Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Eng. James Fransis Mbatia (4 total)

MHE. JOSEPH R. SELASINI (K.n.y. MHE. JAMES F. MBATIA) aliuliza:-
LEKIDIA imeweza kushirikiana na wananchi wa Kata ya Kirua Vunjo Mashariki na kufanikiwa kukarabati barabara za kata hiyo zenye urefu wa kilometa 17 kwa gharama ya shilingi milioni nane, lengo kuu ni ujenzi wa barabara inayoanzia Uchira hadi Kolaria yenye urefu wa takribani kilometa 12 kwa kiwango cha lami; na LEKIDIA wamefanikiwa kufanya harambee na kupata shilingi milioni 130 ambapo shilingi milioni 60 zimetumika kununua mapipa 300 ya lami na kubakiwa na shilingi milioni 70.
Je, Serikali itashirikianaje na LEKIDIA kutekeleza mradi huo kwa ajili ya maendeleo endelevu ya wananchi wa Kata ya Kirua Vunjo Mashariki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa James Francis Mbatia, Mbunge wa Vunjo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Uchira -Kisomachi - Kolaria yenye urefu wa kilometa 12 ilijengwa kwa kiwango cha changarawe kwa gharama ya shilingi milioni 300 kutoka katika Mfuko wa Barabara katika mwaka wa fedha 2013/2014. Barabara hiyo imeendelea kufanyiwa matengenezo ambapo katika mwaka wa fedha 2016/2017 zilitumika shilingi milioni 74.2 ili kuifanya ipitike wakati wote. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imepanga kutumia shilingi milioni 31 kwa ajili ya matengenezo ya kawaida kilometa nane na matengenezo ya sehemu korofi kilometa mbili.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapongeza juhudi kubwa inayofanywa na LEKIDIA. Serikali kupitia Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) itafanya tathmini ya barabara zote nchini pamoja na barabara ya Uchira hadi Kolaria ili kuona namna bora ya kuziboresha barabara hizo kwa kiwango kinachohitajika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kushirikiana na wananchi na wadau wengine wa barabara ili kuhakikisha barabara hiyo inafanyiwa matengenezo kurahisisha usafiri na usafirishaji.
MHE. JAMES F. MBATIA aliuliza:-
Sheria ya Maslahi na Mafao ya Majaji Namba tatu (3) ya Mwaka 2007 Kifungu cha 8; inafafanua kuwa Jaji Mkuu, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji Kiongozi au Jaji wa Mahakama Kuu akifariki dunia akiwa madarakani au baada ya kustaafu, Serikali itagharamia gharama za mazishi na Kifungu cha 10 cha Sheria hiyo kinafafanua malipo ya pensheni na huduma nyingine atakazostahili Jaji wakati wa kustaafu kama ilivyo kwenye Kifungu cha 20 na 21 cha Sheria ya Utumishi wa Umma:-
Je, Serikali haioni busara kuifanyia marekebisho sheria hiyo au vinginevyo ili Majaji waweze kupatiwa huduma muhimu na hasa matibabu wakati wanapostaafu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa James Francis Mbatia, Mbunge wa Vunjo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Malipo ya Mshahara na Mafao ya Hitimisho la Kazi kwa Majaji (The Judges Renumeration and Terminal Benefits Act) na Namba tatu (3) ya Mwaka 2007 katika Kifungu cha 10 na Vifungu vya 20 na 21 vya Sheria ya Mafao Katika Utumishi wa Umma (The Public Service Retirement Benefits Act) Sura ya 371 zinaweka utaratibu wa mafao na stahili za Majaji baada ya kustaafu.
Mheshimiwa Naibu Spika, masharti ya kazi na stahili za Majaji, kwa maana ya Jaji Mkuu, Majaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji Kiongozi na Majaji wa Mahakama Kuu yamefafanua kuwa, Majaji hao wamejumuishwa katika utaratibu wa matibabu kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya afya wawapo kazini na gharama hizo hulipwa na Serikali na hata wanapostaafu wanaendelea kupata huduma hizo kupitia Mfuko huo. Kwa wale waliostaafu kabla ya masharti hayo kuanza kutumika hawanufaiki na Mfuko huo.
MHE. JOSEPH R. SELASINI (K.n.y. MHE. JAMES F. MBATIA) aliuliza:-
(a) Je, kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita Mlima Kilimanjaro umeliingizia Taifa mapato ya fedha kiasi gani kwa njia ya utalii?
(b) Je, ni asilimia ngapi ya mapato hayo yametumika kuweka miundombinu endelevu ya kuuhifadhi Mlima huo?
(c) Je, ni asilimia ngapi ya mapato hayo yametumika katika dhana nzima ya ujirani mwema katika kutoa huduma zinazokuza utu wa wananchi wanaozungukwa na Mlima huo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa James Francis Mbatia, Mbunge wa Vunjo, lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Hifadhi Taifa Tanzania (TANAPA) ni Shirika la Umma ambalo limeanzishwa kwa Sheria Na. 482 ya mwaka 1959 na kufanyiwa marejeo na kuwa Sheria Na. 282 ya mwaka 2002. Shirika linatekeleza majukumu yake ya uhifadhi na kuendeleza utalii katika Hifadhi za Taifa 16.
Kati ya Hifadhi hizo ni hifadhi tano tu ndizo zinazokusanya mapato ya ziada yanayotumika kuendesha Hifadhi za Taifa nyingine 11. Hifadhi hizo ni Serengeti, Mlima Kilimanjaro, Tarangire, Ziwa Manyara na Arusha. Mapato yaliyotokana na Mlima Kilimanjaro na fedha zilizotumika kuweka maendeleo endelevu ya kuhifadhi mlima na kiasi kilichotumika katika dhana ya ujirani mwema kwa wananchi wanaozunguka mlima huo ni kama ifuatavyo:-
(a) Mapato ya Hifadhi ya Kilimanjaro katika kipindi cha miaka kumi, yaani kuanzia mwaka 2007/2008 hadi mwaka 2016/2017 ilikuwa ni shilingi bilioni 471.5.
(b) Fedha zilizotumika kutekeleza majukumu ya uhifadhi ikiwa ni pamoja na kuweka miundombinu ya kuendeleza mlima ni shillingi bilioni 67.5 ambazo kati ya hizo shilingi bilioni 20.89 zilitumika kwa maendeleo na shilingi bilioni
46.6 zilitumika katika uendeshaji wa hifadhi.
(c) Fedha zilizotumika katika kuendeleza miradi ya kijamii katika vijiji vilivyo jirani na Hifadhi ya Kilimanjaro ni shilingi bilioni 2.28.
MHE. JAMES F. MBATIA aliuliza:-
Serikali imekuwa ikitoa huduma ya afya nchini kwa ubia na Mashirika ya Dini na/au Taasisi Zisizo za Kiserikali:-
(a) Je, ni kwa asilimia ngapi ya ubia huo kwa kila upande kati ya Serikali na Mashirika ya Dini au Serikali na Taasisi nyingine Zisizo na Kiserikali?
(b) Kwa kipindi cha miaka 20 iliyopita ubia huu umepata mafanikio kiasi gani na kwa kutumia vigezo gani kwa Hospitali ya Kilema?
(c) Kwa kipindi hicho tajwa hapo juu, je, ubia huo umepatwa na changamoto kiasi gani kwa kutumia vigezo gani kwa Hospitali ya Kilema?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa James Francis Mbatia, Mbunge wa Vunjo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Tanzania inatambua mchango wa sekta binafsi katika utoaji wa huduma za afya hapa nchini. Aidha, Serikali kwa kutambua mchango wa sekta binafsi ilitunga Sera ya Ubia kati za Sekta ya Umma na Binafsi, (Public Private Partnership, 2009) pamoja na Sheria Na.103 ya mwaka 2010 iliyorejewa mwaka 2014 na kanuni zake za mwaka 2011 ambazo zimerejewa mwaka 2015.
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi Machi 2018, jumla ya vituo vya kutolea huduma vilivyopo ni 7,215 (vya umma vikiwa ni 5,361 sawa na asilimia 74 na sekta binafsi ni 1,854 sawa na asilimia 26). Aidha, kati ya vituo binafsi 1,854, vituo 900 sawa na asilimia 13 vinamilikiwa na Mashirika ya Dini. Kati ya vituo hivyo vinavyomilikiwa na Mashirika ya Dini ambavyo vimesaini makubaliano ya kutoa huduma za afya baina ya Serikali na Mashirika ya Dini ni 130 sawa na asilimia 1.8 ambapo hospitali ni 85, vituo vya afya na zahanati ni 45.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inadhihirisha kwamba sekta binafsi ina mchango mkubwa katika utoaji wa huduma za afya hapa nchini. Aidha, takribani asilimia 40 mpaka 70 ya gharama za uendeshaji wa Hospitali za Mashirika ya Dini zinatoka Serikalini kwa ajili ya mishahara ya watumishi, dawa, vifaatiba pamoja na gharama nyingine za uendeshaji wa hospitali hizi.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Kilema ilianza kutumika kama Hospitali Teule ya Halmashauri ya Moshi Vijijini mwaka 1984. Katika kipindi hiki kuna mafanikio mengi yaliyopatikana ikiwa ni pamoja na:-
(i) Kusogeza huduma za afya karibu zaidi na wananchi;
(ii) Kuongeza idadi ya vifaatiba ambavyo vimeboresha utoaji wa huduma;
(iii) Hospitali hii ina jumla ya watumishi 156 walioajiriwa na Serikali ambao wanafanya kazi katika hospitali hii;
(iv) Watoa huduma hususani Madaktari wameongezeka hadi kufikia watumishi tisa; na
(v) Wanapata mgao wa madawa kutoka MSD.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi hiki chote ambapo Hospitali ya Kilema imekuwa ikitumika kama Hospitali Teule imekuwa ikipata changamoto ambazo zimekuwa zikitatuliwa kwa pamoja kati ya Serikali na mmiliki ambaye ni Jimbo la Moshi la Kanisa Katoliki. Baadhi ya changamoto hizo pamoja na kufanyiwa kazi kwa kushirikiana ni ufinyu wa bajeti; upungufu wa watalaam pamoja na uwekezaji katika hospitali hiyo.