Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Zuberi Mohamedi Kuchauka (104 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona. Awali ya yote, nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu aliyeniwezesha kuwepo jioni hii kuchangia mjadala huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda kutoa shukrani za dhati kwa Wanaliwale kwa kuniamini na niko tayari kuwatumikia. Vilevile napenda kuwapongeza wapiga kura Wanaliwale kwa kuiweka CCM kuwa Chama cha Upinzani Jimboni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mjadala wangu nitaulekeza katika maeneo yafuatayo. Kwanza kabisa, msingi wa Mpango. Msingi wa Mpango tumeambiwa ni amani, utulivu lakini nataka nitoe angalizo hapa ni lazima tutofautishe uvumilivu wa watu wachache na amani. Nataka nitumie neno ukondoo, ukondoo wa Wazanzibar tusiuchukulie kama ni kigezo cha amani. Nataka nilihakikishie Bunge lako Tukufu kwamba ukondoo huu tusitegemee kwamba utakuwa ni wa kudumu. Kama tunakusudia huu Mpango utuletee matunda tunayokusudia ni lazima tuhakikishe kweli tunapambana kuhusu suala la amani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango huu tumeambiwa kuna kuimarisha elimu, mimi nitajielekeza kwa upande wa elimu. Hatuwezi kuimarisha elimu tukiwasahau walimu. Walimu wetu maisha yao ni duni sana. Hapa nataka niongelee jambo moja. Walimu wanapewa kazi nyingi sana, mimi naomba tufike mahali hawa walimu tuwapunguzie kazi. Nitoe mfano walimu hawa ndiyo wasimamizi wa uchaguzi nchi hii inapofika kwenye uchaguzi na madhara wanayoyapata ni pale ambapo Chama cha Mapinduzi hakijapita, huyu mwalimu aliyesimamia, aidha ni Mratibu au Mwalimu Mkuu ajira yake iko hatarini. Natoa mfano huu katika Jimbo langu la Liwale leo hii wako walimu ambao waathirika kwa matukio haya. Sasa hatuwezi kuboresha elimu iwapo walimu hawana utulivu, walimu wanaidai Serikali, naomba tuliangalie hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye sekta ya afya. Tusitarajie mpango huu unaweza ukafanikiwa iwapo watu wetu hatujawajenga kiafya. Kwa upande huu wa afya nafikiri siasa imekuwa nyingi kuliko utekelezaji. Kama ambavyo watangulizi walivyosema nchi yetu watu ni wapangaji wazuri sana na mimi nasema huu Mpango tukiamua kuuza kwa nchi yoyote wakiutekeleza miaka mitano ijayo watakuwa mbali sana, lakini kwa Watanzania Mpango huu hatuwezi kufanikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, nchi yetu imekuwa na mipango mingi sana na kitu kikubwa sana nachokiona mimi ni kwamba nchi yetu inaongozwa na mawazo ya watu wachache. Leo hii tukibadilisha Waziri hapa Wizara hiyo itabadilika kwa kila kitu, hatuna common goal kwamba nchi inataka kwenda wapi, hilo ndiyo tatizo letu. Leo hii tukibadilisha Rais anakuja na mambo mengine. Mheshimiwa Mkapa alikuja na Mtwara Corridor baada ya Mkapa kuondoka Mtwara corridor ikafa. Mheshimiwa Kikwete alikuja na maisha bora na yenyewe sijui kama itaendelea. Pia alikuja na Bandari ya Bagamoyo na sijui kama kwa utawala huu kama hiyo bandari bado ipo.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Sasa kwa mtindo huu hatuendi kwamba kila Waziri, kila Rais atakayekuja na la kwake hatuna common goal kama Taifa. Hili limeshatuletea matatizo sana, nitoe mfano kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki tulipozungumzia habari za reli tulilalamika hapa, sisi tulikuwa walalamishi wakubwa sana, watu wa Uganda na Rwanda walipoamua kuondoka kujiunga kutengeneza reli tukaanza kulalamika, mnalalamika nini? Mnachelewa wenyewe halafu mnategemea wao wawasubiri hatufiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze kwa upande wa reli, sidhani kama kweli tuna dhamira nzuri kuhusu hiyo reli ya kati. Hivi unampaje mtu kusimamia reli ya kati ana malori ya usafirishaji zaidi ya 5000, hayo malori ayapeleke wapi? Ana malori ya usafirishaji 5000 halafu mnamwambia asimamie reli ijengwe halafu yeye malori apaleke wapi akafugie kuku? Tuache utani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka Mheshimiwa Rais alipokuwa kwenye Bunge hili kama Waziri wa Miundombinu alisema Sera ya Taifa letu ni kuunganisha mikoa yetu kwa barabara za lami. Nisikitike kusema sisi Mkoa wa Lindi hasa Wilaya ya Liwale inaitwa Wilaya ya pembezoni, kwa mawazo yangu nikajua Wilaya ya pembezoni maana yake ni Wilaya inayopakana na nchi nyingine, lakini ndani ya Tanzania kuna Wilaya za pembezoni. Sisi Liwale tunapakana na Mkoa wa Morogoro, Ruvuma niambieni kama kuna barabara inayotoka Morogoro kuelekea Liwale, hakuna. Hatuongelei barabara za lami tunaongelea hata barabara za changarawe, kutoka Liwale kwenda Tunduru hakuna barabara. Wilaya ya Liwale leo iko pembezoni inapakana na nchi gani? Halafu mnasema tunaweza kwenda sambamba na huu mkakati, huu mkakati nasema kwamba hauwezi kwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, narudi kwenye upande wa amani, tumewapa kazi Polisi kwamba wao ndiyo walinzi wa amani, lakini nipende kusikitika kwamba hao polisi tunaowategemea wanaishi kwenye viota na mtaani. Hivi wewe polisi unakaa mtaani mwanangu anauza gongo utamkamata?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Liwale imekuwa Wilaya mwaka 1975 mpaka leo hawana Kituo cha Polisi. Kituo cha Polisi cha kwanza kilikuwa kwenye gofu la mkoloni, NBC walipojenga nyumba yao wakahamia huko, ile nyumba ilikuwa ni ya mtu binafsi leo hii inamwaga maji kila mahali, mafaili yanafunikwa na maturubai halafu polisi hao hao ndiyo tunategemea walinde amani, hapo tunacheza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba nijielekeze kwa upande wa sekta ya viwanda. Sekta ya viwanda hasa kwa sekta binafsi huku ndiyo tumekwama kabisa. Kama tumefika mahali tunawaacha vijana wetu wahangaike na hawa matajiri wakubwa, eti ndiyo wa-bargain mishahara. Mimi nasikitika jambo moja, sielewi imekuwaje. Zamani nilisikia wale ma-TX walikuwa na vibali vya kuishi miaka miwili leo hii tuna ma-TX kwenye viwanda vya watu binafsi mpaka wafagizi na madereva, sijui Uhamiaji wanafanya kazi gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mpaka naingia hapa Bungeni nina miaka 30 kwenye sekta ya watu binafsi, nimetembea zaidi ya viwanda sita, usiniulize kwa nini nimebadilisha viwanda vyote hivyo, ni kwa sababu nilikuwa sitaki kunyanyaswa. Haiwezekani leo hii tuna ma-TX, mtu ana cheti cha uinjinia ni dereva, ana cheti cha uinjinia anasimamia upakizi wa mizigo kiwandani, hii nchi imeoza, ni kama vile haina mwenyewe. Ndiyo maana nikasema kama ni kutunga sheria sisi tunaongoza kwa kutunga sheria nzuri sana na kama kwa mipango sisi tunaongoza lakini utekelezaji zero. Kama walivyotangulia kusema wenzangu, Waheshimiwa Mawaziri mliopewa dhamana nafuu msikilize Wabunge wa Vyama vya Upinzani wanasema nini, lakini mkiwasikiliza wa huko mtapotea na kama majipu ninyi mtakuwa wa kwanza. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze upande wa kilimo. Kilimo ndugu zangu hakiendeshwi na ngojera hizi za kilimo kwanza wala kilimo uti wa mngogo, tuna matatizo ya masoko. Nikupe mfano Mkoa wa Lindi, Wilaya ya Liwale, sisi tunalima korosho, ufuta, mbaazi lakini wakulima wetu sasa hivi bado wanahangaika. Mwaka juzi mbaazi ilipanda bei watu wakajikita huko, mwaka huu korosho zimepanda bei, ufuta umeshuka. Kwa hiyo, watu bado wanahangaika yaani wanalima kwa kubahatisha kwamba ukilima ufuta ikikuangukia bahati umepanda bei ndiyo unanufaika, ukivuna korosho mwaka huu imepanda bei ndiyo umenufaika. Hizi ngonjera za Kilimo Kwanza bila kutafuta masoko ya mazao yetu hatutakwenda huo mkakati ni wa kufeli. Mimi sijaona kwenye mpango huu wapi kumeelezwa suala kuimarisha masoko. Natoa angalizo hatuwezi kuimarisha kilimo kwa ngojera ya kilimo kwanza wala kilimo uti wa mngogo ni lazima tufanyekazi. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi jioni hii ya leo na mimi nitoe mchango kwenye Wizara hii. Awali ya yote nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha mimi kusimama jioni hii ya leo nikiwawakilisha Wanaliwale, nikifikisha vilio vyao Wanaliwale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaenda huko naomba nitoe utangulizi kidogo maana nasikia watu wanalalamika reli, reli, reli, reli. Mbona haijengwi, mbona haijengwi. Nataka niwape faida moja, tatizo la Serikali yetu ni kutanguliza mipango kabla ya nia au dhamira. Sisi kwenye uislamu tunaamini kwamba, mtu unatakiwa utangulize nia, kwanza nia iwepo utende jambo; haiwezekani katika karne ya 21 Tanzania unasafirisha mafuta kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma kwa gari! Unasafirisha mafuta kutoka Dar es Salaam kwenda Mtwara kwa gari! Bandari Mtwara ipo haiwezekani! Hivi Wajerumani wakati wanajenga ile reli tuliwaona wendawazimu? Wamechukua tu nchi wakajenga reli, sisi leo karne ya 21 tunategemea malori, miaka 54 ya Uhuru hapa hatuendi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wakandarasi mnaowapigia kelele, mnawalalamikia wanajenga barabara, maana gari likipiga kona na barabara nayo inapiga kona! Hawa tutaendelea kuwalaumu, hata aje malaika ajenge hiyo barabara kwa malori yale yanayopita kwenye hizo barabara haziwezi kudumu, cha msingi tubadilishe mindset zetu. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunalalamika kwamba, wenzetu sijui Kenya, sijui Rwanda, sijui nani, wameamua kufanya kazi! Wale wameamua kufanya kazi wametoka maofisini wanafanya kazi. Ndugu zangu Watanzania leo hii Mtanzania ukikabidhiwa mradi cha kwanza ni kutafuta kiwanja, cha kwanza ni kuagiza gari, tunakwenda wapi? Hatuwezi kwenda! Tena basi kama wewe ni Meneja wa Mradi, mradi unakwisha huna nyumba, huna gari, jamii inakucheka, unaonekana wewe fala! Tubadilishe mindset zetu, tuondoe ubinafsi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi nataka niwaambie reli hii kama Waziri huyu aliyekuja leo anadhamira ya kujenga mimi nitaiona. Huwezi kupingana na hawa wafanyabiashara wa malori, mtu ana malori 2000, 3000, 5000, hivi unayapeleka wapi? Nani atakubali reli ijengwe? Tuache kubabaishana, turudi kwenye uhalisia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye viwanja vya ndege. Mheshimiwa Waziri mimi sielewi Mzee Kawawa aliacha usia gani kwa Wilaya ya Liwale, ile miradi yake yote iliyokuwepo yote imefutwa. Sijaelewa kabisa, kabisa tatizo ni nini! Pengine Waziri atakapokuja atanieleza pengine kuna maagizo special Mzee aliyaacha ile Wilaya muisahau kwa kiwango hicho. Sisi Liwale kulikuwa na kiwanja cha ndege leo hii kuna miti unaweza kuchuma hata matunda ule uwanja wa ndege haupo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye upande wa mawasiliano ya simu. Mawasiliano ya simu kwa Wilaya ya Liwale jamani tunaomba mtutoe kisiwani. Mimi namuomba Mheshimiwa Waziri kwa heshima na taadhima muitoe Liwale kisiwani, Liwale kuna tatizo la barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru Mheshimiwa Rais aliyepo madarakani, mnyonge mnyongeni haki yake mpeni, amekuwa muadilifu. Aliulizwa hapa habari za barabara Nangurukulu – Liwale akasema haiko kwenye mpango wa kujengwa kwa lami na kwa kulikumbuka hilo alipokuwa anaenda kuomba kura Liwale hakuja, alijua kwa sababu wameshakataa kwamba hiyo barabara hatowajengea kwa kiwango cha lami na kweli hakujenga na alipoenda kuomba kura hakuenda Liwale kuomba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi namshukuru pengine angekuja nisingekuwa hapa sasa hivi. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hakuna barabara mimi naomba Mheshimiwa Waziri ututoe Liwale kisiwani. Tuna barabara ya Nachingwea – Liwale, kilometa 120, sijaiona kwenye hotuba yako yote. Kuna barabara ya Nangurukuru – Liwale kilometa 230 sijaiona kwenye mpango wako wote, tunakosa nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kwa jinsi Liwale ilivyo na rasilimali za kutosha, tunazo mbuga za wanyama, tunayo mazao ya misitu, tunao wakulima wanalima ufuta, wanalima korosho. Tungekuwa na barabara Liwale tusingekuwa walalamikaji kama tunavyolalamika leo upande wa afya, tunaolalamika upande wa elimu, tungeweza kujenga hospitali zetu. Hizi zahanati tungeweza kuziwezesha kwa mapato ya Halmashauri, leo Liwale imefungwa, Halmashauri inapata wapi mapato?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi namuomba Waziri atusaidie, atuokoe, atuondoe kisiwani. Nimeona kwenye mpango kuna barabara inatoka Mtwara – Newala – Masasi – Nachingwea inarudi Nanganga; nikupe umbo la hiyo barabara ina “U”, chini ya hiyo “U” ndio kuna Liwale, hebu muone Liwale ilivyotengwa. Yaani umechora “U”, umetoka huku umekwenda ile “U” chini ndio kuna Liwale, wameiacha huko chini! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi watu wale wakiona kwamba CCM haiwataki, wana haki au hawana haki? Mmetengeneza “U”, inatoka Mtwara – Newala – Masasi – Nachingwea inarudi Ruangwa – Lindi, Liwale iko chini! Tunawatendea haki watu wale na tunawahitaji?
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ninakuomba kwa heshima na taadhima uiondoe Liwale kutoka kisiwani. Tatizo kubwa ninaloliona hapa, tatizo kubwa, Chama cha Mapinduzi tangu Uhuru mnaongoza hii nchi, lakini hii nchi kila siku inazaliwa upya! Kila tunapobadilisha uongozi nchi inazaliwa upya. Kwa maana ya kwamba, kila Rais anayekuja ana vipaumbele vyake, hatuwezi kufika! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, alikuja Mheshimiwa Mkapa na Mtwara Corridor, Mheshimiwa Mkapa kaondoka na Mtwara Corridor imekufa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sijui kama ipo tena?
Mheshimiwa Mwenyekiti, atakuja huyu na lake, mimi nafikiri, sijui tuseme waongoze milele, sijui kama Rais mmoja abaki tu, sijui tufanyaje? Maana kila tunapobadilisha pamoja kwamba chama ni kile kile, watu ni walewale, lakini mikakati yao ni tofauti kabisa. Utafikiria aliyekuja ni tofauti yaani utafikiri ni chama kingine na nchi ni nyingine...
Mheshimiwa Mwenyekiti, tena kwa kujisifia kabisa kwamba Tanzania inazaliwa upya! Inazaliwa upya kwa kuyaacha yale ambayo yalipangwa awali.
TAARIFA....
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hiyo sijaipokea kwa sababu zifuatazo; amesema Mtwara Corridor bado ipo, anaweza kuniambia Mtwara Corridor ilikuwa ni mradi wa miaka mingapi? Na uliishia wapi? Na ulitengewa fungu kiasi gani? Na ni kwa miaka mingapi? Na utekelezaji wake leo umefika wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mtwara Corridor ilikuwa inatuunganisha sisi mpaka Msumbiji, leo hii huyu mchangiaji aliyetoka hapa anaongelea suala la kutuunganisha na Msumbiji. Eti mtu anakuja anasema Mtwara kule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua hili ni tatizo la watu kutokujua jiografia ya Tanzania. Watu jiografia ya nchi hii hawaijui na ndio maana leo hii ukiongelea barabara ya Kusini mtu anakwambia daraja la Rufiji! Mimi nataka niwaambie daraja la Rufiji halina tofauti na daraja la Ruvu kwa sababu mtu leo anadai barabara ya Kigoma unamwambia daraja la Ruvu, inaeleweka?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio hicho mnachokifanya! Maana tukiwaambia jamani tunahitaji barabara ya Kusini, aah, ninyi Kusini sijui mmetengenezewa daraja la Mkapa. Daraja la Mkapa ndio nini sasa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kuanzia leo hii Kigamboni nako wamepata daraja lile huku Kimbiji, Gezaulole, nani, hawaitaki tena barabara kwa sababu, wanadaraja la Nyerere. Tunakwenda wapi? Mbona tunakuwa wavivu wa kufikiri? Mbona tunakuwa wavivu wa kufikiri! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nafikiri tunahitaji kufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji kufanya kazi nchi hii, tunahitaji watu…
MWENYEKITI: Mheshimiwa, muda wako umeisha, naomba ukae tafadhali.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nitoe shukurani kwako wewe kwa kunipa nafasi ili niwe mchangiaji mmojawapo asubuhi hii ya leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu kwenye Mpango huu ni kama ifuatavyo; Serikali yetu hii ya Chama cha Mapinduzi imekuwa ni Serikali ya kupanga mipango mizuri sana. Hii ni mara ya pili nalisema hili ndani ya Bunge lako Tukufu, lakini tatizo letu kubwa liko kwenye utekelezaji wa ile mipango tunayoipanga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sijui hizi takwimu mnazokuja nazo, hizi za ku-copy na ku-paste zinaletwa kwa sababu ipi? Tunakuwa tumedhamiria nini tunapoleta takwimu ambazo hatuna uhakika nazo na wala hazitekelezeki. Hatuwezi kuwa na mipango na ikatekelezeka iwapo hatuna mikakati iliyowazi ya kuonyesha namna gani tutatekeleza mipango hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitolee mfano takwimu ambayo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati, anasema sera ya nchi yetu ilikuwa kuunganisha mikoa yetu na imekamilika na akaitaja baadhi ya mikoa na akasema ni mikoa michache tu ambayo imebaki haijaunganishwa. Hata hivyo, nashangaa Mkoa wa Lindi - Morogoro haijatajwa katika mikoa ambayo haijaunganishwa. Kwa sababu Mkoa wa Morogoro unapakana na Mkoa wa Lindi kupitia Wilaya ya Liwale lakini hakuna barabara. Mkoa wa Lindi unapakana na Ruvuma katika Wilaya ya Liwale hakuna barabara lakini takwimu hapa zinaonyesha kwamba mikoa hiyo tumeshaunganishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Sera ya Taifa inasema kila kata kuwe na kituo cha afya na kila kijiji kiwe na zahanati. Lengo hili halijafikiwa kama ambavyo Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani amesema, tunadiriki vipi kwenda na mpango wa pili wakati hii mipango yetu ya kwanza haijakamilika, tena imekamilika kwa asilimia 26 tu. Katika Jimbo langu tuna kata 20 lakini tuna kituo cha afya kimoja tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii hapa tunajitapa kwamba tunao uwezo wa kutekeleza mipango hii kwa kutumia rasilimali zetu ambazo nina hakika kabisa hazisimamiwi kama inavyotakiwa.
Ubadhirifu wa rasilimali zetu umekuwa ni mkubwa sana. Tunavyo viwanda, hivyo ambavyo sasa tunasema tunataka kuvifufua, Mkoa wa Lindi kulikuwepo na viwanda vya korosho vikabinafsishwa na havifanyi kazi mpaka leo lakini leo hii tunapokuja kufufua viwanda napata wasiwasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Lindi sasa hivi unazalisha ufuta na korosho lakini kama nilivyosema tuna matatizo ya barabara. Hivi ni mwekezaji gani atayekuja kuwekeza Lindi mahali ambapo hakuna barabara, mahali ambapo hatujajiandaa na miundombinu yoyote? Nitoe mfano halisi, sasa hivi barabara ya Jimboni kwangu imeshafungwa, huwa inapitika kiangazi tu lakini sisi Mkoa wa Lindi ndiyo tunaoongoza wa kuzalisha korosho na ufuta lakini hatuna kiwanda hata kimoja. Mimi siwezi kumvutia mwekezaji yeyote aje kuanzisha kiwanda Liwale wakati ambapo hatuna barabara, umeme wala miundombinu yoyote, huku ni kudanganyana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi sijajua Serikali inavyokuja na hizi takwimu au maelezo ya juu juu wanakuwa wamedhamiria nini kwamba tupitishe tu ili mradi siku ziende au kweli tuko committed na hayo tunayoyaongea au tunayoyadhamiria? Kwa mfano, hapa tumesema malengo yamekamilika kwa asilimia tano, hivi ni kweli? Yaani mpango wa kwanza umetekelezwa kwa asilimia tano au asilimia 26 tunaingia kweli kwa kifua mbele kwa mpango wa pili, mimi sijaelewa na wala sishawishiki kuona kama tuko serious na jambo hili. Hivi tunawezaje kwenda na Mpango wa Pili.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri kikao kilichopita nilisema hapa kwamba hatuko serious. Mpango ule wa kwanza wa kujenga reli tulitekeleza kwa asilimia 5 tu na nikawaambia hapa kwamba hii haifanywi kwa bahati mbaya ila kwa makusudi kwani kuna watu wanataka wafanye biashara za malori, nikasema hapa wakaanza kulalamika. Mipango hii tunayokwenda nayo haiwezi kwenda kama hatuko serious. Mimi naomba Serikali ya Chama cha Mapinduzi kama hamko serious na nchi hii mtuachie na watu wako tayari kutuachia lakini ninyi hamtaki kutoka. Kwa mipango hii hatuwezi kwenda. Tumekuwa wepesi sana wa kuainisha vipaumbele lakini si watekelezaji wa vipaumbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakuja upande wa kilimo, tangu Uhuru tumekuja na sera nyingi za Kilimo Kwanza, Kilimo Uti wa Mgongo lakini hivi kweli hiki kilimo kinaweza kikaimarishwa kwa njia hii na hakuna mkakati wowote wa kuimarisha masoko. Leo hii Waziri anakuja hapa anasema kwamba anataka kushusha bei mazao ya kilimo ina maana wakulima waendelee kuteseka, hiyo ndiyo mipango ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Mtuachie nchi hii kwa sababu mimi ninavyofahamu huwezi kuimarisha kilimo kama haujaimarisha masoko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kwetu tunapata shida, nitolee mfano wa Jimboni kwangu, tunalima korosho na ufuta lakini wananchi wangu wanahangaika kila mwaka. Mwaka huu wakivuna korosho, ufuta unapanda bei, mwakani wanavuna ufuta, korosho zinapanda bei hawajui kinachoendelea.
Leo hii tunakuja hapa na Mpango kwamba tunaanzisha viwanda hatujui hivyo viwanda vilivyokuwepo awali vilienda wapi, wale walioharibu viwanda hivi wamechukuliwa hatua gani hatujui, tunakuja tunavurugana vurugana hapa tu ndani kwamba tuna mipango endelevu.
Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja atueleze, utekelezaji wa Mpango huu hizo hela anazipata wapi? Kwa sababu mipango iliyopita, Serikali ni hii hii, watu ni wale wale imetekelezwa kwa asilimia tano, leo hii mnakuja kutuambia kwamba mnaweza kutekeleza angalau asilimia 50, huo uwezo mnaupata wapi? Au ndiyo kama nilivyosema jana hapa tupo tu kwa ajili ya kuonekana kama sisi tupo Bungeni tunajadili mustakabali wa nchi yetu ili mradi siku ziishe lakini seriousness mimi sijaiona. Seriousness ya Chama cha Mapinduzi kuwahudumia watu wake sijaiona. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nawaambieni Jimboni kwangu tungekuwa tumepakana na nchi mojawapo ningeshawishi lile Jimbo tuliondoe Tanzania. Hata hivyo, kwa sababu tuko katikati hatujapakana na nchi yoyote tutaendelea kubaki kisiwani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi nikiwa na maana halisi. Mimi kwangu hakuna barabara, Kituo cha Polisi, hospitali, maji na nikisema hakuna maji namaanisha. Liwale tumerithi Kituo cha Polisi tulichukua jengo la benki.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba ulinde muda wangu.
NAIBU SPIKA: Muda wako unalindwa, naona kuna taarifa nyingine.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, pili naikataa taarifa kama ifuatavyo. Nimesema Wilaya ya Liwale haina barabara, mimi kila tarehe 15 Septemba na tarehe 15 Julai wananchi wa Liwale wanatoka kwenda Mahenge kwa miguu wanasindikizwa na askari wa wanyamapori na wanatembea muda wa siku tatu mpaka siku nne. Nimesema Liwale hakuna barabara, nimesema Liwale kama ingekuwa vita ile ya mwaka… (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kuchauka, naomba ukae kuna taarifa nyingine.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa hiyo, nakataa Taarifa yake kama ifuatavyo; nimesema na naendelea kusema Liwale sisi hatuna hospitali inayoitwa Hospitali ya Wilaya, nashukuru aliyenipa taarifa ni Naibu Waziri wa Afya atalichukua akitaka kuthibitisha. Sasa hivi katika Wilaya nzima ya Liwale tuna Clinical Officers watatu tu, siyo Madakatari Bingwa ni Clinical Officers watatu tu mahitaji ni Clinical Officers 40, nasema kwa takwimu. (Makofi)
WABUNGE FULANI: Aibu.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, labda uniambie unapotaka kuunganisha mikoa ina maana kwamba tutoke Lindi - Dar es Salaam - Dodoma - Iringa, twende Songea, labda kuunganisha kwa namna hiyo. Nikisema nina hali hiyo ya kusema, nawasemea wana Liwale. (Makofi)
Kwa hiyo, narudi kwenye Mpango. Kama nilivyotangulia kusema kwamba sisi shida yetu ni uhakika wa masoko. Serikali haionyeshi mahali ambapo wananchi hawa watasaidiwa vipi kwa upande wa masoko.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikirudi kwa upande wa maliasili, sisi Liwale tuko kwenye Mbuga ya Selous lakini Liwale haina hoteli ya kitalii, barabara wala kiwanja cha ndege, hatunufaiki kwa chochote sisi kupakana na mbuga za wanyama zaidi ya kuendelea kupigwa na kunyanyaswa. Nimeshamletea Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maliasili taarifa ya mgogoro uliopo Wilaya ya Liwale na Mbuga ya Selous. Sasa anapokuja Naibu Waziri akaniambia kwamba sina haki ya kuiondoa Liwale Tanzania sijamuelewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunanufaikaje na maliasili? Sisi tunapakana na mbuga za wanyama lakini vilevile tulikuwa na uwanja wa ndege enzi zile za Mzee Kawawa, Mwenyezi Mungu amrehemu, tangu Mzee Kawawa amekufa na Liwale imekufa, ule uwanja wa ndege haupo tena pale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi leo hii Serikali hii kwenye Mpango wake huu, labda Waziri atakapokuja kuniambia kama ana mpango wowote, kama kuna mpango wa kuufufua uwanja wa ndege Liwale, kama kuna utaratibu wowote ule wa maliasili, kama wanajenga hoteli au kama wanatutengenezea barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nimetembea vijiji vyote vya Jimbo langu sijakuta hata choo kilichochangiwa na Selous, sijakiona! Sasa unategemea wananchi wa Liwale na Lindi wa-support mpango huu kwa kipaumbele gani ambacho wamepewa au kwa sehemu gani ambayo wamekumbukwa? Labda Waziri atakapokuja kwenye kujumuisha atakuja kunieleza kwamba Liwale au Mkoa wa Lindi kwa ujumla ameuweka katika mpango huu katika maeneo gani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii Liwale bado watumishi hawataki kukaa kule, mawasiliano hakuna siyo ya barabara wala simu. Ndiyo maana nikasema hapa nahitaji Clinical Officers 40, siyo kwamba hawapangwi, wanapangwa lakini hawakai kwa sababu mazingira ya Liwale siyo rafiki. Jamani Chama cha Mapinduzi mtuachie hii nchi. Tuachieni hata miaka mitano tu muone nchi inaendeshwaje. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa na hayo tu ya kusema. Ahsante sana.
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, maelezo yangu kwenye Mpango huu yatajikita katika Wizara zifuatazo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo; ukizingatia mafanikio kidogo kwa ufanisi wa Mpango wa awali kwa maoni yangu tatizo kubwa linaloikabili mipango yetu mingi ni ukosefu wa uadilifu kwa watekelezaji wa mipango yetu. Ikiwa ni pamoja na nchi kukumbwa na tatizo kubwa la rushwa, ukosefu wa miundombinu bora ya reli na barabara kwa maeneo ya uzalishaji mazao ya kilimo. Hatuwezi kuwa na uchumi mzuri mpaka pale tutakapobadilisha mtazamo wetu na kuacha tabia ya uchumi wetu kutumikia siasa, badala ya siasa kutumikia uchumi. Katika kilimo tuna tatizo la masoko ya wakulima wetu, sambamba na ujenzi wa viwanda vidogo vidogo hasa pale ambapo mazao hayo hulimwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu elimu; miongoni mwa sababu za mipango mingi kutofikia malengo ni mfumo mzima wa elimu yetu, elimu inayotoa wahitimu wasiokuwa na uwezo wa kuingia kwenye soko la ajira ya kujitegemea. Elimu ambayo haiwajengei uwezo wa kujitegemea na badala yake wanakuwa mzigo kwa Serikali; vyuo vya VETA pekee ndio ufumbuzi wa hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, maliasili; hatuwezi kukuza sekta ya utalii kama hatupo tayari kufufua vivutio vilivyosahauliwa kama kivutio kilichopo Liwale (Gofu la Mjerumani la vita ya maji maji lililopo Mjini Liwale) hivi ni kweli ili kuingia Selou ni lazima watalii wapitie Morogoro kwa nini Mkoa wa Lindi (Liwale) imeachwa yatima katika utalii wa ndani na nje?
Mheshimiwa Naibu Spika, tunawezaje kuwashirikisha wananchi kushiriki kulinda rasilimali zetu kama hawataona faida ya moja kwa moja itokanayo ya rasilimali zetu. Utatuzi wa migogoro ya mipaka ya hifadhi zetu ni moja ya kikwazo cha sekta hii kushindwa kufikia malengo.
Mheshimiwa Naibu Spika, miundombinu; ugawaji usiozingatia hali halisi wa miradi ya barabara nchini ni moja ya kikwazo katika Mpango huu. Mfano ni Mkoa wa Lindi ambao mpaka leo mkoa huu haujaweza kuunganishwa na Mkoa jirani wa Morogoro kupitia Liwale na Mkoa wa Ruvuma kupitia Wilaya za Tunduru na Liwale. Sio hivyo tu hata barabara ya Nangurukuru-Liwale ambayo ingeendeleza mazao ya korosho na ufuta ambayo sasa yanalimwa kwa wingi katika Mkoa mzima wa Lindi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sekta ya Afya ni sekta muhimu sana ambayo tumeshindwa hata kuboresha afya za watu wetu hasa katika kupunguza vifo vya mama na mtoto. Mfano, katika Wilaya ya Liwale hakuna hadi leo hospitali yenye hadhi ya kuwa hospitali ya Wilaya. Hospitali haina miundombinu yoyote inayofanana na hospitali ya Wilaya. Wilaya nzima ina kituo kimoja tu cha afya Wilaya yenye Kata 20 na Mpango huu haujasema chochote kuhusu ni namna gani ya kupambana na changamoto hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushirikishwaji wa wadau ni muhimu ili mipango yetu iweze kutekelezeka, vile vile uadilifu wa watendaji. Tuongeze bidii ya kupambana na rushwa na uwajibikaji wa pamoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze mchango wangu na Sekta ya Ualimu. Mtiririko mzima wa kuandaa Walimu una kasoro kubwa sana hasa tangu kuchafuliwa kwao kwenda kwenye Vyuo vya Walimu kwa kuwachagua watu wenye ufaulu wa chini kuingia kwenye Vyuo vya Ualimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kitendo cha wahitimu kukaa mwaka mzima wakisubiri ajira kinavunja moyo Walimu wetu. Hata hivyo, kitendo cha Walimu kushindwa kuwapandisha madaraja kwa muda mrefu na pale wanapopanda kushindwa kuwapa stahiki zao, nako ni kuvuruga kiwango cha elimu nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Walimu kufanya kazi nje ya ajira yao, mara nyingi Walimu wamekuwa wakitumikia kwenye kazi kama vile sensa, kusimamia uchaguzi, kuwa Watendaji wa Vijiji nakadhalika. Mwalimu anaposimamia uchaguzi na Chama Tawala kikianguka kwenye Kituo husika, basi huyuo Mwalimu Mwalimu ajira yake huwa hatarini. Ninayo majina ya walimu waathirika na hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Jimbo langu la Liwale ambako CCM ni Chama cha Upinzani, ushauri wangu ni kwamba tuwaache Walimu wabaki madarasani. Pamoja na changamoto nyingi tunazokabiliana nazo ili kujikwamua kutokana na umasikini uliokithiri mahitaji ya Chuo cha VETA Liwale ni muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na Chuo cha Walimu, kwani Walimu wanaotoka nje ya Mkoa wetu wa Lindi wanashindwa kukaa Liwale. Vilevile tunaomba Kituo cha Chuo cha Utalii ili kukuza utalii Kusini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shule za Jimbo la Liwale hazina Wakaguzi na wale wachache waliopo hawana vitendea kazi. Hawana gari hata moja la ukaguzi wala pikipiki. Tunawezaje kuwa na elimu bora, elimu ambayo haisimamiwi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kupanda kwa madaraja ya Walimu kuzingatie kiwango cha elimu. Hakuna utendaji ulio bora kama Mratibu Kata ni Form IV, Mwalimu Mkuu Degree au Mkuu wa Shule Diploma, Mwalimu Degree, hapo hakuna uwiano wowote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya Elimu imeshusha kiwango cha elimu nchini. Leo watoto hawana mitihani ya Mid-term, mitihani ya wiki, Mock – Kata, Mock – Wilaya, wala Mock – Mkoa. Sasa hivi mtoto hupimwa mara moja tu kwa mwaka mzima. Utajuaje maendeleo ya mtoto anayefanya mtihani mmoja tu kwa mhula?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii jioni ya leo nami nitoe mchango wangu kwenye Wizara hii ya Afya. Awali ya yote, nachukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha kusimama hapa katika Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile napenda kutoa shukrani za dhati kwa wapiga kura wangu, Wanaliwale kwa kunikabidhi jukumu hili la kuwawakilisha na sasa hivi ndiyo hiyo kazi naifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, naanza kuwaasa ndugu zangu wa Kambi yetu ya Upinzani. Kambi ya Upinzani ndiyo tuliopewa jukumu la kuishauri Serikali. Serikali hii wanasikia na wanatuelewa. Wenzetu waliobaki kule nyuma, wamepewa kazi ya kushangilia na kupitisha. Sisi ndiyo tunatakiwa tuishauri hii Serikali. Hii Serikali siyo kwamba hawasikii, tatizo la Serikali yetu ni kwamba wako nyuma sana na wakati. Mliwashauri hapa mwaka 2010 kwamba safari za Mheshimiwa Rais hazina tija; Mwaka 2015 wametekeleza; mkawashauri mwaka 2010 kuhusu ufisadi, mwaka 2015 wametekeleza; tatizo ni muda gani wanautumia kuyatekeleza haya tunayowaambia? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, uzuri wa kusema ni kutazamana, ndiyo maana sisi tumetazamana na Mawaziri, wale wako nyuma, kwa sababu wanajua nini tunaongea. Nataka niwape faida moja; tunapochangia Upinzani na Mawaziri wako busy kuandika, kwa sababu wanajua sasa ndiyo wanashauriwa, kule wanasubiri kushangilia na kupitisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa narudi kwa mabosi wangu, Wanaliwale, naomba niwawakilishe. Wilaya ya Liwale ni Wilaya iliyoasisiwa mwaka 1975 na mwasisi wa Wilaya ile ni Waziri Mkuu wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mzee Rashid Mfaume Kawawa. Nakuja kwenye upande wa hospitali; sasa bahati mbaya ya wilaya ile, ina vijiji 76, tuna zahanati 30 tu. Wilaya ya Liwale ina kata 20, tuna kituo cha afya kimoja, mfu. Nasema kituo mfu kwa sababu ni mwaka wa tatu huu, vifaa vimekwenda pale vya upasuaji, viko kwenye maboksi mpaka leo. Havijafunguliwa, mchwa wanakula yale maboksi. Nimeyaona haya kwa macho yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali ya Wilaya ya Liwale ina magari mawili ya wagonjwa; gari moja ndilo ambalo anatumia DMO kama gari la kufanyia kazi na gari moja ndiyo linalotumika kama la kusaidia wagonjwa. Bahati mbaya nyingine ya Wilaya ya Liwale, Mji ule upo; sijui nani anamjua pweza! Barabara zetu ziko mkia wa pweza, kwamba hatuunganishi kutoka kata moja kwenda nyingine, ni mpaka uende urudi, uende urudi. Nakupa mfano wa vijiji vichache vifuatavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutoka Nahoro kwenda Liwale ni kilomita 135, Napata - Liwale Kilomita 120, Liwale - Lilombe Kilomita 65, Kikulyungu - Liwale Kilomita 120. Hawa wanatembea hizo kilomita 120, kufuata huduma Liwale Mjini. Wakifika Liwale Mjini, hospitali yenyewe ndiyo kama hiyo, takwimu hizo nilizokupa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Liwale kwenye zahanati zetu 30 zinahudumiwa na wale mnaita one year course…
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Medical attendant wa one year course ndio wanaohudumu kwenye hizi zahanati. Kichekesho, nimekwenda na DMO kwenye baadhi ya zahanati, tumekuta dawa zimeharibika. DMO anasema hizi dawa zimeharibika kwa sababu hawa wahudumu hawazijui. Wanataka panadol zilizoandikwa panadol. Ukibadilisha boksi siyo panadol hiyo. Hili ni tatizo!
TAARIFA
MWENYEKITI: Taarifa, Mheshimiwa Kuchauka keti kidogo....
MWENYEKITI: Mheshimiwa Zuberi unaikubali taarifa au unaikataa?
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Taarifa yake naikataa, kwa sababu zifuatazo: Waziri Mkuu wa kwanza Tanganyika huru ni Mwalimu Nyerere, lakini Waziri wa Kwanza wa Tanzania ni Mzee Kawawa. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mzee Kawawa ni Waziri Mkuu wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo, uwezo wake wa kuifahamu historia haiwezi. (Kicheko/Makofi)
MWENYEKITI: Endelea!
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Hiyo ni historia fupi tu ameshindwa kuielewa. (Makofi/Kicheko)
MWENYEKITI: Endelea Mheshimiwa na kiti kinakulinda, uko sahihi! (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Afya na Naibu Waziri wa Afya, watu wengi wamewasifia na wanaendelea kuwasifia, nami naendelea kuwasifia, lakini nawapa pole. Nawapa pole kwa sababu jukumu mlilonalo ni kubwa, mazingira ya kazi ni magumu, kwa bajeti hii kwa kweli dhamira yenu ni nzuri, nami nataka niwaambie kwamba ili muweze kuonekana angalau mmetekeleza kidogo, mnahitaji kufanya kazi ya ziada. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama takwimu zinavyosema, bajeti ya Serikali imeongezeka kwa trilioni sita point something, lakini bajeti ya Afya imepungua kwa asilimia 11. Sasa mwone hiyo kazi mliyonayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, narejea kule kule Liwale. Liwale sisi tunayo matatizo, sisi tuna upungufu wa Clinical Officer 40. Mheshimiwa Waziri atakapokuja naomba anieleweshe, hivi DMO anaruhusiwa kutibia? Anaruhusiwa kuingia ofisini kutibu watu? Maana DMO wangu yeye ni mtawala, hajawahi kuingia ofisini kutibia. Sasa sijaelewa, mimi kwa sababu siyo mtaalam sijaelewa. Hapo mtakapokuja, mtanielewesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, jiografia ya Wilaya ya Liwale kiutendaji kuwa na gari moja la wagonjwa ni tatizo. Gari lile likiondoka, watu wengine huku nyuma hawana usafiri tena na ni kilomita kama hizo nilizokupa. Liwale hospitali ile, mimi nimeingia haina X-Ray mwaka mmoja uliopita.
Namshukuru Naibu Waziri, nilikwenda ofisini kwake akanisaidia, akanipa njia ya kupata mtaalam, nikampata mtaalam nikapeleka X-Ray ile ikatengenezwa. Kama Waswahili wanavyosema, “Siku ya Kufa Nyani, Miti yote Huteleza.” Ile X-Ray sasa hivi ni nzima lakini haina mhudumu. Mpiga picha hatuna, kwa hiyo, tumerudi pale pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Wilaya ya Liwale haina ultrasound. Mwezi Januari kuna dada mmoja alikwenda pale kwa lengo la kujifungua, wale akinamama wakaenda kumpima, wakampapasa wakamwambia njoo wiki ijayo. Wiki ijayo yule mama hakufika, tumbo likawa la njano wamemrudisha pale yule mama kafa. Hospitali ya Wilaya ya Liwale!
Mheshimiwa Mwenyekiti, wengi wanamwambia Mheshimiwa Waziri, njoo kwetu, njoo kwetu, mimi sisemi aje Liwale; naomba atusaidie Liwale. Akiona namna ya kuweza kuja, karibu Liwale, aje ajionee haya ninayoyasema. Ile Wilaya imesahauliwa, ni ya siku nyingi, lakini ukienda ukiiangalia utafikiri ni Wilaya ambayo imezinduliwa juzi. Hayo ndiyo matatizo tuliyonayo Wilaya ya Liwale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati napita kuomba kura niliwaambia, sitakubali kuona akinamama wakienda kujifungua wanakwenda kama wameachika; anakwenda na beseni, ndoo, carpet; maana hizi mackintosh wao hawana, kule wanatumia hizi carpet za kawaida. Anakwenda na carpet, ndoo, beseni, wembe, kanga, gloves na sindano. Nikasema sitalikubali hilo. Kwa kuonesha mfano huo, nimepeleka, mackintosh 5,000 mwezi uliopita. Nimeona nianzie hapo, lakini hali yetu ni mbaya, tunaomba msaada wenu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, narudi kwenye upande wa MSD. MSD ni tatizo jamani. Nakumbuka siku moja tulikwenda MSD nikiwa kwenye Kamati ya UKIMWI; yule Mkurugenzi alituambia kwamba tatizo la Halmashauri wanatupa order haraka. Wanatupa order leo, kesho wanataka hela, lakini hii siyo kweli. Sisi Liwale tumepeleka pesa Desemba, shilingi milioni 35. Dawa tulizopata mpaka leo ni za shilingi milioni 20, inaonekana dawa tulizopewa siyo zile tunazozihitaji. Tumepewa dawa zile ambazo MSD wanazo. Mkurugenzi alisema kwamba mkileta pesa, baada ya wiki mbili au wiki tatu mtakuwa mmepata, lakini hii siyo kweli. Huo ndiyo ukweli halisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye CHF. Tarehe 8 Januari, Mkoa wa Lindi ulizindua CHF Kitaifa na mimi mwenyewe nimechangia watu 100 kwenye Jimbo langu, lakini CHF imenitia kitanzi, kwa sababu nimehamasisha Wanaliwale, kabla ya uzinduzi tulikuwa asilimia 10 ya wanajamii wa Liwale, lakini mpaka namaliza tarehe 30 Aprili, tulikuwa tayari tumefika asilimia 46.4 na nikawaahidi Wanaliwale, kufikia Agosti tukiuza ufuta tunataka tusahau masuala ya CHF. Tunataka tuchangie asilimia mia moja. Sasa hiyo imenitia kitanzi. Imenitia kitanzi mimi na Madiwani wangu kwa sababu tuliwaambia, mkienda dirishani mkikosa dawa, njooni kwetu. Sasa vyeti vyote vya dawa vinakuja kwetu. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti vyeti vyote vya dawa vinaenda kwa Diwani, vinaenda kwa Mbunge kwa sababu tuliwaahidi mtoe pesa mtapata dawa; dawa hazipo! Tunawaomba Mheshimiwa Waziri, CHF inatutia kitanzi. Nashukuru mwenzangu Mheshimiwa Bobali aliona mbali, akawaambia wasichange kabisa. Sasa mimi nimeji-commit kwamba tunachanga na kweli wananchi kwa sababu wananikubali, nikiwaambia wanatekeleza. Mwezi Agosti Mheshimiwa Waziri alituahidi tutakuwa tumefikia asilimia mia moja. Naomba Mheshimiwa Waziri, mnitoe kwenye hiki kitanzi. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye hivi mnasema Vituo vya Saratani ya Mlango wa Kizazi. Lindi kuna vituo vinne, Liwale hatuna. Hivi Liwale kuna nini? Jamani, tuoneeni huruma, hata Mzee Kawawa hamumwenzi, simba wa vita! Jamani nawaombeni mtukumbuke na sisi tumo. Kwenye mchango wetu, pato la Taifa tumo! Tunalima korosho kwa wingi, tunalima ufuta kwa wingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie kwenye masuala ya UKIMWI sasa, nakuja kwenye masuala ya UKIMWI. Takwimu zinaonesha wanaotumia dawa za ARV mpaka mwaka 2015 ni watu 700,000 na inakadiriwa mpaka mwisho wa 2016, wanafika watu 900,000, lakini pesa iliyotengwa ni ya watu 200,000. Maana yake mpaka sasa hivi tunasema watu 500,000 hawana dawa. Hiyo ni takwimu sahihi kabisa zinazohusiana na mambo ya UKIMWI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba Mheshimiwa Waziri hili suala la UKIMWI tulipe kipaumbele. Kama kweli dhamira yetu ni kuwasaidia watu wetu, hili suala la UKIMWI tulipe kipaumbele. Vile vile narudi tena kwenye upande wa MSD. MSD hata hizo dawa chache wanazozileta, kwa jiografia ya Liwale na Mkoa wa Lindi ha… (Makofi)
MWENYEKITI: Basi.
MHE.ZUBERI M. KUCHAUKA: Nashukuru kwa kunisikiliza.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami nitoe mchango wangu kwenye Wizara hii ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Kwanza naomba nitoe tu angalizo kwa wasomi wa nchi hii, kwa maana ya kwamba tunasisitizwa sana tusome sayansi, lakini jiografia nayo tuisome. Ukisoma sayansi usiposoma jiografia haina maana. Nasema hivyo kwa sababu zifuatazo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, jioghafia ya nchi yetu inatofautiana kutoka mkoa hadi mkoa, kanda hadi kanda, lakini wataalam wetu wanapotuhudumia wanashindwa kujua hizo jioghafia. Nitoe mfano, wanapogawa pembejeo ile kalenda ya ugawaji wa pembejeo inakuwa ya nchi nzima na inakuwa ya tarehe zinazofanana wakati jiografia ya nchi yetu haifanani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mzuri sisi kanda ya Kusini tunapanda mahindi mwezi wa 12, lakini tumeletewa mbegu mwezi wa tatu. Juzi nimepigiwa simu tumeletewa mahindi ya msaada wa chakula, sisi sasa hivi tunavuna mahindi mwezi Januari sembe Wilaya ya Liwale ilifika kilo moja Sh.2,500/=, kilo hamsini ilikuwa ni Sh.100,000/=, mwone hiyo shida ya chakula. Leo tunavuna mahindi tunaletewa mahindi ya msaada hiyo yote ni kwa sababu hatuijui jiogafia ya nchi yetu. Hili jambo ni muhimu sana na ninyi mnaogawa pembejeo lazima mjue kwamba mkoa fulani unahitaji pembejeo aina fulani tarehe ipi na kwa msimu upi, hilo nilikuwa natoa angalizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vile vile naomba nijielekeze kwenye Bodi ya Mazao Mchanganyiko. Bodi ya Mazao Mchanganyiko ni tatizo, na bodi hii lengo lake lilikuwa ni kuimarisha hayo mazao lakini imekuwa kinyume chake. Nitoe mfano zao la ufuta; sisi Kusini sasa hivi zao la ufuta linakwenda sambamba na zao la korosho, lakini sasa hivi baada ya kuona zao la korosho limefanya vizuri kwenye stakabadhi ghalani tukafikiria ufuta sasa tuuingize kwenye stakabadhi ghalani. Sasa tunauingizaje wakati bodi yenyewe inayoshughulikia mazao mchanganyiko bado haijawa sawasawa? Hakuna sera yoyote ambayo inaelekeza namna ya kutafuta masoko ya hii zao la ufuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Mkoa wa Lindi zao la ufuta ukiondoa korosho linashika nafasi ya pili kiuchumi, lakini tatizo letu kubwa la zao la ufuta ni soko. Hapo naomba nitoe angalizo lingine, kwamba hawa jamaa zetu wa vyama vya ushirika, nimeona kwenye page fulani hapa wamesema kwamba kazi mojawapo ni kufanya utafiti wa masoko. Vyama vya Ushirika hawawezi kufanya kazi ya utafiti wa masoko. Vyama vya Ushirika shida yao kwamba kwanza hawataki ushindani wanataka mtu mmoja a-monoply soko ili na wao wapate. Unapotokea ushindani wa kibiashara kama vile ilivyotokea kwenye korosho mwaka huu wao kwa upande wao ni hasara kwa sababu hawakupata mnunuzi wa pamoja ambaye anaweza akawapa chochote. Kwa hiyo, tukiwaachia Vyama vya Msingi wafanye utafiti wa masoko hapa tutakuwa tunajidanganya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nimesoma ukurasa wa 31 kwenye vipaumbele vya Wizara ya Kilimo. Wametaja vipaumbele kama tisa hivi pale na kimojawapo wamesema kwamba kuwawezesha vijana kushiriki kwenye kilimo, wanashiriki vipi? Nimejaribu kupitia sasa mikakati yenyewe iliyopo baada ya kuorodhesha vile vipaumbele, nikaangalia sasa mikati iliyopo kuiendea vipaumbele, maskini, sijaona chochote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nafikiri kwamba kuweka vipaumbele bila kuwekea mikakati kwamba tunataka tuingize vijana kwenye kilimo, kilimo cha aina gani? Hiki kilimo cha jembe la mkono ambalo Mheshimiwa Waziri wa kwanza wa Wizara hii alisema anataka kuliweka hili jembe la mkono makumbusho, lakini nalo hatuoni mikakati yake? Sasa naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja hebu ajaribu kutuainishia hivi vipaumbele tisa alivyovirodhesha hapa mikakati yako ni ipi kuviendea hivi vipaumbele?

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kwenye kuongeza thamani ya mazao. Hapa kwenye uongezaji thamani ya mazao nimeona kwenye ukurasa wa 37 amesema sijui bodi inakusudia kuleta mashine 14. Hata hivyo, Mikoa ya Lindi na Mtwara sifuri, sasa sielewi sisi kule Mikoa ya Lindi na Mtwara hatutakiwi kuongeza thamani ya mazao yetu au ndio kwa sababu sisi tuko Kusini kama inavyosemwa siku zote? Mimi sijaelewa, kwa sababu hata mashine za kuongeza thamani zilizotajwa hapa kwetu majanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vile vile kwenye hii sekta ya kuongeza thamani wamesema tutashirikisha watu binafsi, lakini kwenye kushirikisha watu binafsi kuna matatizo huko; hatupati wawekezaji kwenye watu binafsi kwa sababu tumeongeza kodi zimekuwa nyingi mno. Ukianzisha hiyo kampuni OSHA atakuja hapo BRELA, sijui nani sijui TBS sijui TFDA, wote wanafanya kazi moja hiyo hiyo. Sasa huyu mwekezaji atakayekuja kuwekeza hiyo faida anaipata wapi? Ndiyo maana hata hapa Waheshimiwa Wabunge wengi wanachangia kwa kusema kwamba, bidhaa zetu zinashindwa kuuzika, zinashindwa kuingia kwenye soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bidhaa zetu zinashindwa kuingia kwenye soko kwa sababu bidhaa zake ziko juu, gharama ya uzalishaji iko juu. Ndiyo maana utakuta dawa ya mswaki leo ikitoka Nairobi inauzwa bei rahisi kuliko inayozalishwa hapa kwa sababu hapa kodi zimekuwa nyingi mno. Hebu jaribu kama Serikali kuna ile wanaita collective responsibility, nafikiri Wizara zote wakae pamoja waangalie tatizo letu liko wapi? Kwa nini bidhaa zetu zinashindwa kuingia kwenye soko?

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile naomba niongelee suala la maghala. Ukiingia ukurasa 36 pametajwa maghala pale panatakiwa kujengwa maghala. Hata hivyo, ukiangalia kwenye Mkoa wa Lindi na Mtwara hakuna ghala hata moja. Yaani Mikoa ya Lindi na Mtwara ni kama vile haipo nchi hii, maana kila sekta wanayoitaja nikipekua hivyo vitabu sioni wapi wameandika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la zao la ufuta. Ununuzi wa zao la ufuta naomba, mwaka huu ilikuwa tuuingize kwenye stakabadhi ghalani lakini tumekwama kwa sababu ya bodi kama nilivyosema. Kwa hiyo, naomba ikiwezekana zao la ufuta mtengenezee bodi yake kwa sababu ni zao ambalo sasa hivi limeshapata umaarufu mkubwa linaiingizia pesa nyingi nchi hii. Kwa hiyo kama ambavyo kuna Bodi ya Korosho basi hilo zao la ufuta waliondoe kwenye mazao mchanganyiko na walitengenezee bodi yake ili na sisi tunaweza kunufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba niongelee zao la ngano. Tanzania tunasindika ngano inayofika tani kama 1,500,000 hivi kwa mwaka, lakini katika hizi tani 1,500,000 Tanzania tuna kama 0.05 percent, ndiyo ngano ya kwetu. Sielewi sera ya nchi yetu hii ni nini? Kwa sababu sasa hivi ukiondoa mchele na mahindi, ngano inaongoza kwa ulaji lakini sioni mkakati wa Wizara wa kuimarisha hili zao ukiondoa tu kwamba linazidi tu kutupotezea pesa zetu za nje. Kwa hiyo, naomba tuone mkakati wa kufufua mashamba ya NAFCO ili na sisi tuweze kunufaika na sekta hii ya viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kuna ukurasa 37 kupitia mradi wa policy and human resource development. Nimeona hapa wamesema kwamba watajenga maghala lakini kama nilivyotangulia kusema, kwamba na sisi wa Mikoa ya Lindi na Mtwara na sisi tunazalisha mazao na tunaomba maghala hayo nasi kule tuwe nayo. Mwaka wa jana tumepata shida sana ya maghala ya korosho, matokeo yake tukapata shida na usafirishaji nao ambapo barabara zetu kama mnavyofahamu ni mbovu. Kwa hiyo, nawaomba sana wanapopanga mikakati yenu, wanaopanga vipaumbele vyenu wajue kwamba Mkoa wa Lindi na Mtwara nako kuna watu nako kuna uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitolee mfano wa zao la viazi. Viazi Mkoa wa Lindi tunapeleka mpaka nchi za nje lakini viazi Mkoa wa Lindi mimi kule kwetu Liwale kiroba kimoja cha viazi ni Sh.10,000/= lakini ukifika Dar es Salaam kiroba kile kile unakuta kinauzwa zaidi ya Sh.100,000/=; hivi hamwoni hii hasara wanayoipata wakulima wa Mkoa wa Lindi na Mtwara?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kabisa, hii yote ni kutokana na shida ya usafiri tuliyonayo katika Mkoa wa Lindi na Mtwara hasa Wilaya ya Liwale, ndiyo maana nikasema kwa umoja wenu kama Serikali kwa collective responsibility wakae kwa pamoja waangalie ni wapi kunapatikana mazao gani na yatafikaje kwenye soko, hatimaye waone kwamba watu wale wananufaika na nchi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa leo nilikuwa sina mengi, naomba tuu nishie hapo ujumbe umefika.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi mchana huu wa leo na mimi nichangie kwenye hoja iliyo mbele yetu.

Awali ya yote kama ilivyo ada na mimi nitoe shukrani zangu za dhati kwa wahudumu wanaohudumu kwenye Wizara hii hasa Mawaziri, lakini siyo Mawaziri peke yao kwa sababu hizi sifa ambazo Mawaziri wanazipata ni kwa sababu ya wale wanaowa-support. Kwa hiyo, nao wanastahili sifa nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli Wizara hii wanaitendea haki, nami nawaombea kwa Mwenyezi Mungu waendelee kuifanya hii kazi kama ambavyo Mwenyezi Mungu atawajalia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba tu Serikali ya Awamu ya Tano, mara zote ninapoanza kuchangia pengine naweza kuonekana kama mlalamishi, lakini ni lazima ukweli usemwe. Nini Kanda ya Kusini tunaikosea nchi hii? Kwa sababu kila ninaposimama kwenye bajeti, ukiangalia Kanda ya Kusini inavyotendewa na kanda nyingine ni tofauti. Kwa nini nasema hivyo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Kanda ya Kusini hatuna Hospitali ya Kanda ya Kusini, lakini kuna Kanda nyingine tayari zina Hospitali za Kanda. Kanda ya Kusini ukiangalia kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri, pesa iliyotengwa haina tofauti na pesa ambazo zimetengwa kwenye Hospitali za Wilaya nyingine, kwenye sehemu nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Kanda ya Kusini tumetengewa shilingi bilioni moja, lakini iko mikoa au wilaya zimetengwa zaidi ya shilingi bilioni mbili mpaka shilingi bilioni nne kwenye Hospitali za Mikoa. Kwa nini Kanda ya Kusini mnatusahau kwa kiwango hicho? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ukiangalia hospitali yetu ya kanda yenyewe kwanza haipo na wanasema ile Hospitali ya Ligula ndiyo ambayo wanaiandaa kuwa Hospitali ya Kanda, lakini hizi shilingi bilioni moja kwanza hatuna uhakika kama zitafika. Tunaomba Serikali ya Awamu ya Tano mwiangalie Kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mzuri tu, maana nikisema lazima nitoe mifano. Kuna huu Mkoa wa Geita umetengewa zaidi ya shilingi bilioni nne, lakini Mkoa wa Geita uko Kanda ya Ziwa. Kanda ya Ziwa wana Bugando, Kanda ya Kaskazini wana KCMC; sisi Kanda ya Kusini hatuna Hospitali ya Kanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sana Mheshimiwa Waziri unayehudumu kwenye hii Wizara uiangalie sana Kanda ya Kusini. Sasa naomba nirejee kwenye nafasi ya utumishi.

T A A R I F A . . .

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naipokea taarifa hii hundred percent. Nafikiri hata mimi nili-overlook tu pale. Kwa hiyo, Geita ni shilingi bilioni tano. Kanda ya Kusini shilingi bilioni moja.

T A A R I F A . . .

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, hapana. Taarifa hii haiwezi kupokelewa kwa sababu mimi nimetoa mfano. Ningeweza kutoa mfano mkoa wowote ule, lakini kwa sababu Mkoa wa Geita ni Mkoa wa watani zangu, ni watoto wangu na wajukuu zangu, nikautolea mfano huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naongelea suala la wahudumu. Suala hili naweza kuliona kama ni janga la kitaifa kwa sababu tatizo hili ni kubwa sana. Pamoja na juhudi kubwa ya Serikali ya kujenga miundombinu ya afya, lakini kama hatujaliangalia suala la watumishi, itakuwa hizi juhudi zote tunazozifanya haziwezi kutuzalia matunda yaliyotegemewa. Kwa mfano, nataka niwaambie kwamba jambo hili kwanza linaweza likapunguza hata ufanisi wa wale watumishi wachache na vilevile kuweza kuwaletea madhara mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano kuna hospitali moja, nurse mmoja alipigwa makofi na mgonjwa. Sababu ilikuwa ni nini? Yule nurse alikuwa peke yake kwenye wodi, kuna akina mama wawili wanajifungua, mmoja akajifungua mapema kuliko yule mwingine. Wakati anamhudumia yule mama, hajamaliza hata kufunga kitovu, yule mama mwingine na mtoto ameshatoka anataka kudondoka. Sasa yule nurse alichokifanya, kuogopa yule mtoto asije akadondoka akafa, mama akapoteza mtoto, aliamua kumwacha yule mwingine kabla hajamfunga kitovu akamhudumia yule mwingine bila kubadilisha gloves. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa yule mama kwa sababu aliona kile kitendo cha kumpokelea mwanae mama ambaye hajabadilisha gloves zenye damu za mama mwingine kwa kuogopa maambukizi ya UKIMWI, akamzaba makofi. Hata hivyo yule nurse alikuwa na mambo mawili ya kuamua, amwache mtoto aanguke afe au ampokee mtoto apate maambukizi aweze kutibiwa. Kwa hiyo, hili suala tunaweza kuliona dogo, lakini ni kubwa sana. Uhaba wa ma-nurse na madaktari ni mkubwa sana. (Makofi)

Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri ulichukulie katika muktadha huo kwamba hili jambo ni la muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nilitaka niongelee kwenye hospitali yangu ya Wilaya ya Liwale. Hospitali ya Wilaya ya Liwale ina wodi tano kama juzi nilivyosema. Wodi moja ya wazazi, moja ya wanaume na nyingine ya watoto. Pia kuna wodi mbili za grade II, lakini kwa night shift panaingia nurse mmoja tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hebu just imagine nurse mmoja anahudumia wodi tano, ufanisi wake utakuwa wapi? Siyo kwamba anakwenda night atapata off, hakuna off kwa sababu ya uhaba wa watumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, niko chini ya miguu yake aiangalie Hospitali ya Wilaya ya Liwale, hali ni mbaya sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naomba nijielekeze kwenye upande wa lishe. Na mimi nitoe utaalam wangu kidogo, ni-declare interest, mimi ni msindikaji wa nafaka kwa taaluma. Tanzania hatuna Sera ya Ulaji na ndiyo maana ulaji wetu unakuwa wa hovyo hovyo na ndiyo maana tunapata magonjwa hayo yasiyoambukiza na mengine yanayoambukiza kama vile kisukari, kwa sababu tunakula hovyo hovyo. Nitolee mfano kwenye nafaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, National Milling wakati ule tunasindika nafaka tulikuwa tunakoboa mahindi asilimia 80, tunatoa unga kwa asilimia 80, lakini leo hii Tanzania tunatoa kwenye hizi coat meal tunatoa asilimia 55 mpaka 60. Maana yake ni nini? Tunakoboa mpaka vitamini zote tunaziondoa, baadaye sasa tukirejea kwenye mahospitali, mtu akipata sukari akienda hospitali ndiyo anaenda kuambwa kwamba ukale dona.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini Serikali isiweke sera tukajua kwamba standard ya sembe ni standard inayokobolewa kwa kiwango gani au mchele, unakobolewa, unapigwa polish mpaka unakuwa mweupe unapoteza kila kitu. Kwa nini Tanzania hatuna sera? Ukienda kwa wenzetu hapo Nairobi maximum rate percent kwamba kukoboa ngano, kwanza tunapoteza nafaka. Kwa mfano, kama asilimia 60 ndiyo flour ambayo inatumika, ina maana asilimia 40 zote unawaachia mifugo. Sasa hata nafaka yenyewe tunapunguza. Ina maana kwamba hata njaa nayo tunaiendekeza sisi wenyewe kwa sababu ya ulaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tukiingia kwenye suala hili la lishe, naomba Serikali waje na sera, ijulikane standard ya ulaji kwamba chakula gani kinaliwa kwenye standard gani na TBS wawe wanafuatilia hizi standard ili kuhakikisha watu wetu wananufaika na masuala haya ya lishe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naomba niongelee kwenye hii Taasisi ya JK na ya MOI. Ukiangalia kwenye jedwali hapa, kamati walishasema hapa kwamba mwaka 2017 wametengewa fedha lakini zilizoenda ni zero. Kwenye Taasisi ya JK ni zero, kwenye Taasisi hii ya MOI ni zero. Sasa pamoja na sifa kubwa, Mheshimiwa Rais juzi alikwenda kwenye Taasisi akawasifia, lakini kwa trend hii ya kutowapelekea pesa mnataka wafanye nini? Kwa nini basi tunatenga hizi fedha wakati hamko tayari kuzipeleka?

Mheshimiwa Naibu Spika, hili jambo nalisema kwenye Wizara hii, lakini linahusu sana Wizara ya Fedha. Kwa sababu Kamati zote zinazokuja mbele yetu hapa, malalamiko makubwa kwenye fedha za maendeleo haziendi. Sasa Taifa gani hili ambalo tunataka kulijenga kwamba tunakusanya pesa kwa ajili ya kulipa mishahara tu, lakini hatutengi fedha za maendeleo? Tunakusudia nini? Hivi tunataka kujenga Taifa la namna gani? Kwa sababu kila Wizara itakayokuja hapa, kila Mwenyekiti anayekuja hapa anasema fedha za maendeleo haziendi.

Mheshimiwa Naibu Spika, afya, fedha za maendeleo haziendi; Taasisi hizi, fedha ya maendeleo haiendi. Sasa ina maana pamoja na kujinasibu kwamba Serikali ya Awamu ya Tano makusanyo yamepanda, hivi tunakusanya kwa ajili ya kulipa mishahara? Kama hatutaki kuwekeza kwenye hizi taasisi kwa kutoa fedha za maendeleo, sidhani kama tunaweza tukafanya kile tunachokusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naomba niende kwenye sera za wazee. Hapa tumeshaweka sheria nyingi sana; kuna dirisha la wazee, sijui kufanyaje wazee, kuna matibabu sugu ya wazee, lakini hawa wazee ni wapi? Kwa sababu hatujapata sheria hapa inayowatambua wazee. Ikiletwa sheria hapa, itaweza kuainisha hawa wazee tunaowakusudia ni wazee wa namna gani?

Mheshimiwa Waziri, kila mwaka tunakuomba utuletee sera hii ya wazee ili hawa wazee tuweze kuwatambua.

Nini tatizo? Kigugumizi ni cha nini cha kuwaletea sheria hawa wazee ili watambuliwe? Mpaka leo hii tunaongelea wazee, lakini wazee wenyewe tunaowaambia tunawatengea madirisha, tunawatibu bure, bado hatujawatambua kwa mujibu wa sheria ni wazee wa aina gani?
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hoja za Kamati zote mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nishukuru na kuwapongeza Wenyeviti wa Kamati, ama kweli ripoti hii wameitendea haki. Vilevile nichukue nafasi hii kumpongeza jemedari wetu, Rais wetu mpendwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa namna anavyoiongoza nchi na kwa namna anavyoonesha mwelekeo, wapi tunataka kwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivyo; lazima niweke kumbukumbu sawasawa, lazima tukumbuke kwamba, mimi sio mtu wa kuweza kunukuu vifungu vya Biblia au Quran lakini zipo sehemu ambazo watu wanasema, kwamba mdomo unaumba, lakini sio hivyo tu, kuna kauli nyingine unaambiwa kwamba sauti ya wengi ni sauti ya Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais Dkt. John Joseph Pombe Magufuli ni zao la dua za Watanzania. Sikuwepo kwenye Bunge lililopita lakini nilikuwa nasikiliza ni namna gani Wabunge walivyokuwa wanaomba kwamba tunataka Rais mwenye msimamo, tunataka Rais anayekwenda kusimamia rasilimali za Taifa hili. Kwa sababu Mwenyezi Mungu anasikia, kilio cha wengi ni kilio cha Mungu, ndiyo akatupatia zawadi tukapata Rais ambaye sasa ni kweli anakwenda kuyatekeleza hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wale ndugu zangu wanaobeza ni kwa sababu ya ubinadamu, kwamba binadamu ameumbwa ni mtu mwenye kusahau. Wameshasahau kwamba wao ndio waliopendelea wakamwomba Mwenyezi Mungu tupate Rais wa namna hiyo, kwa hiyo nilikuwa naweka kumbukumbu sawasawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Wabunge tukumbuke moja ya majukumu yetu ni kutunga sheria. Sasa naomba nitoe ushauri kwa Wabunge; tunapokwenda kutunga sheria lazima tuwe makini kuhakikisha sheria hizi zinakwenda kufanya kazi ile ambayo tumeikusudia, lakini tunapokwenda kufanya kazi hii kwa kulipua matokeo yake tunakuwa wa kwanza kulalamika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimewahi kusikia hapa kuna mchangiaji mmoja alikuwa analalamikia Sheria ya Korosho, kwamba kuna Mkuu wa Wilaya amewakamata watu wanatoa korosho kutoka Msumbiji kuleta Tanzania, lakini wanasahau kwamba kosa lile sisi ndio tumelifanya kwa sababu kwenye Sheria yetu ya korosho ukiangalia tunakataza korosho kutoka nje kuingia Tanzania na sio korosho tu, kuna mazao mbalimbali tumekataza kwenye sheria zetu, kwamba hakuna mtu anayeruhusiwa kutoa mazao nje ya nchi yetu kuyaleta Tanzania. Sasa hawa watekelezaji wanakwenda kutekeleza hizi sharia, bado kwenye Bunge hilihili sisi tunaona kwamba wale wanafanya makosa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tena kuna Mbunge mmoja alikuja akasema kwamba hii ni shame, ni jambo la aibu, kwamba eti kwa nini Msumbiji wanataka kuleta korosho, kuinua uchumi wetu, tuongeze pato letu tunawakataza, lakini anasahau kazi hiyo ameifanya yeye hapa Bungeni na ndiye aliyelipitisha jambo hili. Kwa hiyo, nawaomba Waheshimiwa Wabunge tunapoifanya kazi hii tuifanye kwa umakini, tujue kwamba sisi ni wawakilishi wa wananchi na makosa haya mara nyingi yanafanywa na sisi wenyewe. Kwa hiyo hilo ndilo jambo ambalo nimeona kwamba niweze kulisemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nirejee kwenye utunzi wa sheria. Naomba kuanza na sheria ndogo, Mheshimiwa Mwenyekiti ametoa mapendekezo hapa na ametaja kasoro mbalimbali zinazotokana na utunzi wa sheria ndogo. Kuhusu jambo hili naomba niishauri Serikali, hapa tunasema hizi sheria ndogo, lakini sheria hizi ndizo ambazo ziko karibu na wananchi wetu, ndiko ambako wanakwenda kuzi-practice hizi sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninachoomba kwa Serikali ni lazima tuhakikishe kwamba, hawa Wanasheria tunaowapeleka kwenye halmashauri zetu ni Wanasheria waliobobea katika fani hii ya sheria. Vinginevyo tunapoacha kupeleka Wanasheria waliobobea kwenye halmashauri zetu tunakwenda kuziangusha halmashauri zetu na ndiyo maana tunapata hizi kasoro ambazo zinaletwa kwenye marekebisho ya sheria ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, si hivyo tu, kuna matatizo mengi sana kwenye halmashauri, kuna kesi nyingi sana kwenye halmashauri ambazo halmashauri zinashindwa kwa sababu tu hatuna Wanasheria wenye weledi, hatuna Wanasheria waliobobea na matokeo yake tunashindwa kwenye kesi mbalimbali matokeo yake halmashauri zetu zinaingia kwenye madeni mbalimbali, kulipa fidia na kulipa faini mbalimbali. Hii yote ni kutokana na uchache au weledi wa Wanasheria wetu. Kwa hiyo hapa mimi naishauri Serikali kuimarisha kitengo hiki cha sheria kwenye halmashauri zetu ili tuepukane na hizi adha ambazo tunaweza kuzipata kwenye halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nataka nichangie kuhusiana na uhaba wa upatikanaji wa huduma ya sheria hasa kwenye ujenzi wa Mahakama. Halmashauri zetu nyingi hazina Mahakama; kwa mfano Halmashauri yangu ya Wilaya ya Liwale ni halmashauri ambayo iko tangu mwaka 1975, lakini leo naongea 2019 hatuna jengo la Mahakama ya Wilaya. Si hivyo tu, Wilaya ya Liwale kwa mfano ina tarafa zaidi ya tatu na kata zaidi ya 20, lakini mpaka leo naongea kwenye Bunge hili tuna Mahakama moja tu ya mwanzo; hatuna Mahakama nyingine ya Mwanzo; na hiyo Mahakama yenyewe ya mwanzo ni Mahakama ambayo ilijengwa na wananchi; lakini mpaka leo liko tu jengo la tope na Mhudumu yuko mmoja tu, Hakimu ambaye ndiye Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hapa naweza kuishauri Serikali, kwamba ili tuweze kwenda na wakati na mnajua dunia sasa hivi dunia hii ni kama kijiji; kwa hiyo uhitaji wa Mahakama ni mkubwa sana. Kwa hiyo, naishauri Serikali ipanue hii huduma ya Mahakama ili tuweze kutoa huduma kwa wananchi wetu. Hili jambo ni la muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo kwenye Mahakama za Mwanzo; Mahakama nyingi za Mwanzo zina uhaba mkubwa sana wa wafanyakazi, hasa Mahakimu. Si hivyo tu, kwa sababu ya uchache tulionao kwenye Mahakama imepelekea sasa kuwe na vitendo vingi vya rushwa, ili mtu kesi yake labda iishe mapema, inabidi atoe rushwa. Si hivyo tu, ule upeke kwanza exceptionalist wa mtoa huduma ambaye yuko pale na kesi zile zilikuwa ni nyingi. Kwa hiyo inakuwa ni miongoni mwa vivutio vya kuweza kuendeleza hii rushwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naiomba Serikali, kuna sera inahusu wazee. Ukiingia kwenye huduma mbalimbali unakuta kuna mahali pameandikwa wazee kwanza, mpishe mzee, fanya hivi, lakini ukiangalia kwenye Bunge hili hatujawahi kutunga sheria inayohusu wazee. Hawa wazee ambao wanambiwa wapishwe labda wawahi wazee ni wazee wa aina ipi? Sheria haijawatambua wazee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naishauri Serikali kwamba itulee sheria ya wazee ili hawa wazee ambao tunawaongelea siku zote tuweze kuwatambua, na tukiweza kuwatambua ndipo tutaweza kuwatendea haki. Vilevile tukumbuke sisi wote humu ndani ni wazee watarajiwa. Kwa hiyo naomba niishauri Serikali sikivu ya Chama cha Mapinduzi, ilete hii Sheria ya Wazee ili hawa wazee waweze kutambuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, naomba niishauri Wizara ya Sheria na Katiba. Kumekuwa na tatizo kubwa sana la ucheleweshwaji wa kesi Mahakamani. Jambo hili linakuwa linaongeza sana mlundikano wa mahabusu kwenye magereza zetu. Kwa hiyo naiomba sana Serikali iongeze bidii ili wananchi hawa watendewe haki yao; kwa sababu haki iliyocheweshwa ni sawa kabisa na mtu aliyeikosa haki hiyo. Kwa hiyo naiomba Serikali iongeze watumishi kwenye Idara za Mahakama na vilevile kuongeza ofisi kwenye idara hizi za mahakama ili kesi mbalimbali ziweze kwenda kwa wakati na ziweze kwisha kwa wakati ili kupunguza mlundikano kwenye magereza yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye huo huo utunzi wa sheria; mara nyingi nimeona Serikali ikileta sheria hapa ili zifanyiwe marekebisho; zile ambazo zimepitwa na wakati. Kwa mfano unakuta sheria inataja labla mtu akifanya offence fulani atapata adhabu ya kulipa 2,000 au 5,000. Hizi ni sheria ambapo zimepitwa na wakati. Kwa hiyo Serikali wamekuwa wakizileta hizi sheria hapa kuzifanyia amendment ili kuongeza hivi viwango kulingana na wakati tulionao. Hata hivyo bado tunasahau kuzifanyia marekebisho zile sheria ambazo zitawasaidia wananchi wetu. Mathalani kuna sheria inasema kwamba mwananchi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami jioni ya leo niweze kuchangia hotuba iliyo mbele yetu. Awali ya yote niseme namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai wa kuweza kusimama jioni hii na kutoa mchango wangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, bila kuchelea nataka nitoe vilevile pongezi zangu za dhati kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wateule wote kwa kazi nzuri inayofanywa na vilevile niwaombee dua kwa Mwenyezi Mungu awape umri mrefu ili waweze kuitumikia nchi yetu twende kule ambako Tanzania inataka kwenda.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nianze na kwa nini watu kila wakisimama hapa wanamsifia sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa kweli kama kuna mtu anachelea kumsifia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anafanya dhambi. Yapo mambo ambayo Mheshimiwa huyu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yanafanywa katika nchi hii hayakutegemewa kwa miaka mingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata mimi nilivyokuwa upande wa pili alivyokuwa anaanzisha hii miradi mikubwa nilikuwa na wasiwasi hizi fedha zitapatikana wapi lakini kitu cha ajabu kilichotokea sasa hivi, tuna miradi mikubwa mingi inayofanywa na inafanywa kwa pesa zetu. Kama miradi hii ingeweza kutekelezwa kwenye awamu zilizopita leo Tanzania tusingekuwa hapa tulipo. Sasa kwa nini huyu mtu ambaye ana maono ya namna hii tusimpe sifa, tusimtie moyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna miradi, kwa mfano kuna kuna huo mradi wa Stiegler’s Gorge, kuna ununuzi wa ndege, kuna ujenzi wa reli (SGR), kuna ujenzi wa viwanja vya ndege, tunajenga hospitali wilayani, tunajenga vituo vya afya kwenye kata zetu. Nani ambaye anaweza akasimama kwenye Bunge hili ambaye kwenye wilaya yake hakuna kituo cha afya kinachojengwa? Kwa spidi hii ya ujenzi wa vituo vya afya kama huko miaka ya nyuma tungekuwa tunajenga namna hii, kwa spidi hii leo hii kuna kata ambayo ingebaki haina kituo cha afya?

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunapokwenda namna hii, tunajenga flyover, Dar es Salaam sasa hivi kunakwenda kujengwa flyovers zaidi ya tatu. Jamani, kwa nini tuache kusifia? Ni lazima tutasifia, ni lazima tutam-support na lazima tutamwombea dua Mwenyezi Mungu ampe umri mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, dhana ya Mheshimiwa Rais kutokutoka nje ya nchi hii sasa tunakwenda kuona faida yake. Kwa nini Mheshimiwa Rais alikuwa amesema kwamba hataki kusafiri nchi za nje; yuko tayari kulinda rasilimali za nchi hii ili ziweze kuwanufaisha watu wote na ulinzi wa rasilimali za nchi hii tumeuona kwa sababu katika hali ya kawaida watu walikuwa wanasema kwamba Mheshimiwa Rais hasafiri, tutapataje misaada? Yuko ndani na tunafanya mambo yetu, big up sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nichangie kwenye uwekezaji; kwenye uwekezaji nchi yetu inafanya vizuri, ni kwa sababu kubwa mbili. Kwanza ni kwa ajili ya amani yetu tuliyonayo na usalama, wawekezaji wanahakikishiwa usalama, kwa sababu wanakuwa salama na amani, mali zao zitakuwa salama. Hata hivyo, tunapwaya upande mmoja kwenye uwekezaji, Mheshimiwa Waziri wa Uwekezaji naomba anisikilize hapo; bado tuna tatizo la njoo kesho, njoo keshokutwa, hapa ndipo tunapokwama. Leo hii mwekezaji, nitoe mfano mmoja, jana nimemsikia Mheshimiwa Rais akiwa Mtwara, kuna mwekezaji mmoja pale amewekeza kiwanda, transfoma za umeme kanunua mwenyewe, amekwenda Idara ya Maji wanamwambia atoe milioni 100 wamletee maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa msingi huu hata kama tuna sifa nzuri kwamba bwana Tanzania ukiwekeza mali zako zitakuwa salama, ni nchi yenye utulivu, lakini bado akija ndani hapa anakutana na vikwazo vya njoo kesho, njoo keshokutwa, hili Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana naomba aliangalie kwa makini sana, bado kuna watu kwenye ofisi yake wana tabia ya njoo kesho, njoo keshokutwa. Inawezekana haohao ndio wapinzani wa Mheshimiwa Rais, kwa sababu haiwezekani mpaka leo hii kuna mteule wa Rais hajui mwelekeo wa nchi inapokwenda, hajui Mheshimiwa Rais anataka nini. Wapo watu wanashindwa kufanya maamuzi, wanashindwa kujua kwamba wamewekwa pale kwa sababu gani; Mheshimiwa Waziri naomba alichukue hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nielekee kwenye kilimo; kwenye kilimo kuna matatizo makubwa mawili, kwanza upatikanaji wa pembejeo kwa wakati na masoko. Suala la pembejeo kwangu mimi linachukua nafasi ya pili ukilinganisha na suala la masoko. Tunalo tatizo kubwa sana la wakulima wetu wanahangaika na masoko na ndiyo maana sasa hivi wakulima wanabadilisha mazao kila mwaka. Mwaka juzi korosho Kusini zimefanya vizuri, watu wameacha kulima mpunga, wameacha kulima mazao mengine wamekwenda Kusini kulima korosho, mwaka huu korosho zimeyumba bado wakulima wetu wanahangaika. Kwa hiyo, naomba kwenye upande wa kilimo tujikite sana kwenye kutafuta masoko.

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kwenye upande wa maliasili; upande huu naiomba sana Serikali ije na marekebisho ya Sheria ya Kifuta Machozi. Sisi tunaopakana na hifadhi tunapata shida sana mazao yetu kuliwa na wanyama, lakini hakuna sheria ambayo mkulima yule anapata fidia, kuna Sheria ile ya Kifuta Machozi. Naomba Serikali ije na marekebisho ya sheria, angalau sasa tuanze kufikiria kuwafidia wale ambao mazao yao yataliwa na wanyama wakali.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la umeme, REA; upande wa REA hapa hatujafanya vizuri. Ipo mikoa ambayo imefanya vizuri, ile tu ambayo imepata wakandarasi wanaojielewa, lakini kuna mikoa mingine ambayo imepata wakandarasi wa hovyo, mikoa ile bado REA haijafanya vizuri. Sielewi ni kwa sababu gani, Serikali ilikuwa na vigezo gani mkandarasi mmoja anapewa mikoa zaidi ya mitatu, matokeo yake anafanya mkoa mmoja mingine anasahau. Kwa hiyo, naomba Serikali iangalie upya suala la REA. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano katika Wilaya yangu ya Liwale, katika REA awamu ya tatu, Sehemu ya Kwanza ambayo ilikuwa na vijiji 14 mpaka leo kumewashwa vijiji viwili tu na mkandarasi yule amepotea. Tena kibaya zaidi mkandarasi yule anatuchonganisha sisi na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa sababu tangu alipopewa Mkoa wa Lindi, alikwenda Ruangwa akamaliza alipomaliza vijiji vya Ruangwa amekimbia. Sasa sijui kama aliambiwa kwamba Mkoa wa Lindi una wilaya moja, hatujui. Kwa hiyo naomba sana, suala la REA hawa wakandarasi waangaliwe upya, wale wakandarasi ambao wanaonekana kabisa wanaikwamisha Serikali kufikisha malengo yake waondolewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwamba, asilimia kubwa sisi tunazungukwa na hifadhi, lakini vilevile kuna Sheria ya Misitu. Naiomba sana Serikali, hebu twende turekebishe Sheria ya Misitu, asilimia tano kwa uvunaji wa mazao ya misitu inayopata halmashauri ni fedha ndogo sana ambazo hazilingani na jangwa au na uharibifu mkubwa wa misitu unaofanywa kwenye halmashauri zile.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna fedha ambayo imetengwa kwa ajili ya kupanda miti, kwamba baada ya uvunaji wa miti panakuwa na fedha zimetengwa, asilimia mbili, kitu kama hicho kwa ajili ya kupanda miti, mimi kwenye Halmashauri yangu ya Liwale sijawahi kuona kijiji hata kimoja kimepanda miti zaidi ya kukuta kwenye shule tu, ile miti ambayo inapandwa kwenye bustani za shule. Kwa hiyo, naomba kifungu hiki sasa kiondolewe kipelekwe kwenye halmashauri, ile asilimia inayokwenda hamashauri ifike angalau asilimia 10.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala hili la wazee, leo ni mara ya tatu naliongelea suala hili. Wazee wanatamkwa sana, ukienda kwenye hospitali zetu utakuta kuna labels zimeandikwa pisha wazee, watangulize wazee, lakini bado Serikali haijatuletea sheria ya kuwatambua hawa wazee, hawa wazee tunaokwenda kuwakusudia ni wazee wa aina gani. Ni bora sasa Serikali ikaharakisha mchakato wa kuleta sheria ambayo sasa hawa wazee tunaokwenda kuwatungia sheria wanatambulika.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nijielekeze kwenye suala la elimu maana mimi nadondosha sehemu mojamoja tu. Suala la elimu; suala hili bado hatujafanya vizuri. Tumefanya vizuri kwa kufanikiwa kupeleka watoto wengi shuleni, hili jambo tumefanya vizuri, lakini kwenye ubora wa elimu bado tuna tatizo. Tunacho kitengo chenye kazi ya kukagua, wanaita Kitengo cha Ukaguzi wa Ubora wa Elimu, kile kitengo hakina vitendeakazi, hata magari hawana, mafuta hawana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeweza kufanya ziara, unakwenda kwenye shule unauliza shule hii imekaguliwa kwa mara ya mwisho lini, watakwambia ni miaka miwili, miaka mitatu shule haijakaguliwa. Jambo hili ni jambo ambalo linatakiwa litiliwe maanani, kwamba hiki Kitengo cha Ukaguzi wa Ubora wa Elimu sasa ni wakati kinatakiwa kijengewe uwezo kupewa magari na fedha za mafuta ili kuweza kukagua maeneo yetu haya na hapo ndipo elimu yetu itakapoweza kufanya vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sio ukaguzi peke yake, bado tumuangalie Mwalimu. Jambo kubwa kwenye elimu, mtu wa kwanza kumwangalia ni Mwalimu; je, Serikali imeshafanya tathmini kwamba madeni ya Walimu yamefikia kiwango gani, mpaka leo hii ni walimu wangapi wanaidai Serikali na mpaka leo hii kiasi gani walimu hawa wanadai? Wengine wanadai likizo, wengine wanadai kupandishwa vyeo, wengine madaraja, bado kuna tatizo kubwa kwa upande wa walimu. Kama tukiamua kucheza na walimu maana yake tunakwenda kucheza na elimu. Mimi jambo hili kwa upande wa elimu naomba sana kwamba litiliwe mkazo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho, naiomba Serikali ifanye tathmini kuangalia majengo au mahitaji ya wilaya, kata na vijiji vyetu. Kwa sababu Mheshimiwa Rais amesema hana mpango wa kuongeza sehemu za tawala kwa maana kwamba hawezi kuongeza wilaya, mkoa, kata wala tarafa ni mpaka mahitaji kwenye maeneo hayo yamekamilika. Je, Serikali imeshafanya utafiti?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Halmashauri au Wilaya yangu ya Liwale haina jengo la mahakama, jengo la polisi, Hospitali ya Wilaya wala nyumba ya Mkuu wa Wilaya na ina miaka 43. Kwa hiyo, ni lazima Serikali ije na mpango na takwimu ijue kuna wilaya ngapi zimekosa majengo ambayo yanaitambulisha wilaya, mikoa au kata zetu. Haiwezekani unakwenda kwenye kata hukuti jengo linaloitambulisha kata, hakuna zahanati, kituo cha afya, kituo cha polisi au mahakama ya mwanzo, sasa unasemaje pale ni kata? Ni vitu gani vinavyokwenda kutambulisha maeneo haya? Kwa jambo hili naiomba Serikali iwe makini sana na ije na takwimu sahihi kuhakikisha kwamba haya yote tunakwenda kuyasimamia.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Muda wako umekwisha Mheshimiwa.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na napenda kuunga mkono hoja kwa asilimia mia kwa mia. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mie nitoe mchango wangu kwenye huu Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2021. Awali ya yote nichukue fursa hii kumshukuru au kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna anavyotembea na Ilani ya Chama cha Mapinduzi na kwa namna anavyoangalia ustawi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambie tu wenzangu upande wa pili wananchi wa Tanzania wanahitaji maendeleo, Watanzania wanahitaji ustawi, Watanzania wanahitaji amani, kwa kasi hii ya Dkt John Pombe Joseph Magufuli, kama hawana namna nyingine ya kuendesha vyama watafute kazi nyingine, hii spidi hawatoiweza kwa sababu kama mbinu wanakoendeshea vyama ni kutegemea makosa ya chama tawala au makosa ya Serikali, sasa hivi Serikali ya Awamu ya Tano, hayo makosa ni machache sana kuliko mambo mazuri. Kwa hiyo wananchi wanaiunga mkono Serikali ya Awamu ya Tano kwa sababu inafanya mambo mazuri, kwa hiyo kama wanategemea makosa ya Serikali hii ndiyo waendeshee vyama, basi watafute vyama vingine au watafute njia nyingine au watafute kazi zingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapozungumzia CUF Liwale unazungumzia Zuberi Kuchauka, Zuberi Kuchauka hayupo CUF yuko CCM, wana Liwale hawako tena CUF, kwa hiyo msitegemee kwamba ngoma ya CUF bado ipo Liwale, hiyo nawapa taarifa nyinyi mnaolalamika kila wakati. (Makofi)

MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Taarifa.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ilikuwa ni tanbihi.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kuchauka subiri, taarifa Mheshimiwa Jafary.

T A A R I F A

MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Nampa taarifa mzungumzaji anayezungumza sasa hivi tumefika Liwale, bwana Kuchauka usitudanganye Chama ni taasisi siyo mtu kama wewe umehama basi waliobaki wanaendelea na CUF. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kuchauka.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Siipokei taarifa yake, juzi hapa wamelalamika wamesema Liwale hakuna watu waliochukua fomu, hakuna waliorudisha, Liwale hawajachukua fomu kwa sababu hawapo tena CUF wote wako CCM, ndiyo maana nikakuambia ukiiongelea CCM Liwale unamwongelea Kuchauka.

WABUNGE FULANI: Wacha uongo.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nijirejeshe kwenye Mpango. Mchango wangu kwenye Mpango huu nianze na miradi ya maji; tumefanya vizuri sana kwenye sekta ya elimu, tumefanya vizuri sana kwenye sekta ya afya, lakini bado tunasuasua kwenye sekta ya maji, watu wetu vijijini bado hawajapata maji kwa kiwango kinachoridhisha. Naomba Mheshimiwa Waziri sasa ipo sababu ya kujielekeza kwenye miradi ya maji, tuna miradi mingi sana ya maji, kwanza hapa napenda kumpongeza Waziri wa Maji na Naibu wake, kwa juhudi kubwa wanazochukua kurekebisha idara hii au kurekebisha Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiukweli miradi ya maji imehujumiwa sana, kwa hiyo naomba, kwa kuwa tumefanya vizuri kwenye afya na elimu, basi tujielekeze kwenye maji. Miradi mingi ya maji bado inaendelea kuhujumiwa pamoja na juhudi kubwa zinazoendelea kufanywa. Vile vile hata kwenye utoaji wa fedha kwenye zile certificates za miradi ya maji, bado spidi siyo nzuri sana. Kwa hiyo tunapokwenda kupanga mipango ya mwaka 2021, tuliangalie sana eneo hili eneo la idara ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo moja ambalo naona lilifanikiwa kwenye afya na elimu, ni huu utaratibu ambao Mheshimiwa Rais ameupendekeza wa force account. Ushauri wangu kwenye miradi ya maji basi kuwepo na hizi taratibu za force account kwa sababu miradi yetu ya maji mingi sana inapoteza fedha nyingi sana kwa sababu ya wakandarasi. Wakandarasi wetu wana makadirio ya juu sana kiasi kwamba unapeleka maji kijijini badala ya pale kijijini kuwa na virula tano au sita unakuta viwili au vitatu fedha nyingi zimepotea kwa wakandarasi, lakini tutakapoanza kutumia force account kwenye miradi hii ya maji tunao uwezo wa kusambaza maji pale yakafika kijijini na yakawafikia watu wengi zaidi. Jambo hili ikichukuliwa kwa umakini naona linaweza likatusaidia

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwenye miradi ya kimkakati tulikuwa na miradi ya kimkakati kwenye halmashauri zetu, lakini mwezi uliopita mwishowe Waziri alifuta baadhi ya miradi lakini au amesitisha baadhi ya miradi, lakini kwa nini ilipelekea hili? Jambo hili lazima tulifanyie utafiti tuliangalie kuna hii Sheria ya Manunuzi, napendekeza Mheshimiwa Waziri Sheria ya Manunuzi tuifanyie mapitio kwa sababu miradi mingi sana inakwama au haiendi kwa wakati kwa sababu ya Sheria hizi za Manunuzi ambapo kutafuta mkandarasi mmoja wa mradi inatuchukua zaidi ya miezi mitatu. Unapompa mkandarasi mradi ule anaposhindwa kuutekeleza kwa wakati, tunabadilisha tunatafuta mkandarasi mwingine, naye kumpata mkandarasi mwingine itachukua zaidi ya miezi mitatu mingine, utakuta hapo miezi sita mradi hauja-take off. Kwa hiyo katika jambo hili ushauri wangu ni kwamba Mheshimiwa Waziri tufikie mahali tuone ni namna gani tunakwenda kulitekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine naomba nijielekeze kwenye miradi ya kilimo, asilimia 65 ya wananchi wetu wanategemea kilimo, kwenye hii miradi ya kilimo naomba tuweke msisitizo kwenye idara ya masoko. Kwa sababu mkulima kama ana uhakika wa soko, suala la pembejeo atazitafuta kwa udi na uvumba atazipata kokote atakapozipata, lakini tatizo linakuja kwenye masoko. Kama hatutaweza kuimarisha masoko, juhudi kubwa tunazoingiza kwenye kutafuta pembejeo na kuimarisha kufanya tafiti mbalimbali, kuangalia magonjwa ya mazao na namna ya kuendeleza kilimo, kama hatujaweza kupata masoko ya uhakika juhudi hizi ambazo tunazielekeza kwenye kilimo bado hazitatuletea matunda tunayokusudia. Kwa hiyo, ushauri wangu kwa upande wa kilimo ni uimarishaji wa masoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia huu uimarishaji wa masoko uende sambamba na uimarishaji wa miundombinu ya barabara, yapo maeneo yanapatikana mazao ya kutosha, lakini mazao yale kuyafikia kwenye masoko inakuwa ni shida kubwa na yanapofika kwenye masoko bei inakuwa ni ya juu sana ambayo watu wanashindwa kumudu. Kwa hiyo uimarishaji wa kilimo uendane sambamba na masoko vilevile na uimarishaji wa miundombinu kuhakikisha mazao haya yanafika kwenye soko kwa muda unaotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hii miradi mikubwa ambayo Mheshimiwa Rais anaitekeleza ni jambo zuri sana, nami niseme tu kwamba Watanzania wanamwelewa vizuri sasa Mheshimiwa Rais wetu na nia yake kubwa ya kuipeleka nchi yetu kwenye uchumi wa kati. Hapa napo naweza kutoa ushauri kwamba sasa Serikali tuanze kufikiria katika baadhi ya miradi kuimarisha utaratibu wa PPP ili Serikali iweze kutoa huduma za kijamii kwa mfano kama maji, afya, elimu, ni lazima tuhakikishe kuwa baadhi ya miradi ambayo inatumia fedha nyingi sana fedha zetu za ndani, kuanza sasa kuanza kufikiria kushirikisha hii PPP.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa napo kuna tatizo kubwa la urasimu, naiomba sana Serikali, Serikali ya Chama cha Mapinduzi, Serikali sikivu, Serikali ambayo inapanga mipango inayopangika, mipango ambayo inayotekelezeka, basi na hapo tuendelee kuimarisha uwekezaji, tuendelee kuimarisha ushirika wa watu binafsi na miradi mikubwa Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo Watanzania ambao wanapenda kushiriki kwenye hii miradi mikubwa na midogo, lakini shida kubwa inakuja kwenye mitaji. Hapa napo naomba niishauri Serikali kuangalia namna gani ya kuwashirikisha au kuwapa mitaji au kuwawezesha watu wa sekta binafsi kushiriki kwenye uchumi huu ili tuweze kutoka wote kwa pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sitaweza kukaa chini bila kutaja sekta ya vijana pamoja na ajira. Suala hili la ajira ni muhimu sana, naishauri Serikali ili kuondokana na dhana kwamba mtu yoyote au mhitimu yeyote ategemee kuajiriwa na Serikali, tuanze kufikiria sasa kwamba wahitimu wetu waweze kujitegemea. Watawezaje kujitegemea, ni pale ambapo Serikali itajikita kuimarisha miundombinu ya watu kuweza kujitegemea kama vile kuendelea kuimarisha shule zetu za VETA, shule ambazo zitaandaa wahitimu wetu kujitegemea. Jambo hili ni muhimu sana kwa vijana wetu kwa sababu leo hii kila mhitimu anafikiria kutembea na vyeti akitafuta ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachoshangaza zaidi hata wale ambao wahitimu wametoka kwenye vyuo labda mtu ametoka kwenye chuo cha mifugo, chuo cha kilimo, chuo cha ufundi bado na yeye anatembea na vyeti akitafuta ajira. Hii ni kwa sababu watu wetu bado hatujawajengea uwezo wa kujiajiri.

Kwa hiyo, pendekezo langu pamoja na kuimarisha vyuo vyetu vya VETA na vyuo vya ufundi, bado Serikali ione umuhimu wa kuwawezesha vijana hawa, kuwahamasisha vijana hawa wajiunge kwenye vikundi mbalimbali ili waweze kupatiwa mitaji ili waweze na wao kushiriki kwenye uchumi wa nchi yetu.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja hii ya mapendekezo ya Mpango, tuko vizuri. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kwanza jioni hii ya leo kuchangia hotuba hii ya Wizara ya Nishati na Madini. Kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, bado ananiwezesha kusimama kwenye Bunge lako Tukufu, nikitoa mchango wangu katika Wizara mbalimbali; ni kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu aliyenifanya nisimame hapa niwawakilishe Wanaliwale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema ukweli, sina wasiwasi na dhamira ya Waziri wa Nishati na Madini. Kwanza nakubaliana naye kwa taaluma yake, masuala ya uweledi na ufanisi hilo sina ujuzi nalo, lakini kwa taaluma yake namfahamu vizuri. Wasiwasi wangu ni kwenye utekelezaji, na uwezo wa kuyatekeleza haya ambayo yameanishwa kwenye hotuba hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuweka rekodi sawa nataka niwaeleze Waheshimiwa Wabunge walioko humu ndani, wasione Wabunge wa Kusini wamekuwa walalamikaji sana humu ndani, kwamba kila Mbunge wa Kusini akisimama analalamika kama vile tumeonewa! Kwa kuweka rekodi sawasawa nataka niwafahamishe Waheshimiwa Wabunge, Reli ya Tanga – Dar- es-Salaam iling‟olewa kutoka Mtwara– Nachingwea, wakati ule Mkoa wa Lindi tulikuwa tunalima pamba, mkonge, karanga pamoja na korosho. Wajerumani wakatuwekea ile reli, ili kuharakisha maendeleo, lakini tulivyopata uhuru reli ile ikang‟olewa, ndipo umaskini wa watu wa kusini ulianzia pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunapokuja kulalamika tumeona Mwenyezi Mungu ametupa neema hii ya gesi, sasa ni lazima watu ambao tumeshafanyiwa huko nyuma tuwe waoga. Ndio maana mtu wa Kusini akisimama leo hapa, haiamini hii Serikali ya Chama cha Mpinduzi kwa sababu, wameshatufanyia mengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nijielekeze kwenye madini. Sera ya Madini bado sijaielewa, hata wananchi wangu wa Liwale nafikiri bado hawajaielewa Sera hii imekaakaaje, hasa pale ambapo ardhi ya wanakijiji inapokuja kugundulika pana madini; hawa wananchi wa ardhi ile bado hawaelewi hatima yao na nafasi yao katika rasilimali ile iliyopatikana pale kwenye ardhi yao. Kwa sababu, ninavyofahamu mnufaika wa kwanza wa rasilimali inayopatikana ni lazima awe yule inayomzunguka pale alipo. Pamoja na kwamba, hizo rasilimali ni za kitaifa, lakini mnufaika wa kwanza anapaswa awe yule inayomzunguka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hii kwa Liwale imekuwa ni kinyume chake, sisi Liwale tuna machimbo ya madini yako kwenye Kata ya Lilombe, katika Kijiji cha Kitowelo. Pale wanachimba madini ya sapphire na dhahabu, lakini Ofisi ya Madini iko Tunduru, ndiko mahali ambako kinapatikana kibali cha uchimbaji. Aidha, wachimbaji wadogo ili kupata leseni inabidi uende Tunduru, sasa unafikaje huko Tunduru, sielewi!
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu ukishapata hicho kibali, unakwenda moja kwa moja msituni, machimbo, wanachimba, wakishachimba wanakwenda moja kwa moja Tunduru kwenye mauzo; Halmashauri ya Kijiji na Wilaya haina habari! Nilivyofika kule kwenye machimbo nikalazimika kumtuhumu hata Mkurugenzi wa Halmashauri, pengine naye anajua chochote. Haiwezekani madini yatoke pale Lilombe, wana Lilombe hawajui, Halmashauri haijui, haipati hata thumni! Sasa leo nimesikia ofisi hii imesogezwa imepelekwa Nachingwea!
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutoka Lilombe mpaka Liwale Mjini ni kilometa 60, kwa hiyo, hayo yanayofanyika Lilombe Halmashauri haijui! Sasa hii Sera ya Madini, Mheshimiwa Waziri, atakapokuja nitaomba ufafanuzi kidogo, hii inakuwaje kuwaje? Hawa wachimbaji wadogo tunawasaidiaje? Kwa sababu, nimekwenda mimi kwenye yale machimbo nimemkuta mmiliki mmoja, mchimbaji mdogo, kuna bwana mmoja pale, nafikiri yule alikuwa IGP, Mheshimiwa Mahita! Yeye ana vitalu vyake pale, lakini yeye mwenyewe hayupo pale yupo Tunduru!
Mheshimiwa Mwenyekiti, ina maana wale wachimbaji wakipata madini wanampigia simu, anakuja kuchukua anakwenda au pengine wampelekea ananunua anakwenda, lakini Halmashauri pale haipati chochote, wala kijiji kile hawapati chochote, wanaachiwa mashimo tu na ile ardhi ipo pale! Sasa hapo Waziri atakapokuja naomba anisaidie, hii Sera ya Madini ikoje kwa sababu, sisi ndiyo kwanza tunaingia kwenye hiyo fani kwa sababu, mgodi wetu ule ni mdogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nirejee kwenye umeme. Wilaya ya Liwale ilibahatika kupata umeme miaka ya 77, ndiyo Wilaya ya kwanza kwenye Kanda za Kusini na Nyanda za Juu Kusini kupata umeme wakati ule Mzee Kawawa akaambiwa umeme amefunga kwenye mikorosho, lakini umeme wenyewe ni ule wa mwisho saa nne, mpaka leo miaka 40 bado umeme ni ule ule wa mafuta!
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi hapa wametuonea huruma wakachukua ile mashine kutoka Ikwiriri wakaipeleka Liwale, mashine kuukuu iliyotoka Ikwiriri wakaipeleka Liwale ku-subsdise ile mashine ya zamani ya Mzee Kawawa; lakini kulingana na jiografia ya Liwale, umeme ule wa mafuta, masika kama saa hizi Liwale hakufikiki na mafuta hakuna! Kwa hiyo, mafuta yanapokosekana Liwale inabaki giza, lakini siyo hivyo tu, kutoka Liwale kuja Nachingwea ni kilomita 120. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuna hii Miradi ya REA; umeme wa REA katika Wilaya ya Liwale, ambayo ina vijiji 76 sisi tuna vijiji vitano tu! Tuna Mangirikiti, Kipule, Likolimbora, Mihumo na Darajani, hivi vipo ndani ya kilomita tano kutoka Liwale Mjini, lakini nje ya hivyo zaidi ya hapo hakuna kingine tena kinachopata umeme. Siyo hivyo tu, umeme huu wa gesi umeishia Nachingwea! Nachingwea Liwale kilomita 120, lakini mpaka leo sijaelewa huu mradi wa umeme wa kutoka Nachingwea kufika Liwale umefikia hatua gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimetembea kutoka Liwale kuja Nachingwea katika Vijiji vya Kiangara, Vibutuka, Nagano mpaka Mikunya; nguzo zimewekwa pale, zingine zimechimbiwa, zingine huku zinaanguka huku zinachimbiwa, haieleweki, haielezeki, ukimuuliza meneja hakuna anachosema! Mara pesa bado, hajaleta mkandarasi, hapo alipofikia bado hajalipwa, sijui imekuwa kuwaje, haieleweki ile REA pale Liwale mwisho wake ni lini? Hivi sisi tutabaki gizani mpaka lini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nataka niseme, kama ingekuwa enzi zile za zamani kwamba, ukitoa shilingi inaleta reflection yoyote, ningekuwa natoa shilingi kila Wizara hapa, maana sioni Wizara hata moja ambayo nikasema Wizara hii ina nafuu kwa Liwale. Hata hivyo, hata nikitoa shilingi haina maana yoyote kwa sababu, tumeona hapa mambo yenyewe yanavyokwenda mwisho wa yote tunapiga kura wape, wape, basi; haina maana yoyote!
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, namwomba Mheshimiwa Waziri, kweli atutendee haki, atuondoe gizani; sisi umaskini wetu umechangiwa na haya mambo ya barabara na haya mambo ya umeme, huu ndio unatuletea umaskini, leo hii Liwale hakufikiki, huu umeme wa mafuta magari hayaendi! Hivi huu umeme wa mafuta utafika lini? Halafu umeme wenyewe mwisho saa nne!
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa, muda wetu ndiyo huo!
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze mchango wangu kwa kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri wote na Makatibu wa Wizara hii kwa kazi kubwa na nzuri inayofanywa na Wizara hizi mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kuchangia sasa Ofisi ya Rais, TAMISMI kama ifuatavyo:

Nianze na sekta ya elimu; sekta hii kwa ujumla wake ina changamoto nyingi sana, elimu yetu haijawahi kuandaa wahitimu kuweza kujitegemea hata wale wa elimu ya juu. Changamoto kubwa ni mabadiliko ya mitaala ya mara kwa mara ambako hakuendani na mafunzo kwa Walimu juu ya hiyo mitaala mipya na hata vitabu wakiandaa havitoshi hasa kwa shule za msingi. Vilevile hata miongozo inayotolewa kila kukicha kunachangia kuwavuruga Walimu mashuleni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya uhaba wa Walimu ni kubwa sana nchini, mfano, katika Halmashauri ya Liwale kuna shule nyingi zina Walimu chini ya watano. Shule ya Ndapata, Mtungunyu, Nambinda shule hizi zina Walimu watatu tu kila moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jukumu la kujenga miundombinu ya shule limeachwa kwenye Halmashauri jambo hili limefanya shule nyingi kuwa na miundombinu mibovu sana kwani Halmashauri nyingi zinashindwa kumudu jukumu hili hasa baada ya vyanzo vingi vya mapato vya Halmashauri kuchukuliwa na Serikali Kuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, afya; changamoto zilizopo kwenye sekta ya afya zinafanana kwa kiasi kikubwa na zile za elimu. Uhaba wa watumishi na miundombinu mibovu ya zahanati, vituo vya afya na hospitali za Wilaya hali ni mbaya sana hasa kwenye zahanati na hospitali za Wilaya. Mfano, Halmashauri ya Liwale yenye Kata 20, Vijiji 27 kuna Zahanati 34 tu ambazo zote zinahudumiwa na Manesi Wasaidizi, hazina matabibu wala Madaktari Bingwa wala mmoja na mpiga picha wa x-ray.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, shida ya gari la wagonjwa kwenye hospitali ya Liwale ni kubwa sana. Mapato ya Halmashauri kununua gari ni jambo lisilowezekana kwenye Halmashauri ambayo hata zahanati zilizopo ni chache na miundombinu yake ni duni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri licha ya kupokwa vyanzo vya mapato, lakini Serikali imekuwa bado ikiwapa mzigo mkubwa wa kuhudumia jamii Wakurugenzi wa Halmashauri hizo. Serikali imekuwa haitoi fedha za maendeleo kwa kisingizio cha Halmashauri kutumia mapato ya ndani wakati ikijua kwamba kwenyewe haipeleki fedha za matumizi ya kawaida yaani OC. Jambo hili linafanya halmashauri kushindwa kupanga mapato yake ya ndani kwa miradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Serikali imekuwa haipeleki fedha za miradi ya maendeleo hadi mradi huo uanze kutekelezwa kwa ngazi ya Halmashauri. Jambo hili limekuwa likiongeza umaskini kwenye Halmashauri nyingi hasa zile zisizokuwa na mapato ya kutosha kugharamia miradi hiyo, hivyo Halmashauri kuendelea kubaki nyuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, msimamo huu wa Serikali hauwezi kuleta mgawanyo ulio sawa kwa nchi nzima. Kuna Halmashauri itakayopata fedha nyingi na zingine zikawa hazipati fedha kabisa. Mfano, Halmashauri ya Wilaya ya Liwale haina jengo la hospitali ya Wilaya, jengo la Polisi Wilaya. Miradi hii yote ni miradi ya fedha nyingi na ni miradi muhimu. Kama Halmashauri tukishindwa kuanzisha miradi hii maana yake Serikali haiko tayari kugharamia miradi hii. jambo hili ni vyema Serikali mkaliangalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo; pamoja na kuwa zaidi ya asilimia 70 ya watu wetu ni wakulima, lakini sekta hii haijapata msukumo wa kweli. Wakulima wetu bado wanaishi maisha duni sana licha ya kutumia zana duni kwenye kilimo bado hata hayo mazao wanayopata hawana uhakika wa masoko.

Matamko mengi ya Serikali juu ya kilimo yanachangia kwa kiasi kikubwa kudumza kilimo. Mfano kuzuia watu kusafirisha mazao kufuata soko ni unyanyasaji mkubwa. Ni nani mwenye jukumu la kutunza chakula cha akiba kwa nchi, ni mkulima au Serikali?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ucheleweshaji wa pembejeo za kilimo ni kikwazo kingine cha kumkwamua mkulima. Mfano, hadi leo pembejeo za korosho hazijulikani zitaingia lini nchini wakati mwezi Mei ndiyo mwezi wa kuanza kuweka dawa kwenye mikorosho na hata bei za pembejeo hizo hadi leo hazijulikani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uhaba wa Maafisa Ugani pamoja na vyombo vya usafiri kwa hawa wachache waliopo kunachangia kwa kiasi kikubwa watu wetu kulima bila kuzingatia kilimo cha kisasa kwani wananchi wengi hawafikiwi na watalaam hao. Hivyo, ni vyema Serikali ikahakikisha inakuwa na Maafisa ugani wa kutosha na wawe na vitendea kazi. Vilevile sekta ya kilimo cha umwagiliaji ndiyo kimetupwa kabisa. Miradi mingi ya umwagiliaji nchi nzima imekuwa haikamiliki na fedha zake kuliwa kama hazina mwenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nichangie Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kuhudumu kwenye Wizara hii, Mungu ampe umri mrefu ili aweze kuendelea na jukumu hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la utumishi na watumishi hapa nchini ni hali mbaya sana. Hali ya watumishi nchini kwenye kada mbalimbali ni mbaya. Kilio cha uhaba wa watumishi nchini ni kikubwa sana na hata hao wachache tulionao hali na mazingira yao ya kazi ni mbaya sana kwani walio wengi malipo yao hayalingani na kazi zao. Walio wengi wanafanya kazi kwa sababu tu hawana namna ya kuishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili linapunguza ufanisi na ari ya kazi. Ikumbukwe kwamba baada ya punguzo kubwa la wafanyakazi hapajatokea mkakati maalum wa kuziba pengo hilo. Mishahara ya watumishi wengi, hasa wa kada za chini bado ni midogo sana na ni miaka miwili kama si mitatu haijafanyiwa mapitio.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watumishi wengi hasa wa sekta ya elimu na afya wanafanya kazi chini ya kiwango kwa kuwa kazi zao hazithaminiwi, hivyo walio wengi hufanya migomo baridi, jambo ambalo halina tija kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile mipaka ya kazi sasa haiko wazi kwa wakuu wengi wa mahali pa kazi, wanafanya kazi kwa matamko zaidi kuliko weledi wa kazi. Jambo hili linachagizwa zaidi na kutokuwapa mafunzo au semina kwa watumishi wengi wa umma. Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri walio wengi hawajui mipaka ya kazi zao ndiyo maana kuna migongano mingi kazini. Ubabe ni mwingi kuliko weledi, watumishi wanajazwa hofu badala ya kutiwa moyo na ari ya kazi, kazi za kitaaluma zinafanywa kwa matamko badala ya kitaaluma, hivyo kuondoa ufanisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huko kwenye sekta binafsi ndiko kumeoza kabisa. Wafanyakazi huko hawana taasisi yoyote inayowasimamia, tumeacha watu wa chini wapambane na matajiri wao. Katika mazingira haya ya uhaba wa ajira tunatarajia nini kitatokea kama si watu wetu kunyanyasika na matajiri tunaowaita wawekezaji? Hali ya ajira kwenye sekta hii ni mbaya sana, hakuna anayesimamia mikataba ya ajira zao wala hali bora ya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utawala bora; dhana ya utawala bora ni pana sana na ili itekelezwe ipasavyo kuna haja watu waliopewa dhamana ya kusimamia dhana ya utawala bora waelewe maana ya utawala bora na utawala wa sheria kwani mahali ambapo sheria hazifuatwi hakuna utawala bora. Utawala wa sheria ni dhana nyingine inayowataka viongozi au watawala kufuata sheria kwa mujibu wa Katiba wakijua kuwa roho ya amani ni haki na haki ni kufuata sheria/Katiba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hali ya sasa dhana ya utawala bora imeanza kutokomea kwani watoaji haki wameanza kukiuka dhana ya utawala bora. Sasa hivi tumeanza kujenga Taifa la watu waoga na si watii wa sheria kwani kuna tofauti kubwa kati ya kutii sheria na woga. Mtii wa sheria siku zote atabaki na utii wake, lakini mtu mwoga siku akibadilika akaacha woga basi hapo amani huwa mashakani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, roho ya amani ni haki na wala haitakuwa woga, kulea watu waoga ni kulea bomu katika jamii. Ni vizuri Serikali ikaanza sasa kuwafanya watu watii sheria badala ya kuwajengea woga ambao ipo siku utakwisha. Vitendo vinavyoendelea nchini sasa havina mwelekeo mzuri, vitendo vya watu kutekwa, kupotea na hadi kuuawa ni hatari sana, hasa pale Serikali inapokaa kimya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu matamko ya Viongozi. Uongozi wa Awamu ya Tano umekuja na namna mpya ya kuongoza. Kumekuwa na matamko mengi kutoka kwa viongozi na mara nyingi yamekuwa yakipingana kutoka ngazi moja hadi nyingine. Vile vile kuna viongozi ambao hawafanyi kazi wakisubiri maagizo kwani wakifanya bila maagizo wanaweza wakaondolewa kwenye nafasi zao hata pale anapofanya jambo lililo chini ya mamlaka yake. Watendaji wako ofisini wakisubiri maagizo tu. Uwajibikaji wa pamoja nao umeanza kutoweka, viongozi walio wengi wanaogopa dhana ya uwajibikaji wa pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haki na amani; watu wa kwanza watakaowajibika kwa Mungu siku amani ya nchi yetu ikitoweka ni wale wanaosimamia utoaji haki ambao ni pamoja na polisi, mahakama, Msajili wa Vyama vya Siasa, Tume ya Uchaguzi na Usalama wa Taifa. Taasisi hizi ni muhimu sana wakatenda haki na jamii wakaona haki ikitendeka na haki hiyo lazima iende na wajibu. Hakuna amani bila haki na hakuna haki bila wajibu, naishauri Serikali kusimamia haki ili kulinda amani yetu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia hotuba ya Waziri wa Nishati na Madini kama ilivyowasilishwa leo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Sera ya Madini nchini bado haijaeleweka hasa kwa wananchi wengi wa vijijini, jambo linalowafanya wananchi wengi kunyanyasika hasa pale ardhi yao inapogundulika kuna madini na wao kutakiwa kuhama pengine bila ya hata kujua stahiki zao, zaidi ya kuambulia mashimo. Sambamba na hilo, hata utaratibu wa upatikanaji wa leseni kwa wachimbaji wadogo, hauko wazi hasa kwa watu waishio vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Liwale katika Kijiji cha Lilombe kuna machimbo ya madini ya dhahabu na sapphire, lakini wachimbaji wadogo wanapotaka leseni, hulazimika kwenda Tunduru Mkoani Ruvuma ambako ndiko kuna Ofisi ya Kanda.
Vile vile soko la madini wanayoyapata hulazimika kwenda kuyauzia Tunduru, hivyo Halmashauri ya Liwale haina mapato yoyote yatokanayo na machimbo hayo. Maeneo ya machimbo hayo ni ardhi inayomilikiwa na Kijiji cha Lilombe, lakini inapotolewa leseni wananchi hawa hawashirikishwi katika lolote. Hivyo kuweka mgogoro kati ya wachimbaji hao na Halmashauri ya Kijiji. Nini kauli ya Serikali juu ya mgogoro huu? Kwa nini kusifunguliwe Ofisi ya Madini Liwale? Kwa nini wachimbaji wasilipe ushuru kijijini ili kijiji kipate mapato yatokanayo na ardhi yao badala ya kuachiwa mashimo na mapato yaende mkoa mwingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Liwale iko kilometa 120 toka Wilaya ya Nachingwea ambako kuna umeme wa gesi asilia, lakini kwa masikitiko makubwa hadi leo Liwale inategemea umeme wa mafuta (generator) ambao kutokana na ukosefu wa barabara kuna wakati Liwale hubaki gizani kutokana na kukosa mafuta. Vile vile generator hilo kwa sasa limezidiwa na watumiaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa mradi huu wa REA kwa Wilaya ya Liwale ni wa kusuasua sana hasa baada ya kukosekana kwa umeme wa uhakika. Wilaya yenye vijiji 76 ni vijiji vitano tu vyenye umeme wa REA. Njia kuu ya umeme kutoka Nachingwea hadi Liwale ujenzi wake haujapewa msukumo unaostahili. Kumekuwepo na visingizio vingi, haijulikani kikwazo ni nini na nani kati ya Mkandarasi, TANESCO au Serikali. Namwomba Waziri mwenye dhamana kuhakikisha mradi huu unakamilika ili kusukuma maendeleo ya wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa kiwanda cha kuchakata gesi (LNG – LINDI) ni bora ukaharakishwa sambamba na kulipa fidia kwa wale waathirika wa ujenzi huo. Vile vile ni jambo la kuzingatia kuwa vijiji vyote vinavyopitiwa na bomba hili la gesi ni lazima vipatiwe umeme sambamba na kuwalipa fidia watu wote ambako bomba hili limepita. Hakuna dhambi kubwa itakayofanywa na Serikali hii kama mtawanyima umeme wanavijiji Mikoa ya Lindi na Mtwara. Naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia hotuba hii kwa kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Waziri kwa mikakati yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyo kawaida ya Serikali yetu tatizo kubwa linaanzia pale ambapo Serikali inaposhindwa kutoa fedha zilizotengwa katika bajeti hii. Wizara ya Ardhi kwangu mimi ni kama Wizara mtambuka kwani migogoro mingi husababishwa na maingiliano ya sera kama vile sera ya kilimo, sera ya mifugo, sera ya madini na kadhalika ambazo zote zinaihusu ardhi lakini ni nani anasimamia sera ya ardhi kwa upana wake?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi na umaskini wa watu wetu. Watanzania wengi hasa wa vijijini wanakuwa maskini kutokana na kushindwa kwa Serikali kuwamilikisha ardhi. Hivyo watu hawa hushindwa kuaminika na taasisi za kifedha, hawakopesheki na pale mwananchi anapoomba kupimiwa ardhi yake ili aweze kuwa na hati miliki gharama huwa ni kubwa sana na kuwa na milolongo mingi inayosababishwa na rushwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wengi wanashindwa kuwekeza vijijini kwani kikwazo kikubwa ni vijiji vingi kutokuwa na mipango ya matumizi bora ya ardhi. Kijiji ambacho hakijapimwa kwa matumizi bora ya ardhi kinakosa wawekezaji eti kwa kuwa kijiji husika hakijaingia kwenye mpango wa matumizi bora ya ardhi. Mfano ni jimboni kwangu Liwale wawekezaji wengi wameshindwa kusajili biashara zao kwa kuwa vijiji walivyowekeza havijapimwa kwa hiyo hao wawekezaji kukosa leseni za biashara zao. Yuko mwekezaji ameshindwa kusajili shule kwa kukosa hati miliki ya ardhi kutokana na kijiji kukosa matumizi bora ya ardhi. Vilevile kuna mwekezaji ameshindwa kusajili zahanati kwa kuwa kijiji hakijaingia kwenye matumizi bora ya ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uhaba mkubwa wa watumishi wa kada hii kunafanya gharama ya kupima ardhi na viwanja kuwa ghali sana. Mfano Mji wa Liwale hulazimika kukodi wapimaji toka Wilaya jirani ya Nachingwea hivyo kufanya bei ya viwanja kuwa juu sana na watu kuendelea kukaa maeneo yasiyopimwa. Namuomba Waziri atuongezee watumishi ili kuhakikisha upimaji wa ardhi Jimboni Liwale unafanyika ili kuharakisha maendeleo ya Halmashauri yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro wa ardhi. Wilaya ya Liwale ina mgogoro wa muda mrefu kati ya wanakijiji cha Kikulyungu na Hifadhi ya Mbuga ya Selous. Mgogoro huu umeshaleta maafa tayari watu wanne (4) wamepoteza maisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu upimaji wa vijiji; Serikali iharakishe upimaji wa vijiji ili wawekezaji wanapokwenda vijijini wakute kijiji tayari kimeshafanya mpango wa matumizi bora ya ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nikushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie hoja iliyoko mbele yetu. Kwanza, kama ilivyo ada nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu na kutoa mchango wangu. Kama ilivyo ada vile vile nitoe shukrani zangu na niwapongeze wahudumu wote wanaohudumu kwenye Wizara hii nikianzia na Waziri mwenye dhamana pamoja na Watendaji wote, Makatibu Wakuu na Naibu Mawaziri kwa kazi kubwa wanayoifanya na jukumu kubwa lililo mbele yao. Nawapongeza na kuwapa pole kwa sababu majukumu waliyonayo ni makubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze mchango wangu kwa kuiomba tu Serikali, nchi yetu inaingia kwenye uchumi wa kati; na nchi yetu inasema kwamba yenyewe ni nchi ya viwanda. Ili tuweze kuingia kwenye viwanda tunategemea malighafi kutoka kwenye kilimo. Serikali hii ijaribu kuongea kwa Pamoja; Waziri wa Ujenzi ana vipaumbele vyake, ana barabara zake za kimkakati; ukiingia kwenye kilimo, wana mazao yao ya kimkakati; ukiingia kwenye viwanda, wana viwanda vyao vya kimkakati, lakini haya mambo ukiingia kwenye Serikali hayaendani pamoja. Leo tunazungumza zao la korosho, kahawa, katani, ni mazao ya kimkakati, lakini kwenye Wizara ya Ujenzi hatuyakuti hayo mazao. Hivi leo hii kama Waziri wa Ujenzi hajui korosho zitatokaje Liwale zikafika Lindi, zikafika sokoni, kuna sababu gani ya kusema kuna mazao ya kimkakati? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo sasa tunataka tuwaambie nchi hii kwamba tujenge kiwanda cha korosho kule Liwale, Ndanda, kila mahali ambapo zao lipo. Mwenye shamba lake ajenge kiwanda hapo hapo. Kwa sababu kama kweli tulikuwa tunajua kwamba haya mazao ni ya kimkakati, lazima tuyatengenezee huo mkakati uonekane kwenye Serikali nzima, chain ile ionekane kwamba hili zao la korosho litatoka Liwale, litafika Lindi, litafika Dar es Salaam, litakwenda kwenye soko au litakwenda kwenye viwanda. Kama Serikali hatuunganishi hivi, hatuna maana ya kuwa na mazao ya Kimkakati. (Makofi)


Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kwenye upande huo huo wa barabara. Lifetime ya barabara zetu ni miaka 20, maana baada ya miaka 20 barabara zile zinatakiwa zifanyiwe rehabilitation, iondolewe lami iwekwe nyingine, lakini kwenye nchi kama hii unapoona wenzenu barabara ya zamani inaondolewa, wewe hata lami huijui, mimi napata wasiwasi kama tupo pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye bajeti, kuna barabara ya Dar – Chalinze inafanyiwa ukarabati, inaondolewa ile kwa sababu lifetime imeisha; kuna barabara ya Masasi – Mtwara inaondolewa; kuna barabara ya Dodoma – dar es Salaam, inaondolewa; na kuna barabara ya Arusha – Moshi, inaondolewa. Yaani hizi barabara lifetime yake imeisha, wanakwenda kuondoa hizo lami, waweke nyingine. Hata hivyo hizi barabara hazijawahi kulaza watu njiani, wala hazijawahi kusema kwamba kuna malori ya biashara yamekwama au malori ya mizigo yamekwama kwa sababu ya barabara mbovu, haiwezekani. Hizo barabara zinapitika masika na kiangazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara ya Nangurukuru – Liwale, Nachingwea – Liwale, hazipitiki, nyakati za masika zinasimama. Mkoa wa Lindi hauna barabara za lami. Sasa wananchi wanaotoka Liwale na Lindi wanakwenda kutembelea Dar es Salaam, wanakuta lami zinakwanguliwa na kuwekwa nyingine, hivi wanajihesabu wako wapi? (Makofi)


Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Serikali, hebu tuongee kwa Pamoja, kama kweli tuna dhamira ya kuwahudumia wananchi wetu, lazima tuongee kwa pamoja. Kama hatutaongea kwa Pamoja, bado kuna maeneo yatabaki kuwa nyuma na maeneo mengine yataendelea kwa sababu leo mimi sioni sababu na wala haiingii akilini eti Dodoma – Chalinze wanaondoa lami wanaweka nyingine, mimi Nangurukuru sijawahi kuona lami, Nachingwea – Liwale sijawahi kuona, lami halafu nami napitisha hiyo bajeti, hii haiwezekani! Sitaeleweka! (Makofi)


Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Serikali haka kakeki kalikopo tugawane sawa sawa. Wale ambao tayari wana lami, hebu tuwaache wapumzike kwanza. Sisi ambao hatuna, tupeni hizo lami, kwa sababu na sisi tunachangia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine huko huko kwenye lami, kwenye ujenzi wa barabara zetu, kama hatuko tayari kuangalia specifications za barabara, haya mambo yataendelea kujitokeza, barabara hata miaka 15 haijafika, imeshafanyiwa upembuzi yakinifu na inafumuliwa. Kwa mfano, barabara ya Kibiti – Lindi haina miaka 20 lakini haifai. Inafumuliwa! Kuna barabara ya Wazo – Bagamoyo nayo haijafikisha miaka 15, nayo inafumuliwa. Ukiiangalia, kweli ina haki ya kufumuliwa kwa sababu barabara ni ya hovyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Serikali, pamoja na kwamba tunahitaji wataalam wa ndani, lakini kama kweli tuna uchungu na fedha za nchi hii, barabara hizi ni lazima tuzisimamie ili ziweze kujengwa kwa kiwango kinachotakiwa na kiwe kama ni miaka 20 au 25, tuone barabara inadumu miaka 20. Ninyi wenyewe ni mashahidi mliopita barabara hii ya Dodoma, barabara kwenye kona na lami yenyewe inapiga kona. Kwenye tuta, na lami yenyewe inapiga tuta; wapi na wapi? Tunakwenda wapi?


Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa na mengi sana ya kusema, lakini napata kigugumizi. Nitakwenda kuwaambia nini Wana-Liwale kwamba mimi nimepitisha bajeti ambayo inaondoa lami za zamani na kuweka nyingine na mimi kule sina lami? Sitaweza kupitisha hili, nitakuwa nafanya dhambi. Hapa nami naendelea kufanya dhambi. Kuna mahali pengine barabara hazijaharibika, lakini wanajenga bypass. Bypass sijui ya Dodoma – Iringa. kuna bypass ya Dodoma, Songwe, Dar es Salaam, hizi bypass zinajengwa kwa sababu ni wrong design. Hivi unapitishaje malori kwenye barabara hii hapa ya Dodoma?

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kuchauka, kuna Taarifa.

Mheshimiwa Twaha Mpembenwe.

T A A R I F A

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu nimpe taarifa mzungumzaji, kigugumizi hicho hicho kinachompata yeye kupitisha bajeti hii ya Wizara ya Ujenzi, ndiyo hicho hicho kinanipata mimi katika Jimbo la Kibiti. Barabara ile ya kutoka Nyamisati kuja Bungu jana nimepigiwa simu magari pale yamenasa na abiria pale wamelala.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Kicheko/ Makofi)

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kuchauka, lazima uulizwe kwanza kama unaipokea ama huipokei. Mbona unaipokea haraka haraka! Haya malizia mchango wako.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea taarifa. Sasa nafikiri hapo nimemaliza.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa kumalizia mchango wangu, naiomba Serikali kwanza kuhakikisha kulipa wakandarasi. Jambo hili linatupungizia sana ujenzi wa barabara zetu. Tunajenga barabara chache kwa sababu tunatumia fedha nyingi kujenga barabara chache; na tunatumia fedha nyingi kwa sababu ya riba inayolipwa kwa Wakandarasi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wako Wakandarasi barabara imeisha miaka minne sasa bado Mkandarasi anadai na kwenye bajeti imo. Naiomba Serikali, hakuna sababu ya kuendelea kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina barabara mpya wakati kuna barabara tangu mwaka 2014 imeisha upembuzi yakinifu na hakuna kujengwa. Halafu ukiuliza kwenye vitabu, unaambiwa fedha hazipo. Sasa hizi fedha ni za aina gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atuambie fedha hizi ambazo zinasubiriwa kwenye hizi barabara ambazo zimefanyiwa upembuzi yakinifu tangu mwaka 2014 hazijapatikana na hizi ambazo zinajenga barabara nyingine za mikoa mingine na sehemu nyingine ni pesa za aina gani? Yaani kuna pesa zina label kwamba, pesa hizi za Mkoa wa Lindi au pesa hizi ambazo tunasubiria sisi ni pesa gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu kama ni fedha tunaona barabara nyingine zinajengwa, lakini sisi barabara zetu tunaambiwa fedha hazipo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa, kengele imeshagonga.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa shingo upande. (Kicheko)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, niseme ahsante sana kwa kunipa nafasi jioni hii ili nichangie bajeti iliyopo mbele yetu. Nikushukuru wewe na pia nielekeze shukrani zangu za dhati au pongezi zangu kwa Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote waliomo kwenye Wizara hii, kwa kweli kazi wanayofanya mwaka huu imeonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pongezi za dhati ziende kwa Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan, kwa namna ya aliyoweza kujibu hoja za wananchi mbalimbali kupitia kwa Wabunge wetu kwenye bajeti hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini watu wanaisifia hii bajeti, kwamba kama kumbukumbu zetu zipo vizuri huko nyuma bajeti kuu ilianza kusomwa kabla ya bajeti za kisekta, lakini Serikali ya Chama Mapinduzi ilikuja kubadilisha ule utaratibu, ili kukidhi matakwa haya ambayo yamekuja na bajeti hii, kwamba bajeti za kisekta yale tuliyoyachangia yote ndio yamekusanywa, yameingizwa kwenye bajeti hii. Tunawapongeza sana, tunawapongeza kwamba bajeti imekwenda kujibu hoja za Wabunge na kujibu hoja za Wabunge maana yake ni kwenda kujibu hoja za wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kikubwa zaidi kwenye bajeti hii tunakwenda kujibu masuala ya afya, elimu, maji, umeme na mambo kama hayo. Kuna jambo moja naomba niliongeze kwenye bajeti hii limesahaulika. Tunalo jambo linalozungumzwa kwa jumla ya uhifadhi wa wanyamapori, lakini hapa tumesahau jambo moja kwamba wananchi wale wanaozungukwa na hifadhi za wanyamapori, wanayaonaje matunda ya moja kwa moja kwa kuwepo kwao kwenye hifadhi. Maana leo tunaweza kuzungumza kwamba hifadhi ina faida kwa inaongeza watalii, na mambo mengine kama hayo ya kuinua uchumi, lakini hayo ni mambo ya mbali sana ambayo yanahitaji elimu kubwa kuyaelewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali waende waimarishe WMAs, hapo ndipo wamesahau kwa sababu zile WMAs, wananchi wanahifadhi kwa WMAs ni kwamba wanapopata mapato yao wanajenga shule, madarasa, vyoo. Kwa hiyo wananchi wale wanaozungukwa na hifadhi wanapata ile pinch ya moja kwa moja kwamba kumbe kutokana na hawa wanyama tunapata faida hizi, kuliko hizo ambazo tunatakiwa Wabunge twende tukajieleza, Waziri aje aeleze. Hivyo, kama Serikali wangeimarisha WMAs kwenye maeneo yetu, wananchi wangeweza kupata faida ya moja kwa moja kwa wanyamapori. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapo hapo kwenye WMAs naiomba sana Serikali, kumekuwa na kigugumizi kikubwa sana hata pale ambapo vitalu vya WMAs wakapata wawekezaji, bado yale mafao yao yanakuja kwa kuchelewa sana. Kwa hiyo sasa tunapokwenda kuzunguka kule, wananchi wetu wanapohama mashambani kurudi baada ya kukosa mazao yao, kuliwa na tembo na wanyama wengine wanakosa nini cha kufanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba sana sana, naiomba Serikali, iimarishe WMAs, na kuimarisha WMAs maana yake nini? Kuwasaidia hata kuwatafuta wawekezaji kwenye vile vitalu, vile vile kuvitangaza, unawaachia WMAs watangaze vile vitalu vyao, uwezo wao wa kutangaza ni mdogo sana. Naiomba Serikali kupitia Maliasili waendelee na wao kuitangaza vile vivutio, ambavyo kwenye vile vitalu vinanyomilikiwa na WMAs.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, ambalo naweza kuishauri Serikali katika kuboresha hii bajeti yetu. Jana nimeuliza swali hapa kuhusiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuendelea kufanya upembuzi yakinifu wa barabara mbalimbali nchini. Zipo barabara zimefanyiwa upembuzi yakinifu tangu mwaka 2012, mpaka leo tunatafuta fedha kwa ajili ya kwenda kujenga. Mfano mmojawapo, kuna barabara yetu ya Nachingwea-Masasi, barabara ya Nachingwea – Liwale, barabara ambazo zimefanyiwa upembuzi yakinifu kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini basi Serikali isifikirie sasa isitishe kwanza kuendelea kufanya upembuzi yakinifu ili barabara zile ambazo tayari zimeshafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina, iweze kupata fedha kwa ajili ya kuzijenga. Jambo hili Serikali imelifanya, mwaka huu imepunguza kujenga vituo vya afya, imepunguza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya kwa sababu gani, wapate fedha za kupata vifaa za kumalizia zile hospitali. Naomba na huku kwenye upembuzi yakinifu wafanyeni hivyo, kwamba wajiridhishe barabara ngapi tumeshazifanyia upembuzi yakinifu, zinahitaji fedha ngapi kuzijenga, basi wakasitisha, wakaacha kufanya upembuzi yakinifu kwa barabara zingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, hayo ndio mambo niliona kwamba nije kuwashauri kwa maana kwamba, niwashauri ili waone kwamba wanaweza kupoteza fedha nyingi sana za Serikali. Kwa mfano, nafahamu barabara ambayo imefanyiwa upembuzi yakinifu mwaka 2012, tutakapokwenda kuijenga mwaka 2025 hatutaijenga kwa data zile za mwaka 2012. Kitakachofanyika ni building and design, tunapoteza nyingi. Kwa hiyo nashauri jambo hilo dogo sana walifanye kama ambavyo wamefanya katika sekta zingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, naisifu sana Serikali, tulichangia hapa kutafuta fedha za TARURA, kutafuta fedha za maji vijijini, jambo hili wamekuja nalo vizuri sana, wamekuja kutwambia wameongeza Sh.100 kwenye mafuta; wameongeza tozo kwenye miamala ya simu, jambo zuri, lakini vile vile kwenye line ya simu ni jambo zuri. Hizo fedha mpaka leo tunamwomba Mheshimiwa Waziri, hebu ziwe ring fenced tuzione, kwa sababu zile zilivyo wazi wazi hivi, hazieleweki, haiwezi kuwa sawasawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu zile Sh.100 tuzione moja kwa moja kwamba zile fedha zinakwenda TARURA na hata pale unapoweka mafuta zinaonekana kabisa kwamba imekatwa shilingi kadhaa zimekwenda TARURA kama zilivyo kwenye REA. Leo ukinunua mafuta kwenye REA unaona kabisa kama kuna shilingi kadhaa imeenda REA. Unapofanya muamala kwa simu unaona kabisa kuna shilingi kadhaa zimeenda kwenye REA, tunataka tuone fedha ya mafuta inakwenda moja kwa moja TARURA.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile na zile za kwenye miamala ya simu, tunapofanya miamala ya simu, tuone kwamba hii shilingi kumi imekwenda moja kwa moja kwenye maji vijijini (RUWASA)….

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Hapo ndiyo tutakuwa tumeona vizuri, hiyo ndiyo ring fence ambayo nashauri iwekwe, kwa sababu inaweza kutokea….

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kuchauka kuna taarifa.

T A A R I F A

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Baba yangu anachangia vizuri sana yaani pesa zikifanyiwa vizuri hesabu za mafuta pamoja na kwenye simu zikaenda mahali husika, Taifa hili tutakuwa hatuna shida tena ya barabara. Ahsante sana, nilikuwa nataka nimpe taarifa hiyo tu.(Makofi/Kicheko)

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kama nilivyosema, nilianza kwenye miamala ya simu iende RUWASA na hii ya laini iende maji vijijini, hapo tutakuwa tumefanikiwa, kwa maana kwamba hela ya mafuta inaenda TARURA, hela ya miamala inaenda RUWASA, na hela ya laini inakwenda maji mijini. Huo ndio mchango wangu kwenye bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, mimi ni miongoni mwa Kanda ya Kusini, kwa hiyo kukaa bila ya kuizungumzia korosho nitakuwa sijafanya sawasawa. Nataka niambie Serikali, mazao yote hakuna zao lenye export levy isipokuwa korosho. Lazima tujiulize imetokana na nini hii export levy kwenye korosho. Hii imetokana na kikao cha wadau wa korosho. Walipokaa wadau wa korosho wakasema sisi hili zao za korosho lisiendelee kudumaa tufanye nini? Tukaweka fedha kwenye export levy ili ziweze kurejea kwenye korosho, lakini Serikali baada ya kuona zile fedha ni nyingi na ni tamu wakazihamisha zote wamebebea.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo kwenye kikao cha wadau wa korosho cha mwaka 2020 tumetoa kwa mkulima shilingi 25/= kwenye kila kilo kwa ajili ya kupeleka Naliendele kwenye Chuo cha Utafiti. Tumetoa shilingi 25/= kwenye kila kilo, tumepeleka kwenye Bodi ya Korosho ili Bodi ya Korosho iweze kusimamia zao la korosho. Sasa Muone hii mizigo yote inarudi kwa mkulima. Tunaomba Export Levy irudi kwenye zao la korosho, hata kama siyo hundred percent, lakini mhakikishe angalau hata 50 au 60 zirudi kwenye korosho, vinginevyo zao hili linakwenda kupotea. Nawaomba sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho siyo kwa umuhimu, naomba kuishauri Serikali, tujiondoe kwenye kufanya biashara; tusimamie, tuimarishe Sekta Binafsi. Hatuwezi kuimarisha Sekta Binafsi kama na Serikali nayo itakuwa na taasisi zake zinatamani kufanya biashara. Taasisi zile ambazo zimepewa kusimamia sekta mbalimbali, zenyewe ziwe kama regulator. Siziwe na zenyewe zinafanya biashara, tunakwenda kuharibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, natoa mfano, kuna taasisi moja ya TASAC, kazi yao ilikuwa ni ku-regulate biashara pale bandari, lakini nao pamoja na kwamba tuliwaambia wapitishe zile nyaraka za Serikali tu, leo hata ngano pale kwa Bakhresa wanachukua TASAC. Tunawashauri, tunaomba Serikali, kama tunataka kuimarisha uchumi wa nchi yetu, lazima watu binafsi tuwabebe. Sekta binafsi lazima tuibebe. Tutafute namna yoyote tunavyoweza, Sekta Binafsi ipate nafasi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo, nakushukuru sana. Huo ndiyo ulikuwa mchango wangu kwa leo. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami nitoe mchango wangu. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai na afya njema.

Mheshimiwa Spika, nawapongeze sana Wajumbe wa Kamati wakiongozwa na Wenyeviti wa Kamati zote tatu kwa kuleta ripoti hii ya uchambuzi wa kina kuhusu hii ripoti ya CAG.

Mheshimiwa Spika, naomba nitofautiane kidogo na Wabunge, wenzangu. Pengine utaniongoza; sijajua role yetu kama Wabunge ni ipi katika kuisimamia Serikali? Je, ni kuishauri Serikali tu na kuisimamia? Je, sisi kama Wabunge tuna hakika kwamba tunaisimamia vizuri? Ni nani asiyejua madudu yanayoletwa na sheria ya manunuzi kwenye halmashauri zetu? Nani hajui mwanya mkubwa wa fedha nyingi za nchi hii zinapotea kwa sheria ya manunuzi? Mbunge gani hajui? Tumefanya nini kwa hili? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo Wabunge wengi hapa wametoa mawazo kwamba twende tukawaazimie. Nitoe mfano mmoja, tunataka kumuazimia labda Mkurugenzi wa TANROADS kwa madudu mengi yanayofanywa, na ni kweli kwamba fedha nyingi zinapotea. Hivi ni kweli Mkurugenzi wa TANROADS amepoteza hizi fedha? Sisi kama Wabunge tunaamini Mkurugenzi wa wa TANROADS amepoteza hizi fedha?

Mheshimiwa Spika, unaweza ukamwita Mkurugenzi wa TANROADS akaja na certificates za wakandarasi tatu, nne au tano hazijalipwa. Nani awajibike? Nani anapaswa kuwajibika? Lazima sisi kama Wabunge twende mbali zaidi, siyo tu kuwalaumu watendaji. Wakati mwingine tukizungumza, watendaji wanasema, hawa Wabunge bwana, wanasiasa. Kwa sababu hawaoni tunachokifanya. Hawaoni kwa sababu haya mambo tunayazungumza kila siku.

Mheshimiwa Spika, wakati tunapitia bajeti ya ujenzi hapa, hatukuona tumepitisha fedha kwa barabara zilizoisha? Barabara imeisha mwaka 2021 lakini tumepitisha fedha mwaka huu. Zinakwenda wapi? Zinakwenda kulipa madeni ya Wakandarasi. Nani amezalisha madeni?

Mheshimiwa Spika, tuwe serious kuisimamia Serikali. Hivi ni nani hajui kwenye halmashauri zetu hakuna wahandisi wa kutosha? Katika kuchangia bajeti nilisema, halmashauri zetu hazina wahandisi. Tena wakati ule mimi nilijichanganya kati ya wahandisi na wakadiriaji majengo. Unaweza ukakuta kwenye halmashauri kuna mhandisi lakini hakuna mkadiriaji majengo? Nyumba ya kuingia bati 300, zinanunuliwa bati 400. Nyumba inaingia nondo 10, zinanunuliwa nondo 20. Hatuna mkadiriaji majengo, nani hajui? Nani awajibike?

Mheshimiwa Spika, tunakwenda kumwajibisha Mwalimu Mkuu kwa sababu ujenzi wa shule hajausimamia vizuri. Tunakwenda kumwajibisha DMO kwa sababu kituo cha afya hakijajengwa vizuri, tuko sahihi? Are we serious? Tuna halmashauri ngapi zina wakadiraji majengo? Tuna halmashauri ngani zina wahandisi?

Mheshimiwa Spika, namwonea huruma sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kazi anayoifanya ni kubwa sana na dhamira yake ni njema sana na maono yake ni makubwa sana kwa nchi hii, lakini waliopata dhamana ya kumsaidia Rais wajipime. Kwa sababu akili yangu inakataal unakwenda kwenye halmashauri unakuta madudu.

Mheshimiwa Spika, halafu sasa ukiingia kwenye halmashauri kuna Mkaguzi wa Ndani wa Halmashauri anawajibika kwa Mkurugenzi. Is it fair? Yaani Mkurugenzi ampe mafuta na fedha kwenda kukagua mradi, aende akamkague; atampa? Mkurugenzi atampa usafiri Mkaguzi wa Ndani? Akishaenda kumkagua, hiyo ripoti inasomwa wapi? Siyo sawa, kuna mahali tumepotea. Nashauri, Mkaguzi wa Ndani akae pembeni, awe ni taasisi inayojitegemea. Haiwezekani Mkaguzi wa Ndani akae chini ya Mkurugenzi, amkague Mkurugenzi, siyo sawa.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, mpaka CAG anatuletea madude haya, hivi ni kweli tunasema kwenye Wizara zetu hakuna wakaguzi? TAMISEMI, hakuna wakaguzi? Huku kwenye Maji hakuna wakaguzi? Ujenzi hakuna wakaguzi tumtegemee CAG? Haya madude yapo. Nasi kama Bunge siyo mara yetu ya kwanza kuyaona. Sio CAG peke yake ndio katuonesha! Haya madude yapo!

Mheshimiwa Spika, kuna shida mahali. Kama tuko serious kuna shida mahali. Tuchukulie mfano mwingine, kwenye majengo hayo hayo; hivi ni kweli BOQ ya kujenga darasa moja Dar es Salaam itafanana na ya Njombe? Ndiyo, tunataka majengo yetu yote yafanane kama vituo vya afya vyote; jengo linaweza kuonekana kwa ndani linafanana, lakini ile BOQ ya ndani ni kweli inafanana? Hivi Njombe leo unajenga darasa moja lina feni sita darasani. Umeshafunga mafeni, Njombe, ni kweli!

Mheshimiwa Spika, hayo madarasa yanajengwa Dar es Salaam kwenye joto, Njombe huwezi kuweka feni, lakini unaweza kukuta darasa limejengwa wanakwambia BOQ ndio inavyosema. Hivi Njombe unahitaji dirisha la futi sita kwa sita? Dar es Salaam unahitaji dirisha la futi sita kwa sita kwa sababu ya joto, kuna mahali tunakosea.

Mheshimiwa Spika, nitoe mfano kwenye halmashauri yangu, tumepewa milioni 470 kujenga madarasa. Juzi nilikwenda kukagua, madarasa yote yamekamilika, yote yana feni zinafanya kazi wala umeme hatujui tutapata lini, lakini wamefunga mafeni na kila kitu, lakini hawajajenga choo, hela imeisha. Milioni 28 zimetumika kuingiza umeme kwenye madarasa lakini vyoo havijaisha. Mkurugenzi yupo, Mhandisi yupo, kila mtu yupo na hamna majibu. Ukiwauliza wanakwambia hiyo ndio BOQ, yaani usipofanya hivyo maana yake wewe kibarua chako kiko hatarini.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya umbali uliopo kutoka Liwale kwenda Dar es Salaam ambako wanatakiwa wakanunue vitu vya pamoja wamenunua mpaka bulb, wamekusanya kila kitu kiko stoo, lakini darasa haliwezi kutumika, shule haiwezi kufunguliwa, vyoo hakuna, jengo la maktaba hakuna, fedha zimeisha. Ukienda kuwakagua wametumia vizuri huwezi kuwashtaki. Ndio ile aliyosema kwamba mtu mwingine anaweza akafanya jambo zuri tu kwa nia njema likawa na faida, lakini kwa sababu hajafata Sheria ya Manunuzi akaadhibiwa.

Mheshimiwa Spika, mwingine anaweza aka-mess-up akafanya madudu tu, lakini kwa sababu amefata Sheria ya Manunuzi anaoneka yuko happy. Sasa tufike mahali sisi kama Wabunge, sio tu kuishauri Serikali, twende tuisimamie na inaposhindwa kutekeleza maazimio yetu tuwe na la kufanya. Kama hatuna la kufanya, hapa tutakuwa kama tunapiga story tu, si sawa, kuna shida mahali.

Mheshimiwa Spika, mfano mwingine, MSD inadaiwa na Serikali fedha nyingi tu, lakini halmashauri wanaidai MSD. Sasa ni wajibu wa Mkurugenzi MSD aamue fedha za halmashauri aendeshee taasisi yake, halmashauri wakose dawa au afanyeje sasa?

Mheshimiwa Spika, halmashauri wamepeleka fedha MSD, lakini Serikali hawajapeleka fedha MSD, Mkurugenzi atumie hela zipi kuendeshea ile taasisi? Shida ipo. Lazima kama tuko serious tufumue mifumo yote ya ukusanyaji wa fedha na utumiaji wa fedha, lazima tuwe makini kwamba, fedha tumekusanya kiasi gani, zinakwenda kufanya nini na anayetakiwa kuwajibika ni nani?

Mheshimiwa Spika, leo hii wakienda kumwajibisha Mkurugenzi wanawaonea tu, kule mahali kuna shida. Nimezungumzia Sheria ya Manunuzi, sasa narudi kwenye hoja za CAG. Nafikiri kama Bunge tufike mahali tuseme kama hoja imejirudiarudia ni mara ngapi na kwa muda gani? Tuweke kikomo. Lini hoja ifungwe? Tuweke kikomo na nani awajibike hoja isipofungwa? Vinginevyo CAG anakuja anakwambia hoja zisizofungwa za mwaka 2018 hizi hapa, hoja mpya ni hizi hapa. Nani ambaye amesababisha hoja hazijafungwa? Kwanza nani ameleta hiyo hoja ya ukaguzi? Kuna shida.

Mheshimiwa Spika, sisi Wabunge tunapopitisha bajeti lazima tuwe makini. Tunapopitisha bajeti Wabunge kama kweli tuko serious tuwe makini. Tunapopitisha bajeti ya miradi iliyokamilika lazima tuseme watuambie hizi hela zilichelewa wapi? Barabara imeisha 2018 lakini utakuta bado kwenye bajeti inatengewa fedha, ukiuliza deni la mkandarasi na haliishi, sisi Wabunge tunakubali tu. GAG akija kutustua tunakuwa wakali kwani hakuna kipya mimi ninachokiona hapo kwa CAG alichokileta. Vitu vyote ambavyo kila siku tunaviona, sisi tunabishana sana na Mheshimiwa Waziri wakati tunapitisha Bajeti ya Ujenzi tulibishana naye sana hapa. Akasema hizi fedha tulizopitisha mwaka jana hakuna mradi mpya uliotekelezwa? Akasema hapana zile tumetekeleza mradi uliopita, hatukupitisha hapa? Sasa kitu gani kipya?

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Kuchauka kengele ya pili imegonga…

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, asante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunisimamisha tena hapa nikichangia Wizara hii ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nataka niendelee kuwaasa ndugu zangu wa Kambi yetu hii ya Upinzani, hii Serikali tuendelee kuishauri wale kule tusiwape miongozo wala taarifa, wale ni washangiliaji tuwaache waendelee kushangilia. Sisi tuendelee kuishauri Serikali pengine Mwenyezi Mungu anaweza akawajalia wakaweza kuyasikia na wakayafanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kusema kama ifuatavyo. Kwanza sijaelewa Watanzania tuna matatizo gani? Mwenyezi Mungu atupe nini tufike mahali tuseme Alhamdulillah tumepata tutoke hapa twende mbele? Kwetu sisi madini dhambi, mifugo hatari, kila kitu hatari! Nchi za wenzetu ardhi ni maliasili muhimu sana kwa maendeleo ya mwanadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi ni rasilimali kubwa sana ingeweza kututoa hapa tulipo lakini ardhi hii sisi tunaifanyia nini na kwa nini tunaingia kwenye matatizo ya umaskini wakati ardhi tunayo? Inawezekana kwa sababu ya wingi wetu wa ardhi unatufanya tusijue thamani ya hiyo ardhi. Kwa sababu nchi za wenzetu kuwa na angalau heka 10 tu wewe ni tajiri, unakopesheka, taasisi zote za fedha wanakukopesha lakini ni Mtanzania gani anamiliki ardhi inayomsaidia? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tumefika hapa? Tunatengeneza sera ambazo naona hazina maandalizi. Nitoe mfano pale kwenye Jimbo langu la Liwale, tulipata mwekezaji akajenga shule ya Kiislamu nzuri tu, lakini kupata usajili wa shule hiyo leo ni mwaka wa tano kwa sababu hawana hati miliki. Wakienda kwenye Ofisi ya Ardhi wanaambiwa kijiji ulichojenga hakijaingia kwenye mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa hiyo huwezi kupata hati miliki, tunakwenda wapi? Mtu unaandaa mradi, unakwenda kijijini unatafuta ardhi, wanakijiji wanakupa ardhi, unajenga shule ama zahanati, umeshamaliza sasa unatafuta usajili ukifika Ofisi za Ardhi unaambiwa hicho kijiji hakijapimwa, hakiko kwenye mpango bora wa ardhi, kwa hiyo hatuwezi kukupa hati, hao ni Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii Wizara ya Ardhi naweza kusema ni kama Wizara mtambuka. Kuna Sera za Wizara kibao zimeingia hapa, mkanganyiko ni mkubwa, hatuelewi tunakwenda wapi. Kuna Sera ya Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo, Wizara ya Madini na Wizara inayoshughulika na Misitu, hawa watu wote wanavurugana tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano mwingine, pale kwenye Jimbo langu walikuja hawa jamaa wa TFS, watu wa misitu, wamewapimia watu mpaka kwenye nyumba zao, kwa sababu maskini wale hawajui utaratibu ukoje, walikuja pale wakadanganywa, wakapima mpaka unakosa hata mahali pa kuchimba choo, ukitoka kidogo unaambiwa hapa ni kibao cha TFS. Hapa ndiyo mchanganyiko sasa wa makazi na misitu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu kitu kinachonishangaza hizi taasisi ni za Serikali. Hivi inawezekanaje taasisi ya Serikali inakwenda kijijini inawadanganya wananchi, wanaingia mkenge baada ya miaka miwili, mitatu ukienda kuuliza unaambiwa ni ninyi wenyewe wanakijiji ndiyo mlipitisha hii. Tulipitisha hatukujua hilo na ninyi ni taasisi ya Serikali mlitakiwa mtoe elimu. Sasa inafika mahali wananchi wanakosa mahali hata pa kukata kuni, wanaambiwa Mwenyekiti wenu wa Kijiji ndiyo alisaini lakini alijua hilo? Ndiyo hapo unapopata mkanganyiko kwamba jamani hii Serikali tunakwenda wapi, kwa nini hii neema ya ardhi isiwe ndiyo neema kwetu iwe ni majanga? Kitu gani ambacho tunaweza tukakipata tukakiona kwamba hiki kwetu ni neema? Namwomba Mheshimiwa Waziri ashirikiane na Mawaziri wenzake waangalie hizi sera, hii mikanganyiko inatoka wapi? Wananchi wetu hawa kwa nini tuwadhulumu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee katika upande huo huo wa ardhi. Kule kwangu nimewahamasisha vijana wameunda vikundi vya ufugaji na vya kilimo, lakini wale watu wakiandika andiko watafute wafadhili wanatakiwa wapate hati, mfadhili huyo watampataje? Matokeo yake vijana wale wamekwama, hawana wanachofanya, wakija mjini mnawafukuza, sasa wafanye nini, nani mwenye jukumu la kupima hii ardhi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye viwanja. Liwale bei ya kiwanja ni ghali sana. Nimekwenda nikamuuliza Mkurugenzi kwa nini hii hali ipo hivi? Akaniambia mimi sina wapimaji, nawachukua Nachingwea. Kwa hiyo, nikiwachukua Nachingwea wanakuja hapa nawalipia hoteli na kadhalika, kwa hiyo gharama ya kupima viwanja ipo juu, watu wanashindwa kumudu kununua viwanja. Sasa hili jukumu la kupima viwanja ni la nani? Hivi unawezaje ku-hire wapimaji kutoka sehemu nyingine kwenda sehemu nyingine halafu unakuja kwa mwananchi unamwambia bwana gharama ya kiwanja imekuwa kubwa kwa sababu tuna-hire wapimaji kutoka maeneo mengine, Mheshimiwa Waziri hili ni tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu zote wananchi wetu wako mbele ya maendeleo kuliko Serikali na ndiyo hapo mgogoro unaanza. Mtu anakaa pale kesho na kesho kutwa unamhamisha eti panataka kujengwa hospitali sijui amekaa kwenye makazi yasiyo bora sijui pamefanyaje, mlikuwa wapi? Huyu mtu anaweka nguzo ya kwanza mpaka anamaliza tofali la mwisho anahamia mlikuwa wapi? Ndugu zangu, namtakia kila la kheri Waziri mwenye dhamana, lakini nataka tu nimtahadharishe kwamba uwepo wa ardhi nyingi Tanzania imeonekana hatuithamini, kama tungekuwa tunathamini ardhi leo tusingekuwa hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye majengo kujengwa chini ya kiwango. Naamini Shirika la National Housing lina Wahandisi wengi wa kutosha inafikaje mtu unajenga jengo linakuwa chini ya kiwango, hii ni rushwa! Mkandarasi kuipata hiyo tenda anatumia zaidi ya nusu ya fedha aliyotenda. Hivi ni injinia gani atakwenda kumsimamia yule mkandarasi kumwambia hili jengo umejenga chini ya kiwango wakati tayari ameshachukua hela kutoka kwake, anaupata wapi ujasiri wa kumkemea?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii na mimi nitoe mchango wangu kwenye Wizara hii ya Maliasili. Wizara ya Maliasili ni Wizara ambayo nilikuwa naisubiri kwa hamu sana kwa sababu asilimia 60 ya Wilaya ya Liwale ni Mbuga ya Selous. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sina wasiwasi na weledi, ufahamu na nia ya Mheshimiwa Waziri. Tunalo tatizo kama Watanzania, tunazo fursa nyingi sana Watanzania, lakini maisha yetu fursa hizi hazijawahi kutusaidia. Hivi najaribu kujiuliza nini tatizo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ufahamu wangu mdogo tatizo la Watanzania ni kwamba tumepoteza uzalendo wa nchi yetu, tumetawaliwa na ubinafsi. Hii ndiyo sababu kubwa inayotufanya tushindwe kufikia malengo yetu pamoja na kuwa na rasilimali za kutosha katika nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye vivutio vya utalii hasa malikale. Hapa tunalo tatizo la Watanzania kupoteza historia ya nchi yetu. Tunashindwa kutambua vivutio vilivyopo kwenye nchi yetu ni kwa sababu watu tumepoteza historia ya nchi yetu, hatujui historia ya nchi yetu, tumepoteza hata jiografia ya nchi yetu. Natoa wito kwa Waziri wa Elimu aimarishe somo la historia na jiografia pengine vizazi vijavyo vitaweza kukumbuka haya ninayoyasema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kuisahau Liwale kama utaikumbuka vita ya Majimaji. Lipo boma pale la Mjerumani linaitwa Boma la Mdachi, boma lile pale mpaka leo ziko picha za wahanga wa vita ya Majimaji, ziko sanamu za wahanga wa vita ya Majimaji. Nani analikumbuka Boma la Liwale leo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Liwale tunao mlima ule tunauita Mlima Lukundi, uko Lilombe, mlima ambao ulikuwa na volcano iliyolala, nani anaijua hii? Tumepoteza historia. Naomba turudi kwenye historia, tutaweza tu kuzikumbuka hizi rasilimali zetu kama tutakwenda na historia ya nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Hifadhi ya Selous, asilimia 60 ya Wilaya ya Liwale imezungukwa na Mbuga ya Selous katika vijiji vya Mpigamiti, Barikiwa, Ndapata, Kimambi na Tukuyungu, lakini kuwepo kwetu Selous hakujatusaidia chochote. Nimezunguka katika vijiji hivi nilivyovitaja hatuna alama yoyote kuonesha kwamba sisi tuko karibu na Selous. Hatuna hoteli, hatuna barabara, hatuna miundombinu yoyote wala hatuna kiwanja cha ndege.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaambie kwa Kusini nzima kwa upande wa utalii tumeiacha nyuma. Lindi hakuna hoteli, Mtwara hakuna hoteli. Mtwara ndiko kuna uwanja wa ndege, lakini siyo ule wa Kimataifa kama ambavyo viwanja vingine vipo. Sasa tunategemea ile rasilimali ya Kusini, ule utalii wa Kusini ni nani atakuja kuukumbuka? Kama Mjerumani anaijua Kusini kwa nini Watanzania tusiijue?
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mji wa Liwale kuna kumbukumbu ya Mikukuyumbu, pale ndipo ambapo mmisionari wa kwanza kuja Pwani ya Afrika Mashariki waliuwawa pale. Mpaka leo Wafaransa wanakuja Liwale, wanakuja Mikukuyumbu kuzuru pale, lakini Watanzania hatuna habari hiyo, tumepoteza historia yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu askari wa wanyamapori, mimi nina wasiwasi na askari wa wanyamapori, aidha kwa sababu ya kutokutunzwa vizuri wanafanya haya mambo makusudi kuwachonganisha Serikali na wananchi. Kwa sababu vitendo wanavyovifanya askari wa wanyamapori havilingani na ubinadamu. Mimi nasema hivyo kwa ushahidi, ninayo picha hapa, huyu ni Mwenyekiti wa Kitongoji wa Kijiji cha Kichonda, hana mkono wa kulia, amekatwa mkono mnamo tarehe 08 Septemba, 2015 tukiwa kwenye kampeni na kesi yake imefutwa tarehe 08 Februari, 2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kesi hii kisa chake ni nini, huyu amekatwa mkono akiwa nyumbani kwake. Askari wa wanyamapori wametoka porini wamemfukuza mtu na pikipiki wamesema ameingia pale kijijini wanataka kwenda ku-search. Wanakivamia kile kijiji kufanya searching nyumba kwa nyumba. Mwenyekiti wa Kitongoji akatoka akawauliza, ninyi mmekujaje hapa? Mbona hamna kibali cha polisi? Mbona hamjasindikizwa na polisi? Mbona hamjaja ofisini? Imekuwaje muwaingilie watu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo ni kosa lake lililomfanya akose mkono na file la kesi yote ninalo hapa. Hii kesi imefutwa na Wakili wa Serikali. Wakili wa Serikali anasema silaha zile zilikuwa ni zaidi ya moja, kwa hiyo, haijulikani katika zile silaha ni ipi iliyomjeruhi huyu mkono, yule mshtakiwa ameshindwa kumtia hatiani kuona kwamba je, ni bunduki yake au bunduki nyingine? Ndiyo kesi ikafutwa hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema hawa askari wa wanyamapori wana ajenda ya siri na Serikali yenu, inawezekana hamuwahudumii vizuri, wanafanya mambo kuwachonganisha ndiyo maana watu wengine wote hapa watasema, utampaje adhabu mtu afanye mapenzi na mti ina uhusiano gani? Tunaomba hawa askari waangaliwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu upande wa TFS. Jamani TFS ni taasisi ya Serikali, lakini hii tuiangalie, hawa TFS kwa jinsi nilivyowaona wao kazi yao ni moja tu, kufanya udalali wa mbao na mali za misitu, hawana kazi nyingine wanayoifanya. Ukiwauliza mna mikakati gani ya kuendeleza misitu, hawajui chochote. Wao kazi yao ni kugonga mbao, kugonga mali za misitu, basi wamemaliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala hili la kitanda. Tunaomba hili suala la kitanda mliangalie. Kwa nini Kusini leo hii tumetengeneza vijana wajiajiri, wana viwanda vyao vidogo vidogo vya mbao, lakini havina soko. Ukinunua kiti Liwale, ukinunua kiti Kusini huwezi kukisafirisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hatujui kwamba zile mbao zote wanazotengeneza furniture ni za wizi, maana haiwezekani? Watu wanakwenda mpaka kwenye majumba, kwenye paa. TFS wanafuata mbao kwenye paa zinashushwa. Sasa mbao zimefikaje kule? Hili ni suala ambalo tunatakiwa tuliangalie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao mgogoro kwa upande wa Liwale. Mgogoro ule umetengenezwa kati ya Hifadhi ya Selous pamoja na Kijiji cha Kikulyungu, huu mgogoro ni wa muda mrefu sana. Tatizo lake ni kwamba huu mgogoro wakati walikuja kutengeneza barabara wakasema tutengeneze barabara ili tuweze kufanya patrol, lakini badala yake leo wanasema ule ndiyo mpaka wa Selous. Hata GN hawana, lakini ukienda kuwauliza hakuna wanachofanya zaidi ya kupiga watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikuambie hiki Kijiji cha Kikulyungu leo askari hakuna anayekanyaga, hivi vijiji nimevitaja hapo zaidi ya vitano, ina maana vijiji vyote hivi vikifunga njia Selous askari wa wanyamapori hawaingii. Tutafikia huko iwapo huu mgogoro hautaweza kutatuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, narudi sasa kwenye wanyamapori, tembo, simba pamoja na nguruwe. Kule kwetu ukisikia njaa Liwale imeletwa na nguruwe, ukisikia njaa Liwale imeletwa na tembo, simba kule Liwale ni kama mbwa au kama paka wako wengi sana, tunaomba mje mtusaidie. Tunapokwenda pale kituoni kuomba msaada tunapovamiwa na simba wanatuambia usafiri hawana. Hawana askari wakutosha, watu wetu wanateseka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi kabla sijaja Bungeni nilikwenda kwa Mhifadhi wa Kanda anaitwa Salum, nikamwambia Salum kinachokubakiza hapa ni uvumilivu tu wa hawa watu, siku watakapokataa huna kazi hapa. Haiwezekani watu wanauwawa, haiwezekani watu mazao yao yanaliwa wewe unakuja hapa unaleta nahau. Nikamwambia Salum tafadhali, siku nitakayokuja kusema nimechoka, huna salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mtusaidie, Mikoa ya Kusini mtuwekee hata Chuo kimoja cha Misitu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mchango wangu nianze katika sekta ya utalii. Juhudi ya Serikali katika kutengeneza vivutio vya utalii bado siyo wa kuridhisha kwani kuna vivutio vingi bado hatujaweza kuvitambua na kuvitangaza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu malikale, ukanda wa Kusini kuna vivutio vya malikale kama vile Boma la Mdachi (Wajerumani) lililojengwa miaka ya 1904 -1907 wakati wa vita vya Majimaji Mjini Liwale. Ndani ya boma hili kuna mabaki ya sanamu na michoro ya watumwa kwa ajili ya biashara ya utumwa.
Vilevile katika ukanda wa Liwale kuna milima ya Rondo yenye misitu na vipepeo ambao hawapatikani popote duniani. Tunayo pia bwawa la Mlembe na Kiulumila. Haya ni mabwawa yenye mamba na viboko wenye kuwasiliana na wazee wa mila zetu.
Kuhusu ulinzi wa misitu yetu siyo wa kuridhisha. Kuna Mamlaka ya Uvunaji wa Mali ya Misitu (TFS). Taasisi hii imekuwa kero kubwa kwa watu wanaokaa karibu na hifadhi zetu. Badala ya kuwa na wastawishaji wa misitu wamekuwa waharibifu wakubwa wa misitu yetu. TFS wanatuhumiwa kila mahali kuwa wao ndiyo waharibifu wakubwa wa misitu yetu. Kazi kubwa inayofanywa na watu hawa ni kugonga mihuri tu na kusafirisha mazao ya misitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu migogoro ya mipaka, kumekuwa na migogoro mingi ya mipaka kati ya hifadhi zetu na wanavijiji. Hali hii huchangiwa sana na watendaji wa hifadhi kusogeza mipaka bila kushirikisha jamii husika. Mfano mgogoro wa kijiji cha Kikufungu Wilayani Liwale uliosababishwa na wahifadhi kuhamisha mpaka wa hifadhi bila kushirikisha jamii. Mgogoro huu una zaidi ya miaka kumi sasa. Hadi sasa zaidi ya watu wanne wamepoteza maisha na kuharibu kabisa mahusiano ya askari wa hifadhi na wanakijiji. Aidha, kijiji cha Ndapata wako watu wawili wamepoteza maisha kwa sababu ya mgogoro huu wa mipaka.
Kijiji cha Kichonda Mwenyekiti wa Kitongoji mwezi wa 8 mwaka 2015 amekatwa mikono na askari wa wanyamapori hadi leo hakuna kesi wala fidia juu ya kadhia hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wa Lindi sehemu kubwa ni sehemu ya Selous lakini kwa masikitiko makubwa Mkoa huu hauna manufaa yoyote na Selous. Mkoa wa Lindi hasa Wilaya ya Liwale hakuna hoteli ya kitalii Mkoa wa Lindi pia kiwanja cha ndege cha Mkoa wa Lindi hakijapanuliwa na kuwa na hadhi ya kuwezesha ndege kubwa kutua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Nangurukuru - Liwale ndiyo barabara ingewapeleka watalii kwenye hifadhi hiyo. Kanda ya Kusini haina Chuo cha Misitu Kanda nzima. Eneo kubwa la Hifadhi ya Selous ipo Mkoa wa Lindi Wilaya ya Liwale. Kuhusu ulinzi shirikishi, Serikali imeweza sana kwenye ulinzi wa silaha na mabavu kama njia pekee ya kulinda hifadhi zetu, jambo ambalo halina tija kubwa zaidi ya kuongeza uhasama baina ya wahifadhi na jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu katika hili Serikali ijikite zaidi katika kutoa elimu juu ya ulinzi shirikishi sambamba na kuwaonyesha wananchi faida itokanayo na hifadhi zetu. Kwa mimi nadhani walinzi wa kwanza wawe wale watu wanaozungukwa na hifadhi husika badala ya kutumia silaha zaidi na kuendelea kuua watu na kuongeza uhasama. Mkoa wa Lindi hatujaona faida ya moja kwa moja inayotokana na hifadhi ya Selous zaidi ya kushuhudia mauaji.
Kuhusu uhaba wa watumishi na vitendea kazi, kwa Wilaya ya Liwale uhaba wa watumishi wa wanyamapori kumesababisha hasara kubwa sana kutokana na wanyama kuharibu mashamba ya wakulima. Ukienda kutoa taarifa watakujibu hawana gari au watumishi wa kwenda kuwasaidia watu hao wa vijiji vya Mpigamiti, Barikiwa, Kimambi, Kikulyungu na Ndapata wanakabiliwa na njaa mara kwa mara kutokana na mazao yao kuliwa au kuharibiwa na wanyama kama tembo na nguruwe. Nguruwe wamekuwa ni tishio kubwa sana kwa wakulima wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la watu kuliwa na simba Wilayani Liwale ni kubwa sana hasa baada ya watu kunyang‟anywa silaha zao kwenye Operesheni Tokomeza. Wizara ifikirie namna bora ya kuanza kurudishiwa silaha watu wale ili zisaidie kuimarisha ulinzi vijijini hasa zile silaha ndogo ndogo. Naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze mchango wangu kwa kumwomba na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia uhai na afya na kuniwezesha kutoa mchango wangu kwenye Wizara hii. Katika Wizara hii nitakuwa na mambo makuu matatu au manne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze na migogoro ya ardhi kati ya maeneo ya majeshi na wananchi, yako maeneo mengi, aidha wananchi wamevamia maeneo ya jeshi au wanajeshi wamevamia maeneo ya wananchi. Kwa mfano katika Wilaya ya Nachingwea, ni vizuri sasa mgogoro huu ukaisha kabla haujaleta madhara makubwa. Katika kukabiliana na mambo haya ni vyema sasa maeneo yote ya Majeshi yakapimwa ili kuwapatia Hati Miliki na hivyo kutambulika rasmi kwa mujibu wa sheria. Maeneo ya Jeshi kukosa hati miliki ni jambo baya sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kuishauri Serikali ni kuikamilisha bajeti ya Wizara hii, kwa maana ya fedha za miradi ya maendeleo. Kuacha kutoa fedha za maendeleo katika Wizara hii ni kudhoofisha ulinzi na usalama wa nchi yetu. Kwani hakuna ulinzi endelevu bila ya miradi ya maendeleo hasa kuwa na vifaa vya kisasa na kuendelea kuwa na mafunzo ya mara kwa mara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jambo la kusikitisha sana kuona wanajeshi wetu hawana Bima ya Afya zao pamoja na kuwa na Hospitali za Jeshi. Bima ya afya kwa wanajeshi na familia zao ni muhimu sana, kwani wako wanajeshi ambao wanaishi nje ya Kambi za Jeshi hivyo, wanapopata matatizo ya usiku wanakuwa mbali na Hospitali za Jeshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu malipo ya wastaafu kuchelewa ni jambo la hatari sana kwani wanajeshi hao wameitumikia nchi yetu kwa weledi mkubwa na hivyo kuchelewa kuwalipa ni kutowatendea haki zao. Naishauri Serikali kutoa fedha zote zilizopitishwa na Bunge na zitoke kwa wakati ikiwa na mafao ya wafiwa ambao familia zao zimepoteza wapendwa wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi Kushiriki Shughuli za Kisiasa. Kumeanza kuibuka utamaduni wa kushirikisha wanajeshi kushiriki kwenye shughuli za kisiasa. Jambo hili linaweza kupunguza sifa nzuri ya Jeshi letu, jambo hili ndilo linaloharibu Jeshi la Polisi kwani Jeshi la Polisi huwezi kulitenga na siasa kwani ni jambo la kawaida sana nchini kuona Polisi wakifanya siasa hadharani. Naishauri Serikali kuacha mara moja tabia hii isije ikatuletea madhara makubwa nchini. Wanajeshi waachwe wakae makambini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Jeshi linaloitwa Jeshi la Akiba (Mgambo). Jeshi hili hivi sasa halijapewa kipaumbele kama mwanzo kuanzia bajeti yake mpaka watumishi walioko kwenye halmashauri zetu Makamanda wa Mgambo wa Wilaya na Mikoa hawana vitendea kazi muhimu na fedha za kutosha kuendesha ofisi zao. Maafisa hawa huonekana wakati wa kuandikisha wanamgambo wapya tu na wakati wa kuandikisha vijana wa kwenda JKT. Vile vile vyeti vya vijana wanaomaliza mafunzo ya Jeshi la Akiba (Mgambo) vinachelewa sana na pengine kukosekana kabisa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii kwa dakika tano hizi. Nami nichangie Wizara hii ya Maji. Sina wasiwasi na dhamira ya Mawaziri wote wawili wa idara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wasiwasi wangu ni hizi takwimu. Takwimu hizi tunazoletewa, nina wasiwasi nazo kwa sababu hapa takwimu inasema kwamba, wanaopata maji safi na salama imefikia asilimia 72, hapo ndipo wasiwasi wangu unapoanzia, ndipo hapo unapokuja umuhimu wa kuwepo na Mamlaka ya Maji Vijijini, kwa sababu najua hizi takwimu siyo wao wamezileta ila wao wameletewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano; kwenye jimbo langu tunapata maji kwa asilimia 47 katika mradi wa Vijiji 10, vile ambavyo World Bank walitoa fedha, sisi tumefanikiwa kupata vijiji vitatu tu ambavyo sasa maji yanapatikana. Katika vijiji 76, tumepata vijiji vitatu tu, ambavyo ni Vijiji vya Mpigamiti, Mbaya na Barikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, kulikuwa na mradi wa kutafuta chanzo cha maji kwa ajili ya maji ya Liwale Mjini. Palitolewa pesa, shilingi milioni 200, lakini katika zile pesa, mpaka sasa hivi shilingi milioni 55 zimeshatumika na bado chanzo mbadala cha maji hakijapatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, shilingi milioni 20 zimetumika katika kutafuta chanzo cha maji katika Mji wa Makunjiganga lakini maji hayajapatikana. Shilingi milioni 35 zimetumika katika Kijiji cha Mikunya, pale kumepatikana maji ya lita 5,000 kwa saa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mahitaji ya Wilaya ni lita 25,000 kwa saa. Kwa hiyo, Mkandarasi Mshauri akasema, pampu ile sasa ifungwe kwa ajili ya Vijiji vya Mikunya na Liwale „B‟. Kwa hiyo, chanzo cha maji katika Liwale Mjini bado ni kitendawili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, tulikaa kwenye kikao cha Halmashauri, tukawashauri, badala ya hizi pesa kuendelea kutafuta vyanzo, zitakwisha shilingi milioni 200 bila kupata chanzo mbadala. Tukaiagiza Halmashauri sasa ifanye utaratibu mwingine labda tutafute kuchimba mabwawa; labda tuvune maji kwa mabwawa badala ya kuendelea kutafuta vyanzo mbadala kwa sababu hakuna mahali ambapo itachimba, utapata maji yenye ujazo wa lita 25,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, tuna Vijiji vifuatavyo ambavyo kwa shida ya maji iliyopo Liwale, watu wanahama kuanzia asubuhi wanarudi jioni na ndoo moja. Vijiji kama Kichonda, Kipule Magereza, Kiangara, Mbumbu, Nangano, Kikulyungu, Mkutano, Miluwi na Makata; hivi vijiji watu wanaamka asubuhi, wanarudi jioni na ndoo moja. Sasa ninapoambiwa kwamba kuna asilimia 72 ya watu wanaopata maji, napata wasiwasi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye miradi ya umwagiliaji; tunayo miradi miwili ya umwagiliaji katika Jimbo langu. Kuna mradi wa Ngongowele. Ule mradi wa Ngongowele umeshakula pesa zaidi ya shilingi bilioni moja mpaka sasa hivi zimeteketea na ule mradi umesimama. Tulipokwenda kuwafuata pale, Mkandarasi Mshauri anasema ili huu mradi uweze kuendelea, panatakiwa bilioni nne ili uweze kutumika masika na kiangazi. La sivyo, utumike kwa masika tu, panahitajika shilingi milioni 800.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ule mradi kutumika masika tu, wanakijiji hawako tayari. Wanasema kama mradi unatumika masika tu, sisi masika tunalima. Sisi tulivyokubali huu mradi lengo lilikuwa utumike masika na kiangazi. Kwa hiyo, hata kama zitapelekwa shilingi milioni 800 leo, ule mradi wanakijiji hawako tayari kuupokea kwa sababu hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu mradi wa Mtawango, nashukuru Alhamdulillah kwamba sasa hivi unaendelea vizuri, umefikia asilimia 95. Ushauri wangu, kama ambavyo wachangiaji waliotangulia walisema, kweli tunahitaji Mamlaka ya Maji Vijijini kwa sababu hawa Wakandarasi na Wasimamizi wa miradi hii Vijijini hakuna wasimamizi wa kutosha. Kwa ilivyo jiografia ya Liwale, juzi nilikuwa naongea na Naibu Waziri, nafikiri; ameshindwa kufika Liwale kukagua ile miradi miwili kwa sababu ya jiografia ya Liwale, hakufikiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Liwale tunakwenda sisi tunaokujua, lakini kwa watu kama Mawaziri kama ninyi kufika Liwale inakuwa ni shida. Sasa itakapoundwa hii Mamlaka ya Maji nafikiri hawa ndio wanaweza kufanya usimamizi huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sio hivyo tu, katika Halmashaui ya Wilaya ya Liwale, tunao uhaba wa mafundi kwa maana ya wataalam. Mtaalamu aliyepo pale mwenye cheti ni mmoja tu, wengine wote waliopo ni mafundi wa spana tu wa mitaani. Kwa hiyo, hili nalo ni tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hii miradi ya vijiji hivi vitatu nilivyovitaja, kuna kijiji kimoja kisima kimechimbwa; Kijiji cha Kiangara, kijiji hiki maji ni ya chumvi, hayatumiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru katika hotuba yake Mheshimiwa Waziri, nimeona kuna shilingi milioni 300 nyingine zimetengwa hapa. Naendelea kusisitiza kuhusu usimamiaji wa hizi fedha. Kama tusipopata usimamizi wa kutosha, kitakachotokea ni hiki hiki ambacho kimetokea kwenye hizi shilingi milioni 200 za awali na hii miradi ya kwanza Vijiji 10 na badala yake tukaambulia vijiji vitatu tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hayo, naomba kwa sababu nilipewa tu dakika tano na shida yangu ilikuwa ni hiyo tu, naomba niishie hapo. Ahsanteni sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii jioni hii. Naomba niende moja kwa moja kwenye mchango wangu nikiangalia vipaumbele vilivyoainishwa kwenye huu mpango. Nimesoma vipaumbele vyote vilivyotajwa sijaona kipaumbele cha kilimo na sisi tunajitangaza kwamba tunataka kwenda kwenye Taifa la viwanda. Lakini kwenye miradi hii ambayo imetekelezwa, hakuna mradi hata mmoja wa kilimo uliotajwa hapa. Nikifika na kwenye miradi ambayo inatekelezwa nako vilevile sijapata mradi hata mmoja wa kilimo unaotekelezwa zaidi ya kuona kuna Kijiji cha Kilimo Morogoro. Sasa je, hilo shamba ni la mazao gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, si hivyo tu, ulaji wetu kama Watanzania sasa hivi umebadilika, sasa hivi tunakula sana kwenye mazao ya chakula (ngano) kuliko mazao ya mahindi au mchele kama tulivyozoea. Lakini kwenye mpango huu sijaona mahali popote ilipotajwa kuendeleza hili zao la ngano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na mashamba ya ngano NAFCO, yale mashamba sijui yamepotelea wapi. Na hapa nataka ni-declare interest, mimi ni msindikaji wa nafaka. Ngano hii kiwanda kimoja cha Bakhresa peke yake anasindika tani 2,700 per day na hizi tani 2,700 anazosindika kwa siku zinatoka nje a hundred percent, Tanzania tumelala. Leo hii tunakuja tunasema kwamba tunataka kuimarisha viwanda, hapo napo sijapaelewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nirejee kwenye takwimu, hizi takwimu za Mheshimiwa Mpango bado hazijanishawishi. Kwa sababu kwenye akiba ya fedha, pesa za kigeni, tunasema tunayo akiba ya pesa kuendesha miezi 4.1, hapohapo mwisho kabisa anasema kwamba hii ni zaidi ya lengo la chini kabisa ambalo ni la miezi minne. Huko kuongeza tu kwa pointi moja tayari ni sifa kwetu kuona kwamba tumepiga hatua, lakini je, hizi takwimu zinalingana na takwimu za ongezeko letu Watanzania?
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana unaweza kujisifu kwamba wewe ni mtu wa kwanza darasani kwa kupata asilimia 30, ndiyo hiki ninachokiona hapa, lakini kama kweli tuna nia nzuri ya kuwatendea haki Watanzania, naomba kabla hatujafika kwenye mpango huu turejee kwanza kwenye sensa ya watu waetu ili huu mpango na haya maendeleo tunayojisifu kwamba uchumi wetu unaimarika, unalingana na idadi ya watu tulionao unaowahudumia huu mpango? Ndiyo maana leo hii Serikali inasema uchumi umeimarika, lakini kwa watu tunaokaa nao wanaona hakuna kitu kinachofanyika, ni kwa sababu ule uchumi unaowahudumia ni wengi kuliko hivyo mnavyotarajia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nataka nijielekeze kwenye kufungamanisha maendeleo ya watu na uchumi, hapa napo mmetuacha mbali sana. Leo hii tunaposema hivi, tumeacha vijana wanahangaika, kilimo ambacho kinaajiri watu wengi bado ni kilimo chetu kilimo cha mkono. Zipo taasisi zinakopesha matrekta kwa ajili ya kilimo, lakini hizi taasisi sharti la kwanza uwe na hatimiliki ya shamba. Leo hii nani mkulima wa kijijini anaweza ku-access kupata hatimiliki ya shamba, tunawaacha wapi hawa vijana, na hii tunaposema tunafungamisha maendeleo ya uchumi na watu wetu tumewaacha wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, turejee kwenye sekta binafsi, sekta binafsi sasa hivi ndiyo imechukua ajira kubwa sana, lakini hivi asubuhi hapa nimeuliza swali, ni asilimia ngapi ya Watanzania wana hudumu kwenye hivyo viwanda. Lile swali nimeuliza asubuhi hapa sasa nina messages zaidi ya 100 kwenye simu yangu, watu wanasema kweli wanateseka. Nimepigiwa simu kutoka Arusha, Dar es Salaam, Mbeya, watu wanalalamika, hivi viwanda wanahudumiwa na watu wa nje tu, hakuna Mtanzania anakwenda pale akapata ajira, lakini Watanzania bado tunasema tunahimiza uwekezaji. Lakini je, tunapohimiza uwekezaji tupo tayari kufuatilia hawa wawekezaji kwamba wanakidhi masharti ya nchi yetu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kwa upande wa umiliki wa ardhi. Kumiliki ardhi hapa kwetu tatizo ni kubwa sana na hakuna mtu ambaye anaweza ku-access, mtu wa kijijini akaweza kupata hakimiliki. Upimaji sasa hivi wanasema kwamba eka moja ni shilingi 300,000, kitu kama hicho. Sasa hivi mtu wa kijijini ili aweze kupata shamba la eka 10, 20 atahitaji pesa kiasi gani na atazipata wapi? Kwa hiyo, naona huu mpango, pamoja na kwamba nia ni nzuri, lakini utekelezaji wake na upangaji wake haufanani na hali halisi ya watu wetu wanavyoishi huko vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee kwa upande wa…
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, nianze mchango wangu kwa kuniwezesha kuchangia Wizara hii muhimu kwa ustawi wa wananchi wetu. Katika nchi yetu, tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama bado ni sugu sana. Hata hivyo, bado Serikali haijaonesha nia thabiti ya kupambana na janga hili. Ndiyo maana hadi leo katika bajeti ya Serikali haioneshi umuhimu wa Sekta ya Maji ingawa sera inamtaka mwananchi kupata maji kwa umbali wa mita 400, lakini hadi sasa kwenye Halmashauri zetu tatizo la maji bado ni kubwa sana. Bajeti ya Wizara ya Maji haiwezi kujibu tatizo la maji nchini, kwani fedha zilizotengwa ni kidogo sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Skimu ya Umwagiliaji ni muhimu sana kwa Taifa letu kwa hivi sasa, kwani kilimo cha kutegemea mvua kimepitwa na wakati hasa ukizingatia hali ya mabadiliko ya tabianchi. Serikali bado haijaonesha umuhimu katika sekta hii, kwani miradi mingi ya skimu ya umwagiliaji haijapewa kipaumbele, ndiyo maana hata pale mradi unapotekelezwa chini ya kiwango, Serikali haioneshi nia ya kufuatilia hatma ya miradi mingi ya umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano, katika Wilaya ya Liwale kuna miradi mitatu ya umwagiliaji ambayo kati ya hiyo mradi wa Ngongowele umekufa kabisa japokuwa umeshatumia zaidi ya shilingi bilioni moja. Mradi huu sio watu wa Kanda wala Wizara walioonesha nia ya kujua hatma ya mradi huu na miwili iliyobaki bado nayo inasuasua.

Mheshimiwa Naibu Spika, fedha za Mfuko wa Maji mgao wake bado ni wa kiupendeleo. Sijui ni vigezo gani vinatumika kugawa miradi inayofadhiliwa na mfuko huu. Mfano, katika Halmashauri yangu ya Liwale, sasa ni miaka miwili mfululizo fedha hizi hatujawahi kupewa katika mradi hata mmoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, Liwale ni Wilaya ya zamani sana, lakini hali ya upatikanaji wa maji vijijini ni duni sana na wala sijaona juhudi za Serikali katika kukabiliana na shida hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa kutafuta chanzo mbadala wa maji katika Mji wa Liwale uliokuwa chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia, fedha kiasi cha shilingi milioni 200 zilitolewa mwaka 2014, lakini hadi leo mradi huu umekwama bila maelezo yoyote toka kwa wahusika. Fedha za mradi huu zinaendelea kutumika bila kufikia lengo la kutolewa kwake. Hali ya upatikanaji wa maji katika Mji wa Liwale ni mbaya sana. Namwomba Mheshimiwa Waziri aje Liwale ajionee mwenyewe jinsi watu wa Liwale wanavyoteseka juu ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye mgao wa fedha za Mfuko wa Maji nchini, miradi ya maji vijijini nayo inakumbwa na mgao usiozingatia haki katika kuwafikia wananchi wetu. Katika Jimbo la Liwale hadi leo miradi hii imekamilika katika vijiji vitano tu kati ya vijiji 79. Hii ni ile miradi inayofadhiliwa na Benki ya Dunia. Je, ni vigezo gani vinatumika katika kugawa miradi hii? Katika kitabu cha bajeti, Liwale haijatajwa popote kuhusu miradi ya maji vijijini wala mjini.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze na mchango wangu kwa kuangalia vipaumbele vya mpango wenyewe kuelekea Tanzania ya Viwanda. Nilitegemea kuona kilimo kikipewa kipaumbele katika mpango huu, lakini imekuwa kinyume chake sijaona mahali popote pakitajwa kama kipaumbele kwa kilimo cha mazao kama korosho, pamba, katani, ufuta na kadhalika ilikuwa malighafi katika viwanda hivyo. Hata hivyo, sijaona zao la ngano likitajwa popote wakati sasa ulaji wa watu nchini sasa umebadilika kwani sasa ngano huliwa zaidi kuliko mchele, mahindi na mazao mengine ya chakula.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano katika hili kama ifuatavyo:-
Kampuni ya Bakhresa peke yake kwa siku wanasindika tani 2700 za ngano ambazo zote zinatoka nje ya nchi. Katika miradi iliyotekelezwa hakuna mradi wa kilimo zaidi ya kuona mradi wa kuendeleza Kijiji cha Kilimo Mkoani Morogoro.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu viwanda sijaona kiwanda chochote kilichotajwa katika viwanda vinavyotarajiwa kukuza uchumi zaidi ya General Tyre na makaa ya mawe ya Mchuchuma na Liganga. Katika fungamanisha maendeleo ya kiuchumi na maendeleo ya watu hakuna uhalisia kwani hatujawaandaa vijana nchini kushiriki katika uchumi wa kilimo wala viwanda. Wakulima wetu wanashindwa kuondokana na jembe la mkono kwa kuwa hawakopesheki katika taasisi za fedha. Kwani gharama za kupata hati ya kumiliki mashamba bado ziko juu sana kwani hilo nalo sharti kuu kwa taasisi zinazokopesha vifaa ya kilimo kama tractor, hivyo kuwafanya wakulima kushindwa kulima kilimo chenye tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Kilwa sasa imeanza kutoa madini ya gypsum ambayo sasa yanatumiwa na viwanda vyote vya cement nchini. Hata kusafirishwa kwenye nchi za Zambia, Malawi na Afrika Kusini, lakini sijaona mahali ilipotajwa katika mpango huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika taarifa ya Waziri wa Fedha kwa robo ya kwanza, sekta yenye ukuaji mdogo ni sekta ya usambazaji wa maji safi na udhibiti wa maji taka, pamoja na chakula na malazi, hivyo basi kutarajia kupata maendeleo toka kwa jamii yenye huduma hafifu kiafya ni sawa na kukamua ng‟ombe bila malisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, elimu yetu bado ni ya kutegemea ajira kutoka Serikalini au sekta binafsi kwani wahitimu wetu wameshindwa kupata stadi za maisha kulingana na elimu wanayoipata. Vilevile kama hatutakuwa tayari kuboresha maisha ya Walimu na badala yake kuendelea kuwadhalilisha Walimu kwa kuwapa adhabu mbalimbali kama vile kuwapiga viboko mbele ya wanafunzi hakuinui ari ya Walimu hawa ya kufundisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda; mlundikano wa viwanda katika Mji wa Dar es Salaam hasa kwa viwanda vinavyotegemea malighafi toka nje ungeweza kupunguzwa na kusambaza viwanda hivyo mikoa mingine ya nchi yetu. Ikiwa wawekezaji wangeondolewa kodi kwa wale watakaowekeza nje ya Dar es Salaam ili gharama zilingane na yule aliyewekeza Dar es Salaam. Kwa kiwanda kinachofanana kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia kupanua ajira kwa vijana wa mikoa mingine kwa upatikanaji wa ajira.
Mheshimiwa Naibu Spika, sensa ya watu ni muhimu sana kwa sasa kwani takwimu tunazoletewa leo hazina uhalisia ukilinganisha na idadi ya watu. Hayo maendeleo ya kukua kwa uchumi tunayapima kwa kigezo gani wakati hatuna takwimu halisi ya idadi ya watu wetu. Ndio maana matamko mengi ya Serikali kuhusu huduma za jamii yanakosa uhalisia kwa wananchi wa hali ya kawaida. Haingii akilini mtu kuambiwa uchumi unakua wakati kipato cha mtu mmoja mmoja kinashuka.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumshauri Waziri mwenye dhamana ni bora akazingatia ushauri wa Wabunge ukizingatia ndiyo wawakilishi wa wananchi. Tunashauri kwa niaba yao kulingana na hali halisi ya maisha ya Mtanzania wa hali ya chini wa kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kushika kalamu na kutoa mchango wangu kwa njia hii ya maandishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze mchango wangu kujadili juu ya Mashirika ya Umma yaliyouzwa kwa bei ya kutupwa. Hapa nitajikita zaidi kwenye Shirika lililokuwa la Usagishaji la Taifa (NMC). Shirika hili lilikuwa na Matawi karibu katika kila mkoa lakini uuzwaji wake haukuzingatia thamani ya mali za shirika hilo. Mfano, kiwanda cha mahindi cha Plot 33 hadi leo hakijulikani kama kimeuzwa au hakijauzwa. Ndugu Amani na Ndugu Mwaipopo walikuwa Wakurugenzi wa Shirika hilo wamehodhi kiwanda hiki kwa faida yao, mpaka sasa mgogoro mkubwa baina ya hao niliowataja na mnunuzi wa awali ambaye alishinda tenda ya shilingi milioni mia sita (600,000,000/=).

Mheshimiwa Mwenyekiti, malipo kwa wastaafu, Serikali imekuwa na kigugumizi kikubwa juu ya kulipa wastaafu hasa kwa wale waliokuwa katika mashirika yaliyouzwa. Mfano, wafanyakazi waliokuwa Shirika la NMC Tawi la Kurasini hadi leo Serikali imeshindwa kuwalipa madai yao ingawa kesi yao imekwishaamuliwa. Hata hivyo, wafanyakazi wa TTCL nao wanaidai Serikali mapunjo yao, nao hadi leo hakuna kinachoendelea. Hawa ni watu walioitumikia nchi hii kwa uadilifu mkubwa. Hivyo ni bora Serikali ikamaliza na watu hawa kwa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mafao kwa wazee ambao hawakuwa wakifanya kazi katika mashirika au Serikalini, hawa ni wakulima je, Serikali ina mpango gani na wazee hawa ambao wakati wao walitulisha kwa chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu wingi wa kodi, bidhaa zinazotengenezwa hapa nchini zinashindwa kushindana kwenye soko kwa kuwa gharama za uzalishaji ni kubwa sana zinazochangiwa kwa kiasi kikubwa na wingi wa kodi na wingi wa mamlaka zinazofanya kazi zinazofanana. Mfano, TFDA, TBS, OSHA, FIRE na kadhalika, jambo hili ni muhimu sana kuangaliwa upya, Wawekezaji wanashindwa kuja kuwekeza kwa wingi huu wa kodi na mamlaka za usimamzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwekezaji katika kilimo; sekta hii haijapewa kipaumbele kama inavyostahili shida kubwa hapa ni upatikanaji ardhi kwa wawekezaji. Jambo la uhaulishaji wa ardhi imekuwa ni kikwazo. Mfano, katika Halmashauri ya Liwale imepata mwekezaji wa kilimo cha alizeti lakini hadi leo anahangaika kupata ardhi, ni miaka miwili sasa. Sasa ni kwa namna gani tunaweza kuingia katika uchumi wa kati wakati sekta ya kilimo ambayo inaajiri watu wengi hatuko tayari kuwekeza katika kilimo.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii na mimi nichangie kwenye hotuba hizi mbili. Awali ya yote nichukue fursa hii kuwashukuru sana Wenyeviti wa Kamati kwa hotuba nzuri walizotuletea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mchango wangu niuelekeze kwanza kwenye upande wa maji. Asubuhi nimeuliza swali la nyongeza hapa jibu nililolipata ni tofauti na matarajio. Mimi nimeongelea Mradi wa Ngongowele nimejibiwa mradi wa kijiji kingine tofauti kabisa na mtaa wangu. Mradi wa Ngongowele umegharimu shilingi bilioni nne mpaka sasa hivi hauna maendelezo yoyote yale na hautegemei kuendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika Mji wa Liwale kuna mradi wa World Bank pale kutafuta chanzo mbadala cha maji umegharimu shilingi milioni 200 nao mpaka leo hii unasuasua mradi huo haujaendelea. Kwa hiyo, kwa ujumla wake katika Halmashauri ile kuna shilingi 4,200,000,000, naomba Kamati inayohusika hebu nendeni mkaangalie ili muweze kuishauri Serikali nini cha kufanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika ule mradi wa maji wa vijiji kumi, Liwale nimepata vijiji vitatu tu, kijiji cha Barikiwa, Namiu na Mpigamiti lakini kuna miradi ambayo mpaka sasa hivi imesimama na hakuna kinachoendelea ambayo ni miradi ya kijiji cha Kipule, Kiangara, Mikunya, Mpengele, Kimambi, Nangorongopa, Nahoro na Kitogoro. Kwa hiyo, naiomba Kamati hii kama itapata wasaa hebu iweze kutembelea Jimbo lile la Liwale muone pesa za nchi hii zinavyoharibika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naenda Idara ya Maliasili. Nimeshasimama hapa mara nyingi na nimeshaongea sana, lakini nataka niongelee mgao wa asilimia 25. Kwenye Jimbo langu la Liwale hatujapata huu mgao wa asilimia 25 pamoja na kwamba hatujui asilimia 25 inatokana na mauzo gani lakini walituambia kwamba Halmashauri zote zinazozunguka Hifadhi tutapata mgao wa asilimia 25 kutoka kwenye Serikali Kuu kama ruzuku inayotokana na mauzo ya maliasili ya misitu lakini mpaka leo hii jambo hili halijatekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwenye upande wa Maliasili nikiongelea upande wa malikale. Sisi pale tuna jengo lile la Wajerumani ambalo ni kumbukumbu ya Vita ya Majimaji mpaka leo hii yapo majina kwenye zile kuta, lakini Mheshimiwa Waziri nilisikitika sana nilipouliza hili swali akaniambia kwamba Halmashauri ndiyo tuifanye hiyo kazi ya kuendeleza lile jengo ili kuweka kumbukumbu. Sijui ana maana kwamba sisi tufungue website yetu, tuutangaze utalii wa Liwale kwa kutangaza maliasili ile, mimi sijaelewa. Kwa hiyo, naomba Waziri mwenye dhamana hebu atueleze ile malikale inayopotea pale mpango wake kwa Serikali hii ni nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye upande wa kilimo ambapo tuna tatizo la pembejeo, wengi wameshaliongea kwanza haziji kwa wakati. Mkoa wa Lindi na Wilaya ya Liwale kwa ujumla wake safari hii tumepata viatilifu fake ambavyo vimetupelekea kupata mazao hafifu ya korosho. Ukienda kwa mawakala wale wanaouza pembejeo za kilimo, utakuta ana stock mbili; maana kule kiatilifu kikubwa ni sulphur, anakwambia hii ni sulphur ya ruzuku na hii hapaya kununua. Ukichukua ile sulphur ya ruzuku ni kwamba umeumia, lakini ukichukua ile sulphur ambayo inauzwa cash ndiyo inaweza ikakuletea mazao mazuri.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze mchango wangu kwa maandishi kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kufanya kazi hii ya kuwawakilisha wapiga kura wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upimaji ardhi, ili kuiona Tanzania ya viwanda ni lazima upimaji wa ardhi upewe umuhimu wa kutosha. Kwani hivi sasa uwekezaji wa mashamba makubwa ni mgumu sana kwani vijiji vingi hivi sasa bado havijaingia kwenye mpango wa matumizi bora ya ardhi. Jambo linalofanya Halmashauri kukosa wawekezaji kwenye mashamba makubwa ya mazao ya kilimo na ufugaji wa kisasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano katika Halmashauri ya Liwale yuko Mwekezaji mmoja toka Japan. Huyu ni mzaliwa wa Liwale, mwaka 2015 aliamua kurudi nyumbani na mradi wa kilimo cha alizeti lakini hadi leo anahangaika kupata shamba japo Halmashauri ilishafanya maamuzi ya kumpatia ardhi mwekezaji huyu mzawa. Hatua ya uhaulishaji ardhi ndio kikwazo kikuu kilichobakia katika kukamilisha mradi huu. Namwomba Mheshimiwa Waziri, mwenye dhamana kuhakikisha Mwekezaji huyu anapata ardhi kwa ustawi wa Wanaliwale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali isiziachie Halmashauri shughuli za upimaji wa Vijiji ili kuviingiza katika matumizi bora ya ardhi. Kwani Halmashauri nyingi hazina mapato ya kutosha kumudu kazi hii. Hivyo kuvifanya vijiji vingi kukosa wawekezaji, kwani kigezo cha kwanza cha uwekezaji vijijini ni kijiji kuwa na matumizi bora ya ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uhaba wa watumishi, Wizara hii ina tatizo kubwa sana la upungufu wa watumishi hasa kwenye Halmashauri zetu. Jambo hili linaongeza makazi holela katika Halmashauri nyingi kutokana na uhaba wa viwanja na Halmashauri kushindwa kupima viwanja kwa wakati na jambo linaloongeza rushwa kwa ugawaji wa viwanja na makazi yasiyopimwa. Mfano, katika Halmashauri ya Liwale hatuna Afisa Ardhi mwenye taaluma ya kutosha na hatuna wapimaji wa ardhi tunategemea toka katika Halmashauri ya Nachingwea. Jambo hili linafanya gharama kubwa za upimaji wa viwanja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Gereza la Liwale limechukua ardhi ya wananchi tangu mwaka 1982 lakini hadi leo wananchi wenye mashamba yaliyotwaliwa bado hawajalipwa fidia ya mashamba yao. Naomba Wizara ya Ardhi wakishirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani wamalize mgogoro huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile mgogoro wa mpaka kati ya wanakijiji cha Kikulyungu na Wizara ya Maliasili na Utalii. Ni bora sasa Wizara zote mbili wakashirikiana katika kutatua mgogoro huu. Mgogoro wa Kikulyungu na hifadhi ya Selous ni wa muda mrefu sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi jioni hii ya leo ili na mimi niweze kuchangia hotuba hii ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, kama ilivyo ada, naomba nijielekeze moja kwa moja kwenye hotuba hii nikilenga kwanza hii Taasisi ya Uvunaji wa Misitu (TFS). Kama ambavyo unafahamu 60% ya Wilaya ya Liwale inazungukwa na misitu, kwa hiyo, uchumi mkubwa wa watu wa Liwale unategemea sana maliasili za misitu pamoja na wanyama. Kwa hiyo, naomba moja kwa moja nianzie huko.
Mheshimiwa Spika, namwomba Waziri Mkuu au Wizara inayohusika walete hapa marekebisho ya Sheria ya TFS. TFS kutupatia sisi Halmashauri 5% ya uvunaji wa mazao ya misitu kwa kweli ni kutokututendea haki. Ukienda kuangalia Liwale jinsi magogo yanavyovunwa pale, miti inavyohama na faida wanayoipata Wanaliwale wale kwa 5%, tena hiyo 5% yenyewe namna ya kuipata ni kwa shida kwelikweli. Naomba hii sheria iletwe hapa irekebishwe, 5% ni ndogo sana.
Mheshimiwa Spika, vilevile naomba niuelekeze mgogoro wa Hifadhi ya Selou pamoja na Wanakijiji wa Kikulyungu kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwa nini nauelekeza mgogoro huu kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu? Ni kwa sababu kwenye Wizara husika naona mgogoro huu umeshindikana.
Kwa hiyo, naomba moja kwa moja kwa nafasi hii niuelekeze mgogoro huu kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu pengine tukapata msaada ili wale wananchi wa Kikulyungu wakaepukana na adha wanayoipata leo hii ya kupigwa vibaya na Askari wa Wanyamapori.
Mheshimiwa Spika, baada ya hapo naomba nijielekeze kwenye upande wa takwimu. Sensa ya mwaka 2012 kwa kweli sisi Wilaya ya Liwale imetuathiri sana. Imetuathiri kwa maana ya kwamba, imeonesha wakazi wa Wilaya ile ni kidogo sana. Nitoe mfano ufuatao. Wilaya ya Liwale kwenye Basket Fund tunapata Sh.8,000,000/=, Wilaya ya Nachingwea Sh.18,000,000/=, Wilaya Kilwa Sh.17,000,000/ =, Wilaya ya Ruangwa Sh.21,000,000/=. Basket Fund, Liwale 350, Ruangwa bilioni 1, Kilwa milioni 600, Nachingwea milioni 800 lakini sisi hii idadi tuliyonayo sio kweli kwamba Wilaya ya Liwale yenye Kata 20 ina watu 92, siyo kweli, hii takwimu sio sahihi.
Mheshimiwa Spika, nashindwa kuwaelewa hawa watu wanaosimamia hizi takwimu. Katika Mkoa wa Lindi, Hospitali pekee inayoona wagonjwa wengi kwa mwezi ni Hospitali ya Wilaya ya Liwale lakini ndio hospitali pekee inayopata mgawo mdogo. Naomba nilielekeze hili kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu ili liweze kupatiwa ufumbuzi.
SPIKA: Mheshimiwa Zuberi Kuchauka, kuna taarifa.
TAARIFA...
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napokea taarifa yake kwani haijapingana na nilichokieleza lakini bado narejea palepale, kama takwimu za hospitali zinaletwa kila mwezi kwamba katika Mkoa wa Lindi hospitali inayoona wagonjwa wengi ni ya Wilaya ya
Liwale. Sasa ni mwenye akili gani timamu hiyo hospitali inayoona wagonjwa wengi akaipa mgawo kidogo? Napata wasiwasi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nijielekeze kwenye upande wa hiyohiyo takwimu inatuathiri vilevile kwenye mgawo wa wafanyakazi kwa maana ya ikama ya wafanyakazi. Ikama ya wafanyakazi kwa upande wa elimu, ikama ya wafanyakazi kwa upande wa afya, tuna matatizo sana. Mpaka leo hii ninavyoongea kwenye Bunge hili Tukufu, Liwale hatuna daktari bingwa, tuna uhaba wa madaktari, tuna uhaba wa walimu wa sekondari, lakini ukiuliza unaambiwa kwamba wale waliopo ndio wanafanana na idadi ya watu walioko kule wakati sio kweli. Naomba hizi takwimu zirekebishwe, kama ripoti unaletewa ya idadi ya wanafunzi iweje sasa ushindwe kuitumia ripoti hiyo uende mwaka 2012? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naingia kwenye vyama vya ushirika. Vyama vya ushirika naomba iletwe sheria hapa ili tufanye marekebisho, vyama vya ushirika wawekewe masharti namna ya kuajiri wahasibu. Tumepata matatizo sana mwaka huu, kwenye Chama Kikuu cha Lunali hawajawahi
kupatiwa fedha kama mwaka huu lakini wamevurunda mpaka sasa hivi vyama vya ushirika wameshamaliza pesa lakini wakulima hawajapata hela. Sawa, wale viongozi wa vyama vya msingi tutawapeleka Mahakamani watafungwa au watafilisiwa lakini bado mkulima aliyepeleka korosho yake mwezi wa 10 mwaka jana mpaka leo hajapata hela. Kufungwa au kupelekwa Mahakamani kwa huyu mtu mkulima yule imemsaidia nini?
Mheshimiwa Spika, leo hii mwezi wa Nne tunaandaa mashamba lakini mtu amepeleka korosho mwezi wa 10 mpaka leo hajapata pesa. Ombi langu ni kwamba, Sheria ya Vyama vya Ushirika iletwe hapa, tuwaundie sheria ili ajira za vyama vya ushirika ziendane na taaluma. Kwa sababu
tatizo kubwa tulilolipata safari hii ni watu hawana taaluma ya uhasibu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nijielekeze kwenye Sera ya Wazee. Sera ya Wazee imetungwa nafikiri tangu mwaka 2003 lakini mpaka leo Sheria ya Wazee haijawahi kuletwa kwenye Bunge hili, sijui mmekwama wapi? Naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge hapa ndani sisi wote hapa ni wazee watarajiwa. Tunapolichelewesha hili tunajichelewesha sisi wenyewe na waathirika wakubwa ni sisi, leo vijana, kesho ni wazee.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda kuwapongeza sana wenzetu Zanzibar pamoja na uchumi wao kuwa hafifu lakini wamewakumbuka wazee angalau hata kuwapa Sh.200/=. Leo hii Tanzania Bara tumenyamaza, hata hiyo Sh.10,000/= tuliyoambiwa watapewa mpaka leo haijulikani, tutafikaje huko hata sheria yenyewe haijaletwa hapa? Naomba sana Sheria hii ya Wazee iletwe hapa ili tuone wazee sisi watarajiwa huko mbele tumejiwekea akiba gani?
Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa napenda nizungumzie kuhusu bajeti. Watu wengi sana wamezungumzia kuhusu upelekaji wa fedha kwenye miradi ya maendeleo, kwenye OC, siyo mzuri. Jamani, hapa tatizo siyo upelekaji, hela hakuna! Mimi sidhani kama Serikali wana
pesa halafu hawapeleki! Tuseme kweli kwamba pesa hizo hazipo, makusanyo hayo hayapo! (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba Waziri wa Fedha anieleze pengine mimi kwa sababu ya elimu yangu ndogo sielewi. Hizi figure hizi zinazokuja hapa kila mwaka ambazo hata 50% tunashindwa kuzifikisha zina maana gani? Kuna tofauti gani leo hii tukasema kwamba hii bajeti yetu ni ya
shilingi trilioni 18 badala ya kuweka 30? Shilingi trilioni 18 tunaweza tukaifikia! Kwa nini tunaweka shilingi trilioni 31 ambayo mwisho wa siku hata shilingi trilioni 20 hatufiki! Kuna sababu gani? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba Waziri mwenye dhamana anisaidie ili na mimi nipate uelewa ili siku nyingine nisije nikasimama tena hapa nikauliza kuhusu jambo hilihili. Kwa nini tunaletewa hizi figures kubwa kubwa ambazo hazina mwisho?
Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa naomba niongelee walimu. Kuna tatizo kubwa sana la matokeo. Matokeo ya elimu mwaka huu, kwa mfano kama Mkoa wa Mtwara, Mheshimiwa Spika shahidi, Mkuu wa Mkoa ametimua watu, amepunguza watu lakini mimi nasema hii siyo solution, solution ni kuangalia maisha ya walimu.
Mheshimiwa Spika, walimu wetu tumewasahau na kama tumesahau walimu na elimu nayo tunaisahau. Ahsante sana. (Makofi)
SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Kuchauka. Tupelekee salamu kule Liwale Mjini pale Makunjiganga, Nangano, Kimambi unapoelekea Kilwa, Kikulyungu unapoelekea Nachingwea, Mtawatao kwenye mpunga, Ndapata unapopakana na Selou, Barikiwa. Liwale sio ya kwako peke yako bwana. Mheshimiwa Kakunda.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuanza mchango wangu kwa kuzungumza Sera ya wazee nchini. Sera ya Wazee nchini ilikuwepo tangu mwaka 2003, lakini hadi leo Sheria kwa ajili ya utekelezaji wa Sera hii bado haijaletwa hapa Bungeni ili kukidhi mahitaji ya Sera ya Kitaifa ya wazee kama ilivyopitishwa mwaka 2003. Kumekuwepo kwa ahadi ya muda mrefu ya ulipwaji wa pensheni kwa wazee wote hasa wakulima waliotumikia uchumi wa nchi hii kwa uaminifu mkubwa. Pia kukosekana kwa Sheria hiyo kumefanya ushiriki wa wazee hao kwenye vyombo vya maamuzi kuwa hakuna. Katika ngazi zote za vyombo vya maamuzi, ushiriki wa wazee ni kama hakuna hivyo kuathiri maslahi ya wazee hao. Mheshimiwa Mwenyekiti, kuendelea kwa mauaji ya vikongwe nchini ni matokeo ya madhara ya kutokuwa na
sheria inayowatambua wazee nchini na pia ukosefu wa uwakilishi kwenye vyombo vya maamuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze kwa Wakala wa Uvunaji wa Mali za Misitu (TFS). Sheria na kanuni zinazotumiwa na Taasisi hii ni bora ikafanyiwa marekebisho kwani kwa kiasi kikubwa imekuwa si shirikishi kwa jamii inayoizunguka au jirani na misitu husika. Mfano ushuru au tozo zinazopatikana katika uvunaji huu. Halmashauri zetuupatiwe kiasi cha asilimia tano tu. Kiasi hiki ni kidogo sana ukilinganisha na uharibifu unaotokana na kazi hii. Vile vile ukizingatia ulinzi shirikishi inakuwa ni vigumu sana kwa jamii kuona faida ya misitu hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushiriki wa TFS katika shughuli za maendeleo kwenye vijiji vinavyopakana na misitu midogo sana kitendo kinachochea jamii kutokuona faida ya moja kwa moja ya uwepo wa misitu hiyo. Kamati za Vijiji za uvunaji wa mali za misitu hazina elimu ya kutosha juu ya uvunaji endelevu. Hivyo kufanya wajanja wachache kutumia mwanya huo kuharibu mali za misitu bila jamii husika kunufaika. Kama ilivyo kwa maliasili, vijiji au Halmashauri upatiwa 25% kwa wawindaji, basi na TFS ifikiriwe kutoa kiasi kama hicho cha 25% kwa Halmashauri. Ili Halmashauri iweze kunufaika na uvunaji huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze kwa wapiga kura wangu. Wilaya ya Liwale ni wilaya yenye kata 20 lakini wilaya hii hadi leo ina kituo cha Afya kimoja tu. Jambo linaloifanya Hospitali ya Wilaya kubeba mzingo mkubwa sana. Ukizingatia Hospitali yenyewe tangu ilipopandishwa hadhi toka kituo cha afya miundombinu yake haijaboreshwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, janga kubwa linaloikumba wilaya hii ni mgao mdogo wa fedha za dawa na basket fund. Mfano Mkoa wa Lindi una wilaya tano, wilaya inayopata mgao mdogo ni Liwale ukilinganisha na wilaya zingine. Cha kusikitisha ni kwamba katika Mkoa wa Lindi hospitali za wilaya, Hospitali za Liwale ndio inayoongoza kwa kuhudumia wagonjwa wengi kwa mwezi, lakini ndio inayopata mgao mdogo wa fedha. Basketi fund, Liwale milioni 350, Ruangwa bilioni moja, Nachingwea milioni 800, Kilwa milioni 600, hii si haki. Mateso yanayowapata wana
Liwale ni matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, hivyo, nashauri Serikali ikafikiria vinginevyo badala ya kuacha watu wakiteseka kwa magonjwa na ukosefu wa madawa. Fedha ya dawa Liwale milioni nane, Ruangwa milioni 21, Kilwa milioni 17 na Nachingwea milioni 18.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Madeni ya Walimu; pamoja na juhudi kubwa inayofanywa na Serikali juu ya kumaliza tatizo hili, lakini kasi yake ni ndogo ukilinganisha na ukubwa wa tatizo. Walimu ni wengi sasa wanaodai nyongeza ya mishahara inayotokana na kupandishwa madaraja na
wengine wanaocheleweshwa kupandishwa madaraja ingawa wanakidhi vigezo. Jambo hili linawakatisha tamaa Walimu wengi na kufanya shule nyingi kuwa na matokeo mabaya. Hali za walimu wetu ni mbaya kwa ujumla wanaishi katika mazingira magumu sana. Uhaba wa ajira
tu ndio unaowabakisha huko na si kufurahia ajira yao, kwani walio wengi hawajui hatima yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naomba kuishauri Serikali kuchelewa au kutopeleka Ruzuku ya OC kwenye Halmashauri zetu ni kurudisha nyuma maendeleo ya nchi yetu kwani Halmashauri inashindwa kutekeleza miradi yake ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kutenga fungu la vijana na akinamama. Pengine Halmashauri hutakiwa kutekeleza maagizo ya Kitaifa bila kupewa fungu la fedha za kazi husika ikiwa ni pamoja na michango mbalimbali. Jambo hili hurudisha nyuma mipango ya Halmashauri kwani hulazimika kutekeleza miradi ambayo haikuwa kwenye mpango kazi wa Halmashauri husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwakilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze mchango wangu kwa kumwomba Waziri aje Wilayani Liwale ili kutatua migogoro kwenye Wilaya ya Liwale. Kuna mgogoro wa muda mrefu katika Kijiji cha Kikulyungu na Hifadhi ya Selous. Pia kuna mgogoro kati ya Kilwa na Liwale migogoro hii miwili imeshindikana kwenye ngazi zote, hivyo kuhitaji ngazi ya Wizara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Kanda ya Mtwara ni sehemu ya tatizo katika Halmashauri ya Liwale, kwani imekuwa ikisababisha migogoro badala ya kutatua migogoro. Mfano, Halmashauri ya Liwale imeingia mgogoro na mwananchi baada ya Halmashauri kupima shamba la mwananchi huyo, shamba ambalo lina Hati Miliki ya miaka 99.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri wamepima viwanja bila ridhaa ya mwenye shamba, Kamishna wa Ardhi anajua mgogoro huu lakini hadi leo hakuna hatua iliyochukuliwa. Pamoja na Halmashauri kuvunja sheria ya kupima kwenye ardhi ya mtu inayomilikiwa kihalali, mwananchi huyu ni Ndugu Hemedi Mewile katika Kijiji cha Mangando Wilayani Liwale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujua vigezo vinavyotumika na Shirika la Nyumba la Taifa kujenga nyumba za bei nafuu katika maeneo mbalimbali nchini. Kwani mimi kwenye Halmashauri yangu ya Liwale kuna uhitaji mkubwa sana wa nyumba hizo hasa kwa wakati huu wa mazao ya korosho na ufuta kufanya vizuri. Ni lini Shirika hili litakuja Liwale kujenga nyumba hizi za bei nafuu? Ukizingatia kutokana na shida ya usafiri, hivyo vifaa vya ujenzi ni ghali sana na kufanya wakazi wengi wa Liwale kushindwa kumudu kujenga nyumba bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Msitu wa Nyera-Kipelele umechukua vijiji vingi sana, naomba Serikali kuangalia upya mipaka ya Msitu huu ili wanavijiji wanaozunguka Msitu huu wapate maeneo ya kulima na shughuli nyingine. Mfano, Kijiji cha Kiangara, Kipelele, Naujomba, Miruwi, Mtawatawa na Kitogoro, vijiji hivi havina misitu kabisa kwa shughuli za ujenzi kwani sehemu zote zinamilikiwa na Hifadhi ya Msitu wa Nyera-Kipelele.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi jioni hii ya leo na mimi nitoe mchango wangu kwenye Wizara hii ya Mawasiliano na Ujenzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda nitangulize maneno yale ambayo umetuasa jana hapa, ukatutahadharisha kwamba tusitumie maneno mengine tukaonekana ni wahaini baada ya baadhi ya Wabunge kutoka Mikoa ya Kusini wanapoeleza habari hizi kwa uchungu.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo siwezi kuyarudia hayo maneno usije ukanitoa njiani, lakini nataka niwape hadithi moja, hadithi hii nimeipata miaka ya 1980. Rafiki yangu mmoja aliniambia ukijenga nyumba yako usiweke master bedroom Kusini; ukiweka master bedroom Kusini kuna


uwezekano hata ndoa yako isiwe vizuri na familia yako inaweza kubaki maskini. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, akanieleza yafuatayo; anasema ukiangalia ramani ya ulimwengu hebu angalia Visiwa vya Caribbean vinaona jua labda kwa wiki mara moja, mara mbili. Ukirudi kwenye ramani ya Afrika hebu angalia Afrika ya Kusini mpaka leo hawajapata uhuru, Rhodesia, Msumbiji hawajapata uhuru ni kwa sababu wapo Kusini. Ramani ya Tanzania, angalia Mkoa wa Lindi na Mtwara, wakati ule Mkoa wa Mkoa wa Lindi na Mtwara ndiyo adhabu ya wafanyakazi, ukipelekwa kule wewe ni adhabu. Akaniambia hii yote ni kwa sababu tuko Kusini. Kwa hiyo, ukichora ramani ya Tanzania angalia Mkoa wa Lindi na Mtwara ilivyo nyuma ni kwa sababu tuko Kusini. Akasema njoo uchore ramani ya Dar es Salaam hebu angalia Wilaya ya Temeke na Kinondoni, ana maana kwamba ukiweka master bedroom Kusini utabaki kuwa maskini, ndiyo maana leo mtu wa Kusini akisema anasema kwa uchungu hayo tunayoyasema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, reli inayoongelewa ya Tanga
- Moshi, Mjerumani aliijenga ile reli kutoka Mtwara kwenda Nachingwea. Wakati ule Mtwara na Lindi tulikuwa na pamba, katani, korosho na karanga ndiyo maana akajenga ile reli. Sisi tulipopata uhuru, tukaihamisha ile reli ikaenda Tanga na mkonge ukahamia Tanga, pamba ikahamia Tanga tukabaki maskini. Tunaposema hamtuhitaji nchi hii tunamaanisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mkitaka kuona hilo, je, watu wa Kusini kosa letu kwenye nchi hii ni nini? Hiyo barabara ambayo inaongelewa ya Kibiti - Lindi, mimi wakati nasoma nikiwa form four ndiyo barabara ya Kibiti- Lindi imeanza kuletewa pesa. Mwaka 1984, vifaa vilikuja na Nangurukuru vya kumaliza hiyo barabara, hiyo barabara imeshajengwa na Marais wangapi? Wanne, hiyo iko Kusini.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 1987 natoka Dodoma nakwenda Singida, barabara ni ya vumbi, lakini barabara ya Singida na ya Kibiti - Lindi ipi imeanza kuisha? Mnataka tuseme nini? Naomba Serikali ya Awamu ya Tano mfungue Mikoa ya Lindi na Mtwara. Muufungue Mkoa wa Lindi na Mtwara kwa barabara na kwa mawasiliano, hapo mtakuwa mmetutendea haki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Nangurukuru- Liwale; Nachingwea - Liwale na Liwale - Morogoro zimeshaongelewa sana sina haja ya kuzirudia, lakini kwa sababu mimi ndiyo mwenye hizo barabara wanasema chereko chereko na mwenye ngoma. Wabunge wengi hapa mmesema tuende kwenye sera, Mbunge aliyepita amesema tuende kwenye sera, kama tumeamua kuunganisha Mkoa hadi Mkoa basi nasi mtuunganishe na Morogoro mtungaanishe na Ruvuma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze kwenye Wilaya ya Liwale. Walio wengi hapa wakisimama wanasema Wilaya zao mpya, mikoa mipya, Wilaya ya Liwale ina miaka 42. Sasa kama kuna mtu Wilaya yake mpya anadai barabara na sisi ambao tuna miaka 42 hatuna barabara tuseme nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Liwale haina mawasiliano ya simu, haina mawasiliano ya barabara na leo hii Liwale hapa ninapoongea siwezi kwenda, barabara hakuna na nikienda kule wanaweza wakanipiga hata mawe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu upande wa mawasiliano ya simu. Namuomba Waziri atuletee mawasiliano, kata zifuatazo ili kuweza kupata mawasiliano ya simu ni lazima uende zaidi ya kilometa tano, 10 mpaka
12. Kata ya Mpigamiti, Kikulyungu, Kimambi, Lilombe, Mlembwe, Mkutano, Ngunja, Ngongowele, Ngorongopa, Pengere, Makinda, Mirui, Mikunya, Naujombo, Nahoro, Mtawango, Makololo na Gongowele hizi zote hazina mawasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, kata ya Mpigamiti ndiyo kata anayotoka huyu anayeongea sasa hivi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakuomba sana Serikali ya Awamu ya Tano, hebu muifungue Liwale na Lindi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi nikiwa kwenye Kamati, niliambiwa vigezo vya barabara kupata lami wakasema magari lazima yafike 300, nikawaambia kama kigezo ndiyo hicho, Liwale hatutapata barabara ya lami mpaka Yesu arudi. Kwa sababu karavati walizojenga kwenye hiyo barabara magari makubwa hayaendi na tayari wameshapunguza magari. Mfano, masika kama sasa hivi watu wanazunguka kupitia Lindi, hiyo barabara itafikia magari 300 lini? Siyo kweli kwamba hii barabara haiwezi kufikia magari 300.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri naomba nikuambie barabara ya Nangurukuru – Liwale ukiipa lami, hakuna msafiri atayekwenda Masasi na Tunduru, atakayepitia Lindi au Mtwara lazima wapitie Liwale kwa sababu ndiyo shortcut, lakini leo hii Liwale inaonekana iko kisiwani kwa sababu hatuna barabara.

Kwa hiyo, barabara hii ni barabara ya kiuchumi siyo kweli kwamba ni barabara ya huduma. Liwale tunalima korosho, Mkoa wa Lindi ndiyo tunaongoza, tunalima ufuta, tunalima viazi. Sasa kama siyo uchumi huu ni kitu gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nirejee kwenye ubora wa barabara, juzi tulipokuwa kwenye Kamati tulikagua barabara. Mimi nilisikitika sana yule engineer alinieleza barabara ile haina hata mwaka imeanza kuweka crack, namuuliza anasema unajua hapa wali-estimate vibaya kumbe level ya maji (water table) ile kwamba walikadiria iko juu kumbe iko chini sana, kwa hiyo, barabara imebomoka wanarudia. Nikamwambia hawa wanaofanya feasibility study, sijui upembezi wa kina, wanafanyaje?

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ninavyofahamu kila mita 50 panachukuliwa udongo wanafanya sampling, wanapeleka maabara kupata historia ya hiyo barabara. Ndiyo maana tunashindwa kuwakamata wakandarasi mara nyingi makosa yanakuwa siyo yao. Haya mambo ya upembuzi yakinifu, upembezi wa kina, mtu yuko ofisini anapiga simu tu, eeh bwana hiyo barabara kutoka mahali fulani, kuna mto gani hapo? Huo mto ukoje? Anachora tu, eeh, jamani tuende kwenye field! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haingii akilini mtu aniambie kwamba ile barabara pale maji yanafoka ndiyo maana barabara haidumu, hukuyaona? Hapa tunapoteza pesa bure, lakini tatizo siyo wakandarasi, tatizo kubwa liko kwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina, wataalamu wanabaki ofisini wanafanya upembuzi yakinifu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa tunazungumzia upande wa bandari. Nchi hii ni ya ajabu sana, leo hii hatuna hata lengo kusema kwamba kwenye nchi yetu hii ni mizigo tani ngapi tupitishe majini na mingapi tupitishe kwenye reli. Leo hii Mtwara kuna bandari lakini hii bandari haitumiki. Juzi hapa tumepata shida na mazao ya korosho, Mtwara kumejaa korosho maghala yote, meli hakuna, hii bandari mbona hatuitumii? Tumerogwa na nani sisi? Tatizo liko wapi? Hakuna nchi ya ajabu kama hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii nchi hii bado inasafirisha mizigo mikubwa kwa malori, halafu bado tunawalaumu wakandarasi wanajenga barabara chini ya kiwango, hii si kweli, haiwezekani! Tunayo bandari ya Tanga mwambao wote ule Mtwara, Lindi, Dar es Salaam, Tanga, Bagamoyo bado tunasafirisha mizigo kwa magari, hii ni aibu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri kwamba umefika wakati Serikali wapange kwamba tunataka tusafirishe mizigo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kuchangia hotuba hii kwa kuanza na hali za barabara zetu hapa nchini. Hali ya barabara zetu nyingi ni mbaya hasa majira ya masika ambapo barabara nyingi zinajifunga hasa kwa zile za changarawe na udongo. Hali hii huchangiwa zaidi na wakandarasi kuzijenga chini ya kiwango. Kwa barabara za lami hali ni mbaya pia, barabara nyingi hujengwa chini ya kiwango. Jambo linalo igharimu nchi yetu kutumia fedha nyingi za matengenezo ya mara kwa mara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ubovu wa barabara za lami nchini huchangiwa kwa kiasi kikubwa na kukosa umakini au utaalam wakati wa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ambapo ndio humwongoza Mkandarasi. Kwa ajili hiyo wakandarasi wengi inashindikana kuwatia hatiani kwa sababu mara zote kosa sio lao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nijikite kwenye Sera ya Kitaifa juu ya kuunganisha mikoa yetu kwa barabara za lami. Hadi leo kuna baadhi ya mikoa haijaunganishwa japo mikoa mingine sasa inaunganishwa kati ya wilaya hadi wilaya wakati mikoa mingine haijaunganishwa. Kwa mfano Mkoa wa Lindi na Mkoa wa Morogoro au Mkoa wa Lindi na Mkoa wa Ruvuma. Barabara ya Lindi – Morogoro kupitia Wilaya za Liwale na Ulanga ni muhimu sana hasa kwa sasa ambapo Serikali imehamia Dodoma, kwa sababu Mikoa ya Lindi na Mtwara kuja Dodoma kupitia njia hiyo ni fupi sana; hivyo kuipunguzia Serikali Matumizi ya Mafuta kwa watumishi wa mikoa hiyo, kuja Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nijielekeza Jimboni kwangu Liwale. Liwale ni Wilaya yenye umri wa miaka 42, lakini hadi leo Wilaya hiyo inakabiliwa na tatizo kubwa la mawasilino ya simu na barabaram jambo linaloifanya Wilaya hii kuwa nyuma kimaendeleo. Katika Mkoa wa Lindi Liwale ndiyo Wilaya iliyo mbali zaidi kutoka Mkoani, kama kilomita zaidi ya 300. Barabara ya Liwale – Nachingwea, japo imetajwa katika Ilani ya CCM Lakini sioni juhudi za Serikali katika utekelezaji wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Nanguruku – Liwale ni kama mshipa wa damu kwa Wilaya ya Liwale. Pamoja na kwamba Liwale inaongoza kwa zao la korosho na ufuta katika Mkoa wa Lindi lakini bado wakulima hao wanapata bei ndogo ya mazao yao, jambo linalopunguza pato la Halmashauri na Serikali kwa ujumla kwani wafanyabiashara hutoa bei ndogo kwa sababu ya ubovu wa barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakazi wa Wilaya za Masasi, Tunduru na Nachingwea wangeweza kutumia barabara hii ya Nangurukuru – Liwale kwani ndiyo barabara fupi kwao kwa kwenda na kutoka Dar es Salaam kupitia Liwale, hivyo kuongeza umuhimu wa barabara hii. Pamoja na Liwale kupakana na hifadhi ya Selou, watalii wanashindwa kuja Liwale kwa sababu ya ukosefu wa miundombinu ya barabara na simu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa naomba kupata maelezo ni kipi kianze kati ya miundobinu na simu maendeleo ya watu. Naomba barabara hii ijengwe ili ufuta, viazi na korosho za Wanaliwale ili zipate bei nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mawasiliano ya simu ni muhimu sana lakini hadi sasa ni chini ya asilimia 40 tu ya vijiji 76 vya Wilaya ya Liwale, vina mawasiliano ya simu. Ukiondoa mawasiliano ya simu na barabara hakuna namna nyingine ya mawasiliano kwa wakazi wa Liwale kwani hakuna redio inayosikika Liwale.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze mchango wangu kwa kuishauri Wizara kuzingatia ushauri wote uliotolewa na Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kwani pamoja na kuwa nchi yetu kuwa ya nne (4) Barani Afrika kwa kuwa na aina nyingi za madini, lakini sekta hii haijapewa msukumo wa kutosha ili kuleta tija inayokusudiwa. Bado mchango wa sekta ya madini kwenye Pato la Taifa haulingani na uhalisia. Hivyo basi, Serikali ikafanye uwekezaji wa kutosha katika sekta ya madini ikishirikisha wawekezaji wenye mitaji ya kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, machimbo ya Kitowelo kwenye Kata ya Lilombe ni ya muda mrefu sana lakini hadi leo Halmashauri haijanufaika na chochote. Hii ni kwa sababu soko la madini hayo liko Tunduru Mkoani Ruvuma, hivyo wachimbaji huenda Tunduru bila kupitia kwenye kata au kijiji, hivyo kijiji kukosa mapato.

Mheshimiwa Naibu Spika, vivyo hivyo kuna kampuni ya utafutaji wa madini, kampuni ya GWENA, kampuni hii mkataba wake haujulikani wala haina ushirikiano na vijiji uchimbaji huo unakofanyika kwani elimu ni ndogo sana kwa jamii hivyo kushindwa kusimamia vyema utafutaji huu wa madini. Hivyo Wizara sasa ione umuhimu wa kuwa na Afisa Madini kila halmashauri kwani hapa nchini hakuna halmashauri ambayo haifanyi biashara ya madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, uwepo wa madini aina ya green garnet katika Wilaya ya Ruangwa na Liwale. Serikali haijafanya utangazaji wa kutosha ili kupata wawekezaji katika uchimbaji wa green garnet, hivyo kukosa tija iliyokusudia. Hata hivyo, naishauri Serikali kuangalia upya leseni za utafutaji wa madini kwani wapo wenye hizi leseni wanazitumia kufanya uchimbaji wa madini na si utafutaji au utafiti.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado Serikali haijawekeza vya kutosha kwa wachimbaji wadogo wadogo. Sekta hii imeshindwa kuongeza ajira nchini kwa kuwa wachimbaji wadogo wadogo hawajapewa mitaji ili kupata vifaa na kuboresha mazingira ya kazi zao. Sheria vilevile ikaangaliwe ili kuwe na uwanja sawa kati ya wachimbaji wakubwa na wadogo kwani sasa wachimbaji wananyanyasika sana katika tasnia hii ya madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Sheria ya Madini ikaangaliwe ili kufanya madini yanayotumika katika ujenzi wa barabara ikiwezekana tozo hizi na ushuru mbalimbali zikafutwa ili kupunguza gharama za ujenzi wa barabara zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, naomba kupatiwa majina ya wachimbaji na watafutaji wa madini walioko katika Wilaya ya Liwale. Kwani hadi sasa shughuli hiyo hufanywa holela, hata Mkurugenzi wa Halmashauri hana hiyo takwimu, hivyo hata yeye hajui chochote. Jambo hili haliwezi kuwa sawa kwa kuwa kazi hizi zimekuwa zikifanywa kwenye eneo lake la utawala. Bila kusahau status ya Kampuni ya GWENA na machimbo ya Kitowelo.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii nichangie Wizara hii ya Afya.

Awali ya yote nitoe shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Katibu wa Wizara hii kwa haki walioyonitendea katika kipindi hiki. Mwaka jana nilisimama hapa nikalalamika sana, nikalia sana, kwamba hospitali yangu ile ya Wilaya ya Liwale haina wafanyakazi kwa maana ya madaktari lakini nashukuru Alhamdulillah Mheshimiwa Waziri ameisikia kilio changu amenipa madaktari wawili namshukuru sana nasema ahsante sana. (Makofi)

Pamoja na hilo bado nitaendelea kukuomba kwamba katika zahanati 31 za Wilaya ya Liwale zinaongozwa na enrolled nursing, kwa maana ya kwamba hatuna clinical officers. Wilaya mzima ile ina clinical officer wanne tu. Kwa hiyo, bado tunaendelea kulia pengine kama utapata nafasi hiyo utuongezee hao clinical officers.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile hospitali ile ya Wilaya ya Liwale ina x-ray haina mtaalamu wa hiyo x-ray.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nijielekeze kwenye taasisi moja muhumu sana ambayo ni taasisi ya Mirembe. Taasisi ya Mirembe kama ilivyo umuhimu wake, nimefanya utafiti huu kwa muda wa miezi sita, taasisi ya Mirembe inakabiliwa na matatizo lukuki. Kwanza kabisa ni Ikama ya wafanyakazi, posho ya mazingira magumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapoongea posho ya mazingira magumu Hospitali ya Mirembe inafahamika. Pia madai ya watumishi mbalimbali waliopandishwa madaraja pamoja likizo. Kikubwa zaidi katika taasisi ile ya hospitali ya Mirembe sasa hivi imegubikwa na tatizo kubwa la rushwa. Kwa utafiti nilioufanya, tatizo hili na matatizo mengine yote lukuki niliyoyaorodhesha hapa, tatizo kubwa liko kwenye uongozi wa Hospitali ya Mirembe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiongea na wafanyakazi wa Hospitali ya Mirembe morali ya kufanyakazi imeshuka. Hawana ushirikiano kutoka ngazi ya juu mpaka kwa mtu wa chini. Naomba Mheshimiwa Waziri ufanye utafiti, nenda Hospitali ya Mirembe, Mkurugenzi wa Hospitali Mirembe siyo rafiki kwa wafanyakazi wa Mirembe, na hii inashusha hadhi na morali ya wafanyakazi ya Hospitali ya Mirembe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna wafanyakazi ambao wameshushwa madaraja na wanashushwa na mshahara, hivi mfanyakazi aliyeshushwa daraja, mkashusha na mshahara halafu unamuacha kituo hicho hicho, huo ufanisi wa kazi atautoa wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze sasa kwenye Hospitali ya Wilaya ya Liwale. Hospitali ya Wilaya ya Liwale aina hadhi ya kuitwa Hospitali ya Wilaya, kama ambavyo Katibu wa Wizara ya TAMISEMI anayeshughulikia mambo ya afya alivyosema. Halmashauri pamoja na kwamba tumeambiwa sisi wenyewe ndiyo tuanzishe vipaumbe, kweli sasa hivi tumeshatafuta kiwanja tumeshapata kiwanja, na Inshaallah bajeti inayokuja tunaweza tukaanza ujenzi. Tunaomba Mheshimiwa Waziri support yako tujengee Hospitali ya Wilaya ya Liwale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kama nilivyosema awali Wilaya ya Liwale ina zahanati 31, ina kata 20 lakini tuna kituo kimoja tu cha afya. Hapa napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Naibu Waziri wa TAMISEMI ameweza kutusaidia pesa kidogo kwa ajili ya kuboresha kile kituo chetu kidogo cha afya, naye nasema Alhamdulillah Mwenyezi Mungu ampe umri mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa bado naendelea kusisitiza takwimu za ...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, ninaunga mkono hotuba ya upinzani.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na kuniwezesha leo kushika kalamu na kutoa mchango wangu kwenye hoja iliyo mbele yetu. Pia nichukue fursa hii kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri wote wawili kwenye Wizara hii Dkt. Harison Mwakyembe, Mheshimiwa Naibu Waziri Juliana Shonza pamoja na watumishi wote wanaohudumu katika Wizara hii, wote kwa pamoja nawapongeza sana kwa kufanya kazi kwa weledi na ufanisi mkubwa.

Mheshimiwa Spika, Redio Tanzania, TBC FM hii ni redio ya Taifa lakini usikivu wake katika baadhi ya mikoa ni mbaya sana na mikoa au wilaya zingine hakuna kabisa. Jambo hili linafanya jamii kubwa kukosa habari muhimu zinazohusu Taifa letu. Mfano katika Wilaya ya Liwale Mkoa wa Lindi redio hii haipatikani kabisa. Nimeliuliza jambo mara nyingi bila majibu.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na mchakato wa kutafuta vazi la Taifa. Je, mchakato huu umefikia wapi? Hata hivyo yako mavazi yanayovaliwa hapa nchini hasa na wanawake wakati wakiwa kwenye sherehe mbalimbali. Je, hakuna sheria inayokataza mavazi hayo? Hapa nazungumzia yale mavazi ya nusu uchi yanayoacha maungo wazi.

Mheshimiwa Spika, ziko nyimbo zinazoimbwa na wasanii nyimbo hizo, hufungiwa baada ya wimbo husika kutoka je, hakuna sheria inayokataza wimbo kabla ya kutoka kupitiwa kwanza maudhui yake, kwani kufungia wimbo ambao umeshatoka haisaidii sana kwani tayari huwa umeshaingia kwenye mitandao ya kijamii.

Mheshimiwa Spika, lugha ya Kiswahili ni moja ya tunu ya Taifa letu; kwa nini basi Wizara haina mpango mkakati wa kukikuza Kiswahili ambacho sasa kimeanza kuharibiwa na vyombo vyetu vya habari, viongozi wa kisiasa na wasanii mbalimbali kwa kuchanganya na lugha nyingine kama vile kiingereza (KISWKINGE) jambo hili linaharibu lugha yetu ya Kiswahili, lakini pia yako magazeti yanashindwa kuandika Kiswahili fasaha. Imefika sasa kuwa na Chuo cha kufundisha Kiswahili na kutungwa kwa sheria ya watumishi wote wa vyombo vya habari na wasanii kupitia kwenye Chuo hicho cha Kiswahili ili tunu ya Taifa iweze kuhifadhiwa. Pia Chuo cha Sanaa Bagamoyo kipewe fedha za kutosha na kujengewa uwezo na miundombinu wezeshi. Vilevile chuo hiki kipewe pia jukumu la kusomesha lugha ya kisiasa, sambamba na somo la kukuza uzalendo.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, napenda kutoa shukurani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kusikiliza kilio cha Wanaliwale na hatimaye kutupatia Madaktari wawili hivi karibuni. Namwomba Mungu awaongezee umri mrefu. Hata hivyo, naendelea kusisitiza kuwa tatizo la ikama ya watumishi katika Wilaya ya Liwale bado ni tatizo kubwa. Wilaya ya Liwale yenye Kata 20 na Vijiji 79 ina Zahanati 31 tu na Kituo kimoja cha Afya. Jambo hili linaifanya Hospitali ya Wilaya kuwa na mzigo mkubwa kuliko uwezo wa hospitali hiyo. Zahanati zote zinaendeshwa na enrolled nurses (EN). Wilaya nzima ina Clinical Officer wanne tu. Vile vile kuna mashine ya X-Ray ambayo haina mtaalam wa kupiga picha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na Halmashauri kuwa na mapato kidogo na hivyo kushindwa kujenga hospitali mpya ili kukidhi mahitaji ya sasa kwa hospitali iliyokuwepo, ni ile iliyokuwa Kituo cha Afya cha Liwale Mjini kwani miundombinu ya hospitali hiyo siyo rafiki kwa sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mgao wa madawa kwenye Halmashauri ya Liwale ni mdogo sana hasa ukilinganisha na Halmashauri za jirani. Ni bora sasa Serikali ikatumia takwimu za Hospitali hiyo badala ya kutumia takwimu za mwaka 2012 (sensa). Kwa maneno mengine, kuna wakazi zaidi ya 10,000 wa Wilaya ya Liwale ambao hawana dawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali inatambua kuwepo kwa wazee nchini, kwa nini Serikali haitaki kuleta Sheria ya Wazee nchini ili kuwatambua huko, kuwepo kisheria. Wazee wengi nchini wanaishi kama wakiwa, kienyeji, kwani hawajui hatima yao katika nchi hii. Hawazijui haki zao. Namwomba Mheshimiwa Waziri alete hiyo sheria hapa kwa kuzingatia kuwa wote ni wazee watarajiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa na ukiritimba mkubwa sana juu ya matengenezo na service za mashine za X-Ray nchini. Hadi sasa kampuni pekee iliyopewa kazi hiyo nchi nzima ni Kampuni ya Philips. Je, Serikali haioni imefika wakati sasa wa kutafuta kampuni nyingine, kwani kampuni hiyo imeshindwa kazi? Ubovu wa mashine za X-Ray ni wa nchi mzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya Mama na Mtoto pamoja na kupewa kipaumbele katika Wizara hii, bado utekelezaji wake siyo wa kuridhisha kwani huduma hii bado haijawafikia akinamama wa vijijini mahali ambapo zahanati au vituo vya afya vikiwa mbali na vijiji hivyo. Hata hivyo ni vyema basi Serikali ikawekeza zaidi kwenye miundombinu ya usafiri vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uhaba mkubwa wa fedha ni jambo linalofanya Halmashauri nyingi kukosa dawa licha ya kuwa wanalipa dawa hizo, MSD haina uwezo kuleta dawa kwenye Halmashauri zetu kwa mujibu wa mahitaji ya Halmashauri husika. Vile vile wakati mwingine huleta dawa nje ya wakati na pengine nje ya mahitaji halisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Posho ya Mazingira Magumu (On Call Allowance) kuziacha chini ya Halmashauri ni kutokuwatendea haki watumishi wa kada ya Madaktari kwani vipaumbele vya Halmashauri hutofautiana toka Halmashauri moja hadi nyingine, hivyo kukosa uwiano wa vipato vya watumishi hawa. Hivyo ni bora posho hizi na allowance zake zikachukuliwa na Wizara husika ili zitolewe kwa mazingira yalivyo sasa kwa watumishi wa ngazi husika kutokana na mazingira ya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kuna ubaguzi mkubwa sana wa watumishi kupandishwa madaraja. Kuna watumishi wa muda mrefu hawajapandishwa wakati wapo wa muda mfupi wamepandishwa japo wana vigezo vinavyolingana, jambo linalopunguza morali ya kazi na ufanisi kazini. Vile vile viko vitendo kwa kuadhibu watumishi kwa kuwashusha vyeo na mishahara yao bila kuzingatia sheria za kazi. Jambo hili hupunguza ufanisi wa mhusika na matokeo yake hasira zote huishia kwa wagonjwa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze mchango wangu kwa kumshukuru Mungu kwa kuniamsha salama na kuendelea kunijalia uhai na kunipa uwezo wa kujadili hotuba hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze mchango wangu kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Katibu Mkuu wa Wizara hii pamoja na wakuu wote wa majeshi yetu yote. Kwa kweli, kazi inayofanywa na majeshi wanastahili pongezi na heshima iliyotukuka kwa kuilinda nchi yetu ndani na nje ya mipaka yetu. Askari wetu wanafanya kazi kwa weledi mkubwa, nasema hongereni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuacha kuwaingiza kwenye mfumo wa Bima ya Afya (NHIF) askari wetu sio jambo jema. Familia za askari wetu zinahangaika sana na masuala ya afya kwani hakuna hospitali bora kwenye vikosi/makambi ya majeshi yetu na zipo pia familia zinazokaa uraiani mbali na Kambi za Jeshi, hivyo wanapopata uhitaji wa matibabu wanapata shida sana. Serikali ione umuhimu wa kuwaingiza askari wetu kwenye utaratibu wa bima ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko pia tatizo la malipo ya posho za maaskari wetu. Wako maaskari wengi wanaodai posho mbalimbali kama vile posho za likizo, posho za madaraka na mengine kama hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la pili kwa majeshi yetu ni muda wa kuingia na kutoka kazini. Ili askari awahi kuingia kazini inamlazimu kutoka nyumbani saa 11:00 alfajiri au saa 10:30 na jioni wakitoka saa 11:00 wanafika nyumbani zaidi ya saa 03:00 usiku. Hawa ni wale wanaokaa nje ya makambi ya majeshi yetu, hivyo kuwafanya askari wetu kukosa utulivu wa kikazi maana muda mwingi wanashinda kwenye daladala, hasa kwa askari wanaoishi Dar es Salaam.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii jioni ya leo na mimi nichangie Wizara hii ya Maji. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na kuniwezesha jioni hii kusimama hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze moja kwa moja kwenye Mfuko wa Maji. Wachangiaji walio wengi hapa wameongelea kuhusu Mfuko wa Maji uongezewe fedha kutoka shilingi 50 kwenda shilingi 100 na mimi naunga mkono. Hata hivyo, naunga mkono lakini kwa upande mwingine nasikitika. Nasikitika kwa sababu nimeangalia kwenye hiki kitabu cha Mheshimiwa Waziri kwenye huu Mfuko wa Maji kwangu mimi sijatengewa pesa hata shilingi. Kwa hiyo, pamoja na kuomba kwamba uongezewe fedha lakini kwangu mimi ni majanga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukifungua ukurasa wa 159 - 164 pale pameorodheshwa watu waliotengewa fedha zinazotokana na mradi wa maji katika Miji Midogo lakini Liwale haijatajwa. Kwa bahati mbaya zaidi ikaja ikatajwa ukurasa wa 164, namba 32 pale pametajwa Halmashauri 14 ambazo zimetengewa shilingi bilioni 3.5. Hivi mimi kama mwakilishi wa wananchi wa Liwale pesa hizi zisipofika nazifuatilia wapi? Huoni uwezekano nitakavyokwenda kufuatilia pesa hizi naweza nikaambiwa zimeenda Chato, Mkuranga ama sehemu fulani kwa sababu pale
zimerundikwa Halmashauri zaidi ya 14, nashindwa kuelewa.
(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika Halmashauri yangu ya Wilaya ya Liwale nimeshakwenda kwa Waziri mara kumi kidogo. Nimemwambia kuna mradi wa kutafuta chanzo cha maji mbadala kwa Mji wa Liwale, umeshakula shilingi milioni 200 lakini mpaka leo mradi ule umekufa na maji Liwale hatuna. Namwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha hapa atuambie hatua gani imefikia mpaka mradi ule umekufa?(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwenye Mradi wa Maji Vijijini ambao unafadhiliwa na World Bank, awamu ya kwanza ilikuwa ni vijiji kumi lakini kwenye Halmashauri yangu nina vijiji saba tu lakini bado mpaka leo hii Vijiji vya Kipule, Mihumo na Ngongowele visima vile vimeachwa, vimeishia ardhini hakuna maji mpaka leo. Mheshimiwa Waziri atakaporudi hapa kuhitimisha hoja hii naomba atueleze ni nini hatima ya mradi ule. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sio hivyo tu, nashukuru, Alhamdulilah, Kijiji cha Mpigamiti mpaka sasa hivi kimepata maji lakini kuna Vijiji vya Ngolongopa, Naujombo, Kitogolo, Mtawambo, Mkutano, Makata, Mikunya, Ngunja, Mkundi na Nandimba havina maji kabisa. Kwa hiyo, kwa heshima na taadhima namwomba Mheshimiwa Waziri awahurumie watu wa Liwale. Kama takwimu zinaonyesha kwamba Liwale tuko watu wachache kama ambavyo nimewahi kusema hatustahili kupata maji hayo niyasikie leo. Kama tuko wachache basi watuwekee koki moja moja kila kijiji kuliko kutunyima maji kabisa.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naingia kwenye skimu ya umwagiliaji.Nimeshaongea naMheshimiwa Waziri mara nyingi, kuna miradi mitatu ya skimu ya umwagiliaji Wilaya ya Liwale imegharimu nchi hii zaidi ya shilingi bilioni nne lakini mpaka leo hii ni mwaka wa saba hakuna senti hata moja iliyorudi kutoka kwenye miradi ile. Kwa maana kwamba hakuna mkulima aliyenufaika na miradi ile hasa hasa mradi wa Ngongowele. Niameangalia kwenye kitabu chake ametaja mradi mmoja tu wa Mtawango, mradi wa Ngongowele hautajwi kabisa na huu mradi wa Ngongowele ukienda pale ni ardhi tupu mpaka leo. Nafikiri nimeshakwenda kwake zaidi ya mara tatu. Kama Liwale hawaithamini basi hata hizi pesa za Serikali nazo hawazithamini, shilingi bilioni nne zimeteketea pale hakuna chochote kilichozalishwa nchi hii, tunafikiria kufanya kitu gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, usimamizi wa miradi hasa ya umwagiliaji, nashindwa kuelewa, tukienda kwenye Halmashauri tunaambiwa miradi hii inasimamiwa na Kanda kwamba sisi watu wa Halmashauri hatutakiwi kuhoji chochote. Sasa inapofikia miradi ile haikamiliki nani wa kumfuata? Mheshimiwa Waziri nimeshakwenda kwake zaidi ya mara tatu naulizia, atupe ufafanuzi hii miradi nani afuatwe, watu wa Kanda au watu wa Halmashauri lakini hakuna majibu yoyote ambayo ameweza kunipatia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo basi, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa kuhitimisha anieleze tatizo la maji linatokana na nini hasa Mkoa wa Lindi. Hata kwenye bajeti mkoa ambao umepata bajeti ndogo zaidi ni Mkoa wa Lindi, tatizo liko wapi? Au ile dhana ya Kusini bado mnaiendeleza?Mnataka ile hadithi niliyowapa hapa iwe ya kweli?Jamani naomba tuiangalie Kusini, tuiangalie Lindi. Lindi tunahitaji maji hata kama tuko wachache hao wachache wanahitaji maji, maji hayana wingi wala uchache wa mtu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maana kama upande wa hospitali unaweza kusema kwa sababu tunahudumia watu wachache Madaktari wawili wanatosha, lakini maji nayo je? Tunaomba Mheshimiwa Waziri pamoja na kwamba Wabunge wengi wamesema kwamba Wizara hii ya Maji iongezewe bajeti, naomba atakapoongezewa bajeti kama hili litakubalika basi autazame Mkoa wa Lindi maana bajeti yetu ni ndogo sana. Tena hizo fedha kidogo tulizotengewa ni za wafadhili na siyo za ndani. Kama fedha za ndani hatuna tunategemea fedha za wafadhili itakuwa shida wasipoleta. Mkoa wa Lindi bajeti yetu asilimia kubwa ni ya wafadhili maana yake wafadhili wasipotoa pesa Mkoa wa Lindi tumeambulia patupu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijagongewa kengele ya pili, nilikuwa na hayo machache ya kumweleza Mheshimiwa Waziri. Tena kwa bahati mbaya zaidi kwa sababu ya matatizo ya usafiri nimekosa Mawaziri watatu mwezi wa Kwanza na wa Pili kuja Liwale kutembelea ile Wilaya, Naibu Waziri na Waziri wa Miundombinu ni wamojawapo, walipanga kuja Liwale lakini wameshindwa kuja kwa sababu ya usafiri, barabara chafu na mbaya. Nataka niseme kama Mawaziri hawatakuja nitaendelea kupiga kelele hapa na Mungu anawaona.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii jioni ya leo nami nitoe mchango wangu katika Wizara ya Maliasili. Kwa imani yangu ni kwamba Mawaziri wa Wizara hii ni wasikivu, basi haya nitakayoyashauri hapa, pengine yakawa na tija kwao na kwa Taifa kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze mchango wangu kwa kujielekeza kwenye Hifadhi ya Selous. Kama ambavyo alivyotangulia kusema mama yangu pale, kwamba asilimia 60 ya Selous iko Liwale. Nami nataka kuwapa historia ya Selous pengine Wabunge wenzetu hamuelewi hii ilikuwa kuwaje. Founder wa hii hifadhi ya Selous alikuwa ni Fedrick Selous mnamo mwaka 1879. Mwaka 1905 ndipo hili eneo la Selous likatengwa kama eneo la uwindaji. Siyo hivyo tu mwaka 1922 ndipo eneo hili likahifadhiwa kama game reserve. Mpaka mwaka 1982 UNESCO waliitambua hii kama Hifadhi ya Dunia, hiyo ni historia fupi ya Selous.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na sifa hizi zote zilizonazo Selous lakini lango la kuingilia Selous liko Morogoro. Kwa maana ya kwamba ukanda mzima ule wa Kusini kuanzia Rufiji mpaka Lindi hakuna lango la kuingilia Selous. Sasa wana Selous wale walioko Liwale ambao ndiyo
wahifadhi wa kwanza, mimi naamini kwamba wahifadhi wa kwanza wa hifadhi yoyote ile ni wale wanaozunguka hifadhi. Kwa hiyo, Wanaliwale au Wanalindi kwa ujumla wake ndiyo wahifadhi wa kwanza lakini hakuna lango la kuingilia Selous, kwa maana hiyo basi hakuna manufaa yoyote ambayo wanapata wale ya direct kwa watu waliopo pale Selous.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri hebu aiangalie Selous na aangalie Kusini, mpaka leo hii Kusini hatuna hoteli ya kitalii wala hata barabara ya kufika kwenye hii hifadhi hatuna. Kama mpaka hata Wazungu nao wenzetu wanaithamini kwa kiwango hicho tunawezaje kushindwa hata kuweka barabara ya kuifikia hiyo Selous? Hili ni jambo la kusikitisha sana hasa kwa watu wa Kusini tunaoizunguka hii Selous. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nijielekeze sasa kwenye mamlaka ya Uvunaji wa Mali za Misitu (TFS). TFS ilivyoundwa na lengo lake na inavyofanya kazi, mimi kwa upande wangu naona ni kinyume chake. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Liwale tuna misitu ya aina mbili, kuna msitu wa Nyera Kipelele huu msitu tumeurithi kutoka kwa wakoloni, kuna msitu wa Hangai, huu ni msitu wa vijiji. Msitu huu ni msitu ambao umechangiwa na vijiji kadhaa moja ya vijiji vichache ambavyo vimechangia msitu huu ni Kijiji cha Ngongowele, Mpigamiti, Mikunya, Lilombe, Kitogoro, Mtawango, Mtawatawa, Mitawa, Namakololo, Makirikiti na Kipule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wote wamechangia kuhifadhi hii misitu lakini kinachoshangaza kwenye Kamati ya uvunaji wa misitu hii, Mwenyekiti ni Mkuu wa Mkoa, Mwenyekiti wa Halmashauri hayumo kwenye Kamati ya Uvunaji, Mbunge wa Jimbo husika hayumo kwenye Kamati ya Uvunaji waliopo kwenye Kamati hii ni Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi wa Halmashauri, OCD na watu wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, misitu hii imehifadhiwa na wanavijiji nami kama mwakilishi wa wanavijiji simo kwenye Kamati ya Uvunaji, uvunaji huu unakwendaje? Namwomba sana Mheshimiwa Waziri hebu afikirie muundo wa hii Taasisi ya TFS na uvunaji wa TFS.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, kwenye TFS Halmashauri tunapata asilimia tano ya kile kinachovunwa pale Halmashauri. Naomba sana hata wakati nachangia kwenye hotuba ya Waziri Mkuu nilisema naomba Mheshimiwa Waziri turejeshe hapa hiyo sera ya uundwaji wa TFS ili tuongeze angalau tufike hata asilimia 20 ili tunaozungukwa na ile misitu tuweze kunufaika na ile misitu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti katika nafasi hiyo ya TFS, elimu kwa sababu kuna Kamati za Vijiji ndiyo wanashughulika na mambo ya uvunaji wa hii misitu, lakini wale wanavijiji hawajapata elimu yoyote na wala hakuna semina yoyote inayowafikia. Matokeo yake kinachofanyika sasa mtu anapata leseni, anaenda kuvuna cubic meter 100 na anakata mti akikuta huo mti una pango anauacha, ili uweze kukamilisha mzigo wake maana yake unaacha jangwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanavijiji wale wanasaidiwa vipi? Hakuna elimu yoyote wanayoipata kujua kwamba madhara yanayotokana na ile miti ambayo yule mwekezaji haitaki, ile miti anailipiaje, Halmashauri inapata nini? Matokeo yake Halmashauri tunapata jangwa tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, msitu wa Nyera Kipelele ni msitu tumeurithi kutoka kwa wakoloni, mpaka leo hii harvesting plan ya msitu ule haijatoka. Nimekwenda pale nimepata kitabu cha mwongozo kinaitwa kitabu cha mwongozo wa uvunaji endelevu. Kitabu hicho kwenye Halmashauri kipo kimoja tu na nimekutajia vijiji zaidi ya 20 ambavyo vina hifadhi lakini kitabu cha mwongozo wa uvunaji endelevu kipo kimoja kwenye Halmashauri. Msitu wa Nyera Kipelele mpaka leo hauna harversting plan maana yake ni kwamba huu msitu haujaanza uvunaji, tumeurithi kutoka kwa wakoloni. Sasa hawa ambao wanazungukwa na huu msitu wananufaika na nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo naomba nijielekeze kwenye Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA). Hii taasisi haina ushirikiano na Halmashauri zetu, kwa sababu leo hii wanasema asilimia 25 ya mapato ya uwindaji wa kitalii yanaenda kwenye Halmashauri, huu ni mwaka wa tatu, mwaka wa nne, kila tukifungua kwenye Halmashauri pale kwenye mapato yetu haimo, hili pato haliingi. Nimefuatilia mpaka TAWA, nikawauliza kwanza nilitaka nijue hii asilimia 25 ni ya nini? Sijapata majibu mpaka leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hawa watu wa TAWA hawawezi kutoa ushirikiano, tena nilienda pale wakaniambia kwamba hii sisi siyo Wasemaji wa TAWA nenda kwa Katibu Mkuu. Nimefika kwa Katibu Mkuu wa Wizara sijapata majibu mpaka leo. Tunapata asilimia 25, asilimia 25 ya nini?(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika mambo ya utalii; utalii kwenye Halmashauri ya Liwale kuna boma la Mjerumani nilishalisema hapa, lile boma la Mjerumani ni moja ya kivutio cha utalii. Kwa sababu kumbukumbu yote ya vita ya Maji Maji ukitaka kuongelea leo lazima utalikumbuka lile jengo la vita ya Maji Maji. Vilevile tuna kivutio cha utalii kwenye kaburi la Mfaransa, watalii wanakuja kutoka Ujerumani wanakuja kuangalia pale, kila mwaka wanakuja kuhiji, lakini sisi wenyewe tumelala. Kuna kaburi la Bimkubwa wangu mmoja pale Ndapata, watu wanakwenda kuhiji pale lakini sisi wenyewe tumelala hivi vyote ni vivutio.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi Tanzania tupewe nini na Mwenyezi Mungu ili tuone kwamba tuko duniani. Kama watu wa nje wanaweza kutambua vivutio vyetu vya utalii sisi wenyewe tusivitambue. Mheshimiwa Waziri, najua ni msikivu najua hili ninalolisema atalisikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa naomba niongelee mgogoro wa Hifadhi ya Selous na Kijiji cha Kikulyungu. Mgogoro huu sasa hivi una zaidi ya miaka 10 na umeshapoteza maisha ya watu wanne, namwomba Mheshimiwa Waziri afanye analoliweza, afike Kikulyungu atumalizie huu mgogoro kati yetu na wahifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze sasa katika mchango wa maendeleo unaotokana na hifadhi ya misitu. Mchango wa maendeleo pale kwetu wanasema kwamba ubao mmoja wana utoza sh. 400 kwenye Halmashauri ya Kijiji, gogo moja sh. 1000, hebu fikiria msitu ule unaohamishwa pale, sisi tunaambulia sh. 400! Kwa kweli Mheshimiwa Waziri hizi sheria tunaomba...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze mchango wangu kwanza kwa kumshukuru Mwenyenzi Mungu kwa kuniwezesha kushika kalamu na kutoa mchango wangu kwa njia ya maandishi.

Kwanza kabisa naomba kuchangia juu ya Wakala wa Uhifadhi na Uvunaji wa Mazao ya Misitu (TFS). Taasisi hii imekuwa ni mzigo kwenye Halmashauri zetu, badala ya kuwa taasisi ya uhifadhi yenyewe inaongoza kwa kuharibu misitu vilevile mahusiano ya taasisi hii na jamii au Halmashauri zetu siyo mzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taasisi hii imekuwa haitoi elimu ya kutosha kwa jamii juu ya uvunaji endelevu wa misitu badala yake imekuwa ikiwalinda wavunaji haramu kwa faida ya watendaji wa taasisi. Mfano mzuri ni katika Halmashauri yangu ya Liwale katika Wilaya ya Liwale kuna hifadhi mbili za misitu, kuna msitu wa Angai ambao unahifadhiwa na vijiji 24, na msitu wa Nyera-Kipelele, huu ni msitu wa kitaifa lakini hadi leo msitu wa Nyera - Kipelele bado uvunaji haujafanyika. TFS wanasema mwongozo wa uvunaji haujakamilika lakini wavunaji haramu wanavuna kila kukicha bila ya wahusika kuchukua hatua za kuzuia ujangili huu. Kwa ule msitu wa vijiji bado vijiji havina elimu ya kutosha juu ya uvunaji endelevu jambo linalochangia kwa kiasi kikubwa upotevu wa mapato katika vijiji husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kukosekana kwa uwakilishi wa Mbunge na Madiwani katika Kamati ya Uvunaji wa Rasilimali za Misitu kunaongeza mwanya wa wizi wa mali za misitu. Kamati hii huongozwa na Wakuu wa Mikoa. Je, kuna siri gani inayofanya Meya na Wabunge washindwe kualikwa kwenye Kamati hizi ikiwa wao ni wawakilisi wa wananchi? Vilevile makato ya asilimia tano yanayotengwa kwenye Halmashauri zetu ni kidogo mno kulinganisha na uharibifu wa misitu hiyo, Halmashauri zetu hutegemea misitu katika kukuza uchumi wake, hivyo naishauri Serikali kuangalia upya viwango hivyo ili kuviboresha na kuziongezea uwezo Halmshauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee Pori la Akiba la Selous. Hifadhi hii ni kubwa sana hapa Barani Afrika na duniani kwa ujumla na sehemu kubwa ya hifadhi hii iko Wilayani Liwale, cha kusikitisha hakuna miundombinu yoyote iliyojengwa Liwale katika kuhudumia hifadhi hii. Hata barabara ya kuingia katika hifadhi hakuna, lango la kuingia kwenye hifadhi hii kwa watalii liko Mikumi Mkoani Morogoro jambo linalowanyima fursa za ajira kwa wakazi wa Wilaya ya Liwale na Mkoa wa Lindi kwa ujumla. Hivyo, naiomba Serikali kufikiri kufanya uwekezaji wa kutosha ili wale wanaozungukwa na hifadhi hii waone faida ya kuwa na hifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Mamlaka ya Wanyamapori, pamoja na nia nzuri ya Serikali ya kuanzisha mamlaka hii, utendaji wake bado siyo wa kuridhisha, bado kuna usiri mkubwa na ushirikiano na jamii zinazozungukwa na hifadhi siyo nzuri. Mfano katika Halmshauri yangu ya Liwale hadi leo hatujui hatma ya mgao wetu wa asilimia 25 ya mapato yatokanayo na uwindaji wa kitalii. Hatujui tunayapataje, ukiwauliza wahusika hawana majibu ya kuridhisha zaidi ya kukatisha tamaa. Kitendo cha kuficha taarifa za mapato na kuacha kuweka wazi stahiki za Halmashauri zetu hakioneshi au kinapingana na malengo ya kuundwa kwa taasisi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa sekta ya utalii kwa Kanda ya Kusini bado vivutio vingi havijatangazwa vema au vimesahaulika kabisa. Ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi katika Mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara kuna vivutio vingi havijatangazwa. Mfano, Boma la Mjerumani lililoko Liwale, Kaburi ya Mzungu (Mfaransa) lililoko Mikukuyumbu- Liwale. Kaburi la Bibi aliyesadikiwa kuwa ni Sharifu katika uhai wake lililopo katika kijiji cha Ndapata - Liwale. Vilevile kuna viboko wanaowasiliana na wazee wa kimila walioko Kilwa, pamoja na maji moto yaliyopo katika Mto Rufiji. Hivi vyote ni vivutio vya utalii vilivyosahaulika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu migogoro ya mipaka, kuna mgogoro wa muda mrefu wa mpaka wa kijiji cha Kikulyungu na Hifadhi ya Selous, mgogoro huu umeshachukua roho za watu wanne, ni bora sasa mgogoro huu ukapatiwa ufumbuzi ili amani na usalama vikarejea baina ya jamii na wahifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fidia kwa ndugu Abilahi Njonjo, huyu ni mwananchi aliyejeruhiwa na Askari wa wanyamapori kwa kupigwa risasi kusababisha akatwe mkono. Taarifa zake ziko Ofisi ya Katibu Mkuu wa Wizara akilalamikia namna ya kupata hicho kinachoitwa kifuta machozi ni miaka miwili sasa tangu amekatwa mkono.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mwongozo wa Spika.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Zuberi Kuchauka.

MWONGOZO WA SPIKA

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba mwongozo wako…

NAIBU SPIKA: Kanuni?

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, Kanuni ya 76. Naomba mwongozo wako kwa sababu hii bajeti tunayojadili ni bajeti muhimu sana na haya tunayowaambia tunaiambia Serikali na Serikali ni mtambuka. Humu ndani tuna Mawaziri sita tu, na Naibu Mawaziri wako saba tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano kama haya mambo ya kutokupeleka fedha kwenye bajeti yanahusu Wizara ya Fedha; kuna mambo mengine ya vibali vya ujenzi, GN na nini, inahusu mambo ya Mazingira na nini. Lakini humu tuna Mawaziri sita tu na Naibu Mawaziri wako saba tu; haya mambo yanakwendaje?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba mwongozo wako.

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, amesimama Mheshimiwa Zuberi Kuchauka akiomba Mwongozo wa Kiti kuhusu kuwepo kwa baadhi ya Mawaziri hapa na wengine yeye hawaoni, kwa hiyo, anajiuliza yaani haya tunayozungumza je na wao watayachukua kwa uzito wa namna hii?

Waheshimiwa Wabunge, kwanza, kama alivyosema yeye mwenyewe ni kwamba Serikali ni moja, kwa hiyo, anayesikiliza atafikisha huo ujumbe; moja. Lakini la pili, hata mimi wakati nazungumza nimeeleza hapa kuhusu Waziri wa Ujenzi lakini nikasema pia Waziri wa TAMISEMI, najua nini, humu ndani lazima Waziri wa TAMISEMI atapata taarifa kwamba yeye na Waziri wa Ujenzi wanahitajika kwenda Mbeya.

Maana yake ni nini; hapa tulimsoma Mheshimiwa William Lukuvi, kwamba ndiye msimamizi wa Shughuli za Serikali Bungeni, Waziri Mkuu hayupo. Kwa hiyo, madam yeye amekaa pale, uwe na uhakika kwamba shughuli zote za Serikali humu ndani zinao usimamizi. Kwa hiyo ujumbe wataupata kila mtu vile unavyostahili. (Makofi)

Kwa hiyo, hata mpiga sarakasi ujumbe wake utafika kwenye sehemu inayotakiwa kwa sababu miundombinu anayosema hizi ni zile barabara kubwa. Lakini barabara kubwa haziwezi kufanya kazi peke yake bila barabara ndogo ambazo ni za TAMISEMI. Kwa hiyo, wakati wa TAMISEMI Waziri wa Ujenzi na Manaibu wake walikuwa wanasikiliza kwamba hizi barabara wanazozisema Wabunge zinailisha barabara gani kubwa.

Na sasa na yeye anaposikiliza kuhusu barabara kubwa anazoeleza Mbunge yeyote, barabara kubwa au kama hivi tunavyosema ujenzi wa reli na vitu kama hivyo, wao kama Serikali wanafahamu ni barabara zipi zitatakiwa kulishana namna hiyo.

Kwa hiyo msiwe na wasiwasi Waheshimiwa Wabunge michango yenu ndiyo maana huwa mnazungumza na mimi hapa mbele, na ndiyo kazi yangu. Mnazungumza na mimi, ukishazungumza na mimi usiwe na wasiwasi, hata kama Waziri wa Ujenzi hakuwepo hapa ujumbe ataupata. Ahsante sana. (Makofi)

Itifaki ya Nagoya ya Kusimamia Upatikanaji na Mgawanyo Sahihi wa Faida zitokanazo na Matumizi ya Rasilimali za Kijenetiki.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na mimi kunipa nafasi nitoe mchango wangu katika kuridhia hii itifaki ambayo imewasilishwa leo mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote kama mwasilishaji alivyosema kwamba tunazo faida mbalimbali ameziainisha hapa, faida ambazo tungeweza kuzipata anasema kwamba ni kuimarisha uchumi, kuongeza mazao ya bahari pamoja na ushirikiano wa kikanda. Lakini wazo langu au maoni yangu ni kwamba kwanza kabisa niungane na Kambi Rasmi ya Upinzani yale maoni ambayo wameyatoa naishauri Serikali iendelee kuyazingatia kwa umakini kabisa, kwa sababu tatizo letu siyo tu kuridhia hii mikataba kwanza ni mipango dhabiti ya utekelezaji wa mikataba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Tanzania imekuwa na kawaida ya kusuasua sana kutekeleza mikataba mbalimbali ambayo tunaingia ya Kimataifa. Kwa mfano, sasa hivi tunakwenda kuridhia hii itifaki ambayo tunaizungumzia leo, lakini je, Serikali iko tayari kuleta sheria, kutunga sheria za utekelezaji ambayo itasimamia kwa uhalisia kabisa kulingana na matakwa ya mikataba hii ambayo tunakwenda kuiridhia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ukiangalia tunayo taasisi ambayo kama msemaji aliyepita alisema Taasisi ya Uhifadhi wa Mali/Bidhaa za Bahari. Lakini je, hii taasisi kama Serikali mmeiwezesha kwa kiwango gani ili hayo matakwa yaweze kutekelezeka kama ambavyo tumeridhia? Vilevile kwenye utafiti mara nyingi tumekuwa tukiibiwa rasilimali zetu nyingi za baharini na nchi kavu na hawa watu wanaojiita watafiti. Ni kweli kabisa mara nyingi watafiti wanapofanya utafiti wanaondoka na viumbe hai, wanaondoka na mali zetu, lakini sisi wenyewe tumejidhatiti kwa kiwango gani, hizi tafiti badala ya kufanyika na watu wa nje na wenyewe tuweze kufanya hizi tafiti ili taasisi yetu kwa mfano, Maritime Institute pale Dar es Salaam sijui kwamba na yenyewe imeimarishwa kwa kiwango gani ili tafiti nyingine ziweze kufanyika hapa nchini badala ya kwamba hawa watu wanakuja kutuibia, wakati wenyewe tuna uwezo nalo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ukiangalia mara nyingi Watanzania tumekuwa na kigugumizi sana. Mimi sijaelewa Serikali inakuwaga na kigugumizi cha namna gani, kwa sababu ukiangalia mikataba mingi tuliyoridhia kwanza tunachukua muda mrefu sana kuiridhia na baada ya kuiridhia tunakuwa na kigugumizi sana katika utekelezaji. Naiomba Serikali izingatie ushauri ambao umetolewa na Kambi Rasmi ya Upinzani na Wabunge mbalimbali ambao wanachangia hapa. Hili wote tunajua kwamba tunafanya hivi kwa kuhifadhi mazingira yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kusema ukweli kwa upande wa baharini, kwa kweli Serikali tumesahau sana bahari, kwa sababu ukiangalia uchumi Tanzania tumezungukwa na Pwani kutoka Tanga mpaka Mtwara, lakini ni kiwango gani tunanufaika? Serikali inanufaikaje na fukwe hizi? Tumewekeza kwa kiwango gani? Utakuta uwekezaji tuliouwekeza huku ni mdogo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesema hapa wakati tunachangia bajeti ya kilimo na uvuvi wakasema kwamba sekta binafsi ndiyo wameachiwa wao ndiyo wanunue meli kubwa za uvuvi ili tuweze kuvua na ndio jambo linalopelekea mpaka leo hii tunakula samaki kutoka China. Hivi kweli kwa utajiri huu tulionao Tanzania kuanzia Tanga mpaka Mtwara leo hii hatuna hata meli moja ya uvuvi wa kisasa, hivi tunategemea ulinzi huu wa hizi rasilimali zetu za baharini huyo mlinzi atatoka wapi? Hivi ni kweli hawa Watafiti ambao tunawategemea kutoka nje ndiyo waweze kulinda mali zetu? Kwa kweli jambo hili silioni kama lina tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali kwa dhati kabisa tutoke tuwekeze kwenye bahari ili nasi tuweze kunufaika nayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa hayo machache naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze mchango wangu kwanza kwa kuwapongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa uchapakazi wake katika Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu unajikita mwanzo kwa Kitengo cha Upimaji wa Ardhi, naomba kuishauri Serikali kuongeza kasi ya upimaji wa ardhi kwenye Halmashauri zetu. Kitendo cha kuiachia Halmashauri jukumu la kupima ardhi bila msaada wa Serikali Kuu kutaacha Halmashauri nyingi kuwa na makazi holela kwenye Halmashauri zetu nchini, hasa zile Halmashauri zenye mapato kidogo. Hivyo basi niishauri Serikali kuongeza fedha za upimaji wa ardhi ili kupunguza utaratibu wa urasmishaji wa aridhi ambao hauna tofauti sana na makazi holela.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wilaya yangu ya Liwale yuko Afisa Ardhi ambaye ameleta huu utaratibu wa urasmishaji ambao kwa mazingira ya Wilaya yetu haina uhaba wa ardhi, hivyo nikuombe Mheshimiwa Waziri kumsimamisha mara moja mpimaji huyu ambaye anakwenda kuharibu makazi ya mji wetu wa Liwale.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kwenye Halmashauri yetu inakabiliwa na uhaba mkubwa watumishi wa ardhi kiasi cha kulazimika kuazima wapima toka Wilaya jirani ya Nachingwea ambapo Halmashauri huingia gharama za ziada ya upimaji kwa kuwa mpima toka jirani hulipwa malipo ya ziada nje ya bejeti. Jambo hili huongeza bei za viwanja na kuwafanya wananchi wa kawaida kushindwa kumudu viwanja hivyo na hivyo kuwafanya wandelee kukaa kwenye makazi holela.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wa Lindi, Liwale ndio Wilaya pekee iliyokubali kupokea wafugaji katika Vijiji vya Kimambi, Ndapata na Lilombe. Lakini hadi leo vijiji hivyo havijafanyiwa matumizi bora ya ardhi, jambo linalosababisha migogoro ya ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo niiombe Serikali kuja kuisaidia Halmashauri kufanya matumizi bora ya ardhi katika vijiji hivi.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya Maftaha nami niweze kuchangia. Naomba nianze mchango wangu kwanza kwa kuzishukuru Kamati zote tatu kwa michango yao mikubwa na kuona haya waliyotuletea sisi yanatufaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe angalizo letu moja tu kwamba sisi kama Watanzania ni watu wazuri sana wa kupanga mipango; na mimi ningependekeza tuunde taasisi ya kupanga mipango pengine tukiuza mipango yetu nchi za nje tukapata pesa za kigeni. Kwa sababu tumekuwa wapangaji wazuri sana lakini kwenye utekelezaji tuko zero.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matatizo haya tuliyaongelea wakati tunapanga bajeti hapa, kwamba hizi bajeti hazitoshi kwa maana kwamba hazitakwenda kukidhi matakwa ya kile tunachokitarajia; na hiki ndicho ambacho Wenyeviti wa Kamati wametuletea. Kwa sababu Mwenyekiti wa Kamati amesema kwamba CAG hana resources za kutosha, kwa maana kwamba hana pesa za kutosha kuyaendea majukumu yake na haya tuliyaongea tangu mwanzo kwamba hizi pesa ambazo CAG tunamtengea hawezi kutekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile hata kwenye Kamati zetu za Bunge nazo tumeshindwa kuyaendea majukumu yetu, kukagua miradi iliyopelekewa pesa na Serikali kwa sababu ya tatizo la pesa. Ukienda kwenye halmashauri zetu nako huko watu wenyewe wanakaimu. Sasa ukiangalia bajeti ya Serikali asilimia 70 zinakwenda kwenye halmashauri. Hivi, Waheshimiwa Wabunge kama hawawezi kwenda kukagua miradi, CAG kama hawezi kwenda kukagua hesabu za Serikali, hivi tunatarajia weledi gani tulionao wa matumzi bora, matumizi sahihi ya hizi pesa tunazozipeleka kwenye halmashauri zetu. Hili ni jambo linaloshangaza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwaambie wenzetu mliopata uteuzi au madaraka ya kuisimamia nchi mtuone sisi nasi ni wazalendo. Hayo tunayoyasema tunasema kwa uzalendo kama ambavyo ninyi mnajiona; kwamba ninyi ni wazalendo zaidi kuliko sisi na ndiyo maana hata tunaposhauri mnatuona kwamba tunashauri kama vile tunawapuuza, lakini tunawashauri tukiwa na nia ile ile kwamba na sisi ni wazalendo na tunashauri kwa uzalendo mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye viwanda. Hapa tunapigiwa kelele tu kila siku kwamba viwanda vinafufuliwa, lakini sisi watu wa kusini tunalalamika kwamba kulikuwa na viwanda vya korosho kila wilaya, lakini hakuna kinachofufuliwa hata kimoja na vyote leo hii tunaambiwa vilivyo vingi viko kwenye kesi, kwa hiyo haviwezi kufufuliwa viko kwenye kesi tunabaki kuwa maskini. Kama mama yangu alivyokuwa anasema, kwamba sisi tumebaki kama nchi kama vile haina mwenyewe, hili jambo hata sisi linatuumiza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwenye uwekezaji sekta ambayo kama kweli Serikali ya Awamu ya Tano kama imeamua kuwekeza kwa ajili ya kumkomboa Mtanzania basi sekta mojawapo ambayo ilikuwa ni muhimu ni sekta ya kilimo; lakini sekta ya kilimo imebaki kwenye makaratasi. Mheshimiwa Waziri wa kwanza wa Wizara hii alisema awamu ya tano tunaweka jembe la mkono litakuwa makumbusho, lakini mpaka leo hii tunafika huko katikati jembe la mkulima bado halijaenda makumbusho na sidhani kama litakwenda makumbusho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini bado hata wale wachache wanaojitokeza kuwekeza kwenye kilimo bado hatuwatendei haki. Mimi hainiingii akilini mtu umewekeza, umelima, umevuna mahindi, inatoka Serikali inasema hayo mahindi usiuze halafu NFRA hawanunui, huyu mkulima amewekeza, kwamba amechukua mikopo benki, anailipaje? Yaani tunategemea mkulima yeye ndiye awe food security unit ya Taifa, hii haingii akilini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii kama tulivyosema, kwa mfano kama sasa hivi korosho ndizo zinazofanya vizuri kwenye soko la kimataifa; lakini hizi korosho ni Mwenyezi Mungu tu katupendelea, Serikali haijawekeza mkakati wowote wa kuendeleza zao hili zaidi ya kwenda tu kutafutia soko hapa Vietnam basi, lakini, hakuna mkakati wowote ule ambao umesimamiwa kwamba Serikali imefanya mkakati huu, zao hili la korosho limefika hapa lilipofika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kuna matamko ya viongozi. Naomba hayo matamko ya viongozi lazima yaendane na uhalisia. Tulipokuja kwenye zao la korosho katikati ya msimu tumekuja kuambiwa sulfur itatolewa bure, magunia yatatolewa bure, lakini ukienda kwenye Bodi ya Korosho wanakwambia wao bajeti yao ilikuwa wamesha- order tayari sulfur ya tani elfu tisa, lakini mahitaji halisi ni tani elfu kumi na nane. Sasa tani hizo zingine elfu tisa zinapatikana wapi? Ndiyo maaana sasa hivi kwenye msimu tukahangaika mpaka sulfur ya 35, 000 tumenunua 75,000 lakini lile tamko lilikuja katikati ya mradi. Tunakwenda wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii hapa Mwenyekiti amesema Kodi ya Korosho mpaka leo hii ile asilimia 65 hawajapata lakini leo hii hawa hawa Bodi ya Korosho sasa hivi wanatakiwa waagize sulfur. Itakapofika mwezi wa Nne mwaka huu sulfur inatakiwa imfikie mkulima lakini mpaka leo Bodi hawajapata hela. Ndiyo maana nikasema hili zao la korosho nalo Mwenyezi Mungu tu kataka ndiyo hapo lilipofikia lakini mkakati wa Serikali sijauona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija kwenye uwekezaji wa viwanda vidogo vidogo, kama ambavyo waliotangulia kuchangia walivyosema mimi mwenyewe na-declare interest kwamba na mimi nina kiwanda kidogo cha usindikaji wa nafaka. Mkitaka kujua shida ya nchi hii wewe anzisha kiwanda chako. Atakuja TFDA, atakuja OSHA, atakuja TBS, atakuja bibi afya wa kata, atakuja NEMC, atakuja sijui wa mazingira gani hawa wote wanakuja wanakutafuna, wanakumaliza moja kwa moja, unatamani kwa nini nimeanzisha hiki kiwanda? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa basi hizi taasisi zote basi ziingie kwenye mfumo mmoja, kwamba mtu unakwenda mahali pamoja unalipia hizo taasisi zote, lakini uzunguke leo niende TFDA, kesho niende TBS, kesho kutwa nakwenda OSHA yaani ni vurugu. Kwa kweli…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 na Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi jioni hii ya leo ili nami niweze kuchangia Kamati hizi mbili. Awali ya yote nizipongeze Kamati zote mbili kwa uwasilishaji wa umakini kabisa na kazi nzuri iliyofanywa na Kamati hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, naomba nielekeze ushauri kwa Serikali. Serikali ya Awamu ya Tano au Serikali ya Chama cha Mapinduzi hebu tupunguze umakini unaotupelekea kutokuwa makini. Kwa mfano, mradi huu wa reli ya standard gauge tumesaini mwaka mmoja na Kenya, Kenya wamemaliza lakini sisi kwa sababu ya umakini tumechelewa mpaka leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Bandari ya Dar es Salaam yuko mwekezaji pale alileta ombi lake la kujenga grain terminal miaka kumi na moja (11) imekwisha mpaka leo haijajengwa amekwenda Msumbiji amepewa miaka miwili grain terminal inafanya kazi. Tanzania tuko makini mno, huu umakini ndiyo unaotupozea muda na kuonekana tuko nyuma. Naomba hilo mlichukue kama ni changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niende kwenye hotuba za Kamati mbalimbali. Kamati zote ambazo zimeshawasilisha hapa taarifa zake, tatizo hili la upatikanaji wa fedha kila Kamati lazima iguse. Tunalo tatizo kwenye Serikali ya Chama cha Mapinduzi ya utoaji wa pesa, pamoja na kwamba tulipopitisha bajeti Wizara nyingi zilikuwa zinalalamikiwa kwamba pesa hazitoshi lakini hata zile kidogo zilizotengwa bado haziendi kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili limekuwa likigharimu sana miradi yetu ya maendeleo kukwama. Miradi mingi hapa ambayo leo hii haijatekelezwa tatizo kubwa ni upatikanaji wa pesa. Sasa hatuelewi tatizo hili ni nini na dawa yake ni nini, ni tatizo sugu kwa mimi ninavyoliona.

Mheshimiwa Naibu Spika, ufanisi wa bandari hasa nikianzia na bandari yetu ya Dar es Salaam. Kabla sijaingia kwenye Bunge hili Gati namba saba, moja na mengine tangu mwaka 2008 linatajwa mpaka leo lipo kwenye vitabu tu. Mnaendelea kutuchafulia makaratasi tu Gati namba tatu , namba nne hatuelewi nini kinachoendelea. Tunawaombeni sana sana wote sisi tuna uchungu na nchi hii hebu tufanye kazi tuache kufanya kazi kwa mazoea.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa viwanja vya ndege. Nashukuru Serikali imetuletea takwimu hapa, viwanja vingi vinaonekana vinataka kufanyiwa ukarabati, lakini hivi kweli tunajenga hivi viwanja hivi kwa mikakati ya kiuchumi au kukidhi matakwa ya kisiasa? Kwa sababu mimi kama ungeniuliza mikakati ya kiuchumi ningekutajia viwanja kama cha Mtwara, Kigoma, Songwe - Mbeya na hicho cha Mwanza ambacho mmekikazania.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo kubwa zaidi hatuna vipaumbele, tuna viwanja hapa tumeviandika lukuki lakini mwisho wa mwaka vyote hivi hakuna kilichokwenda. Hivi kwa nini hatuwezi kuamua tu mwaka huu tunashughulika na kiwanja namba A, mwaka mwingine namba B ili twende kuliko kurundika viwanja vya ndege lukuki ambavyo vyote hivi mwisho wa siku hatuwezi kuvifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Bodi ya Wakandarasi kwa mujibu wa sheria ndiyo mlezi wa wakandarasi lakini hivi kweli bodi hii inalea wakandarasi hasa hawa wazawa, tunawajengea uwezo kiasi gani? Mikakati ya kuwajengea uwezo wakandarasi hawa wadogo tunayo, mbona haieleweki? Mimi naiomba Serikali ya Chama cha Mapinduzi sisi wote nchi hii ni ya kwetu, wote ni wazalendo na haya tunayashauri kwa uzalendo mkubwa sana, naomba myachukue. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Kamati pametajwa sera ya kuunganisha mikoa yetu kwa barabara, mikoa kadhaa imetajwa, lakini nisikitike tu Mwenyekiti wangu alisahau tu, Mkoa wa Lindi na Morogoro hajautaja. Lindi na Morogoro unaunganishwa kwenye Wilaya ya Liwale na Wilaya ya Mahenge na hili tumelipigia kelele sana lakini kwenye vitabu hivi bado halijaweza kuonekana. Nawaombeni sana jambo hili ni la muhimu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, upande wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (USCAF). Huu Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote kwa mujibu wa taratibu unachangiwa na makampuni mbalimbali ya simu, hatujapata malalamiko kwamba makampuni haya hayajawahi kuchangia lakini tunapata malalamiko (USCAF) wana uhaba wa pesa. Sasa uhaba huu wa pesa unatoka wapi, iwapo haya makampuni yanachangia? Maana ukienda kuwauliza wanasema miradi mingi haitekelezwi kwa sababu ya pesa lakini source zile za pesa zinapatikana kwamba hawa wanachangiwa na kampuni za simu na zinachangia. Kwa nini pesa hizi Serikali hamtaki kuwapa hawa watu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile mimi niende upande wa madini, kule kwetu Mtwara kuna Kanda ya Mtwara ambayo ofisi yake moja iko Nachingwea, lakini Halmashauri ya Wilaya ya Liwale ina madini na soko lake liko Nachingwea. Sisi watu wa Halmashauri wa Wilaya ya Liwale tunapataje faida zaidi ya kuachiwa yale mashimo iwapo soko la madini liko Nachingwea na mratibu wa Kanda yuko Nachingwea. Naomba Mheshimiwa Waziri atufafanulie hili limekaaje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hotuba hii ya Waziri Mkuu. Awali ya yote, naomba nitoe ombi kwa Serikali ya CCM ya Awamu ya Tano na ombi hili naomba Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Lindi na Mtwara waniunge mkono kwa sababu hii ni hoja yetu sote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa Serikali ya Awamu ya Tano, naomba sana haka kasungura kadogo tulikonako basi tukagawanye sawa sawa, kwa sababu sisi sote tunachangia kwenye haka kasungura. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini naleta hili ombi? Kwa sababu ukipitia bajeti, hii ni bajeti ya tatu, bado Mkoa wa Lindi na Mtwara kwenye bajeti hii tunapata hasa kwenye pesa za miradi wa maendeleo kidogo sana. Kwa ushahidi jana dada yangu Mheshimiwa Hawa Ghasia kalisema hili, kwamba bajeti iliyokwenda kwenye Bandari ya Mtwara ni ndogo. Siyo bandari tu, yeye ameongea hivi kwa busara tu kwa sababu ya mazingira aliyonayo, lakini ukweli ni kwamba bajeti tunayopewa Mikoa hii miwili ni ya shida sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu ukiangalia, juzi tu hapa kuna mradi umetokea wa ukuzaji wa maliasili Ukanda wa Kusini, lakini ukanda wenyewe wa Kusini uliotajwa na kupelekwa zile pesa ni Morogoro, Mbeya, Iringa, Liwale, Lindi haipo, Mtwara haipo na pesa zimetoka. Ni jambo la kushangaza sana! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu Mheshimiwa Masala amesema asubuhi hii, kuna barabara ya Masasi – Nachingwea – Nanganga, ile barabara upembuzi yakinifu umeisha mwaka 2015 lakini mpaka leo pesa zinatafutwa. Ipo miradi kwenye nchi hii imefanyiwa upembuzi yakinifu mwaka 2017/2018 na sasa wakandarasi wako kazini. Suala hili nimewahi kuliuliza, hivi kuna tatizo gani? Kuna barabara nyingine utasikia zimejengwa na fedha za nje, kwa nini hizi bararaba zetu za Liwale, Lindi, Mtwara hazijawahi kupata wakandarasi wa nje? Suala hili ni zito sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuongezea hilo hilo sisi Mwenyezi Mungu alitujalia tukapata gesi asili Mtwara, nafikiri uletaji wa gesi ile Dar es Salaam palitokea vita sana ya maneno na migomo mbalimbali. Leo hii mkoa ambao una tatizo la umeme; kwa siku unakatika zaidi ya mara kumi au mara tano au mara sita ni Mkoa wa Lindi na Mtwara. Kulikoni Mkoa wa Lindi na Mtwara? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ushahidi zaidi, hata Kamati zako za Bunge zinazotembelea kukagua miradi iliyopewa fedha za Serikali, uendaji wa Mkoa wa Lindi na Mtwara ni mdogo sana na wakienda, basi walikuwa wamekusudia kwenda Songea, wakapitia Mtwara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru sana Kamati ya Ulinzi na Usalama imeweza kwenda Mtwara na Lindi, ni kwa sababu tu ya matokeo yale ya Rufiji, inasemekana wale watu wamejificha Lindi na Mtwara, walikwenda kufanya tathimini hiyo kuona kuna nini, lakini siyo kufuata miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sikatai kwamba hakuna miradi ya maendeleo inayokwenda, inakwenda lakini ni miradi midogo sana. Hakuna miradi mikubwa inayovutia Kamati yako ya Bunge kwenda kukagua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali ya Awamu ya Tano tusifanye hivyo. Sisi sote tunachangia kwenye pato la Taifa hili na tuna haki ya kufaidi matunda ya Taifa hili.

Vilevile nakuja kwenye upande wa elimu; upande wa elimu kwa kweli tunacheza, hatujaamua kuwekeza kwenye elimu. Kwa sababu kwa mujibu wa takwimu iliyotoka Hakielimu, wanasema walimu wanaokwenda madarasani kufundisha kwa ari ni asilimia 37. Ina maana wengine wote wanaokwenda ni kwa sababu wameajiriwa, ilimradi tu wanakwenda. Tatizo ni nini? Maslahi yao hayajatekelezwa. Walimu wanafanya migomo ya kimoyomoyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii katika kuboresha, tumeamua kuongeza tatizo lingine. Tumechukua walimu wa sekondari wakafundishe shule za msingi. Matatizo ya huko ni makubwa mno kuliko tunavyofikiria. Zoezi lile zimeendeshwa tofauti na Serikali mlivyopanga. Zoezi lile limeendeshwa kwa ubaguzi mkubwa na kwa uonevu mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana nilikuwa naongea na Afisa Utumishi wa Wilaya yangu, namuuliza mbona kuna malalamiko makubwa sana kwenye hili zoezi? Akanambia hata mimi taarifa hiyo nilikuwa sina, Afisa Elimu amefanya jukumu hili bila kunijulisha. Kweli haya malalamiko ya Watumishi wa Idara ya Elimu hata kwangu yapo. Wameachwa walimu wenye Diploma wanaendelea kwenye shule ya sekondari, wamechukuliwa watu wa Degree wamepelekwa shule za msingi. Kilichofanyika ni watu kukomoana. Wametumia hii loophole kama Mwalimu Mkuu (Head Master) akiona kwamba ana matatizo na mwalimu fulani, anamhamisha anampeleka shule ya msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kule badala ya kuwa shule ya msingi ama kuinua elimu, tumekwenda kufanya kama kule ni jela. Jambo hili haliwezi kukubalika. Ombi langu, Serikali hebu mrudie hili zoezi mwone ni namna gani limetekelezwa kama nia yenu ilikuwa ni nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu vilevile nataka nizungumzie taasisi hii inayoitwa TARURA. Taasisi hii ya TARURA imeundwa kwa nia nzuri kama mnavyodai, lakini taasisi hii mpaka leo hii haieleweki mhimili wake ni upi? Sisi Wabunge hatuna nafasi ya kuihoji TARURA. Halmashauri, Madiwani wetu hawana nafasi ya kuihoji TARURA. Juzi nimeuliza swali hapa Mheshimiwa Waziri anasema, TARURA watapeleka ripoti yao kwenye DCC. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge, hebu tujiulize, ni wangapi tunahudhuria hizo DCC? DCC kwa mwaka zinakaa mara ngapi? Pamoja na kwamba kwa mujibu wa sheria wanatakiwa wakae mara tatu, lakini sina hakika kama kuna Wilaya yoyote ile inayoweza kutimiza hiyo azima ya mara tatu kwa mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba hawa watu wako huru, wanajifanyia mambo wavyotaka. Kuna u-specialist gani wa Meneja wa TARURA wa Wilaya ambaye anamzidi Mhandisi wa Maji, Afisa Elimu na Afisa Maliasili au Afisa Ustawi wa Jamii? Maana hawa wote tunakuwa nao kwenye Baraza la Madiwani. Kwa nini huyu Meneja wa TARURA asiingie kwenye Baraza la Madiwani, ukizingatia hizo barabara anazozihudumia ziko chini ya Halmashauri. Vipaumbele vya barabara gani ijengwe kabla ya ipi, sisi Halmashauri ndio tunajua. Sasa nataka kufahamu, Serikali ije na majibu, kwa nini kuna u-specialist wa TARURA isiende kwenye Halmashauri zetu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nije kwenye uwekezaji; mnaongelea mambo ya uwekezaji, lakini uwekezaji huo una matatizo makubwa sana hata kwa wawekezaji wadogo. Hizi mamlaka za usimamizi zimekuwa ni nyingi sana na tumekuwa tukilia hapa mara kwa mara kwamba kama inawezekana, hizi taasisi nyingine ziunganishwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitaka kujua tatizo la uwekezaji nchi hii hasa kwa wawekezaji wadogo, hebu fungua kiwanda kidogo tu cha kusindika tu sembe, atakuja NEMC, atakuja TFDA, atakuja TBS watakuja sijui TRA, watakuja sijui watu wa OSHA, ni vurugu mtindo mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu sasa ili uweze kuwa mwaminifu ukatekeleza hayo yote, basi kama siyo miezi miwili au mitatu itakuchukua kupitia kwenye hizi taasisi. Kwa sababu ingewezekana hizi taasisi zote zingekaa pamoja au kwenye ile fomu moja ambayo utajaza hawa watu ukawakuta kwenye sehemu moja wakakujazia hizo fomu wakaku-verify ukafanya hiyo kazi, lakini hapana. Leo utakwenda taasisi ya…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili nichangie kwenye hoja iliyo mbele yetu. Naomba nianze mchango wangu kwa maneno mawili: Nangurukuru na Liwale, nitatoa ufafanuzi baadaye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mchango wangu kwa leo kabla ya kusema chochote, kwanza nawashukuru Mawaziri wote wanaohudumu kwenye Wizara hii kwa utendaji wao. Nasikitika tu kwamba wataangushwa na Mheshimiwa Mpango kwa sababu ili waonekane kwamba kweli wanaweza Mheshimiwa Mpango lazima awape pesa. Naomba vilevile kuwashukuru siyo tu Mawaziri na watendaji wote wanaohudumu kwenye Wizara hii na taasisi mbalimbali kwa kazi zao nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze mchango wangu kwa kujielekeza kwanza kwenye mawasiliano. Sekta hii ya mawasiliano kama sitakuwa nimesahau tunao mfuko unaoitwa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, ambao una pesa zake ambazo zimeandaliwa kisheria. Napata mashaka ninaposikia kwamba mfuko huu unashindwa kutekeleza baadhi ya miradi kwa kukosa fedha wakati hawa fedha zao zipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Mpango awape fedha hawa USCAF ili waweze kufanya kazi. Watu wa USCAF wanafanya kazi nzuri sana kwa sababu kwanza kazi zao wanajikita zaidi vijijini ambako kunasemekana huko hakufikiki kibiashara. Sasa kama Serikali ya Awamu ya Tano inasema kwamba ni Serikali ya wananchi wa hali ya chini, basi ni vizuri sana kwenye sekta ya mawasiliano ikawapa fedha mfuko wa USCAF ili waweze kutimiza majukumu yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano katika Halmashauri yangu ya Wilaya ya Liwale haifikiki kwa barabara, redio au mitandao ya simu. Hivi navyoongea kwenye halmashauri ile kuna Kata za Mpigamiti, Ngongowele, Milui, Lilombe, Mkutano, Mtungunyu, Ndapata na Kimambi ili uweze kupata mawasiliano na ndugu zako ni lazima upande juu ya miti au juu ya vichuguu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili linatupa shida sana hata wafanyakazi kama Walimu na watumishi mbalimbali wanashindwa kukaa kwenye maeneo haya kwa sababu ya kukosa mawasiliano. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali iwapatie fedha hawa jamaa wa USCAF waweze kutuhudumia ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niingie kwenye mtandao wa barabara ya Nangurukuru – Liwale. Nashukuru Mheshimiwa Waziri kwa mwaka huu nimeona kwenye vitabu barabara ya Nachingwea - Liwale iko kwenye upembuzi yakinifu na detailed design, nashukuru kwa hilo. Nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri barabara ya Nangurukuru - Liwale kwa maana ya Liwale na Mkoa wa Lindi kwa ujumla wake ni barabara ya kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyoongea pamoja na kwamba zao la korosho limefanya vizuri sana kwenye soko la kimataifa lakini sisi Liwale tunakwama sana, korosho zetu zinakaa ghalani muda mrefu, tunashindwa kufanya minada kwa wakati kwa sababu korosho zetu zinashindwa kutoka Liwale kufika Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri hii barabara siyo tu kwamba ina umuhimu vilevile imeongelewa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi na ni barabara ambayo inarudiwa mara kwa mara. Naomba Mheshimiwa Waziri aitazame barabara hii ya Nangurukuru - Liwale kwa jicho la huruma sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nataka niongelee barabara inayotoka Masasi - Nachingwea – Nanganga. Barabara hii tayari upembuzi yakinifu umekamilika miaka miwili, mitatu ya nyuma iliyopita. Barabara za Masasi - Nachingwea; Nachingwea – Rungwa; Ruangwa – Nanganga; Nanganga - Nachingwea msipoziwekea lami itakuwa ni miujiza kupata lami katika barabara ya Nachingwea - Liwale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nasisitiza Mheshimiwa Waziri waijenge hii barabara ya Masasi - Nachingwea – Nanganga; Ruangwa - Nachingwea ili nami niweze kupata hii barabara ya Liwale - Nanchingwea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nijielekeze kwa upande wa madaraja. Mheshimiwa Waziri atakapokuja mara ya pili ku-wind up ajaribu kuniambia. Kuna miradi mingine utakuta daraja linapangwa moja moja lakini madaraja mengine yamewekwa kwenye makundi. Kwa mfano, sisi kwenye halmashauri yetu kuna daraja linalotuunganisha Nachingewa na Liwale la Mbwemkulu, ni daraja refu na kubwa sana na ndiyo kikwazo kikubwa cha kupeleka korosho Nachingwea mpaka Mtwara na sijaliona kwenye vitabu hapa likikumbukwa. Sijui Mheshimiwa Waziri wana mpango gani na hili daraja la Mbwemkulu linalounganisha Nachingwea na Liwale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nataka nijielekeze kwenye hizi taasisi zilizoko chini ya Wizara hii, kwa mfano TTCL. Tumeamua tuwekeze kwamba TTCL ifanye biashara lakini ina madai makubwa sana kutoka kwenye taasisi zingine za Serikali. Naomba TTCL walipwe pesa zao ili tuweze kuwapima utendaji wao baada ya kupata mtaji. Leo hii hatuwezi kuwapima TTCL utendaji wao wakati hatujawapa pesa, wanadai pesa zao nyingi taasisi nyingine za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nataka niungane na Mtemi Chenge, anasema ni utaratibu mzuri kuamua kujenga reli ya standard gauge lakini ni lazima tutafute fedha au wahisani ili watusaidie speed iongezeke na vilevile Serikali iweze kupumua ili sehemu nyingine napo wapate pesa. Maana leo hii kila tukiamka reli, ndege, as if hatuna shughuli zingine za kufanya kama Serikali. Naomba Serikali mkope pesa kwa mkopo nafuu au kutafuta wahisani ili reli hii tuijenge kwa speed inayotakiwa na Serikali iweze kupumua na kutekeleza miradi mingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee Kampuni ya Meli ya Maziwa Makuu. Kama kweli tumeamua kuifufua kampuni hii ni lazima tukubali tuchukue madeni yake Serikali wawalipe wafanyakazi ili tuwape mitaji hawa watu ndiyo tuweze kuwapima. Nashukuru taasisi nyingi kwenye Wizara hii zimepata viongozi wazuri sana ,tena wazalendo na wenye moyo lakini kama hatutawapa pesa za kutosha, hatutaweza kuwahukumu baada ya miaka miwili, mitatu ijayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze kwenye upande wa bandari. Kuna miradi mingi sana ya bandari imetajwa hapa, lakini nataka niwaambie kwamba sisi zamani Mkoa wa Lindi tulikuwa na Bandari ya Lindi, tulikuwa na meli ya MV Lindi. MV Lindi na Bandari ya Lindi imekufa na kwenye vitabu vya Mheshimiwa Waziri haipo. Naomba sana Bandari ya Lindi nayo waikumbuke kama ni kuifanyia ukarabati au kuijenga upya lakini sisi kama Lindi tunahitaji bandari…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi nichangie hoja iliyo mbele yetu. Kama ilivyo ada watu wamezoea kuwasifia na kuwapongeza Mawaziri mimi leo naomba nisiwapongeze na sababu ya kutowapongeza wanaijua. Siyo kwamba nawachukia ila sababu za kuacha kuwapongeza Mawaziri na watendaji wote wanazijua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na sera ya kumtua mama ndoo kichwani, hivi takwimu tunazopewa huwa zinalenga nini? Kwa sababu takwimu hizi haziendani na uhalisia na ninyi Wabunge humu ndani ni mashahidi siku yoyote pakitokea swali la maji Bunge zima linalipuka kuonesha kwamba hali ya maji nchini ni mbaya. Hata hivyo, ukisoma vitabu, mimi hapa nimesoma nimeambiwa kwenye upande wa vijiji watu milioni 36 wanaopata maji ni milioni 30.9 asilimia 85; lakini bado Waziri akaendelea kusema lakini upatikaji wa maji katika vijiji ni asilimia 58, sababu aliyoitoa ni usimamizi mbovu wa miradi ya maji. Kama kweli tuna sera ya kumtua ndoo kichwani ifikapo mwaka 2020 na huku kutokupeleka fedha kwenye miradi ya maji mbona hizi takwimu zinakwenda tofauti tofauti? Unawezaje kutekeleza hii sera wakati huo huo Serikali haipeleki fedha kwenye miradi ya maendeleo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nashindwa kuelewa hizi takwimu na hizi sera mnataka kumfurahisha nani kwa sababu hazina uhalisia. Kama kwenye miradi ya maji hampeleki fedha halafu mnasema ifikapo mwaka 2020 mnamtua mama ndoo kichwani. Mimi sielewi labda Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha anifafanulie zaidi sera hii maana yake ni nini lakini kama kwa namna hii ya upelekaji wa fedha kwenye Halmashauri zetu au kwenye miradi mbalimbali wa asilimia 22 halafu mnasema ifikapo 2020 mnamtua mama ndoo kichwani mimi siwezi kuelewa na wala sikubaliani na hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba nijielekeze kwenye miradi ya umwagiliaji. Nataka niseme Mheshimiwa Waziri kwenye hii miradi ya umwagiliaji tumefeli. Hakuna Mbunge hapa atasimama atasifia kwamba kweli halmashauri zake kuna miradi ya umwagiliaji imefanya vizuri sana, hakuna. Kwanza mimi naomba niwashauri hebu ondoeni kwanza utata nani msimamizi wa hii miradi ya umwagiliaji. Haiwezekani mradi wa umwagilaji uko Liwale kilometa 400 kutoka Mtwara halafu wasimamizi wa mradi eti wa Kanda watoke Mtwara waisimamie miradi Liwale halafu iende sawasawa, haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu mradi tangu unaanza inatakiwa yule mtaalam awe pale, at least kila baada ya siku mbili au tatu hata kama wiki atoke Mtwara aende Liwale akakague mradi, atakwenda kule mwezi mmoja umepita, wakandarasi wamefanya wanavyotaka halafu miradi inafeli na pesa zinapotea, mnasema kwamba mvua ilikuwa nyingi miradi imeharibika, si sawasawa. Hebu hii miradi mhakikishe inasimamiwa na Halmashauri, kama yule Mhandisi wa Maji yupo Wilayani tumpe huu mradi asimamie, tuone hii miradi ya umwagiliaji itafeli kama ilivyofeli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila nikisimama hapa naongelea Mradi wa Ngongowele. Mradi huu umeshaondoka na shilingi milioni 770 lakini umekufa. Nimeshaomba mara nyingi hapa ule mradi kama itawezekana, nasikia mwaka huu JICA wamekubali kuufadhili basi mtupe sisi halmashauri tuusimamie kwa sababu hawa watu wa Kanda wako mbali sana hata wawe na weledi wa namna gani, kwa shida ya usafiri tuliyonayo na barabara mabovu hizi, atoke Mtwara kila wiki aende Liwale kusimamia mradi wa umwagiliaji si sawasawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nijielekeze kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri amesema kuna mipango ya ushirikishwaji wa ulinzi wa rasilimali maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti,nimeona maelezo tu ni namna gani ushirikishwaji huu upo haieleweki. Mpaka sasa hivi hatujaambiwa wameunda vikosi kazi kwenye vijiji gani, kwenye mabwawa au mito. Huu ushirikishwaji mnaosema hapa kwamba mna mpango wa ushirikishwaji wa ulinzi wa rasilimali maji, kwenye vitabu nimeuona, lakini kwenye uhalisia hatujauona kwamba ni mikakati gani imechukuliwa na Serikali katika kulinda hii miradi ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona tu kweye karatasi imeandikwa lakini sijasikia kumeundwa task force ya namna gani, kijiji gani au halmashauri gani katika kutimiza hili lengo la ushirikishwaji. Kwa sababu haiwezekani Wizara ninyi mnaweza kulinda rasilimali maji bila kuwashirikisha wananchi, ni lazima muwashirikishe wananchi ili miradi hii iweze kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukipitia hii miradi ya maji hata ukiangalia ile miradi ya maji vijijini, fedha nyingi ni za wafadhili, fedha ya Serikali hapa hatuioni hata kama ipo ni kidogo sana na ndiyo hiyo ambayo haiji. Mheshimiwa Waziri nimeshamfuata mara nyingi ananiambia kinachotakiwa pale ni Mhandisi kuleta certificate ya miradi wao watalipa. Nataka niseme kwamba kwenye Halmashauri yangu certificate zipo nyingi kwenye Wizara yako lakini sijapata fedha. Hata bajeti ya mwaka jana nilivitaja vijiji ambavyo havina maji mpaka leo, vya Nangano, Kipelele, Kikuyungu, Naujombo, Kiangara, Mikunya, Kipule, Makata, Mkutano, Mlembwe na miradi ya maji ipo. Sasa sijaelewa hizo certificate ambazo Wizara inadai ni za namna gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nataka niongelee vile vijiji ambavyo tayari vina maji. Vile vijiji ambavyo tayari vina mashine za maji tuna tatizo kubwa sana na mashine hizi zinazoendeshwa na dizeli. Mashine zinazoendeshwa na dizeli kwenye vijiji vyetu tunashindwa kumudu gharama ya maji kwa sababu unakuta ndoo inauzwa kuanzia shilingi 100 mpaka shilingi 200. Kwa mtu wa kijijini yuko tayari aende kilomita tano afuate maji kuliko kutoa shilingi 200 kununua ndoo ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano halisi ni katika Kijiji cha Mpigamiti ambacho kina mradi wa maji sasa hivi una takribani zaidi ya miaka tano lakini pale kijijini wanakosa fedha za kuendesha mradi ule. Kwa sababu mwisho wa siku wanakosa fedha za kununua dizeli kwa hiyo watu hawapati maji. Ushauri wangu ingewezekana kabisa miradi hii wakaanza kuipeleka kwenye solar, miradi ambayo inaendeshwa kwa mitambo ya solar inafanya vizuri sana.

Namshauri Mheshimiwa Waziri hii miradi ya vijiji iliyobaki badala ya kuielekeza kwenye mafuta tuielekeze itumie solar, hapo ndiyo itaweza kufanya vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii sera ya kumtua mama ndoo kichwani naomba niirudie, hebu mtuletee time frame, mtuletee takwimu, mpaka leo hii mmeshafikia asilimia ngapi ya utekelezaji ili tuweze kuona kwamba je, itakapofika mwaka 2020 kweli mtafikia lengo? Hapa mnaleta tu takwimu za ujanja ujanja, hatuletewi ni asilimia ngapi kwamba mpaka sasa hivi mmefika asilimia ngapi, hatujui.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitaka kujua nchi hii tuna tatizo kubwa la maji, leo hii nchi hii kuzindua kisima cha maji anaenda Rais. Hiki kitabu unakiona yaani Makamu wa Rais anamtwisha mama ndoo, anazindua kisima cha maji, hizi kazi wanafanya hata Madiwani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nikichimba kisima pale kijijini kwetu Diwani anaenda kukizindua, lakini leo tunamtuma Rais akazindue kisima cha maji, muone jinsi gani tulivyo mbali. Tuko mbali na uhalisia ndiyo maana inakuwa hivyo yaani inaonekana ni jambo la ajabu mama kutua maji mpaka Rais, Waziri Mkuu, Waziri wanaenda, hizi ni kazi za Madiwani. Tatizo la maji ni kubwa kuliko hivyo mnavyofikiria.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante kwa kupata hizi dakika tano kuchangia Wizara hii ya viwanda. Kwa sababu mimi Liwale hakufikiki kwa barabara, hakufikiki kwa mawasiliano, hakuna umeme wa uhakika sitaongelea kuhusu viwanda ila nitajadili kitaifa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejadili sana namna ya kulinda viwanda vyetu kwa kulingana na ushindani usio sahihi. Lakini hatujajadili namna ya kulinda wafanyakazi wazawa. Tatizo la wazawa viwandani ni kubwa kuliko tunavyolifikiria, na mimi hapa ni-declare interest mimi hapa nimefanya kazi kwenye viwanda vya watu binafsi kwa miaka 25, kabla sijawa Mbunge. Kwa hiyo, ninachoongea hapa ninamaanisha. Nimefanya kazi kwenye viwanda kwa taaluma mimi ni msindikaji wa nafaka. Kwa hiyo, viwanda vyote vya nafaka hapa nchini nimefanya kazi, kwa hiyo ninachokisema namaanisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye nchi za wenzetu mwekezaji anapokuja kutoka nje anapewa limit ya wafanyakazi ambao anaweza kuwaajiri, lakini hapa kwetu ni utitiri. Mheshimiwa Waziri hata wafagizi kwenye viwanda vyetu hivi ni ma-expert. Hata madereva kutoa bidhaa kupeleka kwenye maduka ya jumla nima-expert, hata wasimamizi wa kupakia mizigo kwenye viwanda vyetu ni ma-expert. Kazi ambayo Watanzania wanaweza kufanya kwenye hivi viwanda ni ulinzi na ukuli peke yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili kama Taifa hatutaweza kuliangalia kwa upana wake tutaendelea kusema tunazalisha ajira, lakini ajira zenyewe ni ajira ambazo hazina mashiko. Tunasomesha wahasibu, storekeepers, tunasomesha Maafisa Utumishi lakini hawa wote hawawezi kupata kazi kwenye hizi sekta binafsi.

Pili, nataka niongelee suala la mazingira wezeshi ya uwekezaji. Mazingira ya uwekezaji Tanzania bado hayajawa sawa sawa na mfano mzuri nataka niwaambie kuna mfanyabiashara moja anaitwa Bakharesa alikuwa anataka kujenga grain terminal kwenye Bandari ya Dar es Salaam. Ili mchukua miezi sita kupata kibali, lakini tayari wakati anapata kibali alishakwenda Msumbiji na akapata na kwa nini alitaka kujenga Grain Terminal Dar es Salaam kwa sababu yeye ana viwanda karibu Afrika Mashariki nzima na Afrika ya Kati. Kwa hiyo akitaka kuitumia bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya kuagiza ngano zote kwa ajili ya viwanda vyake vilivyopo Barani Afrika. Lakini kwa sababu ya uzembe na urasimu sasa hivi Grain Terminal iko Msumbiji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, muone namna gani mazingira ya kweli yasivyokuwa rafiki kwa wawekezaji. Lakini sio hivyo tu katika nafasi hiyo hiyo wawekezaji labda hawa wa viwanda vikubwa tutawakosa nchi hii kwa sababu ya sera zetu. Leo hii mwekezaji aliyekuwa kwenye utawala wa Awamu ya Tatu ndio huyo huyo alikuwa fisadi kwenye Awamu ya Nne; mwekezaji aliyekuwa rafiki kwenye Awamu Nne ndio huyo huyo alikuwa fisadi kwenye Awamu ya Tano. Kwa maana hiyo Tanzania hatuaminiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba Chama cha Mapinduzi kinatawala tangu uhuru mpaka leo lakini kila tunavyobadilisha uongozi kwa maana ya Rais basi nchi hii inabadilika kama vile chama kilichotawala pale ni chama kingine. Kwa utaratibu huu hatutawezi kwenda kwa sababu hatuna mwelekeo. Hatuna goal moja ambayo kwamba kila atakaye kuja ataendeleza pale ambapo mwenzake ameacha. Kila Rais anayekuja anataka aanze moja. Hii ni sababu hakuna mwekezaji atakayekuja kuwekeza kiwanda cha miaka kumi. Maana yake tunahitaji viwanda, labda hizo cherehani kwamba kila baada ya miaka kumi Rais akibadilika mtu anafunga vyerehani vyake anaenda sehemu nyingine. Lakini kama tunakusudia kupata wawekezaji wakubwa lazima tujenge uaminifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile naomba niendelee kwenye page 185 ya kitabu cha Mheshimiwa Waziri. Mimi takwimu hizi kidogo zinanichanganya. Yaani wakati sekta ya viwanda mchango wake unaporomoka ndio sekta ya viwanda inakua, yaani sijui sijaelewa kuna majedwali pale yaani pato la Taifa mchango wa viwanda unapungua viwanda vyenyewe ndio vinapanda. Viwanda vikipanda mchango wa Taifa unashuka. Mheshimiwa Waziri mimi utakapokuja hebu uje kunieleza vizuri haya mambo yanakuwaje?

Mheshimiwa Mwenyekkiti, lakini jambo lingine lazima tukubali kwamba wawekezaji nchi hii wanaondoka kwa sababu ya sera zetu mbovu, kama hamkubali lakini lazima tukubali kwamba wafanyabiashara wakubwa wanahama nchi hii kwa sababu ya mazingira si sawasawa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, kwa mara nyingine tena leo nianze mchango kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa kazi nzuri ya kusimamia Wizara hii. Niwapongeze pia watendaji wote ktika Wizara hii na niwatie moyo kwani changamoto ni sehemu ya kazi yao.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Lindi ndio mkoa uliopokea wafugaji waliohamishwa toka Ihefu, walipokelewa katika Wilaya za Liwale na Kilwa. Lakini hapakuwa na maandalizi yoyote ya kupokea mifungo. Mfano katika Wilaya ya Liwale vijiji vilivyopangiwa kupokea mifugo ni vijiji vya Kimambi, Ndapata na Lilombe. Lakini sasa mifugo imesambaa kila kijiji, mbaya zaidi vijiji hivyo havijafanyiwa upimaji wa matumizi bora ya ardhi, hivyo kusababisha migogoro mingi ya ardhi inayosababishwa na kutokuwa na mipaka halisi inayoeleweka kisheria.

Jambo lingine hapakuwa na ushirikishwaji wa kutosha kwa jamii hasa katika nyanja za elimu juu ya namna ya kukaa na wafugaji, ukizingatia kwa asili watu wa Kusini si wafugaji. Palihitajika maandalizi mahususi namna ya kupokea mifugo. Hadi leo sisi wakazi wa Kusini hatuoni faida ya kuwa na mifugo kwani hatuna minada, majosho wala malambo.

Hivyo basi naiomba sana Serikali kuleta wataalam wa ufugaji ili kuelimisha wananchi juu ya faida za mifugo, lakini kama haitoshi tunaomba tupatiwe wataalam wa minada ili kufungua minada ambayo itaweza kukuza kipato cha wafugaji na hata Halmashauri yetu ya Liwale.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Kilimo
MHE. ZUBER M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nichangie na mimi mada iliyopo mbele yetu jioni hii ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nataka niende moja kwa moja kwenye uchangiaji na mchango wangu niuelekeze kwenye vyama vya ushirika. Ushauri wangu kwenye vyama vya ushirika kuna mambo ya kufanya, aidha, turekebishe Sheria ya Vyama vya Ushirika kwa sababu sheria hii bado ina mgongano mkubwa sana. Mimi mwenyewe nimeshuhudia mwaka huu, kwanza nilikwenda na Mkuu wangu wa Wilaya kukagua ghala tukafungiwa mlangoni tukaambiwa hakuna ruksa, sheria hairuhusu hata kuukaribia mlango wa ghala pale ambapo vyama vya ushirika vinafanya biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, si hivyo tu, kuna mgogoro mkubwa sana kwenye vyama vya ushirika kwa sababu mpaka sasa hivi vyama vya ushirika vimepoteza fedha za wakulima wa korosho takribani zaidi ya shilingi milioni 150. Nilipokwenda kumfuata Afisa Ushirika wa Wilaya majibu anayoniambia anasema yeye hana mamlaka kwa mujibu wa sheria ya kukagua vyama vya msingi, wenye mamlaka hayo ni Tume ya Ushirika. Tume ya Ushirika wako mbali sana na hivi vyama vya msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba Mheshimiwa Waziri ajaribu kauangalia Sheria hizi za Vyama vya Ushirika. Haiwezekani Mkuu wa Wilaya, Mbunge, Mkuu wa Mkoa hawaruhusiwi kukagua ama hata kuingia tu kwenye ghala eti Sheria ya Vyama vya Ushirika inakataza na hili ndilo linalotuletea matatizo makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mwingine, mwaka huu kwenye Vyama vya RUNALI na Lindi Mwambao mpaka leo hii hatujui hatma ya sulphur iko wapi. Ukijaribu kuuliza unaambiwa kuna mgongano kati ya Bodi ya Korosho pamoja na vyama vya ushirika. Vyama vikuu vya ushirika bado wanavutana ni nani mwenye haki ya kuagiza sulphur, jambo hili limetuletea matatizo makubwa sana. Wenzetu Mtwara chama chao cha ushirika walishaagiza sulphur na sasa hivi inafanya kazi lakini sisi bado tunababaishwa tu kwamba kulikuwa na mvutano kati ya Bodi ya Korosho pamoja na Vyama Vikuu vya Ushirika kati ya Lindi Mwambao na RUNALI, nani aagize sulphur. Jambo hili Mheshimiwa Waziri naomba mlifanyie kazi ili sheria hii iletwe kama ni kufanyiwa amendment basi ifanyiwe amendment, ionekane mipaka kwamba Mkuu wa Wilaya mpaka wake ni wapi, Mbunge mpaka wake ni wapi na hiki chama cha ushirika kina kazi gani na Bodi ya Mazao mipaka yake iko namna gani, jambo hili limetuletea shida sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine niongelee Maafisa Ugani. Kwa kweli ndani ya Wizara hii Maafisa Ugani wanaonekana kama vile hawana kazi za msingi, wakati huo sisi tunasema kwamba asilimia 80 au 70 ya wananchi wa nchi hii ni wakulima lakini Maafisa Ugani wameonekana kama hawana kazi wamepelekwa tu kule. Kwa mfano, kunapotokea shida ya Maafisa Watendaji wa Vijiji au Kata watu wa kwanza wanaoangaliwa ni Maafisa Ugani. Zamani tulikuwa tunachukua hata Walimu Wakuu lakini sasa hivi kwa sababu imeonekana walimu wakuu ni muhimu sana tukaamua kuwaaacha sasa tumechukua Maafisa Ugani ndiyo tumewafanya Watendaji wa Kata na Vijiji. Tena basi wanafanya kazi ambazo si zao na kwa hiyo ufanisi kwenye utendaji wa vijiji haupo kwa sababu hawajasomea na huku kazi ambayo wamesomea wameiacha haina ufanisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye halmashauri zetu huyakuti mashamba ya mfano kwa sababu Maafisa Ugani wana kazi nyingi, wanakuambia ni muda gani niandae shamba wakati huo huo natakiwa nifanye kazi za utendaji? Kwa nini tumewapeleka huko? Tumewapeleka huko kwa sababu tunawaona hawana kazi, jambo hili linatuharibia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile hata wale wachache waliopo hawana vitendea kazi. Namwomba Mheshimiwa Waziri kama kweli tunataka kusimamia kilimo kitupatie tija basi jambo hili la Maafisa Ugani ni muhimu sana, watengenezewe mazingira na wakafanye kazi ambazo wamesomea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine mimi naona sasa hivi Serikali imeamua kuvuruga kilimo. Zamani mimi wakati nasoma kuna swali unaulizwa pale la jiografia, unatajiwa zao unaambiwa taja mkoa unaolima. Zao la pareto, unataja mkoa unaolima, ukiulizwa chai unaambiwa Rungwe, ukitaja mahindi unaambiwa Iringa lakini leo tumeanza sasa vurugu. Mnataka korosho, pamba na pareto zilimwe nchi nzima, yaani hiyo mnayoanzisha ni vurugu nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, navyofahamu Maafisa Ugani wanagawiwa kulingana na taaluma zao. Kuna mtu aliyesomea mambo ya pamba atapelekwa Mwanza na Shinyanga, watu wengine wamesomea alizeti watapelekwa Singida lakini leo hii mnaanza vurugu mnasema korosho na pamba italimwa nchi nzima hii tunaenda kuvuruga, haiwezekani lazima tuwe na mgawanyo wa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana siku zote tunasema hii Serikali muwe na vipaumbele. Maana ya vipaumbele ndiyo hiyo. Sasa haijulikani ninyi korosho, pareto au chai mnalima wapi ni vurugu tu, haiwezekani. Pamoja na kwamba korosho ni fursa lakini alizeti, pamba na kahawa nazo ni fursa lazima mjipange tugawanye tujue. Mimi wakati nasoma jiografia ilikuwa inanieleza hivyo, nikiulizwa tu chai najua Rungwe, mahindi najua Iringa lakini hii vuruga mnayotuletea mimi sikubaliani nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba nijielekeze kwenye upatikanaji wa mbegu. Upatikanaji wa mbegu hasa za mahindi, maana kule kwetu kijijini kwetu kwenye Kata ya Mpigamiti kule sisi ndiyo tunaolisha…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Nishati
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi nichangie jioni hii ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitoe shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Waziri anayehudumu kwenye Wizara hii, kwa kuiweka Mikoa ya Lindi na Mtwara kwenye Gridi ya Taifa. Tunashukuru sana kwa jambo hili kwa sababu mara nyingi sisi watu wa Kusini tulikuwa tunalalamika mara nyingi mnatusahau sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile na suala la kupeleka meli ya mafuta katika Bandari ya Mtwara na Lindi, tunashukuru mmefanya jambo zuri sana. Hata hivyo, mradi huu nina wasiwasi nao kwa sababu Mikoa mingi ambayo imepitiwa na hii Gridi ya Taifa nimeona nguzo kubwa za chuma ipo lakini kuanzia Mbagala mpaka Mtwara sijaona nguzo ya chuma. Isije tukapigwa changa la macho kwa hizi nguzo za magogo, kama ndiyo hivyo basi tutashukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nataka niongelee REA. REA awamu ya I na II haijafanya vizuri katika nchi hii, kwa sababu sehemu nyingi za taasisi za umma umeme huu haukuzingatiwa lakini kwenye hii awamu ya III naona imezingatiwa. Je, zile sehemu ambazo zilipitiwa na awamu ya I na II kuna utaratibu gani sasa wa kufikisha umeme kwenye hizi taasisi za umma? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu ya III ya REA nayo ina ukakasi wake. Mkoa mzima wa Lindi tumepata mkandarasi mmoja. Mpaka leo mkandarasi wa REA Mkoa wa Lindi bado yuko Ruangwa hajui Liwale ataenda lini, hajui Nachingwea ataenda lini na awamu ya III sehemu ya kwanza mnasema inakamilika mwezi Juni mwakani, lakini hatuelewi awamu hii ya kwanza huyu mkandarasi atafikia wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile walituambia kwamba maeneo ambayo yako mbali na vyanzo vya umeme yatapatiwa na umeme jua. Katika Halmashauri yangu ya Wilaya ya Liwale kuna vijiji ambavyo viko umbali mfupi, kutoka Halmashauri ya Wilaya ni kama kilomita 70 au kilomita 50 kutoka kwenye vyanzo vya umeme,Vijiji kama vya Ndapata, Mpigamiti, Kimambi, Mdunyungu, Milui, Kikuyungu, Lilombe, Mlombwe, Ngongowele, Kipelele, Naujombo, najua kwamba hakuna uwezekano wa kujenga nguzo za umeme kutoka Liwale mjini mpaka kufikia vijiji hivi, naomba nipate ufafanuzi umeme jua katika vijiji hivi utakuja lini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachogomba hapa mambo ya Stiegler’s Gorge hii ni kwa sababu ya falsafa moja kwamba ukiwa muongo lazima usiwe msahaulifu. Serikali hii mlishatuaminisha kwamba gesi ya Mtwara ndiyo muarobaini wa umeme nchi hii, matokeo yake haikuwa hivyo, ndiyo maana watu wanavyoingia kwenye Stigler’s Gorge pamoja na madhara yote haya ambayo tunaenda kuyapata, je, haitakuwa sawa na yale yaliyokuwa kwenye gesi? Maana tuliambiwa kwamba gesi itashusha bei ya umeme, bei ya umeme bado iko juu. Tuliambiwa gesi itakuwa mwarubani wa umeme nchi hii na kuuza nchi za nje, lakini mpaka leo pesa nyingi zimepotea, hatujui hatima ya mradi ule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana sasa tunapoingia kwenye Stiegler’s Gorge ambako tunajua madhara ni makubwa, kwa madhara haya kama kweli hili jambo lililokusudiwa litakwenda kufanyika tunaweza tukavumili haya madhara, lakini kwa kuona matatizo yale yaliyojitokeza kwenye mradi wa gesi ndiyo maana leo hii wananchi wengi na Wabunge wengi wanalilalamikia suala hili. Wanakuwa waoga kwa sababu tusije tukatumbukia kwenye tope kama tulivyotumbukia kwenye gesi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee suala la gharama za umeme nchini. Suala hili Mheshimiwa Waziri inabidi alitupie macho sana kwa sababu linatugharimu kwa kiwango kikubwa sana. Ndiyo maana hata viwanda vyetu vinazalisha bidhaa ambazo zinashindwa kuingia kwenye soko la Kimataifa kwa sababu gharama ya uzalishaji nchini ni kubwa. Leo hii mtu aki-import sukari kutoka nje ya nchi inauzwa rahisi kuliko ya ndani ya nchi. Kwa hiyo, suala la gharama ya umeme linatakiwa liangaliwe kwa makini sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, leo tena naomba kuanza mchango wangu kwenye Wizara hii kwa kuwapongeza Waziri na Naibu Waziri kwa kazi kubwa ya kusimamia Wizara hii nyeti. Hata hivyo naomba kuishauri Serikali katika mambo yafuatayo:-

Kwanza, kwa kuwa tunayo mazao ambayo kitaifa yanaonekana kuwa ni mazao ya kimkakati, ni ushauri wangu kuwa mkakati wa mazao hayo ni lazima uunganishwe na mikakati mingine. Kama vile mikakati ya utafiti ili kuboresha tija ya mazao hayo, uwepo wa miundombinu rafiki ya usafiri ili kuwezesha wakulima wa mazao hayo kuyafikia masoko kwa urahisi.

Mheshimiwa Spika, aidha, kuwepo na mkakati maalum wa kudumu wa kutafuta masoko kwa mazao hayo ya kimkakati utakaowahakikishia wakulima uwepo wa masoko kwa mazao yao. Kwa hali ilivyo sasa masoko ya mazao hayo ya kimkakati sio ya kuridhisha hasa kwa upande wa bei ya mazao hayo.

Pili, kwa zao la korosho ambalo ndio mgongo wa maendeleo kwa Mikoa ya Kusini na Taifa kwa ujumla. Ili kuendeleza zao hilo naiomba sana Serikali kuimarisha kituo chetu cha utafiti pale Naliendele kwa kukipatia chuo hiki fedha za kutosha ili kukiwezesha kuendelea na tafiti mbalimbali.

Jambo la pili naishauri Serikali kuona umuhimu wa kurejesha zile fedha za export levy, fedha ambazo zilikuwa mahususi kwa kuendeleza zao hili la korosho, kwani uzoefu unaonesha kuwa tangu Serikali Kuu kuchukua fedha hizo, uzalishaji wa zao hilo umeshuka sana, hii ni kutokana na wakulima wengi kushindwa kumudu gharama kubwa ya pembejeo.

Nikiendelea kuishauri Serikali katika kuimarisha kilimo chenye tija, liko suala la uhaba wa watumishi wa ugani kwenye Halmashauri zetu, na wale wachache waliopo hawafanyi shughuli za ugani na badala yake wamekuwa wanakaimu kama watendaji wa kata na vijiji na hivyo kusahau kazi zao walioajiriwa nayo. Kutokana na uhaba wa watendaji wa kata na vijiji sehemu nyingi huwatumia wataalamu hawa kama watendaji wa kata na vijiji.

Mwisho niombe Serikali kuifanyia mapitio Sheria ya Ushirika, sheria hii kwa sasa ina mapungufu sana, mfano iko taasisi ya COASCO; taasisi hii badala kuwa mkombozi wa vyama vya ushirika imekuwa adui wa ushirika. Hivyo niombe sana Serikali kuifanyia marekebisho sheria hii ambayo imepitwa na wakati.

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa naiomba sana Serikali kuhakikisha bei za mbegu, pembejeo hasa zinazozalishwa nchini zikawa na bei rafiki kwa wakulima. Kwani hadi sasa wakulima wengi bado wanatumia mbegu zao za asili ambazo tija yake kwa mkulima ni ndogo sana na Serikali bado haijawekeza vya kutosha ili kuhakikisha mbegu zinapatikana kwa bei nafuu.
Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Uamuzi wake wa Kuendeleza Mji wa Dodoma na Kuupa Hadhi ya Jiji
MHE. ZUBEIR M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami nichangie hoja hii iliyoko mbele yetu. Awali ya yote niseme kwamba siungi mkono hoja hii kwa sababu zifuatazo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza sijaelewa kipi kitatangulia? Hivi ni vigezo vinatangulia kuwa Jiji au Jiji ndiyo linatangulia halafu vigezo vifuate? Kwa sababu ukiangalia azimio hili, aya ya pili ya Mheshimiwa mtoa hoja anasema, anaiomba Serikali itenge fedha kwa ajili ya miundombinu ya kuboresha Dodoma. Sasa sijaelewa kwamba ina maana yeye anakubali kwamba bado hatujafikia vigezo vya Dodoma kuwa Jiji. Kwa hiyo, anaiomba Serikali sasa itenge fedha ili Dodoma iwe Jiji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeunga mkono hili azimio kama Mheshimiwa Rais angetamka kwamba nataka kufikia mwaka 2020 – 2025 Dodoma iwe Jiji. Ndiyo maana nasema sasa Serikali ijipange kwamba Dodoma iwe Jiji. Kwa nini nasema hivyo? Kwa sababu ninavyofahamu, Dodoma kuwa Jiji tayari ni mradi. Tayari inatakiwa bajeti itengwe kwa ajili ya Dodoma kuwa jiji. Hii ndiyo sababu leo hii hata kuhamia Dodoma. Tulihamia hivi hivi, kuhamia Dodoma ni mradi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge lako lilitenga bajeti ya kuhamia Dodoma? Leo hii Bunge limetenga bajeti kwa ajili ya Dodoma kuwa Jiji? Sasa mambo yote haya, hakuna mtu anayepinga Dodoma kuwa Jiji, lakini Mheshimiwa Rais angetamka kwamba nataka kufikia mwaka 2020 au 2022 nataka Dodoma iwe Jiji halafu miundombinu ifuate, kama ambavyo mtangulizi wangu alivyosema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Dodoma hatuna stand, leo hii uwanja wa ndege uko mjini pale, wala haufai. Tunahamishia wapi? Tunahamishia Msalato; stand ya bodaboda na kadhalika tunahamishia Nanenane. Maana yake ni kwamba tunataka tutengeneze miundombinu ili Dodoma iwe Jiji...

T A A R I F A . . .

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na taarifa yake siipokei. Nilichokiongea ni kwamba vigezo vitangulie kabla ya kutangazwa kuwa Jiji. Dar es Salaam anayoisema ni kwamba ilitangulia vigezo vya kuwa Jiji. Ile inayoendelea sasa hivi pale ni nyongeza tu. Hatuna maana kwamba Dodoma itakapojengwa kuwa Jiji, hiyo miundombinu ikikamilika haitaendelea tena kujengwa. Maana yake ni kwamba miundombinu itakuwa inaboreshwa kila wakati. Ninachokisema na ndiyo maana CDA ilivunjwa, kwa sababu haikutimiza malengo yaliyokuwa yamekusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Awamu ya Kwanza tangu mwaka 1973 alitangaza kwamba Makao Makuu ya nchi hii iwe Dodoma, lakini akaunda na mamlaka ile ya CDA. Kwa sababu CDA hawakufikia vigezo na ndiyo maana Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano akaja akaivunja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napenda niseme kwamba Bunge lako tukufu ili liweze kuunga mkono hoja hii, basi kauli hiyo ibadilishwe kwamba Mheshimiwa Rais ametamka kwamba kufikia mwaka fulani, Dodoma inatakiwa iwe Jiji. Leo hii Dodoma bado haijakidhi vigezo kuitwa jiji. Kama tukiamua kuweka jiji kisiasa, twende tuliweke jiji kisiasa, lakini vigezo bado havijakamilika.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Viwanda Na Bishara
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vyetu vinashindwa kwenda kwa faida kwa kuwa na mamlaka nyingi za usimamizi zinazofanya kazi zinazofanana kama vile OSHA, TBS, TFDA NEMC na zingine mfano wa hizi. Kwa nini mamlaka hizi zisiunganishwe zikafanya kazi chini ya taasisi moja?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji Serikali yote iongee kwa pamoja kwani ni Serikali ni moja, mfano kuna mazao ya kimkakati, je, vipo viwanda vya kimkakati vinavyokwenda sambamba na mazao hayo ya kimkakati?

Je, Wizara ya Miundombinu inayo miundombinu inayolingana na viwanda, au mazao hayo ya kimkakati, miundombinu ya barabara, bandari na uchukuzi kwa ujumla wake? Je, ni rafiki sawa na mikakati ya Wizara ya Viwanda? Je, Wizara ya Mazingira nayo inaitambua mikakati ya Wizara ya Viwanda na Biashara, kwani kwa uzoefu unaonesha Wizara ya Mazingira inaongoza kukwamisha uwekezaji nchini kwa hoja ya uharibifu wa mazingira.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, naomba pia kuchangia kuhusiana na gesi ya Mtwara, Baada kuanza kwa mradi wa kuchimba gesi Mkoani Mtwara ni matumaini ya watu wa mikoa ya Mtwara na Lindi wawe wa kwanza kunufaika na mradi huu, lakini sasa ni kinyume chake. Mfano, mradi wa gesi majumbani unaanza kutekelezwa Mkoani Dar es Salaam na Pwani na kuiacha mikoa ya kusini Lindi na Mtwara inakotoka gesi. Jambo hili siyo jema hata kidogo.

Mheshimiwa Spika, Kata ambazo hazina umeme kabisa katika Wilaya ya Liwale ni pamoja na Kata za Mpigamiti, Mlembwe, Lilombe, Ngongowele, Mkutano, Kimambi, Mbaya, Barikiwa, Miriwi na Nahoro. Ningetamani kwa awamu hii Kata ya Mpigamiti ingekuwa ya kwanza, Kata anakotoka Mbunge kuko kiza, ni aibu isiyovumilika.

Mheshimiwa Spika, naanza mchango kwa kuwapongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri kwa kazi kubwa ya kusimamia majukumu ya Wizara hii hasa kwenye Mradi wa REA. Hata hivyo, hakuna mafanikio pasipo na changamoto. Ziko changamo kadhaa katika utekelezaji wa mradi huu wa REA.

Mheshimiwa Spika, mfano katika Jimbo langu la Liwale bado umeme huo haujafika katika vijiji vingi. Wilaya ya Liwale yenye Kata 20 na Vijiji 76 kuna Vijiji 34 tu vilivyofikiwa. Tatizo kubwa ni Wakandarasi, wamekuwa wakitoa visingizio vya kushindwa kufikisha vifaa kutokana na ubovu wa barabara. Jambo ambalo halina ukweli, kwani ziko taasisi nyingi zinafanya kila siku na kupeleka bidhaa mbalimbali. Hapa naomba Mheshimiwa Waziri atembelee Liwale kuona uhalisia wa miradi ya REA katika Jimbo langu, bado mahitaji ni makubwa sana.

Mheshimiwa Spika, umbali wa kutoka Nachingwea hadi Liwale ni zaidi ya kilometa 230. Hivyo basi, line ya umeme imekuwa na changamoto nyingi sana kama vile nguzo kuanguka na kuungua moto. Pia kutokana na umbali uliopo, unahitaji pia substation kwa ajili ya kuongeza nguvu ya umeme. Kwani umeme unaofika Liwale tayari unaonekana kuwa na nguvu ndogo.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na mimi kunipa nafasi nitoe mchango wangu kwenye hii bajeti iliyoko mbele yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niombe tu kusema kwamba hii bajeti tatizo kubwa haiakisi maisha ya wananchi wetu wa kawaida na ndiyo maana kuna baadhi ya watu wengine wanasema hii bajeti ni bajeti hewa, kwa sababu ukiangalia kwenye vipaumbele vilivyoandikwa hapa haijaakisi kabisa maisha ya wananchi wetu wa chini. Kwa mfano, kwenye miradi hii ya kipaumbele, ukiiangalia hata kwenye bajeti wamesema kwamba hailetewi fedha za kutosha, hakuna fedha ambazo zimeenda huko fedha za kutosha. Kwa mfano, wamesema kwamba miradi ya kipaumbele kama vile Rufiji. Rufiji mwaka jana ilitengewa shilingi bilioni 220 hivi lakini wakaipeleka shilingi bilioni tatu, sasa unashindwa kuoanisha tatizo liko wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo kubwa ambalo naliona bajeti hii inaanza kuharibika tangu kwenye mipango. Mipango tunayopanga na tunapokwenda kutekeleza tunatengeneza vitu tofauti. Niwatolee mfano, kwenye mipango utakuta kuna miradi ya LNG, Mkuza, kuna huo mradi wa Rufiji, kuna Special Economic Zone, kuna makaa ya mawe, kuna General Tyre, mambo ya barabara na kufungamanisha kwamba uchumi na maisha ya wananchi. Lakini tunapokwenda kutekeleza, tunatekeleza vitu vingine ambavyo havimo kwenye mpango.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano kwenye bajeti iliyopita hapa nimesikia kuna majengo ya Chuo Kikuu ambayo hayakuwemo kwenye mpango, lakini yamejengwa, kuna ujenzi ule wa Magomeni Quarter umeanza kujengwa lakini kwenye mpango haukuwemo, kwenye ukuta pamoja na kwamba ni jambo zuri kwenye huo ukuta wa Tanzanite, haukuwemo kwenye mpango lakini umejengwa. Kwa hiyo, utakuta kuna miradi ambayo inakamilika ujenzi wake, haimo kwenye mpango, lakini ile miradi ambayo imo kwenye mpango hailetewi fedha. Kwa hiyo, kufeli kwa bajeti hii kunaanzia tangu kwenye mipango yetu kwa sababu tunachokipanga sicho tunachokitekeleza. Tunapanga kama Taasisi, kama mpango, Wachumi wanakaa wanapanga lakini inapokuja kwenye utekelezaji mtu anatoa matamko mengine yanafanyika mambo mengine, matokeo yake zile fedha ambazo zilitakiwa ziende huku, zinaenda huku. Kwa hiyo kwa msingi huu, nasema kabisa kwamba bajeti hii haiwezei kukidhi matakwa ya wananchi wetu.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi tunaingia kwenye nchi ya viwanda na uchumi wa kati, hivi kweli kama tunakisahau kilimo, hatutaki kuwekeza kwenye kilimo tuna dhamira kweli ya kwenda kwenye viwanda? Haiwezekani kwenye bajeti ukapanga asilimia 0.4 ziende kwenye kilimo, kilimo ambacho kinaajiri zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania halafu mkasema kweli tuna nia thabiti, mimi siwezi kuunga mkono jambo hili. Kwa mfano, unaona kwamba mifugo imepangiwa 0.1, uvuvi ndiyo kabisa, mmeua mmepangia 0.06 maana yake tuendelee kula wale samaki wa China ambao wanakuja miaka mitatu iliyopita. Sasa tunaposema kwamba hii haiakisi maisha ya wananchi tunamaanisha hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano mimi natoka Liwale, wananchi wangu kule ni wakulima siyo wafugaji, wale ni wakulima lakini sasa naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri, wakulima wale mimi nikawaambie nini kwenye bajeti hii? Sisi zao letu la uchumi kule ni zao la korosho, mmeshalihujumu, zile export levy zimeshapotea, mpaka leo hii hatujui mbolea, pembejeo tunapataje! Hivi mimi watakaponiuliza kwamba bwana eeh! umekaa Dodoma miezi mitatu unachangia bajeti, hivi kama wananchi wa Liwale tumeletewa nini wakulima? Sasa hivi hawana uhakika wa ufuta, yaani bei za ufuta hazijulikani, masoko hayajulikani.

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi hapa mmetangaza kwamba zao la ufuta litanunuliwa kwa stakabadhi ghalani, mmewapa Bodi ya Maghala ndiyo washughulikie hilo, lakini mpaka leo hawajaandaa chochote na ufuta sasa hivi ndiyo uko sokoni, kwa hiyo, mipango hii tuanyopanga haiakisi maisha ya wananchi wetu. Tunaposema hii bajeti siyo rafiki kwa watu wetu tunamaanisha hiyo kwa sababu wengine mipango hii hatunufaiki nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano nakuja kwenye hoja ya kufungamanisha, mnasema kwamba mnaenda kuandaa akaunti moja (collection account) kwamba mapato yote ya nchi hii yakusanywe kwenye akaunti moja halafu Serikali au Hazina ndiyo wagawe. Jambo hili siyo sahihi sana pamoja na kwamba nia yenu ilikuwa ni nzuri. Kwa mwenendo wa upelekaji wa fedha za mafungu haya kwenye Halmashauri zetu au kwenye Taasisi husika na hii sasa mnakwenda kuua. Mmeshaiua Halmashauri, tumejua vyanzo vyote vya Halmashauri mmevichukua mkavipeleka Hazina na hamrudishi, sasa hivi mnaenda kuua mifuko, hii mifuko ambayo ilitengewa fedha maalum.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo sababu juzi nilikuwa nachangia, Waziri wa Fedha nilikuwa nachangia kwamba Serikali hii ya Awamu ya Tano hatuoni fedha zile ambazo zilikuwa za mafungu maalum zamani kiingereza wanaita, kuna fedha ambazo zilikuwa ring fenced, sasa hivi kwenye Awamu ya Tano hizo fedha hazipo tena na sasa hivi ndiyo maana mnaleta hii sera kwamba mnataka kuweka akaunti moja ili muendelee kuua hiyo mifuko na mnapoua hiyo mifuko maana yake, kwanza mlitakiwa mjiulize kwa nini hii mifuko iliundwa, je, yale mahitaji ya hii mifuko imeondoka? Na kama mahitaji ya hiyo mifuko bado ipo kwa nini sasa mnaiondoa? Kuiondoa hii mifuko maana yake sasa mnakwenda kuua malengo yaliyopangwa kwenye hiyo mifuko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa kodi ndiyo maana bajeti zetu zinashindwa kutekelezeka, kwa mfano kwenye miradi ya maendeleo hatujawahi kufika asilimia 50 ya utekelezaji wa bajeti yetu. Pamoja na kwamba mmeongeza, walipa kodi wameongezeka mkumbuke kwamba walipakodi wameongezeka lakini kiwango cha kodi kinachokusanywa kinazidi kupungua. Kwa mfano, kwenye page ya tano ya kitabu cha Mwenyekiti amesema; tatizo la kupungua kwa shughuli za uwekezaji nchini ndiyo sababu inayosababisha uchumi wetu kudorora wameeleza
kabisa kwamba shughuli za uwekezaji zimepungua. Sababu nyingine wamesema mitaji inahamishwa na hapa tulishawahi kuwaambia kwamba wafanyabiashara kwa mazingira haya mliyowawekea sasa hivi wafanyabiashara wanahamisha mitaji. Wafanyabiashara wanahama, tukiwaambia mnakataa, matokeo yake ndiyo haya kwamba watu mitaji wanahamisha na mazingira ya uwekezaji bado siyo mazuri, kodi zimekuwa nyingi hazielewekina usumbufu vilevile. Kwa hiyo, haya mambo yote haya tunashindwa kuelewa, mipango yetu hii inatupeleka wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano kama mnazo hizo mnazoita Economic Zones, pesa hampeleki! Halafu Economic Zone zingine ambazo tayari watu wamelipwa ili kuacha uwekezaji pale uendelee halafu uwekezaji hakuna, maana yake pale kwanza wamepoteza fedha za kulipa watu fidia halafu hatuna mipango. Hatuna mpango ambao tunaweza kwenda kuutekeleza.

Sasa hii mimi nashindwa kuelewa, hasa mmeshindwaje ninyi kama Serikali kufungamanisha kilimo na viwanda? Msitegemee hizi nyanya ambazo mnazikuta hapo Morogoro, hizi nyanya watu wachache wanaweka pale barabarani ndizo ambazo mnataka kuvijengea viwanda. Hebu fungueni milango watu wawekeze kwenye kilimo, watu wakija kuwekeza kwenye kilimo ndipo mtaweza sasa kuendeleza hivyo viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nitolee mfano mmoja, jana Spika alisema hapa anashangaa kwa nini bajeti ya Kenya iko juu kuliko ya kwetu, sababu wenzetu wa Kenya wamejiwekeza kwenye kilimo, sisi tumekataa kuwekeza kwenye kilimo. Asilimia 60 ya nafaka inayosindikwa Kenya ni ya kwao wenyewe lakini sisi asilimia 98 ya nafaka inayosindikwa Tanzania ni kutoka nje. Mfano mzuri mimi nilikuwa msindikaji wa nafaka wa aina ya ngano, asilimia 90 ya ngano inayosindikwa Tanzania ni ya kutoka nje, kwa nini? Ardhi tunayo, tena ardhi nzuri lakini hakuna uwekezaji na wala hamfikirii kutafuta wawekezaji kwenye kilimo cha kisasa, kilimo cha kibiashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.(Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kunipa uzima na kuweza leo kuandika mchango wangu kwenye Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo ni sekta muhimu sana katika nchi yetu japo Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yake anasema kilimo kinaajiri asilimia 65.5 ya Watanzania wote. Jambo hili siyo kweli kwani Watanzania wengi wako vijijini na wanategemea kilimo kwa uchumi wao. Hivyo, kilimo huajiri zaidi ya asilimia 75 ya Watanzania, lakini kwa masikitiko makubwa ni kwamba sekta hii haijapewa umuhimu unaostahili, ndiyo maana Wizara hii imetengewa fedha kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa katika sekta ya kilimo ni uhaba wa masoko ya uhakika na bei ya mazao husika. Hamasa pekee ya kukuza kilimo ni bei nzuri ya mazao na soko la uhakika. Vilevile miundombinu ya barabara ni muhimu sana katika kukuza kilimo nchini, kwani kuna mazao kama vile viazi, nyanya na matunda yanashindwa kulifikia soko kwa kukosa barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la ufuta kwa sasa linalimwa katika maeneo mengi katika nchi yetu. Hivyo ni wakati sasa Bodi ya Mazao Mchanganyiko ikatazamwa upya na ikiwezekana zao la ufuta likaundiwa bodi yake ili kuwapatia tija wakulima kwani hadi sasa tatizo kubwa la
ufuta ni uhakika wa masoko hasa kwenye mikoa ya Kusini (Lindi na Mtwara).

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali ingetilia mkazo sana ili mazao haya yasindikwe nchini badala ya kuendelea kuuza mazao ghafi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mgao wa chakula cha njaa ni bora ukazingatia mahitaji na kufuata jiografia ya nchi yetu. Mfano, Mkoa wa Lindi tunakuwa na uhaba mkubwa wa chakula kati ya miezi ya Desemba hadi Aprili. Hivyo, kuwapelekea chakula mwezi Mei ni sawa, kwani kipindi hiki huwa ni cha mavuno kwa wakulima wengi na shida ya chakula huwa imeisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyo kwa mgao wa chakula cha msaada, mgao wa pembejeo za kilimo ni lazima uendane na mazingira halisi, kwani vipindi vya msimu wa mvua haulingani nchi nzima. Mfano, kwa Mkoa wa Lindi, mazao ya nafaka hupandwa mwezi Desemba hadi Januari na kwa zao la korosho uwekaji wa dawa huanza kati ya mwezi Mei hadi Julai. Hivyo, pembejeo ya zao la korosho zinatakiwa kuwafikia wakulima kati ya mwezi Machi na Aprili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta inayotegemewa zaidi katika usindikaji kwa mazao ya kilimo ni sekta binafsi, lakini Serikali haijaonesha dhamira thabiti ya utekelezaji wa jambo hili. Wawekezaji wengi wanashindwa kufanya hivyo, kwani gharama za uzalishaji hapa nchini ni kubwa sana na hii inatokana na wingi wa mamlaka zinazosimamia jambo hili. Kwa mfano, TFDA, TBS, OSHA, EWURA na kadhalika. Kodi ni nyingi sana hapa nchini, punguzeni kodi kuvutia wawekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nia njema ya kuwa na Vyama vya Ushirika nchini haijatusaidia sana, kwani elimu juu ya ushirika haijatosha, hivyo kupelekea Vyama vya Ushirika kuwa mzigo wa wakulima nchini. Vyama vingi vya ushirika badala ya kukuza masoko ili kusaidia wanachama wao, wenyewe ndiyo vimekuwa kikwazo kwa ustawi wa wakulima, ushindani wa kibiashara katika masoko ya wakulima hakuwapi tija viongozi wa ushirika, hivyo wao huwakumbatia wanunuzi wachache kwa manufaa yao binafsi na siyo ushirika kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ya Liwale tumepata mwekezaji wa zao la alizeti na yuko tayari kujenga kiwanda na uchujaji, lakini hadi leo mwekezaji huyu bado anazungushwa kupata ardhi. Japo Halmashauri ya Liwale ilishampatia ardhi ya kutosha, lakini Kamishna wa Ardhi bado anakuwa na kigugumizi katika jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Wana-Liwale tunaomba mwekezaji huyu apatiwe ardhi ili Liwale tuweze kukuza ajira na uchumi wa Halmashauri yetu.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba leo tena niendelee kuishauri Serikali kwa jambo lake zuri sana la kuweka tozo ya shilingi 100 kwenye mafuta, naomba Serikali iende mbali zaidi kwa kuiwekea wigo fedha hizi ili ziwe kwa ajili ya TARURA tu yaani ziwe ring fenced kama ilivyo kwa fedha za mafuta hata zile za miamala ya simu nazo zielekezwe moja kwa moja (RUASA) maji vijijini na zile za line za simu zielekezwe moja kwa moja maji mijini, kuliko ilivyo sasa fedha hizi zote ziko tu hewani hazijawa ring fenced, hivyo kufanya rahisi kutumika nje ya makusudio.
Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari za Mwaka 2016
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia Muswada huu kwa kuishauri Serikali yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza mwandishi wa habari kutoandika habari za kiuchunguzi au zile zilizoko mahakamani ni kuwanyima watu kupata habari za kina, kwani ni waaandishi wa habari ndio mara nyingi huibua uozo mwingi katika jamii na mara nyingi hata TAKUKURU hutumia taarifa hizi katika kufanya uchunguzi wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo napendekeza kifungu hiki kifanyiwe marekebisho kwani mara zote watendaji kwenye Taasisi za Umma utoaji wa habari ni wasiri sana, hawako wazi hata kwa habari za kawaida. Kuwepo kwa vyombo viwili katika sheria moja kutaleta mgongano wa kiutekelezaji kwani kazi za Bodi ya Wanahabari ingeweza kufanywa na Baraza la Wanahabari ambako ndiko kuna watu wenye taaluma ya habari, lakini si hivyo tu, kuwepo kwa wateule wa Waziri au Rais hakuwezi kukifanya chombo anachokiongoza kuwa huru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, adhabu kwa mwanahabari aliyekutwa na kosa, kunyang’anywa leseni ili asifanye tena kazi ya uandishi wa habari ni adhabu kubwa sana. Lengo la adhabu hii si kutoa funzo ama kumrekebisha mtenda kosa, adhabu hii inakusudiwa kuwatia woga wanataaluma hawa wasifanye kazi kwa uhuru, hivyo kushindwa kuibua maovu yatakayofanywa na watu wenye mamlaka makubwa Serikalini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vyema hayo mambo yanayotajwa kama ni mambo ya siri, uchochezi, uhuru binafsi, faragha yakawa wazi kwani watu wenye mamlaka wanaweza wakatumia mwanya huu kuwazuia waandishi kupata habari kwa kigezo kuwa ni siri na mambo mengine kama hayo. Vilevile kitendo cha masharti ya leseni kuachwa kwa mtu mmoja (Waziri) kunaweza kuwafanya watu wengi kukosa au kufutiwa leseni hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uingizaji wa machapisho nchini. Mamlaka aliyopewa Waziri katika kifungu hiki yasipofanyiwa marekebisho Waziri anaweza akayatumia vibaya. Hivyo mamlaka hayo yakabidhiwe kwenye Bodi ya Huduma ya Habari/Baraza la Habari kuepuka Waziri kuzuia machapisho kwa maslahi binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Makosa Mbalimbali; mtu aliyefanya kosa kwa makusudi kumpa adhabu sawa (moja) na mtu aliyefanya kosa kwa uzembe si sawa kwani huyu wa pili hakukusudia kufanya kosa, hivyo adhabu ni bora zikatofautiana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake aliyoiwasilisha kwa umahiri mkubwa. Nataka nianze mchango wangu kwa kuiasa Serikali kuwa japo upatikanaji wa mapato siyo mzuri sana, lakini hata hicho kidogo kinachopatikana basi kuwe na mgawanyo wa haki, kwani Watanzania wote ni walipakodi wa nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikipitia bajeti zote za Awamu ya Tano. Mgawanyo wa fedha za maendeleo kwa mikoa ya Kusini, Lindi na Mtwara ni kidogo sana. Mikoa hii haina miradi mikubwa ya maendeleo. Jambo hili limekuwa ndiyo chanzo cha kudidimia uchumi wa mikoa hii, hata pale mikoa hii inapokuwa na miradi, basi miradi hiyo haipewi fedha kwa wakati. Mfano, mradi wa barabara ya Masasi – Nachingwea - Nanganga ambayo upembuzi wake ulikamilika tangu mwaka 2015, lakini hadi leo mradi huu haujapatiwa fedha, wakati miradi mingine mipya imekuwa ikipata fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kusisitiza hoja yangu ya mgawo wa fedha za maendeleo kwa Mikoa ya Kusini kwamba siyo wa kuridhisha, hata Kamati zako za Bunge zimekuwa hazifanyi ziara katika mikoa hiyo kwa kuwa haina miradi ya kwenda kukagua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la Serikali kuhamia Dodoma ni kwa kuwa Dodoma ni katikati ya nchi yetu. Hivyo kuweka Makao Makuu hapa ni kuwezesha taasisi na wananchi kufika Makao Makuu ya nchi kiurahisi. Lengo hili halitakuwa na maana kwa wakazi wa Mikoa ya Lindi na Mtwara iwapo barabara ya kuunganisha Mkoa wa Lindi hadi Morogoro haitajengwa, kwani barabara hii ni muhimu sana kwa Mikoa ya Lindi na Mtwara ili kufika Dodoma kirahisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa haipeleki fedha za miradi kwenye Halmashauri zetu kwa masharti kwamba miradi hiyo ni lazima ianze kutekelezwa na Halmashauri husika. Utaratibu huu unaendelea kuziacha nyuma zile Halmashauri zenye mapato madogo ambazo hazina uwezo wa kuanzisha miradi mikubwa kama ujenzi wa Hospitali za Wilaya, majengo ya Mahakama za Wilaya na majengo ya Vituo vya Polisi vya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo naishauri Serikali kuangalia upya utaratibu usio wa haki. Mfano katika Jimbo langu la Liwale, hatuna majengo hayo yote niliyotaja hapo juu na Halmashauri haina uwezo wa kujenga majengo hayo. Kama ni lazima miradi hiyo ianzie ngazi ya Halmashauri, basi Wilaya ya Liwale haitakaa ipate majengo ya Hospitali, Mahakama na Kituo cha Polisi cha Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende kwenye majibu ya Waheshimiwa Mawaziri Bungeni. Kumekuwa na tabia ya baadhi ya Mawaziri kutoa majibu mepesi kwa Waheshimiwa Wabunge bila kuzingatia hali halisi ya mazingira ya swali. Jambo hili linafanya majibu haya baada ya muda yanaonesha Waziri alilidanganya Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano wa majibu haya ni jibu la swali langu kuhusu ujenzi wa jengo la Mahakama ya Wilaya ya Liwale. Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana alinijibu, ujenzi huo utakamilika ifikapo mwaka 2018. Cha kushangaza, hata kwenye Randama ya Bajeti ya mwaka 2018/2019 mradi huu haumo. Je kujibu vile Mheshimiwa Waziri alikusudia nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nizungumzie habari ya Utalii. Kumekuwepo na mradi wa kukuza Utalii Kanda ya Kusini. Cha kushangaza, mradi huu Mikoa ya Lindi na Mtwara haimo. Jambo hili haliwezi kuvumilika kwa wakazi wa mikoa hiyo, kwani ukiizungumzia Kusini juu ya utalii, huwezi kuiacha Hifadhi ya Selous ambayo kwa kiasi kikubwa iko Lindi. Iweje fedha zenye jina la kuendeleza Kusini zipelekwe Mbeya, Iringa na Morogoro, ukaiacha Mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani? Hii siyo sawasawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kuendelea kuitenga Mikoa ya Kusini, hata pale Mungu anapoamua kuiinua mikoa hii. Mfano upatikanaji wa gesi ambako hadi leo hakujasaidia lolote kwani hadi leo Lindi na Mtwara ndiko kuna matatizo ya upatikanaji wa umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuwa na uandikishaji mzuri kwa wanafunzi wa darasa la kwanza, lakini kiwango hiki hakina uwiano mzuri na wahitimu wa darasa la saba. Jambo hili linaashiria kuporomoka kwa elimu yetu, sababu kubwa ni Serikali kutokuwekeza kwa upande wa Walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikama ya Walimu wa Shule za Msingi ni mbaya sana. Mfano katika Halmashauri yangu kuna Shule za Ndapata, Kikulyungu, Norongopa. Shule hizi zina Walimu watatu kila shule. Jambo hili lipo nchi nzima. Tatizo la Walimu ni kubwa sana. Siyo hivyo tu, hata hawa Walimu wachache tulionao hatuwawekei mazingira bora ya kazi zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafiti zinaonesha ni asilimia 39 tu ya Walimu wanaoingia madarasani na kufundisha kwa moyo au ari. Hivyo asilimia 61 wako kazini tu, kwani wamepoteza morali ya kazi, wana migomo ya kimoyomoyo. Kwa ujumla, Walimu wamekosa mtetezi. Watumishi wengi sasa Serikalini wamepoteza morali ya kazi na kubaki na manung’uniko moyoni mwao kwani mishahara yao ni midogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la TARURA, nashauri litolewe ufafanuzi, kwani haiko wazi kwamba fedha hizi za Serikali zinasimamiwa na Mamlaka gani? Kama ni Mhandisi wa Maji, Afisa Elimu, Afisa Kilimo, wote hawa wanawajibika kwa Madiwani. Kwa nini Meneja wa TARURA asije kwenye Baraza la Madiwani wakati barabara zinazojengwa wamiliki ni Madiwani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nachukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia uhai ili niweze kutoa mchango wangu kwenye Wizara hii.

Naomba nianze kuwapongeza Mawaziri wote wawili na watumishi wote wanaohudumu kwenye Wizara hii. Sina budi kushukuru kwa kile kidogo nilichojaliwa kupata kwenye jimbo langu la Liwakle kwa kunipatia watumishi wanne, Mungu awabariki sana.

Sasa naomba kuchangia/kugusia suala la wazee nchini. Imekuwa ni jambo la muda sasa tangu Serikali iahidi kuleta sheria ya wazee humu Bungeni. Kwani pamoja na matamko mengi juu ya wazee kama vile makazi bora kwa wazee, matibabu bure kwa wazee na kadharika.

Mheshimiwa Naibu Spika, mambo haya hayawezi kukamilika bila kwanza kuwatambua hao wazee ni akina nani kwa mujibu wa sheria. Hivyo ni bora sasa sheria hiyo ikaletwa ili tuweze kuwatambua hao wazee. Pamoja na juhudi kubwa inayofanywa na Serikali ya kuboresha miundombinu ya afya juhudi hizi zinaweza zisilete matunda tarajiwa kwa kuwepo na tatizo la uhaba wa watumishi kwenye Wizara halitatatuliwa. Kwa kuwa sehemu kubwa ya watumishi hawa wanashughulikia afya ya watu, hivyo weledi mkubwa unahitajika, hivyo watumishi wachache kuhudumia watu wengi kunawaondolea umakini na kukosa ufanisi, kwa mfano katika Hospitali ya Wilaya ya Liwale ina watumishi wachache sana hospitali ina wodi za grade II, kwa saa za usiku wodi hizi zote zina huduma na wauguzi wasaidizi, ni zahanati nne tu ndio zinahudumiwa na clinical officers wasaidizi. Jambo hili ni baya sana kwani ikitokea akiwa likizo zahanati husika hufungwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Liwale iko mbali sana na Hospitali ya Rufaa ya Sokoine, Lindi. Jambo hili limefanya umuhimu wa kuwa na gari kwani umbali uliopo ni zaidi ya kilometa 300. Hospitali pekee ya karibu ni ya Ndanda iliyoko Masasi, Mkoani Mtwara, kwa sababu hizo uhitaji wa vifaa bora na Madaktari Bingwa ni muhimu sana kwa hospitali ambayo haina usafiri na haina Madaktari Bingwa ni hatari ya wagonjwa kufia njiani ni kubwa sana wakati wakielekea Ndanda kwa kutumia magari ya abiria. Naomba jambo hili lingepewa msukumo wa kipekee.

Mheshimiwa Naibu Spika, maduka ya MSD yameongezeka kuwa msaada mkubwa sana katika idara hii ya afya, hivi imefikia wakati sasa maduka hayo sasa yangepatikana katika Mikoa a Wilaya zote nchini hasa kwenye zile Wilaya ambazo ziko mbali na Makao Makuu ya Mikoa ambako kuna maduka hayo, lakini vilevile pale ambapo maduka hayo yapo basi ni bora dawa zote muhimu zikapatikana ikiwa ni pamoja na vitendea kazi vingine yaani vifaatiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, Bima ya Afya imeonesha kuwa na manufaa makubwa kwa jamii. Changamoto pekee katika utekelezaji wa jambo hili ni elimu duni katika jamii juu ya uchangiaji na uandikishaji wake. Lakini jambo lingine ni tatizo kwenye Halmashauri zetu ni juu ya uchangiaji wa CHF, pamoja na jamii kuendelea kupewa elimu . Lakini mchango wa fedha za kutoka Serikali hazipatikani kwa maana ya tele kwa tele, jambo hili linalea mkanganyio mkubwa kwenye Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa zahanati na nyumba za watumishi sasa jambo hili linaachwa kwenye Halmashauri. Lakini mkumbuke kuwa Halmashauri hizo kwa sasa zina mzigo mkubwa sana. Mfano ujenzi wa maabara za shule za sekondari, nyumba za walimu, vyoo vya shule na walimu na majengo mengine. Hivyo ni bora Serikali ikaona upo umuhimu wa kuzisaidia Halmashauri kujenga zahanati kila kijiji na kituo cha afya kila kata kama Sera ya Taifa inayotaka ujenzi wa vituo vya afya na zahanati ukiachwa chini ya Halmashauri, kwenye Halmashauri zenye mapato kidogo jamii itaendelea kuteseka maana Serikali ya Awamu ya Tano mara zote wanasema hakuna miradi mipya itakayoanzisha mpaka Halmashauri husika yaani Serikali kazi yake ni ku-support tu nguvu za wananchi mahali ambapo wananchi hawana uwezo, patabaki kuwa nyuma kimaendeleo ya kiafya. Na sera ya kuwa na kituo cha afya kila kata haitafikiwa kwani Halmashauri zetu nyingi zina uwezo mdogo na zina mzigo mkubwa sana ikiwa ni pamoja na matamko ya mara kwa mara ya kutoka Serikali Kuu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze mchango wangu kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na leo niweze kuchangia hotuba hii. Mchango wangu kwa leo naomba nianze na sera ya kuunganisha mikoa kwa barabara za lami. Ni wakati muafaka sasa sera hii iwekewe lengo, kwa maana haijulikani ni kwa muda gani sera hii itakamilika kwani hadi leo utekelezaji wake haueleweki. Mikoa mingine tumeanza kuunganisha Wilaya wakati mikoa mingine bado. Mfano, Mkoa wa Lindi na Ruvuma na Lindi na Morogoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, mawasiliano kwa karne hii ni jambo muhimu sana, lakini kutokupewa fedha za maendeleo ni kurudisha nyuma sekta hii, kwani sehemu kubwa ya nchi yetu mawasiliano ya simu ni duni sana. Pamoja na kuwepo kwa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (USCAF), ni jambo la kusikitisha sana kuona fedha za mfuko huu nazo hazipatikani kwa wakati jambo linaloondoa dhana ya kuundwa kwa mfuko huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, USCAF wanashindwa kutekeleza miradi yao kwa kutopewa fedha zao toka Hazina. Mfano katika Jimbo la Liwale lenye kata 20 ni sehemu chache sana kuna mawasiliano ya simu kwenye baadhi ya kata. Hali ni mbaya sana katika Kata za Mpigamiti, Lilombe, Miru, Ndapata, Mlembwe, Mkutano na Ngongowele. Kata hizi hali ya mawasiliano ni mbaya sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Nangurukuru, Liwale ni barabara iliyotajwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015. Hata hivyo, barabara hii ni kiungo muhimu sana kwa uchumi wa Kanda ya Kusini kwa ujumla. Pamoja na barabara ya Nangurukuru - Liwale lipo pia daraja la Mbwemkuru linalounganisha Wilaya ya Nachingwea na Liwale. Vilevile nashukuru barabara ya Liwale - Nachingwea angalau imetengewa fedha kwa ajili ya upembuzi yakinifu. Ni ombi langu, fedha hizo zifike kwa wakati. Pia kuna daraja linaunganisha Kilwa - Liwale katika Kijiji cha Nanjilinji. Naomba ipewe kipaumbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, taasisi zote zilizo chini ya Wizara hii ni bora zikapewa fedha zake kwa wakati ili ziweze kufanya vizuri. Taasisi hizi ni kama USCAF, TTCL, Bandari, MSCL na TAZARA. Taasisi hizi zinakwama sana kwa sababu ya upungufu wa mitaji na fedha za kutekeleza miradi yake ya maendeleo mfano USCAF, wana sababu gani ya kushindwa kutekeleza miradi yao kwa ukosefu wa fedha wakati fedha toka kwenye vyanzo vyao zinapatikana? Vilevile Serikali ilipe malimbikizo ya mishahara ya wafanyakazi wa MSCL ili wafanyakazi wawe na moto wa kufufua shirika hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi ya viwanja vya mikoa ina makundi mawili; kuna vilivyotajwa kimoja kimoja na vingine vimewekwa kwa pamoja. Ninachotaka kujua, ni kwa nini iko hivi? Vile vilivyo pamoja tutajuaje vimejirudia pia kwenye madaraja ya mikoa na barabara za baadhi ya mikoa? Naomba kupata ufafanuzi juu ya jambo hili. Katika bajeti hii Mkoa wa Lindi miradi yake yote iko kwenye makundi hayo hapo juu, yaani yale ya jumla, fedha za Mkoa wa Lindi ni kidogo sana. Barabara ya Masasi – Nachingwea - Nanganga, upembuzi yakinifu umekamilika, lakini ni bajeti ya pili sasa barabara haitengewi fedha wakati huo huo ziko barabara zimekuja nyuma lakini zimepewa fedha za ujenzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naliomba Shirika la Reli kuwalipa askari polisi waliowatumia kusindikiza treni kati ya mwaka 2016/2017 ambao bado wanadai. Askari hawa walifanya kazi kwa uaminifu, lakini malipo yao yamekuwa kitendawili. Gharama za ujenzi wa barabara zimekuwa kubwa kwa sababu ya sheria zetu ambazo kwa kiwango kikubwa hazina faida yoyote. Mfano, Sheria ya Madini, Sheria ya Maji, Sheria ya Mazingira na kadhalika. Mkandarasi hulazimika kuweka gharama za ununuzi wa madini kwa maana ya kifusi na Halmashauri kudai ushuru wa kifusi hicho. Kama vile haitoshi, watu wa mazingira nao wanadai fidia ya uharibifu wa mazingira unaotokana na ujenzi huo kwa kuacha au kufukia mashimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali ingeondoa tozo hizi ili kupunguza gharama za ujenzi wa barabara hizo, kwani hayo maduhuli yote ni ya Serikali moja. Hivyo Serikali ifanye marekebisho ya sheria hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ujenzi wa reli ya kisasa, naungana na ushauri wa Kamati kuwa Serikali ingeangalia sasa kushirikisha watu binafsi au kuomba wahisani kwani kutegemea fedha za ndani pekee kutaifanya Serikali kushindwa kuhudumia sekta nyingine au Wizara nyingine. Hivyo ujenzi unaoendelea sasa kwenye sehemu zilizobaki, jambo hili lingefikiriwa kwa manufaa ya Taifa kwa jumla ikiwezekana hata kukopa mkopo wa masharti nafuu. Kwa sababu ya kiuchumi, kipande cha Isaka na kile cha Kigoma Serikali ingeanza na kuacha Kigoma badala ya Isaka kwani route ya Kigoma ina vivutio vingi vya kiuchumi kuliko Isaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, malipo kwa wakandarasi ni bora yakafanywa kwa wakati kwani kulipa madeni haya kwa riba ni kupoteza fedha za walipa kodi. Wakandarasi wa kigeni wanafaidika sana na riba kuliko hata faida wanayoipata kwenye mkataba husika. Hakuna sababu ya kuingia mkataba na mkandarasi wakati hakuna fedha za kutekeleza mkataba husika.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuanza mchango wangu kwenye Wizara hii kwa kuangalia Tume ya Umwagiliaji kwani ufanisi wa Tume hii ni wa kutiliwa mashaka. Miradi mingi ya umwagiliaji inayosimamiwa na Tume hii ukamilifu wake si wa kuridhisha na miradi mingi imehujumiwa sana kutokana na usanifu wa miradi hiyo kutokuwa wa kuridhisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mradi wa Ngongowele, Wilayani Liwale uliosanifiwa na Tume hiyo Kanda ya Kusini, mradi huu umehujumiwa sana hadi leo mradi huu umekwama sana. Hata hivyo, watu wa Japan wameonesha nia ya kuleta fedha ili kufufua mradi huu lakini tayari watu hao wa Kanda wameanza kutia mikono yao ili kuendelea kuhujumu mradi huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu maji mijini, pamoja na takwimu kuonesha hali ya upatikanaji wa maji mijini ni ya kuridhisha, je, Wizara ina uhakika maji haya yanawafikia wananchi kwani kiwango cha maji kinachopotea njiani ni kikubwa sana. Mfano katika Jiji la Dar es Salaam maji mengi hupotea barabarani kabla ya kuwafikia wananchi kutokana na ubovu wa miundombinu ya maji hasa kupasuka kwa mabomba kunakosababishwa na ukarabati wa barabara na ujenzi holela wa miundombinu ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kumtua mama ndoo, pamoja na nia nzuri ya sera hii lakini utekelezwaji wake si mzuri kwani miradi mingi inashindwa kukamilika kutokana na ukosefu wa fedha na utendaji usioridhisha kutokana na watendaji wengi kwenye Halmashauri zetu kushindwa kuelewa miongozo ya Wizara hii. Mfano pale Waziri anaposema wahandisi watangaze kazi kabla ya kupewa fedha jambo ambalo halitekelezeki na linawachanganya wahandisi wengi wa Wilaya juu ya utekelezaji wake. Ni bora Serikali ikawa wazi juu ya jambo hili kwani miradi mingi vijijini imekwama.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kushindwa kupeleka fedha za miradi ya maji ni kwenda kinyume na sera hii ya kumtua mama ndoo kichwani. Vilevile gharama za maji vijijini ni ghali pengine kuzidi hata gharama za maji mijini, jambo hili limefanya miradi mingi iliyokamilika kushindwa kujiendesha kwa kukosa fedha za kununua dizeli za kuendeshea mitambo ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Halmashauri ya Wilaya ya Liwale ilikuwa na miradi ya kutafuta chanzo cha maji kwa ajili ya Mji wa Liwale baada ya chanzo chake cha mwanzo cha Mto Liwale kushindwa kukidhi mahitaji. Sasa ni miaka minne mradi huu umesimama huku fedha za mradi huu zikiendelea kuliwa bila chanzo hicho kupatikana. Mji wa Liwale unakua kwa kasi na unakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji. Vilevile maji yanayopatikana hayana ubora kwani hayawekwi dawa kwa kuwa hawana dawa wala matanki ya kufanyiwa treatment ya maji, hivyo hulazimika kuyaleta kama yalivyotoka mtoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya takwimu tunazopewa na Mheshimiwa Waziri na uhalisia wake kwani hali ya upatikanaji wa maji nchini ni mbaya ukilinganisha na maelezo ya Mheshimiwa Waziri. Hakuna mji wala kijiji kilicho na utoshelevu wa maji. Hata pale yanapopatikana basi upatikanaji wake ni ghali sana hasa vijijini. Ushauri wangu, ni vyema sasa watendaji walete takwimu sahihi ili sisi Wabunge tuweze kushauri vizuri Serikali ili kutatua tatizo hili sugu la maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kuongeza fedha kwenye Mfuko wa Maji ni bora sasa likatekelezwa ili kuiongezea fedha Wizara hii. Ongezeko kutoka shilingi 50 kufikia shilingi 100 kwani tatizo kubwa la Wizara ni fedha kwa ajili ya miradi yake
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze mchango wangu kwenye hoja hii na mazingira ya uwekezaji. Mazingira ya uwekezaji nchini bado siyo mazuri sana hasa kwa wawekezaji wadogo wadogo

au wazawa. Mazingira haya yanafanya gharama za uzalishaji wa bidhaa nchini kuwa juu kiasi cha kufanya bidhaa zinazozalishwa nchini kushindwa kumudu ushindani wa bidhaa zinazozalishwa nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utitiri wa mamlaka za usimamizi ni kikwazo kingine kwa wawekezaji wazawa, mfano bidhaa moja husimamiwa na mamlaka zaidi ya tano kama vile kiwanda kidogo cha kusindika nafaka husimamiwa na TBS, TFDA, OSHA, NEMC na kadhalika. Taasisi hizi zote zinatoza ada au ushuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kukosekana kwa kiwango maalum cha bidhaa (standard) kunafanya wazalishaji kukosa ushindani ulio sawa kwenye soko. Bidhaa ya aina moja huzalishwa katika ubora au standard tofauti, mfano hapa nchini hatuna kiwango au standard ya bidhaa za nafaka kama sembe na unga wa ngano hivyo washindani hushindania rangi ya sembe bila kujali ubora wake ambao unapaswa upimwe kwa extraction rate toka kwenye maghali ghafiki. Taasisi kama TBS na TFDA wana standard ambayo ndiyo ingekuwa mwongozo kwa wasindikaji wote wa nafaka hivyo kulinda upotevu wa nafaka unaotokana na wasindikaji kukosa standard badala yake wanashindania weupe wa sembe, mchele au ngano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upatikanaji wa malighafi kwa viwanda vidogo ni tatizo lingine hasa kwa yale mazao yanayouzwa kwa njia ya mnada. Wawekezaji wadogo hushindwa kuingia mnadani kushindana na wafanyabiashara wakubwa, hivyo viwanda vidogo vidogo hukosa malighafi baada ya kushindwa kuingia mnadani. Mfano, vikundi vya ubanguaji wa korosho hukosa korosho baada ya akina mama hao kushindwa kuingia mnadani, hawaruhusiwi kununua korosho nje ya mnada.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo naishauri Serikali ione namna nzuri ya kuwawezesha wawekezaji hawa wadogo namna ya kupata malighafi ikiwezekana waruhusiwe kununua nje ya mnada.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwekezaji katika viwanda kwa kiasi kikubwa hutegemea mazao ya mashambani kilimo, wako wawekezaji wanaotaka kuwekeza kwenye kilimo kwanza ili kupata malighafi za viwandani na hatimaye waje kwenye viwanda vya kusindika mazao ya kilimo lakini upatikanaji wa ardhi ni mgumu sana, hasa kwenye vijiji ambavyo havijaingia kwenye mpango wa matumizi bora ya ardhi. Jambo hili limekuwa kikwazo kikubwa kwa wawekezaji wa upande wa kilimo hasa kwa mashamba makubwa, urasimu wa upatikanaji wa ardhi ni lazima ukaangaliwa upya ili uwekezaji katika kilimo uwe na tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwepo wa viwanda nchini kulitegemea kufungua ajira kwa wazawa, lakini kinyume chake ajira nyingi nchini huchukuliwa na wageni hasa kwenye viwanda vya watu binafsi. Wazawa wameendelea kuwa vibarua viwandani. Hakuna namba maalum ya ajira kwa wageni wakati katika nchi za wenzetu mwekezaji anaposaini mkataba wa uwekezaji hupewa idadi maalum ya wafanyakazi wa kigeni lakini hapa kwetu hakuna ufuatiliaji wa sheria hii. Mfano, Uganda mwekezaji wa kigeni huruhusiwa kuajiri wafanyakazi watano tu nje ya nchi yao ili kuwapa ajira wazawa na hao wachache waliopata ajira mishahara yao ni midogo sana na mazingira ya kazi (job security) ni ndogo sana, wazawa wananyanyaswa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sekta ambazo zimesahauliwa katika uwekezaji nchini ni sekta ya kilimo. Pamoja na kuwa na ardhi kubwa yenye rutuba kwa mazao mengi, lakini sekta hii haijatangazwa kama ilivyo sekta nyingine. Wawekezaji wa kilimo cha biashara hapa nchini kinafanywa kwa kiwango kidogo sana. Mfano, hapa nchini viwanda vyote vya ngano vinaagiza ngano kutoka nje kwa asilimia mia moja, hakuna mashamba ya ngano nchini tangu kufa kwa mashamba ya NAFCO.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuende na kauli mbiu ya nchi ya viwanda basi ni vema tukaamua kuwekeza kwenye kilimo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, napenda kuanza mchango wangu kwa sekta hii kuanza na sekta ya uvuvi. Sekta hii haijapewa msukumo wa kutosha kwani hadi leo bado Taifa linaagiza samaki kutoka nje. Pamoja na kuwa ubora wa samaki wa kutoka nje wanatiliwa mashaka, hadi leo hakuna uwekezaji wa kibiashara katika sekta ya uvuvi kwani hadi sasa hakuna meli kubwa ya uvuvi hasa kwenye bahari kuu wala hakuna kampuni yoyote ya sekta binafsi kuonesha uwezo wa kumudu kuingia kwenye sekta ya uvuvi wa kisasa.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwa na maji ya kutosha, ya bahari na maziwa makuu, bado tunaagiza samaki na mazao ya samaki toka nje ya nchi. Tumechoka na samaki wabovu kutoka China, samaki vibua.

Mheshimiwa Spika, ni ipi sera ya Serikali ya Awamu ya Tano juu ya Wizara hii? Kama hakuna fedha za maendeleo zinazopelekwa kwenye Wizara hii pamoja na kuonekana kukusanya vizuri maduhuli ya Serikali bado hata hizo fedha wanazokusanya wenyewe Wizara ya Fedha hawataki kurudisha fedha hizo kwenye Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Ni jambo lisiloeleweka kuona Taifa lenye rasilimali za bahari, maziwa na mifugo ya kutosha bado tunaagiza samaki, nyama na maziwa toka nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, uvuvi haramu unachangia kwa kiasi kikubwa na utendaji mbovu wa watendaji wa Wizara hii kwani si sawa sawa kunyang’anya nyavu baharini, ziwani badala ya kwenye vyanzo vya vifaa au zana hizo zinazoitwa haramu, je, wavuvi wanapata wapi zana hizo? Kwa nini Serikali inashindwa kusimamia uingizajiwa zana hizo haramu badala ya kuwapa hasara wavuvi kwa kuchomewa zana zao?

Mheshimiwa Spika, mifugo sasa nchini inaelekea kuwa balaa badala ya neema kwani hakuna utaratibu wa kueleweka juu ya namna bora ya ufugaji wala namna bora ya uvunaji wa mazao ya mifugo ikiwemo nyama, maziwa, ngozi na mayai. Wafugaji wetu bado ni wafugaji wa kienyeji wa kuhamahama bila kujali Taifa linapata nini juu ya wingi wa mifugo ambayo kwa uhalisia inatuletea migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji.

Mheshimiwa Spika, elimu kwa wafugaji juu ya ufugaji bora wenye tija bado ni ndogo sana. Hivyo, Wizara inatakiwa kuwekeza zaidi kwenye elimu ili watu wafuge kwa tija. Hivyo kuweza kujitosheleza kwa kuwa na viwanda vya kutosha katika kuongeza thamani kwenye mazao yanayotokana na mifugo. Hakuna uwekezaji wa kutosha katika sekta ya mifugo juu ya uchakataji wa mazao ya mifugo.

Mheshimiwa Spika, Wizara haioneshi mipango wala dira ya kutupeleka kwenye ufumbuzi wa changamoto zilizo kwenye Wizara hii, kwa sababu kutokupelekewa fedha za maendeleo kunaonesha wazi kuwa hakuna dhamira ya kutatua changamoto za Wizara.

Mheshimiwa Spika, kutawanya mifugo nchi nzima hakuwezi kuwa ni njia bora ya kukabiliana na changamoto hizo, tumeamua kusambaza mifugo kama tulivyoamua kusambaza mazao ya kilimo, jambo hili tusipolichukulia hatua kwa makini tunakwenda kuifanya Tanzania ya jangwa kwa kuondoa uoto wa asili wa nchi hii.

Mheshimiwa Spika, tunahitaji miradi ya uchimbaji wa malambo, mabwawa na maeneo ya minada hasa kwa mikoa ile ambayo si ya wafugaji kwa asili, mikoa kama ya Lindi na Mtwara bado hakuna malambo, mabwawa wala maeneo ya minada. Jambo hili linafanya mikoa hiyo kutopata faida ya mifugo hiyo kwani hakuna faida ya moja kwa moja kwa jamii kwa kuhamishia mifugo hiyo. Serikali inapaswa kutafuta wawekezaji wa ndani na nje ili kunusuru sekta hii na kukuza pato la Taifa.

Mheshimiwa Spika, maafisa mifugo ni tatizo lingine kwenye sekta ya mifugo, mfano;- Mkoa wa Lindi si Mkoa wa wafugaji. hivyo, idadi ya maafisa mifugo haikuwa kipaumbele, lakini kwa hivi sasa baada ya Serikali kusambaza mifugo nchi nzima hivyo umuhimu wa maafisa mifugo ni mkubwa sana kwa Mkoa wa Lindi hasa katika Jimbo la Liwale ambako hakuna miundombinu yeyote iliyoandaliwa kupokea mifugo. Kwani sasa nyama zinauzwa bila kupima ubora wa nyama na hakuna sehemu maalum kwa ajili ya mnada wa ng’ombe hivyo, Wilaya ya Liwale tunahitaji wataalamu wa mifugo.

Mheshimiwa Spika, kukosekana kwa wataalamu hao kunakuwepo na ufugaji usiotunza mazingira hivyo kuharibu vyanzo vya maji.
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, leo naomba mchango kwenye Wizara hii kwa kujadili namna ya migogoro ya mipaka kati ya hifadhi na vijiji vinavyozunguka hifadhi zetu kwani migogoro hii imedumu kwa muda mrefu na kurudisha nyuma hali ya mahusiano ya wahifadhi na wananchi pia hata na Serikali kwa ujumla. Kwa mfano katika Wilaya ya Liwale kuna mgogoro mkubwa na wa muda mrefu kati ya Hifadhi ya Selous na Kijiji cha Kikulyungu. Hadi sasa mgogoro huu umegharimu maisha ya watu wake katika kijiji hicho. Ni muda mrefu sasa mgogoro huu haujapewa kipaumbele licha ya kugharimu maisha ya watu.

Mheshimiwa Spika, unapozungumza juu ya malikale utakuwa unafanya dhambi kama ukiacha kumbukumbu zilizoachwa wakati wa Vita ya Maji Maji na utawala wa Wajerumani hapa nchini. Wizara bado ina kazi ngumu na muhimu sana ya kutambua majengo na alama mbalimbali za malikale kwa faida ya utalii na urithi wa nchi yetu kwa majengo mengi nchini yamesahauliwa hivyo kupoteza historia ya nchi yetu. Kwa mfano katika Wilaya ya Liwale kuna Boma la Mjerumani, boma hili lina kumbukumbu nzuri na nyingi sana hasa ya Vita ya Maji Maji. Mawe ya kujengea jengo hili yametoka Wilayani Kilwa, zaidi ya kilometa 250 kutoka Liwale, mawe hayo yalibebwa na watumwa.

Mheshimiwa Spika, kuna mabaki na picha za mashujaa na watawala wa Kijerumani waliotawala Ukanda wa Kusini. Kama haitoshi vilevile kuna kumbukumbu ya Mfaransa inayojulikana kama Mikukuyumbu, hapa ndipo mzungu wa kwanza kuingia Liwale aliuawa na mtu ajulikanaye kama Mchimae. Huyu ni mzungu ajulikanaye kama (Mfaransa). Kumbukumbu zote hizo zimesahauliwa sana.

Mheshimiwa Spika, Pori la Akiba la Selous kwa upande wa Ukanda wa Kusini hauna lango la utalii wa picha kwani kuna utalii wa uwindaji tu, jambo hili linakosesha mapato katika ukanda huo na watu wa ukanda huo kukosa kuona faida ya kuwepo kwa Selous Ukanda wa Liwale. Tunahitaji lango la utalii wa picha ili kuongeza ajira na mapato ya Halmashauri yetu ya Liwale.

Mheshimiwa Spika, hadi leo Liwale zaidi ya kushambuliwa na tembo na wanyama wakali hakuna faida ya moja kwa moja kwa wananchi kwa kukosa lango la utalii wa picha. Hivyo, kukosa wawekezaji wa mahoteli na miundombinu mingine ya kiutalii.

Mheshimiwa Spika, Halmshauri zinazopakana na hifadhi zinatakiwa kupata asilimia 25 ya mapato ya hifadhi husika. Naomba Wizara kupitia upya sheria hii kwani kiasi hiki ni kidogo sana kwa sasa, ni bora kiasi hiki kikaongezwa kufikia asilimia 30. Vilevile fedha hizi zinachelewa sana kufika kwenye Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Spika, kuhusu malipo ya kifuta machozi na fidia ya uharibifu wa wanyama pori, fedha hizi licha ya kuwa ni kiasi kidogo lakini hata utaratibu wa upatikanaji wake bado hauko wazi, haueleweki kwa watu wetu jambo linalofanya watu wetu kutopata fidia yoyote licha ya wengine kupata vilema na mashamba yao kuliwa na wanyama kama tembo, nyati na kadhalika. Malipo ya kifuta machozi ni kama danganya toto kwani walio wengi hawapati. Kwa mfano Halmashauri ya Liwale ina muda mrefu sasa watu hawajawahi kupata malipo haya licha ya kuwa na madai ya muda mrefu zaidi ya miaka mitano.

Mheshimiwa Spika, naomba Serikali ipitie upya sheria ya TFS kwani wakala huyu anavuna mazao ya misitu ya vijiji hata ile ya open area kiasi kinachokibaki kwenye Halmashauri ni kidogo sana. Misitu inakwisha lakini Halmashauri inakosa mapato ya moja kwa moja kutoka TFS jambo linaloleta mahusiano ya mabaya kati ya TFS na wananchi wa kawaida kwani hakuna faida ya moja kwa moja kutokana na uvunaji huu wa TFS. Kwa mfano katika Wilaya ya Liwale mahusiano ya TFS na wananchi si mazuri kutokana na watu wetu kutoona manufaa ya moja kwa moja kutoka kwenye taasisi hii.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, naomba nianze mchango wangu kwenye Wizara hii kwa kuangalia upya Sheria ya Kodi hasa kodi ya wafanyabiashara wadogo. Utaratibu wa kuanza kulipa kodi kabla ya kuanza biashara ni utaratibu usiofaa, kwani mlipa kodi utatakiwa kulipia kodi sehemu ya mapato yake. Sasa kitendo cha kulipa kodi kabla ya kufanya biashara, je, hiyo kodi anaitoa wapi? Iwapo biashara husika ikimpa hasara mfanyabiashara, je, sheria hii haioni kuwa inamuonea huyu mfanyabiashara? Jambo hili limekuwa likilalamikiwa na wananchi wengi sana na wengine kushindwa kuingia kwenye sekta hii ya biashara.

Mheshimiwa Spika, suala la ongezeko la mshahara halipaswi kuachwa bila kuangaliwa upya kwani hali ya wafanyakazi nchini ni mbaya sana, gharama za maisha zinapanda kila siku kukicha, sawa na kushuka kwa shilingi yetu dhidi ya dola. Kuacha kuongeza mishahara ya wafanyakazi kunapunguza sana ari ya wafanyakazi hasa sekta ya afya na sekta ya elimu, kwani hivi sasa wafanyakazi wa sekta hizi wana migomo ya kimoyomoyo. Walio wengi kinachowabakiza kazini ni uhaba tu wa ajira nchini.

Mheshimiwa Spika, kuna malalamiko ya muda mrefu juu ya wafanyakzi wa iliyokuwa NMC na TTCL. Wafanyakazi wa iliyokuwa NMC bado wana kesi mahakamani, lakini Hazina wamekuwa wakipiga chenga kwenda mahakamani, hivyo kuchelewesha haki za watu hao.

Vilevile kuna wafanyakazi wa TTCL, hawa walilipwa kwa makundi. Kuna waliolipwa kwa mkupuo kisha wakarudishwa kwenye pensheni ya kila mwezi na kuna kundi lililolipwa kwa mkupuo lakini hadi leo hawajarudishwa kwenye pensheni ya mwezi. Kitendo hiki ni cha kibaguzi kwa wastaafu hao, nao wanashinda Hazina bila majibu.

Mheshimiwa Spika, lingine ni fedha za mifuko maalum kutumiwa nje ya makusudio ya fedha hizo. Kumekuwa na matumizi yasiyofaa kwenye awamu hii ya tano. Mfano, haiingii akilini miradi ya REA kukwama kwa kukosa fedha wakati vyanzo vya fedha hizi vinajulikana na vinalipa vizuri, lakini wakandarasi wa miradi ya REA nchi nzima wanadai. Mfano mwingine ni fedha za kuendeleza zao la korosho. Pamoja na makusanyo mazuri ya export levy, fedha hizo zimeshindwa kwenda kwenye Bodi ya Korosho. Kutumika hovyo kwa fedha hizi kunaondoa maana ya kuanzishwa kwa mifuko hii.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na utaratibu wa taasisi ya TBS na TFDA kukagua na hatimaye kuteketeza bidhaa fake au zisizoruhusiwa nchini. Jambo hili ni jema, lakini ni kwa nini uteketezaji huu usifanywe kwenye viwanda au kwa waagizaji wakubwa badala ya kwenye maduka ya rejareja? Bidhaa kwa mfano ukienda Kariakoo kwenye maduka ya jumla, zinauzwa bila kificho, lakini ukinunua na kuweka dukani kwako ndipo TBS au TFDA wanakuja kukagua na kusema ni bidhaa fake na kesho yake ukienda Kariakoo bado utazikuta zikiuzwa.

Mheshimiwa Spika, kuhusu taarifa ya TRA na Hazina kukosa uhalisia kwenye maisha ya kawaida ya wananchi wetu, Hazina wanasema umaskini wa watu wetu unapungua wakati hali ya watu wetu inazidi kuwa mbaya. Hali ya lishe ni mbaya, watu wanashindwa kununua mahitaji muhimu. Uwezo wa watu kununua bidhaa umepungua sana kadri ya TRA wanavyotangaza kukusanya mapato zaidi ndiyo hali ya watu inavyozidi kuwa mbaya zaidi na hata fedha za kwenda kwenye miradi ya maendeleo zinashindwa kwenda. Hivyo nini faida ya kuwa na makusanyo mazuri wakati miradi yetu ya maendeleo inakwama siku hadi siku? Wizara zote hazipelekewi fedha za miradi ya maendeleo. Je, takwimu za TRA tuziamini? Kama ndivyo, basi kutakuwa na matumizi mabaya ya fedha za walipa kodi.

Mheshimiwa Spika, mgawanyo wa fedha za maendeleo nao ni bora ukaangaliwa upya kwani kwenye mikoa au maeneo yenye michango mikubwa kwenye pato la Taifa hakujapewa kipaumbele katika kuimarisha miundombinu ili kuongeza uzalishaji. Mfano, Mikoa ya Lindi na Mtwara bado hali ya miundombinu siyo nzuri. Mfano, Bandari ya Mtwara, Bandari ya Lindi na Kilwa, Barabara ya Nangurukulu – Liwale na kadhalika. Kuacha kuboresha miundombinu ya barabara hizo nilizozitaja hapo juu ni kudumaza uchumi wa maeneo husika na nchi kwa ujumla.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii ya Ardhi na nichukue fursa kumwomba Mwenyezi Mungu amweke Mbunge mwenzetu ambaye ameitwa mbele ya haki, mahali pema peponi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shida yangu kubwa ni upande huu huu wa migogoro ya ardhi. Pamoja na kwamba Liwale ardhi tunayo kubwa sana, lakini kutokana na uroho wa baadhi ya taasisi wameamua kutuingiza kwenye migogoro mikubwa sana. Sisi Liwale tuna mgogoro mkubwa sana na Selous. Nilikwenda ofisini kwa Mheshimiwa Waziri, majibu aliyonipa aliniambia kwamba mgogoro huu upo ndani ya Mkoa au Kamishna wa Ardhi, atakaposhindwa ndio atampelekea. Naomba nimwambie kwamba hawezi kushindwa akamletea, akimletea maana yake ni kwamba ameshindwa kazi na akishindwa kazi maana yake hataki ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kinakachofanyika pale, ule mgogoro kwa sasa una miaka zaidi ya kumi, haujatatuliwa, sisi na Selous tunagombana. Mpaka sasa hivi watu wanne wamepoteza maisha, kwenye mgogoro ule kati ya Kijiji cha Kikuyungu pamoja na Selous.

Mheshimiwa Mwenyekiti, si hivyo tu, vile vile tuna mgogoro wa ardhi sisi pamoja na Wilaya ya Kilwa, sehemu ya Nanjilinji. Huu mgogoro nao ni wa muda mrefu sana na mgogoro huu ndio ulionipeleka mimi kwa Mheshimiwa Waziri na akanipa hayo majibu kwamba Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa akishindwa ataniandikia. Mkuu wa Mkoa hawezi kushindwa akamwandikia, akishindwa maana yake ameshindwa kazi, lakini bado watu wanaendelea kuteseka. Naomba Mheshimiwa Waziri achukue initiative kwenda kutatua huu mgogoro kati yetu pamoja na Kilwa, pamoja na huu mgogoro wa Selous. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba niongelee huyu Kamishna wa Ardhi wa Kanda ya Mtwara. Mimi kwa kweli kwenye Halmashauri yangu ya Wilaya ya Liwale, migogoro hii kama kweli huyu Kamishna wa Ardhi wa Kanda ya Mtwara, angekuwa anafanya kazi kwa weledi hii migogoro mingine isingekuwepo. Sio hivyo tu, vile vile hata upatikanaji wa hati pale Mtwara; sisi kwanza tuko mbali sana; kutoka Liwale mpaka Mtwara ni umbali mrefu sana, lakini hata ule ushirikiane wake nao ni mgumu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano hawa vijana wa Selous Kijiji cha Kikulyungu, walikuja mpaka hapa Bungeni tukawapeleka mpaka kwa Mheshimiwa Waziri na akaturudisha kwa Kamishna. Kamishna mpaka leo anawazungusha hakuna chochote kinachoendelea na wala hawajui waelekee wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huyo Kamishna wa Ardhi wa Mtwara aliokasimiwa madaraka mimi naona kwamba yeye badala ya kutatua migogoro analimbikiza migogoro, pengine ni kwa sababu ya kuogopa ajira yake, kwamba akionekana ameshindwa basi ataonekana hajafanya kazi vizuri. Kwa hiyo namwomba kabisa Mheshimiwa Waziri kwa nia njema aje Liwale atutatulie hii migogoro ya ardhi kati ya sisi pamoja na Kilwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kwa upande wa watumishi katika Halmashauri yetu. Halmashauri ya Wilaya ya Liwale kuna mtumishi mmoja tu wa ardhi mwenye sifa, waliobaki wengine si watumishi wenye sifa. Matokeo yake sasa kuna tatizo kubwa sana, unapoingia mahali ambako sasa tunataka tupime ardhi kwa matumizi bora ya ardhi tatizo hilo linakuwa kubwa sana kwa sababu uhaba mkubwa sana wa watumishi wa ardhi katika Halmashauri yetu ya Wilaya ya Liwale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, si watumishi peke yake na vifaa vile vile. Mara nyingi tunatumia vifaa kutoka Halmashauri ya Nachingwea, kwa maana ya kwamba hatuwezi kufanya kazi pale mpaka tutafute wataalam na vifaa kutoka Nachingwea, ndipo tuweze kufanya kazi pale kwenye Halmashauri yetu ya Liwale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili limesababisha viwanja Wilaya ya Liwale viuzwe ghali sana kwa sababu mara nyingi tunatumia wataalam kutoka nje; badala ya sisi wenyewe kupewa vifaa vya upimaji tukaenda kupima ardhi ili watu wapate viwanja kwa bei nzuri. Kuna tatizo kubwa sana la vifaa vya upimaji wa ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri ajaribu kuiangalia Halmashauri ya Wilaya ya Liwale hasa kwa upande wa watumishi wa ardhi pamoja na vifaa ili nasi tuweze kufanya matumizi bora ya ardhi. Kwa sababu sasa hivi tunashindwa kupata wawekezaji; mwaka jana tulipata mwekezaji lakini kijiji ambacho ilikuwa aende kikakutwa bado hakijafanyiwa matumizi bora ya Ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na jambo hili sehemu nyingi tunakosa wawekezaji kwa sababu vijiji vyetu vingi havijaingia kwenye matumizi bora ya Ardhi. Hakuna mtu ama Kamishna ambaye anaweza akatoa hati kwa mwekezaji kwenye kijiji ambacho hakijapata matumizi bora ya Ardhi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami kuchangia Wizara hii ya Madini. Awali ya yote, nichukue fursa hii kumpa pole Mheshimiwa Spika na wananchi wa Buyungu pamoja na Viongozi wa CHADEMA kwa kupoteza mwakilishi hapa Bungeni, mwakilishi makini na mahiri. Mwenyenzi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze mchango wangu kwa kuwataka Mawaziri wote watatu wazingatie sana ushauri uliotolewa na Kamati na Nishati na Madini kwani umesheheni mambo muhimu sana. Yapo mambo kumi na moja nimeyaona pale ni muhimu sana, kama kweli dhamira ni kuiondoa nchi hapa ilipo kuelekea kwenye uchumi wa kati basi huu ushauri uzingatiwe sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nijikite kwenye shughuli za utafiti wa madini kama mchangiaji aliyepita amesema kwamba hii tasnia ya madini elimu yake bado ni ndogo sana. Hawa watafiti wa madini wanapoingia kwenye Halmashuri zetu elimu haipo yaani wananchi wanashindwa kujua mipaka ya watafiti ni ipi na wao wananufaikaje, kwa sababu mwisho wa siku wanaachiwa mashimo au mahandaki. Wanakijiji wanakuwa bado hawaelewi ni kwa namna gani wanaweza kufaidika na hizi shughuli za utafiti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitolee mfano katika Kijiji cha Lilombe, kuna machimbo ya muda mrefu sana, yale machimbo yana zaidi ya miaka kumi, kuna madini ya sapphire na dhahabu lakini mpaka leo wananchi wa kijiji kile hawaelewi chochote zaidi na kuambulia mashimo. Nilikwenda kwa Mheshimiwa Waziri kumuulizia akaniambia kwamba ameshindwa kuweka mtu katika Mji wa Liwale kufungua soko pale ili na sisi tupate kunufaika na uwepo wa madini, wakasema yale madini pale wachimbaji wale ni wachache, halafu madini yenyewe siyo mengi kwa hiyo hakuna haja ya kuweka Kamishna pale wa Madini. Jambo hili niungane na mchangiaji mmoja alisema kwamba kuwepo na watu kwenye Halmashauri zetu wanaoshughulika na mambo ya madini iwe ni kwa ajili ya kutoa elimu watu wakajua mahali ambapo madini yanapopatikana wao wanawajibika vipi na kusaidia hawa wachimbaji wadogowadogo ambao wanahangaika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, kutoka Liwale kwenda Tunduru ambako ndiyo kuna soko, kuna umbali wa zaidi ya kilomita 200, mtu anachukua madini kutoka Liwale mpaka Tunduru akaenda kuuza kwa hiyo wanaonufaika na ushuru na mambo mengine ni wale walioko kule, je, kule ambako kuna mashimo kunaachwa nini. Kwa hiyo, jambo hili nalo lifanyiwe marekebisho ili tuone kwamba kuna umuhimu Halmashauri zetu kuwepo na watu wanaoshughulika na mambo ya madini katika kutoa elimu pamoja na mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naomba Sheria ya Madini ifanyiwe marekebisho hasa kwenye madini haya kama mchanga, kokoto na mawe. Panapotokea ujenzi wa barabara kumetuletea migogoro sana na hasa hasa gharama kubwa ya ujenzi wa barabara inatokana na kodi za madini. Ili kujenga barabara unatakiwa upate kifusi, kokoto lakini zenyewe unakwenda kuzilipia.

Mheshimiwa Naibu Spika, unakuta mkandarasi anatenda ile barabara aki-include gharama hizo. Sasa barabara inayojengwa ni Serikali, hayo madini ya Serikali, ifike wakati Serikali iangallie namna ya kurekebisha hii sheria labda kuwa na exemption kwamba kwenye madini ambayo yanakwenda kufanya kazi za kiserikali basi kuwe na exemption yasitozwe kodi na kama yanatozwa kodi basi iwe ndogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naomba niongelee Ofisi ya Madini Kanda ya Kusini ambayo iko Tunduru na wamejenga tawi lao pale Nachingwea lakini bado upatikanaji wa leseni ni mgumu sana hasa kwa wale wachimbaji wadogo wanaotoka kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Liwale. Ni mgumu kwa sababu ni lazima waende Nachingwea wakapate hiyo leseni. Hata vile wanaporudi na hizo leseni soko nalo linawapa shida vilevile.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee suala la uwepo wa madini. Jana nimezungukia kwenye mabanda yale kule nyuma, nimekuta kule kwetu katika Wilaya Liwale na Ruangwa kuna hiyo wanaita green garnet na nikaambiwa haya madini thamani yake ni mara kumi ya tanzanite. Sasa nataka nijue Wizara kupitia kile Kitengo cha Utafiti wa Madini wameyatangaza kwa kiwango gani na mkakati upi umewekezwa kutafuta wawekezaji ili upande wa Kusini uchumi wetu ukaimarika kwa sababu ya upatikanaji wa hayo madini ambayo yameonekana kwamba yenyewe yana thamani kubwa kuliko tanzanite.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli napata ukakasi kidogo, nimesoma kwenye kitabu kile cha Mheshimiwa Waziri kuhusu ukusanyaji wa maduhuli kwenye bajeti ya mwaka 2017/2018 inaonyesha kama maduhuli yameongezeka, imekusanya maduhuli zaidi ya asilimia 103 lakini sasa unakuja kwenye fedha za maendeleo zimekwenda asilimia 0.8. Nashindwa kuelewa inawezekana vipi ng’ombe huyo ambaye unaona ametoa maziwa ya kutosha ndiyo anayenyimwa malisho, tunadhamiria nini, mwisho wa siku tunataka kwenda wapi? Kama Wizara inaweza kukusanya maduhuli ikapindukia lakini kwenye fedha za maendeleo wakawa hawapewi fedha. Bado sijapata ufahamu vizuri tunakwenda wapi, yaani dhamira yetu ni ipi katika hilo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kwenye Wizara hii. Awali ya yote nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha mchana huu wa leo kusimama hapa na kutoa mchango wangu. Vilevile kabla sijasema chochote naomba nitoe pongezi kwa Mheshimiwa Waziri, Naibu Mawaziri, Wenyeviti wa Bodi zote zilizopo kwenye Wizara hii. Vilevile pongezi zangu ziende kwa Katibu Mkuu na Makatibu wote wa kisekta ambao wanahudumu kwenye Wizara hii na bila kuwasahau Wakurugenzi wanaoendesha taasisi mbalimbali zilizopo ndani ya Wizara hii, wanafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kuonyesha kwamba ni namna gani sasa wafanyakazi au wateule hawa wa Mheshimiwa Rais wanaanza kumfahamu Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli anataka kuipeleka nchi sehemu gani, tunataka kwenda wapi. Kwa hiyo, nawapa pongezi, Mwenyezi Mungu awajaalie, awape umri mrefu, waendelee kuhudumu kwenye Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nimeingia kwenye Bunge hili nilitoa hotuba ambayo nilipewa mwongozo na Mheshimiwa Jenista pale. Niliomba kuitoa Liwale kwenye nchi hii kwa sababu ilikuwa kama vile haihitajiki na nikapewa mwongozo kwamba huo ni uhaini. Nilisema Liwale tuitoe kisiwani na leo nasimama hapa napenda kusema rasmi kwamba Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imesikia kilio change, sasa mwelekeo wa kuitoa Liwale kisiwani unakwenda kutoka. Nilisema tuitoe Liwale kisiwani kwa mawasiliano, leo asilimia 70 ya Liwale tunawasiliana, nasema hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa pongezi zangu kubwa sana kwa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, kwa kweli kwa Wilaya ya Liwale umetutendea haki. Napenda kutoa pongezi kwa CEO wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, najua leo hii wanasherehekea miaka 10 ya mafanikio na nawaunga mkono kwa mafanikio waliyoyafikia na kuitoa Liwale kisiwani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, nilisema tuitoe Liwale kwa mawasiliano ya barabara na mara nyingi nimesimama hapa nilikuwa naiongelea barabara ya Nangurukulu - Liwale, Liwale – Nachingwea. Namwambia Mheshimiwa Waziri ahsante sana, kwa sababu barabara hizi nimekwenda nimeziona kwenye maandishi yake tayari ametutengea fedha kwa ajili ya kwenda kufanya upembuzi yakinifu na hatimaye iweze kujengwa kwa kiwango cha lami na naomba Mwenyezi Mungu ajalie hili na tupate fedha hizo ili barabara hii iweze kujengwa kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nijikite kwenye upande wa TAZARA. TAZARA kama ambavyo Mheshimiwa Mwambalaswa amesema, wenzetu wa Zambia wameshapoteza interest na reli hii kwa sababu tayari wana reli mbadala kwa ajili ya uchumi wao, sisi ndiyo tumebakiwa na umuhimu wa kubakia kwenye hii reli. Kwa hiyo, naiomba Serikali hebu wajaribuni kufanya mapitio ya mikataba ya hii reli. Kwanza reli hii kwa kiasi kikubwa kwa upande wa uongozi ipo upande wa Zambia zaidi, ndiyo wenye maamuzi, lakini Wazambia hawa pamoja na kwamba ndiyo wenye maamuzi kwa kiasi kikubwa lakini bado hawahitaji tena hii reli. Kwa hiyo, naiomba Serikali ifanye mapitio ili tuone ni namna gani tunaweza kuihodhi hii reli, ikiwezekana basi kila upande wa- operate kipande chao ili na sisi tuweze kujikwamua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ndiyo maana sasa hivi TAZARA wanakwenda kwa kusuasua hata mishahara yao ni ya kusuasua kwa sababu bado hawajapewa ile full mandate ya kuendesha hii barabara ya TAZARA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi zote nilizozisema kwa ajili ya upembuzi yakinifu wa barabara ya Nachingwea - Liwale na Nangurukuru - Liwale, sasa naomba nirejee Mheshimiwa Waziri barabara inayotoka Masasi kwenda Nachingwea. Barabara hii imefanyiwa upembuzi yakinifu tangu mwaka 2015, leo hii kila unapofungua kwenye bajeti unaikuta barabara hii bado inatafutiwa fedha. Barabara hii ni muhimu sana na kwa nini naiongelea barabara hii, naiongelea barabara hii kwa sababu najua hata hiyo barabara ya Nachingwea – Liwale inayokwenda kufanyiwa upembuzi yakinifu, kama barabara ya Nachingwea –Masasi haitojengwa kwa kiwango cha lami, haiwezi kujengwa barabara ya Nachingwea – Liwale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Serikali waiangalie sana hii barabara ya Masasi – Nachingwea, iende sasa ijengwe, huu ni mwaka wa tatu upembuzi yakinifu umekamilika, naomba Mheshimiwa Waziri aitengee fedha ili barabara hii ijengwe kwa kiwango cha lami. Barabara hii inakwenda sambamba na barabara ya Nachingwea – Nanganga. Barabara hizi mbili zikijengwa kwa kiwango cha lami, napata ahuweni kwamba sasa Liwale – Nachingwea inakwenda kujengwa kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana na napenda kuisistiza Serikali iendelee kuangalia hii barabara, iweze kujengwa kwa kiwango cha lami ili nami kule barabara ya Nangurukuru –Liwale iweze kujengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba niongelee hii taasisi ya MSL. Mheshimiwa Rais ameonesha nia ya kufufua hii taasisi kwa maana tayari tunaweza kujenga meli kama vile tunavyojenga meli zile pale Mwanza - Ziwa Victoria, Ziwa Nyasa na Ziwa Tanganyika, tumeona miradi inakwenda kujenga vivuko na meli. Hata hivyo, hii kampuni bado haijaimarika, kampuni hii bado ina madeni makubwa sana, hata wale watumishi bado wanaidai kampuni kwa kiasi kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali basi ikiwezekana basi madeni haya Hazina wayachukue ili kampuni hii iweze kujiendesha kwa faida. Kwa inavyoonekana na kwa jinsi CEO wa kampuni hii alivyo- committed ni kwamba Serikali watakapowapa full mandate, kampuni hii inaweza ikafanya vizuri na ikatuinua kiuchumi na vilevile ikatusaidia kwenye usafirishaji wa mazao mbalimbali ya bahari na maziwa makuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba niongelee hii kampuni ya TTCL, kampuni hii ni kampuni ya Serikali au Umma, tulitaraji sana kampuni hii iweze kwenda mbali kwa maana kwamba iweze kupeleka mawasiliano vijijini huko mahali ambapo hakuna mvuto wa kibiashara. Tatizo la kampuni hii ni mtaji, kampuni hii ina tatizo kubwa sana la mtaji na kwa nini ina tatizo la mtaji? Ina tatizo la mtaji kwa sababu kampuni hii vilevile ina madeni makubwa inazidai taasisi mbalimbali za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi naiomba Serikali sikivu ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, wawape fedha/mtaji TTCL ili waweze kufika mbali kwa sababu sasa hivi TTCL wapo kwenye mashindano na makampuni mbalimbali, lakini kama hawatakuwa wanapata mtaji wa kutosha, kampuni hii hawawezi kwenda mbele na hawawezi kuingia kwenye ushindani wakashinda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali iendelee kuifutia madeni au ikiwezekana Hazina waifutie madeni basi hii TTCL nayo ili iweze kusonga mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo watu hapa wanabeza ununuzi wa ndege, wanayo haki ya kubeza kwa sababu ili waendelee kubaki kule…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Malizia.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: …ili waweze kuendelea kubaki kule ni lazima waseme hayo wanayoyasema, lakini kwa kweli ununuzi wa ndege una tija kubwa kwa nchi yetu kwa ajili ya kukuza utalii… (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja mia kwa mia. Ahsante. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hutoba hizi za Kamati mbili. Awali ya yote kama Mjumbe wa Kamati ya Miundombinu nataka nichukue nafasi hii kumpongeza Mwenyekiti wetu wa Kamati kwa kuiongoza vyema Kamati ya Miundombinu Kamati ambayo inaongoza kwa upana kwa maana ya sekta nyingi tunazozisimamia, lakini kwa usimamizi wake mahili ndiyo tumeweza kufanikiwa kuleta haya mafanikio ambayo tunayaona leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Rais ambaye anaposema kwamba anataka kuelekea kwenye nchi ya viwanda ni kwamba alijua jambo kubwa sana ambalo anatakiwa kulifanya ni kuuwisha miundombinu na ndiyo maana amewekeza sana kwenye upande wa miundombinu hakuna mtu ambaye hajui ni kwa namna gani nchi yetu sasa hivi kwa upande wa miundombinu hasa ya barabara, viwanja vya ndege, bandari zote hizi zimeenda kufanyiwa kazi na kazi yakiufanisi kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukizungumzia hata huko ziwa Victoria ziko meli mpya zimejengwa na zile za zamani zimekarabatiwa. Lakini hii yote ni katika kuimarisha miundombinu, kuimarisha miundombinu huko ambako kutaelekea kuimarisha uchumi wa Taifa letu. Juhudi hizi kubwa ambazo zinafanya na Mheshimiwa Rais na wananchi wote tunamuunga mkono zipo kasoro mbalimbali ambazo tunakiwa tuzichangie na tuziseme ili Serikali nao waweze kuchukue hili waweze kulifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko suala limezungumzwa na Mheshimiwa Mtaturu suala la TPA, kwa kweli Mheshimiwa Rais amewekeza sana TPA, ameingiza fedha nyingi sana TPA kwa maana ya kuwataka kuimarisha bandari zetu ili hatimaye tuweze kuinua uchumi wetu. Vilevile alienda mbali sana akaonda ukaletwa Muswada, Serikalini tukaletwa Muswada tukaunda hii Taasisi ya TASAC kwa nia hiyo hiyo ya kuimarisha au kuondoa sintofahamu iliyokuwa inapatika kule bandarini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, chombo hiki TASAC tumekiunda kazi zinazofanywa na TASAC sasahivi ni kazi ambazo zilikuwa zinafanywa na watu zaidi ya 2000 huko nyuma, wdau mbalimbali wa sehemu ya bandari. Jambo hili limeipa ugumu sana TASAC kiasi kwamba sasahivi tumezua tatizo jingine kubwa zaidi kwenye sekta ya bandari; tatizo la ucheleweshaji wa mizigo bandarini kama ambavyo aliyetangulia kusema ameshalisema kwamba tayari tumeanza kupoteza wateja wadau mbalimbali wameaza kuamisha mizigo yao kutoka kwenye bandari yetu lakini kikubwa zaidi siyo utendaji mbaya wala uwe sifa ya zaidi ulikuwepo wizi na vitu vingine vya ulaghai wizi mdogo mdogo. Sasa hivi wizi kule hamna wafanyakazi wa bandari, lakini tatizo kubwa linakuwa manpower ya TASAC haiwezi kumudu mzigo uliko pale bandarini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, na naishauri Serikali ukisikia watu wanasema sana ujue kuna jambo hata kwenye hali ya kawaida hapa ukienda barabara ukikuta watoto wanacheza kwenye jalala hebu chukua muda kaa uwasikilize, wasome utajifunza tu. Sasa hizi kilele zinazopigwa hizi pamoja na kwamba wale wanaopiga kelele huko nyuma walishachafuka wanamajina mbalimbali, lakini hebu tuwaangalie hebu twende ndani tuangalie kuna nini kabla hatujaingia kwenye tope zaidi, niliona niliongele hili ili serikali nao mlichukue kwenye Kamati tumelijadili sana, lakini naomba kwa usisitizotu naomba TASAC bandari tuangalie utendaji wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ushauri wangu mwingine kwa upande wa Serikali suala la upembuzi yakinifu wa miundombinu mbalimbalui. Ushauri wangu suala la upembuzi yanikifu uendane na uhalisia, tunayo mikiradi mingi ya muda mrefu imeshafanyiwa upembuzi yakinifu lakini kuna miradi mengine leo inafanyiwa upembuzi yakinifu kabla ile miradi ambayo tumefanya umbembuzi yakinifu mwanzo bado haijakamilika. Kwa mfano barabara ya Nachingwea kwenda Masasi kilometa 45 imefanyiwa upembuzi yakinifu mwaka 2014, lakini barabara ile mpaka leo haijapatiwa fedha za kujenga, tangu 2014 mpaka leo 2020 tumeshafanya upembuzi yakinifu barabara ngapi kabla ya ile; mtaona kwamba bado tulikuwa tunaendelea kufanya umbembuzi yakinifu wakati barabara ambazo tayari tulishazifanyia upembezi yakinifu bado hatujazipatia fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ushauri wangu kabla hatujaanzisha miradi mingine hebu tuangalie ile miradi ambayo tayari tumeshafanyiwa upembuzi yakinifu inapatiwa fedha na hatimaye kujengwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye bajeti iliyopita mfano mwingine kwenye bajeti iliyopita kwenye Jimbo langu la Liwale pale kuna barabara yetu ile Nangurukuru Liwale imeshatolewa fedha za umbembuzi yakinifu, lakini matarajio wananchi wetu tukiwaambia kwamba barabara yetu tayari imeshafanyiwa upembuzi yakinifu ni mategemeo yao kwamba baada ya mwaka mmoja mwaka wa pili, barabara hiyo itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunapowaridhisha wananchi kwamba barabara hii tumeshafanyia upembuzi yakinifu halafu tukachukua miaka 10 bado haijajengwa tunaleta sintofahamu nyingine kwa hawa wananchi ambao tunakwenda kuwasimamia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine naomba niliongelee kuhusu TAZARA, Sheria ya uundwaji wa TAZARA wakati ule TAZARA inaundwa wa Zambia walikuwa wanaihitaji sana, ukiangalia hali ya jiografia kule Msumbiji na Malawi ilikuwa hakuko shwari. Kwa hiyo, TAZARA walikuwa wanahitaji sana hii reli ya TAZARA, lakini miaka hii ya karibuni naomba niiambie Serikali…

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Zuberi

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwani dakika ngapi?

MWENYEKITI: Muda wetu ndiyo huo.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono mia kwa mia. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami jioni hii niweze kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha mimi na ninyi kuwepo hapa tukiwa na afya njema. Vile vile nachukua nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna alivyoweza kuiongoza nchi hii kwa miaka minne mfululizo na hii ni bajeti ya nne ambayo haina ukakasi, tunakwenda kifua mbele.

Mheshimiwa Spika, yaliyofanywa nchi hii ni makubwa sana. Vile vile nataka nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu wa timu yake yote. Mheshimiwa Waziri Mkuu, pongezi za pekee kwanza kwa kumudu speed ya Mheshimiwa Rais. Kwa sababu najua mlianza wengi, lakini wengine wameteremka, watu ambao speed iliwashinda, lakini wewe mwenyewe umebaki katika kiti hicho muda mrefu. Kwa hiyo, nakupa pongezi binafsi kwa kumudu kwenda na speed ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye hotuba hii naomba nijikite sana kwenye upande wa kilimo. Ni ukweli usiopingika, kwenye nchi yetu asilimia 65 ya Watanzania ni wakulima na hapa napenda kuipongeza Serikali, imechukua juhudi mbalimbali za kuimarisha kilimo hasa katika kuwekeza katika tafiti na kuwekeza katika upande wa pembejeo.

Mheshimiwa Spika, jambo kubwa ambalo naomba niendelee kuisisitiza Serikali, kuliangalia kwenye Sekta ya Kilimo hasa kwenye upande wa masoko, tunayo shida kubwa sana ya masoko ya mazao yetu. Nafikiri hapa hata Mheshimiwa Chegeni ametoka kusema hapa, kila mtu anayetoka huko Mwanza anazungumzia pamba na shida kubwa anayozungumzia ni upatikanaji wa fedha kwa wakulima wetu. Upatikanaji huu wa fedha unakwenda sambamba na upatikanaji wa masoko ya mazao yetu.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba tunawekeza kwa kiasi kikubwa sana kwenye pembejeo na kwenye tafiti, lakini tusipokuwa na uhakika wa upatikanaji wa masoko ya mazao yetu, shida kwa wakulima wetu bado itakuwa kubwa sana. Ninapozungumzia soko, naomba nijielekeze vile vile kwenye ushirika. Kwenye ushirika kuna matatizo makubwa na mazito sana. Kuanzia kwenye sheria yenyewe ya ushirika. Hii ni mara ya pili nasema kwamba naiomba Serikali walete Sheria ya Vyama vya Ushirika ifanyiwe mapitio. Pamoja na kwamba hili ni Bunge la mwisho, basi hata kwenye Bunge lijalo hili jambo lifanyiwe mkakati. Sheria ya Vyama vya Ushirika bado ina upungufu mkubwa sana. Hata wenyewe Vyama vya Ushirika ukikaa nao wanakubali kwamba kweli kuna tatizo kwenye Vyama vya Ushirika.

Mheshimiwa Spika, siku moja nilikaa na Afisa Ushirika wa Wilaya, namwuliza vipi bwana, haya mambo yanakwendaje kwenye Vyama vya Ushirika? Mbona vinapoteza fedha za wakulima, wanapoteza mazao, inakuwaje? Anakwambia kwamba hata yeye hana mandate kubwa ya kuingia kwenye Vyama vya Ushirika na kukagua. Mwenye mandate hiyo ya kukagua ni COASCO. Sasa ni lini COASCO inavifikia vyama vya msingi? Ni lini COASCO inafikia vyama vikuu vya ushirika? Kwa hiyo, utakuwa COASCO yenyewe tayari ni mzigo.

Mheshimiwa Spika, hivi leo mimi ninavyozungumza hapa, katika Mkoa wa Lindi hasa Wilaya ya Liwale tuna tani 800 za korosho zimekosa soko, wakulima wanapeleka zile korosho mwezi wa Kumi na Moja, mpaka leo hawajui hatima yao. Kwa hiyo, naomba Serikali ichukulie jambo hili kwa umakini sana, kwamba Vyama vya Ushirika badala ya kuwa msaada kwa wakulima vimekuwa ni mzigo kwa wakulima. Kwa hiyo, naomba Sheria ya Marekebisho ya Vyama vya Ushirika yafanyike.

Mheshimiwa Spika, halafu kwenye hiyo hiyo sheria, Vyama vya Ushirika vimeruhusiwa kuanzishwa na watu 20, sijui watu15; matokeo yake unakwenda kwenye Halmashauri unakuta Vyama vya Ushirika lukuki na vyama vyenyewe vinafanya kazi wakati wa mazao tu. Ina maana wao wakati wa kununua mazao, wananunua mazao, yakiisha wanafunga milango na chama kinaishia pale. Wanasubiri msimu mwingine uje, wanafungua milango, wanachukua korosho za watu, wanauza, wanawaibia, msimu ukiisha wanafunga.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi vyama vya namna hii, sheria iansemaje? Hivi ni wakati gani chama kinatakiwa kifutwe? Yaani chama kisipofikia malengo yake, miaka mitatu, minne chama kinatangaza hasara, wakulima wanadaiwa, mpaka TAKUKURU wanaingia kwenda kudai fedha za wakulima, hicho chama kweli bado kina sababu ya kuishi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba nijike hapo kwenye Vyama vya Ushirika. Kwa kweli Vyama vya Ushirika sheria iletwe, viangaliwe ili kama kweli lengo la Vyama vya Ushirika ni kuwasaidia wakulima, zamani ilisemwa Vyama vya Ushirika vilikuwa vinaweza kusomesha mpaka vijana wa shule wanachama wa Vyama vya Ushirika, lakini leo Chama cha Ushirika kimekuwa ni mzigo kwa mkulima, ndiyo kinachomfanya ashindwe kusomesha.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naiomba Serikali ilichukue hili, Vyama vya Ushirika ni mzigo. Pamoja na nia njema ya kuundwa kwake, lakini Vyama vya Ushirika kwenye sheria, inasema Vyama vya Ushirika vitasaidia wakulima kupata pembejeo na kupata masoko, lakini hivi vyama kweli vinafanya hiyo kazi?

Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri aje na tathmini. Lazima tufanye tathmini tuhakikishe vyama vingapi vinakidhi vigezo na vile ambavyo havikidhi vigezo vifutwe kwa sababu utitiri wa vyama hauna maana kwa wakulima kama wakulima watapoteza mazao yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili naomba nizungumzie suala la ardhi. Ardhi haiongezeki, wanadamu tunaongezeka. Ukienda kule kijijni kuna sheria kwamba kijiji kinaruhusiwa kuuza heka 50, lakini hao mliowapa hiyo mandate ya kuuza heka 50, elimu hiyo wanayo? Ardhi inauzwa sana nchi hii sasa hivi. Uuzwaji wa ardhi umekuwa ni wa holela sana. Ukienda huko vijijini, ardhi inaondoka kweli kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kuishauri Serikali, pamoja na kwamba tumeruhusu vijiji kuuza heka 50, lakini bado wataalam tulionao ni wachache hawakwenda kuwapa elimu wale wanaouza ardhi. Kule vijijini watu hawawezi kuona thamani ya ardhi, wanauza tu; lakini sisi tunaoishi mijini tunajua thamani ya ardhi.

Mheshimiwa Spika, naomba sana, kabla Taifa hili halijaingia kwenye janga la kupoteza ardhi, Serikali mtupie macho kwenye uuzwaji wa ardhi. (Makofi))

Mheshimiwa Spika, liko suala lingine huko kwenye ardhi. Kuna hili suala la urasimishaji. Ndugu zangu, urasimishaji ulikwenda Manzese, ulikwenda Kinondoni kwa sababu tulishindwa kuwapanga wale watu, tayari walishajazana. Leo urasimishaji uko mpaka vijijini. Watu wanakaa holela halafu mtu anakuja anakwambia kuna urasimishaji. Mji unakaa hovyo; hakuna mtaa, hakuna barabara; yaani kuna vijiji ambavyo havina hata sababu ya kuingia kwenye urasimishaji. Ni suala tu la mtendaji kuwahamasisha wananchi wajipange, wapimiwe maeneo yale wakae, kama ni kugawiwa; tena upimaji wenyewe siku hizi ni wa kuchangia.

Mheshimiwa Spika, mimi naomba tuachane na mambo ya urasimishaji hasa kwenye Halmashauri hizi za Wilaya na Vijijini. Tubaki na huu urasimishaji wa Dar es Salaam na Dodoma pengine kama tulichelewa kujipanga.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante, malizia.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba niunge mkono hoja. Napongeza sana Serikali kwa kazi kubwa tunayoifanya, inayotukuka na inayoonekana.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na mchango wangu katika Wizara hii kwa kuishauri Serikali kutekeleza miradi yake ya maendeleo kwa wakati hasa miradi ya nyumba za Askari Polisi na Magereza kwani askari wetu kuishi uraiani kunawaondolea weledi wao na pia kuhatarisha maisha yao, kufuatia mazingira ya kazi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbali na ujenzi wa nyumba za askari vilevile ingeanza ujenzi wa vituo vya polisi vya Wilaya mfano hadi leo Wilaya ya Liwale haina jengo la Kituo cha Polisi cha Wilaya. Jengo linalotumika ni jengo la mtu binafsi ambalo lilipangishwa kwa iliyokuwa Benki ya NBC, jengo hilo sasa ni chakavu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mashamba yanayomilikiwa na Jeshi la Magereza hayana hati miliki ya ardhi, mahali pengine hata jengo la magereza halina hati miliki licha ya kuwa na majengo yaliyokamilika. Mfano, Gereza la Wilaya ya Liwale lililoanzishwa mwaka 1982 lakini hadi leo jengo wanalolitumia ni la tope lenye uzio wa miti. Hata hivyo, wenye mashamba yaliyotwaliwa kipindi hicho bado hadi leo hawajapewa fidia za mashamba yao. Gereza lina miaka 36 sasa lakini wenye mashamba hawajapata haki yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huko nyuma magereza zetu zilikuwa zinajitegema kwa chakula. Je, ni kwa nini sasa magereza zimekuwa mzigo mkubwa kwa Serikali kulisha wafungwa wakati magereza nyingi nchini zina mashamba makubwa na viwanda vya uzalishaji wa bidhaa mbalimbali? Kuna umuhimu gani wa kuwaweka wafungwa magerezani kisha iingie gharama kubwa ya kuwatunza wafungwa hao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na ucheleweshaji mkubwa wa upelelezi wa kesi mbalimbali nchini. Jambo hili limekuwa likichelewesha kesi nyingi kuamuliwa mahakamani. Ni kwa nini kesi hizo zisiwekewe muda maalum ili ikifikia muda huo, basi kesi hiyo iweze kufutwa kwani haina ushahidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwepo na kesi mahakamani kwa muda mrefu kwa kukosa upelelezi, jambo ambalo linaashiria rushwa na kuwanyima haki raia wema. Hata hivyo, wakati mwingine kuchelewa kwa kesi nyingi ni kutokana na matamko ya kisiasa, kwani wako viongozi wanaowaweka ndani bila maelezo ya kutosha na kuwaamuru askari kuwa hakuna kumwachia huru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutekwa na kupotea watu, kumekuwa na matukio mengi nchini ya kutekwa na kuuawa kwa watu wetu, lakini jeshi la polisi na watu wa usalama wako kimya sana na siyo jeshi la polisi tu, hata viongozi waandamizi ndani ya Wizara hii wamekuwa kimya sana katika hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matukio ya mauaji nchini sasa limekuwa ni jambo la kawaida. Cha kusikitisha zaidi ni pale Jeshi la Polisi linapohusishwa na mauaji hayo na huku wengine wakibambikiziwa kesi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi hili pia linahusishwa na utekaji nyara wa raia wema kwa kisingizio cha taarifa za intelejensia. Jambo hili kama wasemaji wanakuwa kimya jamii huamini kinachoandikwa kwenye mitandao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa upatikanaji wa vitambulisho vya Taifa ni mgumu sana na watu wengi bado hawaelewi kinachofanyika kwani ni zoezi linalochukua muda mrefu sana na wala hatujui zoezi hili litakwisha lini. Kila mwaka fedha nyingi zinatengwa kwenye mradi huu lakini utekelezaji wake ni mdogo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vitendea kazi vya Jeshi la Polisi, kumekuwa na uhaba mkubwa wa vitendea kazi katika Jeshi letu la Polisi hasa upande wa magari, mfano Wilaya ya Liwale haina gari la polisi, Wilaya yenye kata 20, tuna gari moja tu. Ikumbukwe kuwa Wilaya ya Liwale ina kituo kimoja tu cha polisi, hivyo kulingana na Jiografia ya Liwale gari la polisi ni muhimu sana hasa kwa Tarafa za Kibutuka na Makata ambako hakuna vituo vya Polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Polisi kuzuia mikutano, kumekuwa ni jambo la kawaida sasa Jeshi la Polisi kuzuia mikutano bila sababu japo Sheria haisemi hivyo. Kwani Sheria inawataka watoe ulinzi kwani hata hao wanaoomba kufanya mikutano wajibu wao ni kutoa taarifa polisi na si kuomba kibali cha polisi, hivyo polisi kuzuia mkutano husika ni kukiuka sheria na kuwanyima raia kupata taarifa mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, polisi kutumia nguvu kubwa, kumekuwa na matumizi makubwa sana katika kuwakamata washtakiwa au watuhumiwa japo bado hawajathibitika kufanya kosa analotuhumiwa nalo. Matumizi haya ya nguvu pasipohitajika yamekuwa yakiwaletea hasara kubwa raia kwa kupoteza mali zao na hata wengine viungo vyao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo ya nguvu hizi ni kuwafanya raia wachukie Serikali yao na Jeshi la Polisi kwa ujumla wake. Watuhumiwa wengi hufika vituoni wakiwa na majeraha makubwa na wengine kuibiwa mali zao.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa uongozi wake mahiri katika kuzisimamia rasilimali za nchi yetu ili ziweze kuwanufaisha wananchi wa nchi hii bila kujali tofauti ya itikadi, dini, kabila, rangi na mipaka ya kikanda. Ama kwa hakika kwa namna Serikali ya Awamu ya Tano inavyotekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ni Serikali ya kupigiwa mfano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ya kielelezo inayotekelezwa nchini ni kielelezo tosha cha kuonesha dhamira ya Rais ya kuona Tanzania mpya, Tanzania ya uchumi wa kati na Tanzania ya viwanda. Miradi kama reli ya SGR, umeme wa maporomoko ya Rufiji, ununuzi wa ndege, ujenzi wa viwanja vya ndege, ujenzi wa barabara za juu Jijini Dar es Salaam, ujenzi wa Hospitali za Wilaya na vituo vya afya, ni mifano michache ya Tanzania mpya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu vitambulisho vya wajasiriamali, naomba visigawiwe kwa idadi sawa kwa kila Wilaya. Ziko Wilaya ambazo zina wajasiriamali wachache, Wakuu wa Wilaya wanalazimika kuwakopesha watu ambao hawana uwezo wa kupata hata hiyo Sh.20,000 na kuwa kero kwa wananchi wanyonge kwani Mkuu wa Wilaya analazimika kumaliza hivyo vitambulisho vya wajasiriamali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu sheria au kanuni za uendeshaji ni bora zikafanyiwa mapitio kwani zingine tayari zimepitwa na wakati. Mfano kwenye zile Halmashauri zinazoongozwa na upinzani, Diwani akikiuka kanuni fulani, Mwenyekiti ana madaraka ya kumtoa nje au adhabu nyingine lakini inapotokea Mwenyekiti amevunja kanuni, kanuni au sharia hizo hazisemi chochote. Kwa namna hii baadhi ya Wenyeviti wanajifanya Mungu watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria ya wazee ni jambo muhimu sana. Ni muda mrefu sasa suala hili limekuwa likisemwa bila utekelezaji. Katika Wizara ya Afya hasa hospitali zetu nyingi, kuna vibao vyenye maneno kama “mpishe mzee” lakini ni mzee gani huyu tunayemzungumzia? Hivyo, umefika wakati sasa sheria hii ikaletwa hapa Bungeni ili hawa wazee wakatambuliwa na sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Liwale ni ya zamani sana ina umri wa miaka 43 lakini haina jengo hata moja la kuitambulisha Wilaya hiyo. Mfano, haina jengo la Mkuu wa Wilaya; jengo la Mahakama ya Wilaya; jengo la Polisi Wilaya na jengo la Hospitali ya Wilaya. Taasisi zote hizo nilizozitaja, zinatumia majengo ya iliyokuwa Tarafa ya Liwale Mjini ndiyo walirithi majengo hayo na kwa kuwa ni ya Tarafa yanashindwa kukizi mahitaji ya ofisi hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Ilani ya CCM ya 2015-2010 barabara za Nachingwea - Liwale na Nangurukuru - Liwale zimeelezwa kuwa ni miongoni mwa barabara zitakazofanyiwa upembuzi na usanifu wa kina. Hivyo, naomba kwa bajeti hii jambo hili litekelezwe. Sambamba na hili, Mikoa ya Morogoro na Lindi bado haijaunganishwa kwa barabara za kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria ya maliasili kuhusu kifuta machozi kwa waathirika wa majanga yanayotokana na wanyamapori kama vile kuliwa mazao yao au kujeruhiwa nashauri ifanyiwe marekebisho. Bora sasa waathirika wakapewa fidia badala ya kile kinachoitwa kifuta machozi ambacho hakitolewi kwa wakati, sheria hii imepitwa na wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kuongeza kasi ya ulipaji wa madeni kwenye taasisi zake. Zipo taasisi zinazoshindwa kujiendesha kwa kukosa mitaji, kwani fedha zao nyingi ziko Serikali Kuu (Hazina). Yako Mashirika na taasisi zinazoidai Hazina fedha nyingi kiasi cha Mashirika hayo kushindwa kujiendesha. Pia, taasisi zingine zingefutiwa madeni yaliyopitwa na wakati na hayalipiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya kilimo inaajiri wananchi wengi sana. Kwa hiyo, Serikali inatakiwa kuipa kipaumbele sana. Hapa mkazo mkubwa uwe kwenye utafutaji wa masoko na uwekezaji katika uchakataji wa mazao ya kilimo. Wakulima wengi hivi sasa wanashindwa kuchagua wajikite na mazao gani kwani bei za mazao zimekuwa zikibadilika mwaka hadi mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, mwaka huu korosho zikishuka wakulima wanahamia kwenye ufuta. Mwaka unaofuata ufuta ukishuka, wakulima wanahamia kwenye mbaazi na mbaazi zikishuka wanahamia kwenye alizeti. Hivyo, nashauri Serikali ijikite kwenye kuimarisha masoko. Hii ndiyo changamoto kubwa sasa kwenye kilimo kuliko hata changamoto za pembejeo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nichukue nafasi hii siku ya leo kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuendelea kuniweka hai na afya njema na leo kunipa uwezo wa kutoa mchango wangu kwenye hoja hii. Pia nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Mheshimiwa Dkt. John J.P. Magufuli kwa kuliongoza Taifa letu kwa uadilifu mkubwa na kwa umahiri anaouonesha katika kusimamia rasilimali ya nchi yetu ili ilete manufaa kwa Watanzania wote. Uongozi unaozingatia, Katiba, usawa, haki, sheria na utu. Jambo linaloendelea kudumisha amani ya nchi yetu. Kwani hivyo ndivyo vielelezo vya amani yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nianze mchango wangu kwa kuishauri Serikali katika mambo yafuatayo:-

Kwanza, Watumishi wa Umma; kumekuwa na uhaba mkubwa sana ya watumishi katika Idara mbalimbali za Sekta ya Umma kama vile afya, elimu, ugani, Mahakama na kadhalika. katika idara nyingi za umma watumishi wengi wamekuwa wakikaimu, nafasi mbalimbali za utumishi, nafasi hizi wanakaimu kwa muda mrefu kiasi cha kuwapunguzia ufanisi katika suala la upungufu wa watumishi. Mfano Wilaya ya Liwale ina upungufu kama ifuatavyo:-

(a) Walimu shule za Msingi upungufu 298;

(b) Afya zahanati na vituo vya afya 261; na

(c) Maafisa Ugani upungufu ni 28.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hawa wachache waliopo, kuna ucheleweshaji mkubwa wa kupandishwa madaraja na pale wanapopandishwa madaraja mishahara mipya huchelewa kutolewa. Hivyo kupelekea Serikali kuwa na madeni mengi au makubwa.

Pili, ni TASAF; nashauri Serikali kufanya utafiti wa kutosha ili wale walionufaika na kuonekana wameshatoka kwenye kaya maskini ili waweze kuondolewa na wengine kupewa hizo nafasi, kwani bado ziko kaya nyingi zenye uhitaji hazijafikiwa na utaratibu huu. Vilevile Serikali ione umuhimu wa kuendelea kushirikisha wanufaika wa TASAF kwenye kubuni miradi mbalimbali, kwani iko miradi iliyoshindwa kufikia mafanikio tarajiwa kutokana na miradi kutokuwa shirikishi kwa wanufaika.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika dhana ya utawala bora Serikali ione umuhimu wa mafunzo kwa wateuliwa wapya juu ya majukumu yao. Uzoefu unaonyesha mara wateule hao wanapotekeleza majukumu yao wengine wanashindwa kujua mipaka ya majukumu yao. Aidha, Serikali ione umuhimu wa kuimarisha au kuboresha Chuo cha Utumishi wa Umma, sambamba na hilo kuwe na utaratibu wa kila mtumishi wa umma awe amepitia kwenye Chuo hicho hata kwa angalau miezi mitatu (3) iwe mara baada ya kuajiriwa au kuteuliwa kwa nafasi au ajira husika. Kama ilivyo kwa Chuo cha Utumishi wa Umma vilevile Serikali ione umuhimu wa viongozi kwenye ngazi mbalimbali wawe pia wamepata mafunzo ya uongozi. Kozi au mafunzo hayo, yatawajengea watumishi au viongozi hao kufanya kazi kwa uzalendo, utaifa na ufanisi mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba Idara ya Polisi na Mahakama kuonekana ina tatizo kubwa la rushwa, lakini rushwa iliyoko kwenye Idara ya Uhamiaji ni ya hatari zaidi na idara hii rushwa zake ni ngumu sana kuzigundua, pamoja na madhara yake ni makubwa sana. kama ilivyo kwa Idara ya Uhamiaji, vilevile Idara/Wizara ya Uwekezaji inakuja kwa kasi kubwa sana jambo linalopunguza ari kwa wawekezaji wa ndani na nje. Hivyo nashauri Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini kutupia macho sana taasisi hizi mbili nilizozitaja hapo juu. Sababu ya kutamalaki kwa rushwa kwenye Taasisi hizi ni kutokana na sababu kuu mbili:-

(1) Upungufu wa watumishi kwenye idara hizo; na

(2) Urasimu mkubwa uliopo unaotokana na watumishi wengi kushindwa kutoa maamuzi hata yale yaliyo chini au ndani ya uwezo wao, hivyo kufanya hali ya njoo kesho, njoo kesho zinakuwa nyingi na kutengeneza mazingira ya rushwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa, napenda kutoa pongezi kwa wateule wote katika Wizara hii wakiongozwa na Waziri mwenye dhamana pamoja na Naibu wake, bila kusahau, viongozi wa taasisi zote zilizo chini yake, kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kulitumikia Taifa hili kwa weledi mkubwa. Kazi hii ya kutukuka inathibitishwa na amani na utulivu uliopo hapa nchini. Kwani ni jambo lililo wazi hakuna amani wala utulivu, mahali ambapo hakuna utawala bora.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ambariki Rais Mheshimiwa Dkt. John J. P. Magufuli.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze mchango wangu kwa kumshukuru Mungu kwa kunipa uhai na kuniwezesha kushika kalamu na kuchangia hoja hii. Pia napenda kuipongeza Serikali kwa kuja na hoja ya kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastic nchini. Kwa hili, pongezi kwanza zimwendee Mheshimiwa Waziri Mkuu kwani yeye ndiye kwa kwanza kuja na tamko hili. Vilevile, nampongeza Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana kwa kuona umuhimu wa jambo hili na kuamua kuchukua hatua, tena niseme hatua hii imecheleweshwa sana hapa nchini, kwani athari za kimazingira juu ya matumizi ya mifuko hii ya plastic ni kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nizungumzie uharibifu wa mazingira utokanao na shughuli za kibinadamu kama vile kilimo cha kuhamahama, biashara ya mazao ya misitu na ujenzi wa miundombinu mbalimbali za kimaendeleo. Mfano, katika Wilaya ya Liwale, Wilaya hii imezungukwa na misitu ya asili; na kwa kuwa huko nyuma hali ya miundombinu ya barabara ilikuwa siyo mizuri, uharibufu wa misitu hii haukuwa mkubwa sana lakini kwa sasa uvunaji wa magogo, mbao na mkaa ni biashara inayokua kwa kasi sana na ni uvunaji usiozingatia sheria na kuwaachia wananchi wa Liwale jangwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiasi cha ushuru Halmashauri inachopata hakiwezi kurudisha uoto wa asili wa misitu hiyo kwani miti imekuwa ikipandwa pembeni mwa majengo ya taasisi za Umma kama shule, hospitali na kadhalika, lakini kule ambako miti hii imekatwa kunabaki kuwa jangwa. Hivyo, napendekeza Wizara ya Maliasili na Wizara ya Mazingira zikafanye kazi kwa pamoja kutafuta namna bora ya kuona misitu au miti inarudishiwa kupandwa pale mti ulipokatwa na Ikiwezekana fedha za upandaji miti ziongezwe na zikasimamiwe moja kwa moja na Halmashauri husika. Kiasi cha asilimia tano cha sasa kinachotokana na uvunaji wa mazao ya misitu kifanyiwe marekebisho ili kiendane na aina au kiasi cha uharibifu unaotokea, hivyo Halmashauri iweze kupanda miti ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu zaidi inahitajika juu ya utunzaji wa mazingira hasa kwenye utunzaji wa vyanzo vya maji. Ufugaji wa samaki pembezoni mwa mito ni bora ukapigwa marufuku, kwani mito mingi sasa imeanza kukauka baada ya watu kuchimba mabwawa ya samaki pembezoni mwa mito. Urinaji wa asali kwa njia za kizamani unachangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa misitu kwa kuchoma moto na kuharibu maisha ya viumbe vingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nichangie kidogo kuhusu Muungano wetu. Kwa kuwa Muungano huu ni wa muda mrefu, kizazi cha leo hakina uelewa wa kutosha kwa nini nchi hizi mbili; Tanganyika na Zanzibar ziliamua kuungana na faida za Muungano wetu na hivyo, kutambua dhamira ya Waasisi wetu. Ndiyo maana kizazi hiki kimeishia kuangalia changamoto tu za Muungano bila kuangalia faida zake kwa pande zote mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, nazishauri Serikali zote mbili za Muungano kuwekeza zaidi kwenye elimu ya kuelimisha jamii ya leo kuelewa Muungano. Pia pale panapotokea changamoto, basi Serikali zote mbili zichukue hatua za haraka kutatua changamoto hizo kabla hazijaota sugu na kuchafua sura nzuri ya Muungano wetu, tena nyingine zinapaswa zitatuliwe na ngazi za Taasisi za chini kama zile za Uhamiaji, TRA na ZRA. Hivyo, naiomba Serikali kulinda na kudumisha Muungano huu kwa gharama yoyote ile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nizungumze juu ya uchafuzi wa mazingira unaofanywa na viwanda vinavyotoa moshi au vumbi mawinguni. Jambo la viwanda vinavyorusha moshi angani na teknolojia iliyopitwa na wakati huchangia kwa kiwango kikubwa uchafuzi wa hali ya hewa ikiwa ni pamoja na magari yanayotoa moshi kupita kiwango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vinavyotoa moshi nashauri viwe vinatozwa tozo za uchafuzi wa mazingira ili iwe kama ni juhudi za kulinda mazingira, kwani sasa nchi za wenzetu viwanda hivi sasa haviko tena na pale vilipo, teknolojia yake haitoi tena huo moshi. Hivyo basi, imefika wakati sasa kuazima teknolojia hiyo ili kulinda mazingira yetu. Viwanda hivi ni kama vile vya cement, chuma na viwanda vya nafaka kama ngano na vile vya kuchakata kokoto na Marumaru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mara nyingine tena naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa hatua mbalimbali katika kuhakikisha haki na utu wa kila Mtanzania unathaminiwa kwa kuimarisha Wizara hii muhimu katika kusimamia usawa na upatikanaji wa Hakimu katika kutafasiri katiba na sheria mbalimbali.

Hata hivyo, nawapongeza pia wateule wote walioko chini ya Wizara hii wakiongozwa na Mheshimiwa Waziri Augustine Mahiga bila kuwasahau watumishi wote walioko katika Wizara hii.

Mmheshimiwa Mwenyekiti, ni Sera ya Taifa kuwa kila kata nchini iwe na huduma ya Mahakama ya Mwanzo na kila Wilaya kuwa na Mahakama za Wilaya, lakini katika Wilaya la Liwale pamoja na kuwa ni Wilaya ya siku nyingi, tangu mwaka 1975 Wilaya hii ina Kata 20 lakini ina Mahakama mbili tu ya mwanzo, yaani ile ya Liwale mjini na ya kata ya Kibutuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Wilaya ya Liwale hadi leo haina jengo la Mahakama ya Wilaya. Jengo linalotumiwa ni lile lililokuwa la Mahakama ya Mwanzo ya Liwale Mjini. Upo uhitaji mkubwa sana wa jengo la Mahakama Wilayani Liwale, sambamba na uwepo wa watumishi wa kutosha. Wilaya pia inahitaji kuwa na Mahakama ya Mwanzo kwenye Kata za Lilombe na Miruwi kwa kuwa kata hizo zina shughuli mbalimbali za uchumi ikiwepo uchimbaji wa madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwezo wa watumishi wa Idara ya Sheria ni mdogo sana jambo linalosababisha Halmashauri zetu kuingia mikataba isiyo na tija na kuzisababishia Halmashauri kuingia kwenye migogoro ya kisheria mara kwa mara. Pia watumishi hawatoshi, kuwepo kwa mwanasheria mmoja kwenye Idara ya Sheria kunapunguza ufanisi kwenye Idara ya Sheria na Halmashauri zetu. Mfano Wilaya ya Liwale ina mtumishi mmoja tu kwenye idara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tume ya Kurekebisha Sheria ni bora ikafanya mapitio ya sheria mbalimbali mara kwa mara kwani zipo sheria nyingi zinazohitaji kufanyiwa mapitio. Ili zifanyiwe marekebisho ziendane na wakati uliopo kwani kuwepo kwa sheria zilizopitwa na wakati ni kuwapora haki wananchi. Mfano sheria inayoruhusu Serikali kumkamata tena mtuhumiwa aliyefutiwa mashtaka na Hakimu baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kushindwa kupeleka mashahidi Mahakamani, ni sheria inayojaza mahabusu kwenye Magereza zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria nyingine ni ile ya maliasili kuhusu kifuta machozi kwa waathirika wa kushambuliwa au mashamba kuliwa na wanyama waharibifu. Ni bora sasa wakapewa fidia badala ya hicho kinachoitwa kifuta machozi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Mwendesha Mashitaka Mkuu imekuwa ni sababu kubwa ya kulundikana kwa mahabusu nyingi; imekuwa ikishindwa kupeleka majalada mbalimbali Mahakamani, hapa ndipo hadi sasa pana rushwa kali sana. Ili jalada lifike Mahakamani, ni lazima mhusika atoe chochote hasa zile kesi kubwa kubwa. Ofisi hii pamoja na changamoto za kifedha, bado kuna utendaji usiozingatia misingi ya Utumishi wa Umma. Ndiyo sababu ya Mahakimu kufuta mashitaka na Mwanasheria Mkuu kuwakamata tena kwa sheria niliyoitaja hapo juu. Wapo mahabusu wengi kwenye Magereza nchini wakisubiri majalada toka kwa DPP.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwamba Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ni vyema ikawa na Wanasheria waliobobea kwenye fani ya sheria na wanaoijua jamii ya Watanzania na mazingira halisi ya nchi yetu, kwani Miswada mingi inayoletwa Bungeni kwa ajili ya kutungiwa sheria na mengine kukosa kabisa uhalisia kiasi cha kudhani watu wanaoandaa Miswada hiyo sio watu wanaotoka katika jamii yetu; kiasi cha kufanya Miswada inayoletwa na Serikali kufanyiwa marekebisho na Bunge pengine ni kwa asilimia zaidi ya 80. Hili huchangia kulifanya Bunge kutunga sheria inayodumu kwa muda mfupi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, kwa hekima na busara kubwa, napenda kuchukua fursa hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na kuniwezesha kushika kalamu na kutoa mchango wangu kwenye Wizara hii muhimu kwa ustawi wa maisha ya jamii yetu.

Mheshimiwa Spika, nianze mchango wangu kwa kuwapongeza Mawaziri wote wanaohudumu kwenye Wizara hii sambamba na watumishi wote walioko kwenye Wizara hii. Pongezi za kipekee kwa askari wetu wa usalama barabarani kwa kazi nzuri wanayoifanya. Japo wapo askari wanaolitia doa Jeshi la Polisi kwa kupenda kwao vipesa vidogo vidogo, ushauri wangu kwa hao wachache wanaochafua jeshi letu ni basi wakadhibitiwa ipasavyo na pale wanapobainika basi adhabu kali iwe juu yao.

Mheshimiwa Spika, nijielekeze kwenye makazi ya Askari Polisi na Magereza. Makazi ya askari wetu bado ni mabaya sana hasa kwa askari wa mikoani na kwenye magereza za pembezoni. Mfano, Wilaya ya Liwale ni wilaya ya tangu mwaka 1975 lakini hadi leo haina jengo la kituo cha polisi wala nyumba za askari licha ya halmashauri kutenga eneo zaidi ya heka 60. Jengo wanalolitumia ni jengo la nyumba ya mtu binafsi. Kitendo cha polisi kukaa uraiani kunawapunguzia weledi wa kazi yao. Pamoja na hivyo lipo pia Gereza la Kipule ambalo lilianzishwa tangu mwaka 1982 lakini hadi leo eneo linalomilikiwa na gereza hili halijalipiwa fidia toka kwa wananchi. Gereza hilo pia hadi leo lina majengo ya udongo na uzio wa miti na kufanya wale wafungwa sugu au wa muda mrefu kulazimika kupelekwa Lindi.

Mheshimiwa Spika, vitendea kazi vya askari polisi; Wilaya ya Liwale imezungukwa na misitu, ni wilaya yenye mtawanyiko mkubwa lakini kuna uhaba mkubwa wa gari la askari polisi. Pamoja na mwaka huu kuletewa gari la Canter nalo ni kubwa linashindwa kuingia kwenye barabara za vijiji au vichochoroni. Hata hivyo napashwa kwa niaba yao nishukuru kwa hilo gari kwani ni hatua moja ya kutatua matatizo la usafiri kwa Polisi wa Wilaya ya Liwale. Ni matumaini yangu Serikali inaona umuhimu wa kuwa na gari la polisi sambamba na nyumba za askari.

Mheshimiwa Spika, katika Idara ya Uhamiaji bado kazi zao wanafanya kizamani sana, bado hawaendi na kasi ya Mheshimiwa Rais. Bado habari ya njoo kesho, njoo kesho ni nyingi hasa kwa raia wanaoomba uraia wa nchi yetu kwa wale wageni wa muda mrefu. Ni bora mwombaji apewe majibu mapema kama anaweza kupata au amekosa sifa za kupata uraia basi ni bora akafahamishwa. Kuacha kumpatia majibu kwa muda mrefu kunajenga mazingira ya rushwa. Ni bora Uhamiaji wakawa wazi kama mtu anakosa sifa za kupata hati ya uraia.

Mheshimiwa Spika, kikosi cha Zimamoto, ni kikosi muhimu sana kwa ulinzi wa mali zetu na ulinzi wa maisha yetu ya kila siku, lakini jeshi hili halijapewa umuhimu unaostahili. Jeshi la Zimamoto hawana magari ya kutosha na vifaa vya kukabiliana na majanga ya moto.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo ziko wilaya ambazo hazina kabisa Jeshi hili la Zimamoto. Mfano Wilaya ya Liwale hakuna Askari hata mmoja wa Zimamoto na hivyo hata raia wa Liwale hawana uelewa wa kutosha juu ya kukabiliana na majanga ya moto, lakini wafanyabiashara bado wanalipa kodi ikiwemo ya zimamoto. Je, wanalipia huduma gani wakati hakuna ofisi ya zimamoto. Je, Mheshimiwa Waziri haoni kuwa watu hawa wanalipia huduma ambayo hawatarajii kuipata?

Mheshimiwa Spika, mimi mpaka leo sioni faida ya watu kukaa magerezani kama wafungwa. Kwa nini wafungwa wawe mzigo kwa Taifa kwa kuwalisha bila wao kujitegemea. Nilitarajia kuona magereza yetu yakijitegemea, huko nyuma, magereza mengi yalikuwa na mashamba makubwa ya mazao ya chakula. Pia kulikuwa na viwanda vya kusindika mazao ya wakulima na kadhalika. Vilevile kulikuwa na viwanda vya mazao ya mifugo na uvuvi na mazao ya misitu. Kwa ushauri wangu kama magereza haziwezi kujitegemea hakuna haja ya kupeleka wafungwa magerezani na hivyo Serikali itafute njia nyingine ya kuwarekebisha wahalifu au wafungwa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuanza mchango wangu kwa kuwapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Makatibu wote wanaohudumu kwenye Wizara hii kwa kazi nzuri na kubwa ya kusimamia elimu nchini, hasa Sera hii ya Elimu Bure. Sera hii imewezesha watoto wengi kupata elimu ambayo ni haki yao ya msingi.

Mheshimwia Mwenyekiti, pia napenda kumshukuru kwa dhati Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, kwa kufanya maamuzi muhimu ya kutekeleza Sera hii ya Elimu Bure ambayo ni hitaji la nchi yetu kwa muda mrefu. Kwa hili Mheshimiwa Rais amethubutu na amefanikiwa kwa ufanisi mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa sasa Taifa letu linaelekea kwenye uchumi wa viwanda, ipo haja kubwa sana ya kuimarisha vyuo vya ufundi kuanzia vile vya VETA hadi vya mafundi mchundo (FTC). Katika kuimarisha vyuo hivi ni bora vyuo vya ufundi visichanganywe na kozi nyingine kama vile kozi ya urembo na ulimbwende. Jambo hili limekuwa likivunja hadhi ya vyuo vyetu. Vilevile, Vyuo vya VETA visiwe kimbilio la wale waliofeli Form Four na Darasa la Saba, ifike wakati hata wale waliofanya vizuri kwenye masomo ya Sayansi wapelekwe VETA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Liwale ndiyo wilaya iliyo mbali sana na Makao Makuu ya Mkoa wa Lindi ambako kuna Vyuo vya VETA, Ualimu na Afya. Hivyo, vijana wengi wanashindwa kumudu kupata elimu ya vyuo hivyo. Hivyo Serikali ione umuhimu wa kutujengea Chuo cha Ufundi, VETA. Halmashauri imeshaanza kujenga maboma mawili ya madarasa, hivyo naiomba Serikali kuokoa nguvu za wananchi kwa kuwapatia Chuo cha VETA. Vijana wengi wanaoshindwa kuendelea na masomo ya juu kwa kukosa nafasi wangeweza kupata elimu hiyo ya VETA kwa karibu badala ya kwenda Lindi ambako ni mbali na gharama ni kubwa. Liwale tuna uhitaji mkubwa wa Chuo cha VETA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanafunzi wa vyuo vya ufundi ni muhimu sana kuhudhuria mafunzo kwa vitendo, lakini wanafunzi wengi wanashindwa kuhudhuria kikamilifu kutokana na changamoto mbalimbali, kama vile nauli za kwenda na kurudi makazini na chakula cha mchana wanapofanya kazi viwandani. Naomba Serikali ifikirie kuwapatia posho za mafunzo viwandani wanafunzi wanaohudhuria mafunzo kwa vitendo. Hakuna maana ya kuwapeleka watoto katika shule/chuo cha ufundi kama elimu hiyo haitaambatana na elimu kwa vitendo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nizungumzie uhaba wa walimu, hasa walimu wa Sayansi. Hapa napenda nianze kwa kuishukuru Serikali kwa kuanza kuajiri walimu. Nishukuru kwa Halmashauri yangu ya Liwale kuwa miongoni mwa Halmashauri zilizopata mgao wa walimu hao japo limekuwa kama tone la damu baharini, kwani uhaba wa walimu ni mkubwa sana Wilayani Liwale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule zetu nyingi zina walimu watatu tu. Shule zenye walimu wengi ni zile zenye walimu wanne. Hata pale RAS anapotaka kufanya mgawazo wa watumishi mkoani anakosa rasilimali fedha ukizingatia katazo linalomkataza RAS kuhamisha mtumishi bila ya kuwa na fedha. Hivyo, naishauri Serikali kutenga fedha mara kwa mara kwa ajili ya kufanya mgawazo kwa walimu hata pale panapokuwa na umuhimu wa kufanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kitengo cha Udhibiti Ubora wa Elimu ni kitengo muhimu sana. Ili kuwe na elimu bora, naishauri Serikali kuongeza uwekezaji katika kitengo hiki kuanzia ikama ya watumishi hadi vitendea kazi ikiwa ni pamoja na magari. Mfano, katika Halmashauri yangu ya Liwale, kitengo hiki hakijawahi kuwa na gari japokuwa mtawanyiko wa kata na shule zetu ni mkubwa sana. Zipo shule hazijawahi kuona Wakaguzi kwa zaidi ya miaka mitano. Ukiuliza watasema hawana usafiri hata wa pikipiki. Hivyo, naiomba sana Serikali kutupatia gari litakalowawezesha wakaguzi na idara ya elimu kwa ujumla. Hadi sasa Idara ya Elimu Msingi na Sekondari wote hawana magari, hali ni mbaya sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali ikaitazame Liwale kwenye Idara ya Elimu ili tutoke kwenye kuburuza mkia kwa Mkoa wa Lindi na Taifa kwa ujumla.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunifikisha kwenye kipindi hiki cha Ramadhani ya mwaka huu, kwani wapo tuliofunga nao mwaka jana, 2018 leo wako mbele ya haki na wengine wameshindwa kushiriki Ramadhani hii kwa hali na maradhi mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa leo naomba nianze mchango wangu kwanza kwa kumshukuru Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Manaibu Makatibu Wakuu na Watendaji wote kwenye wizara hii kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhudumia jamii yetu kwenye sekta hii muhimu ya kulinda afya zetu. Namwomba Mungu awape umri mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kumshukuru Mheshimiwa Waziri kwa bajeti ya mwaka 2018 kwa kunipa watumishi 80 wa Sekta ya Afya, lakini kutokana na uhaba mkubwa tulionao watumishi wale wamekuwa kama tone la damu baharini. Bado Hospitali ya Wilaya ya Liwale yenye wodi nne zinahudumiwa na mhudumu mmoja tu kwa shift ya usiku kutokana na uhaba wa watumishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nitoe shukrani kwenye bajeti hii kwani wilaya yetu imetengewa shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya, maana ile iliyopo ilikuwa ni kituo cha afya, hivyo kushindwa kukidhi hadhi ya kuitwa Hospitali ya Wilaya. Ombi langu ni fedha kuja kwa wakati ili ujenzi huu uanze.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na ujenzi wa Hospitali ya Wilaya na vituo viwili vya afya vya Mpengerewa, Kibutuka, bado Halmashauri ya Liwale inakabiliwa na uhaba mkubwa sana wa gari la wagonjwa (ambulance). Jiografia ya Liwale yenye vijiji 76 ni ngumu sana. Hivyo, namna ya kuwafikisha wamama hasa wajawazito ni ngumu sana, ukizingatia kuwa zahanati zetu hazina wataalamu na vifaa vya kutosha. Kwa hiyo, uhitaji wa gari la wagonjwa ni mkubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kupunguza mlundikano wa wagonjwa kwenye hospitali na zahanati zetu, wakati sasa umefika wa kuimarisha kada ya Mabwana na Mabibi Afya kwenye Kata na Vijiji vyetu. Watumishi hawa ni muhimu sana kwenye jamii zetu. Waswahili husema, “kinga ni bora kuliko tiba.” Elimu ya afya ikiwafikia wanajamii juu ya kutunza afya zetu na mazingira yetu kwa ujumla tutaepuka magonjwa ya mlipuko. Kada hii ya Mabwana/Mabibi Afya ni kama imesahauliwa kwa sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ajira kwa watoto ni jambo linalotishia maisha ya watoto wetu kwani kila kukicha bado ongezeo la ajira kwa watoto mitaani linaongezeka siku hadi siku hasa kwa mijini. Wako watoto wanaosukuma baiskeli kuwatembeza watu wenye ulemavu wa viungo na wasioona kwenye shughuli zao za kuombaomba. Vilevile wako watoto wanaotumwa na wazazi wao kwenda mitaani kupita kuombaomba. Hivyo, naiomba Wizara kuja na mkakati maalum wa kukomesha ajira hizi za watoto na kuwaondoa watoto wanaoombaomba mitaani.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Wananchi wa Tanzania kukosa kuwaingiza kwenye mpango wa Bima za Afya (NHIF) ni kutokuwatendea haki, kwani familia za Maaskari wetu zimekuwa zikihangaika sana hasa zile familia zinazoishi uraiani. Pamoja na kazi ngumu wanazofanya za kulinda nchi yetu, lakini bado hawana uhakika wa afya zao na familia zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sera ya Wazee nchini ni changamoto kubwa hapa nchini kwani hadi leo Serikali haitaki kuleta Sheria ya Wazee ili kuweza kutambua hao wazee. Pamoja na kuwa na matangazo sehemu mbalimbali kama vile “Pisha Mzee”, “Wazee Kwanza”, matangazo ambayo yanashindwa kuwatambua wazee hao, kwani hakuna sheria inayowatambua; kwa nini Serikali inakuwa na kigugumizi cha kuleta Sheria ya Wazee hapa Bungeni ili wazee hawa waweze kutambuliwa? Tukumbuke kuwa sisi sote ni wazee watarajiwa. Hivyo, hiki tunachokifanya ni kujikaanga kwa mafuta yetu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, naomba nianze mchango wangu kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa uhai na afya njema. Pia, nachukua fursa hii kuwapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu, Naibu Makatibu Wakuu, Wenyeviti wa Bodi zote zilizoko kwenye Wizara hii na Wakurugenzi Watendaji wote wa Taasisi zote zilizopo kwenye Wizara hii kwa kazi kubwa ya kumsaidia

Mheshimiwa Rais katika kuwatumikia Watanzania. Nawaombea dua kwa Mwenyezi Mungu awape umri mrefu ili waweze kutimiza ndoto ya Mheshimiwa Rais ya kuona Tanzania mpya. Mwenyezi Mungu awabariki sana.

Mheshimiwa Spika, Barabara ya Nachingwea – Liwale ni barabara muhimu sana kwa Wilaya ya Liwale, kwani ndiyo barabara pekee inayoiunganisha Wilaya ya Liwale na Makao Makuu ya Mkoa wa Lindi. Naishukuru Serikali kwa kuanza upembuzi na usanifu wa kina kwa barabara hii. Nashauri kazi hii iambatane na utafutaji wa fedha ili kuweza kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, Barabara ya Nangurukuru – Liwale ni barabara ya kiuchumi kwa Wilaya ya Liwale. Usafirishaji wa mazao kutoka Liwale hadi Dar es Salaam kupitia Lindi kuna kilometa zaidi ya 750 ukilinganisha na kilometa 500 ukipitia barabara ya Liwale to Nangurukuru. Hivyo, utaona umuhimu wa barabara hii ni mkubwa sana kwa uchumi wa Wana-Liwale na nchi kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, nashukuru tena kuona kwenye bajeti hii kumetengwa shilingi milioni 300 ili kuanza upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kama ilivyo barabara ya Nachingwea – Liwale. Hii pia Wizara ianze kutafuta fedha ili hatimaye nayo pia iweze kujengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mawasiliano, nashukuru kwa kupatiwa mawasiliano kupitia kampuni ya Halotel kwa kutujengea minara kwenye kata tisa ambapo sasa kwa kiwango kikubwa upo unafuu kidogo, lakini bado kuna shida ya mawasiliano katika Vijiji vya Ndapata, Mkutano, Kikulyungu, Nahoro, Kipelele, Mtungunyu na Mtawatawa. Vijiji hivi hali ni mbaya sana katika mawasiliano ya simu.

Mheshimiwa Spika, Reli ya TAZARA bado ni reli muhimu sana kwa nchi yetu. Kwa upande wa Zambia wao kwa reli hii siyo kipaumbele chao tena pamoja na kuwa uongozi wa reli hii kwa kiasi kikubwa unamilikiwa na upande wa Zambia. Wazambia wamekuwa wakifanya vitendo vya kuhujumu reli hii kwa makusudi. Hivyo basi, imefika wakati Serikali yetu ifanye mapitio ya Sheria ya Uendeshaji wa Reli ya TAZARA. Hatua hii ni muhimu na iende sambamba na kuifutia madeni au kuipa mtaji ili iweze kujiendesha.

Mheshimiwa Spika, Chuo cha Mabaharia (DMI) ni chuo kilichosahauliwa kwa muda mrefu ndiyo maana uwepo wa chuo hiki hata kwa jamii hautambuliwi pamoja na kuwa nchi yetu imezungukwa na bahari na maziwa makuu. Sekta ya Uvuvi na Usafiri wa Majini una mchango mdogo katika nchi yetu kutokana na kupuuza chuo hiki muhimu kwa uchumi wa nchi yetu. Nashauri Serikali ianze sasa kuimarisha chuo hiki ikiwa ni pamoja na kukitangaza, kwani sasa chuo hiki hakitambuliwi katika jamii ya Watanzania.

Mheshimiwa Spika, Chuo cha Usafirishaji (NIT) ni chuo muhimu sana kwa sasa, hasa kwa kuwa nchi yetu inakwenda kuimarisha Sekta ya Uchukuzi kwa kujenga reli ya kisasa, ununuzi wa ndege na ujenzi wa meli kwenye maziwa makuu. Hivyo basi, Serikali ione umuhimu wa kuimarisha chuo hiki, kwani ndiyo chuo kinachokwenda kupika wataalam katika Sekta ya Uchukuzi. Chuo hiki ni lazima kipewe fedha za kutosha ili kiweze kujiimarisha kupata wataalam.

Mheshimiwa Spika, sera ya kuunganisha mikoa yetu kwa barabara za lami ni jambo linalopaswa kupewa kipaumbele kwa mikoa yote kwani bado kuna mikoa ambayo hadi leo haijaunganishwa siyo tu kwa barabara za lami, hata kwa barabara za changarawe. Mfano, Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Lindi, mikoa hii, pamoja na kuwa mikoa jirani lakini pia ni mikoa muhimu sana kwa kukuza uchumi wa mikoa hiyo miwili. Hivyo, naiomba Serikali kufanya kila iwezavyo kutekeleza sera hii ya kuunganisha Mikoa ya Lindi na Morogoro kwa barabara ya Liwale – Mahenge (Ulanga).

Mheshimiwa Spika, Uwanja wa Ndege wa Lindi, pamoja na kuwa moja ya viwanja vya zamani nchini, hakijapewa kipaumbele. Hii ni kudumaza maendeleo ya Mkoa wa Lindi sambamba na Bandari ya Lindi. Nashauri Bandari ya Uvuvi ya Kanda ya Kusini ikajengwe Lindi ili kuinua uchumi wa Mkoa wa Lindi.

Mheshimiwa Spika, kwa hayo yote hapo juu, naunga mkono hoja hii muhimu kwa uchumi wa nchi yetu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, leo naomba nianze mchango wangu kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kutoa mchango wangu kwa njia hii ya maandishi. Pia nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa dhamira yake ya kupeleka Tanzania kuwa na uchumi wa kati na nchi ya viwanda na dhamira hii tunaiona kwenye matendo yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza pia Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa kufanya kazi kwa bidii katika kusimamia Wizara hii, pamoja na watendaji wote katika Wizara hii. Hata hivyo, ninayo mambo ya kushauri katika kutimiza kauli mbiu hii ya Tanzania ya Viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kinachowavutia wawekezaji kuja kuwekeza ni utulivu, amani na usalama uliopo lakini mara wanapoonesha nia ya kuwekeza wanakumbana na vikwazo vingi sana ikiwa ni pamoja na utitiri wa taasisi za usimamizi kama vile TBS, OSHA, NEMC, TFDA, FIRE na nyingine kama hizi ambazo kwa uhalisia zote zinafanya kazi zinazofanana. Vilevile urasimu wa njoo kesho, njoo kesho imekuwa ni kikwazo kingine. Kazi ya wiki moja inachukua miezi mitatu hata mwaka mzima. Pia taasisi hizi bado zimegubikwa na rushwa kubwa kubwa na ndogo ndogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado bidhaa zinazozalishwa nchini zina bei kubwa kuliko zinazozalishwa nje. Hii inachangiwa kwa kiasi kikubwa na gharama za uzalishaji nchini kuwa kubwa, kunakochangiwa na wingi wa kodi, nishati ya umeme na mafuta lakini hili la urasimu linagharimu sana nchi yetu. Watu wanaogopa kufanya maamuzi pale wanapohitajika kufanya hivyo, aidha ni kwa kutaka rushwa au kwa kushindwa kuwajibika. Kazi ya kwanza ya Wizara hii ingekuwa ya kulea wafanyabiashara na wawekezaji wa viwanda lakini kinyume chake sasa imekuwa ni maadui wakubwa kwani mfanyabiashara anapokuja Wizarani anaonekana kama msumbufu, badala ya mdau wa maendeleo mwenye kiwanda ni adui wa taasisi zilizo chini ya Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ufungaji wa maduka ya wafanyabiashara na ufungaji wa viwanda haulingani na ufunguaji wa maduka na viwanda vipya. Hii maana yake ni kuwa mazingira ya kufanya biashara nchini ni magumu sana. Ipo haja ya Serikali kukaa pamoja na wafanyabiashara wenye viwanda kuangalia namna nzuri ya kufanya biashara nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kufungamanisha kilimo na viwanda ni jambo muhimu sana lakini utekelezaji wa jambo hilo siyo mzuri sana. Uchakataji wa mazao yetu ya kilimo bado ni wa kiwango cha chini sana. Bado wakulima wengi wakubwa na wadogo hawana masoko ya uhakika wa mazao yao. Hii ni kutokana na ukosefu wa viwanda vya kutosha vya kuchakata mazao hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa naishauri Serikali kama kweli ina nia ya kutekeleza sera hii ni lazima kupunguza masharti na urasimu kwa watu wanaoonesha nia ya kuanzisha viwanda vya kuchakata mazao yetu ya kilimo, uvuvi na ufugaji. Huwezi kufungamanisha kilimo na viwanda kama hakuna viwanda vya kutosha vya kuongeza thamani ya mazao yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, idadi ya wafanyakazi wa kigeni kwa mwekezaji wa nje bado halijakaa sawa, kuna malalamiko mengi sana kwenye sekta hii. Wako wawekezaji walio waajiri wageni bila ya kuwa na sababu maalum tena bila kufuata sheria. Viko viwanda hata madereva, vibarua, fundi saidia na wengine kama hao ni wageni.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia vipo viwanda au wawekezaji wanakataliwa kuajiri watu hao (wageni) hata wale walioko ndani ya sheria. Jambo hili limekuwa likihamasisha rushwa makazini. Serikali ifanye ukaguzi wa mara kwa mara viwandani ili kusimamia sheria hii kwani ajira nyingi zinakwenda kwa wageni, hivi sasa jambo hili limekuwa ni la kwaida sana Watanzania wazawa viwandani wamebaki kuwa vibarua wasiokuwa bali ajira ya mikataba.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Waziri wa Viwanda na Biashara awe mlezi wa wafanyabiashara na wenye viwanda na kusikiliza changamoto wanazopata. Si kweli kwamba wafanyabiashara wote ni wakwepa kodi na ni wezi, je kwa nini watu hawa wanakwepa kodi? Lazima Serikali ije na utafiti kwa nini wafanyabiashara wanakwepa kodi. Kulipa kodi kabla ya kuanza biashara si jambo jema, TRA waangalie vyema jambo hili. Kama ni sheria basi sheria hii iko kinyume na maelekezo wa nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa naishauri Serikali lazima tufanye mabadiliko makubwa ya kisera juu ya namna ya kufanya biashara na uwekezaji nchini kwani kuzilaumu taasisi zinazosimamia sheria hatuzitendei haki. Kama zinaonekana ni kikwazo basi ni bora sheria za kuanzishwa taasisi hizi zikaletwa hapa Bungeni tuzifanyie marekebisho ili kuondoa utitiri wa taasisi hizo maana wote tunakubaliana kuwa taasisi hizi ni kikwazo kikubwa kwa wawekezaji na wafanyabiashara.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, nianze kuchangia hoja hii kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha kushika kalamu na kutoa mchango wangu kwa njia ya maandishi. Kwanza nianze kwa kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri wote watatu pamoja na Makatibu wote kwenye Wizara hii bila kuwasahau Wakuu wa Taasisi zote zilizopo kwenye Wizara hii kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya kwa kipindi kifupi walichopewa kufanya kazi kwenye Wizara hii. Kwa kweli sasa tumeanza kuona matunda ya kazi zenu kwenye Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Liwale ni miongoni mwa Wilaya zinazolima zao la korosho na mazao mengine ya chakula na biashara kama vile ufuta, mbaazi, mtama na muhogo. Tatizo kubwa la wakulima wa Liwale ni upatikanaji wa masoko ya mazao hayo, Wilaya ya Liwale haina soko la uhakika la mazao ya biashara. Shida nyingine kubwa sana katika kilimo ni uhaba wa maghala ya kuhifadhia mazao hasa inapokuja kwenye msimu wa korosho. Mwaka huu korosho kwa mfano zimekaa muda mrefu sana kwenye maghala madogo ya vyama vya msingi, maghala ambayo hayana ubora hivyo kuharibu ubora wa mazao husika. Hivyo naiomba Serikali kuipatia ujenzi wa maghala kwenye halmashauri yetu.

Mheshimiwa Spika, malipo ya korosho kwa Wilaya ya Liwale bado si wa kuridhisha kwani wakulima wote wakubwa bado hawajapata malipo yao japokuwa uhakiki ulishakamilika. Naiomba Serikali kuangalia malipo haya japo msimu wa maandalizi wa mashamba umeshapita na wakulima hao hawajui hatma ya mashamba yao. Pamoja na kauli ya Mheshimiwa Rais alipokuwa ziarani Mtwara kuamuru wakulima wote walipwe, jambo hili kwa halmashauri ya Liwale halijatekelezwa kabisa.

Mheshimiwa Spika, Skumu ya Umwagiliaji ya Kata ya Ngongowele Wilayani Liwale ni ya muda mrefu sana. Hatma ya mradi huu hadi leo hatujui hatma yake licha ya kutengewa fedha kila mwaka; fedha za awali zaidi ya milioni 700 zimeliwa bila mafanikio. Naiomba Serikali kuja na timu maalum ili kufanya ukaguzi ili kuona namna mrdai huu ulivyohujumiwa.

Mheshimiwa Spika, idara ya kilimo katika halmashauri ya Liwale pamoja na changamoto nyingi lakini uhaba wa watumishi wa kada hii ni mkubwa; sambamba na uhaba wa vitendea kazi kama vile magari na pikipiki kwa ajili ya maafisa ugani. Kulikuwa na mradi wa upandaji wa miche ya mikorosho, vikundi mbalimbali vilihamasishwa kuanzisha vitalu vya miche ya mikorosho lakini hadi leo vikundi hivi bado havijalipwa malipo ya upandaji wa miche hii. Watu hawa walichukua mikopo kutoka kwenye taasisi za kifedha hivyo sasa watu hawa wako kwenye hatari. Naiomba Serikali kuwalipa watu hawa madai yao.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Liwale inapakana na Pori la Akiba la Selous hivyo kuna changamoto kubwa sana ya wanyama waharibifu kuharibu mazao ya wakulima. Wanyama hawa ni kama vile nyani, nguruwe, viboko na tembo. Hivyo naiomba Wizara ikisaidiwa na askari wa wanyamapori kuja na mkakati maalum wa kuwasaidia wakulima hawa namna ya kuanzisha vikosi vya misako ya mara kwa mara, misako ambayo inahitaji msaada wa vifaa kama bunduki ndogo, nyavu za kusakia na zana nyingine za kusaidia kupunguza athari za uharibifu huo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, naomba nianze mchango kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha leo kushika kalamu na kutoa mchango wangu kwenye Wizara hii. Kwanza kabisa nianze kwa kuwapongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kazi wanayoifanya kwenye Wizara hii, wao pamoja na watumishi wote kwenye Wizara hii kwa juhudi kubwa wanazofanya za kuwaletea maendeleo katika Sekta hii ya Nishati hasa ya umeme. Wananchi wanaona juhudi yao katika kuwatumikia Watanzania.

Mheshimiwa Spika, kuhusu Mradi wa LNG Lindi; naiomba na kuishauri Serikali kuharakisha mazungumzo juu ya utekelezaji wa mradi huu muhimu kwa nchi yetu. Hata hivyo, katika kuharakisha huko hakuondoi umakini wa kuzingatia maslahi mapana kwa Taifa letu na rasilimali ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, REA awamu ya tatu kwa Mkoa wa Lindi haijafanya vizuri kwani hadi leo vijiji vingi vya Mkoa wa Lindi havijafanikiwa. Mfano Wilaya ya Liwale yenye vijiji 76, katika awamu ya tatu kulikuwa na vijiji 14, ni vijiji vitatu tu hadi leo vimewashwa umeme. Sasa awamu ya tatu, mzunguko wa pili imeanza kutekelezwa kwenye baadhi ya mikoa, Liwale bado tuko awamu ya tatu, mzunguko wa kwanza ambayo hakuna chochote kinachofanyika, japo REA awamu ya pili nayo haikufanya vizuri kwani hadi leo zipo taasisi hazijapata umeme kama vile shule, zahanati na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali kumbadilisha mkandarasi wa Mkoa wa Lindi ambaye ameshindwa kwenda na mkataba. Serikali kushindwa kumbadilisha mkandarasi huyu ni kukiri madai ya mkandarasi huyu kuwa Serikali haitoi fedha, ndiyo maana anashindwa kufanya kazi. Je, ni kweli kuwa Serikali haina fedha za kumlipa mkandarasi huyu?

Mheshimiwa Spika, sambamba na mradi wa LNG – Lindi, naomba kuishauri Wizara kushirikiana na Wizara ya Elimu kukiwezesha Chuo cha VETA Lindi kuanzisha masomo yanayohusiana na masuala ya gesi ili kuwawezesha wakazi au vijana wa Mikoa ya Lindi na Mtwara kushiriki vyema kwenye tasnia hii ya gesi.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo, naiomba Serikali kutoa kipaumbele kwa vijana wa Mikoa ya Lindi na Mtwara, pale inapotokea nafasi kuwawezesha Watanzania kushiriki katika tasnia ya gesi, yaani kimasomo ndani na nje ya nchi ili Wanalindi waweze kuona manufaa ya moja kwa moja kutokana na kugunduliwa kwa gesi katika mikoa hiyo.

Mheshimiwa Spika, mradi wa matumizi ya gesi majumbani ni muhimu sana kwani utasaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira. Pia wananchi wataona moja kwa moja manufaa ya kuwepo kwa gesi hiyo. Mradi wa matumizi ya gesi majumbani kwa Mkoa wa Lindi bado kabisa haujaanza. Kwa hiyo nashauri kufikiria kuanza kwa mradi huu kwa Mkoa wa Lindi.

Mheshimiwa Spika, ninaposema Mkoa wa Lindi naiomba Serikali itambue kuwa Liwale ni miongoni mwa Wilaya za Mkoa wa Lindi hivyo miradi hii inaporatibiwa wakumbuke na Liwale, hata wakandarasi nao wafahamishwe kuwa Liwale nayo iko Lindi. Mfano Kampuni za Shell na Equinor zimeanza kutoa huduma (incentives) kwa Mikoa ya Lindi na Mtwara, lakini Wilaya ya Liwale hawana habari nayo, kana kwamba Liwale haiko Lindi.

Mheshimiwa Spika, naendelea kuishauri Serikali kuendelea kuwekeza kupitia Kampuni ya TPDC kwani sasa kampuni hii haijawezeshwa vya kutosha kuweza kukidhi majukumu yake. Miradi mingi ya kampuni hii imeshindwa kufanya vizuri kutokana na ukosefu wa fedha. TPDC ni lazima ipewe fedha za kutosha.

Mheshimiwa Spika, Liwale nayo iko Mkoa wa Lindi, nayasema haya kwa kuwa Mawaziri wengi huishia Wilaya za Kilwa, Nachingwea, Ruangwa na Lindi na kusema kuwa wamemaliza ziara ya Mkoa wa Lindi. Jambo hili limewafanya hata wakandarasi kuacha kutekeleza miradi mbalimbali kwani wanajua kuwa haitakaguliwa na Waheshimiwa Mawaziri, hakuna Waziri anayekuja Liwale kukagua miradi ya maendeleo ikiwemo REA. Hivyo, namwomba Mheshimiwa Waziri wa Nishati aje Liwale aone haya ninayoyasema. Kati ya vijiji 76, vijiji vyenye umeme havifiki hata 15, hali ni mbaya sana.

Mheshimiwa Spika, mwisho, naiomba Wizara wawaruhusu wawekezaji wa umeme jua, Kampuni ya Power Conner, waweze kutuletea umeme sisi tulio pembezoni tusioweza kufikiwa na umeme wa REA.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uhai na kuweza kuchangia bajeti hii. Katika hatua hii nipende kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri wote pamoja na watendaji wote kwenye wizara hii kwa kazi kubwa wanayiofanya kwa kufanya uchumi wa nchi yetu uweze kukua vyema na huduma za jamii kuimarika. Mawaziri kwa utendaji wao uliotukuka ndiyo sababu ya Mheshimiwa Rais kuwaamini kuendelea kuhudumu kwenye Wizara hii muhimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kusema kweli bajeti hii kwa kaisi kikubwa imekwenda kujibu changamoto mbalimbali kwenye jamii yetu, kwani hakuna bajeti inayoweza kujibu shida za watu wote kwa asilimia 100. Hii ni bajeti iliyozingatia maoni mengi ya Wabunge wakati wakichangia bajeto ya wizara mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia umuhimu wa ujenzi wa Tanzania ya viwanja hivyo ni jambo muhimu sana kuimarisha sekta ya kilimo. Tunapokwenda kuimarisha kilimo cha mazao ya kimkakati, nashauri Serikali kuendelea kuwekeza kwenye mazao ya mbegu za mafuta ya kula kama alizeti, ufuta, nazi na mchikichi, hii itatupunguzia uagizaji wa mafuta ya kula. Pamoja na mazao ya jamii ya mikunde kwani pamoja na hayo mazao hayo husaidia kukuza vipato vya jamii husika na katimaye kwa nchi nzima.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na changamoto za pembejeo lipo pia tatizo la masoko kwa mazao yetu. Hivyo, naishauri Serikali kuimarisha masoko ya mazao na kuimarisha vyama vya ushirika. Hapa naiomba Serikali kuangalia sera na muundo wa Vyama vya Ushirika kwani vyama vingi vimekuwa ni vyama vya msimj wa mazao, mavuno ua mazao yakiisha na vyama husika huwa likizo na vingi havina uwezo wa kujiendesha wala watumishi wenye weledi.

Mheshimiwa Naibu Spika, utalii Kanda ya Kusini bado haujapewa msukumo wa kutosha kwani viko vivutio vingi Kanda ya Kusini Mikoa ya Lindi na Mtwara havijatangazwa. Ukanda wa Kusini tunahitaji geri la utalii wa picha kwa Pori la Akiba la Selous, kwani utalii wa uwindaji hauna nguvu kwa sasa. Mfano Wilaya ya Liwale pamoja na kupakana na Selous hakuna manufaa ya moja kwa moja jwa watu wote, lakini pia Liwale kuna Boma la Mjerumani ambalo halitangazwi kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Sera ya kuunganisha mikoa yetu kwa barabara za lami likapewa msukumo wa kutosha, kwani bado kuna mikoa bado haijaunganishwa kwa barabara hata za changarawe. Mfano Mkoa wa Lindi na Morogoro katika Wilaya za Ulanga na Liwale. Barabara ya Nangurukuru- Liwale ni barabara iliyotajwa mara nyingi hata kwenye ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Hivyo naiomba Serikali ikafikiria kuijenga barabara kwa kiwango cha lami ili kuinua uchumi wa watu wa Liwale na Kusini nzima kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze pia Serikali katika kuimarisha miundombinu ya afya kwa ujenzi wa vituo vya afya, hospitali za wilaya, hospitali za mikoa na zile za rufaa sambamba na upatikanaji wa dawa na vifaatiba, lakini bado tatizo ni kubwa hasa kwa vituo vya afya. Mfano Halmashauri ya Liwale yenye kata 20 zenye jiografia ngumu zina vituo viwili tu vya afya ambapo ujenzi wake unaendelea. Vivyo basi pamoja na shukrani kwa vituo hivyo viwili naendelea kuomba Serikali kutuongezea vituo vingine hasa vile ambavyo wananchi wameanza kuweka nguvu zao katika Kata za Barikiwa, Lilombe na Miruwi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa LNG Lindi ni mradi wa mfano Barani Afrika nan i mradi muhimu sana kwa taifa letu hasa kwa wakazi wa Kusini, hivyo naiomba Serikali kuharakisha mazungumzo ili mradi huu uweze kuanza, kuwa na majadiliano yasiyoisha kutakatisha tamaa wawekezaji wa mradi huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi ya maji ni miradi iliyohujumiwa muda mrefu hapa nchini. Hapa naomba sasa miwapongeze Mawaziri kwenye wizara hii kuwa hatua walizoanza kuchukua. Iko miradi mingi sana ya maji imesimama, mfano katika Halmashauro ya Liwale yenye vijiji 76 ni vijiji 10 tu ndivyo vijiji vyenye miradi ya maji iliyokamilika, vijiji 14 miradi imesimama na vijiji 51 havina maji kabisa. Hivyo naishauri Serikali kupitia miradi yote iliyosimama ba wahusika kuendelea kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria. Viko visima 28 Liwale vimechimbwa lakini havina mtandao wa mambomba, hivyo wananchi kukosa huduma ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuendelea kusambaza mifugo nchi nzima ni lazima liangaliwe upya ni bora kuimarisha ufugaj wa kisasa kuliko hivi sasa wafugaji wanasambaa nchi nzima. Mfano, Wilaya ya Liwale yenye misitu ya asili sasa inaanza kutoweka kutokana na wafugaji kuvamia mapori bila mpangilio matokeo ya haya licha ya kusambaza mifugo tunasambaza pia mapigano ta wakulima na wafugaji.
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hotuba ya Rais. Kama ilivyo ada na kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza naongea kwenye Bunge hili la Kumi na Mbili, naomba nitoe shukurani zangu za dhati kwa Mwenyezi Mungu, nitoe shukrani kwa wapiga kura wangu wa Liwale, nitoe shukrani kwa Chama changu Cha Mapinduzi kwa kuniwezesha kuwepo hapa sasa hivi na kulitumikia Taifa na nawaahidi utumishi uliotukuka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hotuba ya Rais naomba nijikite katika sehemu moja au mbili; sehemu ya kwanza kabisa nizungumzie suala la kilimo. Ni kweli kabisa Mheshimiwa Rais amedhamiria kufufua kilimo, kwa maana ya kwamba kwenda na kilimo cha kisasa na kufanya mapinduzi ya kilimo. Hata hivyo, hatuwezi kwenda na mapinduzi ya kilimo kama hatujawekeza kwenye utafiti. Ni lazima tuhakikishe tunafufua au tunaimarisha vyuo vyetu vya utafiti, vile vile kujikita kwenye bajeti kwa kuongeza zaidi katika sehemu hiyo ya utafiti.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mzuri kwenye zao letu la korosho mwaka juzi kwenye Halmashauri yetu ya Wilaya ya Liwale, kulikuwa na ugonjwa wa mikorosho, ilikuwa inanyauka mizima mizima, ilikuwa inanyauka mpaka inafikia kukauka. Kwenye msimu wa mwaka huu, korosho zile zimezaa vizuri, lakini ukibangua ile korosho yenyewe tayari ndani unakuta imeharibika, kwa maana korosho zimeharibika, kitendo ambacho kimeilazimu Wilaya ya Liwale kuuza korosho zake kwa kiwango kikubwa kwenye grade ya pili. Jjambo hili naiomba Serikali kupitia Waziri wa Kilimo ihakikishe tunapeleka wataalam kwenye mashamba haya ya kilimo ili tuweze kugundua tatizo ni nini. Hii ni kwenye upande huo wa utafiti.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Mheshimiwa Rais kwenye hotuba yake alizungumzia suala la miundombinu. Ni kweli kabisa jambo la miundombinu huwezi kutenganisha na maendeleo ya watu kama hatujawahi kuunganisha miundombinu. Hapa naunganisha na Sera ya Taifa letu ya kuunganisha mikoa yetu kwa barabara za lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niiambie Serikali Mkoa wa Lindi bado haujaunganishwa na Mkoa wa Morogoro kwa barabara za lami. Mkoa wa Lindi tunayo barabara moja tu inaitwa Kibiti – Lindi ambayo ni kama trunk road. Hata hivyo, barabara hii isiposaidiwa na regional roads hatutapata tija yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa naizungumzia barabara inayotoka Nachingwea kwenda Liwale, Nachingwea kwenda Masasi, Ruangwa kwenda Nachingwea, Ruangwa kwenda Kilwa, barabara hizi zisipofunguliwa bado manufaa ya hii trunk road ya Kibiti – Lindi hayataonekana. Naiomba Serikali, pamoja na kwamba tumejikita kwenye kuunganisha mikoa, hizi regional roads tunaweza kuziita feeder roads, ndizo barabara zinazowezesha mazao ya wakulima kufika kwenye masoko kwa urahisi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa hiyo, naiomba Serikali, pamoja na sera ya kuunganisha mikoa Mkoa wa Lindi wauangalie kwa jicho la huruma kwa sababu ni mkoa pekee ambao una barabara moja tu yenye lami ambayo hiyo ni trunk road, regional roads zote ni za vumbi. Naomba sana Mheshimiwa Waziri au Serikali kwa ujumla tuifikirie barabara ya Nangurukuru – Liwale. Barabara hii ni ya kiuchumi na siyo ya kisiasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande huohuo wa miundombinu, tunalo tatizo kubwa sana upande wa wakandarasi. Tunatekeleza miradi mikubwa sana lakini wakandarasi wanachelewa kulipwa. Jambo hili linafanya miradi yetu mingi itumie hela nyingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, barabara inaweza kujengwa labda kwa shilingi bilioni 200, lakini kwa sababu tu mkandarasi amechelewa kulipwa, barabara imeisha ina miaka mitatu, minne mkandarasi hajalipwa, utakuta ile barabara badala ya kujengwa kilometa moja kwa bilioni 1.2 tunajenga mpaka bilioni 1.8 au bilioni 2. Hii yote ni kwa sababu tunachelewa kuwalipa wakandarasi. Kwa hiyo, naiomba Serikali kuhakikisha kwamba wale wakandarasi ambao wanamaliza miradi kwa wakati basi miradi hiyo iishe kwa wakati na wakandarasi waweze kulipwa kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda, hayo tu mawili yananitosha kwa mchango wangu kwenye hotuba hii. Ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi jioni hii niwe mchangiaji wa mwisho kwenye hii hotuba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa watu wengi wameshachangia mambo mengi sana, mimi nataka nianze tu na hii sekta ya kilimo. Ni sekta ambayo imechangiwa karibu na Wabunge wote. Yale mambo ambayo nitayazungumza, siwezi kurudia yale ambayo wenzangu tayari ameshayazungumza. Nataka tu nigusie sehemu moja inayohusu mambo ya masoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba tuna tatizo la utafiti, pembejeo na mambo mengine, lakini soko ni tatizo kubwa zaidi. Kwa sababu wakulima wengi hata wale wadogo wadogo wanaojitahidi kulima, wakihangaika. Nitoe mfano tu, hapa juzi tumesikia kwamba kuna wakulima wa miwa wa Morogoro wamekosa soko, miwa imeungua moto. Leo kuna wakulima Shinyanga wanasema mchele unakosa soko lakini ukienda Mtwara unakuta mchele kilo moja ni Sh.3,000/= mpaka Sh.4,000/=. Tatizo bado Serikali haijajikita kuhakikisha wakulima wetu wanapata uhakika wa kuwa na masoko ya kudumu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wanachangia hapa wanasema wasomi wetu hawako tayari kwenda kwenye kilimo. Jamani, ni msomi gani atakubali kwenda kwenye kilimo akalime heka 10 au 20 za korosho asikie kwamba korosho zimekosa soko? Huyo mkulima ili aweze kujiandaa lazima ataandika andiko, atakwenda benki, atakopa fedha, atafungua shamba la kulima miwa, akihakikishiwa kwamba Kilombero watachukua miwa, inafika mwisho wa msimu, wanakwambia Kilombero wametosheka na miwa, haina soko. Huyo msomi ambaye amechukua fedha kwenye mabenki, amekosa soko, anakwenda kuzilipa vipi pesa alizokopa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mkulima gani ambaye tangu amezaliwa amemkuta baba yake analima kwa jembe la mkono, shangazi yake analima kwa jembe la mkono, hajatoka; halafu yeye aseme mimi msomi nimetoka SUA naweza kulima kwa jembe hili la mkono litanitoa, litamtoa wapi? Kwa hiyo, tusianze kuwalaumu sana wasomi wetu, lakini lazima tuangalie Serikali imejikita vipi kwenye hili suala la kilimo? (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yuko Waziri mmoja hapa hapa, sikumbuki vizuri, 2015 alisema jembe la mkono linakwenda Makumbusho. Lile jembe mpaka leo halijafika Makumbusho. Lazima tuwe wakweli, bado tuna tatizo kwenye sekta hii ya kilimo. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya kilimo vilevile tuiunganishe na sekta ya miundombinu. Wako wakulima vijijini mazao yao yanaharibika kwa sababu ya miundombinu mibaya kulifikia soko. Leo Serikali, sera yetu inajikita kujenga barabara tunasema tunaunganisha mkoa na mkoa, tunajenga trunk road, tunakwenda regional road, lakini tunasahau ziko barabara zinazotakiwa zihudumie wananchi wetu kupelekea mazao kwenye soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano tu Wilaya yangu Liwale, sisi ni wakulima wa korosho wazuri sana, lakini kwa sababu hatuna barabara; kutoka Nachingwea kwenda Liwale ni kilomita 124; Nachingwea korosho wanauza 3,000, Liwale wanauza 2,000 kwa sababu hakuna mfanyabishara yuko tayari kukanyaga pale Liwale kufuata korosho. Mnunuzi akinunua korosho kwa bei ya 3,000 akileta mpaka hata Dar es Salaam itakuwa imefika bei zaidi aliyochukua Mtwara au Lindi. Kwa hiyo, bado kuna tatizo la miundombinu. Kwa hiyo ili kilimo chetu kiweze kwenda sambamba na mpango huu lazima kwanza tufanye mageuzi ya kilimo kwamba tulime kisasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tuhakikishe miundombinu rafiki ya kufikisha mazao haya kwenye viwanda, lakini yapo mazao mengine haya mazao ya msimu, kwa mfano kama nyanya, leo hata ukimwambia mtu afungue kiwanda cha kulima nyanya ambazo zinalimwa miezi miwili, miezi mitatu nyanya hakuna, kile kiwanda anakipeleka wapi, hicho kiwanda anafanya kazi peke yake, maana akishawaajiri watu wanachakata hizo nyanya kwa miezi miwili au mitatu, kiwanda kimefungwa kwa sababu nyanya hakuna. Kwa hiyo ni lazima twende na kilimo cha umwagiliaji. Kama kweli tunajenga kiwanda cha matunda, ni lazima tuhakikishe yule mwenye kiwanda anapata matunda muda wote na anapataje matunda muda wote, ni pale tu tutakapoanza kilimo cha umwagiliaji, lakini hiki kilimo cha kutegemea mvua, hakitatusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunazungumzia mananasi hapa kwa Mheshimiwa Rais mstaafu, kuna mananasi mengi tu, ukienda msimu Chalinze mananasi ni mengi mpaka yanaoza, lakini leo ukifungua kiwanda cha mananasi pale, kitafanya kazi miezi mingapi, miezi miwili au mitatu mananasi yamekwisha, inabidi kiwanda kifungwe na wale uliowaajiri inabidi uwape likizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kuwa na viwanda vya kudumu, ni lazima tuwe na uhakika kwamba tunakuwa na kilimo cha umwagiliaji, kilimo ambacho kitamhakikishia mwenye kiwanda cha matunda kile anapata matunda muda wote. Hili ni jambo ambalo nimeona nilizungumzie kwa namna hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile bado naendelea huko huko kwenye kilimo; tunapokwenda kuzungumzia kilimo cha umwagiliaji, bado ukienda katika skimu za umwagiliaji leo, bado tunatumia mito yaani hatuwezi kuweka skimu za umwagiliaji hapa Dodoma, hakuna mto, ni mpaka uwe pembeni ya mto ndiyo wanatengeneza kile kilimo cha umwagiliaji. Wakati mwingine yanapotokea mafuriko kama haya, ile mifereji yenyewe imevunjika, imeharibika, hakuna kilimo cha umwagiliaji. Naiomba Serikali tafadhali tafadhali, kama kweli tunataka tuisaidie nchi hii, tuwasaidie hawa vijana wa nchi hii, lazima tufanye maamuzi ya kufanya mageuzi ya kilimo, siyo hiki kilimo cha kutegemea mvua wala hiki sio kilimo cha msimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano mwingine, nimefanya kazi kwa Bakharesa miaka zaidi ya 20, wakati ule ngano ilikuwa inauzwa kilo moja Sh.200 nje, ngano ya Tanzania Sh.370. Bakharesa aliamua kwenda kulima ngano Basutu, kilichomkuta alilima mwaka mmoja tu akaacha. Watakuja OSHA hapo, watakuja TFDA, watakuja sijui Ardhi, watakuja watu wa madini, yaani wanakuja kibao. Ile ngano amelima, amevuna, ngano akiagiza India by then ilikuwa 240, ngano alilima Basutu ilifika 400, akaamua kuacha mpaka leo ngano ni shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kweli mpaka leo Bakharesa mimi wakati naondoka mwaka 2014 anasindika tani 1,500 per day, lakini yote hii anaagiza kutoka nje, 100 percent anaagiza kutoka nje. Sasa ni lazima kwanza tujenge mazingira, unajua tatizo lingine linakuja kubwa ni kwamba akionekana mtu anataka kufanya biashara, basi yule anaonekana sijui ameiba hela mahali, sijui anataka kufanyaje, atafuatwa milolongo hapo, itaonekana kama vile hafai, kwanza anaonekana mtu ana hela, hata yule anayekwenda labda anapeleka andiko lake, tayari anaanza kwanza kusachiwa, yaani zile pesa watu wanaanza kugawana kabla hazijafika huko shamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu ulikuwa ni huo tu. Ahsante sana.
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Mpango huu wa Miaka Mitatu wa Taifa letu. Kwanza, naomba nijielekeze moja kwa moja kwenye upande wa miudnombinu. Ni ukweli usiopingika kwamba nchi yetu imeamua kuingia kwenye nchi ya viwanda. Ili tuweze kulifikia lengo hili la kuwa nchi ya viwanda, matarajio yetu makubwa tunategemea kupata malighafi kutoka mashambani. Vile vile, sera ya nchi yetu sasa hivi tuko kwenye kuunganisha mikoa yetu kwa miundombinu ya barabara za lami. Tumeshamaliza baadhi ya mikoa, lakini bado mikoa mingine haijafikiwa. Ni ukweli vile vile tunahitaji kujenga barabara za kiulinzi, lakini ziko vile vile barabara za kuunganisha za kimkakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshafikiria kwamba ili mazao yetu yaweze kufika kwenye hivyo viwanda tunavyokusudia kuvijenga, ni lazima tuhakikishe kule ambako mazao haya yanazalishwa tumepeleka hizo barabara kuwezesha mazao haya kufika kwenye soko au kwenye viwanda. Kwa mfano, ni ukweli usiopingika zao la korosho kwa Mkoa wa Lindi na Mtwara lina mchango mkubwa sana kwenye pato la Taifa, lakini kwenye Mikoa hiyo hiyo ya Lindi na Mtwara ndiyo mikoa ambayo haifikiki kwa barabara za lami kwenye wilaya zake karibu zote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mradi mmoja una miaka zaidi ya mitano sasa wa barabara ya kimkakati wa Kanda ya Kusini, barabara inayotoka Mtwara – Newala – Tandahimba – Masasi - Nachingwea mpaka Liwale. Huu wote unaozungumziwa ni ukanda wa korosho, ndiyo maana mwaka huu tumepata shida sana watu wa korosho kwa sababu mpaka imefika masika korosho bado hazijatoka kwa wakulima kwa sababu hakuna barabara ya kuzifikisha maghalani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napendekeza kwamba kama kweli Serikali inadhamiria kufufua viwanda au kwenda kwenye uchumi wa viwanda lazima tuhakikishe tunayo miundombinu rafiki ya ufufuaji wa viwanda, lakini kama barabara zetu zitabaki kuwa hivi zilivyo, tukategemea kwamba mazao ya wakulima yatafika kwenye masoko au yatafika kwenye viwanda, hapa tutakuwa tunachezeana kiakili. Naomba sana, ufufuaji wa viwanda lazima uende sambamba na ujenzi wa miundombinu. Kweli Taifa letu liko kwenye hatua ya kuunganisha mikoa lakini bado naomba tuingie sasa kwenye barabara zinazounganisha wilaya zetu, hata basi barabara zinazounganisha wilaya zetu na mikoa yetu ili tuone tija ya wakulima. Wakulima wengi wanateseka hawapati pembejeo kwa wakati, hawapati infrastructure yoyote, lakini hata pale wanapojitahidi kulima, mazao yao yanaharibikia mashambani, wanashindwa kuyafikisha kwenye masoko. Jambo hili ni lazima Mheshimiwa Mwigulu alipeleke pamoja kuungamanisha miundombinu na viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine naomba nizungumzie huko huko kwenye miundombinu. Fedha nyingi za Serikali tunazipeleka kwenye halmashauri, tunakwenda kujenga hospitali kwenye wilaya zetu na vituo vya afya, tunajenga madarasa na mabweni shuleni, lakini hizi fedha tunazipeleka kwenye halmashauri ambako hakuna wataalam. Tulipounda TARURA tuliondoa wahandisi wote tukawapeleka TARURA, leo kwenye halmashauri zetu hazina wahandisi, hakuna wakadiriaji majengo. Tunapeleka bilioni 1.5 kwa ajili ya kujenga hospitali ya wilaya, kule unakopeleka yuko Mkurugenzi na watendaji wengine, hakuna mhandisi, nini kinatokea?

Mheshimiwa Naibu Spika, kinachotokea ni kwamba, mahali ambapo mkadiriaji wa majengo akikadiria jengo ili kuezeka bati hamsini anaandika bati 200, zinaenda kununuliwa bati 200 zinakuwa pale jengo limeisha, bati zimebaki, fedha zimeisha. Au jengo lingine ambalo lilitakiwa kuezekwa kwa bati 50 ananunua bati 25, fedha zimeisha, jengo halijaezekwa. Huwezi kumchukulia hatua, hana taaluma hiyo, yuko pale, anafanyaje? Mkurugenzi yuko pale, Mhasibu yuko pale lakini hakuna Mkadiriaji Majengo. Unamchukulia hatua gani huyu mtu ambaye hujamuajiri kwa kwa kazi hiyo? Pangekuwa na Mhandisi pale angeweza kuwajibika, lakini hatuna Wahandisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiondoka hapo, tunayo kada ya wakandarasi. Kwa sababu tumeshaamini kwamba ujenzi kwa force account ni rahisi zaidi kuliko wakandarasi, sasa tumeua hii kada ya ufundi. Naomba jambo hili basi liende sambamba na mitaala yetu ya elimu, wanaendelea kuzalisha wataalam kule wa ujenzi, wakati huku hawawahitaji kuna faida gani? Wakandarasi peke yao ambao wanabaki kidogo ambao tunasema tunataka kulea wakandarasi wazawa, waliobaki ni walioko kwenye barabara tu na ni wachache sana, tena hawana hata mitaji na wala hawafikirii kupata mitaji, lakini wale wakandarasi wa majengo hawana kazi tena nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wizara ya Elimu waondoe hiyo taaluma kwenye vyuo vyetu, hawana kazi! Sisi tumeshaamua kwamba Mwalimu Mkuu ndiyo atasimamia jengo letu, tumeshaamini Mkurugenzi ndiyo atasimamia jengo, tunaamini kwamba DMO ndiyo atasimamia jengo letu, hawa wengine hatuwahitaji! Ndiyo maana tangu tumeunda taaluma mpaka leo hii kwenye halmashauri nyingi hatuna Wahandisi, uongo au ukweli? Naomba sana tulifikirie hilo kwamba tunapeleka fedha nyingi halmashauri, lakini hazina wasimamizi na tutawahukumu kweli lakini tunawahukumu isivyo halali. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nizungumzie suala la uwekezaji. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais, amelizungumza suala hili la uwekezaji vizuri sana, lakini naomba nitoe tahadhari kwa nyie mliopata mamlaka. Hiki kitu cha uwekezaji kiko very delicate. Nimemsikia Mheshimiwa Rais amesema tusiwabughudhi wawekezaji na naunga mkono, tupunguze urasimu kwa wawekezaji lakini tuwe makini. Haiwezekani kazi ambazo Watanzania wanahangaika nazo kila siku wakizitafuta waende wakagawie wawekezaji eti tu kwa sababu tukimkatalia kuajiri ataondoka. Tuwe makini sana hapo. Tusipoangalia ni mwanya mwingine wa kupoteza ajira nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri mimi nimedumu kwenye Sekta Binafsi zaidi ya miaka 30, najua kinachoendelea kule. Wapo watu wana vyeti vya expert, wana vibali vya ma- expert lakini ni wasimamizi tu wa kupakia mizigo kwenye malori. Wapo watu wana kada ya expert kazi yao ni madereva tu wa kuendesha viberenge mle ndani, kupaki paki mizigo kwenye godown, lakini ukiangalia cheti chake, huyo ni expert. Muda wa miaka miwili ukiisha, anaombewa tena kibali. Tuwe makini kwenye nafasi hiyo, tunahitaji wawekezaji, tunawahitaji sana na wafungue milango na wawe rafiki wa wawekezaji, lakini kwa umakini mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hayo ndiyo niliomba niyachangie kwa leo. Naomba kabla hujanipigia kengele, hayo hayo mawili, matatu yatoshe kwa leo. (Kicheko/Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii adimu angalau dakika tano na mimi nichangie hotuba iliyo mbele yetu. Kwa sababu muda ni mchache basi mimi nitautumia muda huu kuongea mambo ya wapiga kura wangu walionituma kuwawakilisha hapa ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunakwenda kukaa hapa zaidi ya miezi mitatu, tunachokifanya hapa ni kugawanya keki ya Taifa letu. Naomba nitoe ushauri kwa Serikali, tunapokwenda kuigawa keki hii lazima tujue jiografia ya nchi yetu inatofautiana sana, maendeleo ya kanda moja kwenda kanda nyingine inatofautiana sana, kutoka mkoa mmoja kwenda mkoa mwingine inatofautiana sana. Kwa hiyo, iwepo juhudi ya makusudi kuangalia ni namna gani ya kuisaidia ile mikoa au zile sehemu ambazo kimaendeleo zipo nyuma au kiuchumi zipo nyuma ili tuweze kwenda pamoja tusiwaache wenzetu. Natoa mfano hata Rais wa Awamu ya Nne aliamua kwa makusudi kuelekeza nguvu nyingi Kigoma, amejenga barabara nyingi sana kule,ili kwenda nao pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tusisahau kuna element moja ilikuwepo tangu zamani kwamba Mikoa ya Kusini ilikuwa ni ya adhabu; miaka ya 80. Naomba niiambie Serikali ile element bado haijafutika, bado ipo pamoja na kwamba Serikali zote Awamu Tano zilizopita zimejitahidi sana kuipunguza lakini hiyo element bado ipo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi leo naongea zipo barabara kwenye nchi yetu zimepitiliza zaidi ya 20, life span ya barabara zetu ni miaka 20, tayari kwenye bajeti hii zipo barabara hizo zinakwenda kufanyiwa upembuzi yakinifu pengine kuondoa ile lami ili waweke nyingine kwa sababu life span yake imekwisha. Hata hivyo, mnapokwenda kufanya hayo mjue kwamba Nangurukuru - Liwale tangu tumepata Uhuru hatujaona lami. Mnapokwenda kufanya hayo mjue kuwa Mkoa wa Lindi hakuna wilaya hata moja ambayo inakwenda mkoani kwa barabara ya lami, ukiondoa Wilaya ya Kilwa na Wilaya ya Lindi Vijijini ambazo ziko kwenye hiyo barabara kubwa ya Kibiti-Lindi. Kwa hiyo, mnapokwenda kufanya hayo mjue kuna mikoa bado ipo nyuma inahitaji juhudi za makusudi kuisaidia ili twende pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano mwingine, Wilaya ya Liwale ni Wilaya tangu mwaka 1975 leo tunazungumza ni miaka 46, lakini Wilaya ile mpaka leo Mkuu wa Wilaya, DED, OCD, Mganga Mkuu, Hakimu wa Wilaya na Polisi OCD hawana ofisi. Kwa mfano mzuri wale Mawaziri waliowahi kutembelea Wilaya ya Liwale wote tunawapokelea kwenye ile rest house ya Selous, vitabu vyote wanakuja kusainia pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, asimame Waziri aniambie kama ameshawahi kuiona Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Liwale; Ofisi ya DED wa Liwale, asimame Waziri yeyote aseme ameshawahi kuona jengo la Polisi Wilaya ya Liwale. Wote tunakusanyika pale kwenye jengo la Selous. Tunaishukuru Selous, wametujengea rest house ambayo ndiyo inatumika mpaka leo. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba sana…

MBUNGE FULANI: Aibu!

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ile wilaya ni ya mwaka 1975 na Mwalimu Nyerere alimpa Waziri wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mzee Rashid Mfaume Kawawa Wilaya ile ya Liwale, lakini wilaya ile iko hoi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawaombeni sana, tunapokwenda kugawa keki hii, tuiangalie mikoa ile ambayo iko chini. Mkoa wa Lindi na Mkoa wa Mtwara ni mikoa ambayo iko nyuma kwa barabara, ndiyo maana tukaomba barabara yetu ile ya korosho inayotokea Mtwara inakwenda Newala – Tandahimba – Masasi – Nachingwea - Liwale mpaka Ruangwa, muikumbuke ili tuweze kuinua uchumi wa watu wa kusini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 –Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa dakika tano hizi nimalizie mchango kwenye Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, niunge mkono hotuba hii lakini kwa sababu ya muda nijielekeze moja kwa moja kwenye mada. Ni ukweli usiopingika tunalo tatizo la watumishi. Hili ni tatizo la Kitaifa kwamba kila Idara kuna upungufu mkubwa wa watumishi. Sasa leo mimi nitazungumzia Idara ya Mahakama hasa Ofisi ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na upungufu mkubwa wa watumishi kwenye Idara hii lakini kuna unyanyasaji mkubwa sana wa watumishi kwenye Idara hii hasa kwenye upandishwaji wa madaraja. Watumishi wengi wa Idara ya Mahakama wanahangaika kutafuta madaraja, hawapandishwi madaraja kwa wakati. Hili nalo limekuwa ni donda kubwa kwenye Ofisi ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninao mfano hapa, nina mtumishi aliyeajiriwa tarehe 4 June, 1990 anaitwa Rashid Ally Libago, mtumishi huyu tangu mwaka 1990 mpaka leo nasimama hapa hajawahi kupanda daraja. Sasa hebu chukulia mshahara wa mwaka 1990, huyu anadumu nao mpaka leo atapata mafao ya shilingi ngapi? Jambo hili linasikitisha sana na barua zake ninazo hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, barua ya mwisho ameandika tarehe 12 Mei, 2020 nayo haijapata majibu mpaka leo. Jambo hili ni la kusikitisha sana na barua yake ya uthibitisho ilikuwa ni tarehe 14 Julai, 1999. Mshahara hapa siusemi lakini jamani tufikirie, hawa watumishi wanafanya kazi kwenye mazingira magumu sana sasa inapotokea mtumishi anafuata haki zake, hili suala la kuzungushwazungushwa nalo sio jambo jema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni la kisera. Ilani yetu inasema tumekusudia kila Wilaya iwe na Mahakama ya Wilaya; lkila Kata kama sio Tarafa iwe na Mahakama ya Tarafa au Kata. Wilaya ya Liwale ni Wilaya tangu mwaka 1975 lakini mpaka leo hatuna jengo la Mahakama ya Wilaya. Jengo linalotumika sasa ni lile lililokuwa na mkoloni ambalo ndiyo ilikuwa Mahakama ya Mwanzo ya Liwale Mjini.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo masika hii ukienda ofisi ya masijala wamefunika maturubai kwa sababu jengo lile linavuja. Kibaya zaidi au cha kusikitisha zaidi bajeti ya mwaka 2017/2018 niliuliza swali la nyongeza hapa Mahakama ya Wilaya ya Liwale itajengwa lini? Mheshimiwa Waziri alitumia sekunde moja tu kunijibu, Mahakama ya Wilaya ya Liwale tunaijenga mwaka 2018, akafunga kitabu akaenda kukaa leo tunazungumza ni mwaka 2021 haijajengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu, tunapouliza maswali hapa na kujibiwa, kama Waziri huna uhakika wa jambo hilo basi jipe muda lakini unapowaambia watu kwamba Mahakama ya Wilaya ya Liwale itajengwa mwaka 2018 watu wanakusikiliza. Mpaka leo mimi wananiuliza, Mheshimiwa Waziri alikudanganya? Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi imeshaanza kusema uongo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naiomba sana Serikali tunapojibiwa maswali kwanza ijulikane kwamba sisi tumeagizwa na wananchi na tunachokisema hapa tunasema kwa ajili ya wananchi, tunaomba tujibiwe kama wanavyotaka waajiri wetu. Wilaya ya Liwale ina Kata 21, Mahakama za Mwanzo mbili tu; ya Liwale Mjini na Tarafa ya Makata, tunaiomba Serikali itufikirie. Nililisema hili wakati nachangia hotuba ya Waziri Mkuu. Miongoni mwa majengo niliyoyataja ambayo hayana sura ya kuitwa Ofisi ya Wilaya ya Liwale, hayana sura hiyo ni pamoja na jengo la Mahakama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nizungumzie suala la Wazee wa Baraza la Mahakama mpaka leo posho yao ni Sh. 5,000 na posho yenyewe haitoki mpaka siku ya hukumu ya kesi. Kuhudhuria kesi hawalipwi, wanalipwa pale kesi inapohukumiwa. Sasa tufikirie hii Sh. 5,000 ni ya mwaka gani na leo tunazungumzia mwaka gani. Hawa watu hawaruhusiwi kukosa, kila kesi ikiitwa wao wanaenda, kesi isipohukumiwa wanatoka kama walivyokuja mpaka hukumu ya hiyo kesi. Kwa shida iliyopo ya kuwa na Mahakimu wachache na vitendea kazi vichache, kesi zetu zinachukua hata miaka minne au mitano, wewe Mzee wa Baraza unasimamia kesi miaka mitano unafukuzia Sh. 5,000. Ombi langu kwa Serikali tufikirie mambo mawili; aidha, kuwaajiri au kuwoangezea hako ka posho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi hii. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi mchana huu nami nichangie Wizara hii mahususi kwa uchumi wa Taifa letu. Awali ya yote kama ilivyo ada nawapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wote. Pamoja na ugumu uliopo kwenye Wizara hii, wanajitahidi kadri ya uwezo wao, kadri Mwenyezi Mungu alivyo wajaalia. Vile vile napenda kusema kwamba mchango wangu leo nitauanza moja kwa moja kwenye uhifadhi wa wanyamapori. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kweli Taifa letu kama mchangiaji aliyepita alivyosema, Serikali ya Awamu ya Tano imedhibiti ujangili, uhifadhi umeongezeka, lakini matokeo ya udhibiti huu ndiyo haya malalamiko ambayo sasa hivi kila kona ya nchi yetu tunayapata, hasa wanyama hawa wanaoitwa tembo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano kwenye Halmashauri ya Wilaya yangu ya Liwale ambako sehemu kubwa ndiyo tunaozungukwa na hifadhi ya Selous, wako wananchi wamehama kutoka mashambani wamerudi vijijini baada ya mazao yao kuharibiwa au kulima na wanyama hao wanaoitwa tembo. Kuna Kijiji kama Ngumbu, Milui, Kikulyungu, Mkutano, Mtawatawa, Barikiwa, Ndapata, Mpigamiti, Lilombe na Kimambi; baadhi ya wananchi wa vijiji hivi tayari wapo vijijini, wamerudi kutoka mashambani baada ya wanyamapori hasa hao jamii ya tembo kumaliza mazao yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali, pamoja na kwamba tumeongeza uhifadhi, lakini bado sasa turejee kwa wananchi tuangalie ni namna gani wananchi wetu tunawakinga na ongezeko hili la tembo? Ongezeko la tembo ni zuri, tunapata mapato mengi, lakini lazima turejee, tuwe na mipango mikakati safi ya kuwanusuru wananchi wetu ili wasiendelee kuteseka na hatimaye kupata majanga ya njaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, naomba nizungumzie suala la kifuta machozi. Sheria ya Kifuta Machozi ni ya muda mrefu sana. Hivi kama mwaka 1974 mtu alikuwa anapewa shilingi 500/= labda kutokana na umbali wa mazao yake yalivyoliwa au shilingi 1,000/=, hivi kweli kiwango kile tunaendelea kukitumia mpaka leo! Nawaomba sana kwa kipande hicho tuongeze kiwango hicho angalau tuangalie namna tunavyoweza kuwasidia wananchi wetu. (Makofi)

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kuchauka kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Ester Bulaya.

T A A R I F A

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nampa Mheshimiwa Kuchauka taarifa katika mchango wake; hili tatizo la fidia ni kero maeneo mengi; na siyo tu ni kidogo, haitoki kwa wakati. Mfano, ni wananchi wa Jimbo la Bunda Mjini, Kata ya Nyatwali; Natwali, Tamau, Serengeti, mbali ya kwamba tembo wanaharibu mazao yao, wanaomba fidia na fidia yenyewe hiyo ndogo haitoki kwa wakati. Kwa hiyo, nilikuwa taarifa. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, niwakumbushe tena. Muda wa kutoa taarifa siyo muda wa kuchangia. Mheshimiwa Kuchauka endelea na mchango wako.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naipokea taarifa yake kwa sababu hata mimi kwangu kuna malalamiko, wananchi wameliwa mazao yao, sasa hivi wana mwaka wa tatu hawajapata fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni hapo hapo kwenye uhifadhi wa Selous. Sasa hivi Serikali imeimarisha utalii wa picha zaidi kuliko utalii wa uwindaji. Naiomba Serikali, ukanda huu wa Selous upande wa kusini kuanzia Kilwa, Liwale mpaka Tunduru, hatuna lango la utalii wa picha, matokeo yake baada ya kupunguza utalii wa uwindaji, umebakia utalii wa picha, lakini sisi kwetu tumebaki hatuna watalii na hatupati mapato yoyote yale.

Kwa hiyo, uwepo wetu wa hifadhi ya Selous tunakuwa kama vile hatuoni yale manufaa ya moja kwa moja. Kwa hiyo, naiomba Serikali kufikiria kuanzisha lango la utalii wa picha kwenye maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine nizungumzie kwenye WMAs. Waziri kwenye ukurasa wa 47 aya ya 59 ndiyo amezungumzia kidogo kuhusu WMAs. Lengo la Serikali kuanzisha WMAs hizi ni kushirikisha wananchi kwenye uhifadhi. Sasa tunawashirikishaje kama kwenye hotuba nzima umetaja kwenye aya moja, tena kamstari kamoja tu? Yaani hawa watu tunawashirikisha vipi? Kwa kweli kama Serikali ilikuja na lengo zuri kuimairisha WMAs ili kushirikisha wananchi kwenye uhifadhi ili wananchi wanaozunguka hifadhi hizo waone faida ya kuwa hifadhi zile, basi naiomba Serikali kuimarisha WMAs na kuona ni namna gani wanazisaidia hata kuwatafutia wawekezaji kwenye vitalu hivi ambavyo wamewekeza hao WMAs. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile fedha zao zinachelewa, hata pale wanapopata mtalii au mwekezaji mwenye Kitalu X, lakini bado mapato yao kutoka Serikalini yanachelewa sana. Hapo naiomba Serikali kuangalia upande wa WMAs. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nije kwenye uhifadhi wa TFS. Bunge lililopita niliuliza swali hapa kuhusu mpango wa uvunaji wa kitalu cha Nyelakipelele. Nashukuru Serikali wameshaleta mpango wa uvunaji wa msitu ule wa Nyelakipelele, lakini uvunaji wa pale ni wa holela. Ukipita hii njia kutoka Nachingwea kwenda Liwale, unapishana na malori usiku, yanabeba magogo. Mengine yana vibali, mengine hayana vibali, mengine yamegongwa na mengine hayajagongwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli naiomba Serikali, pamoja na nia njema ya kufungua uvunaji kwenye hifadhi hii ya msitu wa Nyelakipelele, bado tunaomba itupie macho uvunaji wa msitu huu, kwani ni wa ovyo mno na wala hauzingatii mazingira. Sidhani kama uvunaji ule ni endelevu, kwa sababu uvunaji endelevu ni kwamba watu wanavuna kwa mpango na miti ile lazima ipandwe mingine, lakini kwenye uvunaji wa msitu huo hakuna uvunaji endelevu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nirejee kwenye ikama ya wafanyakazi kwenye Halmashauri zetu. Kwenye Halmashauri zetu utakuta mhifadhi au Afisa wa Wanyamapori yuko mmoja tu. Jambo hili ndiyo linaloleta mgogoro mpaka tunapata matatizo ya wanyamapori, tunashindwa kupata msaada kwa sababu Afisa wa Wanyamapori kwenye wilaya au kwenye Halmashauri, anakuwepo mmoja.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali, Serikali ni moja… (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana. Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Ahsante sana kwa kunipa nafasi. Nami naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia Mapendekezo ya Mpango ulio mbele yetu. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa wasaa kwa kusimama mbele yako kuchangia Mpango huu. Vile vile kama ilivyo ada nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa mambo makubwa anayolitendea Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili niende nalo mbali kidogo kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa namna anavyolipendelea Taifa letu. Huu uongozi wetu sasa ni Awamu ya Sita, lakini katika Awamu zote hizo Mwenyezi Mungu amekuwa akituletea viongozi ambao kwa kweli wana kiu kubwa kuliona Taifa letu linatengemaa na linasonga mbele. Kwa hiyo tushukuru sana kwa Mwenyezi Mungu kwa karma hiyo ambayo ametupa sisi Watanzania, kutupatia Viongozi ambao kila kiongozi anayesimama, anasimama kwa ajili ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shukrani hii haitakamilika kama hatutakishukuru Chama chetu Cha Mapinduzi kwa kulea viongozi, kwa sababu hawa viongozi wote wanapikwa ndani ya Chama cha Mapinduzi. Kwa hiyo chama kiendelee kupika viongozi ili Taifa letu liendelee kutengemaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikirejea kwenye Mpango asilimia 90 kama siyo 95 ya waliochangia kuanzia jana mpaka leo wanazungumzia suala la kilimo, hii ni kuona namna gani kuna umuhimu wa kilimo kwenye Taifa letu. Kwa mtazamo wangu nasema bado kama Taifa hatujaamua kuwekeza kwenye kilimo. Hatujaamua kuwekeza kwenye kilimo kama ambavyo tunawekeza kwa maneno kuipa kilimo hizi semi mbalimbali; siasa ni kilimo, kilimo uti wa mgongo, kama haya maneno yangelingana na matendo yetu, leo kilimo kisingefika hapa tulipofika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefika mahali ambapo Bodi zetu za Mazao zinaendeshwa na wakulima. Leo tunazungumzia mfano mmoja kama Bodi ya Korosho inaendeshwa na wakulima wa korosho. Kila mkulima wa korosho anapouza korosho yake Sh.25 inapelekwa Naliendele kwa ajili ya kuimarisha utafiti. Kila mkulima anapouza korosho yake Sh.25 inakwenda kwenye Bodi ya Korosho.

Kwa hiyo, mtaangalia taasisi zetu za kilimo zinaendeshwa na mkulima, Bodi zetu za Mazao zinaendeshwa na wakulima, Taifa linafanya nini kuhakikisha hivi Vyuo Vyetu vya Utafiti wanavitengea fedha za kutosha, tuweze kufanya utafiti wa kutosha ili tuweze kuzalisha vya kutosha na kufanya kilimo chenye tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi, Serikali kwenye Mpango huu napendekeza ije na Mpango mahsusi ituonyeshe ni wapi tunakwenda kupata mbolea, kipo kiwanda pale kinazungumzwa muda mrefu sana cha LNG. Kile kiwanda kingefanya kazi kutupatia malighafi nzuri sana kwa ajili ya kutengenezea mbolea, lakini leo hii tunakwenda kwenye uhuru wa miaka 60 hatuna kiwanda chochote kile cha mbolea chenye uhakika cha kuweza kukitegemea. Hapo utaona kabisa kwamba bado hatujaamua kuwekeza kwenye kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu; Mpango huu utakapokuja utuainishie kuna mkakati gani kwa ajili ya kuinua kilimo chetu. Kikubwa ambacho nakiona kwamba hii mipango tunayokuja nayo huwa hatujaifanyia tathmini kila baada ya mwaka. Tunapoletewa Mapendekezo ya Mpango huu, vile vile tuambiwe mwaka jana kwenye kilimo tulikuwa tumepanga nini na tumefikia wapi? Kwa nini hatukufikia tulipokusudia kufika na kama tumefika, tumefika kwa nyenzo zipi. Kwa akili yangu ya kawaida nasema hatujafika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala lingine, suala la utalii. Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Samia Suluhu Hassan, ameamua kukuza utalii nchini. Sasa ombi langu kwenye Mpango utakaokuja tuone ni namna gani tunakwenda kupokea hao watalii, tumejiandaa vipi kupokea hawa watalii. Kwa taarifa nilizonazo, hawa wamiliki wa ndege zetu hizi ndogo ndogo ukiachia Air Tanzania, kwanza ni wachache, halafu uwekezaji kwa hapa nchini wanasema ni ghali mno na hizi Regulatory Authorities nazo ni nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi leo hii mtalii gani atakuja, ambaye anaambiwa kutoka Dubai kuja Dar es Salaam ni rahisi zaidi kuliko kutoka Arusha kwenda Mikumi, kweli are we serious? Kama mtu anatoka nje, anakuja kutalii analipa fedha kidogo, kuliko fedha atakayolipa kutoka Arusha kwenda Ngorongoro. Hili jambo naomba mpango utakapokuja watueleze, mama anahangaika huko kuimarisha utalii na huku Mawaziri watuonyeshe kwamba tumejiandaa, tunazo ndege kiasi gani za kupokea hawa watalii kupeleka kwenye hizo hifadhi zetu na kwenda kwenye vivutio vyetu. Tuna ndege kiasi gani? Tuna watoa huduma wangapi? Jambo hili naomba watakapokuja nalo lizungumzwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna jambo hapa kama nimeanza kulisikia sikia kuna azimio la anga la Jumuiya Afrika Mashariki, anga huru la Jumuiya Afrika Mashariki, mpango huu utakapokuja utuambie ikitokea azimio hili kweli likaletwa hapa Tanzania tumejiandaa vipi kulipokea, maana inawezekana mkafungua hili anga mkifungua mnawafungulia watu tu ninyi mna ndege tano wengine wana ndege 1,000 unaingiaje kwenye utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mpango utakapo kuja naomba utuelekeze mpango huu utakapoletwa utuambie tumejiandaa vipi kukabiliana na janga hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nijielekeze kwenye sera mara nyingi tunazo sera ambazo zinamipaka yake labda niseme miaka mitano, miaka miwili lakini tunazo sera zingine ambazo hazina limit na utekelezaji wake umekuwa ni mgumu sana kwa sababu hatuna kipimo. Mfano tumekuja na sera kuunganisha barabara zetu za mikoa na kila mkoa hatujasema mpaka lini, matokeo yake sasa hivi tumehama tunaenda kuunganisha wilaya wakati bado kuna mikoa bado hatujamaliza kuiunganisha na hii ni kwa sababu hatujajipa muda ifikapo mwaka fulani tutakuwa tumemaliza kuunganisha mikoa tuingie kwenye hatua nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sera ambazo zinakuja bila kuwa na muda maalum ndiyo hizo zinakuwa zinatubabahisha tunakuwa hatujui nini tunafanya matokeo yake tunaruka kwenye hatua moja tunaenda hatua nyingine kabla hatua ya pili hatujamaliza, leo hii kuna mikoa bado hatujaweza kuiunganisha lakini tayari tumeshaanza kuunganisha Wilaya kwa Wilaya. Sasa zile Mikoa sijui tumeacha au sera imekufa sijaelewa hapo.

Mheshimiwa mwenyekiti, kwa mfano tuko na sera nyingine kwamba kila kata iwe na kituo cha afya, nashukuru mwaka huu Serikali imekuja na Sera nyingine kwamba siyo kwamba kila kata itajengwa kituo cha afya badala yake tunakwenda kujenga kituo cha afya kwa kimkakati kulingana na uhitaji na mazingira yaliyopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini je, tumeshaletewa tathimini tunapokwenda kuiacha ile sera tunakuja na sera nyinge tumeshaletewa tathimini hapa Bungeni kwamba tuonyeshe kwamba ile sera tuliyokuja nayo ya kila Kata na kituo cha afya imetufikisha wapi? Ina shida gani? Na kama ilikuwa na mafanikio kwa kiwango gani? Kwa hiyo, ninaiomba Serikali kwa hayo machache ilikuwa mchango wangu kwa hayo mambo mawili tu Kilimo, Utalii na hii ya Sera. Ahsante sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi jioni ya leo nami nichangie hoja iliyo mbele yetu. Kwanza kabisa nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha sisi wote kuwepo hapa tukiwa na afya njema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo vibaya kuendelea kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna anavyoiheshimisha Tanzania. Hatuna cha kumlipa mama yule zaidi ya kumwombea dua. ndugu Watanzania tuendelee kumwombea dua Mwenyezi Mungu ampe umri mrefu ili aendelee kuiheshimisha Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utajikita zaidi kwenye Kamati ya Miundombinu kwa sababu nahudumu kwenye Kamati hiyo. Kwa hiyo basi, mchango wangu ni kusisitiza yale ambayo Kamati wameyazungumza. Hapa niseme, naipongeza sana Kamati yangu ikiongozwa na Mwenyekiti wetu, Mheshimiwa Selemani Kakoso kwa kazi kubwa tuliyoifanya mpaka kufikisha Kamati kuweza kuleta taarifa hii hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, msisitizo wangu, naomba niiambie tu Serikali, tunayo sera. Nianze na sera ya kuunganisha mikoa ya Tanzania kwa barabara za lami. Sera hii kama haitekelezeki, siyo dhambi tukaiondoa kama ambavyo tuliondoa sera ya kujenga kituo cha afya kila kata, tukasema tunaenda kujenga kituo cha afya kwa mujibu ya mahitaji. Vile vile kwenye sera hii, kama tunaona hatuwezi kuifikia, basi tuiondoe kuliko kuendelea kubaki hapa wakati utekelezaji wake bado unasuasua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza hivyo kwa sababu, leo kuna baadhi ya mikoa bado kabisa haijawahi kuunganishwa kwenye mikoa hii, lakini tayari tumechangia kwenye kuunganishwa wilaya kwa wilaya kwa barabara za lami. Mfano mzuri Mkoa wa Lindi na Mkoa wa Morogoro bado haujaunganishwa kwa kipande cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kulisisitiza ni kuhusu Sheria ya Manunuzi ya Umma. Kama kuna jambo linatukwamisha Watanzania kwenye hizi Taasisi zetu ni za Umma kufanya biashara au kwenda na ushindani, ni kwa sababu ya Sheria ya Manunuzi ya Umma. Nitoe hapa mfano wa TTCL. Shirika hili lilitakiwa kununua mitambo iliyokuwa imeachwa na Celtel, lakini kwa sababu tu sheria hairuhusu kununua mitambo ya Secondhand, ile mitambo ilinunuliwa na watoa huduma wengine na wanaitumia. TTCL tumeshindwa kuinunua kwa sababu kwenye sheria zetu hairuhusu Taasisi ya Umma kununua vifaa secondhand. Hili jambo naomba liangaliwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huko huko kwenye TTCL, wao wanachukua fedha kutoka UCSAF kwa ajili ya kupeleka minara kwenye sehemu ambazo hazina mvuto wa kibiashara, lakini wale TTCL pamoja kwamba wamepewa miradi hiyo, utekelezaji wao upo chini sana ukilinganisha na watoa huduma wengine. Leo hii Vodacom akipewa shilingi milioni 200, kesho anaingia dukani, ananunua vifaa, anakwenda kutengeneza mradi. TTCL akipewa shilingi milioni 200 ataanza kutangaza tender miezi mitatu; Sijui Bodi ya tender ikae miezi miwili. Mpaka kuja kupata mkandarasi tunachukua miaka mitatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili nalo siyo jema. Kama kweli tunataka kusaidia hizi taasisi zetu za Umma zifanye biashara, basi hatuna sababu ya kuacha kufanya mapitio Sheria yetu ya Manunuzi ya Umma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninaloweza kushauri ni kuhusu TAZARA. Wakati TAZARA inaanzishwa umuhimu mkubwa ilikuwa ni Wazambia walikuwa wanaihitaji zaidi kuliko Watanzania. Lakini leo baada ya maendeleo ya kiteknolojia Wazambia wameshaonesha nia kwamba hii TAZARA hawaihitaji tena, yaani siyo muhimu tena kwao, siyo kipaumbele tena kwao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake ni nini; matokeo yake sisi Watanzania hatuwezi kuweka mtaji pale kwa sababu ukishaweka mtaji pale unakuwa ni mtaji wa nchi zote mbili. Tena sheria yenyewe inaitaja TAZARA kama Zambia ndio wana share kubwa kuliko Tanzania.

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Kuchauka.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, basi baada ya hayo naomba niunge mkono hoja. Ahsante sana kwa kunisikiliza. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba hii ya Waziri Mkuu mchana huu wa leo.

Naomba nianze tofauti kidogo na mwaka jana wakati nachangia hotuba hii. Mwaka jana nilisema Halmashauri ya Wilaya ya Liwale ina miaka 41 lakini haikuwa na jengo hata moja lenye hadhi ya kuitwa Wilaya. Hata hivyo, leo nasimama hapa kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana sana sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa Rais msikivu. Lakini vile vile namshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwakweli hotuba yangu aliitendea haki mwaka jana. Leo nasimama hapa tayari tumeshapokea fedha zaidi ya bilioni moja kwaajili ya kujenga jengo la Halmashauri, tumepokea milioni 500 tunajenga jengo la mkuu wa wilaya, tumepokea milioni 450 tumeanza ujenzi wa mahakama ya wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili ni jambo la kushukuru sana. Tangu tumepata uhuru hatujawahi kupata miradi mingi kwenye Halamshauri ya Wilaya ya Liwale kama tulivyopata mwaka huu. Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni, nasema ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile naomba nijielekeze kwenye mchango wangu kwenye kuboresha baadhi ya mambo machache yaliyojiri kwenye hotuba hii nzuri ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Mimi nianze kuzungumzia upande wa ajira. Kwanza nimshukuru Mheshimiwa Rais, kwa kuonesha nia na kudhamiria kuajiri watumishi wengi zaidi kwenye Wizara yetu ya Afya pamoja na Wizara ya Elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa mchango wangu ni kwamba; ninaomba Serikali izingatie ajira hizi kulingana na jiografia za mahali Halmashauri hizi zilipo. Mimi kule kwangu watu wanakuja kuchukua cheque number tu. Watumishi wengi wanaoajiriwa kuja Liwale wanakuja kwa ajili ya kuchukua cheque number tu. Mwaka juzi nilipata watumishi 81 kwenye kada ya afya, lakini kila tukikaa Kamati ya Mipango na Fedha, watumishi 10 hadi 20 wanahama. Kila mwezi 10 hadi 15 wanahama, kiasi kwamba mpaka leo hii nimerudi kule kule kwenye uhaba wa watumishi. Lakini wakati ule inaajiri kuna vijana walioko kule Liwale wanajitolea kwenye shule zetu na kwenye vituo vyetu vya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwongozo ulisema kwamba wanapoomba ajira basi waende kwa Mkurugenzi waambatishe na CV; yaani Mkurugenzi aandike kuonesha kwamba hawa vijana wamejitolea kwa muda ili waweze kupewa vipaumbele, lakini jambo hili halijawahi kufanyika. Ninao vijana pale wana miaka mitano wengine miaka sita wanajitolea wanataka kufundisha, wanafundisha shule kule lakini walimu wanaokuja kutoka nje wanakuja kuchukua cheque number na wanaondoka. Naomba jambo hili lizingatiwe kwenye suala la ajira ya vijana.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile, kwenye hiyo hiyo ajira wako watu waliomaliza mafunzo, yaani kwenye vyuo vya elimu pamoja na vyuo vya afya kwa mwaka 2019 au 2018 au 2016 lakini wanaajiriwa wengine wa mwaka 2019, 2018 na kwamba waliomaliza mwaka 2016 au 2015 bado hawajapata ajira. Jambo hili nalo liangaliwe. Kwanza wenyewe watakosa umri wa kuajiriwa. Maana kama umemaliza chuo mwaka 2014 leo hii 2022 tayari wanaoomba kuajiriwa utakuta umri umempita. Kwahiyo tutakapoajiri jambo hili mimi ningeomba lizingatiwe sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikitoka huko nielekee kwenye wananyamapori. Suala la wanyamapori hasa kwa sisi wenye halmashauri ambazo tunaishi karibu na hifadhi suala la wanyamapori limekuwa ni kero kubwa sana, hasa kwa upande wa madhara wanayapata wakulima kwa mazao yao kuliwa na wanyamapori. Ipo sera inasema wanapata fidia, lakini fidia zenyewe zinakuwa ni kidogo halafu zinakuja kwa kuchelewa. Ombi langu kwenye upande huu wa wanyamapori, Serikali sasa ione namna ya kuweka askari wa wanyamapori kwenye hizi kata ambazo ziko karibu na hifadhi ili waweze kupata ulinzi. Kata zenyewe ziko mbali, unaweza kukuta kata labda iko kilomita 70 au kilomita 100 kutoka Halmashauri ya Wilaya. Sasa ukitoa taarifa, mpaka anapokuja askari tayari kwenye vijiji vile watu washapata madhara yakutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ombi langu hapa, Serikali ione namna, ikiwezekana tuanze kuajiri polisi kata; yaani wale askari wa wanyamapori wa kata kama ilivyo kwa polisi kata ili tuweze kusaidiana kukabiliana na tatizo hili la wanyamapori kwenye hizi kata ambazo ziko kwenye mipaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nijielekeze kwenye suala la lishe. Pamezungumzwa kwenye lishe; mimi naomba nitoe ushauri, kwa sababu mimi mwenyewe ni mtaalam wa mambo ya usindikaji wa nafaka. Tanzania tuna tatizo kubwa sana kwenye usindikaji wa nafaka. Sisi kitaalam nafaka inasindikwa tuna-extract unga kwa asilimia 85. Lakini kwa utaratibu wa Kitanzania, ili uweze kukoboa watu wanakoboa mahindi mpaka asilimia 60. Kwa hiyo zaidi ya asilimia 40 ya nafaka tunapoteza. Na hii ni kutokana na kwamba sera haijawekwa, vizuri sijui wapo TBS sijui ni TFDA wale ambo sasa hivi wamebadilisha sijui wanaitwa nini sijajua vizuri. Sera zao hazieleweki, hawatoi mwongozo; kwamba ili mtu upate unga kutoka kwenye nafaka inakobolewa kwa asilimia ngapi ili unga uwe na ubora. Sasa hivi mnalisha watu pamba tu, kwa sababu kama mahindi au nafaka yote umeikoboa kwa asilimia 60 unabakiza nini? Tunashindana hata na panya; panya kwenye mahindi anakula kiini kile na lile ganda lote analiacha na sisi ndio tunaneemeka nalo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ipo haja ya kubadirisha sera yetu ya ulaji. Lazima TFDA itoe mwongozo; kwamba kila aina fulani ya chakula, ili ukipate kwenye uhalisia wake kinatakiwa kiwe processed kwa namna gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano, Mikoa ya Njombe, Iringa na Ruvuma ni wakulima wazuri sana wa mahindi lakini ndiyo mikoa inayoongoza kwa utapiamlo; unauliza watu wanapataje utapiamlo ilhali wanakula asubuhi, mchana na jioni? Tena unakuta vitumbo vimepanda kwa ajili ya sembe. Lakini wamekula pamba, hawajala chakula kinachotakiwa. Kwa hiyo ni lazima twende na wakati huo huo tuone namna ya kufika hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine; kulikuwa na miradi ilianzishwa kwenye nchi hii, kwamba kila halmashauri ilitakiwa ilete miradi ya kimkakati. Lengo la miradi ile lilikuwa ni kuongeza mapato kwenye halmashauri zetu. Baada ya mapato mengi ya halmashauri kuletwa Serikali Kuu wakasema sasa halmashauri nendeni mkatengeneze mkakati wa kubuni miradi, na watu wakabuni miradi. Kuna watu walibuni masoko, stendi; na sisi kwenye Halmashauri yetu ya Wilaya ya Liwale tulibuni stendi, tukaletewa fedha lakini fedha zile kutokana na zile sheria zetu za manunuzi ambazo zinachelewa fedha zikaondoka, mpaka leo mradi ule umekufa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ile sera ya kuitaka halmashauri ije na miradi ya kimkakati imekufa? Maana tangu fedha zile zimeondoka huu ni mwaka wa tatu, hazitarajiwi kurudi. Lakini vilevile tulikuwa na mradi mwingine, mradi wa soko, hatuelewi uko wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mimi naiomba sana Serikali, kama kweli tunataka kuendeleza halmashauri zetu na kukuza vipato kwenye halmashauri zetu basi hii miradi ya kimkakati ipewe kipaumbele. Kama miradi iliyochukuliwa fedha zake basi fedha hizo zirudi, na kama hii miradi mingine mipya ianze ili kweli halmashauri zetu zipate mapato ambayo yanaweza kuhudumia jamii zetu mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine naomba nijielekeze kwenye upande wa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Jambo lingine muda wako umekwisha.

MHE.ZUBERI M. KUCHAUKA: Muda umeisha!

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, naomba kuanza mchango wangu kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai.

Pili naomba nikushukuru wewe kwa namna unavyoliongoza Bunge hili la awamu ya tano kwa umahiri mkubwa na weledi wa kiwango cha juu. Pia nitumie fursa hii kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa John J. P. Magufuli kwa namna Mwenyezi Mungu alivyomjalia vipawa mbalimbali inavyomwezesha kuliongoza Taifa letu kwa weledi mkubwa. Na mwisho lakini si kwa umuhimu nitoe pongezi za pekee kwa Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa na unyenyekevu mkubwa aliouonyesha katika kumsaidia Mheshimiwa Rais katika kuliongoza Taifa hili. Pia nimpongeze yeye pamoja na wasaidizi wake katika ofisi yake kwa namna wanavyojituma kulitumikia Taifa hili.

Mheshimiwa Spika, baada ya utangulizi huo sasa naomba nianze mchango wangu kwa kuanza na sekta ya uwekezaji. Pamoja na mazingira mazuri ya uwekezaji nchini lakini bado kuna watendaji hawaendi na kasi ya Rais wetu. Tatizo lingine ni upatikanaji wa ardhi kwa wawekezaji hasa kwa wawekezaji wa mashamba makubwa, kodi nazo kwa wawekezaji sio tu zimekuwa kubwa pia zimekuwa nyingi zinazofanana. Hapa nina maana mamlaka za usimamizi ni nyingi mno zinazofanana kimantiki japo zina majina tofauti.

Mheshimiwa Spika, sekta nyingine ninayopenda kuchangia ni sekta ya ardhi, Taifa letu sasa linakumbwa na tatizo kubwa la uuzwaji holela wa ardhi. Huku vijijini watu wanauza sana bila ya utaratibu. Serikali za Vijiji zimepewa mamlaka ya kuuza si zaidi ya heka 50, lakini wajanja huenda huko vijijini na majina ya ukoo mzima ili wapate ardhi kubwa zaidi. Mfano Mkoa wa Lindi lindi hili la uuzwaji wa ardhi ni mkubwa sana kwa ajili ya mashamba ya korosho na ufuta. Hili linaenda sambamba na uharibifu mkubwa wa mazingira unaosababishwa na ukataji hovyo wa miti kwa kigezo cha kufungua mashamba makubwa.

Mheshimiwa Spika, lingine katika hili ni suala la mipango miji, idara hii ina uhaba mkubwa wa wataalam wa mipango miji jambo linalosabisha miji yetu isipangike na badala yake tunakuja na sera ya urasimishaji. Katika Halmashauri zetu urasimishaji huu unatuongezea matatizo badala ya kutatua tatizo. Naomba kuishauri Serikali kuongeza wataalam wa upimaji na upangaji miji katika Halmashauri zetu nchini.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ninaloomba kuchangia ni juu ya taasisi au idara za Serikali zile zilizotengewa fedha zake kwa mujibu wa sheria, kama vile REA, maji UCSAF na kadhalika. Fedha hizi ni bora zikaenda kwa wakati mara zinapokusanywa kutoka Serikali Kuu kwani iko miradi inayokwama au kuchelewa katika taasisi hizo kwa kigezo cha ukosefu wa fedha na kwa kuwa fedha zilitengwa mahususi kwa kazi hizo basi Serikali ione umuhimu wa kupeleka fedha hizo haraka.

Mheshimiwa Spika, lingine ni kuhusu wastaafu; kumekuwa na ucheleweshaji mkubwa kwa wastaafu kupata mafao yao, kwa sasa muda mfupi zaidi kwa mstaafu kupata mafao yake ni miezi sita. Naiomba Serikali kupunguza muda huu kwani wastaafu hawa huwa ni kama adhabu kustaafu kwao, wakati wengine kama si wote wamelitumikia Taifa hili kwa weledi utumishi uliotukuka. Hivyo basi Serikali ione umuhimu wa watu hawa kupewa stahiki zao mapema iwezekanavyo.

Mheshimiwa Spika, naiomba pia Serikali ifanye utafiti wa kina kuona kama ni Mkoa gani, una umri gani, Wilaya gani ina umri gani au ni Halmashauri gani ina umri, hili litaisaidia Serikali inapojenga majengo yake ya kitaasisi yawe uwiano wa kitaifa zaidi. Mfano ziko Wilaya au Halmashauri za muda mrefu hazina majengo ya Kiserikali, wakati ziko Wilaya mpya au Halmashauri mpya zimekamilika kwa majengo hayo.

Mheshimiwa Spika, Liwale ni miongoni mwa Wilaya za Mkoa wa Lindi, Wilaya hii ni ya tangu mwaka 1975 lakini hadi leo hii Wilaya hii haina jengo hata moja lenye hadhi ya Wilaya. Wilaya ya Liwale, haina ofisi ya Mkuu wa Wilaya, haina jengo la Mahakama ya Wilaya, haina jengo la Polisi la Wilaya, haina jengo la Hospitali ya Wilaya, haina jengo la Halmashauri ya Wilaya. Hii ni mifano michache niliyoamua kuitoa kusisitiza hoja yangu.

Naiomba Serikali kuzingatia ushauri wangu ili kuimarisha umoja wa Taifa letu katika kugawana keki yetu.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema hayo naomba nirudie tena kuishukuru tena Serikali ya awamu ya tano kwa niaba ya Wanaliwale kwa kuendelea kutupatia umeme vijijini, kutujengea vituo viwili vya afya, kutupatia miradi ya maji katika kata nne, Wanaliwale wanamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa yote tuliyotendewa na Serikali yake ya CCM.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, leo naomba nianze mchango wangu, kwanza kumpongeza sana Mheshimiwa Rais mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa muda wake mfupi wa kuongoza nchi yetu baada ya kifo cha Rais wetu wa Awamu ya Tano Mheshimiwa John Pombe Magufuli. Mheshimiwa Samia ameonesha umahiri mkubwa wa kuliongoza Taifa letu, na hatimaye kutuletea bajeti hii ambayo inakwenda kujibu kero nyingi za wananchi wetu na kuboresha uchumi wa nchi yetu. Mimi binafsi nampongeza sana Mheshimiwa Rais na namwombea kwa Mwenyezi Mungu ampe afya njema na umri mrefu wenye manufaa kwake na kwa Taifa letu.

Lakini pia nimpongezi Mheshimiwa Waziri na watendaji wote katika Wizara hii kwa kuja na bajeti nzuri yenye kuzingatia maoni mengi ya Waheshimiwa Wabunge walipochangia Wizara mbalimbali za kisekta. Hii inaendelea kuthibitika kuwa Serikali yetu inayoundwa na CCM ni Serikali sikivu, inayozingatia maoni ya wananchi wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo yote sasa naishauri Serikali kuendelea kusimamia utekelezaji wa bajeti hii nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya utangulizi huo hapo juu naomba sasa kuishauri Serikali kuzingatia yafuatayo ili kuboresha utekelezaji wa bajeti hii:-

Kwanza katika Wizara ya Ujenzi, iko miradi ya aina kuu mbili katika ujenzi wa barabara zetu hapa nchini; miradi ya upembuzi na usanifu wa kina wa barabara zetu, miradi imekuwa ikiigharimu Serikali fedha nyingi na miradi ya ujenzi wa barabara zilizokamilika kwenye hatua hiyo hapo juu.

Katika hatua hii naishauri Serikali kupunguza au kuacha kuendelea na miradi ya upembuzi yakinifu hadi pale barabara zote zilizokwishakamilika katika upembuzi na usanifu wa kina zitakapofikiwa hatua za ujenzi. Nayasema haya kwa kuwa tunazo barabara nyingi zilishafanyiwa upembuzi na usanifu wa kina kwa muda mrefu. Kwa kuwa zinakaa muda mrefu bila kujengwa, na pale tunapokwenda kuzijenga tunalazimika kuzirudia upembuzi upya jambo ambalo linaongeza gharama za ujenzi bila sababu, kwa nini tuendelee kufanya upembuzi kwenye barabara mpya kabla ya ujenzi wa zile zilizokamilika?

Pili ni kuhusu uhifadhi wa wanyama pori; hapa naomba kuishauri Serikali kuja na mpango mkakati wa kuimarisha hifadhi zinazomilikiwa na jamii zijulikanazo kama WMAs. Hifadhi hizi zinamilikiwa na jamii, lakini Serikali isipokuja na mkakati maalum zinakwenda kufa. Kuimarika kwa hifadhi hizi kungepunguza sana manung’uniko katika jamii hasa zile Halmashuri zinazopakana na hifadhi zetu za Kitaifa. Kuimarika kwa WMAs wananchi wetu wanaenda kuona manufaa ya moja kwa moja uwepo wa wanyama hawa, pale ambapo mfano WMAs watajenga darasa au choo na miradi mingine kama hiyo ambayo inaenda kugusa maisha yao ya kila siku.

Mheshimiwa Naibu Spika, WMAs wasaidiwe kutafuta wawekezaji kwenye vitalu vyao na kuvifanyia matangazo ili kuvutia wawekezaji. Sambamba na hilo niiombe sana Serikali kuharakisha malipo yao ya hizi jumuiya yanatolewa kwa wakati. Hapa napo napendekeza malipo hayo yaende moja kwa moja kwenye jumuiya badala ya kupitia TAWA ambako zinachelewa sana kuwafikia walengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, narudia tena WMAs zikifanya vizuri zinasaidia sana kupunguza machungu kwa jamii yanayotokana na athari za wanyamapori. Lakini pia ni ukweli usiopingika kuwa uwezo wa kuzitangaza hifadhi hizi zinazomilikiwa na WMAs wakiachiwa wenyewe ni mdogo sana.
Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo, wa Mwaka 2016
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi jioni hii niwe mchangiaji wa kwanza na mimi mchango wangu utajikita sana kwenye hii Taasisi ya Utafiti wa Kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maneno ya utangulizi, Watanzania tumekuwa Wataalam wazuri sana wa kutunga sheria kama ambavyo tuko wataalam wazuri sana wa kupanga mipango, tatizo letu kubwa liko kwenye upande wa utekelezaji, kwamba ni nani anaingia kwenye utekelezaji. Kwa hiyo, kuja na Muswada huu, Serikali imeleta Muswada huu ni mahali pake kabisa kama ambavyo kauli mbiu inavyosema kwamba tunakwenda kwenye nchi ya viwanda na hatuwezi kwenda kwenye nchi ya viwanda kama tukisahau kilimo na hatuwezi kufanikiwa kwenye kilimo kama hatukuweza kufanya utafiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyotangulia kusema, tatizo langu ni matumizi ya hizi tafiti. Je, tuko tayari kutumia hizi tafiti? Je, tunao wataalam wa kutosha wa kutafsiri hizi tafiti? Je, tuna mikakati ya kufikisha matokeo ya hizi tafiti kwa walengwa? Hapo ndipo ambapo napata ukakasi kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu muundo wa Bodi ya Utafiti wa Kilimo, hapa naona pana upungufu kidogo, sijawaona watu wa Bodi za Mazao, kwa sababu hawa watu wa Bodi za Mazao ndiyo hasa mara nyingi wako na wakulima wa mazao husika, lakini hapa kwenye Bodi hii hawa Watafiti wa mazao sijawaona, badala yake nimekuta hapa hii namba 5(2) kuna Mkurugenzi wa Halmashauri, nafikiria badala ya kumweka huyu Mkurugenzi wa Halmashauri tungemweka Mwakilishi yeyote kutoka kwenye Bodi ya Mazao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija Namba Nne, unakutana na kazi za taasisi, moja ya kazi za taasisi nimeona hapa wameandika kuhamasisha matumizi ya mbegu bora. Matumizi ya mbegu bora ni lazima yaende sambamba na matumizi ya pembejeo za kilimo, sasa nazo hapa sijaona, Ningependekeza kazi mojawapo hawa Watafiti angalau wangepewa ni hii ya kuhamasisha matumizi bora ya mbegu na viuatilifu kama mbolea na pembejeo nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwenye muundo tumeambiwa patakuwa na Baraza, hili Baraza nalo sijaona katika wawakilishi sehemu hii namba 12, sijaona Mwakilishi hapa kutoka Bodi ya Mazao, bado wanaendelea kusahaulika hawa na hawa mara nyingi wana vikao vya Bodi vinakaa at least kila mwaka kufanya tathmini ya mazao mbalimbali. Ningetegemea kwamba pangekuwepo na ripoti ya utafiti ikaletwa kwenye vikao hivi vya Bodi vikatusaidia, lakini hapa napo sijaona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu matokeo ya utafiti. Sijaona mkakati kwenye Muswada huu ni namna gani matokeo ya utafiti yatawafikia walengwa ambao ndiyo hasa wazalishaji. Kwa sababu tunayo matatizo, nikitolea mfano, mimi ni mdau wa zao la korosho, kwenye zao la korosho tunayo matatizo na hawa watu wa utafiti, mara ya mwisho tuliambiwa pembejeo, viuatilifu wanasema vile vya maji ni bora zaidi kuliko vile vya unga. Tukaja tena tukaambiwa lakini vile viuatilifu vya kimiminika (maji) vinatumika masika, wakati korosho sisi tunapulizia kiangazi, sasa bado tunapata mkanganyiko na mkanganyiko huu ulitakiwa tupate majibu kutoka kwa hawa Watafiti wanatusaidiaje, lakini utaona kwamba chain ya kutoka kwa Watafiti mpaka kwa watumiaji sijaiona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikirejea hapo kwenye korosho, tumeletewa mbegu tukaambiwa hizi mbegu ni za muda mfupi. Ni kweli baada ya miaka mitatu hii mikorosho huwa inazaa lakini tatizo lake iko kwenye lifetime ya mkorosho. Ile mikorosho yetu ya asili hata miaka 20 unavuna tu, lakini hii mikorosho ambayo imeletwa na hawa watafiti bado inatupa shida. Utakuta kwamba tunakosa watu sasa wa kuja kututafsiria au kutuelekeza kwamba hii mikorosho itakaa kwa muda gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye jedwali namba moja, sehemu ya tatu. Kuna hawa Wajumbe wa Bodi, inasemwa kwamba pakiwa na mgongano wa maslahi, kuna neno limetumika hapa kwamba ikiwezekana, sijaelewa unaposema ikiwezekana maana yake nini, kwamba it is optional, anaweza aka-declare au la. Mimi naona hapa kipengele hiki nacho kingeweka wazi ili na sisi watumiaji wa hii sheria tuweze kupata ufafanuzi unaoridhisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utafiti, nimeangalia kwenye huu Muswada wote, mkazo kwenye utafiti wa masoko sijauona na tatizo kubwa la mazao ya kilimo ni masoko. Kwa sababu hata ukiangalia upungufu wa uvunaji au uzalishaji unategemeana na soko. Mfano kule kwetu tunalima sana korosho, ufuta na mbaazi, haya mazao yana matatizo ya kubadilishana masoko. Mwaka ambao soko la korosho limepanda, basi mwaka unaofuata litashuka na mwaka ule likishuka watu wanalima mbaazi, mbaazi nazo zikishuka watu wanalima korosho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo watu wetu hawako stable. Sasa na hawa watu wa utafiti nao sijaona, sijui kwa sababu sasa hivi ndiyo wamesema kwenye Muswada huu kwamba tutaimarisha hiki kitengo cha utafiti, lakini bado naona tuna matatizo, tuna-base sana kwenye utafiti wa mazao, kuongeza ubora na wingi labda hivyo, lakini bado kwenye upande wa masoko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mmeona kwenye huu Muswada, kipengele hiki cha maeneo ya utafiti, sehemu ya Nane, kipengele (l) nafikiri ndiyo kimegusia kidogo kuonesha kwamba, yaani kama kuna masoko. Ningetegemea hivi vitu vyote viwili vingeenda sambamba, unapozungumzia utafiti wa kilimo moja kwa moja hapohapo lazima uingie kwenye utafiti wa masoko kwa sababu tatizo kubwa tunalo hapo kwenye upande wa masoko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla basi ningependekeza kwamba ili tuweze kwenda sambamba na utafiti wa kilimo, basi ni lazima twende sambamba na utafiti wa masoko, tena hili la masoko kwenye hii sehemu ya maeneo ya utafiti, yaani imetupwa mbali sana kuonekana kwamba hatuko tayari. Vilevile, tukirudi kwenye utafiti nafikiri kwamba watu wanaoweza kututafsiria hizi tafiti na kutuletea hizi tafiti…
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Kuchauka.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 3 wa Mwaka 2017
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi nichangie Muswada ulio mbele yetu. Awali ya yote napenda nitoe utangulizi kama ambavyo muswada huu unavyosema ni marekebisho ya Sheria mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi tu nataka niwape tahadhari Waheshimiwa Wabunge kwamba moja ya majukumu yetu makubwa ni kutunga Sheria na tunapoifanya kazi hii mimi ningependekeza kwamba tuwe makini kwa maana kwamba tuache mitazamo yetu ya vyama, tuangalie wananchi wetu wametuleta hapa tufanye nini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nasema hivi? Uwepo wa hii Sheria ambayo imetungwa kwenye Bunge lililopita leo tunakuja kufanya marekebisho inaonesha kwamba ni jinsi gani hatuko makini katika kazi hii. Ningeomba sana hasa hasa Waheshimiwa Wabunge wa Chama tawala maana wao wanapitisha hizi Sheria kwa sababu tu Serikali ndiyo imeleta wao wanaona ni sahihi kupitisha kama ilivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi huku tukisema kwamba hili jambo si sahihi tunakuwa tunaonekana kama sisi ni wapingaji tu. Mimi nataka niwaambie Waheshimiwa Wabunge, kwamba kuletwa kwa Sheria ambayo tumeipitisha mwezi uliopita leo inaletwa kuifanyia marekebisho, hatuko makini katika kazi hii na tutahukumiwa kwa hili. Huo ni utangulizi nilikuwa naomba niweke sawa jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nikirejea kwenye point hii ya RUBADA; naunga mkono kufutwa kwa hii Mamlaka ya Mto Rufiji lakini napingana kidogo na mawazo ya Kamati. Kamati wamesema kwamba wameridhika na hili jambo la ufutwaji wa hii lakini je, ni Taasisi gani imetajwa rasmi kwamba ndiyo itashughulika na majukumu yote yaliyokuwepo RUBADA, maana hapa mimi nimepitia nimeona kwamba Serikali itachukua jukumu hili, lakini haijatajwa hata Wizara ipi itashughulikia sasa, kama ni Wizara ya Ardhi,, Wizara ya Maliasili na Wizara gani hasa specific haijatajwa kwamba majukumu yale ya RUBADA yataelekezwa wapi.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile Kamati imependekeza uwepo na Ofisi ya madeni ina maana kwamba hiyo fisi itashghulika na mambo ya madeni tu lakini hii RUBADA ilikuwa na shughuli nyingi na hata haya Mashirika mengine ambayo yamependekezwa hapa, kwamba RAHCO nayo ielekezwe huko. Hata hivyo, hii RAHCO haikushughulika na masuala ya madeni tu yaani jambo ambalo ilikuwa inashulika nayo ni suala siyo la madeni peke yake ambayo yanatakiwa yarithiwe na hii Kampuni au Taasisi hiyo itakayoshughulika.

Mheshimiwa Naibu Spika, naona ingetajwa specific kwamba hiyo Serikali ambayo imeshauriwa iundwe Ofisi ya madeni, basi siyo madeni peke yake na majukumu mengine yote ambayo yalikuwa yanafanywa na RUBADA au na hilo Shirika ambalo litafutwa basi ielekezwe huko. Hilo ndilo lilikuwa jambo ambalo nilikuwa nashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka vile vile nijielekeze kwenye upande wa DAWASCO au DAWASA. Tatizo la maji taka na maji safi kwa mji wa Dar es salaam si tatizo la DAWASCO au DAWASA tu, hili ni tatizo la Wizara nzima, kwamba tuko makini kiwango gani katika kuipatia fedha au kufanya utaratibu ili twende na wakati; kwa sababu Jiji la Dar es salaam linakuwa na ongezeko la watu siku hadi siku; sasa, Wizara ina mikakati gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri kwamba suala a kuiongezea majukumu DAWASCO au DAWASA si solution pekee, kwa sababu solution pekee ni kuchunguza kwa nini DAWASCO imeshindwa kuetekeleza majukumu yake? Hapo ndipo ambapo Wizara au Serikali kwa ujumla wake walitakiwa waiangalie; kwa sababu lengo la marekebisho haya ya Sheria hizi ndogo ndogo lengo ni kuboresha ili jamii au wananchi wapate huduma ambayo inakusudiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa unapokwenda kuongezea majukumu DAWASCO ukaona ndiyo solution pekee badala ya kuangalia ni kwa nini tumefeli katika nyanja hiyo, nafikiri hili si jambo sahihi zaidi. Nafikiri kwamba badala
ya kuiongezea DAWASCO majukumu kama ambavyo imetajwa hapa, ipo haja sasa pengine hata kutengeneza taasisi nyingine ambayo itahusika moja kwa moja na masuala haya ya maji safi na maji taka kwa Jiji la Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa muktadha huo, sina mambo mengi sana zaidi tu napenda kusema kwamba, naunga mkono mia kwa mia maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani, tuyazingatie. Mara zote nataka nirejee Waheshimiwa Wabunge mjue kwamba jukumu letu ni kutunga sheria, haya mambo ya hati za dharura hayatatufikisha popote na sana sana yatatuondolea umakini wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Muswada wa Sheria ya Shirika la Mawasiliano Tanzania wa Mwaka 2017
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii niwe mchangiaji wa kwanza wa Muswada huu. Kwa utangulizi kwanza napenda kushukuru na niseme kwamba, ni Mjumbe wa Kamati ya Miundombinu, kwa hiyo Muswada huu nimeupitia kwa ukamilifu zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu kuishukuru Serikali kwamba imeona kuleta huu Muswada, lakini kabla sijafikia hatua ya kujadili, nataka tu niiase tu Serikali kwamba tatizo letu kubwa sio tu utungaji wa sheria. Jukumu hili sisi kama Wabunge huwa tunalifanya kwa ukamilifu na umakini mkubwa sana, lakini tatizo letu kubwa ni namna gani hizi sheria tunaenda kuzitekeleza hasa kwa wale waliopewa dhamana ya utekelezaji wa sheria hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mtazamo huu, ninavyoiona Serikali ya Awamu ya Tano sasa tunataka kwenda kujielekeza kwenye kufanya biashara kwa sababu mtazamo wa huko nyuma, tulikuwa tumebinafsisha haya Mashirika ya Umma kwa maana kwamba Serikali ilikuwa inajitoa kwenye kufanya biashara ili iweze kusimamia namna ya uendeshaji wa nchi yetu. Sasa kwa mtazamo huu inaonekana kabisa moja kwa moja kwamba tunakwenda kuingia kwenye biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, bado kwa mfano kama hili Shirika la TTCL hatujaambiwa ni kwa msingi gani, ni kwa nini shirika hili lilibinafsishwa likauzwa na Serikali katika mauzo ya shirika hili tulipata kiwango gani. Vilevile sasa hivi tunakuja tunaambiwa hili shirika sasa sisi ndio tumenunua hisa za iliyokuwa Zain ili shirika hili tuweze kulimiliki kwa asilimia 100, lakini bado hatujapata ufafanuzi ni kwa nini tuliliuza na kwa nini leo tunaamua kulinunua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika uundwaji waTTCL, TTCL kama ambavyo Kambi Rasmi ya Upinzani ilivyosema tunalo tatizo la Serikali kutokuwapa mamlaka kamili wale viongozi au wasimamizi wa mashirika haya. Mara nyingi tumekuwa tunaendesha mashirika yetu haya ya umma kwa kauli ama kwa matamko badala ya kuacha ma-CEO wa makampuni haya waweze kuyasimamia kwa weledi. Nikitoa mfano hivi majuzi tu, shirika letu hili jipya la ATCL, ndege imesimama kwa zaidi ya dakika 45 eti inamsubiri Waziri fulani hajafika airport. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii inaharibu kabisa taratibu za uendeshaji wa mashirika haya na sijui Serikali itaepukaje katika hili shirika ambalo tunaenda kuliunda leo lisiendeshwe kwa matamko kama ambavyo ilitokea huko nyuma. Hii ndio sababu kubwa inayopelekea mashirika yetu kushindwa kufanya vizuri kwenye medani za ushindani.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii tunaletewa Muswada wa kuunda shirika la TTCL, lakini ninachoomba Serikali ije na majibu ni kwa namna gani TTCL itaweza kushiriki kwenye ushindani uliopo ambao huko nyuma tumeshindwa kutekeleza. Kama ambavyo Mheshimiwa Waziri amesema, madhumuni makubwa ya kulifufua hili Shirika la TTCL, nasema kulifufua kwa sababu nakumbuka kwamba lilikuwepo, ni kulinda maslahi ya Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha hoja yake ajaribu kutuainishia ni kwa namna gani tunaweza kulinda hayo maslahi ya Taifa, kwa sababu isiwe kama ambavyo sasa hivi inafanywa kufungia magazeti, kuwafanya watu wasiseme ikiwa ndio miongoni mwa mambo ya kulinda Taifa. Hayo yanaweza yakawa ndiyo ambayo Serikali imeona ndio mambo ya kulinda Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili kwa upande wangu naomba Mheshimiwa Waziri atakaporudi kuhitimisha hoja yake, ajaribu kutufafanulia na kuainisha kuweka wazi ni kwa namna gani shirika hili linakwenda kulinda maslahi ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika hili la TTCL kama mjumbe wa Kamati nilishawahi kutembelea, tuliingia pale kwenye ile sehemu ya data center, lakini kwenye Muswada huu wa sheria sijaona mahali ambapo imetajwa ni kwa namna gani kwamba ile data center itatumikaje na hasa kwenye taasisi za Serikali kwamba ni kwa namna gani TTCL mmeamua kuitangaza ile data center ili iweze kutumika kikamilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hivyo tu, kulingana na ushindani wa kibiashara uliopo, Serikali inatakiwa ituambie ni mtaji kiwango gani wanakusudia kuwekeza kwenye hili shirika ambalo tunakwenda kuliunda leo la TTCL. Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama ambavyo Kambi Rasmi ya Upinzani walitoa msisitizo juu ya namna ya uteuzi, kulikuwa na matatizo sana hapa ya uteuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kiongozi anaweza akateuliwa kwa ajili ya kuongoza shirika hili, lakini ni kiwango gani amepewa uhuru wa kuweza kutumia ujuzi na weledi wake, kwa sababu hapa inaonekana kama nguvu kubwa amepewa Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana kutoa, hasa kwenye maelekezo kwa Bodi na Bodi imekuwa ni lazima kuyafuata haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho wa siku shirika hili litakapokosa kufanya yale majukumu yaliyoafikiwa, atakayehukumiwa ni Mwenyekiti wa Bodi na Bodi yake, hatoweza kusema kwamba ameshindwa kuyafikia hayo majukumu kutokana na maagizo ya Waziri. Kwa hiyo, naomba niendelee kusisitiza maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwamba ni lazima hii Bodi tuipe uhuru kamili ili mwisho wa siku tuweze kuihukumu kwa namna ya utendaji wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika hili la TTCL kwa ujumla wake linakwenda kufanya mashindano na mashirika mengine yanayotoa huduma kama hizi. Sasa Serikali imejipangaje namna ya kuiwezesha TTCL kuingia kwenye ushindani huu?

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa, naomba nitoe angalizo kwa Serikali kulingana na matatizo mengi yanayojitokeza ya Serikali kuingilia mashirika yetu. Naomba kwa dhati kabisa kwamba hili ni jambo ambalo Serikali mnatakiwa mlichukue kwa umakini sana, kuacha kuingilia utendaji wa mashirika yetu ili tusirejee kule ambako tulitoka, mashirika haya yalishindwa kufanya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, huo ndiyo ulikuwa mchango wangu kwa leo. Ahsante sana.
Sheria ya Fedha ya Mwaka 2019
MHE. ZUBERI A. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi nitoe mchango wangu kwenye hii Finance Bill ya mwaka huu. Vilevile nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyenipa mimi uwezo jioni hii nisimame nitoe mchango huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna anavyoweza kusimamia maendeleo na kuhakikisha rasilimali za nchi yetu zinawanufaisha watu wote. Jambo kubwa ambalo haliwezi kupingika, jambo alilokuja nalo kuhusu vitambulisho vya wajasiariamali ni muhimu sana, ni ubunifu mkubwa sana na inasaidia sana kupunguza kero mbalimbali ambazo walikuwa wanazipata wajasiriamali wetu wadogowadogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwenye jambo hili, naomba nitoe ushauri kwamba ugawaji wa vitambulisho hivi ni vizuri vikazingatia takwimu ya wajasiriamali wa mahali walipo kwa sababu zipo sehemu za pembezoni kabisa, wilaya au mikoa ya pembezoni vitambulisho vimegawiwa kiasi kwamba hata uwiano wa wajasiriamali wa mahali pale unakuwa haupo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, sasa hivi ukienda Dar-es-Salaam (Kinondoni) vitambulisho vinatafutwa na havionekani lakini ukienda vijijini huko, Ifaraka ndani ndani au Mlimba huko, utakuta kuna wajasiriamali wanapewa mpaka wauza matango, ni kwa sababu tu Mkuu wa Wilaya anavyo vile vitambulisho hakuna wa kuwagawia. Kwa hiyo, zingechukuliwa takwimu sahihi kwamba hivi vitambulisho tunapeleka wilaya gani na kule tunategemea kupata wajasiriamali kiasi gani, lakini wazo la vitambulisho vya wajasiaraiamali ni zuri sana, ni kuboresha tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwaambie Wabunge wenzangu, hakuna mwanadamu akapanga jambo likakosa changamoto. Changamoto ndio chachu ya maendeleo, kwa sababu pasingekuwa na kitu kinaitwa uboreshaji pasingekuwa na changamoto, uboresha mahali ambapo umepata changamoto. Kwa hiyo, jambo hili ninalipongeza sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nawapongeza sana Wizara kwa namna wanavyokwenda kuvilinda viwanda vyetu vya ndani. Hapohapo kwenye kulinda viwanda vya ndani, naomba nitoe mchango wangu lazima Wizara waangalie kwamba gharama ya uzalishaji wa viwanda vyetu vya ndani ni kubwa sana kiasi kwamba tunapokwenda kusema tunaenda kuweka ushuru kwenye bidhaa za nje ili kulinda viwanda vyetu vya ndani tunaweza tuka-create scarcity ya bidhaa hiyo hapa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, kiutaalam mimi ni msindikaji wa nafaka, nimeshashuhudia jambo hili mara nyingi sana. Nitoe mfano mmoja, gharama ya kusindika ngano Tanzania mtu anashindwa kujenga kiwanda cha ngano nje ya Dar-es-Salaam kwa sababu tu hajawekewa exemption ya gharama ya usafirishaji wa malighafi kutoka Bandarini Dar-es-Salaam labda kuipeleka Mwanza au Mbeya. Mtu akijenga kiwanda Mbeya hawezi ku-compete na mzalishaji wa Dar-es-Salaam, lakini mtu aliyejenga kiwanda Uganda, malighafi ikapitia Bandari hii ya Dar-es- Salaam ana uwezo wa ku-compete na mzalishaji wa Dar-es- Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili hata mimi linanipa kutofahamu kidogo kwa sababu inawezekana vipi malighafi ipitie Dar-es-Salaam inakwenda Uganda, inachakatwa kule inaletwa Tanzania ana-compete na mzalishaji mwenye kiwanda Dar-es-Salaam lakini malighafi hiyohiyo huwezi kujenga kiwanda Mbeya kwa sababu utashindwa ku-compete na mzalishaji wa Dar es Salaam? Hapo naomba Serikali Serikali ijaribu kuliangalia suala hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia jambo hili ndiyo linalofanya viwanda vingi vijengwe Dar es Salaam hasa vile viwanda ambavyo tunategemea malighafi labda nusu yake inatoka nje ya Tanzania yaani tuna-import. Maana yake viwanda hivi huwezi kuvijenga nje ya Dar es Salaam ambapo ipo bandari kwa sababu gani? Ukivijenga Mbeya au Mwanza huwezi ku-compete na mzalishaji wa Dar es Salaam kwa sababu Serikali haijafikiria gharama za usafirishaji wa malighafi kutoka Dar es Salaam kupeleka Mbeya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, jambo hilo naomba Serikali walichukue na waliangalie kama kweli tuna nia, kwa mfano hapa wamesema kwamba Wakuu wa Mikoa wameagizwa wafungue viwanda kwenye mikoa yao. Utawezaje kufungua kiwanda ambacho labda nusu ya malighafi inabidi uagize kutoka nje. Ukikijenga nje ya Dar es Salaam, gharama hii ya usafirishaji ile bidhaa utashindwa kuiuza. Kwa hiyo, naomba Serikali ije na utaratibu iangalie namna ya kuviwezesha viwanda hivi kuvipanua pengine viwanda hivi vijengwe hata nje ya Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nataka niongelee suala la hizi bidhaa (transit goods). Mara nyingi, kama nilivyosema mimi ni msindikaji wa nafaka, nimeshafanya kazi zaidi ya miaka 25 kwenye kampuni ya watu binafsi kwenye sekta binafsi. Mnufaika mkubwa wa transit goods ni wafanyakazi wa TRA wale wasio waaminifu, hawa ndiyo wanaonufaika sana na hizi transit goods na huwezi kuwaondoa asilimia 100 wafanyakazi wasio waaminifu TRA. Sasa naomba Serikali ije na utaratibu tunafanyaje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano mmoja, kuna mwaka mmoja, mwaka kama 2005 hivi palikuwa na scarcity kubwa sana ya nafaka. Serikali kwa makusudi ikaamua kwamba nafaka zote ziondolewe ushuru na kweli zikaondolewa ushuru, lakini products zake hazikuweza kushuka. Kwa hiyo, ni nani walikuwa wanufaika wakubwa? Wanufaika wakubwa walikuwa wafanyabiashara na watu wa TRA.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, pamoja na nia nzuri ya Serikali ya kupunguza ushuru kwa lengo la kuwanufaisha wananchi, lakini bado kwenye ufuatiliaji na usimamizi kwamba, je, kile ambacho tumeondoa ushuru, manufaa haya kwa wananchi yamefika? Kwa hiyo, naiomba Serikali iwe na kitengo mahsusi cha kufuatilia hizi nafuu za kodi zinafikaje kwa walengwa. Vinginevyo tutaendelea kuwanufaisha wale ambao ni wafanyakazi/watendaji wa TRA na watu wengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naomba nitoe mchango wangu kama alivyochangia mchangiaji aliyepita kwamba kuna usumbufu mkubwa sana kwenye ofisi za TRA. Yaani mtu ni mlipakodi anakwenda kupeleka fedha kwenye taasisi ya Serikali halafu anasumbuliwa utafikiri yeye ndiyo anakwenda kuomba kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, jambo hili linapunguza vilevile morali ya watu kulipa kodi kwa sababu mfanyabiashara anatakiwa apange siku kwamba leo ni siku ya kwenda TRA, ina maana kama ni duka afunge, kama ni kiwanda kisimame, yeye anakwenda kulipa kodi TRA. Jambo hili ni jambo ambalo wanatakiwa waliangalie sana, jambo la kuliondoa. Jambo hili vilevile linapunguza hata wawekezaji, wengi linawakatisha tamaa pale wanapopata usumbufu wanapohitaji huduma hii muhimu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa na hayo tu mawili, nilitaka niyatolee ufafanunuzi katika mchango wangu wa leo. Vinginevyo naunga sana mkono hoja ya Serikali. Ahsanteni sana kwa kunisikiliza. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa, 2022
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi kuchangia Muswada ulio mbele yetu.

Mheshimiwa Spika, kwanza niseme mimi siyo Mwanasheria lakini yapo mambo ambayo nimeyaona kwenye Muswada huu, naomba niyazungumze, Mheshimiwa Spika utatuongoza tutayaweka wapi ili tujue tunayaweka kwenye nafasi ipi.

Mheshimiwa Spika, ninaishukuru Serikali kwa kuleta Muswada huu kwa sababu sasa hivi kutokana na maendeleo ya kibinadamu, teknolojia na shughuli mbalimbali za kibinadamu, huu Muswada ni mahali pake.

Mheshimiwa Spika, nianze na tafsiri ya neno maafa kwa mujibu wa nilivyoiona aya hii. Wameeleza kuwa maafa ni madhara yanayotokana na majanga ambayo yanajumuisha uharibifu wa mifumo ya kawaida katika jamii ambao unaweza ukasababisha vifo, majeruhi, madhara ya kisaikolojia, upotevu au uharibifu wa mali na kuendelea. Lakini mwisho wa tafsiri hiyo wakasema ni yale ambayo jamii au yule aliyepata madhara hawezi ku-recover, ndiyo yanakuwa sasa yale ni majanga.

Mheshimiwa Spika, sasa shida yangu ni kujua ni nani huyu sasa atakayesema kwamba janga hili haliwezi kuingia kwenye maafa kwa sababu jamii husika inaweza ika-cover, hapa ndipo napata shaka kidogo kwenye hii. Kwamba ni nani sasa huyo ambaye atakuja kusema kwamba kwa extent ya madhara haya yanafaa kuitwa maafa au haya hayafai kuitwa maafa.

Mheshimiwa Spika, hapa niende mbali zaidi, kuna maafa ambayo naomba ni-declare interest, mimi ni mmoja wa wahanga wa maafa yaliyotokana na Uchaguzi wa 2020. Nilichomewa nyumba zangu mbili, nikachomewa na magari matatu. Sisi kwenye ngazi ya Wilaya tukaunda hiyo Kamati ya Maafa ambayo ilikwenda mbali zaidi ikaleta valuer akafanya valuation. Ile ripoti ikapelekwa Mkoani, lakini kwa mujibu wa Sheria hii wakasema maafa hayo hayamo kwenye Sheria ina maana kwamba mimi siyo mnufaika wa maafa hayo.

Mheshimiwa Spika, sasa maana yangu ni nini? Je, mbona hapa kwenye sheria hapajatajwa? Kwamba yakaainishwa hayo maafa halafu wakayaondoa maafa hayo; kwamba maafa yanayotokana na uchaguzi hayatakuwa considered.

Mheshimiwa Spika, na nilikwenda mbali, nilifika mpaka kwa Mkurugenzi wa Uchaguzi majibu yakawa hayo hayo. Ile ripoti ya evaluation ilifika Ofisi ya Waziri Mkuu majibu yakawa yanafanana na hayo. Lakini vilevile hata kwenye Ofisi ya Mheshimiwa Spika nilifika kuomba msaada lakini ikaonekana kwamba si miongoni mwa hayo maafa. Sasa wasiwasi wangu unarejea pale pale. Kwamba, hivi ni nani atakayeweza kusema kuwa maafa haya huyu mtu anahitaji kusaidiwa?

Mheshimiwa Spik,a kwenye sheria hapa nimeona kumeundwa Kamati kuanzia ngazi ya vijiji mpaka ngazi ya Wizara au tusema Taifa, kwenye hizo Kamati za Maafa. Sasa kwenye hizi kamati kwa mfano kama ngazi ya kijiji ni nani kule kwenye ngazi ya kijiji atasema maafa ya extent hii yanafaa kushughulikiwa na ngazi ya wilaya na si ngazi ya Kijiji? Kwamba, huyu mtu inafaa kusaidiwa na ngazi ya mkoa na si ngazi ya wilaya? Wapi panaainishwa kwenye sheria hii ili kujua kwamba kwenye maafa haya yanakwenda kuhudumiwa na nani?

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema, kwamba mimi si mwanasheria. hivyo mimi nitaomba Mheshimiwa Waziri aweze kunifafanulia kwenye baadhi ya sehemu.

(a) Je, ni sura gani kwenye sheria hii inakataza kwamba madhara yote yanayotokana na uchaguzi siyo maafa?

(b) Ni kipimo gani kitakachotumika kujua kiwango cha maafa?

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika Taarifa. (Kicheko)

SPIKA: Mheshimiwa Kuchauka kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko.

T A A R I F A

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru nimeona nimpe taarifa Mheshimiwa Kuchauka. Wakati anachangia na ana-narrate aina ya maafa kwake yaliyompata yeye wakati wa uchaguzi kuchomewa nyumba na gari zake, nimekaa nimetafakari kwa kina nilitaka nimpe taarifa tu kama ni hayo tu ya kuchomewa nyumba na gari kama angekuwa amezikatia bima nadhani ingekuwa taken and care off. (Makofi/Kicheko)

SPIKA: Mheshimiwa Kuchauka hiyo ni ngazi ya kwanza lakini ngazi ya pili hilo jambo linakuhusu wewe mwenyewe, na Kanuni zetu zilitakiwa sasa uwe umeshasema; hayo ndiyo mazingira ya kusema natoa mchango huu lakini naeleza maslahi binafsi; yaani ndio mchango kama huu. Kwa hiyo maslahi binafsi, tena ya kifedha kiasi gani? ndiyo inavyosema sheria yetu lakini malizia mchango wako maana ulianza kwa kujitetea kwanza. Lakini hili jambo unalochangia linakuhusu wewe mwenyewe, na ni hoja yako wewe mwenyewe kwa hiyo mazingira yapo namna hiyo. Malizia mchango wako. (Kicheko)

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, nafikiri pengine hukunisikia nili-declare interest kwenye jambo hili, nilisema kwamba mimi ni mlengwa wa moja kwa moja.

Mheshimiwa Spika, lakini nakubaliana na taarifa yake; pengine ni kwa sababu ile niliyoitaja kwamba mimi si mwanasheria; lakini anapozungumzia masuala ya bima na hapo bado kwenye hii sheria sijaona mahali pametajwa kwamba yaani kama ni nyumba, kama ni mali yenye bima haitashughulikiwa na sheria hii, sijaona. Kwa hiyo, bado hata kama mimi nilikuwa na bima ya magari pamoja na ya nyumba bado, kwa mujibu wa sheria hii, ninavyoona mimi kwa uelewa wangu, ni kwamba bado nilikuwa nahitaji kupata msaada kwenye mfuko wa maafa pamoja na kwamba hizi ni mali zangu zilikuwa na bima. Hii ni kwa sababu hapa kwenye sheria haijatajwa, kwamba mali ambayo itakuwa ni bima haitashughulikiwa na mfuko wa maafa.

Mheshimiwa Spika, sasa swali lingine ambalo nilikuwa nataka niombe Mheshimiwa Waziri atakapokuja anitajie ni kujua ile level niliyoisema. Kwamba maafa haya yanashughulikiwa na nani kwa level ipi? Na ni nani anayeweza kujua kwamba kwa madhara haya hii jamii inaweza ikamudu au haiwezi kumudu? Kwa mfano imetokea madhara kwenye Kijiji, labda shule ikaungua moto; nani atajua kwamba kwa kuungua ile shule kijiji hakina uwezo wa kurudishia ile shule, na kwa hiyo Serikali inahitaji kuingiza nguvu yake pale, au kuiachia kijiji au kumuachia mtu binafsi? Nataka nipate hiyo mipaka ipo sehemu gani kwenye sheria hii?

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, naomba ianishwe mamlaka za zile kamati. Kwamba, kamati ya kijiji inaishia hapa, kamati ya mtaa inaishia hapa, kamati ya wilaya inaishia hapa; ili kuondoa mkanganyiko huu ambao mimi nimeusema. Kwamba, ukishapata yale madhara wewe personally unatakiwa ufuate ngazi ipi; ujue ni ngazi ipi inapaswa ikuhudumie? Na unapokosa huduma uone kwamba sheria haijakutendea haki.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hivyo, naomba niunge mkono hoja.