Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. David Mathayo David (6 total)

MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda sana kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri sana, lakini naipongeza Wizara hii kwa kuwa makini katika kufanya kazi katika sekta hii ya nishati na madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijauliza maswali
mawili ya nyongeza ningependa kuwapa pole wananchi wa Jimbo la Same Magharibi, hususan kata ya Hedaru ambao wamepoteza nyumba nyingi pamoja na mifugo na mazao kutokana na mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia juzi.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu Subhuhana Wataallah, aweze kutupa mvua za kiasi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa napenda kuuliza
maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Swali la kwanza, katika Mradi wa REA Awamu ya Pili, mkandarasi ambaye anaitwa SPENCON alishindwa kufanyakazi na kwa hiyo, vijiji vingi pamoja na vitongoji vingi vya Jimbo la Same Magharibi hususan vijiji 48, umeme haujakamilika kutokana na kwamba, mkandarasi huyo alishindwa kazi.
Je, REA Awamu ya Tatu, vijiji hivi ambavyo vilikosa umeme pamoja na vitongoji vyake, Serikali ina mkakati gani katika kuhakikisha kwamba, vitongoji vyote vinapata umeme na vijiji vyangu vyote vya Jimbo la Same Magharibi katika Awamu hii ya Tatu ya REA?
Swali la pili, je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari baada ya Bunge hili la Bajeti kuongozana na mimi kwenda katika Jimbo la Same Magharibi, ili akajionee mwenyewe vijiji na vitongoji ambavyo havina umeme katika Jimbo langu? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, awali ya yote niungane na Mheshimiwa David kuwapa pole wananchi wake kwa tatizo walilopata.
Mheshimiwa Nibu Spika, kulingana na maswali yake mawili ni kweli kabisa katika utekelezaji wa REA Awamu ya Pili, Mikoa miwili ya Kilimanjaro na Singida haikukamilika ipasavyo na ni kweli kabisa mkandarasi SPENCON hakufanya kazi yake vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kutoa taarifa pia ya hatua za Serikali ambazo zilichukuliwa kutokana na kutofanya kazi vizuri kwa mkandarasi huyo.
Hatua ya kwanza tulichukua asilimia 10 ya mkataba wake ambayo ni retention kimkataba kabisa. Hatua ya pili, kazi hiyo sasa atapewa mkandarasi mwingine ili aikamilishe vizuri na wananchi wa Same waendelee kupata umeme. Lakini hatua ya tatu, tunaendelea sasa kuchukua hatua za kisheria, ili Wakandarasi wa namna hiyo sasa wapate fundisho waache kuwakosesha miundombinu wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David kwamba wananchi wa Same, vijiji vyako vyote 48 vitapata umeme. Naelewa viko vijiji vya milimani kwa Mheshimiwa Dkt. David kijiji cha Muhezi, Malaloni kule Malalo pamoja na kwa Hinka, vitapata umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, kadhalika naelewa vile vijiji 48 anavyosema Mheshimiwa, yapo maeneo kama kule Hedaru, yako maeneo kule ambako Mheshimiwa tumesema Chekereni, Mabilioni pamoja na Jificheni Mabilioni, pamoja na kijiji cha Njiro vyote vitapata umeme. Hivyo, ninakuhakikishia kwamba vijiji ambavyo havijapata umeme kwenye REA II, sasa vyote vitapata umeme. Siyo vijiji tu hata vitongoji vyake na taasisi za umma pamoja na maeneo mengine muhimu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala lake la pili la kuongozana naye, kwanza kabisa niko tayari, ninaweza nikasema utakaponikaribisha utakuwa umechelewa,
ukichelewa sana utanikuta kwenye Jimbo lako, kwa hiyo, niko tayari kutembelea kwenye Jimbo lako.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii niulize maswali mawwili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wananchi wangu wa Kata za Kisiwani, Vumari na Mji Mdogo wa Same wamebanwa sana na Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi; na kwa kuwa Mwenyezi Mungu wakati anaumba dunia alimuumba binadamu akamwambia atawale viumbe vyote viishivyo kwenye maji na kwenye nchi kavu; na kwa kuwa wakati wa uhuru tulikuwa na idadi ya watu milioni 10.3 na sasa hivi tuko takribani milioni 50, tulikuwa na ng’ombe milioni nane sasa hivi milioni 28; tulikuwa na mbuzi milioni 4.4 sasa hivi ni milioni 16.6; tulikuwa na kondoo milioni tatu na sasa hivi ni milioni tano, tulikuwa na nguruwe 22,000 sasa hivi ni milioni mbili, astaghfilillah nimetaja nguruwe wakati ni mwezi wa Ramadhani, mnisamehe sana. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza je, Wizara ya Maliasili na Utalii iko tayari kushirikiana na Wizara ya Kilimo, TAMISEMI pamoja Ardhi ili waweze kutathmini eneo na idadi ya watu pamoja na mifugo wanayofuga ili kusudi kama kuna uwezekano maeneo ya hifadhi za misitu pamoja na Hifadhi za Wanyamapori zipunguzwe ili binadamu waweze kupata maeneo ya makazi pamoja na mifugo na kilimo?
Swali la pili, kwa kuwa Botswana, Afrika ya Kusini na Namibia wameweza kuzuia wanyamapori kutoka kwenye mapori kwenda kwa binadamu ama kwenye wanyama wanaofugwa, je, Serikali iko tayari sasa kuandaa mpango rasmi wa kuweka fence ili wanyamapori wasiweze kwenda kwenye makazi ya watu kuwasumbua na kuwaletea madhara ikiwa ni pamoja na vifo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la kwanza Mheshimiwa Mbunge anazungumzia upungufu wa ardhi kwa ajili ya matumizi ya kibinadamu hasa kwa ajili ya faida ya kiuchumi na kijamii, akihusisha na uhaba au upungufu wa rasilimali ardhi kwa ajili ya shughuli hizo zinazotokana na ongezeko la binadamu na wanyama kama ambavyo amewataja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ufupi Serikali inatambua na kwa kweli ni dhamira ya Serikali kuwafanya wananchi waweze kufanya kazi za kuzalisha mali kwa sababu ni kwa kufanya hivyo tu peke yake ndiyo hata madhumuni makubwa kabisa ya Serikali ya kuiondoa nchi kutoka katika uchumi wa chini kwenda uchumi wa kati yatafanikiwa, ni kwa kufanya kazi tu peke yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili wananchi waweze kufanya kazi lazima waweze kuwa na ardhi au wawe na maeneo ya kufanyia kazi. Kabla hatujaanza kusema kwamba maeneo tunayoyatumia hayatoshi ni lazima kwanza tuone maeneo hayao yanatumikaje hivi sasa, kwa hiyo, hapa ndipo ambapo tunazungumzia juu ya suala la mpango wa matumizi bora ya ardhi.
Kuhusu swali lake tutashirikiana vipi na Wizara nne zile alizozitaja ukweli ni kwamba Mheshimiwa Mbunge anafahamu kwamba tayari tunayo Kamati ya Kitaifa ya Wizara alizozitaja ambayo iko kazini inashughulikia suala hilo na baada ya utafiti wa kitaalam, baada ya kujiridhisha kitaalam tutapitia upya sheria na kuona katika kila eneo kama kweli suluhisho pekee la kuweza kuwafanya wananchi kupata eneo la kufanya shughuli za kibinadamu kama suluhisho pekee ni kugawa maeneo ambayo yamehifadhiwa kwa faida ambazo tunazifahamu ziko lukuki, basi Serikali itazingatia mwelekeo huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kutajitokeza ukweli kwamba bado maeneo tuliyonayo tunaweza kuyatumia vizuri zaidi bila kuathiri maeneo yaliyohifadhiwa basi hatutakuwa na haja ya kupunguza maeneo ya hifadhi isipokuwa tutajiimarisha zaidi katika kutumia vizuri zaidi maeneo ambayo hayajahifadhiwa kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili juu ya kuweka fence, kuweka uzio kwa ajili ya kuzuia wanyamapori kwenda kwenye maeneo ambayo ni ya binadamu, kwa ajili ya maeneo ya makazi ya binadamu na maeneo ambayo binadamu wanafanya shughuli za kibinadamu za kiuchumi na kijamii; napenda tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba huko ambako anazungumzia kwamba udhibiti umefanikiwa njia iliyotumika siyo hii tu peke yake ya kuweka fence, njia ya kuweka fence ni njia mojawapo na inatumika tu pale ambapo ni lazima kuweka fence kwa sababu njia hii ni ya gharama kubwa na si rafiki pia kwa mazingira hata kwa wanyama wenyewe na hata kwa binadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoweza kwa sasa hivi ni kwamba Serikali inalichukua suala hili na kwa kweli tumekuwa tukilifanyia kazi muda mrefu kuweza kuona ni namna gani tunaweza kudhibiti kiwango na kasi ya Wanyamapori kutoka kwenye maeneo yao na kwenda kwenye maeneo ambayo ni ya binadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la msingi hapa vilevile na binadamu na wenyewe tusiendelee na utaratibu ule wa kwenda kukaa kwenye maeneo ambayo aidha ni njia za wanyapori au ni maeneo ya mtawanyiko ya wanyamapori.
MHE. MATHAYO D. MATHAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii kuuliza swali la nyongeza.
Aidha, napenda kumpongeza Naibu Waziri kwa kujibu maswali yake vizuri na kitaalam. Nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, Benki Kuu imepunguza riba ya mabenki ya biashara yanapokopa kutoka kwenye Benki Kuu hadi kufikia asilimia tisa na kwa kuwa pia, imepunguza amana kutoka asilimia kumi hadi asilimia nane ya kiwango cha fedha ambazo mabenki haya ya biashara yanatakiwa yahifadhi Benki Kuu. Je, Benki Kuu imefuatilia na kuona kwamba, mabenki ya biashara yanatoza riba nzuri au yametoa punguzo zuri la riba kwa wananchi ambao wanakopa kwenye mabenki hayo?
Swali la pili, kwa kuwa katika nchi zinazoendelea asilimia 70 ya fedha zinakuwa mikononi mwa wananchi na asilimia 30 inakuwa kwenye mabenki pamoja na Serikali. Je, Benki Kuu imefanya utafiti na kuona, kwa sababu sasa hivi tukiangalia fedha katika mzunguko kwa wananchi wa kawaida zimepungua sana.
Je, Benki Kuu imefanya utafiti na kujua kwamba, fedha hizi ziko wapi ili waweze kutunga Sera ambazo zitarudisha fedha hizi kwenye mabenki ya biashara pamoja na wananchi ili maisha yaweze kuwa mazuri, lakini wananchi pia washiriki vizuri katika shughuli za kujenga nchi yao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tumeshusha kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi na kwa sasa tunafanya ufuatiliaji kuona kwamba, riba zinazotozwa na benki zetu za biashara pamoja na taasisi za kifedha zinashuka ku-respond katika jitihada hizi ambazo zimefanywa na Serikali kupitia Benki Kuu. Tutakapomaliza ufuatiliaji huu na sasa hivi tuko katika vikao mbalimbali na mabenki haya kuona ni jinsi gani sasa wanaweza kurejesha riba chini ili wananchi wetu waweze kukopa, tutaleta taarifa katika Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili, napenda kumwambia Mheshimiwa Mathayo kuwa ni sahihi kwamba asilimia 30 tu ya pesa ndiyo iko benki, asilimia 70 iko kwa wananchi. Kinachoonekana kwa sasa ni kwamba Serikali tumeimarisha mfumo wetu wa ukusanyaji wa kodi. Yule mfanyabiashara aliyekuwa akifanya biashara bila kulipa kodi akijidanganya ile ni faida yake, sivyo ilivyo kwa sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Waheshimiwa Wabunge mtuunge mkono tuweze kukusanya kodi inavyostahiki na ili Watanzania sasa tuishi katika uchumi ambao Taifa letu na wananchi wanastahili kuishi. Kiuhalisia fedha bado iko ya kutosha katika mikono ya wananchi kama alivyokiri yeye Mheshimwa Mbunge aliyeuliza swali kwamba asilimia sabini ya pesa yetu iko kwa wananchi na uchumi wetu unaendelea vizuri.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuuliza swali la nyongeza na pili nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kutupa majibu ya matumaini. Hata hivyo, napenda kusahihisha kidogo wakati wataalam wamekuja mwaka 2015/2016 nilikuwepo na tuliona maeneo mawili ya malambo kwa ajili ya kujenga malambo na maeneo mawili kwa ajili ya majosho na sehemu moja ya kisima kirefu, lakini jibu la Waziri hapa linazungumzia lambo. Kwa hiyo naomba hiyo irekebishwe kwamba ni miundombinu hiyo niliyoitaja.
Mheshimiwa Spika, sasa naelekea kwenye swali la kwanza, je, ni kiasi gani ambacho kimetengwa kwenye bajeti ya mwaka huu kwa ajili ya miundombinu hiyo ambayo nimeitaja katika Jimbo la Same Magharibi na hususani Kata ya Ruvu?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa millioni 100 zinaweza zikatosha malambo mawili na majosho mawili kama kazi hii itasimamiwa na Wizara, lakini kazi hii kama itasimamiwa na Halmashauri milioni 100 inaweza ikatosha josho moja au lambo moja. Je, Serikali sasa iko tayari kwa sababu yenyewe ndio inatoa hizi fedha isimamie kusudi miundombinu hiyo ikamilike kwa bajeti ya mwaka huu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Spika, kuhusu wa usahihi wa nilichokisema ambapo amesema anarekebisha tutaenda kuangalia kuhusu makubaliano yale, lakini kimsingi hakuna kitu kilichoharibika, tutaenda kutekeleza kadiri tulivyoahidi wakati tulipokwenda Jimboni kwake.
Mheshimiwa Spika, vilevile kuhusiana na ni kiasi gani cha fedha ambacho kimetengwa, nimshauri Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa inakuwa ni vigumu kuwa na takwimu sahihi lakini anaweza akanifuata baadaye nikamweleza na ombi lake la kwamba Wizara yenyewe ndio inasimamia ujenzi ule, vilevile tutalichukua na ukweli wa mambo fedha zinazotolewa mara nyingi na Wizara kwa ajili ya kujenga miundombinu huwa tunahakikisha kwamba tunazisimamia ili ifanye kazi iliyoelekezwa.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii niulize maswali mawwili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wananchi wangu wa Kata za Kisiwani, Vumari na Mji Mdogo wa Same wamebanwa sana na Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi; na kwa kuwa Mwenyezi Mungu wakati anaumba dunia alimuumba binadamu akamwambia atawale viumbe vyote viishivyo kwenye maji na kwenye nchi kavu; na kwa kuwa wakati wa uhuru tulikuwa na idadi ya watu milioni 10.3 na sasa hivi tuko takribani milioni 50, tulikuwa na ng’ombe milioni nane sasa hivi milioni 28; tulikuwa na mbuzi milioni 4.4 sasa hivi ni milioni 16.6; tulikuwa na kondoo milioni tatu na sasa hivi ni milioni tano, tulikuwa na nguruwe 22,000 sasa hivi ni milioni mbili, astaghfilillah nimetaja nguruwe wakati ni mwezi wa Ramadhani, mnisamehe sana. (Kicheko)

MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza je, Wizara ya Maliasili na Utalii iko tayari kushirikiana na Wizara ya Kilimo, TAMISEMI pamoja Ardhi ili waweze kutathmini eneo na idadi ya watu pamoja na mifugo wanayofuga ili kusudi kama kuna uwezekano maeneo ya hifadhi za misitu pamoja na Hifadhi za Wanyamapori zipunguzwe ili binadamu waweze kupata maeneo ya makazi pamoja na mifugo na kilimo?
Swali la pili, kwa kuwa Botswana, Afrika ya Kusini na Namibia wameweza kuzuia wanyamapori kutoka kwenye mapori kwenda kwa binadamu ama kwenye wanyama wanaofugwa, je, Serikali iko tayari sasa kuandaa mpango rasmi wa kuweka fence ili wanyamapori wasiweze kwenda kwenye makazi ya watu kuwasumbua na kuwaletea madhara ikiwa ni pamoja na vifo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la kwanza Mheshimiwa Mbunge anazungumzia upungufu wa ardhi kwa ajili ya matumizi ya kibinadamu hasa kwa ajili ya faida ya kiuchumi na kijamii, akihusisha na uhaba au upungufu wa rasilimali ardhi kwa ajili ya shughuli hizo zinazotokana na ongezeko la binadamu na wanyama kama ambavyo amewataja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ufupi Serikali inatambua na kwa kweli ni dhamira ya Serikali kuwafanya wananchi waweze kufanya kazi za kuzalisha mali kwa sababu ni kwa kufanya hivyo tu peke yake ndiyo hata madhumuni makubwa kabisa ya Serikali ya kuiondoa nchi kutoka katika uchumi wa chini kwenda uchumi wa kati yatafanikiwa, ni kwa kufanya kazi tu peke yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili wananchi waweze kufanya kazi lazima waweze kuwa na ardhi au wawe na maeneo ya kufanyia kazi. Kabla hatujaanza kusema kwamba maeneo tunayoyatumia hayatoshi ni lazima kwanza tuone maeneo hayao yanatumikaje hivi sasa, kwa hiyo, hapa ndipo ambapo tunazungumzia juu ya suala la mpango wa matumizi bora ya ardhi.
Kuhusu swali lake tutashirikiana vipi na Wizara nne zile alizozitaja ukweli ni kwamba Mheshimiwa Mbunge anafahamu kwamba tayari tunayo Kamati ya Kitaifa ya Wizara alizozitaja ambayo iko kazini inashughulikia suala hilo na baada ya utafiti wa kitaalam, baada ya kujiridhisha kitaalam tutapitia upya sheria na kuona katika kila eneo kama kweli suluhisho pekee la kuweza kuwafanya wananchi kupata eneo la kufanya shughuli za kibinadamu kama suluhisho pekee ni kugawa maeneo ambayo yamehifadhiwa kwa faida ambazo tunazifahamu ziko lukuki, basi Serikali itazingatia mwelekeo huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kutajitokeza ukweli kwamba bado maeneo tuliyonayo tunaweza kuyatumia vizuri zaidi bila kuathiri maeneo yaliyohifadhiwa basi hatutakuwa na haja ya kupunguza maeneo ya hifadhi isipokuwa tutajiimarisha zaidi katika kutumia vizuri zaidi maeneo ambayo hayajahifadhiwa kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili juu ya kuweka fence, kuweka uzio kwa ajili ya kuzuia wanyamapori kwenda kwenye maeneo ambayo ni ya binadamu, kwa ajili ya maeneo ya makazi ya binadamu na maeneo ambayo binadamu wanafanya shughuli za kibinadamu za kiuchumi na kijamii; napenda tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba huko ambako anazungumzia kwamba udhibiti umefanikiwa njia iliyotumika siyo hii tu peke yake ya kuweka fence, njia ya kuweka fence ni njia mojawapo na inatumika tu pale ambapo ni lazima kuweka fence kwa sababu njia hii ni ya gharama kubwa na si rafiki pia kwa mazingira hata kwa wanyama wenyewe na hata kwa binadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoweza kwa sasa hivi ni kwamba Serikali inalichukua suala hili na kwa kweli tumekuwa tukilifanyia kazi muda mrefu kuweza kuona ni namna gani tunaweza kudhibiti kiwango na kasi ya Wanyamapori kutoka kwenye maeneo yao na kwenda kwenye maeneo ambayo ni ya binadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la msingi hapa vilevile na binadamu na wenyewe tusiendelee na utaratibu ule wa kwenda kukaa kwenye maeneo ambayo aidha ni njia za wanyapori au ni maeneo ya mtawanyiko ya wanyamapori.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuishukuru Serikali kwa majibu mazuri, lakini niwashukuru pia kwamba sasa wataanza kuchimba kisima kirefu kwa ajili ya wafugaji wa Ruvu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi hii ya Serikali ni ya mwaka 2012/2013 na mwaka 2015 wataalamu walikuja Kata ya Ruvu na kubainisha maeneo ya majosho na malambo pamoja na visima virefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa imeshakuwa ni muda mrefu na wafugaji wale wa Kata ya Ruvu wanahangaika sana kuhamisha mifugo huku na kule. Je, Serikali haioni kwamba kwa sasa na hasa kwenye bajeti hii inayokuja ya mwaka 2020/2021 wakatenga fedha za kutosha ili waweze kukamilisha ahadi yao ambayo ilishakubalika mwaka 2012/2013 ili wananchi hao wa Ruvu waweze kupata hii huduma ya malambo na majosho?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kutembelea Wilaya ya Same na kuona maeneo ambayo yanahitaji miundombinu ya mifugo kusudi wafugaji wale waweze kupata miundombinu hiyo na mifugo iweze kupata huduma hiyo kama inavyotakiwa?
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa David Mathayo ambaye ni Waziri Mstaafu wa Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi, na kwamba nijibu maswali yake mawili kama alivyouliza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niko tayari kufanya ziara jimboni kwake mara tu baada ya Bunge hili kumalizika na kwenda kukutana na wafugaji wa maeneo hayo na kukagua miundombinu yao na kutafuta namna ya kuiboresha ili waweze kupata sehemu nzuri ya kunyweshea mifugo yao lakini pamoja na kuogeshea mifugo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili nakubaliana na yeye kwamba katika bajeti hii inayoanza tutaingiza mradi wa lambo katika jimbo lake; ambao umekuwa wa muda mrefu sana kama alivyoeleza mwenyewe, tangu yeye mwenyewe akiwa Waziri na mpaka leo hii ahadi hiyo haijatekelezwa. Sasa safari hii tutaitekeleza kwa kuweka bajeti kwenye mpango wetu wa Serikali ambao tutauanza hivi karibuni.