Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Hassan Elias Masala (30 total)

MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchukua nafasi hii kumshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri ambayo ameyatoa juu ya Mkoa wa Lindi, lakini naomba pia nitumie nafasi hii kuuliza swali moja la nyongeza. Kama ambavyo yeye amekiri, Mkoa wa Lindi kwa ujumla ulikuwa na viwanda vingi ambavyo sasa hivi vyote vimebinafsishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Nachingwea viko viwanda viwili, Kiwanda cha Korosho pamoja na Kiwanda cha Kukamua Mafuta lakini Lindi pia imekuwa na rasilimali ya bahari ambayo tukiitengenezea mazingira bado tunaweza tukatengeneza viwanda vidogo kwa ajili ya usindikaji wa samaki. Pamoja na majibu hayo aliyoyatoa je Mheshimiwa Waziri anatuahidi nini katika mpango huu ambao tunaelekea na tukiangalia Mkoa wa Lindi haujaguswa kwa namna yoyote ile? Asante sana.
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa swali la nyongeza. Kwa ruhusa yako naomba Mheshimiwa Mbunge tusiwahishe shughuli, bajeti yangu inakuja na mambo mazuri kwa ajili ya Mkoa wa Lindi ikiwemo uanzishaji wa kilimo cha muhogo ambako tutakuwa tuki-export nje tani milioni mbili za mhogo nchini China zenye thamani ya dola milioni 300.
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishukuru kwa majibu mazuri ambayo yametolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini sambamba na hilo naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo kampuni ambayo ameitaja Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa muda huo wa miaka nane ambao wamekuwa wanafanya utafiti, wamekuwa wanatumia mashine, wamekuwa wanatumia magari ambayo yamekuwa yanaharibu barabara zinazounganisha, Nditi, Nero, Namakwia pamoja na Lionja.
Je, Mheshimiwa Waziri ananiambia nini kwa niaba ya wananchi wa Nachingwea juu ya fidia ya uharibifu mkubwa wa mazingira ambao unafanywa na kampuni hii? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni eneo la upatikanaji wa leseni. Wananchi walio wengi wanaozunguka Wilaya ya Nachingwea wana kipato cha chini na wanatamani kujinufaisha na rasilimali ambazo zinapatikana katika maeneo yao kama taarifa inavyojionesha, lakini upatikanaji wa leseni hizi umekuwa na mlolongo mkubwa.
Je, Wizara inaweka utaratibu gani rahisi ambao utawawezesha watu wa Nachingwea kujimilikisha na kupata leseni waweze kuchimba wao wenyewe badala ya kuwa vibarua? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya kwanza ameulizia kuhusu uharibifu wa barabara na miundombinu kutokana na shughuli za utafiti. Shughuli za utafutaji ziko za aina tatu. Shughuli ya kwanza kabisa ambayo hufanywa na mtafiti wa madini ni kufanya utafiti angani. Utafiti wa aina hii haugusi ardhi na hauhitaji fidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, utafutaji wa pili ni ule ambao wanaweza wakatumia mimea pamoja na miamba kwa kugusa tu juu ya ardhi na wenyewe hauharibu mazingira, lakini utafiti wa tatu, ni ule ambao mtafiti anahitaji kufanya drilling. Anapofanya drilling sasa anaharibu miundombinu ya barabara na ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa utaratibu huo sasa, napenda kulieleza Bunge lako Tukufu kwamba, taratibu za fidia kwanza kabisa, kama kuna miundombinu imeharibika kwa taratibu za utafiti na uchimbaji, Sheria ya Madini inatoa kifungu cha 96 kuhakikisha kwamba mwenye leseni ya utafutaji au ya uchimbaji wanakaa na mmiliki wa miundombinu kukubaliana aina ya uharibifu na viwango vya fidia. Ikishindikana fidia kwa taratibu za Sheria ya Madini ya mwaka 2010, basi Sheria za Ardhi za 1999 Namba 4 na Namba 5 ya 1999 Vijijini, hutumika kufanya fidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nashauri sana wenye miundombinu hiyo wanaoshughulika na utafiti wakae na Kampuni hiyo wangalie uharibifu halafu waangalie namna gani ya kufidiwa barabara hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni upatikanaji wa leseni za utafiti na uchimbaji wa madini. Natumia nafasi hii kuwaambia tu kwamba taratibu zote za kumiliki leseni za uchimbaji na utafutaji mdogo; utafutaji na uchimbaji mkubwa; zote huzingatia Sheria ya Madini. Utaratibu uliopo, kwa Waingereza wanasema ni first come first served. Anayeomba mapema ndiye anayeanza kufikiriwa kupewa leseni.
Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu wetu wa kutoa leseni ni ndani ya siku 14 tangu unapoomba na unaarifiwa. Ukishaarifiwa na wewe unajibu ndani ya siku 14. Pia mtoa leseni, Kamishna wa Madini kwenye ofisi zetu, anatoa leseni ndani ya siku nyingine 28.
Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, nachukua nafasi hii kusema tu kwamba ni kweli kabisa upatikanaji wa leseni kwa utaratibu wa awali umekuwa ukitumika hivyo.
Hata hivyo, mwaka 2015 tumerekebisha Sheria ya Madini ya 2010, tumeingiza sasa kifungu cha waombaji kuomba leseni kwa kielektroniki, kwa kutumia mtandao. Kwa hiyo, unajaza fomu siku hiyo hiyo, unawasilisha fomu siku hiyo hiyo kwa njia ya mtandao na baada ya siku 28 unapata leseni. Kwa hiyo, nawaombe sana wachimbaji wa vijijini pia wanaweza wakatumia utaratibu huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine tumeboresha leseni kwa kuwegesha karibu na Ofisi za Madini kwenye Kanda zote. Sasa hivi karibu kila mkoa una ofisi tatu au nne za Madini. Kwa hiyo, nashauri basi, ili kupunguza mlolongo wa kuchelewa kupatikana kwa leseni, wananchi walio karibu na Ofisi zetu waende kwenye ofisi zetu ili waombe leseni na kuhudumiwa mapema iwezekanavyo.
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza maswali mawili ya nyongeza;
Swali langu la kwanza ninataka tu nipate ufafanuzi kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri, hii project ya Road to Independence, nimepitia bajeti zote za Wizara ya Ulinzi, nimepitia bajeti ya Wizara ya Utamaduni, sijajua kama anaweza akaweleza wananchi wa Nachingwea ni kipindi gani haswa inaenda kutekelezwa hii program ili tuweze kujua kwa sababu miundombinu ya eneo lile bado inaendelea kuharibika mpaka sasa hivi tunavyozungumza, ikiwemo eneo ambalo ameisha Mheshimiwa Samora Machel.
Swali la pili ambalo ninapenda kuuliza, ni nini kazi za Mabalozi wetu katika nchi hizi ambazo zilinufaika na maeneo haya, ukienda Msumbiji leo hii kuna Chuo Kikuu kinaitwa Nachingwea University kinapatikana pale Msumbiji. Je, hawaoni umuhimu wa kushirikisha Balozi zetu na nchi zilizohusika kuweza kusaidia maeneo haya ili kuweza kuweka kumbukumbu za Viongozi ambao waliishi katika maeneo haya? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza nitatoa utangulizi kwamba historia ya ukombozi wa Bara la Afrika haiwezi kutenganishwa na ushiriki mahiri na wa kujitoa wa nchi yetu Tanzania. Haiwezi kutenganishwa na uwepo wa Viongozi mashuhuri kama Mwalimu Julius Kambarage Nyerere lakini pia na Viongozi wengine wa Bara la Afrika kama kina Nkwame Nkurumah na hao wapiganaji wenyewe wakina Samora Machel wakina Robert Mugabe na wengine. Kwa maana hiyo, hii historia japokuwa ni chungu na japokuwa ni ngumu hatuna sababu ya kusema tunaweza tukadharau kutunza maeneo ambayo historia hiyo inayathamini, kwa maana hiyo eneo hili la Nachingwea ambalo Mheshimiwa Mbunge analizungumzia litapewa kipaumbele kwenye program hiyo ya Road to Independence ambayo nimeizungumzia hapa. Program hii kama anavyosema kwenye bajeti haionekani, naomba mimi na yeye tushirikiane kwa pamoja baada ya kikao hiki cha Bunge kufanya utafiti kwenye vitabu vya bajeti ili tuone ni wapi haswa bajeti hii ya Road to Independence inapatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, inawezekana usiwe mradi ambao unatokana na bajeti ya ndani ukawa ni mradi ambao pengine una ushirika wa hawa wabia anaowasema wakiwemo wafadhili wa maendeleo ama Vyuo Vikuu ambavyo vinapenda kufuatilia historia ya ukombozi wa Bara la Afrika.
Swali la pili, kwamba hatuoni kama Balozi zetu zinaweza zikashirika nchi hizo, Tanzania tulikuwa na jukumu kubwa tu ambao tulijitolea kulibeba la kutafuta ukombozi wa Bara la Afrika na kuwapa nyumba na makazi, mafunzo, chakula na malazi zaidi ya wapiganaji kutoka nchi zaidi ya 12 za Afrika zilizokuwa zinapambana na ukoloni na kwa maana hiyo, hiyo ni heshima ya kipekee ambayo sisi tuliipata kupata wapiganaji wa ukombozi kwenye nchi zao kuja kukaa katika nchi yetu. Heshima hiyo tunaendelea kuipata leo na mwaka jana Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitunukiwa heshima ya kipekee pale AU kwa kupewa jengo la Peace and Security katika Mkutano wa Marais wa Afrika na hivi tunavyoongea hapa katika watu watatu mashuhuri wa Bara la Afrika ambao wanatambuliwa na wamewekewa alama za kipekee pale Addis Abba kwenye Makao Makuu ya AU ni pamoja na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, wengine wakiwa ni Nkwame Nkurumah na mwingine akiwa ni Nelson Mandela.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo, Tanzania itaendelea kuwapokea na kuwapa ushirikiano wapiganaji wote ambao wanapenda kuja Tanzania kwenye maeneo waliyowahi kuishi kama vile kufanya hija na kukumbukia siku ambazo walikuwepo hapa nchini wakipigania uhuru wa nchi zao, ambazo sasa zimekuwa huru.
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika majibu ya msingi ya Mheshimiwa Waziri hayajaonyesha ni muda gani ambao pesa inayotafutwa na Serikali itapatikana. Naomba sasa atoe ufafanuzi wa kutosha ili wananchi wa Nachingwea waweze kujua pesa hii ambayo kimsingi inatakiwa ikae kwenye bajeti, ni wakati gani au ni muda gani ili iwe ni rahisi kwangu kufuatilia kujua barabara hii itajengwa lini ukizingatia upembuzi yakinifu ilishafanyika?
Swali la pili, Mheshimiwa Waziri, naomba nipate vigezo vinavyotumika vya ku-allocate pesa katika barabara zetu kwa kiwango cha lami na ukizingatia barabara ya Nachingwea ni barabara kongwe na ya muda mrefu lakini bado haijatengewa pesa kwa muda huu wote ambao tulitazamia tayari itakuwa imepata pesa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu katika swali la msingi fedha tunatafuta na tunaposema tunatafuta ni kweli tunatafuta. Kwa hiyo, kumjibu ni lini ujenzi utaanza au hizo fedha zitapatika, nafahamu juhudi zake, ameshakuja Wizarani kuhusu hiyo na kwa sababu ya juhudi zake, tumeshatenga shilingi bilioni moja fedha za ndani kwa ajili ya kuanza maandalizi ya kujenga hiyo barabara kwa maana ya kuandaa documents. Natambua jinsi anavyokerwa na barabara hiyo, na mimi ninamhakikishia mara tutakapopata fedha tutamjulisha lini tutaanza kujenga.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu vigezo, ninamuomba Mheshimiwa Mbunge, atambue kwamba kitu cha kwanza kigezo chetu kikubwa ni Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi na katika kitabu kile cha Ilani, kuna barabara zote ambazo tumeahidi tutazijenga, tumeziweka mle ndani. Kwa hiyo, kigezo kikubwa ni hicho, lakini vilevile ahadi za viongozi wetu Wakuu kuanzia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyepita wa Serikali ya Awamu ya Nne na huyu wa Serikali ya Awamu ya Tano, pamoja na viongozi wengine akiwemo Makamu wa Rais. Hivyo ndivyo vigezo tunavyovitumia katika kupanga barabara ipi ishughulikiwe na kwa wakati gani.
Mheshimiwa Naibu Spika, akitaka maelezo zaidi, namkaribisha Mheshimiwa Mbunge aje ofisini, akutane na watalaam ili tuweze kulichakata hilo na likafahamika kwa undani zaidi.
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Pamoja na majibu hayo naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Serikali ina mpango gani wa kukamilisha ujenzi wa masjala za ardhi ambazo zimejengwa katika Vijiji vya Nakalonji, Mbondo, Namatunu pamoja na Nahimba hizo ambazo zilikuwa zinadhaminiwa na watu wa MKURABITA. Maana ni muda mrefu toka zimeachwa mpaka sasa hivi zinataka kupotea?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili nataka nijue, ni nini mantiki ya Serikali kuanzisha Vijiji vya mfano; kwa mfano hivyo vijiji vinne ambavyo nimevitaja ambavyo jukumu hili limeachwa mikononi mwa Halmashauri wakati wanajua Halmashauri zetu hazina uwezo au hazina uchumi wa kutosha kuweza kugharamia kukamilisha hizi hati ambazo mpaka sasa hivi zimesimama na wananchi bado hawajapata?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza alitaka kujua ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa masjala kwa ajili ya kuhifadhia hizo hati miliki za kimila. Kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, kwa sasa Halmashauri inafanya juhudi za kutenga bajeti kila mwaka ili kuweza kukamilisha zoezi hilo. Siyo kujenga tu masjala pia kuna hati 1,170 kama nilivyosema ambazo ziliachwa zilikuwa hazijakamilika kutoka katika hivyo Vijiji vya Mbondo, Nakalonji pamoja na Nahimba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, pale ambapo watakuwa wametenga fedha ya kutosha kuweza kukamilisha, basi zoezi hili la kujenga masjala na kukamilisha zile hati miliki za kimila ambazo ziliachwa na MKURABITA zitakamilika. Hili ni jukumu pia la Halmashauri wenyewe kuhakikisha kwamba zoezi hili linakwisha, kwa sababu lilikuwa limeshaanza vizuri lakini baadaye likaishia katikati.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili anasema nini mantiki ya kuanzishwa vijiji vya mfano katika hili. Mheshimiwa Mbunge labda naomba tu tuelewane kwamba zoezi hili linapofanyika lengo lake kubwa pia ni kuhakikisha kuwa wananchi wanakuwa na maeneo ambayo yapo kiusalama zaidi. Usalama wenyewe ni pale ambapo unakuwa tayari umeshapimiwa eneo lako vizuri, unayo hati yako ya kimila ya kumiliki, hapo tayari unakuwa na uhakika wa eneo lile kuwa nalo salama. Taasisi hizi ambazo pengine zilikuwa zikisaidia zilishindwa kukamilisha malengo hayo na kuona kama vile mradi ule haukuwa mazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia mradi huu ulikumbana na changamoto za ukosefu wa fedha. Lengo la Serikali ni kuhakikisha tunakuwa na Miji iliyo salama lakini miji ambayo pia imepangika. Kikubwa zaidi ni kumwezesha yule mwananchi kumiliki hati yake ya kimila ambayo itamsaidia, hawezi tu kuwa nayo kama hana pia mahali pa kuhifadhia, haya yote yanakwenda katika utaratibu huo wa pamoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba lengo la Serikali kuanzisha Vijiji vya mfano ni la msingi na zuri, tunaendelea nalo na ndiyo maana sasa tunazitaka Halmashauri ambazo zilikuwa na huo mradi katika ile miradi ambayo haikwisha, basi waendelee kuweka pesa kidogo kidogo wakamilishe ili kuweza kufikia ile azma ya Serikali ya kuwa na usalama wa milki kwa watu wetu.
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Katika Wilaya ya Nachingwea tuna jumla ya Tarafa tano. Tarafa nne tayari zimeshafanikiwa kuwa na mitandao ya simu, lakini Tarafa moja ya Kilimarondo mpaka sasa hivi bado hamna mawasiliano ya uhakika na wako watu wa TTCL wameshafunga mitandao yao katika maeneo ya Kata ya Mbondo, Kegei pamoja na Kilimarondo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka leo ninapozungumza ni mwaka wa tatu sasa, bado hawajawasha mitambo yao kwa ajili ya kutoa huduma. Naomba kuuliza swali. Nini mkakati wa Serikali juu ya kuhakikisha maeneo haya yanapata mawasiliano ya uhakika?
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa namna anavyotupa moyo kuhusu uwekezaji uliofanywa na TTCL katika maeneo ya Jimbo lake. Namhakikishia kwamba kuanzia mwezi Septemba, TTCL itafanya mambo makubwa na nitahakikisha katika mambo haya makubwa yatakayofanywa kuanzia Septemba, 2016, eneo hili la Nachingwea ambapo tayari minara imeshajengwa litapewa kipaumbele.
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, lakini pia naomba nitoe pongezi kwa majibu haya ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Sambamba na haya, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa sababu Nachingwea tayari tumeshatenga maeneo na kupitia fedha ya Halmashauri peke yake kwa hizi 5% haiwezi kutosha kuwafikia vijana wengi, sijajua Serikali inatuambia nini ili tuweze kuona namna gani tunaweza kunufaika na fedha zinazotolewa na Mifuko ya Vijana kupitia Taifa badala ya kuachia Halmashauri peke yake?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali la pili, naomba nipate majibu juu ya jitihada gani ambazo zinafanywa kwa vijana wa Mikoa ya Lindi na Mtwara ukizingatia ziko baadhi ya Kanda tayari wameshaanza kuwasogezea huduma za kuwafungulia milango ya kupata ajira ikiwemo Kanda ya Ziwa, vijana wengi wanatakiwa waende kule kwa ajili ya kujiunga na vikundi vya kushona viatu. Lindi na Mtwara tunavyo Vyuo vya VETA, nini kauli ya Serikali juu ya vijana wa kanda hii na hasa vijana wanaotoka Nachingwea ambao hawana chuo cha namna hii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza amesema kwamba, tayari wameshatenga maeneo kwa ajili ya shughuli za vijana na nichukue fursa hii kwanza kabisa kuipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea kwa sababu mwaka 2014 Wakuu wa Mikoa wote walikutana hapa Dodoma na likawekwa Azimio la kuhakikisha kila Halmashauri nchi nzima inatenga maeneo maalum kwa ajili ya shughuli za vijana ambayo tuliyapa jina la Youth Special Economic Zones. Mpaka sasa hivi ninavyozungumza tayari zimeshatengwa ekari 86,000 nchi nzima na Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea nayo ni mojawapo. Kwa hiyo, niwapongeze kwa hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali lake la msingi ni kwamba fedha ya Halmashauri haitoshi, ni kweli! Nataka nikiri kwamba fedha ile haiwezi kukidhi mahitaji. Hata hivyo, tunao Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ambao umetoa mwongozo wa kukopesha SACCOS za vijana katika kila Halmashauri. Nimwombe Mheshimiwa Mbunge awaandae vijana wake, tushirikiane kwa pamoja, wabuni miradi, walete maombi kupitia mfuko ule tumekuwa tukitoa fedha kusaidia vikundi mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyozungumza tumeshakopesha takriban Sh.1,700,000,000 kwa vikundi mbalimbali nchini Tanzania. Ushahidi wa dhahiri kabisa ni katika Mkoa wa Simiyu chini ya uongozi wa Mkuu wa Mkoa wa Mheshimiwa Anthony Mtaka, tumekabidhi fedha kwa vikundi viwili vya kutengeneza chaki na maziwa katika Wilaya ya Maswa na Meatu, takriban Sh. 30,000,000 kwa kila kikundi. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge afanye jitihada hizo, sisi tutakuwa tayari kumuunga mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili anasema ni jitihada gani Serikali imezionesha katika Mikoa ya Lindi na Mtwara. Mheshimiwa Mbunge ni kweli, kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu tuna programu nyingi sana za vijana na sasa hivi tumetangaza programu ya vijana kwenda kupata mafunzo ya kutengeneza viatu na bidhaa za ngozi kule Mwanza lakini siyo kweli kwamba mikoa hii tumeisahau. Mwaka jana tumekuwa na programu kubwa sana katika Mikoa mitano ikiwemo Lindi na Mtwara ambapo tuliwafikia vijana takriban 9,100 kupitia programu inayoitwa Youth Economic Empowerment na mpaka ninavyozungumza hivi sasa vijana wengi wa Lindi na Mtwara walipata mafunzo kupitia VETA na sasa hivi wamejiajiri na wameajiri na vijana wengine. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kupanua wigo wa programu zetu ili ziweze kufika nchi nzima na vijana wote waweze kunufaika.
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini sambamba na hayo naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ya Masasi – Nachingwea – Nanganga inahudumia Wilaya tatu, hivyo umuhimu wake katika mkoa na Taifa unafahamika sana kiuchumi. Majibu aliyoyatoa Mheshimiwa Waziri, naomba niyapokee kwa sababu kwanza wameonesha utashi wa kutenga shilingi bilioni tatu, lakini nilikuwa nataka nijue, kwa urefu wa barabara ile ambao tayari umeshafanyiwa upembuzi yakinifu kilometa 97, kwa kutenga shilingi bilioni tatu ambazo haziwezi kujenga hata kilometa zisizozidi 10, ni nini nia ya Wizara juu ya ujenzi wa barabara hii ambayo imekuwa kero kubwa kwa wananchi wa Mkoa wa Lindi na Wilaya ya Nachingwea kwa ujumla?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, naomba kujua pia kupitia Naibu Waziri, upembuzi yakinifu ambao ulifanyika toka mwaka 2016 uwe umekamilika, umehusisha nyumba za wakazi ambao wamesimamisha shughuli zao. Nilikuwa nataka nijue, katika kiasi hiki cha fedha shilingi bilioni tatu, kinahusisha pia fidia kwa wale wananchi ambao wanapaswa kulipwa ili waweze kupisha ujenzi wa hii barabara? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MWASILIANO:
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina nia ya dhati ya kutaka kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami na ndiyo maana imeshatekeleza hatua ya kwanza muhimu sana ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Kwa nini tumetenga fedha kidogo; kwanza hatujatenga; tunaomba tutengewe fedha kidogo siyo kwa sababu ya kutokuwa na dhamira ya dhati, bali ni kwa sababu ya fedha ambazo Wizara nzima inatarajia kuomba kutengewa imepungua sana ukilinganisha na mwaka uliopita. Kwa hiyo, tutagawana haka kasungura kadogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaanza mwaka huo ujao na miaka inayofuata tutaendelea kukamilisha na hatimaye tutakamilisha hiyo barabara kuijenga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili, naomba nimhakikishie kwamba tunapoanza kujenga na tunapotenga fedha kwa ajili ya ujenzi, inahusisha vilevile na fidia ya maeneo yale ambayo tutajenga katika mwaka huo wa fedha.
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Naomba kupata kauli ya Serikali juu ya zoezi linaloendelea la ugawaji wa pembejeo kwa mikoa ya Lindi na Mtwara hasa kwa sulphur. Mpaka sasa hivi idadi ya sulphur ambayo wamepelekewa wakulima wetu ni kiasi kidogo sana ukilinganisha na mahitaji. Naomba kupata kauli ili tuweze kujua tunawasaidiaje wakulima wa zao la korosho tusiweze kuathiri zao hili ambalo tumekwishaanza kufanya vizuri?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, hili litakuwa fupi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu sulphur, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba sulphur kwa sasa inaonekana kwamba kuna upungufu kwa sababu sulphur hatujaagiza kwa wakati mmoja. Kwa hiyo, tunawaomba Waheshimiwa Wabunge wawaeleze wakulima wao kwamba sulphur ambayo imepatikana sasa wachukue kwa kiwango kilichopatikana, lakini sulphur nyingine iko njiani. Tuliagiza tani 9,000 lakini sulphur nyingine iko njiani.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile niwafahamishe kwamba wanaopata sulphur ni wale walioshiriki katika Mfumo wetu wa Stakabadhi Ghalani, maana yake waliouza korosho msimu uliopita kupitia Vyama vya Ushirika. Kama kuna mtu aliuza kupitia choma choma, maana yake hawezi kuingia katika mfumo rasmi, hatatambuliwa na hatapata sulphur. Kwa hiyo, sulphur iko njiani.
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Naomba kwanza nitambue jitihada ambazo Serikali imefanya kwa kuona umuhimu wa kufufua viwanda hivi Naomba niulize maswali yafuatayo.
Mheshimiwa Spika, mkataba umesainiwa Machi, 2017 na tunategemea kufanya uzalishaji mwezi Septemba mwaka huu, takribani itakuwa miezi tisa. Naomba nifahamu kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, mpaka sasa hivi taarifa nilizonazo ndani ya kiwanda kile kuna mashine zisizopungua 30 zimeshawekwa na mashine hizi ni za manual (za mikono). Sasa nataka nijue mashine hizi ni hii Kampuni ya Sunshine ambayo imeingia mkataba au ni watu wengine ambao wamezileta hizi mashine? Muhimu nilikuwa nataka nijue ambao watu wa Nachingwea wanaufanya.
Mheshimiwa Spika, lakini swali lingine sambamba na hilo, nataka nipate majibu kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, majengo ya kiwanda kile cha korosho mpaka sasa hivi yako chini ya Lindi Pharmacy na yanatumika kama maghala ya kuhifadhia korosho. Je, kiwanda hiki ambacho Wachina wamefanya mkataba nacho ni kiwanda gani ambacho kinaenda kujengwa na kinaenda kujengwa maeneo gani?Au ni majengo yale yale yatatumika?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, napenda nikiri, maswali aliyoniuliza ni undani wa MOU na mimi sijaisoma. Kwa hiyo, nitakwenda kwenye MOU niweze kujua undani wa nani anamiliki nini na nani atapata nini.
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ambayo ameyatoa Mheshimiwa Naibu Waziri, nilikuwa naomba kupata ufafanuzi katika maeneo mawili yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika, ni takribani miezi minne sasa imepita toka Mkataba wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu usainiwe pale Chinongwe, lakini mpaka leo nazungumza, pamoja na majibu aliyoyatoa, kazi kubwa iliyofanyika ni kuweka tu vijiti. Sasa nilikuwa nataka kujua Serikali imekwama wapi kutoa fedha mpaka sasa hivi kwa ajili ya kuanza kazi hii ya kusambaza umeme vijijini?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, nilikuwa naomba nimuulize Naibu Waziri, pamoja na ujenzi wa kituo cha kupoza umeme pale Mahumbika ambacho tuliamini kingekuwa ni tiba kwa tatizo la kukatika umeme kwa Mkoa wa Lindi na Mtwara. Ni jitihada gani za makusudi au za dharura ambazo Serikali itakwenda kuchukua, ili kuwaondoa wananchi wa Mkoa wa Lindi na Mtwara gizani, ukizingatia maagizo ya kufunga mashine yalishatolewa na Mheshimiwa Waziri alipofanya ziara Mkoani Mtwara na aliwapa siku kumi, mpaka leo bado hakuna kilichotekelezwa, naomba kufahamu nini kinaendelea?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, mpaka sasa ni kweli wakandarasi wa REA walishaanza kazi kama anavyosema miezi minne iliyopita na ninaomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge pamoja n Bunge lako Mamlaka ya Umeme Vijijini (REA) wameshalipa kiasi cha takribani bilioni 28 kwa wakandarasi wote kama advance. Nimeongea pia na Mkandarasi wa Mkoa wa Lindi ambaye ni State Grid, yupo anafanya kazi na alikuwa katika Wilaya ya Ruangwa na kati ya vijiji 34 alikuwa amevifikia vijiji 19 mpaka jana na akitoka Ruangwa ataelekea Wilaya ya Nachingwea. Nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kweli Serikali imedhamiria kabisa kwamba vijiji vyote vilivyosalia na kwa awamu hii ya kwanza ni vijiji 3,559 mpaka 2019 umeme vitakuwa vimepeta.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili aliuliza namna gani Serikali inachukua jitihada kumaliza tatizo la umeme Mikoa ya Mtwara na Lindi. Naomba nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge, mkandarasi anayefanya matengenezo ya mashine tisa za kuzalisha umeme Mkoa wa Mtwara ameanza hizo kazi. Vipuri vimewasili kama ambavyo Mheshimiwa Waziri alielekeza na kazi inaendelea. Na mpaka jana mashine sita zenye uwezo wa kuzalisha megawati 12 zilikuwa zinafanya kazi, lakini pia Serikali imechukua hatua imeagiza mashine mbili mpya kwa ajili ya kuzalisha megawati nne kwa thamani ya bilioni nane ambazo zitafika mwakani mwezi wa tatu na zitakuwa zimefungwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo pia Serikali kupitia TANESCO inafanya matengenezo ya mtambo wa kuzalisha umeme Somangafungu ambao unazalisha megawati 7.5. Tuna uhakika, naomba niwathibitishie wakazi wa Mkoa wa Mtwara na Lindi itakapofika Disemba, 31 hali ya upatikanaji umeme Mtwara na Lindi itaboreka. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kunipa nafasi ya kuweza kuuliza swali la nyongeza. Katika moja ya masharti ya mkataba uliosainiwa kati ya Kampuni ya Sunshine na wamiliki wa ghala la Lindi Pharmacy ambayo kilikuwa Kiwanda cha Korosho Wilayani Nachingwea ilikuwa ni kuanza kufanya kazi Septemba, 2017. Lakini mpaka sasa ninapozungumza kiwanda kile hakijaanza kufanya kazi, naomba kupata majibu ya Serikali juu hatma ya kiwanda cha korosho Nachingwea.
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwanza nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia na niseme tu kwamba lengo letu ni kuhakikisha kwamba Mikataba inayokuwa imeingiwa inafanya kazi yake inavyostahili. Lakini kwa sababu suala hili limekuwa ni very specific kwa Kiwanda cha Sunshine na mimi maishani mwangu sipendi kutoa majibu ya kukurupuka au ya uongo, nitalifanyia kazi na nitakuletea taarifa inayostahili.
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza:
Swali la kwanza, kwa sababu mradi huu unagusa Wilaya zaidi ya tatu, Wilaya ya Nachingwea, Wilaya ya Ruangwa pamoja na Wilaya ya Masasi, kiasi cha pesa ambacho kimetengwa ni shilingi bilioni moja. Mheshimiwa Waziri anaweza kuwa tayari kunitajia ni vijiji gani ambavyo vitaanza katika awamu hii ambayo imetengewa bilioni moja, hasa vile vinavyogusa Wilaya ya Nachingwea?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ningependa kujua, mwezi Februari mwaka huu Mheshimiwa Naibu Waziri tulifuatana mimi na yeye ndani ya Wilaya ya Nachingwea kwenda kukagua miradi ya maji ya Chiola, Nampemba pamoja na maeneo ya Mkoka. Miradi ile bado haijakamilika na yako mambo ambayo yamefanyika ambayo siyo mazuri, alituahidi ataleta wataalamu kwa ajili ya kuja kufanya uchunguzi ili tuweze kuchukua hatua za kisheria kwa hujuma iliyofanyika kwenye miradi ile.
Je, Mheshimiwa Waziri anatoa jibu gani kwa Wananchi wa maeneo haya ambayo nimeyataja ambao wanasubiri majibu yake?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa naibu Spika, swali la kwanza, ameuliza katika hii shilingi bilioni moja tuliyoitenga ni vijiji gani katika Wilaya ya Nachingwea ambavyo vitahudumiwa na hii fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna vijiji ambavyo vilikosa maji katika awamu iliyopita ikiwemo Kitandi Nakalonji, Mkotokuyana, tutahakikisha kwamba hivi vijiji katika hii fedha ambayo imetengwa mwaka wa fedha huu tunaouanza tarehe Mosi Julai, tuhakikishe kwamba vijiji hivi pia vinapitiwa. Pia, Mheshimiwa Mbunge atusaidie kuwasiliana na mamlaka ya maji safi MANAWASA ili wakasaidine pia kupanga vijiji vingine zaidi ambavyo vinaweza vikapitiwa na fedha hizi kupitia huu mradi wa maji wa Mbwinji.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kweli nilitembelea Masasi Mkoa wa Mtwara na kwenda kujionea hii miradi ukiwemo mradi wa Chiola ambao nilikuta utekelezaji wake kidogo ulikuwa na mtatizo, baada ya kurudi niliwasilisha taarifa niliyoikuta kwa Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Waziri tayarai alishatoa maelekezo kwa uongozi wa Wizara ili kuunda timu kwenda kuangalia nini kilichojitokeza katika ule mradi na kuhakikisha kwamba uboreshaji unafanyika ili wananchi wa Chiola waweze kupata huduma ya mamji safi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, tumeelekeza kwamba miradi ile ambayo haikukamilika katika awamu ya kwanza, basi Halmashauri kwenye fedha tulizotenga katika Wilaya zihakikishe kwamba zinakamilisha ile miradi ambayo haikukamilika kabla hatujaingia kwenye miradi mipya.
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kazi iliyofanyika Masasi ya kuchimba mitaro, kazi hiyo iliyofanyika pia katika Wilaya ya Nachingwea katika Kata za Naipanga, Chiwindi, Rahaleo, Mkotokweana pamoja na Stesheni. Kupitia nguvu za Mbunge na wananchi tumechimba zaidi ya kilometa 15. Sasa fedha iliyoletwa ni chache na sasa hivi ni mwezi, mabomba yaliyoletwa kwa ajili ya mradi huu yameshindwa kukidhi mahitaji ya mradi mzima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kupata jibu la Mheshimiwa Waziri, ili nguvukazi za wananchi zilizotumika zisipotee, ni lini fedha hii ambayo imeombwa kwa ajili ya mradi huu italetwa ili tuweze kukamilisha kazi ambayo tumeianza? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naye nimpongeze kama ameweza kuhamasisha wananchi kuchimba mtaro wa kilometa 15 ili iwe kazi rahisi kwetu sisi kuweka mabomba. Tayari mabomba mengi yameshapelekwa, yapo Masasi na Nachingwea kwa ajili ya kuyalaza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la fedha, fedha tunazipeleka kulingana na namna tunavyopokea. Kwa hiyo, fedha za Mfuko wa Maji zinazokuja kwa mwezi ni kama shilingi bilioni kumi. Kwa hiyo, hizi ndizo tunazogawana kuwapelekea kila Halmashauri, pale ambapo inaonekana kuna kazi inayoendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kazi ambayo imeanza haitaachwa, tutapeleka hiyo fedha mapema iwezekanavyo.
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Moja ya matatizo makubwa makubwa ambayo tumekabiliana nayo kwa wananchi wanaozunguka Kambi ya Maji Maji kikosi Namba 41 na kikosi cha JKT katika Kata ya Mchonda ni tatizo ya migogoro ya ardhi, na tatizo hili tayari tumesharipoti kwa watu wa Wizara.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kufahamu msimamo wa Serikali au Wizara juu ya fidia ambazo wameahidi kuwalipa wananchi wale ili waweze kuachia yale maeneo?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kuna Kambi nyingi ambazo zina migogoro ya ardhi. Kama ninavyosema mara kwa mara hapa migogoro hii iko ya aina nyingi, kuna migogoro ambayo Jeshi limechukua ardhi lakini wananchi bado hawajalipwa fidia, yapo maeneo ambayo wananchi wamevamia Kambi za Jeshi na na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachoweza kusema hapa ni kwamba tumeweka fedha kwenye bajeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ili kwa yale maeneo ambayo fidia zinahitajika tuweze kulipa ili kumaliza migogoro hii, mwaka wa bajeti haujaisha na nimategemeo yetu kwamba fedha hizo zikipatikana tutatoa fidia kwa wale ambao wanastahili kupewa fidia maana wako wengine ambao wao wamevamia kambi za Jeshi hao hawatalipwa fidia. (Makofi)
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba nichukue nafasi hii kumwuliza swali dogo Mheshimiwa Naibu Waziri; ni nini kauli ya Serikali juu ya kuanza kwa ujenzi wa barabara ya Masasi - Nachingwea - Nanganga?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, kauli ya Serikali ni kwamba pesa inatafutwa, kwa sababu hatua za awali za ujenzi wa kipande hicho cha barabara zilishaandaliwa na zinatekelezwa. Pesa itakapopatikana, barabara hiyo itaingizwa kwenye mpango ianze kutengenezwa kwa kiwango cha lami.
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Spika, naomba nishukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini pamoja na hayo naomba nitumie nafasi hii kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, ni muda mrefu sasa toka fedha hii shilingi bilioni moja itengwe na barabara ambayo imetajwa imefanyiwa sehemu tu ya matengenezo naomba kupata kauli ya Serikali, hizi kilometa 12 zilizobaki ni wakati gani zitamaliziwa kwa fedha ambayo imetengwa?
Swali la pili, naomba kuuliza Serikali imekuwa na kipaumbele cha kuunganisha barabara za Mikoa kama ambavyo jibu la msingi linavyojieleza. Nini mpango wa Serikali wa kukamilisha au kuanza ujenzi wa barabara ya lami kutoka Masasi kwenda Nachingwea, Nachingwea kwenda Nanganga ikiwa ni ahadi ambayo imetolewa kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO:
Mheshimiwa Spika, ni kweli kuna kiasi cha fedha kilitengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii na ilikuwa ni mkakati wa Serikali kulipa madeni. Katika kipindi hiki hadi Desemba Serikali ime-clear madeni kwa makandarasi zaidi ya shilingi trilioni 1.385 kwa maana hiyo hii ni fursa inatosha sasa kuanza kuendelea kutoa sasa mikataba kwa ajili ya ujenzi wa barabara. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge hizi kilometa 12 zitatangazwa na kuanza kutengenezwa wakati wowote.
Mheshimiwa Spika, pia niseme tu ni mpango wa Serikali kuunganisha Mikoa kama nilivyojibu katika jibu la msingi na Mheshimiwa Mwalimu Masala unakumbuka kwamba katika mpango ambao unaendelea kwa ajili ya ujenzi wa barabara kile kipande cha Nachingwea kwenda Nanganga kilometa 46 kitatangazwa wakati wowote, kipo kipande kingine cha Nachingwea - Ruangwa kilometa 45, lakini kuna kipande cha Ruangwa - Nanganga kilometa 58. Pia unatambua kwamba kuna ujenzi wa daraja kule kwenye Mto Lukuledi hii ni dhamira ya Serikali kuweza kuunganisha maeneo haya.
Mheshimiwa Spika, baada ya eneo hili kuwa limekamilishwa itakuwa ni sehemu ya kuunganisha Mkoa wa Lindi na Mkoa wa Ruvuma kwa maana kuwa unatambua kwamba ukitokea Nachingwea kwenda Kilimarondo utakuwa unaelekea kule Mindu upande wa Tunduru tutakuwa tunaunganika na wenzetu wa upande wa Ruvuma. Upande wa Morogoro pia kilometa 129 ukitokea Nachingwea kuelekea Liwale naona Mheshimiwa Kuchauka ananitazama hapa ni kwamba barabara hii sasa tutakapokuja kuanza kutengeneza itakuwa ni sehemu ya barabara ya kuunganisha upande wa Lindi kuelekea Mahenge kule Morogoro.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge nikuombe tu uvute subira ni mpango mzuri wa Serikali kuhakikisha kwamba tunaweza kutengeneza barabara hizi kuunganisha Mikoa na hii itatupa fursa sasa ya kuunganisha barabara ambazo zinakwenda kwenye Wilaya. Kwa hiyo tuvute subira na wananchi wajue Serikali inafanya kazi kubwa kulipa madeni na kutengeneza barabara kwa kiwango cha lami. (Makofi)
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, pamoja na wananchi hao ambao Mheshimiwa Waziri anakiri kwamba hawajalipwa fidia na anakiri kwamba wakati maeneo haya vikosi wanayatwaa hawajalipwa chochote bado vikosi vyetu vimeendelea kuwafukuza wananchi hawa wasifanye shughuli zozote ikiwemo kuokota korosho zao kwa wale ambao walishapanda mikorosho.
Naomba kupata kauli ya Serikali juu hatma ya watu hawa wakati wanaendelea kutengewa hii bajeti ambayo Mheshimiwa Waziri ameisema ili waweze kuendelea kufanya shughuli zao? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili Mheshimiwa Waziri naomba kupata commitment ya Serikali kwa sababu tatizo ni la muda mrefu na Tume nyingi zimeshaundwa na tayari zilishaleta majibu ya kukiri kwamba kuna tatizo.
Ni lini Serikali sasa itaenda kufanya hili zoezi ili tatizo hili liondoke na wananchi wale waweze kujua hatma yao? (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Spika, lazima tukiri kwamba tatizo kubwa limekuwa ni upungufu wa bajeti na kwa maana hiyo kupelekea wananchi wanaostahili kulipwa fidia kuchelewa. Hata hivyo, kulikuwa kuna maamuzi ya makusudi ya kuzuia wananchi kufanya shughuli za kibinadamu katika makambi haya. Sababu kubwa ya maamuzi hayo ni kwamba katika baadhi makambi haya kuna silaha na kuna milipuko ambayo inaweza kuleta athari kwa wananchi na ndiyo sababu wakakatazwa kufanya shughuli za kibinadamu.
Lakini ukiacha tatizo hilo, wapo wananchi ambao wakipewa ruhusa ya kufanya hivyo basi wanafanya maendelezo makubwa, wengine wanajenga hata nyumba ambayo inapelekea uthamini na fidia zao kuwa kubwa mno. Hizo ndiyo sababu zilizopelekea wakazuiwa kufanya shughuli zote za kibinadamu ili kwanza wasidhurike lakini pili wasiendeleze maeneo hayo kwa sababu yatapelekea fidia kuongezeka.
Mheshimiwa Spika, kuhusu commitment ya Serikali kwamba ni lini zoezi hili litakamilika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakapokuwa tumepokea fedha hizi kutoka kwenye bajeti yetu jukumu hili litafanyika mara moja ili tuondokane na tatizo hili la muda mrefu. (Makofi)
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninaomba kupata kauli ya Wizara juu ya ubora wa sulphur ambayo safari hii wakulima wetu wa zao la korosho watakwenda kupata. Ukirejea ripoti ya CAG msimu wa mwaka jana sulphur ambayo imesambazwa kwa sehemu kubwa ubora wake ulikuwa na mashaka makubwa sana; naomba Mheshimiwa Waziri atoe kauli, safari hii sulphur iko katika kiwango gani? Ahsante.
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, sulphur ni kiuatilifu kinachotumika kwenye zao la korosho na taratibu za uingizaji wa sulphur hapa nchini ziko kwa mujibu wa sheria. Tunacho chombo chetu cha TPRI cha kuhakiki ubora wa sulphur kabla ya kuruhusu sulphur hiyo kuingia hapa nchini. Kwa hiyo naomba nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara kupitia TPRI inajitahidi kuhakikisha kwamba sulphur inayoingizwa nchini ina ubora unaokubalika.
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kunipa nafasi ya kuweza kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lililopo Kaliua linafanana na maeneo yangu ya Wilaya ya Nachingwea katika Kata za Kilimarondo, Mbondo, Mateko pamoja na Kiegei. Naomba kupata majibu kutoka kwa Mheshimiwa Waziri nini mkakati wao juu ya kutatua tatizo hili.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Masala, DC wangu mstaafu wa Wilaya ya Kibondo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri Mheshimiwa Masala ni mmoja kati ya Waheshimiwa Wabunge ambao wameleta barua zao za maombi ya minara kwa ajili ya mawasiliano kwenye eneo la Nachingwea. Vijiji vyote alivyovitaja, namuahidi kwamba nitakwenda kule na nitakapokuwa nakwenda kule nitamtafuta ili tuwe naye hata kama kuna maeneo mengine ambayo yana changamoto ya mawasiliano tuweze kuyaona na tuyafanyie kazi ili tuhakikishe kwamba inapofika mwishoni mwa mwaka huu Tanzania inawasiliana kwa asilimia 100. (Makofi)
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri, lakini pamoja na majibu hayo naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, nilitaka nijue Serikali imejipanga vipi au imejiandaa vipi? Kwa sababu wakati Kiwanda hiki cha Mafuta Ilulu kinabinafsishwa, kilikuwa na majengo pamoja na mitambo yake, lakini ukaguzi nilioufanya kwa awamu ya mwisho mpaka sasa hivi huyu mwekezaji anatangaza kukirudisha, kiwanda kile hakina mashine hata moja na amesema kwamba anakirudisha. Nini kauli ya Serikali juu ya mashine ambazo zilifungwa katika Kiwanda kile cha Mafuta cha Ilulu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, nilikuwa nataka nijue; kwa sababu Serikali imetoa hisa asilimia 100 kwa wawekezaji kwa ajili ya Kiwanda cha Korosho, ambapo wawekezaji waliopewa ni Sunshine na mashine walizozifunga pale hazioneshi kama zinaweza zikafanya kazi ambayo tunaikusudia. Kwa nini Serikali isichukue angalau asilimia 51 ya hisa zile ili Serikali iweze kupata gawio lake la moja kwa moja badala ya kutegemea mwekezaji? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa upande wa Kiwanda cha Mafuta cha Ilulu ambacho anadai kwamba mashine zake zimeshaondolewa na kiko katika hali mbaya na kinarejeshwa, ndiyo maana tumesema kwamba tutakipokea kufuatana na taratibu za kisheria. Kwa hiyo, tutaangalia masuala yote ya kisheria pale tutakapoona kwamba mwekezaji huyu anabanwa na masharti hayo, basi hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa kiwanda cha korosho, niseme tu kwamba Serikali ilikuwa imeshajitoa katika kufanya shughuli za uwekezaji na hiyo ndiyo sera yetu. Tunachofanya zaidi ni kuwahamasisha wawekezaji, wao ndio wawekeze na mitaji mingi zaidi iweze kufika na kuwekeza katika nchi. Ila tu katika maeneo yale ambayo tunaamini kwamba pengine kwa mwekezaji binafsi ataona hakuna tija, lakini wakati huo kwa upande wa Serikali tunaona kwamba suala hilo lina manufaa makubwa kwa Watanzania au jamii kwa ujumla, ndipo Serikali inapoingilia na kuweza kuona umuhimu wa kuwekeza.
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Wilaya ya Nachingwea ina jumla ya Kata 36 na tayari inakidhi vigezo vya kupata Majimbo mawili ya uchaguzi na taratibu zote tumeshazifuata. Ni lini Wizara ya TAMISEMI itakwenda kuligawanya Jimbo la Nachingwea ili liwe na Majimbo mawili ya uchaguzi? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipata fursa ya kwenda Wilaya ya Nachingwea na Jimbo la Nachingwea, kwa hiyo najua ambacho Mheshimiwa Mbunge anaongelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo taratibu ambazo zinatakiwa zifuatwe ili Jimbo ligawanywe na hii huwa inapelekwa kwenye Tume ya Uchaguzi ndiyo wenye mamlaka ya kugawanya Majimbo na siyo Ofisi ya Rais, TAMISEMI.
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Maeneo ya Mji wa Nachingwea katika Kata za Namatula, Nangwe, Mteruka, pamoja na Kilimanihewa yamekuwa yanapata maji kwa kusuasua sana, lakini wakati huo huo tuna chanzo kikubwa cha maji kinachotokana na chanzo cha maji ya Mbwinji.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujua mpango wa Serikali juu ya kutoa fedha ili kuweza kufanya utanuzi wa kusambaza maji katika maeneo ambayo nimeyataja.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nampongeza Mheshimiwa Mbunge. Nimepata nafasi ya kutembelea katika Jimbo lake, lakini kiukweli katika kuhakikisha tunatatua tatizo la maji, lazima tuangalie namna gani tunaweza tukatumia kile chanzo kikubwa cha Mbwinji. Sisi kama Wizara ya Maji tuko tayari na tumejipanga katika kuhakikisha tunatafuta fedha ili tuweze kutumia chanzo kile cha maji ili wananchi wake waweze kupata maji safi, salama na yenye kuwatosheleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kupata nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahadi ya kutafutwa pesa kwa ajili ya barabara hii ni ahadi ya muda mrefu sana, lakini pia naomba niweke kumbukumbu vizuri kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, zoezi la kufanyia upembuzi yakinifu barabara hii lilikamilika mwaka 2015 wakati mimi naingia kuwa Mbunge na siyo 2008. Sasa naomba kujua, nini dhamira ya Serikali juu ya kutekeleza ahadi yake ya muda mrefu kuhakikisha fedha ndani ya mwaka huu wa bajeti inapatikana ili barabara hii iweze kufanyiwa kazi kwa kiwango cha lami? Hilo ni swali la kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili ambalo naomba nipate majibu, barabara hii kwa mujibu wa nyaraka nilizonazo, mwanzo kabisa wakati inafanyiwa upembuzi yakinifu ilikuwa inasomeka Masasi – Nachingwea – Nanganga, lakini baadaye ikaja kuanza kufanyiwa kazi barabara ya kutoka Nanganga – Ruangwa – Nachingwea. Sasa hivi majibu yanayotoka, kuna kipande cha kilometa 45 cha kutoka Nachingwea kwenda Nanganga hakisemwi na hakionekani katika maelezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujua msimamo wa Wizara juu ya kioande hili cha Nachingwea kwenda Nanganga ambacho ni kilometa 44.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa umakini na ufuatiliaji wa maendeleo ya Nachingwea lakini siyo Nachingwea peke yake, bali pia maeneo ambayo kimsingi yanaunganika na Wilaya hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba kweli usanifu ulikamilika kipindi cha nyuma, lakini kwa jibu ambalo nimelitoa sasa hivi, kwa yale maandalizi ya kuanza ujenzi huwa kuna kitu ambacho tunaita mapitio. Tunafanya review ili tuweze kutangaza ujenzi wa barabara. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Masala kwamba records ambazo nimeziweka hapa kwa maana ya review ilikuwa ni maandalizi sasa ya kuanza ujenzi. Hivi tulikuwa tunafanya mawasiliano na wenzetu wa upande wa Wizara ya Fedha, fedha zikipatikana tunaanza kujenga barabara hii. Kwa hiyo, nimtoe hofu yeye pamoja na wananchi wa Nachingwea na majirani zake, ni kwamba harakati za kufanya ujenzi wa barabara hii tumezifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la (b); kutokana na review ambayo nimeisema hapa imefanyika ili tuanze ujenzi, haimaanishi kipande hiki cha Nachingwea - Nanganga kwamba tunakiacha. Hiki ni vipambele tu kutokana na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimwambie Mheshimiwa Masala kipande cha Nachingwea - Nanganga na chenyewe kiko kwenye mpango na vile vile tuwasiliane baadaye, atakuja kuona kwenye mpango mkakati wetu baada ya review kwamba tumejipanga vipi kuanza kujenga kwa kiwango cha lami. Kwa maana hiyo ni kwamba tukipata fedha tunaanza ujenzi wa barabara hizi muhimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Mheshimiwa Masala ajue kwamba wakati huo tunajiandaa, tunaendelea kushughulikia maeneo ambayo ni korofi, tunaendelea kushughulikia maeneo ambayo ni maalum, tunaendelea kujenga madaraja. Labda kwa manufaa ya wananchi wa Nachingwea niseme kwamba tumeendelea kukamilisha daraja la Lukuledi ambapo barabara niliyoijibia itapita ili tuwaungenishe vizuri wananchi hawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile tunaendelea kujenga maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Lindi, madaraja ya kule Chumo, kuna daraja Mlowoka, Mtakuja na Nanjilinji. Hii ina maana kwamba maeneo ambayo tumeyatengea fedha za kutosha na maeneo ambayo wananchi walikuwa wanapata usumbufu kupita katika maeneo haya tumeyazingatia. Kwa hiyo, wananchi wa Ruangwa, Nachingwea na maeneo yote ya Lindi, ni kwamba tumejipanga ili tuwahudumie vizuri.
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini pamoja na majibu hayo, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri anakiri kabisa kwamba jengo lile halihitaji tu kufanyiwa marekebisho isipokuwa kujengwa; na kuwa kuwa pia tathmini imeshafanyika toka mwaka 2017/2018, kuna sababu gani sasa za kutenga fedha au kulipeleka jengo hili kwenye mpango wa kujengwa 2020/2021 badala ya mwaka 2019/ 2020?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, naomba kujua nini mpango wa Wizara ya Katiba na Sheria katika kuongeza idadi ya watumishi katika Mahakama zetu hasa Mahakama za Mwanzo? Nachingwea tuna kituo pale kinaitwa Ndomoni, kwa muda mrefu sasa kimefungwa na wananchi hawapati huduma pale. Hivyo, wanalazimika kutembea umbali mrefu kwenda Nachingwea Mjini kufuata huduma ya Mahakama.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA): Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mpango wa Mahakama wa Miaka Mitano wa Kuboresha Huduma za Mahakama hapa Nchini, imeweka pia vipaumbele vya ujenzi. Baada ya taratibu zote hizo kukamilika, limetengenezwa jedwali ambalo ndiyo linaipelekea Mahakama hii kuanza kujenga hizi Mahakama.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa pande wa Nachingwea, kwa sababu tathmini ilikuwa inaendelea kufanyika katika jedwali letu, Nachingwea wenyewe ujenzi utaanza katika mwaka wa fedha 2020/2021 hasa kutokana na kwamba ilikuwa lazima taarifa hizo zikamilike na tayari kuna baadhi ya Mahakama ilikuwa imeshaingia katika mpango wa ujenzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge, ni kweli tunatambua changamoto hiyo lakini kwa sasa kwa sababu Wizara tumeingia makubaliano na Baraza la Ujenzi wa Taifa katika ujenzi wa Mahakama kupitia teknolojia mpya na bei nafuu ya Moladi naamini kabisa kwamba pindi fedha itakapopatikana tutaanza ujenzi wa Mahakama ya Nachingwea ili kuwaondolea usumbufu wananchi wa Wilaya ya Nachingwea.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika swali lake la pili la kuhusu watumishi, ni kweli tuna changamoto katika baadhi ya maeneo, lakini nimwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inaendelea kulifanyia kazi kwa maana ya kuajiri watumishi wengine ambapo tunaenda kupata kibali toka utumishi. Kwa hiyo, pindi ajira hizi zitakapotangazwa na kupatikana, pia Wilaya ya Nachingwea itaangaliwa katika kutatua changamoto hii ya ukosefu wa watumishi katika eneo hilo ili wananchi wa Nachingwea waweze kupata huduma za Mahakama kwa ukaribu lakini na kwa ufanisi zaidi.
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza naomba nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake kwa niaba ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza ambalo nilikuwa naomba kujua, kwa sababu kituo hiki cha kanda ambacho kiko 41KJ kinahudumia wananchi wanaotoka maeneo ya Kilimani Hewa, Nampemba, Mtepeche, Mkotokuyana pamoja na Mandai; pamoja na mkakati ambao Serikali imeusema, hebu aniambie ni mkakati gani ambao Wizara wanaweza wakaufanya kwa haraka ili kuhakikisha wataalam wanapatikana katika kituo hiki ili wananchi waendelee kupata huduma pamoja ukarabati ambao tayari umeshafanyika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili ambalo nilikuwa naomba kujua, ni suala hili la ukarabati wa kituo cha karakana ambacho kiko pale kikosi cha mizinga. Vijana wengi wa Nachingwea sasa hivi wanakosa sehemu ambako wanaweza kwenda kuendelea na masomo yao. Karakana hii kwa sasa inachukua idadi ndogo sana ya wanafunzi au wanachuo. Nini mkakati wa Wizara ili kuhakikisha jitihada hizi za kuihamisha hii karakara kuipeleka VETA unafanyika au kutoa fedha kwa ajili ya kununua vifaa na kuongeza wataalam ambao watakwenda kutoa huduma kwa vijana wa Wilaya ya Nachingwea?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza kwa dhati kabisa Mheshimiwa Masala kwa jitihada zake mbalimbali ambazo anachukua katika kuwasaidia wananchi wa Jimboni kwake Nachingwea. Amekuwa akifanya hivyo hata kwa taasisi na vyombo vilivyopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, katika kujibu swali lake, kwanza kwenye eneo la wataalam kama ambavyo nimejibu katika swali langu la msingi, ni kwamba tayari hivi tunavyozungumza kuna madaktari takribani 300 ambao wanaendelea na mafunzo katika chuo chetu cha Monduli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni imani yangu kwamba madaktari wale watakapokuwa wamekamilisha mafunzo yao, basi miongoni mwao tutawapeleka katika hospitali ile iliyopo katika kikosi cha 41KJ, eneo la Nachingwea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la mkakati wa kuboresha Chuo cha VETA; ni kweli Chuko cha VETA hiki kinasaidia sana na kitaendelea kusaidia zaidi wananchi hususan kwa maeneo ya Nachingwea na maeneo mengine nchini kitakapokuwa kimeimarishwa. Ndiyo maana dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kwamba inakiimarisha chuo hiki ikiwa kimo katika mpango kazi wa Jeshi la Wananchi Tanzania. Miongoni mwa mambo ambayo tunatarajia kufanya ni kuhakikisha kwamba chuo hiki kinaunganishwa na VETA.

Mhehsimiwa Mwenyekiti, hivi sasa tunavyozungumza, ni kwamba tunatoa huduma ile kwa kuazima Walimu kutoka VETA kuja kufundisha, lakini pale ambapo mikakati hii itakapokamilika, tutakuwa tuna Walimu wa kutosha ambao watakuwa pale pale chuoni muda wote. Mbali ya hiyo, tutakuwa tunaweza kuongeza vifaa pamoja na kuimarisha majengo ya chuo hicho ili kiweze kutoa huduma kwa wananchi wengi zaidi wakiwemo wananchi wa Mheshimiwa wa Jimbo la Nachingwea kwa Mheshimiwa Hassan Masala.
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza, naomba kwa ruhusa yako unipe nafasi nitoe pole kwa wananchi wa Mkoa wa Lindi, hasa wananchi wa Kilwa pamoja na Mchinga ambao wamepata maafa ya mafuriko. Sisi kama Wabunge wa Mkoa pamoja na Taifa tunaungana nao na tuko pamoja nao. Pia nikumbushe hoja ambayo ilitolewa na Mbunge mwenzangu jana juu ya kuona umuhimu wa Bunge kuchangia Mkoa wa Lindi, hasa wale wahanga ambao wamepata maafa. Kwa hiyo, kupitia Kiti chako tutaomba mwongozo wako. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hilo, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, Mheshimiwa Rais wetu alifanya ziara tarehe 16 Oktoba, 2019 na katika ziara hiyo Mheshimiwa Naibu Waziri aliambatana na Mheshimiwa Rais. Moja ya ahadi kubwa ambayo aliitoa na ambayo wananchi wa Masasi, Nachingwea na Ruangwa wanasubiria ni kuona utekelezaji wa kile ambacho alikitolea maagizo juu ya kuanza kwa ujenzi wa lami kwa barabara hii ambayo kwa muda mrefu wananchi kwao imekuwa kero. Sasa naomba kufahamu kauli ya Serikali kwa nini mpaka sasa bado maagizo yale hayajaanza kufanyiwa kazi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, Wilaya ya Nachingwea inaungana na Wilaya ya Tunduru Mkoa wa Ruvuma. Kwa muda mrefu wananchi wa maeneo ya Tarafa ya Kilimarondo ambao wanaunganishwa na Mto Lumesule wamekuwa wanapata changamoto kubwa sana ya kupata mawasiliano. Naomba kauli ya Serikali kupitia Wizara, wana mpango gani juu ya kufungua barabara hiyo ya Kilimarondo kwenda Namatunu kutokea Lumesule kwenda kuunganisha Tunduru ili tuweze kufungua barabara hii tuweze kunufaika kiuchumi?

Mheshimi Naibu Spika, ahsante sana.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa Wizara yangu inatekeleza ahadi zote za Ilani ya Chama cha Mapinduzi lakini pamoja na viongozi wetu wakuu wa Serikali. Ni kweli Mheshimiwa Rais aliahidi na sisi Wizara tunalifanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo hatua, baada ya ahadi lazima tujipange na kuandaa bajeti ndiyo tuendelee kutekeleza. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Mbunge na sasa hivi ndiyo tunaandaa bajeti, kwa hiyo tutaendelea kutekeleza hilo lakini pia kumbuka kwamba tunapenda kwanza kukamilisha ujenzi wa barabara zote za mikoa halafu baadaye ndiyo twende kwenye regional roads. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia feeder roads kwa vile kuna TARURA kuna ambazo zitaingia kwenye TARURA lakini kuna ambazo zitatekelezwa na Wizara ya Ujenzi. Kwa hiyo, barabara hiyo aliyoisema kwenda Kilimarondo tutaipitia na kuona kwamba itekelezwe na taasisi gani. (Makofi)
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Waziri moja ya ziara ambazo umezifanya Jimbo la Nachingwea ni katika Kata ya Mbondo, Kijiji cha Chimbendenga. Sasa hivi ni takribani miezi minane toka uondoke ule mradi mpaka sasa hivi haujakamilika. Naomba kufahamu commitment ya Wizara juu ya kukamilisha mradi wa maji Chimbendenga?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge, kiukweli nimefika Nachingwea nimejionea kazi kubwa ambazo anazozifanya siyo katika maji tu hata katika maeneo mengine, lakini kikubwa ambacho ninachotaka kusema moja ya changamoto kubwa sana katika sekta yetu ya maji kulikuwa na wakandarasi wengi wababaishaji lakini hata hao wanaotekeleza wamekuwa katika kusuasua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi hatuna nafasi kama Wizara ya Maji kubembeleza watu. Tunawaomba Wakandarasi wafanyekezi kwa wakati na sisi kama Wizara ya Maji hatutakuwa kikwazo katika kuwalipa fedha zao katika kuhakikisha wanakamilisha miradi ya maji. Ninachotaka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge, tutafanya mawasiliano na wenzetu wa Nachingwea, tukiona mkandarasi anafanyakazi kwa kusuasua tutamnyang’anya kazi tutaifanya kwa wataalam wetu wa ndani ili mradi wetu uweze kukamilika na wananchi wetu waweze kupata huduma ya maji. Ahsante sana.
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Naomba kufahamu, kwa sababu tumebakiza takribani mwezi mmoja ili tuweze kuvuna mbaazi na kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri anakiri kwamba ziko jitihada zimefanyika ikiwemo watu wa Malawi kuwashawishi waje wachukue mbaazi hizi; hebu atuambie mpaka sasa ndani ya mwezi huu mmoja ni maandalizi gani ambayo yamefanyika ili kuwahakikishia wakulima kupata uhakika wa masoko ya mbaazi ambazo wanakwenda kuvuna?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili ambalo nilikuwa naomba kuuliza, hebu watu wa Wizara watuambie pia, watu wa SUA sasa hivi wameanzisha project moja inaitwa Vegi- Leg. Hii project kuna baadhi ya maeneo wanaanza kufanya kazi ikiwemo ndani ya Wilaya ya Nachingwea, kuna Kijiji kinaitwa Mitumbati na Ruangwa wamechukua kijiji kimoja kinaitwa Mibure. Kazi kubwa wanayokwenda kuiandaa ni kuweka utaratibu wa kusindika zao la mbaazi au mazao ya jamii ya mikunde. Hebu watuambie, wao kama Wizara wanashirikiana vipi na watu wa SUA kuhakikisha kazi hii inafanyika kwa wingi katika maeneo yote ambayo yanalima zao la mbaazi?

Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, maandalizi yaliyofanyika kama ambavyo nimezungumza hapo awali, kwanza kwa kushirikiana na TANTRADE lakini na Wizara yenyewe tulifanya ziara ya kutafuta hayo masoko ili kuona kwamba mbaazi zinapokuwa tayari tuweze kujua ni wapi tunapeleka kwenda kuuza.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema ni kwamba sisi wajibu wetu mwingine ni kuwahamasisha wadau mbalimbali na kuwafahamisha wapi wakulima wa mbaazi wapo na waeze kununua, lakini pia kulinda bei ya mkulima ili asionewe wakati wa kuuza mbaazi zake.

Mheshimiwa Spika, kwa kupitia huu mpango ambao umeungumza unaotekelezwa na SUA, kimsingi Wizara yetu kama mratibu inashirikiana na Taasisi zote pamoja na Wizara nyingine katika masuala hayo yanayohisiana na lishe, lakini pia uongezaji thamani wa mazao hayo ya mbaazi pamoja na mazao mengine ili kuweka mazingira wezeshi ya wadau hao kuweza kushiriki kikamilifu na kuweza kuchakata au kuongeza thamani inayostahili.
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwakunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, matatizo ya maji ambayo yametajwakatika Jimbo la Ndanda na huo mradi wa MANAWASA kwa sababu unahudumia Wilaya ya Nchingwea, naomba kufahamu mkakati wa Wizara wa kuhakikisha upanuzi wa miradi hii ya maji katika vijiji vya Nachingwea hasa vijiji vya Namatula pamoja na Mperuka ambako tayari tulishaanza zoezi la kusogeza maji hayo yanayotokana na chanzo cha mto Mbwinji? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nipende kumjibu Mheshimiwa Mbunge, kaka yangu Masala kwa kazi kubwa kwanza anayofanya katika Jimbo lake lakini kikubwa sisi tuna chanzo hiki cha uhakika wa maji, limebaki tu suala la usambazaji. Lakini Mheshimiwa Waziri wangu wa Maji alikwishatoa agizo kwa mamlaka hizi za maji kuhakikisha kwamba inatenga asilimia 20 ya fedha zao za mapato ili kuhakikisha kwamba wanafanya upanuzi.

Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge sisi kama Wizara tutalisimamia hilo katika kuhakikisha vijiji vyake alivyovieleza vinapata huduma hii muhimu sana ya maji.