Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Freeman Aikaeli Mbowe (2 total)

MHE. FREEMAN A. MBOWE Aliuliza:-
Ongezeko la ukubwa wa Serikali na watumishi wake inatokana na kuongezeka mara kwa mara kwa mitaa, vijiji, kata, tarafa, majimbo ya uchaguzi, wilaya na mikoa na hivyo kuongeza ukubwa wa bajeti ya Serikali kwenye mishahara, matumizi mengine (OC) na kusababisha kupungua kwa ongezeko la bajeti ya maendeleo na hata wakati mwingine upatikanaji wake.
(a) Je, ni Vitongoji, Vijiji, Mitaa, Kata, Tarafa, Majimbo, Wilaya na Mikoa mingapi imeongezeka mwaka hadi mwaka kuanzia mwaka 2000 hadi 2015?
(b) Je, ongezeko hili limesababisha vipi ukuaji wa idadi ya watumishi wa Serikali Kuu na Serikali za Mitaa na mishahara imepanda vipi mwaka hadi mwaka kuanzia mwaka 2000 hadi 2015 na ongezeko hilo ni asilimia ngapi ya bajeti ya Serikali?
(c) Je, Serikali haioni sasa umuhimu mkubwa wa kusitisha ukuaji wake ili kuelekeza fedha zinazogharamia utawala kwenda moja kwa moja kwenye bajeti za maendeleo ya wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe, Mbunge wa Jimbo la Hai, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, uanzishwaji wa maeneo mapya ya utawala ikiwemo Mikoa, Wilaya, Majimbo, Tarafa, Kata, Vijiji, Mitaa na Vitongoji unazingatia matakwa ya Katiba ya mwaka 1977 Ibara ya 2(2) pamoja na Sheria ya Serikali za Mitaa Sura 287 na 288 ambazo zimempa Waziri mwenye dhamana wa Serikali za Mitaa madaraka na kuweka utaratibu wa kugawa maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha kuanzia mwaka 2000 mpaka 2015 Mikoa imeongezeka kutoka 21 hadi 26, Wilaya kutoka 114 mpaka 139, Tarafa kutoka 521 hadi 558, Halmashauri kutoka 133 hadi 185, Kata kutoka 3,833
mpaka 4,420, Vijiji kutoka 10,376 hadi 12,545, Mitaa kutoka 1,975 mpaka 4,037, Vitongoji kutoka 57,137 mpaka 64,677. Aidha Majimbo ya Uchaguzi yameongezeka kutoka 239 hadi 268.
Kati ya mwaka 2000 hadi 2015 idadi ya watumishi wa Serikali imeongezeka kutoka wastani wa watumishi 222,792 hadi wastani wa watumishi 405,314. Ongezeko hilo la watumishi limesababisha bajeti ya mishahara kuongezeka kutoka wastani wa shilingi bilioni 668.6 hadi shilingi trilioni 3.05.
Mheshimiwa Spika, azma ya Serikali ni kuongeza huduma karibu na wananchi, hivyo Serikali itaendelea kuzingatia matakwa ya Katiba na sheria zilizopo katika kugawa eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mikoa na maeneo mengine ya utawala. Hata hivyo kigezo cha uwezo wa nchi kiuchumi kitaendelewa kuzingatiwa katika utekelezaji wa azma hii.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI (K.n.y. MHE. FREEMAN A. MBOWE) aliuliza:-
Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa huwapa wananchi fursa ya kuchagua kiongozi na chama wanachotaka sambamba na Ilani za Vyama husika katika kila ngazi ya uchaguzi kuanzia ya Mtaa/Kijiji, Kata, Jimbo na Taifa:-
(a) Je, ni kwa nini Serikali ya CCM hupuuza ukweli huu na kulazimisha Ilani ya Chama chao kutekelezwa nchi nzima kila ngazi bila kujali matakwa ya wananchi kupitia uchaguzi?
(b) Je, katika mazingira ya Manispaa au Halmashauri za Wilaya palipo na uongozi wa Chama tofauti na CCM ni ipi mipaka ya Wakuu wa Wilaya na Mikoa kutoa amri au maelekezo ya kiutendaji?
(c) Je, Serikali haioni kuwa sasa ni wakati muafaka kuweka utaratibu wa kisheria na kikanuni ili kuondokana na mfumo huu kandamizi ambao ni urithi na ukiritimba wa mfumo wa chama kimoja cha siasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe, Mbunge wa Hai, lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Ibara ya 3(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inabainisha wazi kuwa nchi yetu inafuata mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa. Mfumo huo popote pale duniani hukipa Chama Tawala fursa na haki ya kuelekeza kutokana na ridhaa ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, dhana hii ya vyama vingi inatumika pia katika mazingira ya Manispaa na Halmashauri. Vivyo hivyo, mipaka ya Wakuu wa Mikoa na Wilaya kutoa amri au maelekezo ya kiutendaji katika maeneo yao ya utawala, iko kwa mujibu wa Ibara ya 61(4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na vifungu vya 5 (1)-(3) na 14(1)-(3) vya Sheria ya Utawala wa Mikoa, Sura ya 97. Hivyo, Serikali inaamini kuwa utaratibu huu umezingatia demokrasia na kwa sasa hakuna umuhimu wa kuweka mfumo mwingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali haioni ukiritimba wowote katika mfumo uliopo, hivyo sheria na mifumo iliyopo itaendelea kufanya kazi.