Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Prof. Jumanne Abdallah Maghembe (4 total)

MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake. Wizara ya Nishati imesema mara nyingi ndani na nje ya Bunge kwamba katika vijiji ambavyo vinahusika na mradi wa REA watu wote walioko kwenye vijiji hivyo, hata wale ambao nyumba zao ni za majani watapewa umeme. Hata hivyo, katika utekelezaji wa miradi hii Awamu ya Kwanza na Pili katika Wilaya ya Mwanga ni familia chache sana zilizokuwa zimejitayarisha kupewa umeme ambazo zimefungiwa umeme huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeambiwa kwamba nia yake ni kuipa TANESCO biashara ya kuzifungia kaya hizo umeme kwa Sh.177,000/= baada ya mradi kukamilika. Je, sera hii tuliyotangaziwa hapa imefutwa lini ikaja hii ya TANESCO kuchagua watu wachache kuwapa umeme na wengine kuwaacha? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, tuliambiwa kwamba, mkandarasi huyu ambaye ameshindwa kazi ya kusambaza umeme pale awali hawezi tena kupewa kazi katika Wizara ya Nishati na Madini, hasa kazi ileile ambayo yeye alifukuzwa kwa kushindwa kutekeleza. Sasa katika Wilaya ya Mwanga aliyekuwa anatekeleza mradi huu kwa niaba ya SPENCON alikuwa bwana mmoja anaitwa Mrs. Njarita & Company Limited. Sasa Njarita huyo huyo amepewa kazi ya kutekeleza mradi huo kwa jina lingine la Octopus. Je, inatuambia nini au inawezaje kututhibitishia kwamba, huyu aliyeshindwa kutekeleza huu mradi huko nyuma, sasa ataweza kutekeleza round hii? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mheshimiwa Profesa Jumanne Abdallah Maghembe kwa maswali yake mawili ya nyongeza, lakini na kwa kazi nzuri anayofanya katika kufuatilia mahitaji ya nishati katika Jimbo lake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa kwenye ziara wiki iliyopita katika Jimbo la Mheshimiwa Maghembe, kukagua maeneo mbalimbali ambako mradi huu wa REA Awamu ya Pili haukufanyika vizuri, lakini utakubaliana na mimi kwamba, ni kweli kuna mahitaji makubwa na kwa kuwa, hizi kazi zinatekelezwa kwa mujibu wa scope na kwamba, scope ile inakuwa haikidhi mahitaji, lakini Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutambua hilo imekuja na Mradi Mpya wa Ujazilizi (densification).
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu unatekelezwa katika mikoa sita ya awali ya mfano. Ilipofika Mkoa wa Kilimanjaro na wao Mkandarasi Mshauri Elekezi yupo ndani ya mkoa ule kujaribu kufanya feasibility study kwa ajili ya mradi huu, densification kwa maeneo ambayo au kwa kaya ambazo hazijaguswa au taasisi za kijamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimthibitishie Mbunge hakuna ukweli wowote kwamba, zile kaya ambazo hazijaunganishwa nia ya kwamba, iipe kazi TANESCO.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TANESCO ni Serikali ambayo nayo ina kazi ya kusambaza umeme, lakini kwa utaratibu mwingine, lakini si kweli kwamba, kaya hazifikiwi kwa sababu ya kuipa kazi TANESCO. TANESCO itaendelea na kazi ya kusambaza umeme, lakini kama umeme vijijini na ndio maana Serikali imetambua uwepo wa ukubwa wa mahitaji imekuja na huo Mradi wa densification. Kwa hiyo, nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge zile kaya ambazo hazijaunganishwa, zile taasisi za umma ambazo hazijaunganishwa, zitaunganishwa kupitia mradi huu wa densification ambao umefanya vizuri katika Mikoa ya Songwe, Mbeya, Pwani, Arusha, Tanga, Iringa na Mara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ameeleza kwamba mbona mkandarasi yuleyule ndio amepewa kazi na kwamba, Wizara itathibitishaje kwamba kazi zitafanyika. Ni kweli kazi ilifanywa na Kampuni ya SPENCON ambayo ndio ilikuwa main contractor. Huyu Kampuni ya Njarita Octopus walikuwa Sub Contractor. Uchunguzi uliofanyika na Serikali na Wakala wa Umeme Vijijini ulithibitisha kwamba, tatizo lilikuwa kwa main Contractor mwenyewe ambaye ni Spencon si hawa Sub Contractor.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sambamba na hilo nilipokuwa katika ziara tulikuwa na Mkandarasi huyu Njarita na sisi tumempa maelekezo na masharti, ndani ya miezi sita kazi zile zilizoshindwa kufanywa zimalizike na zikamilike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati nzuri nilipokuwa eneo la tukio mkandarasi alikuwa ameshaanza kazi na niliwaomba viongozi wa maeneo hayo, Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya, Waheshimiwa Wenyeviti wa Halmashauri, pia nilizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mama yangu Anna Mghwira kwamba Ofisi yetu au Wizara yetu itasubiria taarifa za mara kwa mara za Mkandarasi huyu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Wakandarasi hawa waliopewa kazi hii tutawafuatilia kwa kila hatua kuona kwamba, makosa yaliyojitokeza awamu zilizopita hayajitokezi tena. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Spika, kwanza naishukuru sana Wizara na Waziri wa Nishati na Madini, kwa jibu zuri sana ambalo ametupatia.

Mheshimiwa Spika, nina maswali madogo mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, katika maeneo ambayo tayari yamepatiwa umeme kule vijijini, wako wananchi wengi sana ambao bado hawajapatiwa umeme kinyume na ahadi ambazo tumepewa hapa Bungeni kwamba kila mmoja atakayepitiwa na nguzo au waya za umeme na yeye atapata umeme. Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba hawa watu ambao wamepitwa bila kufungiwa umeme wanafungiwa umeme kama wenzao waliofungiwa awali?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, katika Tarafa yetu ya Jipe ambayo ina urefu wa kilomita 70 kuanzia mwanzo mpaka mwisho, viko vijiji viwili ambavyo bado havijahudumiwa na mradi wa REA ambavyo ni Vijiji vya Kwanyange na Karambandea. Serikali ina mpango gani wa kuvihudumia vijiji hivi na kuvipatia umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Profesa Jumanne Maghembe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri anayofanya katika Jimbo lake. Nilifanya ziara mwaka jana mwezi kama huu niliona namna ambavyo anashughulika na kero za Nishati katika Jimbo lake.

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza ni kwenye maeneo ambayo yamepitiwa na miundombinu ya umeme mkubwa lakini baadhi ya wananchi hawajapata kuunganishiwa umeme, napenda nimtaarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imepanga Mradi wa Ujazilizi Awamu ya Pili baada ya mafanikio ya Mradi wa Ujazilizi Awamu ya Kwanza.

Mheshimiwa Spika, Mradi huu wa Ujazilizi Awamu ya Pili ambao utaanza Machi, 2019 unahusisha mikoa tisa ya awali ikiwemo Mkoa wa Kilimanjaro lakini baadaye mwezi Julai, 2019 tutaanza Awamu ya Pili katika mikoa iliyosalia. Kwa hiyo, nataka nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba wananchi ambao hawajapata umeme katika vijiji ambavyo miundombinu ya umeme imefika kupitia Mradi wa Ujazilizi watafikiwa na huduma hii ya nishati.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili linahusiana na vijiji katika Tarafa ya Jipe ambapo Mheshimiwa Profesa Jumanne Maghembe, Mbunge wa Jimbo la Mwanga anasema bado havijafikiwa na miundombinu ya umeme. Nataka nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba licha ya Mradi wa Ujazilizi, Serikali pia kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeanza Mradi wa REA Awamu ya Tatu mzunguko wa pili ambapo upembuzi yakinifu umeanza na hivyo vijiji viwili vitafikiwa na miundombinu ya umeme baada ya mradi huo kuanza. Ahsante.
MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwanza ningependa kuwapa pole sana wananchi wa Machame na hasa familia ya Marehemu Dkt. Reginald Mengi kwa msiba uliowapata. Tunamuomba Mwenyezi Mungu aiweke roho haye mahali pema peponi.

Mheshimiwa Spika, sasa niulize maswali mawili ya nyongeza, kwanza, uhaba wa walimu 384 tumepewa walimu 21! Katika shule zetu, shule 50 zina walimu wawili wawili na shule zingine 40 zina walimu watatu watatu, sasa ujue hizo zingine ndiyo… na shule za msingi zina madarasa nane, darasa la awali na madarasa saba, kwa hiyo, hali iliyoko pale ni ngumu sana.

Mheshimiwa Spika, na kwa sababu uhaba huu umetokana na walimu kustaafu, kuhama na kufariki. Suala la fedha halipo hapa, kwa sababu nafasi zipo, na mishahara ipo, ni kwa nini sasa Serikali haichukui hatua ikaajiri bila kutumia visingizio ambavyo havina msingi.

Mheshimiwa Spika, pili, ni lini Serikali itabadilisha urasimu huu, kama mwalimu yupo na yuko kwenye ikama, na amestaafu. Kwa nini Serikali hairuhusu halmashauri ikaajiri kutoka kwenye soko mara moja ili kutoathiri upatikanaji wa elimu katika shule. Inaacha mpaka shule zinakuwa na mwalimu mmoja?

Mheshimiwa Spika, ahsante.

SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, Mwikwabe Mwita Waitara, maswali hayo muhimu sana, Mwanga upungufu wa walimu 300, Kongwa upungufu walimu 1000. Majibu tafadhali.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, ni kweli, tuna upungufu wa walimu wa shule za msingi 66,000 nchi nzima, na upungufu wa walimu wa sekondari 14,000, kwa hiyo, ni kweli kwamba kuna upungufu, ni jambo ambalo liko wazi.

Mheshimiwa Spika, lakini kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, hizi ajira mpya ni ajira za kuziba nafasi. Sasa hivi inayofuata ni ajira zile za kawaida za kila mwaka za kuongeza na kupunguza upungufu uliopo. Kwa hiyo, naomba niwahakikishie kwamba Serikali imeshaliona hili, tulifanya uhakiki, pamoja na watumishi hewa, waliofariki, waliofukuzwa kazi na wengine wamestafu na wengine wameacha kwa sababu mbalimbali. Kwa hiyo, hili ilikuwa ni kuziba nafasi hizi, sasa inakuja ya ajira za kila mwaka za kuweza kuziba kwa utaratibu wa kawaida na hili linafanyiwa kazi na Serikali inajua kwa kweli kuwa kuna upungufu mkubwa nchini wa walimu.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, ni kwamba, ni kuziba nafasi kwa maana ya kutoa kibali kwa halmashauri. Hizi ni ajira, cha muhimu hapa siyo kuruhusu utaratibu usioelekeweka utumike kuajiri walimu, kumekuwa na mambo mengi sana katika halmashauri zetu ambayo yanafanyika katika ajira hizi, kwa hiyo, tunajiridhisha kwanza. Lakini cha muhimu ni kwamba tumekubaliana kama Serikali kuchukua hatua mahususi kupunguza upungufu wa walimu shule za msingi na sekondari.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Spika, nimejibiwa, kwa kuwa nchi yetu itahitaji wanasayansi huko mbele tuendako, na hivi sasa tunavyojenga uchumi wa viwanda. Je, Serikali haioni kwamba hali tuliyonayo katika shule zetu za sekondari ambapo shule za Serikali zina walimu wazuri sana lakini hazina maabara na shule zile za binafsi zina maabara, walimu siyo wazuri kama wale wa Serikali, lakini watoto wale ndiyo wanafaulu mitihani. Serikali ina mpango gani hasa kuhusu kuwaandaa wanasayansi watakaoiendeleza nchi yetu huko mbele? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, nimeona fedha hapa vimetengwa, kwa ajili ya maabara, si maabara peke yake kama ulivyoona swali lenyewe. Nilikuwa nataka nimuulize Waziri, kati ya fedha hizi ni shilingi ngapi zitapelekwa Mwanga kwa ajili ya kusaidia wananchi kujenga maabara ya Msalagambo yale yaliyojengwa sasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, ni kweli Mheshimiwa Profesa ameuliza kwa uchungu na yeye pia ni mwanasayansi ni Profesa katika eneo hilo na tunatambua changamoto iliyopo ya masomo ya sayansi na hasa maabara, lakini niseme, fedha ambazo nimetaja hapa shilingi bilioni 58.2 ni mwaka wa fedha huu 2019/2020, lakini mwaka wa fedha uliopita tumepeleka fedha kwenye shule za sekondari 1964, lakini hapa tulipo tunafanya mchakato wa kupeleka tena fedha za vifaa vya maabara katika shule zetu zaidi ya 2000.

Mheshimiwa Spika, lakini ujue kwamba sisi sekondari za Serikali ni 3632, kwa hiyo tunaamini baada ya mpango huu kukamilika ndani ya mwaka huu mpaka 2020 karibu kila maabara itakuwa na vifaa vya kutosha katika eneo hilo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Profesa nimtoe wasiwasi kwa jambo hili na kwamba tumejipanga namna ya kufanya vuzuri, lakini tumeshatoa maelekezo, maeneo ambayo kuna upungufu wa maabara kuna namna njia mbadala zimefanyika ndiyo maana leo ukiangalia hata pale viwanja vya Jamuhuri kuna maonesho yanafanyika na walimu wetu wamefundishwa kufanya njia mbadala ili tuweze kufundisha watoto wetu kwa vitendo na ufaulu utakuwa unaongezeka kutoka mwaka hadi mwaka.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili la kuuliza, kama ulivyosema, kwamba sina data hapa lakini nadhani baada ya kipindi cha maswali na majibu ninaweza nikampa kumbukumbu, data kamili kwamba yeye katika eneo lake la Mwanga atapata shilingi ngapi katika shule aliyoitaja, ahsante.