Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Vedasto Edgar Ngombale Mwiru (26 total)

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nachukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pia kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia katika mjadala wa Taarifa ya Kamati yangu kwa mwaka 2016. Michango mbalimbali mizuri imetolewa na naitaka Serikali sasa kujipanga na kuona namna bora ya kurekebisha kasoro nyingi zilizoainishwa na Waheshimiwa Wabunge ili kupunguza matumizi mabaya ya fedha za umma na kuongeza ari ya uwajibikaji katika Halmashauri nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na jumla ya wachangiaji 46 ambao wamechangia kwa hoja mbalimbali za Kamati yangu; kati yao 39 wakichangia kwa maneno na saba wakichangia kwa maandishi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia katika maeneo yaliyogusia matumizi yasiyozingatia Sheria ya Manunuzi ya Umma, upelekaji usioridhisha wa fedha kwenye Halmashauri kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, asilimia kumi ya mapato kutochangiwa katika Mfuko wa Wanawake na Vijana, Halmashauri kutopeleka asilimia 20 ya ruzuku kutoka Serikali Kuu katika Serikali za Mitaa na Vijiji na Marekebisho ya Sheria ya Manunuzi ya Umma kwa kuwa sheria hii inakinzana na hali halisi ya bei za bidhaa katika soko na mwisho uwezo mdogo wa kiutendaji wa baadhi ya Wakurugenzi wa Halmashauri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iangalie uwezekano wa kutumia chuo cha mafunzo ya Serikali za Mitaa Hombolo kutoa mafunzo kwa Wakurugenzi wapya wa Halmashauri kama ilivyoshauriwa na Mheshimiwa Issa Mangungu, Mheshimiwa Godfrey Mgimwa na Mheshimiwa Abdallah Chikota. Pia Ndugu yangu Mheshimiwa Silinde alisema na kupendekeza kwamba ni vizuri sasa Serikali iangalie uwezekano wa kuwatumia watumishi wanaotokana na Watumishi wa Serikali ili iwe motisha chanya kwa wale Wakuu wa Idara katika utendaji wa kazi, maana kwa hali iliyopo sasa watumishi wengi katika Halmashauri ile ari ya kufanya kazi imeshuka sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, idadi kubwa ya Waheshimiwa Wabunge ilikuwa inaitaka Serikali itenge bajeti ya kutosha kwa Bunge ili Wabunge waweze kutekeleza majukumu yao kwa kuisimamia Serikali hususan kufanya ukaguzi wa miradi ya maendeleo badala ya kufanya vikao na mahojiano ya ana kwa ana na Menejimenti za Halmashauri hapa Dodoma. Kimsingi ukaguzi ni moja kati ya shughuli muhimu katika kuhakikisha kuwa kuna nidhamu katika matumizi ya fedha za umma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wamechangia hoja ya ufinyu wa bajeti ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi unaosababisha ofisi hii muhimu kushindwa kutekeleza majukumu yake kikamilifu. Hili limezungumzwa na ndugu yangu Mheshimiwa Khatibu na kusema kwamba Serikali inazibana Kamati za usimamizi wa fedha za Serikali, lakini inaibana Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi. Kwa hiyo, mimi situmii ile terminology nyingine aliyotumia Mheshimiwa Khatibu, ila niseme tu kwamba Serikali ilegeze kubana ili basi mambo yaweze kwenda sawasawa. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati za usimamizi wa fedha zinatekeleza majukumu yake kwa kutumia taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, lakini kutokana na ufinyu wa bajeti, mwaka huu CAG ameshindwa kutembelea baadhi ya Halmashauri kufanya ukaguzi na uthibitisho wa majibu ya hoja mbalimbali za ukaguzi. Ufinyu huu wa bajeti usipotatuliwa katika bajeti zinazokuja, kuna hatari ya CAG kushindwa kufanya ukaguzi kabisa na hivyo Kamati hazitaweza kuendelea na majukumu yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwepo na michango mizuri inayohusu usimamizi mbaya wa mikataba na utekelezaji wa miradi ya maendeleo uliobainishwa na Kamati. Naamini kwamba Serikali imeliona hilo na italifanyia kazi hasa kuboresha usimamizi wa mikataba kwa kuwa miradi mingi ya maji katika mwaka wa fedha 2013/2014 na mwaka wa fedha 2014/2015 haikutekelezwa kikamilifu kwa sababu mikataba mingi ilivunjika kabla ya miradi kukamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Leah Komanya, Mheshimiwa Martin Msuha, Mheshimiwa Richard Mbogo kwa kutoa maelezo mazuri juu ya mfumo wa fedha wa EPICOR. Mfumo huu niseme wazi umegharimu Serikali fedha nyingi katika kuziunganisha Halmashauri nchini, lakini utendaji kazi wake hauna tija. Baadhi ya taarifa kwa mfano, taarifa za mali za Halmashauri zinaandaliwa nje ya mfumo. Ifikie wakati Serikali ione kuwa mfumo huu una changamoto nyingi na hivyo haufai kwa mazingira ya sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu wa sasa kupata taarifa za Halmashauri ni mgumu kwa kuwa vitabu vinavyowasilishwa huwa vikubwa mno na mapitio yake huwa magumu mno. Dunia ya sasa inaelekea katika mfumo wa nyaraka laini (electronic filing system). Hili limezungumzwa sana na Mheshimiwa Conchesta Rwamlaza kwamba Kamati inakutana na malundo ya vitabu ambavyo kuvifanyia upembuzi inakuwa ngumu sana. Hivyo Serikali iangalie uwezekano wa kuanzisha mfumo huu kwa Halmashauri nchini. Hii itapunguza hatari ya gharama za kudurufu vitabu hivi ambavyo ni vikubwa na mzigo mkubwa kwa Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mjadala baadhi ya Waheshimiwa Wabunge walishauri Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani kuwa huru na kuwa kipangiwe bajeti ya kutosha ili kiweze kusimamia mwenendo wa fedha za Halmashauri. Wazo hili ni zuri kwa kuwa hata Kamati yangu ilibaini tatizo hili. Serikali iendelee kusisitiza kuangalia namna bora ya utendaji kazi wa kitengo hiki ili kulinda fedha za umma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Pauline Gekul alifafanua kwa undani namna bora ya Mfuko wa Wanawake na Vijana ambavyo unawabagua wazee ambao nao kimsingi wanayo mahitaji ya fedha kwa ajili ya mahitaji ya biashara ndogo ndogo na shughuli nyingine. Kamati iliona hilo na nichukue tena fursa hii kusisitiza uundwaji wa Sheria ya Mfuko huu ili kuongeza tija, ikiwa ni pamoja na kuangalia changamoto ambazo Kamati imeziainisha katika taarifa yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimepokea pia mchango wa Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe kwa maandishi kuhusu suala la Mfuko wa Wanawake na Vijana. Nakubaliana na wazo lake la kuangalia uwezekano wa Serikali kutumia mfumo wa hifadhi ya jamii ili kuhakikisha usalama wa fedha za umma. Kimsingi ushauri wake ni mzuri kwa kuwa una faida za ziada kwa wanavikundi; kama vile utaratibu wa kujiwekea akiba, kupata fao la Bima ya Afya na kupata fursa ya huduma ya SACCOS ili kupanua wigo wa biashara zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, limekuwepo suala la Serikali kuchukua vyanzo vya mapato vya Halmashauri kama vile ushuru wa ardhi na ushuru wa nyumba. Waheshimiwa Wabunge wengi waliochangia wamelalamikia suala hili la Serikali kukusanya ushuru wa ardhi na kutopeleka asilimia 30 katika Halmashauri kama ilivyokubaliwa. Niseme wazi, ushuru huu umefikia wakati kwamba Serikali lazima irudishe katika Halmashauri ili kuongeza wigo wa mapato na kuzipunguzia utegemezi wa ruzuku kutoka Serikali Kuu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wengi waliochangia taarifa yetu, wameshauri Halmashauri kufuata utaratibu katika kutekeleza maagizo kutoka Serikalini. Suala la ujenzi wa maabara limegharimu miradi mingi na Kamati ilibaini kuwa ni moja kati ya sehemu zenye walakini mkubwa katika matumizi ya fedha za Serikali. Sasa lipo suala la utengenezaji wa madawati ambalo pia ni agizo kutoka Serikali Kuu. Naendelea kusisitiza kuwa Halmashauri zifuate sheria, kanuni na taratibu za fedha katika kutekeleza maagizo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia katika taarifa yetu na Kamati inataka Serikali kuleta majibu kwa maandishi juu ya utekelezaji wa yale yote ambayo Kamati tumeyaazimia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho basi niombe sasa Bunge lako Tukufu lipokee na kukubali taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa pamoja na mapendekezo yote yaliyomo katika taarifa hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Nichukue fursa hii kuwaashukuru wachangiaji wote waliochangia katika taarifa ya Kamati yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hii ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya usimamizi wa Hesabu za Serikali za Mitaa imechangiwa na jumla ya wachangiaji 22; kati yao saba walichangia kwa maandishi na 15 walichangia kwa maelezo. (Makofi)

Mheshimiwa Bobali alieleza kuhusiana na aina ya Wakurugenzi waliopo na kama wana uwezo wa kusimamia shughuli za maendeleo. Alieleza pia kwamba Wakurugenzi waliopo hawakupatikana katika mfumo wa watumishi wa umma. Pia alieleza kwamba kuna tatizo katika ukusanyaji wa mapato na hili linatokana na kushuka kwa bei ya mazao ya wakulima. Kamati imepokea ushauri huo na Kamati ilitoa mapendekezo katika taarifa ya mwaka jana kwamba Serikali inatakiwa semina kwa Wakurugenzi ili waweze kufanya kazi ipasavyo. Pia Kamati inashauri Serikali kuhakikisha kila Halmashauri inakuwa na mfumo wa kieletroniki ili basi iweze kuongeza mapato ya Halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Bobali pia ameeleza pia kuhusu tatizo la mradi wa maji. Ameeleza kwamba kuna mradi wa vijiji kumi ambao umeonyesha kutofanikiwa kabisa. Kamati imechukua ushauri huo, Kamati imeliona hilo na katika taarifa yake imeeleza na kutoa mapendekezo kwa Bunge kuazimia kuunda kamati teule ya Bunge kuchunguza matatizo ya maji nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Lubeleje ameishauri Kamati kupewa fedha nyingi zaidi ili kuweza kukagua miradi mingi ya maendeleo na hivyo kuona thamani halisi ya fedha zinazotumika. Tunashukuru kwa ushauri huo na katika taarifa yetu tulieleza kwamba tusingeona vizuri kufanya tu kazi ya mezani, ni vizuri tukatembelea miradi ya maendeleo ili kuona thamani halisi ya matumizi ya fedha za Serikali. Pia alieleza suala la watumishi kukaimu kwa muda mrefu bila kuthibitishwa. Kamati nalo katika taarifa yake imeliona hilo na imeitaka Serikali kuhakikisha kwamba watumishi wasikaimu zaidi ya miezi sita, wathibitishwe ili kuleta tija katika utendaji katika Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Chikota ameeleza kuhusu tatizo la kukaimu kwa Wakuu wa Idara na ametolea mfano halmashauri ya Korogwe ambayo kuna wakuu wa idara 11 wanaendelea kukaimu mpaka sasa, lakini pia ameeleza tatizo la miradi ya maji, ameelezea pia kucheleweshwa kupelekwa kwa fedha za miradi ya maendeleo. Taarifa ya Kamati imezingatia hayo yote na tunashukuru Mheshimiwa Chikota kwa ushauri wako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Selasini ameelezea uwezo wa baadhi ya Wakurugenzi wa Halmashauri zetu, hali ambayo inaleta matatizo na migongano na baadhi ya watumishi.

Suala hili limekuwa likijirudia mara kwa mara na ni kweli Wakurugenzi wengi tulionao sasa hawatokani na mfumo wa utumishi wa umma na hii imeleta tatizo kubwa katika utendaji wa kazi na usimamizi wa shughuli za maendeleo katika Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Gekul yeye alielezea kuhusiana na suala la asilimia 10 ya mfuko wa maendeleo ya vijana na akina mama na alishauri pia hii ihusishe pia wazee. Alieleza pia tukajifunze kutoka Halmashauri ya Babati ambayo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kuchangia fedha hizi. Nichukue nafasi hii kuitaka Serikali iende ikajifunze katika Halmashauri ya Babati tuone namna gani wameweza kuchangia pesa za mfuko huu kwa asilimia 100.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Edward Mwalongo alieleza kuhusiana na tatizo la maji, ameeleza kuna tatizo la wakandarasi washauri na miradi mingi ya maji inaharibika mara tu baada ya kuanza kutumika. Tatizo hili sisi kama Kamati tumelieleza kwa kina na kama tulivyoelekeza tunalitaka Bunge liunde Kamati Teule ya Bunge ili kuchunguza matatizo yote ya maji kwa maana kuna tatizo la miradi ya maji karibu nchi nzima. Katika kila miradi tuliokuwa tumetembelea miradi mingi bado haijafanya kazi vizuri. Kuna tatizo kubwa la usanifu wa miradi hiyo kwa hiyo tumeelekeza Bunge liunde Kamati Teule ya Kibunge kuchunguza matatizo ya miradi ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Musa Mbarouk naye pia alieleza tatizo la kukaimu kwa Wakuu wa Idara na Vitengo kwa zaidi ya miezi sita na ucheleweshaji wa pesa za miradi ya maendeleo. Hili nalo tumelieleza vizuri kwenye maazimio ya Kamati yetu na tunaitaka Serikali itekeleze hilo haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Leah Komanya alieleza kuhusiana na kutojibu hoja za ukaguzi na matumizi ya mfumo wa kihasibu wa EPICOR. Mfumo huu hauna asset model, wakurugenzi wanaweza wakajifanyia mahesabu kwa kadiri wanavyotaka; mfumo huu una cash basis, lakini hauna a clause basis na hii kuleta tatizo katika suala zima la mahesabu. Lakini upo uwezekano pia wa kufanya mahesabu nje ya mfumo. Kamati imeshauri Serikali ihakikishe mfumo wa EPICOR unafanyiwa marekebisho, bado kuna tatizo kubwa la mfumo wa EPICOR ambao tunautegemea kwa kufanya mahesabu katika halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Conchesta Rwamlaza ameeleza kuhusiana na mfuko wa maendeleo ya wanawake na vijana akasema mfuko huu ni muhimu kwa maendeleo ya wananchi lakini utaratibu unaotumika hauko sawa sawa, vikundi vingine vinavyolipwa pesa za mfuko huu ni vikundi hewa. Pia alieleza kwamba mfuko huu unatumika kisiasa; lakini pia alikubaliana na wazo la Mheshimiwa Zitto. Tumepokea ushauri huu na sisi Kamati tumeitaka Serikali ilete muswada wa sheria kwa ajili ya mwongozo wa matumizi ya mfuko huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Kigua ameeleza kuhusiana na miradi ya maji, lakini ameeleza tatizo la makusanyo ya mapato ya Halmashauri. Kamati imeeleza kwa kina matatizo ya miradi na maji na pia Kamati imeitaka Serikali ihakikishe kila halmashauri inatumia mfumo wa kieletroniki ili kuhakikisha kwamba inaongeza mapato ya Halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Zitto Kabwe alileta nyongeza ya kuiomba Serikali iangalie uwezekano wa kuunda Benki ya Maendeleo ya Serikali za Mitaa kwa kutumia asilimia 10 ya mapato ya ndani ambayo itatekeleza wajibu wa kutoa mikopo kwa vikundi vya vijana na wanawake. Vilevile Serikali itafiti uwezekano wa kuanzisha scheme ya hifadhi za jamii kwenye Serikali za Mitaa ili kusimamia mikopo ya vijana na wanawake. Ongezeko hili Kamati tumelikubali lakini pia kamati tulisisitiza kwamba haya yote yataweza tu kufanyika kama Serikali italeta Sheria ya Mwongozo wa Uendeshaji wa Mfuko huu wa Wanawake na Vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Isack Kamwelwe yeye alielezea kuhusiana na matatizo ya maji katika Wizara, akaeleza kwamba Wizara inatoa pesa tu pale ambapo kazi itakuwa imefanyika na Serikali itahakikisha kwamba huduma za maji zinapatikana. Mheshimiwa Waziri nichukue nafasi hii kukueleza kwamba katika ukaguzi tulioufanya tumegundua miradi mingi ya maji haitekelezwi ipasavyo na tatizo kubwa ni kwamba wakandarasi wanavyo- raise certificate Wizara inachukua muda mrefu kutoa pesa hizo na inasemekana ni lazima ukauze sura Wizarani ndipo certificate hizo ziweze kulipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri inatakiwa hili ulifanyie kazi ili kuhakikisha miradi ya maji inatekelezwa ipasavyo. Kamati pia imeliona hilo na kutaka kuundwa kwa kamati teule ya Bunge ambayo itaangalia nini kiini cha matatizo katika utoaji wa huduma ya utekelezaji wa miradi ya maji nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mpango ameeleza kwamba Serikali inapeleka pesa za miradi ya maendeleo tofauti na tulivyoeleza Kamati. Mheshimiwa Waziri nieleze tu kwamba unasema kwamba Serikali inapeleka fedha za miradi ya maendeleo ipasavyo, lakini fedha hizo hazifiki katika Halmashauri na ndio maana miradi mingi ya maendeleo inashindwa kutekelezeka. Kama fedha hizo zingekuwa zinafika kwa wakati miradi ingekuwa inatekeleza bila matatizo na kusingekuwa na malalamiko yoyote kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge na Halmashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Ndalichako ameeleza utekelezaji wa elimu bure na ameeleze ufafanuzi uliotolewa na waraka, kwa mfano suala la chakula kwa wanafunzi. Mheshimiwa Waziri nieleze tu kwamba kauli iliyotolewa na Mheshimiwa Rais ikikuagiza wewe pamoja na Waziri wa TAMISEMI kwamba kuanzia sasa ikipiga marufuku michango yoyote kwa ajili ya uchangiaji katika suala zima la elimu imeleta mkanganyiko mkubwa. Ipo haja ya kutoa tafsiri sahihi ya agizo la Rais na wakati mwingine inashindwa kueleweka kama je, tufate Waraka au agizo la Mheshimiwa Rais. Sasa ninavyoongea kuna shule nyingi huko zimefungwa na watendaji wa Serikali, wakuu wa shule wanapata shida kubwa ya nini kifanyike katika agizo hilo la Mheshimiwa Rais. Kwa hiyo, nitoe wito kwa Serikali kutoa ufafanuzi wa agizo hili la Rais ili kuepusha mkanganyiko unaoweza kujitokeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Jafo ameelezea kuhusiana na hatua zilizochukuliwa kwa Wakurugenzi ambao wameeonyesha kutokuwa na utendaji mzuri, lakini ameelezea suala zima la ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri na pia ameeleza kuna baadhi ya watendaji wamelazimika kulipia hasara walizosababisha na ameeleza pia wako katika vetting kuangalia utendaji wa baadhi ya Wakurugenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili la kufanya vetting, la kuangalia utendaji wa baadhi ya Wakurugenzi tunaliomba lifanyike kwa haraka kwa sababu wananchi wetu na Halmashauri zetu zinapata shida. Wapo Wakurugenzi ambao mpaka sasa utendaji wao haueleweki na hivyo kurudisha nyuma maendeleo katika Halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo naomba kuchukua fursa hii sasa kueleza azimio kubwa la Kamati ambalo lingependa lifanyiwe kazi kwa haraka ni kuhusu kuundwa kwa Kamati Maalum ya Kibunge itakayochunguza sababu za chanzo la tatizo la miradi ya maji kutekelezwa chini ya kiwango au kutotekelezwa kabisa.

Pia nichukue fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Spika, Job Ndugai kumshukuru Katibu wa Bunge Ndugu Stephen Kagaigai, kwa ushirikiano waliouonyesha pamoja na shukrani za dhati kwa Ndugu Athuman Hussein - Mkurugenzi wa Kamati za Bunge, Waziri wa TAMISEMI - Mheshimiwa Jafo na Manaibu wake, Makatibu wa Kamati, Ndugu Dismas Myanjwa, Ndugu Godfrey Kassanga, Ndugu Victor Mhagama pamoja na watumishi wengine wote wa Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa namna ya kipekee nichukue nafasi hii kuwashukuru na kuwapongeza kwa namna wanavyotoa ushirikiano Wajumbe wote wa Kamati ya LAAC kwa kufanya kazi bila kuchoka kuhakikisha kwamba taarifa hii inakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba kutoa hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Usimamizi wa Matumizi ya Fedha za Umma katika Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2017
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhitimisha majadiliano ya Taarifa ya Kamati yako tukufu ya Hesabu za Serikali za Mitaa mbele ya Bunge lako tukufu, naomba kuhitimisha kwa kulieleza Bunge lako tukufu kwamba Kamati ya LAAC ilihoji Halmashauri 58. Kamati iliainisha maeneo yenye matatizo makubwa kwenye Halmashauri zote nchini, kutokana na muda kuwa mfupi wa ufuatiliaji, utendaji na kuhoji kuwa mfupi Taarifa ya Kamati ilibaini mapungufu katika maeneo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ilikuwa ni ubadhirifu wa fedha za miradi ya maendeleo ya Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua kiasi cha shilingi bilioni 3.5 kilichofanyika katika kipindi cha mwaka wa fedha 2012/2013 hadi 2016/2017.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili ilikuwa ni kutotekelezwa kikamilifu kwa mapendekezo ya Kamati na tatu, kucheleweshwa kwa mchakato wa kukamilisha Kanuni za Uendeshaji wa Mfuko wa Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa ya Kamati hii imechangiwa na jumla ya Wabunge watano, hakukuwa na michango ya maandishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijatoa ufafanuzi wa michango ya Waheshimiwa Wabunge naomba nilieleze na kulisisitiza Bunge lako tukufu kuhusiana na mapendekezo ya Kamati ya LAAC katika Ukaguzi Maalum katika Halmashauri ya Kaliua, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa imebainika kuwa kuna ubadhirifu wa fedha za miradi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua kiasi cha shilingi bilioni 3.5 kilichofanyika katika kipindi cha mwaka wa fedha 2012/2013 hadi 2016/ 2017;

Na kwa kuwa hadi sasa Ofisi ya Rais, TAMISEMI imepokea taarifa hizo lakini haijachukua hatua stahiki dhidi ya watu wote walioshiriki katika ubadhirifu huo;

Kwa Hiyo Basi Kamati inaliomba Bunge lako Tukufu liazimie:-

(a) Ofisi ya Rais, TAMISEMI ichukue hatua stahiki dhidi ya wahusika wote walioshiriki katika ubadhirifu huo mara moja kwani suala hili lina sura ya kijinai.

(b) Watumishi wanaohusika moja kwa moja na ubadhirifu huu warejeshwe kwenye kituo hicho ili waweze kujibu tuhuma hizo za jinai.

(c) Taarifa hii ya ukaguzi maalum ikabidhiwe kwenye vyombo vya dola kwa ajili ya kuendelea na taratibu za kisheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Kamati ya LAAC inafanya kazi kwa kupitia Taarifa Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali, ikiwemo pamoja na Ukaguzi Maalum wa Halmashauri ya Kaliua;

Na kwa kuwa Ukaguzi Maalum ni conclusive;

Kwa hiyo basi, watumishi wote waliotajwa na ripoti ya ukaguzi huo kama ilivyoelezwa na kusisitizwa na Mheshimiwa Juma Hamad, Mheshimiwa Tunza Malapo pamoja na Mheshimiwa Felister Bura ikiwemo aliyekuwa Mkurugenzi Dkt. Athumani Kihamia na Wakurugenzi wengine wote waliohudumu katika Halmashauri hiyo kuanzia mwaka 2012 hadi 2017 pamoja na Mkuu wa Mkoa, Ndugu Fatma Mwassa, watawajibika kulingana na mapendekezo ya taarifa ya Kamati hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Tunza Malapo na Mheshimiwa Abdallah Chikota walieleza pia kuhusiana na matumizi mabaya ya shilingi bilioni 12.6 kwa ajili ya ujenzi wa kilometa 4.6 tu katika miradi ya ujenzi wa barabara pale Morogoro ambayo ingeweza kutumika kujenga zaidi ya kilometa kumi. Kamati inasubiri Taarifa ya Ukaguzi Maalum (Comprehensive Specific Audit) katika miradi yote ambayo inatekelezwa chini ya mradi huu wa Urban Local Government Strengthening Program (ULGSP) ili kuweza kuishauri Serikali vizuri juu ya hatua zaidi zinazopaswa kuchukuliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Selemani Zedi alieleza kuhusiana na suala zima la kufutwa kwa malimbikizo ya madeni ya Mfuko wa Wanawake na Vijana na Watu Wenye Ulemavu yanayofikia kiasi cha shilingi bilioni 13.9; Kamati inakubaliana naye. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia alieleza kuhusu suala zima la kutopelekwa kwa fedha za maendeleo zilizopidhinishwa katika bajeti; pia Kamati inakubaliana naye. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini alieleza suala zima la udhaifu wa mifumo ya udhibiti wa ndani; Kamati inakubaliana naye pia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Spika kwa kutuwezesha Kamati kufanya kazi ipasavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota - Makamu Mwenyekiti wangu ambaye tunashirikiana bega kwa bega katika kuiongoza Kamati hii. Vilevile nichukue nafasi hii kumshukuru Ndugu Dismas Muyanja Katibu wa Kamati, Ndugu Victor Mhagama - Katibu Msaidizi wa Kamati, Ndugu Waziri Kizingiti - Msaidizi wa Kamati, pamoja na Wajumbe wote wa Kamati ambao tumekuwa tukishirikiana bega kwa bega kuhakikisha Taarifa ya Kamati hii inakuwa imekamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni matumaini ya Kamati kuwa Serikali itazingatia mapendekezo ya Kamati hii ambayo yatakuwa ni Maazimio ya Bunge lako tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge likubali Mapendekezo ya Kamati hii ya LAAC ili yawe Maazimio ya Bunge lako tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, Naafiki.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pia nachukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu na kwa mara nyingine tena kwa namna ya kipekee niwashukuru wapiga kura wa Jimbo la Kilwa Kaskazini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na suala zima la uwekezaji wa viwanda katika mazao ya bahari. Mikoa ya Kusini ambayo inapakana na Bahari ya Hindi haina viwanda vinavyosindika mazao ya bahari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukumbuke kwamba Mikoa ya Kusini inapitiwa na mkondo wa Kilwa (Kilwa Channel), mkondo ambao unafanya eneo la Kilwa na Mikoa ya Kusini liwe ni miongoni mwa maeneo machache yanayozalisha samaki kwa wingi. Kwa bahati mbaya kabisa mpaka leo baada ya miaka zaidi ya 54 ya Uhuru hatuna kiwanda cha kusindika mazao ya bahari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Lindi pia unapakana na Mto Rufiji na delta za Mto Rufiji. Delta za Mto Rufiji zimetokana na Mto Rufiji ambao unatiririsha mboji nyingi kutoka Mikoa ya Bara. Maeneo haya yanasababisha bahari hii ya kusini iwe maarufu kwa uzalishaji wa kamba. Tunazalisha kamba wengi, lakini kwa bahati mbaya hatuna kiwanda cha kusindika mazao ya bahari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi, sisi watu wa Mikoa ya Kusini tuna mazingira wezeshi ambayo yanaweza kupelekea kuanzishwa kwa kiwanda katika maeneo yetu. Tuna barabara nzuri ya lami, tuna umeme wa uhakika unaotokana na gesi, lakini tuna ardhi ya kutosha. Kwa mfano, katika Jimbo langu maeneo ya Miteja pale, pana ardhi ya kutosha inayowezesha kuanzishwa mchakato wa kuanzishwa kiwanda, lakini kwa bahati mbaya hatuna kiwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na hilo sasa wavuvi wetu kutokana na kukosa hilo bado wanajihusisha na ku-preserve samaki kwa njia ya kukausha, zile njia za kijima kwamba sasa inalazimika wakaushe ili wapate ng‟onda. Bado tunawafanya wavuvi waendeshe shughuli zao katika njia za kijima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme ukianzia maeneo ya Moa - Tanga mpaka Msimbati - Mtwara, kuna viwanda viwili tu vya kusindika mazao ya samaki. Hii haitengenezi ustawi wa wavuvi wetu wa maeneo ya mikoa ya Kusini. Sasa naomba commitment ya Serikali kwamba Mheshimiwa Waziri atakapokuja atuelekeze ana mpango gani wa kujenga kiwanda cha kusindika mazao ya bahari katika maeneo ya mikoa ya Kusini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, niende moja kwa moja kwenye suala zima la uwekezaji katika kilimo cha muhogo. Nilipata kumsikia Mheshimiwa Waziri akisema kwamba Serikali sasa imewezesha kutuletea wawekezaji wa China na wamechagua eneo la mikoa ya Kusini hususan katika Jimbo langu la Kilwa Kaskazini kwamba wataanzisha kilimo cha mashamba makubwa ya mihogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hilo, naipongeza sana na nichukue fursa hii kuwakaribisha wawekezaji hao, waje, maeneo yapo, tuna ardhi ya kutosha, watu wapo na kwa bahati nzuri sasa tuna umeme huu wa REA. Kwa hiyo, wazo la uwekezaji wa kilimo cha muhogo liende sambamba na kujenga kiwanda cha kusindika mazao ya muhogo. Bila kumung‟unya maneno, napendekeza kiwanda hicho kijengwe katika Jimbo langu katika Tarafa ya Njinjo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala zima la kiwanda cha kuzalisha mbolea Kilwa Masoko maeneo ya Kilamko. Wakati harakati za kusafirisha gesi zinaanza kutoka maeneo ya Kilwa kuja Dar es Salaam, kati ya ahadi zilizotolewa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi wakati wa mfumo wa chama kimoja mwishoni mwa miaka ya 1980 ni kwamba gesi ile ije Dar es Salaam lakini watu wa Kilwa waliahidiwa kujengewa Kiwanda cha Mbolea maeneo yaa Kilamko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa ninavyozungumza, hakuna kiwanda zimebakia hadithi. Kilichotokea ni kwamba, watu wa TPDC walichukua zaidi ya hekari 800 maeneo ya Kilwa Masoko na hawajaziendeleza mpaka leo. Kinachotokea sasa ni kwamba wao walisema watawalipa fidia watu 28 tu. Toka mwaka 1989 walipochukua maeneo hayo mpaka leo ninavyozungumza, kuna zaidi ya watu 1,000 wako pale. Kwa hiyo, watu wa TPDC wamekuja lakini kwa msimamo wa kwamba wao watafidia watu 28 tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naitaka Serikali ihakikishe kwamba wakati wa mchakato wa kujenga kiwanda kama mlivyotuahidi, wakati tunakumbuka maumivu makubwa ya kuondokewa na gesi yetu kwenda Dar es Salaam, tuwakumbuke pia wale wananchi ambao wapo katika eneo lile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la muhimu ni kwamba sasa hivi sisi watu wa mikoa ya Lindi na maeneo ya Kilwa ni wazalishaji wakubwa wa zao la ufuta. Wilaya ya Kilwa peke yake inazalisha zaidi ya tani 25,000 za ufuta, lakini mpaka leo bei ya zao la ufuta inasuasua kwa sababu hatuna kiwanda cha kusindika mazao ya ufuta. Sijapata kusikia kama kuna kiwanda cha kusindika mazao ya ufuta. Ninaona tu kwamba Serikali inaendelea ku-entertain kwamba zao la ufuta lisafirishwe kama zao ghafi kitu ambacho kinawaumiza wakulima wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipate maelezo ya Mheshimiwa Waziri atakapokuja atuambie Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha sasa zao hili la ufuta linapata viwanda vya usindikaji ndani ya nchi? Nashukuru, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hotuba hii ya TAMISEMI na Utawala Bora. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha mimi binafsi kuingia katika Bunge lako Tukufu, lakini katika namna ya kipekee kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Kilwa Kaskazini ambao wamenipa dhamana hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na miundombinu ya barabara. Jimbo langu kwa ujumla miundombinu ya barabara ni mibovu na kwa sasa barabara nyingi hazipitiki na hasa zile barabara kutoka Nangurukuru kwenda Liwale, haipitiki, ni mbaya. Sasa hivi kutoka Nangurukuru kupitia Njinjo kwenda Liwale, hakupitiki. Hivyo, inalazimika wananchi wanaotaka kwenda huko watembee au wapite katika umbali wa kilometa zaidi ya 400, wakati kutoka Nangurukuru kwenda Liwale ni umbali wa kilometa 230. Naishauri Serikali ione uwezekano wa kujenga barabara hii katika kiwango cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kuna barabara kutoka Njia Nne kwenda Kipatimo, nayo sasa haipitiki, ni mbovu. Barabara hii inapitia katika Tarafa ya Miteja na Kipatimo. Pia naishauri Serikali ione uwezekano wa barabara hii kuijenga katika kiwango cha lami.
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo langu lipo katika ukanda wa Pwani. Ukanda wa Pwani una matatizo makubwa ya maji, lakini tunayo fursa ya uwepo wa Mto Rufiji. Naishauri Serikali ione uwezekano wa kujenga mradi mkubwa wa maji katika Mto Rufiji utakaosaidia vijiji na rarafa zilizopo katika Wilaya Rufiji na Jimbo la Kilwa Kaskazini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye afya. Huduma za afya katika Jimbo langu bado zinalegalega; huduma zinazotolewa ni hafifu, hakuna dawa katika zahanati, hakuna wahudumu. Tuna zahanati kama sita ambazo zimemalizika kujengwa, lakini hazina dawa wala wahudumu, kama zahanati ya Mwengei, Luyumbu,Marendego, Kipindindi na Nambondo na Hongwe. Zahanati hizi zimemalizika kujengwa lakini mpaka sasa hivi hazijaanza kufanya kazi. Naiomba Serikali iangalie hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika Jimbo langu kuna Hospitali moja tu, hospitali ya Mission. Hospitali hii haina x-ray na tayari wafadhili wa hospitali hii walitoa mashine ya kisasa ya x-ray, lakini kwa bahati mbaya kwa sababu ilichukua muda kupata jengo, ilipata hitilafu na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne alitoa ahadi ya kusaidia kufanya ukarabati wa x-ray hii. Kwa bahati nzuri ilipofikia mwaka 2013 akatoa shilingi milioni 40 kufanya ukarabati wa x-ray hii. Mpaka sasa ninapozungumza x-ray hiyo haijakarabatiwa na pesa zile zipo. Naiomba Serikali ifuatilie ili basi wananchi wangu waweze kupata huduma ya x-ray.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo langu la Kilwa Kaskazini ni dampo la mifugo kutoka Mikoa ya wafugaji. Sasa hivi tuna tatizo kubwa la migogoro ya ardhi, lakini mapigano kati ya wakulima na wafugaji na ni kwa sababu tu wafugaji wote wanaotoka katika Mikoa ya wafugaji wanakuja katika Jimbo langu na kusambaza mifugo yao bila kufuata utaratibu wa matumizi bora ya ardhi.
Naiomba Serikali ihakikishe kwamba inaondoa mifugo yote ambayo ipo katika vijiji ambavyo havikupangwa kuwepo kwa mifugo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni elimu. Tunao mpango wa elimu bure. Huu mpango mpaka sasa naona bado ni kama unalegalega. Mimi binafsi nashauri mpango wa elimu bure uendane sambamba na kuangalia maslahi mapana ya walimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu bure inazungumzia namna ya kumsaidia mwanafunzi, lakini bado haijamwagalia mwalimu. Napendekeza, mpango huu uendane sambamba na kuangalia uwezekano wa kutoa teaching allowance kwa walimu. Walimu wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu, ni vizuri sasa kuangalia maslahi yao. (Makofi)
Mheshimia Mwenyekiti, pia kuna majengo ya Shule na Ofisi za Serikali yanajengwa chini ya viwango. Majengo mengi yanayojengwa sasa, hayawezi kudumu hata kwa miaka kumi, hali ya kwamba majengo ya Serikali yanatakiwa ya kudumu kwa miaka 50 na kuendelea. Serikali iangalie uwezekano wa kusimamia ili majengo yanayojengwa sasa yawe ya kudumu kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la uhakiki wa Watumishi. Suala hili katika eneo langu limezua adha na kuna shida! Tayari Serikali ilifanya zoezi hili kwa mara ya kwanza, lakini sasa inaonekana ni lazima warudie tena kufanya tena kwa mara nyingine. Sasa inawagharimu wafanyakazi. Kwa mfano, wananchi wanaotoka Kijiji cha Nandete kwenda Kilwa Masoko ni ziaidi ya kilometa 140. Mtumishi huyu tayari alishakwenda kwa zoezi hilo kwa mara ya kwanza, lakini analazimika tena aende kwa mara ya pili. Hii inawasumbua sana watumishi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la elimu maalum. Naomba Serikali kwanza ibaini idadi ya walemavu tujue kuna walemavu wangapi. Serikali ijielekeze kutoa huduma stahiki za walemavu. Kila mlemavu ana hitaji lake kulingana na aina ya ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mlemavu wa ngozi anatakiwa apate mafuta maalum ambayo yatamwezesha kumnusuru na athari za miale ya mwanga. Mlemavu kiziwi, anatakiwa apate shime sikio (earing aid), itakayomwezesha kupata athari za uelekeo wa sauti na mlemavu asiyeona anatakiwa apate fimbo maalum itakayomwezesha kupata uelekeo. Naishauri Serikali, huduma hizi zitolewe bure.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kuwasahau walemavu wa viungo, viungo bandia vimekuwa vikiuzwa kwa bei juu, wananchi wetu hawawezi kumudu. Naiomba Serikali, huduma ya viungo bandia itolewe bure. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naiomba Serikali ianzishe Kurugenzi ya Elimu Maalum. Walimu wanaoshughulikia watoto wenye ulemavu, wanafanya kazi kubwa lakini mpaka sasa hatujakuwa na Kurugenzi ya Elimu Maalum.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo langu limepakana na Bahari ya Hindi, lina wavuvi, mpaka sasa wavuvi wanatumia mbinu za kijima kuvua. Naiomba Serikali iwezeshe vifaa vya kisasa kwa wavuvi wale ili waweze kwenda kuvua kwenye maji ya kina kirefu na basi kuweza kupata tija.
Katika Jimbo langu la Kilwa Kaskazini, kuna Tarafa mbili ambazo zinalima kilimo cha michungwa. Katika miaka ya hivi karibuni michungwa imepata changamoto ya ugonjwa ambao unakausha mimea hiyo. Naiomba Serikali ituletee wataalam watakaofanya utafiti wa kugundua ni tatizo gani linaloisibu mimea hiyo kukauka ili basi wakulima wetu waweze kupata tija ya zao hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze katika utawala bora. Mpaka sasa tunapozungumza, jitihada za kufikia viwango vya juu vya utawala bora bado zinakwamishwa. Bado kuna figisufigisu nyingi katika suala zima la uendeshaji wa utawala bora. Bunge lako Tukufu mpaka sasa linafanya shughuli zake kana kwamba tuko jandoni; kwa sirisiri! Hii nafikiri haipendezi na haiwezi ikawa na mchango mzuri wa ustawi wa demokrasia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado mpaka sasa maslahi na matakwa ya maamuzi ya chaguzi zinazofanywa na wananchi hayaheshimiwi. Kilichotokea Zanzibar ni kutoheshimu matakwa ya maamuzi ya wananchi. Naiomba Serikali izingatie utawala bora ili basi matakwa ya maamuzi
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi, lakini nachukua nafasi hii pia kuwashukuru Wajumbe wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kwa kunichagua kuwa Mwenyekiti wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na uzalishaji wa umeme katika kinu cha Somangafungu. Uzalishaji wa umeme katika mtambo huu kwa kweli umekuwa wa kusuasua, umeme unaozalishwa pale unatumika katika Wilaya ya Kilwa na Wilaya ya Rufiji lakini mpaka sasa umeme umekuwa ni wa kukatika katika kila mara. Tulifanya mazungumzo na Mkurugenzi wa TANESCO alikuja pale akatuambia kwamba tayari vipuli vimepatikana kwa ajili ya kufanya marekebisho ya mitambo pale, lakini mpaka sasa hakuna kinachoendelea alituambia baada ya mwezi mmoja mambo yatatengamaa lakini bado umeme unakatikatika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, niongelee kuhusiana na suala zima la umeme vijiji. Katika jimbo langu kuna baadhi ya kata na vijiji havijapata umeme kwa mfano kata ya Miteja - kijiji cha Kikotama, kata ya Mingumbi - kijiji cha Nambondo, kijiji cha Chapita, kijiji cha Nampunga, kata ya Namayuni - kijiji cha Nahama, Namakolo, Naliyomanga, kata ya Chumo - kijiji cha Hongwe, Ingirito na Kinywanyu, kata ya Kipatimo - kijiji cha Mtondowa Kimwaga, Nandete, Pondo, Mkarango bado havijapata umeme, kata ya Kibata kata yote kijiji cha Kibata, Hanga, Nakindu, Mwengehi, Namtende vyote havijapata umeme. Kata ya Kandawale - kijiji cha Kandawale, Ngarambi, Namatewa Natipo havijapata umeme. Kata ya Njinjo - kijiji cha Msitu wa Simba, Kipindimbi havijapata umeme, kata ya Miguruwe - kijiji cha Mtepela na Kingombe na Zinga Kibaoni havijapata umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia katika kata ya Kinjumbi kuna vijiji vya Pungutini, Kitope havijapata umeme. Lakini pia katika Jimbo la Kilwa Kusini kwa Mheshimiwa Bwege kuna kata saba yenye vijiji 31 havijapata umeme, kata ya Pande, kata ya Limalyao, kata ya Nanjilinji, kata ya Likawage, kata ya Mandawa, kata ya Kilanjehanje na kata ya Kitole.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo pia la kuunganishiwa umeme katika vijiji ambavyo tayari vimeshapata umeme. Watu wa REA bado wanasumbua, vijiji vimepata umeme lakini kuunganisha umeme majumbani inachukua muda wakati mwingine ni zaidi ya miezi sita toka mwananchi alipie umeme, umeme anakuwa bado hajaunganishiwa. Kwa hiyo, naomba pia Mheshimiwa Waziri hilo pia uliangalie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuwa jana kupitia vyombo vya habari tuliona Mheshimiwa Rais akizungumza na Mabalozi lakini pia alizungumza na Katibu wa SADC akieleza nia ya Serikali ya kujenga kiwanda cha mbolea pale Kilwa Masoko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kumpongeza, kukupongeza wewe Mheshimiwa Waziri,nimefurahi sana katika hilo na hata kwenye hotuba yako ukurasa wa 37 umeeleza kwamba zimetengwa pesa shilingi bilioni 4.41 kwa ajili ya utengenezaji wa kiwanda hicho, tunashukuru sana. Lakini naomba pia suala hilo liendane sambamba na upanuzi wa…
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa, muda wako umekwisha…
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Ahsante!
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Mchango wangu nitaanza kujielekeza kwa ndugu zangu wa TAMISEMI. Serikali ya Awamu ya Tano toka iingie madarakani haijaongeza nyongeza ya mishahara, lakini pia watumishi wamepandishwa madaraja lakini hakuna mabadiliko ya mishahara kutokana na madaraja waliyopandishwa. Sasa naomba Serikali iwaangalie watumishi ambao watastaafu katika kipindi hiki, kwamba wao walistahili wapate nyongeza hizo kwa mujibu wa sheria, lakini kwa kuwa sasa Serikali imeamua kutofanya hivyo maana yake kuna uwezekano wa watumishi hawa kukosa haki yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali watumishi wataostaafu katika kipindi hiki basi lazima wazingatie kwamba watastaafu kwa kukokotoa kwa hesabu zipi? Kwamba watakokotolewa kwa hesabu zile ambazo kabla mshahara haujabadilishwa au mpaka hapo sasa ambapo Serikali itaamua kuongeza nyongeza hizo za mishahara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni suala la waraka uliotolewa na Serikali kuhusiana na vigezo vipya vya namna gani sasa shule zinaweza zikapata usajili. Kuna waraka mpya umetolewa kwamba ili shule iweze kusajiliwa lazima shule hiyo iwe na madarasa 10, nyumba tatu za Walimu, matundu 10 ya vyoo. Suala hili nafikiri Serikali haijafanya utafiti wa kutosha kwa sababu mazingira ya maeneo ya vijijini ni ngumu sana kwa shule kuwa na uwezekano wa kujenga vyumba 10 vya madarasa, nyumba tatu za Walimu ili waweze kufikia vigezo vya kuweza kupata usajili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali lazima ikumbuke pia wana jukumu kubwa la kuhakikisha linafuta ujinga, linaondoa vijana ambao watakuwa na matatizo ya kushindwa kuhesabu, kusoma na kuandika, sasa kama hili halitazingatiwa maana yake upo uwezekano wa Serikali kuzalisha vijana wengi wenye shida ya kupata ujuzi huo.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali bado haijawaangalia Wenyeviti wa vijiji na vitongoji, wanafanya kazi kubwa lakini bado Serikali haijawaona. Naishauri Serikali ione uwezekano wa Wenyeviti wa Vitongoji na Vijiji waweze kupata posho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mahusiano mazuri kati ya watendaji wa Serikali na wawakilishi wa wananchi kwa maana ya Madiwani pamoja na Waheshimiwa Wabunge. Katika Halmashauri Wakurugenzi wengi wapya walioteuliwa hawana mahusiano mazuri na Waheshimiwa Madiwani na hoja kubwa katika utendaji wao wa kazi, wanasema sisi ni wateule wa Rais, kwa hiyo mara zote, hata katika mambo ambayo yanahitaji kutumia hekima na busara msingi mkubwa unakuwa kwamba sisi ni wateule wa Rais kwa hiyo tunafanya vile tunavyoona. Niishauri Serikali itoe semina kwa Wakurugenzi hawa, lakini pia inatakiwa wawashauri watumie hekima na busara ili kuona kwamba haya mambo yanakwenda katika utaratibu unaotakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la TASAF ambalo limezungumziwa na Waheshimiwa Wabunge wengi, mimi pia kwa msisitizo niseme, Serikali imefanya makosa na lazima ikubali kwamba imefanya makosa. Kwa sababu, wananchi hawa hawakwenda kwa Serikali kuomba msaada kwamba wasaidiwe katika kaya maskini hapana, ilikuwa ni utaratibu wa Serikali. Kama hivyo ndivyo Serikali ilijipanga na ikaweka taratibu zake kwa kutumia Maafisa wake. Kwa hiyo, Maafisa wa TASAF wanapokwenda katika kijiji fulani na kuhitaji kupata vigezo vya nani anastahili apate usaidizi huu, hilo lilikuwa ni jukumu la hao Maafisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kilichotokea sasa hivi wakasema kwamba Serikali imeleta agizo la kwamba vigezo havikufuatwa ili wananchi husika waweze kupata hizo stahili, matokeo yake, kwa mfano katika Jimbo langu la Kilwa Kaskazini katika Kijiji cha Miteja, Mkurugenzi ameagiza kwamba fedha zile ambazo zilipelekwa kwa wananchi ambao hawakustahili zilipwe na Serikali ya Kijiji na Serikali ya Kijiji sasa inatakiwa itoe zaidi ya milioni tano, hii imefanyika katika Kata ya Mandawa na Kata nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niitake Serikali izingatie tena haya maagizo yake, haikuwa ni ombi la wananchi kupata hizo pesa, ulikuwa ni utaratibu wa Serikali, kwa hiyo Serikali lazima hili iliangalie kwa umakini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu vitambulisho vya Taifa; hili suala imefikia mahali kwamba wananchi wanashindwa kuelewa, walikuja hawa watu wa NIDA, wamefanya zile process zote za kupata taarifa kutoka kwa wananchi lakini mpaka sasa hivi, kwa mfano kwenye Jimbo langu la Kilwa Kaskazini wananchi hawafahamu vitambulisho hivyo watavipata lini, Serikali nalo hilo iliangalie ili wananchi wapate vitambulisho hivyo vya Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa ni suala la Mabaraza ya Ardhi; chombo hiki cha baraza la ardhi ni chombo kizuri sana na kimesaidia wanyonge kupata haki zao. Niishauri Serikali ihakikishe chombo hiki kinakuwepo katika ngazi zote. Kwa sasa, chombo hiki kinapatikana katika ngazi ya kijiji na ngazi ya Kata, baadaye ngazi ya Wilaya huwezi kupata chombo hiki, uende mpaka kwenye ngazi ya Mkoa na kule kwenye ngazi ya Mkoa kuna Mwanasheria mmoja tu. Kwa hiyo, naishauri Serikali ihakikishe panakuwa na Baraza la Ardhi la Wilaya ili basi kupeleka huduma hizi kwa wananchi. Pia sisi watu wa Kusini katika Mahakama Kuu Kanda ya Kusini kuna Jaji mmoja tu, kwa hiyo, utoaji wa haki unacheleweshwa kwa sababu Jaji mmoja hawezi kukidhi haja ya usaidizi wa sheria kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ili basi na mimi niweze kuchangia katika hotuba hii ya Wizara ya Miundombinu.
Mheshimwia Naibu Spika, kabla sijaanza nichukue nafasi hii kutoa pole kwa majirani zangu wa Rufiji kwa mafuriko maana kuanzia jana Mto Rufiji umefurika, kwa hiyo, nitoe pole sana, hata yale maghorofa yetu yote yameanguka chini.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na mawasiliano. Katika Jimbo langu la Kilwa Kaskazini kuna kata ambazo bado hazijapata mawasiliano ya simu; kuna Kata za Kibata, Kandawale na Kijumbi hazijapata mawasiliano ya simu, lakini pia kuna vijiji vya Namakolo na Chapita katika kata ya Namayuni havijapata mawasiliano ya simu. Katika kata ya Kipatimu kuna kijiji cha Nkarango na kijiji cha Nandete havijapata mawasiliano ya simu. Niishauri Serikali ijitahidi maeneo hayo niliyoyataja yaweze kupata mawasiliano ya simu.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara; nianze na barabara ya kutoka Nangurukuru kwenda Liwale ambayo ina kilometa 230. Barabara hii ina umuhimu katika mambo makuu matatu; kwanza ni barabara ambayo imepitia katika majimbo matatu, Jimbo la Kilwa Kusini, Jimbo la Kilwa Kaskazini na Jimbo la Liwale, lakini la pili ni barabara ambayo imepita katika Hifadhi yetu ile ya Selous. Kwa hiyo, barabara hii kama ingekuwa imetengenezwa ingetusaidia sana katika utalii. Pia la tatu Waheshimiwa Wabunge tusijisahau, nyakati zile za uchaguzi Wabunge wengi huelekea maeneo ya Liwale, maeneo ya Ngende kwa sababu ya mambo yetu yale, mimi nafikiri ninyi mnayafahamu, lakini cha kushangaza ni kwamba barabara hii inasahaulika. Kwa hiyo, niiombe Serikali, barabara hii ni muhimu sana. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati mwingine nashangaa ni vigezo gani vinatumika kuamua sasa ni barabara ipi ijengwe kwa kiwango cha lami? Kutoka Nangurukuru mpaka Liwale ni mbali sana, Wilaya ya Liwale iko pembezoni kabisa na katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ilieleza kwamba ingefanya upembuzi yakinifu lakini nimeangalia katika hotuba hakuna chochote kilichopangwa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, nikuombe basi uwafikirie wale watani wangu Wangindo na sisi Wamatumbi ili basi na sisi tufaidi matunda haya ya uhuru. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Kwankocho – Kivinje. Barabara hii ni ya urefu wa kilometa tano na ni ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete. Barabara hii inaunganisha barabara inayokwenda Kilwa Masoko na Hospitali ya Wilaya ya Kinyonga pamoja na Mji wa kitalii wa Kilwa Kivinje. Barabara hii imeahidiwa lakini mpaka sasa hakuna chochote kilichofanyika. Niiombe Serikali iijenge barabara hii kwa kiwango cha lami ili basi tupate urahisi wa kwenda katika hospitali ile ya Wilaya ya Kilwa Kivinje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Njianne – Kipatimu. Barabara hii inahudumiwa na wenzetu wa TANROADS lakini inapita katika miinuko ya milima na kuna milima ambayo kama itatengenezwa katika kiwango cha changarawe basi tutaendelea kupata matatizo tu. Niishauri Serikali milima ile kwa mfano Milima ya Ndundu pale Namayuni, Ngoge, Kinywanyu pamoja na na Mlima wa Karapinda pale darajani basi ingewekwa katika kiwango cha lami ili kuhakikisha kwamba barabara ile inapitika kwa wakati wote. (Makofi)
Lakini isitoshe, nikumbushe pia, Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete katika sherehe za kumbukumbu ya Vita ya Majimaji mwaka 2010 kule Nandete aliahidi kujenga barabara kutoka Nandete mpaka Nyamwage, ahadi ile imeota mbawa sijui kama utekelezaji wake unakwenda vipi. Niikumbushe Wizara, Mheshimiwa Rais aliahidi na ningependa kuona utekelezaji wake unafanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, maelekezo yanayotoka kwamba Mkoa na Mkoa utaunganishwa kwa barabara ya lami, lakini sisi Mkoa wa Lindi na Mkoa wa Morogoro hatujaunganishwa kwa barabara. Niishauri Serikali ione uwezekano sasa wa kujenga barabara kutoka Mkoa wa Lindi kwenda Mkoa wa Morogoro, na hii pengine inatengeneza uwezekano mwingine wa kwenda katika Mikoa ya Kusini, isiwe lazima ukitokea Dodoma uende Dar es Salaam, ufike Rufiji, uende Kilwa kwenda Kusini basi ukifika Morogoro uingie Liwale - Nachingwea uende Kusini. Naomba ombi hili lishughulikiwe kwa sababu na sisi watu wa Lindi tuna haki ya kuunganishwa na wenzetu wa Morogoro ili basi kuleta ustawi wa watu hao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie sasa suala zima la ukarabati wa uwanja wa ndege wa Kilwa Masoko. Kwenye bajeti ya mwaka jana tulichangia bajeti lakini hakuna chochote kilichofanyika. Niishauri Serikali iufanyie ukarabati uwanja wa ndege wa Kilwa Masoko kwa sababu ni muhimu sana kwa shughuli za utalii, kama ambavyo mnafahamu Mji wa Kilwa ni mji wa kitalii, ni mji wa kale, watalii wengi wanakuja lakini hatuna uwanja wa uhakika wa ndege, kwa hiyo Serikali ishughulikie suala hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala zima la upanuzi wa Bandari ya Kilwa Masoko. Kilwa Masoko tuna bandari ya asili, lakini mpaka sasa ile bandari haijafanyiwa chochote. Niishauri Serikali ione uwezekano wa kupanua bandari ya Kilwa Masoko ili basi meli kubwa ziweze kutia nanga pale na sisi watu wa mikoa ya Kusini au watu wa Kilwa mazao yetu basi yauziwe pale pale Kilwa, maana Meli kubwa zikija hatutakuwa na sababu ya kupeleka mazao Dar es Salaam. Tunalima korosho, tunalima ufuta, bandari ya Kilwa ikifanya kazi basi mazao yale tunaweza tukayauzia Kilwa na hivyo kupandisha bei ya mazao ya wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kwa masikitiko makubwa nizungumzie suala zima la stand ya mabasi kwa Mikoa ya Kusini. Mikoa ya Kusini kwa jiografia yake, barabara inayosafirisha abiria kutoka Dar es Salaam kwenda Mikoa ya Kusini inatokea maeneo ya Mbagala Rangi tatu, lakini mpaka sasa hatuna stand inayoeleweka ya mabasi kutoka Mikoa ya Kusini. Tunapata shida kubwa maana stand zinazotumika
pale Mbagala Rangi tatu ni stendi za watu binafsi, na kwa sasa kuna ubaguzi mkubwa unafanyika kwa magari yanayotokea Kilwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumelazimishwa kwa magari yanayotokea Kilwa tuka-park uchochoroni huko ambako zina-park daladala hali ya kwamba Kilwa ni mkoa wa Lindi na kuna mabasi mengine ya Mkoa wa Lindi yana- park katika stand ambayo iko barabarani sasa tunashindwa kuelewa ni kwa nini watu wa Kilwa tutengwe?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nichukue nafasi hii pia kuishauri Serikali ijenge stand kwa ajili ya mabasi ya mikoa ya Kusini; kwa sababu kwa jiografia ya Jini la Dar es Salaam haiwezekani mtu anayetoka Mtwara, Kilwa au Lindi kwenda Ubungo, haiwezekani. Kwa hiyo Serikali ifikirie kujenga hiyo stendi ili kuondoa adha hii kwa wananchi wa mikoa ya Kusini.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru, ahsante.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe mchango wangu wa maandishi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika michango ya Waheshimiwa Wabunge katika Wizara hii, wameeleza tatizo kubwa la ukosefu wa X-Ray katika Hospitali zetu. Katika Jimbo langu ambalo lina Hospitali moja ya Shirika la Dini, hatuna huduma ya X-Ray. Jitihada nyingi zimefanyika zikiwemo pamoja na mchango wa Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kuchangia Shilingi milioni 40 mwaka 2010. Nasi Halmashauri kwa upande wetu katika Bajeti ya mwaka huu wa fedha 2017/2018, tumetenga Tanzania Shilingi milioni 20. Hivyo tunaomba Wizara itusaidie kuwasiliana na wenzetu wa Bima ya Afya ili waweze kutukopesha kifaa tiba hicho, kwani tayari tunazo shilingi milioni 60 mkononi ambazo zitaweza kuwashawishi wenzetu kutukopesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 127 inaonesha hali ya Halmashauri. Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa hali yake ya upatikanaji ni asilimia 77. Ukilinganisha na Halmashauri nyingine, Halmashauri hii ni miongoni mwa Halmashauri chache ambazo upatikanaji wake wa dawa bado uko chini. Naomba Mheshimiwa Waziri atakapohitimisha, atuambie ni kwa nini Kilwa? Je, kuna mikakati gani ya kutatua tatizo hili ili kuhakikisha tunapata dawa kama zinavyopata Halmashauri nyingine?

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) inaonesha zaidi ya Tanzania Shilingi bilioni nne zimepotea kutokana na miradi iliyokamilika lakini haifanyi kazi. Katika Jimbo langu la Kilwa Kaskazini, kuna zahanati sita ambazo majengo yake yameshakamilika, lakini bado hazijafunguliwa. Ni Zahanati ya Hongwe, Mpindimbi, Nambondo, Miyumbu, Marendego na Mwengei. Naomba kwa usimamizi wa Serikali izifungue zahanati hizi kwani nguvu za wananchi na Serikali zimepotea bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, katika sakata la vyeti feki, uhakiki wa vyeti, Wilaya yangu imeathirika sana hasa katika Hospitali ya Wilaya ya Kinyonga na Hospitali ya Kipatimu. Madaktari tegemezi wamekumbwa na tatizo hilo. Naomba watakapopanga mgawanyo wa Madaktari kutokana na tatizo hili, Wilaya yangu iangaliwe kwa jicho la huruma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niseme yangu katika Wizara hii ya Maji na Umwagiliaji. Awali ya yote, nachukua nafasi hii kutoa pole zangu kwa wenzetu wa Arusha kutokana na msiba wa wanafunzi. Namwomba Mwenyezi Mungu azilaze roho zao mahali pema peponi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuunga mkono wale wote wanaosema kwamba bajeti ya Wizara hii iongezwe. Kwa ukweli kabisa kama tuna kusudio la kutaka kuwatendea haki wananchi wa Tanzania, basi tuna kila sababu ya kuongeza bajeti ya Wizara hii ili wananchi wakapate maji ya kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, falsafa ya kumtua mama ndoo kichwani, ililenga zaidi kwa wananchi wanaoishi vijijini. Kwa mazingira yetu, sehemu nyingi za mijini zina maji na ikiwezekana miundombinu yake, maji haya yanaenda kabisa mpaka majumbani. Sehemu ambazo bado akinamama wanabeba ndoo kichwani ni sehemu za vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukifuatilia bajeti, bado imekuwa na upendeleo zaidi kwa maeneo ya mijini kuliko maeneo ya vijijini. Jimbo langu ni la kijijini na hakuna mradi wowote wa maji uliotengwa katika bajeti hii. Nimesoma kwenye kitabu hiki hakuna chochote kilichowekwa kule. Sasa ina maana kwamba mwaka huu wa fedha unanipita hivi hivi. Namwomba Mheshimiwa Waziri, wananchi wa Jimbo la Kilwa Kaskazini awaangalie, hakuna chochote alichotenga kwa ajili yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimeangalia pale, Mkoa wa Lindi umetengewa pesa kama 1.1 billion fedha za wafadhili. Basi naomba zile pesa ziwaangalie pia wananchi wa Jimbo la Kilwa Kaskazini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nachukua nafasi hii kupendekeza kuanzishwa kwa Wakala wa Maji Vijijini, kwa sababu vinginevyo basi mgawanyo wa keki hii, wenzetu wa mijini au wenzetu wa baadhi ya Majimbo watakuwa wanapata zaidi kuliko sehemu nyingine. Kwa hiyo, basi uanzishwe Wakala wa Maji Vijijini ili vile vijiji ambako ndiko Watanzania wengi wanaishi waweze kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo, nijielekeze katika matatizo ya maji katika Jimbo langu. Jimbo langu ambalo lina Kata 13, kuna Kata kama sita hivi, bado hazijawa na mradi wowote wa maji. Kuna Kata ya Somanga ambayo iko pale barabarani haina mradi wa maji, Kata ya Kinjumbi, Kata ya Kibata, Kata ya Chumo, Kata ya Namayuni na baadhi ya vijiji katika Kata ya Kipatimu; kuna Vijiji vya Nandete, Intikimwaga, Nandemo, Mkarango na Kijiji cha Nasaya; vyote hivi havina mradi wowote wa maji. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri ayaangalie maeneo hayo nao waweze kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napongeza utekelezaji wa Wizara kwa Mradi wa Maji wa Mingumbi Mitete. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri, tumekuwa tukishirikiana na ule mradi umeelekea kukamilika. Ule mradi unapitia katika Kijiji cha Njia Nne. Namwomba Mheshimiwa Waziri wananchi wa Kijiji cha Njia Nne wapate maji katika mradi ule kwa sababu haiwezekani likapita bomba tu pale halafu wao waliangalie. Ule mradi unaopeleka maji katika Vijiji vya Mingumbi, Poroti, Nangambi na Ipuli, Tingi, Mtandango na Miteja, lakini wale wa Njia Nne wamesahaulika. Kwa hiyo, naomba pia na wale wa Njia Nne waweze kupata maji katika ule mradi.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo, nijielekeze katika matumizi ya chanzo cha Mto Rufiji. Tumekuwa tukiona hapa, vyanzo vyote vikubwa vya maji tayari vinatumika kwa ajili ya matumizi ya maji kwa wananchi wa maeneo hayo. Kuna chanzo cha Ziwa Victoria, Mto Malagarasi na sehemu nyingine; lakini mpaka sasa na nimekuwa nikishauri mara kadhaa, Serikali haijakiangalia chanzo cha Mto Rufiji kwa ajili ya wananchi wa Rufiji na Kilwa. Mpaka sasa yale maji yanapotea tu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Mamlaka ya Uendelezaji wa Bonde la Mto Rufiji wanaita RUBADA. Wapo pale, lakini sioni kama kuna jitihada zozote zinazofanyika, maana hakuna mipango yoyote ya umwagiliaji inafanyika pale; yale maji yanatupita tu hivi hivi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri atakapokuja atuambie ana mpango gani wa kuhakikisha kile chanzo cha Mto Rufiji kinatumika kwa manufaa ya watu wa Rufiji, Kibiti, Kilwa, Kilwa Kusini na maeneo ya jirani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa, nijielekeze katika ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali. Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali anaeleza kuwa kuna zaidi ya pesa shilingi bilioni nne zinapotea kutokana na miradi kukamilika, lakini kutotumika.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na tumefanya ziara za ukaguzi wa miradi maendeleo katika sehemu mbalimbali za nchi hii. Tulichojifunza huko, kuna miradi mingi inakamilika, lakini haitumiki na moja ya miradi hiyo ni miradi ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, kuna mradi kule Nachingwea, kuna mradi kule Tabora, miradi ile imekamilika lakini haitumiki. Tatizo kubwa, kuna shida kubwa kwa Ma-planner wetu wa Halmashauri. Wasanifu wetu, wanasanifu miradi ambayo baada ya kuja kukamilika wananchi wanashindwa kuitumia. Kwa mfano, kuna mradi pale Nachingwea, ili wananchi waweze kutumia ule mradi, basi inahitaji ndoo moja ya maji inunuliwe kwa sh.300/= kitu ambacho wananchi hawawezi kumudu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kuna shida kubwa kwa wataalam wetu wa Halmashauri kusanifu hii miradi. Naomba wataalam wanapokaa na kusanifu hii miradi wawe makini sana na wawashirikishe wananchi kuona namna gani wao wanaweza wakaimudu hiyo miradi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi nitoe mchango wangu katika muda huu wa dakika tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maamuzi ya kuhamisha mifugo kutoka katika Mikoa ya wafugaji kupeleka Mikoa ya Kusini na hasa Mkoa wa Lindi yameleta athari kubwa za mazingira. Na kimsingi hakukufanyika upembuzi yakinifu wa namna gani mazingira yataathirika, maamuzi yale yamepelekea kuathiri sekta ya utalii, mazingira lakini pamoja na kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kijiji cha Ngea kuna zaidi ya mifugo 10,000 iko pale, lakini kijiji hiko hakiko katika mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa ajili ya mifugo. Lakini ndicho kijiji ambacho kina hifadhi ya misitu ya Likonde na Mitalule na mifugo ile ipo ndani mle mle. Kwa hiyo sasa hivi kuna uharibifu mkubwa wa mazingira katika hifadhi ile.
Lakini isitoshe katika kile kijiji kuna Bwawa la Maliwe, bwawa ambalo linatunza viboko wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilifanya ziara kule kina cha maji katika Bwawa la Maliwe kinapungua kwa sababu lile bwawa liko jirani kabisa na Hifadhi za Misitu ile. Hivyo basi kutokana na uwepo wa mifugo maana yake mifugo inapelekea mmomonyoko wa ardhi na hivyo kina cha bwawa lile la Maliwe kinapungua. Kwa hiyo, nichukue nafasi hii kuiomba Wizara ifuatilie katika maeneo hayo ninayoyaeleza kwa sababu vinginevyo mazingira ya uhifadhi wa misitu ni kama yanaenda kuharibika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la wakulima na shughuli zao za kilimo. Wakulima katika msimu wa mwaka huu katika kijiji cha Ngea na vijiji vya jirani ni kama hakuna watakachovuna kwa sababu mazao yote yameharibiwa na mifugo. Kwa hiyo, niiombe Serikali pia iangalie suala hilo ili basi wakulima wetu waweze kuepukana na baa la njaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kushangaza katika jitihada za kuhakikisha kwamba ile mifugo inatolewa pale Serikali ya Wilaya ya Kilwa ilifungua kesi mahakamani ili basi kuwaondoa wale wafugaji. Lakini katika hali ya kushangaza kwenda mahakamani Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kilwa imeshindwa mahakamani na wananchi wanalalamika kwamba inaonekana kuna dalili ya rushwa. Wananchi wanalalamika iweje vyombo vya ulinzi na usalama vimeenda kuwakamata wafugaji katika maeneo ambayo hawakupasa wawepo, lakini wanapoenda mahakamani wanashindwa. Kwa hiyo niombe Wizara ifuatilie suala hilo wananchi wa maeneo hayo wanapatashida sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kuna suala la fidia kutokana na uharibifu unaofanywa na wanyama au kwa mazao au kwa binadamu. Katika jimbo langu la Kilwa Kaskazini tunapakana na Hifadhi ya Selous kuna wananchi wamejeruhiwa na wanyama, lakini taratibu zote zinazofanywa ili basi kupata fidia inachukua miaka mingi kupata fidia kutoka Wizarani. Kwa hiyo, niiombe Wizara kwamba kama ambavyo ninyi mnachukua hatua za haraka pale mwananchi anapomjeruhi mnyama au anapoua mnyama, basi iwe hivyo hivyo pale mnyama anapomjeruhi mwananchi zile fidia zipatikane kwa haraka. (Makofi)

Lakini sio hivyo tuu kuna suala zima la mashamba, kuna ekari nyingi za wananchi zimeharibiwa na ndovu, lakini taratibu zimefuatwa kupitia Maafisa wenu wa Maliasili lakini hakuna chochote kinafanyika baada ya taarifa kufika kwenu. Naomba sana hayo myazingatie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la mipaka kati ya hifadhi hizi na wanavijiji. Kuna tatizo kubwa la mipaka katika kijiji cha Namatewa na kijiji cha Ngarambe. Wananchi wako pale toka siku nyingi lakini sasa hivi inaonekana wenzetu wa Selous wanaidai katika eneo ambalo wananchi wapo wanadai kuwa ni eneo la kwao, kwa hiyo, tayari kumekuwa na migogoro baina ya hifadhi ya Selous na wananchi. Kwa hiyo, niiombe Wizara na hilo lishughulikiwe ili mgogoro uweze kuisha. Ahsante sana, nashukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kusema katika hotuba ya mtani wangu Waziri Mkuu kwa niaba ya wananchi wa Kilwa Kaskazini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na Maadhimisho ya Sherehe za Vita vya Majimaji. Historia inaeleza wazi kwamba Vita ya Majimaji ilianza Kilwa na sababu kubwa ya kwa nini Wahenga wetu wale walianzisha ile vita, ni kwa sababu walikuwa wanakataa kunyanyaswa, wanakataa kunyang’anywa ardhi yao, wanakataa uonevu, lakini walikuwa na ujasiri mkubwa wa kupambana na Mkoloni Mjerumani ambaye alikuwa anatisha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi watu wa Pwani tuna misemo yetu ambayo ina maana na hekima kubwa. Watu wa Pwani tunasema, raha ya maji ya dafu yanywewe kwenye kifuu chake. Maji ya dafu yakinywewa kwenye bilauri hupoteza ladha. Yakinywewa kwenye bilauri hupoteza sifa na harufu yake. Tabia ya dafu ukilipasua ukatoa mzibulio, ukachokoa basi sharti unywe kwenye kifuu chake. Ukichukua yale maji kuyapeleka kwenye bilauri, ladha inapotea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ni nchi inayojitambua. Siamini kama inafanya mambo yake hovyo hovyo. Kila linalotokea ni historia! Katika hali ya mshangazo, watu wa Kilwa tunashangaa kwa nini Sherehe za Vita ya Majimaji zinazogharamiwa na bajeti ya Serikali zinafanyika Songea na siyo Kilwa, Nandete? Hatuelewi! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, waandishi mbalimbali wanazungumzia Vita ya Majimaji. Mwandishi Clement Gwasa anasema, Vita ya Majimaji ilikuwa planned na sababu zake zilianza toka mwaka 1903 na kuja kupigana mwaka 1905. It was very, very planned. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwa ninajiuliza, hivi ni vigezo gani vilivyotumika kuzipeleka zile sherehe zinazotambuliwa na Serikali Songea? Kwa sababu kama hoja ni watu kunyongwa, hata sisi viongozi wetu wa Kilwa walinyongwa. Kinjekitile alinyongwa; na Hassan Omar Makunganya alinyongwa. Ukisoma kitabu cha The Majimaji Uprising kinasema, kiongozi wa ndugu zangu, watani zangu akina Mheshimiwa Jenista, Wangoni wa wakati huo, aliposhawishiwa ajiunge na kumwondoa Mkoloni Mjerumani, yeye alisema hana muda kwa sababu Mjerumani ni rafiki yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ilipofikia wakati wa Vita ya Majimaji, Chabruma aliamua tu kujiunga na mapambano ya Vita ya Majimaji kwa sababu binafsi na sababu yenyewe aligundua kwamba mke wake, Bi mdogo, si mwaminifu katika ndoa. Kwa sababu hiyo akaamua kwenda kwa DC kwenda kulalamika. DC akamwambia kama hivyo ndivyo, basi naomba uniletee ushahidi. Huyu kiongozi Chabruma alishindwa kupeleka ushahidi kwa DC, ndipo basi akaona kumbe hawa Wajerumani hawafai, basi na mimi nitaungana na Wamatumbi kumwondoa Mjerumani. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama sisi tuliamua kupambana vita kwa sababu ya kutetea Utaifa wetu, ardhi yetu na umoja wetu, hivi nani sasa anastahili kupewa heshima kitaifa? Ni yule aliyejiunga na Vita ya Majimaji kwa sababu binafsi au sisi tuliokuwa tuna lengo la kuwaunganisha Watanzania? Haya mambo yanaumiza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania tumefanya mambo mengi, sisi ndiyo Taifa ambalo tulithubutu kuhakikisha kwamba nchi zote kusini mwa Afrika zinapata uhuru. Mwalimu Nyerere kwa sababu zake binafsi akaona hapana, lazima hawa wenzangu wapate uhuru. Sasa kama itatokea mtu akasema heshima hii ya sisi kuthubutu ipelekwe Rwanda, ni kitu ambacho hakieleweki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwa najisikia kutetemeka ninapomwona Mkuu wa Majeshi anaenda pale Songea eti kwamba wale ndio majemedari wa Vita ya Maji Maji. Haieleweki! Naomba mtani wangu, Mheshimiwa Jenista, kalifanyie kazi hili, watu wa Kilwa tupate haki yetu kwa sababu ya ujasiri wa kuthubutu kumwondoa mtawala mkali sana, Mjerumani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri hilo litaeleweka. Nilishauliza maswali hapa, ndugu yangu Mheshimiwa Mwinyi akanijibu vizuri sana, nikataka ufanyike upembuzi wa kihistoria, lakini kuna hoja pia ya sisi waathirika wa Vita ya Majimaji tulipwe fidia kama ambavyo wenzetu wa Kenya wamelipwa, wenzetu wa Namibia wamelipwa. Hakuna chochote kimefanyika, naomba hili lizingatiwe kwa sababu historia ni jambo muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende sasa kwenye suala la watu wenye ulemavu; ukurasa wa 24 na 25 katika hotuba ya Waziri Mkuu anazungumzia suala la watu wenye ulemavu. Anaeleza kwamba Serikali pamoja na wadau wamechangia vifaa kwa watu wenye ulemavu. Amesema wametoa viti mwendo 240, wamechangia magongo ya kutembelea 350, bajaji sita, kofia pana 128, fimbo nyeupe 175, miwani maalum 70, shime sikio 20, vyerehani vinane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wenye ulemavu Tanzania na idadi hii ya vifaa vilivyotolewa na Serikali, nafikiri ni utani kwa watu wenye ulemavu. Walemavu wana mahitaji maalum kutokana na aina ya ulemavu walionao. Kuwa mlemavu siyo planned, ni suala linalotokea kwa bahati mbaya. Serikali bado haijaangalia mahitaji muhimu ya walemavu kutokana na aina yao ya ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mlemavu wa ngozi hakuchagua kuwa mlemavu wa ngozi; na hitaji lake maalum kulingana na aina yake ya ulemavu, ni kupata mafuta maalum ambayo yatamsaidia kupambana na athari za miale ya jua. Sasa kama haya mahitaji hayatolewi bure na Serikali, mimi bado sielewi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mlemavu asiyeona apate fimbo maalum; mlemavu kiziwi apate shime sikio; mlemavu wa viungo apate viungo bandia. Katika hali ya kushangaza, kati ya vitu vinavyouzwa kwa bei ya juu ni pamoja na viungo bandia. Vifaa hivi ni hitaji maalum kwa walemavu kulingana na aina yao ya ulemavu, vitolewe bure na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye ajira ya Watendaji wa Vijiji wa darasa la saba. Kadri siku zinavyozidi kwenda mbele kasi ya watumishi wa Serikali hasa wa kada ya chini kuichukia Serikali inaongezeka. Ni kwa sababu Serikali haijajipanga katika kuhakikisha haki za watendaji wa chini zinazingatiwa. Watendaji wa vijiji wameondolewa kienyeji eti kwa sababu wao ni darasa la saba... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. VEDASTUS E. NGOMBALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi nami nitoe mchango wangu kwa Wizara hii ambayo inahusiana na afya ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nianze kwa kutoa pongezi kwa Serikali kwa kutuwezesha kwa kutupa fedha katika Kituo cha Afya cha Kilwa Masoko shilingi milioni mia tano, Kituo cha Afya Pande, Kituo cha Afya Tindi shilingi milioni mia nne pamoja na ambulance. Tunashukuru sana kwa hilo, lakini pia tunaomba tupate pesa kwa ajili ya Kituo cha Afya Njinjo ili basi huduma ya afya iweze kwenda sawasawa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na suala zima la sera ya huduma bure kwa akinamama wajawazito pamoja na watoto walio chini ya miaka mitano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la sera ya huduma bure kwa akinamama wajawazito pamoja na watoto chini ya miaka mitano. Ni sera inatekelezwa, lakini bado ina changamoto kubwa. Kuna changamoto kubwa kwamba bado huduma hii haitolewi ipasavyo, bado akinamama wanahitajika wajiandae kwa vifaa kwa ajili ya kwenda kujifungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, limezungumzwa suala la delivery kit, naomba suala hili liwe wazi, elimu itolewe, wananchi wafahamu stahili yao kutokana na huduma hii, kama linachangiwa au linatolewa bure ili basi kila mwananchi aweze kupata huduma hii ipasavyo. Kwa hali iliyopo sasa suala hili ni kama limejifichaficha na akinamama wetu kule wanalazimika kuagizwa viwembe, mipira, wanaagizwa kanga; kumekuwa na vurugu na Serikali bado haijaweza kutatua tatizo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nizungumze, kwangu kuna hospitali ya mission. Serikali imeingia mkataba na Hospitali ya St. Mark’s Kipatimu pale na kwa hivyo, akinamama wanatakiwa wapate huduma hii bure, lakini kumekuwa na changamoto katika hospitali hii na hasa pale Serikali inapochelewesha kupeleka pesa katika ule Mfuko wa Basket Fund. Uongozi wa hospitali ukiona Serikali imechelewa kupeleka fedha pale, wanachokifanya ni kuwatoza akinamama wajawazito gharama hizi za kujifungua. Kwa hiyo, hii sera ya utekelezaji huduma bure kwa akinamama wajawazito ni kama haieleweki kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila nilipojaribu kuona sasa baada ya kuwa wamepata hizi pesa wanawezaje kuwarudishia wale akinamama pesa zao, inakuwa ngumu, nimefuatilia mara nyingi, lakini majibu hayajapatikana. Ninao ushahidi wa receipts ambazo wamelipa. Kwa hiyo, ninaomba ulisimamie hili, ili basi wananchi wapate haki zao, kwa sababu ni sera kwamba, huduma ya mama mjamzito na mtoto ni bure, lakini pale pana changamoto kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, katika ule mkataba tunaomba tupate maelekezo ya gharama za huduma zinazotolewa na hospitali hizi. Gharama zimekuwa za juu mno, tupate maelezo tufahamu sasa kwamba, gharama wanazotakiwa kutoa hospitali binafsi ni zipi; gharama zimekuwa juu mno kiasi kwamba wananchi wetu wanashindwa ku-afford. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Wizara ya Afya ilifuatilie hili kwa sababu, wananchi wanapata shida katika suala zima la gharama za matibabu katika eneo langu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la tatizo la maji katika Hospitali ya Wilaya ya Kinyonga, pale Kivinje. Hospitali yetu ya Wilaya ya Kilwa ina tatizo la maji. Mpaka leo wagonjwa wakienda pale suala zima la maji ni kizungumkuti. Kwa hiyo, tunaomba Wizara iliangalie tatizo hili na ilitatue haraka iwezekanavyo kwa sababu, pamekuwa na mashaka ya upatikanaji wa maji katika Hospitali ya Kilwa Kivinje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la ujenzi wa vituo vya afya pamoja na ujenzi wa zahanati. Wananchi katika jimbo langu wamejitahidi kujitolea kujenga zahanati, lakini mpaka sasa zile zahanati zimeisha, lakini bado hazijafunguliwa. Kuna Zahanati za Pungutini, Miyumbu, Marendego, Kipindimbi, Nambondo pamoja na Ongwe. Hizi zahanati zimekamilika kwa nguvu za wananchi lakini mpaka sasa hazijafunguliwa. Tuiombe Serikali ijitahidi kuhakikisha kwamba zahanati hizi zifunguliwe ili wananchi wetu waweze kupata huduma ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la huduma bure kwa wazee. Ni sera ya Serikali kwamba wazee sasa wapate huduma bure, lakini suala hili ni kama halijasimamiwa ipasavyo. Kule kwangu mpaka sasa haieleweki kuna taratibu gani kwa hawa wazee kupata ile huduma. Ilitokea mara moja tu Mkurugenzi alitoa tangazo kwamba wazee wajiandikishe ili waweze kupata utaratibu wa kuweza kupata hizo huduma bure. Hata hivyo, mpaka sasa ni wazee wachache sana wamesajiliwa katika utaratibu ule. Tuombe Serikali itoe elimu zaidi ya namna gani wazee wetu watatibiwa bure, suala hili ni muhimu na ni suala la kisera.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la walemavu. Ndugu yangu Mheshimiwa Mussa hapa amezungumza, nami nimekuwa nikilizungumza mara nyingi. Serikali bado haijaliona kwa kina suala la mahitaji maalum kwa walemavu. Kwa mfano katika Wilaya yangu ya Kilwa, katika Jimbo langu la Kilwa Kaskazini, takribani walemavu wa ngozi 15 tulilazimika kuwapeleka Ocean Road kwa ajili ya kupata matibabu ya mionzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ya kupata hayo matatizo ya ngozi ni kutokana na kukosa hitaji lao maalum la kupata mafuta ya kuwakinga dhidi ya athari ya miale ya mwanga. Tumekuwa tukisema mara nyingi, kama Serikali imeweza kuhudumia mama mjamzito na mtoto wa miaka mitano kwa nini isiweze kutoa mafuta bure kwa walemavu wa ngozi? Hawa walemavu wa ngozi wanaishi katika maisha ya kawaida kabisa na wakati mwingine hawajui hii bidhaa inapatikana wapi? Hili ni lazima lionwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sio hilo tu, sisi sote ni walemavu watarajiwa, lakini mpaka leo Serikali bado hospitali zinazohusika na kutoa viungo bandia zinatoa kwa gharama ya juu mno. Leo ukitaka mguu bandia lazima uwe na milioni tatu, ni hela nyingi kwa mlemavu na hatuwezi kujua mlemavu ni nani? Sijui Serikali inalionaje suala hili? Suala la walemavu, ni asilimia ngapi walemavu katika nchi hii? Kwa nini mahitaji yao maalum yasitolewe bure? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwa mlemavu si suala la kuchagua, kama tunatoa huduma kwa mama wajawazito, tutoe huduma kwa walemavu. Kuwa kipofu, kuwa kiziwi au kuwa mlemavu wa ngozi si suala la kuchagua. Mahitaji maalum kutokana na ulemavu wao ni suala ambalo Serikali inatakiwa iliangalie, sasa nashangaa kwamba leo tuna walemavu wa ngozi tunawapeleka Ocean Road tena kwa kuchangishana ilhali Serikali ipo. Serikali ifanye sensa ya walemavu wa ngozi, vile vile Serikali itoe huduma ya mafuta haya bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nianze kwa kuwapongeza viongozi wa Wizara hii, ndugu yangu Profesa na wasaidizi wake Mheshimiwa Kwandikwa na Mheshimiwa Nditiye kwa namna ambavyo mnatekeleza majukumu yenu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na suala zima la TARURA. Tumeanza na TARURA inafanya kazi lakini bado ina changamoto na kule kwetu Kilwa TARURA hawana vifaa vya usafiri, hawana gari kwa hiyo utendaji wao wa kazi unakuwa ni shida. Kwa hiyo, niombe Wizara iwaone hawa ili waweze kufanya kazi yao vizuri zao sawasawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna hoja ya upembuzi yakinifu katika barabara ya Nangurukuru - Liwale. Imeelezwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwamba barabara hii itafanyiwa upembuzi yakinifu lakini mpaka sasa hakuna chochote kimefanyika. Niiombe Wizara ituangalie watu wa Kilwa, Liwale kufanya upembuzi yakinifu tayari kwa kuijenga barabara ile kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala zima la barabara zinazounganisha mikoa hasa barabara inayounganisha Mkoa wa Lindi na Mkoa wa Morogoro. Mheshimiwa Waziri naomba aliangalie hilo, sisi watu wa Lindi tuna haja ya kuunganishwa na wenzetu wa Morogoro ili tuweze kuwasiliana kijamii na kiuchumi ili mambo yetu yaweze kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna barabara ya Kipatimu - Njia Nne ambayo iko chini ya TANROADS inahudumiwa na hata sasa hivi wakandarasi wako site lakini tuna changamoto kubwa ya miinuko na milima. Kwa hiyo, tuombe Wizara katika milima mikali watuwekee hata vipande vya lami ili ile barabara iweze kupitika wakati wote. Kwa mfano, kuna Mlima wa Ndundu ni mkali sana, Mlima wa Ngoge na Mlima Kinywanyu Wizara ituangalie hivyo vipande viweze kuwekewa lami ili barabara hiyo ipitike wakati wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee sasa suala la mawasiliano ya simu. Katika Jimbo langu kuna Kata ya Chumo, mawasiliano ya simu yapo lakini mnara wa Vodacom uliofungwa pale una matatizo. Unafanya kazi kwa muda wa saa saba hadi nane tu kwa siku, wananchi wangu wanapata hasara kubwa. Ukianza saa tatu mwisho saa mbili usiku baada ya hapo mnara ule haufanyi kazi tena na ni kwa sababu ya chanzo cha umeme pale, wanatumia solar power ambayo nafikiri ina matatizo. Nimeshafikisha tatizo hilo Wizarani naomba mlishughulikie kwa sababu mawasiliano pale ni kama yapo nusu nusu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo kuna Kata ya Kandawale hawana mawasiliano kabisa, kuna Vijiji vya Mkarango, Dandete, Kinjumbi hivi vyote havina mawasiliano ya simu. Naomba basi ndugu yangu Mheshimiwa Nditiye utuangalie na sisi tuweze kupata mawasiliano hayo ya simu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda niongelee suala la mgawanyo wa bajeti ya barabara kwa mikoa. Nimejaribu kufuatilia bajeti za kila mwaka za mikoa inaonekana mgawanyo ni kama haulingani, kuna mikoa ambayo bajeti inakuwa kubwa sana na mingine kila mwaka bajeti inakuwa hafifu sana. Angalau mngejitahidi tuwe tunalinganalingana kwa sababu mikoa mingine kila mwaka bajeti iko juu sana lakini mikoa mingine kama Lindi kila mwaka bajeti iko chini sana. Mheshimiwa Profesa angaliaangalia, hatuwezi kufanana kwa asilimia lakini angalau tulinganelingane kwa sababu hatuelewi mnatumia vigezo gani ya kwamba mikoa mingine bajeti juu na mikoa mingine bajeti inakuwa chini sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna suala la mawasiliano ya redio. Katika bajeti ya mwaka 2016/2017 walisema wangejenga mnara pale Nangurukuru ili na sisi watu wa Kilwa tupate mawasiliano ya Redio Tanzania, lakini mpaka sasa hakuna chochote ambacho kimefanyika. Tunakosa mawasiliano ya redio hasa redio yetu ya Taifa, Redio Tanzania. Tunaomba sasa mnara ule ujengwe, wananchi wanashindwa kuelewa nini kinachoendelea hasa kupitia mawasiliano ya redio. Ni muhimu sana mnara ule ukajengwa ili wananchi wapate mawasiliano ya redio. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la upanuzi wa Bandari ya Kilwa Masoko. Kama ambavyo mnafahamu tunayo bandari yetu pale, lakini mpaka sasa hivi bado haijaonwa. Wizara iione Bandari ya Kilwa Masoko iifanyie upanuzi. Bandari ile ni kama imesahaulika, mtukumbuke na sisi watu wa Kilwa, Bandari ya Kilwa Masoko ipanuliwe kwani itatusaidia sana katika sekta ya utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la upanuzi wa Uwanja wa Ndege Kilwa Masoko. Katika miaka miwili, mitatu iliyopita kulikuwa kuna mpango wa upanuzi wa Uwanja wa Ndege Kilwa Masoko na kuna tathmini ilikuja kufanyika pale ili wale wananchi wanaozunguka uwanja ule waweze kupata fidia lakini mpaka sasa hivi hakuna kinachoendelea, wananchi wale wamebaki pale hakuna uendelezaji wowote unaofanyika na hakuna dalili kwamba ni lini wananchi wale watafidiwa. Kwa hiyo, niiombe Serikali na Wizara iwaangalie wananchi wa Kilwa Masoko ili basi na wao waweze kupata stahiki zao, wafanye mambo mengine kwa ajili ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho na mimi niungane na Wabunge wengine ambao wamejaribu kuelezea shida Waheshimiwa Wabunge wanayoipata ya kusafiri kutoka hapa tulipo kuelekea Area D. Mimi nafikiri Serikali itafute suluhu ya haraka sana kwa sababu haieleweki sehemu ambako Waheshimiwa Wabunge wanakaa namna ya kusafiri inakuwa shida yaani ni kana kwamba Wizara imelala au haioni. Waheshimiwa Wabunge wanapitapita vichochoroni wanaweza wakaibiwa, lakini mazingira yale siyo rafiki. Kwa hiyo, hilo liangaliwe ili Waheshimiwa Wabunge waweze kusafiri comfortable kwenda katika zile nyumba ambazo wanaishi na kufika hapa Bungeni. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili basi na mimi nichangie katika Wizara hii ya Maji na Umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, asilimia 22 ya bajeti ya maendeleo ambayo imekwishatolewa mpaka sasa ni kielelezo tosha kwamba Serikali ya CCM maji siyo kipaumbele chao cha kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya CCM ina kipaumbele cha mipango tu lakini siyo utekelezaji wa mipango hiyo na ndiyo maana mpaka sasa hivi sehemu kubwa ya Watanzania wameshindwa kupata huduma ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niseme kwamba bado Serikali haijafanikiwa kuondoa tatizo la maji kwa wananchi wake kwani wananchi wana shida kubwa ya maji. Sina shida na utendaji wa Waziri na Naibu wake wanajitahidi na kama wangekuwa wamewezeshwa basi mambo yangeweza kwenda sawasawa, lakini tatizo hilo lote kubwa linatokana na Wizara ya Fedha ambayo inashindwa kutoa pesa kwa wakati ili Waziri na Naibu Waziri waweze kutekeleza miradi ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya CCM imekuwa ikijigamba kwamba inakusanya pesa zaidi ya mipango yake, lakini cha kushangaza utekelezaji wa miradi ya maendeleo na maendeleo muhimu kama ya maji inashindwa kutekelezwa, tunashindwa kuelewa. Kama mnakusanya pesa za kutosha kwa nini miradi ya maji ikwame? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali bado haijaliona tatizo hili, sera inaelekeza kumtua mama ndoo kichwani, lakini bado akimama wa vijijini wanapata maji kwa kuyabeba kichwani. Serikali iliangalie hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni suala zima la Azimio la Bunge lako tukufu. Kamati yangu ya Kudumu ya Usimamizi wa Serikali za Mitaa tulipokuwa tunawasilisha taarifa tulitoa angalizo na Bunge likaazimia kuundwe Kamati Teule ya Bunge kwa ajili ya kuangalia utekelezaji wa miradi ya maji. Lile lilikuwa ni Azimio la Bunge na Bunge lilitaka Kiti kihakikishe kinaunda Kamati Teule ya Maji kuangalia utekelezaji wa miradi ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati yangu imefanya ukaguzi wa miradi ya maendeleo tumegundua kuna tatizo kubwa la utekelezaji wa miradi ya maji na ndiyo maana tukaja na pendekezo lile ambalo sasa limeshakuwa Azimio la Bunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi kukikumbusha Kiti, tunaomba Kamati Teule iundwe ili utekelezakji wa miradi ya maendeleo uweze kuangaliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wachangiaji wengi wamejaribu kueleza tatizo la utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya maji ni shamba la bibi. Naomba hiyo Kamati iundwe haraka ili Bunge liweze kuangalia tatizo hili na kutafuta suluhu yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye matumizi ya maji ya Mto Rufiji. Mito yote mikubwa tayari ina miradi mikubwa ya maji, lakini mpaka hivi leo Mto Rufiji maji yake yanamwagika bure tu baharini. Maji ya Mto Rufiji mamba na boko wanaogelea tu, hayajakuwa na faida za moja kwa moja kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa za kijiolojia zinaelekeza kwamba ukanda wote wa Pwani ukichimba maji utapata maji ya chumvi. Kwa hiyo, ili basi kuwezesha kutoa huduma ya maji kwa wananchi wa Ukanda wa Pwani, maji ya Mto Rufiji yatumike. Tunaomba Serikali ianzishe mradi mkubwa wa maji ili basi wananchi wa Ikwiriri, Muhoro, Somanga, Njianne, Miteja, Kilwa Kipatimu, Kibata wapate maji, tunaomba sana katika hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna suala zima la miradi ya maji katika Jimbo langu la Kilwa Kaskazini. Mpaka hivi ninavyozungumza zipo kata ambazo bado hazijapata miradi ya maji. Kuna Kata za Namayuni, Chumo, Kibata, Kinjumbi, Somanga na vijiji vya Mkarango, Mtondo wa Kimwaga na Ndembo katika Kata ya Kipatimu havina mradi wa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni wenzetu wa DDCA walikuja na wakafanya utafiti kwa baadhi ya vijiji lakini wakashindwa kufika katika Kijiji vya Nandembo na Kibata. Niwaombe wafike katika vijiji vile kwa sababu wananchi katika maeneo hayo bado wana matatizo makubwa ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala zima la huduma ya maji katika Hospitali ya Wilaya pale Kilwa Kivinje, bado kuna matatizo makubwa. Tuiombe Serikali ihakikishe hospitali ile inapatiwa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna suala zima la Wakala wa Maji Vijijini na Mijini, limezungumzwa na wachangiaji wengi na Serikali pia ilishaelekeza kwamba ina mpango huo, tunaomba hili jambo lianze kwa haraka. Angalizo ni kwamba, wakati jambo hili litakapoanza Madiwani katika halmashauri zetu wapewe elimu ya kutosha namna gani wakala hii itakavyokwenda kufanya kazi ili kuepusha mgongano ambao unaweza ukatokea.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni suala zima la umwagiliaji. Katika Jimbo langu la Kilwa Kaskazini ambalo lina utajiri wa mabonde hakuna mradi hata mmoja wa umwagiliaji ambao unatekelezwa. Kwa mfano, tuna Mabonde ya Ngamwana, Marendego, Nambacho, Nalulo, Liomanga, hayo ni mabonde ambayo yanatiririsha maji wakati wote lakini hakuna project ya umwagiliaji hata moja. Niiombe Serikali iangalie eneo hilo na sisi tupate miradi ya umwagiliaji ili basi wananchi wetu waweze kujiendeleza kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo mnafahamu eneo la Kilwa na Lindi kwa ujumla wake sisi tumekuwa wapokeaji wa wafugaji. Kuna maelfu ya mifugo yapo katika maeneo yetu lakini mpaka sasa Serikali haijafanikiwa kujenga mabwawa kwa ajili ya kunywesha mifugo hiyo. Kwa hiyo, kunakuwa na mgongano mkubwa kati ya wenyeji pamoja na wafugaji kugombea maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuiombe Serikali ihakikishe maeneo yale yanajengwa mabwawa ya maji ili kuwezesha kunywesha ile mifugo ili tuondokane na migongano isiyokuwa na sababu kati yetu na wafugaji. Tunawapenda wafugaji lakini miundombinu haijaandaliwa. Kinachotokea sasa hivi ni migongano ya kugombea maji. Naomba sana Serikali iliangalie hilo kwa sababu ni jambo muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mradi wa Mingumbi - Miteja ambao uligharimu karibu shilingi 4,750,000,000 umekamilika lakini mara tu baada ya kukamilika haufanyi kazi na haufanyi kazi kwa sababu vifaa vilivyotumika pale ni kama vifaa fake, mabomba yanapasuka hovyo hovyo, ule mradi ni kama mfu ndani ya muda mfupi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo lingine ni kwamba kuna hizi Mamlaka za Watumiaji wa Maji bado hazijapewa elimu ya kutosha kuona ni namna gani zinaweza kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma hii ya maji. Naomba suala hilo liangaliwe…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Niende moja kwa moja kwenye Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi hasa katika Sekta ya Mifugo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimekuwa kila nikipata nafasi ya kuchangia katika Wizara hii, kilio changu ni kuhusiana na suala zima la mazingira wezeshi, mazingira ambayo yanaweza kuwafanya wafugaji wafanye shughuli zao na hii nikiwa na maana kwamba Serikali imefanya maamuzi ya kupeleka mifugo Mkoa wa Lindi na hasa Wilaya ya Kilwa, lakini mpaka hivi ninavyozungumza hakuna chochote kimefanyika kuhusiana na miundiombinu ambayo ingeweza au itaweza kuwasaidia wafugaji wale kufanya shughuli zao ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mapori yote ya Kilwa sasa yamevamiwa na mifugo, lakini hakuna bwawa, hakuna josho kwa hiyo wafugaji wale wanafanya shughuli zao kiholela. Nichukue nafasi hii kuishauri Wizara, naomba mjenge mabwawa na majosho Kilwa ili basi mifugo ile iweze kustawi kama ambavyo tumekusudia. Kwa hali iliyopo sasa ni ugomvi tu baina ya wenyeji wakulima na ndugu zetu wafugaji. Kama ambavyo wanafahamu, sisi watu wa Kilwa hatufugi sisi kazi yetu ni kuvua, kazi yetu kulima, tukiona ng’ombe watoto wanakimbia ndiyo kwanza tumeanza kuona ng’ombe, sasa wameleta kwa maelfu bila kipimo, wanatupa shida, tunapata tabu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii labda mimi naeleza kwa hisia nyepesi nyepesi Mheshimiwa Ulega anafahamu, alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, anafahamu ninachokizungumza, ni mashaka. Kwa hiyo, tunaomba hatuna shida na wafugaji lakini andaeni sasa miundombinu ili sisi basi tufanye shughuli zetu kama wavuvi, kama wakulima na wafugaji wafanye shughuli zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni suala zima la zoezi la upigaji chapa, kuna zoezi hili linaendelea na kusudio lake lilikuwa sasa kuweza kutengenisha wapi sasa wanatakiwa wawepo wafugaji na eneo gani wakulima wataendelea kuwepo na kufanya shughuli zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi hii ni tajiri wa mapori na ardhi ambayo unaweza ukafanya shughuli za kilimo ipasavyo na shughuli za ufugaji, lakini katika hali ya kushangaza, katika program hii, wakulima na wafugaji wanachanganywa na ili kuondokana na hili ndiyo likaja wazo sasa la kupiga chapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, zoezi hili la kupiga chapa linaendeshwa kwa urasimu mkubwa. Tunashindwa kuelewa. Kwa mfano, Lindi tuna Selou, tuna mapori ambayo hayana kazi, lakini wafugaji hawa wanakuja kung’ang’ania kukaa katika maeneo ya wakulima, haieleweki tatizo ni nini. Naishauri Wizara wafugaji wawaweke tofauti na wakulima, tuna maeneo mengi katika vijiji vyetu, wafugaji hawa wanaweza wakafanya shughuli zao tofauti kabisa na wakulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni suala zima la maendeleo ya uvuvi. Kwangu Kilwa ni wavuvi lakini mpaka sasa ukimuuliza mvuvi ni lini alisaidiwa na Serikali hakuna siku ambayo mvuvi alisaidiwa na Serikali na Serikali haijakuja na program yoyote ya kuwasaidia wavuvi.

Naishauri Serikali iwaangalie wavuvi kama ambavyo inawaangalia wafugaji na wakulima. Wavuvi nao waangaliwe, wapewe vifaa vya kisasa, wawezeshwe kwenda kuvua kwenye kina kirefu cha maji ili waweze kupata tija katika shughuli zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hali ilivyo sasa, wavuvi wale wanafanya shughuli zao kienyeji na sasa hivi hizi operesheni za ndugu yangu Mheshimiwa Mpina kwamba kila siku anakuja na programu mpya, inawadidimiza kabisa wavuvi wetu. Kwa hiyo, naomba Serikali ije na programu maalum ya kufanya ustawi kwa wavuvi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wote wanaweza kuwa mashahidi. Leo ukisafiri kwenda Mikoa ya Kusini, sehemu ambayo unaweza kwenda ukasimama ukapata samaki wazuri ni maeneo ya Somanga. Somanga ile ambayo tunapata samaki, lakini hakuna Soko la Samaki. Tasi na changu wananunua kienyeji, hakuna Soko la Samaki. Hii inaonesha namna gani ambavyo Wizara haijapanga kuwasaidia wavuvi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naishauri Serikali, Mheshimiwa Ulega alikuwa Kilwa pale, basi na ndugu zangu wale wa Somanga pawepo na soko ambalo sasa Waheshimiwa wakipita, watapata samaki wa kupaka na wali wa nazi, mambo yanaenda sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na suala zima la makinikia. Mheshimiwa Biteko alikuwa Mwenyekiti na taarifa yake ilikuwa very hot na baada ya taarifa ile matumaini ya Watanzania kupata mafanikio makubwa na pesa nyingi yalikuwa makubwa, lakini mpaka sasa tunavyozungumza hatujui yale matumaini na zile taratibu zimepotelea wapi. Tulitumainishwa kwamba tungepata nyingine lakini mpaka sasa naona mambo yako kimya. Mtakapokuja kuhitimisha Mheshimiwa Waziri tunaomba muwafafanulie Watanzania habari za makinikia na hatima yake imefikia wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala zima la elimu ya madini kwa Waheshimiwa Wabunge. Elimu hii ya madini kwa Waheshimiwa Wabunge haitoshi na siyo Wabunge wote tunatoka katika kanda za madini, wale ambao wanatoka katika Kanda za Madini wana uelewa zaidi kuliko ambao hatutoki katika kanda za madini. Wakati mwingine scope yetu ya kutoa michango inabanwa kutokana na hilo. Kwa hiyo, niombe Waziri basi atutengenezee mazingira tupate semina tuwe na uelewa zaidi katika madini ili basi tuwe tunaweza kuchangia vizuri katika sekta hii ya madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye vitabu vya Wizara tumeelekezwa aina za madini zinazopatikana katika maeneo tofauti tofauti. Naomba nishauri utafiti ufanyike zaidi kwa sababu naamini Tanzania ni tajiri kwa madini na madini yanaweza yakapatikana sehemu yoyote. Kwa hiyo, kama utafiti utafanyika zaidi basi upo uwezekano wa kuweza kugundua madini katika sehemu tofauti tofauti hata kule kwangu Kilwa.

Mheshmiwa Naibu Spika, Kilwa kwetu tukizungumza madini tunazungumzia gypsum, chumvi na gesi, niseme kuhusiana na gypsum. Gypsum inachimbwa Kilwa kwa ajili ya material ya viwanda vya cement lakini kuna changamoto kubwa ambayo ni gharama ya uzalishaji na bei ya soko ya gypsum. Gharama ya uchimbaji wa tani moja ya gypsum ni Sh.27,000, bei ya gypsum kwa viwanda vya cement vya Dar es Salaam ni kati ya Sh.80,000 au Sh.90,000 ukichanganya na gharama nyingine za usafirishaji na ushuru wa Serikali na kodi maana yake hawa wafanyabiashara wa gypsum wanafanya shughuli zao katika mazingira magumu. Tunaomba sana Serikali ije na bei elekezi ya gypsum ili basi wajasiriamali wetu waweze kufanya kazi ambayo inaweza ikawaletea tija.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukitaja madini basi akili zetu moja kwa moja zinatuelekeza kwenye jambo ambalo lina pesa nyingi lakini mchango wa madini katika bajeti ya Serikali ni finyu sana. Nitoe ushauri kwa Serikali bado ipo haja ya kuwekeza ili basi tuweze kuyatumia midini yetu ipasavyo na yatoe mchango mkubwa kwa bajeti ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala zima la madini ya gesi. Madini haya gesi ambayo kwa sisi watu wa Kilwa kwa mara ya kwanza gesi ilipatikana katika Kisiwa cha Songosongo mpaka sasa kuna changamoto kubwa katika madini ya gesi, watu wa Kilwa hatujafaidika nayo moja kwa moja, imefikia hatua hata wale ambao walitakiwa walipwe fidia kutokana na kupisha mradi ule wa bomba la gesi mpaka sasa hawajapata fidia zao. Nichukue nafasi hii kuishauri Serikali iwaangalie wadau wengine ambao walitakiwa wapate tija kutokana na madini haya ya gesi ili basi nao waweze kufaidi matunda hayo ya gesi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Serikali iwe wazi kuhusiana na madini ya gesi, ni aina gani ya gesi tuliyoipata. Gesi tuliyoipata ndiyo hii tunayotumia kupikia majumbani maana wananchi wakiona gesi hizi zinazouzwa wanafikiri ndiyo gesi ambayo tumeipata kutoka kule Songosongo. Tuwe wazi ni gesi hii au ni gesi tofauti, wananchi wafahamishwe maana kuna sitomfahamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunaambiwa uwezekano wa kupata mafuta upo, je, katika machimbo hayo ya gesi yaliyofanyika kuna dalili ya kupata mafuta? Serikali itueleze ni wapi tunaweza tukapata mafuta maana tumetumia gharama kubwa kuchimba gesi kama tulikuwa na tumaini la kupata mafuta Serikali iko kimya haijatueleza chochote kama tutakuja kupata mafuta au lah, maana tunaelezwa gesi na mafuta.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala zima la madini ya chumvi. Sisi tunazalisha chumvi lakini gharama za uzalishaji wa chumvi na tozo zilizowekwa katika uzalishaji wa chumvi ni nyingi sana wajasiriamali wetu ambao wanajishughulisha na shughuli ile hawapati faida. Kwa hiyo, niombe Serikali ipunguze hizo tozo ili basi hawa wajasiriamali wetu waweze kupata faida.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi nami niseme machache katika Wizara hizi mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na TAMISEMI na suala nzima la posho za Wenyeviti wa Vijiji na Vitongozi. Hawa ni viongozi ambao wanachaguliwa kama ambavyo Madiwani, Wabunge na Rais wanavyochaguliwa, lakini hatujaweka utaratibu wa kuangalia haki zao na hasa kuhakikisha kwamba wanapata posho. Napendekeza kwamba kama Serikali Kuu haina uwezo wa kuwawezesha viongozi hawa kupata posho, basi itoe maelekezo maalum katika makusanyo ya ndani ya vijiji husika, viongozi hawa walipwe kutokana makusanyo hayo. Hiyo itawasaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni suala la vitambulisho vya wajasiliamali, zoezi ili limeanza ghafla ghafla na limeleta taharuki kubwa huko kwa wananchi na hasa pale Serikali inaposhindwa kubainisha ni yupi mjasiliamali ambaye anatakiwa apewe kitambulisho? Kumekuwa na sintofahamu, mama mwenye mafungu matatu ya mboga anatakiwa alipe shilingi 20,000/=, mama huyo huyo akiwa na mikungu mitano ya ndizi, anatakiwa alipe shilingi 20,000/= na sehemu nyingine kama kule kwangu mtu mmoja analazimishwa kulipia hata mara tatu kwa sababu ana biashara tatu tofauti. Hiyo ni sintofahamu kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi, vitambulisho hivi vinaenda kubana kabisa mapato ya vijiji na mapato ya Halmashauri. Halmashauri hizi zitastawi vipi kama mapato yake kwa namna tofauti tofauti yanaendelea kuchukuliwa na Serikali Kuu? Naiomba Serikali hilo waliangalie, kwa sababu wananchi sasa wananituma, Mheshimiwa Mbunge, hebu tuulizie, hivi ile kodi ya kichwa imerudi? Maanda sasa kila tukizunguka ni vitambulisho, vitambulisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haipo familia ambayo hahijihusishi na ujasiliamali sasa. Kila familia lazima ifanye ujasiliamali, vinginevyo maisha ni magumu. Sasa kama unafanya ujasiliamali ni shilingi 20,000/=. Maisha kule ni magumu sana, naomba hilo liangaliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusiana na ujenzi wa zahanati kama sera inavyozungumza. Kwa bahati mbaya kabisa, mimi katika Jimbo langu kuna Kata moja aina zahanati hata moja za Serikali. Ile kata inaitwa Kata ya Namayuni. Ile kata ina vijiji sita, kuna kijiji kimoja kinaitwa Kijiji cha Naama, chenyewe wamejitahidi, wamejenga angalau kufikia boma. Naomba Wizara iwasaidie wale wananchi wapate ile zahanati iishe ili basi kata ile nzima iweze kupata huduma kwa sababu wananchi wanatembea kilometa zaidi ya 20 mpaka 50 kufuata huduma za matibabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, bado kuna tatizo la miundombinu iliyokamilika kuendelea kutotumika. Katika Kata ya Mingumbi katika Kijiji cha Lyomanga, Mfuko wa TASAF ulitoa fedha na kujenga zahanati toka mwaka 2009. Mpaka hivi tunavyozungumza, zahanati ile haijatumika na sasa inaelekea kubomoka. Naiomba Serikali ifuatilie hiyo zahanati na ione namna gani pesa za Serikali zinapotea bila kuwa na sababu ili basi ikiwezekana wafanye marekibisho na wananchi wapate huduma ya matibabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la korosho. Nachukuwa fursa hii kuipongeza Serikali na hasa ile kauli iliyotolewa na Mheshimiwa Rais kuhusiana na kwamba itawalipa sasa wakulima wa korosho pamoja na wale kangomba. Nikiri kabisa, sasa angalau tunaishi kwa matumaini, kwa sababu hali mwanzoni ilikuwa ni ngumu sana. Ingawa malipo yenyewe bado hayajafanyika, lakini tunayo imani kwamba siku moja tutalipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hili niseme, Serikali iache tabia ya kuingilia michakato iliyopangwa kwa mujibu wa sheria. Suala la korosho na utata uliotokeza ni kwa sababu tu Bodi ya Mazao Mchanganyiko haina uzoefu wa kusimamia zao la korosho. Katika namna ambayo hatufahamu, ni kwa namna gani Bodi ya Korosho ambayo inatambulika kwa mujibu wa sheria ikawekwa pembeni na badala yake ikachukuliwa Bodi ya Mazao Mchanganyiko ambapo mzigo umewalemea mpaka sasa wanashindwa kufanya malipo kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inajinasibu kwamba imetoa pesa, lakini bodi ile inashindwa kwa sababu haina uzoefu. Kwa hiyo, naomba hili liangaliwe sana. Kwa sababu maamuzi hayo yamepelekea hasara, athari za kisaikolojia, na kudumaza maendeleo, naitaka Serikali iwaombe radhi wakulima wa korosho kwa kitu kilichotokea. Kwa sababu kuna watu wamepoteza maisha, Serikali iwaombe radhi wakulima wa korosho kwa sababu lile lililofanyika, limefanywa kwa makusudi. Kwa hiyo, naomba hilo lifuatiliwe mara moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo napenda niseme ni suala zima la TARURA. TARURA wanafanya kazi vizuri lakini bajeti yao haitoshi. Wanajitahidi, lakini bajeti yao haitoshi. Naitaka Serikali iongeze bajeti TARURA. Nami katika Jimbo langu, naomba TARURA ishughilikie barabara ya kutoka Mbombwe – Anga - Nakindu mpaka Miangalaya; lakini pia ishungulikie barabara ya kutoka Mkarango - Mitole na kutoka Chumo mpaka Mkoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, nikumbushe ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne. Hii nalizungumza kwa mara ya tatu nikiwa humu Bungeni. Rais wa Awamu ya Nne Mheshimiwa Kikwete akiwa katika Sherehe za Kumbukumbu za Vita ya Maji Maji pale Nandete, aliahidi kwamba atajenga barabara kutoka Nandete mpaka Nyamwagi, ile ahadi mpaka sasa haijafanyiwa chochote. Naitaka Serikali ifuatilie utekelezaji wa ahadi ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la ufuta. Jimbo la Kilwa Kaskazini na Kilwa ujumla, sisi ni wakulima wazuri wa ufuta. Mwaka 2018 kulitokea na tatizo kwamba ufuta ambao hauna bodi ulilazimika kusimamiwa na Ofisi ya Mkoa na siyo Halmashauri, matokeo yake yalipelekea mapato ya Halmashauri kupungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2018 tulikwenda TAMISEMI, tulifuatilia sana. Tunaomba zao la ufuta lisimamiwe na Halmashauri na siyo Mkoa kwa sababu zao hili halina bodi na Halmashauri ina uwezo wa kufanya hivyo. Kwa kufanya hivyo, kung’ang’ania kusimamiwa na mkoa, mapato ya Halmashauri yanapungua. Tunaomba sana zao hili lisimamiwe na Halmashauri na siyo vinginevyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nizungumzie kuhusu upandishwaji wa madaraja. Tunaomba Serikali ijitahidi sasa kuona madaraja na mishahara ya watumishi inapandishwa. Watumishi hawa wanafanya kazi kwa kujitolea, wanafanya kazi kwa nguvu kubwa lakini wanakosa motisha kiasi kwamba ufanisi wa kazi unapungua. Kwa hiyo, Walimu, Watumishi wa Afya wote wale wapandishwe madaraja na mishahara iongezeke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nizungumzie kuhusiana na fedha za Mfuko wa Wanawake Vijana na Watu Wenye Ulemavu. Hili limezungumzwa sana na Wajumbe wa Kamati yangu, lakini pia nami niongezee. Tumefanya ziara sehemu mbalimbali, Halmashauri ya Wilaya ya Kahama imefanya vizuri sana na imefanya vizuri katika eneo hilo kwa sababu imefanya maamuzi ya kuchukuwa hizi pesa badala ya kumpa mtu mmoja mmoja ikaandaa utaratibu ambao utaenda kuwasaidia kundi hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iangalie ile model ya Halmashauri ya Kahama, ikiwezekana ifanyike sehemu nyingine. Kwa sababu sasa mianya imefungwa. Mwanya peke yake ambao kama hatutakuwa makini, Watendaji wa Halmashauri wanaweza kutumia kupiga sana pesa, ni katika pesa hizi za asilimia kumi. Kwa hiyo, tuwe makini sana, hizi pesa ikiwezekana tuzielekeze katika namna ambayo tunaweza kufuatilia na walengwa wakapata mahitaji yao stahiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukukumbuke pia katika eneo la walemavu bado walemavu wanashindwa kupata yale mahitaji yao kulingana na aina ya ulemavu waliokuwanao. Tuangalie uwezekano wa kuwasaidia walemavu wasioona wapate fimbo, walemavu viziwi wapate shimesikio, walemavu wa viongo wapate viungo bandia, wapate baiskeli na wale walemavu albino wapate mafuta kwa ajili ya kujinusuru na adhari za miale ya mwanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukijielekeza huko tutakuwa tumewasaidia sana, vinginevyo hii mikopo tunaweza tukaipeleka na isiwe na marejesho. Ni heri tupeleke kwa kuwasaidia Walemavu kwa ulemavu walionao…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Vedasto.

MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na niweze kusema. Nianze na suala zima la Bodi ya Mikopo ya wanafunzi, kuna tatizo ambalo linatakiwa lifanyiwe kazi. Tunawakopesha wanafunzi kwa riba kubwa hali ya kwamba wanasomea elimu ambayo hawana uhakika wa kuja kupata ajira na kwa sababu hiyo, itawachukua miaka baada ya kuwa wamehitimu kuja kupata ajira, matokeo yake watakapokuwa wameanza kupata ajira ile riba inakuwa imeongezeka mara dufu kwa hiyo, wanaanza kazi hali ya kwamba wanamzigo mkubwa wa riba ya Bodi ya Mikopo.. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina hakika kama Bodi ya Mikopo inakusudia, inakusudio la kufanya biashara kusudio la Bodi ya Mikopo siyo kufanya biashara, ni kutoa huduma. Kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Waziri tutoe mikopo lakini tupunguze riba, riba ni kubwa sana kubwa mno na kwa sasa mnakata asilimia 15 ya mshahara kwa hiyo mtumishi anaanza kazi lakini kiasi kikubwa cha pesa tayari kinakwenda kwa Bodi ya Mikopo. Kwa hiyo, naomba hili lifanyiwe kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jingine nizungumzie suala zima la wastaafu na stahiki zao. Tunawapandisha watumishi madaraja kwa maandishi tu na siyo vitendo, tunapandisha madaraja hakuna mabadiliko ya mishahara matokeo yake wanapokwenda kwenye kustaafu mafao yao yanakuwa kiduchu. Ni miaka mingi sasa zoezi la upandishaji wa madaraja limekuwa lakubabaisha babaisha watumishi hawa wanaenda kustaafu kwa mafao kidogo kwa sababu wanapandishwa madaraja lakini bila utekelezaji na matokeo ya mafao yao yanakuwa madogo. Kwa hiyo, niombe Wizara ijitahidi kwamba watumishi na hasa wale wanaokaribia kustaafu wapandishwe madaraja ili basi mafao yao yaweze kuwa angalau manono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jingine ni suala la elimu bure, hii elimu bure Serikali ijipambanue na iwe wazi elimu bure iwe ni kwa suala zima la ada tu, Serikali iwe wazi iwe wazi kwa wadau wa elimu kuchangia elimu na hasa wazazi tamko la elimu bure limeenda kuharibu uelewa na kiasi kwamba wazazi sasa na hasa wa vijijini huko wanaona kuchangia elimu siyo sawa sawa kwa sababu Sera ya Serikali ni elimu bure. Serikali sasa iwe wazi, iwe wazi kwamba suala la kuchangia elimu ni lazima isipokuwa Serikali yenyewe ubure huu unaozungumzia upo kwenye suala zima la ada tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jingine nizungumzie suala la elimu ya watu wazima, hasa suala zima la kisomo cha watu wazima. Wakati wa enzi za Baba wa Taifa suala hili lilisisitizwa sana na Tanzania ikawa ni nchi inayopigiwa mfano kwa kuwa imepiga hatua kwenye kuhakikisha kwamba watu wazima wanapata elimu hasa zile skills tatu za kuandika, kuhesabu na kusoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hili jukumu lilipewa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima sasa hivi hii Taasisi inaonekana hili jukumu lake la msingi kana kwamba wameliacha na wamejikita zaidi kwenye hizi elimu rasmi. Katika maeneo yetu bado kuna watu wengi ambao hawajui kusoma hawajui kuhesabu, hawajui kuandika. Na ukisoma kwenye ukurasa ule wa 38 wa Hotuba yako, unasema ndiyo kwanza mmeandaa mkakati wa kuona namna gani mnajikita katika hili eneo. Nasema mmechelewa mfanye haraka bado tuna watu wengi ambao wanahilo tatizo, huo mkakati wenu uwe wa haraka ili basi kuweza kunusuru watu wengi ambao wanamatatizo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jingine ambalo ningependa niliseme ni suala zima la elimu jumuifu inclusive education. Ukurasa wa 17 umeeleza kwamba Serikali ina mpango mkakati wa kuanzia mwaka 2018/2021 wa kuhakikisha ina mkakati wa hii inclusive education yaani elimu jumuishi lakini mpaka sasa hivi mko katika hatua ya uchapishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona hili suala kama limechelewa sana na tunaposema inclusive education ni nini. Huu ni mpango ambao wanafunzi wa aina yote wale walio na ulemavu na wasio na ulemavu watafundishwa katika darasa moja. Kimsingi suala hili kama litafuatiliwa na kutekeleza litawasaidia sana na litawasaidia sana walemavu kwa sababu kwa kufanya hivyo walemavu wanaweza waka- coop na kujifunza kutoka kwa wenzao ambao wasio walemavu. Lakini kwa kufanya hivyo na wale ambao wasio na ulemavu watakuwa familia na wale wenye ulemavu. Huu ni mpango mzuri sana lakini mpaka sasa inaonekana limezungumziwa kwa miaka mingi lakini utekelezaji wake unachelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe na niishauri Wizara suala hili ni zuri na lifanyike kwa haraka lakini liendane sambamba pamoja na kutoa mafunzo kwa wale walimu ambao hawa-skills za kuwafundisha walemavu. Liendane sambamba na kutoa motisha kwa walimu ambao wataenda kuwafundisha watoto walemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini liendane sambamba na kuwa na idadi kubwa ya walimu katika darasa hilo, kwa sababu katika darasa ambalo linawatoto walemavu na wasiowalemavu, kuwa na mwalimu mmoja ni mtihani lazima kuwepo na mwalimu ambaye hana hiyo skills za kuwafundisha watoto walemavu na yule ambaye ni mwalimu wa elimu maalum. Suala hilo naomba Serikali ilifanye kwa haraka kwasababu kundi hili la watu wenye ulemavu linaendelea kutengwa na kunakuwa na tendency ya kuwa na over protection lakini kunakuwa na tendency ya isolation kwa hiyo tukiwachanganya hawa itawasaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna suala zima la maslahi ya walimu. Walimu hawa wamekuwa wakifanya kazi kubwa kwa ari lakini bado Serikali haijaona namna gari inaweza kuwamotisha. Niombe Serikali itakapokuja basi itoe matumaini kwa walimu kwa kuongeza mishahara yao lakini itoe motisha kwa walimu kwa kuongeza madaraja yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la teaching allowance, teaching allowance Mheshimiwa Ndalichako wewe ni mwalimu kazi ya ualimu ni kazi nzito, walimu tulivushe hili kundi basi lazima tuone uwezekano wa kuwapa teaching allowance kitu hiki kitawasaidia sana na kilifanyika wakati wa mzee Mwinyi teaching allowance inawezekana katika kipindi hiki cha Mheshimiwa Dkt. Magufuli, na hilo mtaliweza kama mnaweza kufanya mambo makubwa makubwa na mazito mazito, fanyeni hili kwa walimu basi, fanyeni tuwarushie hiyo teaching allowance. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala zima la Sera ya Elimu. Wakati wa Baba wa Taifa, Sera yetu ya elimu ilikuwa education for self-reliance elimu inayotolewa basi imuandae mwanafunzi aweze kujitegemea lakini sasa sera yetu na muundo wetu wa elimu ni kama haueleweki, tunatoa elimu tuna watu wanahitimu lakini hawana uwezo wa kujitegemea sasa hivi tumekuwa na fashion ya kuwa na vyuo vingi vinavyotoa degree lakini baada ya kuwa tumekamilisha wanafunzi hawa wamepata degree hawawezi kujitegemea. Kwa hiyo, lazima tuje na mitaala ambayo itamuandaa mwanafunzi ili aweze kujitegemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuungana na Watanzania kwa msiba mzito uliotupata wa Dkt. Mengi. Sisi watu wa Kilwa tunamkumbuka sana Dkt. Mengi. Mwaka 1993 Mzee Kingunge Ngombale Mwiru aliitisha harambee ya kuchangisha ujenzi wa sekondari ambapo Mheshimiwa Dkt. Mengi alitoa milioni 20, tutakukumbuka daima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee suala zima la kuhitaji mtaalam wa mionzi katika Hospitali ya St. Marks Kipatimu. Hospitali hii tayari tumepata X-ray mpya lakini hatuna huyo mtaalamu. Naomba Serikali itupatie huyo mtaalamu ili wananchi waweze kupata uduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili naomba nizungumzie gharama za utoaji maiti katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, kuna changamoto kubwa. Kama ambavyo tunafahamu Hospitali ya Muhimbili ndiyo hospitali kuu ya rufaa, kwa hivyo, wagonjwa wengi wakishindikana wanakwenda pale na upo uwezekano wakatibiwa kwa muda mrefu sana. Sasa ikitokea mgonjwa amepata umauti kuna mtihani mkubwa wa gharama na kinachofanyika pale ni kuzuia maiti isitoke. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na tatizo kubwa sana hili na wauguzaji walio wengi wanashindwa kugharimia gharama hizo na matokeo yake ile maiti inazuiwa na hatimaye huenda kuzikwa na city. Naomba tuangalie upya utaratibu katika suala hili kwa sababu binadamu anastahili heshima na azikwe kwa mujibu wa mila na desturi zake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kiti chako kilishawahi kutoa ruling kikasema kwamba marehemu hadaiwi, sasa hii sijui inakuwaje? Kusudio siyo kukopa ni kupata tiba na ni haki yake, sasa hana uwezo na yeye ameshafariki kwa nini wauguzaji wasiruhusiwe kuchukua maiti wakamzike ndugu yao kwa heshima kubwa? Naomba Serikali iangalie suala hili ni tatizo kubwa, Wabunge tumekuwa tukipigiwa simu mara kwa mara kusaidia katika hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo ningeona niliseme leo ni kuhusiana na suala nzima matibabu ya wazee na hii Sera ya Matibabu Bure kwa Wazee. Ni sera ambayo imeanza kutekelezwa lakini kwa kusuasua. Niishauri Serikali basi ilete Muswada wa sheria ili sasa iwe kwa mujibu wa sheria na siyo sera ili basi wazee wetu wa kuanzia miaka 60 waweze kupata matibabu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la Kituo cha Afya Njinjo pale kwangu, tungeomba Serikali itupatie fedha kama ambavyo vituo vingine vimepata. Kituo kile kimekuwa chakavu sana, tunaomba nacho kipatiwe fedha hizo ili kiweze kutoa huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia wananchi wameanza kujenga Kituo cha Afya Chumo na Somanga. Tunaiomba Serikali nayo itusaidie ili vituo hivi vikamilike.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni suala zima la UKIMWI. Wafadhili wameendelea kujiondoa katika kufadhili ugonjwa huu. Kwa mfano, hawa wenzetu PEPFAR wao wenyewe wamepunguza msaada wao katika suala nzima la UKIMWI kwa kiasi cha dola milioni 119. Hii ni kwa sababu kasi ya kupima bure kufikia asilimia 90 ni kama inaenda kwa kusuasua. Kwa hiyo, ni nini mkakati wa Serikali wa kuwaruhusu wananchi wajipime binafsi kwa kutumia kile kipimo cha mate. Naomba Serikali iharakishe ili wafadhili hawa waendelee kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni suala zima la homa ya ini. Sisi Wabunge tumepata chanjo ya homa ya ini ni vizuri lakini Watanzania walio wengi bado hawajapata chanjo hii. Niiombe Serikali iangalie uwezekano wa kutoa chanjo hii kwa Watanzania wote kwa sababu ugonjwa huu ni hatari na unatishia amani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la bima ya afya kwa wote. Mimi ni miongoni mwa Wabunge tuliotembelea nchi ya Rwanda kuona namna gani wenzetu wanatoa hii bima ya afya kwa wote. Wenzetu wamefanikiwa sana na wanachokifanya ni kuhusisha wahudumu wale wa ngazi za chini, wanawapa majukumu na wao ndio wanafanya ushawishi kwa wananchi lakini wanawa-train kiasi kwamba wawe wanaweza kutoa huduma ya kuzalisha, kuchoma sindano na vitu vya namna hiyo. Niombe Serikali ije na huu Muswada wa Sheria ili basi huduma ya bima ya afya itolewe kwa watu wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. nianze moja kwa moja katika hotuba hii kwenye suala zima la mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya mwaka jana Wizara ilitenga bajeti na ilieleza kwamba, ingejenga minara ya mawasiliano katika vijiji vya Kinjumbi, Mwengei, Nandete, Chapita, Mtende na Mterambuko, hivi vingejengwa kwa kampuni ya TTCL, lakini Vijiji vya Kandawale pamoja na Mtumbempopera vingenjengwa na wenzetu wa Kampuni ya Vietell; mpaka hivi ninavyozungumza bado hakuna chochote kimeanza kufanyika. Niiombe Wizara hizi kampuni zianze kufanya kazi kwa sababu, tayari tumeshawaambia Wananchi na Wananchi wanasubiri kwa hamu kubwa, lakini nishauri pia katika bajeti hii ya mwaka huu niombe vijiji vya Mkarango, Ngarambi, Miteja, Namakolo, Mtepela, Kibata na Ingirito vipate mawasiliano kwa sababu, vijiji hivi havina mawasiliano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jingine niende kwenye suala zima la barabara, awali ya yote katika suala la barabara nichukue nafasi hii kukupongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwani katika ile Barabara ya Nangurukuru – Liwale kilometa mia mbili kama na 30 hivi kwenye Kitabu cha Bajeti yako ukurasa wa 226 nimeona umetenga pesa kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu pamoja na engineering design. Nikupongeze sana kwa hilo, sasa angalao tuna matumaini kwamba, barabara itaenda kujengwa kwa kiwango cha lami, basi tunachosubiri ni utekelezaji. Sambamba na hilo naomba Serikali iiangalie pia, Barabara ya kutoka Tingi – Kipatimu na Ndeti. Nayo basi iingie kwenye kuwekwa bwasi kwenye upembuzi yakinifu, ili basi hatimaye ije kujengwa katika kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo naomba niendelee kukumbusha ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, katika Sherehe ya Kumbukumbu ya Vita ya Majimaji pale Nandete alisema kwamba, yeye angejenga barabara ya kutoka Nandete – Nyamwage. Naomba niwakumbushe barabara hii ni muhimu na ni ahadi ya Mheshimiwa Rais; na nishauri, kijiografia ukitoka Nyamwage kwenda Kipatimu ni kilometa 50 sawasawa na kutoka Njia Nne kwenda Kipatimu, lakini leo hii tukitaka kwenda Kipatimu unalazimika ufike mpaka Nyamwage ambako utaenda kilometa 75 mpaka Njianne ndipo uende Kipatimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa barabara hii ya kutoka Nyamwage kwenda Kipatimu ya kilometa 50 kama ingekamilishwa na ingejengwa kwa changarawe tu, basi ungeturahisishia sana mawasiliano kutoka Nyamwage kwenda Kipatimu. Kwa kupitia barabara hii ukitoka Dar-es- Salaam kwenda Kipatimu ni kilometa 230 tu, lakini kwa kuzunguka tunakwenda kwa kilometa 280. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba barabara hii ambayo inapita kwa Ndugu yangu Mheshimiwa Mchengerwa halafu inakwenda kwangu ijengwe basi, iwe chini ya TANROADS, iimarishwe ili basi tuweze tukapata tukaweza kusafiri kwa mwaka wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo niombe sasa TANROADS waangalie uwezekano wa kuweka vipande vya lami katika milima ya barabara ile ya Tingi – Kipatimu, kuna Mlima Ndundu na Mlima Ngoge, mlima sumbusfu sana. Basi tuwekewe angalao vipande vya lami, ili basi tuweze kusafiri kwa wakati wote, wakati wote tunaweza tukapita kama hivyo vipande vitawekewa vipande vya lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo naomba TANROADS waangalie barabara ya kutoka Ndundu kwenda Somanga imewekwa lami katika kipindi ambacho hakizidi miaka mitatu minne, lakini leo ukienda ile barabara yote imefumuka. Niiombe Wizara makampuni wakati wanatekeleza miradi hii muwe makini sana vinginevyo ni upotevu wa pesa za Serikali kwasababu, barabara ya lami tunategemea ikijengwa angalao ikae miaka 20 na kuendelea, sasa ile barabara imekaa miaka mitatu tu sasa hivi mnarudia tena kufanya ukarabati mkubwa kana kwamba ilijengwa katika kiwango cha changarawe, naomba Wizara hilo waliangalie sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jingine ambalo ningependa nilikumbushe ni suala zima la upanuzi wa Bandari ya Kilwa Masoko. Kilwa pale tuna bandari, lakini ile bandari imekuwa kama haitumiki ni useless, ipo tu. Sasa Wizara naona kama mmetusahausahau, mfanye upanuzi na ikiwezekana muifanye iwe inatumika sasa. Sambamba na hilo naomba muangalie upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kilwa Masoko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kilwa ni Mji wa Kitalii, Mji wa Kilwa ni Mji wa Kitalii, lakini tuna uwanja wa ndege ambao katika bajeti ilisema ingefanya maboresho uwanja ule, lakini hakuna chochote kimefanyika. Naomba tuboreshe ule uwanja, ili basi tuweze kutengeneza fursa ya kupata watalii, Mji wa Kilwa ni Mji wa Kitalii, tuna Mji wa Kale wa Kilwa, tuna Mapango kama ya Nang’oma, tuna Fukwe kwa Mtoni Fumang’ombe na tuna vivutio vingi tu vya utalii, lakini kama uwanja huu ukiboreshwa basi utaweza kuvutia zaidi watalii na hivyo kuifanya Kilwa ipate ustawi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa barabara ya kutoka Nangurukuru kwenda Liwale kwa sasa kuna maeneo bado yanasumbua. Niiombe TANROADS iyashughulikie hayo maeneo, ili basi hiyo barabara iweze kupitika wakati wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ahsante. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie katika Mpango huu wa Maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, niishauri Serikali tupange kuwawezesha wavuvi kwa kuwapa mikopo, zana za kisasa ili basi waweze kwenda kuvuna katika bahari yenye kina kirefu. Hii ni moja ya sekta ambayo imesahauika kabisa, tofauti na sekta nyingine wavuvi ni kama bado hawajapata ule upendeleo wa makusudi wa kutenda kazi zao. Tukifanya hivi tutaongeza kipato cha watu wale lakini tutainua uchumi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine tupange sasa kusitisha uhamishaji wa mifugo. Kulikuwa na maamuzi sasa ya kuhamisha mifugo kutoka maeneo ya Ihefu (Mbeya) kuipeleka Mikoa ya Kusini hasa Mkoa wa Lindi. Mifugo ile sasa imekuwa mingi sana, nafikiri tupange kusitisha zoezi hilo na sasa tujikite na kuboresha miundombinu ya mifugo iliyopo pale. Tumepeleka ile mifugo hakuna mabwawa, malambo na utaratibu wa wapi inakaa na wapi isikae sasa kumekuwa na vurugu. Mimi nafikiri kwa tija bora ya mifugo ile tupange kuboresha miundombinu ili basi ile mifugo iwe productive, hilo litawasaidia sana wale wafugaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kwenye kilimo tuongeze sasa uzalishaji wa mbegu za mafuta. Ni dhahiri shahiri kwamba ukiacha uagizaji wa petroli basi kitu kingine kinachoagizwa kwa pesa nyingi za kigeni ni mafuta ya kula. Bado tunayo fursa ya kuzalisha mbegu hizi za mafuta ili basi tuweze kupata mafuta mengi ya kula ambayo yatapunguza kutumia pesa nyingi za kigeni kuagiza mafuta hayo kutoka nje. Hilo litakuwa ni jambo jema sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tupange pia kuwa na viwanda vya mafuta. Kwa mfano, sisi kule kwetu tunazalisha ufuta mwingi lakini hatuna kiwanda cha ku- process mafuta ya ufuta, ni kama tunazalisha kwa ajili ya kusafirisha ufuta ghafi kitu ambacho kwenye uchumi nafikiri hakiko sawasawa. Tukipanga sasa mpango wa kuwa na viwanda vya ku-process ufuta, vitasaidia kupata hayo mafuta, kutengeneza ajira na kuinua uchumi wa watu wale. Lindi leo tumetajwa kama Mkoa wa mwisho, tunazalisha ufuta mwingi tukiwa na viwanda vikubwa vya ku-process mafuta ya ufuta tutawezesha kupandisha uchumi wa watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine nafikiri sasa tupange kuwa na mtawanyo unaofanana wa uwekezaji wa viwanda. Tunajenga viwanda ni jambo jema na tunaenda kwenye uchumi wa viwanda lakini hivyo viwanda tumeona kama vinajikita sehemu moja. Serikali iangalie uwezekano sasa wa kutawanya, tuangalie kule zinakopatikana malighafi basi na viwanda vijengwe huko. Vitasaidia kutengeneza ajira lakini vitasaidia kujenga ustawi wa miji na kupandisha uchumi wa watu katika maeneo husika. Hilo litakuwa ni jambo jema sana kwa ustawi wa uchumi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka kusema ni kuhusu suala zima la uwekezaji. Tupunguze urasimu katika uwekezaji kwani bado kuna urasimu mkubwa katika uwekezaji. Sisi pale kwetu alikuja mwekezaji kutoka Marekani akitaka kuwekeza katika Bonde la Mto Matandu kwa ajili ya kilimo cha mpunga, ni uwekezaji wa zaidi ya dola milioni 50, uwekezaji mkubwa sana. Sisi Halmashauri tukashawishi Serikali za Vijiji tukatoa ile ardhi lakini kilichotokea basi alitokea tu dalali mmoja akaanzisha longolongo mwishoni yule mwekezaji akaondoka, nafikiri aliamua kuondoka kwa sababu ya urasimu. Serikali ijaribu kufuatilia tupunguze urasimu kwani uwekezaji kama ule ungefanyika ungewasaidia sana wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ule uwekezaji wa miradi mikubwa kwa mfano LNG lakini kiwanda cha mbolea ni jambo jema kama Serikali ingehuisha utekelezaji wake. Limekuwa likizungumzwa lakini utekelezaji wake mpaka sasa naona ni kama umekwenda kwa kusuasua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusiana na uamuzi wa kupunguza kwanza ushuru wa Halmashauri katika yale mazao yanayolimwa na wakulima katika Halmashauri kutoka asilimia 5 mpaka 3 lakini ule uamuzi wa kutotoa ushuru wa korosho umezi-paralyze Halmashauri zetu, Halmashauri zetu hali ni mbaya sana. Hii inachangia pengine hata kufanya wananchi katika Halmashauri uchumi wao kuwa chini na kutajwa kama maskini. Lindi na Mtwara tunazalisha korosho, mwaka jana ushuru ule haukwenda kabisa. Zipo Halmashauri zaidi ya asilimia 90 ya mapato yake zinategemea ushuru wa korosho. Kwa hiyo hilo nalo Serikali iliangalie vinginevyo hawa watu ukisema ni maskini tu inakuwa kama hukuwatendea haki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la maji. Tumekuja na mawazo mazuri kabisa ya kuanzisha Mamlaka ya Maji Mijini na Vijijini, ni jambo jema lakini sasa Serikali ipange kupeleka pesa za kutosha. Katika jambo ambalo bado linaguswaguswa ni suala la maji. Tuna Wakala huyu kwa mfano DDCA wa kuchimba visima bado kabisa kazi haijafanyika. Tuwaongezee pesa waweze kuchimba visima vingi na kufufua ile miradi ya siku nyingi ambayo imekufa ili basi wananchi wetu waweze kupata maji safi na salama na hivyo kuinua uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa ni suala la uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Suala hili la hiki kinachoendelea ni jambo geni kwenye mchakato wetu wa demokrasia na uchaguzi. Ni jambo ambalo limeleta sintofahamu, tumestushwa na tumepigwa na bumbuwazi, kwa nini hili limetokea?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niseme tu hili ni jambo geni na Waswahili wa Pwani wanasema: “Mgeni kumpokea pengine kujichongea”. Sasa hili limekuja tulikemee siyo jambo zuri baadaye litakuja litatusumbua sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi bado wanaendelea kuhangaika kufuata zile taratibu za kupata hizo haki. Tumejiandikisha majina baadaye ukaja uchaguzi wa kuteuliwa, hatukuteuliwa, tukaweka yale mapingamizi bado hatukupata hiyo haki, sasa hivi hatua inayofuata ni kwenda kukata rufaa na rufaa inatakiwa ukakate Makao Makuu ya Wilaya. Sasa kwa jiografia ya Majimbo yetu kutoka vijijini kwenda Wilayani ni mbali sana kiasi kwamba zile siku mbili hazitoshi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali ina nia njema ya kuona hii haki inapatikana, niishauri Serikali iongeze siku kwa ajili ya kukata rufaa. Wananchi bado wanaona kwamba wanataka kutafuta hii haki, kama ambavyo mmeongeza siku za kujiandikisha basi ongezeni siku za watu kwenda kukata rufaa ili kuona wanapata haki zao ili tuweze kwenda kwenye kuchagua viongozi ambao wananchi wanawataka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, ahsante. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge na Utawala na Serikali za Mitaa pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kusema chochote katika michango ya kamati hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze tu kusema kwamba yapo malalamiko kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi na nilitarajia kwamba kwenye taarifa ya kamati basi kuna chochote kingesemwa ili basi kuweka hiki kitu sawasawa. Kwa hiyo, nitake kwamba Serikali ifanyie hili suala kazi, wananchi wanalalamika sana juu ya namna ambavyo uchaguzi umeendeshwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jingine ambalo ningependa niseme ni kwamba zipo Halmashauri ambazo mpaka leo bado hazijapeleka michango ya makato kwa malipo ya Waheshimiwa Madiwani na Serikali isipokuwa makini tutaenda kwenye kumaliza wakati wetu, kwa baadhi ya halmashauri nyingine watashindwa kulipa viinua mgongo vya Waheshimiwa Madiwani. Kwa hiyo, ni jukumu la Serikali kuhakikisha kwamba kila halmashauri inapeka hiyo michango ili basi Waheshimiwa Madiwani waweze kupata stahiki zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala zima la TASAF. Ripoti ya Kamati inaonesha kwamba wafadhili wanatoa fedha lakini Serikali imeonesha kusuasua kutotoa pesa sawa sawa. Kwa hiyo, nachukua nafasi hii kuitaka Serikali ichangie ipasavyo ili basi michango hii iende kwa zile kaya masikini ziendelee kupata kama ilivyokuwa katika utaratibu wa kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la TARURA. TARURA inafanya kazi nzuri na mwaka huu mvua ni nyingi, kwa hiyo barabara nyingi zimeharibika. Kwa hiyo, naiomba Serikali ikubali ushauri wa Waheshimiwa Wabunge wa kuongeza asilimia ya mgawanyo. Kwa kupendekeza, TARURA ipate sasa asilimia 40 ili iweze kushughulikia ipasavyo barabara za mijini na vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepitisha sheria ya asilimia 10 ya mapato ya ndani iende kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu. Zipo Halmashauri zimeanza kutopeleka hizo asilimia 10 kama zinavyotakiwa na sheria na hivyo kuanza kuzalisha madeni. Kwa hiyo, nachukua nafasi hii kuzitaka Halmashauri zote zipeleke ipasavyo hizo asilimia 10 ili basi michango ile iende sawa sawa kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna hii asilimia mbili inayokwenda kwa watu wenye ulemavu. Watu wenye ulemavu wana chagamoto; ukisema waandae makundi ili wakopeshe, wengine wanakosa haki. Kwa mfano, mtu mwenye ulemavu wa akili unamweka katika kundi gani? Napendekeza kwamba watu wenye ulemavu wa aina hiyo, basi wazazi wao washirikishwe kwenye makundi hayo ili basi nao waweze kupata stahiki zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vinginevyo bado inaonekana kuna uwezekano mkubwa kwamba asilimia mbili inayotakiwa kwenda kwa watu wenye ulemavu isiende kwao kwa sababu vikundi vinavyotengenezwa vya watu wenye ulemavu ni vichache sana. Serikali iangalie utaratibu mwingine wa kuweza kuangalia namna gani itawapatia hizi fedha watu wenye ulemavu, ikiwezekana waangalie pia mahitaji yale muhimu ya watu wenye ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nashauri Serikali sasa ilete Muswada wa Sheria kama ilivyozungumzwa kwenye Taarifa ya Kamati kwa ajili ya kusaidia Shirika la Masoko la Kariakoo lifanye kazi sawa sawa. Shirika hili ni la siku nyingi lakini inaonekana lina upungufu wa sheria na linashindwa kufanya kazi yake sawa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nizungumzie suala la pale Jimboni kwangu, Njinjo. Mkoa wa Lindi na Wilaya ya Kilwa na hasa Jimbo la Kilwa Kaskazini tumepatwa na kadhia ya mafuriko, hali ni mbaya sana. Ninavyozungumza, zaidi ya watu 26 wamepoteza maisha ikiwemo watu saba wa familia moja na watu sita wa familia nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyozungumza, katika zile Kata mbili kuna shule nne zimeharibiwa kabisa. Nachukua nafasi hii kuomba wenzangu wa TAMISEMI washirikiane na watu wa maafa wa Waziri Mkuu waangalie namna gani ya kuwasaidia wale watu. Isitoshe kwamba zaidi ya watu 10,000 wamekosa makazi na hivyo kulazimika kupewa viwanja kwa ajili ya kupata makazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia kuipongeza Serikali kwa namna ambavyo imeshughulikia tatizo hili. Naiomba huko ambako wananchi wanakwenda kupewa viwanja, basi Serikali ihakikishe haraka iwezekanavyo inapeleka huduma muhimu ikiwepo shule, miundombinu ya barabara, umeme na maji ili wale wananchi waweze kuishi maisha kama walivyokuwa wanaishi mwanzoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue nafasi hii kuwaomba Jumuiya za Kimataifa, asasi za kiraia, watu mbalimbali kuchangia watu walioathirika na mafuriko. Ikupendeze, hata Bunge lako Tukufu, ikiwezekana, ikikupendeza basi nalo lichangie waathirika wa mafuriko katika Wilaya ya Kilwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue nafasi hii kutoa pole kwa waathirika wote ambao wamekutwa na kadhia hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. VEDASTUS E. NGOMBALE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Nianze na kuwapongeza Mheshimiwa Kigwangwala na Mheshimiwa Kanyasu kwa kazi nzuri, hongereni sana mnakwenda vizuri. Mimi nianze na suala zima la utalii; kwa sababu ya kazi yenu nzuri, sasa tunazidi kupata watalii wengi lakini kuna maeneo ambayo huko mwanzo walikuwa wanapatikana watalii wengi lakini sasa watalii wamepungua. Kwa mfano ukisoma ukurasa wa 94 katika lile jedwali la vyanzo vya kale katika sehemu za Kilwa mwaka 2014, 2015 watalii walifikia mpaka 2700 lakini sasa hivi watalii wamepungua. Sasa hii inaonesha namna gani ambavyo Wizara bado haijajizatiti katika kuendeleza utalii hususan katika eneo la mikoa ya Kusini.

Mheshimiwa Naibu Spika, chanzo kilichotajwa pale ni kimoja tu ilhali sisi tunavyo vyanzo vingi. Kwa mfano tuna chanzo cha Pango la Nang’oma ni pango kubwa tu lakini pale sijaona kama kimefanyiwa chochote. Kutokana na hilo kwa sisi watu wa kusini bado inaonekana neno utalii kwetu ni msamiati, na ni msamiati ambao tafsiri yake hujajua maana yake. Kwahiyo naomba Wizara ijaribu kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kuona namna gani wanajihusisha kwenye utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine ambalo ningependa kusema, niwapongeze kwa kutoa ruhusa sasa ya kufanya ule uwindaji wa wenyeji, sasa wenyeweji wanaweza wakanufaika maana sasa wanyama wamekuwa wengi na sisi tumezikaribia mbuga zile lakini hatupati chochote; kwa hiyo kwa ruhusa hii itawasaidia sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna changamoto moja. Mwaka 2014 kama sikosei kulikuwa na operesheni ile ya Tokomeza ambayo ilisababisha kunyang’anya zile silaha za wenyeji; silaha zote zilinyang’anywa na mpaka sasa hivi ninavyozungumza zile silaha bado hazijarudishwa. Sasa kama mmeruhusu silaha walizokuwa wanamiliki wenyeji kihalali bado mnazo ninyi hilo nafikiri nalo litakuwa tatizo. Nomba Wizara ishughulikie ili warudishiwe zile silaha ili na wao waweze kunufaika kuwinda katika maeneo haya ya wazi kama eneo la Kilwa na sehemu nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kuhusu tembo. Tembo wameongezeka sana, na sisi ambayo majimbo yetu yanapakana na Selou imekuwa shida. Ukitaka kwenda baadhi ya vijiji ni lazima ule-timing kwamba sasa hivi huwezi kupita sasa hivi unaweza kupita. Kule kwangu katika Kijiji cha Mkarango tembo ameshawahi kuua mtu katika kipindi cha miezi miwili iliyopita.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi naomba Wizara ijaribu kuwa na connection nzuri na watu wale wa maliasili ili yanapotokea haya matatizo tunapotoa taarifa kwenu haraka sana waje ili waweze kuwarudisha tembo, vinginevyo basi muangalie njia nyingine ambao zinaweza kusaidia kudhibiti hawa tembo; tembo wamekuwa wengine sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni suala zima la ustawi wa watu wa kusini ambao wanakaribiana na vyanzo na vivutio vya utalii na hususan sisi ambao tunakaribia Pori la Akiba la Selou. Niseme tu kwamba labda Wizara iangalie upya namna ya uwekezaji wa rasilimali hizi za utalii. Sisi kule kusini tuna pori tuna Mji wa Kale wa Kilwa na vivutio vingi lakini mpaka sasa hatuna chochote, yaani hakuna yale manufaa ya moja kwa moja. Kama chuo hatuna hata chuo kimoja cha utalii; basi Wizara angalieni namna ambavyo sisi tunaweza tukanufaika moja kwa moja, maana ukikaribia waridi basi na wewe unukie.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi ni kama tumekuwa watunzaji tu wa yale mapori; na ndiyo maana utalii kwetu kimekuwa ni kitu cha mbali sana. Kwa hiyo Wizara hebu jaribuni kutengeneza kitu ambacho kitakuwa motisha kwa watu wa kusini na wao waukaribie utalii hiyo itatusaidia sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine naomba Serikali ishughulikie mgogoro kati ya Vijiji vya pale Zinga Kibaoni. Kuna Kijiji cha Ngarambi, Kijiji cha Mtepela na Kijiji cha Namatewa na Hifadhi ya Selou bado kuna migogoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, na la mwisho kabisa ninaomba sasa basi hili wenzangu wengi wamelifanya, watu kama kina Samata watumike vizuri ili basi utalii uweze kwenda…(Makofi)

(Hapa kengele ililiakuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Spika, shukrani kwa kunipa nafasi. Nianze kwa kutoa pongezi kwa Waziri na Naibu Waziri, mnafanya kazi nzuri, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi leo nitajikita zaidi katika maeneo ambayo yana tatizo kubwa sana, hasa kwenye suala zima la fidia. Wakati wa utekelezaji wa mradi wa gesi pale katika Kituo cha Somanga Fungu, walipokuwa wanapeleka umeme maeneo ya Rufiji na Ikwiriri wakati wa ujenzi wa njia ile ya umeme TANESCO ilifanya fidia kwa wananchi, lakini ilipofika katika Kijiji cha Somanga walifanya fidia na wakawasahau wananchi tisa.

Mheshimiwa Spika, Nimekuwa nikifuatilia fidia ya wananchi hawa mpaka leo haijapatikana, naomba niwataje. Kuna mwananchi anaitwa Mohamed Mtombwane, Amir A. Mtauka, Athuman Kiwanga, Mpara, Mwinchande Mtauka, Yusuph Masendela, Ally Gumbi, Athuman Mchoro na Rashid Matana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Hawa wananchi wananikera sana na suala hili mara nyingi nakuwa nawasiliana na watu wa TANESCO lakini mpaka sasa fidia zao hazijalipwa, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja basi awaone hawa wananchi, ni muhimu sana hawa wananchi walisahaulika.

Mheshimiwa Spika, lingine, wakati wa utekelezaji wa mradi huo huo, kuna eneo TANESCO walichukua pale Somanga Fungu, kulikuwa kuna eneo la wananchi lakini kuna eneo lilitambulika kama eneo la Kijiji, TANESCO ilifanya tathmini na ikaja kufidia. Wakati inakuja kufidia kwa bahati mbaya sana wananchi wakasema hapana lile eneo siyo la Kijiji ni la wananchi na wakajitokeza wananchi 63. Wakati hilo linafanyika tayari cheque ilishakuwa imeandaliwa, kukawa na mvutano matokeo yake zile pesa zikawa zimerudi tena TANESCO.

Mheshimiwa Spika, Nimefuatilia sana tangu mwaka 2015 mpaka sasa wananchi 63 hawajapata fidia ya yale maeneo na maeneo yale yameshatumiwa na TANESCO. Kwa hiyo naomba sana, wananchi hawa fidia hizo wapate. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine nizungumzie suala la mradi huu sasa kilovoti 400 ambao sasa unaendelea. Mradi huu una malalamiko makubwa sana hasa maeneo ya Somanga. Ifahamike eneo la Somanga ndilo eneo la kwanza ambalo limeanza kutoa umeme wa gesi kutokea Songosongo; lakini katika hali isiyoeleweka Mradi huu wa kilovoti 400 unafanyiwa tathmini na tayari asilimia 79 ya watu wameshaanza kulipwa.

Mheshimiwa Spika, Mradi huu ni wa Somanga fungu Kinyerezi, lakini TANESCO wameanza kulipa Kinyerezi na bado hawaja walipa watu wa Somanga ambako gesi yenyewe imetoka, sasa kuna maneno ambayo hayapendezi maana wale wananchi wananiuliza kwani sisi TANESCO wanatuona malofa au kwa kuwa tuko Kilwa, kwa nini, waanze kuwalipa watu wa Dar es Salaam na siyo sisi ambako gesi yenyewe ndiyo imeanza kutoka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Tumefatilia sana na sasa ni kama mwaka wa nne, mlichukua maeneo yao, wanashindwa kufanya shughuli za Kilimo, lakini bado hamtaki kufanya fidia, nikuombe Mheshimiwa Waziri utakapokuja basi uje na maneno yenye faraja kwa ajili ya malipo ya wale watu wa Somanga ambao wao ndiyo nafikiri ilipaswa wawe watu wa kwanza kufidiwa na si watu wa Kinyerezi kama ambavyo mlifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini jingine, nijielekeze sasa kwenye suala zima la REA, naomba katika awamu hiyo sasa inayokuja basi TANESCO waangalie Kata ya Kandawale, Kata ya Kandawale, Kata nzima haijapata umeme ina vijiji vinne kuna Kijiji cha Kandawale, Mpopela, Ngarambi na Namatewa, lakini katika Kata ya Miguruwe kuna Kijiji cha Zinga, Kibaoni, Mtepela na Kingombe hawajapata umeme, lakini waangalie pia Kijiji cha Mwengei, Mkarango, Namakoro, na Nambondo havijapata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Jingine ambalo ningesema ni suala zima la ujenzi wa Kiwanda cha Mbolea pale Kilwa Masoko. Inashangaza katika bajeti zilizokuwa zinapita taarifa za ujenzi wa Kiwanda tulikuwa tunaona katika hotuba ya Waziri, lakini katika hali ya kushangaza mwaka huu hatujaona chochote hakijasemwa chochote. Sasa Mheshimiwa Waziri awe wazi tu katika aina hii ya gesi tuliyoipata, maana sisi tumepata gesi kavu, gesi ambayo haija-associate na mafuta, je upo uwezekano wa kujenga Kiwanda cha mbolea ambacho kitakuwa kina manufaa, naomba Waziri aje atueleze hili kuliko kuwa tumebaki na matumaini, ahsante. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Naibu Spika, shukrani kwa kunipa nafasi. Nianze na hali ya uchumi hotuba ya Mheshimiwa Waziri inaonyesha kwamba pato letu la Taifa linapanda lakini uhalisia wa mambo hali mtaani ni ngumu, vyuma vimekaza mambo hayaendi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, viashiria vinaonyesha kwamba hali ni ngumu kwa sababu kwanza kwa sasa hata bidhaa tunazosafirisha kwenda nje zimepungua, mazao kama korosho, kahawa kiasi tunachosafirisha kwenda nje kimepungua. Kutokana na hiyo pia kuna hoja ya mikopo katika sekta binafsi imeshuka. Sambamba na hilo mfumuko wa bei umepungua upo chini ya asilimia tano. Sasa wachumi wanatuelekeza kwamba kama hali ndiyo hiyo ya mfumko wa bei, unaweza ukaathiri kwanza ukasabaisha kutovutia wawekezaji, pili mikopo kutolipika.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama hivyo ndivyo ilivyo, mimi siyo mchumi lakini nilikuwa na wazo katika suala moja. Kama mfumko wa bei umeshuka, Wabunge wengi waliposimama wakati wa Bajeti ya Maji walipendekeza Serikali iongeze tozo ya shilingi hamsini katika lita ya mfuta ili basi kupata fedha nyingi pesa nyingi za kutosha kwa ajili ya kuondokana na tatizo la maji. Sasa Mheshimwa Waziri wa Fedha kama mfumuko wa bei umeshuka kwa nini usikubaliane na pendekezo hilo la Waheshimiwa wa Bunge ili basi tukaondokana na tatizo la maji.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika jambo ambalo Serikali ya CCM bado haijashughulikia vizuri ni tatizo la maji, kuna tatizo kubwa sana la maji. Kama tumefanikiwa kwenye umeme kupitia REA kwa utaratibu wa kuweka tozo katika mafuta why not tusifanya katika maji kuna tatizo kubwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, ninamshauri Mheshimiwa Waziri wa Fedha aliangalie suala hili kuna tatizo kubwa miradi ya maji haiendi kwa sababu pesa hakuna. Kwangu kule Kilwa tumefanya contract na watu wa DDCA sasa tuna mwaka wa nne kila siku tunagomba hapa visima havichimbwi kwa sababu DDCA hawana pesa, sasa kama tutakuwa tuna pesa ambazo tumezi- ring fence, nafikiri tunaweza tukafanikiwa kutatua tatizo la maji kama ambavyo tumefanikiwa kwenye umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jingine ni suala zima la mikopo ambayo Benki Kuu imepunza riba kwa benki lakini benki bado hazipunguza riba kwa wateja. Mheshimiwa Waziri wa Fedha ukapokuja hebu tuambie kama Benki Kuu imepunguza riba tena imepunguza sana, kwa nini wateja nao wasipunguziwe riba? Kwa sababu sasa uwezo wa watu kukopa, watu wengi wanaogopa kukopa lakini pia watu wengi wanashindwa kulipa mikopo ambayo wamekwisha kopa. Nalo hilo naomba ulingalie ili basi Watanzania waweze kunufaika.

Mheshimiwa Naibu Spika, jingine niende kwenye suala zima la mifugo na uvuvi. Mheshimiwa Waziri wa Fedha katoa mapendekezo ya kuondoa karibu tozo 15 kwenye sekta ya uvuvi na sekta hii inasimamiwa na Wizara ya Uvuvi na Mifungo, lakini hajaondoa tozo hata moja kwenye sekta ya uvuvi. Mifugo tozo 15 zimeondoka, kwenye uvuvi hata moja hujaondoa tozo. Napata shida kwamba pengine Mheshimiwa Mpina yale mapendekezo yetu ya shida wanazopata wavuvi haukupelekewa labla, nataka niamini hivyo.

T A A R I F A

NAIBU SPIKA: Nani aliyesema taarifa?

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Naibu Spika, nipo hapa.

NAIBU SPIKA: Aaaah! Mheshimiwa Julius Kalanga.

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka kumpa tu taarifa mzungumzaji kwamba siyo busara sana kuendelea kutoa reference ya mapunguzo ya tozo katika mifugo kwa sababu kulikuwa kuna umuhimu wake wa kupunguza. Kama kuna hoja ya kudai punguzo kwenye samaki tudai bila kuona kwamba kupunguza kwenye mifugo maana yake imeathiri haki ya wavuvi, nimeona mijadala hii ikiendelea hivi kanakwamba wafugaji wao hawastahili kupunguziwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo nafikiri tujenge hoja kulingana na mazingira tuliyonayo kuliko ku-justify kwamba tusipunguze kwenye mifugo tupunguze kwenye samaki.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kalanga sidhani hiyo ndiyo hoja ya kwamba mifugo iliyopunguziwa tozo 15 zipungue ili zipelekwe kwenye uvuvi, ni kwamba mifugo tozo zimepungua 15, kwenye uvuvi hakuna nadhani ndiyo hoja ambayo Mheshimiwa Mbunge anajaribu kuiweka hapo.(Makofi)

MHE. VEDASTO E.NGOMBALE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa ufafanuzi.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Vedasto. (Makofi)

MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Naibu Spika, sikusudii kutaka kubagua hizi sekta hapana, hizi sekta zote zinasimamiwa na Waziri mmoja. Waziri na Waheshimiwa Wabunge mnaweza mkawa mashahidi kwa kadhia ambayo imewapata wavuvi kwenye suala zima la kuchomewa nyavu zao, kwenye suala zima la tofauti ya tozo kati ya dagaa wanaovunwa baharini na dagaa wanavunwa ziwani. Kwa mfano, baharini tozo ya kilo moja ya dagaa ni Dola ya Kimarekani 1.5. Ukienda Ziwa Tanganyika tozo ni Dola za Kimarekani ni 1.5, ukienda Ziwa Victoria Dola za Kimarekani 0.16. sasa ni matarajio yetu sasa hii tofauti Mheshimiwa Waziri wa Fedha wewe ndiyo Baba ungekuja kurekebisha kwa sababu kama nchi moja halafu kunakuwa na tofauti ya tozo inatusumbua sana. Sasa tukiona kwamba sekta hii imeshughulikiwa na nyingine haijashugulikiwa ndiyo maana tunataka Mheshimiwa Waziri wa Fedha utusaidie katika hilo.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo ningependa nilizungumzie ni suala zima la korosho, ni dhahili shahili kutokana na maamuzi yaliyofanyika kwenye korosho uchumi umetetereka na hasa wa Mikoa ile ambayo inazalisha korosho. Kwanza mpaka sasa kuna baadhi ya wakulima wengi hawajalipwa na hasa wale wakulima wa chini, hata katika zile pesa ambazo zimelipwa sasa kuna tofauti ya malipo kati ya Wilaya moja na nyingine, kuna Wilaya ambazo zimelipwa mpaka asilimia 90 lakini kuna Wilaya nyingine hata asilimia 50 haijafika.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pendekezo langu na ushauri, korosho zile zipo maghalani na zinazidi kuoza, wapo wafanyabiashara ambao wanataka kununua ninaishauri Serikali na hasa Waziri wa Wiwanda na Biashara Mheshimiwa Rais amekuchangua ili uweze kufanya maamuzi, fanya maamuzi ya kuuza korosho zile hata kwa bei ya chini kwa sababu kadri zinavyozidi kukaa korosho, zinaaharibika ziuzwe sasa angalau tupate nusu hasara.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukweli ni kwamba zile korosho huwezi kuziuza katika bei ile kwa sababu sasa zimeshaanza kuharibia. Sasa nishauri Serikali uzeni angalau tupate chochote kitu ili mambo yaweze kwenda sawa pia wale ambao hawajilipwa walipwe kwa sababu msimu mwingine una karibia.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala zima la bandari. Katika ukurasa namba 28 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha katika kipengele cha tatu anasema ana kusudio la kuwekeza kwenye maeneo ambayo Serikali inaweza kupata mapato zaidi hususan katika uvuvi wa Bahari Kuu kwa kujenga bandari ya uvuvi na ununuzi wa meli za uvuvi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa Serikali ni kama ina kigugumizi kwamba ni bandari gani sasa iwe bandari ya uvuvi. Katika nchi hii kuna bandari nne, kuna Bandari ya Tanga, Bandari ya Dar es Salaam, Bandari ya Kilwa na kuna Bandari ya Mtwara. Bandari hizi tatu tayari Serikali imeshafanya mkakati wa kuziendeleza, lakini Bandari ya Kilwa hakuna chochote ambacho kimefanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapendekeza Serikali sasa iifikirie bandari ya Kilwa kuwa kama bandari ya uvuvi. Bandari ya Kilwa ina historia kubwa, ukisoma historia ya toka enzi ya Ibn Battuta wanaitaja Bandari ya Kilwa, Mvumbuzi Ibn Battuta alipotembea alipofika katika Bandari ya Kilwa alikutana na Mji mkubwa unaovutia. Sasa kama tuna bandari ya kale toka enzi ya Dola ya Kilwa, lakini mpaka sasa Serikali haijakumbuka kuindelezea. Nafikiri sasa Serikali ione umuhimu wa kuingalia Bandari ya Kilwa na iipe kipaumbele ndiyo iwe bandari ya uvuvi hiyo itakuwa hata mizimu itatuona maana hiyo ndiyo bandari ya kale, kwa kufanya hivi tunaweza kupata mapato ya kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana.(Makofi)