Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Maria Ndilla Kangoye (16 total)

MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza napenda kusema kwamba nasikitika sana kwani sijaridhishwa na majibu ya Naibu Waziri, ukizingatia kwamba ametoa mfano mmoja mmoja kwa kila kipengele cha swali langu wakati NGOs zipo nyingi ndani ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nijielekeze katika kuuliza maswali yangu mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa vijana na wanawake ndio engine ya maendeleo ya nchi yetu: Je, ni lini Serikali itaanza kutoa elimu ya ujasiriamali kwa vikundi vya wanawake na vijana kabla ya utoaji wa milioni 50 kwa kila kijiji? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kwa kuwa zipo Taasisi za Kitanzania ambazo zimekuwa zikisaidia vijana wanaoathirika na madawa ya kulevya na tasisi hizi zimekuwa ni chache kulingana na wingi wa vijana hawa, je, Serikali ina mpango gani wa kusaidia taasisi hizi ili ziweze kupanuka na kusaidia vijana wengi zaidi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maria Ndila Kangoye, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu kwenye taasisi hizi mbalimbali?
Serikali haina tu mipango, Serikali imeshaanza utekelezaji wa anachokisema kupitia taasisi mbalimbali. Wizara mbalimbali zinatoa elimu kwenye vikundi mbalimbali ambavyo wanafanyanavyo kazi, lakini pia sisi kwenye Wizara yetu specifically tuna Benki ya Wanawake ambayo imeanzisha utaratibu wa kuanzisha siyo matawi ya benki, lakini kuanzisha vikundi kwenye kila mkoa ambapo wanawake wajasiriamali na hata wanaume na vijana wanapewa elimu ya ujasiriamali na pia wanawezeshwa mitaji kupitia utaratibu ambao wamejiwekea.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, kwamba Serikali ina mpango gani kuhusu kuwawezesha na kuwajengea uwezo vijana? Tayari Serikali inafanya jambo hilo. Namwomba Mheshimiwa Mbunge asiwe na shaka na kazi inayofanywa na Serikali kwa kuwa inafanywa kwa ustadi wa hali ya juu.
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa yapo mashamba ambayo yamebinafsishwa na hayajaendelezwa; je, Serikali ina mpango gani wa kuyarudisha mashamba hayo kwa wananchi ili vijana wa Taifa hili waweze kupata fursa ya kuyatumia mashamba hayo kwa shughuli ya kiuchumi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, tunavyozungumza hivi kuna kikao kinaendelea Ukumbi wa Hazina hapa Dodoma kuzungumzia kuhusu mashamba haya ya Vyama vya Ushirika ambayo hayaendelezwi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi tunajaribu kutengeneza mkakati ambao haya mashamba yanaweza yakatumika katika maana nzuri zaidi ikiwa ni pamoja na kupeleka na kurudisha kwa wananchi kama tunaona kwamba hakuna utaratibu mwingine wa Vyama vya Ushirika kuyatumia. Kwa hiyo, nimwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba hilo analosema litafanyiwa kazi.
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tatizo la fistula limekuwa likiongezeka kadri miaka inavyoenda hususan maeneo ya vijijini; je, Serikali ina mpango gani wa kuelimisha wakunga wa jadi ili kupunguza tatizo la fistula na vifo vya mama na mtoto?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Maria Kangoye, Mbunge Viti Maalum (Vijana) kwa kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiri sitawatendea haki Watanzania kama sitakiri kwamba fistula inawapata wanawake walio katika hali ya chini ambao wako vijijini na kwa sababu ya uhaba wa miundombinu wa vituo vya afya, uhaba wa wataalam, pia usafiri wa kutoka pale nyumbani kwenda kituo cha afya na wanawake wa mijini ambapo kunakuwa na msongamano wa watu katika upatikanaji wa huduma za afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Mheshimiwa Kangoye anataka kujua, Serikali tutawahamasisha au tutawashirikisha vipi wakunga wa jadi ili waweze kuhakikisha kwamba na wenyewe wanashiriki katika kuokoa vifo vya akina mama wajawazito?
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli, asilimia 48 ya wanawake wa Tanzania bado wanajifungulia majumbani maana yake wanajifungulia kwa wakunga wa jadi. Kwa hiyo, Wizara ya Afya itaendelea kuhakikisha tunawapa elimu na kuwaelewesha kwamba wasitoe huduma za kujifungulia kwa hawa wanawake wanaowafuata; wao wawe kama ni sehemu ya rufaa. Mwanamke akienda kwa mkunga wa jadi, basi yeye ampeleke au amhamasishe kumpeleka katika kituo cha afya. Ni jambo ambalo tutalifanyia kazi, lakini pia tumekuwa tukitoa mafunzo kwa wakunga wa jadi jinsi gani ya kuwahudumia wanawake wajawazito ili tuweze kuepusha vifo vya akina mama wajawazito.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana nilisema, tumeamua kuanza kutoa vifaa vya kujifungulia kwa wanawake wajawazito ili kuwa kichocheo cha wao kwenda sasa kwenye vituo vya afya vya kujifungulia badala ya kujifungulia majumbani. Ni jambo ambalo tutalipa kipaumbele. Niwathibitishie Wabunge wenzangu wanawake, mimi ni mama; nimepita labour mara mbili. Kwa hiyo, suala la uzazi salama kwa mwanamke ni suala la kipaumbele kwangu.
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali yangu mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza Vyuo vya Utalii katika Mikoa mingine ya Tanzania hasa katika ngazi ya shahada? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa Mkoa wa Mwanza una makumbusho mbalimbali ya kihistoria yakiwemo ya Kageye na makumbusho ya kabila la Kisukuma yaliyopo Bujola Wilayani Magu, ambayo yamekuwa yakipoteza umaarufu wake kadri miaka inavyoongezeka. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba umaarufu huu wa makumbusho haya unaongezeka ili kuiwezesha Wilaya ya Magu kupata kipato kupitia utalii hasa tukizingatia kwamba Wilaya hii imekuwa na mapato madogo kiasi kwamba, imekuwa haikidhi haja ya utoaji wa asilimia kumi ya mapato yake kwa ajili ya vijana na wanawake?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la kwanza la kuongeza vyuo vya utalii na hasa katika ngazi ya shahada, napenda kutoa maelezo ambayo ndani yake kuna majibu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza, Serikali itaelekeza nguvu zake zaidi kwa sasa katika kuimarisha vyuo vilivyopo, vile ambavyo nimevitaja katika campus tatu, mbili zikiwa Dar es Salaam na moja ikiwa pale Arusha.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tunazingatia kuongeza vyuo zaidi, tutazingatia pia ukweli kwamba kitaalam na hasa unapozungumzia kuongeza mafunzo hayo katika ngazi ya shahada ili wahitimu wenye ngazi ya Shahada waweze kufanya kazi sawasawa na yenye tija, unahitaji zaidi kuwa na wataalam katika ngazi ya kati.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tutaelekeza nguvu zetu zaidi kwa wataalam wa ngazi ya kati sambamba na kuangalia uwiano kati ya wale wahitimu wanaohitimu katika vyuo vya kati ili tuweze kuboresha zaidi utendaji wa wale ambao watakuwa wamehitimu katika ngazi ya shahada hapo baadaye, lakini kwa sasa hivi tuelekeze nguvu nyingi zaidi katika kuzalisha wataalam katika ngazi ya kati.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la makumbusho yaliyoko katika Mkoa wa Mwanza na umaarufu wake unaoendelea kupungua, namwomba Mheshimiwa Mbunge arejee majibu ya maswali yaliyotangulia hapo awali. Hata hivyo, nitarudia pia kwa ufupi kwamba, hivi sasa mpango wa Serikali kupitia Wizara ya Wizara ya Maliasili na Utalii ni kwenda katika kila Halmashauri ya Wilaya nchini na kuorodhesha aina zote za vivutio vya utalii ikiwemo makumbusho mbalimbali ili tuweze kupanga vizuri zaidi namna ya kuweza kuvitunza vile vilivyopo katika hali iliyopo, kuviboresha na kuweza kuvifanya viweze kuchangia vizuri katika uchumi wa Taifa kwa kadri ambavyo tutaweza kuvitangaza zaidi.
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na kazi nzuri ya Serikali, napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; je, ni lini barabara ya kutoka Kilombero - Kivukoni mpaka Mwaya - Ulanga itakamilika kwa ujenzi wa kiwango cha lami? (Makofi)
Swali la pili; je, ni lini ujenzi wa barabara ya kutoka Bigwa mpaka Kisaki itakamilika kwa ujenzi wa kiwango cha lami pamoja na madaraja yake?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiri kwamba barabara hizi ni muhimu na zinahitaji kujengwa kwa kiwango cha lami kama ambavyo Ilani ya Chama cha Mapinduzi imefafanua. Katika barabara zote mbili; moja, hii ya upande huu wa Ulanga Kusini na hii ya upande wa kwa Mheshimiwa Mbena, niwahakikishie kwamba dhamira ya Serikali ni ya dhati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo tumekuwa tukiwaeleza katika vipindi vilivyopita, dhamira yetu ya kujenga barabara hizi iko pale pale na tutahakikisha tunatafuta fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo na kazi hiyo ya kutafuta fedha ya kujenga barabara hizi inaendelea.
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri kutoka kwa Waziri, ningependa kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kumekuwa na utaraibu wa wastaafu kuongezewa mikataba ya kufanya kazi. Je, Serikali haioni kwamba hii ni sababu mojawapo ya ukosefu wa ajira kwa vijana?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kati ya Wilaya saba za Mkoa wa Mwanza, Wilaya sita ambazo ni Sengarema, Ilemela, Nyamagana, Misungwi na Magu, pamoja na Ukerewe, zinategemea asilimia kubwa ya mapato yake kutoka kwenye sekta ya uvuvi. Je, Serikali ina mpango gani wa kuajiri vijana wenye taaluma ya uvuvi ili kuweza kukidhi haja ya elimu ya kilimo cha samaki pembezoni mwa Ziwa Victoria? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza kuhusiana na Serikali kuongezea muda wastaafu au kuwapa mkataba wa ajira, nipende kusema yafuatayo; kwanza kabisa tunao waraka ambao ndio mwongozo unaotoa taswira au mwongozo ni watu gani au kada zipi ambazo zinastahili kuweza kuongezewa mkataba wa ajira.
Nipende tu kusema kwamba kwa sasa kipaumbele kipo kwa marubani, kipaumbele kipo kwa wahadhiri wa vyuo vikuu na hao ndio wanaopewa mikataba. Lakini ni lazima wao pia wanapoomba kuongezewa mkataba wa ajira baada ya kustaafu, ni lazima waweze kuwasilisha mpango wao wa kurithishana madaraka, lakini vilevile ni lazima na wenyewe waweze kutoa wamefanya jitihada gani za kuhakikisha kwamba wanawawezesha watumishi wengine walioko chini yao kuhakikisha kwamba wanaweza ku-take over baada ya wao kuondoka katika nafasi hizo walizonazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali la pili hasa katika ajira za vijana na ameongelea zaidi katika ajira za uvuvi; kwanza nipende tu kusema kwamba Mkoa wa Mwanza katika takribani Wilaya zake nne tunatambua ndizo ambazo zina upungufu mkubwa wa watumishi ikiongozwa na Wilaya ya Buchosa, Wilaya ya Kwimba pamoja na Wilaya ya Ukerewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika ikama ya mwaka huu 2016/2017 nitolee tu mfano katika Wilaya ya Ukerewe, wavuvi wasaidizi takribani watano wamepangiwa na hizo ni katika nafasi chache ambazo zimewekwa katika utaratibu wa ikama ya mwaka 2016/2017. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa kada ambazo zina upungufu mkubwa katika Halmashauri hizo tutazipa kipaumbele ili kuhakikisha kwamba, wanaweza kufanya kazi kwa ufanisi na kwa uweledi mkubwa.
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri kutoka Serikalini, napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa sheria inawataka wavuvi wanaovua katika Ziwa Victoria wakiwemo wavuvi wa Mkoa wa Mwanza kutumia nyavu za inchi sita hadi saba ambazo hazikidhi mahitaji ya uvuvi katika maji ya kina kirefu. Je, Serikali ina mpango gani ya kupitia upya Sheria ya Uvuvi ya mwaka 1973, sheria ambayo ilitungwa kabla hata samaki aina ya sangara hawajapandizwa ndani ya Ziwa Victoria na kuwa imepitwa na wakati? (Makofi)
Swali la pili, je, Mheshimiwa Waziri na Mbunge wangu wa Jimbo la Buchosa, ni lini utakuwa tayari kuja Mkoani Mwanza kukaa na wadau ili kuweza kusikiliza kero zao na changamoto zinazowakumba katika uvuvi ndani ya Ziwa Victoria? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria Namba 22 na maboresho ya kanuni zake kama yalivyofanywa imeweka aina za nyavu ambazo zinaruhusiwa kutumika katika maji baridi, kwa maana ndani ya maziwa yetu; na aina za nyavu ambazo zinaruhusiwa kutumika katika uvuvi baharini. Sasa utafiti ambao umefanywa na wataalamu wetu kwa muda mrefu ulibaini kwamba nyavu zenye matundu size ya chini ya inchi sita zinasababisha uvuvi kutokuwa endelevu ndani ya maziwa yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hii imezingatia pia
aina za samaki waliomo Ziwani na imewekwa ili kuhakikisha kwamba samaki aina kadhaa hawatoweki na aina nyingine wanaendelea kuzaana kwa ajili ya matumizi ya wavuvi wenyewe na watu wengine wanaohusika na suala hili la uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulichokifanya, mimi binafsi nimeshakutana na wavuvi wa Mkoa wa Mwanza na maeneo mengine, siyo mara moja, mara kadhaa na mara ya mwisho tulichokubaliana ni kwamba utafiti wa pamoja ufanyike tena kuangalia mesh size na lile suala la kuunganisha nyavu yaani double tatu, double tisa na kadhalika, ili tuweze kujua kwa kushirikiana ni njia gani sahihi ya kuendesha uvuvi katika Ziwa Victoria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kukutana na hawa wavuvi, mimi nakutana nao kila mara ninapokuwa Jimboni. Ahsante sana.
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza na kwa niaba ya vijana wa Kitanzania ningependa kujua ni lini Serikali itarudisha programu ya michezo katika shule zetu za sekondari na msingi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama alivyozungumza Mheshimiwa Naibu Waziri, kwanza katika suala zima la shule hizi, juzi tumezindua michezo ya UMISETA hapa rasmi, bahati nzuri Kitaifa tumezindulia hapa Dodoma, tuna shule zipatazo 55.
Hata hivyo, tumetoa maelekezo maalum kwa Ofisi
za Mikoa yote sasa programu ya michezo sasa imeishaanza kurudi mashuleni na tumetoa maelekezo kwamba Maafisa Michezo wote waweze kuwezeshwa katika Mikoa yote na katika Halmashauri zote ili kuhakikisha kwamba tunaibua vipaji katika michezo ya watoto wa shule za msingi na watoto wa shule za sekondari.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge naomba nikuhakikishie kwamba Serikali imeshalichukua suala hili na sasa liko katika utekelezaji. Tunawashukuru sana wenzetu wa CocaCola ambao mwaka huu wanafadhili michezo hii ya UMISETA hapa Tanzania, nayo imeishaanza vizuri na tunashukuru sana kwa kweli. (Makofi)
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza kwa niaba ya vijana wa Kitanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, ninapenda kujua ni nini mpango wa Serikali wa kuwapatia vijana wafugaji elimu ya malisho katika ufugaji endelevu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika majibu ya Serikali kwa swali langu la msingi kipengele (b) ni dhahiri kwamba Mkoani Mwanza hakuna vikundi vya vijana/ wafugaji ambao wamejiunga na vyama hivi vya ushirika.
Je, ni lini Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari kuambatana na mimi kwenda Mkoani Mwanza kukutana na maafisa vijana pamoja na maafisa ufugaji ili tuweze kutafuta namna ya kuwawezesha vijana hawa kujiunga na vyama hivyo vya ushirika?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, mpango wa Serikali ni nini wa kuwapatia elimu vijana wa nchi hii juu ya malisho.
Kwanza, kupitia mpango mkakati kabambe kwa maana ya Tanzania Livestock Masterplan ambao tunakwenda kuuzindua sasa katika eneo hili la malisho tumeweka msisitizo mkubwa sana. Nataka niwaambie vijana nchi nzima ya kwamba malisho ni uchumi, leo mbegu kilo moja ya malisho inauzwa takribani 15,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya ng’ombe mwenyewe na mazao yake, lakini uwepo wa malisho mtu ama kijana akijikita katika malisho anao uwezo na uhakika wa kupata kipato chake kitakachomsaidia katika kuendesha maisha yake. Hivyo, Serikali katika kuhakikisha hili tayari tunao mpango wa kuhakikisha mbegu za malisho zinapatikana madukani ili ziweze kuuzwa kama zinavyouzwa mbegu zingine kwa maana ya mbegu za mahindi, mpunga na nyinginezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili la Mheshimiwa Maria Kangoye ni kwenda Mwanza kukutana na kuwahamasisha vijana juu ya shughuli za ufugaji na uandaaji wa malisho; nataka nimhakikishie Mheshimiwa Kangoye niko tayari hata baada tu ya kumaliza Bunge hili kuambatana naye kuelekea Mwanza.
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa TFDA imekuwa na ucheleweshaji wa masuala mbalimbali ya kiukaguzi kutokana na ukosefu wa wafanyakazi wa kutosha. Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza wafanyakazi upande wa ukaguzi ndani ya shirika hili?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze yeye mwenyewe binafsi kwa jitihada zake za kijasiriamali anazoendelea nazo, anafanya social entrepreneurship, anakusudia kuleta sanitary pads kwa ajili ya watoto wa kike, mataulo masafi ya kurudia kufua kwa ajili ya watoto wa kike na ameamua badala ya kuya-import basi azalishe hapa nchini. Nakupongeza kwa hilo na naomba nikwambie kwamba sisi kama Serikali tunatambua jitihada zako na tutakuunga mkono kadri ambavyo inafaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusu ucheleweshaji wa vibali, nafahamu kibali chako kilichelewa mpaka ukakata rufaa kwa Waziri lakini ukweli ni kwamba TFDA kuna changamoto za kuwa na maabara chake na kuwa na bidhaa nyingi japokuwa uwezo wetu umekuwa ukiongezwa siku hata siku. Kwa mfano, sasa hivi TFDA tunaongeza uwezo kwa kuongeza maabara kwenye kila kanda hapa nchini. Kwa hiyo, kila mwaka tunatenga bajeti kwa ajili ya kujenga maabara mpya na kuanzisha kituo kwenye kila kanda. Nafahamu sasa hivi kwenye Kanda ya Ziwa tupo katika hatua za mwisho za kufungua huduma zetu pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, kadri tunavyozidi kutanua wigo wetu wa kuwafikia wananchi ndivyo ambavyo tutazidi kuongeza kasi ya kuwahudumia wateja wetu. Kwa msingi huo, huo ndiyo mkakati wetu kwamba tunaenda kwenye kanda sasa badala ya kubaki na TFDA makao makuu peke yake lakini changamoto ya kuchelewesha kwa kweli ilikuwepo.
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya wanawake na vijana hususan wa Mkoa wa Mwanza napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, kwa kuwa kumekuwa na tabia ya baadhi ya Halmashauri za Wilaya kutokutoa asilimia kumi kwa wanawake na vijana kikamilifu na nyingine kutokutoa kabisa; je, Serikali inachukua hatua gani juu ya Halmashauri hizi zinazokaidi agizo hili la Serikali?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa vikundi vya maendeleo vya wanawake na vijana vimekuwa ni vingi sana na fedha hii imekuwa ikinufaisha vikundi vichache; je, ni lini Serikali itaongeza asilimia hii ili iweze kunufaisha vikundi vingi na ukizingatia kwamba ikifanya hivyo itakuwa imepunguza kwa asilimia kubwa tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimpongeze Mbunge kwa harakati zake kama kijana na kama mwanamke kugombea na kupambana kwa haki za wanawake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kuhusu suala la asilimia kumi, kwamba Halmashauri nyingine hazitengi; katika bajeti ya mwaka wa 2016/2017, tulipotenga bilioni 56.8 tulitoa maelekezo kwa Wakurugenzi wote kwamba commitment ya bajeti ya Serikali katika 10 percent, yaani five ya vijana na five ya akinamama lazima itekelezwe. Katika hili tumeona kwamba mpaka mwezi Machi tumetoa bilioni kumi na saba, lakini mpaka juzi wakati tunafuatilia ina maana fedha zinaongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba niwasihi hasa Waheshimiwa Wabunge, sisi ni wajumbe katika Mabaraza yetu, fedha zile zinakusanywa wala haziendi kwa Mpango haziendi Hazina, zinaishia katika Halmashauri zetu. Lazima kila kinachokusanywa kila mwezi tunapoingia katika Kamati ya Fedha tusikubali kupitisha ile bajeti, fedha zimekusanywa pale, lazima tutenge moja kwa moja five percent ya vijana na five percent ya akinamama ili tuwasaidie watu wetu kule site.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili Wakurugenzi wote ambao tumekubaliana lazima walitekeleze na tarehe 30 mwezi wa sita tutafanya assessment ya Wakurugenzi wote ambao wameshindwa ku-meet commitment hii ambayo ilikuwa ni guideline na maelekezo ya Kamati ya TAMISEMI ya Bunge hili wakati tunapitisha bajeti. Kwa hiyo wakurugenzi wote lazima wajiandae, hiyo ni miongoni mwa assessment tutakayoifanya katika performance ya kufanya kazi zao katika maeneo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, kuongeza ten percent; naomba nimwambie dada yangu, hii ten percent yenyewe inatosha kwa sababu fedha zile kuna nyingine zinakwenda katika maendeleo, posho za Madiwani na posho ya vijiji. Asilimia kumi kinachotakiwa ni compliance tu, kama kila Halmashauri itaweza kutoa kweli asilimia kumi tutaweza kufanya vizuri zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwamba asilimia kumi inatosha, isipokuwa sasa lazima wajue tumetoa maelekezo kwamba katika ile asilimia kumi lazima watenge asilimia mbili kwa ajili ya walemavu katika Halmashauri zetu. (Makofi)
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kabisa naishukuru Wizara kwa lengo lake la kutoa semina kwa Waheshimiwa Wabunge kwa uelewa wa masuala ya uvuvi, lakini kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Mwanza ambao wananufaika na uvuvi wa Ziwa Victoria ambao wengi wao ni wanawake na vijana, napenda kuuliza maswali yangu mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa changamoto nyingi za uvuvi zinatokana na sera na sheria zilizopitwa na wakati ikiwemo Sheria ya mwaka 1972 inayohusisha masuala ya nyavu; je, ni lini Serikali itakaa kuzipitia sheria hizi kwa lengo la kuzirekebisha? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; licha ya Ziwa Victoria kutumika na nchi tatu, yaani Tanzania, Kenya na Uganda, bado kila nchi imekuwa na sera zake juu ya uvuvi. Je, ni lini Serikali itaanzisha mchakato kuhakikisha kwamba kunakuwa na sera moja ya uvuvi katika Ziwa Victoria yaani One Lake, One Policy? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Maria Kangoye kwa kuweza kusimamia vyema kabisa maslahi mapana ya wananchi waliomtuma wa Mkoa wa Mwanza wakiwemo vijana na akina mama. Hongera sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ameniuliza maswali mawili; la kwanza ni juu ya mapitio na maboresho ya Sheria ya Uvuvi. Naomba nimhakikishie kwamba sheria ile aliyoitaja ya mwaka 1970, Sheria Namba 6 ya Uvuvi tayari ilishaboreshwa, ndiyo maana tuna Sheria Namba 22 ya mwaka 2003 ambayo inakwenda na kanuni zake za mwaka 2009 ambayo na yenyewe sasa tuko katika hatua ya kuiboresha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa tunavyozungumza, wataalam wetu katika ngazi ya Serikali, IMTC kwa maana Makatibu Wakuu wanaijadili na baadaye itaingia katika vikao vyetu vya Baraza la Mawaziri ili kuweza kuboreshwa zaidi na hatimaye kwa maslahi mapana ya sekta hii ya uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimtoe hofu Mheshimiwa Maria Kangoye kwamba Sheria yetu ya Uvuvi kabla ya mwaka huu wa 2018 haujakamilika, tutahakikisha kwamba inaingia humu Bungeni kwa ajili ya kuweza kupata baraka na kuboreshwa zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ni juu ya sera moja ya uvuvi, kwa maana ya kwamba Ziwa Victoria ni ziwa ambalo liko shared na nchi tatu, kwa maana ya Tanzania, Kenya na Uganda ambapo sisi kama Tanzania ndio tunaomiliki eneo kubwa la Ziwa Victoria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli na nimwambie tu kwamba katika siku ya tarehe 2 Machi, 2018 Mawaziri wa nchi hizi tatu akiwepo Waziri wetu Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina alishiriki katika kikao ambacho kilikwenda na maazimio.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya maazimio makubwa kabisa ni kuhakikisha kwamba katika kila nchi, zile taasisi zetu za utafiti zinafanya utafiti na kuweza ku- compromise (kuweza kwenda kwa pamoja) juu ya sera zetu, sheria zetu ili zisiweze kugongana; ili wavuvi wote wanaoshiriki shughuli za uvuvi katika Ziwa Victoria wawe wanajua kwamba sheria hii hapa Tanzania, Kenya au Uganda ni sawasawa bila kuvunja sheria za nchi nyingine.
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Vijana na wanawake wengi wa Kitanzania wamekuwa na jitihada kubwa sana katika kilimo hususani cha mbogamboga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali imefanya jitihada zipi za kuhakikisha kwamba bidhaa za shamba zinasindikwa nchini?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi kama ambavyo nimezungumza hapo awali, kwa kupitia miradi ambayo SIDO imekuwa ikiendeleza pamoja na wadau mbalimbali, kwa kweli usindikaji wa mazao sasa hivi umekuwa ni mzuri zaidi. Niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge, inapotokea katika maonesho ya saba saba tafadhalini hebu mpitie muone bidhaa ambazo sasa hivi hawa Watanzania wanazifanya. Ziko katika viwango vya hali ya juu na tutaendelea kuwezesha kuona kwamba wajasiriamali hao wanapata ubora zaidi katika bidhaa zao.
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu hayo kutoka Serikalini, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Ilemela ilifanikisha kuanza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya katika Kata ya Buswero na walifanikisha kukamilisha majengo ya OPD na vilevile jengo la magonjwa ya dharura. Hata hiyo, kutokana na changamoto zilizokuwa pale, wakaona hapafai kuwa na Hospitali ya Wilaya maeneo yale wakaanzisha ujenzi katika Kata ya Bugogwa:-

Je, Serikali haioni kwamba kuna umuhimu wa majengo yale kuanza kutumika sasa kama Kituo cha Afya, kwa sababu yanakidhi haja hiyo ya kuwa kituo cha afya?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, swali langu la pili nianze kwa kuishukuru Serikali kwa kutujengea Kituo cha Afya cha Malya Wilayani Kwimba. Kwa kweli ni kituo kizuri kinatoa huduma kwa wananchi wengi Wilayani humo, lakini kimekuwa na changamoto zifuatazo: hakina Mganga Mkuu na mhusika mkuu pale ni Clinical Officer; vile vile hakina mtaalam wa Maabara, hakina chumba cha upasuaji, hakina Daktari wa Akina Mama na Watoto; na bahati nzuri Naibu Waziri, Mheshimiwa Waitara ameshafika katika hiki kituo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, swali langu ni moja: Je, ni lini Serikali itahakikisha kwamba changamoto hizi zinapungua ili tuweze kupunguza vifo vya akina mama na watoto?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la kwanza Mheshimiwa Maria anauliza juu ya umuhimu wa eneo ambalo lilikuwa limeshaanza kujengwa Hospitali ya Wilaya lakini ikaonekana kwamba hapafai ni bora kikajengwa kituo cha afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze kwa dhati. Hata pia Mheshimiwa Angelina Mabula amekuwa akiliongelea suala hili kwa muda mrefu. Ni adhima ya Serikali kuhakiksha kwamba tunaondoa congestion katika maeno yote. Kwa hiyo, eneo lile na majengo ambayo yameshajengwa, hakika naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, inafaa kabisa kuwa Kituo cha Afya baada ya maboresho machache ambayo yataenda kukamilishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, Mheshimiwa Mbunge pamoja na kwamba amesifia tunashukuru kwa hizo pongenzi kwamba Kituo cha Afya kimeshaanza kufanya kazi nzuri, lakini kinakosa baadhi ya wataalam. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ni azma ya Serikali kwamba yale majengo kwa maana ya vituo vya afya hatujengi ikawa kama picha. Tunataka wataalam wanaohusika ili upasuaji na shughuli zote zinazotakiwa kwenye kituo cha afya ziweze kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Mbunge avute subira. Wakati mwingine kuna watalam ambao ni lazima wawe trained. Kwa mfano, katika upasuaji lazima tuwe na wale watu ambao wanatoa dawa za usingizi na ndiyo maana tumewapeleka kuwa-train. Naamini na kituo hicho ambacho anakiongelea kitapata wataalam hao.
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nianze kwa kuipongeza Serikali kwa majibu mazuri ambayo inaonesha jitihada ya kusambaza maji ndani ya Mkoa wa Mwanza. Pamoja na majibu hayo naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

(i) Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji alivyokuja Misungwi aliahidi kukamilisha malipo ya mkandarasi mradi huu tajwa hapa wenye gharama ya shilingi bilioni 6.1. Lakini mpaka sasa hivi kwa taarifa niliyonayo ni kwamba kuna sintohamu nyingi, mimi ombi langu moja ningependa kujua ni lini Waziri atapata muda wa kuambatana na mimi pamoja na Mbunge wa Jimbo ili tuende tukae na makandarasi na wananchi ili tupate jibu sahihi ya lini watapata maji safi na salama?

(ii) Mara ya Mwisho Mheshimiwa Waziri Mkuu alivyotembelea Misungwi aliahidi mradi wa maji wa Misungwi pamoja na Igokelo kukamilishwa na kukabidhiwa mwezi wa tano. Ikasogezwa ikawa ni mwezi wa nane, leo hii tunavyongea ni mwezi wa tisa. Ningependa kujua ni nini mpango wa Serikali wa kukamilisha mradi huu ili wananchi wa Misungwi waweze kupata maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kiukweli Mheshimiwa Maria Kangoye ni Mbunge king’anga’nizi katika kutetea wananchi wake. Lakini niungane pamoja na Mheshimiwa Kitwanga kwa kazi kubwa wanaifanya katika Jimbo la Misungwi kubwa ambalo ninachotaka kusema utekelezaji wa mradi wa maji unategemea na fedha nataka nimhakikishie mkandarasi anayetekeleza mradi ule shilingi bilioni 6.1 sisi kama Wizara ya maji hatutakuwa kikwanzo na Mheshimiwa Mbunge na kuhakikishia certificate ile na mradi uweze kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili ni kuhusu utekelezaji wa mradi pale Misungwi tuna mradi takribani shilingi bilioni 12 kutokana na kilio cha Mheshimiwa Mbunge Mzee wangu Kitwanga. Wiki ijayo tunakwenda kukabidhi mradi ule ili wananchi waweze kupata maji, na ninataka kumtia moyo Mheshimiwa Kangoye na Mheshimiwa Kitwanga unapotembea na kuzuru wengine naomba usinipite mwokozi, sitowapita nitakuja mwenye Misungwi kushuhudia namna gani wananchi wanaenda kupata maji wiki ijayo. Ahsante sana Mheshimiwa.
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya kutoka Wizarani kwanza nianze kwa kumkumbusha kwamba naitwa Maria Ndila Kangoye siyo kama hivyo alivyonitaja. Nitauliza swali moja la nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, Tanzania ni kati ya Nchi zinazoongoza katika ufugaji Barani Afrika hususani ufugaji wa Ng’ombe, lakini licha ya hivyo tumekuwa nyuma sana katika biashara ya mazao ya mifugo. Ningependa kujua ni nini mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kwamba inakabiliana na upungufu mkubwa wa viwanda vya kuchakata nyama na maziwa nchini?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara, naomba kujibu swali la nyongeza pamoja pia na kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa na mkakati mkubwa na mzuri sana wa kuhakikisha tunapata viwanda vya uchakataji wa mifugo Nchini. Kwa kuanzia kwa haraka haraka hivi sasa, tunavyo viwanda takribani vitatu tunavyovijenga katika Nchi. Kiko kiwanda pale Mkoani Arusha, Wilayani Longido, tunacho kiwanda pale Mkoani Pwani katika Wilaya ya KIbaha, tuna kiwanda kikubwa ambacho tunakitarajia tulichoingia mkataba na Taifa la Misri kitakachojengwa katika Ranch yetu ya Ruvu pale Kibaha pia. Sambamba na kuchakata nyama, tunavyo viwanda ambavyo vinachakata mazao mengine ya mifugo kama vile maziwa.

Mheshimiwa Soika, Serikali inaendelea kuhamasisha sekta binafsi katika kuwekeza kwenye viwanda na mazingira ya uwekezaji katika viwanda hivi vya uchakataji wa mifugo yako mazuri na tunawakaribisha kwa ajili ya kufanya kazi hii.