Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Pauline Philipo Gekul (39 total)

MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA Aliuliza: -

Je, fedha kiasi gani zimepatikana katika opereshini ya kudhibiti utoroshaji wa mifugo nje ya nchi na fedha hizo zitumikaje?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge lako tukufu naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kunipa afya njema na kunipa kibali pia kurudi katika Bunge hili.

Nimshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kuniamini na kuniteua kuwa Naibu Waziri katika Wizara hii. Nishukuru chama changu Chama Cha Mapinduzi pamoja na wananchi wa Jimbo la Babati Mjini kuniamini na kuendelea kunifanya kuwa mwakilishi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi naomba sasa nijibu swali la Mheshimiwa Dkt. Steven Kiruswa, Mbunge wa Longido kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wizara ililazimika kuanzisha operesheni ya kufuatilia utekelezaji wa sheria, kanuni, taratibu zinazosimamia biashara ya mifugo baada ya kubaini ukiukwaji mkubwa uliokuwa ukifanywa na baadhi ya wadau wasiowaaminifu. Operesheni hii ilifanyika kwa awamu tatu, awamu ya kwanza Serikali ilikusanya shilingi bilioni 7.1, awamu ya pili Serikali ilikusanya shilingi bilioni 5.7, awamu ya tatu Serikali ilikusanya shilingi bilioni 3.5.

Mheshimiwa Spika, fedha hizi zinazotokana na operesheni ziliingizwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali na kutumika katika kutekeleza shughuli mbalimbali za Serikali kama zilivyoidhinishwa na Bunge lako tukufu. (Makofi)
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA Aliuliza: -

Kuna mpango wa kujenga bandari kubwa ya uvuvi inayotegemewa kutoa ajira zipatazo 30,000.

Je, ajira kwa upande wa Zanzibar zitakuwa ngapi kati ya hizo?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza mpango wa kujenga bandari ya uvuvi nchini ambapo inaendelea kufanya upembuzi yakinifu, uchambuzi wa awali umetoa mapendekezo ya kujengwa kwa bandari ya uvuvi katika eneo la Mbegani, Bagamoyo. Aidha, uamuzi wa kujenga bandari ya uvuvi ni miongoni mwa vipaumbele vya Taifa, lakini katika sera ya uvuvi ya 2015 lakini Mpango wa Maendeleo Miaka Mitano wa Awamu ya III 2021 hadi 2026.

Mheshimiwa Spika, kukamilika kwa ujenzi wa bandari kunakadiriwa kutoa ajira zaidi ya 30,000 wakiwemo wananchi kutoka Zanzibar, aidha, Serikali itahakikisha kuwa Watanzania kutoka pande zote nchini wananufaika na fursa za ajira, biashara ya mazao ya uvuvi na uwekezaji katika viwanda vya kuchakata mazao ya uvuvi.
MHE. MWANTATU MBARAK KHAMIS Aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwainua Watu Wenye Ulemavu kwa kuwapatia vifaa vya michezo na walimu ili waweze kushiriki mashindano ya kitaifa na kimataifa?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantatu Mbarak Khamis, Mbunge kutoka Baraza la Wawakilishi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ili kusimamia sekta ya maendeleo ya michezo kwa weledi, Serikali imetengeneza Mpango Mkakati wa Maendeleo ya Michezo wa Taifa ambao utazinduliwa rasmi mwezi Septemba 2021. Mpango mkakati huo una malengo ya kuendeleza michezo kwa ujumla wake ikiwa ni pamoja na michezo ya watu wenye ulemavu. Mpango huo unaainisha maeneo yote muhimu yakiwemo upatikanaji wa vifaa, ujenzi na ukarabati wa miundombinu, uendelezaji na upatikanaji wa wataalam na walimu wa michezo.

Mheshimiwa Spika, pamoja na uendelezaji wa mpango huo, Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imekuwa ikiwasaidia wana michezo wenye ulemavu kushiriki katika michezo mbalimbali kwa kuwapatia mahitaji muhimu ikiwa ni pamoja na vifaa vya michezo na wataalam wa mchezo husika. Mathalani mwaka huu wa 2021, Serikali imelipia usafiri, vifaa na posho kwa wachezaji na viongozi wanne kushiriki Michezo ya Paralimpiki inayofanyika nchini Japan – Tokyo kuanzia tarehe 24/08 - 04/ 09/2021. Zaidi ya milioni 15 zimetumika.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2019, Serikali iligharamia timu yetu ya mchezo wa wheel Chair kushiriki mashindano ya Afrika Mashiriki Nairobi Kenya. Mwaka huo huo Serikali iligharamia Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu kwa watu wenye ulemavu kushiriki mashindano ya Bara la Afrika (CANAF) yaliofanyika nchini Angola. Timu hiyo ilifuzu kushiriki mashindano ya Dunia ya mchezo huo yatakatofanyika mwaka 2022 nchini Uturuki.

Mheshimiwa Spika, kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Michezo uliopo chini ya Baraza la Michezo la Taifa, ni matarajio yetu kuwa tutaendelea kuwasaidia wachezaji wenye ulemavu kwa mahitaji mbalimbali ili waweze kushiriki kikamilifu katika michezo ya Kitaifa na kimataifa kwa kuwapatia maandalizi na kuwa na vifaa mbalimbali pamoja na watalaam pale wanapohitaji msaada huo.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. ASIA A. HALAMGA Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa muda mrefu wa kuwatambua na kulinda maslahi ya vijana waliojiajiri katika sanaa ya burudani kama Video Vixen na Video King?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asia Abdukarimu Halamga, Mbunge wa Viti Maalum, Kundi la Vijana kutoka Mkoa wa Manyara, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Video Vixens na Video Kings ni walimbwende, wachezaji, waigizaji, wanamitindo au watu wengine maarufu ambao hushiriki kwenye Sanaa hasa katika muziki wa video (audio-visual) kwa lengo la kuiongezea mvuto kazi husika. Hawa hushirikishwa na wamiliki wa kazi husika kwa makubaliano maalum.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki Na. 7 ya mwaka 1999, anaepaswa kulipwa mrabaha wa kazi ya sanaa ni mtunzi, mbunifu na mtayarishaji (producer) wa kazi ya sanaa husika.

Mheshimiwa Spika, ili kuweza kuifikia na kuivutia hadhira yake, Sanaa hii imekuwa ikiwashirikisha Video Vixen na Video Kings, Serikali ilifanya marekebisho ya Sheria hii kifungu cha 47(b) mwaka 2019 ili kuipa COSOTA mamlaka ya Uhifadhi na Usimamizi wa Mikataba ya kimaslahi kati ya wenye kazi hiyo ya sanaa na vijana wetu hawa.

Mheshimiwa Spika, natoa rai kwa wadau wote wa sanaa ya burudani kuishirikisha COSOTA ili maslahi yao yaweze kulindwa kupitia mikataba.
MHE: RAVIA IDARUS FAINA aliuliza: -

Je, Kwa nini Vyama vya Michezo ikiwemo TFF na TOC vimekuwa vikibadili Katiba zao kwa lengo la kulinda viongozi waliopo madarakani na kudhibiti watanzania wengine wasigombee nafasi katika vyama hivyo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyetupa uhai siku ya leo tukaendelea kutimiza wajibu wetu sisi Wabunge wa Bunge hili. Lakini pia nimshukuru Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan kuniamini tena na kunifanya Naibu katika Wizara hii. Mheshimiwa Rais nakushukuru sana. Lakini la tatu pia, niwatakie kila la kheri wanahabari wote kote nchini na duniani pia katika maadhimisho ya siku yao ya uhuru wa vyombo vya habari.

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ravia Idarus Faina, Mbunge wa Makunduchi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Vyama vya Michezo Tanzania vinasajiliwa kwa Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa na 12 ya Mwaka 1967 na marekebisho yake Na. 6 Mwaka 1971 pia namba 3 ya Mwaka 2018; pamoja na kanuni za msajili za Mwaka 1999.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mahitaji ya kubadili katiba za vyama kujitokeza na kufanyika katiba hizo haziwezi kuanza kufanya kazi, mpaka zisajiliwe upya na Msajili wa Vyama vya Michezo ambaye hupitia upya, kuona kama kanuni zinazosimamia Michezo na Sheria zingine za nchi zimeangaliwa. Iwapo msajili atabaini kuwa suala ambalo limeingizwa katika katiba halina maslahi kwa Chama na Taifa ikiwemo masuala ya utawala bora; Msajili amepewa mamlaka ya kisheria kukataa usajili huo kwa mujibu wa Kanuni za Usajili za Mwaka 1999, kifungu 11(3)(a) na (b).

Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, Shirikisho la TFF na TOC haijawahi kubadili katiba zao kwa lengo la kulinda viongozi walioko madarakani kwa kuwa, mabadiliko hayo yote ya kikatiba ni lazima yakidhi vigezo vya usajili vinavyosimamiwa na msajili wa vyama na vilabu vya Michezo nchini, ikiwemo utawala bora na ukomo wa muda wa uongozi chini ya BMT.
MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuifanya Lugha ya Kiswahili kuwa bidhaa ya kimataifa ili kuendeleza na kukuza utamaduni wetu Duniani?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo napenda kumfahamisha Mheshimiwa Mussa Ramadhan Sima Mbunge wa Singida Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuwa, Serikali imeanzisha mipango kadhaa ya kimkakati ya kukifanya Kiswahili kuwa bidhaa ya Kimataifa. Tayari kanzidata ya wataalam wa Kiswahili imeanzishwa na wataalam 1318 wamesajaliwa. Pamoja na hayo, Serikali imenunua vifaa vya kisasa vya mafunzo ya ukalimani kwa vitendo na matumizi ya TEHAMA katika ukuzaji wa Kiswahili ambayo yametumia zaidi ya milioni 181.8.

Mheshimiwa Spika, tayari tunao mpango wa kufundisha Kiswahili kwa wageni kupitia balozi zetu nje ya nchi. Vile vile, Serikali imeboresha na kuimarisha mafunzo ya stadi za kufundisha Kiswahili kwa wageni. Pamoja na kutoa machapisho ya Kiswahili rahisi kwa wataalam wetu, na pia kwa lengo la kusaidia nchi zilizoonesha nia ya kuingiza Kiswahili katika mitaala yao ya Elimu mfano Afrika Kusini, Namibia, Rwanda na Uganda.

Mheshimiwa Spika, afua ya hayo, mwaka 2019; wakati wa Mkutano wa 39 wa Wakuu na Viongozi wa Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika-SADC Serikali ilifanikiwa kukifanya Kiswahili kuwa moja ya Lugha nne rasmi zinazotumiwa wakati wa vikao na mikutano ya nchi hizo. Naombwa kuwasilisha.
MHE. VUMA A. HOLLE K.n.y. MHE. SYLIVIA F. SIGULA aliuliza:-

Je, nini Mpango wa Serikali kuhakikisha kuwa Timu ya Taifa Stars inafanya vizuri katika Michezo ya Kimataifa?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sylvia Francis Sigula, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha kuwa Timu za Taifa ikiwemo Taifa Stars zinafanya vizuri katika mashindano mbalimbali, kuanzia mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali imeendelea kuboresha maandalizi ya timu zetu kwa kutenga fedha za kuzihudumia timu hizi. Mipango mingine iliyowekwa na Serikali ni ile ya muda mrefu na muda mfupi. Mipango ya muda mfupi ni pamoja na:-

(a) Kushirikiana na TFF katika maandalizi ya kambi za Timu ya Taifa ndani na nje ya nchi.

(b) Kuongeza motisha kwa kutoa posho na bonasi kwa wachezaji na benchi la ufundi la Timu ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mipango ya muda mrefu ni pamoja na:-

(a) Kuwekeza katika michezo ya UMITASHUMTA, UMISSETA.

(b) Kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Michezo nchini.

(c) Mazungumzo yanaendelea kati ya Wizara yetu na Wizara ya Fedha ili kuhakikisha fedha hizi zinatengwa.

(d) Kuanzisha shule maalum za michezo katika kila mkoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mipango mingine ya Serikali iliyopo ni ushirikiano kati ya Wizara yangu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya TAMISEMI juu ya uendeshaji bora wa michezo nchini na mipango ya uanzishaji wa tahasusi za kidato cha Tano zenye somo la michezo.
MHE. NG’WASI D. KAMANI K.n.y. MHE. ASIA A. HALAMGA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Wakandarasi wa Tanzania wanapata fursa ya kujenga Mnara wa Mwalimu Nyerere katika Makao Makuu ya Umoja wa Afrika hasa ikizingatiwa kuwa Serikali ya Tanzania ndio inasimamia ujenzi wa mnara huo?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asia Halamga, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, zabuni Na. SADC/NYERERE ST/02 ilipotangazwa kati ya mwezi Mei na Julai, 2021 ilitoa fursa sawa kwa wakandarasi wote kutoka nchi Wanachama wa SADC. Serikali kupitia Baraza la Sanaa la Taifa ilichukua jitihada za kuwatangazia na kuwahamasisha wadau wote nchini kupitia Shirikisho la Sanaa za Ufundi na Idara za Sanaa za Vyuo Vikuu mbalimbali nchini ili wenye vigezo vilivyoainishwa kwenye zabuni waweze kuomba kazi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu wapo wakandarasi wa Kitanzania walioomba kazi hii sambamba na wenzao kutoka mataifa wanachama wa SADC. Hivi sasa SADC imekamilisha uchambuzi wa nyaraka na muda wowote mshindi atatangazwa baada ya kusaini mkataba.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Kiwanja cha Michezo katika Wilaya ya Hai?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Saasisha Elinikyo Mafuwe, Mbunge wa Hai, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Sera ya Maendeleo ya Michezo ya mwaka 1995, Ibara ya 7 (i) hadi (vii) imetoa maelekezo juu ya ujenzi na utunzaji wa viwanja vya michezo. Sera imezielekeza Halmashauri kutenga maeneo ya viwanja kila wanapopima makazi ya watu na pia kutumia wadau mbalimbali na raslimali zilizopo katika Halmashauri zao ili kuwajengea wananchi viwanja ili wapate mahali sahihi pa kushiriki shughuli za michezo ili kukuza na kulinda afya zao na pia kupata eneo la kutolea burudani za wazi.

Mheshimiwa Spika, kutokana na Mkakati wa Taifa wa utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Michezo wa mwaka 2022 mpaka 2032, nitumie nafasi hii kutoa rai kwa uongozi wa Halmashauri ya Hai na Halmashauri zote nchini pamoja nanyi Waheshimiwa Wabunge wote kuendelea kutenga fedha za ujenzi wa viwanja katika viwanja katika bajeti zetu za Halmashauri husika na kuendelea kuwashirikisha wadau mbalimbali wa michezo katika kukamilisha azma hiyo ya kuwa na viwanja na miundombinu bora ya michezo mbalimbali hapa nchini. Ahsante. (Makofi)
MHE. INNOCENT E. KALOGERIS aliuliza: -

Je, ni lini ahadi ya ujenzi wa uwanja wa mpira Dodoma iliyotolewa na Mfalme wa Morocco itatekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana na kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Edward Kalogeris, Mbunge wa Morogoro Kusini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imefuatilia utekelezaji wa ahadi ya ujenzi wa uwanja wa mpira Dodoma iliyotolewa na Mfalme wa Morocco. Mawasiliano kuhusu utekelezaji wa mradi huo baina ya Serikali ya Tanzania na Morocco bado yanaendelea. Vilevile katika kuhakikisha kwamba mradi huu unatekelezwa Serikali imedhamiria kutafuta fedha kutoka katika vyanzo mbalimbali vikiwemo sekta binafsi na wabia wa maendeleo.
MHE. SULEIMAN HAROUB SULEIMAN aliuliza: -

Je, ni vigezo gani vinatumika kuchagua wachezaji wa timu ya Taifa (Taifa Stars)?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, nikushukuru na kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Suleiman Haroub Suleiman, Mbunge wa Baraza la Wawakilishi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, jukumu la kusimamia timu zote za Taifa ni la Serikali kwa kushirikiana na Vyama na Mashirikisho ya Michezo. Kwa mujibu wa Kamati ya Ufundi ya TFF vigezo vinavyotumika kuchagua wachezaji wa Taifa Stars ni kama ifuatavyo; mchezaji awe raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mchezaji anayecheza katika klabu ya ligi za juu, mchezaji anayepata nafasi na kucheza kwenye klabu husika (playing time), mchezaji awe na ufanisi mzuri wa kucheza (good performance), awe na vigezo katika nafasi anayocheza (fitting the positional profile), pamoja na kuwa na nidhamu ya kiuchezaji na nidhamu katika maisha ya kawaida.
MHE. JANETH E. MAHAWANGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itawekeza katika Sekta ya Michezo hasa kwenye timu za wanawake ili kuibua vipaji kwa watoto?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Janeth Elius Mahawanga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuwekeza katika kuibua, kukuza na kuendeleza vipaji vya michezo ambapo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Shilingi milioni 183.5 zimetengwa kama kianzio katika kutoa huduma kwa timu zetu za Taifa ikiwemo timu za wanawake na Shilingi bilioni 10 zimetengwa kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya michezo.

Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika Timu za Taifa za wanawake ambapo kupitia uwekezaji huu, timu hizi zimeendelea kufanya vizuri katika ukanda wa CECAFA na COSAFA na umewezesha timu ya Serengeti Girls kufuzu mashindano ya Kombe la Dunia nchini India. Ahsante. (Makofi)
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Uwanja wa Michezo katika Mji wa Lushoto?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Shabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sera ya Maendeleo ya Michezo ya Taifa ya mwaka 1995 ibara ya 7(i) – (vii), jukumu la ujenzi na uendelezaji wa miundombinu ya michezo ni jukumu la Serikali Kuu, Mamlaka ya Serikali za Mitaa pamoja na Wadau wa Sekta ya Michezo zikiwemo Taasisi, Mashirika na Watu Binafsi. Hivyo, napenda kuzikumbusha na kuzielekeza halmashauri zote nchini ikiwemo Halmashauri ya Mji wa Lushoto kuzingatia matakwa ya Sera ya Michezo kwa kutenga fedha kutoka katika mapato ya ndani kwa ajili ya kujenga na kukarabati miundombinu ya michezo kwenye maeneo yao. Ahsante.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU aliuliza: -

Je, ni upi mchango wa Serikali Kuu katika ujenzi wa Uwanja wa Kisasa wa Michezo wa Halmashauri ya Mji wa Geita?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa utamaduni, Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Constantine John Kanyasu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sera ya Maendeleo ya Michezo ya Taifa ya mwaka 1995 Ibara ya 7(1) mpaka (7), jukumu la ujenzi na uendelezaji wa miundombinu ya michezo ni jukumu la Serikali Kuu, Mamlaka ya Serikali za Mitaa na watu binafsi. Hata hivyo, tunaipongeza Halmashauri ya Geita Mji kwa ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu ambao umefikia asilimia 75. Hivyo napenda kutoa wito kwa halmashauri zote nchini kuiga mfano wa Halmashauri ya Geita Mji kwa kujenga fedha kutoka mapato yao ya ndani kwa ajili ya kujenga na kukarabati miundombinu ya michezo.

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ipo tayari kutoa mchango wa ushauri wa kitaalamu katika ujenzi wa uwanja wa kisasa wa michezo unaojengwa katika Halmshauri ya Geita Mji, pale itakapohitajika kama ilivyofanya katika halmashauri kadhaa nchini ikiwemo Halmashauri ya Chalinze, Tunduma, Ruangwa na Taasisi kama vile Bandari na Gymkhana. Ahsante.
MHE. DAVID C. CHUMI aliuliza: -

Je, Serikali inakusanya kiasi gani cha asilimia Tano ya zawadi ya washindi wa mchezo wa kubashiri na kimechangia kiasi gani kukuza michezo?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa David Cosato Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 mpaka mwezi Septemba mwaka 2022, Wizara imepokea kiasi cha Shilingi za Tanzania Bilioni 3.4 ikiwa ni asilimia Tano ya mapato yatokanayo na michezo ya kubashiri. Kwa mujibu wa muongozo wa mfuko wa Maendeleo ya Michezo fedha hizi hutumika kuhudumia Timu za Taifa, kutoa mafunzo kwa wataalamu wa michezo na wanamichezo, kuibua na kuendeleza vipaji vya michezo pamoja na kujenga na kukarabati miundombinu ya michezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Timu za Tembo Warriors na Serengeti Girls ni miongoni mwa wanufaika wa hivi karibuni wa fedha hizo katika maandalizi na ushiriki wao kwenye mashindano ya Kombe la Dunia la mpira wa miguu kwa Walemavu na Wanawake chini ya miaka 17 ambapo zilifanikiwa kufika hatua ya robo fainali na kuipandisha daraja nchi yetu katika nafasi za soka Duniani. Ahsante.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO aliuliza: -

Je, ni upi mkakati wa Serikali katika kuziendeleza timu za michezo za watoto?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Husna Juma Sekiboko, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua na kuthamini michezo ya watoto kwa kuwa umahiri wa timu mbalimbali unatokana na ushiriki mzuri wa watoto katika ngazi za chini ambazo hupelekea urahisi wa kuibua na kuendeleza vipaji. Serikali ina mkakati wa kuziendeleza timu za watoto kwa kuhakikisha kuwa kunakuwepo na mashindano mengi yanayohusisha watoto ili kuwajengea uzoefu.

Mheshimiwa Spika, sehemu ya mikakati hiyo ni pamoja na uendeshaji wa mashindano ya UMITASHUMTA na UMISETA, ukarabati wa miundombinu ya michezo katika shule 56 teule za michezo, pamoja na usajili wa vituo vya michezo ya watoto (sports academies). Aidha, Serikali imeendelea kuhamasisha wadau mbalimbali kuandaa mashindano ya timu za watoto na kuwajengea mazingira wezeshi ya kuendeleza vituo hivyo. Ahsante.
MHE. KHADIJA S. TAYA aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kuinua ushiriki wa Watu wenye Ulemavu katika michezo ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa wavu na pete?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Khadija Shaaban Taya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikitoa haki sawa ya ushiriki katika michezo kwa makundi yote ikiwemo watu wenye ulemavu. Moja ya mikakati ya Serikali katika kuinua ushiriki wa watu wenye ulemavu hususani kwenye mpira wa miguu, wavu na pete ni pamoja na kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kushirikisha watu wenye ulemavu katika michezo, kusajili vyama na vilabu vya michezo kwa watu wenye ulemavu, kushirikisha michezo ya watu wenye ulemavu katika matukio yote ya michezo hususani yanayoandaliwa na Serikali, hii ni pamoja na kuziwezesha timu za Taifa za watu wenye ulemavu zinaposhiriki katika mashirikisho mbalimbali ya Kimataifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa michezo imeendelea kuhamasisha ujenzi wa miundombinu ya michezo yenye mazingira rafiki kwa watu wenye ulemavu.
MHE. GEOFFREY I. MWAMBE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itauboresha uwanja wa mpira wa Boma uliopo Masasi Mjini kwa kiwango kinachofaa kukuza na kuendeleza vipaji vya vijana wa Masasi?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Geoffrey Mwambe, Mbunge wa Masasi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sera ya Maendeleo ya Michezo ya Taifa ya mwaka 1995 kifungu cha 7(i) hadi (vii), jukumu la ujenzi na uendelezaji wa miundombinu ya michezo ni jukumu la Serikali Kuu, Mamlaka ya Serikali za Mitaa pamoja na wadau wa sekta ya michezo zikiwemo taasisi, mashirika na watu binafsi.

Mheshimiwa Spika, hivyo, napenda nitoe rai kwa Halmashauri zote nchini ikiwemo Halmashauri ya Mji Masasi kuzingatia matakwa ya sera ya michezo kwa kutenga fedha kutoka katika mapato ya ndani kwa ajili ya kujenga na kukarabati miundombinu ya michezo kwenye maeneo yao kama zilivyofanya Halmashauri za Ruangwa, Geita, Nyamagana, Bukoba na Babati Mjini, ahsante.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO K.n.y. MHE. TWAHA A. MPEMBENWE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Kibiti?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana na kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu nikiwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria nimshukuru Mwenyezi Mungu lakini pia nimshukuru Mheshimiwa Rais kuendelea kuniamini naahidi kwamba nitaendelea kufanya kazi kwa unyenyekevu mkubwa.

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria sasa naomba kujibu swali Mheshimiwa Twaha Ally kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mahakama inaendelea kutekeleza mpango wake wa ujenzi na ukarabati wa majengo katika ngazi zote. Katika mpango huo, Mahakama ya Wilaya ya Kibiti imepangwa kujengwa katika mwaka wa fedha 2023/2024. Aidha, maandalizi ya awali yameshaanza kufanyiwa kazi na kukamilika, ikiwemo usanifu wa mradi, pamoja na maandalizi ya kabrasha za zabuni. Hivyo, mara baada ya bajeti kuanza, utekelezaji wa mradi huu utaanza mara moja. Ahsante.
MHE. ANATROPIA L. THEONEST aliuliza: -

Je, Sheria za Tanzania zinasema nini kuhusu mahusiano ya jinsia moja?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru, na kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria sasa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anatropia Theonest kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria za Tanzania haziruhusu mahusiano ya jinsia moja. Kwa mujibu wa kifungu cha 9 cha Sheria ya Ndoa kinatafsiri ndoa ni mahusiano ya hiyari kati ya mwanaume na mwanamke. Aidha kwa mujibu wa kifungu cha 154 cha Sheria ya Kanuni za Adhabu, Sura ya 16 kinabainisha kuwa kufanya mapenzi kinyume na maumbile ya jinsia ni kosa la jinai ambalo adhabu yake ni kifungo cha maisha jela au kifungo kisichopungua miaka 30 jela.
MHE. CECIL D. MWAMBE K.n.y. MHE. AGNES E. HOKORORO aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kubadilisha Sheria ya Mirathi ya Kiserikali ya mwaka 1925 na Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria napenda kujibu swali la Mheshimiwa Agnes Elias Hokororo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, suala la mirathi hushughulikiwa na sheria tofauti Tatu ambazo ni Sheria ya Kiislam, Sheria ya Kimila na kwa wale wasiotumia sheria hizo, Sheria ya Mirathi ya India ya mwaka 1925 (Indian Succession Act, 1925) ikiwa ni miongoni mwa sheria tulizorithi kupitia Sheria ya The Judicature and Application of Law (JALA) Sura ya 358.

Mheshimiwa Spika, aidha, sheria hizi katika kushughulikia suala la mirathi hutumika sambaba na Sheria ya Usimamizi wa Mirathi, Sura ya 352 ambayo ndiyo sheria mahsusi katika kushughulikia usimamizi wa mirathi yote nchi.

Mheshimiwa Spika, Wizara imeshaelekeza Tume ya Kurekebisha Sheria nchini kufanyia utafiti wa sheria zote zikiwemo Sheria za Mirathi ili kuziboresha na kuondoa vifungu ambavyo vinakiuka misingi ya haki na usawa. Kuhusu Sheria ya Ndoa, Serikali imeshaandaa mapendekezo ya marekebisho ya sheria hiyo na inatarajia kuyawasilisha katika Bunge hili linaloendelea. (Makofi)
MHE. YUSTINA A. RAHHI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali italeta Bungeni Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 kuhusu Ndoa za Utotoni?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yustina Arcadius Rahhi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikumbukwe kuwa Muswada wa Sheria ya Ndoa ulifikishwa kwenye Kamati ya Bunge lako Mwezi Februari, 2021, kufuatia maamuzi ya Mahakama ya Rufani kati kesi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya Rebecca Gyumi, Rufaa Na.204/2017 iliyotokana na kesi Na.5/2016 ya Mahakama Kuu iliyotaka Sheria ya Ndoa ifanyiwe marekebisho ili umri wa mtoto kuingia katika ndoa iwe kuanzia miaka 18. Kamati ya Bunge baada ya kupitia iliona upo uhitaji wa kushirikisha wadau wengi zaidi ili kupata maoni zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kumwarifu Mbunge kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeshakusanya maoni kutoka kwa wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa kidini, viongozi wa kimila, viongozi wa vyama vya siasa, wanafunzi, wataalam mbalimbali wa afya, makundi mbalimbali ya wananchi wakiwemo watu wenye ulemavu. Aidha, tarehe 26 Aprili, 2023, Wizara imeandaa Kongamano la Sheria ya Ndoa litakalofanyika katika Hotel ya Morena, Jijini Dodoma, kesho saa saba. Naomba niwakaribishe Wabunge wote na itakuwa live TBC kwa Watanzania wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara tu baada ya Serikali kukamilisha zoezi hili la mwisho, inatarajia kuwasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ndoa Bungeni katika Bunge hili la Bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE K.n.y. MHE. NJALU D. SILANGA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha Mahakama ya Ardhi chini ya Muhimili wa Mahakama?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Njalu Daudi Silanga, Mbunge wa Itilima kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa utatuzi wa migogoro ya ardhi unaanzia katika ngazi ya Mabaraza ya Ardhi ya Vijiji na Mabaraza ya Kata ambayo yote yana mamlaka ya kufanya usuluhishi. Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya ndiyo yenye jukumu la kutatua migogoro ya ardhi nchini ambapo ikiwa mtu hakuridhika na uamuzi wa Baraza la Ardhi na Nyumba ya Wilaya atakata rufaa kwenda Mahakama Kuu au Mahakama ya Rufani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uwepo wa Mahakama ya Ardhi napenda kumfahmisha Mheshimiwa Mbunge kuwa katika Mahakama Kuu kuna Divisheni maalum ya Mahakama Kuu, Kitengo cha Ardhi. Hata hivyo, Serikali inaendelea kufanya maboresho katika Marabaza ya Ardhi ili kuangalia namna bora ya kuyawezesha ikibidi ihamishiwe katika Muhimili wa Mahakama, ahsante.
MHE. MWANAHAMIS KASSIM SAID aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kupunguza tatizo la watuhumiwa kutopewa dhamana kwa makosa yenye dhamana?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwanakhamis Kassim Said, Mbunge wa Magomeni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, dhamana katika kesi za jinai ni haki ambayo imewekewa utaratibu wa kisheria. Kwa mujibu wa sheria zetu yapo makosa yanayodhaminika na yapo makosa ambayo hayana dhamana. Kifungu cha 148(5) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai Sura 20 kimeainisha makosa yote ambayo hayana dhamana. Hivyo, kwa makosa yote ambayo hayajatajwa na kifungo hicho yana dhamana ambayo ni haki ya mshtakiwa.
MHE. RASHID A. SHANGAZI K.n.y. MHE. USSI SALUM PONDEZA aliuliza: -

Je, lini hatua iliyobakia katika mchakato wa kupata Katiba Mpya itakamilishwa?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, naomba kujibu sasa swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Chumbuni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua umuhimu wa mchakato wa kupata katiba mpya aliunda kikosi kazi kilichoongozwa na Profesa Mukandara ambacho pamoja na masuala mengine, ilikuwa ni kuhuisha mchakato wa Katiba mpya. Katika hilo, kikosi kazi hicho kimetoa mapendekezo ya hatua sita za kufuatwa katika kukamilisha mchakato wa kupata Katiba Mpya. Hatua hizo ni hizi zifuatazo: -

(i) Kuwepo kwa mjadala wa Kitaifa wa kupata muafaka wa masuala ya msingi;

(ii) Kuhuisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba;

(iii) Kuundwa kwa Jopo la Wataalam wa kuandaa Rasimu ya Katiba;

(iv) Rasimu ya Katiba kupitishwa na Bunge;

(v) Kutoa elimu ya uraia; na

(vi) Rasimu ya Katiba kupigiwa kura na wananchi.

Mheshimiwa Spika, baada mapendekezo ya kikosi kazi, tarehe 6 Mei, 2023, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassani, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alimuagiza Msajili wa Vyama vya Siasa kuitisha Kikao Maalum cha Baraza la Vyama vya Siasa wakiwemo wadau mbalimbali kujadili mapendekezo ya kikosi kazi na kupendekeza taratibu za kuzingatia katika kuanzisha mchakato wa kupata Katiba mpya. Ahsante.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza: -

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Mahakama yenye hadhi ya Wilaya katika Wilaya ya Kalambo?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imepanga kuanza ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Kalambo katika mwaka huu wa fedha 2023/2024 ambapo taratibu zote za awali za kupitia michoro na makadirio ya gharama vimekamilika. Aidha, hatua ya kupata Mkandarasi wa ujenzi ipo katika hatua za mwisho. Hivyo, tunategemea muda wowote jengo hili litaanza kujengwa na kukamilika katika mwaka ujao wa fedha, ahsante.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO aliuliza: -

Je, nini mpango wa Serikali wa kuhakikisha kila Kata inakuwa na Mahakama hasa maeneo ya Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ninakushukuru, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria napenda sasa kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Nyangindu Butondo, Mbunge wa Kishapu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inayo azma na dhamira ya kusogeza huduma za haki karibu na wananchi, hususan kwa kujenga na kukarabati majengo ya Mahakama. Katika kutekeleza azma hii, tunao mpango wa ujenzi na ukarabati wa majengo ya Mahakama, katika ngazi zote, kuanzia Mahakama za Mwanzo hadi Mahakama za Rufani.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Mahakama za mwanzo, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kuwa walau kila Tarafa inakuwa na Mahakama ya Mwanzo na baadaye tuweze kwenda hadi ngazi ya Kata kadri upatikanaji wa fedha utakavyoruhusu. Ahsante.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA aliuliza: -

Je, lini Mahakama ya Wilaya ya Nyasa itaanza kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, nikushukuru, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria naomba sasa nijibu swali la Mheshimiwa Engineer Stella Martin Manyanya, Mbunge wa Nyasa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imepanga kujenga Mahakama ya Wilaya ya Nyasa katika mwaka huu wa fedha wa 2022/2023, ambapo taratibu zote za awali za kupitia michoro na makadirio ya gharama zimekamilika, na hatua za kupata mkandarasi wa ujenzi ipo katika hatua za mwisho.

Mheshimiwa Spika, Tunategemea muda wowote jengo hili litaanza kujengwa, na kukamilika katika mwaka ujao wa fedha wa 2023/2024.
MHE. DKT. THEA M. NTARA aliuliza: -

Je, lini Serikali italeta muswada wa sheria ya adhabu kali kwa wanaobaka na kulawiti watoto na wanawake?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Thea Medard Ntara, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa vifungu 130, 131, 131A na 154 vya Sheria ya Kanuni za Adhabu, Sura ya 16, ni makosa ya jinai kwa mtu kubaka na kulawiti. Makosa yote haya adhabu yake ya juu ni kifungo cha maisha jela, na adhabu ya chini ni kifungo cha miaka 30 jela. Aidha, kwa makosa yote hayo yakitendeka dhidi ya mtoto mwenye umri chini ya miaka 10, adhabu yake ni kifungo cha maisha jela. Pamoja na adhabu hizo, Mahakama ina mamlaka ya kutoa amri ya ziada ya kumlipa fidia mwathirika chini ya kifungu cha 131(1) cha Kanuni za adhabu.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali katika kutekeleza maelekezo ya Bunge, inafanya utafiti zaidi ili kuona kama kuna hitaji la kufanya maboresho au marekebisho ya sheria hiyo, ahsante.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza:-

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa jengo la Mahakama Wilayani Mbulu?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ninakushukuru na pia ninamshukuru Mwenyezi Mungu, na naomba sasa kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria niweze kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mahakama ya Wilaya ya Mbulu kwa sasa inaendeshwa katika jengo ambalo ni chakavu na finyu sana kukidhi mahitaji. Aidha, jengo hilo pia lipo kwenye eneo la hifadhi ya barabara na hivyo linapaswa kuondolewa. Katika mpango wetu wa ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Mbulu itajengwa katika mwaka wa fedha 2023/2024 na tayari mshauri elekezi ameshakamilisha usanifu na maandalizi ya zabuni kwa ajili ya kupata mkandarasi wa ujenzi. Ujenzi unatarajia kuanzia mwezi Septemba, 2023 na kukamilika kabla ya Juni, 2024.
MHE. TECLA M. UNGELE aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga jengo jipya la Mahakama ya Wilaya Nachingwea?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ninakushukuru na kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria naomba sasa nijibu swali la Mheshimiwa Tecla Mohamedi Ungele, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutekeleza mpango wa ujenzi na ukarabati wa majengo ya Mahakama katika ngazi mbalimbali ili kuboresha mazingira ya utoaji haki. Katika mpango huo Mahakama ya Wilaya ya Nachingwea imepangwa kujengwa katika mwaka huu wa fedha 2023/2024. Mshauri Elekezi ameshakamilisha usanifu na maandalizi ya gharama za mradi na taratibu za kupata Mkandarasi wa ujenzi zinaendelea.

Mheshimiwa Spika, jengo linatarajiwa kukamilika ifikapo Juni, 2024.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA aliuliza:-

Je, ni lini Muswada wa Ukomo wa Upelelezi wa Kesi utaletwa ili kupunguza msongamano wa kesi unaotokana na upelelezi kutokamilika?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Neema Gerald Mwandabila, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa kifungu cha 225(4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 20, ukomo wa upelelezi katika baadhi ya makosa ni siku 60 na kwa mujibu wa kifungu 225(5), Mahakama imepewa mamlaka kuifuta kesi ambayo upelelezi wake haujakamilika baada ya siku 60.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilifanya marekebisho ya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 20 kupitia Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.1) ya 2022 kwa kuongeza kifungu cha 131A kilichoweka masharti kuwa isipokuwa kwa makosa mazito na makosa yote yanayosikilizwa na Mahakama Kuu watuhumiwa wasifikishwe Mahakamani hadi upelelezi uwe umekalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mkurugenzi wa Mashataka imetoa Waraka Na. 1 wa mwaka 2022, kuhusu Ufunguaji wa Mashtaka na Ukamilishaji wa Upelelezi wa Kesi za jinai uliotolewa tarehe 30 Septemba, 2022 na ulishaanza kutumika tarehe Mosi Oktoba, 2022. Waraka huo unataka upelelezi wa kesi za mauaji, kesi za makosa mazito na kesi zote zinazosikilizwa na Mahakama Kuu ambazo hazihitaji utaalam kutoka taasisi nyingine usichukue zaidi ya siku sitini (60) na zile zinazohitaji utaalam kutoka taasisi nyingine upelelezi usichukue zaidi ya siku tisini (90).
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza:-

Je, lini Serikali itatenga fedha na kuanza ujenzi wa Mahakama ya Mkoa wa Songwe?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria naomba sasa nijibu swali la Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge wa Vwawa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe ulianza katika mwaka wa fedha 2021/2022, na jengo hilo lilijengwa eneo la Vwawa Wilayani Mbozi na lilikamilika Julai, 2022. Aidha, Jengo lilianza kutumika Agosti, 2022 na kuzinduliwa rasmi na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania mwezi Novemba, 2022 ambapo alizindua kwa pamoja na majengo ya Mahakama za Hakimu Mkazi katika Mikoa ya Lindi na Katavi, ahsante.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itarudisha huduma za Mahakama za Mwanzo katika Kata ya Kalya Buhingu?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Nashon William Bidyanguze, Mbunge wa Kigoma Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakama inaendelea na mipango ya kufanya ujenzi na tayari huduma imerejeshwa kuanzia mwezi Julai, 2022 na mpaka sasa wapo watumishi wanatoa huduma kwa kutumia Ofisi za Kata. Kuanzia mwezi Julai 2022 huduma iliporejea hadi Machi, 2023 jumla ya mashauri 38 yamesajiliwa na kusikilizwa katika Mahakama hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango wa ujenzi wa Mahakama, tumepanga kujenga Mahakama ya Mwanzo Mgambo mwaka 2024/2025, ambapo ndiyo Makao Makuu ya Tarafa ya Buhingu. Hivyo, tunatajarajia kuwa wananchi wa Kalya watapata huduma katika Mahakama ya Mwanzo Mgambo. Ahsante.
MHE. ISSA J. MTEMVU aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga Sport Arena katika Wilaya ya Ubungo?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, naomba kujibu swali namba 252 la Mheshimiwa Issa Jumanne Mtemvu, Mbunge Kibamba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inaendelea na mpango wa ujenzi wa Sports and Arts Arena katika Mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma yenye thamani ya jumla ya Shilingi za Kianzania bilioni 550 kwa ushirikiano wa Serikali na Wadau. Wizara imeshakamilisha hatua za awali za kutengeneza michoro ya Arena hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, vikao vya mashauriano baina ya Wizara na Mkoa wa Dar es Salaam vinaendelea ili kukubaliana sehemu ya ujenzi wa viwanja hivyo. Eneo la Luguruni lililopo Manispaa ya Ubungo lenye ukubwa wa ekari 10.5 ni kati ya maeneo yanayotarajiwa kupendekezwa kwa ujenzi wa mradi huo. Baada ya kukamilika kwa hatua hizo, ujenzi utaanza mara moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. VENANT D. PROTAS K.n.y. MHE. JACQUELINE K. ANDREA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati Mahakama ya Wilaya ya Urambo?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Kainja Andrea, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakama ya Tanzania inaendelea kutekeleza mpango wa kuboresha majengo katika ngazi mbalimbali kwa kujenga majengo mapya na kukarabati baadhi ya majengo ya zamani. Aidha, katika mpango huu, jengo la Mahakama ya Wilaya ya Urambo limepangwa kufanyiwa ukarabati mkubwa mwaka wa fedha 2024/2025. Ahsante.
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI aliuliza:-

Je, kwa nini Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania hawafundishi nje ya nchi hata katika Ukanda wa Afrika Mashariki au Nchi za SADC?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Tanzania ina makocha 19 wenye viwango vya CAF A Diploma ambao wanakidhi viwango vya kufundisha nje ya nchi. Hata hivyo, makocha hawa hawafanikiwi kupata fursa za kufundisha nje ya nchi kutokana na historia ya elimu walizonazo. Hivyo basi, Wizara kwa kushirikiana na TFF wanaratibu mpango wa kutoa mafunzo ya Ukocha kwa wanafunzi wa vyuo vinavyotoa mafunzo ya michezo ikiwemo Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya, Butimba na Vyuo Vikuu nchini ili kupata Makocha wenye sifa.
MHE. MOHAMED SAID ISSA aliuliza:-

Je, Serikali inaisaidiaje Zanzibar kupata faida ambazo TFF inazipata katika kuendeleza soka la Tanzania?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia TFF imeendelea kuhakikisha kuwa Zanzibar inanufaika na fedha za misaada kutoka FIFA ambapo hadi sasa miradi kadhaa ya kuendeleza soka imetekelezwa ikiwa ni pamoja na kusaidia timu za Taifa, mashindano ya ndani, mawasiliano na mafunzo kwa wadau wa michezo. Hata hivyo, Serikali inatambua changamoto zilizopo baina ya TFF na ZFF katika uendeshaji soka katika Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kutatua changamoto hizi, Wizara yetu pamoja na Wizara ya Michezo na Vijana Zanzibar zimeitisha kikao maalumu baina ya ZFF na TFF kwa lengo la kutatua changamoto hizo.
MHE. INNOCENT E. KALOGERIS aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga Mahakama za Mwanzo katika Tarafa za Bwakira, Mvuli na Matombo – Morogoro Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, naomba kujibu sasa swali la Mheshimiwa Innocent Edward Kalogeris, Mbunge wa Morogoro Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mpango na Bajeti ya mwaka 2023/2024, Mahakama ya Mwanzo katika Tarafa ya Bwakira, Kata ya Bwakira Chini itajengwa ili kuwawezesha wananchi katika maeneo hayo kupata haki kwa wakati. Tayari zabuni imetangazwa kwa ajili ya kumpata mkandarasi wa ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Mahakama za Mwanzo; Matombo na Mvuha, majengo yaliyopo ni chakavu sana na hivyo kuhitaji ujenzi mpya. Hata hivyo, kutokana na mahitaji makubwa yaliyopo katika maeneo mbalimbali, ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Matombo na Mvuha utazingatiwa kwenye Mpango ujao wa ujenzi wa Mahakama, ahsante.