Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Eng. James Fransis Mbatia (55 total)

MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kwa kuwa lengo la saba la Maendeleo Endelevu ya Duniani ni kuwa na umeme nafuu wa uhakika, endelevu na wa kisasa kwa wananchi wote; na kwa kuwa sekta ya nishati ni sekta nyeti; uzalishaji wa umeme, usafirishaji wa umeme na usambazaji wa umeme, Serikali imefikia hatua gani ya kuhakikisha uzalishaji na usambazaji unakuwa na ubia; na usafirishaji ukamilikiwa na Serikali ili effectiveness katika upatikanaji wa nishati uweze ukawa kwa wote?
Pili, kwa kuwa Kata zilizotajwa kwenye Jimbo la Kibamba, matatizo yake ni sawa sawa na Kata za Kahe Mashariki, Kahe Magharibi, Njia Panda Makuyuni katika Jimbo Vunjo, je, Serikali haiwezi ikaona kwa kuwa hili ni Bunge jipya, ikaleta mpango kazi wa usambazaji wa umeme kwa Majimbo yote ya uchaguzi nchi nzima ili Wabunge waweze kupata ikawa ni rahisi kufuatilia katika Majimbo yao ya uchaguzi? (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwanza swali la usambazaji, siyo kwamba tuna mipango, tunayo miradi. Kwa hiyo, kwa sasa tunaongeza usambazaji wa umeme unaotokea Iringa kwenda Dodoma, Dodoma mpaka Mikoa ya Kaskazini Magharibi, tunatoka kwenye kilovoti 220 kwenda kilovoti 400.
Mheshimiwa Spika, nadhani waliosafiri kwenye hiyo barabara wameona nguzo zile za chuma kubwa, halafu tunajenga transmission line kutoka mpakani mwa Zambia kwenda mpaka Namanga, kutoka kilovoti 220 mpaka kilovoti 400. Ni kwa sababu tunaingia kwenye biashara ya kuuziana umeme kama inavyofanyika duniani kote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukiwa pale Canada unaangalia wanauzia umeme Marekani Niagara Falls, ukiwa kule Iceland, Polland na nchi zote; kwa hiyo, Tanzania inayokuja ni ya umeme mwingi na wa bei nafuu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa nije umeme wa bei nafuu. Ni kwamba kwa sasa hivi ukichukua umeme wote tulionao nchini, hata wa watu binafsi, hatuvuki megawati 1,500; lakini mimi nitachangia siku ya mwisho kuonyesha namna gani tunajenga viwanda vyenye umeme wa bei nafuu.
Mheshimiwa Spika, kama tunataka kuingia nchi ya kipato cha kati miaka 10 ijayo lazima tuwe na Megawati zaidi ya shilingi 10,000/=. Ndiyo maana nakaribisha hata nyie Wabunge kama mnataka kuwekeza kwenye umeme, njooni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, bei ya umeme, wengine wanasema nilisema bei ishuke, haijashuka. Mheshimiwa Mbatia ni hivi nilisema tunapiga hesabu; hizi bei huwezi ukaongea kwenye majukwaa. Kwa hiyo, mategemeo yangu ni kwamba TANESCO na EWURA wanapiga hesabu, nitakaa nao. Umeme sasa hivi tunauziwa kwa senti 12 kwa unit moja. Tunataka kuushusha bei, lakini siyo kwenye majukwaa. Hesabu inapigwa na tarakimu mtazipata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile usambazaji wa umeme kwa wakazi wa Dar es Salaam, katikati ya jiji, kwa mara ya kwanza kabisa tunataka kuachana na matatizo ya umeme. Nyaya zote zinapita chini ya ardhi. Ile ya TANESCO kufukuzana na magari kutafuta wapi nyaya zimeharibika tunataka kuachana nayo kuanzia mwezi wa Nne. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, station ile inatizamana na Hospital ya TMJ ambayo itakuwa inaangalia wapi kuna matatizo. Huo mradi nadhani Mkandarasi nimemwambia ikifika mwezi wa nne, mvua sijui miti imeangukia kule katikati ya Dar es Salaam tutaachana nayo.
Ndugu zangu wa Mbagala na Temeke, tunajenga transfoma kubwa sana ambayo itatatua matatizo ya usambazaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Jimbo la Mnyika kote tunatoa transfoma ambazo zilikuwa za kVA100, kwenda 200.
Kwa hiyo, miradi ndugu yangu ni mingi sana Mheshimiwa Mbunge, tukileta hapa, mimi nadhani tuonane huko huko, field mnaziona. Ahsante. (Makofi)
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri ametuelekeza Watanzania wachangamkie fursa zinazojitokeza katika Soko la Pamoja la Afrika Mashariki na Jimbo la Vunjo ni sehemu ya kuchangamkia fursa hizo especially eneo la Taveta. Sasa lini Serikali itaharakisha ujengaji wa soko la Kimataifa la Lokolova pale Himo ili fursa hizo ziweze kutumika kwa Watanzania?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa soko la analolieleza Mheshimiwa Mbatia ni moja tu ya miradi mingi ambayo Serikali imefanya kuongeza fursa ya Watanzania kushiriki katika biashara ya Afrika Mashariki. Yeye mwenyewe atakuwa ni shahidi kwamba Serikali sasa hivi ina miradi ambayo nusu yake imekamilika ya kujenga vituo vya pamoja kwenye mipaka vinane, tunaita one stop boarder post na tumejenga vituo vizuri sana ambavyo vimeharakisha biashara katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile analolisema Mheshimiwa Mbatia ni suala ambalo tunafikiri ni muhimu kwa Wizara sasa hivi ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa maeneo yote ya mipakani, kwa kweli tuharakishe kumalizia miradi yote ambayo tumeianza na ambayo tunaifikiria ya masoko ya pamoja kwa sababu wenzetu upande wa pili wamechangamkia kweli fursa hiyo. Nadhani huo ni wajibu wa Serikali kuliangalia hilo kwa makini kwa kila mpaka siyo tu kwenye Jimbo la Vunjo.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa sekta ya uvuvi ni muhimu sana katika kukuza uchumi wa Taifa na ni sekta oevu kwa kupata mapato ya Taifa pia kuweza kuwapatia vijana wetu ajira. Serikali imeshafanyia kazi kiasi gani Taarifa ya Chenge One kuhusu sekta hii ya uvuvi hasa wa bahari kuu ambapo Serikali itapata mapato, wawekezaji wataweza kushirikiana na wawekezaji wa ndani ili Taifa letu liweze kujikwamua katika hali ambayo ipo na rasilimali tunayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli naungana naye kwamba sekta ya uvuvi ni sekta ambayo inategemewa sana na Watanzania wengi. Ni sekta ambayo inawaajiri Watanzania 4,000,000, kuna operators mbalimbali wanaofika 400,000 wanaojihususha na shughuli za uvuvi, kwa hiyo ni sekta muhimu sana. Vile vile nikubaliane naye kwamba potential iliyopo ni kubwa na kuna fursa kubwa sana ya kuweza kufanya hili eneo liweze kuchangia zaidi katika maendeleo ya Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kumekuwa na mapendekezo mengi ya namna ya kuboresha ufanisi wa sekta hii ikiwa ni pamoja na ripoti aliyosema ya Chenge One ambayo pamoja na mambo mengine ilipendekeza ni namna gani tunaweza tukapanua wigo wa fursa za uvuvi kwa kutumia bahari kuu. Katika kutekeleza ushauri huu, Wizara ipo katika mpango wa kuchukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha kwamba tunaweza kuanza kunufaika na rasilimali iliyopo katika bahari kuu. Kwa kuanzia, tupo kwenye mkakati wa kuanzisha fishing port. Tunataka tuanzishe bahari ya uvuvi ambayo pamoja na mambo mengine itakuwa rahisi kuratibu namna uvuvi unavyofanywa katika bahari kuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kama nilivyokwishasema hata katika Bunge hili tumeshakutana na Waheshimiwa Wabunge wanaotoka maeneo ya uvuvi na leo hii tena mchana tunakutana. Tunaendelea kupokea mawazo ya Waheshimiwa Wabunge ili tuone namna ya kuboresha sekta hii muhimu katika Taifa letu.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa kuwa dhana ya kuhakikisha Serikali inadhamini kutoa elimu ni jambo la msingi. Tatizo lililopo sasa ni miundombinu katika shule nyingi. Jimboni Vunjo tuna shule zaidi ya 16 ambapo nyingine hazina vyoo na matatizo makubwa kweli, ambapo ni janga hata zile shule kuendelea kufanya kazi sasa kwa sababu zinaweza ikasababisha majanga makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiweka utaratibu ukaufuata inakuwa ni jambo jema. Serikali haioni umuhimu wa kuleta mini budget ili Bunge liweze kutekeleza wajibu wake ili fedha hizo ziumike kwa utaratibu ambao tumejiwekea Kikatiba badala ya Serikali tu kusema inaagiza, inapeleka huku, inapeleka huku, kwa utaratibu ambao haueleweki na unaoleta utata?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA (MHE. GEORGE B. SIMBACHAWENE): Mheshimiwa Spika, ni kweli Mheshimiwa najaribu ku-pause wazo zuri, kubwa na lenye mtazamo mpana. Hata hivyo Serikali imeanza kutekeleza mpango ule wa kuhakikisha kwamba tunatoa elimu ambayo hailazimishi wazazi na hasa maskini kutoa mchango ndipo mtoto aende shule. Hili kusema ukweli ukilitafsiri kijuu juu utaliona ni jepesi, lakini unapomzungumzia maskini, Serikali hii ya awamu ya tano imeanza kujaribu.

Mheshimiwa Spika, tumejaribu kuji-confine kwenye bajeti ya mwaka 2015/2016, maana kwenye bajeti hiyo kuna fedha iliyotengwa na Bunge, lakini kuna ile fedha iliyopatikana. Sasa tumejaribu kucheza kwenye ile difference. Mheshimiwa Rais akasema, basi tuanze kutoa fedha kwa ajili ya uendeshaji wa shule inayoitwa capitation, itolewe in full amount kama ilivyokuwa imepitishwa siku za nyuma shilingi 10,000/= ambapo shilingi 6,000/= itaenda kwa ajili ya kila mtoto shuleni na shilingi 4,000/= itawekwa pamoja kwenye Wizara na kununua vitabu na kuwagawia, kupeleka kwenye mashule. Tumeondoa ile ya kununua vitabu kila mtu anakotaka.

Mheshimiwa Spika, pia Serikali imefidia ada ambapo kwa Shule za Kutwa ni shilingi 20,000/=. Ilikuwa ni lazima kila mtoto, mzazi achangie; imefuta! Pia shilingi 70,000/= kwa watoto wa bweni, Serikali imefuta, imechukua huo mzigo. Pia tutapeleka fedha ya chakula shilingi 1,500/= kwa kila mtoto wa shule za bweni na Shule Maalumu za Msingi. Hizi zote kusema ukweli zilikuwa haziendi vizuri, sasa tunazipeleka kabla ya mwezi. (Makofi)

Vilevile tutapeleka fidia ya mitihani. Mtakumbuka, kila mtoto hasa wa sekondari kidato cha nne alikuwa analipia Sh. 50,000/= kwa ajili ya mitihani. Hizi Serikali itazilipa yenyewe kwenye Baraza la Mitihani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali hii imejipanga kutumia shilingi bilioni 18.77 kwa kila mwezi. Kwa hiyo, nikijibu na swali la rafiki yangu pale ni kwamba fedha hii ni kila mwezi. Hivi sasa tunajiandaa kupeleka nyingine.

Mheshimiwa Spika, kumejitokeza tu changamoto ya idadi ya wanafunzi na records zilizokuja, ndiyo maana fedha zimeenda vibaya, lakini uzoefu tulioupata kwa mwezi huu, sasa naamini mwezi unaokuja tunaweza tukarekebisha hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakubaliana suala la miundombinu kwamba ni changamoto, lakini tumeeleza wajibu wa Serikali, lakini tukaeleza pia wajibu wa wadau wa maendeleo na wazazi katika masuala mazima ya kuhakikisha kwamba Taifa letu linatoa elimu iliyo bora na ambayo ni nzuri na ya kueza kufanya Jamii yetu iweze kubadilika na ku-meet viwango vinavyotakiwa. Ahsante sana.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Waziri anaonaje akishirikiana na Wizara ya Elimu wanafunzi wote wanaosoma masomo ya sayansi kwa A level wapate somo la health and safety ili iwe ni general kwa public ikiwepo sisi Wabunge kupewa elimu kama moto ukitokea kwenye Bunge hili tahadhari inakuaje, milango ikoje na mambo mengine yakoje humu ndani?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Waziri wangu Kivuli wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa umakini kabisa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaongea na mtaalamu kati ya wataalamu wachache tulionao nchini. Tumechukua hoja yake na tutawasiliana na Wizara ya Elimu na namuomba ashiriki kama ambavyo amekuwa akitushirikisha katika mambo mengine ya elimu ili tuweze kufikia huko kwenye eneo ambalo yeye amebobea
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Chanzo cha maji Masokeni kuimarishwa kwa shilingi milioni 759 na miundombinu ya kuhakikisha Vijiji vya Mande na Tella katika Jimbo la Moshi Vijijini ni fedha kidogo kwa kuwa eneo lenyewe ni kubwa, mahitaji ni makubwa. Serikali inaji-commit vipi kuhakikisha kwamba pamoja na fedha hizi watatafuta chanzo kingine cha fedha ili mradi huu ukamilike kama walivyoahidi hapa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Vijijini, Kata nyingine za Kirua Kusini, Mamba Kusini, Mwika Kusini, Kahe Mashariki, Kahe Magharibi pamoja na Makuyuni ambayo ni Mji mdogo wa Himo ambao unapanuka kwa kasi kubwa tatizo la maji ni kubwa sana na Kata ya Mamba Kusini imebidi Diwani aanze kufanya harambee... (Makofi)
MHE. JAMES F. MBATIA: Ndiyo nauliza swali, Serikali inaji-commit vipi kwenye maeneo haya mengine niliyoyataja ambayo maji ni muhimu kwa uhai wao ili waweze kupata maisha endelevu kama raia wengine wa Jamhuri ya Muungano? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa kwamba kwanza walitangaza tenda, halafu mradi ule haujaanza. Hata hivyo, tumeshatoa maelekezo kwa Halmashauri zote ile miradi ambayo haikuanza kwa sababu ya ukosefu wa fedha kwamba miradi hii ndio viwe vipaumbele kwa awamu hii tunavyoanza katika utekelezaji wa bajeti ya 2016/2017, hayo ndiyo maelekezo tuliyoyatoa. Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwamba fedha ni kidogo, ni kweli shilingi milioni 759 haiwezi kumaliza mradi kwa mara moja, lakini ni fedha ambayo unaweza ukatangaza ukampa advance mkandarasi akaanza kujenga. Sasa hivi tunazo fedha za Mfuko wa Maji ambazo tunapeleka kukwamua miradi yote inayoendelea. Kwa hiyo, naomba sana Halmashauri wakaanze kazi fedha hizi zinatosha kupeleka Vijiji vya Tella na Mande. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu yale maeneo mengine ambayo umesema yana matatizo makubwa. Nayo pia tumetoa maelekezo kwamba kila Halmashauri iweke mpango wake katika kutekeleza awamu ya pili ya program ya maji kwamba tukimaliza vijiji kadhaa tunaendelea na vijiji vingine ili tufikishe ile azma kwamba Serikali inataka tukifika mwaka 2020 tuwe na 85% wananchi wanaokaa Vijijini wanapata maji na wanaokaa mijini wanapata kwa 95%. Kwa hiyo, tumeshatoa maelekezo usiwe na wasiwasi Mheshimiwa Mbatia tutakwenda kupeleka maji katika maeneo yote kulingana na namna tulivyopanga bajeti. (Makofi)
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Kwa kuwa swali la msingi hapa ni kituo cha afya; na kwenye Jimbo la Vunjo, Kata ya Marangu Magharibi yenye vijiji saba haina kituo cha afya wala zahanati hata moja, na mpaka sasa Mbunge kwa kushirikiana na wananchi wa kijiji cha Kitowo na Kiraracha tumeweza kufanikisha shilingi milioni 20, na KINAPA wanatupatia shilingi milioni 53 na tunategemea kujenga kwa shilingi milioni 200, commitment ya Serikali itatoa mchango gani ili Kata ya Marangu Magharibi, hasa Kijiji cha Kiraracha waweze kupata huduma ya afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba niwapongeze kwa ile initial stage ya wananchi wako, mmefanya resource mobilization pale mmeweza kupata karibu shilingi milioni hiyo ishirini na kwa ajili ya jambo hilo, nililizungumza katika vipindi mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesema kwanza tumefanya tathmini ya nguvu za wananchi katika maeneo mbalimbali, kuna maboma mengi sana yamejengwa lakini yamefika katikati hayajakamilishwa, ndiyo maana tumewaagiza Wakurugenzi wote wa maeneo mbalimbali kuangalia zile juhudi ambazo wamefanya katika eneo lao, ili mradi katika bajeti hii ya mwaka wa fedha inayokuja tuhakikishe kwamba ajenda ya kwanza ni kukamilisha maboma na maeneo yote. Tukifanya hivi yale maboma ambayo yapo katika stage mbalimbali tutakuwa tumesaidia sana kuwapa support wananchi, lakini hali kadhalika tutakuwa tumejenga vituo vingi vya afya na zahanati tutapunguza tatizo la afya katika maeneo mbalimbali. Kwa hiyo nikushukuru katika hilo. Serikali commitment yetu ni kwamba tumeshafanya hilo zoezi liko katika ground linaendelea na katika mchakato wa bajeti hiyo ni priority yetu katika mpango wa fedha wa mwaka 2017/2018.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa swali la msingi linaulizia vitendea kazi vya elimu, ubora wa elimu, pamoja na mazingira yake yote ambayo ni elimu kwa wote, shirikishi na yenye ubora; mwaka 2013 tarehe 2 Machi siku ya Jumamosi, Mheshimiwa Rais aliunda Tume ya Sifuni Mchome ya kuangalia vigezo vyote hivi. Tarehe 31 hoja binafsi ilikuwa Bungeni kuhusu vigezo vyote hivi. Je, ni lini Serikali italeta ile ripoti ya Tume ya Sifuni Mchome hapa Bungeni ili Wabunge tuweze tukaishauri vizuri Serikali kuhusu ubora wa elimu Tanzania?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ni kweli nafahamu kuna hiyo Tume ilikuwa imeundwa na kuna baadhi ya mambo ambayo yalikuwa yameelezwa kwenye ile Tume; lakini baada ya hapo kuna team mbalimbali ziliundwa ambazo pia nyingine zilikuja kuona hata baadhi ya mapendekezo pengine hayako sawa; yaani hayaendani sawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Wizara tumekuwa tukiendelea kufanya marekebisho kulingana na mahitaji, kwa mfano katika suala la utoaji wa tuzo. Mwanzo zilikuwa zinatumia GPA, sasa hivi tumerudi tena kwenye division. Kwa hiyo, kuna mambo mengi tu ambayo yamekuwa yakifanyiwa kazi kila wakati. Hata hivyo, siyo tatizo kuweza kuwaonesha Waheshimiwa Wabunge nini kilikuwa kimezungumzwa kwenye Tume, lakini pia mabadiliko yanayoendana na uhalisia wa sasa yaliyofanyika.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa swali la msingi linaulizia ahadi ya Serikali na Mheshimiwa Dkt. Magufuli alivyokuwa Waziri wa Ujenzi aliahidi kukamilisha barabara ya Kawawa – Nduoni –Bakula – Marangu Mtoni ambayo ni barabara muhimu sana kwa ajili ya utalii, inajulikana kama utalii road. Alipokuwa anafanya kampeni wakati wa uchaguzi aliahidi pia kwamba itakamilika na imeshajengwa nusu tu kwa lami. Sasa ni lini Serikali itakamilisha barabara hii kwa maendeleo ya utalii na Serikali iweze kupata mapato. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Waziri kivuli wa Wizara hii nadhani anafahamu na tumejadili, ingawa katika kipindi kifupi kidogo hakuwepo lakini nadhani anafahamu kwamba tumekuwa tukijadili utekelezaji wa ujenzi wa barabara mbalimbali na tumesema kwamba kwanza tuzikazanie zile ambazo zina madeni ili tuondokane na madeni na baada ya hapo tutaendelea na hizi zingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hizi zingine kipaumbele cha uhamasishaji wa utalii nacho tulikiweka. Kwa hiyo, nimshukuru alitusaidia kuweka hiki kipaumbele na hivyo mara tutakapomaliza barabara hizi ambazo zina mikataba ya muda mrefu zitafuata hizi barabara zinazohamasisha utalii na vile vile zinazohamasisha viwanda.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la hifadhi ya Mlima Kilimanjaro una eneo la Half Mile au 0.8 ya kilometa, huduma za jamii kwa mfano uvunaji wa majani, uvunaji wa kuni kusafisha vyanzo vya asili vya maji, kwa mfano mifereji, inahusu vijiji 42 vya Halmashauri ya Wilaya ya Moshi. Wakati huu hakuna mahusiano mazuri kati ya wananchi wa vijiji hivi 42 pamoja na Hifadhi chini ya KINAPA hasa wale askari. Serikali haioni ni vema pande zote zinazohusika yaani wawakilishi wa vijiji pamoja na KINAPA ikisimamiwa na Serikali kuweka taratibu na kanuni endelevu zinazoaminika za mazingira ya kisasa ili mahusiano mema kati vijiji 42 na Hifadhi ya Mlima Kilimajora viweze vikawa vya mazingira ya kisasa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ufupi kabisa Serikali inazingatia ukweli kwamba ili uhifadhi uwe endelevu ni sharti wananchi wanaozunguka maeneo ya hifadhi husika, wanaopakana nazo waweze kuona kwamba wao ni sehemu ya huo uhifadhi kwenye hayo maeneo yanayohusika.
Kwa hiyo, njia zote zinazotumika katika kukamilisha malengo ya uhifadhi ni lazima ziwe rafiki kwa wananchi ambao wanazunguka kwenye maeneo hayo. Kwa sasa Serikali inachokifanya ni kuanzisha taratibu za kuwasogelea wananchi kwa ukaribu kabisa na kuwashirikisha, kuwapa elimu kwanza ya manufaa ya uhifadhi wenyewe, pia kuona namna gani wanaweza kushiriki kwenye jitihada za Serikali za kuhifadhi, muhimu zaidi mwishoni kabisa ni kuona namna ambavyo wananchi hawa wanaweza wakanufaika na uhifadhi moja kwa moja ukiacha ule utaratibu wa kunufaika na uhifadhi kwa njia na taratibu za kawaida za Kiserikali.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Tatizo la walimu ni kubwa na ndiyo maana linasababisha hata matokeo ya wanafunzi yanakuwa hafifu. Kwa mfano, Jimbo la Vunjo lina upungufu wa walimu 207, sasa mchakato huu ni lini utamalizika kwa sababu mitihani iko karibuni na hali inazidi kuwa mbaya?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimweleze tu kwamba tunatambua upungufu uliopo katika Wilaya ya Vunjo na nimhakikishie tu kwamba by tarehe 15 Julai, 2017 tunaamini tutakuwa tumefika katika sehemu nzuri. Ahsante.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la msingi lilikuwa linauliza kiasi cha Deni la Taifa hadi sasa. Mheshimiwa Waziri hakujibu kabisa hilo ndiyo swali limeulizwa lakini hakulijibu hilo kabisa! Amekuja na mambo mengine mengi tu.
Kwa kuwa yote aliyosema Mheshimiwa Waziri katika kujibu swali hili ameonesha kwamba mwaka huu wa fedha 2017/2018 Serikali imejipanga kukopa shilingi trilioni 8.83 ambapo wastani kwa mwezi ni sawa na kukopa shilingi bilioni 652 na mishahara ni takribani shilingi bilioni 600. Kwa hivyo kwa mwezi tutakuwa tunalipa mishahara pamoja na kulipa Deni la Taifa. Je, fedha za maendeleo zitapatikana wapi kama tutakuwa tunalipia tu Deni la Taifa pamoja na mishahara?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Serikali ya Awamu ya Tano ilivyoingia madarakani Deni la Taifa lilikuwa ni shilingi trilioni 35 lakini hadi mwezi Machi mwaka huu deni la Taifa limeongezeka na kufika shilingi trilioni 50.8 kwa kasi kubwa namna hii ya kukopa tunalipeleka wapi Taifa letu ambapo tutaweza tukaangamia? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa James Mbatia kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa napenda kuliambia Bunge lako tukufu swali kama lilivyoulizwa ndivyo nilivyolijibu kwa sababu limeulizwa tangu tumepitisha Mpango wa Maendeleo. Mpango wa Maendeleo tunaoutekeleza sasa ni mpango tulioupitisha mwaka 2016/ 2017 na ndio tunaoutekeleza na ndivyo tulivyojibu swali letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu upatikanaji wa fedha za maendeleo; upatikanaji wa fedha za maendeleo unapatikana kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi kwamba tunaimarisha ukusanyaji wa mapato, kwa hiyo, tunaweza kulipa deni letu na deni letu la ndani inakuwa ni rollover.
Kwa hiyo, hiki alichokisema Mheshimiwa James Mbatia inawezekana kabisa kwa sababu hii ni rollover tuna roll mikopo yetu tunaweza kulipa riba yetu na tunaweza kulipa deni letu la nje. Kwa hiyo, tuna uwezo wa kulipa deni letu na tuna uwezo wa kuendelea kutekeleza miradi yetu ya maendeleo kama tulivyofanya mwaka huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ameuliza tunalipeleka wapi Taifa letu. Napenda kurejea kauli yangu niliyoisema ndani ya Bunge lako Tukufu kwamba what matters is not how much you have borrowed but for what have you borrowed; tunakopa ili kutekeleza miradi ya maendeleo, miradi ya kimkakati, miradi inayochochea ukuaji wa uchumi wa Taifa letu na hakuna duniani hata Marekani yenyewe inakopa na inaweza kutekeleza miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunachokiangalia uchumi wa Taifa letu unakuwaje, miundombinu ya Taifa letu inayopelekea ukuaji wa uchumi wetu inatekelezwa kwa kiasi gani. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa nchi ya Tanzania imejengwa na tabaka
zote hasa wakulima na wafanyakazi; na kwa kuwa Serikali ya awamu iliyopita kwenye bajeti ya mwaka 2013/2014 - 2014/ 2015 walitoa ahadi kwenye Bunge hili kwamba watalipa wastaafu wote (wazee wote wenye miaka 60) bila upendeleo wa aina yoyote, wawe wafanyakazi au wakulima.
Nataka kupata kauli ya Serikali ni lini watatekeleza ahadi yao hii ya kuwalipa wazee wote nchi nzima ambao wana zaidi ya miaka 60?(Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimjibu Mheshimiwa James Mbatia, mzee mtarajiwa swali lake ambalo ameliuza kwa niaba ya wazee.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, imetoa ahadi ya kushughulikia suala zima la ulipaji wa pensheni kwa wazee katika nchi yetu ya Tanzania. Naomba nilithibitishie Bunge lako Tukufu mchakato huo umeshaanza na tayari tathmini na study zimeshafanyika za kuona ni utaratibu gani utafanyika wa kuweza kuwalipa pensheni wazee hao, michakato hiyo yote ikishakamilika basi Bunge lako Tukufu litaarifiwa ni lini utaratibu huo wa malipo ya pensheni utaanza. (Makofi)
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kituo cha Polisi Himo kinatoa huduma kwa watu zaidi ya laki tano na kipo mpakani na Serikali ilishaahidi hapa Bungeni tangu mwaka 2013 kwamba itapeleka magari mawili (2) mapya kwa ajili ya kutoa huduma kwenye kituo hicho kutokana na umuhimu wake. Hali sasa ni tete sana, kituo kinatumia pikipiki wako kwenye hali mbaya sana. Je, sasa Serikali ni lini kwa dharura itapeleka magari haya mawili waliyoahidi kwa zaidi ya miaka minne (4) katika Kituo cha Polisi cha Himo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbatia kwamba kama ni ahadi ambayo imetolewa na Serikali ya kupeleka gari katika kituo cha Himo, basi nitaifuatilia nitakapotoka tu hapa, kujua ni kitu gani kinachokwamisha ahadi hiyo isitekelezwe mpaka leo ili tuone jinsi gani tunaweza tukaitekeleza pale tutakapopata uwezo wa magari ya kutosha tuangalie haraka iwezekanavyo tunaweza vipi kutimiza ahadi hiyo ya Serikali ya muda mrefu.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Kata ya Marangu Magharibi yenye vijiji saba haina zahanati hata moja na hasa vijiji vya Kiraracha na Kitowo wako kwenye hali mbaya sana. Mbunge kwa kushirikiana na wananchi wameweka nguvu zao wanajenga zahanati kwa sasa na imefikia hatua za mwisho.
Nini commitment ya Serikali angalau milioni 20 ya dharura, ili kata hii iweze kupata kituo cha afya cha kisasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika fursa niliyopata ya kutembelea Mkoa wa Kilimanjaro nilijionea. Nilienda Moshi Vijijini nikakutana na wananchi wa Kiafeni, nikakuta kwamba hawakai wakasubiri Serikali ifanye, kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge na yeye anakiri na wana utaratibu mzuri, wanasema siku ya utawala wanakwenda kushiriki wananchi kwa ujumla wake. Nguvu ambayo inatolewa na wananchi ukishirikisha na nguvu ya Serikali nina imani hata hiyo kazi ambayo imefanywa na wananchi anaosema Mheshimiwa Mbatia, hakika kwa kutumia uwezo wao wa ndani, kwa maana ya commitment kutoka katika Halmashauri, naomba niitake Halmashauri ihakikishe kwamba wanajibana ili huduma ambayo inahitajika kwa wananchi iweze kufikiwa kwa kumalizia zahanati.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Swali la kwanza, Majaji waliostaafu kabla ya mwaka 2013 ambao siyo wengi, hawako kwenye hali nzuri sana wakati wa kupata matibabu. Serikali haiwezi ikatumia busara hili suala likawa ni la kiutawala (administrative) ili bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria ikawahudumia Majaji hawa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Political Leaders Pension Act ya Mwaka 1981 inaelezea pamoja na watu wengine ambao wanatakiwa kupata pension, angalau wapo kazini kwa miaka 10 ni Wabunge. Je, Serikali haioni busara kuleta Muswada hapa Bungeni ili kufufua Sheria hii ya mwaka 1981 ili Wabunge waweze kupata pension? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la kwanza amezungumza kuhusu Majaji waliostaafu kuanzia mwaka 2013. Kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge ni kweli kwamba, kwa mujibu wa Sheria iliyoanzisha Bima ya Taifa ya Afya, Kifungu Namba 11(3) kinaeleza kuhusu wale watumishi wa Serikali waliokuwa wana-hold Constitutional Office ambao wanaweza kunufaika katika matibabu ya afya. Hata hivyo, katika Kifungu hicho pia, kupitia Sheria hii ya Mwaka 2007 imetamka pia, aina ya watu wanaostahili kupata huduma na stahiki kutokana na sheria ambayo imesomwa ya mwaka 2007.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, katika hili ombi la Mheshimiwa Mbunge la kwamba Serikali ione busara, kwa sababu ni suala ambalo linahusisha pia Sera na Sheria niseme tu kwamba, kama Serikali tunalichukua, lakini siwezi kuweka commitment ya kwamba litafanyika, ni pendekezo limetolewa, linahitaji kwenda kuangalia sera na sheria ambazo zinatuongoza, hasa kuanzia yale mafao ya Majaji, na sheria ambazo pia zinahusika kwa maana ya watoa huduma katika baadhi ya masuala ambayo yanawahusu Majaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili ameuliza kuhusu pension kwa Wabunge. Ombi la Mheshimiwa Mbunge hapa ni kufufua tu sheria, sasa Waheshimiwa Wabunge kwa sababu, masuala haya yanaweza kupitia Tume ya Utumishi wa Bunge na ninyi ndiyo Wabunge, lianzie kwenu kwanza ndiyo lifike Serikalini. Kwa hiyo, hii ni kazi ya Kibunge lianzie katika upande wa Bunge. (Makofi)
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Hospitali nyingi za Wilaya zina mkataba kati ya Serikali na mashirika hasa ya dini, Hospitali ya Kilema ikiwa moja wapo. Tunajenga maabara ya kisasa, nini commitment
ya Serikali katika hospitali ya Kilema ili iweze ikatoa huduma zilizo bora katika Taifa hili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niseme ujenzi wa maabara ni jambo jema sana na sisi Seriali tunaappreciate
hiyo juhudi kubwa inayofanyika na ukiona hivyo
maana yake tunasaidia juhudi za Serikali jinsi gani iweze kusaidia wananchi wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juu ya commitment ya
Serikali katika hilo naomba tuangalie jinsi gani tutafanya katika suala zima la mikataba hata suala zima la watendaji; kwa sababu wakati mwingine tunaweza tukawa na maabara lakini tukawa na watu ambao hawawezi kuendesha vizuri ile maabara. Kwa hiyo, commitment ya Serikali ni kuangalia jinsi gani tutafanya ili maaabara ikikamilika tuweze ku-deploy watu wazuri pale wa kuweza kufanya analysis ya maabara, wananchi wetu wakienda pale waweze kupata huduma bora hata magonjwa yao yaweze kudundulika vizuri zaidi.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Wilaya ya Kilema inahudumia zahanati zaidi ya 13; lakini zahanati hizo zina upungufu mkubwa wa vifaa tiba pamoja na watumishi ambapo zahanati ya Miwaleni imefungwa kabisa kwa kukosa watumishi. Ni nini tamko la Serikali kuhusu watumishi hawa kwenye zahanati zote 13?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka Mheshimiwa Mbatia ali-raise concern hii nadhani wiki iliyopita kuhusu hospitali hii. Mimi nafahamu wazi hata katika zoezi letu hili la uhakiki wa watu walioghushi vyeti, katika sekta ya afya tutakuwa na changamoto kubwa sana ya kukosa wataalam. Ndiyo maana Mheshimiwa Rais juzi alitoa maelekezo kwamba tutakuwa na ajira takribani 52,000 lakini miongoni mwao watakuwa ni wa kada ya madaktari, wahudumu wa afya pamoja na wauguzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimtoe shaka Mheshimiwa Mbunge kwamba katika ajira mpya tutaipa kipaumbele zahanati yake kwa sababu tunajua kuna vifaa vingi vimewekezwa ni lazima tupate wataalam wa kufanya ile. Kwa hiyo, tutalichukulia kwa umakini mkubwa ili kuwasaidia wananchi wa Vunjo waweze kupata huduma.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya maji nchini kwa ujumla siyo nzuri na lengo Namba 6 la ajenda ya 2020/2030 ni maji, upatikanaji wa maji safi, salama kwa wote duniani na Tanzania ni mwanachama. Katika Jimbo la Vunjo sehemu za kata….
Mheshimiwa Mwenyekiti, sawa. Katika Kata ya Mwamba Kusini na Mwika Kusini hali ya maji ni mbaya sana na wananchi wananunua maji ndoo moja kwa shilingi 500.
Je, Serikali inachukuliaje jambo hili kwa dharura ili upatikanaji wa maji uweze kupatikana kwa haraka?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya upatikanaji wa maji nchi ni nzuri kupitia programu ya maendeleo ya sekta ya maji awamu ya kwanza. Tulilenga kutekeleza miradi 1,810, tayari tumeshatekeleza miradi 1,433, tumejenga vituo vya kuchotea maji 117,000 na vituo vyote vingetoa maji vijijini sasa hivi tungekuwa na asilimia 79 ya upatikanaji wa maji safi na salama. Kutokana na mabadiliko kidogo ya tabianchi vyanzo vingi vya maji kukauka sasa hivi hiyo asilimia kidogo imeshuka, lakini tayari tumejipanga kuhakikisha maeneo yote ambayo hayatoi maji tumetenga fedha kwenye bajeti ya mwaka huu tulionao ili hayo maeneo yaweze kupatiwa vyanzo vingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la Vunjo Mheshimiwa Mbunge naomba tukutane, tujadili ili tuone ni namna gani tutatoa kitu cha dharura kuhakikisha wale wananchi wanapata maji.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, majibu ya Serikali ni sahihi yanaendana na lengo la 16 la Malengo Endelevu ya Dunia ya leo. Kwa kuwa Wabunge majukumu yao ni kuwa na uelewa mkubwa na ni sehemu ya viongozi katika jamii, Waziri haoni umuhimu wa kutoa semina kwa Waheshimiwa Wabunge ambapo watapata uelewa wa kutumia muda wao itakiwavyo kwa maslahi ya Taifa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, kwa kuwa Serikali imelitambua hili na inaonekana Waheshimwia Wabunge hawaijui vizuri hata Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; na kwa kuwa zipo sheria vile vile zinazoambatana na Katiba ambapo Wabunge tukipata uelewa na hasa majukumu manne ya Mbunge; la kwanza likiwa kwa Taifa lake; la pili, kwa Jimbo lake la uchaguzi; la tatu, kwa chake cha siasa; na la nne, kwa dhamira yake binafsi ili tuweze kupata uelewa wa hali ya juu namna hiyo na Bunge liweze kujenga maslahi kwa Taifa?
MHE. ANGELLAH J. KAIRUKI - WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kujibu swali moja kama ambavyo umeeleza, ingawa yeye ameweka kama maswali mawili lakini naomba nijikite kwenye swali moja.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na umuhimu wa kutoa semina kwa masuala mbalimbali ya namna ya kutumia muda kuweza kuuliza maswali kama haya, Mheshimiwa Mbunge anayo fursa na anayo haki ya kuweza kuuliza swali lolote. Ndiyo maana sisi kama Serikali tunaona ni fursa muhimu kuweza kutumia Bunge lako Tukufu kujibu maswali kama haya kuweka kuelimisha. Siyo Bunge tu, lakini vile vile Umma mzima wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, suala la namna ya kuelimisha kuhusiana na uelewa wa Katiba, ni jukumu la kila Mheshimiwa Mbunge lakini vile vile na wananchi wote kwa ujumla kuweza kuhakikisha kwamba wanayo elimu ya masuala mbalimbali ya siasa na elimu ya uraia ikiwemo uelewa wa Katiba.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Swali la msingi linaulizia kupata ujuzi na kujiajiri na ifikapo mwaka 2030 kwenye Maendeleo Endelevu ya Dunia, Lengo la Nne ni elimu bora sawa kwa wote. Je, Serikali imejipangaje kuwa na uendelevu wa kutoa masomo kwenye sekondari zetu yaani kwenye mitaala ya sayansi, biashara na kilimo badala ya kulazimisha watoto kuchukua sayansi tu ili iweze ikawa ni endelevu watoto wakaweza kujikita kwenye uelewa wao na stadi ambazo wanazipenda zaidi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru pia kwa swali zuri. Kimsingi hata sasa hivi kwenye baadhi ya maeneo tunazo shule hata za msingi ambazo zinatoa pia mafunzo ya ufundi, lakini vilevile tunaona kwamba kuna haja ya kuwapandikiza watoto wetu ujuzi kuanzia katika ngazi za elimu za msingi, sekondari na kuendelea ikiwemo masuala yanayohusiana na sayansi na mazingira au kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachokiona tu ni kwamba, kuna ugumu wa kusema kwamba kila jambo tunalolihitaji litawekwa kwenye mtaala kwa ajili ya huyo mwanafunzi. Kupitia vipindi vyetu vya elimu ya kujitegemea na mafunzo nje ya vipindi vya kawaida bado hawa wanafunzi wanaweza wakapata pia mafunzo kama hayo.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kituo cha Polisi cha Himo ambacho kinatoa huduma kwa wakazi takribani 400,000 na kiko mpakani, Serikali iliahidi hapa kwamba itafanya ukarabati wa miundombinu ya kituo hicho hasa Ofisi. Sasa ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya tangu mwaka jana na hali ya kituo inazidi kuwa hoi bin taabani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, jibu la suala hili, halitofautiani sana na jibu langu nililojibu mwanzo, kwamba kituo hiki cha Himo ni moja kati ya vituo ambavyo vina changamoto na hasa ukitia maanani kipo karibu na mpakani kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amezungumza. Kitu ambacho kimekwamisha kama ambavyo nimezungumza mwanzo ni suala la bajeti. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge avute subira tuna mpango wa kujenga vituo na kukarabati vituo vingi nchini kama nilivyozungumza katika jibu langu la msingi kwamba tuna upungufu wa vituo katika Wilaya 25 na vituo vingi vipo katika hali mbaya nchini, lakini tutafanya kazi ya kuvirekebisha na kujenga hatua kwa hatua.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Lengo la Nne la Maendeleo Endelevu ya Dunia linasema elimu bora sawa shirikishi kwa wote ifikapo mwaka 2020/2030.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka huu wanafunzi wamefaulu wengi sana ambao wanatakiwa waende kidato cha tano na hasa Shule za Sayansi; lakini kuna tatizo kubwa la wanafunzi wanakwenda kwenye shule hizo hakuna maabara kabisa. Serikali Awamu ya Nne ilianza hili suala la maabara.
Je, nini jukumu la Serikali kwa haraka iwezekanavyo kuhakikisha shule zote za Sayansi zinakuwa na maabara za kisasa ili tujenge Tanzania yenye uwezo wa sayansi na teknolojia?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba wanafunzi wamefaulu wengi sana mwaka huu, ni kama takribani asilimia 27 ya waliofanya mtihani. Na malengo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ilikuwa kwamba tuwe tunapeleka wanaofaulu hawa wafike asilimia 20, isipungue asilimia 20. Kwa hiyo, utaona kazi nzuri imefanywa na Serikali, lakini nichukue nafasi hii kuwapongeza sana walimu wa nchi hii kwa kazi waliofanya na kusababisha ufaulu huu mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kushughulikia kiasi cha wanafunzi 93,018 ambao wamefaulu kwenda kidato cha tano, tumejipanga vizuri tumepeleka kiasi cha shilingi 22,000,000,000 ili kuhakikisha kwamba tunajenga maabara. Fedha hizi zimekwenda toka kama miezi mitatu iliyopita. Ujenzi unaendelea katika shule zote za A-level na hasa zitakazochukua wanafunzi wa combination za sayansi. Ujenzi huo tunahakika kabla shule hizi hazijaanza kupokea wanafunzi utakuwa umekamilika. Kwa sasa hivi tumetawanya watu kutoka ofisini pale Idara ya Elimu, karibu kila Mkoa tumepeleka maafisa wawili kwenda kuhakikisha kwamba wanasimamia kwa haraka ili shule hizi ziweze kukamilika. Kila shule ambayo tutakuwa tunapeleka wanafunzi zitakuwa na maabara zote zinazostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tumeshachukua hatua, tumepeleka fedha hizo na nipende kumshukuru Mheshimiwa Mbunge, kama kuna shule ambayo ipo katika eneo lako basi mtusaidie Waheshimiwa Wabunge wote, kwa sababu fedha zimepelekwa na ziwe kwenye Halmashauri zetu, tusimamie tuwe karibu tuhakikishe kwamba shule zile zinakamilika kabla ya tarehe moja mwezi wa saba. (Makofi)

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Sambamba na majibu mazuri kabisa yaliyotolewa na Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, ningependa pia kumpa taarifa Mheshimiwa James Mbatia kwamba Serikali pia imeshanunua vifaa vya maabara kwa ajili ya shule hizo, kwa hiyo ujenzi utakapokamilika vifaa vipo na wanafunzi watapata vifaa. Nakushukuru.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la hifadhi ya Mlima Kilimanjaro una eneo la Half Mile au 0.8 ya kilometa, huduma za jamii kwa mfano uvunaji wa majani, uvunaji wa kuni kusafisha vyanzo vya asili vya maji, kwa mfano mifereji, inahusu vijiji 42 vya Halmashauri ya Wilaya ya Moshi. Wakati huu hakuna mahusiano mazuri kati ya wananchi wa vijiji hivi 42 pamoja na Hifadhi chini ya KINAPA hasa wale askari. Serikali haioni ni vema pande zote zinazohusika yaani wawakilishi wa vijiji pamoja na KINAPA ikisimamiwa na Serikali kuweka taratibu na kanuni endelevu zinazoaminika za mazingira ya kisasa ili mahusiano mema kati vijiji 42 na Hifadhi ya Mlima Kilimajora viweze vikawa vya mazingira ya kisasa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ufupi kabisa Serikali inazingatia ukweli kwamba ili uhifadhi uwe endelevu ni sharti wananchi wanaozunguka maeneo ya hifadhi husika, wanaopakana nazo waweze kuona kwamba wao ni sehemu ya huo uhifadhi kwenye hayo maeneo yanayohusika.
Kwa hiyo, njia zote zinazotumika katika kukamilisha malengo ya uhifadhi ni lazima ziwe rafiki kwa wananchi ambao wanazunguka kwenye maeneo hayo. Kwa sasa Serikali inachokifanya ni kuanzisha taratibu za kuwasogelea wananchi kwa ukaribu kabisa na kuwashirikisha, kuwapa elimu kwanza ya manufaa ya uhifadhi wenyewe, pia kuona namna gani wanaweza kushiriki kwenye jitihada za Serikali za kuhifadhi, muhimu zaidi mwishoni kabisa ni kuona namna ambavyo wananchi hawa wanaweza wakanufaika na uhifadhi moja kwa moja ukiacha ule utaratibu wa kunufaika na uhifadhi kwa njia na taratibu za kawaida za Kiserikali.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Suala la msingi liliuliza ni lini, maeneo yaliyotajwa yatapata maji, ni lini? Tanzania kijiografia Mwenyezi Mungu ametujalia tunayo maji ya kutosha kwa matumizi ya binadamu na viumbe vingine vyote vilivyo hai kwa kuwa maji ni uhai, tatizo ni namna ya kuvuna maji, kuyatawala maji na kuyatumia maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwenye swali hili la Mheshimiwa Mnyika, ambapo wakazi wenyewe wanatumia maeneo yote aliyoyataja ni zaidi ya milioni mbili uhai wa binadamu hawa kukuza utu wao ni lini watapatia huduma ya hii ya msingi ya kukuza utu wao?
Swali la pili; maeneo ya Jimbo la Vunjo, Kata za Mwika Kusini, Makuyuni, Njia Panda, Kirua Kusini, Mamba Kusini yana tatizo kubwa la maji na wananchi wananunua maji ndoo moja kwa shilingi 500 mpaka shilingi 1,000. Je, Serikali haioni umuhimu wa kutengeneza programu kwa Wabunge wote ikiwemo na Vunjo ndani ya miaka hii mitatu ya kipindi chetu cha Ubunge tuweze tukajua kila programu inatekelezwa kwa muda gani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza kwenye swali la msingi wamesema ni lini. Mheshimiwa Mbunge Mbatia ni kwamba kuhusu maji ya kuyatoa Mtambo wa Ruvu Juu, ambapo juzi Mheshimiwa Rais ameuzindua, maji yako tayari, mradi uliobaki ni wa usambazaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa mkataba huo Mkandarasi anatakiwa kukamilisha mradi huo mwezi Julai mwishoni. Kwa hiyo sijaelewa sasa jinsi anavyoendelea lakini tutauangalia kama utakamilika kama ulivyo, mwishoni mwa mwezi Julai, ni kwamba mwezi Agosti wananchi wataanza kupata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; ni kweli tulikuwa na programu ya kwanza ambayo ilianza kwenye bajeti ya mwaka 2006/2007 imekamilika mwaka 2016 mwezi Juni, ni Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji. Ndani ya programu hiyo tukaibua miradi 1,810 na mpaka tunapozungumza miradi 1,333 imekamilika bado 477.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tumeingia kwenye programu ya pili. Mahitaji ya programu ya pili ni dola za marekani bilioni 1.6 na mpaka ninavyozungumza wafadhili wameshatupatia ahadi ya zaidi ya dola bilioni moja. Kwa hiyo, nina hakika kabisa kwamba, kupitia mpango huu mwingine wa miaka tano, nimhakikishie Mheshimiwa Mbatia kwamba, tutapita maeneo yote, tutatengeneza studies tutatekeleza miradi ili wananchi wa Jimbo lake la Vunjo na vijiji vilivyobaki wafaidi utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Hiyo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Mheshimiwa Spika, lengo la nne la maendeleo endelevu ya dunia ni elimu bora, sawa, shirikishi kwa wote. Suala la mitihani na udanganyifu ni mchakato mdogo to end product. Sasa Serikali ina weka lini au itaanzisha lini chombo cha kudumu cha kuangalia mchakato mzima wa elimu yaani ubora wa elimu, kuwekeza kwenye miundombinu ya elimu kwa walimu, ukaguzi, vyote yaani quality assurance itaanzishwa lini chombo hiki ili elimu yetu, mitihani iwe ni sehemu ndogo tu kama ilivyo nchi ya Finland ambapo asilimia kumi tu ndiyo ile mitihani lakini mchakato mwingine wote wa kumuandaa mtoto unakuwa umeandaliwa na umesiamamiwa na chombo chenye mamlaka na kinachojitegemea? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, wizara imeliona hilo. Ni kwamba kwa sasa hivi kwanza tunaiangalia upya Sheria yetu ya Elimu kwa sababu ni ya muda mrefu na kuna mambo mengi yamejitokeza na hiyo tungependa iendane na uhalisia. Vilevile tunataka kuangalia mfumo mzima wa namna ya ukaguzi. Kwa mfano mwanzo tulikuwa na ukaguzi katika sehemu za kanda na kwenye Halmashauri/kwenye Wilaya zetu lakini sasa hivi baada ya kuongeza shule nyingi, inaonesha kwamba sasa kanda peke yake si sehemu sahihi badala yake tungeweza kuangalia mfumo mzima na tukauboresha zaidi. Hii ni kwa sababu sasa shule za Serikali kwa mfano za sekondari zimeshaongezeka sana.
Mheshimiwa Spika, vilevile tunaona kwamba haitoshi tu kuangalia shule ina walimu wangapi, madarasa mangapi na vyoo vingapi, tunataka tuangalie mfumo mzima, na hivyo wizara sasa hivi inaandaa Mfumo wa Uthibiti na Tathmini kwa ujumla (National Schools Assurance Framework) ambayo itawezesha sasa hata kama unafanyika ukaguzi unakuwa tayari una mwongozo unaokwambia ni nini unatakiwa ufuatilie. Vilevile hata kushirikisha kamati za shule pamoja na walimu na wananchi wenyewe kwa ujumla katika kudhibiti ubora wa elimu Tanzania. (Makofi)
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa maendeleo ya Taifa lolote lile yanatokana na mifumo yake ya elimu inayojali utu wa binadamu; na kwa kuwa Walimu ni sehemu muhimu sana katika uzalishaji wa maendeleo endelevu katika Taifa letu.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kutenga fungu maalum la fedha hata kama ni kukopa ili kuondoa kero hizi katika sekta ya elimu ikiweko nyumba za walimu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbatia ambaye ni mkereketwa mkubwa sana wa sekta ya elimu napenda nimhakikishie kwamba mawazo yake ni sawa tu na mawazo ya Serikali. Hivi karibuni tumekamilisha kukokotoa gharama zinazohitajika kuweza kukamilisha miundombinu inayohitajika katika sekta ya elimu ili tuanze utekelezaji kwa asilimia 100 wa Sera yetu ya Taifa ya Elimu ya mwaka 2014, hilo analoliongea ni mojawapo ya yale ambayo tumeyaingiza katika hizo gharama na gharama za awali katika rasimu inaonyesha wazi kwamba tunahitaji takribani trilioni 13 ili kuweza kukamilisha miundombinu yote inayohitajika.
Naomba Mheshimiwa Mbatia na Bunge lako Tukufu liweze kuwa na subira, tutakapokamilisha tutafanya majadiliano maalum ili tuweze kupata fedha zinazohitajika kwa sekta ya elimu. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Udhaifu katika sekta ya elimu ni mkubwa kwa nchi nzima na hiyo imekuwa ni mjadala kwa muda mrefu na Wabunge hapa wanaulizia miundombinu na mambo mengine kama walimu, mishahara, yapo ni mambo mtambuka. Sasa Serikali haioni umuhimu, ili elimu yetu iweze ikawa sawa, bora na shirikishi kwa wote, tukawa na mjadala wa Kitaifa namna ya kuboresha elimu kwa kuwa ndio tunda la mfumo wa maendeleo yote Tanzania?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. GEORGE J. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimshukuru sanaMheshimiwa James Mbatia kwa kurejea kauli ambayo aliitoa Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, Rais wetu mstaafu kuhusu mjadala wa kitaifa ambao sasa hivi tunafikiria namna ya kuuandaa. Kwahiyo naomba ashiriki na sisi katika kuandaa mjadala huo.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kuna mwingiliano mkubwa wa njia za mawasiliano hasa SafariCom kwenye Jimbo la Vunjo, Rombo na maeneo yanayozunguka mipakani. Serikali ina mkakati gani, labda washauriane ili kuweza kuona mwingiliano huu unaondoka namna gani kwa sababu wewe mtumiaji unalazimika kuingia kwenye roaming bila wewe mwenyewe kutaka na inasababisha gharama kubwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli maeneo mengi sana ya nchi yetu hasa yale ya mipakani kumekuwa na mwingiliano mkubwa sana wa mawasiliano kati ya hizo nchi jirani na Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote na TCRA tumeendelea kuyaainisha maeneo hayo kwa ajili ya kuongeza nguvu minara yetu na kuzuia frequency ambazo ni mtambuka kutoka nchi moja kwenda nyingine kuhakikisha tunazidhibiti ili Watanzania wapate mawasiliano ya Tanzania na nchi jirani ziendelee kupata mawasiliano kutoka nchi hizo.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kama Mheshimiwa Waziri alivyosema ni kwa kweli hospitali hizi zinafanya kazi kubwa sana, lakini hali ilivyo sasa tangu Septemba, 2013, hospitali hizi hazijapewa ruhusa ya kufanya ajira mpya wala ajira mbadala na watumishi wapo pungufu zaidi ya asilimia 50. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuangalia hospitali hizi hasa Hospitali ya Huruma, Kilema, Machame mpaka kule Karatu ambazo zina upungufu wa watumishi kwa zaidi ya asilimia 50?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, mkataba kati ya Hospitali ya Rufaa ya KCMC na Bugando tangu Septemba, 2017 haujakamilika au haujafanyiwa kazi ambapo hospitali hizi haziendeshwi vizuri inavyotakiwa na ni hospitali za rufaa. Je, ni lini Serikali itakamilisha utaratibu huu wa mkataba kati ya Serikali na Mashirika haya ya Dini hasa Hospitali ya Bugando na KCMC?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kwamba baadhi ya hospitali ambazo zimetajwa zimekuwa na changamoto ya rasilimali watu na kadri tunapopata uwezo tumekuwa tunapeleka watumishi. Tunatarajia baada ya Bunge hili la Bajeti tutapata watumishi wa ziada ambapo katika hospitali hizi za DDH na sisi tutapeleka watumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali la pili ameongelea suala la mikataba. Ni kweli Serikali imekuwa inapeleka rasilimali watu na fedha, lakini tumekuwa tunapata changamoto katika baadhi ya hizi hospitali katika usimamizi wa fedha na rasilimali watu ambao tumepeleka. Sasa hivi Serikali inafanya mapitio na pale mapitio haya yatakapokuwa yamekamilika, basi tutaingia mkataba ili tuweze kusimamia vizuri rasilimali fedha za Serikali na watumishi ambao tunawapeleka.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Mwaka 2002 mpaka 2004 tulikubaliana kati ya wadau wa vyama vya siasa na Serikali tuwe na chuo cha kitaifa cha kuandaa viongozi bila kuangalia itikadi za vyama wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu. Je, Serikali imefikia wapi kuhakikisha tunakuwa na Chuo cha Kitaifa cha kuandaa viongozi kwa ajili ya uzalendo wa kitaifa bila kuangalia itikadi za vyama vya siasa ili tuwe na Taifa moja lenye malengo yanayofanana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA, NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali nia na dhamira ni kuendelea kukuza demokrasia ndani ya nchi na makubaliano hayo ya mwaka 2002 tutaendelea kuyafanyia kazi na kuyafuatilia ili lengo hili liweze kutimia la kuwa na chuo cha kuoka wanasiasa ambao tunaamini kabisa kupitia chuo hicho basi tutakuwa tumejenga Taifa la watu wenye uzalendo na ambao watakuwa na ari ya kweli ya kuwatumikia Watanzania. (Makofi)
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, majanga mengi sasa hivi yanasababishwa na binadamu zaidi ya asilimia 96 ikiwepo kwenda kinyume na uumbaji wa dunia ya Mwenyezi Mungu. Sheria hii ya tangu mwaka 1932 mpaka 2007 kwa kiasi kikubwa ni uharibifu mkubwa wa mazingira na hasa barabara za vijijini. International Standard na vigezo vyake vya ujenzi wa barabara huwezi uka-upgrade barabara kutoka stage moja kwenda stage nyingine za vijijini ukafanya mita 60.
Mheshimiwa Spika, barabara hizi zinazoenda vijijini, kwa mfano barabara ya Kawawa - Pakula, Jimbo la Vunjo na barabara ya Himo na Himo - Mwika, kwa nini mnaamua kuchukua mashamba bila fidia na siyo standard? Barabara zinajengwa kwenda juu na siyo kupanua tu kwa horizontally?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ELIAS KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbatia, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza, nitumie nafasi hii kulipongeza Bunge kwa kutunga Sheria hii Na.13 ya mwaka 2007 ambayo kwa kweli ilizingatia sana mabadiliko, ukiisoma Sheria ya mwaka 1932 utaona namna ilivyokuwa. Kwanza ilikuwa ni ndogo sana, ilikuwa na kama section saba tu na ilikuwa inatoa mamlaka makubwa sana kwa wale watekelezaji wa ujenzi wa barabara wanaweza wakafanya maamuzi, sheria iliyowaruhusu. Mabadiliko haya yaliyokuja mwaka 1969 na baadaye kuja hii Sheria Na.13 imetoa nafasi kwa Mamlaka zetu za Barabara kuweza kuzingatia maeneo maalum na kuweza kufanya declaration ya ujenzi wa barabara. Hivyo, sheria ipo vizuri ni vema tu tuendelee kuitekeleza.
Mheshimiwa Spika, nimueleze Mheshimiwa Mbatia niseme kwamba Serikali inalipa fidia kulingana na sheria zilizopo pia lazima tuangalie na mamlaka zetu katika halmashauri. Mamlaka za Barabara zipo kwenye Halmashauri zetu, kwa mfano, sasa hivi tunayo TARURA na TANROADS kwa upande wa Serikali Kuu.
Mheshimiwa Spika, ni muhimu tu tukatazama sheria zote, Sheria za Barabara pamoja na sheria za kusimamia mamlaka zetu ili wananchi waweze kupata haki. Kama jambo hili linaweza kuwa mahsusi Mheshimiwa Mbunge alilete tulizungumze tuone namna nzuri ya kulishughulikia lakini Serikali ina nia thabiti ya kuwalipa wananchi fidia kulingana na sheria zilizopo.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Swali la msingi linasema pia vyanzo sababishi ni ajali na ajali nyingi zimekuwa zikitokea kwa uzembe. Sasa niulize Serikali, Kitengo cha Kupambana na Majanga yaani Risk Management katika Wizara ambapo kuna known risk, known-unknown risk and unknown–unknown risk lakini ajali nyingi zinasababishwa na known-known risk ambazo tunajitakia sisi binadamu. Sasa Serikali ni kwa kiasi gani inaimarisha Kitengo cha Risk Management kitaalamu na kibajeti ili kiweze kupunguza vyanzo vya ajali hizi ambapo maisha ya binadamu hayana thamani?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali tunatambua kwamba kumekuwa na ajali nyingi na hizi tumezizungumza sana kwenye Baraza la Usalama Barabarani. Ziko hatua kabambe nyingi ambazo zinachukuliwa na Serikali ili kuhakikisha kwamba ajali hizi zinapungua. Kwa kipindi hiki kifupi ajali zimepungua lakini tunapenda tuendelee kuzipunguza zaidi na zaidi. Nafikiria tunajaribu kutazama muundo wa Baraza hili sasa ili kuwa na mechanism nzuri ya kuhakikisha kwamba tunazitambua vizuri hizi risk ambazo zipo ili tuweze kuzishughulikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu suala la kupunguza ajali ni letu sisi wote. Kwa hiyo, nitoe tu ombi kwa Waheshimiwa Wabunge tuendelee kushauri wanaotumia vyombo, madereva wetu, madereva wa bodaboda ili wakati Serikali inachukua hatua ni vyema wote tuwe pamoja ili kuhakikisha kwamba tunatoa hamasa, tunatoa elimu na kuwafanya watumiaji wote wa vyombo waweze kutumia barabara vizuri. Pamoja na watumiaji wa miguu, hatari ziko nyingi tunaziona katika majiji na maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tushirikiane ili tuhakikishe kwamba ajali zinapungua na kama ikiwezekana tuziondoe kabisa.
MHE JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Tatizo kubwa la ajira ni mfumo wetu wa elimu ambao hauwapi fursa vijana wetu kuwa creative na innovative, yaani unakuwa na mfumo wa elimu ambao unaangalia miaka 50 unataka uwe na Taifa la namna gani badala ya elimu yetu ya copy and paste. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuhakikisha mitaala yake inaandaa Taifa ambalo linakuwa innovative and creative badala ya copy and paste?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, alichokisema Mheshimiwa Mbunge pia kimeripotiwa na taarifa mbalimbali, moja kati ya changamoto iliyopo ni namna ambavyo tunaweza tukawa tuna vijana wahitimu wenye ujuzi ambao utawapa sifa za kuajiriwa katika soko la ajira.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama ofisi ya Waziri kupitia mpango wa ukuzaji ujuzi, moja kati ya eneo ambalo tumelipa kipaumbele ni hilo. Mwaka jana Mheshimiwa Waziri Mkuu alizindua miongozo kwa ajili ya kuhakikisha vijana wetu wahitimu wa Vyuo Vikuu wanapata mafunzo ya vitendo ili waongeze sifa ya ziada kwenda kuajiriwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikirudi katika msingi wa swali lake ni kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Wizara ya Elimu tunafanya kazi hii kwa pamoja ili kuona namna bora kuja na mitaala ambayo itamfanya kijana wa Kitanzania akihitimu elimu yake awe na sifa za kuajiriwa ili apate nafasi ya kuajirika.

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama alivyosema kwamba kuna hoja ya kuhakikisha vijana wetu wanakuwa wabunifu ili watakapomaliza vyuo kama hawajapata ajira rasmi waweze kujiajiri. Kwa sasa Wizara ya Elimu ina mkakati mkubwa sana kuhakikisha kwamba tunakuza stadi za kazi ili vijana wanapohitimu wasiwe wanaangalia kuajiriwa tu vilevile waweze kujiajiri.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kwa sasa inatekeleza mradi unaitwa ESPJ - Education and Skills for Productive Jobs, mradi ambao unafadhiliwa na Wadau wa Maendeleo kwa dola milioni 100. Moja kati ya malengo yake ambalo ni kubwa, ni kuhakikisha kwamba kwenye shule zetu, vyuo vyetu vijana wanafundishwa stadi za kazi ili wakitoka hata kama hawajapata ajira rasmi waweze kujiajiri.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nitumie fursa hii kuendelea kusisitiza kwamba zamani tunapoenda kusoma shuleni tunafikiria kwenda kuajiriwa, kwa sasa focus tokea mwanzo tunataka watu wajue kwamba ajira ni pamoja na kujiajiri. Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. (Makofi)
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kituo cha Himo kiko mpakani na kinahudumia zaidi ya watu 500,000 na ukiangalia hali ya uhalifu, hasa mambo ya biashara za magendo mpakani ni kubwa. Serikali imekuwa ikiahidi kupatia kituo hiki gari, gari lililopo ni la zaidi ya miaka 10 na tulipewa na CRDB na gari hili limekuwa ni kazi ya Mbunge kulikarabati kila mwaka. Serikali imeshawahi kutoa ahadi zaidi ya mara tatu kuhakikisha wanapeleka gari Kituo cha Himo ili haki ya ulinzi na usalama wa Taifa ni kazi namba moja ya Serikali. Serikali watamke hapa ni lini wanapeleka gari hilo waliloahidi hapa immediately kabla Bunge hili halijamalizika kituo cha Himo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Mbatia amekuwa akiguswa sana na hili suala, nadhani si mara yake ya kwanza kuuliza hapa, mara ya mwisho nilimjibu na narudia jibu ambalo nimempa mara ya mwisho.
Mheshimiwa Spika, tunatambua changamoto za vituo vya Polisi vilivyopo mipakani, kikiwemo kituo cha Himo kama ambavyo amezungumza. Changamoto ambayo tunaipata sasa hivi ni kwamba, bado hatujapata magari mapya. Kwa hiyo, nikazungumza kwamba, tutaangalia sasa magari yatakapokuja yamekuja magari mangapi na wapi panahitaji zaidi.
Mheshimiwa Spika, natambua kituo ambacho amezungumza ni moja kati ya maeneo ambayo yanahitaji zaidi, itategemea wapi panahitaji zaidi sana na idadi ya magari yaliyopo. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge avute subira naamini kabisa kama siyo leo, kesho kama siyo kesho keshokutwa, lakini Serikali inatambua sana umuhimu wa maeneo haya, hasa mipakani kuwa na usafiri imara zaidi ili kudhibiti uingiaji na utokaji wa watu na bidhaa haramu katika nchi yetu.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Miaka mitatu mfululizo iliyopita Madaktari wamekuwa wakihitimu vyuo vyetu vikuu vya humu ndani. Madaktati wako wanasubiri ajira na sekta ya afya ina upungufu wa zaidi ya asilimia 50 ya Madaktari katika vituo mbalimbali na sekta nzima. Je, kwa nini Serikali isi-fast truck ili Madaktari hawa walioko mitaani wakaingia kwenye utumishi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli kwamba tuna uhitaji mkubwa wa Madaktari, lakini pia atakubaliana na mimi kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI imetangaza nafasi na kama hilo halitoshi na Wizara ya Afya nayo imetangaza nafasi kwa ajili ya hao Madaktari na Wauguzi kwa ujumla wake. Naomba nimhakikishie kwamba mchakato upo pazuri, kwa hiyo, hicho ambacho anaulizia kuhusiana na suala zima la ku-fast truck ingekuwa tumechelewa wakati ule lakini kwa sasa hivi tuko hatua za mwisho, naomba avute subira hili litakamilika.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Nini utaratibu wa Serikali katika kuhakikisha wananchi au mashirika mbalimbali wakishajenga zahanati hizi kwa mfano Jimbo la Vunjo Zahanati ya Kochakindo ina zaidi ya miaka mitano ilijengwa na TASAF haina watumishi wala vifaa kwa ajili ya kutoa tiba. Utaratibu wa Serikali ni upi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu kwamba swali la Mheshimiwa James Mbatia linaonekana ni maalum kwa eneo maalum. Kwa hiyo, namwomba sana baada ya kikao hiki leo hii tuweze kuonana ili anipe details.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Vifaa tiba ni tatizo kubwa kwenye hospitali nyingi nchini na utajiri mkubwa tulionao kuliko wote ni afya za mwanadamu.
Mheshimiwa Spika, swali, Wizara hii ina upungufu wa zaidi ya sekta ya afya zaidi ya asilimia 50 ya watumishi. Serikali inaji-commit nini kuhusu kuhakikisha watumishi wa kutosha wa Hospitali ya Newala wanapatikana kwa wakati ili waweze kutoa huduma zinazostahiki?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Hospitali ya Kilema iliyoko Vunjo au ya Halmashauri ya Wilaya ya Moshi ina tatizo la vifaa tiba na watumishi wake kwa wakati huu nesi mmoja anahudumia zaidi ya watu 30 wodini. Serikali inatoa kauli gani hapa ili hospitali hii nayo ipate watumishi wa kutosha pamoja na vifaa tiba kwa ajili ya afya za binadamu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, kuhusiana na commitment ya Serikali ili kuhakikisha kwamba watumishi wa afya wanapelekwa wa kutosha Newala ni kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi. Maombi yao ni kupatiwa watumishi 60 na hii naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbatia kwa niaba ya Mheshimiwa Ajali Akbar kwamba ni commitment ya Serikali kuhakikisha pindi fursa za ajira zitakapokuwa zimetolewa hatutaisahau Newala.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na Hospitali yake ya Kilema ambayo anasema wastani Nesi mmoja anahudumu wagonjwa 30 ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba tunaweka vifaa vya kutosha lakini pia na watumishi wa kutosha. Ndio maana wakati Mheshimiwa Waziri wa dhamana ya ajira alivyokuwa anahitimisha alisema ndani ya Bunge hili tunategemea kuajiri watumishi wa kutosha. Katika watumishi 59,000 watakaoajiriwa sehemu kubwa ni upande wa elimu na afya, naomba nimuhakikishie ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba tunapunguza mzigo mkubwa kwa wahudumu kwa maana ya manesi ili na wao wawe na fursa ya kuweza kuhudumia wagonjwa kwa uzuri zaidi.
Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie na Hospitali ya Kilema tutaikumbuka.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Mkoa wa Kilimanjaro umezungukwa na vijiji 88 ambavyo ni vya ujirani mwema, lakini kwa miaka kumi iliyopita mapato ya mlima huu ilikuwa ni shilingi bilioni 471.5 lakini vijiji vinavyozunguka vimepata shilingi bilioni 2.28 tu ambayo ni chini ya asilimia 0.48 wakati sera ni asilimia 7.5.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haioni umuhimu ili vijiji hivi vipate haki yake badala ya kupata shilingi bilioni 2.6 kwa mwaka, wapate shilingi bilioni 40, TANAPA waweze kukaa na Halmashauri husika za Rombo, Moshi na Hai ili waweke utaratibu ili waweze kupata haki yao inavyostahili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa vijiji vingi vinapakana kabisa na ile hifadhi yetu ya Mlima Kilimanjaro na niseme tu kwamba katika utaratibu wa sera ya ujirani mwema, tunachokifanya sisi katika bajeti nzima ile ya TANAPA tunatenga kati ya asilimia tano mpaka asilimia saba kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ile ya ujirani mwema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatukusema kwamba basi hizi zote asilimia saba ndiyo ziende katika vile vijiji, katika lile eneo husika. Maadam Mheshimiwa Mbatia ameleta haya mapedekezo, tutakaa chini, tutayaangalia na nitaiagiza TANAPA wakae na hizo Halmashauri ili kuona namna gani wanaweza kufaidi zaidi katika huo mradi. (Makofi)
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, barabara za Mkoa wa Kilimanjaro zikiweko za Same pamoja na za Vunjo na mkoa wa ujumla ziko kwenye maeneo ya mwinuko. Na barabara zote hizi, zinavyotengenezwa zinawekewa fedha kidogo ambazo sasa haziendani na hali halisia ya soil property au tabia ya barabara hizo. Je Serikali haioni umuhimu, wa kutafuta aina ya material ambayo ni nzuri na ambayo siyo ghari kama ilivyo beachmen ili kuweza kufanya barabara hizo ziweze zikapitika kwa urahisi na kuongeza uchumi wa Mkoa wa Kilimanjaro na Tanzania kwa ujumla?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, wazo ambalo Mheshimiwa Mbunge anatoa ni wazo jema na sisi Ofisi ya Rais TAMISEMI tumekuwa tukifanya majaribio na tumeanzia Wilaya ya Bihalamuro tulienda na Mheshimiwa Mukasa. Kuna stadi ambayo inafanyika namna ya kuweza kujenga barabara kwa gharama nafuu lakini barabara ambazo zitaweza kudumu kwa kipindi kirefu. Kwa hiyo, ni wazo ambalo tunalifanyia kazi hakika baada ya kujiridhisha juu ya uwezo wa barabara hizo kuhimili kudumu ni wazo ambalo tutalifanyia kazi kujenga barabara zetu kwa gharama nafuu lakini ambazo zitadumu kwa muda mrefu.
MHE. JAMES F. MBATIA: Ahsante sana, Mahakama za Mwanzo za Kilema lile jengo limebomoka kabisa na haifanyi kazi na Marangu inayofanya kazi hali ni mbaya sana na inahatarisha Hakimu na watendaji wote. Serikali inaji-commit itafanya lini ukarabati wa mahakama hizi na kujenga hii nyingine upya kwa sababu utoaji wa haki unakuwa ni mgumu sana katika Jimbo la Vunjo na Wilaya ya Moshi Vijijini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE): Mheshimiwa Spika, swali hili la Mheshimiwa Mbatia litajibu pia maswali ya Wabunge wengi ambao walitaka kusimama. Serikali inatambua upungufu wa Mahakama za Mwanzo nchi nzima na ndiyo maana katika mpango wa miaka mitano tuliyojiwekea katika Wizara wa uboreshaji wa miundombinu, tunakwenda kuyafikia maeneo yote kadri ya bajeti itakavyopatikana.

Mheshimiwa Spika, lakini pia niwaombe Waheshimiwa Wabunge katika Wizara ya Katiba na Sheria tumetengeneza majedwali ambayo yanaonesha Mahakama ya Wilaya, Mahakama ya Mkoa lakini na vilevile ukarabati na ujenzi wa Mahakama Kuu. Kwa hiyo niwaombe Waheshimiwa Wabunge watakaopata nafasi basi waweze kupitia jedwali lile waangalie katika eneo lake ni lini wamepangiwa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo, ya Wilaya na Mkoa.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwa misingi ya elimu bora, sawa, shirikishi kwa wote, elimu ya msingi inaanzia darasa la ngapi mpaka la ngapi na elimu ya sekondari inaanzia darasa la ngapi mpaka la ngapi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa James Mbatia, Mbunge wa Jimbo la Vunjo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa utaratibu tunaotumia tuna darasa la awali, darasa la kwanza mpaka la saba, form one mpaka form four na kidato cha tano na cha sita baadaye elimu ya juu. Ahsante.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Spika, ahsante, nilitaka kujua; kwa kuwa gharama ya kutumia asphalt yaani kujenga lami kama zinavyoonekana ni ya ghali na kwa kuwa ahadi za Mheshimiwa Rais ikiwemo barabara za Himo Mjini, Kahe na ya kwenda Kilema kwenye maeneo ya mwinuko zinahitajika zijengwe ili zipitike wakati wote. Nataka kujua, Serikali imefikia wapi kupitia wataalam kuja na teknolojia nyingine ya kutumia calcium oxide na moram ambayo ni rahisi kuliko hii ya asphalt ili ziweze zikatumike kwenye barabara zote nchi nzima na barabara zote ziweze kupitika kwa sababu ziko kwenye hali mbaya sana?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba kijibu swali la kaka yangu James Mbatia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli gharama ya kutumia asphalt ni kubwa lakini mara nyingi sana mahitaji ya barabara aina gani ya teknolojia ijengwe ni kutokana na jinsi gani ya ile barabara mahitaji yake yalivyo. Ndiyo maana ukiangalia katika ofisi yetu sasa hivi kuna barabara tunazijengwa kwa double surface dressing na hizi cost yake unaona kwamba ina- range katia ya shilingi milioni 300 mpaka milioni 500 lakini barabara ya asphalt inakwenda mpaka one billion per kilometer.

Sasa unakuja kuona ukiangalia hizi barabara ambazo sasa hivi tunazijenga katika miji mbalimbali tunatumia asphalt kwa sababu mizigo inayopita huko na kwa sababu tunalenga katika ajenda ya kiuchumi lazima tutengeneze barabara ambazo zitaweza kupitisha magari mazito kuhakikisha tunachochea uchumi wa eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, ushauri uliozungumza katika kitengo chetu cha ofisi yetu kuna watu wanafanya research maalum kwa aina mbalimbali ya barabara ya madaraja na ndiyo maana hata ukienda kule Kigoma tumeamua sasa hivi kuna teknolijia nyingine tumetoa Belgium ya ujenzi wa madaraja, kwa hiyo hiyo yote ni juhudi ya Serikali kuangalia nini tufanye katika maeneo gani, lengo kubwa ni kuhakikisha Wanancho wote waweze kufika.

Kwa hiyo, ushauri wako unachukiliwa lakini naamini kwamba Serikali inafanya juhudi kubwa kuhakikisha Wananchi wanapata huduma nzuri ya barabara. Ahsante.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Suala hili la hadhi ya mahabusu wetu ni suala nyeti na pana; na kwa kuwa sisi wote humu ndani tunayo nafasi ya kufanya marekebisho katika sheria hizi ili haki ya aina yoyote ya mahabusu iweze ikatendeka; na tumemsikia Jaji Mkuu akisema kwamba pamoja na kuwepo kwa wingi wa mahabusu ni kutokana na kutokufanyika kwa upelelezi na kuukamilisha ndiyo mtu aweze kupelekwa Mahakamani:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuiuliza Serikali, au Serikali kama imesikia kilio cha Jaji Mkuu na ushauri wao, nasi ni Wabunge na tukitegemea tunayo nafasi ya kuweza kufanya mabadiliko ya sheria hizi sasa, maana huwezi kujua kesho, wote hapa ni wafungwa watarajiwa; iwe kwamba, kama ni miezi mitatu upelelezi haujakamilika, basi mfungwa au mahabusu aachiwe au vinginevyo kwa busara itakavyoelekeza sheria hii sasa ifanyiwe marekebisho mahabusu waweze kupata haja na haki zao za kimsingi.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa wingi wa rehema kubwa na ndogo anazotujalia sote hata kufika siku hii ya leo. Vile vile nimshukuru tena Mheshimiwa Rais kwa kuniteua kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbatia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza hadi sasa jitihada hizi zinazofanyika kwa njia hizi tatu ambazo Mheshimiwa Naibu Waziri amezijibu kwenye jibu la msingi ni maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, alipotembelea Magereza likiwepo Gereza la Butimba na akatoa maelekezo kwamba hali ilivyo, Magereza yamezidiwa na mahabusu ndio wengi zaidi na ndiyo maana hatua zinaendelea kuchukuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, DPP amekuwa akifanya jitihada za kutembelea Magereza na kuongea na wafungwa. Pia nasi kama Wizara tumekuwa tukifanya hivyo na ninaamini kabisa kila baada ya muda tutakuwa tunapunguza baadhi ya mahabusu ambao wana kesi ndogo ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua kubwa zinafanyika, nami nadhani iko haja ya jitihada hizi zinazofanyika tukawa tunaleta taarifa hapa kwenye Kamati au kwa njia yoyote ambayo mtaona inafaa kwa sababu ni kweli jitihada zinafanyika. Isipokuwa mchakato wake kama mnavyofahamu, zipo haki za wafungwa, zipo haki za mahabusu na zipo pia haki za waliotendewa makosa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, usilichukulie jambo hili kama ni jepesi. Lazima lichujwe, liangaliwe na upo utaratibu wa kisheria wa kufanya mambo haya. Kwa hiyo, pia tusikimbilie kushabikia tu haki za hawa waliotenda makosa. Ni kweli wanazo, lakini zipo haki pia za waliotendewa makosa. Kwa hiyo jambo hili linahitaji tuli-balance vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani kwa jibu hilo watakubaliana nami kwamba jitihada hizi kwa kweli ni kubwa na zimetokana na maagizo na maelekezo ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Ukiangalia malengo endelevu ya dunia yanaenda kwa vipaumbele. Kipaumbele cha Nne ni elimu bora, sawa Jumuishi/Shirikishi kwa wote. Kipaumbele cha Tisa ni viwanda, ubunifu na miundombinu. Serikali imekuwa ikiwekeza kwa kasi kubwa kwenye miundombinu lakini ili uweze kutekeleza na kusimamia vizuri miundombinu yafaa kuwekeza zaidi ya mara mbili kwenye elimu kabla ya miundombinu. Serikali haioni umuhimu wa kuja na mpango mkakati bila kupepesa macho ili wawekeze kwenye elimu na hasa sayansi ili maabara zetu zikiwa kwenye hali nzuri ikiweko ya Rasesa ambayo Mbunge naijenga kule Vunjo waweze kuwekeza na watoto wetu wawe wabunifu waweze kuendesha karne ya sanyansi na teknolojia na hasa viwanda?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFlSI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa James Mbatia, Mbunge Vunjo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa maoni na mawazo yake mazuri na ya kisayansi. Nimhakikishie kwamba mpango wa Serikali upo mkubwa sana wa kuhakikisha kwamba tunaondoa changamoto hii. Tunaweka mpango mzuri wa kumalizia maabara zetu, kupata mabweni ya kutosha kwa watoto wa kike lakini kupata walimu wa sayansi hasa masomo ya hesabu, fizikia, kemia na biolojia ili masomo hayo yaweze kufundishwa.

Mheshimiwa Spika, lakini wakati tunatekeleza mkakati wa muda mrefu tunao mpango wa muda mfupi. Kama nilivyosema kwenye bajeti hii tunazo fedha na vyanzo vipo katika maeneo mbalimbali. Nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kabla ya mwezi wa pili au wa tatu tutakuwa tumepeleka fedha katika majimbo yetu ili kukamilisha miundombinu ya elimu. Mpango wa mwaka huu tumeelekeza Wakurugenzi na nyie Waheshimiwa Wabunge hakikisheni kwenye mpango mnaoanzisha pale kuwe na kipengele hicho cha kuwekeza katika walimu na madarasa lakini pia maabara katika halmshauri zile.

Kwa hiyo, tukishirikiana na Halmashauri zetu sisi Wabunge na wadau mbalimbali wa maendeleo na Serikali Kuu jambo hili linawezekana. Hatuwezi kuwa na viwanda halafu wageni ndiyo waje kufanya kazi hapa kwetu lazima tuwe na viwanda na vijana walioandaliwa vizuri wafanye kazi katika viwanda hivyo ili tuweze kuwekeza katika uchumi wa viwanda na uchumi wa kati.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana, katika skimu aliyoitaja Mheshimiwa Waziri, skimu ya umwagiliaji wa Kijiji cha Soko na Mawala vilivyoko Kahe katika Jimbo la vunjo pamoja na vile vya Lowa Moshi kwa ujumla vilivyoko kata ya Mogiri, Moshi Vijijini Serikali ina mpango gani endelevu na shirikishi katika kuyavuna maji haya, kuyatawala maji haya na kuyatumia maji haya, ili jamii nzima iweze ikapata elimu endelevu, ili yaweze kutumika kitaalam na kisayansi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, anapenda kujua mipango ya Serikali tuliyokuwanayo ya endelevu kwa ajili ya kutunza upotevu wa maji katika Mkoa huu wa Kilimanjaro, hususan katika Wilaya hii ya Moshi Vijijini. Mipango ya kwanza ni kutoa elimu kupitia kwenye vile vyama vyao vya wakulima wamwagiliaji. Tumewahamasisha wakulima wale wajiunge katika vyama vya watumia maji ya umwagiliaji, ili iwe rahisi sisi kama Serikali na wadau wengine kuwafikia wengi zaidi na kwa wakati kuendelea kuwapa elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia sasa hivi kama tulivyosema programu ya sekta ya kilimo onaongozwa na SDP II na asilimia zaidi ya 59 ya bajeti yake itatekelezwa na sekta binafsi. Tunawahamasisha sekta binafsi zote na kupitia benki yetu ya maendeleo ya kilimo kwa ajili ya kwenda kufanya tathmini na kuainisha fursa zilizopo kwenye kilimo cha umwagiliaji kwa kushirikiana na sekta binafsi hizi zitaendelea kujenga hizo skimu, baadaye wataziendesha na kukabidhi baada ya kurudisha gharama zao walizozitumia.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nchi yetu ya Tanzania tumebahatika kuwa na vyanzo vingi vya umeme ikiwemo umeme wa upepo, Joto ardhi, maji, solar na vinginevyo. Sasa Serikali ina mkakati gani shirikishi na endelevu ifikapo mwaka 2030 kutekeleza kikamilifu lengo la saba la malengo endelevu ya dunia la kuwa na affordable and clean energy?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali zuri la nyongeza la Mheshimiwa Mbatia akiuliza mkakati wa Kiserikali ambapo kufikia mwaka 2020 inaweza ikatekeleza lengo la millennium ambalo amelitaja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza mkakati wa Serikali yetu ya Awamu ya Tano tulivyojipanga ifikapo mwaka 2025 tuna matarajio ya kuzalisha megawatts 10,000. Megawatts 10,000 hizi zitatokana na vyanzo mbalimbali ambavyo amevitaja ikiwemo maji, gesi, nishati jadidifu, joto ardhi, solar na masuala ya upepo. Hivi tunavyozungumza, kwa kutambua umuhimu wa kuwa na energy mix ya uhakika ambapo kuzalisha umeme kutokana na vyanzo mbalimbali kupitia TANESCO, Serikali imetangaza tenda kwa ajili ya kuzalisha megawatts 950 ikiwemo megawatts 600 ya Makaa ya Mawe, megawatts 200 kupitia upepo na megawatts 150 kupitia jua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kuhusu masuala ya joto ardhi, Serikali kupitia tafiti mbalimbali na Taasisi yake ya joto ardhi, imetambua uwepo wa vyanzo vya kuweza kuzalisha umeme kupitia joto ardhi na sasa mpango unaoendelea, tunaishukuru Wizara ya Fedha imeiwezesha Tasisi ya joto ardhi kiasi cha pesa takribani shilingi bilioni 28 kwa ajili ya ununzi wa mashine za kuchoronga visima kwa ajili ya utafiti unaoendelea. Matarajio yetu, tutaanza kuzalisha megawatts 30 kutoka kwenye joto ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimthibitishie Mheshimiwa Mbatia kwamba kwa kweli Serikali inatambua na kuona umuhimu wa kuwa na energy mix ya kutosha kupitia vyanzo mbalimbali na ndiyo maana imejielekeza kwenye umeme wa maji, imejielekeza kwenye umeme wa gesi na miradi mbalimbali inayoendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimthibitishie tu kwamba tulivyojipanga, hilo lengo la millennium litafikiwa na tutakuwa na umeme wa kutosha ambao utaiwezesha nchi yetu pia kusaidia nchi za jirani, nchi za ukanda wa SADC na nchi za ukanda wa Afrika Mashariki. Tumejipanga sasa hivi ujenzi wa njia za kusafirisha umeme unaendelea vizuri katika maeneo hayo ili kuweza kuuza umeme katika nchi za jirani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Kwa kuwa swali la msingi ni kuhusu Hospitali ya Mawenzi na Hospitali ya Mawenzi kusema ukweli imezidiwa sana; namna gani Serikali inaona umuhimu wa kuimarisha hivi Vituo vya Afya kama alivyouliza Mheshimiwa Japhary Michael na hasa Kituo cha Afya cha Kirua Vunjo Magharibi ambapo tangu kimefungulia wa Mheshimiwa Abdu Jumbe mwaka 1973 miundombinu yake ni chakavu sana na wala hakina hadhi ya kuwa Zahanati ili kiimarike kiweze kutoa huduma kama vituo vingine vya afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika kwamba vile Vituo vya Afya vilivyojengwa miaka ya zamani vilikidhi haja kwa kipindi hicho. Ukilinganisha na Vituo vya Afya ambavyo vimejengwa sasa, vile vingine vyote vya zamani vinaoneka vimechakaa.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwanza tulianza kukarabati vile ambavyo vipo lakini pia tukaanza kujenga upya. Ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba vituo vyote vya afya vinakuwa na hadhi ya Vituo vya Afya ili viweze kutoa upasuaji wa dharura kwa mama mjamzito.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbatia, kama ambavyo Serikali imekuwa ikipitia kuona takwimu Vituo vya Afya vipi vichakavu na cha kwake tutakipitia.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, katika kuibadilisha dunia, ku-transform dunia, kigezo cha elimu kimepewa kipaumbele namba nne na kigezo cha elimu bora. Je, fedha hizi zaidi ya bilioni 900 ambazo zimekwenda kwenye shule zetu, kigezo cha kupima zimefanikisha kwa kiasi gani ubora wa elimu na viashiria vyake vyote ukoje!
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba tumepeleka fedha zaidi ya shilingi bilioni 900 kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi la swali la Mheshimiwa Zitto, na Mheshimiwa Mbunge anataka kujua vigezo vya kuonyesha kwamba elimu imeboreka ni kwa kiwango gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, fedha hii inafanya mambo mengi sana ikiwepo ni pamoja na uendeshaji wa shule, usimamizi wa elimu Tanzania umeimarika sana. Tumenunua pikipiki katika Waratibu Elimu wa kata zote nchini, sasa wanaweza ku-move kutoka shule moja kwenda nyingine, maana yake ni kwamba hata utoro rejareja umepungua shuleni, kiwango cha watoto kupata mimba na kuchukua hatua, tuna kesi mbalimbali mahakamani na baadhi ya watu ambao wametuhumiwa kuwapa wasichana wetu mimba wameshafikishwa mahakamani na wengine wamefungwa, kesi ziko katika hatua mbalimbali. Hiyo ni kwa sababu fedha hiyo imekwenda, imepeleka vifaa vya utendaji, pikipiki na imewezesha.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo la pili, tumejenga hosteli maeneo mbalimbali, kitendo ambacho kimepunguza watoto wa kike wengi sasa wanakaa katika shule zetu na utaangalia matokeo mbalimbali, darasa la saba, form four na form six, kiwango cha ufaulu cha watoto wa kike kimeongezeka sana. Tumejenga mabweni na hosteli maeneo mbalimbali, watoto wa kike wengi wanakaa katika maeneo ya shule na usimamizi wao umekuwa ni mzuri zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini elimu msingi bila malipo, sasa hivi tunapozungumza, vijana wetu wa kidato cha nne wanafanya mitihani. Mwaka 2018 wanafunzi ambao walisajiliwa, watahiniwa wa kufanya mitihani, walikuwa 427,000, mwaka huu ni 485,866, maana yake ni ongezeko la wanafunzi ambao wameingia kidato cha nne zaidi ya asilimia 1.37, huu ni ufaulu mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vijana wengi wa Tanzania maskini ambao walikuwa hawana uwezo wa kusoma wa kike na wakiume, wengine walifanya kazi za house girl, wengine walikuwa makuli kwenye masoko, walikuwa wapiga debe, ninapozungumza hapa, vijana wengi kitendo cha Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kuondoa ada katika masomo yao, watoto wengi wapo mashuleni, hata wananchi ambao wanataka ma-house girls wanapata shida sana kuwapata, vijana, wasichana wengi wanasoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, hayo ni kwa uchache, lakini Mheshimiwa Mbatia ni kweli kwamba, yeye anafahamu, hata matokeo ya form six yameongezeka, elimu ya high school imekuwa ni kubwa sana, kwa sababu ya fedha hizi ambazo zimekwenda kuimarisha huduma. Ndiyo maana, hata wananchi ambao walitoa nguvu zao kuchangia kujenga maboma, tumepeleka fedha zaidi ya bilioni 29, angalia halmshauri zote nchini ili tumalize maboma, watoto wetu waendelee kukaa katika madarasa ambayo yapo sawa na wapate matundu ya vyoo. Ahsante.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kanuni ya Muasisi wa Taifa hili, Mwalimu Nyerere ni kwamba binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja. Kanuni ya utu ndiyo inayoibeba dunia leo hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wazee wetu wengi wamechangia Taifa hili kutokana na nyanja mbalimbali, wengine walimu, wafanyakazi wa sekta mbalimbali, madaktari, wauguzi, wakulima, kila mmoja wetu amechangia Taifa hili tukafika hapa tulipo. Nini sera madhubuti ya Serikali na iliyo endelevu kwa ajili ya kuhakikisha wazee wetu wote hawa wanapata huduma za msingi na zinazostahili kukuza utu wao na hasa huduma ya afya ambapo wazee wengi vijijini kwa kweli wanateseka sana, sana, sana?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza lililoulizwa na Mheshimiwa Mbatia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba tukitaka kutafuta mchango wa watu mbalimbali hapa nchini ni karibu kila mmoja ana mchango wake, awe alikuwa mwalimu ametoa mchango wake kwa sababu sisi wote tuliopo hapa tumefundishwa na walimu na si ajabu ni wazee ambao wengine wana hali mbaya. Wako madaktari, manesi na kwa neno la jumla tunalolifahamu ni wakulima na wafanyakazi wote wamechangia maendeleo na ustawi wa nchi yetu hadi ilipofika hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mifano ya wenzetu wengine namna pekee ya kuwaenzi ni mfumo mzuri wa bima ndiyo huwa unaweza kuwatunza wazee hawa vizuri. Kama hatukuwa na mifumo imara sana ya bima kutafuta njia mbadala kwa sasa na kwa ukubwa wa michango mikubwa iliyotolewa haitasaidia kwa sababu huwezi kusema mkulima hakuchangia Taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wako watu ambao wamefilisika baada ya vita ya Uganda kwa sababu walitoa magari na hayakurudi. Tunahitaji kuwa na mtazamo mpana na kutafakari sana tunapokwenda huko. Ndiyo maana wakati mwingine unapofanya jambo kubwa la kujitolea kwa ajili ya nchi yako, sifa na heshima unayoipata ni kwamba wewe ni mzalendo. Neno uzalendo ni kubwa sana na pengine tumekuwa tukitambua michango ya watu mbalimbali kwa kuwapa recognition ya cheti cha Rais. Haya yote yanaonyesha heshima lakini mfumo bora na wenye kueleweka ni mfumo wa bima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwenye matibabu bora Waheshimiwa Wabunge tukatumia nafasi tuliyonayo kutunga Sheria ya Bima inayomhusu kila mwananchi awe na bima kwa ajili ya matibabu. Hii itakuwa ndiyo suluhu ya matatizo ya matibabu, ile Compulsory Health Insurance ndiyo jambo la mana nafikiri tuelekee huko tunaweza tukatatua tatizo la kuwatunza wazee wetu kwa matibabu na hata kwa mambo mengine na hasa afya zao ndiyo muhimu zaidi. Ahsante sana.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ahadi hizi za Rais ziko maeneo mengi na Vunjo maeneo ya Mamlaka ya Mji Mdogo wa Himo iliahidiwa kujengewa barabara kwa lami km 7 na sasa kuna mafuriko eneo la lower area Kahe kuanzia Fungagate, Kahe, Kiomu mpaka maeneo ya Chekereni na Kilema Hospital. Barabara zote hizi ziliahidiwa na Mheshimiwa Rais kujengwa kwa kiwango cha lami na Serikali inajua. Ni lini watatekeleza ahadi hii ya Mheshimiwa Rais?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja dogo la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niseme ni kweli ziko ahadi nyingi za Mheshimiwa Rais lakini katika barabara zimewekewa utaratibu wake. Tunaanza kwanza kukamilisha barabara kuu na zile zinazounga mipaka ya majirani zetu baadaye tutakwenda kwenye barabara za mikoa na tunarudi tena chini kwenye barabara hizo za vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge wewe tulia tu ni kwamba Ilani ya Chama cha Mapinduzi na ahadi za viongozi lazima zitekelezwe.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Spika, nashukuru.

Kwa kuwa majanga yanayosababishwa na binadamu ni zaidi ya asilimia 96 ya majanga yote. Serikali haioni umuhimu wa kuhakikisha kunakuwa na somo rasmi kwenye mfumo rasmi wa elimu wa namna ya kujilinda, kujinga na kujiokoa na majanga hapa nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mabtia, Mbunge wa Vunjo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nao vilevile ni ushauri; nadhani mamlaka husika zimeusikia, lakini kama Serikali tumeuchukua na tutafakari kuona kama kuna haja ya kufanya hivyo kwa wakati huu.
MHE. JAMES F MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, mwaka 2014 Tanzania ilikuwa inashika nafasi ya pili kwa vivutio vya utalii kati ya nchi 133 vyenye kushindana kwenye ubora wa vivutio vya utalii duniani ambapo GDP yetu wakati huo ilikuwa ni asilimia 17 na miundombinu ya utalii ya vivutio ya kutoa ubora wa utalii ilikuwa tunashika nafasi ya 110 kati ya nchi 133.

Je, kwa mwaka huu Tanzania inashika nafasi ya ngapi kwenye ubora vivutio vya utalii duniani na tunashika nafasi ya ngapi kwenye miundombinu bora ya kuchochea vivutio bora vya utalii duniani? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASII NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba miaka hiyo 1984 anayosema Tanzania ilikuwa ni nchi ya pili kwa vivutio na bado ni nchi inayoongoza kwa vivutio vya utalii duniani na hivi karibuni nafikiri uliona mchakato wa kuingiza moja ya vivutio muhimu kabisa ambavyo vilikuwa vinatangazwa kwenye vivutio vya dunia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake kimsingi ili niweze kulijibu vizuri na kufahamu takwimu zote ambazo amezisema ni kwamba lilipaswa kuwa swali la msingi lakini nimuhakikishie Tanzania bado ni nchi yenye vivutio bora na ni nchi ambayo katika Afrika ni nchi ambayo ina vivutio bora zaidi na katika dunia ni nchi ambayo ni huwa nadhani ni nchi ya pili baada ya Brazil.

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, utafiti uliofanyika kati ya mwaka 2012 mpaka 2014 ulitoa taarifa kwamba Tanzania inashika nafasi ya pili kwa vivutio vya nature duniani. Kutokea kipindi hicho mpaka sasa haujafanyika utafiti mwingine wa kuweza kutupa position yoyote ile tofauti na ile ya awali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini matokeo ya katikati ya utafiti huu ambao unafanyika kila baada ya miaka mitano yalitoka Tanzania ilionekana imeshuka kutoka nafasi ya pili mpaka nafasi ya nane kwa vivutio vya nature duniani. Na sababu kubwa iliyosababisha Tanzania kushuka ilikuwa ni uharibifu wa mazingira pia ikiwemo uvamizi wa mifugo na makazi katika maeneo ya vivutio vya utalii vya nature. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kazi kubwa imefanyika katika Awamu ya Tano ya kuwaondoa wananchi ambao wamevamia maeneo hayo, pia kupandisha hadhi baadhi ya maeneo, ninauhakika watakapofikia conclusion ya utafiti huo baada ya miaka mitano ambao ni mwaka huu pengine matokeo ya nafasi ambayo Tanzania inashika katika vivutio vya nature inaweza ikawa imeongezeka zaidi. (Makofi)
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana ukitaka kuangamiza Taifa lolote anza kuangamiza au kuharibu mifumo yake ya elimu inayolinda utu wa binadamu. Mwaka 1979 mabadiliko ya mtaala hayakuweza kukidhi changamoto za mabadiliko ya elimu ya wakati huo na Mwalimu Nyerere akaunda Kamisheni ya Makweta. Sasa ni miaka 37 tangu Kamisheni ile kufanya uchambuzi wa elimu hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, Sera ya elimu ya 2014 na mtaala wake haukidhi changamoto za elimu za sasa za lengo la nne la maendeleo endelevu ya dunia la elimu bora sawa shirikishi kwa wote. Sasa je Serikali haioni umuhimu wa kuweza kuchukua mifumo kama za Finland, Vietnam na kwingine ili tuweze tukaendana na changamoto za elimu za dunia za sasa badala ya kufanya elimu yetu trial and error kama ilivyo sasa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba kwanza nikiri kwamba Mheshimiwa Mbatia ni Mbunge makini sana kwenye masuala ya elimu kwahiyo mara nyingi ushauri wake tunauchukua kama ni ushauri mzuri. Naomba tu nimuhakikishie kwamba Wizara yangu Serikali haijawahi kukaa kimya kufanya mapitio ya mitaala pale inapobidi hata hivyo kama unavyofahamu, ubadilishaji wa mitaala huwezi ukawa unabadilisha kila siku kwa kiasi kikubwa unachofanya ni kufanya mabadiliko madogo madogo kama mwenyewe anavyosema maendeleo na mabadiliko ya teknolojia yanayotokea duniani na tunaendelea kufanya hivyo kila mwaka.

Mheshimiwa Spika, naomba vile vile nimuhakikishie kwamba kwa sasa tunafanya mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 ili tuweze kuhuisha ili iendane na mabadiliko ambayo yametokea na iweze kutupa elimu ambayo ni bora zaidi katika wakati tuliopo. Naomba nimuhakikishie vile vile kwamba wakati tunahuisha Waheshimiwa Wabunge watapata fursa vile vile ya kushiriki katika mjadala ambao utatuletea Sera mpya.

Mheshimiwa Spika, lakini pia kama Mheshimiwa Mbunge atakumbuka wakati tunajadili hotuba ya Wizara yetu tulitoa ahadi ambayo tunataka kuitekeleza ya kufanya mjadala kuwaita wadau tukutane tuongee ili hayo maoni na mengine tuweze kuyachukua katika kujaribu kuboresha sera yetu na hatimaye hata ikiwezekana na kubadilika mitaala iliyopo.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, mwezi uliopita tarehe 15 Mei ilitokea ajali mbaya ikaua watu wanne papo kwa papo na wengine watano wakafa baadae na majeruhi katika Kivuko cha Daraja la Mto Una njiapanda ya kwenda KINAPA ambapo barabara hii ina madaraja manne na madaraja haya ni single deck na sio double deck ambayo yanasababisha ajali na hali sio nzuri.

Je, Serikali kwa udharura huu ambao barabara hii inapitisha watalii pia inayatengenezaje madaraja haya yawe na double deck badala ya single deck ili kuweza kuondoa ajali hizi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbatia amezungumza juu ya ajali, lakini akubaliane na mimi kwamba kunapotokea ajali yako mambo mengi, mengine ni yale makosa ambayo sisi kama binadamu tunayafanya na mengine yapo yanahusisha miundombinu, lakini engineer utakubaliana na mimi tafiti zinaonesha asilimia 80 ya ajali inatokana na human behavior (tabia za kibinadamu).

Kwa hiyo, kwanza nianze kutoa wito tu kwa watumiaji wa barabara wawe makini kwa sababu ninaamini kwamba sehemu ambayo tuna barabara hii kama unavyosema iko na single deck ziko alama ambazo zimeoneshwa kuchukua tahadhari, lakini wako watumiaji wachache wa barabara hawazingatii maelekezo yanayokuwa katika barabara zetu. Kwa hiyo nisisitize hilo tu watumiaji wote wa barabara wazingatie matumizi ya barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala lako la kuitengenza barabara hii katika madaraja hayo manne uliyoyataka kuwa double deck naomba nilichukue kama ushauri tuifanyie kazi tuone kwamba tunaweza kurekebisha kadri itakavyokuwa imewezekana.