Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. William Tate Olenasha (169 total)

MHE. HAMIDU H. BOBALI aliuliza:-
Mkoa wa Lindi unapakana na Bahari ya Hindi na hivyo vijana wengi hujishuhulisha na shughuli za uvuvi ili kujipatia kipato cha kuendesha maisha yao.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kujenga Chuo cha Uvuvi Mkoani Lindi ili kuwaongezea vijana hao ujuzi wa kazi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hamidu Hassan Bobali, Mbunge wa Mchinga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inatambua umuhimu wa kuwafundisha vijana mbinu sahihi za kufanya shughuli za uvuvi, kilimo na ufugaji. Hivi sasa Wizara kupitia Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (Fisheries Education and Training Agency – FETA) imeanzisha Chuo cha Uvuvi Mikindani, Mtwara kwa lengo la kusogeza huduma ya mafunzo ya uvuvi kwa wananchi wakiwemo vijana walioko Ukanda wa Kusini mwa Tanzania, ukiwemo Mkoa wa Lindi.
Ni mategemeo yetu kuwa mafunzo ya muda mfupi; wiki mbili hadi miezi mitatu yataanza kutolewa mwaka huu kwa kudahili wanafunzi 40 na yale ya muda mrefu ya stashahada yataanza mwaka 2017/2018. Ujenzi wa chuo hiki unaendelea ambapo hadi sasa madarasa mawili na karakana imekamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) utaanza kutoa mafunzo ya uvuvi katika Chuo cha Mikindani, Mtwara muda mfupi mwaka 2016/2017 na yale ya astashahada na stashahada yataanza mwaka 2017/2018.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA aliuliza:-
Mwaka 2013 Bunge lilirekebisha Sheria ya Ushirika wa Tumbaku ili iendane na hali ya sasa ya ushirika huo nchini:-
Je, ni marekebisho gani yaliyowanufaisha wakulima moja kwa moja?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Victor Kilasile Mwambalaswa, Mbunge wa Lupa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga Sheria ya Vyama vya Ushirika Na. 6 ya mwaka 2013 ambayo ni kwa ajili ya kusimamia uendeshaji wa shughuli za Vyama vya Ushirika vya aina zote Tanzania Bara na siyo kwa ajili ya Vyama vya Ushirika wa Tumbaku pekee. Sheria hiyo ilianza kufanya kazi mwaka 2014.
Mheshimiwa Spika, marekebisho yaliyowanufaisha wakulima moja kwa moja ni pamoja na:-
Moja, sheria imeruhusu ushindani baina ya Vyama vya Ushirika ili kuongeza ufanisi kwa kuruhusu kuanzishwa Vyama vya Ushirika zaidi ya kimoja vinavyofanya shughuli ya aina moja katika eneo moja, jambo ambalo halikuwepo katika Sheria ya 2003. Hii pia imeondoa migogoro kama ule wa Vyama vya Ushirika vya Mishamo Mkoani Katavi ambapo wakulima wa tumbaku walikuwa na mgogoro mkubwa kiasi cha kutishia amani.
Pili, sheria hii imeweka mazingira ya wanachama wa Vyama vya Ushirika kujiunga na kunufaika na huduma mbalimbali kama zile zinazotolewa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ambazo ni Mafao ya Uzeeni, Fidia, Bima ya Afya na Mikopo. Hadi mwezi Septemba, 2015 zaidi ya wanachama 50,000 wamejiunga na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na kunufaika kwa kupata mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi za Kitanzania bilioni 50 kupitia mpango unaojulikana kama Wakulima Scheme.
Tatu, Sheria imepunguza idadi ya chini kabisa ya watu wanaoweza kuunda Chama cha Ushirika cha Mazao kutoka 50 hadi 20 ili kuwawezesha wakulima kuunda vyama wanavyohitaji kwa wepesi zaidi ilimradi viwe na uhai wa kiuchumi. Vyama vya Ushirika 60 vimeandikishwa kufikia mwezi Disemba, 2015.
Mheshimiwa Spika, nne, Vyama vya Ushirika vimetumia sheria hiyo katika kujihusisha na zaidi ya zao moja na hivyo kuepuka kupata hasara pale ambapo bei ya zao inapokumbwa na misukosuko kama vile kushuka kwa bei. Vyama vya Ushirika wa Tumbaku vya Mkoa wa Tabora vimeanza kuweka mipango ya kuzalisha mazao mengine kaka vile alizeti, karanga na nyonyo ambayo yana soko na bei nzuri.
Mheshimiwa Spika, matokeo ya moja kwa moja ya Sheria mpya ya Ushirika kwa wakulima yataongezeka zaidi mara baada ya kukamilika mfumo wa usimamizi ambao unaainishwa katika sheria hiyo ambao unaanza ngazi ya Wilaya hadi Taifa, utakaotekelezwa kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika ambayo muundo wake tayari umeshapitishwa na Serikali.
MHE. PASCAL Y. HAONGA aliuliza:-
(a)Je, ni lini Serikali itaweka ruzuku kwenye pembejeo za kilimo kama vile mbolea ili kuwapunguzia Wakulima ghaarama za uzalishaji?
(b)Je, ni lini Serikali itaanzisha Mfuko Maalum wa Zao la Kahawa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, ningependa kujibu swali la Mheshimiwa Pascal Yohana Haonga, Mbunge wa Mbozi, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikitoa ruzuku ya mbolea na mbegu za kilimo tangu mwaka 2007/2008. Kwa lengo la kumpunguzia mkulima gharama. Mathalani katika msimu huu wa kilimo Serikali imetoa ruzuku kwenye mbegu bora na mbolea za kupandia na kukuzia kwa mazao ya mahindi na mpunga kwa utaratibu wa vocha kwa kaya laki tisa tisini na tisa elfu mia tisa ishirini na sita mikoani. Aidha, Serikali imeendelea kutoa ruzuku ya madawa na mbegu bora kwenye mazao ya pamba na korosho. Vilevile kwa mazao ya chai na kahawa ruzuku imekuwa ikitolewa kwenye miche bora ili kuongeza uzalishaji na ubora wa mazao hayo.
(b) Mheshimiwa Spika, tasnia ya kahawa tayari imekwishaanzisha Mfuko wa Zao la Kahawa kutokana na azimio la Mkutano Mkuu wa wadau wa kahawa uliofanyika Mei, 2011. Mfuko huu ulizinduliwa rasmi Januari, 2013 na tangu kuanzishwa kwake Mfuko unaendelea kutekeleza majukumu yake kutokana na michango ya wadau.
Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa inayokabili Mfuko huo ni kukosa mitaji ya kutosha kutoa huduma zote zilizokusudiwa kwa kuwa michango ya wadau ni midogo. Mfuko unaandaa mkakati wa kutafuta mtaji kutoka taasisi za fedha ili waweze kuanza kutoa huduma zilizokusudiwa ikiwa ni pamoja na mikopo ya pembejeo kwa wakulima wa kahawa.
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itahakikisha wakulima wanapata pembejeo za kilimo kama mbolea kwa wakati kwa kuwa tatizo hilo limekuwa sugu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Neema William Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum, baada ya kutoa maelezo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa usambazaji wa pembejeo ni wa soko huria na kwamba, wakulima hujinunulia pembejeo wenyewe kutoka kwa Makampuni ya Pembejeo ambao wana Mawakala wao wanaosambaza na kuuza pembejeo Mikoani, Wilayani hadi Vijijini. Kwa upande mwingine Serikali hutoa pembejeo za ruzuku kwa ajili ya mbolea na mbegu kwa mazao ya mahindi na mpunga kwa wakulima wa badhi ya kaya maskini vijijini ili wajikwamue na kadhia ya upungufu wa chakula katika kaya zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo, sasa napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaweka utaratibu kwamba maandalizi ya vocha kwa ajili ya ruzuku ya pembejeo zinakuwa tayari mapema ili ziendane na muda ambao wakulima wanauza mazao yao, ili iwe rahisi kwao kuchangia 50% ya gharama za pembejeo na kujipatia pembejeo mapema. Vilevile Serikali itawalipa makampuni shiriki katika mpango wa ruzuku ya pembejeo mapema iwezekanavyo ili pia watoe huduma bila vikwazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuwahimiza wafanyabisahara wa pembejeo za kilimo, hususan mbegu na mbolea, kuhakikisha kwamba wanapeleka pembejeo kwa wakati. Aidha, Serikali itafanya uchunguzi kubaini mawakala ambao wanachelewesha pembejeo ili kuona namna ya kuwanyima leseni. Tayari Serikali inapitia mfumo wa sasa wa upatikanaji wa pembejeo kwa lengo la kuja na mfumo mpya utakaoweza kuwapatia wakulima pembejeo kwa wakati na kwa bei nzuri. Ahsante sana.
MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza:-
Mfumo wa sasa wa kuwahudumia wakulima wa zao la tumbaku wa Wilaya ya Urambo na Mkoa wa Tabora kwa ujumla una mapungufu mengi yanayowaletea wakulima usumbufu kama vile bei za pembejeo kuwa kubwa kutokana na kuagizwa nje na riba kubwa za benki, masoko ya tumbaku kutokuwa na uhakika na hatimaye kusababisha kushuka thamani ya tumbaku, bei inayobadilika pamoja na uchache wa wanunuzi:-
(a) Je, ni kwa nini hasara inayotokana na matatizo hayo ibebwe na mkulima peke yake?
(b) Je, Serikali imejipanga vipi kuondoa matatizo hayo ili mkulima wa tumbaku anufaike na kilimo na hatimaye ajikwamue kiuchumi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi kujibu swali la Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta, Mbunge wa Urambo, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kuwa yapo maeneo mbalimbali yanayomkosesha mkulima mapato. Maeneo haya ni pamoja na mfumo wa usambazaji pembejeo uliokuwa na mianya mingi inayosababisha madeni hewa, baadhi ya viongozi wa vyama kukopa fedha nyingi kupita uwezo wa vyama wa kuzalisha tumbaku na kadhalika. Kwa sasa Serikali imebadili mfumo huo na kuelekeza wagavi wa pembejeo hizo kuzifikisha moja kwa moja kwenye vyama vya msingi tofauti na utaratibu wa awali wa kupitisha pembejeo kwenye vyama vikuu. Aidha, ili kuwa na uhakika wa soko kilimo cha tumbaku nchini huendeshwa kwa mkataba kati ya wanunuzi na wakulima. Hivi sasa bei hupangwa kabla ya msimu wa kilimo kuanza ili mkulima ajue bei na kiasi anachotakiwa kuzalisha. Tatizo la soko na bei mara nyingi huwakumba wale wakulima wanaozalisha tumbaku bila kuwa na mikataba ambapo hujikuta tumbaku yao ikikosa soko au wakipewa bei ya chini.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua za kukabiliana na changamoto zinazomkabili mkulima wa tumbaku. Hatua hizo ni pamoja na kuboresha mfumo wa upangaji wa bei ya tumbaku ambapo wakulima upendekeza bei yenye tija kwao na kuiwasilisha kwa wanunuzi kupitia vikao vya Halmashauri ya Tumbaku yaani Tobacco Council. Bei hiyo hujadiliwa na hatimae kufikia muafaka. Mfumo huu wa upangaji wa bei umeanza kutumika rasmi msimu wa mwaka 2015/2016. Sanjari na maboresho ya mfumo huu Serikali inaendelea na jitihada za kuongeza wanunuzi wa tumbaku kutoka China ili kuongeza ushindani kumwezesha mkulima kupata bei nzuri. Aidha, Serikali itapitia tozo za pembejeo zinazoingia nchini na kuangalia uwezekano wa kuziondoa ili kumpunguzia mkulimba gharama ya uzalishaji.
MHE. ALLY SALEH ALLY aliuliza:-
Wavuvi kutoka Ukanda wa Uvuvi wa Kisiwa cha Unguja na wale wa Ukanda wa Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani wamekuwa wakifanya uvuvi kwenye maeneo yanayoingiliana, lakini hivi punde wavuvi wa Unguja wameanza kusumbuliwa na kuwekewa vikwazo vya kuvua maeneo ya Tanzania Bara:-
(a) Je, kwa nini wavuvi hao wasumbuliwe na kuwekewa vikwazo?
(b) Je, wavuvi hao hawana haki ya kuvua maeneo hayo?
(c) Je, ni kwa nini Serikali isiwaelimishe juu ya wanachotakiwa kufanya au wasichotakiwa kufanya?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Saleh Ally, Mbunge wa Malindi, lenye vipengele (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, shughuli za uvuvi kwenye maji ya kitaifa na maji baridi si moja ya suala la Muungano. Hivyo uvuvi katika maji hayo husimamiwa kupitia Sheria ya Uvivi, Na. 22 ya 2003 kwa upande wa Tanzania Bara na Sheria ya Uvuvi, Na. 7 ya 2010 kwa upande wa Zanzibar. Uvuvi katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari Kuu, husimamiwa na Serikali zote mbili kupitia Sheria ya Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu, Na.1 ya 1998 na marekebisho ya 2007.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuondoa usumbufu unaoweza kujitokeza kwa wavuvi, Serikali zetu zimeweka utaratibu unaoitwa Dago au uvuvi wa makambi ambao unatoa fursa au ruhusa kwa wavuvi kutoka Zanzibar na Tanzania Bara kuvua bila kusumbuliwa. Kupitia utaratibu huu, wavuvi wanatakiwa kuwa na utambulisho kutoka maeneo yao na kuwasilisha maeneo wanayokwenda kuvua ambao pia huainisha taarifa za uvuvi, zana anazotumia na muda atakaotumia kukaa kwenye Dago.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia majibu ya kipengele (a), wavuvi wa pande zote za Muungano wana haki ya kuvua kwa kufuata utaratibu uliowekwa na kuzingatia maelezo ya Sheria ya Uvuvi katika eneo husika.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatoa elimu kwa wavuvi kuhusu uvuvi endelevu, kwa mfano, kupitia Ofisi za Uvuvi za Halmashauri ambapo mvuvi kabla hajapewa utambulisho, huelimishwa kuhusu utaratibu wa Dago. Vilevile Wizara imeandaa mwongozo wa makambi ambao uko wenye hatua za mwisho kama hatua mojawapo ya kutatua matatizo yanayojitokeza. Hivyo, nawaomba Waheshimiwa Wabunge tuendelee kuwaelimisha wavuvi kufuata sheria na taratibu zilizopo kwa ajili ya uvuvi endelevu kwa vizazi vilivyopo na vijavyo.
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza:-
Mnada wa Magena Wilayani Tarime ulifungwa na kusababisha adha kubwa kwa Halmashauri ya Mji wa Tarime kupoteza mapato ya ushuru wa mifugo inayouzwa nchi jirani ya Kenya, sambamba na ukosefu wa ajira kwa wakazi wa Tarime:-
Je, Mnada huu wa Magena utafunguliwa lini ili kutoa fursa za ajira na kuokoa mapato mengi yanayopotea kwa sasa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther N. Matiko, Mbunge wa Tarime Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mnada wa Magema ulikuwa kati ya minada 10 ya mipakani inayoendeshwa na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Mnada huo ulikamilika kujengwa mwaka 1995 na kufunguliwa mwaka 1996 na ulifanya kazi kwa takribani mwaka mmoja ambapo ng’ombe 104,000 waliuzwa na jumla ya Sh.260,000,000 zilikusanywa kama maduhuli ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza ikiwemo wizi wa mifugo na sababu za kiusalama, mnamo tarehe 14 Mei, 1997, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mara iliagiza mnada huo ufungwe. Ili kuwapatia wafugaji mnada mbadala wa mpakani, Wizara imejenga mnada eneo la Kirumi sehemu ambayo kuna kizuizi asili cha Mto Mara na ujenzi wa Mnada wa Kirumi unaendelea na umekamilika kwa asilimia sitini na unatarajiwa kufunguliwa katika mwaka wa fedha ujao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matunda ya mnada huu yameanza kuonekana ambapo Wizara kwa kushirikiana na uongozi wa mkoa imekusanya jumla ya Sh.221,270,000 kutokana na mauzo ya ng’ombe 9,842, mbuzi na kondoo 4,886 kutoka Mikoa ya Rukwa, Simiyu, Shinyanga, Mara, Mwanza na Kagera.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inatoa wito kwa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kusimamia ipasavyo ukusanyaji wa maduhuli katika minada ya awali ya Mtana, Kewenja, Nyamwaga na Chemakolele. Aidha, ili kupanua wigo wa ukusanyaji wa mapato, Wizara inatoa ushauri kwa Halmashauri za Wilaya ya Tarime kuongeza thamani ya mifugo kwa kujenga kiwanda cha kuchinja, kuchakata, kusindika na kufungasha nyama na bidhaa kadhaa ili kuziuza katika soko la kikanda na nchi za Afrika Mashariki na Kati.
MHE. HAMAD SALIM MAALIM aliuliza:-
Uvuvi ni moja ya vipaumbele vinavyosaidia kusukuma maendeleo ya wananchi wengi wa Tanzania na Taifa letu ni miongoni mwa mataifa maskini duniani:-
Je, Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kwa kiasi gani ili kuwasaidia wavuvi wadogo wadogo wa Tanzania ili kusaidia maendeleo ya Taifa na pia kujikwamua na umaskini uliokithiri?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamad Salim Maalim, Mbunge wa Kojani, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza miradi mbalimbali ikiwemo Mradi wa Maendeleo na Usimamizi Shirikishi wa Uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish) ambao unatekelezwa Tanzania bara na Visiwani. Mradi umelenga kuboresha utawala bora kwenye jamii za wavuvi, kusaidia mitaji, kutoa elimu ya uvuvi endelevu na kuboresha miundombinu ya uvuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (Tanzania Agricultural Development Bank - TADB) na dirisha la Kilimo katika Benki ya Rasilimali (TIB) ili kutoa fursa ya kupata mikopo kwa ajili ya kununua zana za uvuvi. Pia Serikali inaendelea kuwahamasisha wavuvi wajiunge katika Vyama vya Ushirika ikiwemo kuanzisha SACCOS ili kuweza kukopesheka kwenye Taasisi nyingine za kifedha
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kutoa mafunzo kwa wavuvi wadogo ili waweze kuvua katika bahari kuu. Hadi sasa wawakilishi wa wavuvi 99 kutoka Kamati za Uvuvi Zanzibar na Vikundi vya Usimamizi wa Uvuvi (BMUs) Tanzania Bara wamepatiwa mafunzo hayo wakiwemo 47 kutoka Pemba ikiwemo Jimbo la Kojani. Wavuvi hawa baada ya kupatiwa mafunzo hutakiwa kurudi na kufundisha wenzao.
Mheshimiwa Naibu Spika, mafunzo haya ni endelevu na katika mwaka wa fedha 2016/2017 imepangwa wavuvi 50 wapatiwe mafunzo ya namna hiyo. Aidha, Wizara kwa kushirikiana na TAMISEMI imekuwa ikitoa mafunzo kwa wavuvi walio katika Kamati za Uvuvi na BMUs namna ya kudhibiti uvuvi haramu ili kuwahakikishia wavuvi wadogo uvuvi endelevu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza mpango kutoa ruzuku kwa wavuvi wadogo unaolenga kuwasaidia kuoata zana bora na vifaa vya kuvulia zikiwemo injini za boti kwa kuchangia asilimia 40% ya gharama. Katika awamu ya kwanza, injini 73 zimenunuliwa na taratibu za kuzisamabaza zinaendelea.
Vilevile, Serikali kupitia miradi na programu mbalimbali imejenga mialo na masoko ya samaki katika Ukanda wa Ziwa Victoria 29, Ziwa Tanganyika minne na Bahari ya Hindi mitatu. Kuwepo kwa mialo hii kumepunguza upotevu wa samaki baada ya kuvuliwa hivyo kuongeza thamani na bei ya samaki kwa wavuvi wadogo. Naomba kuwasilisha.
MHE. GIBSON B. MEISEYEKI aliuliza:-
Kwa nini Serikali isifanye jitihada za makusudi za kuwatafutia wafugaji mbegu bora za mifugo aina mbalimbali na kuwasambazia wafugaji kwa bei nafuu ili kuondokana na aina za mifugo ambayo haina tija kwa wafugaji?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Gibson Ole-Meiseyeki, Mbunge wa Arumeru Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inafanya jitihada za makusudi kuhakikisha wafugaji wanapata mbegu bora za mifugo kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo uhimilishaji kwa kutumia mbegu bora za mifugo zinazozalishwa katika Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji cha Usa River (NAIC). Katika kipindi cha mwaka 2007/2008 hadi 2015/2016 kituo kilizalisha jumla ya dozi 951,789 za mbegu bora za ng‟ombe na kusambazwa nchini ambapo jumla ya ng‟ombe 871,183 wa maziwa na ng,ombe 80,606 wa nyama walihimilishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, katika jitihada za kuwezesha wafugaji kupata huduma hii kwa urahisi, Serikali imeanzisha vituo sita vya Kanda vilivyopo, Kibaha (Pwani), Lindi (Lindi), Kizota (Dodoma), Uyole (Mbeya), Kituo cha Uchunguzi wa Magonjwa ya Mifugo cha Mwanza (Mwanza) na Mpanda (Katavi). Pia Serikali inaendelea na ujenzi wa kituo kingine cha Taifa cha Uhimilishaji cha Sao Hill kilichopo kwenye shamba la kuzalisha mitamba la Sao Hill (Mafinga-Iringa) kwa lengo la kusambaza huduma hii ya uhimilishaji katika Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Serikali inazalisha na kuwasambazia wafugaji mifugo bora (majike na madume) kwa bei ya ruzuku kutoka katika mashamba yake. Mashamba haya yanazalisha mitamba ya ng‟ombe wa maziwa, mitamba na madume ya ng‟ombe wa nyama, mbuzi wa maziwa na nyama, kondoo na nguruwe. Kwa mfano, mtamba wa ng‟ombe wa maziwa unauzwa kati ya shilingi 800,000 – 1,000,000/= ikilinganishwa na bei ya soko iliyopo ya kati ya shilingi 1,200,000/= na 2,300,000/=. Aidha, katika kipindi cha mwaka 2009/2010 hadi 2015/2016, jumla ya mitamba 4,520 ilizalishwa na kusambazwa katika mikoa yote nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuhamasisha sekta binafsi kuona fursa ya kibiashara katika kuzalisha mbegu bora za mifugo ili kukidhi mahitaji. Aidha, nawashauri Waheshimiwa Wabunge waendelee kuwahamasisha wafugaji wakiwemo wa Jimbo la Arumeru Magharibi kutumia huduma za kuboresha mifugo zinazopatikana kwenye vituo vyetu ili kujipatia mifugo yenye tija.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA aliuliza:-
Je Serikali imejipangaje kuwafidia au kuwapa kifuta machozi wananchi wa Kata za Magawa na Msonga katika vijiji vya Makumbaya, Magewa na Msonga ambao mikorosho kwenye mashamba yapatayo ekari 1000 imeangamia kutokana na ugonjwa wa ajabu na kuwaacha wananchi hawana kitu na hasa ikizingatiwa kuwa baadhi ya maeneo wananchi wanaopatwa na majanga kama haya wamekuwa wakilipwa fidia au hata kifuta machozi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, KILIMO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niamba ya Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Hamis Ulega, Mbunge wa Mkuranga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kawaida Serikali haina utaratibu wa kulipa fidia ya athari za maafa, ila ina wajibu wa kuwahudumia wananchi wake wanapokumbwa na majanga. Wizara yangu ilipata taarifa za kuwepo kwa ugonjwa huo na kuelekeza wataalam kufanya utafiti ili kubaini sababu, namna ya kuzui pamoja na tiba. Baada ya utafiti huo, iligundulika kuwa na ugonjwa huo unasababishwa na kuvu (fungus) aina ya Fussarium wilt. Hivi sasa Taasisi yetu ya Utafiti ya Naliendele inaendelea na majaribio ya viuatilifu vitakavyoweza kutibu ugonjwa huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango uliopo wa kuwasaidia wakulima kama ilivyo utaratibu wa Serikali ni kusambaza miche mipya ya korosho inayohimili ugonjwa katika maeneo yanayoathirika baada ya kupata mahitaji halisi kutoka Halmashauri. Aidha, namshauri Mheshimiwa Mbunge na Halmashauri ya Mkuranga kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kufanya tathmini ya kina ili kuona kama athari za ugonjwa huo zina tishio la watu kufa njaa, ili utaratibu wa kuomba chakula cha msaada ufanyike mara moja kuokoa maisha ya watu wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jitihada hizo kupitia Bodi ya Korosho Tanzania, taarifa za tahadhari zimeanza kutolewa kupitia vyombo vya habari kwa wakulima ambapo pamoja na mambo mengine, wakulima wameaswa kuteketeza mikorosho iliyoathirika na ugonjwa huo na kuepuka kuhamasisha udongo kutoka kwenye naeneo yaliyoathirika kwenda kwenye maeneo mengine.
MHE. SULEIMAN A. SADDIQ (K.n.y. MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA) aliuliza:-
Amani na utulivu ni muhimu sana katika maisha ya binadamu.
Je, ni lini mgogoro wa wakulima na wafugaji katika Wilaya za Mvomero na Kilosa, Mkoani Morogoro utaisha lini ili wananchi waweze kuishi kwa amani na utulivu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christine Gabriel Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kumekuwa na migogoro ya mara kwa mara katika Wilaya za Mvomero na Kilosa ambayo imesababisha uvunjifu wa amani na upotevu wa mali na maisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, uongozi wa Mkoa wa Morogoro umechukua hatua mbalimbali ili kutatua migogoro sugu. Hatua hizo ni pamoja na kupima na kuhakiki upya maeneo ya Kijiji cha Mabwegere, Wilaya ya Kilosa na vijiji vinavyozunguka Bonde la Mto Mgongola ikiwemo Kijiji cha Kambala Wilaya ya Mvomero. Kutokana na upimaji upya wa vijiji hivyo, kupitia Tume ya Taifa ya Matumizi ya Ardhi, kazi ya kuweka mipango ya matumizi bora ya ardhi inaendelea. Lengo ni kupima vijiji vyote na kutenga maeneo ya wakulima na wafugaji ambapo maeneo ya ufugaji yatasajiliwa. Vilevile uongozi wa Mkoa uliunda Kamati ya Usuluhisi wa Mgogoro wa Mabwegere na Kamati hiyo imekamilisha kazi, ripoti iliwasilishwa kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mahitaji ya ardhi ni makubwa katika Mkoa wa Morogoro kutokana na hali ya hewa na rutuba, hali hii ndiyo inasababisha watu kutoka Mikoa mingine kuhamia Mkoa huo kwa ajili ya kilimo na ufugaji. Kutokana na msukumo wa mahitaji makubwa ya ardhi na kuwepo kwa migogoro Mkoa uliamua kufanya tathmini katika Wilaya ya Mvomero na kugundua kuwepo kwa mashamba yasiyoendelezwa. Mkoa ulimwomba Mheshimiwa Rais, afute hati za umiliki wa mashamba hayo na hadi sasa mashamba sita yeye jumla ya hekta 1,880.6 yamefutiwa hati.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa una mpango wa kugawa mashamba hayo kwa wakulima na wafugaji ili kupunguza migogoro baina ya jamii hizo. Mashamba hayo hapo katika vijiji vya Wami Luhindo, katika maana ya shamba lililokuwa la Bwana Karim B. Walji lenye hekta 500, shamba la Bwana Lusingo Kibasisi lenye hekta 200, shamba la Bwana Nicolaus Anthony la hekta 52.3, shamba la Joseph R. Hall lenye hekta 166 na shamba la D. H. Kato Farms lenye hekta 247. Vilevile katika kijiji cha Nguru ya Ndege ambapo kuna shamba la Badrun na Karim Dharamishi lenye hekta 392.6 na katika Kijiji cha Wami Valley ambapo kuna shamba la Emmanuel J. Gereta lenye hekta 545.
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA aliuliza:-
(a) Je, katika kipindi cha mwaka 2010 - 2015, ni ng‟ombe wangapi wametaifishwa na Serikali kwa kuingia katika Hifadhi ya Kigosi eneo linalopakana na Jimbo la Ushetu katika Kata za Ulowa, Ubagwe, Ulewe, Nyamkende na Idalia?
(b) Je, ni utaratibu gani unatumika kuua ng‟ombe wanaoingia kwenye hifadhi; na ni ng‟ombe wangapi waliuawa katika kipindi cha mwaka 2010 - 2015?
NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na utalii, kwa mara nyingine tena, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Elias John Kwandikwa, Mbunge wa Ushetu, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, chini ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 27(1), kila mtu ana wajibu wa kulinda maliasili ya Jamhuri ya Muungano. Aidha, Sheria ya Kuhifadhi na Kulinda Wanyamapori, Na. 5 ya mwaka 2009, vifungu vya 18(2) na 21(1) vinakataza mtu yeyote kuingiza mifugo, kuchunga au kulisha mifugo ndani ya Hifadhi za Taifa, Mapori ya Akiba na Mapori Tengefu. Chini ya kifungu cha 111(1) cha sheria hiyo, mtu aliyepatikana na hatia ya kuingiza mifugo ndani ya hifadhi atanyang‟anywa mifugo hiyo kwa amri ya Mahakama.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na changamoto kubwa ya wafugaji kuingiza mifugo wengi katika Pori la Kigosi wanaohatarisha ustawi wa hifadhi hiyo. Serikali Wilaya ya Ushetu na Mkoa wa Shinyanga wamekuwa wakitoa elimu kwa wananchi juu ya athari ya kupeleka mifugo ndani ya hifadhi kwa Mapori ya Akiba na msimamo wa sheria.
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha mwaka 2010 - 2015 hakuna ng‟ombe waliotaifishwa na Serikali katika Wilaya ya Ushetu.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imebaini kwamba watu wanaopeleka mifugo ndani ya mapori ya Kigosi/Moyowosi ni pamoja na wageni toka nchi ya jirani ambao wanaingia hifadhini na silaha za kivita. Katika jitihada za kuwatoa wafugaji wa aina hii katika hifadhi, maafa yametokea hapa na pale. Askari kadhaa Wanyamapori wamepoteza maisha, mifugo kadhaa wameuawa katika mazingira ya aina hii; hata hivyo Serikali haina sera, sheria, kanuni au utaratibu wa kuua mifugo.
MHE. SILVESTRY F. KOKA aliuliza:-
Serikali kwa nia njema ilirejesha sehemu ya shamba la Mitamba lililopo Kata ya Pangani, Kibaha Mjini kwa wananchi ambao walikuwa wanaishi katika maeneo hayo:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuendelea kurejesha maeneo mengine ya shamba hilo ambayo bado yanakaliwa na wananchi?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Silvestry Francis Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijajibu swali lake namba 66 naomba kutoa maelezo yafuatayo:-
Shamba la Mitamba Pangani linamilikiwa na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Wizara ilipata shamba hili kwa kulipia fidia kwa wamiliki wa asili, ukubwa wa shamba lililokuwa limemilikiwa ni ekari 4000. Hata hivyo, katika kipindi kifupi baada ya wananchi kulipwa fidia, shamba hilo lilivamiwa na wananchi kutoka sehemu mbalimbali na kuanzisha Mtaa wa Kidimu. Katika kutatua mgogoro huo wa uvamizi mwaka 2004, wamiliki Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na Uongozi wa Serikali wa Mtaa huo ziliafikiana kuweka mipaka ya muda.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa 2007 Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ilipima shamba hilo kwa kuzingatia mipaka ya makubaliano yaliyoafikiwa mwaka 2004. Baada ya upimaji kulizalishwa kiwanja Namba 34 chenye ukubwa wa hekta 1037.81 na eneo lililokuwa limevamiwa lilikuwa na ukubwa wa hekta 2963, lilikabidhiwa kwa Halmashauri ya Mji wa Kibaha ili lipangiwe na kupimwa kwa ajili ya wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na upimaji kufanyika bado kuna mgogoro kati ya wamiliki wa shamba na wananchi wanaodai kutolipwa fidia wakati wa utwaaji wa shamba hilo waliokuwa ndani ya shamba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vipindi tofauti Wizara yangu kwa kushirikiana na wamiliki Ofisi ya Mkoa wa Pwani, Ofisi za Wakuu wa Wilaya za Kibaha Mji na Wilaya na wananchi wanaoishi kwenye shamba hilo, tumekuwa tukikutana mara kwa mara kwa lengo la kupata ufumbuzi wa kudumu wa mgogoro huo. Mfano, tarehe 4/3/2016, Timu ya Wataalam kutoka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Halmashauri ya Mji wa Kibaha na Mkurugenzi wa Upimaji na ramani ukiongozwa na Kamishna wa Ardhi Msaidizi wa Kanda ya Mashariki, ilikutana uwandani kwa lengo la kuhakiki mipaka na nyaraka za walalamikaji walio ndani ya shamba. Kwa sasa tunasubiri taarifa ya utekelezaji ambayo bado wataalam wanaendelea kufanyia kazi na mara itakapokamilika tutakuwa na ufumbuzi wa kudumu wa mgogoro huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwepo na tabia ya wananchi kuvamia maeneo ya Serikali na Taasisi zake, ili kuepuka hali hii tunaomba Waheshimiwa Wabunge na Viongozi mbalimbali kila mmoja kwa nafasi yake kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuacha mazoea yaliyojengeka ya kuvamia maeneo ya Serikali na Taasisi zake na maeneo mengine.
MHE. JANET Z. MBENE (K.n.y MHE. SIXTUS R. MAPUNDA) aliuliza:-
Kumekuwa na ongezeko kubwa la kampuni kubwa kuanzisha mashamba ya Kahawa katika maeneo ya Wilaya ya Mbinga na sehemu za Songea Vijijini jambo linalotishia uzalishaji na soko kwa Wakulima wadogowadogo wa Kahawa.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwalinda wakulima wadogo wasimezwe na wakulima wakubwa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi ningependa kujibu swali la Mheshimiwa Sixtus Paphael Mapunda, Mbunge wa Mbinga Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kumekuwepo na ongezeko la kuanzishwa kwa mashamba makubwa ya Kahawa katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na Wilaya za Mbinga na Songea Vijijini. Hali hii inachangiwa na sera na mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyopo nchini. Aidha, uwepo na uanzishwaji wa mashamba makubwa nchini hautishii uzalishaji na soko la kahawa kwa Wakulima wadogo wa Kahawa bali una manufaa yafuatayo:-
(i) Uanzishwaji wa uwepo wa mashamba makubwa unawezesha wakulima wadogo walio karibu na mashamba hayo kujifunza teknolojia mbalimbali zinazotumiwa na mashamba hayo katika kuongeza tija na uzalishaji wa kahawa.
(ii) Baadhi ya mashamba makubwa yanaendesha miradi ya kuwasaidia wakulima wa kahawa walio karibu na mashamba hayo (out growers schemes) kwa kuwapa huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na huduma za ugani, ukoboaji na masoko ya Kahawa yao. Kwa mfano, shamba la AVIV lililopo Lipokela Halmashauri ya Wilaya ya Songea limekuwa likitoa huduma za ugani kwa wakulima wanaolizunguka. Aidha, mpaka sasa kiasi cha miche 550,000 imekwishagawanywa kwa wakulima tangu shamba hilo lianzishwe miaka minne iliyopita.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na manufaa hayo, Serikali ilifanya marekebisho ya Kanuni zinazoongoza tasnia ya Kahawa ili kuwalinda wakulima wadogo wanaoingia makubaliano ya uzalishaji wa Kahawa na makampuni binafsi pamoja na mashamba makubwa.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO aliuliza:-
Mkoa wa Kigoma ni kati ya Mikoa mitatu inayopata mvua nyingi katika nchi yetu kwa wastani na takribani milimita 1,300 kwa mwaka ikifuatiwa na Mkoa wa Katavi.
(a) Je, ni kwanini Serikali haifanyi jitihada ya kuwekeza katika kilimo ili kunufaika na uwepo mzuri wa hali ya hewa?
(b) Je, ni kwanini Mkoa wa Kigoma uliondolewa katika Mikoa na yenye uzalishaji mkubwa na kupata mgao mdogo wa pembejeo?
(c) Je, ni kwanini kituo cha Mbegu cha Bugaga kilichopo Wilaya ya Kasulu kimetekelezwa.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi ningependa kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Nicodemus Nsanzugwanko, Mbunge wa Kasulu Mjini lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa kwa siku za nyuma Mikoa ya pembezoni ukiwepo Mkoa wa Kigoma imekuwa na changamoto nyingi za kimaendeleo kutokana na kukosekana kwa miundombinu muhimu kwa maendeleo. Serikali imefanya jitihada kubwa kuwezesha uwekezaji katika Mikoa hii ikiwa ni pamoja na kukamilisha ujenzi wa miundombinu muhimu kama barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa katika Mkoa wa Kigoma, zinaendelea tafiti mbalimbali za kilimo kwa kushirikiana na wadau wengine kama vile kampuni ya Kigoma Sugar kwa zao la Miwa, na Belgium Technical Cooperation kwa zao la chai kabla ya kuanza kuhamasisha sekta binafsi kwa uzalishaji mkubwa. Aidha, Mkoa wa Kigoma uko katika mpango wa BRN katika kilimo cha miwa (Sugarcane Cluster) ambapo katika mpango huo, mashamba makubwa mawili yameshatambuliwa na wawekezaji kama vile Kigoma Sugar wameshaonyesha nia ya kuzalisha sukari kwa kushirikiana na wakulima wadogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Kigoma umepewa kipaumbele kwa upande wa ruzuku ya pembejeo ambapo ni kati ya Mikoa mitano iliyopewa ruzuku kubwa ya pembejeo kwa msimu wa 2015/2016 kati ya Mikoa 24 Nchini. Hii ni kutokana na umuhimu wake katika uzalishaji mkubwa wa chakula hasa mahindi hapa Nchini. Idadi ya kaya zilizopata ruzuku ya pembejeo za kilimo katika Mkoa wa Kigoma imeongezeka kutoka kaya 60,239 msimu wa 2013/2014 na kufikia kaya 74,000 msimu wa 2015/2016. Aidha, mgao mdogo wa ruzuku ya pembejeo za kilimo kwa wakulima kila Mkoa ikilinganishwa na mahitaji hutokana na ufinyu wa bajeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, shamba la kuzalisha mbegu la Bugaga lenye ukubwa wa hekta 336.906 limekaa muda mrefu bila kuzalisha mbegu kutokana na ufinyu wa fedha. Wizara imeweka mkakati wa kulifufua shamba hilo katika msimu wa 2016/2017 ili liweze kuzalisha mbegu kwa wingi kwa ajili ya wakulima wa Kanda ya Magharibi ikiwemo Wilaya ya Kasulu. Aidha, Serikali inahimiza makampuni na vikundi mbalimbali Mkoani Kigoma kushirikiana na ASA katika shughuli za uzalishaji mbegu za mazao mbalimbali ili kuchangia maendeleo ya kilimo katika Mkoa wa Kigoma.
MHE. JESCA D. KISHOA aliuliza:-
Moja ya njia ya kuimarisha uchumi ni kupunguza uagizaji wa bidhaa nje ya nchi, Taifa linatumia fedha nyingi za kigeni kuingiza mafuta ya kula wakati kuna vyanzo vingi vya mafuta kama vile alizeti - Singida na Michikichi – Kigoma.
Je, ni lini Serikali itaweka msukumo kwa mazao haya katika mikoa hii kwa faida ya nchi na wakazi wa mikoa hiyo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvivi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jesca David Kishoa, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa linatumia fedha nyingi za kigeni kuagiza mafuta ya kula wakati kuna vyanzo vingi vya mafuta kama alizeti na michikichi kwa sababu mbalimbali. Ili kukabiliana na changamoto hii Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imeandaa mikakati inayolenga kuongeza tija na uzalishaji wa mbegu za mazao ya mafuta hususani alizeti ambazo uzalishaji wake umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka.
Aidha, katika Mkoa wa Singida vikundi mbalimbali vimeundwa na taasisi mbalimbali za Serikali na zile zisizo za kiserikali. Mojawapo ya malengo ya vikundi hivyo ni kuongezea thamani kwa maana ya value addition ya zao la alizeti na upatikanaji wa pembejeo ili kukuza tija na uhakika wa masoko kwa wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kigoma ni mkoa pekee nchini unaolima zao la mchikichi kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na maeneo mengine nchini. Hadi sasa mkoa una zaidi ya hekta 18,924 za michikichi zenye tija ya tani 1.6 kwa hekta. Uzalishaji huu bado ni mdogo sana ikilinganishwa na tani 4.0 kwa hekta zinazoweza kuzalishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuongeza tija, mkoa kupitia Halmashauri zake unaendelea kuhamasisha wananchi kufufua mashamba ya zamani ya mchikichi kwa kuyapalilia, kuondoa majina yaliyozeeka na kuanzisha mashamba mapya yatakayokuwa yanapandwa mbegu bora. Vilevile Mkoa kwa kushirikiana na wadau wengine umeshaanza kuzalisha miche bora ya michikichi ambayo itasambazwa kwa wakulima kwa gharama nafuu ili kila mkulima apande miche 137 inayotosha hekari moja.
Pia wajasiriamali wanawezeshwa kupata mashine bora za kusindika michikichi; Serikali Kuu na Serikali ya Mkoa tunakaribisha wawekezaji zaidi kuwekeza katika uzalishaji mkubwa na viwanda vya kati na vikubwa vya kukamua mafuta na bidhaa nyingine zitokanazo na michikichi.
MHE. GIMBI D. MASABA aliuliza:-
Wakazi wengi wa Mkoa wa Simiyu huendesha maisha yao kwa kutegemea kilimo na ufugaji, ambapo Mkoa huo umepakana na maeneo makubwa na mazuri kwa kazi hizo jirani na Mbuga ya Serengeti:-
(a) Je, Serikali itatenga lini maeneo ya kilimo na mifugo kwenye vijiji vinavyopakana na Mbunga ya Serengeti?
(b) Je, Serikali itathamini lini mifugo na mazao ya wakulima hawa kama vile inavyothamini wanyamapori wa mbugani kwani huonekana ni halali kwa wanyama pori kuua/kuharibu mazao ya wananchi wakati siyo halali wananchi kuingiza mifugo au kuchimba hata mizizi ndani ya mbuga ya wanyama?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Gimbi Dotto Masaba, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Matumizi Bora ya Ardhi na kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya zenye vijiji vinavyopakana na mbuga ya Serengeti imeshachukua hatua za kuandaa mipango shirikishi ya matumizi bora ya ardhi ya vijiji vinavyohusika. Tayari vijiji 73 katika Wilaya za Serengeti, Tarime, Bunda na Bariadi vimeshakamilisha mipango hiyo, kinachotakiwa sasa ni kwa Halmashauri hizo kuhakikisha kwamba vijiji ambavyo tayari vina mipango ya matumizi bora ya ardhi vinaitekeleza ipasavyo na kuimarisha usimamizi. Naomba Mheshimiwa Mbunge kushirikiana na Halmashauri husika ili vijiji visivyokuwa na mipango ya matumizi bora ya ardhi navyo viweze kuwa nayo ili faida za mipango hiyo ziwafikiwe wananchi wote.
Mheshimiwa Spika, Serikali inathamini mifugo na mazao ya wakulima na imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kuepusha migogoro kati ya binadamu na wanyama pori na pia kuhakikisha kwamba maisha ya binadamu na mali zao yanalindwa kikamilifu. Hii inadhihirishwa na jinsi Serikali inavyosaidia vijiji kuwa na miradi ya ujirani mwema kwa vijiji vinavyozunguka maeneo ya hifadhi na vijiji hivyo kuwa na mipango shirikishi ya matumizi bora ya ardhi.
Aidha, kwa kutambua umuhimu wa maisha ya binadamu, mazao na mifugo Serikali imeweka utaratibu wa kuchukua hatua za haraka za kufukuza wanyama pori mara inapotokea wameingia katika makazi na mashamba ya wananchi na wakati mwingine inapobidi Serikali hutoa kifuta machozi au kifuta jasho kwa waathirika.
MHE. LEONIDAS T. GAMA aliuliza:-
Kilimo cha mahindi ndiyo shughuli kubwa ya kiuchumi kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma, lakini kumekuwa na bei kubwa ya mbolea na ruzuku hutolewa kwa wakulima wachache tu.
(a) Je, Serikali haioni utaratibu huu wa ruzuku kwa wakulima wachache umekuwa na changamoto kubwa ya kupotea kwa vocha kunakofanywa na watumishi wasio waaminifu?
(b) Je, kwa nini Serikali isitoe ruzuku kwa wakulima wote kupitia taasisi maalum kama TFC na kuacha mfumo huu wa vocha?
(c) Je, Serikali haijui wakulima walio wengi ni maskini na ndiyo wanaowalisha Watanzania wote?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leonidas Tutubert Gama, Mbunge wa Songea Mjini, lenye sehemu (a) b) na (c) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kumekuwepo na changamoto ya upotevu wa vocha za ruzuku ya pembejeo, unaofanywa na watumishi wasio waadilifu kwa kushindwa kusimamia ipasavyo utaratibu huu katika Halmashauri zao. Serikali inaendelea na taratibu za kuwachukulia hatua watumishi wanaohusika na ubadhirifu katika mfumo wa ruzuku za pembejeo; hii ni pamoja na kupelekwa mahakamani wahusika, na baadhi ya kesi zimeishatolewa hukumu ambapo wahusika wanatumikia adhabu mbalimbali ikiwemo vifungo, kushushwa vyeo na kufukuzwa kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili mpango wa ruzuku uweze kunufaisha Wakulima wote nchini, Wizara yangu inaandaa mapendekezo ya mfumo wa ruzuku ya pembejeo ambao utawafikishia wakulima wote pembejeo zikiwa na ruzuku na zipatikane popote nchini na kwa wakati wote na hivyo kuongeza tija na uzalisha na kuwa na uhakika wa usalama wa chakula katika ngazi ya Taifa na kaya. Kwa kupitia mpango huu ni wazi kuwa bei ya mbolea itapungua na hivyo kuwezesha wakulima wengi zaidi kumudu kununua mbolea na kuzitumia ipasavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali ina mpango wa kuwezesha ujenzi wa kiwandakikubwa cha kuzalisha mbolea nchini katika Wilaya ya Kilwa. Tayari wawekezaji wa ujenzi wa kiwanda hicho, wameishapatikana na kwa sasa majadiliano kati ya wawekezaji hao na Serikali yanaendelea. Kama kiwanda hicho kitafanikiwa kujengwa, kitakuwa na uwezo wa kuzalisha mbolea tani milioni 1.2 kwa mwaka, vilevile kampuni ya Live Support System inatarajia kujenga kiwanda cha mbolea katika Wilaya ya Kibaha, kitakachokuwa na uwezo wa kuzalisha tani 500 kwa siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati wa ujenzi wa viwanda vya mbolea hapa nchini, utawezesha upatikanaji wa mbolea kwa gharama nafuu, hivyo kuwezesha wakulima wengi kutumia mbolea na kuongeza tija na uzalishaji. Serikali inatambua mchango wa wakulima wadogo katika kuhakikisha kunakuwa na chakula cha kutosha nchini na inapongeza sana juhudi zinazofanywa na wakulima hao. Aidha, Serikali inatambua umaskini wa kipato walionao wakulima hao na ndio maana inakuja na mipango mbalimbali ya kuwasaidia ikiwa ni pamoja na ruzuku katika pembejeo za kilimo.
MHE. RASHID A. SHANGAZI (k.n.y MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA)aliuliza:-
Wakulima wa zao la tangawizi katika Jimbo la Same Mashariki wanahamasishwa kulima tangawizi kwa wingi kwa matarajio kuwa Kiwanda cha Tangawizi kilichokuwa kinatarajiwa kufanya kazi kingeweza kusaga tangawizi hiyo kwa kiasi cha tani tisa kwa siku; na kwa vile kiwanda hicho hakijaweza kufanya kazi tangu kifunguliwe na aliyekuwa Rais wa wakati huo Mheshimiwa Jakaya Kikwete, tarehe 29 Oktoba, 2012 huko Mamba Miyamba, Wilayani Same Mashariki:-
Je, Serikali inawasaidiaje wakulima hao kupata soko la zao hilo ambalo imeshindikana kuliongezea thamani, processing na matokeo yake wanunuzi ni wachache na wanawapunja sana wakulima wanaponunua zao hilo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Naghenjwa Livingstone Kaboyoka, Mbunge wa Same Mashariki kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Same inaongoza kwa uzalishaji wa tangawizi hapa nchini. Hivyo ushirika wa wakulima wa tangawizi wa kata ya Mamba Miamba uliamua kujenga kiwanda ili kuongeza thamani ya zao hilo.
Baada ya kiwanda hicho kuzinduliwa, kiliweza kusindika zaidi ya tani 100, kabla ya baadhi ya mitambo yake kupata hitilafu na kusitisha usindikaji. Shirika la SIDO lilijulishwa kuhusiana na hitilafu hizo kwa kuwa ndilo lililosanifu na kutengeneza mitambo hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumjulisha Mheshimiwa Mbunge kuwa taarifa nilizopata kutoka kwa Ofisi ya RAS wa Mkoa wa Kilimanjaro ni kwamba tayari SIDO wamekamilisha matengenezo hayo na kinachosubiriwa ni taratibu za makabidhiano.
Mheshimiwa Naibu Spika, soko la tangawizi iliyosindikwa lipo la kutosha ndani na nje ya nchi. Serikali kupitia mradi wa uboreshaji miundombinu ya masoko na uongezaji thamani yaani Marketing, Infrastructure, Value Addition and Rural Financing, kwa kushirikiana na shirika la Faida Mali inaendelea kusaidia ushirika huo kutafuta na kuwaunganisha na masoko ya uhakika, tayari masoko yafuatayo yameishapatikana ambayo ni Kampuni ya Afri Tea ya Dar es Salaam, Kampuni ya Tausi ya Arusha na Kampuni ya Lion Wattle ya Lushoto. Wanunuzi hao wapo tayari kununua tangawizi, iliyosindikwa, mara tu kiwanda kitakapoanza tena kufanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ushirika wa Wakulima wa Tangawizi wa Mamba Miamba, unakabiliwa pia na changamoto nyingine kama vile za uelewa mdogo wa usimamizi na uendeshaji wa kiwanda, ukosefu wa mtaji wa kutosha kwa ajili ya kununua malighafi na gharama za uendeshaji. Changamoto hizo zinapelekea kiwanda kutofanya kazi vizuri. Katika kutatua changamoto hizo, Serikali kupitia wataalam wake wa ushirika na mradi wa MIVARF inaendelea kutoa elimu ya uendeshaji na usimamizi ili hatimaye waweze kuunganishwa na vyombo vya fedha, ili waweze kukopesheka kwa ajili ya kupata mtaji na kuendesha kiwanda kwa faida ya ushirika.
MHE. ALMAS A. MAIGE aliuliza:-
Kilimo cha tumbaku katika Mkoa wa Tabora katika Jimbo la Tabora Kaskazini kinakabiliwa na matatizo ya pembejeo, madeni ya wakulima, viongozi wabovu wa vyama vya ushirika, ukosefu wa wanunuzi, wanunuzi watatu kupanga bei, matatizo haya yanachangiwa na mapungufu ya Sheria ya Ushirika ya Tumbaku:-
(a) Je, ni lini Serikali italeta Sheria za Ushirika na Tumbaku katika Bunge lako tukufu ili zifanyiwe marekebisho?
(b) Kilimo cha tumbaku ni kazi ngumu inayoathiri afya za wakulima. Je, kwa nini Serikali kupitia Bodi ya Tumbaku isiwaagize wanunuzi kuwalipa wakulima posho kwa kufanya kazi inayoathiri afya zao?
(c) Je, ni lini Serikali itatafuta wanunuzi wengine wa tumbaku hasa kutoka China ili kuondoa ukiritimba wa wanunuzi watatu wa tumbaku waliopo sasa nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Almas Athuman Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia mapendekezo ya wadau Bunge lako tukufu lilifanya mabadiliko ya Sheria ya zamani ya Ushirika Namba 20 ya mwaka 2003 hivi karibuni inakuja na sheria mpya ya ushirika namba sita ya mwaka 2013 ambayo utekelezaji wake umeanza. Aidha, endapo kutakuwa na haja ya kufanya tena mapitio au marekebisho ya sheria hiyo kwa kuzingatia maoni ya wadau Serikali haitasita kufanya hivyo. Kuhusu Sheria ya Tumbuka Na. 24 ya mwaka 2001 Wizara kwa sasa inapitia upya ikiwa ni pamoja na kukusanya maoni ya wadau ili ikilazimu iletwe Bungeni kwa nia ya kufanyiwa marekebisho kulinga na hitaji la sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa hakuna sheria, kanuni au utaratibu wowote unaolazimaisha makampuni ya ununuzi wa tumbaku kulipa posho au fidia kwa wazalishaji Serikali inawashauri wadau wa tumbaku kupitia baraza lao kujadili suala hili ili kama wakiona umuhimu wa kutungiwa sheria Serikali ianze kulifanyia kazi.
Aidha, kwa sasa vifaa vya kinga kwa maana ya gloves, gum boots na mask kwa wakulima wa tumbaku vinaingizwa kwenye gharama za uzalishaji wa tumbakuhivyo kuwa sehemu mjengeko wa bei. Wakulima au Vyama vya Msingi wanashauriwa kununua vifaa hivi mara wapokeapo malipo baada ya kuuzwa kwa tumbaku yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikifanya jitihada za dhati za kuongeza ununuzi wa zao la tumbaku ili kuongeza ushindani na hatimaye kuwezesha wakulima kupata bei nzuri. Aidha, kwa sasa kuna jumla ya makampuni manne ya ununuzi wa tumbaku nchini ambayo ni Alliance One Tabacco Tanzania Ltd., Tanzania Leaf Tobacco Company Ltd., Premium Active Tanzania Ltd. pamoja na Japanese Tobacco International Leaf Services.
Mheshimiwa Naibu Spika, licha ya uwezo wa makampuni haya nchini, Serikali bado inaendelea na jitihada za kutafuta wanunuzi wengine wa tumbaku kutoka nchini China na Vietnam ambao baadhi yao wameonyesha nia ya kununua tumbaku ya Tanzania.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA (K.n.y. MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL) aliuliza:-
Shamba la Garagua linalomilikiwa na KNCU lililopo katika Wilaya ya Siha, liliamuliwa liuzwe mwaka 2015 ili kulipa mkopo wa shilingi bilioni nne uliochukuliwa na KNCU na baadaye kushindwa kufanya marejesho ya mkopo huo kwa wakati:-
(a) Je, ni kwa nini Serikali isiwawajibishe viongozi wa KNCU waliousababishia ushirika hasara kwa kuchukua mkopo ambao wameshindwa kuulipa?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuyarudisha mashamba ya ushirika yanayotumika kwa maslahi ya wachache au ambayo ushirika umeshindwa kuyaendeleza katika umiliki wa Halmashauri za Wilaya husika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Godwin Oloyce Mollel, Mbunge wa Siha, lenye vipengele (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Chama Kikuu cha Ushirika cha KNCU Limited kilishindwa kulipa deni la shilingi bilioni 3.4 kutoka CRDB lililokopwa misimu ya 2008/2009 hadi 2010/2011. Ili kubaini sababu za kushindwa kurejesha mkopo, Wizara iliagiza Mrajisi wa Vyama vya Ushirika nchini kufanya ukaguzi na uchunguzi ili kujua kiini cha KNCU kushindwa kulipa deni hilo. Ukaguzi na uchunguzi huo ulibaini hasara ya sh. 3,946,755,736 uliosababishwa na mdodoro wa uchumi na ubadhirifu na uongozi mbovu wa KNCU. Hivyo, Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika ilisimamisha Bodi iliyokuwa madarakani ambayo ilisababisha hasara na kuweka Bodi mpya kama hatua ya awali.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hatua nyingine, Wizara kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika imeanza kuandaa taratibu za kuwachukulia hatua wahusika kwa mujibu wa kifungu cha 15(33) cha Sheria ya Ushirika Na. 6 ya 2013. Aidha, katika kunusuru uuzaji wa mali za KNCU, Mkutano Mkuu wa KNCU uliokaa tarehe 22 Oktoba, 2014 uliazimia kuuzwa kwa shamba la Garagua ili kulipa deni hilo la CRDB na madeni mengine.
(b) Kwa mujibu wa takwimu ambazo Tume ya Maendeleo ya Ushirika inazo, yapo mashamba 96 ya Vyama vya Ushirika nchi nzima yakiwemo 41 Mkoa wa Kilimajaro. Kati ya hayo, mashamba saba yapo Wilaya ya Siha ambapo matatu yanamilikiwa na KNCU na mengine manne yanamilikiwa na Vyama vya Msingi. Mengi ya mashamba haya yamekuwa yakitumika kwa kilimo, ufugaji na ujenzi wa nyumba za makazi ya wanachama na kukodishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa kushirikiana na MKURABITA, TAMISEMI na Vyama Vikuu vya Ushirika nchini inakamilisha maandalizi ya Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi. Mpango huu unatarajiwa kuwasilishwa kwenye kikao kazi kinachofanyika Dodoma, Ukumbi wa Hazina tarehe 27, yaani leo na 28 Juni, 2016. Kikao hicho kitajumuisha Vyama Vikuu vyote vya Ushirika nchini na kukubaliana mkakati wa kuyaendeleza mashamba hayo kwa manufaa ya wanachama na halmashauri kwa ujumla.
MHE. JORAM I. HONGOLI aliuliza:-
Serikali Awamu ya Nne ilianzisha utaratibu wa mbolea za ruzuku ili kuwasaidia wakulima wasio na uwezo wa kununua pembejeo waweze kuzipata na kuboresha kilimo:-
(a) Je, Serikali haioni kama inapoteza fedha nyingi kusambaza pembejeo hizo kupitia mawakala ambao mahali pengine hupeleka mbolea kidogo au wanawasainisha wakulima vocha bila kuwapa mbolea kwa kuwapatia shilingi 5,000 - Shilingi 10,000 na baadaye kurejesha mbolea mahali pengine;
(b) Je, kwa nini Serikali isisambaze mbolea hizo kupitia Kamati za Ulinzi na Uslama kuliko hao Mawakala ambao siyo waaminifu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joram Ismael Hongoli, Mbunge wa Lupembe, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa wako baadhi ya mawakala na watumishi wa Serikali wasiowaaminifu ambao huwarubuni wakulima ili kukiuka utaratibu wa utoaji wa ruzuku uliowekwa kwa manufaa ya mawakala na watumishi wao. Wizara yangu inafanya ufuatiliaji wa karibu na kuwachukulia hatua za kisheria wahusika hao kwani huwakosesha wakulima pembejeo na hivyo kudumaza maendeleo ya sekta kilimo nchini. Aidha, ili kuondoka na mfumo huu Wizara yangu imeunda kikosi kazi cha kupitia gharama za uzalishaji na uagizaji wa pembejeo nchini ili kama kuna uwezekano kuondoa baadhi ya tozo na kodi ili kufanya pembejeo hizo zipatikane kwa bei nafuu. Sambamba na hilo viwanda vya kuzalisha mbolea vinatarajiwa kujengwa hapa nchini katika Wilaya za Kilwa na Kibaha, mategemeo yetu ni kuwa uzalishaji utakapoanza bei ya mbolea itakuwa nafuu kwa wakulima wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, usambazaji wa mbolea za ruzuku umekuwa ukifanywa kwa ushirikiano wa sekta binafsi na Serikali. Makampuni ndiyo yenye mitaji na dhamana ya kuuza pembejeo hizo kwenye mpango wa ruzuku. Serikali inatoa vocha kwa mkulima ambayo ni hati punguzo ya kupunguzia mkulima makali ya bei ya pembejeo. Kwa utaratibu wa sasa Kamati za Pembejeo za Wilaya chini ya Uenyekiti wa Wakuu wa Wilaya, zimepewa jukumu la kusimamia mgawo na usambazaji wa pembejeo katika maeneo yao. Hata hivyo, uzoefu unaonesha kuwa baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wamekuwa wakialikwa katika vikao vya Kamati ya Pembejeo za Wilaya ili kusaidia katika mikakati ya kudhibiti upotevu na ubadhirifu wa vocha za pembejeo.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza:-
Kumekuwa na changamaoto kubwa katika Mkoa wa Ruvuma ambapo vocha na pembejeo za kilimo zinazotolewa zimekuwa hazitoshi na wakati mwingine kuleta mgogoro kwa wananchi wenyewe kwa wenyewe:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza pembejeo za ruzuku katika Mkoa wa Ruvuma?
(b) Je, ni kwa nini Serikali isiondoe kodi kwenye pembejeo ili wananchi waweze kununua wenyewe pembejeo hizo kwa bei nafuu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Ruvuma umekuwa ukipata ruzuku ya pembejeo za kilimo tangu msimu wa 2003/2004 hadi sasa ambapo takribani kaya 80,000 kila mwaka zimekuwa zikinufaika na ruzuku hiyo mkoani humo. Kutokana na changamoto za mfumo wa utoaji wa ruzuku za pembejeo kama vile kuchelewa kwa pembejeo, ubadhirifu, bei kubwa na kadhalika wakulima wachache wamekuwa wakinufaika na ruzuku hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuweza kuwafikia wakulima wengi zaidi katika mikoa mbalimbali ikiwemo Mkoa wa Ruvuma, Serikali inaangalia upya utaratibu wa kutoa ruzuku bila kujali makundi ambao utawezesha wakulima wengi zaidi kunufaika na ruzuku ya pembejeo. Utaratibu huo utakapokamilika umma wa Watanzania utajulishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa kodi za import na excise duties zimefutwa kwa pembejeo za kilimo zinazoagizwa kutoka nje ila bado kuna tozo za bandari na taasisi mbalimbali kama vile TBS, SUMATRA, Taasisi ya Mionzi na kadhalika ambapo baadhi ya tozo hizo ndani yake kuna VAT. Aidha, Halmashauri bado zinatoza cess kwenye mbegu zinazozalishwa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha bei za pembejeo zinakuwa nafuu, Serikali inaangalia uwezekano wa kuondoa au kupunguza tozo mbalimbali kwenye pembejeo zote za kilimo ili kuwawezesha wakulima wengi kununua pembejeo hizo kwa bei nafuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali inaendelea kuweka msisitizo kwa wawekezaji wa nje na wa ndani kuanzisha viwanda vya mbolea na pia kuwekeza katika mashamba ya kuzalisha mbegu hapa nchini. Lengo kubwa likiwa ni kuwapatia wakulima pembejeo za kutosha na kwa bei nafuu ili kuongeza uzalishaji.
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA aliuliza:-
Kumekuwa na ongezeko la Kampuni kubwa kuanzisha mashamba ya kahawa katika maeneo ya Wilaya ya Mbinga na sehemu za Songea Vijijini jambo linalotishia uzalishaji na soko kwa wakulima wadogo wadogo wa kahawa:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwalinda wakulima wadogo wasimezwe na wakulima wakubwa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sixtus Raphael Mapunda, Mbunge wa Mbinga Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kumekuwepo na ongezeko la kuanzishwa kwa mashamba makubwa ya kahawa katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na Wilaya za Mbinga na Songea Vijijini. Hali hii inachangiwa na sera na mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyopo nchini. Aidha, uwepo wa uanzishwaji wa mashamba makubwa nchini hautishii uzalishaji na soko la kahawa kwa wakulima wadogo wa kahawa bali una manufaa yafuatayo:-
Kwanza, uanzishwaji na uwepo wa mashamba makubwa unawezesha wakulima wadogo walio karibu na mashamba hayo kujifunza teknolojia mbalimbali zinazotumiwa na mashamba hayo katika kuongeza tija na uzalishaji wa kahawa.
Pili, baadhi ya mashamba makubwa yanaendesha miradi ya kuwasaidia wakulima wa kahawa walio karibu na mashamba hayo katika maana ya (outgrowers schemes) kwa kuwapa huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na huduma za ugani, ukoboaji na masoko ya kahawa yao. Kwa mfano, Shamba la Aviv lililopo Lipokela, Halmashauri ya Songea limekuwa likitoa huduma za ugani kwa wakulima wanaolizunguka. Aidha mpaka sasa kiasi cha miche 550,000 imekwisha gawanywa kwa wakulima tangu shamba hilo lianzishwe miaka minne iliyopita.
Mheshimiwa Spika, pamoja na manufaa hayo, Serikali ilifanya marekebisho ya Kanuni zinazoongoza tasnia ya kahawa ili kuwalinda wakulima wadogo wanaoingia makubaliano ya uzalishaji wa Kahawa na makampuni binafsi pamoja na mashamba makubwa.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA (K.n.y. MHE. MARGARET S. SITTA) aliuliza:-
Je, ni sababu zipi zinazoifanya Serikali yetu iridhike na utaratibu wenye usumbufu mkubwa unaowataka wakazi wa Tanzania wanaotaka kwenda Uingereza watafute visa kupitia Kenya na Afrika Kusini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI (K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, hapo awali huduma za viza zilikuwa zikitolewa na Ubalozi wa Uingereza, nchini. Ubalozi huo ulihamisha shughuli za utoaji wa viza kutoka hapa nchini kwenda nchini Kenya tarehe 1 Desemba, 2008 na kuanzia tarehe 18 Agosti, 2014 huduma hizo zimehamishiwa nchini Afrika Kusini na siyo Kenya tena.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Serikali ya Uingereza, uamuzi huo ni wa kisera na umefikiwa ili kuleta ufanisi katika utendaji kazi wa Idara ya Viza na Masuala ya Uhamiaji ya Uingereza. Hivyo, mchakato wa utoaji visa za Uingereza unafanyika kikanda. Kwa mantiki hiyo, maombi yote ya viza kutoka
NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT)
15
nchi zote za Afrika Mashariki na Kati, yanafanyiwa kazi katika Ubalozi wa Uingereza, nchini Afrika ya Kusini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, waombaji wa viza hapa nchini wanatakiwa kuwasilisha maombi yao na nyaraka zinazohitajika katika Kituo cha Kuombea Viza, (Visa Application Center) kilichopo Viva Tower Dar es Salaam. Kituo hicho ndicho chenye jukumu la kusafirisha maombi yao kwenda Afrika ya Kusini na kurejesha nyaraka husika kwa waombaji nchini. Mwombaji halazimiki kufuata huduma hiyo nchini Afrika ya Kusini.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, Ubalozi wa Uingereza Nairobi unashughulikia maombi machache ya Visa (restricted number of applications) kwa viongozi wa Serikali na watendaji wengine wenye pass za Kidiplomasia hasa katika hali ya dharura. Maombi hayo yanapaswa kupelekwa moja kwa moja Ubalozi wa Uingereza Nairobi na waombaji wenyewe au kupitia Ubalozi wa Tanzania Nairobi.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuwakumbusha Waheshimiwa Wabunge pamoja na Watanzania wenzangu kwamba zoezi la utoaji visa lina utaratibu wake na moja ya taratibu hizo ni kwamba nchi inayotoa visa ina uhuru wa kuamua ni wapi itatolea visa hizo. Kwa mantiki hiyo, hata Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitia Balozi zake zilizopo nje, inazo taratibu zake za kutoa visa kwa wageni wanaotembelea Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vyema Watanzania ambao wangependa kutembelea nchi ya Uingereza wakazingatia taratibu zilizowekwa za nchi hiyo katika maombi ya visa ikiwemo kuomba visa mapema, kuwasilisha nyaraka zote muhimu na taarifa sahihi ili kuepuka usumbufu usio wa lazima.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA aliuliza:-
Mwaka 2013 Bunge lilirekebisha Sheria ya Ushirika wa Tumbaku ili iendane na hali ya sasa ya ushirika huo nchini:-
Je, ni marekebisho gani yanayowanufaisha wakulima moja kwa moja?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Victor Kilasile Mwambalaswa, Mbunge wa Lupa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba ushirika wa tumbaku kwa ujumla unakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na ubadhirifu katika vyama hivyo, madeni makubwa, tozo na makato mengi na usimamizi hafifu wa Vyama vya Ushirika. Changamoto hizi ni miongoni mwa vitu vilivyochochea kuwepo kwa sheria mpya ya ushirika, Sheria Na. 6 ya mwaka 2013.
Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya marekebisho yanayowanufaisha wanachama wa Vyama Ushirika wakiwemo wakulima wa tumbaku ni pamoja na:-
(i) Kwa kutumia sheria mpya viongozi wabadhirifu katika Vyama vya Ushirika wamechukuliwa hatua. Kwa mfano, katika maeneo yanayolima tumbaku, viongozi wabadhirifu wa Vyama vya Ushirika 26 katika Mkoa wa Ruvuma wakiwemo na Maafisa Ushirika wawili wamesimamishwa kazi na kufikishwa Mahakamani. Viongozi wa Chama Kikuu cha WETCU waliohusika na ubadhirifu Mkoani Tabora, waliondolewa madarakani ili kupisha uchunguzi. Hatua zaidi zimechukuliwa katika Vyama vya Ushirika vya Korosho kwa viongozi watendaji na watendaji 822 kupewa hati za madai katika maana ya surcharge.
(ii) Kuhusu madeni, sheria ya sasa inakataza vyama kukopa zaidi ya asilimia 30 ya mali zake ili kuzuia vyama kuingia kwenye madeni makubwa yasiyolipika. Aidha, sheria ya sasa inaweka usimamizi wa karibu ambapo vyama hivi vitakuwa vikikaguliwa mara kwa mara kuzuia ubadhirifu.
(iii) Kuhusu tozo, kuanzia sasa Mkutano Mkuu utakuwa chini ya Uenyekiti huru utakaochaguliwa na Wajumbe wa Mkutano Mkuu kinyume na hapo awali ambapo Mwenyekiti wa Bodi ya Tumbaku ndiye anayekuwa Mwenyekiti wa Mkutano Mkuu. Lengo ni kulinda maslahi ya wakulima ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa tozo zote zinazoidhinishwa na Mkutano Mkuu zinakuwa na maslahi kwa wakulima wa tumbaku.
(iv) Muundo wa sasa wa Tume ya Ushirika unafanya Maafisa Ushirika wote kuwajibika moja kwa moja kwenye Tume. Hii itaongeza ufanisi na watumishi hawa wa Vyama vya Ushirika kwa ujumla.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza:-
Kuna kodi zinazofikia 26 katika kilimo cha kahawa ambazo zimefanya bei wanayopata wakulima wa zao hilo kuwa kidogo sana ikilinganishwa na gharama za kulima hivyo kuwafanya baadhi ya wakulima kupeleka kahawa yao nchi jirani ambako bei yake ni nzuri na kwa kufanya hivyo nchi inakosa mapato na kudhoofisha zao hilo hapa nchini; na hata Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano alilikemea jambo hilo kwenye hotuba yake ya kulifungua Bunge Jipya aliyoitoa Bungeni Novemba, 2015.
Je, ni kwa nini Serikali isiingilie kati na kufuta kodi hizo kandamizi kwa wakulima?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa kuna changamoto ya kuwepo kwa kodi nyingi siyo tu kwenye zao la kahawa, lakini pia kwa mazao mengine ya chakula na biashara hapa nchini. Kwa mfano, kwa kahawa inayozalishwa Mkoani Kagera ambayo ni aina ya Robusta inapouzwa nje kwa kupitia Vyama Vikuu au Vyama vya Msingi, vyama hivyo hutozwa kodi na tozo mbalimbali zipatazo 26, sawa na makampuni mengine binafsi. Kwa kuwa vyama hivi ni vyama vya wakulima, gharama hizi za kodi na tozo mbalimbali kwa njia moja ama nyingine huenda kwa mkulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kutambua ukubwa wa changamoto hizo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, imedhamiria kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara katika Sekta ya Kilimo kwa kupitia upya taratibu, vibali, tozo, kodi, ushuru na ada mbalimbali zinazotozwa ili kupunguza gharama za kufanya biashara. Tozo, ada na kodi zote zitakazotozwa na Bodi za Mazao na Mamlaka nyingine zitapitiwa upya na kuchambuliwa ili kutoa nafuu kwa wakulima wote ikiwa ni pamoja na wakulima wa zao la kahawa. Kodi zitakazogundulika kurudisha nyuma tasnia ya kahawa zitaondolewa mara moja.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:-
Zao kuu la biashara katika Wilaya ya Bunda ni pamba lakini viwanda vya kusindika pamba vya Ushashi Ginnery na Kibara Ginnery vilivyokuwa vinamilikiwa na MCU (1984) havifanyi kazi tangu mwaka 1990:-
(a) Je, ni lini Serikali itafufua viwanda hivyo ili wakulima wa pamba wapate bei nzuri?
(b) Je, Serikali inatoa tamko gani kuhusu uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo vya kusindika pamba ili kuongeza thamani ya zao hilo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniphance Mwita Getere, Mbunge wa Bunda, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kwamba viwanda vya kuchambua pamba vya Ushashi na Kibara havifanyi kazi tangu mwaka 1990. Viwanda hivi kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge vinamilikiwa na kilichokuwa Chama Kikuu cha Ushirika cha Musoma (MCU) ambacho kwa sasa kipo kwenye utaratibu wa mufilisi ulianza mwaka 1997. Utaratibu wa mufilisi umechukua muda mrefu kutokana na baadhi ya wanachama wa MCU kukata rufaa kwa Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tatu kutaka viwanda hivi visifilisiwe na badala yake ikiwezekana viendeshwe kwa ubia kati ya sekta binafsi, wanaushirika na Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya ushirika imeanza kushughulikia suala la mali za MCU ikiwemo viwanda hivyo ili vitafutiwe utaratibu wa kufufuliwa kwa ubia na vianze kazi ili kuwezesha ulipaji wa madeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Bunda ina ginnery tatu zinazofanya kazi ya kuchambua pamba inayopatikana katika wilaya hiyo. Hivyo wakulima wa Bunda wanapata huduma za uchambuzi wa pamba kupitia ginneries hizo. Aidha, taarifa zilizopo zinaonesha kuwa ginneries zilizopo katika Wilaya ya Bunda bado hazipati pamba ya kutosha na hivyo kufanya kazi chini uwezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inahamasisha sekta binafsi na wadau wengine kuwekeza katika viwanda vidogo vidogo vya kusindika pamba ili kuongeza thamani ya zao la pamba na wakulima wapate faida zaidi. Nia ya Serikali ni kuhakikisha kwamba wakulima wanajengewa uwezo wa kumiliki vinu vidogo vidogo vya kuchambulia pamba katika vikundi vya wakulima na Vyama vya Ushirika. Kwa kuwa tayari Serikali inasambaza umeme vijijini kwa nguvu kubwa kinachofuata sasa ni kujenga mazingira ya kuwawezesha wakulima kumiliki viwanda vya kusindika mazao yao ikiwepo pamba. Hii ndiyo nia na namna ya bora ya kuleta mapinduzi ya viwanda nchini katika Sekta ya Kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali pia inawashauri wamiliki wa vinu vikubwa vya kuchambua pamba wafikirie kuwekeza kwenye hatua zinazofuata za mnyonyoro wa thamani kama kusokota nyuzi katika maana ya spinning, kufuma vitambaa, weaving na kutengeneza nguo (textile).
MHE. MARWA R. CHACHA aliuliza:-
Zao la tumbaku limekuwa likilimwa sana Wilaya ya Serengeti lakini kuna changamoto kubwa ya kukosa masoko.
Je, ni lini Serikali itasaidia upatikanaji wa kampuni zaidi ya moja kwenye ununuzi wa tumbaku ndani ya Wilaya ya Serengeti?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Marwa Ryoba Chacha, Mbunge wa Serengeti kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, majaribio ya kilimo cha tumbaku kibiashara Mkoani Mara yalianza mwaka 2008/2009 kwa lengo la kuwaelekeza wakulima kufuata mfumo wa Tanzania tofauti na hapo awali ambapo walilima tumbaku na kuuza kwa kufuata mfumo wa nchi jirani ya Kenya.
Kimsingi kilimo cha tumbaku mkoani Mara kulikuwa hakijaimarishwa na hivyo kutowanufaisha wakulima kama ilivyo katika maeneo mengine nchini. Aidha, kuendelea kulima tumbaku bila utaratibu maalum kulihatarisha kuenea kwa magonjwa ya tumbaku katika nchi hizi mbili.
Mheshimiwa Spika, msimu wa 2011/2012, Serikali kupitia Bodi ya Tumbaku ilirasimisha kilimo cha tumbaku mkoani Mara ikiwa ni pamoja na Wilaya ya Serengeti. Hatua ya kufunguliwa kilimo cha tumbaku mkoani humo ilitoa fursa kwa kampuni zilizopenda kununua tumbaku mkoani humo kufanya hivyo kwa kuzingatia kanuni na taratibu za zao hilo na pamoja na sheria nyingine za nchi. Hivi sasa Kampuni ya Alliance One ndio kampuni pekee inayonunua tumbaku mkoani Mara.
Mheshimiwa Spika, katika msimu wa 2013/2014 Serikali iliziandikia barua kampuni zote zinazonunua tumbaku nchini kuzijulisha uwepo wa fursa ya kuwekeza katika kununua tumbaku mkoani Mara. Hata hivyo, juhudi hizo hazijaleta matunda yaliyokusudiwa. Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wengine akiwepo Mheshimiwa Mbunge kuzishawishi kampuni hizo kuwekeza Wilayani Serengeti. Aidha, kwa kuwa Tanzania ina wanunuzi wachache, Serikali itaendelea kushawishi wanunuzi wengine hususan kutoka China kununua tumbaku ya Tanzania ikiwa ni pamoja na ya Wilaya ya Serengeti.
MHE. MAGDAENA H. SAKAYA aliuliza:-
Serikali ilifanya ukaguzi maalum kwenye Vyama vya Ushirika vya Mkoa wa Tabora pamoja na Chama Kikuu cha Ushirika (WETCU) tangu mwaka 2014 na kubaini ubadhirifu mkubwa uliofanywa na viongozi kwa kushirikiana na benki mbalimbali.
(a) Je, ni kwa nini mpaka leo ripoti hiyo haijawekwa wazi na hatua za kisheria kuchukuliwa kwa wote waliohusika na wizi huo?
(b) Vyama vingi viko kwenye hali mbaya na havikopesheki na hivyo kupelekea wakulima kukosa pembejeo za kilimo. Serikali ina mpango gani mahsusi wa kusaidia vyama hivyo vya ushirika kwa kuzingatia mchango wa zao la tumbaku kwenye uchumi wa Taifa hili?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Magdalena H. Sakaya, Mbunge wa Kaliua lenye vipengele (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri mwenye dhamana ya ushirika alikabidhi taarifa ya ukaguzi kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) kupitia kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora mnamo tarehe 18 Septemba, 2014 kwa ajili ya kuchukua hatua za kisheria dhidi ya makosa ya jinai yaliyobainika. Mwezi April 2016, Mrajisi wa Vyama vya Ushirika alituma maafisa Mkoani Tabora kufuatilia hatua zilizochukuliwa. Ilibainika kwamba uchunguzi umekamilika na watuhumiwa watachukuliwa hatua za kisheria. Hadi mwezi Juni, 2016 maombi ya kuwafungulia mashtaka watuhumiwa yalipelekwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai akiridhia wafunguliwe mashtaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tume ya Maendeleo ya Ushirika imeanzisha kitengo cha sheria kwa ajili ya kuchukua haraka dhidi ya makosa ya jinai katika vyama. Tume imemwandikia DPP kuomba kibali kwa mujibu wa kifungu cha 133 cha Sheria ya Vyama vya Ushirika ya mwaka 2013 ili wanasheria wake wapewe mamlaka ya kuendesha mashtaka ya kesi zinazohusu Vyama vya Ushirika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vyama vya msingi ambavyo havikopesheki, Serikali inaendelea kuvihimiza Vyama Vikuu vya Ushirika kuangalia utaratibu wa kuvikopesha kwa utaratibu wa kuanzisha revolving fund badala ya kutegemea benki. Chama Kikuu cha Ushirika (WETCU) kilielekezwa kuhakikisha vyama vyake vya msingi 112 kati ya 217 ambavyo havikopesheki viwezeshwe kukopesheka. WETCU imeviwezesha vyama 68 kushiriki kuzalisha tumbaku msimu ujao kwa kutumia fedha za revolving fund. Fedha hizo zinatokana na sehemu ya mgao wake wa ushuru wa iliyokuwa Apex ya tumbaku na sehemu ya ushuru wake jumla shilingi milioni 800. Inatarajiwa kwamba kwa vile fedha hizi ni revolving zitaweza kutumika kuviwezesha vyama vilivyosalia viweze kukopesheka.
MHE. OSCAR R. MUKASA aliuliza:-
Tanzania imekuwa mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa miaka kadhaa sasa, ambapo Watanzania wamekuwa wakijulishwa na Serikali juu ya namna ya ushiriki wa Taifa katika mtangamano huo; ushiriki bora na wenye tija hauwezi kutokana na ushiriki mzuri wa Serikali pekee na mihimili mingine ya utawala bali pia ushiriki wa wananchi kwa ngazi ya mtu mmoja mmoja na kwa namna ya pekee Mikoa inayopakana na nchi za Jumuiya hiyo ukiwemo Mkoa wa Kagera.
(a) Je, kuna mkakati gani wa Serikali kumjengea mwananchi mmoja mmoja na taasisi mbalimbali kushiriki katika Jumuiya hiyo?
(b) Kama mkakati huo upo; je, ni kwa vipi wataufahamu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI (K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa napenda kulieleza Bunge lako Tukufu kwamba jina la Wizara sasa limebadilishwa na imekuwa ni Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Oscar Rwegasira Mukasa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi, lenye vipengele (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi wanachama za Jumuiya ya Afrika Mashariki zinatambua umuhimu wa kuwashirikisha wananchi katika kujenga Jumuiya yao ili kuweza kufikia malengo yanayokusudiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ibara ya 7(1)(a) ya Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki inabainisha kuwa Jumuiya ni ya wananchi, hivyo nchi wanachama zina wajibu wa kuhakikisha wananchi wanajengewa uwezo ili waweze kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mtangamano wa Afrika Mashariki kwa kuzitumia fursa za Jumuiya hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia hilo, Wizara iliandaa Mkakati wa Mawasiliano kwa Umma ulioanza kutekelezwa tangu mwaka 2012. Mkakati huu unatoa mwongozo wa utoaji elimu kwa Umma kuhusu Mtangamano wa Afrika Mashariki kwa makundi mbalimbali na pia ni nyenzo ya kupata mrejesho kutoka kwa wadau.
Mheshimiwa Naibu Spika, tangu kuanza kutekelezwa kwa Mkakati huo, wananchi wamefahamishwa kufahamu mkakati huu kupitia ziara za mipakani, vipindi vya televisheni na redio, vipeperushi, machapisho, makala, mikutano na wafanyabiashara, semina, maonesho mbalimbali kama vile Wiki ya Utumishi wa Umma, Saba Saba, Nane Nane, Maonesho ya Wafanyabiashara Zanzibar na Siku ya Mara pamoja na kuweka mabango kwenye mipaka ya Namanga, Horohoro, Holili, Sirari, Mutukula, Rusumo na Kabanga.
Aidha, mkakati huu ambao upo katika mfumo wa kitabu, umesambazwa kwa wadau kwenye shughuli mbalimbali za elimu kwa Umma zinapofanyika na unapatikana katika tovuti ya Wizara, pamoja na Kituo cha Habari cha Wizara kilichopo katika jengo la NSSF - Water Front, ghorofa ya pili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa sote ni wadau wa mtangamano wa Afrika Mashariki, Wizara inaomba kutoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge kuwaelimisha wananchi katika Majimbo yao pindi wanapoongea nao ili waweze kuzitambua na kuzitumia fursa zitokanazo na mtangamano huo, kwani ni eneo mojawapo linaloweza kuwaongozea kipato na kupunguza tatizo la ajira lililopo nchini.
MHE. HAFIDH ALI TAHIR (K.n.y. MHE. HAMADI SALIM MAALIM) aliuliza:-
Jeshi la Polisi ni chombo muhimu kinacholinda usalama wa raia na mali zao. Askari hawa wanapomaliza mafunzo yao kwa ngazi mbalimbali kama vile Sajenti, Staff Sajenti, Meja na nyingine, hucheleweshwa sana kulipwa maslahi yanayoendana na vyeo vyao:-
Je, ni kwa nini Askari hao hawalipwi kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI (K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Hamadi Salim Maalim, Mbunge wa Kojani, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Askari Polisi hupanda vyeo kama ilivyo kwa watumishi wengine wa umma na vyeo hivyo huambatana na kuongezeka kwa maslahi yao kulingana na cheo kilichopandishwa. Mwaka 2014/2015 jumla ya Askari 1,657 wa vyeo vya uongozi mdogo walipandishwa vyeo mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kumekuwepo na ucheleweshaji wa ulipwaji wa mishahara inayolingana na vyeo katika Jeshi la Polisi. Serikali mara zote imekuwa ikijitahidi kurekebisha mishahara ya vyeo vipya kwa haraka iwezekanavyo kwa Askari waliopanda vyeo. Yapo matatizo ya kiufundi yaliyojikeza wakati wa zoezi la kurekebisha mishahara na kutokea baadhi ya Askari kutorekebishiwa mishahara yao. Hata hivyo, juhudi hufanyika ili kutatua tatizo hilo mara mhusika anapowasilisha malalamiko yake Polisi Makao Makuu. Kitengo cha Maslahi Makao Makuu hupokea malalamiko na kuwasiliana na mamlaka za ulipaji ili kutatua tatizo hili. Aidha, naomba nitoe wito kwa Askari yeyote ambaye amepatwa na tatizo hili awasiliane na viongozi katika Kamandi yake au Makao Makuu ya Polisi, Idara ya Maslahi ili kupata ufumbuzi wa tatizo hili haraka iwezekananvyo.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA aliuliza:-
Wakulima wa tumbaku wamekuwa wakilipwa kwa dola pindi wanapouza mazao yao:-
(a) Je, nani huwapigia hesabu za kitaalamu?
(b) Je, wakulima wote wamefunguliwa akaunti benki?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwanne Ismail Mchemba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo wa kuwalipa wakulima wa tumbaku kwa dola kupitia Vyama vya Msingi ulipendekezwa, ukafanyiwa utafiti na kukubaliwa na wadau wote wa tasnia ya tumbaku. Vyama vya Msingi vya Ushirika vimeajiri Katibu, Meneja na Mhasibu wa kila chama kwa ajili ya usimamizi wa mali na stahiki za kila mkulima mwanachama. Watumishi hawa wana jukumu la kutunza hesabu na madeni pamoja na mauzo ya tumbaku. Ili kuongeza ufanisi katika kazi zao watumishi hao hupewa semina mbalimbali ikiwemo kushawishi bei nzuri ya kubadilisha fedha. Katibu, Meneja na Mhasibu wa Vyama vya Msingi ndiyo wanaohusika katika kubadilisha fedha kutoka dola na kwenda katika shilingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, Serikali imekuwa ikipokea malalamiko kutoka kwa wakulima kwamba watumishi hawa kwa kushirikiana na mabenki wamekuwa wakiwapunja wakulima hasa katika mchakato wa kubadili dola kwenda kwenye fedha za Kitanzania. Wizara yangu inaendelea kuchunguza suala hili na ilipobaini ubadhirifu huchukua hatua stahiki ikiwemo kuwaandikia hati ya madai wahusika.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakulima wengi hawana akaunti binafsi za kupokea malipo ya tumbaku yao waliyouza na badala yake Vyama vya Msingi ndivyo vyenye akaunti. Baada ya vyama hivyo kupokea malipo ya tumbaku za wakulima hutoa fedha hizo kama fedha taslimu na kuzisafirisha hadi katika makao ya vyama hivyo kwa ajili ya kuwalipa wakulima waliouza tumbaku yao. Jambo hili ni hatari na linachochea sana wizi na upotevu wa fedha za wakulima. Hivyo, Serikali inavitaka vyama vyote vya ushirika kuhamasisha kila mkulima kufungua akaunti ili kukabiliana na tatizo hilio na ikiwezekana kufungua akaunti ya dola.
MHE. DEO K. SANGA (K.n.y. MHE. PROF. NORMAN A. S. KING) aliuliza:-
Shamba la Mifugo la Kitulo lililoko Wilaya ya Makete lilianzishwa kwa madhumuni ya kuwezesha wananchi kupata ndama na maziwa kwa ajili ya kukuza uchumi wao, lakini cha kusikitisha, uzalishaji wa ng‟ombe katika shamba hilo kwa sasa umepungua sana kutokana na Serikali kushindwa kusaidia kuimarisha shamba hilo:-
Je, Serikali inafanya jitihada gani kuimarisha shamba hilo ili liweze kusaidia wananchi wa Makete na Mikoa ya jirani kupata ng‟ombe na kukuza uchumi wao?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Profesa Norman Sigalla King, Mbunge wa Makete, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, shamba la kuzalisha mifugo la Kitulo ni kati ya mashamba matano ya kuzalisha mifugo yanayomilikiwa na kuendeshwa na Wizara kwa lengo la kuzalisha mifugo bora kwa ajili ya kuwauzia wafugaji kwa bei nafuu. Shamba hili huzalisha ng‟ombe wa maziwa aina ya Friesian pamoja na maziwa, katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2011/2012 hadi 2015/2016, jumla ya mitamba 365 na madume bora 515 yalizalishwa na kuuzwa kwa wafugaji katika Mikoa ya Mbeya, Njombe, Iringa na Ruvuma. Kati ya mitamba hiyo, 40 iliuzwa kwa wafugaji wa Wilaya ya Makete.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, katika kipindi hicho jumla ya lita 1,963,241 zilizalishwa katika shamba hili na kuuzwa. Shamba hili pia linaendelea kutumika kutoa mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi na wafugaji kutoka vijiji jirani vikiwemo vya Wilaya ya Makete. Katika kipindi hicho, wanafunzi 930 kutoka vyuo mbalimbali vya mifugo hapa nchini na wastani wa wafugaji 250 walipata mafunzo ya vitendo kupitia shamba hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuliimarisha na kuliendeleza shamba hili kwa kuboresha miundombinu ya shamba ikiwepo maeneo ya malisho kwa kupanda na kuwekea mbolea hekta 500 za malisho, kukarabati kilometa 15 za mfumo wa maji, kukarabati na kuweka umeme nyumba 13 za watumishi, kuongeza ubora wa ng‟ombe waliozalishwa na kununua madume bora ya Friesian 12 na kutumia teknolojia ya uhimilishaji wa mbegu zilizotengenezwa kijinsi, kununua mitambo na mashine ikiwa ni pamoja na mashine moja ya kukamulia na tenki moja la kubeba maziwa, magari mawili pamoja na trekta mbili na vifaa vyake kwa ajili ya kuboresha na kurahisisha kazi za shamba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi hizi zimetekelezwa kwa kutumia fedha zinazozalishwa shambani kila mwaka na zinazotolewa kupitia bajeti ya Wizara. Katika mwaka wa fedha, 2016/2017 jumla ya shilingi milioni 105 zitakazozalishwa shambani na zilizotengwa kupitia bajeti ya Wizara zimepangwa kutumika katika kuimarisha na kuendeleza shamba hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inawahamasisha wananchi wa Makete kutumia huduma ya uhimilishaji ili waweze kuzalisha ndama bora kutokana na mifugo yao wenyewe.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:-
Eneo la Buhemba Holding Ground Farm (KABIMITA) linalomilikiwa na vijiji vitatu vya Magunga, Milwa (Wilaya ya Butiama) na Mekomarino (Wilaya ya Bunda) kwa ajili ya kilimo na ufugaji ambalo lilitolewa na Serikali tangu miaka 1970 na 1980 kama kituo cha kukusanyia mifugo (ng‟ombe) na kuwatibu kabla ya kupelekwa kwenye mnada wa ng‟ombe Bukoba; na sasa ni miaka 33 eneo hili linatumiwa na wakazi wa vijiji hivyo kwa ajili ya makazi, kilimo na ufugaji.
Je, ni lini Serikali itatoa tamko rasmi kwamba eneo hilo ni mali ya vijiji hivyo kisheria ili kuondoa dhana ya kuwa eneo hili ni mali ya Serikali?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Buhemba Holding Ground chenye ukubwa wa hekta 2,446 kilijengwa mwaka 1949 na Serikali ya kikoloni kwa ajili ya kukagua, kukarantini na kunenepesha ng‟ombe, mbuzi na kondoo waliokuwa wanauzwa nchi za jirani. Baada ya uhuru kituo hiki kilikabidhiwa kwa Wizara yenye dhamana ya maendeleo ya mifugo hadi mwaka 1975 kilipokabidhiwa kwa Kampuni ya Biashara ya Mifugo Tanzania (KABIMITA) ili kitumike kwa karantini na kunenepesha mifugo kwa ajili ya kuchinjwa katika viwanda vilivyokuwa vinamilikiwa na Tanganyika Packers Limited vya Arusha na Kawe, Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia mwaka 1980 hadi mwaka 1982, kampuni ya KABIMITA ilikitumia kituo husika kukarantini mitamba ya ng‟ombe wa asili kwa ajili ya maandalizi ya kuisafirisha kwenda Uganda kupitia sehemu ya kupakilia mifugo ya Kituo cha Bweri Holding Ground cha Musoma Mjini. Mwaka 1984 Kampuni ya KABIMITA ilifutwa na kituo hicho kilihamishiwa kwenye Wizara yenye dhamana ya maendeleo ya mifugo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 1993, Wizara kwa kutumia fedha za mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) ilianzisha mradi wa uendelezaji wa miundombinu ya masoko ya mifugo ya Tanzania (Tanzania Livestock Marketing Project). Mradi huo uliendeleza kituo hicho kwa kuweka alama za kudumu kwenye mipaka, kujenga ofisi za nyumba na nyumba ya Meneja wa Kituo, kukarabati nyumba za watumishi na kununua vitendea kazi kwa gharama ya shilingi milioni 104.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ya karantini na Holding Ground nchini yanalindwa kwa mujibu wa Sheria Namba 17 ya Kuzuia Magonjwa ya Mifugo ya mwaka 2003 na Sheria ya Nyama Na. 10 ya mwaka 2006. Maeneo haya ni kwa ajili ya matumizi ya mifugo ya biashara ambayo ni lazima iwekwe chini ya karantini ili kufanya uchunguzi wa magonjwa ya mifugo kabla ya kuchinja kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeruhusu wananchi kutumia eneo hilo kwa shughuli mbalimbali huku ikiendelea kuwa chini ya umiliki wa Wizara. Hata hivyo, Serikali inatoa rai kwa wananchi kutopanda mazao ya kudumu na kujenga makazi katika eneo hilo pamoja na vituo vingine vya karantini na Holding Ground nchini.
Aidha, nawaomba Waheshimiwa Wabunge muwaelimishe wananchi juu ya umuhimu wa maeneo haya katika ukuaji wa tasnia ya nyama nchini ili mifugo na bidhaa zitokanazo na mifugo ziweze kukubalika katika masoko yenye ushindani kikanda na Kimataifa.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB aliuliza:-
Baadhi ya wakulima wa Tarafa ya Amani na Muheza wanalima kwa wingi viungo mbalimbali kama pilipili manga, karafuu, hiliki na mdalasini lakini hakuna viwanda kwa ajili ya kusindika mazao hayo.
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia kupata kiwanda wakulima wa mazao hayo kwa ajili ya mazao yao?
(b) Je, Serikali itakuwa tayari kuwatafutia wananchi hao wanunuzi wa uhakika wa mazao hayo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Adadi Mohamed Rajab, Mbunge wa Muheza, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kupitia Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) Mkoa wa Tanga katika mpango kazi wake wa robo mwaka ya pili yaani Oktoba - Disemba, 2016, imeweka mkakati wa kufanya uchambuzi yakinifu (needs assessment) kwa wakulima wa viungo vya vyakula mkoani humo wakiwepo wa Tarafa za Amani na Muheza. Lengo la mkakati huo ni kubaini mahitaji mahususi ya wakulima hao yakiwemo ya kiteknolojia na masoko ili kuzipatia ufumbuzi wa kudumu changamoto wanazokabaliana nazo hivi sasa ya kiwanda cha kusindika mazao hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara imetenga fedha za kuratibu utekelezaji wa mkakati wa kuendeleza mazao ya bustani yakiwemo mazao ya viungo wenye lengo la kuongeza uzalishaji na tija. Vilevile Serikali kupitia Wizara ya Viwanda imekuwa ikitoa teknolojia mbalimbali za usindikaji mazao zikiwemo za mazao ya viungo kwa wakulima wa Mkoa wa Tanga kupitia karakana ya uendelezaji teknolojia (Technology Development Centre) iliyopo Arusha ambapo teknolojia za usindikaji mazao yakiwemo ya viungo hutolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, viungo vinavyozalishwa nchini vina soko la kutosha ndani na nje ya nchi hususani katika nchi za Uturuki, India na Uarabuni. Changamoto ni namna ya kulifikia soko hilo katika viwango na ubora unaotakiwa. Katika Wilaya ya Muheza kuna Makampuni kadhaa yanayonunua viungo na kati ya hayo ni Jumuiya ya Wakulima wa Kilimo Hai Usambara Mashariki (JUWAKIHUMA), Golden Food Product na TAZOP.
Hivyo, Serikali inaandaa mkakati wa kutoa elimu juu ya mbinu bora za uzalishaji wa viungo ili kuinua ubora wa viungo pamoja na mavuno kwa eneo hili kukidhi mahitaji ya makampuni yanayonunua na kuuza viungo ndani na nje ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Shirika la SIDO imekuwa ikiwashirikisha wakulima katika maonesho kwa nia ya kujifunza na kupata masoko. Mathalan kwa mwaka 2015/2016, wakulima wa viungo kutoka Tarafa za Amani na Muheza ni miongoni mwa washiriki wa maonesho ya SIDO Kanda ya Mashariki.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza:-
(a) Je, ni nini maana ya kitendo cha kupiga saluti kinachofanywa na askari?
(b) Je, ni askari wa ngazi gani hupigiwa saluti?
(c) Je, ni maafisa/viongozi wa ngazi gani uraiani katika mihimili ya Serikali, Mahakama na Bunge ambao wanastahili kupigiwa saluti?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, saluti ni salamu ya kijeshi ambayo hutolewa na askari kwa mujibu wa sheria na kanuni za Kudumu za Utendaji wa Jeshi la Polisi (Police General Orders No. 102).
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, askari wote kuanzia cheo cha mkaguzi msaidizi na kuendelea hustahili kupigiwa saluti.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, PGO namba 200 imeainisha taratibu za saluti kwa viongozi wa Serikali na taasisi zingine kama ifuatavyo:-
Askari wa vyeo vyote wanatakiwa kupiga saluti kwa Mheshimiwa Rais na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Kwanza na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania naJaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mawaziri wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katibu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wanapokuwa katika maeneo ya Bunge au Majimboni mwao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, viongozi wengine wanaostahili kupigiwa saluti ni pamoja na Wakuu wa Mikoa na Majaji wanapokuwa katika maeneo yao ya kazi. Aidha, kuanzia askari mwenye cheo cha Konstebo hadi Mkaguzi wanapaswa kuwapigia saluti Wakuu wa Wilaya na Waheshimiwa Mahakimu wote wanapokuwa katika maeneo yao ya kazi.
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR aliuliza:-
Askari wa Wilaya ya Mkoani katika Mkoa wa Kusini Pemba wanakabiliwa na tatizo la uchache wa nyumba za kuishi na ubovu wa ofisi zao:-
Je, ni lini Serikali itawajengea Askari nyumba za kuishi na ofisi za kisasa katika kituo cha Mkoani na Kengeja – Pemba?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI (K.n.y WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Faida Mohamed Bakar, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali inatambua tatizo la uchache wa nyumba za kuishi askari na ubovu wa ofisi zao; kwa sasa Jeshi la Polisi lina mpango wa kujenga nyumba za polisi nchi nzima ambapo kwa awamu ya kwanza zitajengwa nyumba 4,136 katika mikoa 17 ikihusisha Mikoa ya Tanzania Bara pamoja Mikoa ya Unguja na Pemba.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuboresha makazi ya askari na ofisi za polisi kwa awamu kwa kadri hali ya kiuchumi itakavyoruhusu.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI (K.n.y. MHE. YUSUPH SALIM HUSSEIN) aliuliza:-
Kumekuwa na matumizi ya uvuvi haramu wa kutumia mabomu katika mwambao wa bahari ya Tanga na Pemba:-
(a) Je, Serikali inafahamu athari za mabomu yayopigwa chini ya maji?
(b) Je, Serikali imechukua hatua gani kukomesha aina hiyo ya uvuvi.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yussuf Salim Hussein, Mbunge wa Chambani, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inafahamu athari za mabomu yanayotumiwa baharini kwa nia ya kuua samaki na viumbe wengine. Matumizi ya mabomu kwa nia ya kuvua samaki yana athari kubwa kwa samaki na mazingira ya baharini kwa kuwa huua samaki na viumbe wengine, uharibu matumbwawe ambayo ni mazalia na makulia ya samaki, uharibifu wa mazingira na ikolojia ya bahari ikiwemo mfumo wa maisha ya samaki. Pia, ni tishio kwa maisha ya binadamu na usalama wa nchi kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, athari nyingine ni pamoja na kupungua kwa rasilimali za uvuvi, kupoteza kipato, kuongezeka kwa mmomonyoko wa fukwe za bahari; huathiri afya za walaji na shughuli za utalii katika Hifadhi za Bahari na maeneo tengefu. Uharibifu huu unapofanyika unachukua miongo mingi zaidi ya miaka 100 kurudi kwenye hali yake ya awali kutegemea aina ya matumbawe na mazingira yaliyoharibika.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nilitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba mabomu siyo zana ya uvuvi bali ni silaha ya kivita na maangamizi. Aidha, jukumu la kudhibiti uvuvi wa kutumia mabomu, Halmashauri ndizo zenye maeneo ya uvuvi kisheria, Sheria ya Uvuvi namba 22 ya mwaka 2003 na kanuni zake za mwaka 2009 zimekasimu mamlaka ya udhibiti na usimamizi wa rasilimali za uvuvi katika Halmashauri zote nchini. Wizara ina jukumu la kuandaa na kusimamia utekelezaji wa sera, sheria na kanuni zinazotumika katika uhifadhi, udhibiti na usimamizi wa rasilimali za uvuvi nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuongeza nguvu ya kudhibiti uvuvi haramu Serikali ilianzisha mfumo wa kushirikisha jamii katika vikundi vya usimamizi shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (Beach Management Unit) kwa lengo la kuwaelimisha wananchi juu ya athari ya matumizi ya mabomu na uvuvi haramu kwa ujumla na faida za kuwa na uvuvi endelevu kwa manufaa yao na Taifa kwa ujumla ili waweze kusimamia rasilimali hiyo kwani wavuvi haramu hutoka miongoni mwao. Hata hivyo, juhudi hizo hazijaweza kukomesha matumizi ya mabomu katika uvuvi baharini kwa kuwa vyanzo vya mabomu ni kwenye migodi ya madini, ujenzi wa barabara na mengine hutengenezwa kienyeji na wavuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua ukubwa wa tatizo hili Serikali imeunda kikosi kazi kwa lengo la kushughulikia uharibifu wa kimazingira ikiwemo kudhibiti uvuvi haramu na mabomu kinachoundwa na wajumbe kutoka Ofisi ya Rais; Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka; Wizara ya Mambo ya Ndani; Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa; Nishati na Madini; Maliasili na Utalii; Kilimo, Mifugo na Uvuvi; na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na kinakaratibiwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP).
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuziagiza Halmashauri za Ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi kushirikiana na jamii kusimamia kikamilifu udhibiti wa uvuvi wa mabomu, ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua za kisheria wale wanaojihusisha na uvuvi na mabomu.
MHE. OMARY T. MGUMBA aliuliza:-
Wananchi wa Ngerengere wamezungukwa na kambi za Jeshi zaidi ya tatu na kwa upande mwingine shamba la mifugo;
Je, Serikali ina mpango gani wa kupunguza sehemu ya Shamba la Mifugo Ngerengere na kuwapa wananchi, hasa ikizingatiwa kuwa watu wameongezeka sana na ardhi ni ndogo kwa huduma za kijamii?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omary Tebwete Mgumba, Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, shamba la mifugo Ngerengere lililopo Wilaya ya Morogoro Vijijini lina ukubwa wa hekta 4,562, lenye uwezo wa kutunza ng’ombe 1,650 hadi 2,000. Aidha, shamba limegawanywa katika vitengo viwili vya Kiwege na Makao Makuu ambako kundi la ng’ombe wa aina ya Boran hufugwa. Rasilimali zilizopo na miundombinu ya huduma za maji ni pamoja na mabwawa matatu, josho, barabara, mazizi, mabirika ya kunyweshea mifugo, nyumba za watumishi, malisho ya wanyama ikijumlisha idadi ya ng’ombe 827, mbuzi 196 na nguruwe 25.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa ardhi kwa wananchi wa Ngerengere na kwa kuzingatia hilo mwaka 1991 kiasi cha hekta 528 zilipunguzwa kwenye eneo la shamba lililokuwa na hekta 5,090 na kupewa Kijiji cha Ngerengere ili wananchi waweze kugawiwa kwa matumizi yao na shamba kubakiwa na hekta 4,562, ambalo limepimwa na kuwekewa alama na wataalam wa ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa na programu na mikakati mbalimbali ya kuendeleza sekta ya kilimo hususan mifugo. Kutokana na umuhimu wa shamba la Ngerengere kwa wananchi wa eneo hilo Kanda ya Mashariki na Taifa, Wizara katika mipango yake inaendelea kuliimarisha shamba hili na mashamba mengine kwa ajili ya upatikanaji wa mifugo bora na yenye tija kwa ajili ya kukidhi soko la ndani na nje ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, napenda kuwashauri na kuwahimiza wananchi na wafugaji kutumia fursa za uwepo wa shamba la Ngerengere katika kuboresha mifugo na malisho, kufuga kulingana na uwezo wa ardhi, kufuga mifugo yenye tija, pia kutumia mbegu bora za ng’ombe, mbuzi na nguruwe zinazopatikana katika shamba la mifugo la Ngerengere.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA aliuliza:-
Wakulima wa zao la korosho Jimbo la Rufiji wameibiwa zaidi ya shilingi 900,000,000 kwa mwaka 2011 kutoka kwa Vyama vya Msingi vya Kimani, Mwasani, Kibiti na Ikwiriri.
Je, ni lini Serikali itachukua hatua kali dhidi ya vyama hivyo?
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mchengerwa kuna Wandengereko tunakaa maeneo mengine.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2012 Mrajisi wa Vyama vya Ushirika nchini alifanya ukaguzi katika Vyama vya Ushirika wa Korosho katika Mkoa wa Pwani na kubaini upotevu wa fedha wa shilingi 2,655,182,760.46 uliosababishwa na viongozi na watendaji wa Vyama vya Ushirika. Aidha, uhakiki uliofanywa na Ofisi ya Mrajisi huyo unaonesha kuwa wakulima wa korosho wa Mkoa wa Pwani wanavidai vyama vya msingi jumla ya shilingi 3,195,135,103, deni ambalo linatokana na sababu mbalimbali za kibiashara kama vile anguko la bei ya korosho katika soko la dunia. Mchanganuo wa deni hilo kwa kila Wilaya ni kama ifuatavyo; Mkuranga ni shilingi 1,931,224,587, Rufiji shilingi 1,215,018,100, Kibaha Mjini shilingi 758,880, Bagamoyo ni shilingi 10,275,960 na Mafia shilingi 7,857,576.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na ukaguzi huo ilibainika kwamba Mkoa wa Pwani ulikuwa na viongozi 822 wa Vyama vya Ushirika waliodaiwa kuhusika na upotevu wa fedha za wakulima wa korosho. Kwa Wilaya ya Rufuji viongozi 41 wa vyama walibainika kufanya ubadhirifu huo na hivyo kwa kutumia kifungu cha 95 cha Sheria ya Ushirika Na.6 ya mwaka 2013, Mrajisi aliwaandikia hati ya madai na kuwataka kulipa fedha zilizopotea.
Mheshimiwa Naibu Spika, viongozi wa Vyama vya Mwaseni 11, Kilima Ngorongo tisa, Ikwiriri 11 na Kibiti 10 walihusika. Kiasi wanachodaiwa viongozi hao ni shilingi 68,878,188 katika mchanganuo ufuatao:- Mwaseni shilingi 5,152,906, Kilima Ngorongo shilingi 22,104,384, Ikwiriri shilingi 20,549,494 na Kibiti shilingi 21,071,398. Viongozi wa vyama hivi vyote kutoka Wilaya ya Rufiji bado hawajalipa fedha wanazodaiwa na taratibu zinakamilishwa za kuwapeleka mahakamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi tarehe 5 Novemba, 2015 ni viongozi 79 tu kati ya 822 wa Mkoa wote wa Pwani waliokuwa wamerejesha jumla ya shilingi 24,260,163.19. Kwa viongozi ambao hawajarejesha, taratibu zimeandaliwa za kuwafikisha katika vyombo vya sheria ili hatua ziweze kuchukuliwa ambapo hadi tarehe 8/06/2016 tayari majalada 11 yalikuwa yamefunguliwa polisi na kufikishwa katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mkoa wa Pwani.
MHE. JEROME D. BWANAUSI aliuliza:-
Serikali iliwaahidi wakulima wa korosho kupata malipo halali ya mauzo ya korosho kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani.
(a) Je, ni lini Serikali itawahakikishia wakulima wa korosho wa Wilaya ya Masasi wanalipwa malipo yao ya mwisho wanayostahili?
(b) Je, Serikali imekuchukua hatua gani kwa Vyama vya Ushirika ambavyo haviwapi wakulima wa korosho fedha zao kama korosho zilivyouzwa kwenye mnada?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jerome Dismas Bwanausi, Mbunge wa Lulindi, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kuna baadhi ya wakulima wa korosho katika baadhi ya vyama vya msingi ambao hawakulipwa bonus baada ya kuuza korosho zao kama ilivyostahili. Hii ilisababishwa na baadhi ya vyama hivyo kukiuka taratibu za makato ya korosho kama ilivyokubaliwa katika Mkutano Mkuu wa wadau uliofanyika mwaka 2015.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiacha suala la bonus, wakulima wote walilipwa malipo ya awali ya korosho kwa bei elekezi ya shilingi 1,200 na waliongezewa malipo ya pili kutegemeana na bei iliyopatikana sokoni. Nyongeza ya malipo ya pili yalianzia shilingi 800 kwa kilo na kufanya malipo ya chini aliyopata mkulima kuwa shilingi 2,000 kwa kilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa suala la bonus Serikali inafuatilia kuona kama kuna ubadhirifu uliofanyika katika Vyama vya Ushirika kwa kufanya ukaguzi na iwapo itadhihirika, hatua za kisheria zitachukuliwa kwa waliohusika ikiwa ni pamoja na kuamuru wahusika kurudisha fedha hizo na kupelekwa kwenye vyombo vya sheria.
Aidha, katika kuhakikisha kuwa mapunjo ya malipo ya ziada hayatokei tena, Serikali kupitia Bodi ya Korosho imejipanga kuendelea kuvihamasisha na kuvielimisha vyama vya msingi umuhimu wa kukusanya korosho kutoka kwa wanachama wake na kuziuza badala ya kuchukua mikopo yenye riba kubwa kutoka kwenye mabenki na kununua korosho hali inayosababisha malipo ya awamu yasiyokuwa na tija kwa mkulima. Vilevile wakulima wote wa korosho wanashauriwa kufungua akaunti benki kwa lengo la kukabiliana na ubadhirifu wa fedha unaochangiwa na zoezi la usafirishaji wa fedha kutoka benki kwenda kwa wakulima.
MHE. JORAM I. HONGOLI aliuliza:-
Uchumi wa wananchi wa Jimbo la Lupembe na Tarafa ya Lupembe unategemea biashara ya chai lakini kwa muda mrefu sasa wananchi wanataabika kupata soko la chai yao kwa sababu ya kufungwa kwa Kiwanda cha Chai cha Igombola - Lupembe mwaka 2009; na kwa kuwa kiwanda hicho kilikuwa cha wananchi lakini baadaye Serikali ikampata mwekezaji baada ya wananchi kushindwa kukiendesha lakini ukatokea mgogoro kati ya mwekezaji na wananchi ambao umesababisha hasara kubwa kwa wananchi, mwekazaji na Serikali pia.
Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua mgogoro huo ili Serikali iweze kunufaika na kiwanda hicho kupitia tozo ya kodi, ajira na kadhalika na wananchi waweze kuuza chai yao kwenye kiwanda hicho?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joram Ismael Hongoli, Mbunge wa Lupembe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwekezaji wa Kampuni ya Dhow Mercantile East Africa Limited alishinda kesi dhidi ya Muungano wa Vyama vya Ushirika Lupembe (MUVYULU) iliyoamuliwa ilipe fidia inayokadiriwa kuwa shilingi bilioni 28 pamoja na gharama za kuendesha kesi hiyo. Hata hivyo, MUVYULU walikata rufaa na hivyo kesi hiyo bado ipo mahakamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Serikali inasubiri maamuzi ya kesi iliyoko mahakamani kupitia uongozi wa Mkoa, Serikali iliomba Mufindi Tea and Coffee Limited kuangalia uwezekano wa kujenga Kiwanda cha Chai katika Tarafa ya Lupembe ili kuwezesha wakulima wa chai wa eneo hilo kuuza majani ya chai. Mufindi Tea and Coffee Limited ilitekeleza ombi hilo na kuunda Kampuni iitwayo Ikanga Company Limited na kujenga kiwanda katika eneo hilo na kilianza kufanyakazi mwezi Agosti, 2013 na kuzinduliwa rasmi mwezi Novemba 2013 na Rais Mstaafu Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete. Kupitia kiwanda hicho sasa, wakulima wa Lupembe wanauza chai katika kiwanda hicho na kutoa ajira katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kampuni ya Ikanga imeingia makubaliano na wakulima wa Lupembe kwa kuwapatia pembejeo na huduma za ugani ili kuweza kuzalisha chai yenye ubora mfumo ambao Serikali imekuwa ikiusisitiza katika kuendeleza uzalishaji wa mazo ya kilimo. Mwaka 2016 kampuni ya Dhow Mercantile East Africa Limited ilifanya ukarabati katika Kiwanda cha Lupembe ili kiweze kufanya kazi tena.
Hata hivyo, Serikali kupitia Bodi ya Chai imefanya ukaguzi na kugundua kasoro kuhusu hali ya kiwanda hivyo ilitoa leseni ya muda wa majaribio wa miezi mitatu kwa mwekezaji huyo ili kumpa muda wa kurekebisha kasoro zilizodhihirika. Baada ya mwekezaji kumaliza muda wa majaribio Bodi imemuongezea muda wa leseni kwa mwaka mmoja baada ya kujiridhisha na utendaji wake.
MHE. JOSEPH L. HAULE aliuliza:-
Kilio kuhusu migogoro ya wakulima na wafugaji kimekuwa ni cha muda mrefu sana kwa Wilaya ya Kilosa, lakini pia Jimbo la Mikumi, Kata za Tindiga, Kilangali na Mabwegere jambo linalosababisha wakulima kushindwa kwenda mashambani.
Je, ni lini Serikali itakomesha migogoro hiyo isiyo na tija kwa ustawi wa Taifa letu?
NAIBU WAZIRI KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Leonard Haule, Mbunge wa Mikumi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, migogoro ya wakulima na wafugaji katika Kata za Tindiga na Kilangali, inatokana na wakulima kukinga maji ya Mto Miyombo kwa ajili ya umwagiliaji na hivyo kusababisha yasitiririke na kuikosesha mifugo maji. Aidha, mipaka ya vijiji vya Kiduhi na Kilangali haijawekwa bayana kiasi cha kufanya mifugo kushindwa kupita kwenda kwenye maji. Chanzo cha mgogoro wa kijiji cha wafugaji cha Mabwegere ni vijiji jirani kutotambua mipaka ya kijiji hicho.
Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na changamoto ya maji kwa mifugo katika Kata za Tindiga na Kilangali kwa kuanzia katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa imetenga fedha kwa ajili ya kuchimba lambo katika kijiji cha Kiduhi, Kata ya Kilangali.
Mheshimiwa Spika, jitihada mbalimbali zimefanyika katika kushughulikia migogoro ya Mabwegere hadi kuhusisha mahakama. Kwa sasa suala hili linashughulikiwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambapo Waziri mwenye dhamana kwa mamlaka aliyonayo kisheria amemteua Jaji wa Mahakama Kuu ili kufanya uchunguzi wa mgogoro wa Kijiji cha Mabwegere.
Mheshimiwa Spika, ili kuondoa tatizo la migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi iliandaa mkutano wa Wakuu wa Mikoa mwezi Julai 2016, kwa lengo la kupokea taarifa ya utekelezaji wa agizo la Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la kutenga maeneo ya malisho ya mifugo ikiwemo itakayotolewa kwenye mapori ya akiba na hifadhi. Baadhi ya maazimio yaliyofikiwa ni pamoja na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kufanya tathmini ya umiliki wa Ranchi za Taifa kwa lengo la kubaini maeneo ambayo hayatumiki kikamilifu ili wapewe wafugaji. Pia Wizara ya Maliasili na Utalii kufanya tathmini ya Mapori ya Akiba na Hifadhi yaliyopoteza sifa ili yatumike kwa shughuli nyingine ikiwemo ufugaji, hii ni pamoja na kutambua kuwa mapori mengi tengefu ni ardhi za vijiji kwa mujibu wa sheria na hivyo kuendelea kuwa maeneo ya malisho. (Makofi)
MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza:-
Bei za dawa za mifugo na kilimo zinaongezeka siku hadi siku na kufanya mfugaji mdogo ashindwe kupata maendeleo:-
Je, Serikali ina utaratibu gani wa kudhibiti hali hiyo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nassoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kulijulisha Bunge Tukufu kuwa asilimia 99 ya dawa zote za tiba na kinga kwa mifugo zinazotumika nchini huagizwa kutoka nje. Jukumu la uagizaji na usambazaji wa dawa na chanjo hufanywa na sekta binafsi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Mifugo ya mwaka 2006.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa bei za dawa za mifugo katika baadhi ya maeneo zinaongezeka siku hadi siku. Miongoni mwa sababu zinazochangia kupanda kwa bei hizo ni pamoja na:-
Mheshimiwa Naibu Spika, moja, uhaba wa Sekta Binafsi katika baadhi ya maeneo kwa ajili ya kusambaza dawa husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili, baadhi ya wafugaji kutokuwa na taarifa za kutosha kuhusu namna ya kupata pembejezo za mifugo kutoka kwa mawakala halisi au wasambazaji na hivyo kununua pembejeo hizo kupitia kwa watu ambao huuza kwa bei ya juu wenye malengo ya kupata faida kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuongeza upatikanaji wa chanjo na dawa za mifugo na zenye bei nafuu, Wizara yangu kupitia Taasisi ya Chanjo Tanzania, (Tanzania Vaccine Institute) iliyoko Kibaha chini ya Wakala wa Maabara ya Vetenari (veterinary) Tanzania inazalisha chanjo dhidi ya magonjwa ya mdondo kwa kuku pamoja na chambavu na kimeta kwa ng’ombe.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa 2015/2016 taasisi imezalisha dozi 30,396,100 za mdondo, dozi ya chambavu 136,800 na dozi 304,300 za kimeta. Aidha, Baraza la Vetenari Tanzania limeendelea kuchukua hatua stahiki za kuhamasisha Sekta Binafsi kuwekeza katika kuanzisha vituo vya kutolea huduma za mifugo nchini hususan katika maeneo ya wafugaji ili kupanua wigo wa upatikanji wa huduma hizi pamoja na dawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua zingine zinazochukuliwa na Serikali ni pamoja na kuondoa ushuru wa kuingiza dawa zote za mifugo zinazoingia nchini na kodi ya ongezeko la thamani VAT.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuwapunguzia wakulima makali ya bei za dawa Serikali kila mwaka imekuwa ikitoa ruzuku ya dawa kwa ajili ya mazao ya korosho na pamba. Pia Serikali imekuwa ikitoa ruzuku kwa ajili ya miche bora inayostahimili magonjwa kwa ajili ya mazoa ya kahawa na chai. Pamoja na ruzuku hizo Serikali imekuwa ikitoa bure dawa za kudhibiti panya, viwavijeshi, kweleakwelea na nzige. Vilevile Serikali imekuwa ikigharamia ndege ya kunyunyizia dawa hizo ili kudhibiti visumbufu hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni tano kwa ajili ya kununua dawa za kilimo na shilingi bilioni moja kwa ajili ya kununua dawa za majosho.
MHE. OSCAR R. MUKASA aliuliza:-
Biharamulo ni moja ya Wilaya za Mkoa wa Kagera zilizoathirika sana na ugonjwa wa mnyauko wa migomba na hivyo ustawi wa zao hilo kuu la chakula upo mashakani.
Je, Serikali inatoa kauli gani isiyo nyepesi na inayolingana na uzito wa suala hili?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oscar Rwegasira Mukasa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ugonjwa wa unyanjano unasababishwa na bakteria aitwaye Bacterium Xanthomonas Campetris pv. Musacearum. Serikali inaendelea kufanya juhudi za kuudhibiti na kuzuia ugonjwa huu nchini kwa kutoa elimu sahihi juu ya unyanjano kwa wadau wote, madhara, ueneaji na udhibiti wa ugnjwa huu. Maeneo ambayo yamezingatia maelekezo ya udhibiti yamefanikiwa kupunguza kasi ya kusambaa kwa ugonjwa huu. Hata hivyo katika kipindi cha ukame ugonjwa wa black sigatoka umejitokeza Wilayani Biharamulo na kuleta athari kubwa katika zao la migomba. Ugonjwa huu unasababishwa na Fungi. Ugonjwa huu umejitokeza kuanzia mwezi wa Juni mwaka 2016 baada ya kuanza kipindi cha jua. Maeneo yaliyoathirika ni Nyamahanga vijiji vinne, Bisibo vijiji vinne, Ruziba vijiji vinne, Rusahunga vijiji vinne na Biharamulo vijiji vinne.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kupitia kituo chake cha utafiti kimeelekeza wataalam wa kilimo Wilayani Chato kuwashauri wakulima, kuondoa migomba yenye dalili kali za ugonjwa huo na kupanda mbegu aina ya FHIA zinazovumilia ugonjwa huu ambazo kwa sasa mbegu hizi zinapatikana kwa wingi Wilayani humo. Wakulima wakizingatia ushauri huo utasaidia kupunguza usambaaji wa ugonjwa huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, magonjwa ya unyanjano na black sigatoka yanaweza kutokomea iwapo wakulima watafuata kanuni bora za kilimo. Aidha, watafiti wetu na wa nchi za Kanda za Afrika Mashariki wanaendelea kutafiti aina ya migomba yenye ukinzani dhidi ya ugonjwa huu.
MHE. SAVELINA S. MWIJAGE aliuliza:-
Mkoa wa Kagera una mabonde mengi ambayo yanaweza kuzalisha vyakula pamoja na mboga mboga hususan mabonde ya Kalebe, Kagera na Kyabakoba:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuyaendeleza mabonde hayo ili vijana waweze kupata ajira?
(b) Je, ni lini Serikali itawapa mikopo wanawake na vijana ili waweze kujiongezea kipato?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Savelina Silvanus Mwijage, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mikoa yenye fursa nyingi za uwekezaji katika sekta ya kilimo. Aidha, Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mikoa yenye vyanzo vingi vya maji ikiwa ni pamoja na Ziwa Burigi na Ziwa Rwelu na Mito ya Kagera na Rusumo inayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji. Kwa sasa, Serikali inafanya upembuzi yakinifu, usanifu na uandaaji wa makabrasha ya zabuni ya mradi wa mabonde yaliyopo Kagera yanayofaa kwa umwagiliaji chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia ambapo mabonde aliyoyataja Mheshimiwa Mbunge yapo ndani ya mradi huo. Aidha, zoezi la upembuzi yakinifu, usanifu na uandaaji wa makabrasha ya zabuni unatarajiwa kukamilika Aprili 2017 na baada ya hapo Serikali itaendelea kuwasiliana na wafadhili juu ya utekelezaji wa mradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu kwa kushirikiana na halmashauri husika inaendelea kuainisha maeneo yanayofaa kwa kilimo hasa kilimo kinachohusisha vijana na utekelezaji wa mpango na mikakati ya kuhakikisha vijana wengi wanajiajiri kupitia sekta ya kilimo. Suala la upatikanaji wa ajira kwa vijana na wanawake linachukuliwa kwa uzito wa hali ya juu hasa ukizingatia vijana kuwa ni takribani asilimia 67 ya nguvukazi ya Taifa kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) pamoja na wadau wengine wa maendeleo tayari inafanya upembuzi yakinifu kwa kutembelea maeneo mbalimbali nchini ili kuainisha shughuli za vijana pamoja na kuhamasisha kujiunga katika vikundi, kuongea na Serikali za Mitaa ili kubaini changamoto ambazo vijana wanakabiliana nazo wakati wa shughuli zao za kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Wizara zingine za kisekta pamoja na sekta binafsi tayari imetayarisha mkakati wa kuhusisha vijana katika sekta ya kilimo uitwao National Strategy for Youth Involvement in Agriculture wa miaka mitano ambao utasaidia kuweka mzingira bora ya utekelezaji wa mipango kutoka kwa wadau ili kuwanufaisha vijana. Mkakati huu ulizinduliwa mwezi Oktoba, 2016.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM aliuliza:-
Uvuvi ni miongoni mwa sekta inayochangia Pato la Taifa, lakini Serikali imekuwa na kigugumizi cha kuboresha sekta hii wakati tukielekea katika Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati.
Je, Serikali ina mkakati gani madhubuti wa kuboresha sekta ya uvuvi nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Masoud Abdallah, Mbunge wa Mtambile, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imeendelea kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vya kutengeneza zana za uvuvi. Hadi sasa jumla ya viwanda vitatu vya kutengeneza boti aina ya fibre glass na viwanda viwili vya kutengeneza nyavu vimeanzishwa. Aidha, viwanda vya kuchakata mazao ya uvuvi 48 vinavyojumuisha viwanda vikubwa 15 na vidogo 33 pamoja na maghala ya kuhifadhi mazao ya uvuvi 38 yameanzishwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini. Sambamba na hilo Serikali ikishirikiana na sekta binafsi inafanya juhudi ya kutafuta wawekezaji wa kujenga viwanda vya kuchakata samaki aina ya jodari katika huu Ukanda wa Pwani wa Bahari ya Hindi, hili likifanikiwa litawezesha wavuvi kuongeza thamani ya mazao ya samaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imedhamiria kuongeza uzalishaji wa Samaki kupitia ufugaji wa samaki (aquaculture) kutoka metriki tani 10,000 mpaka metriki tani 50,000 ifikapo mwaka 2020. Aidha, Serikali ina dhamira ya kuanzisha vituo vipya vitatu na kuboresha vituo vingine 15 vya uzalishaji wa mbegu bora za samaki, kushirikisha sekta binafsi na taasisi za kitafiti katika kuboresha teknolojia na uzalishaji wa mbegu na chakula bora cha samaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hatua zake za kuendeleza uvuvi wa bahari kuu, Serikali imekamilisha mazungumzo kati yake na Mamlaka ya Bandari ya Dar es Salaam ambapo gati namba sita litatumiwa na meli zinazovua katika ukanda wa uchumi wa bahari, ili kushusha samaki. Aidha, juhudi za ujenzi wa bandari ya uvuvi zinaendelea ambapo tayari mtaalam elekezi wa kufanya upembuzi yakinifu amepatikana.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA (K.n.y MHE. DOTTO M. BITEKO) aliuliza:-
Wakulima wa pamba Wilaya ya Bukombe na Geita kwa jumla katika msimu wa mwaka 2015 walipatiwa mbegu na dawa yasiyokuwa na ubora ambayo hayakuua wadudu.
Je, Serikali inawaambia nini wakulima walioathirika na pembejeo hizo na inachukua hatua gani kuhakikisha jambo hili halijirudii tena?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dotto Mashaka Biteko, Mbunge wa Bukombe kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imepata taarifa kuhusu tatizo lililowapata wakulima wa pamba katika maeneo mbalimbali ikiwemo wale ikiwemo wale wa Mkoa wa Geita kwa kusambaziwa mbegu ambazo hazikuwa na ubora unaotakiwa. Aidha, katika msimu wa kilimo wa mwaka 2015/2016, viuatilifu vilivyosambazwa kwa wakulima vilishindwa kudhibiti wadudu wa pamba kikamilifu katika maeneo mengi ikiwemo Mkoa wa Geita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ununuzi wa pembejeo za zao la pamba unaratibiwa na Mfuko wa Kuendeleza Zao la Pamba (CDTF), usambazaji wa pembejeo hizo baada ya ununuzi unaishirikisha Bodi ya Pamba. Kufuatia taarifa za uwepo wa pembejeo hafifu hususan viatilifu Serikali iliagiza TPRI kufanya uchunguzi wa malalamiko ya wakulima. Uchunguzi ulibaini kwamba kiuatilifu kinachofahamika kwa jina la Ninja 5EC ndicho kilichokuwa kinalalamikiwa na wakulima kwa utendaji hafifu. Uchunguzi zaidi ulionesha kwamba baadhi ya sumpuli za kiuatilifu hicho zilikuwa na kiwango kidogo cha kiambato amalifu (active ingredient) ya kinachotakiwa, hivyo, kiuatilifu hicho hakingeweza kuua wadudu waliolengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa za uchunguzi uliofanywa na TPRI, Bodi ya Pamba, CDTF, wawakilishi wa wasambazaji, wakulima na wadau wengine zimeonesha kwamba viuatilufu hivyo vya Ninja 5EC (Batch Na 2014102001 na KR4003) vilinunuliwa kutoka Kampuni ya Positive Internatinal Limited na kusambazwa na UMWAPA na kutoka Kampuni ya Mukpar Kagera Limited (Batch Na. KR1400451103) na kusambazwa na Mfuko wa Kuendeleza zao la Pamba. Aidha, uchunguzi unaonesha kwamba kuna batches za viuatilifu za mwaka 2014/2015 zilisambazwa pia, ambazo inawezekana kama hazikutunzwa vema ubora ungeweza kuwa na mashaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kwamba matumizi ya kiutalifu hafifu kwa mujibu wa uchunguzi huu kilikuwa na athari kwa wakulima. Kufuatia taarifa hizo za uchunguzi Serikali inakamilisha taratibu za kuchukua hatua za kisheria kwa wale wote waliyohusika na kadhia hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia changamoto za utoaji wa mbegu za pamba ambazo unatokea, Serikali katika msimu wa mwaka 2016/2017 iliamua kufanya majaribio ya utoaji wa mbegu za pamba ambazo zimekuwa zikisambazwa hapo awali bila kujua ufanisi katika utoaji wake. Matokeo ya majaribio ya utoaji yamewezesha kutoa maelekezo kuhusu batches za mbegu za pamba zenye sifa za msingi kusambazwa kwa wakulima katika msimu wa kilimo wa mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuhakikisha jambo hili halijirudii tena, Serikali itaanza kuzalisha mbegu bora za pamba za UKM08 katika mashamba maalum ili hatimaye baada misimu miwili ya kilimo wakulima wote waweze kupata mbegu bora za pamba.
MHE. MUSSA R. NTIMIZI (K.n.y. MHE. MARGARET S. SITTA) aliuliza:-
Pamoja na jitihada za Serikali za kuendeleza kilimo, bado kuna vikwazo vinavyomkandamiza mkulima wa tumbaku ashindwe kujiendeleza kiuchumi:-
(a) Je, hadi sasa Serikali imechukua hatua gani ili kuongeza wanunuzi wa tumbaku ili kuleta ushindani wa bei na kuwa na masoko ya uhakika?
(b) Je, Serikali imechukua hatua gani kuondoa tozo na makato lukuki katika bei ya tumbaku?
(c) Je, Serikali imechukua hatua gani katika kupunguza daraja za tumbaku?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nasi kama Wizara tunatambua kwamba Mheshimiwa Margaret Sitta amekuwa mshauri mkubwa sana, lakini vile vile amesimamia suala la tumbaku nasi tunapenda kutoa pole kwa msiba mkubwa uliompata.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta, Mbunge wa Urambo, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba hapa nchini yapo makampuni machache yanayojishughulisha na biashara ya tumbaku, hivi sasa Serikali kupitia Bodi ya Tumbaku inaendelea kutafuta masoko zaidi ili kuongeza uzalishaji na ushindani wa bei. Hadi sasa Kampuni ya China Sunshine inakamilisha taratibu za kuingiza tumbaku yetu katika soko la China. Vile vile imefanikiwa kupata Kampuni ya Sino Cigarette ya China ambayo inatarajia kununua tumbaku ya Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, Bodi imeshaisajili Kampuni hiyo na kuiruhusu kufanya maandalizi ya ununuzi wa tumbaku. Pamoja na hayo, Soko la Tumbaku Duniani lipo kwenye kampuni kubwa chache zinazofanya biashara, siyo kwa ushindani, bali ni muungano wa ukiritimba (cartel) katika kupanga bei na kiasi cha kununua kutoka nchi fulani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, pamoja na kuwa ushindani ni mojawapo ya vigezo vya kupata bei nzuri, lakini katika zao la tumbaku vipo vigezo vingine vya kuwezesha kupata bei nzuri, ambavyo ni pamoja na ubora, vigezo vya kukubalika sokoni (compliance) na ufanisi katika uendelezaji wa Vyama na Biashara yenyewe katika maana ya efficiency. Hivi sasa Serikali inaelekeza nguvu kwenye kuwezesha zao kukubalika sokoni kwa kuboresha uhifadhi wa mazingira, kuondoa ajira ya watoto na kuongeza ufanisi kwa kuimarisha Vyama vya Ushirika, mazingira ya kufanyia biashara, kuondoa tozo, kodi na gharama za uzalishaji zisizo za lazima.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Wizara zinazohusika inafanyia mapitio tozo na kodi zilizopo katika mazao mbalimbali ikiwemo zao la tumbaku ili kuona uwezekano wa kuziondoa au kuzipunguza. Uchambuzi huo utakamilika kabla ya Bajeti ya Serikali ya mwaka 2017/2018 ambapo tunategemea kuwepo kwa unafuu mkubwa katika makato mbalimbali katika zao la tumbaku na mazao mengine.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, Bodi kwa kushirikiana na wadau wa tasnia ya tumbaku imepunguza madaraja 10 na hivi sasa kuna madaraja 62 badala ya 72 ambayo yatatumika msimu huu wa kilimo katika maana ya 2016/2017. Aidha, wakulima wanashauriwa kuongeza ubora wa tumbaku wanayozalisha jambo ambalo litapunguza madaraja moja kwa moja.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI aliuliza:-
Kuendelea kuwepo kwa uvuvi haramu kunatokana na Serikali kutochukua hatua stahiki kwa wanaofanya vitendo hivyo, hasa watengenezaji na wauzaji wa nyavu haramu, badala yake wanabebeshwa lawama wavuvi peke yao:-
Je, Serikali itakomesha lini tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Raphael Masunga Chegeni, Mbunge wa Busega, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kuwa lipo tatizo kubwa la uvuvi haramu hapa nchini. Katika kudhibiti uvuvi haramu hapa nchini, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kukabiliana na tatizo hili kwa kutoa elimu kwa wadau wanaochangia kuendelea kuwepo kwa uvuvi haramu wakiwemo wenye maduka yanayouza nyavu na zana haramu, wasuka nyavu zenye macho madogo na makokoro, wauzaji wa mabomu , ndoano na zana nyingine zinazozuiliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali imeendelea kufanya doria za kudhibiti uvuvi haramu na kaguzi kwenye maduka yanayouza zana za uvuvi ili kubaini uwezo wa zana haramu kupitia vituo 25 vya doria vilivyoanzishwa Kwenye maziwa makubwa, mwambao wa Bahari ya Hindi na mipaka ya nchi.
Vile vile kwa kushirikiana na Halmashauri, elimu kuhusu madhara ya uvuvi haramu imeendelea kutolewa kwa wadau mbalimbali wakiwemo wavuvi, watendaji wanaohusika na Ushuru wa Forodha mipakani ili kuwa na juhudi za pamoja za kudhibiti biashara ya zana haramu na kuwa na matumizi endelevu ya rasilimali za uvuvi kupitia vyombo vya habari na maonesho ya Kitaifa yakiwemo Siku ya Wakulima (Nane Nane) na Siku ya Mvuvi Duniani ambayo hufanyika tarehe 21 Novemba kila mwaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ushirikishwaji wa jamii za wavuvi katika kusimamia rasilimali za uvuvi unafanyika kupitia vikundi vya usimamizi wa rasilimali za uvuvi (Beach Management Units) 754 vilivyoanzishwa katika maeneo mbalimbali. Pia vipindi mbalimbali vya televisheni na redio vimeandaliwa ili kuonesha madhara ya uvuvi haramu na vitaanza kurushwa hivi karibuni.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hatua hizo, Serikali ikishirikiana na Idara ya Mahakama inaendesha zoezi la Mobile Court ili kuharakisha mashauri ya wavuvi haramu mara wanapokamatwa. Utaratibu huu umeelekezwa uanze kutumika kwenye maeneo yote yenye kukithiri katika uvuvi haramu na vyombo vyote vya dola vinapaswa kutoa ushirikiano stahiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Bunge lako Tukufu nawaomba Waheshimiwa Wabunge ambao ni Wajumbe katika Mabaraza ya Madiwani wazielekeze Halmashauri, Kata, Vijiji na Mitaa kudhibiti uvuvi haramu kwenye maeneo yao na wananchi kutoa taarifa za wavuvi haramu kwa vyombo vya dola ili hatua stahiki zichukuliwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Halmashauri zote nchini zielimishe jamii za wavuvi na wadau wengine kuhusu madhara ya uvuvi haramu ili kusimamia rasilimali za uvuvi na kuwa na uvuvi endelevu kwa ajili ya kuwapatia wananchi ajira, chakula, kipato na mapato kwa Taifa kwa ujumla. Ni kwa njia hii Taifa litaweza kudhibiti uvuvi haramu hapa nchini.
MHE. ROSE K. SUKUM aliuliza:-
Watanzania 89% wanategemea shughuli za kilimo na wengi wanaojihusisha na kilimo ni watu wa kipato cha chini. Serikali katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano ilianzisha Benki ya Kilimo, kwa mujibu wa Mpango huo kuanzia mwaka 2011/2012 hadi 2015/2016 ilitakiwa kutoa kila mwaka shilingi bilioni 100 ili Benki hiyo iwe na mtaji wa shilingi bilioni 500; lakini hadi sasa katika kutekeleza mpango huo Serikali imepeleka shilingi bilioni 60 tu:-
(a) Je, ni lini Serikali itatekeleza matakwa ya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano ya kwanza katika dira ya mwaka 2025 ya shilingi bilioni 100 kila mwaka?
(b) Je, Benki hiyo ina mpango gani wa kuwafikia wakulima wadogo ambao ndio nguzo kuu nchini Tanzania katika kuondoa umasikini wa kipato?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rose Kamili Sukum, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Benki ya Maendeleo ya Kilimo imezunduliwa rasmi mwezi Agosti, 2014. Serikali ina nia thabiti ya kuhakikisha benki hiyo inapata mtaji wa kutosha ili kuiwezesha kutimiza lengo lililokusudiwa la kuwezesha upatikanaji wa mikopo kwa wakulima wadogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kutenga fedha hatua kwa hatua na katika bajeti ya 2016/2017, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 200 ili kuiongezea benki hiyo mtaji. Katika kumaliza tatizo la mtaji, Serikali imejizatiti kuongeza mtaji huo kupitia hati fungani ya mtaji isiyo ya fedha taslimu katika maana ya (Non-Cash Bond) yenye thamani ya shilingi bilioni 800 itakayolipwa kwa kipindi cha miaka sita kuanzia mwaka ujao wa fedha wa 2017/2018.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, kupitia ujio wa Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) yamekuwepo mazungumzo baina ya AfDB na TADB ili kuiongezea mtaji TADB. Kwa vile mkopo huo utakopwa na Serikali, majadiliano baina ya Wizara ya Fedha na Mipango na Benki hiyo yanaendelea ambapo yatakapokamilika, yatawezesha Benki ya Kilimo kuwa na mtaji mkubwa zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa Benki hii wa kuwafikia wakulima wadogo umejikita katika kuvijengea uwezo vikundi vya wakulima ili viweze kukopesheka na kuwa na uwezo wa kurejesha mikopo hiyo. Benki ya Kilimo imeanza kutoa huduma ya mikopo katika mikoa sita ikilenga kuwajengea uwezo wakulima wadogo kwa kushirikiana na Sekretarieti za Mikoa, Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, Mfuko wa Pembejeo na Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika utekelezaji wa mpango huo, Benki ilianza kwa kuvijengea uwezo vikundi 89 vya wakulima wadogo vyenye jumla ya wakulima 21,563 na kati ya hivyo, jumla ya vikundi nane vilitimiza masharti ya msingi ya kuweza kukopa. Vikundi hivyo vipo katika Mkoa wa Iringa na vina wakulima wadogo wapatao 800. Vikundi hivyo nane vimeshapata mikopo yenye thamani ya jumla ya sh. 1,006,822,010/=.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA aliuliza:-
Kumekuwa na mgogoro kati ya wafugaji na wakulima wa Jimbo la Same
Mashariki dhidi ya TANAPA:-
(a) Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwapatia wafugaji hao shamba
darasa kupitia hekta 346,000 zinazofaa kwa ufugaji?
(b) Ili kutatua tatizo la maji na malisho kwa wafugaji wa Same
Mashariki: Je, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi haioni umuhimu wa
kuanzisha mradi wa kuvuna maji ya mvua ambazo hunyesha mara kwa mara?
(c) Je, Waziri yuko yatari kuambatana na wataalam wake
kutembelea Jimbo la Same Mashariki ili kuona ni jinsi gani anaweza kuwasaidia
wafugaji kuanzisha mitambo ya Biogas kwenye mazizi yao pamoja na
kuwaelimisha matumizi bora ya mbolea ya samadi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa KIlimo, Mifugo na Uvuvi,
napenda kujibu swali la Mheshimiwa Naghenjwa Livingstone Kaboyoka, Mbunge
wa Same Mashariki, lenye sehemu (a) (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Shamba darasa la unenepeshaji mifugo limeanzishwa katika Kijiji
cha Ruvu mferejini, Kata ya Ruvu kati ya hekta 2,754 zimepimwa kutokana na
hekta 346,000 zilizoainishwa na vijiji mbalimbali katika Wilaya kwa ajili ya ufugaji.
Uainishaji wa maeneo umefanyika katika Kata zote zinazopakana na mbuga za
Mkomazi na upimaji utafanyika kulingana na upatikananji wa fedha.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaona umuhimu wa kuvuna maji
ya mvua ili kutatua tatizo la maji kwa mifugo katika Jimbo la Same Mashariki;
ambapo kwa kushirikiana na taasisi binafsi ya Women and Youth Empowerment,
Enviro Care and Gender Trust Fund (WOYOGE) na TANAPA, imewezesha ujenzi
wa birika la maji katika Kijiji cha Muheza katika Kata ya Maole na maji yanaingia
katika birika hilo kutokana na chanzo cha maji kutoka Milima ya Mbaga. Aidha,
uvunaji wa maji ya mvua unatarajiwa kutekelezwa kwa ufadhili wa Shirika la
United Nations Capital Development Fund (UNCDF) kwa kukarabati bwawa
katika Kata ya Kalemawe kwa matumizi ya maji kwa kilimo, mifugo, uoteshaji wa
miti na ufugaji wa samaki ambao utasaidia upatikanaji wa maji kwa kipindi cha
mwaka mzima utakapokuwa umetekelezwa.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia CAMARTEC ikishirikiana na
sekta binafsi ya Tanzania Domestic Biogas Program imeendelea kutoa elimu kwa
jamii juu ya matumizi ya biogas katika Jimbo la Same Mashariki ambapo jumla ya
mitambo 106 ya biogas imejengwa katika Vijiji vya Bwambo, Goha, Kirangare,
Bendera, Kihurio, Mtii, Vuje, Njagu, Ndungu, Myombo, Mjema, Maore, Mvaa na
Mpirani. Aidha, Serikali imekwishaanza kutoa uhamasishaji wa matumizi ya biogas
na mbolea ya samadi. Hata hivyo, kukiwa na uhitaji kama alivyoomba
Mheshimiwa Mbunge, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi na kwa sababu inahusu
nishati na Waziri wa Nishati na Madini wanaweza kuambatana na wataalam
wao kutembelea Jimbo la Same Mashariki.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:-

Zao la korosho linakabiliwa na changamoto kadhaa:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa Chuo cha Utafiti wa Kilimo – Naliendele kinapanuliwa ili kiweze kufanya tafiti mbalimbali za magonjwa yote ya korosho badala ya sampuli kupelekwa nje ya nchi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota, Mbunge wa Nanyamba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Utafiti Naliendele ni kituo mahiri cha kufanya utafiti wa kugundua na kutathmini aina bora za korosho zinazotoa mavuno mengi na zinazopendwa katika soko. Vilevile kituo kinafanya utafiti kuhusu mbinu bora za uzalishaji, magonjwa na wadudu wanaoshambulia korosho na utafiti wa kuongeza thamani ya zao la korosho. Pia ni kituo cha kwanza Afrika kutoa mbegu bora za korosho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Naliendele ilipeleka sampuli za korosho nje ya nchi ili kupata ufafanuzi kama vimelea vinavyosababisha ugonjwa wa ukungu au blight ni aina moja au tofauti. Ufafanuzi wa aina hii wa aina za vimelea utasaidia kuweza kupata viatilifu vya ugonjwa huu. Maabara za nje ya nchi ni maalum (specialized laboratories) ambazo hufanya uchunguzi wa magonjwa ya mazao mbalimbali ikiwemo zao la korosho kutoka katika nchi tofauti. Maabara za aina hizi ni ghali kuendesha hivyo kuwa na maabara ya aina hii hapa nchini itakuwa ni hasara kwa vile matumizi yake yatakuwa chini yaani underutilized ukilinganisha na fedha zitakazotumika kujenga na kutunza maabara hiyo.
MHE. HASNA S. K. MWILIMA aliuliza:-

Tarafa ya Nguruka na Uvinza zinalima zao la tumbaku na kuiingizia Halmashauri ya Uvinza fedha nyingi kwenye makusanyo ya ndani lakini wamekuwa wakinyonywa kwenye bei ya uuzaji na upangaji wa viwango vya pamoja vya soko:-
Je, ni lini Serikali itawatumbua wakulima wa tumbaku wa Uvinza ili nao wapate chama kikuu ndani ya Mkoa wa Kigoma na kuwapunguzia gharama za usafirishaji kwenda hadi Tabora?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hasna Sudi Katunda Mwilima, Mbunge wa Kigoma Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa wakulima wa tumbaku kuendelea kunufaika na huduma zitolewazo kupitia vyama vya ushirika. Aidha, kwa mujibu wa Sheria ya Ushirika Na. 6 ya mwaka 2013 na Kanuni za mwaka 2015 ili chama cha ushirika kiweze kusajiliwa kinapaswa, pamoja na kutimiza masharti mengine, kikidhi kigezo cha kuwa na uhai wa kiuchumi katika maana ya economic viability.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa chama kikuu kuanzishwa, uhai wa kiuchumi unazingatia viwango vya uzalishaji kwa mwaka wa vyama vya msingi vinavyohudumiwa na chama kikuu hicho na ufanisi wa mfumo wake wa masoko. Kwa mujibu wa matakwa hayo ya kisheria ili chama kikuu cha ushirika wa tumbaku kiweze kusajiliwa kinapaswa kiwe kinazalisha na kuuza angalau kilogramu milioni kumi za tumbaku kwa mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa katika Mkoa wa Kigoma kipo chama kikuu kiitwacho Kigoma Tobacco Growers Cooperative Union (KITCU). Chama kikuu hicho kinahudumia Wilaya za Kakonko, Kibondo, Kasulu na Uvinza. Takwimu zinaonesha kuwa kutokana na wanunuzi wa tumbaku kupunguza mahitaji ya tumbaku kwa mwaka, uzalishaji wa chama kikuu hicho umepungua hadi kufikia wastani wa kilogramu milioni nane kwa mwaka. Wilaya ya Uvinza ambayo inajumuisha Tarafa za Nguruka na Uvinza inazalisha takriban 55% ya tumbaku yote ya KITCU, ambazo ni takriban kilogramu milioni 4.5. Katika mwaka wa fedha 2015/2016, Wilaya hiyo imezalisha kilogramu 3,586,175 za tumbaku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na taarifa hiyo na umuhimu wa kuzingatia Sheria ya Ushirika katika kuanzisha vyama vya ushirika, kwa sasa chama kikuu kingine cha ushirika kinachojishughulisha na zao la tumbaku katika Mkoa wa Kigoma hakiwezi kuanzishwa. Badala yake Serikali inajielekeza katika kuimarisha nguvu za uzalishaji za KITCU, chama ambacho makao yake makuu yako Nguruka katika Wilaya ya Uvinza ili kiweze kukidhi vigezo vya kiuchumi na kisheria na hivyo kuendelea kuwahudumia wanachama wake kwa ufanisi zaidi, wakiwemo wananchi wa Wilaya ya Uvinza.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA aliuliza:- Katika kampeni zake za kutafuta Urais, Mheshimiwa Rais, Dkt. John Joseph Pombe Magufuli aliwaahidi wananchi wakulima na wavuvi kuboresha maisha yao, ikiwa ni pamoja na kununua mazao na kusaidia vifaa vya uvuvi kwa bei nafuu na mikopo kwa wavuvi. (a) Je, katika bajeti ya mwaka huu azima hii imezingatiwa? (b) Je, ni fedha kiasi gani itatengwa kwa ajili ya kununulia mazao? (c) Je, ni kiasi gani kimetengwa kwa ajili ya mkopo kwa wananchi wanaojishughulisha na uvuvi hasa wale wa mwambao wa Ziwa Tanganyika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Desderius John Mipata, Mbunge wa Nkasi Kusini kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendeleza jitihada zake za kuwajengea mazingira mazuri wakulima na wavuvi na kuhakikisha gharama kubwa za pembejeo na vyombo vya uvuvi zinapungua ili waweze kuzipata kwa bei nafuu kwa kutenga kiasi cha milioni 100 kwa ajili ya ruzuku ya zana za uvuvi, na jumla ya shilingi bilioni 26.99 kwa ajili ya ununuzi wa mazao katika bajeti ya Wizara ya mwaka 2016/2017. Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) umetengewa shilingi bilioni 15, Bodi ya Nafaka na Mazao mchanganyiko shilingi bilioni 8.95. Aidha, ili kuongeza uwezo wa hifadhi kwa ajili ya kuwezesha kutunza mazao mengi zaidi, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula unaendelea kukamilisha ujenzi wa ghala la Mbozi lenye uwezo wa kuhifadhi tani 5,000. Wakala pia unaongeza uwezo wa kuhifadhi kutoka tani 246,000 hadi tani 496,000 kwa kujenga vihenge na maghala katika kanda za Arusha, Shinyanga, Dodoma, Makambako, Songea na Sumbawanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haikopeshi wavuvi bali inaweka mazingira wezeshi kwa wavuvi kupata mikopo yenye riba nafuu. Aidha, Serikali kupitia Benki ya Rasilimali (TIB) imeweka Dirisha la Kilimo Kwanza kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wakulima na wavuvi. Pia Serikali imeanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo, ambayo baadhi ya majukumu yake ni kuwapatia wakulima na wavuvi mikopo yenye riba nafuu. Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imepanga kutoa ruzuku kwa wavuvi kwa utaratibu wa Serikali kuchangia asilimia 40 na wavuvi kuchangia asilimia 60 ya gharama. Ruzuku hiyo itatolewa kwa kuzingatia vigezo vifuatavyo:- (i) Vikundi vya wavuvi vinavyomiliki vyombo vya uvuvi vilivyosajiliwa kisheria ambavyo vinalenga kuvua kwenye maji ya kina kirefu; (ii) Vikundi kuthibitisha uwezo wa kulipa asilimia 60 ya gharama ya vyombo na zana zilizoombwa; na (iii) Maombi husika yanatakiwa yapitishwe na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri husika. Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa rai kwa Waheshimiwa Wabunge kuhimiza vikundi vya uvuvi vilivyo katika majimbo yao vilivyokidhi vigezo kukamilisha taratibu za kuchukua engine hizo. Aidha, vikundi vingine vinashauriwa kutuma maombi kupitia Halmashauri zao na kuwasilisha Wizarani ili viweze kupata engine za uvuvi.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA aliuliza:- Je, ni hatua gani madhubuti Serikali itachukua kwa kampuni zinazoshinda tender (zabuni) za ununuzi wa korosho lakini haziwalipi wakulima kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Hamis Ulega, Mbunge wa Mkuranga kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Mwenyekiti, mojawapo ya masuala ya msingi katika miongozo ambayo hutolewa na Serikali kupitia Bodi ya Korosho Tanzania ni kuwataka wanunuzi wa korosho kulipia kwa wakati korosho wanazoshinda kwenye mnada. Hata hivyo, baadhi ya wanunuzi hukiuka masharti hayo kwa visingizio mbalimbali ikiwemo kushuka kwa ubora wa korosho tofauti na ule uliopo kwenye sales catalogue na kushuka kwa bei ya korosho katika masoko ya nje. Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Bodi ya Korosho imekuwa ikihimiza wanunuzi kufuata sheria, kanuni za taratibu zilizowekwa na mamlaka husika. Aidha, Serikali kupitia Sheria ya Korosho Namba 18 ya mwaka 2009 kifungu cha 17 na kanuni za mwaka 2010 kanuni ya 33, itafungia kampuni yoyote ambayo inafanya biashara ya korosho nchini endapo itakiuka sheria na kanuni ikiwemo ya kutowalipa wakulima kwa wakati ili kubaki na makampuni yanayotii sheria. Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Bodi ya Korosho imefanya maboresho na kutoa mwongozo ulioanza kutumika msimu wa mwaka 2016/2017 kwa kila mnunuzi kuweka dhamana ya fedha taslimu au hundi ya benki kulingana na kiasi cha korosho alizonunua kama dhamana itakayotumika kuwalipa wakulima endapo mnunuzi akishindwa kuwalipa wakulima. Kiwango cha chini ni kununua tani 50, mnunuzi akinunua kati ya tani 50 na 100 atalazimika kulipa shilingi milioni 50 kama dhamana. Kati ya tani 101 na tani 1000 dhamana yake ni shilingi milioni 100 na zaidi ya tani 1001 dhamana yake ni shilingi milioni 300. Dhamana hiyo huchukuliwa mara baada ya Bodi ya Korosho na wahusika wote vikiwemo Vyama vya Ushirika kujiridhisha kuwa mnunuzi alikiuka taratibu na pia adhabu nyingine zinaweza kuchukuliwa dhidi ya kampuni husika.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI aliuliza:-
Wakulima wadogo wadogo wa mkonge wamekuwa wakiuza mkonge kwa Kampuni ya Katani lakini kampuni hiyo imekuwa haiwalipi wakulima fedha zao.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha wakulima wanalipwa fedha zao kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajibu swali na mimi niungane na Waheshimiwa Wabunge wote kumkaribisha Mheshimiwa Ngonyani tena Bungeni, lakini zaidi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumrejesha salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme vilevile kwamba kuna kitu ambacho mimi kimenigusa sana. Muda wote ambao Mheshimiwa Ngonyani amekuwa mgonjwa hakusita kuendelea na majukumu yake ya Kibunge kwani aliendelea kuwasiliana na Wizara yangu kuwatetea wananchi wake na hata hili swali ambalo ameuliza, amepiga simu mara nyingi sana kuulizia madeni ya wananchi wake wanaodai madai ya Katani, kwa hiyo, ameonyesha uwakilishi uliotukuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Steven Hilary Ngonyani, Mbunge wa Korogwe Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na malalamiko ya wakulima wadogo wa mkonge walio chini ya scheme ya Sisal Smallholders and Outgrowers Scheme (SISO) ya kutoridhika na ucheleweshwaji wa malipo yao kwa mkonge unaosindikwa na Kampuni ya Katani Limited. Scheme hii inaendesha kilimo cha mkataba ambapo chini ya mfumo huu Katani Limited ni mnunuzi na msindikaji wa mkonge wa mkulima wakati mkulima ana wajibu wa kupanda, kutunza, kuvuna na kusafirisha mkonge wake hadi kwenye kiwanda (Korona) inayomilikiwa na Katani Limited katika shamba husika kwa ajili ya kusindikwa.
Kwa mujibu wa mkataba kati ya mkulima na Katani Limited, Katani inapaswa kumlipa mkulima fedha zake ndani ya siku 60 baada ya kusindika mkonge wa mkulima, na inapotokea kampuni ya Katani kuchelewesha malipo zaidi ya siku 60, inalazimika kumlipa mkulima malipo hayo pamoja na riba ya asilimia 1.5 ya malipo hayo kwa kila mwezi uliocheleweshwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumetokea ucheleweshwaji wa malipo haya kwa mwaka 2016 kutokana na kuyumba kwa masoko ya mkonge duniani na kushuka kwa bei za mkonge. Kampuni imelazimika kuuza shehena iliyokuwepo japo kwa hasara na hivyo hadi sasa wakulima wanadai malipo ya mkonge waliovuniwa ya miezi mitatu yaani Septemba hadi Novemba, 2016 ambayo hayajalipwa. Malipo ya miezi hiyo mitatu yanatarajiwa kufanyika mwezi Februari, 2017 yaani mwezi huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Bodi ya Mkonge Tanzania imekuwa ikichukua hatua za kuhakikisha kwamba wakulima wanalipwa fedha zao kwa wakati.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:-
Zao la pamba ndilo zao kuu katika Wilaya ya Bunda:-
(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwapatia zao mbadala wakulima wa zao la pamba, baada ya zao hili kuelekea kutokomea kutokana na matatizo ya bei ndogo isiyokidhi mahitaji ya uzalishaji wake?
(b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuongeza uzalishaji wa zao la pamba hasa ikizingatiwa kuwa Wilaya ya Bunda yenye majimbo matatu inategemea viwanda vya pamba katika mapato na ajira?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Serikali bado inaona kuwa kuna tija katika zao la pamba kwa wakulima wa Bunda na maeneo mengine yanayolima pamba nchini kuliko mazao mengine kwa manufaa ya wakulima wenyewe na Taifa kwa ujumla. Hata hivyo, wakulima wanaweza kulima pamba
sambamba na mazao mengine kama vile mazao ya bustani ili kujiongezea kipato. Aidha, kuyumba kwa uzalishaji wa pamba hapa nchini kunasababishwa na changamoto nyingi ikiwemo mabadiliko ya mara kwa mara ya bei katika soko la dunia, kukosekana kwa mbegu bora, upatikanaji na matumizi sahihi ya viuatilifu na mbolea.
Mheshimiwa Spika, hali hii imefanya wakulima wengi wa pamba nchini kuzalisha wastani wa kilo 300 kwa ekari tofauti na kilo 800 zinazopaswa kuzalishwa kwa ekari. Ili mkulima aweze kuona faida ya kilimo cha pamba anayouza kulingana na bei inayopangwa na wadau wakiwemo wakulima, mkulima anatakiwa azalishe zaidi ya kilo 800 kwa ekari ya pamba nyuzi yenye ubora unaotakiwa na soko.
(b) Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali imeandaa mpango maalum wa kuhakikisha kuwa kufikia msimu wa 2018/2019 wakulima wa pamba kote nchini wanatumia mbegu bora za pamba aina ya UKM08 zenye tija kubwa badala ya mbegu aina ya UK91 ambayo imepoteza ubora wake. Mbegu hiyo ya UKM08 inazalishwa katika maeneo ya Meatu, Nzega na Igunga ambayo hayana ugonjwa wa mnyauko. Aidha, Serikali inaendelea kusimamia upatikanaji wa viuatilifu bora na matumizi sahihi ili kuhakikisha wakulima wanatumia na kupata pamba iliyo bora na kukidhi mahitaji ya soko.
Mheshimiwa Spika, katika hatua nyingine, Serikali imeandaa mkakati wa kitaifa wa Cotton To Clothing 2016 – 2020 wenye lengo la kuendeleza mnyororo wa thamani wa zao la pamba ambao utaondoa utegemezi wa bei ya soko la kimataifa kwa kuwekeza katika viwanda vitakavyonunua pamba ya wakulima na hivyo kupunguza uuzaji wa pamba ghafi nje ya nchi. Hatua hii inakwenda sambamba na malengo ya Kitaifa ya kuwa nchi ya viwanda.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-
Serikali imeweka kipaumbele kwenye sekta ya kilimo na kuainisha kwamba mazao ya kilimo yatakuwa moja ya malighafi kwenye viwanda nchini:-
(a) Je, Serikali imeweka mkazo gani kwenye vyanzo vya kilimo ambavyo ndivyo vitakuwa malighafi na kusababisha uzalishaji ukue?
(b) Je, Serikali ina mkakati gani juu ya uhakika wa wakulima wengi zaidi kuingia kwenye kilimo cha umwagiliaji?
(c) Je, Serikali imewekeza kwa kiasi gani kwenye zana za kilimo za kisasa kwa wakulima wadogo na hasa wanawake waishio vijijini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, mchango wa Serikali kwenye sekta ya kilimo ni pamoja na:-
(i) Kutoa ruzuku ya pembejeo za kilimo kwa wakulima ili kuongeza uzalishaji na tija.
(ii) Kutoa elimu ya kilimo bora kwa kutumia mashamba darasa 16,786 na mashamba darasa 44 ya vijana yaliyoanzishwa.
(iii) Kutumia Vituo vya Rasilimali vya Kata 587.
(iv) Kuanzishwa kwa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko ili kuimarisha soko la mazao ya kilimo.
(v) Kukarabati maghala ya kuhifadhia mazao katika Halmashauri ambapo hadi sasa maghala 33 yamekamilika na maghala haya yatanufaisha wakulima wadogo 13,800 kwa kuhifadhi mazao yao.
(b) Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuweka mikakati ya muda mfupi na muda mrefu ili wakulima wengi zaidi waingie kwenye kilimo cha umwagiliaji. Mikakati ya muda mfupi ni pamoja na:-
(i) Kukarabati na kuziboresha skimu za umwagiliaji 37 zenye ukubwa wa hekta 28,612.
(ii) Kuhamasisha matumizi ya teknolojia ya umwagiliaji kwa njia ya matone.
(iii) Kuanzisha na kuimarisha vyama vya wamwagiliaji 442 katika skimu za wakulima wadogo.
(c) Mheshimiwa Spika, Serikali imetekeleza mikakati mbalimbali kwenye zana za kilimo kwa wakulima wadogo na hasa wanawake waishio vijijini ili kuwarahisishia kazi shambani. Kwa mfano, hadi sasa kuna matrekta makubwa 10,283 na matrekta madogo ya mkono 7,350.
Wizara kupitia Mradi wa Sera na Maendeleo ya Rasilimali Watu (Policy and Human Resource Development) imesambaza mashine za kuvuna mpunga 64, kukata mpunga 16 na mashine za kukoboa mpunga 14 katika skimu 14 za umwagiliaji. Mashine hizo zilizosambazwa zitasaidia kuongeza tija na kurahisisha kazi mashambani hususani kwa wanawake.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA Aliuliza:-
Wakulima wa chai wa Wilaya ya Rungwe wanauza majani ya chai kati ya shilingi 230 hadi 240 kwa kilo, wakati wakulima wa Njombe wanauza majani ya chai kwa shilingi 500 kwa kilo huku kukiwa na Bodi moja na ni nchi moja.
Je, kwa nini wakulima wa chai Wilaya ya Rungwe wanalazimishwa kuuza majani mabichi ya chai kwa bei ndogo kuliko wakulima wa chai wa Wilaya za Njombe na Lushoto?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, bei dira ya majani mabichi ya chai hupangwa katika mkutano mkuu wa wadau wa chai ambao ni wa kisheria na hufanyika kila mwaka kabla ya msimu kuanza. Kwa mfano, mkutano wa wadau wa msimu 2016/2017 uliofanyika Njombe wadau walikubaliana bei dira
kuwa shilingi 230. Hata hivyo, kulingana na kifungu cha 49(2) katika kanuni za zao la chai za mwaka 2010, wakulima kupitia vyama vyao wamepewa uwezo wa kujadiliana bei na wenye viwanda ambayo itakuwa zaidi ya bei dira. Kutokana na makubaliano na wakulima Kampuni ya Chai ya Mufindi wanaomiliki viwanda vya Kibena, Luponde, Ikanga na Itona waliwalipa wakulima shilingi 250.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa bei dira hupangwa na kukubaliwa na wadau wote, tofauti ya bei kati ya eneo moja na lingine hutokana na majadiliano kati ya wakulima na wenye viwanda kama ilivyoainishwa kwenye kanuni za zao la chai. Majadiliano hayo ndiyo yaliyopelekea wakulima wa Wilaya za Mufindi na Njombe kulipwa shilingi 250 kwa kilo wakati wale wa Lushoto, Muheza, Korogwe na Kagera wanalipwa shilingi 230 ambayo ni bei elekezi. Kwa upande wa Wilaya ya Rungwe, bei ni kati ya shilingi 240 na 250 ambayo ni juu ya bei elekezi. Tofauti ya bei kwa maeneo hayo inatokana na malipo ya pili, kwa mfano katika mwaka 2015/2016 Kampuni ya Unilever inayomiliki viwanda vya Kibwele, Kilima na Lugoda, imelipa malipo ya pili kati ya shilingi 80 hadi 200 kwa kilo kutegemeana na ubora wa majani ya chai na hivyo kufanya malipo ya jumla kuwa kati ya shilingi 330hadi 400.
Mheshimiwa Spika, kiwanda cha Wakulima Tea Company cha Rungwe hulipa malipo ya kwanza shilingi 240 na ya pili shilingi 29 na kufanya jumla kuwa shilingi 259. Katika mwaka 2016/2017 Kiwanda cha Kibwele kinachomilikiwa na Unilever kinatoa malipo ya pili ya shilingi tatu na jumla kuwa shilingi 253 na Viwanda vya Kilima na Lugoda malipo yatakuwa kati ya shilingi 100 na 200 ingawa vinamilikiwa na kampuni hiyo hiyo. Kiwanda cha Dindira kilichopo Lushoto malipo ya kwanza yatakuwa shilingi 230 na ya pili shilingi saba na jumla kuwa shilingi 237.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA Aliuliza:-
Kampuni ya Chai ya Maruku imekuwa sugu kwa kutowalipa wakulima wanaoiuzia chai pamoja na kutowalipa wafanyakazi wake wenyewe.
Je, ni kwa nini Serikali haichukui hatua ya kuwasaidia wakulima na wafanyakazi hao ili kupata haki yao?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ucheleweshwaji wa malipo ya wakulima na wafanyakazi katika kiwanda cha Chai cha Maruku yalianza Septemba, 2011. Hali hiyo ilitokana na uwezo mdogo wa kifedha wa Kagera Tea Company Limited iliyowekwa na Spearshield Africa Company Limited inayomiliki Kiwanda cha Chai cha Maruku kwa asilimia 75 kusimamia uendeshaji wake ikiwemo ununuzi majani mabichi ya chai kutoka kwa wakulima wadogo. Wakulima hawa wanamiliki asilimia 25 walizopewa na Serikali kufuatia kiwanda hicho kubinafsishwa kwa Spearshield Africa Company Limited kutoka kwa Mamlaka ya Chai Tanzania waliokuwa wanamiliki kiwanda hicho. Mkataba wa mauziano ulisainiwa terehe 25 Septemba, 2001. Sababu nyingine ni tija ndogo ya majani ya chai ikilinganishwa na gharama za uzalishaji.
Mheshimiwa Spika, ili kunusuru wakulima na wafanyakazi wa kiwanda hicho, Serikali kupitia uongozi wa Mkoa wa Kagera, Bodi ya Chai ya Tanzania na Wakala wa Wakulima Wadogo wa Chai Tanzania, kwa nyakati tofauti wamekutana na mwekezaji huyo kumuelekeza atekeleze
wajibu wake wa kulipa wakulima na wafanyakazi. Kufuatia hiyo mikutano, mwekezaji ametafuta fedha na kulipa madeni mbalimbali ikiwemo malipo ya wakulima na wafanyakazi. Mpaka sasa ameshalipa wakulima wadogo malimbikizo yote ya nyuma hadi mwezi Oktoba, 2016 na ameahidi kulipa madeni ya Novemba na Disemba, 2016 ndani ya mwezi Januari, 2017.
MHE. CECIL D. MWAMBE (K.n.y. MHE. MWITA M. WAITARA) aliuliza:-
Baadhi ya wakazi wa Ukonga wanafuga kuku wa mayai na wengine wanatengeneza chakula cha mifugo, shughuli zinazowainulia kipato na kuweza kupata mahitaji muhimu ya kimaisha, lakini shughuli zao zimeathiriwa na watu wanaoingiza mayai toka nje ya nchi:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuzuia uingizaji wa mayai toka nje kwa sababu unaharibu soko la ndani la bidhaa hiyo?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kusimamia malighafi ili chakula cha mifugo kiendane na bei ya mayai na kuku?
(c) Je, Serikali ipo tayari kusimamia wananchi walipwe fidia kutoka kwa wawekezaji wanaoingiza vifaranga wasio na chanjo toka nje ambao wengi wao hufa na kusababisha hasara kwa wananchi wafugaji?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Mwikwabe Waitara, Mbunge wa Ukonga, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia mwaka 2006, Serikali iliweka katazo la kuingiza kuku na mazao yake nchini ili kudhibiti Ugonjwa hatari wa Mafua ya Ndege. Sheria ya Magonjwa ya Wanyama Na. 17 ya Mwaka 2003 na Kanuni zake za Mwaka 2007 na 2010 zinatumika kudhibiti na kukagua uingizwaji katika maeneo ya mpakani, bandari na viwanja vya ndege. Hakuna mwekezaji yeyote anayeruhusiwa kupewa kibali cha kuingiza vifaranga au mayai nchini kwa ajili ya biashara na katika kusimamia hili kuanzia mwaka 2013 hadi 2017, vifaranga 67,500 vilivyoingizwa nchini kinyume na sheria viliteketezwa.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inasimamia ubora wa malighafi za kusindika vyakula vya mifugo kupitia Sheria ya Maeneo ya Nyanda za Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Wanyama Na. 13 ya Mwaka 2010. Changamoto katika kusindika vyakula hivyo ni gharama kubwa ya viinilishe vya protini kutokana na matumizi ya maharage aina ya soya. Maharage haya huagizwa kutoka nje ya nchi hususan Zambia na India. Wizara inaendelea kuhamasisha uzalishaji wa soya hapa nchini katika Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, wapo wawekezaji wachache ambao hupewa vibali maalum vya kuingiza nchini mayai au vifaranga wa kuku wazazi (parent stock) tu. Ukaguzi kwa ajili ya kudhibiti uingizaji wa vifaranga na mayai unaendelea na hatua kali zinachukuliwa kwa yeyote atakayekamatwa kwa kukiuka utaratibu.
MHE. LUCIA M. MLOWE aliuliza:-
Kilimo cha viazi katika Mkoa wa Njombe kimekuwa ni ukombozi kwa wananchi wa mkoa huo. Zao hilo ni la biashara lakini wananchi wameanza kukata tamaa kutokana na kupanda kwa bei za pembejeo, pembejeo kutokufika kwa wakati na kukosa soko la uhakika:-
Je, Serikali ipo tayari kuwaunganisha wakulima hao na kuwa na chama chao kitakachoweza kupigania haki za wakulima hao?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lucia Michael Mlowe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikihimiza makampuni na mawakala wanaosambaza pembejeo za kilimo kuwafikishia pembejeo wakulima kwa wakati kabla ya msimu wa kilimo kuanza. Kutokana na juhudi ya Serikali kwa kushirikiana na makampuni yanayosambaza pembejeo, imewezesha ufikishwaji wa pembejeo ikiwemo mbolea na mbegu bora kwa bei ya soko kwa wakulima kwa wakati. Aidha, changamoto ya kupanda bei ya pembejeo inafanyiwa kazi kwa kuondoa tozo mbalimbali ili kupunguza bei ya pembejeo na kuwezesha wakulima kumudu kununua na kutumia pembejeo hizo. Vilevile Serikali inakamilisha mchakato wa manunuzi ya pamoja (bulk procurement), uondoaji au kupunguza tozo mbalimbali na gharama za usafirishwaji katika mbolea ambao utasaidia kuongeza upatikanaji na kupunguza bei ya mbolea.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inaendelea kuhimiza uzalishaji wa mbegu za viazi kupitia vikundi katika ngazi ya mkulima. Kupitia utaratibu huu wakulima wengi watamudu kununua mbegu za viazi kwa bei nafuu kwa vile zinazalishwa ndani ya kijiji. Pia kupitia SAGCOT wakulima nane wamepata mafunzo ya kuzalisha mbegu za viazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ambazo zitauzwa ndani ya mkoa na hivyo kuchangia upatikanaji wa mbegu za viazi kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ipo tayari kuwaunganisha wakulima wa zao la viazi kwa kutumia taasisi zake katika kuunda ushirika ambao utasaidia kuanzisha chama chao kulingana na taratibu za uanzishwaji wa vyama vya ushirika. Jukumu hili litatekelezwa kupitia tume ya ushirika kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Halmashauri husika katika Mkoa wa Njombe.
MHE. MARGARET S. SITTA Aliuliza:-
Pamoja na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika kutatua matatizo ya wakulima wa tumbaku katika Mkoa wa Tabora akiwemo wa Wilaya ya Urambo.
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuunda Bodi ya Tumbaku (TTB) nyingine ili ianze kazi haraka iwezekanavyo baada ya Bodi ya Tumbaku iliyovunjwa?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha pembejeo za msimu ujao zinamfikia mkulima wa tumbaku mapema wakati huu ambapo bodi husika imevunjwa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI Alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa
Margaret Simwanza Sitta, Mbunge wa Urambo, lenye Sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, A, ni kweli kuwa Serikali imevunja Bodi ya Tumbaku Tanzania kwa lengo la kufanya marekebisho katika utendaji kazi wa bodi. Hatua hii ya kuvunja Bodi ya Wakurugenzi haihusu kusitisha shughuli zinazotekelezwa katika tasnia hii ya tumbaku kwani wapo wataalam wanaoendeleza utekelezaji wa mpango uliopo na kuendeleza soko la tumbaku nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia umuhimu wa uwepo wa Bodi ya Tumbaku nchini kwa maendeleo ya tasnia hii ya tumbaku, utaratibu unaandaliwa wa kuunda Bodi mpya ya Wakurugenzi haraka iwezekanavyo na wananchi watataarifiwa kupitia tamko la Serikali mara baada ya taratibu kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pembejeo za muhimu kwenye zao la tumbaku ni pamoja na mbolea aina ya NPK, mbolea aina ya CAN, nyuzi za kufungia tumbaku wakati wa kuvuna na wakati wa masoko, vipande vya magunia na madawa. Pembejeo hizo huagizwa kupitia vyama vikuu vya ushirika kwa kila eneo kwa kupitia mchakato wa zabuni unaosimamiwa na kuratibiwa na vyama vikuu vya ushirika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia kuwa wakulima wanahitaji huduma muda wote hasa kipindi hiki cha kuelekea masoko ya tumbaku kwa msimu wa 2017/2018, Serikali kupitia Mrajisi wa Vyama vya Ushirika nchini ameshateuwa timu nyingine ambayo ipo Mkoani Tabora ikiendelea kuratibu na kusimamia masuala mbalimbali ya wakulima, ikiwa ni pamoja na kuandaa upatikanaji wa pembejeo kwa msimu ujao. Hivyo, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa, pamoja na Bodi ya WETCU kuvunjwa, lakini kazi za chama kikuu zinaendelea kama
kawaida.
MHE. JUMAA H. AWESO Aliuliza:-
Zao la nazi ni kitega uchumi na chanzo cha mapato kwa wananchi wa Halmashauri ya Pangani lakini zao hili linashambuliwa sana na ugonjwa wa mnyauko ambao umeliathiri zao hilo kwa kiwango kikubwa:-
Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kufanya tafiti kuhusu ugonjwa huo ili kupata dawa inayofaa ili kuwawezesha wakulima waweze kuendeleza kilimo hicho?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jumaa Hamidu Aweso, Mbunge wa Pangani, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ugonjwa wa kunyong’onyea wa minazi (Lethal Dieback Disease) umekuwa ukifanyiwa utafiti kwa zaidi ya miaka 25 na Kituo cha Utafiti Mikocheni. Katika kipindi hicho aina mbalimbali za minazi ya kigeni mifupi na asili mirefu ilichunguzwa ili kuweza kupata minazi yenye ukinzani dhidi ya ugonjwa huo. Aina zote zilionekana kushambuliwa na ugonjwa kwa viwango tofauti. Minazi mirefu kutoka Mkoa wa Tanga na Lindi na aina mbili za minazi mifupi ilionekana kustahimili zaidi kuliko aina zingine ikiwemo aina ya East African Tall (EAT).
Mheshimiwa Spika, aina hizo za minazi inayovumilia ugonjwa huo imepandwa katika shamba la mbegu huko Chambezi na Bagamoyo na mbegu zinauzwa kwa bei nafuu ya shilingi 2,000 kwa wakulima wanaohitaji. Pia Kituo cha Utafiti Mikocheni kinaendelea na uchunguzi wa kubaini wadudu wanaoeneza ugonjwa huu. Aidha, kituo kinaendeleza ushirikiano na taasisi nyingine za Kitaifa na Kimataifa zinazotafiti ugonjwa huu katika kutafuta suluhisho la kudumu la tatizo hili.
Mheshimiwa Spika, tiba ya ugonjwa huu haijapatikana hadi sasa, hivyo, wataalam wanaelekeza kuzuia ugonjwa huu kwa njia mbalimbali ikiwemo kupanda mbegu zitokanazo na minazi iliyoonekana kuwa na ustahimilivu wa ugonjwa; kukata na kuteketeza makuti ya minazi iliyoathirika mara dalili za ugonjwa zinapoonekana; kutopanda miche ya minazi iliyooteshwa katika sehemu zenye ugonjwa; kutoruhusu kusafirisha miche ya minazi kutoka sehemu zenye ugonjwa kwenda sehemu zisizo na ugonjwa; kuangalia matumizi mbadala ya minazi mipevu inayokufa kama kutengeneza samani na bidhaa nyingine zenye thamani; na wakulima kuchanganya mazao kwenye mashamba yao ya minazi ili kupata mazao mengine kutoka katika mashamba hayo endapo minazi yao itakufa kwa wingi kutokana na ugonjwa.
Mheshimiwa Spika, Serikali inashauri Halmashauri ya Wilaya ya Pangani na Wilaya nyingine zilizoathiriwa na ugonjwa huu kuwa na mipango ya kuendeleza zao hili kupitia mipango yao ya maendeleo kwa kuvisaidia vikundi vya wakulima katika Wilaya zao ziweze kupata mbegu zinazostahimili ugonjwa huu na pia kuanzisha vitalu vya miche bora ya minazi.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA Aliuliza:-
Tumbaku ni moja ya zao la biashara ambalo ni muhimu sana kwa Mkoa wa Tabora, lakini ukaushaji wake umekuwa mgumu sana kwa wakulima kutokana na kulazimika kutafuta kuni kwa ajili ya kukaushia tumbaku jambo ambalo linaathiri afya za wakulima hao pamoja na mazingira.
Je, ni lini Serikali itawasaidia wakulima wa tumbaku mkoani Tabora kupata nishati mbadala kwa ajili ya kukaushia tumbaku?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI Alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la…(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila mpangilio)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Subira Mwaifunga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tumbaku ni zao muhimu sana kwa Mkoa wa Tabora na Taifa kwa ujumla, kwani huwapatia wakulima kipato kikubwa na huchangia zaidi ya shilingi bilioni 14 kwa mwaka Mkoani Tabora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kufanya tafiti mbalimbali ili kupata nishati mbadala kwa ajili ya kukausha tumbaku badala ya kuni. Utafiti wa awali uliofanyika ni ule wa kutumia makaa ya mawe na umeme uliofanyika mkoani Iringa ambapo ilibainika kuwa na gharama kubwa kwa mkulima.
Aidha, kuanzia msimu wa kilimo wa 2015/2016, utafiti wa matumizi ya nyasi maalum umeanza kufanyika Mkoani Mbeya na Songwe katika wilaya zinazolima tumbaku. Utafiti huo umeanza kuonesha mafanikio na unatarajiwa kuwasaidia wakulima kwa kupunguza gharama na kutunza mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inasisitiza kuwa wakulima wa tumbaku nchini kutunza mazingira kwa kupanda miti ya kutosha na inayoendana na kilimo chao kwa mujibu wa sheria na kuacha kukata magogo na kutumia magogo kukaushia tumbaku badala yake watumie matawi ya miti. Pamoja na wito huo, Serikali kupitia Bodi ya Tumbaku imeagiza wakulima wote wa tumbaku kwa msimu 2017/2018 watumie majiko sanifu yanayotumia kuni kidogo na yenye ufanisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, majiko haya sanifu yanatumika katika nchi za Malawi na Zimbabwe na yanapunguza sana uharibifu wa mazingira na hayana athari kwa wakulima sababu moshi unapungua sana.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA Aliuliza:-
Serikali ina mpango mzuri wa kuanzisha mfumo mpya wa kutoa ruzuku za pembejeo kwa wakulima ambao utawanufaisha zaidi.
Je, ni lini mfumo huo mpya utaanza kutumika ili wakulima waweze kupata pembejeo kwa wakati wote?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI Alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christine Gabriel Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikitoa ruzuku ya pembejeo za kilimo kwa ajili ya mahindi, mpunga na pamba kwa kutumia mfumo wa vocha kuanzia mwaka 2008/2009 hadi mwaka 2015/2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa vocha umetoa mafanikio mazuri ambayo ni pamoja na kueneza elimu ya matumizi bora ya pembejeo za kilimo kwa wakulima, kusogeza huduma ya upatikanaji wa pembejeo vijijijini na kuongezeka kwa uzalishaji wa mahindi, mpunga na hivyo kuongeza usalama wa chakula katika ngazi ya kaya na Taifa kwa ujumla. Aidha, kumekuwa na changamoto mbalimbali za kiutendaji zilizojitokeza katika kutekeleza mfumo huu hususan katika ngazi ya wilaya na vijiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukabiliana na changamoto zilizojitokeza katika mfumo wa vocha, mwaka 2016/2017 Serikali imetoa ruzuku ya pembejeo kwa kutumia Kampuni yake ya TFC kusambaza mbolea hadi ngazi ya vijiji. Mpaka sasa TFC imesambaza tani 25,100 za mbolea ambazo ni sawa na asilimia 85 ya lengo la mbolea ya ruzuku. Pia makampuni ya mbegu yaliyoingia mkataba na Serikali wa kusambaza mbegu za ruzuku wamesambaza tani 429.4
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kuandaa utaratibu wa kupunguza au kuondoa tozo mbalimbali za pembejeo zinazochangia ongezeko kubwa la bei ya mbolea. Serikali inatarajia kuanza kutumia mfumo wa manunuzi wa pamoja (bulk procurement). Utaratibu huu utawezesha kupunguza bei ya mbolea na hivyo kuweza kuwafikia wakulima wote nchini kwa wakati na kwa bei iliyo nafuu ikilinganishwa na bei za sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo huu wa bulk procurement utaanza kutumika msimu ujao wa kilimo kwa kuanzia; na majaribio ya awali yataelekezwa kwenye mbolea za DAP na UREA.
MHE. NAPE M. NNAUYE (K.n.y. MHE. RASHID M. CHUACHUA) Aliuliza:-
Mfumo mzima wa ununuzi wa zao la korosho kuanzia kwenye ngazi ya Vyama vya Msingi umegubikwa na dhuluma na ukandamizaji mkubwa wa haki za mkulima kwa kila hatua. Hali hiyo imesababisha malalamiko yasiyokwisha ya wakulima wa korosho kila mwaka. Malalamiko ya wakulima ni uwepo wa makato yanayomuumiza mkulima, kutokuwepo kwa uwazi katika kumpata mshindi wa tender, kujitoa kiholela kwa makampuni yanayosababisha kushuka kwa bei ya korosho, kutolipwa kwa bei halali inayouzwa mnadani kwa Vyama vya Msingi, rushwa katika kila ngazi, pamoja na njama kati ya benki na kampuni zinazonunua korosho.
(a) Je, ni lini Serikali itaondoa na kushughulikia malalamiko ya wakulima wa korosho?
(b) Je, ni lini Serikali itadhibiti usambazaji wa pembejeo za ruzuku kwa watu ambao sio wakulima wa korosho?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUZI Alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Chuachua, Mbunge wa Masasi, lenye sehemu (a) na
(b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeshashughulikia malalamiko ya wakulima wa korosho kwa kuondoa makato yasiyokuwa muhimu kama vile kufutwa kwa ushuru wa shilingi 20 kwa kilo kwa ajili ya Chama Kikuu cha Ushirika; shilingi 50 za usafirishaji wa korosho; shilingi 10 kwa kilo kwa ajili ya mtunza ghala na shilingi 10 kwa kilo kwa ajili ya kikosi kazi cha masoko. Aidha, tasnia ya korosho ina utaratibu maalum wa kupanga bei dira kwa kutumia vigezo vinavyokubaliwa kwa wadau wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu manunuzi ya pembejeo za korosho hufanywa kwa pamoja na vyombo rasmi ndani ya tasnia, awali ilikuwa ikisimamiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Korosho na sasa Bodi ya Korosho Tanzania. Kuhusu changamoto za namna ya kufikisha pembejeo hizo kwa wakulima wa korosho, hatua zimechukuliwa kwa kushirikisha Vyama vya Ushirika ili kudhibiti mianya ya pembejeo kwenda kwa wasio walengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu usambazaji wa pembejeo za korosho ambazo ni sulphur ya unga na dawa za wadudu, Serikali imeweka mfumo wa usambazaji wa pembejeo wenye lengo la kuhakikisha kwamba pembejeo hizo zinawafikia walengwa pekee. Utaratibu huo unazingatia kutambua wakulima wenye uhitaji wa pembejeo na hununuliwa kwa kutumia utaratibu wa ununuzi wa pamoja (bulk purchase system) na kusambazwa kwa wakulima kwa kutumia wakala walioteuliwa na kuthibitishwa na Halmashauri husika ambazo huwa zimeandaa orodha ya wanufaika.
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA aliuliza:-
Moja kati ya changamoto zinazowakabili wakulima wa kahawa ni kodi na makato mengi:-
Je, ni lini Serikali itazipiga marufuku kodi zote zinazomnyonya mkulima?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sixtus Raphael Mapunda, Mbunge wa Mbinga Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua changamoto mbalimbali katika uzalishaji wa kahawa nchini ikiwemo kodi na tozo mbalimbali zinazotozwa kwa wakulima na wadau wengine katika tasnia ndogo ya kahawa ambazo zimekuwa na athari katika mapato ya wakulima. Serikali imedhamiria kupunguza na kuondoa kodi na tozo mbalimbali za mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi zisizokuwa na tija ili kupunguza mzigo wa makato kwa wakulima, wafugaji na uvuvi na hivyo kuongeza kipato na kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara katika sekta ya kilimo kwa kupitia upya taratibu, vibali, tozo, kodi, ushuru na ada mbalimbali zinazotozwa ili kupunguza gharama za kufanya biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutekeleza mkakati wa kupunguza kodi, tozo na ada mbalimbali kwa wakulima, Serikali katika mwaka 2016/2017, imefuta baadhi ya tozo katika mazao ya kilimo, ikiwemo ada ya leseni ya kusindika kahawa ya Dola za Kimarekani 250. Aidha, katika mwaka 2017/2018, Serikali imepanga kuondoa na kupunguza baadhi ya kodi, tozo na ada katika mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi, ikiwemo zao la kahawa ili kuongeza mapato ya wakulima na kuboresha mazingira ya ufanyaji wa biashara katika kilimo, mifugo na uvuvi. Mpango wa muda mrefu wa Serikali ni kuhakikisha kodi, tozo na ada mbalimbali ambazo ni kero kwa wakulima wa kahawa zinafutwa na kubakia na kodi, tozo na ada ambazo zina mahusiano na uendelezaji wa zao husika.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU (K.n.y. MHE. HUSSEIN N. AMAR) aliuliza:-
Ili viwanda viweze kufanya kazi kwa ufanisi vinahitaji malighafi ya kutosha.
(a) Je, Serikali iko tayari kutoa bei ya pamba mapema kabla ya msimu wa kilimo kuanza ili wakulima wawe na uhakika wa bei elekezi?
(b) Zao la pamba limekuwa na tatizo kubwa la mbegu zisizo bora na viuatilifu hafifu, je, Serikali imejipanga vipi kwa kuzingatia agizo la Mheshimiwa Rais la tarehe 31 Julai, 2016 alipokuwa akiongea na wananchi wa Geita kwamba hatavumilia kuona wananchi wakiletewa mbegu mbovu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hussein Nassor Amar, Mbunge wa Nyang’hwale, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, bei ya kuuzia pamba ya wakulima hutegemea moja kwa moja bei katika Soko la Dunia ambalo kwa bahati mbaya bei hupanda na kushuka kila wakati. Serikali haipangi bei ya pamba kwa mkulima bali huangalia hali ya bei katika Soko la Dunia katika kupanga bei elekezi ya mkulima. Bei elekezi inapangwa kwa ushirikiano kati ya Serikali, wanunuzi wa pamba na wawakilishi wa wakulima. Aidha, pamoja na mpango wa Serikali wa kujenga viwanda vya pamba kuongeza thamani, Serikali inahamasisha wakulima kufuata kanuni bora za kilimo cha pamba ili kuongeza tija, ubora na baadaye kuwaongezea kipato. Kwa hali hiyo, bei ya pamba hufahamika baada ya kuanza kwa msimu mpya katika Soko la Dunia na kwa hiyo, Serikali haina uwezo wa kupanga bei ya pamba bila kuangalia hali ya Soko la Dunia.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kukabiliana na tatizo la upatikanaji wa mbegu bora za pamba na viuatilifu kwa kutumia Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu Nchini (TOSCI) na kwa upande wa viuatilifu, Taasisi ya Utafiti na Udhibiti wa Ubora wa Dawa (TPRI) ili kuhakikisha kuwa wakulima wanapata mbegu na viuatilifu vyenye ubora mtawalia.
Aidha, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi inafanya rejea ya mfumo bora wa kuzalisha mbegu za pamba kwa maana ya kuuboresha zaidi, hatua hii itasaidia kuongeza upatikanaji wa mbegu bora za pamba kwa wingi na kwa bei nafuu. Aidha, Serikali ina mpango wa kuutumia Wakala wa Mbegu na Mazao kwa ajili ya kufungua mashamba makubwa ya kuzalisha mbegu ya pamba.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza:-
Uhitaji wa zao la pareto duniani ni mkubwa sana kiasi kwamba inahitajika kwa takribani tani 18,000 hadi 20,000 katika Soko la Dunia na Tanzania tuna uwezo wa kuzalisha hadi tani 8,000 tukiwa na mazingira rafiki.
(a) Je, ni kwa misingi gani pareto imepangiwa mnunuzi mmoja tu wa kigeni huku ikiwafungia milango wanunuzi wadogo wa Kitanzania?
(b) Je, Serikali inachukua hatua gani kusimamia bei
ya zao hilo ambayo imeporomoka kutoka shilingi 2,400 katika kipindi cha wanunuzi wengi hadi shilingi 1,500 chini ya mnunuzi mmoja?
(c) Je, Serikali ina mkakati gani wa muda mrefu na muda mfupi wa kuwawezesha wanunuzi wadogo wa Kitanzania kuingia kwenye ushindani na wanunuzi wageni?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, lenye sehemu (a),(b) na (c) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Sheria na Kanuni za Pareto zinamtaka kila mnunuzi kuongeza thamani ya pareto kwa kuzidua sumu ya pareto kupata sumu ghafi. Pia mnunuzi anatakiwa kuwa na maabara ya kupima kiwango cha sumu kwenye maua na kuwalipa wakulima kulingana na kiwango hicho cha sumu. Kwa sasa mnunuzi aliyetekeleza masharti hayo ni Kampuni ya Pareto Tanzania. Serikali inasisitiza mnunuzi yeyote kutimiza vigezo vilivyopo katika sheria na kanuni ili kulinda ubora na soko.
Mheshimiwa Spika, bei ya zao la pareto hupangwa katika Mkutano Mkuu wa Wadau ambao ni wa Kisheria na hufanyika kabla ya mwezi Julai kila mwaka kabla ya kuanza msimu mpya. Mkutano huo, huhudhuriwa na wanunuzi na wawakilishi wa wakulima na viongozi wa Halmashauri zinazolima pareto nchini.
Mheshimiwa Spika, Serikali inasisitiza wakulima kuzingatia kanuni za kilimo bora. Kwa mfano, pamoja na bei ya juu kuwa shilingi 2,200 msimu wa 2012/2013 na shilingi 2,700 msimu wa 2014/2015 ubora wa pareto ulikuwa chini ya asilimia moja. Baada ya baadhi ya wakulima kutekeleza kanuni za kilimo bora cha pareto katika msimu wa 2015/2016, ubora ulifikia asilimia 1.8 na bei ya juu kuwa shilingi 2,700.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, mkakati wa muda mrefu ni kuendelea kuhamasisha wazawa kujiunga pamoja na kukopa ili wawekeze katika viwanda vya kuongeza thamani ya zao la pareto kufikia kiwango cha crude extract na hatimaye kuingia kwenye ushidani na wanunuzi wa kigeni.
MHE. PASCAL Y. HAONGA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaanzisha Chuo cha Kilimo Wilaya
ya Mbozi ili kutoa fursa kwa wanafunzi wengi wanaohitimu kidato cha nne na cha sita Mkoa wa Songwe na maeneo mengine nchini ili waweze kupata mafunzo kwenye chuo hicho?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Pascal Yohana Haonga, Mbunge wa Mbozi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwepo kwa Chuo cha Kilimo katika Wilaya, Mkoa na Taifa ni muhimu kwa kuwa kinasaidia kujenga nguvukazi wataalam na wakulima kifikra na kimtizamo katika kuongeza uzalishaji na tija katika nyanja ya kilimo kwenye eneo husika. Hivyo chuo cha kilimo kikianzishwa katika Wilaya ya Mbozi kinaweza kuchochea maendeleo ya uzalishaji na usindikaji wa mazao yanayozalishwa Wilayani hapo ikiwemo kahawa, mahindi, maharage na matunda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo kuanzisha chuo
cha kilimo kuna gharama kubwa kwa ajili ya kujenga miundombinu, kununua vifaa vya kufundishia na kujifunzia na kuajiri rasilimaliwatu kwa ajili ya kazi za mafunzo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wakati huu vipo vyuo vitatu vya Serikali Mkoani Mbeya vinavyotoa mafunzo ngazi ya Stashahada na Astashahada. Vyuo hivi ni Uyole, Igurusi na Inyala vyenye uwezo wa kuwa na wanafunzi takribani 700 kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kupitia Programu ya Kuendeleza Kilimo (ASDP II) Wizara itaboresha Vyuo vya Kilimo vya Uyole, Igurusi, Inyala pamoja na vyuo vingine kwa kujenga miundombinu, kuongeza upatikanaji wa vifaa, kuongeza rasilimali watu na kadhalika ili viweze kudahili wanafunzi wengi zaidi wakiwepo wanaotoka Wilaya ya Mbozi.
MHE. DKT. MARY M. NAGU aliuliza:-
Watumishi wa yaliyokuwa mashamba ya NAFCO walishinda kesi yao ya madai dhidi ya Serikali na Mahakama kuiamuru Serikali kuwalipa mafao na madai yote lakini Serikali imeendelea kukaa kimya kwa muda mrefu na hivyo kuwanyima haki yao jambo ambalo linasababisha adha kubwa kwa familia zao.
Je, ni lini Serikali itawalipa haki yao waliokuwa watumishi wa mashamba ya NAFCO ikiwemo shamba la Murjanda?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Mary Michael Nagu, Mbunge wa Hanang, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mashamba ya kilimo yaliyokuwa chini ya Shirika la Taifa la Kilimo na Chakula (NAFCO) yaliajiri watumishi 314 kwa nyakati tofauti na kazi tofauti ambapo NAFCO kupitia makampuni hayo iliingia mikataba ya hali bora na watumishi hao kwa lengo la kuboresha maisha yao. Utekelezaji wa mikataba hiyo ulitegemea ufanisi na utendaji wa taasisi husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnamo tarehe 16 Juni, 1996 NAFCO iliwekwa chini ya uangalizi wa PSRC kwa ajili kubinafsishwa kulingana na Sheria ya Mashirika ya Umma ya mwaka 1992. Aidha, baada ya zoezi la ubinafsishaji wa mashamba ya NAFCO, watumishi hao waliachishwa kazi kati ya mwaka 2003 na 2004 ambapo walilipwa malimbikizo ya mishahara yao na mafao mengine, bila kulipwa mafao yanayotokana na mikataba ya hali bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa baada ya kutolipwa madai yatokanayo mikataba ya hali bora, watumishi hao chini ya Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Mashambani Makao Makuu, walifungua kesi ya mdai Mahakama Kuu tarehe 5 Juni, 2004 dhidi ya PSRC na kushinda kesi hiyo ambayo ilichukua miaka minne mpaka mwaka 2008.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watumishi hao walistahili kulipwa mafao ya mikataba ya hali bora kama ifutavyo:-
Mishahara miwili baada ya notisi, magunia matatu ya ngano kwa kila mwaka waliofanyia kazi au fedha badala yake kwa bei ya wakati huo ilipofungwa mikataba, mwisho walipwe misharaha ya miezi minne kila mmoja kwa kila mwaka waliofanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ukweli kwamba madai haya yamepitia vyombo mbalimbali vya usimamizi wa Serikali, hata hivyo, kumekuwepo na madai yasiyo sahihi baada ya uhakiki wa kurudia.
Hivyo, napenda nichukue nafasi hii kuwataka wawasilishe madai hayo ofisi ya Msajili wa Hazina ambayo itashirikiana na Wizara ili tuweze kuyachambua na kujiridhisha ipasavyo iwapo wanastahili kulipwa na hivyo kuiomba Wizara ya Fedha na Mipango kuchukua hatua stahiki.
MHE. FAKHARIA SHOMARI KHAMIS aliuliza
(a) Je, Serikali imejipanga vipi kuzuia uvuvi haramu nchini?
(b) Je, ni meli ngapi zilizokamatwa kwa sababu za uvuvi haramu kuanzia mwaka 2010 – 2015?
(c) Je, ni watu wangapi wametiwa hatiani na hukumu zao zikoje?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomari Khamisi, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na wavuvi haramu, Wizara imeanzisha na kuimarisha vituo 25 vya doria kwenye maziwa makubwa, mwambao wa Bahari ya Hindi na mipaka ya nchi. Vituo hivyo vipo katika maeneo ya Tanga, Dar es Salaam, Kigoma, Musoma, Kagera, Mwanza, Mtwara, Mafia, Kilwa, Horohoro, Kipili, Kasanga, Sota, Sirari, Kasumulo, Mbamba Bay, Tunduma, Kabanga, Kanyigo, Rusumo, Ikola, Geita, Buhingu, Namanga na Murusagamba. Kuwepo kwa vituo hivyo kumeongeza uwezo wa kukabiliana na uvuvi na biashara haramu kupitia operesheni mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada hizi za Serikali, tatizo la uvuvi haramu na biashara ya magendo kwenye mialo, masoko na mipaka ya nchi bado ni kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pia, imeanzisha Kikosi
Kazi cha Kitaifa Mult Agency Task Team ambacho kinafanya kazi ya kudhibiti uhalifu wa mazingira ikiwemo kudhibiti uvuvi haramu hususan matumizi ya mabomu katika shughuli za uvuvi. Wajumbe wa Kikosi kazi hiki ni kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora; Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi; Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi; Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa; Wizara ya Katiba na Sheria; Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Wizara ya Nishati na Madini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wengine ni Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka; Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Baraza la Taifa la Mazingira. Wajumbe kutoka Taasisi nyingine wataongezeka kadri itakavyoonekana inafaa. Kikosi kazi hiki kipo chini ya uratibu wa Wizara ya Mambo ya Ndani. Aidha, Wizara imeendelea kufanya maboresho ya Sera, Sheria na Kanuni za uvuvi ili kuimarisha usimamizi na matumizi endelevu ya rasilimali za uvuvi hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kuwa kwenye maji ya ndani na ya Kitaifa (Inner and territorial waters) uvuvi unaofanyika ni wa kutumia mitumbwi, boti, mashua, jahazi na ngalawa na siyo meli. Kuanzia mwaka 2010 – 2015 jumla ya vyombo 2,795, injini za mitumbwi 118, magari 297 na pikipiki 33 vilikamatwa kwa sababu za uvuvi haramu na utoroshwaji haramu kwenye maji hayo. Aidha, katika Bahari Kuu kuanzia mwaka 2010 hadi 2015 haijawahi kukamatwa meli ya uvuvi. Meli ya Uvuvi Tawariq1 ilikamatwa mwaka 2009.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi tajwa jumla
ya watuhumiwa 3,792 walikamatwa na kesi 243 zilifunguliwa mahakamani. Aidha, jumla ya shilingi 158,559,323 zilikusanywa ikiwa ni faini kutokana na makosa mbalimbali na watuhumiwa 11 wamefungwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Bunge lako Tukufu, nawaomba Waheshimiwa Wabunge ambao ni wajumbe katika Halmashauri waendelee kutoa elimu kwa wavuvi kuhusu madhara ya uvuvi haramu na kuhimiza Halmashauri zao zidhibiti uvuvi haramu kwenye maeneo yao. Pia, jamii za wavuvi na wadau wote washirikishwe katika kusimamia rasilimali za uvuvi na matumizi endelevu kwa ajili ya kuwapatia wananchi ajira, chakula na uchumi wao na Taifa kwa ujumla. Ni njia hii Taifa linaweza kudhibiti uvuvi haramu hapa chini.
MHE. MARTIN M. MSUHA aliuliza:-
Katika msimu wa kilimo wa mwaka 2015/2016 Mawakala wa Usambazaji Pembejeo kwa Vocha katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga wanaidai Serikali jumla ya Sh.824, 000,000/=
Je, Serikali ina mpango gani wa kulipa deni hilo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martin Mtonda Msuha, Mbunge wa Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika msimu wa kilimo wa mwaka 2015/2016, Serikali ilitoa ruzuku ya pembejeo kwa utaratibu wa vocha kwa mikoa 25 ya Tanzania Bara. Kazi ya kusambaza pembejeo hizo kwa kaya za wakulima wanufaika wapatao 999,926 ilifanywa na makampuni na Mawakala wa Pembejeo katika Halmashauri zipatazo 144 zilizonufaika na utaratibu huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kujiridhisha na uhalali wa madai ya makampuni ya Mawakala waliotoa huduma ya pembejeo katika Wilaya hizo, Wizara imefanya uhakiki wa awali ambao umefanyika katika baadhi ya mikoa yenye kiasi kikubwa cha madai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya uhakiki wa awali imefanyika katika mikoa nane kati ya mikoa 25 ya Tanzania Bara iliyopata ruzuku. Matokeo hayo yameonesha upungufu mkubwa katika madai hayo. Hivyo, Mheshimiwa Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango kufanya uhakiki katika mikoa yote kwa makampuni na Mawakala wote waliosambaza pembejeo katika msimu wa 2015/2016 katika kipindi cha mwezi mmoja. Baada ya uhakiki huo madeni yote halali yatalipwa.
MHE. HAWA A. GHASIA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwawezesha wavuvi wa Mtwara Vijijini ili waweze kufanya uvuvi wa kisasa zaidi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kutoa kipaumbele kwa sekta ya uvuvi nchini kwa kutekeleza mikakati yenye lengo la kuendeleza wavuvi wakiwemo wavuvi wa Wilaya ya Mtwara Vijijini ili waweze kufanya uvuvi wa kisasa zaidi. Miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na kuwapatia zana bora za uvuvi, elimu kuhusu masuala ya uvuvi na ujasiriamali, pamoja na kuboresha miundombinu ya uvuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika kuwapatia mitaji wakulima, wavuvi na wafugaji, itawawezesha kupata mikopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo, Benki ya Rasilimali Tanzania na benki za kibiashara kama NMB na CRDB kupitia vyama vya ushirika ili kuboresha shughuli zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kupitia Mfuko wa Pembejeo za Kilimo, Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kuwawezesha wavuvi kununua zana bora za kisasa kama boti, mashine na nyavu ambapo wavuvi wa Mtwara Vijijini pia watanufaika.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, katika mwaka 2017/2018 Serikali itaanza kutekeleza Programu ya Kuendeleza Kilimo Awamu ya Pili (ASDPII) ambapo miradi ya kuwawezesha wavuvi kwa kuwapatia zana bora imeainishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Elimu ya Uvuvi (FETA) inaendelea kutoa elimu ya uvuvi wa kisasa kwa wavuvi na imefungua kituo cha mafunzo Mikindani Mtwara. Pia, Serikali itatoa mafunzo ya uvuvi wa Bahari Kuu kwa wavuvi 50 kutoka Halmashauri za Pwani ya Bahari ya Hindi ikiwemo Mtwara Vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kutoa elimu kwa wavuvi kuhusu matumizi ya zana bora za uvuvi, ufugaji wa samaki, ukulima wa mwani na uongezaji wa thamani ya mazao ya uvuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia mpango kabambe wa uvuvi (fisheries master plan) inaendelea kuboresha miundombinu ya uvuvi ikiwemo mialo na masoko. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara Vijijini, imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa soko la samaki la kisasa katika Kata ya Msanga Mkuu.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM aliuliza:-
Wakulima wamezitumia vyema mvua kwa kulima mazao ya chakula na biashara lakini wanaendelea kupata hasara kubwa kwa kukosa masoko ya uhakika:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa ziada wa kuwapatia wakulima masoko ya uhakika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Masoud Abdallah Salim, Mbunge wa Jimbo la Mtambile kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi inatambua changamoto ya upungufu wa masoko ya uhakika kwenye mazao ya chakula yanayozalishwa kwa ziada hapa nchini pamoja na hasara ambayo wanaweza kupata kwa kukosekana masoko hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mikakati ya Wizara katika kupambana na hali hii ni kuanzisha Mfumo wa Stakabadhi ya Mazao Ghalani ambao unawasaidia wakulima kutunza mazao yao sehemu salama huku wakisubiria bei itakayowapa faida. Vilevile kupitia mfumo huo, wakulima wanahamasishwa kujiunga na SACCOS zilizoko ndani ya AMCOS zinazowasaidia kupata mikopo yenye riba nafuu ili kukidhi mahitaji yao kwa wakati wanaposubiri kuuza mazao yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo huu pia unatia hamasa kwa wakulima kuwa na soko na sauti ya pamoja ambayo inapelekea kuuza mazao yao kwa bei nzuri na siyo kiholela kama ilivyozoeleka kwa wakulima wengi. Pia inawasaidia wafanyabiashara kutumia muda mfupi kununua bidhaa kutoka sehemu moja badala ya kununua kwa kuzunguka kutoka kwa mkulima mmoja mmoja. Hii yote inasaidia kuimarisha masoko ya mazao ya uhakika. Aidha, Wizara itaendelea kuwaelimisha na kuhamasisha wakulima kuuza mazao yaliyokwisha ongezwa thamani ambapo itasaidia kuongeza ubora na bei nzuri za bidhaa hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kutafuta masoko nje ya nchi na kutoa vibali vya kusafirisha mazao na bidhaa za mazao ya chakula kwa wafanyabiashara na kuwahamasisha wafanyabiashara wa ndani kununua sehemu zenye ziada na kuuza sehemu zenye upungufu. Lakini pia Serikali inasisitiza juu ya kufufua viwanda ambavyo vitaongeza soko la uhakika la bidhaa zinazozalishwa na wakulima ili kuendana na mikakati ya Serikali ya Awamu ya Tano.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali na wadau mbalimbali wa kilimo wanaendelea kuhamasisha wakulima kutafuta masoko ya uhakika kama vile kilimo cha mkataba na kuboresha miundombinu ya masoko na barabara ili kuwaunganisha wakulima na masoko. Hii itasaidia kurahisisha usafirishaji wa mazao kutoka mashambani kwenda sokoni, hivyo kupunguza gharama za usafirishaji, muda wa kusafirisha, kiwango cha uharibifu na upotevu wa mazao baada ya mavuno.
MHE. MARTHA J. UMBULLA aliuliza:-
Kwa muda mrefu mawakala wanaosambaza pembejeo wamekuwa wakihujumu wakulima kwa kutowafikishia kabisa au kuwaletea pembejeo ambazo siyo sahihi na kinyume na maelekezo ya Wizara husika:-
(a) Je, Serikali ilishughulikiaje malalamiko ya wakulima wa Wilaya ya Simanjiro?
(b) Je, Serikali imechukua hatua gani kwa mawakala wasio waaminifu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martha Jachi Umbulla, Mbunge wa Viti Maalum, lenye vipengele (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika msimu wa kilimo wa mwaka 2013/2014 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara ilipokea malalamiko kutoka kwa wakulima wa kijiji cha Narakauo kuhusu hujuma ya matumizi mabaya ya vocha za pembejeo za kilimo. Halmashauri ya Wilaya iliunda Kamati ya ufuatiliaji na uchunguzi ili kushughulikia malalamiko hayo. Baada ya uchunguzi ilibaini kuwa kijiji cha Narakauo hakikupelekewa mbolea za kupandia na kukuzia na kasoro zingine za utendaji zilizofanywa na Mwenyekiti wa Kamati ya Vocha na Afisa Mtendaji wa Kijiji. Hatua zilizochukuliwa baada ya kuwasilishwa kwa taarifa ya Kamati Teule ni pamoja na watendaji wa zoezi hilo kufikishwa katika vyombo vya sheria, katika maana ya Polisi na TAKUKURU kwa uchunguzi zaidi, hadi sasa vyombo hivyo vya dola havijatoa taarifa ya matokeo ya uchunguzi huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali ya Wilaya iliamua kuwa mawakala walioonekana kushiriki katika ubadhilifu huo hawataruhusiwa kutoa huduma ya kusambaza pembejeo za ruzuku katika Wilaya hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro imezuia malipo ya mawakala hao pamoja na kuwaondoa katika orodha za mawakala wanaosambaza pembejeo Wilayani humo.
MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS (K.n.y MHE. MBAROUK SALIM
ALI) aliuliza:-
Moja ya jitihada za Serikali za kufufua Kiwanda cha General Tyre kilichopo Arusha ni pamoja na kuendeleza kilimo cha mpira katika mashamba yaliyoko Tanga na Morogoro ili kupata malighafi.
Je, mashamba hayo yana ukubwa gani na umri gani?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbarouk Salim, Mbunge wa Wete, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanda cha Matairi Arusha (General Tyre) bado hakijaweza kuanza kufanya kazi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo uchakavu wa mitambo na teknolojia inayotumika kupitwa na wakati. Serikali imelenga kukifufua kiwanda hicho ambapo imefanya utafiti ili kubaini namna bora ya kukifufua. Taarifa ya awali imeeleza kuwa, mitambo iliyopo ibadilishwe na kuweka mipya inayotumia teknolojia ya kisasa. Vilevile kiwanda kipanuliwe ili kiweze kuzalisha matairi ya aina mbalimbali kwa wingi ili kuzalisha kwa faida na uendeshaji wake uwe chini ya sekta binafsi na Serikali iwe mbia kwa kwa hisa zinazolingana na rasilimali za kiwanda zilizopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, kiwanda hicho na mashamba ya mpira hayana uhusiano wa karibu kwani hakitumii mpira unaozalishwa kwenye mashamba yetu. Hii ni kwa kuwa kinatumia malighafi iliyo katika mfumo wa majora wakati teknolojia ya kugema mpira inayotumika kwenye mashamba yetu inatoa malighafi iliyo katika mfumo wa vipande. Mpira unaozalishwa nchini unatumika katika viwanda vingine kama vile Ok Plastic, Bora Shoes na viwanda vingine vidogo vidogo lakini vilevile unauzwa nje ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, zao la mpira ni moja kati ya mazao ya biashara ambayo yamekuwa yakizalishwa nchini kwa muda mrefu katika mashamba yaliyopo Kalunga - Mang’ula katika Wilaya ya Kilombero Mkoa wa Morogoro na shamba la Kihuhwi lililopo Wilaya ya Muheza Mkoa wa Tanga ambayo yalianzishwa mwaka 1978. Shamba la Kihuhwi lina ukubwa wa hekta 790 na shamba la Kilunga Mang’ula lina ukubwa wa hekta 750. Mashamba ya mpira kwa upande wa Zanzibar yapo Machai na Mselem Unguja yenye hekta 637 na mashamba madogo saba yaliyopo Unguja na Pemba yenye ukubwa wa hekta 633.
Mheshimiwa Naibu Spika, mashamba haya, yaani ya Kilunga na Mang’ula yanazalisha utomvu kati ya tani 0.6 hadi 1.0 kwa hekta kwa mwaka kutokana na miti yake kuwa na umri mkubwa. Kitaalamu uzalishaji wa utomvu huwa kati ya tani 0.8 hadi 1.3 za utomvu kwa hekta kwa mwaka na kupungua kadri ya miti ya mipira inavyozidi miaka 35 tangu kupandwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mashamba ya Tanzania Bara uzalishaji umepungua kutoka kilo 183,420 mwaka 2009 hadi kilo 165,335 mwaka 2014. Kwa upande wa Zanzibar uzalishaji umeshuka kutoka kilo 4,229,226 mwaka 2008 hadi 2,249,021 mwaka 2011.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na kuwa mashamba haya yamezeeka na hayapati matunzo ya kutosha ndiyo maana uzalishaji umeendelea kushuka. Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Taifa yaani NDC imeanza kuendeleza shamba la Mang’ula ambapo kiasi cha miche 212,500 imepandikizwa ili kuongeza uzalishaji wa utomvu. Aidha, Serikali inahamasisha wakulima na wawekezaji kuzalisha zao hili kwa kuwa soko lipo kwa viwanda vingine vya ndani na nje ya nchi.
MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza:-
Ushirika hususani wa mazao hauna maendeleo mazuri na umekuwa ukisuasua kwa sababu mbalimbali.
(a) Je, ni vigezo gani vinatumika kupima na kutathmini maendeleo ya ushirika?
(b) Je, ni hatua zipi zinachukuliwa na Serikali kuboresha mazingira ya ushirika kukua?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shally Josepha Raymond, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, ili kupima na kutathmini maendeleo ya ushirika nchini, Serikali inatumia vigezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ongezeko la idadi ya Vyama vya Ushirika vinavyoandikishwa na idadi ya wanachama kwenye vyama hivyo; idadi ya wananchi wanaopata huduma za kijamii na kiuchumi kupitia Vyama vya Ushirika nchini; uzalishaji na mauzo kupitia Vyama vya Ushirika; mitaji ya Vyama vya Ushirika na Vyama vya Ushirika vinavyouza mazao yaliyoongezwa thamani.
Pia uwekezaji wa Vyama vya Ushirika katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii mfano, huduma za kifedha, shule na majengo ya vitega uchumi; ajira kupitia Vyama vya Ushirika pamoja na thamani na idadi ya mikopo inayotolewa kwa wananchama wake katika kutatua matatizo ya kiuchumi na kijamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, vigezo vingine ni pamoja na kupima ufanisi wa uendeshaji wa shughuli za Vyama vya Ushirika kwa kuzingatia Sheria na Kanuni za Vyama vya Ushirika ikiwemo kupitia Ukaguzi wa mara kwa mara wa nje (external audit) kila mwaka.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali zenye lengo la kuboresha mazingira ya ukuaji wa sekta ya ushirika nchini. Hatua hizo ni pamoja na kuimarisha Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini kwa lengo la kuijengea uwezo wa kiutendaji ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya Maafisa Ushirika katika ngazi ya Taifa, Mkoa na Wilaya na kuendeleza kuwachukulia hatua za kisheria na kinidhamu watendaji wa Serikali, Wajumbe wa Bodi na Watendaji wa Vyama vya Ushirika kwa kushindwa kusimamia sheria katika kutekelza majukumu yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua nyingine zinazochukuliwa ni pamoja na kutoa elimu na kuendelea kuboresha mifumo ya masoko hususan wa Stakabadhi Ghalani; kuendelea kuviwezesha Vyama vya Ushirika kuzitambua kwa kuzihakiki mali zao na kuweka mikakati ya kuziendeleza mali hizo kwa manufaa ya wanachama; kuimarisha usimamizi na ukaguzi katika Vyama vya Ushirika kuzitambua kwa kuzihakiki mali zao na kuweka miakkati ya kuziendeleza mali hizo kwa manufaa ya wanachama; kuimarisha usimamizi na ukaguzi katika Vyama vya Ushirika.
Pia kuwajengea uwezo wanachama; kusimamia upatikanaji wa viongozi waadilifu na wawajibikaji wanaozingatia madili na misingi ya ushirika na pia kushirikisha Wizara za Kisekta na wadau mbalimbali katika kuhamasisha na kuendele za ushirika.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO aliuliza:-
Kumekuwa na tatizo la uagizaji wa dawa za kilimo na mifugo ndani ya nchi zisizokidhi vigezo na bei ya dawa hizo zinaongezeka siku hadi siku na kufanya wakulima na wafugaji wadogo kukosa maendeleo.
(a)Je, Serikali inachukua hatua gani za kuhakiki dawa hizo kabla hazijaingia nchini?
(b) Je, Serikali ina utaratibu gani wa kudhibiti bei hizo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sikudhani Yassin Chikambo, lenye sehemu a na b kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, udhibiti wa ubora na usalama wa dawa na viwatilivu vinavyoingia nchini na ambavyo vipo katika soko unafanywa na Mamlaka mbalimbali za Serikali kama vile Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kwa upande wa dawa za mifugo na Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu vya Kitropiki (TFRI) kwa upande wa viuatilifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza jukumu hili Mamlaka hizo zina mifumo ya udhibiti katika maeneo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, usajili wa dawa zinazoingia nchini; dawa zote na viuatilifu vinavyoingia nchini zinatakiwa kwanza ziwe zimesajiliwa na mamlaka hizo ili kujihakikishia ubora, usalama na ufanisi kabla hazijaingia katika soko la Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukaguzi wa viwanda vinavyotengeneza dawa; ukaguzi huu hufanywa na mamlaka hizo kwa ajili ya kuhakikisha kuwa vinazingatia viwango vya uzalishaji bora wa dawa (good manufacturing practice).
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukaguzi wa kufuatilia dawa katika soko (post marketing surveillance) hufanyika ili kuhakikisha kuwa dawa zilizopo katika soko zinaendelea kuwa na ubora ule ule kama wakati ziliposajiliwa. Sampuli mbalimbali za dawa huwa zinachuliwa katika soko na kupelekwa maabara kwa ajili ya kuzipima kwa minajili ya kudhibiti na kuthibitisha ubora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuwa bei za dawa na viuatilifu zinapangwa na nguvu ya soko lakini Serikali imeondoa ushuru wa forodha na VAT ili kumpunguzia mkulima mzigo wa bei. Aidha, Serikali inaendelea kuzipitia tozo na ada mbalimbali katika sekta ya kilimo na ikionekana inafaa ziondolewe ili kuongeza unafuu kwa mkulima.
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH aliuliza:-
Mazao ya mdalasini na mchaichai yanategemewa sana kama viungo na pia hutumika kutibu afya zetu ndani na nje ya nchi na mazao haya yanastahamili sana ukame na hayategemei mbolea lakini wakulima wengi hawana uelewa wowote kuhusiana na mazao haya; kwa upande wa mchaichai bei shambani ni Sh.250,000/= kwa tani moja na bei ya kiwandani ni Sh.400,000/= kwa kila tani moja:-
Je, Serikali ipo tayari kutoa elimu kwa wakulima ili kuweza kufahamu faida ya mazao hayo ili kuongeza uzalishaji na kukuza uchumi nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naaomba kujibu swali la Mheshimiwa Maida Hamad Abdallah, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mazao ya mdalasini na mchaichai ni miongoni mwa mazao ya bustani yanayozalishwa kwa wingi na wakulima wadogo hususan katika Mikoa ya Tanga, Morogoro na Kigoma. Kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya mazao hayo na faida ya kitabibu na kiburudisho, kumechochea ongezeko la bei na hivyo kupelekea hamasa kwa wakulima kuzalisha zaidi. Hivyo, uzalishaji wa mazao haya umeongezeka kutoka tani 10 za mchaichai mwaka 2010 hadi tani 15 mwaka 2014 na tani 600 za mdalasini hadi 15,000 kwa kipindi hicho hicho.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na ongezeko hilo la mavuno, uzalishaji wa mazao haya hapa nchini unakabiliwa na changamoto mbalimbali hususan mwamko hafifu wa wakulima katika baadhi ya maeneo hivyo kufanya uzalishaji wake kuwa siyo wa kibishara kutokana na kutokuzingatia kanuni bora za kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuongeza hamasa na elimu ya uzalishaji wa mazao ya viungo ikiwemo mchaichai na mdalasini Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na wadau wengine iliandaa mkakati wa kuendeleza mazao ya bustani wa miaka 10 (2011-2021). Pia, Serikali imeandaa mwongozo wa uzalishaji wa mazao yakiwemo ya viungo kulingana na kanda za kiikolojia.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile, kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya, taasisi zisizo za kiserikali na sekta binafsi, Serikali imeendelea kutoa hamasa kuhusu mazao ya bustani ikiwemo mchaichai na mdalasini katika ngazi za Kata, Vijiji kupitia huduma za ugani na maonesho ya nane nane. Hivyo basi, Serikali itaendelea kutoa hamasa na elimu kuhusu kanuni bora za kilimo kwa wakulima ili kuongeza kiwango cha uzalishaji na kuweza kupata mazao bora kulingana na uhitaji wa soko.
MHE. CATHERINE N. RUGE aliuliza:-
Kuna taarifa ya uwekezaji katika Bonde la Mto Mara na Kilimo cha Umwagiliaji cha Miwa na kwamba wawekezaji hao ni Waisrael:-
Je, ni kwa namna gani wananchi watanufaika na ulimaji wa miwa katika bonde hilo ambalo wananchi wamekuwa wakilitumia katika kilimo cha mazao ya chakula, biashara na pia kwa malisho ya ng’ombe?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Catherine Nyakao Ruge, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika jitihada za kuhakikisha Taifa linajitosheleza kwa sukari, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime iliingia makubaliano na Kampuni ya Uwekezaji ya Nile Agro Industries ya Uganda, kuanzisha mradi mkubwa wa kilimo cha miwa na ujenzi wa kiwanda cha sukari. Utekelezaji wa mradi huu unategemewa kuwa na manufaa makubwa kiuchumi kwa wananchi katika Wilaya ya Tarime na Taifa kwa ujumla kutokana na mapato yanayotokana na shughuli za mashambani sambamba na ajira za kiwandani.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu unatarajiwa kuhusisha Wakandarasi wadogo wa hapa nchini na hivyo kuongeza fursa za ajira mpya zipatazo 5,000 kwa wakazi wa Wilaya hiyo, ambapo zaidi ya wakulima 2,000 watanufaika moja kwa moja kwa kujihusisha na kilimo cha miwa. Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime itanufaika kupitia tozo (service levy) zitakazotokana na uzalishaji wa sukari katika mradi huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia kuwa wananchi wamekuwa wakilitumia bonde hilo kwa shughuli zao za maendeleo, Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Tarime inachukua hatua stahiki ili kuepusha migogoro inayoweza kujitokeza. Hadi sasa tayari Serikali imekamilisha mipango ya matumizi bora ya ardhi katika Vijiji Vinne vinavyotegemea bonde hilo, hatua ambavyo imefanikisha kutenga eneo la kiasi cha hekta 6,000 kwa ajili ya mradi huo.
MHE. QAMBALO W. QULWI aliuliza:-
Bei kubwa ya pembejeo hususan mbegu bora ya mahindi imesababisha wakulima wengi kupanda mbegu zilizo chini ya kiwango na hivyo kusababisha uzalishaji hafifu sana, mfano msimu wa mwaka 2015/2016 kilo moja ya mbegu ya zao hilo iliuzwa kati ya shilingi 5,000 hadi shilingi 6,000.
(a) Je, ni nini kinafanya bei ya mbegu bora kuwa ghali sana?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wakulima wa zao hilo kupata mbegu hizo kwa gharama nafuu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Qambalo Willy Qulwi, Mbunge wa Jimbo la Karatu, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, bei ya mbegu bora inakuwa ghali kutokana na gharama halisi za uzalishaji wa mbegu hizo. Mbegu bora zinatokana na tafiti mbalimbali zinazofanywa na watafiti na huchukua muda mrefu kuweza kupata aina mpya ya mbegu.
Pia mbegu bora zinapozalishwa hupitia hatua mbalimbali kama vile usajili wa mashamba, ukaguzi wa mashamba, uchukuaji wa sampuli na upimaji wa mbegu maabara kabla ya kuanza kuziuza kwa wakulima, hatua hizo zote zinachangia mbegu bora kuwa ghali ikilinganishwa na mbegu ambazo sio bora.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia tija inayopatikana kutokana na matumizi ya mbegu bora utaona kuwa bei ya mbegu bora sio ghali. Mfano, ukitumia mbegu bora za mahindi kilo kumi inayotosha ekari moja pamoja na kanuni bora za kilimo inaweza kutoa gunia 25 hadi 30 ikilinganishwa na gunia tano hadi kumi zinazopatikana kwa kutumia mbegu isiyokuwa bora.
(b) Mheshimiwa Spika, katika kukabaliana na changamoto ya bei ya mbegu bora na kwa kutambua uwezo mdogo wa wakulima kuweza kumudu gharama hizo, Serikali imekuwa ikitoa ruzuku ya pembejeo za kilimo ikiwemo mbegu bora ili wakulima waweze kuzalisha kwa tija. Aidha, Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kuimarisha utafiti wa mbegu bora na kuwahamasisha wakulima kuzalisha mbegu za daraja la kuazimiwa ubora (Quality Declared Seeds) ili kuongeza upatikanaji wa mbegu bora katika maeneo ya vijijini.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza:-
Ili kuboresha kilimo na ujasiriamali inahitajika elimu kwa wakulima pamoja na kuwa na vyanzo vya mitaji.
(a) Je, ni lini Serikali itaanzisha Mfuko wa Kuzunguka (Revolving Fund) kwa kila kijiji kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wakulima na wajasiriamali?
(b) Je, Benki ya wakulima ina mtaji kiasi gani na imetoa mikopo katika mikoa gani?
(c) Je, ni lini Benki ya Wakulima itaanza kutoa mikopo kwa wakulima wadogo wa Mbeya Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini, lenye sehemu (a), (b), na (c) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua changamoto ya upatikanaji wa mikopo vijijini hali inayochangia kukosekana kwa mitaji katika kuendeleza shughuli za kilimo na ujasiriamali. Hata hivyo, kwa kuwa suala la kuanzisha Mfuko wa Kuzunguka (Revolving Fund) kwa kila kijiji kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wakulima na ujasiriamali linahitaji fedha nyingi na usimamizi wa karibu kuhakikisha fursa ya upatikanaji wa fedha hizo haitumiwi na watu wachache kwa manufaa yao, Serikali imefanya uchambuzi wa kina ili kuona namna bora ya kusimamia mifuko ya aina hiyo na ambayo itawanufaisha wakulima na wajasiriamali na kuandaa mapendekezo ya mfuko stahiki kwa ajili ya kuridhiwa na Serikali. Juhudi hizo zipo katika ngazi ya maamuzi Serikalini. Aidha, kwa sasa Serikali inawashauri na kuwahamasisha wakulima na wajasiriamali kuunda vikundi au kujiunga na vyama vya kuweka na kukopa yaani SACCOS ili waweze kukopesheka.
Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Juni, 2017 Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania imefikisha mtaji wa shilingi bilioni 65.6 ambayo umepanda kutoa shilingi bilioni 65.3 kama ulivyokuwa katika robo ya kwanza ya mwaka 2017. Kutokana na udhamini wa Serikali, benki imepata mkopo wa bei nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB) kiasi cha shilingi bilioni 209.5 fedha ambazo zinatolewa kwa awamu, ambapo awamu ya kwanza ya shilingi bilioni 104.6 imeshapatikana. Aidha, hadi kufikia Juni, 2017 TADB imetoa mikopo ya jumla ya shilingi bilioni 7.46 katika Mikoa ya Tanga, Morogoro na Iringa ambapo jumla ya wakulima 2,252 wamenufaika na mikopo hiyo moja kwa moja.
Mheshimiwa Spika, TADB inalenga kufungua Ofisi za Kanda nchi nzima ili kurahisisha na kupunguza gharama za upatikanaji wa mikopo. Benki itaanzisha Ofisi ya Kanda Mkoani Mbeya. Hata hivyo, kama ilivyofanyika maeneo mengine, kabla ya ufunguzi wa ofisi hiyo, wakulima wa Mbeya walio katika vikundi watanufaika na mikopo ya TADB kuanzia msimu ujao wa kilimo.
MHE. LATHIFAH H. CHANDE aliuliza:-
Asilimia 85 ya wananchi wa Mkoa wa Lindi ni wakulima wa korosho, ufuta na mbaazi. Pamoja na juhudi kubwa za uzalishaji, wakulima hao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali za ukosefu wa masoko, ucheleweshwaji wa pembejeo na kuongezeka kwa ushuru:-
(a) Je, ni lini Serikali itawashirikisha wakulima hawa katika upangaji bei hasa zao la korosho badala ya Bodi pekee ambayo inapanga bila kuangalia gharama halisi za kulima?
(b) Je, ni lini Serikali italianzisha tena soko la uhakika la mazao ya wakulima baada ya kulifunga lile la awali Wilayani Mtwara?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lathifah Hassan Chande, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ushirikishwaji wa wakulima na wadau wa korosho katika upangaji wa bei ya korosho na mjengeko wa bei ni kwa mujibu wa Sheria ya Korosho ya Mwaka 2009. Kwa hali hiyo, kabla ya kuanza msimu mpya wa soko la korosho, wadau hukutana ambapo Wawakilishi wa wakulima huwa zaidi ya nusu ya wajumbe wote na kukubaliana kuhusu bei dira. Bei hii huzingatia wastani wa gharama za uzalishaji wa korosho ghafi shambani na hali ya soko la nje kwa kipindi kisichopungua miezi sita iliyopita.
Mheshimiwa Naibu Spika, madhumuni ya kuweka bei dira ni pamoja na kumwezesha mkulima kuhimili ushindani wa soko kwa kuwa na uhakika wa kurudisha gharama zake za uzalishaji wa korosho ghafi katika msimu husika, pia juu yake huwekwa asilimia 20 ya faida.
Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu huu wa kupata bei dira ya korosho hufanyika baada ya utafiti wa kina wa gharama za uzalishaji wa korosho na kumsaidia mkulima kupata bei yenye maslahi sokoni kupitia mfumo wa soko wa stakabadhi ghalani. Kwa mantiki hiyo, upangaji wa bei dira ya korosho unashirikisha wakulima na huzingatia gharama halisi za uzalishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara itaendelea kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuanzisha masoko ya mazao mbalimbali kadri itakavyoonekana inafaa.
MHE. PROSPER J. MBENA aliuliza:-
Wakati wa mjadala wa hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi tarehe 22 Mei, 2017, Bungeni, Wabunge wengi walieleza umuhimu wa Serikali kuongeza juhudi za uvuvi kwenye Bahari Kuu na kuitaka Serikali kununua meli kubwa za kuvua samaki kwenye Bahari Kuu:-
(a) Je, Serikali inaweza kueleza sababu zilizofanya Shirika la Uvuvi la Tanzania (Tanzania Fisheries Company-TAFICO) lishindwe kuendelea na biashara ya uvuvi wa Bahari Kuu?
(b) Je, Serikali haioni umuhimu wa kulifufua Shirika hilo la TAFICO?
(c) Je, miundombinu iliyokuwepo ya uvuvi kwa ajili ya TAFICO ikiwa ni pamoja na meli, dry dock na zana nyingi za uvuvi ambazo zilijengwa na kulipiwa na Serikali ya Japan ipo katika hali gani?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Prosper Joseph Mbena, Morogoro Kusini, lenye vipengele (a), (b) na (c), Kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, lililokuwa Shirika la Uvuvi Tanzania (Tanzania Fisheries Corporation - TAFICO) lilianzishwa kwa Sheria ya Makampuni ya Umma Na. 17 ya mwaka 1996. Lengo la kuanzishwa kwa TAFICO lilikuwa ni kuendesha shughuli za uvuvi kibiashara katika maji ya ndani na siyo uvuvi wa bahari kuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 1996, Serikali ilitoa tangazo Na. 322 kuhusu kurekebisha Mashirika ya Umma ili yaweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na tija zaidi ambapo TAFICO ilikuwa ni miongoni mwa mashirika yaliyotakiwa kubinafsishwa au kufanyiwa marekebisho. Kwa msingi huo, shughuli za Shirika la TAFICO liliwekwa chini ya Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC) kwa ajili ya taratibu za ubinafsishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaona umuhimu wa kufufua TAFICO ili Sekta ya Uvuvi iweze kuchangia ipasavyo katika ajenda ya uchumi wa viwanda. Hivyo Wizara imekamilisha waraka wa Baraza la Mawaziri kwa ajili ya mapendekezo ya kutunga Sheria mpya ya Shirika la Uvuvi Tanzania. Suala hili linafanyika kwa kuzingatia ushauri wa kitaalam ili kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali za uvuvi zilizopo ikiwa ni pamoja na uvuvi wa bahari kuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na mabadiliko ya sera ambapo Serikali ilijitoa kufanya shughuli za moja kwa moja za uzalishaji na biashara, Serikali kupitia Msajili wa Hazina iliuza mali za TAFICO zinazohamishika zikiwemo meli na mitambo ya barafu mwaka 2008 na kubakiza mali zisizohamishika yakiwemo majengo ambayo yamekarabatiwa na sasa yanatumika kama Ofisi za Serikali na matumizi mengine. Aidha, kutokana na kukaa muda mrefu bila kutumika na athari za mvua za Elnino, Dry Dock imechakaa na imezama upande mmoja.
MHE. ROSE C. TWEVE aliuliza:-
Pamoja na kwamba sekta ya kilimo ndiyo yenye kuajiri Watanzania walio wengi, lakini sekta hiyo imekuwa na maendeleo hafifu kutokana na watumishi wachache wenye ujuzi wa kutosha na ukosefu wa vitendea kazi kama vile pikipiki, zana za kufundishia na kadhalika.
Je, Serikali ina mkakati gani wa makusudi wa kufanya mapinduzi ya kilimo kwa kuwa na wataalam wa kutosha?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rose Cyprian Tweve, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kuwa Sekta ya Kilimo ni muhimu na ndiyo yenye kuajiri Watanzania wengi, hivyo mapinduzi ya kilimo pamoja na mambo mengine yatachangiwa uwepo na wataalam wa kutosha wenye taaluma na ujuzi stahiki ili waweze kushauri matumizi ya teknolojia na kanuni bora za kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu huo, Serikali imeweka mikakati mbalimbali ili kuleta mapinduzi ya kilimo ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya Maafisa Ugami wenye ujuzi ili kila Kata na kijiji kiwe na Afisa Ugani mmoja. Aidha, Serikali inaendelea kuboresha na kuwezesha Vituo vya Kilimo na Vituo vya Rasilimali za Kilimo za Kata kwa ajili ya kufundisha teknolojia mbalimbali za kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufikia mwaka 2016/2017, Serikali imeajiri Maafisa Ugani 8,756 sawa na asilimia 43 ya mahitaji ya Maafisa Ugani 20,374 katika ngazi ya kijiji, Kata na Wilaya. Jumla ya wataalam wa kilimo 8,000 ngazi ya Astashahada na Stashahada waliohitimu mafunzo katika Vyuo vya Kilimo wameajiriwa katika maeneo mbalimbali nchini. Aidha, Serikali inaendelea kusomesha vijana tarajali na kuwaajiri kulingana na upatikanaji wa rasilimali fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, mikakati mingine ni pamoja na kuboresha huduma za ugani kwa kusambaza teknolojia za kilimo bora kwa wakulima kwa kutumia njia mbalimbali hususan shamba darasa, vipindi vya redio na luninga, mchapisho na Maonesho ya Kilimo - Nane Nane.
Aidha, Serikali itaendelea kutoa ushauri wa kitaalam na kuandaa miongozo na mafunzo ya huduma za ugani, ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa kazi za ugani na kuboresha usambazaji wa teknolojia za kilimo bora kwa wakulima nchini.
MHE. ABDALLA HAJI ALI aliuliza:-
Uzalishaji wa mafuta na gesi ni suala la Muungano na kwa kuzingatia ukweli kwamba visima vya gesi vya songosongo na Mnazi Bay Mkoani Lindi na Mtwara vimekuwa vikizalisha gesi muda mrefu sasa:-
(a) Je, uzalishaji wa gesi kwa siku kwa visima hivyo ni mita za ujazo kiasi gani?
(b) Je, tangu uzalishaji ulipoanza mapato ya fedha yamekuwa kiasi gani kwa mwaka na yanatumikaje?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI (K.n.y WAZIRI WA NISHATI NA MADINI) alijibu:
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdalla Haji Ali, Mbunge wa Kiwani, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa wastani jumla ya futi za ujazo milioni 145 za gesi asilia huzalishwa kwa siku katika visima vya uzalishaji gesi asilia vya Songosongo na Mnazi Bay ambako kiasi cha futi za ujazo milioni 90 huzalishwa kwenye visima vya Songosongo na kiasi cha futi za ujazo milioni 55 huzalishwa katika visima vya Mnazi Bay.
Mheshimiwa Naibu Spika, gesi asilia inayozalishwa hutumika kuzalisha umeme katika mitambo ya SONGAS megawatt 189; Kinyerezi, megawatts 150; Ubungo I megawatts 102; Ubungo II megawatts 129; Somangafungu megawatts 7.5; Tegeta megawatts 45; na Mtwara megawatts 18. Aidha, kiasi kingine cha gesi asilia hutumika kama chanzo cha nishati kwenye viwanda 42 vilivyounganishwa pamoja na matumizi madogo kwenye nyumba kwa ajili ya kupikia na kuendeshea magari.
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha jumla ya shilingi bilioni 488 zimekusanywa kutoka kwenye mauzo ya gesi asilia kwa miaka sita tangu 2011 hadi 2016 sawa na wastani wa kiasi cha shilingi bilioni 81.3 kwa mwaka. Mapato haya huwasilishwa Hazina kwa mujibu wa taratibu husika.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Watendaji wa Vyama vya Msingi vya Mazao (AMCOS) wanapatikana kwa njia ya ushindani na wanakuwa na sifa zinazostahili?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota, Mbunge wa Nanyamba, kama ifuatayo:-
Mheshimiwa Spika, utaratibu wa kuwapata Watendaji wa Vyama vya Ushirika vya Msingi vya Mazao na Masoko (AMCOS) upo kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Ushirika Na. 6 ya mwaka 2013 pamoja na Kanuni za Ushirika za mwaka 2015. Utaratibu umeelekezwa kwa mujibu wa kifungu cha 134 cha Sheria ya Vyama vya Ushirika katika Jedwali la Pili, vifungu vya 14, 15, 16 na 18 kuwa panapotokea nafasi za kazi za Watendaji wa Vyama vya Ushirika katika ngazi zote, vikiwemo vile Vyama vya Ushirika vya Mazao na Masoko, nafasi hizo hutangazwa kwa wananchi kwa muda wa siku 30 ili waombe nafasi hizo kwa ajili ya ushindani.
Mheshimiwa Spika, sifa zinazotakiwa kwa waombaji wa nafasi za Watendaji wa Vyama vya Msingi vya Ushirika, vikiwemo Vyama vya Msingi vya Mazao na Masoko ni kama ifuatavyo; kiwango cha elimu kuanzia kidato cha nne; uelewa wa lugha za kiswahili na kiingereza; uwezo wa kufundishika; majina na anuani za angalau wadhamini wawili (referees); aina ya biashara na shughuli inayofanywa na mwombaji na taarifa nyingine yoyote inayohusika kutoka kwa mwombaji. Hivyo, Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania inahakikisha kuwa Watendaji wa Vyama vya Ushirika vya Msingi vya Mazao na Masoko wanapatikana kwa njia ya ushindani na wanakuwa na sifa zinazostahili kama zilivyotajwa kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Ushirika Na. 6 ya mwaka 2013.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza:-
Serikali inazuia wavuvi kuvua samaki wadogo na hivyo nyavu zenye matundu madogo haziruhusiwi; katika Ziwa Victoria kuna samaki ambao kwa maumbile yao hawawezi kuwa wakubwa kama vile dagaa, furu na hata sato.
Je, Serikali haioni kuwa kwa kuzuia tu nyavu ndogo samaki hawa hawatavuliwa kamwe?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatekeleza Sheria ya Uvuvi Namba 22 ya mwaka 2003 na Kanuni zake za mwaka 2009 katika kulinda na kusimamia rasilimali za uvuvi ili ziwe endelevu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuhakikisha rasilimali za uvuvi zinavunwa katika njia endelevu bila ya kuathiri vizazi vyao, Serikali imepiga marufuku matumizi ya nyavu (dagaa net) zenye macho madogo chini ya milimita nane kwa uvuvi wa dagaa, badala yake nyavu zinazoruhusiwa kwa uvuvi wa dagaa ni kuanzia milimita nane hadi milimita 12.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa uvuvi wa sato na sangara, Serikali imekataza wavuvi kutumia nyavu za makila zenye ukubwa wa macho chini ya inchi sita ili kuvua samaki wakubwa tu. Aidha, samaki hao wanaweza kuvuliwa kwa kutumia mishipi au nyavu za makila kuanzia inchi sita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo kuu la Serikali la kupiga marufuku matumizi ya nyavu zenye macho madogo ni kunusuru kizazi cha samaki kisipotee kwa kuepusha uvuvi wa samaki wachanga kwa manufaa ya kizazi kilichopo na kizazi kijacho. Hata hivyo, kulingana na sheria na kanuni hizo, samaki wa aina zote huvuliwa kwa kutumia nyavu zilizoruhusiwa kisheria na ndiyo maana samaki wa aina zote wanapatikana sokoni.
MHE. QAMBALO W. QULWI aliuliza:-
Miaka ya karibuni zao la mbaazi limechangia kipato kwa wakulima baada ya kupata bei nzuri katika masoko. Katika msimu wa 2016/2017 bei ya zao hili ilishuka hadi kufikia shilingi 900 kwa kilo moja ukilinganisha na bei ya shilingi 2,800 kwa kilo moja kwa msimu wa 2015/2016.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwaunganisha wakulima wa zao hilo na masoko yaliyoko ndani na nje ya nchi ili waweze kupata bei nzuri?
Wapo wanunuzi wa zao hilo, mathalani Kampuni ya Kilimo Market wanachukua mazao ya wananchi na kuchelewa kuwalipa fedha zao. Je, ni nini kauli ya Serikali dhidi ya makampuni ya namna hiyo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Qambalo Willy Qulwi, Mbunge wa Karatu, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
– Mheshimiwa Mwenyekiti, bei ya mbaazi iliporomoka katika msimu wa 2016/2017 katika maeneo mbalimbali nchini kutokana na ongezeko la uzalishaji wa zao hilo katika nchi za China, Brazil, Myanmar, Canada, Msumbiji na Sudan kuliko mahitaji ukilinganishwa na msimu wa mwaka 2015/2016. Ili kuhakikisha kuwa wakulima wanapata soko la uhakika la mbaazi, Serikali kupitia Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko iliandaa Mkataba wa Makubaliano (Memorandum of Understanding – MOU) na Serikali ya India ambao ndiyo wanunuzi wakubwa wa mazao ya jamii ya mikunde hapa nchini ili kuweka mfumo rasmi wa soko la mazao ya jamii ya mikunde hapa nchini. Mkataba huo ulipelekwa India ambako kwa mujibu wa Ubalozi wa India nchini bado wanaufanyia kazi kabla ya kusainiwa na pande zote mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hatua zinazochukuliwa za kuuza mbaazi nchini India, Serikali inaangalia uwezekano wa kuanzisha mfumo wa Stakabadhi Ghalani ambao umeleta matokeo mazuri kwa zao la korosho ili pia utumike kwa zao la mbaazi. Ili mfumo ho utumike ipasavyo na kwa ufanisi, Serikali itawahamasisha wakulima kujiunga katika vyama vya ushirika kwenye maeneo yao na pia kuwa na utaratibu wa kupanga bei elekezi yenye kuzingatia gharama zote za uzalishaji kama ilivyo kwa zao la korosho.
– Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la wanunuzi kuchukua mazao ya wananchi na kuchelewa kuwalipa fedha zao, Serikali itaendelea kutoa maelekezo na kuhakikisha kuwa wanunuzi wote wa mazao nchini wanawalipa wananchi fedha zao mapema iwezekanavyo mara tu wananuapo mazao hayo. Hata hivyo, mfumo rasmi wa soko la mazao ya jamii ya kunde ambao utakuwa chini ya usimamizi wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko utaziba mianya ya wanunuzi holela hivyo kuepusha udanganyifu wakati wa kununua mazao ya jamii ya kunde ikiwa ni pamoja na mbaazi kutoka kwa wakulima.
MHE. JUMAA H. AWESO aliuliza:-
Licha ya Wilaya ya Pangani kubarikiwa kuwa na Bahari ya Hindi lakini wavuvi wa Pangani hawajanufaika ipasavyo na bahari hiyo.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wavuvi wa Pangani mitaji na vitendea kazi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jumaa Hamidu Aweso, Mbunge wa Pangani, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kutoa kipaumbele kwa sekta ya uvuvi nchini kwa kutekeleza mikakati yenye lengo la kuendeleza uvuvi nchini wakiwemo wavuvi wa Wilaya ya Pangani ili waweze kupata ajira, lishe, kipato na kuchangia katika pato la Taifa. Miongoni mwa mikakati hiyo, ni pamoja na kuondoa kodi katika zana za malighafi za uvuvi zikiwemo injini za kupachika, nyuzi za kushonea nyavu (twines) na vifungashio. Kodi hizo zimeondolewa kupitia Sheria ya Ongezeko la Thamani ya mwaka 2014. Vilevile kupitia East Africa Publication on Common External Tariff, injini za uvuvi na malighafi zinazotumika kutengeneza zana mbalimbali za uvuvi na viambata vyake zimepewa punguzo la kodi ili kuwezesha wavuvi kumudu bei za vifaa hivyo. Pia Serikali inatoa ruzuku kwenye zana za uvuvi ambapo mvuvi anatakiwa kuchangia asilimia 60 na Serikali asilimia 40.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Pangani ni eneo la kimkakati katika masuala ya uvuvi na hasa uvuvi wa dagaa katika vijiji vya Kipumbwi na Pangani Mashariki na uvuvi wa pweza katika kijiji cha Ushongo. Serikali imewawezesha wavuvi wa Pangani kwa kuwapatia mafunzo ya kuongeza thamani na uvuvi endelevu wa pweza. Katika mwaka 2017/2018 kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Pangani, Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 20 kwa ajili ya ujenzi wa soko la samaki ambapo fedha imeshapelekwa katika akaunti ya Kata ya Pangani Mashariki ili ujenzi uanze mara moja. Kukamilika kwa ujenzi wa soko hilo kutawanufaisha wavuvi wa Pangani na hivyo kupata mtaji na vitendea kazi katika shughuli za uvuvi. Natoa wito kwa Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Madiwani wa Pangani kufuatilia na kusimamia ipasavyo matumizi ya fedha hizi ili lengo la Serikali la kuwawezesha wavuvi wa Pangani liweze kutimia. Vilevile Mheshimiwa Mbunge aendelee kushirikiana na Waheshimiwa Madiwani na wananchi kupiga vita vitendo vya uvuvi haramu wa kutumia mabomu na hivyo kuhatarisha uendelevu wa rasilimali hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mradi wa Usimamizi wa Uvuvi na Maendeleo Shirikishi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish) imeendelea kutoa mafunzo ya uvuvi endelevu kwa wavuvi ambapo katika Halmashauri ya Pangani, BMUs tatu za Pangani Mashariki, Pangani Magharibi na Boza zimenufaika na mafunzo hayo. Katika mwaka 2017/2018 Serikali itaendelea kutoa mafunzo kwa BMUs zilizobaki za Bweni, Ushongo Sahabu, Kipumbwi, Sange, Mikocheni, Mkwaja na Buyuni ambazo ziko ng’ambo ya Mto Pangani. Pia, Halmashauri ya Pangani imetoa uwakala kwa BMUs nne kati ya 11 za Wilaya ya Pangani kukusanya mapato ya uvuvi ambapo asilimia 10 ya mapato hayo wanapewa BMUs. Fedha hiyo ikitumika vizuri inaweza kuwapatia wavuvi wa Pangani mitaji na vitendea kazi.
MHE. DEVOTHA M. MINJA aliuliza:-
Idadi ya wanafunzi wanajiunga na Vyuo Vikuu vya Mkoa wa Morogoro imepungua kutokana na wanafunzi wengi kukosa mikopo ya elimu ya juu.
Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Devotha Mathew Minja, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutoa kipaumbele katika elimu ya juu nchini, ambapo mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imepanga kutumia shilingi bilioni 427.54 kugharamia mikopo kwa ajili ya wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu. Kiasi hiki ni kwa ajili ya wanafunzi 112,623, ambapo wanafunzi 30,000 ni mwaka wa kwanza na wanafunzi 92,623, ni wale wanaoendelea na masomo. Katika robo ya kwanza kiasi cha shilingi bilioni 147.06 tayari kimeshatolewa kwa wakati, hivyo Serikali haitarajii kuwepo kwa ucheweleshwaji wa mikopo kwa wanafunzi ambao wamekidhi vigezo.
Mheshimiwa Spika, aidha, wanafunzi 3,307 kutoka katika vyuo vitano vya mkoani Morogoro walipata mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 11.49 katika mwaka 2016/2017. Vyuo hivyo ni Chuo Kikuu Kishiriki cha Jordan, Chuo Kikuu cha Mzumbe, Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Morogoro, na Chuo Kikuu cha Sokoine.
Mheshimiwa Spika, suala la mikopo pekee si sababu ya ongezeko au kupungua kwa wanafunzi. Mambo mengine ni pamoja na viwango vya ufaulu alama za ukomo katika udahili, ubora wa vyuo na programu zinazotolewa kulingana na uhitaji wa soko.
MHE.ESTHER A. MAHAWE (K.n.y. MHE. ESTHER M. MMASI) aliuliza:-
Kupitia fursa za ujenzi wa mabweni ya wanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwezi Aprili, 2017.
Je, Serikali imeweka jitihada gani katika kuongeza fursa za ujenzi wa mabweni kwa Taasisi za Elimu ya Juu hususani Chuo cha Ushirika Moshi Mkoani Kilimanjaro ambapo zaidi ya 70% ya wanafunzi wanaishi nje ya chuo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther Mmasi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji katika vyuo vikuu nchini, Serikali imewezesha ujenzi wa mabweni mapya 20 katika chuo kikuu cha Dar es Salaam vyenye uwezo wa kubeba wanafunzi 3,840 na kukamilisha ujenzi wa Chuo Kikuu cha Taaluma cha Tiba (MUHAS). Aidha, Serikali imefanya juhudi za kuainisha hali ya miundominu katika vyuo vya elimu ya juu ili kubaini mahitaji halisi. Baada ya tathmini hiyo, kupitia Mradi wa Malipo kwa Matokeo (P for R) Serikali imeanza ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya vyuo vikuu vya Sokoine, Dares Salaam, Ushirika Moshi na Mzumbe.
Mheshimiwa Spika, Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi kina hostel zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 900 kwa wakati mmoja, idadi hii ni sawa na asilimia 25% ya wanafunzi wote. Ili kuhakikisha mazingira bora ya malazi kwa wanafunzi, chuo kina mpango wa kujenga hostel zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 3,500 kwa wakati mmoja. Mpango huu umebainishwa katika mpango mkakati wa chuo wa miaka mitano.
Mheshimiwa Spika, aidha, kwa mwaka wa fedha 2017/2018 chuo kupitia miradi ya maendeleo ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kinategemea kupatiwa fedha za ujenzi wa hostel zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,000 kwa wakati mmoja. Ujenzi huu ukikamilika utasaidia kutatua kwa kiasi kikubwa tatizo la malazi kwa wanafunzi na hivyo kuchangia katika kufanikisha azma ya Serikali ya kuzalisha wataalam wengi. (Makofi)
MHE. JOHN P. KADUTU aliuliza:-
Miaka mingi iliyopita Serikali iliwahi kuzichukua hospitali, shule na huduma nyingine nyingi kutoka katika mashirika ya dini na baadae Serikali ilirudisha huduma hizo kwa wamiliki wake, Kanisa la Moravian Tabora lilikuwa na eneo la VETA, Serikali wakati wa kurudisha haikurudisha eneo hilo kwa Kanisa hilo.
(a) Je, ni lini Serikali itarudisha eneo hilo kwa wamiliki wake?
(b) Je, Serikali ipo tayari kulipa fidia kwa kuwa na eneo ambalo siyo lake?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia naomba kujibu swali la Mheshimiwa John Peter Kadutu, Mbunge wa Ulyankulu, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnamo mwaka 1973, Kanisa la Moravian Tanzania Magharibi lilikabidhi eneo, majengo na mali inayohamishika na isiyohamishika kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara. Misingi na sababu maalum ambazo zilikubaliwa na pande zote mbili ilikuwa ni kwamba eneo hilo litumike kama chuo cha kufundishia mafunzo mbalimbali ya ufundi. Walengwa walikuwa ni vijana ambao hawakupata nafasi ya kuendelea na masomo ya sekondari baada ya kuhitimu elimu ya msingi na lengo ilikuwa ni kwamba ni kuwapa stadi mbalimbali za ufundi kwa ajili ya kuweza kujiajiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya Serikali kukabidhiwa eneo hilo, lilikabidhi kwa Shirika la SIDO lililokuwa chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwama 1974 ili eneo hilo litumike kuendesha mafunzo ya ufundi. Hata hivyo, mwaka 2002 eneno hilo lilikabidhiwa kwa VETA kwa lengo la kuendelea kutoa mafunzo ya ufundi stadi. Aidha, VETA imeendelea na majuku hayo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Mheshimiwa mwenyekiti, napenda kukifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa Serikali haijarudisha maeneo yote ya kielimu ambayo awali yalikuwa yanamilikiwa na mashirika ya dini bali kuna baadhi ya maeneo ambayo yalirudishwa kwa makubaliano ya pande zote mbili. Aidha, kwa ajili ya manufaa mapana ya Taifa kwa sasa Serikali haina mpango wa kurudisha maeneo mengine kama hayo.
MHE. PASCAL Y. HAONGA aliuliza:-
Kigezo kimojawapo cha kuwanyima mkopo waombaji wa mkopo ya elimu ya juu ni kama muombaji alisoma shule za binafsi.
(a) Je, Serikali haioni kuwa baadhi ya wanafunzi hulipiwa ada ya shule za binafsi na ndugu, jamaa, marafiki na NGO’s hivyo wanafunzi hao wanapofikia elimu ya juu hushindwa kumudu gharama za elimu hiyo?
(b) Je, Serikali ipo tayari kufuta kigezo hicho ili kuwapatia waombaji wa mikopo haki yao ya kupata elimu ya juu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia naomba kujibu swali la Mheshimiwa Pascal Yohana Haonga Mbunge wa Mbozi lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, sifa za msingi za kupata mkopo wa elimu ya juu zinaainishwa katika kifungu cha 17(1) cha Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ya 2004 (Sura ya 178) ya Sheria za Tanzania kama ifuatavyo; awe Mtanzania, awe amedahiliwa kwenye chuo kinachotambulika, awe ameomba mkopo kwa njia ya mtandao, awe hana chanzo kingine cha kugharamia elimu yake. Mbali na sheria, vigezo vingine ni uyatima, ulemavu, uhitaji na mahitaji ya rasilimalwatu kwa ajili ya vipaumbele vya maendeleo vya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa kuwasilisha maombi ya mkopo wa elimu ya juu muombaji hutakiwa kuwasilisha taarifa muhimu zikiwepo shule au vyuo alivyosoma kabla ya kujiunga na elimu ya juu. Bodi ya Mikopo hutumia taarifa hizi ili pamoja na mambo mengine kubaini historia ya uchangiaji wa gharama za elimu katika ngazi ya sekondari au chuo ili kumpangia mkopo stahiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale inapothbitika kwa maandishi kwamba mwanafunzi husika alisaidiwa au kufadhiliwa na ufadhili huo umekoma Bodi ya Mikopo huwakopesha kwa kuzingatia hali zao za kiuchumi kwa wakati huo. Kwa mfano, katika mwaka wa masomo wa 2016/2017 jumla ya wanafunzi 719 waliothibitika kufadhiliwa au kusaidiwa katika masomo yao ya sekondari walipata mkopo.
MHE. ZAYNAB M. VULLU (K.n.y MHE. MARIAM N. KISANGI) aliuliza:-
Ongezeko la watoto wenye matatizo ya afya ya akili na ubongo limekuwa kubwa kwa sasa katika nchi yetu:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha vitengo vya elimu kwa watoto wenye mahitaji maalum (walemavu) wa viungo na ubongo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nassoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua uwepo wa watoto wenye ulemavu wa akili na wenye usonji na jitihada mbalimbali zinafanyika ili kuhakikisha kuwa watoto hao wanapata fursa ya elimu kama watoto wengine. Takwimu za mwaka 2016 zinaonesha kuwa kuna jumla ya wanafunzi wenye ulemavu wa akili na wenye usonji 11,386 katika ngazi ya elimu ya awali na msingi na wanafunzi wenye ulemavu wa viungo 8,115 wanaosoma ngazi ya elimu ya awali, msingi na sekondari.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kupanua fursa za upatikanaji wa elimu na kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa wanafunzi wenye ulemavu nchini. Hatua hizo ni pamoja na:-
Wizara ilitoa mafunzo kazini kwa Walimu wapatao 699 wanaofundisha wanafunzi wenye ulemavu wa akili na wenye usonji kwa lengo la kuwajengea uwezo ili kuinua ubora wa elimu itolewayo; kuboresha miundombinu ya shule ili kukidhi mahitaji ya ujifunzaji kwa wanafunzi wenye ulemavu wa viungo; kuanzisha na kuimarisha vitengo 349 vinavyopokea wanafunzi wenye ulemavu wa akili na wenye usonji nchini; na kufanya mapitio ya mwongozo wa ujenzi wa majengo ya shule za msingi, sekondari na vyuo vya ualimu. Mwongozo huu utazingatia mahitaji maalum ya wanafunzi wenye ulemavu wa viungo ili kuwawezesha kusoma bila vikwazo wawapo shuleni.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inakamilisha uandaaji wa mwongozo wa kufundishia wanafunzi wenye ulemavu wa akili na wenye usonji ambao utasambazwa katika vitengo vyote 349 vinavyopokea wanafunzi hao. Mwongozo huo una lengo la kupanua uelewa wa Walimu juu ya mbinu za kufundishia, matumizi ya vifaa pamoja na saikolojia ya kufundishia wanafunzi hao kwa ubora zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Wizara imetenga jumla shilingi bilioni 3.5 katika mwaka wa fedha 2017/2018 kwa ajili ya ununuzi na usambazaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia pamoja na visaidizi kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum wakiwemo wanafunzi wenye ulemavu wa viungo, akili na wenye usonji.
MHE. ESTHER L. MIDIMU aliuliza:-
Mkoa wa Simiyu hauna Chuo cha Ufundi (VETA):-
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Chuo cha VETA katika Mkoa wa Simiyu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Lukago Midimu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kutekeleza mpango wa kujenga vyuo 43 vya ufundi stadi ngazi ya Wilaya kwa awamu. Kipaumbele ni zile Wilaya zisizo na chuo chochote cha ufundi stadi na ambazo maeneo yake yana miradi mikubwa ya Kitaifa kwa manufaa ya Watanzania. Lengo ni kuongeza fursa za kuwapatia ujuzi vijana zaidi ya milioni moja ambao humaliza elimu ya msingi na sekondari na kuingia katika soko la ajira kila mwaka bila ujuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi sasa Chuo cha Ufundi Stadi Makete kimekamilika na kuanza kutoa mafunzo na vyuo sita vya Wilaya za Namtumbo, Kilindi, Chunya, Chato, Nyasa na Ukerewe vipo katika hatua mbalimbali za maandalizi ya ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vyuo vipya ngazi ya Mkoa katika Mikoa ya Manyara, Pwani, Lindi, Kipawa ICT na Chuo cha Hoteli na Utalii Arusha vimejengwa. Aidha, hatua mbalimbali za maandalizi ya ujenzi wa vyuo ngazi ya Mkoa vya Njombe, Geita, Rukwa, Simiyu na Kagera zinaendelea.
Serikali itaendelea kutenga bajeti ya maendeleo kila mwaka pamoja na kutafuta wafadhili wa ndani na nje ili kuwezesha kujenga vyuo vingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa Chuo cha VETA Mkoa wa Simiyu kwa mkopo wa fedha za Benki ya Maendeleo ya Afrika upo katika hatua za maandalizi. Mshauri Elekezi wa kusanifu majengo na kusimamia ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Mkoa wa Simiyu amekamilisha kazi ya kuandaa michoro, makadirio ya ujenzi na makabrasha ya zabuni mwezi Oktoba, 2017. Hatua zinazofuata ni kutangaza zabuni na kumpata mjenzi mwezi huu wa Novemba na kuanza ujenzi wa chuo mwezi Februari, 2018. (Makofi)
MHE. EDWARD F. MWALONGO aliuliza:-
Elimu ya ufundi ni muhimu ili kuwawezesha vijana kuajiriwa na kujiajiri:-
• Je, nchi yetu ina vyuo vingapi vya Ufundi Stadi vya Umma?
• Je, kuna vyuo vingapi visivyo vya Umma?
• Je, hivi vyote vina uwezo wa kudahili vijana wangapi kwa mwaka?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Edward Franz Mwalongo, Mbunge wa Njombe Mjini, lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu kwa mwaka wa 2016/2017 ilikuwa na jumla ya vyuo vya ufundi stadi 127 vya umma na vyuo 634 visivyo vya umma vilivyokuwa vinatambulika na kusajiliwa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA). Vyuo 501 kati ya 761 vilipata ithibati ya VETA na viliweza kudahili jumla ya wanafunzi 56,420 kwa mwaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, Vyuo vya ufundi stadi vina umuhimu mkubwa wa kuandaa nguvukazi ya kutosha, mahiri na yenye ujuzi unaotakiwa ili iweze kushiriki katika kujenga uchumi wa viwanda wakati tunaelekea kwenye nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa 2016/2017 - 2020/2021 imelenga kuongeza idadi ya wahitimu katika vyuo vya ufundi stadi kutoka 150,000 kwa mwaka 2015 hadi kufikia 700,000 ifikapo mwaka 2021 ili kuongeza fursa za ajira kwa vijana wenye ujuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itakamilisha ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi ngazi ya mkoa katika mikoa mitano na ngazi ya wilaya katika wilaya sita. Aidha, itakamilisha ukarabati wa vyuo vya ufundi stadi katika wilaya mbili. Mkakati uliopo ni Serikali kuendelea kutenga bajeti ya maendeleo kila mwaka pamoja na kutafuta wafadhili mbalimbali wa ndani na nje ya nchi ili kuweza kujenga vyuo vingine.
MHE. HUSSEIN N. AMAR aliuliza:-
Je, katika bajeti ya Serikali 2016/2017 Serikali ilitarajia kuanzisha Vyuo vingine vya ufundi ikiwemo Nyang’hwale?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hussein Nassoro Amar, Mbunge wa Nyang’hwale kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutekeleza mpango wa kujenga Vyuo vya VETA katika Wilaya mbalimbali kulingana na upatikanaji wa fedha. Wilaya zinazopewa kipaumbele ni zile ambazo hazina Chuo chochote cha mafunzo ya ufundi stadi. Lengo ni kuwapatia vijana ujuzi mbalimbali ambao utawawezesha kuwa na sifa za aidha kuajiriwa au kujiajiri.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Sayansi na Teknolojia inatarajia kuanza ujenzi wa Vyuo vinne vya Ufundi Stadi ngazi ya Mkoa katika Mikoa ya Njombe, Rukwa, Geita na Simiyu.
Mheshimiwa Spika, pamoja na Wilaya ya Nyang’hwale zipo pia Wilaya nyingine ambazo zina mahitaji ya kuwa na Vyuo vya VETA, Wizara inatambua hilo na itaendelea kutafuta fedha ili kukabiliana na mahitaji hayo. Tunatarajia kuwa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) cha Mkoa wa Geita kitakapokamilika kujengwa kitakuwa na uwezo wa kutoa mafunzo na huduma kwa vijana kutoka Wilaya zote za Mkoa wa Geita ikiwemo na Wilaya ya Nyang’hwale.
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:-
Kumekuwepo na matangazo mengi ya watu waliopoteza vyeti vya kitaaluma hasa vinavyotolewa na Baraza la Mitihani:-
(a) Je, ni utaratibu gani unaotumika pale mtu anapopoteza cheti ili aweze kupata cheti kingine?
(b) Je, anapata cheti halisi au nakala ya cheti?
(c) Baadhi ya wananchi wanalalamika kuwa kumekuwa na ucheleweshaji mkubwa kwa Baraza la Mitihani wanapoombwa kuwasilisha cheti katika mamlaka fulani ambayo mtu ameomba kazi au nafasi ya masomo na hivyo kusababisha waombaji wengi kukosa nafasi kutokana na ucheleweshaji huo; je, ni taratibu gani mtu anatakiwa kuzifuata ili ombi lake lifanyiwe kazi ipasavyo na kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mhitimu aliyepoteza cheti hupatiwa cheti mbadala au uthibitisho wa matokeo kwa kufuata utaratibu ufuatao:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi kuhusu upotevu wa cheti na kupata hati ya upotevu wa cheti na kupata hati ya upotevu. Lengo la kuripoti polisi ni kupata msaada wa kiuchunguzi ili kusaidia kukipata cheti kilichopotea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbili, kutangaza gazetini kuhusu upotevu wa cheti kwa lengo la kuutarifu umma ili kusaidia kukipata cheti kilichopotea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, endapo hakikupatikana hata baada ya kutangazwa katika vyombo vya habari, mhitimu atajaza fomu ya ombi la cheti mbadala au uthibitisho wa matokeo na kuwasilisha Baraza la Mitihani la Tanzania. Fomu hiyo inapatikana kwenye Ofisi za Baraza la Mitihani Tanzania na pia kwenye tovuti ya Baraza ambayo ni www.necta.go.tz.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nne Baraza la Mitihani Tanzania hufanya uchunguzi wa uhalali wa umiliki wa cheti husika na kutoa huduma stahiki. Wahitimu waliofanya mtihani kuanzia mwaka 2008 ambao vyeti vyao vina picha, hupatiwa vyeti mbadala (Duplicate Certificate) na waliofanya mtihani kabla ya mwaka 2008 hupatiwa uthibitisho wa matokeo ambao hutumwa kwa waajiri wao au mahali pengine kwa mahitaji yaliyotolewa na mwombaji. Hivyo, kundi hili la pili hawapewi cheti mbadala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, cheti mbadala kinachotolewa ni cheti halisi. Hata hivyo, kinaongezewa maandishi yanayosomeka Duplicate kuonesha kuwa cheti hicho kimetolewa kwa mara ya pili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwombaji wa cheti mbadala au uthibitisho wa matokeo hupatiwa huduma baada ya kukamilisha taratibu zinazohitajika na zilizowekwa.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO (K.n.y MHE. ZUBEDA H. SAKURU) aliuliza:-
Baadhi ya Shule na Vyuo nchini vinaendelea kudahili wanafunzi pamoja na kutokidhi matakwa ya sheria mbalimbali.
(a) Je, Serikali inachukua hatua gani kudhibiti vyuo na shule zinazoendelea kudahili wanafunzi huku zikiwa na mapungufu?
(b) Je, mpaka sasa ni vyuo vingapi na shule ngapi zilizofutiwa usajili kwa kutokukidhi matakwa ya kisheria.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, wa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zubeda Hassan Sakuru, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ina taratibu za kudhibiti ubora wa elimu na mafunzo yanayotolewa shuleni na vyuoni kupitia Idara ya Udhibiti Ubora wa Shule katika maana ya shule za msingi, sekondari na vyuo vya ualimu. Baraza la Taifa la Elimu la Ufundi (NACTE) kwa vyuo na taasisi zinazotoa elimu ya kati na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) kwa taasisi zinazotoa elimu ya juu. Shule na vyuo vinavyobainika kukiuka taratibu za utoaji elimu na mafunzo huchukuliwa hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kusitisha udahili wa wanafunzi, kusitisha programu zitolewazo, kupunguza idadi ya wanafuzni waliozidi na kufuta usajili wa taasisi husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2017/2018 Serikali imefuta usajili kwa shule saba za awali na msingi na shule moja ya sekondari. Vilevile vituo 16 vilivyokuwa vimedahili wanafunzi wa elimu ya awali na msingi kabla ya kusajiliwa viliagizwa kuwatawanya wanafunzi hao kwa kuwapeleka katika shule zilizosajiliwa na kufunga vituo hivyo. Katika mwaka 2016/2017 Serikali kupitia NACTE ilifanya uhakiki katika vyuo na taasisi 103 za elimu ya ufundi ambapo vyuo na taasisi 31 zilibainika kuwa na mapungufu na hivyo kufutiwa usajili.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha katika mwaka 2017/ 2018 uhakiki mwingine ulifanyika katika vituo, vyuo na taasisi 454 za elimu ya ufundi ambapo jumla ya vyuo na taasisi 59 za elimu ya ufundi zilibainika kuwa na mapungufu na hivyo walitakiwa kurekebisha mapungufu ndani ya kipindi cha miezi mitatu kuanzia tarehe Mosi Februari, 2018. Chuo kitakachoshindwa kurekebisha mapungufu yaliyobainishwa ndani ya kipindi kilichopangwa kitafutiwa usajili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa vyuo vikuu Serikali kupitia TCU ilifanya uhakiki wa vyuo vyote vya elimu ya juu nchini kati ya mwezi Oktoba, 2016 na Januari, 2017 ili kuhakiki ubora wa elimu inayotolewa vyuoni. Taarifa ya uhakiki ilionyesha mapungufu katika baadhi ya vyuo, kufuatia taarifa hiyo TCU kwa mwaka wa masomo 2017/2018 ilisitisha udahili wa wanafunzi wa Programu za Afya na Uhandisi kwenye vyuo vitano. Vilevile TCU ilisitisha udahili katika programu zote kwa mwaka wa kwanza kwa vyuo 14, aidha, katika mwaka huo wa masomo TCU imedhibiti na kuzuia vyuo vikuu kudahili wanafunzi katika programu ambazo hazijapata ithibati zipatazo 75 katika vyuo vikuu 22.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA (K.n.y MHE. ALLY S. UNGANDO) aliuliza:-
Asilimia 90 ya wakazi wa Delta ya Mto Rufiji katika Kata ya Salale, Maparoni, Mbuchi na Kiangoroni ni wavuvi ambao hutumia mitumbwi isiyo na mashine na ndilo eneo pekee katika mwambao wa Bahari ya Hindi kunapatikana samaki aina ya kamba (prawns) kwa wingi; na kwa kuwa Ilani ya Uchaguzi wa CCM ya mwaka 2015 imeazimu kuwapatia wavuvi wadogo wataalam, vifaa vya kisasa vya uvuvi ili wajiendeleze na kuongeza Pato la Taifa.
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia wananchi wa maeneo hayo semina kuhusu uvuvi bora wa kisasa?
(b) Kwa kuwa mikopo hutolewa kwa vikund mbalimbali; je, Serikali itatoa mikopo kwa vikundi vya uvuvi vilivyopo kwenye maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Seif Ungando, Mbunge wa Kibiti lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imekuwa ikitoa mafunzo ya uvuvi endelevu kwa wavuvi kupitia semina, warsha, vipeperushi, makala, redio na luninga kwa kushirikiana na Halmashauri na wadau mbalimbali. Katika kusambaza teknolojia mbalimbali za uvuvi, katika mwaka 2016/2017, Wizara ilirusha hewani vipindi saba vya redio na kimoja cha luninga vilivyohusu Wakala wa Mafunzo (FETA). Ukuzaji viumbe kwenye maji, uzalishaji bora wa samaki, mbinu za kutambua magonjwa ya samaki na uvuvi endelevu. Aidha, vipindi 19 vilirushwa hewani kwa lengo la kuwaelimisha vijana na kuwajengea uwezo wa kuingia katika uvuvi. Pia Wizara imechapisha nakala 1,000 za mwongozo wa ugani katika Sekta ya Uvuvi kwa lengo la kutoa elimu kwa wavuvi na wakuzaji viumbe kwenye maji.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatekeleza mpango wa kutoa ruzuku kwa wavuvi ambayo inalenga kuwasaidia wavuvi kupata zana bora na vifaa vya kuvulia zikiwepo injini za boti kwa utaratibu wa uchangiaji ambapo wavuvi watangaia asilimia 60 ya gharama na Serikali itatoa asilimia 40. Katika awamu ya kwanza jumla ya engine 73 zimenunuliwa na vikundi 27 kutoka Ukanda wa Pwani katika Halmashauri za Bagamoyo, Mafia, Lindi, Manispaa, Mtwara Mikindani, Temeke, Mkinga, Muheza na Tanga Jiji vimekidhi vigezo. Hivyo, napenda nitumie fursa hii kumuomba Mheshimiwa Mbunge ahimize wavuvi katika Halmashauri ya Kibiti kujiunga katika vyama vya Ushirika vya Msingi ili waweze kutumia fursa hii kwa kuwa mpaka sasa hakuna kikundi kutoka Wilaya ya Kibiti au hata jirani Wilaya ya Rufiji kilijitokeza kuomba zana za uvuvi za ruzuku.
Aidha, Serikali kwa kushirikiana na Shirika la WWF pamoja na Halmashauri ya Rufiji imewezesha wavuvi kuanzisha VICOBA 36 vyenye jumla ya wavuvi 829 na kupewa mafunzo ya ujasiriamali. Pia, Wizara kupitia Mradi wa Usimamaizi wa Uvuvi na Maendelea Shirikishi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish) inaandaa Mpango kazi utakaokuwa na program za vipindi mbalimbali kuhusu usimamizi endelevu wa rasilimali za uvuvi ambazo zitarushwa katika televisheni na radio mbalimbali. Wavuvi wa nchi nzima wakiwemo wa Kibiti watanufaika na elimu itakayotolewa kupitia mpango kazi huo.(Makofi)
MHE. DKT. DAVID M. DAVID aliuliza:-
Serikali iliahidi katika bajeti ya 2012, 2013 na 2014 kujenga Malambo, Majosho na Kisima kirefu kwa ajili ya wananchi na Wafugaji wa Kata ya Ruvu katika Jimbo la Same Magharibi:- Je, ni lini ahadi hiyo itakamilishwa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshiniwa David Mathayo David, Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia bajeti yake na program mbalimbali imeendelea kukarabati na kujenga miundombinu ya maji ya mifugo kwa kutumia vipaumbele kama maeneo yenye mifugo mingi na yale ambayo yanapokea mifugo wakati wa kiangazi. Kupitia utaratibu huo Wizara imeweza kujenga mabwawa na malambo katika Wilaya za Kiteto, Kilindi na Ngorongoro. Aidha, katika bajeti ya mwaka 2013/2014, Wizara ilitenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa malambo katika Wilaya ya Same na Wilaya nyingine.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, Wizara haikupatiwa fedha kwa ajili ya kufanya kazi hiyo. Mwaka 2015/2016, wataalam wa Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Same waliainisha eneo la Kijiji cha Ruvu, Kata ya Ruvu kwa ajili ya ujenzi wa lambo. Mwaka 2017/2018, Wizara imetenga fedha kwenye bajeti yake kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maji kwenye baadhi ya Wilaya ikiwemo Wilaya ya Same.
Mheshimiwa Spika, naendelea kuzishauri Mamlaka za Serikali za Mitaa kuendelea kutenga fedha kupitia bajeti zao kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maji ya mifugo kama malambo, mabwawa na visima virefu ili kupunguza kero ya upatikanaji wa maji kwa mifugo hasa wakati wa kiangazi. Aidha, Wizara itaendelea kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa kujenga na kukarabati miundombinu ya maji ya mifugo kutegemeana na upatikanaji wa fedha.
MHE. CECIL DAVID MWAMBE aliuliza:-
Wananchi wa Jimbo la Ndanda hawako tayari kabisa kuona mfumo wa uuzaji korosho wa stakabadhi ghalani ukiendelea.
Je, Serikali chini ya kauli mbiu “Hapa Kazi Tu” ipo tayari kuondoa kabisa mfumo huo ambao ni kandamizi na hauendani na gharama za uzalishaji?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabla sijajibu lazima niseme kwamba kama Mheshimiwa Cecil Mwambe asingerekebisha swali ningeshangaa sana kama swali la aina hiyo lingetoka kwake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecil David Mwambe Mbunge wa Ndanda kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa Stakabadhi za Maghala ni utaratibu ulioanzishwa kisheria wa namna ya uuzaji wa mazao kwenye maghala kwa wakulima kukusanyia mazao yao kupitia chama chake cha misingi na mazao hayo kupelekwa katika ghala kuu ambapo ubora wa zao huhakikiwa kulingana na Sheria ya Maghala na mkulima kupewa stakabadhi ambayo hutumika kama dhamana ikiwa mkulima atahitaji mkopo wakati akisubiri mazao yake kuuzwa sokoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo huu una mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na wakulima kupata uhakika wa soko, kupanda kwa bei ya zao la korosho ambapo wakulima waliuza korosho zao kwa bei ya ushindani sokoni kwa wastani wa shilingi 2,500 kwa kilo na bei ya juu kufikia hadi shilingi 4,000 kwa kilo katika msimu huu wa 2016/2017. Aidha, mfumo huu pia umewezesha kuongezeka kwa uzalishaji wa zao la korosho ambapo uzalishaji uliongezeka kutoka tani 155,244.64 katika msimu wa 2015/2016 hadi kufikia tani 264,887.52 kwa msimu wa 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, faida nyingine ya mfumo huu ni kwamba wakulima wa korosho kwa sasa wanapata bei za juu kutokana na wakulima kupata bei sokoni kwa utaratibu wa kuvumbua (pride discovery).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ajili hiyo, Serikali haiko tayari kwa sasa kuondoa mfumo wa Stakabadhi Ghalani katika uuzaji wa zao la korosho nchini kutokana na mafanikio hayo, badala yake Serikali itaendelea kusimamia na kuboresha mfumo huu na kuwahamasisha wakulima kuongeza uzalishaji wa korosho zenye ubora ili kujiongezea kipato chao na nchi kwa ujumla.
MHE. HALIMA ALI MOHAMMED aliuliza:-
Tanzania ina dhamira ya kuwa nchi ya uchumi wa kati kwa kujikita katika uchumi wa viwanda; na viwanda vinategemea sana ukuaji wa sekta ya kilimo kwa ajili ya kupata malighafi.
Je, Serikali imewekeza kiasi gani cha fedha kwa ajili ya utafiti wa kilimo (agricultural research) ili kufanya tafiti za kilimo kubaini changamoto zinazodumaza kilimo nchini na kutoa ushauri kwa wakulima ili kuongeza uzalishaji wa kilimo na hivyo kukuza sekta ya viwanda?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Halima Ali Mohammed, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti wa kilimo hapa nchini una lengo kuu la kugundua mahitaji halisi ya mkulima na walengwa wengine. Utafiti wa kilimo hufanywa kupitia vituo 16 vya utafiti vya umma vilivyopo katika kanda mbalimbali na taasisi za utafiti binafsi kama vile Taasisi ya Kahawa (TaCRI), Chai (TRIT) na Tumbaku (TORITA). Serikali imeanza kuboresha mfumo wa utafiti wa kilimo kufuatia kuanzishwa kwa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (Tanzania Agricultural Research Institute
– TARI) ili kuboresha zaidi uzalishaji wa mazao. Taasisi hii ndiyo itakayosimamia na kuratibu utafiti wa kilimo hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kuwekeza katika utafiti kwa kuendeleza rasilimali watu na miundombinu ya utafiti. Idadi watafiti walioajiriwa ni takribani 360 na kati yao asilimia 16 wana kiwango cha elimu cha Shahada ya Uzamivu (Ph.D). Vilevile Serikali imeboresha maabara kuu nne za udongo katika Vyuo vya Utafiti vya Mlingano, Seliani, Uyole na Ukiriguru kwa kuzinunulia vifaa vya kisasa vya kutathmini virutubisho vya udongo/mradi wa kupima rutuba ya udongo na kuchora ramani yenye thamani ya takribani kuthamini ya takribani shilingi bilioni 1.8. Mradi huu utasaidia wakulima na wawekezaji katika sekta ya kilimo kufahamu viwango stahiki vya mbolea na mazao yanayostahili kulimwa katika eneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hutenga takribani shilingi bilioni tatu kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo. Pia vituo hufanya shughuli za itafiti kwa kushirikiana na taasisi za kitaifa na kimataifa. Ni matarajio yetu kuwa mahusiano haya yataboreka zaidi baada ya TARI kuanzishwa rasmi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, utafiti ni mojawapo ya vipaumbele katika Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II). Chini ya programu hiyo uzalishaji na usambazaji wa teknolojia za kilimo utaboreshwa zaidi kwa kuendeleza miundombinu ya utafiti na rasilimali watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika miaka mitano ijayo utafiti utalenga zaidi katika utatuzi wa changamoto zilizokabili mazao yenye tija na yenye kipaumbele kitaifa ili kutekelezwa azma ya kufikia uchumi wa viwanda. Shughuli za utafiti zitakazowekewa mkazo ni pamoja na ugunduzi wa mbegu bora, uzalishaji na upatikanaji wake, magonjwa na wadudu waharibifu, matumizi sahihi ya mbolea, udongo na maji, lishe bora, uhifadhi wa mazao na uongezaji wa thamani ya mazao ili kufikia kilimo chenye tija na cha kibiashara. Jumla ya shilingi 164,532,000,000 zinatarajiwa kuwekezwa katika shughuli za kilimo wa mazao, mifugo na uvuvi kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
MHE. OMAR T. MGUMBA aliuliza:-
Shamba Na. 217 lenye ukubwa wa hekta 63,000 lililopo katika Kata ya Mkulazi, Morogoro Vijijini limepata Mwekezaji Kampuni ya Mkulazi Holding Company Limited kwa ajili ya kuliendeleza kwa Kilimo cha Mazao mbalimbali na uwekezaji wa kiwanda cha sukari. Aidha, wakulima wadogo (out growers) wametengewa eneo la hekta 3,000 tu na Wawekezaji hekta 60,000 kwa ajili ya shughuli zao:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza ardhi ya akiba kwa wakulima wadogo kutoka hekta 3,000 kwenda hekta 23,000;
(b) Je, Serikali haioni kuwa kwa kutenga hekta 3,000 tu itazalisha vibarua wengi wazawa badala ya kuwashirikisha katika uzalishaji ili kuinua hali zao za maisha pamoja na kuongeza Pato la Taifa.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omary Tebweta Mgumba, Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa juhudi anazofanya katika kuhakikisha wakulima wanapata maeneo ya kilimo, napenda kutoa taarifa kuwa, hekta 3,000 za wakulima wadogo wadogo zilizoainishwa na Mheshimiwa Mbunge ziko kwenye eneo la Matokeo Makubwa Sasa. Katika mpango huu inakadiriwa kuwa hekta 250,000 kwa ajili ya wakulima wadogo wa kibiashara na hekta 350,000 kwa ajili ya wakulima wakubwa wa kibiashara zitapatikana na zitalimwa zao la miwa na mpunga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili la Mkulazi ambalo liko kwenye Jimbo la Mheshimiwa Mbunge jumla ya hekta 63,000 zimepimwa na kutolewa Hati Miliki ambayo inamilikiwa na Serikali Kituo cha Uwekezaji (TIC), ambapo hekta 60,000 ni kwa ajili ya wakulima wa mashamba makubwa ya kibiashara ya uwekezaji na hekta 3,000 ni kwa ajili ya wakulima wa mashamba madogomadogo ya kibiashara. Wakulima wadogo watatoka kwenye vijiji vinavyozunguka eneo hilo la uwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uzalishaji wa uwekezaji mkubwa utatumia teknolojia ya kisasa na Kanuni bora za kilimo, kwa kufanya hivyo, maeneo ya wakulima wadogo yatachangia kwa kiasi kikubwa ukubwa wa eneo linalozalisha zao hilo, pia wingi wa ubora wa zao ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje na hivyo kuongeza kipato cha mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushirikishwaji huu hautazalisha vibarua bali utazalisha wakulima na wajasiliamali wengi, ambao watashiriki kikamilifu katika mnyororo wa thamani (value chain) wa zao husika.
MHE. MARTIN M. MSUHA aliuliza:-
Chama Kikuu cha Ushirika ‘Mbinga Cooperative Union (MBICU) kilishindwa kuendesha shughuli zake kibiashara na hatimaye kukabidhiwa kwa mfilisi mwaka 1994/1995 kutokana na madeni pamoja na kuyumba kwa soko la kahawa.
(a) Je, kwa nini mfilisi bado anashikilia mali za Chama hicho badala ya kukabidhi kwa Chama kipya cha Mbinga Farmers Cooperation Union (MBIFACU) kwa muda mrefu kiasi hicho?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kulipa deni la wakulima lipatalo shilingi 424 millioni ambalo liliachwa na MBICU iliyokufa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martin Mtonda Msuha, Mbunge wa Mbinga Vijijini, lenye sehemu (a)na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Chama Kikuu cha Ushirika cha Mbinga (MBICU Limited) kiliacha shughuli zake baada ya kuelemewa na madeni na hivyo kusababisha kufutwa kwenye daftari la Serikali na kisha kufilisiwa. Sababu kubwa na ya msingi ya kufilisiwa MBICU Limited ni kudaiwa na Benki ya NBC na wadai wengine kiasi cha Sh.2,101,365,050/= ambapo ilijikuta ni mufilisi kwa kuwa mali zake zilikuwa na thamani ya Sh.752,814,784/=.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Mfilisi hajashikilia mali zozote za MBICU Limited, baada ya kufutwa kwa MBICU Limited wanachama walianzisha MBIFACU Limited kwa mategemeo ya kukabidhiwa mali za MBICU Limited. Mwaka 2007, wanachama walianzisha MBIFACU Limited, walirudishiwa mali zao na kuahidi kulipa madeni yanayodaiwa MBICU Limited likiwepo deni la Golden Impex Limited lililokuwa na thamani ya Sh.155,000,000/= ambalo lililipwa tarehe 13 Machi, 2012.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya deni hilo kulipwa MBIFACU Limited ilikabidhiwa asilimia sabini ya mali na mfilisi na Bodi ya Uongozi wa MBIFACU Limited ilianza kusimamia mali hizo. Sehemu ya mali ya asilimia 30 iliyobaki itakabidhiwa baada ya Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika kujiridhisha na utekelezwaji wa Mkataba wa Maridhiano yaani MoU baina ya Mfilisi na MBIFACU Limited.
MHE. ESTER A. BULAYA aliuliza:-
Kwa kipindi kirefu sasa Serikali imekuwa na mipango mahsusi ya kuhakikisha kwamba tatizo la walimu wa sayansi linapungua au kumalizika kabisa.
• Je, ni kwa kiwango gani mipango hii imesaidia kupunguza tatizo husika?
• Katika utekelezaji wa mpango tajwa hapo juu, Jimbo la Bunda Mjini na Halmashauri ya Mji wa Bunda imenufaika vipi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ester Amos Bulaya, Mbunge wa Bunda Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na changamoto ya upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi na hisabati kama ifuatavyo:-
(a) Imetenga Vyuo vya Ualimu 10 mahsusi kwa ajili ya kuandaa walimu wa masomo ya sayansi na hisabati.
(b) Kuongeza udahili wa walimu wa masomo ya sayansi na hisabati katika vyuo vikuu vya Serikali ambavyo hapo awali vilikuwa havitoi kozi za ualimu, kama Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) na Chuo Kikuu Mzumbe.
(c) Kutoa kipaumbele cha udahili katika mafunzo ya ualimu wa stashahada na shahada kwa wahitimu wa kidato cha sita wa masomo ya sayansi na hisabati.
(d) Kutoa kipaumbele cha ajira kwa wahitimu wa mafunzo ya ualimu, sayansi na hisabati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilianzisha pia kozi maalum ya stashahada ya ualimu kwa masomo ya sayansi na hisabati ambapo wahitimu wa kundi la kwanza wapatao 1,799 watamaliza mafunzo yao ifikapo Mei, 2018 na kundi la pili la wahitimu wapatao 5,441 watamaliza Mei, 2019.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuboresha ufundishaji na kuvutia wanafunzi wengi kusoma masomo ya sayansi na hisabati na hatimaye kupata wahitimu wengi wa masomo hayo, Serikali imeendelea kuimarisha ufundishaji wa masomo ya sayansi ikiwa ni pamoja na kusambaza vifaa vya maabara na kemikali katika shule za sekondari na kutoa mafunzo kazini kwa walimu wa sayansi na hisabati. Mkakati huo unalenga kupata wahitimu wengi zaidi watakaojiunga na mafunzo ya ualimu wa sayansi na fani nyingine zinazohitaji masomo hayo na hivyo kuendelea kukabiliana na upungufu wa wataalam wa sayansi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Mji wa Bunda ilianzishwa mwaka 2015/2016 baada ya kugawanywa iliyokuwa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda. Kabla ya kugawanywa Wilaya hii ilikuwa na jumla ya walimu 144 wa masomo ya sayansi na hisabati. Katika taratibu za kugawana rasilimaliwatu katika Wilaya hiyo, Halmashauri ya Mji wa Bunda ilipewa walimu 69 wa masomo ya sayansi na hisabati.
Aidha, walimu wa sayansi na hisabati walioajiriwa mwaka 2016/2017 waliopangwa katika Halmashauri ya Bunda Mji ni wanane ambao wamepangwa katika shule za sekondari za Kunzugu, Rubana, Bunda, Wariku, Sazira, Sizaki, Nyendo na Daktari Nchimbi. Serikali itaendelea kuajiri na kupanga walimu wa masomo ya sayansi na hisabati katika Halmashauri hiyo, kadiri watakavyopatikana.
MHE. MUNIRA MUSTAPHA KHATIBU aliuza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuratibu na kuwatambua wasichana wanaokatiza masomo kwa sababu ya ujauzito na wale walionyimwa fursa ya kuendelea na masomo na kuwaandalia mpango maalum wa kujiendeleza kimasomo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Munira Mustapha Khatibu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa inao utaratibu wa kuwatambua wanafunzi wanaoacha shule kwa sababu mbalimbali. Takwimu hutolewa kupitia kijitabu kinachojulikana kwa jina la National Basic Education Statistics in Tanzania (BEST). Kijitabu hicho hutoa takwimu za kielimu ikiwa ni pamoja na idadi ya wanafunzi, walimu na vifaa vya kufundishia na kujifunzia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kupitia Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima hutoa fursa za kielimu kwa makundi tofauti ya walengwa wakiwemo waliokosa nafasi ya kuendelea na masomo ya sekondari kwa sababu mbalimbali kama ujauzito, utoro na utovu wa nidhamu. Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima huendesha Mpango wa Elimu ya Sekondari kwa ujifunzaji huria katika vituo vilivyopo katika Mikoa yote ya Tanzania Bara. Katika mwaka 2017, walengwa 10,420 wamesajiliwa kati yao 7,074 ni wanawake na 4,346 ni wanaume. Aidha, Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima huandaa na kuendesha Programu ya Elimu Mbadala kwa Vijana na Watu Wazima kulingana na mahitaji yao ambapo hutoa mafunzo ya muda mfupi na mrefu kama vile ujasiriamali, stadi za maisha, ufundi wa awali na Programu za Kisomo cha Kujiendeleza kwa Watu Wazima ili waweze kuendesha maisha yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanafunzi wanaoacha shule za msingi, hupata fursa ya kuendelea na masomo kupitia Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Walioikosa (MEMKWA). Pia Serikali ina mpango wa kuimarisha Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs) ili viweze kuongeza wigo wa kudahili wanafunzi kwa nyanja mbalimbali za mafunzo na hivyo kutoa fursa zaidi kwa wanafunzi wanaoacha masomo kwenye mfumo rasmi wa elimu.
MHE. MACHANO OTHMAN SAID aliuliza:-
Kwa muda mrefu sasa Kurugenzi nyingi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki zimekuwa zikiongozwa na Makaimu, hali ambayo inapunguza ufanisi wa kazi.
Je, ni sababu gani za msingi zinazoifanya Serikali kushindwa kuwathibitisha makaimu hao?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA (K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Machano Othman Said, Mbunge wa Baraza la Wawakilishi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuna Kurugenzi mbili ambazo Wakurugenzi wake wanakaimu kwa muda mrefu. Kurugenzi hizo ni Idara ya Miundombinu ya Kiuchumi na Huduma za Jamii na Idara ya Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji.
Aidha, hivi karibuni Kurugenzi nyingine zinakaimiwa na Maafisa Waandamizi au Mabalozi kutokana na baadhi ya Wakurugenzi kustaafu, kuhamishwa na kuteuliwa kuwa Mabalozi kwenda kuwakilisha nchi katika Balozi zetu za Beijing, Paris, Oman, New Delhi. Khartoum na Brussels.
Mheshimiwa Naibu Spika, sababu ya msingi iliyoifanya Serikali kutothibitisha Makaimu Wakurugenzi ni pamoja na Wizara kuwa katika mchakato wa kupitia muundo wake ili kujua idadi halisi ya Kurugenzi zinazohitajika, hivyo kuleta, ufanisi katika kazi. Mchakato wa kupitia muundo huo umekamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa taratibu za uteuzi wa Kurugenzi kwa ajili ya kuthibitishwa na kujaza nafasi hizo zinakamilishwa kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI (K.n.y MHE. SAADA MKUYA SALUM) aliuliza:-
Serikali nyingi duniani zinaunganisha diaspora katika mikakati yao ya kukuza uchumi na huduma za kijamii.
(a) Je, Serikali imefanya mikakati gani ya kuunganisha diaspora katika shughuli za kukuza uchumi na huduma za kijamii?
(b) Je, ni kwa kiasi gani diaspora imechangia uchumi wa nchi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA WAZIRI (K.n.y MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Saada Mkuya Salum, Mbunge wa Welezo, lenye vipengele (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano inatambua umuhimu wa diaspora katika kuleta maendeleo hapa nchini kupitia utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano, mwaka 2016/2017 hadi 2020/2021. Kuelekea uchumi wa kati diaspora ni moja wa wadau. Ili kutekeleza jukumu hili Serikali imeweka mikakati ifuatayo:-
(i) Kuhakikisha kuwa katika kila eneo lenye uwakilishi wetu Ubalozi unawatambua Watanzania wanaoishi katika maeneo hayo pamoja na Watanzania hao kuunda Jumuiya zao.
(ii) Kupitia ziara za viongozi pindi wanapokuwa nchi za nje Serikali imehakikisha kuwa, kunakuwa na utaratibu wa viongozi kukutana na diaspora wa Tanzania ili kuwaeleza masuala yanayotokea nyumbani, hasa fursa za kiuchumi na uwekezaji.
(iii) Serikali imekuwa ikiratibu zoezi la kuwakutanisha diaspora na wadau wa hapa nchini na nje kupitia makongamano, ambapo kumekuwa na jitihada, mijadala yenye tija katika maeneo ya uchumi na maendeleo kwa ujumla.
(iv) Wizara imeunda timu ya kufanikisha uandaaji wa Sera ya Taifa ya diaspora itakayoainisha mikakati na kutoa miongozo kuhusu ushiriki wa diaspora katika kuchangia maendeleo nchini.
(v) Wizara imeelekeza Balozi zetu kusajili Watanzania waliopo katika maeneo yote ya uwakilishi na kuainisha shughuli wanazozifanya, taaluma na ujuzi walionao, ili kusaidia kuwa na takwimu sahihi na kuhusu diaspora wetu na kuweka mazingira wezeshi ya kuchangia maendeleo nchini.
(b) Mheshimiwa Spika, diaspora wetu wamekuwa wakichangia uchumi wa nchi yetu kupitia uwekezaji katika sekta mbalimbali kama biashara, afya na elimu, kama ifuatavyo:-
(i) Kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, yaani 2013 hadi 2017, diaspora kwa ujumla wao walituma nchini kiasi kisichopungua dola za Kimarekani milioni 2282 ikiwa ni wastani wa dola milioni 455 kwa mwaka.
(ii) Jumla ya nyumba 108 za Shirika la Nyumba la Taifa zilinunuliwa na diaspora wetu.
(iii) Mnamo mwezi Julai, 2017 tulipokea Madaktari wa Kitanzania waliopo Marekani, Dakota ambao walikuja kutoa huduma bila malipo katika Hospitali ya Mnazi Mmoja iliyopo Zanzibar.
(iv) Katika kipindi cha mwaka 2015/2017 timu ya Madaktari wa Kitanzania waishio Marekani, kupitia Taasisi ya Afya ya Elimu na Maendeleo – Head Incorporated, walitoa huduma za afya na matibabu katika Hospitali ya Mnazi Mmoja Zanzibar na kukabidhi dawa na vifaatiba vyenye thamani ya dola 459,075; msaada wa mashine ya kupimia saratani ya matiti katika Hospitali ya Lugalo Dar es Salaam yenye thamani ya dola 200,000; huduma za matibabu ya ushauri na ushauri katika Hospitali ya Mwananyamala Dar es Salaam na Hospitali ya Mnazi Mmoja iliyopo Zanzibar, kukabidhi msaada wa vifaatiba vyenye thamani ya dola 300,000.
(v) Jumuiya ya Watanzania nchini Marekani Dakota iliandaa jukwa la afya lililofanyika nchini humo mwezi Novemba, 2017 ambapo walialika taasisi mbalimbali zinazohusika na masuala ya afya kutoka hapa nchini ili kupeana ujuzi na uzoefu walioupata Marekani katika kipindi wanachoishi na kufanya kazi kwa lengo la kuongeza ufanisi katika masuala hayo.
(vi) Diaspora wa Kitanzania waliopo Bujumbura walitafuta soko la bidhaa za wajasiriamali wa Kitanzania walioshiriki katika maonesho ya Juakali yaliyofanyika mwezi Disemba, 2017. (Makofi)
MHE. DKT IMMACULATA S SEMESI aliuliza:-
Kwa ujumla Serikali haiwatumii ipasavyo wanazuoni kama watafiti, hasa katika eneo la tafiti ya sayansi kwa kukuza sekta ya viwanda:-
Je, ni kwa nini vyuo vikuu vya Serikali havipati fungu kwa ajili ya tafiti ili kutoa suluhisho mbalimbali na miongozo ya kimaendeleo yenye misingi ya tafiti kisayansi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Immaculate Sware Semesi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hutenga fedha kwa ajili ya tafiti kupitia Mfuko wa Taifa ya Uendelezaji wa Sayansi na Teknolojia (MTUSATE) unaoratibiwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH). Mfuko huu upo ili kuhakikisha maendeleo ya Sayansi na Teknolojia yanapatikana ambayo ni pamoja na tafiti kufanyika kulingana na vipaumble vya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha kwa ajili ya tafiti kutoka kwenye Mfuko huu hutumiwa kwa utafiti wa ndani ya nchi wakiwemo wanazuoni kwa njia ya ushindani. Aidha pamoja na Wanazuoni kupata fedha za kufanya tafiti kupitia Mfuko wa MTUSATE, washirika wa maendeleo kama vile Serikali za Sweden na Norway hufadhili shule za utafiti kwa kupeleka fedha za utafiti moja kwa moja katika vyuo vikuu mbalimbali kama vile Chuo Kiuu cha Dar es Salam, Chuo cha Ardhi na Chuo cha Tiba ya Afya Muhimbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa MTUSATE imefadhili miradi 102 ambayo ilitekelezwa na Taasisi mbalimbali za utafiti za vyuo vikuu vya Tanzania Bara na Tanzania Visiwani. Kati ya miradi hiyo vyuo vikuu vilitekeleza jumla ya miradi 48 iliyofadhiliwa kwa njia ya ushindani ambayo imegharimu jumla ya shilingi bilioni 4.6.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya vyuo vikuu hivyo ni pamoja na Chuo Kiuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Chuo Kiuu cha Dar es Salam (UDSM), Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya, Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA), Chuo Kikuu cha Sayansi za Tiba, Taasisi ya Syansi na Teknolojia ya Nenson Mandela, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salam na chuo Kikuu Dodoma (UDOM).
Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo ya tafiti zilizofanywa na Wanazuoni zimeonekana kuwa ni tafiti zenye tija katika maendeleo ya uchumi wa viwanda. Baadhi ya matokeo ya tafiti hizo ni pamoja na utengenezaji wa chanjo mseto ya kuku inayostahimili joto ya kukinga magonjwa matatu (mdondo, ndui na mafua) iliyofanywa na SUA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kugunduliwa kwa mbinu bora za kuzalisha vifaranga vya kaa iliyofanya na SUZA, kugunduliwa kwa vifaa kusafishia maji kwa matumizi kwa matumizi majumbani iliyofanya na Taasisi ya Nenson Mandela; usindikaji wa ngozi na mazao ya mifugo ambayo imewezesha kuanzisha kwa mitaala ya astashahada na shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Sokoine iliyofanywa na SUA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kuna udhibiti wa magonjwa yanayiharibu mazao ili kuleta uhakika wa chakula na kuondoa umaskini iliyofanyiwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salam; pamoja na udhibiti wa uharibu wa mazao unaofanywa na panya kwa kutumia mkojo wa paka iliyofanyika na SUA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha kuwa wanazuoni wanafanya tafiti zenye tija Serikali imesaidia uazishwaji wa vituo mahiri (African Center over Excellence) vinne kupitia Benki ya Afrika ambapo takribani shilingi bilioni hamsini zimewekezwa kuendeleza utafiti katika Chuo Kiku cha Kilimo cha Sokoine na Taasisi ya Teknolojia ya Nelsoni Mandela.
MHE. JEROME D BWANAUSI aliuliza:-
Wakati Serikali inafanya juhudi za kuongeza idadi ya Walimu na kulipa stahiki zao:-
(a) Je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kurudisha Chuo cha Ualimu Ndwika badala ya sekondari kama ilivyo sasa?
(b) Je, ni lini Serikali italipa madeni hayo?
NAIBU WAZIRI ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu Swali la Mheshimiwa Jerome Dismas Bwanausi, Mbunge wa Lulindi, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1999, Serikali iliamua kuvibadilisha baadhi ya Vyuo Vya Ualimu kuwa shule za sekondari, Ndwika kikiwa kimojawapo. Uamuzi huo ulifikiwa baada ya utafiti uliofanyika kubaini kuwa vyuo hivi vilikuwa na uwezo mdogo wa kudahili wanachuo kiasi cha kutokuwa na tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na uamuzi huo wa Serikali Chuo cha Ualimu Ndwika kilibadilishwa na kuwa na shule ya sekondari ya wasichana ya bweni kutokana na mahitaji makubwa ya shule za bweni kwa wasichana. Aidha, uamuzi huo ulitokana na changamoto mbalimbali yanayopata wanafunzi wa kike zikiwemo umbali mrefu wa kwenda shule na kurudi nyumbani, baadhi ya jamii ya kutowapa fursa ya kwenda shule na pia vishawishi mbalimbali vinavyopelekea kupata mimba wakiwa masomoni. Hivyo, shule hii ina umuhimu mkubwa katika kumkomboa mwanafunzi wa kike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina jumla ya Vyuo vya Ualimu 35 ambavyo vimekuwa vikidahili wanachuo kutoka nchi nzima. Kuanzia mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali imefanyia upanuzi na ukarabati mkubwa vyuo 24; na katika mwaka wa fedha 2014/2019 vyuo vingine kumi vitapanuliwa kwa lengo la kuongeza nafasi za udahili hivyo kutosheleza mahitaji ya Walimu. Kwa hiyo Serikali itaendelea kuyatumia majengo ya kilichokuwa Chuo cha Ualimu Ndwika kutoa elimu ya sekondari kama ilivyo sasa.
Mhehsimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI imelipa madeni ya Walimu 86,234 yenye jumla ya shilingi bilioni 33,804,082,905 katika kipindi cha mwaka wa 2015/2016 na 2017/2018. Serikali kwa sasa inahakikisha kuwa hakuna madeni yatakayolimbikizwa kwa kulipa stahiki za Walimu kwa wakati.
MHE. JOESPH R. SELASINI (K.n.y. MHE. PASCAL Y. HAONGA) aliuliza:-
Shule za Watu Binafsi zinatoa huduma ya elimu kama zilivyo Shule za Umma, lakini kwa muda mrefu zimekuwa zikikabiliwa na changamoto nyingi sana ikiwa ni pamoja na kodi ya majengo (property tax), tozo ya fire, kodi ya ardhi na kodi nyinginezo:-
(a) Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuondoa baadhi ya kodi zisizokuwa na tija ambazo zimekuwa kero kwa shule za watu binafsi?
(b) Je, Serikali haioni ni wakati sasa wa kuzipatia ruzuku shule binafsi kwa sababu zinashirikiana na Serikali kupunguza tatizo la ajira?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Pascal Yohana Hasunga, Mbunge wa Mbozi, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua na kuthamini mchango wa sekta binafsi katika maendeleo ya elimu nchini ambapo hadi sasa jumla ya shule za msingi 1,432 kati ya shule 17,583 zinamilikiwa na sekta binafsi. Aidha jumla ya shule za sekondari 1,250 kati ya shule 4,885 zinamilikiwa na sekta binafsi. Vilevile kati ya vyuo vikuu 34, vyuo 22 vinamilikiwa na sekta binafsi. Kwa mchanganuo huo ni dhahiri kuwa sekta binafsi ina mchango mkubwa katika kuongeza fursa na ubora wa elimu nchini.
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikishirikiana na wamiliki wa shule binafsi kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo kodi na tozo. Katika kutatua changamoto hizo hadi kufikia sasa Serikali imeweza kuondoa tozo ya uendelezaji ujuzi (Skills Development Levy-SDL) tozo ya zimamoto, kodi ya mabango na tozo ya usalama mahali pa kazi (OSHA).
Mheshimiwa Spika, hii ikiwa ni hatua ya Serikali kuhakikisha kuwa sekta binafsi inakuwa na mazingira rafiki na wezeshi katika kuwaletea Watanzania maendeleo. Hivyo, Serikali kwa kushirikiana na umoja wa wamiliki wa shule binafsi itaendelea kujadiliana na kutatua changamoto zinawakabili ili kuvutia uwekezaji katika sekta ya elimu nchini.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kuzipatia ruzuku shule binafsi, Serikali itaendela kuboresha mazingira ya Taasisi za Fedha ili sekta binafsi iweze kupata mitaji kwa gharama nafuu huku Serikali ikiendelea kupunguza changamoto zilizopo katika shule za umma.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA aliuliza:-
Chuo cha Maendeleo ya Wananchi - Gera ni muhimu katika kuchochea maendeleo:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha utendaji wa chuo hicho?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Dkt. Diodorus Buberwa Kamala, Mbunge wa Nkenge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs) vilihamishwa kutoka iliyokuwa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto katika mwaka wa fedha 2016/2017 kuja Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Kufuatia uhamishio huo Wizara ilitoa kandarasi kwa vyuo vitatu ambavyo ni Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam, Chuo cha Ufundi Arusha na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya kwa ajili ya kufanya uchambuzi wa kina wa hali halisi ya miundombinu na vifaa vya kujifunzia na kufundishia katika Vyuo vyetu vya Maendeleo ya Wananchi kabla ya kuanza taratibu za kuvifanyia ukarabati ikiwemo Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Gera. Vilevile Wizara inaendelea kufanya tathmini ya rasilimali watu kwa vyuo vyote kwa lengo la kujua hali halisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya tathmini kuhusu hali ya vyuo hivyo, Wizara itabaini mahitaji ya wafanyakazi, miundombinu, vitendea kazi na vifaa vya kufundishia na kujifunzia ili kuvipatia ufumbuzi kwa lengo la kuboresha utendaji kazi wa vyuo hivyo kikiwemo Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Gera.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uboreshaji utakaofanyika utalenga kuimarisha utoaji wa mafunzo ya ufundi stadi kwa fani zilizopo kwa sasa. Aidha, fani na stadi nyinigne mpya tofauti na za sasa zitaanza kutolewa katika vyuo hivyo kulingana na mahitaji ya soko la ajira na mahitaji ya jamii husika.
MHE. RASHID A. SHANGAZI (K.n.y. MHE. ESTER M. MMASI) aliuliza:-
Baadhi ya vyuo vikuu nchini vimekuwa na utamaduni wa kutozingatia miongozo ya Serikali Kuu katika kuongoza na kusimamia vyuo vikuu nchini na hata kupeleka kupuuzwa kwa stahiki za wafanyakazi wa elimu ya juu kwa kisingizio cha elimu ya juu inajiongoza na kujisimamia yenyewe chini ya University Charter:-
Je, ni nini kauli ya Serikali katika hili?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ester Michael Mmasi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, uendeshaji na usimamizi wa elimu ya juu nchini unasimamiwa na Sheria ya Vyuo Vikuu, Sura 346 na Kanuni zake za mwaka 2013. Kupitia sheria hiyo, vyuo vikuu vyote nchini vinaelekezwa kuweka mifumo ya usimamizi wa vyuo na kuunda Mabaraza na Kamati za Kitaaluma ili kuhakikisha kuwa usimamizi wa taaluma vyuoni unaenda sambamba na ubora unaotarajiwa. Hivyo, hakuna chuo chenye Hati Idhini (University Charter) ambayo inatekelezwa kinyume na sheria hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, napenda ifahamike kwamba msimamizi mkuu wa Sheria ya Vyuo Vikuu ni Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) ambayo imepewa jukumu kisheria kusimamia ithibati na udhibiti ubora wa elimu ya juu nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia TCU imekuwa na utaratibu wa kufanya ukaguzi wa vyuo vikuu mara kwa mara ili kuona kama vinazingatia sheria, taratibu, kanuni na miongozo ya uendeshaji kulingana na madhumuni ya uanzishwaji wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, TCU imetoa Miongozo ya Ajira kwa Wafanyakazi wa Vyuo Vikuu nchini yaani Minimum Guidelines For Employment, Staff Performance Review and Career Development, 2014 ambayo inatoa dira kuhusu ajira (recruitment), upandaji vyeo (promotion) na uwiano wa kazi (workload) ambazo waajiri wa vyuo vikuu wanatakiwa kuzingatia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande mwingine chuo kikuu kinapobainika kukiuka sheria, taratibu, kanuni na miongozo iliyopo, hatua za kinidhamu zimekuwa zikichukuliwa mara moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na sheria hii, ajira katika vyuo vikuu husimamiwa pia na sheria nyingine zinazohusu kazi na ajira hapa nchini. Hivyo, kama kuna malalamiko yoyote kuhusu watumishi kutopatiwa haki zao za ajira katika baadhi ya vyuo vikuu yawasilishwe Serikalini kwa ajili ya kufanyiwa kazi.
MHE. EDWIN M. SANNDA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatekeleza Sera ya Elimu Bure kwa kidato cha tano na sita ambalo ndilo kundi pekee lililobaki kugharamiwa na Serikali?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekonolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Edwin Mgante Sannda, Mbunge wa Kondoa Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeweka kipuambele cha kuhakikisha fursa sawa ya kupata elimu kwa ngazi ya elimu ya awali, msingi na sekondari, kidato cha kwanza hadi cha nne kwa sababu hii ndiyo ngazo ya elimu ambayo humpatia mhusika study za msingi za kuweza kukabiliana na mazingira yake. Dhana ya elimu bila malipo inazingatia uendeshaji wa shule bila ada wala michango ya aina yoyote ya lazima kutoka kwa wazazi au walezi wa wanafunzi na hivyo kuondoa vikwazo vya uandikishaji na mahudhurio ya watoto shuleni.
Mheshimiwa Naibu Spika, chini ya mpango huu, Serikali inafidia gharama za uendeshaji wa shule ambapo hupeleka fedha moja kwa moja shuleni kama fidia ya ada, chakula cha wanafunzi na fedha za ruzuku ya uendeshaji wa shule (capitation grants). Jumla ya fedha ya kugharamia elimu bila malipo inayotolewa na Serikali kila mwezi kwa ajili ya shule za msingi na sekondari ni shilingi 20,805,414,286.14. Katika hizo, shilingi 5,459,265,929 ni kwa ajili ya shule za msingi na shilingi 10,054,298,857 ni kwa ajili ya shule za sekondari; na shilingi 5,091,850,000 ni posho ya madaraka ya Maafisa Elimu Kata, Walimu Wakuu na Wakuu wa Shule. Serikali pia hupeleka fedha kiasi cha shilingi 6,005,374,781 kwa ajili ya chakula cha wanafunzi wa bweni wa shule za sekondari.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango wa Elimu Bila Malipo umeonesha mafanikio makubwa tangu ulipoanza mwaka 2016. Mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na uandikishaji na uimarishaji wa mahudhurio ya wanafunzi darasani, kwa mfano, watoto wa darasa la awali walioandikishwa wameongezeka kutoka wanafunzi 1,015,030 mwaka mwaka 2015 hadi wananfunzi 1,320,574 mwaka 2017 sawa na ongezeko la watoto 300,544, yaani ongezeko la asilimia 30.
Mheshimiwa Naibu Spika, idadi ya wanafunzi wa darasa la kwanza walioandikishwa imeongezeka kutoa wanafunzi 1,028,021 mwaka 2015 hadi wanafunzi 1,896,584 mwaka 2017 sawa na ongezeko la wanafunzi 868,563 ambalo ni ongezeko la asilimia 84.48.
Aidha, udahili wa wanafunzi wa kidato cha kwanza umeongezeka kutoka wanafunzi 451,392 mwaka 2015 hadi wanafunzi 554,400 mwaka 2017. Hili ni ongezeko la wanafunzi 103,000 ambalo ni sawa na asilimia 22.82. Hali hii imetokana na mwitikio chanya wa wazazi na jamii kuhusu elimu bila malipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na mafanikio ya Mpango wa Elimu Bila Malipo, Serikali inafanya jitihada za kukabiliana na changamoto zilizojitokeza kama vile mahitaji makubwa ya vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo, maabara, madawati, walimu, vifaa vya kufundishia na kujifunzia pamoja na TEHAMA. Aidha, Serikali inaendelea kufanya ukarabati wa majengo ya shule yaliyochakaa. Lengo ni kuhakikisha kuwa elimu inatolewa kwa ubora unaotakiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba kwa sasa Serikali haijaandaa Mpango wa Elimu Bila Malipo kwa ngazi ya elimu ya kidato cha tano na sita bali inaelekeza jitihada zake za kuboresha miundombinu na ubora wa elimu kwa ngazi zote za elimu ikiwemo elimu ya kidato cha tano na sita.
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI aliuliza:-
Wilaya ya Lushoto haina Chuo cha Ufundi (VETA) na kuna vijana wengi waliohitimu elimu ya msingi na sekondari:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga Chuo cha Ufundi (VETA) ili vijana hao waweze kupata elimu ya ufundi ya kuwasaidia katika kujiajiri?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Shaabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi kwa ajili ya kuandaa rasilimali watu watakaotumika katika viwanda ili kufikia lengo la Serikali kuwa na uchumi wa kati unaotegemea viwanda ifikapo mwaka 2025. Vyuo hivi vitasaidia kuwaandaa vijana kwa kuwapatia ujuzi utakaowawezesha kujiajiri na kuajiriwa ikizingatiwa kuwa kundi kubwa la vijana wetu halipati fursa ya kuendelea na masomo ya elimu ya juu.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na mpango wake wa ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi vya Mikoa na Wilaya ikiwemo Lushoto kutegemeana na upatikanaji wa fedha. Lengo ni kila Mkoa na Wilaya kuwa na Chuo cha Ufundi Stadi.
Mheshimiwa Spika, aidha, pamoja na ujenzi wa vyuo hivyo, Wizara itaendelea na utekelezaji wa Mradi wa Kukuza Stadi za Kazi (Education and Skills for Productive Jobs – ESPJ) ambapo katika mradi huu Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vitakarabatiwa ili kuongeza fursa za mafunzo ya ufundi stadi sambamba na elimu ya wananchi. Hivyo, katika kipindi hiki ambacho Serikali inaendelea na jitihada hizi, nashauri wananchi wa mikoa na wilaya zote ambazo hazijawa na vyuo vya VETA kutumia vyuo vya ufundi vilivyopo nchini hususan kwenye mikoa na wilaya jirani ili vijana wetu wapate ujuzi na stadi hizi muhimu kwa maendeleo yao na nchi kwa ujumla.
MHE. JORAM I. HONGOLI aliuliza:-
Je, kwa nini Serikali isiingize kwenye mitaala ya elimu somo la umuhimu wa kulipa kodi ili lifundishwe kuanzia shule ya msingi ili wananchi wapate uelewa wa kodi na waweze kufurahia kulipa kodi kama ilivyo kwa nchi zilizoendelea?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joram Ismael Hongoli, Mbunge wa Lupembe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa elimu ya mlipa kodi katika kumjengea mwananchi tabia, mwenendo na mazoea ya kulipa kodi kwa maendeleo ya Taifa letu. Wizara yangu kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania ndiyo yenye jukumu la kubuni, kuandaa na kuboresha mitaala ya elimu ya awali, msingi, sekondari na vyuo vya ualimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeona umuhimu wa kuingiza elimu ya mlipa kodi kwenye mitaala ya elimu nchini ili kuwajengea Watanzania tabia, mwenendo na mazoea ya kuwa na utamaduni wa kulipa kodi. Katika somo la uraia na maadili kuanzia darasa la III na kuendelea, mtaala umelenga kumjengea na kumuandaa mwanafunzi kuwa mwajibikaji katika kutekeleza majukumu ya kila siku, kuiheshimu na kuithamini jamii yake na kuwa mwadilifu na mzalendo ikiwa ni pamoja na kutekeleza majukumu ya kitaifa ikiwemo kulipa kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kutokana na umuhimu wa kuwajengea vijana tabia kuhusu elimu ya mlipa kodi, Serikali kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania kwa kushirikisha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) itaendelea kuboresha elimu hii ili isisitizwe na kuwekewa mkazo katika mitaala ya elimu kuanzia elimu ya msingi.
MHE. ESTHER A. MAHAWE aliuliza:-
Sera ya Elimu ya mwaka 2014 inaelekeza utoaji wa elimu bila malipo kuanzia ngazi ya chekechea hadi kidato cha nne ikiwemo kuondoa gharama za kulipia mitihani ya kitaifa katika shule za msingi na sekondari lakini wanafunzi wanaosoma katika shule zisizo za Serikali wanalipishwa gharama hizo wakati wazazi wao wanalipa kodi inayowezesha kutolewa elimu hiyo bila malipo:-
Je, ni lini Serikali itafuta ada hiyo ya mitihani kwa wanafunzi wanaosoma katika shule binafsi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajibu swali, naomba nitambue kwamba Mheshimiwa Esther Alexander Mahawe ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wamiliki wa Shule Binafsi Nchini. Lazima tu niseme kwamba katika kipindi cha uongozi wake Serikali imenufaika na ushirikiano mkubwa ambao umefanya Serikali iweze kuwahudumia sekta binafsi katika elimu, tunamshukuru sana Mheshimiwa Esther Mahawe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba sasa kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, nijibu swali la Mheshimiwa Esther Alexander Mahawe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa sekta binafsi katika utoaji wa elimu nchini. Aidha, ili kuhakikisha mazingira rafiki katika utoaji wa elimu, Serikali imekuwa ikifanya majadiliano na sekta binafsi kwa lengo la kuondoa changamoto zinazowakabili. Hadi sasa Serikali imeweza kuondoa baadhi ya kodi na tozo mbalimbali ambazo awali walikuwa wakitozwa mawiliki wa shule binafsi. Mfano wa kodi hizo ni Kodi ya Mabango, Kodi ya Kuendeleza Ufundi Stadi (Skills Development Levy), tozo ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi (OSHA) pamoja na tozo ya zimamoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utekelezaji wa Mpango wa Elimu bila Malipo, Serikali ilifuta ada na michango ya lazima katika shule za umma ngazi ya elimumsingi yaani elimu ya awali hadi kidato cha nne. Ada na michango hiyo iliyokuwa ikilipwa na wazazi au walezi kwa sasa hugharamiwa na Serikali. Mpango huu haukuzihusu shule binafsi pamoja na shule za umma ngazi za kidato cha tano na sita. Hivyo, shule hizo zitaendelea na utaratibu wa wazazi kuchangia gharama za uendeshaji wa elimu ikiwemo kulipa ada za mitihani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya utoaji elimu nchini kadiri uwezo wa kifedha utakavyoruhusu. (Makofi)
MHE. HAWA A. GHASIA (K.n.y MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA) aliuliza:-
Wadhibiti wa Ubora wa Elimu ngazi ya Wilaya wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo uhaba wa vitendea kazi.
• Je, Serikali ina mkakati gani wa kushughulikia changamoto za ofisi hizo ili ziweze kutekeleza majukumu yao?
• Je, ni lini Wizara itapeleka Wadhibiti Ubora wa Elimu katika Halmashauri ya Mji wa Nanyamba badala ya kutegemea wale wa Halmashauri ya Mtwara?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota, Mbunge wa Nanyamba lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa Idara ya Udhibiti Ubora wa Shule kama chombo cha udhibiti wa ubora wa elimu. Kutokana na ongezeko la Halmashauri na Wilaya mpya nchini, kumekuwepo na changamoto mbalimbali katika idara hii ikiwemo upungufu wa Wadhibiti Ubora wa Shule, ofisi na vitendea kazi kama vile magari. Ili kukabiliana na changamoto hizo, Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo ununuzi wa magari, ujenzi na ukarabati wa ofisi pamoja na kuongeza idadi ya wadhibiti ubora wa shule.
Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali imehuisha mfumo wa udhibiti ubora wa shule ambapo kiunzi cha udhibiti ubora wa elimu kimeandaliwa kwa lengo la kuwajengea uwezo wadau mbalimbali wa elimu ili washiriki kikamilifu katika kusimamia ubora wa elimu. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa idara ya udhibiti ubora wa shule inajengewa uwezo ili itimize majukumu yake kikamilifu.
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Nanyamba ni miongoni mwa Halmashauri ambazo hazijafunguliwa ofisi ya udhibiti ubora wa shule. Katika kukabiliana na hii, Serikali imepanga kuanzisha huduma ya udhibiti ubora wa shule katika Halmashauri zote nchini ambazo hazijafunguliwa ofisi, ikiwemo Nanyamba pindi zoezi la kuongeza Wadhibiti Ubora wa Shule litakapokamilika.
Mheshimiwa Spika, aidha, nasisitiza kuwa Wadhibiti Ubora wa Shule waliopo katika Halmashauri mama waendelee kudhibiti ubora wa shule katika Halmashauri hizo mpya wakati Serikali inaendelea na utaratibu wa kuanzisha huduma hii katika Halmashauri hizo. (Makofi)
MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza:-
Tatizo la ada kwa wanafunzi katika shule binafsi nchini linazidi kuongezeka siku hadi siku. Mwanafunzi wa darasa la kawaida katika baadhi ya shule analipa mpaka shilingi milioni tatu hali inayosababisha wazazi wengine kuwapeleka watoto wao katika nchi jirani za Kenya na Uganda ili kutafuta nafuu ya ada:-
Je, kwa nini Serikali isikae na wadau husika ili kupanga ada elekezi kwa wenye shule binafsi?
NAIBU WAZIRI WA WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nasoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua na kuthamini mchango wa sekta binafsi katika maendeleo ya elimu nchini ambapo hadi sasa jumla ya shule za msingi 1,432 kati ya shule 17,583 zinamilikiwa na sekta binafsi. Aidha, jumla ya shule za sekondari 1,250 kati ya shule 4,885 zinamilikiwa na sekta binafsi. Serikali inatambua utofauti wa viwango vya ada kati ya shule za umma na shule binafsi. Vilevile Serikali inatambua utofauti wa viwango hivyo kati ya shule moja na nyingine za binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haitajihusisha na upangaji wa ada kwa shule binafsi bali itaendelea kusimamia viwango vya ubora, taratibu, kanuni na sheria za uendeshaji wa shule zote nchini. Lengo la Serikali ni kuhakikisha watoto wote wa Kitanzania wanapata elimu bora kwa manufaa yao na Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na tofauti ya viwango vya ada na huduma zitolewazo kwenye shule binafsi, nitoe ushauri kwa wazazi kuchagua shule kulingana na uwezo wao wa kulipa ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza kwa watoto na hata kwa wamiliki wa shule hizo.
MHE. FATMA H. TOUFIQ aliuliza:-
Imebainika kuwa baadhi ya Madereva wa bodaboda wamekuwa wakifanya ukatili kwa kufanya ubakaji, ulawiti na kuwapa baadhi ya wanafunzi mimba:-
a) Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti hali hii hasa kwa wale bodaboda wanaowahadaa baadhi ya wanafunzi wa kike?
b) Je, ni wanafunzi wangapi walioripotiwa kupewa mimba na waendesha bodaboda katika kipindi cha miaka mitatu (3) iliyopita?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kuwa kuna wanaume wanaojihusisha na vitendo vya ubakaji, ulawiti na kuwapa mimba baadhi ya wanafunzi. Baadhi ya Madereva wa bodaboda wameripotiwa kujihusisha na vitendo hivyo viovu, vitendo hivyo hutokana na tabia mbaya, vishawishi na changamoto za mazingira kama vile umbali kutoka nyumbani kwenda mashuleni kwa wanafunzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kukabiliana na vitendo hivyo mwaka 2016 Serikali ilifanya Marekebisho ya Sheria ya Elimu Na. 25 ya Mwaka 1978 ambapo mtu atakayepatikana na hatia ya kumpa mimba mwanafunzi akihukumiwa hufungwa miaka 30. Aidha, Sheria ya Kanuni za Adhabu, Sura 16 inabainisha Hukumu ya kifungo cha maisha kwa mtu atakayetenda kosa la kubaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na sheria hizo Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kudhibiti vitendo hivyo kwa kutoa huduma za ushauri na unasihi ambapo shule zimeelekezwa kuwa na Walimu washauri wa kike na kiume. Hivyo, mwongozo wa ushauri na unasihi shuleni na vyuoni umeandaliwa. Vilevile Serikali kwa kushirikiana na wadau inaendelea na ujenzi wa mabweni, hostel na shule katika maeneo ambayo wanafunzi wanalazimika kutembea umbali mrefu.
Mheshimiwa Naibu Spika, wanafunzi hupewa mimba na wanaume mbalimbali, wanaweza kuwa ni wakulima, wafugaji, wafanyakazi au wafanyabiashara wakiwemo Madereva bodaboda. Hata hivyo takwimu za wanafunzi waliyopata mimba hazikokotolewi kwa kuanisha makundi ya wanaume waliowapa ujauzito. Hivyo ni vigumu kupata idadi ya wanafunzi waliyopewa mimba na madereva wa bodaboda.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA aliuliza:-
Serikali iliweka Wilaya ya Mkinga kuwa miongoni mwa Wilaya za kipaumbele kujengewa Chuo cha VETA.
Je, ni lini sasa Serikali itatekeleza ahadi ya kujenga Chuo cha VETA Wilayani Mkinga?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajibu swali naomba kama itakupendeza, kupitia Bunge lako tukufu niwapongeze na kuwatakia kila la kheri vijana wetu 960,202 wanaofanya mitihani ya darasa la saba leo kwenye shule tofauti 16,845. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dunstan Luka Kitandula, Mbunge wa Mkinga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi kwa ajili ya kuandaa rasilimaliwatu watakaotumika katika viwanda na shughuli nyingine za uzalishaji, hasa wakati huu ambapo Serikali imeazimia kufanya nchi yetu kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Vyuo hivi vitasaidia kuwaandaa vijana ili waweze kujipatia ajira kwa kujiajiri au kuajiriwa ikizingatiwa kuwa kundi kubwa la vijana wetu halipati fursa ya kuendelea na masomo ya elimu ya juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na mpango wake wa ujenzi waVyuo vya Ufundi Stadi vya Mikoa na Wilaya, ikiwemo Wilaya ya Mkinga, kutegemeana na upatikanaji wa fedha. Lengo ni kila Mkoa na Wilaya kuwa na Chuo cha Ufundi Stadi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Wizara inaendelea na utekelezaji wa Mradi wa Stadi za Kazi (Education and Skills for Productive Jobs – ESPJ) ambapo kupitia Mradi huu Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC’s) vitakarabatiwa ili kuongeza fursa za mafunzo. Hivyo, katika kipindi hiki ambacho Serikali inaendelea na jitihada hizi, nashauri wananchi wa mikoa na wilaya zote ambazo hazijawa na Vyuo vya VETA kutumia Vyuo vya Ufundi vilivyopo nchini, hususan kwenye mikoa na wilaya jirani ili vijana wetu waweze kupata ujuzi na stadi muhimu kwa maendeleo ya nchi kwa ujumla.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO aliuliza:-
Vitabu ni nyenzo muhimu sana ya kujifunzia lakini kwa muda mrefu sasa wanafunzi hawana vitabu vya kiada:-
Je, Serikali inawaambia nini Walimu na Wanafunzi wa Shule za Msingi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Susan Anselm Lyimo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa vitabu vya kiada kama nyenzo muhimu katika utoaji wa elimu. Kwa umuhimuhuu, Serikali inafanya kila liwezekanalo kuhakikisha wanafunzi wa shule za msingi hawakosi vitabu hivyo. Katika kuhakikisha hilo, Serikali kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 imechapisha jumla ya nakala 10,232,812 za vitabu vya kiada vya darasa la I-III na kuvisambaza katika mikoa yote ya Tanzania Bara. Jumla ya mahitaji ya vitabu vya darasa la nne nchini kote ni vitabu 6,700,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tayari imechapa nakala zote za vitabu vya kiada kwa darasa la IV. Kati ya vitabu hivi jumla ya nakala 4 000,000 vimesambazwa. Vitabu hivi vinaenda kugawiwa kwa uwiano 1:1 yaani kitabu kimoja mwanafunzi mmoja. Serikali inakamilisha zoezi la usambazaji katika Mikoa ya Tanga, Morogoro, Mbeya, Iringa na Ruvuma ambayo ilibaki kupokea nakala za kitabu kimoja kukamilisha idadi ya vitabu sita vinavyohitajika. Zoezi hili litakamilika ifikapo tarehe 15 Septemba, 2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pia imezingatia mahitaji ya Walimu kwa kuchapa na kusambaza vitabu vya kiongozi cha Mwalimu darasa la nne ambapo, jumla ya nakala 190,036 vimechapwa na kusambazwa shuleni. Kwa sasa Serikali inaendelea na uchapaji wa jumla ya nakala 9,000 za vitabu vyote darasa la I-IV kwa ajili ya wanafunzi wenye uono hafifu na nakala 14,000 ya vitabu vya nukta nundu kwa wanafunzi wasioona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utekelezaji wa mikakati ya kuboresha elimu, Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa vitabu vyote vinapatikana ili watoto wote wa Kitanzania wapate elimu iliyo bora.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO aliuliza:-
Sera ya elimu ya mwaka 2014 inatambua elimu ya msingi kuwa ya lazima bila malipo.
Je, Serikali inaweza kuliambia Bunge hili na Taifa kwa ujumla ni lini ulazima huu utatekelezwa kwa vitendo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza naomba vilevile nipokee pole za Mheshimiwa Mbunge na nitazifikisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, lakini Wizara vilevile imezipokea.
Mheshimiwa Mweyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Susan Anselm Jerome Lyimo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeweka utaratibu wa elimu ya msingi kuwa ya lazima na kuweka kipaumbele cha kuhakikisha kuwa kuna fursa sawa ya kupata elimu kwa ngazi hii yaani elimu ya awali, msingi na sekondari hadi kidato cha nne. Kwa sababu hii ndiyo ngazi ya elimu ambayo humpatia mhusika stadi za msingi za kuweza kukabiliana na mazingira yake. Dhana ya elimu bila malipo inazingatia uendeshaji wa shule bila ada wala michango ya aina yoyote ya lazima kutoka kwa wazazi au walezi wa wanafunzi na hivyo kuondoa vikwazo vya uandikishaji na mahudhurio ya watoto shuleni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kwa sasa utekelezaji wa elimu ya msingi ya lazima ni kwa muda wa miaka saba kama inavyoelekeza Sheria ya Elimu iliyopo yaani Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 Sura ya 353.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kutekeleza mpango wa elimu msingi kuwa ya lazima kwa vitendo tangu mwaka 2015/2016 kwa kufidia gharama za uendeshaji wa shule za umma ambapo hupeleka fedha moja kwa moja shuleni kama fidia ya ada, na fedha za rukuzu ya uendeshaji wa shule yaani capitations grands. Serikali pia hupeleka fedha kwa ajili ya chakula cha wanafunzi wa bweni wa shule za sekondari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na mpango huo mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na ongezeko la uandikishaji na kuimarika kwa mahudhurio ya wanafunzi darasani. Aidha Serikali inafanya jitihada za kukabiliana na changamoto zilizojitokeza kama vile mahitaji ya vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo, maabara, madawati, walimu, vifaa vya kufundishia na kujifunzia na kuhakikisha kuwa elimu inatolewa kwa ubora unaotakiwa.
MHE. SELEMANI S. BUNGARA aliuliza:-
Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kilwa kina upungufu mkubwa wa vitanda na hata vichache vilivyopo vimechakaa sana kwani vilinunuliwa tangu mwaka 1969. Mahitaji halisi ya vitanda vinavyohitajika chuoni hapo ni zaidi ya vitanda 50 (double decker):-
Je, Serikali imetenga kiasi gani cha fedha kwa ajili ya ununuzi wa vitanda pamoja na samani nyingine chuoni hapo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Selemani Said Bungara, Mbunge wa Kilwa Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC) kwa ajili ya kuandaa rasilimali watu watakaotumika katika viwanda ili kufikia lengo la Serikali la kuwa na uchumi wa kati unaotegemea viwanda ifikapo mwaka 2025. Vyuo hivi vitasaidia kuongeza fursa ya mafunzo ya ufundi stadi sambamba na elimu ya wananchi (folk education). Aidha, vitasaidia kuwaandaa vijana kwa kuwapatia ujuzi utakaowawezesha kujiajiri na kuajiriwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu wa vyuo hivyo, Serikali imetoa kandarasi kwa vyuo vitatu ambavyo ni Taasisi ya Teknolojia Dar-es-Salaam, Chuo cha Ufundi Arusha na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya ili vifanye uchambuzi wa kina wa hali halisi ya miundombinu, vifaa vya kujifunzia na kufundishia, pamoja na samani katika Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi kikiwemo Chuo cha Maendeleo cha Wananchi Kilwa Masoko. Taratibu za ukarabati zitaanza baada ya kukamilika kwa zoezi hili. Aidha, Wizara inafanya zoezi la kubaini mahitaji ya watumishi katika Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi, zoezi linalotarajiwa kukamilika Julai, 2018.
MHE. OMARI M. KIGUA aliuliza:-
Serikali ya Awamu ya Tano inatoa elimu bure hali iliyosababisha wananchi wengi kupeleka watoto wao shule, huku ufaulu wa wanafunzi kuingia kidato cha tano ukiongezeka:-
Je, Serikali haioni umuhimu wa kila wilaya kuwa na Shule za Kidato cha Tano na Sita kuwa ni wa lazima hasa ikizingatiwa kuwa kuna baadhi ya wilaya hazina shule hizo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua, Mbunge wa Kilindi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kuongeza Shule za Kidato cha Tano na Sita na kuhakikisha zinakuwa kwa kila wilaya hasa wakati huu ambapo wahitimu wa Kidato cha Nne wameongezeka kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge. Hii ndiyo sababu ya Serikali kuelekeza kuwa na Shule za Sekondari za Kidato cha Tano na Sita kwa kila tarafa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa utaratibu huu, Wilaya/ Halmashauri inaweza kuwa na Shule za Kidato cha Tano na Sita zaidi ya moja kutegemea idadi ya tarafa zilizopo. Hivyo, inashauriwa wadau wa Wilaya/Halmashauri ambazo hazina Shule zenye Kidato cha Tano na Sita kushirikiana na Mkurugenzi wa Halmashauri husika kujenga shule au kuongeza miundombinu katika shule zilizopo na kufuata taratibu husika kusajili shule mpya iliyojengwa au kupata kibali cha kuanzisha kidato cha tano na sita katika shule zilizopo. Utekelezaji huo utasaidia kuondoa changamoto ya baadhi ya wanafunzi wenye sifa za kuendelea na masomo ya kidato cha tano kukosa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kukumbusha kwamba Shule za Sekondari za Kidato cha Tano na Sita ni za kitaifa, ambapo hudahili wanafunzi kutoka sehemu mbalimbali za nchi kulingana na tahasusi (combinations) za masomo zilizopo. Hivyo kwa sasa wahitimu wenye sifa kutoka wilaya zote nchini hupangwa katika shule hizo.
MHE. MARY D. MURO aliuliza:-
Uanzishaji wa Vyuo vya Ufundi ulilenga kuwapatia elimu ya vitendo hasa vijana wetu, lakini Chuo cha Ufundi Kibaha kilicho chini ya Shirika la Elimu Kibaha hakina vifaa wala miundombinu ya kujifunzia:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka vifaa pamoja na kufufua miundombinu katika chuo hicho?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mary Deo Muro, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inasimamia Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha kilichokuwa chini ya Shirika la Elimu Kibaha. Chuo hiki ni mojawapo ya vyuo 55 vilivyohamishiwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuanzia Mwaka wa Fedha 2016/2017. Vyuo hivi vina changamoto nyingi za uendeshaji ikiwemo; upungufu wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia na uchakavu wa majengo ya madarasa, karakana, mabweni, nyumba za watumishi na miundombinu.
Mheshimiwa Spika, kutokana na hali ya vyuo hivyo, Serikali imetoa Kandarasi kwa vyuo vitatu ambavyo ni Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam, Chuo cha Ufundi Arusha na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia, Mbeya ili vifanye uchambuzi wa kina wa hali halisi ya miundombinu na vifaa vya kujifunzia na kufundishia katika vyuo hivyo. Baada ya kukamilika kwa zoezi hili taratibu za kuvifanyia ukarabati zitaanza.
Mheshimiwa Spika, aidha, Wizara pia inafanya zoezi la kubaini mahitaji ya watumishi katika vyuo vyote vya FDC. Zoezi hili linatarajiwa kukamilika mwezi Julai, 2018. Baada ya zoezi hili kukamilika, ujenzi, ukarabati na ufungaji wa mitambo na vifaa vya kufundishia na kujifunzia utafanyika kulingana na mahitaji. Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha ni mojawapo ya vyuo vilivyo katika mpango huu.
MHE. HAMAD SALIM MAALIM - (K.n.y. MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED) aliuliza:-
Kwa kuwa huu ni wakati wa Sayansi na Teknolojia na vijana wetu wamekuwa wakizitafuta syllabus za Masomo mbalimbali madukani bila mafanikio:-
Je, Serikali haioni kuwa huu ni wakati muafaka wa kuziweka syllabus hizo mtandaoni?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Muhamed Amour Muhamed, Mbunge wa Bumbwini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inafanya kila jitihada kuhakikisha kuwa wadau wa elimu wanapata mahitaji yao ya Mitaala na Mihtasari kwa lengo la kufanikisha utoaji wa elimu nchini. Katika kuhakikisha hili, Wizara kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania, husambaza Mihtasari nchi nzima. Aidha, ili kukidhi mahitaji kwa wadau mbalimbali, Mihtasari imekuwa ikipatikana duka la TET na maduka ya vitabu nchini ambayo, wenye maduka ya vitabu huenda kununua kwenye duka la TET.
Mheshimiwa Spika, kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia nchini, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kupita TET, imeshaanza kuweka mihtasari kwenye mtandao wa Taasisi ya Elimu Tanzania ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa mihtasari hiyo. Baadhi ya mitaala na mihtasari ambayo tayari imewekwa kwenye mtandao wa Taasisi ya Elimu Tanzania ni Mitaala na Mihtasari ya Elimu ya awali, Msingi na Sekondari.
Mheshimiwa Spika, aidha, lengo la Wizara kwa sasa ni kuweka Mitaala na Mihtasari ya Masomo yote kwenye mtandao ili iwafikie walengwa kwa urahisi na kwa wakati. Wadau wote wa elimu wanashauriwa kutembelea Mtandao wa Taasisi ya Elimu Tanzania (http://www.tie.go.tz) ili waweze kuona na kupakua Mtaala na Mihtasari husika.
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI aliuliza:-
Katika bajeti ya mwaka 2017/2018, Serikali ilitenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha VETA katika Wilaya ya Namtumbo:-
(a) Je, gharama za ujenzi wa chuo hicho hadi kinakamilika ni kiasi gani?
(b) Je, ni lini ujenzi wa chuo hicho utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Eng. Edwin Amandus Ngonyani, Mbunge wa Namtumbo, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
• Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inategemea kukamilisha ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha VETA cha Wilaya ya Namtumbo kwa makadirio ya Sh.6,321,320,292.40.
• Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya ujenzi ilianza mwezi Machi, 2017 na inakadiriwa kuchukua muda wa miezi
18. Hivyo, ujenzi wa chuo hicho unategemewa kukamilika ifikapo Septemba, 2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kutambua umuhimu wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi, itaendelea na ujenzi wa vyuo hivyo kwa ajili ya kuandaa Rasilimali Watu watakaotumika katika viwanda ili kufikia lengo la Serikali kuwa na uchumi wa kati unaotegemea viwanda ifikapo mwaka 2025. Aidha, vyuo hivi vitasaidia kuwapatia vijana wetu ujuzi utakaowawezesha kujiajiri na kuajiriwa.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO aliuliza:-
Mwaka 2017 lilitolewa tamko la kukataza watoto wa shule wanaopata ujauzito kwa sababu yoyote ile kutoendelea na masomo.
Je, kwa katazo hilo, Serikali imejipangaje kuhakikisha kuwa zile sababu zilizo nje ya uwezo wa wanafunzi kuhimili zinapatiwa ufumbuzi haraka?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri, Elimu, Sayansi na Teknolojia naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susan Anselm Jerome Lyimo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua tatizo la wanafunzi wa shule kupata ujauzito wakiwa masomoni kwa sababu mbalimbali zikiwemo zile wasizoweza kuhimili, sababu hizo ni pamoja na kubakwa, kutembea umbali mrefu kufuata shule, na hivyo kupata vishawishi, mila na desturi potofu ambazo humlazimisha au kumuingiza mwanafunzi katika ndoa au mahusiano ya kimapenzi na kukosa mahitaji ya msingi kutoka kwa mzazi, mlezi hali ambayo humlazimisha mwanafunzi kujiingiza katika mahusiano ili aweze kupata mahitaji yake.
Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha sababu hizo zinapatiwa ufumbuzi kwa lengo la kumlinda mwanafunzi wa kike Serikali imetekeleza yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika, imefanya marekebisho katika Sheria ya Elimu Sura ya 353 Toleo la 2002 kupitia Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 2 ya mwaka 2016 ambayo imeongeza kifungu cha 60(a) ambacho kinatamka wazi kuwa mtu yeyote atakaye muweka ujauzito mtoto wa shule atafungwa miaka 30 au kwa kiingereza naomba ninukuu; “Any person who impregnates a primary school or secondary girl commits an offence and shall on conviction, be liable to imprisonment for a term 30 years.” Imeweka mkazo juu ya elimu ya afya ya uzazi na jinsia katika shule za msingi, sekondari na vyuo vya ualimu yaani unasihi ambayo kwa sasa Wizara imeandaa kiunzi kinachoitwa (guidance and counseling with services a guide for counselors and schools and teacher colleges) kwa ajili kutekeleza huduma hiyo.
Mheshimiwa Spika, pia imezifanya shule zote za sekondari za kidato cha tano na sita kuwa na mabweni hosteli kwa ajili ya wanafunzi wa kike; imehimiza ujenzi wa shule za sekondari kila Kata hasa kwenye maeneo yenye wanafunzi ili kupunguza wanafunzi wa kike kutembea umbali mrefu.
Pia Serikali imejenga hosteli katika baadhi ya shule za sekondai za kata kwenye maeneo ambayo wanafunzi wa kike wanalazimika kutembea umbali mrefu ili kufikia shule na kwenye maeneo ambayo kuna mila na desturi potofu ambazo umlazimisha au kumuingiza mwanafunzi katika ndoa au mahusiano ya kimapenzi.
Mheshimiwa Spika, mwanafunzi wa kike anayekatisha masomo anaweza kujiunga na masomo kupita mipango ya elimu inayotolewa na Taasisi elimu ya watu wazima na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) huandaa na kuendesha programu za elimu mbadala kwa vijana na watu wazima kulingana na mahitaji yao kama vile mafunzo ya muda mfupi na marefu ya ujasiriamali stadi za maisha, ufundi wa awali na programu za kimasomo cha kujiendelea kwa watu wazima ili waweze kuendesha maisha.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA (K.n.y. MHE. AIDA J. KNENAN) aliuliza:-
Kila mwaka kuna wanafunzi wanaoendelea na masomo (waliofaulu) na waliofeli wengi hubaki nyumbani kwa kukosa fedha na sifa za kuendelea na masomo:-
Je, Serikali ina utaratibu gani wa kuwasaidia wanaoshindwa kuendelea na masomo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenan, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mwaka Serikali huwapima wanafunzi kupitia Mitihani ya Taifa inayosimamiwa na Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) baada ya kumaliza elimu ya msingi na elimu ya sekondari, ambapo wale waliofaulu huendelea na masomo katika ngazi inayofuata. Kwa wanafunzi ambao hawakufaulu mitihani ya kidato cha nne na cha sita, wanaruhusiwa kufanya tena mitihani kama watahiniwa wa kujitegemea (Private Candidates).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima vipo vituo vinavyotoa masomo ya elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi, kwa kusoma masomo ya kidato cha kwanza na pili kwa mwaka mmoja na kufanya mtihani wa maarifa unaofahamika kama (Qualifying Test) na endapo mwanafunzi atafaulu ataruhusiwa kufanya mtihani wa kidato cha nne kama mtahiniwa binafsi. Katika programu hii, walengwa 10,420 wamesajiliwa katika mwaka 2017; kati yao 6,074 ni wanawake na 4,346 ni wanaume. Aidha, Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima huandaa na kuendesha programu za elimu mbadala kwa vijana na watu wazima kulingana na mahitaji yao. Programu hizo hutoa mafunzo ya muda mfupi na mrefu kama vile ujasiriamali, stadi za maisha, ufundi wa awali na programu za kisomo cha kujiendeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia VETA inatoa mafunzo ya ufundi stadi kulingana na mahitaji ya soko la ajira ambapo jumla ya wanachuo 35,000 wanahitimu kila mwaka katika vyuo 732 vilivyosajiliwa na VETA nchi nzima. Mafunzo wanayopata yanawasaidia wahitimu kuwa na stadi za kuwawezesha kuajiriwa au kujiajiri katika sekta rasmi na isiyo rasmi. Aidha, Serikali inaendelea kuviimarisha Vyuo 55 vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs) ili viweze kuongeza wigo wa kudahili wanafunzi katika nyanja mbalimbali za mafunzo na hivyo kutoa fursa zaidi kwa wanafunzi wanaoacha masomo kwenye mfumo rasmi wa elimu.
MHE. EDWIN M. SANNDA aliuliza:-

Halmashauri ya Mji wa Kondoa imepata eneo la iliyokuwa kambi ya ujenzi wa barabara ya Mela – Bonga pale Kolo kwa ajili ya uanzishwaji wa Chuo cha VETA:-

Je, ni lini Serikali itatekeleza azma hiyo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Edwin Mgante Sannda, Mbunge wa Kondoa Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi kwa ajili ya kuandaa rasilimali watu itakayotumika katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuimarisha uchumi wa viwanda. Hivyo, ujenzi na uboreshaji wa vituo vya mafunzo ya ufundi stadi unaendelea kupewa kipaumbele katika mipango ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na mpango wa ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi vya mikoa na wilaya kutegemeana na upatikanaji wa fedha. Lengo ni kila mkoa na wilaya kuwa na Chuo cha Ufundi Stadi. Aidha, Serikali kupitia Mradi wa Kukuza Stadi za Kazi (Education and Skills for Productive Jobs – ESPJ) inaendelea na ukarabati wa Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs) ikiwemo Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Munguri kilichopo Wilaya ya Kondoa ili kuongeza fursa na ubora wa mafunzo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na ombi la Mheshimiwa Mbunge, mwezi Aprili, 2018, Serikali ilipeleka wataalam wake katika Kambi ya Ujenzi wa Barabara ya Mela – Bonga iliyopo Kolo Wilayani Kondoa kwa lengo la kukutana na Halmashauri na kufanya ukaguzi wa awali wa eneo ili kuona kama miundombinu iliyopo inakidhi kuanzisha Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA). Kufuatia tathmini hiyo, ushauri ulitolewa kuwa majengo yaliyopo yanahitaji maboresho na ukarabati mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili majengo haya yaweze kukarabatiwa na kuanzisha Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), ni jukumu la Halmashauri husika kupitia vikao vyake kuandika barua ya kuomba Wizara kutumia majengo hayo. Hivyo, tunasubiri barua ya Halmashauri husika kuruhusu VETA kutumia miundombinu hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi hiki ambacho Serikali inaendelea na jitihada hizi, nashauri wananchi wa Wilaya ya Kondoa kuendelea kutumia Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Munguri.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA aliuliza:-

Je, kuna utafiti wowote uliofanyika ili kubaini kama adhabu ya kuchapa wanafunzi inaongeza kiwango cha elimu na ufaulu katika shule zetu nchini?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu Sayansi ya Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Athumani Katimba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, zipo tafiti mbalimbali za kielimu kuhusiana na matumizi ya viboko kama njia ya kurekebisha tabia na mwenendo wa mwanafunzi katika kudhibiti nidhamu shuleni. Hata hivyo tafiti hizo zimegawanyika katika makundi makubwa matatu ambayo ambapo zipo zinazokubaliana zinazokataa na zenye msimamo wa kati juu ya matumizi ya adhabu juu ya matumizi ya adhabu ya viboko kwa wanafunzi.

Mheshimiwa Spika, utafiti uliofanywa na Hamza Bakari na Mpoto Tanzania mwaka 2018 unakubaliana na matumizi ya adhabu ya viboko kama njia ya kudumisha nidhamu na hatimaye kuongeza ushiriki wa wanafunzi katika ujifunzaji.

Hata hivyo, tafiti zilizofanywa na Maria Jose Oganda na Kirrily Pells, 2015 (Ethiopia, India, Peru na Vietnam) na Josephine Invocavity, 2014 uliofanyika Tanzania zinasema adhabu ya viboko haina tija na husababisha madhara ya kisaikolojia na kimwili kwa wanafunzi. Aidha, tafiti zilizofanywa na Lomasontfo Dlamini na wenzake 2019 (Swaziland) na Yusuph Maulid Kambuga na wenzake, 2018 (Tanzania) zinasema adhabu ya viboko inaweza kutumika pamoja na njia nyingine ili kudhibiti nidhamu kwa wanafunzi kwa lengo la kuongeza kiwango cha ufaulu shuleni.

Mheshimiwa Spika, katika shule zetu adhabu ya viboko hutumika pale mwanafunzi anapofanya utovu wa nidhamu uliokithiri na hutolewa kwa utaratibu maalum. Kanuni ya 3(1) ya Sheria ya Elimu, Sura ya 353 Marejeo ya mwaka 2002, inasema kuwa adhabu ya viboko shuleni itatolewa iwapo patatokea utovu mkubwa wa nidhamu au kosa kubwa litakalofanywa ndani au nje ya shule ambalo litaishushia shule heshima. Aidha, Waraka wa Elimu Namba 24 wa mwaka 2002 unaelekeza kuwa adhabu ya viboko itatolewa na Mwalimu Mkuu au walioteuliwa kwa kuzingatia ukubwa wa kosa, jinsia, afya ya mtoto na isizidi viboko vinne kwa wakati mmoja. Hivyo Serikali itaendelea kusisitiza matumizi sahihi ya adhabu kwa wanafunzi ili kuleta tija katika ufundishaji na ujifunzaji.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO aliuliza:-

Je, ni fedha kiasi gani zilitumika kujenga mabweni ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yajulikanayo kama H.E Magufuli Hostel?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Susan A. Lyimo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:

Mheshimiwa Spika, mradi wa ujenzi wa mabweni ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yajulikanayo kama Hostel za Dkt. J. P. J. Magufuli ulianza rasmi tarehe 1 Julai, 2016 na mabweni hayo yalikamilika na kukabidhiwa rasmi tarehe 15 Aprili, 2017. Ujenzi huo ulifanywa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kama Mkandarasi na kusimamiwa na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Mheshimiwa Spika, mradi huu uligharimiwa na Serikali kwa kiasi cha shilingi bilioni kumi tu.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kukabiliana na ongezeko la wasichana wanaokatishwa shule kwa sababu ya mimba?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijua:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na ongezeko la wasichana wanaokatishwa shule kwa sababu za mimba, Serikali ilifanya marekebisho ya Sheria ya Elimu Namba 25 ya mwaka 78. Katika marekebisho hayo ya mwaka 2016, mtu yeyote atakayepatikana na hatia ya kumpa mimba mwanafunzi wa shule ya msingi au sekondari atahukumiwa kifungo cha miaka 30 jela.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuwepo kwa sheria hiyo, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kudhibiti ongezeko la mimba kwa wanafunzi, kama vile ujenzi wa mabweni, hosteli na shule katika maeneo ambayo wanafunzi wanalazimika kutembea umbali mrefu. Aidha, huduma za ushauri na unasihi hutolewa kwa wanafunzi ambapo mwongozo wa ushauri na unasihi umeandaliwa. Vilevile mafunzo mbalimbali juu ya stadi za maisha, elimu na afya na uzazi hutolewa kwa wanafunzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kudhibiti mimba kwa wanafunzi, ili kuhakikisha kuwa, wanafunzi wote wanakamilisha mzunguko wa elimu bila kikwazo.
MHE. BERNADETHA K. MUSHASHU aliuliza:-

Miundombinu ya Shule ya Sekondari Rugambwa ilijengwa mwaka 1964 na Sekondari ya Bukoba imejengwa mwaka 1939, hivyo imechakaa sana:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuzifanyia ukarabati shule hizo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bernadetha Kasabago Mushashu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuongeza fursa na kuhakikisha kuwa elimu inayotolewa ni bora, Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika shule na vyuo nchini. Hii ni pamoja na utekelezaji wa mpango wa ukarabati wa shule zote kongwe 88 na sekondari nchini ambapo hadi sasa shule 48 zipo katika hatua mbalimbali za ukarabati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shule ya Sekondari ya Bukoba ni moja kati ya shule zinazoendelea na ukarabati ambapo tayari kiasi cha Sh.1,481,701,194 kimetolewa. Aidha, Shule ya Sekondari Rugambwa ipo katika mpango wa ukarabati awamu ya pili ambao utafanyika katika mwaka huu unaoisha 2018/2019. Tathmini ya kupata gharama halisi za ukarabati (conditional survey) ilishafanyika chini ya usimamizi wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, hivyo ukarabati unatarajiwa kuanza tarehe 15 Aprili, 2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kufundisha na kujifunzia katika shule na vyuo nchini kadiri uwezo wa kifedha utakavyoruhusu.
MHE. JANETH M. MASABURI aliuliza:-

Nchi za China na Singapore zinefanikiwa kwa kiwango kikubwa kwa kuwekeza kwenye ujenzi wa Vyuo vya Ufundi:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kutenga bajeti ya kutosha ili kuwekeza kwenye Vyuo vya Ufundi ambavyo vitasaidia vijana wengi kupata ujuzi na kujiajiri?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Janeth Maurice Masaburi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa nchi kuwekeza katika elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi ili kufikia azma ya uchumi wa kati unaotegemea viwanda ifikapo mwaka 2025. Serikali inaendelea na mpango wa ujenzi wa Vyuo vya Ufundi Stadi vya mikoa mitano katika Mikoa ya Geita, Rukwa, Njombe, Simiyu na Kagera, pamoja na vyuo vya ufundi stadi vya wilaya 13. Aidha, kupitia mradi wa Education Skills for Productive Jobs (ESPJ) vyuo vyote 54 vya Maendeleo ya Wananchi vinakarabatiwa ambapo awamu ya kwanza vyuo 20 vitakarabatiwa na ukarabati upo katika hatua za umaliziaji. Vilevile kupitia mradi huu Chuo cha Ufundi wa Kati (Technical College) kitajengwa katika Mkoa wa Dodoma kuanzia Mwaka wa Fedha 2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kupitia mradi wa East African Skills for Transformation and Regional Intergration Project Serikali inatarajia kuzijengea uwezo taasisi za Chuo Cha Ufundi Arusha, Taasisi ya Teknolojia Dar-es-Salaam (DIT) tawi la Dar-es-Salaam na Mwanza, pamoja na Chuo Cha Taifa Cha Usafirishaji (NIT), ili kuwa vivutio vya umahiri katika sekta za nishati, teknolojia ya habari na mawasiliano, usafirishaji na uchakataji wa mazao ya ngozi. Serikali itaendelea kuwekeza katika elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi kadri uchumi utakavyoruhusu, ili kuongeza fursa na ubora wa elimu na mafunzo hayo nchini kwa lengo la kuleta tija zaidi na manufaa kwa Taifa.
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itapitia upya Sera ya Elimu kwa lengo la kuongeza tija na kuendana na mahitaji ya sasa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapitio au maboresho ya Sera hufanyika kwa vipindi tofauti kulingana na mahitaji ya wakati. Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 ni matokeo ya mapitio yia Sera ya Elimu ya mwaka 1995.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuanza utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, Serikali imebaini changamoto katika baadhi ya maeneo na mengine kuwa na upungufu katika utekelezaji wake. Hivyo, Serikali imeanza mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 kwa kufanya majadiliano na wadau/wataalam mbalimbali kwa lengo la kupata maoni yao na kuhakikisha ushirikishwaji wa makundi yote muhimu unafanyika ili Sera hiyo iweze kuendana na mahitaji ya sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchakato huu wa kupitia upya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 unaendelea na kwa wakati muafaka tutawashirikisha Waheshimiwa Wabunge.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO (K.n.y. MHE. CATHERINE N. RUGE) aliuza:-

Kumekuwa na idadi ndogo ya wasichana wanaodahiliwa katika vyuo vya elimu ya juu katika fani ya sayansi ikizingatiwa kuwa sasa tunaelekea katika uchumi wa viwanda:-

Je, ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha inaongeza idadi ya wasichana katika masomo ya sayansi kuanzia ngazi ya chini mpaka vyuo vikuu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Catherine Nyakao Ruge, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifutavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina dhamira ya kuhakiksha kuwa usawa wa kujinsia katika elimu na mafunzo unazingatiwa. Aidha, Serikali inatambua changamoto zinazosababisha wanafunzi wa kike kushindwa kumaliza mzunguko wa elimu na kupelekea kuwa na idadi ndogo ya wasichana wanaojiunga na ngazi nyingine za elimu hasa katika masomo ya sayansi na hisabati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukabiliana na hali hii, Serikali inatoa fursa zaidi kwa wasichana kwa kuongeza nafasi za udahili kwa kidato cha V-VI katika tahasusi za sayansi ambapo katika shule 141 zinazochukua wasichana wanaosoma tahasusi za sayansi, shule 85 ni za wasichana tu na 56 za mchanganyiko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hatua hizo, Serikali imeendelea na ujenzi wa mbweni na hosteli katika shule na vyuo hasa katika mazingira yenye changamoto ambapo wanafunzi wa kike hupewa kipaumbele kwenye mabweni na hosteli hizo. Vilevile ununuzi na usambazaji wa vifaa vya maabara pamoja na vitabu vya masomo ya sayansi umefanyika ambapo shule za sekondari 1,696 zimepata vifaa vya maabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wanafunzi wote ili wafikie malengo yao katika elimu. Aidha, nitumie fursa hii kuwataka wazazi na jamii kuachana na mila, desturi na mitazamo hasi dhidi ya watoto wa kike kwani ni kikwazo katika maendeleo yao na jamii kwa ujumla.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA aliuliza:-

Wilaya ya Ulanga ina Shule za Msingi zaidi ya 50 na Sekondari zaidi ya 17 lakini haina Chuo chochote ambacho Wanafunzi wanaomaliza masomo kwenye shule hizo wanaweza kujiunga:-

Je, Serikali inasema nini juu ya hali hiyo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Goodluck Asaph Mlinga, Mbunge wa Ulanga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa vyuo vya elimu na mafunzo katika kuandaa rasilimaliwatu itakayochangia katika kufikia azma ya Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali inatekeleza mpango wa kuboresha vyuo vilivyopo kwa kukarabati na kujenga miundombinu mipya pamoja na kuongeza vifaa vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia ili kuongeza nafasi za udahili na kuimarisha ubora wa elimu na mafunzo yatolewayo. Aidha, Serikali inatekeleza mpango wa ujenzi wa vyuo vya VETA za Mkoa na Wilaya kutegemeana na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Ulanga ni moja kati ya Wilaya zenye uhitaji mkubwa wa vyuo vya elimu na mafunzo. Wilaya ina chuo kimoja tu cha ufundi stadi cha Mtakatifu Francis kinachomilikiwa na sekta binafsi. Wakati Serikali inaendelea na jitihada zake za upanuzi na ujenzi wa vyuo, natoa wito kwa Wilaya zote zenye uhaba wa vyuo vya elimu na mafunzo kutumia vyuo vilivyopo nchini.
MHE. ALMAS A. MAIGE aliuliza:-

Waajiri wamekuwa wakilipa Tozo ya Maendeleo ya Ujuzi kwaWafanyakazi (SDL) ya asilimia 4.5 ya mshahara kwa kila mfanyakazi ambayo ililengwa kupelekwa VETA kwa lengo la kuendeleza ujuzi:-

(a) Je, ni asilimia ngapi ya tozo hiyo inapelekwa VETA?

(b) Je, nilini Serikali itarejesha VETA katika Ofisi ya Waziri Mkuu ili kuleta uwiano wa mantiki kuwa VETA inaendeleza ujuzi wa wafanyakazi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Spika,kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Almas Athuman Maige,lenge sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, Tozo ya Kuendeleza Ujuzi, (Skills Development Levy-SDL)ni kodi inayokusanywa na Mamlaka ya Mapato nchini chini ya Sheria ya Kodi ya Mapato na Sheria iliyoanzisha VETA, Sheria Na.1 ya mwaka 1994 iliyorejewa mwaka 2006. Mwajiri anayeajiri wafanyakazi wanne au zaidi anapaswa kulipa tozo hii ambayo ni asilimia 4.5 ya malipo ghafi. Kiwango cha SDL inayopokelewa VETAni theluthi moja ya pato la SDL ambayo ni asilimia 33 ya tozo hiyo.

(b) Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) ilianzishwa ili kuwezesha nguvu kazi kubwa nchini kupata stadi stahiki za ajira kulingana na mabadiliko ya mfuko wa kiuchumi, kisiasa na kijamii. Majukumu makuu matano (5)ya VETAni kusimamia, kuratibu, kugharimia, kutangaza na kutoa mafunzo ya ufundi stadi.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2006VETA ilihamishiwa katika iliyokuwa Wizara ya Elimuna Mafunzo ya Ufundi Stadi, kwa sasa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kulingana na mahitaji ya wakati huo. VETA hufanya shughuli zake kwa kufuata sera na mipango ya Serikali ya muda mrefu na mfupi ili kuhakikisha wakati wote kunakuwa na nguvu kazi za kutosha na yenye ujuzi stahiki kuchangia katika maendeleo ya kiuchumi.Kwa mantiki hiyo, suala la VETA kuwa Wizara gani, itategemea mahitaji ya Serikali kulingana na wakati husika.
MHE. NURU A. BAFADHILI aliuliza:-

Katika kipindi cha miaka ya 1970 wakati wanafunzi wakienda likizo walimu walikuwa wakienda katika vyuo mbalimbali vilivyokuwa jirani na wilaya zao ili kupewa mafunzo au kupigwa msasa (refresher courses) kiasi kwamba walimu walikuwa wanapata ari ya kufundisha vizuri:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kurudisha utaratibu huo kwa walimu kupigwa msasa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nuru Awadh, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kutoa mafunzo endelevu kwa walimu kazini kulingana na upatikanaji wa fedha. Mafunzo hayo yanalenga kuboresha utendaji kazi na kutoa motisha kwa walimu ili kuinua ubora wa elimu nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2018/2019, jumla ya walimu wa Shule za Msingi 1,598 wamepata Mafunzo juu ya Ufundishaji na Ujifunzaji wa Stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK). Aidha, walimu wa Shule za Msingi 200 na Sekondari 198 wamejengewa uwezo katika Ufundishaji na Ujifunzaji wa somo la Hisabati. Vilevile, walimu wa Elimu Maalum 804 wamejengewa uwezo katika Ufundishaji na Ujifunzaji wa wanafunzi wenye Mahitaji Maalum.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, katika mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali imetenga kiasi cha Sh.502,807,348 kwa ajili ya kufanya mapitio na tathmini ya Vituo vya Walimu (TRC) kwa lengo la kuviwezesha kutoa mafunzo kazini kwa walimu kama ilivyokuwa inafanyika hapo awali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali inakamilisha maandalizi ya Kiunzi cha Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini ambacho kitatoa utaratibu wa uendeshaji wa mafunzo hayo ili kuweka msukumo zaidi wa mafunzo kazini. Napenda kutumia nafasi hii kuzihamasisha Halmashauri zote nchini kutenga fedha kwa ajili ya mafunzo kazini kwa ajili ya walimu.
MHE. LUCY S. MAGERELI aliuliza:-

Sera ya cost sharing ilianzishwa ili kuisaidia Serikali kibajeti katika maeneo ya afya na elimu, hadi leo ni bayana kuwa sera hii imeshindwa na hatimaye Serikali kurejea tena katika kugharamia Elimu ya Msingi na Sekondari:-

(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha Elimu ya Tanzania ambayo imeporomoka sana katika shule za Umma inakuwa yenye ubora unaotarajiwa?

(b) Je, Serikali inafanya nini kuhusu madai ya stahiki ya walimu ambazo hazijalipwa kwa muda mrefu sasa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Lucy Simon Magereli, Mbunge wa Viti Maalum, kama lenye vipengele (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, elimu ya Tanzania inaendelea kuimarika siku hadi siku katika Shule za Umma na binafsi. Ili kuhakikisha kuwa ubora wa elimu unaendelea kuimarika zaidi, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia. Mfano, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2018/2019, zaidi ya shilingi bilioni 56.5 zimetumika katika uboreshaji wa miundombinu katika shule 588. Kati ya hizo Shule za Msingi ni 303 na Sekondari ni 288 yakiwemo madarasa 1,190, mabweni 222 na vyoo 2,141.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali imesambaza vifaa vya kufundishia na kujifunzia vikiwemo vifaa vya maabara na kemikali na vifaa vya kielimu kwa ajili wanafunzi wenye mahitaji maalum katika Shule za Msingi na Sekondari. Pia katika kipindi cha mwaka 2017 hadi Aprili, 2019, Serikali imeajiri jumla ya Walimu 17, 884.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Serikali imeendelea kuimarisha Idara ya Udhibiti Ubora wa Shule ambapo imenunua na kusambaza magari 45 ya Udhibiti Ubora wa Shule na pikipiki 2, 897 kwa ajili ya Maafisa Elimu Kata. Pia katika mwaka 2019/2020 Serikali inatarajia kujenga Ofisi 100 za wadhibiti ubora wa shule na kuongeza idadi ya watumishi ili kuongeza ufanisi katika ufuatiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu madai ya stahiki za walimu, Serikali imeendelea kulipa madai hayo yahusuyo mishahara na likizo ambapo kwa kipindi cha Juni hadi Oktoba, 2018 Serikali ililipa zaidi ya shilingi bilioni 16 kwa madai ya malimbikizo ya mishahara. Aidha, hadi kufikia Desemba, 2018 Serikali pia ilipeleka jumla ya shilingi bilioni 5.07 kwenye Halmashauri 184 kwa ajili ya malipo ya likizo za walimu.
MHE. HALIMA A. BULEMBO aliuliza:-

Je, kwa nini mikopo ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu imekuwa ikitolewa kwa ubaguzi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Halima Abdallah Bulembo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu hutolewa kwa mujibu wa Sheria ya Bodi ya Mikopo Sura 178 ya sheria zetu, ambayo inabainisha sifa za msingi ambazo ni; awe ni mtanzania aliyedahiliwa katika masomo ya shahada katika taasisi inayotambuliwa na Serikali; na asiwe na vyanzo vingine vinavyogharamia masomo yake. Kwa mwanafunzi anayeendelea na masomo, awe amefaulu kuendelea na masomo katika mwaka unaofuata.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, bodi ina mamlaka ya kuweka utaratibu wa kubaini wahitaji, hivyo, bodi huandaa mwongozo unaoweka masharti kwa waombaji pamoja na maelekezo juu ya mambo muhimu ya kuzingatiwa kwa waombaji ambao ni yatima, wenye ulemavu au wenye wazazi wenye ulemavu na wale ambao masomo yao ya sekondari au stashahada, yalifadhiliwa. Maelekezo hayo ni pamoja na kuambatanisha uthibitisho wa hali zao.

Mheshimiwa Spika, hakuna ubaguzi wowote katika utoaji wa mikopo, mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu hutolewa kwa watanzania wote wenye uhitaji na walioomba mikopo hiyo kwa kuzingatia sheria, taratibu na vigezo vilivyowekwa. Hivyo, ni vyema waombaji kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na bodi wakati wa uombaji wa mikopo, ikiwa ni pamoja na kujaza taarifa zao kwa usahihi na kuambatanisha nyaraka zote muhimu.
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza:-

Wilaya ya Karatu ilipata mfadhili wa kujenga Chuo cha VETA na ujenzi umekamilika toka mwaka 2017 na tayari majengo yote yamekabidhiwa kwa Halmashauri.

Je, ni lini sasa Serikali itakipa Chuo hicho usajili wa kudumu pamoja na mahitaji mengine kama ilivyo katika vyuo vingine?
NAIBU WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekonolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, vyuo vinavyotoa mafunzo ya ufundi stadi nchini husajiliwa kupitia Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA). Utaratibu wa kuomba usajili huhusisha kujaza fomu inayopatikana katika tovuti ya VETA na kwenye Ofisi zote za Kanda za VETA. Ofisi za kanda hukagua vyuo vilivyoomba na kupewa usajili wa awali (Preliminary Registration). Hii ni hatua ya mwanzo kuelekea kupata usajili kamili.

Mheshimiwa Naibu Spika, usajili kamili hutolewa baada ya kufanyiwa tathmini ambayo inahusisha kutimiza vigezo ambavyo ni chuo kuwa na mfumo wa uendeshaji unaosimamiwa na Bodi ya Wakurugenzi au ya Wadhamini pamoja na menejimenti yenye sifa stahiki za kitaaluma. Chuo kuwa na miundombinu stahiki kwa mujibu wa viwango na vigezo vilivyowekwa. Chuo kuwa na vifaa na mitambo ya kufundishia kwa mujibu wa vigezo vilivyowekwa na chuo kuwa na Walimu wenye sifa stahiki za kitaaluma.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tarehe 26 Novemba mwaka 2019, Chuo cha VETA Karatu kilipewa fomu ya kujitathmini ili kijaze na kuwasilisha ofisi za VETA Kanda ya Kaskazini kwa ajili ya kufanyiwa ukaguzi wa mwisho ili kipate Usajili Kamili yaani Full Registration kwa mujibu wa taratibu za usajili. Hata hivyo, Halmashauri ya Wilaya ya Karatu haijarejesha fomu hii, ili iweze kupatiwa usajili wa kudumu na kuanza kudahili wanafunzi.
MHE. SUSAN L. KIWANGA aliuliza:-

Jimbo la Mlimba lina wahitimu wengi wa Shule za Msingi na Sekondari ambao wanabaki majumbani kila mwaka:-

Je, ni lini Serikali itajenga Chuo cha Ufundi ili vijana hao waweze kupata Ufundi Stadi ili wajiajiri?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susan Limbweni Kiwanga Mbunge wa Mlimba kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua uhitaji wa Vyuo vya Ufundi Stadi katika kuendeleza vijana wake ili waweze kushiriki kikamilifu katika harakati za maendeleo ya nchi yao. Katika kutimiza lengo hili, Serikali imejiwekea mkakati madhubuti wa kuendeleza elimu ya ufundi katika ngazi mbalimbali. Hivyo, Serikali inaendelea na juhudi za kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga Vyuo hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutekeleza mkakati huu wa kuendeleza elimu ya ufundi, Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa kila wilaya na mkoa unakuwa na chuo cha ufundi stadi ili kupanua fursa kwa vijana wetu. Kwa mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali kwa kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inatumia shilingi bilioni 40 kujenga vyuo 25 vya VETA katika ngazi ya Wilaya ambapo sasa hivi vipo katika hatua mbalimbali za ujenzi. Aidha, kwa Jimbo la Mlimba na wilaya nyingine, Serikali inafanya juhudi ya kutafuta fedha kwa ajili ya kuhakikisha mkakati wa kuwa na VETA kila Wilaya unakamilika.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO aliuliza:-

Utaratibu wa marejesho ya Mikopo ya Elimu ya Juu umeendelea kukumbwa na changamoto kubwa hasa baada ya ongezeko la asilimia 6 kama retention fee na hivyo kusababisha wanufaika wa mikopo kushindwa kumaliza kurejesha mikopo hiyo?

Je, kwa nini Serikali isilete Muswada wa mabadiliko ya Sheria husika utakaokuwa na masharti rahisi kwa wanufaika ili waweze kumaliza kulipa mikopo kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Susan Anselm Lyimo Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu hutoza asilimia 6 kwenye salio la deni yaani outstanding loan balance la mnufaika kwa mkopo kama tozo ya kutunza thamani yaani value retention fee. Lengo la tozo hii ni kulinda thamani ya fedha wanazokopeshwa wanufaika wa mikopo ili kuwa na mfuko endelevu utakaoendelea kutoa mikopo kwa wahitaji wengine bila kulazimika kuongeza fedha zaidi kutokana na upotevu wa thamani ya fedha.

Mheshimiwa Spika, kumbukumbu zinaonyesha kuwa wanufaika wanaoanza kurejesha mkopo kwa wakati humaliza kati ya miaka 4 hadi 10 kulingana na kiwango cha mshahara. Hata hivyo, Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya urejeshaji wa mikopo kwa wanufaika ili kuwawezesha kurejesha na kumaliza madeni yao kwa wakati.
MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza: -

Elimu ya Msingi ni muhimu kuwawezesha wahitimu kuzalisha na kuwapatia stadi za maisha lakini wapo wahitimu wa Elimu ya Msingi, Sekondari na Vyuo wasioweza hata kuanzisha bustani za mboga mboga na matunda:-

Je, Serikali inachukua hatua gani kuhakikisha elimu inayotolewa inamwezesha mhitimu kupata ujuzi na stadi za maisha ili aweze kujiajiri?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Shally Josepha Raymond, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kuwawezesha wanafunzi kupata stadi za maisha na kuzalisha limezingatiwa katika mitaala ya ngazi mbalimbali za elimu hapa nchini kwa lengo la kumwezesha mhitimu kupata ujuzi na stadi za maisha ili aweze kujiajiri.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuwawezesha wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu kupata stadi za maisha na ujuzi ili waweze kuzalisha, Serikali imehuisha mitaala ya Elimumsingi kwa lengo la kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji wa stadi mbalimbali za maisha. Kwa mfano, katika shule za msingi, somo la Stadi za Kazi linawajengea wanafunzi stadi za ujasiriamali na hivyo kuwandaa kujiajiri kwa wale watakaoishia ngazi hiyo ya elimu. Kwa upande wa shule za sekondari stadi za ujasiriamali kama vile, kuweka malengo, kuwasiliana na uthubutu zimezingatiwa kwenye mitaala.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali pia imewezesha Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi 54 kutoa maarifa na ujuzi wa ufundi katika fani mbalimbali kwa wahitimu wa Elimumsingi ili waweze kuzalisha kama vile ushonaji, ufundi umeme, uashi na uselemala. Pia, Serikali imeendelea kujenga uwezo wa walimu wa ufundi katika vyuo hivyo ili kuboresha ujuzi wao katika nyanja mbalimbali za kiujuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jitihada hizi za Serikali, jukumu la kufundisha wanafunzi stadi za maisha ni la jamii nzima. Hivyo, naomba kutoa rai kwa wazazi/walezi na jamii kwa ujumla kuwapa nafasi watoto wetu kufanya kazi mbalimbali za nyumbani kulingana na umri wao ili kusaidia kuwafundisha kwa vitendo.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA aliuliza:-

Wapo watoto wengi wenye uwezo (ubongo) mzito kufahamu kusoma au kuandika na hatimaye kubaki shule kwa muda mrefu:-

Je, Serikali ina mkakati gani juu ya kundi hili kubwa la watoto katika kuwaendeleza kielimu ili waweze kujitegemea?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Eilimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu Swali la Mheshimiwa Asha Abdulla Juma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua uwepo wa watoto wenye uelewa tofauti wakati wa mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji ikiwa ni pamoja na watoto wenye uwezo mzito wa kusoma na kuandika. Uwezo huu mzito wa kusoma na kuandika husababishwa na sababu mbalimbali zikiwemo, mazingira yasiyo rafiki nyumbani na shuleni, migogoro ya kifamilia hasa ya wazazi na walezi, kuugua kwa muda mrefu, hofu na kutojiamini. Kwa sababu ya uelewa wao mzito, watoto hao huchukua muda mwingi katika kujifunza.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutatua changamoto hii, Serikali imeendelea kutekeleza Mitaala ya Mafunzo ya Ualimu inayomwezesha mwalimu kuzingatia mahitaji ya makundi mbalimbali ya wanafunzi katika ujifunzaji. Kwa mfano, kuwabaini watoto wenye uwezo mzito katika kujifunza, kupata mbinu mbalimbali za kufundishia na kujifunzia ambazo husaidia watoto hao kujifunza. Vilevile, Serikali imeendelea kutoa mafunzo kazini kwa walimu ili kuimarisha mchakato mzima wa ufundishaji na ujifunzaji kwa kuzingatia mahitaji halisi katika darasa. Kwa mfano, mafunzo endelevu ya ujenzi wa Stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu kwa Darasa la Kwanza hadi la Nne pamoja na Usimamizi wa Elimu ya Awali kwa walimu waliopo kazini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania imeandaa Mitaala na Vitabu kwa ajili ya Elimumsingi ili kuboresha maudhui na njia za ufundishaji zinazomwezesha mwanafunzi kushiriki kikamilifu katika tendo la ujifunzaji. Naomba kutoa rai kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kutoa ushirikiano kwa walimu ili kuweka nguvu ya pamoja katika kusaidia wanafunzi wenye uwezo mzito katika kujifunza kusoma na kuandika.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA (K.n.y. MHE. RHODA E. KUNCHELA) aliuliza:-

Ujenzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo Mkoa wa Katavi ni jambo ambalo linaleta sintofahamu kwa maana ya umiliki wa eneo (Hati) na ujenzi wa Chuo ambao ni miaka sasa bado hakijajengwa na kusababisha jambo hili kuleta usumbufu kwa wanafunzi kwenda Mikoa mingine kutafuta vyuo vya kilimo:-

Je, Serikali ipo tayari kuondoa sintofahamu hii ya ujenzi wa Chuo hicho cha Kilimo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rhoda Edward Kunchela, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inatambua kuwa ujenzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo Katavi lilikuwa ni wazo la Halmashauri ya Mji wa Mpanda. Halmashauri iliingia makubaliano na Chuo cha Royal Agricultural University cha Uingereza kwa ajili ya utekelezaji wa azma hiyo.

Mheshimiwa Spika, mnamo mwaka 2013 Halmashauri ya Mji Mpanda ilileta ombi la kukabidhi mradi huo kwa Wizara na walielekezwa kuwasilisha taarifa rasmi ya maendeleo ya mradi kwa ajili ya hatua stahiki. Hadi sasa Wizara haijapokea taarifa hiyo. Aidha, umiliki wa eneo hilo la chuo bado uko chini ya Halmashauri ya Mji Mpanda.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB (K.n.y. MHE. KHAMIS YAHYA MACHANO) aliuliza:-

Tarehe 19 Agosti, 2019, zaidi ya wanafunzi 100 walisafiri kwenda masomoni China na India na ni ukweli kuwa elimu ya juu ni suala la Muungano:-

(a) Je katika wanafunzi hao ni wangapi wanatoka Zanzibar pamoja na majina yao?

(b) Je, ule utaratibu wa Zanzibar kupewa Scholarship bado unatekelezwa?

(c) Je, ni lini Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia atakutana na Waziri wa Elimu Zanzibar ili kuweka utaratibu mzuri wa masuala ya elimu ya juu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Khamis Yahya Machano, Mbunge wa Chaani lenye vipengele (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, nafasi za ufadhili wa masomo kutoka nchi au mashirika rafiki huratibiwa kwa ushirikiano baina ya pande mbili za Muungano. Mara baada ya kupokea nafasi hizo, Wakurugenzi wenye dhamana ya Elimu ya Juu kutoka pande mbili za Muungano hukutana kwa lengo la kubainisha sifa za waombaji. Matangazo kwa waombaji wote hutolewa kupitia tovuti za Wizara husika. Aidha, zipo nafasi za ufadhili wa masomo ambazo huratibiwa na nchi au shirika linalofadhili.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka 2019/2020 Serikali ya Watu wa China, kupitia Wizara yangu ilitoa nafasi 61 za ufadhili wa masomo. Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, iliratibu zoezi la kuwapata waombaji wenye sifa. Jumla ya waombaji 82 kati ya 662 walioomba walikidhi vigezo na majina yao kuwasilishwa Ubalozi wa China kwa hatua za uchaguzi. Baada ya mchujo uliofanywa na Ubalozi waombaji 61 walipata ufadhili huo.

Kwa upande wa India, nafasi za ufadhili wa masomo kwa mwaka 2019/2020 zilitangazwa na kuratibiwa na Ubalozi wa India ambapo jumla ya Watanzania 24 wamenufaika. Nafasi za ufadhili wa masomo zinapatikana kwa njia ya ushindani kwa kuzingatia sifa na vigezo na pasipo kujali mwombaji anatoka upande upi wa Muungano.

(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu vikao vya Mawaziri, upo muongozo rasmi kuhusu vikao vya pamoja baina ya pande mbili za Muungano na vikao hivyo hufanyika kutokana na uhitaji. Vikao hivyo vipo katika ngazi ya Kamati ya Pamoja, Kikao cha Mawaziri na Kikao cha Makatibu Wakuu.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI aliuliza:-

Kutokana na gharama za pango kuwa kubwa na hivyo kuongeza gharama za uendeshaji kwa Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere kilichopo Mkoani Mara:-

Je, ni lini Serikali itakijengea chuo hicho majengo yake na kuanza kuyatumia rasmi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Spika,kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayani na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joyce Bitta Sokombi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika,Serikali iliamua kuanzisha Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Mwalimu Julius Nyerere Wilayani Butiama kama sehemu ya kumuenzi Baba wa Taifa ambaye aliamini katika umuhimu wa sekta ya kilimo kama uti wa mgongo katika ustawi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius Nyerere cha Kilimo na Teknolojia kimeendelea kufanya shughuli zake kwa muda katika majengo ya Shule ya Sekondari ya Oswald Mang’ombe iliyopo Wilaya ya Butiama.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendeleana ujenzi wa majengo ya chuo (Campus Kuu) ambapo kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ujenzi wa jengo la utawala lenye thamani ya shilingi milioni 200 umefikia asilimia 50. Aidha, katika Mwaka wa Fedha 2019/2020 kiasi cha shilingi bilioni moja kimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mingine. Vilevile, Serikali inaendelea na juhudi za kupata fedha zaidi kutoka vyanzo vingine kama vile miradi ya Benki ya Dunia.
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza:-

Kumekuwa na matamko na makatazo mbalimbali juu ya wanafunzi wanaopata ujauzito wakiwa shuleni:-

Je, matamko na makatazo hayo yamesaidia kwa kiasi gani?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajibu swali naomba kutumia nafasi hii kuwatakia vijana wetu 947,221 wanaofanya mitihani yao ya darasa la saba, naomba niwatakie kila la kheri na Mungu awaongoze katika mitihani yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, matamko na makatazo kuhusu wanafunzi wanaopata ujauzito yanatokana na Kanuni za Elimu za Mwaka 2002, Kanuni Na. 4 ya Sheria ya Elimu ya Mwaka 1978, Sura Na. 353 inayobainisha makosa ya wanafunzi shuleni. Aidha, yanazingatia marekebisho ya Sheria ya Elimu Na. 25 ya Mwaka 1978 yaliyofanyika mwaka 2016. Katika marekebisho hayo, mtu yeyote atakayepatikana na hatia ya kumpa mimba mwanafunzi wa shule ya msingi au sekondari atahukumiwa kifungo cha miaka 30 jela. Sheria hii pia inatoa adhabu kwa mtu yeyote anayesaidia mhalifu aliyempa mwanafunzi mimba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria na makatazo hayo yamesaidia jamii kufahamu umuhimu wa kulinda hadhi na usalama wa mtoto wa kike. Pia, imesaidia kujua adhabu kwa mtu yeyote anayempa mwanafunzi mimba ambapo kesi zimefunguliwa na baadhi ya wahusika wamehukumiwa kifungo kwa kosa hilo. Aidha, elimu, matamko na sheria vimesaidia kupunguza mimba za wanafunzi kwenye maeneo mengi nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeweka mikakati ya kupunguza changamoto kwa watoto wa kike ikiwa ni pamoja na kujenga mabweni na hosteli katika maeneo ambayo wanafunzi wanalazimika kutembea umbali mrefu. Aidha, Serikali pia imeweka mpango wa kusaidia wasichana wanaoacha shule kwa sababu mbalimbali ili waweze kuendelea na masomo. Mpango huo ni kutoa elimu kupitia Vyuo vya Elimu Nje ya Mfumo Rasmi vinavyoratibiwa na Taasisi ya Elimu ya Watu Waziri pamoja na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC).

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe wito kwa wazazi na jamii kwa ujumla kuendelea kutoa ushirikiano wa kuwalinda watoto wa kike na kuhakikisha kuwa taarifa zinatolewa kwa mamlaka husika ili kuhakikisha kuwa mtu yeyote anayemsababishia mtoto wa kike kukosa elimu anakumbana na mkono wa sheria.
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE aliuliza:-

World Vision wamejenga Chuo cha Ufundi katika Kata ya Nyamidaho na kukikabidhi kwa Halmashauri ya Kasulu DC:-

Je, kwa nini Serikali isimalizie ujenzi wa miundombinu midogomidogo na hatimaye kukifanya kuwa Chuo cha Ufundi cha Serikali?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Augustine Vuma Holle, Mbunge wa Kasulu Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa nchi kuwekeza katika elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali imedhamiria kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, kupitia uchumi wa viwanda ambavyo vinaedelea kujengwa kwa kasi kubwa. Kwa sasa Serikali inaendelea na mpango wa kujenga Vyuo vya Ufundi Stadi ikiwa na lengo la kutimiza azma ya kuwa na Chuo cha Ufundi katika kila Mkoa na kila Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetoa jumla ya shilingi milioni 530 kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi wa miundombinu wa ya Chuo cha Ufundi Stadi cha Nyamidaho. Ujenzi umefikia asilimia 80, hatua inayofuata ni kuunganisha umeme, kumalizia ujenzi wa vyoo na kumalizia kazi za nje. Kazi hizi zitakamilika mwishoni mwa mwezi Oktoba, 2019. Aidha, michakato ya manunuzi ya samani na mitambo ya kufundishia na kujifunzia imekwishaanza ili kuhakikisha kuwa chuo hicho kinaanza kutoa mafunzo ifikapo Januari, 2020.
MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED aliuliza:-

Matokeo ya mitihani ya Kidato cha Nne yamekuwa mabaya kwa kipindi kirefu sasa na hali haijapatiwa ufumbuzi wowote:-

(a) Je, nini tamko la Serikali kuhusiana na hali hiyo?

(b) Je, ni juhudi zipi za makusudi ambazo Serikali inakusudia kuchukua ili kupandisha hali ya ufaulu wa wanafunzi hao?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Muhammed Amour Muhammed Mbunge wa Bumbwini lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ufaulu wa wanafunzi katika mtihani wa kidato cha IV umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka ambapo katika mwaka 2018 watahiniwa waliofaulu ni asilimia 78.3 ikilinganishwa na asilimia 77.09 ya mwaka 2017, asilimia 70.35 ya maka 2016 na asilimia 67.91 ya mwaka 2015.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuongeza ufaulu katika ngazi mbalimbali za Elimu. Hatua hizo ni pamoja na kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa kujenga na kufanya ukarabati mkubwa wa miundombinu katika shule ambapo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2018/2019, zaidi ya shilingi bilioni 93.8 zimetumika katika uboreshaji wa miundombinu ya shule 588 zikiwemo (Msingi 303 na Sekondari 285) yakiwemo madarasa 1,190, mabweni 222 na vyoo 2,141, mabwalo 76 na nyumba 99.

Mheshimiwa Spika, Aidha, Serikali imeendelea kusambaza vifaa vya kufundishia na kujifunzia vikiwemo, vifaa vya maabara katika shule na vifaa vya kielimu kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum. Vile vile katika kipindi cha mwaka 2017 hadi Aprili, 2019, Serikali imeajiri jumla ya walimu 17,884.

Mheshimiwa Spika, pia Serikali imeendelea kuimarisha Idara ya Udhibiti Ubora wa Shule ambapo imenunua na kusambaza magari 45 ya udhibiti ubora wa Shule na pikipiki 2,897 kwa ajili ya Maafisa Elimu Kata. Katika mwaka 2019/ 2020 Serikali inatarajia kujenga ofisi 100 za wadhibiti ubora wa shule na kuongeza idadi ya watumishi hao. Hivyo, Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuendelea kuimarisha ubora wa elimu nchini.
MHE. MARIAM N. KISANGI (K.n.y. MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA) aliuliza:-

Serikali imerejesha vyuo vilivyokuwa vya maendeleo kuwa chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Je, Serikali haioni umuhimu wa kukibadili Chuo cha Maendeleo Ikwiriri FDC kuwa VETA ili kubadili fikra za wananchi wa Rufiji, Kibiti na Ikwiriri na hatimaye kuleta mwamko wa elimu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, elimu ya ufundi na mafunzo ufundi stadi hutolewa katika shule na vyuo katika viwango na madaraja mbalimbali kulingana na malengo yake. Katika ngazi ya shule za sekondari, elimu ya ufundi hutolewa ili kumuandaa mwanafunzi kujiunga na vyuo vya ufundi stadi na ufundi wa kati. Vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi huandaa mafundi mchundo na vyuo vya ufundi wa kati huandaa mafundi sanifu. Aidha, vyuo vikuu hundaa wahandisi katika fani mbalimbali zinzohusiana na ufundi.

Mheshimiwa Spika, Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vilianzishwa kwa lengo la kumsaidia wananchi kubaliana na changamoto za kimaendeleo katika mazingira yake kwa kumapatia maarifa na stadi anuwai. Vyuo hivi hutoa elimu ya ufundi stadi katika hatua ya kwanza hadi ta tatu. Pia mafunzo ya ujasiliamali, kilimo, uvuvi, mifugo n.k hutolewa kulingana na mahitaji ya eneo husika.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali haina mapango wa kuvibadili Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi kuwa VETA. Badala yake, Serikali imejikitia katika viboresha vyuo hivyo kwa kuvikarabati na kuviongezea vifaa vya kuviongezea vifaa vya kujifunzia na kufundishia ili viweze kutoa mafunzo bora zaidi. Awamu ya kwanza ukarabati wa Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi 20 ipo katika hutua za mwisho za ukamishaji awamu ya pili inataraji kuanza mapema mwezi Juni, 2019. Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Ikwiriri kilikuwa katika awamu ya kwanza na ukarabati umekamilika. Aidha, katika mwaka wa fedha 2019/2020 Rufiji n miongoni mwa Wilaya zilizotengewa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha Ufundi stadi cha Wilaya cha VETA.
MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza:-

Katika Wilaya ya Urambo kulikuwa na Chuo cha Ualimu ambacho kilisaidia sana kuleta chachu ya maendeleo ya elimu na uchumi kwa wananchi wa Urambo.

(a) Je, ni sababu zipi zilizosababisha Chuo cha Ualimu Urambo kufungwa/kuhamishwa?

(b) Je, Serikali haioni iko haja ya kuangalia upya uwezekano wa kurudisha Chuo cha Ualimu Urambo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta, Mbunge wa Urambo lenye vipengele (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 1995 Serikali iliamua kubadilisha baadhi ya vyuo vya ualimu kuwa shule za sekondari, Urambo kikiwa kimojawapo. Uamuzi huo ulitokana na sababu zifuatazo; mahitaji makubwa ya shule za sekondari hasa katika ngazi ya kata pamoja na maamuzi ya Serikali kuhitimisha utoaji wa mafunzo ya ualimu kwa wahitimu wa darasa la saba Ualimu Daraja la Tatu B ili kuinua kiwango cha elimu na uwepo wa vyuo vingi vya ualimu ambavyo vinatosheleza mahitaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na sababu hizo Serikali ilikibadilisha Chuo cha Ualimu Urambo na kuanzisha Shule ya Sekondari Ukombozi ambayo ni shule ya kutwa.

Aidha, kwa kuifanya kuwa shule ya kutwa yaliyokuwa mabweni yalikarabatiwa na kubadilishwa kuwa madarasa sita na kujenga madarasa mengine sita na kuwezesha shule hiyo kudahili wanafunzi 888 ambapo idadi ya wasichana ni 426 na wavulana ni 462.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina jumla ya vyuo vya ualimu 35 vya Serikali ambavyo hudahili wanachuo kutoka nchi nzima. Kuanzia mwaka 2016/2017 Serikali imefanyia upanuzi na ukarabati mkubwa vyuo 24 katika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali inaendelea kufanya ukarabati wa vyuo vingine kumi kwa lengo la kuendelea kuongeza nafasi za udahili ili kuendelea kutosheleza mahitaji ya walimu nchini.
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA (K.n.y MHE. KITETO Z. KOSHUMA) aliuliza:-

Ili kuelekea Tanzania ya viwanda, Watanzania wanapaswa kuandaliwa vema ili kushiriki kikamilifu katika viwanda vya ndani.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuandaa wataalam mbalimbali watakaotumika katika kuendesha viwanda nchini?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kiteto Zawadi Koshuma, Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2016 Serikali kupitia Wizara Elimu, Sayansi na Teknojia ikishirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu na wadau wengine ikiwa ni pamoja na sekta binafsi na washirika wa maendeleo ilikamilisha na kuanza utekelezajii wa mkakati wa Taifa wa kukuza maarifa (National Skills Development Strategy – NSDS 2016). Mkakati huu ni wa kipindi cha miaka kumi na unaorodhesha mahitaji mbalimbali ya maarifa ambayo wataalam wake wanahitajika ili kuifikisha nchini yetu katika uchumi wa kati wa viwanda tunaoukusudia.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha Watanzania wanaandaliwa vema kushiriki uchumi wa viwanda, Serikali inaendelea kutekeleza mipango mbalimbali ikiwemo kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kama vile ujenzi na ukarabati wa maiundombinu ya shule na kusambaza vifaa vya maabara na kemikali katika shule za sekondari.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Serikali inaendelea na mpango wa ukarabati, ujenzi wa miundombinu, ununuzi wa vifaa vya kisasa vya kujifunzia na kufundishia na kuboresha mitaala katika vyuo na taasisi za elimu. Kwa mfano, ukarabati wa vyuo vya maendeleo ya wananchi, ujenzi na ukarabti wa vyuo vya VETA katika Mikoa na Wilaya pamoja na Vyuo Vikuu nchini. Aidha, katika mwaka 2019/ 2020 Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknojia itaanza ujenzi wa chuo kipya cha ufundi cha Dodoma (Dodoma Technical College) pamoja na kujenga vyuo vya ufundi stadi katika Wilaya 25 ili kuongeza udahili wa wanafunzi katika fani mbalimbali za ufundi.
MHE. RICHARD M. NDASSA aliuliza:-

Wananchi wa Halmashauri ya Kwimba waliombwa kutafuta eneo la kujenga Chuo cha VETA ambapo eneo la ekari 60 lilishapatikana zaidi ya miaka 10 iliyopita na Serikali imekuwa ikiahidi kutenga fedha za ujenzi wa chuo hicho:-

Je, ni lini Serikali itatenga fedha za ujenzi wa chuo hicho?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Richard Mganga Ndassa, Mbunge wa Sumve, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa nchi kuwekeza katika elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali ipo katika jitihada za kuelekea uchumi wa kati kupitia viwanda ifikapo mwaka 2025.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na mpango wa kujenga Vyuo vya Ufundi Stadi ikiwa na lengo la kutimiza azma ya kuwa na Chuo cha Ufundi Stadi katika kila mkoa na wilaya. Ujenzi wa vyuo hivi unafanyika kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Kwimba ni moja ya Kata ya Wilaya zilizopo katika awamu ya pili inayotarajiwa kuanza kutekelezwa mwaka wa fedha 2019/2020. Kwa sasa wananchi wa Kwimba wanashauriwa kutumia Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Malya kilichopo Wilaya ya Kwimba na vingine vilivyo mkoa na wilaya za jirani.
MHE. EDWARD F. MWALONGO aliuliza:-

Elimu ya ufundi ni muhimu sana kwa vijana:-

(a) Je, Serikali ipo tayari kubadili shule moja ya sekondari katika kila Halmashauri na kufanya kuwa shule ya ufundi?

(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kurejesha kozi za ualimu wa ufundi iliyokuwa ikitolewa na Dar es Saalam Institute of Technology?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Edward Franz Mwalongo, Mbunge wa Njombe Mjini, kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa shule za ufundi, hususan wakati huu ambapo inatekeleza dhamira yake ya kujenga uchumi wa viwanda. Ili kufikia lengo hilo, Serikali tayari imekarabati shule za sekondari za ufundi kongwe saba (7) ambazo ni Musoma, Bwiru Wavulana, Ifunda, Tanga, Moshi, Iyunga na Mtwara. Hivyo, kwa sasa Serikali imejielekeza katika kuimarisha shule za ufundi zilizopo ili ziendelee kutoa elimu ya ufundi iliyo bora.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Taasisi ya Teknolijia Dar es Salaam ilikuwa ikitoa mafunzo ya walimu ufundi, kozi hiyo iliitwa Diploma in Technical Education. Baada ya Serikali kuanzisha Wizara mpya iliyokuwa inaitwa Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu, DIT kikiwa chuo kimojapo cha teknolojia kilihamishiwa chini ya Wizara hiyo. Serikali ilifanya maamuzi kuwa kozi ya DTE iendelee kuwepo lakini iendeshwe katika mojawapo ya vyuo vilivyopo chini ya iliyokuwa Wizara ya Elimu na Utamaduni na siyo DIT. Mwaka 1991 kozi ya DTE ilihamishwa toka DIT kwenda Chuo cha Ualimu Kleruu kilichokuwa chini ya Wizara ya Elimu na Utamaduni.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu wa masomo ya ufundi, Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam ina mpango wa kuanza tena mafunzo ya ualimu wa masomo ya ufundi. Vilevile Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya kimeanza maandalizi ya utoaji wa mafunzo hayo ambapo kwa sasa mitaala ya masomo hayo inafanyiwa kazi na Tume ya Vyuo Vikuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali inaendelea kufanya maboresho makubwa katika Chuo cha Ualimu Kleruu pamoja na Chuo cha Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi cha Morogoro (MVTCC) kwa kufanya ukarabati wa miundombinu ikiwepo ujenzi wa mabweni ya wanafunzi kwa lengo la kuongeza nafasi za udahili kwa walimu wa masomo ya ufundi.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA Aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuvutia wawekezaji hasa katika kutumia pumba za mpunga ambazo hutumika katika uzalishaji wa uyoga hasa katika Jimbo la Kilombero?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (UWEKEZAJI) Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijajibu swali, kwa sababu ni mara yangu ya kwanza baada ya uteuzi uliofanywa na Mheshimiwa Rais, naomba nitumie nafasi hii kumshukuru kwanza Mungu kwa kutuweka hai, lakini pia nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuniamini katika nafasi mpya ya Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji. Ahadi yangu kwake ni kwamba nitatumikia nafasi niliyopelekwa kwa uadilifu, uaminifu na kwa kufanya kazi kwa bidii kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo ya mwanzo, naomba sasa kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji, nijibu swali la Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga, Mbunge wa Kilombero, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inavutia uwekezaji wa sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya kilimo kupitia mikakati mbalimbali ikiwemo kuandaa miongozo ya uwekezaji ya mikoa ili kubainisha fursa za uwekezaji za mikoa husika, kuandaa makongamano ya uwekezaji ya ndani na nje na kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Jimbo la Kilombero wanayo fursa kubwa ya kuingia kwenye kilimo cha uyoga kwa kutumia pumba za mpunga kwa kuwa wilaya hiyo ni kati ya maeneo yanayoongoza kwa kilimo cha mpunga nchini. Kwa mfano, Halmashauri ya Mji wa Ifakara inazalisha tani 11,125 za pumba za mpunga kwa mwaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa uyoga una soko kubwa nchini, Serikali imeanza uhamasishaji na kufanya tafiti mbalimbali kuhusu uzalishaji wake. Kwa mfano, Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda (TIRDO) lilianza utafiti na uhamasishaji wa zao la uyoga mwaka 2001 kwa kutumia masalia ya uzalishaji wa kilimo cha viwanda ambapo jumla ya wajasiriamali 1,823 wamefundishwa uzalishaji uyoga ikiwemo uyoga wa dawa aina ya gonagema na shitake kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, TIRDO kwa kushirikiana na taasisi za utafiti inaendelea kufanya tafiti zaidi ambapo mwezi Machi, 2021, imeanza utafiti wa kujua uwezo wa vimeng’enya aina tofauti katika kuongeza uzalishaji wa uyoga na ubora wa uyoga unaozalishwa kilishe (yield and nutritive value).
MHE. EDWIN E. SWALLE aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuvutia Wawekezaji katika kilimo cha Parachichi mkoani Njombe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (UWEKEZAJI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Edwin Enosy Swalle, Mbunge wa Lupembe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufikia mwaka 2020, thamani ya zao la parachichi katika Soko la Dunia inakadiriwa kuwa Dola za Kimarekani milioni 4,800. Kwa Ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara, soko la parachichi linakadiriwa kuwa na thamani ya Dola za Kimarekani milioni 254. Aidha, nchi yetu imeendelea kufanya vizuri katika uzalishaji na uuzaji wa zao la parachichi katika masoko ya ndani na ya Kimataifa kama vile Umoja wa Ulaya, China, India na Kenya. Hivyo, mwaka 2020 kiasi cha Dola za Kimarekani milioni nane kilipatikana kutokana na wastani wa kiasi cha tani 4,000 zilizosafirishwa katika Soko la Kimataifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini na ufanyaji wa biashara kwa kushughulikia kero zitokanazo na ukadiriaji na ukasanyaji wa kodi usio rafiki; upatikanaji mgumu wa ardhi unaochukua muda mrefu kwa ajili ya uwekezaji; changamoto za upatikanaji wa vibali vya kazi na ukaazi; na kuondoa tozo mbalimbali ambazo ni kero katika Serikali za Mitaa. Hadi sasa, jumla ya tozo 273 ambazo zilikuwa kero kwa wawekezaji zimefutwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutekeleza Sera ya Uwekezaji, Serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji ikiwa ni pamoja na kutoa vivutio kama vile misamaha ya kodi kwenye makasha/majokofu (cold rooms) yanayotumika kuhifadhi mazao ya bustani ikiwemo zao la parachichi. Aidha, Serikali ina mpango wa kujenga chumba baridi katika uwanja wa ndege wa Songwe, ambapo ndege za Kimataifa zinazobeba mizigo zitaanza kusafirisha parachichi na mazao mengine ya matunda na mboga mboga moja kwa moja kwenda kwenye masoko ya Kimataifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile, Serikali imepanga kujenga jengo lijulikanalo kama ukanda wa kijani katika bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya kuhifadhi bidhaa na mazao yanayoharibika mapema likiwemo zao la parachichi. Jitihada nyingine ni pamoja na kutafuta masoko ya nje, kuhakikisha upatikanaji wa mbegu bora, kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji, uhifadhi, uchukuzi na usafirishaji. Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wote ikiwemo sekta binafsi katika kukuza uwekezaji wa zao la parachichi.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka vivutio maalum ili kuvutia Wawekezaji kwenye viwanda vya kubangua korosho?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, UWEKEZAJI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota Mbunge wa Nanyamba kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua kuwa korosho ni miongoni mwa mazao matano ya kimkakati yanayolimwa hapa nchini, kuanzia mwaka 2018 Serikali inatekeleza mpango wa uhamasishaji wa kilimo cha korosho katika mikoa yote inayostawisha kwa kuhakikisha upatikanaji wa mbegu bora, huduma za ugani na pembejeo ili kuimarisha upatikanaji wa malighafi kwa viwanda nchini. Hadi sasa, takribani mikoa 20 inazalisha zao hilo kwa viwango tofauti. Msimu wa mwaka 2020/2021 uzalishaji ulikuwa tani 200,010 na kuipatia nchi kiasi cha shilingi bilioni 477.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuimarisha uwekezaji wa viwanda vya kubangua korosho, Serikali imeweka vivutio mbalimbali vikiwemo vivutio visivyo vya kikodi kama vile kuweka mfumo wa soko la awali kwa wabanguaji wa ndani kuanzia mwaka 2020 kwa lengo la kuwawezesha kununua korosho bila kushindana na wanunuzi wanaosafirisha korosho ghafi kwenda masoko ya nje ya nchi na kuwahakikishia malighafi kwa bei nafuu. Katika mnada huo jumla ya tani 2,021.7 kimenunuliwa na viwanda tisa vilivyoshiriki soko hilo la awali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeweka pia vivutio vya kikodi kwa viwanda vya kubangua korosho kupitia Sheria ya Maeneo ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje Sura 373 ikiwemo: Msamaha wa Kodi ya Makampuni (Corporate Tax) kwa miaka 10; msamaha wa asilimia 100 wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa bidhaa za mtaji (capital goods); msamaha wa asilimia 100 wa Kodi ya Zuio (Withholding Tax); na riba ya mikopo kutoka nje; pango na gawio; na msamaha wa asilimia 100 wa Kodi ya Ushuru wa Forodha kwa mitambo na vifaa. Kupitia utaratibu huo, jumla ya viwanda vitano vimesajiliwa na Mamlaka ya Uwekezaji kwa Mauzo Nje (EPZA).

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kubuni na kuweka vivutio mbalimbali vya kikodi na visivyo vya kikodi ili kuvutia zaidi uwekezaji ikiwemo kutenga maeneo maalum kwa ajili ya ujenzi wa viwanda kwenye Halmashauri zinazolima korosho hapa nchini, ambapo maeneo hayo yatakuwa na huduma muhimu kama vile umeme, maji na barabara; na kupitia kodi mbalimbali zinazotozwa katika mitambo, vipuri na vifungashio.
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:

Je, mpaka sasa ni wawekezaji wangapi wamemilikishwa ardhi na kupata Hati kupitia Kituo cha Uwekezaji TIC?
NAIBU WAZIRI OFISI YA WAZIRI MKUU, UWEKEZAJI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, wawekezaji wa kigeni wanamiliki ardhi kwa ajili ya uwekezaji kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi Na.4 ya mwaka 1999. Kifungu cha 20 cha Sheria hiyo kinaelekeza kwamba, Kamishna wa Ardhi atatoa hati ya umiliki wa ardhi (Certificate of Right of Occupancy) kwa jina la Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa ajili ya uwekezaji endapo uwekezaji huo unafanywa na mwekezaji wa kigeni. Kwa kutumia hati hiyo, TIC hutoa Hati ya Umiliki Isiyo Asili (Derivative Right) kwa mwekezaji wa kigeni aliyewasilisha maombi ya ardhi kwa ajili ya uwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya mwekezaji kupewa Hati ya Umiliki Isiyo Asili na TIC, hati hiyo inasajiliwa na Msajili wa Hati (Registrar of Titles) ambaye anatoa hati ya umiliki wa ardhi hiyo (Derivative Title) kwa jina la mwekezaji wa kigeni kulingana na masharti ya uwekezaji husika kama yalivyoainishwa kwenye mkataba wake na TIC.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia utaratibu huo, tangu mwaka 1999 hadi mwezi Mei, mwaka huu, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimewezesha upatikanaji wa Hati za Umiliki Zisizo Asili (Derivative Rights) 401 kwa wawekezaji wa kigeni.