Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Questions to the Prime Minister from Hon. Dr. David Mathayo David (1 total)

MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu swali.

Mheshimiwa Waziri Mkuu, kutokana na sera nzuri za Chama Cha Mapinduzi katika elimu, hususan elimu bila malipo na kutokana na kuongezeka kwa shule za sekondari za kata, enrollment ya wanafunzi imekuwa ni kubwa sana; na hii imesababisha kuonekana kwamba kuna upungufu mkubwa sana wa idadi ya Walimu katika halmashauri zetu. Wakati huohuo wapo zaidi ya Walimu 6,000 ambao ama wanastaafu au wengine wachache kufariki dunia, lakini Utumishi inachelewa kutoa vibali vya kuwaajiri Walimu wale:-

Je, Serikali ina mikakati gani ya kuhakikisha kwamba kasi ya ongezeko la wanafunzi inakwenda na uwiano sawa na kasi ya ongezeko la walimu? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Mathayo David, Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba tumeanza kuona faida ya maazimio na maamuzi ya Rais wetu, Dkt. John Pombe Magufuli ya elimu ya msingi ambayo inaanza kuanzia chekechea mpaka kidato cha nne kwenda kusoma bila malipo yoyote na kuwa na ongezeko kubwa la vijana ambao sasa wanakwenda kusajiliwa darasa la kwanza, lakini pia hata kidato cha kwanza kwenda cha nne.

Mheshimiwa Spika, manufaa haya yanatokana na utaratibu wa awali ambao ulikuwa umezalisha michango mingi sana kwenye shule na kukwaza Watanzania kupeleka watoto wao shuleni. Sasa baada ya kuanzisha elimu bure tumeona pia hata wale watoto wanaotoka kwenye familia zisizokuwa na uwezo wanakwenda sasa shule kupata elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali imeamua kutoka elimu ya msingi mpaka sekondari yote hii tunaita elimu msingi ambayo mtoto ni lazima asome na amalize kidato cha nne na akipata ufaulu anaendelea kidato cha tano kwenye elimu ya juu ya sekondari. Hili pia limefanya kuwe na hitaji la ongezeko la walimu, miundombinu nayo lazima iongezwe na Serikali kote huko inafanya jitihada za kuongeza miundombinu kwa kuhakikisha kwamba kila tunaposajili wanafunzi darasa la kwanza wote waingie madarasani na wakae kwenye madawati.

Mheshimiwa Spika, wanapomaliza darasa la saba wanafaulu kuingia kidato cha kwanza tunahakikisha kwamba tunakuwa na miundombinu ya kutosha ili kidato cha kwanza wanapoanza shule waanze wakiwa darasani na kuendelea mpaka elimu ya kidato cha nne.

Mheshimiwa Spika, wote mnatambua tulitoa maagizo kwa wakurugenzi kuhakikisha kwamba wanafunzi wote waliofaulu mwaka huu wote waingie darasani na waanze kusoma. Ifikapo tarehe 28, Mwezi huu wa Februari, kila halmashauri ihakikishe imeshakamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa, vyoo na nyumba za Walimu ili wanafunzi wanapoingia waweze kuanza masomo yao.

Mheshimiwa Spika, sasa ongezeko hili pia linataka mahitaji ya ongezeko la Walimu na Serikali inaendelea kuwaajiri. Hapa juzi kulikuwa na ajira za Walimu 13,000. Awamu ya kwanza tumepeleka Walimu 8,000, wiki mbili zilizopita tumeshasambaza Walimu 5,000 na bado tunaangalia tunapata ripoti za upungufu wa Walimu kwenye maeneo gani. Bado vibali vya ajira vitatoka na tutaendelea kuajiri kadri tunavyokuwa na uwezo wa kuajiri lakini na mahitaji pia ya elimu. Lengo ni Walimu hawa wawe na vipindi vichache, wawe na urahisi wa maandalizi ya masomo yao na waweze kufundisha na kusimamia vizuri ili kumsaidia mtoto kupata uelewa wa taaluma anayoipata kila siku mahali pa kazi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali yake bado inaajiri na itaendelea kuajiri kuhakikisha kwamba kila shule inakuwa na Walimu wa kutosha kwa masomo yetu yaliyopo kwenye upande wa shule za msingi na sekondari vilevile. Lengo ni kuhakikisha kwamba, wanafunzi wetu wanapokwenda shuleni wakirudi jioni wawe wameshapata taaluma ya vipindi vyote ambavyo vimepangwa, tena kwa uelewa mpana kwa sababu Mwalimu anakuwa na nafasi nzuri ya kuweza kujiandaa. Huo ndiyo mpango wa Serikali wa kuhakikisha kwamba ajira zinaendelea vizuri. (Makofi)