Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Juliana Daniel Shonza (5 total)

MHE. JULIANA D. SHONZA aliuliza:-
Tatizo la maji ni changamoto kubwa sana katika Mkoa wa Songwe na Wilaya zake zote:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwaondolea adha ya maji wanawake wa Mkoa huu hususan Mji Mdogo wa Tunduma ambako hali ni tete zaidi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juliana Daniel Shonza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua adha kubwa ya tatizo la maji inayowakabili wananchi wa Mkoa wa Songwe hususan wanawake. Katika mpango wa muda mrefu wa uboreshaji wa huduma ya majisafi Mkoa wa Songwe, Serikali imekamilisha usanifu na uandaaji wa vitabu vya zabuni kwa ajili ya kuboresha huduma ya majisafi katika Miji ya Mkoa wa Songwe ikiwemo Vwawa ambako ni Makao Makuu ya Mkoa, Itumba, Isongole pamoja na Tunduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na jitihada za kutafuta fedha za kutekeleza mradi huo kutoka kwa wafadhili mbalimbali. Kwa sasa Serikali imewasilisha maombi katika Benki ya Maendeleo ya Ufaransa ya kupata mkopo wa masharti nafuu kwa ajili ya kutekeleza mradi wa majisafi Mjini Tunduma. Pia Serikali imewasilisha maandiko ya miradi ya majisafi kwa Miji ya Vwawa na Tunduma kwenda Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) kwa ajili ya kutafuta fedha za kutekeleza miradi hiyo Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, katika mpango wa muda mfupi wa kuboresha huduma ya maji kwa Miji ya Vwawa na Tunduma, Serikali katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017, itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya upanuzi wa mfumo wa usambazaji wa maji katika miji hiyo.
MHE. JULIANA D. SHONZA aliuliza:-
Benki nyingi nchini zimekuwa na Riba kubwa, hali ambayo inafanya wanawake washindwe kukopa kujiinua kiuchumi. Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka Benki ya Wanawake Mkoa wa Songwe ili wanawake wajasiriamali wanufaike na mikopo hii ya riba nafuu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juliana Daniel Shonza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la Benki ya Wanawake Tanzania ni kusambaza huduma zake katika maeneo yote ya Tanzania ikiwemo Mkoa wa Songwe. Hata hivyo, azma hii inakwamishwa na mtaji mdogo wa benki hii, ndiyo maana kwa sasa imejikita zaidi katika kutoa huduma zake kwa kutumia vituo vya mikopo ambapo hadi sasa benki ina vituo 89 katika mikoa saba ukiwemo Mkoa wa Mbeya ambao hadi mwaka 2015 ulikuwa sehemu ya Mkoa huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango mkakati wa Benki ya Wanawake wa mwaka 2014/2017 ni kufungua angalau matawi matatu kila mwaka. Hii itawezekana tu endapo mtaji wa benki utakuwa kama inavyotegemewa. Hivyo benki itauingiza Mkoa mpya wa Songwe kwenye mipango yake ya upanuzi wa huduma kwa mwaka 2017/2018.
MHE. JULIANA D. SHONZA Aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha miundombinu ya elimu vijijini kama nyumba za walimu pamoja na kulipa malimbikizo ya madeni ya walimu wanayoidai Serikali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juliana Daniel Shonza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inaboresha miundombinu ya shule nchini kupitia mipango na bajeti ya Serikali kwa kushirikisha nguvu za wananchi na wadau wa maendeleo ili kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.
Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali imetenga shilingi bilioni 13.9 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu 1,157 kwa shule za msingi na shilingi bilioni 11.14 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu 661 kwa shule za sekondari. Aidha, kupitia Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES II), Serikali imekamilisha ujenzi wa nyumba 146 kati ya nyumba 183 ambazo kila nyumba wataishi watumishi sita (walimu). Ujenzi wa nyumba hizo umegharimu shilingi bilioni 21.9. Nyumba 37 zinaendelea kujengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 5.5 na zitakamilika tarehe 30 Aprili, 2017.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kulipa madeni ya walimu kadri yanavyojitokeza na kuhakikiwa. Katika mwezi Oktoba, 2015 Serikali ililipa madeni ya shilingi bilioni 20.12 kwa walimu 44,700 na shilingi bilioni 1.107 zililipwa mwezi Februari, 2016 kwa walimu 3,221. Hivi sasa walimu wanadai Serikali madeni yanayofikia shilingi bilioni 26.04 kwa ajili ya walimu waliopo kazini 33,620 na walimu wastaafu 2,134. Deni hilo limewasilishwa Hazina kwa ajili ya taratibu za mwisho za kulipwa kwa walimu wanaodai.
MHE. JULIANA D. SHONZA aliuliza:-
Hospitali ya Vwawa Wilayani Mbozi inakabiliwa na changamoto kubwa ya uhaba wa vitanda vya kulalia wajawazito pamoja na vile vya kujifungulia, pia wodi ya akinamama ni ndogo huku ukizingatia kuwa hospitali hiyo inahudumia Wilaya ya Mbozi na Momba:-
Je, ni lini Serikali itajenga wodi ya akinamama kubwa yenye vifaa vya kutosha ili wanawake hawa waondokane na adha ya kulala wawili wawili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juliana Daniel Shonza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Wilaya ya Mbozi yaani Vwawa ni hospitali iliyopandishwa hadhi kutoka Kituo cha Afya kuanzia mwaka 2001. Kwa sasa hospitali hiyo inahudumia wagonjwa wengi kutoka Halmashauri ya Mji wa Tunduma, Wilaya za Momba, Mbozi na Ileje. Ili kuboresha huduma ya uzazi katika hospitali hiyo, Serikali katika mwaka wa fedha 2017/2018, imepanga kutumia jumla ya shilingi milioni 180 kwa ajili ya ukarabati wa wodi ya wazazi baada ya kujifungua (post natal ward) ambayo itakuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa wengi kwa wakati mmoja na kuondoa msongamano uliopo hivi sasa.
MHE. JULIANA D. SHOZA aliuliza:-
Mkoa wa Songwe ni mpya na unakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa Vyuo Vikuu hata vile vya Ufundi.
Je, ni lini Serikali itakuja na mpango wa kujenga hata kampasi ya Chuo Kikuu kimojawapo pamoja na vile Vyuo vya Ufundi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Juliana Daniel Shonza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT) hivi karibuni itaanza kutoa mafunzo katika kampasi yake ya Myunga iliyopo Wilaya ya Momba, Mkoa wa Songwe. Vilevile kutokana na gharama kubwa ya uwekezaji inayohitajika katika kuanzisha Vyuo Vikuu pamoja na Vyuo vya Ufundi Stadi, wananchi wanashauriwa kuendelea kutumia Vyuo Vikuu na Vyuo vya Ufundi Stadi vilivyopo nchini.