Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Hassan Selemani Kaunje (11 total)

MHE. HASSAN S. KAUNJE aliuliza:-
Jimbo la Lindi Mjini lina eneo la Bahari ya Hindi lenye urefu wa kilometa 112, lakini eneo hilo halina mchango wowote wa maana kwenye pato la Taifa na Manispaa ya Lindi:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuendeleza eneo la bahari katika Manispaa ya Lindi?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Seleman Kaunje, Mbunge wa Lindi Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuendeleza eneo la ukanda wa bahari ya Hindi katika Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, Serikali imeendelea na maandalizi ya mpango wa upimaji wa muda mrefu yaani master plan wa wilaya nzima ambao utaainisha matumizi mbalimbali ya ardhi, yakiwemo uwekezaji, makazi na matumizi mengine. Tayari kibali cha kuandaa mpango huo kimeshatolewa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Halmashauri. Kwa sasa mkataba wa kazi hiyo, uko kwa Mwanasheria Mkuu kwa ajili ya uhakiki yaani vetting ili taratibu za kupata mzabuni ziendelee.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango huo utahusisha uboreshaji wa makazi holela yaani resettlement scheme katika eneo la Mnazi Mingoyo, Mpilipili na Rahaleo ili kuwa na mji wa kisasa katika Manispaa ya Lindi. Kazi zote hizo zinatarajiwa kugharimu jumla ya shilingi bilioni moja hadi kukamilika kwake. Mpango huo utakapokamilika utasaidia Serikali kupata mapato kutokana na aina ya uwekezaji utakaofanyika katika ukanda huo wa bahari ndani ya Manispaa ya Lindi.
MHE. HASSAN S. KAUNJE aliuliza:-
Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2015 - 2020, imeeleza juu ya uendelezaji wa utalii kwa Ukanda wa Kusini kama Program Maalum:-
Je, ni lini Serikali imepanga kuanza mpango huo maalum?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Seleman Kaunje, Mbunge wa Lindi Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2015 - 2020, Sura ya Pili katika aya ya 29 imeainisha program maalum ya uendelezaji wa utalii nchini ikiwemo katika Ukanda wa Kusini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Tano yenye dhamana ya kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi imeandaa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano kuanzia 2016/2017 - 2020/2021 ambao ni sehemu ya pili ya Mpango Elekezi wa miaka 15, (2011/2012 – 2025/2026) na Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2025.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, katika mpango huo wa miaka mitano, Serikali imejumuisha hatua ya kufungua fursa za utalii katika Ukanda wa Kusini kama mojawapo ya hatua muhimu kwa maendeleo ya viwanda na ukuzaji wa uchumi. Ili kutekeleza azma hii, Wizara yangu imejipanga kushirikisha sekta binafsi kuwekeza katika miundombinu ya utalii, kuwekeza na kuendeleza maeneo mengine yenye fursa za utalii, kutekeleza mkakati wa Kitaifa wa Utangazaji wa utalii ili kuwavutia watalii wengi zaidi, kutoa mafunzo ya ukufunzi katika Chuo cha Taifa cha Utalii kwa lengo la kuimarisha mafunzo ya Utalii na kutenga maeneo maalum ya utalii, hususan ya fukwe za bahari na maziwa kwa ajili ya hoteli za kitalii kama maeneo muhimu kwa ukuaji wa uchumi na ustawi wa Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi hicho, Serikali itashirikisha sekta binafsi ili iwekeze katika kuboresha miundombinu na vivutio vya utalii katika Ukanda wa Kusini na kuvitangaza hususan maeneo ya utalii wa kihistoria na kitamaduni kama vile mji wa kihistoria wa Mikindani, Kilwa Kivinje, Pori la Akiba Lukwika-Lumesule na Pori la Akiba la Selous upande wa kusini na maeneo mengine katika Ukanda huo. Aidha, ili kukuza utalii wa baharini na katika fukwe za bahari, Serikali imepanga kutenga maeneo maalum ya utalii hususan kwa ajili ya hoteli za kitalii kando ya Bahari ya Hindi Mkoani Lindi na Mtwara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upana wake, utalii wa Kusini unatarajiwa pia kuboreshwa kupitia program na miradi mbalimbali kwa ushirikiano na wadau wa maendeleo ikiwa ni pamoja na mradi ujulikanao kama REGROW unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kwa gharama ya Dola za Kimarekani zisizopungua milioni 100.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH (K.n.y. MHE. HASSAN S. KAUNJE) aliuliza:-
Kuna migogoro ya ardhi iliyosababishwa na upimaji na ugawaji wa ardhi kwa ajili ya makazi na ujenzi wa taasisi katika Kata ya Rasbura eneo la Mitwero.
Aidha, watumishi wa Idara ya Ardhi walijigawia ardhi kinyume na taratibu na kuiuza kwa manufaa yao. Pia wananchi wanalalamikia fidia na utwaaji wa maeneo makubwa tofauti na michoro iliyomo kwenye nyaraka zilizothibitishwa na Wizara kwa matumizi ya taasisi za umma au binafsi:-
Je, Serikali ipo tayari kufanya uchunguzi au uhakiki wa zoezi zima la upimaji na ugawaji wa viwanja katika eneo hilo?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali Na.375 la Mheshimiwa Hassan Seleman Kaunje, Mbunge wa Lindi Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la Mitwero lililoko katika Kata ya Rasbura ni moja ya maeneo ambayo upimaji wa viwanja kwa ajili ya matumizi mbalimbali katika Manispaa ya Lindi umefanyika. Kwa kawaida, upimaji wa viwanja popote hufanyika kwa kuzingatia Sheria ya Ardhi pamoja na Sheria ya Mipango Miji na kanuni zake ambazo huelekeza upimaji na fidia stahiki kwa eneo husika kabla ya kutwaliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba pamoja na kuwepo kwa utaratibu huu wa kisheria wa upimaji na ugawaji viwanja, yapo malalamiko mbalimbali yaliyojitokeza wakati Halmashauri ya Manispaa ya Lindi ikiwa inatekeleza mradi wa upimaji viwanja katika eneo la Mitwero. Miongoni mwa malalamiko hayo ni wananchi kulipwa fidia ndogo, ucheleweshaji wa malipo ya fidia na utaratibu usioridhisha wa ugawaji wa viwanja.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kushughulikia malalamiko ya wananchi wa Mitwero, nilitoa maagizo kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Lindi kwamba washirikiane na Kamishna wa Ardhi Msaidizi Kanda ya Kusini katika kuyashughulikia malalamiko hayo ikiwemo kurejea uthamini wa maeneo na maendelezo ambayo hayakuthaminiwa wakati Halmashauri ikitekeleza mradi huo ili walalamikaji walipwe stahiki zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi watakaobainika kukiuka maadili ya Utumishi wa Umma pamoja na ukiukwaji wa miiko ya taaluma zao, kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, (TAMISEMI) tutachukua hatua zinazostahili.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Wizara yangu kwa kushirikiana na Manispaa ya Lindi imeshafanya uhakiki na wote waliokuwa na madai yameanza kushughulikiwa kwa kulipwa fidia zao stahiki.
MHE. HASSAN S. KAUNJE aliuliza:-
Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 inasema kuwa idadi ya watu katika Jimbo la Lindi Mjini ni takribani 78,000, lakini takwimu za watu waliojiandikisha NIDA inafika 100,000 na sensa iliyofanywa kupitia Serikali za Mitaa inaonyesha kuwa wakazi wa Lindi Mjini ni zaidi ya 200,000 na Serikali inaendelea kupanga mipango yake ya maendeleo kwa kutumia takwimu za watu 78,000 hivyo kuathiri huduma stahiki za maendeleo.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuangalia upya takwimu hizo ili wananchi wa Lindi Mjini wapelekewe huduma za maendeleo stahiki?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Kaunje, Mbunge wa Lindi Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, idadi ya watu kwa Manispaa ya Lindi (Jimbo la Lindi Mjini) ilikuwa ni watu wapatao 78,841. Kwa madhumuni ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, eneo la Manispaa ya Lindi ni lile linalojumuisha kata 18 za Ndoro, Makonde, Mikumbi, Mitandi, Rahaleo, Mwenge, Matopeni, Wailes, Nachingwea, Rasbura, Matanda, Jamhuru, Msinjahili, Mingoyo, Ng’apa, Tandangongoro, Chikonji na Mbanja. Hivyo basi, tunapozungumzia idadi ya watu 78,841 tuna maana ya idadi ya watu katika kata nilizozitaja hapo juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa uboreshaji wa daftari la wapiga kura, Ofisi ya Taifa ya Takwimu ilitoa makadirio ya idadi ya wapiga kura kwa kila jimbo hapa nchini. Katika makadirio hayo, Jimbo la Lindi Mjini linakadiriwa kuwa na wapiga kura 47,356. Katika zoezi hilo hilo la uboreshaji wa daftari la wapiga kura, Tume ya Taifa ya Uchaguzi nayo ilikadiriwa kuwa Jimbo la Lindi Mjini lina wapiga kura wapatao 42,620. Makadirio haya yalizingatia idadi ya watu kwa Lindi Mjini kama ilivyotolewa na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012.
Baada ya kukamilika kwa zoezi la uandikishaji wapiga kura, Jimbo la Lindi lilionyesha kuwa na wapiga kura 48,850 idadi ambayo ni karibu sawa na ile iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu. Matokeo haya yanadhihirisha usahihi wa takwimu za sense zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, idadi ya watu wapatao 100,000 waliojiandikisha NIDA ni kwa Wilaya nzima ya Lindi, ambayo inajumuisha Manispaa ya Lindi na Halmashauri ya Wilaya ya Lindi na sio Manispaa ya Lindi au Jimbo la Lindi Mjini pekee kama ilivyohojiwa katika swali la msingi la Mheshimiwa Hassan Kaunje.
MHE. HASSANI S. KAUNJE aliuliza:-
Mradi wa Maji wa Ng’apa ambao upo Manispaa ya Lindi ulikusudiwa kuwahudumia wakazi wa Lindi Mjini tangu mwezi Mei, 2015, lakini mpaka sasa mradi huo haujakamilika. Je, ni lini mradi huo utakamilishwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Seleman Kaunje, Mbunge wa Lindi Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu wa Ng’apa unagharamiwa na Serikali kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya kupitia Benki ya Maendeleo ya KfW kwa gharama ya Euro milioni 11.56. Ujenzi wa mradi huu unatekelezwa na Mkandarasi ajulikanaye kwa jina la Overseas Infrastructure Alliance kutoka nchini India. Kazi zinazotekelezwa ni pamoja na ufungaji wa pampu katika visima ambavyo vimeshachimbwa na vina uwezo wa kutoa maji mita za ujazo 7,500 kwa siku; ulazaji wa mabomba ya kusambaza maji; ujenzi wa mtambo wa kutibu maji; ujenzi wa matenki mawili ya kuhifadhi maji; ujenzi wa nyumba ya wafanyakazi, karakana, ghala, nyumba ya walinzi; ujenzi wa mabwawa ya kusafisha maji na ununuzi wa gari moja la majitaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa mradi huu ulitegemewa kukamilika mwezi Mei, 2015. Sababu kuu zilizosababisha kutokamilika kwa mradi huu ni kutolipwa kwa wakati kwa fidia na kasi ndogo ya mkandarasi katika ujenzi wa mradi. Hadi sasa Serikali imefanikiwa kuwalipa waathirika wote wa mradi waliokuwa wamefanyiwa tathmini. Kwa upande wa mkandarasi, Wizara imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kulingana na masharti ya mkataba, ikiwemo kumkata fedha za adhabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua mbalimbali zilizochukuliwa zimewezesha utekelezaji wa mradi kufikia asilimia 85 kwa sasa na mradi unategemea kukamilika mwezi Julai, 2017.
MHE. HASSAN S. KAUNJE aliuliza:-
Hospitali ya Rufaa ya Sokoine Mkoani Lindi inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa maji na ubovu wa vyoo katika wodi zake, pia watumishi wa hospitali hiyo wamekuwa na lugha na huduma duni zinazokera wateja.
Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua changamoto zinazoikabili hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS,TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Seleman Kaunje Mbunge wa Lindi Mjini kama kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kutatua changamoto zinazokabili Haspitali ya Mkoa wa Lindi zikiwemo uchakavu wa miundombinu, katika mwaka wa fedha 2016/2017 iliidhinishiwa kiasi cha shilingi miioni 344 kwa ajili ya kazi ya ukarabati wa miundombinu ambapo fedha zote zimepelekwa.
Vilevile Mkoa umepanga kutumia shilingi milioni 185 kwa ajili ya kujenga kichomea taka (incinerator) ya kisasa na ukarabati wa hospitali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kazi zinazoendelea hivi sasa ni ukarabati wa wodi ya wazazi, wodi ya upasuaji wa wanaume na aidha, katika kutatua tatizo la maji Serikali inakamilisha mradi mkubwa wa maji katika eneo la Ng’apa, Manispaa ya Lindi unaotarajiwa kumaliza kabisa tatizo la maji katika Manispaa ya Lindi. Wodi ya daraja la I. Aidha, mkandarasi atakayejenga kichomea taka ameshapatikana ili kuanza kazi hiyo. Vilevile Serikali ipo katika hatua za mwisho ya kupata mkandarasi kwa ajili ya ukarabati wa wodi ya watoto, jengo la upasuaji (theatre) jengo la huduma ya afya ya kinywa na meno na jengo la huduma ya macho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imepanga kukarabati wodi ya wagonjwa ya akinamama, chumba cha mionzi na jengo la utawala. Ukarabati wa miundombinu utafanyika sambamba na uboreshaji wa mfumo wa maji safi na maji taka.
MHE. HASSAN E. MASALA (K.n.y. MHE. HASSAN S. KAUNJE) aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaanza kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Ngongo - Ng’apa - Milola ambayo ipo chini ya TANROADS?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Seleman Kaunje, Mbunge wa Jimbo la Lindi Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara ya Ngongo - Ng’apa- Milola yenye urefu wa kilometa 42 ni barabara ya Mkoa inayohudumiwa na Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Lindi. Barabara hii ni sehemu ya barabara ya Ngongo - Ruangwa na Nanganga yenye urefu wa kilometa 162.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kutambua umuhimu wa barabara hii imeendelea kutenga bajeti kila mwaka kwa ajili ya kuifanyia matengenezo ya aina mbalimbali ili iendelee kupitika kiurahisi ambapo katika mwaka wa fedha 2017/2018, jumla ya shilingi bilioni 1.149 zimetengwa naa jumla ya kilometa 30 zimefanyiwa matengenezo ya muda maalum.
Mheshimiwa Spika, kuhusu ujenzi kwa kiwango cha lami sehemu ya barabara ya Ngongo - Ng’apa - Milola kilometa 42 kwa sasa kipaumbele ni kukamilisha kwanza barabara za kuunganisha Makao Makuu ya Mikoa pamoja na nchi jirani ndipo barabara za kuunganisha Wilaya zitafuata. Hivyo, barabara hii itaendelea kufanyiwa matengenezo ya aina mbambali kwa kiwango cha changarawe ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka wakati Serikali ikitafuta fedha za kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kama sehemu ya maandalizi ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami. (Makofi)
MHE. DAIMU I. MPAKATE (K.n.y HASSAN S. KAUNJE) aliuliza:-
Kuna mgogoro wa ardhi wa muda mrefu kati ya wananchi wa kijiji cha Mkwaya na mwekezaji Durbali:-
Je, ni lini mgogoro huo utapatiwa ufumbuzi?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Selemani Kaunje, Mbunge wa Lindi Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna mgogoro unaowahusisha baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Lindi ambao wako kwenye Mitaa ya sokoni, Makonde na Mtere ambayo zamani ilikuwa ni sehemu ya Kijiji cha Mkwaya ambao wanasemekana kuvamia na kugawana mashamba yanayomilikuwa na Kampuni ya Indo-African Estate Limited.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro huu si kati ya wananchi hao na bwana Amin Durbali ambaye ni mmoja kati ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Indo-African Estate Limited bali ni kati ya wananchi na Kampuni ya Indo-Africa Estate Limited ambayo ndiyo ina hatimiliki za mashamba hayo yenye ukubwa wa ekari 3,601.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kampuni ya Indo-African Estate Limited ilifungua Kesi Na.17 ya mwaka 2015, ambayo hukumu yake imetolewa Februari, 2018 na kuipa Serikali ushindi. Kinachoendelea sasa ni taratibu za kufuta miliki za mashamba hayo kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi Na.4 ya mwaka 1999 na Kanuni zake za mwaka 2001. Baada ya kufutwa kwa miliki za mashamba hayo, Serikali itaweka utaratibu mzuri wa ugawanaji wa mashamba hayo kwa wananchi.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH (K.n.y. MHE. HASSAN S.
KAUNJE) aliuliza:-
(a) Je, ni lini Serikali itadhamini Wenyeviti wa Serikali za Mitaa ili waweze kupata mikopo kama ilivyo kwa Madiwani na Wabunge?
(b) Je, ni lini Serikali itaanza kuwalipa posho/ mishahara Wenyeviti wa Serikali za Mitaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Seleman Kaunje, Mbunge wa Lindi Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, utaratibu wa Halmashauri na Bunge kudhamini mikopo kwa Waheshimiwa Madiwani na Waheshimiwa Wabunge umetokana na kuwepo kwa utayari wa benki zinazokopesha mikopo hiyo, hususan NMB na CRDB ambazo baada ya kuonesha utayari, makubaliano maalum husainiwa ambayo ndiyo hutoa mwongozo wa namna mikopo itakavyotolewa pamoja na viwango vyake.
Mheshimiwa Spika, utaratibu wa aina hiyo hadi sasa haujawezekana kwa Wenyeviti wa Serikali za Vijiji, Mitaa na Vitongoji kwa kuwa hadi sasa hakuna benki iliyoonesha utayari wa kutoa mikopo ya aina hiyo. Hata hivyo, ipo fursa kwa kiongozi mmoja mmoja kuwasiliana na benki moja kwa moja kwa ajili ya makubaliano binafsi ya mkopo kulingana na kiwango cha amana alichonacho, thamani ya ardhi, nyumba anayomiliki au biashara.
(b) Mheshimiwa Spika, kwa kutambua kazi kubwa inayofanywa na Wenyeviti wa Serikali za Vijiji, Vitongoji na Mitaa kupitia Mpango wa Maboresho ya Serikali za Mitaa, Serikali ilitoa mwongozo kuwa viongozi hao wawe wanalipwa posho inayotokana na asilimia 20 ya mapato ya ndani ambayo hurejeshwa na Halmashauri kwenye Kijiji/Mtaa husika.
Mheshimiwa Spika, changamoto zilizopo za ukusanyaji hafifu wa mapato ya ndani zimekuwa zikisababisha ugumu wa kutekeleza mwongozo huo katika baadhi ya maeneo. Kwa sababu hiyo, Halmashauri zote zimeagizwa zifanye mapitio ya vyanzo vyote vya mapato na ziimarishe makusanyo ya ndani ili ziwe na uwezo wa kulipa posho hizo.
MHE. HASSAN S. KAUNJE aliuliza:-
TANROADS ilifanya upanuzi wa Road Reserve tangu mwaka 2011 ambayo ilihusisha tathmini ya mali zilizopo kwenye maeneo husika:-
Je, ni lini wananchi wa Lindi watalipwa stahili zao?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Kaunje, Mbunge wa Lindi Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa Sheria ya Barabara ya Mwaka 2007 na Kanuni za Menejimenti ya Barabara za Mwaka 2009 iliongeza eneo la hifadhi ya barabara kutoka mita 22.5 mpaka mita 30 kwa barabara kuu na barabara za mikoa kutoka katikati ya barabara kila upande wa barabara. Kwa kuzingatia sheria ya zamani ya barabara (highway Ordinance Cap. 167) wananchi waliojenga ndani ya mita 22.5 kutoka katikati ya barabara wamevunja sheria hivyo Wizara kupitia TANROADS imekuwa ikichukua hatua ya kuweka alama za X nyekundu na wananchi hao wanatakiwa waondoke eneo hilo na hawatalipiwa fidia yoyote kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Spika Wizara kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) imechukua hatua ya kuweka kumbukumbu ya mali zote zilizopo ndani ya mita 7.5 zilizoongezeka kutoka eneo la hifadhi ya barabara la mita 22.5 hadi mita 30 kila upande wa barabara kwa kuziwekea alama ya X ya kijani kwa ajili ya uthamini na malipo ya fidia endapo eneo hilo litahitajika hapo baadaye kwa ajili ya ujenzi na upanuzi wa barabara.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH (K.n.y. MHE. HASSAN S. KAUNJE) aliuliza:-

(a) Je, ni lini Serikali itawadhamini Wenyeviti wa Serikali za Mitaa ili waweze kupata mikopo kama ilivyo kwa Madiwani na Wabunge?

(b) Je, ni lini Serikali itaanza kuwalipa posho/mishahara Wenyeviti wa Serikali za Mitaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Seleman Kaunje, Mbunge wa Lindi Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inalipa posho ya Wenyeviti wa Vitongoji, Vijiji na Mitaa kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani yanayorejeshwa na Halmashauri kwenye Vijiji na yanayokusanywa kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura 290. Madiwani, Wabunge hudhaminiwa kupata mikopo kwenye mabenki na taasisi za kifedha kupitia posho za kila mwezi ambacho ni kipato chenye uhakika kuwezesha kurejesha mikopo hiyo waliyokopa.

Mheshimiwa Spika, mkakati wa Serikali ni kuziwezesha Halmashauri kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kuimarisha makusanyo ya ndani katika vyanzo mbalimbali na kuimarisha uwezo wa Halmashauri kulipa posho hizo kwa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa. Ahsante.