndiyo wataona kwamba kuna utawala bora. Yapo wanayoyasema, wanaenda Mahakamani, wanashtaki, hatua zinachukuliwa, maamuzi yanatoka, lakini bado hawaioni Serikali kama ina utawala bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile wamekuwa wakitushawishi tukubali masharti ambayo kama nchi yetu na tamaduni zetu hatuwezi kuyakubali. Mimi niendelee kuipongeza Serikali iendelee kuwa na misimamo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku zote nimekuwa nikimwambia Rais wangu kupitia Bunge hili pamoja na viongozi waendelee kufanya kazi zao kama walivyojipangia, wasiyumbishwe na mtu yeyote, wasimfuate mtu yeyote maana hawa watu wanawayumbisha kwa makusudi ili siku ya mwisho waje wawaambie kwamba wameshindwa kufanya kazi na waweze kusema. Tumeona miaka mitatu mapinduzi yaliyotekea ni makubwa, maendeleo yaliyotokea ndani ya miaka mitatu ni makubwa, mtu yeyote unayemwambia aangalie anaona, nashangaa wanapokuwa kila saa wanalaumu, kila ni watu wa kubeza…

T A A R I F A

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, namheshimu sana aliyetoa hii taarifa lakini hawezi kunilazimisha hicho kipengele chake kwa sababu yeye ni mfanyabiashara, wote tuongelee biashara hapa ndani. Mimi naongelea kupongeza Serikali yangu kwa kazi kubwa inayoifanya, ndicho nachoongelea mimi na hawezi kuni-drive anapotaka yeye. Tena namheshimu ni rafiki yangu, kutwa ananiambia anataka kurudi CCM huyu wewe muache tu. (Makofi)

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kukutana na wadau wa madini, yote hii ni juhudi kubwa za kutaka kuongeza pato la nchi yake, za kutaka kuongeza uchumi wetu ili Watanzania waendelee kunufanika na matunda yao. Mheshimiwa Rais ambaye anahitaji amani kila siku amekutana pia na Viongozi wa Dini ili kuweka amani katika nchi yetu, kusikiliza kero zao na mambo kadha wa kadha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Rais akutane na wadau wa pamba, tumbaku na kahawa. Mazao haya tunayategemea sana kwa ajili ya kuingiza fedha za kigeni kwenye nchi yetu lakini yanategemewa pia kwenye viwanda vyetu vya ndani na yanatoa ajira kwa vijana wetu na sisi wenyewe. Kwa hiyo, niombe pale Mheshimiwa atakapopata nafasi akutane na wadau wa mazao haya makuu ya nchi yetu ili kuleta tija kama alivyoleta tija kwenye madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia Wizara ya Miundombinu. Umesema leo tujifunze kwa Mheshimiwa Abbasi kutokupiga kelele, tunasikika tu, ngoja nianze kujaribu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe pongezi zangu za dhati kwa Serikali na Wizara nzima ya Ujenzi pamoja na miundombinu, Mheshimiwa Waziri, Manaibu Waziri, Mheshimiwa Nditiye na kaka yangu Mheshimiwa Kwandikwa, tunawapongeza sana kwa kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizipongeze pia taasisi zote zilizo chini ya Wizara hii TPA, SUMATRA, TCRA, RAILWAY, TANROADS, TCAA, TASAC, CATCO, ATCL, UCSAF na zingine zote, kwa kweli wanafanya kazi vizuri sana. Nimeingia kwenye Kamati hii ya Miundombinu muda mfupi tu, nimeona kwa kweli kazi inayofanyika ni nzuri na ni kubwa, tunawapongeza sana na tunataka waendelee kumuuunga mkono Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaanza kuchangia naomba niongee kidogo kuhusu mdogo wangu Mheshimiwa Makamba, jana alichangia akasema kwa nini Serikali imehamisha kitengo cha Wizara kinachohusika na ununuzi wa ndege na kukipeleka Ikulu, wanaficha nini. Naomba tu nimwambie hayupo lakini najua taarifa atazipata kwamba Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kikatiba anayo mamlaka ya kuhamisha Wizara yoyote, kuhamisha Taasisi yoyote ya Serikali, kuipeleka popote anapotaka yeye. Anayo mamlaka ya kuanzisha leo mkoa mpya na kesho kuuvunja, anayo Mamlaka ya kumteua Waziri na kesho kumtumbua na anayo Mamlaka ya kuteuza Katibu Mkuu na kesho kuondoa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kama wanaona kwamba Mheshimiwa Rais alihamisha ile taasisi kwa kuficha kitu sidhani kama wanawaza vizuri, nadhani saa nyingine wanaropoka au wamechanganyikiwa, wakijua kabisa kama Mheshimiwa Makamba anajua kabisa Katiba ya Jamhuri ya Muungano inampa uwezo huo Mheshimiwa Rais. Mfano tulikuwa na Wizara ya Nishati na Madini akazitenganisha, anaficha kitu gani yote hiyo ni kutaka efficiency, kazi zake ziende vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, TAMISEMI ilikuwa chini ya Waziri Mkuu ameihamishia Ikulu anaficha nini? Yote hiyo ni kutaka kazi zisimamiwe vizuri. Kwa hiyo, sisi tunaendelea kumpongeza Rais na tunamwambia aendelee kufanya kazi kadiri atakavyoona mafanikio yatakuwa makubwa na ni mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wanasema Shirika la Ndege halina faida wala maana yoyote. Nimeshukuru kaka yangu Mheshimiwa Abbas ameelezea vizuri faida zake, lakini shirika hili la ndege ni identity, ni utambulisho wetu Watanzania na lina faida kubwa sana. Faida yake si tiketi tu, Emirates, Ethiopia Airline, Quatar hawajawahi kupata faida kwenye tiketi wanapata faida kwenye mambo mengine, kwenye mzunguko kama alivyosema kaka yangu Mheshimiwa Abbas, siwezi kurudia, ndivyo faida inavyopatikana. Kwa hiyo, mambo haya ya kusema ndege hazina maana, ndege zina maana kubwa, naipongeza Serikali yangu imeweka bajeti ya kuongeza ndege nyingine, naomba iongeze ili tuendelee kufanya vizuri jambo ambalo wao hawakutegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kelele zilizopigwa nchi hii ni shirika la ATCL kufa. Leo Mheshimiwa Rais amejitokeza kulirejesha shirika hili ni lazima alisimamie kikamilifu ili isije tena ikajitokeza hali ile kama ilivyokuwa mwanzo. Kwa hiyo, mimi naungana naye mkono kuhamisha kitengo hicho kukiweka Ikulu ili usimamizi wake uwe wa karibu zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika legacy atakazoziacha Mheshimiwa Rais wetu ni pamoja na Shirika la Ndege na reli. Leo reli ya Dar-es-Salaam – Morogoro ya Standard Gauge inayojengwa imeshafika asilimia 50, lakini pia kuna Phase II inayojengwa na yenyewe inaendelea vizuri na tunaomba Mungu iendelee vizuri na iishe ili na sisi Tabora tuingie sasa Phase III. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Uwanja wa KIA kuna hangar ilijengwa muda mrefu, niiombe Serikali iboreshe hangar hiyo ili ndege zetu sasa ziweze kutengenezwa Tanzania. Tuna hangar kubwa mpaka dreamliner inaingia. Kwa hiyo, sioni tena sababu ya kuchukua ndege kuzipeleka nchi za nje kwenda kutengenezwa, tuna ma-engineer zaidi ya 60 ambao wana uwezo wa kutengeneza ndege.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimwombe Waziri na Serikali kwa ujumla ihakikishe imeboresha hangar ile ndege zetu sasa zifanyiwe ukarabati ndani ya nchi yetu na sio kupeleka nje. Hiyo iambatane pia na Uwanja wa Ndege wa KIA uendelee kukarabatiwa, uongezwe parking na mambo mengine kwa sababu uwanja ule sasa umeshakuwa mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jana pia waliongelea kuhusu bandari. Mimi niipongeze Mamlaka ya Bandari, kazi ni nzuri, sasa mizigo inatoka haraka siyo kama ilivyokuwa mwanzo, kwa kweli wanajitahidi kwa kiwango kikubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nimesikia Mkurugenzi wa Bandari amelaumiwa kwa kuwafanyisha watumishi kazi mpaka saa 7.00 za usiku; mimi nimpongeze sana, dunia nzima watu wanafanya kazi saa 24 sehemu kubwa kama zile. Yeye ni kupanga shift zao kwamba nani ataingia mpaka saa 10.00, nani ataingia mpaka saa 5.00 ya usiku na nani ataingia mpaka alfajiri ili kuweka mambo sawa na ili bandari yetu iende na wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi kubwa inayofanywa ya kupanua hizi bandari inabidi ziende na wakati. Kwa hiyo, kitu cha muhimu ni kupanga shift na nawapongeza sana. Yule aliyekuwa analaumu kwa nini wanafanya kazi mpaka saa 7.00 ya usiku nadhani hajatembea, atembee duniani, dunia nzima watu wanafanya kazi saa 24. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naongea kuhusu SUMATRA. SUMATRA kuna kitengo kimeanzishwa kinaitwa VTS (Vehicle Tracking System) ambapo sasa hivi mabasi yetu yamefungwa kifaa hiki akitembea mbio au akifanya nini anaonekana moja kwa moja kule Dar es Salaam. Haya ni maendeleo makubwa sana ya Serikali ya Awamu ya Tano, tunaipongeza Wizara ya Ujenzi na Mawaziri na Manaibu wote kwa kazi hii nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Muda wako umeisha Mheshimiwa, kengele imeshagonga. Ahsante sana.

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii ili nami niweze kuchangia Mpango wa Serikali. Niungane na Wabunge wenzangu kuipongeza Serikali yote kwa ujumla, kumpongeza Mheshimiwa Rais pamoja na watendaji wote kwa mpango mzuri waliotuletea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ufinyu wa muda naomba niende moja kwa moja kwenye hoja. Tuko kwenye kupambana kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa nchi ya uchumi wa kati, lakini na kuendelea Zaidi. Tuko kwenye kukusanya fedha lakini tuwe na matumizi mazuri ili nchi yetu izidi kufaidika, lakini tuendelee kupata maendeleo kama kiu aliyonayo Mheshimiwa Rais wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuingia Kamati ya Kilimo nimejifunza mambo mengi sana. Kuna miradi inaendelea kule kwenye majimbo yetu tulipotoka unakuta mradi wa bilioni nne lakini consultants hawa wanaofanya upembuzi yakinifu wanapata bilioni moja point, unashanga. Ukiangalia consultant ana ma-engineer, ana watu wa NEMC, ana Mhasibu sijui wa mradi, lakini ndani ya halmashauri zetu, ndani ya ofisi zetu za mikoa kuna ma-engineer, kuna watu wa NEMC, kwa nini kazi hizi zisifanywe na ma-engineer wetu wenyewe. Hivyo, hii bilioni moja point ambayo anaenda kupewa sasa huyu consultant ziendelee kufanya kazi kwenye halmashauri, ziendelee kuimarisha miradi mingine na kujenga miradi mingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe sana Serikali, niwaombe Mawaziri wanaohusika pamoja na watendaji wetu, sasa hivi tumefika stage ya kuionea huruma pesa ya Serikali, ma-engineer wetu wafanye hizi kazi. Unaweza ukachukua labda milioni mia mbili ama mia tatu ukasema vijana hawa tumewapa kazi hii wafanye upembuzi yakinifu, basi tutawalipa posho hii, kuliko kuchukua bilioni moja point kumpa consultant ambapo tunao uwezo, tumeajiri watu hao kwenye ofisi zetu, wanalipwa mishahara lakini unaenda kuchukua kampuni binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli unabaki pale pale hizi kampuni ni za kwao wenyewe, ni hawa hawa ma-engineer ndiyo wenye hizi kampuni. Kwa hiyo, naomba kabisa yale mambo yanayowezekana madogo madogo yafanywe na ma-engineer watu wetu wa NEMC walioajiriwa na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuongelea suala la kilimo. Tuko hapa tunaangalia tunavyopata shida ya mafuta, tumekuwa tukiagiza mafuta takribani milioni mia mbili themanini dola kila mwaka. Uwezo tunao wa kulima alizeti, ukiangalia mfano Wilaya ya Manyoni, Mkurugenzi huyo wa Manyoni kama humu ndani yupo kaka yangu Mheshimiwa Jafo, anastahili sifa kubwa, amefanya block farm ambayo ameweka heka elfu 30 za korosho. Leo hii heka zile za korosho wameanza kuvuna, lakini baada ya muda pato la mtu moja moja wa Manyoni litaenda kuimarika. Baada ya muda halmashauri yao itakusanya Cess zaidi ya bilioni 10 na kuhakikisha watajenga zahanati zao, watajenga madarasa yao na watatengeneza madawati yao. Hiyo ni block farm tu moja iliyowekwa na Mkurugenzi mmoja katika nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ajira zitapatikana, kodi italipwa, wakiuza nje Serikali Kuu itapata pesa na kadhalika, lakini mambo mengine mengi mengi yatapatikana hapo. Sasa ninachojiuliza imekuwa halmashauri nyingi kupitia Kamati zao za Fedha wanaenda kutembea pale, wanaenda kujifunza pale, lakini toka wameanza kujifunza hakuna halmashauri nyingine yoyote ambayo imeanza kuweka block farm labda ya alizeti au ya kitu gani ili kuondokana na huu umasikini wa mafuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaweza, Uganda walienda kujifunza pale Manyoni, leo Uganda wameanzisha block farm kama ya Manyoni, sisi kwa nini Tanzania tunashindwa, leo tukianzisha block farm kila wilaya katika mikoa mitano, heka elfu 10 za alizeti zikaangaliwe na Maafisa Ugani wetu, wataalam wetu wakaa pale kwenye block farm, wananchi wakapata ile ardhi kwa bei nafuu, wakapata mbegu za bure au za bei nafuu, tunaweza tukalima alizeti nyingi na tukapata mafuta ya kwetu sisi wenyewe na tukaacha kutoa pesa yetu ndogo hii ya Serikali kuagiza mafuta ambapo tunaacha kufanya huduma za muhimu tunaagiza mafuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ufinyu wa muda niongelee kidogo umwagiliaji. Kule kwetu Tabora tumelitewa bilioni mbili kwa ajili ya kujenga bwawa la umwagiliaji, hakuna kinachoendelea bilioni mbili zimewekwa kule ndani lakini kumelimwa heka kumi na tano tu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Munde.

MHE. MUNDE TAMBWE ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niunge mkono hoja. (Makofi)
Azimio la Bunge la Kutambua na Kuenzi Mchango wa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa Utumishi wake Uliotukuka Pamoja na Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii nami niweze kuchangia maazimio yaliyopo mbele yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naungana na Watanzania wote nami kutoa masikitiko yangu makubwa kwa kuondokewa na Kiongozi wetu. Pia niungane na wenzangu waliotangulia kusema kwamba Bwana ametoa na Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe. Hatuna jinsi zaidi ya kumshukuru Mwenyezi Mungu. Leo Mheshimiwa Dkt. Mpango amesema ni lazima Taifa liendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa demokrasia ile ile iliyopo kwenye nchi ya Tanzania ambayo wenzetu wengine hawaioni, tumeweza kufuata Katiba na kumchukua Makamu wa Rais na kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Napata shida sana kusikia mtu anasema Serikali iliyopita ilikuwa haina demokrasia. Nasema demokrasia ipo na ndiyo maana baadhi ya Wabunge wenzetu vyama vyao viliwakataa, lakini Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikasema ni haki yao kuwa Wabunge. Walikuja hapa wakaapishwa wakati hakuna Bunge. Kwa hiyo, naipongeza Serikali ya Awamu ya Tano, lakini tuko na tunaipongeza na kuiombea kila la heri Serikali yetu ya Mama yetu, Rais wetu, Mama Samia Suluhu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilianza kumfahamu Mheshimiwa Rais wetu wa sasa wakati wa Bunge la Katiba, alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Katiba. Mama huyu alikuwa Mwenyekiti mahiri. Nakumbuka Mzee Samuel Sitta alikuwa ana-deal sana na mambo ya kiutawala. Mama alikaa kwenye mijadala mizito, aliweza kuiamua, Bunge la Katiba lilikuwa liko hot, lakini mama alienda nalo vizuri na hatimaye tulivuka tukamaliza Bunge la Katiba salama salimini. Nina hakika na ninayo kila sababu ya kuwaambia Watanzania, tutaenda kuvuka na kazi itaenda kupigwa na tutafikia malengo yaliyowekwa katika Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina imani sana na Mheshimiwa Rais. Mfano juzi au jana wakati anapokea taarifa ya CAG, maamuzi aliyoyachukua, Watanzania wamempokea kwa mikono miwili. Wameona tuko kule kule kwa mzalendo, ana uchungu na fedha za Watanzania, ana uchungu na wezi na anachukua hatua kama alivyokuwa anachukua mtangulizi wake. Sipati shida kusema Mheshimiwa Mama Samia na Marehemu Rais wetu walikuwa ni Kurwa na Doto, walikuwa wanafanya kazi zao kwa pamoja. Kwa hiyo, niwaambie Watanzania, wawe na imani kubwa kwamba tunakwenda kutekeleza mambo yote tuliyoyaahidi kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesikia mwenzetu mmoja hapa anaongea kwamba Mheshimiwa Rais ahakikishe Katiba mpya inapatikana. Niwaambie tu, wakati Mheshimiwa Rais aliyepo sasa hivi madarakani na aliyekuwa amefariki, walitembea Tanzania nzima kuomba kura kwa Watanzania wakiahidi maendeleo, zahanati, maji, shule, elimu bure na kadhalika. Hawakuweza kuwaahidi Katiba mpya. Msitake kumtoa Rais wetu kwenye reli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiangalia kwenye mitandao, kuna raia mmoja wa Ubelgiji alianza kuandika kwamba tunataka Katiba mpya kwa Rais mpya. Mimi nimweleze tu, hawawezi wao kutupangia, tutajipangia wenyewe na tutakwenda kama tulivyojipangia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nami nimwambie Mheshimiwa Rais, aliwaahidi Watanzania maendeleo, tunataka achape kazi alete maendeleo ili mwaka 2025 tutoke kifua mbele kwenda kuomba kura na hatimaye CCM iibuke kidedea kama kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nami niungane na Wabunge wenzangu kusema kwamba Mungu anaipenda Tanzania. Tendo la leo lililotokea la kumchagua Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Mpango, niseme Mungu anaipenda Tanzania. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Amina.

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, tumekwenda kupata Makamu wa Rais mchapakazi atakayemsaidia Rais wetu kufanya kazi, mzalendo anayechukia rushwa, amekaa Wizara ya Fedha. Nani ambaye hajui Wizara ya Fedha? Leo angekuwa amejilimbikizia mali za kila aina, lakini siyo Mheshimiwa Dkt. Mpango. Ni mchumi aliyebobea. Tuna imani tutakwenda kupandisha uchumi wetu Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kuchangia Wizara ya TAMISEMI. Niungane na wenzangu kumpongeza Waziri wa TAMISEMI na kusema kwamba Wabunge tuna imani naye kubwa kwamba atafanya kazi nzuri kwa sababu tunamfahamu ni mchapa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, awali ya yote, nianze kuipongeza Serikali kwa kutuletea pesa nyingi ndani ya Manispaa ya Mkoa wa Tabora. Mimi ni Diwani ndani ya Manispaa ya Tabora ndiyo maana naongea sana kuhusu Manispaa, lakini pia ni Mbunge wa Viti Maalum wa mkoa mzima. Tulikuwa tunahangaika sana jengo la utawala kwa muda mrefu lakini bajeti hii imetuonesha kwamba tumepewa shilingi bilioni moja kwa ajili ya ujenzi huo, lakini tumeletewa bilioni moja, mia moja hamsini kwa ajili ya hospitali ya wilaya na zahanati tatu; Zahanati ya Igosha, Igombe na Ituru, tunashukuru sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kubwa kabisa ambalo tuna shida nalo sisi wananchi wa Mkoa wa Tabora, la kwanza nimwambie Mheshimiwa ndugu yangu Mheshimiwa Ummy, tuna shida ya kukata Mkoa wa Tabora. Mkoa wa Tabora ni mkubwa, ni mkoa wa zamani, una historia kubwa, lakini haujawahi kukatwa. Imekatwa Mikoa midogo na Mkoa wa Tabora umeachwa.

Nimwambie Mheshimiwa Waziri, Mkoa wa Tabora, Tanga na Morogoro ndiyo mikoa pekee haijakatwa na inasababisha kutopata huduma sawa sawa kwa wananchi. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri, mikoa hii mitatu na yenyewe ikatwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Jimbo la Tabora Mjini lina population karibia watu 400,000, lakini ni Jimbo moja lenye Kata 29. Namwomba Mheshimiwa Waziri apitie majimbo yote aone kipaumbele gani kilitumika kukata haya majimbo? Kuna majimbo yana Kata sita, yana population ya watu 20,000 mpaka 30,000 na kuna jimbo lina watu 400,000. Serikali imetumia mchakato gani kupata haya majimbo? Hiki kitu kinaleta maswali mengi. Unakuta mtu anakata sita… (Makofi)

SPIKA: Hiyo hoja muhimu sana hiyo, maana Kongwa ina watu 400,000 Jimbo moja, endelea Mheshimiwa. (Makofi)

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Hata naongea hapa na Naibu Spika, anasema yeye kwake ana kata 36 zenye population zaidi ya watu 500,000. Tunamwomba sana Mheshimiwa Waziri, hata kwake Tanga Jimbo lile ni kubwa. Sasa yeye labda ataona aibu kujikatia Mheshimiwa Waziri, lakini sisi utukatie. (Makofi)

MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Taarifa jitaje.

T A A R I F A

MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Spika, naitwa Stella Ikupa. Naomba kumpa taarifa Mheshimiwa Munde kwamba hata Dodoma Mjini ina kata 46. (Makofi)

SPIKA: Endelea Mheshimiwa.

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa ya Mheshimiwa Ikupa.

Mheshimiwa Spika, kwa kweli tumwombe Mheshimiwa Waziri apitie majimbo yote na aangalie vigezo. Kama Mheshimiwa Waziri kuna jimbo dogo dogo yaunganishe. Kwa kweli kama nia ni njema na kama mnataka kufuata ukweli, majimbo makubwa myakate.

Mheshimiwa Spika, nirudi kwenye masuala ya watumishi. Tabora Manispaa tuna shida moja; Tabora inaitwa Tabora Manispaa, lakini tuna Kata 12 ziko vijijini. Kwa hiyo, tunapokwenda kwenye mgao wa walimu, tunaambiwa hii ni Manispaa, ina walimu wengi, lakini tuna Kata 12 zina uhaba mkubwa wa walimu.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa nimeongea na Afisa Utumishi anipe idadi kwamba tulikuwa tunatakiwa kuwa na walimu wangapi kwenye ikama na tunao wangapi; lakini nilikuwa njiani nimechelewa kupata. Pia watumishi wa Afya kwenye zile Kata 12 ambazo zipo vijijini ambazo zipo ndani ya Manispaa pia watumishi ni wachache sana, tunaomba msaada wako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali imetuletea fedha nyingi za barabara na ujenzi wa majengo chungu nzima, lakini tuna watumishi wachache sana wa ujenzi. Kwa mfano civil engineer, quantity surveyor na ma-technician wa ujenzi wamekuwa wachache sana kwa sababu tunashindwa kusimamia miradi, hakuna watumishi wengi kama inavyotakiwa kwenye ikama yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pale Tabora tuna Kituo cha Afya kikubwa sana Serikali imetujengea, kina majengo matano, lakini majengo matatu yanafanya kazi. Jengo la operation halifanyi kazi kwa sababu hakuna vifaa vya theatre. Kila kitu kimekamilika, bado vifaa vya theatre. Naiomba sana Serikali ituletee vifaa vya theatre kwenye zahanati yetu ya Mailitano. Pia tuna jengo la Mortuary ambalo tunashindwa kulitumia kwa sababu hakuna yale ma-freezer makubwa ya mortuary. Mheshimiwa Waziri nadhani umenisikia, tunakuomba sana, sana, sana.

Mheshimiwa Spika, vile vile tunayo Hospitali yetu ya Wilaya, Serikali imetuletea fedha nyingi, lakini bado hatujapata fedha kwa ajili ya vifaa tiba kwa ajili ya hospitali yetu ya Wilaya.niiombe sana Serikali iweze kutuletea fedha kwa ajili ya vifaa tiba vya hospitali ile ya Wilaya, kwa sababu mpaka sasa wananchi wa Manispaa ya Tabora wanatibiwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora. Wanasababisha msongamano mkubwa, wanasababisha lawama kubwa kwa madaktari kuonekana hawafanyi kazi ipasavyo, lakini ni kwamba hatuna Vituo vya Afya hatuna Hospitali ya Wilaya; na pale ni mjini population ni zaidi ya watu 400,000. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2017.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia. Kwanza nianze kwa kumpongeza Rais wangu kwa kazi kubwa anayoendelea nayo Mkoani Pwani. Tumeona kwenye vyombo vya habari akifungua viwanda kama sera yetu ya Chama cha Mapinduzi inavyosema. Tunamshukuru Mungu kwa sababu tumeanza kutekeleza ndani ya miaka miwili angalau kuna watu walisema viwanda hivyo vitabaki kuwa historia havitajengwa lakini tumeona Rais akifungua vile viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza pia Waziri wa Fedha na Serikali nzima kwa bajeti yao itakayobaki kuwa ya kihistoria kwa sababu imechukua maoni mengi ya Wabunge. Vilevile, bajeti hii imekwenda kugusa kabisa matatizo ya Watanzania, naipongeza sana Serikali yangu kwa kuonesha dhamira ya waziwazi ya kuwa na nchi ya Tanzania ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiangalia kwenye kitabu cha sheria Part Four inasema Amendment of Excise Management and Tariff Act, Cap. 147 ikiongelea tozo ya shilingi 40. Niiambie Serikali kwamba tumekubaliana kabisa na tozo ya sh.40/= na tunawapongeza sana Serikali kwa kutuleta tozo hiyo. Naomba Serikali yangu, kwa sababu tumekubali kutozwa sh.40/= na kwa sababu wanawake tuna shida ya maji na Watanzania kwa ujumla. Kwa sababu tuliahidi kumtua mwanamke ndoo ya maji, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri hii sh.40/= asilimia kubwa ya pesa hii iende kwenye maji vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kwamba hii bajeti ya 2017/2018, hatuwezi kumaliza matatizo yote ya nchi hii ya maji, lakini tuoneshe concern yetu kwamba kweli tumedhamiria kumtua mwanamke ndoo ya maji kichwani. Kwa hiyo, niombe Serikali ipeleke asilimia kubwa ya pesa hizo katika maji vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bado wenzetu hawa wanasema hii tozo ya sh. 40/= tumewaonea watu wa vijijini ambao wanatumia mafuta ya taa. Mimi bado napingana nao kabisa na naiomba Serikali iwapuuze wala isiwasikilize, kwa sababu miaka yote Tanzania kodi inayokusanywa, kodi ikikusanywa kwenye maliasili na utalii Arusha inatumika nchi nzima, ikikusanywa kwenye madini Geita GGM inatumika nchi nzima, ukikusanywa kwa wafanyabiashara wa Dar es Salaam inatumika nchi nzima, kila mnachokifanya tunakitumia Watanzania wote bila kujali maskini, tajiri, sijui kabila gani, kabila gani, hilo suala hatuna.

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani wenzetu hawa wamedhamiria. Tuliwaambia siku ya bajeti kwamba mbona tunalipa tozo ya Railway Development Levy watu wangapi wanapanda treni? Hii reli inatumiwa na watu wachache, lakini Mtanzania yeyote atakayenunua mafuta analipa kodi hii. Tunalipia REA vijijini siyo wote wa mijini wanataka huo umeme wa vijijini, lakini kwa sababu ni jambo letu sote tunakuwa tunalifanya sote, lakini wenzetu hawa hawakubali.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kushangaza Waziri Kivuli wa Fedha wa Upinzani amekuja hapa amekataa kila kitu, hakuunga mkono hata kitu kimoja kizuri kwenye bajeti hii, ndipo utakapojua hawa watu wana matatizo yao mengine tofauti. Wameikataa bajeti hii wamesema bajeti yote ni mbaya na bajeti hii itaingia kwenye historia ya bajeti mbaya kuliko zote nchini. Ndipo unapoweza kuwaona hawa watu ni watu wa aina gani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumewazoea sana hawa watu kwa sababu kupinga kwao ni kawaida ila hatuna habari nao tunaendelea…

T A A R I F A . . .

MHE. MUNDE A. TAMBWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza yeye ndio anaropoka, yeye na Kambi yake ndio wanaoropoka si mimi, hilo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili wamekosoa na wameshauri, hawakuunga mkono hata kitu kimoja kwenye bajeti na ndilo nililolisema, kwa hiyo yeye ndio ameropoka. Hata Bajeti Kuu hawajawahi kuunga mkono hata neno moja wakasema hili kwa leo mmesema zuri. Angalau Wajumbe wao wa Kamati Kuu ya CHADEMA walimuunga mkono Rais kwenye makinikia, lakini wao wamekataa kila kitu hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hawa watu ni watu wa ajabu sana, mimi nasema aliyewaroga labda amekufa, kila kitu wanakataa. Leo hii wanathubutu kuongea, Serikali ya Awamu ya Tano imefanya nini, hakuna chochote kilichofanywa na Serikali hii; wakisahau kwamba sasa hivi tunajenga reli ya standard gauge ambayo tulikuwa tunatoka Dar-es-Salaam mpaka Mwanza kwa siku tatu lakini leo hii tutatoka kwa saa saba kutoka Dar-es-Salaam mpaka Mwanza, hawaoni yote hayo. Hawaoni kila tulichokifanya hawakioni! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nasema hawa watu tuwahurumie wana laana ya kumkataa Dkt. Slaa.
Muswada wa Sheria ya Shirika la Mawasiliano Tanzania wa Mwaka 2017
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii ili nami niweze kuchangia Muswada uliopo mbele yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naomba nichukue fursa hii kuwapongeza sana Mawaziri wangu wa Chama cha Mapinduzi kwa kazi nzuri waliyoifanya jana. Mawaziri hawa jana wameonesha kabisa kwamba wao wanaendana na kasi ya Mheshimiwa John Pombe Magufuli. Wamejibu vizuri sana, tunawapongeza tunawaomba waendelee kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kuipongeza Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa kuleta Muswada huu wa TTCL kuwa shirika la umma kwa asilimia 100. Kwa nini nasema hivi? (Makofi)

Mheshimia Naibu Spika, TTCL ndiyo mawasiliano yote ya nchi yako pale. Unapoichukua TTCL unaiunganisha na Celtel ni kwamba unaweza ukauza siri za nchi yetu bila wewe mwenyewe kujijua. Kwa hiyo, niipongeze sana Serikali, wamefanya jambo zuri ambalo kwa kweli tutaendelea kuwapongeza siku hadi siku. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tatizo lolote lingetokea tungeshindwa kujilaumu kwa sababu mawasiliano yetu yanaweza yakaingiliwa wakati wowote na wabia ambao wamekuja kuwekeza kwetu. Kwa hiyo, nawapongeza sana wamefanya jambo jema na nawaomba Wabunge wote tuupitishe Muswada huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile huko vijijini ukiwasha Vodacom unapanda kwenye mti, hawaendi sehemu ambazo hazina wateja wengi. Kwa hiyo, Serikali yangu naomba sasa TTCL muipe nguvu na mtaji mzuri ili waweze ku-compete kwenye biashara na mashirika ya mawasiliano yaliyopo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nimefurahi. Sisi tunatoka huko vijijini utakuta mtu akiwasha Vodacom mpaka aende juu ya mti au porini lakini naamini kwa kuwapa asilimia 100 TTCL tutaweza kupata mawasiliano nchi nzima kwa kupitia shirika letu la umma la TTCL.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile niiunge Serikali yangu mkono kwa kuwapa TTCL Mkongo wa Taifa pamoja na Data Centre ili waweze ku-compete vizuri na mashirika mengine kama Vodacom, Airtel na Zantel. Hata hivyo, hili lisiwe sababu ya kuwanyima masafa wenzetu wa Vodacom, Airtel na wengine wowote wanaofanya biashara hizi. Wakiomba masafa na wenyewe wapewe ili waweze ku- compete kibiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napata tabu kwenye kitu kimoja, naona watu wana mawazo sana kwamba labda haitaweza kujiendesha, sijui tumerudi kwenye ujamaa, hivi vitu vimetoka wapi? Mbona China wamedhibiti mawasiliano yao yote na wanajiendesha na wana maendeleo makubwa? Pia Korea na nchi nyingine tofauti tofauti wamefanya hivyo, kwa nini sisi leo tunakuja hapa badala ya kuipongeza Serikali kwa kudhibiti mawasiliano, tunasema tena tuache mawasiliano yaendelee kuendeshwa na wawekezaji? Kwa kweli jambo hili siwezi kulikubali kabisa na tunaipongeza sana Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuache kutishana kwamba kila kitakachofanyika ni ujamaa, hata kudhibiti mawasiliano yetu ni ujamaa, hii itakuwa shida na tutashindwa kufanya kazi. Halafu pia ujamaa siyo dhambi hivyo kama tunavyoiongelea au tunavyoifikiria, ni mambo ya kawaida tu ya kupanga ni kuchagua, kama Serikali yetu imepanga kufanya nini, basi mambo yanakwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe pia Serikali yangu kuweka mtaji mzuri kwenye shirika hili la umma la TTCL lakini pia kupata management yenye uwezo mkubwa. Niiombe Serikali katika hili ndiyo tuangalie sana kuweka Managing Director ambaye ana uwezo na watu wake wa kumsaidia ili shirika letu liweze kwenda vizuri. Kwa mfano, Shirika la National Housing limekaa vizuri linajiendesha kibiashara, tunaamini TTCL litakuwa shirika la kibiashara ili liweze ku- compete na wenzie na siyo lijibweteke lingojee kila siku kupata ruzuku. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona ATCL juzi Mheshimiwa Rais amefufua shirika hili na tunaona jinsi linavyoenda vizuri. Ukisoma taarifa yao ya karibuni utaona kwa muda mfupi wamepata faida ya karibia shilingi bilioni tisa. Kwa hiyo, naamini pia TTCL ikisimamiwa kwa Serikali ya Awamu ya Tano inavyofanya kazi hatutajuta na tutakuwa tumejiwekea kitu kizuri, siri zetu zitakuwa bado zimo ndani kwetu sisi wenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja na naipongeza sana Serikali. Ahsante.