Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Maria Ndilla Kangoye (23 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naitwa Maria Ndila Kangoye, ni Mbunge wa Viti Maalum kutokea Mkoa wa Mwanza nikiwakilisha vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kuanza kwa kumshukuru Mungu kwa kuniwezesha kusimama siku hii ya leo hapa nilipo. Pia nipende kuwashukuru wapigakura wangu ambao ni vijana wa UVCCM Mkoa wa Mwanza pamoja na wanawake wa UWT ngazi ya Taifa kwa kunipa dhamana ya kuwakilisha vijana ndani ya Bunge hili la Kumi na Moja. (Makofi)
Mhehimiwa Mwenyekiti, napenda pia kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi nzuri inayofanya. Nampongeza sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli pamoja na wasaidizi wake ambao ni Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri, Manaibu Waziri pamoja na watendaji wote wa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nijielekeze katika kuchangia hoja iliyopo. Kwanza, nianze kwa kusema kwamba naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja kwani hotuba ya Mheshimiwa Waziri imesheheni mambo mazuri yenye kuleta matumaini katika Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua kwamba Kilimo kimeajiri takriban asilimia 70 ya Watanzania na wengi wao wakiwa ni vijana. Hivyo basi, napenda kuungana na Wabunge wenzangu wanaotokana na Kanda ya Ziwa hasa wale walioongelea zao la pamba kwa kusema kwamba ni kweli zao la pamba limeanza kupunguza uthamani wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wa pamba wamekuwa wakikatishwa tamaa na changamoto nyingi zinazolikabili zao hili. Baadhi ya changamo hizi ni ukosefu wa masoko ya uhakika, lakini kumekuwa na ucheleweshwaji wa pembejeo hususan mbegu na kumekuwa pia na usambazaji wa mbegu ambazo hazioti. Hii imewakatisha tamaa sana wakulima wa pamba. (Makofi)
Mheshimwa Mwenyekiti, labda kwa kwa kutoa mfano, tatizo hili limewahi kutukumba hata kule Wilayani kwangu Magu, katika vijiji vingi vikiwemo kijiji cha Shishani, Kabila, Mwamanga, Ndagalu na vingine vingi. Kwa kuwa Serikali ina mpango wa kujikita katika viwanda napenda kuiomba Serikali ifufue viwanda vya nguo ili kuweza kupata soko la ndani kwa wakulima wa pamba. Naamini viwanda hivi vitaweza kutoa ajira kwa vijana, kama Rais wetu alivyoweza kuajiriwa katika Kiwanda cha Mwatex enzi za ujana wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia kwamba kilimo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa nchi yetu, napenda kuipongeza Serikali kwa kuanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo. Naamini sasa vijana wengi waliojiajiri katika sekta hii wataweza kupata mikopo ya bei nafuu na kuweza kupanua kilimo chao kulingana na teknolojia ya hivi sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine kubwa inayomkabili mkulima wa Kitanzania ni ile ya kutozwa kodi nyingi mpaka mazao yake yanapofika sokoni. Namshukuru Waziri Mkuu, wiki iliyopita amesimama hapa mbele yetu na kutuhakikishia kwamba kodi hizi zitapunguzwa, na mimi ninachoiomba Serikali ni kwamba ianze kutekeleza agizo hilo kwa uharaka ili wakulima waanze kunufaika mapema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na tatizo lingine kubwa. Wakulima hawa wanapofika masokoni, wanakutana na madalali. Madalali hawa wamekuwa kama miungu watu ndani ya masoko haya. Wao ndio wapangaji wa bei na wamekuwa wakitengeneza mazingira ya kukabidhiwa mazao haya; wao ndio wanaouza, ndio wanaopokea pesa na mara nyingi wamekuwa wakiwatapeli wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuiomba Serikali kuweza kuanzisha chombo maalum ambacho kitakuwa chini ya Halmashauri za Wilaya ambacho kitawatambua hawa madalali na ikiwezekana na wao walipishwe kodi kwa sababu hata hiyo pesa wanayopata haina jasho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kanda ya Ziwa hususan Mkoa wa Mwanza ni maarufu kwa ufugaji, lakini kumekuwa na uhaba wa viwanda vya kusindika nyama, maziwa na kuchakata ngozi. Naiomba Serikali itoe kipaumbele kwa kuanzisha viwanda hivi ili kuweza kunufaisha jamii ya ufugaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ifike mahali tuachane na kusafirisha mifugo, ila tujikite katika usindikaji wa nyama, maziwa na usafirishaji wa ngozi ambazo tayari zimekuwa processed. Hili ni suala ambalo linawezekana na nina uhakika kwa Serikali hii inawezekana kabisa. Labda kwa kutoa tu mfano, kuna Ranchi ya Kongwa hapa ya NARCO, imekuwa ikisafirisha nyama kutoka kwenye ranchi yake kwenda sehemu mbalimbali, hata kwenye maduka ya kuuza nyama (butcheries)yaliyoko Dar es Salaam.
Sasa ikiwa suala kama hili tayari lilishaanzishwa tena na vyombo vya Serikali, je, inashindakana vipi kuweka mlologo mzuri ili nyama ya ng‟ombe inayotoka Mwanza iweze kufika Dar es Salaam ikiwa fresh na kuwafikia walengwa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuhitimisha mchango wangu kwa kuiomba Serikali kuiangalia Wilaya ya Ukerewe kwa jicho la pekee. Ukerewe ina visiwa 38; kati ya hivyo, 15 ndivyo vyenye makazi ya kudumu na 23 ni makambi ya wavuvi; na wavuvi wengi ni vijana. Nasikitika kusema kwamba vijana hawa ambao ni wavuvi wamekuwa wakihangaika kutafuta masoko mbali na Ukerewe, ukizingatia kwamba viwanda vya samaki vipo Musoma na Mwanza. Vilevile tukiangalia hali ya usafiri wanaotumia siyo usafiri wa uhakika, yaani usafiri ule siyo salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi tumekuwa tukiwaokota pembezoni mwa ziwa na hii kwa kweli…
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika hotuba ya bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Nianze kwa kumpongeza Waziri pamoja na Naibu wake kwa hotuba nzuri yenye kuleta matumaini kwa Watanzania, lakini niwapongeze sana kwa kazi nzuri waliyokuwa wanafanya kwani haifichiki. Tumeona ujenzi na ukarabati wa hospitali zetu za rufaa lakini tumeshuhudia pia uanzishwaji wa hospitali maalum ya Benjamin Mkapa Ultra Modern Hospital iliyopo hapa Dodoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo, napenda kuikumbusha Serikali kwamba bado haijafikia lengo lililowekwa miaka 15 iliyopita ndani ya Azimio la Abuja linaloitaka Serikali kutenga asilimia 15 ya bajeti yake ya Taifa kwa ajili ya afya. Hapa ninavyoongea sasa Wizara hii imetengewa bajeti chini ya asilimia kumi ya bajeti ya Taifa. Napenda kuiomba Serikali iweze kufikiria upya suala hili na kurejea katika msimamo wa makubaliano hayo na kuwezesha Sekta hii ya Afya kufanya vizuri kwani tutakapowezesha sekta hii tutawezesha pia sekta nyingine kuweza kukua na kufanya vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoani Mwanza zipo changamoto nyingi ambazo zinaikabili sekta hii ya afya. Changamoto hizi tayari zimeshatajwa na Wabunge wenzangu lakini na mimi nitaweka msisitizo japo kwa ufupi. Kuna changamoto ya ucheleweshaji wa dawa kutoka MSD; kumekuwa na wafanyakazi wachache katika sekta hii ya afya; kumekuwa na ucheleweshwaji wa mishahara ya wafanyakazi; kumekuwa na ukosefu wa maduka ya dawa katika hospitali zetu za wilaya na lipo tatizo ambalo limekuwa likisumbua sana la ukosefu wa usafiri wa uhakika kwa wagonjwa wa wilaya zote za Mkoa wa Mwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Wilaya ya Magu ina magari manne ya wagonjwa lakini katika magari manne ni gari moja tu la kituo cha Lugehe ndilo linalofanya kazi, mengine matatu yote ni mabovu na magari haya yamekuwa yakikarabatiwa mara kwa mara bila mafanikio. Kwa kuwa pia Wilaya ya Magu haina mapato ya kutosha, magari haya yamesababisha deni la shilingi milioni 38 kwa ajili ya service zilizokuwa zinafanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Ilani ya Chama changu cha Mapinduzi iliahidi kwamba, itaboresha mazingira ya wafanyakazi wa sekta mbalimbali ikiwemo sekta hii ya afya, napenda kuikumbusha Serikali kwamba ni wajibu wake sasa kutekeleza Ilani hiyo kwa kuweza kutatua changamoto hizi ili wafanyakazi waweze kufanya kazi katika mazingira yanayostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Wilaya ya Sengerema nayo inahitaji ruzuku stahili. Mheshimiwa Ngeleja amesimama mara kwa mara na kuhamasisha suala hili na kuiomba sana Wizara na napenda kuungana naye katika vita hii. Hospitali ya Wilaya ya Sengerema inapata ruzuku ya vitanda 150 tu wakati hospitali hiyo ina vitanda zaidi ya 370 na inategemewa na wakazi wengi wanaoishi ndani ya Jimbo hilo la Sengerema. Ombi hili tayari lipo Wizarani na ni matumaini yetu kwamba Wizara itatupatia jibu zuri ambalo litatuletea matumaini kwa wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimebahatika kuzunguka katika baadhi ya shule za msingi na sekondari ndani ya Mkoa wa Mwanza nikiwa na wanaharakati wanaotoa elimu ya afya ya uzazi. Kwa fursa hiyo ya muda mfupi, nimegundua kwamba ipo haja ya Serikali kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha kwamba wanafunzi wa jinsia ya kike wanapata taulo za kujisitiri ili kupunguza changamoto kubwa ya wanafunzi hawa kutokuhudhuria masomo wakiwa kwenye siku zao. Kwa sababu tayari Serikali inatoa vitabu na madawati mashuleni, naomba suala hili pia liweze kupewa kipaumbele ili kuweza kunusuru wasichana hawa kukosa masomo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati nzuri wapo vijana wa Mwanza ambao wamejitolea kufanya utafiti na wakatengeza washable sanitary towels yaani pedi ambazo zinaweza kufuliwa na kutumiwa zaidi ya mara moja kwa muda mrefu. Naomba Serikali iwasaidie vijana hawa ili bidhaa zao ziweze kuthibitishwa na TBS na endapo zitatufaa bidhaa hizi ziweze kununuliwa na Selikali na kusambazwa katika shule mbalimbali hasa zile zilizopo vijijini. Napenda kumwomba Waziri wa Afya anipokee nitakapowaleta vijana hawa ofisini kwake kwani ni fahari kwa Tanzania kuwa na vijana wabunifu tena wenye kujituma kwa niaba ya nchi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, napenda kusema kwamba naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuipongeza Wizara hii kwa hotuba nzuri iliyojieleza vizuri kwa maslahi ya Watanzania kwa ujumla, pamoja na yote naomba Serikali iweke makazi katika suala lifuatalo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana hasa katika maeneo yanayozunguka migodi yetu. Suala hili limesababisha mauaji ya vijana hawa wanaparamia migodi kuweza kupata chochote kama tunavyosikia mara kwa mara kwenye mgodi wa Nyamongo, Mkoani Mara.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishauri Serikali yangu sikivu, Serikali inayotekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi inayoahidi kupanua wigo wa ajira kwa vijana, iweke mikakati maalum ya kuhakikisha kwamba, migodi mikubwa kama Nyamongo inauza mchanga ambao hauhitajiki na mgodi kwa wananchi ili nao waende kusafisha na kupata japo kidogo katika rasilimali yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini suala hili linawezekana na naamini kwamba, Serikali hii, haitashindwa kuweka utaratibu huu wa wananchi kupata mchanga huo kutoka migodini.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha kusimama ndani ya Bunge hili Tukufu asubuhi hii ya leo, nikushukuru wewe pia kwa kunipatia nafasi ya kuchangia hotuba ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Naibu wake Dkt. Angelina Mabula kwa kazi nzuri wanayofanya, niwape pole kwa changamoto nyingi wanazokumbana nazo ndani ya Wizara hii, kwani zipo nyingi zikiwemo zile za migogoro ya ardhi ambazo zimekuwa ni za muda mrefu na zenye kuhitaji hekima na busara katika kuzitatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa gender sensitivity nipende kumshukuru na kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kumteua mwanamama Dkt. Angelina Mabula kuwa Naibu Waziri wa Wizara hii. Baada ya salamu hizi naomba nijielekeze katika kuchangia hotuba iliyoko mezani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ina hekta milioni 88.6 za nchi kavu na kati ya hizo ni hekta milioni 60 ambazo ni mbuga na zina uwezo wa ku-accommodate ufugaji. Pamoja na kuwa na eneo kubwa la kututosheleza bado kumekuwa na migogoro mingi ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji na migogoro hii imekuwa ikisababisha ulemavu vifo, upotevu wa mali lakini hata wananchi kuhama makazi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua jitihada ya Wizara hii katika kutatua migogoro hii lakini naiomba Serikali ikae itafakari, itafute mbinu mbadala na rafiki kutatua matatizo haya. Hata pale inapowezekana ishirikishe wazee wa kimila katika kuwashawishi wakulima na wafugaji kutumia maeneo maalum yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli zao. Niishauri Serikali kutengeneza mifumo ya kuzuia kuliko kutengeneza mifumo ya kupambana baada ya matatizo haya kufumuka. Kubwa zaidi niishauri Serikali kuhakikisha inafanya utafiti ili iweze kujua vyanzo halisi vya migogoro hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaisihi Serikali kuona haja ya kutambua ufugaji wa asili katika Sera ya Taifa ya Ufugaji ya mwaka 2006, kwani ufugaji huu umekuwa ukichangia asilimia 7.4 ya Pato la Taifa. Kikubwa ni kutengeneza mfumo madhubuti kuhakikisha kwamba ufugaji huu haugeuki kuwa chanzo cha migogoro ya ardhi ndani ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya Sheria ya Ardhi kumekuwa na changamoto kubwa ya wananchi kutokuwa na uelewa wa kutosha wa sheria hiyo, kumekuwa na tafiti nyingi ambazo zimebainisha kwamba wananchi wanaoishi katika ngazi za msingi hususani vijijini wakiwemo wanawake, wakiwemo wafugaji, wachimbaji wadogo na wakulima wamekuwa wakikosa haki katika kumiliki ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kibaya zaidi zipo mila ambazo zinamkandamiza mwanamke katika kumiliki ardhi, mila hizi zimekuwa zikimwaminisha mwanamke kwamba yeye ni wa kuolewa na kusubiri kurithi ardhi kutoka kwa mume wake. Hii tumeona changamoto yake kwamba, yapo baadhi ya makabila yanasadikika kwamba wanawake wao wanawaua waume zao ili waweze kurithi mali. Hii imekuwa ikiwanyima wanawake haki ya kupata, kutumia na kudhibiti ardhi moja kwa moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iweke mpango mkakati wa kutoa elimu ya Sheria hii ya Ardhi katika ngazi ya vijiji ili wananchi waweze kujua haki zao katika kumiliki ardhi. Kama Sheria ya Ardhi Na. 4 na Sheria ya Ardhi ya Vijiji Na. 5 za mwaka 1999 zinavyoainisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la wawekezaji na ardhi; kumekuwa na tatizo la wawekezaji kuhodhi maeneo makubwa ya ardhi na baadhi yao wamekuwa wakitumia sehemu ndogo tu ardhi hiyo, wapo ambao hawajaendeleza kabisa maeneo hayo na kusababisha mapori katikati ya vijiji na mara nyingi mapori haya yamekuwa yakitumika na wahalifu kama maeneo ya kujifichia. Vijana wa Kitanzania wana uhitaji mkubwa wa ardhi ili kuweza kufanya shughuli za kiuchumi, tukumbuke kwamba vijana hawa wa Kitanzania wamelelewa katika mila na desturi za Kiafrika ambapo mali zote ikiwemo ardhi ni za baba, hata pale wanapojitahidi kwenda shule na kuhitimu vyuo vikuu bado wanakuwa hawana fursa kubwa ya kupata ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Wizara hii isitengeneze utaratibu wa kuwagawia maeneo ya ardhi vijana ili nao waweze ku-contribute katika uchumi wa nchi yetu. Kwa kufanya hivi tutakuwa tumepunguza tatizo ambalo limekuwa likijitokeza mara kwa mara la wananchi kuvamia maeneo kama haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu wa kumiliki ardhi, kumekuwa na mlolongo mrefu katika umilikishaji wa ardhi, aidha kwa kupata cheti cha hakimiliki ya kimila ama kwa kupata hati. Hii imesababisha wawekezaji kukosa uvumilivu na kukimbilia katika nchi ambazo zina unafuu katika kumilikisha ardhi. Mlolongo huu mrefu umesababisha Watanzania kuwa wavivu wa kumiliki ardhi kihalali na kwa namna moja au nyingine tumekuwa tukiikosesha Serikali yetu mapato yanayotokana na ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, Ilani ya Chama cha Mapinduzi Ibara ya 37(a) inasisitiza kuimarisha utoaji wa huduma za ardhi. Napenda kuiomba Serikali hii iweze kutekeleza Ilani hiyo ili kuweza kumsaidia Mtanzania kuweza kumiliki ardhi ndani ya muda mfupi. Hili linawezekana kama tu tukiziwezesha Halmashauri zetu za Wilaya kuajiri vijana wa kutosha na Wizara ijikite zaidi katika kampeni nyingi zikiwemo zile za upimaji wa ardhi kuanzia ngazi za Vijiji mpaka za Miji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijahitimisha napenda kuikumbusha Serikali kwamba ilikuja Wilayani kwetu Magu Jimbo la Mheshimiwa Kiswaga ikaomba eneo kwa ajili ya kujenga nyumba za bei nafuu kwa ajili ya wananchi. Napenda kuwataarifu kwamba eneo hilo tayari lipo tunawasubiri tu ninyi mje muwekeze ili wananchi wetu waweze kunufaika kwa kupata nyumba bora kwa bei nafuu. Hata Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu tayari wameshawatengea eneo, tena eneo lipo halihitaji hata fidia ni kazi kwenu kuja kujenga nyumba hizo ili wananchi waweze kupata nyumba bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuhitimisha, napenda kuungana na wenzangu wote kwa kusema kwamba naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa fursa ya kuchangia kwa maandishi. Napenda kuipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa hotuba nzuri, lakini pamoja na yote, napenda kuwataarifu Waziri na Naibu wake kwamba kwa haraka haraka inaonekana watendaji wa Wizara hii wanafanya kazi kwa mazoea na ni wakati sasa wa watendaji hawa kusimamia Katiba ya nchi pamoja na Sera Taifa zinazoigusa Wizara hii ikiwemo Sera ya Taifa ya Mifugo ya mwaka 2006.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wajibu wa Wizara hii kuhakikisha kwamba utalii wa nchi yetu unaimarika kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo ile ya kutangaza vivutio vya utalii vilivyomo ndani ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha kuona nchi nyingine zikijitangaza kuwa na baadhi ya vivutio vilivyopo ndani ya nchi yetu kama come to Kenya and see Mount Kilimanjaro. Hili ni suala la kusikitisha sana pale nchi yetu inaposhindwa kukemea masuala haya kupitia Serikali yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashangaa kwa umri wangu sikuwahi kusikia kitu chochote kuhusu mjusi wa aina ya dinosaur aliyewahi kupatikana hapa nchini Tanzania Mkoa wa Lindi na kupelekwa Ujerumani. Nimekuwa na maswali mengi juu ya hili. Nimekuwa nikijiuliza ni kiasi gani cha fedha Ujerumani inaingiza kupitia huyu mjusi? Katika hizo fedha ni kiasi gani kinaletwa Tanzania na ni kiasi gani kinapelekwa Lindi kwa ajili ya maendeleo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha sana kuona hata mashuleni hili halitajwi popote na kibaya zaidi hata huko Ujerumani hatuna uhakika kama hawa wanataja mnyama huyo katokea Tanzania na kibaya zaidi historia ya mjusi huyu haijulikani na ipo mbioni kupotea kabisa tukizingatia uwepo wa kizazi hiki na kijacho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Wizara husika kutueleza ni shilingi ngapi tunaingiza kama nchi kutokana na mjusi huyu na ni jinsi gani tunafaidi kwa yeye kuwepo huko Ujerumani? Ninaisihi Serikali kumrudisha mjusi huyu nchini ili tuongeze kipato cha Serikali kupitia utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuiomba Wizara hii kuwapeleka Madiwani wa sehemu husika alipopatikana mjusi huyu na baadhi ya Wabunge wakiwemo wanaotoka Lindi kwenda kumuona mjusi huyu ili waje watuhakikishie uhai wake, lakini kikubwa zaidi tupate taarifa ya kujiridhisha juu ya kipato anachoingiza nchini humo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mchango huu, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuchangia hoja iliyopo mezani. Awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu. Pia napenda kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri inayofanya chini ya Rais wetu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Watanzania wengi wana imani kubwa na Serikali hii ya Awamu ya Tano, lakini Watanzania wengi pia wana matumaini makubwa sana na bajeti ya kwanza ya Serikali hii ya Awamu ya Tano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikupongeze wewe pia kwa ujasiri ulionao. Nikuhakikishie kwamba Watanzania wote wanaona ni jinsi gani unavyokitendea haki Kiti hicho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nijielekeze katika kuchangia hoja iliyopo mezani nikianza na sekta ya elimu. Kumekuwa na changamoto kubwa katika ugawaji wa fedha inayotengwa kwa ajili ya elimu. Mara nyingi tumekuwa tukiona kwamba fedha nyingi zimeelekezwa katika matumizi ya kawaida huku maendeleo ya elimu yakipata pesa ndogo na wakati tunajua kwamba maendeleo yamekuwa na changamoto kubwa na nyingi kama za ukosefu wa madawati, madarasa, vyoo, nyumba za Walimu, mabweni na maabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata tukirejea katika mwaka wa fedha wa 2015/2016, tunaona kwamba asilimia 84 ya fedha iliyotengwa kwa ajili ya elimu ilielekezwa katika matumizi ya kawaida huku asilimia 16 tu ikielekezwa katika fungu la maendeleo ambapo nusu yake ilielekezwa katika mikopo ya elimu ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto hii imeathiri sana elimu katika shule zetu za sekondari, primary lakini na vyuo vyetu vya VETA ambapo vimeshindwa hata kukidhi haja ya kuwa na teknolojia ya kisasa. Kwa mfano, mwanafunzi anayejifunza ushonaji katika Chuo cha VETA anatumia cherehani ya kawaida yaani ile ya kutumia miguu na mara nyingi wanafunzi hawa wamekuwa wakitamani kuajiriwa katika viwanda vikubwa let me say kama A to Z cha kule Arusha ambacho kina teknolojia ya kisasa na mashine zake ni za umeme. Ina maana tunawapa mzigo hawa wawekezaji kwa kuanza kuwa-train upya hawa wanafunzi kwa muda mrefu mpaka hapo watakapoanza kufikia ile quality ya ku-produce kile kinachohitajika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali katika ugawaji wa fungu la sekta katika mwaka wa fedha ujao itenge fedha za kutosha kwa ajili ya maendeleo ya elimu. Kwa kufanya hivi, maendeleo yetu yatasonge mbele, lakini pia tutapata nafasi kubwa ya kupata picha ya matumizi ya fedha ya maendeleo ya sekta ya elimu. Kama inawezekana hili fungu la mikopo ya elimu ya juu litolewe katika fungu la maendeleo lihamishiwe katika fungu la matumizi ya kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nijielekeze katika kuchangia masuala yanayohusu Mkoa wangu wa Mwanza. Nianze kwa kuishukuru Serikali kwa kututengea fedha kwa ajili ya meli mpya katika Ziwa Viktoria lakini nishukuru pia Serikali kwa kutenga fedha kwa ajili ya upembuzi yakinifu wa daraja litakalounganisha Kigongo na Busisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaendelea, napenda kutanguliza salamu zangu za masikitiko makubwa kwa Serikali juu ya Mkoa wa Mwanza kuwa mkoa unaoongoza kwa umaskini, kwa kweli ni suala la kushangaza sana na ukizingatia ripoti kutoka BOT inaonesha kwamba Mkoa wa Mwanza ni wa pili katika kuchangia mapato kwa Serikali. Je, hii inamaanisha kwamba Serikali haithamini watu wa Mkoa wa Mwanza? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, labda kwa kukutaarifu tu ni kwamba watu wa Mwanza ni watafutaji wazuri tu na wamekuwa wakijishughulisha na shughuli mbalimbali zikiwemo za kilimo, ufugaji, uvuvi, uchimbaji kule Sengerema na Misungwi, utalii pale Saa Nane Island, ukienda Magu utakutana na museum kubwa ya kabila la Wasukuma lakini ukienda Ukerewe pia utakutana na mawe yanayocheza. Nikuhakikishie kwamba shughuli zote hizi zimekuwa zikichangia mapato kwa Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama kweli Serikali ya Awamu ya Tano ina nia nzuri na Mkoa wa Mwanza, narudia kama kweli Serikali ya Awamu ya Tano ina nzuri na Mkoa wa Mwanza naiomba katika mwaka wa fedha ujao itenge fedha ya kutosha kwa ajili ya miradi ambayo tayari imekwishaainishwa ndani ya mkoa huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna miradi ambayo tayari ilikwishaanzishwa ila haijakamilika na mara nyingi tumekuwa tukipata majibu ya danadana. Naiomba Serikali iweze kuikamilisha miradi hii ili watu wa Mwanza waweze kunufaika na matunda ya michango yao katika pato la Taifa. Miradi hiyo ni kama ule wa maji wa Sengerema, Ukerewe, Misungwi na Magu pale Kisesa na Bujora na maeneo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kumekuwa na miradi mingine ya umeme ambayo bado haijakamilika mpaka hivi sasa. Ipo pia miradi ya barabara ambayo imekuwa ikiongelewa mara kwa mara kama mradi wa barabara ya kutoka Kamanga - Sengerema ambao pia upo ndani ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi na mradi wa barabara kutoka Kisesa - Usagara na barabara nyingine nyingi ndani ya mkoa huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Serikali imeweza kutoa maji Ziwa Viktoria ikayapeleka Shinyanga iweje leo mtuaminishe watu wa Mwanza kwamba Serikali imeshindwa kutoa maji Ziwa Viktoria kuyapeleka Sumve, Magu ama Sengerema, kwa kweli suala hili linatuweka katika hali ya sintofahamu. Serikali inaposema kwamba ina mradi wa maji vijijini imaanishe siyo tusikie kwamba miradi hii inapelekwa mijini kama ilivyokuwa huko nyuma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ina maji mengi sana, tukiachana na maji yaliyopo kwenye maziwa, mito na bahari yapo maji yanayotokana na mvua ambayo mara nyingi yamekuwa yakisababisha maafa ya mafuriko katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Napenda kutumia fursa hii kuishauri Serikali kuanza kufikiria kujikita katika miradi ya kuhifadhi maji katika mabwawa kwa ajili ya matumizi ya binadamu na matumizi mengine. Napenda kutumia fursa hii kuishauri Serikali kukubaliana na wazo la Kamati ya Bajeti la kuongeza Sh. 50 katika tozo ya mafuta ili tuweze kuiwezesha sekta hii ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika sekta ya kilimo tunafahamu kwamba asilimia 70 ya Watanzania ni wakulima na wengi wao wakiwa ni vijana na wanawake. Kwanza kabisa, napenda kuipongeza Serikali kwa dhamira yake ya kupunguza ama kuondoa kabisa ushuru mbalimbali katika mazao ya kilimo. Nimesoma hotuba iliyopo mezani inaonesha kwamba sekta ya kilimo imetengewa shilingi trilioni 1.56 ambayo ni sawasawa na asilimia 4.9 tu ya bajeti ya Serikali tukitoa deni la Taifa. Napenda kuishauri Serikali kuongeza fedha hii kwani haiendani na watu wanaotegemea kilimo. Kwa sababu Serikali…
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
kiti, TTCL ni moja ya mashirika yaliyo chini ya Wizara hii ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Taasisi hii ya TTCL ni kampuni Kongwa, kuliko kampuni zote za mawasiliano Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ni jambo la kusikitisha kwamba TTCL imekuwa nyuma sana katika masuala ya kiteknolojia kiasi kwamba imekuja na wateja wachache sana ikilinganishwa na kampuni nyingine za simu. Napenda kutumia fursa hii kuishauri Serikali yangu kuongeza nguvu ya uwekezaji katika Kampuni hii kama ilivyofanya kwa ATCL kwa kununua ndege ili kusaidia kui-boost ATCL. Ni wakati sasa wa kuiboresha TTCL na sina mashaka na nia nzuri ya Mheshimiwa Rais kwani tayari mmeshamteua kijana mahiri kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na changamoto kubwa hasa katika suala zima la kuongeza nguvu ya ringtones na mimi binafsi nimekuwa nikijiuliza, je, Serikali inanufaika kiasi gani na ringtones hizi? Kwa kuwa zimekuwa zikiingizwa kwenye simu zetu bila hata idhini zetu. Kwa mtazamo wa haraka, ni hakika Kampuni za Simu zinapata fedha za kutosha kutokana na huduma hii. Mashaka yangu makubwa yapo kwenye malipo kwa vijana wenzangu na wasanii wote kwa ujumla pale nyimbo zao zinapotumika kama ringtones.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutumia fursa hii kuishauri Serikali yangu kuanza kulifuatilia suala hili kwa ukaribu kwa kuhakikisha Kampuni za Simu zinalipa mapato yanayotokana na ringtones kwa Serikali na wasanii ambao nyimbo zao zinatumika wanapata stahili zao kwa uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mchango huu, naomba kuunga mkono hoja.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami nianze kwa kuunga mkono hoja na sina mashaka na Serikali yangu ya Awamu ya Tano kwa kazi nzuri inayofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kwa moja nianze na suala zima la udhibiti wa UKIMWI. Napenda kuipongeza Wizara kwa juhudi nzuri inazofanya kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya afya. Hata hivyo, kumekuwa na tatizo kubwa la watoto wanaozaliwa na maambukizi ya VVU. Kwa mujibu wa Kanuni ya Maadili, watoto hawa hawapaswi kupimwa bila idhini ya wazazi. Mara nyingi wazazi hawa wamekuwa hawawapi taarifa ya status zao watoto hawa na tatizo linakuja pale ambapo watoto hawa wanaingia katika mahusiano katika umri mdogo wakiwa shuleni ama mitaani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu zinaonesha kwamba lipo ongezeko kubwa la watoto kujihusisha na ngono katika umri mdogo. Napenda kutumia fursa hii kuiomba Serikali ije na programu nzuri ambayo itawawezesha watoto hawa kuweza kujitambua na kufahamu ni namna gani ya kuweza kujilinda wao pamoja na wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia kuhusu tatizo la hedhi isiyo salama. Kumekuwa na tatizo kubwa sana la hedhi zisizo salama ambalo limekuwa likiwaandama sana wasichana na wanawake ambao wako vijijini lakini na wale ambao hawana uwezo wa kupata taulo salama. Changamoto hii imesababisha matatizo mengi yakiwemo magonjwa mbalimbali yanayotokana na kutumia zana ambazo sio salama kipindi hicho cha hedhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kama mdau mmojawapo wa hedhi salama na napenda ku-declare interest kwamba ni mzalishaji wa taulo ambazo zinatumika zaidi ya mara moja na mara nyingi nimekuwa nikijitolea kutoa bure sehemu mbalimbali ikiwemo mashuleni na magereza. Napenda kuiomba Serikali yangu kuungana na sisi wadau ili pale inapowezekana iweze kutoa pedi hizi kwa makundi mbalimbali yakiwemo ya wafungwa wanawake, wanawake wasio na uwezo lakini pia kwa watoto wa kike ili kuweza kupunguza tatizo la utoro wa shuleni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba moja kwa moja nijielekeze katika Mkoa wangu wa Mwanza. Kwanza napenda nianze kwa kumkumbusha Waziri ahadi ambazo ametuahidi, ipo ile ahadi ya kutuongezea OC katika Hospitali ya Sengerema ambapo OC inayokuja kwa ajili ya vitanda ni ndgo mno kulingana na hali halisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumkumbusha pia Mheshimiwa Waziri ahadi yake ya vitanda katika Kituo cha Afya cha Malya. Alimuahidi Mbunge wangu wa Sumve na sisi tunasubiri ahadi hiyo itimie kwa sababu akina mama wanahangaika sana, wanajifungulia chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ya Magu nitaongelea Kituo cha Afya cha Kisesa, ni kituo ambacho kinahudumia takribani kata tano na tarafa nzima ya Sanjo. Kituo hiki kina uhitaji mkubwa wa x-ray na chumba tayari kimeshaandaliwa vizuri kwa ajili ya mashine hiyo. Hivyo basi, tunaiomba Wizara itushike mkono tuweze kupata mashine hiyo ili wananchi wa Tarafa ya Sanjo wasipate tabu kwenda maeneo ya mbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Ilemela haina Hospitali ya Wilaya. Kwa juhudi ya Halmashauri imeweza kuanza kujenga jengo la OPD. Tunaishukuru Wizara kwa kuweza kuchangia shilingi milioni 300 kwa ajili ya jengo hilo ambalo lina thamani ya zaidi ya shilingi milioni 600. Hata hivyo, bado safari ni ndefu, hospitali nzima gharama yake ni shilingi bilioni 25, hiyo ni kwa ajili ya majengo pamoja na vifaa. Tunaomba sana Wizara ituangalie ili wananchi wa Ilemela wapungukiwe na matatizo ya kwenda katika misongamano ya wagonjwa katika Hospitali ya Bugando pamoja na Sekou Toure.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na yale yote niliyochangia hapo awali, naomba kutumia fursa hii kuchangia yale niliyoshindwa kwa sababu ya muda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Ukerewe Mkoani Mwanza ina changamoto kubwa ya mimba za utotoni na uzazi usio na mpangilio. Jambo hili limezua uwepo wa wategemezi wengi kuliko wanaotegemewa. Hivyo basi, nipende kuiomba Serikali kuliangalia suala hili kwa ukaribu
zaidi na kuweza kuweka mkakati wa campaign ya masuala ya afya ya uzazi na uzazi wa mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru sana AMREF kwa kudhamini theatre za vituo vya afya vya Kata za Muriti na Kagunguli ndani ya Wilaya ya Ukerewe. Tayari miundombinu imekamilika bado tu ukamilishaji wa vifaa husika. Wasiwasi wangu upo kwenye Kituo cha Afya cha Kagunguli ambacho bado hakijapata huduma ya maji salama na katika ziara ya Makamu wa Rais Wilayani Ukerewe, Waziri wa Maji aliagizwa kusimamia suala hilo. Kweli mradi ulianza kwa kasi kubwa na cha kushangaza mradi huo umesimama sasa kwa takribani miezi miwili. Naomba Waziri mwenye dhamana ya maji asikie kilio hiki na atuondoe katika hali ya sintofahamu tuliyonayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na changamoto niliyochangia hapo awali ya ukosefu wa hospitali ya Wilaya ya Ilemela, lipo tatizo lingine la Wilaya ya Ilemela kukosa vituo vya afya vya kutosha. Jimbo la Ilemela lina kata 19 ila cha ajabu ni kwamba lina zahanati tatu tu ambazo hata miundombinu yake haijakamilika. Kwa mfano, Kituo cha Afya cha Buzuruga hakina wodi ya wanaume wakati kinahudumia maelfu ya wananchi kutoka ndani na nje ya Wilaya ya Ilemela. Napenda kuiomba Serikali kukiangalia Kituo hiki cha Afya cha Buzuruga kwa jicho la pekee na kama nilivyosema kuwa hakuna hospitali ya wilaya na vituo vya afya ni vitatu tu wilaya nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ya Kwimba, Jimbo la Kwimba, kipo Kituo cha Afya cha Mwamashimba ambacho hakina theatre na kusababisha wananchi kukosa upasuaji na wengine wamekufa kwa kukosa huduma ya upasuaji pale kunapotokea dharura. Naiomba Serikali kufanya maarifa ili kituo hicho cha afya kiweze kupata theatre ili kunusuru maisha hasa ya akina mama wajawazito.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Kwimba ipo Zahanati ya Buyogo ambayo kwa kweli ni ya mfano. Nitumie nafasi hii kuwapongeza Waganga na Wauguzi wa zahanati hii kwa kazi nzuri. Wamekuwa wakihudumia wananchi wengi kuliko hata hospitali ya wilaya na huduma zao ni nzuri. Mimi leo naungana na Mbunge wa Kwimba kuomba Serikali kuipandisha hadhi zahanati hii ya Buyogo kuwa Kituo cha Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na yote hayo, naomba Wizara itutatulie matatizo ya ukosefu wa maduka ya MSD katika hospitali za wilaya za Mkoa wa Mwanza na tatizo la ukosefu wa Waganga na Wauguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mungu kwa afya njema aliyonijalia. Nitumie fursa hii kuipongeza Wizara kwa hotuba nzuri yenye mipango yenye kuleta matumaini kwa wasanii, wanahabari na wanamichezo.

Mheshimiwa Spika, moja kwa moja nianze kuchangia hoja iliyopo mezani. Kumekuwa na changamoto kubwa ya watoto wa Kitanzania kutokua na ushiriki mkubwa katika michezo. Hivvyo, basi tumekuwa tukijenga Taifa lisilo na hamasa ya michezo. Hivyo basi, nipende kuishauri Serikali kufanya jitihada za kurudisha michezo mashuleni ambayo itaweka wanafunzi katika hali ya kuepuka hata vishawishi. Sambamba na hili, Serikali pia irudishe ushiriki wa wanafunzi katika sanaa na utamaduni kama hapo zamani.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la ukosefu wa timu za kushiriki katika michezo kama volleyball, handball, badminton, table tennis na kadhalika ambayo Tanzania kama Taifa tumekua tukijisahau na kuelekeza nguvu nyingi katika baadhi ya michezo kama mpira wa miguu. Naiomba Serikali iwezeshe ukuaji wa michezo ya aina yote kwa usawa.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kituo cha makumbusho cha Bujora. Hiki ni kituo cha makumbusho ya kabila la Kisukuma kilichopo Mwanza, Wilaya ya Magu. Kituo hiki kimepoteza umaarufu wa hadhi yake hata kupelekea upungufu wa watalii wa nje na ndani kulingana na miaka ya nyuma. Bujora Sukuma Museum inahitaji fedha ili kuweza kuimarishwa na kukarabatiwa kurudi katika ubora wake.

Mheshimiwa Spika, hivyo basi, naiomba Serikali kulisimamia suala hili kwa ukaribu ili kituo hicho kiimarike na kwa kufanya hivyo tutaongoza utalii ndani ya Mkoa wa Mwanza na kwa ujumla Serikali itapata kuongoza ukusanyaji kodi.

Mheshimiwa Spika, baada ya mchango wangu huu mfupi, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuchangia hotuba ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Nianze kwa kuipongeza Wizara kwa hotuba nzuri yenye ufafanuzi unaoeleweka kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI) imekuwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa wataalamu wa kutosha, ninashukuru hotuba imelitambua pia suala hili ni imani yangu kuwa Serikali itaongeza wataalam ambao wengi wapo mitaani hawana kazi na wengi wao pia ni vijana ambao wamekuwa wakihangaika kutafuta kazi kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na changamoto hiyo ya ukosefu wa wataalam wa kutosha, bado taasisi hii ya TAWIRI inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa vitendea kazi, suala ambalo ni muhimu katika kukamilisha majukumu ya taasisi. Pamoja na hilo bado vitendea kazi vilivyopo ni vichakavu na hivyo basi nipende kuiomba Serikali kuipa kipaumbele taasisi hii kwa kuipatia fedha za kutosha ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufasaha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hotuba hii na Mkoa wa Mwanza, kwanza kabisa nianze kwa kuelezea masikitiko yangu makubwa kwa namna Wizara ilivyoutenga Mkoa wa Mwanza. Ukipitia hotuba yote toka ukurasa wa kwanza hadi wa mwisho, hakuna sehemu yoyote utakayokuta mpango wa kuboresha, kutangaza au kuendeleza utalii Mkoani Mwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni suala la aibu sana ukizingatia masuala yaliyopo Mwanza ambayo yangeweza kuvutia watalii wengi na kuliingizia Taifa fedha kupitia utalii. Ni muda mrefu sasa Serikali imekuwa haiuweki Mkoa wa Mwanza kwenye mpango wa kuendeleza utalii nchini, tunajiona kama vile tumetelekezwa na Serikali ukizingatia Awamu hii ya Tano Serikali imebakiza miaka mitatu tu na kwa miaka miwili hii ya mwanzo bado haijaona umuhimu wa utalii wa Mwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda niikumbushe Serikali kuwa Mkoa wa Mwanza una Hifadhi ya Saanane Island ambapo wanyama wengi wapo na kuna kilele kirefu ambacho mtu huweza kuliona Jiji la Mwanza na uzuri wake kwa ujumla. Zipo pia sauti za makumbusho mbalimbali kama Bukumbi ambayo inajenga historia ya dini ya kikristo na muhimu kwa kumbukumbu ya uanzishwaji wa dini hiyo kwa Uganda na Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo pia makumbusho ya Kageye ambapo kuna makaburi ya watafiti au explorers Frederick Barker ambaye alifariki mwaka 1875 kwa kuugua kipindupindu na Dkt. Junker ambaye alitumwa na nchi ya Urusi kuja Afrika kutafiti nchi za Sudan na Egypt.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kipo pia kituo cha makumbusho cha kabila kubwa kabisa la Wasukuma maarufu kama Bujora Sukuma Museum ambapo kuna historia ya chiefdoms zote za kabila hilo lililosambaa katika mikoa minne ambayo ni Simiyu, Mwanza Shinyanga na Tabora. Na kila mwaka kituo hiki huandaa tamasha la kitamaduni maarufu kwa jina la Bulabo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka enzi za utoto wangu kijiji changu cha Bujora kilikuwa kinasheheni watalii kutoka pembe mbalimbali za dunia kuja kujionea ngoma za Kisukuma katika tamasha hili la Bulabo na kwa mwaka makumbusho hayo yalikuwa yanatembelewa na watalii sana. Kama sijakosea na kwa ufahamu wangu duniani kuna jiwe moja tu linalocheza na lipo Wilayani Ukerewe. Pamoja na vyanzo hivyo vya utalii bado Mkoa wa Mwanza unapakana na nchi za Uganda na Kenya, ukivuka Ziwa Victoria na kwa kutangaza utalii wa Mkoa wa Mwanza tungeweza kuvutia wengi kutoka nchi hizo na nyinginezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa Serikali ni kuhakikisha kuwa masuala haya ya utalii Mwanza yanatangazwa na ukweli itafika kipindi na sisi tutachoka kuona Serikali inatusahau kila mwaka na huku vijana wa Mwanza wanahangaika kwa kukosa ajira wakati wangeweza kuajiriwa ama kujiajiri kupitia sekta hii ya utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kulitazama ombi langu kwa ukaribu kwani tunapoteza mapato mengi mno kwa kutokujali kuendeleza utalii wa Mwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mchango wangu huu naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kunipatia afya na kuniwezesha kusimama ndani ya Bunge lako Tukufu. Pia, niipongeze Serikali yangu ya Awamu ya Tano kwa kazi nzuri inayofanya. Niipongeze pia Wizara hii ya Viwanda Biashara na Uwekezaji kwa kazi nzuri na jitihada zake katika kuijenga Tanzania ya Viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa kuanzisha programu ya kuwapa vijana 1,000 elimu ya utengenezaji wa bidhaa za ngozi kutoka katika Chuo cha DIT Mkoani Mwanza na tayari 90 wamehitimu wiki iliyopita na wengine wanaendelea kujiunga na kozi hiyo. Pamoja na pongezi hizo bado ipo haja ya wanafunzi hawa kutafutiwa viwanda ambapo wataweza kufanya internship.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali yangu, kipo kiwanda ambacho kilikuwa chini ya Mwanza Tanneries cha kutengeneza bidhaa za ngozi ambacho kilibinafsishwa na mwekezaji yule hajulikani hata alipo, lakini hata mashine zilizomo mle ndani zimeshatolewa. Nipende kuiomba Serikali yangu sikivu iweze kukirejesha kile kiwanda kwa Serikali, ili wanafunzi waweze kupata sehemu ya kufanyia practicals, na vile vile lakini waweze kupata sehemu ya kufanyia internship na kuajiriwa kama ikiwezekana. (Makofi)


Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya uwekezaji nchini si rafiki kwa wawekezaji wa ndani na nje, hivyo ipo haja ya Serikali kutengeneza mazingira mazuri. Mimi binafsi na-declare interest kwamba ni mmiliki wa kiwanda cha mavazi na taulo za kike. Ninapoongea hapa ninaongea kutokana na kile ninachokifahamu, ni ukweli kwamba hatutaweza kuijenga Tanzania ya viwanda kama hatutakaa na kupitia hizi kodi na tozo mbalimbali ambazo ni nyingi na zimekuwa zikiathiri uwekezaji ndani ya nchi hii. (Makofi)Mheshimiwa Naibu Spika, tozo hizi na kodi zimesababisha bidhaa zetu kuwa za gharama kuliko hata zile zinazotoka nje. Haiwezekani leo mfanyabisahara ambaye ananunua pamba kutoka kwa wakulima inafika hatua ana- prefer kuuza nje ya nchi kwa sababu hatalipa VAT. Pamba hiyo hiyo ikienda nje inatengenezwa nguo, nguo zinaingia ndani bila kulipa VAT, sasa inakuwaje kwamba, viwanda vyetu viuziwe kwa wafanyabiashara wale watalipa VAT na sisi pia huku ndani tuuze na tulipe VAT? Ina maana hatutaweza ku-compete na masoko ya nje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mzuri tunauona kwamba hata mbolea inayotoka Kenya leo hii ni ya bei ndogo ikifika nchini kuliko ile mbolea ambayo tunazalisha hapa. Kwa namna hii hatutaweza kutengeneza Tanzania ya viwanda. Suala hili liangaliwe kwa umakini kwa sababu sasa limeanza kuhamasisha wawekezaji wa ndani ya Tanzania kwenda kuwekeza katika nchi za jirani kwa sababu wanajua wakiwekeza kule wataleta bidhaa zao nchini na hawatalipa VAT. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sina mashaka na kazi nzuri anayofanya Mheshimiwa Waziri na wasaidizi wake wote, lakini kama tunavyofahamu kwamba Wizara hii ni mtambuka na inahitaji cooperation kutoka katika Wizara mbalimbali kama ya Afya, Kilimo, Fedha, Nishati na nyinginezo. Hata hivyo bado inahitaji ushirikiano kutoka Taasisi mbalimbali za Kiserikali kama TFDA, EPZA, TIC, NDC, SIDO, NEMC na nyinginezo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo langu hapa ni urasimu mrefu. Kumekuwa na urasimu mrefu sana katika uwekezaji wa Tanzania ambao umekatisha tamaa viwanda vingi. Kwa mfano, mwekezaji wa kiwanda cha dawa atahitaji kwenda TFDA, NEMC, atahitaji kupitia kwa Msajili wa Kampuni, ataenda TRA na kote anakokwenda kunakuwa na muda mrefu wa kusubiria matokeo ambayo anataka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nipende kuishauri Serikali kuliangalia hilo kwa ukaribu kwa sababu imesababisha sisikupoteza wawekezaji wazuri na wameenda kuwekeza katika nchi nyingine. Kwa mfano kiwanda cha Omnicane ambacho kilitaka kujengwa hapa Tanzania, lakini kutokana na urasimu huu na changamoto hizi nilizotaja hapo awali kimeenda kuwekeza Mauritius ambapo leo kimeajiri wafanyakazi 1,472 lakini kinazalisha umeme kutokana na makapi ya miwa gigawatts 717 ambayo ina-produce katika community inayowazunguka, lakini pia, kwa siku kina-produce sukari tani 8,500. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa tulicheza karata mbovu kwa kweli, kwa sababu sisi ndio tungekuwa tunanufaika na haya. Tuki-compare kwa haraka haraka viwanda vyetu vikubwa ambavyo ni Kilombero na Mtibwa kwa mwaka vinazalisha sukari tani 80,000 ambayo ni production ya siku tatu ya Kiwanda cha Omnicane. Cha kushangaza zaidi pamoja na ukosefu wa sukari ya kutosha ndani ya nchi yetu na experience hiyo ambayo nimeitoa kutokana na kiwanda cha Omnicane bado tunaendelea kuweka mazingira magumu kwa viwanda ambavyo vinataka kuanzishwa hapa vya sukari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mzuri ni kule Tarime. Tarime kuna mwekezaji ambaye yupo tayari kufungua kiwanda cha sukari, lakini kumetokea vita iliyoanzishwa na Mbunge wa Tarime Vijijini ili kukwamisha kiwanda hiki kujengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kiwanda hicho kikijengwa kitanufaisha wananchi wa Tarafa za Ingwe na Inchage ambavyo ni ambavyo ni vijiji vinne vya Biswalu, Mrito Matongo na Kijiji cha Wegita…

T A A R I F A . . .

MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa hiyo siipokei kwa sababu hata wiki iliyopita wananchi wa vijiji hivyo vinne vya Biswalu, Mrito, Matongo na Wegita kijiji wanakotokea wanangu mimi Bhoke na Ryoba walikuja hapa Dodoma na mabasi mawili, wamekuja kuandamana na kuja kuonana na Waziri wa TAMISEMI. Na mimi nimekaa nao, nimepata taarifa hiyo, hata taarifa ya habari ilionesha hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kiwanda hiki kitakapojengwa pale kitanufaisha tarafa za Ingwe na Inchage katika vijiji hivyo vinne ambavyo ni Biswalu, Mrito, Matongo na Wegita, kijiji ambacho wanangu wanatokea Bhoke na Ryoba. Pamoja na hayo yote kiwanda hiki kikijengwa kitatoa ajira kwa wananchi 15,000 lakini kitapunguza changamoto ya ukosefu wa sukari ndani ya nchi hii. Vilevile pia kitaongeza maendeleo katika vijiji hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nipende kuiomba Serikali yangu kuwa makini na suala hili iweze kuingilia kati na kusimamia, ili kiwanda hiki kiweze kuanzishwa kule Tarime.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo yote naomba niunge mkono hoja asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami nianze kwa kuipongeza Wizara kwa hotuba nzuri yenye malengo ya kuinua uchumi wa nchi yetu kupitia kilimo, uvuvi na mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kwamba kilimo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa nchi yetu. Kama tunavyofahamu kilimo kimeajiri takribani asilimia 75 ya wananchi lakini kimeweza kuzalisha chakula almost asilimia 100 ambacho kinatumiwa na wananchi wa nchi yetu hii na
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naomba sana Mheshimiwa Waziri atusaidie Mkoa wa Katavi hasa Wilaya
kuzalisha malighafi nyingi kwa ajili ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na yote hayo bado Serikali imeendelea kutenga fedha kidogo kwa ajili ya Wizara hii ya Kilimo tena kinyume kabisa na Azimio la Maputo ambalo linahitaji Serikali kutenga asilimia 10 ya bajeti yake kwa ajili ya kilimo. Ni wakati sasa wa Serikali kuhakikisha kwamba inalifanyia kazi azimio hili kama kweli tunataka kuijenga Tanzania, hatutaweza kuijenga bila kuendeleza sekta hii ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze sasa kuchangia changamoto za masuala ya Wizara hii ndani ya Mkoa wangu wa Mwanza, nitajikita sana katika masuala ya uvuvi. Kumekuwa na malalamiko mengi kwa miaka mingi kutoka kwa wavuvi ambao wanavua katika Ziwa Victoria na wapo baadhi ya wenzangu ambao tayari wameshatangulia wameliongelea hili lakini jinsi lilivyo nyeti suala hili na mimi nitaendelea kuliongelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama wote mnavyofahamu kuwa mimi ni mwakilishi wa vijana, tena ninayetokana na Mkoa wa Mwanza, ambapo vijana wengi wamejiajiri na kuajiriwa katika sekta ya uvuvi. Hata pale ambapo kunatokea na migomo mbalimbali ya uvuvi lazima vijana hawa wanaathirika kwa namna moja au nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, uvuvi katika Ziwa Viktoria una manufaa makubwa kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa na Taifa kwa ujumla kwa sababu kuna mlolongo wa wafanyabiashara wengi ambao wananufaika kutokana na uvuvi huo. Wapo akinamama ambao wanakaanga na kuuza samaki katika vijiwe mbalimbali; wapo ambao vijana ambao wameajiriwa katika viwanda vya samaki na katika mialo ya samaki; wapo wafanyabishara wanaosafirisha samaki ndani na nje ya nchi; wapo watu ambao kazi yao ni kusafisha tu samaki hawa; wapo wafanyabiashara pia ambao wamenufaika kwa namna mbalimbali kutokana na uvuvi huu wa Ziwa Viktoria na pia wapo mamilioni ya Watanzania wanaotegemea kupata kitoweo kutoka katika ziwa hilo na kupata virutubisho kwa ajili ya kujenga afya yao. Hao ni baadhi tu ya wanufaika wa uvuvi wa Ziwa Viktoria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, unapotengeneza mazingira magumu kwa mvuvi wa Ziwa Viktoria ujue ni namna gani unavyoathiri uchumi wa nchi. Wavuvi hawa hawa wamekuwa wakishirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama katika kuwabaini wale ambao wanavua kwa njia haramu. Hivyo basi wana haki ya kusikilizwa mahitaji yao kwa sababu yamekuwa ni ya muda mrefu na naamini kabisa pale Serikali itakapoamua inaweza kuyatatua matatizo haya na yakafika mwisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wavuvi hawa mara nyingi wamekuwa wakiomba kuruhusiwa kuuza samaki tofauti na bondo. Mabondo yamekuwa ni gharama kuliko hata mnofu wa sangara. Leo hii mvuvi analazimika kuuza samaki pamoja na bondo lake ina maana yule anayenunua ndiyo ananufaika zaidi, wakati wao ndio wanaotoa jasho. Niombe Serikali iweze kuliangalia suala hili, nafahamu ina wataalam wengi ambao wanaweza wakakaa wakamshauri Waziri pamoja na Naibu wake wapate kuliangalia hili na namna gani wavuvi hawa wanaweza kunufaika kutokana na hayo mabondo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mara nyingi wamekuwa wakiomba kuondolewa vikwazo vya kuuza samaki mbichi mzima katika masoko ya nje ya nchi. Wapo wavuvi wakubwa na wadogo, lakini wapo wale ambao wanaweza kusindikika na kupaki, ifike wakati sasa Serikali ione...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuchangia mchana huu wa leo. Awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kunipatia afya ya kuweza kusimama mbele ya jukwaa hili. Pia nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na timu yote ya Wizara ya Afya kwa kazi nzuri wanayofanya. Mungu awabariki ana azidi kuwatia moyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa sijatenda haki kama sitompongeza Mheshimiwa Rais, kwa kazi nzuri anayofanya na kwa usikivu alionao. Tumekuwa tukiona maendeleo mbalimbali hata katika sekta hii ya afya katika ugawaji wa madawa na kuyasambaza, pia hata katika usambazaji wa magari ya kubebea wagonjwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda katika hili niseme ahsante sana kwa Serikali kwa ambulance ambayo tumepoke katika Kata ya Kabila, Jumamosi iliyopita imewasilishwa na Mbunge tunashukuru sana, sisi kama wananchi wa Magu tuna imani sana na Serikali hii na kwamba mnatusikiliza na tutazidi kuwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo bado kuna changamoto kubwa sana ya ukosefu wa watumishi katika sekta ya afya. Zahanati zetu, hospitali zetu zina changamoto kubwa sana, hivyo basi Serikali iliangalie hili kwa ukaribu kama ilivyotoa ajira hapo nyuma ijitafakari tena itoe kulingana na matakwa halisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na changamoto ya ukosefu ya chanjo kupungua kwa kasi bado kumekuwa na tatizo la chanjo ya kichaa cha mbwa. Chanjo hii imekuwa ni adimu imekuwa kama bahati nasibu, naomba Serikali iangalie kwa ukaribu, kwanza ni gharama kwa mwananchi wa kawaida, sindano moja siyo chini ya Sh.30,000, lakini hata kuipata hiyo sindano inaweza ikawa shida, ikakulazimu kutoka nje ya mkoa. Hivyo basi, tunaomba Serikali iangalie kuanzia bei na upatikanaji wake kwani sindano zinazohitajika ni tatu, kwa hiyo Sh.90,000 kwa mwananchi wa kawaida ni kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nimevaa uhalisia wangu, mimi kama champion wa hedhi salama sitajisikia vizuri kama sitaishauri Serikali siku ya leo juu ya hedhi. Suala la hedhi tumekuwa tukilichukulia poa kwa sababu siyo ugonjwa, ndiyo kweli siyo ugonjwa lakini tatizo la hedhi kutokuwa salama ni changamoto kubwa sana na imekuwa ikisababisha magonjwa mengi mno.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri atakubaliana na mimi kwamba dawa nyingi antibiotics wanazosambaza katika vituo vyetu vya afya, katika hospitali zetu zinakuwa consumed na wanawake, wanawake ambao wanatibiwa magonjwa ambayo yanatokana na ukosefu wa hedhi salama, ni lazima tukubaliane na hilo. Ndiyo maana tunasimama hapa na kusema kwamba Serikali iangalie namna ya kuweza kutoa nyenzo za wanawake na wasichana katumia katika siku zao, tunachomaanisha ni kwamba ni bora tu-prevent magonjwa kuliko kuacha yatokee ndiyo tutoe dawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo suala hili ni muhimu sana Serikali kuliangalia, pamoja na kwamba tunafahamu mnayo mambo mengi ya kutekeleza...

T A A R I F A . . .

MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa hiyo kwa niaba ya wanawake wote wa Kitanzania. Kwa hiyo, tunaposema wapewe nyenzo hizi ni kwamba tunataka ku- prevent magonjwa kuliko kutibu na kama tunavyojua prevention is better than cure. Kwa hiyo, tunaamini kabisa Serikali hii sikivu leo hii itaenda kujitafakari upya. Pamoja na kwamba wana mambo mengi tunaamini wanao wadau wengi ambao wanaweza wakawa-aproach wakaweza kuwasaidia katika hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunafikiria huko, tuangalie pia namna ya kupunguza bei ya hizi taulo za kike tuangalie kuanzia VAT kama zinaweza kufutwa zifutwe, kama kuna possibility ya regulate bei ili wanawake wote na wasichana waweze ku-afford itakuwa ni vema zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo nianze kuchangia masuala yanayohusu mkoa wangu.

Katika Wilaya ya Ukerewe Mkoani Mwanza kumekuwa na changamoto nyingi sana za kiafya, kwa wale ambao hawaifahamu Ukerewe Wilaya hii ni muunganiko wa visiwa 38. Kipo Kisiwa cha Irugwa kina changamoto nyingi kwa nini nimekichagua chenyewe tu katika visiwa vyote 38.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwananchi kutoka Irugwa kuifikia hospitali ya Wilaya anachukua takribani saa nne na kuendelea, siyo kwamba katika kisiwa hiki hakuna zahanati, kisiwa hiki ni Kata pia na ina zahanati, lakini cha ajabu ni kwamba ina mtumishi mmoja tu ambaye ni Mhudumu ambaye hana ruhusa hata ya ku-prescribe nusu ya kidonge cha panado kwa mgonjwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wakati sasa wa Serikali hii kusikilza kilio hiki, wananchi wa Irugwa wameteseka kwa muda mrefu, naomba sana uwepo wa haraka sana wa kuwapatia wafanyakazi wa afya kwa sababu wamekuwa wakihangaika kwenda katika hospitali ya Wilaya na ukizingatia kwamba usafiri waotumia si salama…

T A A R I F A . . .

MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kufahamu japo sijaipokea kama ambavyo unataka wewe, kwa sababu nina maana yangu ya kuchangia hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendeleee kusema kwamba usafiri ule siyo salama na kama Serikali imetenga tunashukuru kwa usikivu wa Serikali ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia zahanati hii kuna haja ya kuipanua kuwa kituo cha afya kutokana na wingi wa mahitaji ya wananchi wa pale kwa ajili ya matibabu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ya Kwimba, Jimbo la Sumve tunashukuru sana kwa ahadi ambayo mmetimiza ya kukitengea kituo cha afya cha Malya milioni 400. Ni mara nyingi Mbunge wa Jimbo hilo amekuwa kipiga kelele na mwaka jana nilimpa support ya kusimama hapa, na kuomba kwamba Serikali iangalie ahadi hizo. Akinamama walikuwa wanajifungulia kwenye sakafu, lakini leo Mheshimiwa Waziri ametufuta machozi, wameweza kututengea milioni 400, tunachoomba sasa ni kutupatia milioni 350 ambayo ni ya kununua vitanda na vifaa vya tiba ili shughuli ziweze kwenda kama ambavyo tulikuwa tunatarajia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuchangia hotuba ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa uthubutu mkubwa wa kuwa na nia ya kujenga Tanzania ya viwada. Vilevile niipongeze sana Wizara kwa jitihada zake chini ya Waziri, Mheshimiwa Mwijage, Naibu wake, Mheshimiwa Stella Manyanya, pamoja na Katibu Mkuu, Profesa Elisante, kwa kweli jitihada zenu zinaonekana. Hivyo basi, tunazidi kuwatia moyo, tupo nyuma yenu, tutazidi kuwashauri kadri tuwezavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya yote nipende kumkumbusha Mheshimiwa Waziri kwamba Mkoa wa Mwanza uko tayari kwa ajili ya uwekezaji mpya wa viwanda vipya. Kila Wilaya imeshatenga maeneo kwa ajili ya viwanda. Kwa mfano Magu imeshatanga maeneo Isangijo, Bundirya; Wilaya ya Ilemela imeshatenga Nyamongolo na Sangabuye, na Wilaya nyingine hivyo hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unavyojua kwamba Wanamwanza ni wakarimu, hali ya hewa ya Mwanza ni nzuri, lakini vilevile tupo tayari kuwakaribisha hawa wafanyabiashara wawe wadogo ama wakubwa. Kwa hiyo tunaomba Mheshimiwa Waziri utusaidie sana kutukaribishia na kutupa ushirikiano katika kuwaalika wawekezaji hao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Ilemela ina Kiwanda cha Ngozi cha Mwanza Tanneries. Mwaka jana nilisimama hapa nikaomba Serikali iweze kumnyang’anya yule mwekezaji aliyekuwa amepewa kwa sababu alikuwa amekitelekeza. Ninaishukuru sana Serikali, kupitia Mkuu wa Mkoa wa Mwanza imeweza kukiridisha mikononi mwake. Sasa ninachoomba ni kwamba mtuletee mwekezaji katika kiwanda kile kwani maeneo yale kuna chuo na wanachuo wale wanakosa sehemu ya kufanya field. Kwa hiyo, vilevile itasaidia wanafunzi kupata field na itatoa ajira kwa akina mama na vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unavyojua, pamba ni ajira lakini ni uchumi hususani katika Mkoa wetu wa Mwanza, na wanawake na vijana wanategemea kipato kutoka katika zao hili. Hivyo basi, nichukue fursa hii kumkumbusa Mheshimiwa Waziri kuhusu ule mpango wa kuvifufua viwanda vya kuchambua pamba vya Nyambiti Ginnery na Ngasamo Ginnery ambavyo tunaamini kabisa vitaongeza ajira kwa vijana lakini pia pamba yetu itaweza kuchambuliwa pale pale na kutengeneza nyuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Waziri, kwa sababu hili suala lipo mezani kwake kwa muda mrefu, atakapokuja ku-wind up atueleze ni lini viwanda hivi vitafufuliwa, kwa sababu wananchi wa Kwimba wamekuwa wakihangaika kupeleka pamba yao mbali wakati viwanda vipo pale na vina uwezo wa kufufuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme Wizara hii ya Viwanda imekuwa ikionesha nia nzuri na imekuwa ikifanya kazi nzuri, lakini nashindwa kujua ni kwanini Mheshimiwa Waziri anashindwa kuwa muwazi? Yapo masuala ambayo yanawakwamisha na sisi tunayaona lakini kwa namna moja ama nyingine yeye inabidi admit na aseme na awe aggressive juu yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano zipo hizi associates za Wizara yake kwa ajili ya kujenga viwanda. Kwa mfano iko TRA, TFDA, NEMC, TBS, OSHA na mengineyo kama yapo; hizi taasisi ni muhimu sana katika ujenzi wa viwanda. Pia zimekuwa zikiangusha sana Wizara hii. Kwa nini nasema hivyo zimekuwa na mlolongo mrefu, urasimu mrefu sana wa kutoa vibali. Vilevile kwa namna hiyo tumekuwa tukiwakatisha tamaa wafanyabiashara na wawekezaji wengi sana. Hivyo basi Mheshimiwa Mwijage simama kifua mbele uzikemee na uwe aggressive kama navyosema. Ni lazima useme ili yaweze kusunga mbele kama kweli tuna nia ya kumsaidia Mheshimiwa Rais kutimiza azima yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa mfano leo hii unataka kufungua kiwanda na unapaswa kupata certificate ya TFDA utaambiwa lazima uje ukagulie premises zako. Kitendo cha kumpata afisa kuja kukagua premises inaweza ikachukua miezi miwili/mitatu na bado akifika pale atasema sawa naomba urekebishe hiki na hiki na hiki ukimaliza niite. Kitendo cha kumuhitaji tena inaweza ikachua miezi kama ile ile bado
bidhaa yako umeipelekea TFDA, ipo kule inakaguliwa, kitendo hicho nacho kinaweza kikachukua miezi mingi. Mimi napenda ku-declare interest, kwamba mimi ninakiwanda changu ndiyo, lakini leo ni miaka miwili ninashughulikia kupata leseni na mpaka hivi naambiwa leseni yangu nembo yangu ya TBS ipo tayari lakini mpaka leo hivi sijaipata na hapo mimi ni Mbunge, je, wale wananchi wa kaaida wanafanyaje? Ni lazima tutafakari haya masuala ili tuweze kuisaidia nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu masoko, bado Serikari haijaonesha nia ya kulinda bidhaa za Kitanzania kwa sababu kumekuwa na mambo ambayo yanakwamisha bidhaa hizi. Tukianza katika kodi nyingi ambazo zinatozwa juu ya bidhaa hizi, tukiangalia malighafi ambazo zinaletwa ndani ya nchi zinatozwa kodi nyingi katika bandari yetu. Leo hii bidhaa za kitanzania ni gharama kuliko hata bidhaa zinazotoka nje, hivi unategemea nini? Kwa na namna hii tunauwa viwanda na tunawakatisha tamaa wawekezaji wadogo kwa wakubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshauri Mheshimiwa Waziri, lakini si ushauri kwa sababu ni jambo ambalo nalifahamu, nikukumbueshe kwamba tunao mabalozi wetu nje ya nchi unaweze kuwatumia kututafutia masoko. Vilevile mkae muangalia namna ya kuweza ku-regulate hizi kodi ndogo ndogo ili tuweze kumwezesha Mtanzania kuuza katika bei nzuri na bidhaa zao ziwe katika soko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na malalamiko mengi sana juu ya TRA, hasa pale inapojipangia bei ya bidhaa za wafanyabiashara wanazoagiza kutoka nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii wafanyabiashara wengi wamekuwa forced kususia bidhaa zao bandarini kwa sababu wana-estimate bei kubwa ambazo wanajua wao lakini kodi pia inakuwa kubwa. Kwa hiyo, kunakuwa hakuna haja ya mfanyabiashara yule kutoa kodi kubwa na bidhaa ile isiwe na faida. Kwa hiyo, iko haja ya Serikali kukaa na kutathmini ufanyaji kazi wa hizi taasisi. Tunazipenda sana, tunafahamu umuhimu wake katika kuijenga Tanzania ya viwanda. Hata hivyo kama haitafanya kazi zake kwa ufasihi ni lazima tuzirekebishe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa machache hayo naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia fursa ya kuchangia hotuba ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuwapongeza Waziri pamoja na Naibu wake wakiwemo Katibu Mkuu na Naibu wake pamoja na timu yote ya wataalam wa Wizara hii. Kwa kweli hotuba ni nzuri kwani imesheheni mambo mazuri ambayo yanaeleweka na sisi kama Wabunge kazi yetu ni kushauri pale ambapo kuna mapungufu na ndivyo ambavyo nitafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo, nitakuwa sijatenda haki kama sitampongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kazi nzuri anayofanya ya kusimamia Serikali. Kama tunavyoona leo hii wanafunzi wanasoma bure kutoka shule ya msingi mpaka sekondari. Vilevile tunaona kuna utaratibu mzuri wa kutoa mikopo hata kama mapungufu yapo bado tutaendelea kushauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kufanikiwa kwa wananchi ni kufanikiwa kwa taifa lakini kuwa na elimu pekee bila ujuzi bado siyo suluhisho la kufanikiwa kwa wasomi wa Kitanzania. Hivyo basi, nitumie fursa hii kuishauri Wizara kuhakikisha kwamba inaweka mikakati ya kupitia mitaala iliyopo ili kuweza kutoa fursa kwa wanafunzi ambao wapo mashuleni kushiriki katika michezo lakini katika mafunzo ya kazi za mikono kama ushonaji, ufinyanzi pamoja na ujasiriamali. Kwa upande wa michezo nipongeze Wizara kwa kurudisha michezo ya UMISETA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa nini nashauri hivi? Ni kwa sababu ni wakati wa nchi yetu kujitafakari na kuhakikisha kwamba tunaanza kutengeneza wasomi wasio na fikra ya kuajiriwa tu ila wasomi wenye fikra ya kujiajiri na kuweza kutengeneza ajira kwa wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda niseme tu katika kipindi cha Ubunge wangu ndani ya miaka hii michache nimeweza kutembelea shule kadhaa kwa nia mbalimbali. Naipongeza Shule ya Sekondari ya Misungwi kwa sababu kwa kweli imekuwa ni ya mfano mzuri na ningetamani sana siku moja Mheshimiwa Waziri atakapokanyaga Mkoa wa Mwanza aweze kufika pale ili aone. Kwa kweli shule hii imekuwa ikitoa mwongozo mzuri kwa wanafunzi wake vilevile imekuwa ikiwaandaa kwa ajili ya maisha baada ya masomo chini ya Mwalimu Mkuu Mr. Mbando kwa kweli ni mbunifu na anahitaji pongezi na shule ile inahitaji motisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule ile ina club ya ujasiriamali, wanatengeneza sabuni za maji na mbolea za maji na wanafundisha wanafunzi ujenzi wa nyumba za machupa ya plastiki. Kama haitoshi wanawafundisha wanafunzi wao wa jinsia ya kike kuweza kutengeneza taulo za kike ili waweze kujisitiri katika siku zao. Vilevile kama haitoshi kupongeza kwa hayo imekuwa na Fema Club ambayo imeongoza nchini kwa miaka kadhaa. Kwa hiyo, tunahitaji walimu wabunifu kama hawa na ni mategemeo yetu kwamba hata pale ambapo promotion zinatokea kutoka kwenye ualimu kwenda kwenye Uafisa Elimu, walimu kama hawa akina mwalimu Mbando ndiyo wanaostahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la elimu kwa walemavu, kwa kweli bado haliridhishi, wanafunzi wenye changamoto ya ulemavu ni wengi, shule hizi zimekuwa ni chache mno. Kwa mfano kwa Mkoa wa Mwanza zipo shule tatu tu ambayo ni Shule ya Mitindo iliyoko katika Wilaya ya Miswungwi, kuna shule mbili za Wita na Itumbili katika Wilaya ya Magu. Kwa kweli shule hizi ni chache kulingana na mahitaji. Na uchache huo unalazimisha wanafunzi ambao wana changamoto ya ulemavu kwenda kwenye shule za kawaida ambazo hazina miundombinu inayowafaa, lakini vilevile hakuna wataalam wanaoweza kuwaelimisha vizuri kwa kiwango ambacho kinahitajika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile shule hizi pamoja na uchache wake bado kuna upungufu mkubwa wa hostel. Nikitoa mfano wa shule ya Itumbili iliyoko Magu ina wanafunzi 105, lakini katika hao ni 48 tu ambao wanaweza kuwa accommodated katika mabweni. Kwa hiyo, tunaona umuhimu wa kuongeza hostel katika mashule haya, na ukiangalia wanafunzi wengi wanatoka umbali mrefu, wengine ni wa kubebwa, wanapelekwa shule kwa kubebwa, wengine wanatembea kwa shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ombi langu kwa Wizara hii kwamba iweze kuangalia changamoto hiyo. Kama Mbunge wa vijana kwa nafasi yangu nimeweza kuwafikia mpaka sasa wanafunzi 26 ambao nimeweza kuwagawia baiskeli za watu wenye ulemavu ili waweze kufika shuleni. Sasa najiuliza, kama Mbunge nimeweza kufika hao watu, kwa Serikali hii ambayo inatoa elimu bure ni kwanini isiweze kuwafikia wanafunzi hawa ili at least waweze kupata baiskeli za kuwafikisha shuleni. Mheshimiwa Prof. Ndalichako, ni imani yangu unapokuja kuhitimisha nitasikia neno kuhusu hilo, kama tunaweza kutoa elimu bure na kama tunaweza tukatoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu, ni kwanini tusiweze kuwasaidi wanafunzi hawa ambao wanaenda hata kwenye shule za kawaida kwa mwendo mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumzia kuhusu mikopo nikakumbuka kwamba lipo suala la kipaumbele katika utoaji wa mikopo. Tumeona wanafunzi ambao wamefaulu kwenda vyuo vikuu ambao wanatoka kwenye mazingira magumu wakipata mikopo, wakipewa kipaumbele, lakini tumeona wanafunzi ambao wanasoma masomo ya ualimu na masomo ya sayansi wakipewa kipaumbele. Ni kwanini wanafunzi hawa wenye ulemavu wasipewe kipaumbele katika utoaji wa mikopo pale ambapo wanafaulu kwenda shuleni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na upungufu wa hostel kama ambavyo nimesema hapo awali, kwa wanafunzi wenye ulemavu bado kumekuwa na upungufu mwingi katika shule hizi. Kwa mfano mashine za kupima usiku, vitabu vya nukta nundu, karatasi za kuandika nukta nundu, vifaa...

MWENYEKITI: Ahsante kwa mchango mzuri, mengine utaandika. Mheshimiwa Fatma Toufiq.

MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante naunga mkono hoja na mengine nitawasilisha kwa maandishi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa hii. Nianze kwa kumshukuru Mungu kwa mapenzi yake ya kuniwezesha kuiona siku ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuipongeza Wizara kwa jitihada zake nzuri katika kuiboresha elimu ya Kitanzania, pamoja na juhudi hizo bado kumekuwa na changamoto zifuatazo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa vyoo vya kutosha na maji mashuleni. Mara nyingi unakuta watoto zaidi ya 70 wanatumia tundu moja la choo, hili halikubaliki na Serikali ihakikishe kuwa shule haipewi kibali kama haina matundu ya vyoo ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika suala la maji mashuleni, shule zisipewe vibali vya kuanza kufanya kazi kama hazina miundombinu ya kuvuna maji. Bado maji ni muhimu sana katika afya ya watoto mashuleni hasa wa kike pale wanapokuwa katika siku zao za hedhi, ambapo wengi wamekuwa wakikosa kwenda shule kwa hofu ya kukosa maji pale anapokuwa shule. Maji hayo bado yanachangia katika utoro wa wanafunzi wa kike katika maeneo ambayo hayana maji. Mara nyingi wasichana hawa wamekuwa wakitumika majumbani kutafuta maji hivyo wamejikuta wanaacha shule ama kukosa masomo baadhi ya shule.

Kuhusu utoro wa watoto wasichana mashuleni, unasababishwa pia na ukosefu wa hedhi salama kwa watoto hawa. Pia kwa sababu katika utoaji wa elimu bure vipo baadhi ya vifaa vinavyotolewa na Serikali bure vikiwemo vitabu, chaki hata pen, ni ombi langu sasa kwa Serikali kuanza kutoa taulo za kike mashuleni ili waweze kujihifadhi wanapokuwa katika siku zao za hedhi. Ni imani yangu kwamba kwa kufanya hivyo kilio cha ukosefu wa wasichana kukosa masomo kitapungua. Mfano mzuri, zipo nchi nyingine za Kiafrika ambazo tayari zimefanya hivyo na kupunguza changamoto hii kwa ukubwa. Nchi hizo ni kama Uganda, Kenya, Nigeria, Zimbabwe na nyinginezo ambazo zimekuwa zikitoa taulo za kike za kutumia zaidi ya mara moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala la ukosefu wa madawati, kwanza nianze kwa kuipongeza Serikali katika suala zima la ukusanyaji wa madawati kwa ajili ya shule za Serikali, zoezi ambalo limepunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya ukosefu wa madawati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na utaratibu wa madawati yanayoharibika kusubiri kupelekwa kwenye karakana ya Wilaya kwa ajili ya matengenezo. Ombi langu kwa Serikali ione umuhimu wa madawati haya kuwa yanatengenezwa na wafungwa ili kuepusha madawati hayo kukaa kwa muda mrefu, saa nyingine hata miezi mingi kabla ya kutengenezwa. Ila kwa wafungwa yangekuwa yanatengenezwa hapo hapo mashuleni kwani mara nyingi uharibifu wake huwa siyo mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na yale yote niliyoyochangia pale uliponipa nafasi zipo baadhi ya changamoto za uvuvi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama za kodi za samaki na dagaa mipakani ni kubwa sana, naiomba Serikali kuliangalia hili suala kwa ukaribu ili kunusuru gharama kubwa zinazoelekezwa kwa mvuvi. Lipo suala la Sheria ya Uvuvi ya mwaka 1973 ambayo ilitungwa kabla hata samaki aina ya sangara hawajapandikizwa katika Ziwa Victoria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kwamba sheria hii aiendani na uvuvi wa kisasa, pamoja na yote nyavu hizi za inchi saba bado hazikidhi mahitaji ya uvuvi katika kina kirefu ambapo zimekuwa zikichukuliwa na mawimbi mazito pamoja na makundi ya samaki aina ya sangara. Hii ni kwa sababu nyavu hizo zinakua nyepesi. Hivyo basi, naiomba Serikali kutumia wataalam wake kuweza kutatua tatizo hili ili malalamiko haya yafike mwisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia fursa ya kuchangia hoja iliyopo Mezani. Nianze kwa kuwapongeza Wenyeviti wote wa Kamati zilizowasilisha hoja leo kwa umakini walioonesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuchangia suala la utoaji wa taulo kwa watoto wa kike lililowasilishwa katika taarifa ya Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii katika ukurasa wa 41. Ni kweli, ipo haja ya kumkomboa mtoto wa kike kwa kuwagawia taulo safi, ili waweze kukamilisha malengo yao ya kimaisha hususani ya kielimu. Kwa sababu, nchi nyingine za Afrika zimejaribu na kufanikisha, hakika nasi tutaweza. Suala hili ni zito na uzuri Mheshimiwa Waziri wa Afya ni mwanamke na ni imani yangu kuwa atalisimamia vyema kama tunavyotarajia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu ya kuwa hofu kubwa inaweza kuwa katika kuweka uhakika wa watoto hawa kupata taulo hizi kwa wakati, lakini niihakikishie Serikali kwamba, nchi kama Uganda, Kenya, Ethiopia na nyingine ambazo tayari zimethubutu kufanya hivyo, zimefanikisha kwa kugawa taulo za kufua, maarufu kama reusable sanitary pads ambazo ni bora na zinagawiwa mara moja kwa mwaka hivyo, kuepusha gharama kubwa kwa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua mara nyingi taulo hizi zimehusishwa na ukosefu wa maji, ambako kiukweli ni tatizo tofauti kabisa. Tujiulize tunalalamika watoto kukosa taulo salama, je, wanatumia nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jibu ni matambala yasiyo salama ambayo pia, yanatumia maji kuwekwa katika hali ya usafi. Hivyo, basi ni muhimu Serikali pia, kuangalia changamoto ya maji kwa afya ya hedhi salama kwa sababu, watoto wa kike na wanawake kwa ujumla ni lazima watumie maji bila kujali wanatumia nini wakiwa hedhini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii ya kuchangia kwa maandishi. Nitumie fursa hii kuikumbusha Ofisi ya Waziri Mkuu juu ya ahadi yake ya shilingi milioni 10 aliyotoa kwa ajili ya zahanati ya Maligisu alivyokuwa kwenye ziara Wilayani humo.

Aidha, nichukue nafasi hii pia kumkumbusha Waziri wa Afya ahadi yake ya kuongeza vitendea kazi katika Hospitali ya Sengerema, wagonjwa wanapata shida sana pale wanapolazwa ukizingatia hospitali hii inahudumia wananchi wengi wa Wilayani hapo pamoja na mikoa mingine kama Geita na Kigoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa fursa ya kuchangia kwa maandishi kama ulivyonipatia hapo awali fursa ya kuchangia moja kwa moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa usimamizi mzuri wa Serikali. Pia naendelea kuipongeza Wizara kwa kazi nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Magu, Kata ya Bujora kuna Shule ya Sekondari ya Lunve. Shule hii imekuwa mkombozi mkubwa kwa wanabujora kwani wanafunzi walikuwa wanatembea umbali mrefu kutafuta elimu toka shule za kata za jirani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali kwa mchango wake katika ujenzi wa shule hiyo japo bado kuna mahitaji makubwa na ni hivi karibuni tumepokea shilingi milioni 25 kwa ajili ya madarasa mawili (2). Shule ina majengo sita tu yaliyokamilika huku wananchi wakiendelea kujenga madarasa manne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule haina madawati ya kutosha na wanafunzi wanakaa chini na matundu ya vyoo ni machache kulingana na mahitaji. Naomba sasa Wizara iweze kuiangalia shule hii kwa jicho la tatu ili ipate uwezesho katika mwaka wa fedha ujao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia fursa ya kuchangia hotuba ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa njia ya maandishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza Waziri pamoja na Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanayofanya ya kumsaidia Mheshimiwa Rais kusimamia Wizara kwa uaminifu mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya Wizara ya Viwanda na Biashara imekaa vyema na imeelezea mikakati mizuri ya Serikali ya kuhakikisha tunaijenga Tanzania ya Viwanda. Pamoja na mipango hiyo, bado ipo haja ya WIzara kuhakikisha inakaa na wadau wengine wa viwanda kama Wizara ya Kilimo, Wizara ya Fedha na Taasisi mbalimbali kama NDC, OSHA, NEMC, TFDA, TBS, TRA na nyingine ili kuhakikisha dhamira na mipango mikakati iliyoainisha ndani ya hotuba hii inafanikiwa, kwani kwa asilimia kubwa taasisi hizi kwa namna moja ama nyingine zinakwamisha jitihada za kuijenga Tanzania ya Viwanda kwa kodi na tozo nyingi pamoja na urasimu mrefu wa kupata vibali vya biashara bila kusahau Wizara ya Fedha inayotoa bajeti ndogo ama kiasi kidogo cha fedha kwa ajili ya Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kila leo tunakumbushana kuhusu kilimo kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania lakini mara zote tumekuwa tukijisahau kuimarisha biashara ya kilimo ambayo inatuingizia mapato makubwa na kuongeza ajira kwa Watanzania tena kwa uhakika. Nasema hivyo kwa kumekuwa na changamoto ya wafanyabiashara wa bidhaa za kilimo, wanaouza bidhaa nje ya Bara la Afrika kwa kulazimika kwenda Nairobi ama Holland kupeleka bidhaa zao kwa ajili ya kuthibitishiwa ubora katika maabara zinazokidhi vigezo vya Kimataifa. Pamoja na yote, Tanzania bado haijawa na maabara ya kupima ubora wa bidhaa kama mbogamboga na maua zilizothibitishwa Kimataifa. Ombi langu ni kuwa Serikali iwekeze katika maabara za aina hiyo ili kupunguza adha za wafanyabiashara hao.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na ukosefu wa maabara hizo, bado kuna changamoto za ukosefu wa ndege za kutosha kwa ajili ya usafirishaji wa mboga mboga na maua ambapo wafanyabiashara wengi wamelazimika kusafirisha bidhaa zao kupitia Jomo Kenyatta Airport. Naomba Serikali ihakikishe inaweka mipango ya kuhakikisha kwamba inaweka mazingira ya ndege za aina hiyo kutua nchini kwa wingi kwa ajili ya bidhaa zetu kusafirishwa kwenda katika masoko ya nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia fursa ya kuchangia hotuba ya Waziri wa Nishati kwa njia ya maandishi. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Kalemani, Waziri wa Nishati pamoja na Naibu Waziri wake Mheshimiwa Subira Mgalu kwa kazi nzuri wanayofanya ya kusimamia shughuli nzima ya usambazaji wa umeme katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, pamoja na umakini wa Wizara katika usambazaji wa umeme bado kumekuwa na changamoto ya wakandarasi wa kutekeleza miradi ambapo huchukua muda mrefu tofauti na mikataba inavyotaka. Nazidi kuwapongeza Waziri na Naibu wake kwa kusimamia umeme wa REA. Ombi langu ni kwamba wazidi kusisitiza vituo vya afya na shule yote ili kuweza kurahisisha huduma husika.

Mheshimiwa Spika, kabla sijahitimisha mchango wangu, naomba nimkumbushe Mheshimiwa Waziri kwamba, aliwahi kuahidi umeme wa uhakika Kata ya Kibakwe, Wilaya ya Magu na bado wananchi tunakumbuka ahadi hiyo na tuna matumaini makubwa juu ya utekelezaji wake.

Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi ya kuchangia, naunga mkono hoja kwa asilimia mia.