Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Mariamu Nassoro Kisangi (52 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuzungumzia machache kuhusu hotuba ya Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, napenda nitoe pongezi kubwa sana kwa niaba ya Wabunge wenzangu kwa Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa nchi hii kwa kura nyingi za kishindo, mimi nampa hongera sana na Wabunge wenzangu wote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba uniruhusu niseme maneno yafuatayo kwa niaba ya Wabunge wenzangu kwa Chama changu cha Mapinduzi. Nakipongeza Chama cha Mapinduzi kwa kupata Wabunge 264 katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Haikuwa kazi ndogo, ilikuwa kazi kubwa kweli kweli, lakini ukweli umebaki ukwel, keki ya Bunge imeichukua Chama cha Mapinduzi imewaachia robo. Nakishukuru sana Chama cha Mapinduzi kamati zote za kampeni zilifanya kazi nzuri. (Makofi)
Naomba sasa nichukue fursa ya kipekee kuwashukuru wanawake wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kunichagua mimi nije niwawakilishe katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nawaahidi wanawake wa Dar es Salaam nitawafanyia kazi na sitawaangusha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nirudi kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais alitoa ahadi zake kwamba atakapopata Urais ataunda Baraza dogo la Mawaziri. Hili amelitimiza na ameunda Baraza la Mawaziri lenye Mawaziri 19 tu. Mheshimiwa Rais nampongeza kwa hilo. Pia ametuleta Mawaziri mahiri, wachapakazi ambao tuna imani nao kabisa wataivusha Serikali hii kutoka pale ilipo kuipeleka mbele na kukipatia ushindi au mwenendo mzuri Chama cha Mapinduzi na tuonyeshe kwamba sasa tunataka kutengeneza CCM yenye mabadiliko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la TBC. Kumekuwa na maneno mengi sana kuhusu TBC. Mheshimiwa Waziri ameeleza vizuri sana nini tatizo lakini bado maneno yanazungumzwa. Naomba niliambie Bunge mimi Dar es Salam nina tatizo kubwa la mfumuko wa bei ya vyakula. Wananchi wanahangaika, mchele unanunuliwa shilingi 2,500/= mpaka shilingi 2,800/=. Kama kweli kuna hali kama hiyo mtu mwenye njaa anaweza akangalia TV?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Serikali hili suala la TBC tuliangalie kama alivyozungumza Mheshimiwa Waziri kwamba yako matatizo. Kwa hiyo, haya matatizo ni jukumu letu sisi kama Wabunge kukaa chini na kuyatafakari. Hata hivyo, kuna umuhimu gani wa mimi kuonekana sasa hivi wakati sitafanya chochote Jimboni? Hivi kuongea kwangu kunawasaidia nini? Mimi naomba Serikali inisaidie kupunguza mfumuko wa bei jijini Dar es Salaam, vyakula vimekuwa bei juu sana, hilo mimi kwangu ndiyo naona changamoto. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuchukua zile fedha zote za sherehe ya Uhuru kuja kutujengea barabara ya Kawawa. Kwanza nasema kwa niaba ya Wabunge wale wa Majimbo waliopelekewa zile hela, Jimbo la Ubungo, Kinondoni pamoja na Kawe ambapo barabara ile ndipo ilipo, napenda nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutuletea zile fedha kuondoa msongamano wa magari barabarani.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba wananchi wa Dar es Salaam tunapotaka kufanya maamuzi tuhakikishe tunafanya maamuzi ya kweli kupata watu wa kututetea. Sisi kama Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Rais katupa hizo fedha ili barabara zetu zitengenezwe leo Mbunge wa Dar es Salaam unatoka nje wakati wa kuchangia hotuba ya Rais, hivi wewe ni kiongozi wa wananchi walio wengi au wa walio wachache?
Mimi naomba tuangalie sana nini tunakuja kuwafanyia wananchi ndani ya Bunge hili, tunakuja kuwasemea wananchi wetu tulete maendeleo. Leo mimi ningezungumza na mwenzangu wa Kawe, Ubungo nafikiri Mheshimiwa Rais angepata salamu zetu naye angeharakisha mradi huo. Nawaomba wananchi, CCM sasa ina mabadiliko na sisi tumejifunza, Wabunge tunakuja tukiwa wakali kwa lengo la kuwatetea wananchi wetu. Sasa kazi imeanza na tutafanya hivyo, hatukubali tena. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais, ukurasa wa 15, amesema tutajenga viwanda ili kukuza uchumi lakini pia kuleta ajira kwa vijana. Nimuombe Mheshimiwa Rais pamoja na yote tuangalie viwanda vilivyokufa na vinavyosuasua pia. Kuna viwanda vingi Dar es Salaam kama Aluminium Africa, Metal box, Bora Shoes, National Battery, Tanzania Cables, Mbagala Sheet Glass, Tanita Mbagala, National Milling, Tangold Africa, Urafiki-Ubungo, UFI-Ubungo, hivyo vyote ni viwanda ambavyo miaka hamsini iliyopita vilikuwa vikifanya kazi na leo vingine vimegeuzwa maghala.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia Kiwanda cha TANITA Mbagala kilikuwa kinawapatia ajira kina mama. Kiwanda cha Tanita ni cha korosho kilikuwa kinabeba akina mama leo kiwanda kile kimegeuzwa ghala sijui watu wanahifadhi madudu gani, takataka tupu mle ndani, hivi kweli tutafika kwa hali hii? Niiombe Serikali katika hii sera yetu ya kutaka kuvumbua viwanda hivi tuyaangalie na maeneo hayo ili wananchi na vijana wetu waweze kupata ajira.
Naomba sasa nizungumzie suala zima la elimu. Nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kusema kwamba elimu itatolewa bure kwa ngazi ya shule ya msingi na sekondari. Ninao mfano wa wazi kabisa katika Kata ya Charambe - Mbagala wameandikisha watoto 6,000 wa darasa la kwanza. Hii inaonyesha wazi kwamba kumbe watoto wengi walikuwa wako majumbani wanashindwa kupata kile kiasi cha fedha cha kuingilia shuleni. Kwa hiyo, nampongeza kabisa Mheshimiwa Rais kwa hili wazo lake ambalo amelitekeleza. Pia ziko changamoto kwenye hayo makundi au mchanganuo wa fedha zile na hasa katika fedha za utawala, naomba fungu kidogo liongezwe pale kwa sababu ya walinzi. Pia changamoto ndogo ndogo zinazowakuta walimu hata kupata sukari kilo moja kwa siku angalau na wao wanywe chai kwa asubuhi tu. Niombe sana Serikali hilo nalo liangaliwe. Awamu ya Rais Mkapa ilikuwa zinakuja fedha za capitation kama hizi kulikuwa na fungu la utawala.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaambie Watanzania hizi fedha zitategemea sana utendaji wa Mwalimu Mkuu. Mwalimu Mkuu aliye bora akizisimamia vizuri fedha hizi kwa kweli mambo yatakwenda vizuri. Maana naona yako matatizo yanaletewa Serikali kumbe ni ya ubinafsi wa mtu, amepelekewa fedha ameshindwa kuzitumia vile inavyotakiwa matokeo wazazi wanaleta maneno. Mimi ni mwalimu pia niwaombe walimu wenzangu waunge mkono hizi jitihada za Rais kwa kutumia mafungu hayo vizuri kama vile walivyoagizwa na siyo vinginevyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nichangie upande wa nishati. Hotuba ya Mheshimiwa Rais, ukurasa wa 6, imeeleza itaboresha na itaondoa kabisa matatizo ya kukatikakatika kwa umeme. Naona juhudi kubwa ya Mheshimiwa na nampongeza sana na mfano na sababu ya kumpongeza ninazo. Juzi nimepigiwa simu na watu wa Kigamboni eneo la Ungindoni wanasema haijawahi kutokea, wameomba umeme lakini wameletewa mita majumbani bila ya wenyewe kuwepo. Mita zimepelekwa, wenyewe hawajui, wamepewa namba za simu, mita wameikuta iko nyumbani jambo ambalo halikuwa la kawaida. (Makofi)
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niunge mkono hotuba hii ya Mheshimiwa Rais, nimwambie peleka zile fedha kwenye barabara ya Kawawa mara mvua itakapoisha na siku ya kufungua uniite. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nami kwanza nianze kumshukuru Mungu kwa kunipa uwezo wa kusimama kwenye Bunge lako Tukufu hili katika Bunge hili la Bajeti leo ikiwa mara yangu ya kwanza kusimama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru na kukupongeza sana kwa uendeshaji wako wa Bunge pia napenda nimshukuru Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, pongezi hizi nampa kwa yale yote aliyoyafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitembea nchi nzima kuitangaza Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020/2025, katika ukurasa wa 124 mpaka 141 wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi, Mheshimiwa Rais wetu ameitekeleza kwa vitendo. Ninasema hivyo katika ukurasa wa 31 wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi, kifungu cha 88 kuanzia kifungu kidogo (a) mpaka
(k) ameonesha Ilani ile kwamba kutafanyika ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya, ujenzi wa hospitali za Wilaya, ujenzi wa hospitali za Mikoa, ujenzi wa hospitali za Kanda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hayo yote Mheshimiwa Rais wetu ameyaweza. Pia ameeleza upatikanaji wa vifaatiba, kusafisha damu, dialysis, CT scan, MRI. Hivyo vyote vitafanyika katika sekta ya afya na hayo Mheshimiwa Rais ameyatekeleza kwa vitendo. Pia ameeleza katika ilani hiyo hiyo kuongeza watumishi katika kada ya afya. Hilo linaendelea kutekelezwa lakini limeanza kutekelezeka kwa hayo yote pia amesema matibabu ya kibingwa yapatikane ya figo, moyo, uzazi (kupandikiza uzazi). Hayo yote ndugu zangu yanatekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakina mama tulikuwa na changamoto kubwa ya uzazi kuita ugumba, sasa hivi uzazi unapandikizwa katika hospitali zetu za Dar es Salaam za Tanzania, wanapandikiza uzazi kwa akina mama na tunaweza kupata watoto na jambo la ugumba sasa limeondoka. Hayo yote ni makubwa ambapo ameyafanya Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hayo anayoyafanya kwa kweli tunastahili tumpongeze na tunampongeza sana sana sana kwa sababu ameweza yale aliyoyataka kuyatekeleza, ameyasimamia na yametekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizo napenda sasa nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu wake Waziri, kwa kazi kubwa anayoifanya. Ni Waziri mahiri na Naibu Waziri mahiri wana ushirikiano mzuri kwa kweli tunashukuru. Pia watenda kazi Waheshimiwa Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu na Watendaji wote wa Wizara hii kwa pamoja wanafanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nirudi katika mchango wangu. Mchango wangu nitaanza na Hospitali ya Muhimbili. Kwa kweli mambo mazuri yanafanyika katika Hospitali ya Muhimbili na niipongeze sana Serikali. Nilisimama hapa kuomba wodi ya wagonjwa wa akili Muhimbili kwamba imeachwa ikiwa chakavu, chafu haijapata urekebisho. Hivi ninavyokwambia, wodi imekarabatiwa vizuri bado sehemu chache. Kwa maana hiyo Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi ni sikivu, inachukua maoni yetu na inayafanyia kazi. Wodi ile iko vizuri bado asilimia kama 20 tu kukamilika kabisa. Hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia katika Mfumo mzima wa matibabu. Katika Hospitali ya Muhimbili kumekuwa na mabadiliko na mageuzi makubwa. Mimi nikiwa nje alikuja binti kuniambia amesema mimi nimelazwa pale Muhimbili lakini nilipotoka mama nakwambia angalia baada ya miaka miwili tutazungumza mengine Muhimbili tutakuwa kama India labda. Baada ya miaka miwili mambo niliyoyaona ndani, ananiambia binti tu kama wa miaka 28 umeona nini ananiambia mama siyo ile Muhimbili unayoijua wewe. Muhimbili imebadilika, ina mambo mazuri, ina matibabu mazuri. Kwa hiyo, mimi nalipongeza na wananchi wanapongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi hizo iko changamoto Muhimbili. Changamoto ni wananchi wanaoenda kuangalia wagonjwa bado hawajapata sehemu sahihi ya utulivu. Kule kunakuwa na wagonjwa wengine mahututi hawajiwezi. Mgonjwa wako akiwa mahututi huwezi kuwa na akili ya kukaa nyumbani, kwa vyovyote utakuwa mazingira yale yale unasubiri. Sasa pale unaposubiri inakuwa tatizo. Niiombe Serikali itenge eneo maalum, wale watu wanaosubiri wagonjwa wao wakae huko, wakisubiri wagonjwa wao baada ya masaa matatu manne kwenda kuwaona. Kwa kawaida sisi Waafrika tunafarijika zaidi unapougua ukimuona ndugu yako wa karibu. Utapewa matibabu ya kila aina, utapewa kila huduma na Nesi lakini ukimuona ndugu yako wa karibu unafarijika zaidi. Hivyo hilo nalo tulizingatie kwa sababu wale wagonjwa wanakuwa wanahitaji counsel na kuwa-counsel kwa kwanza kumpa mtu ambaye anampenda ili aweze kupata nafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia naipongeza kuna wodi maalum ya wazazi ambayo imeanza kuzingatia, wao wanakwenda na wenza wao na watu wa kuwahudumia, iko pale Muhimbili hapa jirani na kanisani hapa, kuna wodi nzuri tu ya wazazi lakini bado ni ya kulipia, tumeanza ninayo imani huko tunakoenda tutaangalia mifumo hiyo, kwa sababu hata tunapoenda kwenye nchi za wenzetu mgonjwa amelala pale lakini hapa kunakuwa na kochi la muuguzaji anamuangalia mgonjwa wake. Najua tulikotoka ni mbali na tunakoenda ni mbali. Hapa tulikofika siyo haba, tunamshukuru Mungu kwa yote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sasa nizungumzie Taasisi ya Afya ya Ocean Road ya kansa. Taasisi ile imekuwa na ongezeko kubwa la wagonjwa siku hadi siku, imekuwa na changamoto kubwa ya ucheleweshaji wa vifaa vya matibabu kutokana na taratibu za kikodi. Sasa niiombe Serikali kuwa ile taasisi inategemewa na watu wengi na tunaona wakina mama ndiyo wanaongoza kwenye kuwepo pale wagonjwa wa kansa ya kizazi, lakini pia zaidi siyo kina mama hata akina baba kansa ya tezi dume inazidi kushamiri ukienda unawakuta wengi tu pale wana matatizo hayo. Sasa vifaa vile tunavihitaji kwa afya, inakuwaje tena kunakuwa na tatizo la kikodi?

Mheshimiwa Spika, Serikali iweke mifumo sahihi na iliyo wazi. Leo tunakwenda kununua wenyewe kwa fedha zetu za Tanzania, tunaenda kununua vifaa nje tulete kwenye hospitali yetu ya Ocean Road vinakwama, je, Mfadhili akitaka kutuletea vifaa ndiyo vitaingiaje kama sisi wenyewe vina kwama kwa matatizo ya kikodi. Naomba hilo mliangalie Serikali na Wizara ya Fedha tunavihitaji, tatizo la kansa ni kubwa watu wanahitaji huduma hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nije kwenye hospitali ya Mloganzila, kwa kweli tunashukuru sana hospitali ipo nzuri lakini nayo changamoto yake kubwa ni gharama za matibabu. Wagonjwa, mtu anaumwa akiulizwa unanipeleka wapi? Mlaganzila, aah! naenda kufa mama, nini? Watoto wangu wataweza hizo bili? Eeh! Ile hospitali hivi mfumo wake hasa wa bill ukoje? Mbona watu wanashindwa kuelewa? Kwa sababu mwisho wa yote mtu yule anaugua, anakufa, maiti inakwama, Mbunge hukai Bungeni, unahangaika, unateseka, unaambiwa ukamkopeshe mtu hela za kwenda maiti, nazipata wapi ghafla shilingi milioni saba, nane? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaiomba Serikali siyo Mloganzila tu, Muhimbili, Mloganzila ituwekee mpango sahihi juu ya hizi tiba, watu wanakwama, kila ukienda yaani mpaka tunaogopa, ukifika Muhimbili tu ukienda maeneo ya watu wengi utakumbana na tatizo hilo. Ukiwa Bungeni utakumbana na simu hizo. Kweli tunakwenda pale, wengine tunawaelezea lakini wako watu ambao hamjui hata Mbunge wake, hivi huyu anatokaje?

Mheshimiwa Spika, ninaiomba Serikali iweke utaratibu mzuri utakaoeleweka, kwamba huyu mtu ana uwezo na ikiwezekana mtu aambiwe mapema, umeingia hapa kwenye wodi hii itakubidi ufanye hivi, uweke advance hii ili hapa ukitoka tena isiwe tatizo. Ninaona Mheshimiwa Waziri unatoa taarifa, unajitahidi kutoa taarifa, jamani maiti isizuiwe lakini inafika sehemu hali ni ile ile. Sasa hii kitu sisi kama wananchi tunafanyaje kutoka hapo?

Mheshimiwa Spika, sasa nije kwenye suala zima la afya ya mama na mtoto. Mimi niombe Serikali…

SPIKA: Dakika moja malizia kengele imeshagonga ya pili.

MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, namalizia mchango wangu. Naiomba Serikali iangalie huduma ya afya ya mama na mtoto iwe bure, bure ya kweli. Mama kliniki afanye bure, kwa sababu hata wanaoenda na bima unachajiwa. Sasa kwa nini na sisi tunataka afya ya mama na mtoto iwe bure kwa wote?

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja asilimia mia moja. Sababu ya kuunga mkono hoja ni kutokana na mipango mizuri ya Serikali kwa wananchi wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo la uwajibikaji na maadili ndani ya Serikali, naipongeza Serikali kwa jinsi inavyorejesha nidhamu ya utumishi wa umma. Mheshimiwa Rais na Waziri Mkuu wameonesha kipaumbele chao cha kupambana na mafisadi kwa kuwatoa kazini na kufanyiwa uchunguzi ambao umewezesha wengine kufikishwa Mahakamani, naipongeza sana hatua hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la ukuzaji wa uchumi kupitia mpango wa kufanya mapinduzi ya viwanda, naiomba Serikali pamoja na kuanzisha viwanda vipya, tuangalie na viwanda vyetu vilivyokuwepo zamani, viwanda vifuatavyo tuviangalie kwa umuhimu wake katika Jiji la Dar es Salaam:-
(i) Kiwanda cha Kubangua Korosho cha Mbagala - TANITA
(ii) Bora Shoes
(iii) UFI
(iv) Tanzania Cables
(v) Aluminium Africa
(vi) Metal Box
(vii) Metal Product
(viii) Urafiki Textile
(ix) Banda la Ngozi na viwanda vingine vingi ambavyo kwa sasa hakuna uzalishaji unaoendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu huduma za afya, naiomba Serikali iondoe dhana ya wagonjwa au majeruhi wanaopata ajali kupitia katika Hospitali ya Mkoa badala ya kupelekwa moja kwa moja Muhimbili. Nasema hivyo kutokana na ukosefu wa vifaatiba katika Hospitali za Temeke, Amana na Mwananyamala. Wagonjwa wanaopata ajali mara zote wanapoteza fahamu katika Hospitali za Mikoa na wanafika Muhimbili wakiwa mahututi au wamekufa kabisa. Naiomba Serikali yangu sikivu ibadili utaratibu huu usiwe wa lazima sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mazingira wezeshi; nashukuru Serikali kwa kuwaandalia vijana na akinamama, naipongeza Serikali kwa kuweka bajeti ya shilingi milioni 50 kwa kila Mtaa na Kijiji. Naiomba Serikali iweke mkazo wa kupeleka fedha maeneo yenye ujasiriamali. Maeneo yenye wingi wa vijana na wanawake ni pamoja na Mbagala, Mtoni, Tandika, Gongo la Mboto, Buguruni, Kariakoo, Ilala, Manzese, Mwenge, Kijitonyama, Tegeta, Ubungo, Bunju na Kibamba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo hayo yana wingi wa wananchi ambao wanahitaji kupata mitaji, naiomba Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kuangalia maeneo hayo kwa jicho la upekee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kazi na hifadhi ya jamii, napongeza Wizara na Mheshimiwa Waziri wa Kazi, Mheshimiwa Jenista Mhagama, kwa jinsi alivyoendesha zoezi la kuwatoa wageni walioajiriwa nchini bila vibali, jambo alilolifanya ni kubwa na limesaidia sana. Naomba zoezi hili liwe endelevu kwa maslahi ya wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti,naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayofanya ya kupangua safu ya Viongozi wenye kuingizia Serikali hasara.
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu na Waziri wa Utawala Bora na Katibu Mkuu wa Wizara kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhakikisha katika Ofisi za Serikali kumekuwa na nidhamu ya kazi. Nidhamu ya kazi imerejea kwa wananchi katika upande wa kuwahi kazini na kupunguza utoro wa kazi kwa kiasi kikubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa kuendesha zoezi la watumishi hewa kwa uelevu wa hali ya juu. Nimekuwa nikiona jinsi mnavyotoa maelekezo kwa Ma-DC, Wakurugenzi na Maafisa Utumishi kuzingatia masharti ya Utumishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mafunzo kazini; ni vyema Serikali ikatenga fungu la Semina Elekezi kwa Viongozi/Wafanyakazi wanaopewa nafasi mbalimbali kwa kuwa semina hizo zitawasaidia Watendaji au Viongozi kutekeleza majukumu yao kwa njia sahihi na kwa uhakika zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uzoefu wa kazi kwa vijana wanaoomba ajira mpya; kipengele hiki ni kigumu sana kwa vijana wetu wanaotoka Vyuoni. Kwa nini wale wanaoenda kwenye Ualimu, Udaktari, Uuguzi, hawaambiwi uzoefu wa kazi na wale wanaoajiriwa kwenye Taasisi za Serikali hata kama ni Daktari anatoka Chuoni anaambiwa awe na uzoefu wa kazi tena?
Mheshimiwa Naibu Spika, elimu ya kutoa na kupokea rushwa bado inahitajika kwenye jamii. Kuna baadhi ya Shule za Sekondari zina Club za rushwa. Je, TAKUKURU wanazijua hizo na kuzifuatilia? Ni vyema TAKUKURU wakae na Wizara ya Elimu kuweka suala zima la rushwa katika mtaala wa masomo. Tukilea watoto wetu kwa maono ya kuogopa kutoa au kupokea rushwa, hiyo inaweza kusaidia kuondokana na rushwa katika Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imefanya jambo jema kuondoa au kupunguza matatizo katika kaya maskini kupitia TASAF. Naipongeza Serikali kwa kuwa fedha hizi zimewasaidia sana wananchi wetu kusomesha watoto na kuwasaidia kupeleka watoto Kliniki kupima afya zao. Katika Mkoa wa Dar es Salaam wako wananchi ambao hawakupata nafasi ya kuingia kwenye mpango au kwa uwoga au kwa madhumuni mengine, lakini sasa wako tayari kujiunga. Naomba Serikali iwapokee.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna baadhi ya viongozi wetu wa Serikali za Mtaa ndio wanapotosha watu wa TASAF. Wao waende kwa malengo yao, wasivurugwe na Wanasiasa kwa interest zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba TASAF wasaidie wale wenye UKIMWI, ikiwa ameamua kujiweka wazi pamoja na watoto wenye maambukizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kwenye hotuba hii ya bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda nimpongeze Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoifanya. Anafanya kazi kubwa sana mama yetu. Tunampongeza na kumtia moyo. Tunajua kwenye uongozi kuna changamoto nyingi sana, yako mengi yanazungumzwa, mikataba kuingia hakuanza yeye walianza wengi, lakini maneno yanakuwa mengi. Mimi ninamtia moyo Mheshimiwa Rais aendelee kwa nia yake nzuri ya kutaka kuiopeleka Tanzania mahali pazuri, basi aendelee kufanya kazi na Mungu azidi kumbariki na kumpa afya njema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninawapongeza Waheshimiwa Mawaziri wote kwenye bajeti zao, Waheshimiwa Manaibu Waziri, Makatibu Wakuu wote kwa utendaji wao mzuri mpaka leo hii tunafikia mwisho wa bajeti yetu hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee napenda nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa jinsi alivyoli – handle suala zima la Kariakoo. Nitakuwa mkosefu wa fadhila mimi Mbunge ambaye natoka Kariakoo. Kwa kweli amefanya kazi kubwa na niiombe Serikali yale madai yao wayaangalie kwa sababu miongoni mwa wafanyabiashara wa Karikakoo wengi ni wakinamama. Kwa hivyo, niwaombe muangalie akinamama wale jinsi gani wanaweza kusaidiwa ili kuondoa kero ile, wafanye biashara zao. Wana mikopo na mambo mengi tu lakini niiombe Serikali na nina imani Serikali hii sikivu itayatekeleza yale waliyoyasema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye bajeti hii mchango wangu utajikita katika ukurasa wa 21, 19, 12, 23, 34, 25 na 26 kama muda utaniruhusu, hivyo nitaelekea kwenye miundombinu maji, kilimo, uvuvi na nishati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na upande wa miundombinu napenda kuishukuru Serikali, kwa kweli hali ya Mkoa wa Dar es Salaam kwa upande wa madaraja tumefanyiwa mambo mazuri. Tuna daraja Tanzanite, tuna daraja la Kijazi Interchange, kuna TAZARA, kuna Chang’ombe VETA, kuna Kurasini pale Uhasibu kulikuwa na kero kubwa sana. Magari yalikuwa yanajaa pale Kurasini, sasa hivi tumepata daraja, magari yanakwenda na yanaenda vizuri na tunapata muda wa kwenda kufanya shughuli za kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna madaraja mengine madogo tumejengewa, pale kutoka Bendera Tatu kwenda Gerezani, kuna watu hawakutarajia kama lile jambo linaweza kuwa, ukilinganisha na ile miundombinu ya reli pale chini, watu hawakutarajia. Leo hii pale ukienda utasema siyo Dar es Salaam hii ambayo tumeizoea, huwezi kujua kama hapa ni Keko. Ni jambo la kumshukluru Mungu na tunaishukuru sana Serikali na Mheshimiwa Rais wetu. Miradi ile mingi iliachwa katika awamu iliyopita lakini imeenda kwa kasi katika awamu hii, pia kuna miundombinu ya mwendokasi ya kutoka Mbagala mpaka Gerezani. Hiyo imekamilika tunashukuru sana lakini miundombinu ya kutoka Gerezani tena pia mpaka Gongo la Mboto nao watu wako site, wafanyakazi wako site na kazi inaendelea. Tunapongeza kwa hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kuna changamoto kubwa. Mkoa wa Dar es Salaam hatulimi, tunachotaka kwetu ni barabara. Tunaomba Serikali mradi wa DMDP pamoja na kuzungumza juhudi zako Mheshimiwa Waziri tunaziona hongera sana, tunakaa na wewe, tunakaa na Wizara mbalimbali miundombinu kujua hilo, lakini tunaomba DMDP tu, ije Dar es Salaam. Nasema hivyo kwa sababu Dar es Salaam kama Mji tuna miji yetu. Kwenye Wilaya ya Kinondoni sehemu kama Hananasif - Kinondoni, Kinondoni - Shamba, Mwananyamala, Kijitonyama, Mwenge maeneo yale kwa sasa hayapaswi kuwa na barabara za vumbi, yale ndiyo maeneo yetu ya kujidai katika Mkoa wa Dar es Salaam, kwa hiyo, tunomba Serikali iangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la Ilala Kata ya Mchikichini, Kata hii bado iko katika Wilaya ya Ilala na iko mjini sana, lakini ukiingia kule ndani vumbi tupu. Kwa hiyo, tunaomba sana mradi huu wa DMDP uje ili tuboreshe. Kwenye Jimbo la Segerea, maeneo ya Buguruni, Segerea yenyewe na Kata ya Tabata. Haya ni maeneo ambayo ya kwetu kweli ni maeneo ambayo yana uwekezaji mkubwa na watu wana shughuli kubwa za kiuchumi tunaomba tupate lami. Ukonga yenyewe, maeneo ya Ukonga Kata ya Ukonga pale Magereza, bado ukiingia humo ndani tafrani, hakujatimia, kuna barabara ile moja inayoenda markasi sijaona barabara nyingine, ninaomba Wilaya ya Ukonga nayo pia ipatiwe barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mbagala Rangi Tatu ndiyo center ya Mbagala isipokuwa ukiingia ndani Mbgala kwenye ile Kata ya Kibondemaji ni huruma, hakuna barabara ya lami. Tunaomba tuletewe barabara ya lami kutoka Mbagala Shule ya Rangi Tatu kuelekea Kwa Ndunguru kule bondeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sasa niende kwenye suala zima la nishati. Nimeona Serikali jinsi gani imeweza kuwapatia wananchi wake majiko na kuhamasisha watu kutumia mitungi ya gesi. Lakini mimi niombe kwa vile gesi asilia imeshakuja katika Mkoa wa Dar es Salaam, maeneo ya Mikocheni tayari inatumika, wameshuka mpaka Msasani, niiombe Serikali wawekeze katika gesi asilia. Gesi ile ishuike mpaka Tandale, ishuke iende Manzese, ishuke iende Ubungo, ishuke iende Temeke, ishuke iende Mbagala, ishuke iende Ukonga, ishuke iende Segerea, gesi ishuke iende maeneo ya Buguruni ambako kuna wananchi wengi Watanzania ambao wanaweza wakatumia na hali zao ni ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kama gesi ile mtu ukiwekewa ndani kwa mwezi unaweza ukalipa 10,000 tu kama matumizi yako madogo. Ni kwamba itawapunguzia gharama Watanzania. Kwa hiyo, tunaomba sana tunajua mmetuambia miundombinu yake ya gharama lakini ni uwekezaji, gharama ile italipwa polepole kama tunavyolipa umeme na mambo mengine ina Watanzania pia watakuwa wamenufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije sasa kwenye upande wa maji. Kwenye suala zima la maji tunaipongeza Serikali, kwa kweli miundombinu ya maji inaridhisha, tumepata visima vile vya Mpera na Kimbiji, tunapata maji. Lakini bado kuna changamoto. Wakati wa kiangazi maji Dar es Salaam inakuwa shida. Ni lazima nilitaje Bwawa la Kidunda, tukiwekewa Bwawa la Kidunda hao wananchi wanaotoka mitaa hii ya Mbezi, Kimara, Chuo Kikuu wote wale wanapata maji kutoka Ruvu. Kwa hiy,o tukichimbiwa lile bwawa pale Ruvu itakuwa halikauki. Wakati Mto Ruvu unakauka wataenda kufungulia lile bwawa wananchi wa Dar es Salaam na Mikoa ya Pwani tutapata maji kwa wakati wote. Naiomba sana Serikali waendeleze kama walivyoanza Mheshimiwa Rais amethubutu kwa jambo hili kubwa la kuweka Bwawa la Kidunda kulijenga sasa basi nawaombea heri tufanikiwe hili ili tuweze kupata maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala zima la uvuvi; Dar es Salaam imezungukwa na Bahari Kuu, Bahari ya Hindi imezunguka katika Mkoa wa Dar es Salaam, lakini wavuvi wetu bado. Katika maeneo ya Pemba Mnazi, tunaita Pemba Mnazi ina maana bahari (ukienda pale baharini unakuta bado wavuvi wanavua na vingalawa vidogovidogo) lakini ukienda Kimbiji unakuta kuna bahari, ukija Mji Mwema kuna Bahari, ukienda hapa Feri ndiyo kwenyewe lakini bado utakuta wavuvi wetu hawana vyombo vizuri vya kuvulia samaki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo niiombe Serikali na Wizara husika, waende wakawaone wavuvi wetu wa Mkoa wa Dar es Salaam, hata vile vianikio vya kuanikia dagaa wanaanika katika vitu visivyoeleweka na wengine wanaanika tu chini. Niombe hivi huu uwezeshwaji wa hawa wavuvi sijui wa nini, ni akina nani? Mbona kwetu hatujaona wapate hata boti za kisasa. Tunaomba sana Serikali iwasaidie wavuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuja kwenye suala zima la afya. Kwenye afya, kweli Mkoa wa Dar es Salaam jamani tumejengewa Zahanati na Vituo vya Afya na Hospitali kubwa lakini maboresho ya Haospitali za binafsi yamefanyika ni jambo jema. Hospitali zipo na zipo kweli lakini changamoto kubwa ni Madaktari pamoja na Madaktari Bingwa. Ninashukuru mpango wa Serikali wa kuwazungusha wale Madaktari Bingwa wanatengeneza timu wanahama, leo wanaenda hospitali ya Kigamboni, kesho wanahamia Temeke, kesho kutwa wanahamia Ubungo, keshokutwa wanahamia Amana, Mwananyamala. Hivyo ndivyo wanavyofanya lakini haitoshi ukilinganisha na idadi ya watu walioko Mkoa wa Dar es Salaam ambao sasa tunaelekea kwenye milioni sita kwa mujibu wa sensa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tunahitaji huduma nyingi sana za afya na Madaktari wengi waje watutibu. Nawapongeza kwa hilo lakini naomba tupewe Madaktari na Wauguzi pia. Wauguzi wanafanya kazi kubwa kwenye hospitali zetu tunawapongeza na Madaktari wetu wote, wanafanya kazi nzuri tunawapongeza sana lakini bado tunahitaji ziada. Ziada siyo mbaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. Mwenyezi Mungu akubariki, ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze leo kuzungumzia hoja hii. Kwanza napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kuniwezesha siku ya leo kuweza kusimama katika Bunge lako Tukufu na mimi kuchangia kwenye hoja hizi za Kamati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba niwapongeze Wenyeviti wote wa Kamati zote zilizowasilisha leo hapa, kwa kweli wamewasilisha vizuri sana hongereni sana Wenyeviti wetu lakini pia napenda nipongeze Makamu Wenyeviti wote na Wajumbe wote wa Kamati kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya katika kuwasilisha maoni na mapendekezo yetu katika Kamati hizi husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu kwanza utajikita katika maeneo mawili au matatu iwapo nitapata muda. Kwanza nitaanza katika Wizara ya Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu halafu nitakwenda kwenye Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum na kama muda utakuwepo nitakwenda kwenye Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimpongeze kwanza Mheshimiwa Rais wetu. Mheshimiwa Rais wetu alitoa kauli kwamba miradi yote iliyoanza itakamilika. Mimi nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia miradi ambayo ilikuwa inafanyika katika taasisi zilizopo kwenye Wizara ya Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu. Kupitia kwenye mifuko yetu ya NSSF kulikuwa na miradi mingi ambayo ilianzishwa ikiwemo mradi wa kiwanda cha sukari cha Mkulazi II. Kiwanda kile kwa kweli tulikuwa hatudhani kwamba kiwanda kile kinaweza kukamilika lakini mimi kama Mjumbe wa Kamati na wenzangu wa Kamati tumeshuhudia kwamba kiwanda cha Mkulazi II kimeanza kazi rasmi na kinafanya kazi pamoja na changamoto zingine tu za kimazingira. Hilo ni jambo kubwa kupata kiwanda chetu sisi kama Watanzania kinachomilikuwa na Serikali ubia baina ya NSSF na Magereza siyo jambo dogo ni jambo kubwa nani jambo la kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kutoa fedha kuhakikisha mradi huo unakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi kwenye miradi ya ujenzi wa majengo ya NSSF kule Dar es Salaam majengo ya Mzizima lakini hata mradi mkubwa ule wa Dege ambao ulikuwa ni mtihani katika miaka kadhaa sasa una mwelekeo mzuri. Mradi ule unaelekea kwenye kuuzwa na una majadiliano yanaendelea na Insha’Allah tuna imani mradi ule sasa utakwenda kuuzwa na ile hoja ambayo ilikuwa inatesa miaka yote ya mradi wa Dege sasa tunakwenda kuimaliza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee napenda niipongeze Mifuko yetu yote ya Serikali PSSSF, WCF, OSHA, NSSF na mifuko hiyo mingine yote kwa kufanya kazi nzuri. Kwa kweli matokeo tumeyaona kazi inaendelea. NSSF tunawaona wakiendelea katika miradi yao lakini PSSSF tunawaona jinsi gani sasa wastaafu wanavyopata taarifa zao kwa haraka na pensheni zao zinakuja kwa haraka kupitia mitandao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukikaa wewe kama mstaafu unakuja kushtuliwa na meseji unaambiwa tayari kitu kimeingia huku, siyo jambo dogo. Tukiangalia tulipotoka watu mpaka wakafuatilie huko lakini leo unaambiwa umeingiziwa kiasi gani kwa ajili ya pensheni yako ni jambo kubwa, ni jambo la kupongeza sana sana sana lakini mfuko wetu wa WCF unatoa elimu ya fidia kwa wafanyakazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo wafanyakazi wengi walikuwa hawaelewi hata nini wanapopata ajali kazini wafanye. Sasa hivi kutokana na elimu ambayo wanaitoa tunaona kwamba jamii inaanza kuelewa. Tunachoomba kwa mfuko huu bado elimu iendelee katika maeneo mbalimbali ya kazi. Wapo Watanzania ambao wanafanya kazi kwenye maeneo hatarishi sana, ni vyema mfuko huu ukaenda kutoa elimu katika maeneo ya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na changamoto zao za ukosefu wa watumishi lakini wajipange vizuri kuhakikisha wanaenda kwenye viwanda na maeneo mbalimbali ya taasisi mbalimbali kwenda kuwaeleza wananchi wa Tanzania haki yao kwamba pale wanapopatwa na matatizo wakimbilie wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna mfuko wa OSHA. OSHA watu walikuwa hawaielewi zamani na walikuwa wanaielewa kwa upande wa pili kama kitu fulani korofi hivi lakini sasa hivi Watanzania wameanza kuelewa umuhimu wa OSHA. Tunaona mazingira rafiki katika maeneo ya kazi yanazingatiwa, hii yote ni kutokana na juhudi ambayo wanaifanya wao, kutoa elimu, kuwatembelea, kwenda kwenye maeneo mbalimbali kwa kweli mimi niipongeze sana Taasisi hii inapiga kazi niwaombe waendelee kufanya hivyo na kutoa elimu kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye mfuko wa NSSF. Pamoja na mambo yote mazuri ambayo nimewasifia na kuona kwamba wana miradi lakini pia kwenye mazuri hapaokosi changamoto. Ipo changamoto kubwa ya madeni, Serikali NSSF wanaida Serikali takribani trilioni 13, katika kuchangia miradi mbalimbali lakini pia kwenye madeni yale ambayo ni ya watumishi wa Serikali kuletwa kwenye mfuko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, PSSSF nao vile vile wana madeni mengi ikiwepo takribani bilioni 787 ambazo zipo katika mashirika mablimbali. Mimi niombe madeni haya yalipwe yaongezee ule mfuko, pamoja kwamba madeni hayo ni mashirika ambayo ya Serikali lakini haya mashirika PSSSF na NSSF vitabu vyao vinakuwa havikai vizuri. Tutawasifu, watafanya kazi nzuri lakini kama vitabu vyao vya kimahesabu havijakaa vizuri kazi yao nzuri inakuwa kama ni bure, kumbe kazi hiyo hawajasababisha wao matatizo hayo yamesababishwa na Taasisi nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wote ni wa aina moja tuangalie jinsi gani wa kuondoa haya madeni. Madeni megine ni ya Serikali, kama ni ya Serikali na madeni yale yamekuwa chechefu sasa hayalipiki basi ni bora wakafutiwa madeni hayo na wao waendelee kuendelea na miradi yao mingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye mfuko wa CMA. Hii CMA ni mamlaka ya usuluhishi lakini wana changamoto kubwa sana wa kokosa kusimika mfumo wa kieletroniki. Hii inaendesha kazi yake sambamba na Kimahakama, tunaona jinsi Mahakama sasa zilivyoboreshwa yanaendesha mambo yake yote kupitia mfumo wa electronic. Sasa tuombe Serikali iwape fungu wao wahimize huu mfumo uendelee ili na wao waweze kufanya maamuzi ya yale mashitaka kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja sasa kwenye TAESA. TAESA hii ni Taasisi ambayo inashughulika na kutoa na kusimamia vijana na ajira. TAESA walikuwa ni taasisi ambayo inajitegemea Serikali wakaitoa wakaipeleka Wizarani wakaiweka kwenye benchi ni basic katika Wizara hiyo ya Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu sasa hawa watu hawana bajeti, wanategemea bajeti ya Wizara kupewa fungu. Lakini tunaona crisis ya vijana Tanzania ukosefu wa ajira ile ajenda ya vijhana ni ajenda ya dunia, duniani kote kuna tatizo la vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hii taasisi ilikuwa inawa-train vijana wetu, inawatafutia ajira maeneo mbalimbali tofauti tofauti lakini wanashindwa kuendesha kwa sababu wao kama wao siyo Muhimili unaojitegemea wanaitegemea Wizara na Wizara hii ina bajeti ndogo kwa hivyo wanashindwa kufanya kazi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii TAESA tumeshawaona wengine vijana mbalimbali wanapata ajira zile za intern, watoto wa vyuo wanavyotoka chuoni. Wanapata ajira zile za muda zile mwaka mmoja, miaka miwili lakini hata wengine wanabahatika wanatafutiwa hata ajira za kudumu ni taasisi ambayo inafanya kazi yake vizuri sana. Niombe Serikali wahakikishe kwamba wanatenga fungu kwa ajili ya TAESA. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mariam ahsante sana.

MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kidogo.

MWENYEKITI: Mheshimiwa maliza sekunde 30.

MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake wa Makundi Maalum, nayo vilevile kwa ujenzi na ukarabati wa maeneo mbalimbali ya watoto, makazi ya wazee jambo hilo limefanyika, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu kwa kuhakikisha anaboresha maeneo yote ya makazi ya wazee. Makazi hayo yakikuwa chakavu, hayafai lakini pia ujenzi wa Vyuo vya walemavu ni jambo kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake wa Makundi Maalum haina fungu. Fungu lake ni dogo sana waongezewe bajeti ili waweze kuendeleza program zao ikiwemo zile za watoto na kupinga ukatili wa kijinsia. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa heshima kubwa napenda nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Katibu Mkuu wa Wizara, kwa kazi kubwa wanayofanya ya kupambana na changamoto mbalimbali za Kilimo, Ufugaji pamoja na Uvuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu utajikita katika mambo yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Ufugaji; katika Mkoa wa Dar es Salaam, ufugaji mkubwa unaoendelea ni ufugaji wa kuku wa nyama na mayai. Changamoto kubwa tuliyonayo ni upandaji holela wa bei za madawa na chakula cha kuku. Naiomba Serikali iangalie jinsi gani ya kudhibiti upandishaji bei za madawa ya mifugo.
Watanzania walio wengi wamejiajiri wenyewe kwa kuvua na kufuga kuku wa nyama lakini kadri siku zinavyozidi kuendelea utakuta kwenye supermarkets kumejaa kuku wa kutoka nje na samaki wengi kutoka nchi za nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, uvuvi haramu; napongeza juhudi za Serikali jinsi inavyojitahidi katika kupambana na uvuvi haramu pamoja na juhudi za Serikali bado wapo. Ni vema Serikali ikaongeza juhudi zake kwenye kudhibiti uvuvi huo haramu ambao ni hatari sana kwa uvuvi endelevu wenye tija kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo; nitachangia juu ya kilimo cha mbogamboga na matunda. Kilimo cha mbogamboga na matunda kinachoendelea Dar es Salaam hatuna msaada wowote wa Serikali katika uboreshaji wa kilimo hiki. Tunakiri wako Maafisa Kilimo lakini utendaji wao ni mgumu kulingana na mazingira, pia ufuatiliaji wao ni mdogo. Wananchi wanajilimia wenyewe kama hakuna Wataalam. Je, wataalam hao wanafanya kazi gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, Maafisa Kilimo wako kila Kata, naomba Serikali na Wizara ya Kilimo kukaa na TAMISEMI kuangalia utendaji wa kazi wa Maafisa hao. Mkoa wa Dar es Salaam hatupati unafuu wa pembejeo za kilimo. Mbogamboga ndiyo chakula cha Watanzania walio wengi katika Jiji la Dar es Salaam. Je, Serikali imetuletea mpango gani katika Halmashauri za Mkoa wa Dar es Salaam katika kuboresha Kilimo cha mbogamboga na matunda.
Mheshimiwa Naibu Spika, kukosa soko la mayai; Mkoa wangu una tatizo kubwa la kukosekana kwa soko la mayai. Maeneo ya Kitunda, Chanika, Kibamba, Mbagala, Mbande, Somangira, Gezaulole, Pemba Mnazi na Kisarawe II. Kata zote hizo kuna wafugaji wazuri lakini inafika kipindi soko la mayai linaanguka na wafugaji kukosa mitaji kwa kuwa wanafanya biashara kwa hasara.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naipongeza Wizara ya Elimu kwa mipango mizuri ya maendeleo. Nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Naibu Waziri na Katibu Mkuu kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuhakikisha wanafunzi wetu wanapata elimu bora. Mchango wangu nitauelekeza katika maeneo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, shule za binafsi ni nzuri sana na zinaisaidia sana Serikali kupunguzia mzigo wazazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto iliyopo ni kupanda kwa ada mara kwa mara. Ada kutozingatia hali ya uchumi wa Watanzania na kutuweka katika matabaka na kuongeza ufisadi kwa wazazi kwa kwenda kinyume na maadili ya utendaji kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu TCU, udahili wa wanafunzi wa vyuo vikuu uangaliwe upya, vyuo vya binafsi vinapelekewa wanafunzi wengi kuliko vyuo vya Serikali. Mfano UDOM ni chuo kikubwa na kina mabweni mengi lakini wanalala ndege; badala yake wanajazwa kwenye vyuo ambavyo havina hata hosteli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa wanachuo wa private kwenda TCU ni tatizo kubwa na yawezekana ikawa sababu ya TCU kujichanganya hata kuwapa mikopo hata wasiostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali, watu wanaotaka kujilipia vyuo waende wenyewe kwenye vyuo wanavyovitaka na ada walipe kwenye chuo husika. Mfano sisi wengine ni wazee na fedha tunazo za kulipia unapelekwa TCU ukafanye nini? Usumbufu usio na msingi na kama ni kuhakiki vyeti acha nikahakikishiwe nipewe barua nimalizane na chuo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shule za msingi za english medium. Shule iliyopo Dar es Salaam ni Olymipio na imezaa Diamond; ni shule zilizokuwepo kwa muda mrefu. Je, Serikali kwa nini haioneshi mpango mahsusi wa kuongeza idadi ya shule hizi angalau tukapata katika Wilaya ya Kinondoni moja na Temeke moja kwa kuanzia. Naomba Serikali iliangalie kwani Jiji la Dar es Salaam limekuwa kubwa sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo ya mitihani. Kitendo cha kuwaweka wanafunzi wa shule zetu za kata na shule binafsi zenye uwiano wa mwanafunzi mmoja kwa mwalimu mmoja ni kuwaonea wanafunzi hao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunataka kushindanisha mtu ni vyema umshindanishe na yule aliyekuwepo kwenye level moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja asilimia mia moja bajeti ya Wizara ya Elimu changamoto zilizopo zifanyiwe kazi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kutoa mchango wangu kwa siku ya leo.
Kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya ya kutumbua majipu na kuhakikisha kwamba itapofika Julai aanzishe hiyo Mahakama ya Mafisadi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kweli wanaweza wakasema kulikuwa na mahakama, Mahakama tunazoziona, mimi naishi Dar es salaam, naona kuna Mahakama Kuu, kuna Mahakama ya Rufaa na kuna Mahakama ya Kisutu sijaiona Mahakama ya Mafisadi iliyo wazi, Mheshimiwa Rais ajitahidi kwa kila liwezekanalo alete sheria hapa ya kuanzisha Mahakama ya Mafisadi.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia nimshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais, kwa kututeulia Waziri wa Katiba na Sheria Mheshimiwa Waziri wetu mahiri, muelewa na anatosha kwa nafasi hiyo. Lakini pia nawapongeza Waheshimiwa Makatibu Wakuu. Waheshimiwa Makatibu Wakuu wamewekwa kulingana na elimu zao na taaluma zao katika Wizara hii na nina imani kabisa kwamba watafanya kazi nzuri sana kwa Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wangu hapa duniani kuna matatizo mengi, wewe ni mwalimu, umewafundisha wengi sana lakini kuna baadhi yao watakushukuru na baadhi yao watakubeza. Hayo yote ndiyo mzazi anayopata na ndivyo mzazi alivyo. Unapozaa unaweza ukazaa mtoto mwema na mtoto mbaya yapokee, lakini Mwenyezi Mungu atakulinda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie suala zima linalohusu utumbuaji wa majipu. Katika hotuba ya Upinzani wameeleza kwamba kuna baadhi ya Mawaziri, Wakuu wa Mkoa wanatumbua majipu wakati hawana mamlaka, hiyo siyo kweli!
Mheshimiwa Naibu Spika, utumbuaji majipu utaendelea kufanyika kwa yeyote yule ambaye atakwenda kinyume na maadili ya kazi yake, tena utaendelea utumbuaji huu kwa ngazi za aina mbalimbali. Kama kuna mtu ambaye anaona alitumbuliwa kinyume na taratibu au kinyume na sheria ndiyo maana mahakama zipo, mahakama zimewekwa ili mtu apeleke matatizo yake na hata yule ambaye anaona utumbuaji wake umekwenda kinyume ruhusa kwenda mahakamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nichangie kuhusu fedha za Bunge shilingi bilioni sita. Kwanza nilipongeze Bunge kwa kazi nzuri waliyoifanya, wananchi wetu wanakaa chini, mimi natoka Mkoa wa Dar es Salaam, sasa hivi tumeandikisha watoto wengi sana kuna limbikizo la watoto. Watoto wanasoma wakiwa wamekaa chini hivi leo kuna ubaya gani Bunge kutoa shilingi bilioni sita, kutusaidia Wabunge wote tulioko hapa katika Majimbo yetu tupate madawati.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka wananchi wawaone wenzetu hao wakati wanaomba kura walisema wao ni wazalendo kweli kweli, leo nashangaa uzalendo huu wa kukataa hata kupeleka pesa za madawati katika Majimbo yetu. Jamani hivi tunakokwenda tuko sahihi kweli, kuna mambo ya kubeza, lakini kuna mambo mengine tusifanye masihara kwa sababu wananchi wetu wanapata shida, watoto wetu wanahangaika, wanakaa chini wengine wanakalia vipande vya mawe au matofali. Leo Bunge hili, hivi zile shilingi bilioni sita tulitaka tuzifanyie nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, ninalipongeza sana Bunge hili kwa kuamua, uamuzi wake ni wa busara na waendelee kama kuna pesa ambayo inaonekana haina kazi watuletee tunahitaji bado vifaa zaidi katika afya ya mama na mtoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nirudi katika Mkoa wangu. Katika mahakama za Mkoa wa Dar es Salaam kuna Mahakama ya Mbagala, mahakama hii ina hali mbaya sana, Mahakama ya Temeke, Mahakama ya Magomeni, Mahakama ya Mnazi Mmoja na Mahakama ya Buguruni. Mahakama hizi zote zina hali mbaya, zina zaidi ya miaka 50 toka zimejengwa, Dar es Salaam ni Jiji, Dar es Salaam ni kioo cha Tanzania, tunapokuwa na Mahakama za aina hii katikati ya Mji, inakuwa ni tatizo na wala haioneshi kwamba tunakwenda mbele kama Jiji la Dar es Salaam. Ninaiomba Serikali yangu sikivu ya Chama cha Mapinduzi waangalie kwenye bajeti zao kuboresha Mahakama ukianzia zile zenye hali mbaya Mahakama za Buguruni, Mbagala, Magomeni na ile Mahakama ya Mnazi Mmoja, ziangaliwe kwa jicho la pekee.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika ngazi ya Wilaya, kuna Mahakama ya Wilaya ya Temeke, Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni na Mahakama ya Wilaya ya Ilala. Hizo ni Mahakama za Wilaya lakini hazina hadhi ya Wilaya, niiombe Serikali iboreshe mazingira yale, kubwa zaidi ni zile selo zilizoko katika mahakama hizo. Mahabusu wanajaa mno katika selo zile vyumba ni vidogo, ninaiomba Serikali iwapanulie hivyo vyumba na kuweka madirisha ambayo, yatakuwa yanawasaidia mahabusu katika kuvuta hewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nizungumzie juu ya sheria inayounda Jiji. Kambi ya Upinzani wamesema wamepata Jiji, ndiyo, mmepata Jiji, je, Jiji lile lina faida gani? Mimi ninaiomba Serikali iangalie upya Sheria ya Jiji. Jiji lile ni Serikali ya tatu halina rasilimali yoyote, pale ni utata mtupu, sehemu ilipo Jiji ni eneo la Halmashauri ya Manispaa ya Ilala. Parking ambazo ndiyo mapato ya Jiji zipo kwenye Halmashauri ya Temeke, Halmashauri ya Ilala, Jiji lile ni mgogoro halina rasilimali ya aina yoyote. Nawashangaa wenzangu niliwatarajia leo hapa walete hilo tuliangalie, wao wanafurahia kupata Meya, Meya huyo ataendeshaje wakati hana rasilimali?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tena niungane na Mbunge mwenzangu Mheshimiwa Kiteto kuzungumzia juu ya Sheria ya Mwanamke, sheria hii iangaliwe kwa mapana zaidi kwa sababu Sheria hii ya Ndoa inawaminya sana watoto wa kike, lakini pia..
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana naomba dakika zangu unitunzie.
Ninaomba Sheria hii ya Ndoa iangaliwe tena upya. Kweli mtoto wa kike kwa dunia hii ya leo, Sheria ya Ndoa inasema mtoto wa kike ataolewa akiwa na umri wa miaka 16, bado ni mtoto mdogo sana, ninaiomba Serikali iiangalie kwa mapana yake Sheria hii na iifanyie marekebisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba fursa hii niitumie kukishukuru Chama changu cha Mapinduzi, hususani Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi, kurudisha majina yenye dhana ya fifty-fifty, kweli Chama cha Mpinduzi ndiyo Chama ambacho kinaendeshwa kwa ukweli na uwazi. Imerudisha majina wanawake wawili na wanaume wawili kazi kwetu. Nakipongeza chama changu, kwa uamuzi wake wa busara ambao wameufanya na vyama vingine navyo viige mfano wa Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, mbona hawa wana vurugu! Tulieni ninyi!
Naomba nimpongeze kwa dhati ya moyo wangu Mheshimiwa Jenista Mhagama ambaye ni Katibu wa CCM Bunge, amefanya kazi yake kwa ubora, kwa uzuri ameliendesha Bunge hili vizuri sana, anaachia gari hili na wengine tuje tufuate jinsi gani amefanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja asilimia mia moja na kura Wabunge wa CCM....
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nami kunipa nafasi. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, wote wanawake. Tunategemea kuona ni jinsi gani wanawake mnaweza na sisi tuko nyuma yenu, tutawaunga mkono, tuna imani mtafanya vizuri ninyi akina mama ni walezi. Mungu atawasaidia katika kazi yenu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile ni dakika tano, naomba niende moja kwa moja. Mimi kwa vile ni Mbunge ambaye natoka Mkoa wa Dar es Salaam wenye utitiri wa shule za private, nitakuwa mkosefu wa fadhila au nitakuwa mnafiki iwapo sitazungumzia suala la ada elekezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua kabisa mchango wa sekta binafsi katika maeneo mbalimbali ya maendeleo hususan katika suala zima la elimu. Natambua jinsi gani shule za binafsi zinatubeba kama Mkoa wa Dar es Salaam na kuweza kupata matokeo mazuri. Pia ni wajibu wangu kusema changamoto ambazo wananchi wangu wanazisema kila siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ada za Shule ya Msingi na Sekondari, mpaka sasa imeambukiza na Vyuo Vikuu, ni tatizo. Ada hizi zinapanda kila baada ya muda. Wazazi hao hao ndio wanaokuja kwangu mimi kama Mbunge. Wengine wanashindwa, wanaomba niwasaidie kuwapeleka Olympio. Olympio shule ni moja Mkoa mzima wa Dar es Salaam, ndiyo shule ya Serikali; Olympio na Diamond. Sasa hawa watoto ambao wanashindwa huku, tutawapeleka wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto wale wengine wanapata matatizo wazazi wao hali ya uchumi inakuwa mbaya, wanashindwa kuendelea na shule. Pia kumpeleka mtoto wako shule ya private mara nyingine siyo wingi wa kipato ulichokuwanacho, ila ni utashi wa kupata elimu.
Kwa hiyo, naomba waelewe hata wenzetu, kwamba tunapokwenda kule, siyo kwamba mimi nina hela nyingi. Vijana wetu ambao ni watoto wetu ambao na wao wana watoto wenzao, wanakwenda kule wanakwama. Nao ndio wanaorudisha huku kwamba jamani hizi ada zenu zinazidi. Mtoto wa chekechea shilingi 3,800,000/=; hivi inakuaje? Ndiyo tunajua huduma anayoipata na nini, lakini tuangalie angalau kidogo. Vijana wangu mimi wa Clouds kila siku ndiyo maneno yao, wanasubiri Serikali, ada elekezi, leo mimi Mbunge wao nisimame hapa nisipolizungumzia, kwa kweli sitawatendea haki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, shule za binafsi hazikuanza leo wala jana, kwanini wananchi walilipokea? Tena walipoke vizuri. Leo kila mtu anazungumzia suala la ada; hapa kuna jambo. Naiomba kabisa Serikali, ikae na hao wenye shule tuangalie jinsi gani ya kuweka utaratibu mzuri ili shule zetu ziwe angalau na udhibiti wa aina yake. Shule ya Msingi au Sekondari inafika mpaka shilingi milioni tisa. Hivi leo shule ya shilingi milioni tisa, mtoto yule anaenda; baba yake kafariki, ukienda hawampokei. Wanakushauri ufanye nini, ufanye nini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tusema ukweli, pamoja na utoaji wa huduma, lakini na biashara ipo. Kwa hiyo, naiomba kabisa Serikali; kama isingekuwa biashara, isingetofautiana bei. Sasa inakuwa elimu kama inauzwa; hapa unaona shilingi 200/=, hapa shilingi 300/= au shilingi 3,000/=. Siyo sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tena, pamoja na mambo yote, tuna shule za private, yaani English Medium Dar es Salaam mbili; Olympio na Diamond. Hivi Serikali lini italiona hili suala? Kama wananchi sasa hivi wamekuwa wanapenda watoto wao wasome English Medium kwanini zisiwekwe katika Wilaya ya Temeke, Kinondoni, lakini na mikoa mingine pia ili wale watoto ambao watakwenda huko wakipata matatizo, warudie kwenye shule hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie TCU. TCU Mheshimiwa ni matatizo! Hivi leo udahili wa wanafunzi, mimi mtu mzima nataka kusoma Chuo, naambiwa niende TCU sijui nikapeleke matakataka gani, vitu kibao! Hivi mambo mengine si wanajichanganya wenyewe! Utakuta mkopo unakuja kwangu, mimi nautaka? Hii yote inakwenda na mfumo mbaya. Wanatakiwa wabadilike, warudishe mambo mengine kwenye kwenye Vyuo Vikuu vyenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Vyuoni tumeweka Uongozi, tunawaamini…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa mkakati wake wa kuwezesha katika sekta ya viwanda. Serikali imefungua milango ya uwekezaji kwa kuleta wawekezaji wengi kutoka nchi mbalimbali waje kuwekeza nchini kwetu. Cha kushangaza kuna baadhi ya viwanda vimejengwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo kile cha ASPAM Mbagala. Kiwanda hiki kimejengwa maeneo ya Mbagala kina miaka zaidi ya mitano lakini hakijafunguliwa mpaka leo. Mwekezaji yule anahangaika hajui afanye nini, amewekeza fedha nyingi tena za mkopo mpaka sasa amekufa moyo. Je, Serikali hali hii inatia moyo kwa wawekezaji au inakatisha tamaa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mbunge ambaye ninaishi Mbagala. Masikitiko ya wawekezaji kwa kukosa aina mbalimbali za vibali vinavyowezesha viwanda kuendelea. Niishauri Serikali kuwepo na mshauri wa viwanda ndani ya viwanda ili aweze kusaidia kuwashauri na kuwasimamia wawekezaji hawa kwa kuwa bado tunawahitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vidogo vidogo, naomba Serikali iboreshe SIDO ya Nyerere Road na elimu zaidi itolewe kwa viwanda vidogo vidogo ambavyo Watanzania wanaweza kuvianzisha. Viwanda vya pipi, ubuyu, biskuti na juisi ni viwanda ambavyo katika nchi za China mtu anaweza kuviendesha hata kwenye eneo dogo la nyumbani. Niombe Serikali itoe elimu kwa wananchi wake jinsi ya uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vikubwa kwa mara nyingine tena naomba Serikali sambamba na kuanzisha viwanda vipya iangalie na viwanda vyetu tulivyokuwa navyo muda mrefu na sasa havifanyi kazi tena. Mlundikano wa viwanda vikubwa vya aina moja au vinavyozalisha bidhaa ya aina moja katika eneo moja ni tatizo. Kwa mfano eneo la Mbagala lenye makazi ya watu wamejenga viwanda vya cement viwili kwenye umbali wa robo kilometa ambapo maeneo hayo yana makazi ya watu na viumbe vingine vyenye uhai ni tatizo kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mabadiliko ya matumizi ya maeneo ya viwanda vya Serikali, viwanda vingine vimegeuzwa yard za magari na vingine dampo la uchafu wa chupa na takataka nyingine. Kwa mfano Kiwanda cha Kubangua Korosho na Kiwanda cha Kioo Mbagala (Sheet Glass) kimegawanywa na miundombinu ya uendeshaji wa kiwanda kile umekufa kabisa, vipuli vyote vimechakaa. Nataka kujua kiwanda kile bado kiko Twiga Cement au kimeuzwa? Je, Serikali inafaidika na nini na eneo hilo? Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, naanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuhakikisha nishati ya umeme inapatikana. Nawapongeza Makatibu Wakuu wa Wizara na Wakurugenzi wa taasisi zote zilizopo ndani ya Wizara kwa jinsi wanavyojituma kuhakikisha nchi yetu inaenda vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kutuwekea jiwe la msingi mradi wa Kinyerezi ambao utakapokamilika utakuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa Tanzania. Pia nipongeze Serikali kwa kupata fursa ya ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Uganda kwenda Tanga. Ni jambo jema na lenye tija kubwa kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza EWURA kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma mbalimbali. Hata hivyo, kila panapo mazuri hapakosi changamoto zake. Kwa kweli kumekuwa na lawama nyingine ambazo haziwahusu EWURA, lakini kwa kuwa EWURA ndiyo wanaotoa leseni za mafuta basi lawama zote zitawaendea wao na lazima wazipokee, kwa mfano, ukaguzi wa mazingira. NEMC ni tatizo kubwa kwa wafanyabiashara wa mafuta. Gharama ni kubwa sana kwa watu wa mkoani.
Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali kukaa pamoja na NEMC kuona utaratibu gani mzuri ambao utaifaa kwa kuwasaidia wafanyabiashara. Nami naweka maslahi yangu wazi kuwa ni mdau wa mafuta.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukaguzi wa mafuta ni jambo jema sana, naipongeza EWURA kwa kuwa makini na kazi yao. Kwa uzoefu wangu wa sekta ya mafuta sijaona wakipokea rushwa na hawana mazungumzo na mtu yeyote. Bado nawashauri, EWURA wamezidi kuwa kama mapolisi wapunguze misimamo, watoe elimu kwa wafanyabiashara, tukielimika tutafuata sheria za nchi na mambo yatakwenda vizuri tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa TPDC nitazungumzia juu ya mauzo ya gas. Tumekuwa tukitumia gesi kama chanzo cha umeme peke yake, ni vyema tukaongeza vyanzo vingine vya umeme kama mkaa wa mawe na maji tupate kuuza gesi yetu nchi za nje. Gesi inatakiwa na nchi nyingi za Afrika Mashariki, tungeweza kuiuza nchi ingepata pesa za kigeni zingesaidia kukuza uchumi wetu. Tumepata bomba la mafuta kutoka Uganda mpaka Tanga, basi bomba hilo lingekwenda sambamba na bomba la gesi.
Mheshimiwa Naibu Spika, REA. Nawapongeza sana kwa kazi nzuri ya kusambaza umeme vijijini. Naomba katika Mkoa wa Dar es Salaam wakamilishe umeme maeneo ya Mianzini, Vikunai, Vijibweni na Kisarawe II.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuweke transformer katika maeneo ambayo umeme mkubwa wa kutoka Kigamboni kwenda Pemba Mnazi umepita juu kwa baadhi ya vijiji na wananchi wanaangalia kwa kuwa hakuna transformer.
Mheshimiwa Naibu Spika, TANESCO. Nawapongeza sana kwa kuwa tatizo la kukatika umeme mara kwa mara limepungua kwa kiasi kikubwa sana. Endeleeni hivyo. Mameneja wa TANESCO Wilaya ya Temeke wanafanya kazi nzuri sana na ni wepesi kujibu pale panapotokea hitilafu za umeme. Nampongeza Mkurugenzi na timu yake yote wanajitahidi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja asilimia mia. Uendelezwaji wa Mji wa Kigamboni uendelee kwa kuwa Serikali imeshaanza ujenzi wa Daraja la Nyerere basi na mji ule uendelezwe ili kuleta faida ya lile daraja.
Kuhusu ujenzi wa majumba mapya (NHC) na kuyauza yaliyopo katikati ya mji uangaliwe. Ardhi ikishatumika basi, sasa mwaka 2016 tunauza ardhi, je, kizazi cha miaka 50 ijayo watajenga wapi? Nashauri tukodishe tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Upimaji Viwanja Kiholela. Serikali imeshindwa nini sasa viwanja vinapimwa hovyo na watu kisha wananchi wanadai huduma muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanja vipya vinapimwa lakini mradi wa viwanja 20,000 mpaka sasa watu wamewekeza viwanja vimekuwa mapori hakuna uendelezwaji. Mfano Toangoma, Kisota, Gezaulole na Somangira – Temeke, Serikali inasema nini? Gharama kubwa za rent za nyumba za NHC wakati nyumba hazina ukarabati, maji yamekatwa, umeme wa mashaka lakini rent shilingi 320,000 mpaka 280,000. Hizi sio fedha ndogo kwa mtumishi wa kima cha chini vijana wetu wanashindwa kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama za kununua nyumba ni kubwa sana na nyumba ni ndogo sana huku familia nyingi zikiwa ni kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja asilimia mia.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza na kuunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Waziri kwa asilimia mia moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri pamoja na Katibu Mkuu kwa kazi kubwa wanayoifanya. Mchango wangu utakuwa katika maeneo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utalii wa mambo ya kale ya kihistoria, maeneo mengi ya kihistoria yametelekezwa, hayana maendeleo yoyote. Yapo baadhi ya maeneo yamesambaratika kabisa. Maeneo ya kihistoria iwapo yanaboreshwa na kutengenezwa vizuri yangeweza kuleta mapato makubwa kwa Taifa letu. Tunaenda katika nchi kama China watu walio wengi wanaenda kuangalia Great Wall. Serikali inapata fedha nyingi sana lakini India pia kuna Taj Mahal wanaingiza watalii wengi sana. Je, Tanzania tumejipanga vipi katika kutangaza maeneo yetu ya kihistoria badala ya kutegemea utalii wa mbuga peke yake?
Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali waangalie utalii wa kihistoria na tutangaze maeneo hayo ya kihistoria, matangazo ya utalii hayaonekani katika viwanja vya ndege, maeneo ya bandari na stendi kuu za mabasi. Waongozaji wetu wa watalii walio wengi wako Mkoa wa Arusha na maeneo ya Dar es Salaam na Bagamoyo siyo wengi sana. Lakini ma-tour guide wetu wanazidiwa na wale wa Kenya, Serikali imejipangaje katika kuwajengea uwezo watu wetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, msitu wa Mwandege na misitu mingi iliyopo Mkoa wa Pwani imekuwa ni makazi ya majambazi na wezi. Serikali imefanya vizuri sana kutenga maeneo ya misitu kwa kusaidia kutunza mazingira na kuhifadhi ardhi kwa matumizi ya baadaye.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Dar es Salaam sasa idadi ya watu imeongezeka kwa kiasi kikubwa sana, Mbagala imejaa watu wanaelekea Mkuranga, msitu wa Mwandege uko katikati umezungukwa na makazi ya watu, watu wanaingilia hifadhi na Serikali hakuna wanachosema hatma yake ni kuwabomolea nyumba zao kwani wakati wanajenga Serikali ilikuwa wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itoe baadhi ya eneo la Msitu wa Mwandege wawape Halmashauri ya Temeke watengeneze kituo kikubwa cha mabasi ya Mikoa ya Kusini na eneo linalobaki liendelezwe kama msitu na litunzwe kwa manufaa ya wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu tozo za mazao ya misitu. Gharama za kupitisha kitanda kimoja kutoka Mkoa wa Pwani kwenda Dar es Salaam ni kubwa kuliko ulizonunulia kitanda kijijini. Lakini fedha hizi wanazokusanya kweli zinaenda Serikali? Kwa kuwa tunasikia wafanyakazi wa vituo hivyo walio wengi siyo waaminifu ni vema sasa Serikali ikaangalia nidhamu na uadilifu wa wafanyakazi wa vituo vya ukaguzi wa mali na misitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye Wizara hii ya Ardhi. Kwanza kabisa nimpongeze Rais wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kumchagua Mheshimiwa Lukuvi kuwa Waziri wa Ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais hakufanya makosa, amemchagua Mheshimiwa Waziri mwenye uzoefu mkubwa anayejiweza, yuko makini na tuna imani naye. Pia amemchagua Mheshimiwa Naibu Waziri ambaye ni mwanamama, dada yetu Angelina Mabulla tuna imani naye kubwa sana, tunamtambua vizuri na yeye yuko makini na tuna imani naye kwamba atatusaidia sana sisi wanawake katika matatizo yetu mbalimbali ya ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kama Mbunge wa Viti Maalum ninayetokea katika Halmashauri ya Temeke, kwanza kabisa nitaanza kuzungumzia tatizo la Kurasini. Hii Kurasini hivi Serikali inatambua hayo maeneo ya Kurasini ambayo tunayapigia makelele humu ndani? Mimi ni Mbunge takribani sasa hivi ni miaka sita, kila tulipokuwa tunazungumza kwenye Wizara hii lazima tuizungumzie Kurasini. Kurasini wengine imetuchanganya, imetufanya tukose Diwani wa Chama cha Mapinduzi, imetufanya tukose Mbunge wa Chama cha Mapinduzi, kisa ni malalamiko ya watu wa Kurasini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kurasini watu wale wako kama wako kisiwani, wamezungukwa na magari, matakataka, sijui uchafu wa aina zote, lakini wananchi wale wenyewe kwa jitihada zao wamekwenda kutafuta mtu, wewe mwekezaji tuondoe, kama wananchi wale wamemtafuta wenyewe mwekezaji, hivi Serikali inaona kigugumizi gani kuwatoa wale watu pale, maisha yale ni hatarishi hayafai kuishi binadamu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali kweli ina mipango yake na mipango yake ni mizuri kwamba Kurasini liwe eneo ambalo la uendelezaji na uwekezaji tu wa kibiashara, sasa tunasita nini? Serikali imefanya jambo kubwa sana pale kuweka kile kituo cha biashara, wamewalipa watu mabilioni ya pesa wamekwenda vizuri sasa tumekula ngombe mzima, tunashindwaje mkia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri wa Chama changu cha Mapinduzi, tutakapomaliza Bunge hili aende Kurasini akawaangalie wananchi wale na ayajue matatizo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nizungumzie suala zima la Keko, leo Mheshimiwa Mbunge wa Temeke amewabeba wananchi wa Keko amewaleta hapa, mimi kama Mbunge ambaye niko miaka sita sioni la ajabu, wananchi hawa tumewasemea kuanzia Halmashauri kuhusu ugomvi wao na National Housing. Wameambiwa watatolewa pale watafanyiwa hivi, yote yamekwenda hakuna kinachoendelea, leo linabebwa kundi la watu linaletwa Dodoma, Mheshimiwa Waziri anataka kuwaambia nini, nataka aseme hapa ndani leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa watu wa Keko mgogoro wao Mheshimiwa Waziri auseme hapa ueleweke wazi, vinginevyo tunaonekana sisi tunaokaa humu hatufanyi kazi, kumbe kusema tunasema lakini majibu hayapo. Leo Mheshimiwa Mbunge ana miezi sita sijui ya kuingia humu Bungeni, amebeba kundi analileta hapa ndani, mimi kama Mbunge niliyekuwa humu ndani naona hiyo siyo ajabu. Leo Mheshimiwa Waziri wangu hapa nataka aeleze mgogoro huu National Housing na Keko, hapa ndani ya Bunge wala sitaki akasemee huko vichochoroni, aseme hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nichangie kwenye suala zima la kodi za ardhi. Mheshimiwa Mbunge mwenzangu pale amezungumzia, lakini nataka nirudie, hizi kodi za ardhi zimekuwa tatizo kwa wananchi. Mwananchi anakwenda kulipa anaambiwa sijui lipa premium fee shilingi ngapi sijui! Lipa sijui registration! Unaenda na pay slip sita! Serikali ileile jamani Eeh! Halmashauri, Serikali, Wizara, mtu anapewa vidude vile vya kulipia hata haelewi, wengine ni wazee, ni usumbufu wa hali ya juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri arekebishe. Hivi zile kodi zikilipwa pamoja hawa wahasibu wa Halmashauri na Wizara wanafanya kazi gani? Kwa nini wao wasije huko ndani wakazigawanya? Mtu anatumwa, yaani ni kuchanganyikiwa! Shilingi 1,000 peke yake! Shilingi 300 peke yake! Shilingi 3,000/= sijui peke yake! Hii si shida tu hii? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nizungumzie uendelezwaji wa Mji wa Kigamboni, Wabunge wenzangu wamesema, Mwenyekiti wa Kamati amesema na mimi inabidi niseme. Napata kigugumizi, hivi huu mji upo au haupo? Kama upo kwa nini, wanasema kwamba, ile ofisi iondolewe? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naelewa kabisa Mheshimiwa Waziri katika watu waliotusaidia kupata Wilaya ya Kigamboni na yeye anahusika kutokana na huu Mji wa Kigamboni. Kigezo kikubwa tuliona kwamba, ule Mji wa Kigamboni lazima upate Wilaya yake ili uweze kwenda vizuri. Sasa leo wanalolitenda, hivi Serikali kwa nini iliamua kutuambia kwamba, wanatuwekea Mji wa Kigamboni na sisi wananchi tunautaka, leo unasema ule mji ufutwe? Nataka maelezo ya kina uanzishwaji wa Mji wa Kigamboni umefikia wapi? Nataka Mheshimiwa akija hapa anieleze! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nije kwenye suala zima la National Housing na kodi zao. National Housing gharama za kodi ni kubwa! Unakuta nyumba moja Ilala, Buguruni, Temeke, Magomeni, Manzese, nyumba moja analipa mtu shilingi 320,000 kodi ya mwezi shilingi 280,000! Hivi kweli lengo la kuwekwa National Housing si ndiyo Mtanzania aweze kupata nyumba ya gharama nafuu! Leo Kariakoo majumba ya wananchi wa kawaida yameshuka bei yako chini kuliko ya National Haousing. Nataka nipate majibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine wanatujengea nyumba National Haousing, ndiyo wanafanya vizuri, lakini zile nyumba ni ndogo sana, vyumba kama box, ni vidogo sana ukilinganisha na familia zetu za wananchi wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nichangie katika hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda nimpongeze Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kumteua Profesa Jumanne Maghembe kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii. Tunamtambua Mheshimiwa Maghembe yeye ni profesa, ni mtalaam na tuna imani naye sana kwamba ataweza kuingoza vizuri Wizara hii. Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wake wote wanatosha na wanafaa kuiendesha Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wengine ni Walimu tumetoka mashuleni, tunafundisha watoto nidhamu na nini wafanye au ni wakati gani wazungumze na mazungumzo hayo yatolewe kwa wakati gani? Tunakwazika, tunachanganyikiwa tunapoona zinatolewa sentensi nyingine hazieleweki ndani ya Bunge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba sasa nirudi kwenye hoja yangu. Wabunge wenzangu wamechangia mengi sana, lakini naomba nichangie katika eneo la misitu. Serikali ilikuwa na nia njema sana ya kuhifadhi maeneo ya ardhi yetu kwa kuweka misitu kwa akiba ya baadaye lakini pia katika kusaidia kuboresha mazingira lakini kila panapokuwa na jambo jema halikosi kuwa na ubaya ndani yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hizi hifadhi kwa mfano sisi tunaotoka maeneo ya Mbagala kuna hifadhi ya Mwandege, hifadhi hii haiendelezwi, haina usafi, matokeo yake imekuwa ni makazi ya majambazi. Majambazi yanakuja yanaua watu Mbagala, Temeke, Vituka huko yanakimbilia kwenda kujificha katika msitu huu wa Mwandege. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima nitoe pongezi za wazi kwa Kamanda wangu wa Polisi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Kamanda Siro, amekuwa akifanya operesheni na katika operesheni yake idadi kubwa ya majambazi, majangili, magaidi, yamekamatwa katika msitu huu wa Mwandege uliopo Mkuranga. Hili sasa limekuwa tatizo badala ya raha. Kweli tuna nia njema ya kuhifadhi msitu ule lakini kwa hali ilivyofikia sasa hivi msitu ule ni tatizo kwa wakazi wa Dar es Salaam hususan wakazi wa maeneo ya Mbagala. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua kuna changamoto nyingi sana katika maeneo haya lakini niiombe Serikali sasa hivi Mkoa wa Dar es Salaam una matatizo makubwa ya ardhi lakini pia kuna msongamano wa magari usiokwisha katika maeneo ya Mbagala. Niiombe kabisa Serikali kwa nia njema kwa nini wasipunguze eneo la msitu huu wakatengeneza kituo kikubwa cha mabasi kuondoa ule msongamano uliko pale Mbagala Rangitatu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo hivi huu msitu mwisho wake ni nini? Msitu huo umekuwa ukiingiliwa na wakazi kwenye maeneo yote ya pembezoni lakini wakati watu wale wanajenga nyumba Serikali inawaangalia, kesho na keshokutwa Serikali inakuja kuwavunjia zile nyumba, hawaoni kwamba wanawaonea wale wananchi? Dar es Salaam imejaa, maeneo ya ujenzi yamekuwa machache watu wanaanza kumega kidogokidogo pembeni mwa msitu ule, Serikali inawaona, Maafisa Misitu wapo hakuna wanachowaambia. Sasa mimi kama Mbunge ole wenu mkawaambie wale watu waje wavunje nyumba zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nizungumzie gharama za tozo za misitu. Katika maeneo ya Mkuranga kwenye kituo cha Mkuranga ukitaka kupitisha kitanda kimoja gharama yake unalipia Sh.120,000/=, kitanda hicho kiwe cha zamani, kiwe kipya au kabati liwe la zamani au liwe jipya. Sasa Mkoa wa Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani maeneo ya Mkuranga umeungana, mtu anaweza kuhama kwenye nyumba Mkuranga akahamia Mbagala Temeke, akahama Mwandege akahamia Kongowe. Sasa hizi gharama wakati mtu anahamahama atakuwa anatozwa Sh.120,000/= kila anapohama kutoka huku kwenda kule, hii kweli ni sawa, huu siyo uonevu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali iangalie hiyo sheria inavyosema kwamba watu wanapotoa kitanda au mazao yoyote ya misitu kutoka huku kwenda huku kulipa gharama kubwa. Kitanda cha futi tatu hapa Dodoma kinauzwa Sh.180,000/= wewe unalipiwa ushuru Sh.120,000/= hivi jamani hii ni kweli! Niiombe kabisa Serikali iangalie eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kwenye manunuzi ya mkaa, unakuja pale Mkuranga ukitoka Rufiji unakuta kuna barrier kibao, mbona wenzetu huku Dodoma hakuna barrier za aina ile? Kwa nini kule kumekuwa barriers hizo kila sehemu unatozwa tozo mpaka unachanganyikiwa. Niombe hilo nalo liangaliwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niingie kwenye eneo la utalii. Nitazungumzia utalii wa mambokale au wa maeneo ya kihistoria. Kuna maeneo ya kihistoria yanapotea, maeneo kama Bagamoyo, Kaole, Kunduchi, Isimila, Olduvai Gorge, Mapango ya Amboni, Mikindani, Kilwa Kisiwani, Songomnara, yote hayo ni maeneo ya kihistoria ambayo kama yataboreshwa yangeweza kutuletea mapato makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo haya hayawekewi bajeti nzuri ya kuyaendeleza matokeo yake yanasambaratika, urithi ule wa kihistoria unasambaratika. Kwa hiyo, niiombe Serikali iweke bajeti ya maeneo hayo. Pia maeneo haya hayana information yoyote, hujui hiki kiko wapi wala kile kiko wapi. Kwa hiyo, niiombe Serikali iyatolee maelezo maeneo haya lakini pia iyatangaze. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakwenda kwenye nchi za wenzetu, kwa mfano unakwenda India, unakuta ushawishi mkubwa, wewe kama mgeni unaambiwa nenda Taj Mahal, huelewi, mara nyingine unafuata tu mkumbo lakini sisi mbona tumekuwa kimya! Mtalii anakuja hapa, hakuna maelezo yoyote, hakuna promotion yoyote, unaingia kwenye ndege mpaka unafika Dar es Salaam hata huambiwi kwenye ndege Dar es Salaam utakumbana na kitu gani cha kitalii au ukaone maeneo gani ya kitalii, hili kwa kweli ni tatizo. Niiombe sasa Serikali yetu ibadilike, itangaze vyanzo vyake vya utalii vizuri ili wageni wanapoingia wavitambue na waende wakavitembelee. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie Mkoa wangu wa Dar es Salaam kuwa mji wa kihistoria. Hakuna ambaye hafahamu kwamba Dar es Salaam ndiyo mji mkuu kuliko mikoa yote ya Tanzania lakini wapi Dar es Salaam imewekwa, wapi Dar es Salaam imepangwa kiutalii, tujue Dar es Salaam hii inakwendaje au tunamshawishije mtu wa kutoka nje akiingia Dar es Salaam aweze kutambua kwamba anaingia kwenye mji mkuu, mji bora, mji ambao una mambo yote muhimu, hata uhuru wa nchi hii bendera yake ilipandishwa katika Mkoa wa Dar es Salaam, Uwanja wa Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Serikali, najua mpango huu ulizungumzwa hapa lakini ukaishia, je, imepanga mkakati gani wa kuitangaza Dar es Salaam sasa? Tunataka Dar es Salaam uwe mji wa kiutalii na utangazike na watu walioko nje wautambue. Ndiyo wenye uwanja mkubwa wa Kimataifa, Serikali imejenga ule uwanja, uwanja ule ni wa nini, wa kushusha na kupandisha tu, ni lazima ulete soko la watalii. Kwa hiyo, niiombe Serikali ipange mpango mkakati wa kuitangaza Dar es Salaam kama mji wa kitalii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Hotuba ya Mheshimiwa Waziri ni nzuri na inaeleweka vizuri. Napongeza utendaji wa Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu kwa kazi nzuri wanayofanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mwenyekiti wa Kamati, Makamu Mwenyekiti kwa kuishauri vizuri Serikali. Naomba ushauri wa Kamati uzingatiwe kwa maslahi ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ushauri; Ofisi zetu za ubalozi na maafisa wetu wasaidie katika kuutangaza utalii wa Tanzania. Wasaidie katika kuleta wawekezaji nchini mwetu na mkazo uwe kwenye ujenzi wa viwanda. Serikali iboreshe ofisi zetu za ubalozi kwa kuweka vitendea kazi vya kisasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika utendaji wa Soko la Pamoja la Afrika Mashariki. Elimu iendelee kutolewa kwa Watanzania. Serikali iweke mpango mkakati wa kuwatambua wanafunzi wetu wanaosoma nje ili kupunguza matatizo ya udhalilishwaji wa wanafunzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanafunzi wengi wanakwenda kusoma nchi za nje bila utaratibu. Wanafunzi wanaosoma nje bila kuthibitishwa na TCU kwa nini wao hatuwaingizi kwenye ajira za moja kwa moja?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuangalie kwa kuwa watoto wale ni Watanzania wanakwenda kuchukua ujuzi wa Mataifa mengine si kwa wote lakini wengine tuwape nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kumteua Waziri wa Fedha ambaye anajua vizuri uchumi wa nchi; nampongeza Naibu Waziri kwa utendaji mzuri, napongeza juhudi za Serikali kwa kutuletea Mpango mzuri wa Maendeleo 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mpango nitachangia ukurasa 13, Ujenzi wa Barabara ya Mwendokasi katika Jiji la Dar es Salaam. Naomba Serikali iboreshe mpango wake wa kuendesha mabasi yaendayo kasi kwani usafiri huo ni bora sana na ni msaada mkubwa sana kwa wananchi wetu. Sasa mradi wa mabasi yaendayo kasi yaelekee phase II kutoka Kariakoo kwenda Mbagala.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukamilishaji wa Kituo cha Biashara cha Kurasini. Kituo hiki ni muhimu sana na Serikali sasa imekamilisha malipo ya fidia na kuanza utaratibu wa ujenzi wa ukuta.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vyema kituo hicho kikaendelea kuwepo na kifanye kazi kwa maslahi ya Watanzania na wale wengine wageni wanaotoka nchi za jirani kuja kununua bidhaa zao Kurasini, lakini pia, Kurasini kutakuwa ni mji mzuri wenye maendeleo na mvuto mkubwa wa kibiashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa flyover TAZARA- Serikali iendelee na mpango wake wa ujenzi wa barabara za juu kwa eneo la TAZARA ni jambo la maana sana. Katika kupunguza msongamano katika barabara zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iongeze mtaji Benki ya TIB ili iongezee uwezo wa kukopesha wafanyabirashara, wajasiriamali kwa kuanzisha miradi mbalimbali ikiwemo viwanda badala ya kutumia Mifuko yetu ya Pensheni katika maeneo mengi ya viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo, Mpango uelekeze kwenye kukiendeleza kilimo cha mazao ya chakula na biashara. Pembejeo za kilimo ziwafikie wakulima kwa wakati. Wananchi waweze kuboresha kilimo na kupata mazao mengi ya chakula na biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha standard gauge; ni vyema reli iwepo kwa kuwa itatusaidia sana katika kukuza uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa viwanda ni vyema kabla hatujajenga vipya kwanza tuangalie vile viwanda vya zamani. Tuangalie ni nini kilitufanya tuanguke na tuvifufue angalau vichache, pia viwanda vipya vianzishwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Mheshimiwa Waziri kaza buti, Hapa Kazi Tu.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara kwa kazi nzuri wanazozifanya. Mazingira ni jambo muhimu sana katika maisha ya binadamu. Naiomba Serikali itilie mkazo sana katika suala zima la uhifadhi wa mazingira pamoja na juhudi za Serikali katika kuongeza kasi ya upandaji wa miti, lakini bado kuna mambo mengi sana yanayosababisha uharibifu wa mazingira nayo yafanyiwe kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali wakae pamoja na taasisi nyingine katika kuweka sawa sheria ya mazingira kwa kuwa wananchi wengi wanapotafuta vibali mbalimbali vya ujenzi kunakuwa na vikwazo vingi sana. Mambo yanayowekwa kwa Mtanzania wa kawaida inakuwa vigumu kuyatekeleza kwa haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze Serikali kwa kufuatilia kwa kina kuangalia viwanda ambavyo vinakiuka taratibu za mazingira. Hiyo imesaidia sana Temeke kutokana na matatizo ya Serengeti Breweries.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niwe mchangiaji katika Wizara hii muhimu. Kwanza naomba niipongeze Serikali ya Chama cha Mapinduzi, Mheshimiwa Rais, Waziri Mkuu, Makamu wa Rais, Mawaziri wote wa Serikali pamoja na Makatibu Wakuu wote kwa utendaji wao mzuri uliotukuka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda niwaambie wenzangu wanaosema kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi haikutimiza ilani zake; nawaambia Serikali ya Chama cha Mapinduzi imetimiza ilani yake kwa kiasi kikubwa ndiyo sababu wakachaguliwa Wabunge wengi wa Chama cha Mapinduzi kutoka katika majimbo mbalimbali, lakini pia wakachaguliwa Madiwani wengi wa Chama cha Mapinduzi kutoka katika kata mbalimbali, lakini pia Halmashauri nyingi zimeongozwa na Madiwani, Wenyeviti wa Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukweli ni kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi inafanya mambo mazuri sana. Napenda nimpe pongezi za kipekee Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kwa kazi kubwa anayoifanya katika Mkoa wetu wa Dar es Salaam toka kuchaguliwa kwake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais wetu alipochaguliwa tu, alifanya upanuzi wa haraka wa barabara ile ya Morocco kwenda Mwenge. Pia alifanya ufunguzi wa Daraja la Kigamboni, daraja muhimu sana; alizindua ujenzi wa flyover ya TAZARA, mradi ambao unagharimu shilingi bilioni 99; alifungua mradi wa mabasi yaendayo kasi ambayo yamekuwa msaada mkubwa sana kwa wananchi wa Dar es Salaam ambao walikuwa na tatizo kubwa la msongamano wa magari.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Mheshimiwa Rais alifanya mapokezi ya ndege mbili za Bombadier katika Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam; alizindua mradi wa interchange ya Ubungo, mradi ambao unagharamia pesa kiasi cha shilingi bilioni 177; alizindua ufunguzi wa mradi wa ujenzi wa Mabweni ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; amefungua ujenzi wa reli ya standard gauge kule Pugu, Dar es Salaam, mradi ambao utatumia pesa takribani USD bilioni 1.2; hilo siyo suala dogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais pia alizindua ujenzi wa nyumba za wakazi wa Magomeni; ametoa pesa katika mradi wa Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam ili ukamilike kwa haraka, hiyo siyo kazi ndogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo nawaomba wananchi wangu wa Mkoa wa Dar es Salaam, nami ndio Mbunge wenu kutoka Chama cha Mapinduzi, mlionileta Bungeni nije niwawakilishe, nawaambieni Serikali hii imeamua kwa dhati kabisa kuhakikisha Mkoa wa Dar es Salaam sasa unakuwa mkoa wa utalii, miundombinu yote inaboreka, ndege tumepata; lakini kubwa mimi nilipoingia katika Bunge hili kipindi kilichopita, nilizungumzia juu ya Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam…
TAARIFA...
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunitolea ufafanuzi, maana anaelewa Mwalimu mwenzangu, anajifanya haelewi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi, Serikali ya Tanzania inaongozwa na Mheshimiwa Rais wa Chama cha Mapunduzi na itaendelea kuwa Serikali ambayo inatekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi na yeye Mheshimiwa Waitara anatakiwa atekeleze Ilani ya Chama cha Mapinduzi, atake asitake afanye hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa niendelee. Tunataka kujengewa nyumba za wakazi wa Magomeni na tumesikia kilio cha wananchi wale, jinsi walivyokuwa wanalia kwa kunyanyaswa kuondolewa katika maeneo yao. Wananchi wale leo Mheshimiwa Rais ameona kilio chao; ameamua kwa dhati ya moyo wake kuhakikisha anawapatia makazi bora wananchi wale wa Magomeni. Siyo jambo dogo, ni jambo ambalo sisi kama Wabunge wa Dar es Salaam, tena nampongeza sana Mbunge wangu wa
Kinondoni kwamba yeye alishiriki pamoja na kwamba yuko Upinzani, alishirikiana na Mheshimiwa Rais akaenda pale kwenye uzinduzi wa nyumba zile, hiyo ndiyo siasa. Wanasiasa tufike sehemu, pale yanapofanyika mazuri tuunge mkono, siyo kila kitu tunapinga tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza na kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa hilo tena nasema zile nyumba azijenge kwa haraka, wananchi wale wakae. Sambamba na hao, wananchi wa Ilala Mchikichini nao wanazisubiri kwa hamu nyumba hizo wajengewe na wananchi wa Temeke mwisho nao wanazisubiri. Nimwambie Mheshimiwa Rais na Wizara na Mawaziri, kazeni buti, fanyeni kazi, tekelezeni Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi/ Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wizara hii sasa, nitajikita katika maeneo yafuatayo; kwanza nitachangia katika barabara, bandari, uwanja wa ndege, reli na mawasiliano.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika upande wa barabara, naomba kabisa Serikali pamoja na kumsikia Mheshimiwa Waziri kwamba kuna mpango wa ujenzi wa flyover ya Charambe, naiomba Serikali mpango huo utekelezeke kwa sababu idadi ya watu Mbagala imekuwa kubwa. Kuna msongamano mkubwa kutoka kwenye round about ya Mbagala Rangitatu kuelekea Charambe, Chamazi na Mbande. Mpango huo ukitekelezwa, basi Mbagala yetu sasa nayo itaendelea kuwa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba barabara inayotoka kwenye Daraja la Kigamboni kuelekea Kibada na Kigamboni, hiyo sasa ifanyiwe kazi kwa haraka kwa sababu wakati huu wa mvua barabara hiyo ilikuwa tatizo. Pamoja na daraja zuri tulilojengewa na Serikali, lakini pale upande mwingine kumalizia kile kipande, naiomba Serikali kwa kupitia NSSF wawaamrishe wafanye kwa haraka sana ujenzi ule ukamilike. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali iangalie ujenzi wa barabara ya Nzasa – Kilungule kuvuka kwenda Buza. Barabara hiyo itaungana na ile barabara ya Jet – Davis Corner inayotoka Jet inakwenda Davis Corner. Barabara hiyo ni msaada mkubwa kwa wananchi. Barabara hiyo inawasaidia watu ambapo kunapokuwa na msongamano mkubwa Mbagala Rangitatu, wanaotoka kwenda Airport wanapita Nzasa wanashuka Bondeni wanaunganisha Buza wanaenda wanakutana na ile barabara mpaka Jet, mtu anakwenda uwanja wa ndege kwa haraka sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali, mara nyingi barabara hii imekuwa ikiingizwa kwenye mipango, inatoka; mara inaenda kwenye mpango mwingine. Naiomba sasa Serikali, kupitia Mheshimiwa Waziri wangu akaisimamie, barabara hii ni msaada mkubwa kwa wakazi wa Mbagala. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa Serikali iangalie uwezekano wa kujenga barabara kutoka Mbande kwenda Mipeku - Mkuranga. Wananchi wanapata shida sana hususan akina mama wajawazito, magari hayapiti hata yenye four wheel, lakini wanabebwa kwenye pikipiki kuja Mbande kupata huduma ya afya ya mama na mtoto. Naomba barabara hiyo ijengwe. Ikijengwa barabara hiyo, itakuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wanaotoka Mipeku kuja kupata huduma za afya, hasa akina mama kwenye hospitali au dispensary ya Mbande, Temeke. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nizungumzie upande wa bandari. Pamoja na kazi kubwa inayofanywa na bandari na hasa ile ambayo inaendelea kufanywa ya kuongeza kina cha bandari kutoka geti namba moja mpaka namba saba, lakini naomba sasa bandari itueleze ajira ndogo ndogo zinazotolewa na bandari kwa vijana, nataka mpango wa ajira ndogo ndogo…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Naipongeza sana Serikali, Mheshimiwa Waziri, Manaibu Waziri wote wa Wizara ya Uchukuzi. Fanyeni kazi kwa bidii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakamilisha mchango wangu wa maneno kuhusu barabara. Mabasi yaendayo kasi yaendelee kwa haraka kwenda Mbagala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bandari; ajira ndogo ndogo. Kuwe na mpango madhubuti wa kuzitambua ajira hizo na vijana wa Dar es Salaam hususani Temeke wapate ajira hizo, vile vile mwisho wa siku tupate takwimu za ajira hizo. Fungu la Bandari la Corporate Social Responsibility litolewe kwenye makundi mbalimbali ya wasiojiweza na wazee. Pia akinamama wajasiriamali wadogo watoto wa Kurasini, mama lishe na wauza vinywaji. Bandari iwajengee uwezo na kuwawekea mazingira mazuri ya kuuzia bidhaa zao. Vile vile hata Canteen ya Bandari iwajengee uwezo akinamama walete bidhaa kama vitafunwa ili nao wafaidike na bandari yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Uwanja wa ndege. Ni vyema Serikali ikaelekeza mpango wa mabasi ya mwendo kasi kwenye uwanja huo. Hata hivyo sijaona eneo la biashara kuonesha bidhaa za Tanzania na utalii, je Serikali imepanga vipi eneo hilo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Reli; maeneo ya Shirika la Reli yaliyo mengi yametekelezwa kiasi cha kuwa Mafichio ya wezi na vibaka. Maeneo yatunzwe vizuri ili yatumike baadaye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mawasiliano; matumizi makubwa ya simu yanafanyika Dar es Salaam, lakini ukitoa kodi tunayokata kama wana Dar es Salaam wanatusaidia nini moja kwa moja kama wananchi wa Dara es Salaam? Naomba Makampuni ya simu wakae na sisi Wabunge kuangalia namna bora ya kutuchangia watu wa Mkoa wa Dar es Salaam katika mipango ya maendeleo ya Mkoa wetu. Kikubwa na kuongezeka kwa gharama za simu kumekuwa na matangazo ya uongo kuwa kuna nafuu ya matumizi, ukiangalia dakika hakuna kitu badala yake weekend kuna ongezeko kubwa la gharama za simu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Habari na Utamaduni kwa asilimia mia moja. Nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara. Napongeza Utendaji mzuri wa Wizara na kwa kweli wanafanya kazi nzuri kwa kipindi kifupi.

Mheshimiwa Spika, mchango wangu utajikita katika Utamaduni wa Mtanzania. Utamaduni wa Mtanzania unapotea kwa kuwa kizazi chetu kinafurahia sana tamaduni za kizungu kuliko zetu. Vifaa vyetu vya asili kama mundu, kinu, mchi, kisagio, mtungi, kata, vibuyu na kadhalika vyote vinapotea na hakuna wa kuvirudisha. Je, Serikali ina mkakati gani wa kulinda utamaduni wetu wa asili kwa kuvilinda vifaa vyetu vya asili.

Mheshimiwa Spika, vile vile kwa mazao yetu pia, kwa kuwa shule nyingi ziko maeneo ya mijini utakuta wanafunzi wanashindwa kujua hata mmea wa mahindi ukoje? Naomba Serikali waweke mpango mahsusi wa kuandaa maeneo maalum ya kitamaduni kama vile Kijitonyama kuweka sehemu ya vitalu vya kuonyesha utamaduni wa mazao mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, hiyo itasaidia katika kukuza na kuendeleza utamaduni wetu. Sambamba na hiyo ni mavazi yetu ya asili kama kaniki, kanzu, migolole, shanga, vibwaya na kadhalika. Vifaa hivyo vitunzwe kwa kumbukumbu kwa kuwa vinatoweka sasa.

Mheshimiwa Spika, Sanaa; wachezaji muziki walio wengi wanaume wanavaa nguo vizuri sana lakini wanawake wanavaa nusu uchi. Hali hiyo inatudhalilisha sana wanawake na inatuharibia kizazi chetu kipya kwa kuiga mavazi ya utamaduni ambao si sahihi sana. Serikali itoe kauli kwa wanawake wanaocheza muziki wavae mavazi yao ya heshima pasipo kuwadhalilisha wanawake wenzao.

Mheshimiwa Spika, Mapambo; utamaduni wa kusuka nywele, tumeona watoto wanakua kwa kukazwa nywele na kumfanya mtoto ashindwe kupumua na kupoteza maisha. Serikali itoe angalizo kwa akinamama wenye watoto waangalie watoto wao na wawasuke nywele za kawaida za utamaduni za mikono kwa kuwasaidia watoto mpaka watimie umri wa miaka 12 kwenda juu umri huo mtoto anaelewa baya na zuri.

Mheshimiwa Spika, TBC; ijengewe uwezo iweze kuwa na mitambo mizuri na shughuli za Kiserikali ikiwemo shughuli za Wabunge Majimboni watumie TBC Radio na TV itasaidia hata kuongeza kipato. TBC wajitahidi wawe na mawasiliano katika mikoa yetu ya Tanzania Bara na Zanzibar ili wananchi wetu wafaidi matunda ya Television yetu na Radio yetu ya Taifa.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja asilimia mia moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Mawaziri na Makatibu Wakuu kwa kazi nzuri wanazofanya. Natoa shukrani zangu za dhati ya moyo kutokana na miradi mingi ya Serikali iliyotekelezeka katika Mkoa wa Dar es Salaam. Nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kutuzindulia miradi mbalimbali katika Mkoa wetu wa Dar es Salaam, Mungu ambariki sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri ujenzi wa barabara ya mwendokasi Mbagala sasa mradi ule uanze angalau tupate tumaini.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa barabara ya Nzasa – Kilungule - Buza uangaliwe kwa moyo wa huruma kwani ni barabara muhimu ambayo itasaidia kuunganisha Wilaya ya Ilala na Temeke na Jet ambayo kama mtu anatoka Mbagala anaweza kufika mara moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Temeke Mwisho kwa jina Mbagala Road nayo sasa ijengwe kwa uimara zaidi kwa kuwa imekuwa inabomoka mara kwa mara. TARURA waongezewe nguvu kwa kupewa nyenzo za kufanyia kazi kama greda na vifaa vingine. TANROADS nawapongeza sana kwa kazi nzuri wanazofanya wanajenga barabara nzuri sana kiasi kwamba tunataka barabara zote zichukuliwe na TANROADS, kwa hiyo tusiwapunguzie nguvu bali tuwaongezee nguvu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uwanja wa ndege, naipongeza sana Serikali kwa kuwezesha ujenzi wa uwanja wa ndege mpya wa Dar es Salaam na kutuletea ndege tatu. Tunashukuru sana ukiangalia tulikotoka na tunakokwenda tumepiga hatua kubwa sana. Ombi langu tuboreshe huduma zetu ziende na wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu TBA kwa kweli kuna haja ya kuboresha au kukarabati nyumba zetu na kama hakuna uwezekano tufanye utaratibu ambao mpangaji akifanya ukarabati kisha akatwe katika rent. Miundombinu ya nyumba, mifumo ya maji safi na maji taka imekufa kabisa na hata mafundi wa TBA hawana vifaa vya kufanyia kazi. Nyumba za TBA ni nzuri na zimejengwa kwa uimara wa aina yake tatizo ni kukosa service. Tunaishi miaka kumi hakuna ukarabati wowote siyo vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu TPA naipongeza Serikali kwa ujenzi wa mageti ndani ya Bandari yetu ya Dar es Salaam, nataka kujua Serikali ina mpango gani na Bandari ya Bweni? Fungu la SSR la kutoka bandari pamoja na kutuletea mashuka katika Hospitali yetu ya Temeke namshukuru na kuwapongeza sana kwa moyo wa huruma.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu naomba TPA waangalie na shule zenye watoto walemavu na wenye mtindio wa ubongo ambazo ni Shule ya Mtoni – Maalum, Shule ya Sinza – Maalum na Uhuru Maalum. Shule hizi zina watoto ambao wana mahitaji; kuna wasioona, walemavu wa viungo na akili. Mamlaka yetu iangalie kundi hilo. Nawatakia kila la kheri TPA naona mizigo ni mingi na meli ni nyingi baharini.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja asilimia mia moja.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Wakurugenzi wote wa vitengo mbalimbali vya Wizara ya Afya. Pamoja na juhudi za Serikali za kuisaidia sana Hospitali ya Muhimbili, lakini bado kuna changamoto nyingi ikiwemo ya upungufu wa Wauguzi na Madaktari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwepo na wagonjwa wengi katika Hospitali ya Muhimbili kunatokana na kutoimarika kwa Hospitali za Mikoa na Wilaya, kunasababisha Hospitali ya Muhimbili kuzidiwa na wingi wa wagonjwa. Naomba Serikali iangalie upya na kuzidi kuziimarisha hospitali zetu za Mkoa na Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kuongeza teknolojia ya kupunguza muda wa kupata mionzi. Sambamba na hilo, naomba Serikali wafanye tafiti mbalimbali kutafuta kila kinachosababisha ugonjwa na kuongezeka kwa haraka sana. Kansa inaua watu wengi sana. Kwa sasa inaonekana hakuna dawa kutokana na watu kukosa elimu ya kutosha kutokana na viashiria vya ugonjwa huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na ongezeko kubwa la wagonjwa MOI. Wagonjwa wa mifupa wamekuwa wengi wanakaa kwenye waiting list ya kusubiri operation kwa muda mrefu sana kutokana na kitengo hiki kuzidiwa na wagonjwa, lakini pia upungufu wa Madaktari. Pamoja na kwamba natambua kinachosababisha hayo ni wenye bodaboda, ndio walio wengi na wanasababisha ajali kuwa nyingi sana, majeruhi wamezidi MOI kutokana na ajali za barabarani: Je, Serikali inaisaidiaje MOI kudhibiti ongezeko la ajali za barabarani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali isaidie MOI kwa kuongeza kujengea uwezo Hospitali za Amana, Temeke na Mwananyamala. Serikali ikizijengea uwezo Hospitali hizo za Mkoa wa Dar es Salaam zinaweza kusaidia sana katika kuipunguzia MOI msongamano. Naomba pia hospitali hizo ziweke vitengo vya mazoezi ya viungo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza sana Kitengo cha Emergency cha Muhimbili. Kwa kweli wanafanya kazi nzuri sana kiasi cha kufanya wananchi wajenge imani ya kupona hapo. Kwa kweli wagonjwa walio wengi wanaokuja mahututi wanaamka hapo; kama kufa, wanaenda kufia kwenye wodi kama hawatapata huduma stahiki. Naomba vitengo vya emergency vya Hospitali ya Temeke, Amana na Mwananyamala nazo ziwe na vifaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na juhudi za Mkuu wa Mkoa kuamua kusaidia katika kujenga majengo ya huduma za dharura katika Hospitali za Temeke, Amana na Mwananyamala, lakini naomba Serikali iongeze nguvu kwa kuleta vifaa kwa hizo emergency Unit zilizopo, tupate angalau huduma kwa kipindi hiki cha mpito.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa uamuzi wake wa kujenga vyumba vya upasuaji kwa kila hospitali au zahanati kwa lengo la kuokoa afya ya mama na mtoto. Changamoto kubwa iliyopo Muhimbili imezidiwa na wingi na akinamama; wazazi ni wengi lakini watoa huduma ni wachache na hasa Wauguzi. Kwenye wodi moja unakuta wauguzi ni wawili. Naomba Serikali ituongezee Wauguzi na Madaktari katika Hospitali ya Temeke, Amana, Mwananyamala na Vituo vya Afya vilivyopo katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Dar es Salaam ina ongezeko kubwa la wageni wanaokuja takriban mabasi 300 yanaingia kila siku kutoka mikoani. Hivyo tunahitaji ongezeko la bajeti katika huduma za afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, magonjwa ya akili yameongezeka sana, kwa mfano Hospitali ya Temeke imetoka kwenye wagonjwa watano hadi saba mpaka wagonjwa 105 mpaka 120, lakini hakuna wodi za wagonjwa wa akili katika Hospitali za Mikoa ili kupunguza msongamano wa wagonjwa wa akili Muhimbili. Naomba Madaktari wapewe posho Maalum ya Mazingira Hatarishi ya maisha yao kwani wagonjwa wanaowahudumia ni wa hatari sana. Sambamba na Madaktari na Wauguzi wa Wagonjwa wa Akili, Serikali ifanye utafiti, ni tatizo gani linafanya ongezeko la maradhi ya akili kuongezeka kwa kasi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ugonjwa wa watoto kudondoka ni tatizo kubwa sana. Walianza wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari na sasa wanaanguka hata watoto wadogo ambao hawajaanza shule. Naiomba Serikali iangalie kwa kina, ni nini kimekosekana au ni madini gani yamekosekana mpaka watoto wanaanguka ovyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Vituo vya Madawa ya Kulevya vimezidiwa sana. Kulingana na juhudi za Serikali kupiga vita madawa ya kulevya, ambazo naunga mkono, ongezeko la wagonjwa hao ni kubwa sana na huduma inahitajika sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali iongeze vituo vya Methadone katika Hospitali ya Kigamboni kuwasaidia vijana kuepukana na tatizo la nauli ya kufika Temeke. Pia Kituo cha Muhimbili, Mbagala na Chamazi kinachohudumia wagonjwa wa akili, naomba kiwekwe kituo cha Methadone kusaidia vijana wa Mbagala, Chamazi,

Tuangoma, Kijichi na Mbagala Kuu wapate huduma hiyo kwa urahisi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Serikali kwa kutengea hii Hospitali ya Chanika ambayo itatusaidia sana katika kupunguza idadi ya wagonjwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Muhimbili, wodi ya wazazi mpya, kwa sisi Dar es Salaam tunaita Jengo la Rais Magufuli. Nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuwasaidia akinamama wajawazito. Kwa kweli jengo lile ni mkombozi wa wanawake. Limesaidia sana kiasi cha kujiuliza, wale akinamama kama kungekuwa hakuna jengo lile tungewaweka wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, akinamama wanaruhusiwa saa 8.00 mchana lakini wanatoka hospitali saa 2.00 usiku kusubiri bili za kawaida na Bima ya Afya. Kitengo cha accounts kiongezewe nguvu, kero hii ni kubwa. Usiku una mambo mengi, wazazi wanaweza kuibiana watoto ikawa tatizo kwa hospitali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, asilimia mia kwa mia.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniweka salama na kuweza kuwa na afya njema kwa siku ya leo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kwa umuhimu mkubwa napenda nimpongeze Mheshimiwa Rais wangu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa utendaji wao mwema uliotukuka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nitoe shukrani za dhati kwa Chama cha Mapinduzi - Mkoa wa Dar es Salaam kwa jinsi walivyopata shida, walivyohangaika na uchaguzi na hatimaye tukampata Mbunge mahiri, Mheshimiwa Mtulia wa Kinondoni. Kwa kweli ni jambo la kutukuka katika Mkoa wetu wa Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi kimepata nyongeza ya Mbunge, sasa tuko fifty-fifty. Ahsanteni sana akina mama wote wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa jinsi mlivyowajibika katika kupata nyongeza ya Mbunge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba niende kwenye Wizara ya Afya. Napo napenda nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Makatibu Wakuu na watendaji wote wa Wizara ya Afya kwa kazi kubwa wanayoifanya kuwahudumia wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika huduma za afya katika Mkoa wa Dar es Salaam zimeimarika kwa kiwango kikubwa sana. Napenda niipongeze Serikali kwa jinsi ilivyoimarisha huduma ya afya ya mama na mtoto katika Mkoa wa Dar es Salaam. Nawapongeze sana Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, timu yake, Wakurugenzi na Wakuu wa Wilaya zote za Mkoa wa Dar es Salaam jinsi wanavyoshirikiana katika kuhakikisha wanaboresha huduma za afya ya mama na mtoto katika Mkoa wa Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nitoe shukrani za kipekee kwa Kampuni ya Armson Groups ambayo imeweza kutujengea Hospitali za Afya ya Mama na Mtoto katika Hospitali ya Amana, lakini wanatarajia kwenda Mwananyamala na Temeke pia. Nampongeza sana mfadhili huyu na ninamwambia fungu lako utalikuta kesho kwa Mwenyezi Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nizungumzie juu ya huduma hizi zinazotolewa na Serikali, zizingatie idadi ya watu. Jimbo la Mbagala lina takribani idadi ya watu 1,100,000 lakini mpaka sasa hivi hospitali iliyopo ya Zakiem imezidiwa. Najua juhudi za Serikali wanataka kuboresha Hospitali ya Maji Matitu, lakini naiomba Serikali iiongezee pesa iwe hospitali kubwa. Idadi ya watu imezidi Mbagala na watu wanaongezeka kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naiomba Serikali iangalie eneo la Mbande. Kama ilivyo wanafunzi wa shule, madarasa hayatoshi kila siku, lakini na idadi ya watu inakuwa ni wengi, akina mama ni wengi, huduma inayotakiwa ya afya kule ni kubwa. Wakati tunaangalia maeneo gani tupeleke huduma tuzingatie na idadi ya watu. Akina mama wa Mbande na wananchi wa Mbande ambako wanakutana na Mkoa wa Pwani na Wilaya ya Ilala, pamoja na kazi kubwa iliyofanywa na Serikali ya kuweka ile Hospitali ya Chanika, lakini bado hawa watu wa Mbande wanakuja Zakhiem na Temeke hivyo. Naiomba Serikali iangalie hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niende kwenye Hospitali ya Mloganzila. Hospitali hii ni kubwa na nzuri, naipongeza sana Serikali, lakini bado ina upungufu wa madaktari na wauguzi. Wale ukifika pale unaambiwa mgonjwa wako huruhusiwi kumhudumia. Weka uji, weka maziwa hapo, lakini unakuta wodi nzima ina ma-nurse watatu, wagonjwa 50. Watawanyweshaje huo uji? Hata iweje, lazima kuna wengine watakosa huduma hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kinachonishangaza, lengo la Serikali katika kuanzisha ile Hospitali ya Mloganzila ni kwenda wanafunzi wanaojifunza udaktari na wanaojifunza uuguzi, wakajifunzie. Sasa wale wanafunzi, hivi hakuna wanafunzi wa practical? Wanafanya nini? Kwa nini wasiungane na wale ma-nurse na madaktari katika kusaidia wagonjwa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli madaktari wale na wauguzi wana kazi. Kunywesha kila mmoja umnyweshe na haruhusiwi ndugu yeyote kubaki pale, hili ni tatizo. Naiomba Serikali iangalie, kama imeshindwa kabisa, waache hata ndugu mmoja aweze kutoa huduma kwa mgonjwa wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa Serikali nayo iimarishe vitengo vya mifupa katika hospitali za wilaya na mikoa ili kusaidia mzigo mzito utakaoenda MOI - Muhimbili. Naomba Hospitali ya Muhimbili wangalie gharama… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuna tatizo la ucheleweshwaji wa bili kwa wagonjwa. Hilo ni tatizo kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, mengine nitayaleta kwa maandishi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Katibu Mkuu wa Wizara kwa kazi nzuri. Ninayo maeneo ambayo ningependa niyasemee.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukosefu wa maji safi na salama katika Wilaya ya Kigamboni, Wilaya hii hakuna utaratibu wa upatikanaji wa maji na mfumo wa utoaji wa maji taka. Eneo la Mbagala pamoja na jitihada za Serikali kuchimba visima virefu Mbagala na kusambaza maji lakini bado hatujafikia asilimia 100. Maeneo ya Chamazi, Mbande, Toangoma, Kibondemaji, Mchikichini na Mianzini hata visima vyenyewe ni vya shida.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu visima vya Kimbiji na Mpera, napongeza sana Serikali kwa kuchimba visima, vimekamilika kwa asilimia kubwa. Swali langu kama visima karibu saba vimekamilika kwa nini hakuna utaratibu wa kuanza sasa kusambaza maji angalau kwa kata zilizo jirani na visima hivyo? Kata ya Kisarawe II - Kibada, Pemba Mnazi na zile zilizo jirani tuanze kutumia maji ya visima hivyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mfumo wa maji taka, kwa kweli kuna tatizo la maji taka Kurasini, maeneo hayo yamekuwa ya mjini na mifumo imekuwa ya kizamani. Ni vema tukaangalia vizuri mfumo mzima wa maji taka Wilaya za Temeke, Kigamboni, Ubungo na Kinondoni. Ilala kuna nafuu kidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Bwawa la Kidunda; Serikali iangalie na waweke fedha katika Bwawa la Kidunda kusaidia upatikanaji wa maji kwa uhakika katika Mto Ruvu. Wakazi wa Dar es Salaam tunategemea sana Bwawa la Kidunda kupata maji safi ya kunywa toka Mto Ruvu, lakini kipindi cha kiangazi maji yanapungua, kwa hiyo tunahitaji hilo bwawa lijengwe ili lisaidie.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii ya Viwanda na Biashara. Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha siku hii ya leo kusimama hapa mbele na kuweza kuchangia katika Wizara hii. Pia niipongeze Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhakikisha kwamba tunapata Tanzania ya Viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefurahia kuona hotuba ya Mheshimiwa Waziri inaeleza wazi kwamba nchi yetu imekuwa na jumla ya viwanda 53,876 lakini katika hivyo viwanda vikubwa ni 251, viwanda vya kati ni 173, viwanda vidogo 6,957 na vile viwanda vidogovidogo sana ni 46,495, sio kazi ndogo. Mara nyingi huwa tunatoa mfano kujenga nyumba ni kazi ngumu lakini kusema nyumba hii mbaya ni kazi rahisi sana, unatumia maneno sita tu. Leo hii Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi imefanya kazi kubwa sana ya kuielekeza Tanzania yetu katika uchumi wa viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kusema peke yake hata kule kupiga debe ni kazi. Wananchi wa Tanzania sasa wameelekea katika kuileta Tanzania ya viwanda. Wawekezaji wote sasa wamebadilika na kutaka kuwekeza kwenye viwanda. Si jambo dogo lililofanywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimshukuru na nimpongeze Mheshimiwa Rais wetu, John Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuelezea na kutia nia yake ya dhati kabisa katika moyo wake kwamba anataka kuileta Tanzania katika uchumi wa viwanda. Lengo la viwanda si kwamba anavileta viwanda vile anataka kukuza ajira kwa vijana. Tumekuwa na vijana wetu wengi hawana ajira viwanda hivi vitakavyojengwa vijana wengi watapata ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mazuri yapo lakini changamoto kwa kila binadamu ipo na kwa jambo lolote utakalolifanya utakutana na vikwazo. Vikwazo hivyo vinaweza vikatatuliwa polepole lakini azma ya nchi yetu ni kuipata Tanzania ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuipongeza Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi kubwa inayoifanya sasa naomba nirudi katika mchango wangu na nitachangia kuhusu leseni za biashara. Nimeona wazi kuna eneo wamesema wameweza kutoza faini za kukiuka sheria za biashara takribani shilingi bilioni 9.7. Kitendo hiki cha watu kukiuka kukata leseni na kuingiza pesa kiasi hiki tunaweza kuona ni kizuri lakini ndani yake kuna ubaya, lazima tujiulize kwa nini wananchi wanakiuka?

Mheshimiwa Mwenyekiti, masuala ya leseni na hasa katika Jiji langu la Dar es Salaam imekuwa mtihani. Mama lishe akikaa barabarani hana leseni, mama lishe akijiongeza akasema nikachukue tu kakibanda kadogo niweke hapa sufuria yangu ya wali, vikombe vyangu na meza yangu moja imekuwa shida katika Mkoa wa Dar es Salaam. Mama lishe huyo ataambiwa aende kwanza Manispaa kuomba leseni, ataambiwa nenda TRA ukapate clearance, ukifika TRA hakuachi hivihivi akakupa ile clearance tax clearance ya hivihivi kwamba unakwenda kwanza biashara lazima uanze kulipia si chini ya Sh.300,000. Unawenda halmashauri wanakwambia ulipe leseni hiyohiyo Sh.100,000, unarudi Sh.500,000 imeshaondoka mama lishe huyu biashara hajaanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, akija kuanza biashara miezi mitatu anaambiwa ulipe kodi. Hivi huyu anayejitahidi kuboresha mazingira yake ndiyo sisi tunamuumiza kuliko yule aliyekaa pale anauza bila ya kitu chochote wala usafi. Nakuomba sana Mheshimiwa Waziri uliangalie hili akina mama wa Dar es Salaam kweli wanaendesha kwa kutumia biashara ndogondogo. Sisi katika Mkoa wetu wa Dar es Salaam hatuna mashamba ya kulima kwamba tunaweza kupitisha mazao yetu kwenye ki-carry kidogokidogo kukwepa kodi, sisi tunayo biashara. Biashara zetu ndiyo hizi akina mama kukaanga mihogo, kuuza ice cream lakini yule anayepata mtaji kidogo anahamisha mtaji wake, anauboresha, anaangalia ananunua viti vyake vya plastic sita, anaweka, anafanya biashara. Niiombe Serikali iangalie biashara za namna hii, waangalie jinsi gani watawaelekeza akina mama hawa waweze kulipa leseni vizuri si kwa uonevu, wala kukandamizwa na kodi lakini pia waweze na wao wenyewe kujiendesha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nije TBS. TBS si rafiki wa mfanyabiashara mdogo ni rafiki wa mfanyabiashara mkubwa. Nasema hivyo kwa sababu akina mama wa mkoa wangu wanatengeneza bidhaa mbalimbali zikiwemo sabuni, mafuta ya nazi, majani, mdalasini, wanajitahidi kwa kadri ya uwezo wao lakini wanavyokwenda TBS hawapati ushirikiano wa kuangalia ule ubora wa zile biashara zao hali ambayo inawafanya akina mama hao wakate tamaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimefuatwa na mabinti, nina deni la kulipa hapa Kinondoni, vijana wa filamu badala ya kuonyesha filamu wamejiongeza wakasema wao wawe wajasiriamali, wanatengeneza vitu vyao lakini TBS haiwapi ushirikiano kabisa. Nawaona wanatenga fedha za semina, semina hizo mnawapa akina nani wakati akina mama bado wanahangaika? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nichangie eneo la TANTRADE ambayo sisi tunaita Sabasaba. Niwapongeze sana hawa TANTRADE wanawezesha kuonyesha maonesho mazuri, watu wanajaa, wanapata fedha, lakini sisi kama akina mama wa Dar es Salaam tunafaidika na nini wakati hatuna hata banda?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sikatai kabisa na niwapongeze wanachukua akina mama Tanzania nzima. Sisi Dar es Salaam hatuna mgodi, ardhi ile ndiyo rasilimali iliyoko kwetu na uwanja ule ndiyo tunautegemea angalau na sisi Serikali ituwezeshe kupitia Uwanja ule wa Sabasaba. Leo hii akina mama wa Dar es Salaam wanahenyahenya tu mitaani inafika Sabasaba anaingia kwa tiketi anaenda kuangalia kazi za wenzie yeye kazi yake haipo. Niiombe Serikali, nikuombe Mheshimiwa Waziri utakaposimama unieleze kwamba Mkoa wa Dar es Salaam mwaka huu TANTRADE wako tayari kuwatengea banda angalau tent tu pembezoni na wao waweze kuonyesha bidhaa zao ili na sisi tuweze kufaidika? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna suala lingine kuhusu watoto. Watoto wa Temeke hawana sehemu ya kuchezea. Inapofika Sikukuu ya Iddi na Christmas wanazagaazagaa maeneo yale ya Uwanja wa Sabasaba, hawana pa kuchezea. Hivi Serikali inashindwa nini kuwafungulia watoto wale kucheza mle ndani ya uwanja siku ya Sikukuu ya Iddi na Christmas angalau na wao wafaidike na mradi ule wa Serikali yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyeki, lakini pia katika kuingiza watoto wale wakiletwa wajasiriamali wakaleta bembea na michezo mbalimbali ya kitoto, itaisaidia Serikali pia kuingiza mapato. Kwa hiyo, niiombe Serikali yangu wafanye jitihada ili watoto wetu nao wakafurahie uwanja ule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nichangie kuhusu masoko. Ni ukweli kabisa kuna tatizo kubwa la masoko. Pamoja na kuhangaika kote na viwanda, bado bidhaa zetu zinakosa masoko. Mimi nashindwa kuelewa, bidhaa za Watanzania tunafika sehemu tunahamasisha lakini baada ya kutengeneza kile kitu unakuta gharama yake imekuwa kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa kumpongeza Waziri na Watendaji wote wa Wizara hii. Kazeni mwendo, mwendo huo huo, Mwenyezi Mungu atawasaidia.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja asilimia moa moja. Nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Makatibu Wakuu na watendaji wote wa Serikali kwa kazi kubwa wanayoifanya. Ninao mchango wangu katika mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, naishukuru sana Serikali kwa kutoa fedha za miradi ya kimkakati katika Halmashauri zetu. Ni jambo jema sana na nina hakika kile kilio chetu cha kudai kodi zetu za majengo kimepata majibu. Nashukuru sana Serikali naomba tuendelee hivyo, watukusanye fedha wazirudishe kwenye miradi ya kimkakati.

Mheshimiwa Spika, naomba Serikali isaidie Halmashauri ya Temeke kulichukua deni la CRDB Bank ambazo Manispaa ya Temeke walikopa kwa kulipa fidia katika mradi wa DMDP lakini Halmashauri nyingine walipewa fedha hizo na Serikali. Deni lile ni kubwa na lina riba na chanzo kikubwa kilichoshawishi Halmashauri wachukue ni kodi za majengo ambazo hazipo kwa sasa.

Mheshimiwa Spika, naomba sana Serikali isaidie Halmashauri, vinginevyo tunajisikia vibaya na tutakosa miradi ya kasi kuwa wa kwanza katika kutekeleza maagizo ya Serikali. Serikali wakae na Halmashauri zetu kuangalia biashara gani zinazopaswa kulipiwa kodi na zile ambazo hazitakiwi kulipiwa kodi wananchi waelewe. Kuna biashara zinatozwa kodi lakini ukiangalia mtaji wake ni wa shilingi 500,000 tu. Serikali ina taasisi nyingi za fedha za kusaidia wananchi kupata mikopo na fursa mbalimbali kama UTT na kadhalika. Lakini wananchi hawazitambui, Serikali ifanye juhudi za makusudi kuzifanyia mkakati wa kuziweka wazi kwa wananchi zinaweza kutusaidia kuondoa umasikini.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja asilimia mia hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri kwa asilimia mia moja. Nampongeza Mheshimiwa Waziri na Manaibu wake kwa kazi nzuri wanazofanya, ni nzuri na zinaonekana. Niwapongeze pia Makatibu Wakuu wa Wizara kwa kuendesha vyema Wizara. Naomba changamoto zifuatazo tuzifanyie kazi:-

Ujenzi wa barabara ya Nzasa-Kilungule-Buza; barabara hii ni muhimu sana, Serikali imelipa fidia kwa wananchi kwa lengo la kuingia mradi wa DMDP, lakini mradi huo inasemekana hauwezi kuingia katika DMDP. Je, zile fedha za fidia si tungeweza kujenga barabara angalau kwa nusu kilomita? Je, nini hatima ya barabara hiyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naweka maslahi wazi, mimi nilikuwa Mwalimu; Walimu kuwahamisha kutoka msingi kwenda sekondari ni jambo jema, lakini halijazoeleka katika nchi yetu. Zamani ukirudishwa msingi kutoka sekondari ni demotion. Je, Serikali imewapa elimu Walimu watambue Mwalimu anaweza kufanya kazi msingi au sekondari kwa ngazi ya mshahara ule ule? Je, Serikali imejipanga vipi kuweka Counselors katika Halmashauri zetu kwa kutoa ushauri nasaha kwa makundi mbalimbali yanayofanyiwa mabadiliko ya kimfumo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, utoaji wa vibali vya ujenzi katika Halmashauri zetu; kweli Serikali imefanya vizuri kwa kufupisha muda wa kupata kibali cha ujenzi, lakini kibali kinachotoka Halmashauri hakipewi heshima kama kimepitishwa na wataalam mbalimbali matokeo yake wanakuja wahindi na Ma-architect kutoka maeneo mengine kuvitengua na kudai malipo upya. Kwa nini hawa wanataka kupitia wasiungane na Halmashauri, mwananchi akipata kibali aendelee na ujenzi badala ya kusimamishwa kila mara?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mabasi yaendayo kazi; napongeza Serikali kwa mradi huu ni mzuri na unasaidia. Naomba sasa angalau uanze ujenzi wa mwendokasi Mbagala kwa kuwa hatua iliyobaki ni ulipaji wa fidia ya stendi ya Mbagala Rangitatu. Naomba sasa tuanze ujenzi wa barabara huku tukiendelea na zoezi la stendi, ni jambo jema, nalitakia heri lifanikiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napongeza juhudi za Serikali kwa maboresho ya barabara za Mitaa ya Kariakoo, Gerezani na Upanga kwa kweli inapendeza na kazi ni nzuri kwani maeneo hayo yalikuwa na barabara mbaya sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nawapongeza viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa na Katibu Tawala, Wakurugenzi wa Halmashauri zangu zote za Mkoa wa Dar es Salaam na Wakuu wa Wilaya wote, Ma-DAS wote kwa ushirikiano mkubwa wanaonipa na kuweza kutekeleza majukumu yangu bila kikwazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TARURA waongezewe nyezo za kufanyia kazi kama magreda, makatapira na vifaa vingine vya ujenzi. Kwa kuwategemea wakandarasi wa kukodishwa linapotokea tatizo, hakuna wa kuli-solve haraka sana. TARURA pia waangalie wakandarasi wa kuwapa kazi, kuna tofauti kubwa kati ya barabara za TANROADS na TARURA kwa zile za changarawe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za wanawake na vijana, benki wanazitoza riba lakini halmashauri wana Wahasibu. Kwa nini utaratibu usifanyike fedha zikatolewa katika Halmashauri zetu na kama ni benki kusiwe na riba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, bajeti ipite, maendeleo yafanyike, tupate matokeo ya haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
TAARIFA YA KAMATI YA HAKI, MAADILI NA MADARAKA YA BUNGE KUHUSU SHAURI LA KUDHARAU NA KUDHALILISHA BUNGE LINALOMKABILI MHE. GODBLESS JONATHAN LEMA (MB)
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kwenye azimio hili la Kamati ya Maadili ya Bunge.

(Hapa baadhi ya Wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani walitoka Ukumbini)

SPIKA: Mbona mmeanza kukimbia tena? Mmeshaingia baridi?

MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, kwanza napenda nikupongeze kwa jinsi unavyoliongoza Bunge letu, unatuongoza vizuri kama Wabunge.…

SPIKA: Hapana, mtu yeyote asifanye fujo. Anayetoka atoke. Mtu yeyote asifanye fujo. Leo Bunge hili litaendeshwa kisayansi. Msiwe na wasiwasi. Mheshimiwa Mariam Kisangi.

MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, sawasawa. Wewe ndio kiongozi, tumekuchagua na wewe ndio mwenye mamlaka ya kuweza kupanga taratibu zote za Bunge.

SPIKA: Namwambia Serjeant-at-arms, habari ya watu kutoka hapo nje mara sijui Waandishi wa Habari na nini, marufuku! Anayetaka sijui kuongea ongea nini, nje ya geti.

MHE. MARIAM N. KISANGI: Sawasawa.

SPIKA: Anayetaka kuongea, aongee humu ndani. Naomba Serjeant-at-arm awe macho hapo. Endelea Mheshimiwa Mariam.

MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, nia yako ni njema. Unapomwambia mtu yeyote ambaye amelikosea Bunge kumpeleka kwenye Kamati ya Maadili, kwa maana nyingine ulikuwa unawasaidia watu hawa kwa sababu Kamati ya Maadili siyo Kamati ya kuadhibu mtu tu, bali ni Kamati ambayo inazingatia maelezo ambayo mtu anatoa; na pale anapoomba msamaha, Kamati hii haiwezi kuacha kumsamehe.

Mheshimiwa Spika, lakini watu wanapokuja kwenye Kamati ile na kuendeleza ubabe na kuendeleza maneno yasiyofaa, ile Kamati, sisi ni Wabunge lakini pia tunao uwezo wa kufikiri na kuangalia nini kinachoendelea katika maisha na taratibu za nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Bunge leo ni mhimili. Mhimili wa Bunge unaunganisha viongozi mbalimbali wa Kitaifa wakiwemo Waheshimiwa Mawaziri, Waziri Mkuu, Mheshimiwa Spika mwenyewe na viongozi mbalimbali. Sasa inapotokea mtu akasimama akasema kwamba Bunge ni dhaifu, hatuwezi kukubali.

Mheshimiwa Spika, sisi Waheshimiwa Wabunge tumepata taabu kugombea leo hii kuja kuwawakilisha wananchi hapa. Leo hii akili zote hazipo, ziko Majimboni. Tunapofika hapa Bungeni tukasema dhaifu, ina maana sisi dhaifu? Siyo sawa. Serikali yetu, Wabunge ndio tunaopitisha Bajeti, ndio tunaopitisha miradi mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, leo katika Mkoa wa Dar es Salaam miradi yote muhimu; mwendokasi, barabara nane, miradi kibao imeenda, kazi yote hiyo na Mbunge, iweje leo Bunge hili liambiwe kuwa ni dhaifu? Hiyo haiwezekani.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono azimio hilo. Nasema yote yaliyopendekezwa kwenye Kamati ni sawa sawa. Tuchukulie pia hili Bunge kuna watu mbalimbali wanakuja kujifunza humu ndani ya Bunge. Tunao vijana huko juu, wanafunzi wa Shule za Msingi, Sekondari, Vyuo Vikuu, wanakuja kujifunza katika kwenye Bunge hili, tafiti mbalimbali zinafanyika katika Bunge hili, leo anatokea mtu huko anakuja kusimama kwamba Bunge hili ni dhaifu, sisi tukubaliane naye! Hatuwezi kukubali, tunaungana nawe Mheshimiwa Spika, lazima Bunge letu sasa liwe na nidhamu. Wabunge tuwe na nidhamu, tuangalie mazingira gani ambayo unaweza ukaongea maneno gani.

Mheshimiwa Spika, upotokaji wa maadili unazidi kuwa mkubwa ndani ya Bunge. Kwa maana hiyo, azimio hili la Kamati iwe fundisho sasa kwa Wabunge wengine na viongozi wengine walio nje au ndani ya Bunge kwamba wauheshimu mhimili wa Bunge. Bunge linafanya kazi kubwa sana na linapitisha mipango mbalimbali ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, pia napenda nitoe angalizo kwa Waheshimiwa Wabunge wetu vijana, kama Mheshimiwa Godbless Lema, sisi tunawategemea vijana, sisi ni watu wazima, umri unaenda, tutafika sehemu itabidi tuwaachie vijana hawa waendeleze nchi yetu. Leo Mbunge anasimama anaongea maneno yasiyofaa ndani ya Bunge, anatuambia nini sisi kama wazee ambao tunawatarajia wao tuwape nafasi hizi waendeleze Taifa hili? Je, viongozi kama hawa tukiwapa nafasi wataliacha salama Taifa letu kwa utovu huu wa maadili?

Mheshimiwa Spika, tumekumbana na hii hali kwa muda mrefu, sasa umeamua na sisi tuko tayari kuku-support, hatuwezi kukubali kwamba Bunge liwe mtu anasimama anatukana anafanya hivi na hivi kisha anaachiwa. Hiyo haikubaliki hata kidogo. Lazima taratibu za Bunge zifanywe.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuambiwa huyu Godbless Lema kwamba yeye amekosea aliambiwa siku moja kabla kulikuwa na masaa 24 kwa mtu huyu kutafuta njia mbalimbali za kutubu na kuomba msamaha kwa kosa lake. Bunge kuna taratibu mbalimbali kwa mujibu wa kanuni. Kuna hoja binafsi, kuna kumwandikia Spika, kuna kumwomba Spika, lakini Mbunge huyu hakutaka kufanya taratibu yoyote ya kutaka kujinusuru na kuona kwamba labda kauli ile niliitoa kwa bahati mbaya aweze kupata msamaha.

Mheshimiwa Spika, kwenye Kamati tulimwomba sana; je, kijana wetu huwezi kujutia hilo tatizo lako? Kwa mapenzi makubwa. Anasema mimi nimekubali, kama kufungwa nitafungwa, nimefungwa sana, jambo ambalo siyo sawa.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono Azimio hili la Bunge na niwaombe Wabunge wenzangu kwamba sasa ifike sehemu awe Mbunge gani kama ulivyoongea kwamba awe Mbunge wa Chama gani, bila kujali Chama, wote kwa pamoja tuzingatie nidhamu na maadili ya Bunge.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kujadili hoja hii ya TAMISEMI. Kwanza napenda kuipongeza sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa jinsi ilivyoweza kutekeleza Ilani yake ya Chama cha Mapinduzi; kwa kipindi hiki cha miaka mitatu tumefikia asilimia 90, hali ambayo inawafanya wenzetu wa upande wa kule waanze kutetemeka. Nasema Chama cha Mapinduzi kiko vizuri na Serikali ya Chama cha Mapinduzi iliyoko madarakani inafanya kazi nzuri na tutaona 2020 tumejipanga vizuri, Wabunge wa Chama cha Mapinduzi watatawala katika Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nipongeze Serikali yangu na nimpongeze Mheshimiwa Rais, Dkt. Magufuli kwa utendaji wake mzuri uliotukuka wa kujali wananchi wake katika maeneo mbalimbali bila kujali jimbo hili ni la nani, jimbo hili ni la Chama cha Mapinduzi, jimbo hili ni la Upinzani, Mheshimiwa Rais wetu anafanya kazi kwa ajili ya wananchi wake bila kuangalia tofauti za chama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme nchi yetu, au Serikali yetu ni kweli inaendeshwa katika misingi ya utawala bora, misingi ya utawala bora inazingatiwa na ndiyo sababu tuko hapa. Utawala bora uko katika maeneo mbalimbali; uko katika viongozi lakini uko katika wale wanaoongozwa pia. Ili nchi yetu iwe vizuri, wote tunatakiwa tuendeshe nchi yetu na tuishi sisi kama viongozi kwa kuzingatia misingi, maadili, kanuni na taratibu za nchi yetu, kiongozi ambaye atakwenda tofauti na maadili ya nchi, huyu hatakubalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nije kwenye hoja ya TAMISEMI; kwanza napenda nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Waziri wa Utawala Bora, Naibu Mawaziri wote kwa kazi nzuri. Kwa kweli Serikali yetu imefanya kazi nzuri kwenye ujenzi wa hospitali za mikoa na wilaya wameweza kutoa karibu bilioni 1.5 kwa kila mkoa ambao hauna hospitali za mikoa na zile za wilaya. Pia ujenzi wa zahanati na ukarabati wa vituo vya afya Tanzania nzima, karibu vituo 325 ambavyo umegharimu bilioni 184.67, si jambo dogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika maboresho ya Jiji la Dar es Salaam kwa kweli Jiji la Dar es Salaam sasa hivi limefanyiwa maboresho makubwa sana, lazima tuseme, ni ukweli usiopingika. Dar es Salaam ukienda kila kona unakutana na ujenzi wa barabara, sio kazi ndogo iliyofanywa na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutoa shukrani hizo, sasa nakuja kwenye mchango wangu ambapo nitajikita moja kwa moja katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, ukurasa wa 29, 83 na 87. Naanza na ukurasa wa 29 wa maboresho ya huduma za afya, kweli hospitali na vituo vya afya zimeboreshwa tena siyo vile vya Serikali tu, Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi katika utekelezaji wake wa Ilani kwa kutumia Mfuko wa Bima ya Afya umeweza kukarabari hospitali binafsi pia. Kwa kweli leo hii ukienda zahanati ya binafsi siyo ile iliyokuwa mwaka 47, utakuta ina miundombinu mizuri na iko vizuri kwa kweli zahanati za Mkoa wa Dar es Salaam zipo vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ukarabati huo, niiombe Serikali iiangalie kwa jicho la huruma Zahanati ya Mbagala Zakhem. Kweli Mbagala Zakhem kuna tatizo la ardhi kwamba eneo ni dogo lakini kama Halmashauri tumeboresha Hospitali ya au Zahanati ya Maji Matibu na Charambe ili kusaidia wale wananchi lakini ukweli utabaki kuwa ukweli jiografia ya Mbagala na jinsi Mji wa Mbagala unavyokuwa kwa kasi Hospitali ya Zakhem iko barabarani hivyo inapotokea majeruhi anapelekwa pale baadaye anapelekwa Temeke. Huwezi ukamtoa mtu Mbagala Zakhem ukamrudisha Mbagala Maji Matitu akatokee wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana Serikali, pamoja na mambo yote mazuri tunayofanya tuiangalie hospitali ile kwani kutwa inapokea majeruhi, watu ambao wamejaa pale Mbagala, wafanyabiashara, wajasiriamali na watu wote wanaopata matatizo wanakimbilia pale. Kwa hiyo, Hospitali ile ya Mbagala Zakhem imezidiwa pamoja na kwamba kuna zingine pembezoni lakini ile bado inauhitaji wa aina yake, niombe Serikali iongeze nguvu kusaidia eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye ukurasa wa 83, Tume ya Utumishi ya Walimu, niseme ukweli kwamba bado lipo tatizo kwa walimu. Walimu wanadai hela zao za promosheni mpaka wengine wanafikia kustaafu lakini bado wanadai. Pia walimu wanateseka bado wanadai nauli zao. Ninao mfano wa walimu wa Halmashauri ya Temeke, wale ambao wamestaafu mpaka leo hawajalipwa nauli zao na hela zao za promosheni. Walimu wale wanahangaika wakati wameitumikia nchi kwa uadilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nikiwa mwalimu ambaye nimetoka kwenye elimu ya msingi, walimu wenzangu wananiuliza yaani wewe umefika huko mjengo unatusahau? Nawaambia sijawasahau na ni wajibu wangu kuwasemea. Niiombe Serikali ichukue hatua na ishuke kwenye Halmashauri iwaulize tatizo ni nini mpaka hawa walimu hata anayemaliza leo na bajeti zipo kwa nini hawalipwi? Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri ukaliangalie hilo, walimu ni walezi, wamelea watoto zetu wametulea mpaka wenyewe Wabunge hapa wote tumepitia kwenye elimu, kwa hiyo naomba waendelee kuwajali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye ukurasa wa 87, mradi wa DMDP, nitoe shukrani za dhati kabisa kwa Serikali kwa uwezeshwaji wa mradi huu. Mradi huu umeleta maendeleo makubwa katika Jiji letu kwani sasa limebadilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Mbagala Kijichi huwezi kudhani kama ni Mbagala ile, barabara zimetawala, soko la kisasa na miradi kadha wa kadha imejengwa. Pia katika maeneo ya Yombo Vituka, Kilakala, Tegeta, Mikocheni, Buguruni, Ilala, Upanga, Temeke, Chang’ombe, barabara ile imepanuliwa kwa mradi wa DMDP, ni jambo kushukuriwa. Vilevile barabara ya Ubungo, Kibamba na Gerezani, zimeshughulikiwa, kwa kweli hali za barabara zetu katika Jiji la Dar es Salaam ni nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tunasimama hapa ndani mimi na Mheshimiwa Mnyika tunazungumzia barabara ya Kibwegele – Kibamba, leo hii Mnyika amenyamaza kimya anahangaika tu na mambo yake ya Mahakama. Hii yote ni kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na Serikali katika Jimbo la Kibamba na Mkoa mzima wa Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende kwenye upande wa mabasi yaendayo kasi, kwa kweli niipongeze Serikali sasa mabasi yaendayo kasi mradi ule unatekelezeka. Tayari fidia zimelipwa na unaanza kujengwa kwa mabasi yanayoanzia kutoka Gerezani kwenda Mbagala Rangi Tatu. Tunamshukuru sana Mungu na Serikali yetu kwa kuliwezesha hilo. Mradi ule utakapokuja pale Mbagala Rangi Tatu maeneo ya Mbagala, Charambe, Kiburungwa, Mianzini yatapanda thamani kutokana na miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini najua penye jambo jema hapakosi changamoto. Kweli mradi wa mabasi ya mwendo kasi hivi karibuni umeleta umeleta changamoto kubwa kwa hasa yale yanayotoka Mbezi, Kimara kwenda mjini, kweli kumekuwa na uhaba. Nikushukuru sana Mheshimiwa Waziri jinsi ambavyo unakwenda kufuatilia kwa karibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiulize Serikali ule uhaba wa mabasi unatokana na nini? Niishauri Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kama ina fedha nyingi pamoja na mabasi yake ya utalii basi yale mabasi ya utalii iongezewe nguvu Halmashauri ya Jiji waweze kununua mabasi ya akiba iwapo kutatokea tatizo lolote basi mabasi yetu wenyewe ya Serikali au Halmashauri ya Jiji yawe yanaingia kwenye miundombinu ya mwendo kasi kuwasaidia wananchi wa Dar es Salaam.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Mariam.

MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, naipongeza Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, iendelee hivyo hivyo. Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu na Makamu wa Rais wote kwa pamoja pigeni kazi wananchi wanawaamini. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi kwa Serikali Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri na Makatibu Wakuu kwa kazi nzuri wanazozifanya za ujenzi wa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, NEMC; naomba Serikali waangalie utendaji wa NEMC kwani washauri wanachukua fedha nyingi kuliko Serikali. Waangalie mradi gani unahitaji upembuzi wa muda mrefu na mengine kama imeshapitishwa na Halmashauri NEMC wapitishe kwa haraka. NEMC na taasisi nyingine kama EWURA na wengine wakae pamoja na kutafuta njia nyepesi ya kuwasaidia wawekezaji wa mafuta (naweka maslahi wazi ni mdau). Badala ya kulipa malipo makubwa mara moja, nashauri katika kukuza na kuendeleza uwekezaji waweke tozo ambazo zinaweza kulipwa kila mwaka, hii itasaidia hata wawekezaji wadogo kuweza kumudu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mifuko ya plastic; naipongeza Serikali kwa uamuzi wake wa kupiga marufuku kwani mazingira yetu yaliharibika vibaya kutokana na mifuko kujaa ardhini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Muungano; naipongeza Serikali kwa kujitahidi kutatua kero za Muungano kwa kiasi tulichofikia inatia moyo sana. Tudumishe Muungano wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri na Katibu Mkuu kwa kazi nzuri wanazofanya. Nashukuru kwa kuimarisha huduma ya afya ya Mama na Mtoto hali ambayo imesababisha katika Hospitali ya Temeke mwezi Machi hakuna kifo cha uzazi. Yote hayo yametokana na kuimarika kwa huduma zote za afya ya Mama na Mtoto katika Hospitali ya Temeke.

Mheshimiwa Naibu Spika, mambo yafuatayo yazingatiwe (changamoto):-

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba mashine za CT Scan kwa Hospitali za Mkoa wa Dar es Salaam, Temeke, Mwananyamala na Amana. Hospitali hizo hazina mashine za kufulia nguo, mashuka mpaka yapelekwe Muhimbili jambo ambalo linafanya kipindi fulani mashuka yanapungua hospitalini.

Mheshimiwa Naibu Spika, gharama kubwa za matibabu kwa hospitali zinazopitia Wakala wa CRDB, unatakiwa ununue kadi kwa Sh.10,000 au utumie ya Wakala kwa Sh.2,000 kila unapokwenda hospitali. Mifumo ya Serikali itumike, kwani inaweza kusaidia zaidi wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, malipo ya fedha kwa maiti ni changamoto kubwa. Mtu anapofariki na deni la dawa anatakiwa kulipiwa na ndugu, unafikia wakati ndugu wanashindwa kulipia hapo viongozi tunashirikishwa na maiti kukaa muda mrefu. Naomba Serikali watoe ufafanuzi kuhusiana na jambo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, unapoenda na mgonjwa mara nyingine Emergeny Muhimbili unamlipia mgonjwa, tena unapewa bill ya dawa usiku Sh.500,000 na zaidi, lakini baada ya sekunde unakuta mgonjwa amefariki. Kutokana na panic unaacha kila kitu, kwa nini tusiwe na kianzio cha dawa kwa wagonjwa wanaokuja kuanza matibabu kabla ya kupewa bill?

Mheshimiwa Naibu Spika, hospitali/zahanati ya Mbagala Zakhem imezidiwa sana, eneo ni dogo na wananchi wanaohitaji huduma ni wengi sana kutokana na kukua kwa Mji wa Mbagala na ongezeko kubwa la watu. Pamoja na jitihada za halmashauri kujenga zahanati ya Maji Matitu na Charambe, lakini jiografia inakataa kwa kuwa mgonjwa akitoka Zakhem anaenda Temeke na Zakhem ni katikati ya Mji wa Mbagala. Naomba Serikali isadie hata kujenga ghorofa la OPD kwa wagonjwa wa kawaida.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, hoja hii ya Bajeti ya Serikali. Nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Makatibu Wakuu na Watendaji wote wa Serikali kwa kazi nzuri na ngumu wanazozifanya kuhakikisha nchi yetu inaenda vizuri. Bajeti ya Serikali iliyosomwa ni nzuri sana na imegusa maeneo mbalimbali, lakini pia, kuondoa tozo ambazo zilikuwa kero kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na Bajeti ya Serikali kwa jinsi ilivyowasilishwa pamoja na Mpango wa Maendeleo wa Taifa na utekelezaji wake kama inavyoonesha katika ukurasa 138. Kwa kweli, mambo mengi yaliyopo katika mpango yamefanikiwa kwa kiasi kukubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, maoni yangu kwa upande wa biashara ni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza natoa pongezi kwa Serikali kwa kutoa muda wa miezi sita kwa wafanyabisahara wanaoanza biashara na kulipa kodi kwa muda huo. Kwa kweli, hii ilikuwa ni shida kubwa kwa wafanyabiashara wenye mitaji midogo. Shukrani sana kwa kulitekeleza hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, naomba kwanza kuweka maslahi yangu wazi kuwa, mimi ni mdau wa sekta ya mafuta. Tatizo kubwa la wawekezaji wa mafuta na gesi na hata wawekezaji wengine ni vibali vya kuanzisha ujenzi wa biashara ambavyo, lazima ufike EWURA, NEMC, OSHA, Bodi ya Majengo, Bodi ya Architect, TRA, Halmashauri/ Manispaa, Ardhi, Bonde la Mto/Visima. Kwa kweli kazi hiyo ni kubwa sana mara nyingine unatamani kuacha kuwekeza. Ushauri wangu, kwenye One Stop Centre ya uwekezaji kuwepo na wahusika hao wote ili wananchi wanapotaka kuanzisha biashara wanawaona. Ni bora kulipa gharama kubwa wakati mmoja kuliko usumbufu usiokuwa na mwisho.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, biashara ya mafuta kwa maoni yangu naona ilikuwa imekaa vizuri, tatizo ni wale mawakala ambao wanalipwa Sh.2,830,000/= kwa mwaka, lakini mashine zinapoharibiwa wanakuwa wazito kuja kurekebisha, ndio tatizo. Kwa maoni yangu naona mfumo wa EFD za vituo vya mafuta ukiboreshwa hali itakuwa nzuri zaidi kwa kuwa, sekta ya mafuta ilikuwa na ubabaishaji mkubwa sana, lakini kwa kutumia mashine hizi Serikali imepata kodi zake na hali imezoeleka tusibadilishe kwa haraka mfumo uliopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Bandari; naungana na Serikali kwa kuruhusu watu kuingia bandarini kutoa mizigo yao, lakini ulinzi uboreshwe kwa kuwa, mizigo ni mingi. Tukiingia wote inaweza kuwa ni vurumai ndani ya bandari japo kwa upande mwingine wataamsha na kuleta uhai wa bandari.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa kupongeza Serikali kwa kudhibiti mfumo wa bei na hasa katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Nazi iliuzwa mpaka 500/= na vitu vyote bei ilishuka ghafla na kuwa chini, haijawahi kutokea kwa miaka zaidi ya 10, sijawahi kuona hali hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kunipa nafasi niweze kuchangia katika Wizara hii. Kwanza kabisa napenda kumpongea Mheshimiwa Waziri na Manaibu Waziri wake, Makatibu Wakuu na watendaji wote wa Wizara hii kwa utendaji wao mahiri katika Serikali yetu. Lakini napenda nitoe salamu za pongezi kwa Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uamuzi wake wa busara wa kununua ndege sita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi ni Wabunge tunafika sehemu lazima tuwe wa kweli nchi yetu kwa kukosa ndege ilipwaya. Leo anatoka mtu anasema kwamba ndege hizi hazina faida zina hasara kubwa lazima tuwe wa kweli faida ya ndege huwezi kuiona hivi hivi, kuna mambo hayawezi kuonekana moja kwa moja. Kwanza ndege zinasaidia katika eneo la utoaji wa huduma kwa haraka katika nchi lakini pia ndege itasaidia kutangaza Utalii, pia zinasaidia kutuletea fahari yetu kama Watanzania na sisi tunapoona Twiga wetu wa ATCL anaruka kutoka kwenye nchi yetu kwenda kwenye nchi jirani kama mtanzania na mzalendo kwa kweli unajisikia moyo wako una amani kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia ndege hizo ziteleta fedha zitasaidia katika kuongeza mapato ya Serikali kupitia uwekezaji utakaoendelea kutokana na kutangazwa kwa Utalii na mambo mbalimbali katika nchi za jirani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo napenda tena nimpongeze Mheshimiwa Rais tena wa Jamhuri ya Muungano kwa kuwa Rais wa Watanzania wote bila kujali ametoka katika mkoa gani. Nasema hayo kwa uzalendo mkubwa nikiwa na ushahidi kwa yale yaliyotendeka katika Mkoa wa Dar es Salaam. Katika Mkoa wa Dar es Salaam katika kipindi kifupi kumefanyika miadi ifutayo;

(i) Lilikamilika daraja la Kigamboni,

(ii) Flyover ya TAZARA ya Mfugale,

(iii) Interchange ya Ubungo imeanza,

(iv) Barabara nane Kimara kufika Kibaha mradi huo umeanza,

(v) Ujenzi wa daraja la Mlelakuwa umekamilika,

(vi) Ujenzi wa daraja la Salenda umeanza na uko kwenye hatua nzuri, Kuanza kwa barabara na miundombinu ya mwendokasi kutoka Gerezani, Bendera Tatu mpaka Mbagara Rangitatu. (Makofi)

(vii) Ujenzi wa Uwanja wa ndege wa Kimataifa umekamilika kwa asilimia 90 ,

(viii) Ujenzi wa reli na upanuzi wa bandari gate namba 13 umekamilika bandari ya Dar es Salaam, maboresho makubwa ya barabara katika Mkoa wa Dar es Salaam kupitia mradi wa DMDP kwa kweli yameleta sura nyingine kabisa katika Mkoa wa Dar es Salaam. Hayo yote yametokana na uzalendo wa Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano ambaye yeye kujali nini ni Rais wa Watanzania wote akaona pamoja na kuhama kwa Makao Makuu kutoka Dar es Salaama na kuwa Mji wa kibiashara basi mambo haya yameboreshwa.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutoa pongezi hizo kwa Serikali sasa naomba nijikite mchango wangu katika ukurasa wa 24 barabara ambazo zimekamilika ziko katika upembuzi yakinifu. Barabara ambayo iko kwenye upembuzi yakinifu ni barabara ya Kibada, Tudwi, Songani, barabara hii kwa kweli yaani ni ya muda mrefu kila wakati ipo kwenye upembuzi wananchi wa kule Tundwi Songani wako katika hali mbaya sana mvua zinaponyesha wanakuwa hawana mawasiliano kabisa. Niiombe Serikali yangu waangalie kwa jicho la huruma wananchi wale wanaokaa Tundwi Songani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia barabara nyingine ambayo ipo kwenye upembuzi na kuanza ni barabara ya Mbagala Rangi Tatu, Kongowe pamoja na daraja la Mzinga. Niiombe Serikali hii barabara ni muhimu sana watu wote wa Kusini lazima wapite kwenye daraja la Mto Mzinga lakini daraja lile sasa hivi limewekwa daraja la muda lile la kijeshi hakuna hata pembezoni sehemu ya kupita watu watu wakiwa kundi hawawezi kuvuka pale. Kwa hiyo, niiombe Serikali waharakishe barabara hii kwa ajili ya watu wanaoelekea katika mikoa ya Kusini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kuna barabara ya Kongowe, Mji mwema Kivukoni tunaomba barabara hiyo iko kwenye mpango kabisa wa kujengwa kweli barabara hiyo itakapojengwa waangalie jinsi ya kuiongeza upana, barabara sasa ni finyu na mji wa Kigamboni sasa umekuwa tumekuwa na Wilaya mpya ya Kigamboni, kwa hiyo, barabara ile pamoja na kuboreshwa bado waongeze upana wa barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara ya Kitunda, Kivule kwenda Chanika Msongola. Barabara hii muda mrefu inajengwa vipande lakini hatuelewi kwa nini Mheshimiwa Waziri nakuomba sana utakaposimama uje unieleze hii barabara ya Kitunda, Kivule kwenda Msongola ina matatizo gani mpaka haiendelezwi? Wananchi wa kule wamechoka. Mbunge ninayetoka Dar es Salaam wameniomba nije nikuombe na utakapomaliza Bunge uende pale ukaeleze wananchi wa kule hivi ni sababu gani zinakwamisha ujenzi huu usiende vizuri? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nije kwenye barabara ya Nzasa, Kilungule, Mwanagati, Buza. Barabara hiyo kila nikisimama hapa Bungeni hebu Mheshimiwa Waziri unionee huruma wananchi wa kule bado kunahitaji daraja la Kilungule kwenda Mparange wananchi wanavuka daraja la miti kama wako kijijini kumbe ni Jiji la Dar es Salaam ile hali haipendezi nikuombe Mheshimiwa Waziri kila siku tunaambiwa pesa iko tayari kila kitu kiko tayari mkandarasi atatangazwa kesho, kesho hii itaisha lini? Naomba sasa barabara hii itekelezwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nichangie kwenye eneo la bandari, napenda kutoa pongezi kutokana na taarifa kwamba bandari imefanya vizuri, kama inafanya vizuri basi ndio tunavyoomba niombe sasa liko tatizo bandari baada ya mkumbo wa vyeti feki hakuna waajiriwa wengi walitoka, sasa hivi Serikali inawatumia SUMA JKT kuajiri vibarua. Natoka Mbagala lazima nikatishe bandarini kila siku watoto wale wanajaa pale nje wanasubiri kibarua cha shilingi 9000 lakini sasa tuone kibarua kile niiombe Serikali tumuamini kuna Mkurugenzi wa Bandari na ni Mkurugenzi mahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama ni Mkurugenzi mahili kwa nini hamna maeneo ambaayo mkaangalia jinsi ya kufanya mkataba leo hii anaajiriwa dereva wa kumbeba Mkurugenzi anamtoa Mkurugenzi wadogo wadogo hawa anamtoa Dar es Salaam mpaka Dodoma kutwa analipwa 9000 jamani hivi kweli tuangalie kada za kuiachia SUMA JKT lakini tuangalie sekta nyingine vitu vingine kama vinaangalia basi watu hao wapewe hata mikataba midogo. Mtu yupo daktari pale na yeye anachukuliwa kama kibarua nurse anapewa 9000 kwa kutwa jamani hii kitu hapana lazima tuangalie na level. Kama tunakwenda kuwachukua hawa watu wadogo, vibarua vidogo hivi wa SUMA waende lakini maeneo mengine makubwa basi Mkurugenzi apewe mamlaka ya kuangalia mikataba midogo ili wale watu wafanye kazi yao vizuri wasiwe na tamaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niombe Serikali fungu la CSR linatolewa kwa jamii katika Mamlaka ya Bandari naomba sana nimewaona sisi kama Dar es Salaam hatuna kitu kingine tunawategemea wao niliwaona mara moja wakitoa magodoro shule ya uhuru lakini nawaomba tena waangalie kwa jicho la huruma watoto wenye mahitaji maalum wenye magonjwa ya usonzi wenye usonzi Sinza maalum, Mtoni maalum wale tukiwapa huduma jamani wana mahitaji makubwa Mamlaka ya Bandari kama inaingiza faida basi rudisheni kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije sasa kwenye reli nashukuru sana na naipongeza sana Serikali kwa kujenga reli ya standard gauge kwa kweli pale Dar es Salaam tu ukifika pale gerezani imeanza kubadilisha sura ya Jiji. Pia kuna mpango wa reli za mjini Dar es Salaam , reli hizo zitakuwa zikitoka uwanja wa ndege Mbagala, Chamazi, Buguruni, Kibaha, Bunju mpaka Bagamoyo ni jambo jema tunaiombea Serikali mambo haya yaende vizuri ili hii treni iweze kukamilika. (Makofi)

MWENYEKITI: Maliza.

MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naomba barabara ya kutoka Mbuyuni Kawe, kuelekea Mbweni barabara ile iko ufukweni haina taa giza kubwa, wananchi wa kule wanapata shida naunga mkono hoja asilimia 100 ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia kwenye Wizara hii ya TAMISEMI.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge lako Tukufu, kwanza napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuwa na afya njema mpaka kufikia siku ya leo. Napenda niwatakie Ramadhan Kareem Waislam wote nchini Tanzania, wawe na mfungo bora na wenye amani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nataka niwashukuru wapiga kura wangu wote wa Mkoa wa Dar es Salaam, kwa kweli wamenifanyia jambo kubwa sana. Nawashukuru sana nami nawaaidi mbele yako kwamba nitawatendea haki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee pia niwapongeze na kuwashukuru wagombea wenzangu 300 wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kunipa support kubwa sana kwa sababu pamoja na kujiombea wao walikuwa wananiombea na mimi pia. Nashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nije kwenye Wizara ya TAMISEMI, napenda nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI kwa kuteuliwa kwake na sina mashaka naye maana ni ndugu yangu ambaye ninauhakika na utendaji wake wa kazi. Pia nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri na Makatibu Wakuu wote wa Wizara hii ya TAMISEMI, nina hakika kwamba watatutoa pale tulipo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije sasa kwenye mchango wangu na utajikita katika maeneo manne; elimu, afya, barabara na masoko kama muda utakuwepo. Kuhusiana na suala nzima la elimu nitaanza kwanza na hoja ya walimu. Walimu wana masikitiko makubwa, walimu wa shule za msingi na sekondari waliostaafu wana madai yao ya nauli huu sasa ni mwaka wa tano.

Mheshimiwa Naibu Spika, walimu hawa Tanzania nzima Shule za Msingi na Sekondari wanadai fedha zao za nauli, wamelitumikia Taifa hili kwa amani kwa utulivu na kwa moyo wao wote na kwa sababu kazi ya uwalimu ni wito na moyo. Leo hii walimu wanastaafu wanahangaika wanakwenda kwa Wakurugenzi, kuna wengine wanawapa majibu mazuri, lakini kuna wengine wanawapa majibu yasiyofaa, wanawaambia nendeni TAMISEMI fungu lenu haliko katika halmshashauri. Hii ni kero kubwa, naomba Serikali sasa itoe majibu walimu hawa stahiki yao ya nauli au mizigo ipo au haipo. Kama imefutwa basi ni bora waambiwe watulie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, walimu hawa wanataka kuja huku Dodoma, mimi wananiuliza wewe mwalimu mwenzetu umetoka hapa kwenye shule ya msingi leo umekwenda Bungeni unashindwa kututetea hata sisi walimu wenzio tunapata tabu. Mimi nasema walimu wenzangu leo wanisikie, naomba Serikali iwaangalie walimu hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia naomba niishauri Serikali wangu, walimu hawa miaka ya nyuma walikuwa wanalipwa kwenye halmashauri zetu nikiwepo mimi, nimelipwa fedha yangu ya mizigo milioni moja laki tatu kwenda kwetu Lindi sikuwa na tatizo lolote, huu mpango ulivyokuja kubadilka wa kutoka huku kuja kwenye Serikali Kuu ndiyo shida ilipoanzia. Sasa naomba kuuliza hii shida itaendelea kuongezeka mpaka lini? Niombe Serikali sasa iwe na mpango. Mheshimiwa Waziri mdogo wangu, naomba akija hapa aje na majibu, walimu wake wanateseka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuzungumzia masuala ya walimu, sasa nizungumzie suala la elimu ya shule ya msingi. Niombe Serikali sasa ije na mpango maalumu wa kukarabati sasa shule za msingi zilizo kongwe. Nimeona imekarabati vizuri shule za sekondari zilizo kongwe, lakini sasa twende kwenye mpango maalumu wa kukarabati shule za msingi zilizo kongwe. Kuna shule za muda mrefu, kwa mfano Shule ya Msingi Kisiwani, Kigamboni sasa hivi majengo yake baada ya ujenzi wa barabara yamekuwa mafupi mno kiasi kwamba imekuwa kama vibanda. Niombe Serikali katika mpango wake wa ukarabati waiangalie Shule ya Msingi ya Kisiwani, Kigamboni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia ipo Shule ya Mchikichini, Mbagala, pale kuna uwanja mkubwa ambao Samatta aliweka television kwa ajili ya kuangalia, lakini ukienda kwenye majengo ya shule ile inatia huruma, mabati yote yamekwisha kwa kutu. Pia ipo Shule ya Nzasa, Mbagala ambayo ina historia kubwa ya kutoa wanafunzi wengi kwenda sekondari; wazazi wengi walikuwa wanaigombania shule hiyo ili watoto wao waufaulu, leo hii shule hiyo baadhi ya majengo ni chakavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ipo Shule ya Msingi Baruti katika Halmashauri yangu ya Ubungo inahitaji ukarabati. Pia ipo Shule ya Msingi Buguruni na Shule ya Msingi Mbezi Beach. Shule ya Mbezi haiendani na mazingira ya Mbezi Beach naomba shule iendane na mazingira ya Mbezi Beach. Pia Shule za Msingi za kwanza kabisa Uhuru na Msimbazi nazo zinahitaji ukarabat. Hizi nimetoa kama mfano tu lakini shule zote kongwe naomba ziangaliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoke eneo hilo niende kwenye eneo la afya. Naipongeza Serikali kwa kujenga hospitali za wilaya 102 nchi nzima, ni jambo kubwa, naipongeza sana Serikali yangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo naomba waangalie baadhi ya hospitali katika Mkoa wa Dar es Salaam ambazo zimezidiwa. Hospitali ya Palestina Sinza kwa kweli ni ndogo lakini inategemewa sana; mgonjwa yeyote anayetoka kwenye hospitali ndogo anakwenda Palestina, kama Mungu akijalia itakapoisha Hospitali yetu ya Wilaya ndiyo atapelekwa huko.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana, kengele imeshagongwa.

MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, naomba sana na Hospitali ya Mbagala Zakiem na Vijibweni ziangaliwe kwenye bajeti. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja hii iliyopo mbele yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuchaguliwa kwake kwa kura za kishindo kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kuipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa jinsi walivyouwezesha Mkoa wetu wa Dar es Salaam. Usiposhukuru kwa kidogo basi hata ukipata kikubwa huwezi kushukuru, ni lazima niipongeze na kuishukuru Serikali kwa yale yaliyofanyika katika Mkoa wetu wa Dar es Salaam. Kwanza kupata Daraja la Kigamboni; Daraja la Mfugale TAZARA; Interchange Ubungo ya Kijazi; na ujenzi wa Daraja la Selander ambao umeanza na unaendelea vizuri ila nitaiomba Serikali waharakishe katika kulimaliza daraja hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia ujenzi wa barabara ya Bagamoyo. Barabara hii imejengwa vizuri lakini ina changamoto kubwa sana. Changamoto yake kubwa ni kwamba mvua inaponyesha inajaa maji katika maeneo yote. Hatuelewi hivi upembuzi yakinifu uliofanyika katika eneo lile hawakuliona hilo? Barabara ni nzuri na tunatarajia kweli itafungua uchumi katika maeneo hayo lakini ina changamoto ya kujaa maji. Niiombe Serikali wakaangalie hiyo barabara ina matatizo gani mpaka inajaa maji tena inajaa kwa kupitiliza kama bahari, ni nini kimetokea pale? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile niipongeze Serikali kwa ujenzi wa daraja au interchange nyingine ya Uhasibu Chang’ombe na pale VETA. Miradi hiyo yote yote inaendelea na kandarasi wako site, naipongeza sana Serikali kwa kutufanyia mambo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee sasa barabara za Ubungo, tuna wilaya mbili; Wilaya ya Ubungo na Wilaya ya Kigamboni ni mpya hazina mitandao mikubwa ya barabara. Kwa hiyo, naiomba Serikali izingatie kwamba wilaya hizi ni mpya na tumeweka makao makuu ya wilaya na halmashauri lakini hayafikiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nije katika barabara za Ubungo. Tuna wilaya mbili; Wilaya ya Ubungo na Wilaya ya Kigamboni ni wilaya mpya, hazina mitandao mikubwa ya barabara. Kwa hiyo, naiomba Serikali izingatie kwamba Wilaya hizi ni mpya na tumeweka Makao Makuu ya Wilaya na Halmashauri, lakini Makao Makuu ya Wilaya na Halmashauri hizo hayafikiki. Kwa mfano, katika Wilaya ya Ubungo barabara ya Makabe kupitia Msakuzi hadi Mpiji, barabara hii ni muhimu sana katika kuwezesha wananchi wa maeneo haya kufika katika Ofisi zao za Wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna barabara kubwa ya Kibwamba - Kibwegere mpaka Mpiji; barabara hii ni kubwa na imetupa shida sana katika kampeni zetu. Naiomba Serikali ianze ujenzi wa barabara hii angalau kwa kilometa moja, wananchi wa Kibamba waone kwamba angalau Serikali yao inawajali. Pia niombe barabara ya Kimara mwisho kwenda Segerea kupitia Bonyokwa, barabara hii ni muhimu ambayo inaunganisha wilaya mbili; Jiji la Ilala na Halmashauri ya Ubungo. Naiomba sana Serikali waiangalie barabara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nije katika Jimbo la Kigamboni. Jimbo hili ni mtihani, hakuna barabara. Barabara ya lami ambayo ipo kuanzia Mji Mwema kwenda Pemba Mnazi, bado haijafikia kilometa hiyo, inaishia Somangira. Pia barabara hii inakubwa na changamoto kubwa ya kuharibika haribika. Mara tu inaanza kujengwa ni viraka viraka, sasa hii hali inakuwaje? Naiomba sana Serikali, kama wanajenga, basi wajenge barabara imara kulingana na uchumi wa eneo lile. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ile mwanzoni Mji wa Kigamboni ulikuwa haujajengeka, lakini sasa Kigamboni imejengeka ina viwanda, ina magari makubwa. Kwa hiyo, wakijenga wasiweke lami ya mparazo, wahakikishe wanaweka uimara wa sawa sawa kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara ambayo tunaiomba toka mimi nimeanza kuwa Mbunge humu ndani mpaka leo hii, barabara ya kutoka Kibada kwenda Kisarawe II, kwenda Pemba Mnazi kupitia Kimbiji; barabara hii jamani tumeiomba mimi toka naanza Ubunge kila nikisimama naomba barabara hii. Naomba Serikali sasa waianzishe. Hii barabara ni ahadi ya Mheshimiwa Rais Marehemu kwamba sasa Mji wa Kigamboni unaenda kufunguliwa na barabara ikiwepo barabara hiyo. Naomba sana Serikali waiangalie.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Muda umeisha Mheshimiwa.

MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na yote naipongeza sana Serikali kwa yale waliyoyafanya.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ya hotuba ya Waziri wa Maliasili na Utalii kwa kumpongeza sana Waziri, Naibu Waziri na Katibu Mkuu kwa kazi nzuri wanayoifanya katika Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni yangu kwa Wizara, naomba utalii wa ndani uimarishwe kwa kufanya promotion au ku-promote utalii wa ndani na hasa kuimarisha cultural heritages site zetu. Watalii wa ndani waje waone Makumbusho zetu na maeneo mentioned ya urithi wa Utamaduni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu mwingine, Serikali sasa ijipange kuhakikisha wanaanzisha Plantation Museums ambazo zitasaidia watoto wetu kujifunza. Tunakoelekea, wanafunzi wa mijini hawatakuwa na sehemu ya kujifunza kwa vitendo na kwa kuona uhalisia wa mazao mbalimbali

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Mawaziri wote kwa ytendaji mzuri katika Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Spika, mchango wangu utajikita katika maeneo yafuatayo; miundombinu, afya, maji na elimu.

Mheshimiwa Spika, nianze na miundombinu; naomba Serikali iangalie upya mradi wa DMDP, uangaliwe upya kwa umuhimu wa Jiji la Dar es Salaam na hasa Wilaya ya Kigamboni na Ubungo ziwe kipaumbele. Lakini pia barabara ya Nzasa - Kilungule nayo sasa ikamilike. Mradi umechukua muda mrefu sana. Barabara hii ni muhimu sana kwa wakazi wa Buza na wale wanaoenda Mbande na Kongowe.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa afya, naipongeza Serikali kwa ujenzi wa vituo vya afya, naomba Serikali iangalie jinsi ya kupanua Hospitali ya Mbagala Zakhiem kwani imezidiwa, idadi ya wagonjwa ni kubwa sana.

Kwa upande wa elimu, naipongeza Serikali kwa ujenzi wa madarasa mapya, lakini niiombe Serikali sasa iangalie ukarabati wa shule kongwe na hasa maeneo ya Mkoa wa Dar es Salaam.

Kuhusu suala la maji, niiombe Serikali waendelee na mpango wake wa ujenzi wa Bwawa la Kidunda ndio suluhisho la upatikanaji wa maji kwa muda wote katika Mkoa wa Dar es Salaam. Naomba sana Serikali itekeleze mradi huo. Mradi wa Visima vya Kimbiji na Mpera sasa ukamilike ili wananchi wa Kigamboni na Mbagala waweze kupata maji safi na salama.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote wa Serikali kwa utendaji wao uliotukuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kulipa promotion za wafanyakazi, ni jambo jema, naipongeza sana Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa ninayoiona ni pale mfanyakazi anapostaafu kuna baadhi ya waajiri wanamsafirisha mfanyakazi wanapewa stahiki zao na wengine hawapewi mfano kada ya ualimu, wengine wanapewa na wengine hawapewi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali ije na majibu je, stahiki hiyo ipo au imefutwa na kama ipo utaratibu wake ukoje? Nataka ufafanuzi mzuri utolewe vinginevyo nitashika shilingi. Mtumishi anapobadilisha kada anaweza kutoka kwenye mshahara wake ambao unaweza ukawa wa juu lakini kule anakoenda akashushwa mshahara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli lengo la kubadilisha kada ni kutaka kupata zaidi, lakini mtu anaposhushwa kiwango cha mshahara hatuoni tuna viashiria vya rushwa na wizi katika maeneo ya kazi? Jambo hili liangaliwe namna nzuri ya kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na nampongeza Mheshimiwa Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote wa Mahakama.

Mheshimiwa Spika, kwa kweli naipongeza sana Seikali kwa kujenga Mahakama ya Temeke. Nilikuwa Mbunge wa vipindi vilivyopita nilikuwa nataka ikamilike sana kuhusu Mahakama ya Temeke, sasa tumepata Mahakama Maalum yenye kila kitu mpaka chumba cha kunyonyeshea Watoto, hongereni sana.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hayo Mahakama za Wilaya zote za Mkoa Dar es Salaam zimejengwa na ziko vizuri sana. Ombi langu naomba Serikali iangalie Mahakama ya Mwanzo Mbagala; hali ni mbaya Mbagala. Idadi ya watu Mbagala ni kubwa na mahitaji ni makubwa sana. Naomba Serikali iangalie sana Mbagala.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono na tumekuwa na mobile mahakama maeneo ya Chanika na zile za pembezoni, shukrani sana.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kupongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuwasilisha vizuri hotuba yake nzuri na utendaji wake mzuri sana, ameonesha weledi mkubwa sana katika uongozi wake. Pia nawapongeza Mawaziri wote waliopo kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kazi kubwa wanazozifanya kuhakikisha nchi yetu inapiga hatua kimaendeleo. Nawapongeza pia Makatibu Wakuu wote kwa utendaji uliotukuka.

Mheshimiwa Spika, mchango wangu utajikita katika suala zima la ajira kwa vijana. Nchi yetu kumekuwa na tatizo kubwa la ajira kwa vijana wetu, lakini pia kuna vijana ambao wapo katika ajira zisizokidhi haja na mfano vijana wanaofanya vibarua TPA, wanafanya vibarua kwa miaka 10 lakini ajira zinapotokea wanaletwa wengine na wale wanaofanya kazi ya kibarua wanaendelea kuwa vibarua. Mfumo wa kutumia wakala wa vibarua kama vile SUMA JKT unadumaza maendeleo ya upatikanaji wa ajira kwa sababu wanatoa ajira za kutwa na hakuna njia nyingine.

Naiomba sana Serikali iangalie upya utaratibu wa utoaji ajira kwani kuna vijana wengi wanajitolea bure kutoa huduma kwa zaidi ya miaka mitano, lakini ajira zinapotokea hawapewi kipaumbele. Hali hiyo sio nzuri inakatisha tamaa sana kwa vijana wetu. Vijana wanaojitolea wapewe kipaumbele. Niipongeze Serikali kwa kuja na utaratibu wa intern kwa vijana, ni jambo jema, lakini vijana wengi wako intern lakini tuhakikishe kuwa hao walio intern wanapata ajira za kudumu.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kunipa nafasi niweze kuchangia kwenye Wizara hii muhimu ya Maji. Kwanza kabisa napenda nimpongeze Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kumpa hongeza sana kwa kazi kubwa anayoifanya ya kutatua mambo mbalimbali changamoto mbalimbali za wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais tumeona juzi imekuja changamoto ya mafuta Mheshimiwa Rais amewajibu wananchi wake kwa kuweka ruzuku ya bilioni 100 ili kuwapunguzia kasi ya bei ya mafuta wananchi wa Tanzania waweze kupata huduma hiyo kwa gharama nafuu. Hilo siyo jambo dogo Mheshimiwa Rais wetu anafanya kazi kubwa sana anahangaika huku na huku kuhakikisha watanzania wanapata huduma zote muhimu kwa gharama nafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya hapo naomba sasa nirudi kwenye Wizara yetu ya Maji nakupongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Maji, Naibu Waziri pamoja na Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhakikisha wanakwenda kumtua mama ndoo kichwani na kuhakikisha sasa wananchi wa Tanzania wanakwenda kupata maji safi na salama.

Mheshimiwa Spika, nikipongeze Chama cha Mapinduzi pia katika Ilani yake ya CCM sura ya kwanza kipengele cha kwanza ukurasa wa tatu Ilani inasema Serikali itaongeza idadi ya wananchi wanaopata huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama vijijini kutoka asilimia 47 mpaka kufikia zaidi ya asilimia 70 katika kipindi hiki kinachokuja. Hili ni jambo kubwa ninapoanza kutaka kuzungumza katika Wizara hii ya Maji ninaona jinsi gani mipango ya bajeti inavyokwenda sasa kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa vitendo. Nakipongeza Chama chetu cha Mapinduzi kwa kuisimamia vizuri Serikali na hata katika bajeti hii sasa tunakwenda kufanya hiyo kazi kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye bajeti hii nitazungumzia masuala ya ujenzi wa bwawa la Kidunda. Mkoa wa Dar es Salaam unategemea kupata maji safi na salama katika chanzo kikuu cha Bonde la Ruvu. Lakini katika kipindi hapa nyuma tumeona ilitokea ukame Mkoa wa Dar es Salaam tukawa tunapata maji kwa mgao. Lakini katika bajeti hii inaelekeza sasa inakwenda kutengeneza bwawa la Kidunda, naipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kuamua hilo na niombe hili bwawa la Kidunda sasa litengenezeke ndiyo mwarobaini pekee wa upatikanaji maji fulltime katika Mkoa wa Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimemuona Mheshimiwa Waziri wakati ule wa ukame alikuwa anaingia kwenye mabonde anaingia huku na huku tunaumia Mheshimiwa Waziri utaliwa na mamba suluhisho ni kujenga bwawa la Kidunda. Kwa nini nasema bwawa la Kidunda Mkoa wa Dar es Salaam wenye watu takriban kwa mujibu wa sensa 2012, 5,465,420 wanategemea maji kwa asilimia kubwa kutoka kwenye mto Ruvu.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Ilala ina takriban watu 1,534,489 hao wanategemea maji kutoka mto Ruvu, Wilaya ya Kinondoni yenye takriban watu 1,164,174 inategemea maji kutoka huko kwenye hilo bonde la Ruvu. Ubungo yenye takriban watu 1,058,597 wanategemea kupata maji huko ya mto Ruvu. Lakini pia Temeke nayo yenye watu takriban 1,510,000 wanategemea kupata maji kutoka mto Ruvu lakini kama haitoshi kupitia DAWASA hiyo hiyo Kibaha mjini na vijijini Chalinze yenye watu takriban watu 233,000 wanategemea kupata maji kutoka chanzo cha Ruvu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niombe Kisarawe, Bagamoyo hao wote kupitia DAWASA tunategemea maji ya mto Ruvu suluhisho la tatizo la maji yapatikane saa zote iendane na idadi ya watu. Dar es Salaam chanzo cha Ruvu kimeanza toka sasa toka Uhuru sasa ni karibu miaka 60 hakijapatikana chanzo mbadala zaidi ya visima vya Kimbiji na Mpera lakini mradi huu bado haujakamilika. Sasa Serikali iende ikaandike historia mpya kwa kuweka hifadhi ya maji katika Bonde la Mto Kidunda.

Mheshimiwa Spika, kwa nini nasema hivyo kutokana na mabadiliko ya tabia nchi kumekuwa na mafuriko mengi yanatokea maji mengi yanapotea kwa mpito yanatoka kwenye mto Ruvu yanaingia baharini lakini baada ya hizo mvua kupita ukame unarudi suluhisho lake ni maji ya Kidunda lakini maji haya hayataisaidia mkoa wa Dar es Salaam yatasaidia Mkoa wa Pwani, Mkoa wa Morogoro hilo bwawa la Kidunda litasaidia katika Mkoa wote wa Morogoro katika kuchachua uchumi, uvuvi na kilimo lakini na sisi wa Dar es Salaam tunapata maji ya uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mji wa Dar es Salaam unakua kwa kasi enzi hizo inawekwa hiki chanzo cha Ruvu kuwa chanzo pekee ile Kariakoo haikuwa hivyo leo Kariakoo magorofa yote yale yanatumia maji yanayotoka mto Ruvu. Sasa niombe Serikali hili bwawa la Kidunda tena nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kuliweka katika mpango hili bwawa. Tumekuwa muda mrefu linaingia toka mimi nimeingia hapa Bungeni linaingizwa kwenye bajeti linatoka linaingizwa linatoka hivi lini linatekelezwa. Sasa nimuombe Mheshimiwa wangu Rais atengeneze historia mpya katika Tanzania kwa kuamua sasa kulijenga hili bwawa la Kidunda.

SPIKA: Mheshimiwa Mariam Kisangi kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Kalogeresi.

T A A R I F A

MHE. INNOCENT E. KALOGERESI: Mheshimiwa Spika, nataka kumpa taarifa mchangiaji ni ukweli usiofichika suluhi la Dar es Salaam ni bwawa la Kidunda ambalo linajengwa katika Wilaya ya Morogoro Vijijini Jimbo la Morogoro Kusini ambapo natoka na sisi wana Morogoro Kusini tumejipanga kuhakikisha kwamba vikwazo vyote ambavyo vitakwamisha ujenzi wa bwawa hili vitaondoka Jumatatu nitakuwa na Mkurugenzi wa DAWASA kule kuhakikisha kwamba mambo yanakwenda vizuri.

SPIKA: Mheshimiwa Mariam Kisangi, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, taarifa hiyo naipokea kwa mikono miwili na naomba sana Wizara ilisimamie hilo tuweze kupata maji wote mikoa yote hiyo ineemeke. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nije kwenye mchango wangu wa pili kuhusu chanzo cha maji cha Visima vya Kimbiji na Mpera niipongeze sana Serikali mradi huu umekuwa ukisuasua kwa muda mrefu angalau sasa umeanza kuleta matumaini tunaona kwamba katika kata kama za Mjimwema, Kibada kumeanza mpango wa kusambaza mabomba. Lakini changamoto kubwa ambayo wasiwasi umewaingia wananchi wa maeneo hayo ni kuangalia jinsi ya gharama za maji.

Mheshimiwa Spika, kama ulivyoongea Mheshimiwa Waziri tunakuomba kama ulivyosema kitu chema kinaigwa. Hebu tuendane na vile wanavyofanya wenzetu wa umeme vijijini tuangalie mipango mahsusi ambayo itamwezesha mwananchi kuwekewa maji na walau kulipa kwa kiasi kidogo aendelee kufanya matumizi ninasema hivyo kwa sababu watu wameanza kuogopa hata kukwepa kuletewa hayo maji.

Mheshimiwa Spika, lakini pia niombe sasa huu mradi wa visima vya Kimbiji na Mpera sasa uwawezeshe wananchi angalau wa Wilaya ya Kigamboni wote waweze kupata maji safi na salama. Maji haya yaende kwenye Kata yenyewe ya Kisarawe II, yaende mpaka Mwasonga, yaende Tunduisongani, yaende Pembamnazi, yaende Kimbiji lakini pia maji hayo…

SPIKA: Muda wako umeisha Mheshimiwa Mariam.

MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na kuipongeza sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa utendaji wake mahiri ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja ya Bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri anayoifanya pamoja na msaidizi wake Naibu Waziri. Wote mnafanya kazi nzuri bila kuwasahau Makatibu Wakuu wa Wizara kwa kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Spika, mchango wangu utajikita katika maeneo yafuatayo; nikianza na Maafisa Ugani; napongeza Serikali kwa kuwapa pikipiki Maafisa Ugani waweze kuwafikia wakulima. Tatizo maafisa hawa wako Wizara ya TAMISEMI pamoja na Waziri kuwa na nia njema na kilimo, lakini hawa Maafisa Ugani hawawajibiki katika Wizara yake. Niiombe Serikali waangalie mfumo wa utawala wa Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu uchimbaji wa mabwawa; kutokana na mabadiliko ya tabianchi na ukosefu wa mvua naungana na Serikali kuchimba mabwawa na kufanya kilimo cha umwagiliaji tuweze kupata mazao mengi ya chakula na biashara.

Kwa upande wa rasirimali watu; Serikali itoe kibali cha ajira kwa Wizara hii kwani kuna taasisi hakuna watumishi wa kutosha kama TFC, ni vyema Wizara ipewe kibali.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Hongereni sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa uamuzi wake wa busara wa kuendelea kutenga fedha za ujenzi wa Bwawa la Kidunda, bwawa ambalo ni faraja kubwa kwa wakazi wa Mkoa Dar es Salaam na Pwani kupata maji kwa wakati wote.

Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Makatibu Wakuu na watendaji wote wa Serikali kwa kazi nzuri kuhakikisha kuwa Mkoa wa Dar es Salaam tunapata maji safi na salama isipokuwa changamoto yetu kubwa ni kupungua kwa maji na mabomba kupasuka na kupoteza maji mengi sana; naiomba Serikali iendelee kupambana na changamoto hizo.

Mheshimiwa Spika, naomba Serikali ikamilishe miradi ya maji ya Dar es Salaam pamoja na Mradi wa Visima vya Maji vya Kimbiji na Mpera sasa ukamilike na maji yasambazwe kwenye Wilaya ya Kigamboni yote na Temeke, Mbagala pia Jimbo la Ukonga.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu Serikali ikafanye utafiti wa maji tuweze kuchimba visima virefu maeneo ya Mvuti Dondwe nao wananchi wa Ilala wapate chanzo kipya cha maji. Ni matumaini yangu chanzo hicho kitawasaidia sana.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja naipongeza sana Serikali kwa utekelezaji na juhudi zake, endeleeni hivyo Mungu atasimama nasi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kuja na wazo la kupitia upya mitaala yetu. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Makatibu Wakuu kwa utendaji mzuri katika sekta ya elimu.

Mheshimiwa Spika, mchango wangu utajikita katika walimu wa vijijini kufundisha kutoka asubuhi mpaka saa 11 kasoro jioni, lakini walimu wa mijini wanamaliza kazi saa 8.30 mchana.

Mheshimiwa Spika, walimu wote mijini na vijijini, walimu wa vijijini wote wanahitaji muda wa ziada wa kujiandaa na masomo lakini pia kufanya kazi za kujiongezea kipato kama vile kilimo na ufugaji. Naomba sana sana muda wa kazi uwe ni mmoja.

Mheshimiwa Spika, elimu ya watu wazima ni jambo la muhimu, kuna wanaokosa elimu kwa sababu mbalimbali lakini pia kuna watu wazima wanaotaka kujiendelaza, hivyo Serikali iweke mpango wa kuendeleza elimu ya watu wazima.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja ya Wizara hii, pia naipongeza Serikali kwa bajeti hii, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Makatibu Wakuu na watendaji wote wa Serikali kwa kuisaidia Wizara kuweza kutekeleza majukumu yake.

Mheshimiwa Spika, mchango wangu utahusu Maafisa Ustawi wa Jamii wanafanya kazi kubwa sana na wanafanya maamuzi ya kesi mbalimbali za wakubwa na Watoto, lakini hawapewi posho yoyote kwa kazi kubwa wanazofanya. Utakuta wanaamua kesi moja kuanzia asubuhi mpaka usiku. Kazi kubwa sasa wanafanya maafisa hawa.

Mheshimiwa Spika, naipongeza sana Wizara hii kwa kutoa mikopo kwa vijana na kuwezesha mikopo hiyo kurudishwa. Si jambo rahisi sana kwa wakati tulionao hongereni sana.

Mheshimiwa Spika, ombi langu ni vyema wale wanaohusika na fedha za Halmashauri wakajifunze kwa Wizara hii.

Kuhusu ongezeko la watoto watukutu mitaani naomba sana Serikali isaidie kuwatoa watoto wanaoombaomba mitaani kwani wanajifunza tabia mbaya. Ni bora waombe watu wazima lakini wasiwe na watoto wao.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja asilimia mia moja bajeti hii ipite kwa kishindo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja ya Wizara hii ya Uchukuzi.

Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa kutoa fedha nyingi sana za kujenga barabara na madaraja katika mkoa wetu. Kwa kweli naipongeza Serikali kwa ujenzi mkubwa wa madaraja likiwemo la Tanzanite, Kurasini, TAZARA Mfugale na Inter Change ya Kijazi, kwa kweli madaraja hayo yamebadilisha sura ya Mkoa wa Dar es Salaam.

Aidha, napongeza kwa ujenzi wa barabara za mwendokasi Mbagala na Gongo la Mboto; naishukuru sana na kuipongeza Serikali.

Mheshimiwa Spika, mchango wangu; naomba mradi wa DMDP uje katika Mkoa Dar es Salaam kutusaidia katika barabara za mitaa na naomba ujenzi wa barabara uende sambamba na taa za barabarani kwa kuwa barabara zetu zimekuwa na giza sana.

Kuhusu bandari ya Dar es Salaam, kwa kweli utendaji wa bandari ni wa kusuasua kwa muda mrefu na hasa eneo la operation, Wakurugenzi wa Bandari wamekuwa wakipata tuhuma mbalimbali kutokana na mifumo yetu kutosomana. Sasa naiomba Serikali tuangalie upande mwingine wa shilingi kufikiria kumuweka mwekezaji wa kuendesha bandari upande wa operation. Mwekezaji aendeshe bandari na kuboresha miundombinu, na sisi atupe faida yetu, cha msingi ni kuangalia mkataba uwe win win na maslahi ya wafanyakazi wetu yazingatiwe kulingana na mkataba wao wa kazi.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na nakupongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na watendaji wote wa Serikali bila kusahau Wakurugenzi wa Taasisi zetu zote zilizo chini ya Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, ushauri wangu naomba uzingatiwe.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naunga mkono hoja kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. Samia Suluhu Hassan anafanya kazi kubwa sana ya kuliongoza Taifa letu. Napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri pamoja na Makatibu Wakuu wote kwa utendaji uliotukuka katika sekta ya ardhi, Mungu awabariki sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utajikita katika maeneo yafuatayo nikianza na urasimishaji; kwa kweli Mkoa wa Dar es Salaam tulipokea vizuri sana, lakini tuliingiliwa na watu ambao hawana maadili, wakavuruga na wakachukua fedha za watu na hati hazijatolewa mpaka leo hii. Wananchi hawajui hatma yao. Tunaomba Serikali itoe maelekezo jinsi watakavyofanya usuluhishi wa jambo hilo tuweze kwenda mbele.

Pili ni kuhusu ujenzi wa makazi ya gharama nafuu; naomba Serikali iangalie jinsi ya kujenga nyumba za gharama nafuu zisiwe na bei kubwa. Gharama kubwa za nyumba zinazosababisha nyumba hizo kuishi wenye fedha badala kuishi wananchi wenye kipato kidogo na kipato cha kati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kodi ya ardhi; wananchi wengi wamekuwa na madeni makubwa ya kodi ya ardhi ni vyema Serikali ikafanya mahesabu ya madeni wakaangalia wastani wa makusanyo yao kama ni machache kuliko madeni Serikali iweke punguzo la kodi kwa kipindi cha mpito wananchi wengi waweze kulipa kodi hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuiwezesha Wizara hii kuipatia fedha kuweza kupata kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo iliyopo kwenye Wizara hii. Nampongeza sana sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri pamoja na Katibu Mkuu bila kumsahau Naibu Katibu Mkuu.

Mheshimiwa Spika, mchango wangu kwa leo sina zaidi ya kuipongeza Wizara hii. Ukiangalia tulikotoka na tulipofikia Serikali imepiga hatua kubwa sana. Nilikuwa na maneno mengi siku za nyuma lakini sasa sina maneno zaidi ya kupongeza. Napongeza pia kuja na mkakati wa nishati bora ya kupikia, kweli ni ukombozi kwa mwanamke, shukrani kwako Mheshimiwa Waziri na timu yako yote kwa jambo kubwa mlilofanya la kuwajali wakina mama wa Tanzania, mbarikiwe sana.

Mheshimiwa Spika, ombi langu naomba mradi wa usambazaji wa gesi asilia utengewe fedha ya kutosha, gesi ifike Mbagala, Tandale, Gongo la Mboto na maeneo ya pembezoni. Nawashukuru sana sana na kuwapongeza sana Mheshimiwa Waziri na timu yako, endeleeni hivyo na Mungu atasimama na ninyi.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 7) wa Mwaka 2019 (Toleo la Kiingereza)
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Muswada huu wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali. Kwanza napenda nimpongeze Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa kuleta Muswada huu hara sana Bungeni kwa njia ya dharura. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda nimpongeze Mheshimiwa Spika kwa kupokea Muswada huu kwa haraka na yeye kuufanyia kazi kwa haraka. Pia napenda nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu na wasaidizi wake akiwemo Mheshimiwa Jenista Mhagama, Waziri wa Uratibu wa Bunge, kwa kufanya kazi hizi kwa umahiri mkubwa sana lakini pia kwa haraka sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda nimshukuru sana Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu kwa kuweza kuwasilisha vizuri Muswada huu wa sheria ya mabadiliko ya sheria mbalimbali. Napenda pia nimpongeze Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Katiba na Sheria kwa kuweza kuujadili Muswada huu kwa umahiri mkubwa sana pamoja na Wanakamati wote. Pia niwapongeze Makatibu wa Kamati hiyo ya Katiba na Sheria kwa kufanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu katika Muswada huu wa Mabadiliko ya Sheria Mbalimbali utajikita katika maeneo makuu matatu; kwanza, Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa VVU na UKIMWI, Sura ya 43; Sheria ya Bandari, Sura ya 166; na Sheria ya Wanyama, Sura ya 156.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na Sheria ya Udhibiti wa VVU na UKIMWI, nitachangia katika eneo ambalo mchangiaji mwenzangu alianza kuzungumzia. Katika eneo la umri wa mtoto kuwa na hiari ya kupima UKIMWI ni mtoto wa miaka 15. Nakubaliana kabisa na maelezo ya Serikali na yale yaliyotolewa. Mtoto wa miaka 15 ni mtoto ambaye angalau anakuwa amemaliza shule ya msingi sasa anakwenda sekondari, kwa maneno mengine tunasema kwamba katika umri huo wa miaka 15 mtoto angalau ameweza kujitambua.

T A A R I F A

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpa taarifa mama yangu, Mheshimiwa Mariam Kisangi kwamba kwa sasa hivi watoto wengi wanaomaliza darasa la saba ni kuanzia miaka 12 hadi 13 na sio miaka 15 kama ilivyokuwa zamani.

MWENYEKITI: Taarifa hiyo.

MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa yake siitambui kwa sababu mimi ni Mwalimu wa shule ya msingi, najua mtoto anapokelewa kuanzia miaka sita, saba na kuendelea na anamaliza miaka 15 au 14 kwa wengine, sio wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. MARIAM N. KISANGI: …nimesema sio wote…

MWENYEKITI: Order, order!

MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kabisa katika suala zima la sheria hiyo, nakubaliana na mapendekezo ya Serikali, Serikali imefanya jambo la maana, umri huo ndiyo unaofaa. Haya ni masuala ya maisha ya watu, kwa fikra zangu, hivi mtoto wa miaka 12 hata kama ndiyo, atakuwa amemaliza darasa la saba, ni kadogo hivi, unakapeleka kale kaende kakajipime kakaelezwe, kakapewe mambo mbalimbali ikiwemo jinsi huo UKIMWI na mambo yake jinsi umeupataje na jinsi ya kujihifadhi. Hivi mtoto wa miaka 12 unaanza kumwelekeza matumzi ya condom, hivi kweli mnalitakia heri Taifa hili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nieleze wazi, katika masuala ya maisha na watu tusifanye ushabiki, haya ni maisha ya watu na wale ni watoto wetu.

MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la umri huu wa miaka 15…

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tu nimpe taarifa dada yangu, Mheshimiwa Mariam Kisangi, kwamba mtoto wa darasa la tano tu anapewa mimba kwa hiyo tayari anakuwa ameshaelewa ni nini kinachofanyika. Naomba tu Mheshimiwa dada Kisangi usifikiri kwamba watoto wanaomaliza darasa la saba wote wanakuwa na miaka 15, hapana, mtoto anamaliza darasa la saba…

MWENYEKITI: Ahsante; Mheshimiwa Mariam Kisangi.

MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa yake siipokei kwa sababu masuala ya mimba na uzazi na masuala ya UKIMWI, hapa tunazungumzia masuala mazima ya uambukizi wa VVU.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaposema kwamba mtoto wa miaka kumi tuna-assume kwamba hayo maambukizi ameyapata kutoka kwa wazazi wake. Jambo ambalo hakatazwi kupima lakini atapimwa kwa uangalizi wa wazazi wake au kwa uangalizi wa mlezi wake, lakini mtoto wa kwenda mwenyewe kwa Daktari na kuomba kupimwa UKIMWI anatakiwa awe na umri wa miaka 15.

MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. MARIAM N. KISANGI: Umri ambao katika sheria za kidini au sheria… wewe acha Ukigambini wako hapa…

MHE. LUCY S. MAGERELI: Taarifa.

MHE. MARIAM N. KISANGI: Wewe acha Ukigamboni wako hapa. Analeta ushabiki wa Dar es Salaam hapa.

MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti…

MWENYEKITI: Waheshimiwa, muda wake ni dakika tano tu, kaa chini.

MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, usinilindie muda wangu.

MBUNGE FULANI: Asikulindie?

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwakasaka, jiandae Mheshimiwa Amina Mollel.

MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, sijamaliza muda wangu.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kisangi, muda wako umekwisha.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 6) wa Mwaka 2019 (Toleo la Kiingereza)
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia muswada huu muhimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa napenda niipongeze Serikali nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Bunge, Sera na Wenye Ulemavu, Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu, Naibu, Mawaziri, Uchukuzi, Fedha, Naibu Waziri wa Maji, Makatibu Wakuu, Watendaji wa Serikali, lakini kipekee napenda kumshukuru, Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria Ndogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mwenyekiti huyu kwa kweli ni mtu muhimu sana na amenipa somo leo kwa mara ya kwanza katika Bunge lako tukufu, namimi najaribu kuchangia muswada wa sheria kutokana na elimu ambayo nimeipata kwa Mwenyekiti huyu, pia naomba niwapongeze Wajumbe wote wa Kamati ya Sheria Ndogo kwa kazi kubwa walioifanya na ushirikiano wao.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Muswada huu ya Mabadiliko ya Sheria Mbalimbali mchango wangu utajikita katika sehemu ya pili; Marekebisho ya Sheria ya EWURA Sura namba 414, lakini pia utajikita katika Sheria ya Michezo ya Kubahatisha Sura Namba 41, lakini pia nitazungumzia kidogo Sheria ya Vivuko Sura 173.

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze sana Serikali kwa mara nyingine muswada huu kuleta kwa hati ya dharura, mimi nafikikiri ni jambo muhimu sana na tumpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwajali makundi mbalimbali ambayo yalibanwa na sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Muswada wa Sheria wa EWURA naomba nichangie katika maeneo yafuatayo; kwanza kabisa suala ambalo lilikuwa linawaudhi wengi na linatukera watu wengi ni pale ambapo Waziri wa Nishati alikuwa hana mamlaka ya kuweza kuamua chochote kwa sababu EWURA ilikuwa chini ya Wiizara ya Maji, Muswada huu muhimu sasa unamrudisha Waziri wa Maji na Waziri wa Nishati kufanya kazi pamoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika masuala ya mafuta ndiyo masuala makubwa katika uchumi wa nchi yetu na masuala haya yote yalikuwa yanasimamiwa na Waziri wa Nishati, leo hii katika maamuzi Mheshimiwa Waziri wa Nishati hakuwa na maamuzi, lakini muswada huu muhimu umeleta marekebisho katika eneo hilo, sasa Waziri wa nishati na Waziri wa Maji watafanya kazi pamoja, watatoa maamuzi ya pamoja, lakini pia watapitia taarifa zote kwa pamoja na hata kwenye bodi, Wajumbe wa Bodi watachaguliwa kutoka kwenye pande zote mbili, mimi niipongeze sana Serikali kwa hilo jambo muhimu walilolifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili katika sehemu hiyo ya pili muswada huu wa sheria unampa Mkurugenzi uwezo wa kufifilisha makosa. Naomba ni declare interest kwamba mimi ni mdau katika eneo hilo, masuala ya makosa wafanyabiashara wengi wa mafuta katika miji mbalimbali walikuwa wanafanya makosa, lakini mwisho wa makosa yao wanaambiwa wasubiri bodi, wanafungiwa miezi mitatu, miezi minne na wengine wanakimbilia kwa Mkurugenzi, lakini Mkurugenzi yule alikuwa hana meno, muswada huu unampa meno Mkurugenzi wa EWURA kwamba sasa awe na uwezo iwapo mfanyabiashara ataleta shida na akakubali makosa yake basi Mkurugenzi atakuwa na uwezo wa kumfifilishia kosa lake na kuweza kulipa faini inayotakiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia muswada huu umetoa nafasi kubwa kwa na uhuru mkubwa kwa wananchi pale wanapoona kwamba makosa hayo waliopewa hawaridhiki nayo wamepewa uhuru wa kwenda mahakamani. Ni jambo jema sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye suala zima la interest, nakubaliana kabisa na Serikali na maamuzi yao kwamba lazima tuweke interest ili kujenga imani kwamba unapokopa deni lazima ulipe, naomba waangalie kwenye regulation yao kwamba waweke hizi interest zinazotolewa wazi, isiwe zimefinywa finywa wajuwe kwamba kosa fulani litalipiwa faini kiasi fulani na interest itakuwa vipi na kosa fulani itafanywa hivi natambua EWURA wana kanuni zao, nitaiomba Serikali kwenye hizo kanuni zao basi waweke wazi masuala yote kama vile Serikali ilivyoweka wazi katika eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niseme suala hili limechelewa, lakini nimeona kabisa juhudi za wazi za Mheshimia Rais katika kuboresha mazingira ya biashara yawe rahisi katika Taifa letu. Ni jambo zuri na ni jambo ambalo huwa tunafikiri sheria hii itakaposainiwa wananchi na wafanyabiashara wetu wataifurahia sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye Sheria ya Michezo ya Kubahatisha; lengo la muswada huu ni kuhakikisha pia wanadhibiti, lakini pia kuipa bodi mamlaka ya kufanya ukaguzi, ukamataji na ufilisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona mara nyingi wananchi wetu ambao wanacheza michezo hiyo ya kubahatisha wamekuwa wakipata matatizo ambayo hakuna wa kuyatatua, sasa bodi imepewa mamlaka kama mfanyabiashara au mwenye bahati nasibu anafanya vitu visivyoeleweka, lakini pia anashindwa kulipa kodi, anashindwa kulipa watu wake basi sheria hii itashika mkondo wake, itamkamata na kumfilisi, lakini katika kufanya kazi hiyo naiomba Serikali katika kuangalia nao sheria zao waangalie kwamba haki itendeke, siyo kwa vile tumewapa mamlaka hayo wakafanye mambo yasiyofaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia sheria hiyo imeongeza wigo wa kutoa leseni ya michezo ya kubahatisha, tunashuhudia katika tv kwamba kuna michezo aina mbalimbali, mingine inachezwa hapa nchini na mingine inachezwa nchi za nje, sasa ile ya nchini walio tayari watapewa leseni, lakini sheria hii pia inaweka security bond kwa yeyote yule atakayefanya biashara hii.

Mheshimiwa Spika, hiyo security bond itasaidia sana kwa sababu tumeona wanacheza michezo, wanawaahidi watu milioni mia tano, lakini unaambiwa yule mtu hajapata hiyo pesa. Sasa Serikali inamsimamia Mtanzania ambaye atakuwa amecheza huo mchezo, lakini akulipwa hii security bond itasaidia kumlipa lakini na yeye pia itamsaidia iwapo atakuwa ametenda kosa aondolewe kwenye eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nichangie sehemu ya sita, ibara ya 165 kupanua wigo wa matumizi ya vivuko; kweli kabisa tunatambua umuhimu wa vivuko vya Serikali vinatakiwa viwekewe nafasi, lakini hiyo adhabu iliyowekwa tuangalie mbele na nyuma, kuna wakati katika maeneo ambayo yanawekwa vivuko vya Serikali kunatokea hatari, kwa mfano kama hivyo Kivuko cha Kigongo sijui, huko kama vivuko kama Kigamboni maeneo hayo mara nyingine kinaweza kikawa kime-fail engine, viboti vidogo vidogo huwa vinakuja kuokoa wananchi; sasa je, sheria hiyo itakuwaje? Kwa hiyo, niombe kwenye kanuni za uokoaji, lakini katika kanuni nzima ambazo zitaongoza kwenye eneo hili basi waangalie jinsi gani hivyo viboti vidogo vidogo iwapo itatokea dharura au ajali yoyote kuweza kuingia kwenye eneo la vivuko.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi sina mengi, niishukuru sana Serikali, nimshukuru Mheshimiwa Jenista Mhagama kwa jinsi anavyoliongoza Bunge kwa kweli tunampongeza sana mama huyu usiku na mchana mpaka kinaeleweka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana lakini nimshukuru Mwenyekiti wangu tena kwa mara nyingine kwa kuniwezesha na mimi leo kuanza kuipenda sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)