Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Freeman Aikaeli Mbowe (15 total)

MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri sana ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, hili tatizo siyo la Mheshimiwa Mbunge aliyeuliza peke yake, ni tatizo la nchi nzima, kwamba kumekuwa na tatizo kubwa la kushindwa Sasa swali kwa Mheshimiwa Waziri; ili tuweza kujenga Taifa moja lenye kuheshimu kwamba vyama vingi vya siasa ni takwa la kikatiba kwa mujibu wa Ibara Na. 3 (1) na (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwamba nchi yetu ni ya vyama vingi vya siasa; hatuoni kama kuna sababu za msingi za Serikali kukemea watumishi wa Serikali ambao wanafikiri wana haki ya kutenda haki kwa chama kinachotawala lakini kutokutenda haki kwa vyama vingine ambavyo ni tofauti na Chama cha Mapinduzi? (Makofi)kutofautisha majukumu ya Chama cha Mapinduzi na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tatizo la baadhi ya watumishi katika Serikali kufikiria wao ni sehemu ya Chama Tawala, limekuwa ni tatizo kubwa ambalo linapekea kutokutenda haki katika maeneo mengi sana ya Taifa letu. Swali la Mheshimiwa Mbunge siyo kwamba linajenga tu misingi ya kibaguzi, linajenga misingi ya kichochezi kwamba nihaini kuwa kwenye chama kingine tofauti na Chama cha Mapinduzi; na jambo hili liko katika ngazi mbalimbali za utawala katika nchi yetu. (Makofi)
MHE. ANGELLAH J. KAIRUKI - WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Spika, kwanza niseme tu kwamba swali hili sisi binafsi kwa upande wa Serikali hatujaliona kama ni la uchochezi na ndiyo maana tumeweza kulijibu na ninaamini upande wa pili wameweza kufurahia majibu ambayo tumeyajibu kwa sababu tumetenda haki kwa mujibu wa Katiba. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na kwamba watumishi wengine wamekua labda hawatendi haki kwa vyama vingine, kwa kweli sidhani kama ni sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Watumishi wa Umma wanatakiwa watekeleze sera za Serikali; wanatambua kwamba kuna Mfumo wa Vyama vingi vya Siasa, lakini vilevile wanatambua kwamba ipo Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ambacho ndicho Chama kinatawala katika wakati husika. Kwa hiyo, hawana jinsi, wanatumikia kwa kufuata Ilani ya chama kilichopo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukiangalia kwa wao, pamoja na kwamba wanatumikia chama kilichopo madarakani, yapo makatazo. Hawatakiwi kujionyesha dhahiri kwamba wanahusika katika masuala ya kisiasa. Ndiyo maana ukiangalia katika sehemu (f) ya Kanuni zetu za Kudumu za Utumishi wa Umma za mwaka 2009 imeeleza ni kada gani ambazo hazitakiwi kujihusisha na masuala ya kisiasa. Naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Spika nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii.

Mheshimiwa Spika, majeshi yetu ni vyombo vya ulinzi na usalama, na ni vyombo ambavyo wote tunastahili kuviheshimu, lakini kwa muda sasa kumekuwa na utamaduni wa kuwatumia askari kutoka Bara kuwapeleka Zanzibar, kuwaandikisha Zanzibar wakati wa uchaguzi na kuwatumia kupiga kura katika mazingira ambayo hayapo wazi.

Je, Mheshimiwa Waziri una taarifa za upelekaji wa vikosi Zanzibar kwa jukumu moja tu la kupiga kura na kisha kurejeshwa Bara?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, kwanza tutambue kwamba majeshi yetu ni ya Muungano. Kwa maana hiyo, Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania anaweza kupangiwa kufanya kazi yake sehemu yoyote ya Jamhuri ya Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kuhusu kuandikishwa kupiga kura, Mheshimiwa Mbowe nataka uelewe kwamba utaratibu wa kupiga kura Zanzibar unafahamika na uko wazi. Huwezi kwenda leo ukaandikishwa, ukapiga kura. Ili uweze kupiga kura, ni lazima uwe ni Mzanzibari mkaazi. Hiyo ipo na ushahidi tunao. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, ambacho tunaweza kusema hapa kwa ufupi ni kwamba wanajeshi wanapopelekwa Zanzibar ni kwa ajili ya kulinda usalama wakati wa uchaguzi.
MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza
swali.
Mheshimiwa Spika, hali ya ukame wa chakula katika nchi yetu, kimsingi inasababishwa
na matatizo mawili makubwa. Tatizo la kwanza na matatizo yote mawili yanatokana na maji.
Aidha, kunakuwa na ukame kwa maana ya kukosekana kwa maji, ama kunakuwa na mafuriko
kwa maji kuwa ya ziada. Suluhisho la kudumu la tatizo la chakula katika maeneo mengi ya nchi,
mbali na Serikali kuendelea kutoa misaada ufumbuzi wa kudumu wa tatizo la muda mrefu ni
kufanya water management kwa njia mbili.
Mheshimiwa Spika, kwenye maeneo yenye mafuriko kufanya flood management na
kwenye maeneo yenye ukame wa maji kufanya water conservation yaani hifadhi ya maji
hususani wakati wa mvua.
Mheshimiwa Spika, sasa swali ni hili, kwa nini Serikali isiweke mpango maalum kupitia
Halmashauri za Wilaya mbalimbali kwa kila Halmashauri kuwa na mpango wake wa kuangalia
namna bora ya uhifadhi wa maji kwa wakati wa mafuriko, vilevile uhifadhi wa maji wakati wa
msimu wa mvua ili yatumike kwa ajili ya unyweshaji maji. Vilevile utaratibu wa uzuiaji wa
mafuriko (flood management) wakati wa mafuriko ili tuepukane na hili tatizo la chakula kwa
utaratibu wa kudumu zaidi?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri Mkuu
naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mbowe kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, wazo la kuvuna maji ya mvua tutalileta kwenye awamu ya pili
ya programu ya maji. Ni wazo la msingi kwamba ni lazima sasa tuelekee kuvuna maji ya mvua.
Pia masuala ya kuweza kuzuia mafuriko ni jambo ambalo tutalifanya kwenye program ya pili.
Kwa hiyo, tutaleta mpango huo ambao kila Halmashauri tutaangalia kwamba kila mwaka
ikiwezekana wawe na mpango wa kuweza kujenga mabwawa madogo madogo ambayo
yako chini ya uwezo wao. Wizara ya Maji itakwenda kusimamia na miradi mikubwa ya strategic
dams hiyo itasimamiwa na Wizara ya maji.
MHE. FREEMAN H. MBOWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kumuuliza swali Mheshimiwa Waziri.
NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT)
17
Maadam Mheshimiwa Waziri ameeleza kwamba maelekezo ambayo Serikali Kuu inatoa kwa Serikali za Mitaa yanasimamiwa ama yanasimamia msingi wa nia njema na kwa sababu tunakubaliana katika utawala wa nchi, nia njema haiwezi ikazidi utaratibu uliowekwa kwa sheria, kanuni na taratibu za kiutawala na kwa sababu kumekuwepo na tatizo kubwa sana la muingiliano wa maelekezo hususan kwenye zile Hamlashauri za Wilaya ama Manispaa ambazo zinaongozwa na vyama tofauti na Chama cha Mapinduzi.
Je, ili kuweka utawala wa sheria, unaoheshimu mifumo yetu ya kiutawala iliyowekwa na sheria, Waziri haoni kwamba ni muhimu na busara sana Serikali ikatoa tamko katika Bunge hili kwamba viongozi katika ngazi ya Wilaya kwa maana ya Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa waache kuingilia majukumu ya Halmashauri za Wilaya na Manispaa ili kuruhusu maamuzi ya vikao vya Madiwani na wengine kufanya kazi kwa mujibu wa taratibu za sheria?
Mheshimiwa Spika, kwanza naomba tuweke kumbukumbu sawa sawa, lengo letu Serikali za Mitaa zimewekwa kwa mujibu wa Katiba Ibara 145 na utekelezaji wake unaelezewa katika Ibara 146; kwa hiyo, maana yake ni chombo halali ambacho kiko kwa mujibu wa sheria. Nimesema pale awali maelekezo hasa ya kutoka Serikali Kuu, maana yake kikubwa zaidi yanania njema kama Mheshimiwa Mbowe ulivyorejea hapa. Lakini anasema jinsi gani Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wasiingilie maamuzi, kinachofanyika ni kwamba Wakuu wa Mikoa na Wilaya sio wanaingilia, wanachokifanya ni nini? Kinachotakiwa hasa cha msingi ni kuona kama utaratibu unakiukwa pale Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya ana haki ya kuweza kuliingilia hilo jambo lisiharibike kwa ajili ya maslahi ya umma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nina imani haiwezekani kikao halali cha baadhi ya Madiwani kimefanya ambayo hakuna utaratibu wowote uliokiukwa Mkuu wa Mkoa au Wilaya atakuwa ameingilia. Lakini kama kuna jambo linaenda kinyume na Mkuu wa Mkoa yupo, naye anaona jambo linaharibika kwa makusudi mbele yake ni lazima aingilie hapo ilimradi kuweka mambo sawasawa. Kwa sababu mwisho wa siku ni kwamba watu wanatarajia kwamba Serikali hiyo iliyowekwa kwa mujibu wa sheria basi itatimiza majukumu yake kama wananchi walivyoipa ridhaa itawaongoza katika kipindi hicho mambo yanayohitajika yaweze kufikiwa na yaweze kufahanikiwa. Kwa sababu sasa hivi Tanzania tunaongozwa kwa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 - 2020.
Mheshimiwa Spika, lengo kubwa ni kwamba kuanglia kama Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya aharibu utaratibu wa Baraza la Madiwani lakini wanahakikisha kwamba utekelezaji wa Ilani unakamilika kama ilivyokusudiwa na wananchi walioichagua Serikali hiyo.
MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana na namshukuru Mheshimiwa Waziri na nampa pole sana kwa ajali iliyompata.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, ni kweli nia ya kupeleka maeneo ya kiutawala karibu na wananchi mambo yanaweza yakachochea maendeleo kwa upande mmoja, lakini vilevile yanaweza kupeleka huduma jirani na wananchi, lakini je, Serikali haioni kwamba kutokana na kukua kwa mahitaji ya shughuli za kimaendeleo katika nchi yetu utakuwa wakati muafaka kuangalia upya Sheria ya Ugawaji wa Mikoa, Wilaya na maeneo mengine ya kiutawala ili kuokoa fedha zinazopelekwa katika utawala kwenye bajeti ya Taifa na kuzielekeza zaidi katika bajeti ya maendeleo? Hilo ni swali la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kufanya hivyo, huoni kwamba Serikali inaweza ikajikuta inapeleka zaidi fedha kwenye ujenzi kwa mfano wa hospitali, shule badala ya kujenga nyumba za watumishi ama za viongozi mbalimbali ambao wanaongezeka idadi na kuleta mzigo mkubwa kwenye bajeti? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe, Mbunge wa Hai kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kama tulivyojibu katika jibu letu la msingi kwamba ugawanyaji wa maeneo ya kiutawala unazingatia sheria zilizopo hizi mbili, Sura 287 na 288 za Serikali za Mitaa lakini zinabebwa na msingi wa Katiba. Lakini pia kubwa ni ushirikishwaji na hitaji la wananchi kwa sababu hatugawi tu, tunagawa kwa sababu msingi wake ni kurahisisha huduma kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikuoneshe takwimu; wakati Morogoro yenye ukubwa wa square kilometer 77,522.08 ni Mkoa mmoja, Kilimanjaro, yenye size 13,209 ni Mkoa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wakati Tabora yenye ukubwa wa size ya square kilometer 76763.03 lakini Kilimanjaro ina size hiyo. Lakini nyingine wakati Jimbo la Liwale tu lina ukubwa wa size ya square kilometer 34300.92 Hai ina square kilometer 1011. Tukisema kwamba tusiendelee kugawa, tukasitisha kama Mheshimiwa Mbunge anavyosema uwiano uko wapi katika kutoa huduma za wananchi? (Makofi)
Mheshimia Spika, mahitaji haya ya sheria kuangaliwa upya kwa msingi wa kusitisha pengine sio jambo la busara sana, pengine tufikirie kama nia ni kupunguza matumizi ya Serikali, kuunganisha hivi visehemu vidogo vidogo ili viwe sehemu moja, viwiane na maeneo mengine makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili hizo issue ni fedha, haya ndiyo matumizi ya fedha kwa ajili ya kuhudumia watu. Kwa hiyo hauwezi ukabanwa kwamba matumizi ya fedha, kwani zinatakiwa ziende wapi? Si ziende zikahudumie watu? Kwa hiyo swali la pili, Serikali itaendelea kutenga/kugawa maeneo haya kwa msingi wa mahitaji kwa kuzingatia Katiba na sheria zilizopo. (Makofi)
MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kuwepo na mabweni katika shule kwa ajili ya kidato cha tano na sita ni jambo muhimu ama sharti muhimu la kupata nafasi ya kuwa na shule ya kidato cha tano na sita, na kwa sababu kazi ya ujenzi wa mabweni katika maeneo mengi imeweza kufanywa na wananchi wenyewe na Serikali ikaongezea nguvu zake; na kwa sababu vilevile sera ya Serikali katika ujenzi wa kidato cha tano na sita ni kupata wananfunzi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi ili wachanganyikane, jambo ambalo ni jambo jema.
Serikali haioni kwamba kwa wale wananchi ambao wapo tayari kujenga mabweni ya kidato cha tano na sita; maeneo kama hayo yanapojitokeza wapewe kipaumbele katika kupata nafasi zaidi katika shule hizo? Japo na nafasi nyingine itolewe kwa wananchi katika Mikoa mingine? (Makofi)
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS TAMISEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli na tunashukuru kwanza wananchi kwa dhati kabisa. Katika maeneo mbalimbali na hata katika pitapita yangu karibuni wananchi wengi sana wameamua ku-invest sana katika suala zima la kuhakikisha kwamba wanaboresha shule zao. Na hili limetusaidia sana kwa sababu shule nyingi katika kipindi hiki cha kati tumeweza kupata shule za kidato cha tano na kidato cha sita lakini nguvu kubwa katika upande wa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na hili naomba nikiri wazi kwamba sisi kama Serikali tutapenda kuweka kipaumbele cha kutosha kabisa jinsi gani tutafanya kuweka nguvu zaidi katika maeneo hayo; lengo kubwa ni kwamba Watanzania hawa na vijana wetu wanaofaulu kidato cha nne waweze kupata fursa. Kwa sababu mwaka huu ukiangalia kuna maeneo mbalimbali tulipata wanafunzi walifaulu zaidi hata ukilinganisha na idadi ya shule tuziokuwa nazo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbowe swali lako ni jambo la msingi na Serikali hii tutaipa jicho la karibu zaidi; lengo kubwa ni kwamba vijana wa Tanzania waweze kupata fursa ya elimu katika nchi yao.
MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa mujibu wa takwimu ambazo Mheshimiwa Naibu Waziri ametupatia, Deni la Taifa sasa mpaka Juni mwaka huu limefikia shilingi trilioni 51 na bilioni 40. Kiwango hiki cha fedha ni almost mara mbili ya bajeti ya Taifa. Wakati huo huo ukigawanya deni hili kwa Watanzania milioni 45 kila Mtanzania leo atakuwa anadaiwa shilingi 1,134,222.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kukopa ni muhimu katika wakati mwingine ili kuweza kusukuma mbele shughuli za kimaendeleo, lakini ulazima wa kukopa kwa kiwango ambacho tunaweza kukilipa kwa wakati ili Taifa liondokane na mzigo wa riba pamoja na kulimbikiza madeni liweze kujielekeza mapato yake zaidi katika kushughulikia mipango ya maendeleo, ni vyema tuwe na kiwango cha ku-control ukopaji wa Serikali.
Sasa swali langu la mwisho ni hili, tutakumbuka wakati wa Awamu ya Tatu, wakati wa Mheshimiwa Mkapa, Tanzania ilikuwa mojawapo ya nchi zilizokuwa zimepata sifa ya kuwa miongoni mwa nchi zilizosamehewa madeni kupitia mpango wa HIPC (Heavily Indebted Poor Countries) ambapo Deni la Taifa liliweza kusamehewa na likashuka chini ya dola bilioni 10 na almost tulikuwa tunamaliza Deni la Taifa.
Je, ni kwa nini Serikali sasa hivi, kwa sababu bado mpango wa HIPC upo chini ya World Bank na IMF, ni kwa sababu gani Serikali isione uwezekano tena wa kufanya initiative ya kurudishwa katika Mpango HIPC ambao unasimamiwa na World Bank na IMF ili tupunguze mzigo huu wa madeni na hizo pesa tuzielekeze zaidi kwenye shughuli za kimaendeleo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haijaondoka kwenye mpango huo wa kusamehewa madeni na bado tunaendelea na mchakato huu kwa kushirikiana na IMF pamoja na World Bank. Zipo nchi ambazo zilikuwa katika mpango wa kuhakikisha tunasamehewa madeni kama nchi yetu lakini zilisitisha kutokana na migogoro ambayo ipo ndani ya nchi hizo, moja ya nchi hizo ilikuwa ni Iraq, Iran pamoja na nchi nyingine zenye migogoro ambazo zilisitisha sasa kusamehewa madeni. Hivyo bado tunaendelea na mchakato huo kuendelea kuwashawishi wadau hao wa maendeleo ili waweze kutusamehe madeni haya.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa ya kitaalam, lakini nilitaka kuongezea nyongeza tu na kuwatoa hofu Watanzania kwenye kile alichosema Mheshimiwa Mbowe kwamba ukiligawa deni hilo kwa kila Mtanzania.
Kwanza hakuna siku Watanzania watagongewa mlango wakigawanywa Deni hilo la Taifa na wala katika Taifa lolote hakuna utaratibu wa kupima deni kwa kuangalia mgawanyo wa ujazo wa watu bali Deni la Taifa linapimwa kufuatana na uwezo wa nchi kimapato inavyokusanya na inavyoweza ku-service deni hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo tunapoangalia kukua kwa deni tutakiwa pia tuangalie miundombinu ya nchi yetu imekuwa kwa kiwango gani kwa sababu wazo hilo linafuatana na uamuzi wa nchi inayochukua kwenye miundombinu, hata hivi sasa Waheshimiwa Wabunge tunavyoongelea standard gauge ya reli, tunavyoongelea miradi mikubwa mikubwa kama ya bandari tutakuwa tunaongelea uwezo wa nchi yetu kuweza kuendesha miradi, lakini ujenzi wake utategemea njia hizo hizo za kuweza kukopa. Ndiyo maana hata mataifa makubwa ambayo yameendelea leo hii yana madeni makubwa lakini yana uwezo wa kulipa madeni hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimoja tu ambacho natakiwa nimhakikishie Mheshimiwa Mbowe ambacho Serikali inakifanya, haikopi kwa ajili ya matumizi ya kawaida. Serikali inapokopa kwa mara zote inakopa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambayo itazalisha kulipa deni hilo. (Makofi)
MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa imekuwa ni tabia ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi kutoa ahadi ambazo zinaonekana tamu kwa wananchi wakati wa uchaguzi. Tukikumbuka kwamba katika Awamu ya Nne ulianzishwa mpango wa mabilioni ya Jakaya Kikwete ambao ulikufa bila kueleza Bunge au Watanzania kuwa umekufaje; na kwa sababu sasa hivi ni mwaka mmoja umepita tangu tumemaliza uchaguzi na Baraza la Mawaziri linajua kwamba hadi robo ya kwanza ya mwaka wa fedha ya mwaka 2016/2017 inakwisha kuna Wizara kadhaa hazijapata fedha za maendeleo.
Sasa namuuliza Waziri ni miujiza gani itakayotumiwa na Serikali hii ambayo leo imefilisika ambayo leo imeshindwa kutoa mikopo ya wanafunzi wa chuo kikuu kwa maelfu kwamba inaweza…
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nauliza ni miujiza gani Serikali iliyofilisika itakayotumia kutafuta fedha hizi shilingi bilioni 960 badala ya kuwadanganya wananchi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kwanza kwamba Serikali hii haifanyi kazi kwa miujiza, Serikali hii inafanya kazi kwa mpangilio wa bajeti tuliojiwekea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na uthibitisho wa kwamba jambo hili litatekelezeka ni kama tulivyoweza kuwashangaza Watanzania kwa kutoa elimu bure kwa mabilioni ya fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulivyoweza kuwashangaza Watanzania kwa kutekeleza miradi mingine mikubwa na hata ununuaji wa ndege, tulivyoweza kuwashangaza Watanzania kwa utekelezeji wa Ilani yetu kwa mambo mengine mbalimbali ninaomba niwathibitishie Watanzania fedha hizi zitatolewa na Watanzania watazipata na Serikali hii haitafanya kazi kwa miujiza itafanya kazi kwa mpango wa utekelezaji wa bajeti ya wananchi tuliojiwekea. Na fedha hizo zitafika pia hata katika majimbo ya wapinzani katika nchi ya Tanzania.
MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Mambo ya Ndani inakabiliwa na upungufu mkubwa wa magari na ninamshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kukiri kwamba wanapungukiwa sana magari, vitendea kazi pamoja na ofisi. Vilevile wana upungufu mkubwa wa rasilimali watu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa swali langu, siku za karibuni, kwenye upande wa Jeshi la Polisi ndani ya Wizara ya Mambo ya Ndani pamejitiokeza utaratibu ambapo Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wanalitumia Jeshi la Polisi kuwalinda wao binafsi wakati kuna matatizo makubwa ya kiulinzi katika Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa swali langu ni hili, nikitoa mifano halisi, katika Mkoa wa Arusha, Mkuu wa Mkoa wa Arusha analindwa na section nzima ya Jeshi la Polisi, ana motorcade, ana ving‟ora asubuhi mpaka usiku. Sasa magari kama mawili au matatu yanamhudumia Mkuu wa Mkoa na section nzima ya Jeshi la Polisi ambayo ina askari tisa na ving‟ora na hata Wakuu wa Wilaya wamejipa utamaduni huo sasa.
Je, ni nini itifaki ya Kitaifa kuhusu ulinzi wa Viongozi kama hata hawa Mawaziri wenyewe hawalindwi na Askari, lakini Wakuu wa Mikoa leo wanajilundikia Askari badala ya Askari kwenda kwenye lindo, ma-OCD wote siku hizi hawafanyi kazi ya ulinzi wanafanya kazi ya kulindana na kufuatana na Wakuu wa Wilaya. Tunaomba Wizara watueleze leo, ni nini sera ya Serikali kuhusu itifaki hii na matumizi mabaya ya Jeshi la Polisi?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kwenye utendaji wa kazi kwenye ngazi za Mikoa na Wilaya, Mkuu wa Mkoa ni Mwenyekiti wa Ulinzi na Usalama wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya ni Mwenyekiti wa Ulinzi na Usalama wa Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, panapokuwepo na jukumu hasa ambalo linapohusisha shughuli za kiulinzi na nje ya ofisi, ni sahihi Mkuu wa Mkoa ama Mkuu wa Wilaya kuambatana na timu yake kwenda katika eneo husika. Inapotokea Mkuu wa Mkoa anakwenda ofisini kwake ama Mkuu wa Wilaya anakwenda ofisini kwake, maana yake OCD ama RPC ama wengine na wenyewe watakuwa kwenye ofisi zao. (Makofi)
Kwa hiyo, mimi kwa mazingira ambayo nimekuwa nikipewa ni pale ambapo hawa viongozi wanakwenda katika eneo la tukio ambalo linahusisha ulinzi na usalama. Huo ndiyo muogozo kwamba kama wanaelekea katika eneo ambalo linahusisha ulinzi na usalama ni sahihi viongozi hawa kwenda na timu zao kwa sababu ni mambo ya kiusalama na sehemu ya kutolea maelekezo, lakini siyo wakati wa kwenda ofisini on daily routine, unless kama wanafanya hivyo itakuwa maeneo ambayo kila mmoja anaenda kwenye ofisi na ofisi hizo ziko katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo, kwa maelekezo haya, ni kwamba viongozi hawa wanapokwenda kwenye majukumu ambayo yanahitaji maelekezo na ni ya kiulinzi na usalama na wao ndio Wenyeviti wa Ulinzi na Usalama itifaki inataka hawa watu wawe na hao viongozi kwa ajili ya maelekezo ya site, lakini wanapoenda kazini na hawa viongozi wengine nao wanaendelea na majukumu yao.
MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya swali la nyongeza.
Kwa kuwa matatizo ya vyama vya msingi vya ushirika katika Wilaya ya Siha, yanafanana sana na matatizo ya Vyama vya Msingi vya Ushirika katika Wilaya ya Hai; na kwa sababu Vyama vya Msingi vya Ushirika katika Mkoa wa Kilimanjaro vimehodhi maeneo makubwa sana ya ardhi, ambayo kimsingi kwa Mkoa wa Kilimanjaro ndiyo backbone ya economy ya Mkoa ule kwenye upande wa kilimo; na kwa kuwa kumekuwa na shutuma nyingi za muda mrefu ambazo pengine zimelindwa kwa kiwango kikubwa na sheria yenyewe ya ushirika, ambayo inatoa limited power kwa mtu mwingine yeyote kuingilia vitendo na kazi za ushirika:-
Je, Serikali haioni sasa kwa sababu ya matatizo haya ya muda mrefu yaliyokithiri, ni wakati muafaka wa ku-review Sheria ya Ushirika; na kabla ya kui-review Sheria ya Ushirika, kuangalia kwa kina matatizo ya Vyama vya Msingi vya Ushirika katika Mkoa wa Kilimanjaro ili kuweza sasa kuweka mapendekezo sahihi ya kurekebisha sheria ile?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza kuhusiana na kufanya mapitio katika Sheria ya Ushirika, Wizara ya Kilimo bahati nzuri wapo. Niseme tu kama Serikali tumekuwa tukifanya hivyo kwa sheria mbalimbali siyo hii tu ya ushirika; na naamini Wizara husika itaweza kulichukua na nina uhakika watakuwa wameshaanza mapitio kwa sababu ni suala endelevu kila mara kungalia sheria inakidhi mahitaji ya wakati husika.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na Serikali kuviangalia Vyama hivi vya Ushirika kama vina matatizo, napenda tu kusema kwamba katika Mkoa wa Kilimanjaro hata hivi sasa tunavyoongea tayari Vyama vya Ushirika vinne vimefanyiwa uchunguzi na tayari vyama vitatu uchunguzi umeshakamilika, kimebakia kimoja. Naamini matokeo ya uchunguzi hayo yataweza kutangazwa huko baadaye ili kuona ni hatua gani iweze kuchukuliwa.
Mheshimiwa Spika, vile vile tumeshafanya uchunguzi katika Chama Kikuu cha Ushirika cha KNCU na tumefanya uchunguzi katika Chama cha Tanganyika Coffee Curing CompanyLimited na siyo kwa Vyama hivi vya Ushirika peke yake. Tumefanya pia uchunguzi katika SACCOS nne na tayari mbili zimeshafikishwa Mahakamani na mbili zinaendelea na uchunguzi.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbowe, kwa kutambua umuhimu wa Vyama hivi vya Ushirika kwa wakulima, tutakapoona kuna harufu au chochote kinachoashiria vitendo vya rushwa au vitendo vingine vya ubadhirifu wa mali za umma, tutahakikisha kwamba hatua stahiki zinachukuliwa.
MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu tatizo la Mji wa Kahama kama sahihi kabisa alivyozungumza Mheshimiwa Naibu Waziri linafanana kwa njia moja au nyingine na ahadi za Rais alizotoa wakati wa kampeni, ni kweli Rais wakati wa kampeni alitoa ahadi ya kujengea Halmashauri ya Wilaya ya Hai kilometa tano za lami katika Mji wa Hai katika kipindi chake cha uongozi. Na ni kweli kwamba hivi majuzi Rais alivyokuwa katika ziara kwenye Mkoa wetu wa Kilimanjaro aliulizwa kuhusu ahadi yake na Rais akauliza vilevile Halmashauri imegawiwa fedha kiasi gani katika mwaka huu wa fedha kwa ajili ya Mfuko wa Barabara. Taarifa ambazo Rais alipewa ni fedha ambayo ilikuwa imepangwa kwenye bajeti ambayo ni shilingi bilioni 1.3 lakini hiyo fedha haijapokelewa kwa sababu haijatolewa na Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, natambua kwamba Rais aliagiza kwamba TAMISEMI wakafanye uchunguzi, nakaribisha sana TAMISEMI mkafanye uchunguzi, lakini ukweli ni kwamba fedha pekee ambayo ilishapokelewa ni kama shilingi bilioni 300 ambayo ni lazima mtambue kwamba Wilaya ya Hai ina zaidi ya kilometa 200 za barabara zinazoteleza za milimani ambazo ni lazima zifanyiwe routine maintanace.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sasa Mheshimiwa Naibu Waziri ni wewe kutoa commitment ya kwenda kufuatilizia alichokizungumza Rais, lakini vilevile kukumbushia ahadi ya Rais ya kilometa tano za Halmashauri ya Wilaya ya Hai katika Mji wa Hai, bado ni muhimu sana kwa sababu Mji unakuwa kwa kasi na una zaidi ya wakazi 50,000 ambao kwa kweli hawana hata robo kilometa ya lami katika Mji wa Hai ukiacha barabara ya kwenda Arusha. Mheshimiwa Waziri naomba commitment yako.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA
NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni na hata baada ya kampeni amekuwa akiahidi kufanya mambo mbalimbali hasa anapoona maeneo fulani yana matatizo. Katika eneo la barabara ametoa ahadi maeneo mbalimbali ikiwemo Kasulu kilometa sita na hapa Mheshimiwa Mbowe anasema kilometa tano na hasa barabara za milimani, lakini ameahidi maeneo mengi, Waheshimiwa Wabunge wana ahadi na wana kumbukumbu hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge, kwamba ahadi za Mheshimiwa Rais zitatekelezwa na kwa sababu bado tunao muda na tutaangalia kama utaratibu mzuri ni wa kuzingatia wakati wa bajeti zetu lakini nafahamu mnafahamu kwamba bajeti zetu huwa zina ukomo, kwa hiyo tutajaribu kuangalia namna ya modality nzuri ya kuweza kutekekeleza hili tukimshirikisha aliyeahidi.
Pia nitoe rai tu kwa wenzangu kwamba wakati tunaposimamia ahadi za Mheshimiwa Rais pia tuwe tunakumbuka kuishi naye vizuri na kumheshimu. Ahsante sana.(Makofi)
MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tatizo linalowakabili wananchi wa Mbozi kwenye suala la Hospitali ya Wilaya kwa kiasi kikubwa linafanana na la Hospitali ya Wilaya ya Hai katika Mkoa wa Kilimanjaro. Hospitali hii ya Wilaya ya Hai ilianza kujengwa zaidi ya miaka 10 iliyopita wakati huo Mji wa Hai ukiwa na wakazi wasiofika 10,000 na Mji wa Hai leo ni mji unaokua kwa kasi kuliko miji yote katika Mkoa wa Kilimanjaro ikiwa katika kipindi cha miaka kumi, Mji wa Hai umefikisha zaidi ya wakazi 50,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali hii imekuwa inajengwa awamu kwa awamu lakini kuna tatizo moja kubwa la msingi ambako wanaume na wanawake wanalala katika wodi moja. Jambo hili nimeli-witness mwenyewe na nimetembelea hospitali hii wiki iliyopita kushuhudia hali hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachomwomba Naibu Waziri katika hatua ya sasa, kutokana na hali ya unyeti wa hospitali hii na ikiwa vilevile ni hospitali ambayo iko katika barabara kuu ya Arusha-Moshi ambayo inahudumia wagonjwa wote wanaopata ajali katika barabara ile, rai yangu kwa Mheshimiwa Waziri ni kutenga muda wake tuweze kutembelea pamoja hospitali hii kwa pamoja tuone uzito wa tatizo lililopo kisha Serikali itutafutie ufumbuzi wa kudumu kuhusu tatizo hili. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba niseme takriban wiki tisa kama sio kumi zilizopita nilikuwa pale Hai. Nilienda kuitembelea hospitali ile na niliweza kubaini mchakato mkubwa unaofanywa na injinia wetu katika lile jengo la akinamama linalojengwa pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli nimefarijika na nimefurahi sana kwa mkakati uliopangwa. Kwa kutumia hizi Force Account kazi kubwa inafanyika pale. Kwa hiyo, jambo la msingi ni kwamba kama Serikali pale kuna kazi kubwa tunaendelea kuifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme nimekubali wazo
hilo la kwenda pamoja lakini tayari nimeshakwenda na tumesha-identify na nimeshatoa maelekezo nini wanatakiwa wafanye. Namshukuru sana DMO wetu pale kwa kazi kubwa inayofanywa na menejimenti ya hospitali ile. Hata hivyo, nimetoa maagizo sasa waangalie rasilimali zilizokuwepo kama majengo yaliyokuwepo pale nini kifanyike, wapange mpango mzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi kubwa tunayokwenda kufanya ni kukamilisha lile jengo kubwa linalojengwa ambalo ni la mfano na mimi nimetolea mfano hata nilivyokwenda Siha kule nikawaambia kwamba igeni kwa wenzenu wa Hai kwa kutumia Force Account, kutumia fedha ndogo na kufanya mabadiliko makubwa katika sekta ya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imeweka nguvu kubwa pale. Hata hivyo, nina mpango wa kwenda Hai na Waziri wangu amepanga hilo kwa sababu Mheshimiwa Rais ameshaelekeza lazima tukahakiki suala zima la matumizi ya fedha na miundombinu ya barabara, kwa hiyo, tutakwenda tuone jinsi gani tutafanya ili hospitali ile iweze kuwahudumia vizuri wananchi wetu wa Hai.
MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Majeshi yetu na hususan Jeshi la Wananchi ndicho chombo ambacho tunakiamini sana kwamba kina wajibu wa kulinda mipaka yetu na usalama wa raia na nchi yetu katika ujumla wake.

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni katika mpaka wa Namanga tulishuhudia kupitia vyombo vya habari vurugu kubwa zilizofanywa upande wa Kenya ambapo magari, abiria na mizigo kutoka Tanzania yakiwemo magari yalizuiliwa na wananchi wa Kenya na kusababisha vurugu kubwa katika mpaka ule. Mheshimiwa Waziri anatupa tamko gani kama Waziri wa Ulinzi kuhusu usalama wa nchi yetu katika mpaka ule na nini kilipelekea tukio lile likafanyika likasababisha vurugu zile?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Freeman Mbowe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Jeshi la Ulinzi lina wajibu wa ulinzi wa mipaka lakini Vyombo hivi vya Ulinzi na Usalama vina majukumu tofauti. Suala la usalama wa raia ni suala la Polisi na kuna vyombo vingine vingi vya ulinzi na usalama ambavyo vina majukumu ya kulinda usalama katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, nachoweza kusema ni kwamba mpaka wetu kati ya Tanzania na Kenya kwa upande huo hauna tatizo lolote. Ulinzi upo pale wa kutosha na hizi vurugu zilizotokea nadhani lilikuwa ni jukumu la vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuhakikisha kwamba wanalishughulikia. Taarifa nilizonazo ni kwamba suala hili limeshughulikiwa na lilimalizwa. Kwa maana hiyo hatutarajii matukio kama haya yaendelee kutokea.
MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana tukaona mambo haya ya uchaguzi ni mepesi lakini amani ya Taifa hili itapotea ama itaathirika kama tukipuuza masuala ya uchaguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, subsidiary legislation zozote zinazotungwa katika nchi hii leo, lazima kwa njia moja au nyingine ziwe ratified na Bunge. Sheria ndogondogo tunazozitunga kabla hazijaanza kutumika kimsingi zinastahili kuletwa kuwa ratified na Bunge. Vikao vya wadau vinavyokaa ni maoni wala vikao vya wadau vinavyokaa kujadili subsidiary legislation ama legislation yote haviwezi kuwa mbadala wa Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Sheria Ndogo ya Bunge haijawahi kuona kabisa au kupitia na kuthibitisha ama kuzi-accept ama kutoa maoni kanuni hizi zilizotungwa na TAMISEMI. Ninachouliza Mheshimiwa Waziri atueleze katika utamaduni huo ambako tayari kanuni zimeshaingizwa kazini, Kamati ya Sheria Ndogo ya Bunge haikuzipitia kwa kisingizo kwamba wadau walizipitia ambao sio Bunge. Je, jambo hili ni sahihi? (Makofi)
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe maelezo kidogo kuhusu suala ambalo ameliibua Mheshimiwa Mbowe, amesema kwamba sheria ndogondogo zinapotungwa lazima kuletwa Bungeni kabla ya kuanza kutumika, hiyo kwa mujibu wa utaratibu siyo sahihi na bahati nzuri Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Sheria Ndogo yupo hapa ataeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria Ndogo huwa zikishatayarishwa zinapelekwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ajili ya uchambuzi yaani vetting na baada ya hapo Mwanasheria Mkuu wa Serikali humrudishia Waziri husika na Waziri yule anazi-gazette halafu baada ya hapo zinapelekwa kwenye kikao kinachofuata cha Bunge kwenye Kamati ya Bunge ya Sheria Ndogo kwa ajili ya kuchambuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongeze kusema mtu anaweza kusema labda mchakato huo hautoi nafasi ya kuweza kuziangalia vizuri zile sheria ndogo, kimsingi sheria ndogo zote zinatungwa chini ya sheria mama na ipo misingi ya kisheria inayoelekeza namna gani sheria ndogo zitungwe na mojawapo ya misingi hiyo ni kwamba isipingane kimsingi na sheria mama. Na inapotokea kuna changamoto moja au mbili ile Kamati ya Bunge kuhusu sheria ndogo kutoa maoni na maelekezo yake na kama kuna changamoto yoyote inarekebishwa, kwa hiyo, hakuna tatizo kabisa katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kwa Mheshimiwa Waziri na kwa sababu swali langu litafanana kidogo na swali la Kasulu linahusu Mji mdogo sio Mji mdogo, Mji wa Hai ambao zamani ukiitwa Bomang’ombe Makao Makuu ya Wilaya ya Hai.

Mheshimiwa Spika, mji huu ni Mji ambao unakuwa na kwa kasi kuliko pengine Miji yote katika Mkoa wa Kilimanjaro ukiwa ni mkoa ni Mji ambao unaunganisha Mikoa ya Kilimanjaro na Arusha na Manyara kwa upande wa Simanjiro. Mji huu sasa hivi unakaribiwa kuwa na takribani na wakazi zaidi ya 100,000 na unahudumia eneo lenye viunga vya karibu watu 200,000 kuanzia Mkoa wa Manyara, Mkoa wa Arusha, Mkoa wa Kilimanjaro na ni get way to the Kilimanjaro international Airport ambapo ni karibu sana na uwanja wa ndege wa Kimataifa na of course ndio njia na lango la kuingilia katika Mlima Kilimanjaro ambao ni chanzo kikubwa sana cha mapato kwa Taifa letu.

Mheshimiwa spika, sasa Mji huu ukiacha barabara Kuu ya Lami inayotoka Arusha kwenda Moshi na inayotoka kwenye ene la Hai kwenda Sanyajuu katika Jimbo la Siha Mji huu hauna barabara hata moja ya lami. Sasa katika kupanga Miji ni pamoja na ujenzi wa barabara za lami ili ujenzi na upangaji miti uwe kamili ni lazima uendane vilevile na mitaro ya maji pamoja na ujenzi wa barabara za lami.

Mheshimiwa Spika, halmashauri zetu sasa hivi hazina uwezo wowote wa kuweza kufanya miradi mikubwa ya kiwango hiki. Na natambua hapo nyuma kidogo kulikuwa kuna program kuna project ya sustainable cities ambalo nafikiri limekuwa funded na World Bank ambayo ilichagua baadhi ya Miji ambayo kwa umuhimu wake wa kiuchumi iliweza kuwekewa miundombinu ya barabara za lami. Na hata Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni za 2015 Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli alitoa ahadi ya kujenga barabara kilomita 5 za lami ambazo kwa bahati mbaya bado tunazisubiri kwa hamu sana.

Mheshimiwa spika, sasa Mheshimiwa Waziri katika utaratibu huo wa kupanga Miji nini kifanyike ili Miji muhimu kama hii ambayo inahudumia watu wengi na ni sura ya Taifa inaweza kufanyika ili ipate lami? Nini kifanyike katika hiyo mipango Miji kuikamilisha kwa kujenga miundombinu ikiwemo barabara za lami? (Makofi)
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa spika, master plan haijengi miundombinu master plan ni dira ya kuonesha mahitaji ya mpango au mahitaji ya huduma ndani ya Wilaya. Master plan wenye Wilaya yenu mtapanga kutaka kujua barabara zipite wapi, maeneo ya mazishi ni wapi, maeneo ya makazi ni wapi, maeneo ya biashara na huduma mbalimbali. Kwa sababu hata mkiwa na fedha ya barabara kama hamna maeneo mliyopanga kujenga barabara hazitafanya kazi na ndio maana mnakuwa na hela halafu mnaamua kufanya vyovyote au mnavunja nyumba za watu hovyo. Kwa hiyo, la kwanza nakushauri Mheshimiwa Mbowe pangeni master plan ili muone uhitaji wa leo mnahitaji kuwa na barabara kiasi gani, za saizi gani, za lami na kila kitu na mahitaji mengine.

Mheshimiwa Spika, then mkishapanga master plan kuainisha maeneo hayo mtakuja kuyapima lakini baadaye sasa ndio mtawaomba sasa huduma mbalimbali na kuziwekea bajeti ili ziwemo kulingana na master plan iliyopo.

Kwa hiyo, nimelichukua ombi lako hilo, lakini nashauri kama nilivyosema kwa Mheshimiwa Mbunge mwenzangu wa Kasulu naomba halmashauri yako mkae kama council katika miradi kingi mnayobuni pale Hai basi mbuni utengenezaji wa master plan kama hamna mtu wa kuwaelekeza pale Moshi kuna Kanda na nimepeleka pale mtalaam mbobezi Afisa Mipango Miji Mkurugenzi Msaidizi wa Kanda mnaweza mkamualika yule bure akaja kuwapa maelekezo na utalaam wa awali wa namna ya kutayarisha master plan ya Hai ili iweze kuwaoneshea huduma zenu zipangwe namna gani katika Wilaya ya Hai.

Mheshimiwa spika, lakini hilo jingine ulilosema nakushauri kwa sababu Wizara ya TAMISEMI iko hapa Dodoma pengine ukipata fursa ungepita pale kwenye Ofisi za TAMISEMI ili angalau hayo majibu mengine ya lini zitajengwa hizo barabara uweze kujibiwa pale ofisini.