Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Martha Moses Mlata (40 total)

MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Na mimi kama swali la msingi lilivyoongea kuhusu Mkoa wa Simiyu kuunganishwa na mikoa mingine, ni wazi kwamba Mkoa wa Simiyu bado haujaunganishwa na Mkoa wa Singida ambao unapitia katika Daraja la Sibiti – Mkalama - Nduguti - Iguguno. Nataka nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri, je, anafahamu kwamba Daraja la Mto Sibiti ndilo kiunganishi kikubwa katika Mkoa wa Simiyu na Singida na mpaka sasa mkandarasi hayupo site? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kwamba Daraja la Sibiti ni muhimu katika mawasiliano kati ya Mkoa wa Simiyu na Singida na ndiyo maana kazi kubwa inafanywa sasa kutokana na matatizo yaliyotokea ili kuhakikisha mawasiliano yanakuwepo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mkandarasi, kwa kuwa fedha za kulipa madeni ya wakandarasi tumeanza kupata ambapo huyu naye ni mmoja kati ya wakandarasi wanaotakiwa kulipwa ili waendelee na kazi. Mara fedha zitakapopatikana, mkandarasi atarudi site ili aweze kukamilisha kazi ambayo alisaini kuifanya.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa hapa Bungeni tumekuwa tukipitisha fedha nyingi sana kwa ajili ya kwenda kutatua matatizo ya maji kule vijijini ikiwemo Mkoa wa Singida, lakini yamekuwa ni mazoea kwamba ma-engineer wanakwenda kuchimba maji maeneo ambapo hakuna maji ya kutosha na hivyo fedha nyingi kupotea.
Je, Serikali ni lini itakuja kutuletea idadi ya fedha ambazo zimepotezwa kwa sababu ya ma-engineer kwenda kuchimba maji kwenye maeneo ambayo hakuna maji matokeo yake wananchi wanaendelea kuteseka na adha za maji? Ni lini Serikali itatuletea figures hizo? Asante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, suala la maji chini ya ardhi ni gumu sana na tuchukulie mfano Mkoa wa Tabora. Mkoa wa Tabora ulifanyiwa study na Wajapani na waka-confirm kwamba chini kuna maji, lakini wamekwenda kuchimba maji yamekosekana kutokana na mfumo wenyewe wa miamba chini ya ardhi. Kwa sasa Wizara ya Maji imetengeneza utaratibu mpya kwamba, study ya maji pamoja na uchimbaji utafanywa na mtu mmoja. Kitu tulichokiona ni kwamba, study inafanywa na Mhandisi Mshauri, anayekuja kuchimba ni mwingine na unakuta tunapoteza pesa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kitu tulichokifanya sasa hivi kwamba, pale tutakapotoa fedha kwa ajili ya kuchimba visima tunatafuta Mkandarasi mmoja na huyo huyo ndiyo anafanya study. Ili akifanya study akichimba kama maji hayakupatikana basi pesa hatutamlipa na kuhakikisha kwamba huo upotevu wa pesa unakuwa haupatikani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye hoja ya pili, tutafanya tafiti na tutatoa taarifa kwenye Bunge hili kuona ni fedha kiasi gani ambazo zimepotea baada ya huo utaratibu wa kuchimba visima na maji hayapatikani.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante. Ni kweli kama alivyosema Naibu Waziri kwamba Serikali itaendelea kutekeleza ahadi za Serikali ya Awamu ya Tano. Naomba nimuulize kama anafahamu pia kwamba kuna mradi wa barabara kutoka Singida – Irongero – Mtinko - Meria mpaka inaungana na Mkoa wa Manyara ambayo pia ilikuwa ni ahadi ya Rais aliyemaliza muda wake. Je, yuko tayari pia kuiingiza barabara hii katika mchakato wa kuikamilisha mapema ili wananchi wale wasiendelee kusubiri kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martha Mlata kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, anachosema Mheshimiwa Mlata ni kweli na juzi nilikuwa katika Mkoa wa Singida na hiyo barabara ni miongoni mwa barabara ambazo nimeziona. Jambo la kufurahisha zaidi katika barabara hiyo, Waziri mweye dhamana ya Miundombinu alipita na kuna daraja la Sibiti ambapo amesema katika bajeti ya mwaka huu mchakato wa lile daraja tayari umeshatengewa fedha kuona ni jinsi gani litaweza kujengwa. Kwa hiyo, commitment ya Serikali ni kuhakikisha kwamba barabara ile inajengwa na tukijua wazi kwamba kwa watu wanaoenda kwa mfano katika Mkoa wa Simiyu, kitendo cha kupita Nzega ni changamoto kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mlata kwamba jambo hili liko katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. Kwa hiyo, ni commitment ya Serikali kuangalia katika miaka mitano tutafanya vipi ili mradi wananchi waweze kupata fursa za maendeleo.
MHE. MARTHA M. MLATA:Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante namshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri kwenye kiwanda hiki.
Lakini kwa kuwa sisi sote Wabunge tuliokuwepo awamu iliyopita ni mashahidi kwamba Mbunge aliyekuwa wa Jimbo lile Mama Anne Kilango Malecela, kwa jua, kwa mvua usiku na mchana alipigania kiwanda kile kwa fedha zake, akakianzisha na mpaka sasa wananchi wale wananufaika.
Je, Serikali haioni kwamba ni hakika inapaswa kumuunga mkono Mbunge yule ili kiwanda kile kiweze kutoa ajira nyingi sana kwa Wanasame na Watanzania kwa ujumla?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba kama isingekuwa ni juhudi za Mheshimiwa Anna Malecela inawezekana tusingekuwa tunazungumza leo kuhusu kiwanda hiki na hivyo kuwa na swali kama hili Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yeye amejitahidi sana na kama mnavyokupunga Waheshimiwa Wabunge mwaka 2012 yeye ndiyo alifanya jitihada akamualika Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na akaenda kufanya harambe kubwa iliyofanikisha ujenzi wa kiwanda kile. Nimfahamishe tu Mheshimiwa Mlata kwamba Mama Anne Kilango Malecela pamoja na kwamba siyo Mbunge tena anawasiliana na Wizara yangu kwa karibu sana ili kuhakikisha kiwanda hiki kinafufuliwa na kinaweza kuendelea. (Makofi)
Kwa hiyo, naomba mahali popote alipo afahamu kwamba kiwanda hicho hatujakitupa na ikiwezekana tunafanya jitihada kwamba wakati wa ufunguzi vilevile awepo, wakati tunavyofungua upya baada ya matengenezo ahsante sana.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwanza naishukuru Serikali kwamba tukiwauliza maswali hapa kuwaomba waende kwenye maeneo, maeneo mengine wameshafika. Namshukuru sana Mheshimiwa Jafo kwani ametembelea barabara nilizokuwa nimeziomba za kule Msingi na Kinyangiri.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Ikungi ni moja kati ya Wilaya kubwa sana ambayo haina mtandao wa barabara na wananchi wamekuwa wakipata shida sana kufika kwenye Makao Makuu ya Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi hususan Jimbo la Ikungi Magharibi ambao wamemwamini sana Mheshimiwa Magufuli na kumpa kura nyingi sana; ni lini sasa Serikali itaenda kule ikaangalie mzunguko wa barabara zile Puma, Ihanja, Iseke pamoja na Mwintiri hadi Igilasoni? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Martha Mlata kwamba, changamoto tunazozipata katika Wilaya ya Ikungi, nina uhakika baada ya wewe sasa kuwa Mwenyekiti wa Mkoa wa CCM utatusaidia ili tuweze kuzitatua moja kwa moja ili wale wananchi wanapoambiwa nia ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi kufanya maendeleo wasirudishwe nyuma kwa kukataa kushiriki katika masuala ya maendeleo kutokana na changamoto ambazo tunazo katika hiyo Wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba sisi watu wa miundombinu tutashirikiana naye kuhakikisha kwamba eneo hilo, changamoto zote za miundombinu tunazitatua ili Wilaya ya Ikungi iwe na hadhi kama Wilaya nyingine za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa tatizo la lumbesa linasababishwa na viroba ambavyo vina vipimo tofauti tofauti. Kwa kuwa nchi yetu ilikuwa na kiwanda cha magunia ambayo yalikuwa na kipimo na ujazo ulio sawasawa.
Je, Waziri yupo tayari kwenda kukifufua kiwanda kile ili tuweze kuwa na vipimo vinavyolingana kuepuka kuwadhulumu wananchi wetu? Ahsante.
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la viroba au vifungashio vyenye ukubwa tofauti suluhisho lake ni kuwa na mizani kwenye buying centre ambao utabainisha kilo stahiki, ukubwa wa gunia sio hoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la viwanda vya magunia, kwa nini viwanda vya mgunia vya Tanzania vilikufa ikiwemo kile cha Kilimanjaro. Magunia yanayotoka nchi za Asia ikiwemo Bangladesh yanapoingia East Africa hayatozwi ushuru, magunia yanayotengenezwa na viwanda vya Tanzania yanatozwa ushuru katika mazingira hayo lazima tuanguke. Kwa hiyo, mapendekezo ni kwamba lazima tuangalie ulinganisho wa ushuru na gharama za bidhaa zinazotoka nje na zinazoingia ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili limeshafikishwa kwa wahusika na tutaweza kulishughulikia namna hiyo. Kwa hiyo, viwanda vya Kilimanjaro, Singida na Tanzania nzima vitaweze kufufuka kwa namna hiyo.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kama ilivyo kwenye vijiji vya Msanga, Kawawa na kadhalika katika Jimbo la Chilonwa, ndivyo ilivyo katika Wilaya ya Mkalama kwenye kata ya Msingi pamoja na kata ya Kinyangiri, vijiji vya Ishinsi pamoja na Kidi na Lelembo, vijiji hivi mvua inaponyesha vinakuwa ni kama kisiwa kwa sababu vimezungukwa na mito ambayo haina madaraja, hivyo wagonjwa wanapougua wakibebwa kwenye machela hawawezi kuvuka na matokeo yake wengine wanaweza wakapoteza maisha.
Je, Serikali inasemaje kuhusu kuwawekea madaraja ya kuvuka wakati wote vijiji hivi nilivyovitaja? Ahsante
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme kwamba kwanza tumelipokea ombi hili, bahati nzuri ni kwamba siku ya tarehe 25 Juni, Mbunge wa Mkalama amenialika kwenda Jimboni kwake kwa ajili ya kukabidhi madawati.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii maana yake ninazungumza ni Jumamosi hii inayokuja, nitakapofika kule Mkalama, miongoni mwa maeneo ya kuyatembelea baada ya kuhakikisha tunazindua baadhi ya ile miradi ambayo Mbunge amekusudia ikiwepo madawati na mambo mengine, lakini tutakwenda kutembelea maeneo haya ikiwezekana tuweze kubaini nini kinatakiwa kifanyike ili wananchi wa Jimbo la Mkalama waendelee kupata huduma.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante. Wilaya mpya ya Mkalama pamoja na kwamba ilitengewa fedha kwa ajili ya kujenga Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya hiyo, fedha hizo zimeonekana hazitoshi kwa sababu nyingi zimeenda kulipa tu fidia na hivyo kushindwa kuendelea kujenga ofisi hiyo. Naomba Mheshimiwa Naibu Waziri atuambie wako tayari sasa kuiongezea fedha Halmashauri hiyo ili iondokane na adha ya kupanga majengo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya mpya ya Mkalama katika orodha yangu ya zile Halmashauri nilizozizungumza ni miongoni mwa Halmashauri ambayo imo kwenye orodha. Jukumu letu sisi Wabunge kwa umoja wetu tuhakikishe bajeti ya Serikali inapita na tutaiomba sasa Wizara ya Fedha bajeti tuliyoipanga mwaka huu iweze kupatikana ili Mkalama kama tulivyoipangia bajeti katika mwaka huu iweze kupata fedha, ujenzi uweze kuendelea ile Halmashauri iweze kusimama vizuri. Kwa hiyo, Mkalama ni miongoni mwa Wilaya ambazo tunaenda kuzifanyia kazi katika mwaka huu wa fedha.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
Barabara inayounganisha Mkoa wa Singida, kwenda Wilaya ya Mkalama, ambayo inaunganisha pia Mkoa wa Simiyu, kupitia daraja la Sibiti kwa hali ya mshangao sana mkandarasi alifika site lakini akaondoka, sasa nilikuwa namuomba Naibu Waziri, yuko tayari kwenda kusaidiana na wananchi wale kushangaa ni kwa nini mkandarasi aliondoka site?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi na Mheshimiwa Waziri wangu, tutajigawa kuhakikisha kwamba maombi haya ikiwa ni pamoja na la kwake tunayatekeleza. Labda niombe hapo hapo Waziri wangu aniruhusu, kati ya Kiluvya na Daraja la Sibiti, mimi aniruhusu niende kwenye Daraja la Sibiti.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza naishukuru sana Serikali kwa kuleta maji katika Mji wa Singida. Mahali ambapo mitambo, mashine na matanki yale yalipo katika Kata ya Mwankoko ambako ndiko maji yanatoka kwenda kwenye Mji wa Singida wao wenyewe hawana maji. Je, Serikali sasa iko tayari kutumia yale maji kuwasambazia wananchi wa Kata ya Mwankoko ili na wenyewe waweze kufaidi maji ambayo yako kwenye chanzo cha eneo lao?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nijibu kwamba Serikali iko tayari na ndiyo malengo yetu kuhakikisha kwamba sehemu ya chanzo cha maji wananchi waliopo pale lazima tuwaheshimu kwa sababu kwanza wamelinda kile chanzo hawajakiaribu, kwa hiyo lazima wafaidi juhudi waliyoifanya na pili wataendelea kulinda miundombinu yetu.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante. Ningependa tu kumwuliza Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba kwa kuwa hoteli hizi ambazo ni maalum sana, ambazo zinaitwa ‘za Kimataifa’, zinazojengwa kwenye maeneo maalum, zimekuwa zikichukua ajira za wafanyakazi wengi kutoka nje, zile ambazo ni muhimu sana na kuwaacha wazawa wakifanya kazi zile ndogo ndogo kwenye hayo mahoteli makubwa. Je, Serikali inajipanga vipi kuhakikisha kwamba nafasi zile kubwa zinachukuliwa na wazawa kuliko wafanyakazi kutoka nje?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli kwa ufupi kabisa! Ukweli ni kwamba mfanyabiashara anapotafuta mtu wa kumwajiri ili aweze kutoa huduma katika eneo lake la biashara, lazima atakuwa anatafuta mtu ambaye atamwezesha kupata tija katika biashara yake. Kwa hiyo, hilo linakuwa ni suala la ushindani.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeliona jambo hili kwamba kwa upande wa nchi yetu, tunao upungufu kwa kiwango fulani juu ya kuweza kushindana katika masoko haya ambayo yanahusisha ushindani wa Kimataifa. Kwa hiyo, hatua ya kwanza ambayo tutaifanya ni ile ambayo tunaboresha zaidi Vyuo vyetu ili tuboreshe zaidi wananchi wetu, waingie, wajifunze; lakini siyo kujifunza tu darasani, wakitoka pia waweze kufanya kama walivyojifunza.
Mheshimiwa Naibu Spika, mambo mengine, kwa mfano ya hospitality ni zaidi hata ya kujifunza darasani, lakini pale ni lazima mtu uweze ku-gain competencies ambazo zitaweza kukuwezesha kupambana kwenye soko la ajira; lakini haitafikia wakati tukaweza kumlazimisha mfanyabiashara kumwajiri mtu; isipokuwa tutajenga mazingira ya kuwawezesha Watanzania wawe washindani wazuri zaidi.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na kwamba sheria hii ni nzuri lakini naamini kwamba bado elimu haijatolewa vizuri kwa wananchi hasa walioko pembezoni. Naibu Waziri, ningependa kujua, kwamba kumekuwa pia na tabia ya watu wahalifu ambao wanatumia namba za simu za watu wengine kwa kuwaibia watu wengine. Ukienda kwenye truecaller unakuta ni jina la Martha Mlata na namba ni ya kwake lakini aliyetumia ni mtu mwingine, je, hili nalo anatuambia nini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, sababu mojawapo kubwa ya kutaka kutekeleza kuondoa simu feki ni pamoja na hilo ambalo Mheshimiwa Martha Mlata amelieleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba ukiwa na simu feki, makosa haya yanapotendeka si rahisi Polisi ku-trace, inakuwa ngumu sana kufuatilia tukio hilo lilipotokea kwa sababu zile simu feki hazijawa registered na haziwezi kuwa registered kwa sababu utengenezaji ni tofauti na jinsi ilivyoandikwa na hakuna namba ya utambulisho katika zile simu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ndugu zangu, ili tuweze kuhakikisha kazi hii tunaifanya kwa ukamilifu na kwa uzuri zaidi, nawaomba sana tuwahimize ndugu zetu wahakikishe simu zote zinasajiliwa na zile ambazo hazijatoka katika watengenezaji rasmi na hazina namba za utambulisho nafahamu kwamba kuanzia tarehe 16 saa sita usiku zitaondolewa katika matumizi. Lengo kubwa ni ku-improve katika utekelezaji wa haya ambayo Mheshimiwa Mlata ameeleza.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri lakini naomba, kwa sababu Singida ni center ambapo watu wengi wanaosafiri wanapita mkoa ule na unaona kabisa zile nyumba za maaskari pale kushoto baada ya uwanja wa Namfua. Sasa yuko tayari kuanzia pale kabla hajaenda mikoa mingine ili zile nyumba zikatengeneze sura ya Mkoa wa Singida?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Martha Mlata, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Singida na Tabora siyo mbali basi tutazingatia pendekezo lake.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nilikuwa naomba kumuuliza Naibu Waziri kwa kuwa REA wamejitahidi sana kusambaza umeme vijijini, lakini TANESCO hawaingilii kwenda kuanza kusambaza umeme kwenye maeneo mengine ambayo yameanzishwa hasa ya uzalishaji, mfano Kata ya Gumanga kuna kiwanda cha kusindika nyanya, umeme haujapelekwa Mkalama. Nilikuwa naomba kuuliza ni kwa nini TANESCO sasa wasiende kuanza kusambaza umeme? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji alivyotaja Mheshimiwa Mlata kwanza kabisa viko kwenye Mpango wa REA, lakini sambamba na Mpango wa REA bado TANESCO wanapeleka nguzo. Nimhakikishie tarehe 15 mwezi uliopita Mheshimiwa Mlata tulimpelekea nguzo 20 za umeme ambazo zitafungwa kuanzia tarehe 20 mwezi unaokuja. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mlata vijiji vyako vyote vya Manga pamoja na ulivyotaja Mkarama vitafungiwa umeme kupitia REA pamoja na TANESCO.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri akijibu swali mojawapo hapa Bungeni kuhusu mradi wa umeme wa upepo Singida alisema kwamba Serikali inakamilisha mkataba na taratibu za kusaini kati ya Kampuni ya Wind East-Africa na kwamba mwezi Februari mradi huo utaanza. Naomba atusaidie, je, maneno yale ni kweli au bado? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilichowaeleza ni kweli kwanza, lakini cha pili nifafanue tu kwamba mradi wa REA unaokwenda kuendelea umeshaanza na mpaka tarehe 31 mwezi Machi, wakandarasi watakuwa wameshaingia mikoa yote kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa REA unaoendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa upande wa umeme wa upepo kule Singida nimesema mradi wa Wind East-Africa pamoja na Geo Wind wanakamilisha taratibu za kimikataba na kufikia mwezi Juni ndiyo wataanza rasmi. Kwa wanaoanza Februari na mwezi Machi ni miradi ya REA na ile miradi ya upepo itaanza kuanzia mwezi Juni na kuendelea.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri lakini naomba nimuulize. Hivi kwenye habari ya wagonjwa haya mambo ya kodi yanatoka wapi jamani kwenye magari yao? Kwa sababu hiyo sio biashara ni huduma. Kwa hiyo, naomba aniambie hiyo ni biashara au ni huduma kwenye masuala ya VAT? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kama Serikali tumeiona changamoto hiyo na tumeanza kuifanyia kazi. Niwaahidi Waheshimiwa Wabunge kwamba tunapokuja na sheria mpya jambo hili yawezekana
likawa limepatiwa ufumbuzi.
Mheshimiwa Spika, nia ya Serikali yetu ni kuhakikisha wananchi wetu wanapata huduma hasa za afya katika mrengo ulio mzuri na bila usumbufu wowote. Kwa hiyo, niwahakikishie tu Waheshimiwa Wabunge kwamba jambo hili Serikali tumeliona na hasa hili la kodi ya VAT ambalo liko chini la Wizara ya Fedha na Mipango. Ahsante. (Makofi)
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba Mheshimiwa Naibu Waziri anisaidie, kwanza napongeza kasi ya usambazaji wa umeme lakini kuna tatizo la nguzo kwenda chache.
Naomba aniambie katika kata ya Bumanga kwenye kiwanda cha akina mama cha kusindika mbogamboga, msitiki, kanisa na shule walikosa nguzo hivyo hamna umeme, ni lini mtapeleka nguzo hizo ili waweze kupata umeme? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile Mheshimiwa Mlata ameniambia kwamba kuna tatizo la nguzo, nitawasiliana na wataalam leo hii ikiwezekana mwisho wa wiki hii au wiki ijayo ziweze kupatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kusema kwamba kwa sasa nguzo, mashine na transfoma zinapatikana hapa nchini hatuagizi kutoka nje. Kwa hiyo, uhakika wa upatikanaji wa nguzo pamoja na vifaa vingine utakuwa ni rahisi zaidi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mlata tutafuatana lakini mwisho wa wiki hii au wiki ijayo nguzo zitapatikana.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa katika majibu yake Mheshimiwa Waziri amesema kwamba changamoto kubwa ni kutokana na ratiba za wanafunzi wanaomaliza form six kwenda Chuo Kikuu muda ni mdogo na wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne mpaka kuja kuingia cha tano waliofaulu ni miezi nane. Je, anaonaje kuleta sheria hapa ili tuje tubadilishe wawe wanaenda JKT wakati wanasubiri kwenda form five?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema wakati nawasilisha bajeti yangu, kwamba wazo hili lilikuja ni wazo zuri, tulikubali kwamba tutalichukua tukalifanyie kazi kwa sababu kuna wadau wengi wakiwemo Wizara ya Elimu, tupitie nao kwa pamoja tuone uwezekano wa jambo hili. Kwa maana hiyo baada ya mazungumzo na wadau tutaweza kulitolea uamuzi.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kujua kama mfumo anaosema Mheshimiwa Naibu Waziri unasaidia pia kukusanya data za malipo ya nyimbo za wasanii ambazo zinatumika kama miito kwa sababu ni mara nyingi wamekuwa wakidhulumiwa na kutokujua ni kiasi gani wameuza? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, hatujaanza kulifuatilia eneo hilo, lakini tukishakamilisha mfumo huu wa Total Revenue Assurance, nina uhakika tutaingia huko. Kikubwa hapa ni mikataba kati ya wasanii na hawa watoa huduma. Ni kazi ya sisi kupitia huu mtambo kuhakikisha tunasimamia mikataba yao na hatimaye tunawanufaisha wasanii. Hilo nadhani litaweza kufanyika, ngoja tusubiri mtambo huu ukamilike katika mfumo wake wa Total Revenue Assurance.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na Serikali kuweka mikakati mizuri ya kuhakikisha inapunguza vifo vya akina mama, nilikuwa naomba; wewe unatambua sasa hivi kuna Watanzania wengi walioko vijijini na mitaani wanaoteseka, wanaoumwa na kuugua maradhi yanayotibika lakini wamekosa fedha za kutibiwa hospitali mpaka wanagundulika na vyombo kama televisheni au redio au waandishi kwa sababu ya kukosa pesa.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia watu hawa? Kwa mfano kuna kijana mmoja anaitwa John ambaye ana maradhi makubwa ya moyo amegundulika na Clouds Television, je, Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia wagonjwa hawa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwanza nivipongeze vyombo vya habari na Watanzania wote ambao wamekuwa katika nyakati tofauti wakichangia gharama za huduma kwa Watanzania wenzetu ambao wanakuwa wamekosa uwezo wa kufanya hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo niseme tu kwamba Serikali ina utaratibu wa kutoa misamaha kwa kila Mtanzania ambaye atashindwa kumudu gharama za huduma ya afya kwa sababu huduma za afya ni haki ya msingi ya kila Mtanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo nitoe rai, kama kuna Mtanzania ametozwa gharama ambazo hawezi kuzimudu, kuna utaratibu wa kufuata kueleza hali yake kwamba hana uwezo wa kumudu gharama hizo kupitia kwa Maafisa Ustawi wa Jamii waliopo kwenye Halmashauri zote na kwenye hospitali zote. Afisa Ustawi wa Jamii akifanya uchunguzi na akathibitisha kwamba kwa kweli Mtanzania huyu mwenzetu ameshindwa kumudu gharama za matibabu alizopewa basi Afisa Ustawi wa Jamii ata-write-off msamaha, ataandika msamaha kwenye fomu zake na Mtanzania huyu atapata huduma hizo bure bila gharama yoyote ile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo ni watu sasa wauelewa utaratibu huu na sisi Waheshimiwa Wabunge tuwaeleweshe Watanzania wenzetu, wanahabari pia wawaeleweshe Watanzania wenzetu, wala hakuna sababu ya kwenda kuchangishana kwenye vyombo vya habari ili ukapate huduma kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa sababu kama huduma hiyo ipo na huna uwezo wa kulipa muone Afisa Ustawi wa Jamii utapewa msamaha na utatibiwa bure hapo hapo Muhimbili.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Kwa kuwa wanawake wanaoishi katika Manispaa ya Singida na maeneo yanayozunguka Manispaa hiyo wamekuwa wakipata huduma kwenye Hospitali ya Mkoa pamoja na Sokoine lakini idadi yao ni kubwa kiasi kwamba inawazidi wale watoa huduma hali kukiwa na Hospitali ya Rufaa ambayo imeshajengwa tayari lakini bado Wizara haijaleta huduma yoyote kuboresha pale ili huduma zianze na kuokoa maisha ya wanawake wengi. Ni lini sasa Serikali italeta huduma kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida ili kuokoa maisha ya wanawake? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza nimpongeze yeye lakini pia nimpongeze RMO wa Singida rafiki yangu Dkt. Mwombeki kwa jitihada mbalimbali ambazo wanazifanya kuboresha huduma za wana Singida. Wamekuwa wakifanya mikakati mbalimbali ikiwemo kujenga hiyo Hospitali ya Rufaa mpya, nzuri na ya kisasa kabisa.
Mheshimiwa Spika, pia wamekuwa mkoa wa kwanza kuanzisha huduma za outreach, huduma za kuwafuata wananchi na kuwapa huduma za kibingwa kwenye vijiji vyote. Naona Mheshimiwa Spika sasa hivi hata hapa mkoani kwako zimefika na juzi zilikuwa pale Kongwa lakini waanzilishi ni Mkoa wa Singida. Niwaombe Wabunge wote wa-support mpango huu, wawasiliane na RMO wa Mkoa wa Dodoma ili waone ni namna gani wanaweza wakazipeleka hizi huduma kwenye mikoa yao.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya bashirafu hiyo, jibu langu ni kwamba tayari huduma zimeshaanza kwenye Hospitali ya Rufaa anayoizungumzia lakini tunakwenda kwa awamu. Katika hatua ya kwanza tumeanza kutoa huduma za outpatient lakini kadri tunavyoendelea kuboresha huduma na kupata pesa za kuweza kuijengea uwezo hospitali ile, ndivyo tunapanda ngazi na kuongeza huduma moja baada ya nyingine.
Mheshimiwa Spika, kuanzisha hospitali siyo jambo dogo, linataka muda, rasilimali na hatutaki kukurupuka kwa sababu tunataka tuitendee haki hospitali ile nzuri ambayo imejengwa chini ya usimamizi wa RC aliyekuwepo Mheshimiwa Parseko Kone. Ahsante.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Natambua kwamba tatizo la uhaba wa maji linawakumba sana wanawake wote Tanzania. Nilikuwa naomba Mheshimiwa atusaidie hasa kwenye Mkoa wetu wa Singida, hakuna mradi wowote mkubwa wa maji ambao umeanzishwa kwa ajili ya kuokoa tatizo la maji katika Mkoa wa Singida.
Je, ni lini sasa Serikali itaenda kuwakomboa wanawake wa Mkoa wa Singida kwa tatizo la maji? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli watu wanaopata adha kubwa katika suala la maji hasa vijijini ni akina mama na Serikali inatambua jambo hilo na ndiyo maana katika mwaka huu wa fedha 2017/2018 tumetenga shilingi bilioni 237. Hizi zinakwenda kwenye Halmashauri zote katika kutekeleza miradi ambayo iko vijijini na hususan miradi hiyo ikikamilika itakuwa imeondoa hii adha ya akina mama wanaopata shida ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali kama tuna mpango wa kupeleka mradi mkubwa, katika bajeti ambayo imetengwa hiyo ya shilingi bilioni 237, kwanza tunataka tukamilishe miradi ambayo tayari Serikali ilishawekeza. Kwa hiyo, ikishakamilika miradi hii tutaangalia mahitaji sasa ya ziada na tutaona namna gani tuweze kutafuta mradi mkubwa wa kuweza kuwafikishia wananchi wa Mkoa wa Singida. (Makofi)
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naiomba Serikali itoe tamko hapa kuwaeleza wananchi wa Ilongelo, Mdida, Singa, Mtinko, Nkungi hadi Haydom kwa ahadi yao waliyoahidiwa na Rais wa Awamu ya Nne kwamba barabara ya lami itajengwa kutoka Singida kupita maeneo hayo hadi Haydom lakini sasa hivi hakuna kinachoendelea. Naomba Serikali iwaambie wananchi hao. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Martha Mlata, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Singida na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa huo, kama ifuatavyo:- (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba juhudi zake za kufuatilia ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami hatimaye zitazaa matunda kwa sababu ahadi ambayo ilitolewa na Rais wa Awamu ya Nne tunayo na nimhakikishie kwamba ahadi hiyo tutaitekeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaenda kutekeleza ahadi hizi awamu kwa awamu kama ambavyo nimekuwa nikimueleza yeye pamoja na Wabunge wenzake wanaofuatilia sana barabara hii, barabara hii inaunganisha Wabunge wengi sana.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri na kuitaja Singida, naomba atusaidie kwamba makampuni yale ambayo yanachukua leseni halafu wanakaa nayo muda mrefu bila kufanyia kazi na hivyo kuwafanya wachimbaji wadogo wasiende kufanya uchimbaji kwenye maeneo yenye madini kama Londoni, Sambaru, Muintiri, Sekenke pamoja na Mkalama. Ninaomba atoe tamko hapa kwa makampuni hayo na ni lini atatekeleza? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia sasa na kuanzia huko nyuma na tunaendelea kufanya hivyo. Naomba nichukue nafasi hii kutoa rai kwamba wachimbaji wote ambao hawayafanyii kazi maeneo yao, Serikali itayachukua na huo ni utaratibu wa kisheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Madini kifungu Na. 36(1), Sheria Namba 14 ya mwaka 2014 inakataza mwekezaji yeyote kushikilia maeneo bila kuyaendeleza. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mlata kwamba wananchi wa Sekenke, Sambaru, Londoni, Muintiri na wananchi wengine wote tunawapatia maeneo kutokana na wawekezaji ambao hawayaendelezi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili niwahakikishie na niwaombe sana Watanzania kwamba sasa tunatekeleza sheria. Maeneo yote ambayo yalikuwa hayafanyiwi kazi na wawekezaji na hasa wawekezaji wa nje, lakini hata wawekezaji wa ndani ambao walikuwa hawayaendelezi, sasa sheria inaanza kuchukua mkondo wake. Maeneo tutayachukua, tutayatumia kwa ajili ya wachimbaji wadogo waweze kupata maeneo ya uhakika kwa ajili ya kujipatia kipato.
Kwa hiyo, namshukuru Mheshimiwa Mlata, kama ambavyo siku zote anafanya; na Kampuni ya Ashanti Mining ambayo iko kwake, tunafanya mazungumzo nayo ili ikiwezekana na yenyewe iweze kuachia maeneo kwa ajili ya wananchi wa Singida.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza niipongeze Serikali kwa mkakati mkubwa inayoweka kuhakikisha wananchi wote kwenye vijiji wanapata maji. Hata hivyo, tukirudi nyuma historia ni kwamba Serikali ilipochimba visima iliachia Kamati za Maji kuendesha visima hivyo. Je, Serikali kwa sababu imejizatiti kupeleka maji kila kata na vijiji, ina mpango gani ya kuchukua wale wanafunzi wenyeji waliomaliza Kidato cha Nne wakajifunze Chuo cha Maji kwa ajili ya kuja kusimamia visima hivyo ili viweze kutumika kwa muda mrefu. Mheshimiwa Naibu Spika, ni hilo. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru. Pia nimshukuru sana Mheshimiwa Mbunge, mama yangu, kwa swali zuri, lakini kikubwa na sisi tumepokea ushauri. Tulivyoanzisha miradi ya maji na kuhakikisha wananchi wanapata maji, lakini lazima kuwe na usimamizi, tukaona haja ya kuwashirikisha wananchi katika kuhakikisha kwamba, kunakuwa na jumuiya za watumiaji maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na nia njema ya kuweka jumuiya ya watumiaji maji, lakini kumekuwa na changamoto za aina yake. Sisi kama Wizara ya Maji tumekuwa na Chuo cha Maji kipo pale Ubungo; ni fursa pia niwahamasishe vijana wenzangu wapate nafasi ya kufika pale na sisi kama Wizara tutaangalia namna ya kuweza kuwasaidia katika kuhakikisha na wao wawe sehemu ya kumiliki miradi ile ya maji. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Naibu Spika, asante kwa kuwa swali la msingi linafanana kabisa na Wilaya mpya za Mkalama pamoja na Ikungi na wanatimiza vigezo vyote ambavyo Waziri amevitaja hapa.
Je, Serikali ni lini sasa italeta huduma za hospitali za Wilaya katika Wilaya hizo za Mkalama na Ikungi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Mkalama ni Halmashauri mpya na imegawanyika kutoka Halmashauri ya Iramba, tunaenda kuhakikisha tunaboresha kile kituo cha afya cha Inimbila kwa sasa lengo kubwa ni kwamba kiweze kuwa na suala zima la upasuaji kuondoa haya mambo ya referral system, ambapo tunajua kwamba jambo hili tukilifanya litasaidia sana wananchi wa Jimbo la Mkalama kuweza kupata huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, hali kadhalika katika kituo cha afya cha Ikungi tunaenda kuweka uboreshaji mkubwa wa miundombinu ya afya ambayo kwa wananchi wa eneo lile wataweza kupata huduma mzuri hivi sasa ambapo kama nilivyosema awali tumeingiza katika mpango ule wa vituo vya afya 100 ambao Serikali iko katika hatua za mwisho kwa sababu kila kitu kimeshakamilika, tegemeeni Waheshimwa Wabunge katika maeneo hayo Serikali imewasikia na itafanya mambo hayo kwa kadri iwezekanavyo. (Makofi)
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Wanawake wa Kongwa, Singida na wa nchi nzima wanasubiri utekelezaji wa kauli ya kumtua mwanamke ndoo. Leo hii Mheshimiwa Waziri anajibu swali kwa kusema kwamba mkandarasi alipata mkataba mwaka 2014 mpaka sasa eti wana mazungumzo. Naomba Mheshimiwa Waziri aendane na kauli ya kumtua mwanamke ndoo kwa kusitisha kwa haraka mikataba inayosuasua ili tuwaokoe wananchi wa Tanzania. Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa katika utekelezaji wa kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata maji, tulianzisha hii Programu ya Maji na tukawapa hawa Wakurugenzi wa Halmashauri kusimamia miradi mingi. Toka tumeingia Awamu ya Tano, kitu cha kwanza tulichofanya tumeikwamua miradi mingi iliyokuwa imesimama baada ya fedha kuanza kwenda.
Mheshimiwa Spika, hatua ya pili, tunafanya mapitio ya mikataba yote ya hovyo ambayo ilikuwa imeingiwa halafu wanafika mahali wamekwama. Kwa hiyo, mikataba ile ambayo ilikwenda vizuri miradi imekamilika na sasa hivi kati ya miradi 1,800 miradi 1,300 imekamilika, bado hii 400 ambayo inaendelea kwa hatua mbalimbali.
Kwa hiyo, katika hii 400 kuna baadhi ya mikataba ambayo tunafanya mapitio kama huo mradi wa Nyang’wale ambao kidogo una figisu figisu kwamba mkataba wa kujenga matanki na kupeleka mabomba ni watu tofauti. Sasa mikataba ikiwa ya namna hiyo unakuta mmoja akizembea, utekelezaji unakuwa hafifu. Kwa hiyo, azma ya Serikali ya kuhakikisha kwamba tunamtua mama ndoo iko pale pale.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mkoa wa Singida unastawisha sana zao la alizeti na wananchi wa Mkoa wa Singida wameelewa sana dhana ya viwanda. Sasa tatizo linakuja kwenye zao la alizeti kwa sababu Serikali haijaweka msisitizo katika kuleta ruzuku ya mbegu ili zao lile lilimwe kwa wingi kukidhi viwanda vinavyojengwa Mkoani Singida. Ahsante.
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inao mkakati mahsusi wa zao la alizeti ambao mkakati huo pamoja na mambo mengine umelenga kwanza kuongeza uzalishaji wa alizeti hapa nchini na usindikaji wa mazao yanayotokana na alizeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati huu kwa kuanzia umeanza kwanza na kuhakikisha kwamba upatikanaji wa mbegu bora za alizeti unakuwa na utoshelevu. Tumeshapata sasa aina nne za alizeti variety mpya ambayo tija (productivity) yake ni kubwa kuliko mbegu hizi ambazo au variety hizi ambazo tumekuwa tunatumia hapa nchini kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo ni kweli kwamba kwa miaka ya nyuma mbegu ya alizeti ilikuwa haitoshi, mbegu yenye ubora lakini sasa mbegu inayoweza kutoa mafuta megi zaidi na katika kiwango kidogo imeshapatikana, ni variety hizo nne na zitaanza kusambazwa kwa wakulima hapa nchini.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ya Iramba, Tarafa ya Ndago, Kata ya Ndago kwenye Magereza ya Ushora ambayo yana “A” na “B”, Ushora pamoja na Mirungu kulikuwa na msitu mkubwa na miti mikubwa ambayo ilikuwa ni chakula cha tembo lakini wafungwa wale wamemaliza ile miti hadi wale wanyama wamehama kule. Waziri ananiambia nini kuwapelekea miti wale wafungwa wakapande waturudishie msitu wetu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Martha Mlata, alipokuwa kwenye Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira alikuwa anazungumzia sana juu ya ukataji wa miti hovyo kwenye Gereza la Ushora. Mimi niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wote na niwakumbushe kwamba suala kulinda, kutunza na kuhifadhi mazingira kwa mujibu wa kifungu namba sita cha Sheria Namba 20 ya mwaka 2004 sote tunawajibika kufanya hivyo. Tuendelee kuhakikisha kwamba zile taasisi ambazo ziko kwenye maeneo yetu yakiwemo magereza, shule, hospitali wahakikishe kwamba wanatumia nishati mbadala kama ambavyo Mheshimiwa Waziri alivyoelekeza.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Martha Mlata kupitia swali lako hili, naendelea kuzitaka taasisi zote ambazo tulishazielekeza wasiendelee kukata miti kwa ajili ya nishati, waendelee kutumia nishati mbadala na katika siku ya Mazingira Duniani ambayo tunaanza tarehe 30 Mei mpaka tarehe 5 Juni, 2018 kutakuwa na maonesho ya…

…watu mbalimbali katika kutumia nishati mbadala. Mheshimiwa Martha Mlata nitakuwa tayari kuambatana na wewe kwenda Gereza la Ushora, ahsante sana.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nampongeza Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri.
Kwa kuwa amezungumzia mikakati ya Serikali katika kuhakikisha inatunza na kuhifadhi vyanzo vya maji, ninaomba kujua, kwa kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais ilishawahi kutoa maelekezo kwa Wakurugenzi wote nchi nzima iweze kubaini vyanzo vyote vya maji na kupeleka orodha ili Serikali sasa ije na mkakati wa kutekeleza, siyo kwa ajili ya kuweka mikakati ya kufikiria kuanza; je, mkakati huo na agizo hilo limetekelezwa kwa kiwango gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa sababu Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba Serikali ina mpango wa kufufua vyanzo; kuliko kusubiri kuja kufufua vyanzo ambavyo vilishakufa, Singida tuna maziwa mawili, Singidani pamoja na Kindai na ukienda Singidani lile ziwa limeshaanza kujaa tope. Je, kuna mkakati gani sasa wa kuja pale Singida ili mje muondoe lile tope, kina cha maji kibaki kama kilivyokuwa mwanzo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze swali la msingi Mheshimiwa Catherine Magige kwa namna ambavyo anawakilisha Mkoa wake wa Arusha na wananchi wa Arusha wanadhani yeye ndiye Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa Ofisi ya Makamu wa Rais ilishatoa agizo kwa Wakurugenzi wote nchi nzima kubaini na kuorodhesha vyanzo vya maji na tuliwapa muda wa kutosha, lakini mpaka sasa ni mikoa mitatu tu kati ya mikoa yote ambao wamewasilisha orodha ya vyanzo vya maji pamoja na changamoto zake. Sasa mikoa mingine wameshindwa kutekeleza agizo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachofanya sasa ni kuhakikisha kwamba orodha ya Halmashauri zote nchini ambazo hazijawasilisha orodha ya vyanzo vya maji, tunaiwasilisha kwa Waziri Mkuu wa nchi yetu ili aweze kuamua hatma ya Wakurugenzi hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Martha Mlata naye amekuwa akifuatilia sana kero za Mkoa wa Singida hasa upande wa mazingira. Napenda nimhakikishie Mheshimiwa Martha Mlata kwamba maziwa mengi katika nchi yetu likiwemo hilo la Singidani yamekuwa yakijaa tope kutokana na shughuli za kibinadamu. Sasa nitamwagiza Mkurugenzi wa Mazingira wa nchi yetu aambatane na timu yake washirikiane na Halmashauri ya Wilaya ya Singida na ya Mji wa Singida ili waweze kuona ni mikakati gani tunayoweza kuifanya kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunadhibiti hali hiyo. Ahsante sana. (Makofi)

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri kuhusu vyanzo vya maji katika Halmashauri zote, napenda kulipa taarifa Bunge hili kama nyongeza ya majibu kwamba mwaka 2006 wakati wa kuandaa Programu ya Maji nchi nzima ilifanyika stadi ya vyanzo vya maji nchi nzima. Kwa hiyo, kwa Wakurugenzi siyo kazi mpya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa agizo kwa Wakurugenzi wote, ndani ya mwezi mmoja waweze kuwasilisha Ofisi ya Makamu ya Rais hivyo vyanzo vya maji vyote kwa sababu wanavyo katika vitabu vyao. (Makofi)
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naomba hili swali la wananchi niseme ifuatavyo wa Singida. Kwanza namshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli alipokuja Itigi kufungua barabara ya Chaya-Tabora, aliwahaidi wachimbaji wote wadogo atamsimamia Shanta aweze kuwalipa fidia na nashukuru wamelipwa kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo Kamati ya Ulinzi na Usalama ilipeleka maombi kwa ajili ya wachimbaji wadogo ili wapatiwe leseni, wachimbaji hao walijiunga kwa makundi matatu ambao 1,000 wa Wilaya nzima ya Ikungi, ambao ni Dhahabu ni Mali, lakini Mang’oni Mining pamoja na Aminika na Serikali ilishapokea maombi hayo. Hivyo naomba kupatiwa majibu ya Kamati ya Ulinzi na Usalama inayoongozwa na Mheshimiwa Mtaturu ambaye ni DC wa Ikungi. Ni lini leseni zitapelekwa na wachimbaji hawa wakapewa maeneo yao, ahsate sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, vikundi vilivyoomba hivyo vitatu alivyovitaja Mheshimiwa Mbunge ni kwamba tayari wamekwishapewa maeneo ya kuchimba, mojawapo wakiwa ni Imarika, ni kikundi chenye watu 193 walipewa dola za kimarekani milioni 25 na waliweza kununua vifaa na walianza kazi za uchimbaji. Tatizo lililotokea ni kwamba sasa hivi waliingia kwenye madeni kwa sababu walikosa yaani utaratibu mzuri wa kuweza manage pesa zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Wizara tunataka sasa hivi wachimbaji wote wadogo tumejipanga tutawapa maeneo mengi kwa mfano pale Muhintili tutawapa leseni zaidi ya mia moja na sabini na kitu. Hizo leseni tutawapa, lakini vilevile kama Wizara tunataka kuendelea kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo waweze kuchimba kwa faida waweze kuchimba vizuri na waweze ku-manage fedha zao vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutafanya hivi kwa sababu tumegundua kuna tatizo kubwa la wachimbaji wanapopata fedha nyingi wanakosa ule ujuzi wa kuweza kumiliki zile fedha. Hiyo inawafanya waende kutumia vibaya na waweze kuingia kwenye umaskini tena. Hivyo tumejipanga tutatoa elimu vizuri na tutahakikisha kwamba wachimbaji wetu wanachimba kwa tija.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Napenda kumueleza Mheshimiwa Waziri kuna bwawa katika Kata ya Urugu, Wilaya ya Iramba ambalo limekuwa na manufaa makubwa sana kwa muda mrefu kwa wananchi wanaoishi kwenye kata ile lakini sasa hivi linaelekea kupotea kwa sababu tope linajaa. Je, ni lini Serikali sasa itakwenda kusaidia wananchi wale ili tope lile liondolewe na shughuli zile ziendelee?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mama yangu Mheshimiwa Martha Mlata kwa jinsi ambavyo anashughulikia Mkoa wa Singida kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nilielekeza Idara yangu ya Umwagiliaji watengeneze teknolojia ya kuhakikisha kwamba inaondoa matope kwenye mabwawa kwa sababu mabwawa mengi yamejaa tope na leo wanakuja kunipa taarifa. Nipongeze sana Mkoa wa Singida, katika mikoa ambayo imeyatunza mabwawa na mifugo inapata maji kwa zaidi ya asilimia 60 ni Mkoa wa Singida. Kwa hiyo, Mheshimiwa Martha Mlata nalifanyia kazi, teknolojia ikishapatikana tunataka tuyaokoe mabwawa yote.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Spika, ahsante na ubarikiwe kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Spika, tunaposubiri ujenzi wa barabara kutoka Handeni - Singida na Waziri amezungumzia ubora wa barabara ile tukitambua kuna milima na mabonde. Nini kauli ya Serikali kuhusu ubora wa barabara ya kutoka Sekenke - Shelui ambayo imekuwa ikiua watu takribani kila mwezi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, kwanza nikupongeze sana Mheshimiwa Martha Mlata kwa kufuatilia barabara za Singida na kila wakati tumezungumza ndani na nje ya Bunge, unafuatilia sana hizi barabara.
Mheshimiwa Spika, nimuahidi tu Mheshimiwa Martha na watumiaji wa barabara hii wakiwemo wananchi wa Singida kwamba tumeiona barabara hii. Barabara hii hatutaitazama upande wa Sekenke tu, tutaitazama kutoka Singida Mjini tunakwenda mpaka Misigiri tunashuka Sekenke. Tumetenga fedha ya kuweza kufanya usanifu wa barabara hii kwa sababu imekuwa ni ya muda mrefu na imechakaa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Singida na Watanzania kwa ujumla kwamba sasa hivi tunakwenda na teknolojia mpya kwa barabara hiyo kama unavyoona kwa ile miteremko ile lami inakimbia. Kwa hiyo, tutaiangalia ili tuitengeneze kiasi kwamba ubora wake uwe mkubwa zaidi na watumiaji wa barabara watumie vizuri na pia kupunguza ajali ambazo zimekuwa zikitokea mara kwa mara. (Makofi)
MHE. MARTH M. MLATA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa kuwa hivi karibuni Serikali imewaondoa madereva wengi ambao ni wazoefu kwa sababu wao ni darasa la saba na kuwaajiri vijana wadogo kwa sababu wao wana-qualify ama kidato cha nne na kuendelea, lakini bila uzoefu na tumeshuhudia sasa ajali zimeanza kuwamaliza viongozi wetu. Serikali haioni sasa hilo ni bomu kubwa sana inatengeneza kwa ajira za vijana ambao hawana uzoefu kwa kuwamaliza watu? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana dada yangu Mheshimiwa Martha Mlata kwa swali nzuri na swali lenye mantiki. Nachoweza kusema tu ni kwamba Idara yetu ya Usalama Barabarani itaendelea kufuatilia masuala ya uzoefu kuhusu uendeshaji wa vyombo hivi vya moto. Hata kwenye swali la msingi tulipotoka kwenye upande wa bodaboda ndivyo vitu ambavyo tumeendelea kuwasisitizia kwamba mtu anajifunza ndani ya robo saa na baada ya hapo anabeba watu watatu kwenye pikipiki yake. Kwa maana hiyo hata upande wa magari tutaendelea kuongea na wenzetu kwa upande wa magari haya ya Serikali ambayo ameyaongelea, waweze kuzingatia suala la uzoefu wa anayeendesha gari hiyo pamoja na mwendo ambao anatakiwa kuendesha gari hiyo.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa Mikoa ya Singida, Simiyu, Tabora na Shinyanga pia ina vivutio vyake; ukienda utakutana na akina Mtemi Chenge, Chifu Mayenga, Mtemi Gerege na wengine wengi.
Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kutembea mikoa hiyo ili tumwonyeshe vivutio hivyo aweze kuviingiza kwenye ramani ya utalii kwenye mikoa hiyo? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa katika mikoa yote aliyoitaja ina vitu vingi na ina historia ndefu ya utamaduni wa Mtanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie kwamba nipo tayari wakati wowote kuongozana kwenda kutembelea mikoa hiyo na nitaomba wakati naenda tuongozane naye ili kusudi aweze kunionesha maeneo yote hayo na Serikali iweze kuyachukua na kuyatangaza ipasavyo. (Makofi)
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pia nashukuru kwa majibu mazuri sana ya Naibu Waziri na naipongeza Serikali kwa sababu imeendelea kuimarisha sana Sekta hii ya Sanaa, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa sasa Serikali inatambua umuhimu wa vijana kujiajiri kupitia sanaa; je, haioni sasa umefika wakati muafaka kuboresha vitengo vya Maafisa Utamaduni ambao kwa sasa hawana vitendea kazi. Ili waweze kuwapatia magari na fedha kwa ajili ya kuwafikia vijana hasa walioko vijijini na wenye vipaji?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa vijana wengi sasa wamejitokeza kuonesha ufundi stadi wao katika sanaa mbalimbali, lakini kuna uharamia mkubwa sana katika mitandao, kuna fedha nyingi zimebaki kule. Je, Serikali haioni sasa umefika wakati muafaka wa kurasimisha zile kompyuta ambazo zinatumika kuuza miziki ya Wasanii, ili Serikali yenyewe ipate mapato, lakini na Vijana waweze kupata mapato kupitia mitandao hiyo? Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa napenda kumpongeza kwa sababu amekuwa ni mpambanaji mkubwa sana ndani ya Bunge ya masuala yote ambayo yanahusu Sanaa pamoja na Wasanii.
Mheshimiwa Spika, sasa nikija katika swali lake ambalo ametaka kujua Serikali ina mpango gani katika kuboresha maslahi ya Maafisa Utamaduni Nchini. Nikiri kwamba sisi kama Serikali tunatambua kwamba, Maafisa Utamaduni nchini kote wanafanya kazi kwenye mazingira magumu. Hata hivyo, kwa sababu tunatambua pia kwamba sisi kama Wizara ya Habari, Maafisa Utamaduni wako kwenye Wizara ya Habari Kisera, lakini kiutendaji wanawajibika chini ya Wizara ya TAMISEMI.
Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kumuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba, Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya TAMISEMI, tutaendelea kushirikiana kuhakikisha kwamba tunaboresha, mazingira ya Maafisa Utamaduni nchini. Kama haitoshi nimhakikishie kwamba kwa sasa hivi, Wizara ipo katika hatua za mwisho kabisa za kuhuisha na kuboresha ile Sera yetu ya Utamaduni ya mwaka 1997 ili basi iweze kuendena na mazingira ya sasa.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili, ameuliza kuhusiana na kurasimisha kompyuta ili kuweza kutunza haki za Wasanii. Mheshimiwa Mbunge nimhakikishie kwamba, tunatambua kabisa kwamba kumekuwa na changamoto kubwa sana ya wizi wa kazi za sanaa. Sisi kama Serikali zipo jitihada mbalimbali ambazo tumezichukua katika kukabiliana na uharamia huo wa kazi za sanaa nchini. Si tu katika kurasimisha kompyuta, lakini kuna jitihada mbalimbali mojawapo ikiwa ni kutoa elimu kwa Wasanii wetu ili waweze kujua ni namna gani ya kuweza kuhifadhi kazi zao, lakini vile vile waweze kusimamia haki zao, kwa sababu changamoto kubwa imekuwa ni wao wanaingia mikataba ambayo haizingatii maslahi yao.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo kama Wizara tumefanya, ni kuhakikisha kwamba, sasa hivi tumeunda Kamati ambayo inapitia Mikataba yote ya Wasanii. Ni hivi juzi tu tumeshuhudia Waziri wangu Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe akilivalia njuga suala la Mzee Majuto kudhulumiwa haki yake na nimhakikishie kwamba kwa sasa hivi tumefika kwenye hatua nzuri. Kwa hiyo, tunaamini kabisa kwamba Kamati hiyo itakapokamilisha kupitia hiyo mikataba yote ya Wasanii nchini, Wasanii wataweza kunufaika na kazi zao.
Mheshimiwa Spika, kama haitoshi mwisho kabisa kwa sasa hivi, Wizara tuko katika kwenye mazungumzo na wenzetu wa Wizara ya Viwanda ili basi ile Idara ya COSOTA iweze kurudishwa kwenye Wizara ya Habari, Sanaa na Utamaduni.
Ili basi matatizo yote ambayo yanawahusu Wasanii yaweze kushughulikiwa na Wizara Moja. Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Tarafa ya Ilongero iliyopo Wilaya ya Singida Vijijini ambayo iko kwenye bonde la ufa haijawahi kupata umeme tangu REA I na II na ya sasa imeanza kutekelezwa. Kuna Kituo cha Afya ambacho hawawezi kutoa huduma kwa sababu hakuna umeme. Je, ni lini sasa Serikali itawapatia umeme wananchi wale au Waziri aongozane tu nami twende kwenye Tarafa ile akashuhudie ili aweze kuwahimiza wakandarasi waweze kukamilisha umeme katika bonde lile? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mlata, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa natambua kwamba Kata ya Ilongero iko kwenye mpango wa upelekaji umeme katika awamu inayoendelea. Hivi sasa mkandarasi ameshakaribia maeneo yale, ametoka Marendi kwa Mheshimiwa Mwigulu na wiki ijayo atakwenda Ilongero ambapo kuna Kituo cha Afya. Kwa hiyo, nimpe uhakika Mheshimiwa Mlata kwamba atafika kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuongezana na Mheshimiwa Mlata, mimi sina wasiwasi, kama kawaida yangu nitaambatana na Mheshimiwa Mlata tukatatue kero za wananchi. Ahsante sana.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kupigania afya yangu, sasa hivi naendelea vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kumekuwa na upotoshwaji mkubwa sana kwa watu wasioitakia mema nchi hii, wamekuwa wakiweka dosari ambazo hazipo kwenye suala hili la uchaguzi. Je, Serikali imejipangaje kuwaelimisha zaidi Watanzania ukweli ambao wamekuwa wakifanya hivyo na uchaguzi umekuwa ni huru na ndio maana wapinzani ni wengi ndani ya Bunge, Madiwani, Wenyeviti na kadhalika. Mmejipangaje kuwaelimisha Watanzania hawa wanaopenda amani katika nchi yao? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, kwanza nampongeza na kumpa pole sana kwa kupata shida ya afya na Mungu amemjalia na aendelee kuimarika Mbunge mwenzetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni swali muhimu sana, nasema ni muhimu kwa sababu ni kweli kwamba hata swali la msingi la leo utaona ni swali ambalo limejaa tu hofu bila sababu yoyote ile kwa sababu uchaguzi wa Serikali za Mitaa si kwamba unaanza kufanyika kwa mara ya kwanza Tanzania leo mwaka huu, ni uchaguzi ambao tumefanya awamu kadhaa huko nyuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na bahati nzuri niliyesimama hapa pia nimekuwa Mwenyekiti wa Serikali za Mitaa kupitia chama cha upinzani CHADEMA kama ingekuwa uchaguzi sio huru mwenyewe mwaka 2014 nisingekuwa Mwenyekiti wa Serikali za Mitaa pale Kivule, nilishinda uchaguzi na nikawa Mwenyekiti wa Mtaa kupitia chao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili; uchaguzi wa nchi hii ni huru, nilikuwa Mbunge kupitia CHADEMA, nilishinda kwa kanuni hizihizi na Katiba hiihii iliyopo na leo nimesimama mbele yako kama Mbunge kupitia Chama cha Mapinduzi. Hii yenyewe inaonesha kwamba uchaguzi wa Tanzania ni huru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye Serikali za Mitaa, mchakato wa uchaguzi huu kanuni zimeandaliwa na wadau waliitwa wakatoa maoni yao, tukachakata na wataalam wakashauri kanuni hii hapa imeshatolewa na Mheshimiwa Waziri wa Nchi ameshatoa nakala hizi kwa Wakuu wa Mikoa wote na vyama vya siasa wanazo hizi kanuni. Hakuna mtu ambaye amekuja mbele ya Watanzania akakosoa kifungu chochote kwenye kanuni kwamba kimekinzana na Katiba kina mapungufu, wamepokea na wameridhia, tunaendelea na mchakato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeenda mbali zaidi, tumetoa mwongozo kwa wapiga kura, hapa inaeleza nani ana sifa za kugombea, mchakato ndani ya chama namna mbalimbali za michakato na usimamizi na imetaja nani anapaswa kusimamia uchaguzi na imewakataa mpaka Watendaji wa Kata ukisoma vizuri. Kwa hiyo, nitashangaa sana watu ambao wanakuja hapa wana hofu ya Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tarafa, Watendaji na watumishi wa Serikali lakini kanuni imeeleza ni nani ambaye anapasa kusimamia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitabu cha tatu ambacho kimetolewa ni Mwongozo kwa Mpiga Kura na kanuni imeeleza kama mtu yeyote ama asasi za kiraia anataka kutoa elimu ya uraia, kuchunguza ndani na nje kanuni imetoa mwongozo kuna utaratibu wa kufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme kwamba Serikali imejipanga vizuri sana kuendesha uchaguzi wa Serikali za Mitaa na utasimamiwa na Waziri mwenye dhamana na Watanzania wapo tayari sana kufanya uchaguzi huru na haki, wapate viongozi wao, wazingatie maelekezo ya Serikali ili tupate viongozi ambao watatuwakilisha. Wananchi wasiwe na hofu, uchaguzi utasimamiwa na vyombo vipo na kama kuna mtu yeyote ambaye ana jambo lolote ambalo anadhani kwamba linataka maelezo, Ofisi ya Rais – TAMISEMI ipo wazi, tunawakaribisha tupate maoni tujadiliane kwa maana ya kuboresha,

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwanza naomba nishukuru sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuweza kukamilisha daraja la Sibiti na hiyo ni kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Singida pamoja na Simiyu kwa thamani ya daraja lile nilikuwa naomba nimuulize mheshimiwa Naibu Waziri, ili tuweze kuwa na dhamani ya daraja lile ni ujenzi wa Barabara ya lami unaotoka Iguguno, Nduguti, kupita Sibiti, Meatu na kuendelea mpaka Bunda ili wananchi wale waweze kufanya shughuli za maendeleo. Je, ni lini Serikali itaanza Ujenzi huo kama ilivyoahidi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Mlata kwa sababu umekuwa umefuatilia barabara zote za Mkoa wa Singida na ninafahamu hata sasa tuna ujenzi mkubwa mwingine unaendelea katika daraja la Msingi ili tuweze kuwaunganisha wananchi wa Wilaya ile ya Kiomboi na waweze kupita nao Sibiti. Kwa hiyo, tunaendelea na ujenzi na ujenzi unaendelea vizuri, lakini niseme tu kwamba mkakati mkubwa wa kuiboresha barabara hii ambayo ni muhimu sana itapunguza pia wasafiri wanaokwenda Arusha, wanaokwenda Manyara, wanaokuja Singida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kukamilika daraja lile tunajenga kiwango cha lami kilometa 25 ili eneo lote la bonde hili ambalo lilikuwa na changamoto kubwa wananchi waweze kupita vizuri ujenzi ule unaendelea kilomita 25.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunakamilisha usanifu wa barabara hii muhimu ambayo inaunganisha mikoa ya Kanda ya Ziwa tukipita Sibiti tunakwenda Haydom tutakwenda Ndogobeshi, itakwenda hadi Mbulu itoke Karatu. Kwa hiyo, juhudi kubwa zinafanyika kuiboresha barabara hii muhimu na itawafanya wakazi wote wa Manyara wakazi wote wa Arusha waweze kupita barabara hii kwa sababu itapunguza zaidi kilomita mia mbili kwa mtu anayekwenda Mwanza, Simiyu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaendelea na kazi nzuri kubwa inafanyika, vuta subira na kwakweli ninashukuru sana kwa ushirikiano unaotoa Mheshimiwa Mbunge kwa kutupa information nyingi ili tuweze kuwaudumia wananchi wa Singida.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza naomba niipongeze Serikali kwa juhudi kubwa ambazo imefanya kwa kurejesha Vyama vya Ushirika. Hata hivyo, kumekuwa na malalamiko mengi sana kuhusu vyama hivi na matatizo yake ni mengi. Wakulima wanapokuwa wamepeleka mazao yao mara nyingine hawalipwi kwa wakati au fedha zao kupotea kabisa. Sasa nataka kuiuliza Serikali, je, itakuwa tayari yenyewe kama Serikali kuweza kufidia pale ambapo Vyama vya Ushirika vimeshindwa kuwalipa wakulima hawa fedha zao kwa wakati ama kuwafanya wakulima wapate bima zao za mazao ambazo zinakuwa ni kwa ajili ya majanga mbalimbali kama mafuriko, nzige, ukame na kadhalika, pamoja na kutokulipwa iwe ni kama janga mojawapo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Martha Mlata, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kuhusu suala la bima; wakati wa Nane Nane Serikali ilizindua Bima ya Mazao. Nitumie nafasi hii kuwahamasisha wakulima kuhakikisha kwamba wanajikatia insurance za mazao yao. Pamoja na hatua hiyo kama Serikali na Wizara tumeanza kupitia gharama za bima ya mazao na hivi karibuni tutakutana na insurance companies ambazo zinatoa bima katika sekta ya kilimo ili tuweze kukubaliana nao na kutengeneza road map itakayo-guide suala la insurance. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Ushirika, napenda tena kurudia kusema ndani ya Bunge hili Tukufu. Ushirika haununui mazao, wao ni conduit ya kumkutanisha mkulima na mnunuzi. Tunatumia Ushirika kama sehemu ambayo wakulima wadogo wadogo watapeleka mazao yao na watakuwa na bargaining power juu ya hatima ya mazao yao. Vilevile niseme pale ambapo Chama cha Ushirika kitashiriki katika ubadhirifu wa kumuibia mkulima, tutawachukulia hatua stahiki na kali kama ambavyo tumekuwa tukifanya. Navyoongea sasa hivi viongozi wa ushirika sehemu mbalimbali ambao wamekula fedha za wakulima wako magerezani na wamechukuliwa hatua na kupelekwa kwenye kesi za uhujumu uchumi. Hivi karibuni tumewaweka ndani viongozi wa Chama cha Chai cha MVYULU kilichopo Wilaya ya Lupemba ambao walikuwa wamejibinafsishia mali za wakulima ziwepo magari, mashamba na nyumba na tutaendelea kufanya namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaeleze Watanzania na Waheshimiwa Wabunge hatuwezi kukimbia changamoto. Ubadhirifu ulikuwepo hatuwezi kuua mfumo mzuri wa sekta ya kilimo kwa sababu ya viongozi wabadhirifu. Sisi kama Wizara tutasimamia kuhakikisha kwamba ushirika unakuwa safi na kuweza kufikia malengo ya Serikali. (Makofi)