Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Dr. David Mathayo David (10 total)

MHE. SHALLY J. RAYMOND (K. n. y MHE. DKT. DAVID M. DAVID) aliuliza:-
Je, mradi wa maji tambarare ya Mwanga na Same hadi Korogwe umefikia hatua gani na wananchi wategemee utakamilika lini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Same, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatekeleza mradi mkubwa wa kupeleka maji katika Miji ya Mwanga na Same pamoja na Vijiji vya Wilaya ya Mwanga, Same na Korogwe vilivyopo kandokando ya bomba kuu. Mradi huu utakapokamilika unatarajia kuhudumia watu 456,931. Ujenzi wa mradi huo umegawanywa katika awamu mbili. Awamu ya kwanza inahusisha ujenzi wa chanzo cha maji, mitambo ya kusafisha maji na miundombinu ya kusafirisha na kusambaza maji katika miji ya Mwanga na Same. Awamu ya pili inahusisha ujenzi wa miundombinu ya kupeleka maji katika vijiji 38 vilivyo kandokando ya bomba kuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu ya kwanza imepangwa katika loti tatu. Utekelezaji wa loti ya kwanza unahusisha ujenzi wa chanzo cha maji katika Bwawa la Nyumba ya Mungu, ujenzi wa mtambo wa kusafisha maji na kulaza bomba la urefu wa kilomita 12.8 kutoka kwenye chanzo hadi kwenye matanki ya kituo cha kusukuma maji Kisangara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, loti ya pili inahusu ujenzi wa miundombinu ya kupeleka maji katika Mji wa Mwanga ambao upo katika hatua ya manunuzi. Tayari zabuni zimetangazwa ili kumpata mkandarasi mwenye sifa. Aidha, fungu la tatu la ujenzi wa miundombinu ya kupeleka maji katika Mji wa Same utekelezaji wake unaendelea na mkandarasi yupo katika hatua ya maandalizi ya ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa mradi wa Same - Mwanga - Korogwe awamu ya kwanza unatarajiwa kukamilika Disemba, 2019. Ujenzi wa awamu ya pili ambayo inahusisha kupeleka maji katika vijiji vilivyo kandokando ya bomba kuu haujaanza kutokana na ukosefu wa fedha. Serikali inaendelea kutafuta fedha za utekelezaji wa awamu hiyo.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID aliuliza:-
Vijiji 48 vya Jimbo la Same Magharibi vyenye zaidi ya kaya 2,943 havijapatiwa umeme wa REA japokuwa vina mahitaji makubwa ya umeme.
Je, ni ipi ratiba ya kuwasambazia umeme wananchi hawa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa mradi kabambe wa usambazaji umeme vijijini awamu ya tatu umeanza nchi nzima tangu Machi, 2017. Mradi huu unajumuisha vipengele vya miradi vitatu vya Densification, Grid Extension pamoja na Off Grid Renewable.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi zitakazofanyika ni kuongeza wigo wa usambazaji umeme katika vijiji, vitongoji vyote, taasisi za umma na maeneo ya pembezoni ambayo hayajafikiwa na miundombinu ya umeme, ikiwa ni pamoja na visiwa.
Mradi wa REA Awamu ya Tatu utakamilika mwaka 2020/2021. Vijiji vya Jimbo la Same Magharibi vitapatiwa umeme kupitia mradi huu wa REA Awamu ya Tatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya kupeleka umeme katika vijiji hivyo itahusisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 67.81. Ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa 261, ufungaji wa transfoma 43 pamoja na kuwaunganishia umeme wateja 2,457.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi hii itagharimu shilingi bilioni 10.8.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID aliuliza:-
Mkomazi Game Reserve (sasa Hifadhi ya Taifa Mkomazi) ilianzishwa kabla ya Uhuru wakati tukiwa na idadi ndogo ya watu na mifugo.
Je, Serikali haioni kwamba sasa ni wakati muafaka wa kusogeza mipaka ya Hifadhi ya Taifa Mkomazi ili wananchi wa Kata za Visiwani, Mji Mdogo wa Same na Vumari wapate maeneo ya kuishi, kilimo na ufugaji?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hifadhi ya Taifa Mkomazi imetokana na kupandishwa hadhi kwa Pori la Akiba la Mkomazi – Umba kupitia Tangazo la Serikali Namba 27 la mwaka 2008. Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi ilirithi mipaka ya lililokuwa Pori la Akiba la Mkomazi – Umba mipaka ambayo ilitambulika kisheria kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Namba 275 la mwaka 1974.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi ni sehemu muhimu ya mfumo wa kiikolojia na toshelezi kwa idadi ya wanyamapori waliopo hifadhini kujipatia mahitaji yao ikiwemo malisho, maji na maeneo ya mazalia hivyo kufanya hatua za kupunguzwa kwa eneo kusababisha athari hasi ikiwemo baadhi ya wanyamapori kutoka nje ya hifadhi kwa ajili ya kujitafutia mahitaji yao muhimu na hatimaye kusababaisha kuongezeka kwa migogoro kati ya binadamu na wanyama pori.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009 hairuhusu kufanyika kwa shughuli za kibinadamu ndani ya hifadhi ikiwepo kilimo, ufugaji na uchimbaji madini. Hivyo, kutokana na sababu hizi za msingi za kiuhifadhi, kwa sasa Serikali haioni haja ya kusogeza mipaka ya hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, isipokuwa kwamba Serikali itaendelea kupokea kutoka kwa wananchi na wadau wengine maoni yatakayozingatia matakwa ya sheria na taaluma ya uhifadhi. (Makofi)
MHE. MATHAYO D. MATHAYO aliuliza:-
Je, Serikali ina mikakati gani ya kuongeza ukwasi katika benki na kwa wananchi wa kawaida ili washirikiane na Serikali katika kujenga uchumi wa mtu mmoja mmoja, kaya na taifa kwa ujumla?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mathayo David Mathayo, Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kufikia malengo ya Serikali ya kuimarisha uchumi na kudumisha utulivu wa mfumuko wa bei, Benki Kuu hutekeleza Sera ya Fedha inayolenga kudhibiti ukwasi ili uendane na mahitaji halisi ya uchumi. Kati ya Julai, 2016 na Julai, 2017 kiwango cha ukwasi katika mabenki kwa ujumla wake kiliongezeka kutoka asilimia 35.53 hadi asilimia 38.41 kwa mtiririko huo. Kiwango cha ukwasi wa asilimia 38.41 ni kizuri zaidi katika uchumi ikilinganishwa na kiwango cha chini cha asilimia 20 kinachotakiwa na Benki Kuu ya Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuimarika kwa ukwasi kwa mwaka 2017 kunatokana na hatua mbalimbali za kisera zinazochukuliwa na Benki Kuu. Miongoni mwa hatua hizo ni kutoa mikopo ya muda mfupi kwa mabenki, kununua fedha za kigeni katika soko la jumla la fedha za kigeni (Interbank Foreign Exchange Market) na kushusha riba inayotozwa kwa benki za biashara na Serikali wanapokopa Benki Kuu kutoka asilimia 16 hadi asilimia 12 mwezi Machi, 2017 na kutoka asilimia 12 hadi asilimia tisa mwezi Agosti, 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua nyingine iliyochukuliwa na Benki Kuu ni pamoja na kushusha kiwango cha sehemu ya amana ambayo mabenki yanatakiwa kuhifadhi Benki Kuu kutoka asilimia 10 hadi asilimia Nane (8) kuanzia mwezi Aprili, 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa na Benki Kuu, hali ya ukwasi katika sekta ya fedha, hususan benki ni nzuri na hakuna vihatarishi vya kuleta madhara hasi katika uchumi wetu. Aidha, Benki Kuu itaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha masoko ya fedha kwa lengo la kuhakikisha kwamba, yanaendeshwa kwa ufanisi na ushindani na hivyo kusaidia kuongeza ukwasi miongoni mwa mabenki na taasisi nyingine za kifedha.
MHE. COSATO D. CHUMI (K.n.y. MHE. DKT. DAVID M.
DAVID) aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itapeleka mawasiliano ya simu za mkononi katika kata za Jimbo la Same Magharibi hususani Kata za Msindo, Mshewa, Mhuzi, Vumari, Vuudee, Tae, Suji, Gavao, Saweni na Ruvu Jiungeni?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Vijiji vya Kata za Vumari, Suji na Ruvu Jiungeni vitafikishiwa huduma ya mawasiliano kupitia utekelezaji wa mradi wa Kampuni ya Simu ya Viettel. Utekelezaji wa mradi chini ya Kampuni ya Viettel unapaswa kukamilika mwezi huu wa Novemba, 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Vijiji vya Kata za Mhezi, Msindo, Mshewa, Vuudee, Tae, Gavao na Saweni vinafanyiwa tathmini na Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote na vitaingizwa katika orodha ya miradi ya mfuko itakayotekelezwa kulingana na upatikanaji wa pesa.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID aliuliza:-
Serikali iliahidi katika bajeti ya 2012, 2013 na 2014 kujenga Malambo, Majosho na Kisima kirefu kwa ajili ya wananchi na Wafugaji wa Kata ya Ruvu katika Jimbo la Same Magharibi:- Je, ni lini ahadi hiyo itakamilishwa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshiniwa David Mathayo David, Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia bajeti yake na program mbalimbali imeendelea kukarabati na kujenga miundombinu ya maji ya mifugo kwa kutumia vipaumbele kama maeneo yenye mifugo mingi na yale ambayo yanapokea mifugo wakati wa kiangazi. Kupitia utaratibu huo Wizara imeweza kujenga mabwawa na malambo katika Wilaya za Kiteto, Kilindi na Ngorongoro. Aidha, katika bajeti ya mwaka 2013/2014, Wizara ilitenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa malambo katika Wilaya ya Same na Wilaya nyingine.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, Wizara haikupatiwa fedha kwa ajili ya kufanya kazi hiyo. Mwaka 2015/2016, wataalam wa Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Same waliainisha eneo la Kijiji cha Ruvu, Kata ya Ruvu kwa ajili ya ujenzi wa lambo. Mwaka 2017/2018, Wizara imetenga fedha kwenye bajeti yake kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maji kwenye baadhi ya Wilaya ikiwemo Wilaya ya Same.
Mheshimiwa Spika, naendelea kuzishauri Mamlaka za Serikali za Mitaa kuendelea kutenga fedha kupitia bajeti zao kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maji ya mifugo kama malambo, mabwawa na visima virefu ili kupunguza kero ya upatikanaji wa maji kwa mifugo hasa wakati wa kiangazi. Aidha, Wizara itaendelea kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa kujenga na kukarabati miundombinu ya maji ya mifugo kutegemeana na upatikanaji wa fedha.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID aliuliza:-
Mkomazi Game Reserve (sasa Hifadhi ya Taifa Mkomazi) ilianzishwa kabla ya Uhuru wakati tukiwa na idadi ndogo ya watu na mifugo.
Je, Serikali haioni kwamba sasa ni wakati muafaka wa kusogeza mipaka ya Hifadhi ya Taifa Mkomazi ili wananchi wa Kata za Visiwani, Mji Mdogo wa Same na Vumari wapate maeneo ya kuishi, kilimo na ufugaji?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hifadhi ya Taifa Mkomazi imetokana na kupandishwa hadhi kwa Pori la Akiba la Mkomazi – Umba kupitia Tangazo la Serikali Namba 27 la mwaka 2008. Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi ilirithi mipaka ya lililokuwa Pori la Akiba la Mkomazi – Umba mipaka ambayo ilitambulika kisheria kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Namba 275 la mwaka 1974.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi ni sehemu muhimu ya mfumo wa kiikolojia na toshelezi kwa idadi ya wanyamapori waliopo hifadhini kujipatia mahitaji yao ikiwemo malisho, maji na maeneo ya mazalia hivyo kufanya hatua za kupunguzwa kwa eneo kusababisha athari hasi ikiwemo baadhi ya wanyamapori kutoka nje ya hifadhi kwa ajili ya kujitafutia mahitaji yao muhimu na hatimaye kusababaisha kuongezeka kwa migogoro kati ya binadamu na wanyama pori.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009 hairuhusu kufanyika kwa shughuli za kibinadamu ndani ya hifadhi ikiwepo kilimo, ufugaji na uchimbaji madini. Hivyo, kutokana na sababu hizi za msingi za kiuhifadhi, kwa sasa Serikali haioni haja ya kusogeza mipaka ya hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, isipokuwa kwamba Serikali itaendelea kupokea kutoka kwa wananchi na wadau wengine maoni yatakayozingatia matakwa ya sheria na taaluma ya uhifadhi. (Makofi)
MHE. VENANCE M. MWAMOTO (K.n.y. MHE. DKT. DAVID M. DAVID) aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itapeleka waganga, watumishi wa afya pamoja na vitendea kazi katika zahanati za Same Magharibi zilizojengwa kwa ushirikiano wa wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt.David Mathayo, Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua tatizo la upungufu wa watumishi wa sekta ya afya katika Jimbo la Same Magharibi, ambapo mahitaji ni watumishi 867 lakini waliopo ni 287, upungufu ni watumishi 585.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imepeleka watumishi wapya 10 wa sekta ya afya katika jimbo hilo. Katika mwaka wa fedha 2018/2019, Halmashauri ya Wilaya ya Same imeomba kibali cha kuajiri watumishi wapya 104 wa sekta ya afya ambao watapangwa katika vituo vyenye upungufu mkubwa wa watumishi.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID aliuliza:-

Serikali iliahidi katika Bajeti ya mwaka 2012/2013 kujenga malambo, majosho na kisima kirefu kwa ajili ya Wananchi wafugaji wa Kata ya Ruvu Jimbo la Same Magharibi?

Je, ni lini ahadi hiyo itakamilishwa?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mhe. Dkt. David Mathayo Mbunge wa Jimbo la Same Magharibi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia bajeti yake pamoja na program mbalimbali imeendelea kukarabati na kujenga miundombinu ya maji ya mifugo katika maeneo mengi ya ufugaji hapa nchini ili kupunguza tatizo la maji hasa wakati wa kiangazi kikali. Katika Mwaka huu wa Fedha 2019/2020 Wizara imetenga fedha Jumla ya shilingi 700,000,000 kwa ajili ya kujenga visima kumi na kukarabati mabwawa kumi katika mikoa kumi Tanzania Bara. Katika utekelezaji wa mpango huo, kisima kimoja kinatarajiwa kuchimbwa katika Wilaya ya Same, hususan Kata ya Ruvu ili wafugaji waweze kupata maji kwa ajili ya mifugo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka huu wa fedha 2019/2020 Wizara imetenga fedha kwa ajili ya kukarabati majosho 161 nchi nzima ili kudhibiti magonjwa yaenezwayo na kupe, mbung‟o na wadudu wengine. Mpaka sasa, majosho 46 yamekamilika, majosho 95 ukarabati unaendelea na majosho 20 ukarabati bado haujaanza. Aidha Wizara imejenga josho moja la kisasa Wilayani Bariadi. Pia Halmashauri mbalimbali zinakarabati majosho 288 na zinajenga majosho mapya 84. Kwa Halmashauri ya Same josho moja linakarabatiwa na Wizara katika Kata ya Ruvu-Muungano na matatu yanakaribatiwa na Halmashauri yaliyopo kwenye vijiji vya Mwembe, Bangalala na Mkonga. Mikakati ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya mifugo inaendelea kadri fedha zinapopatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Napenda kuchukua fursa hii kutoa rai kwa halmashauri zote hapa nchini ikiwemo Halmashauri ya Same kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya kujenga, kukarabati na kuendeleza miundombinu ya mifugo katika maeneo yao kwa kutumia fedha zinazopatikana kutokana na makusanyo ama tozo za mifugo.
MHE. ANNE K. MALECELA (K.n.y. MHE. DAVID M. DAVID) aliuliza:-

Je, ni lini Serikali kwa kushirikiana na Mashirika ya Simu itawapelekea huduma ya simu wananchi wa Kata za Msindo Mshewa, Mhezi, Vumari, Vudee, Tae, Suji, Gavao, Saweni na Ruvu Jiungeni?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano Kwa wote imetoa ruzuku kwa ajili ya ujenzi wa minara ya mawasiliano katika Wilaya ya Same ambapo wakazi zaidi ya 13,531 wamefikiwa na huduma za mawasiliano katika Kata za Bombo, Maore, Mshewa, na Ruvu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa wote imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kufikisha huduma za mawasiliano nchi nzima. Kwa upande wa Same Magharibi, Serikali iliviainisha Vijiji vya Kata za Vumari, Suji na Ruvu Jiungeni ili kuangalia mahitaji halisi ya mawasiliano na hatimaye vimeingizwa katika orodha ya vijiji vya zabuni ya Awamu ya Nne. Zabuni hiyo ilitangazwa tarehe 18 Julai, 2019 ambapo mwisho wa kurudisha vitabu vya zabuni hiyo ni tarehe 3 Oktoba, 2019, ikifuatiwa na tathmini ya zabuni husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Mshewa imefikishiwa huduma za mawasiliano ambapo minara miwili (2) ya tigo imejengwa na kuihudumia kata hii. Pamoja na jitihada hizi na uwepo wa minara hii baadhi ya maeneo ya kata hii yanaonekana kuwa na changamoto za mawasiliano. Kata hii itafanyiwa tathmini zaidi ili kubaini maeneo mahususi ambayo bado yana changamoto ya mawasiliano ili yafanyiwe kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasialiano kwa wote (UCSAF) imevipokea vijiji vya kata za Msindo, Mhezi, Vudee Tae, Gavao na Saweni na itavifanyia tathmini kuangalia mahitaji halisi ya mawasialiano na kasha kuviingiza katika orodha ya vijiji vya zabuni zitatazotekelezwa kulingana na upatikanaji wa fedha hususani katika mwaka wa fedha 2019/2020.