Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. Godwin Oloyce Mollel (11 total)

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ieleweke kuwa wananchi wa Siha siyo kwamba wanachukia polisi kuwepo katika eneo hilo lakini kilichoonekana ni kwamba watu wameongezeka sana katika eneo hili na ushahidi upo kwamba wameshakufa watoto wanne na tarehe 18/08/2016 kuna mtoto ambaye risasi ilimfuata nyumbani na mpaka sasa ana ulemavu. Maswali yangu mawili ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Serikali isione ni busara sasa na ni wakati muafaka ikafuata ushauri wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Siha ya kwamba mazoezi ya polisi yapelekwe katika eneo la heka 500 ndani ya NARCO lakini hilo eneo likagawanywa katika sehemu tatu? Sehemu ya kwanza ni kutoa eneo ambalo litasaidia kupunguza ukata wa ardhi kwa wananchi wa Siha hasa walioko upande wa milimani, sehemu ya pili ikatolewa kwa ajili ya kufanya utalii wa kimila. Kama mnavyokumbuka mwaka huu Waziri wa Utamadumi alikuja pale na alifanya tukio kubwa ambalo linafanyika East Africa yote kwa ajili ya utalii. Kwa hiyo, Wizara ya Utamaduni na Idara ya Mambo ya Kale ikakabidhiwa chini ya Halmashauri eneo lingine kwa ajili ya kufanya utalii wa kimila. Eneo linalobaki tukajenga Chuo Kikuu cha Polisi badala ya kufanyia mazoezi yanayowaathiri wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ni kwamba…
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Huwa sichanganyikiwi mkiongea sana. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, wananchi walioumia na huyu mtoto aliyepata ulemavu Serikali iko tayari kutoa fidia lakini vilevile Waziri kutembelea kuwaona waathirika?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo alilopendekeza ametaja kwamba ni eneo la NARCO na NARCO iko chini ya Wizara nyingine na Wizara husika wana mpango wa matumizi wa eneo hilo. Ninachotambua ni kwamba ni kweli Wilaya ya Siha pamoja na Mkoa mzima wa Kilimanjaro una matatizo makubwa ya ardhi. Mkoa pamoja na Wilaya kwa kushirikisha Wizara ya Ardhi mara kwa mara wamekuwa wakiangalia mpango bora wa matumizi ya ardhi na sisi kama Wizara ya Mambo ya Ndani ni sehemu ya Serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata eneo. Hata hivyo, kwa sasa yale niliyoyasema kwenye jibu la msingi yanasimama kwa maana tunatarajia kupima eneo lile ambalo linatumika kwa ajili ya mafunzo, kuweka alama na wananchi hawa waweze kutafutiwa maeneo mbadala ambapo mazungumzo yameendelea katika maeneo tofauti na Waziri wa Ardhi alishafika kule kuweza kuangalia njia bora ya kuwapatia vijana maeneo ya ardhi kwa ajili ya matumizi mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hili ambalo amelisemea la kijana aliyeumia, kwa niaba ya Wizara na Serikali nitoe pole na tumepokea hayo ambayo ameyasema kama mapendekezo. Tutaongea na wataalam tuone ni kitu gani wamekuwa wakifanya punde yanapotokea mambo ya aina hiyo.
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kushukuru Wizara ya Kilimo, vilevile kumshukuru Rais. Nimemweleza hili, nimeona cheche kidogo. Niseme, kwa kuwa tumeshamkamata aliyekuwa Mkurugenzi wa Siha na amewekwa ndani kwa muda kwa ajilii ya tuhuma kama hizi za ufisadi, lakini sh. 1,600,000/= ambazo zimeshushwa siyo za kweli. Amesharudisha ambaye sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Mara, Charles Mlingwa na risiti tunazo. Tulimtafuta tukamkamate, lakini tukakuta amezungukwa na Jeshi la Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile kwa kuwa Mkuu Mkoa wa Kilimanjaro Meck Sadiq amemtishia Meneja wa TAKUKURU wa Mkoa wa Kilimanjaro, kwamba hizi tuhuma anazozichunguza ni za uongo, swali langu la kwanza ni kwamba. Je, Serikali inatoa commitment gani kuhakikisha watuhumiwa wote wa ufisadi ndani ya ushirika na KNCU Mkoa wa Kilimanjaro, wamefikishwa mbele ya sheria; na kutuhakikishia watamlindaje Mkuu wa TAKUKURU anayezuiliwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro kufanya kazi zake? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; je, Serikali inatupa commitment gani kwamba Charles Mlingwa ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Mara, vilevile Meck Sadiq ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, bado wanastahili kupeperusha bendera ya Tanzania na vilevile kupigiwa saluti na majeshi yetu ya Tanzania kama Wakuu wa Mikoa na kumwakilisha Rais baada ya vitendo hivi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Spika, kwanza kuhusiana na swali lake la kwanza, kwamba Serikali inatoa commitment gani kuhakikisha kwamba watuhumiwa wanafikishwa Mahakamani au wanafunguliwa mashtaka? Nimhakikishie kwamba tunaendelea na chunguzi mbalimbali na pindi chunguzi hizo zitakapokamilika na itakapothibitika pasipo shaka kwamba wanayo hatia au wana hoja ya kujibu Mahakamani, basi kwa hakika watuhumiwa watafikishwa Mahakamani.
Mheshimiwa Spika, kwa swali la pili kwamba Afisa wa TAKUKURU wa Mkoa anaingiliwa ama anazuiwa kufanya kazi zake na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, niseme kwamba siyo kweli. Ukiangalia kama nilivyoeleza katika jibu la msingi, TAKUKURU kama chombo, kinao uhuru wa kufanya kazi zake bila kuingiliwa na imekuwa ikifanya hivyo. Hata katika jibu la msingi nilieleza, tayari kulikuwa kuna mkutano wa wanaushirika, tena Mheshimiwa Meck Sadiq huyo huyo aliitisha na waliweza kusomewa taarifa ya TAKUKURU pale na aliweza kuridhika na ndiyo maana mpaka leo kunakuwa na utulivu na uhimilivu katika eneo hilo.
Mheshimiwa Spika, endapo ataona ana malalamiko dhidi ya Wakuu wa Mikoa hao, basi asisite kuwasilisha malalamiko stahiki na aweze kuchukuliwa hatua.
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Hospitali ya Wilaya ya Siha inafanana sana na Wilaya ambayo imetangulia kuulizwa hapa, na Mheshimiwa Waziri aliitembelea Hospitali yetu ya Wilaya ya Siha na ameona kwamba tuna wagonjwa wa nje tu, hatulazi lakini juhudi zinaendelea na hata wiki hii wananchi wamejitolea kuchimba msingi kwa ajili ya kuendeleza hospitali yetu na changamoto kubwa tuliyonayo ni watumishi, hospitali yetu haina watumishi na hata tukifikia mahali pa kulaza na kuweza kufanya operation na huduma nyingine
hatutakuwa na watumishi na madaktari.
Je, anatuambia nini kwa sababu ndani ya mwaka
huu tutaanza kulaza na kufanya operation, je, ni mkakati gani wa dharura utafanyika ili hospitali hiyo iweze kupata watumishi wa kutosha na kazi ianze?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli nilifika pale Siha na nilivyofika pale licha ya hilo suala la watumishi
lakini nilitoa maagizo. Serikali tumepeleka fedha pale kwa ajili ya kuhakikisha tunamaliza miundombinu katika ile floor ya juu, lakini nilitoa maagizo kwa sababu matumizi ya fedha zile, vikao vilivyokaa kwamba inaonkana fedha zile zilikuwa zinakwenda kutumika isivyo halali. Imani yangu ni kwamba katika eneo la Siha, utawala wa Siha utakuwa umefanya utaratibu mzuri jinsi gani tunaenda kupata value for money jengo lile linakamilika wananchi waweze kupata huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala zima la
watumishi sasa, Serikali inasema sio Siha peke yake, isipokuwa katika maeneo yote tuna changamoto sana ya watumishi na hasa katika suala zima la uhakiki tulivyopeleka hivi sasa
kuna watu wengine walikimbia vituo. Kwa hiyo, imani yangu ni kwamba kwa sababu tuna mchakato hivi sasa wa suala zima la ajira nadhani Wizara ya Utumishi itakapokuwa tayari basi kibali kitatoka kuhakikisha kwamba tunapata waajiriwa mbalimbali katika sekta mbalimbali hasa ikiwa sekta ya afya na watakuja kule Siha kuwahudumia wananchi wa Siha.
MHE. DKT. GODWIN A. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, hili suala la dawa linaonesha ni tatizo sugu na swali langu ni kwamba ukilinganisha vituo vya afya vya binafsi na hata maduka ya binafsi na MSD, dawa ambazo hazipatikani Serikalini mara nyingi zinapatikana kwenye vituo binafsi.
Mheshimiwa Spika, je, Mheshimiwa Naibu Waziri anaweza kutuambia ni kwa nini vituo binafsi vinakuwa na dawa zote wakati Serikali inashindwa kuwa nazo na imekuwa ni tatizo sugu, tufanye nini kama nchi?
Mheshimiwa Spika, hapa amezungumzia suala la morphine pamoja na ku-control, lakini ni dawa ambayo kwa kweli inahitajika kwenye vituo vya Serikali kwa sababu watu maskini wanateseka sana. Pamoja na control hizo zote ambazo tunazisema lakini kwa kuzingatia hizo control ni muhimu hizo dawa ziwepo kwenye vituo vyetu. Unatuambia nini kwa sababu kwa kweli hili ni suala sungu na ni aibu kwa Seriali kwa sababu kwanza tunanunua kutoka kwa mtengenezaji, kwa nini hatuna dawa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, ahsante naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mollel...
Mheshimiwa Spika, basi nachangua kujibu lile la kwanza, kwamba kwa nini kwenye baadhi ya vituo vya Serikali hakuna baadhi ya dawa wakati kwenye private zipo.
Mheshimiwa Spika, ukweli ni kama nilivyoeleza kwenye majibu yangu ya msingi lakini pia kwenye maelezo ambayo nimeyatoa kwenye maswali mbalimbali ya nyongeza ambayo yamekuwa yakiulizwa hapa Bungeni ni kwamba huko tunakotoka hali ya upatikanaji wa dawa ilikuwa chini sana na sababu zilikuwa nyingi.
Mheshimiwa Spika, sababu mojawapo ilikuwa ni hiyo ya maoteo kujua mahitaji ya Halmashauri zote nchini kabla mwaka haujaanza na hii ni kwa mujibu wa sheria kwamba inatakiwa kila Halmashauri kufikia Januari ya kila mwaka wawe wameleta maoteo yao ya mahitaji ya dawa MSD na MSD ijipange kununua kadri ambavyo itaweza na kadri ambavyo inajua kwamba mahitaji ya dawa yametathminiwa na Halmashauri husika. Sasa mwaka jana tulikuja kugundua Halmashauri nyingi hazikuwa zikileta maoteo kwa hivyo unakuta Halmashauri wana pesa, halafu MSD ana bajeti ndogo kiasi kwamba hawezi ku-meet mahitaji ya Halmashauri ambao wana pesa zao tayari. Ndiyo maana tukaanzisha hii saa 24 kutoa kibali cha kwenda kununua kwenye private sector.
Mheshimiwa Spika, sababu nyingine ni kwamba dawa nyingi hazipatikani hapa nchini kwenye viwanda na sisi tuna maelekezo ya Mheshimiwa Rais ya kununua dawa moja kwa moja kutoka viwandani na sasa ili tuweze ku-meet hayo maelekezo tulikuwa tunapaswa kufanya mambo yafuatayo; tutanue mtaji wa MSD na ndicho ambacho tumekifanya. Mheshimiwa Rais ametuongezea bajeti ya dawa kutoka shilingi bilioni 31 mwaka juzi mpaka shilingi bilioni 251.5 mwaka jana na mpaka shilingi bilioni 299 mwaka huu. Tatizo la fedha sasa limeanza kupungua kwa hivyo sasa tuna uwezo wa ku- order dawa kadri ambavyo tunaona mahitaj ya nchi yatakuwa katika mwaka husika na kupanga schedule ya supply kila baada ya miezi mitatu itakuwaje.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, baada ya kufanikisha hilo, ndiyo maana nimesema pale awali, mahitaji ya dawa sasa tuna uwezo wa kuya-meet katika nchi kwa wastani wa asilimia 80 na kuna baadhi ya Halmashauri ambazo zina viongozi wazuri ma-DMO wazuri, Wakurugenzi wazuri wanaweza kufika mpaka asilimia 90. (Makofi)
Kwa hiyo, tukisema kuna baadhi ya dawa hazipo Serikalini na kuna baadhi ya dawa zipo kwenye private sector ni kweli, lakini angalau sisi tumehakikisha kwenye ile list ya essential medicines, dawa 138 za muhimu zaidi tunazo na kuna zile tracer medicine 30 tunazo wakati wote. Kwa hiyo, kuongelea kwamba dawa fulani ipo huku private na huku Serikalini haipo linaweza likawa ni suala kidogo relative lakini objectivity yake ni kwamba angalau tuna uhakika makundi yote ya dawa yanapatikana, anti-biotics zipo, anti inflammatories zipo dawa zote essentials zinapatikana kwenye vituo vya kutolea huduma vya Serikali.
Sasa hivi mimi nazunguka sana pengine kuliko Mheshimiwa Mbunge, sijapata malalamiko ya dawa tena takribani mwaka mzima umepita. Nakushukuru.
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, ahsante, hapa tunachokisema ni katika nchi ambayo kuna upungufu mkubwa wa dawa, lakini vilevile unaona kuna dawa ambazo zinaharibika na tunatumia mabilioni ya fedha kuteketeza hizo dawa. Mheshimiwa Waziri wa Afya hawezi akafikiri kwamba kuna umuhimu wa kutizama kwamba inawezekana kuna ufisadi kati ya MSD na viwanda vikubwa vya dawa kugeuza nchi yetu kama dumping space ya dawa, atuletee kuja kututhibitishia hapa Bungeni kwamba hakuna ufisadi kati ya wanaonunua dawa katika nchi hii na viwanda vikubwa? Nikwambie Waziri sikurupuki, hebu tufanye hiyo kazi uone kama hujakuta kuna shida hapo. (Makofi)
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, kwanza nataka kumsahihisha Waziri Kivuli jambo moja, hakuna upungufu mkubwa wa dawa Tanzania na kati ya jambo kubwa ambalo Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli amelifanya ikiwemo katika Jimbo lako ni kuongeza bajeti ya dawa.
Mheshimiwa Spika, na dawa muhimu zaidi na Mheshimiwa Dkt. Mollel unajua, tunaposema upatikanaji wa dawa tunapima dawa 135 na katika Halmashauri yako ya Siha zipo. Nataka kuonesha mfano kwa sababu swali hili lilikuwa ni la Njombe, Njombe walikuwa na bajeti ya dawa shilingi milioni 43 kwa sababu ya jitihada za Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, bajeti ya dawa ya Njombe ni zaidi ya shilingi milioni 150 kutoka shilingi milioni 43. Kwa hiyo, tusikariri taarifa zilizopitwa na wakati. Kama mnataka kumtendea haki Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, mtendeeni haki kwa kumpima ni kiasi gani amewekeza katika upatikanaji wa dawa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la pili; Mheshimiwa Dkt. Mollel wewe ni mtaalam, kuna international standard za dawa kuchina, dawa ambazo zinaruhusiwa ku-expire. Kama umenunua dawa za milioni 100 zisifike asilimia tano ya kiasi cha milioni 100. Tanzania dawa zinazochina ni asilimia 1.8, tupo chini ya kiwango cha kimataifa cha asilimia tano. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa nini dawa zinachina Tanzania? Tunazo changamoto na namshukuru sana Mheshimiwa Jafo, kuna tatizo kubwa la maoteo. Watu hawaleti mahitaji halisi ya dawa lakini Mheshimiwa Jafo amechukua hatua na sasa hivi TAMISEMI wanajipanga kuleta maoteo halisi ya dawa.
Mheshimiwa Spika, hatua kubwa ambayo tumechukua, kwa nini dawa zinachina ni dawa za misaada. Unakuta sisi tumenunua dawa kwa ajili ya kutibu malaria unaletewa tena dawa za misaada. Tumechukua mwongozo, sasa hivi hatupokei dawa ya msaada ambayo either imekaribia kuharibika muda au dawa hiyo tayari tunayo katika bohari ya dawa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niliona nimpe shule Mheshimiwa Dkt. Mollel kwa sababu yeye ni mtaalam. (Makofi/Vigelegele)
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Wilaya ya Siha kwenye Kata Ngarenairobi na Ndumeti wananchi hawana maeneo ya kulima pamoja na makazi, wamekaa kwenye mabonde wakati wamezungukwa na heka zaidi ya elfu hamsini na sita za Serikali lakini kukiwepo na mashamba makubwa sana ya ushirika ndani ya Wilaya ya Siha ambayo hayatumiki kama inavyotakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumwomba Waziri kama atakuwa tayari kufuatana na mimi baada ya Bunge hili tukatizame mazingira ya Wilaya ya Siha na huko Ndumeti pamoja Ngarenairobi na maeneo mengine tuweze kuamua namna ya kupanga hiyo ardhi kubwa sana iliyoko Siha kwa matumizi ya wananchi kwa ajili ya kilimo, makazi lakini vilevile kutenga maeneo ya viwanda na uwekezaji mwingine kwa ajli ya Serikali na sera iliyopo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa la Siha na maeneo kama hayo ni uwekezaji mkubwa ambao unafanywa na wananchi wachache. Kwa hiyo, tungependa tupate kwanza mpango wa Halmashauri yake halafu ndiyo tuweze kuufanyia kazi. Ahsante sana.
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niuliza kwamba Wilaya ya Siha inafanana sana na Nyamagana tuna hospitali mpya ya Wilaya ambayo Waziri wa TAMISEMI Mheshimiwa Jafo alikuja akashirikiana na sisi kufanya kazi nzuri ya kuhakikisha hospitali hiyo inaweza
kulaza na kufanya upasuaji. Lakini sasa tuna changamoto, pamoja na vifaa lakini tuna upungufu wa asilimia 74 ya watumishi. Je, Waziri atakuwa tayari tukae na yeye kujadili kwa namna ya dharura namna ya kusaidia hospitali hiyo? (Makofi
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mollel kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli nilifika Siha na ni kweli hata takriban wiki moja na nusu nilikuwa naongea na Mkuu wa Wilaya yako ya Siha na bahati nzuri katika kazi kubwa tunayoenda kuifanya katika umaliziaji wa hospitali tatu za awali ikiwepo Mvomero na Hospitali ya Siha na maeneo mengine tunaenda kufanya hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, jambo hilo hata bila kukaa tumeshalimaliza tayari kwa ajili ya maslahi mapana ya wananchi wa Tanzania. (Makofi)
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Hata hivyo, nitumie fursa hii kuwashukuru wananchi wa Siha kwa kuniamini tena na kuhakikisha hawa wanaosema muda nawapiga kipigo ambacho hawajawahi kukisikia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna barabara yetu ya kutokea Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kwenda kwenye Kata ya Biriri kukutana na barabara inayotokea Sanya Juu kuelekea mpaka KIA (Kilimanjaro International Airport), kwa mwaka jana ni katika barabara mbili ambazo zilikuwa zipandishwe hadhi kuingizwa TANROAD ikashindikana ikawa imepanda barabara moja ya Mwanga. Nataka kumuuliza Waziri mwaka huu basi isidunde kama zawadi ya watu wa Siha kwa uamuzi wa busara walioufanya. Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI) - MHE. JOSEPH S. KANDEGE:
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpongeze na kumkaribisha sana Dkt. Mollel na kumhakikishia kwamba yuko katika nafasi ambayo ni salama sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la kupandisha hadhi barabara ambayo anaiongelea ili iwe chini ya TANROAD.
Mheshimiwa Naibu Spika, wewe ni shuhuda kwamba Waheshimiwa Wabunge wengi tulikuwa tunapenda barabara za Majimboni kwetu zipandishwe zichukuliwe na TANROADS, lakini ni kwa nini tulikuwa tunataka zichukuliwe na TANROADS? Ni kutokana na namna ambavyo barabara ambazo ziko chini ya TANROADS zimekuwa zikihudumiwa kwa namna nzuri. Ndiyo maana kama Bunge tukaona kwamba ni vizuri tukaanzisha chombo ambacho kitakuwa kinafanya kazi madhubuti kama ambavyo zimekuwa zikifanywa na TANROADS.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie, kwa kasi ambayo tumeanza nayo na jinsi ambavyo TARURA imeanza kufanya kazi, nimtoe mashaka, barabara ambayo anaisemea chini ya TARURA itakuwa na hadhi na ubora sawa na barabara ambazo zinatengenezwa chini ya TANROADS.
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Siha inafanana na wilaya iliyotajwa hapo lakini kwa tofauti kidogo, Halmashauri ya Siha ina magulio, haina masoko. Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano alishatoa maelekezo kwamba akinamama wanaotandaza bidhaa chini na wale ambao ni wa chini kabisa wasidaiwe ushuru.
Mheshimiwa Spika, cha kusikitisha kabisa jana katika Wilaya ya Siha wananchi kwenye soko la Sanya Juu wameenda kulazimishwa kulipa ushuru kwa kutumia polisi na wananchi waliposema Rais alishasema sisi tunaotandika chini tusilipe waliambiwa Rais huyo huyo ndiye anasema tukusanye kodi na bado yeye anatuvuruga kwenye kukusanya kodi, lipeni ushuru na polisi wakapelekwa sokoni na wananchi walipata taharuki sana.
Mheshimiwa Spika, sasa naomba nielezwe kwamba tunawezaje kuwasaidia hawa akinamama ambao ni vipenzi vya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tayari alishatoa maelekezo na yamekuwa yakipuuzwa na Halmashauri zetu. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, maelekezo aliyotoa Mheshimiwa Rais kwamba wale akina mama ambao wanapanga bidhaa zao ikiwa ni pamoja na wale ambao wanauza ndizi wasibugudhiwe ni msimamo ambao uko thabiti, hauyumbi hata mara moja. Kama kuna Mkurugenzi yeyote ambaye hataki kutekeleza kauli na maelekezo ya Mheshimiwa Rais tafsiri yake ni kwamba Mkurugenzi huyo hajitaki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nikuhakikishie, leo wakati naingia nilimwambia Mheshimiwa Mollel katika maeneo ambayo nina wajibu wa kwenda kutembelea ni pamoja na Jimbo lake hii ni pamoja na kwenda kutazama eneo la ujenzi wa hospitali mpya ya wilaya. (Makofi)
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania, vilevile Waziri Mkuu na Mawaziri kwa kazi kubwa ambayo inafanywa kwenye eno hili la ardhi. Najua nia njema ya Waziri aliyejibu swali langu, namfahamu vizuri lakini nimpe taarifa kwamba katika majibu aliyonipa bado umeendelea ule utaratibu wa baadhi ya watendaji wa Serikali wasio waaminifu kupotosha kwenye vitu ambavyo ni vya msingi.

Mheshimiwa Spika, nikianza na baadhi ya majibu yaliyotolewa hapa, mojawapo ya jibu lililotolewa ni jibu ambalo Waziri Mwanjelwa aliwahi kulikataa na kutoa maelekezo tofauti lakini bado jibu hilo hilo limeendelea hapa. Kuhusu exemption tuna barua ya Wizara ya Viwanda ikionesha kwamba mojawapo ya mashamba yaliyopewa exemption, mwaka 2014 Shamba la Gararagua limeuzwa lakini mwaka 2012 tayari mwekezaji aliyenunua mwaka 2014 tuna barua ya Wizara ya Viwanda inayoonyesha kwamba alipewa exemption mwaka 2012.

Mheshimiwa Spika, leo tukiwa hapa hatujui tuna wananchi wetu wa Kata ya Levishi, Kijiji cha Mese mashamba yao ya kahawa yamechukuliwa na TANAPA, Donumoru wananchi sasa hivi wa Kilolepori wanaishi nje, wamebomolewa nyumba zao. Leo hatujui mpaka wa Siha na Wilaya ya Arusha lakini bado huko chini tuna watu ambao wanafanyakazi hiyo. Vilevile kwenye Wizara ya Kilimo tutaona kwamba…

SPIKA: Mheshimiwa Mollel swali sasa.

MHE.DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nakwenda kwenye swali langu sasa.

SPIKA: Swali moja kwa moja.

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, je, Mawaziri wa Wizara husika watakuwa wako tayari kufuatana nami sasa ili twende kwenye maeneo husika kwa sababu tuna Wazungu wanaouza mashamba ya Siha ili wapate mtaji wa kuendeleza maeneo mengine na kuchapa watoto ndani ya Wilaya ya Siha na nitawapa ushahidi hapa?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, Wizara ya Kilimo na Wizara ya Ardhi zitakuwa tayari sasa kukaa chini baada ya Tamko la Rais ili tuone ni namna gani tunaweza tukawapatia wananchi wa Ngarenandume makazi zaidi ya 38,000 wanaoishi kwenye heka 500?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Dkt. Mollel, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Mollel kwa namna anavyofuatilia migogoro ya mashamba ya ushirika katika Jimbo lake la Siha.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Dkt. Mollel angependa kusikia commitment ya Serikali kama tuko tayari kuambatana naye kwenda Jimbo la Siha ili kutatua migogoro hii. Jibu ni kwamba tuko tayari na mara tu baada ya Bunge tutaelekea katika Jimbo la Siha ili kuangalia migogoro hii katika mashamba ya ushirika. Pia kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, azma ya Serikali ni kuhakikisha tunakarabati ushirika kwa manufaa ya wananchi wetu.
MHE. DKT. GODWIN A. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Wizara ya Kilimo imefanya kazi kubwa sana kwenye maeneo ya kufufua haya mazao ya mkakati lakini vilevile kushughulikia Vyama vya Ushirika. Katika Mkoa wa Kilimanjaro vile vile kazi kubwa imefanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuomba, ukienda Wilaya ya Siha Vyama vya Ushirika vingi vina matatizo. Kwa mfano, ukienda Sanya Juu utakuta wanachama 1,800 wameibiwa, SACCOS yao imekufa na fedha zimepotea, lakini ukienda kwenye mashamba yote yaliyoko Wizara ya Siha, ukienda Kashashi kuna ushirika wenye shida. Kwa hiyo, utaona kuna matatizo ya ardhi lakini kuna suala zima la kufufua zao la kahawa.

Mheshimiwa Waziri nilikuja ofisi kwako kukuomba twende Wilaya ya Siha na upate siku isiyozidi mbili za kutosha kwa ajili ya kuangalia matatizo yote haya. Sasa ni lini sasa utaweza kuja hapo ili ushirikiane na Comrade Ndaki Stephano Muhula, Mkurugenzi mzuri sana wa Wilaya ya Siha ili tuweze kufikia muafaka mzuri wa kufufua ushirika kwenye Wilaya ya Siha?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali dogo la Mheshimiwa Dkt. Mollel kwamba lini niko tayari kwenda? Tukimaliza Bunge hili mimi na yeye tukae, tupange ratiba, tuweze kwenda Hai pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ushirika na ubadhirifu unaoendelea Kilimanjaro, nataka tu nimhakikishie kwamba kuna timu yetu inaendelea na kufanya tathmini na niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwamba yeyote atakayekuwa ameshiriki kula fedha za Ushirika, awe ndani ya Serikali au kwenye Vyama vya Ushirika, tutawachukulia hatua.