Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Pauline Philipo Gekul (13 total)

MHE. KUNTI Y. MAJALA (K.n.y. MHE. PAULINE P. GEKUL) aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itamaliza tatizo la ulipaji wa ushuru wa huduma ambao ni asilimia 0.3 unaotozwa kutoka mitandao ya simu ambao kwa sasa Halmashauri zimeshindwa kukusanya ipasavyo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI (K.n.y. WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Pauline P. Gekul, Mbunge wa Babati Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, suala la ulipaji wa ushuru wa huduma za mawasiliano ambao ni asilimia 0.3 limekuwa ni tatizo kwa pande zote mbili yaani Halmashauri ambazo ndiyo zinakusanya kwa upande mmoja na kampuni za mawasiliano ambazo anakabiliwa na ugumu wa kuzilipa kwa upande mwingine.
Mheshimiwa Spika, suala hili limejadiliwa na wadau kwa kuongozwa na Wizara yenye dhamana na Mawasiliano na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Mheshimiwa Spika, napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMESEMI), hivi sasa inafanyia marekebisho Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa Sura 290 ili kuwezesha kukusanya ushuru wa huduma wa mawasiliano pamoja na maeneo mengine.
Mheshimiwa Spika, hatua hii litasaidia sana kupatia ufumbuzi tatizo lililoelezwa na Mheshimiwa Mbunge kwa mapato kukusanywa sehemu moja na Halmashauri zote kupata mapato stahiki. Rasimu ya Sheria hiyo ikikamilika inatarajiwa kujadiliwa katika kikao cha wadau hivi karibuni
MHE. PAULINE P. GEKUL aliuliza:-
Je, ni kwa nini Serikali imekuwa hairudishi katika Halmashauri zetu 30% ya mauzo ya viwanja?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Pauline Philipo Gekul, Mbunge wa Babati Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara yangu haikuwahi kuwa na utaratibu wa kurudisha asilimia 30 za mauzo ya viwanja kwa Halmashauri, kwa sababu mauzo ya viwanja hufanywa na Halmashauri husika wanapokuwa na mradi wa viwanja katika maeneo yao na Wizara hupokea ada ambazo zinahitajika kisheria katika uandaaji wa hati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia 30 ya fedha ambazo zilikuwa zinarejeshwa Halmashauri ni kodi ya ardhi ambapo katika mwaka wa fedha 2015/2016, Wizara ilipeleka mgao wa Sh. 3,541,212,774.01 kwa Halmashauri zote nchini na Halmashauri ya Babati ilipokea jumla ya Sh. 24,138,421.39.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Wizara imekuwa inakumbwa na changamoto kadhaa katika kurejesha asilimia 30 ya fedha za makusanyo. Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na:-
(i) Halmashauri nyingi kutotuma taarifa za makusanyo kwa wakati ili kuiwezesha Wizara kufanya ulinganisho wa kiasi kilichopokelewa na kile kilichokusanywa.
(ii) Baadhi ya Halmashauri kutumia fedha za makusanyo kabla ya kuziwasilisha kwenye akaunti ya makusanyo ya maduhuli inayosimamiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
(iii) Wizara kupatiwa mgao mdogo wa fedha unavyopokelewa Wizarani kutoka Hazina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya mwaka 2016/2017, Serikali imeondoa utaratibu wa marejesho ya retention ya asilimia 30 ya makusanyo ya fedha zote zinazoingia katika Mfuko Mkuu wa Hazina. Aidha, Wizara yangu kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI tutaangalia namna bora ya kuweka utaratibu wa utoaji wa fedha kwa ajili ya uendeshaji wa sekta ya ardhi katika Halmashauri zetu.
MHE. PAULINE P. GEKUL Aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itafanya tathmini ya miradi ya maji ya visima kumi katika vijiji inayofadhiliwa na Benki ya Dunia?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Pauline Philipo Gekul, Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika ilifanya tathmini ya awamu ya kwanza ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji mwaka 2015 ambapo katika Halmashauri ya Mji wa Babati, Serikali ilipanga kutekeleza miradi ya maji katika vijiji vya Mutuka, Chemchem, Kiongozi, Malangi, Managhat, Halla, Himti, Haraa, Nakwa na Imbilili. Ujenzi umekamilika katika vijiji vinne vya Mutuka, Himti, Chemchem na Managhat ambapo wananchi wanapata huduma za maji. Ujenzi wa miradi mingine katika vijiji sita unaendelea na umefikia hatua mbalimbali za utekelezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itahakikisha inazifanyia kazi changamoto zilizojitokeza katika kutekeleza awamu ya kwanza ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji. Baadhi ya changamoto hizo ni kuchelewesha manunuzi ya miradi, upungufu wa wataalam wa maji, kukosa wataalam wabobezi wa taaluma za kifedha pamoja na baadhi ya maeneo yaliyokusudiwa kuchimba visima kukosa maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Halmashauri zote zinaendelea kupewa mafunzo ili kujenga uwezo wa kusimamia miradi, kusajili na kuunda vyombo na kuimarisha usimamizi wa mfumo wa ukusanyaji wa takwimu za miradi ya maji vijijini ili kuwa na takwimu sahihi.
MHE. PAULINE P. GEKUL aliuliza:-
Serikali iliwahi kuliahidi katika Bunge hili kuwa inafanya mapitio ya Sera ya Elimu Bure na kwamba ingeleta Bungeni mambo yanayohitaji kuboreshwa:-
Je, ni lini mapitio hayo yatakamilika?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wangu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Pauline Phillip Gekul, Mbunge wa Babati Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iliamua kuondoa malipo ya ada kwa elimu msingi inayojumuisha elimu ya awali pamoja na darasa la kwanza hadi kidato nne kama utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 Ibara ya 3.1.5 na Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015-2020 Ibara ya 52(a). Lengo la Sera hii ni kuhakikisha kuwa watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanapata fursa hiyo bila kikwazo chochote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na umuhimu wa maamuzi hayo ya Serikali kwa ustawi wa wananchi na Serikali kwa ujumla mwezi wa Februari mwaka 2017 Wizara ilifanya ufuatiliaji kuhusu utekelezaji wa Sera hii ili kubainisha mafanikio na changamoto kwa lengo la kuimarisha utekelezaji wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kuwa Serikali itatumia matokeo na mapendekezo ya ufuatiliaji uliofanyika kutatua changamoto zilizojitokeza ili kuhakikisha lengo la Serikali la kutoa fursa kwa watoto wote wenye umri wa kwenda shule linafikiwa.
MHE. PAULINE P. GEKUL aliuliza:-
Halmashauri ya Mji wa Babati inaidai NFRA ushuru wa zaidi ya shilingi milioni 90 katika kipindi cha mwaka 2014/ 2015.
Je, ni lini fedha hizo zitalipwa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Pauline Philipo Gekul, Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika msimu wa ununuzi wa nafaka mwaka 2014/2015 Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ulinunua tani 1,127.826 za mahindi zenye thamani ya shilingi 6,063,913,000 kutoka kwa wakulima na vikundi vya wakulima katika Mji wa Babati. NFRA ilipaswa kulipa kwa Halmashauri ya Mji wa Babati ushuru wa shilingi 181,917,390 ambazo ni asilimia tatu ya thamani ya mahindi yaliyonunuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2014/2015 Wakala ulilipa ushuru wa mazao kwa tani 4,400,000 zenye thamani ya shilingi 66,000,000 na kubaki na deni na deni la ushuru wa mazao kwa tani 7,727.686 zenye thamani ya shilingi 115,917,390.00. Hata hivyo, kutokana na ufinyu wa bajeti wakala ulishindwa kulipa kiasi chote cha ushuru kwa wakati kutokana na kuongezeka kwa ununuzi wa mahindi zaidi ya melengo yaliyopangwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2015/2016 Wakala ulilipa deni lote la ushuru wa mazao kwa Halmashauri ya Babati kwa awamu mbili ambapo tarehe 10 Agosti, 2015 ulilipa shilingi 23,000,000 na kumalizia deni la shilingi 92,917,390 tarehe 27 Januari, 2016. Aidha, kwa sasa Wakala umelipa ushuru wa mazao kwa Halmashauri zote ilikonunua mahindi na hakuna deni lolote kuhusu ushuru wa mazao.
ABDALLAH A. MTOLEA (K.n.y. MHE. PAULINE P. GEKUL) aliuliza:-
Kuna mkanganyiko wa kutoza ada ya ukaguzi kati ya TFDA na Halmashauri kwa wafanyabiashara wale wale.
Je, ni kwa nini chanzo hiki cha mapato kisiachwe kwa Halmashauri?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Pauline Philipo Gekul, Mbunge wa Babati Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, majukumu ya TFDA yanatekelezwa kwa mujibu wa Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi Sura ya 219. Kutokana na uhaba wa rasilimali watu na ili kusongeza huduma karibu zaidi na wananchi, baadhi ya majukumu ya TFDA yamekasimishwa kwa Wakurugenzi wa Halmashauri kwa mujibu wa Kanuni za Kukasimu Madaraka na Majukumu (The Tanzania Food, Drugs and Cosmetics (The Delegation for Powers and Functions) Order (GN No. 476) za mwaka 2015. Kwa mujibu wa Kanuni hizi, ada zote za udhibiti zinazotozwa kwa majukumu yaliyokasimiwa kwa Halmashauri hutumiwa na Halmashauri zenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kusisitiza kuwa ada zinazotozwa na Halmashauri kutokana na udhibiti wa chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuhakikisha kuwa watumiaji bidhaa hizo wanalindwa afya zao ipasavyo.
MHE. PAULINE P. GEKUL aliuliza:-
Kata ya Sigino na Vijiji vyake vyote katika Jimbo la Babati Mjini haina kabisa maji safi na salama:-
Je, ni nini mkakati wa Serikali wa kuipatia maji safi na salama Kata hiyo pamoja na Vijiji vyake?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Pauline Philip Gekul, Mbunge wa Babati Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba vijiji vyote vinne katika Kata ya Sigino ndani ya Halmashauri ya Mji wa Babati vyenye wakazi 11,895 havina huduma ya maji safi na salama. Hata hivyo ziko hatua mahsusi zinazoendele. Mnamo tarehe 29 Mei, 2017, Halmashauri ya Mji wa Babati ilisaini mkataba wa Sh.487,470,000 kujenga mradi wa maji katika Kijiji cha Imbilili ambao ulipangwa kukamilika tarehe 30 Juni, 2018 lakini Mkandarasi Black Lion Limited amebainika kuwa na uwezo mdogo kwani hadi sasa ametekeleza kazi kwa asilimia saba tu. Naishauri Halmashauri ambapo Mheshimiwa Pauline Gekul ni Diwani, itathmini haraka hali hiyo na ichukue hatua haraka kwa manufaa ya wananchi.
Mheshimiwa Spika, hatua nyingine kubwa inayoendela ni utekelezaji wa mkataba kati ya Halmashauri na Mkandarasi Maswi Drilling Company Limited kuchimba visima virefu katika Vijiji vya Sigino, Singu na Haraa kwa shilingi milioni 94.5 ambao umefikia asilimia 25 na utakamilika tarehe 30 Juni, 2018. Usanifu na ulazaji wa mabomba yakayosambaza huduma za maji safi na salama kwa wananchi utaanza mwaka 2018/2019 kwa kutumia Sh.611,137,000 ambazo zimetengwa kutekeleza mradi huo. Ahsante.
MHE. PAULINE P. GEKUL aliuliza:-
Ziwa Babati limejaa magugu maji na Halmashauri haina bajeti ya kusafisha ziwa hilo kwa maana ya kuondoa magugu hayo. Je, ni lini Serikali itasaidia kuondoa magugu hayo ili kulinusuru ziwa hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Pauline Gekul, Mbunge wa Babati Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, magugu maji ni moja ya viumbe vamizi wageni (Invasive Alien Species) ambayo ni moja ya changamoto kubwa inayokabili mazingira yetu nchini. Baadhi ya maeneo yaliyoathirika na mimea ya aina hi ni pamoja na Ziwa Jipe, Ziwa Victoria, Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro. Athari za mimea vamizi wageni kama magugu maji ni kusambaa kwa kasi katika eneo lilivamiwa pamoja na kusababaisha kutoweka kwa baionuai asili katika eneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kubaliana na tatizo hili, nchini Ofisi ya Makamu wa Rais imeitisha mkutano wa wadau uliofanyika terehe 4 Septemba, 2018 ili kushirikiana na wadau katika kutafuta ufumbuzi wa kukabiliana na tatizo hili kitaifa ikiwa ni pamoja na Ziwa Babati. Mkakati huu utakuwa ni muendelezo wa mkakati wa Kitaifa wa kuhifadhi mazingira ya pwani, bahari, maziwa, miti, mabwawa wa mwaka 2008.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkutano huo wa wadau umeandaa mapendekezo ya hatua za kuchukua kitaifa kukabiliana na nchangamoto za uharibinfu wa mazingira unaotokana na mmea vamizi wageni katika magugu maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua juhudu za Halmashauri ya Babati na Bonde la Maji la Kati ambapo imeandaa andiko la mradi unaoihusu uhifadhi wa mfumo wa ikolojia wa Ziwa Manyara ambapo Ziwa Babati ni moja ya sehemu ya mfumo wa ikolojia hiyo. Katika andiko hilo, uondoaji wa magugu maji katika Ziwa Babati ni moja ya shughuli za mradi huo. Serikali inaendelea na utaratibu stahiki kuwashirikisha washirika wa maendeleo kupata fedha za kutekeleza mradi huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juhudi izngine zilizochukuliwa na Halmshauri ya Mji wa Babati ni pamoja na kuweka mabango ya makatazo ya shughuli za binadamu ndani ya mita 60 ya eneo la ziwa. Mabango 20 yaliwekwa maeneo yaliyozunguka Ziwa Babati, kutoa elimu ya hifadhi ya mazingira na kuhimiza kilimo cha makingamaji katika maeneo ya Kata za Bagala, Babati, Mangala, Singe na Bonga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kudhibiti shughuli za kilimo na ufugaji katika eneo la Ziwa Babati na vilevile Halmashauri ya Mji wa Babati imepata Muwekezaji wa shughuli za kitalii karibu na eneo la Ziwa Babati na moja ya makubaliano ni kuondoa magugu maji katika eneo la ziwa hilo. Taratibu za kufikia makubaliano zinaendelea na Ofisi ya Makamu wa Rais itashirikiana na Halmashauri husika kwa kutoa wataalam wakati wa kuondoa magugu maji katika ziwa hilo.
MHE. PULINE P. GEKUL aliuliza:-
Vijiji vya Imbilili, Hitimi na Managha katika Jimbo la Babati Mjini havina mawasiliano ya simu. Je, ni lini Serikali itavipa vijiji hivyo minara ya mitandao ya simu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Pauline Gekul, Mbunge wa Babati mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ilifanya tathmini katika Kijiji cha Imbilili kata ya Singino, Himiti Kata ya Bonga pamoja na Kijiji cha Managha Kata ya Singena kwa kuangalia hali halisi ya mawasiliano pamoja na idadi ya wakazi. Vijiji hivyo viliingizwa katika orodha ya vijiji vinavyohitaji huduma ya mawasiliano. Vijiji hivyo vyote viliweza kupelekewa mawasiliano kupitia Kampuni ya Viettel ambayo inamilikiwa kampuni ya Halotel kwa ajili ya mawasiliano. Hata hivyo ninazo taarifa kwamba minara hiyo haifanyi kazi vizuri sana na nimetuma timu ya wataalamu kwenda kuhakikisha kwamba kuna tatizo gani katika minara hiyo kwa ajili ya kuhakikisha wanapata mawasilino wananchi wa eneo hilo.
MHE. PAULINE P. GEKUL aliuliza:-

(a) Je, ni lini wananchi wanaodai fidia kutokana na barabara ya mchepuo kutoka Arusha – Singida na Arusha – Dodoma katika Mji wa Babati watalipwa fidia?

(b) Je, ni lini ujenzi wa barabara hizo utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Pauline Philip Gekul, Mbunge wa Babati Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa mchepuo kutoka barabara za Arusha – Singida na Arusha – Dodoma kwa Babati Mjini (Babati Baypass) unatekelezwa kwa pamoja na mradi wa barabara ya mchepuo wa Bwawa la Mtera (Mtera Baypass) katika barabara ya Iringa – Dodoma chini ya ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB). Aidha, taratibu za ununuzi wa kumpata Mhandisi Mshauri atakayefanya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina upo katika hatua za mwisho ambapo kazi ya upembuzi yakini na usanifu wa kina itakayotekelezwa na Mhandisi Mshauri itahusisha pia usanifu wa mwelekeo ulio bora na sahihi wa barabara ya mchepuo kwa kuzingatia vigezo vya kitaalam kama vile gharama za ujenzi, uhifadhi wa mazingira pamoja na usalama wa watumiaji wa barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulingana na hadidu za rejea alizopewa Mhandisi Mshauri ni pamoja na kutambua watu na mali zao watakaoathiriwa na mradi. Baada ya Mhandisi Mshauri kukamilisha jukumu la kitaalam; tathmini ya mali za wananchi zitakazoathiriwa na mradi itafanyika kwa kufuata sheria na taratibu na hatimaye fidia kulipwa kwa walengwa kwa kuzingatia sheria zilizopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kukamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina pamoja na maandalizi ya nyaraka za zabuni, kazi hii itatangazwa ili kumpata mkandarasi wa kujenga barabara hiyo.
MHE. PAULINE P. GEKUL aliuliza:-

Je, ni lini wananchi wanaodai fidia ya maeneo yao yaliyopitiwa na mradi wa KV 400 katika Jimbo la Babati Mjini watalipwa.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Pauline Philip Gekul, Mbunge wa Babati Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linatekeleza mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Singida hadi Namanga kupitia Arusha. Mradi huu unahusisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 400 yenye urefu wa kilomita 414 na upanuzi wa vituo vya kupozea umeme vya Singida na Arusha na usambazaji wa umeme katika vijiji 14 vinavyopitiwa na mradi. Gharama za mradi huu ni Dola za Kimarekani milioni 258.82.

Mheshimiwa Naibu Spika, ulipaji fidia ulianza mwezi Agosti, 2018 baada ya kukamilika kwa zoezi la uthamini na uhakiki wa mali na mazao yatakayoathirika na utekelezaji wa mradi. Hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Machi, 2019 fedha zaidi ya shilingi bilioni 31.87 zimeshalipwa kwa waathirika 2,815 kutoka Wilaya za Arusha, Monduri, Babati pamoja na Hanang’.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Wilaya ya Babati, fedha zaidi ya shilingi 6,200,800,000 zimeshalipwa kwa wananchi 995 hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Machi, 2019. Wananchi 86 waliobaki watalipwa fedha zao shilingi milioni
638.18 wakati wowote baada ya kukamilika kwa zoezi la uhakiki linaloendelea.
MHE. PAULINE P. GEKUL aliuliza:-

Miundombinu mibovu ya barabara zinazoelekea Hifadhini husababisha Watalii kuwa wachache Mathalan; barabara inayotoka Iringa Mjini hadi Hifadhi ya Ruaha kilometa 104 ni ya vumbi na vilevile barabara ya kutoka Babati Mjini hadi Tarangire kilometa 20 ni ya vumbi:-

Je, ni lini Serikali itajenga barabara hizo kwa kiwango cha lami ili kuwavutia Watalii wengi zaidi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Pauline Philipo Gekul, Mbunge wa Babati Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya kutoka Iringa Mjini kuelekea Hifadhi ya Taifa Ruaha ambayo inajulikana kama barabara ya Iringa – Msembe ni barabara ya Mkoa inayosimamiwa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADs) Mkoa wa Iringa. Barabara hii ina urefu wa kilomita 104 kati ya hizo kilomita 18.4 ni za lami na kilomita 85.6 ni za changarawe. Barabara hii inapitia katika maeneo muhimu ya makumbusho ya Mtwa - Mkwawa (Kalenga), maeneo yenye kilimo cha Mpunga na Mahindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu wa barabara hii, TANROADs imefanya Upembuzi yakinifu, Usanifu wa kina na kuandaa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami. Kazi hii imefanywa na Mhandisi Mshauri M/s ENV Consult (T) Ltd wa Dar es Salaam na tayari imekamilika. Ambapo jumla ya shilingi billioni 4.22 zimetengwa Katika mwaka wa fedha 2019/2020 kwa ajili ya maandalizi ya kuanza ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu kupitia Taasisi zake imekuwa ikishirikiana na Mamlaka zingine kuhakikisha kwamba barabara mbalimbali zinazoelekea maeneo ya Hifadhi zinapitika wakati wote kwa kufanya ukarabati wa mara kwa mara. Kwa mfano, Hifadhi ya Taifa Tarangire imeshirikiana na TARURA kurekebisha barabara ya kutoka Minjingu kwenda Tarangire yenye urefu wa kilometa 7 na barabara ya kutoka lango la Sangaiwe kwenda kijiji cha Usole – Mwada – Sangaiwe kwa kufanya matengenezo ya kuchonga na kuweka moram.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, usanifu wa barabara ya Minjingu – Tarangire kilometa saba kwa kiwango cha lami umekamilika na sasa inatafutwa fedha kwa ajili ya ujenzi. Barabara kutoka Babati Mjini hadi Hifadhi ya Taifa Tarangire kilomita 20 inafanyiwa ukarabati wa mara kwa mara kila mwaka kwa ushirikiano kati ya TARURA na Hifadhi ya Taifa Tarangire.
MHE. PAULINE P. GEKUL aliuliza:-

Je, ni lini Shamba la Singu Estate litarudishwa kwa wananchi wa Kata ya Sigino kama alivyoahidi Mheshimiwa Waziri Mkuu wakati alipofanya ziara katika Jimbo la Babati Mjini mwaka 2017?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Pauline Philipo Gekul, Mbunge wa Babati Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Shamba la Singu namba 679 lenye Hati namba 11837 ambalo ukubwa wake ni hekta 1,260 sawa na ekari 3,080 lipo kilomita tano kutoka Mji wa Babati Mkoani Manyara linamilikiwa na Kampuni ya Agric. Evolution (T) Co. Ltd. Mnamo mwaka 2004 Mji wa Babati ulipandishwa hadhi na kuwa Halmashauri ya Mji, hatua iliyopelekea kubadilika kwa Sheria za uendeshaji wa Mamlaka hiyo na pia kuanzisha mchakato wa kubadilishwa kwa shamba hili kutoka matumizi ya kilimo na kuwa na matumizi mbalimbali ya kimji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria zilizotumika katika mchakato wa kubadilisha matumizi ya shamba la Singu zilimlazimu mmiliki wa shamba hilo kurejesha hati ya umiliki wa shamba ili liweze kubadilishwa kuwa na matumizi mbalimbali ya ardhi ya jumla. Baada ya hati hiyo kurejeshwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi iliridhia mabadiliko hayo na kupitisha rasmi mpango wa kina wa matumizi ya ardhi katika eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, makubaliano yaliyofanyika kati ya mwenye shamba, Halmashauri ya Mji na wananchi wa kijiji cha Singu ni kama ifuatavyo; kijiji kipatiwe ekari 50 kwa ajili ya huduma za jamii kama vile shule, zahanati na kadhalika ili ziwanufaishe wananchi wa Singu. Wananchi waliokuwa wamejenga ndani ya eneo la ekari 200 kwenye shamba hilo wasitolewe bali wapimiwe na kumilikishwa viwanja katika maeneo waliyojenga.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara aliyoifanya katika Kijiji cha Singu mwezi Agosti mwaka 2017, wananchi na uongozi wa kijiji kwa ujumla wao waliweza kuridhia uendelezaji wa eneo hilo kimji ili waweze kunufaika na huduma zitakazopatikana na kwamba wananchi wa Singu watapewa kipaumbele katika ugawaji wa viwanja hivyo. Kuanzia mwaka 2017 hadi sasa mambo yafuatayo yamefanyika;

(i) Umeandaliwa mpango kabambe wa mji kwa miaka 20 ijayo ambapo Singu ilipangwa kama mji wa pembezoni;

(ii) Umeandaliwa upangaji wa kina;

(iii) Upimaji wa viwanja umefanyika;

(iv) Utengenezaji wa barabara katika eneo la mradi umefanyika na;

(v) Juhudi za usuluhishi wa mgogoro kati ya Mwekezaji na wananchi wa Singu zimefanyika kupitia uongozi wa mkoa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na muafaka kupatikana na wananchi kupewa zaidi ya ekari 800 na kumilikishwa maeneo yao kisheria.