Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. William Tate Olenasha (320 total)

MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ya kumwuliza Mheshimiwa Waziri maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri hakujibu swali langu. Nimeuliza, Serikali haioni umuhimu wa kujenga Chuo cha Uvuvi Lindi, nikimaanisha Mkoa wa Lindi, siyo Mikindani Mtwara.
Mheshimiwa Spika, pia kwa mujibu wa hotuba ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa humu Bungeni tarehe 20 Novemba…
MBUNGE FULANI: Hukuwepo!
MHE. HAMIDU H. BOBALI: Aidha, nilikuwepo au sikuwepo lakini kuna Kitabu. (Makofi)
Mheshimiwa Rais anasema, katika kutatua tatizo la ajira nchini, ataweka mkazo katika sekta tatu; viwanda, kilimo na uvuvi. Mimi nilitegemea, Serikali ingekuja na mkakati wa kuanzisha hivi vyuo katika kila mkoa ambapo tumepakana na bahari ama kuna maziwa. Waziri anajibu, watatoa mafunzo ya muda mafupi kwa watu arobaini arobaini.
Mheshimiwa Spika, watu 40 sidhani kama ni mkakati huu anaozungumzia Rais. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atueleze kwamba huu msisitizo alioutoa Mheshimiwa Rais ndiyo huu wa kuchukua watu arobaini arobaini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kwa sasa hamna chuo kinachojengwa Mkoani Lindi, lakini tulichokuwa tunaelezea ni kwamba tayari kuna jitihada ya kujenga vyuo kama hivyo katika maeneo mbalimbali nchini na tayari kuna chuo ambacho kipo karibu na Mchinga. Ni kweli kwamba Mheshimiwa Rais alielezea kuhusu umuhimu wa kujenga vyuo hivyo, lakini tayari tumeanza kwenye baadhi ya maeneo.
Mheshimiwa Spika, tayari kuna vyuo vinafanya kazi, kwa mfano tayari kuna Chuo cha Mbegani ambacho kinatoa mafunzo chenye uwezo wa wanafunzi 120; tayari kuna Chuo Kibirizi, Kigoma na Chuo cha Nyegezi Mwanza nacho kinatoa mafunzo.
Kwa hiyo, kadri tunavyozidi kuendelea, tunazidi kuanzisha vyuo katika maeneo mbalimbali na hatimaye ikiwezekana maeneo yote au Mikoa yote ambayo imezungukwa na maji, yatakuwa na vyuo hivyo. Vilevile tunatambua kwamba hatuanzishi tu vyuo kwenye maeneo ambayo yapo karibu na bahari kwa sababu tunachosisitiza siyo vyuo tu vya uvuvi katika maeneo ya bahari na maziwa, lakini hata siku hizi tunakazania sana kuhusu suala la ufugaji wa samaki (aquaculture). (Makofi)
Kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba mpango upo lakini tumeanza taratibu kwasababu hatuwezi tukaanza katika maeneo yote. Nashukuru sana.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, japokuwa swali langu halijajibiwa kifasaha na imekuwa ni mwendelezo wa kukiuka Kanuni namba 46(1) na hii ni kawaida tumeona sijui inamaanisha nini. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza:
Kwanza, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kupunguza bei ya mbolea ili kuwapunguzia wananchi gharama za kilimo?
Pili, ni lini Serikali itapunguza ushuru na tozo mbalimbali katika zao la kahawa ili kuwapunguzia wakulima mzigo maana wakulima wametwishwa mzigo kwa muda mrefu sana. Wamekuwa na tozo nyingi, ushuru mkubwa kwenye kahawa mwisho wa siku hawanufaiki. Sasa ni lini Serikali itapunguza ushuru na tozo mbalimbali katika zao la kahawa ili kuwapunguzia wakulima mzigo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kwanzaa kuhusu kupunguza bei ya mbolea, Serikali imejipanga kuhakikisha kwamba inachukua hatua zinazotakiwa ili kuhakikisha kwamba bei ya mbolea inayotumika katika mazao mbalimbali inapungua. Kwa wiki za hivi karibuni Wizara yangu imekuwa ikikutana na wataalam wake kuangalia ni namna gani tunaweza tukaondoa kero mbalimbali zilizopo katika sekta ya kilimo ikiwa ni pamoja na kuondoa kero ya bei ya mbolea ambayo kwa kweli imelalamikiwa na wananchi wengi.
Mheshimiwa Spika, lakini (b) ameulizia kuhusu kuondoa tozo mbalimbali zinazokabili mazao mbalimbali katika sekta yetu ya kilimo. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kuwa Wizara imekuwa ikipitia upya tozo zote zinazotolea ili kuona ni namna gani tunaweza kupunguza.
Mheshimiwa Spika, katika kufanya hivi nafikiri yeye mwenyewe ameshiriki katika Mkutano ambao Mheshimiwa Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi ameuitisha hivi karibuni wa Wabunge wanaotoka maeneo ya mazao haya ili kuangalia changamoto zilizopo lakini vilevile kupata mapendekezo yao ya namna ya kutafuta suluhu. Nimhakikishie tu kwamba, Wizara inapitia upya kuhusu hizo tozo kwa sababu ni kweli wananchi wanalalamikia na muda siyo mrefu tutapata mrejesho kamili kuhusu namna gani Serikali itapunguza au kuondoa moja kwa moja baadhi ya hizo tozo. Nashukuru sana.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri. Kwa kuwa hatuna muda nitauliza swali moja tu la nyongeza na swali langu liko hivi. Kwa kuwa, kumekuwa na mlolongo mrefu wa upatikanaji wa pembejeo za kilimo kwa wakulima.
Je, Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kutafuta njia mbadala ili kufupisha mlolongo huo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Serikali iko kwenye mpango tayari wa kupitia mfumo wa kutoa pembejeo ili kuleta mfumo ambao utaleta ufanisi zaidi katika ugawaji wa pembejeo ambao sisi tunaamini kwamba siyo tu kwamba, utarahisisha upatikanaji wa pembejeo kwa wakati, lakini vilevile kwa bei nafuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni kama mnavyofahamu tumekutana na Wabunge wote wanaotoka maeneo wanayolima mazao muhimu ili kupata mawazo yao ya namna ya kuboresha mfumo huu. Nawaahidi kwamba, katika bajeti inayokuja, Serikali inakuja na mapendekezo ya mpango mpya kabisa ambao utaondoa hii kero na changamoto, ili isiwepo tena. Nashukuru sana.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri amekiri kwamba mfumo uliopo una matatizo katika kumhudumia mkulima. Lakini Serikali inashiriki kikamilifu katika kupanga bei katika mfumo mzima. Sasa kwa kuwa Serikali inashiriki kwa kupitia wakala wake bodi au council, je, Serikali haioni kwamba inawajibika kubeba sehemu ya hasara anayopata mkulima?
Kwa kiasi gani mmefaulu kupata wanunuzi zaidi kutoka China ili soko liwe la haraka na wakulima wanufaike?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, Tobacco Council au Halmashauri ya Tumbaku inawakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya tumbaku. Serikali yenyewe haihusiki moja kwa moja katika kupanga bei lakini imeweka tu utaratibu ambao wadau wenyewe wanaweza kukaa kukutana kwa uhuru wao na kupanga bei. Hata hivyo, Serikali imechukua hatua mbalimbali za kuhakikisha kwamba bei ya tumbaku inaendelea kuwa nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kwamba tokea mwaka 2013 Bunge hili lilipitisha Sheria mpya ya Vyama vya Ushirika, utaratibu mpya wa Vyama vya Ushirika ni utaratibu ambao pamoja na mambo mengine unawaruhusu wakulima wa mazao mbalimbali kuendesha shughuli zao kwa kuwa na uhuru zaidi. Lakini vilevile mpango ule umeunda Tume ya Ushirika ambayo inakuwa karibu na Vyama vya Ushirika ili kuwezesha kuondoa kero zilizopo. Tunafikiri kwamba utaratibu huu utaleta ufanisi zaidi katika kilimo cha tumbaku pamoja na mazao mengine ikiwa ni pamoja na kusaidia katika suala la bei.
Lakini nitumie tu fursa hii kuwawelezea vilevile Waheshimiwa Wabunge kwamba pamoja na changamoto nyingi zilizopo kwenye sekta ndogo ya tumbaku, tunafikiri sekta ndogo ya tumbaku ni eneo ambalo limeanza kuonesha mifano ya kufanikiwa. Hii ni kwa sababu ndiyo sekta ndogo ya pekee ambayo mkulima anakuwa na uhakika wa kuuza zao lake tokea siku ya kwanza anapoanza kuweka mbegu shambani kwa sababu ni kilimo cha mkataba. Kwa hiyo, tukiondoa changamoto zilizopo tunafikiri ni eneo ambalo bado inawezekana kupata mafanikio makubwa. Lakini vilevile tungependa kutumia fursa hii kuwaeleza wakulima…
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, namalizia. Kuwafahamisha kwamba kufanikiwa kutumia mfumo wa mkataba utasaidia tu kama kila mtu akiheshimu mkataba. Kwa mfano, mwaka huu tayari wakulima wanafahamu inatakiwa wazalishe tumbaku kiasi gani, tunaomba wale ambao hawako kwenye mkataba usizalishe tumbaku kwa sababu ukizalisha hautaweza kupata mnunuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kipengele cha pili cha swali ni kwamba ni kiasi gani na kwamba tumefikia wapi na kuwapata wanunuzi kutoka China.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inajitahidi kuongea na wafanyabiashara kutoka China, tumefika hatua nzuri sana kilichobakia sasa ni wao kumaliza taratibu za nchi mwao ili nao waweze kuingia kwenye mfumo rasmi wa kununua tumbuku ili kuondoa ukiritimba ambao mpaka sasa hivi nchi nzima kampuni zinazonunua tumbaku ni nne tu.
Kwa hiyo, tunafikiri kampuni zikiwa nyingi maana yake tunaondoa monopoly na hivyo bei itakuwa nzuri nashukuru sana.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa masikitiko makubwa sana nimefedheheshwa na majibu ya Wizara kwa sababu amenijibu kuhusiana na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na mimi nimeuliza kuhusiana na Halmashauri ya Mji wa Tarime ambapo Mnada wa Magena upo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali yangu, kwa kuwa katika majibu yao ambayo hayajakidhi wametamka dhahiri kwamba walifunga mnada huu kwa sababu za wizi wa ng’ombe na usalama. Kwa kuwa Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi imeanzisha Kanda Maalum ya Tarime - Rorya ambapo hivi sasa usalama umeimarika ingawa bado wanaongelea suala la wizi. Vilevile wameainisha kwenye majibu yao kwamba 1996 tu waliweza kupata Sh.260,000,000 na sasa hivi 2015 wanapata Sh.212,000,000, hawaoni kuwa Serikali inapoteza mapato mengi sana kwa kutokuanzisha ule mnada ambao ulikuwa umeshajengwa ambapo kwa sasa hivi unaweza kupata zaidi ya Sh.1,000,000,000? Hilo ni swali la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni dhahiri kabisa na hata kwenye majibu yao wamesema Mnada wa Mtana, Kewenja, Nyamwaga na Chemakolele ipo katika Halmashauri ya Wilaya na ni dhahiri kabisa pia kwamba huu mnada ulihamishwa kwa sababu za kisiasa kwa sababu huwezi ukasema Kirumi ipo mpakani na Kenya. Napenda kujua sasa ni lini Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi itaacha siasa iweze kufanya mambo ya kimaendeleo na Mnada wa Magena ufunguliwe ili wananchi wa Tarime wafaidike? ((Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kupoteza mapato, ni kweli kabisa kuna changomoto kwamba Serikali ingeweza kupata mapato mengi zaidi kwa kuendelea na mnada ule. Hata hivyo, katika hali iliyopelekea mpaka mnada husika ukafungwa, ukweli wa mambo ni kwamba hata kukusanya mapato ilikuwa haiwezekani. Kwa sababu Serikali ina jukumu la msingi la kulinda amani na usalama, kwa kweli ilikuwa haiwezi kuendelea kuruhusu mnada ule utumike wa sababu watu mali zao zilikuwa zinapotea na walikuwa wanatishiwa maisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi, hakuna shughuli za kiuchumi ambazo zilikuwa zinaenda kama ilivyotarajiwa. Kwa hiyo, pamoja na kwamba ingeweza kupata mapato lakini haikuwezekana kuendelea kuwa na shughuli yoyote katika hali ambayo si salama. Hata yeye mwenyewe amekiri kwamba kulikuwa na hali ya kutishia amani na usalama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mnada husika kufungwa na mwingine kuanzishwa kisiasa, nimhakikishie tu Mheshimiwa Matiko kwamba kilichopelekea mnada huu kufungwa na mwingine kuanzishwa siyo sababu za kisiasa ni kwa sababu ulinzi na usalama wa wananchi wa Tarime ulikuwa ni wa muhimu zaidi. Vilevile nimhakikishie tu kwamba kwa hali ya sasa mnada ule mpya unafanya kazi kama ile iliyokuwa inafanywa na mnada wa awali. Cha maana ni wananchi kupata fursa ya kuuza mifugo yao kwenda nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama kuna mnada ambao unafanya kazi ileile vizuri zaidi na hauhatarishi usalama, kwa vyovyote vile Serikali itachukua uamuzi wa kuhakikisha kwamba mnada huo unaendelea badala ya kufikiri kwamba ni lazima kurudi kwenye mnada ambao kwa kweli uendeshaji wake ulikuwa unatishia ulinzi na usalama.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa Mnada wa Magena katika Mji wa Tarime unafanana na mnada ambao unaitwa Mnada wa Kimataifa wa Pugu lakini ukifika hakuna mazingira yoyote ya kimataifa ambayo unaweza ukaonyesha. Ng’ombe wote wanaofugwa mikoani mimi katika Jimbo la Ukonga kule Pugu ndiyo nawapokea na nawalisha watu wa Dar es Salaam. Naomba nijue, ni lini sasa Wizara hii itahakikisha jina la Mnada wa Kimataifa wa Pugu linasadifu na mazingira ya Pugu kwa maana ya malambo, umeme na huduma zingine? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mnada wa Magena ni Mnada wa Mpakani wakati Mnada wa Pugu ni Mnada wa Upili, kuna tofauti kubwa. Hata hivyo, naungana naye kukiri kwamba kuna changomoto nyingi ambazo zimejitokeza katika uendeshaji wa Mnada wa Pugu. Bado kuna fursa kubwa ya kuufanya mnada ule uwe na hadhi nzuri zaidi kuliko ilivyo sasa. Nimhakikishie tu kwamba tayari hatua zinachukuliwa ili kuboresha huduma katika Mnada wa Pugu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mwenyewe baada ya kupata uteuzi wa Mheshimiwa Rais, nilikwenda kutembelea Mnada wa Pugu na kuangalia hali ilivyo na tayari tumetoa maelekezo hatua mahsusi zichukuliwe ili kuboresha huduma pale ikiwa ni pamoja na huduma za maji na kuimarisha utaratibu wa kukusanya mapato. Kwa sasa karibuni Mnada wa Pugu utakuwa unatuma mfumo wa kukusanya mapato wa kielektroniki. Hata Mheshimiwa Waziri mwenyewe ameshatembelea Pugu. Kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba baada ya muda Mnada wa Pugu utaendeshwa katika hali ambayo ni nzuri zaidi ili kuweza kuchangia katika pato la Taifa.
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Waziri ametuambia hapa kwamba kuna sharia zinazosimamia suala hili lakini sijui kama ana taarifa kwamba watu hupigwa na kunyang’anywa mali zao na lini jambo hili litakoma ili sheria ifuate mkondo na siyo kunyang’anywa mali zao na kupigwa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Waziri amesema kwamba kuna elimu inatolewa juu ya watu hawa wa Dago ambapo kwa Wazanzibar ni jambo asili na la muda mrefu tu kutoka Bara kuja Unguja kama vile watu wanavyotoka hapa kwenda Dago Zanzibar. Je, Waziri anajua kwamba hiyo elimu anayoisema haijaenea kiasi cha kutosha ndiyo sababu ya sokomoko linalotokea katika eneo la wavuvi hawa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa kwamba watu hupigwa na kunyang’anywa mali zao hazijafika rasmi Wizarani. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba pale tutakapopata taarifa hizi tutachukua hatua stahiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nimueleze kwamba nafahamu kuna changamoto nyingi zinatokea katika Kambi za Dago hasa maeneo ya Mafia, kuna changamoto nyingi ambazo zimeripotiwa. Wizara yangu ina mkakati na mimi mwenyewe nimepanga kwamba mara nitokapo kwenye Bunge hili nitaelekea Mafia kwa sababu mbali na alichosema Mheshimiwa Mbunge tayari Wabunge wengi wa ukanda huo na hasa wanaotoka maeneo ya Mafia wameleta changamoto nyingi ambazo zipo, nitaendelea kufahamu changamoto zilizopo kule ili kuweza kuzipatia suluhu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nitumie fursa hii kupitia Bunge hili kuwasihi wananchi kwamba utaratibu wa Dago ni utaratibu mzuri lakini ni mzuri tu kama unafuatwa. Kama wavuvi wakiwa wanatoka eneo moja kwenda lingine bila kufuata taratibu ni vigumu sana Serikali kutoa msaada wowote. Kwa hiyo, ni vizuri tufuate taratibu na sheria zilizopo ili kuondoa vurugu ambazo zinatokea kwenye Dago.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la nyongeza la pili lilitaka nijibu kama kuna elimu inatolewa Zanzibar. Nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa taarifa tulizonazo sisi ni kwamba elimu hiyo inatolewa kote na mara nyingi inatolewa kwenye halmashauri anapokwenda kuvua mvuvi siyo kule anapotoka. Kwa hiyo, tunaendelea kusisitiza kwamba kama kuna upungufu katika elimu inayotolewa, tutaendelea kuwasiliana na mamlaka husika kuhakikisha kwamba elimu hii inatolewa kwa wavuvi wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa sekta ya uvuvi ni muhimu sana katika kukuza uchumi wa Taifa na ni sekta oevu kwa kupata mapato ya Taifa pia kuweza kuwapatia vijana wetu ajira. Serikali imeshafanyia kazi kiasi gani Taarifa ya Chenge One kuhusu sekta hii ya uvuvi hasa wa bahari kuu ambapo Serikali itapata mapato, wawekezaji wataweza kushirikiana na wawekezaji wa ndani ili Taifa letu liweze kujikwamua katika hali ambayo ipo na rasilimali tunayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli naungana naye kwamba sekta ya uvuvi ni sekta ambayo inategemewa sana na Watanzania wengi. Ni sekta ambayo inawaajiri Watanzania 4,000,000, kuna operators mbalimbali wanaofika 400,000 wanaojihususha na shughuli za uvuvi, kwa hiyo ni sekta muhimu sana. Vile vile nikubaliane naye kwamba potential iliyopo ni kubwa na kuna fursa kubwa sana ya kuweza kufanya hili eneo liweze kuchangia zaidi katika maendeleo ya Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kumekuwa na mapendekezo mengi ya namna ya kuboresha ufanisi wa sekta hii ikiwa ni pamoja na ripoti aliyosema ya Chenge One ambayo pamoja na mambo mengine ilipendekeza ni namna gani tunaweza tukapanua wigo wa fursa za uvuvi kwa kutumia bahari kuu. Katika kutekeleza ushauri huu, Wizara ipo katika mpango wa kuchukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha kwamba tunaweza kuanza kunufaika na rasilimali iliyopo katika bahari kuu. Kwa kuanzia, tupo kwenye mkakati wa kuanzisha fishing port. Tunataka tuanzishe bahari ya uvuvi ambayo pamoja na mambo mengine itakuwa rahisi kuratibu namna uvuvi unavyofanywa katika bahari kuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kama nilivyokwishasema hata katika Bunge hili tumeshakutana na Waheshimiwa Wabunge wanaotoka maeneo ya uvuvi na leo hii tena mchana tunakutana. Tunaendelea kupokea mawazo ya Waheshimiwa Wabunge ili tuone namna ya kuboresha sekta hii muhimu katika Taifa letu.
MHE. ALLY M. KEISSY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mwambao wa Ziwa Tanganyika wavuvi wengi wanatoka DRC-Congo. Cha ajabu wanakata leseni kwa bei kama mvuvi mwenyeji wa Ziwa Tanganyika. Je, ni lini Serikali itachukua hatua ili wavuvi kutoka nchi za jirani walipie leseni kama inavyotakiwa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Keissy kwa sababu amekuwa akifuatilia kwa karibu sana changamoto mbalimbali za uvuvi na hasa katika maeneo ya Jimbo lake. Tumepata taarifa kwamba kuna wavuvi wanaotoka nchi za jirani wanavua katika maziwa yetu. Kwa vyovyote vile, hii ni kinyume na sheria. Tunaomba Waheshimiwa Wabunge taarifa kama hizi tuendelee kuzipata. Tukitoka hapa mimi mwenyewe nitachukua hatua za makusudi za kufuatilia ili tuweze kujua nani amehusika, tuwajue Maafisa wa Halmashauri wanaotoa leseni kwa watu hao ili kuweza kuchukua hatua stahiki.
MHE. HAMAD SALIM MAALIM: Mheshimiwa Naibu Spika nafurahi sana kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri. Pamoja na majibu yake mazuri, nafurahi kwa kukubali kwamba kuna mradi unaotoa mafunzo na mitaji kwa wavuvi, lakini naomba niseme kwamba, mradi huu kuna bado katika Jimbo langu ambako kuna wavuvi wengi haujafika. Sasa naomba maelezo yake ni lini mafunzo na mitaji hii katika Jimbo langu la Kojani ili kuwafaidisha wavuvi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba katika mipango ambayo imepita, Jimbo la Mheshimiwa halikuwepo katika mpango, lakini katika bajeti inayokuja nitakuhakikishia kwamba wananchi wa Jimbo lako vilevile watapata mradi huo.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Meiseyeki, swali la nyongeza.
MHE. GIBSON B. MEISEYEKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika nchi yetu tukizungumzia hasa mifugo, ng‟ombe hawa wa nyama ni aina ile ambayo inachukua muda mrefu sana kumtunza ng‟ombe kufika angalau kilo 100 unaweza kuchukua karibu miaka minne au mitano ng‟ombe kufikisha kilo 100. Sioni commitment ya Serikali hapa hasa ukilinganisha kwa hii bei ambayo wameitaja hapa shilingi laki nane kwa milioni moja kwa mtamba.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii bei ni kubwa sana na sidhani kama, labda naomba ku-declare interest, mimi ni mfugaji na ni mkulima pia. Hii bei ya shilingi 800,000/= na shilingi 1,000,000/= ndiyo bei iliyoko sokoni, sasa kuambiwa kwamba hii ndiyo bei yenye ruzuku sitakubaliana na hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba kupata commitment ya Serikali katika kubadilisha hasa aina ya mifugo tuliyonayo, ni lini Serikali itakuja na bei ambayo ni affordable kwa wakulima wetu ili tuweze kubadilisha mbegu hizi za hawa ng‟ombe ambao wanachukua muda mrefu kuongeza uzito?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, ni Tanzania ndiyo nchi pekee duniani ambayo maziwa ni rahisi kuliko maji ya kunywa, ni lini Serikali itakuja na bei elekezi ya lita moja ya maziwa ya ng‟ombe ili iweze kuwa na tija kwa wafugaji ambao wanahangaika sana na mifugo, lakini hawapati chochote kutokana na nguvukazi yao hiyo na pengine inaweza kuwahamasisha vijana zaidi kushiriki kwenye ufugaji. Ni lini Serikali itakuja na bei elekezi ya lita moja ya maziwa fresh ya ng‟ombe ili wakulima wetu waweze kupata tija?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kwa bei ya sasa ya mitamba inaonekana kwamba iko juu, lakini kama nilivyosema ukilinganisha na bei iliyoko kwenye soko bado kuna ruzuku.
Kama nilivyosema tofauti inafikia kwenye mitamba yenye ruzuku ya Serikali ni kati ya shilingi 800,000/= na 1,200,000/= wakati kwenye soko inafikia kati ya 1,2000,000/= hadi 2,300,000/=. Kuna tofauti hapo, lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha kwamba bei hii inashuka ili wafugaji wengi waweze kumudu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tunamshauri Mheshimiwa Mbunge pamoja na Wabunge wengine, tujaribu kutumia huduma za uhimilishaji kwasababu zinakuwa bei yake ni afadhali zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu bei elekezi, bei ya maziwa kama bidhaa nyingi nchini kwetu zinaamuliwa na kanuni za soko. Tunachoweza kusema ni vigumu kuweka bei elekezi lakini tunachofanya kama Serikali ni kujaribu kuweka mazingira mazuri ya uchakataji wa maziwa, kujenga viwanda ili bidhaa za maziwa ziweze kupata bei.

WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri wa Kilimo, Ufugaji na Uvuvi, napenda niongeze jibu moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili tuweze kujenga uchumi wa viwanda na tuwe shindani lazima mazao ya chakula yawe ya bei nafuu. Kwa hiyo, wakulima wanaofuga ng‟ombe, wajibu wa Serikali ni kuwawezesha ili bei ya maziwa iwe chini, bei ya chakula iwe chini, wafuge na kuzalisha kwa tija kusudi uwekezaji Tanzania uwe nafuu, viwanda vya dunia nzima vije Tanzania. Nawapongeza wakulima wa maziwa na bajeti yetu itawasemea.
MHE. ABDALLAH HAMISI ULEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu haya mazuri ya Serikali naomba sasa niulize majibu ya maswali mawili ya nyongeza.
(a) Je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kuongozana na mimi kwenda Jimboni Mkuranga katika vijiji hivi vya Magawa, Msonga Makumbeya na vinginevyo pata athari hii ili aweze kujionea yeye mwenyewe na kuona namna iliyobora zaidi ya kutusaidia?
(b) Ningeomba niulize Serikali sasa ipo tayari kuhakikisha kwamba viuatilifu kwa maana ya sulfur, iweze kupatikana kwa wingi na kwa wakati katika Jimbo letu la Mkuranga ili kuepusha madhara haya ya ugonjwa wa mikorosho na kuhakikisha uzalishaji mkubwa zaidi ili kuwaondolea wananchi wangu umaskini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ombi lake la kutaka tuongozane naye kwenda Jimboni tumelipokea na ninamuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa namna ambavyo amekuwa akifuatilia hili suala tayari tulishapanga kufika Mkuranga na kipindi cha bajeti kitakapoisha mimi binafsi nitaongozana naye kwenda Mkuranga ili kujionea hali halisi na kuangalia namna ya kuwasaidia wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili ni kweli kwamba kumekuwepo na changamoto ya upatikanaji wa viwatilifu kwa wakati hasa sulfur na huko nyuma tayari kumeshatokea matatizo kwa sababu hiyo, kama nakumbuka mwaka 2011 kulikuwa na changamoto wakatia wa matumizi ya kiatilifu cha aina eugenol 880, lakini kwa sasa Wizara kwa kushirikiana na Bodi ya Korosho imejipanga vizuri kuhakikisha kwamba viwatilivu hivyo na hasa sulfur zinapatikana kwa wingi na kwa wakati. Hivyo, ninamuahidi kwamba changamoto hii imeshafanyiwa kazi.
MHE. SULEIMAN A. SADDIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Ni kweli kuna juhudi mbalimbali zinazoendelea kufanyika katika Wilaya ya Mvomero kuondoa tatizo la wakulima na wafugaji, na kwa kweli Serikali imefanya kazi kubwa kupitia Waziri Lukuvi, Mheshimiwa Simbachawene pamoja na Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, tunawashukuru Mawaziri hawa, wamefanya ziara mbalimbali. (Makofi)
Swali la kwanza, kwa kuwa juhudi ambazo tunaendelea kuzifanya kama Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero zinahitaji bajeti, na kwa kuwa tayari Mawaziri hawa tumeshawapa bajeti zetu ili tuondoe mgogoro huu na wakulima na wafugaji wawe na maeneo yao. Je, ni lini Serikali itatoa fedha ambazo tuliziomba na fedha zile ziko kwenye bajeti?
Swali la pili, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kuna mashamba sita yamerudishwa, na mashamba mengine zaidi ya 29 bado hayajarudishwa.
Je, lini Waziri mhusika pamoja na Mheshimiwa Rais, watayafuta yale mashamba yaliyobaki ili tuwagawie wananchi maeneo ya wakulima na wafugaji?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la bajeti, Wizara ya Ardhi pamoja na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwenye bajeti yake imetenga fedha pamoja na mambo mengine kwa ajili ya matumizi bora ya ardhi, vilevile kwa ajili ya kuweka miundombinu ya huduma za mifugo, kwa ajili ya Wilaya ya Mvomero.
Kuhusu swali la pili, tayari mashamba mengine yameshapelekwa Wizara ya Ardhi ili yaweze kufutiwa hati. Wilayani Kilosa mashamba 73 yenye ukubwa wa ekari 429,625.3 tayari yameshabainishwa na kupelekwa ili yaweze kufutwa. Vilevile Wilayani Mvomero mashamba 84 yenye ukubwa wa ekari 119,382.6 nayo yameshapelekwa Wizara ya Ardhi ili kufanyiwa kazi. Lengo ni kwamba haya mashamba yote yakiweza kufutiwa hati baada ya hapo utaratibu utakaofuata ni kuwagawia Wafugaji na Wakulima ili kuweza kuondoa tatizo kubwa lililopo la ardhi na hatimaye kupunguza migogoro hiyo ya ardhi.
MHE. SILVESTRY F. KOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru na kumpongeza Waziri na Serikali kwa kuamua kurejesha takribani hekta 2963 kwa wananchi. Pamoja na kazi hiyo nzuri ya Serikali kwa wananchi ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika urejeshaji huo wa eneo hili kuna eneo dogo la takribani ekari 300 tu, ambalo lina zaidi ya kaya 250 ambalo halikufikiriwa katika mpango huu na ambapo limewafanya wananchi hawa wanaokaa katika eneo hili sasa wakae kwa mashaka na kujiona kwamba wao ni wanyonge kwa sababu hawakuwekwa katika mpango huu ambao uliwarejeshea maeneo wenzao.
Swali langu la kwanza, je, ni lini sasa Serikali itaamua kurejesha eneo hili dogo ili kuwatendea haki kama ilivyotenda haki kwa wananchi wengine na wananchi hawa wa Vingunguti waweze kujiona kwamba wametendewa haki kama hao wengine.
Swali la pili, kwa sababu Serikali imekuwa na nia njema na imechukua hatua mbalimbali, ni lini sasa Mheshimiwa Waziri pengine akishirikiana na Waziri wa Wizara ya Mifugo atatembelea eneo hili la Pangani maarufu linaitwa Vingunguti, ili tuweze sasa kukaa na wananchi na kupata ufumbuzi wa kudumu kutokana na mgogoro au tatizo hili la wakazi wa eneo hilo?
himiwa Naibu Spika, naomba nikiri wazi tu kwamba Serikali haiwezi kuendelea kurudisha maeneo kwa wananchi, hasa katika hilo eneo ukizingatia kwamba eneo la awali lililokuwa na ukubwa wa hekta 4000 wananchi walipewa eneo la hekta 2963 sawa na asilimia 74 ya eneo lote. Hivyo kuendelea kulimega ni kufifisha pia azma ya Wizara ya Kilimo na Mifugo, katika kuendelea kuzalisha mitamba bora ambapo tunahitaji kuwapeleka wafugaji wetu katika maendeleo ya kuwa na ufugaji bora na endelevu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili niseme tu kwamba, Wizara imekuwa na nia ya dhati kufika katika lile eneo na kukutana na wananchi na hasa kukutanisha pande zote mbili, ukizingatia mara ya mwisho tumekuwepo kule tarehe 4/3/2016, lakini kama hiyo haikutosha Wizara yangu iko tayari kuendelea kukutana nao ili muafaka uweze kufikiwa.
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Hizo huduma zinazosemekana kuwa zinatolewa kwa out growers, Je kuna mkakati maalum au inategemea na huruma ya huyo mwekezaji mkubwa?
Swali la pili linahusiana na soko; Kwa kuwa sasa hivi huu utaratibu wa minada ya Kahawa unaathiri kwa kiasi kikubwa mapato yanayopatikana kwa wakulima wadogo. Je, Serikali iko tayari kuruhusu wakulima wa kahawa na wao wenyewe kujitafutia masoko katika maeneo ambayo ni nish kwa ajili yao ili na wao waweze kupata mapato makubwa zaidi kwa ajili ya kahawa yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, Je, hii minada ni lazima iwe Kilimanjaro tu, hatuwezi kuwa na minada katika maeneo makubwa ambayo Kahawa inalimwa? Ahsante sana
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, moja, kuhusu huduma zinazotolewa na Wakulima wadogo kwenye out grower schemes hamna mkakati wowote maalum ambao umewekwa, isipokuwa uhamasishaji umekuwa ukifanywa ili mashamba hayo yaweze kutoa huduma mbalimbali ikiwepo kama nilivyosema kuwasaidia kupata teknolojia nzuri zaidi, kuwasaidia katika ukoboaji, kimsingi mashamba yale yanaangalia ni nini wanahitaji kwa ajili ya kuongeza tija katika uzalishaji wao na katika kupata masoko.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inachofanya ni kujaribu kuhamasisha na kuwashauri waweze kutoa huduma mbalimbali ambazo zitawasaidia wakulima wale wanaozunguka kuweza kupata tija katika uzalishaji
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu masoko; Serikali kimsingi haikatazi wakulima kujitafutia masoko ilimradi wafuate taratibu ambazo zimewekwa ili kusiwepo na uholela pia vilevile ili wakulima wetu waweze kulindwa na mifumo ya kinyonyaji, kwa sababu ukiachia tu iende kiholela, wakulima wetu wanaweza wakaumia. Kwa hiyo kimsingi, masoko yanaweza kutafutwa na tayari kuna wakulima ambao wanauza Kahawa moja kwa moja nje lakini ilimradi taasisi zinazohusika na udhibiti zifanye kazi ili wakulima wasiweze kuonewa.
Pia, aliuliza kuhusu Je ni lazima soko la kahawa likafanyike tu Kilimanjaro. Kimsingi kuna aina tatu ya uuzaji wa kahawa. Kwa kutumia soko la Moshi, wakulima wanaweza wakauza moja kwa moja nje pia kuna utaratibu wa kutumia manunuzi ya wakati lakini kimsingi Serikali iko tayari kufikiria namna bora ya kuendesha soko la kahawa ikiwa ni pamoja na kuruhusu uanzishwaji wa masoko mengine kwa maeneo ambayo yana uzalishaji mkubwa.
MHE. ESTHER M. MMASI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii nami niweze kuuliza swali la nyongeza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Waziri, kupitia mpango wa AGOA ambao Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama sehemu ya ushiriki Nchi za SADC, tumepewa ridhaa ya kutumia soko la Marekani bila kuwepo na vikwazo vya kodi.
Je, Serikali inatupa commitment gani kuona vijana wahitimu wa Vyuo Vikuu wanaweza kutumia fursa hii ya mpango wa AGOA kuondokana na suala zima la tatizo la ajira? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa naibu Spika, ni kweli kwamba mpango wa AGOA unatoa fursa ya kuweza kuuza mazao yetu nje, na ni kweli vilevile kwamba ni fursa ambayo ikitumiwa vizuri inaweza ikawasaidia vijana wetu kujiajiri na kuondokana na adha iliyopo sasa ya ukosefu wa ajira. Kwa hiyo Wizara iko tayari kushirikiana na vijana wowote ambao wako tayari kujiingiza katika uuzaji wa kahawa ili kuitumia fursa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika bajeti yetu ya mwaka huu tumetenga baadhi ya fedha ili kuweza kuona namna ya kuwasaidia vijana waweze kuingia kwenye kilimo na tutaanza eneo la Rufiji, lakini tuko tayari kufikiria namna nyingine ya kuweza kuwasaidia vijana wengi waweze kuingia katika uzalishaji huo hasa katika eneo alilosema la kahawa.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Wilaya ya Nkasi, kuna Ranchi ya Kalambo ambayo iligawiwa kwa wafugaji block kama kumi, kila block heka 3000 mpaka 2500 kila mfugaji, block kumi. Lakini hizo block kumi hakuna ng‟ombe zilizopelekwa baadhi ya blocks na baadhi ya waliochukua hizo block ni wajanja hawana mfugo hata mmoja wanakaa wanakodishia wafugaji.
Je, Serikali iko tayari kupitia upya Ranchi ya Kalambo ili kugawa upya kwa wafugaji ili kuondoa matatizo ya wafugaji na wakulima nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba kuna changamoto kubwa sana katika ranch ya Kalambo na ranch nyingine ambazo zinamilikiwa na NAFCO, hasa zile ambazo zimegawiwa kwa Wawekezaji.
Nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge kuwa kwa sasa Wizara inafanya tathmini ya kuangalia namna uwekezaji ule ulivyofanywa ili ikigundulika kwamba kuna wawekezaji walipewa ranchi za NAFCO lakini hawatumii ipasavyo wanyang‟anywe na kupewa kwa wafugaji na wawekezaji wengine ambao watatumia inavyotakiwa.
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Pamoja na majibu ya Waziri katika majibu yake ya msingi amekiri kwamba Serikali inachukua hatua kuhakikisha kwamba wanatatua migogoro inayohusiana na wafugaji na hifadhi.
Sasa swali, Waziri utakuwa tayari kuongozana na mimi kuelekea Mkoani Simiyu kwenda kutatua migogoro inayoendelea katika vijiji vya Nyantugutu, Lumi na Longalombogo kwenda kutatua migogoro hiyo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili wananchi wa Wilaya ya Meatu na Wilaya ya Maswa wengi wao hawana maeneo ya kuchungia mifugo yao. Je, Serikali itakuwa tayari kurudisha Pori la Akiba la Maswa ili wananchi hawa waweze kutumia kama malisho, kwa sababu pori hilo limekosa sifa ya kuwa Hifadhi ya Taifa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kwanza kuhusu kama nitakuwa tayari kuandamana na yeye ndani ya Bunge hili kwenda kutatua migogoro, nimshauri Mheshimiwa Mbunge kwamba labda baada ya kikao cha leo tukutane nimshauri zaidi namna ya kutatua hili kwa sababu itabidi aongee na watu wa maliasili kwa sababu Wizara yetu hasa haihusiki na migogoro kati ya hifadhi na wananchi lakini nitamshauri namna ya kufanya hivyo na nitamshauri vizuri.
Mheshimiwa Spika, kuhusu Pori la Akiba la Maswa kutolewa kwa ajili ya wafugaji nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba mimi ni jirani yake, mimi natoka Ngorongoro nafahamu changamoto iliyopo kati ya wafugaji na pori la Maswa.
Mheshimiwa Spika, kuna mkakati ambao unaendelea sasa Serikalini kama ulivyosikia wiki iliyopita Waziri Mkuu alivyozungumza wa kuangalia namna ya kuondoa migogoro hii, vilevile kuangalia namna ya kutafuta ardhi kwa ajili ya wafugaji ikiwa ni pamoja na kutafuta uwezekano wa baadhi ya maeneo ambayo yamepoteza hadhi ya kihifadhi ili wafugaji waweze kugaiwa.
Mheshimwia Spika, hili linaendelea siwezi kusema moja kwa moja sasa kwamba, Pori la Maswa ni moja kati ya haya maeneo lakini kuna mipango ya kujadili suala kama hilo. Nimueleze Mheshimiwa Mbunge kwamba pamoja na migogoro hii kuongezeka lakini bado kama Taifa tuna jukumu la kuhifadhi wanyama, tunafahamu kwamba ni rasilimali muhimu, tusipohifadhi baada ya muda inawezekana tusiwe na wanyama pori ambao wanaendelea kuletea nchi yetu fedha za kigeni lakini vilevile sifa. Nashukuru sana.

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, naomba nitoe mawazo kuhusu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kama mtakuwa mmeangalia takwimu za sensa ya mwaka 2012 mtaona kabisa katika ile Sensa ya Watu na Makazi kwamba eneo la asilimia 10 la surface area ya Tanzania Bara limetengwa kwa ajili ya mifugo, eneo hilo bado halitumiki ipasavyo. Niseme tu kwa sababu muda mwenyewe ni mfupi kwamba Serikali haina mpango wa kuhuisha maeneo ya hifadhi kuwa maeneo ya kuchunga. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka pia niseme kwamba wote kabla hatujawa Wabunge hapa baada ya kushinda uchaguzi tuliapa kiapo cha uaminifu cha kuilinda, kuihifadhi na kuitunza Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sehemu ya 27 ya Katiba hiyo inasema; kila mtu anao wajibu wa kulinda maliasili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
MHE. LEONIDAS T. GAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii nishukuru kwa majibu ya Wizara, lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa wananchi wa Songea Mjini na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla wanapata shida sana ya kupata mbolea kwa wakati, mbolea huchelewa sana kufika. Lakini vilevile wanakopwa mahindi yao, pamoja na kununua mbolea kwa bei kubwa, lakini wamekuwa wakikopwa mahindi yao na NFRA matokeo yake wakulima hawa wanaendelea kuwa maskini, wanateseka sana.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa wakulima hawa wanapata haki yao kwa muda unaostahili?
Swali la pili, mwezi Disemba mwaka jana Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, alifanya ziara Songea Mjini; na alipata bahati ya kutembelea ghala la hifadhi ya mahindi la NFRA. Alikutana na matatizo mengi ya wananchi pale NFRA; na akatoa maagizo na agizo moja alitoa la kwamba NFRA hivi sasa inunue mahindi moja kwa moja kwa wakulima badala ya walanguzi. Lakini la pili alitoa maagizo kwamba bei elekezi ya Serikali ihakikishe inamfikia mkulima wa kawaida kule anakolima; na ya tatu aliagiza kwamba magunia ambayo yamekuwa yakitolewa kwa walanguzi, na kwa hiyo kuwalangua wakulima wa kawaida. Alipiga marufuku akataka magunia yote wapelekewe wakulima wa kawaida wa mahindi.
Sasa nataka niulize je, Wizara imejipangaje kuhakikisha inasimamia maagizo haya ya Waziri Mkuu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama alivyosema kwamba, mbolea mara nyingi hazifiki kwa wakati, na imekuwa ikiuzwa kwa bei ya juu; na ndio maana nimeeleza katika jibu langu la msingi kuwa tupo katika mkakati wa kuhakikisha kwamba ruzuku zinapatikana kwa bei nafuu, kwa kujaribu kuhuisha utaratibu mzima unaotumika kwa sasa wa kupeleka pembejeo kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba katika msimu utakaokuja, maana yake tukianza kutekeleza Bajeti yetu ya mwaka unaokuja wa fedha, hatutasikia tena kitu kinachoitwa utaratibu wa vocha wa kupeleka pembejeo kwa wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, tutakuwa na utaratibu mpya kabisa, na tunaamini kwamba kwa kiasi kikubwa itaondoa shida iliyopo. Lakini vilevile nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba tatizo lingine ambalo linatokea Ruvuma kama ilivyo katika maeneo mengine nchini; ni kwa sababu malipo ya mahindi kwa wakulima yanachelewa kwa sababu kunakuwa na walanguzi wa kati. Nimfahamishe tu kwamba kwa sasa utaratibu huo utaondolewa, wakulima wanakuwa wanalipwa moja kwa moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vile vile nipende kujibu swali lake la pili la nyongeza, kuhusu ziara ya Waziri Mkuu aliyofanya ya tarehe 6 Januari mwaka huu Ruvuma; ambapo pamoja na mambo mengine alitoa maagizo matatu kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge.
Moja ni kuhusu kuwaondoa watu wa kati nimueleze Mheshimiwa Mbunge kwamba maagizo ya Waziri Mkuu sisi tunayafanyia kazi, na nimhakikishie kwamba kuanzia sasa mahindi yatanunuliwa moja kwa moja kutoka kwa wananchi na sio kupitia kwa watu wa kati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vile vile kuhusu bei elekezi, nimueleze kwamba kuanzia sasa bei ile ya dira bei elekezi ambayo inatolewa na NFRA bei hiyo ndio inatumika kununua mahindi ya wananchi; na hakuna mtu yeyote atakayeruhusiwa kwenda kupunguza bei hiyo, kwa hiyo watu wa kati hawataweza tena kufanya biashara kama hiyo.
Lakini vilevile kuhusu magunia na vifaa vingine, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, agizo la Waziri Mkuu kuhusu hili linatekelezwa; na kwamba sasa magunia yanapelekwa moja kwa moja kwa wananchi, na sio kupitia kwa watu wa kati.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jibu lako zuri, naomba niulize swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa moja ya usumbufu mkubwa wanaopata wakulima ni suala la usambazaji wa pembejeo ambao haufiki kwa wakati. Lakini tatizo kubwa ambalo linasababisha hilo ni mawakala kutokufikisha kwa wakati na mawakala wamekuwa wakilalamika kwamba hawalipwi pesa za usambazaji. Mpaka leo ninavyozungumza kuna baadhi ya mawakala waliosambaza mwaka jana ambao walikuwa wanafanya kazi hiyo kwa niaba ya makampuni makubwa, kama TFC na MINJINGU, hawajalipwa. Sasa Serikali haioni kwamba tutaendelea na hili zoezi la kuwasaidia wananchi na kutowasaidia wengine wanaosambaza ni makosa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kama alivyosema kwamba kumekuwa na ucheleweshwaji wa malipo kwa mawakala wanaotoa huduma za ruzuku. Nimuhakikishie tu kwamba tatizo hilo linashughulikiwa sasa na Wizara inaandaa malipo ili utaratibu wa kuwalipa uweze kuanza bila kuchukua tena muda. Lakini nimueleze kwamba kama nilivyosema nilipokuwa najibu swali la nyongeza la
Mheshimiwa Gama ni kwamba utaratibu mzima unaotumika kwa sasa ni mbovu ndio umetuleta hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni utaratibu ambao hauwanufaisha walengwa, watu ambao wamenufaika sana na mfumo tulionao sasa wa pembejeo ni wajanja wachache. Mara nyingi pembejeo hizo hazifiki kwa wananchi, lakini hata pale zinapofika zinachelewa, kwa hiyo nilichosema ni kwamba Wizara yangu iko katika hatua za mwisho za kukamilisha utaratibu mpya ambao ni tofauti na huu ili kuweza kuondoa changamoto hii. Pembejeo ziweze kufika kwa wakati na kwa bei ambayo wananchi wanamudu, lakini vilevile kusiwe tena na malalamiko haya ya ucheleweshwaji wa mawakala kulipwa.
MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR:Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mbali na tatizo la upatikanaji wa mbolea kwa wakati kwa wakulima, lakini kuna tatizo kubwa la elimu juu ya utumiaji wa mbolea hizo kwa hao wakulima.
Je, Serikali imejipangaje juu ya kutoa elimu endelevu,kwa utumiaji wa mbolea hizo, hususani kwa wakulima wanawake ili kupatikane mazao ambayo yana tija?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kama alivyosema kwamba kuna changamoto kubwa ya elimu na ufahamu miongoni mwa wakulima wetu, kuhusu utumiaji wa pembejeo. Nikiri kabisa kwamba moja kati ya matatizo ya matumizi ya pembejeo kuweza kuongezeka nchini kwetu, ni kwa sababu ya hamasa ndogo ambayo wananchi wanayo. Kwa hiyo, sisi tunaamini kwamba zoezi la kutoa elimu na uhamasishaji lazima liende sambamba na utoaji wenyewe wa ruzuku ili hatimaye wananchi waweze wenyewe kujinunulia kwa sababu utaratibu wa kutoa ruzuku kwenye pembejeo sio endelevu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Ofisi zetu za Kilimo na Maafisa wetu wa Kilimo walioko kwenye Halmashauri, wanaendelea kutoa elimu na kuamasisha wananchi, kuhusu umuhimu wa kutumia pembejeo na hii ni bila kuchagua jinsia, wakulima wote wanapatiwa elimu hii na tunaendelea kuhamasisha wananchi wetu waweze kutumia pembejeo.
MHE. EDWARD F. MWALONGO:Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi, naomba nimuulize Naibu Waziri je, katika suala la ruzuku hiyo ambayo inakuja Serikali inaonaje sasa ikatoa upendeleo kwa wakulima kwamba mkulima awe ndio mwenye kuchagua mbolea anayoihitaji kwa ajili ya mazao anayolima badala tu ya kulazimisha kwamba mkulima ni lazima achukue mbolea ya kupandia mahindi, ama ni lazima achukue mbolea ya kupandia mpunga?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana naye kabisa kwamba kumekuwepo na changamoto ya utaratibu wa kuwalazimisha wakulima wote kuchukua mbolea inayofanana na ruzuku nyingine zinazofanana. Nimhakikishie tu kwamba kwa sababu pendekezo lake linakuja katika wakati muafaka, wakati tunajaribu kurejelea utaratibu huu, tutahakikisha kwamba tunaweka utaratibu wa kuwafanya wakulima vilevile waweze kuwa na uchaguzi kutegemeana na kitu wanacholima.
MHE.RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, lakini ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa kiwanda hiki inaonekana ni teknolojia ya zamani ambayo wenzetu wa SIDO ndio ambao wameitengeneza kama alivyosema Mheshimiwa Waziri. Je, ni lini sasa Serikali itakwenda na wakati na kuwaletea wananchi hao kiwanda ambacho kinaendana na teknolojia ya kisasa ili pia kiweze kuwanufaisha wananchi wa Kata za Lugulu, Mpinji, Bombo, Vunje Maole na Ndungu?
Swali la pili, kwa kuwa katika Jimbo la Mlalo pia ni wakulima wazuri wa tangawizi na Mheshimiwa Naibu Waziri amejibu kwamba Kampuni ya Lion Wattle inanunua tangawizi, na mimi nataka nimwambie kwamba sio ukweli.
Je, Serikali ina mpango gani wa kututafutia wafanyabiashara wanaoeleweka ambao watakuja kununua mazao haya ya tangawizi katika Kata za Mbaramo, Mnazi, Wangwi pamoja na Honde?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu teknolojia inayotumika katika kiwanda cha Same, nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba tuko tayari kupitia upya na kufanyia tathimini kiwanda kile ili kuangalia kama teknolojia yake imepitwa na wakati; na ikionekana hivyo tuko tayari kuwasaidia wana ushirika ili kuweza kutafuta fursa ya kuweza kutafuta kiwanda na teknolojia ambayo inaendana na wakati. Tunaamini kwamba hii itatusaidia katika kupanua uwezo wa kiwanda ili iweze vile vile kuchukua na kusindika tangawizi kutoka maeneo mengine ikiwemo maeneo ya jirani kama Lushoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la nyongeza la pili, kuhusu kampuni ya Lion Wattle, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Ofisi yangu iko tayari kukaa na yeye. Tujadiliane kuhusu hoja hii anayoileta sasa kwamba ana wasi wasi na ukweli kwamba hiyo kampuni inanunua tangawizi. Kwa hiyo tuko tayari vizuri ni mtu ambaye anakuja ofisini kwangu mara kwa mara. Namkaribisha tena tuongee tupitie na tufananishe taarifa tulizonazo, lakini tuko tayari vilevile kuwasaidia wakulima wa Jimboni kwake Mlalo ili kuweza kupata masoko ya tangawizi ikiwa ni pamoja na yale makampuni mengine ambayo nimeyataja.
MHE. MARTHA M. MLATA:Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante namshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri kwenye kiwanda hiki.
Lakini kwa kuwa sisi sote Wabunge tuliokuwepo awamu iliyopita ni mashahidi kwamba Mbunge aliyekuwa wa Jimbo lile Mama Anne Kilango Malecela, kwa jua, kwa mvua usiku na mchana alipigania kiwanda kile kwa fedha zake, akakianzisha na mpaka sasa wananchi wale wananufaika.
Je, Serikali haioni kwamba ni hakika inapaswa kumuunga mkono Mbunge yule ili kiwanda kile kiweze kutoa ajira nyingi sana kwa Wanasame na Watanzania kwa ujumla?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba kama isingekuwa ni juhudi za Mheshimiwa Anna Malecela inawezekana tusingekuwa tunazungumza leo kuhusu kiwanda hiki na hivyo kuwa na swali kama hili Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yeye amejitahidi sana na kama mnavyokupunga Waheshimiwa Wabunge mwaka 2012 yeye ndiyo alifanya jitihada akamualika Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na akaenda kufanya harambe kubwa iliyofanikisha ujenzi wa kiwanda kile. Nimfahamishe tu Mheshimiwa Mlata kwamba Mama Anne Kilango Malecela pamoja na kwamba siyo Mbunge tena anawasiliana na Wizara yangu kwa karibu sana ili kuhakikisha kiwanda hiki kinafufuliwa na kinaweza kuendelea. (Makofi)
Kwa hiyo, naomba mahali popote alipo afahamu kwamba kiwanda hicho hatujakitupa na ikiwezekana tunafanya jitihada kwamba wakati wa ufunguzi vilevile awepo, wakati tunavyofungua upya baada ya matengenezo ahsante sana.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niulize swali la nyongeza.
Kwa kuwa Jimbo hili la Same Mashariki linafanana kabisa na Jimbo la Mbulu Vijijini kwa mahitaji. Same Mashariki wanalima kitu kinachoitwa tangawizi, Mbulu Vijijini tunalima vitunguu na tuna tatizo hili la soko. Je, Serikali ina mpango gani kusaidia wananchi wa Mbulu Vijijini kwa zao hili la vitunguu swaumu maana yake ni maarufu sana pale Bashineti Mbulu ili kuhakikisha kwamba maisha haya yanakwenda vizuri?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa tunatambua kwamba wananchi wa Mbulu wako makini na ni kati ya wazalishaji wakubwa sana wa vitunguu nchini. Serikali iko tayari kukaa na Mheshimiwa Mbunge kuangalia changamoto ambazo zipo katika soko la vitunguu ili wananchi waweze kupata soko la uhakika. Kwa sababu ni jirani yangu yeye anatoka Mbulu na mimi Ngorongoro namkaribisha vilevile tutumie ujirani huo kuongea ili niweze kuwakaribia zaidi wananchi wake na kutoa msaada ambao anauhitaji.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kuniruhusu niliulize maswali mawili ya nyongeza licha ya majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, soko la tumbaku duniani limeendelea kupungua haraka na kwa hivyo hivi karibuni wakulima tumbaku Tabora watakosa mahali pa kuuza tumbaku. Je, Serikali haioni ni muhimu kuanzisha mazao mengine ya biashara kama ufuta, karanga na alizeti?
Swali langu la pili, matatizo ya wakulima wa tumbaku sasa hivi yanatokana na usimamizi mbovu au mdogo unaotekelezwa na bodi yetu ya tumbaku. Hawana uwezo wa hela na hawa vilevile rasilimali watu na kweli kuacha zao la tumbaku liluke luke kama vile kuku hana kichwa.
Je, Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kuiboresha Bodi ya Tumbaku au kuboresha kitu kingine mamlaka mengine ya kusimamia zao la tumbaku ili wakati huu tunahangaika na tumbuka lakini wakulima wawe na hali nzuri ya mauzo ya tumbaku? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, moja kabisa nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba soko la tumbaku linaendelea kuleta changamoto siku hadi sikuhii ni kwa sababu kama mnafahamu Waheshimiwa Wabunge tumbaku ndiyo zao la pekee ambalo hata yule mtumiaji anapiga vita toka siku ya kwanza anapoanza kuitumia. Mnafahamu kwenye tumbaku zote kwenye pakiti za tumbaku imeandikwa tobacco is dangerous to your health, kwa hiyo, imefanya watumiaji wengi wa tumbaku kujiondoa duniani na hasa wale wanaotoka Ulaya Magharibi na Marekani. Soko la tumbaku siku hizi limehamia kwa kiasi kikubwa katika Bara la Asia hasa China lakini nikubaliane naye kwamba ni soko ambalo tunaendelea kupata changamoto katika ununuzi wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nakubaliana nay eye kabisa kwamba njia mojawapo ya kuwafanya wananchi wetu wasiweze kupata mdororo wa uchumi ni kuwashauri kutoweka mayai kwenye kapu moja na kuzalisha mazao mengine ambayo nayo yana tija hususan mazao ya karanga na alizeti ambayo yanaendana vizuri kabisa na hali ya hewa na udongo wa Mkoa wa Tabora.
Kwa hiyo, Serikali imekuwa ikiwahamasisha wananchi siyo wa Tabora tu wasijiingize kwenye kilimo cha zao moja kwa sababu tumeona athari za wananchi kufanya hivyo lakini wajaribu kulima azao mengi iwezekanavyo ili pale zao moja linapopata changamoto waweze kuwa na uchumi wasije wakapata matatizo. Kwa hiyo, nakubaliana naye kabisa kwamba Serikali tutachukua hili na tutafuta namna ya kufanya uhamasishaji wa wananchi kuingia kwenye kilimo kingine lakini huku tukiendelea kutafuta masoko ya tumbaku kwa sababu niseme siyo kwamba masoko hayapo moja kwa moja, ni suala la kutafuta masoko mengine kwa hiyo tutaendelea kufanya hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la nyongeza la usimamizi wa tumbaku, nakulibaliana naye kabisa kwamba bodi yetu ya tumbaku imekuwa na changamoto nyingi sana hususan katika eneo la fedha, lakini vilevile katika eneo la rasilimali watu. Kwa sasa Wizara inajitahidi kusaidia katika kutatua changamoto hizi na tayari mwaka huu kama mnavyoona kidogo soko la tumbaku limeweza kuendeshwa vizuri kwa sababu bodi wamepata baadhi ya fedha, lakini tutaendelea kuboresha hali katika bodi yetu na wazo lake kuhusu kutafuta njia mbadala kama bodi haijafanikiwa nimueleze tu kwamba Serikali inalichukua hili tuangalie kama Bodi ya Tumbaku ikishindwa kufanya kazi labda kama tunaweza tukatafuta kitu kingine ili mradi kwamba tunajua kwamba hata hicho kingine nacho fedha na itahitaji rasilimali watu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mwisho kabisa mimi nimshukuru Mheshimiwa Almas Maige amenifundisha mengi sana katika eneo hili la tumbaku, ni mtu ambaye nakaa naye kabisa ni mzoefu, kwa hiyo, nitaendelea kumuomba ushauri ili tuweze kuleta ufanisi kwa wakulima wetu wa tumbaku si wa Tabora tu, lakini vilevile tunafahamu changamoto zilizopo Chunya, Mpanda, tunafahamu zilizoko Namtumbo, zote Wizara inashughulikia, nashukuru.
MHE. OMAR T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa matatizo yaliyoko Tabora Kaskazini ya kukosa soko la tumbaku na bei zake kushuka yanafanana kabisa na matatizo yaliyopo katika jimbo langu la Morogoro Kusini Mashariki hususan katika zao la bei ya ufuta, ukizingatia kwa mfano mwaka jana bei ya ufuta ilifika mpaka shilingi 2500 mpaka 3000 lakini mwaka huu 1500, 1600 mpaka 2000. Na kwa kuwa mazao haya yanategemea soko la dunia na soko la dunia kila siku bei zinashuka kama alivyosema Mheshimiwa Waziri katika jibu lake la msingi kwenye tumbaku na mazao mengine. Je, Serikali ina mpango mkakati gani wa kuwafidia wakulima kwa kutoa ruzuku hasa pale bei zinaposhuka katika soko la dunia ndogo kulinganisha na gharama za uzalishaji wa mazao hayo hususan ufuta katika vijiji vyangu na jimbo langu na Tanzania kwa ujumla?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba zao la ufuta nalo lina changamoto zinazofanana na ile ya tumbaku pamoja na kwamba kuna baadhi ya maeneo tunafahamu ambayo zao la ufuta ni kama sasa ndiyo tegemeo. Tutajaribu kuangalia ni nini hasa kinatokea katika wakulima wa ufuta Morogoro Kusini ili tuweze kuangalia namna ya kuwasaidia wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali haijaweza kuja na mkakati wa kufidia wakulima pale soko la dunia la ufuta linapotetereka lakini tumekuwa tukiangalia uwezekano wa kuwasaidia wananchi kuweza kupata mikopo na ndiyo maana tumeanzisha Benki ya Kilimo, lakini vilevile tuna mfuko wa pembejeo tunaamini haya yote pamoja na ruzuku tunayotoa kwenye mazao inamsaidia mkulima pale wanapopata mtikiso wa bei katika soko la dunia. Kwa hiyo, niko tayari kulichukua hili na tutaenda kulifanyia kazi.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri na mimi naomba kuuliza swali moja dogo la nyongeza. Kwa kuwa katika sheria ya ushirika ya mwaka 2013 tuliwaondoa watu wa APPEX kwenye mchakato wa kupata pembejeo za Vyama vya Ushirika wa Tumbaku, kwa sababu walikuwa hawana tija tukawabakiza Vyama vya Wilaya ambavyo vinawasimamia Vyama vya Msingi. Na hivi Vyama vya Wilaya vinaonekana navyo ni mzigo katika kupata pembejeo kwa Vyama Msingi vya wakulima wa tumbaku. Je, Serikali inasemaje kuhusu kuwaondoa hawa watu wa wilaya ili Vyama vya Msingi vikope vyenyewe kwenye mabenki?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kama alivyosema kwamba Sheria mpya ya Ushirika Na. 6, 2013 ambayo imeanza kufanya kazi mwaka 2015 imeleta muundo mpya wa kitaasisi ya namna ya kuendesha vyama vya ushirika ikiwa ni pamoja na kuondoa utaratibu ule wa vyama vya APPEX, ilionekana kwamba msululu wa vyama vingi unaleta changamoto na kuleta gharama ambazo siyo lazima kwa mkulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, pendekezo lake ni kuhusu Vyama vya Wilaya kwamba navyo vinaleta mzigo katika uendesha wa Vyama vya Ushirika nimfahamishe tu kwamba Wizara inakaribisha mapendekezo yote ya kurekebisha sheria yoyote pale wadau wakihisi kwamba inakuwa na tija zaidi kama maboresho yakiletwa sisi tuko tayari kusikiliza na hatimaye kuleta Bungeni. Kwa hiyo, nimkaribishe Mheshimiwa Victor na wadau wengine kama wanataka tuirejele tena upya sheria ambayo tumeipitisha miaka miwili tu iliyopita sisi tuko tayari kuwasikiliza ndiyo kazi yetu, kwa hiyo karibu sana.
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri na nia nzuri ya Serikali ya kumpunguzia mkulima wa tumbaku makato mengi ambayo yanafanya mkulima huyu asipate tija ya zao la tumbaku, kuna shida ya makato ya mkulima yanayotokana na ujenzi wa ma-godown ambayo ma-godown yale yalijengwa kwa mkataba wa CRDB na kupatikana mkandarasi kwa kupitia CRDB. Ma-godown yale hayana tija yamedondoka mpaka sasa hayafanyi kazi lakini mkulima wa tumbaku anaendelea kukatwa mpaka sasa. Je, Serikali inasema nini kuhusu hili?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama anavyosema Mheshimiwa Mbunge kwamba kumekuwepo na changamoto nyingi za makato ambayo yanaendelea kufanya bei anayopata mkulima katika zao laki kuwa ndogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikijaribu kupitia hizi tozo ili tuweze kuona namna ya kuzipunguza, tunafahamu changamoto anayoizungumzia ya maghala na katika wiki hii Mheshimiwa Waziri wa Kilimo aliitisha kikao cha Bodi ya Tumbaku, kikao ambacho kilikaa kwa masaa sita na moja kati ya masuala ambayo bodi imeelekezwa kuifanyia kazi ni hili la ma-godown madeni ambayo wakulima wanaendelea kulipa kila wakati na katika kikao kile wameelekezwa kuleta jibu haraka iwezekanavyo. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hili linafanyiwa kazi na tutapata jibu sahihi muda siyo mrefu.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pia nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Naomba sasa niulize maswali mawili ya nyongeza; je, Serikali iko tayari kukisaidia Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Pwani (CORECU) ili kiweze kujijenga na kuwasaidia wakulima wa Mkoa wa Pwani hasa wakulima wa korosho wa Wilaya ya Mkuranga waweze kuuza korosho zao kwa bei nzuri lakini pia kupata pembejeo ya sulphur kwa kuwasaidia Chama Kikuu cha Ushirika (CORECU) kulipa deni wanalodaiwa na Benki ya CRDB?
La pili, kuwasaidia Chama Kikuu cha Ushirika (CORECU) kuweza kuyatwaa tena maghala yake yaliyomilikiwa na watu binafsi yaliyopo kule Ukonga, Dar es Salaam?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inasaidia na imekuwa ikikaa mara kwa mara na CORECU ili kukabiliana na changamoto mbalimbali katika kusaidia wakulima wa korosho katika Mkoa wa Pwani, ikiwa ni pamoja na wanaotoka katika Jimbo la Mheshimiwa Mbunge. Tayari Wizara imeisaidia CORECU kuweza kulipa sehemu kubwa ya deni ambalo wanadaiwa na CRDB. CRDB walikuwa wanadai CORECU shilingi bilioni 3.5, lakini Serikali ikawasiliana na BOT ili kuweza kulipa asilimia 75 ya principal sum ya deni ambalo walikuwa wanadaiwa kwa sababu BOT alikuwa ni guaranter katika mkataba wa deni lile.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tayari imeshalipwa bilioni 1.2 na sasa hivi tunavyoongea bado CORECU wanadaiwa bilioni 2.4, lakini bado tunaendelea kuongea na CRDB ili waweze kuangalia namna ya ku-restructure lile deni ili Chama cha Ushirika cha CORECU waweze kulipa kwa muda mrefu zaidi wasije wakauziwa mali zao. Vilevile, Wizara kwa kushirikiana na Bodi ya Korosho imejiandaa kuhakikisha kwamba pembejeo zinapatikana kwa wakulima wote wa korosho hususan pembejeo ya sulphur kwa ajili ya mikorosho.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, linahusu maghala ambayo yanamilikiwa. Nimechukua ombi la Mheshimiwa Mbunge na tayari alishafika ofisini kufuatilia hili, nimweleze tu kwamba majadiliano yanaendelea ndani ya Wizara kuangalia ni namna gani bora ya kuweza kurudisha yale maghala kwa wenyewe halali ambao ni Chama cha Ushirika cha CORECU. Ahsante.
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa matatizo haya ya KNCU yanafanana na matatizo yaliyopo katika Chama Kikuu cha Ushirika cha MAMCU cha Mkoa wa Mtwara na Vyama vyake vya Msingi, nataka niulize swali; kwa kuwa wakulima wa korosho wa Wilaya ya Masasi wanadai bilioni nne ambazo ni malipo ya tatu ya malipo ya korosho na hadi sasa kumekuwa na ubabaishaji mkubwa juu ya kupatikana kwa malipo hayo. Je, Mheshimiwa Waziri atatoa maelekezo gani kwa Mrajis wa Vyama kuhakikisha kwamba anafanya uchunguzi wa haraka ili wananchi wale waweze kulipwa malipo yao?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama alivyosema kwamba changamoto ya CORECU ni changamoto ambayo ipo katika Vyama vya Ushirika vingi, vingi vina madeni. Namwomba sana Mheshimiwa Mbunge, tukitoka hapa leo tukutane ofisini kwangu niweze kupata hili analosema kwa mapana na marefu ili tuanze kufanyia kazi mara moja na nimfahamishe tu kwamba, tayari kuna kikao kinaendelea huku cha Vyama Vikuu vya Ushirika na itakuwa ni fursa vilevile ya kulizungumzia katika wakati huu. Kwa hiyo nimwahidi tu kwamba, tutalifanyia kazi.
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa yapo mashamba ambayo yamebinafsishwa na hayajaendelezwa; je, Serikali ina mpango gani wa kuyarudisha mashamba hayo kwa wananchi ili vijana wa Taifa hili waweze kupata fursa ya kuyatumia mashamba hayo kwa shughuli ya kiuchumi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, tunavyozungumza hivi kuna kikao kinaendelea Ukumbi wa Hazina hapa Dodoma kuzungumzia kuhusu mashamba haya ya Vyama vya Ushirika ambayo hayaendelezwi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi tunajaribu kutengeneza mkakati ambao haya mashamba yanaweza yakatumika katika maana nzuri zaidi ikiwa ni pamoja na kupeleka na kurudisha kwa wananchi kama tunaona kwamba hakuna utaratibu mwingine wa Vyama vya Ushirika kuyatumia. Kwa hiyo, nimwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba hilo analosema litafanyiwa kazi.
MHE. MPAKATE D. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa matatizo ya ushirika yameenea katika maeneo yote ya nchi yetu ya Tanzania, na kwa kuwa Sheria Na. 6 ya Mwaka 2013 ilianzisha rasmi Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania. Je, ni lini Serikali itaifanya Tume hii iwe na uongozi wa kudumu kwa kuteua Mwenyekiti wa Tume pamoja na Makamishna wa Tume ili ushirika usimamiwe vizuri?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa anavyosema kwamba Tume ya Ushirika bado inakabiliwa na changamoto ya uongozi, nimhakikishie tu kwamba mapendekezo kuhusu uongozi tayari yapo mezani kwa Waziri, kwa hiyo muda mfupi tutasikia kukamilika kwa uteuzi wa viongozi wote wa Tume ya Ushirika.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi na maswali mawili.
Swali la kwanza, kwa kuwa vocha hizi zimekuwa zikichelewa kuwafikia wakulima na wakati mwingine zimefika wakati wakulima wameshapanda mazao yao au wameshakuzia mazao yao.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba mbolea hizi zinafika mapema ili kabla hawajaanza maandalizi ya mashamba haya ikiwezekana ziwe zimeshafika?
La pili, kwa kuwa mbolea hizi za ruzuku zimekuwa zikitolewa kwa wakulima wa mazao ya chakula pekee, Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa mbolea za ruzuku kwa wakulima wadogo hasa wa mazao ya biashara kama vile chai ili waweze kuongeza uzalishaji na hatimaye waweze kuongeza kipato chao?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kama Mheshimiwa Mbunge alivyosema kwamba kwa utaratibu wa sasa pembejeo zinachelewa sana kwa wakulima, nimfahamishe tu Mheshimiwa mbunge kwamba katika mwaka ujao wa fedha Wizara yangu inaubadilisha utaratibu mzima wa kupeleka ruzuku kwa wananchi. Kwa hiyo, tunategemea kwamba changamoto kama hizi kuhusu ucheleweshaji wa pembejeo hautatokea tena.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ni kuhusu mpango wa Serikali wa kutoa ruzuku kwa pembejeo kwa ajili ya wakulima wote zaidi tu ya wale wanaofanya kilimo cha mazao ya chakula hususan mahindi na mpunga. Nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba ruzuku ya pembejeo hutolewa vilevile katika mazao mengine ikiwemo kwa mfano Korosho, Pamba, Kahawa, kwa kutumia taratibu za mifuko kwa ajili ya mazao hayo na vilevile kuna utaratibu wa kuhakikisha kwamba pembejeo vilevile zinatolewa katika zao la chai. Kwa hiyo, utaratibu huu vilevile unatayarishwa na Mheshimiwa Mbunge atapata taarifa pindi itakapokamilika.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Katika maelezo ya Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba ruzuku ya pembejeo pia inapelekwa kwenye zao la pamba. Mheshimiwa Waziri unajua kwamba mpaka leo hakuna ruzuku yoyote inayopelekwa kwenye zao la pamba, kwenye mbolea pamoja na mbegu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia ruzuku katika zao la pamba linatolewa kwa utaratibu tofauti na ule unaotolewa katika mahindi na mpunga. Kwenye zao la pamba ruzuku inatolewa katika mbegu, kwa hiyo, niko tayari kuongea na Mheshimiwa Mbunge tujaribu kupitia yale ambayo yeye anayafahamu kuhusu hili lakini nimfahamishe tu kwamba kuna ruzuku inatolewa lakini ni katika utaratibu ambao ni tofauti kidogo. Kama nilivyosema mazao mengine kama kahawa, korosho vilevile ruzuku inatolewa lakini mara nyingi ni kwa kupitia mifuko maalum ambayo imeundwa kwa ajili ya mazao hayo. Lakini niko tayari kuongea naye tuangalie kuhusu hili.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Kwa kuwa, Wilaya ya Lushoto ni ya wakulima wa mbogamboga na matunda hasa maeneo ya Mkuzi, Kishangai, Boeloi, Ubili, Lukozi, Baga na Mazumbai na wakulima hawa hawapati ruzuku za pembejeo. Je, Serikali ina mpango gani sasa kuwapatia wakulima hawa pembejeo ili na wao waweze kunufaika kama wakulima wengine wa nafaka?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kama tulivyosema kwamba siyo mazao yote hupata ruzuku, nilifahamishe Bunge lako Tukufu kwamba mpango wa kutoa ruzuku ambao umeanza kwa muda sasa kuanzia mwaka 2003 umekuja kwa sababu ya kufanya mambo makuu matatu:-
(i) Kuongeza uzalishaji wa chakula, lakini vilevile kujaribu kuwafanya na kuwahamasisha wakulima waweze kutumia mbolea na mbegu bora.
(ii) Kuwasaidia wakulima ambao wana kipato cha chini kuweza kuongeza tija. Tumeanza na baadhi ya mazao kama nilivyosema kwa sasa Serikali inatoa ruzuku na pembejeo kwenye mazao makuu mawili katika maana ya Mpunga na mahindi lakini vilevile kwenye yale ya biashara kupitia bodi zao lakini pale tutakapoona kwamba inafaa tutaendelea kuongeza utaratibu wa kupatikana kwa ruzuku kwa mazao yote.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba nilieze Bunge lako Tukufu kwamba lengo la kutoa ruzuku siyo kufanya wakulima wawe wategemezi lengo ni kuwafanya wao waone umuhimu wa kutumia pembejeo. Kwa hiyo, kama wakulima wenyewe wanauwezo wa kujinunulia pembejeo bila kupata ruzuku.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo;
Kati ya kero zinazowakabili wakulima, mojawapo ni hii ya upatikanaji wa mbolea na bei yake wakiwemo wakulima wa tumbaku. Je, ni lini Serikali itaondoa kodi na tozo mbalimbali zinazoifanya mbolea ipatikane kwa gharama kubwa, tukiamini kwamba zikiondolewa kodi hizo na tozo mbalimbali mkulima atapata nafuu ya mbolea na pembejeo zingine na kwa msingi huo ataweza kulima zaidi.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba tozo na kodi mbalimbali zinachangia gharama ya pembejeo hususan mbolea kuwa kubwa. Nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari Serikali imefanyia marekebisho baadhi ya tozo hizo na kodi kama mlivyosikia wakati Waziri wa Fedha anawasilisha bajeti, tayari kuna marekebisho kwenye baadhi ya tozo za zao la korosho lakini vilevile pamba na tunaendelea taratibu kuboresha katika maeneo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niwafahamishe tu Waheshimiwa suala la kodi haliwezi kuwa ni suala la siku moja kwa sababu ni lazima mijadala ifanyike miongoni mwa wadau wa setka mbalimbali vilevile kodi ni suala la uchumi huwezi kuondoa zote kwa siku moja, nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba tunaendelea kuzifanyia kazi taratibu ili hatimaye kuwe na mazingira ya kikodi ambayo hayamuumizi mzalishaji mdogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba, tatizo lingine linalosababisha bei ya mbolea kuwa kubwa ni kwa sababu tunaagiza kutoka nje, nimpe habari njema kwamba kwa sasa kuna mikakati ya kujenga viwanda viwili vikubwa vya mbolea nchini; moja kitajengwa Kibaha na kingine kitajengwa Kilwa. Tunaamini kwamba uzalishaji wa mbolea ukifanyika nchini kwetu itakuwa ni rahisi zaidi wakulima kupata mbolea kwa bei ambayo ni nafuu.
MHE. JAQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ambayo kimsingi sijaridhishwa nayo ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kilimo, nina maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Ruvuma una wakazi zaidi ya watu 150,000 na ruzuku/vocha zinazotolewa kwa maana ya pembejeo za kilimo ni karibu kwa watu 80,000 ni wazi kuwa hazikidhi haja. Swali langu, naomba anieleze leo ni lini Serikali itaondoa angalau ushuru kwa maana ya cess kwa wakulima ili pale wanapotoa mazao yao shambani wasitozwe tozo yoyote ile?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, mawakala wa pembejeo za kilimo ambao wamehudumia kwa maana ya kuikopesha Serikali kwa msimu wa mwaka 2015/2016 mpaka sasa hawajalipwa pesa zao. Naomba Waziri anipe majibu mazuri na ya kina kwamba ni lini Serikali itawalipa mawakala hawa ambao wamehudumia wananchi katika Wilaya mbalimbali za Mkoa wa Ruvuma za Nyasa, Mbinga, Songea, Namtumbo pamoja na Ruvuma ikiwepo pia hata maeneo mengine yote ya nchi yetu ya Tanzania? Hawa watu wanafanya biashara kwa kukopa kwenye benki na sasa hivi imefika mahali wanashindwa kurejesha mikopo yao. Naomba anipe majibu ya kina.
NAIBU WAZIRI KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ni lini Serikali itaondoa ushuru, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari Finance Bill inayotegemewa kuja katika Bunge hili tumependekeza kwa Wizara ya Fedha, baadhi ya hizo tozo ziondolewe. Kwa hiyo, tunategemea tutakapoleta Waheshimiwa Wabunge mtatuunga mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nieleze tu kwamba kuna tozo nyingi ambazo zimekuwa zikiongeza bei ya pembejeo kwenye mjengeko wa jumla ambazo nyingi kwa kweli zinaleta matatizo kwa wakulima na tutahakikisha nyingi zitaondolewa. Vilevile tufahamu kwamba suala la kodi ni la kisheria, kwa hiyo, kuna baadhi ya kodi ambazo tutaziondoa taratibu lakini kimsingi Wizara yangu ipo kwenye utaratibu mzima wa kuhakikisha kwamba baadhi ya hizi kodi zinaondoka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili la mawakala ambao hawajalipwa, nikiri kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna mawakala ambao hawajalipwa mpaka sasa. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kuwa tayari Wizara imejipanga kuhakikisha kwamba tunamaliza madeni yote ya mawakala ili wasiendelee kupata vikwazo kama wanavyopata, wengi wanauziwa mali zao kutokana na mikopo. Tunawasihi mawakala wote wapeleke certificate zao kwa sababu tayari utaratibu wa kuwalipa unaandaliwa. Nashukuru sana.
MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwa kuwa tatizo hili la pembejeo hasa mbegu bora ni tatizo ambalo kwa kweli linatakiwa sasa lishughulikiwe kwa kina na kwa kuwa Mungu ameijalia Wizara hii ya Kilimo kupata Waziri na Naibu Waziri ambao ni wachapa kazi na ni mahodari, je, kutokana na uhaba wa mvua, Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Wizara wapo tayari kuharakisha tafiti za mbegu ambazo zitaendana na mazingira ya sasa
NAIBU WAZIRI KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua wazi kwamba changamoto ambazo tunazipata katika kilimo chetu ni pamoja na mabadiliko ya tabia nchi na hivyo kuhitaji mbinu za kisasa za kuweza kupata pembejeo na hasa mbegu ambazo zinaendana na hali halisi ya mvua ambayo tunapata. Taasisi yetu ya Taifa ya Mbegu (ASA) imejikita sana sasa katika kufanya utafiti wa mbegu ambazo zinaendana na mazingira yetu na hali halisi ya mvua ambayo tunapata.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari Serikali imewekeza sana katika utafiti wa mbegu, kwa hiyo, tunaamini kwamba kadiri muda unavyokwenda tutapata mbegu ambazo zinaendana na mazingira yetu. Vilevile nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa pamoja na changamoto kubwa tuliyonayo kwa sasa ambayo takribani asilimia 60 ya mbegu zote zinazotumika nchini zinatoka nje, tumeelekeza nguvu nyingi katika kuzalisha mbegu ndani ya nchi na tunashirikiana na sekta binafsi katika shughuli hii. Nashukuru sana.
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuvishirikisha Vyama vya Msingi na AMCOS kwenye hiyo contract farming badala ya ku-deal na wafanyabiashara binafsi ambao wale hawamgusi moja kwa moja mkulima, wao wako zaidi kwa ajili ya ununuzi wa kahawa siyo uzalishaji wa kahawa.
Mheshimiwa Waziri huoni sasa ni wakati muafaka kwa ile AMCOS ya Kimuli ya kule Utili sasa ishirikishwe na zile „AMCOS’ nyingine za Miyangayanga, Utili na sehemu nyingine?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kama alivyosema, ni kweli kwamba kama AMCOS zingekuwa zinashirikishwa ingeweza ikawa na manufaa kwa wakulima wengi. Nimweleze tu Mheshimiwa Mbunge kuwa, kwa kutambua umuhimu wa kushirikisha wakulima katika contract farming, tayari Wizara kwa kushirikiana na Bodi ya Kahawa ilishaifanyia marekebisho Sheria ya Kahawa ya mwaka 2001 pamoja na Kanuni zake za mwaka 2012, ili kuweka utaratibu kwa yeyote yule ambaye anataka kuingia katika kilimo cha mkataba katika maana ya contract farming aweze kuingia katika namna ambayo haitamnyonya wala kumuumiza mzalishaji mdogo.
Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo, zile AMCOS ambazo zinataka kuingia katika mkataba wa kilimo na wazalishaji wakubwa, tayari kuna utaratibu wa kufanya hivyo. Kwa hiyo, ni suala la wenyewe kujiweka sawa na Bodi ya Kahawa itawahakikishia kwamba wanaingia katika mikataba ambayo haitawanyonya.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, nilikuwa na kesi nimeshinda…! Kwa hiyo nipo tena kazini kama kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tofauti na Mbinga, wakulima wa kahawa wa Mkoa wa Kilimanjaro hususani Jimbo la Rombo wanaelekea kukata tamaa, wengi wao wanang‟oa kahawa wakibadilisha na mazao mengine. Tatizo ni kwamba gharama ya uzalishaji wa kahawa ni kubwa sana wakati bei ya kahawa ni ndogo. Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka ruzuku katika zao la kahawa ili kuwapa motisha wakulima wa kahawa tena kahawa ile tamu ya Arabica ndiyo inayong‟olewa, ili kahawa isije ikafa katika Mkoa wa Kilimanjaro?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa kwamba kwa miaka ya karibuni zao la kahawa limepata changamoto nyingi sana, hususan bei kwa wakulima wetu. Serikali imechukua hatua kadhaa ili kukabiliana na changamoto hii ikiwa ni pamoja na kuanzisha Mfuko wa Kahawa (CDTF) ili uweze kusimamia zao la kahawa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba wanatoa pembejeo kwa wakulima kwa bei ambayo ni nafuu.
Mheshimiwa Spika, tayari katika mazao mengine, hususan zao la korosho, tumegundua kwamba kwa kuanzisha Mfuko ni rahisi Mfuko ule kuwasaidia wakulima kupata pembejeo kwa bei ambayo ni nzuri na hivyo basi kuwaondolea gharama ambazo katika mjengeko wa bei zinawafanya wapate bei ambayo siyo nzuri. Kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba, tayari Mfuko huu upo, umeanza kazi na mtaji bado unaendelea kujengwa ili uweze kuwasaidia sasa wakulima wa kahawa waweze kupata bei nzuri.
Mheshimiwa Spika, nashukuru sana.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa nchi ya Tanzania ilikuwa koloni la Mwingereza na hivyo kuwa na mahusiano mazuri mpaka hivi sasa. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuishawishi sasa Serikali ya Uingereza ili waweze kurejesha huduma hiyo hapa nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI (K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumweleza Mheshimiwa Mbunge kwamba utaratibu huu mpya wa Serikali ya Uingereza ni wa duniani kote, siyo kwa Tanzania tu. Kwa hiyo, siyo kwamba ni sisi pekee ndio tumebanwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nimweleze tu kwamba kuhamishwa kwa Kituo cha Kuchakata Visa za Uingereza kwenda Pretoria nchini Afrika Kusini hakujaathiri utoaji wa visa. Sana sana kinachotakiwa kwa sasa ni kwamba ujipange mapema, ufanye maombi mapema, lakini kimsingi muda umebaki vilevile, gharama ni zile zile. Kwa hiyo, wao walichofanya ni kupunguza gharama zao za kuchakata visa kwa kuhakikisha kwamba wanaipa Kandarasi Kampuni ya Tele-Performance, badala ya wao wenye kufanya hiyo kazi. Kwa hiyo, namhakikishia tu kwamba hakuna madhara makubwa ambayo yametokea kwa sababu hiyo.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mlolongo wa tozo kwenye zao la tumbaku ambazo anatozwa mkulima, ilikuwepo tozo ambayo, kabla ya marekebisho ya Sheria hiyo ya 2013 kulikuwa na AMCOS, Ushirika wa Msingi, Ushirika wa Wilaya na Ushirika wa Taifa ambao ulikuwa Morogoro wakijiita APEX. Sasa sheria hii iliporekebishwa hawa watu wa APEX waliondolewa na kuondolewa kwao ina maana tozo ambayo mkulima alikuwa anakatwa ili ikafanye uendeshaji wa APEX, ilikuwa aidha irudi kwenye AMCOS au iondolewe. Je, hiyo imeondolewa au imerudi kwa mkulima? La kwanza hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, wote hapa tumemsika Mheshimiwa Waziri Mkuu anasema baada ya Bunge hili atakwenda Tabora akaangalie matatizo yaliyomo kwenye eneo hili la tumbaku.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na matatizo haya pia kuna tatizo la wanunuzi wa tumbaku. Makampuni ya kununua tumbaku hapa nchini yako matatu tu na mwaka 2015 yameanza ukiritimba wa kutokununua tumbaku yote ya wakulima. Je, Wizara inasemaje au ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba tumbaku yote ya wakulima inanunuliwa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu tozo iliyokuwa inalipwa kwa APEX, nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge kuwa tuko katika utaratibu wa kupitia tozo zote katika mazao yote na tutaleta taarifa hivi karibuni Bungeni, Waziri wa Fedha atawasilisha Finance Bill na hiyo Finance Bill pamoja na mambo mengi itaonesha maeneo ambayo tumependekeza kuondoa au kupunguza kodi ambazo hazina maana. Kwa hiyo, zinashughulikiwa na atapata taarifa karibuni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na ununuzi na soko la tumbaku, ni kweli kabisa kama alivyosema, tunatambua changamoto iliyopo katika soko la tumbaku kwa sababu pamoja na mambo mengine, kuna ukiritimba mkubwa kwa sababu makampuni yanayonunua ni matatu tu. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba pamoja na suala la soko, ni suala la dynamics duniani, lakini nimhakikishie tu kwamba Wizara yangu tayari inafanya jitihada ili kuhakikisha kwamba tunapata wanunuzi wa ziada ili kuondoa ukiritimba.
Mheshimiwa Naibu Spika, mipango hii imekuwa ni pamoja na kufanya majadiliano na The China Confederation of Industries ili kujaribu kuwaleta wanunuzi wa tumbaku kutoka China. Nimweleze tu kwamba tumeshafikia hatua nzuri na baada ya muda siyo mrefu tuna hakika kwamba kutakuwepo na wanunuzi wa ziada kutoka China ili kuweza kuleta ushindani na hatimaye wakulima wetu waweze kupata bei nzuri.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kuniruhusu nami niulize swali la nyongeza kwa niaba ya wakulima wa tumbaku. Kwa vile sheria hii ya ushirika pamoja na sheria ndogo Na. 42 iliyounda Bodi ya Tumbaku zimeendelea kuwa na upungufu mkubwa, ni lini Serikali italeta sheria hizo mbili hapa katika Bunge lako ili zifanyiwe marekebisho na kwa faida ya wakulima na zao la tumbaku nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Sheria ya Ushirika kufanyiwa marekebisho pamoja na ile inayounda Bodi ya Tumbaku, nimwambie kuwa Sheria ya Tumbaku ndiyo imepitishwa tu karibuni haina hata miaka mitatu, imeanza kufanya kazi tu mwaka 2015 pamoja na kwamba ilipitishwa kuanzia mwaka 2013.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba, kuna maeneo ambayo yanahitaji marekebisho, itabidi tufuate utaratibu wa kawaida na hatimaye sisi kama Wizara tutahakikisha kwamba inakuja Bungeni. Vivyo hivyo kwa sheria inayounda Bodi ya Tumbaku, tukipata mawazo kutoka kwa wadau mbalimbali kwamba inahitaji kufanyiwa marekebisho tutafanya utaratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni vigumu kwa sasa kumwambia kwamba, tutaileta kwenye Bunge hili lini kwa sababu bado kama Wizara hatujapata malalamiko makubwa au mapendekezo kutoka kwa wadau mbalimbali ya kuweza kurekebisha.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Katika jibu Mheshimiwa Naibu Waziri anasema Serikali imedhamiria na kodi zinazotozwa zitapitiwa, ina maana kazi hiyo haijaanza?
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli akiwa kwenye kampeni pale Bukoba, tulimwambia kuhusu kodi hizi na tozo nyingi sana na akasema kwamba atakapokuwa Rais akiteua Waziri wa Kilimo, Waziri wa Fedha na Waziri wa Biashara wakishindwa kuondoa kodi hizi atawatumbua. Leo yapata karibu miezi sita tangu wameteuliwa watu hawa na hakuna kodi hata moja ambayo imeondolewa. Je, hawa Mawaziri wako tayari kutumbuliwa?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Rweikiza Mjumbe wa Kamati Kuu ambaye kwa nafasi yake ya Ujumbe wa Kamati Kuu naye anaweza akamtumbua Waziri yeyote. Nimhakikishie tu kwamba kwa kuwa kodi hizi zinahusisha taasisi zaidi ya moja, hivi tunavyoongea, tayari timu ya wataalam ambayo inaandaa Muswada wa Sheria ambao utaletwa hapa Bungeni ambao ndiyo unaopanga mapato na kodi zitakazofanyika katika mwaka wa fedha unaokuja, inakamilisha kazi yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wengine, haya yote ambayo tumekuwa tukiyasema, hasa hili ambalo Mheshimiwa ametoka tu kulisema, sisi Waheshimiwa Mawaziri tumepigia mstari kwenye kitabu cha hotuba ya Mheshimiwa Rais. Jambo hili alilolisemea Mheshimiwa Rweikiza, liko ukurasa wa 17 paragraph ya tatu kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais wakati analizindua Bunge hapa na tuko kwenye hatua za mwisho za kulitekeleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaamini tutakapokuwa tunajadiliana Finance Bill baada tu ya bajeti kubwa ya Serikali, mambo haya yanayohusu tozo za kero ambazo kimsingi Mheshimiwa Rais tayari alishayatolea maelekezo wakati anatupa kazi hii, sisi tutakwenda kulikamilisha na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na timu yake wanaendelea na kazi ya kutengeneza hiyo Finance Bill.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, ni ukweli usiopingika kwamba zao la pamba bei yake ni ndogo mno ukilinganisha na uzalishaji wake. Ni lini Serikali itafanya mikakati ya dhati ya kupandisha bei ya pamba?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, hivi viwanda vidogo vidogo ambavyo kwa swali la msingi wamevitaja kwamba vitaanzishwa kwenye Wilaya ya Bunda hasa jimbo langu la Bunda ni lini vitaanza?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba ikilinganishwa na nchi nyingine pamba yetu haipati bei nzuri. Hii inasababishwa pamoja na mambo mengine na ukweli kwamba wakulima wetu wengi wanauza pamba ikiwa ghafi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba wakulima katika vikundi vyao wanajengewa uwezo wa kumiliki viwanda vidogo vidogo ili waweze kuchambua pamba kwa sababu faida kubwa kwenye pamba ipo katika hatua nyingine za mnyororo kama kuchambua ambayo wakulima wetu hawashiriki. Hiyo kazi imefanywa na watu wachache. Kwa hiyo, tunataka tuwajengee uwezo waweze wenyewe kumiliki viwanda vidogo vidogo kama vya alizeti ili waweze kufaidika na mazao mengine yanayotokana na pamba kama mafuta pamoja na cotton seed.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile bei ya pamba inashuka kutokana na ukweli kwamba wakulima wetu wanakuwa na gharama kubwa za uzalishaji ikiwa ni pamoja na kununua pembejeo kwa bei ambayo ni ghali. Ndiyo maana Serikali imechukua maamuzi ya kuangalia namna ya kupunguza tozo na kodi mbalimbali zinazotozwa kwenye pembejeo ili kuondoa gharama kubwa za uzalishaji na hivyo baadaye wakulima wetu waweze kupata bei nzuri wakati wanapouza pamba yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, viwanda kama nilivyosema, mkakati wa kujenga viwanda vidogo, nafikiri mlishasikia bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara, kwamba katika Awamu hii ya Tano tunataka kujenga uchumi wa viwanda na hasa viwanda vile vinavyotumia malighafi inayopatikana hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kwamba pamba kama tungekuwa na viwanda vya kutengeneza nguo, kusingekuwa na haja hata ya kuhangaika ya kuuza pamba yetu nje. Kwa hiyo, ni kweli kabisa kwamba kuna mkakati mkubwa sasa wa kuhakikisha kwamba tunarudi kuwa na viwanda vya kutengeneza nguo ili pamba iweze kupata bei nzuri zaidi.
MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Mheshimiwa Naibu Waziri amezungumzia sana kuhusu kuwawezesha wakulima ili waweze kujenga viwanda, lakini pia amekiri kwamba pembejeo ni bei ghali sana kwa wakulima wetu. Sasa nikijaribu kuangalia bajeti iliyopita juzi tu kwa Wizara hii, bajeti ya mbolea imeshuka shilingi bilioni plus, imekwenda mpaka around shilingi bilioni 20.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa gap hiyo ya kushuka kwa bajeti ya mbolea kutaenda kuondoa ukali wa bei kwenye mbolea na kutawasaidia vipi wakulima kuondokana na kuzalisha katika hali ngumu sana na kuendelea kuwa maskini? Vinginevyo tutakuwa tunaendelea kupiga porojo tu hapa.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Pamoja na ukweli kwamba katika bajeti kulikuwa na changamoto kuhusiana na fedha za pembejeo, lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara kwa sasa inaandaa utaratibu mpya wa kutoa ruzuku katika pembejeo ambao utaruhusu wakulima wengi zaidi kuliko ilivyo sasa kuweza kunufaika na ruzuku na kwa bei nafuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika utaratibu wa sasa, wote mmesikia malalamiko kwamba pamoja na kwamba Serikali ilitoa fedha nyingi, kwa mfano, katika mwaka wa fedha unaokwisha Serikali ilitoa shilingi bilioni 78 kwa ajili ya ruzuku, lakini mnafahamu utaratibu unaotumika sasa unaowafanya wachache wanufaike na mara nyingi ruzuku ile haiendi kwa wananchi. Sasa Serikali inakuja na utaratibu ambao inawezekana kwamba mbolea zote zikawa na ruzuku na zikapatikana nchini kama tunavyosema, kama bidhaa nyingine na siyo kwa wakulima mmoja mmoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, pamoja na changamoto iliyopo, haitaathiri nia ya Serikali na uwezo wa Serikali kuweza kuwapatia wananchi pembejeo kwa bei nafuu.
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili ya nyongeza.
Wilaya ya Serengeti ni Wilaya ambayo kimsingi tunazungukwa na wanayama kila kona na zao pekee ambalo kimsingi Tembo hali ni tumbaku, Mheshimiwa Spika, unakumbuka nimekuandikia barua kuhusu issue ya Tembo wamehamia Serengeti wamekula mazao yote; wananchi kwa sasa hawana chakula, zao ambalo kimsingi lilikuwa likiwanufaisha na kuwaokoa wananchi wa Serengeti ni tumbaku, kwa sasa tumbaku haina soko hata kampuni ya Alliance One iliyopo nasikia mwakani inaondoka.
Sasa swali Mheshimiwa Waziri Serikali hii ya Awamu ya Tano kipaumbele chake ni viwanda ni lini mtajenga kiwanda cha ku-process tumbaku Tanzania?
La pili, uko tayari wewe Waziri na mimi Mbunge wa Jimbo la Serengeti kuambatana na wewe kwenda kuwasikiliza wakulima wa tumbaku wa Serengeti na kuwatafutia hayo makampuni uliyosema?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kwanza nakiri kabisa kufahamu changamoto inayoletwa na wanyama waharibifu kwa wakulima wa Serengeti kama ilivyo katika maeneo mbalimbali katika nchi yetu. Mimi nafahamu maeneo ya Serengeti kwa sababu ni jirani zangu, sisi Ngorongoro tulichokifanya ni kwamba wanyama tumewatumia kama fursa ili hata pale wakituletea taabu tuone kwamba tunaweza vilevile tukanufaika na hao wanyama.
Hata hivyo changamoto ya tumbaku kama zao la biashara wote tunafahamu, tumbaku ndio zao la pekee duniani ambalo hata wale wanaotaka wanufaike nalo hawakubali kulipigia debe linunuliwe. Leo hii nina hakika Mheshimiwa Mbunge na hata wale wanaotoka maeneo mengine wanaolima tumbaku nikiwaambia twendeni nje tukapige debe ili watu wanunue sigara nina hakika hawataungana na mimi, ndio changamoto ya tumbaku, ni zao ambalo limeshetanishwa duniani yaani limekuwa demonized.
Mheshimiwa Spika, ni zao ambalo pamoja na kwamba tuko tayari kunufaika nalo lakini dunia nzima inapiga vita tumbaku na hii imesababisha bei ya tumbaku iendelee kudorora na wanunuzi wa tumbaku wameendelea kuwa wachache siku baada ya siku. Leo hii nchini tuna wanunuzi wanne tu kampuni hiyo anayosema ya Alliance One, tunao Premium, TLTC na GTI na duniani kote makampuni makubwa hayazidi manne yanayonunua tumbaku. Kwa hiyo, ni shida ambayo ni ya dunia nzima lakini pamoja na changamoto hiyo Serikali inaendelea kutafuta fursa katika masoko ambayo yanaelekea kuanza kujitokeza hasa soko la China. Wizara inaendelea na majadiliano na Ubalozi wa China tuone ni namna gani tunaweza tukapata fursa katika soko la China.
Mheshimiwa Spika, lakini vilevile tunaangalia uwezekano wa kupata fursa katika soko linaloibukia la shisha katika maeneo ya Uarabuni, nchi kama Misri lakini kwa sasa wananchi wetu tunaendelea kuwaeleza umuhimu wa kuangalia uwezekano wa kulima mazao mengine kwa sababu inavyoelekea soko la tumbaku duniani litaendelea kushuka kwa sababu ya aina ya zao lenyewe, ni zao ambalo linapigwa vita, zao ambalo lina madhara kiafya, kwa hiyo, tunaendelea kuwashauri kwamba tutafute mazao muafaka.
Mheshimiwa Spika, kuhusu ujenzi wa kiwanda cha kuchakata tumbaku nchini nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ya Awamu ya Tano inaweka mazingira wezeshi pamoja na kushawishi sekta binafsi kujenga viwanda vya tumbaku.
Mheshimiwa Spika, tuna baadhi ya viwanda vya tumbaku, kuna kiwanda kikubwa kipo Morogoro lakini tunaendelea kuwahamasisha sekta binafsi kama wanaweza wakaanzisha kiwanda cha kuchakata tumbaku sina hakika kama hata nikiandamana na Mheshimiwa Mbunge kwenda Serengeti kwamba mimi ninaweza nikapeleka kiwanda kule lakini tutaendelea kuwahamasisha sekta binafsi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu Serikali inafanya nini kuhusiana na uharibifu ambao unaendelea, nilishaongea na Mheshimiwa Mbunge kwamba mimi niko tayari kuongea na Wizara ya Maliasili ili kuangalia ni namna gani Serikali inaweza ikawafidia wananchi ambao mazao yao yanaharibiwa na Tembo.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha sana tangu tarehe 18 Septemba, 2014 mpaka leo ni miaka miwili; taarifa ilikabidhiwa na mpaka leo hakuna hatua zozote zilizochukuliwa za kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haioni kuendelea kuchelewa kuchukua hatua kwenye masuala ya msingi kama haya yanayohusu masuala ya kilimo wakati tunasema kilimo ni uti wa mgongo; inazidi kudidimiza kilimo ambacho ndio hasa sehemu kubwa ya uchumi wetu na hivyo Serikali ipo tayari sasa kuchukua hatua za haraka kuhakikisha wale wote waliohusika wanafilisiwa kwanza mali zao wakati hatua za kuwafikisha mahakamani zinafuata?
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili hakuna kilimo chenye tija bila kuwa na ushirika wenye nguvu; COASCO ambayo imepewa jukumu la kukagua vyama vya ushirika Tanzania imeshindwa kabisa kutimiza wajibu wake. Serikali sasa haioni sababu kuweza kukabidhi jukumu la ukaguzi wa Vyama vya Ushirika kwa Ofisi ya CAG ili watimize wajibu huu? Fedha zinazoibiwa ni fedha za Watanzania, ni fedha za wakulima lakini pia ni fedha za Serikali. Ili jukumu hili likaguliwe na Ofisi ya CAG na hivyo kuweza kusaidia kilimo na wananchi kwa ujumla. Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kukubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba hatua za kuwachukulia wahusika kuwapeleka mahakamani imechukua muda mrefu. Hata hivyo, nimueleze tu kwamba ni changamoto ya jumla katika sekta yetu ya kutoa haki na ndio maana kuna hatua mbalimbali zinaendelea ndani ya Serikali ili kuhakikisha kwamba haki inapatikana kwa haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge baada ya kuona kwamba baada ya kuona kwamba utaratibu wa kuwatumia wanasheria wanaotoka kwa DPP; Wizara yangu kwa kupitia Tume ya Ushirika tayari imeandika barua ya kuomba ruhusa ya kuwatumia wanasheria waliopo kwenye Tume ya Ushirika ili wao waweze kuhusika katika kuendesha kesi za ushirika. Nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba pindi ombi letu hilo litakapokubalika na tunalifuatilia kwa karibu sana; wanasheria wetu watahakikisha kwamba kesi hizo zinaendeshwa kwa haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusu COASCO; napenda vilevile kukubaliana na hoja ya Mheshimiwa Mbungekwamba COASCO imekuwa ikituletea matatizo na changamoto katika ukaguzi wa Vyama vya Ushirika. Badala ya kutumia Ofisi ya CAG kwa sasa Wizara yangu inafanya utaratibu wa kurekebisha kasoro za kiutendaji zilizopo ndani ya COASCO ili iendelee kutoa huduma za ukaguzi kwa haraka kwa sababu wao ndio wanatambuliwa kwenye Sheria ya Ushirika Namba Sita ya mwaka 2013 kama ndio wakaguzi wa vyama hivi vya ushirika. Tunatambua changamoto tunaifayia kazi, nashukuru sana. (Makofi)
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru; kwa kuwa Kanda ya Ziwa tunategemea kilimo na zao la pamba limekufa, tukahamasisha wakulima wetu walime zao la mpunga kama zao la biashara na bahati nzuri Mwenyezi Mungu akatujalia mpunga ukaiva wa kutosha na Rais wa Jamhuri ya Muungano alizunguka kwenye kampeni akisema wakulima hawatafungiwa masoko kwa kuwa wanalima kwa pesa zao na nguvu zao wenyewe.
Kwa kuwa Serikali imezuia wananchi na wafanyabiashara wa mpunga kupeleka nje, wakulima wetu kule wameivisha mpunga hawana sehemu ya kuweka huko nje na tunaenda kwenye msimu wa mvua. Je, Serikali ina mpango gani kama haijataka kufungua soko wa dharura wa kuweza ku-protect kile chakula kilichopo nje? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kurekebisha, Mheshimiwa Mbunge amesema Serikali imekataza wafanyabiashara kupeleka mazao nje, kauli sahihi ni kwamba Serikali imesitisha huku tukiweka utaratibu sawa kwa sababu tunajaribu kuangalia tuwe na utaratibu mzuri zaidi wa kuruhusu chakula kiende nje kwa sababu kuna hatari kubwa kwamba tukiendelea kufanya holela kama ilivyo sasa nchi yetu inaweza ikaingia katika janga la njaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka huu Ukanda mzima wa Kusini mwa Afrika unakabiliwa na njaa, nchi 13 kati ya nchi 15 za Jumuiya ya Kiuchumi ya Kusini mwa Afrika (SADC) zinakabiliwa na njaa ikiwemo Afrika ya Kusini. Utaratibu ambao tumekuwa tukiutumia kupeleka chakula nje ulikuwa unatoa fursa chakula chote kiishe bila kufuata utaratibu. Kwa hiyo tulichofanya ni kwamba tumefanya tathmini ya taratibu ambazo tunatumia ili kuja na utaratibu ambao utaturuhusu na kuwaruhusu wafanyabiashara wetu waweze kupeleka nje lakini katika hali ambayo haitatuacha katika hali ya njaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba utaratibu huo karibia unakamilika na muda si mrefu, namhakikishia kupitia Bunge lako tukufu kwamba utaratibu wa kawaida wa kupeleka chakula nje kwa wafanyabiashara utaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wavute subira, Serikali ya Awamu ya Tano haina nia ya kukwamisha wafanyabiashara na Watanzania kutumia mazao yao kibiashara, sisi wenyewe tunatafuta masoko, lakini lazima tufanye kwa njia ambayo sio holela kwa sababu tuna majukumu vilevile ya kuhakikisha kwamba nchi yetu haiingii katika baa la njaa.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Naibu Spika nashukuru na namshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania inashiriki kwenye mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kama Taifa, lakini iko haja ya kutafuta namna ambavyo Wilaya na Halmashauri ambazo zinapakana na nchi jirani zinazoshiriki kwenye Jumuiya hii kuzitumia fursa ambazo wigo wake unaishia kwenye Wilaya zinazopakana na nchi hizo.
Kwa kuwa Biharamulo inapakana na Rwanda kijiografia na kimiundombinu; na kwa kuwa wananchi wa Biharamulo kwa kushirikiana na Mbunge wao wameshazitambua fursa lakini wanahitaji nguvu ya kidiplomasia ya ngazi ya kitaifa kuhakikisha tunazichukua; je, Waziri yuko tayari kuleta nguvu ya uchumi wa kidiplomasia Biharamulo kuzungumza nasi ili tuzitumie?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; je, Waziri yuko tayari kuambatana na mimi akiwa pamoja na wataalamu wa diplomasia ya uchumi kutoka Wizara yake ili tukae na wataalam wa Biharamulo tuzitumie fursa hizo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba Wilaya na jamii ambazo zipo mipakani zina nafasi kubwa zaidi ya kushiriki katika fursa zinazopatikana kwa mtangamano wa Afrika Mashariki na ni kweli kabisa nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara iko tayari kabisa kuangalia ni namna gani inasaidia jamii na Wilaya zinazopakana na nchi za jirani ili kuweza kutumia fursa hizo. Naomba nimweleze tu kwamba, hilo siyo kwamba ndiyo linaanza sasa, ni kwamba kama nilivyoeleza katika swali la msingi, tayari Wizara inatoa elimu na ufahamu kwa wananchi kutambua fursa zilizopo ili waweze kuzitumia.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuhusu Wizara kuandamana naye ili kufika Jimboni na kuangalia hizo fursa, naomba nilichukue hili, nitamshauri Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje ili waangalie namna ya yeye au Naibu Waziri na timu yake waweze kwenda kwa Mheshimiwa Mbunge ili waweze kuangalia namna ya kutumia hizo fursa kwa ukaribu zaidi.
MHE. HAFIDH ALI TAHIR: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ucheleweshaji wa malipo ya Askari hawa wanapomaliza mafunzo Mheshimiwa Waziri haoni kama yanasababisha suala la rushwa ili Askari hao wapate maslahi yao?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili, inakuwaje Serikali inachelewesha maslahi ya Askari hao wenye vyeo wakati wanajua kwamba Askari wamekwenda mafunzoni na watamaliza mafunzo hayo muda fulani. Kwa nini wasiwatengee mapema ili tatizo hili liondoke?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kwamba ucheleweshaji unaleta mambo ya rushwa, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba utaratibu wa kurekebisha changamoto hizi uko wazi kwa hiyo haimlazimishi Askari yeyote ambaye anadai malimbikizo ya mishahara yake kutoa rushwa. Serikali inatambua kuhusu deni hili na tayari katika bajeti iliyopita ya Wizara ya Mambo ya Ndani imetengwa fedha kwa ajili ya kulipa malimbizkizo haya. Kwa hiyo, niwahakikishie tu Askari ambao wanadai malimbikizo kwamba wasubiri kwa sababu malimbikizo hayo yatalipwa haraka iwezekanavyo katika bajeti inayokuja.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili kwamba kwa nini ucheleweshaji unatokea, nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba ucheleweshaji uliotokea umetokea kwa sababu za kitaalam kwamba wakati Maaskari wameenda kwenye mafunzo mwaka 2013 kibali cha kwenda mafunzo pamoja na ikama ilikuwa imeombwa lakini kwa bahati mbaya ikawa imechelewa na Askari wakawa wameenda kwenye mafunzo na walipotoka kwenye mafunzo wakapandishwa vyeo wakati bado ikama haijatoka.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na Askari ambao wameathirika kuwa ikama hiyo imeshatoka sasa. Kwa hiyo, malipo yao yako njiani, wafuate tu taratibu ambazo zinafahamika ambapo katika Jeshi la Polisi ni lazima wawasilishe madai yao ya salary arrears kwenye Kamandi ya Maslahi ya Makao Makuu na watapatiwa fedha zao bila kuchelewa. Nashukuru.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Naibu Waziri amesema kwamba watumishi ambao wameajiriwa na ushirika huo wanapewa semina mbalimbali za kitaalamu na kwa kuwa kama tunavyofahamu suala la hesabu kwa nchi yetu ni tatizo, hawajui hesabu, je, Serikali inajua kwamba mpaka hivi sasa wanunuzi wa tumbaku ambao wamejitawala wanadaiwa na wakulima shilingi bilioni 14 za mwaka 2014/2015 ambazo hawajalipwa mpaka sasa? Je, Serikali inasemaje kufuatilia suala hilo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, mpaka hivi sasa soko la mwaka huu halijaanza, linasuasua na unapochelewa kupima tumbaku maana yake unapunguza kilo za tumbaku. Je, Serikali inasema nini kufuatilia suala la soko la tumbaku kwa sasa hivi ili liweze kukamilika kwa muda muafaka?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kama anavyosema kwamba wakulima wa tumbaku wa Tabora na wa mikoa mingine wanadai fedha nyingi, wanawadai vyama vya ushirika pamoja na wanunuzi wa tumbaku. Serikali imekuwa ikiendelea na jitihada za kuhakikisha kwamba fedha hizi zinalipwa. Tayari mafaili ya watu waliohusika na ubadhirifu mkubwa katika Mkoa wa Tabora yameshawasilishwa Polisi taratibu nyingine ziendelee ili wahusika waweze kupelekwa mbele ya sheria ikiwezekana wakulima waweze kupata fedha zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu soko la tumbaku, ni kweli kama Mheshimiwa alivyosema kwamba suala la soko la tumbaku bado linasuasua na Serikali imekuwa ikijitahidi kufanya njia mbalimbali ili kuhakikishia wananchi kwamba soko halitapata shida. Jitihada hizi ni pamoja na kuhakikisha kwamba wanapatikana wanunuzi wengine wa tumbaku ili kuondoa ukiritimba wa wanunuzi wachache ambao mara nyingi wao ndiyo wanaoamua bei lakini vilevile wao pekee ndiyo wanaendesha soko la tumbaku. Tunaamini kwamba wanunuzi wengine wakipatikana itaondoa tatizo hili na italeta ushindani na hivyo kuondoa tatizo katika bei na soko la tumbaku.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari tulishaahidi kwamba tukitoka kwenye Bunge hili tutaenda Tabora na maeneo mengine kwa wadau wa tumbaku tujadiliane namna bora ya kuboresha zao la tumbaku. Nimhakikishie tu kwamba pamoja na Mheshimiwa Mwigulu Nchemba kuhama, ambaye ndiye aliyetoa ahadi, ahadi ile ilikuwa ni ya Wizara na iko pale pale. Niwahakikishie tu kwamba tukimaliza bajeti Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi ataelekea Tabora kwa ajili ya kwenda kuongea na wadau kuhusu masuala ya tumbaku.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa wakulima wa tumbaku wamekuwa wakikopwa na pesa zao zinachukua muda mrefu sana kuja kulipwa, Serikali ina utaratibu gani wa kuwasaidia wananchi hawa wanaolima tumbaku hasa Mkoa wa Tabora kuhakikisha kwamba wanalipwa pesa yao na riba kama wanavyofanya mabenki?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa utaratibu wa tumbaku kuchukuliwa na baadaye ndipo wakulima hulipwa kumesababisha matatizo makubwa sana na ndicho hasa chanzo cha kurundikana kwa madeni mengi ya wakulima kutoka kwenye Vyama vya Ushirika. Tunafahamu kwamba mfumo mzima wa ushirika siyo kwenye tumbaku tu lakini katika mazao mengi una changamoto na ndiyo maana Bunge hili lilifanya uamuzi mzuri sana wa kuleta Sheria mpya ya Tumbaku, Sheria Na.6, 2013 ili kuondokana na changamoto hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaendelea kuimarisha ushirika ili isitokee tena kwamba wakulima wanachukuliwa tumbaku yao na wanakaa miaka mingi bila kulipwa. Kwa hiyo, tunaamini kwamba kwa mfumo huu wa ushirika ambao tunauleta sasa haitawezekana tena wananchi kukopwa lakini tunahakikisha kwamba tumbaku ya wananchi inakuwa inalipwa moja kwa moja. Badala ya kuchukua kwanza na kulipa baadaye ni kwamba tutakuwa tunatumia mfumo kama ule wa korosho ambapo tumbaku ikishakusanywa kwenye Vyama vya Msingi wanunuzi wanakuja kununua pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inafahamu changamoto hii, inafanyiwa kazi na tunaamini katika mfumo uliokuja wa Vyama vya Ushirika utarekebisha matatizo makubwa ambayo yametokea. Vilevile sheria hii imeweka mazingira mazuri sana ya kuwabana na kuwafikisha katika vyombo vya sheria si tu wafanyakazi wa Vyama vya Ushirika lakini vilevile hata Maafisa Ushirika ambao wanashirikiana katika kuwahujumu wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilieleze tu Bunge lako Tukufu kwamba changamoto kubwa iliyoletwa na mfumo wa ushirika ambao tunauondoa ni kwamba kumejengeka utatu usio mtakatifu kati ya viongozi wa Vyama vya Ushirika, mabenki na watendaji wa Serikali. Kwa hiyo, tunahakikisha kwamba utatu huu ambao umeleta matatizo kwa wananchi unavunjwa ili wananchi waweze kupata haki yao na kusiendelee kutokea changamoto katika zao la tumbaku.
MHE. JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba nimuulize Waziri swali dogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Bodi ya Tumbaku inafanya kazi ndani ya Serikali na kwa maagizo ya Serikali; na kwa kuwa Bodi ina upungufu wa fedha unaosababisha kutokupatikana wanunuzi wengi wa kutosha, je, Serikali iko tayari kuwaongezea Bodi ya Tumbaku pesa ili waongeze wanunuzi wa tumbaku na kuongeza masoko? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Bodi ya Tumbaku inakabiliwa na changamoto za fedha. Hata hivyo, Serikali imekuwa ikijaribu kuangalia uwezekano wa Bodi za Mazao kujitegemea zaidi badala ya kutegemea ruzuku ya Serikali. Kwa hiyo, utaratibu ambao unatumika ni kuhakikisha kwamba Bodi ya Tumbaku inaweza ikapata fedha za kujiendesha yenyewe bila kupata ruzuku kubwa kutoka Serikalini. Ndiyo maana tunafikiria kuwa na Mfuko wa Bodi ya Tumbaku kama ilivyo kwenye korosho na kahawa ili wadau wenyewe waweze kujiendesha bila kuingiliwa na Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimueleze vilevile Mheshimiwa Mbunge kwamba suala la soko la tumbaku ni zaidi ya ukosefu wa fedha kwa Bodi ya Tumbaku. Soko la tumbaku linaathirika na namna zao linavyochukuliwa duniani. Wote mnafahamu kwamba tumbaku ndiyo zao la pekee ambapo kunakuwa na vita sana kwa hiyo inafanya wanunuzi wengi mara nyingine wasijiingize kwenye tumbaku. Hata hivyo, tunaendelea kutafuta aina zingine za tumbaku ambazo zinawavutia watumiaji wengi hasa Wachina.
Mheshimiwa Naibu Spika, watumiaji wa China wanapendelea tumbaku inayozalishwa Zimbabwe. Kwa hiyo, tumeongea na Bodi ya Tumbaku wajaribu kuangalia ni namna gani tumbaku ambayo inazalishwa katika maeneo mengine kama Zimbabwe na ambayo inapendwa na watumiaji wengi wa China inaweza ikaoteshwa nchini. Kwa hiyo, jitihada zinaendelea kwa ajili ya kuweza kuimarisha bei ya tumbaku.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri alipojibu maswali ya nyongeza amesema kwamba makampuni ya wanunuzi ni machache yako kama matatu na yanafanya kiburi kwa sababu kwao ni cartel na amesema kwamba Wachina wana nafasi ya kununua tumbaku hapa kwetu kwa sababu Wachina ni wengi sana hapa duniani. Je, Serikali inasemaje kuyaleta Makampuni ya Kichina kuja kununua tumbaku hapa Tanzania na kuwapunguzia wakulima adha wanayopata?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba Serikali inatambua changamoto inayoletwa na ukiritimba katika ununuzi wa zao la tumbaku. Ndiyo maana Wizara yangu imechukua hatua kadhaa ili kutafuta wanunuzi wengine. Nipende tu kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba wiki mbili zilizopita tumekutana hapa Dodoma na Balozi wa China ili kuangalia uwezekano wa kuwapata wanunuzi zaidi. Tumeongea nao ili confideration of China Industries waweze kuruhusu kampuni zao ziweze kuja kununua tumbaku Tanzania, mijadala hiyo inaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tumeongea na watu wa Vietnam ili kuangalia uwezekano wa kuwapata wanunuzi kutoka Vietnam. Kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba jitihada zinaendelea na tuna hakika kwamba wanunuzi wengine wa tumbaku watapatikana.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Wilaya ya Makete ndipo ambapo kituo kinachozalisha mitamba katika wilaya hiyo na wananchi wa Wilaya ya Makete ndiyo wamekuwa miongoni mwa wanaofaidi na mikoa mingine jirani kama alivyosema:-
Swali, hivi sasa Serikali imejipangaje kuona sasa Halmashauri jirani za Mkoa wa Njombe hususan Wilaya ya Wanging‟ombe, Njombe, Ludewa, Halmashauri ya Mji wa Makambako na Lupembe zinafaidika kupata mikopo ya kuwakopesha mitamba hii ili iweze kuzalisha katika halmashauri hizi wananchi waweze kunufaika? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili; kwa kuwa wananchi wa Wilaya ya Makete walitoa eneo kubwa sana kwa kituo hiki na eneo hilo bado kubwa halitumiki, Serikali imejipangaje kuona wananchi wa Wilaya ya Makete wanakopeshwa mitamba hii ili waweze kupata eneo ambalo limekaa tu halitumiki waweze kunufaika nalo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ni namna gani Serikali imejipanga kutoa fursa kwa wananchi wa Halmashauri ambazo zimepakana na shamba ili kujipatia mikopo kwa ajili ya kuweza kujiendeleza katika ufugaji; Wizara ipo tayari kushirikiana na Halmashauri hizo ili waweze kuona fursa zilizopo katika Benki ya Kilimo, lakini vilevile katika Benki ya TIB na NMB ili waweze kupata fursa ya kupata mikopo na kuwekeza katika ufugaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kama Wizara ina mpango wa kugawa ardhi kwa wananchi wanaozunguka shamba hilo; napenda kusema kwamba pamoja na Serikali kutambua umuhimu wa Sekta Binafsi na wananchi mmoja mmoja kujihusisha katika ufugaji; kwa sasa Serikali inaona kwamba ni vizuri shamba hilo likaendelea kubakia mikononi mwa Wizara ili liweze kutumika kwa ajili ya watu wengi zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile Wizara inatambua kwamba huko nyuma jitihada za kubinafsisha ardhi pamoja na mali nyingine za Wizara, hazijazaa matunda makubwa sana; na mpaka leo hii viwanda vya nyama ambavyo tumebinafsisha pamoja na viwanda vya ngozi, lakini vilevile blocks za ranchi za Taifa, uzoefu umetuonesha kwamba hatujapata mafanikio makubwa sana katika kuendeleza Sekta ya Mifugo kwa utaratibu huo.
Kwa hiyo, Serikali na Wizara inalenga kuwekeza zaidi katika mashamba hayo na katika sekta kwa kusimamia yenyewe badala ya kubinafsisha mashamba hayo.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, je, ni lini Serikali yetu sikivu itafanya tathmini ya hali halisi ya maeneo haya ambayo ukienda kwenye maeneo hayo kuona hali halisi; na kwa bahati nzuri katika eneo hili kwenye Bunge lililopita niliuliza swali na Waziri wa Kilimo enzi hizo, Mheshimiwa Mwigulu na Naibu mwenyewe nashukuru sana kwa kufika kwenye maeneo yangu; hali halisi ya eneo hilo halipo, watu wameshajenga. Sasa je, ni lini Serikali itafanya tathmini ya hali halisi kujua maeneo haya ambayo wanamiliki hewa kumbe wananchi wote walishakali na kujenga shule za msingi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kutokana na Sheria Namba 17 na Namba 10 alizozitaja Mheshimiwa Naibu Waziri zimechelewa sana kwa wananchi wa Kijiji cha Mikomalilo, kwa sababu walishajenga na kulima mazao ya kudumu. Je, ushauri wake sasa haoni umechelewa sana ili kuwashauri watu walime mazao ambayo siyo ya kudumu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu umuhimu na haja ya kufanya tathmini kuangalia hali halisi ya eneo la Holding Ground husika, Serikali inafahamu tosha kwamba ndiyo wananchi wamekuwa wakilitumia hilo eneo tokea miaka ya 1980; lakini kwa sasa hata pamoja na kwamba kuna maeneo ambayo yamevamiwa, hata yale ambayo yamebaki bado sisi tunaona kwamba ni muhimu kwa ajili ya matumizi ya Wizara na tusingependa kutumia kigezo cha kwamba kimevamiwa kuruhusu sasa; kwa sababu itamaanisha kwamba katika maeneo mengine wananchi vilevile wanaweza kuvamia.
Kwa hiyo, jitihada iliyopo sasa ni kuangalia namna gani tunaweza kunusuru maeneo yaliyobaki.
Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, tukiruhusu maeneo yote ya Serikali yachukuliwe na wananchi baadaye Serikali ikihitaji maeneo tunaanza tena ugomvi na mgogoro na wananchi kwa sababu Serikali mara kwa mara itahitaji maeneo kwa ajili ya maendeleo ya kiujumla kwa ajili ya maendeleo ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jibu hili la swali la kwanza la nyongeza, vilevile linajibu swali la pili kwamba tamko hili la kusema wananchi wasijenge, halijachelewa. Hata mwaka 1980 waliporuhusiwa, makubaliano ilikuwa ni kwamba wasipande mazao ya muda mrefu na wala wasijenge.
Kwa hiyo, wananchi wamekuwa wakifahamu na ndiyo maana hata Mheshimiwa Mbunge leo analiuliza hili swali wakati anafahamu kwamba huo ndiyo utaratibu uliokuwa ukitumika tokea mwaka 1980.
Kwa hiyo, sisi kama Wizara hatujachelewa, kilichotokea ni kwamba wananchi hawajafuata makubaliano ambayo tuliwekeana tokea eneo hilo lianze kutumika na wananchi mwaka 1980.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, ni kweli kabisa kwamba viungo vina soko kubwa ndani na nje ya nchi kwa sababu mimi mwenyewe naona jinsi hawa wanunuzi wa kutoka nje wanavyohangaika wakati wa msimu pale Muheza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza, ni lini Wizara itawapeleka wataalam hao kuhakikisha kwamba wanainua ubora wa wakulima hao waweze kujua namna ya kulima vizuri pamoja na kuhifadhi mazao hayo ambayo wanayazagaza nje nje tu?
La pili, kama ambavyo Wizara imesema kwamba imetenga fedha za kusaidia bustani pamoja na wakulima wa hivi viungo, mna uhakika gani kwamba wakulima wangu wa Amani na Muheza fedha hizo ambazo zimetengwa watazipata?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ni lini wataalam wa Wizara wataenda kushirikiana na wakulima katika Jimbo lake ili kuweza kuwa na kilimo cha tija, nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba utaratibu wa kutoa taaluma na uelewa kwa wakulima ni utaratibu ambao ni endelevu kupitia Maafisa Ugani.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua kwamba kuna changamoto ndiyo zinawakabili, lakini katika bajeti yetu na ile ya TAMISEMI zimetengwa fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Maafisa Ugani wanafanya kazi na kuweza kuwafikia wakulima ili waweze kuzalisha kwa tija zaidi.
Vilevile labda nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sababu Pemba tuna kiwanda kizuri sana ambacho kinachakata viungo, tutashirikiana na Halmashauri ili kuona namna gani wakulima wanaweza vilevile wakaendelea kutembelea kiwanda hicho na kujifunza kinachofanyika ili pamoja na kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara, tuangalie ni namna gani tunaweza vile vile kuwa na kiwanda kinachoweza kuchakata viungo ili tufikie ufanisi kama walivyofikia wenzetu kutoka Pemba.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwamba tutafanya vipi kuhakikisha kwamba fedha zilizotengwa zinawafikia wakulima; nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ya Awamu ya Tano inatembea katika ahadi zake. Kwa hiyo, yale yote ambayo tumepanga na kutenga kwa ajili ya wakulima wetu, tutahakikisha kwamba tunafuatilia ili ziweze kuwafikia bila kupotea.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nashukuru Mheshimiwa amenijibu vizuri ambapo Watanzania wameweza kufaidika na hili swali langu, lakini nitakuwa na maswali mawili ya nyongeza. Ni kwa nini askari wamekuwa hawatimizi wajibu wao hasa kwa viongozi wa kisiasa wakimemo Waheshimiwa Wabunge? (Makofi)
Swali la pili, ni kwa nini Serikali isitoe maelekezo au waraka kwa askari wake ili suala hili liwe linakwenda sambamba na utekelezaji wake na viongozi wengine ambao tayari wamewataja katika waraka huu.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI (K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI): Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kwa nini askari hawatimizi sharti hilo la taratibu zao za kazi za kupiga saluti kwa viongozi na hasa Waheshimiwa Wabunge, naomba nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba askari wote wanafahamu kwamba wanatakiwa kufanya hivyo. Askari yeyote ambaye atapatikana na kosa la kutotimiza matakwa hayo ya kanuni zao kawaida huchukuliwa hatua za kinidhamu; ikiwa ni pamoja na kukatwa mshahara, adhabu ya kutoondoka kambini inaitwa confinement to barracks, adhabu ya kucheza paredi, lakini vilevile adhabu ya kufanya usafi kambi au inaitwa extra duties.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimweleze Mheshimiwa Mbunge pamoja na Waheshimiwa Wabunge wengine kwamba mara nyingine unakuta kwamba sio rahisi askari akafahamu kwamba Mheshimiwa ni Mbunge, lakini vilevile askari unaweza ukakuta kwamba katika namna alivyokutana na Mheshimiwa Mbunge anaweza asimtambue kwa sababu aidha hauko na bendera kwenye gari lako, lakini vile vile ukienda kwenye mazingira na kufanya vitendo ambavyo haviendani na nafasi yako ile ya Ubunge, inakuwa ni vigumu yeye kukupigia saluti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, vilevile niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge kwamba saluti hiyo tunastahili kwa sababu ya heshima ya cheo na dhamana ambayo tumepewa kama viongozi. Kwa hiyo, tunaomba badala tu ya kudai saluti lakini vilevile tuwe viongozi wenye maadili ya uongozi na ndiyo kama usipopewa heshima hiyo ni rahisi kumripoti askari yule kwa wakubwa zake na akachukuliwa hatua. Hata hivyo, kama nilivyosema askari wetu wote wanafundishwa kuhusu hizi orders na mara nyingi wanatekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kwamba kwa nini Serikali isitoe maelekezo askari waweze kufuata taratibu hizi. Naomba nitumie fursa hii kwa askari wote nchini wahakikishe kwamba wanafuata Police General Orders No. 102 ili waweze kutenda yale yote ambayo wanatakiwa kufanya ikiwa ni pamoja na kutoa saluti kwa viongozi wote kama wanavyotakiwa. Ahsante sana.

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri ameyaeleza kwa kirefu nilipenda pia niongezee kwa upande wa vyombo vile vya binafsi. Pia kumejitokeza vyombo hivyo vinapokuwa katika sehemu zake za lindo kutokuwa na heshima na kuzingatia viongozi wanapokuwa wanahitaji kupata huduma ikiwemo huduma za kibenki. Kwa hiyo, naomba pengine pia hilo liweze kuzingatiwa wakati pia taasisi hizi zinapowaweka hawa askari wao kwenye malindo kujua kwamba wanafanya kazi zinazoendana na ethics za kiuaskari, kwa hiyo ni vyema kuzizingatia. Ahsante.
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri Masauni huwa ana kawaida ya kutembelea mikoa mbalimbali ili kuona matatizo ama changamoto za askari na hata Pemba alifika na yeye mwenyewe alijionea tatizo sugu lililopo katika Mkoa wa Kusini Pemba, Wilaya ya Mkoani kituo cha Mkoani na kituo cha Kengeja, zile ofisi zinavuja. Je, Serikali itakubaliana nami kwamba hela hizi zilizopangwa na nyumba hizo zitakazojengwa zianzie katika ofisi za kule Mkoa wa Kusini Pemba Wilaya ya Mkoani na kule Kengeja ili kuwaondoshea askari hao usumbufu mkubwa wanaopata? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa kutokana na tatizo kubwa la ukosefu wa nyumba za askari hasa kule Pemba; askari wengi wanakaa katika nyumba za kupanga ambazo zipo mbali sana na vituo vyao vya kazi. Je, Serikali ipo tayari kuwaondoshea tatizo hili askari hao kwa kuwakopesha vifaa vya usafiri lakini vifaa hivyo viwe na riba nafuu ili kuwaondoshea tatizo hilo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI (K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kama alivyosema kwamba Kusini Pemba kuna changamoto kubwa kama nilivyosema kwamba nchi nzima kuna changamoto ya nyumba za polisi kiasi kwamba kuna upungufu mkubwa. Katika kutimiza azma ile ya Serikali ya kuhakikisha kwamba askari wetu wanapata nyumba nchi nzima tutaanzia kwenye maeneo yale ambayo tunafikiri kuna tatizo zaidi na Kusini Pemba ni moja kati ya maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mbali na kujenga nyumba mpya kama nilivyosema katika majibu ya swali la awali ni kwamba Serikali vilevile iko kwenye utaratibu wa kukarabati nyumba kwa kuanzia na yale maeneo ambayo yana shida zaidi. Kwa hiyo, nimwahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Kusini Pemba ni moja kati ya maeneo ambayo yameonekana yana changamoto kubwa na mpango huo wa kufanya ukarabati pamoja na ujenzi vilevile utahusisha kule.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kutoa mikopo ya riba nafuu kwa ajili ya kununulia vifaa naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ni moja kati ya masuala ambayo yanafanyiwa kazi ili askari wetu hasa wale ambao hawana nyumba waweze kufika kazini bila matatizo yoyote.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza niishukuru Serikali kwa kutoa maneno mazuri ndani ya Bunge hili ila nilikuwa na swali moja la nyongeza. Kwa kuwa suala la utalii ni suala muhimu sana kwa Watanzania na kwa kuwa Zanzibar na Pemba na Tanga watalii wengi walikuwa wanakwenda kwa ajili ya kuogelea ndani ya bahari. Pia kwa kuwa tatizo hili limewaathiri kwa kiwango kikubwa sana watalii wanaotoka nje kwa ajili ya kuja kufanya utalii katika eneo la pembezoni mwa bahari. Je, Serikali inaweka hatua gani ya dharura kwa kuhakikisha suala hili linachukuliwa maamuzi ya haraka ili watalii waendelee kuwepo katika eneo la bahari?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa biashara au uvuvi wa kutumia mabomu unaathiri sana biashara ya utalii na hususani katika Ukanda wa Pwani ambao Mheshimiwa ametaja. Kama nilivyosema Serikali imeamua sasa kuchukulia suala la uvuvi haramu kwamba ni suala la kiusalama; niwafahamishe tu Waheshimiwa Wabunge kwamba kuna uhusiano wa karibu sana kati ya ugaidi, uvuvi wa kutumia mabomu lakini vilevile kutumia mabomu au vilipuzi ambavyo havina leseni katika machimbo yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Serikali imeamua kuchukulia hili suala kwamba sio suala la uvuvi; kwa sababu hamna uvuvi unaitwa uvuvi wa mabomu, pale mtu anapotumia mabomu kuvua hapo anakuwa anafanya maangamizi ya samaki na viumbe vingine baharini na sio uvuvi. Kwa hiyo, tumeamua kulichukulia kwamba ni suala la usalama na ndiyo maana kwa sasa halishughulikiwi moja kwa moja au peke yake na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi lakini vile vile linashughulikiwa na vyombo vya usalama.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kufanya hivyo; Serikali imeanzisha vituo vitano vya kudhibiti uvuaji wa samaki wa aina hii na moja kati ya vituo iko Tanga na Pemba ili kuhakikisha kwamba udhibiti unafanyika wa karibu sana. Naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tokea utaratibu huu uanze mwaka 2015 tayari kuna maendeleo makubwa sana na uvuaji wa kutumia mabomu umepungua kwa kiasi kikubwa. Kwa hiyo, Serikali itaendelea kuhakikisha kwamba linafanyiwa kazi ili liweze kwisha moja kwa moja.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuuliza swali la nyongeza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri. Mheshimiwa anafahamu kwamba tangu ulivyomalizika mradi wa MACEMP hakuna juhudi zozote ambazo zimechukuliwa na Serikali za kuwawezesha wavuvi katika masuala mazima ya zana pamoja na utaalam wa uvuvi na ndiyo maana wavuvi sasa wanatumia zana ambazo siyo sahihi. Je, anakubaliana na hilo na wanachukua hatua gani katika kulitatua?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba tokea uishe mradi wa MACEMP kumekuwepo na changamoto nyingi sana lakini naomba tu nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba uvuvi haramu au wa kutumia zana ambazo haziruhusiwi za uvuvi hauwezi kuruhusiwa kwa sababu yoyote ile kwa sababu kimsingi ni vitu ambavyo vinapingana na sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nieleze tu kwamba wavuvi wote kabla hawajapewa leseni ya uvuvi wanakuwa wamefahamishwa na wamefundishwa kuhusu uvuvi haramu ni nini na kwamba ni nini kinatakiwa watekeleze. Kwa hiyo, Serikali inaendelea kuwaomba wavuvi wote nchini kufuata taratibu ambazo tayari wanafahamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba pamoja na mradi wa MACEMP kwisha bado jitihada za Serikali za kuwapatia wavuvi mafunzo pamoja na nyenzo bora za uvuvi zinaendelea na ndiyo maana katika bajeti yetu ambayo mliipitisha Waheshimiwa Wabunge tuliainisha kabisa namna ambavyo tutajaribu kugawa na kusaidia vikundi kuweza kuwa na zana bora za uvuvi.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, Sheria ya Mipango Miji Namba Nane ya Mwaka 2007 inasema mashamba ya kilimo na mifugo kwa mijini na mamlaka za miji yasizidi ukubwa wa heka tatu. Ukizingatia Ngerengere sasa hivi ni mamlaka ya mji mdogo na shamba lile lina ukubwa wa zaidi ya hekta 4,562 ambazo ni sawa na heka 10,036, ambapo ni kinyume na sheria hii namba nane ya mwaka 2007. Je, Serikali haioni uwepo wa shamba hili katika Mamlaka ya Mji wa Ngerengere inakiuka sheria hii namba Nane na ukizingatia Serikali inafuta mashamba mengi sasa hivi kwa kuzingatia shabaha hii kwa wananchi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Halmashauri ya Morogoro ina ardhi kubwa nje ya Mamlaka ya Mji wa Ngerengere, je, Serikali iko tayari wakatupa ardhi hiyo kwa ajili ya maendeleo ya Mji wa Ngerengere na Serikali tukawapa ardhi nyingine kwa ajili ya kuendeleza shamba la mifugo, kwa kuzingatia Sheria ile Namba Nane ili iwe nje ya hapo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama alivyosema kwamba Sheria Namba Nane ya Mipango Miji ya mwaka 2007 pamoja na mambo mengine inakataza kuwepo na mashamba yanayozidi heka tatu ndani ya maeneo ya mji. Nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba pamoja na kwamba shamba la Ngerengere mipaka yake iko karibu na mjini lakini eneo linalotumika hasa kama shamba ni mbali kidogo na mji. Pale karibu na Ngerengere eneo kubwa la shamba hilo ni makazi ya wafanyakazi, kwa hiyo shamba lenyewe liko mbali na mji, kwa hiyo haivunji hasa Sheria Namba Nane kwa sababu shughuli zenyewe za kufuga ng’ombe hazipo karibu na hapo, ziko nje kidogo ya mipaka ya Mji Mdogo wa Ngerengere.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili, kwamba kwa nini Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Vijijini isifikirie kutoa ardhi mbadala? Nafikiri anachosema Mheshimiwa Mbunge kina mantiki, kwa hiyo, ni suala la taasisi husika za Kiserikali ikiwa ni pamoja na halmashauri pamoja na Wizara ya Ardhi kujadiliana na kuangalia uwezekano wa kupata ardhi nyingine ili kuliondoa shamba hili ili labda liweze kutumika kwa ajili ya matumizi mengine ya mji. Kwa hiyo, ni suala ambalo linazungumzika, nafikiri ni kitu ambacho kinaweza kikafanyika. Nimshauri Mheshimiwa kwamba mjadala huu alifuatilie na aanzishe katika mamlaka husika ili utatuzi uweze kupatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo nimweleze vile vile Mheshimiwa Mbunge kwamba mashamba ya mifugo kuwepo karibu na mijini mara nyingine inasaidia kwa sababu inawasaidia wananchi walioko karibu na maeneo yale kuweza kupata ajira, wanaweza vile vile wakapata maziwa na nyama kwa bei rahisi zaidi. Kwa hiyo, ni suala la kuangalia ni nini kinafaa katika mazingira yale.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipatia fursa ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Migogoro kati ya wakulima na wafugaji imekuwa ikiongezeka, wakulima, wafugaji dhidi ya hifadhi na ukuaji wa miji kama swali la msingi lilivyokuwa limeulizwa. Nakumbuka kwamba katika Bunge hili swali hili limeshawahi kuulizwa na ikatakiwa kwamba Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi; Wizara ya Ardhi; Wizara ya Maliasili; wakae pamoja kuangalia utaratibu wa kuhakikisha kwamba kunakuwa na mipango mizuri ya matumizi bora ya ardhi. Je, Wizara hizi zimeshakaa na hatua waliyoifikia ni ipi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama alivyosema kwamba migogoro ya aina hii imekuwa mingi sana katika nchi yetu, lakini vile vile ni kweli kwamba tayari tulishaahidi na tulielekezwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu, Wizara zile zinazohusika na suala hili zikutane ili kujaribu kutafuta suluhu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango huo bado upo, lakini tulisema ni baada ya Bunge la Bajeti. Kama anavyofahamu bado hatujarudi hasa maofisini kukaa kwa pamoja, lakini nimwahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba suala hilo bado tunalipa kipaumbele kikubwa sana, ni tayari ni maagizo kutoka kwa viongozi wetu. Kwa hiyo, tukitoka kwenye Bunge hili nimwahidi tu kwamba hilo ni moja kati ya masuala ya kwanza ya kwenda kutekeleza kama Wizara mbalimbali na kama Serikali. Nashukuru sana.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, nina maswali mawili ya nyongeza, lakini nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ambayo yamenipa faraja kuliko majibu ya juzi yaliyotolewa na Waziri wa Maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza la nyongeza, katika kuwasaidia wakulima hao hao, bajeti ya Wizara hii ya Kilimo na Mifugo kwa mwaka huu wa fedha 2016/2017 imetenga maeneo ya kipaumbele na katika maeneo hayo ya kipaumbele Rufiji si maeneo ya kipaumbele kwa mujibu wa bajeti hii ya mwaka 2016/2017. Kama Wizara hii ingeweza kutoa kipaumbele kwa Rufiji inamaanisha kwamba tatizo la sukari hapa nchini lingeweza kwisha kabisa kwa Serikali kuwekeza na kutengeneza viwanda vikubwa vya sukari. Nataka nifahamu hawa wataalam waliomsaidia Mheshimiwa Waziri kuandaa bajeti hii wana elimu gani, darasa la saba au ni form four? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, Serikali kupitia Wizara hii ya Kilimo ilituletea sera ya kutuletea RUBADA. RUBADAhii wamekuwa wabadhirifu wakubwa wa fedha za umma ambao pia ni madalali wa viwanja na mashamba, wamesababisha anguko kubwa la uchumi Rufiji kwa kushindwa kusaidia kuleta wawekezaji katika kilimo lakini pia kushindwa kusimamia Bonde la Mto Rufiji? Nataka nisikie kauli ya Mheshimiwa Waziri hapa ni lini ataifuta hii RUBADAna kutuletea mradi mkubwa wa kilimo kwa ajili ya Wanarufiji? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu elimu ya watendaji walionisaidia kutayarisha majibu haya, nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kama zilivyo Wizara nyingi za Serikali zina wataalam waliobobea katika fani mbalimbali. Kwa hiyo, kuhusu uwezo wao hatujawahi kuutilia maanani. Kuna changamoto ndiyo katika utekelezaji tunadiriki kusema hivyo lakini haitokani na uwezo wa wataalam wetu. (Kicheko)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri unamaanisha hamjawahi kuutilia mashaka na siyo maanani? (Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile nijibu swali lake kuhusu RUBADA. Ni kweli kabisa kama alivyosema Mheshimiwa Mchengerwa kwamba kumekuwepo na changamoto nyingi kuhusiana na RUBADA lakini Serikali imeifanyia marekebisho makubwa RUBADA. Mnafahamu kwamba tayari tumeshabadilisha uongozi na tunaendelea kufanyia marekebisho na bado tunaamini kwamba RUBADA itaendelea kuwa ni chombo muhimu katika lengo la Serikali la kutumia Rufiji kama sehemu muhimu sana kwa ajili ya kilimo.
Vilevile nimfahamishe Mheshimiwa Mchengerwa kwamba hatujaitenga Rufiji katika vipaumbele vyetu na ndiyo maana katika nchi nzima sehemu ya pekee ambayo imepata fedha katika bajeti yetu kwa ajili ya kilimo kwa ajili ya vijana ni Rufiji. Kwa hiyo, nimfahamishe tu kwamba Rufiji ni sehemu muhimu sana, ni bonde ambalo ni muhimu sana kwa kilimo katika nchi yetu na tutaendelea kulitumia kwa ajili ya kilimo cha mazao mbalimbali ikiwa ni pamoja na namna ya kutatua changamoto tulionayo ya sukari, tunafahamu ni bonde muhimu sana. Kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba hatujaisahau Rufiji, hatujaisahau RUBADA tutaendelea kufanyia kazi changamoto zilizopo ili tuweze kutumia eneo hilo vizuri.

WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na majibu sahihi. Nilitaka tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa sababu mara kwa mara amekuwa akija hata ofisini kufuatilia jambo hili pamoja na mambo mengine ya wapiga kura na mimi niwapongeze wapiga kura wake kwa kumpigia kura na kwa kweli anastahili kuwa mwakilishi wao. Nimhakikishie kwamba mimi binafsi baada ya Bunge la Bajeti nitapanga ziara na nitaongozana naye kwenda kupita haya maeneo yote ambayo amekuwa akiyalalamikia na ambayo amekuwa akiyaleta ili Serikali iweze kuchukua uamuzi tukiwa kwenye eneo la tukio.
MHE. JUMAA H. AWESO: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwa kuwa matatizo ya Jimbo la Rufiji yanafanana kabisa na Jimbo langu la Pangani katika sekta ya kilimo na uvuvi. Nataka nijue ni lini Serikali itakuwa tayari kuwakumbuka wavuvi pamoja na wakulima wa zao la korosho katika Jimbo langu la Pangani?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa changamoto za Pangani zimefanana kwa kiasi kikubwa na Rufiji na nimweleze tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kama alivyosikia kwenye wasilisho la Wizara ya Fedha kuhusu bajeti ya Serikali, korosho ni moja kati ya mazao ambayo tayari tuna mkakati mkubwa sana wa kuhakikisha kwamba wananchi wanapata ahueni. Mmesikia tunaondoa tozo tano ambazo zimekuwa za usumbufu mkubwa kwa wananchi wetu. Tunategemea kwamba bei ya korosho itaendelea kuimarika na kuwa nzuri kwa sababu tayari tozo ambazo zilikuwa ni kero ziko mbioni kuondolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nimhakikishie kwamba hata kuhusu uvuvi, nina hakika alifuatilia tulipowasilisha bajeti yetu, tumeweka mikakati mizuri sana ya kuhakikisha wavuvi wetu wananufaika na mipango mbalimbali ya Serikali ukiwepo mpango wa kutoa mikopo kwa ajili ya vikundi vya wavuvi, kutoa elimu kuhusu uvuvi mzuri lakini kuwasaidia wavuvi wetu kuweza kupata nyenzo za uvuvi. Kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba wananchi wa Pangani katika uvuvi lakini vilevile katika kilimo hawajasahauliwa na Serikali. Hata hivyo, kwa sababu ni Mbunge makini na mara nyingi sana tumeongea naye, nimhakikishie tu kwamba kwa yale ambayo anafikiri tunahitaji kuelekeza nguvu zetu zaidi, naomba tukutane naye na ikibidi niko tayari kuandamana naye kwenda Pangani tukaangalie changamoto zilizopo.
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nishukuru majibu ya Naibu Waziri. Swali langu la kwanza, kwa kuwa malipo ya bonus ni haki ya wakulima kwa maana ni malipo ya tatu ya korosho na wananchi wale tangu mwezi Disemba wanazungushwa kupata fedha yao. Je, Serikali haioni kuna haja ya kutoa kauli sana kwamba wananchi wale waweze kulipwa fedha zao? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kwa kuwa mchanganuo wa fedha zinazopaswa kulipwa kwa wakulima ulishatolewa Bodi ya Korosho tangu Aprili na Serikali imepata kigugumizi hadi sasa kutotoa kauli ya wananchi wale kulipwa na Waziri naye aliahidi kuja pale. Je, leo Waziri anaweza kutoa kauli ya Serikali kuhusu ujio wake katika eneo hilo? Pia ni kwa nini asitoe tamko kuwaambia vyama kuanzia sasa wawalipe wakulima?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kuhusu bonus ni kweli kabisa kwamba wananchi wamepunjwa bonus mpaka Sh.200 katika kilo. Kama nilivyosema awali, Serikali inaendelea na uchunguzi kuhusu ubadhirifu ambao umefanywa na Vyama vya Ushirika ili wale wote ambao wamehusika na mapunjo hayo waweze kuchukuliwa hatua za kisheria. Nitumie fursa hii kuvitaka Vyama vya Msingi kuhakikisha kwamba wakulima wanapata salio la bonus yao ambayo hawajalipwa mpaka sasa hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili la sisi kwenda, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mara baada ya Bunge la Bajeti tutafanya utaratibu kwenda kuongea na wananchi na kufuatilia kwa ukaribu zaidi ili waweze kulipwa bonasi yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie fursa hii kuwaeleza na kuwashauri Waheshimiwa Wabunge pamoja na wananchi wa maeneo yanayolimwa korosho kwamba kinacholeta changamoto kubwa katika malipo stahili kwa ajili ya korosho ni kwa sababu Vyama vya Msingi pamoja na wakulima wanachukua madeni kutoka kwenye mabenki ili kuwalipa wakulima kabla korosho ile haijapata mteja.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaendelea kuwashauri kwamba wawe na subira, wasiwe na haraka ya kwenda kuchukua mikopo, badala yake wakusanye korosho kwa utaratibu wetu ule wa stakabadhi ghalani ili korosho ile iweze kununuliwa na hivyo kuondokana na utaratibu ambao inabidi ulipe interest za benki. Mara nyingine viongozi ambao siyo waadilifu wa Vyama vya Ushirika pamoja na Maafisa Ushirika wanatumia mtindo huo kama ni mwanya wa kuwaibia na kufanya makato ambayo yanawafanya wakulima wasiweze kupata fedha wanayostahili. Wawe na subira, waweke korosho yao, wauze kwa pamoja, waache kuchukua kwanza mkopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na tatizo la soko la chai kuna tatizo kubwa sasa linaendelea katika Mkoa wangu wa Manyara kuhusu soko la mbaazi. Wafanyabiashara wamekataa kununua mbaazi kabisa katika Wilaya ya Babati na katika Wilaya zote za Mkoa wa Manyara na wakulima wamebaki na mbaazi zao kwa sababu India mwaka huu ambao walikuwa wanunuzi wakubwa wao wamelima, Uganda wamelima na Kenya wamelima.
Naomba nipate kauli ya Serikali juu ya wakulima hao wa mbaazi katika Mkoa wa Manyara ambao wameshindwa kuuza mbaazi zao kwa sababu wafanyabiashara wamegoma kabisa kununua mbaazi hizo.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kama anavyosema Mheshimiwa Mbunge kwamba bei ya mbaazi imetetereka katika miezi ya hivi karibuni na si jimboni kwake tu lakini Tanzania nzima. Soko la mbaazi limetikisika siyo nchini kwetu lakini ni duniani kote, wanunuzi wakubwa ambao wamekuwa wakinunua mbaazi yetu katika siku za hivi karibuni hawajaendelea na utaratibu ule wa kununua kwa bei ile kwa hiyo imepelekea mtikisiko utokee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inalifahamu hili, inajaribu kulifanyia kazi ikiwa ni pamoja na kuangalia uwezekano wa kupata wanunuzi mbadala. Nikubali tu kwamba ni kweli kabisa mbaazi imeshuka bei kwa baadhi ya maeneo kama Lindi na Mtwara imeshuka mpaka hata kufikia shilingi 500 kwa kilo ambayo ni tofauti kabisa na ilivyokuwa huko nyuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, suala hili tunalifahamu na tunalifanyia kazi na nimuahidi tu kwamba pale Serikali itakapopata suluhu tutamtaarifu kwa niaba ya wananchi wake wa Babati.
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu imeeleza kwamba kufunguliwa kwa Ubalozi kutategemea masuala ya kibajeti; je, Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kufungua ile tunaita Honorary Consul kwa sababu ile haina gharama zozote ambazo Serikali itaingia zaidi ya kupata tu mtu ambaye ni mwaminifu na mwadilifu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kufungua Honorary Consuel ambapo siyo suala lenye gharama kibajeti kama ambavyo Serikali imejibu katika swali la msingi, ni jambo la msingi kwa sababu litawezesha kufungua fursa zaidi za kiuwekezaji siyo tu katika Sudan ya Kusini, lakini pia katika maeneo mengine ambako Serikali imeshindwa kufungua Balozi kwa sababu ya ukosefu wa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa kufungua fursa hizi za uwakilishi wa heshima, tunapanua wigo wa kuongeza uwekezaji na biashara na hivyo kuongeza mapato ya Serikali ambayo mwisho wa siku wananchi wa Mafinga na Tanzania kwa ujumla watanufaika katika kuboresha huduma zao za kijamii. (Makofi)
Je, Serikali iko tayari pia sasa kufungua Uwakilishi wa Heshima katika Mji wa Lubumbashi ambako kuna fursa kubwa za kibiashara baina yetu sisi Tanzania na nchi ya Demokrasia ya Kongo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli alivyosema Mheshimiwa Mbunge kwamba kufungua Uwakilishi wa Heshima ni njia mojawapo ya kuwa na uwakilishi wa nchi yetu katika nchi nyingine, lakini vilevile kuna utaratibu wa Kikonseli lakini na ule utaratibu wa kawaida wa kufungua Ubalozi wenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, hizo ni kati ya njia ambazo tungeweza kutumia nchini Sudan Kusini, lakini kwa sasa Wizara inafikiria zaidi kujipanga kufungua Ubalozi kamili badala ya kufungua Consul au kutafuta Uwakilishi wa Heshima. Hii ni kwa sababu nchi ya Sudan Kusini ni moja kati ya wanachama wa Jumuya yetu ya Afrika Mashariki, kwa hiyo, ningependa kuwa na Ubalozi kamili.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wakati bado tunaelekea kule, tunajipanga, nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kitendo cha nchi ya Sudan Kusini kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki inatoa fursa nyingi sana na inarahisisha wananchi kuweza kunufaika na fursa zilizoko kule hata bila kuwepo na Ubalozi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unaruhusu pamoja na mambo mengine urahisi wa kusafirisha bidhaa, lakini vilevile huduma na kazi kwenye hizi ambazo ni wanachama.
Kwa hiyo, tayari kuna mazingira mazuri ambayo yanarahisisha wananchi kuweza kunufaika na hizo fursa hata bila kuwa na uwakilishi wa kiheshima bila kuwa na Consul au kuwa na Ubalozi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema Wizara inajipanga, tunatambua umuhimu wa Sudan Kusini kama wanachama wa Afrika ya Mashariki, tunatambua fursa lakini huko ndiyo tunaelekea, lakini tunajipanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile Mheshimiwa Mbunge amezungumzia kuhusu kufungua Uwakilishi wa Kiheshima Lubumbashi. Napenda kumjibu Mheshimiwa Mbunge kwamba, ni kweli kabisa tunatambua fursa zilizopo Lubumbashi, tunafahamu fursa zilizopo katika ukanda huo wa DRC, lakini kwa sasa Serikali na Wizara imejielekeza zaidi katika kuimarisha shughuli za Kibalozi kwa sababu tunafikiri bado inakidhi matakwa hayo ya fursa zilizopo, nashukuru sana.
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, kwanza ninasikitika sana kwa majibu ya Naibu Waziri anaposema kwamba wafugaji hawapati maji kwa sababu wakulima wamekuwa wakikinga hayo maji, nadhani wana upungufu wa research. Inaonesha kwamba mto Mkondoa na mto Miyombo inafika mpaka sehemu ambazo wafugaji wapo na tatizo lao kubwa siyo maji, tatizo lao kubwa ni malisho. Ndiyo maana wameonekana sehemu za Malangali wakilisha katika sehemu za mashamba ya watu na sehemu ambazo watu wamehifadhi mazao yao.
Mheshimiwa Spika, lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Tindiga pamekuwa siyo mahali salama kwa watu kuishi na kwa kilimo kwa sababu wafugaji wameonekana ku-take over maeneo yale na hapa nnavyozungumza na wewe pamekuwa na mauaji kila mwezi; tarehe 8 Juni ameuawa kijana anaitwa Ally Mbarouk Makakala na juzi tarehe 6 Septemba wameuawa watu wawili Elia Emmanuel Mbwane na Ramadhani John Mashimba.
Je, Serikali inawahakikishiaje usalama wa wakulima wa pale Tindiga lakini pia inawahakikishiaje usalama wananchi wa Tanzania ambapo suala la migogoro ya wakulima na wafugaji limeonekana kuwa kero kubwa sana hapa nchini? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa Mkuu wa Mkoa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa ilikuja Tindiga na kutoa baadhi ya maagizo ambayo mpaka sasa hayajafanyiwa kazi na kupelekea vifo vya hao watu wawili vilivyotokea juzi.
Je, Naibu Waziri pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani wapo tayari kuambatana pamoja na mimi kuelekea Tindiga kuona hali halisi ya mauaji na hali ya kutotulia katika Jimbo la Mikumi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kama Mheshimiwa Mbunge haridhiki na maelezo yangu nafikiri bado tuna fursa ya kuangalia suala hilo ili tuweze kupata maelezo mengine na ninamuahidi kwamba tukitoka hapa nitakaa naye tuone namna gani tunaweza tukapata taarifa ambazo zitatusaidia kuboresha hiyo ambayo tunayo ili tuweze kufanya yale ambayo ni ya muhimu kwa ajili ya kushughulikia mgogoro huo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunafahamu mauaji ambayo yametokea Mheshimiwa Mbunge amewasiliana na sisi. Tunafahamu kwamba ni sehemu ya changamoto kubwa tuliyonayo nchi nzima ya migogoro ya wakulima na wafugaji. Ndiyo maana kama nilivyoeleza katika swali la awali Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara zingine ikiwepo Wizara ya Ardhi, Wizara ya Maliasili na TAMISEMI tayari kuna timu ya Wizara hizo inafanya ground work kuja na mapendekezo ambayo yatatusaidia kuondoa migogoro tuliyo nayo. Kwa hiyo, naamini Mheshimiwa Mbunge akiwa na subira na katika muda ambao siyo mrefu tutafikia muafaka wa namna ya kusuluhisha matatizo haya.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili kwamba maagizo ya Kamati ya Ulinzi na Usalama hayajatekelezwa. Vilevile nipo tayari nikitoka hapa kuwasiliana na Mheshimiwa DC wa kule kujua ni kwa nini maagizo yale hayajatekelezwa, ikibidi kama anavyopendekeza mimi mwenyewe sitasita kuandamana naye kwenda Jimboni kwake kuangalia hali hii. Pamoja na kwamba tayari nafahamu aliyekuwa wakati huo Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba tayari alishafika kwenye eneo hilo. Serikali hatutaki hii migogoro iendelee na pale panapotakiwa tufanye jambo lolote la kunusuru na kusuluhisha tutafanya hivyo. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba siyo shida kwenda Jimboni kwake kuangalia hii hali. Nashukuru sana. (Makofi)

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu sahihi aliyoyatoa. Niseme tu na mahali pote wasikie kwamba hakuna shamba lolote ambalo linafanana na thamani ya maisha ya mwanadamu, wala hakuna kundi lolote la mifugo ambalo linafanana na maisha ya mwanadamu. Kwa hiyo, hakuna mgogoro wowote ule ambao unaleta uhalali wa kuua mwanadamu.
Mheshimiwa Spika, kwa kutumia kigezo hiki nitoe maelekezo katika Mkoa husika na Wilaya husika kuwasaka wowote wale waliohusika na mauaji hayo na sehemu yoyote ile ambako watatumia vigezo vya mgogoro kuua watu, wakamatwe na wafikishwe kwenye mkono wa sheria. Kama watatumia kigezo cha mob nielekeze katika Kijiji husika ambacho watapoteza maisha ya mwanadamu, wakamate vijana wote wenye nguvu ambao wanaweza wakawa wawefanya hivyo ili kuweza kupekua na kuweza kupata wale waliofanya kazi hiyo. Kama Magereza hayatoshi wawaachie huru vibaka wote walioiba simu na vitu vidogo vidogo, wakamate wale wanaoua watu wawekwe ndani ili tuweze kukomesha utaratibu wa watu kuua wananchi wasiokuwa na hatia na kuwasababishia matatizo. (Makofi)
MHE. SULEIMAN A. SADDIQ: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.
Kwa kuwa Wilaya ya Mvomero kuna migogoro mikubwa sana ya wakulima na wafugaji zaidi ya Wilaya ya Kilosa na kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero imefanya mikakati mbalimbali kupunguza migogoro hii na zipo juhudi kubwa sana zilifanyika na aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba alifika mara mbili na aliahidi kutupatia fedha kwa ajili ya kujenga majosho na malambo; fedha ambazo hadi leo hazijapatikana. Majosho na malambo yale yatasaidia ng’ombe wale kwenda kupata maji katika maeneo ambayo yapo nje ya mashamba ya watu.
Je, Serikali ipo tayari kutimiza ahadi hiyo ya Waziri ili tuweze kupata fedha za kujenga malambo na majosho Mvomero? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa kwamba aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Mwigulu Nchemba alitoa ahadi kuhusu miundombinu hiyo ya malambo na majosho. Nipende tu kusema kwamba alifanya hivyo kama Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi na hakufaya kama binafsi. Kwa hiyo, ahadi aliyoitoa bado ipo kwenye Wizara yangu hajahama nayo. Ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara yangu itaendelea kuwasiliana na Halmashauri ya Mvomero ili kuhakikisha kwamba ahadi yetu hiyo ya Wizara inatekelezwa. (Makofi)
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi.
Kama alivyoeleza Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba migogoro hii ya wakulima na wafugaji inasambaa karibu maeneo mengi hapa nchini ikiwa ni pamoja na katika Jimbo la Lulindi katika Vijiji vya Sindano, Maparawe, Mapili pamoja na Manyuli.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari kuja kule kusaidiana na kusuluhisha matatizo yaliyopo kati ya mpaka wa Tanzania na Msumbiji hususani katika eneo la kando kando mwa Mto Ruvuma ambako wananchi wengi ndio hulima lakini tayari kuna uvamizi mkubwa wa wafugaji ambao sasa upotevu wa amani umeanza kuwepo katika eneo hilo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, changamoto za migogoro ya wafugaji na wakulima na migogoro ya ardhi ya aina mbalimbali ni kweli kwamba ipo karibia kila kona ya nchi yetu. Kwa hiyo, pamoja na kwamba tupo tayari kwenda kila Jimbo katika kila kona ya kuangalia namna gani ya kutatua, Wizara na Serikali kwa ujumla inafikiria kutafuta suluhu ya jumla; suluhu ambayo itasaidia katika maeneo yote badala ya kila wakati labda Waziri na Naibu Waziri kukimbia kila mgogoro unapotokea. Kwa sababu mnafahamu Waheshimiwa Wabunge kwamba nchi yetu ni kubwa inawezekana tukashindwa kufika kote kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo nimeshafika Lulindi kwa Mheshimiwa Bwanausi lakini nilienda kushughulikia kero nyingine kabisa ya korosho. Kwa hiyo, bado ni Tanzania yetu hiyo hiyo kama inaelekea kwamba utatuzi wa jumla hautaweza kushughulikia kero aliyoileta Mheshimiwa Mbunge, nipo tayari kwenda kule na labda itakuwa vilevile ni fursa ya kwenda kumalizia viporo vya korosho nilivyoviacha.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali langu la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ninalo swali la nyongeza.
Kwa kuwa wananchi wengi wa Mkoa wa Dar es salaam na hasa katika maeneo ya Kitunda, Mvuti, Chanika, Mbande, Pugu, Somangila, Kisarawe II, Kibada, Vijibweni, Yombo, Kunduchi, Mabwepande na Kibamba wote wanategemea kupata vipato vyao na hasa akina mama kwa kwa kazi ya kufuga kuku wa nyama na kuku wa mayai, lakini bei ya dawa zimekuwa kubwa sana kiasi kwamba akina mama hawa wanashindwa kuuza bidhaa zao, wanashindwa kuuza kuku wa mayai na kuku wa nyama kwa gharama ambayo ingeweza kuwapa faida.
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga maduka au kuweka dawa katika vituo vya mifugo vya Serikali ambavyo viko katika Wilaya zote Tanzania nzima ili wafugaji hawa waweze kupata nafuu ya bei za dawa kuliko vile wanavyolanguliwa na wafanyabiashara mbaimbali ambao wao hawana uchungu sana na wananchi, wao wanatafuta kipato?
Swali la pili, kwa kuwa Serikali imeonyesha wazi lengo lake kwamba kuna Kituo cha Tiba cha Kibaha kinaweza kuzalisha chanjo mbalimbali; je, Serikali ina mkakati gani wa kukiongezea nguvu kituo hiki ili iweze kuzalisha chanjo kwa wingi, wananchi waweze kupata chanjo hizo kwa bei nafuu na wao waweze kuboresha vipato vyao?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kama alivyosema kwamba kuna changamoto kubwa sana ya upatikanaji wa dawa za mifugo, vilevile kwamba bei imekuwa ni bei ambayo wakulima wengi, wafugaji wengi hawawezi kustahimili. Mkakati wa Serikali kwa sasa ni kujaribu kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi ili iweze kutoa huduma hizo, huo ndiyo mwelekeo wa sera tuliyonayo ya mwaka 2006.
Hata hivyo, Serikali kwa kutambua kwamba tayari utaratibu huo una changamoto Serikali inafikiria zaidi kuangalia ni namna gani tunaweza tukawezesha na tukahamasisha ujenzi wa viwanda dawa hizo ziweze kuzalishwa nchini ili bei ipungue. Kwa sababu kinachofanya dawa kwa kiasi kikubwa ziwe ghali ni kwa sababu nyingi tunazitoa nje ya nchi, kwa hiyo kuna utaratibu ndiyo maana tunahamasisha sana kuhusu ujenzi wa viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ili kuteremsha na kufanya bei ya dawa hizo kuwa nafuu Serikali imeendelea kupitia wigo wa kodi na tozo mbalimbali ambazo ziko kwenye dawa ili hatimaye dawa hizo ziweze kupatikana kwa urahisi zaidi. Serikali inaendelea kutumia Maafisa Ugani kufanya uhamasishaji na kutoa elimu ili wananchi wenyewe waweze kuona umuhimu wa kutumia dawa ili kuweza kunusuru mifugo yao isife.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili kwamba Serikali ina mpango gani wa kuongezea kiwanda kilichopo Kibaha nguvu, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inaweka mazingira wezeshi ili sekta binafsi waweze kujenga viwanda zaidi. Kwa hiyo, tuko tayari kushirikiana na viwanda hivyo kwa sababu kuna viwanda vya Farmers Center, vilevile kuna kiwanda cha Multivet Services kwa hiyo zote hizi tutaendelea kufanya nao kazi na kutoa msaada ambao watahitaji ikiwa ni pamoja na msaada ambao watauhitaji ikiwa na nafuu za kodi ili waweze kuzalisha zaidi ili wakulima wetu na wafugaji wetu waweze kupata dawa kwa haraka lakini na kwa bei ambayo ni nzuri. (Makofi)
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Kwanza ni amani yangu kwamba wataalamu waliopelekwa kutoa ushauri wa kupelekwa Wilayani Chato ila wamepeleka Wilayani Biharamulo.
Pili maelezo kidogo tatizo hili limekuwepo kwa miaka mingi na tumekuwa tunapata majibu mara nyingi kutoka Serikalini ambayo kwa kweli hayajaweza kukidhi kulingana na ukubwa wa tatizo. Tulisikia swali la kisera kuelekea kwa Waziri Mkuu mwezi wa saba likapelekea kiti chako Mheshimiwa Naibu Spika kutoa maelekezo kwamba Serikali ichukue hatua na ilete majibu hapa.
Sasa swali langu kwa sababu hali halisi inaonesha kabisa kwamba tatizo hili ili likabiliwe kuna mambo matatu lazima yafanyike la kwanza utafiti ili kuja tatizo ni nini ambalo tayari...
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu je, Mheshimiwa Naibu Waziri uko tayari kufanya kikao maalum na Wabunge wa Mkoa wa Kagera ili tuone namna gani tunaweka mikakati ya kutafuta utashi wa kisiasa wa kukabili tatizo hili, lakini namna ya kutafuta na kuwashirikisha wadau wengine wa maendeleo wa ndani na nje ya nchi na hata private sector ndani ya Tanzania ili tukabiliane na tatizo hili? Kama uko tayari, upo tayari kwa muda wa karibuni, muda wa kati au muda wa mbali?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nilipotaja Chato nilisahau Biharamulo, lakini mimi ndiyo sijasoma kwa hiyo nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Biharamulo nayo imo.
Kuhusu ombi lake la kufanya mkutano, tayari nimeshawasiliana na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi na ameahidi kwamba tukitoka kwenye Bunge hili atafanya mkutano na Wabunge wanaotoka Mkoa wa Mwanza vilevile Mkoa wa Kagera ili kuangalia namna ya kuweza kushughulikia tatizo hili, kwa hiyo kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge tayari tumepokea na tutafanya haraka tuweze kukutana nao. (Makofi)
MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Wakati wa Bunge la Tisa hili suala nililiuliza ikawa upembuzi yakinifu, sijui upembuzi yakinifu unachukua miaka mingapi kuweza kukamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama suala langu linavyosema na yeye mwenyewe Mheshimiwa Waziri amekiri, Mkoa wa Kagera sisi hatujawahi kuomba chakula; tunachoiomba Serikali ni kuwapa elimu wana-Kagera waweze kuwa na chakula cha kutosha. Kama hivi sasa tuna matatizo ya njaa, lakini ni mara ya kwanza, tungekuwa na utaalam wa kilimo cha umwagiliaji tusingekuwa na matatizo ya njaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, ni lini Serikali itaupa kipaumbele Mkoa wa Kagera kwa kila kitu? Kwa kuwa kila kitu tunachokisemea kinakuwa ni kesho, kesho, hata na haya maafa itakuwa ni kesho. Ni lini Serikali itaona huruma kwa kuwapa elimu vijana na wanawake wakawa na chakula cha kutosha pamoja na chakula cha kuleta uchumi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, kama Mheshimiwa Mbunge alivyosema, kwamba upembuzi huwa unaelekea kuchukua muda mwingi kuliko ilivyopangwa, lakini kama nilivyosema tunatarajia sasa utakamilika mwaka unaokuja. Kwa hiyo baada ya hapo hatutakuwa tunazungumzia tena kuhusu kuchelewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, kuhusu Serikali kupeleka wataalam wa kilimo, nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba, tayari katika Serikali za Mitaa katika Halmashauri zetu tuna Maafisa Ugani wa Kilimo ambao wanafanya kazi za kutoa elimu kwa ajili ya kilimo na Wizara yangu imeweka mazingira wezeshi ya kisera ya kuhakikisha kwamba wataalam hao wanaotoa elimu wanatoa elimu sahihi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mara nyingi vikwazo vimekuwepo kwamba hawana nyenzo, hata hivyo Serikali inaendelea kuboresha shughuli za ugani ili wananchi waweze kunufaika na elimu ya kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba, kuhusu vijana, Wizara yangu iko tayari muda wowote kushirikiana na Mheshimiwa Mbunge ili kuangalia namna gani tunaweza kuwawezesha vijana kushiriki katika kilimo. Tayari katika Bunge hili kuna Mbunge mmoja, ambaye anashirikiana vizuri sana na Wizara yangu, Mheshimiwa Ester Mmasi, ambaye kupitia kwake na jitihada zake kwa vijana, tayari tumewafikia vijana 500 na tayari tumewapatia ardhi katika maeneo mengi; tayari tuko katika jitihada za kuwaunganisha na mabenki kwa ajili ya kupata mikopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimkaribishe sana Mheshimiwa Mbunge aje ofisini kwetu, tukae, tuongee tuangalie namna gani tunaweza tukawasaidia vijana wa Kagera ili waweze kuondokana na tatizo la ajira. Vilevile, niseme kwamba, tunawapongeza sana watu wa Mkoa wa Kagera kwa sababu ni kweli kama alivyosema kwa miaka mingi sana wamekuwa wakijitosheleza kwa chakula na hata sasa ambapo changamoto za mabadiliko ya tabia ya nchi yametokea, Serikali yao bado itaendelea kuwa nao ili kuhakikisha kwamba, wanaweza kukabiliana na hizo changamoto ili waendelee kujitegemea kwa chakula.
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na swali zuri lililoulizwa juu ya ajira ya kilimo kwa vijana wa Mkoa wangu wa Kagera, Serikali katika bajeti ya mwaka 2016/2017, ilionesha nia na dhamira ya dhati ya kuinua ajira kwa vijana. Je, Serikali imefikia wapi katika utekelezaji wake katika sera ya ajira ya vijana katika sekta ya kilimo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba katika mpango wetu wa bajeti ya mwaka huu tuna mikakati mingi ya kuwasaidia vijana kupata ajira kwenye sekta ya kilimo. Kama nilivyokwishasema, tayari Wizara inashirikiana na vijana wengi ili kuhakikisha kwamba wanajihusisha katika shughuli za kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari vijana wengi tumewasaidia kuingia kwenye Vyama vya Ushirika, lakini vilevile tayari vijana tunawaunganisha katika fursa za mikopo. Mfano mzuri, ni fursa iliyopo katika benki ya NMB ambayo tayari wametenga shilingi bilioni 500 kwa ajili ya kilimo cha biashara na kwa wale vijana ambao wameunganika katika vikundi kama wale niliosema wanaosaidiwa na Mheshimiwa Ester Mmasi tayari tunaongea na NMB ili waweze kutoa mikopo kwa ajili ya vikundi hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile NMB wako tayari kutoa elimu ya kilimo kwa ajili ya vijana ambao watapata mkopo. Vilevile, katika kutekeleza kusudio letu la kuhakikisha vijana wanapata ajira kupitia kilimo, tumetenga hekari 220 katika bonde la Rufiji ili liweze kuwa shamba darasa ili vijana wengi waweze kuelewa namna zaidi ya kujihusisha na kilimo. Kwa hiyo, kama ninavyosema kuna mipango hiyo na Mheshimiwa Halima namfahamu ni mtu ambaye anawapigania sana vijana nae vilevile ili…
Ili aweze kupata maelezo zaidi, namkaribisha…
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Taasisi nyingi za fedha zinawakwepa wakulima na wafugaji kuwapatia fursa za mikopo, lakini nashukuru katika maelezo yake sasa hivi amefafanua hasa kwa wakulima. Sasa je, Serikali ina mikakati gani hasa kuwapa wafugaji mikopo ili waweze kuendeleza mifugo yao?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema kilimo na mikopo iliyopo, pamoja na fursa zingine tunamaanisha vilevile ufugaji pamoja na uvuvi si kilimo cha mazao pekee.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, napenda tu kuuliza swali dogo kwa Mheshimiwa Waziri.
Kwa kuwa Bodi ya Pamba muda mwingi iko Dar es Salaam na Makao Makuu yako Dar es Salaam, na kwa kuwa Mkoa wa Simiyu ndio Mkoa unaoongoza kulima pamba hapa nchini. Je, Serikali inatoa tamko gani kwa wakulima ambao wamekuwa wakipata mbegu hizi na dawa ambazo haziwasaidii na wala hawapewi fidia. Ni lini Bodi hii itahamia karibu na Mikoa ambayo inazalisha pamba?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi ameshatoa agizo la Bodi ya Pamba kuhamia Mwanza na kwa taarifa tulizonazo ni kwamba wanatakiwa wawe wamehama kabla ya tarehe 10 mwezi huu.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa jinsi Mheshimiwa Waziri alivyojibu swali lake, kwamba bado hawajagundua nani ambaye amesababisha tatizo, lakini Serikali iliji-commit kulipa fidia. Sisi tunaotoka Kanda ya Ziwa suala la pamba limekuwa ni issue kubwa sana.
Je, Mheshimiwa Waziri, tatizo la pamba likijitokeza tena, uko tayari kujiuzulu kwa sababu majibu yako tayari unajikanganya hapa?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri kama ofisi inawezekana anavyosema Mheshimiwa Mbunge alitoa majibu ya kusema Serikali italipa fidia. Lakini hizo fedha ni fedha ya umma ambayo haiwezi ikalipwa tu bila kujiridhisha kwa kweli kwamba anayelipwa anastahili na kwamba Serikali inayo liability katika hilo jambo. Kwa hiyo, ni lazima kuwa na uhakika kwamba kwanza kweli Serikali inayo liability katika hilo jambo, lakini pili anayelipwa anastahili kulipwa hizo fedha na ndiyo maana hatua hizi zinafanyika. Kama nilivyosema kwenye suala la viuatilifu, tumekwisha jiridhisha beyond doubt nani wamehusika na hilo kosa la kusababisha dawa zisiwe na effect katika kuua wadudu kama ilivyotarajiwa na kwa hiyo hawa watachukuliwa hatua kama sheria inavyotaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hata kwenye mbegu, tutakapajiridhisha exactly ni nani muhusika kwanza hawa watachukuliwa hatua na kama ni Serikali, itakuwa na wajibu wa kulipa tutafanya namna hiyo.
MHE. MUSSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru wewe na pia kwa kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri; lakini katika majibu yake Serikali imekiri kwamba wanunuzi hawa wa tumbaku wana muungano wa ukiritimba katika kupanga bei na kiasi cha tumbaku cha kununua. Wanapenda kuangalia gharama za mkulima katika kuzalisha zao lake ndipo wapange bei, lakini sisi hatujui wao wanauza shilingi ngapi katika Soko la Dunia. Je, ni hatua gani Serikali inachukua katika kumsaidia mkulima huyu wa tumbaku katika kupata bei nzuri?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Serikali ililitangazia Bunge kwamba kupitia WETCU wana mpango wa kufufua Vyama 64 vya Wakulima wa Tumbaku ambapo wanachama wa vyama vile walichangishwa sh. 100,000/= kila mmoja katika kufanikisha zoezi hilo, lakini leo WETCU na makampuni wamewanyima wakulima hawa pembejeo, lakini vile vile wanasema kwamba soko la kununua tumbaku ile hakuna. Wakulima tayari wameshalima na utaratibu wote wameshamaliza na hawajui watauzia wapi tumbaku hiyo. Je, Serikali inawaambia nini wakulima hawa wa tumbaku ambao tayari sasa wemeshalima tumbaku yao na wanasubiri mauzo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba biashara ya tumbaku inaendeshwa kwa cartel; kuna makampuni machache duniani ambayo ndiyo yanaamua kila kitu, yanaamua kiasi, lakini vile vile yanaamua bei. Ni kweli vile vile kwamba mara nyingi kampuni zinazonunua tumbaku zenyewe hazina tabia ya kuonesha faida na gharama zao lakini wanataka wakulima na wazalishaji waoneshe.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikiendelea na majadiliano na haya makampuni na kwa sasa makampuni hayo yamekubali kutuonyesha gharama zao pamoja na faida wanazopata ili tuweze kulinganisha wakati wa kuamua bei dira. Kwa hiyo, kuanzia msimu unaokuja, Serikali vile vile sasa na wadau wengine watafahamu upande wa pili wa hali halisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na wakulima ambao wamelima tumbaku lakini hawajawekwa kwenye utaratibu wa ununuzi, kauli ya Serikali ni kwamba tumbaku inazalishwa na inauzwa kwa kupitia Vyama vya Ushirika, ni kilimo cha mkataba. Ni vigumu sana kumhakikishia mkulima soko kama hakukuwa na makubaliano kabla ya kilimo. Kwa hiyo, tunaendelea kuwakumbusha wakulima kwamba ni vizuri wapitie utaratibu wa Vyama vya Ushirika ili kuweza kuingia mkataba na makampuni yanayonunua tumbaku kwa sababu ni zao ambalo hupati bei nje ya utaratibu wa kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tutaendelea kuboresha mfumo ikiwa ni pamoja na kuboresha Vyama vya Ushirika kwa sababu changamoto kubwa iliyopo katika zao la tumbaku ni kwa sababu vyama vingi vya ushirika vina madeni. Mkoa wa Tabora ni Mkoa wa mfano kabisa, kwa hiyo, mara nyingi sana imetokea kwamba wakulima wengi hawataki kuuza kwenye mfumo wa Vyama vya Ushirika kwa sababu vyama vinadaiwa. Kwa hiyo, Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya Vyama vya Ushirika.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba nimwulize Mheshimiwa Naibu Waziri swali moja la nyongeza. Kwa kuwa Serikali inatambua mchango wa zao la tumbaku kwenye uchumi wa Taifa hili na hivi tunavyoongea makampuni kwenye Vyama vya Ushirika hawajatoa makisio kabisa maeneo mengine na maeneo mengine wametoa makisio madogo sana, kiasi kwamba wakulima wengi mwaka huu wanashindwa kwenda kulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Serikali iweke commitment hapa, itafanya utaratibu gani wa haraka kuhakikisha makampuni haya yanatoa makisio kwenye Vyama vya Msingi ili wakulima ambao wanalima miaka yote waweze kulima kwa sababu ndiyo sehemu ya maisha hayo? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa katika msimu unaokuja, makisio yamekuwa ni ya kiasi kidogo kuliko msimu uliopita. Makisio ya msimu unaokuja ni kilo milioni 55.9 wakati msimu uliopita ni kilo milioni 60. Kwa hiyo, maana yake ni tumbaku kidogo itanunuliwa ukilinganisha na msimu uliopita.
Mheshimiwa Naibu Spika, shida hii imetokea kwa sababu kulikuwa na kutoelewana katika bei ya dira kati ya makampuni na Vyama Vikuu. Kwa hiyo, Serikali inachojaribu kufanya ni kuweka mikakati ili makubaliano ya bei yaweze kufanyika mapema ili katika msimu mwingine tusije tukapunguza hizi kilo, ila ziongezeke.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunachoweza kusema kwa sasa ni kwamba, tayari makubaliano yameshatokea, sisi tunaangalia huko mbele kuhakikisha kwamba tunaongeza kilo ambazo zitanunuliwa.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali na kwa kiwango kidogo kitakachozalishwa mwaka huu:-
Je, Serikali imejipanga vipi kutatua tatizo la ukosefu wa classifiers ambao wanafanya msimu wa zao kuwa mrefu sana? Ni lini Serikali itakuja na bajeti ya kutosha kwa ajili ya kuajiri classifiers ambao watasaidia kutatua tatizo la tumbaku?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa Wizara na Serikali inatambua changamoto iliyopo kwa sababu kuna upungufu wa classifiers. Bodi ya Tumbaku iko katika hatua za kuhakikisha kwamba, changamoto hiyo inaondoka na tunaamini kwamba, kwa kiasi kikubwa tunapoelekea kwenye msimu mwingine wa tumbaku tatizo la classifiers halitakuwepo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nitumie fursa hii kuwaomba Waheshimiwa Wabunge wafahamu kwamba, ili kuweza kupata bei nzuri ya tumbaku na kuweza kuuza tumbaku nyingi zaidi ni lazima vile vile tumbaku yetu tufanye iweze kushindana. Kwa sasa tumbaku yetu inakabiliwa na changamoto kubwa. Imekuwa ni vigumu sana kuwapata wanunuzi kwa sababu hatutunzi mazingira na vile vile kwenye kilimo cha tumbaku tunatumia watoto kitu ambacho hakitakiwi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata ukiwa na tumbaku nzuri namna gani, ni lazima vilevile uangalie mazingira ambayo umezalisha. Kwa hiyo, tuhakikishe kwamba, tunapanda miti, tunafuata masharti yote, lakini vilevile watoto wasifanye kazi kwenye mashamba ya tumbaku.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali madogo mawili. Swali la kwanza, kwa kuwa hizi zana haramu, yaani nyavu pamoja na zana nyingine zinatengenezwa na viwanda vilivyoko hapa nchini na zinaagizwa kuingia hapa nchini na wafanyabiashara: Je, Serikali inachukua hatua gani kwa hao watu ambao wanaleta zana haramu hapa nchini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa wavuvi haramu hasa ni watu ambao wanajitafutia riziki zao, wengi wamenyang’anywa zana zao na kuchomwa moto ili kuitikia agizo la kisheria la nchi: Je, Serikali ina mpango gani kuwasaidia hao wananchi ambao maisha yao yote yanategemea uvuvi lakini kwa sasa hawawezi kufanya kwa sababu wanakiuka sheria? Wanasaidiwaje kupata mikopo angalau waweze kuendesha maisha yao, lakini pili kufundishwa namna endelevu ya kufanya uvuvi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali haijaishia tu katika kukamata makokoro na zana nyingine haramu zinazotumika katika uvuvi, lakini vile vile kuhakikisha kwamba, pale yanapotengenezwa na yanapotokea, vilevile wanaohusika wanakamatwa.
Waheshimiwa Wabunge, kama mtakumbuka, ni karibuni tu meli iliyoingia katika bandari ya Dar es Salam ilishikwa ikiwa imebeba zana mbalimbali za uvuvi zikiwepo zana za kutengeneza makokoro na nyavu ndogo ambazo inaaminiwa zingeweza kutengeneza mpaka nyavu 20,000. Huo ni mfano tu wa kuonesha kwamba siyo tu tunakamata wavuvi, lakini vile vile hata viwanda na hata katika kuingiza vile vile tunadhibiti.
Mheshimiwa Naibu Spika, ifahamike tu kwamba, ugumu unaotokea ni kwamba zana za uvuvi au vifaa vinavyotumikia kutengeneza zana za uvuvi vile vile zinatumika kutengeneza vitu vingine ambavyo ni halali. Kwa mfano nyavu, siyo kwamba unakuta hasa kwamba ile bidhaa inayotoka kiwandani ni haramu; inaweza ikawa inatumika kwa ajili ya vitu vingine ambavyo vinaruhusiwa kisheria. Kwa hiyo, kidogo inaleta shida, lakini pale tunapobaini moja kwa moja kwamba ni kifaa au ni zana ambayo inaenda kutumika kufanya uvuvi haramu au kutengeneza zana za uvuvi haramu, tunachukua hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, ni kuhusu msaada gani Serikali inatoa kwa wavuvi wadogo? Nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali kupitia Wizara hii, imeweka utaratibu wa kuhakikisha kwamba wavuvi wadogo wanaweza kupata mikopo kupitia katika Benki yetu ya Kilimo, lakini vile vile kuna mikopo ambayo inapatikana kwa ajili ya pembejeo kupitia Mfuko wa Pembejeo. Tayari Benki ya Uwekezaji ambayo nayo ina fursa kwa ajili ya mikopo na Wizara pia inakopesha vikundi mbalimbali vya wavuvi. Kwa hiyo, kuna fursa mbalimbali kwa vikundi na wavuvi ambao watahitaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiacha fursa zilizopo kwa ajili ya kutoa mikopo, Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri mbalimbali imeendelea kutoa elimu kuhusu uvuvi endelevu na uvuvi bora kwa kupitia vikundi mbalimbali vya Beach Management Unit na tayari katika maeneo mengi ya nchi yetu, elimu hii imetolewa, lakini kama nilivyosema tunatoa elimu kupitia vyombo vya habari kama television na tunaamini imesaidia sana kupunguza tatizo la uvuvi haramu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunavyofahamu, uvuvi haramu ni kama uhalifu mwingine. Hata watu wakiwa na elimu namna gani, bado mara nyingi kuna tabia ya wahalifu kuendelea kuwepo, lakini Serikali itaendelea na jitihada za kupambana na uvuvi haramu.
MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa wananchi wa Jimbo la Mchinga wameamua kuitikia wito wa kupambana na uvuvi haramu especially uvuvi wa mabomu na wameanzisha BMU katika maeneo ya Mchinga, Mvuleni, Kijiweni na Ruvu. Je, nini kauli ya Serikali kwenye kuzisaidia na kuzijengea uwezo hizi BMU ili ziweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niwapongeze sana wananchi wa Mkinga na ukanda huo wa Pwani kwa sababu ni kweli kwamba wameitikia ombi au mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kwamba tunatokomeza uvuvi haramu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, nipo tayari kuongea naye ili tuone namna gani ya kusaidia Halmashauri yake ili waweze kutoa msaada na elimu kwa wananchi ambao wako kwenye Beach Management Units. Kwa hiyo, naomba kwa kuwa yuko kwenye Kamati yangu, tukitoka hapa, tuongee, tuangalie namna ya kusaidia.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa Majimbo yote ya Kanda ya Ziwa tunategemea uvuvi na tumekuwa tukiona kweli jitihada za Serikali katika kupambana na wavuvi haramu kuchoma nyavu na vitu vingine; lakini zile samaki zinazovuliwa na wavuvi haramu zinauzwa viwandani. Hatujawahi kuona hata siku moja operation inapelekwa kwenye viwanda na kwenye maduka. Je, Mheshimiwa Waziri anatuhakikishiaje Wabunge wa Kanda ya Ziwa atafanya lini ziara na kulifanya zoezi hili kuwa endelevu kwenye maduka na viwanda vinavyonunua samaki zinazovuliwa na wavuvi haramu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, vita dhidi ya uvuvi haramu kama tulivyosema ni vita kwa mtu yeyote ambaye anajihusisha na uvuvi haramu kuanzia uagizwaji wa zana ambazo zinatumika kwenye uvuvi haramu wenyewe, lakini vile vile hata kwenye samaki na biashara ambayo inatokana na uvuvi haramu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, hii vita haimbagui mtu yeyote, haitamwacha mtu yeyote na tayari Mheshimiwa Waziri alishatoa tamko kwamba watu wote wanaojihusisha na uvuvi haramu wamepewa fursa ya ku-surrender vifaa vile kwa sababu kuna operation kubwa. Nimwahidi tu kwamba, hiyo operation itakapokuja itaenda vile vile kwenye viwanda na mtu yeyote ambaye anajihusisha na biashara ya uvuvi haramu.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Kabla ya swali langu la nyongeza, nataka nieleze masikitiko yangu makubwa
kwa jinsi aliyempa Mheshimiwa Waziri taarifa hii alivyoipotosha. Mheshimiwa
Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi namheshimu sana na inabidi kueleza
ukweli kwamba upotoshaji huu, itabidi huyu aliyempa hizi taarifa za uwongo amchukulie hatua. Kwa mfano, hapa ilipoandikwa kwamba, TANAPA
wakishirikiana na WOYOGE Trust Fund wameshajenga birika ni uwongo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza na-declare interest, hii WOYOGETrust
fund mimi ndiyo Mwenyekiti wake. Huu mradi mwaka jana nilimuuliza Waziri wa
Maliasili na Utalii, kwamba wanyama wale wameharibu sana miundombinu
ambayo nilikuwa nimewasaidia wananchi kule kwa ufadhili wa Ubalozi wa Japan
na Waziri akakubali kwamba watarekebisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, basi
nimwambie tu kwamba, Waziri amepotoshwa maana TANAPA hawajaja kujenga
chochote kwanza ndiyo naambiwa mradi umeenda kwenye Bodi na kwamba
hata haujapitishwa. Wamempotosha sana.
Swali langu la nyongeza ni kwamba je, Waziri haoni kuna umuhimu wa
kuweka kituo cha artificial insemination, kwa kuzingatia kwamba madume
yanayopelekwa kusaidia wafugaji yanakufa, maana wafugaji wanayaswaga
nayo yale yanataka yafanyiwe zerograzing? Naomba ajibu swali hilo.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika,
kuhusu taarifa tulizotoa kupishana na taarifa aliyonayo yeye, niko tayari kukaa
naye kuangalia kwa nini yeye ana taarifa tofauti na ile ambayo tunayo kama
Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu artificial insemination ningependa
kumjulisha Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari huduma za artificial insemination
zinatolewa karibu kabisa na Jimboni kwake akifika tu kituo cha Tengeru, huduma
hizi zinaweza kupatikana vilevile niko tayari kukaa naye na kumwelekeza zaidi
namna ya wafugaji wake watakavyoweza kunufaika na huduma hii.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa
kunipa nafasi. Jimbo la Same Mashariki ni Jimbo ambalo lina ardhi nzuri kwa
kilimo cha tangawizi: Je, Mheshimiwa Waziri kwa nini huoni sababu wataalam
wake kushirikiana na wataalam wa TANAPA kuwapa elimu wananchi wa eneo
hili wakalima kilimo cha tangawizi ambacho hakidhuriwi na mifugo,
tukaondokana na mzozo wa wakulima na wafugaji?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni
kweli kabisa kama alivyosema kwamba eneo la Same kutokana na hali ya hewa na aina ya udongo inafaa sana kwa zao la tangawizi, tayari Wakulima wa Same
ni wakulima mahiri wa zao la tangawizi, na tayari Serikali kwa kushirikiana kwa
karibu sana na aliyekuwa Mbunge wa Same Mheshimiwa Anne Kilango
Malecela, ambaye tunashukuru amerudi kwenye Bunge hili walishajenga
kiwanda kwa ajili ya kuchakata tangawizi kama njia ya kuwaongezea wakulima
faida zaidi.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kama alivyosema kwenye jibu lake la msingi kwamba kituo hiki kinafanya tafiti mbalimbali lakini wanashindwa kuhaulisha yale maarifa wanayopata kwenye tafiti zao kwa wakulima kwa sababu hawana fedha za kutosha za kuweza kwenda kwa wakulima Mtwara, Lindi na Pwani na kuwapa matokeo mapya ya utafiti. Serikali ina mpango gani wa kukiongezea fedha kituo hiki ili waweze kuwafikia wakulima wengi wa korosho? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kiuatilifu muhimu katika uzalishaji wa zao la korosho ni sulfur dust. Napenda kujua mpango wa muda mfupi wa Serikali wa kuhakikisha kwamba inawashawishi wawekezaji wakubwa waje kujenga kiwanda cha kutengeneza sulfur Mikoa ya Lindi na Mtwara ili sulfur hiyo iuzwe kwa bei ya chini kama ilivyo sasa hivi kwa viwanda vya mbolea badala ya kuagiza sulfur hii kwa fedha nyingi za kigeni kutoka nchi za nje?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kumekuwepo na changamoto ya kibajeti itakayowezesha Kituo cha Naliendele kuhaulisha teknolojia ya korosho kwa wakulima na Serikali mwaka hata mwaka bado inaendelea kuongeza bajeti, lakini lazima niseme kwamba mafanikio makubwa ambayo tumepata kwenye zao la korosho na hasa katika msimu uliopita umechangiwa vilevile na teknolojia ambayo imetoka Naliendele. Kwa hiyo, nakubali kwamba kuna haja ya kuongeza bajeti na Serikali iko tayari kufikiria katika bajeti inayokuja lakini lazima vilevile tuseme kwamba pamoja na changamoto hiyo Naliendele imesaidia sana katika kukuza zao la korosho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ujenzi wa kiwanda cha sulfur, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba namna mojawapo ya kupunguza gharama kubwa za sulfur kwa wakulima wetu ni kuhakikisha kwamba tunazalisha katika viwanda vyetu vya ndani. Nipende tu kumhakikishia Mheshimwa Mbunge kwamba tayari Mheshimiwa Waziri wa Viwanda anafuatilia ujenzi wa kiwanda cha sulfur akishirikiana na Mheshimiwa Hawa Ghasia. Kwa hiyo, tunatumaini kwamba kitakapojengwa changamoto hii itakuwa imeondoka.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami napenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri swali dogo la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama lilivyo swali la msingi, kwa zao la kahawa na migomba kuna ugonjwa uitwao mnyauko kwa jina lingine unaitwa ugonjwa wa manjano. Ugonjwa huu umeshambulia migomba pamoja na kahawa. Je, Serikali imefanya utafiti upi ili kulipatia ufumbuzi zao hili lisije likapotea?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba kati ya magonjwa ambayo yameleta changamoto katika zao la migomba na kahawa ni ugonjwa wa mnyauko na kwa kipindi fulani umeleta matatizo makubwa sana katika Mkoa wa Kagera. Serikali ilichukua hatua mahsusi za kutafuta namna ya kuzuia ugonjwa huo na tayari kwa kiasi kikubwa kwa sababu ya kampeni kubwa iliyofanyika kuudhibiti, Serikali ilishaudhibiti na sasa hali siyo mbaya sana.
MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, tarehe 16 Desemba 2016, wadau wote wa zao la tumbaku walikuwa na mkutano Morogoro na mgeni rasmi alikuwa ni Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Dkt. Tizeba. Katika mkutano huo vyama vililalamika kuhusiana na kuwa na madeni ya muda mrefu yanayowasababishia kukosa mikopo ya pembejeo kwenye mabenki. Mheshimiwa Waziri alitoa tamko kwenye mkutano huo hapo Morogoro kwamba mabenki sasa wachukue yale madeni ya muda mrefu badala ya kuvibebesha mizigo vyama vya msingi yapelekwe moja kwa moja kwa mwanachama au mkulima mmoja mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikitika kwa msimu huu, mabenki hayajatekeleza agizo la Mheshimiwa Waziri kutaka madeni yale yaelekezwe kwa mtu mmoja mmoja badala ya vyama. Je, nini kauli ya Serikali kwa wakulima wa vyama vya msingi kwenye zao hili la tumbaku waliokosa mkopo wa pembejeo kwenye msimu huu wa 2016? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, kilimo cha tumbaku kinahitaji utunzaji wa mazingira na kwa mujibu wa kanuni ya zao hili kila mkulima anatakiwa kwenye hekta moja anayopanda tumbaku apande miti 150 na miti 200 apande kwenye mashamba yanayomilikiwa na vyama vya msingi. Kwenye Halmashauri yetu ya Uvinza vyama vya msingi tulivyonavyo vinahitaji jumla ya hekta 240 sawa na hekari 600. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuvisaidia vyama vya msingi vya zao la tumbaku kupata maeneo ya kupanda miti?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kama alivyoeleza kwamba mwaka jana Mheshimiwa Waziri alitoa kauli ya kuelekeza namna bora ya kulipa madeni ya muda mrefu yanayovikabili vyama vya msingi na alielekeza kwamba ufanyike utaratibu ili madeni yale yaweze vilevile kulipwa na wale wanaodaiwa moja kwa moja badala ya kuleta mzigo kwenye chama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado huu ndiyo msimamo wa Serikali. Serikali itaendelea kufuatilia kwamba kwa nini hili halijatokea kama ilivyotakiwa kwa sababu tunaamini kuendelea kuvibebesha vyama vya msingi mzigo ndiyo chanzo cha vyama hivyo kuporomoka na hatimaye zao la tumbaku kuanguka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utunzaji wa mazingira, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge ana uelewa mzuri sana kuhusu namna zao la tumbaku linavyotakiwa kuendeshwa kwamba ili uweze kuzalisha tumbaku ambayo ina vigezo vya kimataifa lazima iwe environmentally compliant (ikidhi vigezo vya mazingira) na ndiyo maana kuna hitaji la kupanda miti. Nitaongea na Mheshimiwa Mbunge ili niangalie namna ya kuongea na Halmashauri za Mkoa wake kuhusu namna ya kupata ardhi kwa ajili ya kupanda miti hiyo ambayo inatakiwa kwa ajili ya zao la tumbaku.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, nina swali moja la nyongeza. Kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri ameonyesha kwamba wako mbioni kujenga ghala mjini Sumbawanga lakini ameonyesha na sehemu mbalimbali ambazo ni centre, ni sehemu za mijini mijini. Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme kwamba kwa upande wa Sumbawanga ambako barabara sasa inaimarika an kutokana na hali ya hewa nzuri, maeneo ya uzalishaji zaidi yako Wilayani. Je Serikali haioni kwamba iweke mkazo katika kujenga maghala katika maeneo ya uzalishaji kama vile Nkasi, Sumbawanga Vijijini, Kalambo, Matei kule maana yake kuna barabara za lami ili iweze kupunguza pia hasara ya kwenda kuyafuata mazao hayo na kuleta Sumbawanga?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba mara nyingine kumekuwa na changamoto ya kuweka huduma ya maghala kwenye maeneo ambayo hakuna uzalishaji, lakini kwa sasa kwa sababu bado hatuna maghala mengi, Wizara inaweka maghala kwenye maeneo ambayo yako katikati katika maeneo ambayo ni rahisi kuweza kupata mazao kutoka kwenye Wilaya mbalimbali. Lakini kadri uwezo utakavyoongezeka, nia ni kujenga katika Wilaya zote tuwe na maghala ya kuweza kuhifadhi chakula.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kimsingi swali langu linafanana na swali namba 107 linakwenda Wizara ya Kilimo. Kimsingi ninataka kufahamu, tukiwa tunaelekea kwenye uuzaji wa korosho msimu uliopita tumeshuhudia Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Mtwara (MAMKU) viongozi wake, watendaji wakuu wakishikiliwa kwa ajili ya uchunguzi kutokana na ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala hili pia limejitokeza katika vyama vikuu vya TANECU, Lindi Mwambao, Ilulu pamoja na Chama Kikuu cha Mkoa wa Pwani. Tumeona Mheshimiwa Waziri Mkuu akichukua hatua kwa viongozi hawa wa Chama Kikuu cha MAMCU sasa tunataka kufahamu kutoka kwa Waziri amejipangaje na yeye kuwachukulia hatua viongozi wa vyama vikuu nilivyovitaja kwa sababu ya kudhulumu na matumizi mabaya ya pesa za wakulima za korosho katika Mikoa ya Mtwara, Lindi pamoja na Pwani? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kama alivyosema katika msimu uliopita wa korosho kumekuwepo na changamoto nyingi sana kuhusu malipo kwa wakulima wa korosho na ndiyo maana Waziri Mkuu alichukua hatua ya kuhakikisha kwamba sheria inachukua mkondo wake kwa watu wa MAMCU, lakini vilevile mtunza ghala wa Chama cha Msingi cha Ushirika ambapo kosrosho ziliweza kupungua bei na tunavyozungumza tayari wahusika wamefunguliwa kesi ya kuhujumu uchumi na kesi inaendelea mahakamani, lakini vilevile tunawahakikishia wakulima wale ambao wamepata changamoto hiyo ya fedha zao kutolipwa kwa kiwango ambacho kilitarajiwa kwamba Chama cha Ushirika ambacho kilisababisha korosho zile ziweze kuingia kwenye sales catalogue wao watalazimika kurudisha ile tofauti ili mkulima asije akapata tatizo lolote. Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tunafahamu kwamba changamoto iliyotokea Mtwara lakini vilevile Nanyumbu tunafahamu vilevile imetokea Mkoa wa Pwani kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari Serikali inachunguza changamoto hizo, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara kashafanya uchunguzi huo na tumepata repoti.Lakini vilevile Waziri Mkuu mwenyewe aliagiza ufanyike uchunguzi wa kina na repoti iko tayari Serikali inapitia taarifa zile ili wale wote ambao wamehusika wakiwemo viongozi na watumishi wa MAMCU, TANECU na vyma vingine vya ushirika kama KORECU ambao watakuwa wamehusika watachukuliwa hatua za kisheria. Cha maana zaidi, wakulima wale ambao hawakupata malipo stahiki kwa sababu ya vurugu au uzembe wa watumishi wa Vyama Vikuu au Vyama vya Msingi tunawahakikishia kwamba fedha zao zitalipwa.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize swali moja la nyongeza. Kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa ina upungufu mkubwa sana wa chakula pamoja na Wilaya za Mkoa wa Dodoma na Mkoa wa Singida; na kwa kuwa Serikali imekiri kwamba kuna Halmashauri za Wilaya 55 ambazo zina upungufu mkubwa sana wa chakula na Serikali ina chakula cha kutosha kwenye maghala. Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni lini Serikali itaanza kusambaza chakula cha bei nafuu kwasababu hivi sasa debe la mahindi ni shilingi 20,000 na mfuko wa sembe ni shilingi 40,000 ni lini Serikali itaanza kusambaza chakula cha bei nafuu Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa pamoja na hizi Halmashauri 55?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Waheshimiwa Wabunge, kama mnavyokumbuka tulishakuja kwenye Bunge hili mapema kueleza na kutoa taarifa ya tathmini ya kina ambayo Wizara imefanya kuhusiana na usalama wa chakula na katika taarifa ile kama mlivyosikia Waheshimiwa Wabunge tuliweza kuainisha maeneo ambayo yana upungufu mkubwa, lakini vilevile katika taarifa ile tulieleza kwamba Serikali imejidhatiti vilivyo kuhakikisha kwamba upungufu ambao unaelekea kutokea kati ya mwezi Januari na Aprili kwamba utashughulikiwa. Mheshimiwa Mwenyekiti, nimahakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba taratibu zinaendelea ili kuhakikisha maeneo yale ambayo yana upungufu kwamba wananchi wanapata chakula cha bei, nafuu kwa hiyo, naomba uvute subira taratibu zinaendelea.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda kuuliza maswali ya nyongeza mawili kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, tatizo la upatikanaji wa
pembejeo kwa zao la pamba ni la muda mrefu sana karibu miaka 17 au 20. Ni lini sasa Serikali itakuwa na mikakati maalum ya kumaliza tatizo hili la pembejeo kwa wakulima wa pamba kwa sababu limekuwa sugu kwa muda mrefu?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; ni muda mrefu sana Serikali tumekuwa tukipandisha bei ya pamba kwa kutegemea soko la dunia. Ni lini sasa Serikali itatengeneza mkakati wa kupata bei ya wakulima wa pamba kwa kutegemea soko la ndani?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuboresha upatikanaji wa pembejeo za pamba. Hatua mojawapo ambayo imeshafanyika ni kuanzishwa kwa Mfuko Maalum wa Wakfu wa Pamba (CDTF), ambao kazi yake kubwa ni kugawa na kuhakikisha pembejeo zinapatikana kwa bei nafuu kwa wakulima wa pamba, kazi ambayo tayari imekuwa ikiendelea kwa miaka kadhaa sasa.
Mheshimiwa Spika, lakini vilevile Serikali inaendelea na mpango wa kuvifufua na kuboresha utendaji wa vyama vya ushirika ili viweze kusimamia upatikanaji wa pembejeo katika maeneo hayo. Jitihada hizi zinahusisha kwa mfano kufufua Chama cha Ushirika cha Nyanza ili kiweze kufanya kazi kuwasaidia wakulima wa pamba lakini vilevile vyama vingine kama SHIRECU, navyo vilevile kazi ya kuvifufua
inaendelea.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na namna gani Serikali inaendelea kuboresha soko la ndani, napenda kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba, mkakati tulionao kwa sasa
ni ule wa mwaka 2016-2020 wa kujaribu kuhakikisha tunaboresha mnyororo mzima wa thamani kutoka kwenye pamba hadi kufikia kwenye nguo. Katika mkakati huo, Serikali
inahakikisha kwamba tunajenga viwanda na kuhamasisha ujenzi wa viwanda ndani ili nguvu kubwa isielekezwe tena katika kutafuta soko la nje bali kutumia soko la ndani ambalo tunaamini tunalo. Kwa sababu kwa idadi ya Watanzania
iliyopo kama tutaweza kutengeneza nguo ambazo zitatumika ndani, tunaamini kwamba bei ya pamba itaendelea kuimarika.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa, zao la pamba linafanana kabisa na matatizo ya zao kubwa la tumbaku la Mkoa wa Tabora; na
kwa kuwa, Mkoa wetu wa Tabora unategemea sana zao la tumbaku. Zao la tumbaku limekuwa na tozo kuanzia 19 mpaka 38 zinazomuumiza mkulima wa tumbaku na kusababisha mkulima huyu faida yake yote kwenda kwenye matozo 38. Je, Serikali ina mpango mkakati gani wa kuhakikisha inapunguza tozo hizi ili mkulima wa tumbaku apate faida kama ilivyopunguza tozo kwenye kilimo cha korosho?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba, kati ya changamoto ambazo wakulima wa mazao hapa nchini wanapata ni tozo nyingi ambazo zinaendelea kuongeza changamoto kubwa
katika uendeshaji wa kilimo. Namwomba Mheshimiwa Mbunge asubiri kusikia hotuba ya bajeti yetu kwa sababu mwaka huu wa fedha unaokuja, Wizara imeamua kuondoa karibu nusu ya tozo zote ambazo ziko kwenye mazao.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, sitaki kuwahi kuanza kueleza yaliyoko kwenye hotuba yetu ya bajeti, lakini nimweleze tu kwamba Serikali tayari ilishatambua changamoto hiyo; viongozi wetu wakuu, Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Makamu wa Rais na Mheshimiwa Waziri Mkuu kila wakati wamesisitiza kwamba tuondoe tozo hizo. Kwa
sasa Wizara imeondoa tozo kwa 50% lakini kama
ninavyosema tukija na maelezo yetu ya bajeti ataona ni tozo gani zimepungua.
Mheshimiwa Spika, vilevile Mheshimiwa Mbunge
atakumbuka kwamba, hivi karibuni katika jitihada za kuondoa changamoto zilizopo kwenye zao la tumbaku (Tabora), Mheshimiwa Waziri Mkuu alienda kule na anajua yaliyotokea kule. Sasa changamoto ya chama kikubwa cha WETCU kuweza kuhudumia vizuri wakulima tayari
inashughulikiwa pamoja na mambo mengine kwa kugawa iwe ni vyama viwili lakini vilevile ubadhirifu ambao umefanyika tayari wahusika wameshachukuliwa hatua.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kimsingi kuna mikakati mingi ambayo inaendelea ya kuhakikisha kwamba tunaboresha zao la tumbaku. Vilevile nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba Jumamosi hii tumeitisha Mkutano wa Wadau wa Tumbaku na nachukua nafasi hii kumkaribisha tarehe 7 kwenye huo mkutano ili aangalie ni
mikakati gani mbayo tumeweka. Nashukuru sana.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika,
nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Kwa kuwa, zana alizozitaja Mheshimiwa Naibu Waziri zinatumiwa zaidi na wanaume na zinarahisisha zaidi kazi kwa
wanaume, hususan, kwenye kaya zenye uwezo. Je, Serikali ina mkakati gani wa kutoa zana ambazo zitamrahisishia mwanamke kulima mwenye kipato duni kama ninavyomwona mwanamke aishiye Mkoa wa Simiyu? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili. Ilani ya Chama cha Mapinduzi imekusudia kutoa ajira zaidi. Kwa kupitia malighafi za mazao, si tu ajira zitatoka katika viwanda bali pia katika mazao ambayo yatauzwa na wakulima. Je, Serikali
ina mkakati gani wa kuhakikisha inatoa mbegu ambazo zitaleta tija katika kilimo cha mtama na alizeti katika Mkoa wa Simiyu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Spika, jitihada mbalimbali ambazo Serikali inachukua kuboresha kilimo za kugawa na kuleta zana za kilimo zinawasaidia wakulima wote wakiwemo na wanawake. Tunaamini kwamba tukiweza kuwa na zana za kilimo za kisasa, wanufaika wa kwanza watakuwa ni wanawake kwa sababu wao hasa ndio kwa kiasi kikubwa
wanajihusisha na kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini vilevile Wizara kupitia Mfuko wa Pembejeo imeweka utaratibu wa kuweza kukopesha zana za kilimo kwa bei nafuu na wanawake kwa kupitia vyama vya ushirika lakini vikundi mbalimbali ni wanufaika wakubwa wa huduma hii. Vilevile Wizara kwa kupitia Benki
ya Maendeleo ya Kilimo inatoa mikopo kwa ajili ya pembejeo. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge aweze kuwasiliana na sisi ili kuwaunganisha akinamama wakulima
wa Simiyu ili waweze kupata huduma hii.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na kugawa mbegu za mtama na alizeti, katika mwaka wa fedha unaokwisha na hasa baada ya changamoto ya mvua kutokuwa nzuri, Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali iligawa zaidi ya mbegu milioni 14 za mtama. Vilevile tumegawa mbegu za alizeti kwa wakulima mbalimbali nchini wakiwepo na wakulima wa Mkoa wa Simiyu.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kwa kuwa matatizo yaliyopo Simiyu yanafanana sana na matatizo yaliyopo Mkoa wa Geita na Kagera, Serikali imetangaza wafugaji watoke kwenye Pori la
Kimisi na Burigi na wakatii sheria. Sasa wale askari wanaoendesha ile operesheni wanazifuata ng’ombe vijijini kilometa saba mpaka kumi na kuzirudisha porini na baadaye kuwafilisi wananchi hawa. Je, ni nini kauli ya Waziri kuhusiana
na uonevu unaoendelea kule Burigi na Kimisi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Spika, ni kweli kama alivyoeleza kwamba tayari katika zoezi linaloendelea la kuondoa mifugo katika misitu na hifadhi kuna changamoto ambazo zimeripotiwa. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara imepokea changamoto hizo na inaendelea kujadiliana ndani ya Serikali kuangalia namna ya kuzitatua kwa muda mfupi.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, jibu la Mheshimiwa Waziri halijaniridhisha. Bodi ya Chai Rungwe imeweka wanunuzi wa chai wa aina mbili, wako WATCO na Mohamed Enterprises. Mohamed Enterprises amekuwa akinunua chai ya wakulima kwa bei nzuri na
WATCO ikawa inanunua chai kwa bei ya chini, lakini cha kushangaza Serikali ikaamua kumwambia Mohamed Enterprises aombe kibali upya, mpaka sasa tunaongea Mohamed Enterprises hana kibali cha kununua chai ya
wakulima na hii inapelekea wakulima kuuza kwa bei inayotaka Serikali ambayo ni ya chini.
Swali langu la kwanza, Serikali iko tayari kuvunja Bodi hiyo ili tuweze kupata watu tunaowaamini watakaotetea
wakulima wa chai wa Rungwe? (Makofi)
Swali langu la pili; Serikali iko tayari na Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuongozana na mimi kwenda kuonana na wakulima wa chai na kusikiliza kero za wakulima wa chai wanavyoteseka kwa muda mrefu? Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Spika, naomba nianze na hilo la pili, nitakuwa tayari kuandamana naye muda wowote kuanzia sasa kwenda kusikiliza kero za wakulima wa chai. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali la nyongeza la kwanza, kama nilivyoeleza bei ya chai hupangwa kwenye mkutano wa wadau ambayo kawaida inakuwa ni bei ambayo tunasema ni bei dira. Maana yake ni bei ambayo hairuhusiwi mtu yeyote kumlipa mkulima chini ya hapo, lakini
Kanuni za zao la chai zinaruhusu majadiliano yafanyike kati ya mkulima na mnunuzi, maana yake wanaweza wakakubaliana bei kuwa juu ilimradi isije ikawa chini ya kile ambacho kimewekwa kama bei dira. Kwa hiyo, tofauti anayoiona Mheshimiwa Mbunge kuhusu wanachotoa WATCO na Mohamed Enterprises
inatokana na majadiliano yale ya ziada ambayo kanuni inaruhusu.
Mheshimiwa Spika, vilevile ningependa kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kwamba tofauti ya bei hutokana na ukweli kwamba kunakuwa na tofauti ya ubora wa chai moja kutoka mkulima mmoja hadi mwingine, kwa hiyo mara nyingine kuna makampuni yanaamua kulipa kitu tunachoita bonus au malipo ya ziada kutokana na ubora wa chai, ndiyo maana tunaendelea kuwashauri wakulima wetu wajaribu kulima chai kwa viwango vinavyotakiwa ili kuwa na ubora ambao utawafanya wapate bei nzuri zaidi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kuvunja Bodi ya Chai kwa sababu hiyo, katika hali kama hii inakuwa ni vigumu kusema kwamba wao wanahusika moja kwa moja, kama nilivyosema kama Mheshimiwa Mbunge haridhiki na majibu ambayo nimeyatoa niko tayari kukutana naye ili niendelee kumuelewesha zaidi, pia kuandamana naye kwenda kwa wakulima wa chai.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Kwa vile tatizo la Rungwe ni sawasawa na tatizo linalowapata wakulima wa tangawizi wa Jimbo la Same Mashariki na kwa vile wakulima hao walipata tatizo kubwa tangu walivyosaidiwa na SIDO mpaka leo kiwanda hakifanyi kazi na wameshauriwa kwamba waunde Kampuni na LAPF wamekuwa tayari kusaidia kuingia
katika Kampuni hiyo. Je, Wizara inawezaje kuwasaidia hawa wakulima ili wasije wakaingia tena katika tatizo walilolipata ambalo mpaka leo kiwanda hakijaweza kufanya kazi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Spika, Serikali au Wizara iko tayari kukutana na Mheshimiwa Mbunge pamoja na wakulima wa tangawizi ili kuangalia namna gani bora wanaweza wakatumia hicho kiwanda kwa manufaa yao na hivyo kuondokana na matatizo ambayo yameshatokea huko nyuma.
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Spika,
nashukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza. Kwa vile viwanda vya chai vipo Mufindi na katika majibu ya Waziri ameeleza vizuri sana viwanda vya Unilever na Mufindi Tea Company na ni kweli kabisa kwamba wakulima wa Mufindi wanapata shida sana kuhusiana na
bei ya chai na makampuni makubwa yanakopesha wakulima mbolea halafu wanakatwa kwenye bei ile ya chai mwisho wa siku wale wakulima hawapati kitu chochote.
Je, Serikali haioni kwamba kuna umuhimu wa
wakulima wadogowadogo wale wa Mufindi Serikali ikasimamia wakajenga kiwanda chao, badala ya kuuza majani mabichi waweze kuuza majani makavu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa kwamba kuuza majani ghafi husababisha bei kuwa ndogo na ndiyo maana Serikali ya Awamu ya Tano inaweka jitihada katika uchumi wa viwanda. Tunaamini kwamba tutakapojenga viwanda vingi
maana yake wakulima wetu watakuwa na faida zaidi. Kwa hiyo, Wizara iko tayari kushirikiana na wakulima wa Mufindi na wakulima wa chai wa maeneo mengine ili kuendelea kuongeza viwanda vya chai tuweze kufanya uchakataji badala ya wakulima kuendelea kuuza chai ghafi. Nakubaliana nae kwamba ni kitu na Wizara itafuatilia.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kadri ya muuliza maswali, kipengele namba (c) kinasema je, Serikali ipo tayari kusimamia wananchi walipwe fidia kutoka kwa wawekezaji wanaoingiza vifaranga wasio na chanjo toka nchi za nje?
Kimsingi kwenye jibu lake haja-commit, hajasema kama Serikali sasa hivi iko tayari kuhakikisha wafugaji wale wanaopata hasara wanalipwa fidia yao, kwa hiyo tunaomba Serikali itoe neno kwenye hili. Pia itueleze kama hali ni hii basi izuie kabisa watu wasiingize vifaranga ambavyo havina chanjo.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kutokana na kuongezeka kwa gharama za uzalishaji hasa wa chakula kama alivyosema yeye mwenyewe na tumeona gharama kubwa sana kwenye chakula cha mifugo. Kwa kipindi hiki ambapo kuna tatizo kubwa la chakula na njaa, Serikali haioni sasa umefika wakati iondoe angalau kodi fulani ili kuweza ku-compensate wakulima katika kupata chakula chenye bei nafuu na wananchi waweze kununua kuku kwa bei nafuu?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu fidia, kimsingi suala la fidia halitokei kwa sababu kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, kimsingi ni kinyume cha sheria na taratibu kuingiza kuku na mayai kutoka nje, kwa hiyo wale ambao
wanaingizwa kwa taratibu ambazo sio rasmi, wanaingizwa kwa utaratibu wa njia za panya. Kwa hiyo, kimsingi Serikali imeweka utaratibu kuhakikisha kwamba hairuhusu uingizwaji, hivyo kutokea na ndiyo maana tumesema tayari
katika kipindi cha miaka minne tumeteketeza vifaranga zaidi ya 67,000. Hata hivyo, tunachotaka kutoka kwa Mheshimiwa Mbunge ni kuonesha ushirikiano kama wanaweza wakatuonesha watu ambao wanaingiza vifaranga na mayai kinyume na taratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na gharama ya vyakula vya mifugo, hasa kuku, kama nilivyosema vilevile ni kweli kwamba kuna gharama kubwa sana katika kutengeneza vyakula vya kuku kwa sababu kiinilishe kinachotumika ni maharage ya soya ambayo hatuzalishi hapa nchini. Kwa hiyo, hatua ambazo tunazichukua ni
pamoja na kuhamasisha wananchi walime zao la soya.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kupitia hotuba ya bajeti ya Wizara yetu kwa ajili ya mwaka wa fedha unaokuja, Serikali imechukua hatua kadhaa kupunguza kodi na tozo za mazao na bidhaa mbalimbali ili basi vyakula vya kuku na mazao mengine viweze kupatikana kwa bei nafuu. Kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba suala la kodi na tozo litashughulikiwa.
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza:-
Swali la kwanza, kwa kuwa tatizo la pembejeo
limekuwa la muda mrefu na ni sugu katika Mkoa wetu wa Njombe. Je, Serikali iko tayari sasa kuanzisha Kiwanda cha kutengenezea mbolea katika Mkoa wa Njombe?
Swali la pili, kwa kuwa Mkoa wa Njombe ni kati ya
Mikoa inayotoa viazi au inayolima viazi kwa wingi; Njombe peke yake inalima au inatoa viazi tani 900,000 kwa mwaka, lakini tatizo ni kwamba soko limeingiliwa na watu wa Kenya.
Je, Serikali iko tayari sasa kuwazuia watu wa Kenya wasilete viazi nchini Tanzania ili wakulima wetu wa viazi waweze kuwa na soko zuri?
NAIBU WAZIRI KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na Serikali kujenga Kiwanda cha Mbolea Njombe; Serikali ya Awamu ya Tano inahamasisha ujenzi wa uchumi wa viwanda, kwa hiyo, tuko tayari kushirikiana na Mbunge pamoja na wadau wengine wowote ambao wanataka kuanzisha Kiwanda cha Mbolea- Njombe. Vilevile ni lazima niseme kama nilivyosema, tunategemea bei ya pembejeo ishuke kuanzia mwaka unaokuja kwa sababu karibuni tutaanza utaratibu wa kuagiza mbolea kwa pamoja (Bulk Procurement). Kuhusiana na suala la ushindani wa Wafanyabiashara kutoka Kenya; kimsingi tunabanwa na itifaki za Kikanda kuhusiana na biashara, kwa hiyo ni vigumu moja kwa moja kuwazuia wakulima wa Kenya isipokuwa tunachofanya ni kujenga mazingira ambayo wakulima wetu wanaweza wakazalisha kwa tija ili waweze kushindana na wafanyabiashara wengine kutoka Kenya.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nipende tu
kumweleza Mheshimiwa Mbunge kwamba ushindani siyo mbaya na mara nyingi Wakenya wanapokuja kununua viazi kutoka kwetu ni kwa sababu kuna tofauti kati ya msimu wa viazi kuzalishwa Njombe na Kenya, kwa hiyo tusiogope
ushindani lakini tujizatiti zaidi tuweze kuzalisha kwa tija ili tuweze kushindana.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu. Pamoja na majibu yako na jitihada kubwa inayochukuliwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu katika kutatua changamoto za zao la tumbaku, naomba niulize maswli ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, msimu wa kuuza tumbaku, yaani msimu wa masoko ya tumbaku ni sasa, ni mwezi huu wa nne, Serikali inatoa kauli gani kuhusu yafuatayo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza uongozi wa AMCOS ambao umefutwa kutokana na agizo la Serikali na kuwaacha bila uongozi kipindi hiki ambacho masoko yanaanza? Serikali inasema nini kuhusu suala hili? Ikiwemo AMCOS ya Utenge na Nsenga ambazo hazina uongozi hadi
sasa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Serikali
inasemaje kuhusu kuwasaidia wakulima ambao
wamejitahidi wao wenyewe kutokukopa, lakini hatimaye wamejikuta wanabebeshwa madeni yasiyowahusu na kuwaacha hoi kiuchumi. Serikali inatoa kauli gani? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uuzaji wa tumbaku katika mazingira ambayo uongozi wa AMCOS umefutwa au umesimamishwa; taratibu zitaendelea kushughulikiwa kwa kupitia Chama Kikuu katika maana hiyo WETCU na kama nilivyokwishsema tayari WETCU imewekewa utaratibu wa mpito, ili kuweza kufanya kazi zake kama kawaida. Kwa hiyo, kama kuna AMCOS ambazo hazina uongozi uuzaji wa tumbaku utaendelea kushughulikiwa na chama kikuu cha
ushirika, lakini vilevile kwa kushirikiana na vyombo vingine kama Maafisa Ushirika, lakini vilevile kwa kupitia watendaji ambao bado wapo kwenye Bodi ya Tumbaku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Mheshimiwa Mbunge ameuliza kuhusu wakulima ambao wanalazimika kubeba mzigo wa madeni ambayo yametokana na wao kuwepo kwenye vyama vya ushirika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kati ya sababu zilizosababisha Mheshimiwa Waziri Mkuu kuchukua maamuzi mazito kuhusiana na WETCU na Bodi ya Tumbaku ni kwa sababu kulikuwa na usimamizi mbovu sana kuhusiana na madeni ya vyama vya ushirika, hali ambayo ilisababisha
wakulima kimsingi kubebeshwa madeni ambayo kwa kiasi kikubwa hata matumizi ya fedha ambazo zimekopwa utaratibu wake haufahamiki sawasawa. Kwa hiyo, hatua ambazo zinachukuliwa ni ili kuondoa hiyo hali, ni ili ifahamike kwamba, mikopo ambayo inachukuliwa inafanya kazi gani, lakini vilevile ni kuwawajibisha wale ambao wamekopa fedha na kuzitumia kwa njia ambazo ni kinyume na taratibu.
MHE. JUMAA H. AWESO: Mheshimiwa Spika, tunapozungumzia suala la minazi ndiyo uchumi na ndiyo maisha ya wananchi wa Pangani. Ukisoma majibu ya sasa wamefanya tafiti lakini hawajajua mdudu ambaye anaeneza ugonjwa huo na wala hakuna tiba kama UKIMWI. Kwa kuwa, mnazi ndiyo uchumi, je, Serikali haioni haja sasa ya kuangalia nchi ambazo zinalima zao hili la mnazi kwa wingi ili kupata ushauri kujua namna gani tunaweza kuokoa zao hili la mnazi. (Makofi) Swali la pili; naomba sasa nipate commitment ya Waziri kwa kuwa tunaona jitihada zinazofanyika mpaka sasa hakuna majibu sahihi yaliyoweza kupatikana. Je, ili kuweza kuwaokoa wananchi wa Pangani kuondokana na umaskini kwa nini wasitupe zao mbadala ili kuhakikisha kwamba badala la mnazi tuwe na zao ambalo linakimu maisha ya wananchi wa Pangani? Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba imechukua muda mrefu sasa mdudu anayeambukiza ugonjwa huo kuweza
kufahamika, lakini zaidi tiba kuweza kupatikana. Wizara na Serikali inaendelea kushirikiana na Taasisi za Kitaifa na
Kimataifa ili kuangalia namna ya kutafuta tiba ya ugonjwa huu.
Mheshimiwa Spika, tunashirikiana na Taasisi za nchi zinazoongoza kwa kuzalisha minazi kama nchi za Indonesia,
Ufilipino, India na Brazil ili kuangalia namna gani ya kuhakikisha kwamba ugonjwa huu tunautokomeza kama nilivyosema. Kwa sasa tunaangalia namna ya kudhibiti ili usiweze kuleta madhara makubwa zaidi wakati tunaendelea kutafuta tiba.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu Serikali kutafuta zao mbadala; nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali na Wizara inafahamu jitihada ambayo yeye pamoja na Mheshimiwa DC Zainab Abdallah wa Pangani wanafanya katika kuleta zao la korosho Pangani. Nilipotembelea Pangani miezi michache iliyopita niliona
jitihada kubwa zinazofanywa na Mheshimiwa Mbunge pamoja na DC na Halmashauri ili kujaribu kuwashawishi na
kuwahimiza wananchi wapande mikorosho kama zao mbadala wakati Serikali inaendelea kutafuta tiba ya ugonjwa
wa minazi.
Mheshimiwa Spika, vilevile Serikali inaendelea kuangalia namna gani tunaweza tukahimiza matumizi ya mazao mbalimbali yanayozalishwa na mnazi. Kwa sababu mnazi ndiyo zao la pekee duniani ambalo hakuna chochote
ambacho hakitumiki, kuanzia mizizi mpaka matunda yote inatumika. Kwa hiyo, tunajaribu kuhimiza kwa mfano
uchakataji wa mbata ili kuweza kutengeneza mafuta ya kupikia na kujipaka. Waheshimiwa Wabunge mnafahamu kwamba mafuta ya nazi hayana lehemu katika maana ya cholesterol wala hayana mzio katika maana ya allergy. Kwa hiyo, tunaangalia uwezekano wa kuendelea kutumia products za mnazi kama njia mojawapo ya kuwasaidia wakulima wa minazi.
MHE. YOSEPHER F. KOMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Katika majibu ya msingi ya Waziri amesema ugonjwa unaotokana na minazi haujapatiwa ufumbuzi. Katika Mkoa wa Tanga, tuna Chuo cha MATI Mlingano, Chuo cha Utafiti. Je, Serikali ina mpango gani wa kukifufua kile chuo ili wakulima wa mazao mengine kama korosho, mkonge, michungwa waweze kupata uhakika wa mazao yao?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Spika, tunafahamu umuhimu wa Chuo na Kituo cha Utafiti cha Mlingano. Mimi mwenyewe katika ziara yangu ya Mkoa wa Tanga nilipata fursa ya kutembelea pale, kuangalia changamoto zilizopo na tayari Wizara iko kwenye mkakati wa kutatua changamoto mbalimbali ambazo tuligundua katika kituo hicho ili iweze kuwasaidia wakulima wa Mkoa wa Tanga na maeneo mengine ya Tanzania katika kuboresha kilimo.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na majibu ya Naibu Waziri ambayo hayaridhishi vizuri, napenda nimuulize maswali madogo mawili ya nyongeza.
Je, Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kwenda kutoa elimu kwa wakulima hawa ili badala ya kutumia hayo magogo ambayo wanasema, basi waweze kutumia hayo matawi ili kuweza kukausha tumbaku zao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kuhakikisha wakulima hawa hawatumii tena kuni kwa sababu wanakata sana miti na badala yake walete hiyo nishati mbadala kwa haraka ili wakulima hawa waweze kuacha kukata miti?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu elimu, Serikali imeendelea kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kutumia majiko sanifu na vilevile athari za mazingira zinazotokana na ukataji wa miti. Kwa hiyo, ni kitu ambacho kimekuwa kikiendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namsihi tu Mheshimiwa Mbunge pamoja na Wabunge wengine wanaotoka maeneo yanayolima tumbaku, waendelee kuwaelimisha wananchi wetu kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira katika kilimo cha tumbaku kwa sababu tumbaku yetu inaweza ikawa na bei nzuri kwenye soko kama tutakuwa na tabia ambazo zinahifadhi mazingira. Inaitwa compliance, ni moja kati ya vigezo vinavyoangalia ubora wa tumbaku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, kwa sasa Serikali inahimiza matumizi ya majiko sanifu na kuanzia msimu huu unaokuja, haitaruhusiwa tena kutumia majiko ya aina nyingine; itakuwa ni lazima kila mkulima atumie majiko sanifu wakati wa kukausha tumbaku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na nishati mbadala, kama nilivyosema, tayari tafiti zimeshafanyika kuangalia kama umeme na makaa ya mawe yanaweza yakawa nishati mbadala, lakini kwa sasa ilionekana kwamba nishati hizo zinakuwa na gharama kubwa kwa mkulima. Kwa hiyo, njia ambayo inaoneka ni ya gharama nafuu lakini vilevile ni rafiki kwa mazingira, ni kutumia majiko sanifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunamwomba Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wengine waisaidie Serikali kuendelea kuhimiza wakulima wetu watumie njia hiyo wakati wa kukausha tumbaku.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri na Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya ngongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia 75 ya wakulima hapa Tanzania wakiwemo wakulima wa Mkoa wa Morogoro wanategemea kilimo kwenye uchumi wao. Serikali ina mkakati mzuri wa kupunguza bei kwenye mbolea kusudi iweze kuwa nafuu kwa wakulima. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuanzisha viwanda vya mbolea hapa nchini sambamba na Kiwanda cha Minjingu na Kiwanda cha Mtwara kinachotegea kujengwa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, mbolea hasa ya DAP pamoja na UREA ni mbolea ambayo zinatumika sana kwenye kilimo chetu, DAP ikiwa ni mbolea ya kupandia na UREA ikiwa ni mbolea ya kukuzia. Hapa nchini tuna mbolea ya Minjingu ambayo inazalishwa Manyara.
Je, mbona haijawekwa kwenye mkakati huu kusudi wananchi waweze kupata hamasa ya kutumia mbolea ya Minjingu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la Serikali kuanzisha viwanda, ni kweli kabisa kwamba Serikali ya Awamu ya Tano moja kati ya mikakati yake ya kuendeleza uchumi ni kuhakikisha kwamba kunakuwa na viwanda nchini. Kwa hiyo, Serikali imekuwa ikihimiza na kuweka mazingira wezeshi ili sekta binafsi na wadau wengine waweze kuanzisha viwanda nchini. Kwa sasa Serikali iko katika mikakati ya kushirikiana na sekta binafsi kuanzisha kiwanda cha mbolea Mkoani Lindi kwa kutumia gesi; na utaratibu huo ukikamilika, tunaamini kwamba mahitaji mengi ya mbolea yatakuwa yamepata suluhu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna kiwanda cha mbolea kinajengwa Kibaha, kwa hiyo, tunaamini kwamba kadiri miaka inavyokwenda, tutakuwa tunazalisha mbolea zetu humu nchini, kuliko kuagiza ambayo inatusababishia kuwa na gharama kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba katika utaratibu wa bulk procument (uagizaji wa mkupuo) tunaanza na mbolea za DAP na UREA, lakini baadaye tutaingia kwenye mbolea nyingine kama NPK na mbolea nyingine ambazo zinatumika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kwa nini hatujaweka mbolea ya Minjingu katika utaratibu huu? Ukweli wa mambo ni kwamba tunapozungumzia kuhusu uagizwaji wa mkupuo, tunazungumzia kuhusu mbolea kutoka nje.
Hata hivyo, bado kuna fursa ya kuendelea kuhimiza kiwanda cha Minjingu kiongeze uzalishaji, kwa sababu kwa sasa uwezo wao kwa mwaka ni tani 50,000 wakati mahitaji yetu ya mbolea ya aina hiyo kwa mwaka ni zaidi ya tani nusu milioni. Kwa hiyo, vilevile kuna suala la uwezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Serikali iko tayari kushirikiana na Minjingu waongeze uzalishaji ili mbolea yao iweze kutumika kwa wingi zaidi.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri na pamoja na kazi nzuri ambayo imeanza kufanywa ya kusaidia kuongezeka kwa bei ya zao la korosho kwa Mikoa ya Lindi, Mtwara na Pwani ambao ni wakulima wazuri wa korosho, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, je, Serikali haioni sasa umefika wakati wa kuweka kiwango cha elimu kwa viongozi wanaoongoza Vyama vya Msingi, kwa sababu ni moja ya changamoto kubwa sana ambayo imesababisha migogoro mikubwa kwenye Vyama vya Msingi na inasababisha hasara kubwa kwa wakulima wakorosho? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, moja ya changamoto kubwa kwenye biashara ya korosho ni utaratibu wa wanunuzi wa korosho kutengeneza cartel, kutengeneza muungano wa pamoja ambao unakwenda kuathiri bei ya mnada kwenye ununuzi wa korosho. Sasa Serikali inachukua hatua gani kukomesha utaratibu huu? Kwa sababu kwa kweli, kwa namna moja ama nyingine umeathiri sana wakulima wa zao la korosho na bei inaendelea kushuka kila kunapokucha na hata sasa ambapo bei imekwenda vizuri, msimu ujao mpango huu wa cartel ukiachiwa ukaendelea, wakulima wetu wataendelea kupata umaskini na nchi yetu haitasonga mbele.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuungana na Mheshimiwa Nape kwamba zao la korosho ni zao la muhimu sana kwa mikoa inayolima hususan Mikoa ya Lindi na Mtwara. Katika msimu uliopita mikoa sita inayolima korosho, kwa uchache waliweza kuingiza shilingi bilioni 700 katika kipindi kifupi kwa ajili ya kuuza korosho. Yote imetokana na jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano ya kuendeleza zao la korosho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba, kiwango cha elimu kwa Watumishi wa Vyama vya Ushirika, ni kitu kikubwa. Kimsingi tunategemea kurekebisha sheria ili kuweza kuongeza kiwango hicho, lakini tunasisitiza vilevile kwamba elimu pekee siyo kigezo, tunahitaji watu waadilifu, lakini zaidi watu ambao wanafahamu taratibu za tasnia ya korosho inavyoendeshwa. Kwa hiyo, tutaleta marekebisho, lakini vilevile tutaangalia vitu vingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na namna ya kudhibiti cartel, kwa kutambua kwamba huko nyuma wanunuzi walikuwa wanatumia utaratibu huo wa cartel kuharibu bei ya korosho, kwa sasa tunaendesha minada kwa uwazi zaidi ili isitokee watu wakatengeneza utaratibu na watumishi wa Ushirika, vilevile na wa Vyama vya Ushirika wasio waaminifu ili kujitengenezea utaratibu ambao wanunuzi ni hao hao na hivyo kuweza kuharibu bei.
Kwa hiyo, kwa sasa kuna utaratibu wa kuuza korosho kwa uwazi zaidi, lakini vilevile pale mnunuzi atakaposhinda zabuni ya kununua korosho inatakiwa aweke dhamana ili baadaye asije akaacha kununua ili baei ije ishuke. Kwa hiyo, utaratibu huo unashughulikiwa.
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri na yenye matumaini kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa muda mrefu unaosemwa na Serikali, umesemwa kwa miaka mingi sana. Hata mwaka 2015, Rais wetu mpendwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli katika kampeni zake alisema hakuna zao lenye tozo na kodi za ajabu ambazo hazi-exist duniani kama zao la kahawa, alisema lina kodi 26. Mwaka jana ametoa kodi moja tu ya usindikaji wa kahawa dola 250, bado kuna kodi 25, hatuoni commitment ya Serikali kwenye hili. Mbona tumefanikiwa kwenye korosho mwaka jana imefuta kodi zote na wananchi wakulima wa korosho wanaishi vizuri? Naiomba Serikali iji-commit kwenye hili mwaka huu iondoshe hizo kodi zote kwa sababu haya matumaini tumeyachoka.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama anavyosema Mheshimiwa Mbunge kwamba suala la tozo, kodi, limekuwa likizungumziwa kwa muda mrefu na ni kweli vilevile kwamba Mheshimiwa Rais wakati wa ziara yake ya kampeni ni moja kati ya masuala ambayo aliahidi kwamba atayafanyia kazi. Sisi kama Wizara tumeendelea kutekeleza sio katika zao la kahawa tu lakini katika mazao yote ya biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Sixtus Mapunda kwamba tarehe 22 Mei, tutakuja na mapendekezo ya kufuta tozo mbalimbali katika mazao ya biashara. Katika hili nimuahidi kwamba tutavuka mategemeo yake. Siku hiyo ya tarehe 22 mimi mwenyewe nitahakikisha namwita aje Bungeni kusikiliza. Katika hili tutaleta, sisi tunasema mapinduzi makubwa, tutaondoa tozo nyingi sana sio katika kahawa pekee bali katika mazao yote ya biashara.
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniona. Suala la kahawa kule kwetu kuna kata zaidi ya tano zinalima kahawa; Kata ya Mriba, Nyanungu, Itirio na maeneo mengine ya Tarime Mjini pia Kitale wanalima kahawa. Watu wa maeneo mengine wamefyeka kahawa zao kwa sababu wanaona ni kilimo kisichokuwa na tija. Mwenzangu amelalamikia kodi na tozo, ni kweli zipo, lakini kule kwetu nalalamikia bei. Ukichukua bei za kahawa zinazonunuliwa kwa mfano upande wa Kaskazini, japo bado zipo chini, ni tofauti na za Tarime na maeneo mengine ya kule Mara. Ukichukua bei zilizoko Kenya, sisi tuko mpakani, Kenya bei iko juu…
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Kenya mpakani bei inakuwa juu kuliko sisi. Sasa nauliza Serikali ni kwa vipi watu wengine wote bei zao zinakuwa tofauti na sisi? Ni kwa nini wasifanye bei hiyo ipande ili wakulima wale wasifyeke kahawa zao iwe ni kati ya zao ambalo linawapatia faida?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa Mheshimiwa Mbunge anavyosema kwamba nchi za jirani bei ya kahawa ni nzuri kuliko bei tuliyonayo nchini. Moja kati ya sababu zinazofanya bei yetu ya kahawa iwe chini ukilinganisha na nchi za jirani ni kwa sababu ya utitiri wa tozo na kodi ambazo zinafanya ile bei anayopata mkulima kuwa ndogo. Ndiyo maana nimesema mwaka huu tutapunguza tozo na kodi kuzidi mategemeo yenu kwa wakati wowote ule.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kodi hizi sio kwamba zina athari tu kwa bei ya zao hili kwa wakulima lakini zina athari katika mazingira ya ufanyaji biashara. Wawekezaji na wanunuzi wengi wa kahawa hawaji Tanzania kwa sababu kimsingi mazingira ya kufanya biashara ni magumu, ikisababishwa pamoja na mambo mengine na utitiri wa kodi na nyingine zinawagusa wao moja kwa moja. Kwa hiyo, tunapopunguza zitakuwa na faida sio tu ya kuongeza bei anayopata mkulima lakini vilevile kuwavutia wanunuzi wengi zaidi ili ushindani uwe mkubwa na hivyo bei kuongezeka. Naomba naye asubiri tarehe 22 ataona mapinduzi haya ambayo tunayazungumzia.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, mazingira ya swali hili yanafanana kabisa na mazingira ya wakulima wa Wilaya ya Mbozi na hasa katika Jimbo la Vwawa. Kwa kuwa, moja ya gharama kubwa ambazo wakulima wa kahawa wanazipata ni pamoja na kusafirisha kahawa yao kupeleka kwenye mnada kule Kilimanjaro. Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba Mnada wa Mloo unafunguliwa ili kupunguza ushuru na tozo mbalimbali ambazo zinawakabili wakulima wa zao la kahawa wa Wilaya ya Mbozi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba mnada mkubwa wa zao la kahawa upo Moshi. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba katika jitihada za Serikali za kuboresha mazingira ya zao la kahawa suala la minada na mahali panapofanyika ni moja kati ya masuala tunayofanyia kazi. Kwa hiyo, avute subira, nina hakika muda sio mrefu tutakuwa na suluhisho katika hili.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Uhaba wa mbegu bora uliokuwepo mwaka 2015/2016 na kiwango kidogo cha ubora wa dawa ya pamba uliokuwepo mwaka 2015/2016 umeendelea kuwepo 2016/2017. Sasa swali langu la kwanza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri, ni kwa kiwango gani Wizara imejiandaa kumaliza tatizo hilo mwaka 2017/2018?
Swali langu la pili, wakati wa kampeni Mheshimiwa
Rais alipokuwa Kanda ya Ziwa aliagiza Bodi ya Pamba ihamie karibu na wazalishaji wa zao la Pamba. Sasa swali langu, ni kwa kiwango gani uwepo wa Bodi ya Pamba Kanda ya Ziwa umesaidia kuhakikisha kwamba zao hili la pamba linapata uzalishaji mkubwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kuhusu ni lini Serikali itaongeza kiasi au kiwango cha mbegu za pamba ili kukidhi mahitaji ya wakulima, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika msimu unaokuja wa kupanda pamba, tayari Bodi ya Pamba kwa kushirikiana na Mfuko wa Pamba wameweka mikakati kuhakikisha kwamba kutakuwa na mbegu za kutosha.
Mheshimiwa Spika, vilevile nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba siyo suala la kuongeza tu kiasi cha mbegu inayopatikana, lakini vile vile kuhusu ubora wake.
Mhshimiwa Spika, Bodi ya Pamba kwa kushirikiana
na Wizara na vituo vyetu vya utafiti, tayari kwa muda sasa tunafanyia utafiti mbegu aina ya UKM08 ambayo haina tatizo la ugonjwa wa unyaufu na hivyo tuko mbioni kuondokana kabisa na mbegu UK91 ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikileta usumbufu.
Mheshimiwa Spika, tunaamini kwamba tunapofikia mwaka 2018/2019 tayari mbegu hii mpya, yenye ubora ambayo haina magonjwa itakuwa imeingia sokoni na ifikapo mwaka 2020, mbegu aina ya UK91 itakuwa imeondoka sokoni moja kwa moja. Kwa hiyo, katika miaka hii michache inayokuja tutahakikisha kwamba tuneondokana kabisa na adha ya ugonjwa na ubora usio mzuri wa mbegu ya pamba.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu Bodi ya Pamba kuhamia katika maeneo ambayo yanazalishwa pamba, nimfahamishe tu kwamba agizo lile la Mheshimiwa Rais tayari limeshatekelezwa, Bodi ya Pamba wameshahamia Mwanza na kwa kiasi kikubwa tayari imesaidia sana kwa sababu watendaji wanaoshughulika na zao la pamba kila siku tayari wapo karibu nao. Kwa hiyo, inakuwa ni rahisi wao kuweza kufika katika Ofisi za Bodi za Pamba na kupata huduma, lakini vilevile watendaji wenyewe maana ni rahisi wao kufika katika maeneo ya wakulima na kutoa huduma zinazotakiwa.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kupewa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kumshukuru Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo kwa mkutano tuliofanya na wakulima na wawakilishi wa Wanunuzi mwishoni mwa mwaka 2016.
Mheshimiwa Spika, katika mkutano huo tulikubaliana kuwa wanunuzi wadogo wapewe leseni ya muda na vile vile wajiunge kwenye vikundi na pia hii Kampuni ya pareto ambayo ilikuwa imebinafsishwa kutoka Serikalini kulikuwa na asilimia 10 ambazo walipewa wakulima. Vilevile katika hicho kikao tulikubaliana kuwa zichunguzwe hizo asilimia kumi ziko kwa nani kwa vile wakulima hawakupewa hizo asilimia kumi.
Mheshimiwa Spika, pamoja na makubaliano yote hayo, hakuna hata kimoja kilichozingatiwa na leo hii kuna kampuni mpya mbayo imejenga kiwanda eneo la Inyara, Mbeya ambayo imezingatia vigezo vyote na ilipewa leseni ya kununua pareto kwenye vijiji viwili tu kati ya vijiji zaidi ya 20 vinavyolima pareto. Sasa ni kwa nini Serikali isiboreshe hii Bodi ya Pareto ili tuweze kuboresha kiwango cha zao la pareto?
Mheshimiwa Spika, nashukuru.
La pili vilevile nilitaka kupata uhakika wa Serikali, kwa sababu inavyoelekea hakuna ushindani sasa hivi, watatuhakikishia vipi ya kwamba hawa ambao wametimiza vigezo vyote wanaruhusiwa kununua pareto ili inunuliwe kwa ushindani? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kwanza nikiri kwamba Mheshimiwa Njeza amekuwa akifuatilia sana maslahi ya wakulima wake wa pareto, kahawa na mahindi. Kwa hiyo, tumekuwa naye karibu sana. Vilevile nikiri kwamba tulifanya kikao na wakulima, mkutano ambao ulitusaidia sana kupata makubaliano kuhusu namna bora ya kuendesha zao la pareto.
Mheshimiwa Spika, kutokana na mazungumzo yetu, baadhi ya masharti ambayo wakulima na wawakilishi wao tulikubaliana watekeleze, bado wako mbioni kutekeleza na hivyo bado tunasubiri kutoka kwao.
Mheshimiwa Spika, vile vile kuhusiana na leseni ya kampuni za kununua pareto; nilieleze tu Bunge lako Tukufu kwamba zao la pareto ni zao lenye masharti tofauti kidogo na mazao mengine kwa sababu tunachoruhusu kipelekwe nje siyo pareto ghafi, siyo maua, bali ni sumu ghafi. Katika maana hiyo, ili uweze kupeleka nje lile zao ni lazima uwe na kiwanda.
Mheshimiwa Spika, tunafanya hivyo kwa sababu huko nyuma wakati tulikuwa tunaruhusu kupeleka maua nje, kiwango cha pareto yetu kilishuka sana kwa sababu hatukuwa tunaweza kudhibiti ubora wa sumu inayopelekwa nje, ndiyo maana tukaleta ili kunusuru zao lisije likaanguka nchini. Tukaleta kigezo kwamba ni lazima uweze kuwa na kiwanda ili uweze kuzidua au kuchakata na kuwa sumu ghafi.
Kwa hiyo, kampuni yoyote ambayo imekidhi masharti hayo, katika hali ya kawaida tunaruhusu inunue pareto. Kampuni ambayo anaizungumzia ya TAN Extract ya Mbeya ambayo ndiyo imeingia tu sokoni na kutimiza masharti, tutaendelea kutoa leseni ili waweze kununua pareto maeneo mengine zaidi ya vijiji ambavyo wanatoa sasa.
Vilevile nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa hatujaona kwamba tatizo ni Bodi ya Pareto lakini ni kanuni na sheria ambayo tumewekeana wenyewe kama wadau na Serikali iko tayari kuirejea na kuangalia upya sheria na kanuni hizo kama itaonekana inafaa.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii niulizes swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, matatizo yaliyopo huko Mbeya Vijijini yanafanana kabisa na matatizo waliyonayo wakulima wa Itigi. Wakulima wa Itigi wanalima mazao mbalimbali yakiwemo mazao ya biashara na mazao ya chakula, lakini wanategemea sana Kampuni hii ya Tanganyika Packers ambalo limetelekezwa na sasa wanalitumia. Mheshimiwa Naibu Waziri alifika pale na aliona hamasa ya wananchi kutaka shamba lile lirejeshwe kwa wananchi kupitia Halmashauri yao.
Je, ni lini sasa Wizara hii italirudisha shamba lile kwa wananchi kwa sababu kampuni hii inayolimiliki ilishafilisika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba wakati wa ziara yangu Itigi, niliona changamoto ya ardhi waliyokuwanayo wananchi, pamoja na kuwepo na shamba ambalo ni kama limetelekezwa na hivyo kuhitaji jitihada za kuangalia namna ya kuwapatia.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari mchakato wa kuangalia namna ya kuligawa shamba hilo unaendelea. Wizara yangu kwa kushirikiana na Msajili wa Hazina inatayarisha waraka wa kwenda Baraza la Mawaziri ili hatimaye shamba hilo liweze kugaiwa kwa utaratibu ambao utaonekana unafaa ikiwa ni pamoja na kugawa kwa wafugaji na wakulima wa Itigi.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ya kuuliza swali la nyongeza. Wilaya ya Hanang kama ilivyo Wilaya ya Siha inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa Ardhi na tuna mashamba ambayo yalikuwa chini ya NAFCO ikiwemo Basotu Plantation na tuliomba kwamba shamba hili lirudi kwa wananchi; Mheshimiwa Waziri anaweza kutueleza ombi letu limefika wapi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mary Nagu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa kwamba kuna maombi ya Shamba la Basotu Plantation ambalo lilikuwepo mikononi mwa NAFCO liweze kugaiwa kwa wananchi. Utaratibu ambao ulikuja kubadilika baadaye ni kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’ ikabidhiwe hilo shamba ili wenyewe waweze kukodisha kwa wakulima wadogo, kwa sababu tayari jitihada za kugawa mashamba mengine ililileta mgogoro mkubwa sana ambao ulikuwa unatishia amani.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa sasa utaratibu ambao umetumika ni huo wa kujaribu kukabidhi kwa Halmashauri huku jitihada zikiendelea za kuangalia namna bora ya kuweza kuligawa. Kwa hiyo, namtaka Mheshimiwa Mbunge aendelee kuwa mvumilivu tukiangalia utaratibu huu ili huko mbele ya safari tuweze kuligawa kwa utaratibu.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa mpango wa Serikali kwa sasa ni kuelekea Tanzania ya viwanda na hakuna viwanda ambavyo tunaweza kuvipata bila kuboresha kilimo. Hii ni sawa na kwamba unapanda mchicha unategemea kuchuma machungwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa pia hauwezi kuboresha kilimo bila kuwekeza kwenye vyuo vya kilimo. Je, Serikali ipo tayari kuboresha kituo cha mafunzo ya wakulima ambacho kipo kijiji cha Mbozi, kata ya Igamba, Jimbo la Mbozi ili kiwe chuo kamili, kwa maana tayari kituo hiki kipo na wakulima walishaanza kupata mafunzo pale tangu mwaka 2012?
Swali la pili, kwa kuwa vyuo vingi vya kilimo nchini kikiwepo Chuo cha Kilimo cha Uyole, vipo katika hali mbaya sana, Serikali imevitelekeza, miundombinu ni mibovu, havina wataalamu. Je, Serikali ipo tayari sasa kuboresha vyuo vyote vya kilimo nchini ili sasa tuweze kwenda na hii suala la nchi ya viwanda?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye majibu ya swali la msingi, Serikali ina nia ya kuendelea kuboresha vyuo vyetu vya kilimo, kuboresha kule ni zaidi tu ya kuviongeza idadi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaamini kwamba tukiweza kuimarisha na kuboresha huduma zinazotolewa na vyuo vilivyopo sasa sio lazima kuongeza vyuo vingine. Kwa sasa nchini kwetu tuna vyuo 14 vya kilimo katika kanda sita za kilimo. Sasa tunachofanya ni kuendelea kuziboresha ili ziweze kutoa huduma nzuri zaidi badala ya kuelekea kujenga utiriri wa vyuo ambavyo havina quality nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge nimuelekeze tu kwamba kituo anachozungumzia wakati huko mbele tunaweza kufikiria kufanya chuo kamili lakini kwa sasa vyuo vitatu ambavyo vipo mkoa jirani wa Mbeya tutaendelea kuviimarisha na kuviboresha ili viweze kutoa huduma kwa watu wa Mbozi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili, jibu hilo pia linatumika kwa vyuo vyote nchini, kama nilivyoeleza kwenye jibu la msingi. Serikali sasa inaanza kutekeleza Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Mifugo awamu ya pili ya ASDP II, moja kati ya matarajio katika kutekeleza mpango huu ni kuendelea kuboresha vyuo vyetu vya kilimo ikiwa ni pamoja na kuongeza kukarabati majengo, kuajiri rasilimali watu ya kutosha ili viweze kudahili wanafunzi wengi na kutoa elimu ya kilimo ambayo ni bora.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waingereza wanasema justice delayed is justice denied, na kwa vile imechukua muda. Je, Msajili wa Hazina, Hazina na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi watakuwa tayari sasa kukamilisha uhakiki huu na kuwalipa hao wanaodai ambao walikuwa wafanyakazi wa NAFCO?
Swali dogo la pili, ili tumalize migogoro iliyo kwenye mashamba ya NAFCO, je, Serikali iko tayali sasa kurudisha shamba la Basutu plantantion kwa wananchi ambao wana upungufu wa ardhi mapema inavyowezekana?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba justice delayed is denied, vilevile justice hurried is justice buried. Kwa hiyo, katika mukhtadha huo tunaendelea na uhakiki ili haki itendeke pande zote, tunatambua kwamba imechelewa lakini haki katika hili ni pamoja na Serikali kuweza kulipa malipo ambayo ni stahiki kwa sababu tukiyaharakisha sana inawezekana hata baadhi ya wafanyakazi wale tukawapunja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jitihada zinaendelea na tunashirikiana na Wizara ya Fedha taratibu zikikamilika wananchi wake wa Hanang ambao anawasimamia vizuri sana watalipawa haki zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali la pili la Basutu plantantion ni kweli kabisa kama anavyosema Mheshimiwa Dkt. Nagu kwamba shamba lile baada ya kuwekewa utaratibu ambao Halmashauri wanakodisha kwa wananchi, tayari kuna malalamiko yametufika kwamba utaratibu ule haujaweza kufanya lile ambalo lilitegemewa. Kuna malalamiko kwamba kuna wajanja wameingilia vilevile wale walengwa ambao walikuwa ni wananchi wa kawaida, maskini, wakulima wadogo wao inaelekea hawajanufaika katika mpango huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara bado inaendelea kulichunguza suala hili na ikibainika kwamba lile lengo ambalo tulikusudia halifikiwi, Wizara itachukua utaratibu mwingine kuhusiana na shamba la Basutu plantantion.
MHE. FAKHARIA SHOMARI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake marefu lakini yametoa elimu kwa Watanzania. Naomba kuuliza maswali mawili madogo.
Kwa kuwa katika kupambana na uvuvi haramu baharini na katika maziwa yetu, jambo linaloonekana ni kwa mvuvi anaevua uvuvi wa haramu kwa sababu anapatikana na nyavu zenye macho madogo; na yeye ndiye hutiwa hatiani. Kuna usemi unaosema mkamatwa na ngozi ndiye mwizi. Sasa swali, je, Serikali inasemaje kwa wale wenye viwanda vya kutengeneza nyavu, wanaoleta, wanaouza, ambao wao ndio source kubwa ya kutufanyia huu uvuvi haramu kutokana na vifaa wanavyovileta, kuliko huyu mvuvi ambaye ameuziwa akaenda akaifanya hii kazi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Wizara italeta lini Bungeni Sheria ambayo itaweza kuwadhibiti hawa waletaji, wenye viwanda pamoja na wauzaji ili tuweze kuwadhibiti kisheria pamoja na hawa wanaozitumia nyavu hizi? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, niruhusu nitambue kweli jitihada za Mheshimiwa Mbunge za kufuatilia masuala ya uvuvi. Si mara ya kwanza yeye kuuliza maswali katika Bunge hili, lakini amekuwa akiwasiliana na Wizara kuonesha concern yake kuhusiana na masuala mbalimbali ya uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kuhusu kwamba ni kwa nini wavuvi tu wanaokamatwa na nyavu ndio wanachukuliwa hatua za kisheria. Nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge, kwamba kwa sababu kutumia nyavu ambazo haziruhusiwi kisheria ni kosa la kisheria, yoyote yule atakayehusika kwa namna moja au nyingine katika utengenezaji, uuzaji, usafirishaji, utumiaji wa nyavu hizo anakuwa amekiuka sheria vile vile, kwa hiyo hakuna ambaye ataachwa.
Mheshimwia Mwenyekiti, kwa hiyo, kama kuna kiwanda ambacho kinatengeneza nyavu ambazo haziruhusiwi, kama kuna mfanyabiashara atafanya, kama kuna dalali, mtu yoyote atakayejihusisha kwa namna moja au nyingine sheria itachukua mkondo wake. Ni kweli kabisa si wavuvi tu ndio wanakamatwa lakini tayari tumeshakamata bidhaa za kutengenezea nyavu kama hizo, lakini vile vile hata wafanyabiashara ambao wanahusika wameshachukuliwa hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la
pili kwamba lini tutabadilisha sheria yetu ya uvuvi ya mwaka 2003 ili sasa kushughulikia kwa utaratibu zaidi makosa mbalimbali yanayopelekea watu kujihusisha na uvuvi haramu. Nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari Wizara inafanya utaratibu wa kupitia sheria ile; lakini si sheria ile tu, tunaanza kufikiria sasa kama nchi kwamba suala la uvuvi haramu ni zaidi tu ya uvuvi, inahusisha vile vile mambo ya ugaidi, lakini vile vile inahusisha uhujumu uchumi. Kwa hiyo ikiwezekana sheria nyingi zitarekebishwa ili hili suala tuweze kulishughulikia kwa mapana zaidi na kwa ufanisi zaidi.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kumuuliza swali moja Mheshimiwa Naibu Waziri. Kwa kuwa Taasisi ya Hifadhi ya Bahari Mafia, imeshindwa kazi yake ya msingi ya kuzuia uvuvi haramu na uhifadhi na hivi sasa inauza visiwa na maeneo Wilaya Mafia. Je, Sasa Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kuondoa uongozi wa juu pale na kubadilisha kuleta uongozi mwingine?Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, jana tulielezea kwamba hakuna visiwa ambavyo vimeuzwa Mafia isipokuwa sheria tu zimefuatwa kukodisha Kisiwa cha Shungimbili kwa miaka 20 kwa Mwekezaji wa Hoteli. Vile vile kama kuna ushahidi wowote ule ambao utaonesha kwamba, maafisa anaowazungumzia wameshindwa kufanya kazi yao au wamejihusisha na vitendo ambavyo ni kinyume na sheria, lakini vile vile na maadili ya kazi yao, naomba Mheshimiwa Mbunge atuletee na sisi bila kusita tutachukua hatua.
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Kwa vile madeni haya yamechukua muda mrefu; je Serikali iko tayari kufikiria kulipa pamoja na riba kwa Mawakala hao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kumekuwepo
na tatizo la pembejeo ambazo hazina ubora; je, Serikali ina mpango gani kuimarisha ukaguzi wa maduka ya pembejeo za kilimo ili kuhakikisha wananchi hawa wanapata pembejeo zenye ubora stahiki? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na madeni ulipwaji wake kucheleweshwa na hivyo kustahili kulipwa riba; nimweleze tu Mheshimiwa Mbunge kwamba ucheleweshwaji wa ulipwaji umetokana vilevile na kasoro ambazo hata Mawakala wenyewe wanahusika katika kasoro hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuliambia Bunge lako Tukufu kwamba suala la pembejeo limekuwa ni moja kati ya maeneo ambayo kuna wizi mkubwa sana wa fedha za umma. Kwa hiyo, ukiona kwamba kuna ucheleweshaji kidogo ni kwa sababu tunataka tufanye malipo sahihi, hatutakubali tena fedha za umma ziibiwe na wajanja wachache kwa kisingizio kwamba huduma imetolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, pamoja na kwamba tunathamini mchango mkubwa sana wa Mawakala wa Pembejeo katika kuendeleza Sekta yetu ya Kilimo, lakini niwaeleze tu kwamba hili ni eneo ambalo Serikali imepoteza fedha nyingi sana. Katika ukaguzi wa awali ambao tumefanya kama Wizara katika mikoa nane ambayo imepata ruzuku kubwa, walikuwa wanadai shilingi bilioni 36. Kati ya hizo ni shilingi bilioni nane tu ambazo zimeonekana zinaweza kulipwa bila utata. Kwa hiyo, unaweza kuona ni kwa kiasi gani tumekuwa tukipoteza fedha nyingi kwa kukimbilia kulipa haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, naombeni wale mnaotoka maeneo ambayo pembejeo ya ruzuku imepelekwa, mtufahamishe upungufu unatokea kule. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Keissy kwa sababu yeye amekuja mbele na kutueleza kuhusu udanganyifu uliofanywa na Mawakala katika Jimbo lake. Vilevile juzi Mheshimiwa Flatei Massay, naye kaeleza upungufu uliotokea Wilayani kwake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaendelea kulipa madeni yale ambayo ni sahihi, lakini kwa bahati mbaya sana kuna Mawakala ambao hawana makosa lakini wanapata matatizo kwa sababu ya makosa ya Mawakala ambao sio waaminifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile lazima niseme udanganyifu huu haukufanyika na Mawakala peke yao, hata Maafisa wa Serikali wamekuwa ni sehemu ya mfumo mbovu ambao umekuwa ukiibia fedha Serikali. Kimsingi tu, katika Serikali ya Awamu ya Tano hili hatutaki litokee na ndiyo maana tumebadilisha mfumo na kwa sasa hatuna tena mfumo wa vocha.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Swali lililoulizwa na Mheshimiwa Martin Mtonda kuhusu madai ya Mawakala wa Pembejeo Mbinga Vijijini linafanana kabisa na tatizo lililopo Wilaya ya Masasi Mkoa wa Mtwara na hasa Jimbo la Ndanda; kwamba katika msimu wa kilimo wa mwaka 2016 wakulima wa korosho na hapa Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri kwamba hasara nyingine huwa zinasababishwa na watumishi wa Serikali wasio waaminifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jambo hili pia limetokea Mtwara kwa wakulima wa korosho baada ya wamiliki wa maghala kwa kushirikiana na Watendaji wa Chama Kikuu cha Ushirika kuwaibia wakulima pesa zao na kesi zinaendelea kwenye Mahakama. Je, Serikali haioni sasa ni wakati wa kutoa pesa zilizopo kwenye Mfuko wa Wakfu na kufidia hasara hii waliyoipata wakulima wakati wao wanaendelea na wale watu waliopo Mahakamani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na uwezekano wa Serikali kulipa fedha ambazo kwa sasa zipo kwenye Mfuko wa Wakfu kwa ajili ya kufidia zile fidia, ingekuwa ni jambo jema, lakini kwa sababu suala lenyewe bado liko Mahakamani, ni vizuri tukasubiri tupate majibu, kwa sababu inawezekana kule Mahakamani, wale ambao tunafikiri wamesababisha hasara ikaja ikatokea uamuzi tofauti. Kimsingi tunataka kila mtu abebe mzigo wake ili kama wale watakuwa wamehusika kulingana na hukumu ya Mahakama, wenyewe watabeba jukumu la kurudisha fedha za wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachofanya sisi kama Serikali ni kuhakikisha kwamba matatizo kama haya hayatokei tena. Ndiyo maana tunavyozungumza, tayari Bodi za Vyama vya Ushirika zaidi ya 200 Mtwara na Lindi zimevunjwa, ni kwa sababu tunajaribu kuwalinda wakulima wasiendelee kuibiwa na watu wachache ambao sio waaminifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile hizo kesi ziko Mahakamani na Afisa yeyote wa Ushirika au wa Serikali ambaye atabainika kuhusika katika upotevu wa fedha za wakulima, naye vilevile atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuboresha ubora, ni swali ambalo liliulizwa awali ambalo linahusiana na hili. Sasa hivi Serikali ina mpango wa kuagiza mbolea kwa mkupuo (bulk procurement) na hii itasaidia sana sisi tuweze kuchagua mbolea ambayo tunahakikisha kwamba inakuwa na ubora. Kampuni yetu inayohusika na ubora wa mbolea itahakikisha kwamba mbolea yote inayoingia ni bora lakini vilevile hata kwa mbegu…
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona. Mwaka 2016 Mheshimiwa Waziri Mkuu alifanya ziara Mkoani Rukwa na alipata nafasi ya kuonana na Wakala wa Mkoa wa Rukwa. Kama tunavyojua, Mkoa wa Rukwa ni mchangiaji mkubwa sana wa uzalishaji wa chakula hapa nchini. Mpaka sasa hakuna kilichopatikana katika madai haya na Wizara imekuwa ikitoa majibu ya namna hii hii kila siku; haioni kama inadidimiza kilimo katika nchi hii? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mawakala wamekata tamaa na ndiyo walikuwa wanatusaidia mkoani kwetu na sasa chakula kitapungua Mkoa wa Rukwa kwa sababu ahadi ya Waziri Mkuu ambaye aliongea na Mawakala, haijatimizwa kwa sababu ya majibu ya kila siku kama haya.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba majibu yamekuwa ni kama haya kwa sababu huo ndiyo ukweli, kwamba ni vigumu sana sisi kukimbilia kulipa madeni ambayo tunafahamu kuna wizi ndani yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sasa hivi tunachofanya ni kuhakikisha kwamba tunaondokana na mfumo ambao unarahisisha wizi na ndiyo maana mfumo wa kununua mbolea kwa mkupuo hatutakuwa tena na tatizo la kuanza kuwa na madeni kwa sababu mbolea itakuwa inanunuliwa dukani kama Coca Cola. Kwa hiyo, tunachosema, watuvumilie tu, hatuwezi tukalipa fedha ambazo ni wazi ni za wizi. Tuna ushahidi.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba inaondoa migogoro hii ya upatikanaji wa pembejeo za kilimo na kwetu sisi wakulima wa korosho, hapa juzi Serikali imetutangazia kutupatia sulphur kwa maana ya pembejeo ya kilimo bure. Je, Serikali imejipangaje katika usambazaji wa sulphur hii ya bure ili iweze kutufikia kwa wakati na ya kutosha?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakuja kueleza wakati wa hotuba ya bajeti yetu Ijumaa kuhusiana na hatua mbalimbali ambazo tumechukua kuboresha mifumo ya usambazaji wa pembejeo katika mazao mbalimbali ikiwepo zao la korosho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, niseme tu kwamba sulphur itagawiwa kwa utaratibu ambao umewekwa na Bodi ya Korosho. Kimsingi, hatuamini kwamba itawezekana tena sulphur ichelewe, kwa sababu kwa sasa maana yake inakuwa inatolewa bure na yule ambaye anagawa inakuwa ni Bodi. Kwa hiyo, tusubirie tutasikia kuhusu huo utaratibu.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu marefu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini kwa kweli nashindwa hata kusema kama Mbunge ninayewakilisha wavuvi yaani nikirudi Jimboni sina hata cha kuwaambia kufuatana na haya majibu ambayo yapo, kwa sababu ukiangalia nilitegemea aniambie angalau bajeti ya mwaka huu zimetengwa fedha kiasi fulani kwa ajili ya wavuvi angalau wa Jimbo lako au wa Tanzania kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo ninaweza kwenda kuwaambia wakulima mwaka huu kiasi cha pembejeo kilichotengwa kwa sulphur na dawa za maji, kila kitu nina uwezo wa kwenda kusema, lakini kwa wavuvi sina.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia suala la mabenki aliyozungumza, mabenki ni ya kibiashara na wavuvi hawana dhamana yoyote ya kuwaunganisha. Katika haya mafunzo, unataka kutoa mafunzo ya Bahari Kuu kwa mwambao wa bahari kutoka Moa mpaka Mtwara wenye Wilaya zaidi ya 14, wavuvi 50 ambao kwa mimi naona ni sawa na kijiji kimoja tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, labda Mheshimiwa Waziri aniambie mgawanyo wa hao 50; wavuvi ambao anataka kuwapatia mafunzo ya uvuvi wa Bahari Kuu kila Wilaya wanawapa wangapi ili na mimi ninavyorudi Mtwara Vijijini nikaseme kwamba watapewa kiasi hicho?
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, tulikuwa na mradi wa MACEMP ambao ulifanya vizuri sana katika kuwasaidia wavuvi, hivi mpango huo umefikia wapi au umekufa au kwa nini tusichukue mafunzo tuliyoyapata kutoka kwenye MACEMP tukahamishia Serikalini, tukatekeleza sisi wenyewe?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli anaposema Mheshimiwa Hawa Ghasia kwamba imekuwa ni vigumu kuweza kusema ni fedha gani zimetengwa kwa ajili ya Wilaya yake ya Mtwara Vijijini, lakini natambua kwamba Mheshimiwa Ghasia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, kwa hiyo, ana uelewa zaidi wa namna bajeti katika sekta ya uvuvi inavyotengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi tu wanaoshikilia hasa bajeti ya kuendeleza uvuvi ni Halmashauri. Kwa hiyo, kama Diwani anayeshiriki katika mijadala katika Halmashauri ya Mtwara Vijijini najua kwamba itakuwa ni rahisi yeye kufuatilia zaidi. Niliyoyazungumza mimi ni ya kisera zaidi kwa sababu amezungumzia kuhusu mipango, lakini pale nimeonesha kidogo fedha ambazo zinasimamiwa na Wizara.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile niko tayari kukaa naye tujadiliane niweze kumwonesha hiyo mikakati kwa ufasaha zaidi. Kuhusiana na MACEMP ni kweli kabisa kama anavyosema, MACEMP umekuwa ni mradi ambao umekuwa na mafanikio makubwa na ndiyo maana yale tuliyojifunza kutoka MACEMP tumeweza kuweka katika Programu ya kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili ili kuweza kuyachukua yale mazuri na kuweza kuyajengea mkakati ili wavuvi wetu waweze kunufaika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la namna gani wale wavuvi 50 watakavyogawanywa, niko tayari vilevile kukaa naye tuangalie namna gani katika hao kuna ambao watatoka Mtwara Vijijini, lakini niseme kigezo ni uwezo wa kuvua katika Bahari Kuu. Tunaweza tukafikiri kwamba ni wachache, lakini sio Watanzania wengi, sio wavuvi wengi wa kawaida ambao wanaweza wakajihusisha na uvuvi wa Bahari Kuu.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwa kuwa kuna changamoto lukuki katika Sekta ya Uvuvi na kwa kuwa wavuvi hao wameongezeka mara dufu zaidi ya asilimia 90 kwa miaka 10 iliyopita pamoja na vyombo wanavyotumia, lakini haviendi sambamba na nini wanachokipata.
Serikali haioni sasa ijikite kwenye ku-promote acquaculture na mariculture kwa ajili ya maendeleo ya Sekta ya Uvuvi nchini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Sware ametabahari sana katika masuala ya uvuvi, kwa hiyo, anafahamu fika kwamba katika Mpango wa Maendeleo wa Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili, moja kati ya masuala ambayo yametiliwa mkazo sana ni namna gani ya kujenga uwezo wa wavuvi na Watanzania wengi kushiriki katika ufugaji wa viumbe kwenye maji katika maana ya acquaculture.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba acquaculture ndiyo hasa tunakoelekea tunavyozungumzia kuhusu blue economy. Kwa hiyo, ni kweli kama alivyosema, lakini ni kweli kwamba tumewekea mkakati. Tunataka ikiwezekana kila Halmashauri iwe na mkakati wa kuhakikisha kwamba wananchi wanafuga samaki, badala ya kuendelea kutumia rasilimali tulizonazo za uvuvi ambazo kwa kiasi kikubwa zimepatwa na changamoto kutokana uvuvi usio endelevu.
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naomba niulize swali moja la nyongeza. Mkoa wa Songwe hususan Wilaya ya Ileje iko katika ukanda River Songwe Basin na kulikuwa kuna mpango katika mojawapo ya vitu vya kufanya katika mradi ule wa kuwa na mabwawa kwa ajili ya kufugia samaki na mpaka sasa hivi watu walizuiwa kutumia eneo hilo la Bupigu kwa sababu hiyo.
Je, Mheshimiwa Waziri anaweza kutueleza ni lini sasa mpango huo utafanyika ili vijana wetu wapate ajira na vipato? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama anavyosema kwamba mpango uliokuwepo wa kuanzisha mabwawa ya samaki katika eneo la Buhengwe umesimamishwa kutokana na haja ya kuangalia athari zinazoweza kutokea za mazingira. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie kwamba pindi tathmini hiyo itakapokamilika, jibu sahihi au mwelekeo utafahamika.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nina maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
La kwanza, Serikali imesema kwamba wanaendelea kuwahamasisha wakulima kutafuta masoko ya uhakika, lakini hata pale ambapo wakulima wanavuna mazao yao ya ziada hawaruhusiwi kuuza mazao hayo nje ili kujipatia kipato cha ziada. Baya zaidi ni kwamba Wakala wa Hifadhi ya Chakula wa Taifa, (National Food Reserve Agency - NFRA) hawapatiwi fedha za kutosha kununua mazao ya wakulima pale ambapo yanakuwa ni mengi, jambo ambalo linasababisha wakulima hawa kupata hasara kubwa. Je, Serikali ina mkakati gani wa ziada kuhakikisha kwamba, NFRA wanapewa fedha za kutosha ili kununua mazao ya wakulima pale ambapo yanakuwa ni mengi? La kwanza.
La pili, ni kwamba wanaonunua mazao ya wakulima, wafanyabiashara ndogo ndogo katika masoko ya Temeke, Tandika, Buguruni, Mbeya na maeneo mengine mbalimbali, Mabibo, Mwananyamala, kote huko wana malalamiko makubwa kwamba mzunguko wa pesa kwa ujumla wake, basi umekuwa ni mdogo, wafanyabiashara hawa wamepigika; umaskini unakua, hawana uhakika wa mambo ambayo wanayafanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali sasa ituambie mkakati wa ziada kuhakikisha kwamba wafanyabiashara ndogo ndogo wanaofanya biashara za mazao ya wakulima katika masoko mbalimbali nchini mnawahamasisha kiasi gani ili kuweza kupata mikakati yao ya ziada ya kujiongezea kipato cha uhakika? Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwanza kwamba ni lazima tufahamu kwamba, lengo la Serikali la kuzuia kuuza chakula nje ni kwa ajili ya maslahi ya Taifa. Ni lazima tuangalie hali yetu ya chakula ikoje, tukifananisha na majirani zetu wanaotuzunguka.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunavyozungumza, nchi za Ukanda wetu wa Afrika Mashariki watu zaidi ya milioni 20 mwaka huu wanategemewa kuwa na njaa ambayo haijatokea hivi karibuni. Ethiopia pekee watu milioni nane wana njaa; Sudani ya Kusini watu 4,600,000 wana njaa, Somalia watu 6,100,000 wana njaa; Rwanda kuna shida; nchi za pekee ambazo zina ziada ya chakula katika ukanda wetu ni Zambia, Malawi na Uganda. Katika mazingira kama haya, kama Taifa ni lazima tutangulize maslahi ya Taifa mbele na ni lazima tuhakikishe kwamba tumejitosheleza huku ndani kuliko kukimbilia kuuza chakula nje. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nataka nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba na hili ni lazima tuseme kwa uwazi, biashara inayofanyika ya kupeleka chakula nje siyo biashara, ni utoroshaji wa chakula. Mwaka 2016 mnafahamu huku ndani karibu mtutoe macho Waheshimiwa Wabunge kwa kusema kwamba kulikuwa na upungufu wa chakula. Mwaka huu tusipoangalia hali itakuwa ni mbaya zaidi. Kwa hiyo, ni lazima tuendelee kuhakikisha kwamba tunakuwa na usalama wa chakula ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile soko la chakula lipo ndani. Hatutaki tuwakimbize wakulima wetu waanze kuuza wakati wanalanguliwa. Bei wanayopata sasa hivi siyo nzuri. Mkulima ambaye anasubiri, anaweza akauza kwa urahisi zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo mafupi, niseme sasa kwamba NFRA mkakati ambao tumejipanga, kwa sasa tunaanza kwanza na kuimarisha au kujenga uwezo wetu wa kuhifadhi. Kwa sasa tuna uwezo wa kuhifadhi chakula tani 251,000 tu. Tumepata shilingi bilioni 100; tunajenga maghala ili tuweze kuongeza uwezo huo kufikia tani 500,000. Ni kitu cha kwanza kwa sababu hata tukisema tununue, hatuna mahali pa kuhifadhi. Kwa hiyo, tunaongeza uwezo wa kuhifadhi. Baada ya hapo, NFRA itaongezewa uwezo wa kununua mahindi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kwa sababu NFRA haijaanzishwa kwa ajili ya kufanya biashara ya chakula, imeanzishwa kwa ajili ya hifadhi ya usalama wa chakula. Bodi ya Mazao Mchanganyiko tunavyozungumza Serikali imeshaagiza vinu vitatu vikubwa kwa ajili ya kuongeza uwezo wa kusindika katika vinu vya Dodoma, Mwanza na Iringa.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo ni kwamba, Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko iweze kununua chakula kingi na kusindika na kuuza nje. Huko ndiyo tunakoelekea. Kwa hiyo, naomba tuvute subira, hayo yatafanyiwa kazi, lakini hatuwezi tukakimbilia kuanza kuruhusu chakula kiondoke nchini kiholela.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu masoko, Mheshimiwa Mbunge amezungumza kuhusu changamoto iliyoko Temeke na masoko mengine ya mjini kama alivyosema. Mkakati ambao Serikali inafanya, tunawashauri na kuwasaidia wafanyabiashara wadogo wadogo waweze kujiunga kwenye SACCOS, waweze kujiunga kwenye Vyama vya Ushirika ili iwe ni rahisi wao kupata mitaji kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo, lakini vilevile Benki za Biashara kwa sababu mara nyingi sana suala la mitaji linaweza likatatuliwa kwa kuwezesha kupata mikopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Serikali kwa sababu tunaposema kwamba uwezo wa mzunguko wa fedha umekuwa ni mdogo, mikakati yote ambayo tunaijenga kama Serikali ni kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wananchi wanakuwa na uchumi imara ambao utawasaidia kuendelea kufanikiwa zaidi. (Makofi)
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Naomba kupata kauli ya Serikali juu ya zoezi linaloendelea la ugawaji wa pembejeo kwa mikoa ya Lindi na Mtwara hasa kwa sulphur. Mpaka sasa hivi idadi ya sulphur ambayo wamepelekewa wakulima wetu ni kiasi kidogo sana ukilinganisha na mahitaji. Naomba kupata kauli ili tuweze kujua tunawasaidiaje wakulima wa zao la korosho tusiweze kuathiri zao hili ambalo tumekwishaanza kufanya vizuri?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, hili litakuwa fupi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu sulphur, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba sulphur kwa sasa inaonekana kwamba kuna upungufu kwa sababu sulphur hatujaagiza kwa wakati mmoja. Kwa hiyo, tunawaomba Waheshimiwa Wabunge wawaeleze wakulima wao kwamba sulphur ambayo imepatikana sasa wachukue kwa kiwango kilichopatikana, lakini sulphur nyingine iko njiani. Tuliagiza tani 9,000 lakini sulphur nyingine iko njiani.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile niwafahamishe kwamba wanaopata sulphur ni wale walioshiriki katika Mfumo wetu wa Stakabadhi Ghalani, maana yake waliouza korosho msimu uliopita kupitia Vyama vya Ushirika. Kama kuna mtu aliuza kupitia choma choma, maana yake hawezi kuingia katika mfumo rasmi, hatatambuliwa na hatapata sulphur. Kwa hiyo, sulphur iko njiani.
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Naomba pia nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri, nina maswali madogo ya nyongeza.
Swali la kwanza, wakulima hasa wa jamii ya wafugaji wanapopelekewa pembejeo kwa maana ya mbegu, mbolea na madawa, pale ambapo hawana maelekezo mazuri ya uelewa wanazikataa pembejeo hizo na hivyo kuwanufaisha wale mawakala kwa kujinufaisha kuziuza tena.
Je, Serikali ina mikakati gani kuhakikisha kwamba wanapowapelekea pembejeo wakulima wa jamii ya wafugaji na wengineo ambao hawana uelewa mzuri wanawaelekeza vizuri ili waweze kunufaisha kilimo chao?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Tarafa ya Dongobesh katika Wilaya ya Mbulu kwa msimu uliopita hawakupelekewa kabisa mbolea na mbegu na dawa kwa ajili ya pembejeo za kilimo kwa msimu uliopita. Nini kauli ya Serikali pale ambapo inatokea tatizo kama hilo hasa tukiwa katika harakati za kuboresha kilimo tunakoelekea kwenye Tanzania ya viwanda?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba jamii za wafugaji lakini vilevile Watanzania walio wengi/wakulima hawana ufahamu mzuri kuhusu umuhimu na namna ya kutumia mbolea kwa ajili ya kuendeleza kilimo chao. Katika kushughulikia changamoto hii Serikali imekuwa ikiimarisha huduma za ugani ili wananchi waweze kupata elimu na ufahamu mzuri ili waendelee kutumia mbolea kwa namna inavyotakiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu kwa kushirikiana na Serikali za Mitaa - Halmashauri zetu, tunaendelea kutoa miongozo ile vile kutoa elimu kwa Maafisa Ugani ili waweze kutoa taarifa sahihi na elimu inayotakiwa kwa ajili ya wakulima wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile katika kuhakikisha kwamba huduma za ugani zinaendelea kuboreshwa, Wizara yangu imebuni Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Sekta ya Kilimo (ASDPII) ambao utekelezaji wake unaanza katika mwaka wa fedha na moja kati ya masuala yanayotiliwa mkazo sana ni masuala ya ugani na tunategemea kuendelea kuimarisha vituo vya rasilimali za kata (World Resource Centre) ili ziendelee kutoa teknolojia muhimu ya kilimo na elimu ili wananchi waweze kuweza kutumia mbolea na kufanya kilimo ambacho kinakuwa na tija zaidi.
Pia Wizara kwa sasa imejipanga kutumia huduma za ugani mtandao (E-extension services) ili iwe rahisi hata kwa kutumia tu simu za mikononi wananchi waweze kupata taarifa muhimu kuhusiana na namna ya kutumia mbolea lakini vile vile kuhusiana na taarifa zingine muhimu za kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la nyongeza
la pili kuhusiana na kata ya Dongobesh kutopata pembejeo katika msimu uliopita, nimueleze tu Mheshimiwa Mbunge kwamba katika msimu uliopita siyo maeneo yote nchini yalipata pembejeo za kilimo zile za ruzuku, kwa sasa Wizara imejipanga ili makosa kama haya na upungufu kama huu usitokee tena, kuhakikisha kwamba mbolea inapatikana dukani kama CocaCola.
Waheshimiwa Wabunge, wote mnakumbuka kauli maarufu ambayo Waheshimiwa Wabunge najua mnaipenda sana ya Mheshimiwa Mwigulu alipokuwa Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi, hilo alilokuwa anasema limetima kuanzia msimu unaokuja mbolea ya DAP na UREA itapatikana nchi nzima kwa bei ambayo itakuwa na dira ili kuhakikisha kwamba hatutakuwa tena na upungufu na bughudha zingine ambazo zimekuwa zikitupata katika kusambaza pembejeo za kilimo. Nashukuru sana. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa pembejeo nyingi mwaka huu mawakala wengi walipewa muda wa kupeleka kwa wakulima na hazikufika kwa wakulima mwaka huu, mawakala wameshapewa na Kamati ile ya pembejeo za Wilaya na sasa pembejeo hazijafika.
Je, Serikali inatuambia nini kwa pembejeo hizi ambazo hazijafika wakulima bado wanasubiri na msimu umeshapita?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Flatei kwa sababu suala alilolileta kwenye swali la nyongeza limekuwa ni suala ambalo amelifuatilia mara nyingi sana Wizarani. Kimsingi amekuwa ni Mbunge mzalendo kama mlivyo wengi humu ndani. Ameniletea orodha ya Mawakala ambao walichelewa kuleta pembejeo Jimboni kwake lakini bado wanataka kulipwa. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Wakala ambaye hakuweza kuleta pembejeo kwa wakati hatalipwa. Kimsingi Wizara na Serikali haiwezi kulipa kwa huduma ambayo haijatolewa.(Makofi)
MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu marefu ya Mheshimiwa Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshiwa Naibu Spika, katika majibu yake Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba mashamba haya yamekuwa ya muda mrefu na uzalishaji wake umekuwa mdogo sana. Pia mashamba haya yanatumia hekari nyingi sana, kwa hiyo, yamechukua sehemu kubwa ya ardhi ya Tanzania. Pamoja na kukiri kwamba hakuna uhusiano baina ya Kiwanda ya General Tyre na mashamba haya. Namuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, je, Serikali iko tayari kuleta matumizi mbadala ya mashamba haya kwa sababu hayalisaidii Taifa?(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Kiwanda cha General Tyre si kiwanda kipya ni kiwanda cha zamani sana na kilikuwa kinazalisha. Hata hivyo, marekebisho yake naambiwa yafanyiwa utafiti, ukiuliza utafiti, ukiuliza utafiti, hakimaliziki kiwanda kufanyiwa utafiti ili kuzalisha. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri haoni kwamba hatujawa tayari kuingia katika Tanzania ya viwanda kwa mwendo huu?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kuhusu mipira au zao la mpira kuchukua ardhi kubwa na hiyo ardhi kutoweza kutumika kwa tija zaidi, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa mashamba ya mpira tuliyonayo hayajachukua ardhi kubwa sana. Tunachofikiria sasa kama Wizara na Serikali ni kujaribu kutafuta ardhi nyingine ili tuongeze uzalishaji wa mpira. Kwa sasa tunafikiri mpira soko lake limeimarika tena hata jirani nchini Kenya kuna soko, lakini vilevile China kuna soko kubwa. Kwa hiyo, sasa tunajaribu kuangalia namna ya kuwekeza tena kwenye mpira ili liwe tena ni zao ambao wakulima wetu wanaweza kunufaika nalo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa sasa hatufikirii ile ardhi iende kwenye matumizi mengine lakini tunachofanya ni kuendelea kuimarisha mashamba yaliyopo lakini vilevile kujaribu kuongeza ardhi nyingine ili kilimo cha mpira kiweze kupanuka. Vilevile kujaribu kuimarisha teknolojia ambayo tunatumia kwa sasa ili iweze kuendana na mahitaji ya sasa ya soko la mpira duniani.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kuhusiana na General Tyre. Kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, Serikali inaendelea kufanya tathmini kuhusu namna bora ya kurejesha tena Kiwanda cha General Tyre kiingie katika uzalishaji. Kimsingi tulichosema ni kwamba taarifa ya awali inaonyesha kwamba tunahitaji kuboresha teknolojia iliyopo, lakini vilevile mfumo wa uendeshaji uwe ni kwa utaratibu wa kushirikiana na sekta binafsi kwa maana ya PPP ili Serikali iweze kubakia na hisa chache tu na hasa zile zinazolingana na mali au uwekezaji ambao Serikali tayari umeshaufanya, lakini huku Serikali ikijaribu kuvutia wawekezaji ili iendeshwe kwa ubia na sekta binafsi. Kwa hiyo, siyo kwamba Kiwanda cha General Tyre kimetupwa lakini ni kwamba sasa jitihada zinaendelea ili kukifufua ili kiweze kufanya kazi tena.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Katika nchi yetu ajali za barabarani zimekuwa nyingi sana na moja kati ya sababu za ajili hizi ni matairi ya mitumba yanayoagizwa kutoka nje. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, labda niseme Tanzania ni nchi pekee ambayo inaagiza matairi ya mitumba ikijua kabisa kwamba matairi haya yanakuwa yamemaliza muda wake na inaweza ikawa kisababishi kikubwa cha ajali. Sasa wakati tukisubiri kiwanda hiki kufufuliwa, hadithi ambayo imekuwa ni ya miaka mingi, je, Serikali ina mpango gani wa kupiga marufuku uingizaji wa matairi yaliyotumika katika nchi ambayo yanasababisha ajali?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba ajali za barabarani zimeendelea kuongezeka nchini na inawezekana kama anavyosema Mheshimiwa Mbunge kwamba matairi yasiyo na ubora ni moja kati ya visababishi. Kimsingi suala la ajali za barabarani ni suala ambalo Serikali linalichukulia kwa uzito sana, ni kero kubwa inaondoa maisha ya wananchi wetu. Kwa hiyo, Serikali inaangalia ni namna gani ya kudhibiti ajali hizo ikiwa ni kuangalia visababishi kama hilo la matairi, kwa sababu kuna visababishi vingine mfano uendeshaji usiozingatia utaratibu, uendeshaji kupita speed inayotakiwa, lakini vilevile madereva kulewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi Serikali inaangalia suala la ajali katika ujumla wake na visababishi vile itahakikisha inavifanyia kazi ili tuendelee kupunguza ajali barabarani. Kwa hiyo, kama hilo la matairi ni moja ya visababishi kwa vyovyote vile Serikali inalifanyia kazi.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, shamba la Kihuhwi ambalo
lipo Wilayani Muheza ni kweli lilikuwa linalima mpira na linaendelea kulima mpira na lilikuwa lina- supply kwenye kiwanda cha General Tyre - Arusha. Sasa hivi shamba hilo ni moja ya mashamba ambalo limeshafutiwa hati na Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Naibu Waziri, haoni sasa kutokana na matatizo ya Kiwanda cha General Tyre - Arusha, mikakati ifanyike kiwanda hicho kiwe na mashine za kisasa na kihamishiwe Wilayani Muheza ambapo nafasi tunaweza kutoa na kiwe karibu na malighafi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge anapendekeza kwamba tuhamishe Kiwanda cha General Tyre tupeleke Muheza. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari kuna timu inafanya kazi ya kuangalia namna bora ya kufufua Kiwanda cha General Tyre.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nimhakikishie tu kwamba nitawapelekea pendekezo la kuangalia kama inawezekana kupeleka Muheza, lakini zaidi zaidi ni vizuri vilevile kuangalia uwezekano wa kuanzisha kiwanda kipya Muheza.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ili wananchi waupende ushirika ni pamoja na kuona kuwa mali zao ziko salama na wananufaika.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuuliza Serikali, kwa Vyama vya Ushirika ambavyo mali zake zimetapanywa yakiwemo mashamba, viwanja, nyumba, hususani KNCU, Serikali inasaidiaje ili kurejesha mali hizo ili wananchi wanufaike? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Serikali inasaidiaje mikataba mibovu iliyoingiwa na Vyama vya Ushirika na wale ambao wamechukua mali za vyama hivyo iletwe ili irekebishwe wananchi hao waweze kuona sasa ushirika wao unaendelea vizuri?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba baadhi ya mali za Vyama vya Ushirika zimetapanywa na hazitumiki kwa utaratibu unaotakiwa na ndiyo maana Wizara yangu kwa kushirikiana na Maafisa Ushirika nchini kote kwa sasa wanafanya tathmini kuhusiana na mali zote za Vyama vya Ushirika ili kujua ni zipi ambazo hazitumiki, zipi ambazo zimeingia mikononi mwa watu binafsi kinyume na taratibu, kwa lengo la kuhakikisha kwamba zile ambazo zimechukuliwa kinyemela ziweze kurudi, lakini vilevile ili mali hizo za ushirika ikiwa pamoja na ardhi ziweze kutumika katika mazingira ambayo yanaleta tija zaidi na kwa manufaa ya ushirika na wana ushirika wenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile Mheshimiwa Mbunge ameuliza swali la pili kwamba tunafanyaje kurejesha mali ambazo zilichukuliwa kinyume na taratibu. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa tokeo Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, tumechukua hatua kadhaa za kuhakikisha kwamba uovu uliokuwa ukifanyika katika Vyama vya Ushirika hautokei tena. Kwa hiyo, wale wote ambao wamehusika katika kufanya ubadhirifu na upotevu wa mali za ushirika wanachukuliwa hatua za kisheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile hata viongozi wa Vyama vya Ushirika ambao nao wanakuwa ni sehemu ya ubadhirifu huo tumeendelea kuwachukulia hatua. Ni hivi karibuni tu tumevunja Bodi za Vyama vya Ushirika zaidi ya 200 Mtwara na Lindi. Vilevile mmesikia yaliyotokea Nyanza, jitihada zinaendelea kurudisha mali za Ushirika wa Nyanza. Pia tunajitahidi kuendelea kusaidia vyama vingine ambavyo siku za nyuma kimsingi taratibu zilikiukwa na mali zao kwenda nje kwa watu binafsi bila kufuata utaratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na maswali haya na jitihada za Serikali, naomba niendelee kuwaomba Waheshimiwa Wabunge wahamasishe wanaushirika wawaeleze kwamba ushirika ni wa kwao, Serikali yenyewe inasaidia. Kwa hiyo, inatakiwa wenyewe wawajibike kuhakikisha kwamba mali za ushirika zinalindwa na pale kasoro zinavyotokea basi watoe taarifa kwa Serikali ili tuweze kuchukua hatua.
MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Naomba nianzie pale ambapo Naibu Waziri wa Kilimo ameishia, kwamba Bodi ya Nyanza (Nyanza Cooperative Union) na yenyewe pia imekuwa ikilegalega. Je, ni kwa namna gani Serikali inaweka mikakati ya kuhakikisha wakulima wa pamba Mkoani Mwanza wanafaidika na Nyanza Cooperative Union na kushirikishwa katika vikao vinavyoendelea katika Bodi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, jitihada zinazoendelea kushughulikia changamoto ambazo zimekikumba Chama cha Ushirika wa Nyanza ni kwa ajili ya kuwanufaisha wakulima wa pamba ambapo kimsingi chama kile kilianzishwa kwa ajili ya kuwasaidia. Kwa hiyo, tunavyojaribu kurudisha mali zile ambazo zilichukuliwa kinyume na taratibu, tunaamini baadaye zitaendelea kuwaongezea wakulima wa pamba wanachama wa Nyanza katika kuendeleza zao la pamba. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba maboresho ambayo tunayafanya na ufuatiliaji ambao tunaufanya yote lengo lake kubwa ni kuwasaidia wakulima wa pamba.
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Kwa kuwa matatizo yaliyoko sehemu nyingine ya Vyama vya Ushirika ni sawa na tatizo lililoko kwenye Mkoa wa Pwani kwa Coastal Region Cooperative Union - CORECU, majengo yake kutaka kuuzwa na kununuliwa na wajanja wachache. Je, Serikali ina kauli gani juu ya ku-rescue hali hiyo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba Chama Kikuu cha Ushirika cha Pwani - CORECU kimekuwa kikipita katika wakati mgumu pamoja na mambo mengine kwa sababu ya madeni makubwa ambayo yameendelea kutishia uhai wa chama hicho. Hivi tunapozungumza CRDB ambao wamekuwa wakikidai chama hicho fedha nyingi, tayari walishaenda mahakamani na taratibu zilianza za kutaka kuuza mali za CORECU. Ni suala ambalo limetokana na mchakato wa kimahakama lakini pamoja na hayo, Serikali na Wizara inaendelea kufanya majadiliano kuangalia namna gani ya kunusuru mali zile zisiuzwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee kurejea kusema kwamba naomba Waheshimiwa Wabunge tutoe elimu kwa wanaushirika kwamba wao ndiyo hasa inatakiwa wawe watu wa kwanza kulinda mali za ushirika. Kwa sasabu wanapoingia kwenye mikataba ambayo inahatarisha mali zile, baadaye ni vigumu sana Serikali kusaidia kwa sababu inakuwa ni suala la kisheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Serikali ilisaidia sana kujaribu kuondoa changamoto ya CORECU kwa sababu hata kwenye mkopo ambao wanadaiwa Serikali ilishasaidia kulipa baadhi ya fedha, nafikiri imelipwa zaidi ya shilingi bilioni moja. Hata hivyo, nimueleze Mheshimiwa Mbunge kwamba jitihada zinaendelea kuangalia ni namna gani ya kunusuru mali za CORECU zisiuzwe.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Zaidi ya nusu ya Vyama vya Ushirika nchini havijafanyiwa ukaguzi kazi ambayo ilipaswa kufanywa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika. Kutokana na uwezo mdogo wa Tume yetu wa kifedha na watendaji tumeshindwa kufanya hivyo. Serikali ina mkakati gani wa kuiwezesha Tume ya Ushirika iweze kufanya kazi yake kikamilfu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge kwamba kumekuwepo na changamoto ya kufanya ukaguzi kwenye Vyama vyote vya Ushirika. Kwa sasa Wizara na Tume ya Ushirika imejipanga kuhakikisha kwamba katika mwaka unaokuja wa fedha Vyama vyote vya Ushirika vinakaguliwa, lakini zaidi kuweka mfumo ambapo utaratibu wa ukaguzi utakuwa unafanyika mara kwa mara bila kukosa.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nilipenda niseme kama ifuatavyo:-
Suala la uingizaji wa dawa za kilimo zisizokidhi vigezo limekuwa sugu katika nchi yetu. Hata hivyo Mheshimiwa Waziri ameeleza mamlaka mbalimbali ambazo zinahusika katika kuhakiki hizo dawa na uingizaji. Nilipenda kujua ni hatua zipi zimekuwa zikichuliwa kwa makampuni hayo ambayo yamekuwa yakileta dawa ambazo hazikizi vigezo; hasa kwa sabau zinaleta mzigo mkubwa kwa wakulima wetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Serikali inaendelea kupitia tozo mbalimbali katika sekta ya kilimo ili kuona uwezekano wa kuziondoa tozo hizo. Nilipenda kujua kwamba zoezi hilo la kupitia hizo tozo ambazo zimekuwa mzigo kwa wakulima wetu litaanza lini ili kuleta unafuu kwa wakulima wetu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na uingizwaji wa dawa ambazo hazikidhi viwango ni kweli kabisa kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge kwamba tuna changamoto hiyo. Hata hivyo Serikali imeendelea kudhibiti na kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha tatizo hilo linamalizika ili kuhakikisha kwamba wakulima wetu hawaathiriwi na viuatilifu ambavyo si salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya hatua ambazo tunazichukua ni kwamba pale tunapogundua, kwamba Kampuni fulani imeingiza dawa ambayo si sahihi, mara nyingi Kampuni ile inafutiwa leseni, lakini vile vile kama ni maduka tunayafunga, lakini tayari vile vile kuna kesi nyingi ambazo ziko Mahakamani kwa watu na Makampuni ambao wamebainika kuvunja taratibu za Kisheria kuhusiana na viuatilifu pamoja na dawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana 2016 tulifanikiwa kukamata viuatilifu lita 14,600 ikiwa ni sehemu ya ufuatiliaji wa kawaida wa kuhakikisha kwamba wakulima wetu wanapata viuatilifu na dawa salama. Ifahamike tu kwamba viuatilifu vingi ambavyo vinaingia ambavyo havikidhi viwango vingi vinatoka nje na hiviingizwi kwa utaratibu wa njia rasmi, zinapitia katika uchochoro, katika panya roads. Kwa hiyo, mara nyingi wahalifu kila wakati wanagundua njia mpya ya kuhakikisha kwamba wanakwepa mkono wa Sheria lakini Serikali imeendelea kuhakikisha kwamba kila wakati yule ambae anahusika anachukuliwa hatua za kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na tozo, nafikiri Mheshimiwa Mbunge amekuwepo, kwa sababu sasa tunaendelea na mjadala wa Wizara yetu, kwamba tayari Wizara imependekeza kufuta tozo 108, tozo ambazo tunahakika zikifutwa zitamsaidia sana mkulima, mfugaji na mvuvi wa Tanzania katika kuendelea kunufaika na kilimo, ufugaji na uvuvi wao. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge aendelee kufuatilia kwa sababu tayari tumeishaondoa hizo tozo, lakini Wizara inaendelea kuongea na Wizara zingine ambazo zinasimamia baadhi ya tozo ili tuendelee kuziondoa au kuzipunguza.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa viuatilifu hivi kwa kweli imekuwa ni hasara kubwa sana kwa wakulima, na kwa kuwa wakulima wa Jimbo la Bariadi na Jimbo la Busega katika msimu huu wamelima sana zao la mahindi lakini limeshambuliwa na funza, kitu ambacho kimesababisha watapata uhaba wa chakula, je, Serikali inachukua hatua gani za makusudi ili watu hao wanaoingiza viatilifu ambavyo havifai na viko chini ya viwango wanadhibitiwa na wanapewa adhabu kali?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye maelezo yangu ya awali; kama Mheshimiwa Mbunge anawafahamu watu au makampuni ambao wameingiza viuatilifu ambavyo haviko katika ubora unaotakiwa kisheria tutawachukulia hatua. Hata leo hii hii akinipa list yao tutaanza kufanyia kazi na kuchukua hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kuwafungia na kuwaondolea leseni ya kuagiza na kuuza viuatilifu lakini vile vile kuwapeleka Mahakamani kwa sababu ni kinyume cha Sheria kuuza dawa na viuatilifu ambavyo havina ubora.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Naomba Mheshimiwa Naibu Waziri unisikilize vizuri. Msimu uliopita wa mwaka juzi, wakulima wa pamba wote wa Kanda ya Ziwa walilazimishwa kutumia dawa ya kuua wadudu inayoitwa Ninja. Dawa hiyo ilikuwa inasambazwa na Bodi ya Pamba na haikusaidia kabisa na pamba iliharibika kabisa kwa sababu haikuwa na ubora. Niliuliza swali hapa Bungeni nikaahidiwa na Serikali kwamba, na yenyewe imethibitisha kwamba suala hilo ni kosa la uhujumu uchumi, kwa hivyo, wahusika watapelekwa mahakamani na wakulima watalipwa fidia ya gharama waliyotumia kununua ile dawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kujua kwamba Serikali imefikia wapi katika utekelezaji wa hilo jibu ambalo Serikali iliniambia hapa Bungeni?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama anavyosema Mheshimiwa Mbunge kwamba iligundulika kwamba ilitokea matatizo makubwa kwa wakulima wa pamba waliotumia kiuatilifu ambacho kilikuwa kinatiliwa shaka kuhusu ubora wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea na uchunguzi kubaini ni nini hasa kilitokea, kwa sababu tayari kuna mvutano kuhusu je, suala lilikuwa ni ubora wa dawa, namna ya matumizi, namna ya matunzo au ni suala la wakulima wenyewe walivyotumia ile dawa. Kwa hiyo, Serikali bado inaendelea na uchunguzi, lakini pale itakapobainika kwamba ni kweli kabisa kwamba suala ni kuhusu ubora sheria zitachukua mkondo wake. Kama nilivyosema, itakuwa ni pamoja na kuwafungia na kuwachukulia hatua wale wote ambao wamehusika. Vile vile ikibainika kwamba kampuni ambazo zili-supply hiyo dawa kwa Bodi ya Pamba wao watawajibika moja kwa moja katika kuhakikisha kwamba wakulima wanalipwa fidia. Hata hivyo kama nilivyosema suala hili bado linachunguzwa, tufahamu hasa kiini kwa sababu bado kuna mvutano kuhusu sababu hasa yenyewe iliyosababisha tatizo hilo.
MHE. DKT. CHRISTINA G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nashukuru kwanza kwa majibu mazuri ya Serikali, hata hivyo lakini nina maswali mawili mafupi. Swali la kwanza, kuwa wakulima wengi sasa hivi wamechangamkia kilimo cha miembe na kwa kuwa Serikali imetoa mwongozo wa mafunzo kwa Maafisa Kilimo 117 tu; na kwa kuwa ni vikundi 19 tu vimepewa mafunzo; je, Serikali haioni haja kuweka mpango wa kutoa mafunzo zaidi ya maafisa kilimo ili kuweza kueneza kilimo hiki cha miembe ambacho kimechangamkiwa sana na wananchi sasa hivi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Serikali imekiri kuwa imeanza utafiti, naipa pongezi na kwa kuwa mpaka sasa hivi Serikali imetoa starter kit kwa kikundi cha wakulima ambacho kinalima maembe tu. Hiki kikundi cha wakulima sana kimejikita Mkoa wa Pwani ambapo Mikoa ya Morogoro, Tanga mpaka Zanzibar, Tabora wanalima maembe na kwa kuwa ni lita 560 tu za kivutia wadudu zimetolewa tu. Je Serikali haioni kuwa kuna umuhimu wa kutoa starter kit angalau moja kwa mikoa hii inayolima miembe na kuongeza hii dawa ya kivutia wadudu kwa mikoa hii ili wakulima waweze kuendelea na kilimo hiki cha miembe?
Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia nawapa hongera sana vijana wangu wa SUA na wajasiriamali na Chuo cha SUA ambao wanaeneza miche ya miembe, hongereni sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kwanza nakubaliana nae kwamba mafunzo zaidi kwa Maafisa Kilimo yanahitajika na kwa fursa hii namwelekeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Engineer Mtigumwe aandae mafunzo zaidi na hasa kwa maeneo yaliyotajwa ambayo yanazalisha maembe zaidi.
Mheshimiwa Spika, swali la pili kuhusu kugawa starter kit na dawa hii ya eugenol ya kivutia wadudu nayo nakubaliana nayo tutaangalia uwezekano wa kupata fedha zaidi ya kuweza kueneza hizi starter kit kwa vikundi vya wakulima zaidi ya hicho kikundi kimoja kilichopata.
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninalo swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hamasa pia mkakati wa Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya kuhamasisha uendelezaji wa zao hili, lakini bado hadi sasa kipo kiwanda kimoja tu kinachopokea mazao haya ambapo kipo Kisiwani Pemba. Je, Serikali inawaambia nini wananchi katika uendelezwaji wa viwanda hasa katika mkakati huu wa uendelezaji wa viwanda nchini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba kwa sasa bado kuna changamoto kubwa ya kuwa na viwanda vya usindikaji kwa ajili ya mazao ya mdalasini na mchaichai na kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge, kwa sasa tuna kiwanda kimoja kikubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili tuweze kuongeza thamani katika mazao haya, ni lazima tuchukue hatua za makusudi kuhakikisha kwamba kunakuwa na viwanda vya kutosha. Kwa sasa sambamba na kutafuta fursa za kujenga viwanda, Serikali bado inatilia mkazo zaidi kuongeza uzalishaji kwa sababu uzalishaji uliopo wa sasa ni mdogo sana kuweza kuvutia uwekezaji kwenye viwanda. Kwa hiyo, rai yetu kwa Waheshimiwa Wabunge wanaotoka maeneo yale yanayolima mchaichai na mdalasini waendelee kuhamasisha wakulima walime zaidi ili tuweze kuwa na uzalishaji wa kutosha wa kuweza kuvutia viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii kuwafahamisha Waheshimiwa Wabunge kwamba mdalasini na mchaichai ni mazao ambayo wengi wetu hatujui faida zake, lakini ukweli wa mambo ni kwamba ukiacha faida ya mazao haya kwa burudani kama kinywaji lakini vilevile inatibu magonjwa mengi. Hata hivyo, nilivyokuwa nasilikiza swali lile Namba 21 la Mheshimiwa Khatib Said Haji hata zile changamoto alizoelezea kwa ufahamu wangu ni kwamba hata mdalasini na mchaichai navyo husaidia kuondoa changamoto hizo.
MHE. CATHERINE N. RUGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri maswali mawili ya ngongeza. Katika jibu lako la msingi Mheshimiwa Naibu Waziri, ameonesha kwamba kuna mpango wa matumizi bora ya ardhi katika vijiji vinne na tayari hekta 6,000 zimeshapangwa kwa ajili ya mradi huo. Ni dhahiri kulikuwa na wananchi wa vijiji hivyo wanaozunguka Bonde la Mto Mara ambao walikuwa wanafanya shughuli zao za kilimo, ufugaji na uvuvi wa samaki. Napenda kujua; Je, Serikali imetenga eneo gani mbadala na fidia ili wananchi waendelee kunufaika na shughuli zao sambamba na uwekezaji huo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; Mkoa wa Mara umekuwa uki-experience vipindi virefu vya ukame vinavyotokana na mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira. Je, Serikali imejipangaje kuhakikisha uwekezaji huu hauendi kuathiri bioanuwai pamoja na mfumo mzima wa Serengeti Ecosystem ambayo Bonde la Mto Mara ni sehemu ya mradi huo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama kuna wananchi ambao wataathirika katika mradi huo ni dhahiri kwamba hatua zozote zitachukuliwa kuhakikisha kwamba madhara hayo yatapunguzwa ikiwa ni pamoja na kampuni ambayo itahusika katika kufanya uwekezaji kulipa fidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile mradi huu ni mradi wa siku nyingi sana, umekuwa ukifikiriwa tokea miaka ya sabini, kimsingi eneo lile lina hekta 14,000 na kwa muda huo wote jitihada zimekuwa zikifanyika kuwaeleza wananchi kwamba sehemu hiyo itatumika kwa ajili ya shughuli ya kilimo cha miwa na kiwanda cha sukari, lakini kama kuna wananchi ambao wataathirika watafidiwa kwa taratibu zilizopo za sheria zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Mheshimiwa Mbunge ameuliza swali muhimu sana linalohusiana na athari za kimazingira ambazo zinaweza zikajitokeza kwa maji ya Mto Mara kutumika kwa ajili ya shughuli ya kilimo vilevile kwa ajili ya shughuli ya kiwanda kile. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kabla mradi haujaanza ni lazima tathmini ya kina ya mazingira ifanyike ikiwa ni pamoja na tathmini ya kijamii ili athari zozote zile ambazo zinaweza zikajitokeza ziweze kuangaliwa na ikiwezekana kama athari zile zitakuwa ni mbaya sana mradi usiendelee.
Mheshimiwa Naibu Spika, ikolojia ya Serengeti ni muhimu kwa ajili ya nchi yetu. Kwa hiyo kwa vyovyote mradi wowote ambao una hatari ya kuathiri katika njia mbaya hautaweza kuendelea. Nimhakikishie tu kwamba ni lazima tathmini itafanyika ili kuzuia uharibifu wowote.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize maswali madogo ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali madogo mawili:-
Kwa kuwa, dhamira ya Serikali hii ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha wananchi wake wanajitegemea hasa katika suala la chakula, pia kuhakikisha wananchi hawavamii hifadhi zilizotengwa kwa ajili ya kuhifadhi wanyama na misitu ya hifadhi. Pia kwa kuwa eneo langu la Itigi eneo wananchi ni asilimia 35 tu, asilimia 65 ni eneo ambalo limetengwa kwa ajili ya hifadhi ya Wanyamapori ya Rungwa, Muhesi na maeneo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, shamba hili ndiyo shamba lenye rutuba na ndiyo shamba ambalo lina kiwango kizuri cha kufanya wananchi waweze kunufaika na kujitegemea kwa chakula na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kilimo alipokuja Itigi katika mkutano wake wa hadhara na wananchi aliwaambia na kuwahakikishai wananchi kwamba shamba hili sasa litarudishwa kwa wananchi;
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kilimo na shamba hili liko kwenye Wizara ya Kilimo, aliwadanganya wananchi wa Itigi kwamba atawarejeshea shamba hili?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa Kampuni hii ya Tanganyika Packers ilishafilisika, haipo kisheria na ilishafutwa, je, sasa Serikali iko tayari kutekeleza yale ambayo Mheshimiwa Rais alipokuja Itigi alisema kwamba atawasaidia wananchi wa Itigi shamba hili ili liwanufaishe jamii nzima?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa nilipofika Itigi nilitoa ahadi kwamba Serikali itachukua hatua kuhakikisha kwamba shamba analolizungumzia litarudi kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimfahamishe Mbunge kwamba utaratibu huo umeshaanza kwa sababu Wizara ambayo awali ndiyo ilikuwa inamiliki hilo shamba imeshawasilisha taarifa kwa Treasury Register ili utaratibu wa kurudisha utaratibu kwa wananchi na hasa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi iweze kufanyika. Kwa hiyo, naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba siyo uwongo, hatukudanganya lakini mchakato unaendelea.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nasikitika kwa majibu ya Naibu Waziri kwa kusema kwamba mbegu hizi sio ghali. Mbegu hizi ni ghali. Mkulima anapotaka kupanda walau eka moja tu ambayo hata haiwezei kutosha chakula chake cha mwaka inabidi atumie zaidi ya shilingi 60,000 sasa kama shilingi 60,000 kwa eka sio ghali sijui Waziri ametumia kipimo gani!
Mheshimiwa Spika, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Asilimia kubwa ya mbegu hizi pia zinatoka nje ya nchi na zinazalishwa katika mazingira tofauti na ya wakulima wetu jambo ambalo pia zinapoingizwa nchini inaongeza gharama hizi kwa mfano mbegu aina ya seedco, mbegu aina ya hybrid. Sasa miaka ya nyuma tulikuwa na Shirika letu la TANSEED lilikuwa linasaidia sana wakulima kupata mbegu hizi.
Je, Serikali ina mpango gani wa kufufua Shirika la TANSEED au mashirika mengine ya aina hiyo ili mbegu hizi ziweze kuzalishwa hapa nyumbani katika mazingira ya wakulima wetu hatimae bei pia iweze kupungua.
Swali la pili, asilimia 60 hadi 80 ya mahindi yote yanayolimwa nchini yanatumika kwenye kaya zetu. Asilimia 20 tu inaingia kwenye eneo la biashara, lakini changamoto ambayo wananchi wetu wanakutana nayo ni suala la uhifadhi wa mazao haya kwa kipindi chote cha mwaka. Mifuko ya kuhifadhia mahindi aina ya PICS (Purdue Improved Crop Storage) pamoja na hata zile dawa za shamba shumba, hizo bei kwa kweli zko ghali kiasi kwamba wakulima wanashindwa kuzinunua na mazao yao yanaharibika.
Je, Serikali iko tayari sasa kuingiza pembejeo hizo za uhifadhi wa nafaka ili zipunguze bei, wananchi wazipate kwa bei rahisi wakati zikiwa kwenye ruzuku. Nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimuombe sana jirani yangu asisikitike kwa sababu nitajisikia vibaya sana, Karatu ni jirani na Ngorongoro kwa hiyo ningependa sana afurahi.
Mheshimiwa Spika, vilevile nimweleze kwamba akifanya mahesabu sawasawa kwa kweli mbegu bora siyo ghali, kwa sababu mfuko wa kilo kumi wa mbegu ya mahindi aina ya OPV ni shilingi 40,000 wakati bei ya chotara ni shilingi 30,000.
Sasa katika mfuko wa kilo kumi unaweza ukatumia kwenye heka moja ambayo unaweza ukapata gunia mpaka 30 na gunia moja Karatu inauzwa shilingi 50,000 maana yake gunia moja tu ukipata kwa mwaka unaweza ukahudumia heka moja na ukapata magunia mengine mengi. Kwa hiyo, ni suala la hamasa wananchi kuelewa umuhimu wa kutumia mbegu bora.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo niendelee kujibu maswali yake kwamba ni kweli kama alivyosema kwamba bado tunaagiza asilimia kubwa ya mbegu zetu kutoka nje, lakini kwa sasa Wizara na Serikali imejikita katika kuondoa tatizo hili ASA ambayo ndiyo Kampuni yetu ya Taifa ya Kuzalisha Mbegu, wameelekezwa sasa watumie mashamba yao mengi waliyonayo katika maeneo mbalimbali kwa mfano Mbozi, Bugaga, Msamba na Kilingali, Dabaga, Ngaramtoni ili kuongeza uzalishaji wa mbegu bora. Vilevile Serikali imeondoa vizingiti vilivyokuwa kwenye Sheria ya Mbegu ili kampuni binafsi ziweze sasa kwa urahisi zaidi kuzalisha mbegu ambazo zimetafitiwa na taasisi zetu za utafiti. Kwa hiyo, tunategemea tunavyozidi kwenda hiyo changamoto ya kutojitosheleza kwa mbegu itapungua na katika wa mkakati mpango wetu wa kilimo wa pili wa SDP II kuna mkakati mkubwa sana wa kuongeza uzalishaji wa mbegu.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ni kuhusiana na uhifadhi wa chakula, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa Wizara imejikita katika kuongeza uwezo wetu wa kuhifadhi chakula kwa sasa tuna uwezo wa kuhifadhi nafaka ya tani 250,000 lakini tayari tumesaini mkataba na makampuni mawili ili kujenga maghala saba katika maeneo mbalimbali, ikiwepo ghala itakayojengwa Babati ili tuweze kuongeza uwezo wetu na hatimaye kufikia tani 500,000. Tunaamini katika miaka miwili ijayo tutakuwa na uwezo wa kuhifadhi nafaka tani 500,000 na hivyo wakulima wake wa Karatu wakitaka wanaweza wakahifadhi kwa mpango maalum ambao utawekwa na NFRA katika ghala na kihenge kitakachojengwa Babati.
Mheshimiwa Spika, vilevile nimhakikishie kwamba mifuko ile ya kuhifadhi nafaka ambayo haingiliwi na wadudu kama mifuko ya PICS kwa sasa inapatikana kwa bei nzuri sana. A to Z wanazalisha mifuko ile kwa bei ya jumla ya wastani wa shilingi 2,700 kwa mfuko kwa hiyo kwa mkulima ambaye anahitaji mifuko mingi kwa kweli shilingi 2,700 kwa kuhifadhi mazao yale kwa muda mrefu bado ni bei ambayo inahimilika lakini vilevile Serikali inafikiria kuendelea kupunguza gharama za kikodi katika uzalishaji wa mifuko hiyo ili kwa mfano hiyo mifuko ya PICS iweze kupatikana kwa bei nzuri zaidi.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kupata tafsiri ya jina langu.
Mheshimiwa Spika, kwa kweli nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali yanayotia moyo, pamoja na kuwepo na jitihada za kuweka mfumo mzuri wa masoko, bado mfumo wa masoko umedhoofishwa na kuwepo kwa wanunuzi wachache ambao wamekuwa wakiwadidimiza wakulima kwa bei isiyokuwa ya ushindani.
Swali la kwanza, je, ni kwa nini zao la pareto lina mnunuzi mmoja ambaye anajipangia bei anavyotaka mwenyewe?
Swali la pili, je, ni kwa nini tumeshindwa kuanzisha soko la bidhaa (commodity exchange) ambayo imekuwepo toka mwaka 2014?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Spika, kwa nini soko la pareto lina mnunuzi mmoja. Naomba nimueleze Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kipindi kirefu pareto imekuwa inanunuliwa na mtu kwa sababu masharti yaliyopo katika ununuzi wa zao la pareto ni kwamba ni lazima mnunuzi awe na kiwanda kwa sababu kinachouzwa kwenye pareto siyo maua ni ile sumu. Sasa kama hatujui kiwango cha sumu kilichopo kwenye maua ni vigumu sisi kujua bei ambayo wakulima wetu wanapata vilevile ni vigumu hata kukokotoa kodi ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, naomba nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa kuna kiwanda cha pili kimejengwa Mbeya, kwa hiyo tunaamini kwamba kitaongeza ushindani. Nafahamu ameshaniletea malalamiko mara nyingi sana kwamba pamoja na kuja na hichi kiwanda bado kuna vizingiti vya kuhakikisha kwamba kiwanda cha pili nacho kinaruhusiwa kununua pareto, naomba tu nimhakikishie yeye pamoja na wakulima wake kwamba mimi mwenye nitafuatilia kuhakikisha kwamba huyu mnunuzi mpya aliyeingia sokoni anaruhusiwa kununua bila vizingiti vyovyote.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili la commodity exchange. Ni kweli kwamba kwa muda sasa Serikali imekuwa ikifikiria kuanzisha mfumo wa commodity exchange kama namna mojawapo ya kutafuta masoko kwa ajili ya mazao yetu. Ili tuweze kuanzisha mfumo wa commodity exchange ambayo kimsingi ni mfumo wa kisasa zaidi wa stakabadhi ghalani unaotumia teknolojia kubwa zaidi na unaoweza kuunganisha mazao yetu katika soko la dunia tunahitaji vitu vingi sana ikiwa ni pamoja na teknolojia yenyewe ni lazima tuwe na maghala ambayo yanakidhi sifa za Kimataifa, vilevile lazima tuweze kufanya na uzalishaji ule wa bidhaa ambao unapatikana kwa quality ile ambayo inahitajika na kwa viwango ambavyo soko la dunia linahitaji.
Kwa hiyo, tunafikiri kwamba wakati tunaendelea kuboresha mazingira yetu ya ndani tutaendelea kwa sasa kutumia utaratibu wa stakabadhi ghalani na tumeona mafanikio makubwa sana kwenye korosho na tayari tunaelekea kutaka kuuza mazao mengine kama mbaazi, ufuta kwa kutumia utaratibu huo. Kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba hatujalitupa lakini bado tunaboresha mazingira ili iweze kufanikiwa kwa urahisi zaidi.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Ingawa Serikali ina mpango sana wa kufungua mabenki ya wakulima, je, Serikali haioni kama tatizo hiyo benki inafilisika kwa kuwa wakati wa msimu mkulima analazimishwa asiuze mazao bei anayotaka? Kwa mfano, mahindi kule kwetu yanashuka bei, mengi hakuna mahali pa kupeleka.
Je, Serikali haioni kwamba iweke sheria mtumishi abanwe mshahara wake ili asiutumie hovyo ili wakati wa matatizo awasaidie majirani zake kama vile wakulima wanavyofanywa ili wasiuze mazao wasaidie sehemu zenye njaa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Spika, nashukuru unaelekea kunilinda tusifungue suala hilo kwa sababu ni jambo zito lakini naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, kwa sasa tunatambua changamoto ambayo imeletwa na zuio la kuuza mahindi nje kitu ambacho kimefanyika na Serikali kwa nia njema. Kwa sasa Serikali inajitahidi kuongea na WFP ya Serikali ya DRC Congo vilevile Sudan ya Kusini ili kuangalia namna ya wakulima wetu kuweza kuuza mahindi nje.
Mheshimiwa Spika, naomba tu niendelee kusema kwamba zuio hilo halina nia mbaya lakini tunajitahidi kuhakikisha kwamba nchi yetu inakuwa na usalama wa chakula. Vilevile tunajaribu kuangalia kama tutapata fedha ili NFRA iweze kununua mahindi mengi zaidi lakini Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko nayo imekaribia kupata mkopo wa kununua zaidi ya tani 10,000. Kwa hiyo, tunaamini pamoja na changamoto iliyopo tutahakikisha kwamba baadhi ya mahindi ya wakulima yataweza kununuliwa.
Mheshimiwa Spika, kubwa zaidi tunaendelea kutoa rai kwa wafanyabiashara wanunue mahindi maeneo ambayo yanapatikana kwa wingi ambayo bei yake bado ni nzuri na wapeleke maeneo ambayo hayajapata mavuno vizuri, kwa mfano mwaka huu tuna uhaba wa chakula Mwanza, Simiyu, Shinyanga huko kote kunahitajika chakula. Kwa hiyo, wafanyabiashara wetu watumie kama fursa kwa sababu mara nyingine tunaposema tutoe fursa ili wakulima wetu wauze mahindi nje, ukweli wa mambo wanaouza mahindi nje siyo wakulima ni walanguzi. Mara nyingi mkulima bei anayoipata bado ni ndogo ile ile wala haifanani na ikikaa kidogo na akauza baadaye ndani.
Mheshimiwa Spika, vilevile lengo letu la kuongeza uwezo wetu wa kuhifadhi chakula ni ili wakulima wetu waweze kuhifadhi ili ikiwezekana wauze kwa utaratibu wa stakabadhi ghalani ambayo wanaweza wakapopeshwa fedha na mabenki kwa kutumia akiba yao ambayo itakuwepo kwenye maghala.
MHE. LATHIFAH H. CHANDE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Serikali ilisema kwamba itagawa sulphur bure na matokeo yake sulphur iliyogaiwa, nyingi ilikuwa ni feki na nyingine ilikuwa imeshapitwa na muda, yaani ime-expire. Hii inaweza kupelekea kuharibu zao hili la Korosho. Sasa Je, Serikali ikiwa kama mdhibiti, ilikuwa wapi mpaka hii sulphur ikaweza kuingia nchini na hadi kumfikia mkulima?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili ni kwamba, sasa hivi Mkoa wa Lindi wamelima kwa wingi zao la choroko na mbaazi ambalo wamekosa soko hadi kupelekea gunia moja la kilo 100 kuuzwa kwa Sh.15,000/=.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hapo miaka ya nyuma, Bunge hili lilipitisha Sheria ya Exchange Commodity ambapo ilikuwa na mpango wa kuanzisha Exchange Commodity Market na mpaka dakika hii tayari Ofisi kwa ajili ya Exchange Commodity Market imepatikana na hadi savers zimekuwa set up lakini hakuna operation zozote zinazoendelea; kitu ambacho soko hili la Exchange Commodity lingeweza kuwasaidia wakulima waweze kupata soko la uhakika kwa ajili ya mazao mbalimbali. Sasa je, Serikali ina mpango wa kuanza lini operations katika Commodity Exchange Market? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na viuatilifu au sulphur feki au iliyopitwa na wakati, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote kwamba hakuna sulphur feki wala iliyopitwa na wakati ambayo imesambazwa kwa wakulima. Naomba yeyote mwenye ushahidi wa mkulima mmoja tu ambaye ameuziwa au amepewa sulphur feki au ambayo imepitwa na wakati anipe ushahidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nawahakikishia kwamba hakuna sulphur feki wala ambayo imepitwa na wakati ambayo imesambazwa kwa wakulima. Kilichotokea katika taarifa zile mlizoona kwenye vyombo vya habari ni kwamba kulikuwa na sulphur ambayo iko kwenye maghala ambayo imepitwa na muda, ime-expire lakini haikuwa kwa ajili ya kugawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili la commodity exchange, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba utaratibu wa commodity exchange hautafuti soko, yaani siyo kwamba ukishatumia commodity exchange basi unakuwa na uhakika wa soko. Kama soko halipo ni kwamba halipo tu. Commodity exchange haina tofauti kimsingi na utaratibu wa sasa tunaotumia wa stakabadhi ghalani. Tofauti yake kidogo tu ni kwamba yenyewe inatumia teknolojia zaidi, lakini kama hakuna mnunuzi hutapata kwa kutumia commodity exchange.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, nimhakikishie kwamba Serikali kwa sasa imejiwekeza zaidi katika kuimarisha utaratibu tulionao wa stakabadhi ghalani kwa sababu ili tuweze kufikia kwenye commodity exchange tunahitaji vitu vingi. Tunahitaji kuwa na maghala ambayo ni ya kisasa zaidi, tunahitaji teknolojia, tunahitaji kuweza kuzalisha kwa utaratibu unaotakiwa na masoko ya nje lakini vilevile tunahitaji wakulima wetu waweze kuzalisha kwa viwango vile ambavyo vinahitajika. Kwa hiyo, kwa sasa jitihada ya Serikali siyo kwenye commodity exchange, tutaelekea kule, lakini kwa sasa tunaweka nguvu nyingi kwenye utaratibu wa stakabadhi ghalani.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali inaendelea na jitihada za kutafuta soko kwa ajili ya mazao ya mikunde. Changamoto iliyotokea ni kwamba India ambayo ndiyo nchi inayonunua mazao ya mikunde, kwa mwaka huu wana ziada ya asilimia 30 na ndiyo maana mbaazi zetu, dengu zetu na choroko zimepata changamoto. Hata hivyo kwa kupitia Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kununua mbaazi za wakulima, lakini huko mbele ya safari tunagemea tuanze kuuza zao hilo la mbaazi kwa utaratibu wa stakabadhi ghalani tukiamini kwamba kuuza kwa pamoja kutasaidia bei iwe nzuri zaidi. (Makofi)
MHE. PROSPER J. MBENA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nashukuru majibu ya Serikali hasa kwa kubaini umuhimu wa kulirudisha hili Shirika la TAFICO kufanya uvuvi hasa kwenye bahari kuu, nadhani wamechukua ushauri wetu, naomba kuwapongeza. Nina swali moja tu la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa uvuvi ni sekta muhimu sana hasa katika sera hii ya Serikali ya uchumi wa viwanda: Je, ni lini Serikali itasaidia Jimbo la Morogoro Kusini kuleta wataalam wake kufanya utafiti kwenye mito mikubwa yenye utajiri mkubwa wa samaki na dagaa ili nao waweze kuchangia kwenye uchumi huo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ombi lake ni kwamba, Serikali iweze kupeleka wataalam Jimboni kwake wakafanye utafiti. Naomba nilichukue tukaliangalie ndani ya Wizara ili ikiwezekana wataalam waweze kwenda kule.
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri. Pamoja na maelezo hayo, Mheshimiwa Waziri atakubaliana nami kabisa kwamba kumekuwa na dhana potofu kuwa kilimo kimekuwa kama last resort. Hata ukiongea na watoto wetu wa shule, ukiwauliza unataka kuwa nani? Mmoja atakwambia daktari, mwanasheria, engineer na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nilitaka nipate maelezo ya Mheshimiwa Waziri, ni mikakati gani sasa kama Wizara au incentives gani mmeziweka ili iwe kivutio kwa hawa Watanzania na vijana wetu ambao kuna tatizo kubwa la unemployment? Hilo ni la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, katika maelezo yangu ya mwanzo niliongelea suala la wataalam nashukuru kuwa Mheshimiwa Waziri ameli-address lakini kwenye ukosefu wa vitendea kazi, Watanzania wamekuwa wakiwalaumu sana wataalam hasa hawa Maafisa Ugani kuwa wamekaa tu Maofisini, lakini ukiangalia tatizo kubwa ni ukosefu wa vitendea kazi. Sasa napenda nipate maelekezo, ni mkakati gani kama Wizara mmeweka kuhakikisha hawa wataalam wetu wanapata vitendea kazi kama vile pikipiki na zana za kufundishia ili tuweze kuleta mapinduzi ya hii Sekta ya Kilimo? Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kuweka mazingira ya kilimo kuvutia watu wengi zaidi hususan vijana, naomba nimahakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa kilimo kinavutia sana na ndiyo maana hata baadhi yenu Waheshimiwa Wabunge ni wakulima hodari. Kwa hiyo, kizuri kinajiuza, kilimo kinalipa, tayari kuna watu wengi wamenufaika na hivyo niwasihi tu vijana kwamba kilimo kina manufaa. Vilevile Serikali imeweka mazingira mazuri sana ya kuwavutia vijana na ndiyo maana tumeweka taratibu za wao kupata mitaji, tumeanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo, tuna Mfuko wa Pembejeo, lakini vilevile hata Benki za binafsi zinatoa mikopo. Kwa hiyo, niseme tu kwamba kilimo kinavutia, kuna uwezeshaji, kwa hiyo, vijana wanakaribishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ni kuhusiana na wataalam, Maafisa Ugani kutokuwa na vitendea kazi. Hili limezungumzwa sana, lakini mara nyingi vilevile imekuwa ni ksingizio. Kinachohitajika kwa Afisa Ugani anapokuwepo kwenye eneo lake la kazi ni elimu ile aliyonayo ajaribu kuitumia kuwafikishia wananchi. Mara nyingi katika ngazi ya kijiji huwezi kulalamika kwamba kwa sababu sina pikipiki, basi siwezi kuwafikia wananchi. Watendaji wengine wa Serikali walioko katika ngazi hizo wanafanya kazi zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, pamoja na ukweli kwamba kuna hitaji la kuhakikisha kwamba hivyo vitendea kazi viweze kupatikana lakini tunawasihi kwamba isiwe ni kisingizio. Lazima watumie elimu ambayo wanayo kwa sababu ni ajira yao ili kujaribu kuhakikisha kwamba wananchi wanapata elimu ya kilimo bora.
MHE. ABDALLA HAJI ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa masikitiko tu kidogo kwamba hili suala tunasema ni la Muungano lakini katika majibu ya Naibu Waziri naona hakutaja upande wa pili hata neno moja, sijui kama tumo au hatumo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Sheria ya Mafuta na Gesi ni ya Muungano na hivyo kila nchi inastahiki kupata gawio stahiki kutokana na mauzo ya gesi. Je, ni kiasi gani cha gawio kilichopelekwa kwa Hazina ya Zanzibar tangu mauzo haya ya gesi yafanyike?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kitaalam tunaambiwa kwamba gesi inayozalishwa Tanzania ni gesi safi kabisa, yaani haihitaji gharama kubwa kufanyiwa mchakato kwa matumizi. Sasa tulitegema kwamba umeme unaotokana na uzalishaji kutokana na gesi hii ungekuwa rahisi kwa watumiaji lakini kila siku umeme unapanda bei. Ni kwa sababu gani? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI (K.n.y. WAZIRI WA NISHATI NA MADINI): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama alivyosema kwamba suala la gesi asilia ni suala la Muungano kwa mujibu wa Ibara ya 4 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 na Nyongeza ya kwanza ya Katiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu gawio la Zanzibar kutokana na mapato ya gesi ni suala la takwimu, ningeomba niweze kulifanyia kazi halafu niweze kumpatia Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili kwamba katika hali ya kawaida gesi inatakiwa iweze kuzalisha umeme ambao ni bei rahisi, naomba nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba huo ndiyo ukweli na toka tuanze kuzalisha umeme kwa kutumia gesi tumeweza kuokoa fedha nyingi sana. Kwa mwaka inakadiriwa tunaokoa dola za Kimarekani bilioni 1.6 ambapo kama tungetumia umeme wa kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimweleze tu kwamba pamoja na bei ya umeme kuendelea kubadilika badilika lakini bado itabakia kwamba tokea tumeanza kutumia umeme wa gesi tumeweza kupunguza gharama kubwa sana za fedha tunazotumia katika kuzalisha umeme.
MHE ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwanza, Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa shahidi kwamba kuna ukiukwaji mkubwa wa sheria kwa sababu kuna watendaji wengi wa hizo AMCOS ambao hawana sifa zilizotajwa kisheria. Kwa hiyo, napenda kujua Serikali inatoa kauli gani kuhusu AMCOS ambazo zimeajiri watendaji ambao hawana sifa?
Mheshimiwa Spika, pili, kutokana na kazi kubwa ambazo wanazifanya watendaji hawa wa AMCOS hasa wale wa Mikoa ya Mtwara na Lindi ambao sasa hivi wanashughulikia zao la korosho na wanashughulika na fedha nyingi sana, Serikali ina mpango gani wa kuwajengea uwezo kwa kuandaa mafunzo maalum ili kupunguza ubadhirifu na upotevu wa pesa ambao siyo wa lazima? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Spika, kabla sijajibu, naomba nikiri kwamba Mheshimiwa Chikota ni mmoja kati ya Waheshimiwa Wabunge wanaofuatilia sana masuala ya ushirika kwa niaba ya wananchi wake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie tu kwamba kama kuna mfanyakazi yeyote na mtendaji wa Chama cha Ushirika ambaye hajakidhi matakwa ya kisheria, kimsingi huyo amekaa mahali ambapo siyo pake. Kama ana ushahidi wa watendaji ambao wameajiriwa kinyume na taratibu au kinyume na sifa ambazo nimezitaja kwa mujibu wa sheria, naomba anipe orodha yao na mimi nitashughulika nao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, anasema kwa nini Serikali haitoi mafunzo au kuwajengea uwezo watendaji wa vyama vya ushirika, naomba nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba moja kati ya kazi ya Vyama vya Ushirika, hasa Vyama Vikuu, ni kuhakikisha vilevile kwamba watendaji wa Vyama vya Msingi wanajengewa uwezo. Kwa hiyo, tunaendelea kusisitiza kwamba Vyama Vikuu vishirikiane na Vyama vya Msingi kuhakikisha kwamba wanatoa elimu ya mara kwa mara kwa watendaji wa Vyama vya Msingi. Vilevile, nitumie fursa hii kuwaagiza Maafisa Ushirika katika wilaya zote wahakikishe kwamba wanatekeleza jukumu lao la msingi la kuendelea kutoa elimu na kuwajengea uwezo viongozi pamoja na watendaji wa Vyama vya Ushirika.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri anakiri kwamba hili tatizo la watendaji wasiokuwa na sifa ni moja ya tatizo kubwa sana kwenye zao la korosho na Serikali inatambua kwamba msimu wa korosho uliomalizika tumepata upotevu mkubwa sana wa pesa.
Sasa Serikali haioni wakati umefika wa kubadilisha sifa zinazotumika za kuwapata hawa watendaji? Nasema hivyo kwa sababu kiwango hicho kidogo cha elimu ni moja ya sababu ya wao kuzungukwa na watendaji wa mabenki na watendaji wengine wanaohusika katika mfumo na matokeo yake pesa nyingi sana zinapotea na wakulima wanapata hasara. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Spika, ni kweli kama Mheshimiwa Mbunge anavyosema, kwamba mara nyingine elimu na uwezo mdogo wa watendaji wa Vyama vya Ushirika inaweza ikawa kikwazo kikubwa cha wao kuweza kufanya kazi kwa ufanisi, hasa pale kiwango kikubwa cha fedha kikiwa kinahusika. Naomba nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba sheria haisemi kwamba ni lazima mtu awe na elimu ya kidato cha nne, inasema kuanzia. Kwa hiyo maana yake, hata kama kunakuwa na waombaji wa nafasi zile wana elimu zaidi bado wanaweza kuchukuliwa.
Mheshimiwa Spika, naomba nisisitize kitu kimoja, kuwa na elimu kubwa mara nyingine siyo kigezo cha uadilifu na tabia njema. Leo hii tunafahamu Vyama vyetu vya Msingi ni vyama vya wakulima, vinashughulikia maslahi ya watu wa kawaida, ukija kupeleka wataalam, wanaweza wakawa wataalam wana elimu nzuri lakini vilevile wakawa wataalam wa kupiga. Kwa sababu hata huko Serikali Kuu na maeneo mengine unasikia kwamba mara nyingine wapigaji ni watu ambao elimu zao ni kubwa. Kwa hiyo, tutaendelea kuangalia ni namna gani ya kuboresha mazingira ya utendaji wa Vyama vya Ushirika, lakini kwa sasa sheria haimkatazi mtu mwenye degree au masters kuwa Mtendaji wa Chama cha Msingi. (Makofi)
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante napenda kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inawapatia wakulima pembejeo kwa ajili ya kilimo na wafugaji hivyo hivyo. Kwa upande wa uvuvi Serikali mna mkakati gani wa kuhakikisha na wenyewe mnawawezesha badala ya kila siku kuchoma nyavu zao na kuacha wakiwa maskini? Mwisho, naipongeza timu yangu ya Yanga. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hilo la Yanga, sitalijibu, siyo sehemu ya swali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba katika ruzuku ya kilimo, wavuvi hawajasahauliwa. Wizara ina utaratibu ambapo inatoa ruzuku kwa wavuvi wanaotaka kununua injini za boti. Kwa hiyo, kama kuna Mheshimiwa Mbunge yeyote ambaye ana vikundi vyake vya wavuvi ambao wanataka kununua boti, Serikali inatoa ruzuku ya asilimia 40 kwa vikundi vinavyonunua injini za boti. Kwa hiyo, ruzuku ipo. (Makofi)
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Wananchi wa Jimbo la Manyoni Magharibi ni wananchi ambao nao wanapenda kitoweo cha samaki. Kwa kuwa hatuna bwawa wala ziwa.
Je, Serikali iko tayari kushirikiana nami Mbunge wao na vikundi vya vijana na akina mama wa Itigi kuweza kuanzisha mabwawa ya samaki?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafurahi kusikia kwamba Mheshimiwa Mbunge anataka kuhamasisha vijana wake wa Jimbo la Manyoni Magharibi ili kuwekeza katika ufugaji wa samaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimfahamishe tu kwamba Wizara iko tayari kushirikiana naye ili mradi afuate utaratibu ambao unatakiwa nao ni kwa kupitia Halmashauri ambayo yeye mwenyewe ni Diwani.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa hii. Naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Keissy kwamba Wilaya ya Hanang ina Ziwa Basutu na ina samaki wengi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa hatuna polisi wa kutosha na ndiyo maana tunashindwa kudhibiti hawa wavuvi wanaotumia nyavu ndogo ndogo. Je, Serikali haioni kwamba itakuwa vizuri sana kuwahamasisha wananchi wa Tanzania kuanzisha mabwawa mengi ya kufugia samaki na wazungu wanaita aqua culture kama namna ya kuwafanya wavuvi wakawa na samaki wa kutosha na wakaacha kutumia nyavu ndogo ili waweze kuendelea kuishi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikiri kwamba Jimboni kwa Mheshimiwa Dkt. Mary Nagu kuna uvuvi katika Ziwa Basutu ambao wananchi wake wanategemea sana na Serikali inatambua fika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nakubaliane naye kwamba kwa sasa jitihada kubwa duniani ni kuelekea kwenye uvuvi ambao tunaita ufugaji wa samaki (aqua culture) na tunatambua kwamba hata hapa kwetu, Serikali tayari imechukua jitihada za kutosha kuhahakisha kwamba tuna-diversify sasa kutoka kwenye uvuvi wa kutumia maji kuelekea kwenye ufugaji wa samaki. Ndiyo maana kuna mikakati mbalimbali inaendelea. Kuna Waheshimiwa Wabunge wanafahamu kwamba sasa kuna ufugaji unaitwa ufugaji wa vizimba (cage culture).
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile hata aqua culture sasa hivi Serikali inawezekeza katika ufugaji wa samaki kwa utaratibu wa aqua culture na tayari kuna vituo ambavyo vinazalisha vifaranga.
Kwa hiyo, kama kuna Mheshimiwa yeyote anataka kuwekeza au kusaidia wananchi wake wawekeze katika ufugaji wa samaki, awasiliane na mimi ili nimwelekeze pa kupata vifaranga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari kuna mradi mkubwa unaitwa Sawfish ambao unajaribu kuhahakisha kwamba tunaanchia nafasi, rasilimali zetu za uvuvi kwenye maji ya kawaida kwa kuweza kuwekeza kwenye ufugaji wa samaki kwenye nchi kavu. Kwa hiyo, tuna jitihada hizo ndani ya Serikali.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali. Dhamira ya Serikali ya kuanzisha Benki ya Kilimo ilikuwa ni kuwainua wakulima nchini. Wakati Serikali inafikiria kuanzisha Benki ya Kilimo ilikubali kutoa mtaji wa shilingi bilioni 800, lakini fedha iliyotolewa ni shilingi bilioni 60 tu na benki hii imeshindwa kabisa kuwahudumia wakulima wa nchi hii.
Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wakulima wanapata mikopo na wanalima kilimo chenye tija? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwakajoka, nafikiri limekaa sawa kwa sababu linaendena hasa na jitihada ya Serikali kujaribu kuwekeza na kuwasaidia wavuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa anavyosema Mheshimiwa Mbunge kwamba huko nyuma kulikuwa na jitihada kujaribu kuhakikisha kwamba Benki ya Maendeleo ya Kilimo inapata shilingi bilioni 800. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa benki hiyo imeweza kupata shilingi bilioni 246 tayari zimeshaingia benki na yote itaelekezwa katika kilimo ikiwa ni pamoja na kilimo cha mazao, uvuvi na ufugaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge labda tukitoka hapa leo anione nimfahamishe taratibu za kuweza kupata hizo fedha kwa ajili ya wavuvi wake. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba hizo fedha zimepatikana.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la kuzuia uvuvi wa nyavu ambazo hazistahili, hazifai ni ni zuri na wavuvi hawa wanapokamatwa wanapata taabu sana, nyavu zinaharibiwa, wanakamatwa, wanawekwa ndani, na kadhalika, lakini hawa wavuvi hawajitengenezei nyavu hizi, wanazinunua madukani. Kwa nini wasikamatwe wale wanaoziuza ili ziondolewe? (Makofi)
Swali la pili, kwa jinsi ninavyofahamu, Tanzania hakuna kiwanda cha nyavu, kama kipo hakifanyi kazi. Nyavu hizi zinatoka nje ya nchi, zinaagizwa nje ya nchi, zinaingia Tanzania na Wizara ipo. Kwa nini Wizara isizuie nyavu hizi ambazo haziruhusiwi zisiingie? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba siyo wavuvi pekee wanaolazimika kufuata Sheria ya Uvuvi kulingana aina ya nyavu wanayotakiwa watumie. Mtu yeyote yule ambaye anajihusisha na shughuli ambayo inapelekea kutumia nyavu ambazo hazitakiwi kutumika, anakuwa ametenda kosa kwa mujibu wa Sheria ya Uvuvi Namba 22 ya mwaka 2003 na Kanuni zake 2009.
Kwa hiyo, mtengenezaji, msafirishaji, dalali, mtumiaji, mtu yeyote yule ambaye anaingia katika mfumo wa kuhakikisha kwamba nyavu hizo zinapatikana vilevile anakuwa ametenda kosa la kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda kuwaeleza Waheshimiwa Wabunge kwamba lengo la Serikali siyo kujaribu kuwabana na kuwaletea matatizo wavuvi, wao hasa ndio wanufaika wa kwanza na jitihada za Serikali za kulinda rasilimali za uvuvi kwa sababu tusipolinda, baadaye hawatakuwa na cha kuvua. Ndiyo maana tunasisitiza zitumike nyavu ambazo zitafanya uvuvi uwe endelevu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la pili, kwamba kwa nini tusizuie nyavu ambazo zinatoka nje, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tunazuia hata mwaka 2016 tulikamata nyavu pamoja na vifaa vingi ambavyo vilitoka China vilikamatwa bandarini na Serikali inaendelea kufuatilia mtu yeyote yule ambaye anaingiza nyavu ambazo haziruhusiwi.
Lakini vilevile lazima niwafahamishe Waheshimiwa Wabunge changamoto iliyopo ni kwamba mara nyingine nyavu nyingine zinasokotwa kienyezi.
Kwa hiyo, watu wananunua nyuzi ambazo zinapatikana kwa ajili ya matumizi mengine halafu wanakwenda kutengeneza nyavu ambazo hazitakiwi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuhakikisha kwamba tunadhibiti uingizwaji wa nyavu zile lakini vile vile utumiaji wake katika maeneo mbalimbali nchini.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami naomba kumwuliza Mheshimiwa Naibu Waziri swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa vijana wengi wamekuwa wakijiajiri kwa kupitia uvuvi wa bahari kuu, lakini vijana hawa hawana mitaji ya kuendeleza sekta hii ya uvuvi.
Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha vijana hawa wanapatiwa angalau mikopo ya bei nafuu ili wapate kujiendeleza katika sekta hii ya uvuvi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu vijana kufanya uvuvi katika bahari kuu, taarifa tulizonazo ni kwamba hakuna vijana wanaofanya uvuvi katika bahari kuu. Bahari kuu ni suala lingine, ni gumu kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na vijana wanaojishughulisha na uvuvi katika maji ya kawaida na maji ya Kitaifa tunafahamu. Zanzibar mradi wa Sawfish umetoa dola milioni 11 kwa ajili ya kuwezesha wananchi wajishughulishe na shughuli za uvuvi. Labda Mheshimiwa Mbunge tunaweza tukaonana tukitoka hapa leo nimhabarishe na nimpe taarifa vizuri zaidi ili aangalie namna ya kuwasaidia vijana wake wawekeze katika uvuvi.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kuna utaraibu mzuri wa kuzuia hizo nyavu zisizoruhusiwa, lakini samaki katika maziwa yetu; Ziwa Victoria kuna samaki aina ya sato, nembe, sangara na samaki wengine; lakini kuna utaratibu mzuri katika bahari yetu hasa uvunaji wa samaki aina ya kamba, kwamba wanavunwa baada ya muda fulani halafu wanasimama. Ili samaki hawa waweze kukua katika Ziwa Victoria; sato na samaki wengine; kwa nini sasa tusiwe na utaratibu wa kuzishirikisha nchi za Kenya, Uganda na Tanzania ili kusudi samaki hawa wawe na tija, badala ya kuvua samaki wadogo wadogo tuwe na muda wa kuwavuna? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Ndassa kwa sababu inaelekea ana ufahamu wa ndani kabisa kuhusiana na masuala ya uvuvi. Kimsingi Ziwa Victoria kabla ya miaka ya 1980 samaki aina ya nembe, furu na gogogo walianza kupotea, lakini siku hizi tayari wameshaanza kuonekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la kusimamisha au kusitisha uvuvi katika Ziwa Victoria majadiliano yanaendelea katika ukanda wetu wa Afrika Mashariki kuangalia kama hilo ni suala ambalo linaweza likafanyika. Kwa sababu kimsingi hata sisi Tanzania tukisimamisha leo wenyewe na wengine wakiwa wanaendelea, haitakuwa na faida kwa sababu samaki wale ni migratory. Ukifanya uamuzi katika nchi moja halafu wakaendelea kuvuliwa katika nchi nyingine, bado hautakuwa umepata nafuu yoyote. Kwa hiyo, majadiliano yanaendelea na utafiti vile vile unaendelea. Matokeo yakishatolewa, basi uamuzi sahihi utachukuliwa.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa. Kwa kuwa Serikali imepiga marufuku uvuvi wa majongoo bahari Kisiwani Mafia; wakati huo huo majongoo bahari yanavunwa kule Zanzibar upande wa pili wa Muungano.
Je, Serikali sasa haioni ni wakati muafaka kuruhusu uvuvi wa majongoo bahari kuendelea Mafia?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama anavyosema kwamba uvuvi wa majongoo bahari umepigwa marufuku Mafia, kwa sababu kimsingi kwa namna ulivyokuwa unaendelea ulikuwa unaharibu sana matumbawe. Kwa sababu kuvua majongoo bahari inabidi uzame ndani uende kwenye mazalia ya samaki na ni lazima uingie kwenye miamba ndiyo uweze kuvua majongoo bahari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Zanzibar wao wanaendelea kufanya, lakini nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba suala la uvuvi katika maji yale ya kawaida siyo suala la Muungano. Kwa hiyo, Zanzibar wanakuwa na sheria zao na sisi tuna sheria zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri anachosema Mheshimiwa Mbunge ni kwamba ni vizuri katika kujenga ule ushirikiano tuwe na maamuzi ambayo yanaweza yakafanana na hasa yale ambayo yanasaidia pande zote mbili kuendelea kuimarisha na kulinda rasilimali za uvuvi.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Wavuvi wa Ziwa la Babati wamekuwa wakipata taabu sana kwa Ziwa Babati kufungwa miezi sita kwa mwaka ilhali wavuvi hawa wanategemea uvuvi katika kuendesha maisha yao.
Mheshimiwa Naibu Waziri, yuko tayari kufika Ziwa Babati na kushauriana na watalaam wa Halmashauri ya Mji wa Babati ili kupata mbegu ya samaki ambayo itatumika kwa mwaka mzima badala ya kama ilivyo sasa ambapo wavuvi hao huvua kwa miezi sita tu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kama niko tayari kwenda Babati kwenda kuongea na Halmashauri kuhusiana na hili, mimi sina shida na niko tayari hasa tukiandamana na yeye mwenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba kufungwa mara kwa mara kwa Ziwa Babati ni utaratibu wa kawaida katika small water bodies yaani maji madogo. Kama usipodhibiti ni rahisi uvuvi ukafanyika na ukamaliza kabisa bioanuwai iliyopo ya samaki. Kwa hiyo, ni uataratibu wa kawaida. Hata ukisikia Bwawa la Nyumba ya Mungu limefungwa, ni kawaida. Kwa hiyo, Serikali inafanya hivyo ili kuwasaidia wananchi wako wa Babati. Lengo siyo baya, lakini tunatambua kwamba tusipodhibiti baada ya muda hakutakuwa hata na samaki mmoja katika Ziwa Babati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini akitaka twende, tutaenda.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Wananchi tunaowapa elimu kwa ajili ya ufugaji wa samaki katika maeneo mbalimbali, wamekuwa wanahamasika na wanajenga mabwawa ya samaki lakini wanakosa vifaranga kwa muda mrefu, zaidi ya miaka miwili mpaka mitatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mpango gani kuhakikisha maeneo yote ambayo tunatoa elimu ya ufugaji wa samaki, tunanunua mashine za kutosha za kutotoa vifaranga vya samaki ili wananchi wale waweze kupata vifaranga kwa urahisi, lakini kwa bei nzuri waweze kunufaika na ufugaji wa samaki maeneo wanayokaa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kupitia Bunge lako Tukufu nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba hakuna ukosefu wa vifaranga vya samaki. Kwa sasa kama kuna mtu yeyote ambaye anataka vifaranga, awasiliane na Wizara. Kimsingi vifaranga vya samaki mbalimbali wanazalishwa katika vituo vyetu vya uvuvi.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge kama wananchi wake wanataka kuwekeza katika ufugaji wa samaki, anione nimwelekeze namna ya kupata vifaranga vya samaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nimfahamishe
Mheshimiwa Mbunge kwamba hata kwenye Ziwa Victoria Serikali imejipanga, kuna mradi ambao tunauanza katika mwaka huu wa fedha unaokuja wa kuwekeza vifaranga vya zaidi ya milioni 50 katika Ziwa Victoria ili kuendelea ku-boost uzalishaji wa sangara na sato. Kwa hiyo, kama kuna upungufu wowote Mheshimiwa Mbunge anaweza akaniona.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, mbaazi inayolimwa Tanzania bado ina uwezo wa kuingia katika soko lililoko India kutokana na viwango vya ubora ambayo inayo. Nashukuru kwamba Serikali imesema imeandaa makubaliano na mkataba umesainiwa wa kuwasaidia wananchi wetu waendelee kupata bei nzuri.
Je, Serikali iko tayari sasa kusukuma majadiliano hayo ili wananchi wetu waweze kunufaika kuanzia msimu wa kilimo ambao unaendelea sasa hivi baada ya kuvuna?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa biashara ya kuuza mbaazi nje ndiyo hiyo ambayo sasa haitabiliki. Je, Wizara hii iko tayari sasa kuanza mazungumzo na Wizara ya Viwanda na Biashara ili kupata viwanda vya kusindika zao hilo tuweze kuuza nje bidhaa iliyosindikwa ili kuongeza thamani na pia kutoa ajira kwa watu wetu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kufuatilia mkataba na Serikali ya India ili utekelezaji wake uweze kuanza kazi mapema iwezekanavyo ili wakulima wetu waendelee kunufaika bila kuchelewa.
Kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tunalisukuma, lakini wanaochelewesha kwa sasa siyo sisi ni upande wa India, wao wanaangalia mazingira ya hapa kwetu kwa sababu wameongea na nchi zingine za Kenya na Msumbiji, kimsingi wanajaribu kuangalia options mbalimbali, lakini sisi tutaendelea kuongea nao ili kufanikisha huo mkataba ili uanze mapema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu viwanda, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba ni kweli kabisa kati ya mikakati tuliyonayo ya kuweza kutafuta soko zuri la mbaazi na mazao mengine ya jamii ya mikunde ni kuwa na viwanda vya kuchakata hapa ndani ili tuweze kushindana katika soko la Kimataifa. India yenyewe ambayo ndiyo mnunuzi wa asilimia 27 ya mbaazi na mazao ya mikunde duniani wanauza katika nchi zingine baada ya kuchakata. Kwa hiyo, nasi tukiwa na viwanda itatusaidia sana tuweze kupata masoko mengine ikiwepo na masoko mazuri kama ya Marekani na Ulaya. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari hiyo ni moja kati ya mikakati ambayo tunafikiria kama Serikali.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mkoa wa Manyara kwa ujumla wake unazalisha sana zao la mbaazi hususan katika Jimbo langu kata ya Singe, kata nzima na mnapita barabarani pale kama mnaenda Arusha ni mbaazi na imestawi. Hata hivyo, kwa kuwa hakuna viwanda vinavyochakata zao hili na Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri na kwa kuwa bei hii imekuwa ikishuka kila mwaka, wananchi wetu wamekuwa wakipata hasara.
Je, Serikali haioni kwamba ni vizuri wakanunua zao hili wao kama wanavyofanya kwa zao la mahindi kwa NFRA ili wao watafute soko badala ya wananchi wetu kuendelea kupata hasara maana hata viwanda havijaanza sasa kutekeleza?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kwa sasa bado hatuna viwanda vya kuchakata siyo zao la mbaazi tu lakini mazao mengi yakiwepo mazao mengine ya jamii ya mikunde kama njegele, dengu, choroko na lentili na hiyo inaleta changamoto katika upatikanaji wa soko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kwa sasa Serikali haina mpango wa kununua zao hilo kutoka kwa wakulima, lakini tunachofanya ni kujaribu kwenda kule kwenye soko lenyewe India na ndiyo maana tayari tumeshaingia mkataba wa awali ili wananchi wetu waweze kuuza kwa uhakika zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, soko la India kwa sasa hata kama tukifanikiwa kupata tatizo litakuwa ni sisi kuweza kuzalisha kiwango ambacho wanahitaji. India kimsingi wana mahitaji makubwa na ndiyo maana tunafikiri njia sahihi na njia ambayo itawakomboa wakulima ni kutafuta hilo soko pamoja na kwamba kama tulivyosema tutaendelea kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya kuchakata mazao mbalimbali hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niseme kwamba changamoto nyingine iliyopo katika uuzaji wa mbaazi na mazao mengine ni mfumo wetu wa soko. Nimshauri Mheshimia Mbunge pamoja na Wabunge wengine wahamasishe wakulima waanzishe vyama vya ushirika kwa sababu ni mfumo ambao utawasaidia kuuza kwa pamoja na kwa urahisi zaidi.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyo kwenye matatizo ya mazao ya mbaazi vivyo hivyo kuna tatizo la zao la ufuta, lakini tatizo kubwa la mazao haya ni Bodi ya Mazao Mchanganyiko. Ni nini kauli ya Serikali katika kuiboresha hii Bodi ya Mazao Mchanganyiko iwe na mipango endelevu ya kuendeleza haya mazao ili wananchi wetu waweze kupata soko la uhakika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Wizara na Serikali inaendelea na mikakati ya kuboresha Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi. Changamoto iliyopo kwa sasa ni namna gani tunaweza tukaanzisha utaratibu wa kusimamia mazao mengi ambayo hayana mfumo wa kuyasimamiwa. Kwa hiyo, kwa sasa Bodi inaendelea na mchakato wa kuangalia namna gani ya kuweza kusimamia kila zao kwa utaratibu wake kama ilivyo kwenye mazao mengine ya biashara. Kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari Serikali inafahamu hilo na linafanyiwa kazi, Bodi inajitayarisha kuangalia namna ya kusimamia siyo zao la ufuta tu lakini vilevile mazao mengine.
MHE. JUMAA H. AWESO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niishukuru Serikali kwa kuondoa kodi katika zana hizi za uvuvi. Kitu ambacho nataka nimuulize Mheshimiwa Waziri pamoja na kuondoa kodi na kuleta tozo kwa asilimia 40 kwa wavuvi wa Pangani lakini Serikali haikuwa wazi ni namna gani au utaratibu gani ambao unatakiwa ufuatwe na vifaa hivi vinapatikana wapi ili wavuvi hawa hususani wa dagaa waweze kupata zana hizo kwa ukaribu na rahisi?.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, nataka nimuulize Mheshimiwa Waziri Serikali ina mkakati gani wa kujenga bandari ya uvuvi hususani katika ukanda huu wa Pwani ya Mkoa wa Tanga kwa mantiki ya meli kubwa zinazovua bahari kuu kwa maana ya kuhaulisha, kuuza na kutoa takwimu sahihi kuhusu suala zima la uvuvi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na utaratibu unaotakiwa kufuatwa ili wavuvi waweze kupata punguzo katika zana za uvuvi, nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kimsingi wavuvi wake wanaotaka kupata ruzuku ya vyombo vya uvuvi wanatakiwa wajiunge katika vikundi, lakini vilevile wachangishane fedha, wakishakuwa na fedha ya kununua kwa mfano injini ya boti wanawasilisha maombi yao Halmashauri ambao watawaelekeza namna ya kupata zile zana halafu Serikali itachukua asilimia 40 ya gharama ya chombo ambacho wanataka kununua. Mheshimiwa Aweso kwa sababu ni Mbunge kijana ambaye amekuwa akihangaikia sana wananchi wake kwa muda mrefu sana, nimuahidi tu kwamba kama anataka kupata ufafanuzi mzuri zaidi hata leo mchana anaweza akaja ofisini kwangu tukaongea ili wananchi wake wasiendelee kuchelewa kupata huduma hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu bandari ya uvuvi, wakati tunawasilisha bajeti yetu tulitoa maelezo marefu sana kuhusiana na mikakati mbalimbali ambayo kama Serikali tumeweka ili kuendelea kuboresha namna ya nchi kunufaika na uvuvi katika bahari kuu. Moja ya mikakati hiyo ambayo tulisema ni pamoja na kuanza na mchakato wa kujenga bandari ya uvuvi. Katika bajeti ya mwaka unaokuja, Wizara imetenga fedha za kufanya upembezi yakinifu ili tuweze kujua ni mahali gani hasa ambapo panafaa kuweka bandari ya uvuvi. Bandari ya uvuvi yenyewe gharama za awali ambazo tumekadiria tunafikiri inaweza ikagharimu zaidi ya…
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Jimbo langu la Ulanga tumebahatika kuwa na mto mkubwa sana, Mto wa Kilombero lakini wananchi wanaoisha maeneo yale hawajawahi kunufaika na chochote kile kuhusu uvuvi.
Je, sasa Wizara iko tayari kutoa ushauri wa kitaalam na vifaa ili wananchi wanaoishi karibu na mto ule wanufaike na shughuli za uvuvi na Serikali ipate mapato? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara na Serikali iko tayari kuwasaidia wananchi wake waweze kuvua katika Mto Kilombero. Nimhakikishie tu kwamba huduma hii inapatikana katika Halmashauri ambapo yeye mwenyewe ni Diwani na vilevile niwashauri Waheshimiwa Wabunge wote kwamba huduma za namna ya kuwasaidia wananchi katika sekta ya uvuvi na sekta zote za Wizara yangu yaani kilimo na mifugo, sehemu nzuri ya kuanzia ni kwenye Halmashauri na sisi wenyewe tunashiriki lakini kama nilivyosema kwa Mheshimiwa Aweso, hata Mheshimiwa Mlinga anaweza akaja nikamuelekeza zaidi.
MHE. CATHERINE N. RUGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la uvuvi haramu kwa kutumia nyavu zenye matundu madogo na baruti limekuwa la muda mrefu kwenye Ziwa Victoria, lakini pia maziwa mengine hapa nchini. Ni nini mpango wa Serikali kuwekeza kwenye vizimba (fish cadge) njia ambayo ni salama na yenye ufanisi ili kuwawezesha vijana wa Kanda ya Ziwa kuendelea kujiajiri katika sekta ya uvuvi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba katika Ziwa Victoria hakuna uvuvi wa mabomu, uvuvi uliopo ni uvuvi wa kutumia zana ambazo hazijaruhusiwa kutumia makokoro na zana zingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi Serikali inaendelea kutoa elimu kwa wavuvi ili waachane kabisa na uvuvi ambao sio endelevu na katika hili tunahakikisha kwamba tunashirikiana na Halmashauri na vilevile Mheshimiwa Mbunge tunaomba na yeye atusaidie ili kuendelea kuhamasisha wavuvi wa kule anakotoka ile wafanye uvuvi ambao unaendana na taratibu za sheria.
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na Serikali kuondoa baadhi ya kodi katika sekta ya uvuvi na vilevile kujenga Soko la Kisasa la Samaki Pangani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namuuliza Mheshimiwa Waziri, je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Chuo cha Uvuvi katika Mkoa wa Tanga kama kile kilichopo Mwanza?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ujenzi wa chuo anachosema, Serikali itafikiria ombi lake kulingana na uwezo wa kibajeti lakini kwa sasa tunaendelea kuimarisha vyuo vilivyopo vya VETA ili kuweza kuendelea kutoa huduma hata wakati huko mbele tunafikiria kujenga vyuo vingine kadri uwezo utakavyoruhusu.
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Spika, nimemsikiliza Waziri amesema Serikali haitarajii kuwepo kwa ucheleweshwaji wa mikopo kwa wanafunzi ambao wamekidhi vigezo.
Mheshimiwa Spika, wiki iliyopita mamia ya wanafunzi wenye vigezo walikuwa wakishinda katika Bodi ya Mikopo wakifuatilia upatikanaji wa mikopo. Wengi wa wanafunzi hao wanatoka katika familia maskini, na Bodi ya Mikopo vigezo wanavyoviangalia ni ufaulu. Wanafunzi wengi ambao wanasoma katika shule binafsi zikiwemo Feza na nyinginezo wana ufaulu wahali ya juu ukilinganiswa na shule za Serikali. Hata hivyo hivi sasa wanafunzi hao wanaotoka kwenye shule za private ambao wana ufaulu mkubwa wanapata fursa hii ya mikopo ikilinganishwa na wanafunzi maskini wanaotoka katika shule za Serikali. Je, ni lini Serikali sasa itaangalia vigezo stahiki vya wanafunzi ambao wana uhitaji wa kuingia vyuo vikuu?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, lengo la kuanzishwa kwa Bodi ya Mikopo ilikuwa ni kwa wenye uhitaji, lakini sasa lengo lile limebadilika na sasa hivi mikopo inatolewa kwa kozi, kwa mfano wanaosoma udaktari, engineering wanapata mikopo kwa asilimia 100. Ni nani amesema kwamba nchi hii haihitaji accountants? Nani amesema nchi haihitaji waandishi wa habari? Nani amesema haihitaji lawyers? Naomba majibu ni kwa nini sasa Serikali isiangalie namna ya kutoa mikopo kwa kuangaliwa mahitaji ya wanafunzi wa hali ya juu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, nianze kwa kusema kwamba leo hii Wizara yetu itatoa Kauli ya Serikali kuhusiana na masuala ya udahili na mikopo, kwa hiyo tutaelezea kwa kirefu kidogo.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo itoshe tu kwa ajili ya maswali ya nyongeza niseme yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika, kuhusu wanafunzi kuandamana kwa sababu ya kucheleweshewa mikopo, naomba nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba Bunge hili lilipitisha shilingi bilioni 427 kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza na wale wanaoendelea.
Mheshimiwa Spika, wanafunzi wa mwaka wa kwanza wanaotegemea kupata mikopo ni 30,000. Tayari Serikali imetoa mikopo kwa wanafunzi 29,578. Tofauti na huko nyuma wakati huu fedha ilitangulia kwenye bodi, wanafunzi ndio wanaenda kuomba, wakati huko nyuma fedha zilikuwa zinachelewa. Tayari Serikali imeshatoa shilingi i bilioni 147 kwa ajili ya robo ya kwanza ya mwaka. Kilichotokea ni kwamba taratibu za udahili ambazo wakati huu wanafunzi wenyewe ndio walikuwa wanachagua vyuo ndizo zimechelewesha utolewaji wa mikopo na ndiyo maana kuna hawa wanafunzi wachache ambao bado hawajapata mikopo. Lakini kama ninavyokwambia tayari wanafunzi 29,578 wameshapata mikopo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili linalohusu vigezo vinavyotumika. Naomba nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna vigezo vikuu vinne vinavyotumika kwaajili ya kutoa mikopo.
Mheshimiwa Spika, kigezo cha kwanza ni uyatima, kigezo cha pili ni ulemavu, kigezo cha tatu ni uduni halafu kingine ni ile kuangalia masomo ya kipaumbele kulingana na mipango ya maendeleo ya taifa. Sasa wanapochanganya vigezo hivi vyote ndipo tunapata idadi ya wale wanafunzi ambao watapata mikopo. Kwa hiyo baadaye Mheshimwa Waziri atakapotoa taarifa atatoa takwimu kuonesha kwamba vigezo hivi vimezingatiwa na wanafunzi wale ambao tunasema wanastahili zaidi ndio hasa wamekuwa walengwa na ndio wamepata mikopo. Nashukuru sana.
MHE. JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa fursa ya kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Kwanza, ni vigezo gani viliifanya Serikali kurudisha mali za madhehebu mengine kama hospitali ya KCMC, Bugando na mashule na kwa nini isirudishwe mali za Kanisa hili la Moravian?
Swali la pili, kwa kuwa mgogoro huu na utata huu umechukua zaidi ya miaka 44, je, sasa Serikali ipo tayari kukaa katika meza ya majadiliano na Kanisa kumaliza utata huu uliodumu kwa miaka hiyo 44? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba baada ya zoezi lilioendelea baada ya miaka ya 1960 ya shule nyingi zilizokuwa chini ya mashirika ya dini kupelekwa Serikalini kwa makubaliano maalum, lakini baadaye kuna baadhi ya huduma kama za hospitali ambazo zilirudishwa.
Naomba tu nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba urudishwaji wa hospitali zile na baadhi ya huduma imefanywa kwa makubaliano maalum na madhehebu ya dini, vivyo hivyo hata shule ambazo zimeendelea kubakia Serikalini ambazo zamani zilikuwa ni shule za taasisi za kidini, kubakia Serikaini vilevile ni suala la makubaliano. Kwa hiyo, Serikali itaendelea kusaidia na madhehebu ya dini na mashirika mbalimbali na sekta binafsi katika kuendeleza elimu ikiwa ni pamoja na kuendelea kuzihudumia shule hizo kwa sababu inafanyika kwa maslahi mapana ya Taifa. Ifahamike kwamba miaka ya 63 zoezi hilo lilivyochukuliwa kulikuwa na makubaliano kama njia mojawapo ya kuhakikisha kwamba kunakuwa na usawa wa utoaji huduma na hususani elimu Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili kwamba ni lini majadiliano yatafanyika na Kanisa la Moravian kuhusu eneo la Chuo cha VETA tunachokizungumzia, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa hakuna mgogoro wowote uliopo katika umilikaji wa eneo hilo kwa sababu tokea lilipotolewa mwaka 1973 ilifanyika kwa makubaliano na makubaliano hayo bado yanafanya kazi, changamoto kidogo ambayo imetokea ni kuhusu chuo kuendelea kutumika kwa malengo yale ambayo ilianzishwa nayo na malengo yenyewe ilikuwa ni kuwasaidia wanafunzi ambao wamekosa fursa ya kwenda katika elimu ya sekondari sasa hili linaweza likajadiliwa lakini mgogoro haupo kwenye umiliki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu kwamba, Wizara yangu na Serikali iko tayari kuendelea kushirikiana na Kanisa la Moravian, ni washirika wetu tokea siku nyingi sana tokea miaka ya 1970, tunawashukuru sana, tutaendelea kujadiliana nao namna bora ya kutumia chuo hiki kwa maendeleo ya Taifa.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Waziri katika Jimbo la Kahama, Kata ya Mwendakulima kuna mgogoro wa muda mrefu sana kati ya Kanisa la Katoliki na Kijiji cha Mwendakulima na sasa ni mtaa juu ya ardhi ambayo Kanisa hili limemiliki.
Mheshimiwa Waziri, je, uko tayari kwenda na mimi katika Jimbo hili na Kata hii kuweza kutatua mgogoro huu maana umekuwa ni wa muda mrefu na unaleta hali ya kutoelewana kati ya Kanisa na wananchi wa Mwendakulima? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimahakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba niko tayari kwenda naye katika eneo hilo na ikiwezekana kuwashirikisha wenzetu wa Wizara ya Ardhi tuone mgogoro huo namna ya kusuluhisha, lakini kwa kuanzia hata leo niko tayari tukutane mimi na yeye tujadiliane kuhusu hili.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Mbulu Mjini limekuwa na migogoro ya ardhi hususani shule zetu za msingi na sekondari na kwa sasa karibu shule mbili ziko mahakamani kwa ajili ya kutetea ardhi zake.
Je, Serikali haiwezi kuchukua utaratibu sasa wa kuhakikisha kuwa maeneo yote ya shule za msingi na sekondari nchini zinapata kupimwa ili ziweze kuepukana na adha hii ya migogoro ya ardhi kwa taasisi hizi za Serikali?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama anavyosema, Serikali inahitaji kupima hayo maeneo naomba tu nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari kuna mkakati na maelekezo madhubuti ili taasisi zote za umma hususani shule kuhakikisa kwamba maeneo yao yote yanapimwa na kupatiwa hati ili kuondoa migogoro ambayo inaweza ikatokea pamoja na uvamizi.
MHE. PASCHAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, siku za hivi karibuni tumeisikia Bodi ya Mikopo imeongeza masharti au vigezo vipya kwa wakopaji, kwa mfano wale viongozi wanaojaza fomu za maadili ya viongozi wa umma wakiwepo Madiwani nao pia ni miongoni mwa watu ambao watoto wao wananyimwa mikopo. Kwa kuwa tunajua kabisa kwamba Madiwani hawana mishahara na wanategemea posho ambayo ni kidogo sana je, Serikali haioni kwamba, huu ni unyanyasaji ambao kwa namna yoyote hauvumiliki na hitakiwi kuufumbia macho unaofanywa na Bodi ya Mikopo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, siku za hivi karibuni wote tunajua kabisa kwamba Bodi ya Mikopo imeongeza makato kwa wanufaika wa mikopo. Kwa mfano awali ilionekana kwamba, wanufaika wa mkopo walikuwa wanalipa wanarejesha asilimia nane ya mkopo waliokuwa wamekopa kwa maana ya makato ya asilimia nane, lakini kwa sasa wanakatwa asilimia 15. Hali hii imesababisha wale wanufaika wa mkopo kama walimu na watumishi mbalimbali ambao walikuwa wamebakisha fedha kidogo ambazo walikuwa wanapata mwisho wa mwezi, leo hawana mshahara hata kidogo na kuna watumishi wanaacha kazi. Je, Serikali haioni ni wakati muafaka sasa kurudi kwenye asilimia nane ya makato, ili angalao watumishi hawa waliocha kazi waweze kurudi makazini na maisha yaweze kwenda vizuri? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli alivyosema kwamba katika mwaka huu wa masomo kuna vigezo vimeongezwa kwa ajili ya watu ambao hawastahili kupata mikopo, ikiwa ni pamoja na viongozi wa umma wanaojaza fomu za Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa umma. Lengo la kufanya hivyo ni kwamba, tunajaribu kuhakikisha kwamba mkopo ule unatumika kwa wale ambao hawana uwezo kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuhusu Madiwani kama wana uwezo au hawana uwezo tunajaribu kuangalia kipato chao wanachoweza kupata kwa mwaka na kulinganisha na Watanzania wengine wengi ambao hawana kipato kabisa. Kwa hiyo, lengo ifahamike tu ni kwamba ni kujaribu kutoa fursa kwa wale ambao hali yao ni mbaya zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hitaji la sasa la kwamba waombaji wa mikopo ambao wanatakiwa kurudisha wanakatwa asilimia 10 inatoka kwenye mshahara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nilifahamishe Bunge lako Tukufu kwamba mkopo ule ukishachukua kigezo cha pekee cha kwamba unatakiwa kurudisha fedha ni kwamba wewe umekopa, maana yake ilitakiwa pale unapomaliza shule uanze kurudisha.
Sasa kwa muda mrefu sana ule mkopo umekuwa unashindwa kuwanufaisha watu wengi kwa sababu watu wengi hawarudishi na ndio maana sasa tumelazimisha kwamba, ni lazima kwamba, mtu ambaye atakuwa amepata ajira aweze kulipa kwa asilimia 15 ya mshahara wake, lakini vilevile kuna kigezo kingine ambacho tumeweka kwamba, tunatoa kipindi cha mpito au grace period ya miezi 24 toka mwanafunzi amalize shule, lakini baada ya hapo kama hajaanza kulipa tunaanza vilevile kutoza riba ya asilimia
10. Lengo ni kwamba tunahitaji kuufanya mfuko ule uwe endelevu ili wananchi wengi waweze.
Waheshimiwa Wabunge nafahamu kuna baadhi ambao nao wanadaiwa mikopo, katika siku hizi za karibuni tunakuja na orodha ya wale ambao ni wadaiwa sugu. Kwa hiyo, nawaombeni ushirikiano…
MHE. ZAYNAB M. VULLU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Swali la kwanza, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, bado inaonekana kuna tatizo la uhaba wa Walimu. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inatoa Walimu wa kutosha ili waweze kufika kwenye Halmashauri zetu. Pia kuwa uwezo wa kupata Walimu wengi kwa sasa hivi haupo, je, hakuna haja ya kwamba wachukue Maafisa Afya kwenye Kata zetu waweze kusaidia watu ambao wana watoto wenye matatizo ya akili? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa, tatizo la ugonjwa wa akili au usonji linaongezeka nchini. Je, chanzo cha tatizo hilo ni nini, ni lishe duni, uhaba wa madini wakati mama anapokuwa mjamzito au ni nini kinachopelekea mpaka kuwa na idadi kubwa ya watu wenye ugonjwa wa akili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama alivyosema kwamba kwa kiasi fulani kuna changamoto ya kuwa na Walimu wa kutosha kwa ajili ya kuwafundisha watoto wenye matatizo ya akili na usonji. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba pamoja na changamoto hiyo Wizara imejipanga kuhakikisha kwamba katika siku za huko mbele tatizo hilo linaondoka.
Mheshimiwa Naibu Spika, mikakati hiyo imeanza kwa kujenga chuo cha kisasa cha kufundishia Walimu cha Patandi. Tunajenga The State of Art College kwa ajili ya kufundisha Walimu watakaotoa huduma kwa wanafunzi wenye mahitaji hayo. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba siyo kwamba Serikali haijajipanga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile wazo lake alilopendekeza kwamba tuwatumie Maafisa Maendeleo ya Jamii tutalifikiria kuangalia namna tutakavyoweza kufanya kazi pamoja na kwamba tunafahamu kwamba unahitaji watu maalum ambao wanajua saikolojia na namna nzuri ya kuwafundisha watoto hao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na chanzo, kuna vyanzo mbalimbali vinavyosababisha watoto wazaliwe wakiwa na hayo matatizo. Mojawapo ni suala la alcoholic disorders hasa kwa akinamama wajawazito. Ni muhimu sana kujua kwamba tayari kuna tafiti zinaonesha kwamba kama mzazi akiwa mjamzito atakuwa mlevi sana inasababisha mara nyingi mtoto kuzaliwa akiwa na haya matatizo. Sababu ya pili ni kwamba magonjwa mengine ni ya kurithi, kwamba watoto wanazaliwa kwa sababu wamerithi kutoka kwa wazazi na kuna sababu nyingine, kwa vyovyote vile nina uhakika wenzetu wa afya wanaweza wakawa na taarifa sahihi zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kama wameongezeka au hawajaongezeka, kama Wizara ya Elimu tunachofahamu na tunachofanya ni kwamba, tunajua tumeendelea kuongeza uwezo wetu wa kuwapokea wengi zaidi. Ndiyo maana kama ninavyosema, tumeendelea kutenga fedha kila mwaka; mwaka huu tumetenga shilingi bilioni 3.5 kuhakikisha kwamba wanafunzi wale katika shule za msingi na sekondari wanapata vifaa vya kuwafundishia. Vilevile hata katika ujenzi wa majengo wa sasa ukienda kwenye shule za msingi yanajengwa ili yaweze kukidhi mazingira maalum ya wanafunzi wa aina hii. (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII,
JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, nataka kuongeza maelezo mafupi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali sasa hivi ina mkakati, imeonekana kwamba siku 1,000 za mwanzo za mtoto baada ya kuzaliwa iwapo atapata tatizo la utapiamlo zinamuathiri sana katika kukua vilevile kiakili. Kwa hiyo, sasa hivi Serikali kupitia Taasisi yake ya Lishe, imeweka mkakati wa kuhakikisha kwamba siku 1,000 za mwanzo mtoto anapata lishe nzuri ili kuhakikisha kuwa anakua vizuri na anapata uwezo mzuri wa kuweza kuwa na akili sawasawa.
MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuweza kuwapatia wanafunzi hususan wa shule za msingi angalau mlo mmoja kwa siku?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ni lini Serikali itahakikisha kwamba wanafunzi watapata angalau mlo mmoja kwa siku, naomba nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari kuna utaratibu unaoendelea kwenye shule nyingi nchini kuhakikisha kwamba wanafunzi wanapata uji wakiwa shuleni. Hata hivyo, katika Mpango wetu wa elimu bila malipo, tayari tunafikiria kufanya maboresho ili masuala kama haya ya mlo vilevile yaweze kuchukuliwa
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Jimbo la Lupembe katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, tuna shule moja ya Matembwe ambapo watoto wenye ulemavu tofauti tofauti wanasoma pale na tuliomba vifaa vya kufundishia na kujifunzia wanafunzi kutoka Wizarani au Serikali lakini mpaka sasa bado hatujapata. Nataka kujua ni lini Serikali italeta vifaa kwa ajili ya kuwawezesha watoto wale waweze kupata elimu vizuri, kwa kuwa vifaa sasa hivi hawana? Ahsante.(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka uliopita 2016/2017, tulitoa vifaa kwa shule 213 za msingi na shule 22 za sekondari. Mwaka huu tumetenga shilingi bilioni 3.5 kwa ajili ya kununua vifaa. Naomba Mheshimiwa Mbunge aongozane nami nikitoka leo Bungeni ili anieleze mazingira ya shule yake tuweze kuweka kwenye utaratibu wa kugawa vifaa katika bajeti ya mwaka huu.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwanza kabisa niipongeze Serikali kwa mpango wake wa kujenga chuo kila Mkoa. Kwa kuwa vijana wengi Mkoa wa Simiyu hawana kazi na ukosefu wa ajira unasababisha vijana wengi kujiingiza kwenye vitendo vya uhalifu. Namwomba Naibu Waziri anihakikishie, ni lini sasa huo ujenzi utaanza Mkoani Simiyu ili vijana wajifunze ujuzi waweze kujiajiri wenyewe waondokane na umaskini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, kwamba kwa namna tulivyopangilia tutajitahidi tusitoke nje ya mipango yetu, ujenzi unatakiwa uanze Februari mwaka kesho.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi hicho wakati tunasubiri chuo kikamilike, tunaendelea kuwasihi vijana wa Simiyu na wengine wa Tanzania waendelee kuachana na uhalifu kwa sababu inawezekana isiwe tiba ya changamoto iliyopo.
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Elimu ya ufundi ni muhimu ili kuwawezesha vijana wetu kuajiriwa au kujiajiri. Je, ni lini Serikali itajenga Chuo cha VETA Wilayani Lushoto?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye swali la msingi, Serikali kwa sasa ina mpango wa kujenga vyuo 43 katika Wilaya mbalimbali hapa nchini, tayari tumeanza taratibu katika wilaya saba.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo letu ni kwamba Wilaya zote nchini katika wakati mmoja au mwingine zinakuwa na Vyuo vya VETA. Kwa hiyo, hata kwake Mheshimiwa Mbunge, Lushoto, kwa vyovyote vile ni sehemu ya Tanzania na ipo katika mipango hii. Naomba tu avute subira kama Waheshimiwa Wabunge wengine vilevile nitakapowaeleza, kwa sababu Serikali imedhamiria kwamba itaendelea kujenga vyuo hivi kadri ya fedha zitakavyopatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nimwombe Mheshimiwa Mbunge pamoja na Waheshimiwa Wabunge wengine kwamba inakuwa ni rahisi zaidi Serikali kuingiza mikono yake au jitihada kama wananchi wenyewe wamehamasika. Kwa hiyo, pale tunapoona wananchi wenyewe wameanza kujichangisha na kuhamasika inakuwa ni rahisi hata Wizara kutumia fedha ambazo zinapatikana kusaidia.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi.Pamoja na Serikali kuendelea kujenga vyuo katika Mikoa na Wilaya, tuna tatizo kubwa sana la Walimu wa Vyuo vya VETA, kwa sababu tuna chuo kimoja tu cha Morogoro ambacho ndicho kinachotoa Walimu. Je, Serikali inatusaidiaje kuhakikisha kwamba Vyuo hivi vya VETA vinavyojengwa na vilivyopo ambavyo vina tatizo kubwa sana la Walimu vinakuwa na Chuo kingine cha Walimu ili kuweza kutatua tatizo la wanafunzi, watoke pale wakiwa wamekamilika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama anavyosema kwamba kuna changamoto ya kuwapata Walimu wa Vyuo vya VETA. Nimhakikishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba mkakati wa kuhakikisha kwamba elimu ya ufundi inapatikana nchini kwa wingi na ubora zaidi ni pamoja na kuhakikisha kwamba tunakuwa na Walimu wa kutosha. Kwa hiyo, katika mikakati ya Wizara kuna mkakati wa kuhakikisha kwamba Walimu pia wanapatikana.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Serikali iliahidi kwamba maeneo yenye vyuo vya wananchi (FDCs) itaviongezea uwezo ili viweze kutoa elimu ya ufundi kwa ufanisi zaidi. Je, ni lini Serikali sasa itatimiza hiyo azma katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi, Njombe Mjini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ujenzi wa Vyuo vya VETA nchini unasuasua sana na Jimbo la Njombe Mjini lina shule 11 za sekondari, kuanzisha fani ya ujenzi ama umeme gharama yake ni nusu ya gharama ya kujenga maabara ya kemia ama ya baiolojia. Je, Serikali ipo tayari kuzifanya Shule za Sekondari Mgola na Luhololo kuwa shule za Sekondari za Ufundi kwa fani mbili kwa majaribio (pilot project)?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu jitihada za Serikali katika kuboresha Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs); naomba nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara tayari imepata ufadhili wa kuweza kukarabati vyuo 30 kati ya 55 tulivyonavyo vya wananchi. Lengo ni kuhakikisha kwamba vyuo hivi vinarudi katika utendaji bora zaidi, vilevile ikiwezekana waendelee kutoa elimu ya ufundi kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Chuo chake cha Njombe Mjini nimweleze tu kwamba ni fursa imejitokeza kwamba tayari tumepata dola milioni 120 kwenye mradi unaoitwa Education and Skills for Productive Jobs (ESPJ), fedha hizi zinapatikana lakini kwa ushindani. Kwa hiyo hata Chuo chake cha Njombe Mjini inabidi washindane kuomba fedha hizi ili Wizara iweze kuja kufanya tathmini na kuangalia kama ni chuo ambacho kinahitaji kukarabatiwa, ni fursa ambayo ipo. Kwa hiyo nimweleze tu kwamba fedha zipo tutatangaza muda sio mrefu ili waweze kuziomba.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mpango wa kurejesha vyuo vyote 55 vya wananchi virudi katika hali yake ya zamani, viwe vyuo vizuri ili viendelee kusaidia kutoa mafunzo katika maeneo mbalimbali ya elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ni kuhusiana…
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na Shule zake za Sekondari za Mgola na Luhololo kuruhusiwa kuwa shule za ufundi hili linajadilika. Nimwombe Mheshimiwa Mbunge kama wao kama Njombe Mjini wanakubali zibadilike kuwa shule za ufundi sisi tuko tayari kama Wizara tufanye majadiliano na kwa hakika itawezekana. (Makofi)
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Maswali Namba 75 na swali Na 76 yanafanana lakini Mheshimiwa Naibu Waziri katika majibu yake ambayo ni mazuri sana amesema kwamba palipo na wananchi na kama wamehamasika na wameshajitolea kuanza kazi za ujenzi wa vyuo kama hivi, Serikali iko tayari kuweza kuwapa mkono.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Bunge lililopita, Serikali iliwakubalia wananchi wa Wilaya ya Busega kutenga eneo kwa ajili ya kuanzisha Chuo cha Ufundi Stadi (VETA). Je, wazo hili la Serikali bado liko palepale au limebadilika?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyosema mwenyewe, kama tayari kuna ahadi thabiti ya Serikali kuhusiana na chuo chake cha VETA Busega, leo hii haiwezi ikabadilika. Kwa hiyo, tuendelee na majadiliano tokea tulipoacha kutoka kwa wenzetu ili tuone namna bora ya kutekeleza ahadi hiyo. (Makofi)
MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Naibu Spika nakushukuru sana kwa kuniona. Kwa kuwa, hivi karibuni Serikali kupitia Waziri Jafo ilitangaza kwamba au ilitoa agizo kila mkoa utengeneze viwanda 100 na kwa kuwa vyuo hivi vya ufundi ni muhimu sana. Je, ni lini Serikali itaanza kutoa ruzuku kama ilivyokuwa ikiahidi mara kwa mara kwenye vile vyuo ambavyo ni vya wananchi, kule kwangu kuna vyuo vya Mawelas, KVTC, Imani ili azma hiyo ya Serikali iweze kutimia haraka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza katika moja kati ya majibu yangu leo, kwa kuanzia tunaanza na ukarabati kabla hatujaanza kufikiria kutoa ruzuku tunaanza kwanza na ukarabati, kama nilivyosema tumepata Dola milioni 120 tunaanza kukarabati vyuo 30 kwanza kati ya 55.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Komu achukulie kama ni hatua mojawapo kufikia hicho anachotaka ili vyuo vyake viweze kushindania fursa hii ya kukarabatiwa; baadaye sasa vikishakuwa katika hali nzuri ya kuchukua wanafunzi ndiyo tuanze kufikiria masuala mengine kama ruzuku. Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwa kuwa swali langu lilikuwa la Wilaya ya Nyang’hwale na nimejibiwa kimkoa, Nyang’hwale imeshajipanga tayari na imetenga maeneo ya kuweza kujenga Chuo cha Ufundi. Je, Serikali imeshaweka ndani ya mpango 2018/2019 mpango huu wa kujenga VETA katika Wilaya ya Nyang’hwale?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Serikali huwa mipango yake inaenda taratibu na Nyang’hwale ina vijana wengi ambao hawana ujuzi. Je, Serikali iko tayari kuchukua angalau vijana 50 na kuwapeleka katika maeneo mengine mbalimbali nchini kwenda kujifunza ujuzi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, kuhusu kama katika bajeti ya mwaka 2017/2018 tumetenga fedha kwa ajili ya kujenga Chuo cha VETA Nyang’hwale; nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba tunajitahidi kutenga fedha kadri tunapopata kwa ajili ya kujenga Vyuo mbalimbali vya VETA. Kwa sasa hakuna fedha ambazo zimetengwa kwa ajili ya Nyang’hwale; lakini nimwahidi tu kwamba kwa sababu mpango wetu ni kuhakikisha Wilaya zote zinakuwa na Vyo vya VETA tutaendelea kupangilia na kutafuta fedha na kujenga kadri inavyowezekana.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kama tuko tayari kupeleka vijana 50 kwenye Vyuo vingine nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, kama wao watajipanga kama Wilaya sisi tuko tayari kushirikiana nao kuhakikisha kwamba vijana hao wanapata nafasi katika Vyuo vingine.
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. La kwanza litalenga wale waliofanya mitihani kabla ya mwaka 2008 ambao hawapewi cheti mbadala. Kwa mujibu wa majibu ya Serikali badala ya kupewa cheti wanapewa uthibitisho na mara nyingi uthibitisho huu mtu anakuwa ameomba ili uelekezwe ama sehemu anayoomba kazi anayoomba kujiunga na masomo zaidi.
Sasa Serikali haioni umuhimu wa hata hawa ambao walipoteza Cheti ambao walihitimu kabla ya mwaka 2008, kuwafanyia utaratibu wa kuwapa hiyo duplicate?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa mara nyingi watu wanaoomba Baraza la Mitihani liwasilishe hizo taarifa kama vyeti kule walikoomba kazi au masomo, vyeti hivyo mara nyingi uthibitisho upo kwamba, vimekuwa vinachelewa na hivyo kuwasababishia watu hao ama kukosa hizo nafasi za kazi walizoomba au nafasi za masomo.
Je, Serikali haioni haja ya kuwa na mifumo kama ya vyuo vya elimu ya juu ambapo mtu ambaye amepoteza cheti anaweza akapewa nakala hata mbili tatu akazitunza mwenyewe, midhali Serikali na Baraza la Mitihani limejiridhisha kwamba, huyo mtu kweli alihitimu masomo hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu wahitimu waliomaliza shule kabla ya mwaka 2008, kwa sasa imekuwa ni vigumu kuwapatia vyeti mbadala kwa sababu wakati huo vyeti havikuwa vinabeba picha za wahitimu. Kwa hiyo tukitaka kubadilisha maana yake ni lazima tutafute picha za wale wote ambao wamemaliza shule kabla ya 2008. Kwa vyovyote vile ni kazi kubwa, hata hivyo, sio jambo ambalo haliwezekani kufanyika kwa hiyo, nalibeba tukajadiliane ndani ya Serikali kama linatekelezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ni kuhusu kuchelewa kupatiwa nakala au cheti mbadala au uthibitisho kwa wale ambao wanakuwa wamepoteza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto iliyopo ni kwamba, mara nyingi watu wanaenda kuomba vyeti mbadala au uthibitisho pale wanapokuwa na uhitaji. Ushauri wangu kwa Watanzania wote ni kwamba, kila mara unapopoteza cheti usisubiri mpaka uhitaji kutumia cheti hicho ndio ukaanze kutafuta mbadala au uthibitisho. Ukishapoteza anza taratibu za kuanza kutafuta, ili ikitokea kwamba, unahitaji iwe ni rahisi kwa sababu, tayari unakuwanacho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kwa sasa kwa mwombaji yeyote yule, ukiomba inachukua angalau siku 30, lakini hizo ndiyo siku nyingi ambazo kinaweza kuchukua, ni maximum. Inaweza ikawa chini ya hapo na kwa sasa hivi kwa kweli, Baraza la Mitihani la Taifa ni moja kati ya Taasisi za Serikali zinazofanya kazi kwa ufanisi mkubwa sana kwa hiyo, mara nyingi hazifiki hata hizo siku ukikamilisha taratibu zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu pendekezo lake la kutumia utaratibu unaotumiwa na vyuo vikuu la kutoa nakala, naomba nilibebe, ni wazo zuri, tukaangalie namna ya kutekeleza, ili ikiwezekana tunapotoa cheti tutoe nakala kadhaa ili mtu aweze kutumia pale atakapopoteza. Ahsante.
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa taarifa zinaeleza kwamba, vyeti vimekuwa vikizalishwa nje ya nchi. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuzalisha vyeti hapa nchini ili zoezi la kuvitoa liwe rahisi zaidi? Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa nilizonazo mimi vyeti vinatengenezwa hapa hapa nchini, tuna vifaa vya kisasa, Baraza la Mitihani lina vifaa vya kisasa sana na ni taasisi ambayo kwa ufanisi wake nchi nyingi sasa hivi zimeanza kuja kujifunza namna tunavyofanya. Kama Mbunge ana taarifa tofauti na hizi naomba tuonane baada ya Bunge hili ili nijue kwa nini yeye ana taarifa ambazo si sahihi.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na jitihada za kudhibiti ubora wa elimu hapa nchini ikiwa ni pamoja na kuanzia shule ya awali mpaka vyuo vikuu, naishukuru Serikali kwa juhudi hizo kwa sababu siku zote Upinzani tumekuwa tukizungumzia suala la ubora wa elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka kujua ni nini hatma ya wanafunzi katika vyuo vile ambavyo vimefutiwa usajili wakiwa tayari wanaendelea na masomo? Kwa mfano, unakuta vijana hao tayari walishalipa ada lakini na muda wao. Je, Serikali inatuambia nini au inawaambia nini wanafunzi ambao tayari walikuwa kwenye masomo lakini wakaondolewa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kweli kwamba huu ukaguzi ni mzuri sana lakini kumekuwa na ubaguzi mkubwa kwenye ukaguzi kwa maana ya shule za msingi za Serikali na zile za private, hali inayopelekea kuwa na double standard, kwa sababu wanafunzi wa shule za private kila mwanafunzi anatakiwa alipe shilingi 5000 kwa ajili ya ukaguzi, lakini wanafunzi wa shule za Serikali ni bure. Hamuoni kwamba kwa ubaguzi huu ndiyo inayopelekea kuporomoka kwa elimu hasa kwenye shule za Serikali na ndio sababu kunakuwa na matokeo mabaya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uwezekano wa wanafunzi wanaondelea na vyuo kuathirika na hatua ambazo tunachukua wakati wa kuhakikisha kwamba kuna ubora katika vyuo vyetu.
Naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kila wakati tunapochukua hatua tunahakikisha kwamba wanafunzi hawataathirika lakini ifahamike kwamba kwa sababu tokea awali vyuo hivyo vinafahamu kuhusu utaratibu ambao wanatakiwa wafuate, pale tatizo linapotokea maana yake wenyewe watatakiwa kurejesha gharama hizo kwa wanafunzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuhusiana na tofauti aliyotaja ya ada ya ukaguzi kati ya shule za Serikali na zile za watu binafsi, Serikali haioni kwamba tofauti hiyo ina athari zozote zile katika ubora wa elimu. Ni utaratibu tu ambao umewekwa wa kuhakikisha kwamba hiyo ada inalipwa lakini hatuoni kwamba shilingi 5000 kulipa kwa shule binafsi kwamba ina athari katika ubora wa elimu.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, kwanza nina masikitiko kwamba majibu ambayo ametoa Mheshimiwa Waziri, ama wataalam wake hawaijui sekta ya uvuvi na wanaelekea zaidi kwenye shughuli za mifugo au itakuwa kuna danadana za hapa na pale. Nina maswali mawili ya nyongeza yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kufikia mkakati wa Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati, Serikali imekuja na majibu wanasema wanataka kuanzisha viwanda vitatu vya kutengeneza boti aina ya fibre glass. Tanzania ya viwanda
kuelekea uchumi wa kati wanataka kutengeneza boti sasa ndogo (fibre glass), Serikali ituambie ina mkakati gani wa kuweza kununua meli za uvuvi za kisasa kwenda kwenye bahari kuu ambapo watavua samaki ambao wanavuliwa na nchi nyingine? Hiyo, tunataka mkakati wa ziada, sio mnasema mnataka kununua fibre glass? Fibre glass kwenye uchumi wa kati, Tanzania ya viwanda? Maajabu makubwa haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, wanasema Serikali kwamba sekta ya uvuvi hii wanataka kuboresha maisha ya wavuvi, wametenga wana shilingi milioni 400 kwa ajili ya kuboresha ruzuku za uvuvi na mambo mengine. Shilingi milioni 400 Mheshimiwa! Wavuvi ni maskini, shilingi milioni 400 ndio kitu gani? Kwenye bahari na kwenye maziwa? Serikali ituambie mna mkakati gani wa ziada kuboresha maisha ya wavuvi hasa wadogo wadogo sio shilingi milioni 400. Ndio Tanzania ya viwanda kuelekea uchumi wa kati hiyo? Tupe majibu ya uhakika, Serikali inasemaje juu ya kuboresha maisha ya wavuvi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Masoud kama ifuatavyo:-
Kuhusu uwekezaji wa ununuzi wa meli kwa ajili ya uvuvi katika bahari kuu nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali yenyewe haina nia ya kununua meli, lakini kinachofanywa ni kuweka mazingira wezeshi na kuhamasisha sekta binafsi iweze kuwekeza katika ununuzi wa meli pamoja na uvuvi katika bahari kuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Shilingi milioni 400, nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba hiyo ni sehemu ndogo tu shilingi milioni 400 zilizotolewa kwa ajili ya kuwawezesha wavuvi ni sehemu ndogo tu ya jitihada mbalimbali zinachokuliwa na Serikali kwa ajili ya kuendeleza sekta ya uvuvi.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, kwa kunipa nafasi. Wakazi wa Wilaya ya Nkasi karibu nusu wanakaa mwambao wa Ziwa Tanganyika ambapo wanajishughulisha na shughuli ya uvuvi. Serikali kupitia Mkuu wa Mkoa imepiga marufuku kabisa shughuli za uvuvi kufanyika mchana na kufanyika kwa kutumia vifaa vyovyote vya kielektroniki kama vile tochi na taa za solar ambazo zinatoa mwanga mdogo tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa wavuvi wamekaa na wamechanganyikiwa hakuna kazi yeyote wanayoifanya na hawawezi kuendesha maisha yao kwa sasa hivi. Kwa hiyo, naiomba Serikali ione namna ambavyo wataiona changamoto hii kwa namna ya pekee kwa sababu wananchi hawana namna ya kujisaidia kwa sasa. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kama alivyosema kwamba katika siku za karibuni kumetokea hali ya sintofahamu kwa wavuvi wa Ziwa Tanganyika kutokana na katazo ambalo limefanywa na Serikali. Wabunge wanaotoka katika ukanda huo wengi wamekuwa wakija ofisini kwetu kufuatilia akiwepo Mheshimiwa Keissy, yeye nimeongea naye sana kuhusu hili.
Nimhakikishie tu kwamba kilichotokea ni mkanganyiko kidogo kuhusu kanuni ambayo hairuhusu uvuvi kwa kutumia jenereta na kwa kutumia solar ya zaidi ya wati 50; maelekezo sahihi tumeshayatoka kwa hiyo tunaamini katika siku chache hili litakuwa limeshakamilika na wavuvi wataendelea kuvua kama kawaida.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Naomba kwa namna ya kipekee kabisa wakati nikijielekeza kuuliza swali hilo niipongeze sana Serikali yetu ya Awamu ya Tano kwa kazi nzuri inayofanya ya kuwalinda wakulima wetu na wananchi wetu wa hali ya chini. Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hiyo pia nimpongeze Mkuu wetu wa Mkoa Engineer Evarist Ndikiro kwa kazi nzuri aliyoifanya mwaka wa jana wa kuyalazimisha Makapuni mawili ya Alpha Choice na Kaisari ambayo yaligoma kuwalipa kwa wakati wakulima wa korosho wa vijiji vya Msonga, Kalole, Mkuranga mjini na Kimanzichana Kusini. Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jibu la msingi la Mheshimiwa Waziri anaeleza kwamba wanapochelewesha…
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Ahsante sana. Wanapochelewesha kulipa malipo ya wakulima wa korosho huchelewa. Je, Serikali ipo tayari sasa kuhakikisha inawasimamia ipasavyo na madhubuti kabisa wanunuzi hao ili wawe wanaondoa mazao yao katika maghala yetu mapema iwezekanavyo ili mzigo mwingine wa wakulima uingie kwa wakati na waweze kupata pesa za kuinua maisha yao?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaona zao la korosho kama mfano wa namna ambavyo tunaweza tukafanya kilimo chetu kifanikiwe. Mafanikio makubwa na ya kihistoria ambayo yamepatikana katika korosho katika msimu uliopita ni kielelezo tosha cha namna Serikali ya Awamu ya Tano inavyotaka kushughulikia changamoto za kilimo. Kwa hiyo, hatutakubali mtu yoyote aje avuruge mafanikio yetu na ndiyo maana hizo kanuni zimeweka wazi kama unaenda ku-bid kununua korosho ni lazima kuweka dhamana. Hiyo inatusaidia kuwashughulikia wanunuzi wababaishaji ambao wanaenda ku-bid lakini baadaye korosho zinahifadhiwa halafu baadae wanakuja kulalamika kwamba zimepoteza sifa. Kwa hiyo, kwa sasa haiwezekani tena na niwahakikishie tu wakulima na Waheshimiwa Wabunge kwamba mtu yeyote ambaye ameshinda tender ya kununua korosho atalazimika kulipia na haiwezekani baadaye akaja kuleta malalamiko mengine, kwa hiyo, hilo halitatokea.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti nashukuru sana. Tatizo hili la wazabuni kushinda tender na baadae kuchelewesha huduma kwa Watanzania kwa muda uliokusudiwa imekuwa tatizo kubwa katika nchi yetu. Mifano ya wazi zipo katika Halmashauri za Wilaya ya Mbulu kwa miradi ya maji na miradi ya afya. Mifano hiyo ni kama ambavyo kupewa tender makampuni ambayo hayana uwezo na hatimaye baadaye kuchelewesha huduma hizi. Je, Seriakli yetu sasa kutokana na hali hii ambapo tenda hutolewa na wataalam ndani ya Halmashauri, inachukua hatua gani kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata huduma kwa wakati uliokusudiwa kutokana na muda wa mikataba?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba nilichozungumzia kwenye korosho ni zile taratibu ambazo tumeweka kwa ajili ya korosho, lakini ukweli wa mambo, kuna utaratibu wa kawaida wa kisheria kuhusiana na mambo ya tender. Sheria yetu ya manunuzi inaweka wazi namna tender inavyotakiwa kuendeshwa, lakini vilevile inaweka masharti kuhusiana na utekelezaji wa miradi kwa yule ambaye ameshinda tender na kwa vyovyote vile hairuhusiwi kisheria mtu ambaye ameshinda kutelekeza ile kazi kama kuna mapungufu ambayo yametokea ni vizuri kuangalia katika kesi zenyewe ili wale ambao wamehusika waweze kuchukuliwa hatua za sheria.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Moja ya sababu zinazofanya ucheleweshwaji wa malipo ya korosho ni pamoja na tamko la Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, alitamka kwamba korosho zote za Mkoa wa Lindi na Mtwara zipitie Bandari ya Mtwara kitendo ambacho bandari ya Mtwara ilishindwa kusafirisha korosho hizo kwa wakati na wanunuzi wakaacha kulipa kwa sababu korosho zao mpaka ziingie kwenye maji ndipo waendelee kufanya malipo. Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, sababu ya pili; ni kwamba hata hayo makampuni mnayosema kwamba mnayadhibiti pale ambapo yanakuwa yanachelewesha kulipa lakini bado kuna mtindo wa hayo makampuni kubadilisha majina. Unalifutia jina kampuni hili, mwenye kampuni ni yule yule anatengeneza kampuni nyingine…
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Je, Serikali inatoa kauli gani namna ya kukabiliana na matatizo hayo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kama alivyosema kwamba kitendo cha kuelekeza korosho ipelekwe nje kupitia Bandari ya Mtwara ilikuwa ni moja kati ya sababu ambazo zilipelekea ucheleweshwaji wa malipo na kuvuruga kwa kiasi fulani soko la korosho. Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo nimueleze Mheshimiwa Mbunge kwamba Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa na Serikali kwa ujumla walifanya hivyo kwa nia njema. Tulitaka vilevile kujenga Bandari ya Mtwara kama moja kati ya bandari zetu, kwa hiyo, ilikuwa ni kwa nia njema. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile hata ilipotokea changamoto ile ya mizigo kurundikana bandarini, Serikali ilikuwa rahisi kuchukua hatua na kuruhusu ipitie Bandari ya Dar es Salaam. Kwa hiyo, baadae tatizo hilo liliisha. Kuhusu hili la makampuni kutumia majina mbalimbali, ni tatizo kubwa, tunatambua kwamba unakuta mtu mmoja au watu wale wale wanakuwa na kampuni zaidi ya kumi, wana-bid katika soko lile lile. Lakini nikueleze tu kati ya mabadiliko makubwa ambayo tumefanya ni hilo la kuleta kanuni na utaratibu ambao ni lazima kuweka security bid ili baadaye ukishashinda tender baadaye huwezi kukimbia na kusema kwamba sitakuja kuchukua korosho. Kwa sasa ni lazima uchukue kwa sababu usipochukua, fedha zako tayari ulishaziacha na Serikali itawalipa wakulima.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza siyo kweli kwamba amelipa madeni hadi Oktoba mwaka jana. Madai ninayo bado yapo mengi yana zaidi ya mwaka mmoja, miaka miwili sasa nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, inakuaje Serikali inampa mtu kiwanda kwa mikataba na kwa utaratibu unaokubalika anashindwa kutimiza wajibu wake ambao ni pamoja na kulipa bei za wakulima na mishahara ya watumishi Serikali
inamuangalia tu mwekezaji huyo, anasema hapa ameahidi ambapo siyo kweli kama nilivyosema na Serikali inamuangalia tu huyu inasema ameahidi halafu inamuachia?
Swali la pili, wakulima hawa ambao hawalipwi hela yao ya chai ndiyo wakulima hawa ambao wanalima kahawa. Tumesema humu mara nyingi kahawa ina bei hafifu. Wizara ni hiyo hiyo ya kilimo imeagizwa na Mheshimiwa Rais iondoe kodi kwenye zao la kahawa, kodi ziko nyingi karibu
30. Kwa nini mpaka leo kodi hazijaondolewa na wakulima hawa wanazidi kuumia, kwenye chai wanaumia na kwenye kahawa wanaumia? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Spika, kuhusu kama ni kweli au siyo kweli kwamba tayari haya malipo yamefanyika, mimi nipo tayari kukaa na Mheshimiwa Mbunge ili tufananishe taarifa tulizonazo, kwa sababu kwa ripoti ambayo ninayo na ambayo ni ya Serikali inaonesha kwamba kuna malipo yamefanyika lakini niko tayari kukutana nae, tujadili tuone
taarifa sahihi ni ipi.
Mheshimiwa Spika, vilevile mazingira ya kampuni
ambayo anazungumzia ni magumu kidogo kwa sababu wakulima wenyewe ni wamiliki vilevile wa hisa kwenye kampuni ile kwa hiyo ilipobinafsishwa na Serikali wakulima wa chai vilevile nao waliweza kupata asilimia fulani. Pamoja na changamoto ambazo zimekuwepo bado wakulima nao vilevile ni wamiliki wa kiwanda kwa kiasi kikubwa, lakini kama nilivyosema Serikali imekuwa ikiendelea kuwasiliana na kiwanda ili kuondoa hizo changamoto ambazo zimetokea.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la pili, ni kweli kama Mheshimiwa Mbunge alivyosema kwamba kumekuwepo na manung’uniko ya haki kabisa kuhusu tozo na kodi nyingi ambazo zimepitiliza katika zao la kahawa na mazao mengine. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge
kwamba siku tutakaposoma hotuba yetu kwa ajili ya mwaka ujao wa fedha awepo maana yake tutaziondoa tozo mwaka huu mpaka nyingine mtatuomba tuzirudishe.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, ni jambo la kushangaza na
kusikitisha kwa sababu wafanyakazi mimi nina malalamiko yao, nina document nitaweza kumletea Mheshimiwa Waziri hawajalipwa wale wafanyakazi na wengine wamefikia mahali pa kustaafu hawajapata hata pesa zao. Kile kiwanda
kimebaki kubadilishwa na wasimamizi mara kwa mara kwa ajili ya kutaka kuwadhulumu wafanyakazi pamoja na wakulima. Ni lini Waziri utakwenda pale kuhakikisha wewe mwenyewe kwamba wafanyakazi wameshalipwa? Mheshimiwa Spika, nina uhakika hawajalipwa hata senti tano.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Spika, kama nilivyokwishasema kwa
Mheshimiwa Rweikiza, niko tayari kukutana na Waheshimiwa Wabunge ili tufananishe taarifa tulizonazo. Taarifa sisi tuliyonayo ni kwamba tayari kuna malipo ambayo yamefanyika siyo yote sawa, lakini niko tayari kama nilivyosema kukutana nae ili tuangalie kwamba nani ana taarifa sahihi na vilevile Wizarani au Serikalini kama kuna Afisa
ambaye ameniletea mimi taarifa za uongo atachukuliwa hatua.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nianze kwa
kupongeza Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa ushirikiano wanaonipa kuhakikisha kwamba tunapata zao jipya Tanzania, zao linaloitwa stevia kupitia Jimbo langu la Ngara.
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi tayari wameshatoa kibali cha kuingiza mbegu ya zao la stevier zao ambalo ni sukari ambayo ni anti-diabetes, antipressure lakini zao ambalo ni zao la kuinua kipato cha Watanzania. Pamoja na kutoa kibali hicho kwa sababu ni
zao geni tunahitaji kufanya utafiti kwanza na tayari Wizara imeelekeza Kituo cha Utafiti Maruku ambacho kiko Mkoa wa Kagera kushirikiana na Kampuni ya East African Stevier and Agro-Investment kufanya utafiti wa zao hilo lakini tatizo ni fedha za kufanyia utafiti. Je, Wizara ya kilimo, Mifugo na Uvuvi wako tayari kutenga pesa ili kuwezesha kituo cha utafiti Maruku kushirikiana na Kampuni ya East Africa Stevier kutoa pesa ili kuweza kufanya utafiti huu na hatimae zao hilo liweze kuanzishwa katika nchi yetu ya Tanzania na kuleta mabadiliko ya uchumi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Gashaza kwa jitihada na ubunifu ambao ameufanya Jimboni kwake katika kutafuta mazao ambayo yana tija kwa wakulima. Kimsingi tumekuwa tukishirikiana naye kama Wizara ili kuangalia namna ya kuleta nchini zao la stevier
ambalo huko maeneo mengine linakolimwa lina tija kubwa sana. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kama ambavyo tayari tumeshashirikiana naye katika hatua za kusajili hilo zao, Wizara iko tayari vilevile kushirikiana naye na wananchi wake katika kufanya utafiti katika kituo chetu cha Maruku ili zao hilo liweze kuanza kulimwa nchini na Wizara iko tayari kutenga bajeti ya kawaida ya utafiti kwa kituo hicho ili utafiti huo uweze kufanyika.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa majibu haya ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Waziri katika majibu katika majibu ya msingi ameeleza kwamba Wilaya za Kibiti, Rufiji na Wilaya yangu ya Mkuranga ni miongoni mwa Wilaya ambazo wavuvi wake hajaomba mikopo. Inawezekana kabisa kutokuombwa kwa mikopo hii ni kutokana na ukosefu wa elimu ya kuweza kuwafahamisha na kuwawezesha waweze kuwa na uelewa wa kuomba hii mikopo.
Sasa swali langu, naomba Mheshimiwa Naibu Waziri aniambie moja kwa moja ni lini tunaweza tukashirikiana sisi na wao ili kwa haraka zaidi Watanzania hawa wa Kisiju, Kibiti Delta na Rufiji mpaka Bagamoyo waweze kutumia fursa hii ya mikopo inayotolewa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Ulega siyo mgeni sana kwenye Ofisi ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, kwa hiyo, naendelea kumkaribisha amekuja mara nyingi sana kufuatilia changamoto za wananchi wake, aje ofisini hata akitaka leo mchana tuongee na tuangalie namna ya kufikisha elimu hii kwa ukubwa zaidi kwa sababu tayari Halmashauri zinatakiwa zitoe elimu kwa wavuvi na kuwafahamisha kwamba kuna fursa hiyo. Kama nilivyosema niko tayari kukaa naye tuweke mkakati wa kupeleka elimu zaidi.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wavuvi hata ho wa maeneo ya Rufiji na maeneo mengine wanaojishughulisha kwa mambo ya uvuvi wametengeneza Beach Management Units na hizi BMUs zina uongozi. Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa Wizara ya Kilimo pamoja na Halmshauri husika wakawa wanaviongezea nguvu hizi Beach Managementi Units kwa kuwasaidia kielimu hata na masuala ya kifedha?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama anavyosema vikundi vya usimamizi wa rasilimali za uvuvi katika mwambao au tunaziita Beach Management Units ni kweli imekuwa ni fursa ambayo inaweza ikatumika katika kutoa elimu, lakini vilevile kutoa misaada mbalimbali ambayo inaweza ikawasaidia wavuvi kufanya shughuli za uvuvi katika utaratibu ambao ni endelevu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wowote ambao Serikali imetoa elimu tumetumia sana Beach Management Unit, Serikali ndiyo imesaidia kuzianzisha lakini niendelee kumsihi Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wote kujaribu kuhimiza Halmashauri zao ambao kimsingi wao wanakaa kwenye Baraza la Madiwani kuendelea kutoa elimu kwa kupitia Beach Management Units lakini vilevile kuhakikisha kwamba tunatenga raslimali kwenye halmashauri zetu ili hiyo elimu iweze kutolewa kwa urahisi zaidi.
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipa nafasi niweze kusema kuuliza swali moja la nyongeza.
Tunatambua kwamba katika kupambana na uvuvi haramu hawa Beach Management Units wamekuwa wakisaidia sana, lakini kwa bahati mbaya sana walikuwa hapati kipato cha moja kwa moja, kwa hiyo wakati mwingine wanageuka wao nao kushiriki katika uvuvi haramu.
Je, ni lini Serikali itaanzisha huu ufugaji wa samaki kwa njia ya cage ambao utakuwa unawapatia vile vikundi wa Beach Management Units kipato cha ziada ili waendelee kutunza maeneo yetu haya ya Uvuvi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue kwanza nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mathayo kwa sababu amekuwa mmoja kati ya Wabunge ambao wamejitahidi sana kuhakikisha kwamba wavuvi wao wanaingia katika ufugaji wa samaki vilevile uvuvi ambao ni endelevu, tunatambua jithata hizo zimezaa matokeo mazuri sana kwani katika eneo analotoka uvuvi haramu umepungua sana. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba ufugaji wa samaki kwenye vizimba (cage culture) ni moja kati ya aina ufugaji wa sasa ambao Serikali imeamua kuhimiza wananchi wajihusishe nao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inachofanya ni kutoa elimu pamoja na kuweka mazigira wezeshi ambayo wavuvi mbalimbali wanaweza wakajihusisha katika cage culture kwa hiyo katika BMUs lakini vilevile kwa wavuvi mmoja mmoja kama kuna ambao wanataka kuingia katika ufugaji wa samaki katika vizimba Wizara yangu iko tayari kushirikiana na Halmashauri wanazotoka ili kutoa elimu ya njia sahihi ya kuweza kufanya ufugaji wa samaki kwenye vizimba.
MHE. SAUMU H. SAKALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina swali moja la nyongeza. Katika jibu la msingi la Mheshimiwa Waziri ametaja Wilaya ambazo zitapata fursa wavuvi hao Wilaya ya Pangani hakuitaja. Sasa ningependa kufahamu wana mpango gani na wavuvi wa Pangani hasa ukizingatia nao pia kuna uvuvi wa prawns, lakini pia wamesahaulika sana katika elimu, kitu ambacho wangeweza kupata elimu wangeweza kupata hiyo mikopo ambayo ingewasaidia katika suala zima la uvuvi. Ahsante (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, orodha ya Halmashauri au Wilaya ambazo nimetaja ni zile ambazo tayari zimeshanufaika na mpango huo wa wavuvi kupatiwa asilimia 40 ya fedha kwa ajili ya kununua vifaa vya uvuvi hasa injini za boti. Kwa hiyo, ninachosema mpango huu upo na unapatikana kwa Halmashauri zote ili mradi wenyewe wajipange na wakidhi vigezo halafu tutaoa asilimia 40.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Pangani, mimi nimefika Pangani na watu wa Pangani nawapenda sana, Mheshimiwa Aweso nilikutana naye kule. Kimsingi niliwaahidi kwamba wakijipanga kwenye vikundi, nipo tayari kuwasaidia waweze kupata asilimia hiyo 40. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwambia vilevile mheshimiwa Mbunge wapangeni wavuvi wenu katika vikundi, watafute fedha asilimia 60 halafu baada ya hapo tutawasaidia kupata hiyo asilimia 40 waweze kununua injini na waweze kufanya uvuvi kwa njia ambayo ni rahisi zaidi. (Makofi)
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuuliza swali la nyongeza na pili nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kutupa majibu ya matumaini. Hata hivyo, napenda kusahihisha kidogo wakati wataalam wamekuja mwaka 2015/2016 nilikuwepo na tuliona maeneo mawili ya malambo kwa ajili ya kujenga malambo na maeneo mawili kwa ajili ya majosho na sehemu moja ya kisima kirefu, lakini jibu la Waziri hapa linazungumzia lambo. Kwa hiyo naomba hiyo irekebishwe kwamba ni miundombinu hiyo niliyoitaja.
Mheshimiwa Spika, sasa naelekea kwenye swali la kwanza, je, ni kiasi gani ambacho kimetengwa kwenye bajeti ya mwaka huu kwa ajili ya miundombinu hiyo ambayo nimeitaja katika Jimbo la Same Magharibi na hususani Kata ya Ruvu?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa millioni 100 zinaweza zikatosha malambo mawili na majosho mawili kama kazi hii itasimamiwa na Wizara, lakini kazi hii kama itasimamiwa na Halmashauri milioni 100 inaweza ikatosha josho moja au lambo moja. Je, Serikali sasa iko tayari kwa sababu yenyewe ndio inatoa hizi fedha isimamie kusudi miundombinu hiyo ikamilike kwa bajeti ya mwaka huu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Spika, kuhusu wa usahihi wa nilichokisema ambapo amesema anarekebisha tutaenda kuangalia kuhusu makubaliano yale, lakini kimsingi hakuna kitu kilichoharibika, tutaenda kutekeleza kadiri tulivyoahidi wakati tulipokwenda Jimboni kwake.
Mheshimiwa Spika, vilevile kuhusiana na ni kiasi gani cha fedha ambacho kimetengwa, nimshauri Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa inakuwa ni vigumu kuwa na takwimu sahihi lakini anaweza akanifuata baadaye nikamweleza na ombi lake la kwamba Wizara yenyewe ndio inasimamia ujenzi ule, vilevile tutalichukua na ukweli wa mambo fedha zinazotolewa mara nyingi na Wizara kwa ajili ya kujenga miundombinu huwa tunahakikisha kwamba tunazisimamia ili ifanye kazi iliyoelekezwa.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza na nitakuwa nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya changamoto zilizojitokeza kwenye msimu wa korosho mwaka wa jana ni pamoja na wizi uliofanyika katika maghala ya YURAP yaliyoko Masasi kwa kushirikisha wamiliki wa ghala lakini pamoja na viongozi wa mkoa walibariki jambo hili; na sasa hivi kuna kesi zinaendelea mahakamani kwa ajili ya kuweza kupata haki ya wakulima wale. Sasa tunataka kufahamu Serikali haioni haja ya kuwalipa wakulima pesa zao, kwa sababu walikuwa wanatoa michango kwenye mfuko wa kuendeleza zao la korosho wakati ninyi mnahangaika na wale wezi wenu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, sasa hivi tunaelekea kwenye msimu wa kilimo na wananchi wanaendelea kutayarisha mashamba yao kwa ajili ya msimu wa korosho ujao. Hata hivyo kumekuwa na sintofahamu kubwa sana kuhusiana na pembejeo baada ya Serikali kutangaza kwamba itapeleka pembejeo za bure. Sasa tunataka kufahamu, ni lini pembejeo zitawafikia kwa asilimia 100 ili waweze kutayarisha mashamba yao, kwa sababu wanategemea zinatolewa na Serikali tena kwa bure? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajibu maswali yake ningependa kusema kwamba zao la korosho ni moja kati ya mazao ambayo yamefanikiwa sana katika miaka ya karibuni. Mwaka huu korosho ndiyo imeongoza kwa kuiingizia nchi yetu fedha za kigeni kati ya mazao yote, imeipiku tumbaku. Vilevile katika msimu huu Serikali imefanikiwa kuwapatia wananchi wa mikoa inayolima korosho shilingi bilioni 800. Kwa hiyo, tunapozungumza korosho tunazungumza mafanikio makubwa sana ya Serikali ya Awamu ya Tano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kuhusu utaratibu wa Stakabadhi Ghalani tunaelekea sasa kwenye mazao mengine hususan Kahawa, lakini vilevile na mazao ya jamii ya mikunde.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maswali yake, ni kweli kwamba kuna mapungufu yametokea ikiwa ni pamoja na mapunjo ya fedha za wakulima. Kama mnavyofahamu, tayari kuna watumishi wa MAMCU wamepelekwa mahakamani na kufunguliwa mashtaka ya kuhujumu uchumi. Vilevile katika fedha ambazo zimepotea tayari Serikali imesha- recover shilingi bilioni 1.5 na hizo zitaenda kwa wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu pembejeo naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tani 9,000 za sulfur tayari zimeishaingia nchini na sulfur hiyo inagaiwa bure na iko njiani kuelekea kwenye mikoa inayolima korosho ili wananchi waweze kugawiwa, nashukuru sana. (Makofi)
MHE. HALIMA ALI MOHAMMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante sana, pamoja na majibu marefu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetangaza Tanzania ya viwanda na bila ya malighafi kutokana na mazao ya kilimo na uvuvi basi hatuna viwanda Tanzania.
Je, ni kwa nini Serikali haijajielekeza katika kilimo cha umwagiliaji maji ambapo Tanzania tuna mito mingi na mabonde mengi ili kuhakikisha basi tunakuwa na malighafi za kutosha kwa kipindi cha mwaka mzima? (Makofi)
La pili, kwa nini sasa Serikali haiwekezi katika mazao ya maua ambayo pia yanategemewa kuingiza income katika nchi yetu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama Mheshimiwa Mbunge alivyosema kuna uhitaji wa kuwekeza zaidi katika kilimo cha umwagiliaji na nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge katika Programu ya Kuendeleza Sekta Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) kilimo cha umwagiliaji ni moja kati ya masuala ambayo yamewekewa mkakati mkubwa. Kwa hiyo, tunaamini huko mbele tunakokwenda kilimo chetu kitabadilika kwa sababu tutawekeza zaidi kwenye umwagiliaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili; sekta ya maua ni moja kati ya sekta za kilimo ambazo Serikali inatilia mkazo. Ukienda Kaskazini mwa Tanzania, Kilimanjaro na Arusha kuna mashamba makubwa sana ya maua, lakini kwa ujumla wake horticulture ni moja kati ya maeneo ambayo vilevile tumeyawekea mkakati. Kwa asilimia kubwa kilimo cha maua kinaiingizia Serikali fedha za kigeni. Lakini ni kweli otential kubwa namna ya kuhamasisha kilimo cha maua.
MHE. JOSHUA S. NASSARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, msingi wa swali langu unajikita kwenye suala la utafiti. Mataifa yote yaliyoendelea duniani ni yale ambayo yamefanya tafiti na kuzitumia tafiti hizi iwe ni kwenye masuala ya kielimu, teknolojia, kilimo au move ya viwanda kama ambavyo tumekuwa tunasema kwa sasa kwenye nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni kwa namna gani basi Serikali inatuhakikishia kwamba tafiti za kilimo zitafanyika na ziweze kutafsiriwa na kufika chini kwa wananchi kwa maana ya kwenda kwenye uhalisia ili hali kwenye bajeti ya Serikali tu ambayo tunamaliza sasa hivi peke yake, kwenye fedha za maendeleo Wizara ya Kilimo haijapata zaidi ya asilimia 30. Sasa ni kwa namna gani tunawahakikishia Watanzania tafiti na tafsiri yake na kufika chini ili ziende kwenye uhalisia kwenye kilimo?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, tafiti ambazo zinafanyika katika vituo vyetu 16 vya utafiti, kawaida huteremka moja kwa moja kwenda kwa wakulima kupitia huduma za ugani. Ndio maana kwa miaka ya karibuni kumekuwepo na maendeleo makubwa sana katika kilimo chetu, Serikali itaendelea kuongeza bajeti ya ugani ili tafiti zile ziweze kuwafikia wakulima na hatimaye kilimo chao kiweze kuwa kizuri zaidi.
MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwa kuwa sekta ya kilimo, uvuvi na ufugaji ni sekta ambayo inapata shida sana kwa wananchi wetu. Ni lini Serikali itaona sasa wakati umefika kuwapa elimu ili wakanufaika na kilimo, mifugo na uvuvi wakaacha kuwa wanakamatwa mara kwa mara hasa wavuvi wanachomewa nyavu zao ni kwasababu hawapati elimu. Lini Serikali itajikita sana kuwasaidia hao wananchi maskini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu swali la Mheshimiwa Nassari, niseme tu kwamba Serikali hufikisha elimu kwa wakulima, wafugaji pamoja na wavuvi kupitia huduma za ugani na nieleze tu kwamba katika uvuvi kawaida tunatumia beach management unit kama njia sahihi ya kuwafikia wavuvi walio wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu mara nyingi hata wavuvi wanaofanya uvuvi haramu sio kwamba hawajui kwamba ni tatizo lakini wanafanya kwa kukusudia. Hata hivyo, Serikali itaendelea kutoa elimu na kusisitiza wananchi wetu wafanye uvuvi ambao unakubalika kisheria.
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa mujibu wa majibu ya Serikali niliyonayo mezani jibu la Mheshimiwa Naibu Waziri halijakamilika bado part ‘B’. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri itabidi nikutane na Mheshimiwa Msuha ili tuone ni kwa nini anafikiri swali langu au swali lake halijajibiwa vizuri. Kwa sababu sisi tulivyoliangalia tumejiridhisha kwamba alichotaka tumekijibu kwa sababu kimsingi aliuliza maswali mawili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza kwa nini Mfilisi bado anashikilia mali za chama hicho na tumejibu kwamba mfilisi hashikilii. Akauliza swali la pili, je, Serikali ina mpango gani wa kulipa deni la wakulima ambalo la shilingi milioni 424, hili nalo tumesema Serikali inaendelea kuangalia utaratibu wa kulipa. Kimsingi Serikali imeji-commit kwamba itaendelea kulipa. Sasa kama anaona bado halijajibiwa, nafikiri hakuna tatizo niko tayari kukutana naye, tujadiliane kwamba kwa nini anahisi bado halijajibiwa.
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Na mimi nikupongeze kwa kurudi salama, tuliku- miss pia.
Mheshimiwa Spika, elimu ya kisasa ya sheria sasa hivi ina-encourage kupunguza misongamano kwenye Magereza, wanapokwenda kwenye Mahakama wahakikishe wanapunguza misongamano na kuwapeleka watu Magerezani bila sababu.
Mheshimiwa Spika, kama swali la msingi ambavyo limeulizwa ukienda kwenye Magereza yetu, kuna msongamano mkubwa sana. Kwa mfano, Gereza la Segerea ambalo nili-happen kulitembelea juzi, capacity yake ni mahabusu 700, lakini sasa hivi lina mahabusu na wafungwa 2,400. Wanalazimika watu kulala upande mmoja mmoja kwa zamu baada ya muda tena inapigwa alarm, halafu wageukie upande mwingine. Huu ni ukiukwaji kabisa wa haki za binadamu. Kuna watoto wengi ambao wako under age wamekaa pale, wengine wanatakiwa waende shuleni. Hii tuna-cripple Taifa la baadae, wala hatuwasaidii wale watoto ambao wako Magerezani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa swali langu; kwa kuwa hii modern law inafundisha kupunguza mahabusu kwa kadri iwezekanavyo wasiende Magerezani; ni kwa nini Serikali imekuwa ikipeleka wanasheria kutetea kesi za Serikali ambao wamekuwa wakilazimisha wale ambao wanaweza wakapata bail waende kukaa mahabusu, kama ambavyo kesi zetu sisi zilikuwa zina bail, lakini Mawakili wa Serikali wakawa wanalazimisha twende kule tukaongeze msongamano?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, mahabusu kuwekwa ndani kwa muda mrefu siyo suala tu la kwamba Serikali haitaki kesi ziishe mapema, lakini kuna sababu nyingi za msingi za baadhi ya watuhumiwa kutoachiwa.
Mheshimiwa Spika, moja, mara nyingine ni kwa sababu ya usalama wao. Kwa mfano, kama ni watu ambao wametenda makosa ambao unahisi kwamba wakienda nje wanaweza wakapata matatizo, mara nyingi Serikali inajaribu kuwalinda. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ya pili, kuna watuhumiwa ambao wakitoka nje wanaweza vilevile kwenda kuharibu ushahidi. Kwa hiyo, Serikali inaangalia hivyo vitu vyote. Siyo suala la kwamba hutaki kesi iishe, lakini yawezekana unapowaachia kurudi, wanaenda kusababisha kesi ichelewe kwa sababu wataharibu ushahidi. Nashukuru sana. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Ni kweli kabisa kwamba msongamano kwenye Magereza yetu Tanzania, Tarime na hata Segerea nilipoenda ni mkubwa sana.
Mheshimiwa Spika, swali langu la nyongeza ambalo nauliza hapa, Mheshimiwa Waziri wakati anatoa takwimu za gharama kwa wafungwa, amesema ni shilingi 1,200 kwa chakula. Nilipokuwa Segerea kwenye swali langu ninaloenda kuuliza, kule kuna wamama wamefungwa wanadaiwa shilingi 150,000 mathalani, lakini amefungwa miezi sita. Kwa gharama ambazo amezitoa Mheshimiwa Naibu Waziri unakuta zinavuka pale tena mpaka shilingi 270,000. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna mama ambaye amefungwa miezi sita, anaumwa ugonjwa wa fibroid ana-over breed, kila siku jioni ambulance inampeleka Amana.
Je, ni kwa nini Serikali isitumie busara ya zaidi kwa hawa akina mama ambao wengine wana watoto wachanga ambao unakuta wanafungwa kwa kesi za shilingi 100,000 au 200,000 wasiweze kuzi-waive uki-compare na gharama ambazo wanaenda kuhudumia kwenye ile jamii? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, suala la kwamba fedha ambayo wanadaiwa ni kidogo, ni suala la kisheria. Kwa hiyo, kama Mheshimiwa Mbunge anafikiri sheria ile imepitwa na wakati na haitendi haki, ni rahisi yeye kuleta hoja Bunge hili libadilishe sheria kwa sababu sheria ndiyo zinasema hivyo. (Makofi)

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nipongeze kwa majibu mazuri yaliyotolewa. Nataka tu kumuomba Mheshimiwa Mwalongo kwa ile hoja ya jambo mahususi alilolileta kwamba baada ya Bunge, basi tuonane ili nilipate vizuri kwa sababu jambo lake alilolileta lile ni mahususi ili tuweze kulifanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ambazo tumezipata, niweke tu kumbukumbu sawa, siyo kila Magereza yana msongamano. Tuna baadhi ya Magereza ambako katika mikoa ile kiwango cha uhalifu ni kidogo, hata msongamano Magerezani ni mdogo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilienda Mkoa wa Lindi, Gereza lilikuwa na uwezo mkubwa kuliko kiwango cha wahalifu. Hivyo hivyo, nilienda kwa Mheshimiwa Shangazi kule, kiwango cha Gereza la kule ni kikubwa kuliko wahalifu walioko mle.
Kwa hiyo, nitoe rai kwa Watanzania na jamii nzima ya Watanzania kuepuka kufanya uhalifu kwa kweli, kwa sababu sisi kama Serikali hatupendi watu kuwa magerezani, lakini tunawapeleka kwa sababu ya uhalifu wanaoufanya.
Mheshimiwa Spika, hatuwezi tukaacha wahalifu wakawa nje na kama watu watafanya uhalifu, ni kwamba wataenda magerezani. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwanza ninachoweza kusema Mheshimiwa Waziri katika mgawanyo takwimu wamekuongopea, Halmashauri yangu imepata walimu ambao hawafiki hata 60; ni 58 tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalotaka kusema, hao wanane Bunda sisi hawatutoshi. Hisabati mahitaji ni 55 waliopo 20 peke yake, fizikia mahitaji 27 waliopo 10 peke yake, biology mahitaji 32 waliopo 15 chemistry kidogo
ndio mmejitahidi mahitaji 29 waliopo 21 bado wanane. Ukiangalia yaani hao tuliogawanywa na mahitaji kwa ujumla wake ni 68. Ni lini Serikali mtatupa Bunda walimu wa sayansi? Tumechoka Bunda kuwa miongoni mwa Wilaya zinazofanya vibaya katika masomo, swali la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, tunajia TEA ina- deal na masuala ya infrastructure. Hivi kwa nini Serikali msitenge fedha za kutosha, mkawapa TEA wakajenga pia na nyumba za walimu mbali na kwamba kuna changamoto kwenye shule za walimu ili pia walimu wawepo shuleni kuepuka usumbufu ambao unajitokeza na kusababisha watoto kufeli halafu hatimaye tunalaumiana mnaanza kuwafukuza wao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu upungufu wa walimu uliopo katika shule za Jimbo lake; ni kweli kwamba kuna upungufu wa walimu wa sayansi nchi nzima na ndiyo maana katika jibu langu la msingi nimeeleza mikakati iliyopo ya kuhakikisha kwamba, tunaondokana na upungufu huo.
Kwa hiyo, naomba nimhakikishie tu kwamba tunafahamu kwamba kuna upungufu na si kwake tu. Kwa hiyo tutaendelea kuhakikisha kwamba, upungufu huo unafanyiwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kujiingiza zaidi katika kujenga shule za walimu, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kutegemeana na bajeti ambayo TEA wanatengewa ambayo kimsingi kwa miaka mitatu sasa mfululizo wanatengewa shilingi bilioni 10, itaendelea kujenga nyumba za walimu, lakini ikumbukwe kwamba jukumu hasa la TEA ni suala la kuongeza ubora, lakini vilevile kuhakikisha kwamba kuna upatikanaji wa elimu na suala la usawa yaani access, equity na quality.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, TEA haikuundwa ili ichukue majukumu yote ya miundombinu za shule katika Halmashauri zetu. Jukumu la kujenga miundombinu katika shule ambazo ziko chini ya Serikali za Mitaa litabakia kuwa jukumu la Serikali za Mitaa.
Kwa hiyo, nimuombe Mbunge pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote kwa sababu sisi wenyewe ni Madiwani tuendelee kuwahamasisha wananchi washirikiane na Serikali kujenga miundombinu kwa ajili ya shule za msingi na shule za sekondari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini TEA vilevile na hasa nyie Waheshimiwa Wabunge mkiwaongezea bajeti kwa sababu nyie ndiyo hasa mnaongeza bajeti itaendelea kufanya hayo kuhakikisha kwamba kunakuwa na usawa, ubora lakini yale maeneo ambayo yatakuwa na upungufu yaweze kupatiwa kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nieleze utaratibu kwamba ukiacha mbali la Halmashauri yenyewe kuomba TEA waweze kupatiwa fedha kwa ajili ya ujenzi lakini vilevile Wizara kwa kushirikia na Ofisi ya Rais, TAMISEMI tunakusanya takwimu, kwa hiyo, tunajenga miundombinu kulingana na takwimu ambazo tumepata za nchi nzima. Nashukuru sana. (Makofi)
MHE. MUNIRA MUSTAPHA KHATIBU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Elimu ya Watu Wazima imekuwa ni elimu dhaifu ndani ya mikoa yetu, ndani ya mikoa yetu iko chini yaani mikoa mingine hata haitambuliki kama kuna Elimu ya Watu Wazima. Je, Serikali ina mpango gani wa kusaidia na kuboresha elimu hii ya watu wazima ili waweze kukabiliana na majukumu yao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri amesema Serikali ina mpango wa kuimarisha Vyuo vya Maendeleo (FDCs). Je, ni lini sasa Serikali itaimarisha Vyuo hivi vya Maendeleo ya Wananchi ili vijana waweze kupata elimu katika vyuo hivi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake kwamba Elimu ya Watu Wazima imedhoofika katika baadhi ya maeneo, ni suala la mtizamo lakini kama tulivyosema rekodi tulizonazo ni kwamba karibia katika mikoa yote kuna vituo kwa ajili ya kutoa Elimu ya Watu Wazima. Mheshimiwa Mbunge labda kama atakutana na mimi ataniletea orodha ya mikoa ambayo anafikiri haifanyi kazi lakini nimhakikishie kwamba Elimu ya Watu Wazima bado ipo pale. Ni ukweli vilevile kwamba kadri tunavyozidi kuimarisha na kuboresha elimu ya mfumo rasmi mahitaji ya Elimu ya Watu Wazima kwa baadhi ya watu yanaanza kuonekana kwamba yamepungua lakini ukweli wa mambo ni kwamba bado kuna watu wengi ambao wanajifunza na kupata elimu kwa kupitia Elimu ya Watu Wazima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile swali lake kuhusiana na namna Serikali inavyoboresha Vituo vya Maendeleo vya Wananchi (FDCs), nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa Serikali inatekeleza Mpango unaoitwa ESPJ ambao pamoja na mambo mengine utajenga na kukarabati miundombinu ya Vyuo vya Wananchi 55 na baadae tutahakikisha watakuwa na rasilimali watu wa kutosha. Lengo ni kuhakikisha kwamba tunaendelea kupata fursa ili vijana wengi waweze kujifunza stadi za kazi na ufundi na hasa kwa sasa hivi ambapo tunakazania kuhakikisha kwamba tunaingia kwenye uchumi wa kati ambapo rasilimali watu wa aina hiyo inahitajika.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali ndogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Tano ni Serikali sikivu sana kwa wananchi wake hali iliyopelekea mpaka imewarudisha kazini watumishi wa darasa la saba. Swali langu, je, ni lini sasa Serikali itatoa tamko la kuwarudisha masomoni wasichana wote waliopata ujauzito na kuthibitishwa na Mahakama kuwa walibakwa kwani kwa kutowarudisha ni kuwanyima haki yao ya kupata elimu lakini vilevile ni kuwapotezea ndoto zao? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba hata sisi Serikali kwa kweli hatupendi na hatutaki kusikia vitendo vya uonevu dhidi watoto wa kike, kwa sasa mfumo wetu wa elimu umepangwa katika namna ya kuhakikisha kwamba wanafunzi ambao wanapata ujauzito wanapata fursa ya kusoma lakini nje ya mfumo rasmi.
Kwa hiyo, kuna fursa nyingine nyingi za kusoma kama nilivyosema katika swali langu la msingi kwa kupitia Elimu ya Watu Wazima na Vyuo vya Ufundi. Serikali haitarajii na naomba niweke wazi kuwarudisha wanafunzi ambao wamepata ujauzito kwa njia yoyote ile. Ni kwa sababu tukifanya hivyo maana yake tunahalalisha na kuhamasisha ngono shuleni wakati mila na sheria zetu haziruhusu ngono katika ngazi hizo maana yake shule za msingi na shule za sekondari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na kubakwa, tunaposema kwamba hawaruhusiwi kuendelea na elimu katika mfumo rasmi siyo kwamba ni adhabu kwa kujifungua, tunachochukulia ni kwamba tayari ana mtoto na hivyo tukifanya hivyo tunakuwa tumefungulia milango ya vitendo kama hivyo kuendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kuna fursa zingine ambazo watoto wale wanaweza kutumia kupata elimu, zipo.
MHE. MACHANO OTHMAN SAID: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Wizara naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika majibu ya msingi Mheshimiwa Waziri amesema kwamba kumekuwa na Makaimu kwa sababu bado kuna muundo mpya unatengenezwa, lakini Ofisi ya Mambo ya Nje Zanzibar inakaimu karibu miaka miwili na ukiacha kukaimu, pia wana uhaba wa staff na samani za Ofisi katika Ofisi ya Zanzibar.
Je, ni lini Wizara hii itashughulikia Ofisi ya Zanzibar ili iwe sawa na sehemu nyingine za Muungano?
La pili, miongoni mwa Kurugenzi zisizopungua 12 za Makao Makuu ya Wizara hii zote haziongozwi na Mzanzibar hata mmoja na kwa sababu Wizara hii ni kioo cha Muungano, Mheshimiwa Waziri anatuahidi nini katika muundo mpya kwamba Kurugenzi nyingine zitapata wafanyakazi kutoka upande wa pili wa Muungano?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Machano kwa namna anavyowakilisha maslahi ya Zanzibar katika Bunge la Jamhuri ya Muungano. Siyo mara ya kwanza kumsikia akifanya kazi hii kwa weledi mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile niseme tu kwamba ni kweli kuna changamoto alizozitaja kwenye Ofisi ya Zanzibar nimwahidi tu kwamba Serikali imejipanga kuhakikisha changamoto hizo zinafanyiwa kazi haraka iwezekanavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la Wakurugenzi waliopo idadi yao Wazanzibar kuwa ni wachache, nimhakikishie tu kwamba Wizara ina Idara 14; siyo 12 kama yeye alivyosema. Nimhakikishie tu kwamba katika uteuzi utakaofanyika, bado Serikali itaendelea kuhakikisha kwamba kigezo kukubwa inakuwa ni weledi, lakini kuangalia kwamba pande zote za Muungano zinawakilishwa vilivyo katika Wizara. Nashukuru sana. (Makofi)
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, diaspora kwa umoja wao wamekuwa wakipigania kurudi nyumbani kufanya kazi. Tangu Awamu ya Tano ianze ni diaspora wangapi wameajiriwa katika sekta ya umma ili kutumia ujuzi wao katika kuisaidia Serikali?
Swali langu namba mbili, ni jinsi gani Serikali inawapa fursa diaspora katika uchumi wa viwanda? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA (K.N.Y WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI): Mheshimiwa Spika, kama nilivyosikia swali ni kama moja hasa kwamba ni namna gani Serikali imejipanga kutoa fursa kwa ajili ya diaspora wetu.
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikifanya makongamano ya mara kwa mara na diaspora ili kuweza kuwaonesha fursa zilizopo waweze kuwekeza nchini kwa sababu tunatambua potential kubwa iliyopo kwa diaspora kama ilivyo katika nchi nyingine.
Mheshimiwa Spika, vilevile kwa kutambua umuhimu na potential ya diaspora wetu Serikali sasa iko mbioni kuja na sera mahsusi ya diaspora ili kuweza kuweka mazingira mazuri ya namna ambayo wanaweza kushiriki katika kuchangia maendeleo ya nchi yetu.
Kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, tayari kuna mipango inaendelea na diaspora tayari wameshaanza kuwekeza katika maeneo mbalimbali. (Makofi)
MHE. DKT IMMACULATA S SEMESI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi, nina maswali mawili ya ziada.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa inafahamika kwamba vyuo vikuu ni chachu ya maendeleo kwa sababu wanazalisha hawa wataalam na wanavumbua au wanaleta suluhisho katika shughuli mbalimbali. Swali lilivyojibiwa kwa upande MTUSATE linaonesha kwamba MTUSATE wameshafadhili miradi 102, kati ya hiyo miradi 44 kutoka vyuo vikuu na shilingi bilioni 4.6 ndio zilizotumika. Hata hivyo, kwa bahati mbaya haiku-indicate ni muda gani. Je kipindi cha miaka 10, 20 au 30 kwa kuzingatia umuhimu wa sekta ya hizi ya elimu ya vyuo Vikuu na issue za tafiti?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, ni kuhusu utengaji wa fedha na upatikanaji wa fedha ambazo zinaelekezwa COSTECH. Mwaka wa fedha 2017/2018 zilitengwa bilioni 13.6, kati ya hizo bilioni bilioni tatu ni fedha za nje. Mwaka huu unaokuja wa fedha zimetengwa bilioni 9.5 kutoka kwenye mfuko wa ndani. Viwango hivi vya fedha ni vidogo sana lakini ningependa kujua kati ya hizi fedha zinazotengwa zinazowafikia COSTECH ni kiasi gani ili ziweze kushuka kwenye hivi vyuo vikuu husika kwa ajili ya tafiti? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha ambazo nimezungumzia kwamba tayari zimeshatolewa kwa ajili ya vyuo vikuu kwa ajili ya utafiti ni fedha ambazo zimetengwa kuanzia mwaka 2015/2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili, kwamba ni kiasi gani ambacho kimeshatolea COSTECH ni suala la takwimu, naahaidi nitakapotoka hapa nitampatia takwimu sahihi Mheshimiwa Dkt. Sware.
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, lakini pia niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano ya Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwajali Walimu na kuhakikisha kwamba inalipa malimbikizo yao, lakini nina maswali mawili ya nyongeza; kwanza sababu zilizotolewa na Serikali ya kukiondoa chuo hiki kuwa sekondari kwa sasa si sababu muhimu sana, kwa hiyo bado tunasisitiza Mheshimiwa Waziri kwamba. Je, hawaoni kwa kukiondoa Chuo kile cha Ualimu cha Ndwika kumefanya Kanda ya Kusini kuwa na vyuo vichache vya ualimu hivyo bado umuhimu wa chuo kile kurudi Serikali iutazame upya?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, pamoja na kulipa malimbikizo ya Walimu lakini je, nini mikakati ya Serikali kuhakikisha sasa malimbikizo haya ya Walimu hayarudii kama ilivyokuwa mwanzo?
NAIBU WAZIRI ELIMU SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ukanda wa Kusini, au niseme mkoa anaotoka Mheshimiwa Mbunge tayari una vyuo vingine vitatu vya ualimu. Mkoa wa Mtwara una Chuo cha Ualimu cha Kitangali kilichopo Newala, lakini vile vile kuna Chuo cha Ualimu cha Mtwara Ufundi pamoja na Mtwara Kawaida. Hata hivyo, ifahamike kwamba vyuo hivi vyote ni vyuo vya kitaifa na udahili wake unawachukua wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ukweli huu kama Mheshimiwa Mbunge bado anafikiri kuna haja ya kurudisha shule hiyo ya sekondari kuwa chuo, nimshauri tu wajipange wakae katika halmashauri yao, walete mapendekezo wizarani na kwa vyovyote vile si msahafu, kama kuna haja za msingi bado Serikali inaweza kufikiria kurudi huko tulipotoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la pili, ni kweli kwamba kwa sasa Serikali imejipanga kuhakikisha kwamba hakuna tena madeni ya Walimu ambayo yatajilimbikiza. Hatua mbalimbali tayari zimeshachukuliwa ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku sasa, kwa mfano kuhamisha Walimu kwa utaratibu wa kawaida bila kuwalipa stahiki zao. Vile vile kuhakikisha kwamba kila mwajiri anatenga fedha kwa ajili ya likizo za Walimu, lakini pia pale wanapostaafu kuhakikisha kwamba fedha za kusafiri zinakuwa zinatolewa. Kwa hiyo tunachofanya sasa ni kuhakikisha kwamba hakuna kulimbikiza tena madeni ya Walimu na inawezekana tu kufanya hivyo kama stahiki zao zote zitalipwa kwa wakati muafaka.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali lanyongeza kutokana na swali namba 101 la Mheshimiwa bwana Jerome Bwanausi. Kwa muda mrefu pia Serikali imekuwa ikiwakopa wazabuni na kusababisha madeni makubwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo Chuo cha Wauguzi Masasi, Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Masasi, Ndanda High School pamoja na Chidia Sekondari yanayotisha wazabuni hawa kufilisika lakini pia…
…wanataka kusitisha kutoa huduma zao; sasa swali langu, ni lini Serikali kwa makusudi kabisa itaamua kuwalipa wazabuni wa ndani hasa wa vyakula katika hizi shule zetu za mabweni?
NAIBU WAZIRI ELIMU SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba swali la Mheshimiwa Cecil Mwambe halina uhusiano wowote na swali la msingi, lakini nipende tu kusema kwamba kwa sasa Serikali imejidhatiti vilevile kuhakikisha kwamba inalipa madeni yote ikiwa ni pamoja na madeni ya wazabuni. Hata hivyo, ifahamike kwamba madeni yote yatalipwa tu baada ya uhakiki kufanyika, kwa sababu huko nyuma kuna madeni mengi yamelipwa lakini hayakustahili kulipwa.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, nnakushukuru na nashukuru kwa majibu ya Serikali. Kabla sijauliza maswali mawili ya nyongeza naomba tu jina la muuliza swali lisomeke kama Pascal Yohana Haonga siyo Pascal Yohana Hasunga. Baada ya masahihisho hayo kidogo naomba niulize maswali yangu mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, mara nyingi Serikali imekuwa ikizungumzia na kutoa matamko kuhusu ada zinazopangwa na shule za binafsi ikionesha kana kwamba Serikali ina mpango wa kuweka kiwango fulani cha ada bila kuzingatia gharama ambazo shule hizi zinaingia katika kusomesha wale watoto na kuendesha shule zao. Je, kwa nini Serikali isiwaachie wamiliki wakapanga hizi ada wenyewe ili wazazi ambao wanaweza wakamudu ada hizo waenda kwenye shule bila kikwazo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, mara nyingi shule zinapanga taratibu zao za namna ya kuwafanya hawa watoto waweze kufaulu, kwa mfano, kuwawekea mitihani kutoka kwenye daraja fulani kwenda kwenye daraja fulani, lakini Serikali pia inaonesha haifurahishwi na jambo hili. Je, kwa nini Serikali isiache hizi shule zikapanga utaratibu wa kuwafanya hawa watoto waweze kufaulu kulingana na sera na taratibu za shule zenyewe? (Makofi). Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la Serikali kutoingilia maamuzi ya shule za binafsi katika kuamua ada. Naomba nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa Serikali inaendelea na majadiliano na sekta binafsi ya namna bora ya kuratibu suala hilo badala ya Serikali yenyewe kutoa maelekezo ya gharama ambazo zinatakiwa zilipwe.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu shule za binafsi zinaendeshwa na watu binafsi, lakini vilevile kwa sababu ni biashara na ni biashara ambayo maana yake mtu anayetaka kwenda kununua au kupata hiyo huduma yeye ndiyo aangalie uwezo wake, tunafikiri bado kuna busara ya kuendelea kujadiliana nao namna bora ya kuhakikisha kwamba kunakuwa na gharama ambazo zinahimilika badala ya Serikali yenyewe kuanza kutoa bei au gharama elekezi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili kwamba Serikali isiingilie taratibu za shule binafsi za kuweka viwango vya ufaulu. Wakati tunatambua kwamba ni kweli ni vizuri sekta binafsi katika uendeshaji wa shule ikaachiwa nafasi ya kuamua wenyewe namna wanavyodhibiti ubora. Ni kweli kwamba udhibiti wa ubora ni suala la kisera na kisheria, kwa hiyo, haiwezekani Serikali ikakaa moja kwa moja ikaruhusu kila mtu ajiamulie namna anavyodhibiti ubora katika shule yake.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa sasa ilichoamua ni kwamba tutaendelea kushirikiana na Umoja wa Wamiliki wa Shule Binafsi ili kuangalia namna ya kuboresha sheria na taratibu zilizopo ili ziwawezeshe kupata ubora ule, lakini bila kuvunja sheria za elimu kwa sababu hata kama shule ni za binafsi, lakini ni nchi moja, Serikali ni ile ile, sheria ni zilezile, hatuwezi tukaruhusu kila mtu akajiamulia anavyotaka kwa sababu siyo kila mwenye shule binafsi amekuwa akitumia uhuru huo vizuri.
Mheshimiwa Spika, kuna baadhi ya wanafunzi wamefukuzwa shule kinyume na sheria, kuna wengine wanakaririshwa kwa kuonewa, kuna wanafunzi unakuta wa Form Four wanafukuzwa shule tu kwa sababu hajafikia kiwango fulani. Tunachosema ni kwamba tutaendelea kuwaruhusu kuboresha hayo mazingira, lakini sheria na taratibu lazima tuzifuate na ndiyo maana tunaendelea kufanya nao mjadala kwa pamoja.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwa kuwa mwaka 1975 Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kushirikiana na Shirika la SIDA alianzisha vyuo vya FDC kwa nia ya kutoa ujuzi kwa akina mama wajasiriamali na vijana ili waweze kuongezewa ujuzi na hivyo kuweza kujiajiri; na kwa kuwa Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Nkenge imeandaa mpango mkubwa wa kutoa ujuzi kwa wajasiriamali akinamama na vijana, je, Wizara iko tayari kushirikiana na Ofisi ya Mbunge wa Nkenge katika kutekeleza mpango huo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri alitembelea Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Gera na akakuta zaidi ya shilingi milioni 100 zilizotolewa kwa ajili ya kukarabati zilifanya kazi ndivyo sivyo; na kwa kuwa alitoa maelekezo palepale wale waliofanya kazi chini ya viwango warejee tena kwa gharama yao, je, maelekezo ya Mheshimiwa Waziri yametekelezwa au imebaki kama ilivyokuwa kabla ya kutoa maelekezo yake? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kama tuko tayari kushirikiana na Ofisi ya Mbunge, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tuko tayari kushirikiana naye kwa sababu lengo letu ni moja, tunataka vile vyuo viweze kufanya kazi ili tuendelee kupata nguvukazi ya ufundi na stadi mbalimbali katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ni kuhusu maelekezo yaliyotolewa juu ya ukarabati uliofanyika ambao haujakwenda vizuri. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba maelekezo na uamuzi wa Wizara uko palepale, tutaendelea kufuatilia kuhakikisha kwamba maelekezo yale yanatekelezwa.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona na naomba niulize swali dogo la nyongeza kuhusiana na mada hii iliyoko mezani.Kwa kuwa Wilaya ya Longido haina chuo hata kimoja, chuo chochote cha Serikali; na kwa kuwa Wilaya hii ya Longido ni ya wafugaji kwa karibu asilimia 100 na ni wilaya ya uhifadhi wa wanyamapori kwa sababu tuna maeneo ya WMA na ya uwindaji, je, Serikali haiwezi kuja kutujengea VETA hasa inayolenga tasnia ya ufugaji mifugo na uhifadhi wa wanyama na mazingira na ikiwezekana Chuo cha Walimu wa Sayansi kwa sababu kuna uhaba mkubwa wa Walimu wa sayansi nchini na tuna ardhi ya kutosha na maji ya Kilimanjaro yanakuja?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba mikoa na wilaya zote nchini zinakuwa na vyuo vya VETA. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tumeanza kwenye baadhi ya maeneo ambako tayari kuna ujenzi unaendelea na kuna mipango ya kuhakikisha kwamba wilaya zote zinakuwa na vyuo vya VETA. Kwa hiyo, hata Longido tutafika na wakati tunafanya hivyo, tutaangalia zile fani ambazo zitawasaidia wananchi wa pale kuweza kujiendeleza.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya maswali mawili ya nyongeza. Kwanza, napenda kuiuliza Serikali, je, imepangaje kusaidia vyuo vikuu vijiendeshe kwa mujibu wa sheria za nchi lakini bila kuathiri uhuru wa utoaji wa taaluma?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ubora wa elimu inayotolewa na vyuo vikuu vyetu imekuwa ni ya kutia mashaka na inashindwa kuwaandaa vijana kujiajiri lakini pia kushindana kimataifa. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuboresha mitaala ya elimu ya vyuo vikuu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaheshimu uhuru wa vyuo vikuu (academic freedom) na mara nyingi sana Serikali haitaingilia namna vyuo vikuu vinavyoendeshwa. Hata hivyo, uhuru huo lazima ufanyiwe kazi ndani ya sheria. Kwa hiyo, vyuo vyote vinatakiwa viwe na uhuru lakini uhuru wake uko kwenye mipaka ambayo imewekwa na sheria, kanuni na taratibu. Ndiyo maana chuo kikuu chochote, kiwe cha Serikali au binafsi ambacho hakifuati sheria, kanuni, taratibu na miongozo hatutasita kukichukulia hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili kwamba ni namna gani tunajaribu kuboresha quality ya elimu katika vyuo vikuu vyetu, jibu lake linafanana na hilo ambalo nimeshatoa kwamba Tume ya Vyuo Vikuu ambayo ndiyo hasa imepewa kazi ya kuhakikisha kwamba inadhibiti ubora wa elimu katika vyuo vyetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia itaendelea kuhakikisha kwamba taratibu zile zinafuatwa na ndiyo maana tunafanya tathmini ya kila mara na vyuo vikuu vile ambavyo havitakuwa vimefuata taratibu zile vitafungiwa. Ndiyo maana kwa mwaka huu vyuo 19 vimefungiwa na programu 75 za vyuo 22 zimesitishwa. Tunachosema tu ni kwamba ili tuweze kuwa na ubora unaotakiwa, tutaendelea kuchukua hatua ili elimu yetu iendelee kuwa bora.
MHE. EDWIN M. SANNDA: Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza; kama alivyoeleza Naibu Waziri mpaka sekondari elimu bure, lakini pia ukienda Chuo Kikuu kwa elimu ya juu tunayo mikopo ya wanafunzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kundi lililobaki ni kidato cha tano na cha sita. Kwa kuwa changamoto ya uwezo wa kugharamia elimu iko pia kwa wananchi hasa ambao nao wanakwenda kidato cha tano na cha sita ambapo imepelekea baadhi yetu nikiwemo mimi kuweka mpango mahsusi kwenye Majimbo yetu ya kuwalipia wanafunzi wanaofaulu kwenda kidato cha tano na cha sita; pamoja na changamoto ya uwezo wa Serikali; je, Serikali sasa haioni umuhimu wa kulijumuisha kundi hili la kidato cha tano na cha sita kwenye Mpango wa Elimu Bure? Hilo ni swali la kwanza. (Makofi)
Swali la pili. Ili mpango wowote ufanikiwe, ni lazima kuwe na lengo na dhamira ya dhati ya kuhakikisha jambo hili linafanikiwa na kuwekewa mikakati. Kama tunavyozungumzia kwenye upande wa maji, tunasema mpaka 2020/2021 tuwe tumefikia asilimia 85 ya Watanzania wawe wanapata maji safi na salama; je, Serikali haioni umuhimu sasa kuweka muda mahususi kwa maana ya time frame na malengo lini tutaanza kutoa elimu bure kwa kidato cha tano na cha sita kama ilivyo kwenye maeneo mengine? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaingia kwenye maswali, naomba nikiri kwamba Mheshimiwa Sannda ni mmoja kati ya Wabunge wanaofuatilia sana masuala ya elimu. Pale Wizarani amezoeleka sana kiasi kwamba haulizwi tena kwamba anataka kuonana na nani? Kila siku utamkuta yupo mlangoni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kama Serikali ina nia ya kuhakikisha kwamba hata kidato cha tano na sita nao wanapata mpango ule wa elimu bure, kwa sasa Serikali imeweka nguvu nyingi katika kukabiliana na changamoto ambazo zimejitokeza baada ya elimu bila malipo kuanza kutekelezwa, lakini baadae kadri fedha na uwezo utakapoimarika tutafikiria hata kwa elimu ya kidato cha tano na sita.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwamba kwa nini angalau tusiweke basi mpango wa muda mrefu; nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba pamoja na kwamba haionekani kwenye mipango yetu kuhusu muda, lakini nia yetu kama Serikali ni kuhakikisha kwamba kadri uwezo unavyoongezeka kuendelea kutoa changamoto zinazowakabili wananchi kwenye Sekta ya Elimu na ikiwezekana huko mbele kadri uchumi wetu utakapoimarika kama nchi, hakuna shida hata mpaka Chuo Kikuu inaweza ikawa elimu bure kama ilivyo kwenye baadhi ya mataifa ya Ulaya.
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri. Naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa Chuo cha VETA kiko mbali sana na Wilaya ya Lushoto na hii imesababisha vijana wengi wa Lushoto kukosa fursa ya kujiajiri na kuajiriwa, je, Serikali haioni kwamba imefikia wakati sasa kuchukua hatua za haraka ili kuwajengea chuo hicho vijana wa Lushoto waweze kupata elimu hiyo ya ufundi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali pili, kwa kuwa kuna majengo ya TBA na majengo yale yana karakana ya Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto. Je, Serikali haioni sasa kuwa kuna haja ya kurudisha majengo hayo katika Wizara ya Elimu kwa nia ya kufungua Chuo cha VETA katika majengo hayo ili vijana wa Lushoto waliokosa elimu hiyo ya ufundi kwa muda mrefu waweze kuipata sasa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Shaabani Omari Shekilindi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kuhusu ni lini Serikali itajenga Chuo cha Ufundi Stadi Lushoto, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kama nilivyoeleza kwenye jibu la msingi, Serikali itaendelea kujenga Vyuo vya Ufundi Stadi katika wilaya na mikoa yote kadri fedha zitakavyopatikana. Kwa hiyo, kwa sasa nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba fedha zikipatikana Serikali itajenga Chuo cha Ufundi Lushoto kama itakavyofanya katika maeneo mengine.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu majengo ya TBA kama ni wakati sasa wa kurudishwa Wizara ya Elimu ili yaweze kutumiwa kama Chuo cha VETA, naomba nimshauri Mheshimiwa Mbunge kwamba hili linawezekana lakini wao waanzishe mchakato katika ngazi yao ya halmashauri, wawasiliane na TBA. Wakishapata yale majengo kwa maana ya wakiruhusiwa, sisi Wizara ya Elimu tuko tayari kuja kuyakagua na kuangalia kama yanafaa kuwa VETA na hatimaye tukiona yanafaa hatuna kipingamizi, tutahakikisha kwamba majengo yale yanageuzwa kuwa VETA.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Waziri kwa kujibu maswali vizuri lakini pia nina swali moja la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania wengi hawana uelewa wa kulipa kodi, wanapoenda dukani kununua bidhaa wanalipa gharama ya zile bidhaa lakini pia wanalipa na Value Added Tax (VAT) asilimia 18 na wauzaji wakati mwingine hawawapi risiti na mwisho wa siku kodi hii ambayo wananchi wanalipa inapotoea. Je, ni lini sasa Wizara ya Elimu itaiagiza Taasisi ya Elimu (TET) kwa kushirikiana na TRA ili waanze kufanya kazi ya kuboresha mitaala hii ili Serikali isipoteze kodi kupitia wananchi kutokuwa na uelewa lakini pia na wauzaji wa hizi bidhaa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hongoli, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kutoa elimu kwa mlipa kodi, TRA kwa sasa wanaendesha zoezi hilo nchi nzima. Kwenye shule zetu nyingi wameanzisha club za kodi ambazo pamoja na mambo mengine wanafunzi wanaelezwa kuhusu umuhimu wa kulipa kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu ili kufanya sasa kodi iwe ni kitu ambacho kinafahamika zaidi, Wizara yangu iko tayari kushirikiana na TRA kuboresha mitaala iliyopo ili kuendelea kuwajengea vijana wetu ufahamu na umuhimu wa kuwa wazalendo ikiwa ni pamoja na kulipa kodi. (Makofi)
MHE. ESTHER A. MAHAWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina na maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa bajeti ya Wizara ya Elimu inapopangwa inahusisha wanafunzi wote wanaotakiwa kuanza elimu yao ya msingi na sekondari na kwa kuwa wazazi wa hawa wanafunzi wanakuwa tayari wamechangia bajeti kuu ili kuweza kusomesha wanafunzi hawa kwa kupitia elimu bure. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka kuendelea kuondoa kodi na tozo ambazo sio lazima kwa wazazi hawa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa moja ya malengo ya fedha za mitihani ni pamoja na kutafsiri mitihani kazi ambayo kimsingi ni jukumu la Baraza la Mitihani na siyo kwamba wazazi hawa wanaosomesha watoto katika shule ambazo sio za Serikali ni matajiri. Je, Serikali haioni kwamba kwa kuondoa tozo hizo watapata nafasi ya wanafunzi wengine wengi kusajiliwa katika shule hizo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Esther Mahawe, kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi kuboresha mazingira ya wao kuwekeza katika elimu. Tutaendelea kuboresha mazingira yaliyopo ili waweze kuwekeza kwa urahisi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba niseme kwamba sekta binafasi wamekuwa walipaji wazuri wa kodi na wanatambua umuhimu wa kodi katika maendeleo ya Taifa. Kwa hiyo, pamoja na kwamba tupo tayari kujadiliana nao kuhusiana na namna ya kuweza kupunguza hizo kodi lakini bado tutaendelea kusisitiza kwamba ni vizuri wote tukashirikiana ili kuhakikisha kwamba baadhi ya gharama ambazo ni muhimu ziweze kulipwa na wale ambao wanaweza kuchangia. (Makofi)
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya Elimu ya 2014 ya Elimu Bila Malipo inaonekana kuwa ni sera ya ubaguzi ambayo inawabagua watoto wanaosoma kwenye shule binafsi. Mbali tu ya kuwalipisha ada za mitihani lakini sasa Serikali imekwenda mbali kwamba wanaosoma shule binafsi hawawezi hata kupata mikopo ya elimu ya juu. Hivi ni kigezo gani Serikali imekitumia cha kujiaminisha kwamba watoto wanaosoma shule binafsi ni watoto wa matajiri? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwaa Mtolea, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kwamba Sera ya Elimu Bure ni ya kibaguzi, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba sio ya kibaguzi bali elimu bure tunazungumzia katika sekta ya umma. Kwa hiyo, lazima tutofautishe sekta ya umma na sekta binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuhusiana na watoto ambao wamesoma shule binafsi kutoruhusiwa kupata mikopo ni suala tu la kuangalia kwamba kati ya mtu ambaye anaweza kulipa milioni mitatu au milioni nne kwenda shule ya msingi na sekondari na yule ambaye hawezi, ni yupi utamuangalia wakati wa kutoa mkopo? Ni suala la kuangalia nani mwenye mahitaji zaidi siyo suala la kibaguzi. Bajeti iliyopo ni kidogo na wahitaji ni wengi lazima tuchague na tunatoa zaidi kwa wale ambao wanahitaji zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwa wanafunzi wale ambao wamepata bahati ya kusomeshwa labda na wafadhili, Serikali haiwanyimi mikopo, tunachotaka ni ushahidi kwamba kweli wamefadhiliwa. Tutahitaji barua kutoka kwa mfadhili kuonyesha kwamba mwanafunzi amefadhiliwa. Kwa hiyo, sio ubaguzi ni suala tu la ni namna gani tunafanya kazi ili huduma hiyo ya elimu iweze kutolewa kwa wote kwa usawa. (Makofi)
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kuuliza maswali ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Mji wa Nanyamba ina umri wa zaidi ya miaka mitatu tangu kuanzishwa kwake, je, mchakato wa kuanzisha ofisi mpya ya udhibiti ubora inachukua muda gani ikiwemo ni pamoja na kupata vitendea kazi pamoja na watumishi wa kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Halmashauri mama ambayo ni Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, bajeti ambayo imetengewa na imepelekwa na Serikali imeweza kukagua shule 18 tu kati ya shule 106; je, Serikali inapoilekeza ikakague Nanyamba kwa bajeti ipi ambayo imeipeleka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, kuhusu ni muda gani inahitajika kazi ya kuanzisha ofisi ya udhibiti ubora itachukua, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hakuna muda maalum, yote inategemeana na upatikanaji wa fedha na tunachosema tu ni kwamba kwa sasa tumejipanga kwamba tutahakikisha kwamba Wilaya zote zinakuwa na wadhibiti ubora. Kwa hiyo, tutaendelea kutafuta fedha ili kuhakikisha kwamba ofisi hizo zinakuwepo.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili kwamba Halmashauri mama ya Mtwara yenyewe bado haijaweza kufanya ukaguzi kwa kiwango kikubwa.
Naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba lengo letu ni kuhakikisha kwamba kadri tunavyoendelea tunapanua uwezo wa wadhibiti ubora wetu kuweka kufanya udhibiti ubora. Kwa hiyo, hata kama sasa kiwango cha udhibiti ubora kilichofanyika bado ni kidogo lakini lengo letu ni kuendelea kuongeza fedha ili tuhakikishe kwamba tunaweza tukafanya hiyo kazi kwa ufanisi na kwa wingi zaidi.
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Katika jitihada za kuendelea kuinua ubora wa elimu suala la kuimarisha kitengo hiki cha udhibiti ubora ni suala ambalo kwa kweli halina mjadala. Hali ilivyo sasa hivi wale wenzetu pale ni kama wamevunjika moyo na wamekata tamaa kwa kukosa motisha.
Mheshimiwa Spika, je, ni lini sasa Serikali itawaweka hawa watumishi wa kitengo hiki kwenye viwango kama ilivyo maafisa elimu au walau waweze kupewa posho za madaraka kama zilivyo za Walimu Wakuu, Wakuu wa Shule na Wataribu wa Elimu Kata? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, Serikali inachukua hatua mbalimbali kujaribu kuboresha namna tunavyofanya udhibiti ubora. Kitu cha kwanza kikubwa ambacho kimefanyika ni kubadilisha mfumo wenyewe.
Mheshimiwa Spika, huko nyuma tulikuwa tunazungumzia kuhusu ukaguzi au tulikuwa tunawazungumzia wakaguzi wa shule, sasa hivi mfumo ule umebadilika tunasema ni udhibiti ubora. Mfumo ambao wanaohusika sio wale wadhibiti ubora tu lakini hata walimu wenyewe na wadau wengine kama wazazi kwa mfano kama kuna watu wanamiliki shule binafsi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mfumo uliopo sasa ni mfumo ambao ni shirikishi; tunaamini mfumo huo utatusaidia kwa sababu kila mmoja wetu anahusika.
Mheshimiwa Spika, vilevile changamoto ambazo zipo kama nilivyosema kwenye jibu la msingi kwa mfano kama magari, vitendea kazi na idadi ya Wadhibiti Ubora wenyewe kama nilivyosema Serikali inaendelea kuboresha na kwa kuanzia nafikiri karibuni tutagawa hata magari kwa zaidi Halmashauri 40 kama sehemu hiyo ya jitihada zetu za kuhakikisha kwamba tunaondokana na upungufu wa vitendea kazi vilivyopo.
Mheshimiwa Spika, vilevile tuna mpango wa kujenga ofisi zaidi ya 50 kwenye Halmashauri zetu, lengo ni kuhakikisha kwamba tunaendelea kuboresha huduma ya udhibiti ubora.
Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kusema kwamba kwa sasa hatutegemei tena tuwasikie Wadhibiti Ubora wakifanya kazi za kipolisi, ni lazima washirikishe wadau wote wakati wanafanya zoezi la udhibiti ubora.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kutoa elimu bure, lakini kwa kuwa Serikali imesema wazi na inaonesha wazi kwamba mjadala na watu wenye shule binafsi kwa ajili ya kupunguza hizi ada bado haujafanyika; na kwa kuwa baadhi ya shule za msingi za binafsi zimekuwa na mtindo wa kuwalundikia watoto wadogo maswali kutoka 100 mpaka 1,200 kuja kufanya nyumbani, hali ambayo inawafanya watoto wengine waogope kwenda shule kwa kuwa hajamaliza homework na watoto wengine kufanyiwa kazi hizo na wadada wasaidizi wa nyumbani. Je, Serikali inatoa tamko gani kwa walimu ambao hawatumii njia za ufundishaji zinazofuata misingi ya kazi ya ualimu na matokeo yake watoto wanafundishwa na watu wasiokuwa na taaluma ya ualimu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa wazazi wengi wamepeleka watoto katika shule binafsi kwa malengo mbalimbali. Lengo kubwa lingine lilikuwa ni kuwaanda watoto wao kuweza kufanya vizuri katika masomo ya sekondari na chuo kikuu, lakini wazazi wa Mkoa wa Dar es Salaam wamepata sintofahamu juu ya hatma ya watoto wao kukosa mikopo ya kusomea vyuo vikuu wakati maisha yana kupanda na kushuka. Je, Serikali inawaambia nini wazazi wanaosomesha watoto wao katika shule binafsi?
NAIBU WAZIRI WA WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mariam Kisangi ambaye ni mwalimu mbobezi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la kwanza kuhusu kutoridhika kwake na namna baadhi ya walimu wa shule za binafsi wanavyoendesha mambo yao, naomba tu nisisitize pamoja na kwamba shule ni za binafsi, mitaala, sheria, kanuni na miongozo ni ya umma. Kwa hiyo, hata kama tukitoa ruhusa wamiliki wa shule binafsi waweze kuendesha shule lakini ni lazima wafuate taratibu, sheria na sera iliyopo. Kwa hiyo, tunategemea kwamba kwa kutumia mfumo mpya ambao tumeuleta wa udhibiti ubora ambao kimsingi kila mtu sasa ni mdhibiti ubora kuanzia Kamati au Bodi za Shule vilevile shule zenyewe, tunategemea kwamba upungufu wowote ambao utatokea, utashughulikiwa na wadhibiti ubora ili kanuni zilizopo ziweze kufuatwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile lengo la Serikali la kuingia kwenye mchakato wa kuja na Bodi ya Kitaaluma ya Walimu ni kuhakikisha kwamba walimu wanaofundisha kwenye shule zote ikiwa ni pamoja na shule binafsi ni wale tu ambao watakuwa wana viwango vinavyohitajika lakini ni walimu ambao watakuwa wameandikishwa. Kwa hiyo, tunategemea katika mwaka huu tutakuja na Muswada ili kuhakikisha kwamba mwalimu yeyote ambaye atafundisha ni yule tu ambaye amethibitika kwamba amehitimu na ana ubora unaohitajika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali la pili kuhusu wasiwasi wa wazazi wa wanafunzi ambao wamesoma katika shule za binafsi kupata mikopo ya kwenda katika elimu ya juu, naomba niendelee kuweka wazi jambo ambalo tumekuwa tukizungumza. Bajeti ya mikopo kwa ajili ya wanafunzi wanaoenda vyuo vya elimu ya juu kwa mwaka ni shilingi bilioni 427 wakati wanafunzi ambao tunategemea kuomba mikopo kwa mwaka ni kama 70,000. Mwaka huu wa fedha unaoisha tuliweza kuchukua wanafunzi 30,000 na kwa mwaka unaokuja tunategemea kuongeza idadi hiyo kufikia wanafunzi 40,000. Katika hali ambayo fedha iliyopo inaweza kuwachukua wanafunzi kiasi fulani, ni lazima tufanye uchaguzi. Uchaguzi wetu utaangalia uwezo wa wazazi kulipa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mwanafunzi aliyesoma katika shule binafsi inachukuliwa moja kwa moja kwamba ana uwezo wa kulipa chuo kikuu. Mfano mzuri tu ni kwamba shule nyingi za binafsi nyingine ada zinafika hata shilingi milioni 30 na nyingine unakuta ada ya chini kabisa ni Sh.1,500,000 lakini University of Dar es Salaam kwenye baadhi ya masomo ni mpaka Sh.1,000,000 na Chuo Kikuu Mzumbe ni Sh.1,300,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunachoomba ni kwamba wale watoto ambao hawana uwezo kabisa tuwape nafasi kwanza kabla hatujawachukua wale ambao historia yao inaonesha kwamba wana uwezo wa kulipa. Hata hivyo, kama itadhihirika kwamba kuna mwanafunzi ambaye alipata msaada wa kulipiwa shule za binafsi katika ngazi ya primary na secondary, tutahitaji tu ushahidi, vinginevyo naye atapata ufadhili.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi kwa kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa waajiri wengi nawapotoa nafasi za ajira, wanahitaji waombaji ambao wanaomba wawe na experience na wanachuo wengi wanaomaliza vyuo wanakuwa hawana uzoefu. Je, Serikali ina mpango gani kuwasaidia wanavyuo wanapotoka vyuoni waajiriwe bila kuulizwa experience?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba, siyo kazi zote zinahitaji uwe umepata uzoefu. Kuna kazi ambazo zinatangazwa ambazo wanachukuliwa wanafunzi waliotoka vyuoni moja kwa moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kama nilivyosema lengo la kuanzisha mfumo wa elimu ambao vilevile unafundisha stadi za kazi ni kuhakikisha kwamba hata tunapokuwa mashuleni tayari kuna uzoefu ambao tumekuwa tumeupata. Ndiyo maana hata Serikali kwa sasa inawekeza sana kwenye elimu ya ufundi ili wanafunzi wanapokuwa mashuleni na vyuoni wawe tayari wameshaanza kufanya practicals ili wakienda kwenye ajira kwamba wawe tayari wanaweza kuajiriwa. (Makofi)
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa suala la ubakaji na ulawiti linazidi kuongezeka; je Serikali haioni imefika wakati wa kuwa na hotline maalum ya kutoa taarifa za ukatili kwa wale ambao wanapata tatizo hilo?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa Serikali imeweka mpango mzuri wa kuwa na dawati la jinsia. Kwa nini Serikali isiweke utaratibu wataalam hawa wakaenda kutoa elimu katika shule zetu mbalimbali hapa nchini? Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi maswali yake yote mawili ni kutoa ushauri na mapendekezo, nimhakikishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba mapendekezo ambayo anayotoa, nitayafikisha Serikalini tuone namna ya kuyafanyia kazi. (Makofi)
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu haya hayaridhishi hasa ukizingatia kwamba ahadi hii ya Serikali ni ya muda mrefu takriban miaka saba sasa. Pale Mkinga tunategemea uwekezaji mkubwa sana wa kiwanda kikubwa cha cement, uwekezaji wa takriban dola bilioni tatu. Uwekezaji ambao utavutia takriban viwanda 11. Sasa kwa muktadha huo, nini mkakati wa Serikali wa kuleta Chuo cha Ufundi pale Mkinga ili vijana waweze kupata stadi zitakazowawezesha kuingia kwenye uchumi huu wa viwanda? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wenzetu wa Singapore kwa kutambua changamoto ya ajira katika nchi yao, wametumia mfumo ambao umewawezesha kuondoka kwenye tatizo, mfumo wa ku-link mafunzo ya VETA na maeneo ya kimkakati ya uzalishaji (industrial park) je, Serikali iko tayari kujifunza kutoka kwa wenzetu ili tuondokane na tatizo tulilonalo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naelewa sana Mheshimiwa Kitandula anaposema jibu langu la msingi halijamridhisha kwa sababu kwa kweli kwa miaka mitatu sasa amekuwa kila wakati yupo Wizarani akifuatilia ujenzi wa VETA ya Wilayani kwake Mkinga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kupitia Bunge lako Tukufu nimhakikishie Mheshimiwa Kitandula kwamba tayari mchakato wa kujenga Chuo cha VETA Mkinga umefikia katika hatua za mwisho. Serikali kwa kushirikiana na kampuni ya Dubai inayoitwa Planet Core iko katika hatua za mwisho za kuingia mkataba wa PPP ili waweze kujenga vyuo kumi nchini kikiwepo Chuo cha VETA cha Mkinga. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba awe na subira kidogo tu kwa sababu kile ambacho amekuwa akitafuta kwa muda mrefu sasa kiko mbioni kutekelezwa. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Ukiangalia kwenye majibu ya msingi ya swali langu Waziri anakiri kabisa kwamba bado mpaka sasa hivi wanasambaza vitabu vya darasa la nne na kimsingi darasa la nne wamefanya mtihani. Kwa hiyo ina maana kuna wanafunzi wamekosa vitabu na wamefanya mitihani na hawa watoto pia wanafanya mitihani ya kufanana. Je, Serikali haioni hili ni tatizo kubwa na kwamba ni lazima sasa watoto wapate vitabu kwa wakati kwa sababu tunajua Walimu nao wana matatizo yao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; mwaka 2016 Taasisi ya Elimu ilitayarisha vitabu na vitabu hivyo vikaondolewa kwa sababu vilikuwa vibovu sana, lakini mwaka 2018 wametengeneza tena vitabu na baadhi ya vitabu vina matatizo. Je, Serikali haioni kwamba Taasisi ya Elimu imeshindwa kazi yake kwa sababu vile vitabu vilikuwa zaidi ya bilioni 100 tulivyoambiwa na kwamba sasa Serikali haioni kuna haja ya kuwa na ushindani na Sekta Binafsi ili vipatikane vitabu ambavyo vitakuwa bora ili watoto wetu waweze kupata elimu bora? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kumekuwepo na changamoto ya kuhakikisha kwamba vijana wetu wa darasa la nne wanapata vitabu kwa wakati. Hata hivyo, kama nilivyoeleza sasa tunaelekea kukamilisha zoezi la kusambaza vitabu hivyo nchi nzima. Kwa hiyo nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba changamoto hiyo sasa tuko mbioni kuachana nayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hili la vitabu anavyosema vina makosa tulishatoa rai kwamba kama kuna yeyote mwenye kitabu kati ya vitabu hivi ambavyo tumechapisha ambaye ameona au anahisi vina makosa atuletee kwa sababu sisi ka Wizara na kama Serikali. Mchakato ambao tumeutumia kuja na vitabu vipya umetuhakikishia kwamba kuna ubora mkubwa sana katika vitabu vipya ambavyo vimetoka kwa hiyo namwomba Mheshimiwa Mbunge na wengine wote ambao wao wana vitabu ambavyo wanafikiri vina makosa wavilete kwetu na tutaviangalia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu tayari kulikuwa na vikaragosi vinazungushwa mtaani kumbe vilikuwa ni vikaragosi vya vitabu vya Kenya. Kuna watu wengi ambao wanajaribu kuichafua Serikali na kuchafua mfumo wetu wa elimu. Kwa hiyo, naombeni mwenye chochote kile ambacho anafikiri ni makosa alete tuangalie kwa sababu sisi tunajiridhisha kuwa vitabu havina makosa.
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza napenda nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake marefu, hata hivyo, nataka nimuulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, nataka nimwambie elimu ya juu ni suala la Muungano na amejibu katika majibu yake ya msingi kwa wanafunzi ambao wameweza kupata kwa mwaka huu ni 33,920. Nataka nimuulize, je, kati ya hao Wazanzibari ni wangapi nataka nijue? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, napenda niipongeze sana Serikali kwa kuweka vigezo vya kuwatambua zaidi yatima na watu wenye hali ngumu katika mikopo hii. Kuna taarifa ambazo zipo na ambazo zina ushahidi, wengi ambao wanaokosa basi ni hawa yatima na hawa wenye hali ngumu. Hii inapelekea kuomba kwetu sisi Wabunge ili tuweze kuwawezesha waweze kupata elimu hii ya juu. Je, Serikali inasemaje kuhusu hili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimeeleza sifa za upatikanaji wa mikopo hapo awali sifa kuu ni hizo ambazo niliziainisha na kwa kweli tumekuwa hatusemi zaidi kwamba nani Mzanzibari nani Mtanzania bara, na hiyo ni kwa sababu gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza hata kwa hali iliyopo katika maisha yetu ya kawaida ni vigumu sana hata kuwatenganisha hawa wanafunzi kwa sababu unaweza kukuta kuna mwanafunzi wa Zanzibar yuko Tanzania Bara na anasoma na mwanafunzi wa Tanzania Bara anasoma Zanzibar. Kwa hiyo tunachoangalia zaidi ni vile vigezo na sifa zinazostahiki waweze kupata mikopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, katika suala hili la hawa wenye uhitaji maalum kukosa mikopo, niseme tu kwamba Serikali imekuwa ikizingatia sana na kwa wale ambao wana mazingira hayo ninayoyasema ikithibitika watasaidiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano katika mwaka huu wa 2017/2018, jumla ya wanafunzi 7,073 waliopata mikopo kati yao 1,224 ni wale ambao wenye mzazi mmoja na 5,849 ni wale ambao pia walikuwa hawana wazazi, lakini wenye ulemavu ni 626 kwa hiyo kimsingi niseme tu kwamba Serikali imekuwa ikizingatia sana uhitaji. (Makofi)
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kunipa na mimi niulize swali la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, suala la mafunzo ya ufundi ni muhimu sana vijijini, sana, kwa hiyo naunga mkono kwa kweli suala la kuhimiza uimarishaji wa utoaji wa elimu ya ufundi vijijini, kwa sababu wengi hawaendelei na kidato cha kwanza na hata wanaomaliza kidato cha nne hawana mahali pa kwenda. Je, Serikali ina mpango gani wa kuimarisha hivyo vituo alivyokuwa anazungumzia Mheshimiwa Susan lakini pia FDCs ili viweze kutoa ufundi unaotakiwa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYASI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Margaret Sitta, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kama anavyosema Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna umuhimu mkubwa sana wa kuhakikisha kwamba tunaendeleza elimu ya ufundi nchini. Naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali imejipanga kuhakikisha kwamba tunaboresha mazingira ya elimu ya ufundi. Kwa kuanzia kama alivyouliza, katika bajeti ambayo wametupitishia ya mwaka unaokuja, Wizara ya Elimu itakarabati vyuo 30 vya FDCs, vile vyuo vya wananchi, kati ya 55 vilivyopo. Tumetenga zaidi ya shilingi bilioni 10 kuhakikisha kwamba vile vyuo vinakarbatiwa lakini tunajaribu kuangalia mahitaji yao ya wafanyakazi ili kuhakikisha kwamba sasa vinafanya kazi katika hali nzuri zaidi.
Mheshimiwa Spika, vilevile naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika azma hiyo hiyo ya kujaribu kuendeleza elimu ya ufundi, Wizara yangu inatekeleza mradi wa unaotiwa ESPJ wa dola zaidi ya milioni 100. Mradi huu kimsingi unajaribu kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji katika vyuo vyote vinavyotoa elimu ya ufundi katika katika ngazi zote. Kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba ni kweli tunatambua umuhimu na ndiyo maana tunachukua hatua mbalimbali.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, ni kweli ule msemo ukishangaa ya Musa utaona ya firauni, ukishangaa ya Musa utaona ya CCM.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inaweza kutuambia kwamba ilitudanganya kwa sera hii kwa sababu ilisema elimu msingi ni darasa la kwanza mpaka la sita. Leo wanasema elimu ya msingi ni darasa la kwanza mpaka la saba kwa sheria ya mwaka 1978. Sasa wako tayari kuwaambia wananchi kwamba sasa wanafunzi watakuwa wanasoma darasa la kwanza mpaka la saba na kwamba ile sera ilikuwa ya kutudanganya? Hilo la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa sasa wamekiri kwamba elimu msingi kwa maana ya elimu ya awali mpaka kidato cha nne haiwezekaniki, tena na sasa ni elimu ya msingi ya darasa la kwanza mpaka la saba.
Sasa nataka kujua hiyo, mitaala ambayo tayari walishaihuisha ya kuanzia darasa la kwanza mpaka darasa la sita kwa maana ya kwamba la saba lilikuwa halipo, wataenda tena kukaa na kutunga mingine au watafanyaje? Nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kwamba Serikali imedanganya kwa kubadilisha elimu msingi kuwa miaka saba badala ya ile sita iliyokuwa imesemekana katika sera ya elimu ya mwaka 2014, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hakuna kosa lililofanyika kwa sababu sera ni njozi, ni vitu ambavyo unatarajia kufanya katika kipindi cha muda mrefu, kwa hiyo, hakuna ulazima wa kufuata sera kwa asilimia 100. Kitu ambacho ni lazima kufuata ni sheria na Sheria yetu ya Elimu ya mwaka 1978 mpaka leo hii ndio sheria ambayo inatuongoza na ndio inatutaka tufuate elimu msingi ya miaka saba bila kukosa.
Kwa hiyo, kama tunataka tuhakikishe ile miaka sita inakuwa kisheria hatuna budi kubadilisha sheria na ndio kazi hasa ya Bunge hili. Kwa hiyo, kama yeye anaona kwamba ni lazima kufanya hivyo aje na mapendekezo na sisi hatuna shida.
Lakini niseme vilevile kwamba waingereza wanasema don’t fix that which is not broken, hatujaona shida na elimu ya miaka saba katika shule ya msingi. Waheshimiwa wote mlioko huku wote mmesoma katika mfumo huo. Kuhusu kwamba tulishapendekeza busara ikikujia nyingine wakati wowote ili mradi ni kitu kizuri haina shida, hakuna kosa lililofanyika na tutaendelea kwa miaka saba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la mitalaa, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kurekebisha mitaala yetu ili tuendane na maamuzi yoyote ambayo tutakuwa tumechukua kwa wakati huo. Nashukuru sana.
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jibu lisilokamilika kutokana na kwamba mimi niliulizia Kilwa lakini amejibu kwa pamoja. Ni lini sasa uchambuzi wa kina na hali ya halisi utakamilika ili vyuo hivyo vipate huduma inayohitajika? Hilo ni swali langu la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Chuo cha Maendeleo cha Wilaya ya Kilwa kina mafunzo ya udereva, lakini mpaka sasa hivi hakuna gari la kujifunzia. Ni lini Wizara itapeleka gari katika Chuo cha Maendeleo Wilaya ya Kilwa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Bungara, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu zoezi litakamilika lini, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, zoezi hilo litategemea kukamilika mwezi ujao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu chuo kupatiwa gari, kama tulivyosema tunafanya tathmini ya kuangalia vitu vinavyohitajika ikiwa ni pamoja na vifaa vya kujifunzia na kufundishia. Kama gari ni moja kati ya vitu vitakavyoonekana kwamba vinahitajika basi Serikali itajipanga ili kuweza kuhakikisha kwamba linapatikana kadri uwezo utakavyoruhusu.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Karagwe ina idadi ya watu wasiopungua 350,000 lakini tuna A Level moja tu ya Bugene Sekondari na haina maktaba hata moja, lakini pia ina upungufu wa madarasa yasiyopungua 17. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri baada ya Bunge hili yuko tayari kuambatana na mimi akajionee hali ilivyokuwa mbaya pale Bugene Sekondari? Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Innocent Bachungwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge ni kama amewahisha shughuli kwa sababu swali linalofuata linahusiana vidato vya tano na sita. Hata hivyo, mimi sina shida niko tayari kwenda naye jimboni kwake, kuna maeneo maarufu sana nataka nifike kule kama Chamchuzi. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba sina shida na kwenda kwa hiyo tutaongea tuone umuhimu wa kufanya hivyo.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi nami niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto zilizopo kwenye Chuo cha Maendeleo Kilwa zinafanana kabisa katika changamoto zilizopo katika Chuo cha Bandari kilichopo Tandika pala Temeke ambako chuo hicho kilianza kufundisha wanafunzi kabla hakijapata ithibati, hivyo wanafunzi wote walio-graduate kuanzia mwaka 2016 kurudi nyuma hawakupewa vyeti vyao mpaka hivi leo. Jambo hili limezua mtafaruku mkubwa, wanafunzi hawa hawajui hatima yao, wanashindwa kuendelea na masomo zaidi na wanashindwa kupata ajira. Nilitaka kujua kauli ya Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wanafunzi hawa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mtolea, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama anavyosema kwamba kuna changamoto katika Chuo cha Bandari. Changamoto hiyo imeshafika Wizarani kwetu na kwa sasa tunaishughulikia na wanafunzi watapatiwa majibu muda si mrefu.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Elimu lakini nina maswali madogo mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, natambua jitihada za Wizara ya Elimu za kuanzisha Shule za Sekondari za Kata lakini ni ukweli usiopingika kwamba wananchi wengi baadhi ya maeneo wanashindwa kupeleka watoto wao maeneo ya mbali, mfano Jimbo la Kilindi ambako wazazi hawana uwezo wa kupeleka watoto wao kidato cha tano na cha sita. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kushirikiana na halmashauri yetu ambapo tumeshafanya jitihada kubwa kutembelea Shule za Sekondari za Kilindi Girls, Kikunde na Mafisa ambazo tayari zina miundombinu kwa ajili ya kupata sifa ya kuwa na kidato cha tano na sita? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kigua, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kama niko tayari katika kutembelea shule za jimboni kwake kama alivyotaja, mimi niko tayari kuzitembelea lakini naomba tu niendelee kusizisitiza kuwa Shule za Kidato cha Tano na Sita ni shule za kitaifa. Kwa hiyo, hata kama tukijenga Kilindi bado haitakuwa kwa ajili ya wanafunzi wa kutoka Kilindi tu, watatoka wanafunzi Tanzania nzima.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa matatizo ya Kilindi yanafanana kabisa na yale matatizo ya shule za Mbagala. Niishukuru Serikali kwa kujenga madarasa mengi katika shule ya Msingi Majimatitu na Mbande. Shule hizi zilikuwa zinaandikisha wanafunzi 6,000 kila mwaka, kwa kweli watoto hawa ni wengi. Je, Serikali haioni haja ya kuandaa shule ya sekondari za high school katika maeneo ya Chamazi, Mbande, Nzasa na Charambe katika Jimbo la Mbagala ili watoto wanaomaliza sekondari waende kwenye high school maeneo hayo hayo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mariam Kisangi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, kwa halmashauri ambazo zinahitaji kuanzisha Shule za Kitado cha Tano na Sita, utaratibu ni kwamba wao wenyewe wajipange na wajenge miundombinu husika baadaye waombe kibali kutoka Wizara ya Elimu na sisi tutaangalia na tukijiridhisha kwamba inafaa hatutakataa kuzisajili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kusema kwamba kwa sasa kama kuna changamoto ya wanafunzi wa kutoka Mbagala kuweza kupata elimu ya kidato cha tano na sita karibu bado fursa zipo katika shule nyingine za kitaifa kwa sababu kimsingi kidato cha tano na sita zote ni shule za Kitaifa.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Jimbo la Sumve lina shule za sekondari 17 ikiwemo Shule ya Sekondari ya Talo ambayo inazo sifa zote kama vile miundombinu na tumeshaleta maombi Serikalini. Je, ni lini sasa shule hiyo ya sekondari itawekewa kidato cha tano na sita?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ndassa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimeendelea kusema kwenye majibu yaliyopita, Wizara ya Elimu ipo tayari kupokea maombi ya kutoka kwenye halmashauri zinazofikiri zinataka shule ziweze kupatiwa ruhusa ya kuendesha kidato cha tano na sita. Sisi tutakachofanya tutaenda kujiridhisha na hali ya miundombinu kuangalia kama kweli kuna mazingira ya kukidhi kuanzishwa kidato cha tano na sita. Kama nilivyosema, lengo letu kama Wizara tunataka angalao tuhakikishe kwamba katika kila tarafa kuwe na kidato cha tano na sita. Kwa hiyo, tukiangalia mazingira kama yanaridhisha sisi hatuna shida. Kwa hiyo, naomba waanze wao walete mapendekezo Wizarani na sisi tutayafanyia kazi.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa elimu ya bure ni kuanzia darasa la kwanza mpaka darasa la kumi na mbili, lakini kidato tano na sita hawamo. Hawa wote ni watoto wa mtu mmoja, kuna sababu gani za msingi form five na six wakaachwa kusamehewa karo? Naomba Waziri atoe maelezo kwa sababu wote ni watoto wake, kwa nini hawa waachwe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Lubeleje, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama alivyosema kwamba watoto wote ni watoto wa Taifa hili kwa hiyo haitakiwi kuwa na ubaguzi. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba lengo la Serikali siku zijazo kadri uwezo utavyoruhusu tutatoa elimu bure ikiwezekana mpaka chuo kikuu bure. Kwa sasa, kutegemeana na hali halisi ya kifedha, tutaendelea kwanza kuimarisha miundombinu na mazingira katika shule za ngazi ya elimu msingi, kuanzia shule za awali mpaka kidato cha nne na kuendelea kutoa elimu bure na uwezo ukiongezeka hatuna shida kuongeza kidato cha tano na sita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kama mnavyofahamu Serikali inatoa mikopo kwa ajili ya wanafunzi wa elimu ya juu. Tunatoa shilingi bilioni 427 kila mwaka kwa sasa. Kwa hiyo, anachosema ni kitu cha kweli. Kwa kweli siku zijazo uwezo utakapoongezeka hata kidato cha tano na sita nayo itakuwa ni elimu bure.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika majibu ya Mheshimiwa Waziri anasema kwamba kwa mujibu wa sera angalau kila tarafa iwe na shule ya sekondari ya kidato cha tano na sita; na sisi Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki tumeshaanza ujenzi huo katika tarafa zote tatu za Mkuyuni Ngerengere na Nelson Mandela. Shule ya Nelson Mandela tulishamaliza bado bwalo kumalizia juu. Je, Serikali iko tayari kutuunga mkono kumalizia bwalo ili mwezi wa saba wanafunzi waanze, ukizingatia mwaka jana zaidi ya wanafunzi 60 wamekosa kwenda katika hizo shule za kitaifa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mgumba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kama Serikali iko tayari kuwaongezea nguvu kukamilisha bwalo na anataka limalizike mwezi wa saba, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba pamoja na nia ya Wizara ya kuendelea kusaidia ujenzi wa miundombinu bado muda wa matayarisho utakuwa ni muhimu kwa sababu kipindi cha mwezi mmoja kwa kweli kina changamoto katika taratibu za kawaida za kupata fedha. Hata hivyo, halmashauri yake walete mapendekezo na sisi tutajipanga ili tuweze kuwasaidia katika mipango mingine ijayo. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Jimbo la Mbulu Vijijini na Halmashauri ya Mbulu tumejenga Shule ya Kidato cha Tano na kila kitu tayari na Mheshimiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI amekuja kuigagua. Tumetuma maombi na Naibu Waziri anafahamu tunahitaji kuianzisha mwaka huu na kila kitu tayari. Je, kibali hicho kinatoka lini ili mwaka huu watoto hawa waingie shuleni na kusaidia Tanzania ya elimu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Flatei, Mbunge wa Mbulu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Mheshimiwa Mbunge amekuwa akifuatilia sana kuhusu shule anayosema na ombi lao liko mezani kwenye Wizara yetu. Naomba tu nimhakikishie kwamba tutalishughulikia mapema iwezekanavyo ili ikiwezekana katika mwaka wa masomo unaofuata wanafunzi wa kidato cha tano waweze kuingia katika shule anayosema.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Katika jimbo letu la Babati Mjini tuna A – level moja (Babati Day) lakini Serikali walitupa mwongozo kwamba tutafute A – level nyingine na sisi halmashauri yetu tukapendekeza Sekondari ya Kwaangw’, Kata ya Maisaka. Mheshimiwa Naibu Waziri anapafahamu sana hapo maana anapita, tukawekeza nguvu zetu zote pale, sasa halmashauri haina vyanzo vya kutosha na A – level hiyo inatakiwa ianze mapema. Mheshimiwa Naibu Waziri Serikali sasa iko tayari kutuongezea nguvu ili hiyo sekondari ya A – level ianze mapema?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya Wizara yetu ambayo Wabunge wametupitishia kwa ajili ya mwaka unaokuja tumetenga shilingi bilioni 168 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu katika taasisi mbalimbali za elimu kwa ngazi mbalimbali; kuanzia shule za msingi mpaka vyuo vikuu. Kwa hiyo, Wizara ina fedha za kusaidia ujenzi wa miundombinu. Tunachotaka kutoka kwenu Waheshimiwa Wabunge na mkiwa sehemu ya Mabaraza la Madiwani leteni maombi nasi tukijiridhisha kwamba kuna mahitaji hatutasita kuwasaidia. Kwa hiyo, nimshauri Mheshimiwa Gekul kwamba sisi tuko tayari kupokea maombi yenu lakini leteni kwa taratibu zilizowekwa.
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakurushukuru. Serikali itakubaliana na mimi kwamba sekta binafsi ina mchango mkubwa katika elimu. Mwaka jana wanafunzi takriban 19,000 waliokuwa wanaingia kidato cha tano walikosa nafasi katika shule za Serikali. Mheshimiwa Naibu Waziri, hamuoni imefika wakati sasa kuzipunguzia kodi shule binafsi ili hawa wanafunzi wanaokosa nafasi katika shule za Serikali waweze kumudu ada elekekezi katika shule binafsi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Halima Bulembo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba sekta binafsi ina nafasi nzuri sana katika kusaidia maendeleo ya sekta ya elimu. Serikali itaendelea kushirikiana nao ili kuondoa changamoto zinazowakabili ili waweze kuwekeza kwa urahisi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari tumeshaondoa tozo na kodi kubwa nne ambazo zilikuwa zinawaletea changamoto. Tupo tayari kujadiliana nayo ili kuangalia ni namna gani tunaweza kuboresha mazingira ili waweze kuwekeza kwa urahisi zaidi.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekondari ya High School ya Kaliua inapokea watoto kutoka Tanzania nzima na ina watoto wegi sana lakini kuna upungufu mkubwa sana wa mabweni ya wasichana na wavulana. Pamoja na juhudi za halmashauri za kuendelea kujenga bado mahitaji ni makubwa sana. Serikali iko tayari sasa kupeleka nguvu katika Sekondari ya High School ya Kaliua ili watoto wale wapate mabweni ya kutosha kwa sababu hivi tunavyoongea baadhi ya wavulana wanakaa kwenye madarasa kwa kukosa mabweni ya kulala?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sakaya, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ipo tayari kuangalia uwezekano wa kusaidia kujenga miundombinu katika shule aliyosema. Kama nilivyosema kwenye maswali mengine tunahitaji kupata maombi, ni lazima halmashauri yenyewe ituletee maombi ili tuangalie ni namna gani tanaweza kusaidia. Kwa hiyo, tuko tayari kujenga miundombinu, tumeshajenga mingi katika nchi nzima lakini tunaangalia vilevile na bajeti. Kwa hiyo, alete maombi yataangaliwa pamoja na maombi mengine.

MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Amekiri kwamba kuna matatizo lakini swali langu la kwanza linasema, kama hivyo ndivyo, wanafunzi wamemaliza wakiwa hawana ufundi wowote, kwa sababu kile chuo kilikuwa cha madarasa kwa ajili ya vijana wetu na kilikuwa kinafundisha udereva hamna magari, karakana hamna, madarasa mabovu na wameondoka wakiwa hawana ujuzi wowote na intake yao imekwisha. Je, Serikali ina mpango gani kwa ajili ya vijana hao, baada ya kurekebisha upungufu huo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa hakuna vifaa vya kufundishia miundombinu hakuna na bado intake hii wanachukua wanafunzi, nini kauli ya Serikali katika hilo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwamba pamoja na upungufu uliopo katika Chuo cha FDC Kibaha, elimu iliyokuwa inatolewa inakidhi viwango stahiki vya ufundi ambao Chuo kile kimesajiliwa kwa ajili ya kutoa. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba wale vijana waliomaliza Serikali imejiridhisha kwamba wamekuwa wakipata mafunzo vinginevyo chuo kile kingeshafungwa.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili kwamba ni namna gani sasa tunarekebisha hiyo hali, nimeshamjibu kwenye jibu letu la msingi kwamba tayari tupo kazini, tunafanya tathmini ili kuweza kujua upungufu uliopo katika vyuo vyote 50 vya FDC ili sasa tuanze utaratibu wa kukarabati, na kuweka mazingira mazuri ya kujifunzia na kufundishia ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba kuna nguvukazi ya kutosha ili elimu inayotolewa iweze kuwa bora kuliko sasa. Kwa hiyo, nimwambie tu asubiri tayari zoezi linaendelea.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa nami kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Chuo cha Ufundi VETA, Dodoma kilijengwa muda mrefu na kilikidhi kwa wakati ule na sasa hivi kuna ongezeko kubwa sana la vijana na miundombinu bado ni ile ile; je, Serikali haioni kwamba umefikia wakati wa kuongeza majengo na miundombinu ili kiendane na hadhi ya Jiji? Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwamba Serikali ina mpango wa kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji katika vyuo vyote nchini, na sio Vyuo vya Ufundi tu. Kwa hiyo, tutaendelea kuangalia vyuo vile ambavyo vinahitaji matengenezo na ukarabati pamoja na kuongezewa Majengo, ili tuweze kufanya hivyo kadiri bajeti itakavyoturuhusu.
Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie tu kwamba, hata Chuo cha Dodoma nacho ni moja kati ya vyuo tulivyonavyo na kwa vyovyote vile kulingana na upatikanaji wa fedha tutaangalia uwezekano wa kukipanua.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Moja ya Malengo ya Umoja wa Mataifa ni kuhakikisha kwamba hakuna anayeachwa nyuma na katika vyuo vingi hasa vya Ufundi, havizingatii mahitaji ya kundi maalum la watu wenye ulemavu na hivyo wamekuwa wakiachwa nyuma. Ni nini sasa, jitihada za Serikali katika kuhakikisha kwamba ili tunaendana sambamba na kauli hizo za Umoja wa Mataifa, watu wenye ulemavu hawaachwi nyuma?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Amina Mollel, kwa kweli amekuwa ni mtetezi mkubwa sana wa haki za watu wenye mahitaji maalum. Nimhakikishie tu kwamba, Wizara yangu imejipanga vizuri kuhakikisha kwamba changamoto ambazo zilikuwepo huko nyuma za kutotoa msisitizo mkubwa kwenye mahitaji maalum ya watu wenye ulemavu, kwa sasa tunahakikisha tunajaribu kutoa kipaumbele.
Mheshimiwa Spika, kwa kuanzia Wizara ya Elimu ina Kitengo Maalum kinachohusika na elimu ya mahitaji maalum. Vilevile kwa sasa tumetoa maelekezo kwamba katika ujenzi wowote ule utakaofanywa kwa fedha za Serikali ni lazima tuhakikishe kwamba mahitaji na mazingira ya watu wenye mahitaji maalum yanatiliwa maanani.
Mheshimiwa Spika, ukiacha hivyo, Serikali imewekeza sasa vilevile kwenye kutafuta Walimu na Wataalam wengine kwa ajili ya kuendeleza elimu ya watu wenye mahitaji maalum. Ndio maana tumefanya ukarabati mkubwa sana katika Chuo cha Patandi na tunaamini kwamba tunavyoendelea mbele, tutaendelea kuhakikisha kwamba kunakuwa na Walimu na wafanyakazi wengine ambao wana elimu ya kuweza kusaidia wanafunzi na watoto wenye mahitaji maalum. Kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba Serikali inayafanyia kazi vizuri sana.
MHE. HAMAD SALIM MAALIM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Wizara, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Wizara imekiri kwamba si mitaala na mihtasari yote iliyoko kwenye mtandao. Je, lini Wizara itahakikisha kwamba mitaala na mihtasari yote hii inapatikana kwenye mtandao?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, mabadiliko ya mitaala na mihtasari yanayofanywa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia huwa inachuka muda mrefu sana kutufikia kule Zanzibar na hiyo kupelekea wanafunzi wetu kuathirika sana wakati wanatumia mitaala na mihtasari ile mikongwe. Je, ni lini Wizara itahakikisha kwamba mitaala hii na mihtasari hii inafikia Zanzibar kwa wakati ili waweze kujitayarisha katika masomo yao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, kuhusu ni lini tutaweka mitaala na mihtasari yote kwenye tovuti, naomba nimhakikishie Mbunge kwamba kama nilivyosema, kwenye jibu la msingi kwamba tumeshaanza na tayari baadhi ya mitaala na mihtasari inapatikana. Sasa kuhusu ile ambayo bado, nimhakikishie kwamba Serikali, itachukua hatua kuhakikisha kwamba tunaweka kwenye tovuti haraka na mapema iwezekanavyo.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na changamoto iliyoko Zanzibar naomba nimhakikishie kwamba nimeipokea, tunaenda kuifanyia kazi ili kuhakikisha kwamba nako mihtasati na mitaala iwe inapatikana kwa wakati.

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Labda tu nihakikishe kwamba utaratibu ambao uko kwa sasa hata mitaala inapofanyiwa mapitio kunakuwa na ushirikiano kati ya upande wa Tanzania Bara na upande wa Zanzibar na hata katika Bodi ya Taasisi ya Elimu pia kunakuwa na wawakilishi ambao wanatoka upande wa Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, hivyo, inawezekana pengine changamoto ipo katika usambazaji inapokuwa imefika kwenye Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, lakini kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri tumelipokea, tutahakikisha kwamba, kama kuna mahali popote kuna mkwamo, basi iweze kufika, lakini ushirikiano ni mkubwa katika hatua zote tangu maandalizi.
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, hata hivyo naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Wananamtumbo hawafahamu ni majengo gani yanayojengwa na wapo wanaosema kwamba linajengwa jengo la bwalo la chakula, nyumba za wakufunzi, nyumba za kulala wanafunzi, kwa hiyo wanahisi tu hawajui. Je, Serikali iko tayari kuwaeleza wananchi wa Namtumbo kwanza, hizo hisia zao kama ni sahihi na kama sio sahihi ni majengo gani yanayojengwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Mheshimiwa Profesa Ndalichako alipofika Namtumbo watu walikuja kupata taarifa baada ya yeye kuondoka na walipobeba ngoma zao kwenda kumshangilia wakakuta hayupo, je, yupo tayari hicho chuo kitakapokamilika ama yeye, kwa sababu wakimwona yeye ni sawa wamemwona Mheshimiwa Rais au kiongozi yeyote wa ngazi ya juu aje akifungue kile chuo ili wale wananchi waondoe kiu yao ya kutaka kuwaona viongozi wao wanaowapenda?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ni majengo gani yanajengwa katika ujenzi unaoendelea, naomba nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa majengo ambayo yanajengwa ni jengo la utawala, karakana za ufundi seremala, uashi, bomba, umeme wa majumbani na maabara ya komputa. Majengo mengine ni pamoja na madarasa, maktaba na stoo ya generator lakini katika awamu zitakazokuja tutajenga majengo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali la pili kama Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kwenda wakati wa ufunguzi, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa namna Serikali inavyotilia mkazo suala la ufundi na namna ninavyomfahamu Mheshimiwa Waziri anavyosisitiza masuala hayo Wizarani, nina hakika kwamba atakuwa tayari kwenda katika ufunguzi lakini hata baada ya kusikia kuna ngoma hata mimi nafikiri nitaungana naye. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.
MHE SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na nashukuru kwamba Serikali inatambua kwamba kuna changamoto nyingi za watoto wao kushindwa kwenda shule.
Mimi nilikuwa mmoja wa Wajumbe katika Kamati iliyozunguka nchi nzima kuangalia ni jinsi gani watoto hawa wanaweza kurudi shuleni na Serikali kama mtakumbuka mwaka 2017 Naibu Waziri alisema tayari wameshaandaa mwongozo wa jinsi gani ya kuwarudisha watoto hawa shule. Lakini ghafla bin vuu mtu mmoja tu Mheshimiwa Rais akatoa hilo katazo.
Mheshimiwa Spika, sasa swali langu, ninaomba kujua kwamba Serikali imeshafanya tathimini ya kuona kuna athali gani za kijamii, kiuchumi na kisaikolojia kwa watoto hawa wa kike pamoja na watoto wanaozaliwa ni athari zipi hasa zinaweza kuwapata hasa ikizingatiwa kwamba hii sheria baba wa watoto hao nao atakuwa amefungwa miaka 30 hawaoni kwamba kutakuwa na athari kubwa sana?
Mheshimiwa Spika, swali la pili nchi nyingi pamoja na Zanzibar wanafunzi wanaopata ujauzito wanaendelea na shule, sasa hili jibu kwamba kuna elimu ya watu wazima. Serikali haioni kwamba hawa watoto wanaopata ujauzito wa miaka 12 mpaka 15, 16 ni watoto wadogo sana kiasi kwamba wakienda kwenye hiyo elimu ya watu wazima wanaenda kukutana na watu wazima. Lakini vilevile elimu hiyo ya watu wazima haiku coordinated hata kidogo na kwa maana hiyo wanawapelekea watoto hawa kufanya pia, mapenzi hawa watu wazima kwa vyovyote vile watawapa washawishi.
Serikali haioni kweli kuna kila sababu ya kuwapatia watoto hawa special education…
...ili waweze kuendelea na masomo yao?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Lyimo ni mwalimu tena mzoefu na ni Mjumbe wa Kamati ya Maendeleo na Huduma za Jamii. Kwa hiyo, haya masuala anayafahamu sana lakini ameamua kuleta mjadala. Lakini naomba maswali yake kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kuhusu kwamba katizo la wanafunzi wanaopata ujauzito kurudi mashuleni limetolewa na Mheshimiwa Rais naomba nimsahihishe kwamba katazo hilo limekuwepo toka mwaka 2002 kwa mujibu wa kanuni inayoitwa The Expulsion and Exclusion of Students from School Regulation 2002 iliyoanzishwa kwa mujibu wa kipengele cha 60(o) ya Sheria ya Elimu ya mwaka 1978. Kwa hiyo, alichofanya Mheshimiwa Rais ni kusisitiza kitu ambacho kilishaamuliwa toka siku nyingi.
Mheshimiwa Spika, vilevile kuhusiana na swali lake la pili kwamba elimu ya watu wazima haiwafai wale wanafunzi kwa sababu bado ni wadogo.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema yeye ni mwalimu Serikali imeamua kuchukua uamuzi huo kwa sababu ya kumlinda mtoto.
Mtoto ambaye anapata ujauzito mara nyingi akirudi shuleni anakuwa ananyanyapaliwa na wenzake. Kwa hiyo, hata yeye mwenyewe ata ukimruhusu aendelee na shule bado hawezi kuwa katika mazingira mazuri kisaikolojia. Lakini vilevile ni kwa sababu tunataka tuweke wazi kwamba hatutegemei wanafunzi wetu katika umri mdogo waendelee kufanya mapenzi wakiwa shuleni kwa sababu inawaathiri katika masomo yao. Kwa hiyo, ni suala la kuchagua na sisi tumechagua kwamba hatutaki tuchanganye mapenzi na elimu katika huo umri mdogo.
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 iliahidi kujenga VETA katika kila Wilaya. Je, ni lini sasa Serikali itaanzisha mkakati wa kujenga VETA katika kila Wilaya ili kuwasaidia vijana kupata ujuzi wa kuweza kujiajiri? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama alivyosema kwamba Ilani ya Chama cha Mapinduzi imeainisha kwamba Serikali itajenga VETA katika kila Wilaya. Serikali imeanza ujenzi wa VETA katika baadhi ya Wilaya na mpango upo wa kujenga VETA katika kila Wilaya na kila Mkoa, lakini tunajenga kadri fedha zinavyopatikana. Kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba mpango upo pale pale. (Makofi)
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza Mkoa wa Rukwa hauna chuo chochote cha ufundi cha VETA na Serikali hapa imetuahidi mara nyingi kwamba tutapata chuo hicho. Je, ni lini chuo hicho kitajegwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Chuo cha Maendeleo ya Wananchi cha Chala kinaendesha shughuli zake kwenye majengo ya Kanisa Katoliki na kwa kuwa Kanisa Katoliki wanahitaji majengo yao na wananchi wameanza kuchukua hatua ya kujenga majengo mengine ili kuhamishia huko chuo, je, Serikali iko tayari badala ya kufanya ukarabati kwenye majengo yale yaliyokuwa ya mission wahamishie juhudi hizo kwenye wazo hili la wananchi ambapo wanajenga majengo kwa maana kuhamisha Chuo cha Chala?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mipata, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na Mkoa wa Rukwa kutokuwa na Chuo cha VETA, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba lengo la Serikali ni kujenga vyuo vya VETA katika mikoa na wilaya zote. Kwa hiyo, tuna mpango wa kujenga chuo katika Mkoa wa Rukwa kama tutakavyofanya katika mikoa mingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la kuangalia uwezekano wa kuwaunga mkono wananchi katika kujenga chuo wilayani kwake badala ya kutumia kile cha Chala, nafikiri walete maombi Wizarani na sisi tutakaa nao. Kimsingi Wizara tuko tayari kuwaunga mkono wananchi na wilaya ambazo zenyewe zinaanza kujenga na kuwasaidia hata kwenye miundombinu kadri hali ya fedha itakavyoruhusu.
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nachukua fursa hii kushukuru na kupongeza majibu mazuri ya Serikali. Pia niseme tu kwamba ushauri wa kuendelea kutumia Chuo cha Munguri kilichopo sasa tumeupokea na tunaendelea kuutumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu, uwepo wa VETA utaongeza sana na kupanua wigo wa fursa za elimu ya ufundi ili kuendeleza azma yetu ya viwanda. Siyo hivyo tu, lakini pia kuongeza ajira kwa vijana. Swali; je, Serikali imejipangaje kuhakikisha kwamba maboresho haya mliyoyasema yanaingizwa kwenye Mpango na Bajeti ya VETA ili azma hii itekelezwe kwa haraka?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, naelekea huko mzee, swali la pili, azma ya kuwa na VETA ina maslahi mapana sana kwa wanachi, siyo tu kwa wananchi wa Jimbo la Kondoa Mjini, lakini kwa Kondoa nzima kama Wilaya. Pia uwepo wa Taasisi ya kitaifa kama hii yenye hadhi ya VETA na sasa Kondoa ni Halmashauri ya Mji, itaongeza tija kubwa sana kwenye kuchangamsha uchumi wa Kondoa. Swali je, Serikali inatupa commitment gani ya kuhakikisha inaharakisha mchakato huu mara tu baada ya kupokea hiyo barua kutoka Kondoa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama anavyosema Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kweli amekuwa akifuatilia kuhakikisha kwamba majengo yale yanatumiwa kwa ajili ya VETA. Naomba nimhakikishie kwamba kwa sababu Serikali ina azma na imedhamiria kujenga VETA kila Wilaya na kila mkoa, sisi tukikuta kwamba kuna majengo ambayo yamekuwa tayari tunakimbilia kwa sababu gharama ni ndogo kwa sababu tunataka tuweze kuwaletea wananchi maendeleo na kupata ile elimu ya ufundi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimhakikishie mbele yako kwamba pindi sisi tutakapopata barua ya kutuhurusu tutumie yale majengo tutaendelea na utaratibu wa kukarabati ili wananchi wa Kondoa waweze kupata ile huduma. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Wizara yetu hatuwezi tukawa kikwazo cha yeye kufanikiwa lengo lake hilo kwa ajili ya wananchi wake. Kwa hiyo naomba nimshauri wakakae na halmashauri yake watupatie barua, wakinipa kesho mimi niko tayari hata mwenyewe kwenda kukagua eneo lile ili tuweze kuendelea na taratibu zinazofuata.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza.

Kwanza nianze kwa kupongeza maamuzi ya Serikali ya kutoa elimu bure kwa shule za msingi na shule za sekondari na sisi wote ni mashahidi ni kwa namna gani maamuzi haya yameweza kuleta tija kwa Taifa letu. Aidha, nina maswali mawili ya nyongeza.

Kumekuwa na matukio ya adhabu za kuchapa wanafunzi zilizopitiliza mashuleni ambazo zimesababisha madhara makubwa ya kisaikolojia na kwa wakati mwingine zimesababisha vifo vya wanafunzi. Japokuwa kuna mwongozo wa namna gani adhabu hizi za kuchapa...

SPIKA: Mheshimiwa Zainab swali.

MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Okay, japokuwa kumekuwa na mwongozo wa namna ya kutumia adhabu hii ya kuchapa wanafunzi mashuleni lakini mwongozo huu umekuwa hauzingatiwi.

Je, Serikali inatoa kauli gani kuhusiana na masuala haya ya adhabu mashuleni?

Swali la pili, je, wenzetu ambao wamefanikiwa katika sekta ya elimu walifanikiwa kwa sababu ya kuwapo kwa adhabu hizi za kuchapa wanafunzi mashuleni au walifanikiwa kwa sababu ya kuwekeza katika mifumo, mitaala pamoja na miundombinu ya ufundishaji?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba utekelezaji wa kanuni na waraka unaohusiana na viboko bado haujafuatwa kikamilifu. Kwa hiyo, naomba nitumie nafasi hii kuwataka viongozi wote wanaosimamia elimu pamoja na walimu, kuhakikisha kwamba wanafuata Waraka ule Namba 24 wa mwaka 2002, lakini vilevile Kanuni ile inayofahamika kama The Corporal Punishment Regulations wa mwaka 2002.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ifahamike kwamba kwa wale walimu ambao hawatafuata waraka na kanuni hiyo,
wanakuwa wanafanya kosa na wanaweza kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa sheria inaitwa The Teacher Services Act ya mwaka 1989 kama ilivyorejewa mwaka 2002. Kwa hiyo, nawataka wote wafuate taratibu hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la pili kwamba wenzetu wamefanikiwa vipi kuboresha elimu bila kutumia adhabu ya viboko.

Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishe Mheshimiwa Mbunge, pamoja na Wabunge wengine ni kwamba viboko havitumiki Tanzania pekee, hata Marekani huko ambapo ndio tunafikiri wameendelea sana majimbo 19 kati ya majimbo 50 ya Marekani mpaka leo hii yanatumia viboko. Naomba nimwambie kwamba Serikali haitumii tu viboko kama njia ya kuboresha elimu, kuna mengine mengi tunafanya, tunaendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia, viboko ni sehemu ndogo tu na tena tunatumia kidogo sana. Kwa hiyo asije akafikiri kwamba sisi tunatumia viboko tu. Kwenye hilo la viboko hatupo peke yetu duniani tunafahamu mtindo wowote wa kufundisha lazima uhusishe adhabu na zawadi (punishment and rewards).
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, mimi nakubaliana na wewe kuwa bila viboko wanafunzi hawawezi wakaenda. Lakini kwa nini Serikali isitoe aina ya mfano wa kiboko ambacho kinatakiwa kitumike kuchapia wanafunzi? Tumeshuhudia walimu wakikata kuni kwa ajili ya kwenda kuwachapia wanafunzi; kwa hiyo watoe kiboko cha mfano.l
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, kuhusu ni aina gani ya kiboko kinaruhusiwa kanuni ile ya mwaka 2002 (The Corporal Punishment Regulations) inasema kwamba fimbo au kiboko kinachotumika ni kile ambacho kiko flexible yaani hakijakakamaa ndicho kinasema hivyo, kwa hiyo, sio kwamba ni fimbo yoyote unaweza ukachukua ukamchapa nayo mtoto. Kwa hiyo, tayari sheria imeeleza kwamba ni kiboko cha aina gani ni kiboko ambacho ni kilaini, hakija kakamaa.
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa vile tafiti zimeonesha moja kwa moja kwamba zinakinzana, kuna zinazokubali na zinazokataa na kuonesha na sababu zake.

Sasa je, kwanini Serikali haijikiti zaidi katika kutafuta adhabu mbadala yenye tija zaidi na kuliacha suala la viboko mikononi mwa wazazi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, kama wewe mwenyewe ulivyosema, suala la viboko ni suala vilevile la mila. Hata sisi Serikali tukisema leo hatutaruhusu viboko, nina hakika wazazi wengi wataendelea kuwachapa wanafunzi na hapa Bungeni nina hakika tukiwauliza wazazi walioko huku kwamba ni wangapi wanachapa viboko, inawezekana wote tukakuta wanafanya hivyo.

Sasa Serikali kama nilivyosema, kwa sababu adhabu inayotumika mashuleni sio viboko peke yake, hata hivyo kama nilivyosema tutaendelea kutumia viboko kwa njia ambayo haina madhara. Tukifuata ule waraka kwa kweli adhabu ya viboko wala hata isingetolewa kwa kiasi kikubwa.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona.

Mheshimiwa Spika, ile bakora ulioitumia wewe kumchapia yule jamaa nadhani ilikuwa ni bakora maalum sana. Sasa nilikuwa nataka niulize swali kwamba ni aina gani ya material yatakayotumika kutengeneza hicho kiboko cha kuchapia wanafunzi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema, kanuni hazielezi kuhusu ni material gani itumiwe kutengeneza fimbo, lakini wanasema iwe ni fimbo ambayo haijakakamaa ambayo ni laini.

Mheshimiwa Spika, naomba niendelee kusisitiza kwamba, tunaporuhusu viboko haturuhusu uchapaji ambao una madhara kwa mwanafunzi. Kwa hiyo hata kama unatumia kiboko tumia kile ambacho hakina madhara na kwa njia ambayo haidhuru. Vilevile sheria imeelekeza kwamba unachapa wapi, wanasema unachapa mkono au kwenye unachapa kwenye makalio, sio kichwa au mgongo. Kwa hiyo, sheria ile ikifuatwa vizuri, kanuni zile zikifuatwa, tusingekuwa tunapata madhara ambayo tunapata kwa sasa hivi.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu. Mabweni haya yana ghorofa nne nne na ni majengo 20. Bei hii ilileta maneno mengi sana na tukaomba CAG afanyie special audit. Nataka kujua ni jengo gani la ghorofa nne yenye kuchukua wanafunzi takriban 3,840 kwa majengo yote inaweza ghorofa moja kugharimu shilingi milioni 500 tu?

Mheshimiwa Spika, la pili, nataka kujua baada ya TBA kuyajenga majengo yale ndani ya miezi minne yalikuwa na nyufa nyingi, maarufu kama expansion joint ambazo sisi tunavyojua ni lazima jengo liwe nalo, lakini expansion joint
hizo zilienda mpaka kwenye floor na mpaka kwenye madirisha. Nataka kujua ni kwa sababu gani mabweni hayo yalimomonyoka na ni je ni gharama kiasi gani imetumika sasa kuweza kurekebisha hasa ikizingatiwa kwamba TBA hivi majuzi tu Mheshimiwa Rais aliwafukuza kwenye kazi mbalimbali. Je hili jengo ambalo sasa hivi limetengewa bilioni moja ni hao hao TBA pale kwenye hayo Magufuli Hostel watajenga au wamepata mkandarasi mwingine?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:

Mheshimiwa Spika, kuhusu hitilafu alizosema zimetokea na hususan zile zinazohusishwa na expansion joint naomba nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba expansion joint sio hitilafu, expansion joint imekusudiwa kuwekwa kwenye maghorofa yale ili kuweza kuhimili changamoto ambazo zinaweza zikatokea, ni kazi ya kitaalamu na wala sio upungufu na tayari tulishatoa maelezo marefu sana kuhusu hili.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na upungufu mwingine mdogo mdogo uliotokea, hii ni kawaida ambayo inatokea katika ujenzi na tayari ilisharekebishwa na kwa sababu tayari mkandarasi aliyepewa kazi bado alikuwa katika kipindi cha liability alirekebisha yeye mwenyewe na tayari ilishakwisha na hakukuwa na fedha za ziada ambazo zilitumika kurekebisha changamoto hiyo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu gharama naomba nimhakikishie Mheshimiwa Susan Lyimo kwamba jengo hilo limegharimu shilingi bilioni 10. Sasa kama yeye anatilia shaka kuhusu ukweli huo ambao namweleza labda yeye atuletee mahesabu yake ya kuonesha kwamba imegharimu zaidi, lakini hizi ni fedha za umma, zimelipwa kwa mujibu wa taratibu, taarifa rasmi ambayo naileta Bungeni ni kwamba imetumia shilingi bilioni 10 na hakuna fedha nyingine yoyote iliyotumika ukiacha fedha ambazo zimetumika kwa ajili ya kufanya masuala mengine ambayo ni nje ya scope ya kazi ile ambayo walipewa TBA.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nashukuru kwa majibu niliyopatiwa na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ongezeko la watoto wetu wanaoendelea kupata mimba bado limeshika kasi. Ni juzi tu tumepata habari kwamba kuna mwalimu amewafanya wake zake watoto wa primary karibu 10. Wako wanaopata mimba kwa kubakwa, wako wanaopata mimba kwa kushawishiwa na wako wanaopata mimba kwa bahati mbaya yoyote ambayo inatokezea lakini huwa siyo dhamira, dhamira hasa ni watu hawa wapate haki ya kielimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili ni zito sana…

MWENYEKITI: Swali sasa.

MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Sheria Na. 5 imetoa adhabu ya miaka 30 kwa yule mharibifu.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Abdullah, nipe maswali.

MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza, nataka niiulize Serikali ni lini hasa itakaa chini itizame upya kadhia hii inayowakuta watoto wa wanyonge, wafanyakazi na wakulima, wasichana ambao wanakosa haki yao kielimu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, lini Serikali itatafuta mbinu mbadala ya kuwasaidia watoto hawa ambao wanakosa haki yao ya kimsingi? Hili jambo linauma sana, lazima Serikali itazame upya.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika jibu langu kwenye swali la msingi, Serikali inachukua hatua kadhaa kuhakikisha inadhibiti tatizo hili. Kubwa ambalo limezungumziwa ni mabadiliko ya sheria ambapo imekuwa ni kosa la jinai kwa mtu yeyote kumpa mimba mwanafunzi wa shule ya msingi au sekondari. Tunachoomba na Waheshimiwa Wabunge ni mabalozi wazuri katika hili, Serikali ina dhamira ya kuhakikisha kwamba wale wote wanaokutwa na makosa haya wanachukuliwa hatua kwa mujibu wa sharia na kama tulivyosema tumeweka kifungo cha miaka 30.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi kinachotokea ni kwamba ushirikiano kutoka kwa wazazi wa wanafunzi ambao wameathirika unakuwa siyo mkubwa. Pindi tutakapopata ushirikiano na ushahidi ukiwepo, Serikali itaendelea kuchukua hatua kuhakikisha kwamba wale wahusika wote wanachukuliwa hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili tunachukua hatua zipi kuhakikisha kwamba wale wanafunzi wanaoathirika wanaendelea na safari ya masomo? Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba mwanafunzi kupata mimba haimaanishi kwamba ndiyo mwisho wa safari yake ya masomo. Serikali imeweka taratibu kadha wa kadha ili kuhakikisha wanafunzi wale bado wanapata fursa nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fursa hiyo ipo katika maeneo matatu makubwa; moja Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima ina utaratibu wa kutoa elimu nje ya mfumo rasmi. Napenda kutoa taarifa kwamba kwa mwaka jana kuna wanafunzi 10,000 ambao wamehitimu kidato cha nne kupitia utaratibu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima na 6,000 ni wasichana. Tunaamini kwamba baadhi yao ni wanafunzi wale ambao walikatisha masomo kwa sababu ya mimba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia Wizara ya Elimu kwa kushirikiana na UNICEF tunaendesha Mradi wa Elimu Changamani kwa wanafunzi ambao wameshindwa kuendelea na shule kwa sababu ya kupata ujauzito. Pia, Serikali imeendelea kuimarisha elimu ya ufundi, kwa hiyo, wanafunzi ambao hawajaweza kwenda sekondari au ambao wameshindwa kuendelea kwa sababu ya kupata ujauzito kuna fursa vilevile ya kupata elimu ya ufundi na tumeendelea kuimarisha na elimu hiyo sasa hivi ni bora.

Kwa hiyo, tunachosema kimsingi, hata kama mwanafunzi amepata ujauzito sio mwisho wa safari yake ya masomo kuna fursa nyingine na kuna wengi ambao wamenufaika. Nina hakika hata baadhi ya Wabunge kwenye Bunge hili wamenufaika na mipango hii ya Serikali.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tatozo la mimba utotoni pia linawahusu sana watoto wenye ulemavu walio nje ya shule na ambao wako ndani ya shule. Je, Serikali inawanusuru vipi hawa watoto wenye ulemavu na mimba za utotoni?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Toufiq, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu niliyotoa kuhusu watoto wa kike wanaokatishwa safari ya masomo kutokana na mimba, vilevile yanaweza yakatumika kwa ajili ya watoto walemavu kwa sababu tunachosema Wizara yetu na Serikali kwa ujumla inahakikisha kwamba hakuna mtoto yoyote wa Kitanzania atakayekosa elimu kwa sababu yoyote ile. Sisi tunachotaka ni ushirikiano kutoka kwa wazazi kwa sababu tayari Serikali ina mipango ya kuhakikisha kwamba yeyote yule anapata elimu bila kujali changamoto yoyote imempata katika safari yake.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nina swali moja dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mikakati ya Serikali ya kuweza kutoa adhabu kali na sheria ya kifungo cha miaka 30 kwa wale ambao wanawapa mimba wanafunzi lakini inaonekana bado wanafunzi wanapata mimba na idadi inaongezeka. Je, Serikali ina mkakati gani wa ziada kwa baadhi ya madereva wa bodaboda wanaowachukua wanafunzi wetu ambapo wamekuwa wakilalamika kwamba wanatendewa vitendo visivyo za kutoa elimu ya kutosha kwa madereva hao wanaowachukua wanafunzi kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Masoud, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, jibu langu nilitoa katika majibu yangu ya swali la msingi kwamba Serikali inachukua hatua kadha wa kadha. Moja ni kuzuia na tunazuia kwa njia mbili na kubwa kupitia kitu tunachoita deterrence; kwa kuwaadhibu wale wanaofanya makosa ili wengine wasije wakafanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu changamoto ambayo watoto wanapata wakiwa wanaelekea shuleni, Serikali imeendelea kujenga shule karibu na wananchi lakini vilevile kwenye maeneo ambayo shule ziko mbali tumejenga mabweni. Vilevile tunatoa elimu kwa umma na wanafunzi kwa kupitia huduma za unasihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nachotaka tu kusema ni kwamba Serikali inajua hili ni tatizo kubwa lakini hatujakaa kimya tumeendelea kufanya kila linalowezekana kuhakikisha kwamba hayatokei. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kutokana na takwimu tulizonazo tatizo haliongezeki limepungua.
MHE. BERNADETHA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Bukoba Sekondari ina umri wa miaka 80, Rugambwa Sekondari ina umri wa miaka 55 lakini pamoja na uzee shule zote zilipitiwa na tetemeko na Bukoba Sekondari ikaja vilevile ikaezuliwa na kimbunga. Kwa niaba ya Mkoa wa Kagera na wanafunzi wanaosoma katika shule hizo, naipongeza sana Serikali kwa kutoa Sh.1,481,000,000 kwa ajili ya kukarabati Bukoba Sekondari na kuahidi kukarabati Rugambwa mwaka huu kuanzia mwezi huu wa Aprili. Kwa kuwa Rugambwa wakati wa tetemeko nyumba za walimu na zenyewe zilianguka na nyingine zikaathirika sana, hadi leo Mkuu wa Shule hana mahali pa kuishi, je, Serikali ina mpango gani wa kuwajengea nyumba za kuishi walimu wa Shule ya Sekondari Rugambwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, shule zote mbili, Bukoba Sekondari na Rugambwa zinahitaji kumbi za mikutano. Bukoba Sekondari haina ukumbi kabisa, Rugambwa ukumbi wake ni mdogo sana unachukua watoto 300 wakati wako wanafunzi karibu 700/800. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwajengea kumbi za mikutano ili wanafunzi wapate mahali pa kufanyia mitihani na kufanyia mikutano?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba kwa dhati kabisa na kwa furaha kubwa nipokee shukrani na pongezi za Mheshimiwa Mbunge kwa kazi ambayo Serikali imefanya katika shule zake. Lazima niseme kwamba Mheshimiwa Mushashu ni moja kati ya Wabunge makini sana katika Sekta ya Elimu na tumeendelea kufarijika na uzoefu wake mkubwa kama Mwalimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maswali yake, kwanza kuhusiana na nyumba za Walimu katika Shule ya Rugambwa, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunavyozungumza tayari Serikali inafikiria kujenga nyumba nane za Walimu katika shule ya Rugambwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na kumbi za mikutano katika shule zote mbili, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia ikiwa ni pamoja na miundombinu katika shule zake kadiri uwezo wa fedha utakavyoruhusu.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kupata nafasi hii. Tatizo lililopo Bukoba ni sawa na tatizo lililopo katika Mkoa wa Mara hasa Jimbo la Bunda Vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunda Vijijini tuna Shule za Sekondari 12…

MWENYEKITI: Uliza swali Mheshimiwa.

MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naweka hoja vizuri ili swali lieleweke. Ili mtoto awe na usikivu mzuri darasani, mazingira ya shule zile ni mabaya sana, maboma hayajamaliziwa, kwa hiyo, ili mtoto awe na usikivu darasani ni vizuri kuwe na miundombinu mizuri na mazingira mazuri. Je, ni lini Serikali itahakikisha inajenga na kuzimalizia zile Shule za Sekondari katika Jimbo la Bunda Vijijini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika shule zetu na ndiyo maana Serikali imeendelea kutenga fedha kwa mabilioni kuhakikisha kwamba tunaondoa changamoto ya miundombinu katika shule zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu katika mwezi wa Januari ilitoa shilingi bilioni 56 kwa shule tofauti 500 nchi nzima. Lengo lake ni kuendelea kupunguza changamoto za miundombinu katika shule hizo. Hata Mkoa wa Mara na Bunda anapotoka Mheshimiwa Mbunge nao wamefaidika na mpango ule wa ujenzi kupitia mradi wa kulipa kulingana na matokeo (EP4R).

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Wizara ya TAMISEMI hivi karibuni imetoa fedha kwa ajili ya kumalizia maboma nchi nzima. Naomba Mheshimiwa Mbunge awasiliane na Halmashauri yake kupata taarifa sahihi kwa sababu fedha hizo zimeenda nchi nzima. Kama bado kuna upungufu ni nia ya Serikali kuendelea kukabiliana na changamoto hizo kadiri uwezo wa fedha utakavyoruhusu.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nashukuru kwa kunipa nafasi. Naipongeza Serikali kwa kutupatia fedha Korogwe Girls za ukarabati wa shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati mbaya sana katika ukarabati ule bweni moja la Thabita limeshindikana kabisa kukarabatiwa kutokana na ubovu wa bweni lile.

Je, Serikali itakuwa tayari sasa kutupatia fedha ili tuweze kujenga jengo hilo kutokana na watoto 120 kwenda kutawanywa kwenye mabweni mengine?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mary Chatanda pale Wizarani kwangu ameshatengewa kiti kwa sababu kila wakati amekuwa akija Wizarani kufuatilia changamoto za miundombinu kwa ajili ya shule zake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sababu siyo mara ya kwanza kuleta changamoto hii, Wizara yangu imejipanga kuondoa hiyo kero moja kwa moja ili watoto wetu waweze kusoma katika mazingira mazuri.
MHE. JANETH M. MASABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Natambua Serikali imefanya vizuri sana katika sekta hii ya elimu, lakini nina maswali madogo ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa, hivi sasa kwa wastani kwa wahitimu wa vyuo vikuu ni kati ya 10 kwa mmoja kwa wahitimu wanaohitimu vyuo vya ufundi, yaani wasimamizi 10 kwa mtendaji kazi mmoja badala ya msimamizi mmoja kwa watendaji kazi 10. Je, Serikali inasema nini juu ya hili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika umuhimu huo wa vyuo vya ufundi ambako ndiko kunakozalisha kundi kubwa la watenda kazi ambalo kundi hili ndilo linajiajiri lenyewe. Je, Serikali inasema nini juu ya kuweka uwekezaji mkubwa katika vyuo vya ufundi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Janeth Masaburi kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ukweli kwamba, kwa sasa hakuna uwiano mzuri kati ya watendaji au wafanyakazi katika sekta ya ufundi katika ile maana ya kwamba, wale watendaji wa kada ya kati pamoja na kada ya chini na wale wa ngazi za juu. Serikali ndio maana imechukua maamuzi ya kuongeza udahili katika vyuo vyetu ili tuendelee kuwapata wataalam wengi ambao baadae watatusaidia kujaza ombwe hili na hivyo kurekebisha hali hiyo, ili tuwe na uwiano mzuri katika wafanyakazi wetu katika sekta ya ufundi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili kwamba, Serikali inafanya nini kuwekeza katika vyuo vya ufundi. Kama nilivyosema kwenye jibu langu katika swali la msingi, Serikali inachukua hatua kadhaa za makusudi kuhakikisha kwamba, tunaongeza, sio tunaongeza vyuo vingi, lakini vilevile tunaongeza udahili pamoja na ubora wa vyuo hivyo ambavyo vinatoa fani mbalimbali za ufundi. Ndio maana tunapozungumza sasa tunajenga vyuo 13 vya wilaya, lakini tutajenga vyuo vitano vya mikoa, ambavyo vile vya mikoa vyenyewe vinagharimu shilingi bilioni 118, lakini pia hatujaishia hapo, tunakarabati Vyuo vyote 54 vya Wananchi vile tunaviita FDCs.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo ni kuweza kuwa na vyuo vingi vyenye ubora mzuri, ili tuongeze udahili, ili tuendelee kuwapata mafundi wengi kwa sababu, watatusaidia katika azma yetu ya kujenga uchumi wa viwanda, lakini vilevile kuongeza fursa za ajira. Kwa sababu, kama mnavyofahamu ni rahisi vijana wengi kujiajiri wakisoma ufundi; lakini pia, tunaendelea kujenga vyuo vya ufundi wa kati na ndio maana tumewekeza katika kujenga chuo kikubwa Dodoma, chuo ambacho kina hadhi kama ilivyo DIT na Arusha Technical College.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona. Wananchi wa Mafia kwa kushirikiana na Mbunge wao wamejenga chuo cha kisasa kabisa cha VETA na kukamilisha taratibu zote, lakini mpaka leo Wizara haijatoa usajili. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri sasa atakuwa tayari kutoa usajili kwa ajili ya VETA ya Mafia?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dau, Mbunge wa Mafia, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dau amekuwa akifuatilia sana suala la VETA ya Mafia. Kwa kweli, kuna wakati hata mimi na yeye kidogo tulitofautiana kwa sababu, aliona kwamba, hatufanyi kazi kwa kasi ambayo anaitaka kwa hiyo, nampongeza sana kwa sababu, amekuwa akifuatilia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, VETA ya Mafia imekuwa na changamoto mbili kubwa ambayo ni changamoto ya vifaa, hasa kwenye fani za ushonaji, lakini vilevile Walimu ambao wana viwango vinavyohitajika, ili VETA iweze kusajiliwa. Nimemwahidi Mheshimiwa Mbunge na ninaendelea vilevile kumwahidi kupitia Bunge lako Tukufu kwamba, Wizara yangu iko tayari kusaidiana na yeye pamoja na wananchi wake wa Mafia ili changamoto hizo tuweze kuziondoa na tuweze kutoa usajili mapema kwa ajili ya chuo chake.
MHE. SHAABAN O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Wilaya ya Lushoto ni wilaya kongwe na bahati nzuri Waziri Mheshimiwa Ndalichako alitembelea Wilayani ya Lushoto na akaona hali halisi ilivyo. Je, ni lini Mheshimiwa Waziri utatuma wataalam wake kwenda kuona majengo yale ya Halmashauri, ili ikimpendeza tuweze kuanza sasa kukarabati majengo yale na watoto wetu waanze kusoma masomo ya VETA?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shekilindi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba, leo hii tukitoka mimi na yeye tutapanga ni lini tutawapeleka hao watendaji kule.
MHE. SUSAN A. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mheshimiwa Naibu Waziri anapojibu anaelezea suala zima la kujenga vyuo kila wilaya na mkoa, lakini hawajazungumzia changamoto kubwa ya tatizo kubwa la Walimu wa ufundi stadi. Je, wanapojenga hivi vyuo kila mkoa na kila wilaya wana Walimu kwa sababu, wana Chuo kimoja tu cha Ualimu wa Ufundi Stadi kule Morogoro, ni lini wataongeza au waapanua chuo kile au kujenga chuo kingine, ili tupate Walimu bora ambao wataweza kuhimili au kwenda kwenye hivi vyuo ambavyo vinajengwa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susan Lyimo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba, kuna upungufu huo na Serikali inatambua na tumeanza hatua za makusudi kuhakikisha kwamba, tunaongeza upatikanaji wa Walimu katika vyuo vyetu vya ufundi.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Zamani tulikuwa na shule za msingi ambazo zilikuwa zinatoa mafunzo ya ufundi, lakini pia, tulikuwa na sekondari za ufundi. Je, ni kwa nini sasa Wizara isizifufue zile shule angalau kila kata iwe na shule moja ambayo inatoa mafunzo ya ufundi, ili kuwawezesha vijana ambao hawajafanikiwa kwenda sekondari kupata stadi na mwisho wakaweza kujiajiri na vilevile tukateua sekondari katika kila tarafa sekondari moja iwe sekondari ya ufundi, ili vijana wanaokosa kuendelea na kidato cha tano waweze kujiajiri?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hongoli kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba, kuna haja ya kuongeza fursa za mafunzo ya ufundi katika ngazi mbalimbali na ndio maana Serikali inajaribu kwa kuanzia kujenga vyuo, lakini badaye tutaangalia uwezekano wa kurudi kwenye shule za sekondari na shule za msingi ambazo ni za ufundi. Kwa sasa zipo shule baadhi za sekondari ambazo zinatoa ufundi vilevile.
MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshukuru kwa maelezo ya Mheshimiwa Waziri aliyoyatoa kuhusu umuhimu wa elimu ya ufundi na Halmashauri ya Wilaya ya Kigamboni ni wilaya mpya ambayo ina fursa nyingi sana zinaweza kuwasaidia vijana kujiajiri wenyewe. Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga chuo cha ufundi katika Halmashauri ya Kigamboni, ili kuwaepusha vijana wetu na gharama kubwa ya nauli wanayolipa katika kivuko kuvuka kwenda mjini kutafuta huduma hiyo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Magereli, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema Serikali ina mpango wa kujenga vyuo vya ufundi vya wilaya katika Wilaya zote ikiwemo na Wilaya ya Kigamboni. Naomba nimshauri vilevile Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wengine wote kwamba, pale ambapo wao wenyewe na wananchi wao watakuwa wameanzisha jitihada ya kujenga chuo inakuwa ni rahisi sisi kuja kuongezea kuliko tunapoendelea kusubiri nchi nzima tujenge.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Serikali ninayo maswali mawili ya madogo ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa Sera ya elimu ya mwaka 2014 imetamka wazi kwamba elimu ya msingi itaishia darasa la sita na hadi hivi tunavyozungumza Serikali bado haijatekeleza katika eneo hilo. Je, Serikali inatuambiaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni kwa kiasi gani Sera hii ya Elimu inazingatia ubora wa elimu, hasa ukizingatia kwamba miongoni mwa mikoa ambayo huwa haifanyi vizuri katika mitihani mbalimbali ni Mkoa wa Tanga. Sasa nataka kujua ni kwa kiasi gani Sera hii ya elimu inazingatia suala zima la ubora wa elimu kwa maana ya quality assurance? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Rashid Shangaz, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kujibu, naomba nitumie nafasi hii kusema kwamba Mheshimiwa Shangazi amekuwa akifuatilia suala hili na masuala yote yanayohusiana na elimu na kwa kweli kwa nafasi yake hakuna ubishi kwamba ni moja kati ya Wabunge bora kabisa ambao wamewahi kutokea katika Bunge hili. Swali lake la kwanza ni hilo kwamba kwa nini hatujatekeleza wazo lile la Sera la kuishia darasa la sita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jibu letu ni kwamba Sera siyo Msahafu, kwa hiyo Serikali inabadilisha Sera kadiri inavyoona kwamba inafaa kulingana na mahitaji ya wakati huo. Kwa sasa busara imetujia upya kwamba elimu kuanzia darasa la kwanza mpaka la saba siyo kitu kibaya, kwa hiyo hatuna haja ya kubadilisha na ndiyo maana tumebakia na mfumo wa zamani na hatujavunja sheria, Sera siyo lazima itekelezwe, Sera unatekeleza na unabadilisha kadiri unavyoona inafaa. Kwa sasa tuko kwenye mapitio na ni moja ya mambo ambayo tuliona kwamba hatutatekeleza na tutaendelea na utaratibu wa zamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuhusiana na ubora wa elimu ni kweli kwamba Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, imeweka msisitizo mkubwa katika masuala ya udhibiti ubora wa elimu na ndiyo maana kumetokea mabadiliko makubwa sana katika mfumo wetu wa udhibiti ubora. Zamani tulikuwa tunasema ni ukaguzi wa elimu lakini siku hizi tunadhibiti ubora, lakini vile vile mtindo mpya wa kudhibiti ubora ni wa kiushirikishwaji zaidi unawaleta wadau wote kushiriki katika kudhibiti ubora wa elimu, lakini vilevile kama wote mnavyojua sasa tuko katika mikakati mikubwa ya kuhakikisha kwamba Wadhibiti Ubora wanawezeshwa kwa kupata vifaa na ofisi. Kimsingi tumeweka mikakati mikubwa sana ya kuhakikisha kwamba elimu yetu inakuwa bora. Moja kati ya masuala ambayo tunayafanyia kazi katika mapitio ya Sera ni kuendelea kuweka mifumo ambayo itawezesha kudhibiti ubora wa elimu.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja dogo la nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mapitio ya Sera ya Elimu na kuweka mikakati ya ubora wa elimu, ni mara kadhaa hapa Bungeni Serikali imekuwa ikiahidi kuboresha maslahi ya walimu ikiwemo posho ya kufundishia (teaching allowance). Vilevile kwenye sherehe mbalimbali za walimu katika maeneo kadhaa Serikali wamekuwa wakiahidi kuboresha posho ya kufundishia (teaching allowance) lakini hadi sasa waliopata fedha hizo ni Wakuu wa Shule na Waratibu wa Elimu. Naomba kujua kama Serikali iliwadanganya walimu na lini fedha hizo zitatolewa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali na Mheshimiwa Masoud, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli katika azma ya kuboresha elimu maslahi ya walimu na wafanyakazi wengine katika sekta ya elimu ni kitu muhimu. Ndiyo maana kwa sasa Serikali inajaribu kupitia upya utaratibu mzima wa maslahi ya watumishi wa umma kwa jumla wakiwemo na walimu ili baada ya hapo tuweze kuwa na maslahi ya walimu ambayo yataenda na wakati wa sasa lakini vilevile ili waweze kufanya kazi yao vizuri katika sekta ya elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusu swali la madeni, naomba nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ilijikita kwanza katika zoezi la kufanya uhakiki ili kubaini madeni ya kweli. Baada ya hapo tayari baadhi ya malipo yalishafinyika na mengine yataendelea kulipwa.
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mwezi Januari, 2019, Wizara ya Elimu ilitoa Mwongozo juu ya Muundo wa Bodi za Shule kuanzia shule za msingi mpaka Serikali. Katika muundo ule, Wizara imeelekeza katika shule ya sekondari na shule za msingi muundo utoe nafasi kubwa sana kwa walimu ambapo watakuwa watano lakini pia wazazi au nje ya walimu wanakuwa watatu. Je, katika maana nzima ya makusudio ya Bodi kwenda kuangalia ufanisi wa taaluma na majengo na mambo yanayoendelea shuleni, Wizara haioni kwamba jambo hili limekosewa na kwamba linahitaji lirekebishwe haraka sana kabla hapajaharibika?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba hivi karibu tumetoa Mwongozo mpya wa Bodi za Shule na lazima niseme kwamba baada ya kuutoa tumegundua kuna maeneo ambayo yangeweza kuwa bora zaidi na mojawapo ni hilo alilosema Mheshimiwa Kikwete. Naomba nimhakikishe kwamba tayari Wizara inaupita upya tena Mwongozo ule kwa kushirikiana na wadau ili tuwe na Mwongozo ambao utakotupeleka mbali zaidi.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri na mikakati yote ya Serikali bado idadi (ratio) ya wasichana kwa wavulana katika vyuo vyety vya elimu ya juu ni ndogo sana katika masomo ya sayansi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua kwamba baadhi ya vyuo, kwa mfano Chuo Kikuu cha Dar es Salaam siku za nyuma kilikuwa na programu ambayo ilikuwa inawasaidia wasichana ambao wamepata point chache wanakuja kwenye hiyo programU walau miezi miwili ili waweze sasa kujiunga na vyuo lakini programU hiyo sasa haipo na bado tunahitaji sana wasichana kuendelea na masomo. Swali la kwanza, je, ni lini programu kama hizo zitarudishwa ili kusaidia wasichana kwa kuwa tunatambua mazingira magumu wanayowapata wasichana huku chini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, pamoja na kwamba wanajenga mabweni au hosteli katika vyuo na shule zetu lakini bado tuna tatizo kubwa sana la uhaba wa mabweni ambayo yangewasaidia wasichana hawa kuweza kujiunga na vyuo vya elimu ya juu kuweza kuweka uwiano wa kijinsia siyo tu katika vyuo lakini hata katika masuala mazima ya siasa maana tunapata wanawake wachache kwa sababu hiyo. Ni lini mtatekeleza hilo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Susan Lyimo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Chuo Kikuu cha Dar es Salaam siku za nyuma kilikuwa na mpango ambao ulifanikiwa sana wa kuwasaidia wanafunzi wengi wa kike kuweza kujiunga na masomo ya sayansi. Mpango ule muda wake ulishaisha lakini kwa sasa tayari kuna majadiliano ya kurudisha au kuanzisha programu inauhusiana na suala hilo na katika hali ambayo itawahusisha watoto wa kike wengi zaidi katika vyuo vingine, kwa hiyo, majadiliano yapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sisi kama Serikali tunachofanya ni kuboresha elimu kwa ujumla wake pamoja na kutoa hamasa na kuomba wananchi na wadau wote washirikiane katika kuondoa mila na fikra potofu ambazo zinafanya watoto wa kike waogope kwenda kuchukua masomo ya sayansi. Nashukuru kwamba leo tumetembelewa na wanafunzi wa kike wa sekondari. Naomba nitumie nafasi hii kuwaeleza kwamba sayansi na hisabati ni ya kila mtu na siyo kwa ajili ya wanaume tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali lake la pili kuhusiana na ujenzi wa mabweni na hosteli, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara yangu mwezi Januari ilipeleka katika shule na vyuo tofauti 560 shilingi bilioni 56 ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kujenga miundombinu katika shule na vyuo vyetu na kati ya fedha hizo, nyingi zimeenda vilevile katika kujenga hosteli na mabweni. Yeye mwenyewe anajua baadhi ya vyuo kwa mfano Chuo cha Ardhi na Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere tunajenga hosteli kwa ajili ya wanafunzi lakini maarufu kwa utetezi wake wa Hall 2 na Hall 5 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa sasa vimetengewa shilingi bilioni nne. Kwa kweli katika vyuo vyetu tunajitahidi kujenga mabweni na hosteli za wanafunzi.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Ili watoto wa kike waweze kufanikiwa katika masomo ya sayansi wanahitaji uwepo wa walimu. Tuna tatizo kubwa sana kama nchi ya walimu wa sayansi na hasa hasa physics. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakisha shule zetu zinapata walimu wa kutosha wa physics?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwalongo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama alivyosema kwamba ili watoto wa kike waweze kufanikiwa kuchukua masomo ya sayansi ni lazima kuwa na walimu na ndiyo maana Serikali imekuja na mikakati thabiti ya kuhakikisha kwamba walimu wanapatikana. Wote tunakumbuka kwamba Serikali ilipeleka wanafunzi wale waliokuwa UDOM kwenda kusoma masomo ya sayansi na tunategemea wataanza kuingia sokoni kwa ajira za hivi karibu. Pia katika vyuo 35 ambavyo tunavyo, Serikali imeamua sasa kutenga vyuo vichache kati ya hivyo vinakuwa ni vyuo vinavyofundisha sayansi. Kwa hiyo, tunaendelea kuongeza fursa na udahili katika vyuo vya elimu vinavyotoa walimu wa sayansi.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Napenda nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri wa Elimu, kumekuwa na malalamiko mengi ya wanawake kwamba hawapati nafasi za kutosha katika shule kuanzia sekondari, vyuo na vyuo vikuu. Sasa ni mkakati wa Serikali kwamba wanawake wakifikia hapo waanze kubinywa au wanawake wenyewe wamezoea kudekezwa tu?

MWENYEKITI: Hebu tusaidiane kidogo, unauliza vizuri lakini hilo neno kudekezwa linyooshe tu.

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri aseme kuna mkakati kwamba wanawake wanabinywa au sasa wao wenyewe wanataka wasaidiwe tu kwenda vyuoni?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti nilichokuwa nazungumzia katika maswali yangu yaliyopita ndiyo inajionyesha dhahiri hapa kwamba ni suala la mila, desturi na fikra potofu dhidi ya uwezo wa watoto wa kike kuweza kuendelea na kufanya vizuri kama watoto wa kiume.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waheshimiwa Wabunge kila mmoja katika nafasi yake ajielekeze kwenye ukweli kwamba mtoto wa kike ana uwezo sawa na mtoto wa kiume, kwa hiyo, tuwasaidie waweze kusonga mbele.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba nimpongeze Mkuu wangu wa Wilaya kwa jitihada zote za kunyanyua elimu ya Ulanga Bi. Ngoro Malenya.

Mheshimiwa Spika, chuo anachoongelea Mheshimiwa Waziri ni cha mission na kinachukua wanafunzi wachache sana na fani chache ambazo haziendani na rasilimali zinazopatikana Ulanga kama madini, misitu na uvuvi. Wanafunzi wanaomaliza Ulanga kidato cha nne kwa mwaka ni 1000 hadi 1200 na hiki chuo kinachukua wanafunzi chini ya 150.

Mheshimiwa Spika, kwa nini sasa Serikali isishirikiane na misheni ili kuongeza kukipanua chuo hiki ili kiweze kuchukua wanafunzi wengi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kuna eneo ambalo tulilitoa kwa ajili ya VETA wajenge Chuo cha Ufundi eneo la Mwaya. Je, Serikali inasemaje ipo tayari kutoa hela kwa ajili ya kuanza ujenzi wa chuo hiki?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ni kweli kama tulivyosema kwamba Wilaya ya Ulanga kwa sasa ina chuo kimoja tu cha binafsi lakini tumeshauri kwamba wananchi wa Ulanga waendelee kutumia vyuo vingine vilivyopo, kuna vingi vipo katika Mkoa wa Morogoro lakini vilevile nchi nzima kwa sababu ndio utaratibu tunaoutumia kwa sababu sio kila Wilaya ina vyuo.

Mheshimiwa Spika, vilevile kuhusiana na Serikali kushirikiana na wa-misionari wanaoendesha Chuo cha Mtakatifu Francis, naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa Serikali haina utaratibu wa kuendesha vyuo kwa utaratibu wa PPP. Tupo tayari kuona ni namna gani tutajenga Chuo cha Ufundi Stadi Ulanga kwa sababu hata hivyo ni mpango wa Serikali kujenga chuo cha Ufundi Stadi kila Wilaya na Mkoa.

Kwa hiyo, kuhusu eneo ambalo limetengwa, wizara yangu haina shida ya kushirikiana na Wilaya ya Ulanga kuangalia namna gani kile chuo kitajengwa kwa sababu tayari ni mpango wa Serikali kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja dogo.

Mheshimiwa Spika, Serikali ina mpango gani wa makusudi kuweza kujenga Chuo cha VETA katika Wilaya ya Kaliua ili vijana wa Kaliua ambao wanakua haraka sana ni wengi wanaokosa nafasi za kuingia masomo ya juu waweze kupata stadi za kazi na ujuzi waweze kujiajiri na tunapoelekea kwenye uchumi wa kati na uchumi wa viwanda?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba nitumie nafasi hii kulieleza Bunge lako tukufu na ningeshukuru kama Waheshimiwa Wabunge wote watasikiliza kwa sababu jibu nitakalotoa linafanana kwa kila Jimbo kwa sababu jibu ni hilo hilo.

Mheshimiwa Spika, azma ya Serikali ni kujenga VETA katika kila Wilaya na Mkoa. Kwa sasa tunavyoongea kuna ujenzi unaendelea katika Wilaya 17 Vyuo vya VETA lakini vilevile kuna VETA tano zinaendelea kujengwa. Sasa mpango wetu ni kwamba nikuhakikisha kila Wilaya inapata VETA kwa hiyo tutaendelea kujenga nyingi iwezekanavyo kulingana na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, ushauri wa ujumla ambao ningependa kutoa kwa Waheshimiwa Wabunge, ukiweza kujiongeza na kwenda mbele zaidi katika kujenga sehemu inakuwa ni rahisi Serikali kuleta fedha kwa sababu hata hivyo tunachotaka ni kuongeza nafasi za udahili kwa wengi nchi nzima.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, ni majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia. Je, yupo tayari kufuatana na mimi kwenda kuangalia eneo ambalo tayari Wilaya ya Uyui tumeliweka kwa ajili ya VETA?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, sina shida ya kuandamana na Mheshimiwa Mbunge na akipenda vilevile anaweza akawa na Wabunge wa Viti Maalum wa Mkoa husika wakati wa kutembelea eneo hilo. kwa hiyo, tukitoka tutapanga ili tuweze kutembelea huko.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, kwa vile tozo hii ya asilimia 4.5 ya mshahara wa mfanyakazi ni kubwa kuliko tozo zote duniani. Siyo Afrika tu, dunianina hapa Afrika Mashariki tozo hii inatozwa asilimia 1.2 Kenya tu, tena kwa ajili ya sekta moja ya utalii. Swali la kwanza, je, Serikali haioni umuhimu wa kupunguza tozo hii ili kufanya utendaji wa biashara hapa nchini uwe rahisi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, hapa Tanzania tunafanya biashara au kazi kwa utatu, yaani Serikali, Wafanyakazi na Waajiri,VETA kuwa chini ya Wizara ya Elimu, imetutoa katika mfumo huo. Je, Serikali haioni sasa ni muhimukurudisha VETA chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ambako kuna Kazi, Ajira na Mafunzo.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Almas Maige kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuhusu kwamba SDL tunayotoza sisi ni kubwa kuliko zote zinazotozwa duniani, siwezi kuwa na uhakika kuhusu hilo. Hata hivyo, concern au hoja ya kupunguza kodi hiyo au tozo hiyo tayari imeshawasilishwa Serikalini. Hata juzi wakati wa Maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi Chama cha Waajiri Tanzania waliileta kwa msisitizo mkubwa na Mheshimiwa Rais aliitolea maelekezo kwamba Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayehusika na masuala ya Kazi na Ajira ajaribu kuwakutanisha utatu ule ambao Mheshimiwa Maige ameusema, yaani Serikali, Wafanyakazi na Waajiri ili waweze kujadiliana wapate muafaka kuhusu namna bora ya kuratibu tozo hii.

Mheshimiwa Spika, watakapokutana, itabidi sasa jambo hilolipelekwe kwenye kikosi kazi kinachohusiana na mambo ya kodi, yaani ile Tax Reform ili waweze kujadili na ikiwezekana mapendekezo yaweze kutolewa na ikibidi sheria ije Bungeni irekebishwe ili sasa tuwe na tozo ambayo imekubalika na pande zote.

Kuhusiana naswali lake la pili kwamba kwa nini VETA isihamishiwe Ofisi ya Waziri Mkuu ambaye ndiye hasa inahusika na masuala ya ajira. Kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, Serikali ni ileile. Kwa hiyo, kuhusu kwamba jambo fulani linatakiwa liwe wapi wakati fulani, ni masuala ya maamuzi tu ya muda na inategemea sana kwa wakati huo, kwamba umuhimu au mahitaji yanahitaji iwekwe wapi. Kwa vyovyote vile, masuala ya ufundi stadi ni suala la elimu vilevile. Kwa hiyo, siyo kwamba kuna shida ikiwepo kwenye Wizara ya Elimu, lakini kama tunavyosema, itaendelea kubadilika kulingana na maamuzi ya Serikali kwa wakati husika.
MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, mbali na hayo masomo yaliyokwishafundishwa kuna somo la TEHAMA ambalo sasa hivi linafundishwa katika shule mbalimbali lakini kuna baadhi ya walimu katika shule za msingi hawana ujuzi wa kutumia kompyuta. Je, Serikali ina mpango gani ya kuwapa mafunzo walimu hao ili tuendane na wakati huu wa utandawazi na digitali?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa walimu wanafanya kazi zao vizuri na tunastahili kuwapa motisha. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapa ile Teaching Allowance kama walivyowapa Wakuu wa Shule pamoja na Waratibu ili nao waweze kuipenda kazi yao na kupata morali ya kufundisha?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nuru Awadh, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la kuwajengea walimu uwezo katika masuala ya TEHAMA, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa TEHAMA ni kati ya maeneo mapya ambayo lazima walimu wote wajengewe uwezo kwa sababu katika enzi tulizopo sasa TEHAMA ni moja ya vitu muhimu katika elimu. Kwa hiyo, katika mipango ya Serikali TEHAMA ni moja kati ya maeneo muhimu ambayo walimu watajengewa uwezo na hili litafanyika kulingana na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la motisha, naomba nimjibu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kuboresha maslahi ya walimu kadiri ya uwezo utakavyoruhusu. Siku za mbele hata masuala ya motisha ni moja kati ya masuala ambayo yanaweza yakaangaliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu mimi ni Naibu Waziri wa Elimu, naomba nitumie fursa hii vilevile kuwatakia kila la kheri vijana wetu 91,440 wa Kidato cha Sita na wale 12,540 wa Vyuo vya Ualimu ambao leo wanafanya mitihani yao ya mwisho. Hata hivyo, nitoe rai kwao kwamba wafuate sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza mitihani na kamwe wasije wakajihusisha na vitendo vya wizi na udanganyifu katika mitihani.
MHE. OTHMAN OMAR HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, hadi natuma swali hili Mei 8, 2017, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ilikuwa inadaiwa na TANAPA zaidi ya shilingi bilioni 3 za Tanzania. Je, deni hili limeshalipwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Wizara kupitia Shirika lake la AICC inamiliki majengo ya kutosha pale Mjini Arusha ambapo ingetumia majengo yale ingewezesha mahakama hii kufanya shughuli zake kwa ufanisi mkubwa sana. Je, Mheshimiwa Waziri haoni upo umuhimu kuhamisha mahakama hii huko inakokodi na kuipeleka katika majengo haya ya AICC ili kuokoa matumizi yasiyokuwa ya lazima?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Othman Haji, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba TANAPA inadai fedha ya pango kwa ajili ya ofisi za Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu lakini taratibu zinaendelea ili ziweze kulipwa. Hata hivyo, naomba nimueleweshe Mheshimiwa Mbunge kwamba siyo mahakama ndiyo inadai Serikali bali ni Serikali na Serikali. Kwa hiyo, ni suala la kawaida, pesa hiyo italipwa muda ukifika na kama nilivyosema mchakato unaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la pili kwamba kwa nini majengo ya AICC yasitumike kama ofisi za mahakama hiyo. Naomba nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari Serikali imetafuta hekari 20 Arusha kwa ajili ya kujenga ofisi za mahakama hiyo na taratibu za ujenzi zimefika mbali sana. Kwa hiyo, tunategemea baada ya muda mfupi ofisi hizo zitajengwa na hakutakuwa na haja ya kwenda kubanana kwenye Ofisi ya AICC. Hata kama mahakama hiyo ingeenda kwenye majengo ya AICC labda suala lile lile la kudaiwa na TANAPA lingeweza kujirudia. Kwa hiyo, tunachotaka kufanya ni kujenga ofisi ambazo zitatosha na changamoto hii haitatokea tena.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo hili la wanadiplomasia kutolipa kodi za pango halipo tu Arusha lakini pia lipo kwenye baadhi ya Balozi. Kwa mfano, Ubalozi wa Palestina nchini umepanga katika jengo linalomilikiwa na Halmashauri ya Temeke toka mwaka 2003 na mpaka leo hawajawahi kulipa kodi hata shilingi moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri imejaribu kufuata hatua mbalimbali za kudai ikiwa ni pamoja na kuripoti ofisi ya Wizara ya Mambo ya Nje lakini hakuna lolote lililofanyika. Tunahofia kuwaondoa kinguvu kwa sababu ya kulinda hiyo image ya ushirikiano wetu. Je, Mheshimiwa Waziri upo tayari leo kuwapa notice Ubalozi wa Palestina kwamba ndani ya miezi mitatu kuanzia leo wahame katika jengo hilo huku Halmashauri ikiendelea na taratibu nyingine za kudai deni lao?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mtolea, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba kuna utaratibu wa kidiplomasia wa kudaiana kati ya Serikali na Serikali na kwa vyovyote haiwezi ikawa kwa kupitia matamko ya Bungeni. Kwa hiyo, naomba tu nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba hili suala linafanyiwa kazi. Madeni yapo kila mahali, ni kawaida, awe na subira, nina hakika Serikali italifanyia kazi na changamoto hii itaondoka.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Wizara ya Mambo ya Nje imekuwa na madeni mengi hasa kwenye Balozi za nje ambazo Mabalozi wetu wanaishi na ni tabia ambayo inatuletea image mbaya kama taifa. Je, ni lini Serikali italipa hayo madeni ya pango za nyumba za Mabalozi wetu katika nchi mbalimbali za dunia hii tuliyopo sasa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwakagenda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge hili katika bajeti zake za miaka ya hivi karibuni limekuwa likitenga fedha mara kwa mara kwa ajili ya kulipa madeni hayo. Kwa hiyo, naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ni kweli madeni yapo na kila wakati madeni ni sehemu ya maisha lakini Serikali itaendelea kulipa kadiri uwezo unavyopatikana. Hata hivyo, mkakati mkubwa wa Serikali sasa ni kuzuia madeni mengine kutokea kwa kulipa madeni kwa wakati. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie kwamba suala hili litafanyiwa kazi.
MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Katika swali hili Serikali imeeleza inalipa Dola za Marekani 38,000 kwa mwezi ambazo ukipiga kwa mwaka ni takribani shilingi bilioni 1 na Serikali imeanza kulipa kuanzia 2008, kwa hiyo, ni takribani shilingi bilioni 9 kama all facts are being equal zimelipwa. Wizara hii ina experience kwenye ujenzi wa hosteli za chuo kikuu pale walisema block moja iligharimu shilingi milioni 500, ukigawanya kwa wastani wa hizo shilingi bilioni 9 kwa kipindi hiki kungeweza kujengwa maghorofa kati ya 18 mpaka 20.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hali kama hii, ni kwa nini Serikali imeachia hali ikae muda mrefu na ni lini hasa ujenzi huu utafanyika ili pesa zisiendelee kutumika kwa kiwango kikubwa namna hii kwenye kulipa kodi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba gharama hizo ni kubwa, hata hivyo, ujenzi wa majengo ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu ni suala la kimkataba na wala haliamuliwi na Serikali peke yake, inabidi kukaa kukubaliana, michoro. Kwa hiyo, ni suala ambalo sio sisi wenyewe, ingekuwa ni kawaida kwamba ni la kwetu tungeshajenga lakini kama nilivyoliarifu Bunge lako Tukufu, tayari hatua za ujenzi zimefika mbali. Tumeshapata eka 20, michoro tayari, kwa hiyo muda wowote jengo hilo litajengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba avute subira sanasana ucheleweshwaji umetokea kwa sababu majadiliano yanaendelea kuhusu namna gani jengo hilo lijengwe kwa sababu sio letu peke yetu lazima tuongee na Mahakama ya Afrika pamoja na Umoja wa Afrika.
MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Ni kwa bahati mbaya tu kwamba Serikali inatoa majibu na takwimu ambazo haziakisi ukweli. Katika jibu la Mheshimiwa Waziri, hizi takwimu alizozitoa pia nazo haziakisi ukweli kwa sababu ukikokotoa kiasi cha takwimu anazozitoa na ukilinganisha uhitaji ulivyo inaweza kukupa jibu ya kwamba elimu yetu inaporomoka badala ya kukua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, anaposema Serikali imetoa shilingi bilioni 56.05 katika shule 588, kati ya shule 17,174 maana yake wamehudumia shule 3% tu. Sasa ukiangalia kama hapo takwimu hii inakwamba elimu inakua ama inaporomoka.

Mheshimiwa Naibu Spika, shule zetu zina hali mbaya sana na nina mfano halisi ambao uko mita 1,000 kutoka majengo ya Bunge, Shule ya Msingi Medeli, hii shule haina vi…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Lucy, naomba uulize swali tafadhali. Naomba uulize maswali yako.

MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Naibu Spika, hili suala ni sensitive kidogo, tafadhali naomba takwimu kidogo.

NAIBU SPIKA: Aaah, sasa siwezi kukupa dakika zako. Swali lako peke yake ni dakika sita. Sasa ukitumia dakika mbili kwenye swali moja la nyongeza maana yake muda wako umekwisha tayari, ndiyo maana nakukumbusha uulize swali.

MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Naibu Spika, basi katika takwimu hizo ambazo unaziona kwamba 3% tu ndiyo imehudumiwa: Je, mazingira haya duni ambayo yanazikabili shule zetu, elimu itakuwa inakua ama inaporomoka?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Madai ya walimu ni moja kati ya mwarobaini muhimu sana wa kutanzua kuporomoka kwa elimu ya Tanzania. Katika hili naomba nimwombee dua njema mdogo wangu Mwalimu Hilda Galda John Bura aliyefariki tarehe 05 na tukamzika ambaye naye amefariki akiwa anaidai Serikali madai haya haya ya walimu. Je, kwa takwimu hizi za shilingi bilioni 15.07 alizotoa Mheshimiwa Waziri, ni asilimia ngapi ya madai yote ya waalimu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu takwimu ninazozitoa kwamba haziakisi hali halisi, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba takwimu hizo nilizotoa ndiyo takwimu rasmi. Pia shule ambazo tumeweza kujenga na kuboresha miundombinu ni katika kipindi fulani. Nimeweza kuainisha kwamba ni kutoka mwaka 2017 mpaka sasa, haimaanishi kwamba huko nyuma hakukuwa na kitu ambacho kimefanyika, lakini haimaanishi kwamba siku za usoni hatutafanya kitu kingine. Kwa hiyo, shule 588 katika kipindi cha miaka mitatu siyo kitu kidogo. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie tu kwamba Serikali itaendelea kuboresha miundombinu kadiri ya upatikanaji wa fedha utakaporuhusu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuhusu malimbikizo ya madeni ya walimu naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali ya Awamu ya Tano imejitahidi kwa kiasi kikubwa kupunguza madeni hayo. Kwa sasa tunachojaribu kufanya ni kuhakikisha kwamba madeni mapya hayatokei. Tunalipa stahiki za walimu pale zinapohitajika.

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri. Nimesimama hapa kuweka msisitizo kwamba Serikali inafanya kazi vizuri sana katika kuhakikisha kwamba inaboresha Sekta ya Elimu. Hii takwimu ambayo imetolewa hapa ni mfano wa Mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo. Haijajumuisha shilingi bilioni 29 ambazo Ofisi ya Rais, TAMISEMI ilizitoa kwa ajili ya kukamilisha maboma; haijajumuisha shughuli ambazo Halmashauri zetu katika bajeti zao zinatenga.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Lucy Magereli kwamba Serikali iko vizuri, mwenye macho haambiwi tazama. Ukienda unaona hata shule kongwe zilivyoboreshwa, zinapendeza, zilikuwa majengo mabovu. Kwa hiyo, watupe muda, Serikali tutaendelea kufanya kazi yetu vizuri.
MHE. DKT. SULEIMAN ALLY YUSSUF: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana jambo la kwanza nataka nimwambie Mheshimiwa Naibu Waziri nimerekebisha waliodhurumiwa katika haki za Binadamu. Na ningeweza kujibu sana lakini sio wakati wake. Maswali yangu mawili, kituo cha haki za binadamu LHRC Tanzania huwa kinaweka wazi matukio yote makubwa ambayo yanayotokea nchini yakiwemo utekwaji, uteswaji, upoteaji, upigwaji risasi, kuonyesha bastola hadharani….

MWENYEKITI: Uliza swali sasa.

MHE. DKT. SULEIMAN ALLY YUSSUF: Ubambikizwaji…

MWENYEKITI: Uliza swali sasa

MHE. DKT. SULEIMAN ALLY YUSSUF: Ripoti za Serikali hazibebi mambo mazito kama haya.

Swali la pili, nataka kujua ni challenge zipi ambazo serikali inazipata inapokwenda kutoa ripoti zake katika vikao vya kimataifa huku kukiwepo na ripoti mbadala za ndani zinazo kinzana na ripoti za Serikali?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, ni kweli Legal Human Right Center mara nyingi hutoa ripoti yenyewe inavyoona kuwa mambo ya haki za binadamu yamekuwa yakiendelea nchini, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba sheria zetu zina ruhusu na inatoa uhuru wa maoni sio Legal Human Right Center hata watu binafsi mashirika mengine sio ya kiserikali kwa hiyo wanaongea mengi. Lakini katiba na sheria zetu zimetambua hasa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwamba ndio imepewa jukumu la kikatiba la kuhakikisha kwamba haki za binadamu zina heshimiwa na ndio imepewa fursa ya kusikiliza malalamiko mbalimbali. kwa hiyo, yoyote yule mwenye malalamiko na manunguniko kuhusiana na uvunjifu wa haki za binadamu pamoja na ufunjivu wa taratibu za utawala bora waweze upeleka kwenye Tume kama inavyotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ni changamoto gani tunapata huko tunapoenda nje kuhusiana na haki ya haki za binadamu, naomba nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba changamoto kubwa kuliko zote ni uposhwaji mkubwa sana unaofanywa na sio tu taasisi mbalimbali lakini vilevile mtu mmoja mmoja ikiwa na baadhi na wanasiasa. Lakini kama anavyofahamu hivi karibuni Serikali imeamua kuchukua hatua kuhakikisha kwamba kila upotoshwaji unaotolewa unajibiwa pale unapotolewa kwa sababu mara nyingi ni kwa ajili ya kuchafua sifa njema ya Taifa letu.
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru, wanafunzi wengi waliokuwa wanasoma shule binafsi wamekuwa wakinyimwa mikopo ya elimu ya juu kwa kigezo kuwa wazazi wao wana uwezo wa kuwalipia. Je, ni kwa nini sasa Serikali isifute kigezo hicho kwa sababu si wanafunzi wote wanaosoma binafsi wana uwezo, lakini wengine wamekuwa wakienda binafsi kwa kukosa nafasi katika shule za umma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Halima Bulembo ni kati ya Wabunge wanaowakilisha vijana Bungeni na hakika na hili sidhani kama ni la mjadala, amejitahidi sana katika miaka hii muhimu kufanya kazi yake vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina hakika vijana wenyewe wanamfuatilia na hata anapouliza swali hili sasa la leo, ni katika jitihada hizo za kuwakilisha vijana katika Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sheria yetu inayotuongoza kwenye mikopo haibagui watoto wanaosoma kwenye shule binafsi. Sheria inataka tu tutumie vigezo vile vya kuangalia uwezo wa mtu kujilipia masomo ya chuo kikuu. Kwa hiyo, kinachofanyika ni kwamba, waombaji wote tunawafanyia kitu kinaitwa minutes testing, wanajaza fomu, tunangalia taarifa na kuangalia kama wanaweza wakajifadhili. Kwa hiyo, mtu anaweza akawa amesoma kwenye shule binafsi, lakini kumbe amefadhiliwa, tunachoomba, kama mtu amefadhiliwa, alete ushahidi, alete kiambatisho wakati anajaza fomu.

Mheshimiwa Spika, mwaka huu, kuna wanafunzi 500 ambao wamesoma shule binafsi, wengine wamesoma mpaka Feza School, lakini kwa sababu wameleta uthibitisho wa kwamba wamesomesha na wazazi wao hawana uwezo, tunawasomesha. Kwa hiyo, naomba niendelee kutoa rai na ufahamu kwamba, kusoma kwenye shule binafsi siyo kigezo cha kukosa mkopo! Tunaaangalia uwezo, inawezekana mtu amesoma lakini kafadhaliwa.

Mheshimiwa Spika, naomba vilevile ifahamike kwamba, tuna rasilimali kidogo na tuna wahitaji wengi, ndiyo maana, kama tukipata fursa ya kutoa mikopo, tutatoa kwanza kwa wale ambao hali zao ni mbaya zaidi, kabla hatujatoa kwa wengine kwa sababu tunataka tulete ulinganisho katika elimu. Tunafanya kitu kinachoitwa equity, kwa hiyo, hakuna upendeleo, ni sheria ambayo imetungwa na Bunge hili, ndiyo inatuelekeza.

Mheshimiwa Spika, na katika miaka hii tumefanikiwa kuendelea kuongeza wigo wa wanafunzi wengi kupata mikopo na ndiyo maana mwaka huu tumeweza kuongeza kutoka wanafunzi 41,000 wa mwaka wa kwanza, hadi kufikia wanafunzi 45,000. Nina hakika tutaendelea kuboresha taratibu hizo za kutoa mikopo na ikiwezekana huko mbele ya safari, kadri uwezo utakavyoruhusi, inawezekana hata kila mtu yeyote anayetaka mkopo akapata. Isipokuwa tunapenda kuendelea kusisitiza kwamba ule ni mkopo. Kwa hiyo, kama mzazi ana uwezo wa kumsomesha mwanaye, asitafute mikopo kwa sababu baadaye atawajibika kulipa.
MHE. SUSAN A. LYIMO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, pamoja na majibu ya Serikali, kilio kikubwa cha wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu ni pamoja na tozo ya asilimia moja kwa ajili ya administrative costs za bodi. Nilitaka kujua, Serikali haioni kwamba huku ni kuwaibia wanafunzi? Kwa sababu tunajua tuna bodi nyingi ambazo hazitegemei makato ama ya watumishi au ya wafanyakazi wake, ni kwa nini Bodi ya Mikopo unawatoza wanufaika asilimia moja kwa ajili ya administrative costs za bodi!
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba, Serikali inatoza tozo ya asilimia moja kama management costs kwa ajili ya mkopo unaotolewa kwa wanafunzi wa elimu ya juu, lakini ifahamike kwamba, kazi ya kuweza kufuatilia na kutoa mikopo ile ina gharama kubwa na ni kawaida katika utoaji wa mikopo, kwamba mkopo ule vilevile uweze kugharamia uendeshaji wake, vinginevyo inahitaji utafute fedha za ziada ili kuendesha ule mkopo.

Mheshimiwa Spika, asilimia moja anayosema Mheshimiwa Mbunge, inatozwa mara moja, haitozwi kwa mwaka. Kwa hiyo, ni one off payment na ukiangalia, ukilinganisha sisi tunachotoza na nchi zingine, sisi tunatoza asilimia ndogo sana, hata kwenye tozo zingine kwa ujumla wake. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hii ni muhimu kwa ajili ya kuhakikisha kwamba utoaji wa mkopo unafanyika kwa ufasaha zaidi.

Mheshimiwa Spika, na nimhakikishie tu kwamba, asilimia hiyo moja, imetuwezesha katika hii miaka minne kuongeza marejesho ya mikopo kutoka shilingi bilioni 23 toka mwaka 2015/2016 mpaka sasa kufikia bilioni 183 mwaka huu. Ile fedha inatusaidia kufuatilia kwa sababu watu ambao hawataki kutoa ni wengi, ina gharama. Kwa hiyo, naomba ajue tu kwamba lengo letu siyo kuwaumiza wanafunzi wala wazazi lakini ni kuhakikisha kwamba mikopo ile inarejeshwa na inatolewa kwa utaratibu ambao ni mzuri na yeye mwenyewe ni shahidi, yeye mwenyewe ameshatusifu mara nyingi kwamba tumefanikiwa sana kwenye elimu ya mikopo ya elimu ya juu.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi. Ukosefu wa Ofisi za Bodi ya Mikopo kwa upande wa Zanzibar umekuwa ukileta usumbufu mkubwa sana kwa wazazi na wanafunzi kusafiri kuja Dar es Salaam kwa ajili ya huduma hizo.

Mheshimiwa Spika, ukizingatia hali duni ya wazazi, ni lini Serikali itasogeza huduma hizo kwa upande wa Zanzibar. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kumekuwepo na changamoto hiyo ya ofisi kutoka Zanzibar, lakini naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwamba tayari kuna jitihada za kuhakikisha kwamba ofisi inakuwepo Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, pia, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, pamoja na ofisi kutokuwepo, bodi ya mikopo imeendelea kurahisisha namna ya kuomba mikopo na kurejesha, kiasi kwamba unaweza ukafanya maombi na kurejesha popote ulipo kwa sababu siku hizi kuna teknolojia, lakini naomba vilevile nimhakikishie kwamba bado kuna jitihada za kuhakikisha Zanzibar nayo inakuwa na ofisi.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kwa kuwa Sera ya Elimu ni kuwa na VETA katika kila Wilaya na kwa kuwa Wilaya ya Karatu tumeshaonesha mfano huo wa kuwa na VETA kupitia Wafadhili wetu na ni ukweli kwamba kutokana na mapato ya ndani ya halmashauri siyo rahisi kukiendesha Chuo hiki Je, Serikali sasa iko tayari kukichukua Chuo hiki na kukiendesha?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kwa kuwa Wafadhili hao mpaka sasa wanaendelea kutoa fedha za uendeshaji na wanaendelea kujenga baadhi ya miundombinu, na kwa kuwa wanaweza kukoma wakati wowote Je, Serikali sasa kupitia Wizara iko tayari katika Bajeti ya mwaka unaokuja 2020/2021 kutenga fedha kwa ajili ya uendeshaji wa Chuo hiki?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama anavyosema Mheshimiwa Mbunge kwamba inawezekana kabisa kwamba katika mazingira ambayo halmashauri au basi Mamlaka ya Serikali za Mitaa inashindwa kuendesha VETA kuna uwezekano mkubwa wa halmashauri hiyo kuweza kuipa VETA na VETA ikaweza ikabeba majukumu yote ya uendeshaji pamoja na gharama zote ambazo zinahusika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ushauri wangu ni kwamba kama Halmashauri ya Karatu inaona kwamba kwa sasa haiwezi kuendesha Chuo hiko kikamilifu na kutimiza malengo yake kinaweza kikaomba VETA iweze kuimiliki na hivyo kuiendesha moja kwa moja na kuondoa changamoto ambazo wanazipata.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kuhusu kwamba kama inawezekana fedha zikatengwa katika Bajeti inayokuja kwa ajili ya Chuo hiko baada ya wafadhili kuanza kushindwa kumalizia. Ushauri wangu ni kwamba ni vigumu kwa sasa VETA au Wizara kuipangia fedha kwa sababu inachukuliwa kwamba bado ni Chuo cha Serikali za Mitaa katika maana kwamba bado ni Chuo cha halmashauri kwa hiyo wakitaka fedha zitengwe na Serikali Kuu ni lazima kwanza waanze utaratibu ule wa kuipeleka VETA.
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante majibu ya Waziri ni kama vile ya kukopi na ku-paste sasa nimeuliza swali kama Mbunge wa Halmashauri ya Mlimba pamoja na kuwa kuna halmashauri nyingine zimeshaanza kupata hizo hela na zinajengwa lakini kila mtu analia na pale panapo mbana. Sasa Halmashauri ya Mlimba yaani kwa miaka mitatu mfululizo wanafunzi waliomaliza Kidato cha Nne takribani milioni nne laki nane na themanini na saba wako mtaani ukiachilia mbali wa darasa la saba. Sasa na pale Mlimba katika Kituo cha Mpanga Utengule kuna majengo kabisa yapo kwa hiyo Serikali haiwezi kuwa na gharama kubwa kwenda kujenga majengo mengi.

Je, kwa nini Serikali isiende kwenye Kituo hiko cha Mpanga kwenda kukiboresha ili wanafunzi hao wanaozagaa mtaani waanze pale baada ya kujenga majengo makubwa hayo tunayosubiri kwa miaka mingi na watoto wanazidi kupotelea mtaani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuboresha hizo Shule za Sekondari au za Msingi kuwepo na Kitengo cha Ufundi ili hawa wanafunzi hata kama wakifeli kuingia darasa la juu wawe tayari wamepata miundombinu ya kiufundi katika maeneo haya katika Shule zote Tanzania? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kuhusu kama jibu langu ni la kukata na kupaka yaani cut and paste naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hata swali ambalo ameniuliza nalo siyo jipya sana linaulizwa mara nyingi kwa hiyo majibu yanakuwa ni yale yale siyo kwamba lenyewe ndiyo limeanza kuulizwa leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo kuhusiana kama inawezekana Serikali kutoa fedha ili kuendeleza Kituo ambacho tayari kipo ili kiwe Chuo cha VETA naomba tu nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kama kuna Taasisi ambayo tayari inatumika na inaonekana inafaa kuwa VETA bila kuvunja matumizi au kuondoa matumizi ya sasa Serikali iko tayari kufikiria lakini ni baada vilevile ya kufanya tathmini ya kuhakikisha kuwa inafaa kwa ajili ya kuachwa Chuo cha VETA.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake kuhusu Serikali kuboresha au kuanzisha mafunzo ya Ufundi katika Shule zote naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari kuna Mpango madhubuti wa kuboresha baadhi ya Shule zetu za Ufundi lakini kwa sasa jitihada kubwa tunaweka katika kuanzisha Vyuo vya VETA kila Wilaya kuliko kila Shule ya Sekondari kuwa Shule ya Ufundi kwa sababu vilevile ina mahitaji makubwa hasa ikichukuliwa kwamba tunahitaji kuwa na Walimu wa kutosha.
MHE. SUSAN A. LYIMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na niseme tu kwamba majibu ya Waziri hayajaniridhisha hata kidogo kwa sababu swali langu lilihoji matatizo makubwa yaliyopo lakini na kama tuna haja ya kuleta Sheria ndani Bunge lakini bado hajajibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili ya nyongeza, ukiangalia hata jibu lake ni kweli kwamba bado kuna tatizo kubwa ndiyo sababu wanasema wanaendelea kuboresha, lakini baada ya nyongeza ya asilimia 15 takwimu zinaonyesha toka mwaka 1994 wakati Bodi ya Mikopo imeanzishwa au Sheria hii imeanzishwa kati ya Wanufaika takribani 500,000 ni wanufaika 11,000 tu wameweza kurejesha Mikopo mpaka mwaka jana kwa maana ya kwamba ni asilimia 2.3 tu na hapo bado Sheria ilikuwa haijaongezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa swali langu, Waziri au Serikali haioni kwamba nyongeza hii kubwa ya makato yatapelekea sasa Wanafunzi badala ya kulipa ndani ya miaka 4 au 10 ambayo anasema Mheshimiwa Naibu Waziri sasa hivi itaenda mpaka miaka 30 kiasi kwamba wanafunzi hawa wanufaika watakuwa ama wameshafariki au wamestaafu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Serikali za Wanafunzi zimekuwa ndiyo daraja kati ya Serikali na Serikali Kuu kwa maana ya Wizara pamoja na wanafunzi wenyewe na kwa muda mrefu na mimi kama Mshauri wa Wanafunzi nilivyokuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Viongozi hawa wa Wanafunzi wamekuwa wakipata madhara makubwa sana ikiwa ni pamoja na kufukuzwa wakati wanadai madai ya Wanafunzi kwa sababu wote tunajua kwamba Wanafunzi wa Elimu ya Juu wanahitaji Mikopo. (Makofi)

SPIKA: Tatizo unahutubia sasa Mheshimiwa Susan.

MHE. SUSAN A. LYIMO: Mheshimiwa Spika, nilitaka nimalizie.

SPIKA: Eeh malizia kwa kuuliza swali.

MHE. SUSAN A. LYIMO: Mheshimiwa Spika, wanahitaji mikopo kwa ajili ya kusoma lakini Wanafunzi hao wanakaa zaidi mwezi mmoja bila kupata Mikopo hii, wanapodai wanafukuzwa wakati matatizo makubwa ni kwa Wizara yenyewe pamoja na Vyuo kutopeleka majina.

SPIKA: Basi sasa inatosha. (Makofi)

Mheshimiwa ...

MHE. SUSAN A. LYIMO: Mheshimiwa Spika, sasa nilitaka kujua…

SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri majibu na Profesa alitaka aongezee anasema matatizo ni wewe mwenyewe Wizara. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Waziri majibu tafadhali.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, kuhusu kwamba inachukua muda mrefu sana kwa Wanafunzi hao wanaodaiwa Mikopo kurejesha Mikopo uzoefu wetu Wizarani unaonyesha kwamba tatizo halipo kwa sababu ya value retention fee ipo kwa sababu ya watu kutotaka kurejesha Mkopo.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2015 tulipoingia Madarakani urejeshwaji ulikuwa ni shilingi bilioni 23 kwa mwaka lakini baada ya kuweka jitihada napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba mwaka huu tunategemea urejeshwaji utakuwa shilingi bilioni 200 kwa mwaka, mwaka jana ilikuwa bilioni 183.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, shida haipo katika fedha ile, tozo ya kulinda thamani ipo katika watu wenyewe kuhamasika kurejesha Mkopo. Kwa hiyo, kwa sababu tumeweka jitihada kubwa katika urejeshwaji wa Mkopo tumeanza kuona kwamba warejeshwaji wengi wanaanza kurejesha.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kuhusu kama tuna mpango wa kuleta Marekebisho ya Sheria uzoefu wetu unatuonyesha kwamba Sheria ya sasa na hasa kama ilivyorekebishwa na Bunge hili mwaka 2016 bado inakidhi mahitaji ya utoaji wa Mikopo nchini, lakini pia kama Mheshimiwa Mbunge anaona kwamba kuna haja ya kuleta Marekebisho ya Sheria hiyo ndiyo kazi ya Bunge. Lakini angalau sisi kama Serikali tunaridhika na Sheria ya sasa haijatupa shida yoyote tunachoendelea kusema tu ni kwamba wale waliokopeshwa warejeshe Mikopo kwa sababu usiporejesha kwa wakati ndiyo deni lile linaongezeka na inakuwa ni vigumu kulipa.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili la kuhusu Serikali za Wanafunzi, nafurahi sana kwamba nimesikia swali hili kutoka kwake kwa sababu ni kweli kwamba Mheshimiwa Susan Lyimo kwa muda mrefu alikuwa ni anafanya kazi kwenye Ofisi ya Mshauri wa Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kipindi kile ambacho migomo ilikuwa ni mingi sana. Lakini tunachosema ni kwamba kilichotokea hivi karibuni katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ilikuwa ni kuturudisha nyuma, tulishaondoka kule hatupo tena kwenye enzi ya kuanza kuvutana na Wanafunzi kuhusiana na Mikopo.

Mheshimiwa Spika, Mikopo siku hizi, fedha za Mikopo zinatolewa na Serikali angalau miezi miwili kabla ya Vyuo kufunguliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kinachotokea hili ninaweza nikawahakikishia kwa sababu niko Wizarani kwa zaidi ya miaka miwili, na tena Mheshimiwa Rais mwenyewe anafuatilia kila, tatizo sasa hivi siyo fedha hazitoki Serikalini inakuwa ni changamoto ya michakato ya ndani ya Vyuo na hata kilichotokea kwenye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ilikuwa ni sehemu ndogo sana ya wanafunzi ambao bado taarifa zao zilikuwa hazijakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, hatutakaa tukubali wanafunzi ambao sisi ndiyo tunawapa Mikopo kama Serikali kuitishia Serikali kwamba msipotoa fedha katika masaa sabini na mbili wataandamana. Sio tu kwamba inapingana na Sheria na taratibu za kuendesha Vyuo Vikuu lakini hata katika maadili ya kawaida ya Kitanzania mtoto hawezi kumpa mzazi ultimatum kwamba Baba usipoleta karo nakuja nyumbani na utaniona, kwa hiyo, tunaendelea kuwachukua hatua kwa mujibu wa Sheria zilizopo. (Makofi)

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niongezee majibu mazuri ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri ameyasema, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Susan Lyimo Waziri mwenzangu wa Elimu yeye akiwa ni Waziri Kivuli na swali lake kuhusiana na Serikali za Wanafunzi.

Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii kuwahakikishia Bunge lako Tukufu kwamba Serikali inatambua na kuthamini mchango wa Serikali za Wanafunzi na inatambua kwamba Serikali za Wanafunzi ni daraja muhimu kati ya Wanafunzi na Uongozi wa Chuo lakini pia kati ya Wanafunzi na Serikali kwa ujumla pale ambapo kunakuwa na changamoto za Wanafunzi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ningeomba tu hizi Serikali za Wanafunzi ambazo tunazitambua na kuthamini michango yao watumie njia ambazo ni taratibu zinazotambulika katika kuwasilisha changamoto zao.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la kuchelewesha ulipaji wa fedha kwa ajili ya Wanafunzi, nirudie kusema jambo ambalo Mheshimiwa Naibu wangu amelisema Serikali imekuwa ikitoa fedha miezi miwili kabla ya Chuo kufunguliwa.

Mheshimiwa Spika, kinachotokea na kilichotokea mwaka huu kwa baadhi ya Wanafunzi wapo Wanafunzi ambao anasaini fedha yake ya kutumia ile boom ya chakula na malazi lakini anakuwa hasaini kwenye sehemu ya ada za Chuo kwa sababu ile hela haiendi kwake.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kilichofanyika Vyuo vimeangalia kuna Wanafunzi ambao walikuwa wamefika mwaka wa tatu lakini alikuwa hajasaini fedha ya malipo ya Chuo kwa mwaka wa pili na kwa mwaka wa kwanza na kinachotokea asiposaini zile hela Bodi ya Mikopo inazirejesha kwa hiyo, Wanafunzi walikuwa ni wanufaika wa Bodi ya Mikopo lakini walikuwa wanaonekana wanadaiwa kwa sababu hawakuwa wamesaini.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba nichukue nafasi hii kuwasihi Wanafunzi kuhakikisha wanakamilisha taratibu zote ambazo zimewekwa ili waweze kupata fedha zao kwa wakati kwa sababu fedha za Mikopo zipo na Serikali hii inakuwa inazitoa kwa wakati. (Makofi)
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nianze kwanza kumpongeza Rais wetu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kutoa elimu bure ambayo imewezesha kila mtoto sasa atoke akasome na hakuna dadalea tena nyumbani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la msingi nimesisitiza elimu ya msingi kuwezesha wanafunzi kwenda kufanya kazi zao baada ya masomo kwa wale ambao hawataendelea. Naomba kuuliza maswali kwa Serikali, la kwanza, kwa kuwa wanafunzi hao tunaowaona barabarani na nyie mkiwa mashahidi wanatoka nyumbani alfajiri saa kumi na moja na kurudi nyumbani saa kumi na mbili hoi bin taabani, kwa maana muda mwingi wako shuleni na shuleni ndiko wanakoweza kufundishwa, kwa nini sasa katika elimu ya msingi walimu wasiwe na mtaala ambao watafufua zile bustani ndogondogo toka wakiwa wadogo wawe na interest ya kilimo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kipindi cha nyuma tulikuwepo na sekondari za mchepuo, tulikuwa na sekondari ya mchepuo wa kilimo, mchepuo wa biashara, mchepuo wa sayansikimu na kadhalika. Baada ya hayo yaliyotokea hapo katikati na michepuo ile kufutia, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kurejesha tena aina ile ya mitaala ili mwanafunzi akitoka pale pamoja na kulelewa nyumbani na wazazi, kulelewa shuleni, lakini taifa ka kesho liwe bora kama nyie mlio hapa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Shally Raymond, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na umuhimu wa Serikali kurejesha bustani mashuleni, naomba nimhakikishe Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sehemu kubwa wanafunzi bado wanapata fursa za kujifunza kilimo kidogo kidogo hasa maeneo ya vijijini lakini changamoto wote tunafahamu ni maeneo ya mjini ambapo ardhi ni changamoto kubwa. Ndiyo maana tunaendelea kusisitiza kwamba jamii, familia waisaidie Serikali nao waweze vilevile kutoa stadi hizo kwa vijana, kwa sababu lazima tuseme pia kwamba maisha ya kisasa yanahusika kwa kiasi kikubwa katika kuondoa ari na hamasa ya vijana kujihusisha na vitu kama hivyo. Wazazi wengi wanapenda watoto wao wakacheze na play station, kuangalia TV, video games kuliko kujifunza stadi za maisha. Ndiyo maana tunasema, ndiyo Serikali itaendelea siyo tu kuboresha mitaala lakini kuweka mazingira wezeshi ili wanafunzi waweze kupata hizo stadi za kazi lakini kama nilivyosema ni jukumu letu wote. Kwa hiyo, tunomba tusaidie ili tuweze kufanikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na kubadilisha mitaala ili turudi nyuma, naomba nichukue mawazo yake, siyo baya tutaendelea kuboresha mitaala yetu ili iweze kutoa elimu bora na yenye manufaa kwenye vijana wetu. (Makofi)
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kunipa nafasi ili niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, takribani watoto 115 waliomaliza darasa la saba mwaka jana na kufanya mtihani kutoka Jimbo la Ngara katika Shule ya Msingi Kumnazi walifutiwa mtihani na wazazi wa watoto hao kwa umoja wao walimwandikia Katibu Mkuu Baraza la Mitihani barua ya tarehe 10 Desemba lakini mpaka sasa hivi hawajapata majibu. Watoto na wazazi wamechanganyikiwa ukizingatia ni watoto yatima na wengi wao ni watoto wa maskini. Nini kauli ya Serikali kuhusu suala hili?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwanza swali hili halina uhusiano na swali la msingi ambalo nilikuwa najibu lakini naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Gashaza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu barua ambao wazazi wale wameandika kwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Mtihani, naomba nifuatilie nijue barua hiyo majibu yake yanatoka lini. Hata hivyo, ifahamike tu kwa umma na kwa Waheshimiwa Wabunge kwamba ni kosa kujihusisha na uhalifu wa mitihani. Kwa hiyo, pale mtuhumiwa atapobainika kwamba kweli amehusika hatua stahiki zinachukuliwa na hatua hizo inakuwa ni pamoja na kumfutia mtihani na matokeo. Kwa hiyo, ifahamike tu kwamba kwa kweli ni kosa lakini nitaenda kufuatilia halafu nitampa jibu.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii. Nashukuru sana kwa majibu mazuri, ya kina na yenye maelezo ya kutosha na kwa kiasi kikubwa suala langu limepata ufafanuzi kwa swali la aliyeuliza kabla yangu lakini nitakuwa na maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti baadhi ya utawala wa shule ambao huwa unawazuia watoto wenye uwezo mdogo au uwezo wastani kufanya mitihani yao ya mwisho na kuwalazimisha waende wakajiandikishe kama private candidates kwenye vituo vingine wakati wakijua kufanya hivyo ni kuwapunguzia moral na kuwavuruga kiasi kwamba wanawazidishia kutofanya vizuri lakini pia ni kuwabagua watoto hawa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni kwa kiasi gani Serikali imejipanga kushirikiana na wazazi na walezi kuona kwamba Kamati za Ahule zinasaidia kupunguza kadhia hii kwa watoto hao wenye uwezo pungufu katika masomo yao? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Asha Abdulla Juma kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaeleze Waheshimiwa Wabunge pamoja na Watazania kwa ujumla kwamba ni kosa kumbagua mtoto yeyote kwa sababu yoyote. Wote ni watoto wa Kitanzania na tena Serikali inatoa msisitizo zaidi kwa wale ambao wana changamoto mbalimbali za ujifunzaji. Kwa hiyo, ikibainika kwamba kuna mwalimu au kiongozi yeyote wa elimu ambaye anawabagua watoto wenye changamoto ya uzito katika kujifunza kwa kweli ni kosa na atachukuliwa hatua za kisheria. Naomba nimtake Mhshimiwa Mbunge kama ana ushahidi kuhusu hili alete kwetu na sisi hatutasita kuchukua hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuhusu nafasi ya Kamati na Bodi za shule katika kutatua changamoto hii, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge ni kwamba lengo zima la kuanzisha Kamati za shule katika Shule za Msingi na Bodi katika Shule za Sekondari ni pamoja na kuangalia changamoto kama hizi ili kuhakikisha kwamba sheria, taratibu na miongozo ya Serikali inatiliwa mkazo katika usimamizi wa elimu. Kwa hiyo, tuendelee kuwaunga mkono kwa sababu ndiyo kazi yao hasa.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kutokana na jibu la msingi kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, tunaomba Serikali iweze kufuatilia majibu ya chuo hiki kwa sababu ni muhimu kwa wana-Mpanda kwa sasa.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kama ilivyo kwa wana- Mpanda, Shirika la la Utafiti la Uyole lina kituo pale Kijiji cha Nkana katika Wilaya ya Chunya, wameanzisha utafiti kwa muda mrefu, lakini mpaka sasa Wizara ya Elimu haijaweza kuwezesha utafiti ule kuendelea kwa ukosefu wa fedha. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha katika utafiti ule ili watu wa Nkana na Uyole, Mbeya, waweze kuendeleza shughuli za kilimo na kuweza kuwasaidia Watanzania? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mhesimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kunchela, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuhusu ombi lake la sisi tufuatilie kuhusu chuo hicho, naomba nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kufuatilia, lakini majibu ambayo tumetoa sasa ni kwamba sisi tumeomba taarifa kutoka kwa Halmashauri ya Mji wa Mpanda lakini mpaka sasa hatujapata taarifa. Kwa sababu yeye anatokea kule, nafikiri itatusaidia sana kama angeweza kusukuma kwa kushirikiana na Halmashauri yake ili tuweze kupata taaarifa hiyo ili tujue hatua za kuchukua.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na utafiti huo ambao anauzungumzia wa Uyole, naomba nifuatilie kwa sababu hajasema ni utafiti gani ili niweze kujua ni nini hasa ambacho kinampa changamoto Mheshimiwa Mbunge.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, alichouliza Mheshimiwa, Je, Kati ya wanafunzi hao ni wangapi waliotoka Zanzibar pamoja na majina yao. Swali hili limeletwa zaidi ya mwezi mmoja na, kwa maana hiyo wizara haijawa tayari kutaka kujibu na ninaomba utumie kanuni yako swali hili lije tena. Baada ya hayo, tuendelee hivyohivyo, kwa kuwa suala hili la Muungano wala siyo hisani wala fadhila, ni la Muungano, kwa mujibu wa Katiba ambayo umeisaini wewe bwana Chenge, ukurasa mwisho 124. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ndiyo inayoshughulikia masuala yote ya elimu ya juu, Wizara ya Elimu ya Zanzibar kukosa fursa hii. Je, ni lini watakaa kuweka utaratibu huu Zanzibar vijana hawa wakapata masomo kuhusu Elimu ya Juu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, tokea kuanza Serikali ya Awamu ya Tano, kwa kweli karibu mwaka wa nne, vikao hivyo vimefanyika mahali gani na wapi, kama Mheshimiwa Waziri ni mkweli wewe. Tuwe wakweli, hii si fadhila wala hisani, kwa mujibu wa Katiba hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jaku kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge, kwamba nafasi za ufadhili zinazotolewa kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hutolewa kwa Watanzania wote bila kujali wanatoka upande gani wa Muungano. Wakati tunatangaza nafasi hizo, kawaida hakuna sifa au hakuna hitaji la wewe kusema kwamba unatokea upande gani wa Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge anaponitaka mimi nije na orodha ya wanafunzi wangapi wamenufaika wanaotoka Zanzibar, ananipia kazi ambayo kawaida hatuifanyi, kwa sababu sisi tunachofanya tunapopata nafasi, tunakaa na wenzetu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, kupitia sifa zile halafu tunawachagua wanafunzi wa Kitanzania, bila kujali wanatoka wapi. Kwa hiyo, hatuwaambii waandike kama wanatoka Zanzibar au wanatoka Bara. Kwa hiyo, orodha ambayo ananiomba sisi hatuna! Kwa sababu hatuchukui wanafunzi kwa kuzingatia sifa hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nimhakikishie kwamba Wizara yangu inashirikiana vizuri sana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar na kila wakati tunahakikisha kwamba pande zote za muungano zinapata manufaa sawa bila ubaguzi!

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia lazima afahamu kwamba nafasi hizi hutolewa na wale wanaoomba wanatakiwa washindane. Kwa hiyo, mara nyingine ukisema tuanze kukaa na kusema tuanze kuchukua watu kulingana na wametoka wapi, tunaweza tukashindwa kwa sababu kule wanakwenda kushindana na wanafunzi wa nchi zingine. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie kwamba, asijenge ubaguzi kichwani, sisi hatuna ubaguzi, tunakaa na wenzetu na wala hakuna malalamiko yoyote ambayo yameshakuja kwamba kuna Wazanzibar ambao washindwa kupata nafasi hizi.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Spika, ahsante.

Mheshimiwa Spika, kama tunavyojua, Butiama ni sehemu ambako kila mtu anaelewa Butiama ni nani ametokea kule. Aliyetokea kule ni Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na chuo hiki kina umuhimu mkubwa sana, na tunajua kabisa kilimo ni uti wa mgongo, na vijana wengi sasa hivi wanakimbilia kujiajiri kwenye kilimo. Nataka kujua ni lini Serikali itatenga pesa za kutosha ili chuo hiki kiweze kukamilika badala ya kutegemea pesa au vyanzo kutoka Benki ya Dunia; ukizingatia Serikali haina ajira za kutosha kwa vijana?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; Mhehsimiwa Waziri anasema ujenzi wa majengo umekamilika kwa asilimia
50. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kutembelea chuo kile ilia pate uhakika kama kweli zimefika asilimia 50? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Sokombi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya msingi; ni kutokana na nia ya dhati ya Serikali ya kumuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ndiyo maana tumeamua kuanzisha Chuo cha Kilimo na Teknolojia Butiama. Hata hivyo, kama nilivyosema, kumekuwepo na changamoto kiodgo kwenye suala la upatikanaji wa ardhi. Hata pale kwenye shule ya Oswald Mang’ombe Serikali bado haijapata hati kwasababu Mheshimiwa Nimrod Mkono ambaye ndiye aliitoa kwa Serikali bado kuna michakato inaendelea. Hata hapo tunapojenga sasacampus kuu katika kituo cha uhamilishaji cha Butiama bado kuna changamoto ya radhi;na ni vigumu Serikali kuweka fedha nyingi kwenye eneo ambalo bado hati yake haijapatikana.

Mheshimiwa Spika, lakini kama nilivyosema, Serikali tayari imeshatenga shilingi bilioni moja kwenye bajeti ambayo tunaitekeleza sasa. Kwahiyoni matumaini yetu kwamba masuala ya radhi yakishakamilika, Wizara na chuo kikishakuwana hati inakuwa ni rahisi kuweka fedha nyingi zaidi.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo tayari tumeshatoa shilingi milioni 200 angalau kuanza ujenzi;kama tunavyosema juu ya majengo yale, hasa jengo la utawala ambalo linajengwa kwa fedha za TEA limefikia asilimia 50.

Mheshimiwa Spika, kuhusu ombi la Mheshimiwa Mbunge; kwamba,je, niko tayari kwenda Butiama na kuhakikisha kama ni kweli imafikia asilimia 50? Sina shida kuamabata na Mheshimiwa Sokombi tena nitakwenda kwa furaha sana ili tukaangalie kama jengo hilo kweli limefikia asilimia 50.
MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kuishukuru Serikali kwa kazi nzuri inayoendelea ya kujenga hiki Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, mawazo ambayo mwenyewe aliyaasisi na yakapokelewa na Mbunge wetu Mheshimiwa Mkono ambaye alitoa hata maeneo ningependa kuuliza swali moja la nyongeza kama ifuatavyo:-

Kwa kuwa, kutokana na changamoto ya radhi, Serikali ilishajipanga na tukaainisha maeneo kupitia kikao cha RCC Mkoa wa Mara, kwamba kuna majengo ambayo yapo katika Chuo cha Kisangwa-Bunda na kuna majengo mengine ambayo yako katika Chuo cha Shirati, na kuna majengo ambayo yako katika Chuo cha Wananchi-Bweri; na yale majengo yaliyopo yanaweza hata kupokea watoto.

Ningependa kujua, kwa kuwa Serikali bado inaendelea na mchakato na kwa kuwa pale kuna wafanyakazi sasa ni takribani miaka mitatu hawana kazi ya maana ya kufanya, ni lini sasa Serikali itawapanga watoto waende kuanzisha masomo pale wakati tukisubiria sasa fedha nyingi kwa ajili ya kuongeza majengo na maeneo mengine, ikiwa ni hatua muhimu sana ya kujenga mawazo ya Baba wa Taifa ambaye kwa kweli alijitoa, alitoa mpaka eneo, alijenga mpaka na Bwawa la umwagiliaji ambalo wananchi wameendelea kulilinda kwa muda mrefu sana?

SPIKA: Mheshimiwa Amina kwahiyo unapendekeza ihamishwe Butiama iende Bunda…

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Inabaki pale pale…

SPIKA: …na huko ulikotaja; hebu weka vizuri swali lako.

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Spika, kwa mawazo yaliyokuwepo ni kwamba chuo kitaanzia pale na watoto watakuwa pale na majengo ya kusomea yapo, watakapokuwa…

SPIKA: Pale una maana ya Butiama?

MHE. AMINA N. MAKILAGI: …ni Butiama ila wanapkwenda field kwa ajili ya masomo kwa vitendo kuna maeneo mengine ambayo yako ambapo wangekwenda kufanya practice.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Makilagi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kumekuwepo na mapendekezo mbalimbali ya namna ya kuanzachuo kile wakati tunasubiri ujenzi uanze. Hata hivyo Wizara imekuwa ikiangalia vilevile athari ambayo inaweza ikatokea kama tutatumia majengo ya vyuo vilivyopo ambavyo navyo vina umuhimu Kitaifa katika chuo ambacho tunaanzisha. Kwahiyo busara ambayo sisi tumeifikia ni kwamba hatuna haraka sana tusije tukavuruga utaratibu uliopo kwenye vyuo vingine kama hivyo anavyotaja lakini tusubiri mpaka hiki tuanze kujenga.

Mheshimiwa Spika, lakini pia kuhisiana na maeneo ya kufanya mazoezi, kwasababu Chuo kile sehemu kubwa itakuwa ni kwa ajili ya kuwasaidia wakulima kuweza kufanya mafunzo mafupi ya kilimo, Wizara inaendelea kutafuta ardhi katika maeneo ya jirani ikiwemo pamoja na Wilaya ya Serengeti ili tuweze kuwa na sehemu ya kufanyia mazoezi. Kwahiyo naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba nia ya Serikali iko pale pale, chuo kile kitaanza na naomba wavute subira, lakini naomba wote kwa ujumla wao tusaidiane kuondoa changamoto za upatikanaji wa ardhi pale kwenye Chuo cha Uhamilishaji lakini vilevile katika kuweza kupata eneo lile la Oswald Mang’ombe tuweze kupata hati ili hatimae chuo kiweze kumiliki.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Mtama lina shule za sekondari mbili ambazo zinapokea vijana waKidato cha Tano na Kidato cha Sita. Shule ya Sekondari Nyangao na Shule ya Sekondari Mahiwa. Mwaka jana Naibu Waziri wa Elimu alipotembelea Jimboni Mtama alipoenda kuiona Shule ya Sekondari Mahiwa alikuta majengo yake yamechoka na yamekuwa ya muda mrefu na akaahidi kwamba Serikali itatoa fedha kusaidia ukarabati wa majengo hayo.

Je, Serikali iko tayari kutekeleza ahadi yake kwa wananchi wa Jimbo la Mtama?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba nilitembelea Jimbo la Mheshimiwa Nape na ni kweli kwamba alinisihi nimsaidie shule yake iweze kupata miundombinu ili iweze kuwa bora na hatimaye kuwa shule ya Kidato cha Tano na Kidato cha Sita. Naomba niendelee kumuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imepanga kupeleka fedha katika Awamu ya Nane ya Mpango waEP4R, kwa hiyo, ahadi yetu iko palepale na itatekelezwa.(Makofi)
MHE. AIDA J.KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Kutokana na majibu ya Serikali, Serikali yenyewe inakiri kwamba kuna changamoto mbalimbali zinazopelekea mtoto wa kike kupata ujauzito. Lakini inasema ina mpango wa mtoto huyu wa kike aliyepata ujauzito kusoma elimu ya watu wazima ambayo ni nje ya mfumo rasmi. Kuna wanawake ambao wana familia zao wanasoma degree, wanapata Master’s na Ph.d ambao ni mfumo rasmi. Serikali haioni kwa kufanya hivyo ambao tunawaita ni watoto wakasome elimu ya watu wazima ni kuwaongezea adhabu nyingine?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Serikali pia imekiri kwamba umbali mrefu nao unachangia watoto wa kike kupata ujauzito. Kwa kuwa Mkoa wa Rukwa nao umekuwa kinara kwa watoto wa kike kupata ujauzito, Mkuu wetu wa Mkoa amekuja na oparesheni ambayo ina kauli mbiu ambayo inasema, Niacha Nisome. Je, Serikali iko tayari kumsaidia fedha kwa ajili ya kujenga hosteli?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na hilo la pili, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari Serikali inasaidiana na wananchi kwenye halmashauri zao kujenga hosteli na mabweni kwa ajili ya kuondoa changamoto ya watoto wa kike ambao wanatembea umbali kwenda shuleni. Kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba tuko pamoja na Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa kuhakikisha kwamba azma yake hiyo inafanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na lile swali lake la kwanza, kwamba kwa maoni yake siyo haki kuwanyima watoto ambao wamepata ujauzito kuendelea na masomo katika shule za kawaida. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba lengo la Serikali ni zuri kwa sababu tunajaribu kumlinda hata mtoto yule anayezaliwa kwa sababu watoto wale ambao wanapata mimba wanakuwa baadaye wanawabeba wenzao. Ukiwapeleka katika shule za kawaida hawatapa mazingira mazuri ya kuweza kuwalea. Kwa hiyo, tunamjali mtoto yule aliyezaliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tumeweza kujifunza vilevile kwamba hata watoto hao ambao wamepata ujauzito, mara nyingi wakienda kwenye shule za kawaida zile ambazo wametoka wanakuwa wananyanyapaliwa, kwa hiyo tunawawekea mazingira mazuri ambayo yatawasaidia kusoma kwa uhuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, wanapoenda kusoma kwenye Vituo vya Elimu ya Watu Wazima, inawasaidia kusoma katika utaratibu ambao…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri kwa kifupi sana.

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwahakikishie kwamba tutaendelea kuwasaidia na kwa kweli vituo hivyo ambavyo viko 500 nchi nzima vya watu wazima vimewasaidia watoto wengi wa kike kuendelea na masomo katika ngazi zinazofuata.
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nishukuru kwa majibu mazuri na niishukuru Serikali kwa shilingi milioni 500 ambayo mmetuletea kwenye Chuo cha Nyamidaho, naamini kwamba mwakani kinaanza kufanya kazi kama alivyosema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na hayo, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, ni dhahiri kwamba hata baada ya kupokea fedha hizo, ujenzi utakapokuwa umekamilika, bado tutakuwa na uhitaji wa jiko, bwalo la kulia chakula, bweni la wanafunzi wa kiume pamoja na uzio kwa ajili ya usalama wa wanafunzi ambao watakuwa wanasoma kwenye chuo kile pamoja na nyumba za watumishi, maana hakuna mpango wa kujenga nyumba hata moja ya watumishi. Je, Serikali ina kauli gani kuhusu haya mahitaji ambayo yatakuwa yamebakia?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Waziri yuko tayari kuongozana na mimi kwenda kuona mazingira jinsi yalivyo ili iweze kutoa msukumo katika kumalizia mambo haya na kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya watoto kusoma kwenye Chuo cha Nyamidaho?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Vuma, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama utaniruhusu, kabla ya kujibu maswali hayo, naomba nitumie nafasi hii kwa msisitizo mkubwa kueleza ni namna gani Mheshimiwa Mbunge amehusika katika kupatikana kwa chuo hiki. Kwa kweli lazima niseme, kama isingekuwa yeye, kwa namna alivyokuwa anatusumbua, mpaka pale ofisini anafahamika kama king’ang’anizi, chuo hicho kisingepatikana. Naomba nitumie nafasi hii kumpongeza na nimuombe Mungu wapiga kura wake wasikie kwamba kwa kweli amejitahidi na napenda kumpongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kama Serikali iko tayari kuongeza majengo na miundombinu mingine ambayo bado kuna upungufu, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba punde chuo kitakapoanza mwaka 2020 kama tunavyotarajia, tutaangalia upungufu uliopo na kuendelea kuboresha na kuongeza kadri uwezo wa fedha utakavyoruhusu. Kwa hiyo, naomba nihamhakikishie kwamba hatutaishia hapa, tutaendelea kukiboresha chuo kile ili Wanakasulu na Watanzania wengine waweze kusoma katika mazingira mazuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuandamana naye, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba niko tayari kuandamana naye. Pia najua kwenye mkoa wake wapo vilevile Wabunge wa Viti Maalum ambao nao vilevile wamekuwa wakisaidia kusukuma ujenzi wa vyuo hivi, nao vilevile wakiwepo itasaidia tutaandamana kwenda kuangalia chuo hicho. Nashukuru sana.
MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED: Mheshimiwa Spika, ahsante pamoja na majibu ambayo Serikali imetoa ambayo ni ya kawaida sana hayako katika uhalisia yako much shallow kwa kweli katika swali langu la msingi lililenga zaidi ufaulu wa wanafunzi kutoka kidato cha IV kwenda kidato cha V, sio labda majengo zaidi aaah! Ni kiasi gani asilimia ngapi inafaulu kutoka IV kwenda V na pia lilenga zaidi kwenye subject matter.

Sasa je, Serikali inajiridhishaje hata hizi takwimu ulizonipa nina mushkeli nazo nitaomba zaidi kama ziko takwimu za ufaulu kutoka IV kwenda V nipatiwe kwa Tanzania nzima. Sasa swali langu la nyongeza ni hili. Je, Serikali kupitia Wizara inayohusika inajiridhishaje kwamba zile competences zilizoainishwa kwenye syllabus zinafikiwa? Hapo ndiyo ulipo mushkeli wangu.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge amesema majibu yetu yamekuwa ya kawaida na ni shallow. Ukweli wa mambo tumejibu kutokana na swali alilouliza yeye kauliza matokeo ya mtihani wa kidato cha IV yamekuwa mabaya kwa kipindi kirefu sana na hali hii haijapatiwa ufumbuzi wowote na maswali ikawa ni nini tamko la Serikali kuhusiana na hali hiyo, lakini vile vile akauliza kuhusu juhudi.

Mheshimiwa Spika, sasa tamko la Serikali nililokupa ni kwamba tumekupa takwimu kuonyesha kwamba ukiangalia kuanzia mwaka 2015 mpaka sasa kumekuwa na ongezeko la ufaulu katika mitihani ya Kidato cha IV kutoka mwaka hadi mwaka. Mwaka huu tumefikia asilimia 78, wakati mwaka 2015 tulikuwa asilimia 67. Sasa kama unataka kujua ni kiasi gani cha hao wanaoenda kidato cha V hapo sasa ungeleta swali lingine au ungeuliza kwenye swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, na kuhusiana na hilo suala alilouliza la competences naomba nimuhakikishie Mbunge kwamba tunajaribu kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha kwamba elimu yetu inakuwa bora na ndiyo maana nimeorodhesha hatua au mambo mbalimbali ambayo tunayafanya ikiwa ni pamoja na kujenga miundombinu, ikiwa ni pamoja na kuajiri walimu, tunapitia mitaala, tumehuisha mfumo wa udhibiti ubora. Kimsingi tulipo sasa ni bora kuliko tulikotoka na nimuhakikishie tu pamoja na Mheshimiwa Wabunge wengine kwamba Serikali itaendelea kuweka mkazo ili kuendelea kuboresha elimu yetu.
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi kwa vile suala la elimu kwa ujumla wake siyo suala la muungano na kwamba Baraza la Taifa la Mitihani pamoja na elimu ya juu ndiyo vya muungano. Sasa swali langu liko hapa Sera za elimu pamoja na mitaala kwa vyovyote itakuwa ni tofauti baina ya Zanzibar na Tanzania Bara.

Sasa kwa nini Serikali zetu mbili kwa lengo la kuimarisha elimu Tanzania zisikae pamoja zikatengeneza sera ya elimu na mitaala inayofanana ili kuinusuru Zanzibar kila mara kutokea kumi za mwisho? Ahsante; dhamira ni kuimarisha muungano.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge anashauri kwamba Serikali zetu mbili zikutane na kujaribu kukaa ili kuangalia uwezekano wa mitaala yetu iweze kufanana. Ni wazo ametoa sio wazo baya kwa sababu ni nchi moja tutaenda kuliangalia sio kitu ambacho hakiwezekani.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana ukitaka kuangamiza Taifa lolote anza kuangamiza au kuharibu mifumo yake ya elimu inayolinda utu wa binadamu. Mwaka 1979 mabadiliko ya mtaala hayakuweza kukidhi changamoto za mabadiliko ya elimu ya wakati huo na Mwalimu Nyerere akaunda Kamisheni ya Makweta. Sasa ni miaka 37 tangu Kamisheni ile kufanya uchambuzi wa elimu hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, Sera ya elimu ya 2014 na mtaala wake haukidhi changamoto za elimu za sasa za lengo la nne la maendeleo endelevu ya dunia la elimu bora sawa shirikishi kwa wote. Sasa je Serikali haioni umuhimu wa kuweza kuchukua mifumo kama za Finland, Vietnam na kwingine ili tuweze tukaendana na changamoto za elimu za dunia za sasa badala ya kufanya elimu yetu trial and error kama ilivyo sasa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba kwanza nikiri kwamba Mheshimiwa Mbatia ni Mbunge makini sana kwenye masuala ya elimu kwahiyo mara nyingi ushauri wake tunauchukua kama ni ushauri mzuri. Naomba tu nimuhakikishie kwamba Wizara yangu Serikali haijawahi kukaa kimya kufanya mapitio ya mitaala pale inapobidi hata hivyo kama unavyofahamu, ubadilishaji wa mitaala huwezi ukawa unabadilisha kila siku kwa kiasi kikubwa unachofanya ni kufanya mabadiliko madogo madogo kama mwenyewe anavyosema maendeleo na mabadiliko ya teknolojia yanayotokea duniani na tunaendelea kufanya hivyo kila mwaka.

Mheshimiwa Spika, naomba vile vile nimuhakikishie kwamba kwa sasa tunafanya mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 ili tuweze kuhuisha ili iendane na mabadiliko ambayo yametokea na iweze kutupa elimu ambayo ni bora zaidi katika wakati tuliopo. Naomba nimuhakikishie vile vile kwamba wakati tunahuisha Waheshimiwa Wabunge watapata fursa vile vile ya kushiriki katika mjadala ambao utatuletea Sera mpya.

Mheshimiwa Spika, lakini pia kama Mheshimiwa Mbunge atakumbuka wakati tunajadili hotuba ya Wizara yetu tulitoa ahadi ambayo tunataka kuitekeleza ya kufanya mjadala kuwaita wadau tukutane tuongee ili hayo maoni na mengine tuweze kuyachukua katika kujaribu kuboresha sera yetu na hatimaye hata ikiwezekana na kubadilika mitaala iliyopo.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza maswali ya nyongeza.

Kwa kuwa wananchi wa Rufiji wamekuwa na shida kubwa kupata Chuo cha VETA rufiji, pamoja na juhudu za Mbunge wao kupambana kutafuta jinsi gani ya kupata Chuo cha VETA ndio sababu akaona hata kuna haja kubadilisha vyuo vya FDC labda wanafunzi wa Rufiji waweze kupata elimu hiyo ya VETA, na Kwa kuwa Serikali sasa imeshatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa VETA - Rufiji ni jambo la shukrani na pongezi sana kwa Serikali, je, Serikali sasa ni lini ujenzi huo utaanza rasmi.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Kwa kuwa katika Mkoa wa Dar es Salaam kuna Chuo kikubwa sana cha VETA Kipawa, chuo hiki ni kikubwa mno, lakini hatujawahi kuona matangazo mbalimbali juu ya elimu inayotelewa hapo au ni mwaka gani wa mafunzo ambao unaanza lini na lini wanafunzi waweze kuhamasika kujiunga na Chuo cha VETA Kipawa?

Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kukitangaza hiki Chuo cha VETA Kipawa ambacho Serikali imewekeza fedha nyingi sana na chuo ni kizuri mno, ili wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali waweze kujiunga na chuo hiko?
NAIBU WAZIRI ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, kuhusiana na lini ujenzi wa Chuo cha VETA cha Rufiji kitaanza, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba fedha zimetengwa katika mwaka wa fedha unaokuja na fedha hizo zipo, kwa hiyo, siyo za kutafuta. Kwa hiyo, ujenzi utaanza mara moja, Rai yetu kwa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji ni kwamba watupatie eneo lenye hati ili ujenzi uanze bila kuchelewa.

Mheshimiwa Spika, lakini pia swali lake la pili kuhusiana na Chuo cha VETA Kipawa, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba VETA nchi nzima kawaida inakuwa na utaratibu wa kutangaza nafasi za masomo katika vyuo vyake vyote lakini kama Mheshimiwa Mbunge anaona haitoshi katika Chuo cha Kipawa naomba nitumie fursa hii kumuagiza Mkurugenzi Mkuu wa VETA ahakikishe kwamba matangazo yale yanatolewa na aongeze kasi na wigo wa kutangaza nafasi mbalimbali za VETA zote nchini.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Chuo cha VETA Ludewa kilipaswa kiwe kimeshakamilika toka mwaka jana mwezi wa nane, lakini mpaka leo hivi ninavyozungumza Chuo cha VETA kile Ludewa hakina dalili na mkandarasi hayupo. Je, ni lini Chuo cha VETA Ludewa kitakamilika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba kwanza nitumie nafasi hii kukiri na kuweka wazi kwamba Mheshimiwa Deogratias Ngalawa amekuwa akifuatilia sana ujenzi wa Chuo cha Ludewa au Chuo cha VETA Mkoa wa Njombe.

Mheshimiwa Spika, uchelewaji wa ujenzi wa chuo husika umetokea kwa sababu mkandarasi ambaye alipewa kazi ya kujenga chuo kile alifanya madudu na Serikali ilibidi kusitisha mkataba. Kwa sasa tayari mfadhili wa mradi ambaye ni Benki ya Maendeleo ya Afrika tayari ameshatupa ruhusa ya kutangaza kandarasi upya. Kwa hiyo, kwa sasa tupo katika hatua za kumpata mkandarasi mpya ili ujenzi uweze kuendelea.

Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ujenzi utaanza mara tu Mkandarasi mpya atakapopatikana na hatutegemei ichukue tena muda mrefu.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya mimi kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa sasa hivi tuna Sera ya Elimu Bure ambayo imeleta ongezeko kubwa sana la wanafunzi wanaojiunga na shule na kwa kuwa bado hata private sector inaendelea kujenga vyuo vya ualimu.

Je, Serikali sasa haiwezi kuona kwamba, kuna umuhimu wa kuiweka Urambo kama eneo mojawapo ambalo Serikali itajenga kwa siku zijazo kutokana na mahitaji makubwa naamini ya walimu yanayohitajika sasa hivi kutokana na ongezeko la wanafunzi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyosema mwenyewe kwa sasa Serikali haina lengo la kuongeza vyuo vingine vya ualimu kwa sababu tuna vyuo 35 na siku hizi fikra ya Serikali ni kujaribu kuboresha zaidi na kupanua zilizopo kuliko kujenga utitiri wa vyuo na ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa kwa watu wa Tabora kuna vyuo viwili vya ualimu tayari, Chuo cha Walimu Ndala na kile cha Tabora, lakini kama mwenyewe anavyosema labda huko mbele kama itatokea haja ya kuhitajika kujengwa chuo kingine sio vibaya kufikiria ombi lake, lakini kwa sasa lengo ni kujaribu kuongeza ubora wa vyuo vilivyopo badala ya kukimbilia kujenga vyuo vingi ambavyo havina ubora.
MHE. RUKIA AHMED KASSIM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini bado nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa tatizo kubwa tulilonalo katika nchi yetu kwenye mazingira ya biashara ni mfumo wa kodi kuwa kuwa hauko wazi: Je, ni lini sasa Serikali itaandaa mfumo wa kodi ambao utakuwa wazi katika mazingira haya ya ufanyaji biashara?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa sababu nchi yetu katika uwezeshaji ufanyaji wa biashara imeambiwa ni nchi ya 144, Rwanda ambayo ni nchi ndogo ni ya 29, Kenya ni nchi ya 40: Je, Serikali haioni kwamba tutapoteza wawekezaji katika halali hii ili tuweze kujirekebisha?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA): Mheshimiwa
Naibu Spika, kuhusiana na mazingira yetu ya kodi kuwa wazi, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imekuwa ikipitia mazingira ya kodi kila wakati na ndiyo maana hata kwenye kila Bunge, mara nyingi tumekuwa tukipata mapitio ya kodi mbalimbali ili kuendelea kuboresha mazingira yetu ya kodi yaweze kuwa ya kishindani na yaweze kurahisisha biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba pamoja na changamoto ambazo bado zipo, Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali la pili la namna gani tunaweza tukaboresha mazingira yetu ya uwekezaji, kama nilivyosema kwenye jibu letu la msingi, Serikali imeshachukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na kukaa na wafanyabiashara kujadiliana nao mazingira au changamoto wanazozipata. Ndiyo maana tumekuja na Blue Print kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kibiashara. Tutaendelea kufanya reforms; na ndiyo maana hata juzi Mheshimiwa Rais aliwaita wafanyabiashara akakaa nao mkutano wa masaa mengi akisikiliza kero zao. Lengo ni kupata changamoto na mawazo yao ili kuboresha mazingira ya biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hili litaendelea na baada ya muda siyo mrefu, mazingira yetu yataboreka, yatakuwa mazuri na itaendelea kuvutia wawekezaji kutoka nje.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nami naomba kuongezea majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda katika swali la pili la nyongeza la Mheshimiwa Rukia Kassim kuhusiana na wepesi wa kufanya biashara. Kwanza kabisa nimhakikishie kwamba tutakapoenda katika mwaka ujao kwa nafasi ya Tanzania tutakuwa tumefanya vizuri zaidi. Changamoto ambayo tunayo ukizingatia na maboresho ambayo sasa hivi Serikali imeyafanya, huwa katika upimaji wa nafasi ya nchi katika wepesi wa kufanya biashara, kipimo chao deadline ni mwezi wa Tano wa kila mwaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kwa sasa Juni - Julai mambo mengi yamefanywa na Serikali. Juzi tu nilikuwa na mkutano pamoja na Benki ya Dunia Washington na Dar es Salaam, kuhakikisha kwamba tunawasilisha vielelezo vya kuonyesha ni namna gani kama nchi tumefanya maboresho mbalimbali na tumepiga hatua katika kuboresho viashiria vile 11 ambavyo vinatumika katika kupima wepesi wa kufanya biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu kusema kwamba, tumepata muda wa kuongezewa mpaka Ijumaa ijayo kuweza kuwasilisha vielelezo vingine vya namna gani tumeweza kufanya makubwa na marekebisho katika mifumo yetu ya kufanya biashara, ikiwemo kuanzisha biashara, ufungaji wa biashara, taratibu za biashara mipakani pamoja na nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu kusema kwamba tumepata muda wa kuongezewa mpaka Ijumaa ijayo kuweza kuwasilisha vielelezo vingine vya namna gani tumeweza kufanya maboresho makubwa na marekebisho katika mifumo yetu ya kufanya biashara ikiwemo kuanzisha biashara, ikiwemo ufungaji wa biashara, ikiwemo taratibu za biashara mipakani pamoja na nyingine. Kwa hiyo, niwatoe hofu Watanzania niwatoe hofu Wabunge kila mmoja atimize nafasi yake tujitahidi kuona ni kwa namna gani tunaboresha huduma hizi na ninaamini itakapofika mwaka 2020/2021 ripoti yetu na nafasi ya Tanzania tutaweza kufanya vizuri zaidi.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili tumepata pia utaratibu tutawaita wataalam wa Benki ya Dunia Makao Makuu pia waweze kuja ili kuweze kutoa mafunzo na kutoa maelekezo kwa wale viungo au focal point wa mazingira ya biashara ya kila Wizara na kila Taasisi maana yake tunao watu hawa, ili waweze kuona ni kwa namna gani watapaswa kufanya maboresho zaidi. Tunaamini tulishafanya kitu kama hiki mwaka 2016 na ilitusaidia sana kama nchi tuliweza kuvuka na kuimarika nafasi takribani saba. Kwa hiyo, tunaamini kati ya mwaka huu mpaka mwaka 2021 tutaweza kufanya vizuri zaidi, muhimu kila mmoja atimize wajibu yake. (Makofi)
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi ya maswali mawili ya ngongeza. Kwanza niipongeze Serikali kwa majibu mazuri na tunaona mikakati wa Serikali kuelekea Tanzania ya viwanda.

Swali la kwanza, tayari katika mikakati hiyo shule nyingi za sekondari zimejenga maabara ili kutengeza wataalam kwa ajili ya Tanzania ya viwanda, ni lini sasa Serikali watapeleka vifaa vya maabara katika shule za sekondari ambazo zimeshatekeleza ujenzi wa maabara?

Swali la pili, katika Wilaya Malindi tuna Chuo cha Maendeleo Sofi nashukuru Serikali wanakifanyia ukarabari chuo kile lakini kina uhaba mkubwa wa walimu. Je, ni lini Serikali itapeleka Walimu katika chuo cha Sofi ambapo ukarabati wake karibu unakamilika? Nakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ni lini Serikali itapeleka vifaa vya maabara katika maabara ambayo imekamilika naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tumekuwa tukipeleka vifaa vya maabara mara kwa mara kadri maabara zinapokamika. Naomba nimhakishie kwamba kwa shule zile ambazo sasa zimekamilisha Serikali inataendelea kupeleka vifaa vya maabara na hata kwenye bajeti ambayo Bunge hili imepitisha vilevile tumeweka fedha za maabara ili kuhakisha kwamba vifaa vinapatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na Chuo cha Maendeleo ya Wananchi cha Sofi naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba utaratibu ule wa kukarabati vyuo vya wananchi (FDC’s), hauishii tu kwenye ukarabati vilevile inaenda kwenye mambo mengine ya kuboresha mazingira yote ya kujifunzia na kufundishia ikiwa ni pamoja na kuajiri walimu, wakufunzi lakini na wafanyakazi ili vyuo vile viweze kuendeshwa kwa uzuri zaidi ndiyo maana tulifanya kitu kinachoitwa conditional survey ya kujaribu kuangalia ni mahitaji yapi yanahitajika ili vyuo vyote viweze kupata mahitaji yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie kwamba tayari tulishafanya tathmini ya nini kinahitajika na punde ukarabati utakapokamilika vilevile nimhakikishie kwamba watapata wakufunzi. (Makofi)
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kwanza niipongeze Serikali kwa kukubali na kupokea ombi la Wilaya ya Kwimba yenye majimbo mawili kwamba itaanza ujenzi huo kwenye mwaka wa fedha 2019/2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa sababu Madiwani wa Wilaya ya Kwimba ambao sasa wamesharidhia kama walivyoombwa na VETA wenyewe kwamba ile hati ambayo ilikuwa imeandikwa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba ihame sasa iende VETA kazi ambayo imeshafanywa na tumeshapeleka hati hiyo kwenda kubadilishwa, nini hatua inayofuata sasa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, si vibaya kujua maoteo ya gharama ya ujenzi wa chuo hicho. Je, gharama hiyo ni shilingi ngapi hadi kikamilike?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Richard Mganga Ndassa, Mbunge wa Sumve, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tunapokea pongezi zake lakini naomba nimhakikishie kwamba pindi wao watakapokuwa wamekamilisha taratibu za kupata ardhi na hati wawasilishe Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ili mchakato wa ujenzi uweze kuanza mara moja. Nina hakika utaratibu ukikamilika mradi utasimamiwa vizuri kwa sababu Mheshimiwa Mbunge amebahatika vilevile kuwa na DC mahiri na mzuri sana Mheshimiwa Senyi. Kwa hiyo, nategemea kwamba fedha zile zikipatikana mradi ule utaenda vizuri.

Kuhusu maoteo ya gharama za mradi ule kwa sasa Wizara imefikiria kwamba tutahitaji angalau shilingi bilioni 1.5 kama matumizi ya awali. Hata hivyo, Wizara iko tayari kuweka fedha kwenye mradi kadri mahitaji yatakavyotokea.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Awali ya yote niipongeze sana Serikali kwa jitihada ambazo zinaendelea, niombe basi speed iongezeke kuwaandaa walimu, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, ufundi ni ujuzi wa jambo lolote lile. Je, Serikali inaonaje sasa ikabadilisha mtizamo wa kuanza kujenga vyuo vya ufundi vikubwa na vyenye gharama kubwa badala yake iende kwenye fani ambazo zinahitaji fedha kidogo na kazi za mikono kwa vijana wa Tanzania kama vile kilimo na ufugaji? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Njombe tuliahidiwa kukarabatiwa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi. Chuo kile ni kichakavu sana kinachukua wananfunzi wachache sana. Je, Serikali imefikia wapi katika ahadi yake ya kukarabati Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Njombe Mjini?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Edward Franz Mwalongo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Serikali kujielekeza zaidi kwenye vyuo vidogo badala ya vile ambavyo vina gharama kubwa, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inaendesha vyuo vya aina zote; vidogo, vya kati vilevile vikubwa. Yeye mwenyewe ni shahidi kwamba Serikali kwa sasa imeweka fedha nyingi katika kukarabati Vyuo vya Wananchi lengo lake ni ili wananchi waweze kupata kozi ambazo zinaendana na shughuli ambazo wanafanya. Kwa hiyo, kwenye maeneo ya kilimo kunakuwa na vyuo ambavyo viatoa elimu ya ufundi wa masuala ya kilimo au shughuli nyingine yoyote ambayo wananchi wanafanya. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie kwamba wazo lake hilo siyo baya na tayari Serikali inalifanyia kazi na ndiyo maana kuna vyuo vya aina mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la Chuo chake cha Wananchi kwamba ni lini kitaanza kukarabatiwa, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa tumeanza na ukarabati wa vyuo 20 kati ya vile vyuo 55 na tunategemea vile vingine vilivyobaki ukarabati utaanza mwezi ujao. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie kwamba yeye na wananchi wake wawe tayari kwa sababu ukarabati unakwenda kuanza.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.

Nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini bado specifically ninataka kusikia angalau kwenye takwimu jinsi ambavyo Serikali inawekeza haraka kutumia pumba hizi kwa sababu zinaharibu mazingira na hivi ninavyozungumza na wewe zimesababisha Mto Kilombero kujaa maji na kusababisha mafuriko kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza ni kwamba ni kiasi gani Serikali inawekeza haraka iwezekanavyo kutumia pumba hizi ambazo Mheshimiwa Naibu Waziri amesema ni tani 11,000; zinakwenda wapi pumba hizi? Ni kwamba uwekezaji wa haraka unatakiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; hawa wakulima wadogo wadogo wa kilimo cha uyoga tayari Halmashauri yetu imewakopesha katika vikundi na wanaendelea kulima, changamoto kubwa wanayoipata ni katika vifungashio, mifuko ile ya kupandia.

Je, Serikali haiwezi kutafuta wawekezaji watakaoruhusu mifuko hii ya kupandia ipatikane kama ambavyo imefanyika kwa wauza mikate kwa sababu sasa hivi kuna katazo la Serikali la mifuko ya nylon?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (UWEKEZAJI): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Asenga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kwamba kwa nini Serikali haijawekeza; naomba nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba zao la uyoga ni zao ambalo ni kama ndiyo linaanza. Kwa hiyo, bado tunahitaji kufanya utafiti na kutoa hamasa kubwa ili wananchi waweze kufahamu umuhimu wa kulima hilo zao, lakini pia tuweze kuwa na elimu basi hata ya namna ya kulipanda na kulihudumia.

Kwa hiyo, Serikali imeanza kwa kutoa uhamasishaji na kufanya tafiti mbalimbali. Sasa huko mbele ya safari tunaamini kwamba taarifa ambayo itatokana na tafiti hizo, na wananchi wakihamasika basi inakuwa ni rahisi kuvutia wawekezaji wengine na hata kutoka nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na upatikanaji wa vifungashio; ni swali zuri na sishangai kwa sababu ni Mbunge makini, namfahamu tokea siku nyingi. Lakini naomba nilibebe ili tushirikiane na Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira pamoja na wenzetu wa Wizara ya Kilimo, tuangalie ni namna gani tunaweza tukapata vifungashio vizuri zaidi kwa ajili ya kuzalisha vimeng’enya kwa ajili ya uzalishaji wa uyoga.
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nashukuru pia kwa majibu mazuri ya Serikali kuhusu swali hili. Ninalo swali moja tu la nyongeza.

Kwa kuwa zao hili la parachichi limeanza kupata msukumo mkubwa na wananchi wengi wanaendelea kulima zao hili katika mikoa mbalimbali hapa nchini ikiwemo mikoa ya nyanda za juu kusini hasa katika Mikoa ya Mbeya, Njombe, Songwe na Rukwa ; na wananchi wengi wanalima zao hili kwa njia za asili bila kufuata taratibu za kilimo bora: Je, Serikali haioni haja sasa kulisimamia zao hili kwa ukaribu ili wakulima walime kwa tija kwa kuzingatia kilimo bora cha parachichi. (Makofi).
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (UWEKEZAJI): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama nilivyosema kwamba zao hili la parachichi ni kati ya mazao ambayo kwa sasa kwa kweli yameleta matumaini makubwa kwa ajili ya kuwanufaisha wananchi wetu. Ndiyo maana kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, Serikali imeanza kuweka mikakati ya kuhakikisha kwamba wananchi wanaweza wakazalisha zao hili kwa wingi zaidi na katika mazingira bora zaidi ili kuweza kukidhi ushindani uliopo Kimataifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba sehemu ya mkakati huo ni pamoja na Wizara ya Kilimo kuanza kujikita kutayarisha mkakati wa kulima mazao ya mboga mboga. Mkakati unaoanzia mwaka 2021 mpaka mwaka 2030 ambao pamoja na mambo mengine utahakikisha kwamba kunakuwa na mbegu bora, kunakuwa na kilimo ambacho kina tija; pia Serikali imeanza kuangalia zaidi katika masoko hayo ya Kimataifa ambayo tumesema kwa kweli ni mengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukijaribu kuangalia uzalishaji wetu bado ni tani 4,000 wakati dunia nzima zinahitajika zaidi ya tani 2,000,000. Kwa hiyo, fursa bado zipo na ndiyo maana tumeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanaweza wakazalisha kwa ubora zaidi.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa utaratibu huu wa mfumo wa soko la awali huwa unawakutanisha wenye viwanda na wakulima lakini hauna ushindani kwa sababu bei ni ndogo na wakulima hawavutiwi kupeleka korosho zao kama ilivyo kwenye minada mingine ya kawaida, kwa sababu wakulima wanaona kama ni kangomba ya aina fulani tu: Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka top up kwa bei ile inayotolewa na wawekezaji ili kuhakikisha kwamba wawekezaji hawa wanapata korosho katika soko?

Swali la pili, kwa kuwa viwanda hivi vimeajiri vijana wengi na akina mama wengi; na kwa sasa hivi viwanda takriban vyote vinafanya kazi chini ya uwezo wake kwa sababu ya changamoto mbalimbai ikiwemo ukosekanaji wa malighafi kwa sababu hawapati korosho mnadani: Je, Serikali inatoa kauli gani sasa kwa wawekezaji ambao wameshafungua viwanda nchini na wale ambao wanatarajia kufungua viwanda vipya?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuwepo kwa changamoto ya upatikanaji wa korosho kwa sababu wakulima hawana imani na mfumo wa soko la awali, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Chikota kwamba kwa sababu ndiyo mfumo umeanza, Serikali itaendelea kuchukua jitihada kuboresha ili kuweza kuvutia wakulima waone kwamba ile siyo kangomba, bali ni soko ambalo lipo lenye lengo la kuhakikisha kwamba viwanda vya ndani vinapata korosho kwanza kabla havijauza nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu changamoto hiyo aliyozungumzia kwamba ajira zile hazizalishwi kwa sababu viwanda havipati korosho, naomba nimhakikishie kwamba katika utaratibu huo huo wa kushughulikia changamoto ambazo zipo katika soko la awali, Serikali itaendelea kufikiria namna bora ya kuhakikisha kwamba korosho inapatikana ili viwanda hivi na vingine ambavyo tunategemea kuvutia viwezwe kuanzishwa, viweze kutoa ajira kwa ajili ya vijana wetu.