Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Kassim Majaliwa Majaliwa (1 total)

MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza:-

Je, Serikali inatoa elimu gani kwa vijana waliopo mashuleni/vyuoni ili kujikinga na tatizo sugu la utumiaji wa dawa za kulevya nchini.
WAZIRI MKUU alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imejipanga na imekuwa ikitoa elimu kwa vijana waliopo Mashuleni na vyuoni ili kujikinga na tatizo la matumizi na biashara ya dawa za kulevya. Ikumbukwe, mwaka 2017, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alianzisha rasmi Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ambayo licha ya kupambana na biashara hiyo, Mamlaka hii imejikita katika suala zima la utoaji wa elimu juu ya tatizo hilo kwa Umma wakiwemo vijana waliomo mashuleni na vyuoni kama moja ya vipaumbele vyake muhimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hadi sasa, mamlaka imeweza kutoa elimu mashuleni na kutengeneza mwongozo wa uendeshaji wa vilabu vya kupinga matumizi ya dawa za kulevya mashuleni na wakati mwingine kutumia Vilabu vya UKIMWI mashuleni kuzungumzia pia suala la tatizo la Dawa za Kulevya. Sambamba na hilo, Mamlaka kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wanafanya utaratibu wa kuingiza suala la dawa za kulevya katika mitaala ya kufundishia wanafunzi wa mashuleni na vyuoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, elimu imekuwa ikitolewa na Mamlaka kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Taasisi za Serikali, Asasi za kiraia pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo kupitia vyombo vya habari kama vile Televisheni, Redio, Magazeti na mitandao ya kijamii pamoja na matamasha. Aidha, Mamlaka imekuwa ikitumia hafla maalum za kitaifa kama vile siku ya Kupambana na Dawa za Kulevya Duniani, Mbio za Mwenge wa Uhuru, Sikukuu ya Sabasaba, Sikukuu ya Nanenane pamoja na siku ya UKIMWI Duniani ili kutoa elimu kwa Umma.