Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Selemani Said Bungara (5 total)

MHE. SELEMANI S. BUNGARA aliuliza:-
Mradi wa ujenzi wa Barabara ya Singino/Kivinje maarufu kama Barabara ya Kwa Mkocho ni ahadi ya Serikali iliyotolewa na Rais Mstaafu, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, karibu miaka 10 iliyopita. Aidha, kwa kipindi chote cha miaka 10 ujenzi wa barabara hiyo umekuwa wa kusuasua ingawa barabara hiyo ni kiunganishi kwa wananchi hasa wagonjwa wanaokwenda kutibiwa hospitali ya wilaya:-
(a) Je, ni nini kauli ya Serikali ya Awamu ya Tano juu ya ukamilishwaji wa ahadi hiyo?
(b) Je, Serikali inatoa maelezo gani kwa wananchi juu ya kuchelewa kukamilishwa kwa ujenzi wa barabara hiyo kwa kipindi cha miaka 10 sasa?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Selemani Said Bungara, Mbunge wa Kilwa Kusini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Singino/Kivinje – Kilwa ni barabara inayohudumiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa. Katika mwaka 2012, Mheshimiwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne aliahidi kutenga fedha kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa ili barabara hiyo ijengwe kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ilisaini mkataba na kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami kwa gharama ya shilingi bilioni 1.478. Hata hivyo, mradi huo haujakamilika na mkandarasi amekimbia eneo la mradi. Wakati wa ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, aliagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Lindi, kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tathmini ya mahitaji ya fedha zinazotakiwa ili kuendelea kujenga kwa kiwango cha lami barabara hii yamefanyika na ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara hii unatarajiwa kuanza pindi fedha zitakapopatikana.
MHE. SELEMANI S. BUNGARA aliuliza:-
Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kilwa kina upungufu mkubwa wa vitanda na hata vichache vilivyopo vimechakaa sana kwani vilinunuliwa tangu mwaka 1969. Mahitaji halisi ya vitanda vinavyohitajika chuoni hapo ni zaidi ya vitanda 50 (double decker):-
Je, Serikali imetenga kiasi gani cha fedha kwa ajili ya ununuzi wa vitanda pamoja na samani nyingine chuoni hapo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Selemani Said Bungara, Mbunge wa Kilwa Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC) kwa ajili ya kuandaa rasilimali watu watakaotumika katika viwanda ili kufikia lengo la Serikali la kuwa na uchumi wa kati unaotegemea viwanda ifikapo mwaka 2025. Vyuo hivi vitasaidia kuongeza fursa ya mafunzo ya ufundi stadi sambamba na elimu ya wananchi (folk education). Aidha, vitasaidia kuwaandaa vijana kwa kuwapatia ujuzi utakaowawezesha kujiajiri na kuajiriwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu wa vyuo hivyo, Serikali imetoa kandarasi kwa vyuo vitatu ambavyo ni Taasisi ya Teknolojia Dar-es-Salaam, Chuo cha Ufundi Arusha na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya ili vifanye uchambuzi wa kina wa hali halisi ya miundombinu, vifaa vya kujifunzia na kufundishia, pamoja na samani katika Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi kikiwemo Chuo cha Maendeleo cha Wananchi Kilwa Masoko. Taratibu za ukarabati zitaanza baada ya kukamilika kwa zoezi hili. Aidha, Wizara inafanya zoezi la kubaini mahitaji ya watumishi katika Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi, zoezi linalotarajiwa kukamilika Julai, 2018.
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE (K.n.y. MHE. SELEMANI S. BUNGARA) aliuliza:-

Hospitali ya Wilaya ya Kilwa haina Jokofu la kuhifadhi maiti na pia majengo yake mengi ni chakavu:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kununua jokofu jipya sambamba na kukarabati majengo ya hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE.MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Selemani Saidi Bungara, Mbunge wa Kilwa Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti Hospitali ya Wilaya ya Kilwa (Kinyonga)ni miongoni mwa Hospitali Kongwe za Wilaya hapa nchini na imekuwepo tangu mwaka 1965. Kwa kutambua umuhimu wa Hospitali hiyo, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imekua ikifanya ukarabati na upanuzi wa majengo mbalimbali ya kutolea huduma kama ifuatavyo:-

Mwaka wa Fedha 1996/1997, ukarabati wa miundombinu mbalimbali ya hospitali ulifanyika pamoja na ujenzi wa kliniki ya Mama na Mtoto; Mwaka 2010 ulifanyika ujenzi wa Jengo la Huduma za UKIMWI (CTC); Mwaka 2012 ulifanyika ujenzi wa jengo la wazazi; na Mwaka 2017 ulifanyika ujenzi wa jengo la mama ngojea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Wilaya ya Kilwa ina jokofu moja la kuhifadhia maiti lililonunuliwa mwaka 1996. Hata hivyo, jokofu hilo lina uwezo wa kuhifadhi mwili mmoja tu. Serikali inaendelea nautaratibu wa kukamilisha hatua za kuanza ujenzi wa jengo jipya la kuhifadhia maiti kwenye hospitali hiyo sambamba na ununuzi wa jokofu jipya la kisasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kukarabati miundombinu ya vituo vya kutolea huduma za afya nchini kwa kadri ya upatikanaji wa rasilimali fedha utakavyokuwa.
MHE. SELEMANI S. BUNGARA aliuliza:-

Kituo cha Afya Kilwa Masoko kinakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo uhaba wa watumishi, upungufu wa dawa, upungufu wa vitanda, magodoro, mashuka, vifaa tiba, kipimo cha sukari, kipimo cha damu, uchakavu wa majengo na pia kituo hicho hakina gari la kubebea wagonjwa hali ambayo ni kero kubwa kwa wagonjwa wanaohamishiwa Hospitali ya Wilaya iliyo umbali wa zaidi ya kilometa 25:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kutatua changamoto zinazokabili Kituo hicho cha Afya ili kuondoa adha kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Selemani Said Bungara, Mbunge wa Kilwa Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya Kilwa Masoko kilipatiwa kiasi cha shilingi milioni 500 katika mwaka wa fedha 2017/2018 kwa ajili ya ukarabati na upanuzi ambapo ujenzi na ukarabati wa majengo sita ya kituo umekamilika. Aidha, baada ya ujenzi na ukarabati kukamilika, kituo kimepokea vifaa tiba mbalimbali kwa ajili ya kuboresha huduma hususan za upasuaji ambapo hadi Oktoba, 2019 kituo kimepokea vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi 332,916,070/=. Hali ya upatikanaji wa dawa zote muhimu (Tracer medicine) katika Kituo cha Masoko ni asilimia 87.

Mheshimiwa Spika, kituo kina jumla ya watumishi 30 wa kada mbalimbali za Afya ikiwa ni upungufu wa watumishi 22. Kituo kina nafasi ya vitanda 55, vitanda vilivyopo ni 31 na mashuka 126. Idadi ya vitanda vilivyopo vinakidhi mahitaji kwani kwa sasa kituo kinapokea wagonjwa wa kulazwa angalau watano kwa siku. Kwa sasa Halmashauri ina gari maalum ambalo hutumika kubeba wagonjwa katika kipindi cha dharura.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutafuta rasilimali fedha za kutatua changamoto zilizopo ikiwa ni pamoja na kununua gari la wagonjwa kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Kilwa Masoko.
MHE. SELEMANI S. BUNGARA aliuliza:-

Uvuvi haramu unazidi kushamiri siku hadi siku hasa kwenye maeneo ya Songosongo, Somanga, Njianne, Kivinje hadi Pwani ya Bushungi. Aidha, maeneo haya kuna bomba la gesi linapita na hivyo kujenga hofu ya uwezekano wa mlipuko pamoja na uharibifu wa mazingira kwenye maeneo tajwa.

(a) Je, Serikali ina mpango gani madhubuti kukabiliana na tishio hilo sugu?

(b) Kwa kuwa wanaofanya hujuma hizo wamejiandaa kwa kuwa na boti maalum katika kuendesha huduma hizo; je, Serikali haioni haja ya kuleta boti za doria zenye uwezo wa hali ya juu ili kulinda bahari na bomba la gesi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Selemani Said Bungara, lenye vipengele (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na uvuvi haramu, Wizara inatekeleza mikakati mbalimbali ikiwemo kuanzisha vituo vya doria kwenye maziwa makubwa, mwambao wa Bahari ya Hindi na mipaka ya nchi. Imeanzisha Kikosi Kazi cha Kitaifa (Multi Agency Task Team), ambacho kinafanya kazi ya kudhibiti uhalifu wa mazingira ikiwemo kudhibiti uvuvi haramu hususan matumizi ya mabomu katika shughuli za uvuvi. Kufanya opereshini za mara kwa mara mfano Operesheni Jodari kwenye Ukanda wa Pwani na Operesheni Sangara, Ziwa Victoria, kuanzisha na kuimarisha vikundi vya usimamizi shirikishi wa rasilimali za uvuvi (BMU) pamoja na kufanya maboresho ya Sheria na Kanuni za Uvuvi ili kuimarisha usimamizi na matumizi endelevu ya rasilimali za uvuvi hapa nchini. Juhudi hizi zimezaa matunda hususan katika Ukanda wa Pwani ambapo uvuvi wa kutumia mabomu kwa maana ya milipuko umepungua kwa takribani asilimia 99.

Mheshimiwa Spika, Serikali itendelea kupambana na tatizo la uvuvi haramu hususan wa mabomu kwa kuhakikisha vituo vya doria vinapatiwa vitendea kazi ikiwemo boti za kisasa ili kuimarisha ulinzi wa rasilimali za uvuvi na miundombinu ya gesi kwa faidi ya kizazi cha sasa na vijavyo.

Mheshimiwa Spika, nitoe rai kwa Waheshimiwa Wabunge kuendelea kuiunga mkono Serikali yao kwa kukemea na kupiga vita uvuvi harama katika maeneo yao.