Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Julius Kalanga Laizer (9 total)

MHE. CECILIA D. PARESSO (K.n.y. MHE. JULIUS K. LAIZER) aliuliza:-
Kwa muda mrefu kumekuwa na mgogoro wa mipaka kati ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania na Kijiji cha Lashaine Wilayani Monduli, lakini mwaka 2011 yalifikiwa makubaliano chini ya Mkuu wa Wilaya kuwa mipaka yenye mgogoro isomwe upya kwa kutumia GPS na wananchi wa kijiji cha Lashaine wamekuwa wakisubiri zoezi la kusomwa upya mipaka kwa muda mrefu.
Je, Serikali itakamilisha lini makubaliano haya kwa kutumia GPS kusoma mipaka upya ili kumaliza mgogoro huo?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Julius Laizer, Mbunge wa Monduli, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, vijiji vinavyozunguka eneo la Jeshi la Monduli vimekuwa na migogoro ya mipaka na Jeshi kwa miaka mingi. Katika kumaliza migogoro hiyo, Wizara yangu kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Monduli ilifanya vikao na makubaliano ya mipaka eneo la Jeshi na kulipima kwa kutumia vifaa vya kisasa yaani GPS mwaka 2004. Eneo la Jeshi lilipunguzwa kutoka ukubwa wa hekta 94,000 hadi hekta 86,966 ili kupisha makazi ya raia wa vijiji jirani yaliyokuwa yameingilia eneo la Jeshi kikiwemo Kijiji cha Lashaine.
Mheshimiwa Spika, tatizo la mpaka wa Jeshi upande wa Kijiji cha Lashaine ni kuzibainisha beacons zilizowekwa ili wananchi waweze kuziona kwa wazi kwa mujibu wa ramani iliyosajiliwa yaani boundary recovery.
Mheshimiwa Spika, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Laizer kuwa azma yetu ya kufufua mpaka huo bado ipo na tutafanya hivyo tutakapopata fedha za kutekeleza jukumu hilo.
MHE. JULIUS K. LAIZER aliuliza:-
Mheshimiwa Rais alipokuwa anaomba ridhaa ya kuchaguliwa kuwa Rais wa Tanzania mwaka 2015 aliahidi kuwa Serikali itakarabati mabwawa matatu ya josho, mto Mbu na Olkuro:-
(a) Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hiyo ili wananchi wa Esilalei waweze kupata maji kwa ajili ya mifugo yao?
(b) Je, ni lini Serikali itawapatia wananchi wa Sepeko na Lepurko maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS- TAMISEMI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Julius K. Laizer, Mbunge wa Monduli, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika mwaka wa fedha 2016/2017, imekamilisha usanifu kwa ajili ya ukarabati wa mabwawa ya Joshoni na Olkuro na kubaini kuwa shilingi bilioni 1.45 zinahitajika kwa kazi hiyo. Mahitaji hayo yatazingatiwa katika mpango wa bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/2019.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea
na utekelezaji wa miradi ya maji katika Vijiji vya Lendikinya Kata ya Sepeko ambao unatekelezwa kwa gharama ya shilingi milioni 868.07. Kazi imefikia asilimia 35 na itakamilika mwezi Octoba, 2017 kwa kuzingatia mkataba. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imeidhinisha shilingi milioni 639.5 kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji katika Kijiji cha Nanja ambacho kipo Kata ya Lepurko ambao utahudumia pia shule ya Sekondari ya Nanja, Kata ya Sepeko.
MHE. JULIUS K. LAZIER aliuliza:-
Hivi karibuni Serikali ilitoa maelekezo kwa Wakuu wa Mikoa kusimamia urejeshwaji wa mashamba makubwa ambao hayakuendelea yakiwemo ya Wilaya ya Monduli.
Je, ni lini Serikali itakamilisha mchakato wa kufuta mashamba 25 katika Wilaya ya Monduli ambayo mchakato wake kwa ngazi ya Halmashauri umekamilika?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Julius Kalanga Laizer Mbunge wa Monduli kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia maelekezo ya Serikali kwa mikoa kusimamia urejeshwaji wa mashamba yasiyoendelezwa nchini, Wizara yangu imekuwa ikipokea mapendekezo ya kubatilisha miliki za mashamba na viwanja ambavyo wamiliki wake wakiuka masharti ya kumiliki ardhi kwa kutoendeleza, kutelekeza au kuendeleza kinyume na masharti au kutolipa kodi ya pango la ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2015 Halmashauri ya Wilaya ya Monduli ilifanya ukaguzi kwa mashamba 25 ambayo yalikuwa hayajaendelezwa. Katika ukaguzi huo ilibainika kuwa kati ya mashamba yaliyokaguliwa, mashamba 12 hayakuwa na nyaraka kamili za umiliki, kwa maana ya barua ya toleo au hati na hivyo kutokuwa halali kwa kubatilishwa kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri iliwasilisha mapendekezo ya kufutwa mashamba 13 tu na Wizara yangu imekamilisha utaratibu wa kubatilisha miliki za mashamba hayo yote 13 yaliyopo katika maeneo ya Mswakini Juu, Lolkisale na Maserani yenye ukubwa wa jumla ya ekari 131,873.35 Mashamba haya yamerejeshwa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli chini ya usimamizi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa ajili ya kuandaliwa mpango wa matumzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, nichukue fursa hii kuwakumbusha Halmashauri kuwa maeneo yanayorejeshwa kwao wakumbuke kuwa na mpango mzuri wa matumizi ikiwepo kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji pamoja na matumizi mengine ya wananchi. Hata hivyo hadi leo Wilaya na Mkoa hawajaleta mapendekezo rasmi ya kutumia ardhi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu inaendelea kupokea na kushughulikia mapendekezo ya kubatilisha milki za mashamba mengine kutoka Halmashauri mbalimbali nchini baada ya wamiliki kupewa ilani kwa mujibu wa sheria.
MHE. JULIUS K. LAIZER aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya ukarabati wa mabwawa matatu katika Kata ya Esilalei ambayo aliahidi tangu mwaka 2015?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Julius Kalanga Laizer, Mbunge wa Monduli, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika mwaka wa fedha 2016/2017 ilikamilisha usanifu kwa ajili ya ukarabati wa mabwawa ya Joshoni na Olkuro yaliyopo Halmashauri ya Monduli na kubaini kuwa shilingi bilioni 1.45 zinahitajika kwa ajili ya kazi hiyo. Serikali katika mwaka wa fedha 2018/2019 imetenga kiasi cha shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya Halmashauri ya Monduli kutekeleza miradi ya maji vijijini ikiwemo ukarabati wa mabwawa hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi ya maji katika vijiji vya Lendikinya, Kata ya Sepeko ambao unatekelezwa kwa gharama ya shilingi milioni 868. Kazi imefanyika asilimia 75 na inatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba 2018 kwa kuzingatia mkataba. Aidha, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imeidhinisha shilingi milioni 639 kwa ajili ya ujenzi wa Mradi wa Maji katika Kijiji cha Nanja ambacho kipo Kata ya Lepurko ambako utahudumia pia Shule ya Sekondari ya Nanja, Kata ya Sepeko. Ahsante sana.
MHE. CECILIA D. PARESSO – (K.n.y. MHE. JULIUS K. LAIZER) aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatoa fidia stahiki kwa wananchi ambao mazao yao yaliharibiwa na wanyamapori tangu mwaka 2010 hadi 2017 katika maeneo ya Mswakini, Makuyuni, Naiti, Mbuyuni, Lokisale na maeneo mengine Wilayani Monduli?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Julius Kalanga Laizer, Mbunge wa Monduli, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la wanyamapori wakali na waharibifu ni kubwa na linajitokeza katika zaidi ya Wilaya 80 nchini. Uharibifu mkubwa wa mali na madhara kwa binadamu vikiwemo vifo husababishwa na tembo, mamba, nyati, kiboko, simba na fisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uharibifu unaotokana na wanyamapori kwa sehemu kubwa unasababishwa na ongezeko la watu na shughuli zao ambazo mara nyingine zinafanyika katika maeneo yaliyo karibu na hifadhi au kwenye mapito ya wanyamapori. Aidha, mabadiliko ya tabianchi yamechangia pia katika kubadili mzunguko na mtawanyiko wa asili wa wanyamapori wakati wa kutafuta mahitaji muhimu, hususani chakula na maji. Hali hiyo kwa ujumla wake imeongeza ukubwa wa tatizo la muingiliano wa binadamu na wanyamapori na kusababisha uwepo wa matukio mengi ya uharibifu wa mali na madhara kwa binadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuzingatia changamoto zilizopo, Wizara yangu kwa kushirikiana na halmashauri ya Wilaya ya Monduli, inaendelea kukabiliana na tatizo la wanyamapori wakali na waharibifu kwa kufanya doria za udhibiti wa wanyamapori hao katika maeneo mbalimbali ya Wilaya hiyo kulingana na taarifa za uharibifu zinazowasilishwa na wananchi husika. Aidha, Wizara itaendelea kutoa elimu ya njia mbadala ya udhibiti wa tembo na wanyamapori wengine katika Wilaya ya Monduli na maeneo mengine, mathalani matumizi ya uzio wa kamba zilizopakwa mchanganyiko wa pilipili na oili chafu, matumizi ya matofali ya kinyesi cha tembo kilichochanganywa na pilipili na mizinga ya nyuki kuzunguka mashamba ambayo tembo huogopa na kuondoka maeneo hayo. Sanjari na hayo, Wizara itaendelea kuelimisha wananchi kuhusu njia bora za kujikinga na wanyamapori wengine kwa kuhimiza ujenzi wa nyumba bora na imara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Kanuni za Kifuta jasho na Machozi za Mwaka 2011, Serikali imekuwa ikitoa fedha kidogo za kuwafariji wananchi kwa kuwalipa kifuta jasho kwa uharibifu wa mali (mazao na mifugo) na kifuta machozi kwa madhara kwa binadamu (vifo na majeruhi). Katika kutekeleza mpango huo, jumla ya shilingi 48,015,000 zililipwa kwa wananchi 251 wa vijiji vya Wilaya ya Monduli waliokidhi vigezo vya kulipwa kuanzia mwaka 2010 hadi mwezi Aprili, 2018.
MHE. JULIUS K. LAIZER aliuliza:-

Tatizo la maji Jimbo la Monduli limeongeze kwa sasa baada ya Mabwawa zaidi ya 43 kati ya 51 kujaa tope na mengine kupasuka:-

(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa muda mfupi na muda mrefu wa kuwapatia maji wananchi wa Esilalei, Makuyuni, Mswakini na Ohukai kabla ya mwaka 2020?

(b) Mradi wa maji ya kisima cha Ngaramtoni umefika katika Kata ya Monduli Mjini na Engutoto; je, ni lini Serikali itasambaza maji kwa wananchi wa Vijiji vya Lashaine, Ar Katan na Meserani chini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Julius Kalanga Laizer, Mbunge wa Monduli, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika juhudi za kuwapatia maji wananchi wa Esilalei Makuyuni, Mswakini na Otukai kabla ya mwaka 2020 Serikali imekuwa ikijenga mabwawa ya kuhifadhi maji katika Wilaya ya Monduli kutokana na Wilaya hiyo kukosa vyanzo vya uhakika vya maji kama vile chemchem na vyanzo vya maji chini ya ardhi. Kwa upande wa Vijiji vya Makuyuni na Mswakini vinapata maji kupitia visima virefu vilivyochimbwa kwenye vijiji hivyo na vijiji vya Esilalei na Otukai vinapata maji kupitia vyanzo vya Bwawa ya Otukai, Esilalei na JKT Makuyuni.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2017/2018 Serikali ilitekeleza mradi wa maji wa Ngaramtoni ambapo awamu ya kwanza ilihusisha huduma ya usambazaji katika kijiji cha Meserani Juu. Awamu ya pili itahusisha usambazaji wa maji katika Kijiji cha cha Meserani Chini na kazi hiyo inategemea kuanza mwezi Julai, 2019. Kwa mwaka wa fedha 2018/2019 Halmashauri ya Monduli imetengewa jumla ya shilingi bilioni
1.2 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji. Serikali itaendelea kutenga fedha na kutoa fedha ili kuhakikisha hadi kufikia mwaka 2020 vijiji vyote vya Arktana, Nanja, Esilalei, Makuyuni, Mswakini, Otukai na Mti Mmoja vimepatiwa huduma ya maji.
MHE. JULIUS K. LAIZER aliuliza:-

Tanzania ni nchi ya tatu (3) Afrika kwa kuwa na idadi kubwa ya takribani mifugo milioni 25 lakini sekta hii bado mchango wake katika pato la Taifa ni ndogo ukilinganisha na idadi ya mifugo tuliyonayo:-

(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga viwanda vya nyama, ngozi na maziwa hapa nchini ili kuongeza thamani ya mazao yatokanayo na mifugo?

(b) Je, ni lini Serikali itaanza kutoa ruzuku ya madawa kama Ndigana Kali, Homa ya Mapafu na dipu kwa wafugaji wetu nchini?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Julius Kalanga Laizer, Mbunge wa Monduli lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ina mkakati wa kuendeleza Sekta ya Mifugo nchini kwa kuboresha kosaafu, malisho, kuelimisha wafugaji kuhusu ufugaji wa kisasa, kuimarisha utafiti na kuweka mazingira bora ya kuvutia wawekezaji katika ujenzi wa viwanda vya kusindika na kuongeza thamani mazao ya mifugo. Aidha, Wizara kupitia Taasisi ya NARCO imeingia mkataba na Kampuni ya NECAI ya Misri kujenga kiwanda cha kusindika na kuongeza thamani ya mazao ya mifugo katika Mkoa wa Pwani (Ruvu). Aidha, viwanda kumi na nne (14) vya nyama na maziwa vipo katika hatua mbalimbali za ujenzi kikiwemo kiwanda cha kisasa cha Elia Foods Overseas Ltd kinachojengwa katika Wilaya ya Longido kitakachokuwa na uwezo wa kuchinja ng’ombe 400 na mbuzi 2,000 kwa siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia mkakati wa kudhibiti magonjwa ya mifugo, Wizara imenunua na kusambaza kiasi cha lita 8,823 za dawa ya kuogesha mifugo (dipu) kwa ruzuku ya asilimia 100 katika mikoa yote ya Tanzania Bara. Aidha, Serikali imewezesha uzalishaji wa chanjo muhimu nchini zikiwemo chanjo za Homa ya Mapafu ya Ng’ombe (CBPP) kupitia Taasisi ya TVLA pamoja na kuanzisha mfumo wa ununuzi wa dawa, chanjo na viwatilifu kwa pamoja (Bulk Procurement) ili kurahisisha usimamizi na upatikanaji wa pembejeo hizi kwa urahisi na kwa bei nafuu.
MHE. JULIUS K. LAIZER aliuliza:-

Mji wa Mto wa Mbu ni mji wa kitalii na unaingiza mapato mengi ya kitalii; lakini unakabiliwa na tatizo la miundombinu ya barabara;

(a) Je nini mkakati wa Serikali kuupatia Mji wa Mto wa Mbu angalau km 5 za lami?

(b) Je Serikali ina mpango gani wa kuanza ujenzi wa barabara ya Mto wa Mbu mpaka Loliondo kwa kiwango cha lami ili kusaidia mradi wa kimkakati wa magadi Engaruka?

(c) Je ni lini Serikali itatimiza ahadi ya Mhe. Rais ya kuweka lami barabara ya Ngarasha mpaka Monduli Juu kwa Sokoine?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Julius Kalanga Laizer, Mbunge wa Monduli, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini – TARURA imekamilisha usanifu wa barabara za Mji Mdogo wa Mto wa Mbu kwa kiwango cha lami zenye jumla ya urefu wa kilometa 9 ambazo ujenzi wake utagharimu jumla ya shilingi bilioni 7.32. Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya ujenzi ambao utafanyika kwa awamu.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Mto wa Mbu – Loliondo ina urefu wa kilometa 247 na ipo chini ya Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS). Serikali imeanza kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami. Katika mwaka wa fedha 2019/20 kiasi cha Shilingi bilioni 87 kimetolewa kwa ajili ya kujenga kipande chenye urefu wa kilometa 49 na ujenzi umefikia asilimia 43. Serikali itaendelea kujenga barabara hii kwa awamu kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.

(c) Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Ngarasha mpaka Monduli Juu kwa Sokoine yenye urefu wa kilometa 11.66 iko chini ya Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS). Wakala wa Barabara unaendelea na usanifu wa barabara hiyo. Kwa sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo unaotarajia kuanza pindi usanifu wa barabara hiyo utakapo kamilika.
MHE. JULIUS K. LAIZER aliuliza:-

(a) Je, ni lini Serikali itapeleka umeme wa REA kama ilivyoahidi katika vijiji vya Munjere, Baraka, Mbaasha, Lepurko, Mti Mmoja, Arkatan, Arkaria, Mfereji, Ndonyonaado, Mswakini, Naitolia, Emurua, Lashaine, Orkenswa, Engaaroji, Oldonyolengai na Naalarami?

(b) Je, ni lini Serikali itapeleka umeme katika Shule ya Sekondari Oldonyolengai ambayo laini imefika tangu mwaka 2015 lakini mpaka sasa umeme haujawaka?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati napenda kujibu swali la Mheshimiwa Julias Kalanga Laizer, Mbunge wa Monduli lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imedhamiria kufikisha ueme katika vijiji vyote visivyo na umeme nchini ifikapo mwezi Juni 2021. Kulingana na mpango wa kupeleka umeme katika vijiji 64 Wilayani Monduli vijiji 16 vilishapatiwa umeme vikiwemo vijiji vya Arkatani na Mti Mmoja ni miongoni mwa vijiji vya Wilaya ya Monduli vilivyopata umeme kupitia awamu ya pili ya mradi wa kusambaza umeme Vijijini (REA II). Aidha, vijiji vya Arkaria, Lepurko na Mbaasha vitapatiwa umeme kupitia mradi wa REA III mzunguko wa kwanza unaoendelea.

Mheshimiwa Spika, kazi za mradi zinahusisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 48.75 na njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa 40 na ufungaji wa transfoma 20. Jumla ya wateja wa awali 720 wataunganishiwa umeme na gharama za mradi ni shilingi bilioni tatu. Mradi unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2020.

Vijiji vingine vya Munjere, Baraka Mfereji, Ndonyonaado, Mswakini, Naitolia, Emurua, Lashaine, Orkenswa, Engaaroji na Naalarami vitapata umeme kupitia REA III mzunguko wa pili utakaoanza kutekelezwa kuanzia mwezi Julai, 2019 na kukamilika mwezi Juni, 2021.

(b) Mheshimiwa Spika, Shule ya Sekondari Oldonyolengai iliyopo Kata ya Engaruka imeshapatiwa umeme kupitia Mradi wa REA III mzunguko wa kwanza unaoendelea kutekelezwa Wilayani Monduli.