Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Khadija Nassir Ali (9 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa masikitiko makubwa naomba kuchangia mawazo yangu baada ya kupitia kitabu cha hotuba ya Wizara ya Maliasili na utalii. Nimesikitishwa sana kuona hotuba yenye kurasa zisizopungua 120 kutoelezea vizuri mipango na mikakati ya sekta ya utalii Zanzibar. Sote tunajua contribution ya Zanzibar kwenye sekta hii ya utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Wizara yako inajitihada za makusudi katika kuhakikisha utalii wa Zanzibar unainuka na unatambulika zaidi duniani, ila kiukweli wazawa hawafaidiki ipasavyo. Inasikitisha kuona hata mpishi wa hoteli ni foreigner, sitaki kuamini kwamba wazawa hawana elimu ya kutosha ku-operate hoteli na sehemu nyingi za kitalii. Ni kwa nini Wizara isichukue juhudi za kuboresha mitaala katika vyuo vyetu vya utalii vilivyo ndani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama sitapata maelezo mazuri kutoka kwa Mheshimiwa Waziri wakati wa ku-wind-up nakusudia kushika mshahara wa Mheshimiwa Waziri.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama hapa nikiwa mwenye afya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile, napenda kuipongeza Serikali yangu ya Awamu ya Tano kwa kasi iliyoanza nayo, imani yangu, Tanzania yetu iko kwenye mikono salama chini ya Serikali ya CCM. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi hizo, sasa naomba kujikita moja kwa moja kwenye michango yangu, ambapo nitaanza kuongelea suala la ajira kwa vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuipongeza Serikali kwa juhudi inazochukuwa kuhakikisha vijana wanapatiwa ajira. Pamoja na jitihada hizi bado tunauhitaji mkubwa wa ajira kwa vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa Serikali hizi milioni 50 ambazo zinatakiwa kwenda kwenye kila Kijiji zingetumika kuanzisha Community Bank katika kila Wilaya, ambayo vijana na makundi mengine yangeweza kukopa kwa masharti nafuu na kuweza kujiajiri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa niongelee issue ya elimu. Naipongeza Serikali kwa kuanzisha elimu bure hadi kidato cha nne. Huu ni mwanzo mzuri wa kuweza kuwajengea fursa sawa watoto wote nchini kwa kuwajengea uwezo. Naiomba Serikali iweze kwenda mbele zaidi hadi kidato cha sita kufanya kuwa elimu bure. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile, napenda kuishauri Serikali ione namna ya kutoa mikopo kwa wanafunzi wanasoma Kada za Afya na nyingine ambazo tunahitaji sana kama Taifa mfano wa Kada hizo ni kama Kada ya Utabibu, Ukunga na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa niongelee suala la kodi katika Sekta ya Utalii. Sekta ya Utalii inachangia asilimia 12 ya Pato la Serikali kwa Tanzania Bara na asilimia 27 kwa Tanzania Visiwani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, average ya Watalii kwa mwaka ni milioni moja na hii average imekuwa stagnant kwa zaidi ya miaka mitatu. Hii inatokana na Imposition ya kodi ambazo hazina tija katika Sekta hii. Ushauri wangu kwa Serikali iangalie upya hizi kodi na kuzifuta ili tuweze kuinua Utalii wetu kwa kiwango kikubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitakuwa sijajitendea haki nisipoongelea issue ya CAG. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya PAC, naelewa umuhimu wa CAG naelewa kazi zake na naelewa umahiri wake. Wenzangu waliopita wameongelea sana kwa kirefu na kwa kina zaidi. Namwomba Waziri atakaposimama kwa ajili ya majumuisho atueleze ni jinsi gani atakavyoweza kupata fedha za kumwongeza CAG ili aweze kufanya kazi zake kwa umahiri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa leo sina michango mingi, naunga mkono hoja, ahsante!
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Usimamizi wa Matumizi ya Fedha za Umma katika Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2017
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, na mimi kuweza kunipatia nafasi ya kutoa maoni yangu juu ya hoja ambayo iko mbele yetu. Kwanza kabisa nipende kuzipongeza Kamati zote mbili kwa kuweza kutuletea taarifa iliyosheheni maoni na mapendekezo ambayo yana maslahi mapana ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, labda tu niwakumbushe wenzangu ambao wanajifanya kusahau kwamba hawafahamu msingi wa Kamati hizi mbili kitu gani ambacho wanatakiwa kufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, msingi wa kazi za Kamati ya PAC...

MBUNGE FULANI: Ooohhh Khadija.

MHE. KHADIJA NASSIR ALI: …zinatokana na taarifa iliyokaguliwa na CAG. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitawaelezea machache tu ili waweze kurudisha kumbukumbu zao na hisia zao karibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati iliweza kubaini mapungufu na madhaifu mbalimbali katika ripoti ya CAG, nitayaelezaa machache. Kamati yetu iliweza kubaini mapungufu katika makusanyo ya mapato yetu ya nchi. Lakini baada ya Kamati ya PAC kuishauri Serikali iliweza kuleta mfumo mzuri wa makusanyo wa mapato yetu na sasa hivi tunaweza kuona tija, ya mapato yetu ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati yetu iliweza kubaini mapungufu katika mikataba yetu ya madini baada ya Kamati yetu kuishauri Serikali iliweza kuchukua hatua mbalimbali. Kamati yetu iliweza kubaini upungufu wa kiutendaji, kwenye mashirika na taasisi zetu za umma, baada ya Kamati kuishauri Serikali iliweza kuteua Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu, na sasa hivi Mashirika yetu yanaweza kufanya kazi vizuri baada ya kuweza kuweka ile mianya ambayo ilikuwa iko wazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati yetu iliweza kuona mapungufu katika ufanisi wa kazi katika Halmashauri zetu. Baada ya Kamati yetu kuishauri Serikali, Serikali imeweza kuzidisha ufanisi, sasa hivi Halmashauri zetu nyingi zimeanza kupata hati safi katika mchakato wetu wa Ukaguzi. (Makofi)

MHE. BONIPHACE M.GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

WABUNGE FULANI: Endelea wewe, endelea.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Getere.

T A A R I F A

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Khadija Nassir unaipokea taarifa hiyo?

MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea taarifa hii. Hiyo ni moja ya kati ya…

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Taarifa.

MHE. KHADIJA NASSIR ALI: …na utekelezaji wa Serikali baada ya kupata maelekezo ya…

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Bungara.

T A A R I F A

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Khadija Nassir unaipokea taarifa hiyo?

MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa hiyo siipokei, Mheshimiwa Zitto ni kati ya wahasibu ambao tupo hapa Bungeni, tupo very competent, yeye ni mmoja kati ya wengi ambao tupo wazi na macho kuangalia ufanisi wa Kamati na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuendelea. Kamati yetu pia iliweza kubaini madeni ya Serikali kwenye taasisi na mashirika yetu ya umma, lakini baada ya kamati yetu kuweza kushauri Serikali, Serikali imeweza kuanza kulipa madeni hayo na sasa mashirika na taasisi zetu za umma zimeanza kufanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo sasa naomba niende kwenye uwekezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo. Napenda kuipongeza Serikali yangu na ninapenda kuwashauri Wabunge wenzangu, kwa vile Serikali yetu ni sikivu, inasikia maelekezo ya Kamati na ushauri mmoja mmoja wa Wabunge tuendelee kufanya kazi yetu ya kikanuni kuisimamia na kuishauri Serikali katika mambo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali yetu imeanza kwenye uwekezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo. Tumeona Serikali imewekeza kwenye mradi wa SGR ambayo inaenda kuipa vijana ajira zaidi ya 3,000. Mradi huu unaenda kutoa uboreshaji wa Wilaya zaidi ya 16 nchini na kutoa uwezeshaji wa vijiji zaidi ya 120 katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Serikali imewekeza katika ununuzi wa ndege, ndege hizi zitarahisisha usafiri wa wananchi na kutatua changamoto katika sekta ya utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Serikali imeweza kuwekeza katika miradi mikubwa ya umeme ambayo ita- stabilize uwezeshaji na uwekezaji katika miradi ya viwanda vya ndani. Mradi huu pia utachangia na kumwezesha Mtanzania mmoja mmoja katika kuweza kujikimu kimaisha. (Makofi)

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inafanya mambo mazuri sana…

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ulinde muda wangu.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Bungara taarifa.

T A A R I F A

MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, tumezoea kuwaona wanachukua muda mwingi kupotosha, lakini sasa tumeamka na tupo tayari kuwaeleza wananchi nini Serikali inafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kueleza hayo naomba sasa niende moja kwa moja katika utekelezaji wa miradi mikubwa ambayo Serikali yetu imejikita…

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ulinde muda wangu.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwakajoka.

TA A R I F A

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Khadija Nassir unaipokea taarifa hiyo?

MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, siipokei taarifa yake. Kwanza tu nimueleze kati ya majukumu ya Kamati ya PAC ni kusimamia mashirika changa na kusimamia mashirika ambayo yameanza kazi yake. Kwa hiyo miradi ambayo tunaielezea hapa ni miradi ambayo tumeianzisha sisi na kuisimamia kama Kamati ya PAC. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa niendelee na mchango wangu ambao nitajikita kuelezea…

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa ya mwisho hiyo inayomuhusu Mheshimiwa Khadija Nassir, Mheshimiwa Yussuf.

T A A R I F A

NAIBU SPIKA: Sawa, Mheshimiwa Khadija Nassir unaipokea taarifa hiyo?

MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, siipokei taarifa yake na kwa vile walizoea tantalila na kwa vile walizoea baada ya kuimba nyimbo zao hatuwajibu walijua kwamba hakuna watu specific wa kuweza kuwajibu tantalila zao. Naomba niwaambie hivi uwekezaji ambao Serikali imefanya… (Makofi)

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbilinyi kwa Mheshimiwa Khadija Nassir nimesema ile ilikuwa ni taarifa ya mwisho, Mheshimiwa Khadija Nassir una dakika mbili malizia muda wako.

MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuendelea na naomba ulinde muda wangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nielezee fursa ambazo tutazipata…

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mbilinyi unasubiri kunyolewa Mbeya 2020.

MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama mradi wa SGR tutaweza kupata nafasi za ajira 2,500 nchini, uchumi wa Wilaya zaidi ya 16 na uchumi wa vijiji zaidi ya 106.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapo hapo naomba nitoe ushauri, kwa vile Serikali imejikita katika kuwekeza katika miradi mikubwa naomba wakati wananza kuwekeza katika miradi mikubwa waweze kuanzisha miradi wezeshi ili tuweze kupata muda sahihi ambao tunatakiwa kuutumia katika uwekezaji. Pia kiasi sahihi ambacho tunaweza kukitumia katika uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, kama kwenye mradi wa SGR tungeweza kuanzisha mradi wa kokoto, mradi wa chuma na miundombinu mizuri kabla ya kuanzisha huo mradi wa SGR tungeweza kupata specific term ambayo tutaitumia katika mradi wa SGR lakini pia tungeweza kubana matumizi katika uanzishaji wa mradi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile, mimi ni mwanakamati nimeshatoa maoni mengi sana kwenye Kamati…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee kuongelea changamoto zinazowakabili watu wenye mahitaji maalum (viziwi). Kumekuwa na changamoto kubwa sana kwa wenzetu hasa soko la ajira haliwapi fursa kuweza kupata nafasi za kazi na fursa za kujiajiri; ushauri wangu Serikali iangalie mitaala maalum itakayoweza kuwapa wenzetu hawa fursa ya kuingia kwenye soko la ajira ili waweze kuona tija ya elimu wanayopatiwa.

Masomo ya dini (Bible knowledge na Islamic religion) kupatiwa thamani kwenye ufaulu wa wanafunzi; Serikali imekuwa ikilipa mishahara kwa walimu wanaosomesha masomo ya dini shuleni na pia Serikali imekuwa ikiingia gharama kuandaa mitihani kwa masomo hayo bila ya kupatiwa thamani kwenye ufaulu. Kwa vile kila mwanafunzi anatarajiwa kuwa muajiriwa mtarajiwa na kwa kila mwajiriwa anahitaji miongozo ya kiroho, Wizara sasa ina haja ya kuona namna ya kuipa thamani masomo haya kwenye ufaulu wa wanafunzi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. KHADIJA N. ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru nami kwa kunipatia nafasi ya kuchangia kwenye Wizara hii ya Fedha na Mipango. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya ya kuweza kusimama hapa leo lakini pia napenda kuwapa heri ya mfungo wa Ramadhani Waislam wote duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile dakika zangu ni chache, naomba sasa nijikite moja kwa moja kwenye mchango wangu na nitaanza kuongelea mtiririko mzima wa fedha za miradi ya maendeleo. Mwaka wa fedha 2015/2016, fedha zilizotengwa kwenye bajeti ya miradi ya maendeleo ilikuwa ni bilioni 1,031.7 na kwa mwaka wa fedha 2016/2017, fedha zilizotengwa ilikuwa ni bilioni 791.9.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ingawa Serikali imepunguza budget ceiling ya hizi fedha za maendeleo lakini bado tatizo la kupeleka fedha hizi kwenye miradi imekuwa ni changamoto kubwa. Mfano, katika mwaka wa fedha wa 2016/2017, Wizara iliidhinisha jumla ya shilingi bilioni 791.9 lakini mpaka kufikia Machi, 2017 Serikali ilikuwa imepeleka jumla ya shilingi bilioni 18.8 ambayo ni sawa na asilimia mbili tu ya bajeti ambayo imeidhinishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali juu ya hili ni kwanza, Serikali kupitia Bunge iidhinishe bajeti ambayo itaweza kwenda ipasavyo na siyo kuidhinisha bajeti kubwa ambayo haitaweza kwenda. Bajeti za Wizara ziendane na kasi ya makusanyo ya mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa pili; muda muafaka sasa kwa Serikali kuhakikisha fedha zote zinazoidhinishwa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo zipatikane kwa wakati ili kuendana na kasi ya Mheshimiwa Rais ya kujenga Tanzania ya viwanda. Ushauri wangu wa tatu; Serikali isitegemee sana fedha za wafadhili kwa sababu fedha hizi hazina uhakika wa kutosha, zinaweza kuja au zisije au zikaja kwa kuchelewa na hili linaweza kuathiri maendeleo ya miradi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijamaliza kuongea kwenye hili suala naomba Waziri atakapokuja kuhitimisha anipe majibu ya maswali haya yafuatayo:-

Huu mpango wa Serikali kuhamia Dodoma; Je, Serikali imetumia kiasi gani cha fedha katika mpango huu? Pili; Je, mpango huu umeathiri vipi fedha za umma ambazo zingeweza kupelekwa kwenye miradi ya maendeleo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niingie kwenye suala la misamaha ya kodi. Serikali imekuwa ikitoa misamaha ya kodi kila mwaka lakini bado misamaha hii haitolewi kwa uwazi kwa maana ya kwamba mimi na wewe na wananchi wengine hatujui misamaha hii inatolewa kwa vigezo gani. Wabunge na wananchi tunahitaji kujua projection ya misamaha hii lakini pia tunahitaji kujua uhalisia wa misamaha hii, pia ushauri wangu kwa Serikali ni kwanini isiwe ina-publish misamaha hii ili tuweze kujua kiwango na watu ambao wanasamehewa hizi kodi ni akina nani na wanatolewa kwa vigezo gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nigusie kidogo issue ya deni la Taifa. Kwa mwaka wa fedha 2016/2017 malipo ya deni la Taifa ilikuwa ni bilioni 8,000 matumizi ya kawaida kwa mwaka huu yalikuwa ni bilioni 8,009.3 na kwa mwaka wa fedha 2017/2018 malipo ya deni la Taifa yanatarajiwa kuwa bilioni 9,461.4 na matumizi ya kawaida yanatarajiwa kuwa bilioni 9,472.7. Naipongeza Serikali kwa hili, kwa kuwa wameweza kuongeza bajeti ya malipo ya deni la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yangu kwa Serikali ihakikishe kuwa fedha hizi zinatolewa kwa wakati ili nchi iondokane na madeni yanayosababisha nchi kulipa fedha nyingi yaani ile fedha inayotoka kama riba ingawa Serikali inasema kwamba deni la Taifa ni himilivu lakini lazima Serikali iendane……………..

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa vile dakika nilizonazo ni chache naomba sasa niende moja kwa moja kwenye kuelezea hali halisi ya kibishara inayoendelea Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi zote zilizoungana na visiwa kama Tanganyika ilivyoungana na Visiwa vya Zanzibar hutumia visiwa hivyo kama strategic center za kibiashara kutokana na geographical position za visiwa. Kwa bahati mbaya sana mpaka sasa Serikali yetu haijaona umuhimu wa kutumia Zanzibar kama center ya kibiashara kwa maslahi ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miezi michache iliyopita Tanzania Bara ilipatwa na shortage ya sukari ambayo kwa taratibu za Serikali ilizozichukua sina mashaka nazo, hatua ambazo Serikali imechukua ku-solve tatizo hili pia sina mashaka nazo. Mashaka na malalamiko yangu makubwa kwenye hili ni baadhi ya Watendaji wa Serikali kulichukua hili jambo na kulitekeleza kinyume na maagizo ambayo yametokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ambayo inaendelea sasa kwenye bandari yetu, Wazanzibar au wananchi wetu hawana ruhusa hata ya kuingiza sukari kilo mbili kwa ajili ya matumizi yao binafsi. Tatizo hili limekuwa kubwa mpaka sasa wananchi wetu hawawezi kuingiza hata kilo mbili za matumizi yao ya kawaida. Kisa tu tamko lilitoka, kibali hakijatoka na utekelezaji huo umekuwa namna hiyo ambayo naielezea. Kwa masikitiko makubwa sana nathubutu kusema kwamba bado sijaona faida ya kibiashara ndani ya Muungano wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuelezea malalamiko yangu, naomba sasa nielezee juu ya Wabunge ambao wamebeba agenda ya kuibeza Zanzibar na Wazanzibari kwa ujumla. Kuna baadhi ya Wabunge humu wamebeba agenda ya kuibeza Zanzibar na Wazanzibari kwa ujumla na wamekwenda mbali mpaka kujiita kwamba wao ndiyo wababe wa Wazanzibari. Niwaambie tu, mbabe wa Wazanzibari ni Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein ambaye ndiye Rais wetu na hakuna mbabe zaidi ya huyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kueleza hayo, naomba sasa nijikite kwenye mchango wangu moja kwa moja na nitaanza kuelezea hali ya kiuchumi nchini. Ukurasa wa nane umeelezea viashiria vya kiuchumi vinaonesha kuwa katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Septemba, 2017, uchumi ulikua kwa asilimia 6.8. Sina mashaka na maelezo haya na kwa vile hotuba hii haijaonesha ni viashiria gani ambavyo vimepima ukuaji uchumi huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuangalie ripoti ya REPOA na takwimu ambazo imeonesha. Ripoti ya REPOA inaonesha kwamba mwaka 2014 asilimia 22 ya Watanzania walikuwa wanashinda na njaa wakati mwaka 2018 asilimia 27 ya Watanzania wanashinda au kulala na njaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ripoti hii pia imeonesha hali ya ajira nchini. Ripoti hii inaonesha kwamba vijana wa Kitanzania asilimia 43 walikuwa na imani kuwa Serikali itatengeneza ajira wakati mwaka 2018 ni vijana asilimia 31 tu ndiyo wenye imani kuwa Serikali itatengeneza ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ripoti hii pia inaonesha hali ya ufukara nchini. Kwa mwaka 2014 asilimia 64 ya Watanzania hawakuweza kumudu maisha yao wakati kwa mwaka 2018 ni asilimia 76 ya Watanzania hawakuweza kumudu maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia tuangalie ripoti ya Serikali kupitia Taasisi ya NBS ambayo inaonesha hali ya udumavu kwa mwaka 2014 ni asilimia 34.4 ya watoto nchini walikuwa wamedumaa, wakati kwa mwaka 2018 asilimia 34.7 ya watoto nchini wamedumaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ripoti hiihii pia imeonesha vifo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza kabisa, napenda kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri lakini pia napenda kuipongeza Serikali kwa ujenzi wa maktaba mpya na ya kisasa. Maktaba hiyo ndiyo kubwa kwa East Africa nzima. Maktaba hiyo inakwenda sasa kuwapata watafiti wetu nguvu na ufanisi wa kuweza kufanya tafiti zao vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maktaba hiyo pia inakwenda kuwaisaidia wanafunzi wa elimu ya juu nchi nzima kuweza kufikia yale mahitaji ambayo yalikuwa yanatakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vie muda wangu mchache, naomba sasa niende moja kwa moja kwenye mchango wangu. Suala la kwanza ambalo nitaliongelea ni Sera ya Elimu versus Sera ya Uchumi wa nchi. Nchi zote duniani, Sera ya Elimu ndiyo inatoa dira na mwelekeo wa Sera ya Uchumi wa nchi. Kama tunavyofahamu, Wizara ya Elimu ndiyo mdau na ndiyo yenye dhamana ya kuleta rasilimali watu ambao wataweza sasa kujenga uchumi wa nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakwenda kwenye uchumi wa viwanda na uchumi huu kwa kiasi kikubwa sana unahitaji rasilimali watu, wenye elimu na ujuzi wa level ya kati, sio level ya juu. Kama tutakubaliana na hilo, niiombe sasa Serikali yangu, nafahamu inasikia na ina lengo la kui-support hii Sera ya uchumi, iende sasa ikaboreshe mitaala katika vyuo vyetu vya stadi za kazi, iende ikaboreshe mitaala na ufanisi katika vyuo vyetu vya VETA. Kwa sababu hizo ndiyo taasisi ambazo zitatuletea nguvukazi ya vijana na watu ambao wataendesha viwanda vyetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuongea hayo, naomba sasa kidogo niende nikagusie masuala ya watu wenye mahitaji maalum hasa wale wenzetu ambao wana shida ya kusikia au kwa lugha rahisi, viziwi. Hawa watu wenye kundi maalum hili wanakutwa na changamoto kubwa. Changamoto kubwa ni kwa sababu hawana uwezo wa kufanya mawasiliano ya moja kwa moja na watu wa kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto hii inasababisha hata ufanisi wao katika masuala ya elimu wakiwa shuleni unakuwa mgumu sana kiasi kwamba huwa wanakosa msaada kwa wenzao. Rai yangu kwenye hili, napenda kuishauri Serikali ione sasa umuhimu wa kuanzisha elimu ya lugha ya alama iwe kama somo katika shule zetu ili sasa hawa wenzetu waweze kufaidika na mfumo wa elimu wa nchi yetu.

Mheshimiwa Menyekiti, katika kufanya hili, hatuendi tu kuwasaidia watu ambao hawana uwezo wa kusikia kwa vile soko la ajira kwa wakalimani sasa hivi ndani na nje ya nchi liko very hot. Tunakwenda ku-create ajira kwa vijana ambao sasa watakuwa wamepatiwa elimu ya lugha ya alama kwa maana ya kwamba tutapata wakalimani ambao watapata ajira ndani na nje ya nchi yetu. Kundi hili lina changamoto nyingi sana. Hiyo ya kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee ya pili. Kati ya vyuo ambavyo tunavyo nchini, ni vyuo vinne tu ndiyo ambavyo mpaka sasa vina wakalimani, kiasi kwamba kuna wanafunzi ambao wanafanikiwa kufika mpaka ngazi ya shahada, wanafika vyuoni na huwa wanakosa misaada ya kuweza kuendelea au ku-cope kwa sababu hawana vyuo husika au hawana vyuo maalum kwamba hawa vyuo vyao specifically ni hivi. Huwa tunawachanganya pamoja na wanafunzi wengine na wakifika kule wanakosa wakalimani wa kuweza kuwasaidia kuweza ku-cope na masomo.

Mheshimiwa Waziri, naomba hili ulichukue. Tuna watu wenye ulemavu wa kusikia ambao ni very genius, wanahitaji msaada mdogo tu wa wakalimani ili na wao sasa waweze ku-cope vizuri na masomo wakiwa vyuoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine kwa hawa wenzetu ni suala zima la ajira. Kila anayesoma ndoto yake ni kuweza kutumia elimu yake kumfikisha au kuweza kutumia elimu yake kumkwamua kwenye masuala ya kiuchumi, lakini kwa bahati mbaya sana bado Serikali…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Muda wako umekwisha.

MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Eh!

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi kwanza kabisa nipende kuungana na viongozi wote ambao wameweza kutoa pole kwa Taifa letu na kwa dunia nzima kwa ajili ya hili janga la corona. Lakini pia nitoe pongezi kwa Serikali kwa namna ambavyo imekuwa ikikabiliana na hili janga.

Mheshimiwa Spika, pongezi pia kwa Serikali ya Awamu ya Tano kwa jinsi ambavyo imeweza kujipambanua kufanya mageuzi makubwa sana ya kimaendeleo katika sekta mbalimbali.

Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu imeeleza mambo tofauti tofauti ambayo kama nchi na Serikali tumeweza kuyafikia. Hotuba hii imeeleza ukuzaji wa fursa za ajira kwa vijana, lakini pia imeeleza vizuri uboreshaji wa miundombinu kwa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa. Hotuba hii pia imeeleza ufufuaji wa shirika ndege, ufufuaji wa mali za ushirika, ulinzi wa rasilimali zetu za nchi, ukarabati wa miundombinu ya elimu, uboreshaji wa huduma za afya na maji, upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa mijini na vijiji.

Mheshimiwa Spika, mafanikio haya niliyotaja na mengi ambayo sijayataja yanakwenda sasa kutekeleza moja kwa moja azma ya kuchochea uchumi wetu kwenda sasa kuwa uchumi wa viwanda. Baada ya pongezi hizo sasa niweze kwenda moja kwa moja kwenye mchango wangu na nitaanza kuelezea ukuzaji wa fursa za ajira kwa vijana.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeeleza hapa namna ambavyo imeweza kubuni uzalishaji wa ajira ambazo ni rasmi na zile ambazo sio rasmi, lakini takwimu ambayo Mheshimiwa Waziri Mkuu ameitoa kwenye hotuba yake inaonesha kwamba ajira ambazo sio rasmi ni nyingi sana nchi kuliko zile ambazo ni rasmi. Vile vile tunafahamu ajira ambazo sio rasmi zinahitaji mambo mawili makuu; la kwanza mafunzo wezeshi, lakini pia vitendea kazi baada ya vijana kupatiwa mafunzo ambayo Serikali imeanza kuyatoa.

Mheshimiwa Spika, nafahamu Serikali ina Mfuko wa Maendeleo kwa Vijana na umekuwa ukifanya vizuri sana, lakini kutokana na uhitaji kuwa mkubwa Mfuko huu umeanza kuelemewa kwa mahitaji ambayo kama nchi tupo nayo. Sasa kwa kuzingatia hayo nina ushauri ambao nitatoa kwa Serikali.

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza, Serikali iweze kupunguza masharti kwa taasisi za fedha ili vijana ambao wataweza kupatiwa yale mafunzo waweze kupata mikopo ya kuweza ku-practice yale masomo ambayo watayapata na kuweza kujiajiri. Tunafahamu tulifanya marekebisho ya Sheria za Taasisi za Fedha ambayo yamekwenda sasa kufuta huduma ya VICOBA na zile taasisi ndogo ndogo ambazo mitaani zilikuwa zinawasaidia vijana na akinamama. Sasa tunaomba vijana watakapotoka kwenye zile incubation programmes waweze kupata angalau hata kama sio benki za biashara, benki ya maendeleo ambayo itaweza kuwapatia mikopo kwa masharti naafuu.

Mheshimiwa Spika, ushauri wa pili, kumekuwa na msongamano na uhaba wa vyuo vya stadi za kazi, sisi kama vijana tumelia sana hapa Bungeni angalau kila wilaya iweze kuanzisha Chuo cha VETA na kama wilaya hazitaweza basi angalau hata mkoa. Vyuo hivi ndio ambavyo vinakwenda sasa kutoa zile stadi za kazi ambazo tunazihitaji katika kukuza au kufikia ule uchumi ambao tunaita wa viwanda. Sasa hapa tumeona vyuo ambavyo vinatoa stadi hizo za kazi ni vichache nchini, lakini pia msongamano umekuwa mkubwa. Naomba Serikali iweze kulichukua hilo na kuweza kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, la tatu, Serikali iweze kuwa na takwimu ya vijana ambao wana vipaji maalum kwa hizi stadi za kazi. Pia serikali iweze kuwa na takwimu ya vijana ambao tayari wameshapewa mafunzo ya kujiajiri. Kwa kufanya hivyo tutaweza kuona sasa ile elimu inashuka kwa jamii ambazo vijana inawazunguka, lakini pia tutarahisha kwa Serikali katika kuhakikisha kwamba vijana ambao hawana ajira wanaweza kupata hizo taaluma ambazo zinahitajika.

Mheshimiwa Spika, la mwisho kwenye hili, napenda kutoa ushauri kwa Serikali angalau iweze kufikiria namna ya kutoa intensive internship programs kwa wale wanavyuo ambao wamemaliza. Tumekuwa na changamoto ya vijana kukataliwa katika ajira kwa kigezo cha uzoefu. Kwa kufanya hivi tutawawezesha sasa waajiri waweze kuwa comfortable kutuajiri sisi vijana ambao tunatoka chuoni moja kwa moja kwa sababu tayari wanakuwa na uhakika tumepata mafunzo ya kutuwezesha kuingia kazini vizuri.

Mheshimiwa Spika, baada ya hilo nitakwenda moja kwa moja kuongelea hali ya uchumi.

Mheshimiwa Spika, tumeona hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu imeongelea ongezeko la ukuaji uchumi, nawapongeza sana Serikali kwa hilo na niwapongeze Serikali kwa usimamizi mzuri wa ukusanyaji wa mapato. Pia niwapongeze Serikali kwa kuandaa mfumo mzuri wa ukusanyaji mapato. Kwa hayo mawili ndiyo results ambazo tunaziona sasa hivi. Vile vile kwenye hili ningependa kushauri mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza, Serikali ifanye jitiahada ya kuangalia walipakodi wapya; tumekuwa tukiwakamua walipa kodi wale wale wa zamani bila ya kuangalia kwamba kila mwaka Serikali ina uwezo wa kukusanya walipakodi wapya na wakaweza kuingia katika kuchangia pato la Taifa.

Mheshimiwa Spika, pili, ningependa Serikali ione namna kuweza kuwatambua wajasiliamali ambao hawana ajira rasmi na kwa nchi hii ndio wengi. Tukiweza kuwatambua tukawapa elimu, tukaweza pia kuwashirikisha katika ukuzaji huu wa uchumi, nadhani watakuwa tayari na wao kuweza kuunga mkono jitihada za Serikali na wao wakaweza pia kuingia katika kukuza pato la nchi.

Mheshimiwa Spika, tatu, kuna wafanyabishara wengini na wajasiliamali ambao sasa hivi wamekuwa wakitumia ukuaji wa teknolojia katika kufanya biashara zao yaani online business na wana make money kuliko hata hawa ambao wameweza ku-estabilish biashara zao kwenye hii proper arrangement.

Mheshimiwa Spika, nchi zote duniani wafanyabiashara wakubwa ambao wamechipukia ni wale ambao wameweza kuona fursa katika ukuaji wa teknolojia. Nasema hivi sio kuwabana au kuwaminya, lakini naamini wao na mimi na sisi wengine Watanzania tupo tayari katika kushirikiana na Serikali kukuza pato la Taifa. Sasa tutakapowawekea protection, tutakapowaona na kwamba na wao ni part ya watu ambao wapo tayari katika kushirikiana na Serikali wataweza kuwa wa msaada mkubwa sana katika kukuza uchumi wa nchi, pia tutaweza kuwaona miongoni mwetu na wao pia wataweza kufaidika katika hili.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Spika, ya mwisho?

SPIKA: Ndiyo.

MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)
Sheria ya Fedha ya Mwaka 2019
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Kwanza kabisa nipende kuunga mkono hoja ambayo iko mbele yetu, lakini pia nipende kuongea machache tu kabla sijatoa mapendekezo yangu katika hoja hii ambayo tuko nayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka uliopita katika kipindi kama hiki cha kujadili mapendekezo ya maboresho ya sheria ya mbalimbali, mimi nikiwemo na wenzangu tulisimama kuongelea issue ya double taxation kwenye umeme ambao unakwenda Zanzibar na hili ndilo ambalo linanipa faraja leo kuweza kusimama tena, kwa sababu baada ya kupiga kelele nyingi Serikali yetu imeweza kusikia na sasa hivi suala hilo limekwisha. Kwa hiyo, nipende kuipongeza Serikali kwa hilo, lakini pia nipende kutoa mapendekezo machache tu na sitatumia muda mrefu kwenye ongezeko la thamani ya kodi kwa bidhaa ambazo zinakwenda Zanzibar.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunavyofahamu kwamba, kipato cha Mzanzibari wa chini kabisa ni kidogo uki-compare na kipato cha Mtanzania bara wa kawaida na kwa hili linapelekea sana sana kufanya maisha ya wazanzibari kuwa magumu. Tumekuwa na tatizo la double taxation kwa bidhaa ambazo zinakwenda Zanzibar. Hili limepelekea kuwa na mzunguko finyu sana wa biashara kule Zanzibar na ukizingatia kwamba Zanzibar ni kisiwa, uchumi wake tunategemea sana kwenye mzunguko wa biashara lakini pia kwenye masuala la utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nafahamu, mapendekezo yote ambayo sasa tutayapitisha, yatakwenda kuathiri makusanyo ya kodi ambayo tunayapata kwa sasa hivi, lakini tusiangalie tu ukusanyaji wa kodi, tuangalie namna gani ambavyo tutaweza kuwapunguzia ugumu wa maisha wananchi wa kawaida wa Tanzania visiwani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu, hata sasa nikipendekeza kwamba, wale wafanyabiashara ambao hawana uwezo wa kununua bidhaa kutoka kwenye viwanda, hata nikipendekeza waweze kupewa exemption, tutatoa mwanya kwa wale wafanyabiashara ambao siyo waaminifu kuweza kukwepa kodi. Kwa hiyo, sitaki kwenda huko, lakini nina mapendekezo machache tu kwenye hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwanzoni huko nyuma, zaidi ya miaka 25 tulikuwa na utaratibu wa tax refund na hili lilikuwa linakwenda vizuri sana, japokuwa lilikuwa na changamoto ndogondogo kama vile fedha kurudi kwa wakati na mambo mengine. Sasa napendekeza kwamba, utaratibu ule urudi, lakini tuufanyie maboresho yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaweza kuona namna ya kuweza kufungua akaunti, separate ya kuweza kuingiza hizi fedha ili zitakapotakiwa sasa kurudi kusiwe na mkanganyiko au kusitokee changamoto yoyote. Kwa kufanya hili tutaweza kuwawezesha wale wafanyabiashara kule Zanzibar sasa kuweza kutanua wigo, lakini pia kuweza kuwasaidia wananchi wa kawaida kupunguza ule ugumu wa maisha ambao upo kule sasa hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nataka kupendekeza, kama hilo pia tutaona, au Serikali itaona kuwa halifai kwa sasa hivi, tuone basi namna ambavyo tunaweza kufuta ongezeko hili ili sasa visiwani kule, biashara ziweze kushamiri, lakini pia maisha yaweze kuwa marahisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi langu kwenye hili lilikuwa ni hilo, naamini kwamba Serikali italifanyia kazi na sisi tuweze kuona manufaa, lakini pia tuweze kuona matunda ya biashara kwenye nchi yetu. Nashukuru sana. (Makofi)