Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Prof. Jumanne Abdallah Maghembe (31 total)

MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, utalii ili uweze kuendelea vizuri na uweze kuboresha Pato la Taifa ni pamoja na ushirikishwaji wa wananchi wanaoishi kando kando ya Hifadhi hizi za Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina mgogoro sasa hivi wa wafugaji zaidi ya ng‟ombe 5000 kwa vijiji vya Kijereshi na Nyamikoma katika Jimbo la Busega ambao wamekamatwa kwa sababu ya askari wa Game Reserves kuwasukumizia kwenye hifadhi ili waweze kutoza fedha hawa wafugaji. Hii mifugo ina zaidi ya siku tatu imefungiwa kwenye pori. Hivi kweli kama tunataka ushirikishaji mzuri na uhifadhi wa maliasili zetu.
Je, Serikali inachukua hatua gani sasa kuruhusu hiyo mifugo, kwa sababu ng‟ombe hawana tatizo, ili waweze kuachiwa…

MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu ni kwamba ninaomba tamko la Waziri wa Maliasili kuhusiana na mifugo hii ambayo imeingizwa kwenye hifadhi kinyume cha utaratibu na kwa nini imeendelea kufungiwa kule isiachiwe? (Makofi)
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa…

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Nakushukuru kwa kunipa nafasi kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Chegeni, Mbunge wa Busega, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, wanavijiji wanaopakana na Mbuga ya Serengeti katika eneo la Busega na vijiji hivyo ambavyo Mheshimiwa Mbunge amevitaja, wameingiza ng‟ombe zaidi ya 6000 katika eneo lao na ng‟ombe hao wamekamatwa na Askari. Jana usiku nimetoa maagizo kwamba ng‟ombe hao waachiwe na wanavijiji wachukue ng‟ombe zao bila kuchelewa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kusisitiza kwa wafanyakazi wa mbuga ya Serengeti kuwaachia ng‟ombe hao mara moja. (Makofi)
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa vile swali la Mheshimiwa Kabongo limefanana na matatizo yaliyoko katika Mbuga za Wanyama za Mkomazi; na kwa vile nilishaongea na Waziri wetu wa Utalii, kaka yangu Mheshimiwa Profesa Maghembe kwamba tembo wanatoka Mkomazi National Park wanaingia kwenye Loresho tulilowatengenezea wafugaji na inaharibu sana sehemu hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa TANAPA tuliwaeleza tatizo hili na kwamba watusaidie kuboresha intake ili maji yawe mengi wakati wanatafuta jinsi ya kuwapelekea tembo wale maji. Je, Waziri anaweza kunisaidia kueleza atachukua hatua gani ya dharura kuhakikisha kwamba yale maloresho na tenki letu la intake lililoharibiwa na tembo na wanyama wengine linaboreshwa ili wafugaji waendelee kupata maji wakati wanatafuta jinsi ya kusaidia wanyama hawa? Ahsante.
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, tutachukua hatua mbili. Kwanza ni kuhakikisha kwamba tunaongeza upatikanaji wa maji katika eneo ambalo hao tembo wanatoka kule kwenye National Park na pia tutafanya ukarabati wa maeneo ambayo yameharibiwa katika vijiji ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameyataja. (Makofi)
MHE. MARWA R. CHACHA: Nina maswali mawili. Kwanza, naomba niwaambie tu kwamba Serengeti wanaishi binadamu, siyo wanyama peke yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukija Serengeti ni aibu sana, yaani utafikiri haipo Tanzania. Hatuna maji, hatuna lami, hatuna chochote, yaani faida tunayoipata sisi kuishi Serengeti National Park ni tembo kula mazao ya wananchi na kuua watu. Hiyo ndiyo faida tunayoipata.
Sasa mimi nimeuliza kwamba kwanini Wizara tusipate sehemu ya gate fee au bed fee? Hivyo vilikuwa ni vyanzo vya mapato vya Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti. Kwa sasa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti haina chanzo chochote. Ukija kwenye kwenye service levy, wamechukua vyote, hakuna kitu. Sasa sisi own source tunatoa wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kwenye maelezo ya Naibu Waziri, amesema kwamba wamewahi kuisaidia Wilaya, mimi nimekuwa Diwani tangu mwaka 2010 sijaona mradi wowote wa TANAPA.
MHE. MARWA R. CHACHA: Swali la kwanza, kwa kuwa ni majirani zetu, ninyi watu wa TANAPA naomba mtujengee game post kila kata katika kata kumi, ili kuzuia tembo, sisi tulime tu, hamna shida. Tunahitaji game post. Hata gari la kufukuzia tembo hatuna.
Swali la pili.

MHE. MARWA R. CHACHA: Swali la pili, kwa kuwa sasa makampuni haya yameenda Mahakamani kuishitaki Serikali, Mwanasheria wetu unasemaje kuhusu hili? Maana sasa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti hatuna own source? (Makofi)
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kuacha siku nyingine, jana nilikaa na wananchi wa Serengeti katika ofisi yangu wakiandamana na Mheshimiwa Mbunge kuelezea tatizo la single entry katika Pori la Serengeti ili ifanyiwe marekebisho, wananchi wa Serengeti ambao wana WMA waweze kufaidika zaidi na pori la Serengeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimewasikiliza na tatizo lao tuko kwenye hatua ya kulitatua. Kwa hiyo, siyo kweli kwamba wananchi wa Serengeti hawafaidiki na kitu chochote.
Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vilivyo na hizi WMA ambavyo vinapakana na Serengeti vinapata shilingi milioni 300 kila mwezi kutokana na biashara ya WMA hizi. Kwa hiyo, siyo kweli kabisa kwamba hawafaidiki na kitu chochote.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, tuko tayari kuongeza ulinzi katika maeneo ya mipaka na katika mwaka huu unaokuja wa fedha tumepanga tujenge vibanda vitatu kwa ajili ya askari ili kuhakikisha kwamba tunasaidiana na Wilaya katika kuwalinda wananchi na hivi sasa tayari tuna magari ambayo yanazunguka kule kuhakikisha kwamba tunasaidia kupunguza hasara ambazo wananchi wanaweza kupata kutokana na wanyama waharibifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kushirikiana na Wilaya ili kuhakikisha kwamba tunapunguza madhara haya.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona.
Naomba kumwuliza Waziri, kwa kuwa mbuga ya Hifadhi ya Mkomazi iko katika Wilaya za Same, Mwanga na Lushoto na kwa kuwa lengo la hifadhi hizi ni kuongeza Pato la Taifa. Je, ni lini Serikali itajenga mlango wa kuingilia katika mbuga ya Hifadhi ya Mkomazi katika eneo la Kivingo, Kata ya Lumbuza ili na Wilaya ya Lushoto nayo iweze kuchochea Pato la Taifa? Ahsante.
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu inafanya study hivi sasa ya kuangalia namna ya kuongeza milango ya kuingia katika Pori la Mkomazi na iko tayari kufungua mlango wa kuingia Mkomazi kutoka katika Jimbo la Mheshimiwa Mbunge.
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize maswali madogo ya nyongeza. Nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri. Kwa kuwa Askari wa Wanyamapori ni wachache na kwa kuwa hifadhi zimekuwa zikiwatumia Askari wa Wanyamapori wa kujitolea kwa kufanya doria na kwa kuwa askari hawa wanapofanya kazi kama maeneo ya Kigosi kwenye mipaka ya Jimboni kwangu wamekuwa na utaratibu wa kufanya doria na kujilipa. Haoni sasa wakati umefika Serikali ichukue hatua kukomesha tatizo hili ili kuondoa migogoro kwa wafugaji? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Sheria ya Uhifadhi inatoa fursa ya wananchi kushiriki katika uhifadhi kwa kutumia vikundi vya kijamii pamoja na vikundi ambavyo vipo vijijini. Je, Serikali iko tayari kuweka msukumo wa aina yake ili kuhakikisha kwamba vikundi vya jamii ikiwepo sungusungu wanahusika katika uhifadhi ili kupunguza migogoro?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Askari wa Wanyamapori ni wachache lakini pia malipo yao na mishahara yao ni midogo sana. Kuanzia mwaka 2016/2017, Serikali italigeuza jeshi au askari hawa wa wanyamapori kuwa jeshi usu au paramilitary force ili kushughulikia ujuzi na uwezo wao, lakini pia kuangalia kwa undani mafao na mishahara yao ili wawe walinzi thabiti katika kulinda maliasili zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli pia kwamba vikundi vya wananchi hata vikundi vya sungusungu vinaweza kulisaidia sana Jeshi la Wanayamapori katika kulinda na kuhifadhi maliasili zetu. Serikali imechukua wazo hili zuri na tutalifanyia kazi ili tuone ni jinsi gani vikundi hivi vinaweza kusaidiana na askari katika kuhifadhi mali zetu.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana Mwenyekiti, na pia nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri, lakini nina maswali madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mradi wa haya madini adimu duniani pamoja na joto ardhi ni muhimu sana kwa uchumi wa viwanda, naomba commitment ya Serikali, moja, je, ni lini wataanza uchimbaji wa joto ardhi ili tuweze kutumia kwenye viwanda vyetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, na pili, naomba pia commitment ya Serikali pamoja na mradi wa Ziwa Ngozi, je, Serikali imetoa leseni ngapi za uchimbaji na uzalishaji wa madini na nishati ya joto ardhi katika sehemu zingine hapa kwetu Tanzania? Ahsante.
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, juu ya ni lini tunaanza, utafiti umeshafanyika, unaonesha kwamba ili upate umeme wa joto ardhi unahitaji kuwa na temperature ambayo iko katikati ya nyuzi 180 mpaka 240 celsius. Sasa bahati nzuri hii ya Ngozi iko zaidi ya 240. Kwa hiyo, kinachofuata sasa kwa miezi michache ni kwamba inabidi tuchoronge miamba pale chini tuweze kujua kuna mvuke kiasi gani ambao utaendesha mashine ya kuzalisha umeme wa kiasi gani. Kwa hiyo, tutatoa hiyo tarehe baada ya kujua tuna mvuke wa chini kiasi gani yaani steam.
Mheshimiwa MWenyekiti, na leseni ngapi zimetolewa, ni kwamba tumeshatengeneza ramani ya nchi nzima ambayo inaonesha maeneo yote ambayo tunaweza kuendeleza joto ardhi. Kwa sasa hivi ukiacha ya Ngozi, Mbeya eneo lingine ni la Luhoi kilometa kama 70 Kusini Mashariki mwa Dar es Salaam, halafu na lingine liko sehemu za Kusini mwa Morogoro na Ziwa Natroni kwa hiyo maeneo ni mengi lakini tunaenda hatua kwa hatua.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mgogoro uliopo kati ya Wananchi wa Buger na Hifadhi ya Taifa ya Manyara ni sawasawa na mgogoro uliopo kati ya Hifadhi ya Mkungunero na wananchi wa vijiji 11 vya Wilaya ya Kondoa. Katika mgogoro huo wananchi wameuawa, Askari wa Hifadhi ya Mkungunero wamekufa na mgogoro huu ni wa muda mrefu na tumeiomba Serikali washughulikie mgogoro huo na wananchi wanaomba kilometa 50 tu ili mgogoro umalizike.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mawaziri waliopita wametembelea na wamefanya mikutano na wananchi wa vijiji 11 wa Wilaya ya Kondoa pamoja na Chemba. Je, Mheshimiwa Waziri ni lini mgogoro wa wananchi wa Wilaya ya Kondoa, vijiji 11 utaisha kati ya Hifadhi ya Mkungunero na wananchi hao?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kujibu swali la nyongeza kuhusu Mbuga ya Mkungunero. Wizara yangu pamoja na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, imeandaa mpango wa kupima maeneo yote ambayo yana mgogoro kati ya wananchi na Hifadhi za Taifa ili kufanya juhudi za kutatua matatizo haya moja kwa moja.
Mh
MHE. ESHER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, wananchi ambao wanazungukwa na hifadhi kwa Mkoa wa Mara, Tarime, Serengeti, Bunda Mjini na Bunda, wamekuwa wavumilivu sana. Hivi tunavyozungumza hakuna mwaka ambao tembo hawatoki kwenye hifadhi na kuja kwenye vijiji, nazungumzia kwenye Jimbo langu, Kijiji cha Serengeti, Tamau, Kunzugu, Bukole, Mihale, Nyamatoke na maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni tulienda na Mheshimiwa Jenista, akajionea mwenyewe tembo wanavyoharibu mazao ya wananchi, lakini bado fidia ni ndogo, shilingi 100,000/= mtu anaandaa shamba kwa milioni 10. Hivi karibuni Mheshimiwa Waziri wa Utalii na Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu…..

MHE. ESTER A. BULAYA: Komeni basi, kelele niongee!

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Jenista wamepeleka magari mawili na askari sita kuhakikisha yale mazao ya wananchi yanalimwa. Tunaposema ni lini Serikali mtatafuta ufumbuzi wa kudumu ili hao wananchi waepukane na njaa wakati wana uwezo wa kulima na lini ufumbuzi wa kudumu utapatikana badala ya kupeleka magari na askari kwa ajili tu ya kulinda mazao ambayo yako shambani?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa fursa ya ziada ya kujibu swali la Mheshimiwa Ester Bulaya kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu alikuwa kule na alitoa ahadi, alijionea mwenyewe na kutoa ahadi kwamba Serikali itafanya juhudi ya kupeleka magari na askari wa ziada ili kuhahakikisha kwamba tembo hawaharibu mazao ya wananchi. Ni wiki moja na nusu sasa magari yale yako kule yanafanya kazi na tunaamini kabisa kwamba hii ni hatua ya kwanza ya Serikali kulishughulikia jambo hili kwa hatua za kudumu.

Mheshimiwa Spika, tumeanza pia kutumia ndege ambazo hazina rubani, tumeanza majaribio katika Wilaya ya Serengeti na Wilaya ya Bunda ili kuzitumia ndege hizi kuwatisha tembo na kuwaondoa katika maeneo ambayo wako karibu na mashamba ya watu na tunategemea kwamba jambo hili litatatuliwa kwa kudumu kwa kutumia utaratibu huo wa teknolojia.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa wananchi wa Kasulu wengi wao kwa kutokujua mipaka inaishia wapi; wamekuwa wakilima mpakani mwa pori la Kagera Nkani na kwa sasa mazao yao yako tayari wanahitaji kuvuna.
Je, Serikali iko tayari kumuagiza Mkuu wa Wilaya awaruhusu wananchi waweze kuvuna mazao yao huku utaratibu mwingine ukiwa unaendelea?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, maagizo yametolewa mahususi kabisa kuhusu suala hilo kwamba Wizara pamoja na Wakuu wa Wilaya wawaruhusu wananchi ambao wamelima ndani ya hifadhi zetu waweze kuvuna mazao yao kabla hawajaondoka katika maeneo hayo.
Kwa hiyo, nimkumbushe tu Mkuu wa Wilaya juu maagizo hayo na awaruhusu wananchi wachukue mazao yao.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona swali langu ni dogo tu ambalo linafanana na swali la msingi la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, utamaduni uliokuwepo wa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa miaka ya nyuma uliruhusu wananchi wanaoishi kando kando mwa maeneo ya hifadhi waliruhusiwa kuvua samaki kwenye mabwawa hususan wananchi wa Jimbo langu la Rufiji wa maeneo ya Luwingo na utaratibu huu ulienda sambamba na kata zote; kata ya Mwasenimloka, kata ya Ngolongo pamoja Kagira, naomba kufahamu Wizara ya Maliasili na Utalii inaweka utaratibu gani sasa ili kuweza kuwasaidia wananchi wa maeneo haya katika kuchimba mabwawa ya samaki ili wananchi hawa wawekeza kuuza samaki hizo kuwasaidia kwa ajili ya kuwapeleka watoto wao shuleni? Ahsante.
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, katika majibu ya msingi ya Mheshimiwa Naibu Waziri alielezea kuhusu masuala ya kimkakati ambayo ni lazima tuyashughulikie katika kuendesha hifadhi hizi na kutokana na mabadiliko ambayo yametokea katika maeneo ya mipaka ya hifadhi zetu zote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, suala hili ni moja ya masuala ya mkakati na tutajadiliana na wananchi na hasa kwenda kabisa katika maeneo hayo ili tukubaliane na wananchi namna ya kutumia maeneo hayo ya kuvua na pale inapowezekana tuwasaidie wananchi kuwa na mabwawa yao wenyewe ili kusiwe na sababu yao kwenda ndani ya hifadhi.
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Nataka kumwuliza Mheshimiwa Waziri; kwa vile utalii ni moja kati ya tegemeo kubwa la uchumi wa nchi yetu. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwajengea uwezo Mabalozi hasa walioko nchi mbalimbali za Latin America na America kuwa na uwezo wa kuweza kufanya ushawishi na kuweza kuunganisha Mashirika ya Kitalii yaliyoko katika nchi hasa za Ujerumani na Ufaransa kuweza kuja katika nchi zetu hizi na kuwa na mfano wa nchi ambazo wameweza kufanikiwa sana tukilinganisha nchi za Mauritius na nchi nyinginezo za Mashariki ya mbali ambazo zimefanikiwa sana katika suala hili la utalii?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nakushukuru sana kwa kuniona, lakini napenda nianze kwa kweli kwa kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Sera ya Serikali ya economic diplomacy, hii ni moja ya nguzo ya kujenga mapato ya Serikali kwa kuzitumia Balozi zetu kutusaidia katika kutangaza utalii katika maeneo yao na tayari tumeanza kuandaa vitini ambavyo tutawapelekea Mabalozi ili hata mgeni akiingia kwenye Ubalozi wetu, ajue tayari ni vitu gani viko Tanzania. Kwa hiyo, tunawaomba Waheshimiwa Wabunge, tusaidiane katika jambo hili ili kuweza kufanikisha sera hii.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa, wananchi wanaoingia kwenye hifadhi ya misitu siyo kwamba wanaingia kwa sababu ya ukatili ni kwa sababu ya kukosa maeneo ya kuishi na kulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano; wananchi wa Wilaya ya Kasulu wanaoingia kwenye pori ya Hifadhi ya Kagerankanda ni kwa sababu watu wameongezeka, ardhi ni ile ile, maeneo ya kilimo yamekuwa ni kidogo. Je, kwa nini, Serikali isiwaruhusu waendelee kulima wakati Serikali inaandaa utaratibu mwingine wa kupima mipaka. (Makofi)
Swali la pili; kwa kuwa, ongezeko la watu ni kubwa sana, kwa nini, Serikali isitenge baadhi ya maeneo ya misitu ili wananchi waruhusiwe kuishi na kuwapunguzia tatizo hili la kuhangaika kutafuta maeneo ya kulima?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba wako wananchi ambao wameingia na wamejenga ndani ya maeneo ya misitu na wanakaa humo kufanya shughuli za kibinadamu. Sheria zetu za nchi zinakataza wananchi kuingia na kujenga, kulima ndani ya hifadhi zetu. Kwa hiyo, naomba niwahamasishe wananchi hawa wafuate sheria na wafuate sheria bila shuruti. Kwa hiyo, waondoke kwenye maeneo ya hifadhi na washirikiane na Halmashauri pamoja na Serikali za vijiji vyao kuwapangia maeneo mengine ya kuishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ongezeko la watu ni phenomena ambayo inatokea dunia nzima. Siyo jambo la Tanzania peke yao, kama ambavyo mmeona, nchi ambazo zinaendelea na zile ambazo zimeshaendelea, idadi ya wakulima inaendelea kupungua mpaka kufikia asilimia 20 katika nchi nyingi za Ulaya au kule Marekani, hii inatokana na watu kufanyakazi zingine, siyo lazima wote tuwe wakulima, kufanya kazi zingine ambazo mahitaji yake ya ardhi ni madogo kama vile ufugaji wa samaki, ufugaji wa nyuki kuanzisha viwanda vidogovidogo kama nilivyoeleza kwenye swali langu la msingi ili kuhakikisha kwamba maisha yetu yanaendelea, lakini na misitu yetu inakuwepo ili maisha yetu yaendelee kwa ustaarabu ambao unatakikana.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri ambayo anajitetea na kijificha katika msitu wa njugu. Ni-declare interest mimi ni mtaalam wa misitu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilichouliza ninataka kujua Serikali ina mkakati gani mahsusi wa kuongeza idadi ya wanafunzi katika chuo kile ili kukabiliana na paragraph ya mwanzo ya majibu yako. Ieleweke kwamba tunaposema wataalam wa misitu (foresters) hasa ni wale certificate na diploma kwa sababu wale ndiyo field officers na kukosekana kwa wale ndiyo sasa hivi deforestation imeongezeka na afforestation imepungua.
Mheshimiwa Spika, nataka kujua mkakati upi wa Serikali wa kuongeza idadi ya wanafunzi wa certificate na diploma katika chuo kile ili kukabiliana na hali hii tuliyonayo katika nchi yetu ya uharibifu wa misitu na mazingira? (Makofi)
Swali la pili, mheshimiwa Waziri, Chuo cha Misitu cha Olmotonyi katika miaka ya 1980 kilikuwa na hadhi ya Kimataifa, sijui leo; na kilikuwa kinapokea wanafunzi kutoka nje ya nchi. Je, Serikali inasema nini katika kukiboresha chuo hiki kikaendelea kupokea wanafunzi kutoka nje ikawa ni moja kati ya source of income za Serikali hii, kuipatia fedha za kigeni? Nashukuru!
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Yussuf kwa maswali yake mazuri.
Mheshimiwa Spika, kwanza ni uwezo wa chuo kuongeza wanafunzi na katika jibu la msingi hapa, tumepanua chuo ili kiweze kuwa na hall ya mhadhara mmoja ambao unaweza sasa kubeba wanafunzi 200 kwa wakati mmoja. Tumepanua na nafasi nyingine na hasa kuboresha maktaba ili iwe bora zaidi na iweze kuwa na rasilimali za vifaa vya kujifunzia bora zaidi. Kwa kufanya hivyo tunaweza kuongeza wanafunzi wengi zaidi na kufanya chuo kitoe mafunzo mazuri zaidi.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba huko nyuma, Chuo cha Olmotonyi kilikuwa kinachukua wanafunzi kutoka nje ya nchi, lakini katika ngazi hii ya cheti na ngazi ya diploma, hii ni ngazi ya msingi sana kama elimu ya msingi kwenye mafunzo haya ya misitu.
Mheshimiwa Spika, katika mafunzo haya ya misitu nchi nyingi ambazo zilikuwa zinaleta wanafunzi kwetu zimejijengea uwezo wake wa kutoa mafunzo ya msingi. Siku hizi wanafunzi wa Kimataifa wanakuja kusoma kwenye chuo chetu cha misitu kilichopo kwenye Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine ambacho ndicho chuo bora zaidi kwenye fani ya misitu kuliko vyuo vyote Barani Afrika.
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Nina swali la nyongeza eeh.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nilikuwa nasubiri umalize kwanza. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba sasa nimuulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ripoti ya Maendeleo ya Dunia ya mwaka 2010 inaitaja Tanzania kama nchi yenye malikale adimu na urithi wa utamaduni wa Taifa ambao ungeweza kuongezea nchi yetu kipato na kukuza uchumi wetu. Nataka kujua sasa, Tanzania inafanya nini katika kutumia malikale zake hizo adimu kama Olduvai Gorge, Laetoli, Kolo na Kilwa Kisiwani ili iweze kuiongezea nchi yetu kipato? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kwa kuzingatia umuhimu na mchango wa malikale za Taifa letu katika kukuza uchumi, mnamo mwaka 2007 aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, aliagiza nyayo hizo ziweze kufukuliwa ili watalii wengi zaidi waweze kutembelea eneo hilo na nchi yetu iweze kujipatia kipato.
Mheshimiwa Naibu Spika, inasikitisha sana katika majibu ya Mheshimiwa Waziri, anasema hakuna kusuasua kwa ufukuzi wa nyayo hizo ilhali sasa hivi inapita miaka 10 tangu agizo hilo litolewe na hadi hivi sasa tunavyozungumza, bado nyayo hizo hazijafukuliwa. Kwa hiyo, ninachotaka kujua, wananchi wa maeneo yale ambao wanazungukwa na ile historical site wananufaikaje kwa uwepo wa hiyo historical site? Ahsante.
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Napenda kumhakikishia Mheshimiwa Chakoma kwamba Serikali imechukua hatua mbalimbali za kuhakikisha kwamba maeneo yetu haya ya urithi wa Taifa yanaletwa katika kiwango ambacho kinaweza kutumika na kutuzalishia mapato katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la Ngorongoro, eneo hilo limefukuliwa na wataalam kutoka Tanzania, Spain pamoja na Marekani na kuvumbua nyayo nyingine ambazo zinaonesha kwamba wanadamu hao wanaitwa Zamadamu, walikuwa wanaishi pale wakiwa wanatembea upright miaka milioni 3.6 iliyopita. Nyayo hizo mpya ambazo ziligundulika, zilifunguliwa mwezi Machi, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hilo pia linajenga museum kubwa, eneo la mapokezi, maktaba na kuonesha vitu mbalimbali ambavyo vitavutia sana watalii watakaotembelea eneo hilo. Aidha, Serikali inaendelea kuyafufua na kuyakarabati maeneo mengi ya Malikale ambayo Mheshimiwa Chakoma ameyataja na kwamba maeneo haya yakiwekwa katika utangazaji wetu wa utalii yatakuwa na mvuto mkubwa na yataongeza mapato ya Serikali kwa kiwango kikubwa sana.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Spika,
ninakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, miongoni mwa gharama kubwa ambazo Hifadhi ya Ngorongoro inatumia ni pamoja na kumtunza faru Fausta ambaye chakula chake kwa mwezi ni shilingi milioni zaidi ya 64. Naomba kufahamu, Serikali ina mpango gani juu ya faru huyu Fausta ambaye analigharimu Taifa au hifadhi ile kwa fedha nyingi sana kwa mwezi na
hata kwa mwaka?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, napenda kukushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Gekul kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli yuko faru Fausta pale
Ngorongoro na amewekwa kwenye cage kwa sababu amekuwa mzee sana na amekuwa ananyemelewa na magonjwa aina mbalimbali na lengo ni kuhakikisha kwamba maisha yake yanaendelea utafiti na takwimu ambazo zinakusanywa kwa ajili ya faru huyu zinaendelea, kwa sababu wanyama hawa ni wachache sana nchini hivi sasa na kila takwimu ambayo tunakusanya na kuilinganisha na maisha halisi ya wale ambao wako kwenye pori ni muhimu kwa
maisha ya wale wengine ambao wanaishi humo.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kufanya kazi hii kuna gharama, lakini hizi ndiyo gharama halisi za uhifadhi. Namuomba Mheshimiwa Mbunge aendelee kutuamini kwamba tunafanya jambo hili kwa nia njema na kwamba takwimu zinazopatikana zinathamani halisi kwa ajili ya
uhifadhi wa wanyama hawa.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri. Pamoja na majibu hayo naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Jumapili tulikuwa na semina inayohusu mambo ya utalii, na kwenye jarida hili kulikuwa na taarifa ambazo zilikuwa na upungufu juu ya vivutio hivi. Sasa Je, Waziri yuko tayari kutembelea visiwa vya Ukerewe na kushuhudia vivutio hivi ili awe Balozi mzuri na mwenye taarifa zilizo sahihi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, suala la ukuzaji
na uendelezaji wa vivutio hivi mbali na kuvitangaza inategemea zaidi ubora wa miundombinu ya kuvifikia vivutio hivi; na kwa kuwa Halmashauri zetu hazina uwezo wa kutosha wa kuboresha miundombinu hii, sasa Serikali iko tayari kuboresha miundombinu ya kufikia vivutio hivi hasa Jiwe linalocheza la Nyaburebeka la Kisiwani Ukara? (Makofi)
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niko tayari kabisa kutembelea vivutio hivyo pamoja na Mbunge, Mheshimiwa Mkundi bila wasiwasi wowote na tutapanga safari hiyo mwezi Agosti mwaka huu.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba vivutio vyote vya utalii vinakuwa vizuri zaidi kama vinafikika na raia na watalii wanaotaka kuvitembelea. Wakati tutakapotembelea tutafanya tathmini ya vivutio hivyo na kuona ni namna gani juhudi hizi zitakamilika ili vivutio hivyo vifikike.
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na swali la msingi ambalo niliuliza kuhusu vivutio, Mji wetu wa Iringa ni Mji mkongwe ambao una historia kubwa ya Mtemi wetu Mkwawa jinsi alivyopambana na Mjerumani. Ni juhudi zipi za makusudi ambazo zinafanywa na maliasili kuhakikisha kwamba mji huu wa Iringa na historia kubwa ya Mtemi Mkwawa inaendelea kujulikana katika dunia nzima na Tanzania kwa ujumla?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ni hatua nyingi zinafanywa kuboresha utalii katika eneo zima la Kusini mwa Tanzania, lakini hususan Mji wa Iringa na viunga vyake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tumefungua makumbusho ya historia ya Iringa na utemi wake kule. Pili, Serikali inapanua Uwanja wa Nduli kama ulivyoona kwenye bajeti. Vile vile Serikali imepanga kujenga barabara kutoka kwenye geti la Ruaha kuja Ruaha Mjini. Shughuli hii tumeishughulikia sana na Mheshimiwa Lukuvi katika kuitekeleza pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Miundombinu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2016 tumeanza kwa mara ya kwanza kuwa na Maonesho ya Utalii Kusini mwa Tanzania na yalikuwa Iringa na mwaka huu maonesho hayo ni makubwa zaidi. Waheshimiwa Wabunge, nawakaribisha mje kushiriki katika maonesho hayo. Ahsante.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri na ambayo yanatia matumaini. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kutambua kwamba kuna vivutio hivyo katika Jimbo la Ngara, kama maporomoko hayo, lakini bado hifadhi hizo za Burigi na Kimisi na bado kuna vivutio vingine kama pango lililokuwa linasafirisha watumwa kutoka Burundi kupitia Tanzania, pango la Kenza Kazingati, kuna mlima mrefu kuliko milima yote Mkoa wa Kagera, kuna mito miwili ambayo unaweza ukafanya boat riding na ili vivutio hivi kufanya kazi na kupata watalii ni lazima kuboresha miundombinu ya barabara na viwanja vya ndege, sasa tuna uwanja wa ndege wa Luganzo. Je, Wizara iko tayari kuboresha uwanja huu wa ndege wa Luganzo ambao unaweza ukasaidia kuleta watalii na wakafanya utalii katika eneo hilo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Ngara ilitegemea kupata gawio la asilimia 25 kutokana na utalii wa uwindaji katika Hifadhi za Burigi na Kimisi. Hata hivyo, takribani miaka 30 iliyopita tangu Hifadhi ya Burigi imeanzishwa na miaka takribani 12 tangu Hifadhi ya Kimisi imeanzishwa ni mwaka jana tu ambapo tumeweza kupata gawio la shilingi milioni 7, gawio ambalo ni dogo. Sasa nahitaji nipate ufafanuzi kwamba shilingi milioni 7 hizi zilitokana na mapato ya kiasi gani na ni wanyama kiasi gani waliowindwa katika hifadhi hizi mbili? (Makofi)
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Gashaza kwa ufuatiliaji wake wa karibu na mawazo mazuri katika kuendeleza na kuboresha maeneo haya kama maeneo yanayovutia watalii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kuna uwanja wa ndege ambao umekuwa unatumiwa na wawindaji katika eneo lile ambao urefu wake ni mita 1,700. Tutatuma wataalam wetu wanaoshughulika na masuala ya uwindaji ili washirikiane na TAA katika kuboresha uwanja huu ili kuhakikisha kwamba vivutio hivi vinaweza kufikiwa kwa urahisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la uwindaji, Wizara yangu itafuatilia zaidi malipo ambayo yamefanywa ili kuona ni namna gani tunaweza kuboresha ushirikiano kati ya wawindaji, Wizara na wananchi wa Ngara, ili kuboresha hali ya uwindaji katika eneo hilo.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Ahsante kwa majibu Mheshimiwa Naibu Waziri. Swali la kwanza, napenda kujua Serikali imefikia hatua gani kwenye kulipa fidia au kuboresha mazingira ya wanakijiji wa Uvinje vis-a-vis TANAPA?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Serikali imejipangaje kwa vijiji vile vinavyozunguka au vilivyo ndani ya Saadani kuona vinashirikishwaje katika shughuli za kitalii ili kudumisha au kuboresha uchumi wao? (Makofi)
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza linahusu fidia kwenye vijiji alivyovitaja. Kwa kuwa hadi nasimama hapa bado nilikuwa sijapata taarifa zilizokamilika kuhusiana na madai hayo, nimuahidi nikitoka hapa anipe kwa ufafanuzi vijiji hivyo ni vipi na kwa nini vinastahili fidia ili niweze kuangalia tumefikia katika hatua gani pale Wizarani kuweza kukamilisha utaratibu huo wa kuwalipa fidia ikiwa watakuwa wanastahili kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili la namna gani Wizara au Serikali inashirikisha vijiji vinavyozunguka maeneo ya Hifadhi ya Saadani katika masuala ya kuendeleza vivutio, utaratibu wetu kwa kawaida ni kwamba kila wakati tunapofikiria kuanzisha mradi, wadau wa kwanza kabisa na hii nimeisema hata katika swali la msingi, kwamba uendelezaji wa vivutio katika hifadhi zote unashirikisha jamii zinazozunguka katika maeneo ya hifadhi na Serikali pamoja na mashirika binafsi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hata kwa upande wa vijiji alivyovitaja katika Hifadhi hii ya Saadani tumeweza kuwashirikisha kwa mujibu wa taratibu tulizonazo lakini kama ana mawazo ya kuweza kuipatia Serikali ili tuweze kuboresha zaidi namna ya kuweza kushirikisha wananchi hawa au wadau hawa wanaoishi kwenye maeneo ambayo ni jirani na hifadhi basi tupo tayari kupokea ushauri huo tuweze kuboresha zaidi taratibu zinazotumika katika kuboresha vivutio kwenye maeneo ya hifadhi.
MHE. JUMAA H. AWESO: Mheshimiwa Spika, nikushukuru. Ili kuboresha sekta hii ya utalii ni pamoja na kuboresha miundombinu yake. Ukiangalia hii mbuga ya Saadani barabara ambayo inaifikia mbuga ile ni mbovu na haipitiki kwa muda wote. Je, Wizara hii haioni haja sasa ya kukaa na Wizara ya Miundombinu ili kuhakikisha kwamba inaijenga barabara hii ya Tanga - Pangani - Saadani ili watalii waweze kufika kwa urahisi?Ahsante sana.
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ni kweli ili utalii uweze kwenda sawasawa, ili tuweze kupata idadi kubwa ya watalii, ili watalii wakija waweze kufurahia kuwepo kwenye hifadhi zetu na kwenye maeneo yetu ya vivutio, wakae muda mrefu zaidi ili waweze kutumia fedha zaidi na kuweza kuboresha pato zaidi ni lazima mazingira hapo ambapo tumeweka vivutio yawe bora zaidi ikiwa ni pamoja na miundombinu ya usafiri lakini pia hata malazi. Upande wa malazi kwa kiwango kikubwa hili ni eneo ambalo linafanywa au linatekelezwa na sekta binafsi.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa miundombinu kama barabara ukweli ni kwamba eneo hili linatekelezwa na Serikali, lakini pia hata ndani ya Serikali, barabara zile ambazo zinaelekea kwenye hifadhi kutoka kwenye maeneo mengine ya miji jirani, hizi ni barabara ambazo zinatekelezwa kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Kwa upande wa barabara ambazo ziko ndani ya hifadhi, kwa mfano barabara zilizoko ndani ya Hifadhi ya Saadani, hili ni jukumu la Wizara ya Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa barabara pamoja na matengenezo yake ya kuweza kuzifanya zipitike hili ni jukumu ambalo linafanyika na Wizara kwa kupitia Shirika la TANAPA ambalo ni Shirika la Hifadhi za Taifa. Katika bajeti ya mwaka huu TANAPA wametenga fedha kama ambavyo tunatenga kila mwaka kazi yake ni kuboresha miundombinu kwa maana ya kuboresha iweze kupitika mwaka mzima hata msimu wa mvua, lakini pale ambapo inawezekana kupasua barabara mpya kutegemeana na bajeti na uwezo wa kifedha, basi utekelezaji wa mradi huo utaendelea.
Mheshimiwa Spika, kuhusu barabara aliyoitaja ya Tanga – Pangani – Saadani, hii ni barabara ambayo tutashirikiana na wenzetu wa Wizara ya Miundombinu ili kuhakikisha kwamba barabara hiyo inajengwa kwa mujibu wa taratibu tulizojiwekea na hasa pale ambapo bajeti itakuwa imeweza kuruhusu.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasikitika sana. Majanga ya tembo katika Mkoa wa Mara na Tanzania kwa ujumla ni makubwa sana, lakini majibu ya Waziri yamekuwa ni mepesi sana. Nitanukuu, naambiwa kwamba kuanzia mwaka 2015 mpaka 2016 ni matukio 128 na mwaka 2016 mpaka 2017 wamepunguza hadi 105, kwa maana hiyo matukio waliyoweza kuyapunguza ni 23 tu. Hatuoni kwamba itachukua muda mrefu sana mpaka kuhakikisha kwamba tatizo la tembo hapa Tanzania kwa ujumla litakuwa bado ni tatizo kubwa sana kwa wananchi?
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine, hawa tembo zamani wananchi walikuwa wanajichukulia wenyewe hatua mikononi na tembo hawa walikuwa hawasumbui wananchi. Lakini kwa sababu Serikali imeona kwamba tembo ni wa thamani kuliko binadamu, na ukiua tembo ni shida unafungwa miaka mingi, na tembo akiua binadamu ni halali. Sasa naomba Mheshimiwa Waziri aje na majibu mazuri kwa wananchi wa Mkoa wa Mara, je, warudi kule kule wajichukulie hatua mkononi? Kwa sababu ile nyama ya tembo inaliwa na wanasema kwamba aidha…
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, ni kweli kwamba uvamizi wa tembo katika maeneo ya wananchi ni changamoto kubwa katika maeneo ya Bunda, Tarime na Serengeti. Hata hivyo Serikali inachukua kila aina ya hatua kuhakikisha kwamba inapambana na kuzuia hali hii, na orodha ya hatua ambazo zimechukuliwa nimezitaja. Pamoja na hayo, tunaendelea na utafiti wa kuweza kutambua njia nyingine bora zaidi za kukabiliana na jambo hili. Na Mheshimiwa Mbunge atakuwa ni shahidi kwamba wafanyakazi wetu pamoja na wafanyakazi wa Halmashauri wanafanya juhudi kubwa sana ya kusaidia wananchi katika jambo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, si kweli kabisa kwamba tembo ni bora kuliko wananchi. Lakini ni jambo lisilopingika kwamba wanyamapori ni rasilimali kubwa yetu sisi sote kama wananchi wa Tanzania na tunawashukuru sana wananchi wa Mara kwa juhudi kubwa ambazo wanafanya kusaidia nchi nzima katika kuwahifadhi wanyama hawa.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, uko utaratibu kama si sheria au kanuni katika nchi hii, kwamba mifugo ya wananchi au wananchi wenyewe wakiingia kwenye hifadhi kuna tozo inawakuta. Je, Mheshimiwa Waziri haoni ili kuondokana na hili tatizo la wanyama kutoka nje umefika wakati sasa wanyama wakitoka nje kwenye maeneo ya wananchi, tozo hiyo hiyo ambayo wananchi wanatozwa wakiingia kwenye hifadhi nayo itozwe? Nakushukuru. (Makofi)
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, wanyamapori si binadamu na wanyamapori hawana akili za kibinadamu, ni wanyama wa porini. Kwa hiyo, tujitahidi sana kuwalinda kwa kuwaeleza askari wanyamapori pale wanapotokea na mimi nasema kwa kweli ni furaha kubwa kwamba kwa mara ya kwanza sasa tembo wameongezeka kutokana na hali mbaya ya ujangili iliyokuwepo hapa nchini na sasa wanaonekana, wanakuja mpaka kwenye maeneo ya watu. Rai yangu kwa kweli tushirikiane ili tuwataarifu askari wanyamapori pale wanyama hao wanapotokea na sisi tunachukua hatua haraka iwezekanavyo kila tukio la namna hii linapotokea.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri katoa majibu mazuri sana, lakini mimi nina concern moja kubwa kwamba hawa tembo madhara yao ni makubwa sana katika Wilaya ya Busega ambayo inapakana na Wilaya za Bunda na Serengeti. Maelezo ya Mheshimiwa Waziri katika majibu yake amesema kwamba hawa tembo wanazidi kudhibitiwa, lakini mwishoni amesema kwamba tembo wameongezeka zaidi, sasa sijaelewa kwamba sasa kwa vile wameongezeka zaidi madhara yatakuwa makubwa kwa wananchi. Serikali sasa kupitia Wizara yake ina mkakati gani kuwaokoa wananchi ambao wanasumbuliwa na tembo kwa kusababishiwa hasara kubwa zaidi?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, huko nyuma nchi yetu ilikuwa na tembo wengi sana, wanafika 110,000, hivi sasa hatua tuliyofikia hapa wanyama hawa walipunguzwa sana na ujangili wakafika chini ya 10,000. Sasa hivi ndiyo idadi hiyo inaanza kukua na tunaanza kuwaona. Katika eneo lile la Serengeti na eneo la Maswa tunafanya utafiti kuangalia kama tunaweza kujenga uzio wa kuwatenganisha watu, mashamba yao na hifadhi. Tunafanya mazungumzo na wawekezaji wakubwa hapa nchini kwetu na mazungumzo yanaelekea vizuri. Sikupenda nifike mahali ninasema jambo hili, lakini Serikali inalichukulia jambo hili kwa uzito mkubwa sana na ndiyo maana tunafanya utafiti wa uwezekano wa kujenga uzio wa kilometa 140 tuone kwamba italeta afueni kiasi gani katika kuwadhibiti wanyama hawa.
MHE. SULEIMAN A. SADDIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa Mikumi National Park imepakana na Wilaya ya Mvomero na kata za Doma, Msongozi, Melela, Malaka pamoja na Mangaye; kwa kuwa wanyama waharibifu wanaingia sana katika mashamba ya wakulima na wanaharibu sana mazao ya mahindi, mpunga, nyanya na kadhalika na kwa kuwa tembo wengi sana wameshafanya uharibifu mkubwa, je, Serikali sasa iko tayari kuongeza Askari wa Wanyamapori katika maeneo hayo angalau kila kata kuwe na askari mmoja ili kuondoa tatizo ambalo wananchi wanakabiliana nalo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Wilaya ya Mvomero ina upungufu mkubwa wa vitendea kazi, je, Serikali iko tayari sasa kuisaidia Wilaya ya Mvomero vitendea kazi pamoja na masuala mengine ya usafiri ili tuweze kukabiliana na hali hiyo? (Makofi)
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba wanyama wakali na waharibifu wameongezeka katika maeneo mbalimbali hapa nchi na katika eneo la Wilaya ya Mvomero wanyama hawa wameongezeka sana katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Saddiq Murad Mbunge wa Mvomero, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi pamoja na Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Wilaya tumetembelea hayo maeneo ambayo yamezidiwa sana na uvamizi wa wanyama wakali na waharibifu. Wizara itaongeza askari kusaidiana na wale walioko katika Wilaya ya Mvomero ili kupambana na kadhia hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Wizara itashirikiana na Halmashauri ya Mvomero kwa kuipa vitendea kazi zaidi pamoja na kuwasaidia katika usafiri ili waweze kukabiliana na tatizo hili ambalo limeongezeka sana katika Wilaya hiyo. (Makofi)
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Tatizo la viboko lililopo katika Jimbo la Ulanga linafanana sana na tatizo la viboko lililopo Kisiwani Mafia. Wananchi wa kata za Ndagoni, Baleni na Kirongwe wameharibiwa mazao yao na ng’ombe wao wameuwawa na viboko waharibifu. Kutokana na ongezeko kubwa sana la viboko hawa na Kisiwa cha Mafia ni eneo dogo, je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kutoa ruhusa tuanze kuwavuna viboko hawa kwa sababu kule ni kitoweo pia? Ahsante. (Kicheko)
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue fursa hii kumpa pole sana Mheshimiwa Dau na wananchi wake wa Mafia kwa kadhia hii ambayo imewakumba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua ambayo tutachukua ni pamoja kutuma wataalamu waende wakafanye sensa ili tujue kwamba kuna viboko wangapi katika eneo hilo na tuweze kuangalia kama kuna uwezekano wa kuweza kuwavuna hao viboko ili kupunguza madhara yake kwa wananchi wa eneo la Mafia.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la wanyama waharibifu ni kubwa sana katika Jimbo langu la Bunda Mjini na Jimbo la kaka yangu Boni. Sisi wananchi wa Mkoa wa Mara hatuhitaji kuomba chakula na mwaka jana Mheshimiwa Waziri wa Sera, Uratibu na Bunge, Mheshimiwa Jenista alikuja akaliona tatizo hilo na Mheshimiwa Waziri mwenyewe anajua, tatizo la tembo kuharibu mazao ya wananchi, kuua wananchi pamoja na mali zao. Sasa nataka kujua, ni lini Serikali mtahakikisha mnakuwa na mkakati wa kudumu wa kumaliza tatizo hili katika vijiji vyote vinavyozunguka hifadhi? (Makofi)
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba katika Mkoa wa Mara na hasa Wilaya za Bunda, Serengeti, Tarime na Wilaya za maeneo yale kuna kadhia kubwa sana ya wanyama waharibifu wanaotoka hasa katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kuingia katika mashamba na wakati huu ambapo mavuno yanakaribia ndiyo kadhia hii inaongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua za muda mfupi, mwaka tutachukua hatua ya kuongeza askari na magari ya patrol ili kuhakikisha kwamba kama mwaka jana tunawaokoa wananchi na tatizo hili.
Pili, tunazungumza na washirika wetu wa maendeleo kuona ni namna gani tunaweza kuweka fensi ya kilometa 140 ili kuangalia kwa majaribio kama itakuwa ni suluhisho la tatizo hili.
MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri baada ya kero hiyo kurekebishwa lakini bado driver guides wanapofika pale getini wanatakiwa kuandikisha majina ya wageni ambao wanawapeleka Ngorongoro ama Serengeti. Kwa hiyo, hilo nalo bado linaleta usumbufu mkubwa kwa sababu counter inayotumika katika uandikishwaji pamoja na ku-submit zile risiti ni moja. Je, Mamlaka haioni kwamba kuna ulazima sasa na umuhimu wa kuongeza madawati yale ya kutolea huduma hiyo ili kuokoa muda wa wageni unaopotea pale getini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa biashara yoyote inahitaji huduma bora kwa wateja yaani customer care na hili limeonekana likikosekana maeneo ya geti la Lodware na Naabi Hill. Je, Mamlaka haioni kwamba wafanyakazi wale wanahitaji kupatiwa indoor training ya mara kwa mara ili kuweza kufanya utalii wa ushindani na nchi jirani ambako customer care iko juu? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nishukuru sana kwa maswali mazuri ambayo Mheshimiwa Mahawe ameyauliza. Maswali haya ni relevance kabisa kwa kazi ambayo tunaifanya pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza suala la kuongeza madawati tumeliona na pale kwenye lango kuu kutoka Karatu unavyoingia Ngorongoro tumeongeza watendaji kazi kwa ajili ya kuwatambua watu ambao wanataka kuingia ndani ya hifadhi. Shughuli hii ni muhimu kwa sababu za usalama, lakini pia kwa sababu ya kuweza kukagua mapato tuliyokusanya na watu ambao wameingia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini napenda nimueleze Mheshimiwa Mahawe kwenye swali lake la pili kwamba ni kweli wafanyakazi wanahitaji kupatiwa mafunzo ya mara kwa mara ili kuongeza ubora wao katika customer care, lakini pia katika kushirikisha na kutoa maelekezo kwa wageni. Kwa hiyo, shughuli hii tutaendelea kuifanya kila siku na tunategemea kwamba itaongeza ufanisi wa eneo hili.
MHE. OMARY H. BADWEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa utozaji huu wa ushuru na kodi mbalimbali kutoka Wizara hii ya Maliasili na Utalii katika maeneo mbalimbali mahali pengine umekuwa ama haukufikiria vizuri au umekuwa kero. Kwa mfano katika mazao ya ubuyu na ukwaju, mazao ambayo yana bei ndogo sana kwa maana ya shilingi 100 kwa kilo na katika masoko ya Dar es Salaam na maeneo mengine ya miji yanauza kwa shilingi 200. Mazao haya yamekuwa yakivunwa ama na kina mama wenye kipato cha chini au vijana na watu wengine ambao wanapambana na umaskini.
Hata hivyo, Wizara hii kupitia Maliasili wanatoza shilingi 350 kwa kilo na imewafanya sasa wafanyabiashara hawa washindwe kabisa kufanya hii biashara kwa sababu bei yenyewe ni ndogo na sasa inafikia shilingi 500 baada ya ushuru huu.
Je, Mheshimiwa Waziri anafikiria nini juu ya kufuta ushuru huu ili kuwasaidia wale wafanyabiashara wadogo wadogo waweze kupambana na umaskini? (Makofi)
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba katika tozo za mazao ya misitu na mazao katika sekta ya utalii zingine ni kero sana kwa wananchi. Moja ya tozo hizo ambazo ni kero kwa wananchi ni tozo ya matunda ya ubuyu na matunda mengine ya misituni ambayo wananchi wanakusanya na kupeleka kuuza. Napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba tozo hizi ambazo ni kero zitafutwa pamoja na hii ya kutoza kodi ya ubuyu. (Makofi)
MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kumekuwa pia na kero katika sekta ya uwindaji katika utoaji leseni hasa kwa wazawa. Soko hili limemilikiwa zaidi kwa wageni kuliko wazawa. Kwa mfano, leseni ya uwindaji kwa mwaka unalipa dola 600 na tena unalipa dola 200.
Je, Wizara haioni umuhimu wa kuwapa wazawa zaidi ili pia waweze kulinda hifadhi zetu? (Makofi)
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka uliopita wa uwindaji unaoishia mwezi Juni, 2017 vitalu vilivyokuwa vimetolewa asilimia 85 walipewa wazawa na ni vitalu asilimia 15 tu ambavyo walipewa wageni. Kwa hiyo, siyo kweli kwamba utoaji wa vitalu unawapendelea wageni.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Kijiji cha Kasapa wanakabiliwa na changamoto inayofanana na wananchi wa Kijiji cha Nyakanazi. Mwaka huu walikosa kabisa maeneo ya kulima baada ya wahifadhi wa msitu wa TFS Kalambo kuweka mipaka ya eneo lao na kuonekana kijiji na maeneo yote wanayolima, yako ndani ya hifadhi na kwa kuwa Halmashauri tayari imeanza mchakato wa kuliona hilo.
Je, Serikali iko tayari kuungana na mawazo ya Halmashauri pamoja na Ward DC ya Kijiji cha Sintali ili wananchi hawa waweze kupata eneo la kulima?(Makofi)
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na napenda kujibu swali la Mbunge makini sana wa kule Nkasi Kusini, Mheshimiwa Desderius Mipata kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mipata ameleta tatizo hilo tayari kwenye Wizara yetu na nilimuahidi kwamba tutakwenda tuliangalie suala hilo katika site huko na tutafanya maamuzi baada ya hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ahadi yangu iko pale pale na Serikali itatekeleza kama ambavyo itaona inafaa. (Makofi)
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na swali la msingi ambalo niliuliza kuhusu vivutio, Mji wetu wa Iringa ni Mji mkongwe ambao una historia kubwa ya Mtemi wetu Mkwawa jinsi alivyopambana na Mjerumani. Ni juhudi zipi za makusudi ambazo zinafanywa na maliasili kuhakikisha kwamba mji huu wa Iringa na historia kubwa ya Mtemi Mkwawa inaendelea kujulikana katika dunia nzima na Tanzania kwa ujumla?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ni hatua nyingi zinafanywa kuboresha utalii katika eneo zima la Kusini mwa Tanzania, lakini hususan Mji wa Iringa na viunga vyake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tumefungua makumbusho ya historia ya Iringa na utemi wake kule. Pili, Serikali inapanua Uwanja wa Nduli kama ulivyoona kwenye bajeti. Vile vile Serikali imepanga kujenga barabara kutoka kwenye geti la Ruaha kuja Ruaha Mjini. Shughuli hii tumeishughulikia sana na Mheshimiwa Lukuvi katika kuitekeleza pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Miundombinu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2016 tumeanza kwa mara ya kwanza kuwa na Maonesho ya Utalii Kusini mwa Tanzania na yalikuwa Iringa na mwaka huu maonesho hayo ni makubwa zaidi. Waheshimiwa Wabunge, nawakaribisha mje kushiriki katika maonesho hayo. Ahsante.