Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Prof. Jumanne Abdallah Maghembe (8 total)

MHE. ELIAS J. KWANDIKWA aliuliza:-
Serikali imekuwa ikitumia waajiriwa wa muda (vibarua) ambao hawana ujuzi, uadilifu wala taaluma ya uhifadhi:-
(a) Je, ni vibarua wangapi walitumiwa katika Hifadhi ya Kigosi kwa kipindi cha miaka mitano (2010-2015)?
(b) Je, Serikali ilikuwa imetenga kiasi gani cha fedha na ni kiasi gani kililipwa kwa vibarua hao?
WAZIRI WA MALIASILI NAUTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Elias John Kwandikwa, Mbunge wa Ushetu, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya shughuli ambazo hazihitaji ujuzi mahsusi kama usafishaji wa ofisi, kufyeka barabara na mipaka ya hifadhi. Kazi hizo hutolewa kwa wananchi waishio kando ya hifadhi ikiwa ni njia mojawapo ya kuwapatia kipato na kukuza mahusiano mema kati Serikali na wananchi hivyo kuwapa faida za moja kwa moja za kiuchumi kutokana na kuwepo jirani na hifadhi. Aidha, wapo vibarua ambao hufanya kazi zinazohitaji elimu na ujuzi mahsusi wa wastani kama vile ukatibu muhtasi na udereva ambao huhitaji kuwa na vyeti na leseni zinazoruhusu kufanya kazi hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kawaida hakuna kibarua anayefanya kazi za kiuhifadhi moja kwa moja kwani kazi hizo zinahitaji taaluma, ujuzi na uzoefu wa masuala ya uhifadhi wa wanyamapori katika viwango vinavyokubalika na taaluma yenyewe. Ajira za vibarua hutolewa kulingana na mahitaji ya ofisi, hivyo wanaokidhi vigezo hupewa mikataba ya ajira kwa kipindi kisichozidi miezi mitatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Pori la Kigosi kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2010 - 2015 jumla ya vibarua 240 walifanya kazi za muda kama kufyeka barabara na mipaka na kusaidia kufanya usafi wa kambi na miradi ya maendeleo kama vile ujenzi wa nyumba, ukarabati wa majengo kwa kushirikiana na Askari wa Wanyamapori.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi hicho jumla ya shilingi milioni 27.8 zilitumika katika kuwalipa vibarua hao. Aidha, kampuni zinazoendesha shughuli za utalii katika mapori huajiri vibarua kwa ajili ya shughuli zao.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza:-
Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na malalamiko baina ya wakulima na Mamlaka ya Mapori ya Hifadhi ya Misitu, kwa sababu ya kuongezeka kwa watu lakini ardhi haiongezeki, hivyo kufanya ongezeko hili la watu wakose ardhi kwa shughuli zao za kilimo na mambo mengine yahusuyo ardhi:-
Je, ni lini Serikali italeta Bungeni Muswada wa Sheria husika ili kufanya marekebisho katika mipaka ya Hifadhi hizo ili kupata eneo la kilimo kwa wananchi walioongezeka ambao hawana maeneo ya kilimo.
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Genzabuke, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa idadi ya Watanzania inaongezeka siku hadi siku, ambapo 75% ya watu hao wanaishi vijijini na kwamba wananchi wengi wa vijijini wanategemea rasilimali za misitu na ardhi kwa ajili ya maisha yao. Pia, inaeleweka wazi kuwa kasi ya ongezeko la idadi ya watu linachangia katika kuongezeka kwa mahitaji ya mazao ya misitu na ardhi kwa ajili ya kilimo, ufugaji pamoja na makazi. Kukosekana kwa mipango ya matumizi bora ya ardhi ya vijiji, inachochea kuongezeka kwa kasi ya uharibifu wa misitu na ukosefu wa ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mahitaji makubwa na umuhimu wa ardhi katika kukidhi mahitaji ya wananchi na maendeleo ya kiuchumi, Serikali inatambua misitu ni muhimu kwa maisha ya viumbe hai, katika kupunguza hewa ukaa, kulinda hewa safi, kupunguza joto la ardhi, kutunza vyanzo vya maji, upatikanaji wa nishati na shughuli mbalimbali za kibinadamu. Hivyo, kwa kutambua umuhimu wa ustawi wa maisha ya wananchi na uhifadhi wa misitu, Serikali inaendelea kuchukua hatua zinazozingatia uwiano kati ya mahitaji ya maendeleo ya wananchi na uhifadhi wa misitu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua changamoto zinazotokana na upungufu wa ardhi, Wizara inawashauri wananchi wote na Serikali za Vijiji vyote vinavyozunguka misitu ya hifadhi kushirikiana na sekta husika katika kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi itakayolenga kutenga maeneo kwa matumizi mbalimbali kufuatana na mahitaji katika maeneo yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu itaendelea kutoa ushirikiano katika kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi ikiwa ni pamoja na hifadhi ya misitu. Vilevile, tunawaomba Waheshimiwa Wabunge kuwahamasisha wananchi kutumia mbinu za kilimo bora chenye tija na kuibua shughuli nyingine za kiuchumi ambazo hazihitaji matumizi makubwa ya ardhi kama vile ufugaji wa samaki, ufugaji wa nyuki, uanzishaji wa viwanda vidogovidogo na shughuli nyingine ambazo ni rafiki wa mazingira.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN aliuliza:-
Karibu theluthi moja ya ardhi ya Tanzania ni misitu na kuna uhaba mkubwa wa watalaam wa misitu nchini.
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kukiboresha Chuo cha Misitu cha Olmotonyi?
(b)Je, kila mtalaam wa misitu aliyepo leo anasimamia hekta ngapi za eneo?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yussuf Salim Hussein, Mbunge wa Chambani, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna upungufu wa watalaam wa misitu nchini. Kwa sasa kila mtalaam wa misitu aliyepo anasimamia jumla ya hekta 25,000 za misitu. Kimsingi uwiano huu ni mara tano zaidi ya uwiano unaokubalika Kimataifa wa mtaalam mmoja kwa hekta 5, 000. Kwa kutambua hali hii, Wizara yangu imeanza kutatua tatizo hili kwa kuboresha miundombinu ya Chuo cha Misitu Olmotonyi.
Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na Serikali ya Norway inatekeleza mradi wa kuwezesha jamii kupitia mafunzo ya shughuli za usimamizi shirikishi wa mistu na mabadiliko ya tabianchi. Mradi huu unalenga kukijengea chuo uwezo kwa kukarabati nyumba za watumishi saba, kuimarisha maktaba ya chuo kwa kuweka samani, vitabu vya kiada na vitabu 137 vya mada 22 tofauti, vifaa 62 vya kufundishia, kompyuta 15 na kutoa mafunzo ya kompyuta kwa wakutubi watano; ukarabati wa mtandao wa mawasiliano na kuunganisha chuo na Mkongo wa Taifa.
Mheshimiwa Spika, pia mradi unaendelea na ujenzi wa bweni moja lenye uwezo wa kuchukua wanachuo 100 na ukumbi wa mihadhara wenye uwezo wa kuchukua wanachuo 200 kwa wakati mmoja. Vilevile mradi umewajengea uwezo wa kutumia mbinu bora za kufundisha wahadhiri 16 wa chuo hicho. Mradi unatoa mafunzo kwa jamii ya vijijini kuhusu kuhifadhi misitu na shughuli mbadala za kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, kupitia mradi huu, Serikali inatoa ufadhili kwa wananfunzi wa ngazi za cheti na ngazi za diploma ili waweze kukamilisha mafunzo yao katika chuo chetu.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miaka mitatu, kuanzia mwaka 2013/2014 mpaka 2015/2016, Wizara kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania imegharamia ukarabati wa nyumba tisa za watumishi, kumbi za chakula na mikutano; na ununuzi wa kompyuta mbili na basi aina ya Tata kwa ajili ya usafiri wa wanafunzi wanapokwenda kupata mafunzo nje ya chuo.
Mheshimiwa Spika, kutokana na hatua hizi, chuo kumeongeza uwezo wake wa kupokea wanafunzi wengi zaidi na kuwajengea uwezo wawe wataalamu mahiri katika ngazi ya masomo yao.
MHE. ALEX R. GASHAZA aliuliza:-
Maporomoko ya maji ya Rusumo yanapatikana katika Jimbo la Ngara nchini Tanzania na Wilaya ya Kirehe nchini Rwanda kwenye mpaka wa Tanzania na Rwanda na maporomoko haya yanaweza kuwa kivutio kizuri cha kitalii.
Je, Serikali iko tayari kufanya utafiti katika eneo hili ili liweze kurasimishwa kwa ajili ya shughuli za kitalii ili kuongeza pato la Wilaya na Taifa kupitia sekta hiyo ya utalii?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Alex Raphael Gashaza, Mbunge wa Ngara, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa maporomoko ya maji ya Rusumo yaliyopo Wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera, yana uwezo wa kuwa kivutio kizuri cha utalii katika Kanda ya Ziwa Victoria. Wizara iliwahi kutembelea eneo hilo na kushauri kuwa linaweza kutembelewa kama kivutio. Maeneo mengine yanayoweza kujumuishwa katika maporomoko hayo kama kivutio ni maeneo ya hifadhi za Burigi na Kimisi, Bioanuwai ya pekee katika katika misitu ya asili ya Minziro, mapango ya watumwa katika Kata ya Kenza na maporomoko ya maji katika Msitu wa Rubare pamoja na maji ya moto katika Msitu wa Mutagata.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara iko tayari kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Ngara kufanya utafiti unaoweza kuendeleza na kurasimisha maporomoko hayo na mandhari yake kuwa kivutio cha utalii kitakachoongeza pato la Wilaya na Taifa kwa ujumla.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI (K.n.y. MHE. MARY D. MURO) aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha Mbuga ya Saadani iliyoko Mkoa wa Pwani ili kuongeza pato kwa wananchi walio kando ya mbuga hiyo?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mary Deo Muro, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Sera ya Taifa ya Utalii ya 1999 inaelekeza vema jamii zinazoishi ndani au jirani ya maeneo ya hifadhi kushirikishwa katika uhifadhi, uendelezaji na usimamizi wa vivutio vya utalii ikiwa ni pamoja na kunufaika kutokana na mapato yatokanayo na shughuli za utalii katika maeneo husika.
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kwamba miundombinu bora na ya kutosha na huduma bora kwa watalii ni miongoni mwa sababu za msingi za kukua kwa shughuli za utalii katika Hifadhi za Taifa na kuongezeka ka idadi na shughuli za watalii na hivyo kuongezeka kwa pato la Taifa litokanalo na utalii ikijumuisha ajira za kudumu na za muda pale zinapojitokeza; kukua kwa soko la bidhaa zitokanazo na shughuli za kiuchumi za wananchi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya jamii na uwekezaji kwenye vijiji inayohusisha sekta za afya, elimu, maji na mazingira.
Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuboresha miundombinu katika Hifadhi ya Taifa ya Saadani ikiwa ni pamoja na kujenga daraja la muda kuunganisha hifadhi na Mji wa Bagamoyo na Jiji la Dar es Salaam. Aidha, katika mipango ya muda mfupi na muda mrefu, Serikali itakamilisha ujenzi wa daraja la kudumu katika eneo la daraja la muda; kuboresha miundombinu ya malazi kwa wageni ambapo Kampuni ya mwekezaji ijulikanayo kama “Camden Hospitality Group” inakamilisha taratibu za kujenga kambi ya kudumu ya vitanda 30 na kuboresha miundombinu ya barabara na huduma nyingine za utalii ndani ya hifadhi.
Mheshimiwa Spika, Wizara pia inakamilisha utafiti wa wanyamapori waliokuwepo siku za nyuma na wakatoweka ili kuona uwezekano wa kuwarejesha kutoka katika maeneo mengine walikokuwa wameelekea. Wizara itaendelea kuboresha zaidi utangazaji wa vivutio vyenye upekee vya Hifadhi ya Taifa ya Saadani. Jitihada zote hizi zinatarajiwa kuongeza pato kwa wananchi waishio jirani na Hifadhi ya Taifa ya Saadani.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI aliuliza:-
Katika Mkoa wa Mara kuna usumbufu mkubwa unaosababishwa na tembo. Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti tembo hao?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joyce Bitta Sokombi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na madhara yanayosababishwa na wanyamapori, hususan tembo, Serikali imechukua hatua mbalimbali ili kunusuru maisha na mali za wananchi waishio kando ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Kwanza, Serikali imeunda timu ya udhibiti wa wanyamapori hatari na waharibifu ambayo inajumuisha watumishi 14 kutoka kikosi dhidi ya ujangili kilichopo Bunda, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Pori la Akiba Ikorongo – Gurumeti, Halmashauri ya Wilaya na Gurumeti Reserves. Lengo ni kuhakikisha kwamba tukio lolote la uvamizi wa tembo linashughulikiwa mara moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kuweka minara (observations towers) ambayo askari wanyamapori wanatumia kufuatilia mwenendo wa tembo ili pale wanapotoka nje ya hifadhi, hatua za kuwadhibiti zichukuliwe na tatu, kuweka mizinga ya nyuki pembezoni mwa mashamba ili tembo wanapoingia katika mashamba wafukuzwe na nyuki.
Nne, kutumia ndege zisizokuwa na rubani (unmanned aerial vehicles) kwa ajili ya kufukuza tembo. Mafunzo ya kutumia ndege hizo yametolewa kwa watumishi kwa kushirikiana na Shirika la World Animal Protection.Kwa ajili hiyo, Pori la Ikorongo limepewa ndege moja, Halmashauri ya Serengeti imepewa moja na Kikosi Dhidi ya Ujangili Bunda kimepewa ndege moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, tano, kuendelea kutoa elimu ya uhifadhi kwa jamii ili wananchi waepuke kulima katika shoroba za wanyamapori. Sita, kuendelea kufanya utafiti na kushauri wananchi kulima mazao ambayo hayavutii kuliwa na wanyamapori na saba, kuhamasisha Halmashauri ya Wilaya kuandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na jitihada hizi, matukio ya uvamizi wa tembo yamepungua kutoka 128 mwaka 2015/2016 hadi 105 katika mwaka 2016/2017. Aidha, katika mwaka 2015/2016, tembo waliweza kufanya uharibifu hadi umbali wa kilometa 30 kutoka kwenye hifadhi, lakini kwa mwaka 2016/2017 umbali huo umepungua hadi kilometa 12 tu.
MHE. SULEIMAN A. SADDIQ (K.n.y. MHE. GOODLUCK MLINGA) aliuliza:-
Kumekuwa na ongezeko kubwa la wanyama waharibifu kama vile viboko na tembo kwenye maeneo ya mashamba katika Kata za Ruaha, Chilombola, Ilonga, Ketaketa, Mbuga ya Lukande na Lupilo.
Je, Serikali ina mpango gani kuzuia uharibifu huo wa mazao?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Goodluck Mlinga, Mbunge wa Ulanga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kumekuwepo na ongezeko la wanyama wakali na waharibifu katika maeneo mbalimbali nchini yakiwemo Kata ya Ruaha, Chilombola, Ilonga, Ketaketa, Mbuga ya Lukunde pamoja na Lupilo. Kutokana na madhara yanayosababishwa na wanyama waharibifu hususan tembo na viboko, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kunusuru maisha na mali za wananchi. Hatua hizo ni pamoja na:-
(a) Kufanya doria za wanyamapori wakali na waharibifu ili kudhibiti madhara ya wanyamapori hao kwa kutumia Askari Wanyamapori waliopo katika Pori la Akiba Selous eneo la Ilonga, Kikosi Dhidi ya Ujangili pamoja na Askari Wanyamapori katika Halmashauri ya Wilaya Mahenge;
(b) Kutoa elimu ya uhifadhi kwa jamii kuhusu kujiukinga na wanyamapori wakali na waharibu wakiwemo tembo na viboko;
(c) Kuendelea na mbinu mbalimbali za kupunguza madhara yatokanayo na uvamizi wa tembo na kukuza kipato kwa mfano matumizi ya mizinga wa nyuki, oil chafu na kilimo cha pilipili kuzunguka mashamba na kadhalika; na
(d) Aidha, Wizara imekuwa inafanya majararibio ya kutumia ndege zisizokuwa na rubani yaani drones kwa ajili ya kufukuza tembo pindi wanapovamia makazi na mashamba ya wananchi.
MHE. ESTER A. MAHAWE aliuliza:-
Kadi za kulipia Ngorongoro zimekuwa kero kwa wageni na wahudumu kwani muda mwingi umekuwa ukipotea wakati kufanya malipo.
Je, ni lini Serikali itafanya marekebisho ili kuwe na mfumo wa kadi kama za TANAPA?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ester Alexander Mahawe, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Manyara, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imebadilisha mfumo wa malipo na utoaji wa vibali vya kuingia katika Hifadhi ya Ngorongoro.
Mfumo huu mpya kabisa ujulikanao kama Ngorongoro Safari Portal ulianza kutumika tarehe 01 Februari, 2017 na umeonyesha ufanisi mkubwa ikiwa ni pamoja na kuondoa kabisa msongamano wa wageni katika malango ya kuingia kwenye hifadhi na kuongeza ufanisi katika makusanyo ya mapato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo huu mpya uko kwenye mtandao wa internet na hivyo huwezesha wakala wa utalii kulipa na kupata vibali moja kwa moja kwa njia ya mtandao bila kulazimika kufika katika ofisi, kwenda benki au malango ya kuingia katika Hifadhi za Ngorongoro.