Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Nape Moses Nnauye (17 total)

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. FIFA inaitambua TFF kuwa ndio chombo chenye mamlaka ya kusimamia mchezo wa soka Tanzania.
Je, TFF ni Tanzania Football Federation au TFF ni Tanganyika Football Federation? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama jibu ni Tanzania Football Federation; je, TFF ina mamlaka gani juu ya chombo cha ZFA kule Zanzibar? Kama jibu ni Tanganyika Football Association; ni kwa nini hamjaiandikia FIFA na kuiambia kwamba ZFA haihusiki na mambo ya Chama cha Soka cha Tanzania? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, tatizo la baadhi ya viongozi kule Zanzibar kutotii sheria za nchi siyo tu liko kwenye mambo ya siasa, sasa limehamia mpaka kwenye mambo ya michezo. Hivi tunavyozungumza Makamu Mwenyekiti wa ZFA amekipeleka Mahakamani Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA), jambo ambalo FIFA wakiamua kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria zao, ni kwamba Tanzania itafungiwa uanachama muda wowote kuanzia sasa.
Je, Serikali inatoa tamko gani juu ya viongozi wa vyama vya soka wasiotii na kuheshimu sheria zilizowaweka kwenye madaraka yao?
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, WASANII NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, la kwanza, TFF ni Tanzania Football Association na siyo Tanganyika Football Association. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, ni Tanzania Football Federation na mamlaka yake yanakwenda mpaka Zanzibar… (Kicheko/Makofi)
SPIKA: Jamani, mbona Mheshimiwa Nape akiongea mnachemka sana upande wa pili? (Kicheko/Kelele)
Mheshimiwa Nape, endelea kujibu maswali.
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI. WASANII NA MICHEZO: Wanajua mimi kiboko yao! (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, ameuliza na ametoa mfano wa viongozi ambao wamepeleka masuala ya michezo Mahakamani. Taratibu za michezo duniani zinajulikana; na kama kuna watu wamepeleka michezo Mahakamani, kwa kweli hukumu yake kwa FIFA inajulikana. Kwa hiyo, tutachukua hatua tuangalie namna ambayo watarudi kwenye utaratibu wa kawaida ili kuepusha kuchukuliwa hatua za kufungiwa michezo.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza, kwa kuwa Mbulu walishapewa ahadi ya kujengewa uwanja na Olympic na sasa wale wameondoka na eneo hilo lipo mpaka sasa na wananchi wa Mbulu wamekubali kutoa eneo hilo. Je, Serikali haioni ndiyo sasa wakati wa kuja kuwekeza au kujenga kituo hicho Mbulu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa wanariadha wazuri ambao wamevunja rekodi ya dunia mpaka leo na haijawahi kuvunjwa mfano Philbert Bai ambao wamekuwa msaada mkubwa kwa Tanzania, je, Serikali haioni sasa ndiyo muda muafaka wa kujenga kituo hicho Mbulu kwa sababu uwezo wa Mbulu na uoto wa asili na hali ya hewa inawaruhusu wanariadha kuweza kufanya mazoezi na kushinda Olympic?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Serikali inatambua kazi nzuri iliyofanywa na wanariadha wanaotoka Mbulu wakiwemo akina Philbert Bai na wenzake. Tunakubaliana na hoja kwamba kama eneo lipo ambalo kwa kweli halitahitaji fidia na litaondoa hii haja ya mazungumzo ya kupata eneo, tutashauriana na Serikali ya Mkoa wa Manyara kuona namna ambavyo tunaweza kulitumia eneo hilo kwa ajili ya kujenga kituo hiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana naye kwamba kwa kutambua mchango wa wanariadha kutoka Mbulu na namna nzuri ya kuwaenzi nadhani ni vizuri tukaangalia namna ya kujenga kituo hiki Mbulu kwa kuzingatia mazingira hayo.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kuna msemo wa Kiswahili unaosema samaki mkunje angali mbichi. Ujenzi wa kituo hicho hautakuwa na maana kama hatujawekeza huku chini. Tunatambua kwamba wakati Serikali inapanua elimu walihakikisha kabisa viwanja katika shule zetu za msingi havipo kwa maana kwamba walijenga shule za pili. Je, Serikali inasema nini kuhakikisha kwamba shule zetu za msingi zina viwanja ili watoto waanze kucheza riadha au michezo mingine ili sasa hivi vituo wanavyovijenga huku juu viwe na maana?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza siyo kweli kwamba Serikali ilihakikisha kwamba shule hizi hazina viwanja. Bahati mbaya iliyotokea yako baadhi ya maeneo ambapo suala la kutenga viwanja vya kutosha halikuzingatiwa wakati wanapanga mipango na maeneo mengine viwanja vilichukuliwa vikabadilishwa matumizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeendelea kusisitiza kwanza katika kila mpango wa ardhi kuhakikisha tunatenga maeneo ya michezo siyo tu kwenye shule, lakini maeneo ya michezo yatengwe kwenye makazi ya watu ili kurahisisha watu kushiriki michezo kwenye maeneo yao ya makazi. Pili, tumeendelea kukagua na kurudisha maeneo ambayo yamevamiwa na kubadilishwa matumizi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Waheshimiwa Wabunge ninyi ni Madiwani tusaidieni mambo mawili. La kwanza, hakikisheni hakuna mipango ya matumizi ya ardhi inapitishwa wakati hakuna maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya michezo.
Pili, shule hizi zinaendeshwa na kumilikiwa na halmashauri zetu. Sisi Waheshimiwa Wabunge ambao ni Madiwani tukiwa wakali kwenye kubadilisha matumizi ya maeneo yetu bila shaka viwanja vitapatikana na michezo yetu itaendelea. Nakubaliana na wewe michezo ili iendelee lazima ianze ngazi ya chini, habari ya kuanzia ngazi ya juu tutapoteza muda wetu bure.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu mazuri. Niulize maswali yangu mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa kilichopelekea kuunda Tume hii mpaka kwenda Zurich ilikuwa ni swali ambalo liliulizwa hapa ndani na Mheshimiwa Hafidh Ali na imekuwaje Serikali imeshindwa kutoa jibu mapema mpaka leo baada ya kuuliza swali ndiyo majibu yamekuja?
Swali la pili, kwa kuwa kutotambuliwa kwa ZFA na FIFA kutapelekea bado kuwa na timu ya Taifa moja na kwa kuwa TFF na ZFA zinaposhiriki Kimataifa zinapata tatizo la ukosefu wa fedha na hivyo kupelekea timu zetu za Taifa kufanya vibaya, je, Serikali sasa haioni ni wakati muafaka kuzichukua timu za Taifa wakati zinaposhiriki kwenye mashindano ya Kimataifa ili tusiendelee kuwa kichwa cha mwendawazimu?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mwamoto kwa mchango wake mkubwa kwa michezo ya nchi yetu, hasa kwa michezo ya hapa Bungeni kila asubuhi namkuta uwanjani anafanya kazi nzuri, namshukuru sana.
(a) Ni kweli kwamba suala hili la mvutano kati ya ZFA na TFF limechukua muda mrefu sana. Limekuwa likijadiliwa kwa muda mrefu pamoja na magizo ya Serikali kwamba jambo hili liwe limemalizika, moja ya sababu pamekuwa na mivutano na tumeshuhudia mivutano mikubwa kwenye ZFA kwa maana ya uongozi, lakini juzi wamefanya uchaguzi na tunaamini sasa hali ya ZFA imetulia na Serikali tutaweka juhudi za kutosha kuhakikisha kwamba ZFA na TFF wanakaa chini na kusaini makubaliano. Lakini sababu ya pili, walipokaa mara ya kwanza wakatengeneza makubaliano, upande mmoja wa pande hizi mbili ulisita kusaini hayo makubaliano mpaka leo. Kwa hiyo, tutakachofanya tutaweka nguvu kuhakikisha pande hizi mbili zinakuja pamoja, zinasaini makubaliano na utekelezaji wa makubaliano yale unaanza kutekelezwa.

(b) Sehemu ya pili ya swali lake ameuliza kama Serikali sasa iko tayari kufadhili timu ya Taifa. Kwa kweli nchi yetu ina michezo mingi na haiwezekani Serikali ikatenga pesa kwa ajili ya michezo yote. Tunachofanya ni kuviwezesha vyama vya michezo nchini kwanza viwe na vyanzo vya mapato vya kutosha kufadhili na kuendesha michezo, lakini pia kuhamasisha sekta binafsi na wafadhili wengine waweze kusaidia kazi hii ya kufadhili michezo nchini na wako ambao wamekuwa wakifanya vizuri, ndiyo mana ligi zetu nyingi zinakwenda vizuri.
MHE.HAMIDA M. ABDALLA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Waziri, kwa majibu yake yenye matumaini.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Mikoa hii ya Lindi tuna majina mengi sana, tunaitwa Mikoa ambayo imesahaulika, Mikoa iliyokuwa pembezoni, Mikoa ya Kusini. Tunapata hofu sana tunapokosa matangazo na matangazo kusikika katika eneo la mjini tu, wakati Wilaya ya Nachingwea ina kata 34, na wanahitaji kupata matangazo. Ningependa Mheshimiwa Waziri atuthibitishie wananchi wa Wilaya ya Nachingwea ni lini atapata fedha ili kwenda kujenga mtambo huu?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimthibitishie tu kwamba tumeweka kipaumbele kwenye Mikoa ambayo iko pembezoni ambayo kwa kweli usikivu wa vituo vyetu vya Taifa umekuwa mdogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, binafsi nimefanya ziara kwenye Mikoa 13 ya pembezoni lakini kwa Mkoa wa Lindi ambapo mimi natoka na Waziri Mkuu anatoka, na sisi ni waathirika wa tatizo hili, nataka nikuhakikishie kwamba imefanyika tathimini na hivi tunavyoongea juzi Katibu Mkuu wa Wizara yangu ametoka huko pamoja na Mkurugenzi wa TBC wakiangalia namna tunaweza tukaanza hiyo kasi ya uboreshaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tu nikumbushe kwamba juzi Waheshimiwa Wabunge wamepitisha bajeti ya Wizara yangu na moja ya eneo ambalo tunawekeza kwa nguvu kubwa ni kuhakikisha tunaongeza usikivu. Wakati wa bajeti tulieleza hapa kwamba zaidi ya Wilaya 81 usikivu wa redio yetu hausikiki, kwa hiyo katika mipango yetu tutakwenda awamu kwa awamu na kipaumbele tutatoa kwa ile Mikoa ya mipakani na Mikoa inayoitwa ya pembezoni.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa redio ya Taifa (TBC)haipatikani kabisa katika maeneo ya Lushoto hasa maeneo ya Makanya, Mlolo, Mlalo, Lushoto na Bumbuli.
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga mitambo hiyo ili wananchi wa Wilaya ya Lushoto waweze kupata taarifa za nchi kama wananchi wengine?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza kwenye swali la nyongeza la Mheshimiwa Hamida, bahati nzuri kwenye hotuba yangu ya bajeti hapa tuliorodhesha Wilaya ambazo tutaboresha usikivu wake na Wilaya anayotoka Mheshimiwa Mbunge ni katika Wilaya tulizozitaja kabisa kwenye hotuba ya bajeti tuliyoiwasilisha hapa Bungeni.
Kwa hiyo nataka nikuhakikishie kwamba tathimini imekamilika, sasa kwa kuwa mmepitisha jana Finance Bill hapa fedha zitaanza kutoka na tutaweka kipaumbele kwenye eneo lako. Nikupongeze kwa kazi nzuri unayofanya kuwatetea wananchi wa Jimbo lako.
MHE. MASHIMBA M.NDAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile pia usikivu wa Redio ya Taifa ni dhaifu sana kwenye Mkoa wa Simiyu na kwa vile hakuna mwakilishi Mkoa wa Simiyu anayewakilisha TBC wala Redio ya Taifa. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwa na mwakilishi Mkoani na pia kuboresha usikivu huo?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mikoa ambayo nilitembelea mwanzoni ni pamoja na Mkoa wa Simiyu na nilipofika ni kweli nilikuta tatizo la TBC kutokuwa na mwakilishi. Hii ilitokana na kwamba Mkoa huu ulikuwa ni sehemu ya Mkoa wa Shinyanga. Kwa hiyo, TBC ilikuwa na mwakilishi pale Shinyanga, ulipopatikana Mkoa mpya taratibu zilikuwa zinafanyika za kupata mwakilishi pale, bahati mbaya taratibu hizo zilikuwa zinakwenda taratibu. Nilipotoka pale tumeagiza na taratibu hizo zimekamilika na sasa Mkoa wa Simiyu utakuwa na mwakilishi wa TBC na hivyo kazi za TBC zitafanyika vizuri katika Mkoa wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, bado liko tatizo la usikivu kama ilivyo katika mikoa mingine ambayo inakabiliwana tatizo hilo na Mkoa wa Simiyu ni katika mikoa ya kipaumbele katika uboreshaji wa matangazo ya Shirika la Utangazaji la Taifa.
MHE. ALLY M. KEISSY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Waziri ametembelea mpaka Wilayani kwangu Nkasi kule na kujionea mwenyewe jinsi matatizo ya mawasiliano ya Redio TBC hayafiki kule kwetu. Ni lini sasa bataweka mkazo ili watu wanaokaa mwambao mwa Ziwa Tanganyika waache kutegemea matangazo kutoka DRC Congo?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI,SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba katika Mikoa michache ambayo nimeitembelea ni pamoja na Mkoa wa Rukwa na Jimboni kwake Nkasi na nimpongeze kwa juhudi walizozifanya Halmashauri ya Wilaya Nkasi kwa kuanzisha redio yao na inafanya vizuri sana. Ni kweli pia kwamba usikivu wa Shirika la Utangazaji la Taifa kwa Wilaya ya Nkasi ni mbovu na baadhi ya maeneo yakiwemo ya Kabwe na maeneo mengine kwa kwa kweli wanasikiliza matangazo kutoka nchi jirani ya Congo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema tumeweka mkazo mkubwa kuhakikisha mikoa hii ya pembezoni tunaimarisha usikivu wa Shirika letu la Utangazaji la Taifa ili wananchi wetu waache kusikiliza redio za nchi jirani ikiwezekana watu wa nchi jirani wasikilize redio yetu na Shirika letu la Utangazaji wa Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie katika maeneo yote niliyotembelea kwa bahati nzuri, baada ya ziara yangu Mkurugenzi wa TBC Dkt. Rioba amekwenda huko nilikopita, na kuhakikisha kwamba yale niliyoyaagiza yanatekelezwa; na nichukue nafasi hii kumpongeza Mkurugenzi wa TBC kwa kazi nzuri anayofanya, ya kulibadilisha Shirika letu la Utangazaji na mimi naamini kwamba kwa kasi yake mambo yatakwenda vizuri.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ni haki ya kila mwananchi hasa Mtanzania kupitia kodi zao kusikiliza redio ya Taifa hasa TBC. Je, ni lini Serikali sasa itaweka booster yake ya TBC katika Mji Mdogo wa Itigi ili na wananchi wale wasikie redio yao ya Taifa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuambatana na mimi kwenye gari yake yenye redio nzuri ili atakapofika Itigi asikie matatizo yaliyoko pale?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba usikivu wa redio hasa Redio ya Taifa pale Itigi siyo mzuri lakini hii imetokana na mabadiliko ya teknolojia kutoka Mediam Waves (MW) kwenda FM. TBC kwa sasa inamalizia zoezi la kufanya uchambuzi wa kuangalia mahali ambapo tunatakiwa kuweka booster na maeneo mengine tunalazimika kupeleka mtambo. Sasa ni lini usikivu utaboreka, ni pale utaratibu huu wa kufanya uchambuzi utakapokamilika na ni hivi karibuni kwa sababu tupo mwishoni kabisa, upembuzi ukimalizika tutaamua sasa Itigi tunaweka mtambo au booster.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, mimi kama Waziri wa Habari nipo tayari kuambatana naye na yeye anajua kwamba Singida ni nyumbani kwetu. Najua usikivu pale ni mbovu ndiyo maana tunafanya kila liwezekanalo kazi hii ikamilike mapema tuweze kuongeza usikivu wa Redio ya Taifa kwenye eneo la Mheshimiwa Mbunge.
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante! Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina swali moja la nyongeza. Kwa kuwa umbali wa kutoka Songea na Mamba Bay - Nyasa bado ni mrefu, Serikali haioni haja ya kufunga mitambo angalau kwenye milima ya Mbuji ili kuongeza usikivu katika tarafa hizo zilizotajwa?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upembuzi uliyofanyika, huu mtambo utakaofungwa Mbamba Bay utakuja kukutana na mtambo uliofungwa hapa Matogolo na kwa pamoja usikivu utaongezeka badala ya kufunga kwenye Kata ya Mbuji kama anavyosema. Ni upembuzi wa Kitaalam umefanyika na hili likifanyika tutaongeza usikivu katika eneo lake na kwa sababu ni matokeo ya utafiti tunaamini hili likifanyika basi hayo ambayo Mheshimiwa Mbunge anayaombea hapa yatakuwa yamefanyika na usikivu utaongezeka.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. TBC na Radio ya Taifa ndiyo visemeo vya Serikali. Je, wakati mnaboresha mitambo, Serikali ina utaratibu gani wa kuwapeleka wafanyakazi wa TBC na Radio ya Taifa kwenda nje kujifunza ili kusudi waendane na teknolojia ya sasa, kuwapeleka nje kwenda kusoma?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Ndassa kwa kazi nzuri anayofanya ya kutetea tasnia ya habari kwa sababu na yeye mwenyewe ana background ya habari. Pili TBC imekuwa na mipango mizuri ya kuwapeleka wafanyakazi wake kwenda kuongeza ujuzi wao nje ya nchi, lakini pia na kuwaalika Wataalam mbalimbali kuja hapa kwa ajili ya kuongeza ujuzi wao. Mfano mzuri, wenzetu wa China wamekuwa wakitusaidia sana, wafanyakazi wengi wanakwenda kujifunza. Hata hivi tunapoongea wako wafanyakazi ambao wanaongeza ujuzi wao China, lakini tunao Wachina ambao wako hapa kupitia ushirikiano wa TBC na Star Times, nao wanaongeza ujuzi wa watu wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaamini program hizi zitaendelea na tutaendelea kuziboresha mara kwa mara ili wafanyakazi wetu waendane na kasi ya mabadiliko ya teknolojia duniani.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Spika, naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa sasa hivi suala la michezo Tanzania ni sawasawa na mgonjwa na unapokuwa na mgonjwa aidha umpeleke kwenye maombi, hospitali au kwa mganga wa kienyeji.
Sasa kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amekiri na anajua tatizo hilo na tatizo kubwa limekuwa ni kwamba Serikali imeshindwa kuwekeza kutoka chini kwa maana ya kwenye shule za msingi, UMISHUMTA, UMISETA na michezo mingine na kuifuta, sasa Serikali inasemaje kuhusu kufufua michezo hiyo kwa nguvu zote na kupanga bajeti ya kutosha? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa michezo ni ajira na Serikali ilikiri yenyewe kwamba itahakikisha inapeleka ajira kwa vijana kupitia michezo; na michezo inaleta pato la Taifa kwa mfano nchi kama Nigeria, Cameroon na Ghana imekuwa ni pato, sasa Serikali kwa nini imesahau kwamba hiyo itakuwa ni pato kubwa kwa nchi yetu na kuitelekeza michezo? Naomba jibu. (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, la kwanza Serikali haijafuta michezo ya UMISHUMTA, UMISETA kama ambavyo imekuwa ikikaririwa, isipokuwa mwaka huu kilichotokea ni kwamba michezo hii iliahirishwa kwa muda, kwa sababu ya kuwa na maandalizi ambayo hayakuwa yanaridhisha na hivyo tukasema ni vizuri tujipange upya ili michezo hii iwe na maana.Kwa muda mrefu sasa michezo ya UMISHUMTA, UMISETA imekuwa ikifanyikakama matamasha ikifikia kilele mwishoni hakuna matokeo yanayoendelezwa baada ya michezo ile.
Mheshimiwa Spika, Serikali inajipanga kuhakikisha kwamba, michezo hii sasa inapofikia kilele chake wale wanaofanya vizuri wanapelekwa kwenye shule maalum zitakozotengwa kwenye Mikoa na Wilaya kwa ajili ya kuendeleza vipaji vyao badala ya kutokea kama ambavyo imekuwa ikitokea, michezo ile ikimalizika watoto wanarudi kwenye shule zao na vile vipaji vinapotea.
Mheshimiwa Spika, lakini la pili kwamba suala la uwekezaji kwenye michezo. Ni kweli michezo inahitaji uwekezaji mkubwa, kwa uwekezaji mdogo hatutapata matokeo ya kutosha. Serikali haijatelekeza michezo kama ambavyo nimejibu katika jibu la msingi kwamba Serikali itaendelea kutenga fedha kwenye bajeti zake, lakini na kuangalia vyanzo vingine ambavyo hata wenzetu wamekuwa wakivitumia kuendeleza michezo. Vyanzo vingine ni pamoja na pesa zinazotokana na Bahati Nasibu za Taifa. Duniani kote Michezo ya Bahati Nasibu ya Taifa ndio ambayo imekuwa ikifadhili michezo badala ya kutegemea hii bajeti ndogo.
Mheshimiwa Spika, niendelee kutoa wito kwa sekta binafsi kushirikiana na Serikali kusaidiana katika kuwekeza katika michezo, tumeona sasa tunakoelekea michezo itakuwa ni biashara kubwa, italipa na hivyo natoa wito kwa wadau mbalimbali kuwekeza katika michezo wakishirikiana na Serikali na tukifanya hivyo tunaamini tutapata matokeo mazuri.
MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nilikuwa na maswali mawili madogo ya nyongeza kama ifuatavyo:-
La kwanza, mwanamke ni tunu katika uumbaji wa maisha ya mwanadamu na kwa kuzingatia mila na desturi zetu za Tanzania nilikuwa nataka kujua Serikali inawashirikisha vipi viongozi hawa wa dini wakishirikiana na wasanii hao pamoja na majibu yake aliyotoa juu ya elimu kwa umma na umuhimu wake?
La pili katika Serikali ya Awamu ya Nne iliyopita Waziri husika alikuwa ameunda Kamati ya Vazi la Taifa ambalo nchi zawenzetu wengine wa hapa Afrika, ndio kutambulisha Utaifa wao nilikuwa nataka Mheshimiwa Waziri atueleze jambo hili limefikia hatua gani na mikakati yake endelevu? Ahsante.
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, la kwanza juu ya ushiriki wa viongozi wa dini na makundi mengine katika jamii katika kuhakikisha sanaa yetu inatumika vizuri na haimdhalilishi mwanamke.
Mheshimiwa Spika, nikiri kwamba kwanza ni kweli kwamba mwanamke ni ana hadhi yake katika jamii na hasa katika jamii zetu za Kiafrika na nimpongeze sana Mheshimiwa Mary Mwanjelwa kwa namna anavyopigania hadhi ya mwanamke katika Taifa letu. (Makofi)
Wizara yangu inatoa wito si tu kwa viongozi wa dini hawa wasanii wetu wamo katikakati ya jamii zetu, hawa wasanii ni watoto wetu, ni ndugu zetu na wanaingia kwenye nyumba mbalimbali za ibada na kukutana na viongozi wetu wa dini, natoa wito kila mmoja wetu aone kwamba kuna umuhimu wa kila mmoja kushiriki na kuwahamasisha wahakikishe wanazingatia maadili ya Mtanzania katika shughuli zao za sanaa.
Mheshimiwa Spika, nataka nilihakikishie Bunge lako ikiwa jamii itayakataa matendo yanayofanywa na wasanii, wasanii hawa wataacha kufanya hayo matendo, lakini ikiwa jamii inayashabikia na kuyapenda, wasanii hao wataona ndio fashion na wataendelea kufanya. Kwa hiyo, hata kama sisi tukihamasisha namna gani kama jamii haitayakataa na kuyaona hayafai, kila Mtanzania akaona mwanamke akidhalilishwa amedhalilishwa mzazi wake, amedhalilishwa ndugu yake, haya matendo yatakoma katika jamii yetu.
Kwa hiyo nadhani ni suala la jamii yetu zaidi kuyakataa na kuwatenga kijamii wale ambao wanafanya shughuli za kuwadhalilisha akina mama wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili la Vazi la Taifa na wakati wa bajeti niliulizwa hili swali na nililitolea ufafanuzi, ni kweli ulifanyika mchakato wa kutafuta Vazi la Taifa hapa lakini tulikuja kugundua kwamba ule mchakato tukiendelea nao mpaka mwisho tunaweza tukajikuta tumetoka na vazi la viongozi na sio Vazi la Taifa. Jamii yetu Watanzania tuna makabila 126 kila kabila lina aina yake ya kuvaa, mnaweza mkaendeleza mkafanya mchakato mkafika mwisho halafu mnakwenda mnawaambia Wamasai waache mavazi yao wachukue hili la kwenu, iko hatari ya kuwa na vazi la viongozi na badala ya kutengeneza Vazi la Taifa. Sasa tukatoa wito kwamba kwa ule mchakato ulipofikia ulipendekeza vazi la kanga kuwa ndio vazi preferable ambalo kwa kweli watu wanaweza wakalitumia. Lakini tunaogopa kufikia mahali pa kutengeneza vazi tukalilazimisha na likabaki kuwa vazi la viongozi.
Mheshimiwa Spika, lakini hata hayo mataifa mengine ambayo yana mavazi ambayo yanaonekana yanawakilisha Utaifa wao hawakufanya mchakato wa kufikia Vazi la Taifa. Ilikwenda ikatokea wakajikuta wana vazi, likapendwa na walio wengi na likarasimishwa. Hapa tukiendelea na mchakato huu tutatengeneza vazi la viongozi na halitakuwa Vazi la Taifa letu.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Wananchi wa Karagwe tunamkumbuka Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa push-up za kihistoria alizozipiga pale Kayanga. Je, Serikali mnaonaje kama mkitusaidia kujenga uwanja wa Wilaya pale Kayanga ili tuweze kumuenzi Rais wetu kwa ule ukakamavu alioonyesha kwa vijana wa Karagwe? Nashukuru sana
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kweli kwamba push-up kwa mara ya kwanza zilipigwa kwenye eneo ambalo Mheshimiwa Mbunge anasema, hii ilithibitisha uwezo wa Rais John Pombe Magufuli wa afya yake, lakini pia ulionyesha kwamba Serikali atakayoiunda ni Serikali ya Hapa Kazi Tu tofauti na wenzetu mgombea wao nadhani hiyo kazi ilikuwa ngumu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Wizara kwa kushirikana na Halmashauri anakotoka Mbunge tunaweze kuzungumza kuona namna ya kushauriana kuweka kumbukumbu hii muhimu ya Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi nzuri inayofanywa. Kwa hiyo, Wizara na Halmashauri ambapo anatoka Mbunge tutakaa pamoja tuzungumze tuone namna ya kuweka hii kumbukumbu muhimu.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, natoa shukrani zangu kwa Mheshimiwa Waziri kwa majibu ya kutia matumaini. Lakini nataka ieleweke kwamba Wilaya ile ya Liwale ipo mbali sana na makao makuu ya Mkoa, Wilaya ya Liwale haina usafiri, haina barabara za kutosha yaani za kuaminika, Wilaya ya Liwale haina mtandao wa simu unaoaminika, Wilaya ya Liwale haina usikivu wa redio. Sasa muone jinsi Wilaya hii ilivyo kisiwani, hawa ni miongoni mwa walipa kodi wa nchi hii, sijui kama kodi zao watanufaika nazo vipi? Nashukuru kwa jibu la kwanza nimepata timeframe na mimi nitafuatilia kuhakikisha hii timeframe inafikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa swali la pili napata wasiwasi, nimepata tu majibu ya moja kwa moja. Nahitaji kujua ni lini Redio Tanzania itasikika Liwale? Hapa nimepewa tu majibu ya jumla jumla. Mwisho kabisa hapa amesema kwamba mpango wa muda mrefu sasa hata huo mpango wa muda mfupi nao haujatajwa, huo ni wa lini? Naomba nipatiwe majibu.
vipi? Nashukuru kwa jibu la kwanza nimepata timeframe na mimi nitafuatilia kuhakikisha hii timeframe inafikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa swali la pili napata wasiwasi, nimepata tu majibu ya moja kwa moja. Nahitaji kujua ni lini Redio Tanzania itasikika Liwale? Hapa nimepewa tu majibu ya jumla jumla. Mwisho kabisa hapa amesema kwamba mpango wa muda mrefu sasa hata huo mpango wa muda mfupi nao haujatajwa, huo ni wa lini? Naomba nipatiwe majibu.
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona. Nami ni mdau mkubwa wa michezo na hasa mchezo wa soka. Mchezo wa soka ni mchezo unaopendwa nadhani kuliko mchezo wowote duniani na ni mchezo ambao unaweza kutumika kuwa kiunganishi muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, kulikuwa na tuhuma za rushwa katika suala hili kwa kuwa, mchezo huu ni kipenzi cha watu wengi, je, Waziri anaweza kuliambia Bunge hili kwamba, ni lini sasa uchunguzi huu utafika mwisho na wahusika kuchukuliwa hatua ambazo zinatakiwa kuchukuliwa? Ahsante sana.
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema TAKUKURU wanakamilisha utaratibu. Wakati mwingine uchunguzi wa makosa hasa ya rushwa ambayo kwa namna moja ama nyingine wahusika wa pande mbili wanakuwa wamekubaliana huwa yanaweza yakachukua muda mrefu na wakati mwingine kupata uhalisia wake inakuwa ngumu, lakini habari nilizonazo ni kwamba, TAKUKURU wako hatua za mwisho za kukamilisha uchunguzi huo na baada ya kukamilisha uchunguzi huo, hatua zinazostahiki zitachukuliwa.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Wizara hii inashughulika na habari, utamaduni, sanaa na michezo. Kwa idhini
yako, naomba uniruhusu niulize swali la michezo. Timu yetu ya vijana under 17
imebahatika kwenda kwenye fainali itakayofanyika Gabon Aprili, ni mwezi
mmoja tu sasa umebaki. Je, Serikali pamoja na TFF tunajiandaa namna gani ili
timu yetu hii isiende kushiriki bali iende kushindana na kuleta ushindi katika nchi
yetu?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu
Spika, ni kweli kwamba Serengeti Boys wamefanya vizuri sana katika mchezo wa
mpira wa miguu katika nchi yetu na kuiletea heshima nchi yetu. Nichukue nafasi
hii kuwapongeza kwa moyo wao wa dhati ambapo wamejitahidi kupambana
na kwa kweli wanafanya vizuri. Kama Serikali, kwanza nilihakikishie Bunge lako
kwamba tumeshiriki kikamilifu kwa wao Serengeti Boys kufanikiwa kufika pale
walipofika ikiwemo kutafuta rasilimali kwa wadau. Niwashukuru sana wadau wa
sekta binafsi ambao wamekuwa wakijitolea kuhakikisha timu yetu hii inafanya
vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kwa kushirikiana na TFF tumejipanga
kwamba Serengeti Boys watakwenda kupiga kambi ya mwezi mzima kabla ya
kwenda kwenye fainali za mashindano haya. Serikali ikishirikiana na wadau wa
sekta binafsi, tutahakikisha zinapatikana rasilimali za kutosha kuhakikisha vijana
hawa wanapiga kambi yao, lakini pia wanakwenda kuchukua kombe na siyo
kushiriki. Kila tukiangalia uwezekano wa kushinda, ni mkubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe Waheshimiwa Wabunge na
Watanzania kwa pamoja tuungane pamoja kwa dua zetu na rasilimali zetu
kuhakikisha kwamba Serengeti Boys wanakwenda na wanarudi na ushindi hapa
nchini.