Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Prof. Jumanne Abdallah Maghembe (25 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na ninapenda kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa hotuba nzuri iliyotoa malengo thabiti ambayo yamenukuliwa duniani kote kama hotuba ya mfano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuniamini na kunipa dhamana ya kuiongoza Sekta ya Maliasili na Utalii. Wasemaji wengi wameeleza changamoto zilizopo katika sekta hii, lakini kwanza nilikuwa nataka niwahakikishie ndugu zangu kwamba Sekta ya Maliasili ukiondoa misitu inachangia uchumi wetu kwa asilimia 17, lakini ukiongeza misitu mchango wake unafika asilimia 23 ya uchumi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mchango huo, sekta hii ndiyo ya kwanza kutupatia fedha za kigeni kwa kuchangia asilimia 25 ya fedha zote za kigeni.
Pamoja na mchango huu, sekta hii ndiyo inahakikisha tunapata maji, inahakikisha mvua zinakuwa za kuaminika, inahakikisha tunapata watalii wengi sana kutoka maeneo yote duniani. Sekta hii pamoja na changamoto zilizopo, ina ubora katika nchi yetu kuliko nchi zote za Kiafrika, na ni ya pili duniani kote ukiacha Brazil kwa ubora dunia nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu hiyo ni muhimu tupambane sana na changamoto ambazo zinaikabili; ya kwanza ikiwa ujangili. Hili tunapambana nalo kwa kuwafanyia utafiti majangili. Hivi sasa wamebadilisha sana njia zao za kuwaua wanyama ambao wanawahitaji katika mapori yetu. Tembo wanauawa kwa kupewa sumu na wanyama wengine wanapewa sumu tena kwa aina ambayo kwa kweli ni ya kusikitisha sana. Na sisi tunabadilisha mwendo wetu wa kushughulika nao.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi tunafanya majaribio ya ndege ambazo hazina marubani, kwanza kuhakikisha kwamba zinaondoa migogoro kati ya wananchi wenye mashamba na mapori ya akiba na mapori tengefu, lakini pia kuhakikisha kwamba tunaona shughuli za binadamu pamoja na majangili katika maeneo ambayo yana maliasili.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumechukua hatua pia ya kuongeza wafanyakazi ambao wanashughulikia ulinzi wa wanyamapori kutoka askari 1,506 mwaka 2014 na sasa wamefikia askari 2,064. Aidha, tumeongeza vitendea kazi kwa sehemu kubwa sana na tumelitengeneza Shirika la Tower ambalo kazi yake itakuwa kulinda maliasili zetu kwa karibu zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ni kubwa sana na Waheshimiwa Wabunge mmelisema kwa uchungu mkubwa ni uharibifu unaofanywa na wanyamapori katika mashamba na katika maeneo tunakoishi. Tutashirikiana na Wizara ya Ardhi, Wizara ya Mazingira na Wizara ya Kilimo na Mifugo ili kuhakikisha kwamba migogoro hii inaondoka mapema iwezekanavyo. (Makofi)
Aidha, tunachukua hatua mbalimbali za kuhakikisha kwamba mapato yetu kutoka kwenye maliasili zetu yanaongezeka. Kuacha sasa, wizi ule mdogo mdogo unaotendeka ndani, malengo yetu ni kuongeza watalii kutoka 1,100,000 hivi sasa na kufika 3,000,000 mwisho wa mwaka 2018 tukilenga kwamba utalii sasa utupatie asilimia 40 ya mapato yote ya Taifa letu. Ndugu zangu naomba tulinde maliasili zetu. Ahsanteni sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda niwashukuru sana ndugu zangu mnaotutia moyo. Napenda niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wa Chama changu na Wabunge wa Upinzani. Tangu jana hapa hoja zilizotolewa, kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri, unaweza kuziita very constructive. Zilikuwa hoja nzuri sana za kujenga. Zilikuwepo chache ambazo zina miiba, miiba, ndiyo ubinadamu, lakini hoja ambazo zimetolewa hapa kwa kiasi kikubwa zimetujenga, nasi tunatoka hapa tukiwa tumejiamini zaidi katika kazi ambayo tunaifanya ya kuhakikisha kwamba nchi yetu inafaidika zaidi na maliasili ambazo tunazo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge 90 wameleta michango yao kwa maandishi. Na mimi nawaheshimu na ninawashukuru sana. Nimesoma michango ile, kama ingesemwa hapa, pangekuwa na hewa nzuri zaidi, maana ilikuwa ni michango mizuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, waliochangia kwa kuongea hapa Bungeni ni Waheshimiwa Wabunge 55; kwa kweli hii ni faraja kubwa sana na muda kama mlivyoelezwa, siyo rafiki sana. Nitajaribu kutoa majibu kwa upana na ninamshukuru sana Mheshimiwa Makamba, Mheshimiwa Profesa Muhongo, Mheshimiwa AG na wengine wote ambao mmetusaidia katika kujibu maswali kwa utangulizi mzuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme hivi, maliasili zetu na sisi wanadamu na wanyama na viumbe vingine vilivyo chini ya group kubwa la wanyama, tunaishi na mimea yetu kwa mtindo unaoweza kuuita symbiotic, yaani tunaishi kwa kusaidiana. Bila rasilimali zetu hizi za maliasili, tusingeweza kuishi na bila sisi, hizi rasilimali zisingekuwepo. Ninaposema sisi, nina maana ya sisi binadamu na viumbe wote ambao wapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maliasili zetu za misitu na nyuki, wanyamapori na utalii zinatuwekea mfumo wa ikolojia ambao ndiyo unakuwa muhimili mkubwa wa maisha yetu. Hewa tunayotoa sisi kama hewa chafu ili tuweze kuishi inavutwa na majani na kutumika kuzalisha chakula cha majani. Mimea yetu, miti na mimea mingine ndiyo chanzo kikubwa cha kurekebisha mvua yetu, kurekebisha joto katika dunia.
Katika Tanzania, Mwenyezi Mungu ametujalia, tumekuwa na aina tofauti sana, nyingi za mimea na viumbe wengine ambazo zinapatikana Tanzania peke yake na hazipatikani mahali pengine popote duniani na ndiyo maana tuna msingi mkubwa wa utalii kupita nchi zote duniani ukiacha Brazil. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maji ambayo ndiyo uhai wetu yanatoka kwenye misitu yetu na hifadhi zetu nyingine. Maji haya ndiyo tunayotumia nyumbani, ndiyo tunatumia kwa kilimo cha umwagiliaji, tunazalishia umeme kwa miaka mingi katika nchi yetu na ndiyo inaendesha viwanda vyetu. Maliasili hizi tumeelezwa hapa mara nyingi, ni msingi mkubwa wa pato letu la Taifa na zinatuletea asilimia 25 ya fedha zote za kigeni tunazopata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikia hapa na Mheshimiwa Naibu Waziri amejibu vizuri, kwamba tuna mradi wa zaidi ya dola milioni 200 wa kujenga misingi ya utalii Kusini mwa Tanzania. Tutaviboresha viwanja vya ndege, tutaboresha barabara kutoka kwenye viwanja hivyo mpaka kwenye hifadhi zetu na kwa sababu hiyo, wale ambao wamepisha Ruaha ili iwe mbuga yetu kubwa, waliopisha Kitulo, waliopisha Katavi wakae mkao wa kula, maana tunatengeneza mradi ambao utaboresha utalii katika maeneo haya ambayo yana sifa nzuri sawa sawa au hata kuzidi hizi mbuga nyingine ambazo tunazitumia kwa sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya matatizo makubwa ambayo tunayo katika kuboresha utalii Kusini mwa Tanzania, ni bei ya tiketi za ndege. Kutoka Arusha mpaka Kigoma dola 1,800 kwenda na kurudi kwa dola 1,800 unaweza kutoka Dar es Salaam ukaenda New York na kurudi. Kutoka Dar es Salaam kwenda Mpanda; kutoka Dar es Salaam kwenda Iringa ni ajabu bei za ndege zilivyo kubwa.
Kwa hiyo, hatua ya kwanza ambayo tunachukua, tunaanzisha vituo vya kuzipa ndege mafuta katika viwanja hivyo vya ndege ili kuhakikisha kwamba hakuna kisingizio kwamba lazima tutue Tabora kwanza, tutue Dodoma kwanza ndipo twende, kwa hiyo, ni lazima bei ipande. Pia tumeishauri Serikali inunue ndege ndogo kama hizi Fokker Friendships ambazo zinaweza ku-service viwanja vyetu hivi ambavyo ndiko watalii wetu watakapokuwa wanakwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hifadhi zetu ndiyo kiini cha utalii wetu na zinalindwa kwa sheria kama ambavyo tumesema na kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge mmetueleza, mmerudia; Sheria ya Wanyamapori hasa sehemu ile ya 18(2), Sheria ya Misitu na Sheria ya Mazingira. Sheria hizi zinatutaka tulinde, tuhifadhi na tuendeleze maliasili zetu. Hizi siyo sheria za kwanza ambazo zinatulazimisha tuangalie shughuli zetu; wote tunajua watu ambao wamejenga kwenye hifadhi za barabara katika maeneo mengi nchini kwetu wameondewa na hata bila fidia kwa sababu wameingilia hifadhi ya barabara na watu ambao wamejenga kwenye mabonde. Kwa hiyo, siyo mara ya kwanza kuhakikisha kwamba tunasimamia Sheria za Uhifadhi kama ambavyo zimetungwa na Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niliambia Bunge lako Tukufu kwamba japo nchi nyingine za jirani zina sheria na zinavyozitekeleza zinakuwa za imla sana; kwa mfano, nchini Kenya ukiingia kwenye Hifadhi ya Taifa na huna sababu ya kuwa hapo, wanapiga risasi bila kukuuliza swali na nchini Botswana, hivyo hivyo. Nchini Tanzania hatuwezi kufanya hivyo, hata kama tunaingia kwenye matatizo ambayo wakati mwingine tunakuwa nayo.
Kwa hiyo, nimesikiliza kwa makini na nimesikia kwamba wafanyakazi wa wanyamapori, wafanyakazi wa misitu na walinzi wa hifadhi zetu wakati mwingine wanakuwa na roho mbaya sana. Wanapiga raia, hatukuwatuma kuwapiga raia; wanapiga mifugo risasi, hatukuwatuma kupiga mifugo risasi. Pia hatukuwatuma kuchoma nyumba za watu; hatukuwatuma kuwaumiza watu. Kwa hiyo, Wizara yangu itachukua hatua kali pale ambapo tutathibitisha kabisa kwamba askari alipiga watu, tutamchulia hatua kali sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hiyo, baada ya kikao hiki cha Bunge, tutawaita wahifadhi wote tuangaliane kwenye macho, tuelezane tabia nzuri ya kufuata huko kwenye hifadhi zetu na wale ambao hawatafikia kiwango cha weledi tunachokitaka, tutakapobadilisha hili Jeshi la Uhifadhi hatutawaingiza kwenye Paramilitary Force ambayo tunaijenga. Tutapeleka wale tu ambao wana weledi na uaminifu wa kutosha wa kuhakikisha kwamba Watanzania wamewaajiri ili walinde maliasili zetu, lakini hawakuwaajiri ili wawapige, wawaumize, wapige risasi ng‟ombe zao au wapasue nyumba zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na mjadala ambao umeendelea hapa, nimeelewa kwamba katika maeneo mengi bado wakulima wanavuna mazao yao. Kwa sababu hiyo, ninawaomba wenzangu huko, Wakuu wa Mikoa kwamba wasiwabughudhi watu wakati wanapovuna mazao yao; na hivyo wawaache hao ng‟ombe kwanza mpaka watu wamalize kuvuna ndipo watekeleze agizo la Waziri Mkuu ambalo amelitoa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala ambalo lisememwa hapa la huyu mtu anayeitwa Green Miles Safari ambaye alifutiwa leseni, akafutiwa na vitalu vyake vyote; kwa nini Serikali imemrudishia leseni na kitalu chake?
Mheshimiwa Spika, ni vizuri Bunge lako Tukufu likajua kwamba katika eneo la Natron kabla ya mwaka 2011 kulikuwa na vitalu viwili; Natron North na Natron South; na kwamba baada ya kuweka tathmini katika vitalu hivi, vitalu vile vilionekana ni vikubwa sana na kwa hiyo, vikagawanywa tukatoa vitalu vinne. Majina yake siyo muhimu, lakini moja ya hicho kitalu kilipewa Green Miles na kingine akapewa Wengert Windrose Safaris. Green Miles Safari ni Mwarabu na Wengert Windrose ni Mmbarekani. Kwa hiyo, siasa za Kimarekani na Kiarabu zimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yule Mmarekani aliyekuwa na hicho kitalu chote kikubwa alisema eneo alilopewa Green Miles ndilo eneo zuri zaidi na yeye amewekeza zaidi hapo, kwa hiyo, hataki kuondoka. Anataka abaki na hicho kitalu chake hata kama hakupewa na Serikali. Idara ya Wanyamapori imejaribu kusuluhisha jambo hilo ikashindwa. Wengert Windrose akaenda Mahakamani kupinga jambo hilo kisheria. Kabla kesi hiyo haijamalizika, ikatolewa DVD hapa ambayo inaonesha watu waliokuwa wanawinda katika kitalu kimoja cha Green Miles huko Selous, siyo Lake Natron; huko Selous walifanya makosa na kuwinda kinyume na kanuni za uwindaji zilivyowekwa. Wale wote ambao mtapenda kuiona hiyo DVD tutakuwa tayari ku-share tuwaoneshe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya ile DVD kuoneshwa hapa, Mheshimiwa Waziri aliongea na vyombo vya habari, akasimamisha leseni, akasimamisha na vitalu vyote vya Green Miles Safaris. Tarehe 30 Machi, 2015 Mahakama ikaamua, ikasema kitalu alichopewa Green Miles ni haki yake. Mahakama Kuu ya Tanzania sehemu ya biashara, ni haki yake, kwa hiyo, aruhusiwe kuendelea na kazi yake.
Kwa hiyo, ukiangalia ile Sheria ya Wanyamapori Kifungu cha 38(12)(c) ndiyo inayompa Waziri mamlaka ya kugawa vitalu, lakini pia mamlaka ya kumnyang‟anya mtu kitalu. Hata hivyo ukiangalia ile mamlaka ya kunyang‟anya kitalu inasema; “Waziri hatamnyang‟anya mtu kitalu kama mtu huyo hakuonekana ana hatia na Mahakama ya Tanzania.” Sasa huyu mtu hakuonekana ana hatia na Mahakama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tulichofanya ni kutekeleza sheria na kutekeleza maamuzi ya Mahakama yetu. Kwa hiyo, hakuna jambo ambalo limefanyika hapa ambalo halikufanyika kwa utaratibu unaotakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, huyu bwana, alirudishiwa kitalu chake na amerudishiwa leseni ya kuwinda. Hata hivyo, wale wafanyakazi wa Serikali walioshiriki na wafanyakazi wa Green Mile Safaris na kuonekana kwenye ile DVD, tunaandaa utaratibu na charges tumeshapeleka kwa DPP ili waweze kufunguliwa mashitaka kwa kosa la kuwinda kinyume cha Kanuni. Sasa huwezi kwenda kumnyonga baba kama mtoto wake ndio ameua mtu. Kama mtoto wake amaeua mtu na ni mtu mzima, yule mtoto ana-face makosa yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia niongee kidogo kuhusu TANAPA. Nawashukuru sana wengi ambao mmewapongeza TANAPA kwa kazi nzuri ambayo wanafanya. Napenda pia niseme, sentensi moja moja kwanza kwamba, Serikali haichukui mapato ya TANAPA na kuyaweka kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali, kilichobadilishwa ni TANAPA na mashirika mengine yote ya umma, zile akaunti zake zote za makusanyo, zinafunguliwa Central Bank. Kwa hiyo, wakishapokea pesa kwenye Commercial Bank, ile Commercial Bank ina-transfer mapato yale kwenye Central Bank. Wakifanya matumizi, wanachukuwa fedha kule kwenye Central Bank na kutumia kama kawaida. Cha muhimu ni kutaka kujua kwa uhakika mashirika haya yote tulionayo, mapato yake ni kiasi gani, yanatumikaje na kwa wakati gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya madawati ya thamani ya shilingi bilioni moja, ambayo ni madawati 16,500, ambayo tulimkabidhi Mheshimiwa Makamu wa Rais wiki iliyopita, yametoka kwenye bajeti ya TANAPA ya Corporate Social Responsibility, siyo kwamba tumechukuwa fedha za mipango ya kazi ya TANAPA na kutengenezea madawati, hata kidogo!
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda at this juncture nieleze kidogo kuhusu haya madawati yote ambayo yatatolewa na Wizara ya Maliasili na Utalii. Shirika la TANAPA limechangia madawati 16,500, katika Wilaya 55 na kila Wilaya itapata madawati 300 ambayo yatakaliwa na wanafunzi 300 mara tatu; na hizi ni zile Wilaya zinazozunguka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, imechangia madawati 2,000 katika Tarafa ya Ngorogoro yenye thamani ya shilingi milioni 140 na itatoa madawati mengine 10,000 kuchangia Mfuko wa Madawati wa Wizara; TFS itatoa madawati 20,000 na kutoa meta za ujazo za magogo 15,000 za misitu kama mgao maalum kwa kikosi cha Magereza na madawati mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri zitaruhusiwa kuyanunua kutoka kwenye mashamba yetu mbalimbali bila kutoa mrahaba, lakini kulipa asilimia 25 ya mrahaba kwa ajili ya fedha zinazotakiwa katika kurudishia kupanda miti katika meneo hayo yatakayokatwa. Jumla ya madawati 168,500 yatatolewa na haya yana uwezo wa kukaliwa na wanafunzi 505,050.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niende kwa haraka katika suala la concession fees. Ni kweli kwamba mwaka 2007 nilipokuwa Waziri wa Maliasili na Utalii tulitangaza concession fee ya kitanda dola 50. Baadaye watoa huduma wakakataa mchango huo, wakaenda Mahakamani mwaka 2007 na mwaka 2008 ndiyo Mahakama ikahamua. Kwa hiyo, kilichotokea hapo katikakati, Mahakama ilikuwa haijaamua. Sasa hivi tunangojea Bodi ya TANAPA ikamilike kuteuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya TANAPA ni tofauti kabisa katika kuunda Bodi na sheria nyingine. Wizara imefanya inayotakiwa kufanya na tunangojea hatua ya mwisho ya kukamilisha uteuzi huo na baada ya uteuzi huo, Bodi itapitia concession fee mpya na ikishapitia tutai-gazette na kuanza kutumika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine lililosemwa hapa na nafuu niliseme linahusu lodge ya Mikumi. Tender ilishatangazwa, mjenzi ameshapatikana na tunangoja mjenzi huyo ajikusanye, aanze kujenga lodge hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la wabeba mizigo, wapishi na waongoza misafara katika Mlima Kilimanjaro; Wizara ya Kazi, Wizara ya Maliasili tulikutana na Vyama hivi na wale wenyewe wanaohusika, wakatengenezeana mkataba wa malipo na tukaweka msimamo. Wale watoa huduma, lazima wawalipe wale wabeba mizigo, wapishi na waongoza misafara kabla hawajaanza kupanda mlimani na wasiwarushe pesa zao. Kwa hiyo, tunangoja tuone utekelezaji unavyokwenda na hivi sasa wana mikataba na bei ya kupanda ni dola 10 kila siku kwa mbeba mizigo; dola 15 kila siku kwa mpishi, nadhani na dola 30 kwa mwongoza msafara. Kwa hiyo, hilo liko vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Mlima Kilimanjaro ni kweli kwamba kuna uchafu sana katika njia ya kupanda na njia zote zile. Suala la kutengeneza vyoo na maeneo mengine ya kupumzika liko mikononi. Tender ya Kimataifa ilitangazwa ili kupata vyoo ambavyo vinageuza kinyesi kiwe vumbi (powder) ili kupunguza uchafu kule juu ya mlima. Kwa sababu vyoo vyenyewe vinavyotakiwa ni vingi na bei ya kuvijenga vyote ni zaidi shilingi bilioni moja, ilitangazwa Kimataifa na tender ilikwishatolewa kwa Kampuni ya Korea ya Kusini, lakini Bodi ikija, Mwenyekiti ndio atasaini hiyo. Maana tender ya zaidi ya shilingi bilioni moja ni lazima isainiwe na Mwenyekiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nataka kuliongelea hapa linahusu Watanzania wanaopewa ruhusa wenyewe au kampuni zao kufanya biashara ya wanyama hai. Wanyama hai wanaoruhusiwa kwa sasa, baada ya ile scandal ya kubeba twiga ndani ya ndege na kusafirisha nje ya nchi, wanyama wanaohurusiwa sasa ni primates hawa wadogo wadogo; nyani, tumbili na hawa wanyama wadogo, aina ya kenge, reptiles, ndege aina mbalimbali pamoja na wadudu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, imeonekana kila siku tunapata taarifa ya Watanzania kusafirisha Wanyama nje ya nchi bila utaratibu; bila vibali, bila ruhusa, bila kitu chochote. Wanyama wanakamatwa Hong Kong, Thailand, Eastern Europe, wanakamtwa kila mahali! Hawa waliokamatwa na tumbili juzi, siwezi kusema jambo hilo kwa sababu liko mahakamani, lakini limefikishwa mahakamani kwa sababu kuna ushahidi kabisa kwamba walikuwa wanafanya michezo. Halafu wanyama hawa wanaosafirishwa nje, hata wale ambao wanakatazwa na conference of parties, wanapelekwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuna jina chafu huko kwa sababu ya watu ambao wanapeleka wanyama hai bila utaratibu. Hakuna utaratibu mzuri uliowekwa kuhakikisha kwamba tunaweza kudhibiti biashara hata hii biashara hii ikaipatia Taifa pesa, wale tumbili walikuwa wanapelekwa for medical research.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu anayekuja kupeleka wale wanyama wala hafanyi declaration ya aina yoyote kwamba wale wanyama wanakwenda kutumika kwa ajili gani? Kama wanaenda kutumika kwenye zoo, unaweza kuelewa; hawana faida kubwa sana ambayo unaweza kusimama imara ukasema hakuna ruhusa kupeleka; lakini wengine wanapelekwa kwa ajili ya utafiti wa dawa. Kwamba huyu nyani ni jamii ya mtu, tukitumia dawa ya namna hii kutibu hiki, inaweza kuponya au haiwezi kuponya? Tutumie kiasi gani? Tumtibu kwa muda gani ili huu ugonjwa upone? Dawa ikipatikana, ile kampuni inapata billions of dollars na sisi tunabaki na nyani aliyeuzwa kwa dola 15.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuanzia leo hivi nilivyosimama hapa, ninasimamisha kwa muda wa miaka mitatu usafirishaji wote wa wanyama hai kutoka Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba, wanyama wakubwa, swala, pundamilia, twiga, hawakubaliwi, lakini bado wanasafirishwa, bado wanaibiwa, kwa hiyo, tunasimamisha. Hata chawa wa Tanzania hatasafirishwa nje ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi hiki cha miaka mitatu, Idara ya Wanyamapori itajipanga na kuweka utaratibu unaofaa ili Serikali ikiangalia na wenyewe unafaa, ndiyo biashara hiyo iweze kuruhusiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, liko tatizo la Sao hill. Muda hauko rafiki sana, lakini mradi wa misitu ya kupanda wa Sao Hill ulianzishwa kwa minajili ya kujenga kiwanda cha karatasi. Wakati umeanzishwa, ulianzishwa pia mradi wa kujenga kiwanda cha karatasi pale Ruvu, Kongowe. Kiwanda kilipangwa kijengwe Morogoro, unapoingilia Mto Ruvu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi ule wa Ruvu ulikuwa umepangwa kwa pine ile ya Carribean ambayo haikuweza kukua katika mazingira yale. Pine iliyoanzishwa kule Sao Hill; pine ya Ellioti iliota na kukua vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, baada ya magogo kukua, kiwanda cha Sao Hill kikajengwa kama Kiwanda cha NDC, SU (Shirika la Umma). Tulipoendesha kikatushinda, tukakiuza kama ambavyo sasa kinamilikiwa na mtu binafsi. Sasa wakati tunacho kiwanda chetu, mi-pine ambayo tulikuwa tunatumia ya miaka 14, hiyo ndiyo inatumika kuzalisha paper, ndiyo kawaida, dunia nzima! Unaangalia ule mti, uone wakati ambao fiber ile ya kutengenezea paper ni ndefu kupita wakati wote; na kwetu hapa Tanzania, pale Sao Hill ni miaka 14.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, miti ile ya miaka 14, haifai kupasua mbao. Ndiyo maana wao walikuwa na mkataba na Serikali wa kuuziwa miti ile ambayo ni michanga na midogo ambayo huwezi kupasua mbao kwa shilingi 14,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, actually mwaka 2007, ukiangalia bajeti ambayo tulisoma hapa, yale magogo ya kutengenezea karatasi yalikuwa yanauzwa shilingi 1,700. Tuliyapandisha bei hapa mwaka 2007, ndiyo ilifika hapo; na magogo yale ya kupasua mbao yalikuwa shilingi 18,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu mtu aliyenunua kiwanda hicho, naye alinunua kwa lengo lile lile, kutengeneza karatasi. Kile kiwanda ambacho kilijengwa pale na NDC, kilijengwa kutengeneza craft paper.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mipango iliyokuwepo ni kwamba kile ambacho kitajengwa pale Bagamoyo, ndiyo kitamalizia craft paper kuwa karatasi hii nyeupe ambayo tunatumia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ndiyo maana unaona yanayotokea pale. Kwanza wamepewa bei ile ya chini ya pulp na bei hiyo ni tofauti na wale ambao wanatengeneza mbao. Kwa sababu bei ya paper na mbao ni tofauti kabisa. Ukiwa na kiwanda cha karatasi kinachonunua magogo kwa bei ya timber, hakiwezi kuuza karatasi barabarani, ndiyo jambo muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kilichotufikisha pale ambapo wanatumia magogo makubwa kama wale wanaopasua mbao, ni ule muda uliotumika kuanzia tuliposhindwa kukiendesha mpaka tulipopata mwekezaji. Ile miti yote ambayo ilikuwa kwa ajili ya kuzalisha paper, ikawa imekuwa magogo makubwa, lakini hakuna eneo kubwa zaidi ambalo lilipandwa.
Kwa hiyo, ile yote ikawa lazima igawanywe, nyingine itengenezwe paper kwa bei ya paper and pulp na nyingine itengeneze mbao na ndiyo sad story ya pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa cha muhimu wananchi wa Mufindi, Njombe, Mbeya na Morogoro mpande miti kwenye mashamba yenu. Pale Sao Hill penyewe kuna four thousand hectors ambazo wananchi wanaweza kupanda miti yao. Mpande miti ile, ikiwa midogo, mnaweza kuiuza kama pulp and paper, lakini mkiacha ikiwa mikubwa mnaweza kujikwamua kiuchumi kama Mheshimiwa Mbunge wangu wa Viti Maalum alivyosema kwa uchungu sana na mimi namuunga mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu itaendelea kuwapa miche bure ili muweze kupanda miti katika eneo lote hilo na mjitegemee hapo badaye, mjikwamuwe kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niseme kwamba suala hili la migao ambalo limelalamikiwa hapa, na mimi nimelalamikiwa. Nimesema mgao mpaka kwanza tuupitie ule utaratibu wake na ndiyo tutatoa mgao. Mwaka huu hakuna mgao mwezi wa sita na labda hata mwezi wa saba hautatoka mpaka tumejua namna ya kuugawa vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa bado nina karatasi nyingi hapa, lakini muda ndiyo umekwisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti napenda nikushukuru sana kwa nafasi hii, mapema kabisa niseme kwamba naunga mkono hoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumzia juu ya utalii na namna ambavyo tunaweza kuuboresha utalii wetu. Nianze tu kwa kusema kwamba utalii wetu unachangia asilimia 17.5 ya mapato yetu yote ya mwaka ya Taifa na asilimia 25 ya fedha zote za kigeni tunazozipata. Aidha, inatoa ajira kwa watu laki tano, ajira za moja kwa moja na Watanzania milioni moja wamejiajiri wao wenyewe katika utalii na potential ya kuongezeka ni kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sekta ya utalii ikiwa na mchango wake mkubwa huu na ukizingatia kwamba hata mtu anayenunua sukari, unga, misumari kwenye duka la mtaani analipa VAT. Hutegemei kwamba sekta ambayo inachangia karibu moja ya tano ya pato lote la Taifa nchini ifanye biashara hiyo bila kulipa au kuchangia mapato ya kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utakumbuka wakati ulipokuwa Mwenyekiti wa Kamati hii ya Bajeti mwezi Juni mwaka 2015 mliwaita wadau wengi sana kuzungumza nao na kuangalia namna ya kupanua wigo wa kodi hapa nchini. Mwezi Juni mwaka 2015 mlikutana na wadau wa utalii na kuwapa taarifa kwamba mmeona kwamba huduma za utalii ni moja ya maeneo ambayo mnafikiria kuyaongeza kwenye wigo wa kodi. Wakati ule Wadau wakaomba mwaka mmoja ili waweze kujiandaa na kweli kwa mwaka ule 2015/2016 wakapewa ahueni hiyo na mwaka 2016/2017 ndiyo kodi hii ikaingizwa kama mapendekezo ya Kamati yetu hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa ni-propose hata tabasamu kidogo kwamba Kamati hii imekuwa na mchango mkubwa katika kuiangalia bajeti na kuongeza mapato ya Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, VAT inatumika duniani kote, nchi jirani yetu iliondoa VAT katika kipindi hiki cha mwaka 2016/2017 kwa sababu maalum. Katika mwaka 2013/2014, Watalii walioingia kule walikuwa milioni mbili lakini mwaka 2015/2016 waliteremka wakafika milioni moja nukta tatu. Kwa sababu hiyo wakaona labda wakiondoa VAT watarudisha watalii wafike kiwango kile ambacho kilikuwa nyuma na ninyi mnajua wote kwamba ilitokana na Ugaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka huu wa kwanza wa kutoza VAT hatujaona negative impact ya VAT kwenye idadi ya watalii. Napenda pia niseme kwa sababu muda wenyewe ni mfupi sana na niwapongeze Waheshimiwa Wabunge…
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba kuchukua fursa hii kukushukuru sana wewe binafsi na Bunge lako Tukufu kwa kupokea, kujadili na kutoa maoni na ushauri pamoja na maelekezo katika maeneo pengine kufuatia hotuba ya makadirio ya bajeti ya Wizara yangu kwa mwaka 2017/2018. Aidha, namshukuru sana Mheshimiwa Atashasta Nditiye, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa uchambuzi na maoni kuhusu utekelezaji wa bajeti ya mwaka huu wa fedha unaokuja na Maoni ya Kamati Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka 2017/2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Maoni na Ushauri wa Kamati umegusa maeneo ya ufinyu wa bajeti, ushirikishaji wa mamlaka nyingine za Serikali na wananchi, utangazaji wa utalii, migogoro ya ardhi kati ya maeneo yaliyohifadhiwa na wananchi, mgongano wa sheria, uwekaji wa mipaka, utatuzi wa mgogoro wa Loliondo…
udhibiti wa ujangili na masuala kuhusu maendeleo ya sekta ya utalii nchini. Ushauri na maoni haya ya Kamati utazingatiwa na wizara na tutaufanyia kazi kwa jinsi ambavyo tutaweza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nafasi hiyo hiyo namshukuru Mheshimiwa Esther Nicolas Matiko, Msemaji wa Kambi ya Upinzani wa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kutoa maoni ya kambi yake na maoni hayo na yenyewe tumeyapokea na tutayaangalia kwa makini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba yetu imejadiliwa na Waheshimiwa Wabunge kwa undani sana; jumla ya Waheshimiwa Wabunge 142 walijadili bajeti yetu. Waliochangia kwa mdomo walikuwa Waheshimiwa Wabunge 76 na walioleta maandishi kama mchango wao ni Waheshimiwa Wabunge 66.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda ambao umenipa na michango ambayo imeletwa ukubwa wake, ubora na umuhimu wake hatutaweza kuyatendea haki mawazo yote haya yaliyotolewa katika hotuba hii ya dakika 30. Ninachowaomba na kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge ni kwamba tumepokea michango hii na tumeifurahia kwakuwa critical review ya performance ya Wizara ya Maliasili na Utalii na tutaichukua kwa hali hiyo na kushughulika nayo mpaka tupate majawabu. Tunategemea kabisa kwa ushirikiano ambao umeonyeshwa hapa, willingness ya Waheshimiwa Wabunge kushiriki na kutusaidia hakuna litakaloshindikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nianze kujibu masuala ambayo yamejitokeza na yamejitokeza kwa nguvu, si kwa umuhimu kwamba yale ambayo hatutayafikia siyo muhimu, ni kwa sababu tu ya muda.

Kwanza nitaongelea juu ya Kamati ya Wizara tano ambayo imeundwa kwa ajili ya kutatua migogoro ambayo inaisibu Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Kilimo, Wizara ya TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu na pengine inasibu Wizara ya Mazingira lakini ikiwa chini ya Uenyekiti wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati hii imeundwa na Kamati ilipoundwa imepitia taarifa zote za migogoro ya ardhi na migogoro mingine ambayo ni kati ya wananchi na Serikali katika maeneo mbalimbali ya nchi hii. Jumla ya ripoti 19 zimepitiwa na ni zote ambazo zimetokana na Bunge, Serikali yenyewe na kadhalika. Ripoti hizo zikaifanya Kamati ikatembelea mikoa kumi kama sampuli ya maeneo ambayo yameguswa na ripoti na ikaja na migogoro 1,246 ambayo inahitaji kutatuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ikawasilisha migogoro hiyo kwa makatibu wakuu ambao nao tarehe 8 Mei, 2017 wakaiwasilisha kwa timu ya Mawaziri wanne. Tukaipokea ripoti ile na tukaona kwamba Kamati ile iendelee na kazi ili iweke mkakati wa utekelezaji wa ripoti ambayo wameileta. Tumewakea timeframe na kwamba kabla ya tarehe 10 Juni, 2017 wataiwasilisha ripoti yao kwa Makatibu Wakuu wa Wizara sita na tarehe 10 Mawaziri wa Kilimo, Maliasili, TAMISEMI, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais tutakutana chini ya uenyekiti wa Waziri wa Ardhi kuiangalia ripoti hiyo na mkakati wake wa utekelezaji kabla hatujapeleka ripoti hiyo kwa viongozi wetu kwa kupata kibali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo,nataka niwaombe sana wale wote ambao wameongea hapa kwa hisia kubwa juu ya migogoro iliyopo kati ya hifadhi zetu na mifugo, kati ya hifadhi zetu na wakulima, kati ya hifadhi zetu na watu waliojenga katika maeneo mbalimbali kwamba wavute subira kwa sababu hili jambo linafanyiwa kazi na kazi hii inafanywa kwa nguvu sana na kwa usimamizi wa Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tutapata majawabu na hatutateteleka katika kuyatekeleza. Nimemsikiliza sana Mheshimiwa Joseph Musukuma, classmate wangu Profesa Anna Tibaijuka jana na nimewasikiliza sana Waheshimiwa Wabunge wenzangu wakina Mheshimiwa Kanyasu, Mheshimiwa Joseph Kakunda na Mheshimiwa Cosato Chumi, nimewasikiliza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimewasikiliza na wengine na jambo hili tunakwenda kulitekeleza, lakini wakati tulipokuwa tunasikiliza mambo haya pia tumejifunza vitu hapa maana yametolewa madarasa aina mbalimbali. Kutokana na madarasa hayo tumejifunza kwamba kuma muingiliano mkubwa sana wa shughuli za kibinadamu na uhifadhi. Hili ni jambo ambalo lazima tuanze nalo. Pili ni kwamba tunahitaji kilimo kwa ajili ya kushiba kwetu vile vile kwa ajili ya kujenga uchumi wa nchi yetu, lakini kilimo kinahitaji maji kwa ajili ya umwagiliaji. Kwa sababu hiyo kama tunataka kumwagilia maji na tunaongea na kusema kwamba hatuwezi kuwa na tija katika kilimo lazima tuhifadhi misitu kule ambako maji yanatoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji sana mifugo, na mimi ninaamini kabisa kwamba hili ni giant kubwa ambalo limelala. Mchango wa mifugo bado hatujauona. Mchango wa mifugo ule unaouona kule Uholanzi, kwenye ile cattle belt ya Marekani, hujauona hapa. Potential ya hilo giant ipo na giant hilo linahitaji maji, giant hilo linahitaji mvua, giant hilo linahitaji kutunzwa na linahitaji liepushwe na magonjwa na maambukizi mengine ya mifumo ya ikolojia ambayo inaweza kuzingatiwa na hifadhi zetu. Kwa hiyo, tunahitaji misitu itupe mvua, itupe maji, itupe hewa na itupe bidhaa nyingine zile za kiikolojia ili maisha yetu yaweze kuwa bora na vilevile ili tuweze kufanya shughuli zetu hizi za uchumi, kilimo, mifugo na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji sana wanyamapori na Mwenyezi Mungu ametupa wanyamapori hawa sisi Watanzania kwa ajili ya utalii. Kama mmejumlisha tarakimu vizuri hapa sekta hii ya utalii inachangia asilimia 21.4 ya Pato la Taifa ukijumlisha aslimia 3.9 ya misitu na asilimia 17.5 ya utalii na wanyamapori. Lakini wanyama hawa wanatusaidia pia katika kutafuta dawa kwa maisha yetu ya baadaye, ni viumbe ambavyo lazima tuwe nao ili kuhakikisha maisha yetu na longevity ya maisha yetu. Kwa hiyo, wakati umefika, kwa kweli, na amesema hapa Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati. Sisi katika kujifunza mambo yaliyopita hapa ndani tumejifunza kwamba wakati umefika sasa tusiwe na makampuni zaidi ya manne ndani ya sekta hii ya wanyamapori, tuwe na kampuni hii moja tu ambayo itapunguza gharama katika uendeshaji. Tutafundisha Jeshi la Wahifadhi na jeshi hilo tutakalolitengeneza ni jeshi moja tu ambalo litakuwa na malezi chini ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania ili kujenga nidhamu, kuheshimu haki za binadamu na kufanya kazi kama ambavyo maslahi ya Taifa yanahitaji. Kwa hiyo, jeshi hilo ambalo tunaliandaa hivi sasa (Jeshi Usu) litakuwa na chain ya command moja na litawajibika kijeshi kwa makosa ya haki za binadamu na usaliti wa Taifa au usaliti wa uchumi wa nchi yetu. Kwa hiyo, hilo ni moja ya masomo ambayo tumejifunza hapa.

Waheshimiwa Wabunge wengi wameongelea kwa uchungu juu ya utalii. Kwanza niseme kwamba tumefurahi sana kupata michango hii ya utalii, lakini nimeona katika maono yetu na definition ya utalii naona kama kuna tofauti hivi ya mawazo. Sisi tumetumia maana ya utalii kama inavyotumiwa na United Nations Tourism Organisation, hiyo ndiyo definition; ya mtu anayeondoka pale alipo kusafiri kwenda nchi za nje au kutoka pale alipo kwenda mahali pengine kwa shughuli inayozidi saa 24 lakini haifikii mwaka mzima akiondoka nyumbani kwake; hata kama anakwenda kwa biashara, anakwenda kwa vitu vingine, lakini wakati akiwa kule atakuwa anatoa huduma ambazo mtalii akifika mahali anazipata kama kukaa kwenye hoteli na kutumia huduma za aina hiyo kule anakokwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo takwimu ambazo tumezitoa ni takwimu ambazo zimekusanywa vizuri sana na timu ambayo inaundwa na Wizara yangu ya Maliasili na Utalii, Jeshi la Uhamiaji, Benki Kuu ya Tanzania, Kamishna wa Utalii kule Zanzibar na huduma zetu za kiuchumi wa ndani ya nchi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Msemaji wa Kambi ya Upinzani wakati ukiwa na nafasi nitakupa hizi takwimu ili uweze kuona ni jinsi gani tumezikokotoa na ni jinsi gani ambavyo ile thought process imekwenda na kwamba zile takwimu ambazo umetupa hapa si za kweli. Tumepata mawazo, na ni kweli kwamba utangazaji wetu wa vivutio vya utalii bado ni mdogo kwa sababu ya fedha ambazo tunazo. Hata hivyo Serikali imeondoa hatua ya kwanza na inakwenda mbele na mwelekeo ambao tunao na mipango ambayo tunayo inatuwezesha sasa tupige hatua kubwa katika kuujulisha ulimwengu kwamba yule giant wa utalii anayeitwa Tanzania sasa ameanza kutembea. Kama mnavyokumbuka, sisi kwa tathmini ya World Economic Forum ya mwaka 2014, sisi ni wa pili baada ya Brazil kwa kuwa na vivutio vizuri, hasa vile vya nature, tukifuatia Brazil huku duniani, hakuna nchi nyingine tena. Lakini kuanzia mwaka 2014, tukafika mwishoni mwa 2015, tumeanza kushuka kwa sababu tumekuwa na maono tofauti kwa jinsi ambavyo tunaviona hivi vivutio vya utalii. Wengine kati yetu wanayaona ni maeneo mazuri ya kuchunga ng’ombe, wengine wanaona ni maeneo mazuri ya kupeleka utalii, wengine wanaona ni maeneo mazuri ya kulima, na kwa sababu ya vitendo hivi mbalimbali tumefika mahali sasa tumefika Taifa la nane katika mataifa ya duniani katika ubora wa vivutio vyetu vile ambavyo ni natural.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nataka niwaombe ndugu zangu, tuvilinde hivi vivutio vyetu vya utalii kama tunavyoweza kuweka mboni na kulinda macho yetu, na hatujachelewa. Hatujachelewa kwa sababu nina imani kabisa hii Kamati yetu itaweka matumizi mengine hapa, matumizi mengine hapa na utalii na uhifadhi hapa na tutarudi kule ambapo tulikuwa. Katika Bara la Afrika kuna vivutio vya kimataifa, vya kidunia 50, kati ya hivyo 50, vivutio vya kwanza nane vinatoka Tanzania. Tusiharibu jambo hili zuri namna hii kwa kuwa tu tunataka tuoneshe kwamba sisi we are on top of the world and we can use it for anything, tusifanye hivyo. Tulinde na tuangalie ni kitu gani kinaleta ugali ndani ya midomo yetu, na kule kwingine tuangalie ni namna gani ambavyo sasa tutaboresha kilimo. Hatuwezi kulima sasa mashamba kwa kukimbilia kulima hekta 200 ili tupate magunia 200 ya mahindi, lazima tulime hekta 10 tupate magunia 200. Lazima tufuge vizuri tupate maziwa, tupate nyama na mazao ya kufuga mazuri ili tufurahie nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo changamoto katika utalii. Moja ya changamoto iliyotajwa hapa ni leseni. Ndugu zangu nawaomba mnielewe, leseni za biashara zinatolewa kwenye categories mbalimbali. Leseni ni kibali cha kufanya biashara, sio kodi. Mtu mwenye kaduka kwenye mtaa tunapoishi anakata kodi lakini kodi ya mtu mwenye duka la mtaani ni tofauti na kodi ya Kampuni ya Mabasi ya Shabiby, ni tofauti na kampuni ya ndege na ni tofauti na kampuni za aina nyingine. Katika utalii, tangu mwaka 1992 leseni ya kufanya utalii ni dola 2000. Nimewawekea kwenye bag sheria zote ambazo zinaongoza maliasili na Sheria ya Utalii nimewawekea mule ndani na zile kanuni za leseni na namna ya kufanya hiyo biashara nimewawekea kwenye lile bag; naomba mzisome na mzielewe vizuri. Mtu anayepandisha watu Mlima Kilimanjaro akapandisha kundi la watu kumi, kila mtu mmoja kwa bei ya sasa analipa dola 4,000. Kama wako kumi watalipa 4,000 mara kumi na mtu yule anaweza kupandisha makundi matano mpaka sita ya watu hao kwa mwaka. Mimi nina rekodi kule kwenye Wizara kwa hiyo najua. Kwa hiyo huwezi kusema kwamba ni mdogo asilipe leseni ya dola 2,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nadhani interpretation hapa na udogo na ukubwa una tofauti. Udogo na ukubwa unaangaliwa kwenye kulipa corperate tax, wakati wa kulipa kodi ile asilimia 30 ndiyo unaangalia mdogo kwa sababu ya biashara yake ilivyo ndogo na mkubwa kwa sababu biashara yake ni kubwa. Lakini katika kukata leseni, ni lazima tuangalie biashara kama biashara ya kawaida na tumeanza kupanua utalii katika zones mbalimbali, katika kanda mbalimbali. Upande wa Kusini, tunaboresha miundombinu katika mbuga za wanyama za Ruaha, Selous, Mikumi na Ruangwa pamoja na Kitulo. Serikali pia kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imekwenda ikakagua barabara kutoka Iringa mpaka kwenye lango la Hifadhi ya Ruaha. Kwa hiyo, tuko njiani kuboresha maeneo yale, lakini kikubwa ni kwamba kuboreshwa kwa ATCL kumesaidia sana na kutasaidia sana kupunguza gharama za ndege za kwenda kutembelea Hifadhi za Ruaha, Ruangwa na Kitulo na kwa hiyo, kufungua lango la Kusini mwa Tanzania. Hivyo hivyo, tumefanya kazi kubwa sana ya kupeleka zile Kampuni za Utalii za Kimataifa katika mbuga yetu ya Katavi, kwenye ufukwe wa Ziwa Tanganyika na katika Hifadhi yetu ya Gombe kule Kigoma, na kuanzia mwezi Aprili, 2017 tumeanza kupata watalii kutoka Uyahudi kwenye sekta hiyo ya Magharibi, na Air Tanzania imetusaidia sana kupokea wageni wanapofika Dar es Salaam na kuwarusha kwenda Kigoma na kutoka Kigoma kwenda Mpanda. Kwa hiyo, kazi inaendelea, naomba mtuunge mkono. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge nimesikia sana malalamiko makubwa kuhusu mkaa. Ndugu zangu, mkaa unasababisha ukataji wa asilimia 80 ya miti yote inayokatwa hapa Tanzania. Sisi tunaelewa kabisa kwamba bado tunahitaji wananchi wetu watumie mkaa katika vijiji, watumie kuni na katika miji midogo hii watumie mkaa kwa ajili ya maisha yao. Lakini huu mkaa unaokatwa unatengeneza tani milioni 2.3 za mkaa kila mwaka na zaidi ya nusu ya mkaa huu unaingia Dar es Salaam. Kiini macho tu. Maana kutoka Dar es Salaam mwingine unakwenda Zanzibar na kutoka Zanzibar unakwenda Oman na unakwenda Mombasa. Mkaa unakatwa kwenye hifadhi zetu za Magharibi za Burigi, kule Moyowosi, Kigosi, unakatwa unachomwa kule unakwenda nchi jirani za DRC, Burundi na mataifa ya kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ambacho ninataka niwaambie ndugu zangu ni kwamba hatuwezi kukubali miti yetu ikatwe kwa ajili ya kupeleka mkaa Kenya na majirani wengine. Tunataka mkaa ukikatwa utumike hapa Tanzania. Kwa hiyo, hatujakataza kuchoma na kuuza mkaa ndani ya Tanzania na mtu ambaye anafanya hivyo anavunja sheria na ninataka niseme, kuzungusha mkaa ndani ya mji au ndani ya vijiji au maeneo ambayo watu wanaishi kwa baiskeli au kwa pikipiki, hakuna mtu aliyekataza. Kinachokatazwa ni wale ambao wana-smuggle mkaa kutoka misituni kwa ajili ya kupeleka nchi za nje na kupeleka kuuza kwenye maeneo ambayo haina kibali cha kuuza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka kwanza tuanze vizuri, cha kwanza, nimeambiwa wapo watu wengi sana wamekamata baiskeli za watu, zipo baiskeli malundo na malundo. Nimeambiwa kuhusu malundo yaliyopo Kasulu, nimeambiwa kuhusu malundo yaliyopo Geita, nimeambiwa kuhusu malundo yaliyopo Ushirombo na maeneo mengine. Kuanzia leo, Maafisa wa Misitu wote wa maliasili wanaagizwa warudishe baiskeli za watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaagiza kwamba Maafisa Maliasili, Maafisa Misitu, Maafisa Wanyamapori walioshika pikipiki za watu, baiskeli za watu na vifaa vya wananchi ambavyo havina kesi mahakamani, waviachie mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo watu ambao wanasaidia sana nchi hii kwa kupanda miti katika maeneo yao na mashamba yao, na mimi nataka niwape pongezi kubwa kwa kufanya kazi hii kwa niaba ya Taifa. Watu hawa wengi wapo katika Wilaya za Njombe, Wanging’ombe, Mufindi, Mafinga, Kilombero na Morogoro. Nataka niseme hivi, Wizara na Serikali hatuna tatizo na watu hawa kuchagua matumizi ya miti yao.

Aidha, hatuna tatizo na watu hawa kukata miti yao wakati wanapotaka. Lakini tungependa kuwashauri, kwamba kama ni miti ambayo inatakiwa kutumika kwa ujenzi au kutengeneza vifaa kama hiki ambacho ninaongelea hapa, ni vizuri miti ili iachwe ikomae ili vifaa vile viweze kuwa vya kudumu na miti yao iweze kuwa na faida kwao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa sababu wapo watu wengi sana wanaofanya biashara ya magogo na mazao mengine ya miti, ni muhimu Maafisa Misitu waweze kuhakikisha kwamba hii inatoka kwenye mashamba yao na kwa sababu hiyo wasiwabugudhi, lakini wote ambao wanatoa kwenye mashamba ya Serikali, katika Misitu ya Serikali, Misitu ya Vijiji na Misitu ya Halmashauri ni lazima wapate vibali na leseni za kuvuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti viko vitu vingine hapa ambavyo vilisemwa kwa hisia kubwa sana nami najisikia kwamba labda nipate muda niviseme tu hata kwa sentensi mbili. Hapa kimesemwa Chuo cha Nyuki cha kule Tabora kwamba chuo kimefungwa, kama Kituo cha Utafiti kimehamishiwa Arusha. Sasa nataka kusema, hii siyo kweli. Chuo cha Tabora kipo na Chuo cha Utafiti wa Nyuki Tabora kipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo kile ni muhimu sana kwa sababu kulikuwa na uvumi wakati fulani kwamba asali inayotokana na miombo kule Tabora ina nicotine, kwa hiyo, haifai kuuza nchi za nje. Kituo kile ndiyo kimechukua sampuli za aina mbalimbali za asali kutoka maeneo yote ya Tabora; maeneo yanayolimwa tumbaku na yale ambayo hayalimwi tumbaku na hakuna tofauti ya kihesabu yaani statistical kati ya uwepo wa nicotine kwenye asali inayotoka ndani ya misitu ambapo hakuna kabisa tumbaku na ile ambayo inayotoka katika maeneo ambayo yako karibu na tumbaku. Nyuki wenyewe wana uwezo wa kuchagua na kutengeneza zao zuri. Kwa hiyo, nataka kile chuo kiendelee kukaa pale na tutashirikiana na Waheshimiwa Wabunge wa Tabora kuhakikisha kwamba tunakijenga na kukiendeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliambiwa computer ziliondolewa, computer hazijaondolewa. Kama wameondoa watazirudisha, kesho ukifika pale utazikuta. Gari halijaondolewa limepelekwa kutengenezwa. Gari ni la mwaka 1989 na ni Land Rover ile ya zamami. Kwa hiyo, nimewaagiza kwamba wawaletee gari nyingine ili waweze kufanya utafiti vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo limesemwa hapa likanigusa sana ni akina mama kuliwa na mamba wakati wanachota maji kwenye Mto Ruvuma. Hili limeletwa hapa na Mheshimiwa Bwanausi ambaye amelieleza kwa uchungu mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuwahakikishia tu akina mama wa Lulindi kwamba tuko pamoja, tumetuma wataalam wa kupima maeneo ambayo yana maji ya chini ya visima ili kuhakikisha kwamba hakuna mwana mama anakwenda kuchota maji kule kwenye mto. Nasi tutatoa fedha ili visima hivyo viweze kujengwa na kuhakikisha kwamba akina mama hawaliwi na mamba wakienda kuchota maji. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mambo hapa ambayo bado nilikuwa nataka niyaseme, lakini kwa kweli muda tu ndiyo unanishika mkono na mimi nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii. Nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba tutawapa majibu mazuri kwa maswali yenu yote ambayo mmeuliza na tutaomba msaada wenu katika kuendeleza sekta hii ya maliasili na utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa leo naomba ushirikiano wenu katika kupitisha bajeti ya Wizara ili tuweze kwenda kufanya kazi. Naomba kutoa hoja.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.5) wa Mwaka 2019 (Toleo la Kiingereza)
MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii ya kuchangia katika Muswada ulio mezani wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 5) wa Mwaka 2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka nimpongeze sana Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, nimpongeze sana Waziri wa Katiba na Sheria na nimpongeze Katibu Mkuu wa Wizara hii kwa kazi nzuri ambayo wanafaya na juhudi wanazofanya katika kuhakikisha kwamba sheria tulizonazo ambazo zina ugumu wa utekelezaji zinafanyiwa marekebisho na kutuletea marekebisho ambayo mengi tunayakubali na yale ambayo yanakuwa na matatizo tumeyajadili kwa pamoja, kwa sehemu kubwa tumekuwa na muafaka na tunapendekeza kabisa Bunge lako Tukufu iyakubali marekebisho haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kusema machache katika jambo hili, jambo la kwanza ambalo ningependa kuongelea ni juu ya usajili wa kadi za simu. Mapendekezo yaliyopo mezani kama vile yanamuacha yule anayeuza kadi hizo, kadi ambazo hazikusajiliwa mtu anayekutwa nazo mapendekezo yalikuwa apate faini ya shilingi milioni tano au kifungo. Sasa ukifikiria kwamba wakulima na watu vijijini ndiyo wanaweza kununua kadi hizi na wakati mwingine wananunua wasipojua kwamba hazikusajiliwa basi jambo hili tukaona ni vizuri ili tusije tukajaza watu kwenye jela basi tupunguze hiyo faini ifike milioni Moja. Na tunamshukuru sana AG na Serikali kwa kukubali marekebisho haya ambayo tumeyafanya kwenye kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ingekuwa muhimu sana kwamba yule anayeuza kadi lazima anajua kama kadi hii imesajiliwa ama haikusajiliwa. Sasa sheria ingembana huyu zaidi kuliko yule ambaye ameuziwa kutumia na kwamba mtu anayeuza kadi ya namna hiyo anaturudisha nyuma na kutufanya kama Shamba la Bibi fulani hivi wanaoweza kuja watu wakatumia mawasiliano yetu bila utaratibu kamili. Kwa hiyo, tunaomba sana watu wa namna hii wachukuliwe hatua kali zaidi na sheria isiwe na huruma na watu wa namna hii, kwa sababu athari ya kutosajili kadi ni kuwaibia wananchi hasa katika mitandao hii ya M-pesa, TigoPesa na kadhalika. Pia inaweza kutumiwa na maharamia, watu ambao ni magaidi ambao wanaweza kutumia mitandao ya namna hii kuweza kujipenyeza katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa pamoja na marekebisho hayo, ningependa nipendekeze kwamba Wizara na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iende mbele zaidi katika marekebisho ya sheria hii. Jambo la kwanza, sheria iangalie namna ambavyo inaweza kuzuia matumizi mabaya ya kadi za simu. Kwa mfano, mtu anayeingilia kadi ya mwingine na kuzungumza naye kama vile huyo aliyeingiliwa ndiye anayeongea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo huu wa kuingilia simu za watu na kutoa taarifa ambazo siyo za kweli umekuwa mwingi sana katika mitandao yetu. Mimi mwenyewe nina experience ambapo mtu ameingilia simu ya Kiongozi wa Chama cha Mapinduzi na kutoa maagizo kama vile ni yeye, lakini kumbe ni mtu ambaye ameingia visivyo halali, hilo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili katika mitandao hii ya simu tunapotuma pesa, tunaponunua vifurushi na tunapofanya miamala mbalimbali humu ndani unakuta wamekuletea jinsi ambavyo muamala ule, bei yake ni nini, kodi ni kiasi gani na kadhalika lakini sina uhakika ile VAT inayoandikwa katika miamala yetu kweli inaingia Serikalini. Kwa hiyo, Serikali inapoteza mapato mengi sana wakati huu ambapo hatuna pesa. Kwa hivyo, sheria hii ingetafuta namna ya wale wenye mitandao kutekeleza miamala hii kama ambavyo wameandika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ambalo ningependa nilishauri sana ni mitandao hii kudanganya wateja. Unanunua kifurushi unapiga simu unaandika dakika ulizotumia, unapiga tena unaandika unakwenda kama ulikuwa una dakika 200 ukifikisha dakika 45 wanakwambia dakika zako karibu zinakwisha, ukipiga tena wanakukatia katikati. Wizi unatokea sana katika mitandao. Kwa bahati mbaya mimi kwa experience yangu simu yangu ya Vodacom inaniibia sana muda wa maongezi. Nataka niseme hapa kwamba wakati umefika kwa Serikali kuingilia mitandao hii ili isiendelee kuwaibia wananchi. Tumepata nafasi hii ya kuongea hapa, watu wa Vodacom wasikie kwamba sio vizuri kutuibia pesa zetu tunazoweka huko kwenye mitandao hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo nilikuwa napenda nilizungumze ni suala la Sheria hii ya Sanaa ambayo ni Sura 204. Tunafurahi kwamba mnaendelea kuleta maboresho katika kuboresha sheria hii lakini ukiwasikiliza Wasanii wenyewe inaonekana kama tunaweka viraka tu kwenye sheria ambayo kwa kweli ilikuwa inatakiwa iandikwe upya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hii imekuwa ya zamani ni ngumu sana kwa utekelezaji wa wasanii wetu, ni vizuri kwa mfano haya mabaraza kama BASATA, COSOTA na kadhalika yaunganishwe yawe kitu kimoja ili iwe rahisi kwa wasanii wetu wanaotunga miziki yao, wanaofanya ulimbwende unaitwa?

MHE. RITTA E. KABATI: Ulimbwende. (Kicheko)

MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, yote hayo ya urembo na fasheni za nguo, ilitakiwa hiki kitu kiunganishwe kwa pamoja kuwe na sheria moja na ambayo itakuwa ya kisasa na inayoweza kuwavumilia wasanii wetu kuliko sheria ambayo ipo sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wenyewe zile attitude zetu kwa wasanii ingekuwa ni vizuri zibadilike. Kwa mfano, ngoma zetu za kienyeji za makabila mbalimbali zipo tofauti sana, lakini unaweza kukuta wacheza ngoma ile ya kikabila wamevaa sketi fupi ya majani imezunguka chini na sehemu kubwa ya mwili iko wazi! lakini wasanii wa siku hizi wakivaa sketi fupi tunapiga kelele, hatuna uvumilivu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani lazima tujue kwamba miziki hii tunaiuzia dunia na hiki kitu ni biashara, kama wangevaa suti kama hii niliyovaa waseme wanaenda kupiga muziki ule, hakuna mtu atanunua muziki wa namna hiyo. Kwa hiyo, lazima tuwe wavumilivu na tulinganishe miziki ya kisasa na miziki ile ya zamani ili tuwape nafasi wasanii wetu waweze ku-perform. (Makofi)

T A A R I F A

MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba unilindie muda wangu. Hili ndilo jambo hasa ambalo nilikuwa nasema lazima tuwe tolerant, lazima tuwe na uvumilivu. Tukiona mtu amevaa tofauti na ambavyo tumevaa sisi tusianze kudhani kwamba amevunja utamaduni. Utamaduni wetu lazima tuulinde iwezekanavyo lakini pia lazima turuhusu sanaa na ubunifu uweze kufanya kazi. Tusifanye mambo haya… (Makofi/Kicheko)

MBUNGE FULANI: Upo vizuri Profesa.

MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwangu la muhimu hapa ninalotaka ni kwamba sheria hii iandikwe upya na iletwe kama sheria mpya na ambayo inakwenda na wakati wa siku hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti…

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Aah! Ndiyo maana ya kuwa Profesa. (Kicheko)

T A A R I F A

MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.

MWENYEKITI: Umeipokea taarifa?

MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua mazungumzo kwenye Bunge lazima turuhusu yaendelee. Ninachoomba mimi unilindie muda wangu niweze kusema niliyotaka kusema, halafu kila mtu hapa ni Mbunge amekuja kuwakilisha watu wake kutoka kwenye Jimbo lake, atayachukulia jinsi anavyoweza. Tumshukuru Mungu kwa kutupa akili za namna mbalimbali na ndiyo maana ya Bunge.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika marekebisho ambayo yameletwa ya Baraza la Mitihani, lengo ni kudhibiti na kuhakikisha usalama wa mitihani, lakini ni muhimu sana kwamba katika kufanya hivyo, mitihani inakuwa katika mikono michache sana ili kuzuia uvujaji wa mitihani hiyo. Kwa hiyo, Kamati ambazo zinaundwa katika Mikoa na Wilaya ni vizuri zipewe majukumu mahsusi kabisa kwamba ni za kuhakikisha usalama na kuhakikisha ufuatiliaji na uchunguzi kama kuna tatizo lolote la uvujaji ambalo limepatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ningependa kutoa mapendekezo katika Sura ya 340 juu ya mabadiliko yanayopendekezwa katika Sheria ya Vipimo (Weight and Measures). Ni vizuri sana kwamba sheria sasa inateua watu mahsusi ambao watakuwa wanapitia vipimo katika maeneo mbalimbali na kuhakikisha kwamba vinafuata utaratibu na usahihi au accuracy ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili ni muhimu sana na labda hata limechelewa kidogo lakini tunaishukuru Serikali kwamba imelileta sasa kwa sababu katika eneo hili kuna matatizo mengi hasa katika kilimo na wengi wetu tunajua juu ya vipimo vya lumbesa na watu wanaonunua mazao yaliyopo shambani kabla mazao yale hayajavunwa na kupimwa. Ni vizuri Serikali iongezee mabadiliko katika sheria hii ili kuhakikisha kwamba pamoja na mtu kununua mazao yaliyopo shambani kabla hayajapimwa, wakati ambapo yanavunwa mazao haya yaweze kupimwa ili mkulima ihakikishwe kwamba kweli amepata thamani sahihi ya mazao yake yote ambayo ameyalima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami ningependa sana katika mjadala ambao nimeuona unaweza kutokea huu wa Baraza la Sanaa. Ningependa tuendelee kujadiliana ili tuweze kutoka na sheria ambayo ina uvumilivu wa kazi za wasanii na kuwaachia sehemu wavute hewa ili waweze kufanya biashara wanayofanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nikushukuru sana kwa kunipa fursa hii niongee machache kwa kutoa ufafanuzi kwenye hoja za msingi na nzuri ambazo zimetolewa na Waheshimiwa Wabunge.
Kwa kuwa huu ndiyo mwanzo wa mjadala wetu wa Bunge la Bajeti basi tutakuwa na fursa zaidi ya mara moja, ya kuendelea kueleza yale ambayo Waheshimiwa Wabunge wameyaleta na kwa sasa tu niwashukuru sana wale ambao wameongelea suala la utalii ambalo nitalitolea ufafanuzi kidogo katika mawasilisho yangu haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge walioongelea juu ya sekta yetu wako kumi na wengi wao waliongea juu ya Utalii kama ambavyo nilisema. Jana Mheshimiwa Mbunge mmoja alitupa takwimu kidogo, ni kweli kwamba mchango wa sekta ya utalii katika uchumi wetu ni mkubwa na unafikia asilimia 17.5 ya Pato la Taifa na inachangia asimilia 25 au robo nzima ya mapato yote, hii inatokana na watalii 2,200,000 ambao wanakuja kwetu sasa. Hii ni takwimu ambayo ilifikiwa mwaka 2014 na ninategemea sasa hivi tunakokotoa tumefika karibu mwisho wa kukokotoa idadi ya watalii waliokuja mwaka 2015.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nitoe ufafanuzi kidogo kwamba mwaka 2010 ni kweli walikuja watalii 800,000 na wale waliohesabiwa mwaka 2014 walikuwa hao 1,200,000 na kwamba kulikuwa na ongezeko hapo karibu watalii 500,000 katika kipindi hicho. Siyo kwamba, katika miaka hiyo watalii waliokuja ni hao 500,000 gawanya kwa sita au 89,000 kama ilivyosemwa. Maana yake ni kwamba hao 89,000 ni wale wanaongezeka kila mwaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kutoka 500,000 mwaka 2006, wakafikia 800,000 mwaka 2010, laki tisa, milioni moja, milioni 1.2 ni ongezeko na hiyo 900,000 ni kwa mwaka. Tofauti kati ya milioni 1.2 na 800,000 ile ndiyo ongezeko lililotokea katika kipindi hicho, siyo kwamba katika mwaka mzima waliingia wale ambao wameongezeka tu, hata kidogo!
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba fursa zetu za utalii ni nyingi na kwamba watalii ambao wanakuja hao milioni 1.2 ni wachache sana. Lakini katika uchache wao ndiyo waliochangia robo ya mapato yetu yote ya kigeni hapa nchini. Kwa hiyo, tuna lengo la kuongeza mapato haya kutoka bilioni 2.3 ya sasa na kuyafikisha bilioni tano mwaka 2020.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia mwaka huu tataanza mpango kabambe kabisa wa kutangaza kwenye masoko ya ndani na yale ambayo yanatuletea watalii wengi katika nchi yetu. Tutatangaza Marekani ndiyo nchi ya kwanza kutuletea watalii, mwaka 2014 ilileta watalii karibu 500,000, tutatangaza Uingereza, Jamhuri ya Muungano wa Kijerumani, (Federal Republic of Germany), Italia na nchi zile ambazo zinatuletea watalii wengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, tuna lengo la kushirikiana na United Arab Emirates ili watalii wale wanaofika Dubai milioni 27 kwa mwaka, angalau milioni tatu waweze kuja Tanzania kama sehemu ya safari yao kule Dubai. Kwa hiyo, kuongeza watalii wetu kwa idadi hiyo na tunaamini kabisa kwamba baada ya mipango hii kutekelezwa tutakuwa tumefikia mapato ya dola za Kimarekani bilioni tano kwa mwaka na kuongeza idadi ya Watanzania walioajiriwa katika utalii moja kwa moja 500,000 mpaka wafike milioni 1.2 na wale ambao wanaohudumia utalii kutoka milioni moja kufika milioni mbili.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, sekta hii ni muhimu sana na sisi wenyewe tumejiandaa kwa kuyalinda haya mapori ambao ni nje ya TANAPA na nje ya Mamlaka ya Ngorongoro kwa kuanzisha mamlaka mpya inaitwa Tanzania Wildlife Authority. Italinda mapori tengefu, italinda game reserves na italinda na maeneo ambayo yako wazi ili kuhakikisha kwamba wanyama katika maeneo hayo wanatumika kwa faida ya Taifa.
NAIBU SPIKA: Kengele ya pili hiyo Mheshimiwa Waziri!
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru sana ndugu zangu baada ya hutuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kujadiliwa basi, tutaendelea kutoa ufafanuzi. Mimi naunga sana mkono hoja hii, ahsante sana!
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kumpongeza Mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa kwa hotuba nzuri ya Bajeti. Aidha, hotuba hii nzuri inatokana na kazi nzuri ya timu hii mahiri ya Wizara hii inayojumuisha Waziri, Naibu Waziri, Makatibu Wakuu na Wafanyakazi wa Wizara na Mashirika yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wetu wa Kilimanjaro una majimbo ya uchaguzi tisa. Kati ya hayo majimbo mawili tu ndiyo ya Chama Tawala cha CCM na yaliyobaki saba yako chini ya Chama cha Upinzani cha CHADEMA. Kwa bahati mbaya majimbo yanayoongozwa na CCM yalikuwa hayapewi fedha za utengenezaji wa barabara. Fedha karibu zote za kutengenezea barabara zinapangwa kutengeneza barabara katika Majimbo yanaongozwa na Upinzani. Msemo wa Wananchi wa Kilimanjaro umekuwa, kama mnataka barabara zenu zitengenezwe muwe chini ya CHADEMA. Napenda sasa nichukue fursa hii kuishukuru Serikali na hasa Wizara ya Ujenzi kuwa Bajeti ya mwaka huu 2017/2018 imejibu kilio cha wananchi wa Mwanga kwa kutenga fedha kuhudumia barabara ya Mwanga – Kikweni – Lomwe na Vuchama – Ngofi. Tuna imani kubwa kuwa hatua hii itasaidia sana kuleta imani ya wananchi wa Mwanga kwa Serikali yao na Chama chao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua zilizochukuliwa sasa zinatekeleza ahadi za Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano aliyetembelea barabara hii mwaka 2015 akiwa Waziri wa Ujenzi. Hivyo napenda kwa niaba ya wananchi wa Mwanga kumshukuru sana Mheshimiwa Rais.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nichangie katika hoja hii ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Muda wa dakika tano ni mdogo sana, lakini nataka niseme na kuipongeza sana Serikali kwamba katika sekta hii tumetoka mbali sana, tulikuwa tukisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza tunapitia Nairobi, safari ya siku moja tunakwenda siku mbili. (Mkakofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tumeanza kujenga reli, tunaboresha Shirika la Ndege la Tanzania na tunaboresha communication nchi nzima, tusikate tamaa, pale tunapopata matatizo madogo madogo kwani hizi ndio changamoto za maendeleo na tuwe tayari kupambana nazo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu mwezi Aprili, mwaka 2015 Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa Waziri wa Ujenzi alitutembelea kukagua barabara inayojengwa kwa lami kutoka Mwanga kwenda Usangi mpaka Uchamangofi. Barabara hiyo sasa inajengwa kwa nguvu kubwa kabisa na nataka nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri ambayo anaifanya na kwa kazi ambayo anatufanyia pale kwenye Jimbo la Mwanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipande cha barabara hii ambacho kimebakia cha kutoka Kikweni kwenda Msangeni – Kifula – Mwaniko mpaka Uchamangofi na chenyewe kimetengewa fedha katika bajeti hii na napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Mawaziri na watendaji wake wote kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya bila kuchoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata mkisikia kuna watu wanatoa hoja kuwapinga sana wapuuzeni, nendeni mbele kwa sababu hata Marekani leo inawekeza bado kwenye miundombinu, hata Uingereza ina kazi ya kuwekeza kwenye miundombinu. Matatizo tunayopata sasa hayawezi kwisha, kila siku yatakuwepo na kila siku tuwe tayari kupambana nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia niishukuru Serikali kwa kupandisha daraja barabara mbili, moja kutoka Lomwe - Ndolwe - Kilomeni - Lembeni kuwa barabara ya TANROAD na nyingine kutoka Kilya - Kitichamungu - Nyabinda - Kagongo - Lang’ata - Tingatinga - Kifaru na katika bajeti hii naona shilingi milioni 565 zimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo. Napenda nichukue fursa hii kuishukuru sana Wizara inayohusika, lakini pia kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri sana ambayo anafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, muda wa dakika tano ni mdogo sana, lakini napenda niseme kwamba katika barabara moja ambayo ndiyo kubwa sana ya TANROADS katika Wilaya yangu ya Mwanga kutoka Kifaru - Kigonigoni - Kichwa cha Ng’ombe kuna maeneo ambayo yameharibika sana na barabara wakati huu haipitiki kabisa kwa sababu ya mvua. Nawasihi sana, namsihi sana Mheshimiwa Waziri afanye kila juhudi ili eneo la kutoka Kisokoro - Kigonigoni - Mvuleni liweze kutengenezwa ili wananchi waweze kushughulika na shughuli zao za biashara kama ambavyo wamekuwa wanafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sana pia nihimize kwamba maeneo ambayo hayafikiki kwa mtandao wa simu yawekewe juhudi maalum kule katika Bwawa la Nyumba ya Mungu na maeneo ya Kisangara Juu na Jipendea yapate minara mipya ya mawasiliano ili wananchi waweze kuendelea…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Harrison G. Mwakyembe, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kazi nzuri iliyotukuka. Naipongeza Wizara kwa kazi nzuri, hotuba na Mipango mizuri, hivyo naunga mkono hoja hii kwa furaha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, chemchemi ya michezo ni vijana wetu vijijini. Chemchemi hii ikihifadhiwa, ikaendelezwa huliletea Taifa sifa na faraja ya kushinda katika mashindano ya Wilaya, Mkoa, Taifa na Kimataifa. Kwa sababu hiyo niliomba na bahati nzuri nikaahidiwa na Waziri tangu Mei, 2016 mipira 100 football kwa ajili ya kuendeleza mpira wa miguu ngazi ya Kata. Mipira hii niliahidiwa na Waziri wakati huo 2016 kama mchango wa kuendeleza League ya mpira wa miguu Wilayani Mwanga (Maghembe Cup).

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri anikumbuke kutekeleza ahadi yako hii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii kuzipongeza sana hotuba nzuri sana zilizotolewa na Mawaziri wetu wa Nchi, Mheshimiwa Suleiman Jafo na Mheshimiwa George Huruma Mkuchika. Mawaziri hawa mahiri wanafanya kazi nzuri sana, wao pamoja na wasaidizi wao wote. Hivyo, naunga mkono hoja zao zilizo Mezani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Mwanga ina baraka ya kuwa na milima mirefu katikati ya wilaya na tambarare mbili; moja Mashariki ya Milima katika Ziwa Jipe na moja Magharibi ya Milima ulipo Mji Mkuu wa Mwanga na Bwawa la Nyumba ya Mungu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali yetu ya Wilaya iko Usangi juu kabisa milimani. Awali mwaka 1980 tulipopewa hadhi ya Wilaya ya Mwanga, kilichokuwa Kituo cha Afya Usangi kilipandishwa hadhi kuwa Hospitali ya Wilaya, lakini tangu kipandishwe hadhi, hakijafanyiwa ujenzi na ukarabati ili kifikie kiwango cha hospitali ya wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa Waziri wangu Mheshimiwa Suleiman Jafo; atume timu ya wataalam wafanye mahitaji halisi ya Hospitali ya Wilaya ya Mwanga iliyopo Usangi. Baada ya assessment hiyo aiunganishe hospitali hii kwenye vituo vya afya vinavyoboreshwa na World Bank ili itengenezwe, ipanuliwe na ipatiwe vifaa stahiki kama hospitali nyingine za wilaya. Tupatiwe Madaktari na wafanyakazi stahiki ili Hospitali ya Wilaya ya Mwanga ifanye kazi kama hospitali ya wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya TAMISEMI ihakikishe kuwa viongozi wote wa Idara ya Afya (15) waliohamisha ofisi zao toka Hospitali ya Wilaya Usangi na sasa wako Ofisini kwa Mkurugenzi wa Wilaya (DED) Mjini Mwanga, warudi hospitalini wakatoe huduma ya afya kwa wananchi badala ya kuwa Makarani wa DED. Uamuzi huu ulifanywa na BMW, lakini uamuzi haujatekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kwanza hii niweze kuchangia katika hoja hii iliyoko mezani ya Waziri wa Elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta hii ya elimu imekuwa inapitia mabadiliko makubwa sana katika kipindi cha miaka kumi mpaka 15 sasa. Kwa hiyo, ningependa kwa dhati kabisa nimpongeze Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kufanya uamuzi ambao ni wa kijasiri wa kutoa elimu bure ya msingi. Huu ni uamuzi mkubwa sana kwa sababu katika hatua tuliyonayo sasa ya elimu Rais amekubali tupanue access na kwa kuanza ameondoa fees katika elimu ya msingi ambayo ni kuanzia darasa la kwanza mpaka form four. Kwa hiyo, pamoja na kupanua access kwa watoto wengi kupata elimu hii amepanua pia elimu ya msingi kutoka darasa la saba mpaka form four. (Makofi)

Napenda pia kwa nguvu hizo nipongeze viongozi wa Wizara ya Elimu na hasa binti yangu Mheshimiwa Profesa Joyce Ndalichako kwa kazi nzuri sana anayoifanya katika Wizara ya Elimu. Tunakupongeza sana Mheshimiwa Joyce, this is very good. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa labda ningetoa mfano huu wa access kwa sababu mwaka 2003 wakati mimi ni kipindi changu cha kwanza cha Bungeni hapa vijana waliomaliza O-Level (form four) walikuwa 46,000; mwaka jana vijana hao waliomaliza O-Level walikuwa wanakaribia 400,000; kwa hiyo, utaona access imepanuka kweli kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuendeleza elimu hatua ya kwanza kabisa ni kupanua access, lakini sasa kilichoko mbele yetu baada ya kupanua access lazima sasa tujenge ubora katika elimu yetu, kwa sababu mahali tulipofika sasa tumefika mahali ambapo watoto wanafika darasa la saba wanaweza wasijue kusoma na kuandika. Watoto wanafika form four hawawezi kuandika barua, hivi sasa graduate lawyer hawezi kuandika judgment ya kiingereza. Kwa hiyo, hatua tuliyonayo sasa lazima tuweke mkakati wa kuboresha elimu yetu ili viwango vilingane na hii access ambayo imepanuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika level ya elimu ya msingi ukiangalia matokeo ya mitihani utakuta kwamba kwa miaka yote wala siyo miaka mitano wala siyo miaka sita, watoto wa darasa la saba wanaofaulu mtihani wa kumaliza elimu ya msingi wanaofaulu mtihani wa hesabu hawazidi asilimia 17 kila mwaka ni hivyo na wanafunzi wanaofaulu mtihani wa Kiingereza katika ngazi hiyo ya msingi hawazidi asilimia 21. Kwa hiyo, kama watoto hawajui hesabu, kama watoto hawajui kiingereza ambacho sasa hatua inayofuata ndicho kinakuwa lugha ya kufundishia haiwezekani watoto hao waweze kupata elimu bora.

Kwa hiyo, jambo la kwanza ambalo tunatakiwa tufanye lazima tuangalie vitabu vinavyotumika, lazima tuwafundishe walimu wetu, tuwe na uhakika kwamba kweli Walimu hawa wanaofundisha wana stadi za kufundisha watoto katika ngazi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe mfano katika mwaka 2007 Wizara ya Elimu ilitoa mtihani wa hesabu wa darasa la saba wa mwaka 1994 ikawapa walimu wa Mkoa mmoja sitautaja ambao wanafundisha hesabu. Watoto wa Mkoa ule walifaulu kwa asilimia 17, lakini walimu waliokuwa wanafundisha hesabu wali-pass kwa asilimia 12.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivi utaona kwamba tatizo siyo watoto peke yao na walimu hawana zile study zinazohitajika. Wizara sasa imefika wakati ichukue hatua katika kiingereza itengeneze vitabu vya kufundishia watoto. Sisi ambao tulifundishwa mwanzoni na vitabu vile vya kiada vinavyoitwa New Oxford English Course for Schools, tulijua kiingereza vizuri sana katika ngazi ile. Mimi sioni sababu gani vitabu vile visihaririwe upya na kuletwa vikafika level hii ya leo vikatumika kufundishia watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti umefanywa katika Wilaya ya Moshi Vijijini na umeonesha kwamba matokeo mazuri yanaweza kupatikana. Hivyo hivyo ni muhimu sana tuandike vitabu vipya vya hesabu vya kufundishia watoto, haikubaliki kwamba asilimia 17 tu ya watoto ndiyo wanaoweza kufaulu hesabu. Tuandike vitabu vipya, tunayo ile Taasisi inaitwa Institute of Education itumike na wataalam tulionao kwenye Vyuo Vikuu watumike kutengeneza vitabu hivi ili viweze kufundisha watoto wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ngazi ya sekondari tumepanua sana na katika kupanua kuna vitu ambavyo tulifanya lakini bado. Katika ngazi hii wananchi walifanya juhudi kubwa sana ya kujenga zile shule za sekondari za kata. Walijenga kwa mikono yao wao wenyewe na walipata mafanikio makubwa. Ni muhimu tunavyoongea upanuzi wa elimu ya sekondari tuwapongeze sana wananchi wa Tanzania kwa kiu waliyokuwanayo na nguvu walizotumia kujenga shule za sekondari. Lakini bado ujenzi wa shule za sekondari haujakamilika, bado ujenzi wa shule za kata haujamalizika na hatua iliyofikiwa siyo hatua ya wanavijiji tena, hatua iliyofikiwa ni ya Serikali sasa kwa makusudi kabisa ichukue hatua ijenge maabara zote ambazo zimebaki katika shule za sekondari za kata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Jimbo langu katika shule zangu 25, wananchi….

T A A R I F A . . .

MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemsikia.

Katika ngazi hizi za msingi maana yake, elimu ya msingi na elimu ya sekondari liko jambo lingine kuacha maabara ambalo ni muhimu sana na jambo hili ni Idara ya Ukaguzi wa Shule. Idara ya Ukaguzi wa Shule imekufa, hakuna ukaguzi maana yake kuna Wakaguzi lakini hawana bajeti, kuna ukaguzi lakini hawawezi kwenda shuleni kukagua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu elimu ni kama bidhaa nyingine, sema hii ni bidhaa ya thamani kubwa kupita zote, wakati umefika sasa tungeunda commission wale walimu wote walioko kule kwenye ukaguzi wangekuwa kwenye Tume ya Ubora wa Elimu. Tungeunda Education Quality Control Commission ambayo itakuwa chombo huru chenye uwezo wa kuandikisha shule, chenye uwezo wa kukagua ufundishaji, chenye uwezo wa kuwasimamia walimu wanaofundisha na kama hawafanyi vizuri kuwateremsha cheo, wale wanaofanya vizuri kuwapandisha vyeo na shule zile ambazo zinafanya hovyo kabisa kuzifuta ili kuhakikisha kwamba elimu inapanda kutoka hapo ilipo inakwenda mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika elimu ya juu tumefanya maendeleo makubwa sana katika kupanua upatikanaji wa elimu ya juu. Sasa hivi tunavyo vyuo vikuu karibu 63, lakini hivyo vyuo vikuu sijui nisemeje maana yake viko very heterogeneous. Viko vyuo ambavyo ni vyuo vikuu kweli kweli, lakini viko vyuo vikuu ambavyo ungekuwa unahusishwa navyo ungesema jamani siyo mimi, mimi sitaki kukaa huko. Kwa maana hii vyuo vikuu ni lazima vikaguliwe very rigorously na hii commission yetu ya Vyuo Vikuu Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono lakini inaelekea yule dada alininyima dakika zangu sikupewa.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami nijadili hoja yetu hii ya Wizara ya Fedha kuhusu bajeti kuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kabisa kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu wake na wataalam wao kwa kweli kwa bajeti nzuri sana mwaka huu. Kwa mara ya kwanza wale waliokuwa wanategemea kwamba bei za bia na soda ndiyo zitakuwa uti wa mgongo wa bajeti nadhani wameona kwamba kuna watu wanafikiri na kufanya kazi nzuri ya kutengeneza bajeti ya maendeleo ya nchi hii na mimi nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo makubwa ambayo wamefanya ni kuanza sasa kuelekea kwenye harakati za kuvutia sana wawekezaji. Hatua ya kupunguza Kodi ya Mashirika au Corporate Tax, utaratibu mpya uliowekwa wa kumpa Waziri mamlaka ya kuweza kusamehe kodi na hasa pale ambapo tulikuwa tunatoza kodi kwenye misaada ambayo tunapewa na nchi za nje, hizi ni hatua nzuri sana. Hatua hizi nzuri zimefanywa pamoja na kuandaa Investment Blue Print mpya kwa nchi yetu na tunategemea kabisa kwamba hatua hizi kwa pamoja zitaongeza uwekezaji wa wawekezaji wanaotoka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nitoe mapendekezo ambayo yanajenga hatua ambazo zimechukuliwa. Jambo la kwanza, Serikali ingefikiria kupunguza VAT kutoka 18% angalau ifikie 15%. Jambo la pili, Serikali ingefikiria kuwatambua wawekezaji wa ndani kama ambavyo inawafikiria wawekezaji wa nje. Kwa sababu kwa vyovyote vile, hata kama tutavutia wawekezaji wengi sana kutoka nje lakini watakaojenga uchumi wa Tanzania na watakaokuwa wengi katika uwekezaji ni wawekezaji wa ndani, wawekezaji wadogo, wa kati na wakubwa katika nchi yetu. Hawa ndiyo watakuwa uti wa mgongo katika uchumi wetu, hili ni jambo muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kufanya hivyo, ni muhimu Serikali ifikirie kupunguza riba ya mikopo kutoka kwenye mabenki yetu. Riba ya mikopo katika benki zetu inakatisha tamaa sana uwekezaji. Wawekezaji wa nje wanachukua mikopo kwenye benki zao kwa riba ya asilimia
1.5 mpaka asilimia 2, wawekezaji wa kwetu wanachukua mikopo kwa asilimia 21, ikiwa rahisi sana ni asilimia 15, hawawezi kushindana kwa vyovyote vile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kwamba kwa miaka 10 tumekuwa tunasukuma sana jambo hili na ni kama limeshindikana. Majirani zetu Wakenya walikuwa na hali kama hii, Bunge lao likachoka kusukuma Central Bank kupunguza riba na wakatunga sheria kwamba benki zisizidishe interest level fulani wanapotoa mikopo kwa ajili ya uwekezaji. Nasi hatuna haja sasa ya kujikusanya kama Bunge na kulazimisha benki yetu, lakini Serikali ifikirie kupunguza riba ili wawekezaji wa ndani waweze kukopa na kushindana na wale wa nje.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la lingine mwekezaji ni yuleyule. Wahenga wa Kipare wanasema kama unampenda jongoo lazima upende na miguu yake. Wawekezaji wa ndani kabla hawajaanza kufanya biashara wakapata faida ambayo ndiyo inatakiwa itozwe kodi wanakadiriwa kodi kwa maana wanatakiwa walipe kodi kwenye mkopo waliouchukua kuandaa uwekezaji, sasa haiwezekani! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutajengaje kada ya wawekezaji wa ndani kama tunaanza kuwakata kodi hata kabla hawajaanza kuzalisha? Napenda tuanze kufikiria wawekezaji wa ndani na wenyewe wapewe tax holiday, wawekezaji wa nje tunawapa five years tax holiday, tufikirie kuwapa tax holiday wawekezaji wa ndani, angalau hata miaka miwili. Mapendekezo yangu yangekuwa kwamba kama tunaweza kuwangojea wawekezaji wa nje miaka mitano tusishindwe kumngojea mtu mwenye duka mtaani miaka mitatu ndiyo aanze kulipa kodi wakati amejizatiti katika biashara yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda sana niliseme ni juu ya mashirika yetu haya yanaitwa Regulatory Institutions. Hizi Regulatory Institutions zetu kama EWURA, SUMATRA, TBS na mashirika yote haya ambayo yanatoa huduma hiyo, yanaundwa kwa lengo la kutoa huduma lakini yakianza kazi yanaanza kazi kama mashirika ya kukusanya mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, alisema hapa juzi Mbunge wa Singida Mjini, Mheshimiwa Sima, kwamba mashirika haya yote yangekuwa managed chini ya paa moja (one roof) yalipwe mchango mmoja tu halafu yawe yanatoa huduma kwa wawekezaji. Yanasumbua sana wawekezaji na uwekezaji unakuwa mgumu kwa sababu hiyo. Hayo ndiyo yalikuwa muhimu kwangu niliyoyaona katika upande wa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, kwa ingenuity hiihii ambayo wametumia katika kuangalia kodi waangalie pia maeneo ambayo yanaweza kuleta mapato makubwa kwa Serikali kwa uwekezaji mdogo. Nitatoa mfano mmoja, hapa kwetu Tanzania tuna hekta ambazo ziko chini ya umwagiliaji 489,000. Uzalishaji katika haya mashamba ya umwagiliaji ya hekta 489,000 kwa uzalishaji wa mpunga ni kama tani moja mpaka tani moja na nusu kwa hekta moja. Kwa ujumla tunapata kama tani 700,000 kutokana na haya mashamba ambayo yameandaliwa kwa umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama wakulima wangefundishwa kilimo bora cha kulima mpunga na wakalima mara mbili kwa mwaka, hekta moja ingeweza kutoa tani 10 mpaka 15 kama wanalima misimu miwili kwa sababu wananyeshea. Kwa uzalishaji huo tungeweza kuwalisha mchele watu wa Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Kongo, Zambia, Mozambique na Malawi, wote ambao wananunua mchele kutoka nchi za nje. Hesabu ambazo nime…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, calculation ambayo nimefanya hapa juu ya bahasha kwa mwaka mmoja tungeweza kupata dola bilioni 3 mpaka bilioni 7 kutoka kwenye mpunga peke yake.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi nichangie katika mdahalo huu wa mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo na Mwongozo wa Bajeti kwa ajili ya mwaka wa fedha unaokuja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niipongeze kwanza Serikali kwa kutuletea mpango mzuri, na ningependa sana niweke msisitizo hapa na kuweza kumu-encourage Dkt. Mpango kwa kazi nzuri anayoifanya kule Wizara ya Fedha. (Makofi)

Mimi nitachangia kitu kimoja tu katika sekta moja ya elimu, na nitachangia juu ya kuboresha utaratibu wa kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu. Ndugu zangu wote mnajua kwamba tunatoa karibu shilingi bilioni 500 kila mwaka, lakini kwenye vyuo vikuu bado wanabaki wanafunzi wengi hawapewi mikopo, wanafunzi wanalalamika, vijana wanalalamika, wazazi wanalalamika na watu wale ambao wanalea watoto na kuwapitisha katika elimu wanalalamika sana.

Sasa kwa mtaji huu wa shilingi bilioni 500 tukiweka marekebisho kidogo tunaweza kuwapa mikopo wanafunzi wote ambao wanapata elimu ya juu na hapa ndio ninapotaka kutoa mapendekezo.

Pendekezo la kwanza, ni kwamba badala ya mikopo kutolewa na Serikali, Serikali ishirikiane na sekta binafsi ili kuhakikisha kwamba sekta binafsi ndio inatoa mikopo, kwa hiyo mikopo itoke kwenye benki za biashara.

Pili, mikopo itolewe kwa wanafunzi wote ambao wamejiunga na wana sifa za kupata elimu ya juu. Na mikopo hiyo itolewe bila riba kwa watoto wanaokopeshwa na kwa sababu watoto watakopeshwa wote, kiasi cha mikopo kitapanda kitafika mpaka shilingi bilioni 800/bilioni 900 hata trilioni moja. Lakini kwa sababu inatoka kwenye sekta binafsi haiwezi kuwa na pressure kubwa katika bajeti ya Taifa.

Kwa hiyo katika utaratibu huu Serikali itakuwa na wajibu wa kuzilipa benki riba ya mikopo hiyo. Kwa hiyo, kwa estimates ambazo nimeweka hapa kwenye karatasi hapa juu ya bahasha, kama mikopo inakuwa bilioni 500 kama ambayo inatolewa sasa benki ziki-charge riba ya asilimia 10 Serikali italipa shilingi bilioni 50 kila mwaka. Lakini kama benki zita- charge asilimia 20 basi Serikali italipa shilingi bilioni 100 na hii ni badala ya kulipa mikopo shilingi bilioni 500. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, benki zinatoa mkopo kwa wanafunzi ambao watalipa principal wakati wameshapata degree zao, Serikali itakuwa inalipa riba ya mikopo hiyo mpaka mwanafunzi amalize na mwanafunzi anatakiwa apewe time frame ya kulipa na kumaliza na time frame ipo katika mikopo ambayo inatolewa sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napendekeza kwenye kipindi cha sasa mpaka kwenye bajeti itakapotangazwa hapa mwaka kesho Serikali ije na mpango ambao itashirikiana na benki kuhakikisha kwamba watoto wote ambao wanakwenda chuo kikuu kila mmoja anapata mkopo na kila mmoja analipiwa riba na Serikali, watoto watafurahi, wazazi watafurahi, wapiga kura watafurahi na Serikali itapunguziwa kiasi ambacho inatoa na kulipa kama mchango wake kwa mikopo kwa wanafunzi wanaokwenda chuo kikuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo ningependa niliseme sasa kwa sababu nina muda kidogo katika kuboresha elimu ya sekondari nchini kwetu maja ya matatizo tuliyonayo shule hazina maabara kwa miaka sita mpaka saba sasa Serikali inawahimiza wananchi wajenge maabara katika shule zile za kata, kwenye Wilaya yangu mimi nina shule 25 na ni shule mbili tu ambazo zimeweza kujenga maabara tatu zinazotakiwa, sasa mwaka huu. Serikali ije na bajeti ya kusaidia wazazi wanaojenga maabara za shule za sekondari hili shule zote ziweze kuwa na maabara kwa sababu tumenunua vifaa, lakini vifaa vyote vimewekwa stoo kwa sababu hakuna hakuna maabara kwenye shule zetu za sekondari na haiwezekani tuwe na wana sayansi ambao wanafundishwa bila maabara, hakuna wanasayansi wanaopatikana bila kupatikana maabara ya kufundishia msingi wa sayansi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo, mwaka huu wala tusipeleke huko mbele na hizo pesa ambazo tunaweza ku- save kutokana na kupungua kwa mikopo inayotolewa na serikali tunaweza kuzitumia kujenga maabara zote zikakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho katika Mkoa wa Kilimanjaro na hasa Wilaya za Mwanga na Same kwa miaka
15 hatujapata walimu hata siku moja, walimu wanagawanywa lakini mikoa ile haipati sababu mwanzoni walikuwa wanasema wana walimu wengi kupita maeneo mengine ya Tanzania.

Kwa hiyo, walimu wanastaafu wanaondoka, wanafariki wanazikwa, wanahamishwa wanakwenda mikoa mingine lakini nafasi zao hazijazwi. Kwa miaka 15 katika Wilaya ya Mwanga tunahitaji walimu 1,005. Sasa hivi tuna walimu 601 na upungufu mkubwa kabisa wa walimu 384 sasa kwenye shule zetu za msingi kuwa na walimu wawili, watatu, wanne, ndiyo maximum, watoto wanakaa shule hawafundishwi, nafasi za walimu zipo na nafasi hizo zina mishahara yake maana wale watu waliostaafu wameacha nafasi zile zina mshahara, mtu aliyefariki ameacha nafasi ile ina mshahara, mtu aliyehama amehama amechukua nafasi nyingine Wilaya nyingine pale Mwanga nafasi yake ipo. Nimeiomba Serikali kwenye bajeti iliyopita, nimewapelekea Mawaziri wahusika barua kwa ajili ya kuwakumbusha nataka nikumbushe tena. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanafunzi wa elimu ya msingi wa Wilaya ya Mwanga hawana walimu hata kidogo tunaiomba Serikali kwenye mpango huu Serikali ituletee walimu 384 ili watoto waendele kufundishwa, na kufurahia elimu ya bure iliyoazishwa na Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii nina unga mkono hoja iliyopo mezani kwetu.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, nitoe mchango wangu katika hoja ambazo ziko Mezani.

Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kuzipongeza sana Kamati zote ambazo zimewasilisha ripoti zao leo asubuhi. Napongeza ushirikiano mkubwa ambao Serikali inaendelea kutupa katika kufanya kazi yetu ya Uwakilishi hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitazungumzia mambo machache tu kwa sababu na muda wenyewe ni mfupi sana. La kwanza nianzie hapa alipoishia rafiki yangu Mbunge wa kutoka kule Njombe, ambaye amemaliza kuongea, kwamba katika Wilaya yangu kule Mwanga kuna upungufu mkubwa sana wa Walimu. Leo asubuhi Mwalimu Mkuu wa Shule ya Kijijini kwangu kule Kirongaya, ameniambia kuanzia Jumatatu ijayo kutakuwa na Walimu wawili tu katika Shule ya Msingi ya Kamwala ambayo ndiyo shule ya kijijini kwangu.

Mheshimiwa Spika, katika Wilaya ya Mwanga Walimu watatu ndiyo wastani wa Walimu katika Shule za Msingi. Nimepiga kelele hapa kweli kweli, leo niongeze tena kelele hiyo. Nimemwandikia rafiki yangu Mheshimiwa George Mkuchika, Waziri wa Utumishi, nimemweleza Waziri wa Elimu, nimemweleza Waziri wa TAMISEMI. Sielewi ni kwa sababu gani tatizo hili halijaweza kutatuliwa.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu Walimu ambao wamepungua ni wale ambao wamestaafu; na kwa sababu hiyo mishahara yao ipo. Sasa inachukuaje mwaka mzima kutatua tatizo dogo namna hiyo wakati Walimu mtaani wako wamejaa tele na shuleni Walimu watoto wako wenyewe hawana Walimu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naendelea kuihimiza Serikali iliangalie jambo hili kwa huruma kabisa ili watoto wasiendelee kupoteza maisha yao wakiwa shuleni wanacheza peke yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, nimeliona huku kwenye mitandao yetu kama Wabunge, kuna mjadala unaendelea, Waheshimiwa Wabunge wanajadili kwamba labda tubadilishe lugha ya kufundisha katika ngazi ya sekondari na ngazi ya Chuo Kikuu, tufundishe kwa Kiswahili. Ukiangalia matokea ya Mtihani wa Form IV wa mwaka 2018 haya yaliyotoka wiki iliyopita, utakuta tatizo kubwa kabisa katika shule zetu ni watoto kutojua Hesabu. Ukienda mbele, ukiangalia vizuri zaidi utakuta watoto wetu hohehahe kabisa katika Kiswahili chenyewe. Wanasema niletee ugari na wari, akuna shida badala ya hakuna shida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, watoto wetu wana shida kabisa katika ufahamu wa Kiingereza, anasema I will come yesterday. Watoto wana tatizo kubwa kabisa, ukienda utakuta watoto wetu wana matatizo makubwa sana katika sayansi; biolojia, fizikia na kemia. Sasa huko mbele Madaktari na Wachumi tutapata wapi? Kwa hiyo, tushughulikie tatizo lenyewe, tuwapeleke Walimu ambao wanafundisha masomo haya tuwajengee umahiri wa kufundisha masomo haya ya Hesabu, Kiswahili na Kiingereza sio kubadili lugha ya kufundishia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuwapeleke Walimu tuwafundishe kwa sababu huko shuleni hawa watoto ambao wanasema I will come yesterday ndio wanapata degree, wanakwenda kufundisha English na wakiwa wanafundsiha wanafundisha hiyo hiyo I will come yesterday. Kwa hiyo, tufanye juhudi tuwafundishe Walimu wajenge umahiri katika masomo yao, ili tuweze kuacha Taifa ambalo litaweza kushindana katika uchumi wa dunia, litaweza kupambana katika masuala ya utafiti, litaweza kupambana katika kujenga nchi yetu, tusifanye mambo cosmetic yaani tusifanye vitu hivi kama vile mtu unaweka vipodozi mwilini, tusifanye mambo cosmetic. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tufundishe Walimu vizuri ili wapate umahiri wa kufundisha Kiingereza, Hesabu na Kiswahili na watoto waanze kujua zile KKK (Kusoma, Kuandika, Kuhesabu); wajue table na wabebe hata vile vijiti vya kuhesabia ili wajenge kabisa umahiri katika hesabu. Hakuna Taifa ambalo linaweza kuendelea watu hawajui hesabu, wamefika form four wanajua hesabu kwa asilimia 19, mambo magumu haya. Hili ni janga kabisa, kwa hiyo tulichukulie kwa nguvu inayotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho, napenda nirudie jambo ambalo nimelisema tena huko nyuma kwamba, watoto wanaokwenda kwenye vyuo vikuu wanahangaika sana na suala la mikopo. Katika mwezi huu uliopita wa Oktoba watoto wamefungua vyuo vikuu, nilikuwa kule Jimboni kwangu, nimeletewa watoto 15 ambao ni watoto yatima, wengine na mimi nafahamu ni watoto yatima, lakini hawakupewa mkopo. Sio kwamba lile baraza lina shida hapana, mikopo yenyewe haitoshi, kwa hiyo kuna watakaopata na wataokosa; wanafanya kila kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna siku moja nimekwenda pale, nimeongea na wale vijana wa Bodi ya Mikopo nimeona mazingira ambayo wanafanyia kazi. Serikali katika bajeti iliyopita ilitoa shilingi bilioni 500, jamani shilingi bilioni 500 sio kidogo, ni pesa nyingi sana. Kwa hiyo, Serikali ina dhamira thabiti kabisa ya kusaidia watoto wapate mikopo. Sasa sisi ndio lazima tuwe wabunifu, Serikali ikishatupa shilingi bilioni 500 tuwe wabunifu. Tusifanye mambo business as usual, tuwe wabunifu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumepata bilioni 500, tumewapa watoto hao tuliowapa lakini pia mwaka kesho tutapewa tena labda bilioni 600 kwa sababu watoto wataongezeka, bilioni 700; hivi tunaweza, hatuwezi. Kwa hiyo, lazima tubadilishe gia, tuziambie benki zetu zitoe mikopo ili kila mwanafunzi wa chuo kikuu apate mkopo. Akishaingia chuo kikuu kama anataka mkopo apate mkopo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali kazi yake kuangalia ile mikopo, benki zina…

SPIKA: Ahsante sana Profesa.

MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Spika, ngoja nimalize kitu kimoja. Benki zinataka riba kiasi gani, Serikali ihangaike na riba na watoto wahangaike na mkopo wakati watakapomaliza shule zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami nichangie katika Wizara hizi mbili ambazo zote kiongozi wake ni Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Napenda nipongeze sana kwa kazi nzuri ambazo zinafanywa katika Wizara zote hizi mbili. Pia ningependa niwashukuru sana Waheshimiwa Suleiman Jafo, Mheshimiwa George Mkuchika na Waheshimiwa Manaibu Waziri wote kwa kazi nzuri ambayo wameifanya katika kuendeleza Wizara hizi. Unaweza kuseka chochote lakini Wizara hizi zinafanya kazi nzuri sana na ni vizuri tuzipongeze, tuzipe moyo ili waendelee kuwaletewa Watanzania maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa muda wenyewe wa kuongea ni mchache nitapenda sana nizingatie maendeleo kule kwenye Jimbo langu. Nikianza na sekta ya afya; napenda sana niipongeze tena Wizara hii ya TAMISEMI kwa kuvipangia ujenzi vituo hivi 95 katika bajeti hii ambayo tunaijadili sasa. Hata hivyo, Mheshimiwa Suleiman Jafo atakumbuka kwamba nilimletea rasmi kabisa matatizo niliyonayo katika Wilaya ya Mwanga katika hospitali yetu ya Wilaya ambayo awali ilikuwa ni kituo cha afya na kupandishwa kuwa hospitali ya Wilaya, Mwanga ilipokuwa Wilaya, kwamba tangu mwaka 1979 hadi leo hakuna kitu kingine kilichofanywa juu ya kituo cha afya kubadilishwa kuwa hospitali ya Wilaya. Hivi sasa majengo yamechakaa, theatre zimechakaa, vitendeakazi vimechakaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Jafo kwa kutuma timu ambayo ilikwenda ikafanya tathmini ya hospitali ile na kuona matatizo yaliyopo, lakini katika orodha hi ya hospitali 95 siioni hospitali ya Wilaya ya Mwanga. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri tafadhali ikiwezekana twende sisi wawili tukaangalie pamoja ili uone shida kubwa ambayo ipo. Hivi sasa theatre karibu inafungwa kwa sababu hakuna vitendeakazi, hakuna vifaa tiba, mortuary jengo limeanguka na majengo kwa ajili ya kuwapa uhifadhi wafanyakazi, nyumba za wafanyakazi hakuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri atusaidie kama anavyosaidia kwenye Wilaya zingine ili hospitali hii iweze kutumika vizuri. Aidha, naendelea kushukuru na kupongeza sana katika hatua kubwa zilizofanywa za kujenga na kuboresha vituo vya afya na sisi katika Wilaya ya Mwanga awali tumepata shilingi bilioni 1.4 kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Kisangara na Kituo cha Afya cha Kigonigoni. Tunaendelea kushukuru na fedha ambazo zimepangwa katika bajeti hapa kwa ajili ya kukamilisha Kituo cha Afya cha Kifaru. Hata hivyo, bado wananchi wa Mwanga wamejenga vituo vingine viwili ambavyo ni karibu kumalizia kama hicho cha Kifaru, Kituo cha Afya cha Mwaniko na cha Kileo ambapo tunawaomba sana fedha zikipatikana basi tuwasaidie wananchi kukamilisha. Wameshajenga, wamebakiza vitu vidogo sana ambavyo wangetupatia shilingi milioni 400 hivi, basi maneno yote yangekuwa tayari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha katika sekta hi ya afya, wananchi wa vijiji sita katika Wilaya ya Mwanga wanaendelea kujenga zahanati na karibu zinakamilika. Zahanati hizi za Kituri, Mrigeni, Lembeni, Nyabinda, Lang’atabora na Vanywa ziko karibu kabisa kukamilika, wananchi wamejenga mpaka wamepaua lakini wamechoka. Tunawaomba sana katika huu utaratibu wa kumalizia maboma, ya kwao siyo maboma wameshapaua, basi watusaidie kukamilisha zahanati hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili kubwa ambalo nataka niliongelee ni suala la elimu. Katika Wilaya ya Mwanga na hasa katika elimu ya msingi nimesema hapa mara nyingi shule zetu hazina Walimu kabisa. Kati ya shule 117, shule 50 zina Walimu wawili, wawili peke yake na shule zingine 40 zina Walimu watatu, watatu, sasa utapiga hesabu mwenyewe uone ni ngapi ambazo zina Walimu wanne. Hakuna shule ambayo ina zaidi ya hapo labda zile ambazo ni za watoto wa mahitaji maalum.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ya Mwanga hatuhitaji Walimu wapya. Tunachoomba Serikali itupe ni Walimu ambao watachukua nafasi za Walimu waliostaafu, wale ambao wamefariki au wale ambao wamehamishwa na Serikali kwenda maeneo mengine kufanya kazi. Kwa hivyo, sioni sababu ya kuchukua mwaka na nusu kulishughulikia jambo hili. Watoto wanateketea, wanapotea, hawana Mwalimu wa kuwafundisha, Walimu wawili wakiingia kwenye madarasa saba, watoto wa madarasa matano wanabadilisha shule inakuwa soko. Kwa hivyo, tunawaomba sana, hatuombi Walimu wapya, mishahara yao ipo kwa sababu wale waliokuwepo walikuwa na mishahara na hakuna sababu yoyote ya kutotupa Ealimu kwa sababu Ealimu wako barabarani hawana kazi. Kwahiyo nawaomba tena…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Profesa kwa mchango wako mzuri.

MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami nichangie hoja iliyopo mezani kwetu hapo ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa miaka 15, nchi yetu imekuwa katika harakati kubwa ya kupanua upatikanaji wa elimu na juhudi kubwa zimefanywa ili elimu imfikie kila mtoto wa Tanzania. Napenda sana niipongeze Serikali ya Chama cha Mapinduzi na hasa Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa wanayofanya hasa kwa kukubali baada ya kupanua elimu hii, kuitoa bure. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana Waziri wa Elimu aliwasilisha bajeti ya Wizara ya Elimu na kwa muda tuliopo sasa katika kupanua elimu, bajeti ile imeitendea haki Wizara hii ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Kwa hiyo, napenda sana nimpongeze Waziri, Naibu Waziri na viongozi wote wa Wizara kwa kazi nzuri ambayo inaonekana kufanywa. Kwa upande wetu kwa wakati huu kazi kubwa ni kuboresha elimu, kuishauri Serikali pale ambapo inaweza kufanya vizuri zaidi katika kutekeleza suala hili la kuboresha elimu hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitaka kuboresha elimu, jambo la kwanza lazima uwe na walimu. Niendelee kusema kwamba tunaendelea kuiomba Serikali ihakikishe kwamba inapeleka walimu wengi wa kutosha hasa katika shule za msingi. Wiki iliyopita, sisi katika Wilaya ya Mwanga tumepewa walimu wachache; tuliomba walimu 386, tumepewa walimu 30 hivi na tunategemea kupewa wengine mwezi wa Sita. Kwa hiyo, mwezi wa Sita utakapofika tungependa tuone significant kabisa walimu wa kutosha kabisa ili waweze kufundisha watoto wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kusema kuhusiana na bajeti hii kwamba ili elimu ya Tanzania iboreke, ni muhimu Serikali ichukue hatua ya kuboresha Idara ya Ukaguzi. Wafanyakazi wa Idara ya Ukaguzi wengi wanaomba kuondoka kwa sababu mishahara, madaraja na marupurupu yao na nafasi ya kazi wanayokuwa nayo siyo nzuri kama wale ambao wanaofanya kwenye kufundisha na kusimamia elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, jambo la kwanza ambalo napenda kupendekeza, Wizara iangalie Idara ya Ukaguzi wa Shule na imlinganishe Mkaguzi Mkuu wa Shule na Kamishna wa Elimu. Kule kwenye mikoa, Mkaguzi Mkuu wa Kanda awe sawa sawa na wale Manaibu RAS wa kule kwenye mikoa na wale wafanyakazi ambao wanafanya kwenye Idara hii waweze kupewa vyeo sawa sawa na Maofisa wa Elimu wanaoshiriki katika kuendesha elimu katika Wilaya zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, ni muhimu sana idara hii ipatiwe vifaa; magari na vifaa vya ukaguzi ili kuhakikisha kwamba wanaweza kuwafikia walimu na kwamba ripoti ya ukaguzi wa shule na ukaguzi wa kila mwalimu katika kufundisha unaongezea katika sifa za mwalimu kupandishwa madaraja na kupandishwa vyeo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, tunapotaka kuboresha elimu ni muhimu sana tulenge tunafanya nini? Katika miaka ya kwanza miwili ya shuleni, ni vizuri sana tuache kuwafundisha kila kitu watoto wa Darasa la Kwanza na la Pili. Tulenge kuwafundisha vitu vitatu peke yake kwa miaka ile ya kwanza mitatu ya shule; Darasa la Awali, Darasa la Kwanza na Darasa la Pili tuwafundishe zile K tatu; Kusoma, Kuandika na Kuhesabu na namna ya kutumia namba katika maisha. Tuache kuwafundisha masomo yote, tuwafundishe hivyo vitu vitatu tu ili wakitoka hapo wamevishika na wanaweza kujifunza mambo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ngazi hii ya elimu ya msingi na hata sekondari, ni muhimu sana tuboreshe hii mitaala na tutunge sasa vitabu ambavyo vina tija, vinaweza kuwafundisha watoto wetu wakajifunza, wakaelewa kinachofundishwa. Tusiongee juu ya joto la mwili wakati tunaongea juu ya homa, tuongee juu ya Malaria; tutibu Malaria tusitibu joto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hiyo, ni muhimu sana tutunge vitabu vizuri na katika kila somo kuwe na wataalam waliobobea katika somo hilo ambao wanatoka kwenye taasisi za nchini humu, taasisi za Serikali kama Vyuo Vikuu, taasisi zisizo za Serikali, Vyuo vya Ualimu na hata Shule zetu za Sekondari na Msingi. Tutoe wataalam wa masomo hayo ambao wataandaa mitaala, vitabu vya kutumia na wale ambao watafanya review, wataviangalia kama vinafikia standard inayotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili katika ngazi hiyo ni kwamba katika sekondari, shule zetu nyingi hazina maabara. Tumeacha kazi ya kutengeneza na kujenga maabara, tumewaachia wanavijiji. Wanavijiji hawajui sayansi na hawana uwezo wa kujenga maabara, lakini tumewaachia. Hii ni kwa sababu katika hatua ya upanuzi tulifika mahali hela zimetuishia, lakini kwa sasa hatuna sababu yoyote ya kuwaaachia wanavijiji watujengee maabara ya sekondari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninapendekeza kabisa Wizara ya Elimu itenge fedha kwa makusudi kabisa, ijenge na kumalizia maabara zote ambazo zipo huko kwenye Shule zetu za Kata. Hili litatusaidia, tukisema tunataka kuongeza wanasayansi, tuanze kuwafundisha wanasayansi. Hivi sasa haiwezekani. Tunavyo vifaa vya maabara lakini vimewekwa stoo na vikiwa stoo haviwezi kufundisha watoto. Kwa hiyo, ninashauri sana tujenge maabara na tufanye hili jambo liwe la makusudi kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, niliwahi kupendekeza hapa kwamba ni muhimu sana tuwapatie watoto wote mikopo ya kusomea katika Vyuo Vikuu. Katika hotuba ambayo imesomwa jana tumeletewa na Waziri, juhudi kubwa sana imefanywa kutafuta fedha kwa ajili ya mikopo lakini mimi nadhani hakuna sababu yoyote…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Profesa. Mheshimiwa Dkt. Tisekwa halafu jiandae Mheshimiwa Mama Salma.

MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Kamwelwe, kwa kazi nzuri sana anayoifanya kuiongoza Wizara hii. Niwapongeze sana Manaibu Waziri Mheshimiwa John Kwandikwa na Mheshimiwa Engineer Atashasta Nditiye na Makatibu Wakuu wote kwa kazi nzuri.

Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu kwa kutujengea barabara ya Mwanga – Kikweni – Vuchama – Ngofi – Kiriche - Lomwe kwa kiwango cha lami. Sisi Wanamwanga tunamshukuru sana. Pia tunawashukuru sana kwa kuzipandisha barabara za Lembeni – Kilomeni - Ndorwe na barabara ya Kirya - Lang’ata Bora - Kifaru kuwa barabara za TANROADS.

Mheshimiwa Spika, suala langu la tatu ni mawasiliano, tunaishukuru sana Serikali kwa kulea uwekezaji katika mawasiliano. Hakika karibu nusu ya Watanzania wanamiliki simu ya mkononi, aidha, bei za kutumia mitandao ya simu zimeendelea kushuka. Hata hivyo, makampuni ya simu yanatumia ujanja na control ya system nzima kuwaonea na hata kuwaibia wananchi wanaotumia mitandao yao. Unanunua kifurushi cha GB 15 kwa Sh.20,000/=, kwa siku saba, unatumia GB 3 kwa siku zote saba, halafu GB 12 zinamezwa kwa kuwa siku saba zimekwisha. Huu ni wizi, mtumiaji wa simu akinunua kifurushi ni chake, lazima atumie mpaka kiishie ndiyo anunue kipya. Huu ndiyo utaratibu wa kununua na kuuza mali.

Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa fursa.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii
MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Kwanza naunga mkono hoja ambazo ziko mezani. Napenda sana kuzipongeza hizi Wizara ambazo tunazijadili hapa moja kwa moja na kuzilenga Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Wizara ya Afya. Kwa kweli wanafanya kazi nzuri sana na tuwapongeze wenzetu kwa sababu wanatumia muda mrefu na wanafanya kazi kubwa ambapo ni vizuri mtu akifanya vizuri tumwambie hongera, apate moyo zaidi wa kufanya vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, muda siyo rafiki sana, nitaongea na kukumbusha hapa Kamati zetu kwamba kwa miaka miwili hapa nimekuwa naongea na kupongeza juu elimu jinsi ambavyo inapata pesa nyingi. Nimesikia mtu mmoja anasema pesa hizo hazitoshi. Haziwezi kuja kutosha hata siku moja, lakini fedha ambazo zinatengwa na Serikali shilingi trilioni 4.4 ni sawa sawa dola bilioni 2.2. Dola bilioni 2.2 kwenye elimu peke yake, hebu angalieni nchi za Afrika, nchi ambayo inatumia dola bilioni mbili katika kutoa elimu ya watoto wake, ziko chache kweli kweli! Kwa hiyo, tuipongeze Serikali ya Tanzania kwa kazi nzuri hii ambayo inafanywa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kazi hiyo nzuri, napenda kukumbusha, bado kule Mwanga tuna walimu wachache sana. Walimu wa Shule za Msingi kule Mwanga ni wachache kweli kweli! Wastani wa walimu kwenye shule zetu za msingi kule Mwanga ni walimu wawili au watatu. Tuna madarasa nane kwenye shule moja ya msingi. Kwa hiyo, walimu watatu wakiingia kwenye madarasa matatu, watoto wengine waliobaki kwenye madarasa matano, wanaendesha soko huko na kucheza darasani. Kwa hiyo, kuomba tupate walimu zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda niseme pia kwamba kwa kweli Wizara ya Afya pamoja na kuipongeza, niipongeze tena, wamejenga Vituo vya Afya zaidi ya 300 katika kipindi kifupi hiki, wanastahili kupongezwa. Katika kazi hizi nzuri na watu tuko milioni 55 huwezi kudhani kwamba itakuwa kama maua, haiwezekani. Kutakuwa na shida shida kama hizi za wazee na hizi shida tutaendelea kuzitatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuendelee kuungana pamoja kama Wabunge na Serikali yetu tusaidie kutatua haya matatizo. Napenda nikumbushe kwamba huko nyuma tulikuwa tunajenga Vituo vya Afya sisi wenyewe; wananchi wenyewe na Serikali inatusaidia. Tunajenga Zahanati na Serikali inatusaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kule kwenye Wilaya yangu ya Mwanga nina Vituo vya Afya vitatu ambavyo vimejengwa na karibu vimekwisha na vimejengwa na wananchi njia ya msaragambo. Hivi vituo tunaiomba Serikali na sasa wakati huu ndiyo mnapanga bajeti, mtusaidie kuvimaliza ili vile sawa sawa na hivi ambavyo vimeletwa na Serikali na kupigwa mara moja na kumalizika; sasa vile ambavyo wananchi wamejenga karibu wanamaliza na nguvu zao zimetumika kiasi kikubwa sana, basi mtusaidie kuvimaliza. Tuna Kituo cha Afya cha Kileo na Kitu cha Afya cha Mwaniko ambavyo tunaomba Serikali itusaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, tuna Zahanati sita ambazo tunaomba mtusaidie. Zahanati ya Kituri imekamilika na wananchi wamefanya juhudi kubwa, wamepaua na wamemalizia almost complete, lakini nasikia wametumia mabati gauge 30 na Injinia wa Wilaya anasema wang‟oe mabati. Sasa nafikiri kwamba jambo hili tulifikishe kwenye Wizara ya Afya. Maana hata kama wananchi walikuwa hawana mabati, wana nyasi peke yake, basi wamejenga kituo chao ndiyo hicho, waruhusiwe kukitumia, wasiambiwe wang‟oe mabati kwa sababu ni nyumba ya Serikali. Nyumba ya Serikali ingeng‟oa mabati kama Serikali ingeleta hayo mabati mengine. Kwa hiyo, tunaomba wananchi wasaidiwe Zahanati ifunguliwe mapema, maana wametumia fedha nyingi sana kuijenga.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna zahanati pia Lembeni, Mlingeni, Vanua kule Ndorwe, Buchama, Ndambwe na Kitoghoto ambapo Zahanati hizo karibu zimekamilika, lakini wananchi wanahitaji msaada kidogo tu wa Serikali ili waweze kuzitumia Zahanati hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, napenda nitoe mapendekezo hapa kwamba jamani tuna Shule za Sekondari sasa zinatosha, watoto wetu wa kutoka Shule za Msingi karibu wote niseme, wabaweza kwenda Sekondari, lakini kuna tatizo kubwa kwenye Sekondari zote hizi. Ni Sekondari chache tu ambazo wananchi wamemaliza ujenzi wa maabara. Ina maana kwamba wanafunzi wetu wanajifunza sayansi kwa nadharia tu, hakuna mahali ambapo wanajifunza physics kwa kufanya practical; hakuna mahali wanajifunza biolojia kwa kufanya practical; na hakuna mahali wanajifunza kemia kwa kufanya practical.

Mheshimiwa Naibu Spika, kujenga maabara siyo kitu rahisi na kuwapa wananchi wa vijijini kazi ya kujenga maabara na hawajui maabara maana yake ni nini, ni kutaka vitu vingi sana kutoka kwa wananchi wa vijijini. Tunaomba sana jamani, katika bajeti hii inayokuja, Serikali itenge angalau shilingi bilioni 200 imalize hizi maabara zote ili watoto wetu wa shule hizi za Kata waweze kufaulu mtihani wa Form Four kama wale ambao wanasoma kwenye shule za private, kwa sababu watoto wetu hawa wanafanya sayansi kinadharia.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo nataka nimalize nalo...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Profesa, ahsante sana.

MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Ooh, my goodness!

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Mheshimiwa Japhet N. Hasunga (Mb) na Naibu Waziri Mheshimiwa Omary T. Mgumba na Mheshimiwa Innocent L. Bashungwa kwa kazi nzuri ya kuiongoza Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Spika, nimependa nichangie kwa sababu naona nchi yetu inapoteza fursa kuboresha mazao na kuzalisha mazao mapya.

Mheshimiwa Spika, moja kwa kutotenga fedha za uhakika katika utafiti wa mazao na kilimo kwa ujumla. Mbili, kupiga marufuku utafiti na controlled test ya uhandisi jeni (genetic engineering. Katika eneo la utafiti, fedha tunazotenga katika agricultural research zinapaswa ziongezeke ili kukabiliana na changamoto za kuboresha mazao hasa kuongeza uzalishaji kuangalia udongo, kukabiliana na wadudu fungi, virusi na nematodes.

Mheshimiwa Spika, aidha, kumekuwa na kupanua marufuku ya genetically Modified Crops (GMO’s). Awali sheria ilikataza majaribio ya GM crops katika mashamba au kuzalisha mazao hayo ya majaribio katika mashamba. Jambo hili lilizuiliwa kisheria kwa kuweka strict liability clause. Tangazo la Katibu Mkuu wa Wizara hii Mhandisi Mathew J. Mtigumwe likapiga marufuku kabisa utafiti wote, kwenye maabara, kwenye utafiti nje ya maabara na shambani. Jambo hili limefanywa bila kujali kuwa Tanzania ndiyo nchi ya kwanza Africa katika utafiti huu (tulikuwa mbele ya nchi zote Afrika katika kutafiti wa GMO. Tumefunga maabara na kuwatawanya wanasayansi na watafiti wetu.

Mheshimiwa Spika, hatua hii inasikitisha na kuturudisha nyuma sana. Hakuna kubisha kuwa tabianchi imebadilika kwa haraka na inaendelea kubadilika. Mazao tunayotumia ikiwa hatutayabadili kuweza kuendana na mabadiliko hayo, keshokutwa tutakuwa taifa lenye njaa sana. Wakati huo, tutakuwa hatuna majibu ya changamoto ya mvua kidogo, mvua inayonyesha kwa wiki tatu badala ya miezi mitatu, ongezeko la joto (evaporation) ongezeko la aina ya wadudu na idadi yao, virusi na visumbufu vingine, upungufu wa unyevu kwenye hewa na kwenye udongo.

Mheshimiwa Spika, maamuzi yetu yanatuchelewesha sana. Nchi yetu imefanya utafiti tayari na kuwa na mbegu yake ya GMO cotton (inaitwa Bt cotton Duniani). Hii ni kwa kuwa takriban nchi zote duniani zinazolima pamba zinazalisha na kutumia Bt cotton. Mfano wa nchi hizo ni India, Pakistan, China, Russia, USA, Brazil, Uganda, Kenya, Sudan, Egypt, Nigeria, Niger , Mali, Burkina Faso n .k. Ukiangalia ni Tanzania tu ambayo inakataza wakulima wake kutumia mbegu za Bt. Cotton.

Mheshimiwa Spika, Bt cotton inatoa longer lint (hivyo bei bora); inazalisha 3,000 kg cotton/na ukilinganisha na mbegu za kienyeji tunazotumia. Inakinzana na wadudu na visumbufu vya pamba hivyo huhitaji kupulizwa dawa (viuatilifu) mara tatu badala ya mara sita mpaka saba kwa msimu, na huhimili upungufu wa unyevu kwenye udongo. Aidha, kwa Tanzania ni muhimu kutumia Bt cotton kwa kuwa inakinzana na red american ball worm, hivyo kwa kutumia Bt cotton hatuna haja ya kuzuia kilimo cha pamba katika Wilaya ya Chunya, Rufiji, Lindi, Mtwara, na Wilaya zingine za Kusini.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii; na kama ilivyoada ningependa kutoka sakafu ya moyo wangu niwapongeze sana Mheshimiwa Waziri na Naibu wake na Wizara kwa ujumla kwa kufanya kazi nzuri sana ya kusambaza umeme katika nchi yetu. Kazi mnayofanya inaonekana nasi ni wajibu tuwapongeze.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kazi nzuri na kubwa kila siku lazima kunakuwa na mashimo na madoa ambayo lazima yanyooshwe. Ningependa niende kwenye jimbo langu; niseme mpaka mwisho wa mwaka uliopita wananchi wa vijjini kule Mwanga walikuwa wakinunua umeme wa shilingi 5,000 wanapata unit 43 za umeme. Mwisho wa mwaka jana ukawa ndio mwisho wa furaha. Tangu mwaka huu uanze shilingi elfu 5 ile ile wananunua unit 13 umeme umepanda kwa asilimia 330.

Mheshimiwa Naibu Spika, niliuliza juu jambo hili wakati wa briefing na Mheshimiwa Naibu Waziri akinipa jibu sijui niliite jibu la namna gani; akasema watu wa mwaka wote waliopewa umeme wameanzisha viwanda kule nyumbani. Kwa hiyo kwa sababu wameanzisha viwanda wanapata umeme kwa bei ya watu wenye viwanda. Sasa nimetafuta vile viwanda kule Mwanga sijaviona. Mheshimiwa Waziri ninakuomba kesho ukifanya majumuisho hili jambo la kuwabagua watu wa Mwanga kama wamekuwa watu wa viwanda wote liachwe. Watu wa Mwanga wapate umeme wapate umeme kama wananchi wa Tanzania wanaoishi vijiji.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, muda ni mdogo, lakini ningependa nizungumzie kidogo nizungumzie juu ya REA III. Nimshukuru Mheshimiwa Waziri na Naibu wake walitembelea kwenye jimbo langu, na kazi kwa kweli kwa span imefanya; lakini yapo maeneo ambayo span inayotolewa ya kuwafungia watu umeme inatuletea matatizo kule vijiji. Kwa mfano kwenye Kijiji changu cha Kigonigoni wananchi wanaotaka umeme wapo 380. Watu waliopo kwenye scope ya kupewa umeme ni watu 38, na kijiji chote watu wanakaa mahali pamoja si kijiji ambacho kimesambaa kwenye eneo kubwa; ukiongeza nguzo hamsini unawapa wote umeme. Sasa ninaelewa mambo ya span na mambo ya menejimenti, lakini na ninyi muelewe siasa pia na mtupunguzie malalamiko ya wananchi. Kama kinachotakiwa ni nguzo 50 leteni nguzo ... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Spika, nilizungumza juu ya hoja hii, lakini muda wa dakika tano ni mdogo sana. Hivyo nina jambo la pili ambalo ni kuhusu ubora wa mafuta ya petroli na dizeli hapa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, katika Bunge la 10, Bunge lilichukua hatua ya pekee ya kuzuia wenye vituo vya mafuta kuchakachua mafuta ya petroli na dizeli kwa kuichanganya petrol + kerosene na diesel + Kerosene. Lengo la wafanyabiashara ni kupata faida kubwa sana. Hivyo, Bunge likapandisha bei ya kerosene iwe karibu sawa na diesel au petrol.

Mheshimiwa Spika, kwa muda wa miaka mitano sasa tatizo la kuchakachua mafuta ya petrol na diesel limerudi upya. Takriban vituo vyote vya mafuta leo katika Miji ya Mwanga, Moshi, Arusha, Dodoma, Dar-es-Salaam, Morogoro, Singida, wanauza mafuta yaliyochakachuliwa. Yaelekea kuwa, wafanyabiashara wanaoleta mafuta ya taa kwa bei rahisi kutoka nje (bila kodi) na kuyasambaza nchi nzima. Nchi yetu inapata hasara kubwa sana kwa kutumia mafuta ya kuchakachua, yanaharibu magari, pump, mitambo na viwanda.

Mheshimiwa Spika, haya yote yanatokea na EWURA wapo. EWURA walishindwa kazi ndiyo maana Bunge likachukua hatua. Sasa mafuta yanachakachuliwa sana, huu ni wakati wajue kuwa si heshima kuendesha ufisadi. Waziri wawajibishe MD na Management yote ya EWURA, weka watu walio tayari kufanya kazi na Dkt. John Pombe Magufuli.
Muswada wa Sheria ya Bodi ya Kitaalam ya Walimu Tanzania wa Mwaka 2018
MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kukushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami nitoe mchango mdogo katika Muswada huu ambao uko mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza jambo hili la kutaka kuanzisha Bodi ya Taaluma ya Ualimu limeshughulikiwa kwa muda mrefu. Kwa kweli napenda nimpongeze sana kwa dhati kabisa Waziri wa Elimu, Mheshimiwa Prof. Ndalichako kufanikiwa kulileta jambo hili hapa Bungeni kwa sababu linahitajika sana. Hongera sana Mheshimiwa Prof. Ndalichako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuwashukuru Mawaziri wa Elimu ambao walihudumu katika Wizara hii tangu mwaka 2006. Namshukuru hasa Mheshimiwa Mama Margaret Sitta ambaye alilianzisha jambo hili kwa nguvu mpya kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na kupanuka kwa elimu haraka haraka katika miaka hii 20 iliyopita au miaka hata 30 hivi iliyopita, kumekuwa na walimu wa aina nyingi sana ambao wameingia kufundisha katika shule zetu. Mwanzoni tulikuwa na Universal Primary Education au ile ilikuwa inaitwa UPE na tukawa tunafundisha walimu wakati mwingine waliitwa hata Voda fasta. Kuanzia mwaka 2006 tulikuwa na upanuzi mkubwa katika shule za sekondari katika kila kata. Kwa hiyo, tukawa tumepanua sana idadi ya mahitaji ya ualimu katika ngazi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi hicho hicho kumekuwa na upanuzi mkubwa sana katika elimu ya juu na hasa katika vitivo vinavyofundisha walimu kwa ajili ya sekondari na shule za msingi. Kwa sababu hiyo, hii Bodi ni muhimu sana katika hatua hii ili kuweza kuhakiki walimu mbalimbali ambao wako darasani wanafundisha watoto wetu. Lengo kubwa hasa ni kuhakikisha kwamba uhakiki huu unatuletea ubora katika elimu yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2008 - 2015 kulikuwa na uajiri wa walimu uliotoka walimu 7,000 katika shule za msingi mpaka karibu kufikia walimu 30,000. Haiwezekani kwamba wote hawa walikuwa ni wazuri na wenye sifa za kutosha. Kwa hiyo, wakati huu ni muafaka kuwa na Bodi hii itakayoweza kuwahakiki na kuweza kuhakikisha kwamba walimu wanaofundisha wana sifa stahiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nichomekee hapa hapa kwamba katika mikoa mingine wakati walimu walikuwa wanaongezeka sana kwenye shule za msingi na sekondari iko mikoa ambayo ikuwa haipatiwi walimu kwa sababu awali ilikuwa na walimu wengi kupita mikoa mingine. Moja ya mikoa hiyo ni Mkoa wa Kilimanjaro na Wilaya yangu ya Mwanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na mabadiliko ya kiasili, walimu wanakuja, wanazeeka, wanastaafu, wanaondoka, wengine wanakufa na wengine wanahama, Walimu waliokuwa wameajiriwa katika Wilaya yangu mwaka 2001 wamepitiwa na mkumbo huo na hivi sasa kuna upungufu wa walimu 390. Wastani wa idadi ya walimu katika shule zetu za msingi ni walimu wawili au watatu. Nami naamini katika Wilaya nyingine kama Same na hata Hai na nyingine mkoani pale, ziko namna hiyo hiyo. Nawaomba wakati huu Wizara ya Elimu, Ofisi ya Rais, TAMISEMI waende wapitie ikama, kwa sababu nafasi hizi zilizoko zina mishahara, watusaidie kuajiri walimu mapema iwezekanavyo, kwa sababu shule watoto wanakaa bure, hawafundishwi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nasema haya, nimeisoma hii sheria vizuri, nashauri kwamba walimu wale wanaofundisha kwenye vyuo vya ualimu, lakini pia walimu wale ambao wanafundisha vitivo vya walimu watakaokuja kufundisha kwenye shule za msingi na sekondari na wenyewe walazimike kusajiliwa kwa sheria hii. Kwa kufanya hivyo itasaidia kuhakikisha kwamba kweli wale wanaofundisha walimu wanawafundisha kwa kuwa na sifa stahiki katika kufanya kazi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni suala la nidhamu na maadili. Walimu wetu ambao wanafundisha huko na hawa ni wachache sana, lakini hawana maadili yanayotegemewa kwa mwalimu anayefundisha kwa kujenga malezi bora katika shule. Ndiyo maana katika hizi siku za karibuni kumekuwa na walimu ambao wanapiga watoto mpaka wanakufa; kuna walimu ambao wanakuwa na mahusiano ya kimapenzi na watoto; na kuna walimu ambao kwa hulka hawawezi kutekeleza wajibu wao. Katika haya ni muhimu sana Bodi katika Kamati zake ambazo zimependekezwa ziwe kali sana katika kuhakikisha kwamba kila mwalimu aliyesajiliwa na Msajili wa Walimu au Mrajisi awe na sifa stahiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, ni kitu cha kupendeza kwamba Bodi hii sasa ikishamfukuza mwalimu anayefundisha kwenye shule za Serikali, mwalimu huyo hawezi kwenda kuajiriwa kwenye shule za binafsi. Hii itahakikisha kwamba mtu ambaye sio mwalimu hawezi kufundisha kwenye public school na private school.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wazazi watakuwa na mahali ambapo wanaweza kwenda wakalalamika kama wanadhani kwamba watoto wao hawatendewi haki. Hili jambo ni muhimu sana. Nami nawashauri sana, pamoja na tofauti zetu za kiitikadi, tuiunge mkono Serikali kwa nguvu zote, Bodi hii ianzishwe na…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naunga sana mkono Serikali katika kuleta Bodi hii na msisitizo wangu ni kwamba wote tuiunge mkono na ianze kazi mara moja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuruku sana kunipa nafasi ya awali kabisa kuchangia hoja ambayo ipo mezani. Kwanza ningependa sana niwapongeze Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, nimpongeze Naibu wake na timu yote ya Katibu Mkuu kwa kazi nzuri ambayo wamefanya, inaonesha wazi kabisa kwamba katika bajeti ya mwaka huu wamesikiliza sana na kuyaleta yale mambo ambayo tuliyapendekeza katika bajeti ile ya mwaka jana. Kwa hivi tunawapongeza sana kwa kuwa wasikivu na kuleta mapendekezo ambayo na sisi tunaweza kuongeza nyama ili mapendekezo haya yaweze kuwa mazuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, imefurahisha sana kwamba Mheshimiwa Waziri ameshughulikia zile kero ambazo ni ndogo ndogo na zinawasumbua sana wawekezaji, kero zile ambazo zimewekwa na TBS, TFDA, OSHA, EWURA, SUMATRA na wengine. Hizi tunawapongeza sana kwa kuziondoa, lakini ninafikiri kwamba mngekwenda mbele zaidi. Uchumi wetu unategemea sana usafirishaji na hasa usafirishi wa nchi ambazo zinatuzunguka. Moja ya kero kubwa sana ya watu ambao wanasafirisha bidhaa kupitia nchini kwetu na wafanyabishara walioko kando kando ya nchi kama Mwanza, Kigoma na kadhalika, ni kusimamishwa barabarani mda mrefu kabisa na polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, polisi wanakuwa ni wasumbufu wakubwa sana na nilikuwa namsikiliza hapa Waziri Waziri Mambo ya Ndani akitoa amri, ningependa utoe amri kwamba watu walio na mzigo yao wakishakaguliwa mara moja, wakakaguliwa mahali pengine mara ya pili waachwe waende nyumbani. Wanyarwanda wanachangua kutoka Kigali kwenda Mombasa kuchukua bidhaa zao kwa safari ya kilometa 7,200 round trip badala ya kutoka Kigali kuja Dar es Salaam ambayo round trip ni kilometa 3,200 kwa sababu tu magari yanaokwenda round trip ya kilometa 7,600 yanakwenda na kurudi mapema zaidi ya yale ambayo yanapitia Tanzania. Kwa hivi tuchukue hatua kali kabisa tuhakikishe kwamba polisi hawatuharibii biashara ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ningependa tuchukue hatua ambazo zitatusaidia katika bajeti ambazo zinakuja. Moja hatua hizi ni kuweka msisitizo sana kwenye kilimo. Kilimo kimetajwa na ripoti zote za kamati ambazo zimewasilishwa hapo. Nitatoa mfano mmoja tu katika nchi yetu tuna maeneo ya umwagiliaji ya hekta 485,000 za umwagiliaji. Kama tungelima mpunga kwa kutumia kilimo cha kisasa, kutumia mbegu nzuri, kutumia mbolea ku-control magugu vizuri uzalishaji kwenye mashamba yetu ungefikia tani nane kwenye hekta moja, lakini uzalishaji wetu kwenye kilimo hiki cha umwagiliaji ni tani 1,500 na tunalima mara moja tu kwa mwaka kama vile kwenye mashamba ya kawaida yanayongojea mvua wakati katika mashamba haya ya umwagiliaji tungeweza kulima mara mbili hata mara tatu kwa mwaka kutegemeana na mbegu ambayo tungeweza kuchagua na kwa kuwafundisha wakulima, kwa kuwekeza katika kuwafundisha wakulima tungeweza kupata kwenye bajeti yetu mpaka dola bilioni tano/kumi kwa mwaka kutokana na mauzo ya mpunga kwa nchi za jirani zinazotuzunguka. Kwa hiyo, hebu tuweke nguvu kidogo kuwafundisha wakulima na ituletee mchango huu mkubwa ambao unaweza kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni uwekezaji katika utafiti wa kilimo ni mdogo sana, literal hakuna uwekezaji kabisa na bahati mbaya mwaka jana mwishoni kuna Mhandisi mmoja ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo alifuta uhandisi wote wa biotechnology na uhandisi jeni, nadhani alikuwa amechanganya uhandisi, uhandisi jeni na uhandisi wa mabomba na mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu umeona mwaka huu, nusu ya nchi imepata mvua za masika kuanzia mwisho wa mwezi Mei na mvua hizi kwa mazao tuliyonayo tunategemea mvua mwezi Februari, sasa kama hatufanyi uhandisi jeni, tunategemea nini hapo kesho? Wakati mabadiliko makubwa haya ya tabianchi yakitukumba, yapo mazao ambayo tunayapanda kwa siku hizi kiaibu kabisa. Kwa mfano, kwa nini tunatumia mbegu ya hovyo ya pamba wakati ambapo nchi zote duniani zinatumia bt cotton na sisi wenyewe tunavaa nguo wote hapa za bt cotton, lakini tunakataza Wakulima wetu wasitumie bt cotton wakaongeza uzalishaji mara tatu, wakazalisha pamba yenye nyuzi ndefu, wakapunguza kupuliza dawa mara tatu, badala ya kupuliza mara saba, wakapunguza, wakapiga mara tatu/mara nne. Wakapunguza na wadudu ambao wanakula pamba halafu tukaruhusu pamba iweze kupandwa nchi nzima kuanzia Chunya mpaka Lindi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafanya hivyo tumepiga marufuku Kusini kote huko kwa sababu pamba tunayopanda hapa nchini tunawalazimisha wananchi wanapanda ka pamba kale kanazalisha kilo 300 za pamba kwa hekta. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ni muhimu sana tutoke pale tulipofika, maana pale nyuma tulikuwa tunaruhusu utafiti wa uhandisi jeni, tunaruhusu watu wa-test mazao ya uhandisi jeni kwenye controlled environment, lakini sasa tumepiga marufuku kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maabara zetu zilikuwa ndiyo nzuri kupita zote Afrika nzima, zote tumefunga na wataalam wetu waliokuwa wazuri kupita Afrika nzima tumewasambaza kila mahali, wako frustrated. Mimi nadhani turudi pale tulipotoka, tufanye utafiti maana wananchi wetu kama wa Bukoba wasingeacha kula ndizi wakageukia ugali kama tungekuwa tuna-test mazao haya ya uhandisi jeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika ugonjwa wa mnyauko wana sayansi wetu waligundua kwamba ukiondoa gene ile ambayo ina udhaifu na virusi ya mnyauko, ukaweka gene ya pilipili hoho ndizi zinakuwa ambazo hazina mnyauko, sasa pilipili hoho tunapika, wakati tunapika matoke, sasa kama tukiiweka kwenye mgomba ina shida gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ni lazima tubadilike na ni lazima tubadilike na tuende pamoja na dunia huwezi kuwa unavaa nguo za bt cotton halafu unawazuia wakulima wako wasikuze bt cotton wakati Kenya wanakuza bt cotton, Uganda wanakuza, Sudan wanakuza, Egypt, Mauritania, Nigeria wote wanakuza na nchi zingine zote duniani zinakuza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ukisema hii bt cotton ni mbaya, sasa uzuri wake ungekuwa nini, kwa sababu nguo ulizovaa ni za bt cotton, kwa hiyo nilikuwa nataka niishauri Serikali hili ni Serikali kwamba ifikirie upya marufuku yaliyopigwa katika utafiti wa uhandisi jeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nilikuwa nataka nipige tena debe juu ya maabara...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali (Na. 2) wa Mwaka 2019 (Toleo la Kiingereza).
MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kutoa mawazo kidogo tu katika Muswada huu. Ni siku 17 tu wachimbaji wadogo walitoa matatizo yao mbele ya Mheshimiwa Rais na kwa speed aliyofanya kuleta Muswada huu, anastahili tumpongeze sana, Mheshimiwa Rais wetu Dkt, John Pombe Magufuli. Hii ni kazi nzuri na tusiibeze kwa njia yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nimeangalia kifungu cha 26 cha sheria hii ambacho kinaongelea juu ya import permit. Wako watu wanachimba na kutafuta madini hapa Tanzania kutoka Thailand; wako watu wanatoka nchi hata ya Afghanistan wanachimba hapa; wako Wa-Senegal wanachimba hapa na wanaondoka na madini yetu, kwa sababu wanapokwenda nyumbani kwao kule, wanapokelewa kama wao ni mashujaa.

Mheshimiwa Spika, sisi tunakuwa Wakatoliki zaidi ya Pope. Mtu anakwenda anachimba madini yake popote anapoyachimba, naomba tukifute hiki kifungu kilichorekebishwa na Serikali, kinaitwa 86 (a) katika mabadiliko haya ya Serikali. Hiki kifungu nawaomba sana; na uzee wangu leo nataka niwapigie magoti, tukifute kabisa. Mtu yeyote ambaye ameleta madini huku Tanzania, afanye declaration ndani ya soko anapouzia ili Serikali iweze kuweka record. Kusiwe na application yoyote kule mpakani au application yoyote huko njiani, apeleke madini mpaka sokoni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi zote hizi za dunia zinajengwa kwa mambo mengi; na yako mambo mengi ambayo katika Bunge lililoko wazi namna hii, hatuwezi kusema kila kitu. Kwa hili, imenibidi nikuombe sana kwamba nisimame na nili- convince Bunge lako Tukufu katika hili. Tufute hiki kifungu cha 26 kabisa. Kama Mheshimiwa Waziri anataka kukileta kwa namna, akiweke kwenye kanuni ya kumtaka mtu aliyeleta madini afanye declaration kwenye soko.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.4) wa Mwaka 2019 (Toleo la Kiingereza)
MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii nami nichangie walau neno katika mabadiliko haya ya Sheria Mbalimbali (Na.4) ya Mwaka 2019. Kwanza niseme wazi kama mimi naunga mkono hoja hii iliyoko mbele yetu.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati naunga hoja basi nichomekee vitu viwili, vitatu. Kwanza ningependa sana nimpongeze Mheshimiwa Rais pamoja na Azimio letu la jana basi niongeze kumpongeza kwa jinsi walivyo endesha Mkutano wa 39 wa SADC. Pili ningependa sana nimpongeze rafiki yangu na Shemeji yangu Mheshimiwa Miraji Mtaturu kwa kuchaguliwa na kuapishwa kuwa Mbunge wa Singida Mashariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niingie katika sheria yetu hii ambayo iko mezani na kwanza nimpongeze sana Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kazi nzuri waliyofanya katika kuleta marekebisho ambayo yako mbele yetu lakini pia niongeze sauti yangu kwa kazi nzuri ambayo imefanywa na Mawakili wetu wa Serikali katika kesi ambayo wameshinda tena wameshinda kwa akili kubwa sana. Mwenyezi Mungu aendelee kuwabariki nasi wajue tuko nao katika kutetea mali zetu popote zilipo duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya vitu ambavyo vimenikuna sana katika hoja hii iliyoko mezani ni Mabadiliko ya Sheria ya Vizazi na Vifo, Sura 108 kwamba sasa Serikali itagatua mamlaka yale ya kutoa vyeti vile vya uzazi na vifo katika vijiji, kwamba Mtendaji wa Kijiji pale kijijini kwangu atafanya kazi hiyo na itapunguza adha ambayo wananchi wanapata. Mfano, nilikuwa nazungumza na Mgosi Mheshimiwa Shangazi kwamba watu wake wanatoka kwenye kijiji cha Mnazi wanakwenda mpaka Korogwe halafu wapande mlima waende mpaka Lushoto, kilometa 170 ndiyo warekodi kizazi au unatoka kwenye Tarafa yangu ya Jipendea kule kwa Kihindi unakwenda mpaka Lembeni mpaka unafika Mwanga kilometa 70, halafu urudi zingine 70 kwa ajili ya kusajili uzazi tu au kusajili kifo. Kwa hiyo, ndiyo unakuta Watanzania wengi wanakuwepo lakini hawakusajiliwa wanapotakiwa sasa wawe na nyaraka zile za uzazi hawana. Kwa hivi hili ni jambo la kimapinduzi na sote tunaliunga mkono kwa nguvu zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo ni muhimu sana katika suala hili ni kuweza kujua wananchi wa Tanzania ni akina nani? Kwa sababu katika kijiji Mtendaji wa Kijiji anawafahamu watu wote pale. Sasa watu wakijitokeza tu kutoka eneo lolote kwenda kwenye Mji Mkuu wa Wilaya kujiandikisha wanaweza kuandikishwa wale waliomo na wale ambao hawamo. Kwa hivi, jambo hili ni jambo zuri na tunaliunga mkono kwa nguvu zote zile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sura hii pia imerekebisha uasili wa watoto au adoption of children katika maeneo yetu. Kwa hivi hii sheria sasa inakuwa sheria ya kisasa na mambo tunakwenda nayo ni yale ya kilimwengu yaliyoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nimeliona limefanywa kwa uzuri kabisa ni Sheria inayorahisisha Uendeshaji wa Masuala ya Jinai na Mashtaka katika maeneo mbalimbali kufuatana na marekebisho ambayo yametokea katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Kwa kweli mimi sikuwa na mambo mengi ya kufanya katika kazi hii nilipenda niseme hayo tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana na Mungu akulinde. (Makofi)