Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Kiteto Zawadi Koshuma (17 total)

MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali fupi la nyongeza.
Wilaya ya Ilemela ilikuwa ina mradi ambao ulikuwa unatakiwa kukamilika mwaka 2014, mradi huu ambao ulitakiwa kuwanufaisha Kata za Wilaya ya Ilemela ikiwepo Kata ya Kayenze, Sangabuye, Shibula, Monze na Buswelu ambayo ni Kata Mama ya Wilaya ya Ilemela.
Je, ni lini mradi wa tenki hili la kutoa maji Wilaya ya Ilemela utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mradi umekuwepo Wilaya ya Ilemela na ulishindwa kukamilika. Tulipata matatizo kidogo baada ya kuanza Programu ya Sekta ya Maji Awamu ya Kwanza iliyoanza mwaka 2007, programu ilizinduliwa na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, lakini kwa sababu fedha nyingi tulikuwa tunapata za wafadhili, ule mchakato wa manunuzi, kwa mfano mwaka 2007 ndiyo programu ilianza, lakini kuja kupata no objection ya kuanza kusanifu tuliipata Disemba mwaka 2009, utekelezaji wa miradi ukaanza mwaka 2012. Kwa hiyo, hicho ndiyo kitu ambacho kilifanya miradi mingi isikamilike.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa tunatoa ahadi kwamba miradi yote ambayo haikukamilika tunaanza nayo tukamilishe ndiyo tunaingia kwenye miradi mipya. Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie kwamba Kata zako zote za Wilaya ya Ilemela katika Programu ya Pili ya Mpango wa Maji itafikiwa na itakamilika.
MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa barabara ya Nyakato – Buswelu - Mhonze ina urefu wa kilometa 25 ambapo kilometa 6 ni urefu wa barabara kutokea Nyakato National kuelekea Buswelu Wilayani. Serikali pamoja na kutoa kilometa 2.4 ambapo katika hizo kilometa 1 ilitengwa shilingi milioni 500 na sasa wametenga shilingi bilioni 1.16. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuongeza kilometa 4 ili kuweza kuifanya barabara hiyo kufika Wilayani?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Rais aliyepita wa Awamu ya Nne aliahidi kuijenga barabara ya Kamanga – Sengerema kwa kiwango cha lami na barabara hiyo inawasaidia wanawake wa Vijiji vya Katungulu, Kasomeko pamoja na Nyamililo kufanya kazi zao za kiuchumi. Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kiteto Zawadi Koshuma, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, umuhimu wa kuongeza fedha ili kuhakikisha ile barabara inafika Makao Makuu ya Wilaya, Wizara inautambua na ndiyo maana hata katika mwaka wa 2016/2017 tumeongeza kiwango cha fedha tulichotenga. Nimhakikishie Mheshimiwa Kiteto Zawadi Koshuma kwamba juhudi zake hizo zitazaa matunda kwa kadri fedha zitakapokuwa zinapatikana mwaka hadi mwaka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali la pili kwa barabara ya Kamanga – Sengerema, naomba tu nimjulishe kwamba yale ambayo tuliyaeleza katika swali kama hilo hilo hapo nyuma tulidhamiria. Tuna dhamira ya kujenga hiyo barabara na tutaendelea kwa hatua zile ambazo tulizieleza. Tutaanza na masuala ya feasibility study pamoja na detail design kama ambavyo Wizara imepanga.
MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kumuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa shule zilizoko pembezoni katika Wilaya ya Ilemela huwa zinasahaulika katika mgao wa madawati. Mfano wa shule hizo ambazo ziko pembezoni mwa Wilaya ya Ilemela ni Shule ya Bugogwa, Igombe, Isanzu, Kisuni, Kilabela, Kabangaja na zinginezo. Katika shule hizo ambazo ziko pembezoni wanafunzi ambao wanakaa chini ni wa kuanzia darasa la kwanza mpaka la tatu. Je, Serikali inatoa tamko gani kuwa madawati yanapokuwa yamegawiwa, kwa mfano nikiangalia hapa katika majibu yake inaonekana pesa iliyotengwa yatapatikana madawati 4,000 kwa bei ya Sh.50,000 kwa kila dawati, je, Serikali inanihakikishia vipi kwamba shule hizi za pembezoni zitapata mgao huo wa madawati?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili…
SPIKA: Mheshimiwa umeshauliza mawili tayari.
MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimeuliza moja. Swali la pili, je...
SPIKA: Mheshimiwa Kiteto samahani. Mheshimiwa Waziri kati ya hayo mawili utachagua moja la kujibu, haya endelea na swali la pili.
MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Je, Serikali haioni sasa kwamba ni wakati wa kuruhusu Halmashauri za Mkoa wa Mwanza kutumia msitu wa Buhindi ambao haujavunwa kwa muda mrefu sasa, miti ivunwe kwa ajili ya kutengeneza madawati ili kukidhi tatizo hili sugu la madawati katika Mkoa wa Mwanza? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Koshuma amezungumza agenda muhimu sana hapa, upelekaji wa madawati katika maeneo ya pembeni. Kwa uzoefu wangu nilipotembelea maeneo mbalimbali siyo madawati peke yake, hata Walimu tunaowapeleka katika migao mbalimbali wengi sana wanaishia maeneo ya mijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama mlikuwa mnafuatilia vyombo vya habari juzi juzi nimetembelea shule moja ya Manispaa ya Dodoma iliyoko pembezoni hata mgao wa madawati haufiki kule na nikatoa maelekezo sasa shule hiyo ina madawati ya kutosha. Kwa hiyo, natoa maelekezo kwa Wakurugenzi wote wa Halmashauri wahakikishe madawati yanafika maeneo ya pembezoni hasa tukizingatia kwamba shule za pembezoni huwa zinasahaulika.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika ziara zangu nitakazozifanya utaratibu wangu utakuwa uleule, sitatoa taarifa ni shule gani nakwenda kuitembelea na Mkurugenzi ambaye nitafika katika Halmashauri yake, niki-pick shule nikikuta hakuna madawati maana yake ameshindwa kukidhi vigezo na maelekezo ya Serikali za Mitaa. Kwa hiyo, naomba nitoe onyo kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni kuhusu kutumia msitu, kuna misitu ya vijiji na mingine ni ya Serikali Kuu. Nadhani Ofisi ya Mkuu wa Wilaya itaangalia utaratibu na kuona tunafanyaje na kama kuna uwezekano msitu huo uweze kutumika. Vilevile nizishauri Halmashauri, wakati mwingine mbao zinakamatwa badala ya kukaa mpaka zinachakaa wakati Halmashauri ina shida ya madawati, tuangalie namna ya kufanya mbao zile ziweze kutumika kwa ajili ya kuondoa tatizo la madawati katika shule zetu.
MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Kwa kuwa lengo la Serikali ni kutoa huduma za afya kwa mama wajawazito bure, hiyo ni nia nzuri; lakini katika Mkoa wa Mwanza, baadhi ya visiwa vimekosa huduma za afya kwa sababu ya ukosefu wa Vituo vya Afya pamoja na Zahanati; Visiwa hivi viko katika Wilaya ya Buchosa ambavyo ni visiwa vya Soswa, Nyamango, Chamagati, Gembale, Nayonzwa pamoja na Kata ya Buryaheke kule Wilayani Buchosa. (Makofi)
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba katika visiwa hivyo kunajengwa Vituo vya Afya ili kuwasaidia akinamama wajawazito wasitembee umbali wa zaidi ya kilometa 40 kupata huduma za afya?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mkakati wa kwanza, kila mwaka tunatenga fedha kwenye bajeti kwa ajili ya kuboresha huduma za akinamama wajazito na watoto. Mkakati wa pili, tayari Serikali inafanya mkakati wa ku-optimize huduma zinazotolewa kwenye Vituo vya Afya, ndiyo huo niliouzungumza wakati nikijibu swali la Mheshimiwa Aysharose, kwamba tunahakikisha vituo vyote ambavyo vimesajaliwa kama Vituo vya Afya, vinatoa huduma optimally, yaani huduma za upasuaji na huduma za kimaabara kama ambavyo Sera ya Afya inaelekeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa tatu umetangazwa juzi na Mheshimiwa Waziri wa Afya wakati wa Mkutano wa Global Financing Facility (GFF), ambapo tutajenga vituo 100 vipya vya afya na kufanya maboresho kwenye vituo hivyo kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma za akinamama wajawazito na watoto.
MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Spika, nashukuru.
Kwa kuwa akina mama wengi wajawazito hususani vijijini wamekuwa wakipoteza maisha wakati wa kujifungua kwa sababu ya kukosa huduma ya kupangiwa kufanyiwa operation kabla ya siku ya kujifungua, hii imekuwa ikitokana na kwamba akina mama hawa hawapati elimu pale wanapokuwa wanakwenda katika vituo vya afya kwa ajili ya kliniki, hawaambiwi kwamba inawezekana kama mtu anakuwa na matatizo basi afanyiwe operation ya kupanga. Serikali imekuwa ikisisitiza operation za dharura, na hata katika majibu ya Waziri, amesisitiza sana katika huduma za vituo vya afya kutoa upasuaji wa dharura.
Je, Serikali haioni umuhimu sasa wa kutoa mwongozo katika vituo vya afya kwamba wanapotoa elimu kwa akina mama wajawazito wawaelimishe juu ya elimu ya kupata upasuaji wa kupanga ili kuokoa maisha ya mama na mtoto?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Kwanza, napenda yeye mwenyewe pamoja na Wabunge wote wafahamu kuwa suala la kupunguza vifo vya wanawake wajawazito wakati wa kipindi cha uzazi ni suala systemic, hakuna mkakati mmoja unaoweza kulipatia ufumbuzi. Nikisema ni suala la kimfumo ninamaanisha kwamba ni lazima mfumo mzima uweze kufanya kazi ndipo tuweze kushusha vifo vya akina mama wajawazito katika kipindi cha kujifungua. Kwa maana hiyo ni rai yangu kwamba sisi Waheshimiwa Wabunge kwenye Halmashauri zetu tushiriki kwenye vikao vya kufanya maamuzi ili tuweke kipaumbele kwenye kujenga vyumba vya upasuaji, maabara, na Serikali tutatimiza wajibu wetu wa kupeleka watumishi wenye ujuzi wa kutoa huduma ambazo zitawezesha vituo vyetu vya afya nchini viweze kutoa huduma za upasuaji wa kupanga kama anavyozungumza Mheshimiwa Kiteto.
Mheshimiwa Spika, kwamba elimu inatolewa ama haitolewi, elimu inatolewa kila siku kwa akina mama wote wanaofika kliniki, pia niwapongeze akina mama wote nchini kwa kuelewa umuhimu wa kuhudhuria kwenye kliniki za uzazi kipindi wanaposhika ujauzito kwa sababu kiwango cha mahudhurio kimeongezeka sana kutoka takribani asilimia 56 miaka kumi iliyopita mpaka kufikia kiwango cha asilimia 86 kwenye miaka ya karibuni. Hivyo ni kwamba uelewa sasa umeongezeka, akina mama wanadai huduma za kliniki ziwepo, sasa kazi ni kwetu kuzitoa huduma hizo.
Mheshimiwa Spika, napenda kulipa taarifa Bunge lako Tukufu kwamba Tanzania ina vituo vya afya vipatavyo 489 tu, katika hivyo ni 113 tu vinavyotoa huduma za upasuaji na hii ni changamoto ambayo ipo kwenye Halmashauri zenyewe kwamba zikamilishe katika vituo hivi 489 vianze kutoa huduma za upasuaji na ndiyo kazi ninayoifanya kila siku kwenye ziara zangu.
MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
Kwa kuwa mitaala ya elimu Tanzania inazingatia misingi na mahitaji ya kijamii hususan masuala ya utandawazi. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuweka somo la computer katika shule za sekondari na msingi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi tayari Serikali ilishaanza kuweka masomo ya computer au TEHAMA kwa ujumla katika shule zetu, isipokuwasiyo shule zote ambazo tayari zimeshapata hizo fursa kutokana na miundombinu halisi. Lakini kupitia hii miradi ya REA ambayo sasa karibu kila kijiji kinakuwa na umeme, vilevile karibu taasisi zote za umma ikiwemo shule zitakuwa na umeme. Kwa hiyo, tunaamini kwamba eneo la TEHAMA litaweza kupata nguvu zaidi na tayari wizara inafanyia kazi kuhakikisha kwamba wanafunzi wengi wanapata fursa ya kupata mafunzo hayo.
MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Naomba nianzie pale ambapo Naibu Waziri wa Kilimo ameishia, kwamba Bodi ya Nyanza (Nyanza Cooperative Union) na yenyewe pia imekuwa ikilegalega. Je, ni kwa namna gani Serikali inaweka mikakati ya kuhakikisha wakulima wa pamba Mkoani Mwanza wanafaidika na Nyanza Cooperative Union na kushirikishwa katika vikao vinavyoendelea katika Bodi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, jitihada zinazoendelea kushughulikia changamoto ambazo zimekikumba Chama cha Ushirika wa Nyanza ni kwa ajili ya kuwanufaisha wakulima wa pamba ambapo kimsingi chama kile kilianzishwa kwa ajili ya kuwasaidia. Kwa hiyo, tunavyojaribu kurudisha mali zile ambazo zilichukuliwa kinyume na taratibu, tunaamini baadaye zitaendelea kuwaongezea wakulima wa pamba wanachama wa Nyanza katika kuendeleza zao la pamba. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba maboresho ambayo tunayafanya na ufuatiliaji ambao tunaufanya yote lengo lake kubwa ni kuwasaidia wakulima wa pamba.
MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa SIDO ndiyo mlezi wa viwanda vidogo vidogo pamoja na vya kati ambapo tunatarajia viwanda hivi viweze kuelekea katika kuwa viwanda vikubwa na hivyo kuweza kuwezesha uchumi wa viwanda kuendelea hapa nchini Tanzania na Waziri amekiri kabisa kwamba Serikali inalitambua hilo na imekuwa ikitenga fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, utakubaliana na mimi kutenga fedha na kupeleka fedha ni kitu kingine. Kwa taarifa nilizonazo kabisa ni kwamba Serikali kwa mwaka 2015/2016 ilitenga shilingi milioni 500; mwaka 2016/2017 Serikali ilitenga shilingi bilioni 2.4; na kwa mwaka 2017/2018 kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri, Serikali imetenga shilingi bilioni 7.14.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali pamoja na kutenga fedha hizi zimekuwa haziendi. Kwa maana hiyo, tunategemea nini?
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kauli mbiu ya viwanda ambayo tumeona Mheshimiwa Rais amekuwa akiisema kweli itaweza kutimia kwa mwenendo huu wa kutokupeleka fedha? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, wanawake wa Mkoa wa Mwanza wamekuwa wakijishughulisha na shughuli za viwanda vidogo vidogo, lakini changamoto kubwa waliyokuwanayo ni kukosekana kwa vifungashio ambavyo wanavipata kwa gharama za juu sana na hivyo kushindwa kujiendeleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujua kwamba Serikali inawezaje kuwasaidia wanawake wa Mkoa wa Mwanza ili waweze kupata kiwanda cha vifungashio ili waweze kujikwamua kiuchumi? (Makofi)
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nikiri na ninakubaliana naye. Ujenzi wa uchumi wa viwanda endelevu unatokana na viwanda vinayoitwa LGI (Local Grown Industries) siyo hizi FDI. Hawa wanatafuta green pasture, wataondoka na Serikali inalitambua hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2016 tulipaswa kupewa shilingi bilioni 2.4, hatukupewa. Tumeiomba Serikali tupewe shilingi bilioni 7.04; nina imani Serikali itatoa pesa hizo na ninazifuatilia. Napenda niishie hapo na Kamati yangu imefanyia kazi na tusipotoa pesa hizo, hivi viwanda tunavyoita FDI, hao ni kware. Huwezi kulisha kware ukawaacha watoto wa kuku. Naomba niishie hapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la vifungashio ni tatizo kwa wajasiriamali wadogo wote. SIDO tumeamua kuwekeza katika kiwanda cha vifungashio na hicho kitatoa vifungashio kwa akina mama wote na wajasiriamali wadogo. Nachukua firsa hii kuwahimiza wajasiriamali wanaoweza kuwekeza kwenye biashara hii wawekeze katika vifungashio. Tunatumia pesa nyingi za kigeni kuagiza vifungashio kutoka nje ya nchi.
MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Pamoja na majibu ya Serikali, imesema kwamba hawana ushahidi na Serikali ina mkono mrefu, je, ni kwa nini Mheshimiwa Waziri katika Wizara yake wasiweke mkakati wa operation maalum ili kuweze kuwakamata wahalifu hawa ambao wamekuwa wakizorotesha uchumi wa wavuvi? Hilo ni swali la kwanza.
Swali la pili, kwa kuwa wavuvi wengi Kanda Ziwa wakiwemo wavuvi wa Mkoa wa Mwanza na mikoa ya jirani kama vile Kagera ikiwepo Kata ya Kerebe ambayo iko Bukoba, Ukerewe pamoja na Kalebezo na Kayenze wamekuwa wakiteseka sana na uporaji wa mali zao, hizi bodi pamoja na samaki, suala ambalo limekuwa likizorotesha sana uchumi wa wavuvi, je, ni lini sasa Serikali itatimiza ahadi yake ambayo imekuwa ikiahidi kwa takribani miaka kumi sasa ya ununua boti ambazo zinaweza zikafanya doria ili kuwakamata hawa wahalifu ambao wanawapora wavuvi mali zao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na mkakati, mkakati upo na kuna mahitaji ya task force ambayo inahusisha wadau mbalimbali na majukumu yake makubwa ni kukabiliana na uhalifu katika maeneo ya majini. Kama ambavyo nimejibu katika swali la msingi kwamba mikakati hiyo ikiwemo katika eneo ambalo anazungumzia Mheshimiwa Mbunge ya Ziwa Victoria, tulipeleka hiyo timu na tukaweza kubaini upungufu kadhaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu wenyewe ambao umeelekezwa ni kwamba kuna umuhimu wa kuweza kupata boti zaidi zenye uwezo mkubwa zaidi kwa ajili ya kukabiliana na uhalifu huo. Ndiyo maana nikamweleza katika jibu la msingi kwamba Serikali inafanya jitihada kuweza kupata boti hizo za kisasa ili kuweza kudhibiti hali hiyo. Kuhusiana na kwamba wahalifu hawa wanatoka ndani au nje; ndiyo maana nimemwambia kwamba tunashirikiana na nchi jirani ili kuweza kuwabaini na kuwachukulia hatua za kisheria kupitia Wizara yetu ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kituo cha Kulelea Wazee Bukumbi Mkoani Mwanza kinakabiliwa na changamoto ya kukosa uzio na hivyo kuhatarisha usalama wa Wazee hawa ambao tunawapenda sana. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuweka mkakati kwa ajili ya kuweka uzio katika vituo vyote hapa nchini Tanzania ambapo pia ni vichache vya hawa Wazee ili kuhakikisha usalama wa wazee hawa?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua changamoto ya Makazi ya Wazee ya Bukumbi na makazi mengine kama ya Mwanzagi ambayo nayo yamekuwa na changamoto kama hiyo. Tunaendelea kutenga fedha kwa awamu na nimuahidi Mheshimiwa Mbunge tu kwamba, katika mwaka huu wa fedha tutatenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa kituo cha Bukumbi.
MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Serikali; kwa kuwa fedha za basket fund pamoja na mambo mengine kutumika pia kupunguza vifo vya mama na mtoto. Hata hivyo fedha hizi zimekuwa zikienda taratibu na pia zina chelewa sana kufika. Kwa mfano the first quarter kwenda kuanzia Julai - Septemba zinaenda Desemba tena mwishoni kabisa na baadhi ya vituo kutokupata kwa mfano Kituo cha Ihelele kilichopo Misungwi pamoja na Hospitali ya Bukumbi hazija pata kabisa fedha.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kifedha tofauti na mfuko wa Basket Fund ambao unatolewa na wafadhili kuhakikisha kwamba vifo vya mama na mtoto vina pungua? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, tunashukuru Mheshimiwa Waziri wa Afya alifika Mkoa wa Mwanza na akatembelea katika Kituo cha Karume na kuangalia kazi iliyofanyika katika Kituo cha Karume kwa pesa ambazo zimetolewa na Serikali, lakini pia Mheshimiwa Waziri alihaidi kukipatia fedha kituo cha afya kilichopo Buzuruga fedha kwa ajili ya kutengeneza theater ambapo kwa sasa kituo kile hakitoi huduma za upasuaji na kituo ambacho kinategemewa sana.
Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi hiyo ili kuendelea kupunguza vifo vya mama na mtoto katika Mkoa wa Mwanza?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Kiteto Koshuma kwa kupigana kiume na kike katika kuimarisha afya ya uzazi na mtoto ikiwemo wasichana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza kwamba fedha za Basket Fund zina chelewa nini mkakati wa Serikali katika kutafuta fedha za ndani. Kwanza kuhusu fedha za Basket Fund tumefanya mashauriano na wadau ambao wanachangia mfuko wa afya wa pamoja. Moja ya makubaliano ambayo tumeyafanya na Waziri wa Fedha akiwemo ni kwamba fedha hizi sasa watajitahidi kuzitoa kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika bajeti yetu ya mwaka 2017/2018 tumetenga rasilimali fedha za ndani kwa ajili ya kuimarisha huduma za uzazi ikiwemo kuhakikisha uzazi salama. Kwa mfano katika huduma za uzazi wa mpango kwa mara ya kwanza tumetenga bilioni 14 na zimetoka, fedha za ndani kwa ajili ya huduma za uzazi. Lakini tumetenga fedha pia kwa ajili ya kujenga maabara za damu katika mikoa mitano na tumetenga fedha pia kwa ajilia ya kujenga vyumba vya upasuaji katika vituo vya afya. Kwa hiyo sambamba na fedha za Basket Fund lakini pia tunazo hela za ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, kuhusu Kituo cha Afya cha Buzuruga, ni kweli tumepata fedha za Basket Fund bilioni 15.5 na tunategemea pia kupata fedha kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya kuboresha vituo vya afya ili kuviwezesha kutoa huduma za uzazi za dharura.
Nitumie fursa hii kuelekeza tena fedha hizi sio za kujenga mabwalo ya kulia chakula, si fedha za kujenga ukuta sifedha za kujenga mambo ambayo hayahusiani moja kwa moja na huduma za afya ya mama na mtoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua vituo vya afya vina changamoto nyingi lakini hebu tujikite katika kumuokoa mama mjamzito na mtoto mchanga baadae tutakuja kujenga wodi za kufunga vidonda lakini kwetu sasa hivi hicho sio kipaumbele, nakushukuru sana.
MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana; kwa kuwa Halmashauri nyingi sana zinakabiliwa na changamoto ya kuwa na mapato madogo na hivyo kushindwa kabisa kutenga fedha hizi za asilimia 10, asilimia tano wka vijana na asilimia tano kwa akina mama kwa ukamilifu.
Je, Serikali inachukua hatua gani kwa Halmashauri ambazo hazitengi kabisa na hata tuliona katika bajeti ya mwaka jana kuna Halmashauri mbili zilikuwa zimetajwa kwamba hazijatenga kabisa fedha hizi za akinamama na watoto, lakini hatujaona Serikali ikiwachukulia hatua. Je, Serikali inachukua hatua gani kwa Halmashauri ambazo hazitengi kabisa fedha hizi za akina mama?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna excuse yoyote ambayo itasababisha Halmashauri isamehewe eti kwa sababu makusanyo yake ni kidogo. Kwa sababu hata kama ungekusanya shilingi moja, shilingi moja hiyo tunachotaka asilimia 10 ya shilingi moja si ya kwako. Wewe ni kama conduit tu unatakiwa pesa hiyo iende kwa wanawake na vijana.
Kwa hiyo, kama ambavyo tulisisitiza juzi katika jibu ambalo alijibu mwenzangu tutachukua hatua kali kwa Halmashauri yoyote na hasa Wakurugenzi wahakikishe kwamba asilimia 10 ya kutenga katika mapato ya ndani sio option, it’s a must! Na yeyote ambaye hatatekeleza hilo hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.
MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, lakini wakulima wa pamba katika mikoa ambayo inahusika kulima pamba kama vile Mikoa ya Shinyanga, Simiyu na kwingineko bado ni wakulima wadogowadogo. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha wakulima hawa wanakuwa wakulima wakubwa ili kuleta tija katika zao hili la pamba ambalo ni zao la kibiashara linalotegemewa hapa nchini Tanzania ili kuongeza Pato la Taifa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri Mkuu alifika Mkoa wa Mwanza na kufanya kikao na wadau wa pamba na kuwaahidi kwamba atarudi tena mwezi Mei ili kuweza kupanga bei ya pamba kwa msimu huu ambao unakuja; naomba kuiuliza Wizara, je, ni kwa nini isione kwamba waweze kupandisha bei ya pamba kutoka Sh.1,200 kwa msimu uliopita hadi Sh.2,000 kwa msimu ambao unakuja kwa sababu zao hili la pamba ndiyo dhahabu ya Mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Simiyu na mikoa mingineyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote naomba kuchukua fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge, mdogo wangu Mheshimiwa Kiteto Koshuma kwa maswali yake mawili mazuri ya nyongeza na vilevile kwa jinsi ambavyo anafuatilia zao hili la kimkakati Tanzania, zao la pamba.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza na swali lake la kwanza; ni kweli kwamba uzalishaji wa pamba ulikuwa ukishuka na kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, Serikali tumejipanga kwamba sasa hivi tutakuwa na mfumo bora wa uzalishaji wa zao la pamba kwa maana ya uzalishaji wa mbegu ile niliyoisema kwenye jibu langu la msingi, UKM08 na vilevile tuweze kuzalisha pamba zaidi kwa kuzingatia kwamba kitakuwa ni kilimo chakisasa na ni mfumo bora wa mbegu hii ambayo tumeianzisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwenye swali lake la pili, naomba niseme kabisa kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu wetu amekuwa ni champion kabisa katika zao hili la pamba na mpaka sasa hivi ameshafanya mikutano na wadau mbalimbali kuhusu zao la pamba; mikutano zaidi ya sitana leo hii pia tunakutana na wadau wengine wa pamba, jana pia Mheshimiwa Waziri Mkuu alifanya tena mkutano mwingine na ginners wote wa pamba.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie mdogo wangu, Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali tumejipanga safari hii kuhakikisha kabisa kwamba zao la pamba litakuwa pia ni zao bora na litaendelea katika uzalishaji, ukizingatia tumeshaanzisha hii mbegu nyingine mpya niliyoisema ya UKM08.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tarehe 26, mwezi huu wa Nne, wadau wote wa pamba tutakusanyika kwa ajili ya kuangalia indicative price ya zao la pamba itakuwa ni shilingi ngapi. Kwa maana hiyo, naomba Mheshimiwa Mbunge mwezi huu kabla ya mwisho wa mwezi tutakuwa tumeshajua bei ya zao la pamba itakuwa ni shilingi ngapi.
MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali imekiri kuwa ilitenga shilingi bilioni mbili kwa mwaka 2017/2018, lakini ikapeleka kiasi cha fedha shilingi bilioni moja. Mkoa umejiwekea malengo ya kumaliza jengo hili ifikapo mwaka 2020 lakini Serikali inapeleka fedha kidogo kidogo. Pia kwa mwaka 2018/2019 Serikali tumeona tena imetenga kiasi cha fedha shilingi bilioni mbili, uzoefu umekuwa ukionesha kwamba fedha zinapelekwa kidogo kidogo na hivyo kukwamisha ukamilishaji wa majengo mengi ambayo yanakuwa yanajengwa katika hospitali zetu za mikoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu, je, Serikali ina mpango gani mkakati wa kuhakikisha kuwa fedha hizi ambazo zimetengwa kwa mwaka 2018/2019 zinapelekwa zote lakini pia fedha ambazo zilitengwa kwa mwaka wa fedha 2017/2018, bilioni moja iliyobaki na yenyewe pia inapelekwa na kumalizia fedha zingine ili jengo hili liweze kwisha na kuondoa msongamano uliopo pale katika hospitali ya Sekou Toure?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, uzoefu unaoyesha kwamba majengo mengi yanajengwa lakini yanapokamilika, vifaa haviendi kwa wakati, watumishi hawapelekwi kwa wakati. Je, Serikali imejiwekea mpango gani mkakati kuhakikisha kwaba jengo hili litakapokamilika ifikapo 2020 basi watumishi wanapekwa, vifaa vinapelekwa ili kuweza kuokoa maisha ya mama na mtoto.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) (K.n.y. WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO):
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimejibu katika jibu langu la msingi Serikali imetenga jumla ya bilioni 30 ambazo katika hizo bilioni 30 kiasi cha bilioni 10 zinaenda kutumika kuhakikisha kwamba tunafanya ukarabati na pia bilioni 20 zinaenda kutumika kwa ajili ya kujenga hospitali za rufaa katika Mikoa ya Njombe, Geita, Simiyu, Songwe na Mara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, ni azma ya Serikali kuhakikisha maeneo yote yale ambayo kuna msongamano kama ilivyo hospitali ya Sekou Toure ambayo nina hakika Serikali imeanza kutoa pesa na yeye mwenyewe amekiri bilioni moja imeshatoka. Nimhakikishie kwa kadri pesa itakavyokuwa imepatikana hiyo bilioni nyingine itatoka ili ziweze kumalizia kazi iliyokusudiwa, kwa sababu lazima tuhakikishe kwamba inakamilika kwa muda tuliojipangia 2020.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili anaulizia juu ya suala zima la kupatikana vifaa pamoja na watalaam wa kuweza kutoa huduma kama ambavyo tumetarajia. Naomba nimhakikishie yeye mwenyewe Mheshimiwa Mbunge ni shuhuda kwamba sasa hivi Serikali imetangaza nafasi kwa ajili ya kuajiri watumishi kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI, lakini pia kupitia Wizara ya Afya. Ni wajibu wetu kuhakikisha kwamba watumishi wanapatikana, hilo naomba nimwondoe shaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusu suala zima la vifaa tumekuwa tukipeleka pesa moja kwa moja MSD ili pale ambapo hospitalii zinakamilika na vituo vya afya vinakamilika vifaa navyo vinapelekwa mara moja.
MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza kabisa naomba nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya kwa sababu ni miongoni mwa Mawaziri ambao wana ushirikiano mkubwa sana katika Wizara hii ya Afya.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Waziri amekiri kwamba Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya utaletwa Bungeni na kwa kuwa wananchi wengi waishio vijijini na mijini hawana uelewa mkubwa kuhusiana na huduma hii ya bima ya afya. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha wananchi wanapata uelewa wa kutosha, ili waweze kujiunga na bima ya afya na kuweza kupata huduma nzuri?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, ni kweli, sasa hivi tuna takribani asilimia 34 ya Watanzania ambao wapo katika mfumo wa bima na tunatambua kwamba Serikali imeendelea kuboresha sekta ya afya na huduma zimezidi kuboreshwa, lakini uwezo wa wananchi kugharamia matibabu umekuwa ni moja ya changamoto. Sisi kama Wizara tumeendelea kujikita kuhakikisha kwamba tunatoa elimu kwa umma na tumeendelea kufanya uhamasishaji na tunajaribu kuja na vifurushi vipya ambavyo vinaweza vikajibu baadhi ya hizi changamoto za uwezo wa wananchi kuweza kugharamia matibabu.

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto alikuwa katika mikoa ya Kusini katika kuhamasisha fao jipya la washirika ili hawa wakulima ambao wako katika mazao ya mkakati basi na wao waweze kupata cover ya bima hii ya afya. Sisi kama Wizara tutaendelea kufanya hivyo kuhakikisha kwamba jamii nzima ya Watanzania wanakuwa katika mfumo wa bima ya afya.
MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Spika, pamoja na sheria kuelekeza umri wa kuajiriwa kazini, bado ajira nyingi zinapotangazwa hapa nchini hutoa sharti la kuwa na uzoefu wa kazi, kuanzia umri wa miaka mitano na kuendelea, na hivyo hii huwaondolea fursa vijana wengi wanaotoka vyuoni kutokupata ajira.

Mheshimiwa Spika, hivyo, naomba Serikali itoe majibu hapa kwamba ni lini itatoa tamko kwa waajiriwa kuondoa sharti la vigezo ili kuwapa fursa vijana wanaotoka vyuoni, isipokuwa tu kwa zile ajira ambazo zinahusu nafasi za juu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE): Mheshimiwa Spika, kwa kutambua kwamba kumekuwepo na changamoto kubwa sana kwa vijana wahitimu wa vyuo vikuu na vyuo vya elimu ya juu kupata kazi kwa kikwazo cha uzoefu. Ofisi ya Waziri Mkuu katika utekelezaji wa programu ya ukuzaji ujuzi nchini, imeanzisha program maalum kabisa ambayo Mheshimiwa Waziri Mkuu alizindua miongozo yake ya mafunzo ya Uanagenzi na mafunzo ya Vitendo Kazini (Internship). Ambayo hivi sasa kwa mujibu wa utaratibu tuliouweka, tunawachukua vijana kutoka vyuo vikuu, kutokana na fani walizonazo na makubaliano ambao.

Mheshimiwa Spika, sisi Serikali tumeingia na chama cha waajiri na sekta binafsi, tunawapeleka katika kampuni husika kwenda kufanya kazi kivitendo, ambako wanakaa miezi sita mpaka miezi 12 na baadaye mwajiri katika eneo husika, anampatia cheti cha kumtambua kama ni mwanachuo ambaye amekaa kwake katika fani husika kwa miezi 12 ili baadaye ikitangazwa nafasi ya ajira ya kazi ambayo ameifanyia kwa vitendo, iwe pia ni sehemu ya yeye kumsaidia kupata ajira, kwa maana ya kutumia ule utambulisho wa kwamba tayari ameshafanya kazi katika mwajiri husika.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kama Serikali na sisi tumeliona jambo hilo, na ndiyo maana tumeweka nguvu kubwa sasa hivi katika kuhakiksiha kuwa tunawajengea ujuzi vijana wetu ili waweze kuwa na sifa za kuajirika na baadaye kuwasaidia kupata ajira pasipo kikwazo cha uzoefu.
MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu ya Serikali, lakini kwa umuhimu mkubwa sana wa suala hili, Serikali nimeuliza ni hatua zipi zinazochukuliwa, lakini Serikali imeniletea majibu kusema kwamba sheria imetungwa. Sheria tumeitunga sisi wenyewe Wabunge na tumeipitisha sisi wenyewe na imesainiwa na Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Spika, lakini je, ni hatua gani zimechukuliwa? Ndiyo lilikuwa swali langu la msingi, lakini nasikitika kwamba halijajibiwa kwa sababu hakuna hatua amabazo zimeonyeshwa kuchukuliwa katika halmashauri ambazo hazitengi fedha hizi na ukizingatia kwamba fedha hizi zinasaidia maendeleo ya kiuchumi kule kwa yale makundi maalumu ambayo yametajwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba Serikali iweze kusema ni hatua zipi ambazo zimechukuliwa hasa baada ya Serikali ya kutungwa kwa sheria.

Mheshimiwa Spika, lakini pia, kwa kuwa zipo halmmashauri ambazo zina changamoto ya mapato, je, Serikali ina mkakati gani wa kuzisaidia halmashauri hizo ili ziweze kutenga asilimia 10 ya haya makundi ili waweze kuchochoe maendeleo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza ni kweli alitaka kujua hatua, lakini nimesema kwenye jibu la msingi kwamba, sheria hizi na kanuni zimetungwa mwaka jana 2018 na mwaka huu wa bajeti tumepitisha fedha ambazo zinakwenda kwenye mwaka 2019/2020. Sasa hizi halamshauri ambazo zitashindwa kutekeleza sheria hii, baada ya sheria hii kuwa in place, tumetangaza kanuni wanazo, then hatua zitachukuliwa dhidi ya hawa watu ambao wamekuwa wakichukua hizi fedha. Kwa sababu mwanzoni sheria haikuwepo na kanuni hazikuwepo ilikuwa halmashauri inatenga kwa kujisikia. Hayo ndiyo majibu ya Serikali na Mheshimiwa Mbunge avute subira.

Mheshimiwa Spika, na maelezo ya nyongeza ni kwamba, kwa bahati nzuri halmashauri zote, mikoa yote na wakurugenzi, kwenye mwaka huu wa fedha wakati wa mjadala wa bajeti ya TAMISEMI, kila Mkurugenzi alikuwa anaji- commit kwamba anarudi kwa hii awamu ya robo ya nne ya mwisho, ni lazima wakamilishe kutenga fedha kwa kiwango tulichokubaliana na mwaka wa fedha wa bajeti ujao, kama kuna mkoa utakuja bila kukamilisha zoezi hili na niwaombe Waheshimiwa Wabunge kwenye ziara zetu katika majimbo na wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya, nendeni kwenye halmashauri, Wakurugenzi wawaonyeshe fedha zilizotengwa, vikundi vilivyokopeshwa, miradi ambayo imeanzishwa ili mtupe taarifa tuweze kuchukua hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, anauliza habari ya changamoto za mapato. Nimezungumza vilevile kwenye jibu la msingi, hata kama halmashauri inakusanya shilingi 100, imeelekezwa, ndani ya hicho ilichokusanya kidogo hicho, itenge asilimia 10 ya fedha hizo baada ya kuondoa mapato lindwa. Kwa hiyo, katika hoja hii na katika sheria hii na kanuni zetu, hakuna halmashauri ambayo itapata utetezi wa kwamba mapato ni ya chini. Hatukumlazimisha apeleke bilioni mbili, bilioni 10, bilioni 100, tumesema, 10% ya makusanyo ya mapato lindwa.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.