Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Selemani Said Bungara (7 total)

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa jibu lililotolewa na Mheshimiwa Waziri. Hata hivyo, namwomba sana, kwa kuwa Mheshimiwa Rais Magufuli ameagiza hii barabara ijengwe na mpaka sasa hivi anasema kwamba wanatafuta fedha ili ijengwe, naomba sana waitafute hiyo fedha barabara hiyo ijengwe. Pamoja na hilo, nataka niulize swali la nyongeza; kwanza; je, tathmini hiyo ni shilingi ngapi katika barabara hiyo iliyotathminiwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; katika kampeni ya mwaka 2015, Rais Dkt. Magufuli alipokuja Kilwa aliwaahidi watu wa Kilwa kama atashinda Urais atajenga kilometa tano katika Mji Mdogo wa Kilwa Masoko. Sasa pamoja na kwamba ahadi za Rais hizi hazitekelezwi kwa wakati. Je, ni lini ahadi hii ya Mheshimiwa Dkt. Magufuli kwa sababu Urais alishaupata, na yule Bwana akisema jambo basi linakuwa hivyohivyo anavyosema. Je, ni lini itatimizwa ahadi hii ya kilometa tano katika Mji wa Kilwa Masoko?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, wataalam wetu wa TANROADS walikwenda kufanya tathmini ya barabara hiyo na tukagundua kwamba inahitajika takribani bilioni tatu kwa ajili ya kukamilisha barabara hiyo. Mwezi huu uliopita tu Halmashauri zilipelekewa takribani milioni 400, sasa tunaamini kazi iliyopo mbele yetu ni kutafuta bilioni 2.6 kwa ajili ya kukamilisha barabara hiyo. Mheshimiwa Rais alinipa jukumu hilo na nitahakikisha kwamba pesa hizo tunazitafuta ili barabara hiyo iweze kukamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusu ahadi iliyotolewa na Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni kuhusu ujenzi wa kilometa tano Mjini Kilwa Masoko. Ahadi zote alizotoa Mheshimiwa Rais tumezichukua na tunazifanyia kazi na tutahakikisha hivi karibuni tutaanza kuzitekeleza moja baada ya nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na Kituo cha Kipatimo ambacho amesema Mbunge mwenzangu wa Kilwa Kaskazini, Mbunge wa Kilwa Kusini kuna kituo cha Polisi ambacho kimejengwa na wananchi lakini bado kumalizika kule Kijiji cha Nanjilinji. Je, Mheshimiwa Waziri, unaweza kutusaidia ili kituo hicho kimalizike?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Kituo cha Nanjilinji ni miongoni mwa vituo vingi ambavyo vimejengwa kwa nguvu za wananchi ambavyo vinahitaji kukamilika. Hiyo ni dhamira ya Serikali, kuhakikisha kwamba vituo vyote hivyo nchi nzima ambavyo vimejengwa kwa nguvu za wananchi vinakamilika, siyo tu kwa sababu ya faida na manufaa ya matumizi ya vituo hivyo, lakini pia kwa kuweza kutokuwavunja moyo wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Kituo cha Nanjilinji, pale ambapo hali ya kifedha itakaa vizuri, tutakimaliza pamoja na vituo vingine, lakini Mheshimiwa Mbunge vilevile anaweza akatumia fursa hiyo kusaidia kuweza kufanikisha ujenzi huo kwa kuhamasisha wananchi wake ama wadau kuendeleza jitihada hizi za Serikali na Serikali pale ambapo uwezo utakuwa tayari basi tutavimaliza.(Makofi)
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mji Mdogo wa Kilwa Kivinje kuna vitongoji tisa ambavyo vyote havina maji; na kuna mradi mkubwa wa maji ulikuwa wa kutoka Mavuji kuja Kilwa Kivinje, mpaka sasa hivi hatujajua hatima yake. Je, Waziri anazungumzia vipi upatikanaji wa maji katika Mji Mdogo wa Kilwa Kivinje?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Kivinje naufahamu uko baharini, lakini juzi nilimpa Mheshimiwa Mbunge shilingi milioni 500, tumetoa fidia kwa ajili ya kutunza eneo la chanzo cha maji. Kwa hiyo, chanzo hicho sasa tutatekeleza mradi mmoja mkubwa wa kuchukua maji yaliyo baridi pale na kuyapeleka katika eneo la Kivinje. Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi Ilani ya Chama cha Mapinduzi iko makini, itatekeleza huo mradi kuhakikisha wananchi wa Kivinje wanapata huduma ya maji.
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jibu lisilokamilika kutokana na kwamba mimi niliulizia Kilwa lakini amejibu kwa pamoja. Ni lini sasa uchambuzi wa kina na hali ya halisi utakamilika ili vyuo hivyo vipate huduma inayohitajika? Hilo ni swali langu la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Chuo cha Maendeleo cha Wilaya ya Kilwa kina mafunzo ya udereva, lakini mpaka sasa hivi hakuna gari la kujifunzia. Ni lini Wizara itapeleka gari katika Chuo cha Maendeleo Wilaya ya Kilwa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Bungara, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu zoezi litakamilika lini, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, zoezi hilo litategemea kukamilika mwezi ujao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu chuo kupatiwa gari, kama tulivyosema tunafanya tathmini ya kuangalia vitu vinavyohitajika ikiwa ni pamoja na vifaa vya kujifunzia na kufundishia. Kama gari ni moja kati ya vitu vitakavyoonekana kwamba vinahitajika basi Serikali itajipanga ili kuweza kuhakikisha kwamba linapatikana kadri uwezo utakavyoruhusu.
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuuliza swali kuhusu kilimo cha korosho. Juzi wakulima wa korosho wamelipwa fedha chini ya kiwango ni theluthi moja ya haki yao. Je, Mheshimiwa Waziri unawaambia nini wakulima hawa, hizi fedha ndiyo basi au watalipwa zingine na sababu gani ambazo zimefanywa hawakuweza kulipwa hela zote?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tunafahamu malipo yote wanayopaswa kulipwa wakulima wa korosho ni zaidi ya bilioni 723 na mpaka sasa tumelipa zaidi ya bilioni 633. Bado kuna wakulima ambao wanadai Serikali bilioni 100 hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka wiki iliyopita tulipeleka zaidi ya bilioni 50 na malipo yanaendelea mpaka sasa hivi na kama anachokizungumza, kama tunavyofahamu, wanunuzi wa korosho kabla Serikali hatujaweza kuokoa hali ilivyokuwa, walikuwa zaidi ya 100. Lakini mwaka huu mnunuzi ni mmoja tu na ukizingatia kwamba hii benki ya maendeleo ya kilimo na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko ilikuwa haijajiandaa katika ununuzi huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ilipaswa mjue kwamba Mbunge ungeipongeza Serikali na Bodi ya Nafaka na Mazao mchanganyiko kwa hatua ilizochukua mpaka leo tumeweza kulipa zaidi ya bilioni 633 na mnunuzi akiwepo mmoja kitu ambacho kilikuwa hakuna kwenye bajeti badala ya kusema kwenda kwenye…

MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu hayo kuhusu Wilaya ya Kilwa, lakini Wilaya ya Kilwa kwenye Hospitali ya Wilaya kuna uhaba mkubwa wa maji: Je, Serikali inatuambia nini kuhusu jambo hili la Hospitali ya Wilaya kupata maji ya uhakika na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji, sisi kama Serikali na Mheshimiwa Mbunge anatambua, ni miongoni mwa jitihada ambazo tunazifanya katika kuhakikisha tunatatua tatizo la maji katika Jimbo lake la Kilwa Kusini. Yupo katika mpango wa miji 28, lakini kama unavyotambua, suala la hospitali ni suala la dharura sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikubaliane na Mheshimiwa Bungara tukutane baada ya saa saba ili tuwasiliane na wataalam wetu tuangalie ni namna gani tunaweza tukawapatia wananchi wake huduma haraka katika suala zima la maji.
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, kwanza nakushukuru sana na ninakupongeza kwa kutupatia tablet hizi. (Makofi)

Pili, hili swali niliuliza mwaka 2016, lakini naishukuru Serikali leo wamejibu kwa vitendo. Kweli Kituo cha Afya Masoko sasa hivi utasema upo Ulaya, nashukuru sana. Pamoja na shukrani hizo; je, ni lini Serikali itatimiza au itakamilisha wafanyakazi 22 waliobakia ili kituo kiendane sawasawa na kilivyo? Swali la kwanza hilo.

Swali la pili; kwa kuwa hakuna gari maalum ya wagonjwa hiyo unayosema, lakini kwa kuwa umenipa matumaini kwamba mtatafuta gari nyingine: Je, lini hiyo gari ya Kituo cha Afya cha Kilwa Masoko itapatikana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, niruhusu nipokee pongezi za Mheshimiwa Bungara, maana huwa zinatolewa mara chache sana. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, katika swali lake la kwanza anauliza ni lini upungufu wa watumishi 22 utatatuliwa ili hadhi ya Kituo cha Afya ambacho anasema ni sawa na kuwa Ulaya kitaweza kutoa huduma kukiwa na ikama ambayo inatakiwa?

Mheshimiwa Spika, naomba niendelee kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kama ambavyo ameendelea kuiamini Serikali ya CCM ikiahidi inatekeleza na utekelezaji ni pamoja na swali ambalo aliliuliza, nami nampongeza kwa kuuliza swali na Serikali tumemjibu kwa vitendo. Naomba nimhakikishie ni azma ya Serikali kuhakikisha maeneo yote ambayo Vituo vya Afya vimefunguliwa tunapeleka watumishi kwa kadri nafasi za ajira zinavyopatikana na Kilwa hatutasahau.

Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili anaulizia suala la kuwepo gari. Gari lililopo aina ya Maruti linafanya kazi, lakini kama tulivyokiri katika majibu yetu kwamba ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba tunapata gari zuri zaidi kwa kushirikiana Halmashauri yake, ni vizuri nao katika bajeti; maana kama kuna Halmashauri ambayo inafanya vizuri katika makusanyo ni pamoja na Halmashauri yake maana zao la ufuta linaingiza fedha nyingi. Ni vizuri nao Halmashauri wakatenga na sisi Serikali tukashirikiana ili gari ziweze kupatikana kwa ajili ya wananchi.