Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Khadija Hassan Aboud (64 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami napenda kuchukua nafasi hii kumpongeza Rais wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Mheshimiwa Waziri Mkuu na Makamu wa Rais mama yetu, dada yetu mpendwa, Mama Samia Suluhu Hassan kuwa mwanamke wa kwanza Makamu wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianzie na suala la kutatua kero na changamoto za muungano. Naomba kuipongeza Serikali kwa hatua zake na Kamati na Tume zilizoundwa katika kutatua kero na changamoto hizi za Muungano mpaka hapa tulipofikia ambapo sasa Zanzibar iko huru kujiunga na taasisi zozote za Kimataifa, inaruhusiwa kukopa, Tume ya Haki za Binadamu imeanzishwa Zanzibar na mengi mengineyo. Ninachosisitiza tu harakati hizi ziendelee katika kuboresha maslahi ya Watanzania nje na ndani ya Zanzibar.
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mazingira si suala la Muungano lakini mazingira na mabadiliko ya tabianchi ni suala la Kimataifa. Zanzibar imo ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo naomba jitihada zile za kuisaidia Zanzibar katika kunusuru visiwa vile iendelee. Kwa sababu utafiti uliofanywa tayari maeneo 48 ya visiwa vya Unguja na Pemba yameathirika kimazingira. Baadhi ya visima vya maji matamu vinatoa chumvi, baadhi ya mashamba yanatoa chumvi na kuna mmomonyoko wa ardhi. Hivyo basi, naomba jitihada hizi ziendelee katika kuinusuru Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila ya mazingira hakuna nchi. Hivyo naomba Wizara hii ya Mazingira iongezewe fedha katika kuinusuru nchi yetu na hasa katika maeneo ya fukwe za bahari na visiwa tengefu. Katika maeneo hayo wavuvi wanatumia uvuvi haramu, wanaharibu matumbawe na kuathiri mazingira ya visiwa hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nashangaa, humu ndani ya Bunge tumekuja kutete maslahi ya Watanzania wote, lakini bado kuna wenzetu wanang‟ang‟ania madaraka. Tayari Kisiwa Panza na kwingine maji yameanza kufukia visiwa hivyo watatawala nini hawa visiwa hivi vikishafukiwa na bahari? Mimi naomba Jamhuri ya Muungano iingize nguvu zake zaidi katika kunusuru visiwa hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nijielekeze katika suala la Muungano. Imesemwa hapa Muungano wetu umefifia na hauna hali ya kuridhisha na wakati wowote unaweza ukavunjika. Mimi naamini Muungano wetu kwa nguvu za viongozi wetu na Watanzania wote umeimarika zaidi na una nguvu zaidi na unajulikana Kimataifa zaidi kuliko hapo mwanzo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niingie katika suala la majeshi. Kwanza napenda kumpongeza Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Tanzania. Napenda kumpongeza Waziri wa Ulinzi kwa kazi nzuri waliyoifanya katika kulinda uhuru na usalama wa wananchi wa visiwa vya Zanzibar katika chaguzi zote mbili. Uchaguzi wa Zanzibar umefanyika kihalali kwa kufuata Katiba na sheria zote za uchaguzi. Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein ndiye Rais wa Zanzibar mpaka mwaka 2020. Naomba Bunge lako lisitumike kama mahali pa kujadili masuala ya Zanzibar, masuala ya Zanzibar yako kwenye Baraza la Wawakilishi.Wamesusa, watu wamekula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasikia malalamiko mengi kwamba Tume imevunja uchaguzi. Napenda niwakumbushe katika mwaka 2008 chama kimoja cha upinzani hapa Tanzania kilifuta matokeo ya uchaguzi wa Mwenyekiti wa Vijana kwa sababu tu hawakumtaka ambaye anapendeza kwenye chama chao na wakakaa hawana Mwenyekiti mpaka mwaka 2011, hao pia wanafuata demokrasia? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea suala la ulinzi katika maeneo tengefu, naomba litumike Jeshi la Ulinzi la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania katika kulinda hayo maeneo tengefu ya visiwa ambavyo wavuvi haramu hutumia kujificha kufanya uharibifu wa mazingira na pia maficho ya wahalifu. Naomba jambo hili litiliwe maanani kwa sababu wao ndiyo chanzo cha uharibifu wa mazingira katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni imani yangu kupitia Bunge lako Tukufu viongozi wetu mahiri wataendeleza mshikamano, udugu, upendo uliojengeka kwa miaka mingi mpaka kufikia miaka 52 ya Muungano wetu kwa vitendo. Mimi sina shaka na hilo, Serikali iko tayari na sisi raia tuko tayari kutii sheria za nchi. Kwa wale ambao hawatii sheria za nchi basi sheria itachukua mkondo wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naomba nimalizie kwa kuwaombea nguvu zaidi viongozi wetu wote, Mawaziri wetu wote na sisi Wabunge, sote tutekeleze majukumu yetu tuliyotumwa na wananchi na si kuwa walafi wa kutafuta madaraka kwa njia za mgongo wa nyuma. Uchaguzi umeshafanyika, wananchi wanahitaji maendeleo, hawahitaji porojo za kisiasa au za mwanasiasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nachukua fursa hii kuwapongeza viongozi wote wa Wizara kwa juhudi kubwa za kuendeleza elimu kwa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Chama cha Walimu Tanzania, CWT ishauriwe kupunguza mchango kwa Walimu au kuondoa kabisa. Pia michango waliochangisha waoneshe ni kwa namna gani imewasaidia walimu ili walimu wanufaike na michango yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bodi ipange mpango mkakati wa kufuatilia wanafunzi ambao wamepata ajira au kujiajiri lakini mpaka sasa hawajarejesha mikopo ili fedha hizo zisaidie kuongeza idadi ya wanafunzi kukopeshwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti,, wanafunzi wa kike waliopata bahati mbaya ya ujauzito nashauri Wizara iwaruhusu kuendelea na masomo baada ya kujifungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara isaidie ujenzi wa mabweni ya wasichana katika maeneo ya vijijini ili kuwanusru wasichana wetu wadogo.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwanza napenda kuwapongeza Kamati zote tatu zilizotuletea ripoti zao hizi pamoja na ripoti ya CAG. Kwa kweli wamekaa na kuchambua na wametulea vitu ambavyo tunaweza kujadili asubuhi hii ya leo. Naunga mkono hoja za kamati zote tatu.

Mheshimiwa Spika, mimi nitajielekeza kwenye kipengele ambacho kinahusu fedha za dharura ambazo zinatumiwa na halmashauri pale ambapo kunatokea majanga, maafa na maradhi ya mlipuko.

Mheshimiwa Spika, inapotokea maradhi ya mlipuko hayana dakika wala saa; lakini wanapoomba vibali halmashauri Wizara husika inachelewa sana kutoa majibu ya vibali vile na hapo inasababisha wavunje sheria kwa kutumia fedha ambazo hazikuidhinishwa.

Mheshimiwa Spika, hoja yangu hapa, ili kuepusha isiwe kichaka cha upotevu wa fedha nyingi cha kutumia kipengele cha kwamba maradhi ya mlipuko au majanga na maafa Wizara iandae aidha, kitengo maalum au wahusika maalum ambao watapokea barua na watafanyia kazi kwa haraka kwa dharura iliyojitokeza ili kuepusha matumizi ambayo hayakuidhinishwa na au kuwa, kama nilivyosema mwanzo, kuwa kichaka cha utumiaji wa fedha za umma bila matarajio yaliyokusudiwa.

Mheshimiwa Spika, hapa inakuja hoja, je tusubiri kibali cha matumizi au tuachie watu wafe? Sasa inapokuja hoja kwamba tuwaachie watu wafe ndipo halmashauri na wahusika kutumia fedha bila kupata kibali. Hili suala lina hoja nzito kwa sababu huwezi kuwaacha watu wakafa wakati fedha unazo lakini fedha hizo ni madhumuni ya watu walewale ambao unatakiwa kuwaoongoza lakini wakifa wote unaomuongoza nani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikijielekeza kwenye mchango wangu kuna ripoti ya CAG kuna hasara ya shilingi takriban milioni 56 ambazo wamelipwa watumishi hewa, watumishi waliostaafu, watumishi waliokufa na watumishi ambao hawapo kazini kabisa. Hapa ni upotevu mkubwa wa fedha za umma ambazo zinahitaji fedha zile zielekezwe katika kutumia fedha hizi katika mambo mengine ambayo yanahusu maendeleo ya nchi, ya wananchi na watumishi wengine.

Mheshimiwa Spika, nikiunganisha hapo hapo kwenye suala la watumishi, kwenye ripoti ya CAG kuna madeni ambayo yanahusu bilioni 160 ambayo hawajalipwa watumishi, pamoja na milioni 96 ambazo ni posho na mengine haya kwa ajili ya watumishi ikiwemo uhamisho, likizo na vitu vingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, watumishi hawa ndio tunawategemea wasimamie fedha zetu, watumishi hawa ndio tunategemea wakakwamue maendeleo ya wananchi na wasimamie fedha na maendeleo ya wananchi. Lakini tunapowavunja moyo na kuwakatisha tamaa, malimbikizo mengine yanafika miaka kumi, mitano, sita mpaka mtumishi anakufa mrithi wake anakufa fedha hizi anapewa nani? Anakuja kupokea mtu ambaye hausiki kabisa hajamsaidia lolote yule mtumishi aliyetumia nguvu zake.

Mheshimiwa Spika, ukiwahoja halmashauri ni mkakati gani ambao wameweka kulipa watumishi hao mabilioni haya wanatenga fedha kidogo sana ambazo kwa kutenga fedha hizo inaweza ikachukua muda mrefu, takriban miaka kumi hajamaliza madeni.

Mheshimiwa Spika, tutafute hatua za haraka na dharura ili kuhakikisha tunapunguza angalau nusu ya madeni ya watumishi wetu ili watumishi hawa wasitumie fursa hii ya kuhujumu kwa sababu hawalipwi likizo, uhamisho, mishahara, na matibabu. Sasa ili wasihujumu, wasifiche mapato wafanya kazi zao kwa weledi na kwa uaminifu na wao stahiki zao zinatakiwa zilipwe kwa wakati. Wajibu unaendana na haki. Sasa, sasa, ili atekeleze wajibu wake mtumishi apate haki zake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naendelea. Kuna uvujaji mkubwa wa mapato katika halmashauri ambako hawakusanyi mapato kutoka kwenye vyanzo vingi, na hapa kuna upotevu mkubwa wa fedha za Serikali na fedha za umma. Kwa mfano kuna ushuru wa mazao, chanjo na machinjio ambako zaidi ya bilioni 14 hazikukusanywa kwenye baadhi ya halmashauri; tumeikuta katika ripoti ya CAG.

Mheshimiwa Spika, huu uvujaji wa mapato au kutokukusanya mapato kunaitia hasara kubwa Serikali, kwa sababu haya mapato tunayotaka kuyakusanya ndiyo tunatakiwa tuwalipe watumishi, tulipe vikundi, kufanyia shughuli nyingine za maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikiongezea hapo hapo kwenye ukusanyaji wa mapato, mfano ukusanyaji unaohusiana na kilimo, mifugo na uvuvi ndani ya halmashauri watenge percent ambayo itasaidia kuendeleza zile sekta, tuziziachie Wizara peke yake. Kule kuna uvuvi, kilimo, ufugaji, zitengwe fedha kwaajili ya kuongeza majosho, kusaidia uboreshaji wa kilimo na mabwawa. Hii ni kwa sababu ndio ushuru wa kilimo chenyewe au uvuvi na mifugo yenyewe. Kuonekane basi kuna faida kuendeleza kile kilimo katika ile halmashauri kwa sababu wanachukua fedha kutoka kwao hayo ni maoni kwa sekta zinazohusika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelea, kuhusu mfuko wa wanawake, vijana na wenye ulemavu, hili ni takwa la kisheria kupeleka 4:4:2, lakini baadhi ya halmashauri hawafikishi hiyo asilimia kwa hivyo vikundi, na inasababisha sasa kuzorota kwa ile azma ya Serikali ya kumkomboa mwananchi kiuchumi na kupunguza umaskini wa kipato. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hii mifuko kuna takriban bilioni 47.01 hazijakusanywa kwenye mamlaka 155, bilioni 47 hazijakusanywa kwenye mamlaka 155.

Mheshimiwa Spika, hapa inabidi tutafakari na tujiulize; kweli fedha hizi zitapatikana? Waliohusika na kupewa hiyo mikopo wapo? Hivyo vikundi viko? Uhakiki umefanyika ili kuhakikisha vikundi hivi viko hai na vinafanya uzalishaji? Kama vinafanya uzalishaji na havirejeshi mikopo basi ni suala letu sisi wahusika kufuatilia hiyo mikopo. Lakini kama baadhi ya vikundi havipo ni kwamba tuna haja sasa ya kuhakikisha fedha hizi zinakwenda kwa walengwa husika ambao wana miradi mahususi ya uzalishaji ili fedha hizi zirudi zikasaidie wengine katika kujikwamua na umaskini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano halmashauri badala ya kuwapa fedha wahakikishe vile vikundi wanavipa ujuzi kwanza ndipo baadaye wanavipa vifaa na vitendea kazi. Wavisimamie ili kuhakikisha wao wenyewe wananufaika lakini na Serikali fedha zake zinarudi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapo kuna baadhi ya halmashauri hawapeleki ile asilimia 40 na asilimia 60 kwenye miradi ya maendeleo. Hili ni takwa la kisheria, inatakiwa fedha ziende kama ilivyotakiwa ili kuimarisha miradi ya kiuchumi na miradi mingine ya kijamii katika halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikimalizia la mwisho nakuja kwenye uhaba wa watumishi, uhaba wa watumishi umejitokeza katika sehemu nyingi za halmashauri zetu. Hapa nitoe rai. Halmashauri itenge fedha za kusomesha na kuwajengea uwezo wale watumishi waliopo, wasisubiri tu uajiriwe na Serikali kuu ilete kwa sababu wao wana fedha na wana watumishi. Kwa mfano, kwenye sekta ya hesabu na sekta ya mambo ya kimtandao (TEHAMA). (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sekta hizi mbili ndiyo zinachangia sana kwenye uvujaji na upotevu wa mapato katika halmashauri, tukiweka wataalam, halmashauri ikiwa na mpango mkakati wa kusomesha watu wake wale wale walio ndani ofisini kuwajengea uwezo watu wa hesabu na TEHAMA hakutakuwa na upotevu na ubadhirifu mkubwa wa fedha wataweza kuweka hesabu zao sawa na kujua wanafanya nini.

Mheshimiwa Spika, naipongeza sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, nampongeza Mheshimiwa Rais, anajitahidi sana kuhangaika huku na kule kutafuta fedha kwa ajili ya wananchi wetu. Ni wajibu wetu sisi tumuunge mkono kuhakikisha fedha hizi zinatumika ipasavyo ili kuwaletea wananchi wetu maendeleo, na kuwapunguzia upungufu na umaskini wa kipato. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata nyumbani kama unahangaika kuomba, kukopa, unachuna uso unakwenda kwa ajili ya watoto wako, lakini watoto wakawa wanaharibu, hawatumii ipasavyo roho yako inanyonga, inaumia na inachukia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuwaunge mkono viongozi wetu wote waliopo madarakani kwa kuhakikisha kwamba tunawasaidia katika kuokoa fedha na katika kuwasaidia wananchi kuwaletea maendeleo.

Mheshimiwa Spika, ahsante, nakushukuru na naunga mkono hoja zote. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Awali ya yote napenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza kwa dhati kabisa Timu yetu ya Serengeti Girls kwa ushindi waliopata kwa kuwakilisha kwenye Kombe la Dunia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuipongeza sana Wizara hii ya utamaduni kwa kazi kubwa wanazofanya katika kuhakikisha sanaa, utamaduni, michezo vinaleta tija katika Taifa hili, lakini pia vinaleta tija kwa wanamichezo na wasanii wenyewe. Pia nampongeza sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa dhati kabisa kwa kupenda na kukuza michezo na vipaji vya wanamichezo mbalimbali, kuvithamini na kutaka vipaji hivyo viendelezwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naanza na mchango wangu katika eneo la lugha ya Kiswahili. Napongeza kwanza taasisi zote zinazojihusisha na uendelezaji na ukuzaji wa Kiswahili, zikiwemo BAKITA, BAKIZA, kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuendeleza Kiswahili ambapo kwa mchango wao huo umefanikisha leo Kiswahili kuwa lugha inayotumika kwa kazi kwa Afrika, lakini pia ni lugha ambayo inatumika kikanda na kimataifa. Nawapongeza sana. Kiswahili ni bidhaa, Kiswahili ni ajira, lakini Kiswahili ni utambulisho wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lugha ya Kiswahili imesheheni maneno mengi ambayo tumetohoa na mengine tumeazima kutoka lugha mbalimbali. Kiswahili chetu hiki kimeunganishwa na kutohoa maneno mbalimbali ikiwemo Kiingereza, Kijerumani, Kiarabu, Kiajemi, Kichina, Kijapani, Kigiriki, Kihindu ambapo Kihindu kuna Kihindu, kuna Punjab, kuna Hindu kuna Ghujrat yote haya yapo katika Kiswahili, tumetohoa na kuazima haya maneno. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutohoa na kuazima huko Kiswahili hiki kimetohoa kwenye vyakula, wanyama na kwenye mambo mbalimbali. Kwa mfano, nataka kutoa mifano michache tu, kwenye lugha ya Kihindi tumetoghoa chapati, fenesi, bagia, kachori, achari, karakana, madhubuti, tamasha, kitabu, pesa, meza, bangili, gari na mengineyo. Kiarabu tumetohoa ghali, amiri, dhambi, ridhaa, kasi, dhaifu, nafsi, kalamu, hifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiendelea kwenye Kijerumani tumetohoa neno soli. Kwenye Kigiriki tumetohoa neno lami, kwenye Kireno tumetohoa neno gereza, dama, lakini kwenye Kiajemi tumetohoa bahati, bahati nasibu, jambazi, balungi, hili balungi ni tunda. Kijapani tumetohoa judo, kichinchiri, kichinchiri maana yake ni kitoto kidogodogo kinachokuakua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna maneno tumetohoa ambayo yanaingiliana na lugha nyingine. Mfano, soko Kiswahili lakini Kihindi ni sok na Kiarabu ni suuq. Kiswahili dua, kiarabu dua, kihindi dua. shukurani Kiswahili, shukria Kihindi, lakini shukra Kiarabu na mengi mengineyo kama madarasa, madras na madrasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nataka kujenga hoja, kwenye Kingereza tumetohoa penseli, pencil, baskeli, bicycle, ringi, ring na mengi mengineyo, hayo ni machache tu. Ninachotaka kusema tunataka kutumia Kiswahili kwa kuunganisha na kuongeza utalii nchini. Utalii nchini kwa kutumia Kiswahili, wanaotaka kujifunza Kiswahili wanakuja nchini na wengine wanataka Walimu wapelekwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hoja yangu ni hapa, kilio huanza mfiwa ndipo na wa mbali akalia, lakini pia, kibaya chako si chema cha mwenzako, tutukuze Kiswahili chetu. Kiswahili ni hazina, Kiswahili ni rasilimali ya nchi, tukikitumia vizuri, tukikiendeleza vizuri tutapata tija kubwa kupitia lugha yetu ya Kiswahili duniani na kuitangaza nchi yetu ya Tanzania tukiunganisha na kutangaza utalii wa nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa ninachotaka kusema katika kukiendeleza Kiswahili, tujitahidi basi tutumie lugha nyepesi, lugha ambayo inaweza kusomeka, kuandikika na kujifunza. Nimetoa mifano kwamba, hapa tumetohoa, mfano neno television linatumika karibu ulimwenguni kote television; Sudan television, Comoro television, Kifaransa télévision. Sasa maneno kama haya, tujaribu ndio tunataka tutumie maneno yetu ya kibantu, maneno yetu ya asili, lakini tutumie maneno mepesi kwa sababu kuna maneno tunayatumia sasa hivi hata mimi Mswahili nafikiri vile kitu gani vile? Nafikiri, nikishindwa natumia lile la Kiingereza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa lugha isiwe ngumu. Zamani lugha yetu inasema lugha nyepesi, mwananchi au wageni wanaifahamu kwa urahisi zaidi. Kwa hivyo, tuendeleze, tutohoe pia maneno yetu ya kibantu, lakini mengine ambayo ni magumu sana tumeyasahau, sitaki kuyataja hayo maneno yanajulikana, magumu. Unakifikiri kitu mara tatu, vile nini, vile nini? Hata ukilipata. Sasa hapa tuboreshe Kiswahili kiwe chepesi lugha inayoweza kuzungumzika ili kujenga ule uimara na watu kuja kujifunza kwa wingi Kiswahili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Kiswahili tunataka kiwe kama ajira, nashauri vijana wetu wajifunze lugha zaidi ya mbili kwa maana ya Kiswahili, achanganye Kiingereza na Kifaransa au Kiswahili, Kingereza na Kihispania, ili lile soko la ajira la ukalimani, soko la ajira la kusomesha, liwe linapatikana kwa urahisi kwa vijana wetu kujua lugha zaidi ya mbili au tatu. Hiyo itasaidia zaidi kukitangaza Kiswahili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiendelea na mchango wangu napongeza sana wasanii hapa nchini kwa kazi kubwa mbalimbali wanazofanya kuhakikisha sanaa inakua. Nashauri Serikali iendelee kuinua na kuibua vipaji vipya na kuviendeleza, lakini katika kuinua vipaji vipya hivyo tuangalie na sheria hasa kule kwenye halmashauri kuna sheria nyingi zinakandamiza wasanii wasije juu kwa sababu ya kodi na ushuru mkubwa au malipo makubwa ya vibali kwenye halmashauri. Msanii ndio kwanza anataka kuanza anaambiwa lipa 70,000, ndio kwanza, atajitangaza vipi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuweke muda maalum, kikundi kimeshakua, baadaye tuwatoze hizo kodi au tuwatoze hizo tozo, ili tuibue vikundi, kuwe na motisha fulani ya kuibua vile vipaji tuviendeleze. Vinaibuliwa vingi, lakini vinaishia hukohuko chini, wakati mwingine ni sheria tu kandamizi ambazo hazitaki kuinua vipaji vya wasanii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiendelea hapo sekta ya utamaduni. Utamaduni ni mpana sana, ni mpana kwa maana binadamu anapozaliwa anazaliwa kwenye utamaduni, analelewa kwenye utamaduni, anakuwa kwenye utamaduni, harusi ni utamaduni, mpaka anazikwa binadamu anazikwa kwenye utamaduni kutokana na eneo husika na nchi husika. Kwa hivyo, suala la utamaduni ni utambulisho mkubwa wa nchi, tunataka kuliendeleza ili liendelee kuitangaza nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiendelea kuwapongeza wasanii, kuna suala moja linajitokeza, haki miliki. Wasanii wetu haki miliki zao bado zinadhulumiwa, kwa maana kuna nchi au mataifa wanatumia nyimbo zao wanazibadilisha lugha, lakini mdundo, muziki ni uleule, wimbo ni uleule na wanapata fedha nyingi kupitia hizo nyimbo zetu za Watanzania wetu wakiwemo akina Diamond na wenzake, tulinde haki zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano kuna wasanii wa zamani wa nyuma wameimba nyimbo nyingi, lakini zinaimbwa na sasa hivi, anaonekana mmiliki ni yule wa sasa hivi, lakini kumbe ile nyimbo ni ya zamani na imetungwa zamani. Tuweke kumbukumbu wimbo huu umetungwa lini? Muimbaji alikuwa nani? Aliyetia sauti ni nani? Aliyetunga shairi ni nani ili kizazi na kizazi kiweze kujua wimbo huu ulikuwa ni wa nani? Hata kama utaimbwa tena mara ya tatu, mara ya nne, basi mmiliki awe na haki zake kwa uhalisi wake anapata zile kutokana na jasho lake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sanaa tunaipenda. Tunasikia wasanii mara wanafungiwa, hivi, nataka niongee kidogo tu; mimi niliwahi kutumikia chombo cha sanaa, niliwahi kuwa Naibu Mkurugenzi Idara ya Sanaa Zanzibar, tulikuwa na chombo kinaitwa Sensor Board, muziki, shairi lolote kabla halijatoka linakwenda kwenye Sensor Board kwanza. Hii inaifanya taasisi ya muziki ule wasipate hasara baadaye ya kuja kufungiwa muziki wao, lakini inataka mashirikiano ya pamoja kati ya wasanii na hivi vyombo. Wawe wakweli na wa wazi kupeleka mashairi yao, maudhui yao, ili wasije wakafungiwa na kupata hasara isiyokuwa ya lazima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mambo yanaepukika. Tujitahidi kuwaonesha sanaa zenye kupendeza, lakini…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Wizara iwasaidie wakulima wa mazao ya baharini:-
(i) Kuwatafutia masoko ya uhakika wakulima wa zao la mwani;
(ii) Kusaidia kuwapatia elimu juu ya mbegu bora ya mwani inayokubalika katika masoko ya nje ya nchi; na
(iii) Kuhamasisha wawekezaji wawekeze katika kujenga viwanda vya usindikaji wa mazao ya bahari, mfano mwani na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara iongeze juhudi katika kudhibiti uingizaji wa bidhaa zisizo na ubora unaokubalika kwa matumizi na zinazohatarisha maisha ya mtumiaji na hasa bidhaa za chakula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uanzishaji wa viwanda uzingatie ujenzi wa viwanda visivyoharibu mazingira, malighafi zake ziwe zinapatikana hapa nchini, Wizara iweke vipaumbele vya aina ya viwanda tutakavyoanza navyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho napongeza juhudi za Wizara katika juhudi zake za kufufua viwanda na kuanzisha vipya kwa nia ya kuongeza pato la Taifa na kupunguza tatizo la ajira kwa wananchi na kuweza kunyanyua hali zao za maisha. Ahsante.
Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa pongezi kwa Mheshimiwa Waziri na uongozi wote wa Wizara na taasisi zake na wasanii wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sanaa za kazi za mikono na sanaa za ufundi zipewe msukumo zaidi ili kuwawezesha vijana wengi kutengeneza na kujifunza sanaa hizo ili waweze kujiajiri na kupunguza umaskini wa kipato pamoja na kuongeza Pato la Taifa. Maigizo na filamu zinazokiuka maadili ya Mtanzania zisiruhusiwe kuoneshwa katika jamii ili kupunguza mmomonyoko wa maadili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lugha ya Kiswahili ipewe msukumo zaidi ili Kiswahili kiweze kuwa ni mojawapo ya lugha yenye nguvu na iweze kuzungmzwa na nchi nyingi duniani. Hivyo itapelekea Watanzania kupata ajira zaidi katika kufundisha lugha ya Kiswahili. Pia Kiswahili kitaongeza umaarufu wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa juhudi zake za kuhakikisha Wizara inatekeleza majukumu yake kama inavyotarajiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utalii naishauri Wizara iweke mkakati madhubuti katika kudhibiti mapato yatokanayo na utalii. Watalii wanaotembelea Tanzania walipie hapa nchini kuepusha upotevu wa mapato. Elimu na matangazo juu ya vivutio vya utalii vilivyopo nchini ipewe kipaumbele ili kuongeza idadi ya watalii kuitembelea Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu misitu, upandaji wa miti uwe mara mbili zaidi ya miti inayokatwa. Nishati mbadala ya kupikia itasaidia kupunguza matumizi ya mkaa ambapo itasaidia kupunguza miti kuchomwa kwa kutengeneza mkaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, usafirishaji wa mbao nje ya nchi udhibitiwe zaidi pamoja na kupunguza kiwango cha mbao zinazosafirishwa nje ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vibali vya ukataji na uvunaji miti katika mashamba ya miti, kwa mfano SAO Hill na kwingineko upatikanaji wake ni wa shida sana, hata muombaji aliyetimiza masharti yote. Kuna upendeleo na wanyonge ni shida sana kupata vibali hivyo. Nashauri upangwe utaratibu mzuri katika utoaji vibali vya uvunaji miti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na nawatakia kazi njema.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naipongeza Wizara kwa kazi nzuri ya kuitangaza Tanzania. Nina ushauri ufuatao:-
(i) Abiria wanaosafiri nje ya nchi wakaguliwe kwa uhakika ili kudhibiti Watanzania kukamatwa na madawa ya kulevya;
(ii) Wizara itenge fedha kwa ajili ya dharura kwa Balozi zetu kwa madhumuni ya kuwasaidia Watanzania wanaofika Ubalozini kuomba wasaidiwe baada ya kupata matatizo makubwa huko ugenini; na
(iii) Ofisi ya Makao Makuu ya Kiswahili ipewe vitendea kazi na fedha ili ifanye kazi zake kwa umahiri mkubwa ikiwa ni pamoja na kukitangaza Kiswahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namtakia Waziri kazi njema katika kutekeleza majukumu yote.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza utendaji kazi mzuri kwa Viongozi na Watendaji wote wa Wizara na Taasisi zake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TTCL, iimarishwe zaidi kwa vitendea kazi vya kisasa ili iweze kufanikisha malengo yake kwa kufikia kutoa huduma za mawasiliano katika maeneo na vijiji vyote ndani ya Tanzania kwa ufanisi mkubwa. Mitandao ya simu ya Tigo, Airtel, Vodacom haina nguvu katika baadhi ya maeneo na maeneo mengine mawasiliano hakuna kabisa huko Zanzibar, hivyo waongeze nguvu ili wateja wapate huduma katika sehemu zote huko Zanzibar mfano, Chukwani, Mji Mkongwe na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi za Serikali na Taasisi zake watumie huduma za simu za TTCL pia wahimizwe kulipa madeni kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Posta, liongeze nguvu na kujipanga zaidi katika huduma ya kusafirisha pesa na kupokea fedha kwa njia ya haraka ili watu wavutike kutumia huduma yao badala ya kutumia mawakala wengine wa kupokea na kupeleka fedha nchi mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja. Nawatakieni kazi njema na nguvu katika kutekeleza majukumu ya kuwatumikia Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Kwanza kabisa na mimi napenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza Wizara ya Ulinzi, Mheshimiwa Waziri na jopo lake lote, napenda pia kuwapongeza Mkuu na Wakuu wa Majeshi yote ya Ulinzi na Usalama wa Tanzania kwa kazi nzuri wanayoifanya ya ulinzi wa raia na Tanzania kwa jumla ndani na mipaka yote ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kuanza kuchangia sasa hivi ni kuhusu kuvamiwa kwa maeneo ya kambi za Jeshi. Kama ilivyoelezwa na Wajumbe waliotangulia, kambi zetu nyingi zimevamiwa na maeneo ya raia. Nataka kuishauri Wizara yako Mheshimiwa Waziri tuangalie kambi ambazo zimeathirika sana na kuvamiwa na raia, tuombe Serikali tubadilishe maeneo ya kambi tupeleke maeneo mengine ambayo yapo nje zaidi na maeneo ya wananchi. Hayo ni kwa sababu ya kunusuru maisha ya wananchi waliozunguka katika maeneo yale, lakini pia usalama wa jeshi lenyewe, pamoja na vifaa vilivyokuwemo ndani ya kambi za Jeshi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumzie kidogo kuhusu mapato yanayopatikana na shughuli za utendaji katika majeshi. Naomba Wizara yako kwa kupitia Wizara ya Fedha kama kuna mapato yanazalishwa na majeshi yanakwenda Serikalini, basi iwekwe percent kidogo ibakie pale ili waweze kujiendesha kwa shughuli nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa limezungumzwa suala la wanajeshi wastaafu kuwa waganga wa kienyeji. Baada ya mtu kustaafu kazi ya aina yoyote, ana uhuru wa kufanya analolitaka; na uganga wa kienyeji ni fani, siyo kila mtu anaweza. Kama mtu ana fani yake, sheria haimbani kuwa mganga wa kienyeji, kuwa mshona cherehani, kuwa mtengeneza baiskeli, kuwa fuundi makenika, anaweza! Huo ni uhuru wa raia kufanya anachokipenda! Katika uganga wa kienyeji huo anapata mapato mengi kuliko mimi ninayefanya kazi Serikalini nilivyokuwa kwa wakati huo. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, nami nizungumzie kidogo suala hili la majeshi kwenda Zanzibar, kubakwa kwa demokrasia, kuingilia uchaguzi. Ninachosema, Jeshi la Wananchi wa Tanzania ni Jeshi la Wananchi wote wa Tanzania kama jina lake lilivyo. Lina uhuru na lina haki ya kikatiba ya kufanya kazi popote ndani ya Jamhuri ya Tanzania kuanzia Kigoma mpaka Kisiwa Panza mpaka Tumbatu na kazi ya ulinzi ni kazi ya jeshi hili. Kwa wale ambao hawakufurahishwa na kitendo kile, mimi nawahesabu ndiyo wale ambao walikuwa wanataka kuhatarisha amani ya nchi. Kwa sisi ambao tulikuwa tunataka tuwe huru, tufanye uchaguzi kwa amani, tulifurahi sana kuwepo kwa jeshi letu la ulinzi wa Tanzania kuja kutulinda. Wananchi walifurahi, walikuwa wako huru, hawana mashaka kama walivyokuwa mwanzo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya Zanzibar ilikuwa inajulikana, wakati wa uchaguzi hali ilikuwa tete, wananchi wanaogopa hata kwenda kununua sukari nje, wanashindwa. Kila asubuhi kukicha unasikia milipuko Kibanda Maiti; milipuko Darajani; milipuko, kumezungushwa uzio. Hivi ninyi mlikuwa mnataka kufanya nini hasa? (Makofi)
Mimi nauliza kulikuwa kuna nia gani na nchi yetu hata leo imekuwa jeshi kila mahali linazungumzwa. Jeshi nalipongeza wamefanya kazi nzuri, wameilinda Zanzibar kama sehemu ya Jamhuri ya Muungano ambayo ni wajibu wao na wamelinda raia wa Zanzibar kama ni raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Napenda kulipongeza kwa dhati jeshi letu liendelee na juhudi zake hizo za kulinda amani ya nchi na nchi yetu ya Tanzania kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, uchaguzi wa Zanzibar umefanyika kwa kufuata sheria zote za uchaguzi za Zanzibar. Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein ndiye Rais wa Zanzibar, ataiongoza Zanzibar kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. Nawashauri, tunasikia maneno mengi hapa kuhusu uchaguzi wa Zanzibar, lakini kama kweli walikuwa na nguvu ya umma inayowakubali kwa nini walikataa kuingia kwenye uchaguzi na wao wana mtaji wa kutosha? Kwa nini wamekataa mechi ya marudio? Kama kweli wana mtaji wa kutosha wa wapiga kura, ilikuwa hakuna sababu ya kukataa kuingia kwenye uchaguzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Zanzibar …
TAARIFA....
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Naibu Spika, siipokei kwa sababu kazi ya jeshi ni ulinzi wa nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kidogo suala la ajira. Naomba kama yalivyozungumzwa, hawa vijana waliokwenda kupata mafunzo ya JKT ndio wafikiriwe kwanza katika ajira za jeshi. Pia napenda kushauri kwamba hili jeshi letu la JKT ligawe aina ya mafunzo. Kuwe na mitaala ambayo inawahusisha wanafunzi wa vyuo wanapokwenda kupata mafunzo yawe ya aina nyingine na mafunzo ya vijana wanaoandaliwa kuwa wanajeshi au askari yawe ya aina nyingine kwa maana kwamba hapa tutaepuka kuwafundisha mambo yote ya kijeshi vijana ambao baadaye watakwenda kuajiriwa kwenye taasisi nyingine za umma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu nyumba za askari wetu wa Jeshi, na mimi nasisitiza kwamba awamu hii nyumba zijengwe Unguja. Nashauri kutokana na uhaba wa ardhi wa Kisiwa cha Unguja, basi sijaona ramani zao lakini nashauri nyumba hizi zisiwe nyumba ndogo ndogo badala yake ziwe nyumba za ghorofa ili kutumia eneo dogo kwa nyumba nyingi na baadaye eneo litakalobaki huko mbele lije litumike kwa nyumba nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jeshi letu ni kubwa, limekua, tofauti na jeshi la mwaka 1964 na 1967. Kwa hiyo, kwa sababu jeshi letu limekua, lazima kutakuwa na mahitaji mengi na changamoto nyingi. Kwa hiyo, la kufanya tu ni Serikali kuongeza bajeti katika jeshi hili katika Wizara hii na ifikirie zaidi kutatua matatizo mbalimbali ya Wanajeshi wetu na hasa wakati wa kustaafu walipwe viinua mgongo vyao kwa wakati muafaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nami napenda kuipongeza Wizara hii ya Mambo Nchi za Nje kwa juhudi kubwa inayofanya pamoja na Mabalozi wetu walioko nchi za nje wanaoiwakilisha Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli Balozi zetu zilizoko nchi za nje zinafanya kazi kubwa wakati fedha zinazopelekwa ni chache ukiachilia mbali kucheleweshwa kwa baadhi ya mahitaji yao. Pia Balozi zinafanya kazi kubwa kuwapokea Watanzania wanaopata matatizo wakiwa nje ya nchi mfano kama Oman, India, Marekani, Uingereza ambapo wengi wao huenda kwa sababu zao binafsi kama kutafuta ajira baadaye kutelekezwa na waajiri wao, wengine wanakwenda kwa matibabu wanaishiwa fedha na wanakimbilia kwenye Balozi zetu za Tanzania na Balozi zinafanya kila jitihada kuhakikisha wananchi hao wanarejea Tanzania. Napenda kuzipongeza sana Balozi zetu zilizoko nchi za nje kwa uvumilivu wao huu na upendo kwa Watanzania wenzao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri tumearifiwa kwamba Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki imehamia rasmi Zanzibar. Mimi napenda tu kusisitiza kwamba Kamisheni hii ipewe kipaumbele cha vitendea kazi ili iweze kufanya kazi zake vizuri. Kwa sababu kwa kutumia lugha yetu ya Kiswahili tutaongeza ajira kwa vijana wetu, pato la Taifa na tutaitangaza nchi yetu Tanzania duniani kote. Kwa hivyo, kuamua Kiswahili makao makuu yake kuwa ndani ya nchi yetu ya Tanzania ni fahari kwetu sote Watanzania katika umoja huu wa Afrika Mashariki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ninalotaka kuliongelea sasa hivi ni elimu juu ya fursa za kiuchumi na biashara katika masoko ya Afrika Mashariki. Wananchi wetu wa Tanzania wengi hawaelewi ni mbinu gani na njia gani za kufanya biashara katika masoko hayo ya Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ninalotaka kulizungumza hapa kwa mashirikiano ya pamoja kwa Wizara hii ya Mambo ya Nje na Wizara ya Mambo ya Ndani kuhakikisha wanadhibiti wasafiri Watanzania na abiria wengine wanaopitia Tanzania kupitia viwanja vyetu vya ndege kwa usafirishaji wa madawa ya kulevya. Tatizo hili linalipa aibu sana Taifa letu wanapokwenda nchi za nje tukaambiwa watu hawa wametokea Tanzania au ni raia wa Tanzania. Udhibiti ufanyike pale kwenye viwanja vyetu vya ndege, madawa haya ya kulevya yasitokee nchini kwetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoomba kwa Mabalozi wetu walioko nchi za nje watumie fursa hiyo kuitangaza Tazania na kutafuta mialiko mbalimbali kama matamasha ya kiutamaduni na biashara yanayokuweko katika nchi hizo wawalete Tanzania ili wananchi wetu waweze kufika huko. Hili nina ushahidi nalo kwa sababu mimi mwenyewe nilishawahi kuwa Naibu Mkurugenzi wa Utamaduni na Mambo ya Sanaa nilikuwa natafuta mwenyewe mialiko kwa viongozi na wasanii kutoka Zanzibar kwenda kuitangaza Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapofika katika baadhi ya Balozi na vikundi vyangu vya utamaduni hata wao wanakuwa hawaelewi kwamba kuna fursa za namna hiyo katika nchi zao. Kwa hiyo, ninachoomba wafanye utafiti na wawe wanatafuta mialiko kama hiyo ya maonesho mbalimbali ili Watanzania waweze kushiriki na kuitangaza nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Spika, kwanza naipongeza Serikali na Wizara kwa ujumla katika juhudi zake za kuendeleza michezo, sanaa na utamaduni nchini. Serikali iweke mkazo zaidi katika kuipa nguvu lugha ya Kiswahili kwa kutumia lugha hii katika shughuli na hafla mbalimbali za kitaifa na kimataifa ili lugha yetu hii iweze kuongeza idadi ya watumiaji na pia kuongeza soko la ajira kwa Watanzania.

Mheshimiwa Spika, utamaduni; Serikali iendelee na juhudi za kutoa elimu kwa wananchi juu ya mila potofu zinazoathiri afya za wananchi. Serikali iendelee na juhudi za kutoa elimu kwa wananchi juu ya tamaduni zinazokandamiza wanawake, watoto na jamii kwa ujumla. Wasanii wapewe elimu ili wasiitumie sanaa kudhalilisha wanawake kwa mavazi yasiyoendana na maadili ya Mtanzania.

Mheshimiwa Spika, TBC iongezewe nguvu ya vitendea kazi, rasilimali fedha, watumishi wa kutosha ili redio na TV ziweze kusikika na kuonekana nchi nzima.

Mheshimiwa Spika, ahsante na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri na Wizara kwa ujumla katika utekelezaji wa kazi za kuendeleza utalii hapa nchini Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni/ushauri; Wizara iendelee na kazi ya kuibua vyanzo vipya vya utalii na kuvitangaza duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Tanzania Forest Fund (TFF), Kamati iliyoundwa kuangalia jinsi ya kutoa fedha za utafiti wa kuendeleza misitu Tanzania, uhifadhi wa misitu na viumbe wadogo wadogo kuna malalamiko kwamba wanaopewa fedha hizo baadhi yao hawakidhi vigezo na baadhi hawajishughulishi na shughuli hizo kabisa. Nashauri ufuatiliaji wa karibu juu ya fedha hizo za Serikali zilizotolewa kama zimetumika zilivyokusudiwa. Kabla ya kutolewa fedha hizo ukaguzi ufanyike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nawatakia utekelezaji mwema wa majukumu yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Na mimi napenda nikuunge mkono kwa kazi yako unayoifanya ya kusimamia sheria na kanuni zetu za Bunge. Endelea kusimamia sheria na kanuni za Bunge ili kulinda heshima ya Bunge letu. (Makofi)
Napenda kuchukua nafasi hii kuipongeza Wizara ya Fedha, Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na viongozi wote wa Wizara hii kwa juhudi zao za kuhakikisha nchi yetu inapiga hatua za maendeleo. Naomba niwatie moyo, endeleeni na kazi, sisi tuko nyuma yenu kuwasaidia pale ambapo panahitajika kutoa msaada wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kutoa mchango wangu kwenye Tume ya Pamoja ya Fedha. Napenda tu kutoa msisitizo kwamba Tume hii ifanye kazi zake na kama kuna upungufu urekebishwe na kama kuna upungufu wa watendaji basi nafasi hizo zijazwe ili Tume hii ifanye kazi yake vizuri na kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie kuhusu mashirika ya Serikali kama NIC na TTCL. Haya ni mashirika yetu ya Serikali lakini hali yake siyo nzuri kiutendaji na katika ukusanyaji wake wa mapato au kupata mapato. Ni vyema sasa taasisi za Serikali ikayatumia mashirika yetu ya Serikali ili kuongeza mtaji na fedha zaidi katika mashirika hayo. Mfano TTCL, taasisi zote za Serikali zikitumia mitandao hii ya TTCL nafikiri tutaweza kuwaongezea mtaji wa kuendesha shughuli zao na litaanza kunyanyuka pamoja na mashirika mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna taasisi ambazo zinafanana katika shughuli zake za utendaji mfano TRL na RAHCO, TBS na Weights and Measures Agency. Hebu Serikali sasa iangalie taasisi za namna kama hiyo ambazo kazi zake zinafanana au zinakaribiana iziunganishe ili zifanye kazi kwa pamoja na kwa ufanisi zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie kuhusu ukusanyaji wa mapato katika bandari bubu. Ni kweli kabisa fedha nyingi zinapotea katika bandari bubu. Kwanza ni kuziorodhesha bandari zote bubu za Tanzania na baadaye kujua ni mbinu gani ambazo wanatumia katika kupitisha bidhaa. Kwa kufanya hivyo tutaweza kudhibiti upotevu wa mapato na bidhaa za magendo. Kwa kupitia bandari bubu si ukwepaji tu wa kodi uliopo huko bali pia zinatumia kupitisha bidhaa ambazo haziruhusiwi mfano nyara za Serikali zinapitishwa na zinakwenda katika maeneo mengine na zinasafirishwa. Mfano, zinaweza zikapitishwa bandari bubu za Tanga na Zanzibar na kusafirishwa huko zinakokwenda kama China na kwingineko. Kwa hivyo, ulinzi na ukaguzi madhubuti ufanyike katika bandari bubu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi natilia mkazo Sheria ya Manunuzi kama wenzangu walivyoiongelea, iletwe hapa ili ifanyiwe marekebisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitilie mkazo kuongezewa mtaji Benki ya Kilimo kwa sababu benki hii kutokana na mpango kazi wake imejipanga kwenda katika mikoa yote ya Tanzania. Tatizo lao ni mtaji wa kufika na kufungua ofisi katika mikoa yote ya Tanzania. Kama itaongezewa mtaji itaweza kuwafikia wananchi wote huku waliko ili kuwasaidia wananchi katika miradi midogo midogo ya kilimo, uvuvi, ufugaji na mingineyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine tutilie nguvu ukwepaji wa kodi, najua hili mnalifanyia kazi. Nataka kuuliza, kulikuwa na uwakala wa ukusanyaji wa VAT kati ya Tanzania Bara na Visiwani kila mmoja ni wakala wa mwenzake. Sasa sijui mpango huu mpaka sasa unaendelea au umesimama? Pia naomba tudhibiti mfumko wa bei, kila kukicha mfumko wa bei unakuwa mkubwa na unakuwa mzigo mkubwa kwa wananchi katika kununua bidhaa za kujikimu kimaisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni hii Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Mifuko hii ni vema ikaangalia masharti ya wanachama wake ili kupunguza baadhi ya masharti ili isiwe mzigo kwa wananchama wa mifuko hii. Mfano umri wa kulipwa pensheni wakati wa kustaafu inamlazimisha mwanachama lazima afikishe miaka ile waliyoitaka wao na pengine kungekuwa na nafasi ya kustaafu mapema akalipwa haki zake angeweza kustaafu na nafasi zile zikajazwa na vijana wengine ambao wanataka kuajiriwa. Kwa kipengele hicho kinafanya mtu abakie tu kusubiri kulipwa pensheni kwa sababu kama hukufikisha umri huo huwezi kulipwa pensheni yako. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nisisitize kuhusu ukusanyaji wa mapato kwa jumla. Naomba wafanyabiashara wahamasishwe zaidi kutumia hizi mashine za kieletroniki na mashine hizi zisiwe kwa baadhi tu ya watu, ziwe kwa wafanyabiashara wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja, nawatakia kheri katika ufanisi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali, Wizara ya Elimu na viongozi wote wa Wizara ya Elimu kwa juhudi kubwa za kuendeleza elimu nchini kwa manufaa ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na waliopendekeza watoto wa kike wanapopata ujauzito wakiwa bado wanafunzi waruhusiwe kurejea shuleni baada ya kujifungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ya watu wazima iimarishwe zaidi ili kuwasaidia wale vijana walioacha shule mapema na waliokosa kwenda shule kwa sababu mbalimbali zikiwemo umaskini wa familia zao.


Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ya ufundi ipewe nguvu na shule za ufundi zipatiwe vifaa vya kisasa ili wanafunzi wanapomaliza waweze kujiajiri, pia waweze kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja na nawatakia kazi njema.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kwa dhati kabisa kuwapongeza Viongozi wetu Wakuu wa nchi, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Viongozi wote wa Serikali pamoja na Wizara hii ambayo leo tunajadili bajeti yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mazingira ni suala pana na linahitaji mbio za haraka ili kunusuru nchi yetu. Kama lilivyoelezwa na Wizara yenyewe na hatua mbalimbali ambazo wanachukua napongeza kwa jitihada hizo ziendelee na wazo la kuongeza fedha katika bajeti ya Wizara hii ni muhimu kwa sababu ndiyo urithi wa nchi yetu na vizazi vijavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, historia ya Muungano ni pana, hivi sasa vizazi vingi tuliopo tumezaliwa baada ya Muungano. Kwa mantiki hiyo, vijana sisi ambao wengi wetu ni raia wa Tanzania tunaoishi sasa tunaupenda na tuko tayari kuupigania kwa nguvu zote Muungano wetu huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nigusie changamoto za Muungano. Nashauri changamoto za Muungano pale zinapotatuliwa zitangazwe bayana kila mwananchi azielewe, kwa sababu ni changamoto nyingi zimefanyiwa marekebisho na zimeshafanyika kazi lakini bado wananchi hawaelewi. Nasisitiza pia ushirikiano wa sekta ambazo siyo za Muungano, kwa sababu raia wa nchi mbili hizi au wa Jamhuri ya Muungano wanatumia fursa mbalimbali kwa nchi zote mbili Zanzibar na Jamhuri ya Muungano kama hospitali, elimu na mengineyo, pamoja na utamaduni na mila zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa jina la sasa Tanzania una umri wa miaka 53, ni chombo muhimu sana kwa maisha na maendeleo ya Watanzania na hasa Wazanzibari wapenda amani, utulivu na maendeleo. Yeyote anayebeza au kudharau Muungano huu na kuwa hautakii mema tunamjua ni mmoja katika maadui wa nchi yetu. Dunia, Afrika na majirani zetu wanafahamu kwamba Tanzania ni nchi ya amani na hususan ikiwemo Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Muungano huu na Mapinduzi ya Zanzibar, majaribio mengi ya vitimbakwiri yalifanyika kutaka kudhoofisha au kuondosha kabisa, lakini kwa uimara wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Muungano wa Tanzania majaribio hayo yameshindwa. Moja kati ya jaribio hilo ambalo limeshindwa lilisababisha kifo cha muasisi wa Mapinduzi na Muungano Mheshimiwa Abeid Amani Karume, lakini kwa uimara wa Serikali zetu majaribio hayo yameshindwa na yataendelea kushindwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie miradi ambayo inatokana na fedha na mambo yanayohusu Muungano. Naomba nichukue nafasi hii kwa kifupi sana kwa wale wasiofahamu umuhimu na maendeleo ya Muungano. Kwanza ni ulinzi na usalama, hilo sina shaka nalo ni faida moja ya Muungano, nikigusia kwenye elimu kuna miradi mikubwa ya uanzishwaji wa shule za sekondari 19 pamoja na ujenzi wa Chuo cha Benjamin Mkapa kule Pemba, hizo ni faida za Muungano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukarabati wa shule sita za sekondari zikiwemo shule tatu zilizomo katika Jimbo la Mheshimiwa Ally Saleh shule ambazo ni Forodhani, Hamamni na Tumekuja, zimo ndani ya Jimbo moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Mifuko hii ya Muungano tumepata mafunzo ya Walimu ambapo jumla ya Dola za Kimarekani milioni 42 zilitumika kwa mkopo wa Benki ya Dunia zilizokopwa na SMT. Pia kuna dola milioni 10 kwa ujenzi wa school mpya sita Unguja na nne Pemba. Hayo ni matunda na mafanikio ya Muungano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hayo tu, kuna miundombinu ya barabara ikiwemo Mkapa road Mkoa wa Mjini Magharibi, kuna barabara Pemba zilizojengwa kwa Mfuko huu wa Muungano.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi juzi tu tarehe 4 Julai, Mkopo wa India wa USD 92.1 milioni kwa ajili ya mradi mkubwa wa maji Mkoa wa Mjini Magharibi. Pia kuna uimarishaji wa miundombinu ya maji mijini na vijijini kwa mkopo wa ADB wa dola milioni 21. Pia tumesikia leo miradi ya mazingira kupitia TASAF na mifuko mingineyo kuhifadhi mikoko, ujenzi wa kuta, kuzuia bahari, bahari inakula visiwa vyetu lakini Mifuko ya Muungano inakwenda kusaidia kulinda bahari isile visiwa vyetu kule Zanzibar. Pia kuna miradi mikubwa ya mikopo ya SMT ndiyo inayodhamini Zanzibar pale ambapo itashindwa SMT inalipa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tulivyoona Mifuko ya TASAF imesaidia wajasiriamali wetu wadogowadogo, pia imesaidia masoko, ujenzi wa vituo vya afya na zahanati, imesaidia kaya maskini, yote hayo ni matunda na faida za Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijamaliza naomba niunge mkono hoja kwa asilimia mia moja. Muungano wetu imara tutaulinda, tutaudumisha, kwa maslahi wa wananchi wote wa Tanzania, vizazi vya sasa na vizazi vijavyo. Dunia inaona, Afrika inaona na sisi tuko imara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha ahsante sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Naibu Spika. Awali ya yote, nachukua nafasi hii kuwapongeza kwa dhati sana Mawaziri wetu wawili hawa; Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara ya Maji kwa ufuatiliaji wao wa karibu na kutenda kazi kwao kwa umakini katika kusaidia Taifa letu kuondokana na shida ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ni moja kati ya nchi tano za Afrika zenye wingi wa maji na maji yanayofaa kwa matumizi ya binadamu. Tatizo letu labda ni kwenye changamoto za utaalam na rasilimali fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nijielekeze kwenye hii taasisi ya Wakala wa Uchimbaji Visima na Mabwawa (DDCA). Hii ni taasisi ya Serikali, unapokuja ushindani mara nyingi wanashindwa kwa sababu wana bei zao ambazo zimewekwa kwa kiwango.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachoshauri ni kwamba Halmashauri zetu zitumie hii Mamlaka ya DDCA katika uchimbaji wa visima na mabwawa, kwa sababu hawa wana utaalam wa kutosha na pindi wamechimba kwa bahati mbaya maji hayakutoka, huwa hawadai malipo. Taasisi binafsi wanatuchimbia visima na mabwawa na baadaye wanadai malipo na maji huwa hayatoki. Nashauri iongezewe nguvu na vifaa vya kisasa kabisa ili zile kanda ambazo wameweka ziweze kufanya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakwenda kwenye mfuko wa maji. Nami nakubaliana na waliotangulia kwamba ile shilingi 50 sasa iongezeke kwenye bei ya mafuta, ya kukatwa kwenye mafuta, ile tozo ili ifikie shilingi 100.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naishauri Serikali iangalie zaidi kwenye simu. Kwenye simu kuna fedha nyingi sana, tuangalie vyanzo vingine vya kuongeza huu mfuko na tuangalie haya Mashirika ya Simu. Mashirika ya Simu yanaingiza fedha nyingi, lakini wanavyowekeza kwenye maendeleo ya wananchi ni kidogo. Katika huu Mfuko wa Maji nashauri kwamba vijijini wapewe asilimia kubwa ili kuimarisha miundombinu ya maji huko Vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ninaloliona hapa kwenye VAT ni katika madawa ya kutibu maji. Kwenye madawa ya kutibu maji hii VAT inapelekea sasa maji yawe bei kubwa ambapo kuna baadhi ya mamlaka wanashindwa kujiendesha hata kulipa bill za umeme. Naomba liangaliwe suala hilo kwenye madawa ya kutibu maji ili kumshushia mwananchi mzigo wa kulipa bill kubwa ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, kwenye mikoa yetu, mkoa wa chini zaidi unaolipa bei ndogo ni 640 Moshi, na DAWASCO wanalipa 1,663 kwa unit, lakini bei hizi bado kwa Tanzania ukilinganisha na nchi za nje, mfano Denmark kwa unit ile ile inayolipwa Moshi shilingi 650 wao wanalipa shilingi 7,658. Ukienda nchi ndogo ambayo inalipa bei ndogo na ina utaalam wa kutosha, ni China; inalipa shilingi 902, lakini Moshi tunalipa shilingi 640. Hili nataka kutoa mchanganuo mdogo zipo nchi mbalimbali na bei zake.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuchangia Chuo cha Maji. Chuo hiki kiongezewe nguvu na vifaa vya kutosha ili tupate wataalam wa maji huko vijijini na kwenye Manispaa zetu. Kikiimarishwa Chuo hiki tutapata wataalam watakaosaidia kwenye Mikoa yetu na Wilaya zetu; mfano kwenye kitengo cha drill cha uchimbaji wa Visima, hiki kipewe msukumo mkubwa wa wataalam ili tuweze kuwatumia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nami niongezee kuchangia kwenye uvunaji wa maji ya mvua ambapo suala hili liwe ndiyo kauli mbiu yetu. Tuanze na sisi Wabunge humu ndani kwenye majumba yetu na maeneo yetu tujiwekee akiba ya maji ya mvua. Nafahamu kuna nchi baadhi ya maeneo maisha yao yote wanaishi kwa maji ya mvua tu, hawana maji mengine yanayotumia, kwa sababu wapo juu ya milima, milima ni jiwe hawapati maji, maji yao ni ya mvua tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, maji ni afya. Kwa kuwa maji ni afya tukiwekeza zaidi kwenye maji, tutapunguza hata ununuaji wa madawa ya kutibu binadamu na hasa watoto wadogo ambao wanaathirika sana na maradhi mbalimbali ya maambukizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tukipata maji tutamsaidia mwanamama au mwanamke kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi, atapata muda wa kutosha wa kulea familia, atapata muda wa kutosha wa kujiajiri na kuinua kipato chake, badala ya kutumia muda mrefu kuhangaika kutafuta maji. Kwa hiyo, nashauri tuwekeze zaidi kwenye Mfuko huu wa Maji ili tuweze kumsaidia mwananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiendelea, naamini kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi ikiongozwa na Rais wake, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu na Mawaziri wote, wana nia na dhamira ya dhati kabisa katika kuhakikisha wananchi wa Tanzania wanaondokana na shida ya maji na shida mbalimbali zinazotukabili. Mambo huenda kwa awamu, awamu baada ya awamu, hatua baada ya hatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini Wizara imejipanga vizuri katika kutekeleza mpango kazi wao waliotuandikia katika bajeti yao. Naishauri Serikali zile pesa walizoomba zitoke na zitoke kwa wakati...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote kwanza naomba kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza na Kambi ambazo zimezungukwa na maeneo ya raia. Naomba Serikali ilishughulikie suala hili kwa haraka kwa sababu tayari kuna baadhi ya maeneo ya kambi ukipita nje yanayofanyika ndani ya Kambi ya Jeshi yote raia wanayaona. Mfano Kambi ya Mwanyanya inahitaji ukarabati wa kujengewa ukuta. Pia naomba Serikali sasa ilipe fidia lakini pia izungumze na Serikali kupata maeneo mengine kwa ajili ya Jeshi, maeneo yawe ni ya Serikali yasiyohitaji watu kulipwa fidia ili kuweka akiba kwa hapo baadaye kwa ujenzi wa Kambi na matumizi mengine ya Jeshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ajira za JKT, nashauri pia isiwe kwenye vikosi vya Jeshi tu lakini pia hata ajira za taasisi nyingine za Serikali na Serikali kwa ujumla iwafikirie vijana wetu hawa wanatoka katika Jeshi la Kujenga Taifa ili wapewe kipaumbele kwa sababu vijana hawa tayari wameshafunzwa uzalendo, ujasiri pamoja na maandili ya kuitumikia nchi na Taifa kwa jumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalipongeza Jeshi letu kwa kukabiliana na vitendo mbalimbali viovu vinavyofanyika katika mipaka yetu ndani na nje ya Tanzania ikiwemo kudhibiti mambo ya uharamia na mambo mengine yote yanayojitokeza yanayoashiria mambo ya kigaidi na mengineyo. Nalipongeza sana Jeshi letu kwa kazi nzuri linayoifanya katika kusaidia mambo mbalimbali yakiwemo majanga na maafa yanayotokea ndani ya nchi, wamekuwa mstari wa mbele sana kutoa msaada wa hali na mali na nguvu zao zote katika kuhakikisha wananchi wanaishi kwa amani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe pongezi za dhati kabisa kwa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Tanzania, Waziri wa Ulinzi, Mkuu wa Majeshi, Kamanda wetu wa Majeshi na Majeshi yote nchini Tanzania kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kulinda nchi yetu, mipaka yetu na raia kwa ujumla. Kama ilivyotokea kuashiria kwa uvunjifu wa amani uliotokea Zanzibar wakaenda pale kwa ajili ya kulinda amani ya nchi na hawakwenda kushiriki uchaguzi wamekwenda kusimamia amani ya nchi na wameifanya kwa uzalendo mkubwa na nchi sasa iko shwari nchi iko salama, mipaka ya nchi yetu iko salama, tunawashukuru wanajeshi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachokiomba mahitaji yao ya msingi tuwasaidie, yakiwemo marupurupu na mambo mengine ya kupandishwa vyeo na madaraja ili waweze kufanya kaz zao kwa weledi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ninaloliomba, mwenzangu alichangia kuhusu vituo hivi vya afya, ni kweli vituo vya afya na Hospitali za Jeshi zinatoa msaada mkubwa sana kwa raia. Naomba ziongezewe vifaa na ziongezewe watalaam na kuwapatia mafunzo zaidi ikiwemo kuwapatia mafunzo wanajeshi wetu ili kukabiliana na hatari zinazojitokeza za kimataifa za uharamia na ugaidi. Naomba mafunzo hayo yaendelee kutolewa zaidi kwa wanajeshi wetu na hasa vijana wadogo ambao ni nguvu kazi kubwa ya Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho niongezee tu kwa kusema kwamba Jeshi letu ni imara, Jeshi letu linafanya kazi nzuri, na ninakipongeza kwa dhati kikosi kile ya Makomandoo wa Jeshi. Mheshimiwa Waziri kikosi kile ukione kwa jicho lingine zaidi la huruma kwa sababu ndicho kikosi ambacho tunakitegemea yatakapotokea majanga na maafa makubwa ndani ya nchi yetu, lakini Mwenyenzi Mungu naomba yasitokee hayo, nchi yetu iendelee kuishi tuishi kwa amani na salama, mipaka yetu iwekwe salama, na nchi yetu iwekwe salama. (Makofi)

Mheshimwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Naanza na NFRA. Kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa ambayo hayatabiriki naomba sasa hii NFRA iongezewe nguvu, iongezewe fedha ili kwanza iweze kununua mazao ya kutosha na kwa wakati na kwa bei muafaka. Pili iongezewe fedha ili tuweze kuhifadhi mazao yetu kwa njia za kisasa zaidi na tuepukane na ile kuhifadhi katika maghala twende kisasa zaidi ambapo mazao yetu yatakaa kwa muda mrefu zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kuhusu ukulima na ufugaji unaohifadhi mazingira. Nashauri Wizara ya Kilimo ishirikiane na Wizara ya Maji hawa wafugaji ambao wana mifugo mingi wahamasishwe na wapewe elimu ya kuhifadhi maji ya mvua kwa ajili ya mifugo yao huko wanakoishi. Katika ukulima nashauri Serikali ihimize zaidi hasa wale wanunuzi wakubwa mfano wa tumbaku, waje na yale majiko ya kisasa ya kukaushia tumbaku ili kuepusha ukataji wa miti yetu kiholela ambayo inatumika kukaushia tumbaku. Naomba yale majiko ya tumbaku yapewe hamasa zaidi ili yatumike tumbaku yetu ikaushwe kwa majiko ambayo hayahitaji kukata miti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza uvuvi wa bahari kuu kwa Serikali kuamua kwa makusudi kujenga au kuendeleza gati namba sita na gati namba tatu ya kule Zanzibar kwa ajili ya kupokea na kuhifadhi samaki wa bahari kuu. Naomba hili Serikali ilitilie mkazo, hizo bandari zimalizike kwa haraka ili nchi yetu iweze kupata mapato ya fedha za kigeni na ajira kwa vijana wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwamba Serikali yetu ina dhamira ya dhati kabisa katika kumsaidia mkulima na mvuvi wa Tanzania. Kwa maana hiyo kwa makusudi imeondoa tozo mbalimbali na kodi mbalimbali zitakazomsaidia mvuvi na mkulima. Dhamira nyingine ya dhati ni kuweka ununuzi wa pamoja wa mbolea, hizi zote ni mojawapo ya dhamira za dhati za kuwasaidia wakulima wetu na mvuvi ili waondokane na tabu ndogo ndogo zinazowakabili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na naipongeza Wizara kwa marekebisho ya baadhi ya kanuni za mamlaka katika uvuvi wa bahari kuu. Naomba Kanuni hizi zitumike kwa haraka ipasavyo ili ziweze kutuletea mapato katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naongeza kwenye Benki ya Kilimo, nashauri benki hii iongezewe mtaji ili iweze kusaidia wananchi kulima ikiwemo kuhamasisha vikundi vidogo vidogo vya vijana na wanawake kuwapa mkopo ili Wizara ya Kilimo itoe utaalam wa ukulima na utengenezaji wa mbegu bora ili wananchi wetu wapate mbegu bora ambazo zitaendana na soko, uchumi wa kati na uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Kamati kwa kazi nzuri ya kufuatilia kazi kwa umakini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, michango. T.F.C ipelekwe Wizara ya Kilimo ili Wizara ya Kilimo iweze kuisimamia na kuifuatilia kwa karibu ili kuleta ufanisi wa kazi zake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Kilimo iweke utaratibu wa kukutana na wadau wote wa kilimo angalau mara mbili kwa mwaka ili kubaini matatizo na changamoto zinazokabili sekta ya kilimo. Pia, Benki ya Kilimo iongezewe mtaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maji; kuwekwe utaratibu wa ufuatiliaji wa miradi ya maji kote nchini ili kuhakikisha vifaa na miundombinu ya maji vina ubora unaohitajika kwa mradi husika ili kubaini wakandarasi wasiofuata masharti na mikataba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tozo ya mafuta iongezwe iwe Sh.100 ili kuongeza mtaji katika Mfuko wa Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uvuvi; Serikali iharakishe ujenzi wa bandari ya uvuvi na ununuzi wa meli ya uvuvi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naunga mkono hoja. Naipongeza Serikali ya CCM katika juhudi za makusudi za kuwasaidia wananchi hasa wanawake na watoto kupata afya bora na huduma nyinginezo za kijamii. Naishukuru na kuipongeza Serikali kwa hatua iliyochukua kuanzisha matibabu ya kupandikiza figo na upasuaji wa moyo hapa nchini. Pia naipongeza Serikali kwa kuanzisha chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi kwa wasichana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri, naiomba Serikalii iangalie namna ya kupunguza bei ya vifaa vya kujifungulia kwa mama wajawazito ili akina mama wasio na uwezo waweze kumudu gharama za vifaa hivyo. Serikali ijenge vituo vya kuwasaidia vijana walioathirika na madawa ya kulevya na bangi ili warudi katika hali yao ya kawaida na waungane na wananchi wenzao katika ujenzi wa Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mayoma kwa akina mama yanazidi kuwa tatizo kwa wanawake ni vyema ufanyike utafiti juu ya ukubwa wa tatizo hilo na baadae elimu itolewe kwa wanawake waende hospitali kabla ya matatizo hayajawa makubwa na kusababisha madhara mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho naipongeza Wizara na viongozi wote wa Wizara kwa juhudi kubwa wanazofanya katika kuisimamia Wizara na utekelezaji wa majukumu yote kwa bidii, waendelee na moyo huo. Pamoja na Madaktari Bingwa akiwepo Dkt. Janabi, ahsante.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja hii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nachukua fursa hii kuipongeza Serikali, Mheshimiwa Waziri, viongozi na watendaji wote katika jitihada zote katika kuhakikisha sekta zote za Wizara hii zinafanya kazi kwa maslahi ya kuwaletea wananchi maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, michango/ushauri kuhusu Shirika la Posta; Serikali iongeze fedha ili shirika liweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na kuweza kukabiliana na ushindani na kuongeza kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi. Serikali ione umuhimu wa kununua meli ya abiria kwa usafiri wa baharini kati ya Dar es Salam na Zanzibar kwa madhumuni ya kuwasaidia wananchi wanyonge ili waweze kumudu gharama za usafiri kwani usafiri wa kampuni binafsi au mtu binafsi bei zake ni za juu sana kwa mwananchi mnyonge na abiria wanahitaji huduma hiyo wanazidi kuongeza siku hadi siku.

Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika letu la Simu (TTCL); nashauri zitafutwe fedha za ziada ili shirika liweze kupanua wigo zaidi wa kutoa huduma za kuwafikia wananchi katika maeneo yote ya nchi yetu Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, TBA ikague nyumba zake zote na kuzifanyia matengenezo zile ambazo zinahitaji matengenezo ili nyumba hizo zisiendelee kuharibika zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naunga mkono hoja, Hapa Kazi Tu, Mheshimiwa Waziri piga kazi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. KHADIJA H. ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii kuipongeza Serikali, Wizara ya Habari pamoja na Mheshimiwa Waziri na wasaidizi wake wote katika Wizara hii kwa jitihada zao wanazofanya kuhakikisha wanafikia malengo waliyojipangia katika kuendeleza sekta zote zilizomo ndani ya Wizara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kushauri yafuatayo:-

(i) Wizara iongezewe fedha ili iweze kutekeleza majukumu yake.

(ii) TBC inahitajika nchini kote hivyo Serikali iendelee na juhudi za kuwajengea uwezo wafanyakazi ili waendane na hali ya sasa ya teknolojia ya habari. Aidha, TBC ipatiwe mitambo ya kisasa na yenye nguvu ili iweze kusikika na kuonekana ndani na nje ya nchi kwa muda wote.

(iii) Wizara iweke msukumo na mkakati maalum katika kuiendeleza lugha ya Kiswahili ikiwemo shughuli zote za kiserikali itumike lugha ya Kiswahili, mikutano yote inayofanyika nchini itumie lugha ya Kiswahili kwa lengo la kuongeza ajira kwa Watanzania, kuongeza idadi ya watumiaji wa Kiswahili na kuifanya lugha yetu hii itumike duniani kote.

(iv) Wizara kupitia taasisi zake zote iendelee na juhudi zake wanazochukua kuhakikisha maadili, mila na desturi za Watanzania zile zilizo bora zinalindwa na wasisite kuzuia au kufungia nyimbo, michezo, filamu na sanaa zote zinazokiuka maadili ya nchi yetu na Watanzania kwa ujumla.

(v) Wizara ihamasishe na kufufua michezo ya zamani ambayo imepotea ambayo inaweza kuongeza tija kwa Taifa na wananchi kwa kuongeza kipato na kulinda isipotee kabisa.

(vi) Sanaa na utamaduni ni vyombo vyenye nguvu sana katika kuitangaza nchi. Hivyo juhudi za Wizara za kuitangaza nchi yetu kupitia sanaa mbalimbali ziongezwe kwa lengo la kuitangaza zaidi nchi yetu ya Tanzania duniani kote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri aendelee kupiga kazi kwa manufaa ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa jitihada zake za makusudi inazochukua katika kuhakikisha wananchi wa Tanzania wanapata maji safi na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara kwa kuhangaika kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama na kushughulikia miradi ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kuunganisha DAWASCO na DAWASA, ni jambo jema kwa watumiaji wa maji, ufanyike uchunguzi kwa DAWASCO na DAWASA kuhusiana na madeni, hasara na changamoto zote zilizopo katika taasisi hizo. Katika chombo hicho kipya kitakachoundwa watendaji watakaopewa kukiendesha wateuliwe wale ambao wana maadili na waaminifu ili kuepusha matatizo hasara na madeni ya lazima.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali na Wizara iendelee na juhudi zake za kutafuta fedha kwa madhumuni ya kuongeza miradi ya maji nchini ili Watanzania wapate huduma hiyo muhimu ya majisafi na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa jitihada zake za makusudi za kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara iendelee na mikutano ya mara kwa mara na wadau, wawekezaji na wafanyabiashara ili kubaini changamoto, matatizo na vikwazo vinavyowakabili ikiwemo kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuendeleza sekta ya viwanda ni lazima kuiendeleza sekta ya kilimo, uvuvi na mifugo vipewe kipaumbele ili kupata malighafi za kupeleka viwandani, malighafi zitoke hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wawekezaji wa viwanda vya maziwa wana changamoto ya kodi mbalimbali hivyo ni vema eneo hilo liangaliwe upya. Wafanyabiashara wadogo wadogo kama mama lishe na wajasiriamali wadogo wanasumbuliwa sana kuhusu kodi, hawana uwezo wa kulipa kutokana na faida kuwa ndogo. Serikali iangalie jambo hili ili wananchi wetu wanyonge waweze kujikwamua na umaskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nalipongeza Jeshi la Ulinzi kwa kazi nzuri na ya kizalendo inayofanya kuhakikisha nchi yetu na mipaka yake ipo salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Tanzania kwa uongozi wake bora wa kulisimamia Jeshi letu la Tanzania. Nampongeza Waziri wa Ulinzi wa Jeshi la Kujenga Taifa, Watendaji wote wa Wizara na Wakuu wa Majeshi wote nchini kwa usimamizi wa majeshi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali ijitahidi kuongeza bajeti kwa Wizara hii kwa lengo la kuongeza ufanisi wa kazi zake na kutekeleza majukumu yake kwa wakati. Vile vile Wizara iongeze kuelimisha majeshi yetu katika vitengo vya uhandisi na teknolojia ya kisasa ili kukabiliana na changamoto mbalimbali za sayansi na teknolojia zinazojitokeza. Pia majeshi yetu kujitosheleza na wataalam hao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kambi za Jeshi zilizopo karibu na makazi ya raia au kuzungukwa na maeneo ya raia ziangaliwe ili yasije yakatokea madhara kwa raia wa maeneo hayo. Pia juhudi za Wizara za kuwapatia wanajeshi wetu makazi bora ziendelee kwa lengo la kuwapatia wanajeshi wetu maisha bora na yenye utulivu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Spika, naipongeza Serikali katika jitihada zake za kuhakikisha wafugaji na wavuvi wananufaika na kazi zao wanazofanya katika kujitafutia kipato, kudhibiti uvuvi haramu, kuhifadhi mazingira na kudhibiti rasilimali za bahari na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali iweke mazingira wezeshi kwa wawekezaji katika sekta ya maziwa kwa kuangalia tozo na kodi mbalimbali zilizopo katika sekta hiyo ya maziwa. Serikali iwekeze fedha za kutosha katika uzalishaji wa viumbe kwenye maji ili kuongeza mazao hayo, kuongeza ajira na kuongeza pato la Taifa.

Mheshimiwa Spika, elimu ya ufugaji wa samaki na viumbe wengine waishio kwenye maji ipewe msukumo mkubwa kwa vijana katika Halmashauri zote nchini.

Mheshimiwa Spika, nawatakia Mawaziri utekelezaji mwema wa majukumu yao ya kazi. Ahsante sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Kilimo
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote, napenda kuchukua nafasi hii muhimu kuishukuru Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi na Mheshimiwa Rais kwa jitihada zake anazochukua siku hadi siku kuhakikisha kilimo kinakua na wakulima wanapata unafuu. Mfano, kuwapunguzia kodi mbalimbali na tumeona kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri kuna changamoto nyingi za kodi na tozo mbalimbali zinakwenda kutatuliwa na kupatiwa ufumbuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuipongeza Wizara na Serikali kwa ujumla, Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na viongozi wote wa Wizara. Tumeshuhudia juzi uwekaji wa jiwe la msingi la maghala na vihenge vya kisasa kabisa ambavyo vitachangia kwa kiasi kikubwa kuhifadhi mazao yetu yasiharibike na kupata soko na vilevile katika vihenge na maghala hayo, tutakuwa na uhakika wa usalama wa chakula hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, usalama wa chakula ni muhimu kwa sababu ni usalama wa Taifa. Tutakapokosa chakula hata hayo majeshi yetu yatashindwa kutulinda sisi na mipaka yetu. Kwa hiyo, nashauri Kitengo hiki cha NFRA kiongezewe fedha zaidi ili kuweza kununua mazao mengi kwa ajili ya usalama wa chakula lakini pia kuwasaidia wakulima wetu kupata masoko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyotambua kwamba karibu asilimia 65 ya malighafi za viwanda zinategemea mazao ya kilimo. Ni vyema sasa sekta hii ya kilimo ikaongezewa fedha zaidi ili kuhimili mahitaji yote ya kilimo ndani ya nchi yetu na kupata malighafi za viwanda vyetu ili tuweze kupata ajira kwa vijana wetu katika kilimo, viwanda na kuongeza Pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuliboresha au kulifanikisha suala hili ni lazima tujikite zaidi kwenye kilimo cha umwagiliaji. Kilimo cha umwagiliaji kitakuwa ndiyo nguzo muhimu ya kumkomboa mkulima mkubwa na mdogo kwa sababu mabadiliko ya hali ya hewa au mabadiliko ya tabia nchi yanayumbayumba na hivyo kusababisha kilimo chetu pia kiwe kinayumbayumba na hakina uhakika. Kwa hiyo, tukiwekeza zaidi kwenye sekta hii ya umwagiliaji tutaweza kupata masoko ya ndani na nje na tutapata malighafi za viwanda vyetu. Hilo liende sambamba na miundombinu ya barabara kule ambako kunazalishwa mazao mengi ili mazao hayo yasiharibike shambani na yaweze kufika kwenye maeneo ya masoko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mbegu bora ni la msingi zaidi. Ili kupata mbegu bora ni lazima tuviimarishe kwa kuviongezea mtaji vituo vyetu vya utafiti kama TARI na vinginevyo. Tukiviongezea fedha vituo hivi vikafanya utafiti wa mbegu bora tutaweza kupata mbegu bora ambazo zitasaidia hata kukabiliana na upungufu wa mafuta na sukari ambao tunao hivi sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kuishauri Serikali iongeze fedha au ipeleke fedha kwenye TFRA kwa sababu ya majukumu yake. Hii ni kutokana na hali ya sasa hivi ambapo kuna milipuko ya magonjwa na wadudu mbalimbali wanaoharibu mimea yetu, ni bora tukajua ni viuatilifu gani vinafaa kwa maeneo gani na kwa wadudu gani waharibifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuimarisha sekta binafsi ili iwekeze katika kilimo cha wawekezaji wadogo na wakubwa, ni vyema kukajengwa mazingira mazuri kwa wawekezaji hawa ili waweze kuwekeza kwa kiwango kikubwa. Hii ni pamoja na hatua mbalimbali zilizoanza kuchukuliwa na nyingine ziko kwenye mikakati ya kuchukuliwa ya kuangalia kodi na tozo mbalimbali ili kuwawezesha wawekezaji wetu kuvutika na uwekezaji katika sekta ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, katika kuwekeza katika fani ya kilimo ni lazima kuwe na zana bora za kilimo. Kwa hiyo, ni vyema Benki ya Kilimo ikaongezewa mtaji ili itoe mikopo kwa wafanyabiashara au wakulima ili waweze kukopa vifaa vya kilimo kama matrekta kwa bei nafuu. Vinginevyo tutafute njia mbadala ya kuhakikisha wakulima wetu katika kila kijiji wanapata trekta na zana bora za kilimo na baadaye walipe kidogokidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili linatakiwa liende sambamba na teknolojia ya usindikaji. Teknolojia yetu ya usindikaji iliyopo sasa tunapoteza mafuta mengi katika mashudu. Kwa hiyo, ni vyema tukapata teknolojia mpya na ya kisasa ili kuhakikisha mafuta yetu mengi hayapotei katika mashudu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, kuna masuala ya ushirika. Suala la ushirika limeongelewa sana na tumelieleza kwenye Ilani yetu ya Uchaguzi ukurasa wa 112, Ibara ya 57(a) ambayo inasema, kuhakikisha kuwa shughuli zote zenye mwelekeo wa ushirika zitapewa msukumo stahiki kwa kuhamasisha na kusimamia kwa nguvu uanzishwaji wa vikundi vya ushirika kama vile SACCOS na vinginevyo, vyama vya mazao, ufugaji na vinginevyo. Mwisho inamalizia hapa, ushirika ndiyo silaha kuu ya wanyonge na nguzo kuu ya ujenzi wa siasa ya ujamaa na kujitegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kufuata kipengele hicho cha Ilani, vyama vya ushirika tulivyonavyo, kama kuna makosa madogomadogo ni vyema sasa tukayafanyia marekebisho, tukaviunda upya ili kweli viwe mkombozi wa mkulima mnyonge na wanyonge wengine hapa nchini Tanzania. Kwa sababu tumeona kwamba ndiyo nguzo kuu na silaha na mkombozi wa mnyonge kwa njia ya ujamaa na kujitegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya mwaka jana tulikamata shilingi hapa ya Mheshimiwa Waziri kuhusu zao la minazi. Mwaka huu kitabu hiki cha Waziri sijaona akiongelea kuhusu zao la minazi. Zao hili ni la biashara, sasa hivi tunaagiza nazi kutoka nje ya nchi na kama sisi Tanzania tutaimarisha kilimo chetu cha minazi tutaweza kusafirisha nje ya nchi mazao yatokanayo na minazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kwa mara nyingine kuwatakia kheri, wafanye kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza kabisa, napenda kuchukua fursa hii kuipongeza sana Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi katika kutekeleza majukumu yake ya kuhakikisha tunapata uvuvi endelevu na pia tunaliongezea Taifa fedha za kigeni kupitia Sekta hizi za Ufugaji na Uvuvi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sekta ya Ufugaji na Uvuvi ni sekta muhimu sana kwa sababu ni sekta ambayo kwanza pia inatupa usalama wa chakula ndani ya nchi; lakini pili, inaongeza ajira; tatu, inaongeza pato la Taifa, lakini pia inatupa lishe bora. Ni vyema sasa Serikali ikaona kuna haja ya kuongeza msukumo zaidi katika sekta hizi ili kuongeza pato la Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, katika Sekta ya ufugaji, wafugaji wanahitaji mipango bora ya malisho na maji, wanatakiwa wapewe elimu juu ya uvunaji wa maji ya mvua ili waweze kujenga mabwawa na malambo kwa ajili ya kulishia mifugo yao. Natumai wafugaji wakipewa elimu hii wataweza kuchukua baadhi ya mifugo na kuwekeza katika sekta hii ya upatikanaji wa maji na malisho; pia kunatakiwa wafugaji na wavuvi waendelee kupewa elimu ya juu ya uhifadhi wa mazingira.

Mheshimiwa Naibu Spika, naelekea kwenye bidhaa za ngozi, kuna bidhaa nyingi za ngozi ambazo hazitumiki, na badala yake zinakaa zinapotea. Nawashauri Serikali, kwa vile viwanda ambavyo sasa hivi vinachakata ngozi, ile ngozi ya ziada ambayo haitumiki ni bora kukatengenezwa mazingira rahisi ili ngozi zile zikauzwa badala ya kubaki na kuwa hazifai au kuharibika au kuoza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Sekta ya Maziwa; sekta hii ina changamoto nyingi kwa wawekezaji wa viwanda vya maziwa. Changamoto pia inamkuta hata yule mzalishaji mdogo wa maziwa kwa sababu maziwa mengi yanaharibika njiani kutokana na miundombinu ambayo siyo rafiki kwa mkulima wa maziwa na tukizingatia kwamba bidhaa hi ya maziwa haichukui muda kuharibika.

Mheshimiwa Naibu Spika, pale wazalishaji wadogo wa maziwa wanapokwenda kupeleka maziwa kiwandani hawana vyombo vya kupooza maziwa hayo ili yachukue muda mrefu yawafikie viwandani na watumiaji wengine. Ni vyema sasa tukahamasisha, au Serikali ikatafuta mpango wa vipoozeo vya maziwa kuwapa hawa wakakopa kwa kupitia mabenki, kwa kupitia vikundi mbalimbali, waweze kupata vipoozeo vya maziwa ili maziwa yao yakae muda mrefu na yamfikie mtumiaji bila kuharibika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye sheria za uvuvi, sheria hizi wavuvi wengi hawazifahamu, hizo sera hawazifahamu. Kwa hiyo ni vyema sasa wavuvi wetu wakaelekezwa juu ya sheria, sera na kanuni mbalimbali za uvuvi kwa sababu inaelekea kuna baadhi ya sheria zimeandikwa kwa lugha ya Kiingereza ambazo wavuvi wetu hawazifahamu. Kwa hiyo, naipongeza Wizara kwa kutafsiri hii sheria kwa lugha ya Kiswahili ambayo itakuwa ni lugha nyepesi kwa wavuvi wetu kuweza kuifahamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kinachotakiwa baada ya tafsiri hiyo, zishushwe chini sasa kwa wavuvi wenyewe ili wazifahamu na wapewe mafunzo elekezi ya kufahamu sheria hizo na sera za uvuvi. Tukiwafundisha kanuni na sera za uvuvi kutapunguza huo uvuvi haramu tunaoupiga vita. Sisi sote tunajua kwamba uvuvi haramu ni janga la Taifa, linaharibu mazingira, linaharibu mazao yetu ya samaki na mazao mengine ya baharini. Sasa ni vyema wavuvi wetu wakapewa elimu zaidi ya kufahamu sheria, kanuni, vitu gani vinafaa kwa uvuvi na vitu gani havifai, nyavu ziwe na ukubwa gani, elimu hii iendelee kutolewa mara kwa mara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na hiki Kiwanda cha Sunflag ambacho kinazalisha nyavu inaelekea nyavu zake hazina ubora. Kwa sababu wavuvi wakitumia mara moja au mara mbili nyavu zimeshavurugika, zimeshakatika, hivyo tunamtia hasara mvuvi mdogo maskini ambaye amejichuma pesa zake ndogondogo akaweza kununua nyavu. Sasa tuangalie upatikanaji wa nyavu bora na vivulio bora vya samaki ili tusimuongezee mzigo mvuvi wetu mdogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, inapotokea samaki, mvuvi amevua kwa bahati mbaya, kuna masikitiko na malalamiko, samaki ambaye hahitajiki kwa wakati ule, samaki ni samaki ndani ya bahari, unapopitisha nyavu anaweza akaingia na mwingine ambaye hahitajiki. Basi jambo lile lisichukuliwe kwamba yule mvuvi kafanya makusudi akalipishwa faini, akachomewa nyavu, akachomewa vyombo. Kwa hiyo hili suala linatakiwa lichukuliwe kwa umakini wake na kujua katika bahari kuna vitu vingi na vitu hivyo vinaweza vikajichomeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna tatizo la mipaka ya leseni za uvuvi, wale wavuvi wanatakiwa waelezwe leseni zile wanazokata zinatumia mipaka gani. Kwa sababu bahari haina mipaka, imeanzia Zanzibar, Kilwa, Dar es Salaam, Kimbiji, inazunguka, na mvuvi anataka kutafuta samaki ili asipoteze muda wa kukaa kutwa kucha nzima baharini bila ya samaki, kwa hiyo hizi leseni zinazotoka hebu zitolewe kwa ufafanuzi ili wavuvi waelewe mipaka yao ya kuvua ni ipi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi, kwa sababu wakienda eneo lingine wanatozwa faini wanaambiwa wakate leseni nyingine. Sasa hizi leseni zimegawiwa kwa viwango gani, au akate leseni ya aina gani ili aweze kuvua sehemu yoyote ya Tanzania? Hili linatakiwa lifanyiwe kazi na wavuvi wetu waelezwe ili kuepusha hizo kasoro ndogondogo zinazojitokeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Wizara kwa kutengeneza huo mfumo wa kuzalisha samaki ambao sasa wavuvi wetu watajua wapi samaki wapo na watavua kwa wingi gani. Kwa hiyo, hili nalipongeza, ni jambo zuri na linatakiwa liwe endelevu kwa wavuvi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza pia Serikali na Wizara kwa kutaka kuifufua na kuiboresha TAFICO. TAFICO ikifufuliwa na ikiboreshwa ikawekewa miundombinu na mitaji, itaweza kufanya kazi za uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zana bora za uvuvi, zana bora za uvuvi kwa wavuvi wetu zinahitajika kwa sababu wataepuka kubahatisha kuvua. Kazi ya uvuvi ni ngumu na inahitaji uvumilivu wa hali ya juu. Wavuvi wanapokwenda baharini ukaona upepo unavuma huna uhakika kama mvuvi atarudi au harudi, atakuwa salama au hawi salama, atapotelea wapi. Tumeshuhudia Tanzania tunapokea wavuvi kutoka Comoro wengi tu ambao wamepotea baharini siku saba, siku nane na Watanzania wanapotea kuelekea nchi nyingine. Kwa hiyo, hii kazi ni ngumu, siyo kazi rahisi, inataka ujasiri. Kwa hiyo, ni vyema wavuvi wetu sasa tukawaendeleza ili wapate zana bora za uvuvi za kujua wapi samaki wapo, kwa ukubwa gani, kwa wingi gani, kwa kina gani cha maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nichangie kuhusu uvuvi wa Bahari Kuu, naomba Serikali imalize hii michakato ya ujenzi wa bandari za uvuvi na ununuzi wa meli ya uvuvi. Kwenye uvuvi wa bahari kuu hakuna haja ya kuwekeza, Mwenyezi Mungu ameshawalea mwenyewe samaki, ameshawakuza sasa hivi kazi yetu sisi wanadamu ni kwenda kuwavua. Kwenye uvuvi wa bahari kuu kuna samaki wengi ambao nchi za duniani wanafaidika na uvuvi huu. Tutaweza kuongeza Pato letu la Taifa na tutaweza kutengeneza miundombinu mingi kupitia uvuvi wa bahari kuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nikiendelea kwenye uvuvi huu wa bahari kuu, kuna mgao wa fedha, mgao huu unahusu Serikali mbili. Naomba usicheleweshwe, ugawiwe kwa maeneo yote Bara na Zanzibar, ili Sekta ya Uvuvi iweze kusonga mbele badala ya kubakia tu hazipelekwi. Kwa sababu kuna miundombinu mingi ya kupanua Sekta ya Uvuvi bado hatujafikia na tunahitaji mapato ya kutosha ili tuwekeze kwenye Sekta hii ya Uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Wizara, lakini pia nakipongeza Chuo kile cha Uvuvi cha Kigoma. Bila kutumia senti hata moja ya Serikali wameweza kufufua chuo kile kwa fedha zao wenyewe, wamejibinya, wameweza kufufua kile chuo na kuongeza wanafunzi wa kusomea mambo ya uvuvi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Spika, naipongeza Wizara, Mheshimiwa Waziri kwa utendaji na usimamizi mzuri katika kuhakikisha mali na rasilimali zetu za asili zinatunzwa na pia kukuza na kuinua sekta ya utalii nchini.

Mheshimiwa Spika, ushauri, katika kutekeleza nia njema ya Serikali kwa kuweka Mfuko wa Misitu, huoni vyema Wizara ikafuatilia kwa karibu zaidi juu ya wanufaika wa mfuko huo kama wanakidhi vigezo husika kwa lengo lililokusudiwa ili kuepuka wajanja kuitumia fursa hiyo na wale walengwa husika kukosa fursa ya kupata (fund) hizo kwa lengo la kutekeleza azma ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, Serikali iendelee kuelimisha juu ya kulinda na kuhifadhi uoto wa asili. Mali Kale zitunzwe, zifanyiwe ukarabati na zilindwe ili ziweze kubaki kuwa ni urithi wetu wa Taifa kwa lengo la kuhifadhi historia na kuongeza vivutio vya utalii. Kuangalia namna ya kupata nishati mbadala yenye gharama nafuu kwa wananchi ili kuepusha ukataji wa miti kwa madhumuni ya kutengeneza nishati ya kuni na mkaa. Upatikanaji wa miti upewe mkazo wa pekee kunusuru nchi kuwa jangwa. Baada ya kupandwa kuwe na ufuatiliaji wa karibu kuhakikisha miti hiyo inakuwa vizuri.

Mheshimiwa Spika, ahsante naunga mkono hoja endeleeni kuchapa kazi kwa manufaa ya Watanzania.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Wizara, Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara, Mabalozi wetu wote wanaowakilisha Tanzania kwa jitihada kubwa ya kuitangaza nchi yetu pamoja na kuitafutia misaada mbalimbali kwa maendeleo ya nchi yetu na wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, michango na ushauri:-

Mheshimiwa Naibu Spika,Wizara hii ipelekewe fedha kwa wakati ili kutekeleza majukumu yake kwa muda muafaka. Pia fedha za maendeleo ziongezwe ili kutekeleza miradi mingi ambayo inahitajika kwa muda huu na baadaye kwa maslahi ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vyema Serikali ya Muungano ijenge jengo jipya la Ofisi ya Mambo ya Nje huko Zanzibar. Serikali iombe kiwanja kwa SMZ na ijenge jengo jipya na la kisasa kulingana na kazi na mahitaji husika.

Mheshimiwa Naibu Spika,Wizara iendelee na juhudi za kuwatafutia ajira vijana wa Tanzania nchi za nje na Taasisi nyingine za Kimataifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania waishio nchi za nje ambao wamepata mafanikio na maendeleo makubwa, wahamasishwe zaidi kuja kuwekeza nchini kwao Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, Balozi zetu ziongezewe fedha ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itenge fedha kwa madhumuni ya kufanyia matengenezo Balozi zetu nchi za nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naunga Mkono hoja. Nawatakia utekelezaji mwema wa majukumu ya kazi na kulitumikia Taifa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa jitihada mbalimbali za kuwezesha Wizara na Taasisi zake zote zinazotekeleza majukumu yake pamoja na changamoto zilizopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali ione namna ya kuongeza fedha katika Wizara na Taasisi zake ili majukumu ya kazi zao yatekelezwe kwa ufanisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji lipatiwe zana na vitendea kazi vya kisasa ili Jeshi hili liweze kukabiliana na majanga, maafa na matukio mbalimbali yanayotokea nchini yanayohitaji uokoaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Polisi lipatiwe vitendea kazi ili liweze kukabiliana na uhalifu na ulinzi wa nchi, wananchi na mali zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwamba wahamiaji haramu wakikamatwa warudishwe kwao au waachiwe waendelee na safari yao nje ya nchi yetu kuepusha mlundikano wa mahabusu katika Magereza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Askari yeyote ambaye anakiuka maadili ya kazi yake kwa kuchafua Jeshi la Polisi, Magereza, Uhamiaji na kadhalika, wachukuliwe hatua za kinidhamu ili kulinda heshima ya majeshi yetu hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nawatakia utekelezaji mwema. Naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii kuipongeza Serikali kwa juhudi kubwa sana za kuwaletea wananchi maendeleo. Nawapongeza viongozi wetu Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mawaziri wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu/Bunge kwa utendaji wa kazi ulio bora katika kuongeza juhudi za kuwatumikia wananchi wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, masuala ya Muungano; naipongeza Serikali yangu kupitia kikao chake cha Baraza la Mawaziri kuridhia kuondosha kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa kiwango cha asilimia sifuri kwa umeme unaouzwa kwa Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO) kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) sambamba na kufuta malimbikizo ya deni la VAT la shilingi bilioni 22.9 kwa Shirika la umeme (ZECO).

Mheshimiwa Spika, ulinzi na usalama; navipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi kubwa wanayofanya kuhakikisha nchi yetu iko salama na ulinzi wa raia na mali zao.

Mheshimiwa Spika, miundombinu; Serikali imefanya juhudi kubwa katika kuimarisha sekta hii kama viwanja vya ndege, barabara, reli na hasa reli ya mwendokasi, naipongeza Serikali pia. Nashauri kuongeza uwekezaji katika eneo la bahari kwa meli za abiria, mizigo na uvuvi.

Mheshimiwa Spika, nashauri Serikali iendelee na juhudi za kuweka mazingira wezeshi zaidi kwa wawekezaji wa ndani na wa nje ya nchi ili sekta ya uwekezaji izidi kuimarika ili kuongeza pato la Taifa, kuinua uchumi na kuongeza ajira kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Nawatakia utekelezaji mwema wa majukumu ya kazi zenu.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kuipongeza sana Serikali kwa mpango mzuri wa maendeleo uliotuletea ikiwemo kuipa kipaumbele Sekta ya Kilimo. Kwenye mpango Serikali itaendelea kuimarisha sekta ya kilimo kwa kusaidia upatikanaji wa pembejeo, masoko na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nijielekeze katika ukulima wa mbogamboga. Katika kilimo hiki cha mbogamboga sasa hivi vijana wamehamasika sana na wakulima wadogo hujiunga katika vikundi au mmoja mmoja katika kilimo hiki cha mbogamboga. Kwa bahati njema sana mazao ya mbogamboga yanahitajika ndani ya nchi lakini pia nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo ni moja usafiri wa ndani kuhakikisha mazao haya yanafika kwa wakati katika maeneo husika lakini pia usafiri wa nje wakati wanapopata tenda za kusafirisha mazao hayo nje ya nchi kunakuwa na tatizo la usafiri kwa kuzingatia kwamba mazao mengi ya matunda na mbogamboga yanatoka kwenye Mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya na kwingine. Ni vyema sasa Serikali ikaimarisha Kiwanja cha Ndege cha Songwe ili wakulima na wasindikaji na wazalishaji wa maeneo hayo wapate urahisi wa kusafirisha mazao yao nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine katika ukulima huu wa mbogamboga napenda niongelee kuhusu suala la vifaa vya kilimo na hususani vifaa vya kilimo vya mbogamboga kama green house. Vifaa hivi vya kilimo vinatozwa VAT vya asilimia 18 na kwa maana hiyo sasa mkulima mdogo au kijana aliyemaliza masomo yake anataka kujiingiza kwenye ukulima huu wa green house, vifaa hivi vinakuwa ni vya bei kubwa sana. Hivyo, anashindwa kuwekeza kwa maana ya vifaa vyenyewe kwamba vifaa vya ujenzi, vifaa vya mipira ya kumwagilia na vinginevyo vinakuwa na gharama kubwa sana ambapo vijana na wakulima wadogo wanashindwa. Naomba Serikali iliangalie hili kwa upana ili kupunguza VAT hii ya asilimia 18 kwa vifaa vya uzalishaji wa matunda green house na nyinginezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea dhamana ya mikopo kwa wakulima wadogo na vikundi vidogo vidogo vya wakulima imekuwa ni tatizo kupata mikopo kutokana na kwamba hawana dhamana yoyote ambayo itawalinda kupata mikopo hiyo. Naomba sasa Serikali itafute njia bora zaidi na nyepesi zaidi ambayo itakuwa kama ni dhamana kwa vijana wetu na vikundi vyetu vidogo vidogo vya wakulima kuweza kukopesheka. Kwenye sekta hiyo ya kilimo kuna tatizo pia kwenye kodi kubwa VAT ya vifungashio. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vMheshimiwa Mwenyekiti,ifungashio vya mazao ya kilimo na mbogamboga imekuwa na VAT kubwa ambapo wakulima wanashindwa sasa kuhimili vile vifungashio vyenye ubora ambavyo vitaweza kusababisha kusafirisha mazao yao nje ya nchi na badala yake wanajikuta mazao yao tunauziana wenyewe hapa ndani ya nchi na tunakosa soko la nje lakini pia tunakosa fedha za kigeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hili Mheshimiwa Waziri alizingatie kwenye vifungashio pia vya mazao ya kilimo na mbogamboga. Kwa sababu sasa hivi wawekezaji wetu wa kilimo wanaagiza vifungashio kutoka nje ya nchi na kuviingiza Tanzania. Tufanye mipango sasa vifungashio hivi vizalishwe ndani ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na tozo nyingi ambazo zinamfanya mwekezaji kuwa na mlolongo mkubwa wa tozo mbalimbali. Naiomba Serikali sasa iziangalie tozo hizi ziweke mazingira wezeshi itakayomfanya mwekezaji awe analipa eneo moja tu na kumaliza shughuli zake na kuanza kuwekeza, tujenge mazingira wezeshi kwa wawekezaji wetu wa nje na ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea hapo hapo ssa hivi naigusa sekta ya maziwa. Sekta ya maziwa inatupa lishe lakini pia inatupa afya bora na kwa kuzingatia kwamba maziwa yanapozalishwa yanakuwa na matatizo na mambo madogo madogo ambapo tunahasishwa sasa tunywe maziwa yaliyosindikwa ambayo ndiyo yenye ubora kwa afya zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia hilo kwenye uwekezaji wa sekta ya maziwa nako pia kuna mlolongo mkubwa wa kulipa vitu mbalimbali kama hiyo mambo ya fire, VAT na vinginevyo ni vingi sana mpaka wazalishaji wa maziwa wanashindwa sasa kuhimili vile vikwazo vidogo, naomba hizi changamoto ndogo ndogo Serikali iziangalie kwa hawa wawekezaji wa maziwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kwenye sekta hiyo ya maziwa ukiondoa hayo mlolongo wa mambo hayo mambo yanatakiwa kulipa, kwenye kuwekeza maziwa, maziwa yanayozalishwa kwa muda mfupi hayatozwi VAT lakini ukizalisha maziwa ya muda mrefu yanatozwa VAT. Kwa maana hiyo sasa wawekezaji wanawekeza kwenya maziwa ambayo ya muda mfupi ambayo hayatozi VAT.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vyema sasa tukaliangalia hili ili wawekezaji wetu wawekeze maziwa muda mrefu ili waweze kusafirisha nje ya nchi kwa sababu yatakuwa yanadumu kwa muda mrefu na tutapunguza lile tatizo la sisi kuagiza maziwa kutoka nje na kuyaingiza ndani ya nchi kwa sababu ya kwetu sisi ni ya muda mfupi yake yanatoka nje ya muda mrefu, hili nafikiri tuliangalie sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea kwenye sekta ya maji kwa kuwa tuliomba tuongezewe Sh.50 kwenye lita ya mafuta kwa ajili ya Mfuko wa Maji, nashauri Serikali kama hili haliwezekani tutafute njia mpya njia mbadala ya kuongezea huu Mfuko wa Maji ili tuweze kutatua matatizo ya maji ndani ya nchi yetu. Kilio kikubwa kimekuwa kwenye maji na tumeweka kwenye mpango kilimo cha umwagiliaji. Kilimo cha umwagiliaji tutahitaji maji, tutahitaji mabwawa, tutahitaji visima. Kwa hivyo ni vyema pia tukaliangalia ili kuongeza kwenye Mfuko wa Maji ili tuweze kujenga hayo mabwawa, visima na miundombinu mingine ya umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea kwenye sekta ya uvuvi, ni vyema pia Serikali ikaiangalia kwa upana wake sekta ya uvuvi. Sekta ya uvuvi ni eneo moja ambalo litaipatia Tanzania fedha za kigeni, litaipatia ajira vijana wetu pia tutapata lishe bora kwa kula samaki ambapo watakuwa wengi tunawavua hapa nchini. Pia tujikite katika uwekezaji, naomba Serikali, hii bandari ya uvuvi ipewe kipaumbele ili imalizike na baada ya kumalizika kwa bandari ya uvuvi, Serikali sasa tumeshajikita katika kununua ndege sasa tujikite tena pia Serikali kwenye kununua meli ya uvuvi. Naipongeza Serikali kwa hilo, tumenunua ndege sasa tujikite tena tujipange, tujifunge mkanda, tununue meli ya uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea na suala la umeme. Umeme ni uchumi, umeme ni siasa na umeme ni usalama. Huduma hii ya umeme katika bajeti ya mwaka jana tulizungumzia kuhusu suala la umeme Zanzibar baina ya ZECO na Shirika la Umeme TANESCO. Tunaomba sasa huu mchakato umalizike kwa kuwa mtumiaji wa umeme wa Zazibar inabidi alipe VAT mara mbili kwa sababu tukinunua umeme tunalipa VAT, mtumiaji mdogo analipwa VAT sasa ni vyema sasa VAT hii iwekewe mikakati iwe inalipwa sehemu moja tu ili kumpunguzia mzigo mwananchi mdogo ili asielemewe na mzigo na kwa sababu hii ndio maana kumekuwa na malimbikizo makubwa sana ya umeme kule Zanzibar kwa sababu suala hili bado halijapita ufumbuzi wapi VAT hii ilipwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea kwenye huduma za mama, afya na mtoto; naipongeza Serikali kwa kulipa kipaumbele suala la afya ya mama na mtoto. Pia naiomba Serikali kila kwenye kituo cha afya basi iweke chumba cha kujifungulia mama na mtoto na chumba pia cha kupumzika baada ya kujifungua ili kuweka usalama wa mama na mtoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa hatua mbalimbali za kusamehe kodi mbalimbali za kilimo ikiwemo mambo ya ngozi na mambo mengine ya kilimo. Hapa naipongeza Serikali sana kwa kuliona hili, lakini pia nataka Serikali itupie macho katika haya mambo niliyoainisha kwenye sekta ya maziwa, sekta ya mbogamboga na sekta nyingine za uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kuipongeza sana Serikali kwa mpango mzuri wa maendeleo uliotuletea ikiwemo kuipa kipaumbele Sekta ya Kilimo. Kwenye mpango Serikali itaendelea kuimarisha sekta ya kilimo kwa kusaidia upatikanaji wa pembejeo, masoko na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nijielekeze katika ukulima wa mbogamboga. Katika kilimo hiki cha mbogamboga sasa hivi vijana wamehamasika sana na wakulima wadogo hujiunga katika vikundi au mmoja mmoja katika kilimo hiki cha mbogamboga. Kwa bahati njema sana mazao ya mbogamboga yanahitajika ndani ya nchi lakini pia nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo ni moja usafiri wa ndani kuhakikisha mazao haya yanafika kwa wakati katika maeneo husika lakini pia usafiri wa nje wakati wanapopata tenda za kusafirisha mazao hayo nje ya nchi kunakuwa na tatizo la usafiri kwa kuzingatia kwamba mazao mengi ya matunda na mbogamboga yanatoka kwenye Mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya na kwingine. Ni vyema sasa Serikali ikaimarisha Kiwanja cha Ndege cha Songwe ili wakulima na wasindikaji na wazalishaji wa maeneo hayo wapate urahisi wa kusafirisha mazao yao nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine katika ukulima huu wa mbogamboga napenda niongelee kuhusu suala la vifaa vya kilimo na hususani vifaa vya kilimo vya mbogamboga kama green house. Vifaa hivi vya kilimo vinatozwa VAT vya asilimia 18 na kwa maana hiyo sasa mkulima mdogo au kijana aliyemaliza masomo yake anataka kujiingiza kwenye ukulima huu wa green house, vifaa hivi vinakuwa ni vya bei kubwa sana. Hivyo, anashindwa kuwekeza kwa maana ya vifaa vyenyewe kwamba vifaa vya ujenzi, vifaa vya mipira ya kumwagilia na vinginevyo vinakuwa na gharama kubwa sana ambapo vijana na wakulima wadogo wanashindwa. Naomba Serikali iliangalie hili kwa upana ili kupunguza VAT hii ya asilimia 18 kwa vifaa vya uzalishaji wa matunda green house na nyinginezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea dhamana ya mikopo kwa wakulima wadogo na vikundi vidogo vidogo vya wakulima imekuwa ni tatizo kupata mikopo kutokana na kwamba hawana dhamana yoyote ambayo itawalinda kupata mikopo hiyo. Naomba sasa Serikali itafute njia bora zaidi na nyepesi zaidi ambayo itakuwa kama ni dhamana kwa vijana wetu na vikundi vyetu vidogo vidogo vya wakulima kuweza kukopesheka. Kwenye sekta hiyo ya kilimo kuna tatizo pia kwenye kodi kubwa VAT ya vifungashio. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vMheshimiwa Mwenyekiti,ifungashio vya mazao ya kilimo na mbogamboga imekuwa na VAT kubwa ambapo wakulima wanashindwa sasa kuhimili vile vifungashio vyenye ubora ambavyo vitaweza kusababisha kusafirisha mazao yao nje ya nchi na badala yake wanajikuta mazao yao tunauziana wenyewe hapa ndani ya nchi na tunakosa soko la nje lakini pia tunakosa fedha za kigeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hili Mheshimiwa Waziri alizingatie kwenye vifungashio pia vya mazao ya kilimo na mbogamboga. Kwa sababu sasa hivi wawekezaji wetu wa kilimo wanaagiza vifungashio kutoka nje ya nchi na kuviingiza Tanzania. Tufanye mipango sasa vifungashio hivi vizalishwe ndani ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na tozo nyingi ambazo zinamfanya mwekezaji kuwa na mlolongo mkubwa wa tozo mbalimbali. Naiomba Serikali sasa iziangalie tozo hizi ziweke mazingira wezeshi itakayomfanya mwekezaji awe analipa eneo moja tu na kumaliza shughuli zake na kuanza kuwekeza, tujenge mazingira wezeshi kwa wawekezaji wetu wa nje na ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea hapo hapo ssa hivi naigusa sekta ya maziwa. Sekta ya maziwa inatupa lishe lakini pia inatupa afya bora na kwa kuzingatia kwamba maziwa yanapozalishwa yanakuwa na matatizo na mambo madogo madogo ambapo tunahasishwa sasa tunywe maziwa yaliyosindikwa ambayo ndiyo yenye ubora kwa afya zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia hilo kwenye uwekezaji wa sekta ya maziwa nako pia kuna mlolongo mkubwa wa kulipa vitu mbalimbali kama hiyo mambo ya fire, VAT na vinginevyo ni vingi sana mpaka wazalishaji wa maziwa wanashindwa sasa kuhimili vile vikwazo vidogo, naomba hizi changamoto ndogo ndogo Serikali iziangalie kwa hawa wawekezaji wa maziwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kwenye sekta hiyo ya maziwa ukiondoa hayo mlolongo wa mambo hayo mambo yanatakiwa kulipa, kwenye kuwekeza maziwa, maziwa yanayozalishwa kwa muda mfupi hayatozwi VAT lakini ukizalisha maziwa ya muda mrefu yanatozwa VAT. Kwa maana hiyo sasa wawekezaji wanawekeza kwenya maziwa ambayo ya muda mfupi ambayo hayatozi VAT.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vyema sasa tukaliangalia hili ili wawekezaji wetu wawekeze maziwa muda mrefu ili waweze kusafirisha nje ya nchi kwa sababu yatakuwa yanadumu kwa muda mrefu na tutapunguza lile tatizo la sisi kuagiza maziwa kutoka nje na kuyaingiza ndani ya nchi kwa sababu ya kwetu sisi ni ya muda mfupi yake yanatoka nje ya muda mrefu, hili nafikiri tuliangalie sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea kwenye sekta ya maji kwa kuwa tuliomba tuongezewe Sh.50 kwenye lita ya mafuta kwa ajili ya Mfuko wa Maji, nashauri Serikali kama hili haliwezekani tutafute njia mpya njia mbadala ya kuongezea huu Mfuko wa Maji ili tuweze kutatua matatizo ya maji ndani ya nchi yetu. Kilio kikubwa kimekuwa kwenye maji na tumeweka kwenye mpango kilimo cha umwagiliaji. Kilimo cha umwagiliaji tutahitaji maji, tutahitaji mabwawa, tutahitaji visima. Kwa hivyo ni vyema pia tukaliangalia ili kuongeza kwenye Mfuko wa Maji ili tuweze kujenga hayo mabwawa, visima na miundombinu mingine ya umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea kwenye sekta ya uvuvi, ni vyema pia Serikali ikaiangalia kwa upana wake sekta ya uvuvi. Sekta ya uvuvi ni eneo moja ambalo litaipatia Tanzania fedha za kigeni, litaipatia ajira vijana wetu pia tutapata lishe bora kwa kula samaki ambapo watakuwa wengi tunawavua hapa nchini. Pia tujikite katika uwekezaji, naomba Serikali, hii bandari ya uvuvi ipewe kipaumbele ili imalizike na baada ya kumalizika kwa bandari ya uvuvi, Serikali sasa tumeshajikita katika kununua ndege sasa tujikite tena pia Serikali kwenye kununua meli ya uvuvi. Naipongeza Serikali kwa hilo, tumenunua ndege sasa tujikite tena tujipange, tujifunge mkanda, tununue meli ya uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea na suala la umeme. Umeme ni uchumi, umeme ni siasa na umeme ni usalama. Huduma hii ya umeme katika bajeti ya mwaka jana tulizungumzia kuhusu suala la umeme Zanzibar baina ya ZECO na Shirika la Umeme TANESCO. Tunaomba sasa huu mchakato umalizike kwa kuwa mtumiaji wa umeme wa Zazibar inabidi alipe VAT mara mbili kwa sababu tukinunua umeme tunalipa VAT, mtumiaji mdogo analipwa VAT sasa ni vyema sasa VAT hii iwekewe mikakati iwe inalipwa sehemu moja tu ili kumpunguzia mzigo mwananchi mdogo ili asielemewe na mzigo na kwa sababu hii ndio maana kumekuwa na malimbikizo makubwa sana ya umeme kule Zanzibar kwa sababu suala hili bado halijapita ufumbuzi wapi VAT hii ilipwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea kwenye huduma za mama, afya na mtoto; naipongeza Serikali kwa kulipa kipaumbele suala la afya ya mama na mtoto. Pia naiomba Serikali kila kwenye kituo cha afya basi iweke chumba cha kujifungulia mama na mtoto na chumba pia cha kupumzika baada ya kujifungua ili kuweka usalama wa mama na mtoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa hatua mbalimbali za kusamehe kodi mbalimbali za kilimo ikiwemo mambo ya ngozi na mambo mengine ya kilimo. Hapa naipongeza Serikali sana kwa kuliona hili, lakini pia nataka Serikali itupie macho katika haya mambo niliyoainisha kwenye sekta ya maziwa, sekta ya mbogamboga na sekta nyingine za uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwanza kabisa nachukua fursa hii kuipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa jitihada zake zote inazofanya kuwasaidia wananchi wa Tanzania katika kuwaletea maendeleo na pia kuwasaidia kupata huduma muhimu ikiwemo ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naanza na Mfuko wa Maji ambao ni chanzo muhimu sana cha upatikanaji wa fedha za kusaidia maendeleo ya maji na tumeona ufanisi wake kwa kipindi hiki kwa kufanyiwa mpango na Serikali kutoza tozo ya shilingi 50 kwa kila lita. Ombi langu kwa Serikali, tuongeze tena shilingi 50 kwa kila lita ya mafuta ya petroli na dizeli ili kuufanya mfuko huu ukusanye jumla ya shilingi bilioni 316, fedha hizi zikipatikana zitasaidia sana miradi ya maji vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, taasisi za maji au Mamlaka za Maji zinakabiliwa na madeni makubwa ya maji kwa takribani shilingi bilioni 38. Naishauri Serikali ili Mamlaka za Maji ziweze kujiendesha na kuongeza huduma za maji kwa wananchi, madeni haya yalipwe kwa haraka ili mamlaka zetu ziweze kujiendesha na kutanua huduma za maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naipongeza Wizara ya Maji kwa kuanzisha prepaid meter ambazo zitasaidia sasa, wale wadaiwa sugu wa maji watakuwa hawana tena njia ya kukwepa kulipa madeni hayo. Namshauri Mheshimiwa Waziri, hizi prepaid meter watakapozifunga, wazianzishe kwa wale wadaiwa sugu wa madeni makubwa ya maji, muanzie huko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maji yanahitaji dawa za kusafishia na kutibu. Katiba dawa za kusafishia na kutibu maji, naishauri Serikali iondoe au ipunguze kodi ili dawa hizi zipatikane kwa nafuu ili kumpunguzia mzigo mwananchi kwa sababu dawa hizi zinagharimu fedha nyingi na ni lazima tuzipate ili tusafishe maji yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashauri au nakubaliana na wazo la Wizara kwa kuhamasisha wananchi sasa katika Halmashauri, Wilaya na Mikoa na maeneo yote yanayojengwa, uvunaji wa maji ya mvua. Maji ya mvua uvunaji wake baada ya kutengeneza miundombinu inakuwa ni rahisi na salama na hayahitaji tena madeni makubwa ya kulipia umeme katika kuyavuta maji. (Makofi)

Kwa hiyo, tukihamasishana sisi wananchi katika uvunaji wa maji ya mvua, hii itasaidia sana kutatua baadhi ya matatizo hasa kwenye kilimo na mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naipongeza Wizara kwa kuanzisha Wakala wa Maji Vijijini. Wakala wa Maji Vijijini itaisaidia sasa Wizara kusimamia moja kwa moja miradi ya maji lakini pia itasimamia moja kwa moja matumizi ya fedha za miradi ya maji na kufuatilia maendeleo yake kwa haraka zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikiendelea, niongelee kuhusu Tume ya Umwagiliaji. Tume hii ndiyo chemchem na chimbuko la kilimo cha umwagiliaji. Hivyo ni vyema basi fedha zinazotengwa kwa ajili ya Tume ya Umwagiliaji zipelekwe kwa wakati na pia kutafuta vyanzo mbalimbali vya fedha vya kusaidia Tume hii ya Umwagiliaji ili kuweza kutekeleza majukumu yake, kwani kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa na mabadiliko ya tabianchi kilimo chetu kimekuwa kinayumba. Kwa hiyo, kilimo cha kumwagilia ndiyo kilimo kitakachomkomboa mwananchi wa kijijini katika kukamilisha azma ya kujiletea uchumi wa maendeleo, uchumi wa viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna upungufu mkubwa wa wataalam wa maji na umwagiliaji, naishauri Wizara inayohusika na kuajiri itoe kibali sasa, Wizara iajiri wataalam hao wa maji na pia wataalam wa umwagiliaji ili kuweza kutekeleza majukumu ya kumsaidia mwananchi katika kilimo bora na pia kumsaidia mwananchi kule aliko kijijini kwenye Mamlaka za Maji na Halmashauri kuweza kupata wataalam wa maji na miundombinu ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda kuipongeza Serikali kwa hatua iliyochukua ya kukaribia kukamilisha zile fedha za miradi ya maji ya Mfuko wa India ambazo fedha hizi zikipatikana zitasaidia miji 17 ya Tanzania kupata maji. Hapo tutakuwa tumetatua tatizo kwa kiasi fulani la upungufu wa maji ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika kudhibiti maji yasipotee, hatua ya Wizara ya kutengeneza miundombinu ya maji iliyo chakavu na kutengeneza mingine mipya ili kudhibiti maji yasipotee kiholea, nashauri suala hili litiliwe mkazo. Katika kutengeneza miundombinu hiyo ya maji na kuanzisha mingine mipya, tuangalie ubora wa vifaa, mitambo na miundombinu hiyo kwa sababu inaelekea kuna baadhi ya vifaa na miundombinu ni mpya lakini tayari imeshakuwa chakavu na inavujisha maji ovyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika uhifadhi wa vyanzo vya maji, naipongeza Serikali kwa kuhifadhi vyanzo vya maji vyote nchini na pia kuongeza vyanzo vipya vya maji na kuvifanya kuwa maeneo tengefu. Hili la uhifadhi wa vyanzo vya maji linahitaji sote wananchi tulipe kipaumbele kwa sababu baadhi ya vyanzo vya maji wananchi wanavichafua kwa makusudi. Kwa hiyo, jitihada za wazi zinahitajika katika kuhifadhi vyanzo vyetu vya maji ambavyo ndiyo chanzo kikuu cha maji. Tuvihifadhi na tuviwekee uangalifu wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende kwenye Chuo cha Maji, hiki ndiyo chuo ambacho kwa Tanzania hii kinatoa wataalam wa maji na wataalam wa uchimbaji wa visima na mambo mengine.

Mheshimiwa Spika, nashauri chuo hiki kiendelee kuongeza wanafunzi na kuongezewa fedha ili tupate wataalam wengi wa maji, tuwasambaze vijijini kote ili wakasaidie miradi ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu Wakala wa Uchimbaji Visima (DDCA), nashauri Serikali, kwa sababu hiki kitengo ndiyo kinachosaidia kuchimba visima na mabwawa ndani ya nchi yetu, kiongezewe mitambo ya kisasa na wataalam wa kisasa wanaoweza kuchunguza maji ndani ya Tanzania yetu, wapi yapo, yapo kwa kima gani, kwa ukubwa gani, kwa mita ngapi ili tuweze kufanya kazi ya uchimbaji wa visima kwa usahihi zaidi na kuepusha kuchimba visima ambavyo baadaye havitoi maji.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hii DDCA inatakiwa ijengewe uwezo wa kutosha na vijana wetu watakaotoka DDCA wasambazwe wilayani na mikoani ili kusaidia uchimbaji wa visima, mabwawa na utengenezaji wa mabwawa ya kuvunia maji ili wananchi tuvune maji na tupate maji kwa uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho namalizia kwa kusema naipongeza Wizara kwa jitihada zake. Suala la maji ni la msingi, wananchi tunahitaji maji, mimea inahitaji maji, wanyama wanahitaji maji. Suala la maji sasa hivi Serikali tumejitwisha kwenye mabega, inafaa kwa wakati huu tuliweke kichwani liwe ndiyo agenda kubwa ya maji katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana nakushukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Awali ya yote na mimi napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyeniweka hadi leo kuwa nina afya na uzima. Kwanza, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchukua nafasi hii adhimu kuipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi, inayoongozwa na jemedari wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli; Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan; Waziri Mkuu pamoja na Mawaziri wote waliomo ndani ya Wizara hii ya Ofisi ya Waziri ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Dada yangu Jenista Mhagama na Mheshimiwa Angellah Kairuki, pamoja na Naibu Mawaziri wote kwa nzuri wanayoifanya katika kutekeleza majukumu yao na kuwaletea wananchi wetu maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti ya mwaka jana nilichangia kuhusu kusamehewa VAT kwa umeme tunaouziwa kutoka TANESCO kwenda ZECO Zanzibar. Napenda nichukue nafasi hii kwa heshima kubwa kwa niaba ya Wazanzibar kuipongeza kwa dhati Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Marais wetu wawili kwa kutafakari na kufikiria hili kwa lengo la kuimarisha Muungano kwa vitendo na kuudumisha kwa kutusamehe deni la umeme la shilingi bilioni 22.9 na pia kutuondelea VAT kwenye umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili litaongeza ari ya pamoja kwamba Tanzania tuna dhamira ya dhati kuelekea kwenye uchumi wa viwanda kwa sababu viwanda vingi vinategemea umeme. Kwa hiyo, kupungua kwa bei ya umeme kutaongeza chachu ya wawekezaji Zanzibar, ajira itapatikana na uchumi utakua kwa pande zote mbili za Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia na kuipongeza Wizara hii ya Uwekezaji kwa kuendelea kuandaa mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara na wawekezaji ndani ya nchi. Naomba juhudi hizo ziendelee kwa kupunguza changamoto mbalimbali zinazowakabili wawekezaji wetu ili kuongeza uwekezaji katika sekta mbalimbali na hatimaye kuongeza ajira, kukuza uchumi na kufikia hatua ya uchumi wa kati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili naipongeza sana Wizara ya Kilimo lakini pia naipongeza Wizara ya Mifugo kwamba tayari wameshaanza kuanzisha viwanda vya nyama pamoja na usindikaji wa ngozi. Kama tunavyofahamu ngozi yetu ilikuwa haina soko lakini sasa ngozi yetu itapata masoko kwa kusindikwa hapa nchini na pia kuanzisha viwanda vya nyama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuleta vitambulisho vya wafanyabiashara au wajasiriamali wadogo ili waweze kufanya biashara zao bila ya kubughudhiwa. Pamoja na hilo napenda tuendelee kuzishauri Halmashauri zetu ambazo baadhi yao zinawabughudhi hawa wafanyabiashara na wajasiriamali wadogowadogo kwa kuwatoza kodi ndogo ndogo. Mheshimiwa Rais amelikemea hilo, kwa hivyo na sisi tumuunge mkono kwa kulikemea ili wafanyabiashara na wazalishaji wetu wadogowadogo waweze kufanya biashara zao bila kubughudhiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika uwekezaji tuhakikishe malighafi za ndani zinapata masoko na yataanzia kwenye viwanda vinawekezwa hapa nchini. Nashauri tuhakikishe viwanda vyetu vinavyowekezwa hapa nchini vinatumia malighafi zetu za ndani ili kuwapa wakulima wetu masoko, masoko yetu yaanzie humu ndani ya nchi kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo, ili tupate masoko na bidhaa bora ambazo zitahitajika katika viwanda vitakavyoanzishwa ni lazima tuwekeze vizuri kwenye sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi kwa kuendeleza utafiti ili tupate mbegu bora za mifugo na kilimo ili bidhaa zetu kwenye viwanda hivyo ziwe na tija. Tuwe na bidhaa chache tunazozalisha lakini tunapata tija kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala la uvuvi, naomba Serikali iendelee na harakati za kuwekeza kwenye uvuvi wa bahari kuu. Nashauri iwekeze kwa kujenga gati za uvuvi na kununua meli uvuvi kwa ajili ya kujipanga sasa kuingia kwenye soko la kimataifa kwa uvuvi wa bahari kuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuipongeza Serikali kwa juhudi mbalimbali inayochukua katika kuwaletea wananchi wetu maendeleo ikiwemo kupunguza kodi na tozo mbalimbali kwa bidhaa mbalimbali za kilimo na ufugaji. Serikali imepunguza tozo na naomba iendelee kuangalia tozo mbalimbali ambazo zinakwamisha wawekezaji na wazalishaji wetu wadogo wadogo. Nashauri Serikali iendelee kukaa na wawekezaji na wazalishaji wadogowadogo ili kubadilishana mawazo na kutatua na kuzivumbua changamoto mbalimbali zinazokwamisha shughuli za maendeleo katika nchi yetu ili uwekezaji wetu uwe mzuri na wenye tija. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namalizia kwa kuipongeza Serikali kwa kuwa nchi yetu sasa iko salama, mipaka ya nchi iko salama, shughuli za maendeleo na kiuchumi zinafanyika kwa sababu nchi iko salama, kuna utawala bora, maendeleo yanapatikana, juhudi zinaonekana, wananchi wanafurahia maendeleo, reli zinajengwa, miundombinu inaimarishwa, barabara zinajengwa na ndege watu wanakosa nafasi. Sasa hivi watu wanapotaka kusafiri kwenda nje wanaambiwa ndege ya Air Tanzania imejaa wanaanza kuhangaika kutafuta ndege maeneo mengine ili waweze kusafiri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Spika, kwanza nachukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa juhudi kubwa na mchango wake mkubwa katika kuinua Sekta za Michezo, Sanaa na Utamaduni.

Mheshimiwa Spika, naipongeza Wizara na Viongozi wa Wizara kwa kazi kubwa na ya uzalendo mkubwa katika kuzisimamia sekta zote za Wizara na kufikia hatua nzuri ya mategemeo kwa Taifa na wananchi. Napenda kuwatia moyo waendelee na juhudi hizo wanazozifanya, michezo na sanaa imekua na imeleta sifa kubwa kwa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, nashauri Wizara iendelee kuendeleza vipaji vya wanamichezo pamoja na wasanii wetu sambamba na kuvumbua vipaji vipya. Serikali iendelee kuwatambua na kuwaenzi wasanii na wanamichezo kwa mchango wao mkubwa walioutoa katika Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kupitia vyombo na Taasisi zake zinazohusika na kutoa elimu ya maadili, viendelee kutoa elimu juu maadili mema kwa wasanii, waigizaji na wanamichezo ili waendelee kuwa kioo kwa jamii.

Mheshimiwa Spika, Kiswahili, Serikali na Wizara kwa ujumla naipongeza kwa kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili; lugha yetu hii imezidi kuzungumzwa duniani. Hivyo, nashauri juhudi hizo za kukiendeleza Kiswahili ziendelee kwa lengo la kukiongeza nguvu duniani kote, kuitangaza nchi yetu kupitia lugha yetu hiyo ya Kiswahili, kudumisha utamaduni pamoja na kuongeza soko la ajira kwa wataalam na watumiaji wa Kiswahili hapa nchini kwetu.

Mheshimiwa Spika, michezo ya zamani ambayo yana faida na mchango kwa Taifa na wanamichezo wenyewe ambayo imepotea au haina nguvu ifufuliwe na kupewa msukumo. Nashauri Serikali iongeze fedha kwa Wizara hii ili kukamilisha majukumu yao. Mwisho Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wote wa Wizara nawapongeza kwa kazi nzuri ya kuendeleza kazi zote zilizomo ndani ya Wizara.

Mheshimiwa Spika, ahsante na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nakushukuru kwanza naanza kwa kuunga mkono hoja hii, pili nachukua nafasi hiI kuipongeza sana Serikali kwa juhudi na dhamira yake ya dhati kabisa katika kuwapatia watanzania maji safi na salama, napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa wanavyojitoa kwao kuhakikisha wananchi wa watanzania wanapata maji na kufuatilia miradi ya maji vijijini huko iliko pamoja na Mijini, nawapongeza sana Waheshimiwa Mawaziri wetu na watendaji wote kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kuhakikisha watanzania tunapata maji safi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo, maji ni uhai, maji ni afya, maji ni uchumi na kwa maana hiyo maji yakiwa ni uchumi kilimo kinahitaji maji, ufugaji unahitaji maji, mimea, miti na sisi binadamu tunahitaji maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi nashauri Serikali iongeze fedha za maendeleo katika kuhakikisha miradi hii ya maji inafanikiwa, na katika kuongeza fedha hizo za maendeleo naungana na Wabunge wenzangu waliosema kwamba katika mfuko wa maji tunahitaji kuongeza fedha ili
tutekeleze miradi ya maji, Serikali itafute vyanzo vya mapato kuhakikisha mfuko huu unakuwa mkubwa ili kuhakikisha miradi ya maji inatekelezeka ili kufikia malengo yetu tuliyojiwekea ifikapo mwaka 2020. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuchelewa au kusuasua kwa miradi hii ya maji baadhi ya miradi ya maji imekwama kutokana na ucheleshaji ulioko bandarini kukosekana kwa misamaha ya kodi kwa vifaa vya maji. Ucheleweshaji huo unakwamisha pia utekelezeji wa miradi mbalimbali ya maji, pamoja na hilo ucheleweshaji pia unakuwa kwenye utoaji wa vibali vya kazi kwa wataalam wa maji ambao wanatoka nje ya nchi, wanachelewa kupata vibali vya kazi kwa hivyo miradi hii inachelewa kuanza kutoka na kukosekana kwa wataalam hao. Hili ni la kufanyia kazi kwa Wizara zinazohukia ikiwemo TRA pamoja Wizara ya Mambo ya Ndani ili kuhakikisha masuala haya tunayafanyia kazi kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utekelezaji wa miradi kuna changamoto nyingi zinakwamisha utekelezaji wa miradi, ikiwemo upungufu wa wataalam wa maji, Wizara inahitaji wataalam wa maji wapatao 3,910. Hili ni pengo kubwa sana kwa sababu kukosekana kwa wataalam hawa 3,910 wa kusimamia miradi katika maeneo yetu mbalimbali ya Tanzania inachangia sana kukwamisha utekelezaji wa miradi hiyo na pia kusababisha kununuliwa kwa vifaa ambavyo viko chini ya kiwango na utekelezaji wa miradi ambayo iko chini ya kiwango. Naomba Serikali isaidiane kutekeleza kazi hii ya kutoa vibali vya ajira kwa wataalam hawa wa maji ili waajiriwe na wakasimamie miradi yetu ya maji vijijini huko tunakohitaji mahitaji ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukwamisha pia upanuzi wa miradi ya maji katika miradi hii ya maji kuna madeni karibu bilioni 29 ni zaidi ya bilioni 21 Mamlaka za Maji zinadai kwa Taasisi za Serikali. Hili linakwamisha sana Mamlaka za Maji, kutengeneza miradi ya maji pamoja na kutanua hiyo miradi yenyewe ya maji huko vijijini, tunaomba madeni haya Serikali itafute mbinu ya kuyalipa au kuyakata huko huko Wizara ya Fedha ili mamlaka hizi zipate fedha zake zitekeleze miradi hii. Naipongeza sana Wizara kwa kazi iliyoanza ya kuweka prepaid mita ili kutatua tatizo hili la madeni. Lakini nashauri pamoja na kuongeza hizo prepaid mita hizo zilizokuwepo zianzwe kufungwa kwenye hizo Taasisi ambazo ni wadaiwa sugu wa maji wakawafungie huku badala ya kuwafungia wananchi, waanze na hizo Taasisi ambazo zinadaiwa mabilioni haya ya fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika miradi midogo midogo ya maji huku vijijini wananchi wanapata mzigo mkubwa wa kufidia au kulipia gharama za dizeli. Nashauri miradi hii mingi ya Vijijini ambayo ni miradi midogo midogo basi tuende na kutumia Solar System ambazo zitakuwa na betri zake ili hata wakati wa mvua ziweze kufanya kazi kusukuma maji katika visima hivi. Hii itapunguza gharama za uendeshaji wa miradi ya maji, pia itampunguzia mzigo mwananchi wa chini ambaye hana uwezo au kipato chake ni kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nashauri uhamasishaji wa nguvu ufanyike pamoja na kutoa elimu kuhusu uvunaji wa maji ya mvua. Maji yetu ya mvua ni salama hayahitaji madawa, yanahitaji tu kuwekewa miundombinu ili tuyavune tuweze kuyatumia. Na katika kupanda mimea maji ya mvua yana rutuba kuliko maji mengine yoyote, hata huo ujenzi wetu uzingatie miundombinu ya uvunaji wa maji ya mvua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nashauri uhifadhi wa vyanzo vya maji, elimu itolewe katika kuhamasisha wananchi juu ya kuhifadhi vyanzo vya maji na utunzaji wa mazingira. Na katika kuhamasiha wananchi nashauri Wizara pia itambue sasa mwananchi mmoja mmoja au vikundi, au taasisi vitakavyokuwa vinahifadhi vyanzo vya maji na vinatunza mazingira viwatambue na kuwapa tunzo au motisha maalum ili iwe hamasa kwa wengine nao kushawishika kutunza vyanzo vya maji na kuhifadhi mazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho namalizia kwa kusema kwamba maji safi na salama ndiyo yanayozaaa maji taka. Kwa hivyo kama maji safi na salama ndiyo yanayozaa maji taka ni vyema basi miundombinu ya maji safi iende sambamba na miundombinu ya maji taka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, naipongeza Serikali kwa yote yanayofanywa tuko pamoja Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri tuko pamoja kukusaidia katika kutatua changamoto hizi, kukushauri kila tunapohitajika. Naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: AhsanteMheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwanza kabisa napenda kuipongeza Serikali, napenda kuipongeza pia Wizara ya Kilimo, Mheshimiwa Waziri, Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara ya Kilimo kwa juhudi kubwa wanayoifanya kuhakikisha kilimo cha Tanzania kinakua, kinakua endelevu na chenye tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuipongeza Serikali na Mheshimiwa Rais kwa kuitoa Tume ya Umwagiliaji kwenye Wizara ya Maji na kuipeleka kwenye Wizara ya Kilimo. Tume hii kupeleka kwenye Wizara ya Kilimo imefika hasa pahali pake; kwa maana kwamba Wizara ya Kilimo sasa itaitumia Tume hii ya Umwagiliaji kwa kukuza kilimo chetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Tume hii ya Umwagiliaji lazima sasa Wizara ijipange vizuri ili kuhakikisha Tume hii watendaji wake wanafanyakazi kwa uadilifu na weledi. Ili kuifanya Tume hii ya Umwagiliaji iweze kufanya kazi zake vizuri ni vyema sasa miundombinu yote ya umwagiliaji inayohusu kilimo iangaliwe upya kuhusu kodi; ikiwemo mitambo ya kuchimbia mabwawa, vifaa vyote vya umwagiliaji pamoja na mitambo ya kuchimbia visima vya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiliangalia hili la kodi miradi ya umwagiliaji itakuwa na wananchi watahamasika sana kulima kilimo cha umwagiliaji. Kutokana na hali na mabadiliko ya tabia nchi kilimo cha umwagiliaji ndiyo mkombozi wetu wananchi wa Tanzania. Kwasababu kilimo hiki kitakuwa endelevu na cha muda wote kwa maana hiyo viwanda vyetu sasa vitapata malighafi ya kutosha na kwa muda wote. Pia kilimo cha umwagiliaji kitatuweka vizuri katika usalama wa chakula na kilimo cha biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea, katika kuimarisha kilimo chetu nchini ni vyema sasa tukawekeza zaidi kwenye utafiti. Tuingize nguvu zetu nyingi katika utafiti katika kupata mbegu bora ambazo zitatoa mazao mazuri yenye tija. Kwa faida ya kilimo hiki ni vyema sasa tukaziimarisha hizi taasisi zetu za utafiti kama TARI, Taasisi zetu za kutayarisha mbenu kama ASA, tukazipa mitaji ya kutosha ili ziweze kufanyakazi zake vizuri kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania na hasa wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuipongeza Serikali na Wizara ya Kilimo kwa kuanzisha kitengo cha kutafuta masoko ya kilimo. Kitengo hiki kitakuwa mkombozi na mtatuzi wa changamoto za mazao yetu ya kilimo katika masoko mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuipongeza Wizara ya Kilimo kwa kuanzisha mradi wa kudhibiti sumu kuvu. Sumu kuvu ilikuwa ni tatizo kwa mazao yetu; na kwa vile mwananchi alikuwa hajui sumu kuvu ni nini kwahiyo baadhi ya wananchi walipoteza maisha kutokana na kula vyakula vilivyokuwa na sumu kuvu. Kwahiyo naipongeza hii Wizara kwa kuliona hili na kuhakikisha kwamba mazao yetu yanakuwa hayana sumu kuvu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naipongeza Serikali kwa kuongeza bajeti ya kilimo. Bajeti ya kilimo imeongezeka. Pia napenda kuishauri Serikali iendelee kuongeza bajeti ya kilimo ili kukidhi matakwa na mahitaji yote ya Wizara ya Kilimo na taasisi zake zote. Bajeti ikiongezeka taasisi zote zitapata fedha na miradi ya kilimo itaongezeka kwa kupata mbegu bora viuatilifu bora na mengineyo. Naipongeza Serikali kwa kuona nakupunguza tozo mbalimbali za kilimo, lakini pia naishauri Serikali iendelee kuangalia tena uwezekano wa tozo na vikwazo au changamoto mbalimbali inazokabili sekta hii ya kilimo ili wananchi wahamasike kulima kilimo chenye tija na kilimo cha biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati imechambua kwa kina sana kuhusu zao la korosho, naipongeza sana kamati kwa ushauri wake kwa Serikali, na ninaamini kwamba Serikali haina nia mbaya na wananchi au wakulima wa korosho. Wakulima wa korosho watalipwa na watapata haki zao kwasababu najua Serikali iko mbioni sasa kuhakikisha madeni yote yanalipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nyongeza tu, na mimi napenda kuongeza kwenye korosho kwamba waangalie pia na wadai wa korosho wa mwaka 2017/2018, kwa sababu nako huku kwenye vyama vya ushirika vimewatapeli wananchi wetu wakulima wa korosho kwa madai yao ya mwaka huu. Kwa hiyo Serikali itakapoandaa mchakato wa kuwalipa wananchi na wakulima wa korosho iangalie pia na wale wa mwaka wa jana; kwa sababu tunataka kilimo cha korosho kiwe endelevu na chenye tija mazao yaongezeke tupate mazao ya biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo naipongeza sana Wizara ya Kilimo kwa jitihada mbalimbali za kuendeleza kilimo nchi Tanzania na Serikali yetu kwa ujumla ya Chama cha Mapinduzi na Mheshimiwa Rais wetu kuhakikisha kwamba kilimo kinakua, kilimo chenye tija kwa ajili ya biashara na mtaji au rasilimali muhimu na mali ghafi kwa viwanda vyetu tunavyovijenga.

Mheshimiwa Mwenyekiti,, naunga mkono hoja, ahsante sana, nakushukuru kwa kunipa nafasi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza naanza kwa kuunga mkono hoja ya Wizara hii na kuipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kazi kubwa wanayoifanya kuhakikisha sasa Tanzania yetu inapata mafanikio katika Sekta hii ya Mifugo na Uvuvi. Napongeza mikakati na mipango yote iliyopangwa na Wizara na naomba Serikali na sisi wadau tuhakikishe tunaungana na Serikali na Wizara hii kuhakikisha mipango yetu hii inafanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi na shukrani hizo na pia naipongeza Wizara kwa kuanzisha kupitia upya Sheria ya Uvuvi na hasa pale walipoamua kwa makusudi kabisa kuwashirikisha wadau wote wa sekta hii ya uvuvi nchini kote Tanzania. Pamoja na hilo pia, naipongeza Wizara kwa kutafsiri Sera ya Uvuvi. Kama tunavyofahamu wavuvi wetu wengi ni masikini hawajasoma Kingereza kwa hivyo naipongeza Wizara hii kwa kuamua kuitafsiri sasahivi ile Sera ya Uvuvi, ili kila mvuvi aweze kutambua sera hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza Wizara kwa kufufua Shirika la TAFICO. Najua mambo mengi yameshafanyika huko TAFICO, lakini pia naomba sasa Serikali iangalie hili jambo ambalo ni mwingiliano wa kisheria na kanuni na majukumu ya utendaji wa kazi kati ya Wizara hii ya Uvuvi na Wizara nyingine za Serikali. Jambo hili likifanyiwa kazi kuna changamoto nyingi zitaweza kutatuka. Pia naomba Serikali iangalie tozo mbalimbali kati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Wizara nyingine, kuna tozo zinaingiliana na hivyo kuleta mkanganyiko katika utekelezaji wa majukumu ya kazi ya Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi naomba nigusie kidogo uvuvi wa bahari kuu. Napongeza sana mchakato wa Wizara na mchakato wa Serikali ulioanza wa ujenzi wa bandari ya uvuvi. Naomba mchakato huo sasa pia uanze na uendelee kwa upande wa Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuhusu uvuvi wa bahari kuu. Sisi kisiwa chetu cha Zanzibar hatuna rasilimali nyingine isipokuwa bahari, tumezungukwa na bahari, mapato yetu yanategemea sana bahari. Naomba sana Serikali iangalie sasa zile tozo ambazo zinatozwa kwa wanaoomba kuvua kwenye bahari kuu, yaani zile leseni za uvuvi ziangaliwe upya zile kodi na tozo ili angalau na sisi hizi leseni zikitolewa nchi yetu nayo itapata mapato kupitia hii sekta ya uvuvi wa bahari kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niingie kwenye sekta ya ukuzaji wa viumbe kwenye maji. Naipongeza sana Wizara na imepeta fedha hivi karibuni kwa ajili kuimarisha sekta hii ya ukuzaji wa viumbe kwenye maji na hasa ufugaji wa samaki. Pamoja na hilo liende sambamba na Maafisa Ugani ili wawe na teknolojia mpya katika ufugaji samaki na mazao mengine ya bahari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia huu ufugaji hautaki elimu kubwa sana; kwa hivyo naomba kile chuo cha uvuvi kinachofundisha mambo ya ufugaji samaki kiangalie ile mitaala au vile vigezo vya kuingia kwenye chuo kile cha kujifunza ufugaji wa samaki, kwa sababu tunaona hata majumbani watoto wadogo wa miaka saba wanawafuga wale gold fish na wanauza; kwa maana hiyo haitaki elimu kubwa. Hivyo vijana waliomaliza darasa la saba wakiwezeshwa, wakipewa mitaji na wakipewa elimu hii ya ufugaji samaki tunaweza kutatua tatizo la ajira kwa vijana wetu wa darasa la saba na vijana wa form four kwa sababu elimu inayohitajika si kubwa sana. Tuandae programu za muda mfupi za kuwafundisha hawa vijana ambao wamemaliza shule mapema ili wajiajiri kwenye sekta hii ya uvuvi na ufugaji wa samaki pamoja na kuwasaidia njia bora za kupata mikopo kwa gharama nafuu au kwa masharti nafuu waweze kukidhi kupata hivyo vifaa vya ufugaji wa samaki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na huduma mbalimbali za kuwasaidia wavuvi wetu naomba sana Serikali ione Wizara kwamba huduma za kijamii kama vile vyoo, vituo vya afya, vituo vya Polisi kwenye maeneo yale ya madago wanakovua wavuvi vipewe kipaumbele kwa sababu kule nako wanaishi binadamu na kunatokea milipuko ya maradhi, lakini pia kunatokea na hujuma mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo naomba Serikali na Wizara iendelee kuwaboreshea wavuvi wetu zana bora za uvuvi ili kupata uvuvi wenye tija na wenye faida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naelekea kwenye Wakala wa Maabara na …

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Khadija malizia, kengele ya pili imelia.

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia kwa kuipongeza Wizara hii kwa kuanzisha viwanda vya ngozi, viwanda vya usindikaji maziwa na viwanda vingine vipya vya usindikaji wa nyama. Tuko pamoja tunawapa nguvu viongozi wetu hawa, Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Maafisa wote, (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Spika, kwanza naipongeza Serikali yetu inayoongozwa na Rais wetu mpendwa Mheshimiwa John Magufuli kwa kazi kubwa sana inayofanya katika kuwaletea wananchi maendeleo na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi wa CCM kwa kiwango kikubwa.

Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa usimamizi mzuri wa Wizara hii pamoja na wasaidizi wake. Naipongeza Serikali kwa ujenzi na kuimarisha miundombinu, uboreshaji wa huruma za afya na elimu ikiwemo kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.

Mheshimiwa Spika, nashauri Serikali itenge fedha za kutosha ili kuwezesha kukabiliana na majanga na maafa yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.

Mheshimiwa Spika, mengine nakubaliana na mipango ya Serikali. Nashauri kupunguza kodi kwa vifaa vya kujikinga na maradhi. Ahsante.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema hii aliyotupa Chama chetu cha Mapinduzi kushinda ushindi wa kishindo na baadhi yetu kuturejesha Bungeni. Nampongeza sana Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi kwani leo Chama cha Mapinduzi na wanachama wake kinatimiza miaka 44 tangu kuzaliwa kwake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa napenda kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kauli yake aliyoitoa ndani ya Bunge hili kwamba atashirikiana bega kwa bega na Rais wa Zanzibar pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhakikisha kwamba Zanzibar inasonga mbele kiuchumi na wananchi wake wananyanyuka kiuchumi. Amedhihirisha hilo kwa kusema kwamba kwenye uvuvi wa bahari kuu anapeleka meli nne Zanzibar ambapo meli nne hizo zitasaidia Zanzibar katika dhana yake ile ya uchumi wa blue. Zanzibar sasa imejipanga kuingia kwenye uchumi wa blue na hapa Mheshimiwa Rais wa Muungano ameonesha dhamira yake ya dhati Zanzibar kuingia kwenye uchumi wa blue. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, najihusisha sasa kwenye sekta ya kilimo. Mheshimiwa Rais kwenye hotuba yake ameonesha dhamira ya dhati kwamba sasa anataka kumnyanyua mwananchi mdogo mdogo na mkulima mdogo mdogo, mvuvi pamoja na wafugaji ili waweze kupata tija ya kilimo chao, tija ya uvuvi wao na tija ya mifugo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali, Mheshimiwa Rais aliahidi kuwapunguzia kero wakulima na wavuvi na ameonesha kwamba tumepunguza tozo na kodi mbalimbali 114 ambazo zinamlenga mvuvi, mkulima na mfugaji na amesema wazi kwamba ataendelea kuangalia kero na tozo mbalimbali ambazo zinawagusa wakulima, wavuvi na wafugaji. Mheshimiwa Rais ameonesha dhamira ya dhati kuwasaidia wakulima wa bustani ambapo wakulima wa bustani walikuwa na changamoto kubwa sana katika usafirishaji wa mazao yao. Kwa hivyo sasa Serikali imepanga kununua ndege ambayo itasaidia kupunguza changamoto za kusafirisha mazao hayo ya bustani ambayo mazao ya bustani yana soko kubwa katika nchi za nje, tatizo ilikuwa jinsi ya kuyafikia masoko hayo. Mheshimiwa Rais ameonesha dhamira kwamba sasa masoko hayo yatafikiwa na wakulima watapata faida ya mazao yao wanaozalisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha kwamba kilimo chetu kinakuwa bora na endelevu na chenye tija, lazima sasa tuwekeze kwenye mbegu bora, mbegu ambazo zitalingana na udongo wa nchi yetu na mazingira yake na maeneo husika, lakini mbegu ambazo zitaangalia mazingira yanayohusika linapolimwa zao husika. Ni vema sasa tukaziimarisha taasisi zetu zinazohusiana na uzalishaji wa mbegu pamoja na viuatilifu ili viweze kutatua changamoto ya mbegu na viuatilifu kwa wakulima wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiendelea katika kilimo, naunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais za kutaka sasa kilimo kiwe kilimo cha kisasa, kilimo chenye tija ambacho kitakuwa kilimo cha umwagiliaji. Sasa ili kuhakikisha kwamba kilimo cha umwagiliaji kinafanikiwa ni vyema sasa tukaimarisha pia kwenye sekta ya maji ambayo itasaidia kwenye viwanda, ukulima, uvuvi na ufugaji. Tukipata maji ya kutosha kwa wananchi lakini pia maji ya kuimarisha kilimo chetu, nashauri Serikali Mfuko wa Maji uongezewe fedha ili kukidhi mahitaji hayo ya wananchi. Nasema hivi kwa sababu fedha ambazo zimetumika kwenye Mfuko wa Maji zimeonesha kutoa mafanikio makubwa katika kutatua changamoto za maji na hivyo tukiongeze fedha kwenye mfuko wa maji, tutaisadia sasa TAWASA ili iweze kukabiliana na changamoto za maji vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia, naomba nimpongeze sana Rais wa Jamhuri ya Muungano, wasaidizi wake wote, Mheshimiwa Spika, wewe mwenyewe kwa kulisimamia Bunge letu hili tukaweza kutekeleza yote ambayo tumefikia kwa sababu kazi ya Bunge ni kuishauri Serikali na kuisimamia. Bunge hili Bunge hili lilifanya kazi hiyo na ndiyo maana maendeleo haya yakafikiwa na nategemea wataendelea kufanya hivyo na sisi Wabunge tuko pamoja na wao na Serikali yetu kuhakikisha tunafikia pale tulipokusudia, kumpa Rais wetu imani na kumpa Rais wetu hamu ya kututetea na kutuletea maendeleo. Ameonesha dhamira ya dhati kwamba yeye ni Rais wa wanyonge na anatetea wanyonge.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Spika, kwanza nachukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa juhudi na hatua mbalimbali anazochukua kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama.

Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri na watendaji wake wote kwa kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Mheshimiwa Spika, naomba kuishauri Serikali; kwanza Wizara iendelee na jitihada za kudhibiti upotevu wa maji; pili, kulinda na kuhifadhi vyanzo vya maji; na tatu, kuongeza matumizi ya mita za LUKU (prepaid meter) kwa matumizi ya majumbani ili kuepusha mtumiaji wa maji kuchelewa kulipa bili za maji pia kumsaidia mwanachi kulimbikiziwa madeni ya maji.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, ahsante.
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba Ardhi na Mbingu hashindwi na walimwengu apangalo yeye huwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nampongeza Rais wetu na wasaidizi wake. Hapo walipotufikisha wametufikisha mbali, Watanzania tunajionea wenyewe maendeleo yaliyofikiwa katika kuwasaidia wananchi kwenye huduma mbalimbali za kijamii, kiuchumi na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara ya Fedha na wasaidizi wake wote kwa hotuba nzuri walizotuletea za mipango na makadirio. Naunga mkono hoja zote zilizowasilishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza na sekta ya kilimo. Kilimo kimeelezwa kwenye Mpango wa Mwaka Mmoja na wa Miaka Mitano. Naunga mkono hatua mbalimbali zilizoelezwa kwenye hotuba zote za kuimarisha kilimo kama uti wa mgongo wa kumuinua mwananchi mmoja mmoja na kuinua nchi kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo kina sekta nyingi lakini nitagusia kilimo ambacho kitahifadhi mazingira yetu. Ardhi yetu tunaihitaji sisi kama tulivyoikuta lakini pia na kuvirithisha na vizazi vijavyo. Nahamasisha kilimo kilimo hai na kilimo hifadhi. Kilimo hai na kilimo hifadhi kinalinda ardhi yetu ili iweze kutumika kwa miaka mingi lakini pia kinatoa mazao ambayo hayana kemikali ambapo kwa sasa ni mazao yenye bei sana katika soko la dunia na wananchi duniani wanayahitaji mazao ya aina hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo cha bustani ni kilimo ambacho sasa hivi kinaleta hamasa sana kwa vijana na wanawake kwa sababu kina soko kubwa nje ya nchi. Hata hivyo, lazima sasa tupange ardhi yetu, ardhi ya kilimo, ufugaji, viwanda, majengo na mengineyo. Kilimo hiki ukataji wa miti ni mkubwa, tunakata miti mikubwa ya kudumu tunalima bustani. Kwa hivyo, kilimo hiki kina fedha nyingi lakini pia kizingatie hali ya mazingira na hali ya nchi yetu kulingana na mabadiliko ya tabia nchi yanayotukabili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na waliosema kuhusu mbegu bora. Mbegu bora zinahitajika ili kwendana na mazingira ya nchi yetu, udongo wa nchi yetu na hali ya hewa. Kwa maana hiyo sasa ni vizuri kuwekeza kwenye utafiti. Utafiti unahitaji wataalam na elimu hii ni ya muda mrefu, nashauri Serikali, kuna wataalam wetu wa utafiti ambao wamestaafu lakini sasa wanatumikia nchi za jirani, watafutwe waungane na hawa waliopo ili waje kuendeleza soko hili la kuzalisha mbegu bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo cha umwagiliaji ndiyo muarobaini kutokana na hali ya hewa na mazingira ya tabianchi. Kilimo cha umwagiliaji kinatupa usalama wa chakula lakini kitatoa mazao bora kwa ajili ya malighafi za viwandani. Nashauri Sekta ya Maji iimarishwe ili yapatikane maji ya kuhudumia mifugo, viwanda, ukulima na sisi wananchi tupate maji safi na salama. Juzi nilisema Mfuko wa Maji umefanya kazi nzuri sasa unahitaji kujengewa uwezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na uzalishaji wa malighafi za viwandani, lakini pia wakulima wana changamoto kubwa baada ya kuzalisha mazao yao, hakuna usafiri wa kutoka kwenye maeneo yanayozalisha hivyo vyakula kuyafikia masoko ya mijini. Mfano maziwa ni bidhaa ambayo inaharibika kwa muda mfupi sana kwa hivyo barabara za vijijini zikiwa mbaya, wakulima wa maziwa wanapata hasara na Taifa letu pia linapata hasara ya kukosa pesa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ujenzi wa maghala na vihenge, naipongeza Serikali imefika hatua kubwa na mipango inaonesha kuna maendeleo makubwa katika ujenzi wa vihenge. Pia katika kuhifadhi chakula na usalama wa chakula, naishauri Serikali mwananchi mmoja mmoja naye aweze kuhifadhi chakula chake kwa mwaka mmoja au miwili. Kwa maana hiyo, kuna viwanda vya wawekezaji hapa nchini tayari wanazalisha mifuko ya kilo 100 na 200 kwa maana ya mwananchi aweze kuhifadhi mazao yake. Ni vyema viwanda vile vikapunguziwa kodi na tozo mbalimbali ili mwananchi aweze kumudu gharama za kununua ile mifuko aweze kujihifadhia mwenyewe chakula chake na watu wake huko nyumbani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nagusia kidogo Sekta ya Uvuvi. Uvuvi wa Bahari Kuu tunaipongeza Serikali kwa ununuzi wa meli za uvuvi, bandari za uvuvi na maghala ya kuhifadhia samaki. Kwa vile chombo hiki ni cha Muungano, nashauri Shirika la Uvuvi la TAFICO, kuna mpango wa kuliimarisha, naomba sana na Shirika la Uvuvi la Zanzibar (ZAFICO) mambo haya yaende sambamba ili kuwekeza zaidi katika uchumi wa bahari kuu. Katika Mipango ya Miaka Mitano, nashauri na bandari moja ya uvuvi kule Zanzibar nayo ijengwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye sekta hiyo ya uvuvi, napenda kuchangia kwenye ukuzaji wa viumbe kwenye maji. Sekta hii ni sekta ambayo haitumii nguvu kubwa. Ni vyema sasa na wala haihitaji elimu kubwa, wale vijana wetu waliomaliza darasa la saba, waliomaliza masomo darasa la tano na la nne, wanaweza kufanya hii sekta ya viumbe kwenye maji. Nina ushahidi mtoto wa darasa la tatu anafuga mwenyewe samaki wa gold fish, anawalisha biscuit tu na anawauza kwa watalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana sekta hii inawezekana kwa vijana wetu wa darasa la saba na la tano kufanya sekta ya ukuzaji wa viumbe kwenye maji, kwa sababu ni sekta ambayo haihitaji elimu kubwa, haihitaji utaalam mkubwa. Tukiwekeza hapa tutapunguza wale vijana ombaomba wanaozunguka mitaani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ile Mifuko yetu ya ujasiriamali ya vikundi vya vijana ni vyema sana zikaandaliwa program maalum za vijana hawa, baada ya kumaliza masomo ndio wakapewa ile mitaji sasa kwa sababu tayari wameshapata ujuzi, wameshapata uelewa na kazi watakuwa wanaipenda, kwa hivyo, watakuwa wanafanya kitu ambacho wanakipenda, kwa hivyo, kutakuwa na ufanisi mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nakuombea dua wewe uendelee kutuongoza vizuri. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais na timu yake aendelee kutuhudumia sisi wananchi tunamhitaji, tunampenda na tunampongeza sana kwa juhudi zake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuamsha salama siku hii ya leo. Nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa Hotuba yake nzuri yenye kuleta mustakabali mwema katika Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote naanza kuchangia kwenye sekta ya mazingira, nchi yetu ya Tanzania ni nchi ambayo ina Bara, ina na Visiwa kwa pande zote mbili za Muungano. Sisi tumerithi nchi yenye Bara na Visiwa, ni vyema na sisi tukawarithisha vitoto vyetu nchi ikiwa kamilifu, kama ilivyo kwa maana ya Bara na Visiwa vyake.

Mheshimiwa Spika, kutokana na mabadiliko ya tabia nchi kuna changamoto kubwa katika maeneo ya fukwe na maeneo mengine ya maziwa kwamba, tayari bahari au maji yanapanda juu na kuyafikia maeneo ya makazi ya watu. Kuna visiwa duniani tayari vimeshapotea kwenye ramani ya dunia, kwa hivyo na sisi ni vyema tukahifadhi mazingira yetu ili visiwa vyetu visije vikapotea kwenye ramani ya dunia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye sekta hiyo hiyo ya mazingira tumeambiwa na kwenye Hotuba ya bajeti kwamba, Wizara ina mpango wa kuzuia utumiaji wa kuni, makaa. Lakini ni vyema pia, kuna baadhi ya uzalishaji mali katika sekta ya biashara, unatumia kuni nyingi na hivyo ni vyema tukaangalia hasa kwenye kukausha tumbaku. Tumbaku inatumia miti mingi katika kukausha. Ni vyema sasa Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mazingira ikakaa pamoja, ili kuweka namna bora ya ukaushaji wa tumbaku kwa kutumia mashine nyingine za kisasa ambazo hazitumii kuni na mikaa na kukata miti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kuna Taasisi zisizo za Kiserikali nyingi tu, zinajihusisha na uhifadhi wa mazingira na uoto wa asili. Ni vyema Taasisi hizo zikatambuliwa rasmi kwasababu, kuna baadhi ya Taasisi nimezikagua, wanatumia fedha zao mfukoni kuhifadhi mazingira na uoto wa asili. Wengineo wana misitu karibu ya heka (10), (15) wanahifadhi wenyewe uoto wa asili. Kwa hivyo, ni vyema katika hiyo mifuko inayokuja, ikaangalia pia na hizi Taasisi zisizo za Kiserikali iweze kutekeleza jukumu letu hili kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikija kwenye upande wa Muungano, Muungano wetu jana umetimiza miaka (57) na leo imeongezeka siku moja. Muungano huu unakwenda haukutembea na ndio maana kila kitu kinachokuwa kinakuwa na changamoto zake. Na Muungano wetu unakuwa kwasababu kuna changamoto za makuzi. Naipongeza Serikali kwa kutatua changamoto mbalimbali ambazo zinajitokeza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaiomba Serikali, iendelee na hatua hizo za kutatua changamoto hizo kwa wakati muafaka na kuzitangaza kwa wananchi. Kwasababu, wanufaika wa Muungano huu ni nchi na wananchi ni vyema pande zote mbili za Muungano zikafaidi matunda ya Muungano kwa maana Bara na Visiwani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, changamoto mbalimbali zikitatuliwa wananchi watakuwa na furaha na Muungano wetu. Changamoto za kibiashara, changamoto za kiuchumi, changamoto za ajira kama zilivyosemwa. Mambo haya yakienda sambamba na sawia mambo mengi yatatatuliwa kutokana na changamoto za Muungano.

Mheshimiwa Spika, nikiendelea, Tanzania ni nchi ya amani, Tanzania viongozi wote walioanza kuiasisi Tanzania kutokea Hayati Mzee Karume na Mwalimu Nyerere na viongozi wote waliofuatia, wameuimarisha Muungano wetu kwa vitendo na waliopo ni matumaini yetu watauendeleza kama walivyosema wenyewe, wameahidi. Mheshimiwa wetu Rais Samia, Makamu wa Rais, Rais wetu wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi wako sambamba na maamuzi na mapendekezo ya watangulizi wao nawapongeza kwa hilo na sisi tuko nyuma yao kuwaunga mkono, kuhakikisha Muungano huu unadumu milele na milele kwa faida yetu tuliopo na faida ya vizazi vijavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jina la Tanzania ni jina zuri sana, jina lenye haiba, jina lenye mvuto nampongeza aliyetunga jina hili la Tanzania kwa dhati ya moyo wangu. Jina limetupatia heshima kubwa sana, jina la Tanzania. Ni vyema sisi wananchi wa Tanzania tukatunza amani yetu ya Tanzania kama jina letu lilivyo lina mvuto wa haiba ya Tanzania.

Naomba tumpe muda Rais wetu, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu watuletee maendeleo ya nchi yetu na kutekeleza majukumu yote yaliyoachwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli wako na dhamira ya dhati kabisa kuwaletea wananchi maendeleo. Si vyema kwa sasa hivi wakaanza kuwachokonoa, ni muda mfupi tu wana malengo makubwa, wana maono makubwa ya kutuletea maendeleo sisi watanzania. Naomba tuwape ushirikiano, tuwape imani zetu kama tulivyo. Kiungo kikubwa cha Muungano wetu kinaashiria pia kwenye hili Bunge lako.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru na ninakupongeza wewe na Naibu wako kwa kuliongoza Bunge letu hili vizuri kwa salama na Bunge letu tukatekeleza majukumu yetu kama tulivyopangiwa kutoka pande zote mbili za Muungano tukiwa wawakilishi wa wananchi wa pande zote mbili za Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi iko salama, mipaka ya nchi iko salama. Ni matumaini yangu kwamba, na sisi wananchi tutahakikisha kuunga mkono viongozi wetu na vyombo vyote vya usalama, kuhakikisha nchi yetu hii itakuwa salama kwa faida yetu na vizazi vijavyo.

Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia, Tanzania ina jina kubwa na ina historia kubwa, Muungano wetu uendelee kudumu kwa maslahi yetu na vizazi vijavyo. Ahsante nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwanza naunga mkono hoja hii. Lakini pia naipongeza Wizara ya Maji, Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wote katika juhudi zao za kila siku za kuhakikisha wananchi wa Tanzania wanapata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuliona hili na dhamira yake ya dhati ya kumtua mwanamama ndoo kichwani. Ambapo ameahidi kwamba, atauongezea nguvu mfuko wa maji kwa kutafuta vyanzo vipya vya kuongeza nguvu katika mfuko huu wa maji. Napongeza sana juhudi za Wizara kwa kukamilisha utekelezaji wa miradi 422 ya maji mijini na vijijini, pamoja na kupunguza gharama za uwekezaji kwenye miundombinu ya maji. Naomba juhudi hizo ziendelee ili kuokoa pesa nyingi za Serikali kwa ajili ya uwekezaji wa miradi ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara ina upungufu mkubwa wa wataalam wa maji, naishauri Serikali ione umuhimu wa kuajiri hawa wataalam wa maji, ili kwenda kusimamia miradi ya maji huko mijini na vijijini. Ikiwa pamoja na kuwatumia wataalam wetu waliobobea ambao kwa sasa wamestaafu, angalau wawatumie kwa kipindi kifupi cha mwaka au miaka miwili ili kuongeza nguvu katika kuwekeza huduma hii ya maji kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maji ni muhimu kwa wananchi kwa maana ya binadamu, maji yanahitajika kwa wanyama, maji yanahitajika pia kwa miti na mimea yetu. Kwa hivyo, suala la maji ni suala la msingi na ninaipongeza Serikali kwa juhudi hizo kwa kuona tunafikia ile asilimia tuliyojiwekea kwa upatikanaji wa maji safi na salama mijini na vijijini. Lakini pia, napongeza juhudi za Serikali kwa maana ya Wizara ya Maji wameliona hilo sasa, kwa kuhifadhi au kuvuna maji ya mvua. Hili ni jambo jema ambalo litasaidia sasa kupunguza zile changamoto za maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama tunavyojua maji ya mvua ni maji mazuri na yenye rutuba kwa kilimo. Kwa hivyo, tukihifadhi na kuvuna maji haya ya mvua yatakwenda kusaidia sana kwenye sekta hii ya uwekezaji wa kilimo lakini pia kwa matumizi mengine ya binadamu. Uvunaji wa maji ya mvua ni jambo la msingi kwa kuzingatia kwamba tunapoteza maji mengi na yanaharibu miundombinu yetu. Kwa hivyo, tukiyavuna na kuyahifadhi kwa kuyatumia kwa mahitaji yetu yote kwa viumbe sisi binadamu na wanyama, na kwa matumizi mengine ya kijamii yakiwemo mambo kama mfano, wakivuna maji ya mvua watu wa magereji wanaotumia maji mengi sana katika ukoshaji wa magari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hivyo tungeweka msisitizo pia kwa hawa wanaotumia mambo ya ukoshaji magari wakavuna maji ya mvua ili kusaidia kupunguza yale maji safi na salama kutumia kwa mambo ya magari na mambo mengine. Kuna madeni makubwa sana kwenye Wizara hii ya Maji, ni vyema sasa Wizara ya Fedha ikawakata moja kwa moja wale wadaiwa sugu maana kuna wadaiwa na wadaiwa sugu. Sasa wale wadaiwa sugu wale Serikali ikate moja kwa moja ili fedha zile zikasaidie kuhakikisha kwamba, miundombinu ya maji inakarabatiwa, tunadhibiti upotevu mkubwa wa maji ili sisi tunaopata maji ambao hatulipi basi zile fedha zisaidie kwenda kutengeneza miundombinu na wale wenzetu ambao hawapati maji waweze kupata maji tuwalipie hizi fedha Serikali ikate moja kwa moja hizi fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na pia, hawa wadaiwa sugu naiomba Wizara prepaid meter zianze huko kwao kwasababu, wameonesha kwamba wao hawalipi kwa hivyo zile prepaid meter zikaanze kwa wadaiwa sugu wa maji, ili tuweze kupata fedha zetu za maji tuwekeze zaidi kwa wananchi wengine wapate maji. Nimalizie kwa DDCA - Wakala wa Uchimbaji Visima na Mabwawa. Naomba Serikali iwekeze pale kwasababu, sasa miundombinu waliyonayo ya vifaa ni hafifu haviwezi kuchimba kina kirefu cha maji. Visima virefu vya maji inahitaji tuagize mitambo na wataalam kutoka nje waje watusaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukiwekeza pale tukisomesha wataalam wetu tukawa nao sisi wenyewe na tukawekeza mitambo ya kutosha pale ya kuhimili kuchimba kina kirefu cha maji, tunaweza tukaokoa pesa nyingi za Serikali na kupunguza urasimu wa utendaji katika kufanya kazi hii ya DDCA. Naomba Uwakala huu uongezewe nguvu na uwezo na kuwekewa wataalam wazalendo ili tukafanye kazi ya kutafuta maji, kwenye ardhi kuna maji ya kutosha.. (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Spika, nakushukuru naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuamsha salama mpaka jioni hii ya leo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa napenda kutoa pongezi za dhati kwa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Tanzania, Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan, lakini napenda kuwapongeza Wakuu wa Majeshi yetu yote. Napenda sana kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa inayofanywa ambayo inahakikisha usalama wa nchi yetu, ulinzi wa nchi yetu na pia kushughulikia mambo mbalimbali ya ustawi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli napenda kuwapongeza kwa dhati majeshi yetu haya ya ulinzi, nchi iko salama, mipaka ya nchi yetu iko salama na hii inatokana na umahiri wao, lakini uzalendo wao, kujitoa kwao, kujituma kwao na kuwa waadilifu, wakweli na wasikivu kwa nchi yao na Taifa lao. Nawapongeza pia na majeshi yetu yote nchini Tanzania kwa kazi kubwa wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiendelea na mchango wangu kwenye Jeshi la Kujenga Taifa; kazi kubwa inafanyika ya kuandaa vijana wetu, lakini na mimi napenda kuishauri Serikali, katika maandalizi yetu haya ya vijana wetu wa Jeshi la Kujenga Taifa tuendelee kuwapa skills ambazo zitawasaidia kujiajiri, lakini pia zitasaidia kuongeza kipato chao, lakini kipato cha nchi na uchumi wa nchi. Na Jeshi letu hili la Kujenga Taifa tuhakikishe wanaporudi kwenye mitaa yetu au kwenye maeneo yetu wanatumika vizuri na sio badala yake kutumika vibaya. Tuwape scheme au skills ambazo zitawafanya watumike vizuri kwa jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiendelea jeshi letu la ulinzi limeanza tangu mwaka 1964 na katika miaka hiyo ya 1964 kwa mfano kwa upande wa Zanzibar mwaka 1964 kumekuwa na kambi nyingi za kijeshi ambazo kwa maeneo hayo kwa wakati huo ilikuwa ni porini na wananchi hawajawahi kufika huko, lakini kwa mazingira ya sasa hivi baadhi ya kambi zimezungukwa na raia. Tayari zimezungukwa na maeneo ya wananchi, hata magari, madaladala baadhi ya maeneo yanapita chini ya kambi. Wasiwasi wangu ni kwamba kunaweza kukatokea hatari ya kambi yenyewe au hatari kwa kambi yenyewe au kwa wananchi ambao wako jirani na kambi, apa ndio ushauri wangu unapokuja.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vyema sasa jeshi letu au Wizara yetu hii ya Ulinzi ikawasiliana na Serikali zetu kubadilisha matumizi ya maeneo yale na kuomba maeneo mapya kwa ajili ya kuzihamisha zile baadhi ya kambi ambazo ni hatarishi kwa maisha ya wananchi, lakini pia ni hatarishi kwa jeshi lenyewe. Na kwa kipindi cha mpito nashauri kuna baadhi ya kambi ukipitia nje unawaona walioko ndani na kinachofanyika ndani. Ni vyema basi tukazungusha uzio angalao ile staha ya ile kambi ipatikane, wakati tunajiandaa na kutafuta mbadala wa kambi nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na hayo yako kwa maeneo mengi ya nchi yetu, kambi zimezungukwa na maeneo ya rai ana raia wamekuwa jirani na hizo kambi na nyingine ndio wanachunguliwa mpaka ndani wanaona kinachofanyika ndani. Lile ni jambo hatarishi kwa kambi zetu na usalama wa wanajeshi wenyewe waliomo mle ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine kwenye mipaka ya nchi, naomba Serikali ilione hili la kuhakikisha tunaongeza fedha ili mipaka sahihi ya nchi yetu iwekwe ili kuepusha mkanganyiko wa kugombaniana mipaka na kuleta taharuki kwa nchi. Sasa tuko salama, lakini miaka inakwenda na mambo yanabadilika na mahitaji yanaongezeka kwa kila nchi kwa hivyo ni vyema tukawekeza pia kuchanganua mipaka yetu kwa usahihi baina ya nchi na nchi, baina ya maeneo na maeneo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea na mimi kuchangia kwamba jeshi letu lipewe nyenzo za kisasa zinazolingana na teknolojia ya kisasa na vijana wetu wanajeshi wapewe mafunzo yanayolingana na hali ya kisasa na mabadiliko mbalimbali ya kidunia yanavyojitokeza katika ulinzi wa nchi, mipaka ya nchi na usalama wenyewe wa nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kulipongeza jeshi let una vikosi vyote vya ulinzi kwa kazi kubwa wanayoifanya kuhakikisha nchi yetu iko salama, lakini pia nawapongeza yanapotokea majanga, maafa. Kwenye furaha na kwenye shida wanakuwa pamoja na wananchi bega kwa bega kuhakikisha nchi yetu inafanikiwa katika matukio yote likiwemo tukio la juzi tu la tangu kumuaga na kumsindikiza mpendwa wetu, Rais wetu mpendwa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye sasa ni Hayati Dkt. John Pombe Magufuli. Jeshi hili halikulala usiku wala mchana, lilifanya kazi kubwa kuhakikisha kwanza nchi iko salama, wananchi wako salama na mambo yote yanatekelezeka kwa wakati muafaka na hakuna tatizo lolote lililojitokeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hilo tuwape hongera kwa umahiri wao pamoja na majemadari wao, makamanda wao kwa kazi kubwa wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jeshi letu ni tiifu na bila ya utiifu jeshi hili kusingekuwa na amani hii tunayoizungumza hivi sasa, lakini nalipongeza jeshi letu ni tiifu sana, ni wasikivu na naomba wapokee pongezi zangu hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na katika kuwapongeza hivyo na wao tuwaone kwa sababu mcheza kwao hutunzwa. Wanatusaidia, wanatufurahisha, wanatutengenezea mambo yetu na sisi tuwatunze, tuwaone kwa mahitaji yao zikiwemo nyumba bora, mishahara minono, marupurupu mengine ambayo yatawasaidia kustawisha maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia naomba niunge mkono hoja, nakushukuru sana kwa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na ninapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kuniamsha salama asubuhi hii ya leo.

Mheshimiwa Spika, nikiendelea kwanza sina budi kutoka pongezi za dhati kwa Wizara hii Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara hii kwa juhudi mbalimbali wanazofanya kuhakikisha sekta zetu mbili za uvuvi na mifugo zinapiga hatua na kumsaidia mwananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninakubaliana na maoni ya Kamati kwamba Bajeti ya Wizara hii ni ndogo, utoaji wa fedha hauendi kwa wakati, hivyo inachangia kurudisha nyuma mipango kabambe ambayo imepangwa na Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninashauri Serikali itoe fedha kwa wakati na iongeze bajeti kwa ajili ya kutatua changamoto na kupiga hatua mbele mbalimbali za maendeleo, kwa sababu Wizara hii ina mchango mkubwa katika kuongeza pato la Taifa. Tutapata fedha za kigeni kupitia Wizara hii, tutaongeza ajira, lakini pia Wizara hii itatusaidia kwenye usalama wa chakula kwa maana tutapata vitoweo, maziwa na vitu vinginevyo ambavyo vitasaidia usalama wa chakula katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninakubaliana na mawazo ya Kamati kwamba sheria za uvuvi na mifugo na kanuni zake zifanyiwe haraka zikamilike ili kutatua changamoto za wavuvi na wawekezaji wa uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikiendelea ninakuja kwenye sekta hii ya uvuvi, kwenye uvuvi wa bahari kuu nawapongeza sana Serikali kwamba sasa tunaingia kwenye uchumi wa blue kwa vitendo na imesema hapa katika bajeti ya mwaka 2021/2022 itanunua meli mbili za uvuvi kwa kuanzia. Sasa mimi ninataka niiambie Wizara kwakuwa chombo hichi DSFN cha Kitaifa meli mbili za uvuvi za Zanzibar zitanunuliwa kwa awamu gani ya bajeti? Naomba hapo nayo ituweke sawa ili tujue tunafanya nini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye uwekezaji wa viumbe kwenye maji, hapa pana soko kubwa sana la ajira kwa vijana na wanawake. Eneo hili litakwenda kutatua changamoto za ajira kwa vijana na wanawake, lakini pia itaongeza kipato cha mwananchi mmoja mmoja, kitaongeza kipato kwa vikundi, lakini pia kipato kikubwa kwa Taifa, kwa sababu tutawekeza kwenye hii sekta, tutauza nje. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, uingizaji mkubwa wa samaki kutoka nje hivi kweli hata saladini tunaagizia kutoka nje, vibua vile ambavyo vimejaa nchini mwetu, lakini tunaagiza kutoka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninachotaka kusema hapa kuna vyuo ambavyo vinatoa mafunzo ya ufugaji wa samaki vyuo vile ninawashauri serikali iwe na programu tofauti, programu ya muda mrefu na ya muda mfupi, zile za muda mrefu ziendelee kwa wale wanaotaka utaalamu zaidi, lakini zile za muda mfupi ziwe kwa vijana wetu hawa wa kati na kati ambao watatoka kupata ajira wakaanzie miradi yao. Ninashauri ili kuvutia uwekezaji katika sekta hii kwa wananchi mbalimbali wale wataalam ambao wamepata mafunzo kwenye vile vyuo vyetu vya mafunzo Wizara iwe inawatangaza, waweke kumbukumbu zao na wajulikane wako wapi ili mwananchi anapotaka kuanzisha huu mradi ajue mtaalam nitampata wapi wa kunisaidia kutengeneza huu mradi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na wale vijana ambao tunawapatia mafunzo kwa program ndogo ndogo zile zitakazoundwa na Wizara ninashauri kuna mifuko ile ya vijana ya uzalishaji mali ya wanawake sasa badala ya kuwapa cash watengeneze ile miundombinu, hawa vijana wameshapata mafunzo, watengenezewe miundombinu, wajengewe mabwawa, vifaa na vifaranga waanzishe, hii itakuwa chachu kwa vijana wengine watakapoona wenzao wanafaidika na wao kutaka kujifunza utaalamu huo wa ufugaji samaki na wa viumbe kwenye maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia kwenye ufugaji wa samaki na viumbe kwenye maji sio samaki tu, pweza, na nini, lakini kuna madini pale yanapatikana madini ya lulu. Madini ya lulu yanahitajika sana duniani, yana soko kubwa, tunayapata kwa kupitia ukuzaji wa viumbe kwenye maji, kuna lulu zinapatikana baharini, lakini lulu tunaweza tukazitengeneza wenyewe kwenye vizimba vyetu, lulu ni madini makubwa duniani yanahitajika sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikiendelea kwa dakika zangu chache zilizobaki labda nijikite kidogo kwenye suala la ufugaji. Wizara ijitahidi sana ufugaji wenye kuhifadhi mazingira ya nchi kwa maana zile Ranchi za Taifa, Kamati imeshauri vizuri, zile Ranchi za Taifa na nyongeza yangu hii iwe kama shamba darasa sasa kwa wafugaji ili kuwepo na mabwawa, kuwepo na malisho, halafu kuwe na program kuwachukua wale wenye ng’ombe wengi wafugaji wakubwa waliopo kwenye Mikoa yetu waje pale wajifunze namna ya kuhifadhi mazingira, yaani wafuge kitaalamu, wavutike na ile ranchi kwamba hapa tukifanya hivi na sisi tunaweza tukafanya kwa sababu wakirudi kule kwenye maeneo yao waanzishe hiyo miradi kwa sababu uwezo wa kuanzisha wanao kwa sababu wana ng’ombe wengi wanaweza wakauza wakaanzisha hayo malambo na vitu vingine vya kulishia wanyama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hivi tunaweza tukawekeza mabwawa kwenye maeneo, lakini bado wafugaji hawahamasiki kukaa pale pale wanaendelea bado kuendelea kuhama hama lakini tukifanya programu maalum…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Khadija muda wako umekwisha.

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuamsha asubuhi ya leo tukawa salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kuipongeza hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha, hotuba ya bajeti ya Serikali na mpango wa Maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii kumpongeza sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa mama Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi mbalimbali anazozifanya katika kuhakikisha nchi yetu inasonga mbele kukuwa katika uchumi pamoja na kuinua maisha ya mwananchi mmoja mmoja katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ally Mwinyi, kwa juhudi zake mbalimbali anazofanya katika kuhakikisha Zanzibar inakwenda mbele na inasonga mbele kiuchumi na kimaendeleo pamoja kunyanyua hali za wananchi wa Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha Naibu wake, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu kwa kazi nzuri wanayoifanya na mashirikiano ya pamoja hadi kufikia kutuletea bajeti nzuri ambayo inaenda kutatua changamoto za wananchi mbalimbali, changamoto za wakulima, wavuvi, wafanyabiashara na wananchi kwa jumla nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri na wizara yake kwa kututambua sisi asasi zisizo za kiserikali - NGOs akatuweka katika bajeti yake kwamba na sisi tumechangia katika uchumi wa Taifa kwa kweli taasisi zisizo za kiserikali nazo zinafanya kazi kubwa katika kunyanya maisha ya mwananchi, kutatua changamoto za wananchi, kutatua changamoto za ajira, lakini kuinua uchumi wa nchi ni vyema sasa michango yetu nayo ikatambuliwa na dhamani gani tumewekeza katika mazingira yote, katika maeneo yote ya sekta zote za uchumi maendeleo ya jamii na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kupongeza bajeti hii kwa kuondoa ushuru katika mazao ya Kilimo, Ufugaji, Viwanda na Biashara. pamoja na kuondoa ushuru huu wa forodha, tusisahau kuzingatia mazingira katika bajeti zetu zote tuhakikishe kwamba pamoja na mambo yote tunayoyafanya kuilinda nchi yetu na mazingira na mabadiliko ya tabia nchi, na katika bajeti imo, Mheshimiwa umetenga fedha kwa ajili ya mazingira, ni vizuri sana tukawa na fedha zetu za ndani za kuwekeza katika kuhifadhi mazingira yetu ya nchi na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili napenda kuchangia kwamba pamoja na mambo yote tunayoyafanya ya kuwekeza lakini tutenge ardhi katika maeneo muhimu ikiwemo uhifadhi wa misutu, uhifadhi wa uoto wa asili, uhifadhi maeneo tengefu kwa ajili ya kulinda mazingira ya nchi na kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili napongeza Serikali kwa kuondosha ushuru katika uwekezaji wa mbolea na viwanda vya mbolea ni kweli itasaidia kutatua changamoto za mbolea katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nashauri katika uwekezaji huo huo wa mbolea tusisahau mbolea zetu za asili kwa maana ya kuhifadhi ardhi yetu iendelee kudumu na kutumika milele na vizazi vijavyo. Naamasisha pia katika mipango inayokuja tuwekeze pia katika kilimo hifadhi na kilimo hai, kilimo hifadhi na Kilimo hai kitakwenda kulinda afya ya mimea yetu na mazao tunayozalisha hayatakuwa hayana chemical, lakini pia tutahifadhi ardhi na udogo wa nchi yetu kwamba usiendelee kuharibiwa na chemical za viwandani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea katika hicho hicho kilimo, kuna kilimo cha mazao ya bustani na mboga mboga, kilimo hiki kimetokea kuwa na soko kubwa duniani na tunaingiza fedha nyingi za kigeni kupitia kilimo hiki cha bustani na mboga mboga.

Narudia kusisitiza kwamba Kilimo hiki kuna baadhi ya maeneo wanakata miti mikubwa wanaondosha uoto wa asili badala yake tunakwenda kupanda bustani na mazao ya mboga mboga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili tulitizame kwa upana wake pia na ndiyo nikasisitiza kwamba tuweke na maeneo ya kuhifadhi uoto wa asili na misitu kwa maana kila bidhaa zikiwa nyingi huko duniani na sisi kilimo tutaongeza kupanua maeneo, tukipanua maeneo tunakata miti ya asili, tunakata na misitu, lakini tunapanda mboga mboga, naomba hili tuliweke angalizo katika mipango yetu ya maendeleo kwa kila mwaka, na hii nakuja pale kusisitiza kwamba kupima maeneo yapi ya Kilimo, yapi ya ufugaji, yapi ya viwanda, na yapi ya uhifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea naipongeza Serikali kwa kuondoa ushuru wa ongezeko la thamani katika taa za solar, pamoja na vifaa vya kutengenezea solar, lakini katika hapa nilikuwa nauliza Serikali inijibu kwamba katika kusamehe hizi tozo na kodi inaunganisha na ile mitambo ya kusukuma maji katika visima vyetu kama hicho hakipo nashauri Serikali mitambo ya kusukuma maji katika visima vyetu viondolewe kodi. kwa sababu uwekezaji wa visima vya maji kwa kutumia diesel na petrol tumegundua kwamba ni gharama kubwa ya uendeshaji na hivyo mzigo unamwelemea mwananchi anayetumia maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nia ya Serikali yetu, ni ya Rais wetu ni kuhakikisha mwanamama anamtua ndoo kichwani lakini wananchi kwa ujumla wanapata maji safi na salama. Kwa hivyo tukipunguza kodi kwenye vifaa vya kusukumia maji katika visima vya maji itasaidia kupunguza gharama za uendeshaji wa visima vya maji na maji yatapatikana kwa bei nafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea kwenye Sekta ya uvuvi naipongeza Serikali sana, sasa tumejipanga katika uvuvi, uvuvi wa bahari kuu na Serikali ina mpango wa kununua meli za uvuvi. Ushauri wangu pamoja na kujiingiza kwenye uvuvi huo mkubwa kwa kununua meli uvuvi wa Bahari Kuu, uvuvi wa Kisasa tusisahau wavuvi wetu wadogo wadogo, wavuvi wetu wadogo wadogo na wao waende sambamba na ukuaji huo wa uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu bado zana zao ni duni, zana zao hafifu mvivu anapokwenda baharini anajua kwenda lakini uhakika wa kurudi hana kwa sababu atakachokutana nacho baharini hajui kama ni mawimbi makali au ni dhuruba, au atapata samaki au hapati, kwa hivyo uchumi huu mkubwa tuwachukue wavuvi wetu wadogo wadogo ambao wametusaidia mpaka kufika hapa kwamba uvuvi bado Tanzania upo tuwawezeshe kwa zana za kisasa ili na wao tuwainue kiuchumi lakini pia waongeze mapato ya Taifa na waweze kujiajiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia nasema hivi naipongeza sana Serikali tumuunge mkono Rais wetu atuletee maendeleo nampongeza Makamu wa Rais, nampongeza Waziri Mkuu, nampongeza Rais wa Zanzibar kwa juhudi kubwa anazofanya katika kuwaletea wananchi maendeleo na sisi wananchi tuko bega kwa bega kuhakikisha maendeleo haya tunayapata yanawafikia wananchi wetu, yanatufikia na sisi wenyewe na vizazi vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, ahsante sana, nakushukuru naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante awali ya yote napenda kuipongeza sana Wizara ya Fedha na Kamati yake ya bajeti kwa Mpango huu ambao sasa umetuletea na sisi tuuchakate na kuongeza mawazo yetu. Kwa dhati kabisa kwanza napenda kumpongeza Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kutimiza mwaka mmoja, lakini pia napenda kumpongeza kwa hotuba yake nzuri sana aliyotoa wakati wa sherehe zile ambayo inaleta maono na mwanga mkubwa kwa maisha ya Wazanzibar na Watanzania kwa ujumla pia kuinua uchumi wa nchi na uchumi wa Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea natoa pongezi sana kwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mama Samia Suluhu Hassan kwa ukakamavu wake na ushupavu wake na uthubutu wake katika kuliongoza Taifa letu na kutuletea sisi wananchi wa Tanzania maendeleo katika kukamilisha miradi iliyoanzishwa na kuibua miradi mipya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najielekeza kwenye sekta ya kilimo, katika kuimarisha na kuinua sekta ya kilimo kwa maana ya kupata mazao bora na mazao yenye tija na kuinua uchumi wa nchi na kuongeza ajira ndani ya nchi nashauri Serikali iwekeze kwenye viwanda vya mbolea ndani ya nchi. Kama majirani zetu wanakuja kuwekeza viwanda hapa nchini malighafi za uzalishaji zinatoka hapa ndani ya nchi kwanini sisi wenyewe tusiwekeze kwanini wao waweze wana nini sisi tushindwe tuna nini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini uwezo huo tunao wa kujenga viwanda vya mbolea kwa sababu tumewekeza miradi mikubwa sana ya kimaendeleo na ya kimkakati na sasa hivi yako ukingoni kukamilika. Naamini tukiwekeza kwenye viwanda vyetu vya mbolea kwa sababu tutakuwa tunaangalia nini mahitaji ya ardhi yetu na udongo wa nchi yetu tutajua afya ya udongo wa nchi yetu kwa kutumia wataalamu wetu kwenda kupima afya ya udongo na kujua ni mbolea gani ambazo zinahitajika kwa mahitaji ya nchi zikiwemo hizo UREA, MPK, mbolea ya samadi tutajua tunahitaji mbolea gani kwa mahitaji ya wananchi wetu katika kuinua kilimo chetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hapo hapo kilimo tuwekeze pia kwenye viwatilifu bora kwa sababu kuna hatari ya kuingiza viwatilifu ambavyo viwatilifu vile vinakwenda kuathiri mazao ya wananchi baada ya kutumia nguvu kubwa ya uwekezaji matokeo yake baada ya kuvuna wanaharibu mazao yote na hili nimelishuhudia kuna kijana mmoja alijitokeza kulima mipapai, mipapai kaimwagilia imekubali lakini ikafanya ukungu mweupe akaenda kutafuta dawa baada ya kupata dawa mipapai yote imegeuka dume hakupata hata papai moja. Sasa hapo tunaona kwamba tunahitaji viwatilifu bora ambavyo vitasaidia wakulima wetu. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Bashe sijui kama yuko hapa mipapai imegeuka dume yaani baada ya kiatilifu! Mheshimiwa Khadija endelea. (Kicheko)

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo hili nishalizungumza mara nyingi ambalo mimi binafsi linaniuma sana tunasema tunakwenda kusomesha wataalam wabobezi wa uzalishaji wa mbegu bora ubobezi wa mbegu unahitaji taaluma kubwa na inachukua muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sasa tuna wataalamu wetu wabobezi na walishafanyakazi na research kubwa na wakazalisha mbegu lakini wamestaafu. Matokeo yake wazalishaji mbegu bora wale wamechukuliwa mataifa jirani wanazalisha mbegu na zinarudi Tanzania tunazinunua tena sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali katika hili hebu tuangalie kwenye hiki kipengele cha ajira kwa hawa wataalamu wenye ujuzi maalum na adimu tunafanyaje ili waendelee kutusaidia kwa sababu kama wanaweza kuzalisha nje ya nchi mbegu inamaana tayari akili zao zinafanyakazi na hawajachoka wanaweza wakaendelea nchini kuzalisha zile mbegu na mbegu zikatapakaa kwa wananchi wetu bila ya kupata hasara ya kutumia mbegu ambazo hazina uhakika na hazina ubora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji kilimo cha kukidhi mahitaji yetu kwa maana ya sisi wenyewe lakini akiba ya chakula na kuwekeza pia kwenye uzalishaji wa nje kupata fedha za kigeni. Nashauri Serikali kilimo biashara kianzie sokoni kwa maana tutizame soko linahitaji nini na mazao ya ubora wa kiwango gani ili sasa wakulima wetu wanaotaka kujiingiza kwenye kilimo biashara wajue wanalima mazao gani? Kwa ubora gani? Uhifadhi wa mazao pale ghalani na vifungashio kwa ubora gani? Ili hilo soko liweze kupatikana kwa urahisi. Kwa sababu tusilime tu bila kujua soko linahitaji nini na kwa wingi gani na kwa ubora gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea kidogo nakuja kwenye mabadiliko ya tabianchi na upande wa mazingira kwa sababu na mimi mwenyewe ni mdau wa mazingira kwa sababu na mimi nahifadhi uoto wa asili kule Tabora. Masuala ya mabadiliko ya tabianchi liwe suala la kitaifa pamoja na kutegemea fedha ambazo zitatoka kwa wafadhili, lakini tuwe na bajeti yetu wenyewe ndani ya nchi ambayo tutaitumia kwa mabadiliko ya tabianchi kipindi hicho yatakapotokea majanga na maafa mbalimbali. Kwa sababu mabadiliko ya tabianchi yatakwenda kuathiri hata hicho kilimo ambacho tunakipigania, uvuvi pamoja na uzalishaji wa mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango umesema watahamasisha matumizi ya nishati mbadala na mimi naunga mkono matumizi ya nishati mbadala hasa kwa wakaushaji wa tumbaku kule Tabora, wapatiwe nishati mbadala kukaushia tumbaku kwa sababu wanakata miti mingi na wanaharibu mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango huo huo wa kuhifadhi mazingira naomba Wizara zote za Serikali ambazo zinakuwa na miradi mikubwa ya kimkakati wanaharibu sana ikolojia na mazingira mfano, anapoweka umeme kuna ukataji wa miti mingi, kwenye mawasiliano, kwenye barabara kuna uharibifu mkubwa wa ikolojia, vyanzo vya maji na mambo mengine.

Nashauri kila Wizara inapokuwa na miradi yake ya kimkakati naya kimaendeleo itenge fedha kwa ajili ya kurejesha uharibifu wa mazingira ambao waliharibu kwa kukata miti na kuharibu ikolojia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamesema hapa wataongeza upandaji miti, tunashauri kwamba tusiwe tunapanda miti sasa tugeuze msamiati tuwe tunaotesha miti kwa maana ukisema kupanda miti tunaipanda baadaye mingine inaachwa haikui, lakini tukiiotesha ina maana tuishughulikie mpaka ile miti ikue.

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naunga mkono hoja. (Makofi/Kicheko)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nitumie nafasi hii kumpongeza Waziri wa Fedha, kwa mpango wake mzuri aliotuletea kwa mustakabali mzima wa Taifa letu. Nitumie nafasi hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan. Pia nimpongeze kwa dhati kabisa Mheshimiwa Rais wa Zanzibar ndugu yetu Hussen Ali Hassan Mwinyi kwa ushirikiano wao wa pamoja katika kuwaletea wananchi wa Tanzania maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee, na nitajielekeza kwenye sekta za uzalishaji ikiwemo kilimo, mifugo na uvuvi. Naipongeza Serikali kwa kuwekeza fedha nyingi katika sekta hizi za uzalishaji ambazo lengo lake ni kuimarisha sekta hizi kwa manufaa ya Watanzania. Ni vyema sasa uwekezaji huu mkubwa unaowekezwa na nchi yetu tuone matokeo makubwa pia ya uwekezaji huu kwa sababu ni fedha nyingi sana zimewekezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu inategemea sana usalama, hasa usalama wa nchi kwa maana ya mipaka, usalama wa ndani ya nchi kwa maana ya wananchi na mali zao, lakini hapo hapo inategemea usalama wa nchi kwa maana ya chakula. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuelekeze zaidi kuwekeza kwenye NFRA, kwa ajili ya kujiwekea usalama wa chakula ndani ya nchi pindi tutakapofikwa na majanga, maafa na maswaibu mbalimbali ndani ya nchi yetu ambayo yanasababishwa na mambo mengi ikiwemo mabadiliko ya tabia nchi na mambo ya dunia yanayojitokeza. Kwa hiyo kwenye NFRA tukiwekeza vya kutosha ule usalama wa nchi utakamilika, kwa maana ya mipaka, raia, mali zao na usalama wa matumbo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea hapo hapo kwenye sekta ya kilimo, tumeona kwenye mipango kwamba kuna mipango inafanywa kwa ajili ya uwekezaji kwenye sekta ya kilimo, kuimarisha tafiti, kuimarisha mambo ya mbegu bora. Pia kwenye suala la mbolea kuna watafiti wetu wamegundua kilimo ambacho kinaitwa kilimo hai na kilimo hifadhi. Hiki kilimo hai na kilimo hifadhi kinakwenda kulinda na kuhifadhi ardhi na udongo wa nchi yetu na pia kinatoa matunda bora ambayo hayana kemikali zozote za viwandani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwaunge mkono watafiti hawa ili elimu hii isambae kwa wananchi wetu waweze kulima bila kutegemea mbolea ambazo wakati mwingine zinakwama kufika kwa wakati, wakajitengenezea wenyewe mbolea zao na mambo yao mengine ya ughani kwa kutumia kilimo hifadhi na kilimo hai. Tumeona matunda yanayolimwa kutokana na kilimo hai na kilimo hifadhi ni matunda mazuri na yana soko kubwa katika soko la dunia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango wa kilimo, nashauri tujielekeze sasa kwenye mpango wa muda mfupi na mpango wa muda mrefu, kwa baadhi ya mazao. Tuna uhaba wa sukari, mafuta ya kula na ngano ndani ya nchi. Ni vyema sasa tukajipangia mipango kumaliza tatizo japo kuna zao moja la sukari, ama ngano, ama mafuta; ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, miwili au mitatu. Tuache tabia ya kuagiza nje mazao haya kwa sababu ardhi tunayo ya kutosha, wataalam tunao, fedha tushapata, mitaji kama hii kwenye kilimo. Basi tuseme ndani ya miaka mitatu au minne tutaachana na kuagiza sukari ama unga wa ngano, ama mafuta ya kula. Tujielekeze hivyo tuzalishe ndani ya nchi, tujitosheleze, pia tuweze kupata soko la nje kwa mazao tutakayozalisha ndani ya nchi huku tukiendelea na mazao yetu mengine ya biashara yakiwemo mazao ya bustani, mbogamboga na mazao mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikitishwa sana kwa taarifa ya Kamati kuona kwamba Serikali imewekeza fedha nyingi kununua vitendea kazi vya Maafisa Ugani ikiwemo pikipiki, lakini kumbe kuna baadhi ya pikipiki zile hazifanyi kazi iliyokusudiwa eti kwa tatizo tu la kukosa mafuta. Tunawekeza fedha nyingi kwa Maafisa Ugani, tumewapa vitendea kazi, Serikali imetoa ili wawafikie wakulima lakini kweli inashindikana mafuta ya kuweza kuwafikia wakulima wale. Kamati imeelekeza kwamba halmashauri zitenge fedha kwa ajili ya kugharamia mafuta. Lakini haya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi, kuna kodi inachukuliwa pale kwa halmashauri sasa si ndio hapo pa kuwekeza ili ile kodi iwe kubwa zaidi tuongeze mapato kwa sababu kilimo kikikua na mapato yanakua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea kwenye sekta ya uvuvi tumeona hapa kuna nchi zinaendeshwa uvuvi katika dunia. Tujielekeze zaidi kwenye uvuvi wa Bahari Kuu kama mipango ya Serikali na pia tiliimarishe Shirika la TAFICO na ZAFICO kwa sababu uvuvi wa Bahari Kuu ni chombo cha Muungano. Kwa hiyo kwa upande wa TAFICO zinawekezwa fedha lakini bajeti haikidhi kwa sababu TAFICO inahitaji uwekezaji mkubwa, kwa maana ya kuwekeza fedha pale TAFICO kulifufua. Shirika linahitaji gati na mitambo ya baridi ya kuhifadhia Samaki, shirika linahitaji kila kitu kwa maana na hata baadhi ya majengo tayari yameanza kumomonyoka kwakuwa yanaliwa na dahari. Pale uwekezaji wake ni mkubwa hivyo ni lazima tuwekeze fedha za kutosha ili kulifufua hili shirika kwa haraka, kwa sababu ni muda mrefu sasa tunazungumzia TAFICO lakini TAFICO yenyewe bado haijaanza kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye samaki hatuhitaji mbolea, ugani wala kupalilia. Samaki tunachokitaka ni kuhifadhi matumbawe na kuweka mazingira ya kudhibiti uvuvi haramu, tuvue, hakuna hasara nyingine pale inapayotikana, Mwenyezi Mungu katujalia ile baraka ya Samaki tunawaacha, na Samaki wanatembea kokote duniani, yeyote anaweza akamvua, huwezi kumwekea mipaka. kwamba mimi ninamzuia mpaka shirika langu la TAFICO liwe salama ndipo tuweze kufanya kazi ya kuvua Samaki. TAFICO ikifufuliwa ikapewa mtaji wa kutosha tutaanza kuvuna rasilimali ya bahari kwa wingi zaidi na bila ya gharama kubwa. Gharama yetu ni uwekezaji kwenye TAFICO.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nagusia sekta ya maji ambayo imezungumzwa sana, na mimi nashauri kwenye jambo moja. Kuna gharama kubwa ya uendeshaji wa maji katika visima kwa kutumia nishati ya umeme. Ni vyema sasa Serikali ikaona namna ya kupunguza kodi au ongezeko la thamani (VAT) au kutoa ushuru mwingine kuhakikisha hizi mashine za solar za kupandishia maji na kuendesha mitambo ya maji ili kupunguza gharama kubwa kwa wananchi kule vijijini ya kutumia nishati ya umeme…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante…

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Awali ya yote napenda kuipongeza sana Wizara na watendaji wake wote.

Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa juhudi alizochukua kukutana na asasi zisizo za Kiserikali ambazo zinafanya kazi ya kuhifadhi mazingira. Wana asasi wamefarijika sana kwa kuwatambua kwa sababu sisi wana asasi zisizo za kiserikali tunafanya kazi kubwa sana kuisaidia nchi hii kuhifadhi mazingira yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kututambua kwako Mheshimiwa Waziri tumefarijika sana. Tunachoomba, tunapokuja Wizarani kwako, sisi wana asasi utupe ushirikiano wa kutosha ili tuweze kutekeleza majukumu yetu pale ambapo tuna kwama.

Mheshimiwa Spika, kwenye suala la mazingira, naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa juhudi zinazofanywa katika kuhifadhi mazingira ikiwemo upandaji miti. Hata hivyo nataka niishauri Serikali, kwa msamiati wa upandaji miti, ni bora sasa twende na msamiati wa Uoteshaji wa Miti. Kwa sababu tunapopanda miti, baadaye hatujui inakua au haikui; lakini tukiotesha tutaifuatilia tangu tumeipanda mpaka inakua na kuona imefika hatua gani? Tunapanda miti mingi lakini mingi inakufa njiani, kwa hiyo, ni bora tuoteshe miti ili kuisimamia miti hii tuone inakuwa endelevu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nijikite kwenye upande wa Muungano. Muungano wetu umefikisha miaka 58, ni safari ndefu, tumeanza mbali; na Muungano huu ni Tunu na Hazina ya Tanzania. Mpaka kufikia miaka 58 Muungano huu umepitia changamoto nyingi sana mpaka kufikia hapa. Changamoto ya kwanza ya kuhakikisha Muungano huu hauendelei, ni pale alipouawa Rais wa Kwanza wa Zanzibar Mheshimiwa Abeid Amani Karume. Hilo ndilo jaribio la kwanza la kutaka kuona Muungano huu hauendelei. Tusishangae kwamba bado Muungano huu kuna watu wanautazama kwa jicho la husuda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika miaka 58, chochote kinachokua kinakuwa na changamoto. Katika kukua kuna changamoto za Muungano, na changamoto hizi hazitaisha kwa sababu Muungano huu unakua na nchi inabadilika na dunia inabadilika na miundombinu inabadilika. Kwa hiyo, changamoto zitaendelea kujitokeza kila Muungano huu unapoendelea kukua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninachoshauri, Serikali iendelee kuzitatua changamoto hizi pale zinapojitokeza kwa wakati muafaka ili kuepusha manung’uniko, chuki na kejeli kwa Muungano huu. Tukizitatua changamoto zetu kwa wakati muafaka, Muungano huu utaendelea kudumu na kupendwa kwa muda wote na hakutakuwa na manung’uniko na chokochoko zozote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni imani yangu na ni imani ya Watanzania kwamba viongozi wetu wana dhamira ya dhati katika kuuendeleza Muungano huu kwa vitendo kwa faida ya nchi zetu mbili za Muungano kwa maana ya Zanzibar na Tanzania Bara. Dhamira zao za dhati zilianzia kwa waasisi wa Muungano huu; Marehemu Mheshimiwa Abeid Amani Karume na Marehemu Mzee Nyerere. Hao ndio waasisi. Marais waliofuatia baada yao, akina Mzee Jumbe, Mzee Mkapa, Mzee Ali hassan Mwinyi na mpaka sasa tunaye Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akishirikiana na Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni imani yangu kwamba wataendeleza nyayo na mema yote yaliyoanzishwa na waasisi wa Muungano huu kuutekeleza na kuusimamia Muungano huu kwa vitendo kwa maslahi ya wananchi wa Tanzania, maslahi yetu Watanzania na vizazi vijavyo vya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Awali ya yote napenda kuchukua nafasi hii adhimu kumpongeza sana na kwa dhati Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa dhamira yake ya dhati kuhakikisha kilimo cha Tanzania kinakua na kuhakikisha kwamba sekta za uzalishaji zinapatiwa fedha ili kuinua uzalishaji nchini katika kupambana na hali ya uchumi wetu, kuingiza fedha za kigeni, kutatua matatizo ya wananchi wetu na hasa wakulima ili waweze kulima kilimo chenye tija na waweze kupata faida ya jasho lao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo limedhirika wazi baada ya Mheshimiwa Waziri wa Kilimo kukabidhi vitendea kazi kwa Maafisa Ugani wetu pamoja na vifaa mbalimbali ikiwemo vifaa vya kupimia afya ya udongo. Hiyo ni dhamira ya dhati na huo ni mwanzo mzuri wa kuona kwamba sasa tunakwenda kupiga hatua katika sekta hizi ya kilimo na uzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo napongeza pia mpango wa Wizara ambao unakwenda kutoa ruzuku kwa wakulima wetu hivi karibuni. Pamoja na na kutoa hizo ruzuku bado naishauri Serikali kuwekeza zaidi kwenye viwanda vya mbolea vya hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwekezaji umeanza kwa kiwanda cha mbolea na vingine vilianza huko nyuma, naishauri Serikali iendelee na uwekezaji kwa wananchi wetu wa hapa ndani pia wawekeze kwenye sekta hii ya viwanda vya mbolea, kwa sababu, mbolea ni silaha kubwa katika kilimo popote duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, itakapotokea changamoto nyingine zozote duniani kwenye sekta hii ya mbolea basi na sisi tuwe na akiba yetu ya mbolea hapa nchini tuweze kukidhi mahitaji yetu ya wakulima wetu ndani ya nchi, ikiwemo kupanda kwa bei ya mbolea mara kwa mara, kupanda kwa mambo mbengine yatakayojitokeza ya kimazingira na mabadiliko ya tabianchi, lakini na sisi tukiwa na viwanda vyetu vya mbolea hapa nchini, ambavyo vitakwenda kuzalisha mbolea zinazolingana na udogo wa nchi yetu kutokana na mazingira tofauti tofauti ya nchi yetu, itakwenda sana kumkomboa mkulima wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea na mchango wangu, Mheshimiwa Waziri amegusia kuhusu kuzalisha mbolea asili, nami nakubaliana naye katika kuzalisha mbolea asili. Mbolea asili ziende pamoja na viuatilifu asili. Tunavyo viuatilifu vyetu asili na Wizara kupitia vitengo vyake vya utafiti vimeshafanya utafiti kwa baadhi ya viuatilifu, ni vema viuatilifu hivyo vikatangazwa wananchi wakavijua na kuweza kuvitumia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sekta hii ya kilimo kumeongezwa fedha kwenye utafiti, huduma za ugani, umwagiliaji, tunaomba katika fedha hizi zilizoingizwa nyingi kwenye bajeti hii ya kilimo, bado tunahitaji fedha zaidi za uwekezaji mkubwa katika kilimo. Fedha hizi zilizoingizwa zilizowekwa kwenye bajeti tunaomba zitoke kwa wakati, kwa sababu zinapotoka mwisho wa mwaka kilimo kinakwenda kwa miongo na bado hatujajiweka sawa kwenye umwagiliaji, hivyo inapokuja fedha miongo ile imeshapita, fedha zile zinakuwa sasa zimekuja mwisho. Tunaomba fedha zije kwa wakati zikafanye kazi kwa wakati kulingana na mazingira ya kilimo kwa Mikoa tofauti, hali ya hewa tofauti na kilimo tofauti katika mazingira tofauti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea, niongelee kuhusu utoshelevu wa mafuta. Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imejipanga kuhakikisha kuna utoshelevu wa mafuta nchini. Nami naipongeza Wizara kwa mikakati mbalimbali. Tunaomba sote tu-support Wizara ya Kilimo kufuatia watendaji wake, tuunge mkono juhudi za Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo mambo ya mafuta, Wizara imewekeza hivi sasa kuliimarisha zao la nazi kwa kutoa miche 2,000. Miche 2,000 ni kidogo mno, kwa sababu kuna baadhi ya maeneo mafuta wanatumia tu kwa sababu hawana la kufanya, lakini matumizi makubwa ni nazi. Kwa hiyo, tukiimarisha hili zao la nazi, litakwenda kupunguza ule upungufu wa mafuta uliopo nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna haja ya kujipanga katika mazao ya biashara na mazao ya kukidhi mahitaji yetu ya nchi. Kwenye mazao ya biashara tuangalie soko liko wapi? Mazao gani yana soko? Halafu turudi kwa wakulima, tuhamasishe wakulima wetu walime vipi. Hapo hapo tuimarishe uhifadhi na vifungashio ili mazao yetu yawe na ubora. Vifungashio pia ni sehemu ya kuvutia biashara kwani biashara ipendezayo ndiyo inunuliwayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiacha suala la vifungashio, sasa niipongeze Serikali kwa kuwekeza mtaji mkubwa kwenye Benki ya Kilimo. Benki hii itakwenda kumkomboa mkulima mdogo. Tunaiomba Serikali, kila inapoweza kuongeza mtaji kwenye Benki hii, iendelee na juhudi za kuongeza mtaji ili tuone wakulima wetu wananufaika na kuweza kukidhi mahitaji ya kilimo ikiwemo vitendea kazi ili wavutike na biashara hii ya ukulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubalina na Wizara katika kuuboresha ushirika, ufanyiwe kazi kwa haraka kutatua zile changamoto na pia kutazama udhaifu uliopo kwenye ushirika na kuyaboresha kwa muda huu muafaka ili ushirika uweze kumkomboa mkulima wetu mdogo ambaye anahitaji sana nguvu ya kusaidiwa na Taasisi hii ya Ushirika ambayo ndiyo taasisi tunayoiona kwa sasa inayoweza kumpunguzia matatizo mkulima katika kuhifadhi mazao yake ambayo yanapotea na pia kumtafutia soko la uhakika katika kuuza mazao yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza sana juhudi zinazofanywa na Wizara kuwekeza Ofisi za Umwagiliaji katika Halmashauri au Wilaya zote za Tanzania. Tunachoomba kwa Mheshimiwa Waziri, hao wahusika wapewe ushirikiano na Wizara na Taasisi zilizopo katika maeneo husika ili waweze kufanya kazi zao kwa uadilifu na kumsaidia mkulima katika sekta hii ya umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikimalizia, niseme kilimo ni biashara, kilimo ni utatuzi mkubwa kwa wananchi wa Tanzania. Naiomba Serikali, kila itakapokuwa na uwezo, basi iwekeze katika sekta hii ya kilimo. Tumpe moyo Mheshimiwa Rais wetu, kwa dhamira yake ya dhati ya kuinua sekta hii na Mheshimiwa Waziri anajipanga vizuri, tunaomba tumpe support kabisa ili tuweze kumkomboa mkulima mdogo aweze kupata tija kwa anachokivuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa hii nafasi. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuamsha asubuhi hii ya leo tukaweza kuja kujadili bajeti hii muhimu kwa nchi na kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kuipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia napenda kupongeza Wizara zote mbili ambazo zinahusika na mambo mawili haya ya Muungano na Mazingira. Nikiendelea, kwanza napenda kuwapongeza wananchi wa Tanzania kwamba, keshokutwa tu tunatimiza miaka 59 ya Muungano wetu wa Tanganyika na Zanzibar. Muungano ambao umeleta sura na nuru ya Taifa letu katika dunia nzima. Ni Muungano wa kupigiwa mfano, tunatakiwa sisi tuliourithi kutoka kwa waliouasisi kuundeleza na kuutunza kwa vitendo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Serikali na vikao mbalimbali vya kutatua changamoto mbalimbali za Muungano zinazojitokeza, napenda kuipongeza Serikali kwa jitihada hizo inazozichukua siku hadi siku. Pia napenda kukubaliana na maoni ya Kamati kwamba mgawanyo wa ajira na uwiano wa watumishi katika sekta za Muungano ufanyiwe kazi na uwe uwiano ule uliopangwa ili kuhakikisha pande zote mbili za Muungano zinanufaika na utumishi huo na ajira hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiendelea, najikita kwenye upande wa mazingira. Napenda kuipongeza Serikali kwa juhudi mbalimbali inazochukua katika kuhakikisha nchi yetu inatunza mazingira, tunadhibiti mabadiliko ya tabianchi kwa ujumla na shughuli mbalimbali za uhifadhi wa mazingira. Napenda nichangie mambo yafuatayo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na pongezi hizi, naipongeza Serikali kwa kuwekeza miradi ya mazingira mbalimbali kwa upande wa pande zote mbili za Muungano, na upande wa kwetu Zanzibar tumepata miradi ya kujenga tuta, ukuta, kuhifadhi maji chumvi yasiingie. Pia, tumepata mradi wa majiko ambayo yanatumia nishati mbadala ili kuepusha ukataji wa miti na kuni. Vile vile mradi ambao utasaidia wananchi wa Pwani wasipasue mawe ili kujengea kwa kupewa boti kama mbadala wa biashara zao na kujiingizia kipato.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto bado ziko, hasa kwa upande wa visiwa. Visiwa vyetu vinaliwa na maji ya bahari na kuna hatari ya kupoteza uhalisia wa visiwa hivi. Tanzania ni Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambayo sasa ni Tanzania na ndani ya Tanzania kuna visiwa ambavyo vinahitajika duniani. Tudhibiti visiwa hivi visichukuliwe na bahari na baadaye vikapotea kabisa kwenye ramani ya dunia. Tanzania ni bara na visiwa vyake na hasa maeneo ya pwani. Maeneo kama ya Nungwi, Kizimkazi, Makunduchi, Mkoani, haya tayari maji yanapanda juu na yameshaathiri makazi ya wananchi na huduma mbalimbali za kijamii. Ni vyema sasa tukawekeza zaidi kuhifadhi visiwa hivi kwa sababu maji ya bahari yana nguvu kubwa yanapoingia kwenye maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiendelea naomba nichangie kuhusu hapo hapo kwenye mazingira. Ukataji wa miti bado umekuwa mkubwa. Ukataji wa miti hauendani na uwekezaji wa miti. Tufanye tathmini ya kutosha, uwekezaji wetu wa miti unaendana na uhalisia wa miti iliyoota? Kwa sababu, tunawekeza fedha nyingi katika kupanda miti, lakini hatuna uhakika wa kutosha kwamba miti ile yote iliyopandwa inakua na inastawi. Tukiangalia Mkoa wa Dar es Salaam tu, mkaa unaotumika kwa mwezi ni tani ngapi? Kila tani kwa wastani ni miti mingapi? Miti mingapi kwa wastani ni hekta ngapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tutazame hapo, tani zinazotumika kwa mwezi na miti inayokatwa kwa mwezi; kwa maana mti tunajua unatoa kiasi gani, kilo ngapi, halafu tuone sasa tani zilizokatwa miti ni hekta ngapi? Je, na upandaji wa miti unawiana na ukataji ule wa miti? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiendelea, Tanzania tuna ardhi ya kutosha, tuna misitu, tuna eneo kubwa, lakini kuna fedha nyingi zimewekezwa kwenye mambo ya hewa ya ukaa. Kwenye hewa ya ukaa bado Tanzania hatujasaini, lakini kuna nchi ambao ni majirani zetu wa Afrika ikiwemo Kenya, Burundi, inatarajia kusaini; Gabon, Mozambique, Malawi, wameshasaini mkataba ambapo katika mkataba huo kuna ajira zitapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ajira zitakazopatikana kwa ajili ya uwekezaji kwenye hewa ya ukaa na fedha nyingi zitapatikana kwenye hewa ya ukaa. Kama ajira milioni 30 zinategemea kupatikana ifikapo mwaka 2030, lakini pia inatarajiwa kupata fedha kwa kupitia biashara karibu Shilingi trilioni 14, sisi tumekwama wapi? Au kuna masharti magumu ambayo hayaendani na mila na desturi zetu? Kama hakuna masharti ya namna hiyo, basi tunapaswa na sisi kujiunga na kusaini, ili tuweze kufaidika na hizi fedha na uwekezaji wa ajira mkubwa ambao unapatikana kwenye hewa hii ya ukaa ambayo tayari nchi jirani zetu wameshajiunga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ninalotaka kuishauri Serikali, ni kwenye utunzaji wa mazingira…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili hiyo.

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa hii nafasi. Kwanza napenda kuipongeza Wizari yetu hii ya Mifugo na Uvuvi; Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wake wote wa Wizara. Kwa kweli wametuletea bajeti ambayo imegusa kila sekta na matarajio yetu wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza kwa dhati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuiona Sekta hii ya Uvuvi na Mifugo kwamba hii ni sehemu ambayo Serikali yetu itainua kipato cha mwananchi mmoja mmoja, kitaongeza ajira, na lakini pia kitaleta uchumi mkubwa ndani ya Nchi yetu. Tunafahamu kwamba kuna baadhi ya nchi hapa duniani zinaendeshwa kwa uvuvi tu na nyingine kwa mifugo tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza na pia nampongeza kwa dhati Rais wa Zanzibar kwa sababu kwenye uvuvi wa Bahari Kuu ni chombo cha Muungano na ndiyo maana Mawaziri wetu wote wawili wako hapa na kila mwaka tunawaona. Nawapongeza sana kwamba na kule Zanzibar sasa kuna mikakati madhubuti ya kuhakikisha Zanzibar nayo kwa kushirikiana na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitia chombo hiki cha uvuvi wa Bahari Kuu kinataka kuwekeza kwenye Sekta hii ya Uvuvi wa Bahari Kuu. Nawapaongeza sana Serikali zote mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea, naipongeza Wizara kwa kusamehe na kuondoa tozo mbalimbali katika Sekta zote; za Uvuvi, Mifugo na mambo yanayohusiana na mazao hayo, ikiwemo Sekta ya Maziwa. Sekta ya Maziwa ilikuwa ina changamoto nyingi sana huko nyuma kutokana na tozo mbalimbali ambazo zinakwamisha ukuaji wa sekta hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tozo nane zimesamehewa au zimeondolewa katika Sekta ya Maziwa. Ninachokiomba sasa, tuendelee kuhamasisha uwekezaji wa viwanda vya maziwa kwa maziwa yanayodumu kwa muda mrefu ili kuokoa maziwa ya wafugaji wetu yasiharibike na sisi kuepuka kuingiziwa maziwa ambayo virutubisho vyake vimeongezwa baadhi ya mambo ili kuathiri afya zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, usalama wa chakula pia unapatikana kwenye Sekta hizi mbili; Mifugo na Uvuvi. Naipongeza sana Serikali kwa kutaka kuwekeza katika Sekta hizi. Nikiendelea, Serikali inawekeza fedha nyingi sana kwenye Sekta ya Ufugaji kwa kuwajengea mabwawa wafugaji wetu huko waliko. Cha kusikitisha, uwekezaji ule unatuvunja moyo kwa maana haufikii viwango vile ambavyo vinatarajiwa. Ninachokiomba kwa Wizara, pamoja na kwamba maeneo ya wafugaji yako ndani sana, wawe na ufuatiliaji wa mara kwa mara kuhakikisha malambo na mabwawa hayo yanajengwa kwa viwango vinavyostahili ili kuzuia kupoteza fedha za Serikali, na walipa kodi ambao ni wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Sekta hii ya Mifugo, bado mfugaji hafaidiki na soko au fedha kutokana na bidhaa yake ya ufugaji. Tumepata masoko kutoka nje ya nchi, majirani zetu tunao, lakini kiunganishi hapa kinakuwa kikwazo, kwa sababu wanakutana na madalali. Madalali ndio wanaokwenda kwa wafugaji, wanawachukua ng’ombe mpaka Dar es Salaam, wanawakabidhi wale wafanyabiashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba hii ni Sekta binafsi lakini kuwe na kiungo, kama kituo kuhakikisha mnunuzi anajua afike wapi ili aweze kuwapata hawa ng’ombe kupitia kwa mkulima au mfugaji mwenyewe ili afaidike zaidi yule mkulima na mfugaji, sio dalali. Kuna udalali mkubwa hapo unaofanyika kwenye Sekta hii ya Mifugo. Kwa hiyo, tuendelee kuimarisha sekta zetu au tasnia zetu za utafiti kwenye uvuvi na kwenye mifugo. Hapo ndiyo tutapata malisho bora, tutapata mbegu bora, na mazao bora kwa ajili ya sekta zote mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nigusie uvuvi wa Bahari Kuu. Muda mwingi tulikuwa tunapiga kelele kuhusu sekta hii kuwekeza katika uvuvi wa Bahari Kuu. Naipongeza kwa dhati Serikali, sasa imejikita kuingia kwenye Sekta ya Uvuvi wa Bahari Kuu, kwa maana ya kwamba imeagiza meli mbili za uvuvi kwenye ujenzi wa Bandari ya Uvuvi kule Kilwa, tumeona mambo yameanza. Tunachoomba sasa, Serikali iwekeze fedha kwa haraka ili bandari ile imalizike, meli hizo zinunuliwe, na vifaa vyake vingine vijengwe ili tuingie kwenye Sekta ya Uvuvi wa Bahari Kuu, nasi tuweze kufaidi rasilimali alizotupa Mwenyezi Mungu kwa kupitia bahari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea kwenye uvuvi wa Bahari Kuu, izungumzie Shirika la TAFICO. Nimeona mipango mingi ambayo imepangwa kwa ajili ya kulifufua hili Shirika ili lianze kazi. Shirika hili linahitaji uwekezaji mkubwa, linahitaji fedha nyingi kwa sababu miundombinu yake inatumia gharama kubwa. Tusione shida kuwekeza, kwa sababu tukiwekeza leo tutafaidika kesho. Tunapowekeza zaidi kwenye Shirika la TAFICO tutavuna zaidi mabilioni kwa mabilioni ya fedha na tutaongeza ajira, tutaongeza ukuaji wa uchumi na pato la Taifa. Shirika hili ni muhimu, litatukomboa kwenye sekta ya uvuvi, tutakapoingia kwenye uvuvi wa Bahari Kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulifanye hili Shirika lianze kazi haraka, liungane na bandari ya uvuvi tuingie kwenye uvuvi wa Bahari Kuu, tufaidi. Tusiwe kila siku tu tunapiga kelele, Bahari Kuu, Bahari Kuu! Bahari imejaa Samaki, nchi za nje wanakuja na meli zao wanavua, sisi tumekaa. Mwenyezi Mungu katuruzuku hii rasilimali, tuitumie, tuwekeze, tukavuna zaidi ya tunachowekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea, nimeona kwenye Wizara, Serikali ina mipango ya kuwasaidia wavuvi wadogo wadogo kwa zana za uvuvi. Tuendelee kuwasaidia wavuvi wetu kwa mikopo nafuu ili waingie kwenye Sekta ya Uvuvi na wao wafaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uvuvi ni kazi ngumu. Unapotoka kwenda kuvua, unajua kwenda, hujui kurudi. Ikikukuta dhoruba huko, unaweza ukapotea baharini na usirudi, au kwenye visiwa usirudi, au ukapotelea nchi jirani baada ya miezi mitatu ndiyo unaokotwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uvuvi una hali ngumu, tuwawezeshe wavuvi wetu wavue kisasa na kwa tija. ikiwepo kuzifanyia marekebisho sheria na sera mbalimbali za uvuvi, iwe ni yenye manufaa kwetu na wavuvi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea, kuna mfumo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia kwa kusema, tuendelea kuvua na kufuga kwa kuhifadhi mazingira ya nchi, ili kunusuru nchi yetu isije ikawa jangwa na mabadiliko ya tabianchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii jioni ya leo. Kwanza napenda kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuona umuhimu kwenye sekta hii ya kilimo kwa kuongeza fedha katika bajeti kila mwaka, kuanzia mwaka jana. Fedha zinaongezeka kila bajeti inapokuja. Ninampongeza kwa juhudi mbalimbali anazohamasisha Wizara hii iweze kufanikisha malengo na majukumu yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara; Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wake wote kwa mikakati madhubuti waliyojipangia katika kupaisha sekta hii ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona katika bajeti Wizara imejipanga na mikakati madhubuti ya kuhakikisha sasa tunaingia kwenye sekta ya kilimo, kilimo chenye tija, kwa maana ya kwamba kuwekeza katika vitendea kazi kwa Maafisa Ugani, viuatilifu, utafiti pamoja na umwagiliaji. Fedha zikiingizwa kwa wakati, na tukipata fedha nyingine zaidi, kilimo chetu kitakuwa cha hali ya juu na chenye tija kwa manufaa ya mkulima, na kuongeza pato la Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo kina utashi na kina hamasa kwa kupata masoko. Masoko ndiyo yanayosababisha kuongeza utashi na hamasa kwa mwananchi na mkulima kulima zaidi, kwa maana atapata tija katika kilimo chake. Kwa hiyo, sasa kilimo kianzie sokoni halafu kije shambani kwa maana ya kwamba masoko ambayo tuna uhakika nayo tuhamasishe wakulima wetu walime zaidi pamoja na mazao mengine ya kujikimu wenyewe yaendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara ya Kilimo, inafanya jitihada kubwa kutafuta masoko ya wakulima. Jitihada hizi zikiungana na Wizara ya Biashara, masoko ya wakulima wetu yatakuwa makubwa zaidi. Masoko siyo ya nje tu, ni pamoja na masoko ya ndani kwa maana ya kuwekeza viwanda kwa ajili ya malighafi za wakulima, kusindika na kuyaongezea thamani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi leo nataka nijikite kwenye kilimo hasa kilimo cha asili. Nimeona kwenye bajeti, kuna mpango wa kuhuisha mbegu zetu za asili na kuzifanya ziwe nyingi zaidi. Mbegu za asili tunajua, zina virutubisho vingi na havina kemikali. Kwa hiyo, kwa mbegu za asili tutapata mazao yenye uhakika pia wa afya zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nahamasisha na kuishauri Wizara iendelee na juhudi hizo za kuwahamasisha wakulima wetu kuweka mbegu zile za wakulima ambazo ni mbegu za asili, tuwaongezee utaalamu, tuwape taaluma ya kuweza kuzalisha mbegu zile zaidi. Usalama wa chakula ni pamoja na usalama wa mbegu. Tukiwa na mbegu zetu, itakapotokea zahama yoyote huko duniani, sisi tuna mbegu zetu na kilimo chetu kitaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo tukiunganisha na umwagiliaji, kilimo kile kitakuwa na tija kwa kutumia kilimo hifadhi na kilimo hai. Kilimo hai kinatumia mbolea zetu za asili kwa maana ya mbolea ya samadi, kwa hiyo, tunazuia udongo wetu na ardhi yetu kuharibiwa, na wataalamu wapo. Tuchukue wataalam hawa na utaalam wao kuongeza kwenye wakulima wetu wa kawaida namna ya kulima kilimo hifadhi na kilimo hai, pamoja na kutumia mbegu zetu za asili. Kilimo hai kinahifadhi ardhi, kinahifadhi udongo na tunapata vyakula vyenye virutubisho ambavyo havijaadhiriwa na kemikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna viwanda vya mbolea ndani ya nchi. Bado kuna haja ya kuongeza viwanda vya mbolea ndani ya nchi na viwanda ambavyo vitakuwa vinamilikiwa na wananchi wa hapa nchini kwa maana ya kudhibiti soko la mbolea kutoka nje, tutauziana hapa wenyewe, na pia mbolea hiyo wazalishe mbolea ambayo inalingana na mahitaji ya udongo wetu na mahitaji ya ndani ya kilimo chetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri tuhamasishe viwanda vya mbolea na vikiwemo viwanda vya mbolea vya asili kama hii ya samadi, tuifanyie marekebisho ili iweze kutumika katika ardhi ya kilimo kwa ajili ya kuhifadhi udongo wetu na kuhifadhi ardhi yetu na kuwasaidia wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mbolea ni silaha kubwa kwenye kilimo. Chochote kikitokea duniani kama majanga, maafa, tukiwa na viwanda vyetu ndani ya nchi, vinavyotosheleza wakulima wetu, kutakuwa hatuna tatizo lolote kwa sababu tunao mtaji wetu wa mbolea na mbegu ndani ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kuwasaidia wakulima ruzuku ya mbolea. Jihada hizo ziendelee, lakini pia uhamasishaji wa viwanda vyetu vya mbolea vya ndani ya nchi, uendelee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, napenda kuipongeza Serikali kwa mradi wa BBT uliobuniwa na Wizara ya Kilimo, kwa kweli utakwenda kumkomboa kijana na mwanamke. Nami naongezea kwamba, Wizara ya Kilimo itafute dirisha lingine ambalo litamsaidia mkulima ambaye hana elimu kabisa, au kaishia madarasa ya chini kabisa, hana utaalamu wa kuingia kwenye mitandao, hasomi hata gazeti, hana hata kile kisimu cha tochi. Yule naye anahitaji kupata fursa kama hii ili naye aweze kumiliki ardhi na kuendesha kilimo. Wizara ibuni mbinu muafaka itakayomshirikisha mkulima mdogo yule aliyeko kijijini ambaye hana fursa nyingine yoyote ya kitaalam ili naye aweze kumiliki ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwasaidia kwa njia hiyo, tutakuwa tunaweka uwiano sawa wa kumiliki ardhi kama keki yetu ya Taifa aliotujalia Mwenyezi Mungu tuweze kuipata kwa usawa wa elimu za aina zote, rika zote na jinsia za aina zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia kwa kusema, nawapongeza sana Wizara, waendelee na jitihada zao hizo, tunawaunga mkono, tutaendelea kuwashauri pindi inapobidi, kwa sababu tunaona mwelekeo upo, tutatoka hapa. Dhamira ipo ya kutoka hapa, nchi imedhamiria na Wizara imedhamiria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Azimio la Bunge kuhusu Mapendekezo ya Kuridhia Itifaki ya Biashara ya Huduma ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ya Mwaka 2012
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Napenda kuipongeza Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kutuletea kuridhia Itifaki hii ya SADC. Nawapongeza wote wa hapo Wizarani kwa juhudi zao mbalimbali za kuhakikisha nchi yetu inakwenda kunufaika na fursa mbalimbali zilizopo katika SADC na sehemu nyingine katika dunia yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na mapendekezo ya Kamati kwa kuishauri Serikali. Kati ya nchi tano ambazo hazijaridhia Azimio hili na Tanzania imo, leo hii tunakwenda kuridhia Azimio hili kwa manufaa ya nchi yetu, manufaa ya Watanzania na manufaa ya wafanyabiashara wetu wanaotoa huduma mbalimbali katika nchi. Tutanufaika na fursa mbalimbali zikiwemo biashara za huduma kama vile elimu, afya, usafirishaji na mambo mengine yanayohusu kutoa huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, limezungumzwa hapa suala la kwamba tutapata fursa ya kukitumia na kukieneza Kiswahili katika ukanda huu wa SADC. Ushauri wangu kwa Serikali, tuitumie vema fursa hii ya uwekezeaji kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania na vijana wetu ambao tayari ni weledi wa Lugha ya Kiswahili. Tuhakikishe Tanzania tunaendelea kukihakikisha Kiswahili ni cha Tanzania kuepusha soko hili likatekwa na nchi nyingine wakajifanya wao ndiyo wakuu wa Kiswahili. Nashauri tuendelee kuhamasisha vijana wetu kutumia fursa hii ya ajira kwa soko la kueneza Kiswahili kwa fani mbalimbali ualimu, ukalimani, uhadhiri na mambo mengine ya kuandika vitabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakwenda kunufaika pia na fursa nyingine kwa upande wa mazingira, tutanufaika pia kwa fursa za watoa huduma ikiwemo mawasiliano elimu na afya. Naishauri Serikali tuweke mazingira mazuri kwa watoa huduma wetu tulionao na Serikali kuanzisha kitengo maalum ndani ya Wizara cha kuibua fursa ambazo watakwenda kuwekeza katika hizo nchi nyingine za SADC. Kwa sababu, isiwe wao wanakuja kwetu tu kutumia fursa zetu lakini sisi hatupati kwenda. Ni vyema sasa tukawasaidia wafanyabiashara wetu hawa wa huduma namna ya fursa zilizokuwemo kwenye nchi za wenzetu za SADC ili tuwe tunabadilishana uzoefu na maarifa wao wanakuja na sisi tunakwenda. Tukifanya hivyo na sisi tutajitangaza zaidi kwa fursa mbalimbali za uwekezaji katika nchi nyingine za SADC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusaidie kuwawezesha kimitaji wafanyabiashara wetu watoa huduma, kwa sababu bado kuna hili tatizo la mitaji ya kutosha. Tuwasaidie namna ya kupata mitaji katika benki ili na wao waingie kwenye huu ushindani kwenye kuwekeza katika nchi mbalimbali za SADC ili tupate hayo manufaa na sisi ya kuingia kwenye SADC. Tukifanya hivyo wafanyabiashara wetu watoa huduma watakuwa na wao na ujasiri watakuwa na uelewa na weledi wa kuwekeza na watatoka uoga kwa sababu wakati mwingine ni hofu tu lakini tukiwatoa hofu tukawapa elimu na tukawapa maarifa ya kuingia, wataweza kuingia kwenye ushindani huu wa soko la kutoa huduma mbalimbali katika nchi za SADC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Bunge likubali kuridhia Azimio hili ili tuendane na wakati tusiwe tumeachwa nyuma twende sambamba na hali ya mabadiliko ya dunia ya sasa ili kuibua fursa za uwekezaji kwa wananchi wa Tanzania fursa za ajira, fursa za masomo na fursa nyingine za kuinua uchumi wa nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Nami niendelee na kuwapongeza Wizara Mheshimiwa Waziri, Katibu Mkuu na timu yake kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuendeleza sekta zote zinazohusiana na Wizara yao. Pia napenda kukushukuru Mheshimiwa Waziri, kwani kwetu kule Zanzibar anajitahidi sana kuweka ushirikiano wa pamoja na kutoa msukumo katika mazingira yote ya utamaduni na kuhakikisha yanakwenda sambamba na Tanzania Bara. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri, aendelee na juhudi zake hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda inabidi moja kwa moja nichague moja la kusema hapa. Najielekeza kwenye lugha ya Kiswahili. Lugha ya Kiswali ni ajira, lugha ya Kiswahili ni rasilimali na pia lugha ya Kiswahili inaitangaza Tanzania katika Sekta ya Utalii. Kuna utalii sasa unafanyika kupitia lugha ya Kiswahili, kwamba watalii wanakuja kusikia hiyo lugha ya Kiswahili, kuona nchi yenyewe ambayo imeanzisha Kiswahili na kuona utamaduni wa Mswahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea kwenye hiyo hiyo lugha ya Kiswahili; ili kukamata soko la ajira ni lazima Wizara hii iongezewe fungu la fedha katika kuwaandaa vijana wetu kwa soko la ajira la ukalimani na ualimu, kwa maana ya kwamba tuwaongezee uwezo na idadi ya lugha ambazo ataweza kwenda kutafsiri na kufanya ukalimani, isiwe tu Kiswahili na Kiingereza, bali na lugha nyingine za kigeni wawe wanazimudu ili kudhibiti hili soko la ajira lisije likachukuliwa na mataifa mengine ambao sasa hivi wao ndio wanajifunza Kiswahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiswahili chetu kinajulikana Afrika, kinajulikana duniani sasa hivi na kinaipaisha Tanzania, lakini tukiimarishe Kiswahili chetu kiwe imara. Kiswahili ni mchanganyiko wa lugha mbalimbali duniani; Kiarabu, Kiingereza, Kiajemi na lugha nyingine. Kwa maana hiyo, Kiswahili ni mchanganyiko wa lugha. Neno lenyewe Swahili, linatokana na neno la Kiarabu, kwamba ni pwani, pwani. Pia Waturuki wanatumia neno hilo hilo swahil kwa maana ya pwani. Kwa hiyo, ni lugha ya Pwani na utamaduni wa pwani ukaenea duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2022 nilisema na leo narudia tena kwa uchache tu. Kuna maneno tunayatumia ambayo yameungana; Kiswahili, Kiarabu, Kiingereza, mfano taabani, kanuni, madrasa, dhuluma, Askari, barafu; haya ni Kihindi, Kiarabu na Kiswahili tunayatumia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nikwambie sasa, bendera na safari ni neno la Kihispania; vurumai ni neno la Kigiriki, tunalitumia; pashiani, reshani Kijerumani kuna hela, kuna zahanati. Hapa natoa mfano mdogo tu tuone. Hoja yangu ni kwamba tunapotunga haya maneno ya Kiswahili tutumie maneno rahisi na mepesi kama lugha yenyewe, isiwe sasa hivi Kiswahili ni kigumu. Kimekuwa kigumu sana na hapo wanapokaa kuyatunga haya maneno, ushirikishwaji unakuwaje kwa pande zote mbili; Baraza la Sanaa, Baraza la Kiswahili la Taifa na Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKITA na BAKIZA)? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, chombo hiki sasa hivi kimemaliza muda, naishauri Serikali itapokiunda, iangalie upya muundo wake kama unakidhi vigezo vya sasa na kuitangaza Kiswahili duniani? Kama haukidhi, tufanye marekebisho, tutafute Waswahili wabobezi ambao wapo, waingie kwenye hizi sekta waweke sawa Kiswahili chetu ili kiendane na hadhi na ubora unaotakiwa, kuliko kujaza tu maneno hata hayaeleweki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshatoa mfano kwamba Kiswahili ni mchanganyiko wa maneno. Lugha nyingi zinategemeana kwenye maneno mbalimbali yenyewe huko kwenye Kijerumani, Kifaransa, Kigiriki na Kitaliano, yanaingiliana siyo kwenye lugha yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea, nataka nitoe mfano mdogo kwa watu ambao wamekineemesha Kiswahili, wamekitangaza Kiswahili duniani na kukistawisha. Nina wengi, lakini kwa uchache tu, napenda kumtaja Prof. Mohamed na Dkt. Abdallah, hawa walikuwa walimu katika Vyuo Vikuu vya Uganda na Kenya ambao wanafunzi wao sasa wameshalikamata soko la Ghana na Nigeria, wanasomesha huko Kiswahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye sekta ya utangazaji kuna watu wamekichangia Kiswahili tangu miaka ya 50 na 60 nchi mbalimbali. Mfano, Watangazaji kuanzia miaka ya 1950, kuna Bwana Ahmed Rashid Ally, Sauti ya Afrika, Sauti ya Ukombozi, Cairo; kuna Maimuna Fassy, sauti ya Marekani; Abdulrahim Kaktan, Radio Deutsche Welle; Abdala Mbamba, sauti ya America; Ahmed Rajab BBC na wengine Radio Moscow Abdul Wahidah Hassan Shehe. Tukiendelea, Radio Japan, Rahman Mohamed Dahman, ambaye alitokea Radio Deutsche Welle; Umul Kheir; hao ni wengi na baadhi tu akiwemo Bw. Ramadhani Ally ambaye alitangaza Idhaa ya Kiswahili Czechoslovakia Idhaa ya Prague, pia alitangaza Berlin na baadaye Radio Deutsche Welle, mpaka akastaafu. Mwingine Radio Beijing, Miraji Mpatani, Haroub Othman; tukiendelea, kuna na wengi Radio China. Naomba tuwaenzi, tuwatambue. (Makofi)

Mheshimiwa mwenyekiti, mwisho niseme hivi, neno la Tanzania lina nuru na linapaa duniani. Aliyetunga jina la Tanzania alikuwa ni mwanafunzi kwa wakati huo, ametumia kipaji chake na uwezo wake. Kama ingewapendeza, miaka 60 ya Muungano, Jamhuri ya Tanzania akaletwa huyu mtu tukamwona na Taifa likamtambua kutokana na jambo zuri aliyotufanyia Taifa letu, Tanzania inapaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nakushukuru naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Awali ya yote napenda kuipongeza sana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiongozwa na Rais wetu mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan, pia napenda kuipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na ndugu yetu Dkt. Hussein Ali Hassan Mwinyi, kwa pamoja na juhudi zao zote wanazofanya kuhakikisha wananchi wa Tanzania wanapata maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Waziri wa Fedha, Naibu Waziri wa Fedha, Katibu Mkuu na timu yake yote katika kutupambania sisi Watanzania kutatua changamoto mbalimbali zinazotukabili pamoja na bajeti nzuri hii waliotuletea, nawapongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea na mchango wangu napenda nijielekeze kwanza kwenye sekta ya kilimo. Bajeti ya Kilimo sasa hivi imefikia bilioni 970.8. Ni safari ndefu, tumeanza mbali, napenda kuipongeza Serikali kwa juhudi hiyo katika kutatua changamoto za wakulima pia kujiwekeza kwenye kilimo chenye tija kwa mwananchi mkulima lakini pia kwa faida ya Watanzania wote na Taifa letu kupata fedha za kigeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuipongeza sana bajeti hii kwa kupunguza na kuondosha baadhi ya tozo na kodi mbalimbali kwenye sekta za uzalishaji ikiwemo kilimo, mifugo na uvuvi pamoja na sekta zingine za kijamii. Napenda kuipongeza bajeti hii kuna mambo yametugusa sisi wananchi kwenye sekta zetu tunaofanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea na mchango wangu kwenye sekta hii ya kilimo. Napenda kuishauri Serikali kwanza naipongeza Serikali kwa kuongeza ruzuku kwa mbolea lakini naishauri tuendelee kujenga viwanda vingine vipya vya mbolea. Kwa zile malighafi za mbolea zinazopatikana ndani ya nchi tuendelee kujenga viwanda vyetu vya mbolea ili kukabiliana na changamoto hii, pia kukabiliana wakati itakapojitokeza majanga mengine na maafa huko duniani kwa sababu mbolea ni silaha kwenye kilimo chetu. Kwa hiyo, tukiwa na mbolea nyingi ya kutosha hapa nchini, tutaweza kutatua changamoto zetu bila kuagiza nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye sekta ya sukari. Bodi ya Sukari na Wizara ya kilimo imejipanga vizuri sana kuhakikisha tunakwenda kuongeza tija katika sukari lakini pia kuacha kuagiza sukari huko siku za baadae. Pamoja na hilo nia na dhamira ya Wizara ya Kilimo na Bodi ya Sukari ni kufufua Chuo cha Sukari kwa sababu sasa hivi tuna shida ya wataalam wa sukari hapa nchini, inalazimika wazalishaji kuagiza wataalam nje ya nchi. Kwa hiyo, mimi nashauri andiko lao hili lifanyiwe kazi ili kile chuo kifufuliwe na wanafunzi waanze kusoma ili tupate wataalam wetu wa sukari hapa ndani ya nchi tuepushe na tatizo la kuagiza wataalam mara kwa mara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea na mchango wangu kwenye sekta ya uvuvi, nasisitiza tu uwekezaji Bahari Kuu uendelee ili tuweze kuingia kwenye sekta hii ya uvuvi wa Bahari Kuu pamoja na kulifufua shirika la TAFICO liongezewe fedha kwa haraka ili lianze kazi na mambo haya yaende sambamba kwenye sekta ya uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mazingira nashauri na mimi masuala ya nishati mbadala. Kutafutwe mbinu ya kupunguza gharama kwa mtumiaji mdogo wa chini ili kila mtumiaji mwananchi aweze kumudu gharama hizi za kutumia nishati mbadala ili kuepusha ukataji wa miti ambao unaharibu mazingira ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ajira Serikali inajipanga sana sekta mbalimbali kuhakikisha vijana wanapata ajira, lakini kwenye ajira kuna wanaopenda kilimo, wanaopenda uvuvi, wanaopenda na kazi nyingine. Lakini kuna na wengine kila mtu kwa kipaji hake na utashi wake anapenda kile ambacho anakipenda. Mimi nashauri bado tuling’ang’anie soko la ajira kwenye lugha ya Kiswahili. Sasa hivi vyuo vingi duniani vinaanzisha mitaala ya lugha hii ya Kiswahili, bado hili soko linaandamwa na nchi jirani. Tujipange kuhakikisha hili soko tunalikamata sisi Watanzania kwa sababu sisi ndiyo wenye chimbuko la Lugha ya Kiswahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea najikita kwenye amani na utulivu wa nchi. Bila ya amani bila utulivu wa nchi haya yote tunayoyapanga hayatatekelezeka ila nia ya Serikali ni kuhakikisha kila mwananchi anaishi kwa amani na utulivu katika nchi yetu. Napenda kuwapongeza Marais wetu kwa juhudi kubwa wanayochukua kuhakikisha amani na utulivu wa nchi unakuwa sambamba na hali halisi ya maendeleo ya nchi. Wanajitoa nawapongeza kwa uvumilivu wao na ustahimilivu wao, mengi yanawakuta wanayabeba, binadamu kapewa kifua cha mbele na cha nyuma, yote wanayabeba kulingana na hali halisi inayojitokeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba viongozi wetu na wasaidizi wake ninyi Mawaziri wetu, muendelee kumpa moyo Mheshimiwa Rais, pia nasi tunaendelea kuwapa moyo ili mambo yetu ya kuwaletea wananchi wa Tanzania maendeleo yafanyike. Ninachotaka kusema baniani mbaya lakini kiatu chake dawa. Viongozi wetu wanahangaika kutafuta miradi, kutafuta pesa kwa ajili yetu sisi Watanzania lakini sisi tunajifanya hatuoni. Naomba sasa Watanzania tuheshimu na tuthamini juhudi zetu zinazofanywa na viongozi wetu mbalimbali kwa sababu lililopo baharini lisubiri ufukweni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote yanayofanyika kuna siku tutayaona na tutayafaidi sote, siyo hao viongozi wanayoyaleta. Sote Watanzania kila pembe tulipo, mafanikio haya tutayafaidi na tutajivunia hapo baadaye. Ndiyo maana nikasema lililoko baharini lisubirie ufukweni, tutaona na mwenye macho haambiwi tazama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ada ya mja kunena, uungwana ni vitendo, tenda watu wataona, majisifu weka kando, viongozi wetu wanatenda hawajisifu na tutayaona. Ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi hii awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kwanza kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa dhamira yake ya dhati kabisa kuhakikisha sekta zetu hizi za uzalishaji kilimo, Mifugo na uvuvi vinakwenda sasa kumuinua Mtanzania na kuinua uchumi wa Taifa hili, na hayo hayatekelezi kwa maneno bali anatekeleza kwa vitendo kwa maana kubwa kwamba sekta hizi ameziongezea bajeti katika matumizi yake kwa kipindi cha mwaka huu bajeti yetu ya Wizara hii imefikia bilioni mia moja tunapongeza sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulea mimba ni kazi lakini kulea mwana ni kazi zaidi Serikali, Rais wetu, Viongozi wetu Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wanahangaika huku na kule kutafuta fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati na kimaendeleo. Tunaomba fedha hizi zitumike kwa dhamira zilizokusudiwa zisiende kutumika kwa matumizi mengine kwa maana ya kwamba Serikali kupitia Wizara hii iwe wakali na iwe wasimamizi wazuri kuhakikisha fedha hizi zinafanya kazi zilizokusudiwa kwa maslahi ya wananchi wa Tanzania na Tanzania kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia sekta ya mifugo, sekta ya mifugo ina changamoto nyingi lakini kutokana na mpango wa Bajeti hii tuliyopewa na Mheshimiwa Waziri baadhi ya changamoto nyingi zinakwenda kutatuliwa kutokana na fedha zitakazoingizwa kwenye bajeti tunaomba fedha hizi Mheshimiwa Waziri na wanaohusika na utoaji wa fedha, fedha hizi ziende kwa wakati na zitoke zote ili zikatekeleze hayo majukumu yaliyopangwa kumuinua mfugaji kumuinua mvuvi wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye uwekezaji katika sekta hii ya mifugo suala la ngozi, ngozi zetu bado zina changamoto katika soko la dunia masoko yapo lakini ngozi hazikidhi viwango. Wizara imetoa mpango wamesomeshwa Maafisa Ugani kwenda kuangalia madaraja ya ngozi, lakini hawa maafisa ugani wanatakiwa kufanya zaidi ni kumuelimisha mfugaji namna ya kuhakikisha ile ngozi haiharibiki na inapata madaraja ya juu mfano kuwapiga mikwaju hovyo wale wanyama ng’ombe inaharibu sana ngozi na inakosa thamani kuwachoma choma hovyo sasa hapa elimu itolewe kwa wafugaji kwamba sio nyama tu lakini hata ngozi ni bidhaa kubwa ambayo itamsaidia kuinua kipato chake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, soko la ndani kwa maziwa lipo natoa mfano ASASI anapata asilimia 60 tu ya mahitaji yake kutokana na uwezo wa kiwanda ana ukosefu wa asilimia 40 ili kukidhi mahitaji ya kiwanda nashauri kwa vile miundombinu ya uwekezaji pale ipo eneo karibu na ASASI basi tuongeze uhamasishaji wa ufugaji bora katika maeneo yale vijana tuwahamasishe wafuge kisasa tupate mazao bora ya maziwa kwa maana tayari soko kwenye eneo lile lipo la uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo ni soko la ndani wala sio soko la nje na hivi sasa mfano Kiwanda cha ASAS kina mpango wa kutengeneza maziwa ya muda mrefu kwa maana ya maziwa ya unga kwa hivyo watahitaji sana malighafi ya maziwa. Hilo soko lipo kwa maeneo ya Iringa. Nikiendelea kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Serikali imezuia kiwanda cha kuchinja Punda na wameomba kwamba uwekezaji ule sasa ubadilike matumizi wachinje mbuzi, kondoo na ng’ombe hapa inaonekana kwamba soko la punda ni kubwa na linaweza likaongeza uchumi wa nchi na linaweza likatoa ajira kubwa kwa vijana na wanawake na wafugaji kwa jumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Wizara ihamasishe ufugaji wa punda ili kukidhi masoko ya hawa wawekezaji waliokuja kuwekeza punda ili tuweze kupata fedha za kigeni lakini tuongeze ajira kwa vijana wetu hapa inaonekana punda wanatakiwa sana huko duniani sasa kama sisi punda wetu wamepungua tumezuia sasa hawa waliokuwepo tuongeze uzalishaji wawe wengi zaidi ili tupate hilo soko la punda duniani na vijana wetu wapate ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ufugaji mnahamasisha tuwekeze zaidi kwenye malambo kwa maana ya mabadiliko ya tabia nchi, yanaharibu sana upatikanaji wa uhakika wa maji. Nashauri wafugaji na wavuvi waitumie benki ya kilimo ile benki siyo ya kilimo peke yake, tutoe elimu kwa wafugaji wetu na wavuvi kwamba benki ya kilimo inawahusu wao pia wafugaji na wavuvi. Kwenye sekta ya uvuvi kwanza nipende kuchukua fursa hii kuwapongeza wavuvi wote Tanzania kwa kazi kubwa wanayoifanya. Uvuvi ni kazi ngumu unatoka usiku unaacha nyumba na watoto, unakwenda baharini hujui kama utafika au hufiki, hujui kama utakwenda au utarudi, hujui kama utavuna au hauvuni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kazi tu ya kubahatisha vyombo vyenyewe ni duni hali ya bahari tunaijua haina muda haina wakati wakati wote inapata wazimu huko baharini. Nashauri Serikali iongeze uwekezaji kuinua wavuvi wadogo wadogo ili kunusuru Maisha yao lakini kupata tija ya kipato chao kwa muda wote huu wanafanya kazi tunapata lishe tunapata vitoweo lakini bado hali ya mvuvi ipo chini na duni na hana kipato cha uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea ufugaji wa viumbe kwenye maji Wizara imeweka mpango mzuri napongeza Serikali kwa mpango huu tuimarishe na tushajirishe vijana wetu kuingia kwenye uwekezaji wa uvuvi kwenye maji, hivi viumbe maji sio samaki tu kuna kaa, kaa wana faida kubwa na wana fedha nyingi za kigeni lakini kuna majongoo, majongoo yanatakiwa sana duniani na yana fedha nyingi za kigeni kupitia majongoo, lakini katika uvuvi huu wa viumbe kwenye maji tunapata madini ya Lulu pale, tukiwafundisha wavuvi wetu namna ya kutengeneza Lulu tutapata fedha za kigeni kupitia madini ya Lulu, Lulu ni madini na yanapatikana kupitia viumbe kwenye maji na yanafugwa, Lulu haichimbwi, lulu inapatikana baharini na lulu inatengenezwa kwenye vizimba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye uvuvi wa bahari kuu Serikali ihakikishe kwamba tunawekeza zaidi kwenye bahari kuu, mipango na mikakati mingi tumeiona tunaomba mpango hii ifanikiwe kwa sababu tunahimiza uvuvi wa bahari kuu tunataka kulitumia shirika la TAFICO, Shirika la TAFICO linahitaji uwekezaji mkubwa linahitaji fedha nyingi kwa sababu ukiliangalia hayo maeneo yake ya uwekezaji tayari mmomonyoko bahari inakwenda kula yale majengo, kwa hivyo kwenye uwekezaji ule wa majengo kunahitaji fedha nyingi kuzuia bahari yale majengo yasiharibiwe na maji ya bahari yakianza kupanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Naibu Waziri wake na Watendaji wote wa Wizara ya Fedha kwa bajeti nzuri yenye kutatua changamoto mbalimbali za wananchi wa Tanzania ikiwemo wakulima, wafugaji na wavuvi na wafanyabiashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa pia ndiye Mwenyekiti wetu wa Chama cha Mapinduzi kwa kuiongoza nchi yetu kwa kutumia busara na weledi wa kuhakikisha nchi yetu inavuka salama katika matukio mbalimbali yaliyotukumba ya kidunia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza na sekta ya kilimo. Naipongeza Serikali kwa kuweka bajeti kubwa kwenye Wizara ya Kilimo ambapo sasa kilimo chetu kitakwenda kuwa kilimo chenye tija lakini kilimo kitachomkomboa mkulima mdogomdogo na mkubwa pia kuongeza uchumi wa nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na bajeti kubwa hiyo ya kilimo ambapo nitakwenda kujikita kwenye kilimo cha umwagiliaji, mambo ya viuatilifu, Maafisa Ugani, tunayo mazao ya biashara ambayo wakulima wetu wanapata tija kupitia biashara na Serikali inapata mapato. Naomba kuishauri Serikali pamoja na mazao yetu ya biashara nashauri kwamba kutokana na changamoto zetu za ndani ya nchi tuchague mazao fulani ya kimkakati kwa maana ya kwamba tujikite kwa kipindi cha miaka miwili au mitatu Tanzania tunakwenda kuondokana na tatizo ama la mafuta ya kupikia, sukari au jambo jingine ili tukifika hatua hiyo tukaweza kujitosheleza na tukaweza kuuza baadae tunajiwekea kipindi kingine kutatua changamoto nyingine ambayo inatukabili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu sekta ya uvuvi, naipongeza Serikali kwa hatua mbalimbali za kuinua uvuvi hapa nchini, kwa kununua vifaa mbalimbali vya uvuvi na kuwasaidia wavuvi wetu. Katika kuimarisha uvuvi wa Bahari Kuu lazima taasisi mbili ziimarishwe ambayo ni TAFICO na ZAFICO. Kwa upande wa TAFICO bado miundombinu yake haijawa kamilifu na kwa bajeti hii itachukua muda kukamilika pamoja na bajeti iliyotengwa nashauri Serikali itafute fedha zaidi ili kuhakikisha TAFICO inafufuka na inafanya kazi zake. Kwa sababu kwenye TAFICO kuna miundombinu ambayo inagharimu fedha nyingi ikiwemo vyumba vya kuhifadhia samaki, vyumba vya kuweka majokofu ya baridi, inatakiwa kutengenezwa gati, inatakiwa kujenga majengo. Majengo ambayo sasa yapo kwenye fukwe ambazo fukwe zinaliwa na bahari, kwa hivyo, panahitajika fedha za kutosha ili kulifufua hili Shirika la TAFICO liweze kujikimu na kujikita katika uzalishaji utakapofika huu uvuvi wa Bahari Kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza Serikali pia kwa kuwekeza kwenye sekta ya maji kwa kununua mitambo na vitendea kazi vya kuchimba visima na mabwawa na hili ndiyo hasa dhamira ya Serikali kwamba kumtua ndoo mwanamke kichwani pia kuhamasisha kilimo, ufugaji na uvuvi. Kwa hivyo, vitu vitatu hivi vimeenda sambamba naipongeza sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo kwenye sekta ya mazingira tumeona kwenye bajeti yetu ya Serikali kuna mambo ya mazingira yanakwenda kutekelezwa, lakini mazingira tuyatazame kwa ukubwa na upana wake kulingana na mabadiliko ya tabianchi. Mabadiliko ya tabianchi yanaharibu sana mazingira yetu, kwa hivyo ni vizuri kuwekeza zaidi kwenye kuhifadhi mazingira yetu ili tubaki na nchi ikiwa salama na ubora wake kama ulivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha katika bajeti hii kutambua mchango wa asasi zisizo za Kiserikali katika kuinua uchumi wa Taifa, kuinua uchumi wa wananchi na kuleta maendeleo katika jamii yetu, nampongeza sana kwa kutambua mchango wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naongozea pale katika kuwekeza sekta ya kilimo tumeona kuna fedha hapa zimetengwa Bilioni 6.1 kwa ajili ya kumalizia kiwanda cha mbolea. Bado naendelea kusisitiza mbolea ni silaha, tunahitaji mbolea ya kutosha kwa ajili ya kilimo chetu hapa nchini, mbolea za aina mbalimbali kutokana na udongo wetu na mazingira yetu. Kwa hivyo, kuna haja Serikali kuwekeza zaidi kwenye viwanda vya mbolea ili tuweze kujitosheleza hapa nchini kwa mbolea na tuache kuagiza nje mbolea. Kwa sababu ardhi tunayo, malighafi tunayo na fedha tunaweza tukapata katika maeneo mbalimbali kama hizi tulizozitafuta na tutafute kuhamasisha wananchi wa humu ndani ya nchi kuwekeza katika sekta ya viwanda vya mbolea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua nafasi kumpongeza Mheshimiwa Waziri katika bajeti yake katika ukurasa wa 74 ameeleza kwa hisia jinsi ya kukitumia Kiswahili na kukienzi Kiswahili. Kiswahili ni fursa, Kiswahili ni ajira, Kiswahili ni bidhaa, pindi tukikitumia vizuri Kiswahili nchi yetu tutazidi kuitangaza na hapa tuunganishe na tuongeze na utalii wa lugha, utalii wa lugha utatuongezea mapato katika nchi na kuitangaza nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utalii si kwa watu wa rangi ya aina Fulani, sasa hivi tunapata watalii wa Afrika wenzetu wanaokuja Tanzania kwa sababu tu ya lugha ya Kiswahili na wakifika hapa Tanzania wanapata fursa ya kuona hivyo vivutio vingine vya utalii kwa maana walikuja tu kwa sababu ya kuona hiyo Tanzania inayosifika na lugha ya Kiswahili inayokua duniani wanataka kuja kuona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachosisitiza hapa tuwekeze kwenye watalaam, tuwape motisha wataalam wetu wa lugha ya Kiswahili pia tuweke motisha kwa wanafunzi waweze kujikita katika kusoma Kiswahili na kukisomea na kuwa watalaam, kwa maana ya kuwapatia mikopo na motisha mbalimbali ili tukipende Kiswahili kama tunavyopenda masomo ya sayansi na Kiswahili nacho tukipe kipaumbele. Hayo ni mawazo yangu kwamba wasomi wa Kiswahili tuwaongezee weledi kwa maana ya kwamba tuwekeze wajifunze lugha zaidi ya mbili ndiyo soko linapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiswahili chetu tusiruhusu kikatekwa, ninachotaka kusema sasa hivi kuna lugha zinazungumzwa kwamba Kiswahili kimeanzia nchi fulani kimekuja Tanzania kimefia mahali fulani. Kiswahili ni mali yetu Watanzania tusikubali kikaporwa ikawa kama Mlima Kilimanjaro, sasa hivi Kiswahili ni rasilimali ya nchi tukienzi, tukitunze, tuhakikishe kinakua na kitambulisha nchi yetu, wajanja wasije wakatupora lugha yetu na ndiyo maana nasisitiza tuwekeze kwenye lugha ya Kiswahili kwa kuhamasisha vijana wetu wasome lugha zaidi ya moja au mbili ili tupate soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kiswahili tunapokwenda kupeleka watalaam katika nchi fulani ambayo hawazungumzi kiingereza sisi tunapata nini? Tuhakikishe na zile nchi wanafundishwa wanafunzi wetu lugha nyingi kama Kifaransa, Kibelgiji, Kireno, kwa sababu sisi tunawapa lakini baada ya muda Walimu wetu watakua hawana tena kazi, watafundishana wenyewe kwa wenyewe hilo tuweke angalizo. Watafundishana wenyewe kwa wenyewe ndani ya nchi kutokana na zile lugha zao za ndani wanazozitumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano kuna nchi inaongea Kifaransa baada ya muda hawa watu wetu wakifika huko Wafaransa watachukuana na nchi nyingine za Kifaransa watakwenda huko watasomeshana, ndiyo maana nasema tuwape na sisi tuchukue kwa maana na sisi tupate zile lugha zingine za Kifaransa, Kireno, Kigiriki tuzipate Watanzania, tusibaki tu na Kiswahili na Kiingereza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho namalizia kwa kuipongeza sana Serikali, tumuunge mkono Rais wetu katika kuwaletea wananchi maendeleo tupo nae bega bega. Ahsante sana naunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira wa Mwaka 2018
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza naomba kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.

Pili, naipongeza Serikali kwa kuleta Muswada huu muhimu kwa wakati huu muafaka. Muswada huu unalenga kuwa na usimamizi bora wa rasilimali ya maji na utakuwa unaleta maendeleo endelevu na ufanisi katika kuwaletea wananchi maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la Taifa kuhusu upatikanaji wa majisafi na salama kwa wastani kwa vijijini kufikia 85% ifikapo mwaka 2020 na wastani wa mijini kufikia 95% ifikapo mwaka 2020. Kwa hiyo basi, naipongeza Serikali pia kwa kuanzisha Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) ambao sasa utasaidia kuwakomboa wananchi wetu wa vijijini kupata majisafi na salama na kufikia hiyo asilimia iliyowekwa na Taifa ifikapo mwaka 2020. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Muswada huu pia utatatua changamoto zilizopo ambapo kuna changamoto nyingi katika utekelezaji wa majukumu ya maji. Mfano, majukumu ya msingi ya usimamizi wa maji ambao unasimamiwa na Wizara ya Maji lakini pia majukumu hayo hayo yanasimamiwa na Wizara ya TAMISEMI. Kwa hiyo, Muswada huu utakwenda kuainisha majukumu pamoja na wahudumu wa maji ambao wanasimamia kwenye Wizara hizi mbili Muswada huu utakwenda kutatua changamoto hizo. Pia utakwenda kutatua mwingiliano wa kisheria katika kutoa huduma za maji na usafi wa mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hii mpya itawezesha miradi ya maji vijijini kusimamiwa na wataalam kupitia Wakala wa Maji Vijijini na Wakala wa Maji Mijini wenye taaluma ya kutosha. Pia sheria hii ikipita, itakwenda kuainisha majukumu ya Mamlaka za Maji Mijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye huu Mfuko wa Maji naiomba Serikali iongeze vyanzo vipya vya mapato ili kuhakikisha mfuko huu wa maji unafanya kazi iliyokusudiwa katika kutatua tatizo la maji mijini na vijijini na hasa huko vijijini ambapo kuna asilimia kubwa ya wananchi wanaopata taabu na changamoto za maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, kwenye jedwali la kwanza Ibara ya 5, nami naungana na mapendekezo ya Kamati ya kuweka 50% kwenye uteuzi wa Wajumbe wa Bodi kwa sababu zilizoelezwa kwamba mwanamke ndiye hasa anayejua changamoto na upatikanaji wa maji, ndiye anayekesha kutafuta maji. Kwa hiyo, wakiwemo pale angalau 50% au kuzidi, basi watakuwa na uelewa na utatuzi mzuri wa kusaidia changamoto hizi za maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya 14 inayohusu makosa na adhabu, naungana na mawazo ya Kamati kwamba adhabu hizi zitenganishwe kulingana na makosa; makosa ya mtu binafsi kwa matumizi ya maji majumbani, lakini makosa ya matumizi ya maji ya viwandani kwa maana ya maji ya kibiashara. Kwa hiyo, adhabu hizi zitenganishwe kutokana na makosa ya mtu aliyofanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali ifanye marekebisho pale kwamba kwa mtu binafsi iwe ni shilingi 500,000/= mpaka shilingi milioni tano kulingana na kosa alilofanya na shilingi milioni tano hadi shilingi milioni 50 kwa taasisi kubwa au kwa uharibifu mkubwa uliofanya kutokana na uharibifu wa miundombinu ya maji. Tunatambua kwamba kuna changamoto hizo za watu wabaya kuchafua miundombinu ya maji kwa makusudi au kwa tama zao za binafsi na za kibiashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye maeneo ya hifadhi ya vyanzo vya maji naiomba Wizara inayohusika na Mamlaka zinazohusika ziharakishe basi kutenganisha maeneo ya hifadhi ya maji na vyanzo vya maji ili kuepusha usumbufu kwa wananchi kupata hasara baadae. Kazi hii ifanyike kwa haraka kuweka mipaka ya vyanzo vyote vya maji na vyanzo vyote vya maeneo tengefu kwa ajili ya maendeleo ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba Serikali sasa ilete haraka hapa Bungeni sheria zote ambazo zinakinzana na sheria hii itakayotungwa leo kwa sababu kuna sheria nyingi ambazo zinakinzana na sheria ambayo tutaitunga leo ili kuhakikisha tunapata maji safi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naipongeza Serikali kwa juhudi zote za kuwaletea wananchi maji na dhamira yake ya dhati kwa kuwasaidia wananchi wa Tanzania na hasa mwanamke kumtua ndoo kichwani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)
The Water Resources Management (Amendment) Act, 2022
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Awali ya yote napenda kuipongeza Wizara ya Maji kwa kutuletea Muswada huu kwa mustakabali wa maisha ya sisi wenyewe na vizazi vyetu vijavyo na mustakabali mzima wa taifa letu katika sekta hii ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na mapendekezo yote yaliyowasilishwa kwetu na Serikali kuhusu Muswada huu wa rasilimali za maji. Nakubaliana na mapendekezo ya Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji kwa kusaidia na kushiriki kwao katika kutoa maoni ya kuhakikisha kwamba Muswada huu unafanikiwa na kuleta tija kwa mustakabali wetu sisi wananchi na vizazi vyetu vijavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, umuhimu wa Muswada huu wa rasilimali za maji ni kwa faida yetu sisi na vizazi vijavyo. Kwasababu kumekuwa na uharibifu mkubwa katika vyanzo vya maji, lakini pia kuna upotevu mkubwa wa rasilimali za maji ambazo bado hazijawekewa sheria. Kwa muktadha huo sasa, sheria hii itasaidia utunzaji, uhifadhi na ulinzi wa rasilimali za maji. Kwa sababu, kwanza niuhifadhi, pili ni kutunza na la tatu ni kulinda. Kwa hiyo, Muswada huu umekuja kwa wakati mwafaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kifungu cha 44, kuandikwa upya naungana nacho kwa sababu ya kutenganisha kosa la mtumiaji maji ambaye ana kibali na mtumiaji wa maji ambaye hana kibali. Hapa kumekuwa na changamoto. Kwa wanaokuwa na vibali, wanakuwa na vibali lakini kwasababu anakibali anatumia zaidi ya kibali, kibali kinamruhusu afanye jambo kadhaa na kadhaa lakini yeye anaongeza mara tatu, mara nne na kupelekea uharibifu wa vyanzo vya maji. Na kwa hawa ambao hawana vibali wanatumia mwanya wa kusema kwamba wao hawaelewi, kwamba kuna sheria zinazohusu udhibiti wa vyanzo vya maji na rasilimali za maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana kabisa na huu Muswada kwa kurekebisha hiki kipengele ili kuwafanya hao wenye vibali wanatumia mwanya wa kupata kibali kujinufaisha zaidi na utumiaji wa rasilimali za maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kifungu cha 37 cha sheria mama kuongeza Kifungu Kidogo cha 4. Kifungu hiki kinahusu udhibiti wa maeneo tengefu. Tuna maeneo yetu tengefu, lakini katika maeneo haya tengefu kuna shughuli za kibinadamu bado zinaendelea kufanyika. Sasa katika kudhibiti haya maeneo tengefu sheria hii itatoa ufafanuzi wa namna ya kulinda na kudhibiti maeneo tengefu. Kwa mfano maeneo tengefu ya visiwa, visiwa vinatumika na wavuvi, wavuvi wale wanapotumia visiwa hivi ambavyo ni maeneo tengefu wengine hawajui, wengine wanajua lakini kwa kujifanya hawajui.

Kwa hivyo, elimu kuhusiana na maeneo tengefu itolewe zaidi. Kwamba wananchi wanatakiwa wajue ni sheria gani zinambana mtumiaji huyo na uharibifu gani akiufanya na adhabu gani atapata. Imewekwa adhabu kwenye Muswada huu, ni vizuri. Walichofanya ni kuongeza baadhi ya adhabu kwasababu adhabu za nyuma zilikuwa hazilingani na makosa. Makosa mengine ya uharibifu wa maji adhabu zake zinakuwa kama robo tu ya hasara. Serikali inaingia hasara kubwa kurejesha ule uharibu alioufanya yule mtumiaji wa vyanzo vya maji. Serikali inaingia hasara kubwa kuliko kile ambacho anatakiwa alipe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana, kwa mfano amefanya uharibu wa gharama ya milioni 50. Serikali inataka kuingia gharama ya kurejesha ile kwa milioni 50, lakini nyuma adhabu ilikuwa; kwa mfano, kama analipa milioni moja au laki tano hapo utalinganisha uharibifu alioufanya na hasara. Sasa kwa adhabu zile ilikuwa uharibifu unaendelea kwasababu yule anayefanya uharibifu hapati madhara yoyote isipokuwa kapata faida kubwa kwa kufanya ule uharibifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuzungumzia kuhusu utunzaji wa rasilimali za maji. Hii ni kwa faida yetu sisi wananchi, binadamu, wanyama, miti na viumbe vingine; pia sekta za uzalishaji ikiwemo kilimo, mifugo na mambo mengine ya kimaendeleo katika nchi yetu vinatumia maji. Hivyo, ni vyema sasa uhifadhi wa mazingira, kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, liwe ni suala la mkazo. Katika sekta zote za Wizara zote kuwe na kifungu na fungu maalum litakalohusika na uhifadhi wa mazingira yetu ili yatusaidie kutunza nchi yetu, kutunza mazingira yetu.

Mheshimiwa Spika, uhifadhi wa vyanzo vyetu vya maji ambavyo ni rasilimali tuliyopewa na Mwenyezi Mungu, rasilimali hii ni kwa faida yetu sote na vizazi vijavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Muswada huu utajenga mustakabali mwema wa taifa letu katika kuhifadhi vyanzo vya maji na uhifadhi wa maji kwa ujumla. Kama leo tukiupitisha Muswada huu, nashauri Serikali itoe elimu katika maeneo husika kwa njia husika, nyepesi ambazo zitawafikia walengwa huko waliko, na si tu kutumia radio na magazeti bali kuwafuata wahusika huko waliko, kujumuisha wananchi na uongozi wa pale. vilevile kutoa elimu kwa eneo lililowazunguka, ikiwa ni eneo la vyanzo vya maji ama ni eneo tengefu au ikiwa ni eneo la bonde; waelewe maana ya kutunza bonde lao, kutunza vyanzo vyao vya maji na kutunza maeneo tengefu ili kudhibiti hasara itakayotokea hapo mbele. Pia na wao wasipate adhabu ambazo hazistahiki kwa kutojua maana ya uhifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuwapongeza taasisi isiyo ya kiserikali ya TAWASANET, mtandao wa maji na usafi wa mazingira Tanzania kwa juhudi zao za dhati kwa wanavyoisaidia Serikali katika shughuli mbalimbali ikiwemo kutoa elimu, kuhifadhi mazingira ya vyanzo vya maji. Mtandao huu umefanya kazi kubwa sana maeneo mbalimbali ya Tanzania. Nawapongeza sana, nawataka na wengine waendelee kusaidia nchi katika uhifadhi wa mazingira, vyanzo vya maji na utunzaji kwa ujumla wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho; nimalizie mchango wangu kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwekeza fedha nyingi katika sekta ya maji. Dhamira yake ya kuwekeza fedha nyingi katika sekta ya maji kumsaidia mwananchi, akiwemo mwanamke, kupata fursa ya kupata maji katika sekta za uzalishaji, matumizi ya kibinadamu lakini kuongeza uchumi na Pato la Taifa letu kwa kupitia sekta hii ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuunge mkono juhudi hizo kwasababu kama ilivyosemekana, maji ni uhai, maji ni kila kitu; na kama ilivyoelezwa hapa, kwamba vita nyingine itakayokuja duniani uwezekano mkubwa ikawa vita ya maji na sisi tumepakana na mabonde, tumepakana na mito ambayo inaruunganisha na nchi nyingine jirani. Kwa hivyo, uhakiki na utumiaji sahihi wa maji ni muhimu kwa nchi yetu. Sheria zifuatwe ili kuona usawa unapatikana katika kutumia rasilimali hizi zote za maji, ikiwemo maziwa na mito kwa nchi zote ambazo tunaungana katika kutumia maji hayo hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho; nakushukuru kwa nafasi hii, naipongeza Wizara na Serikali kwa ujumla kwa utekelezaji wa majukumu mbalimbali na kusimamia rasilimali za maji pamoja na kusimamia miundombinu ya maji inayoharibiwa na kutoa adhabu inayostahiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nakushukuru sana.