Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Mariamu Ditopile Mzuzuri (11 total)

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi. Naomba nitangulize shukrani zangu kwa Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya na kuweza kusimama hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kumpongeza Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kutimiza ahadi yake. Alisema kipindi cha kampeni, yeye akiahidi anatekeleza. Kwa Wana-Dodoma ametuletea Makao Makuu na kweli Serikali imeshahamia. Kipindi cha kampeni wananchi waliilalamikia CDA kwamba amethubutu, ameivunja mamlaka ya ustawishaji. Sisi tunamwambia tuko naye bega kwa bega, tunasema uungwana ni vitendo asubirie 2020, Dodoma tuko naye pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nyongeza tu ni kwamba Serikali tunaomba sasa muda muafaka umefika wa kuleta muswada wa Sheria ya Makao Makuu. Leo hii tunajadili Wizara nyeti, tunajadili maisha robo tatu ya Watanzania. Kwa mujibu wa hotuba yako Mheshimiwa Waziri, umesema kwamba sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi, imeajiri zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania.

Waheshimiwa Wabunge, everybody is entitled to his/ her opinion, lakini lazima tuseme ukweli. Wao wanaosema tumeganda wakati Sudan inategemea chakula kutoka Tanzania, Kenya wanategemea mahindi kutoka Tanzania, Uganda wanategemea mahindi kutoka Tanzania na mazao mengine! India wanategemea chorosho, choroko, dengu, mbaazi zote zinatoka Tanzania. La msingi ni kwamba tunatakiwa tuishauri Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii naomba niwaambie, Waziri wa Fedha na Naibu Waziri, naomba mnisikilize. Mipango yenu ni kwamba tunataka kupeleka nchi kwenye uchumi wa viwanda, tunataka kuwa na uchumi wa kati, tuwekeze kwenye kilimo, mifugo na uvuvi. Kilimo, mifugo na uvuvi ni afya, kilimo, mifugo na uvuvi ni ajira, itampunguzia kaka yangu Antony Mavunde adha aliyokuwa nayo. Kilimo, mifugo na uvuvi ni fedha na uchumi, kilimo, mifugo na uvuvi ni amani. Tukiwa na njaa tutaweza kuwa na amani?

Kwa hiyo, Waziri wa Fedha na Mipango, ukipeleka hela kwenye kilimo, mambo yako yote, mpango wa maendeleo utafanikiwa kwa asilimia 200. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi, lawama nyingi sana zimemwendea Mheshimiwa Waziri. Namfahamu Mheshimiwa Waziri. Nimeshalima naye, ni mkulima mzuri sana. Tena bahati nzuri analimia hapa hapa katika Mkoa wetu wa Dodoma. Mheshimiwa Waziri amekua kama mtoto wa mfugaji, kazaliwa kwenye jamii ya ufugaji, anatoka Kanda ya Ziwa, anaelewa uvuvi. Ukikaa na Mheshimiwa Waziri, maono aliyokuwanayo kwa Wizara yake ni makubwa, lakini hana fedha, atafanya nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nieleze umuhimu wa utafiti, sayansi na teknolojia katika kilimo. Kwa Kiingereza tunasema, science and technology innovation in agriculture. Tunasikitika, bajeti ya ugani iko wapi? Bajeti ya utafiti ikoje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma kitabu chote, leo hii nchi yetu ina watu takriban milioni 50, baada ya miaka 10 tutakuwa na watu zaidi ya milioni 65. Hakuna mpango mkakati wa kutuvusha kutupeleka huko na yote Mheshimiwa Waziri siyo kosa lake; huna utafiti, uta-project vipi? Utapangaje mipango yako vizuri kama hujafanya utafiti?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na yote, niwaambieni, dunia nzima kati ya watafiti wanaoheshimika ni Tanzania. Kigoma Watanzania walifanya utafiti wa mbegu ya michikichi ambayo Malyasia ndio wanatumia. Leo hii niwaambieni, kuna Mtanzania mmoja alikuwa Serikalini, amefyatuliwa risasi juu, amechukuliwa na Bill Gates Foundation Marekani kama mtafiti na aliombwa abaki kule afundishe masomo ya kilimo, lakini amechukua uzalendo wake, amerudi Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umuhimu wa utafiti naomba niwaambieni Serikali, leo hii mjiulize kwenye uvuvi, Ziwa Victoria sisi ndio wenye sehemu kubwa, lakini ukienda kwenye statistics za dunia, Uganda imetupita, yenyewe ni ya sita katika uvuvi wa Ziwa Victoria. Sisi ni wa nane, kwa nini? Leo hii tujiulize Bukoba kahawa mwaka 1978, miaka 30 na kitu iliyopita walikuwa wanazalisha zaidi ya tani 140,000, lakini leo kwenye kitabu mmeona, tuna-project kuvuna tani 47,000 kwa sababu hatujafanya tafiti ya kuendeleza hizi kahawa. Miche imekuwa mikuu, haizalishi, imekuwa dormant. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba tu niwaeleze umuhimu wa science and technology innovation. Leo hii tunafurahi hapa kusema kwamba tunalisha East and Central Africa, lakini tusipojipanga vizuri, tunu hii tuliyopewa na Mwenyezi Mungu tutaikosa, Malawi wamejipanga kwenye pamba. Malawi ni nchi ndogo, lakini leo hii inaenda kutupita kwenye uzalishaji wa pamba kwa sababu ya tafiti na kujipanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kuongelea suala la mbegu. Tumejaribu sana kuendeleza kilimo. Nashukuru Serikali ilijaribu kutoa matrekta, lakini hebu tuweke azimio, Mheshimiwa Waziri, kaa chini. Vituo unavyo, mahitaji unayajua, sitaki kuzungumzia sana yaliyokuwemo humu. Hebu tusonge mbele, tuwafunge watu midogo. Tuweke azimio kwamba Serikali ihakikishe kila mkulima anapata mbegu bora. Wakulima wetu wamekuwa wanatumia nafaka. Nendeni mkasome muone tofauti ya mbegu na nafaka (seed and grain). Mkulima analima heka yake moja, akivuna mahindi, yale yale aliyoyavuna, anahifadhi anaifanya mbegu. Siyo mbegu! Atajikuta alivuna mawili atabaki na moja. Kwa hiyo, tuweke azimio, uwezo huo tunao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, naomba kuzungumzia Mkoa wangu wa Dodoma. Mkoa wa Dodoma unafanya tremendous kwenye kilimo, ingawa watu wanajua kwamba ni kame. Msimu wa mwaka 2013/2014 Tanzania iliuza tani 860,000 China, kati ya hizo tani 300,000 ufuta umetokea hapa Dodoma. Tuna maonyesho ya Nane Nane. Pale inaonekana mazao yote yanawezekana. Kwani ile ardhi ya Nane Nane ni ya wapi? Ni Arusha? Siyo ya Dodoma! Lakini humu sijaona Mheshimiwa Waziri. Nina vijana wengi na kila siku nawapigia kelele waingie kwenye kilimo. Hebu tuhamishe basi ile Nane Nane tuipeleke Chamwino, tuipeleke Kondoa, tuipeleke Chubi. (Makofi)

Mheshimiwa Ally Saleh kauliza kuhusu shamba kubwa, twende Chubi kwa Mheshimiwa Kijaji ukaone shamba kubwa za hizo heka unazosema na mwekezaji ujifunze. Tembea, no research, no right to speak. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naongea kwa sababu niko field, najua raha ya kilimo, najua machungu ya kilimo, najua mafanikio na ninajua tukiweka nguvu kidogo, tutafika mbali. Nataka sana vijana. Vijana wanataka red market, wanataka mitaji, hatuna sehemu ya kuwapeleka zaidi ya kilimo. Tuwekeze jamani! Leo hii haiwezekani, nchi ya Egypt ina River Nile peke yake. Source ya River Nile ni Lake Victoria. Kale ka-Nile kanatokana na Lake Victoria wanakatumia, wanafanikiwa vibaya mno! Sisi wenye Ziwa Victoria, wenye Ruvu na mito kibao hatuongei, kwa nini tunashindwa kutumia hizi fursa? Tumeona mwenyewe Mheshimiwa Waziri umeshasema hii ndiyo sekta ambayo inaleta pesa kuliko zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nigusie kwenye uvuvi katika Ziwa Victoria, kuna samaki anaitwa sangara. Sangara jamani…(Makofi)

(Hapa kengele ililie kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi kuweza kutoa mchango wangu kwenye Wizara hii ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo moja naomba nilitolee ufafanuzi. Serikali iliyokuwepo madarakani ni Serikali ya Chama cha Mapinduzi; Serikali ya Awamu ya Tano ya Chama cha Mapinduzi na inatekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015/2020. Sasa leo hii unatofautishaje Serikali ya Chama cha Mapinduzi na Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Awamu ya kwanza ilikuwa ni ya CCM, ya pili ya CCM, ya tatu ya CCM, ya nne ya CCM na ya tano ya CCM. Leo hii Mheshimiwa Rais Magufuli akizindua kiwanda ambacho jiwe la msingi liliwekwa na Kikwete hapo kuna tatizo gani? Maana watu wanaleta hoja ambazo hazina mashiko. Tumepewa nafasi hii kutoa michango naomba tutoe michango ambayo inaleta tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mdogo tu mimi Mzaramo nitatoa mfano, leo hii kaka yangu Kubenea ameenda kuoa baada ya harusi akitembea na mke wake watu watamsifu, Kubenea una mke mzuri, alimlea yeye? Ni kwa nini wasisifie wazazi waliomlea yule mke. Nimetolea
mfano, utapewa sifa wewe mume wa yule mke ingawa hujamzaa wala hujamlea wewe. Kwa hiyo, mafanikio ambayo leo hii tunajivunia ya awamu ya tano yanatokana na misingi mizuri ya Chama cha Mapinduzi na Serikali zake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais alivyokuwa anaomba ridhaa ya kuongoza nchi hii wimbo wake mkubwa ulikuwa kwamba tutajenga Tanzania yenye viwanda na ninampongeza. Mheshimiwa Rais ameanza kuweka mikakati ya kitaifa ambayo itatupeleka kwenye uchumi wa viwanda. Uwekezaji kwenye reli ulio kwenye kiwango cha standard gauge, kinaenda kuwekeza kwenye uchumi wa viwanda. Ununuzi wa ndege ambao tunafufua Shirika letu la ATCL leo hii lazima tutambue tunasafirisha minofu ya sangara kwenda nje ya nchi, tunasafirisha maua, tunasafirisha mboga mboga. Leo tumeanza kununua ndege za abiria ndogo mpaka kubwa, najua huko mbele tutaenda kununua ndege za kusafirisha mizigo. Kwa hiyo, zile bidhaa zetu tutazisafirisha kwa shirika letu, tuta-enjoy economies of scale. Kwa hiyo, lazima tutambue kwamba uwekezaji huu kwamba Mheshimiwa Rais anasimamia kauli yake na kwa level yake ya juu kabisa ameonesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye uwekezaji wa Stiegler’s Gorge kwenda kuzalisha umeme yote hii tunaona kwamba tunaenda kuelekea kwenye uchumi wa viwanda. Waliokuwepo chini ya Mheshimiwa Rais, Waheshimiwa Mawaziri hususani Waziri Mwijage, kama uthubutu wa Mheshimiwa Rais kuwekeza kwenye haya mambo je, wewe unaendana naye? Kila saa anasimama Mheshimiwa Rais kuwaambia wasaidizi wake hivi kweli mnaelewa mimi ninayoyahitaji? Je, mnasoma mimi nini ninachokitaka? Tunakuomba Mheshimiwa Mwijage lazima ujiulize mtu akikusifia makofi matatu hayazidi. Kwa hiyo, je, unaendana na ajenda? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba, mimi nina neno moja kwa Mheshimiwa Waziri naomba uwe serious kwenye hii ajenda ya viwanda na uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tatu tunaenda kujenga viwanda na viwanda tayari vipo vya ndani tunavilindaje? Maana kuanzisha kiwanda ni jambo moja, lakini kuvifanya viwanda hivi viwe endelevu na vizidi kukua lazima tuweke ajenda muhimu je, Mheshimiwa Waziri naomba ukiwa unakuja kujibu hoja utuambie una mipango mikakati gani gani ya kulinda hivi viwanda ambavyo tunavianzisha? Unaweza ukaanzisha viwanda vikatoa bidhaa visinunulike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunawaambia wananchi wetu tuwe wazalendo tununue bidhaa za ndani, lakini unaweze ukakuta nguo kutoka China ina bei nafuu kuliko nguo iliyotengenezwa Mwatex na haya matatizo tunasababisha wenyewe, viwanda vya ndani vinaonewa, urasimu ni mwingi, umangimeza umejaa, utitiri wa kodi na usumbufu ambao hauna sababu. Mwenye kiwanda atafuatwa Halmashauri, atafuatwa na Mbunge, Diwani, OSHA na Wizara, yaani imekuwa ni usumbufu. Tunawaambia wawekeze hela, tunawapa pressure katika kurudisha mitaji yao na kuweza kujiendeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano mdogo, leo hii mtu akileta nyuzi ama nguo kutoka nje ya nchi, ataleta estimates za uongo atawekewa kodi ndogo, lakini huyu mwenye kiwanda ndani atakuwa charged kodi nyingi, hatimaye cost of production inakuwa kubwa anashindwa kufikia break even, anafeli. Kwa hiyo, lazima tuangalie na tuwe na mikakati. Naomba na nasisitiza ukiwa unajibu hoja unijibu kwamba una mikakati gani katika kulinda hivi viwanda na uwekezaji wa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu chochote lazima kiwe na washika dau. Waheshimiwa Mawaziri wote kwa ujumla hasa Waziri wa Viwanda, jamani msiwaogope wafanyabiashara na wawekezaji, hii inaenda kwenu Waheshimiwa Mawaziri na watendaji, mfanyabiashara ataomba appointment na kuonana na Waziri au mtendaji mtamkwepa, mnamkwepa nini. Yule ndiye mdau wako, kaa naye ujue changamoto zake na yeye umueleze mambo na mikakati ya Serikali. Utapigiwa simu na mwekezaji aah naogopa, hutaki kumuona wa nini? Utapata wapi information za kukusaidia? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mtu mla rushwa atakuwa mla rushwa tu, rushwa zina aina nyingi sana kupatikana, kwa hiyo, tusiwekewe hawa watu. Pia nikupongeze MheshimiwaMwijage maana naona jana ulialika wadau wako wamiliki wa viwanda akiwemo Mzee wangu Kilua mmiliki wa Kilua Group. Kwa hiyo, hilo nalo nikupongeze, lakini wengine wote tusiwaogope hawa ni wenzetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasema when government walks, business community runs. Kwa hiyo hawa ni wadau wetu tusiwakwepe, tukae nao tujue changamoto tuweze kusaidiana kupeleka gurudumu la maendeleo mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala naomba niliweke vizuri na na-declare interest kwamba mimi ni mkulima na ni mchuuzi wa mazao. Kwa hiyo, nikiongelea natafuta soko la ufuta nafuatilia kwenye soko la dunia na vilevile nchi za wenzetu hali yao ya kuvuna, maana lazima tuelewe si Tanzania peke yake duniani ndiyo inayolima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa tu mtambue kwa mujibu wa FAO, India ndiyo nchi ya kwanza inayolima mbaazi duniani, lakini India ndio nchi ya kwanza ambayo pia inanunua mbaazi duniani. Yote ni kwa sababu India ndiye mtumiaji wa kwanza wa mbaazi, tofauti na chakula India anakamua mbaazi mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichotokea msimu wa mwaka 2017/2018 kuhusu mbaazi maana shutuma nyingi zinakwenda kwa Serikali, penye kushauri tushauri ukweli, penye kukosoa tukosoe ukweli na kwenye kusifia tusifie ukweli. I am talking because I know. Mimi nilikuwa nafuatilia suala la mbaazi, kilichotokea msimu uliopita India ili-over produce mbaazi. (Makofi)

Mimi nilikuwepo kule na nikaenda Lower House Bungeni kwao na siku hiyo nilikuta mjadala Wabunge wa Upinzani wamewachachamalia Serikali wakiwaambia najua mmeenda nchi za Afrika ikiwemo Tanzania mmekubaliana kwamba mta-import mbaazi kutoka kwao, sasa wakulima wetu wamelima hawana soko, tunaomba muweke ban kwenye importation ya mbaazi kutoka nchi za Afrika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tuliaothirika sio Tanzania peke yake ni pamoja hata na jirani zetu Malawi ambao wanalima kuliko sisi. Kwa hiyo, sasa usiwe wimbo wa kuikosoa Serikali; mnyonge mnyongeni haki yake mpeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ndiyo maana naunga mkono jibu la Naibu Waziri alilosema kwamba hata na sisi tujifunze kula mbaazi, sisi ni Wabunge tumeaminiwa lazima tujiongeze kwenye kudadavua mambo, hajamaanisha ukapike nyumbani kwako, tu-cultivate tabia ya sisi wa kwanza kutumia bidhaa tunazozizalisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nikaenda mbali nikasema ili Serikali muwe mfano, basi kule magerezani na mashuleni tunapeleka vyakula tuwafundishe kule kula mbaazi instead of maharage ili ninyi muanze kama mfano. Sisi tunapoenda Mjimboni mwezi mtukufu wa Ramadhani watu mnaongelea mafuta, sukari tuseme na mbaazi, hata kiafya ni nzuri. Kwa hiyo, lazima sisi tuwe mfano, bidhaa zetu sisi tuwe watumiaji wa kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ndicho kinachotukuta, ufuta wote tunautoa nje kwa sababu hatujui umuhimu. Unaambiwa duniani hata hii alizeti tunaongea cholesterol free it’s not true, mafuta ambayo hayana rehemu kabisa ni mawili, mafuta ya ufuta na mafuta ya nguruwe (pig fat), that is the truth. Kwa hiyo, leo hii tunasafirisha ufuta wote kwenda nje kwa sababu hatupo aware kuhusu... (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi naunga mkono hoja nawashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehma mwenye kurehemu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, napenda kukushukuru wewe, Mheshimiwa mtani wangu, maana niliona mbona napitwa, muda unazidi kwenda na mimi sipati nafasi. Napenda ni-declare interest, mimi ni mkulima. Tumezoea kusikia mtoto wa mkulima, mtoto wa mfugaji, mimi ni mtoto wa kishua, lakini ni mkulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuanza kwa kusema, naipongeza Tanzania, napongeza Serikali zote za Chama cha Mapinduzi kuanzia Awamu ya Kwanza, ya Pili, ya Tatu, ya Nne na hii ya Tano.
Waheshimiwa Wabunge wenzangu, huu mchezo hauhitaji hasira na msema ukweli mpenzi wa Mungu. Kama wewe unasema tupo nyuma, India wanatambua korosho bora inapatikana Tanzania, dunia inatambua mwaka 2015 kwa mujibu wa FAO kati ya nchi 10 duniani zinazoongoza kwa kuzalisha ndizi, Tanzania imo. Pamoja na yote, tumo kwenye ramani. Serikali zetu zimekuwa zikihangaika na kilimo na zinazidi kuboresha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Rais, ametuletea wahusika ambao watatuvusha. Nina uhakika kipindi hiki cha 2015 na ninamwomba Mheshimiwa Rais, hii timu wasiibadilishe mpaka tufike 2025; Mheshimiwa Mwigulu na mwenzake watatuvusha mbali sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo ya kuyaboresha ili tufike mbali. Cha kwanza ni sera, kwa sababu kuna vitu tunashangaa tu. Leo hii haiwezekani mbegu inayozalishwa hapa nchini iwe inatozwa ushuru mkubwa kuliko mbegu inayoagizwa kutoka nje. Kwa sababu wataalam wanasema, mbegu inatakiwa ifanyiwe tafiti mahali husika. Kuna factors nyingi za hali ya hewa na aina ya udongo uliopo. Kwa hiyo, tukibadilisha hizi sera zetu, namwomba Mheshimiwa Waziri akae chini apitie sera zilizopo, je, zinaendena na wakati? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi zitamsaidia yeye maana kuna watu wameshaanza kumtisha, na mimi nikakumbuka, ametaja baadhi ya Mawaziri ambao walipitia Wizara yako leo hii hawajarudi, nikakumbuka na baba yangu mdogo yumo kipenzi changu Mheshimiwa Adam Malima, na yeye alipita huko hajarudi, lakini nasema kwamba Mheshimiwa Mwigulu utaiweza na itakufikisha sehemu ambapo wewe unapaota, angalia hizi sera! (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo moja limechangiwa sana na watu hapa, mimi ni mwana maendeleo, ni kijana, ninalinda interest ya kundi kubwa ambalo lina-constitute hii nchi. Kuna watu mnawasema vibaya, jamani wafanyabiashara wamo humu, kuna biashara ambayo haina channel of distribution? Kwenye biashara lazima una producer, una mtu wa katikati ambaye anapeleka kwa final consumer. Kwa nini kwenye kilimo huyu mtu wa kati anapigwa sana vita? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliomba ridhaa kwa Wana-Dodoma hususan vijana kuja kuwawakilisha, mimi mkisema hivyo mnaniumiza. Nina vijana wengi sana ambao wanafanya biashara za mazao na naomba kuwasemea, wanafanya kazi kubwa kuisaidia Serikali kuendesha kilimo. Hawa watu wana-invest kule. Ninyi mnapochelewa kupeleka mbegu, hawa ndio wanaenda kuwapa wakulima mbegu na muda mwingine inaweza kutokea mvua hazijatosha, hawajapata kitu. Hela zao wao ndio zinakuwa zimepotea.
Naomba tuwaendeleze hawa, tuone ni namna gani ya kuimarisha mahusiano baina ya wakulima na hawa vijana wetu. Haiwezekani leo hii tumsifie kijana Mtanzania anayeenda kuchukua nguo China kuja kuuza, tumkandamize huyu ambaye aliamua kufanya kazi na mkulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo mengi, nimeshauri sana tangu niwe Mbunge kwa sababu nina interest na kilimo na ninajua kilimo ndiyo cha kututoa.
Napenda kuzungumzia vijana. Kuna kundi moja la vijana ambao ni wahitimu wa Vyuo Vikuu, imekuwa kwao tatizo ni ajira, lakini wapo ambao wanajitolea, mmojawapo ni mimi. Tangu nilipomaliza diploma niliamua kuingia kwenye kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaelekea kwenye uchumi wa viwanda, lakini hawa vijana kutumia vile vyeti vyao tu kama collateral na Serikali iwasimamie vizuri, waweze kuwezeshwa kufanya kilimo chenye tija na cha biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unaweza ukaunda kundi la hawa wahitimu mmoja akiwa mtaalam kutoka SUA mwingine awe accountant, mwingine awe mtu wa procurement, mwingine awe marketing; wakiungana hao wakaenda shambani na ukawawezesha kwa nyenzo, wakaenda kulima, wakauza, watafanikiwa na wao wenyewe watakuwa ni source ya ajira kwa vijana wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo mengi sana ya kuchangia, nitaandika kwenye mchango wa maandishi. Tunataka kumtoa Mtanzania kwenye kilimo cha jembe, Mheshimiwa Mwigulu thubutu na utaweza. Weka sera ya kila kijiji kiwe na trekta. Tuna vijiji 19,200 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012; ukipiga hesabu ya trekta moja farm track ya milioni 35 na hiyo ni bei ya hapa Tanzania, inakuja hesabu ya kama shilingi bilioni 600.7. Ukithubutu utaweza kwa awamu, sio vijiji vyote vitahitaji! Utaweza na utakuwa umeacha trade mark ambayo haitafutika mioyoni mwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri, kwa kuwa tunataka tuweke uchumi wa viwanda, tufanye kilimo cha biashara. Naomba tuanzishe agricultural zones, ifahamike. Ukanda ambao unalima ndizi, u-concetrate, uboreshe mbegu nzuri za ndizi ambazo tutaweza ku-export. Tunaweza kwenda Bukoba na Mbeya hawa wakawa zones za kulima ndizi, machungwa kwa watani zangu Tanga, mananasi kwa watani zangu Wasukuma Geita, pamoja na kwa kaka yangu Mheshimiwa Ridhiwani, ikawa ni zone kwa ajili ya mananasi. Tuna kilimo cha maua, leo hii Songwe, Mbeya, Iringa Arusha na uzuri miundombinu ipo, kuna airport, we can export fresh flowers to Europe and elsewhere in the world. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikirudi kwetu Kanda ya Kati tukazanie kwenye alizeti, ufuta, choroko, dengu, mbaazi and I tell you Tanzania ni nchi ya tatu katika Afrika ku-produce mbaazi. Tunatengeneza mbaazi nzuri kweli! Mpwapwa kwa Mzee Lubeleje ndio wanatengeneza the best karanga in the world ambayo inatoa mafuta mazuri. Kwa nini tusitumie fursa hii kwa ajili ya kupata kipato kikubwa katika nchi yetu?
MHE. MARIAM D. MZUZURI: Kwa hiyo, nashukuru sana. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti ni suala muhimu linalowezesha kupata taarifa sahihi na kuwezesha kuweka mipango mbalimbali ya nchi. Ili kupata maendeleo endelevu katika michezo, ni muhimu kuwa na taarifa sahihi zilizofanyiwa utafiti. Serikali imefanya tafiti nyingi kama vile michezo kwa watu wenye ulemavu, michezo na UKIMWI, haiba na michezo na kadhalika. Bado kuna maeneo mengi ya michezo yanahitaji kufanyiwa tafiti ili kuongeza tija katika sekta ya michezo nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo tatizo la kukosekana mfumo endelevu wa kuviendeleza vipaji vinavyoibuliwa na kuwa na miundombinu isiyokidhi mahitaji. Vilevile somo la elimu ya michezo limekuwa halifundishwi kikamilifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya mwaka 2002 hadi 2007 kulifanyika utafiti uliofanywa na Idara ya Elimu ya Michezo na Utamaduni ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ulioonyesha kwamba vipindi vya masomo ya michezo katika shule za sekondari za Serikali na binafsi vimekuwa vikitumika kufundisha masomo mengine badala ya elimu ya michezo na michezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, tafiti hizi zilibainisha ukosefu wa walimu wenye sifa stahiki za kufundisha elimu ya michezo kuwa ni changamoto kwa shule za Serikali na binafsi nchini. Nashauri Mheshimiwa Waziri aanze na shule za binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokuwepo kwa mfumo na utaratibu mzuri wa ufuatiliaji na tathmini katika michezo kumeendelea kuathiri upatikanaji wa taarifa na mapato halisi yanayotokana na ajira za wanamichezo. Hali hii imeathiri wachezaji na wadau mbalimbali kuwekeza katika sekta hii ikilinganishwa na nchi kama Nigeria, Ivory Coast, Ghana na Afrika ya Kusini ambazo zimefanikiwa kupitia michezo. Mheshimiwa Waziri, hili linaendana sambamba na sanaa, hususan muziki wa kizazi kipya. Kwa mfano, Diamond ndiye msanii anayelipwa zaidi kuliko msanii yeyote Afrika Mashariki na Kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka Disemba, 2015, Tanzania ilikuwa na wachezaji takribani kumi wanaocheza michezo ya kulipwa nje ya nchi. Tisa ni wa soka na mmoja wa mpira wa kikapu. Hata hivyo, mtazamo wa jamii haujajielekeza kutambua kuwa michezo ina michango katika kukuza uchumi wa nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshauri Mheshimiwa Waziri, tuweze kutafuta wabia zaidi tuweze kujenga sports academy kama ile Jakaya Kikwete Sports Academy, ikiwezekana kila mkoa au angalau kila kanda kwa kuanzia.
Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Uamuzi wake wa Kuendeleza Mji wa Dodoma na Kuupa Hadhi ya Jiji
MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Awali ya yote napenda kusema kwamba naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Simbachawene kwa asilimia mia moja. Pia nampongeza Mheshimiwa Rais, kwa kweli amekuwa kwa hakika akiwa ni mtekelezaji mzuri wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Kwa kulifanya Dodoma kuwa Jiji, tuna uhakika sasa kweli Makao Makuu ya nchi yapo Mkoa wa Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, narejea tena kumpongeza Mheshimiwa Rais na nimwambie, mimi kama mwakilishi wa vijana kutoka Mkoa wa Dodoma ambao sisi ndio tupo zaidi ya asilimia 60 ya population kwamba hilo tumelipokea na kwa kweli tutapokea changamoto zote na Dodoma kweli litakuwa Jiji. Niseme tu, kwa hili kumrudishia, tunajua mtanange 2020 upo, atashinda kwa asilimia kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna nchi za wenzetu hapa Afrika zimeweza. Mfano Nigeria na ya pili, South Africa. Kama wao wameweza na sisi tutaweza. Kwa hiyo, kama kuna mtu yeyote ambaye hajaunga mkono hoja hii, ajue kwamba sisi tumeweza na tutaweza. Kwa hiyo, la msingi tu apande pamoja na sisi tushirikiane kwa ajili ya kuhamisha Makao yetu Makuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, Mheshimiwa Rais alisema Morogoro kwamba katikati pazuri. Dodoma tumelala katikati ya nchi ya Tanzania na tunaona barabara imejengwa chini ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi, kuunganisha Iringa, Arusha na nchi ambazo zipo Kanda ya Ziwa. (Makofi)

Kwa hiyo, kuweka Makao Makuu hapa katikati kutarahisisha hata uchumi wa ujenzi wa viwanda na huduma zote. Mtu kutoka Arusha ili apate huduma za Kiserikali hawezi kuzunguka kwenda mpaka Dar es Salaam. Mtu kutoka Iringa, Mbeya ni rahisi kufika Dodoma kupata huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme jamani, katikati pazuri. Kweli Mheshimiwa Rais tunamshukuru, naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali (Na. 2) wa Mwaka 2019 (Toleo la Kiingereza).
MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwa kweli leo hii nitajikita kwenye kuongelea mchuzi wa zabibu. Kila siku nikiwa nachangia masuala ya kilimo nasema tujikite kwenye agricultural zone. Leo hii kulibeba zao la zabibu kwa Mkoa wa Dodoma, ndio mambo yenyewe tunaenda kuyatengeneza vizuri. Msimu uliopita wakulima wetu zabibu ziliozea kwenye mashamba na sababu inajulikana. Wale wenye viwanda vikubwa hapa Dodoma ambao CETAWICO pamoja na Alko Vintage yake matanki yao ya kuhifadhi michuzi yalijaa kutokana na tozo ilivyokuwa kubwa walishindwa kwenda kuuza ule mchuzi, kwa hiyo effect yake ikashuka kwa mkulima, walishindwa kuuza zabibu, zabibu zikaoza. Kwa hiyo, niseme hatua ya kupunguza punguzo kubwa sana litaenda kuwahakikishia soko la zabibu za wakulima wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waswahili wanasema usione vinaelea vimeundwa. kwa namna ya kipekee nikupongeze umekuwa pioneer kwenye kutetea punguzo hili; mbele ya Waziri Mkuu na Rais uliongea. Mwingine pia Mbunge wangu wa Dodoma Mjini Mheshimiwa Anthony Peter Mavunde ambaye anajinasibu kwa kusema yeye ni mtumishi wa watu (De populo servorum) sijui kama nimepatia Kigogo hiki. Mbele ya Rais tarehe 3 Novemba, wakati wa ufunguzi wa NMB aliomba hili punguzo mbele ya Waziri Mkuu na Mbele ya Makamu wa Rais aliomba hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna siku nimeambatana naye mpaka Ofisi za TRA akitetea punguzo hili, hawezi kujisemea humu ndani lakini naomba niwahakikishie wakulima wote wa Dodoma Mjini kwenye hili Mbunge wenu amelipigania na fadhila mumrudishe 2020 kijana wenu, aliwasemea na kweli amehakikisha yeye ni mtumishi wenu. Atapita bila kupingwa, hilo linajulikana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nasema mbona tunaanza kusutana? Wameongea wamesikika, mambo yamerekebishika wanaanza tena kusuta ooh! Mheshimiwa Dkt. Mpango hasikii, amesikia. Asingerekibisha wangesema nini? Kwa hiyo, ifike hatua kama kweli tunashauri ili mambo yawe vizuri, basi tusifie tuendelee kuongezea nyama sio tunaanza tena kusutana sutana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, napenda pale pale uliposema wewe kuhusu hii import permit. Jamani hata kwenye suala la uchenjuaji walivyosema kwamba kama kuchenjua kufanyike kwenye mkoa ule ule ambao, tumeona effect yake. Kulikuwa wanaoleta madini yao kutoka Congo na Kenya kuja kuchenjua, tumekosa mapato kutokana na hilo. Kama leo vijana wetu wanapata uwezo wanaenda huko Mozambique na wapi kuchukua madini kuja ku-process hapa kwa nini tuanze kuleta vikwazo? Kwa kweli kwenye hili Mheshimiwa Waziri wa Fedha kama vile tunavyom-appreciate yeye ni msikivu na mwelewa, hebu aangalie namna ya kuliweka sawa. Yote haya tunataka vijana wetu wapate ajira na vilevile nchi yetu iweze kupata mapato kama wanavyofanya Awamu ya Tano wanajenga vituo vya afya, tunaona kodi, hata TRA acheni wachukue kodi ya majengo, wananchi wanaona namna Serikali ya Awamu ya Tano inavyorudi kwao na mapato yanatumika vizuri na kwa uwazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa nafasi uliyonipa. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa fursa hii ya kuweza kuchangia katika hoja zilizo mbele yetu. Kwa vile ni mara yangu ya kwanza kusimama mbele ya Bunge hili Tukufu, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa Rehema, kwa kuniwezesha kuwa mwakilishi wa vijana katika Bunge hili Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijikite moja kwa moja kwenye mchango wangu. Naanza na asilimia tano ya mikopo kwa vijana kutoka kwenye mapato ya ndani ya Halmashauri zetu. Naomba kuishauri Serikali kwamba hili jambo ni la kutilia mkazo maana limekuwa kama ngonjera. Kila siku watu wanaongelea kwamba kuna 10% Halmashauri zinatakiwa zitoe 5% iende kwenye vikundi vya akinamama na 5% ziende kwenye vikundi vya vijana lakini haifanyiki hivyo.
Mheshimiwa Spika, sasa kwa Serikali hii ya Awamu ya Tano na kasi yake iliyoanza nayo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi basi tunasema na hawa watu wa Halmashauri wajue kwamba huu ni wajibu, ni lazima watoe hizi fedha. Pia siyo kutoa tu zipangiwe utaratibu maana hii ni mikopo, lengo lake ni kwenda kuwasaidia hawa vijana waweze kufanya kazi, waweze kuinua kipato chao na vilevile hizi pesa zirudi ili vijana wengine wapate hiyo fursa. Kwa hiyo, uwekwe utaratibu mzuri wa kuzikopesha na kuzirudisha ili ziwe endelevu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri awaambie Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya walisimamie kwa karibu jambo hili. Huu ni mpango wa Serikali lakini tumeona kuna vyama vingine vya siasa sijui wanalewa madaraka, juzi tu wameanza kutoa hundi, ooh, mapesa ya UKAWA, mapesa ya UKAWA ya wapi? Basi na sisi wa CCM kwenye Halmashauri tunazoziongoza tuanze kusema ni hela za CCM. Kwa hiyo, naomba ifahamike kwa wananchi kwamba huu ni mpango wa Serikali na siyo mpango wa vyama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye elimu. Napenda kuipongeza Serikali hii, tangu tulipokuwa tunaomba ridhaa kwa wananchi tulisema kwamba tuko kwa ajili ya kuwasaidia wananchi. Mmethubutu na mmeweza kuleta elimu msingi bila ya malipo, kazeni buti mwende mbele. Kitu chochote chenye neema lazima kiendane na changamoto. Tumeona udahili umeongezeka baada ya kuwawezesha wananchi kwani ile Sh. 20,000/= tu ya kumpeleka mtoto wake shule ilikuwa inamshinda.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kutokana na neema hii kuna vitu vimeambatana nayo, kuna upungufu wa madarasa, Walimu, matundu ya vyoo halikadhalika na kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya hawa Walimu wetu. Nashauri katika kila Halmashauri waweke mpango mzuri wa kuweza kutatua matatizo ambayo yanaambatana na neema hii bila kusahau madawati. Pia niwakumbushe tu ameshaongea Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba kila Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi zile mbao mlizozikamata jamani ziende zikatengeneze madawati, ameongea bosi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niongelee kuhusu sekta ya afya katika upatikanaji vifaa tiba na dawa. Hii imekuwa changamoto ambayo najua Serikali inajaribu kuikabili kutwa kucha. Tunaelekea kwenye uchumi wa viwanda, tukaeni chini tuna wataalam, Wizara yetu ya TAMISEMI ikishirikiana na Wizara ya Afya, Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Wizara ya Viwanda na Biashara kwani hatuwezi sisi kama Tanzania kuwa na viwanda ambavyo vitatengeneza dawa? Nina uhakika malighafi za kutengenezea dawa zipo.
Mheshimiwa Spika, Watani zangu Wahaya mtu akiumwa kichwa hanywi panadol ana dawa zake anazitumia. Nina uhakika malighafi za kutengeneza dawa tunazo, hiyo itatuokoa kwanza tutakuwa tunazalisha dawa zetu hapa, tutapata kipato soko lipo na pia dawa zitakuwa zinapatikana kwa bei nafuu na tutawaepuka hawa matapeli ambao wanatafuta fursa ya kuleta dawa ambazo zimepitwa na muda na siyo nzuri kwa matumizi ya binadamu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kuzungumzia mradi wa uendelezaji miji ya kimkakati. Kwa Mkoa wetu wa Dodoma huu mradi umetusaidia sana kwenye maeneo ya Kisasa, Nkuhungu, Mjini Kati na Kikuyu. Kwa kweli mradi huu ulivyotekelezwa hapa mmetupa moyo, kweli mnatuheshimu kwamba hapa ni Makao Makuu ya Chama na Serikali. Kwa hiyo, naomba mradi huu uendelee kwenye sekta zingine za miundombinu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kugusia Tume ya Utumishi wa Walimu. Hiki kimekuwa ni kilio kikubwa sana kwa Walimu wetu. Tunajua mchango wao katika maendeleo ya Taifa letu kwa sababu aliyekuwa anaajiri Mwalimu ni mwingine, aliyekuwa anashughulika na kuwalipa Walimu ni mwingine, aliyekuwa anashughulika na kumpandisha cheo Mwalimu ni mwingine, aliyekuwa anashughulika na malipo ya Mwalimu ni mwingine, lakini Tume hii ya Utumishi itakuja kuwa mkombozi wa Mwalimu, hongera sana kwa Serikali yetu. Kwenye bajeti hii tumeona mmeshawawekea fungu lakini tunaomba kwa siku za karibuni muweze kukamilisha taratibu zote ili hii Tume ipewe meno ianze kazi haraka sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nigusie kidogo mipango ya matumizi bora ya ardhi. Wataalam wetu katika Halmashauri wakishirikiana na Viongozi wa Vijiji, Kata, pamoja na Wilaya na Madiwani wapange mipango bora ya ardhi kwa sababu huko ndiko kwenye wananchi na wanajua changamoto zinazotokea na ambazo zinaleta ugomvi kati ya wakulima na wafugaji. Tukikazania huko hili tatizo litakuwa historia kwa sababu wananchi wanaumia jamani. Sisi tupo huku lakini wananchi wa Kongwa tunaumia sana kwa hii migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia napenda tu kugusia kwa hawa watumishi wa Halmashauri, kuna hawa Mabwana Kilimo, Mabwana Mifugo na Maafisa Biashara, majipu tusiangalie wale wanaofuja pesa tu tuwaangalie hata wale watumishi ambao hawatoi deliverance. Wananchi wetu wanajitahidi kujikwamua kwa kuendesha shughuli za kilimo na biashara lakini hawa wataalam hawawasaidii. Vijana wengi wapo hapa Dodoma wanafanya biashara ya uchuuzi wa mazao lakini hakuna Afisa Biashara hata siku moja kamfuata kumpa ushauri wa kitaalam. Vilevile Serikali ifike kipindi iwasaidie na kuwa-guarantee hawa vijana waweze kupata mikopo na wakopesheke. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kuongelea makusanyo ya mapato. Mheshimiwa Waziri Mkuu ameshaongea, Halmashauri wasipofikisha 80% ya ukusanyaji wa mapato waliokadiriwa zitafutwa. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu hii kauli iwe ni ya kweli, kama Halmashauri haijafika hicho kiwango basi ifutwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kugusia kwa juu tu kuhusu TASAF III, TASAF inasaidia sana. Tumeona TASAF I, TASAF II na sasa hivi tupo kwenye TASAF III ni kweli inasaidia wananchi wenye kipato cha chini na kaya maskini. Tunaomba TASAF iendelee na moyo huohuo, kelele nyingi na matatizo tuliyokutana nayo huko ni ya kisiasa kwa sababu wenzetu walisema, ooh, hizi hela zinakuja kwa ajili ya kampeni, siyo kweli, zinasaidia wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kuongelea PCCB, tumeona utendaji kazi wao mzuri, wanashughulikia masuala ya rushwa lakini kwenye ripoti zao tumeona wakiongelea, ooh, tume-save fedha kiasi fulani lakini kuna rushwa fulani sijui kwa nini inafichwa. Rushwa hii inaumiza kweli kweli, inawaathiri watu kisaikolojia, inasababisha watu wapate magonjwa, wengine hata wakate tamaa za maisha, ni section 25, rushwa ya ngono hasa kwa mtoto wa kike.
Mheshimiwa Spika, mtoto wa kike tangu elimu ya msingi anasumbuliwa na rushwa ya ngono, kwenye elimu ya sekondari anasumbuliwa na rushwa ya ngono, akija chuo kikuu anasumbuliwa na rushwa hii ya ngono, akija kwenye kazi anasumbuliwa na rushwa ya ngono. Jamani kama kesi zipo tunaomba zielezwe ili hawa mabinti wasifiche na waseme haya matatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na naunga mkono hoja kwa asilimia mia mbili.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Kilimo
MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kutoa mchango wangu. Natangulia kwa kusema kauli inayosema nitasema ukweli daima fitina kwangu mwiko. Naenda kuchangia ukweli siyo fitina wala majungu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, napenda kuwapongeza viongozi wetu wakuu wawili: Rais wa nchi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na Waziri Mkuu, wameonekana namna gani wana dhamira ya dhati kuwasaidia Watanzania. Katika ziara zake zote Mheshimiwa Rais lazima atatue matatizo ya wakulima, hata Waziri Mkuu tumeona akihangaika kwenye kahawa, korosho, tumbaku kwa kweli hawa viongozi wetu kwenye hili wanapaswa kupongezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Dkt. Tizeba ni swahiba wangu lakini leo naomba nimwambie uswahiba baina yangu mimi na yeye haujazidi uswahiba niliokuwa nao na wakulima wa nchi hii. Najua jasho wanalolitoa, najua jinsi gani wanavyojikwamua na mazingira magumu lakini wanataka kupatia uchumi wetu kipato kikubwa. Kwa hiyo, leo hii nasimama kwa niaba ya wakulima wangu wa Chubi, Chamwino, Dodoma Mjini, Kondoa, Chemba, Soya, kote naomba niongelee machungu yanayowapata na naongea kwa facts. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na zao la mahindi. Tanzania ilishatoka kwenye kilimo cha subsistence, hatulimi mahindi kwa ajili ya chakula, tunalima mahindi kwa ajili ya biashara na chakula. Leo hii ripoti yake yeye mwenyewe inamsuta amesema tumezalisha zaidi ya asilimia 120, kwa hiyo, suala la yeye kulinda food security asiende kuwaumiza watu ambao tunawaambia walime kwa ajili ya biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mwenyewe ni kijana ambaye ni mkulima, nina mwaka wa saba kwenye kilimo lakini I regret to say ni mwaka wa kwanza sijalima. Nina gunia 6,500 juzi nimetoka kuzitupa zimeoza, tunaelekea wapi? It is very simple, Mheshimiwa Tizeba anakwenda kushauri viongozi wetu wakuu anawalisha matangopori kwa nini? Leo hii tayari tuna ziada na kiada ya mahindi anaenda kuweka zuio la ku-export mahindi lakini anaruhusu mahindi yaingie basi si angeacha tuminyane wenyewe ndani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkulima hajaomba mbegu hasa sisi wa Kanda ya Kati, Dodoma tunalima katika hali ngumu, anasema ili kwa Mheshimiwa Musukuma wasife njaa atuumize sisi. Musukuma ana madini, ana ziwa kule anavua samaki, sisi tunategemea kilimo, kilimo chenyewe ni cha machungu kweli kweli hatupati lolote kutoka Serikalini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii mahindi yameoza hali ni mbaya, anajibu majibu kirahisi oh hao wachuuzi, kwani wachuuzi wanaenda kununua na mawe yale mahindi? Mkulima kitu chochote akishavuna, amekaa miezi saba anasubiria kitu chini ya ardhi hajui hatma yake, anavuna mahindi yeye anachotaka apate hela aendelee na maisha, alipie watoto ada, aweze kula, aweze kujitibu anasema simply wachuuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mkiwasema wachuuzi ndiyo vijana wangu wengi wa hapa Dodoma wamejiajiri katika sekta hiyo na hawa ndiyo wa kuwasaidia. Hebu tutathmini leo hii exporters wangapi wana asili ya Kitanzania? Sasa kama hatutowashika hawa mkono kuwapandisha tutazidi tu kuwa na wale wageni ambao ndiyo wanapeleka mazao nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni-regret sana kwenye mahindi kwa kweli basi angalau ungesema tunakataza kutoa nje lakini tusiingize kutoka nje ya nchi. Leo hii Zambia wameingiza mahindi mengi Mtwara, Lindi mpaka Himo, mahindi yetu yamekwama hakuna soko, huo ndio ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye tumbaku, kwa sababu anajitetea sana Mheshimiwa Waziri. Uongozi una vitu viwili, sawa bajeti anapelekewa ndogo lakini kuna utashi, Waziri ana utashi gani, hapa umesoma hotuba yako hata hatujasisimkwa sisi kama wakulima. Bajeti ya kwanza aliongea Mheshimiwa Mwigulu hapa kila mtu alisisimka kama mkulima alisema kabisa sasa hivi yale mageti hakuna kuzuia magunia ya wakulima muwaache. Alienda kutatua kero ambayo inamgusa mkulima wa kawaida, but now nothing my friend, nothing. Sawa Waziri anapelekewa bajeti ndogo lakini utashi, ameaminiwa na Mheshimiwa Rais apeleke kilimo kwa ajili ya kuleta uchumi wa viwanda lakini ndiye yeye anavuruga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, world market price ya tumbaku, Cost, Insurance and Freight mpaka Vietnam ilikuwa kilo moja ni dola 2.20. Wanunuzi wetu hapa walikuwa tayari kwa sababu ununuzi wa tumbaku ni pre-order, walikuwa tayari kununua zaidi ya order waliyotaka lakini wakaomba wanunue kwa dola 1.3 lakini Mheshimiwa Waziri akakataa huku akijinadi kwamba ana wanunuzi. Akaenda nasema tena tangopori akamlisha Mkuu, akamlisha Mheshimiwa Waziri Mkuu lakini Wabunge wa Tabora huku walichachamaa wakasema mbona wanunuzi wanazuiwa kununua na tumbaku zinakaa muda mrefu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumbe inavyosemekana Waziri alisema kwamba wanataka kununua kwenye 0.8 lakini ilikuwa wanataka kununua kwa 1.3. Kilichotokea mvua imenyesha, hawana vihenge wale, hawana sehemu ya kuhifadhia, wanalima ili wauze waweze kuendelea na maisha mengine, tumbaku zimeharibika, zimeshuka thamani, mwisho wa siku wameuza kwa 0.8 USD. Kwa hiyo, zile pesa walizopata wameenda kulipa tu madeni hakuna chochote yaani kwa kweli wenzangu Wabunge wa Tabora watakuja kusema hali halisi, mimi ni Mbunge wa nchi nzima kwa hiyo lazima niliongelee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye korosho. Picha tunayoipata kwenye korosho kwa kweli niwaambieni siyo juhudi za Wizara, ni kudra ya Mwenyezi Mungu. Tuna advantage kwamba msimu unapoanza sisi ndiyo nchi ya kwanza ya kuvuna korosho, kwa hiyo, tunakuta makampuni mengi yanahitaji ile korosho. Ndiyo maana mpaka leo korosho ina bei ya juu tunapoona kwenye minada. Vilevile in the world Tandahimba, Newala, Masasi na Mtwara ndiyo ambao wana-produce korosho nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, I was in India, nilienda kuongea na watu kwa ajili ya kuwauzia korosho bahati mbaya niliharibu kwa sababu nilikuwa na rafiki yangu kutoka Ghana, wale waliniambia Ghana nao wana korosho nzuri but still virgin hawajagundua, basi maneno yale hayajaenda kushoto wala kulia, Ghana wamezindua Mpango wa Miaka Kumi wa Kunyanyua Kilimo cha Korosho, tusubiri tutakayoona, hatuna mipango endelevu. Bodi ya Korosho wanai-disturb, korosho ni zao la biashara, linaenda vizuri, linaleta mapato, ghafla unasema sulphur ipelekwe bure waliomba, ndiyo mahitaji ya wakulima? Mmeshindwa kuzifikisha kwa wakati korosho zikaingia magonjwa hakuna dawa ya kutibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, magunia, minada imeanza, mtu ana korosho zake nyumbani hamna magunia na yaliyomo chini naomba vyombo vya ulinzi na usalama vikachunguze mnajua wenyewe. Haya leo hii wamerudi tena nyuma, kwa nini tuna-disturb industry? Wamerudi nyuma tena wanasema ooh sulphur hatuzitoi bure, mliombwa mtoe bure? Kwa nini mna-disturb wakulima na watu wanaenda katika njia nzuri? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mipango endelevu tuliyokuwa nayo leo hii badala ya kutoa korosho kama raw material tunaenda kuongeza miche. Mimi napenda kwamba kila sehemu tulime korosho kwa sababu it is a green gold lakini nilitoa hapa mchango mwaka wa kwanza nikasema tuweke agricultural zone, kila sehemu hapa ina zao lake, kwa nini tusikazanie huko? Unaniletea mikorosho Dodoma hakuna hata Afisa Kilimo mmoja aliyefundishwa utaalamu, hiyo mikorosho ikiota asilimia 10 najiuzulu Ubunge, iko majumbani imekauka. Unawapelekea watu hujawapa utaalam, tena system unayo, kuna Maafisa Ugani kila Kata na Kijiji, waite wape elimu halafu ndiyo usambaze, hamtoi elimu mnaenda kugawa mikorosho, tutaona mwisho wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu mimi niwashauri kidogo tu, tuweke mazingira mazuri, huwezi ukampa mazingira sawa mtu anaye-process korosho na yule anayeitoa nje, hebu tuwa-favor hawa. Kuna kitu kinaitwa opportunity cost ingieni.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati Kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019
MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa fursa hii ya kuweza kuchangia kwenye taarifa ya Kamati hizi mbili. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu aliotujalia afya na uzima kuweza kukaa kwenye kikao hiki leo.

Mheshimiwa Spika, mimi ni mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini lakini pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati. Kwa hiyo nipende kumshukuru sana na kumpongeza Mwenyekiti wetu wa Kamati Mheshimiwa Kitandula kwa uongozi wake mahiri na kutuongoza vema. Tunamuombea afya na uzima ili aendelee katika majukumu yake. Pia nipende kuwashukuru sana wajumbe wa kamati hasa wale wanashiriki katika vikao na ziara kikamilifu; lakini pia niwatie joto wale ambao wanategatega katika kazi za kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kamati yetu inafanya kazi na wizara mbili, Wizara ya Nishati pamoja na Wizara ya Madini, nipende kuwapongeza sana sana Waheshimiwa Mawaziri wa Wizara hizi pamoja na Manaibu wake, pamoja na Makatibu Wakuu lakini bila kuwasahau wataalam wa wizara hizo. Kwa kweli wanafanya kazi kubwa katika kutafsiri maono ya Mheshimiwa Rais ya kuleta uchumi wa kati na Tanzania ya viwanda. Pia kubwa lile la kutaka sisi kujitegemea kama taifa huru. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sekta ya nishati, nirudie kuunga mkono kauli ya mchangiaji aliyepita Mheshimiwa Peter Serukamba ambaye amesema kwa uthubutu wa Viongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano kweli yanafanyika mapinduzi makubwa na ya kihistoria. Kwenye sekta ya nishati leo hii mtu anavyosema kwamba tuna umeme wa ziada, ndivyo taifa linatakiwa liwe kwa sababu ulichonacho na huku una mipango endelevu lazima uwe na ziada na uwe na mipango ya kuongeza zaidi na zaidi. Huwezi kusema ninahitaji thelathini na nina hiyo hiyo thelathini halafu ukasema wewe ni taifa linaloendelea. Kwa hiyo tunapoongea kwa sababu wamesema ooh, wateja ni hawa tu na huku tuna umeme wa ziada. Taifa lolote lenye mipango endelevu na ambalo liko katika process ya maendeleo lazima liwe na ziada. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeona mafanikio makubwa ya miradi hii ya umeme vijijini, awamu ya kwanza, awamu ya pili na sasa tuko kwenye awamu ya tatu ambayo ina mafanikio makubwa. Ilipanga kupeleka umeme kwenye vijiji 4,651; miezi 19 ya utekelezaji tayari vijiji 3,269 vimeshafikiwa na umeme ambayo ni sawa na asilimia 70 ya malengo waliyojiwekea. Wilaya ya Tarime ambayo ina majimbo mawili ina vijiji 88, kwenye vijiji 88 tayari vijiji zaidi ya 46 vina umeme, vijiji zaidi ya 26 vimeshaingia kwenye bajeti ya mwaka huu kazi zinaendelea kusimamisha nguzo na nyaya ili umeme uwake kwenye vijiji hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini katika nchi za Afrika ni takribani mataifa kama manne tu ikiwemo Nigeria ambao wanafanya process hii ya ku- electrify rural areas. Lakini kati ya yote sisi Tanzania tuko bora hata Angola wamekuja nyuma yetu wamekuja kujifunza Tanzania kufanya electrification kwenye vijiji vyao, kwa hiyo kazi inafanyika na sio kazi ndogo ni kazi kubwa kweli kweli.

Mheshimiwa Spika, zipo changamoto lakini uzuri wa viongozi wetu ni wasikivu. Tuliwaambia wigo (scope) ni mdogo ndio maana Wizara kupitia REA wakasema tulete awamu ya tatu mzunguko wa pili ili kufanya ujazilizi kwenye maeneo ambayo yamerukwarukwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zipo changamoto za vifaa kwamba hawa wakandarasi wanakuwa kidogo wana uzito katika kutekeleza majukumu na visingizio kwamba hawapati vifaa, lakini nashukuru kwa ushauri wa Kamati Serikali tumesikia juzi walikuwa na mkutano na wakandarasi kwa maana sasa wanachukua maoni yetu na kuyafanyia kazi. Bunge kazi yake ni kuisimamia na kuishauri Serikali, ukiacha kupitisha bajeti. Mafanikio mema ya Serikali ndio mafanikio yetu sisi Bunge. Sasa leo hii ukisimama kama Mbunge na kubeza mafanikio ya Serikali labda kwa vile ndio uki upande wa kukataa, lakini ukweli upo na unaonekana.

Mheshimiwa Spika, Shirika la TANESCO ni shirika la umma. Serikali hii ilipoingia madarakani Awamu ya Tano TANESCO ilikuwa ni shirika la madeni na shirika ambalo lilikuwa linaendeshwa kwa kupokea ruzuku kutoka Serikalini. Lakini leo tunavyoongea TANESCO inalipa madeni, TANESCO haipokei ruzuku, TANESCO haizalishi madeni, TANESCO inasonga mbele. Tunasema mapinduzi makubwa leo hii tuna ziada ya umeme, lakini bado Serikali hii kwa kutumia fedha za ndani ambazo Bunge hili ndio limeidhinisha tuna ujenzi wa umeme kwenye Bwawa la Rufiji la Nyerere. Kwa hiyo kwa kweli mambo ni makubwa na sisi kama Kamati/Wajumbe tuwatie moyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kwenye sekta ya madini kwa kupitia sheria zile mbili za mwaka 2017 lakini pia mabadiliko ya sheria ndogo ya mwaka 2019 tujivunie, Tanzania leo hii madini ni mali ya Watanzania. Leo kuna masoko ya madini, leo kuna kipengele kwa kuanzisha Tume ya Madini, kuna kitu kinaitwa local content. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mpaka mayai, kabichi yalikuwa yanaingizwa kutoka nje ya nchi, leo mama wa kawaida pale nyumbani kwa Mheshimiwa Spika anauza mayai mgodini. Sasa kama hatutofurahi kuona kwamba haya manufaa yanashuka kwa wananchi wa chini tunalipenda Taifa letu, utabeza mambo yote haya ambayo yanamgusa mpaka Mtanzania wa kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hii kule Geita inajenga refinery ambayo itaenda kutalisha haijawahi kutokea kwenye historia ya nchi. Kwanza hiyo refinery Afrika Mashariki ndio itakuwa ambayo ni modern kuliko zote, itaweza ku-process zaidi ya tani 100 ya dhahabu kwa mwaka. Dhahabu yote inayozalishwa Kanda ya Ziwa itakuwa inapandishwa thamani pale. Mambo ni makubwa nan i mengi lakini tumeona mapato, Mheshimiwa Rais alisema hatutaki sisi ndio haya mambo sasa hivi tunapiga watu wa Marekani. Wewe Marekani umemzuia sisi Mkuu wa Mkoa wetu ni mtu mkubwa, yule ni president appointee, sasa leo unamzuia asiingie nchini kwako na sisi tusijibu kisa wanatupa hela za msaada ndio maana tunataka kujitegemea ili mtu anapotoa kisu na sisi tunatoa panga msichukue tafsiri nyingine nimetumia mfano maana kwa kunani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hii tuna shirika la Twiga Mining Company hayo siyo mafanikio? Kweli hatuendi kwenye uchumi wa kati. Leo hii Tanzanite kwa ujenzi wa ukuta ilikuwa inapatikana Tanzanite kilo 147.7 leo tunapata kilo 949; mapato kwenye madini yametoka kutoka bilioni 196 mwaka 2016 mpaka bilioni 310 inachangia katika pato la Taifa utasema mambo hayajafanyika! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, huwezi kujua umuhimu wa hivi vitu kama hujatoka nje ya mipaka ya Tanzania. Ulinipa heshima kwenda kushiriki round table ya viongozi wa nchi wa SADC kwenda kutoa maoni namna gani ya kubadilisha policies na sheria ili kuboresha extractive industry iweze kutufaidisha sisi kama wazawa, kila nchi ilikuwa ina-present mawazo, Tanzania tulikuwa ni nchi mfano, a model country. Walisubiri sisi tuwasilishe ili wao waweze kupata dondoo. Nakushukuru na ahsante. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge
MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Ninukuu maneno ya Mheshimiwa Rais wetu Kipenzi Mama Samia Suluhu Hassan aliyozungumza pale Dodoma UDOM akiwa anaongea na viongozi wa dini mbalimbali. Alisema, Wabunge tulieni, acheni kudemka. Sasa sijui hatukumwelewa! Kwa sababu leo hii wananchi wetu wana changamoto nyingi, wanatutaka sisi Wabunge wao tuje hapa tuielekeze na kuieleza Serikali namna gani ya kuunga mkono juhudi za Rais wetu ili Tanzania ifike kwenye nchi ya ahadi. Leo hii tunapoteza masaa yote kwa ajili yao kudemka na kutafuta kiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kaka yangu Bishop Gwajima anajua ni namna gani ninampenda na tunaongea mambo mengi, lakini mimi siyo mnafiki. Nilimwandikia ujumbe mfupi kwenye WhatsApp nikamwambia kaka hapa umepotoka. Hatukatai kutokukubali chanjo; na ndiyo maana msimamo wa Serikali chanjo ni hiari, lakini mwenzetu huyu anatumia vibaya kanisa lake kwenda kuweka tuhuma nzito kwa viongozi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, unaposema viongozi wamepewa fedha, Mheshimiwa Rais amepokea rushwa, ndicho unachomaanisha. Ukisema viongozi wetu chanjo wanazopigwa wanadanganya, unamaanisha Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Spika ambaye kwa kweli ndio anayetuongoza hapa, Waziri Mkuu na wote waliochanja wanawadanganya Watanzania. Ni vizuri mmemwita mbele ya Kamati ameshindwa kuleta vielelezo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kawe kwenye chama chetu waligombea wengi. Kawe kwenye Uchaguzi Mkuu viligombea vyama vingi na alitupa mzigo mkubwa sana. Ilibidi twende Roman Catholic tufute mambo aliyoyasema, ilibidi twende kwa Waislamu tufute mambo aliyoyasema, chama kimemwamini, wananchi wa Kawe wamemwamini, ana majukumu ya kuwatumikia wananchi wa Kawe, arudi kwenye mstari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kaka yangu Mheshimiwa Jerry Silaa kwanza sisi kama vijana wenzake; sijui wasomi wenzake wanasheria, maana mimi sio penguin; tumesikitishwa mno na drama zako. Umeitwa kwenye Kamati, jishushe brother, tuna safari ndefu. Unamtunishia misuli Ndugai, mwenzako kawa Mwenyekiti, Naibu Spika, Spika miaka kumi. Kongwa mimi mwekezaji kule, wanampenda huyu hawataki hata astaafu. Umekuja na begi zima unaanza kuongea kauli za shoo shoo, umejibiwa na vitu viwili; salary slip na kitabu hiki chenye maslahi na mwongozo wa kazi za Mbunge. Unajiita Wakili Msomi, nami nili-post picha yako kabisa umevaa joho. Kaa ujitathmini, Taifa lilikuwa linakuhitaji, umeshajitia doa. Rudi kwa Mungu wako, rudi kwa wazazi wako, rudi kwa viongozi wako, chutama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli mimi niseme naunga mkono Azimio la Kamati, lakini adhabu ni ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa suala alilolifanya Gwajima ni uhaini. Sisi kama Watanzania tunayemwamini Rais wetu, mimi kama Mwanachama wa CCM ambaye namwamini Mwenyekiti wangu, anapaswa kupewa adhabu. Kama anaona Uaskofu ni mkubwa, atuachie Ubunge wetu. Wapo wana-CCM wengi mahiri wa kuweza kuleta maendeleo makubwa. Kawe ilicheleweshwa chini ya upinzani, tunataka iende mbali. Kwa hiyo, naomba adhabu iwe ya juu kabisa kwenye Bunge na pia hatua nyingine za kinidhamu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi kama vijana tunaipenda nchi hii, hatuko tayari kuona mtu yeyote akikwamisha juhudi za Serikali yetu chini ya Rais ambaye kwa kweli siku zote mama huyu hakuchukua fomu kugombea Umakamu wa Rais; Mama huyu hakutaka Urais, alimsindikiza mgombea wake wa Urais kunadi Ilani ya Chama. Yaliyotokea ni ya Mwenyezi Mungu. Ndiyo maana tunasema ni chaguo la Mungu, hana kundi huyo. Kwa hiyo, tunaomba kwa kweli adhabu ziwe kali mno na baada ya hapo vyombo vingine vya mamlaka viwape adhabu. Hakuna lingine. Ahsante sana. (Makofi)

SPIKA: Umesahau kutoa hoja tu. (Kicheko)

MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021
MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa fursa hii. Nianze kwanza kuipongeza Kamati yangu ya Nishati na Madini chini ya Mwenyekiti wetu Mheshimiwa Dunstan Kitandula. Kwa kweli tumefanya kazi kubwa sana na tunashauriana na Serikali ili sekta yetu ya nishati na madini iweze kuwa na tija katika Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijikite kwenye ushauri ambao hasa ni endelevu. Kwa kweli shirika letu hili la TANESCO ni kubwa mno na nishati yetu hii ya umeme inahitaji mipango mikakati ambayo ni endelevu. Leo hii Taifa letu ambalo tayari tumeshaanza kuchochea uchumi wa viwanda tuna umeme wa Megawatt 1,600 na tunajiona kwamba tuna umeme wa kutosha na wa ziada, lakini ukienda duniani na kujifunza utaona tuko nyuma sana na tumechelewa kujipanga vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii nchi ya Afrika Kusini ambayo ina population ya watu takribani milioni 59.3 ina uwezo wa kuzalisha umeme Megawatt 52,000 na bado wananunua umeme kutoka nchi Jirani ya Msumbiji na Namibia. Kwa hiyo, ukiangalia Rule of Thumb, kwenye nchi ya Afrika Kusini moja tu, kwamba Megawatt 1,000 ni sawa sawa na watu milioni moja, huo nindiyo uwiano wa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi leo katika nchi yetu tuko takribani milioni 60 lakini tuna umeme ambao ni Megawatt 1,600 na tukiona namna tulivyojipanga ni kwamba 2025 tunategemea kuwa na Megawatt 5,000. Mwaka 2044 tunajipanga kuwa na Megawatt 18,000. Sasa tukajifunza kwa wenzetu na nchi hii ya Afrika Kusini, hivi tunavyoongea, wana hali mbaya ya umeme kuliko sisi. Leo South Africa wana mgao wa umeme na baadhi ya maeneo hakuna umeme kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia nature ya matatizo, tunafanana; uchakavu wa miundombinu na kutokufanya periodic maintenance ya hivi vituo vyetu vya kupooza. Kwa hiyo, naona kikubwa kwa shirika letu, napongeze sana uteuzi wa Mheshimiwa Waziri pamoja na MD wa TANESCO, tunaamini nyie ni vijana, basi hebu kaeni chini mtumie vipawa vyenu muweze ku-plan, kwa sababu Wagogo wanasema: “If you fail to plan, then you plan to fail.” Tunataka kwenda kwenye uchumi wa juu, wa viwanda, lazima tuwe na umeme toshelevu ili kuepuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye jambo lingine la kuzuia, huko tunakoenda kwenye planning, ushauri wangu mwingine kuna kitu kinaitwa live line technology. Kwa sababu tumeona, walitutangazia siku kumi ili wafanye marekebisho kwenye vituo, lazima wakate umeme. Ila dunia ya sasa hivi, kuna kitu kinaitwa live line technology; ni mfumo unaoruhusu uendelee na ukarabati wa umeme bila ya kukata umeme. Huko ndiko dunia ilipo. Najua ni gharama, lakini ni bora utumuke leo kwa gharama kubwa lakini kuokoa hasara kubwa ambazo tunaweza kuzipata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naona ukitumia hii live line unaweza kubadilisha nguzo bila kukata umeme, unaweza ukaunganisha watu wapya bila kukata umeme, unaweza ukabadilisha vikombe bila kukata umeme, unaweza kubadilisha transformer bila kukata umeme, unaweza kufanya marekebisho na matengenezo kwenye vituo vya kupooza bila kukata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hilo nalo tuliangalie. Ni uwekezaji mkubwa, lazima tuwafunze wataalamu wetu. Yapo mashirika binafsi hapa hawana tu uwezo wa kifedha, lakini TANESCO ikikaa nao kuona namna gani ya kuwawezesha ili tuingie na sisi kwenye utaalam huo, haya matatizo yataweza kuondoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nchini kwetu tuna tatizo kubwa la radi. Kuna baadhi ya maeneo yanakaa muda mrefu bila kupata umeme kwa sababu ya radi, lakini huko duniani kuna technology inaitwa comby Unit; kuna kifaa kinawekwa kwenye transformer…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja za Kamati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. (Makofi)