Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Juliana Daniel Shonza (13 total)

MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona. Kwa kuwa tatizo la Maswa linafanana kwa ukaribu kabisa na tatizo la Wilaya ya Momba, kwa sababu Wilaya ya Momba haina hospitali ya Wilaya. Kipindi cha kampeni Mheshimiwa Rais alituahidi kutupatia majengo ya pale Chipaka yatumike kama hospitali ya Wilaya. Nataka kujua, je, Serikali ina mpango gani wa kutupatia majengo yale ili yatumike kama Hospitali ya Wilaya ya Momba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Momba hatuna hospitali ya wilaya pale na siyo hospitali ya wilaya hata zile infrastructure za wilaya yenyewe, halmashauri hatujakaa vizuri. Momba kwa sababu ni eneo jipya, mkakati wetu ni kuweza kuimarisha, lakini kwa sababu kuna majengo tayari, kikubwa zaidi ni kwamba wataalam watatakiwa kufika pale kufanya assessment ya hayo majengo.
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri katika ziara yangu ambayo nitaanzia Mkoa wa Iringa kuanzia tarehe 17 vilevile nitafika na maeneo ya Momba. Nikifika Momba, nitaomba wanifikishe katika yale majengo. Lengo letu ni nini? Tubainishe jinsi gani wananchi wataweza kupata huduma hizi. Kwa hiyo, namshukuru sana Mheshimiwa Juliana Shonza kwa juhudi kubwa anayofanya kwa ajili ya wananchi wa Momba.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Katika jibu la msingi Mheshimiwa Waziri amesema kwamba usanifu umekamilika katika Miji ya Isongole, Vwawa pamoja na Tunduma, lakini nisikitike kusema kwamba neno usanifu umekamilika bado haliwezi kuleta matumaini kwa akina mama wa Mkoa wa Songwe ambao wanapata shida kubwa sana ya maji. Kwa hiyo, napenda kuomba Mheshimiwa Waziri aniambie kwamba ni lini mradi huo utaanza katika maeneo hayo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili la nyongeza kama tunavyojua Mkoa wetu wa Songwe ni mkoa mpya na lengo la kuleta Mkoa mpya ni kusogeza huduma karibu na wananchi. Huduma mojawapo ni huduma ya maji ili akinamama wale wa Mkoa wa Songwe waweze kupata huduma kama inavyostahili. Hata hivyo, nioneshe masikitiko yangu makubwa kwamba mpaka sasa, hasa…
MWENYEKITI: Naomba uulize swali tafadhali!
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nauliza. Kwa maeneo ambayo ni ya pembezoni, mfano kule Ibaba, Ileje, ukienda Mkwajuni Wilaya ya Songwe, ukienda Iwula, ukienda Kamsamba bado miundombinu ya maji haijakaa vizuri. Naomba kupata jibu la Mheshimiwa Waziri kwamba ni lini Serikali itajenga miundombinu mizuri ya maji, hasa kwa maeneo ambayo ni ya pembezoni?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa jinsi anavyofuatilia upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi wake na kwa sababu ni Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum nafikiri wananchi hawakupoteza kura zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ameniuliza maswali mawili ya nyongeza, ni lini miradi hii iliyofanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina itaanza. Kama nilivyojibu katika swali la msingi kwamba, tayari sasa hivi Serikali inafanya majadiliano na wafadhili kwa ajili ya kupata mikopo ya masharti nafuu. Hii miradi ni mikubwa, uwezo wa Serikali tunaendelea lakini bado siyo mkubwa sana kiasi cha kuweza kutekeleza miradi mikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge amesema kwamba kuna Miji ya Mkoa wa Songwe, Mkoa ni mpya, kuna maeneo mengi bado hayajapata huduma ya maji. Serikali inaendelea, tumeanza programu ya kwanza ya maendeleo ya maji mwaka 2006/2007, programu ya kwanza ya miaka mitano imekwisha mwaka 2015 Disemba. Sasa hivi tumeanza programu ya pili, kwa hiyo ile miradi ambayo haikukamilika, miradi ambayo haikuanza katika awamu ya kwanza, basi tutaianza na kuikamilisha katika awamu ya pili.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Katika majibu ya msingi ya Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba benki hii kwa sasa inajikita katika kutoa huduma kwa kutumia vituo vya mikopo. Sasa nataka nijue kwamba ni lini wanawake wa Mkoa wa Songwe watapata kituo angalau kimoja ili waweze kujiinua kiuchumi?
Swali la pili, kwa kuzingatia kwamba madhumuni ya uanzishwaji wa benki hii ni kuwainua wanawake wanyonge, hususan wanaoishi vijijini, ambao hawana uwezo wa kumiliki ardhi wala nyumba kama ilivyo kwa wanawake wangu wengi wa Mkoa wa Songwe, lakini masharti ya mikopo ya benki hii kimsingi hayatofautiani sana na masharti ya benki nyingine. Je, Serikali haioni kwamba kuna umuhimu wa kurekebisha masharti haya ya mikopo ya benki ili basi wanawake wa Mkoa wa Songwe waweze kunufaika?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda nimpongeze kwa kuwajali wanawake wa Mkoa wa Songwe, yeye akiwa kama Mbunge wa eneo hilo na mimi nikiwa kama Balozi wa Wanawake.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza ni lini tutafungua angalau kituo kimoja cha mkopo kwenye Mkoa huo. Naomba nimpe taarifa kwamba tayari tuna kituo kimoja Songwe, maeneo ya Tunduma na kwamba tayari tumemwambia kwenye jibu letu la msingi kwamba tunauweka Mkoa wa Songwe katika mpango wetu wa kufanya kazi wa mwaka 2017/2018. Hivyo mtaji utakaporuhusu basi tutaufikiria mkoa huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, naomba na yeye atuhurumie kwa kutambua kwamba tayari benki yetu inajitanua kidogo kidogo na kwa sababu Songwe imemeguka kutoka Mkoa wa Mbeya, ambao tayari una vituo 11 vya kutolea mikopo, atuhurumie twende na maeneo mengine, kama kumwongezea basi tutamwongezea kidogo sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, kuhusu masharti ya mikopo kwenye Benki ya Wanawake; tayari Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto alikwishatoa maelekezo Siku ya Wanawake Duniani mwezi wa Machi mwaka huu, kwamba Benki ya Wanawake iweke utaratibu mpya wa kushusha masharti na gharama za kutoa mikopo kwa wanawake ili wanawake wenye kipato cha chini waweze kumudu gharama za kurejesha mikopo hiyo bila usumbufu wowote. Tayari maelekezo haya ya Mheshimiwa Waziri yanafanyiwa kazi na Benki yetu ya Wanawake.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwenye bajeti ya mwaka huu tayari tumeweka provision, ambapo kutakuwa kuna fungu maalum la pesa litakalokwenda moja kwa moja kwa wanawake wenyewe, badala ya kutumika katika administrative activities za benki.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Kwa kuzingatia kwamba Mkoa wa Songwe ni mpya na ni mkoa ambao uko mpakani, lakini kiongozi ambaye anahusika na mambo ya ulinzi na usalama wa Mkoa wetu wa Songwe ambaye ni RPC anaishi kwenye nyumba ambayo ni sawa na gofu. Nilitaka kupata kauli ya Serikali kwamba ni lini RPC wa Songwe atapatiwa nyumba nzuri?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua changamoto ambayo inakabili makazi ya RPC kule Songwe hasa ukitilia maanani kwamba mkoa huu ni mpya, kwa hiyo utakumbana na changamoto mbalimbali na unahitaji muda mpaka kuweza kukaa sawa. Kwa kulitambua hilo basi, nikiamini kabisa kwamba tuna programu kabambe ya ujenzi wa nyumba za makazi kwa askari ambazo tumekuwa tukizizungumza hapa kila siku, tutaangalia huo uwezekano kufikia utaratibu huo ama utaratibu mwingine wowote ili tuweze kurekebisha hilo jambo, tunalifahamu na tutalifanyia kazi.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona, kwa kuwa tatizo la maji lililopo Urambo linafanana kwa ukaribu kabisa na tatizo la maji lililopo katika mji wangu mdogo wa Mlowo, na kwa vile katika Mji huo kuna mto uitwao Mto Mlowo.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kuchimba mabwawa katika mto huo ili kuhakikisha kwamba wananchi wa mji mdogo wa Mlowo, hususani wanawake ambao Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba ndio wachotamaji wakubwa wanaondokana na adha hiyo ya mji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ametuomba kwamba tuna Mto Mlowo na akinamama wanakwenda kuchota maji Mto Mlowo, sasa haoni kwamba kuna umuhimu wa kuchimba mabwawa?
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshaagiza tayari kwamba Halmashauri zote zifanye utafiti na zilete mapendekezo ili Serikali iweze kutenga fedha kuhakikisha kwamba kila Halmashauri na tumeomba kwamba kila Halmashauri kila mwaka ihakikishe inachimba bwawa moja. Kwa hiyo, Mheshimiwa Shonza naomba na wewe ni Diwani, tusaidiane kwenye vikao vyetu tuelekeze kwamba Wakurugenzi na wahandisi wa maji wa Halmashauri zetu wafanye utafiti ili tuweze kupata maeneo ya kuchimba mabwawa tuweze kuondoa hii kero ya maji.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Waziri, lakini ni wazi kwamba kwa miaka mingi sana Serikali haijatoa kipaumbele kwa suala la nyumba za walimu. Kwa mfano, kwenye majibu ya Mheshimiwa Waziri amesema kwamba kwa mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali imepanga kujenga nyumba 1,818, ukiangalia nikitumia Mbozi kama case study ya Mkoa wa Songwe, kuna uhaba wa nyumba za walimu 1,432. Je, ni lini sasa Serikali italeta mpango kabambe wa kumaliza tatizo la nyumba za walimu hasa wa vijijini ili iwe kama motisha?
Swali la pili, Mheshimiwa Waziri ambacho nilitaka kufahamu kwamba je, ni lini madeni hayo ya walimu yataanza kulipwa kwa sababu ukisema kwamba yamepelekwa tu Hazina bado haileti tija kwa walimu wa Tanzania. Ninataka kujua kwamba ni lini rasmi madeni hayo yataanza kulipwa?
Mheshimiwa Spika, ninakushukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI): Mheshimiwa Spika, najua Mbunge anaguswa sana na sekta ya elimu na nikupongeze sana kwa sababu ukiwa kijana lazima uguswe na elimu.
Mheshimiwa Spika, katika majibu yangu ya msingi na mkakati wa Serikali nimezungumza pale awali. Kwa vile tumebaini changamoto ya nyumba za walimu ndiyo maana Serikali katika bajeti ya mwaka huu tunaoenda nao imetenga takribani shilingi bilioni 13, hii ni kwa ajili ya nyumba za walimu wa shule za msingi peke yake, lakini shilingi bilioni 11 kwa ajili ya shule za sekondari. Hata hivyo, commitment katika mpango mwingine wa MMES II, nimezungumza hapa karibuni nyumba zipatazo140 tumeshazikamilisha.
Mheshimiwa Spika, naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge katika ziara zangu katika Mikoa mbalimbali, miongoni mwa mambo ninayoyatilia kipaumbele sana ni kukagua ujenzi wa nyumba za walimu. Naomba niwapongeze Wabunge wote kwa ujumla wetu katika maeneo yetu nilipopita nimekuta ujenzi wa nyumba za walimu kwa kweli unaenda kwa kasi sana. Kwa vile katika commitment ya Serikali imeshatenga hizi fedha, naomba niwaambie fedha tunaendelea kuzipeleka katika Halmashauri zetu, lengo kubwa walimu waweze kupata mazingira salama ya kuweza kuishi.
Mheshimiwa Spika, katika suala zima la madai ya walimu, nimesema kwamba sasa hivi tumeshahakiki deni la shilingi bilioni 26.04 na haya ni madeni yasiyo ya mshahara. Maana yake Serikali haiwezi kulipa madeni lazima kwanza kuweza kuhakiki, ndiyo maana nimesema zoezi la uhakiki limeisha Oktoba, 2016. Sasa hivi ni mchakato ambao upo katika Wizara ya Fedha kwa utaratibu wa mwisho wa kuweza kulipa. Kwa hiyo, naomba tuwe na subira tu kwa sababu kigezo kikubwa ni kwamba ni lazima deni lihakikiwe na madeni haya yameshahakikiwa na naomba niwaambie walimu wa Tanzania kwamba wawe na subira kipindi siyo kirefu, Hazina kwa kadri inavyojipanga, madeni haya yanaweza kulipwa walimu mbalimbali ili mradi wapate haki zao.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona. Kwa kuzingatia umuhimu wa magari ya zimamoto katika Mikoa yetu, lakini mikoa mingi mipya hususan Mkoa wa Songwe unakabiliwa na ukosefu wa magari ya zimamoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kupata kauli ya Serikali kwamba je, Serikali ina mpango gani wa kutuletea
magari ya zimamoto katika Mkoa mpya wa Songwe? Ahsante.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa
ufuatiliaji wake na siyo tu jambo la zimamoto, bali masuala mazima yanayohusu idara zilizopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ikiwemo Makao Makuu ya Polisi katika Mkoa mpya wa Songwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu Songwe ni moja ya mikoa mipya, lakini una bahati ya kuwa karibu na uwanja
wa ndege. Tutaupa kipaumbele kama Mkoa mpya lakini pia kama mahitaji ya Mji ambao upo karibu na Mji wa Tunduma ambao unakua kwa kasi, ambao mara nyingi sana Mheshimiwa Juliana Shonza amekuwa akitetea masuala ya maendeleo ya mkoa huo na miji hiyo.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona. Kwa kuwa tatizo lililopo Manonga linafanana kwa ukaribu kabisa na tatizo lililopo katika Mkoa wa Songwe na kwa kuzingatia kwamba Mkoa wa Songwe ni mpya, lakini mpaka sasa Wilaya za Mbozi, Ileje, Momba pamoja na Songwe hazina vyuo vya ufundi. Je, ni lini Serikali itajenga vyuo vya ufundi katika wilaya hizo ili kuwasaidia vijana wa Mkoa wa Songwe kuweza kuondokana na tatizo la ukosefu wa ajira? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ninavyofahamu ni kwamba Wilaya ya Songwe ni miongoni mwa maeneo ambayo yamo kwenye mpango, nafahamu kuna kiwanja kilishatengwa eneo la Makutano, kwa hiyo, muda ukifika tutafanya hiyo shughuli ya ujenzi.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Waziri japokuwa niseme kwamba majibu haya hayaridhishi na wala hayajatosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la msingi nilitaka kujua kwamba Serikali ina mpango gani wa kujenga wodi mpya ya akinamama katika Hospitali hii ya Wilaya ya Mbozi ukizingatia kwamba hospitali hii inahudumia wilaya mbili mpaka sasa. Hali halisi ilivyo pale kuna vitanda 25 tu vya akinamama vya kulala baada ya kujifungua lakini kwa siku wanawake wanaozalishwa katika hospitali hiyo ni wanawake 42 mpaka 50. Kwa hiyo, kukarabati hili jengo hakuwezi kusaidia. Kwa hiyo, swali langu la msingi nataka kujua kwamba Serikali ina mpango gani wa kujenga wodi ya akinamama mpya na kubwa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, katika
swali langu la msingi pia nataka kujua kwamba Serikali ina mpango gani wa kujenga Hospitali ya Wilaya ya Momba?Hili jambo nimekuwa nikilipigia kelele sana katika Bunge hili kwamba mpaka sasa Wilaya ya Momba hawana Hospitali ya Wilaya. Hali hiyo inapelekea usumbufu sana kwa sababu mara nyingi wanalazimika kuja kutibiwa katika hospitali ya Mbozi ambayo pia nayo jengo lake ni dogo. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Naibu Waziri aniambie ni lini sasa Serikali itajenga Hospitali ya Wilaya ya Momba? Ahsante.(Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge, haya yote yanatokana na needs za Wabunge wenyewe tunavyokaa katika vikao vyetu. Kwenye vikao vyetu ndipo ambapo tunaweka priority nini kifanyike. Eneo hili priority ya kwanza imeonekana ni lazima tutenge shilingi milioni 180 kwa ajili ya kufanya ukarabati huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba niseme mipango hii yote inaanzia kwetu sisi Wabunge katika maeneo yetu tunapofanya needs assessment au tunapopanga mipango yetu. Hata hivyo, nimhakikishie Mheshimiwa Juliana kwa jinsi anavyopigania haki za akinamama na watoto Serikali tutafanya kila liwezekanalo kuona jinsi gani tutafanya kwa sababu pale Vwawa sasa hivi ndiyo kama Makao Makuu. Licha ya ukarabati huu, lakini tutaangalia nini kingine kifanyike lengo kubwa ni akinamama na watoto hasa wanaozaliwa waweze kuwa katika mazingira salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Hospitali ya Momba, niliongea na Mkuu wa Mkoa wetu wa Songwe, Mama Chiku Gallawa wakati tunafanya mikakati ya ukarabati wa vituo vya afya 100, hili jambo aliweka kama priority na aka-identify kwamba Momba haina Hospitali ya Wilaya. Tulibadilishana mawazo tukaona lile eneo la awali ambalo limepangwa kuwa Makao Makuu ya Halmashauri ya Momba kile kituo cha afya cha pale tukiwekee miundombinu ya kutosha ili wananchi wa eneo lile waweze kupata huduma ya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Juliana kwamba tutafanya kila liwezekanalo kuhusiana na hoja hii na kwamba katika Makao Makuu ya Momba tunaenda kufanya uwekezaji mkubwa sana ndani ya kipindi hiki hiki kabla ya mwezi wa saba. Kilio cha wananchi wa pale ni kwamba wanapata shida na Serikali tumesikia kilio hiki, tutaenda kufanya kazi kubwa na ya kutosha kuwasaidia akinamama na watoto wa maeneo yale. (Makofi)
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona. Tatizo lililopo Mfenesini linafanana kwa ukaribu kabisa na tatizo ambalo lipo katika Mkoa wa Songe na ukizingatia kwamba Mkoa wa Songwe ni mpya na umekuwa na changamoto kubwa sana za kiuhalifu. Changamoto kubwa iliyopo ni suala la usafiri kwa Jeshi la Polisi hususan katika Wilaya mpya ya Songwe. Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka magari katika Mkoa wa Songwe hususan katika Wilaya mpya ya Songwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua Mikoa na Wilaya mpya nyingi zina changamoto sio tu za magari pamoja hata na vitendea kazi, ofisi na nyumba. Kwa hiyo, ni kipaumbele cha Wizara yetu kuona kwamba tunapopata vifaa na uwezo wa kuweza kuimarisha vitendea kazi katika maeneo hayo, tunaangalia mikoa hii ambayo ni mipya ukiwemo Mkoa wa Songwe.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Kampasi ya DIT iliyoko Myunga anayoizungumzia Mheshimiwa Naibu Waziri yalikuwa ni majengo ya TANROADS ambayo kwa sasa ni takribani mwaka mmoja umepita tangu Serikali ipeleke Walimu wanne, lakini hakuna maandalizi mengine yoyote yanayoendelea pale kuonyesha kwamba hicho chuo kitafunguliwa hivi karibuni. Kwenye jibu la msingi Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba hicho chuo kitafunguliwa hivi karibuni.
Mheshimiwa Naibu Waziri anatuhakikishia vipi wananchi wa Wilaya ya Momba pamoja na Mkoa wa Songwe kwa ujumla kwamba hicho chuo kitakuwa bora kwa sababu mpaka sasa maandalizi yake ya ufunguzi ni hafifu sana?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; katika Wilaya ya Ileje kuna chuo cha VETA ambacho kimejengwa kwa jitihada kubwa za Halmashauri pamoja na JICA, mpaka sasa chuo hicho hakijafunguliwa kwa sababu ya ukosefu wa vifaa. Je, Serikali sasa haioni kwamba kuna umuhimu wa kukiongezea nguvu chuo hicho ili kiweze kufunguliwa na hatimaye kiweze kutumika kama chuo cha VETA kwa Mkoa wa Songwe ukizingatia kwamba mpaka sasa Mkoa wa Songwe hakuna chuo cha VETA? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Chuo cha Myunga, kwanza nichukue nafasi hii kuwashukuru sana wenzetu TANRODS kwa kukubali kambi hiyo itumike kwa ajili ya kutoa mafunzo kupitia Chuo cha DIT. Kimsingi ni kweli kwamba ile kambi haikuandaliwa kama Chuo cha Ufundi, kwa hali hiyo ilibidi kuanza kufanya taratibu zinazostahili ikiwa ni pamoja na kuangalia ni course zipi zinaweza zikafanyika kwa kuanzia katika eneo lile. Vvilevile kupata mahitaji muhimu kama umeme, pamoja na miundombinu ambayo itakuwa sahihi katika ufundishaji na ujifunzaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shughuli hiyo imekamilika lakini tumekwama hasa katika suala la umeme na tumeona tutaanza na umeme wa Solar mna generator lakini baadaye tunategemea kupitia umeme vijiji mahali hapa patakuwa pameshapata umeme na kuweza sasa kutoa mafunzo makubwa zaidi kwa mujibu wa fursa zinazotolewa katika kampasi za vyuo vyenye uwezo wa kutoa mafunzo kuanzia ya ufundi wa sanifu mpaka degree.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika swali la pili kuhusiana na Chuo cha Ileje. Suala hili limekuwa pia likifuatiliwa na Mheshimiwa Janeth Mbene na tulikuwa tumetoa maelekezo baada ya Mkuu wa Wilaya kuja ofisini kwetu. Tulilokuwa tunaliomba kwao ni wao kuongeza eneo lile ukubwa kidogo lakini wakati huo kutupa sisi hati baada ya kupitia mikutano yao ya Halmashauri za Wilaya na RCC ili sasa kuhamisha ile ardhi kuwa katika mikono ya VETA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo sisi tutaendelea na hayo tumeshayafanya maeneo mengi ikiwemo Busekelo. Kwa hiyo, ninachoomba tu kwamba wao wenyewe wajitahidi katika kuongeza jitihada katika hilo. (Makofi)
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jitihada kubwa za Serikali za kumaliza tatizo la maji katika Mji wa Tunduma, bado changamoto kubwa imebaki kuwa kukosekana kwa chanzo cha uhakika katika Mji wa Tunduma. Je, nini mkakati wa Serikali wa kutekeleza ahadi aliyotoa Mheshimiwa Rais wakati wa uchaguzi ya kuvuta maji kutoka chanzo cha uhakika kilichopo katika Mji wa Ileje? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Juliana Shonza, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Songwe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, chanzo cha uhakika cha maji kwa Mji wa Tunduma kama alivyoongelea chanzo cha maji kutoka Ileje, feasibility study inaendelea kufanyika na mara itakapokamilika basi mradi ule utatengewa fedha kwa awamu na utekelezaji utaanza mara moja. Vile vile kwa nyongeza pale Tunduma nimeshafika na kuona namna gani bora ya kuweza kupatikana kwa maji kwa sababu miundombinu ya awali tayari ilikamilika Mheshimiwa Mbunge niseme tulishaweza kumpa maelekezo Meneja wa Maji Mkoa, RUWASA na yule Engineer ni Engineer ambaye tunamtegemea katika Wizara na anafanya kazi vizuri sana. Hivyo, nikuhakikishie shida ya maji katika Mji wa Tunduma inakwenda kuwa historia. (Makofi)
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kata 29 za Wilaya ya Mbozi, Kata tatu za Bara, Kilimpindi na Nyimbili bado hazijapelekewa umeme. Naomba kufahamu ni lini Serikali itapeleka umeme katika kata hizo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shonza kuhusu kupeleka umeme katika kata alizozitaja katika Jimbo la Mbozi. Katika Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili wa REA iliyoanza Machi tutahakikisha tunapeleka umeme maeneo yote ambayo yalikuwa hayajapata umeme. Hivyo na yeye atakuwa mmojawapo kati ya wale watakaopata umeme katika awamu hii.