Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi) (31 total)

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza:-
Kumekuwa na changamaoto kubwa katika Mkoa wa Ruvuma ambapo vocha na pembejeo za kilimo zinazotolewa zimekuwa hazitoshi na wakati mwingine kuleta mgogoro kwa wananchi wenyewe kwa wenyewe:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza pembejeo za ruzuku katika Mkoa wa Ruvuma?
(b) Je, ni kwa nini Serikali isiondoe kodi kwenye pembejeo ili wananchi waweze kununua wenyewe pembejeo hizo kwa bei nafuu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Ruvuma umekuwa ukipata ruzuku ya pembejeo za kilimo tangu msimu wa 2003/2004 hadi sasa ambapo takribani kaya 80,000 kila mwaka zimekuwa zikinufaika na ruzuku hiyo mkoani humo. Kutokana na changamoto za mfumo wa utoaji wa ruzuku za pembejeo kama vile kuchelewa kwa pembejeo, ubadhirifu, bei kubwa na kadhalika wakulima wachache wamekuwa wakinufaika na ruzuku hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuweza kuwafikia wakulima wengi zaidi katika mikoa mbalimbali ikiwemo Mkoa wa Ruvuma, Serikali inaangalia upya utaratibu wa kutoa ruzuku bila kujali makundi ambao utawezesha wakulima wengi zaidi kunufaika na ruzuku ya pembejeo. Utaratibu huo utakapokamilika umma wa Watanzania utajulishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa kodi za import na excise duties zimefutwa kwa pembejeo za kilimo zinazoagizwa kutoka nje ila bado kuna tozo za bandari na taasisi mbalimbali kama vile TBS, SUMATRA, Taasisi ya Mionzi na kadhalika ambapo baadhi ya tozo hizo ndani yake kuna VAT. Aidha, Halmashauri bado zinatoza cess kwenye mbegu zinazozalishwa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha bei za pembejeo zinakuwa nafuu, Serikali inaangalia uwezekano wa kuondoa au kupunguza tozo mbalimbali kwenye pembejeo zote za kilimo ili kuwawezesha wakulima wengi kununua pembejeo hizo kwa bei nafuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali inaendelea kuweka msisitizo kwa wawekezaji wa nje na wa ndani kuanzisha viwanda vya mbolea na pia kuwekeza katika mashamba ya kuzalisha mbegu hapa nchini. Lengo kubwa likiwa ni kuwapatia wakulima pembejeo za kutosha na kwa bei nafuu ili kuongeza uzalishaji.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza:-
Katika Ilani ya CCM 2016/2017 Serikali imeahidi kuinua kipato cha mwananchi mmoja mmoja:-
Je, ni lini Serikali itaanza kutoa fedha kiasi cha shilingi 50,000,000 kwa kila Kijiji au Mtaa ili kuwasaidia wananchi kuboresha mitaji yao?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Ruvuma, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imetenga shilingi bilioni 59.5 katika bajeti ya mwaka 2016/2017 chini ya Fungu 21, kwa ajili ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 ya kupeleka shilingi milioni 50 kwa kila kijiji. Fedha hizo zitatolewa baada ya kukamilisha taratibu mahususi zinazolenga kuhakikisha uwepo wa tija, katika matumizi ya fedha hiyo. Hivyo namwomba Mheshimiwa Mbunge Jacqueline, asubiri utekelezaji wake kuanzia mwaka wa fedha 2016/2017. Mara baada ya kukamilika kwa mfumo na muundo wa utekelezaji wa zoezi zima, ambapo kazi hii imeshaanza kufanyika.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza:-
Mkoa wa Ruvuma una jumla ya Wilaya sita zenye Majimbo tisa ya uchaguzi, unakabiliwa na tatizo kubwa la maji:-
Je, ni lini Serikali itapeleka maji safi na salama katika Mkoa wa Ruvuma?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mpango wa utekelezaji wa miradi ya maji vijijini ulioanza mwaka wa fedha 2006/2007, Mkoa wa Ruvuma ulipangiwa vijiji 80. Kati ya vijiji hivyo, vijiji 76 vilipata vyanzo vya maji na Vijiji vinne vya Mchoteka, Nakapanya, Mtina na Muhuwesi katika Halmashauri ya Tunduru vilikosa vyanzo. Miradi ya maji katika vijiji 43 imekamilika na miradi mingine ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka 2016/2017, Mkoa wa Ruvuma umetengewa jumla ya shilingi bilioni 13.17 kwa ajili ya miradi ya maji vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea na mipango ya kuboresha huduma ya maji katika Miji ya Songea, Mbinga, Namtumbo na Tunduru ya Mkoa wa Ruvuma. Kwa Mji wa Songea, Serikali imekamilisha mradi wa ukarabati wa chanzo cha maji cha Mto Ruhila Darajani kwa gharama ya shilingi bilioni 2.6 ambapo umeongeza kiasi cha maji lita milioni sita kwa siku. Mradi huo umekamilika mwezi Februari, 2016 na sasa upo kwenye majaribio. Kukamilika kwa mradi huo kumewanufaisha wakazi 164,162 wa Manispaa ya Songea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mpango wa muda mrefu Serikali imekamilisha usanifu wa kina na uandaaji makabrasha ya zabuni kwa ajili ya uboreshaji huduma ya maji katika Miji ya Tunduru, Namtumbo na Mbinga. Utekelezaji wa miradi hiyo utagharimu Dola za Marekani milioni 7.3 kwa Mji wa Tunduru, Dola milioni 12.08 kwa Mji wa Namtumbo na Dola milioni 11.86 kwa Mji wa Mbinga.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na jitihada za kutafuta fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA (K.n.y. MHE. JACQUELINE
N. MSONGOZI) aliuliza:-
Barabara ya Makambako - Songea yenye urefu wa kilometa 295 imeharibika sana na inahitaji kufanyiwa matengenezo.
Je, ni lini Serikali itakarabati barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la Serikali ni kuifanyia ukarabati kwa kiwango cha lami barabara ya Makambako hadi Songea yenye urefu wa kilometa 295 ili kupunguza gharama na muda wa kusafiri kwa watumiaji wa barabara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania –TANROADS, tayari imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na utayarishaji wa nyaraka za zabuni. Lengo la kazi hiyo ni kuikarabati barabara hiyo kwa kiwango cha lami na kazi hii imefanyika kwa kutumia fedha za mkopo kutoka Benki ya Dunia.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ukarabati kwa kiwango cha lami barabara ya Makambako hadi Songea. Aidha, Wizara kupitia Wakala wa Barabara Tanzania inaendelea kuifanyia matengenezo barabara hii kwa kutumia fedha za Mfuko wa Barabara ili iendelee kupitika wakati Serikali inatafuta fedha za kuifanyia ukarabati kamili.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza:-
Wakati Rais akiwa katika kampeni aliahidi kuwa ataondoa ushuru na kodi ndogo ndogo zinazoleta usumbufu kwa wajasiriamali wadogo wadogo kama vile machinga, wachuuzi wa mboga mboga na matunda, mama lishe, waendesha bodaboda na kadhalika, lakini mpaka sasa ahadi hiyo haijatekelezwa. Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imefanya uamuzi wa kufuta ushuru unaotozwa kwa wafanyabiashara ndogo ndogo wasio rasmi na wanaofanyia biashara katika maeneo yasiyo rasmi wakiwemo mama lishe, wauzaji mitumba wadogo, wauza mboga mboga, ndizi na matunda. Vile vile, wafanyabiashara walio nje ya maeneo maalum ya kibiashara wenye mitaji chini ya shilingi 100,000 hawaruhusiwi kulipa ada, tozo na kodi za aina yoyote.
Mheshimiwa MWenyekiti, uamuzi huu umeanza kutekelezwa kuanzia tarehe 1 Julai 2017 baada ya marekebisho ya Sheria ya Fedha ya mwaka 2017 iliyotangaza kufuta ushuru na kodi kero kwa wafanyabiashara wadogo wadogo. Hatua inayoendelea sasa hivi nikuwatambua wafanyabiashara wadogo wote ili kuwapatia vitambulisho maalum vya kazi wanazozifanya. Hivyo, Serikali imetekeleza kwa vitendo ahadi hii iliyoko katika Ilani ya Chama Tawala ya mwaka 2015 inayolenga kuwapatia unafuu wa maisha wananchi wa hali ya chini kiuchumi ili waweze kukua na kuchangia vizuri katika uchumi wa Taifa lao. (Makofi)
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kufufua Kiwanda cha SONAMCU kilichopo Songea Mjini?
(b) Je, Serikali ipo tayari kuwaongezea gawio la uzalishaji wa tumbaku wananchi wa Wilaya ya Namtumbo?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania ambayo ni msimamizi wa vyama vya Ushirika Tanzania imewezesha kukamilisha mkataba kati ya mnunuzi mwingine wa Tumbaku Kamouni ya Premium Active Tanzania Limited na Chama Kikuu cha Ushirika cha Wilaya za Songea na Namtumbo (SONAMCU Ltd.) wa miaka saba na mkataba huu umeboreshwa zaidi kwa kuweka kipengele cha tumbaku yote inayozalishwa Songea lazima isindikwe katika Kiwanda cha Tumbaku kilichopo Songea Mjini. Mkataba huu tayari umeshasainiwa na umeshaanza msimu huu wa mwaka 2018/2019 ambao utadumu kwa miaka saba hadi mwaka 2025/2026. Vyama vyote vya msingi vimeingia mkataba na Chama Kikuu cha Ushirika (SONAMCU) ili kudhibiti tumbaku yote itakayozalishwa Songea na Namtumbo kusindikwa katika kiwanda cha tumbaku kilichopo Songea Mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi huu wa Februari, kampuni hii itawaleta wahandisi wawili kutoka nchi ya Italia ambao watafika Songea na kushirikiana na Mkoa ili kuandaa gharama halisi za ukarabati na mtambo mwingine utakaoagizwa Italia ili tumbaku yote itakayozalishwa kuanzia msimu huu wa 2018/2019 isindikwe katika Kiwanda cha Songea Mjini. Serikali ina matumaini kuwa kiwanda hiki kitafunguliwa na kuanza upya kazi ya usindikaji wa tumbaku ifikapo mwezi Julai, 2018 hivyo kuwezesha kutoa ajira kwa wananchi zikiwemo ajira za kudumu na za msimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkataba wa ununuzi wa tumbaku uliopo sasa kati ya SUNAMCU na Premium Active Tanzania Limited umeanza kuongeza uzalishaji wa tumbaku kwa wananchi wa Wilaya ya Namtumbo kutoka kilo 250,000 za mwaka 2017/2018 hali kufikia kilo milioni moja kwa mwaka 2018/2019. Aidha, mkataba unaonesha kila mwaka kutakuwa na ongezeko la uzalishaji wa tumbaku kutoka kwa mnunuzi aliyeingia mkataba kufuatana na ubora na mahitaji ya soko la nje ya nchi.
Hata hivyo, Serikali inaendelea kuboresha mazingira na fursa ya wanunuzi wengine watakaojitokeza wenye mahitaji ya tumbaku. Ikumbukwe kuwa ongezeko hutokea endapo tu kuna mwenendo mzuri wa biashara katika soko na ongezeko la uzaishaji. Ahsante sana.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza:-
Kituo cha Afya cha Mji Mwema katika Manispaa ya Songea kinahudumia watu zaidi ya laki mbili lakini kinapata mgao wa dawa sawa na vituo vingine vya afya:-
(a) Je, Serikali ina mpango wa kukiongezea dawa kituo hiki ili kipate mgao wa dawa na vifaa tiba kama Hospitali ya Wilaya?
(b) Je, ni lini Serikali itakamilisha vifaa vya upasuaji katika Kituo cha Afya cha Mji Mwema?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inafanya mgawanyo wa fedha za dawa kulingana na idadi ya watu wanaopata huduma katika kituo husika. Takwimu za Wizara za mwaka 2015 zinaonesha kituo hicho kinahudumia wananchi 20,000. Kama kuna mabadiliko ya idadi ya wananchi wanaopata huduma katika kituo hiki ni vyema takwimu hizo ziletwe Wizarani na Mganga Mkuu wa Wilaya husika ili marekebisho yaweze kufanyika. Kwa kuwa hiki ni Kituo cha Afya, hakitapata mgao kama Hospitali ya Wilaya mpaka pale ambapo kitapandishwa hadhi ya kuwa Hospitali ya Wilaya.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kukamilisha upatikanaji wa vifaa vya upasuaji wa Vituo vya Afya nchini kikiwemo cha Mji Mwema chini ya mpango wa Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa (BRN). Mpango huu ni wa miaka mitatu na umelenga kupunguza vifo vya akinamama kwa asilimia 20. Katika kipindi hicho cha 2015 – 2018, Vituo vya Afya nchini vitaboreshwa ili kutoa huduma za upasuaji hasa kwa akina mama ambao wameshindwa kujifungua kwa njia ya kawaida. Serikali pia itaboresha idadi ya wataalam na upatikanaji wa dawa hasa za mpango wa mama na mtoto.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza:-
Benki ya Kilimo ipo kwa ajii ya kumwezesha mkulima wa Tanzania aweze kufanya uwekezaji wenye tija katika kilimo:-
(a) Je, ni lini Serikali itapeleka Benki ya Kilimo katika Mkoa wa Ruvuma ili wananchi waweze kukopeshwa?
(b) Je, Serikali ipo tayari kupunguza riba kwa pesa anayokopeshwa mkulima kutoka katika benki hiyo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mpango Kazi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania wa miaka mitano (2017 – 2021), benki inakusudia kuanzisha Ofisi za kikanda katika Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Kusini, Kanda ya Kati, Kanda ya Ziwa, Nyanda za Juu Kusini pamoja na Zanzibar. Kutokana na ufinyu wa rasilimali fedha, benki itatekeleza mpango wake wa kusogeza huduma karibu na wateja wa awamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufikia 30 Juni, 2018, Ofisi ya Kanda ya Kati itakuwa imefunguliwa ambayo pia itakuwa ni Makao Makuu ya Benki ya Kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya ufunguzi wa Ofisi ya Kanda ya Kati kukamilika, benki itafanya uchambuzi wa fursa zilizopo kikanda na hivyo kuchukua hatua na taratibu za kufungua Ofisi nyingine kulingana na upatikanaji wa rasilimali fedha.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania inatoa mikopo kwa kutumia mfumo wa makundi:-
(i) Kundi la kwanza ni wakulima wadogo wadogo kwa riba ya 8% – 12% kwa mwaka;
(ii) Kundi la pili ni la miradi mikubwa ya kilimo kwa 12% – 16% kwa mwaka;
(iii) Kundi la tatu ni wanunuzi wa mazao kwa 15% – 18% ; na
(iv) Kundi la mwisho ni mikopo ya ushirika ambapo riba yake inaendana na hali ya soko na matumizi ya mkopo huo. Hata hivyo, majadiliano kuhusu kiwango cha riba yanaweza kufanyika kulingana na historia ya mkopaji.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza:-
Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne alitoa ahadi ya kujenga theatre pamoja na vifaa vyake vya upasuaji katika Wilaya ya Namtumbo, Mji Mdogo wa Lusewa. Ahadi hii ni ya muda mrefu na wananchi wamekuwa wakiteseka kutokana na ukosefu wa huduma hiyo jambo ambalo limesababisha vifo hasa kwa akinamama wajawazito na watoto:-
a) Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi huo?
b) Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga nyumba ya Daktari katika Kituo cha Afya cha Lusewa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa jengo la upasuaji katika Kituo cha Afya Lusewa ulianza mwaka 2015. Ujenzi uliendelea katika mwaka wa fedha 2017/2018 ambapo fedha zilipelekwa moja kwa moja kwenye akaunti ya kituo. Jengo la OPD limekamilika isipokuwa sakafu ya chumba cha upasuaji. Kituo hicho kitawekwa katika kipaumbele na kutengewa bajeti katika mwaka wa fedha 2019/2020 ili kukamilisha ujenzi unaoendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, ili kuboresha huduma za afya kwa mama na mtoto, Serikali imeweka kipaumbele na kutoa jumla ya shilingi bilioni 3.6 kwa ajili ya ukarabati wa vituo vya afya nane katika Mkoa wa Ruvuma ambapo kati ya fedha hizo, shilingi milioni 900 zimetolewa kwa vituo viwili vya afya vilivyoko katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ambavyo ni Kituo cha Afya Msakale na Matemanga. Vituo vingine vilivyopokea fedha katika Mkoa wa Ruvuma ni Kalembo (shilingi milioni 500), Mkili (shilingi 400), Namtumbo (shilingi milioni 400), Madaba (shilingi milioni 400), Mahukuru (shilingi milioni 500) na Mchangimbole (shilingi milioni 500).
Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati huu wa Serikali unalenga kuimarisha huduma za dharura na upasuaji kwa mama wajawazito.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itawalipa Mawakala wa Pembejeo za Kilimo fedha zao ambazo walikopesha Serikali tangu mwaka 2014/2015?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, wifi yangu kama ifuatavyo:-
Mhesimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2014/2015 Serikali ilitoa ruzuku ya pembejeo kupitia vikundi vya wakulima na benki jamii badala ya utaratibu wa vocha za pembejeo uliokuwa unatumika awali. Utaratibu huu ulitumika kwa lengo la kuwajengea uwezo wakulima kuweza kukopa na kujipatia pembejeo wao wenyewe. Serikali ilitakiwa kuchangia asilimia 20 ya gharama za pembejeo zinazotosheleza ekari moja tu. Utaratibu huu ulikuwa utumike nchi nzima, lakini Mikoa iliyotekeleza ilikuwa ni Morogoro, Njombe, Iringa, Manyara, Mbeya, Ruvuma, Rukwa na Tabora tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu ilipokea na kupitia nyaraka mbalimbali za Makampuni na Mawakala wa Pembejeo 23 zenye madai ya jumla ya shilingi 7,180,914,669 waliofanya kazi ya kusambaza pembejeo zenye ruzuku msimu ule wa kilimo 2014/2015.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uhakiki wa awali umefanyika kwenye mikoa kumi. Kupitia uhakiki huo wa awali imejiridhisha pasipo shaka uwepo wa upungufu kwa baadhi ya Makampuni na Mawakala kwa madai waliyowasilisha ikiwemo kukosekana kwa nyaraka za manunuzi, kutokuwepo kwa mikataba ya kazi, kukosekana kwa orodha ya wakulima wanufaika katika vijiji husika na kukiukwa kwa taratibu za utoaji wa pembejeo kwa wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na matokeo ya uhakiki huo wa awali kuwa na upungufu mkubwa katika madai hayo, Mheshimiwa Waziri Mkuu aliiagiza Wizara ya Fedha na Mipango kufanya uhakiki wa kina katika Mikoa yote na kwa Mawakala wote ili kubaini uhalali wa madai hayo ili madeni halali yaweze kulipwa. Taarifa rasmi ya uhakiki huo itatolewa mapema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kwa pembejeo zilizogawiwa kwa msimu wa mwaka 2016/2017 ambapo Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) ilipewa jukumu la kusambaza mbolea na baadhi ya Kampuni na Mawakala wa Mbegu walisambaza mbegu bora, uhakiki pamoja na ukaguzi wa mahesabu unaendelea. Uhakiki huu utakapokamilika, taarifa itatolewa mapema. Ahsante.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza:-

Barabara ya Likuyufusi – Mkenda yenye urefu wa kilometa 123 inayounganisha nchi mbili za Tanzania na Msumbiji, bado haijaanza kujengwa kwa kiwango cha lami:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Likuyufusi – Mkenda yenye urefu wa kilometa 123 ni barabara kuu inayounganisha nchi mbili za Tanzania na Msumbiji na inahudumiwa na Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS).

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kutambua umuhimu wa barabara hii iliamua kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa lengo la kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami, kazi ambayo ilikamilika mwaka 2013. Katika Mwaka wa Fedha 2018/2019 shilingi bilioni 5.86 zimetengwa kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwepo kwa uchimbaji na usafirishaji wa makaa ya mawe katika Kijiji cha Muhukuru kilicho kilometa 74 kutokea Songea katika barabara hiyo, kumesababisha kuongezeka kwa magari mengi na mazito yanayobeba makaa ya mawe. Kufuatia hali hiyo, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) imeamua kufanya mapitio ya usanifu wa kina (Design Review) ili kukidhi mahitaji halisi yaliyojitokeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kazi hiyo kukamilika, Serikali itaendelea kutafuta fedha zaidi kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA (K.n.y MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI) aliuliza:-

TPB ni Benki ya Serikali na inamilikiwa na Serikali kwa zaidi ya asilimia 90 lakini Taasisi za Serikali na Mashirika ya Umma yanatumia Benki nyingine katika huduma za Kibenki:-

(a) Je, ni nini msimamo wa Serikali katika kutumia huduma za Kibenki?

(b) Watumishi wa Serikali na Viongozi wote wa Serikali wanatakiwa kutumia TTCL katika huduma za mawasiliano ya simu. Je, kwa nini Watumishi na shughuli zote za Serikali zisianze kutumia huduma za Kibenki kupitia Benki hiyo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu
(a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, biashara huria ya sekta ya fedha ilianza tangu mwaka 1991 mara baada ya kupitishwa kwa Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 1991, pamoja na Kanuni zake. Kupitia sheria hiyo, Wawekezaji mbalimbali walifungua Benki binafsi hapa nchini na hivyo matumizi ya huduma na bidhaa za benki kuanza kuamuliwa na nguvu ya soko ikiwa ni pamoja na huduma na bidhaa za Benki za Serikali. Benki ya TPB, kama ilivyo kwa benki nyingine haina budi kujiimarisha na kujitangaza yenyewe kwa lengo la kuuza bidhaa zake na hatimae kuvutia wateja zaidi ikiwa ni pamoja na Taasisi za Serikali na Mashirika ya Umma.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia misingi ya nguvu ya soko, Benki ya TPB imefanikiwa kujitangaza na kuimarisha huduma zake na hivyo kuvutia baadhi ya Taasisi za Serikali na Mashirika ya Umma kutumia bidhaa zake. Miongoni mwa huduma za benki ya TPB zinazotumiwa na Taasisi za Serikali na Mashirika ya Umma kwa sasa ni pamoja na akaunti ya muda maalumu, akaunti ya biashara, malipo kwa njia ya mtandao, kubadilisha fedha za kigeni, kukusanya mapato ya Serikali, kulipa mishahara ya watumishi, mikopo kwa watumishi, kulipa pensheni za wastaafu pamoja na mikopo kwa wastaafu wanaolipwa pensheni zao na Serikali pamoja na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

(b) Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sera, Sheria, Kanuni, Taratibu na miongozo iliyopo ya uchumi huria, Serikali haina Mamlaka ya kumlazimisha Mtumishi au Taasisi ya Umma kutumia huduma za benki yoyote, ikiwemo benki ya TPB. Hivyo basi, ni jukumu la Benki ya TPB na benki nyingine kuboresha mifumo ya huduma na bidhaa zao ili kuvutia Watumishi wa Umma, pamoja na Taasisi za Umma kuanza au kuendelea kutumia huduma zao.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza:-

Barabara ya Likuyufusi – Mkenda yenye urefu wa kilometa 124 inayounganisha Tanzania na Mozambique mpaka sasa bado haijajengwa kwa kiwango cha lami.

Je, ni lini Serikali itapeleka pesa na kuanza ujenzi huo kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Likuyufusi – Mkenda yenye urefu wa kilometa 124 ni barabara muhimu kutokana na ukweli kwamba inaunganisha nchi mbili za Tanzania na Msumbiji na pia inahudumia wananchi wengine wa vijiji vya Mkenda/Mitomoni hadi Likuyufusi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), ilifanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hii kwa kumtumia Mkandarasi Mshauri M/s Crown Tech. Consult (T) Ltd. wa Dar es Salaam ambaye alikamilisha kazi hiyo mwaka 2012. Baada ya kukamilika kwa usanifu huo, kulijitokeza ongezeko kubwa la matumizi katika barabara hiyo kutokana na kugundulika na kuanza kuchimbwa kwa makaa ya mawe katika eneo la Muhukuru pamoja na matarajio ya uwekezaji wa shamba la miwa na kiwanda cha sukari eneo la Nakawale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na mabadiliko hayo, Wizara yangu kupitia TANROADS inapitia upya usanifu wa awali ili kuzingatia mahitaji ya sasa. Kazi hiyo imeshaanza na inatarajiwa kukamilika mwezi Juni 2020. Baada ya kukamilika kwa kazi hiyo, Serikali itajua gharama halisi za ujenzi na kuanza kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza:-

(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kufufua Kiwanda cha Tumbaku cha SONAMCU kilichopo Songea Mjini?

(b) Je, Serikali haioni umuhimu wa kuanzisha pia Kiwanda cha Usindikaji wa Samaki wanaotoka Ziwa Nyasa?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania ambayo ndiyo msimamizi wa vyama vya ushirika Tanzania imewezesha kukamilisha mkataba wa makubaliano ya kufufua kiwanda cha SONTOP kilichopo Songea Mjini kati ya Chama Kikuu cha Wakulima wa Tumbaku yaani SONAMCU na kampuni inayonunua tumbaku Mkoa wa Ruvuma inayoitwa Premium Active Tanzania Limited. Kampuni hiyo ilitoa kiasi cha dola za Kimarekani 3,050,000 kama dhamana kwa ajili ya kukifufua kiwanda hicho kinachomilikiwa na Chama Kikuu cha Wakulima wa zao hilo.

Vilevile vyama vyote vya msingi vimeingia m kataba na Chama Kikuu cha Ushirika - SONAMCU ili kudhibiti tumbaku yote inayozalishwa Songea na Namtumbo kusindikwa katika Kiwanda cha Tumbaku kilichopo Songea Mjini. Pindi kiwanda kitakapoanza uzalishaji chama hicho kitakuwa kinakatwa kiasi cha fedha kama sehemu ya marejesho kwa kampuni tajwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kuanzisha Kiwanda cha Samaki katika mwambao wa Ziwa Nyasa ni la muhimu sana na ni sehemu ya mpango wa Serikali kupitia mpango wa uwekezaji yaani investment guide wa Mkoa wa Ruvuma. Wilaya ya Nyasa imetenga eneo lenye ukubwa wa hekari 345 eneo la Kilosa kwa ajili ya ujenzi wa viwanda husika. Vilevile Serikali imeshaanza kuweka mazingira wezeshi ya miundombinu kwa kupeleka umeme wa uhakika wa kilovott 33 na ujenzi wa barabara ya lami kilometa 67 kutoka Mbinga hadi Mbambabay wenye thamani ya shilingi bilioni 129, meli mbili za mizigo yaani MV Ruvuma na MV Njombe na kuimarisha mtaji nguvukazi kwa kujenga Hospitali ya Wilaya ya Nyasa na vituo vya afya kwa thamani ya shilingi takriban bilioni 3.54.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Wizara kwa kushirikiana na mkoa inaendelea na jitihada ya kutafuta wawekezaji mbalimbali wakiwemo wa viwanda vya kusindika samaki. Hivi sasa Serikali kupitia taasisi zake za SIDO na TAFIRI zimekuwa zikifanya mafunzo ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya awali kwa wavuvi wa eneo hilo kuhusu uvuvi, usimamizi na uzalishaji wa samaki pamoja na huduma kwa wateja (customer care).

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kupitia Corporate Social Responsibility ya Mradi wa Barabara ya Mbinga – Mbamba Bay wilaya iliainisha mradi wa uwezeshaji wa kuongeza thamani mazao ya samaki wenye thamani ya takriban shilingi milioni 455 ili kuongeza tija ya mradi husika.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga barabara ya Likuyufusi - Mkenda yenye urefu wa kilometa 124 kwa kiwango cha lami ili kufungua zaidi fursa za kiuchumi kati ya nchi yetu na Msumbiji?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Likuyufusi – Mkenda yenye km 124 ni barabara muhimu kwa kuwa inaunganisha Nchi ya Tanzania na Msumbiji kupitia Mto Ruvuma.

Aidha, barabara hii inahudumia wasafiri wanaotumia uwanja wa ndege wa Songea wanaotokea Nchi jirani ya Msumbiji na maeneo mengine ya Mkoa wa Ruvuma. Vile vile, barabara hii ni muhimu kwenye suala la ulinzi wa mipaka ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu wa barabara hii, Serikali ilikamilisha usanifu wa kina wa barabara hii chini ya Kampuni ya Crown Tech - Consult Limited ya Tanzania. Hata hivyo, kufuatia uchimbaji wa makaa ya mawe kwenye eneo la Mhukulu lililopo kilomita 80 kutoka Songea na kilomita 60 kutoka Likuyufusi, Wizara ya Ujenzi kupitia TANROADS, ilikamilisha mapitio ya usanifu wa kina wa barabara hii (mwaka 2020) ili iendane na mahitaji na mazingira ya sasa. Vile vile, katika Mwaka huu wa Fedha 2020/2021, Daraja la Mkenda limetengewa shilingi milioni 110 kwa ajili ya kuendelea na usanifu wa kina.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imepanga kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami kwa awamu ambapo katika Mwaka wa Fedha 2020/2021 shilingi bilioni 1.59 zimetengwa kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kilomita 10. Kazi inatarajiwa kuanza mwezi Aprili, 2021 baada ya kukamilisha taratibu za manunuzi. Aidha, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni
1.346 kwa ajili ya matengenezo mbalimbali ili barabara hii iweze kupitika majira yote ya mwaka.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga vituo vya afya katika Kata za Tinginya, Muhimba, Kalulu, Mindu, Nalasi Magharibi na Nalasi Mashariki Wilayani Tunduru?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha huduma za afya katika ngazi zote nchini ikiwemo Wilaya ya Tunduru. Katika kipindi cha kuanzia mwaka 2017 hadi 2020 Serikali imejenga na kukarabati Vituo vinne (4) vya Afya vya Mkasale, Matemanga, Mchoteka na Nakapanya Wilayani Tunduru kwa gharama ya shilingi biloni 1.5. Aidha, katika Mwaka wa Fedha 2020/2021 Serikali imetenga shilingi milioni 200 kwa ajili ya kukamilisha maboma manne (4) ya zahanati katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru.

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kwamba mahitaji ya vituo vya kutolea huduma za afya ni mengi nchini, ikiwemo Wilaya ya Tunduru. Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga na kukarabati vituo vya kutolea huduma za afya nchini ikiwemo vituo vya afya kwenye Kata za Tinginya, Muhimba, Kalulu, Nalasi Magharibi na Nalasi Mashariki katika Wilaya ya Tunduru kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza:-

Mheshimiwa Naibu Spika, je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Lumecha – Londo – Kilosa kwa Mpepo, inayounganisha mkoa wa Ruvuma na Morogoro kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Lumecha, Londo, Kilosa kwa Mpepo ni sehemu ya barabara Kuu ya Mikumi, Kidatu, Ifakara, Lupiro, Malinyi Kilosa kwa Mpepo, Londo hadi Lumecha yenye jumla ya kilometa 512 ambayo inaunganisha Mikoa ya Ruvuma na Morogoro. Kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hii ulikamilika mwaka 2018 ikiwa ni lengo la Serikali kujenga barabara yote kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, hadi sasa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Mikumi hadi Kidatu kilometa 35.2 na ujenzi wa Daraja la Magufuli lenye urefu wa mita 384 pamoja na barabara unganishi yenye urefu wa kilometa 9.142 umekamilika. Aidha, ujenzi wa sehemu ya Kidatu – Ifakara ambayo ina urefu wa kilometa 66.9 unaendelea na umefikia asilimia 22.6.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa barabara hii kuanzia Lupilo, Malinyi Kilosa kwa Mpepo, Londo hadi Lumecha, Serikali inaendelea kutafuta fedha za kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami ikiwemo sehemu ya Lumecha, Londo hadi Kilosa kwa Mpepo. Aidha, wakati juhudi za kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami zikiendelea, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania yaani TANROADS Mkoa wa Ruvuma na Morogoro itaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hii kutoka Ifakara, Lupiro, Malinyi, Kilosa kwa Mpepo, Londo hadi Lumecha kila mwaka ili iweze kupitika majira yote ya mwaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha huu wa 2020/2021, barabara hii imetengewa jumla ya shilingi milioni 3,610.54 kwa ajili ya matengenezo mbalimbali. Kati ya fedha hizo shilingi milioni 985.585 ni kwa ajili ya sehemu ya barabara ya Lumecha, Londo ambayo iko Mkoa wa Ruvuma, ahsante. (Makofi)
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza:-

Kituo cha Afya Msindo kilichopo Wilayani Namtumbo kinapata mgao mdogo wa dawa usiokidhi mahitaji: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza mgao wa dawa katika Kituo cha Afya Msindo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya Msindo kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo kilipandishwa hadhi kutoka Zahanati na kuwa Kituo cha Afya tarehe 26 Machi, 2014. Kituo hiki kimekuwa kikipokea mgao wa dawa kama Zahanati badala ya Kituo cha Afya kwa kuwa Halmashauri haikuwasilisha maombi husika kadri ya utaratibu. Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo imeendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na changamoto hiyo ikiwemo kutumia fedha za makusanyo zinazotokana na uchangiaji wa huduma za afya kwa ajili ya ununuzi wa dawa. Wastani wa upatikanaji wa dawa muhimu katika kituo hiki ni asilimia 87.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeielekeza Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo kuwasilisha rasmi maombi ya mgao wa fedha za dawa za Kituo cha Afya Msindo kupitia ruzuku ya Serikali Kuu ili mgao huo urekebishwe na kukiwezesha kituo hicho kupatiwa mgao wa dawa wenye hadhi ya Kituo cha Afya, ahsante.
MHE. VITA R. KAWAWA K.n.y. MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kupelekea maji katika Vijiji vya Lingusenguse, Lusewa, Namwinyu, Mchomoro na Luchiri Wilayani Namtumbo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nia ya Serikali ni kuhakikisha huduma ya upatikanaji wa maji inaboreshwa katika Wilaya ya Namtumbo, ambapo kwa sasa hali ya upatikanaji wa huduma ya maji Wilayani humo ni asilimia 69. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali inaendelea kuboresha huduma ya maji katika Halmashauri hiyo ambapo katika Vijiji vya Lingusenguse, Lusewa na Mchomoro kazi zinazoendelea ni pamoja na ukarabati wa pampu ya mkono, ujenzi wa chanzo, ukarabati wa tanki la ujazo wa lita 50,000, ujenzi wa vituo vya kuchotea maji (16) na ulazaji wa bomba la kusambaza maji urefu wa kilomita tisa. Kazi zote zinatarajiwa kukamilika mwezi Januari, 2022.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Kijiji cha Namwinyu ujenzi wa mradi utaanza robo ya tatu ya mwaka 2021/2022 na utahusisha uchimbaji wa kisima kirefu, vituo vinne (4) vya kuchotea maji, ulazaji wa bomba kilomita tatu (3) na ujenzi wa tanki la kuhifadhia maji la lita 90,000.

Mheshimiwa Spika, katika Kata ya Luchili wananchi wa Vijiji vya Namanguli, Misufini, Chengena na Kilangalanga wanapata huduma ya maji kupitia visima 24 vinavyotumia pampu za mkono. Katika mwaka 2021/2022, Serikali kupitia RUWASA itachimba visima virefu viwili (2) na kujenga miundombinu ya kusambaza maji. Kazi hizo zinatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2022.

Mheshimiwa Spika, kukamilika kwa utekelezaji wa miradi hiyo kutaondoa tatizo la maji katika vijiji vilivyotajwa. (Makofi)
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha bei ya mbolea inashuka hadi kufikia kiwango cha Wakulima kumudu kuinunua ili kuiepusha nchi yetu kukumbwa na janga la njaa?
WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum, lenye eneo (a), (b) na (c), kwa pamoja kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inakiri kwamba bei ya mbolea katika Soko la Dunia na hapa nchini imepanda kwa msimu wa mwaka 2021/2022 ikilinganishwa na msimu wa mwaka 2020/2021. Kupanda huko kwa bei hakutokani na Serikali au wafanyabiashara wa ndani kupandisha bei, bali kumetokana na kupanda kwenye Soko la Dunia na wakulima wote duniani wameathirika na upandaji huo uliotokana na athari za UVIKO. Mfano, hadi kufikia mwezi Januari, 2022 bei ya Urea ni Dola za Kimarekani 700 kwa tani ikilinganishwa na Dola za 350 kwa msimu wa 21, sawa na ongezeko la asilimia 100.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto za kupanda kwa bei za mbolea nchini, Serikali inachukua hatua za muda mfupi na muda mrefu. Hatua za muda mfupi zilizochukuliwa mpaka sasa ni pamoja na kununua mazao ya nafaka kwa bei ya juu kuliko bei ya soko ambapo mahindi yalinunuliwa kwa bei ya shilingi 500 badala ya 200.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kuhakikisha kwamba bandari zetu zinatoa kipaumbele cha kushusha mbolea ili kupunguza tozo za bandarini, ununuzi wa mbolea kwa mfumo wa (BPS) katika baadhi ya mazao mfano Tumbaku. Matumizi ya reli kusafirisha mbolea katika maeneo ambapo reli inapita. Matumizi ya mbolea mbadala kama NPS na NPS-Zinc na kuruhusu ushindani kwenye uagizaji wa mbolea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua za muda mrefu zilizochukuliwa ni pamoja na kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vya mbolea. Kutokana na uhamasishaji huo, Kampuni ya Itracom Fertilizers kutoka Burundi inaendelea na ujenzi wa kiwanda cha mbolea Mkoani Dodoma chenye uwezo wa kuzalisha tani 600,000 za mbolea na tani 300,000 za chokaa kwa mwaka. Wawekezaji wengi zaidi wanaendelea kujitokeza kutoka nchi mbalimbali kama vile Misri na Saudi Arabia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekutana na uongozi wa kiwanda cha mbolea cha Minjingu kujadili namna kiwanda hicho kinavyotakiwa kuzalisha mbolea kulingana na mahitaji ya udongo na kuongeza uzalishaji wa mbolea kutoka tani 30,000 hadi kufika 100,000 kwa mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inatambua umuhimu wa mbolea katika uzalishaji wa mazao ya chakula ili kuihakikishia nchi Usalama wa Chakula. Kutokana na tathmini iliyofanyika ambayo iliangalia changamoto hii pamoja na utabiri wa mvua, ulioonesha hatutapa mvua nyingi kwa miaka miwili iliyopita, bado maoteo ya uzalishaji yanaonesha nchi itaweza kujitosheleza katika chakula. Mpaka sasa maeneo mengi ya nchi yanaendelea kupata mvua nzuri. Matumizi ya mbolea yapo kwenye asilimia 50 ya kawaida ya mazao ya shambani. Kwa hali hiyo, Wizara ya Kilimo inapenda kuwahakikishia wananchi kwamba, nchi haitakumbwa na janga la njaa.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA K.n.y. MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka ruzuku kwenye majiko madogo ya gesi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha nchi inafikia zaidi ya asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2032. Miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na kufanyika kwa mjadala wa Kitaifa wa nishati safi ya kupikia, kuunda kikundi kazi kwa ajili ya uratibu, kutenga fedha katika bajeti ya 2023/2024 kwa ajili ya shughuli za nishati safi ya kupikia, kuanzisha mfuko wa nishati safi ya kupikia pamoja na kuzitaka taasisi zote zenye watu zaidi ya 300 kama vile shule, vyombo vya ulinzi na usalama, Magereza na kadhalika, kutumia nishati mbadala kupikia ikiwemo gesi na kuachana na matumizi ya kuni na mkaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini inatarajia kutekeleza mradi wa majaribio kwa kutoa ruzuku ya asilimia 50 ya gharama zote (jiko, gesi, mtungi pamoja na vifaa vinavyohusiana). Katika Awamu hii vifaa vipatavyo 100,000 vitasambazwa katika Mikoa 25 ya Tanzania Bara. Naomba kuwasilisha.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kuwawezesha wachimbaji wadogo wanawake kwa kuwapa mikopo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha wachimbaji wadogo hususan wanawake wanapata mikopo, Serikali kupitia STAMICO imepanga kununua mitambo mitano (5) midogo ya uchorongaji (utafiti madini) ambapo taratibu za ununuzi wa mitambo hii zinakamilishwa hivi sasa. Mitambo hiyo itawazesha wachimbaji wadogo kujua kiasi cha mashapo yaliyopo katika maeneo yao. Aidha, STAMICO imeingia makubaliano ya ushirikiano (MoU) na baadhi ya mabenki nchini kutoa mikopo kwa wachimbaji wadogo wakiwemo wanawake. Benki hizo ni CRDB, NMB na KCB ambapo katika utekelezaji wa makubaliano hayo, benki hizo zimejengewa uelewa wa sekta ya madini na namna nzuri ya utoaji mikopo kwa sekta hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Madini imekuwa ikiwahamasisha wachimbaji wadogo hususan wanawake kujiunga katika vikundi ili kurahisisha utoaji huduma mbalimbali zinazolenga kuwawezesha kupata fedha, vifaa vya uchimbaji na uchenjuaji wa madini. Ahsante sana.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza: -

Je, ni kwa nini Serikali haijagawa fedha kwa ajili ya ufugaji wa vizimba vya samaki katika Ziwa Nyasa?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Ruvuma, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ili kufuga samaki kwa vizimba inabidi kuainisha maeneo yanayofaa ziwani kwa kuzingatia vigezo vya kisheria na kitaalam. Katika awamu ya kwanza Serikali ilitoa fedha katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa Victoria ambayo ilishakidhi vigezo vya kisheria na kitaalam baada ya kufanyiwa tathmini katika Mwaka wa Fedha 2021/2022 na 2022/2023.

Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2023/2024, Serikali kupitia Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI) imepanga kufanya tathmini ya kimkakati ya mazingira (Strategic Environmental Assessment) katika Ziwa Nyasa ili kuanisha maeneo yanayofaa kwa ufugaji wa samaki kwa vizimba kwa kuzingatia vigezo vya kisheria na kitaalam. Pia (TAFIRI) itaanza ufugaji samaki kwa majaribio kwa kushirikiana na wananchi kufanya uzalishaji wa vifaranga vya samaki aina ya magege (Oreochromis karongae) na ufugaji wake kwa vizimba. Hatua hii inalenga kuwajengea uwezo wananchi ili waweze kuendelea na ufugaji pindi taratibu zitakapokamilika.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kupeleka umeme katika Kata ya Mletele Wilayani Songea?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kata ya Mletele katika Manispaa ya Songea ina jumla ya mitaa sita ambayo ni Mletele, Makemba, Liumbu, Nonganonga, Mdundiko na Mji Mwema. Mitaa mitano ya Mletele, Makemba, Liumbu, Nonganonga na Mdundiko tayari ina umeme. Mtaa wa Mji Mwema tu ndiyo bado haujafikiwa na umeme.

Mheshimiwa Spika, mtaa huu tayari umefanyiwa tathmini na utapata umeme kwa kuweka miundombinu itakayogharimu shilingi 115,767,782.60 katika Mwaka wa Fedha 2023/2024. Nashukuru.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA K.n.y. MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza: -

Je, lini Barabara ya Majengo – Ruvuma – Subira - Muungano itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeshaanza mipango ya ujenzi wa Barabara ya Majengo – Ruvuma - Subira na Muungano kwa kiwango cha lami ambapo katika Mwaka wa Fedha wa 2023/2024, jumla ya shilingi milioni 517.50 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami nyepesi kilomita moja.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. JACQUILINE N. MSONGOZI aliuliza: -

Je, lini Serikali itatoa fidia kwa Madaktari na Manesi wanaopoteza maisha wakihudumia Wagonjwa wa Magonjwa ya Mlipuko?

NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Msongozi Ngonyani, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua na kujali mchango mkubwa wa Watumishi wanaohudumia wagonjwa wa magonjwa ya milipuko wakiwemo Madaktari na Wauguzi. Aidha, napenda kufahamisha Bunge lako tukufu kwamba Serikali hutoa fidia kwa watumishi waliofariki kwa sababu za kuwahudumia wagonjwa, wa magonjwa ya mlipuko kwa Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi Sura ya 263, marejeo ya Mwaka 2015 kupitia Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi Tanzania. Fidia zinazotolewa ni pamoja na gharama za mazishi na pensheni kwa wategemezi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA K.n.y. MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kudhibiti mabadiliko ya tabianchi ambayo yamekuwa tishio kwa usalama wa viumbe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge Wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeandaa sera, mikakati na mipango ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambayo inatoa elimu na namna bora ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa wadau wote muhimu wakiwemo wananchi katika maeneo yote nchini.

Mheshimiwa Spika, wananchi wanahamasishwa kuacha shughuli zinazochangia uharibifu wa mazingira na kusababisha athari za mabadiliko ya tabianchi zikiwemo kukata miti ovyo, kuepuka kilimo kisichoendelevu katika vyanzo vya maji, kuepuka ufugaji unaoharibu mazingira pamoja na uvuvi haramu. Vilevile, Serikali inachukua hatua kwa kuanzisha na kutekeleza miradi ya kuzuia madhara ya mabadiliko ya tabianchi.

Mheshimiwa Spika, napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kuwa Serikali inaendelea kusimamia sera, mipango na mikakati ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambayo inapatikana kwenye tovuti ya Ofisi ya Makamu wa Rais (www.vpo.go.tz )

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu kuhusu hewa ya ukaa ili wananchi waelewe na wanufaike na elimu hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, biashara ya kaboni (biashara ya hewa ukaa) ni moja ya mbinu za kupunguza uzalishaji wa gesijoto (mitigation) ambayo iliridhiwa katika Itifaki ya Kyoto ikizitaka nchi wanachama kupunguza uzalishaji wa gesijoto iliyorundikana angani. Biashara hii ipo katika masoko ya aina mbili ambayo ni Soko la Hiari/Huria (Voluntary Carbon Market) na Soko la Umoja wa Mataifa (Official Carbon Market).

Mheshimiwa Spika, Serikali imeandaa Mwongozo wa Biashara ya Kaboni pamoja na Kanuni zake za mwaka 2022. Aidha, elimu kuhusu biashara ya kaboni hadi sasa imetolewa kimakundi ikiwemo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira, Wizara zote za kisekta pamoja na taasisi zake, Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya wote, Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mkoa na kwa wadau mbalimbali. Aidha, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kutoa elimu ya mazingira kwa Umma ikiwemo ya biashara ya kaboni.

Mheshimiwa Spika, ni matumaini ya Serikali kwamba kupitia jitihada hizo wananchi watapata uelewa na kunufaika na biashara ya kaboni. Nakushukuru.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza: -

Je, kuna mango gani wa kudhibiti Tembo wanaoharibu mazao na kujeruhi wananchi Kata za Mindu, Kahulu na Tinginya -Tunduru?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante; kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Vijiji vingi katika Wilaya ya Tunduru vinapakana na Hifadhi ya Taifa ya Nyerere na ushoroba wa wanyamapori wa Selous Niassa ambao ni mapito ya wanyamapori kati ya Tanzania na Msumbiji.

Mheshimiwa Spika, Wizara imechukua hatua zifuatazo: -

(i) Kuomba kibali cha kuajiri Askari wapya 600 ambao watasambazwa kwenye maeneo hatarishi ili kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu. Sambamba na hilo, Wizara ina mkakati wa kuanzisha vituo vya kikanda vya Askari katika maeneo yenye changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu;

(ii) Kutoa mafunzo kwa askari wa wanyamapori wa vijiji; na

(iii) Kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna bora ya kupunguza athari zinazotokana na wanyamapori wakali na waharibifu.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka ruzuku kwenye nishati ya gesi ili wananchi waweze kumudu kununua?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Sera ya Taifa ya Nishati ya Mwaka 2015 inaielekeza Serikali kuchukua hatua madhubuti za kufanikisha matumizi ya nishati safi na vifaa sahihi vya kupikia. Kwa sasa Serikali inakamilisha kuandaa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa lengo la kuhakikisha asilimi 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo Mwaka 2033. Hivyo, Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali kutatua vikwazo vinavyokwamisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kupunguza gharama za upatikanaji wa nishati safi, vifaa na majiko sanifu ya kupikia, ahsante.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha viwanda vya uzalishaji wa vyakula vya mifugo nchini?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji na kuhamasisha ujenzi wa viwanda nchini vikiwemo viwanda vya vyakula vya mifugo ambavyo vingi vinatumia malighafi za kilimo kama vile mahindi, soya na mashudu ya alizeti.

Mheshimiwa Naibu Spika, uzalishaji wa vyakula vya mifugo vilivyosindikwa umeongezeka kutoka tani 1,380,000 mwaka 2021/2022 hadi tani 1,580,000 mwaka 2022/2023. Aidha, viwanda vipya 22 vya kuzalisha vyakula vya mifugo vimesajiliwa katika mikoa nane kwa maana ya Arusha vinne, Kilimanjaro vitatu, Dar es Salaam vinne, Morogoro viwili, Iringa vitatu, Mbeya kimoja, Pwani vitatu na Shinyanga viwili na hivyo kufanya viwanda vya kuzalisha vyakula vya mifugo kuongezeka kutoka 199 mwaka 2021/2022 hadi 221 mwaka 2022/2023.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vya uzalishaji wa vyakula vya mifugo na kuhakikisha kuwa vyakula vinavyozalishwa vinakuwa na viwango stahiki kulingana na mahitaji ya mifugo husika.