Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Josephine Tabitha Chagulla (7 total)

MHE. JOSEPHINE T. CHAGULA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Namshukuru sana Waziri kwa majibu yake mazuri na ya kututia moyo wananchi wa Mkoa wa Geita. Nina swali moja tu la kumuuliza. Kwa kuwa vijana wetu wangependa sana kujiajiri au kuajiriwa, lakini hawana ujuzi; je, Serikali iko tayari kuwapa ujuzi?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, hili ni kwa Waheshimiwa Wabunge wote na Watanzania wote. Katika kila Mkoa kuna Ofisi ya SIDO. Mojawapo ya kazi ya SIDO ambayo analipwa pesa na Serikali ni kutoa elimu ya ujasiriamali kwa watu wote. Semina na mafunzo yale yanatolewa bila gharama.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Chagula, awasiliane na Meneja wa Geita, aandae vijana wake waende wapate elimu hiyo, halafu kuanzia hapo tuone watajiendeleza namna gani.


WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WATU WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwanza kabisa naomba nikubaliane na sekta ambayo inaongozwa na Waziri mwenye dhamana ya Viwanda na Biashara kupitia SIDO ili kutengeneza ujuzi na kuajiri vijana wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuliarifu Bunge lako Tukufu kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Kitengo kinachoshughulikia Kazi, Vijana na Ajira katika bajeti ya mwaka 2016/2017, Serikali imetenga fedha ambazo zitatumika kwa makusudi mazima kuongeza ujuzi kwa vijana mbalimbali walioko katika nchi ya Tanzania na ili kuwafanya vijana hao; kwanza, waweze kujiajiri wao wenyewe, lakini vilevile waweze kuajiriwa katika viwanda vilivyopo na vitakavyoanzishwa katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunawahakikishia Waheshimiwa Wabunge kwamba, shilingi bilioni 15 zilizotengwa zinaweza kutoa msaada mkubwa sana wa kuongeza ujuzi kwa vijana wa Tanzania na kukabiliana na tatizo hili la ukosefu wa ajira.
MHE. JOSEPHINA T. CHAGULA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri. Naomba nimwulize swali moja tu la nyongeza. Kwa kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa sana la wagonjwa wa kisukari katika jamii yetu na inavyoonekana, jamii bado haijapata uelewa mkubwa kuhusu kujikinga na ugonjwa huu wa kisukari. Je, Serikali haioni ni muda muafaka kuja na mpango mkakati wa kutoa elimu kwa jamii ili kuweza kujikinga na baadhi ya vyakula pamoja na kubadilisha staili ya maisha yetu tunayoishi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda kumshukuru Mheshimiwa Josephina Tabitha Chagula, Mbunge wa Viti Maalum kwa swali lake la nyongeza. Nalijibu kwanza kwa kutambua ushiriki wake yeye mwenyewe kwenye mazoezi kila siku asubuhi na baadhi ya Wabunge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, napenda kuwatambua Waheshimiwa Wabunge wote wanaounda timu ya Bunge Sports Club kwa jitihada wanazozifanya kuamka asubuhi na mapema na kwenda kushiriki kwenye mazoezi. Natoa rai kwa wananchi wote kufuata mfano mzuri anaouonesha Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wote na mimi mwenyewe kwa kushiriki kwenye mazoezi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo tu tunajenga afya zetu lakini pia sisi kama viongozi tunatoa mfano bora kwa wananchi wote kushiriki kwenye shughuli mbalimbali za kijamii, lakini pia kufanya mazoezi kwa ajili ya kulinda afya zetu. Kufanya hivyo, siyo tu kunajenga miili yetu, lakini pia kunaipunguzia gharama Serikali. Takwimu zinaonesha kwamba kufikia mwaka 2020 mzigo wa magonjwa duniani utakuwa mkubwa kiasi cha kufikia kiwango cha asilimia 73 na katika mzigo huo nchi za Afrika zinatarajiwa kuchukua share kubwa kuanzia mwaka huo wa 2020 niliyoutaja.
Mheshimiwa Naibu Spika, sababu ya hayo ni kwamba dynamics za maisha ya binadamu kwenye nchi zinazoendelea kama ya kwetu zimebadilika sana, hususan kwenye maeneo ya mijini ambapo lifestyle sasa imekuwa ni watu kukaa kwenye magari, watu kutokujishughulisha na shughuli mbalimbali ambazo ni physical ambazo zinaweza zikapunguza sukari mwilini na matokeo yake mzigo wa magonjwa ya kuambukiza unaongezeka siku hata siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inaendelea kuwaelimisha wananchi kupitia vyombo mbalimbali vya habari, lakini pia ikishirikiana na wadau mbalimbali kama Tanzania Diabetes Association ambayo napenda kuitambua kwa mchango wake mkubwa kwenye kupambana na ugonjwa wa kisukari.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge tushiriki kwenye kuelimisha jamii kwenye majimbo yetu na ku-support michezo ili kuwaokoa watu wetu. (Makofi)
MHE. JOSEPHINE T. CHAGULA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba nimuulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la ukosefu wa nyumba za kuishi watumishi katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale ni kubwa sana; watumishi hawa hulazimika kutembea umbali wa kilometa 50 mpaka 80, lakini wengine wanaishi Mkoani kabisa Geita ambako ni umbali wa kilometa 100. (Makofi)
Je, Serikali haioni kuna haja sasa ya kuharakisha majengo haya ili watumishi hawa waweze kuishi karibu na ofisi zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, tumekisikia kilio hiki, ndiyo maana mwaka huu tumetenga bajeti ya shilingi milioni 850.
Nawapongeza kwa sababu mshauri ameshaanza zile kazi za awali; ramani imeshapatikana na bajeti iliyolipwa pale kwa shilingi milioni 177, pesa iliyobakia inaonekana mkandarasi aliyepatikana hawezi kuanza kufanya kazi. Ndiyo maana tumesema kwamba mwaka huu tumetenga shilingi milioni 850, lengo letu kubwa ni kwamba tukichanganya na zile za mwanzo sasa, mkandarasi aweze kuingia site na hii kazi iende kwa haraka.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mchakato huu wa bajeti tutaharakisha fedha hizi ziende mapema ili mradi ujenzi uweze kuanza kwa wakati ili kuondoa kero kwa watumishi hawa ambao wanasafiri katika umbali mrefu.
MHE. JOSEPHINE T. CHAGULA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na ya kutia moyo wananchi wa Nyang’hwale.
Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya cha Kharumwa kilipopandishwa hadhi na kuwa Hospitali ya Wilaya ya Nyang’hwale lakini bado hakijapata watumishi wa kutosha kulingana na hadhi hiyo ya Hospitali ya Wilaya. Je, ni lini Serikali itapeleka watumishi wa kutosha pamoja na vifaa tiba vya kutosha katika Hospitali hiyo ya Wilaya ya Nyang’hwale?(Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kumekuwa na msongamano mkubwa sana katika Hospitali zetu hizi za Rufaa kama vile Bugando na kwingine ukitaka kuonana na Daktari Bingwa; je, Serikali, haioni ni muda muwafaka sasa kuweza kupeleka Madaktari Bingwa wa watoto pamoja na akina mama katika hospitali zetu za Wilaya, ili kuondoa usumbufu huo usiokuwa wa lazima kwa wananchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, ni kweli kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge ndiyo maana kwa haja ya Waheshimiwa Wabunge wa Geita hasa ndugu yangu Mheshimiwa Hussein Omar na Mheshimiwa dada yangu Josephine, katika Kituo hiki cha Afya cha Kharumwa kwanza, jambo kubwa tutakalolifanya, licha ya zile bajeti ambazo wenyewe wamezitenga, hivi sasa tutaenda kufanya ukarabati mkubwa wa kituo kile, tutajenga theatre ya kisasa. Lengo kubwa ni kwamba, wale Wasukuma wenzangu wa pale waweze kupata huduma nzuri. Kwa hiyo tutawekeza juhudi hii ya kutosha katika kile, kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge naomba nikutoe hofu katika hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo tunafahamu kwamba changamoto kubwa ni changamoto ya wataalam na bahati nzuri kama ninavyofahamu hata zoezi hili la uhakiki wa watumishi hewa kwenye maeneo mbalimbali tumepata ripoti kwamba idadi ya watumishi hasa katika sekta ya afya, imeathirika sana. Pamoja na watumishi hewa, lakini pia kuna suala zima la ku-forge vyeti. Sasa hivi Serikali iko katika harakati mbalimbali za kuwaajiri watumishi wapya. Naomba nikutoe hofu Mheshimiwa Josephine kwamba tutakapotoa ajira hizi mpya, ambazo si muda mrefu Wizara ya Utumishi watatoa maelekezo nini cha kufanya, tutaelekeza watumishi katika eneo letu hili la Nyang’hwale ili wananchi wa eneo lile waweze kupata huduma nzuri.
Mheshimiwa Spika, kuhusu hoja hii nyingine ya msingi hasa suala zima la madaktari bingwa ni kweli na ndiyo maana leo hii, hasa magonjwa yale ya akinamama, wakati mwingine watu wengi wanatoka mikoani wanaenda Dar es Salaam kwa ajili ya kwenda kuwaona gynecologists. Na kwa sababu hii Serikali yetu inaangalia jinsi gani itafanya ili kuweka uwiano mzuri katika kada mbalimbali zitakazoajiriwa, lakini lazima kuelekeza hawa wataalam katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, tukifanya hivyo tutapunguza hii changamoto ya wananchi ambao wengi wao kwenda muhimbili au kwenda sehemu nyingine yoyote ya mbali kwa kujisafirisha inakuwa kazi kubwa. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge nasema hoja yako imekubaliwa, na katika hili Serikali tutafanya kila liwezekanalo kuhakikisha kwamba tunapeleka watalaam bingwa katika maeneo yetu haya.
MHE. JOSEPHINE T. CHAGULA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nampongeza sana na kumshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na ya kututia moyo wananchi wa Mkoa wa Geita, lakini nina swali moja tu la nyongeza naomba nimuulize.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, Benki ya Wanawake iko Mjini Dar es Salaam, lakini asilimia kubwa ya wanawake wanaishi vijijini. Je, Serikali ina mpango gani basi wa kuweza kupeleka Benki ya Wanawake katika Mikoa yote, ikiwepo Mkoa wangu wa Geita? (Makofi)
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Chagula kwa maswali yake mazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Benki ya Wanawake imefungua matawi mawili Dar es Salaam, lakini tuna madirisha ya kutoa huduma katika Halmashauri takribani 20.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, habari njema ambazo nataka kumfahamisha Mheshimiwa Josephine Chagula ni kwamba, tulikuwa katika misukosuko kidogo, lakini tumefanya Forensic Audit ya Benki ya Wanawake na tumeweka Bodi mpya, lakini pia tuna a very dynamic young man ambaye ndiye Mkurugenzi Mtendaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sasa hivi tuko tayari, tutaongea na wenzetu wa Hazina ili sasa watukamilishie ule mtaji ambao Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne aliuahidi ili sasa tufungue matawi katika Mikoa yote na lengo letu ni kuhakikisha wanawake wanapata mikopo yenye masharti nafuu kuliko benki nyingine. Ahsante sana.(Makofi)
MHE. JOSEPHINE T. CHAGULA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza niishukuru sana Serikali kwa mkakati huo, pia nimshukuru sana Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na ya kutia moyo. Nina swali moja tu la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Mkoa wa Geita imekuwa ikihudumia wagonjwa wengi sana kiasi kwamba inaelemewa kabisa. Hii ni kutokana na mapungufu makubwa yaliyopo katika Hospitali zetu za Wilaya. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuweza kuboresha hospitali zetu hizi za Wilaya ili kupunguza msongamano wa wagonjwa uliopo katika Hospitali yetu ya Mkoa wa Geita? Ahsante.
(Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi Serikali ina nia njema ya kuhakikisha kwamba, kwanza si kuimarisha Hospitali za Wilaya, tunaanzia kwanza kuimarisha vituo vya afya ndiyo maana pesa nyingi sana imepelekwa ili kupunguza ule msongamano ambao wananchi watalazimika kwenda hospitali ya Wilaya. Kama hilo halitoshi tunajua kabisa, ili kuweza kupunguza mlundikano kwa wananchi ambao wangependa kwenda hospitali za mikoa ni kuwa na uhakika wa kutibiwa katika hospitali za wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwatake wananchi na Halmashauri zetu zote nchini, wahakikishe kwamba, maeneo kwa ajili ya kujenga hospitali za Wilaya yanatengwa kwa kufuata viwango ambavyo vinatakiwa na Halmashauri kwa kutumia own source waanzishe na Serikali itaweka mkono wake. (Makofi)
MHE. JOSEPHINA T. CHAGULA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na ya kujitosheleza. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa mahitaji ya maji katika Mji wa Geita na vitongoji vyake ni makubwa mno ukilinganisha na maji tunayopata; mahitaji halisi ni lita milioni 15 kwa siku, lakini maji tunayopata ni lita milioni nne kwa siku. Kwa hiyo, tuna upungufu wa lita milioni 11 ambayo ni sawa na asilimia 29 kwa siku. Je, Serikali haioni kuna haja sasa ya kuongezea nguvu na uwezo Mradi wa Ziwa Victoria ili tuweze kupata maji ya kutosha kulingana na mahitaji yetu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kuna mradi wa maji katika Wilaya ya Nang’hwale. Mradi huu ni wa siku nyingi sana, hivi sasa ni miaka sita tangu uanzishwe, bado wananchi wanateseka wanahangaika kwa kupata maji. Naishukuru Serikali kwa kuweza kutenga shilingi bilioni moja kwa ajili ya maji katika Wilaya ya Nang’hwale, je, Naibu Waziri yuko tayari sasa kwenda Nang’hwale ili akajionee hali halisi ya mradi ule ambao sasa hivi ni miaka sita haujakamilika na wananchi wanaendelea kuteseka mpaka sasa? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Chagula, yeye ni mama na anadhihirisha kwamba mama wajibu wake ni kuhakikisha familia inapata maji. Nimkumbushe kwamba Serikali tayari imeshatekeleza awamu mbili za Programu ya Kulinda Ziwa Victoria, awamu ya kwanza ilikamilika na awamu ya pili imekamilika Desemba, 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi tumeanza awamu ya tatu na katika awamu hii Mheshimiwa Chagula, tayari tumepanga kutekeleza miradi kutoa maji Ziwa Victoria kupeleka Ilemela, Buchosa, pale Geita, Katoro Buseresere. Pia tunatarajia haya maji tutapeleka hadi Mbogwe. Hili eneo la Mbogwe linaweza likapata maji kutoka eneo la Katoro, Buseresere au kutoka Msalala.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, mradi huu utahusisha pia kupeleka maji Buhongwa, Sumve na Usagara. Majadiliano na wafadhili wakiwemo European Investment Bank, Benki ya Maendeleo ya Afrika, yanaendelea vizuri na pia tutahakikisha kwamba hili eneo la Geita Mjini ambao ni mkoa mpya nalo limeingizwa ili tuweze kuongeza kiwango cha maji katika hilo eneo.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kuhusu Nyang’hwale, kwa bahati nzuri nimetembelea Nyang’hwale nikakuta ule mradi umekaa muda mrefu sana. Nilitoa maelekezo na kila siku tatu naongea na Mbunge wa Nyang’hwale ili awe ananipa progress nini kinaendelea. Ameniridhisha kwamba mkandarasi sasa yuko site. Na mimi sasa kwa sababu ameomba kwenda na Mheshimiwa Naibu Waziri, nampa kibali hapa hapa Mheshimiwa Mbunge aende naye. (Makofi/Kicheko)