Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Kemirembe Rose Julius Lwota (7 total)

MHE. KEMIREMBE J. LWOTA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itapeleka x-ray na CT-Scan kwenye Hospitali ya Sekou Toure Mkoani Mwanza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kemirembe Julius Lwota, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Mkoa wa Mwanza ya Sekou Toure ina mashine mbili za x-ray ambazo zilinunuliwa na Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto mwaka 2002. X-Ray hizo zinafanya kazi pamoja na kuwepo kwa matengenezo ya mara kwa mara kutokana na uchakavu wake. Aidha, hospitali hiyo haina mashine ya CT-Scan na kwamba huduma hiyo inapatikana katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wizara ya Afya imeanza mradi wa kusimika vifaa vya kuangalia mwenendo wa afya za wagonjwa na vifaa vya uchunguzi vikiwemo CT-Scan katika Hospitali za Rufaa za Mikoa utakaotekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na Uholanzi. Mpango huu utakapokamilika utasaidia Hospitali nyingi za Mikoa za Rufaa kuwa na vifaa muhimu kwa ajili ya huduma ya afya.
MHE. KEMIREMBE J. LWOTA Aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha miradi ya maji inayojengwa Wilayani Sengerema katika Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa inakamilika haraka na kuwanufaisha wananchi wa Buchosa hasa mradi wa maji wa Lumea - Kalebezo na Nyegonge?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Sika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kemirembe Julius Lwota, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, miradi mitatu inayohudumia vijiji nane katika Halmashauri ya Buchosa inaendelea kujengwa ambayo ni mradi wa maji Lumea - Kerebezo - Nyegonge, mradi wa maji Nyakalilo - Bukokwa na mradi wa maji Luchili - Nyakasungwa hadi Igwanzozuna.
Ujenzi wa mradi wa maji Lumea - Kalebezo - Nyegonge ulianza kutekelezwa mwezi Machi 2013 kwa gharama ya shilingi bilioni 1.69 kwa sasa mradi huo upo katika hatua za mwisho za majaribio ya mitambo pamoja na miundombinu na utaanza kutoa huduma ifikapo Juni, 2017.
Mradi utakapokamilika utanufaisha wakazi 16,000 wa vijiji vya Kalebezo na Nyegonge.
MHE. KEMILEMBE J. LWOTA aliuliza:-
Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa ni miongoni mwa Halmashauri mpya zilizoanzishwa mwaka 2015 na watumishi 98 walihamishiwa kutoka Halmashauri za Sengerema, Misungwi, Ilemela, Jiji la Mwanza, Kwimba na Magu lakini watumishi hawa hadi sasa hawajalipwa fedha za uhamisho:-
Je, ni lini Serikali itawalipa stahiki zao watumishi hawa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kemilembe Julius Lwota, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa ni miongoni mwa Halmashauri zilizoanzishwa Julai, 2015 baada ya kugawanywa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema. Watumishi 98 waliohamishwa Buchosa kutoka Halmashauri za Sengerema, Ilemela, Jiji la Mwanza, Kwimba na Magu wanadai jumla ya shilingi 354,075,500 na tayari madai ya shilingi 44,531,000 yamelipwa kwa watumishi 16. Hadi Disemba, 2016 Halmashauri imebakiwa na madeni ya uhamisho kwa watumishi 88 wenye jumla ya shilingi 292,531,000. Madeni hayo yaliyobaki yamewasilishwa Wizara ya Fedha na Mipango kwa ajili ya uhakiki ili yalipwe.
MHE. KEMIREMBE J. LWOTA aliuliza:-
Je ni lini Serikali itaanza ujenzi wa duka la dawa la MSD kwenye Hospitali Teule ya Sengerema?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri Wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kemirembe Julius Lwota, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika hospitali za umma, Serikali iliagiza maduka ya dawa yafunguliwe kwenye hospitali za umma. Kama sehemu ya utekelezaji wa agizo hilo, bohari ya dawa imeshafungua maduka katika hospitali za Muhimbili, Mount Meru, Ruangwa, Sekou Toure, Mbeya, Katavi na Chato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huu wa kuanzisha duka la dawa katika hospitali una faida kubwa ambazo ni pamoja na kuunga mkono dhamira ya kuleta dawa na vifaa tiba karibu na wananchi; kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa bei nafuu na kwa ubora kwa Watanzania; kuunga mkono kwa vitendo juhudi za Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na TAMISEMI katika kudhibiti kuongezeka kwa gharama za huduma za afya; kuondoa utegemezi wa fedha kutoka Serikali Kuu na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa dawa na vifaa tiba kwa wakati wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kutekeleza agizo hilo kwa Tanzania nzima, inaonekana itahitajika rasilimali watu na rasilimali fedha nyingi sana ambapo bohari ya dawa ilikubaliana na TAMISEMI kuwa hospitali zilizo chini yake zifungue maduka yao zenyewe na MSD itatoa ushauri wa kitaalamu pamoja na kuziuzia dawa na vifaa tiba.
MHE. KEMIREMBE J. LWOTA aliuliza:-
Je, ni lini ujenzi wa Daraja la Kigongo Busisi utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kemirembe Julius Lwota, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mradi wa ujenzi wa Daraja la Kigongo – Busisi pamoja na barabara unganishi unatekelezwa katika hatua mbili. Hatua ya kwanza, ambayo tayari upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na uandaaji wa nyaraka za zabuni. Upembuzi yakinifu ulikamilika tarehe 11 Julai, 2017. Aidha, kwa sasa Mhandisi Mshauri ambaye ni Kampuni ya Cheil Engineering Ltd kutoka Korea Kusini akishirikiana na AFRISA Consultant pamoja na Apex za Tanzania anaendelea na kazi ya usanifu wa kina na kuandaa nyaraka za zabuni. Kazi ya usanifu wa kina zimepangwa kukamilika mwezi Julai, 2018 kwa gharama ya shilingi bilioni 2.8.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kukamilika kwa kazi ya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na uandaaji wa nyaraka za zabuni gharama halisi za ujenzi wa daraja zitafahamika. Baada ya gharama kufahamika, Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa daraja hilo.
MHE. STANSLAUS S. MABULA (K.n.y. MHE. KEMIREMBE J. LWOTA) aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itahakikisha umeme wa uhakika kwenye Kata za Wilaya ya Nyamagana, Mkoa wa Mwanza?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishari napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kimirembe Julius Lwota, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Nyamagana ina jumla ya Kata 18 ambazo ni Nyegezi, Mkolani, Buhongwa, Rwanhima, Mkuyuni, Mabatini, Luchelele, Igogo, Pamba, Nyamagana, Mirongo, Isamilo, Mbungani, Mahina, Igoma, Butimba, Muhandu na Kishiri. Kata zote hizi zinapata umeme wa Gridi ya Taifa japo baadhi ya maeneo ya Kata hayana umeme wa uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia TANESCO inaendelea kujenga miundombinu ya umeme na kusambaza umeme katika maeneo yote ya nchi yetu. Katika bajeti ya mwaka 2017/2018 Shirika la Umeme (TANESCO) limetenga jumla ya shilingi bilioni nane na milioni mia saba thelathini kwa ajili ya kujenga, kukarabati na kuboresha miundombinu ya umeme ya Mkoa wa Mwanza ikiwepo Wilaya ya Nyamagana na Kata zake ili kuhakikisha umeme unapatikana kwa uhakika. Hadi kufikia mwezi Machi, 2018 jumla ya nguzo 519 za umeme wa kati wenye msongo wa kilovoti 11 na 33 na nguzo 188 za msongo wa voti 400 katika Kata za Nyamagana na maeneo mengine ya jiji la Mwanza vimebadilishwa, pia vikombe 807 vilikuwa vimevunjika vimebadilishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha kilometa 33 za msongo wa kati na madogo zimesafishwa kwa kukata miti pamoja na kubalisha waya kwa kilometa 22 zilizokuwa zimechakaa. Zoezi hili la ukarabati linaendelea ili kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maboresho hayo yamewezesha kuimarika kwa upatikanaji wa umeme katika Mkoa wa Mwanza ukilinganisha na kipindi cha nyuma. Aidha, kukamilka kwa mradi mkubwa wa kusafirisha umeme wa msongo kilovoti 400 kutoka Iringa hadi Shinyanga kumechangia kwa kiasi kikubwa kuimarika kwa umeme katika Mkoa wa Mwanza. Zoezi la ukarabati na matengenezo ya miundombinu ya umeme ni endelevu na kiasi cha fedha shilingi bilioni nne kimependekeza katika bajeti ya mwaka huu 2018/2019 kwa ajili kuboresha miundombinu ya umeme ya uhakika Jijini Mwanza.
MHE. STANSLAUS S. MABULA (K.n.y. MHE. KEMILEMBE J. LWOTA) aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kumalizia ujenzi wa maboma ya Zahanati yaliyoanzishwa kwa juhudi za wananchi pamoja na kuyawekea vifaa tiba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kemilembe Julius Lwota, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mwaka 2017 Serikali ilifanya tathmini kubaini idadi ya maboma nchi nzima ambayo ni Vituo vya Afya, Zahanati na nyumba za watumishi na kubaini kuwa kuna maboma 1,845 ambayo yanahitaji jumla ya shilingi bilioni 934 ili kukamilishwa.

Mheshimiwa Spika, Serikali iliona ni vigumu kukamilisha maboma hayo kwa pamoja kutokana na upatikanaji wa fedha. Hivyo, ikabuni mkakati wa kujenga na kukarabati Vituo vya Afya 350 nchini vilivyochaguliwa kwa kutumia vigezo ambavyo ni uhitaji mkubwa wa huduma za dharura na upasuaji wa akina mama wajawazito, sababu za kijiografia na umbali mrefu ambao wananchi wanatembea kupata huduma za dharura.

Mheshimiwa Spika, vilevile, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2017/2018 na 2018/2019, jumla ya maboma 207, Vituo vya Afya sita, Zahanati 191 na nyumba kumi yalikamilishwa kwa fedha kutoka Mradi wa Mfuko wa Pamoja wa Afya na Mapato ya Ndani ya Halmashauri.

Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii kuzielekeza Halmashauri zote nchini kutenga fedha kwenye makusanyo yake ya ndani na kuendelea kushirikisha wananchi na wadau wengine wa maendeleo kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa maboma wakati Serikali ikiendelea kutafuta fedha za ujenzi na ukarabati wa maboma hayo.