Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Julius Kalanga Laizer (8 total)

MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Mkoa wa Katavi na Mkoa wa Kigoma ni Mikoa ambayo haijafaidika na miradi ya REA Awamu ya Tatu kwa sababu ya walioomba tenda kugombania tenda na kushtakiana Mahakamani. Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua huo mgogoro ili wananchi wa Mikoa hiyo waweze kupata huduma ya REA awamu ya tatu?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Kakoso kwa swali lake zuri. Nichukue fursa hii kuwapa pole na kuwaomba radhi wananchi wa Mikoa ya Kigoma na Katavi, lakini ameuliza Serikali ina mpango gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka nimtaarifu suala hili lipo Mahakamani. Kwa kuwa, Mahakama ni chombo pekee ambacho kinatoa haki, sisi kama Serikali ya Awamu ya Tano tutasikiliza maamuzi ya Mahakama, kwa hiyo mgogoro huu utatatuliwa na Mahakama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimwambie kwa kuwa, Mamlaka ya Manunuzi (PPRA) hawakuwa na kipingamizi katika suala la mchakato, Wakala wetu wa Nishati Umeme Vijijini (REA) wameanza mchakato wa kumpata mkandarasi mpya, lakini kama yatatokea maamuzi mengine ya Mahakama tutaendelea kuyaheshimu, lakini kwa mpango ndani ya Wizara tunaamini kuanzia Machi 2018 Mkandarasi mpya atapatikana. Ahsante sana.
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniona.
Kwa kuwa, katika Halmashauri ya Njombe Mji kuna tatizo kubwa la maji na Serikali imekuwa ikiahidi kuwasaidia wananchi kutatua tatizo hili la maji kupitia mradi wa Hagafilo lakini hakuna dalili yoyote.
Je, ni lini sasa Serikali itaanza kutekeleza mradi huo ambao imekuwa ikiwahaidi wananchi siku zote? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Njombe ni miongoni wa Miji 17 itakayofaidika na mkopo kutoka Serikali ya India wa dola milioni 500, kwa hiyo nikukuakikishie pamoja na wananchi wa Njombe kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi imeshajipanga tayari, mwaka wa fedha unaokuja tutasaini mikataba na kuekeleza mradi wa kuchukua maji kutoka mto Hagafilo na kuhakikisha kwamba Mji wa Njombe sasa unakuwa na maji.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kuwa na sheria ni zuri kwa upande mmoja, lakini kwa upande wa pili Halmashauri zetu zinakabiliwa na matatizo makubwa ya kiuchumi. Sasa Serikali inatoa tamko gani kuhusu kuziwezesha Halmashauri zetu hizi kuweza kukusanya pesa za kutosha ili ziweze kuwalipa watu hawa ambao ni muhimu sana kwenye maendeleo ya vijiji vyetu?(Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala zima la ukusanyaji wa mapato la Halmashauri kuwa katika hali ngumu ya uchumi, kwanza ni commitment yetu wote Wabunge na Madiwani kuhakikisha kwamba Halmashauri zetu zikusanye vizuri. Kwa sababu, miongoni mwa kigezo kimojawapo cha existence ya Halmashauri lazima iweze kukusanya mapato ndiyo maana imepewa ridhaa kuwa Halmashauri kamili. Katika hili sasa ndiyo maana katika kipindi hiki kilichopita tumetoa maelekezo mbalimbali katika suala zima la ukusanyaji wa mapato, hasa kutumia mifumo ya electronic.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, katika maeneo mbalimbali tuna- success story kwamba leo hii kwa kutumia mifumo ya electronics tumepata mafanikio makubwa. Sasa maelekezo yangu nadhani twende katika compliance vizuri katika matumizi mazuri ya hii mifumo, kuna mahali pengine mifumo ipo, lakini haitumiki vizuri, watu wana-divert kutoka katika mifumo ya ukusanyaji wa mapato hivi, mifumo ile sasa inajukana ipo, lakini wengine hawapati manufaa katika hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwasihi sana Wakurugenzi wote katika Halmashauri zote twende kuhakikisha kwamba katika idara zetu za fedha tunazisimamia vizuri. Lengo kubwa ni kwamba, mapato yaliyopangwa kupitia Mabaraza ya Madiwani yaende kukusanya vizuri ili tukuze mapato katika Halmashauri zetu. (Makofi)
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya sheria ya zamani ya mita 60 kwa ajili ya kuhifadhi vyanzo vya maji, ilianza katikati ya mto mita 60 mpaka pembezoni mwa mto na mwaka jana tukairekebisha ikaanza mwisho wa mto na kuendelea, iliwaathiri wananchi wengi sana waliokuwa na mashamba ya asili wakati huo, ambao sasa hivi ndio wanakumbwa na hili tatizo la kuondolewa katika maeneo yao ya asili kama walivyofanya kwa Mheshimiwa Mbowe ambaye amekaa kwenye hilo shamba karibu miaka 80 iliyopita.
Je, Serikali imejipanga namna gani kufidia hawa wananchi kwa sababu marekebisho ya sheria ya mwaka jana yaliwakuta wananchi wakiwa wanaishi katika maeneo hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu katika utaratibu wa kisheria, mambo haya katika vyanzo hivi, maeneo chepechepe, maeneo oevu, yanakuwa defined katika mazingira mbalimbali katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa sababu kuna sheria ambayo imetungwa, kwa sababu tunajua kwamba kuna Waziri mwenye dhamana katika Ofisi ya Makamu wa Rais na bahati nzuri alipita mpaka Mkoa wa Arusha, Mkoa wa Kilimanjaro na Mikoa mingine, wakifanya ufafanuzi wa hizi sheria na utaratibu wake ukoje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu maamuzi yote yanaenda katika suala zima la mipango shirikishi, imani yangu kuwa ni kwamba, zoezi hili linapokwenda na ndio maana nirejee jibu langu la msingi, linapokwenda sasa kufanyika kubaini maeneo mbalimbali, kwamba hawa watu uhalisia wake ukoje, naamini maamuzi sahihi yatafanyika lakini baada ya kufanya jambo hili kuwa shirikishi zaidi kama tulivyoelekeza katika suala zima la Jimbo la Arumeru Magharibi.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ni zaidi ya miaka miwili na nusu imepita tangu upembuzi yakinifu wa barabara ya Karatu- Mbulu- Haydom ufanyike. Je, ni lini sasa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hiyo utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nafurahi kwamba Mheshimiwa Mbunge amekiri kwamba upembuzi yakinifu ulikwishafanyika na usanifu wa kina umekwishafanyika. Kwa hiyo, hatua zinazofuata Mheshimiwa Mbunge ni kwamba tunatafuta pesa kwa ajili ya kulijenga eneo hilo kwa awamu, na hivi karibuni zitakapopatikana utaona wakandarasi wanaingia pale barabarani kwa ajili ya kuanza kutekeleza mradi huo.
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nampongeza Naibu Waziri kwa majibu mazuri lakini pamoja na majibu hayo nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, utetezi wa mkandarasi kwamba kulikuwa na changamoto za kupata vibali vya ujenzi kwa kweli haina mashiko kabisa kwa sababu mimi kama Mbunge na Mkurugenzi wangu tulishirikiana na mkandarasi huyu vibali vikapatikana kwa muda mwafaka na akajenga minara miwili ikakamilika pamoja na kujenga msingi wa mnara mmoja wa tatu. Ni muda wa mwaka mmoja na nusu sasa minara hiyo haijawashwa. Ni lini atakamilisha kazi hii kwa sababu tunahitaji mawasiliano Manyoni?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, utoaji wa huduma za mawasiliano umeligawa jimbo langu, kwa mfano, Kata ya Makulu na hasa Kijiji cha Hika hakina mawasiliano kabisa hata upande juu ya mti huwezi kuwasiliana na watu na unakuwa umeshajitenga na dunia kabisa.
Je, ni lini Serikali italeta huduma hii ya mawasiliano katika kata hii, hasa katika Kijiji cha Hika? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inazo taarifa za kuchelewa kuwashwa kwa minara hii ambayo Mheshimiwa Mbunge ameitaja katika eneo hili la Sanza na Sasilo. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba mwishoni mwa mwezi huu au mwanzoni mwa mwezi unaokuja hii minara hii itawashwa. Kwa hiyo nakuhakikisha Mheshimiwa na nikupongeze sana kwa kufuatilia juu ya suala hili na niwahakikishie wananchi kwamba sasa watapata mawasiliano muda siyo mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, niseme tu kwamba eneo hili la Makulu Mheshimiwa Mbunge amelitaja kwamba tunayo orodha ya vijiji vingi ambavyo tayari viko kwenye hatua sasa ya kuweka minara tunavyo vijiji 369 orodha ninayo hapa Mheshimiwa Mbunge. Lakini pia tunakamilisha hatua za manunuzi mwanzoni mwa mwezi ujao tutakuwa na orodha nyingine mpya ya vijiji vingi tu ambavyo tutaenda kujenga minara.
Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge kwa ujumla kwamba Serikali imejipanga kuhakikisha maeneo ambayo yana shida ya minara na mawasiliano hafifu tunaendelea kuyaboresha ili wananchi Watanzania kwa ujumla waweze kupata mawasiliano ambayo ni muhimu katika harakati za maendeleo.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, katika majibu ambayo ameyatoa ametaja mradi wa maji katika Kijiji cha Muhange ambao unapata maji kutoka Mto Mgendezi kwenda Muhange Centre na kwenda Muhange ya Juu. Hata hivyo mradi huu sasa maji yanayotoka hayafai kwa matumizi ya binadamu kwasababu ni machafu. Lakini vilevile mradi huu haukukamilika kama ilivyokusudiwa. Je, nini kauli ya Serikali kuhusiana na mradi huu?

Pili, kutokana na mradi wa maji na changamoto hizi ambazo nimezitaja, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kufuatana nami ili akazione hizo changamoto na hatimaye kutoa suluhu ya miradi hii?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Aloyce Kamamba kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nipende kusema nimesikitika kuona kwamba Mheshimiwa Mbunge anasema maji ni machafu na mradi haujakamilika vizuri kwa sababu swali lake la pili ni ombi la kuambatana na mimi nipende kukuhakikishia Mheshimiwa Mbunge mara baada ya Bunge hili tutakwenda pamoja na nitakwenda kujihakikishia na wakati tunaendelea kukamilisha session hii ya Bunge ninatoa maagizo kwa Meneja wa eneo lile aweze kuwajibika haya maji yaweze kufanyiwa treatment kadri ya utaalamu wetu wa Wizara ili wananchi waweze kupata maji safi na salama. (Makofi)
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kunipa nafasi. Kwanza kabisa niwapongeze Serikali kwa kutujengea Mahakama Kuu nzuri na ya kisasa katika Jimbo la Shinyanga Mjini. Swali langu Mahakama ya Wilaya, Mahakama ya Mwanzo na Mahakama ya Hakimu Mkazi imechakaa sana, actually ilijengwa tangu kipindi cha ukoloni. Nini mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba Mahakama hizo zinakarabatiwa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Makamba kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama tulivyoeleza katika mpango wetu kwamba tumetenga fedha za kukarabati majengo yote chakavu nchini na kujenga mapya katika maeneo yale ambayo yana uhitaji huo. Ninakuahidi tu Mheshimiwa Mbunge uvute subira kidogo utaona kazi inaendelea kule kwa ajili ya ukarabati.