Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Anthony Calist Komu (21 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia Mapendekezo ya Mpango huu wa Mwaka 2019/2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilivyosoma kuanzia tu ule ukurasa wa kwanza nikaanza kupata wasiwasi baada ya kuona kwamba miradi ya kimkakati kwa kweli imekuja mingine mipya lakini ile ambayo ilikuwepo siku zote tunaizungumza haijaelezwa kwamba ni kwa nini imeondoka na imefikia wapi katika utekelezaji wake? Siku za nyuma tulikuwa na miradi ya kimkakati kama Mradi wa Makaa ya Mawe Mchuchuma na Chuma cha Liganga; Mradi wa Magadi Soda ya Engeruka; Mradi wa Kiwanda cha Matairi (General Tyre) na Kurasini Logistic Centre. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiacha kwamba hatujui ni kwa nini sasa miradi hii haipo tena ukweli na taarifa mbalimbali zinaonyesha kwamba hakuna chochote ambacho kimefanyika katika kuikamilisha hii miradi. Miradi hii imechukua pesa nyingi za walipa kodi na nyingine ni mikopo. Kwa hiyo, tungependa sana kufahamu ni kwa nini hii miradi imeachwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine cha muhimu sana ni kwamba ukiiangalia miradi hii kwa karibu ni miradi ambayo kweli ingetupeleka kwenye maendeleo ya viwanda lakini imeachwa. Sasa ni mapenzi tu ya watu ambao wako kwenye madaraka sasa hivi au ndiyo utaratibu wa kuendesha nchi yetu? Napenda nipate maelezo kuhusiana na jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, tumekuwa tukizungumza karibu muda wote wa Serikali ya Awamu ya Nne hasa mwishoni juu ya uchumi wa gesi. Leo ukiangalia katika mapendekezo haya sioni namna ambayo tunakwenda kutumia hiyo fursa ya uchumi wa gesi. Hili na lenyewe napenda nifahamu ni nini hasa kilichopelekea hali hii? Sababu ninazozisikia ni kwamba eti sisi kama Watanzania hatutanufaika sana kutokana na mikataba ambayo imekuwepo. Napenda kujua, hivi kweli ni sahihi kuchimbia hiyo rasilimali ambayo tumepewa na Mungu na kuwaachia hao au tukazungumze nao na kuona ni namna gani tutafanya? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia fursa ambazo zingepatikana kutokana na uchumi wa gesi, kuna ajira zaidi ya 7,000 kutokana na vile viwanda ambavyo vingeweza kuanzishwa kule kama vya mbolea, cement na vya gesi yenyewe. Yote hayo tumeyakimbia na kwenda kuingia kwenye mambo mengine ambayo kwa kweli mimi siku zote naita ni kucheza kamari kama ule mradi wa ndege. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii vilevile inaacha maswali mengi juu ya Serikali hizi ya CCM. Hivi hakuna mahusiano kati ya Serikali iliyotangulia na hii ya sasa hivi? Au tuamini kwamba hizo Serikali zote zilizopita zilikuwa ni za wapigaji tu na ndiyo zimeifikisha hii nchi sasa inakuwa kama ndiyo inaanza upya? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiachana na hiyo, ukweli ni kwamba tungefuatilia uchumi wa gesi na ile miradi mingine ya kipaumbele, leo tusingekuwa tunakwenda kuingia kwenye mgogoro wa kwenda kwenye Stiegler’s Gauge ambapo tunakwenda kugombana na jamii ya Kimataifa. Vilevile sustainability ya huo mradi unaacha maswali mengi, kwa sababu kuna mambo ya mabadiliko ya tabia nchi, pia kuna uchumi wa utalii ambao tunakwenda kuua bila sababu yoyote ya msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine kwenye hii ni ushirikishaji wa wadau ambao imetamkwa huku, lakini ukienda kuangalia hali halisi sasa hivi ya nchi yetu ni tofauti. Unapozungumza ushirikishaji wa wadau ni pamoja na kushirikiana na jamii ya Kimataifa. Nataka ni-echo hoja aliyotoa hapa Mheshimiwa Mchungaji Msigwa kwamba sisi tumeamua kujitenga na dunia. Kama Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ameamua kutokuhudhuria mikutano yote mikubwa hata ya Umoja wa Mataifa, nafikiri ni lazima sisi kama Bunge tuchukue nafasi yetu, tushauri, tuseme siyo sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama suala ni gharama, ukienda pale UN unakuwa na fursa ya kukutana na viongozi wengine wa dunia kwa kutumia gharama hizo za kukupeleka wewe UN. Sasa kinachotufanya tusiende kwenye Jumuiya ya Madola, tusiende kule Davos ni nini? Hivi sisi kweli tunaweza kuwa kisiwa tukaishi wenyewe tu humu humu ndani kama kuku anaatamia halafu tukaweza kuvuka kweli? Kwa hiyo, naomba sana Bunge lako liangalie jambo hili na kuliwekea utaratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kushirikisha wadau vilevile ni kuangalia haki kwa wadau, is not one way traffic. Siyo suala la kwamba Serikali inaweza ikafanya tu jinsi inavyotaka kwa wadau. Leo wako wafanyabiashara wakubwa kwenye nchi hii ambao wako ndani kwa visingizio mbalimbali. Siungi mkono ufisadi lakini nafikiri kuna haja ya kuchukua hatua za makusudi wale wote ambao wamewekwa ndani kwa sababu mbalimbali, kesi zao au mashauri yao yafanywe kwa haraka ili waweze kurudi kufanya kazi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumweka ndani mtu ambaye ana uchumi mkubwa kwa maana ya uwekezaji katika hii nchi, maana yake ni kufunga vilevile shughuli zake za kiuchumi. Hii vilevile inawatisha wawekezaji wengine kuingia kwenye biashara na Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende kwenye uchumi wa viwanda ambao ni kaulimbiu ya Serikali ya Awamu ya Tano. Taarifa zinaonyesha kwamba sasa hivi tuna viwanda zaidi ya 52,000, maana hivyo viwanda ukivigawa kwa Majimbo tuliyonayo hapa kila mtu angepaswa aone kwake kuna viwanda kama 300 hivi, lakini kule Moshi Vijijini hatuna kiwanda hata kimoja. Hata ukimwuliza ndugu yangu Mheshimiwa Japhary hapa au ndugu yangu Mheshimiwa Selasini hapa, hatuna viwanda 10. Sasa hivyo viwanda vinajengwa wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua kwamba Serikali haijengi viwanda bali inajenga mazingira wezeshi kwa ajili ya viwanda kuwepo. Serikali hii imekuwa ikituambia kwamba itafidia yale maeneo ya EPZ na SEZ, itakuwa inatengeneza mazingira mazuri kwa ku-harmonize zile mamlaka za udhibiti, itakuwa inarejesha yale maeneo na viwanda ambavyo vilibinafsishwa lakini havifanyi vizuri lakini kwenye mambo yote hayo ambayo Serikali inapaswa kufanya ni sifuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Halima amesema hapa na akatoa data sana kwenye hiki kitabu cha Hotuba ya Kambi ya Upinzani, ukienda kwenye ule ukurasa wa 70, anasema tulipaswa na Serikali inasema siku zote, tunaweka nguvu kwenye kilimo na mifugo kwa ajili ya kupata malighafi kwa ajili ya viwanda hivi ambavyo tunavipigia debe. Mheshimiwa Halima ametuambia hapa kwamba kwenye kilimo katika mwaka 2016/2017 tumetekeleza bajeti kwa asilimia 2; mwaka 2017/2018 tumetekeleza bajeti kwa asilimia 11. Ukienda kwenye mifugo, tumetekeleza kwa asilimia sifuri mwaka 2017/2018. Pia hizo bajeti hazitoshi, ni finyu, lakini pamoja na ufinyu wenyewe bado tunakwenda kutoa sifuri halafu tunasema tunajenga uchumi wa viwanda. We are joking! Tunafanya utani na haya mambo na tunawatania Watanzania, hatuwatendei haki. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ANTHONY C. KOMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa naongea kwa mara ya kwanza katika Bunge hili, nichukue fursa hii kumshukuru Mungu na mimi kuwepo hapa. Zaidi niwashukuru wananchi wa Moshi Vijijini kwa maamuzi waliyofanya ambayo yameweza kunifanya nikawa mwakilishi wao, Mungu aendelee kuwaimarisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kabla sijaenda kwenye mchango niweke record sawasawa. Wakati ule tukiwa tunafanya semina hapa, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alisema wakati akijaribu kutuaminisha kwamba yeye ni Mwanasheria wa kila kitu. Mwanasheria Mkuu wa Mihimili yote, alisema yuko mtu mmoja alilishtaki Bunge katika Mahakama ya haki ya Afrika Mashariki na yeye akaenda kulitetea Bunge kule kama Mwanasheria Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ndiye niliyeishtaki lakini sikulishtaki Bunge. Niliishtaki Serikali ya Jamhuri ya Tanzania na nilimshtaki Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Kesi yangu ni reference Na. 7 ambayo ni Anthony Calist Komu versus Attorney General of United Republic of Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kesi hiyo nilishinda, Mwanasheria Mkuu amekata rufaa na nina uhakika nitamshinda tena ili wanilipe vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende kwenye kazi hii ambayo iko mbele yetu. Kama mwenzangu aliyenitangulia alivyosema, kama unataka kukamua ng‟ombe ni lazima umlishe vizuri, vinginevyo utakamua damu. Ukienda kwenye haya Mapendekezo ya Mpango, idadi ya watu na pato la kila mtu. Mapendekezo haya yanasema, nchi hii itakwenda kwenye kipato cha kati, na itakwenda kwenye kipato cha kati kwa sababu hapa wamefanya makadirio. Wanasema kipato cha Mtanzania kinakua na sasa hivi kimefikia dola za Kimarekani 1,043, maana yake Shilingi 1,724,716 kwa mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukifanya hesabu utaona kwamba kila Mtanzania anapaswa awe anapata kipato cha Shilingi 1,043,000 na pesa kidogo. Sasa nauliza, hivi kweli ni Watanzania wangapi wana kipato hicho siku ya leo? Kima cha chini cha mshahara kwenye viwanda vyetu, viwanda vya Wahindi, Wachina ni Sh. 100,000 na hilo huwezi kulichukua kama ni pato ambalo mtu anakwenda nalo nyumbani kwa sababu bado hujatoa gharama za kumuwezesha yeye kwenda kutekeleza wajibu huo unaompa kwa Sh. 100,000. Maana yake ni lazima alipe nauli, ale mchana halafu ndipo sasa apate kitu fulani. Ma-house girls mmewahi kusema chapa Bungeni kwamba wanapaswa kulipwa Shilingi 80,000 kwa mwezi. Ma-bar maid ambao ni wengi sana katika nchi hii. Sasa hizi takwimu zinatu-mislead na hapa ndiko tunakokwenda kukamua ng‟ombe ambaye hatumlishi vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye viwanda vingi, ukienda kwenye mashamba, sisi tuna mashamba yale ambayo yalikuwa nationalized kule Moshi vijijini, watu hawaajiriwi, watu wanakuwa vibarua kwa miaka mitatu, minne, mitano. Akifika ule muda wa kuambiwa aajiriwe anapewa likizo isiyokuwa na malipo au anakuwa terminated halafu anaomba tena akianza anaanza upya tena. Sasa kwa utaratibu huo ni lazima tuangalie sana mipango yetu na hizi takwimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, madeni. Niko hapo hapo kwa Mtanzania. Tukitaka kwenye uchumi huu wa kipato cha kati ni lazima tuwe na sekta binafsi ambayo ina nguvu. Leo haya madeni yanayozungumzwa na bahati mbaya yanayowahusu watu wa ndani, sekta binafsi ambayo ilikuwa inaongozwa na Mheshimiwa sana Rais Magufuli, Rais wetu wa Awamu ya Tano; Wakandarasi wanadai madeni makubwa sana. Sasa, ukiangalia katika Mpango huu wote hakuna mahali ambapo inaonesha kwamba Serikali imejipanga kulipa haya madeni hasa ya watu wa ndani (Wazawa). Sasa hii sekta binafsi ambayo ndiyo yenye mchango mkubwa sana katika huu Mpango, kwa sababu ukisoma huu Mpango utaona kwamba mapato ambayo ni ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona katika ule mwelekeo uliyoletwa hapa au hata ukifanya mapitio ya Mpango wa Kwanza wa Miaka Mitano, utaona kwamba ni wastani wa trilioni 8.9 ndizo ambazo zinapaswa kutumika kila mwaka. Lakini katika hizo trilioni 8.9, 2.9 ndizo ambazo ni mapato yetu ambayo naweza kusema Serikali ina uwezo nayo. Trilioni sita zinapaswa kutoka kwenye Sekta binafsi na washirika wa maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hakuna mkakati wa makusudi, wa kuhakikisha sekta binafsi inalindwa, inalipwa ili kutoa huduma na inalipwa kwa wakati, hatuoni kama tunaanza kuzika huu mpango kabla haujaanza. Kwa hiyo, naishauri sana Serikali iliangalie hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ukienda kwenye Sekta ya Elimu utaona kwamba kuna mambo mazuri yanayozungumzwa, tuna madarasa fulani tunajenga, tuna hiki tunajenga, lakini siamini kama kuna review ya yale ambayo yalikwishafanyika, kwa sababu kungekuwepo na review, toka nimekuwa Mbunge nimetembea karibu Kata zote za Jimbo langu, hakuna Kata hata moja ambayo nimekwenda nikaacha kukuta kuna madarasa ambayo hayafai, yameshakuwa condemned, hakuna vyoo, unakuta shule ina watoto 370 haina choo. Shule ina watoto 188 haina choo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali iwe inafanya na kile kitengo cha ukaguzi kwenye mashule wapo tu, hawana fedha, hawafanyi ukaguzi. Kwa hiyo hakuna ripoti za hali halisi ilivyo kwenye field. Hivyo hivyo kwenye sekta ya maji, hapa wanasema maji ni asilimia kadhaa, lakini ukienda kwenye reality, unakuta kwamba hakuna hayo wanayoyazungumza. Kule kwangu wanasema Kata ya Uru Kusini ina maji, Kata ya Uru Kaskazini ina maji.(Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ANTHONY C. KOMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nami nianze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa masikitiko kwamba kwa kweli ukiitazama hii hotuba yake kuanzia mwanzo mpaka mwisho pale anapokwenda kuomba pesa. Ukijiuliza kwamba ni kitu gani kimoja ambacho kitakuwa kimekamilika baada ya kwisha mwaka huu wa fedha ambao tunauzungumzia, hakuna hata kimoja kitakachokuwa kimekamilika kinachoweza kutupeleka kwenye uchumi wa viwanda na biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge na Serikali kwamba tunapojadili haya mambo, tuwe serious kidogo. Tuangalie kwamba ni wapi tunataka kupeleka nchi hii? Kama ni suala la kujaribu kuwa masters wa kila kitu halafu mwisho wa siku tunajikuta kwamba we are master of none, kwa kweli tutakuwa tunawadanganya wananchi wetu. Hilo ndilo ninaloliona, kwa sababu tunasema kwa mfano tunataka kuwa na viwanda vya kimkakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumza kwa miaka nenda rudi kuhusu Mchuchuma na chuma cha Liganga. Tunasema hivi ni viwanda vya kimkakati, lakini ukienda kuangalia fedha zilizotengwa ni kwa ajili ya kwenda kufidia ili watu wapishe maeneo yale kwa ajili ya ujenzi. Ni kwa ajili ya kukamilisha upembuzi yakinifu; lakini tunasema mwakani miezi mitatu ijayo tutaanza uzalishaji. Huu ni uongo! Haya ni maigizo! Hizi ni nyimbo! Sasa nyimbo za aina ya namna hii ni lazima tuachane nazo tuzungumze vitu ambavyo ni tangible, yaani vitu ambavyo vinashikika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema kwamba hivi ni viwanda vya kimkakati, lakini share zetu sisi kwenye chuma cha Liganga na Mchuchuma tuna share 20. Sasa share 20 nafasi yetu ya ku-influence mambo kwenye hiyo miradi, iko wapi? Kwa hiyo, bado tunakwenda kucheza kwenye mikono ya wabia wetu ambao ndio watakaokuwa na influence. Kwa hiyo, hatuwezi kujidai kwamba hivi ni viwanda vya kimkakati wakati hatuna mkakati wowote wa kuhakikisha vinaanza, hatuna makakati wowote wa kuhakikisha kwamba, tunavimiliki ili tuwe na influence.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana, Waziri atakapokuja hapa atuambie ni mikakati gani ambayo ni tangible (inayoshikika), ambayo ni mahususi ya kutufanya kweli twende kumiliki hayo maeneo ambayo yanaitwa ni ya kimkakati na ni lini haya maeneo kweli kwa maana ya fedha kwa maana ya bajeti yanaweza yakaanza na tukaona hapa kweli tunapiga hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumza kwenda kwenye uchumi wa kati, wakati huo huo tunazungumza habari ya kuwa na private sector yenye nguvu, lakini ukiangalia Serikali yetu ndiyo ambayo inajitahidi kwa nguvu zake zote kuua private sector. Ukienda kwenye deni la Taifa, unakuta tunadaiwa zaidi ya shilingi trilioni 29 sijui, kama sijakosea figures, lakini 1.3 trillion ni madeni ya ndani ambapo ni Wazabuni mbalimbali waliofanya kazi na Serikali, watumishi wa Serikali na Wakandarasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunapokwenda kwenye huu uchumi wa kipato cha kati tunaenda na nani, kama Serikali kazi yake kubwa ni kuhakikisha kwamba hawa wazawa hawanyanyuki? Mwaka 2015 kuna Mhandishi mmoja alijiua kwa sababu kampuni yake ililemewa na madeni ya Ukandarasi, kwa sababu ya Kandarasi mbalimbali alizofanya kwenye Serikali, akajiua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kuwe na affirmative action ya kuhakikisha kwamba tunawanyanyua wazawa. Ukienda kwenye ile sheria ya mwaka 2004 ya kuwezesha wazawa waweze kushiriki kwenye uchumi na yenyewe ina walakini mkubwa. Naona Waziri Muhongo hayuko hapa, lakini mwaka 2015 nafikiri kuna mtu mmoja alitaka kuwekeza kwenye gesi na ni mtu maarufu, Dkt. Regnald Mengi akaambiwa yeye level yake ni uchuuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka Mheshimiwa Waziri leo atuambie, ili uwe mzawa unayeweza kupewa hadhi ya kuwekeza kwenye vitu ambavyo siyo vya uchuuzi, unapaswa uwe na uchumi wa namna gani? Kwa sababu uchumi wa Mengi kwa jinsi tunavyojua, ni uchumi mkubwa. Kama ni fedha anaweza akawanazo nyingi; kama ni mali zisizohamishika ambazo zinaweza kuwekwa dhamana, anazo ambazo watu wanazifahamu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama huyo anaambiwa kwamba ni mchuuzi, akachuuze, kwa vyovyote Watanzania walio wengi watakuwa wamekwazika sana na watakuwa wanaogopa kujitokeza kwa sababu watajipima, hivi mimi na Dkt. Regnald Mengi, naweza kwenda? Inawezekana ndiyo maana Mheshimiwa Waziri hapa kila siku anahamasisha watu wajitokeze, hawajitokezi kwa sababu havijatolewa vigezo vya Watanzania ili washiriki kwenye uwekezaji wanapashwa wawe na nguvu zinazofanana namna gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri na hili naweza nikashika mshahara wako kama hautokuja vizuri. Kwa sababu ni suala la kisera, utuambie ni uwezo wa namna gani unatakiwa ili Watanzania nao waweze kushiriki katika kuwekeza kwenye uchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni laxity ya Serikali ya CCM, yaani uzembe wa Serikali ya CCM na kutokufuatilia mambo kwa Serikali ya CCM. Kwa sababu tumeambiwa hapa viwanda vimekufa, lakini viwanda hivi vimekufa na Mheshimiwa Waziri ametuambia katika taarifa zake mbalimbali kutoka kwenye Kamati kwamba viwanda vingine vilitumika kama dhamana kukopa kwenye mabenki, lakini mikopo hiyo haikwenda kutumika kwa ajili ya kuendeleza viwanda, ilitumika kwenye vitu vingine, Serikali ilikuwa wapi? Serikali ilikuwa wapi wakati mtu anakopa fedha akasema anakwenda kufua kiwanda akaenda akafanya mambo mengine ya kwenda China akaenda kuchukua bidhaa kwa ajili ya uchuuzi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachelea kusema kwamba, kama tabia hii haitabadilika, kama mienendo ya namna hii haitabadilika, bado tutaendelea kupata matatizo kwa sababu hizi benki ambazo tunataka kuanzisha, zitaanzishwa, pesa zitawekwa kule, watakopa tena, kwa laxity hii hii ya Serikali za CCM, mambo yatakuwa yale yale, business as usual. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana tuangalie ni namna gani. Limezungumzwa suala la kulinda viwanda vya ndani, well and good, lakini unavyozungumza suala la kulinda viwanda vya ndani, usiangalie tu uagizaji wa bidhaa kutoka nje; jiulize vile vile ni kwa nini bidhaa za nje zinakuwa bei rahisi? Zinakuwa bei rahisi kwa sababu mazingira yetu ambayo kimsingi ni jukumu la Serikali kuyafanya yawe yanayofanya viwanda vya kwetu vizalishe bidhaa zinazoweza kushindana kibei, ni magumu. Watu wamechangia hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Meshimiwa Peter Surukamba asubuhi alizungumza akaorodhesha…
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naomba nichangie. Kwanza nawashukuru sana na nawapongeza sana Kamati kwa kazi nzuri ambayo wamefanya kwa sababu, kwa kweli, wamezungumza kitu kile ambacho kinapaswa kuzungumzwa.
Mheshimwa Mwenyekiti, watu wengi wameshazungumza kuhusiana na deni la Taifa. Naomba niweke mstari tu kwamba sisi kama Bunge tusiposimama kwenye nafasi yetu na kuiambia Serikali kinachopaswa kufanyika, tunaweza tukajikuta tuko kwenye hatari kubwa na tukawa mufilisi; tukawa hatuwezi kukopesheka na tukawa vile vile hatuwezi kuhudumia Watanzania ambao tunapaswa kuwahudumia. Hii ni kwa sababu ukiangalia kwenye maandiko ya Kamati inaonesha kwamba deni linakua kwa asilimia 18. Hili ni jambo la hatari.
Mheshimwa Mwenyekiti, wakati deni hili linakua, kuna mambo ambayo yanafanywa na Serikali ambayo yangeweza kufanywa kwa namna nyingine ambayo ingeweza ikawa na tija zaidi kwa Serikali. Kwa mfano, tumenunua ndege kwa pesa taslimu; ule ni mradi wa kibiashara ambao ungeweza ukaachwa ukakopa wenyewe, ukajiendesha wenyewe, uka-service hiyo riba wenyewe; lakini tumeenda kununua cash.
Mheshimwa Mwenyekiti, lakini wakati huo huo tunakopa, tena tunakopa ndani kwa kiwango ambacho ni kinyume hata na kiwango kilichoidhinishwa na Bunge hili. Maana yake ukiangalia huku, tumekopa tukazidisha asilimia 32. Naomba sana Bunge hili lisimame mahali pake liiambie Serikali iache tabia za aina hiyo, kwa sababu inakwenda kutuingiza kwenye hatari ambayo itakuja kuwa tatizo kubwa sana. (Makofi)
Mheshimwa Mwenyekiti, kutokupeleka fedha kwa wakati kwa miradi mbalimbali, hili ni jambo lingine ambalo linaonekana kama ni rahisi tu; lakini ukweli ni kwamba usipopeleka fedha kwenye mradi kwa kadri ilivyoelekezwa, maana yake unalipa watumishi wengi bila kazi yoyote. Unakuta watu wapo kwenye Serikali, mashirika mbalimbali na Halmashauri, hawana kazi ya kufanya, lakini mwisho wa mwezi lazima walipwe mishahara. Sasa tukiendelea na tabia hii, tunakwenda kwenye jambo ambalo ni tatizo kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kwenye kuchelewa kupeleka fedha au kushindwa kupeleka fedha maana yake ni nini? Miradi ile ambayo ilikusudiwa, gharama zake za kuitekeleza zinaongezeka na mahali pengine inaleta migogoro. Unakuta mahali ambapo kulipaswa kufanyiwe fidia ya labda shilingi bilioni 10, unaambiwa sasa ni shilingi bilioni 20 na hiyo gharama kwa vyovyote inabebwa na Serikali na kodi za wananchi. Kwa hiyo, tunaendelea kuweka mzigo mkubwa zaidi kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa nilizungumzie, ni kuwa na mipango mingi ambayo kimsingi haitekelezeki. Kwa mfano huku, unaona mahali ambapo Kamati imebainisha kwamba miradi ambayo inapaswa kutekelezeka; kwa mfano, mradi wa makaa ya mawe Mchuchuma na Liganga, hili ni jambo ambalo lipo kila siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme kwamba jambo hili pamoja na kwamba wamesema linaweza likatekelezwa robo ya kwanza ya mwaka huu wa fedha. Jambo hili halitawezekana kwa sababu mpaka sasa hivi fidia peke yake ya kuwahamisha wale wananchi ambao wanapaswa wapishe mradi huu haijafanyika. Kama haijafanyika, ukiangalia urasimu unaotakiwa kwa vyovyote haitawezekana kukamilisha hilo zoezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba tunakuwa na vitu vingi ambavyo hatuwezi kuvitekeleza. Tunashindwa kuwa na vipaumbele. Kwa hiyo, nashauri kwamba tuwe na vipaumbele vichache ambavyo tuna uwezo navyo na hivyo vipaumbele, kwa sababu Serikali ilishasema kwamba mradi huu ni wa kimkakati, maana yake ingekuwa ni jambo la busara sana kama Serikali ingeelekeza nguvu zake zote kwenye haya mambo machache ambayo yana input kubwa kwenye uchumi wetu ili yakifanyika, tuweze kupiga hatua haraka na tukaendelea kweli kama ambavyo inaelezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiendelea na hadithi hizi za kwenye makaratasi za kueleza kwamba hili litafanyika halafu, yaani kama bluffing tu, kwamba “funika kombe mwanaharamu apite,” yaani tunaliambia Bunge kwamba jambo hili litatekelezeka, lakini ukweli ni kwamba inaendelea kuwa hadithi. Nimemsikia Mheshimiwa Ndassa akisema, kwa sababu Mheshimiwa Ndassa ni mtu senior sana kwenye hili Bunge, kwa maana ya kukaa muda mrefu kwenye hili Bunge; akisema hiyo hadithi, kwamba toka ameingia Bungeni na labda ataondoka Bungeni, huo wimbo umekuwepo wa Mchuchuma na Liganga. (Makofi)
Mheshimwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana sasa tupige hatua, tuwe na vipaumbele vichache ambavyo tunaweza kuvifanyia kazi, bajeti ambayo ni realistic, inayotekelezeka na tuifanye kulingana na time. Kitu kingine ambacho kinasikitisha sana ni kwamba mambo haya yanashindikana, lakini yapo mambo ambayo hayajapangiwa bajeti; hayapo mahali popote, unaona yanatekelezwa.
Mheshimwa Mwenyekiti, nimemsikia Mheshimiwa Rais akiwa kule Magomeni anasema natoa shilingi bilioni 10 kujenga nyumba; lakini huu mradi wa Mchuchuma kwa ajili ya fidia inayotakiwa pale ni shilingi bilioni 15. Hivi ni kwa nini hakushauriwa kwamba hili jambo la kwenda kufanya fidia kule mchuchuma ni la muhimu zaidi kuliko kwenda kujenga nyumba pale Magomeni? Kwa hiyo, naomba sana Bunge lako liibane Serikali katika jambo hili ili haya mambo yaweze kufanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la uzito unaotakiwa kutolewa kwa ajili ya sekta binafsi. Sekta binafsi ina mchango mkubwa sana kwa uchumi wetu. Nafikiri zaidi ya asilimia 57 ya uchumi wetu unategemea sekta binafsi. Ukiangalia mwenendo wa Serikali ya Awamu ya Tano kwenye suala la sekta binafsi, ni kana kwamba tunarudi kwenye ujamaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikia juzi hapa kwamba, limetolewa agizo kuwa nyumba zote za Serikali sasa hivi zitajengwa na Tanzania Building Agency. Hii ni kampuni kama kampuni nyingine; na kimsingi agency hii kazi yake siyo kujenga.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni lazima tuishauri Serikali na Serikali iwe wazi, ituambie tunakwenda wapi? Sisi tunakwenda kwenye ujamaa au tunakwenda kwenye ubepari au tunakwenda kwenye ile mixed economy. Kwa sababu kimsingi ni kama tumechanganyikiwa hatujui tunapokwenda. Sasa matokeo yake ni kwamba tunaua private sector.
Mheshimwa Mwenyekiti, dada yangu hapa, Mheshimiwa Esther Matiko amezungumza habari ya madeni ambayo yanaibana sekta binafsi. Hili la kuibagua sekta binafsi kwenye kandarasi za Serikali na lenyewe linaua private sector ambalo ni tatizo kubwa na inaweza ikatuletea matatizo makubwa kwenye uchumi wetu.
Mheshimwa Mwenyekiti, hatupaswi kushangaa ni kwa nini uchumi unadorora…
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru Mheshimiwa Waziri na wasaidizi wake kwa jitihada walizofanya na hasa kutukumbuka sisi watu wa Moshi Vijijini. Katika Hotuba ya Mheshimiwa Waziri katika Sub-vote 2005 - Roads development divisions kasma 4115 (vii) inaonesha tumetengewa sh. 811,000/= Kiboroloni – Kiharara – Tsuduni – Kidia kilomita 10.8.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka wa fedha unaoishia wa 2016/2017, tulitengewa shilingi bilioni 2.583; lakini mpaka leo hakuna hata shilingi moja iliyotolewa kwa barabara hii ambayo ni muhimu sana. Ukiacha shughuli nyingine za kiuchumi zilizopo katika maeneo inapopita barabara hii ambazo nyingi ni za kitalii, barabara hii ndiyo iendayo kwa wakwe wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, nyumbani kwa Mama Anna Mkapa. Ni imani yangu kuwa inafaa sana kuwaenzi wazee wetu hawa kwa kuwapa barabara nzuri. Naomba sana bajeti ya mwaka jana isipotee, zifanyike jitihada za makusudi ili kazi hii iweze kuanza kupitia fedha za mwaka unaoishia wa 2016/ 2017.

Mheshimiwa Mwenyekiti, chini ya miradi ya barabara za mikoa (kasma 4132) 2017/2018, Mkoa wa Kilimnjaro kuna ukarabati wa Kibosho Shine – Mto Sere Road). Upgrading to Dar es Salaam of Kibosho Shine – kwa Raphael International School Road, kilomita 27.5 zimetengwa shilingi milioni 128.00.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ilikuwa ni ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na ilianza kujengwa kwa kiwango cha lami takribani kilometa saba. Naomba sana Mheshimiwa Waziri aangalie uwezekano wa kukamilisha ahadi hii kwa ukamilifu wake kwa kiwango cha lami. Aidha, tumetengewa Rehab, Uru – Kishumudu Parish – Materuni Road, kilometa nane shilingi milioni 61.00. Barabara hii ilijengwa kwa kiwango cha lami miaka ya 1970 mwanzoni, imebomoka karibu yote. Mwaka wa jana 2016 ilijengwa sehemu ndogo kwa kuondoa lami ya zamani na kuweka mpya urefu wa takribani kilometa 1.5.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiasi hiki cha shilingi milioni 61.1 ni kidogo mno kuendeleza kazi hii ambayo imeliliwa mno na wananchi wa maeneo hayo. Barabara hii ni njia ya utalii kwenda Mlima Kilimanjaro Maanguko ya Mnambeni na katika mashamba ya kahawa. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri aliangalie upya suala hili la barabara hii, si vema kurudi nyuma, yaani kutoka lami kwenda changarawe. Tuko tayari kusubiri kwa kujengewa kidogo kidogo lakini lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni kuhusu kujengwa kwa kiwango cha lami barabara ya Mamboleo – Shimbwe ambapo ni ahadi ya Rais wa Awamu ya Tano, Dkt. John Joseph Pombe Magufuli. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri, mikakati ya kuanza kutekeleza ahadi hii ianze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wa kiujumla. Ingekuwa ni vema sana kama Wizara ingefanya survey ambayo ingeiwezesha Wizara kutambua mahitaji halisi ya kila barabara kwa maana ya kazi/mahitaji mahususi eneo kwa eneo. Mara nyingi nimeona kazi zikifanyika kwa mazoea tu wakati ingewezakana labda barabara A katika eneo fulani ikajengwa kwa kiwango cha lami hata kwa robo kilometa ikasaidia sana barabara hiyo kudumu kuliko kuiwekea changarawe na kushindilia na mvua moja tu ikaibomoa yote au ikaacha kupitika kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Moshi Vijijini linapakana na Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro katika kata za Kibosho Magharibi, Kibosho Kati, Okaoni, Kibosho Mashariki, Uru Kaskazini, Uru Shimbwe na Uru Mashariki ambako kwa muda mrefu mahusiano kati ya wahifadhi na wananchi yamekuwa mazuri sana. Kumekuwepo na eneo linalojulikana kama half mile ambalo ni eneo la hifadhi, lakini wananchi toka enzi za wakoloni waliruhusiwa kufanya shughuli za kibinadamu kama kuokota kuni, kupata majani ya mifugo na ndipo vilipo vyanzo vya maji vingi vinavyolisha jimbo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni kufuatia agizo la Mheshimiwa Waziri Mkuu la kuweka mipaka ya hifadhi upya mbali na kukataza kabisa eneo la half mile kutumika kwa shughuli za binadamu kwa masharti yaliyokuwepo mipaka mipya imechukua sehemu ya maeneo ya wananchi ambayo wamekuwa wakiyamiliki toka miaka ya 1940. Jambo hili limeleta mtafaruku mkubwa katika vijiji vya Sisimaro na Omarini huko Okaoni pamoja na Kibosho Kati, Singa Juu na Kibosho Mashariki. Ninaiomba Wizara kufuatilia jambo hili na kuona namna ya kuwapa wananchi husika maisha mbadala.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nianze mchango wangu kwa kueleza masikitiko yangu juu ya kauli ya Mheshimiwa Elibariki Kingu, kijana mdogo ambaye kwa kweli niliamini kwamba angekuwa ni mtu makini, mtu ambaye anasema ukweli na mtu ambaye angekuwa analiongezea hili Bunge hadhi (value) kuliko kuzungumza vitu ambavyo kimsingi mtu yeyote anayesikiliza, hataelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wewe umetoa sifa, leo umetoa complement kwamba katika hotuba ambazo zimeshatolewa hapa ndani ya Bunge kutoka upande huu, hii ni moja ya hotuba ambazo ni role model. Sasa anatokea mtu mmoja anasimama na anasema ukurasa wa kwanza mpaka wa mwisho hakuna kitu chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza huu ni uongo. Maneno kama haya yakivumiliwa ndani ya Bunge hili, maana yake hata hadhi ya hili Bunge na Kiti chako wewe mwenyewe vitakwenda kuathirika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Nilichokuwa nataka kusema ni kwamba waliosoma hiki kitabu kwa sababu wanacho, kina ushauri mwingi sana. Mtu akikushauri, maana yake anakupa alternative. Sasa huyu Mheshimiwa Kingu anavyosema hakuna ushauri wowote, ni malalamiko na hakuna mkakati wowote; Mheshimiwa Lwakatare amerejea hapa maeneo ambayo yanaonesha mkakati ambao unaweza ukatumika kama mbadala.

Kwa hiyo, naomba iingie kwenye record kwamba Mheshimiwa Kingu amesema uongo na amejaribu kupotosha na kwa kweli kitu alichofanya kinafedhehesha hata Bunge lenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naamini kwamba utakuwa umetunza muda wangu, kwa sababu kwa kweli umetumika ndivyo sivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kusema na hii ni kauli ambayo nairudia mara kwa mara kwamba ni vizuri Serikali ikaweka vipaumbele vichache. Tukiwa na vipaumbele vichache, maana yake tunaweza kujipima na kujua kwamba tunatoka wapi na kwenda wapi.

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wengi hapa wamezungumza habari ya Mchuchuma na Liganga. Kama tungekuwa tunajiwekea vipaumbele na tukaamua kujua kwamba ni kipi ambacho tunataka kukifanya na kwa wakati gani, haya malalamiko ambayo yameelezwa hapa yasingekuwa yamejitokeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo napenda kulishauri kwa nguvu zote ni suala la Serikali kufanya biashara, kujiingiza katika shughuli za kiuchumi moja kwa moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda Waheshimiwa Wabunge tuwe kitu kimoja na tuishauri Serikali kwa nguvu zetu zote kama Bunge kwamba suala hili ni jambo ambalo huko siku za nyuma lilishafanyiwa uamuzi na baada ya kufanyiwa uamuzi ingekuwa ni busara kama tunataka kutoka hapa tukapata muafaka sasa wa Kitaifa kwamba sasa tunaondoka kwenye utaratibu huu, kwenye utamaduni huu, kwenye sera hii tukaenda kwenye huo utaratibu mwingine wa Serikali kufanya biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbuka mchango wa Mheshimiwa Shabiby ambaye alizungumza hapa from practical point of view kwamba yeye ni mfanyabiashara na akashauri kwa nguvu zake zote kwamba hata hii biashara ya ndege ambayo Serikali imeamua kuingia, kama tunataka ifanikiwe, Serikali ikae mbali na hiyo management ambayo imewekwa kwa ajili ya kuendesha hiyo biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ukichukua mifano kama hiyo, utaona kwamba ni vigumu na haitawezekana kabisa kwamba Serikali ikafanya biashara. Tunao mfano mmoja ambao ni mdogo. Juzi juzi hapa; na bahati nzuri wewe mwenyewe ndio ulihusika kikamilifu, mlikabidhi Serikali shilingi bilioni sita kwa ajili ya kwenda kutengeneza madawati. Wakaamua kutengeneza madawati yale kwa kutumia vyombo vyake vya Ulinzi na Usalama (SUMA JKT na Magereza). Mpaka tunavyoongea hapa siku ya leo, shilingi bilioni sita madawati hayajaweza kukabidhiwa kila mahali ambapo yalipaswa kupelekwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi mwenyewe katika Halmashauri yangu ya Moshi hatujapewa hayo madawati kwa sababu tuliambiwa tukachukue hayo madawati kule Nachingwea na watu wengine wengi bado wanadai hayo madawati. Katika utaratibu wa namna hii, unakuta kwamba malengo ambayo yamepangwa hayawezi kufikiwa; hakuna tija wala ufanisi. Huo uamuzi wa Serikali ambao ulikuwa sahihi sana wa kutumia fedha zile wa kwenda kutatua tatizo la madawati, maana yake haikuwezekana. Kwa sababu kama kweli kulikuwa na kero ya madawati, mpaka leo miezi kadhaa hayajafika sasa tunafanya kitu gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia jambo lingine ambalo ni la msingi sana kwenye masuala haya ya viwanda na biashara, hili suala la Serikali kushindana na wadau wa biashara katika nchi; na lenyewe linayumbisha sana uchumi wetu. Kwa mfano, sasa hivi Serikali imeamua kwamba fedha zake zote zitoke kwenye benki za biashara na benki binafsi ziende kukaa Benki Kuu kwa sababu tu wanafikiri kwamba zile fedha za Mashirika au za Serikali zinatumiwa na benki zetu kwa ajili ya biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, nini jukumu la Serikali katika kufanya nchi istawi kiuchumi? Mahali pengine Serikali inatoa hata ruzuku kwa ajili ya benki zisianguke, zifanye vizuri; lakini kwetu pesa ziko pale, hazina kitu chochote ambacho kinainyima Serikali, Serikali inaamua tu kuwa na wivu fulani, kuwa na msimamo ambao ni hasi kwa wafanyabiashara wake na benki zake, zinakwenda kuwekwa Benki Kuu, zinakaa pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukijiuliza, hivi huo uchumi ni uchumi gani ambao unakufanya wewe uone wivu dhidi ya benki zako kufanya vizuri? Kwa sababu benki zikifanya vizuri, maana yake hiyo ni ajira inayotokana na watu wanaofanya kazi ndani ya benki. Benki zikifanya vizuri, zitakopesha watu ambao watakwenda kufanya biashara. (Makofi)

Mheshimia Naibu Spika, hata haya aliyouliza Mheshimiwa Lwakatare pesa ziko wapi, niseme pesa ziko Benki Kuu kwa sababu zimeondoka kwenye mzunguko wa kawaida. Kwa hiyo, ni vizuri Serikali ikaelewa kwamba inao wajibu wa kujenga mazingira rafiki na wezeshi kwa ajili ya watu na sekta binafsi kufanya biashara kama hizo Benki na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna maamuzi mengi ya Serikali ambayo yanafanywa bila kujali kwamba biashara au uchumi katika nchi utaathirika kwa kiasi gani. Haya nimeyaeleza kwenye hotuba yangu, lakini napenda nitie msisitizo kwenye jambo hili kwa sababu ni jambo ambalo linaathiri sana biashara na mara nyingi ukikutana na wafanyabiashara, ukikutana na wenye viwanda na wawekezaji, malalamiko yao ni hayo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, unajua jinsi ambavyo Serikali inakuwa au wanakuwa wakali inapokuwa kwamba wanadai labda fedha kwa ajili ya ushuru, wanadai fedha kwa ajili ya kodi…

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Komu. Muda wako umekwisha.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na mimi kupata nafasi ya kuchangia huu Mpango ambalo ni jambo muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa sehemu ile kwenye hotuba ya Waziri, Mheshimiwa Dkt. Mpango, ambapo anazungumza kwenye ukurasa wa tano juu ya kuweka nguvu kwenye maeneo ambayo yanawahusu watu walio wengi. Anasema tuweke nguvu kwenye maeneo hayo ambayo ni kilimo, uvuvi, pembejeo na mitaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninachojiuliza na ambacho mimi naona kwamba ni shida kubwa sana katika huu Mpango ni uhalisia wa hilo tamko ambalo ameliweka hapa na mambo ambayo yanafanyika. Kwa sababu tunapaswa tujiulize tukienda kwenye kilimo tuna mikakati gani ambayo inashikika ya kufanya mapinduzi ya kilimo, uhalisia hauko hivyo. Na kama hatutarekebisha hali hii kwa kweli tutaendelea kubaki watu wa kusema maneno tu na hakuna kitu ambacho kitakuwa kinafanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mabonde makubwa, tuna mabonde tisa ambayo ni Rufiji, Kihansi, Pwani na kadhalika. Lakini ukijiuliza kuna mipango gani ya makusudi ya Serikali ambayo inafanya haya mabonde yaweze kuleta mapinduzi ya kilimo, ukweli ni hakuna. Na nimeangalia kwenye ukurasa wa 19 wa hotuba ya Mheshimiwa Dkt. Mpango anasema katika utekelezaji wa bajeti iliyopita wameweza kutenga vyanzo vya maji 78 na kutangaza kwamba haya ni maeneo tengefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni utani, kwa sababu kwa taarifa ambayo sisi tulipata kwenye Kamati yetu ya Mazingira, Bonde la Kihansi peke yake lina vyanzo 901, katika vyanzo hivyo ni asilimia 27 tu ambayo imeshatambuliwa, kuwekewa mipaka na kutangazwa kama ni maeneo ambayo ni tengefu. Maana yake kuna maeneo zaidi ya 600 hayajafanyiwa chochote na maana yake ni kwamba hayawezi kutumika vizuri kwa ajili ya kuleta mapinduzi ya kilimo. Kwa hiyo, katika hali kama hii unaweza ukasema kwamba hatuko serious na hatumaanishi haya ambayo tunayasema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Kamati yetu vilevile ya mazingira tulianzisha hapa Mfuko wa Mazingira na ukazinduliwa na Mheshimiwa Rais na wako watu wa muhimu nawenye uwezo mkubwa sana kwenye ule Mfuko wa Mazingira. Lakini mfuko huu ulitengewa shilimhi bilioni mbili mpaka leo tunavyozungumza, Serikali imetoa shilingi milioni 34 tu kwa ajili ya huo Mfuko wa Mazingira, sasa katika hali kama hiyo tunapigaje hatua. Ukienda kuangalia kwenye eneo hilo la kilimo tuna Benki inaitwa ya Kilimo hapa, hiyo Banki ya Kilimo inafanya nini, Serikali imeipa nguvu kiasi gani ili iweze kufanya mapinduzi ya kilimo katika nchi hii, nimeangalia wametoa mikopo ya kama shilingi bilioni 6.5 kwa watu 2000 na kitu maana yake ni wastani wa kama shilingi milioni 2.6 kwa mtu mmoja. Tunaweza tukafanya mapinduzi ya kilimo katika nchi hii kwa stahili ya namna hiyo!

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kule Moshi kulikuwepo na mradi unaitwa Moshi Lower Irrigation Scheme ambao huu uligharamiwa na Wajapani, baada ya Wajapani kuondoka ekari ambazo zilikuwa zimekwishatayarishwa na kujengewa miundombinu zilikuwa 1,100 na zilikuwa na uwezo wa kuhudumia watu zaidi ya 4,500 leo hii tunapozungumza kutokana na uchakavu, kutokana na mabadiliko ya tabianchi leo ni ekari 417 tu ambazo zinatumika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni wazi kwamba tunarudi nyuma hatupigi hatua na kama Serikali haitachukua hatua za makusudi za kuwekeza kwenye maeneo kama haya na kuangalia maeneo ya miradi ya namna hiyo katika nchi nzima tutaendelea kuwa maskini na hatuwezi kufanya hatua yoyote. Tukienda kwenye uchumi wa viwanda, ni lazima tukubaliane na watu wengi hapa wamezungumza kwamba tunataka kujenga uchumi wa aina gani, uchumi wa kijamaa au wa kibepari au wa kati, kwa sababu ukiangalia tunazungumza kuwa tunataka kujenga uchumi wa viwanda lakini unaona kwamba Serikali bado inarudi kule ambapo tulishatoka miaka mingi. Leo hii Serikali inamiliki TTCL kwa 100%, leo hii Serikali inamiliki kiwanda cha General Tyre kwa 100%, leo hii TBA inafanya kazi za ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi wajibu ule wa Serikali ambao tunauzungumza wa kujenga mazingira wenzeshi, unaendanaje na hali kama hii? Lakini tunazungumza uchumi wa viwanda tumetenga maaneo kwa miaka mingi EPZ na ZSS, na baada ya kuyatenga hakuna hatua za makusudi na uwekezaji wa makusudi katika hayo maeneo kwa ajili ya kujenga miundombinu, kwa ajili ya kuyafanya yale mazingira yaweze kuwa wezeshi, kwa ajili ya kulipa fidia hakuna hatua ambazo za kulizisha. Matokeo yake ni kwamba tunatarajia wawekezaji waje, wajenge barabara, waweke umeme na waweze kujenga viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri atuambie ni mtu exposed sana na sina matatizo naye, ni wapi hapa duniani hata kule China ambapo ardhi ilitengwa halafu...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Maji ambayo ni bajeti muhimu. Kwa maoni yangu ni bajeti ambayo ingepaswa iwe labda namba mbili baada ya bajeti ya Wizara ya Elimu kwa umuhimu. Maji ni uhai si uhai wa binadamu tu isipokuwa uhai wa viumbe na hata uhai wa uchumi wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuangalia hali ya maji nchini. Waziri amejaribu kujenga picha kwamba tuna hali nzuri sana katika Afrika Mashariki kwa sababu kiasi cha maji sasa hivi kwa maana ya mita za ujazo kilichopo kwa ajili ya matumizi ya kila mtu ni 1,800 kama alivyosema na akasema sisi ni wa kwanza Afrika Mashariki. Nataka Bunge lielewe, kwa mujibu wa taarifa za wataalam wa Wizara hali yetu ya maji si nzuri kwa sababu ifikapo mwaka 2025, tutakuwa tupo chini ya kiwango ambacho kinahitajika kwa binadamu mmoja, tutakuwa tumefikia mita za ujazo 1,500 na tutatangazwa kama nchi yenye uhaba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia uwekezaji unaofanywa kwenye maji inaonekana wazi kabisa kwamba huko ndiko tunakokwenda. Kwa hiyo, kutulinganisha sasa hivi na walemavu wengine haitusaidii sana, ni lazima tuzungumze hali halisi na kwamba hali yetu ni mbaya na uwekezaji wetu hauashirii hata kidogo kwamba tutazuia kwenda kwenye nchi ambayo ina uhaba mkubwa wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu leo tunavyozungumza katika vijiji vyetu vyote ni asilimia 46 tu ya watu wenye maji salama na maji safi. Sasa hili si jambo la kujisifia. Ukiangalia fedha ambazo zimetengwa kwa ajili ya bajeti ya maji hazioneshi kama tunaweza tukajiondoa hapa tuliko kwa sababu ni fedha kidogo, lakini vilevile pesa hizo zikishatengwa hazipelekwi na mahali pengine inakwenda sifuri kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimejitahidi kusoma kidogo na hawa watu wa Wizara wamefanya kazi kubwa sana, wametengeneza miradi yote ya maji katika nchi hii kwenye hiki kitabu na zipo hapa. Wameonesha ili miradi yote ya maji iweze kukamilika tunahitaji shilingi trilioni 32.4 lakini leo pesa tuliyotenga, tumetenga shilingi bilioni 20 maana yake ni kwamba tunahitaji miaka 1,200 ili tuweze kukamilisha kilichoandikwa humu, tunatania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia mwaka jana pesa ambazo zilitengwa kwa ajili ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji shilingi bilioni sita, wamesema hapa kwamba hiyo bajeti imetekelezwa kwa asilimia 12 lakini waseme vilevile kwamba fedha za ndani hazikwenda hata shilingi moja, zimekwenda asilimia sifuri, fedha za nje ndizo zilizokwenda shilingi bilioni 2 ambazo ndizo zinazofanya asilimia 12. Katika hali ya namna hii tunatania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini maana ya kuwekeza kwenye maji ni nini? Maana ya kuwekeza kwenye maji ni kuwa na ajira ya uhakika, chakula cha kutosha na kuacha ku-import chakula kutoka nje. Leo kwa taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania tunaagiza chakula kutoka nje cha shilingi bilioni 888.5 kila mwaka. Hizi fedha tungeweza tukazi-save, ndiyo maana sisi watu wa upinzani tunashangaa kweli kweli mnavyoshangilia hapa kuhusu kununua ndege cash. Hivi tuna-luxury gani ya kwenda kuwekeza shilingi trilioni moja kwenye ndege wakati kila mwaka tunapoteza shilingi bilioni 800 kwa ajili ya kununua chakula kwa sababu hatuwekezi kwenye maji? Tukiwekeza kwenye maji tukaokoa hizo fedha maana yake ni kwamba kila mwaka tungeweza kununua hizo ndege sita kwa mpigo, lakini kweli tumeanza na ndege ndiyo maana sisi tunawashangaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ni hali ambayo kama hatutabadilika, tukaamua kuchagua vipaumbele ambavyo ni sahihi, vipaumbele vinavyowagusa watu wetu, vipaumbele ambavyo vinatufanya tuweze kupiga hatua kwa namna ya kuweza kuchochea uchumi wetu bado tutaendelea kuingia katika hatari na kama nilivyosema tunakwenda sasa ku-approach danger zone kwamba tutakuwa nchi ambayo wanaita kwa kiingereza water stress.

Nashauri tuangalie upya na hili ni Bunge tusimame kama Bunge tuisimamie na kuishauri Serikali iache haya mambo ambayo ni ya kujenga impression wakati hali yetu ni mbaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti nikienda kwenye miradi hii ambayo imetangazwa humu, iko miradi ya umwagilaji ya toka mwaka 2004 haijaisha. Katika miradi 312 ni miradi 55 tu ambayo imeweza kukamilika maana yake ni asilimia 17. This is very serious. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti kama Wabunge wengine walivyosema unavyokwenda kumpa mkandarasi pesa kidogokidogo, unakuta kuna mradi ambao unapaswa ujengwe kwa shilingi bilioni sita unapeleka shilingi bilioni 900, hauko serious. Tabia hii ni lazima tuibadilishe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye jimbo langu. Kule kwenye la Moshi Vijijini tuna mradi mmoja wa Kata ya Old Moshi Magharibi na niliwahi kuuliza kwenye swali la msingi hapa ulitangazwa toka mwaka 2012, tukaambiwa mkandarasi atakwenda site, kila tukiuliza tunaambiwa utaanza mwaka unaofuata mpaka leo huo mradi wa vijiji vya Telamande haujaanza. Naomba Waziri akija hapa atuambie huo mradi utaanza lini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii asilimia 46 wanayosema kwamba kuna maji, wanahesabu mpaka yale mabomba ya Moshi Vijijini yaliyojengwa na Lucy Lameck mwaka 1975 ambapo miundombinu yake imeshachakaa na vyanzo vingi vya maji hayo vimeshakauka, kwa hiyo na vyenyewe wanahesabu kwamba kuna maji. Ndiyo maana kuna watu wengine watu wa Kaskazini wasubiri kwa sababu wanafikiri kule kuna maji, sisi kule tuna shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kata yangu moja inaitwa Mabogini ina vijiji kumi ni vijiji vinnetu vina maji. Kule Mtakuja kwa Wamasai, Mserikia, Mawala kwa Mheshimiwa Mbatia, Mikocheni TPC hakuna maji, watu wanatafuta maji kama wanavyotafuta mafuta ya taa au petroli. Kwa hiyo, tunaomba muangalie mambo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mradi mkubwa ambao ulijengwa na Wajapani unaitwa Moshi Lower Irrigation Scheme. Mradi ule ni wa kisasa sana lakini na wenyewe kwa sababu hakuna maintenance fund, hakuna watumishi wenye weledi wa kuweza kusimamia machines ambazo zimeachwa kule, hakuna mashine hata moja inafanya kazi na sasa hivi unaanza kubomoka na huko kwenye hatari vilevile ya kwisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, huu utaratibu wa kutokupeleka fedha kwenye Wizara mbalimbali na hasa hii ya Maji maana yake ni kwamba there is no value for money kwa zile pesa za matumizi tunazotoa, unalipa mtu ambaye humtumii. Maana yake ni kama unatoa sadaka au ruzuku tu na hii ni matumizi mabaya ya fedha za walipa kodi wa nchi hii. Ni lazima tusimamishe hayo mambo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba sana Bunge lako liielekeze Serikali ichukue vipaumbele vichache vyenye matokeo makubwa kwenye uchumi wetu, iweke nguvu hapo na imalize miradi hiyo. Leo tunaenda kushika Stigler’s Gorge, hatujaangalia uchumi wa gesi kule umeendaje, tunaenda kuangalia Stigler’s Gorge kuna Mchuchuma na Liganga ambao unaweza kutupa umeme hatuendi, sasa tukifanya hayo mambo kwa mtindo huo hatutaweza kufika.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Spika, nami nikushukuru kwa kunipa nafasi kuchangia bajeti hii ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Wizara ambayo kimsingi ndiyo inayobeba kaulimbiu ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano, Dkt. Joseph Pombe Magufuli.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hiyo kaulimbiu ya Mheshimiwa Rais lakini uhalisia kwa maana ya bajeti haupo. Kwa sababu 2015/2016 bajeti ya kwanza ya Mheshimiwa Rais, utekelezaji kwenye bajeti ya maendeleo kwenye Wizara hii ilikuwa ni asilimia 5 tu, 2017/2018 ikawa asilimia 9.47. Katika hali ya namna hii ukiunganisha hiyo kaulimbiu na majigambo yote yaliyokuwepo na dhamira ya kutaka kuona kwamba tunakwenda kwenye uchumi wa viwanda haipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye ripoti ya CAG ambayo inaangalia ufanisi kwenye viwanda vidogo vidogo na vya kati ambavyo mahali popote duniani ndiyo moyo wa mapinduzi ya uchumi wa viwanda, anasema hali si nzuri, bajeti kwenye sekta hiyo imeendelea kushuka katika ngazi zote maana yake mpaka kule kwenye halmashauri zetu, si zaidi ya asilimia 16, kwa hiyo, bado uhalisia unaendelea kuonekana kwamba haupo. Mafunzo kwenye viwanda hivi vidogo vidogo kwenye sekta hii bado yameendelea kushuka, CAG anasema yako kwenye wastani wa asilimia 7 tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye Vituo vya Maendeleo ya Teknolojia ambavyo vilianzishwa na Mwalimu Nyerere mashine ambazo zinatumika mpaka leo zina umri wa miaka 40, amesema Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, siyo sisi tunaosema. Sasa seriousness iko wapi? Ukiangalia CAG anasema, sekta ya viwanda vidogo vidogo na kati inaporomoka kwa asilimia 30 ikilinganishwa na kukua kwake kwa asilimia 5.6. Kwa hiyo, kauli mbiu ya Mheshimiwa Rais ya kujenga Tanzania ya Magufuli ya Viwanda haina uhalisia wowote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mwenyekiti wa Kamati alivyokuwa anazunguza hapa amezungumzia mazingira ya kufanya biashara Tanzania. Mpaka tunavyoongea hapa sasa hivi sisi ni wa 137 duniani kati ya mataifa 190 kwa mazingira rahisi ya kufanya biashara. Kinachokwenda kupeleka huo ugumu ni nini? Ni matamko ya viongozi wetu wa siasa wa upande huu wa CCM ambayo yanafanya mazingira yetu yawe si ya kutabirika na kwa sababu hiyo uwekezaji unakuwa ni mgumu katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukitaka kupata kupata kibali cha kuanzisha kiwanda hapa pamoja na mbwembwe zote anazosema Mheshimiwa Waziri hapa unaweza ukatumia miezi kadhaa. Kuna marufuku zinatolewa tu kila siku na hata wafanyabiashara waliomo humu ndani wamekuwa wakilalamika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni-declare interest nilikuwa kwenye Kamati ya Viwanda na Biashara, tulikutana na tatizo hili ambalo Mwenyekiti amelizungumza hapa vilevile la vibali vya sukari ya viwandani. Vipo viwanda ambavyo tunapozungumza sasa hivi vimefungwa kama Kiwanda cha SAYONA kule Dar es Salaam kutokana na sukari yao kuzuiliwa bandarini tangu mwezi wa nane eti uhakiki unafanyika na ukimuuliza Mheshimiwa Waziri anasema hili liko kwa tajiri mwenyewe. Kwa hiyo, masuala kama haya yanaleta shida. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kuna masuala ya hizi mamlaka zetu za udhibiti, TRA, ubabe mtupu na urasimu ambao hausaidiaa nchi hii. Nimeona kwenye magazeti ya leo TRA sasa wanawaomba wafanyabiashara walifunga biashara zao warudi. Hizi kauli za kukinzanakinzana zinatupa shida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jana Waziri wa Fedha alikiri kwamba hali ni mbaya na ndiyo maana bajeti hazitekelezeki. Hawawezi kukusanya mapato kwa sababu ya hii mikanganyiko ambayo ipo kwenye uendeshaji wa Serikali yetu. Kwa hiyo, tunawataka waache hayo mambo ambayo wanafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ni kushikashika vitu vingi bila ya kuwa na jambo moja ambalo tumeamua kulifanya kwa sababu ya tafiti ambazo tumefanya na tukalikamilisha. Mheshimiwa Zitto hapa amezungumzia Mchuchuma na Liganga. Hivi kweli kama tuna akili sawasawa, tumefanya tafiti zetu na tumedhamiria kweli kuleta mapinduzi na kukomboa watu wetu ni kwa nini hatuutekelezi mradi huu? Tuna mradi wa Bwawa la Kidunda pale Morogoro ambalo linahitaji Dola za Marekani milioni 251 ili tupate umeme, ajira, kusaidia kilimo chetu, ku-stabilize Mto Ruvu na maji kwa ajili ya viwanda lakini jambo hili linaendelea kuwa ni hadithi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati huo huo nilisema hapa juzi, nchi hii inaagiza chakula kwa mwaka kulingana na takwimu za Benki Kuu ya kwetu sisi bilioni 888.5. Hivi jamani hii Serikali haina uchungu na nchi hii? Hivi hawaoni kwamba tungechukua hizo Dola bilioni 251 tukawekeza pale Kidunda tungeweza tukaokoa hizo bilioni 888.5 na baada ya hapo tukaenda sasa kuwekeza katika mambo mengine ambayo kwa kweli mimi naita ni mambo ya kishamba tu, ya kujionyesha. Eti na sisi tuwe na ndege kwa kuwekeza trilioni moja tena sisi kwa sera ya nchi yetu tumeshakubaliana kwamba twende kwenye Private Public Partnership (PPP) hatufanyi. Tungeweza tukaweka hayo masuala ya ndege kwenye hiyo PPP, sasa hivi tunajenga reli ya standard gauge ambayo ni kitu cha maana na muhimu sana lakini tukaenda kwenye utaratibu huo. Tunachukua pesa za Watanzania, badala ya kuwekeza kwenye mambo ya msingi ambayo yatawapa matokeo ya haraka na yatakayosaidia kupiga hatua kwa haraka.
Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Uamuzi wake wa Kuendeleza Mji wa Dodoma na Kuupa Hadhi ya Jiji
MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia azimio hili na nianze kwa kueleza masikitiko yangu kuhusiana na azimio hili kwa sababu kwa maoni yangu ni azimio ambalo kwa kweli ni lenye ubaguzi kwenye nyanja nyingi. Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema ni azimio lenye ubaguzi kwa sababu kwanza ukiangalia hili azimio, linataka kufanya historia kama inaanza leo kwamba Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ndio ambaye amefanya hili Jiji la Dodoma au huu Mji wa Dodoma kuwa ndiyo Makao Makuu na kuwezekana kuwa Jiji. Mheshimiwa Mwenyekiti, mchakato wa kuifanya Dodoma ikawa kama ilivyo leo na Mheshimiwa Simbachawene amerejea hapa kwamba wakati Mheshimiwa Rais anazungumza kwenye Mkutano wenu Mkuu, alizungumza kwamba vipo vitu ambavyo vimeshawezesha sasa Dodoma kuwa ni mahali panaweza kuwa Makao Makuu. Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa leo azimio hili lingekuwa na maana sana na ningeliunga mkono kama lingetambua vilevile watu wengine ambao wamefanya mambo makubwa mpaka tukawa jinsi tulivyo leo. Mheshimiwa Mwenyekiti, wako watu wamejenga hili Bunge, wako watu waliojenga barabara za kuja Dodoma, wako watu waliojenga Chuo Kikuu cha Dodoma. Hivi leo Rais Dkt. Magufuli amefanya nini ambacho ni muujiza?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais, Mheshimiwa Magufuli ametangaza, tena ametangaza bila kuzingatia sheria. Amepoka mamlaka ambayo sio yake.

Siyo, nenda karejee Sheria ya Mipango Miji kifungu cha 7(2) uone nani mwenye mamlaka ya kutangaza Mji kuwa Jiji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunataka kuonesha Bunge hili kufanya kwamba fedha anazotumia Rais, Mheshimiwa Dkt. Magufuli ni za kwake za mfukoni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge hili ni lazima lijirudishe mahali pake liwe na hadhi na kwamba ndilo linaloombwa pesa. Serikali inapaswa kuja hapa kuomba pesa na siyo sisi Wabunge kuwa ni chombo cha kushangilia na kupongeza wajibu wa mtu anaopaswa kufanya. Hilo ndilo sikitiko langu la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sikitiko la pili ni aina ya ubaguzi unofanywa katika kutekeleza mambo mbalimbali katika nchi. Sisi Moshi tulifanya michakato yote ya kuwa jiji kwa zaidi ya miaka mitano na tumetumia fedha nyingi za ndani na za nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiofichika kwamba Mheshimiwa Rais siku moja kabla ya Mei Mosi ya mwaka 2017 alikuja akakaa mahali na watu ambao sisi watu wa Moshi hatuwajui, akaamua kufuta mchakato mzima wa Moshi kuwa Jiji. Sasa hili sijambo la kushangilia. Ni jambo la kusikitisha. (Makofi)

Mhesimiwa Mwenyekiti, la mwisho, mpango huu ni mpango wa kukurupuka. Ni mpango ambao unasababisha mateso makubwa kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nieleze kwa masikitiko makubwa kwamba mwezi uliopita tumepoteza watumishi watatu wa TIC wakiwa wanakuja Dodoma.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia bajeti hii. Nianze kwa kusema hili suala la utekelezaji duni wa bajeti kwa kweli ni tatizo kubwa ambalo lisipopatiwa ufumbuzi itatuwia shida sana. Kwa sababu naona na najiuliza kweli kwamba ni kwa nini tunakaa kwenye hili Bunge na kupoteza muda mwingi namna hii na kufanya uchambuzi kama tunavyofanya na Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Mpango pale anakuja na yote haya aliyokuja nayo, lakini mwisho wa siku kunakuwepo na utekelezaji mpaka wa sifuri kwenye baadhi ya maeneo ambayo ni ya msingi sana kama ilivyorejewa hapa na watu mbalimbali kama kilimo na umwagiliaji.

Mheshimiwa Spika, sasa hii inaondoa maana ya Bunge hili, vilevile na nimekuwa nikisema mara kwa mara kuna tatizo la kutumia fedha vibaya. Kama unapeleka fedha zile zinazoitwa za matumizi ya kawaida na OC ambazo hakuna kazi inayokwenda kufanyika. Kwa sababu hizi fedha tunazotoa kama matumizi ya kawaida ni ili zikafanye mambo fulani fulani ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, kama hili jambo halitarekebishwa kama Wabunge na chini yako tutakuwa sisi tunatumia fedha za wananchi ambao ni walipa kodi vibaya. Kwa hiyo ningekuomba sana tuweze kuungana kwa pamoja kama Wabunge tuwaulize Serikali tatizo liko wapi, kwa nini wasije na bajeti ambayo ni ina uhalisi inayotekelezeka ili tukipitisha hapa tunajua kwamba tumefanya kitu ambacho kinakwenda. Wengine ni waathirika wakubwa wa huu utekelezaji duni wa bajeti.

Mheshimiwa Spika, nina miradi kule kwenye Jimbo langu, miradi ya barabara 2016/2017, barabara moja ambayo inatoka Kiboroloni inakwenda Kikarara inapita kule Suduhi mpaka kule Kidia imetengewa fedha shilingi bilioni 2.5 haikuja hata shilingi. Mwaka 2017/2018 ikatengewa fedha shilingi milioni 810 haijaja hata shilingi. Safari hii nimeona tena Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi ameitengea shilingi bilioni moja na yenyewe sijui niseme itakuja tena sifuri au namna gani.

Mheshimiwa Spika, umesoma kule kwetu unajua kwamba barabara zetu kujengwa kwa kiwango cha lami si luxury ni suala la lazima. Kwa sababu ya hali halisi ya aina ya udongo wetu kule. Vivyo hivyo tuna mradi mmoja wa Telamande - Old Moshi toka mwaka 2012 unazungumzwa kwenye makabrasha yote haujaanza mpaka leo. Sasa katika hali ya namna hii naona ni fedheha kwa Serikali na hata kwa Bunge lako ambalo linakaa hapa na kutumia fedha nyingi kiasi hiki kupitisha vitu ambavyo kimsingi sijui niseme havipo au ni hewa au ni namna gani. Kwa hiyo ni vizuri tukawaomba Serikali wakija hapa watueleze ni kwa nini mambo yanakwenda hivi.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni sekta binafsi. Sekta binafsi ni kichocheo kikubwa na ni engine mahali popote pa uchumi. Leo asubuhi uliuliza hapa ni kwa nini Kenya wako kama walivyo, ni kwa sababu wanaheshima na commitment kwa private sector. Sisi katika Taifa letu tunazungumza kila siku kitu kinachoitwa PPP, niulize leo ni mradi gani ambao unaendeshwa kwa huo utaratibu wa PPP, hakuna! Hata hivyo, tunashindwa kufanya mambo kwa sababu hatuwapi fursa watu wa sekta binafsi.

Mheshimiwa Spika, katika Kamati yetu ya Kilimo, Mifugo na Maji tumekuwa na ziara juzi hapa huko Nyanda za Juu Kusini, Njombe, tukakuta wawekezaji wanalalamika. Wakati wanapoagiza vitu kwa ajili ya kuwekeza hapa kuna unafuu wanaopewa wa kodi, lakini wanaambiwa na Serikali walipe fully, walipe kodi zote halafu wa-claim. Hizo pesa hazirudishwi na hata zikirudishwa zinarudishwa baada ya muda mrefu sana, jambo ambalolinaondoa imani kwa Serikali, linaondoa imani kwa wawekezaji na sekta binafsi. Sasa wenzetu huko duniani hawako hivyo.

Mheshimiwa Spika, kuna kiwanda cha Chai kule Njombe na nasikia Mheshimiwa Rais anakwenda huko, ni vizuri wanadai bilioni 8.2, hawajarudishiwa. Tanga wanadai bilioni 17 hawajarudishiwa, tulipita wakati fulani kule Mwadui tukakuta hivyo hivyo bilioni 12. Sasa katika hali ya namna hii tutakuwa hatujengi uchumi wetu na hatuwatendei haki watu wa sekta binafsi.

Mheshimiwa Spika, mfano mwingine mzuri kuna Wakala wa Mbolea, walifanya kazi hapa wanadai zaidi ya bilioni 64, lakini kirahisi tu Serikali imesema hawadai baada ya uhakiki. Ukienda kuwauliza mpaka leo watu wanadaiwa na mabenki na mbolea zilikwenda, lakini shauri ya technicalities tu unakuta kwamba wameambiwa hawadai. Sasa hali kama hii kwa kweli haiwezi ikatupeleka mahali pazuri.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni kuwa na miradi mingi na ambayo kila siku tunaanza miradi mipya, wamezungumza watu hapa asubuhi. Tuna miradi kwa mfano, tukienda kwenye eneo la umeme, tuna uchumi ambao tulihubiriwa sana uchumi wa gesi. Hivi ni tatizo gani limeingia kwenye kile kitu tulichokuwa tunazungumza habari ya uchumi wa gesi.

Mheshimiwa Spika, nasikia mpaka leo tunafanya utilization ya 6.8 basi katika uchumi wa gesi na pesa zote ambazo tumewekeza. Sasa katika hali ya namna hiyo ni jambo ambalo linaacha maswali mengi. Pia kuna suala la Mchuchuma na Liganga, kuna suala la bwawa la Kidunda yote haya yangetupa umeme.

Mheshimiwa Spika, sasa kama watu hawa wangeamua wakashika mambo machache na wakayafanyia kazi kwa ukamilifu leo tusingekuwa tunaenda kuhangaika na vitu kama Stiegler’s Gorge, ambayo mimi na naomba iinge kwenye record kwamba siungi mkono hilo suala la Stiegler’s Gorge kwa sababu ni jambo ambalo linakwenda kuleta athari kubwa sana kwa uoto wetu wa asili na wanyama wanaoishi kule Selou na sioni ni kwa nini. Kwa sababu tungefanyia kazi vyanzo hivi vya umeme ambavyo tunavyo tungeweza tukafika mbali zaidi.

Mheshimiwa Spika, mwisho niseme kwamba chema chajiuza kibaya chajitembeza, hivi kweli hizi sifa zote tunazoandika huku hatuwezi kuacha tu historia ikaja ikasema tuliyoyafanya na ambayo tumeshindwa kuyafanya?

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018
MHE. ANTHONY C. KOMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Nianze na mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mazingira ni kitu cha muhimu sana na ni kitu ambacho ni cha kufa na kupona, kwa sababu bila mazingira binadamu anaweza kuwa hatarini kutoweka kama viumbe vingine ambavyo vinatishika sasa hivi kutoweka. Uwekezaji unaofanywa katika mazingira hauakisi hali hiyo. Kwa hiyo, niungane na Kamati kwamba iko haja ya Bunge kuisukuma zaidi Serikali kuona umuhimu wa mazingira na kuwekeza inavyotakiwa katika mazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hii kauli ya Mheshimiwa Rais ya juzi kwamba watu sasa wanaruhusiwa kufanya shughuli za kibinadamu kwenye maeneo yale ambayo ni tengefu na maeneo ya vyanzo vya maji. Sisi hatuna ugomvi na hilo, lakini tunasema kama kweli tunataka kufanya kazi kwa misingi ya kisheria na ili isiwe hii ni kugawa peremende kwa sababu za kiuchaguzi, halafu baada ya uchaguzi wananchi waje wapate taabu kama wanavyopata kwenye maeneo mengine, Serikali ilete sheria, ilete mapendekezo ya marekebisho ya sheria, tuijadili hapa Bungeni, tuipitishe, ili watakaokwenda kufanya shughuli za kibinadamu kwenye maeneo hayo ambayo Mheshimiwa Rais ameyasema, yaweze kuwa salama hata baada ya uchaguzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hivyo, niende sasa kwenye Kamati ya Viwanda na Biashara. Kumekuwepo na kutokutekeleza mikakati mbalimbali ambayo tunaiweka. Hii mimi nasema kinachofanyika kwa kweli ni matamko tu, siyo mkakati. Ukiangalia, kuna mambo mengi ambayo yametajwa katika mpango wetu wa miaka mitano wa maendeleo. Leo ukiangalia ni kwa kiasi gani tunatekeleza yale ambayo tumeyaazimia, utashangaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwepo na miradi ya kimkakati, mfano ujenzi wa viwanda ambavyo vinaweza vikachochea mageuzi ya viwanda katika nchi hii. Hivyo viwanda viko vingi. Kuna Kiwanda cha General Tyre, Mheshimiwa Lema amesema sana hapa, hakuna chochote pamoja na uwekezaji mkubwa ambao unazidi zaidi ya shilingi bilioni 20 ambao umekwenda kule. Pesa zile zimetupwa tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mradi wa Mchuchuma na Liganga, kuna zaidi ya shilingi bilioni 20 nazo zimetupwa tu. Kuna Mradi wa Magadi Soda Engaruka, kuna zaidi ya shilingi bilioni sita zimekwenda kule, hakuna chochote kinachoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika hali kama hiyo, nafikiri ipo haja ya kuangalia upya; na ili Bunge liweze kufika mahali pa kutoa maelekezo kwa Serikali, ili tuwe na vipaumbele ambavyo tunavifanyia kazi na tusiwe na haya matamko ambayo kwa namna moja ama nyingine yanaendelea kutumika kama vichochoro kwa ajili ya kutengea fedha na kupiga fedha. Kwa sababu ukiangalia Kamati inavyosema, Kiwanda cha General Tyre ni kama hakipo tena na hakitawezekana, lakini utashangaa mapendekezo ya bajeti yatakapokuja hapa, wanasema tunahitaji shilingi fulani kwa ajili ya kwenda kufanya utafiti, na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipo Kiwanda cha Urafiki ambapo sisi Tanzania ni wabia kwa asilimia 49, lakini kwenye Hotuba ya Kamati hapa wamesema kuna fedha zilikopwa na wabia wenzao wale wa China, wameandika pale Yu 217,000 lakini Kamati inasema haifahamu hizo fedha zilikwenda wapi na zilifanyia nini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Kamati inasema hivyo, mwakilishi wetu pale ambaye ni Serikali, hajui kwamba hizo fedha zilizokopwa zilikweda kufanya nini na ziko wapi? Sasa katika hali ya namna hiyo ni kitu ambacho kwa kweli, kinaleta kichefuchefu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hiyo miradi, kuna mtu alizungumza hapa akasema tunawasifia Serikali ya Awamu ya Tano kwa kufanya radical change. Sasa radical change kwenye kitu gani? Ingekuwa radical change mngetuambia leo mnajenga Mchuchuma na Liganga. Ingekuwa ni radical change mngesema mnajenga Engaruka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nim-quote Mheshimiwa Waziri Stephen Wassira. Wakati fulani akiwa anawasilisha Mpango wa Mapendekezo ya Mpango wa Taifa wa mwaka 2014/2015 alisema hivi: “Kwa upande wa Mradi wa Magadi Soda Bonde la Engaruka, Arusha, kazi ya kuchonga mashimo 12 kwa ajili ya uhakiki wingi na ubora na magadi umekamilika, ambapo imebainika kuwa eneo la Engaruka lina magadi yenye mita za ujazo bilioni 4.68 kiasi ambacho ni kikubwa kutosheleza uchimbaji wa magadi soda kwa zaidi ya miaka 400. Upatikanaji wa magadi soda utasaidia katika viwanda vya madawa, sabuni, nguo, rangi na viwanda vya kuchakata chuma.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilivyosoma hii, nikajua kumbe ndiyo maana Mheshimiwa Stephen Wassira anataka kurudi tena agombee Urais. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko Bwawa la Kidunda ambapo tungelijenga, linahitaji uwekezaji wa shilingi bilioni 251, leo tusingekuwa tunaenda kwenye Stiegler’s Gorge kwa sababu tungepata umeme, tungepeta maji ya kumwagilia, tungepata uchumi mkubwa wa miwa, utalii na uvuvi. Sijui tumelogwa na nani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna uchumi wa gesi ambao ulihubiriwa sana, lakini leo tumeshafika 7% tu ya utilization, mbali na uwekezaji mkubwa tuliouweka pale kujenga bomba kutoka kule Mtwara mpaka Dar es Salaam kwa pesa ya mkopo ambayo tunapaswa tulipe miaka na miaka na hakuna chochote ambacho mnasema. Leo mnasema mnafanya radical change, mnafanya radical change kwenye kitu gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya biashara; na hapa nataka nimrejee ndugu yangu Mwalimu wangu Mheshimiwa Dkt. Mpango. Katika hali ya biashara, wakati wanawasilisha mapendekezo ya hali ya uchumi alisema watahakikisha kunakuwepo na kufungamanisha uchumi na maendeleo ya watu. Wakasema watajenga mazingira wezeshi kwa ajili ya uwekezaji, na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hawa Waheshimiwa walivyoingia madarakani, kwa mujibu wa Benki yetu Kuu ya Tanzania, ile economic monthly review, deni la ndani, ambapo walisema vilevile watalipunguza, Novemba, 2015, lilikuwa shilingi trilioni 7.9. Leo, yaani mwaka 2018 kwa takwimu za Benki Kuu ya Tanzania, deni la ndani ni shilingi trilioni 14. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hiyo radical change iko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye Tanzania World Bank Economic Update, Report Number 11, utakuta umasikini katika nchi hii kwa kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Tano, wamezalisha watu masikini kwa miaka hii mitatu, milioni mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye urahisi wa kufanya biashara, hali imeendelea kuwa mbaya. Kuanzisha biashara tulikuwa wa 129 mwaka 2015, leo ni wa 162. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vibali vya ujenzi tulikuwa wa 126, leo ni 156. Kusajili mali (property) tulikuwa wa 133, leo ni 142. Kupata umeme tulikuwa wa 83, hapo tumepiga hatua kidogo kwa moja, tuko 82 sasa hivi. Biashara mpakani tulikuwa wa 180, leo wa 182.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hii ni kwa sababu ya sera mbaya, ni kwa sababu ya misururu ya kodi, ni kwa sababu ya taasisi nyingi za udhibiti, ni kwa sababu ya kukosekana one stop window; ni kwa sababu ya Sheria za Kodi zisizokuwa rafiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi Serikali imeamua kufanya biashara na kuacha jukumu lake la msingi la kisera la kuwa facilitator, kuwa mwezeshaji; imeamua kuwa mshindani. Mifano ipo. Leo tunafanya biashara ya kwenye ATCL kwa asilimia 100, that is very wrong.

Sasa leo tunaenda kununua korosho.

MBUNGE FULANI: Wamelipa mikopo ya benki.

MHE. ANTHONY C. KOMU: Leo tunaenda kuingia kwenye biashara ya korosho kwa asilimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, akili ya kawaida, sisi tulipaswa tufanye subsidy, tulipaswa tu subsidize. Kama walikuwepo wafanyabiashara waliotaka kununua ile korosho kwa shilingi 2,700/=, sisi tungewaongezea hiyo shilingi 600/= tukawakopesha. Leo tungekuwa tunahitaji shilingi bilioni 200 tumalize biashara ya korosho. Leo tunataka shilingi bilioni 900, tumechukua Jeshi letu la Wananchi wako kule wanapigana vikumbo na wananchi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeua kabisa mfumo wa korosho. Baada ya mwaka huu kwisha, nani atanunua tena korosho? Mwaka kesho tena Serikali wataenda kununua korosho? Mmeua Bodi ya Korosho, mmeshindwa kui-replace? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na hili tatizo la korosho, kwa mujibu wa hii economic review, maana sijui Economic Review ya Benki yetu ya Tanzania, kwenye balance payment tume-experience deficit ya dola milioni 500. Halafu mnasema mnafanya radical change. Ipi? (Makofi)

MBUNGE FULANI: Wapi?

MHE. ANTHONY C. KOMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninawaomba sana; wafanyabiashara waliokuwa wanafanya biashara za ku--supply stationaries sijui kwenye Jeshi la Polisi, waliokuwa wanafanya biashara ya kuchapa vitu mbalimbali, leo wanaofanya ni TISS, Usalama wa Taifa. Wanaenda kufanya… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Nakushukuru kunipa nafasi kuchangia hii Wizara, ambayo kwa kweli ni Wizara nyeti, ni Wizara muhimu sana, ni Wizara ambayo kwa kweli inasimamia uhai wetu. Maana yake hali ya maji, isipokuwa nzuri hatuwezi kuwa na Kilimo kizuri, hatuwezi kuwa na hali nzuri ya hewa, hatuwezi kuwa na mazingira mazuri na kwa kweli hatuwezi kuendelea. Kwa hiyo, ni jambo la muhimu sana sana kuzungumza haya mambo ya maji na kuyazungumza katika hali ya umakini wa hali ya juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba nimemsikiliza Waziri vizuri, nimesikiliza Kamati na bahati nzuri niko kwenye Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji, kwa hiyo nafahamu vizuri, niseme kwa kweli, kwamba bado hatujawa serious vya kutosha katika kuwekeza katika maji, kwa sababu ukiangalia tu kitakwimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi asilimia 51 ambazo tunazizungumza, tunazungumza bilioni 106 ambazo ni fedha zinatokana na ule mfuko wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika fedha za ndani, za vyanzo vingine ambazo ni bilioni 284, tumetoa bilioni 48 tu sawa na asilimia saba. Sasa ni vizuri Wabunge wakaelewa, na mtu mwingine yoyote anayeona kwamba tuna tatizo kubwa la maji, akaelewa kwamba hatuko serious kiasi hicho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kama tumetenga pesa, halafu tunatoa asilimia saba, tunataka tufanye maendeleo ambapo viwanda vyetu vinategemea maji. Chakula chetu kinategemea maji, mazingira yetu yanategemea maji, hali ya hewa inategemea maji, halafu tunatoa asilimia saba we are not serious. Kwa hiyo nafikiri tuna tatizo hapa la vipaumbele vyetu, kupanga ni kuchagua najua kuna matatizo makubwa mengi, ambayo tunataka kufanya, lakini tunalinganisha maji na nini? Katika nchi hii? Ni kwa nini hatuwekezi kwenye maji vya kutosha? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sana, kwamba Waziri akija hapa na kwenye ukurasa wa 22 wa kitabu chetu hiki cha Kambi Rasmi ya Upinzani, tumesema fedha ya nje imetoka asilimia nne, ni kwa sababu randama inasema hivyo. Kwa hiyo, na Waziri akija hapa tumuombe, hizo bilioni 188 za nje, hata kwenye Kamati, kwa kweli hazikuletwa wakati huo. Kwa hiyo, aje atuambie zimetoka wapi? Na zimekwenda kufanya nini kwenye hiyo miradi ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoka hapo na mbaya zaidi, leo pamoja na kwamba changamoto za maji zimeongezeka, lakini bajeti ya maji inapungua. Mwaka jana kwenye hii bajeti tunayoimaliza sasa hivi, tulikuwa na bilioni 673 kwa ajili ya maendeleo, safari hii ni bilioni 610 zaidi ya asilimia nane drop kwa hiyo unaweza ukaona, kwamba ni tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa takwimu zenyewe za Waziri hapo, inaonyesha kwamba nchi yetu sasa hivi iko kweye red line, kwenda kwenye nchi ambazo zina uhaba mkubwa wa maji duniani. Kwa sababu kiwango cha chini, ni meta za ujazo, 1,700 kwa mtu mmoja kwa mwaka. Leo sisi tuko kwenye 1,952 ukilinganisha na mwaka wa 1962 tulivyopata uhuru, tulikuwa 7,000 na kitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaweza kuona ni namna gani, tunaenda kwenye danger zone kwa hiyo nilikuwa naomba sana, kwamba tuendelee kufanya jitihada. Sasa watu wamezungumza hapa, kwamba miradi inaenda kwa kusuasua na Serikali inachangia sana, wakati tunafanya ziara, tulikuta miradi haitekelezwi kwa sababu unakuta mahali ambapo kuna mradi unatekelezwa, mradi mkubwa mzuri unaohitajika sana lakini unaambiwa kwamba vifaa viko bandarini toka mwezi wa kumi na mbili mpaka mwezi huo wa nne ambapo tulikuwa tunapita kwenye hizo ziara havijatoka, kwa sababu msamaha wa kodi haujatolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini waliosaini Mkataba na wakasema kwamba kutakuwepo na msamaha wa kodi ni Serikali yenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Serikali saa nyingine inajishika mashati, tunaomba wafanye coordination na Mheshimiwa Jenista yuko hapa, awaratibu hao watu wake, ili tusije tukakutana kutana na hivyo vitu vya aina hiyo kwa sababu implication zake ni kubwa, miradi inachelewa na gharama zinapanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba sana, hilo lizingatiwe, niende Moshi, kule kwenye Halmashauri ya Moshi, tunaambiwa kwamba hali yetu ya maji ni nzuri, nataka niseme hali si nzuri, kwa sababu hiki kinachosemwa ni pamoja na miradi ambayo ilijengwa miaka ya sabini wakati wa Lucy Lameck wanasema bado inafanya kazi. Ukienda kule kwenye Kata kadhaa, Kata ya Kimochi, ukienda kule old Moshi, ukienda kule uru, (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo vyanzo vyenyewe vya maji vilishakauka. Kuna mito ambayo ndiyo ilikuwa ina kuwa source ya maji ilishakauka, kuna chemchem nyingine hazipo tena, mabomba yamechakaa, kwa hiyo, niombe sana, kwamba kama alivyozungumza, Mbunge mmoja hapa ifanyike review tuweze kujua hali halisi ya upatikanaji wa maji ukoje na tusipofanya hivyo tunajivuna leo kwamba tuna bajeti kubwa ya afya ni kwa sababu watu wanaugua sana, na magonjwa mengine yanasababishwa na kutokuwa na maji salama. (Makofi)

MHE. JOHN W. HECHE: Sixty percent ya …

MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Moshi, kuna, na nitoe pongezi sana kwa Mamlaka ya maji pale Moshi, inaitwa MUWASA, inafanya kazi nzuri. Lakini niwaombe sana Wizara, kwamba kuna madeni makubwa wanadai, Majeshi yetu, Chuo cha Polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanadai Magereza zaidi ya bilioni mbili, walipwe hizi fedha. Ili waweze kufanya huu ukarabati ninao uzungumza, waweze kupanua maeneo mengine kupeleka maji. Tunao mradi mmoja sasa hivi ambao unatekelezwa kule, Kata ya mabogini, tunahitajia kama bilioni 1.8. Waziri ameshaniahidi kwamba wanapeleka hizo hela. Nakuomba sana Mheshimiwa Waziri, hizo fedha ziende na tusingekuwa na tatizo kiasi hicho kama hizi fedha zetu ambazo Mamlaka yetu imeshatoa service kwa Serikali yenu halafu hamlipi? Kwa hiyo niwaombe sana kwamba mpeleke hizi fedha ili hiyo miradi iweze kutekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema kwamba Kamati imeshauri, Kamati yetu ya Kilimo, Mifugo na Maji imeshauri kwamba ni usanifu wa miradi inavyofanyika iwe comprehensive iwe inazingatia mambo yote ya muhimu kuwepo na provision kwa ajili ya maji taka. Kuwepo na provision kwa ajili ya fidia, kuwepo na provision kule maji yanakopita. Wale, hata kama haijengwi sasa hivi, lakini designing izingatie hilo. Ili kule maji yanakopita, kwa mfano tumeenda kule Arusha, kuna mradi ambao unatoka Jimbo la Siha kilomita 64 kwenda Jimbo la Longido, hapo katikati kuna watu wana uhitaji mkubwa wa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hakukuwepo na provision yoyote kwa ajili ya kuwapa maji kwa ajili ya mifugo, na kwa ajili ya matumizi ya binadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake ni kwamba huu mradi utakuwa hatarini siku zote, lakini ukienda pale Arusha Mjini kuna mradi mkubwa unatekelezwa, lakini ukienda kuangalia ni namna gani, design imezingatia land acquisition na kule mabomba ya maji taka yatakapopita unaona bado kwamba watu wana jikanyaga kanyaga. Ndiyo maana unakuta kwamba miradi mingi inaanza, lakini kwenye process unaambiwa kwamba usanifu ulikosewa na sasa mradi umepanda kutoka bilioni fulani mpaka bilioni fulani, sasa ili tuondokane na hilo nafikiri ushauri wa Kamati uzingatiwe. Lingine ambalo tuliliona ni Kampuni moja kupewa miradi mingi kwa wakati mmoja, na matokeo yake, kunakuwepo na visingizio mbalimbali katika kuitimisha hiyo miradi na hili tatizo tuliliona pale Arusha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa hiyo tuwaombe sana Mheshimiwa Waziri na watu wake, wafuatilie mambo kama hayo na wahakikishe kwamba hayajirudii. Nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii ambayo ni muhimu sana katika ustawi wa taifa letu kwa sababu tukiwa na tukiweza kufanya biashara vizuri, tunaweza tukafanya mambo mengine mengi ya kijamii na tukaweza kwenda vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze alikoishia ndugu yangu Mheshimiwa Mashimba Ndaki, ambaye tumesoma darasa moja kwamba ili tulinde viwanda vyetu, ni lazima tuwe na mazingira yanayotabirika. Katika nchi yetu, tuna tatizo kubwa sana la mazingira ya biashara yasiyotabirika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi huu uliopita tu, TRA walitoa tangazo la kupiga marufuku vinywaji vyote ambavyo havina stika ya kieletroniki kwamba ikifika tarehe 30 ya mwezi uliopita, hivyo vinywaji vyote vitakuwa vimekoma na havitakuwa na thamani tena. Hiyo marufuku inavyofanyika sijui walizingatia nini kwa sababu hivyo vinywaji vilinunuliwa katika utaratibu wa kisheria na vina stika ambazo zinatambulika na vimeshasambazwa katika nchi nzima. Maana yake vinywaji hivi vinapatikana Dar es Salaam, vinakwenda kwenye jimbo fulani, labda la ndugu yangu Mlimba kule Ifakara, sasa unavyowaambia unawapa siku chini ya 30 kwamba wavirejeshe vyote viweze kupata stika nyingine na wasipofanya hivyo, hiyo biashara itakuwa imekoma, kwa kweli ni kitu cha ajabu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Naibu Waziri nilimweleza na amelifanyia kazi. Katika hali ya namna hiyo, inatupa shida na ndiyo maana biashara inasinyaa kila kukicha katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, kuna masuala haya ya kurejesha VAT. Tumeambiwa hapa kuna burden ya zaidi ya shilingi bilioni 45, sasa ni nani anakuja kuwekeza hapa wakati hana uhakika wa kuridishiwa kile ambacho kiko kwenye mkataba? Kwa hiyo, katika hali kama hii, inatupa shida sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mazingira ya kufanya biashara ni magumu sana. Ndugu yangu Mheshimiwa Bashe alisema jana kuhusu habari ya kuanzisha kiwanda cha kusindika maziwa. Leo tunavyozungumza, nchi yetu inazalisha maziwa lita bilioni 2.4 kwa mwaka lakini maziwa tunayosindika ni lita kama milioni 37 tu. Hii ni kwa sababu ya mlolongo wa kodi ambazo zipo, jana Mheshimiwa Bashe alisema ni 26, mimi ninalo andishi hapa, ni tozo na kodi 28. Taasisi au mamlaka ambazo zinakwenda kushughulika na wewe siku ukiamua kuanzisha kiwanda cha kusindika maziwa ni 11 na taasisi moja inaweza ikarudi hata mara nne kwenye hiyo biashara yako.

Mheshimiwa Naibu Spika, wenzetu wa Kenya, leo wanazalisha maziwa lita bilioni tano kwa mwaka, wanasindika zaidi ya lita bilioni tano kwa mwaka. Leo Uganda wanazalisha lita bilioni 2.4, wanasindika zaidi ya lita laki tano kwa siku, sisi tuko kwenye laki moja na elfu hamsini.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ndugu zangu ili uanzishe kiwanda cha kusindika hapa Tanzania, unapashwa ulipe zaidi ya shilingi milioni 33 ndiyo kiwanda kianze kuzalisha. Sasa tunang’ang’ania milioni 33 lakini tunapoteza ajira na kodi ambazo tunaweza tukazipata kwa kuwepo na viwanda vingi, tunapoteza mapato ambayo yanatokana na bidhaa zinazotokana na maziwa ambazo ziko zaidi ya 20. Sasa jamani, hii ni akili gani? Tumelogwa na nani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa hiyo hatutumii fursa ambazo tunazo ambazo tumepewa na Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye hoja ya tatu, nayo ni sakata la korosho. Nasi kwenye ukurasa wa 42 kwenye kitabu chetu cha Maoni ya Kambi ya Upinzani Rasmi Bungeni, tumesema watu wawajibike. Hapa nataka niwe very specific; na niliombe sana Bunge hili linisikilize na lichukue hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuliingia mkataba na kampuni inaitwa INDO Power ya Kenya. Siku tulivyoenda kuingia mkataba Serikali ilikwenda pale, Mawaziri kadhaa walikwenda pale akiwepo Waziri wa wakati huo wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi na Gavana wa Benki Kuu alikuwepo pale. Katika watu waliozungumza, Kabudi alizungumza, akasema Kampuni hii ina weledi, ina uzoefu, ina uwezo wa kifedha na hata huyo mmiliki wa kampuni hiyo alikuja kwa ndege binafsi ya kukodi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Gavana wa Benki Kuu akasema alifanya due diligence kuona kwamba kampuni hiyo ina weledi wa kutosha na uwezo wa kutosha wa kufanya hiyo biashara. Baada ya miezi minne, ile biashara, kama Watanzania walivyosema na Mheshimiwa Rais alisema, Watanzania siyo wajinga. Walisema hii kampuni ni ya kitapeli, haina uwezo huo. Waliandika kwenye mitandao. Baada ya miezi minne imeonekana kampuni ile haina uwezo, imeshindikana na ile biashara imekufa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi kweli Bunge hili linakubali Mheshimiwa Kabudi aendelee kubaki na Uwaziri wake, mtu ambaye kila kukicha anamdanganya na kumfanya Mheshimiwa Rais aendelee kupotoka hivi! Hapa duniani Rais wa nchi akilalamika, Rais wa nchi akilia, kinachoweza kumsaidia ni Bunge la nchi. Kama Bunge la nchi likishindwa, basi tunamuachia Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri tusifike hapo ndugu zangu, Bunge lako Tukufu lichukue hatua ili hawa watu wawajibike. Kabudi; na ningefurahi sana angekuwepo hapa; Kabudi, mnakumbuka masuala…(Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Komu, ni Mheshimiwa.

MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Profesa Kabudi, nafurahi kama angekuwepo hapa, kwa sababu mnakumbuka issue ya makinikia, mnakumbuka issue ya Sheria ya PPP, mnakumbuka issue ya sheria ya kulinda rasilimali za nchi hii, mnakumbuka issue ya Sheria ya Takwimu; haya mambo yana utata. Kwa hiyo, naliomba Bunge hili lichukue hatua dhidi ya Kabudi, awajibike. Hawa wengine ndugu zangu hapa akina Kakunda, Mheshimiwa Japhet Hasunga, hawa ni watu ambao wako kwenye basi tu, lakini anayeendesha hili basi, ni Kabudi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana, tusije tukamfanya Rais wetu aonekane kwamba ni mtu tu ambaye analialia jambo ambalo siyo heshima kwa Bunge hili na siyo heshima kwa Watanzania walio...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, nitoe shukrani kwa ujenzi wa miradi miwili iliyosimamiwa na MUWASA katika Jimbo la Moshi Vijijini, ule wa Mang’ana ulionufaisha vijiji vya kata ya Uru Kusini na Uru Kaskazini na ule wa Kaloleni unaonufanisha vijiji vya kata ya Mabogini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji aliahidi kupanua miradi ya MUWASA ili vijiji vilivyobaki katika kata ya Mabogini viweze kunufaika vyote yaani Mtakuja, Msarekia, Muungano na Remiti. Aidha, kata ya Kimochi sehemu kubwa ya miundombinu ya maji ni ya miaka mingi sana na imechakaa sana, inahitaji ukarabati na mahali pengi kujengwa upya. Tunahitaji Serikali kuja kufanya tathmini na kuchukua hatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa Mbokumu unaohudumia vijiji vya Tema, Kiwalaa na Korini Kusini na Kaskazini umekamilika lakini kuna malalamiko mengi sana juu ya kiwango cha ubora wa kujengwa kwake. Naomba Wizara ije ione ukweli huu na kuchukua hatua kwa kuwa mradi huu haufanyi kazi vizuri. Maji mengi bado yanapotea njiani na virura vingi havitoi maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho tunahitaji Wizara kuonesha kuunga mkono mifereji yetu ya asili katika vijiji vyetu vyote vya Moshi Vijijini kwani mingi inahitaji ukarabati mkubwa kidogo ambao wananchi wenyewe hawawezi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. ANTHONY C. KOMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wote katika Wizara hii kwa kazi wanazozifanya katika mazingira mazuri kutokana na kutokuwa na rasilimali za kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mazingira ni suala la kufa na kupona kutokana na umuhimu wake kwa viumbe vyote duniani ikiwa ni pamoja na sisi binadamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu haijatoa uzito unaostahili kibajeti kwa eneo hili. Nichukue fursa hii kuiomba Wizara kufuatilia maombi yangu ya mara kwa mara ya kuja Jimboni kwangu kuona athari mbalimbali zinazosababishwa na mabadiliko ya tabianchi ukanda wa tambarare katika Kata za Arusha Chini, Mabogini, Old Moshi Magharibi na Kahe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri yetu imefanya jitihada na kupata mshirika toka Ujerumani Jiji la Kiel ambalo linatusaidia sana kufanikisha mradi wa mazingira wenye lengo la kurejesha miti ya asili ambayo ni rafiki wa mazingira katika eneo letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana Mheshimiwa Waziri aje aone jitihada hii, aitambue na Serikali ione jinsi ya kuchangia na kupanua mradi huu kuhusu manufaa ya maeneo mengine katika Taifa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Spika, naomba nami nichangie hotuba ya Waziri wa Mambo ya Ndani kutokana na umuhimu wake katika suala zima la usalama wa raia na mali zetu.

Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri amesema katika vipaumbele vya Wizara yake ni kuhakikisha amani na utulivu unaendelea katika nchi yetu na kuhakikisha kuwa wanajitosheleza kwa chakula kupitia miradi inayoendeshwa chini ya Jeshi la Magereza. Haya ni malengo mazuri sana na ya kuungwa mkono lakini ni lazima ukweli huu hapa chini uzingatiwe.

Mheshimiwa Spika, moja, amani na utulivu ni tunda la haki na uzingatiaji wa sheria kwa kila mtu yaani watawala na watawaliwa, raia na viongozi. Suala la kuzuia mikutano ya hadhara na sasa karibu shughuli zote za kisiasa za wanasiasa ni uamuzi usio sahihi, wa haki na wala siyo wa kisheria. Hii inaweza kuwa sababu ya uvunjifu wa amani siku za baadaye. Ni vyema Jeshi letu la Polisi likatumia weledi wake kuhakikisha shughuli za kisiasa zinafanyika kulingana na sheria na mtu mmoja mmoja anayetumia fursa hii vibaya achukuliwe hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Spika, hivi majuzi nimeona katika vyombo vya habari Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara akitoa maelekezo na vitisho kwa OCD wa Tarime eti awakamate Wabunge wa CHADEMA waliofanya mkutano wa hadhara huko Tarime Mjini na kama hatawakamata basi aondolewe mara moja katika nafasi yake. Hii inatia mashaka sana kauli kama hizi zinapoachwa bila ukemeaji wowote kutoka kwa Waziri mwenye dhamana. Naomba atakapokuja kuhitimisha na hili alitolee maelezo na kukemea tabia hii ili Jeshi letu liendelee kuaminiwa na kuheshimiwa na watu wote.

Mheshimiwa Spika, mbili, pawepo na ushirikiano wa karibu baina ya Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Katiba na Sheria na Idara ya Mahakama juu ya uwepo wa mahabusu wengi ambao kwa sababu mbalimbali wanakaa katika magereza yetu kwa muda mrefu bila mashauri yao kuamuliwa au hata kuanza kusikilizwa tu. Masuala kama haya yanatumia gharama nyingi sana za jeshi letu mfano chakula, magari, rasilimali watu na hata hali ya afya ya mahabusu wenyewe kutokana na msongamano wa mahabusu wa aina hiyo.

Mheshimiwa Spika, hotuba ya Mheshimiwa Waziri imeeleza katika ukurasa wa 11 na 12 jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali kukabiliana na uhaba/uchache wa Vituo vya Polisi na nyumba za askari. Katika Jimbo la Moshi Vijijini, sisi wananchi wa Jimbo hili, Kata za Uru Kusini, Shimbwe, Uru Kaskazini na Uru Mashariki wamejenga kituo kikubwa cha kisasa sana cha Class ‘C’ na kimekamilika. Nilishamuarifu Mheshimiwa Waziri juu ya kukamilika kwa kituo hiki nikimuomba aje kukipokea na kutambua mchango wa wananchi hawa wa zaidi ya Sh.100,000,000. Naomba wakati Waziri atakapokuja kuhitimisha hoja yake atuambie ni lini atakuja kupokea kituo hiki.

Mheshimiwa Spika, kwa maombi yangu kwa niaba ya wananchi ninaowawakilisha TANAPA (KINAPA) wameunga jitihada hizi za wananchi na kujenga nyumba kwa ajili ya askari watakaohudumu katika kituo hiki, nayo imekaribia kukamilika. Jitihada kama hizi zilishafanyika pia katika Tarafa ya Kibosho ila sasa uhudumiaji wa kituo hicho ambacho kilijengwa katika Kata ya Okaoni leo kinahitaji ukarabati na huduma nyingine kama gari la uhakika kutokana na ukubwa wa eneo linalohudumiwa na kituo hicho.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Spika, kwanza nipongeze uongozi mzima wa Wizara kwa jitihada wanazofanya kukabiliana na changamoto mbalimbali katika sekta ya kilimo pamoja na ufinyu wa raslimali walizonazo.

Mheshimiwa Spika, ili tuweze kufanya mapinduzi ya kilimo katika Taifa letu ni lazima tuamue kama Taifa kwa makundi kuwekeza vya kutosha katika kilimo na hususani katika Nyanja ya umwagiliaji.

Mheshimiwa Spika, katika Jimbo langu la Moshi Vijijini kwa miaka mingi tulishaingia katika kilimo cha umwagiliaji na kwa bahati nzuri tulipata mradi mkubwa wa umwagiliaji kwa ushirikiano na nchi ya Japan Mradi unaoitwa Moshi Irrigation Scheme. Mradi huu umekuwa ni mkombozi mkubwa kwa watu wetu hasa katika Kata za Mabogini, Arusha chini na Old Moshi Magharibi.

Mheshimiwa Spika, mradi huu sasa unakabiliwa na changamoto kuu tatu.

(i) Maji hayatoshi hivyo zinahitajika fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu iliyopo katika mradi huu kuepusha maji mengi kupotea na kulinda vyanzo vya maji hayo.

(ii) Wakulima wa mpunga katika mradi huu wameunda ushirika wao na kwa muda mrefu wamekuwa wakiomba wakabidhiwe vifaa vilivyoachwa wakati wa kuanzishwa kwa mradi huu ikiwa ni pamoja na mashine ya kukoboa mpunga mpaka leo hawajakabidhiwa mashine.

Mheshimiwa Spika, naomba Waziri afanye kila linalowezekana wakulima hawa wajibiwe kilio chao.

Mheshimiwa Spika, changamoto ya tatu ni barabra inayoingia katika mradi huu inayoitwa Funga Gate – Mabogini – Chekereni – Kahe; kipindi kirefu cha mwaka barabara hii haipitiki kabisa jambo ambalo linaathiri sana ustawi wa mradi huu.

Mheshimiwa Spika, katika mpango wa kuendeleza kilimo awamu ya pili zipo fedha zilizoainishwa kwa ajili ya kuboresha miundombinu katika miradi ya umwagiliaji. Naiomba Wizara iratibu vizuri fedha hizi na kwa kushirikiana na TARURA ili barabara hii iweze kutengenezwa ikiwezekana kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mifereji ya asili huko nyuma imekuwa ikisaidiwa katika ukarabati wake na Serikali kupitia Ofisi ya Kanda ya Tume ya Umwagiliaji. Kwa muda mrefu support hii imekoma matokeo yake ni kwamba mifereji mingi imeanza kufa jambo ambalo ni hatari sana kwa ustawi wa watu wa Moshi Vijijini. Mifereji kama Makeresho wa Kata ya Kibosho Magharibi, mfereji wa Makupa, Metro na mingine mingi karib kata zote 16 inahitaji ukarabati mkubwa.

Mheshimiwa Spika, naiomba sana Wizara irejee utaratibu wake wa zamani wa kusaidia mifereji hii kwa kuwa mahitaji ya sasa wananchi hawawezi kuyamudu kwa nguvu zao wenyewe.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuwapa pole sana viongozi na watendaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kazi kubwa wanayofanya pamoja na changamoto za rasilimali kidogo. Naiomba Wizara hii muhimu kwa uchumi wetu ione umuhimu wa kutembelea Jimbo la Moshi Vijijini kwa ajili ya kutambua vivutio vya utalii katika Kata za Old Moshi Mashariki na Uru Mashariki (Materuni) ambapo kuna maanguko ya maji (water falls) ya ajabu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, vivutio hivi havijaweza kuwa vyanzo vya maana vya mapato kutokana na miundombinu ya barabara na vyoo kuwa mbaya sana. Nikilinganisha na vyanzo vya aina hiyo mahali pengine duniani naona kinachokosekana kwetu ni matangazo na kuboresha miundombinu tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, niombe Wizara ikaone mti ulio katika Kata ya Mbokomu ambao ni mrefu kuliko yote Barani Afrika na wa sita duniani. Watu toka sehemu mbalimbali duniani toka ugundulike wamekuwa wakiutembelea, jambo ambalo linaweza kusababisha madhara kwa mazingira ya eneo hilo, hasa uoto wa asili ikiwa hapatakuwepo na utaratibu wa kuuendea mti huo na hifadhi yake. Mti huu unaweza kuwa chanzo cha mapato pia.
Muswada wa Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira wa Mwaka 2018
MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru sana kwa kunipa nafasi kuchangia muswada huu ambao kwa hali halisi ni muswada muhimu kwa sababu unashughulikia jambo ambalo siku zote tumekuwa tukiambiwa maji ni uhai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kazi kubwa ambayo ilifanya na Kamati kupitia muswada huu na niishukuru sana Serikali kwamba ilikubali lile jina waliloleta RUWA kubadilika kuwa RUWASA kama sisi tulivyokuwa tumependekeza kwenye Kamati na sababu kubwa ya kuweka lile neno sanitation liweze kuonekana ni ili kuanzia kwenye jina watu wajue kwamba suala la kujenga miundombinu au kuweka fursa ya kujenga hiyo miundombinu baadae wakati wanasanifu mradi wowote wa maji ni jambo la muhimu na la msingi sasa. Kwa sababu kama alivyosema ndugu yangu Mheshimiwa Jitu Soni, kumekuwa na zana potofu kuwa kijiji hakuhitajiki sana hiyo miundombinu, lakini baada ya muda fulani hivyo vijiji vinabadilika kuwa miji na matokeo yake tunakuja kukumbana na bomoa bomoa kwa sababu ya kutokuzingatia mambo kama haya wakati tunasanifu miradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende kwenye zana hii nzima ya umuhimu wa RUWASA na hapo niungane na maoni Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni pale waliposema kwamba kuanzisha tu wakala hakutoshi ni lazima tuangalie ni kwanini hizo changamoto ambazo Waziri amezizungumza hapa kwenye hotuba yake kwamba miradi imekuwa ikijengwa lakini baada ya muda zile mamlaka kule chini au zile bodi za watumia maji kushindwa kuihudumia na kuiendeleza ile miradi imekuwa ikifa. Sasa kuanzishwa kwa huu wakala maana yake ni lazima kuwe na tofauti, ninachojiuliza ni kwamba tofauti itatoka wapi kama hatuta ongeza rasilimali kwa maana ya fedha, kwa maana ya vitendea kazi, kwa maana ya watendaji ambao wenye weledi waende kule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama tutafanya kama tulivyofanya TARURA uchukue ma-engineer wale waliopo pale Halmashauri uhamishe ukawafanye kuwa independent entity halafu usiwaongezee kitu chochote maana yake bado kunaweza kuwa na hata tatizo kubwa zaidi kuliko hata tulilokuwa nalo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nasema kama hayo yatafanyiwa kazi basi sioni shida yoyote tunaweza kwenda vizuri. Na tatu ni ushirikishwaji wa Serikali za Mitaa kwenye Ibara 48 kuna mambo mengi yameanishwa pale kwa kweli niipongeze Serikali kwa hiyo hatua kwa sababu tofauti na wakati ule tunaanzisha TARURA angalau hapa kuna
mwelekeo ambao umetolewa kwa namna fulani halmashauri zinaweza zikapata ushirikishwaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukienda kwenye Ibara ya 49 unaona nguvu zimetolewa zaidi yaani ulazima wa kutoa taarifa na mipango umetolewa zaidi kwenye DCC na RCC ambavyo ni vyombo tu vya mashauriano na hata muda wake wa kukutana ni mara chache sana katika mwaka na wakikutana wanakutana kwa muda mfupi na wanakuwa hawana ufahamu wa kutosha kwenye haya mambo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Serikali ianglie uwezekano wa kufanya ni lazima mipango ya wakala hii na maendeleo ya utekelezaji wa shughuli zake yatolewe kwa lazima kama taarifa kwenye Mabaraza ya Madiwani ambao ndio wenye watu, ndio ambao wana maslahi mapana kwenye masuala mazima ya maji kule chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimeleta hapa amendment ambayo na ninafikiri Serikali itaizingatia na nitawaomba Wabunge kama ikibidi tushirikiane kwenye hili ili tuweze kuweka mambo yakaenda vizuri na hapa nirejee, nilikuwa namsikiliza Mheshimiwa Rais akiwa anazungumza kule Chato na Baraza na Madiwani aliwaambia kwamba ni lazima wazimamie kikamilifu rasilimali za Halmashauri. Sasa sioni itawezekanaje hii azma ya Rais kama hatutawapa/ hatutafanya hizi wakala zikawa na ulazima wa kupeleka taarifa kule kwa sababu kuna msemo wa kingereza unasema information is power, sasa ukishawanyima watu hawa uwezo wa kupata habari itakuwa shida kuweza kufanya hayo ambayo Rais anatamani yafanyike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo lipo kwenye hotuba ya Mheshimiwa Mgimwa - Mwenyekiti wa Kamati ni kupitia sheria nyingine hasa ile Sheria ya Usimamzi wa Rasilimali za Maji Sheria Na. 11 nafikiri ya mwaka 2009. Kuna mambo mengi ambayo yameshapitwa na wakati, kwenye sheria za nchi hii kuna sheria inasema ukitaka kuvuna maji ya mvua kama unavuna zaidi ya lita 20,000 unapaswa uwe na kibali maana yake ukivuna maji zaidi ya lita 20,000 na ukaja, huyo mtu mwenye mamlaka ya kutoa hicho kibali akaja akakukuta umefanya hivyo maana yake utakuwa umetenda kosa na unaweza ukawajibishwa. Sasa sheria za namna hiyo zimeshapitwa na wakati lazima zinagaliwe upya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisikiliza juzi juzi Mheshimiwa Rais alikuwa anazungumzia kufanya shughuli za kibinadamu kwenye ule upana wa mita 60 kwenye vyanzo vya maji. Ni kweli kwamba ile sheria inapswa ingaliwe upya kwa sababu mito ambayo inapita mjini hivi kweli bado tunahitaji mita 60 kwa ajili ya shughuli za kibinadamu kwa hiyo kuna mambo kama hayo ya kufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna makatazo mengine hata kwenye hii sheria bado yapo ambayo kwa kweli Serikali inapaswa ingalie kwa mfano pale wanaposema kwamba zisifanyike shughuli ambazo ni za kujenga miundombinu kwa ajili ya matumizi labda ya bustani au domestic use. Sheria za aina hiyo ni very conservative, zinafanya watu washindwe kufanya maendeleo ambayo kweli yanandaena na mahitaji na sayansi au maendeleo ya kisayansi yaliyopo leo.

Kwa mfano kuna mahali nimeona kwenye sheria hii wanasema kwamba mambo anaweza kufanya bila ruksa, maana yake kuchimba kisima ambacho kinachimbwa kwa mkono hicho ndicho ambacho hakiruhusiwi (shallow hand dig dam wealth) hicho ndicho kinaruhusiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwenye karne hii tunazungumza habari ya kujenga visima kwa kutumia jembe la mkono! Maana yake leo nikienda nikajenga kisima pale nyumbani kwangu ambacho nimetumia labda nimeleta bulldozer au greda au excavator nikachimba kwa sababu nimetumia kitu ambacho sio kwa kutumia mkono maana yake inaweza ikaonekana kwamba nimefanya kosa na nikahukumiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo kama haya ni mambo ambayo ninaiomba sana Serikali na Bunge lako yatizamwe na kuondolea vitu vya namna hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna masuala yanayohusu fidia, masuala ya fidia hayajapewa uzito ambao unastahili. Kwa hiyo, sisi kwenye Kamati na hata kwenye hotuba ya Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani jambo hili limesisitizwa na ninaiomba sana Serikali ione kwamba ni jambo la muhimu. Kwa sababu tusipofanya hivyo hawa ma-engineer wetu na wataalam wetu wanavyosanifu hiyo miradi na kwenye vichwa vyao vikaonekana vikawa havikumbushwi kwamba kuna suala la fidia ndipo hapo ambapo unakuta kwamba watu wanaleta mradi na wakishaleta mradi wanasema Serikali Kuu itakuja kufidia au mfadhili atakuja kufidia au hakuna fidia. Jambo hili kwa kweli linakuwa si sahihi hata kidogo na si haki kwa wale ambao wanafanyiwa vitu vya namna hiyo. Kwa hiyo niombe sana, suala la fidia liwe ni suala ambalo ni la lazima na lizingatiwe tangu wakati wa usanifu wa mradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo limezungumzwa vilevile na wachangiaji walionitangulia ni kuhusu suala la tafsiri ya matumizi mabaya ya maji. Tuliomba sana kwenye Kamati kwamba tafsiri ya matumizi mabaya kwenye maji itolewe na iwekwe kwenye sheria ili wale maofisa ambao wanahusika na kusimamia hizi rasilimali za maji waweze kuongozwa vizuri katika kulishughulikia jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona maeneo mengine maofisa wanaohusika wakikuta tu vijana wanateka maji na wanatumia kuoshea magari wanaambiwa wanafanya matumizi mabaya ya maji na wanapewa adhabu ambazo ni za ajabu kabisa, adhabu ambazo zinaweza zikalinganishwa na mtu ambaye anateka maji ya kwenda kufanya irrigation. Kwa hiyo kukwepa mambo kama hayo ni vizuri kungekuwepo na tafsiri na hiyo tafsiri iwekwe kwenye sheria ili kila mmoja aweze kuongozwa na hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusu hii dhana ya kutoruhusu kujenga miundombinu kwenye vyanzo vya maji. Wanasema kwamba hata kama unatumia maji kwa ajili ya matumizi labla ya nyumbani, yale ya kibinadamu, lakini ukiteka hayo maji kwa kutumia miundombinu ambayo imejengwa maana yake ni kosa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hii dhana nayo inadumaza maendeleo kwa watu wetu. Kwa sababu inawezekana kwamba mimi nina bustani, lakini nina pump, badala ya kuchota maji kwa ndoo na kwenye kichwa kutoka kwenye mto ninaweka pump pale nachota maji namwagia ile bustani ambayo inaeleweka kwamba ni bustani inahitaji labda ndoo kumi au lita 200; nikafanya hiyo kazi na nikaifanya kwa muda mfupi na kwa ufanisi mkubwa nikaondoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mtu mwingine akienda kuchota kwa wheel barrow, akachota lita 1000, kwa sababu tu hajajenga miundombinu hata kuwa ametenda kosa, lakini mimi ambaye nitatumia pump nikachota lita 200 nitakuwa nimefanya kosa. Sasa dhana kama hizi ninafikiri zinadumaza watu wetu na matokeo yake ni kwamba tutaendelea kurudi nyumba badala ya kwenda mbele. Kwa hiyo, niiombe sana Serikali kwamba na hili ilizingatie ili liweze kupata usahihi katika maendeleo ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo niseme ninaunga mkono sana hotuba na maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na ningeiomba sana Serikali iyazingatie kwa sababu ukweli ni kwamba sisi ni kioo chenu na kama unataka kupendeza ni vizuri ukajiangalia kwenye kioo kabla ya kutoka. Kwa hiyo, Mheshimia Waziri kabla ya kutoka na hii sheria ni vizuri ungetizama mara mbili mara tatu maoni haya ili ukatoka ukiwa uko vizuri zaidi wale ambao wanataka kukutakia mambo mabaya wakute kwa kweli tayari umeshawa pre-empt. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo baada ya kusema hayo nakushukuru sana. (Makofi)