Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Dr. Godwin Oloyce Mollel (19 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nashukuru kupata fursa hii kuweza kuchangia, nitachangia maeneo machache ya dawa na bima kwa wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa dawa, tumepokea malalamiko mengi yanayohusiana na ukosefu wa dawa na tunakiri kuyapokea malalamiko hayo na sisi tunapenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba sasa Wizara imechukua mwelekeo mpya wa kihistoria wa kuboresha upatikanaji wa dawa nchi hii ili huu wimbo ukosefu wa dawa ufikie tamati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mabadiliko gani? Tumeamua kwa dhati kama wazalendo kuanza sasa kununua dawa sio kwa middle men, sio kwa washitiri yaani unaletewa dawa unanunua kwa mtu wa tano aliyenunua kutoka kiwandani. Tunakwenda kiwandani huko huko kuzinunua hizi dawa na hivi ninavyosema MSD tayari imeshapeleka order toka Novemba mwaka jana kupitia bilioni 43 zilizokuwa zimetolewa na Serikali na makontena yako bandarini yanakuja mapema Machi yanafika. Yakifika hizo dawa zitakuwa nyingi na zitasambazwa na vituo vitanunua kwa bei nafuu dawa hizo tofauti na awali. Kwa hiyo kuanzia Machi mwanzoni hapa dawa zitakuwa zimeingia nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiacha hilo, MSD imechukua mwelekeo sasa wa kuanza kutengeneza dawa kupitia viwanda vyake, imeongezea hilo jukumu na linaendelea kukamilishwa ili lianze. Hata hivyo, kuna vile viwanda ambavyo Serikali tulikuwa tuna-share ndogo, kwa mfano pale Keko, shares zimepanda mpaka asilimia 70 na tayari MSD alishazalisha dose milioni 25 za erythromycin mwaka jana Desemba na kuzisambaza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tunahamasisha wawekezaji wa viwanda vya dawa nchini waache kuwekeza Ulaya maana gharama inakuwa kubwa, wanakuja kuwekeza hapa nchini kwetu. Sambamba na hilo, sisi wenyewe tumefanya mabadiliko makubwa kwenye Hospitali zetu za Kanda, Taifa pamoja na Hospitali za Mikoa zinachukua direction ya kutengeneza zile dawa na vifaatiba vidogo vidogo ambavyo viko ndani ya uwezo wetu. Yote hii ni kupunguza mzigo mkubwa wa Serikali kununua vitu hivi kutoka kwa middle men. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee suala la vifaa. Kwenye direction hii tuliyoichukua vifaatiba vikiwemo vya dialysis vinavyotesa sana wananchi pamoja na kwamba tunaimarisha suala zima la kinga, watu wasipate magonjwa haya yasiyoambukiza, lakini gharama zitashuka kutoka 300,000 mpaka 100,000 kwa maamuzi haya ambayo tumeyachukua. Hata ule mpango wa SADC kuanza kuipa contract MSD sasa utatekelezeka vizuri. Sambamba na vifaa hivyo kutakuwepo na uwekezaji kwenye oxygen plants ili tuache kuwa tunanunua oxygen kutoka kwenye maeneo ambayo ni bei ghali sana kwa sababu tutawekeza na ku- produce hapa nchini na vifaa vya uzazi na watoto na ICU, yaani kwenye yale magonjwa ambayo ni very critical. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kidogo kuhusu vituoni; dawa zinapotea sana, tunafanya ukaguzi wa kihistoria nchi hii. Tunaomba ushirikiano wa Wabunge na Bunge lako Tukufu. Tutachukua maamuzi ya kihostoria vile vile; kwa wale wanaodokoa dawa na kupoteza dawa sambamba na kuhujumu mapato yatokanayo na ukusanyaji wa dawa. Kwa hiyo tunapodhibiti kuanzia kwenye production, tunakuja kudhibiti kwenye matumizi, tutakuwa tumehitimisha wimbo wa upungufu wa dawa katika nchi hii na tutaulizana kwani mwanzoni ilikuwaje? Utakuwa ni wakati muafaka ambapo nchi imefunguka chini ya kiongozi wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli anayetupa ujasiri, maana vita sio wingi wa silaha, ni ule ujasiri wa kutumia silaha uende mbele. Kwa hiyo, nathibitisha kwamba suala hili linakwenda vizuri na kuanzia Machi tutegemee dawa, tamati ya ukosefu imefikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Bima ya Afya kwa wote tumelipokea kwa mikono miwili, tunakamilisha huu Muswada ambao utaingizwa huko Bungeni ili tuwe na Bima ya Afya kwa wote na hii itachangia sana kumaliza matatizo ya wananchi wetu wengi wanaoshindwa kupata huduma stahiki mahali popote. Tunapofanya haya mabadiliko yanakwenda sambamba na kusogeza hizi huduma karibu na wananchi. Kwa mfano huduma za dialysis, sasa hivi tunaanza kuongelea kwenye hospitali za mikoa, kwa sababu baadhi ya hospitali za mikoa kama kumi zimeshapelekewa mashine. Tulishindwa kuzianzisha kwa sababu ya gharama ya kuvipata hivi vifaa. Kwa hiyo kuelekea Machi tutakuwa tayari tunaanza kutoa hizo huduma kwa sababu tuna access ya dawa na vifaa kwa bei rahisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepokea mambo mengine yote, tutayafanyia kazi na kuyaleta kwenye Bunge lako Tukufu la Bajeti kipindi kinachokuja. Hivyo, naomba kuwasilisha. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL):
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ni mara ya kwanza kusimama hapa, kwanza nimshukuru Rais wetu mpendwa, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini tena na kuniteua kuendelea kumsaidia katika eneo hili la afya. Vilevile, nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango kwa kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa mentoring nzuri anayotufanyia wakishirikiana na Chief Whip, Mheshimiwa Mama Jenista Mhagama ambapo kwa kweli imetusaidia sana kurahisisha shughuli zetu. Pia nikushukuru wewe na Mheshimiwa Spika kwa ushirikiano mzuri ambao mnatupa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nijielekeze kwenye hoja za Waheshimiwa Wabunge. Kabla ya kuanza, niseme tu kwamba sitaweza kuwataja kwa majina wote waliochangia lakini wakati Waziri atakapohitimisha ataonyesha michango yenu na wote waliochangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kujibu hoja za Kamati ambapo kimsingi zimefanana na zimegusa yale ambayo vilevile yamechangiwa na Waheshimiwa Wabunge. Hoja ya kwanza ilikuwa ni kuhusu kuongezeka kwa bajeti kwenye eneo la akina mama na watoto ili kupunguza vifo vyao. Katika eneo hilo Wabunge wengi vilevile wamechangia lakini utaona kwa bajeti ya mwaka 2021 ilikuwa ni shilingi bilioni 55 na sasa imeongezeka imefika shilingi bilioni 63. Maana yake kuna ongezeko la bilioni kadhaa hapo ambazo sasa zinaenda kuongeza nguvu kwenye yale maeneo ambayo yanaenda kutuongezea kasi kwenye kupunguza vifo vya akina mama na watoto. Pia utaona vituo vya kufanyia upasuaji kwa maana ya kupasua kutoa mtoto tumboni vimejengwa 304 na tayari vifaa tiba kwa ajili ya upasuaji huo vimeshawekwa kwenye vituo 238.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo hilo hilo Mheshimiwa Dkt. Thea Ntara, amezungumzia upandikizaji wa mimba. Tumelichukua jambo lake ambalo kwa kweli kwenye kutengeneza Bima ya Afya kwa Wote, lakini kwenye ongezeko hili la bajeti na eneo hilo linaenda kuongezwa nalo ili kuchukuliwa uzito ambao Mheshimiwa Mbunge ameuzungumzia.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Mheshimiwa Dkt. Thea na Mheshimiwa Hawa Chakoma Mchafu walieleza suala la tohara kwa akina mama ambalo nalo hili linaongeza vifo vya akina mama. Waziri wetu anapouliza wanaume mpo huwa anataka tuelekeze nguvu kwenye eneo hilo, tu-address magonjwa yanayotuhusu sisi wanaume na yale ambayo yanaumiza akina mama ambapo sisi tunaweza tukawa solution. Sisi Wabunge tunaotokea maeneo yenye changamoto hiyo kama Umasaini au Ukuriani ambapo hali ni mbaya zaidi tuungane na tutengeneze utaratibu wa pamoja tukaenda kuhamasisha na sisi tukawa watu wa kwanza kulizungumzia hilo kwa uzito unaostahili.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya pili ya Kamati ambayo vilevile Wabunge wengi wameizungumzia ni suala la watoto njiti. Kamati ilizungumzia hasa Muhimbili lakini utaona kuna upanuzi walikuwa na vitanda 66 tu lakini sasa vimeongezwa vimefika 130. Vilevile ukiangalia Muhimbili kwa mwaka akina mama wanajifungulia pale ni 54,000, lakini watoto njiti kati ya hao 54 ni 14,400. Kwa hiyo, hapa ili tuweze kutoka vizuri eneo hili Serikali imeongeza bajeti kutoka shilingi bilioni 37.8 hadi shilingi bilioni 52.2. Pia ongezeko la bajeti ya shilingi bilioni 55 hadi shilingi bilioni 63 nalo linaenda ku-address eneo hili na kutatua tatizo ambalo linasababisha yatokee matatizo ambayo Wabunge na Kamati yetu imeyaainisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo limeibuka ni eneo la Bima ya Afya, wengi wamezungumzia matatizo yalioko kwenye eneo hili. Vilevile Kamati imeshauri suala la ushirikishwaji kwamba kabla ya kuleta Bima ya Afya kwa Wote hapa Bungeni wananchi na wadau mbalimbali washirikishwe. Serikali imechukua ushauri huo na kabla ya Muswada huo kuja hapa Bungeni wadau wote watashirikishwa kuanzia wananchi na watu wengine wowote ambao utawagusa na tunaamini na ninyi kama sehemu muhimu sana mtaingiza input ambazo zitaondoa matatizo mengi yaliyoko kwenye Bima ya Afya iliyopo kwa sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo Kamati imelizungumzia lakini na Waheshimiwa Wabunge pia wamegusia ni kuhusu ushirikishwaji wa sekta binafsi kwenye suala la Bima ya Afya. Sisi tunasema wakati Muswada huu utaletwa Bungeni mtaona umeweka kipengele ambacho kinaruhusu sekta binafsi kushiriki kwenye eneo la bima.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo limekuja ni wateja wa NHIF kukosa huduma lakini likagusiwa suala la CHIF. Tulichokuja kugundua wakati tunasikiliza kwa makini kuna wakati watu wanachanganya wanasema bima akimaanisha CHIF na wakati mwingine anasema bima akimaanisha bima ya afya ile kubwa ambayo inatolewa kwa wafanyakazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunachoweza kusema hapa ni kweli tatizo hilo liko na linasababishwa na upungufu wa madawa kule chini. Ukienda kwenye eneo la CHIF wananchi wamehamasishwa sana kukata zile kadi zao lakini wanapokuwa na kadi zao wanapokwenda kwenye dirisha la dawa wanakuta hamna dawa, kwa hiyo, thamani ya ile kadi aliyoikata inakosa maana. Tumeenda baadhi ya maeneo kwenye wilaya hata wananchi wenye bima hii ya afya kubwa kama walimu hata wafanyakazi wa afya wanapokuwa maeneo remote huko vijijini wakikosa dawa kwenye vituo vyetu na hakuna duka lenye dawa zote kwenye eneo lao inabidi asafiri kilometa nyingi ambapo anatumia shilingi 10,000 kufuata dawa ya shilingi 3,000. Tunachosema wakati tunakuja kwenye Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote, lakini wakati tunaelekea kwenye kuboresha upatikanaji wa dawa kwenye vituo vyetu haya matatizo yote yataenda kutatuliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni eneo la Corona. Watu wengi wamezungumzia Corona na ni namna gani tunafanya. Kwanza, niwaondoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge kwa sababu kwanza kuna Kamati ya Rais ambayo inafanya kazi hiyo na inatoa ushauri mzuri sana kwa Serikali na hilo linaendelea vizuri. Hakuna kitu kipya hapa ambacho kimeanzishwa kwa sababu kama mnakumbuka Mheshimiwa Rais wetu Hayati Dkt. John Pombe Magufuli akiwa Kagera alitushauri Wizara ya Afya msipokee vitu, lakini msifanye vitu bila kufanya upembuzi yakinifu. Hicho ndicho anachoendeleza Rais wetu wa sasa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameunda Kamati Maalum ambayo itaangalia kwa umakini ni nini kinaingia na nini kinafanyika kwa ajili ya usalama wa watu wetu. Mheshimiwa Rais ameendeleza umakini kwenye hilo hilo na Kamati hiyo inashauri vizuri sana kuhakikisha mambo ambayo tunaenda kufanya ni yale ambayo yataboresha usalama wa watu wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Gwajima amesema jana kwa uchungu mkubwa sana na hasa akitilia hofu kwenye eneo la chanjo. Amezungumzia chanjo za RNA na DNA na ameuliza chanjo zingine ni vitu gani. Ukweli ni kwamba Serikali inajua na ndio maana kuna Kamati Maalum ya wataalam yenye Maprofesa na watu wengine waliobobea na wanajua kwamba kuna hizo chanjo za RNA na DNA. Zile za RNA zinaingia kwenye seli lakini zinasemekana haziendi kwenye nuclears kwa maana ya kugusa DNA. Hata hivyo, watu wetu wanaangalia ukweli huo ni wa kiasi gani kabla sisi hatujasema lolote ndio maana ya timu hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna zile ambazo ni za DNA ambapo wametumia adenovirus ambao ni virus kutoka kwenye chimpanzee, wanachukua DNA ya virus wa Corona halafu wanachanganya na adenovirus ambayo ni type 5 unakuta katikati kuna virus huyo wa Corona pembeni na pembeni kunakuwepo na DNA ambayo anatokana na adenovirus ndiyo anaingizwa mpaka kwenye nuclear halafu baadaye anatengeneza hizo protini. Ndiyo kazi ya Maprofesa wetu na Rais ameelekeza nguvu zote pale ili wajihakikishie hiyo adenovirus na vitu vingine haina matatizo mengine? Kwa sababu tunajua genetic makeup moja hai-present kitu kimoja, unaweza ukasema unataka kutengeneza protini hizi lakini kumbe hiyo sehemu ilikuwa na uwezo wa kutengeneza protini zingine ambazo zinaweza zikawa na madhara kwa watu wetu. Timu hiyo ndiyo inafanya kazi hiyo kuhakikisha tunajibu maswali haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuwahakikishie kabisa Serikali ya Tanzania haibishani na dunia au WHO, wala Tanzania haijioni yenyewe ni kisiwa, inakubaliana na mambo yote yanayotokea kisayansi na afya katika dunia. Ubishani hauko kati ya Serikali au Wizara na mtu yeyote, ubishani uko kati ya wanasayansi kuhusu usalama wa kitu tunachoenda kufanya. Kwa hiyo, huo ni ubishani sio kutofautiana, hapana! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaulizana kisayansi unaposema hiki kinaingia kwenye cell hakikuzi DNA, ukizingatia tunajua kwenye eneo la mimea (Genetic Modified Foods) wakati fulani mapapai yalikuwa modified genetically yakatoa mapapai mwaka wa kwanza baada ya miaka miwili yakatolewa mapapai lakini hayana mbegu. Kwa hiyo, sasa tunajiuliza haya maswali, je, kwa binadamu usalama uko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, tukubaliane kwamba dunia inakoelekea mwisho wa siku chanjo nyingi baadaye zitakuwa zinatengenezwa na RNA na tunaenda kwenye genetic therapy. Kwa hiyo, hatuwezi kubishana na dunia na sayansi iliyopo, anachofanya Amiri Jeshi wetu Mkuu ni kwamba hata kama tunakubaliana na dunia tuhakikishe tuko salama kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ni kwenye tiba ya asili, Wabunge wengi wamezungumzia eneo hili na tumechukua mawazo yao yote. Mpaka sasa wataalam wa tiba asili na tiba mbadala 27,793 wameshasajiliwa, vituo 1,003 vimesajiliwa, dawa 49 zimesajiliwa lakini mafunzo yamefanyika kwa wataalam wa tiba asili 335.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka kwenda mbali zaidi ndiyo maana utaona Serikali yetu imepeleka fedha NIMR kwenye sehemu ya utafiti, hatutaki tu kuishia kusema huu mti unatibu, unaupika huo mti halafu unapata juice yake halafu unakunywa, tunataka watu wa NIMR wakae chini wajue ndani ya huo mti ni molecule gani ziko ndani yake ambazo ndiyo zina sifa ya tiba. Pia hizo molecule ziwe extracted vitu vingine vinatupwa tunaanza kutengeneza syrup na vidonge, huko ndiko tunakotaka kuelekea. Kama mnavyojua quinine inachukuliwa kwenye magome ya miti inaenda nchi zingine mwisho wa siku inatolewa kile kinachotibu inarudi kama sindano tunakuja kutibiwa hapa malaria. Kwa hiyo, tunataka tufike kwenye sayansi kubwa na ndio muelekeo wa Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ni suala la CCBRT kusajiliwa...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Sekunde 30, kengele imeshagonga.

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL):
Mheshimiwa Naibu Spika, tayari CCBRT imesajiliwa, hivyo, agizo la Kamati limeshatekelezwa. Tunatambua mchango mkubwa unaofanywa na CCBRT na Kamati ilitembelea kwa kweli Mkurugenzi wa CCBRT anafanya kazi kubwa na sisi kama Wizara tutampa ushirikiano mkubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwanza nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii lakini kwa kutusimamia kwenye hiki kipindi kigumu kidogo naanza kuona matumaini tumekaribia na mwisho, lakini tumshukuru Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais lakini Mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye siyo tu kwamba amekuwa kiongozi wetu lakini amekuwa mentor wetu. Wabunge ni mashahidi akija Majimboni kwetu anatuita Wabunge wenzangu nasi anatuita Mawaziri wenzangu wakati mwingine tunaenda kwa Waziri Mkuu tunaongea tunajisahau tupo na Waziri Mkuu baadaye tukitoka sisi tunajiuliza hivi pale tuliharibu lakini anakuwa ametuvumilia, tunakushukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwashukuru ninyi Wabunge wenzangu mmetuchanganya Mheshimiwa Ummy Mwalimu alikuwa ananiambia haya madeni tutayalipaje, lakini mmetuheshimisha na wakati mwingine tunawaza sasa je, tutaitunzaje, shida siyo kuambiwa mmefanya vizuri shida nitutatunzaje hiki mlichokiaminisha kwetu. Lakini mimi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Ndugu yetu Makubi tulikuwa tunashangaa tukiwa nje kwamba ule umahiri wa Mheshimiwa Ummy Mwalimu ambao tunauona sisi na ninyi mnauona tunasema ahsanteni sana Wabunge wenzangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwaambie Waheshimiwa Wabunge Mheshimiwa Kingu na wenzangu ambao tulikuwepo Bunge lililopita, nilipokwenda kwenye uchaguzi 2020 tulikuwa tukipigiwa kura na tukizungumzia performance zilizofanywa kwenye Wizara ya Afya, aliyetusaidia tukafika hapo ni huyu Mheshimiwa Ummy Mwalimu ambaye tunae leo. Niseme tu alipokuja Wizara ya Afya akasema sisi tunaanzia strategy inayoitwa Samia Suluhu Hassan strategy ya 1.3 Trilioni ambayo imekuja yote ikaelekea kwa wananchi akatwambia tukae chini, akaita watu wanaosimamia mradi wa investing to people akakaa nao bila kuwagombeza akapunguza kwenye posho, akapunguza kwenye semina, akapunguza kwenye nini, leo tunazo Bilioni 10 tunaenda kujenga hospitali ya akina Mama Dodoma huyo ndiyo Mheshimiwa Ummy Mwalimu.

Mheshimiwa Spika, hata siyo muda na ninafiriki mtaona kwenye Majimbo kama 100 fedha zinakuja Bilioni 7.8 ambazo hazikuwa kwenye bajeti kabisa, ni katika kukaa kupunguza kwenye posho, kupunguza kwenye nini zikapatikana Bilioni 7.8 na ndani ya wiki zilizopita zimepelekwa TAMISEMI kwa ajili ya kuja kwenye Majimbo yenu, huyo ndiyo Ummy Mwalimu ambaye mmesema hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, alikuja tulikuwa tumepanga ilipangwa kwenye bajeti ya kawaida na kwenye utaratibu wa kawaida ilipangwa kwamba tununue ambulance 503 akasema hebu niachieni niwapigie UNICEF alipowapigia UNICEF makubaliano yaliyofanyika kule ambulance 503 tukajikuta kwa kununua kupitia UNICEF tunanunua ambulance 663 maana yake zimeongezeka ambulance 160. Maana yake nini Waheshimiwa Wabunge tunapozungumzia sasa hivi suala la ambulance kila Jimbo linaenda kupata ambulance mbili. Jana alikuwa anatuambia tuhangaike kwenye Global Fund tutafute nyingine 150 Mungu akisaidia inawezekana zikaendelea kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wenzangu, Dada yangu Msambatavangu Jesca amezungumizia suala la tiba ya akili, jana tulikaa vilevile Mheshimiwa Waziri akawa anasema hebu tuitishe Kongamano la Afya ya Akili. Tena nilikuwa namwambia hapa lile kongamano unaweza nimuombe akubali awe ni Balozi kuhakikisha kwamba tunapigania suala la Afya ya Tiba ya Akili. Niwaambie tu, shida moja afya tumekuwa tukiliangalia kwamba tatizo la maendeleo ya jamii tu, lakini tiba vilevile ni suala la uchumi. COVID ilivyokuja tulizungumzia COVID kama ugonjwa lakini tukazungumzia kama suala la kiuchumi, lakini leo ukizungumia kuanzia mtoto anapozaliwa inavyobebwa mimba unapompa lishe na mambo mengine yanakuja kutokea hayo ambayo anayasema Mheshimiwa Mbunge pale na kwamba hata tunapotoa fedha nyingi kwa wanawake kule vijijini, kwa vijana halafu outcome ya fedha tunayo dish kule kwa ajili ya kukuza uchumi na kufanya mambo mengine, inapokuwa haitokei ina mahusiano makubwa sana na lishe na namna gani tunavyofanya lishe kuanzia watu wanapokuwa wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile wenzetu sasa hivi mashindano tunakwenda dunia ambayo tunaizungumzia dunia ya artificial intelligent, wafanyakazi watakaotakiwa kesho kutwa siyo wafanyakazi wenye uwezo wa kufanya kazi ni wafanyakazi wenyewe uwezo wa kufikiri nakuja na mawazo mapya. Kama hujaboresha lishe, kama hujaboresha tiba ya afya ya akili huwezi kupata hiyo kaliba ya watu ambao ni innovative na wenye uwezo wa kufanya mambo hayo. Ndiyo maana nasema Mheshimiwa Waziri amesema hapa hilo kongamano akilitayarisha ni muhimu Wabunge wote tushirikiane.

Mheshimiwa Spika, tumshukuru Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kipindi kidogo cha mwaka huu mmoja, kwenye hospitali yetu ya Ocean Road tumekwenda kwenye Afrika nzima kuna nchi nne tu ambazo zinazalisha mionzi tiba zinaviwanda za mionzi tiba. Leo tunaenda kuingia kwenye historia ya Afrika kuwa nchi ya tano kwa Afrika kuzalisha mionzi tiba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana tulikuwa tunazungumzia mgonjwa wa Mheshimiwa Saashisha ambaye amechelewa pale tukigojea mionzi tiba itoke kwa ndege siku ya Jumatano kutoka Afrika Kusini. Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kiwanda kimefikia asilimia 95 na sasa ndani ya miezi mitatu tunaenda kuzalisha hapa, na watu wetu watatibiwa hapa na nchi zinazotuzunguka zitaanza kuja hapa kwetu. Ukizungumzia hospitali yetu ya Ocean Road kwa maana ya uboreshaji uliofanyika pale utakwenda pale nchi 16 zinakuja pale kuchukua ujuzi wa namna gani unaweza kufanya mionzi tiba, ukienda JKCI mpaka kuna watu wametoka nchi zingine za Ulaya wanakuja kutibiwa pale, siyo tu kwa sababu moja kwamba kule wanatoa standard ya Ulaya lakini kwa bei rahisi zaidi. Kwa maana hiyo tunapozungumzia Wabunge suala la medical tourism Serikali yetu imejipanga na Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan amejipanga vizuri kwenye eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, amesema waziri hapa suala la upandikizaji wa Uroto na amesema Waziri hapa kwamba kwa Afrika kwa Mashariki na Kati sisi wenyewe ndiyo tunafanya, lakini Waheshimiwa Wabunge muelewe kitu walichofanya Rais wetu kwa kipindi hiki kidogo cha mwaka mmoja, kufanya Uloto kwa mgonjwa mmoja alikuwa anapelekwa India kwa thamani ya Milioni 250 kwa mgonjwa mmoja, leo hapa Tanzania baada ya Rais wetu kununua vifaa na vipo Muhimbili inafanyika kwa Shilingi Milioni 70 na anafanyiwa mgonjwa bure, maana yake tunaokoa Milioni 180 zinakwenda kufanya shughuli zingine za maendeleo. Hayo ndiyo mambo tukisema Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan anaupiga mwingi hiyo ndiyo maana yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunapozungumzia suala zima la ubora wa huduma. Kwa kweli ukizungumzia ubora wa huduma utazungumzia suala la dawa, utazungumzia suala watumishi, utazungumzia masuala mengine yote na upatikanaji, vilevile kwenye ubora wa huduma utazungumzia suala la ujenzi, majengo ambayo yanajengwa na mmeona wenyewe kwamba yamejengwa tunaenda kujenga EMD’s kwenye Wilaya zetu, tunaenda kujenga ICU’s na kuweka vifaa, lakini utazungumzia kusomesha wataalamu.

Mheshimiwa Spika, leo kama Tanzania watu wanatoka nchi zilizotuzunguka kuja kujifunza kwa wataalam wetu kuzungumzia nayo ubora wa huduma unazungumzia teknolojia nayo, kwamba tuwe na high standard ya teknolojia ambayo wakati mwingine tunaweza tukawa na mtaalam hapa lakini kama hatuna teknolojia inabidi mtu wetu aende kufuata kule, tukinunua teknolojia hapa ni gharama rahisi zaidi kumleta mtaalam kutoka nje akaja kutusaidia kwenye teknolojia iliyopo hapa na ikawa gharama zaidi na akawatibu wagonjwa wengi zaidi kwa muda mfupi na kwa gharama nafuu. Kwa hiyo hayo yote yanaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mmezungumzia suala la incentive, kwamba Madaktari wetu waache kukimbiakimbia kwenda sehemu tunafanya nini. Tunachowaambia tunampongeza sana Professor Mohamed Janabi wa Hospitali ya Jakaya Kikwete, amefanya kazi kubwa sana nzuri, Madaktari wake wanabaki pale pale na wanafanya na hawakimbiikimbii na Mount Meru hospitali wamefanya hivyo. Tutachukua model ya JKCI na model ya Mount Meru Hospital ambayo imeboreshwa pale halafu tuone ni namna gani tuna roll out kwenye nchi nzima ili iweze kufanyika namna hilo na lile ambalo mmeshauri Wabunge hapa liweze kufikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la damu salama kwa kweli damu hainunuliwi, damu hakuna sehemu damu wametembea nayo watu, tunaendelelea kuboresha Mheshimiwa Waziri ameitisha kikao na hii ilikuwa ni kuhakikisha kuboresha kwamba wataalam wetu wanapelekwa.

Mheshimiwa Spika, unajua wakati mwingine unaweza ukampeleka Mkurugenzi wa kukusaidia masuala ya damu kwenye Kanda lakini huyo mtu hata hawezi kuitisha kikao tu cha ukoo wake, unataka aitishe watu wakubali kutoa damu. Tunataka kuwaweka watu sasa ambao wana uwezo wa ku- mobilize kutumia mbinu mbalimbali kuhakikisha watu wanakuwa tayari kutoa damu.

Mheshimiwa Spika, mmezungumzia suala la tiba asili nakwenda haraka haraka, kama tulivyokwisha kusema tayari Rais wetu ametoa Shilingi Bilioni 2.8 zinakwenda kufanya utafiti pale NIMR kuhusu tiba asili mbalimbali. Pia kuna muda ambao Waziri wetu Mheshimiwa Ummy Mwalimu hivi karibuni ataenda kufungua hospitali ya tiba asili iliyopo kule Meru. Ni hospitali ambayo inatumia miti shamba kutoka Mlima Meru kutoka kule Umasaini lakini mengine kutoka Ulaya. Unaingiza kwenye maabara ya kawaida ya kisasa, inaingizwa kwenye vipimo vya kawaida vya kisasa lakini ukifika duka la dawa unapewa dawa za tiba asili.

Mheshimiwa Spika, wanaotibu ni Madaktari wazalendo lakini supervisors ni Wazungu wawili kutoka Australia, kwa namna hiyo tutachanganya ujuzi wa mwenzetu kutoka nje na sisi wenyewe tukimaliza tunaweza tukaboresha tibaasili zetu na kama ambavyo Mheshimiwa umesema tutatembelea Momba tutakuja Momba na tuangalie namna ya kufanya na kuhakikisha kwamba na wenzetu wa tibaasili kuhakikisha wanaweka hayo mambo sawa.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga.

NAIBU WAZIRI WA AFYA: Imeshagonga, nakushukuru mimi natoa hoja ili la TMDA na TBS mimi nafikiri tutaendelea kuwasilishiana kwenye Serikali na Waziri amelichukua litaenda kufanyiwa kazi kwa sababu ni kweli chakula ni sehemu muhimu sana lakini chakula usipo control tutapata matatizo ya figo, kansa na mambo mengi. Waziri amelichukua kwa uzito. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Daktari Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuniamini mimi na Mheshimiwa Ummy Mwalimu kuiongoza Wizara ya Afya. Sisi tunachomhakikishia ni kwamba hatutamwangusha.

Mheshimiwa Spika, namshukuru Makamu wa Rais na Waziri Mkuu kwa miongozo yao ya wakati wote ambayo imekuwa ikitusaidia mimi na Mheshimiwa Ummy Mwalimu katika kazi zetu.

Mheshimiwa Spika, nikushukuru wewe kwa usimamizi mzuri na ushauri mzuri kwa wakati wote ambao tunafanya shughuli zetu za kibunge hapa. Wabunge wamesema hapa, wakaniona mimi ni sawa wamemwona Mheshimiwa Ummy Mwalimu, na wakimwona Mheshimiwa Ummy Mwalimu ni sawa wameniona mimi. Maana yake ni kwamba, niwaambie tu ukweli, sisi Wizara ya Afya tunajigamba sana, tunaye Waziri wetu, dada yetu, mshauri wetu, lakini ni mtu ambaye hata kabla wewe hujasema, tusitaje sana majina ya Mawaziri, yeye tayari alishaniambia hakuna sababu ya kulitajataja. Sisi tupige kazi, hudumia Wabunge, twendeni mbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo niseme machache na mnisikilize kwa umakini nioneshe tuna Rais wa namna gani, na ni kwa namna gani kwa kipindi kifupi ameweza kufanya kazi kubwa ambapo kwa upande wangu mimi, matatizo yote ambayo mnayaona hapa, yeye Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametupandisha mlima, na sasa tunachokiona mbele yetu ni kichuguu, na kichuguu hatutakipanda, tutaenda kukivuruga.

Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye hospitali zetu za kanda, ukianza hospitali za kanda na za Taifa, kwa mwaka huu mmoja, zimepelekwa zaidi ya shilingi bilioni 51.4. Ukienda kwenye hospitali zetu za mikoa peke yake, ujenzi tu, zimeenda shilingi bilioni 54.2. Ukirudi kwenye hospitali zetu hizi za mikoa pamoja na za Taifa, fedha zilizokwenda kwa ajili ya vifaa tiba ni shilingi bilioni 290.9, ni fedha nyingi sana. Maana yake ni nini? Hizo fedha zimefanya mapinduzi makubwa sana ambayo mmeyaona hapa. Waziri wetu ameonesha mtoto ambaye ametibiwa hapa na ni huduma ambayo tulikuwa tunaenda kuipata nje kwa zaidi ya shilingi milioni 250. Leo anatibiwa ndani ya Tanzania kwa shilingi milioni 30 na kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukienda kwetu pale Muhimbili, Hospitali ya MOI utakuta leo tulikuwa tunaenda kwa zaidi ya shilingi milioni 80, wenzetu wanapokuwa na vivimbe chini ya ubongo, tunawapeleka India kwa ajili ya kuwatibu hivyo vivimbe kwa zaidi ya shilingi milioni 80. Leo wanapona ndani ya Tanzania kwa shilingi milioni saba, bila kufungua kichwa, wanaingiza mashine kwenye pua na wanatoa vivimbe chini ya sakafu ya ubongo na mtu anarudi nyumbani kwake amepona.

Mheshimiwa Spika, maana yake nini? Hizo fedha zimeokolewa, ni fedha ambazo zilikuwa ziende nje, halafu sasa zimebaki ndani ya Tanzania zipo kwenye mzunguko wetu ndani ya Tanzania zinasaidia wananchi. Ndiyo maana umeona leo wamekuja Zambia, Rwanda na Malawi juzi mmeona watu wetu wamekwenda kule. Maana yake Rais wetu amepunguza rufaa kwenda nje kwa asilimia 97. Maana yake sisi na wenzetu waliokuwa wametuzunguka, tulikuwa tunaenda kupanga foleni India kwa pamoja. Rais wetu amefanya kazi kwa asilimia 97, leo tunabaki ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, siyo hivyo tu, na wenzetu tuliokuwa pamoja tunapanga foleni nje kule India, leo amewarudisha, wanatibiwa ndani ya Tanzania. Ni kazi kubwa sana imefanywa na Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maana yake ni nini? Ndiyo maana nasema, nawaambia tusiwe na wasiwasi kwa sababu bado tuko na Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, tuko naye, tutakuwa naye mpaka 2025 na tunakuwa naye mpaka 2030 na ataendelea kupiga kazi kubwa ya namna hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yamezungumziwa masuala ya upatikanaji wa dawa kwenye vituo vyetu na zahanati zetu. Nawaomba Waheshimiwa Wabunge, hili suala la upatikanaji wa dawa lina sehemu nyingi. Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshafanya kazi yake, ametoa fedha kwa ajili ya dawa kusambazwa kwenye maeneo yetu.

Mheshimiwa Spika, nitoe mfano wa Ngara. Mbunge wa Ngara hapa alikuja akamlalamikia Mheshimiwa Waziri wa Afya, akamwambia kwamba kuna shida ya wizi wa dawa kule. Mheshimiwa Waziri wa Afya akanituma na Mbunge wa Ngara akatoa Press kwenye wilaya yake akilalamika kwamba kuna wizi wa dawa. Mheshimiwa Waziri wa Afya akanituma niende Ngara, nilipofika Ngara, Mheshimiwa Mbunge wa Ngara akanionesha summons ya kutoka Mahakamani. Akaniambia; “amenishtaki DMO, amenishitaki Mfamasia, wananiambia nimewachafua kwamba wameiba dawa.” akaniambia, “wamemwambia nikiongea na wewe usiwaguse, wana-withdraw hii summons ya shilingi milioni 600 wanayokudai.” Nikamwambia, usiogope, sisi tutaenda mbele. Hata kitendo cha kutishia Bunge kwa kutumia mwanasheria, hicho kinatosha kuwaondoa hapa.

Mheshimiwa Spika, tulipoingia kwenye kikao, wataalamu wetu walifanya kazi, tukatoa mikoba kwenye Kamati ya Ulinzi na Usalama, na Ushahidi. Wote pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama tukakubaliana kwamba DMO na Mfamasia watoke kwenye Wilaya ya Ngara. Wametoka, na leo ukimwuliza Mbunge wa Ngara, anakwambia dawa zipo kwenye wilaya yake.

Mheshimiwa Spika, ninachokisema hapa ni nini? Anakwambia dawa zipo kwenye wilaya yake. Ninachosema, suala ni kwamba mafisadi wana ushirikiano. Sisi watu wema tunakosa kushirikiana. Ninawaomba Wabunge, suala la kupambana na wizi wa dawa tusaidieni. Amesema Waziri wa Afya, ameshatoa maelekezo kwamba kuanzia sasa tukienda kujenga uwezo wa timu zetu za mikoa na wilaya tutajenga uwezo pia wa timu za ulinzi na usalama za wilaya ili waweze kufanya. Hata hivyo, Waheshimiwa Wabunge, tushikane mkono, tushirikiane pamoja tutandike wezi. Wangapi wananikubalia hilo? Piga makofi. Tuko pamoja? (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, haiwezekani Wilaya ya Siha wezi waibe, haki ya Mungu siji kulalamika Bungeni, namalizana nao huko, kama ni Serikali itanikuta Siha nikishughulikia majambazi. Kwa hiyo, nawaomba leo Wabunge wote tukitoka hapa, sisi ni Madiwani tusikubali dawa yoyote ipotee. Tusingojee kuja kulalamika Bungeni.

Mheshimiwa Spika, kuna eneo lingine linaloitwa Mshitiri. Hili eneo la Mshitiri ni kijiwe kingine cha kuiba. Nimewaambia Wabunge na kote ninakopita kwa ma-DMO, nawaambia mkiona Mshitiri analeta bei kubwa mwondoeni. Nimekwenda Nzega kwa Mheshimiwa Bashe, Mshitiri amehonga watu huko ndani, dawa ndani ya hospitali ni bei ghali kuliko nje kwenye duka la Mshitiri aliyechaguliwa. Tulichokisema, tukamnyoosha Mshitiri, sasa hivi kule kwa Mheshimiwa Bashe mambo yanaenda vizuri. Ninachowaomba Waheshimiwa Wabunge, twendeni tukashirikiane pamoja kwenye eneo hili la kushughulika na wezi.

Mheshimiwa Spika, Ndugu zangu niwaambie kitu kimoja. Wengine mmetaja masuala ya ambulance hapa, lakini amesema Waziri wetu, Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa fedha, zimenunuliwa ambulance 727. Wakati huo, Waziri wetu alipoona kulikuwa na taratibu za kimanunuzi zinazotuletea mambo ya ajabu, akakataa, akasema hatununui kwa kufuata hizi taratibu za kimanunuzi, twendeni tukatafute mtu wa kutuuzia moja kwa moja na matokeo yake tukaongezewa kutokana na kuokoa zile fedha, zikaongezeka ambulance 168. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maana yake ni nini? Wote pamoja tukiungana kupambana na ufisadi kuanzia kwenye eneo la manunuzi na kuanzia tunapotoka majimboni haki ya mama hizi fedha mama yetu anayopeleka kule zitafanya kazi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naulizwa na mtu mmoja ananiambia kwanini fedha za afya zimepelekwa kwenye maji wakati ule wa corona? lakini nikamwambia Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan anajua hesabu. Alijua ukipeleka dola moja kwenye maji, unapunguza dola nne upande wa afya na ukipiga mahesabu ya teknolojia aliyoileta hapa Tanzania halafu ukapiga hela zilizotolewa dola zilizookelewa kwenda nje unajua huyu ni Rais anaejua nifanye nini? Niokoe dola, wakati wenzangu nje dola zimewaishia yeye ana dola ndani.

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana wenye akili walikaa wakasema huyu astahili tena kuitwa Samia Suluhu Hassan aitwe Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kwa sababu amepiga mahesabu ikaonekana wenzetu sasa wanapita kwenye ugumu mkubwa sana wa kiuchum, lakini sisi tuna nafuu kwa sababu Rais wetu kila kitendo anachokifanya kinabakiza dola nyingi ndani ya nchi badala ya kutoa dola nyingi nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kusema kimoja, Mheshimiwa pale Mbeya kwako tulikuwepo na Kamati ya Bunge, tukawa tunatembelea na wananchi walikuwepo, tukawa tunatembelea majengo ya hospitali ya mikoa zaidi ya bilioni saba. Tumekwenda lile jengo la mama na mtoto ambalo limegharimu zaidi bilioni 19 pamoja na vifaa kuna MRI, kuna CT – Scan.

Mheshimiwa Spika, wananchi wakaniambia kabla ya wewe kuwa Mbunge, walikuwa wanaota sugu kutoka huku kuja Muhimbili kutafuta huduma. Lakini baada ya wewe kuwa Mbunge leo wananchi wa Mbeya Mjini wanabaki wanapata huduma za kinamama za kibingwa bobezi ndani ya Mbeya wanapata MRI ndani ya Mbeya, wanapata CT – Scan ndani ya Mbeya na tunataka kuwataarifu watu wengine wananchi wa Mbeya Mjini hawataota tena sugu kutoka Mbeya kwenda Dar es salaam wanataka kutulia na Dr. Tulia wao, waanataka kutulia na Dr. Tulia wao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalizie la mwisho kwamba leo ndani ya Tanzania Afrika kuna nchi nne tu, ambazo zina kiwanda cha kuzalisha mionzi dawa. Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan amejenga kiwanda Ocean Road na sasa tunaenda kuwa nchi ya tano Afrika kwa kuzalisha mionzi dawa na mionzi dawa hiyo kila mwaka ilikuwa inatusababisha tutoe bilioni tano nje ya nchi sasa zinabaki ndani ya Tanzania.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. DKT. GODWIN A. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishukuru kwa kupata nafasi. Kwanza nakubaliana na wenzangu wanaosema mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni nami niseme tu katika migogoro ambayo nimewahi kumletea Mheshimiwa Waziri kuhusu ardhi ndani ya Wilaya yetu ya Siha, nimeeleza hata ya kufanya na kuyafuatilia na amefika katika Wilaya ya Siha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimeona wanavyoshirikiana na Wizara ya Kilimo kutatua migogoro iliyoko eneo la Ushirika. Vile vile niseme kwamba leo tujielekeze zaidi wapi atakapokwenda kukwama wakati anafanya shughuli zake ili ajipange mapema zaidi na nimwombe anayemwakilisha Waziri Mkuu, ili aweze kunisikiliza kwa makini na kumfikishia ujumbe huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya Wilaya ya Siha, tuna migogoro ya mipaka kati ya Arumeru na Longido, lakini sikuwepo siku mbili ,tatu hizi wananchi kati ya Arumeru na Siha wamebomoleana nyumba upande wa Arumeru wamebomoa nyumba moja lakini Siha kwa sababu Mkuu wa Wilaya kafika pale tena kafika amelewa, lakini alipofika pale ame-provoke wananchi kati ya pande zote mbili zimebomolewa nyumba nne za Arumeru, lakini ikabomolewa na ofisi ya mtendaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekwenda pale kazi ilikuwa ni rahisi, ilikuwa tu kukutanisha wananchi pande zote mbili na kuwaelewesha na kukaa chini mkondo wa sheria ufuate sehemu yake, lakini Mkuu wa Wilaya ya Siha alitaka nguvu zitumike kuliko akili. Niseme tu nimshukuru OCD Meru na Siha, lakini na Mkuu wa Wilaya ya Meru angalau anasimama kwenye nafasi yake kama tunavyotaka aende. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunapoongea hivi najua migogoro ambayo nimewaandikia, lakini migogoro ambayo ameandika Mkuu wa Wilaya ya Siha baada ya maagizo ya Mheshimiwa Waziri, mgogoro ambao nimekuwa nikiusisitiza kila siku, leo tunapoongea hivi matrekta mawili yamebomolewa na wananchi, nimepata meseji sasa hivi lakini gari la polisi limevunjwa kioo, huyo ndiyo Mkuu wa Wilaya tuliyenaye.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanasemaje? Wananchi wanasema na baadhi ya watumishi, wananchi walipoona yule mwekezaji kwenye Kata ya Songu, alipokuwa anaenda kwenye Kata ya Songu kulima hilo eneo ,wananchi walimzuia. Walipomzuia wakamtaka Mkuu wa Wilaya na uongozi wamzuie kwa sababu bado wana mgogoro, wao wanasema eneo ni lao na wenyewe wawekezaji wanasema eneo ni lao, wakataka tu kwamba azuiliwe na yeye asilime ili waendelee na mchakato wa kawaida, lakini Mkuu wa Wilaya akaagiza polisi waje wakamate watu. Polisi wakatumia nguvu nyingi wakakamata na viongozi, ndiyo yaliyofikia, hayo sasa ndiyo matatizo tuliyonayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sana nashukuru Mheshimiwa Waziri alikwenda kwenye Wilaya ya Siha, lakini nimwambie kuondoa Mkuu wa Mkoa ambaye alikwenda naye baba, wengine wote ni watuhumiwa, Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi na hata juzi tulimuuliza amekodisha heka nyingi ambazo haziruhusiwi, tena beacon zimepimwa amewapa watu viwanja, halafu wakaenda tena kukodishwa halafu zikalimwa wakang‟oa zile beacon, anatuambia tutafute shilingi milioni mia moja kwa ajili ya kurudishia beacon, hiyo ndiyo Serikali ya Wilaya tuliyonayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe na nimwombe Mheshimiwa Waziri pamoja na Waziri wa Kilimo, twende ili wathibitishe ninayosema kwa maneno yao hawathubutu kumwambia ukweli. Akienda cha kwanza kiongozi akifika pale anaambiwa yule Mbunge ni mkorofi, ana fujo, lakini kiukweli mimi sina fujo wala huwa mimi siyo mkorofim isipokuwa nataka watu waende kwenye focus ambayo ndiyo tunaitaka nchi hii ifike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekubaliana kwamba, tunataka kuipeleka Tanzania iwe ni nchi ya pato la kati, hamna namna yoyote tutakuwa nchi ya pato la kati na narudia tena, ni lazima kama tunajenga viwanda, basi watakaotengeneza malighafi kwa ajili ya hivyo viwanda wawe ni Watanzania wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani tukatengeneza kiwanda, sawa tunakubali na mwekezaji wa kiwanda awe na sehemu ya kutafuta malighafi, lakini ili kuwapeleka nao Watanzania waweze kumiliki uchumi wa nchi yao, ni lazima nao waweze kuzalisha malighafi ambayo itatumika kwenye hivyo viwanda, ndicho tunachokisema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano Wilaya ya Siha, nilisema tena hapa tunaweka 130,000, hivi tungesema tunatoa eka 10,000 tunahakikisha nao watu wa Siha wanamiliki au Watanzania wanamiliki, sio lazima watu wa Siha wakamiliki zile 120,000, tukawekeza tutapunguza migogoro. Leo umeona Mheshimiwa lile shamba la maparachichi ni zuri, lakini ndani ya Wilaya ya Siha ni mojawapo ya wilaya hazina pato, inasemekana baraza lao livunjwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini ukienda kwa wawekezaji wanakwambia kwanza tumechoka viongozi wako wa Wilaya sisi ndiyo tunatengeneza magari, sisi ndiyo tunawapa hela na vitu vingine, tunakuomba uende ukasema tuwe tunadaiwa kile tunachostahili, tena tupeleke kwenye maendeleo yaonekane na wananchi. Kama mimi nasema uwongo, naombeni twende tuthibitishe haya ninayosema na niko tayari kuwajibika kama nasema uwongo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme hivi, tukiwamilikisha namna hiyo tutapunguza migogoro, kama mkulima mwekezaji amewekeza kwenye zao fulani, nao wakulima wakawekeza kwenye zao hilo hilo kwa kupewa ardhi, kwa sababu wanatumia soko moja na wakatumia eneo moja kuuza, urafiki utakuwepo na migogoro haitakuwepo na upendo kati ya wawekezaji na wananchi utakuwa mkubwa sana. Hicho ndicho tunachokisema, hatusemi hatutaki wawekezaji, sisi tunasema tunataka wawekezaji lakini tunataka tunapofikiria uwekezaji tufikirie sustainability ya uwekezaji wenyewe kwamba uwekezaji wenyewe utadumu vipi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu huyu huyu Mkuu wa Wilaya nilishawahi kumwambia, wala mimi siyo Mbunge wakati huo nilikuwa mfanyakazi wa kawaida tu. Nikamwambia migogoro wa Endarakwai ambao ameandika hapa eka 5,000 wakati ni eka 11,000, nikamwambia fanya hivi, fanya hivi, akakataa akasema yeye ni dola na hatuwezi kumfundisha. Tuliona kilichotokea, nyumba zimechomwa na mabilioni yamepatikana na ni aibu kwetu kama nchi na ni aibu kwetu kama wilaya, wawekezaji kuvamiwa halafu inarushwa nje, je, na tunataka tuwekeze, tukitaka tuwekeze wakati tunatangaza sehemu zetu za uwekezaji, watu waki-google wakiona wawekezaji wamevamiwa tunakosa uwekezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunataka watu wenye hekima ambao wanajua kupeleka uwekezaji pamoja na wananchi bila kuwa na migogoro ili watu waipende nchi yetu. Nilikuwa naangalia leo hata Ujerumani wanatangaza wanaomba wawekezaji watoke nje, hata sisi tunawahitaji, lakini tunawahitaji kwa namna ambayo itamfanya Mtanzania afaidike, mwekezaji afaidike lakini na mtu ambaye anakaa katika eneo husika afaidike, ndiyo uwekezaji tunaousema. Tunamshukuru Mheshimiwa Waziri anaona hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri aangalie watu hao wasimkwamishe kwa sababu hapewi ukweli. Leo shamba ambalo limechomwa matrekta hajawahi kwenye ofisi yake kuambiwa, lakini siku zote tunasema kwa sababu wana maslahi. Mashamba ya ushirika alikuja Waziri wa Kilimo, Naibu Waziri wa Kilimo, Mkuu wa Wilaya wananchi walimzomea kwa masuala ya ardhi, lakini kwa nini ndani ya mashamba ya ushirika ni wao wanalima wananchi hawapati mashamba? Kama nasema uwongo twendeni halafu niko tayari wala msiseme nimesema kwenye Bunge siwajibiki, niwajibike kama nasema uwongo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe hili limfikie Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba, sisi tunapenda hiyo nafasi ya Ukuu wa Wilaya, lakini huyo ambaye anakaa mpaka saa nane bar, dereva anakaa kwenye gari na gari la Serikali la kodi ya wananchi, sisi tumechoka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatutaki mtu anayesababisha Serikali idharauliwe, tunataka Serikali ya Tanzania iheshimike, watu waheshimu Serikali ya Tanzania. Unapokwenda kwa wawekezaji Mkuu wa Wilaya mzima unaongoza Serikali halafu unapewa vitu vidogo vidogo unaidhalilisha Serikali yetu na hatutakuwa tayari. Nilimwambia Mkuu wa Mkoa, huyu Mkuu wa Wilaya anatusumbua na tukamweleza, nikamwambia nitakuja kuomba hapa ahamishwe ikishindikana wananchi wa Siha hatupo tayari Serikali ya Tanzania kuaibishwa, tutamtoa wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kweli kwa sababu anatudhalilisha, anafanya vitu ambavyo ukienda kwa mzungu akikuona mweusi anakudharau, hatuko tayari. Kwa hiyo, niseme bila kuathiri juhudi nzuri zinazo…
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa
Mwenyekiti, nashukuru kupata fursa hii lakini kabla sijasema naomba niweke sawia mambo mawili yaliyojitokeza jana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mtu jana alijaribu kuonesha kwamba Mwenyekiti wa Kambi Rasmi ya Upinzani ni mtu wa kawaida, lakini naomba niweke rekodi vizuri, Mheshimiwa Freeman Mbowe, alikipokea Chama cha Demokrasia na Maendeleo kikiwa na Wabunge watano, lakini amekipeleka na akafika mahali mpaka ikaundwa UKAWA na leo Bunge hili lina Wabunge kutoka upinzani zaidi ya 100. Lakini ameweza kuunganisha nguvu na hata akatuletea magwiji wa siasa kutoka huko kwenu ambao wakikaa kimya CCM wote mnakusanyika kufukiria kwa nini yupo kimya. Kwa maana hiyo Mheshimiwa Freeman Aikael Mbowe ni profesa wa sayansi ya siasa, niweke rekodi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile jana kuna baba yangu alisema kwamba mama yetu Ruth Mollel kwamba eti kwa sababu amewahi kuwa kiongozi mkubwa katika nchi hii hastahili kuwa kwenye chama cha upinzani kwa sababu ana siri za Serikali. Ninataka niwaambie kwamba CCM sio masijala ya siri ya Tanzania. CCM ni chama kama chama kingine cha siasa, CCM ni kana CHADEMA ni kama CUF na mtu yeyote haijalishi ameshika nafasi katika nchi hii anaruhusiwa kuwa kwenye chama chochote ilimradi havunji Katiba ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefanya utafiti kuanzia miaka ya 1970 mpaka 2016 nimegundua ili kutekeleza mpango kazi wa mwaka mmoja katika nchi hii unahitaji miaka mitatu mpaka minne kwa hiyo sitazungumzia pesa kwa sababu nchi hii haina pesa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitakwenda kujikita tubadilishe fikra kwa babu fikra ndiyo tatizo leo kwa hiyo tukibadilisha namna tunavyofikiri nchi hii itakuwa na pesa na tunaweza kukabiliana na matatizo yaliyotukabili mbele. Wakati nawaza hilo, nikafikiria, hivi katika kubadilisha fikra na kuisadia nchi hii, solution ni kubana demokrasia? Ni kuzuia uhuru wa kutoa mawazo ya Bunge? Ni kuhakikisha vyombo vya habari havifanyi kazi yake vizuri? Nikagundua la hasha, kuruhusu uhuru wa mawazo ndipo tutakapogundua magwiji wa fikra katika nchi hii.


Mheshimiwa Mwenyekiti, sifa ya magwiji wa fikra ni watu wenye uwezo wa kufikiri katika upeo ulipitiliza ubongo na sifa yake ni kwamba huko hakuna unafiki, hakuna uzandiki, hakuna u-CCM wala u-CHADEMA, tunalifikiria Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme, Rais wa Marekani alipokuwa anamkabidhi Makamu wake kazi, alimwambia naamini akili zako sana, akamwambia ninakupa mission ya kupeleka nchi yetu iwe nchi ya kwanza kufanya miujiza katika sayari ya mars. Tujiulize sisi tunapokabidhiana madaraka, tunakabidhiana madaraka kwa ajili ya kuishughulikia upinzani, kwa ajili ya kubonyeza demokrasia, tunakabidhiana madaraka kwa ajili ya kufanya nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tujiulize kwa nini Marekani wanataka kwenda mars, wanataka wawepo, pamoja na mambo mengine, wawe wanaitazama dunia wakiwa mbali wanaiangalia Tanzania, wanaangalia mabara yote na mtu yeyote akitaka kuigusa Marekani wakati akiwa katikati ya Bahari ya Atlantiki, anagongwa kabla hajaifikia Marekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tujiulize sisi kama nchi, hivi tunajisifia kwa kutegua mtego wa Mheshimiwa Nape kuongea na waandishi wa habari halafu tunasema tumetumia akili na Usalama wa Taifa una akili sana katika nchi hii! Nchi yetu leo tunauliza maswali ya msingi kwamba Ben Saanane yuko wapi? Hatuna hata uwezo wa kueleza yuko wapi na ninategemea kwamba Usalama wa Taifa ndiyo darubini ya nchi, ndiyo maana tunaita TISS, ile ‘I’ ndicho kitu cha msingi; intelligence! Uwezo wa kutazama na kuona mambo yasiyoonekana kwa macho ya kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nchi inahangaika, Mwenyekiti wa Kambi ya Upinzani anasema, tuombe basi msaada Uingereza kwa watu wenye darubini ya kutazama mambo yasiyoweza kuonekana, tunazunguka zunguka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme hivi, hii nchi siyo ya CCM, siyo ya CHADEMA, ni yetu wote Watanzania. Ni lazima tuanze kufikiri ni namna gani tunaweza kuisaidia Tanzania na tunatokaje sehemu hiyo ambayo sasa tupo. Juzi hapa na jana limejadiliwa suala la East Africa. Tumeingia kwenye uchaguzi na ningependa sana Spika angekuwepo hapa. Unajua ukiwa umelala uko nusu usingizi, huwa kuna akili nzuri zinakuja, lakini hizo akili huwa zinakuja wakati kuna msiba umetokea mkubwa wa mtu ambaye mnampenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipokuwa hapa kwenye msiba wa Sitta, Mheshimiwa Spika ndipo alipofikia akagundua sisi tunapita tu hapa duniani, akasema anatamani sana kufikia hata nusu ya utekelezaji wa Mheshimiwa Sitta, lakini juzi tumefanya uchaguzi wa East Africa hapa, yamefanyika madudu. Nataka umwambie Mheshimiwa Spika, huu mtego wa uchaguzi wa Afrika Mashariki ni mtego ambao unamfanya hata aweke milestone ya kwanza kumwelekea Sitta, hata kufikia nusu ya Mheshimiwa Sitta. Ndiyo mtego wa kwanza ambao tunampa Bunge hili. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vita kuhusu East Africa na uchaguzi wa East Africa siyo kati ya CCM na CHADEMA, ni kati ya Tanzania na dunia ya kibiashara na vita vya kibiashara vya kidunia. Tunahitaji akili kubwa kama ya Mheshimiwa Masha ambaye amewahi kuwa kiongozi ndani ya Serikali, anajua Usalama wa Taifa vizuri namna ya kushirikiana nao, anajua nchi hii ili tuweze kuunganisha nguvu tupambane kwenye vita vya kidunia katika uchumi wa dunia, siyo kutafutana na kutafuta CHADEMA nani mzuri nani mbaya. Hicho ndicho tunachokifikiria; tuache kuwaza katika akili ndogo. Bahati nzuri, tunaye Mheshimiwa Waziri mzuri, msikivu na mwelewa tumtumie, ni fursa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu yangu Waziri wa TAMISEMI nikwambie tu, unaye Naibu wako mzuri ambaye ametuonesha mfano mzuri wa utawala bora, Mheshimiwa Jafo.

Mheshimiwa Jafo amekuja kwenye Wilaya ya Siha, ametuunganisha wana-CHADEMA na wana-CCM tukaanza kuwaza tu kuhusu maendeleo ya Wilaya yetu, akaacha mambo ya uchama ili twende mbele. Tunataka viongozi kama hao, hatutaki watu ambao wanakuja kwa shughuli za Kiserikali wanaanza kufikiria mambo ya vyama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu, usalama wa nchi ni uchumi. Tujiuize maswali ya msingi, Usalama wa Taifa kama ina microscopic eyes na tunazungumzia hapa na wakati mwingine tukizungumzia Usalama wa Taifa watu wanafikiri tunadhalilisha Usalama wa Taifa, hapana tunatafutia Usalama wa Taifa uhuru wake na waanze kupelekwa Usalama wa Taifa watu wenye akili kubwa, ndicho tunachokipigania hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tujiulize Kagoda ilivyokuwa imetokea, Richmond, EPA; Usalama wa Taifa walikuwa wapi? Leo Rais anahangaika na makontena huko, tujiulize kama hilo wazo la kuruhusu makontena yaende nje lilikuwa baya, Usalama wa Taifa walikuwa wapi wasimshauri Mheshimiwa Rais? Tujiulize kama Mheshimiwa Rais leo atakuwa amekosea kuzuia hayo makontena, Usalama wa Taifa wako wapi kama Mheshimiwa Rais wetu atakwenda kukosea kwa maana ya uamuzi huo anaofanya? Hiyo ndiyo akili tunataka nchi yetu isaidiwe na iongozwe kwa namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu tujiulize hivi hawa watu wanaompelekea Mheshimiwa Rais message kwamba kuna muuza duka huko amemtukana halafu muuza duka anakwenda kusimama na Rais Mahakamani eti ana kesi na Mheshimiwa Rais, ni nani huyo anayempelekea Mheshimiwa Rais anaanza kufuatilia mambo madogo madogo katika nchi kama hii maskini ambayo asilimia 48 ya bajeti yake inategemea misaada kutoka nje? Kuna mambo makubwa ya kumwelekeza Mheshimiwa Rais ili ayafikirie, siyo kuwa na kesi na watu wadogo wadogo wa mtaani kwenye shughuli za simu. Tuanze kutafakari, tuanze kufikiria, tuipeleke nchi yetu inavyotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua nawatibu akili, mimi ni Daktari wa binadamu, tuanze kuwaza, Mheshimiwa Mwinyi unanielewa. Ukianza kuona mtu ana Ph.D halafu anajipendekeza kwa mkubwa kwa sababu tu huyo mkubwa anafanya mambo ya uteuzi, ni mojawapo ya kujitambua na kupima kwamba uwezo wako wa kufikiri ni mdogo, hata kama ulifaulu, ulikuwa na IQ ndogo tu ambazo zingekuwezesha kufaulu matokeo darasani, lakini IQ ni ndogo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu tuanze kujipima IQ, zetu ni kwa nini mtu mwenye Ph.D anajipendekeza kwa mtu mkubwa? Inakuwaje zero inapigiwa salute na majeshi yetu? Mheshimiwa Mama Ndalichako anza kujiuliza, hivi kuna leakage gani inapitisha zero mpaka inakuwa Mkuu wa Mkoa katika nchi hii? Inatokeaje? Hatuwezi kukubali hicho kitu. Hizo zero hatuzidharau, tujiulize, hivi kama yeye ameweza ku-shake nchi mpaka Ph.D inampigia salute, tujiulize sisi wenye Ph.D na huyo mwenye zero ni nani mwenye akili zaidi? Hilo ndiyo la msingi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tujiulize, mimi nawarudisha, siwezi kuzungumzia tena maji maana naona…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Muda wako umekwisha!

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Nakumbuka kuna Bunge lililopita ambalo tulifanya kazi kubwa sana ya kutunga Sheria ambayo ingesaidia kuboresha, kulinda demokrasia, lakini kuhakikisha vyama vyetu vya siasa vinaendeshwa kwa kufuata sheria na taratibu, lakini leo tumekuwa na vyama ambavyo vimegeuka ni SACCOSS ya kikundi cha watu wachache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wenzetu wa CHADEMA wamekuwa na kikao chao cha Kamati kuu lakini maswali ya msingi yaliyoibuka kwa Wabunge wa CHADEMA na baadhi ya Wajumbe wa Kamati Kuu ni kwamba walimtaka Mwenyekiti wao aweze kuwasaidia moja michango yao ambayo wamekuwa akiwachangisha ili iweze kusaidia chama kujipanga kwenye uchaguzi ambao unakuja.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wakawa wanamuomba kwamba kuna ruzuku ambayo imekwisha ingizwa na Serikali huko nyuma na ile michango ambayo tayari kama milioni 600 na mingine ambayo Wabunge, mwenyewe nadai milioni 18 kule! Nadai milioni 18 kwa hiyo, naomba hapa ile sheria itumike ili hata na mimi tutakaporudishiwa hela na mimi 18 zangu zirudi huku na Watara apate ya kwake. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na Wabunge wakumwambia Mheshimiwa wao kwamba kama sisi tusisusie huu uchaguzi, twendeni kwa sababu ni fursa ya sisi kufanya siasa lakini tuchukue pesa ambazo tumepata za ruzuku lakini michango ya Wabunge ambao tumekuwa tukisema inakusanywa inawekwa akaunti maalum kwa ajili ya uchaguzi. Wakasema uchaguzi huu ndiyo wenyewe sasa, twendeni tukafanye siasa hata kama kuna maeneo wenyeviti wameweka mpira kwapani hawajajiweka, lakini tutapita kufanya siasa. Wabunge wameomba hilo ili wazunguke hii nchi nzima kila kijiji wapate pesa waende huko, pesa hamna! Sasa wamekimbilia kwenye siasa rahisi za kusema kwamba uchaguzi sio huru na haki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wakawa wanazungumzia suala la watendaji na wakurugenzi kufoji sijui kufanya nini. Wao waliwaambia watu wao na walipita kwa semina zao na kuwaambia hakikisheni hamfanyi hivyo halafu wao wanafanya siasa rahisi huku juu kuonesha kwamba hakuna uhuru wa kufanya uchaguzi. Haya nilitaka kuomba kwenye hiki kipengele kwamba kama tulitunga sheria na kama kweli tunataka tupate vyama ambavyo maana yake uwepo wa vyama vya upinzani vinasaidia sana kwenye maendeleo kwa sababu vinajenga amsha amsha na vinaamsha chama ambacho kinatawala. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tutaruhusu watu wachache watuulie vyama hivi vya upinzani maana yake siasa na maendeleo yetu yataenda kupata shida. Tunataka tumuombe Msajili wa Vyama vya Siasa sasa aanze kuitisha kufuatilia hivi vitu kwa makini na kama nitakuwa nimesema uwongo, niko tayari na mimi kuitwa pale juu na kwenda kujieleza kama nitakuwa nimesema uongo kwamba hawa ndugu zangu hawaibiwi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuondokane kwa sababu wanasema mambo yanavyokwenda usalama unapata matatizo, nchi hii haitakuwa salama. Kuliko watu watengeneze mambo halafu wahatarishe usalama wa nchi yetu, ili kunusuru hilo twendeni tukaone ukweli, Watanzania wajue ukweli, watu waache kuchonganisha wananchi na Serikali yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na nimewashauri huko nyuma wakati CUF wanagombana nikawaambia mbona hii game rahisi wakati nikiwa kule. Mchukueni Sharif pale anakuja anakuwa Katibu Mkuu wa CHADEMA mambo mengine yanaenda, siasa inakuwa bora kwa sababu ni kijiwe na mtu mmoja, walimkataa ameenda ACT wanaanza kupiga kelele.

Mimi nimeamua niseme hilo kabla sijaingia masuala ya maendeleo kwa sababu hili ni muhimu sana kwa usalama na heshima ya nchi yetu Kimataifa, hao watu wanachafua nchi yetu sana. Naomba tufanye hilo na Msajili afanye hiyo kazi lakini kama Serikali ina n amna ya kufuatilia ruzuku yake, ifuatilie niko pole pole naenda Mahakamani kudai milioni 18 zangua mbazo hazijafanya kazi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Wabunge wetu wamechangia kwenye…

MWENYEKITI: Sijakuelewa, Mheshimiwa Mollel kuna hela zinatolewa kwa Waheshimiwa Wabunge na Spika sijui, hela za namna gani?

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimechangia 500,000 kwa miaka mitatu kila mwezi na niliandika mwenyewe barua kweli, sipingi! Lakini ukweli ni kwamba haijatumika kwenye lengo tulilopanga. Sasa hivi watu wamepiga kitu kwapani, wamekula hela, wamejenga mahoteli wenzao wanatesema hapo, ukiwaona wamechoka hapo Mheshimiwa Silinde hapo usimuone ndugu yangu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Viti Maalum wamedaiwa 1,500,000.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Nina uhakika hiyo Taarifa ni muhimu sana.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waitara nimekuona, kuhusu taarifa.

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, nashukuru. Waheshimiwa Wabunge naomba nimpe Mheshimiwa Mbunge anaendelea kuchangia Godwin Mollel Mbunge wa Siha Taarifa kwamba na mimi ni miongoni wa wanaodai Chama hicho za zamani shilingi milioni 18 kwa sababu tulikuwa miaka mitatu pale kwa hiyo Mheshimiwa kwenye kesi ambayo utafungua na mimi nitaku-join ili tukadai hizi hela Mahakamani. (Makofi/Kicheko)

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea Taarifa hiyo na namkumbusha

Mheshimiwa Waitara yeye ni milioni 19 na pesa kwa sababu yeye alichelewa kidogo kurudi huku. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, twende kwenye eneo la kilimo. Viti Maalum ni 1,500,000 na bado wanachangishwa 2,000,000 na wengine wamechelewa kikao fulani wakapigwa faini 2,000,000 na watu wakapiga kwapani wala haikuifanya kazi ya chama. Hiyo ndiyo CHADEMA halafu inasema tuna taka uadilifu katika nchi, uongozi wenye maslahi, sijui vitu gani! Hapa tunataka kujenga nchi, tuko serious, hatutaki vijiwe na CHADEMA wale wanaotaka kuiua CHADEMA hatutakubali. CCM itatetea CHADEMA isimame CHADEMA kama chama. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninaenda kwenye eneo la kilimo. Wabunge wengi wamechangia na wakaonesha kwamba kilimo kinachangia asilimia 28 ya pato la Taifa lakini kwa mwaka huu ukuaji wake ni asilimia 5.3. ni ukweli kwamba kilimo ni sehemu nyeti sana kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu. Nilitaka kuomba Wizara ambazo zinahusika ukitaka kumsaidia mkulima sio kumpa pembejeo, ukitaka kumsaidia mkulima ni kumtafutia masoko ya mazao yake, sio kutenga, ni kutafuta masoko ya mazao yake. Kutembea kwenda sehemu mbalimbali na kutafuta masoko kwa ajili ya mazao husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitaka kumsaidia mkulima inawezekana kweli wakati mwingine tunajaribu kudhibiti mazao kutoka nje ili kudhibiti mfumuko, lakini hasara yake nini? Unaweza ukawa undhibiti mazao kutoka nje kwa ajili, najua sasa hivi limeondolewa lakini hasara yake inawezekana ndiyo iliyotuathiri mwaka huu tukashuka madhara yake ni kwamba wananchi wanaweza wakaachana na hayo mazao ambayo walikuwa wanayazalisha mahindi wakaachana nayo wakaenda kwenye mazao mbadala halafu mwisho wa siku ukajikuta unatumia fedha za kigeni kununua mahindi na mwisho wa siku ukapandisha bei ya shilingi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri tuuachie uhuru wa watu kuuza popote na Serikali ifanye juhudi ya nguvu sana kutafuta masoko sehemu mbalimbali kahawa na mazao mengine yote ambayo wananchi wetu wanayalima kwa namna hiyo hatutakuwa na haja ya kuuza pembejeo kufanya nini, wananchi wenyewe watatafuta vitu vyao na Serikali itaachana na mizigo ya kutaka kupeleka pembejeo na vitu vingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ya pili nilitaka tujikite zaidi kutoa elimu kwa sababu Serikali imefanya kazi kubwa mno. Leo tukizungumzia vile vile kilimo kushuka katika Taifa letu maana yake ni kwa sababu hatuna viwanda, kwa sbabau tukiwa na viwanda ambavyo vinachakata aina ya mazao tunayozalisha maana yake ni kwamba wananchi wetu watapata masoko ya kuuza mazao yao na hata kilimo na uzalishaji utapanda ndiyo maana tuna bwawa la Nyerere ambalo tunatengeneza umeme. Ukiwekeza kwenye eneo la umeme ukazalisha umeme wa kutosha maana yake kutakuwepo na viwanda huku Tanzania kwa sababu umeme tulionao leo hata tukisema tutaweka viwanda, hatutakuwa na umeme wa kutosha na tutakapokuwa na umeme wa kutosha hata ujenzi wa viwanda na bei ya umeme itashuka na viwanda vingi vitatengenezwa na mwisho wa siku tutamnyanyua mkulima wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanaposema kwamba uwekezaji kwenye kilimo ni mgumu, ninachokiona kuna umuhimu wa kuelimisha watu kwamba uwekezaji unaofanyika kwenye barabara, umeme, treni na ndege mwisho wa siku uwekezaji huo wote unakuja kumsaida mkulima wetu kwa sababu atasafirisha mazao kwa urahisi, mkulima wetu atapata umeme wa bei rahisi, mkulima wetu akipata umeme wa bei rahisi na kiwanda kinapata umeme wa bei rahisi maana yake viwanda vitafunguliwa vingi. Wakulima wetu, Kenya ndege zinapishana kupeleka mazao yanayozalishwa na wakulima wa Kenya kupeleka huko nje na sisi maana yake ndiyo maana tunasema na ndege.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninachosema unapotazama kilimo usitazame kilimo kama ni shilingi ngapi inailetea kilimo moja kwa moja. Tazama ni vitu gani ambavyo vinaweza vikasaidia kilimo na ni vitu gani ambavyo ukiviunganisha mwisho wa siku input yake inaenda kuingia kwenye kilimo. Ndiyo namna hiyo tun apotaka kutazama bajeti ya kilimo ni shilingi ngapi na tukaona. Inawezekana unaona hela iliyopelekwa kwenye kilimo ni kidogo lakini hali halisi hela ni nyingi sana kwa sababu input zote hizo zinakuja kusaidia malighafi ambazo zinazalishwa ndani ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye eneo la maji, niseme kuna hela nyingi sana zinapelekwa kwenye maji na watu wengi wamekua wakichangia kuhusu hilo. Nafikiri kuna umuhimu sana nisiongee sana kwa sababu imeshasemekana. Kuna umuhimu wa kutumia force account nayo kwenye eneo la maji kwa sababu tunaibiwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Siha tu coverage yetu ya maji ni asilimia 87 lakini…

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa. Malizia.

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamuomba tu Naibu Waziri au Waziri wa Maji hapa twende tena Siha, kile kikundi cha mafisadi wa maji waliokwenda Mkoani na sehemu zingine kumzuia asifanye utekelezaji wa mambo ambayo yatasaidia wananchi wa Siha kufanya bill ndogo ya uuzaji wa maji bado kinatusumbua kule. Twende halafu tushushe bei ya maji kwa ajili ya wananchi wa Siha. Ahsante sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Dkt. Mollel kwa mchango wako. Dah! Kumbe watu wanazoa mahela hapa, hatari kubwa! Na nyie mnatoa tu, nyie vipi? Hatari kubwa! Inahitaji tuwasaidie kwakweli. Waheshimiwa Wabunge, lakini ofisi yangu haihusiki kukata hela ya mtu yeyote. Hatufanyi hiyo biashara sasa hivi.

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeibiwa sana tusaidie ndugu yangu.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nianze kwa kusema kwamba mpaka 2100 yaani miaka 81 kutoka sasa Tanzania inakadiriwa kuwa ni nchi ya sita kwa idadi ya watu duniani lakini itakuwa ni nchi ya pili kwa Afrika ikiongozwa na Nigeria, tukifuatiwa na DRC, Ethiopia na Uganda. Kwa hiyo, mambo yote ambayo tunayafanya leo na mipango ambayo tunaipanga leo ni kujipanga kwa ajili ya kupokea hiyo idadi ya watu na changamoto kwa ajili ya hiyo idadi ya watu. Kwa muda mrefu tulikuwa tukitamani Serikali inayofikiri miaka 100 mbele siyo inafikiri kwa miaka mitano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali kubwa linaloendelea hapa ni kwamba Serikali hii imekuwa akipanga bajeti kwa ajili ya vitu na sio kwa ajili ya watu. Nianze kwa Wilaya ya Siha, nikija kwenye eneo la barabara, Serikali hii imepeleka shilingi bilioni 52 na barabara ya lami inaendelea kujengwa ndani ya Wilaya ya Siha. Ukienda kwenye TARURA, barabara za kuunganisha vijiji kuna kata moja ya Ivaeni pamoja na Kashashi ilikuwa ili watu waliotofautiana mita 200 kukutana wanazunguka kilometa saba. Serikali hii imepeleka shilingi milioni 960 na sasa wananchi wanaungana kwa kupitia daraja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake ni nini? Leo utakuta Mbunge anasimama hapa anasema kwamba Serikali hii inapeleka fedha kwenye vitu hapo hapo analalamika kwamba bei ya petroli imepanda kijijini kwa sababu barabara imekatika, unashindwa kuelewa huyu kiongozi anataka nini kifanyike. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwenye Wilaya ya Siha, Serikali hii na bajeti hii, Wilaya ya Siha ina vijiji 100 umeme umefika vijiji vyote, ina vitongoji 168 umeme umefika vijiji 125 bado vitongoji 43, ni Serikali hii hii ya Chama cha Mapinduzi. Hii maana yake ni nini? Ukipeleka umeme vijijini wananchi wataongezea mazao yao thamani na watapata karibu huduma zinazohitaji umeme na hata mzunguko wa fedha unaongezeka kwenye vijiji vyao. Hiyo ndio maana yake, tunaposema tunawekeza kwenye umeme mfano Stigler’s Gorge tunapandisha thamani ya maisha kule vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata leo ukiangalia Korea ya Kusini na Korea ya Kaskazini, Korea ya Kusini ni tajiri kuliko Korea ya Kaskazini hata kama unapita usiku utaiona Korea ya Kaskazini kuna giza lakini utaiona Korea ya kusini kuna mwanga wa kutosha. Maana yake umeme ndiyo chanzo kikubwa sana cha kusisimua maendeleo ya wananchi. Kwa maana hiyo, tunaposema tunawekeza kwenye umeme wa uhakika na kwa sababu umeme wa maji ndiyo wa bei rahisi mpaka sasa hakuna mwingine, dunia sasa hivi inafanya utafiti namna ya kuwekeza kwenye umeme huu wa uranium na kuweka ndani ya bahari ambapo ni salama zaidi na utatoa umeme rahisi na sisi wangetufikirisha pamoja na sisi kuwekeza kwenye huu umeme wa maji sasa tuanze kufikiria na kujifunza wenzetu wanafanya nini kwenye uranium, hilo ndilo tungelitegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukija kwenye afya kwenye Wilaya ya Siha. Bajeti hii na Serikali hii imepeleka shilingi bilioni 9 Hospitali ya Kibong’oto na shilingi bilioni 1.75 tunajenga Hospitali ya Wilaya. Maana yake ukipunguza magonjwa, huduma ya akina mama na watoto na life span inaongezeka, hiyo ni michango ya kugusa maendeleo ya watu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unakwenda kwenye maji, kwenye kata zingine imepelekwa shilingi bilioni 1.8 kwa ajili ya vijiji 17 na shilingi bilioni 1.75 kwa ajili ya vijiji 13. Maana yake ukipeleka maji vijijini unapunguza magonjwa lakini akina mama muda wa kwenda kuchota maji unapungua. Baada ya muda hata muda wa kufanya kazi za maendeleo unaongezeka lakini magonjwa ambukizi yanapungua na unaongeza maisha ya watu na uzalishaji. Kwa hiyo, hoja ya kusema hii bajeti ni ya vitu siyo ya watu ni uongo uliotukuka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye umwagiliaji sisi kwetu tuna shilingi milioni 380 kwenye Kata ya Levishi na shilingi milioni 450 kwenye Kata ya Kashashi. Maana yake ni kwamba wananchi wanaenda kumwagilia mazao yao kwa kilimo cha umwagiliaji. Kwa hiyo, maana yake ni bajeti ya watu na inayoenda kukugusa maisha ya watu siyo bajeti ya vitu kama ambavyo wenzetu wanataka kutuaminisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo wenzetu walewale leo wanasema kwamba idadi ya watalii kwenye Taifa hili haiongezeki na wanasema pato la utalii haliongezeki. Watu wamefanya utafiti wameona kwamba wenzetu ambao tunashindana nao kwenye utalii wana ndege na wanasafirisha watalii kwa ndege zao wanaanza kupitisha kwenye nchi zao ndiyo watalii waweze kuja Tanzania. Maana yake sisi Watanzania pesa ya kwanza wanayotoka nayo Ulaya wanapita nazo kwanza kwenye nchi yetu chenchi ndiyo inafika kwenye nchi yetu. Sasa leo tumenunua ndege anaibuka yule yule anayesema kwamba pato na idadi ya watalii haiongezeki anasema kwamba unanunua ndege haigusi maisha ya watu. Haya ndiyo mambo tunayoyasema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunazungumzia suala la ajira, tunatakiwa tufikiri sana na tunawekeza kwenye elimu, tunaenda kwenye dunia ya artificial intelligence, vitakuja viwanda hapa mtu atakuja na roboti tatu halafu anahitaji watu wenye uwezo wa kufikiri. Ndiyo maana Mheshimiwa Profesa Ndalichako kuna hela nyingi zimewekezwa kwenye elimu na mabweni yanajengwa kwenye maeneo mbalimbali, uwekezaji unafanyika kwenye elimu ili tufike hapo kwa sababu ajira ijayo ndugu zangu siyo hii mnayoipigania hapa ambayo leo inagharimu asilimia 43 ya pato la TRA, ni ajira ambayo inahitaji mtu kufikiri siyo kufanya casual job. Miaka ijayo artificial intelligence, roboti ndiyo zitakuwa zinafanya kazi sasa wanatakiwa watu creative na innovative. Twendeni tukatengeneze watu creative na innovative kwa sababu ndiyo ajira itakayokuwepo siyo aina hii ya ajira ambayo tunaifikiria sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina malalamiko kutoka kwa wenzangu wazuri wa CHADEMA wameniambia jambo niombe kuwasaidia na Watanzania wazuri. Wameniambia kwamba kuna kiongozi wao mmoja mkubwa amekopa ndani ya chama shilingi milioni 600 akaenda kuwekeza Morogoro lakini huo mradi ulivyoshindikana anataka sasa kugeuka hiyo pesa iwe ulikuwa ni mradi wa CHADEMA usiwe tena mradi wa kwake yeye binafsi. Wakaniambia nisaidie hapa kuiokoa hiyo mali ya CHADEMA na tuiombe TAKUKURU iende pale na hata ikiwezekana kwa sababu tunataka maendeleo yanayogusa watu basi hayo matrekta ambayo yanabadilishwa majina na hizo mali kwa sababu hizo pesa ni ruzuku na ni kodi ambayo Mheshimiwa Dkt. Mpango umekusanya, sasa hiyo kodi ambayo Mheshimiwa Dkt. Mpango umekusanya ikaenda CHADEMA halafu mtu mmoja amechukua anataka kuwapakazia CHADEMA baada ya yeye kukopa tunataka ikachunguzwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mashamba ya ushirika kule Siha na Hai tunataka sasa yale matrekta yachukuliwe yaende kwenye hayo mashamba na ichunguzwe tuletewe ukweli hapa. Wakati kule Hai tunaendelea kuchunguza, Sabaya anaendelea kuchunguza kale kataasisi cha kihuni, tuendelee kufanya na hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwenzangu anapenda kusema kansa hapa. Kansa maana yake ni nini? Cell zote za mwili zinakuwa controlled na central nervous system. Maana yake cell moja iki-jump ikawa haisikiliza ubongo inakuwa inajigawanya bila kusikiliza ubongo unataka nini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia Serikali ya Tanzania na Chama cha Mapinduzi kuna control system kutoka juu mpaka chini na akisema Mheshimiwa Rais basi chini tunafuata lakini CHADEMA sasa hivi wanatafutana wamekuwa kansa wenyewe, kila mmoja yuko kivyake kama cell ya kansa. Kwa hiyo, kufafanua vizuri kansa ni CHADEMA wala siyo kama yeye anavyofikiri ni Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namsikia Kiongozi Mkuu, namheshimu sana kaka yangu Mheshimiwa Selasini lakini naunga bajeti mkono, hebu rekebisha kansa kwenye chama chako watu wasikilize kama central nervous system. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, basi kusema namsikia kiongozi namheshimu sana Mheshimiwa Selasini, lakini naunga bajeti mkono hebu rekebisha kansa kwenye chama chako watu wasikilize kama sisi tulivyosikiliza. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia, nijikite kwenye ripoti ya Kamati kwenye eneo la Bohari ya Dawa. Kwanza niwashukuru kwa sababu wameonyesha kwamba hali ya dawa imeboreka na hasa baada ya Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kupeleka bilioni 333.8, lakini kuweka utaratibu ambao kila mwezi bilioni 15 zinakwenda Bohari ya Dawa na sasa hali inaendelea kuwa nzuri.

Mheshimiwa Spika, vile vile wamezungumzia kutokuwepo na viwanda vya kuzalisha dawa. Kwa rekodi nzuri ya Bunge kwa hii miezi ambayo Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan amekuwepo madarakani tumekwenda sasa kujenga Kiwanda cha Kuzalisha Dawa kule Njombe na kimefikia asilimia 70 ya ujenzi na kitaenda kuzalisha vidonge vya kutosha nchi nzima kwa siku mbili. Pia kinajengwa kiwanda cha kuzalisha gloves ambacho kitakidhi 85% ya nchi nzima.

Mheshimiwa Spika, Kiwanda chetu cha Keko kimeenda kufufuliwa na sasa kinafanya kazi na kinazalisha zaidi ya dawa 12 kwa sasa. Wakati huo huo kimeanzishwa Kiwanda cha Kuzalisha Mionzi Dawa ambacho kiwanda hicho kwa Afrika Mashariki ni sisi peke yetu tutaenda kuwa nacho na kwa Afrika kuna nchi tano tu ambazo zinamiliki kiwanda hicho. Maana yake ni nini, tulikuwa tunaagiza dawa kutoka Afrika Kusini, sasa tutakuwa tunapata dawa hapa hapa Tanzania na Nchi za Afrika Mashariki zitakuwa zinaagiza hapa nchini kwetu.

Mheshimiwa Spika, wamezungumzia suala la deni la MSD, ni kweli kulikuwa na deni la bilioni 281 na kulikuwa na kazi inayoendelea ya kuhakiki deni hilo. Kwa sababu kila wakihakiki wanakuta kuna kiasi kikubwa cha fedha ambacho kilikuwa siyo halali, kimeshahakikiwa kama milioni 90 na tayari zimelipwa bilioni 39. Wakahakiki tena bilioni 126 wakakuta kuna madeni feki bilioni 4.7 na hii bilioni 126 sasa inaenda kulipwa ambazo zimehakikiwa tayari.

Mheshimiwa Spika, ukizungumzia eneo la Bohari ya Dawa kwa maana nyingine huwezi kuzungumzia bila kuzungumzia uwajibikaji na utendaji mzuri kuanzia juu mpaka kufika chini. Nakumbuka Wabunge tuliripoti hapa kwenu na tukawaeleza jinsi ambavyo kulivyokuwa kuna upotevu wa dawa kwenye maeneo yetu. Tukitaka kweli tufike mahali dawa zipatikane kwa wingi, ni muhimu sana hili suala la kusimamia dawa liwe ni shirikishi, maana yake sasa tunatakiwa twende kujua vyanzo ambavyo vinafanya dawa zipatikane kwenye hospitali zetu za halmashauri na sehemu zingine na vyanzo kuna basket fund, kuna own source na MSD.

Mheshimiwa Spika, sasa wakati mwingine tulivyowaelezea upatikanaji wa dawa hapa kwetu jinsi tulivyoibiwa, tulichotaka ni kwamba tunataka tushuke mpaka chini Baraza la Madiwani na hata vituo vyetu kule chini watendaji na Wenyeviti wa Vijiji na Madiwani wawe ni sehemu ya kusimamia uadilifu huo na kupata ripoti zote zinazotokana na dawa ili tuweze kusimamia kwa umoja wetu.

Mheshimiwa Spika, nafikiri kwa upande wetu hayo ndiyo ambayo yalikuwa yanatuhusu sisi na majibu yake ni hayo. Niseme tu kwenye eneo hili la kuzalisha dawa maana yake tiba mionzi, Kamati yetu ya Bunge ya Huduma za Jamii iliomba ikifika asilimia 80 ya ujenzi wa hicho kiwanda watembelee na asilimia 80 ya hicho kiwanda imefika na tumeshaandika barua kwako kwa ajili ya Kamati ya Bunge kutembelea kukiangalia kile kiwanda.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kukushukuru wewe na kulishukuru Bunge lako Tukufu kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya. Lakini zaidi nimshukuru Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa nini ninamshukuru Rais wetu; hapa Bungeni mmetupitishia trilioni 1.1 kwa ajili ya shughuli mbalimbali za afya, lakini yeye kwa kutumia mbinu nyingine tumepata nje ya bajeti zaidi ya bilioni 891.5. Siyo kazi rahisi; una trilioni 1.1 halafu nje ya bajeti inapatikana fedha karibia na hizo zilizopo kwenye bajeti.

Mheshimiwa Spika, hizi fedha zimepunguza rufaa za nje kwa zaidi ya asilimia 97. Tulikuwa na hospitali mbili tu za mikoa ambazo mpaka mwezi Februari zilizokuwa na CT scan, lakini sasa hospitali zote za mkoa zitakuwa na CT scan. Leo kwa mwezi Oktoba na Novemba tunakwenda kugawa X-ray machines 174 kwa nchi nzima kwa Wabunge wote na hakuna wilaya ambayo haitaguswa. Hii ni kazi kubwa sana ambayo Rais wetu ameifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, unakumbuka Mheshimiwa Rais alikwenda pale Muhimbili akapewa ripoti kwamba kuna watoto zaidi ya 500 ambao wana ulimi mkubwa wanaosubiri kwenda nje kutibiwa India. Rais wetu aliagiza pale na vifaa vililetwa na sasa watoto wote wametibiwa ndani ya nchi, hawajaenda nje, na wapo kwenye familia zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende sasa kwenye hoja. Kulikuwa na hoja nyingi lakini naomba niende kwenye tatu. Hoja ya kwanza ni bima kutorejesha gharama za matibabu. Kwa mwaka 2021/2022 kwenye halmashauri zote madai yalikuwa bilioni 29.6 na sasa zimerejeshwa bilioni 26.6, kwa maana kuna asilimia nane ndiyo bado hazijarejeshwa kutokana na sababu mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, sisi tumekwenda mbali zaidi na tumekwenda kwenye maeneo mbalimbali tumeangalia tatizo hili. Nitolee mfano sehemu moja ya Mkoa wa Kigoma. Tulikwenda tukawakuta kwenye bima tu peke yake walikuwa wanapata milioni 70 kwa mwezi, lakini tulipokaa kwa kushirikiana na Wabunge, Serikali ya Mkoa na watumishi wa hospitali husika, walifanya mabadiliko na sasa ukienda Hospitali ya Mkoa wa Kigoma wanapata zaidi ya milioni 200 kwa mwezi kupitia bima.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hatukuwa tunapoteza tu pesa kwenye eneo la marejesho lakini kulikuwa na pesa ambazo hazikuwa zinadaiwa nyingi sana kwenye eneo letu. Hilo eneo tumeshaliboresha. Na kuna makubaliano yanaendelea na TAMISEMI na Bima kuhusu pesa hizi ili waweze kupelekewa vifaa na vitu vingine ambavyo vitatiokea kule upande wa bima.

Mheshimiwa Spika, hoja ya pili ni kuisimamia MSD kupeleka vifaa kulingana na mahitaji. Moja, kuna hatua mbalimbali zilipendekezwa, hatua zote ambazo zilipendekezwa kwa ajili ya kuchukuliwa kutokana na matatizo yaliyokuwepo kwenye mfumo wa dawa zimeshachukuliwa.

Mheshimiwa Spika, vilevile, baada ya kuchukua hatua hizo tukaenda mbali zaidi tukasema kwamba kuna mambo yaliyokuwa yanasababishwa na masuala ya manunuzi, ucheleweshaji ulikuwa unasababishwa na manunuzi. Tulichokifanya pale tumeweka mikataba ya muda mrefu ili kuondoa hayo mambo ambayo yanachelewesha upatikanaji wa dawa kutokana na sheria za manunuzi kuchukua muda mrefu kila hitaji linapotokea.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na tatizo la halmashauri zetu kupeleka fedha MSD lakini dawa hazipelekwi kule kwenye halamshauri zetu. Tulichokifanya hapa, kwa fedha ambazo tayari halmashauri wanazo, kama MSD hana dawa hizo, ndani ya saa 24 atoe OS ili halmashauri waweze kwenda kununua dawa sehemu nyingine badala ya kuchukua fedha na kuzipeleka MSD na wanashindwa kupeleka dawa sehemu husika.

Mheshimiwa Spika, zaidi ya hapo, tunakwenda kushirikiana na kamati zetu za ulinzi na usalama kwenda kufika zaidi, tushirikiane pamoja kwenye kufanya kazi kwenye medicine audit na kutengeneza mfumo ambao tutaona dawa inapotokea MSD mpaka inaposhuka halmashauri na jinsi dawa zinavyotumika. Mfumo uweze kuonekana upande wa TAMISEMI na upande wa Afya, tuhakikishe kunakuwepo na control kubwa ya dawa na vifaatiba.

Mheshimiwa Spika, eneo la tatu ni eneo la uteketezaji wa dawa. Moja; kwa nini kumekuwepo na dawa nyingi zilizoteketezwa. Tumeona kwamba kulikuwepo na mabadiliko makubwa ya tiba, hasa kwenye eneo la Ugonjwa wa UKIMWI, maana kwenye eneo hilo mwaka 2018 na 2021 kumekuwepo na mabadiliko makubwa sana kwenye eneo la tiba. Lakini wakati mabadiliko yanafanyika kuna dawa tayari zilikuwa zimepelekwa kwenye site. Hizo dawa hazikutumika kwa sababu ya hayo mabadiliko na ni dawa zenye thamani ya bilioni 16.

Mheshimiwa Spika, wakati huohuo kumekuwa na mabadiliko ya teknolojia ambayo nayo yamesababisha vitendanishi aina mbalimbali vyenye thamani ya bilioni sita kuharibika. Na fedha hizi ni zile za wadau, na mara nyingi wanapeleka pesa lakini wakati huohuo wanakuja na mambo kama haya. Hilo tumekwenda nalo kulishughulikia.

Mheshimiwa Spika, sasa ni kwamba vitu hivi vyote vitafanyika kupitia Mfuko wa MSD, siyo kufanyika tena direct kwenda kwenye mikoa yetu ili tuweze kufanya reconciliation na kuondoa hili ambalo limeonekana hapa.

Mheshimiwa Spika, kwenye mfumo wetu wa dawa wa manunuzi ya kawaida…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Sekunde 30, malizia.

NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwenye mfumo wetu wa kawaida kumekuwa na asilimia nane kweli ya upotevu wa dawa kama hiyo. Tumeshashughulikia maeneo yaliyokuwa na shida, kama alivyosema Waziri wa TAMISEMI, kuna mabadiliko makubwa sana yamefanyika, wakuu wa idara na mambo mengine. Wakati huohuo tunataka, ndiyo maana tunasema tunakwenda kukaa na kamati za ulinzi na usalama, tumekwenda Nzega tumekuta ndani ya hospitali duka la dawa linauza dawa bei ghali kuliko maduka yaliyozunguka hospitali. Lakini ni mkakati uliotengenezwa palepale ndani.

Mheshimiwa Spika, maana yake nini; tukishirikiana kwa pamoja, dawa hazitaharibika kwa sababu watu sasa wanakwenda kununua dawa nje ya hospitali badala ya ndani na zinabaki zinaharibika. Hayo yote tumeshayafanya.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kufika hapa. Vilevile niwashukuru wananchi wa Wilaya ya Siha kwa kuniamini kwamba naweza nikawawakilisha. (Makofi)
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Jafo anamjua Mwanri vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuchangia kwa kusema kwamba kama kweli tunataka kuitoa Tanzania kutoka sehemu moja kwenda nyingine ni lazima tuwe na tafakuri ya juu sana katika kuamua ni namna gani tunatumia rasilimali za nchi yetu. Hata hivyo, nimshukuru Rais John Pombe Magufuli kwa sababu kwa muda mrefu watu wamekuwa wakisema kwenye jengo hili kwamba kuna ufisadi, kuna ubadhirifu wa rasilimali za nchi, yeye amekuwa shahidi namba moja, twendeni tukapambane na huo ufisadi. Amekuwa shahidi yetu kwamba yaliyokuwa yanasemwa kwa miaka yote ni kweli kabisa. Sasa wote kwa umoja wetu bila kujali vyama vyetu twendeni tujikoki silaha zetu tukapambane kwa ajili ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuzungumzia ardhi kwa Wilaya ya Siha. Wilaya ya Siha ina eneo kubwa la ardhi ambayo haitumiki inaitwa ardhi ya Serikali ni zaidi ya heka 32,000, zipo tu na hakuna matumizi yoyote. Vilevile ardhi ambayo haiendelezwi vizuri inayosemekana Ushirika wameishika ni zaidi ya heka 14,000 na ardhi ambayo inasemekana wawekezaji wamemiliki ni zaidi ya heka 39,000. Ukijumlisha heka zote unakuta kuna heka 120,000 na zaidi. Unakuja kugundua ardhi hiyo kwa heka ni zaidi ya wananchi wa Wilaya ya Siha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Lukuvi, Waziri wa Ardhi na Mawaziri wengine wahusika nimewaeleza na wamenisaidia, wamenisikiliza vizuri. Niseme karibuni Wilaya ya Siha, karibuni Mkoa wa Kilimanjaro kwa sababu ni mkoa mdogo sana na matumizi yake ya ardhi yanatakiwa yaangaliwe kwa jicho tofauti na kwingine ambako kuna mapori makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niombe, tuna shamba ambalo lina ukubwa wa heka 3,429 linaitwa shamba la Gararagua. Ni shamba ambalo linasemekana linamilikiwa na KNCU. Shamba lina miundombinu ya maji ndani yake ambayo ndiyo backup ya maji ndani ya Wilaya ya Siha na kwenye Halmashauri lakini shamba hili anauziwa mwekezaji ambaye anakuja kulima maparachichi na mwingine kufuga kufuga kuku. Tuna uzoefu na huo uwekezaji wa maparachichi, nimeuliza ndani ya Wilaya ya Siha unaiingizia Halmashauri shilingi ngapi hamna chochote zaidi ya maparachichi yaliyoharibika kulipiwa ushuru wa geti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwekezaji huyu anataka kuongezewa eneo lingine ukipiga bei kwa kila heka yeye anaenda kuchukua kwa Sh.2,000,000 kwa heka moja. Ni heka moja yenye maji ndani yake thamani yake ni kubwa mno. Tutafute tafakari ya juu ya namna gani tutatumia hiyo ardhi kwa maslahi ya Taifa letu. Kwa sababu tukimjenga mwananchi wa chini ili aweze kuzalisha vizuri, alipe kodi na akapata ardhi nzuri ndivyo ambavyo tutaweza tukasema tunaweza kutekeleza bajeti tuliyonayo kwa sababu hatutegemei hela kutoka Serikali Kuu, tunategemea hela kutoka kodi wanazolipa wananchi wa chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nionye tu kuhusu shamba hili, mwekezaji ambaye alipewa na KNCU kwa muda wote wa miaka mingi toka nikiwa mtoto akichangisha Sh.50,000 kwa kila mwananchi kukodisha kulima mazao. KNCU wanasema wanataka kuuza hili shamba kwa sababu wana deni la Sh.4,000,000,000 wanalodaiwa na CRDB.
Mheshimiwa Mwenyekiti, msimamo wetu kama Wilaya na Mkoa kabla ya kusema unauza shamba hili, tujiulize aliyechukua Sh.4,000,000,000 kutoka Halmashauri kwa nini alishindwa kurejesha? Kama ni jipu litumbuliwe kabla ya kwenda kusema unaenda kurudisha hela za CRDB. KNCU inajulikana kwamba imekuwa kidonda ndugu kwa Mkoa wa Kilimanjaro kwa kuua zao la kahawa na kufanya mambo mengine ambayo wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro hawaridhika nayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuonyesha kuna tatizo hapa, nimetembelea mashamba zaidi ya 23 niliyoyazungumzia lakini nilipofika katika hili shamba la Gararagua mwekezaji aliyeko pale aliagiza walinzi wake wanizuie nisiingie kwenye shamba. Nilipoingia alienda Polisi kusema nimemwingilia shambani kwake. Cha kusikitisha amepiga simu toka Dar es Salaam, Polisi na Serikali ya Wilaya ya Siha ikawa inakimbiakimbia inanitafuta mimi, nikajiuliza kazi ya Mbunge ni nini? Sisi tumechukua silaha zetu tunakwenda kutumbua majipu watu wachache ambao wanahisi majipu yao tunaenda kuyatumbua wanaiamsha Serikali yetu inapingana na sisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa kwenye Wilaya au Mikoa yetu kuna shida moja mnapokuja ziara. Nashauri muanzishe utaratibu mzuri kama aliouanzisha Mheshimiwa Mwigulu kwamba kabla ya kwenda eneo fulani anaonana na watu wa eneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye eneo la la elimu. Nielezee kitu cha tofauti, imesemekana elimu ni kitu ambacho tunaenda kukiangalia kwa jicho lingine. Nimshukuru Mheshimiwa Ndalichako, naamini unaweza ukaenda ukafanya hilo lakini tuangalie pamoja na kwamba tutaboresha shule, tutaboresha kila kitu lakini tuna eneo ambalo tunatakiwa tuliwekeze nalo ni eneo la mtoto na uwezo wa akili wa mtoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, twendeni tuwekeze katika lishe ya watoto wetu ili tunapowapeleka shule basi ukuaji wa ubongo uwe umekua vizuri ili aweze kupata kile kinachotakiwa. Kwa sababu wenzetu wametuzidi kiteknolojia siyo kwa sababu tu wana rasilimali nyingi au wana vitu vingi ni kwa sababu wana watu wenye uwezo wa kufikiri zaidi ya kufikiri katika ubongo (thinking beyond the brain). Tunatakiwa na sisi tuanze kujenga watu wenye uwezo huo ili tuweze kuwekeza kwenye teknolojia. Kama hatujawekeza vizuri kwenye ubongo wa mtoto kwa maana ya ukuaji pamoja na elimu nzuri hata kama tutajenga vyuo vikuu vizuri namna gani hatutakuwa na ubongo wa kuweza kuelewa teknolojia ambayo tunaitaka tuitengeneze.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala kilimo. Wilaya ya Siha ni Wilaya mojawapo iliyozunguka Mlima Kilimanjaro lakini utalii huo haufaidishi Wilaya ya Siha na vilevile tunahitaji tuboreshe miundombinu iliyozunguka Wilaya hiyo. Ukiangalia barabara ambayo inapitia ile Kisimiri Corridor kwenda Londrosi Gate imechimbika sana na Rais ameahidi kuishughulikia na nasikia kwamba tayari procurement imeshafanyika kwa ajili ya kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami imebaki kusainiwa mkataba. Naomba hilo suala liharakishwe kwa sababu magari yamekuwa yakianguka katika barabara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuboreshe eneo la kilimo, wananchi wamekuwa wakizalisha mazao mengi lakini wakati wa mavuno mipaka yetu imekuwa ikufungwa. Nina zao moja katika Jimbo la Siha ambalo wananchi wako tayari kulima hata mashimo wanyeshee nalo ni zao la nyanya. Cha kushangaza wanapovuna mahindi mengi wanakosa pa kuuza. Naomba ikiwezekana wananchi wakivuna waruhusiwe kuuza popote wanapoweza kuuza ili kuhamasisha mazao ya chakula kuzalishwa na hata wananchi wawe tayari kuchimba mashimo watafute maji ili wanyeshee na tutaweza kuzalisha chakula kwa wingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kilimanjaro na Wilaya yaSiha wamekuwa wakizalisha zao la kahawa. Naomba Waziri wa Kilimo tusaidiane…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha
kwa muda wa mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umemalizika.
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. DKT. GODWIN A. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba hii, lakini niseme kwamba wote tunakubaliana kwamba tunaipeleka nchi yetu kuwa ni nchi ya viwanda na nchi ya pato la kati. Kuipeleka nchi hii kwenye nchi ya viwanda na nchi ya pato la kati haitawezekana kama hatutazingatia kilimo ambacho kitamshirikisha kila Mtanzania kumwingiza kwenye uchumi huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna shida moja ambayo tunatakiwa tuifute kwenye vichwa vyetu ya kujiamini kama sisi tunaweza, lakini kuwaamini Watanzania na wakulima wetu walioko kule wanaweza hata kuliko watu wanaotoka nje kuja kuwekeza katika nchi hii. Nikitolea mfano Wilaya ya Siha, ni Wilaya ambayo imebarikiwa kuwa na ardhi nzuri na yenye rutuba na iliyozunguka Mlima wa Kilimanjaro; ni ardhi ambayo ukihesabu ekari zake ni karibu mara mbili ya idadi ya watu wa Siha wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, imekuwa ikiaminika kwamba sisi watu wa Siha hatuna uwezo wa kuwekeza wala wa kulima, inatakiwa waje watu wengine kutoka nje wawekeze ndiyo wenye uwezo huo. Leo, nashukuru maana jana nilikuandikia kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu kuhusu Gararagua kidogo hukunijibu nikawa na hasira kidogo, lakini nilivyokuona umeshika ng„ombe hapa, nikakupenda bure, kwa hiyo, sikushughulikii! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo watu wameitana siri siri kule Mkoani kwangu, wanajadili kuuza shamba la Gararagua. Wanajadili kuuza ardhi ya Siha kwa sababu wanaamini sisi Watanzania hatuna uwezo wa kuwekeza. Bado tunazungumza kuwatoa watu wa Tanzania waingie kuwa ni watu wa uchumi wa kati, haiwezekani kama hatutafika mahali tukaamini Watanzania wanaweza na kupitia Watanzania tunaweza tukawekeza kwenye ardhi iliyopo Tanzania na tunaweza tukawekeza kwenye kila kitu na rasilimali zilizopo Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hatusemi „tusikubali uwekezaji,‟ tunawapenda wawekezaji, tunapenda uwekezaji kutoka nje, lakini tunahitaji uwekezaji wenye maslahi kwa Umma. Tunahitaji uwekezaji ambao mwisho wa siku uwekezaji huo unamfanya mwekezaji huyo apate alichokuja kukichukua, lakini unafanya nchi ipate, lakini Mtanzania wa kawaida naye apate kutokana na uwekezaji huo. Ndiyo uwekezaji ambao tunausema na tunauhitaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumezungumzia masuala ya mifugo. Bahati nzuri Profesa jana alikuwa anasema ukifuga unapata sh. 8,000/=, lakini mimi nina kaka yangu anamiliki ng‟ombe zaidi ya 450 na kila miaka mitano anavuna mara nne na anavuna kila mwaka milioni 150. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hizi hoja za theses za watoto wa Kizungu wanaposoma Masters huwa mara nyingi hazitusaidii. Ninachoweza kusema ni kwamba tukiwekeza kwenye kilimo, kwenye mifugo tunachoweza kutupa tu ni sauti ya hiyo mifugo! Mifupa ni pesa, ngozi ni pesa, nyama ni pesa, kwato ni pesa, pembe ni pesa, damu ni pesa na kila kitu ni pesa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na wanaosema tunahitaji tufuge mifugo kwa kiwango kulingana na ardhi tuliyonayo, lakini kuna shida iliyotokea, wazee wetu huko nyuma walikuwa wanamiliki ardhi kimila, wanamiliki Communal Owned Land, lakini ilikuja ikaonekana kwamba ardhi hizo ni tupu na wawekezaji wakapewa. Wakulima wanakosa pa kulima, wafugaji wanakosa pa kufuga, matokeo yake wakulima na wafugaji wanakutana kwenye maeneo ambapo mkulima hana ardhi wala mfugaji hana ardhi wanaishia kugombana bila sababu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tuseme, hata kama tunazungumzia popote ambapo kuna matatizo ya kifugaji; wafugaji kupigana na wakulima, wakulima na wafugaji ni ndugu, ni Watanzania wamoja ila ni mfumo umewafanya wagombane. Twendeni sasa kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu, hebu amka nenda mkatusaidie sasa tuhakikishe wakulima na wafugaji hawapigani tena kwa sababu wanapendana, ni Watanzania wanataka kuwa wamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bila ku-undermine kazi ambayo inafanyika na Wizara ya Kilimo kule Siha kutusaidia kuhakikisha tunamaliza migogoro, lakini niseme kuna suala la KNCU. KNCU imekufa! KNCU haifai! Leo wanataka kuuza shamba la Gararagua shilingi bilioni 12; walipe shilingi bilioni nne CRDB, shilingi bilioni nane ziende KNCU. Kama wameua KNCU, unawapelekea shilingi bilioni nane za nini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali, hata kama basi Serikali haina, Hazina ilipe shilingi bilioni nne. Kama inaonekana uwekezaji huo ni mzuri, wananchi wapate ekari za kuwekeza kwa pamoja. Waziri Mkuu nakushukuru, nikikueleza unanielewa na nimekueleza sasa hivi, umenielewa vizuri. Niseme tu kwamba, kama kuwekeza, tumesema tuna vijana wa Vyuo Vikuu wanamaliza, tuwekeze hicho kilimo kinacholimwa na huyo Mzungu, tuwape mikopo halafu walime, Watanzania waendelee na hiyo shilingi bilioni nne isiende KNCU. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
MHE. DKT. GODWIN A. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsanteni sana, nawashukuru…
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kusema ili Taifa lolote liweze kuendelea linahitaji viti viwili vya msingi. Taifa linahitaji uchumi shirikishi na siasa shirikishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na uchumi shirikishi. Ili uweze kuwa na uchumi shirikishi katika nchi ni lazima kuwepo na motisha ya kufanya watu wako waweze kuwa wanatafakari kwa kina na kuwa wabunifu wazuri na kutengeza mifumo ambayo itakujenga uchumi wa nchi yao. Nitolee mfano wa Bill Gates wa Marekani ameweza kukaa chini na kugundua na kutengeneza fursa za kiuchumi kwenye eneo la computer na huko akawa tajiri na akatengeza uchumi wake na akatengeza ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchumi ambao siyo shirikishi ni ule uchumi ambapo anatokea fisadi mmoja mwenye fedha zake, anakamata nchi, anaenda kwenye eneo moja tuseme la mawasiliano, anakamata zile fursa, anazuia watu wengine kuingia kwenye hizo fursa anakuwa tajiri peke yake na anakamata mpaka Ikulu. Mojawapo ya uchumi usio shirikishi ni uchumi ambao mtu anaweza akaja akachukua ardhi ya Tanzania, akachukua hati, akaenda akakopa fedha na asiendeleze, akawazuia Watanzania kutumia ile ardhi na hakuna kitu chochote ambacho Watanzania wanakipata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana utasikia wenzangu wa upande wa pili wanalalamika sana ambao wameshindwa hata kutumia milioni 400, sielewi kwa nini tunahangaika na watu kama hao kusikiliza ushauri wao. Ndiyo maana Mheshimiwa Lema leo kwa mara ya kwanza pamoja na kujua migogoro ya ardhi iliyopo kwenye Mikoa ya Kilimanjaro na Arusha amesimama hapa anapinga watu kunyang’anywa ardhi na Wizara ya Ardhi. Anakataa kwa sababu anajua kwamba wanaotaka kumpeleka Hai kwenda kugombea Ubunge ni hao mafisadi ambao tayari Kilimanjaro wamepandishwa kama wahujumu uchumi. Hicho ndicho kinamfanya Mheshimiwa Lema leo aweweseke…

MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Lema nimeshazuia taarifa, nitakupa baadaye.

MHE. GODBLESS J. LEMA: Ajenge hoja, zuia matusi Mwenyekiti.

MWENYEKITI: Sasa unabishana na Kiti Mheshimiwa Lema?

MHE. GODBLESS J. LEMA: Zuia matusi Mwenyekiti.

MWENYEKITI: Dkt. Mollel wewe ni Daktari tunategemea utatoa mchango kwa kutumia lugha ya Kibunge.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Lema aliwatukana hapa Mawaziri.

MWENYEKITI: Wewe Jacqueline Msongozi kaa kimya. Endelea Mheshimwa Mollel. (Makofi)

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakusheshimu sana lakini tunajua kuna watu wanafadhiliwa kuingia kwenye siasa na watu wachafu na ndiyo tunawadhibiti. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Kama ulivyonunuliwa wewe.

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la siasa shirikishi ni kama kazi ambayo nchi yetu leo imefanya kuwa na Muswada ambao utafanya leo mwanamke wa Tanzania hii ijulikane ni mfumo gani utamfanya afike hapa Bungeni na siyo aletwe kutoka mfukoni mwa watu wachache. Leo tumepitisha Muswada ambao utafanya rasilimali za vyama vyetu, tuna vyama ambavyo akigombana Mwenyekiti na watu wengine hatujui mwisho wa siku mali ziko wapi. (Makofi)

WABUNGE FULANI: Ooooooooo.

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, hizo ndiyo siasa shirikishi tunazosema. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema kwamba tunaishi kwenye dunia ambayo ina rasilimali za kudumu na zinaisha. Ili nchi iweze kuendelea ni lazima sheria zote ambazo zinatungwa katika Taifa zielekeze kuzisimamia rasilimali hizo na kuziweka katika chain ambayo izitafanya ziwe endelevu. Katika kuwekeza kwenye rasilimali ambazo zina tabia ya kuisha, fedha ambazo zitapatika ni lazima ziwekezwe ili zikiisha basi pato la Taifa liweze kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitataja sehemu ambazo ni muhimu sana kuwekeza, kwanza, kuwekeza kwenye human capital kwa maana ya rasilimali watu na ndiyo ambacho Serikali inafanya inawekeza sana kwenye elimu. Pili, kuwekeza kwenye human made capital kwa maana ya miundombinu ndiyo maana unaona Serikali inawekeza kwenye Stiegler’s Gorge, treni, barabara, ndiyo kazi Serikali inafanya. Sehemu ya tatu ni kuwekeza kwenye innovation na technology, ugunduzi pamoja na teknolojia. Ugunduzi ninaozungumzia ni kuwekeza katika eneo litakalovumbua watu wenye uwezo wa kufikiri katika hali ya utupu, kukaa chini na kugundua. Leo Israel ni jagwa lakini kwa sababu watu wake wana uwezo wa kufikiri katika hali ya utupu, mimea inapewa dawa specifically siyo kurusha kama tunavyorusha sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tuna hizi rasilimali zinazohisha na tunataka kuwekeza huko tujue wenzetu katika mataifa mengine rasilimali zao zimekwisha. Wamefika mahali sasa wanatoka nje ya mataifa yao kwenda kutafuta maeneo ya kuwekeza ili waweze kuhakikisha usalama wa nchi yao kiuchumi. Ndiyo maana utakuta baadhi wanaweza kutumia vyama vya siasa au mtu mmoja mmoja kuvuruga baadhi ya mambo ambayo yanawazuia wao kuwekeza kwenye rasilimali za Taifa husika. Ndiyo maana utaona…

T A A R I F A

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, Selasini unajua vizuri ni yule rafiki yako wa pale Moshi ame-supply vitu substandard. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana sisi tulipokuwa upande ule wa Selasini, Selasini akituongoza kwa sababu walishaweka mkakati…

KUHUSU UTARATIBU

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, Paroko nimepokea hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipokuwa upande ule walianza na mkakati wa kuhakikisha wanazuia Serikali yetu isiwekeze kwenye maeneo haya ya kimkakati. Tukajipanga namna ya kuzuia na kukwamisha Serikali ili isiwekeze katika eneo hilo. Mwenzetu Mheshimiwa Tundu Lissu akaonyesha kuwa kinara wa kuzuia hilo, yakatokea mambo mawili. Jambo la kwanza ikaonekana kwamba anatengeneza umaarufu binafsi lakini ya pili kwa sababu ni watu ambao wamepanga kuuza hili Taifa wakatuma watu wakampiga Tundu Lissu na kumuumiza… (Makofi)

WABUNGE FULANI: Ooh, ooh.

KUHUSU UTARATIBU

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nipo tayari kuthibitisha. Namna ambayo nitathibitisha kwanza leo tu jioni hii nitatoka nje, isisemekane nimesema twende Mahakamani lakini CHADEMA waniletee matumizi yao yote ya ruzuku na hela wanazotoa nje wanatumia kufadhili nini? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa Daktari niliyewakilisha CHADEMA kwenye postmortem ya mabomu ya Arusha nilipotoka nikaiambia CHADEMA, Mheshimiwa Mbowe, Mheshimiwa Lema na Mheshimiwa Selasini walikuwepo ni Mkutano wa Kanda, kwa sababu kilio chetu tunasema hatuamini Serikali kwenye kuchunguza kuna vitu nimeviiba huko ndani twendeni tupeleke kwa Mkemia Mkuu wa Afrika Kusini walikataa, waseme kwa nini walikataa na walikuwa na ruzuku. Wanapinga suala la Mheshimiwa Tundu Lissu, Chacha Wangwe kilimtokea nini baada ya kutaka Uenyekiti? (Makofi)

T A A R I F A

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, anasahau kilio alichotoka kulia hapa Serikali isaidie, mimi nilikuwa kada mwaminifu, nikafanya kazi za chama lakini walinikwamisha wao, nikagundua kwamba wanajua kinachoendelea. Mnajua Mheshimiwa Zitto leo asingekuwa hai kwa kilichomtokea kama siyo Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi kumlinda. (Makofi)

T A A R I F A

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru aliyenijibu hapa ni mmojawapo wa wale waliokuwa wanatengeneza njama za kumng’oa Mbowe. Kwa hiyo, kuna uthibitisho dhahiri hapa kwamba huko kuna mafia wa kutosha. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaeleze tu…

T A A R I F A

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea taarifa kwa sababu tulikuwa pamoja na tulikimbia umafia kwa ajili ya nchi yetu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kulikuwa na plan namba moja ya kuzuia Serikali isifanye kazi, katikati ya plan namba moja Lissu akapigwa risasi ili kusisimua watu waivuruge Serikali yetu. Plan namba mbili ndiyo inaendelea Ulaya ambayo ni mwendelezo wa kufadhiliwa na wale watu wachafu. Mimi sisemi kuwa kuna nchi yoyote inafadhali ila ni watu wachafu ambao ni wezi wa rasilimali za kidunia. Tunataka kuwapa taarifa kuwa hakuna rasilimali ya Tanzania mtakayoweza kuipekea nje ilhali Watanzania wapo na leo tunawaambia ukweli. Tanzania haiuzwi kwa makubaliano ya ninyi kufika Ikulu, mkifika Ikulu mtasimamia nini? (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutambua na kuelewa vizuri ni namna gani ambavyo tunaweza tukaifikia Tanzania ya viwanda, lakini bila kusahau viongozi wa Wizara. Hata hivyo, napenda kuwakumbusha kwamba pamoja na kwamba kuna juhudi nzuri sana ambazo Wizara inafanya, lakini Rais anafanya tusipuuze sana malalamiko haya ambayo yanasemwa na Wabunge, lakini kuna mambo yanayotokea chini kwa watendaji ambayo tunatakiwa kukiri na kujaribu kuyafanyia kazi kama ambavyo Wizara ya Maji imekiri na ipo tayari kufuata chini ili kuweka mambo sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kusema kwamba tunajua kwamba ukisema unatengeneza kiwanda, huna namna ya kuwa na kiwanda wakati bei ya umeme ipo juu. Leo katika Tanzania hii umeme tunanunua unit kwa maana ya dola senti 10, lakini Uingereza ni 0.12 ya senti, maana yake huwezi ukajenga kiwanda cha nguo hapa Tanzania kwa umeme wa namna hiyo kwa standard ya nguo iliyotengenezwa Uingereza ukauza soko la nje. Kwa maana hiyo, hakuna namna yoyote mtu anaweza akawekeza kwenye kiwanda cha nguo ndani ya Tanzania. Rais wetu amelijua hilo, amewekeza kwenye Stiegler’s Gorge.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, utaona na watu wanasema Wizara hii ni Wizara mtambuka; uwekezaji unaofanyika kwenye Wizara ya Miundombinu, Wizara ya Afya na Wizara ya Elimu, yote mwisho wa siku unaenda kuonekana kwenye kuboresha hii Sera ya Viwanda na kuboresha kwenye eneo la viwanda. Kwa mfano, ukienda kwenye afya tunaposema tunaboresha afya na kupeleka hela kwenye afya, maana yake tunaenda kuboresha siyo afya tu kwa maana ya watu kutibiwa lakini tunaenda kuwaboreshea huduma akinamama na mwisho wa siku watazaliwa watoto wazuri tutafanya lishe, tutaendelea na tutapata watoto wenye akili nzuri kwa sababu kwenye viwanda siyo tu suala linalosaidia viwanda ni kwamba kuleta teknolojia kutoka nje, innovation na ugunduzi ni vitu ambavyo vinasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, utakuta leo SIDO yetu wana-copy vitu kutoka nje lakini hawawezi kwenda zaidi ya hiyo ku-copy kutoka nje. Rais anapowekeza kwenye eneo la afya maana yake generation inayokuja mbele tutaweza pamoja na ku-copy lakini na sisi tutaweza kugundua na tutaweza ku-compete kwenye soko la uwekezaji na ugunduzi na hasa viwanda sasa vitaanza kuonekana vina tija kwenye Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kwenye elimu; leo kwenye elimu tunawekeza kwenye VETA. Leo tumeambiwa tunajenga Vyuo vya VETA zaidi ya 26 mwaka huu, hii maana yake ni input ya Serikali kwenye kuwekeza kwenye viwanda, mwisho wa siku zile pesa zilizokwenda kule zinarudi kuingia kwenye viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile utaona watu wanazungumzia bandari; mimi niseme kwamba Rais Kikwete yupo vizuri sana, alianza huo mradi lakini akaona kidogo kuna shida akasema Morogoro walisema mimi ni mpole mpole lakini naenda kuwaletea chuma, mkali zaidi na mzalendo. Ametuletea mwisho wa siku akamkabidhi faili akamwambia hebu chunguza vizuri hata Stiegler’s Gorge akamkabidhi yote. Rais akaangalia akahakikisha uwekezaji utakaowekezwa kwenye Stiegler’s una manufaa kwa Taifa akaupitisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, akaenda Bagamoyo akaangalia akasema hatuna bandari ambayo tunaiuza Tanzania, tuna bandari ambayo tunataka kuwekeza. Akapiga breki yule mzalendo akasema ngoja nitulie niweke na wakati huo akichukua ushauri kutoka Spika na watu wengine namna nzuri ambayo tutawekeza kwenye bandari zetu zote kuanzia Mtwara mpaka Bagamoyo na tutaelekea mpaka Tanga na hatutaki mtu atakayekuja ku-dictate terms hapa ni namna gani tunaendesha hili Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilihama nikaja upande huu na kauli mbiu yangu ya kwanza nilisema naenda kuungana na wazalendo ambao watalinda rasilimali za Taifa hili. Tumekuja kuungana na mtu ambaye ningekuwa ni profesa wa chuo kikuu, Rais Dkt. John Pombe Magufuli ningempa Ph.D ya heshima ya sheria ya kuwa profesa wa uchumi na uongozi. Ameanzisha mambo mengi, wengi walikuja hapa wakifikiri haiwezekani, imethibitika inawezekana; Dodoma leo tupo hapa na jiji linakua. Ameanzisha Stiegler’s, watu waliogopa na inaenda, na amesoma chemistry lakini amefanya mambo ya uchumi ya kustaajabisha, ndiyo maana mimi leo nasema nashukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata ukiangalia China, China ambayo leo imeendelea vizuri, kabla ya kufungua mipaka kuingia kwenye foreign direct investment walifunga mipaka wakajihakikishia kwamba wana nguvu ya kutosha ya negotiation na wana nguvu ya ndani, ndipo sasa wakafungua mipaka na wanaenda kizalendo na ndiyo maana leo Marekani na China wanabishiana kwenye masuala ya biashara na… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza Waziri, lakini zaidi niwapongeze wananchi wa Nzega kwa kutuletea jembe. Nimpe Waziri salamu zake kwa wale ambao tulijipanga Muhimbili kumchagua akawa Rais wetu wamemwambia kwamba, hawakukosea walijua yeye ni kichwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu, naenda kutumia kigwanomics naomba Mheshimiwa Waziri anisikilize vizuri sana. Wilaya ya Siha ni wilaya pekee Tanzania ambayo iko katikati ya milima miwili mikubwa na Wilaya ya Siha tulishajipanga kwenye cable cars zile za kupanda kwenye milima na tulitenga eka 800 kwa ajili ya kufanya shughuli mbalimbali pamoja na hizo cable cars na mambo ya utalii. Tayari tumeshawakabidhi TANTRADE eka 200 zimebaki 600, aje kwetu Siha uchukue eka 600 ili tuweze kujipanga na ni mkakati mzuri kwa sababu, tukifikiria kutengeneza cable cars tukaanza kuitafakari Wilaya ya Hai, Wilaya ya Siha, tukiangalia vizuri tunaweza kupanga hizo cable cars ninaamini ni kitu ambacho kita-boost sana kuongeza pato la Wizara ya Maliasili.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba, Wilaya ya Siha iko katikati ya milima mizuri miwili, lakini imezungukwa, utakuta huku kuna Mlima Meru ambao kuna hifadhi, lakini kwa Kaskazini kwake kuna corridor ambayo wanyama wanapita kutokea huku upande wa Meru na kwingine Tarangire kuelekea upande wa Kenya. Maana yake ni utalii, lakini kunakuwepo na ule wakati wa kupanda Mlima Meru, ukipanda Mlima Kilimanjaro sio tu unapanda moja kwa moja kwenda Mlima Meru ukipitia Siha, unapanda Mlima Meru, lakini Mlima Kilimanjaro wakati unapanda Mlima Kilimanjaro unakutana na hifadhi na unakutana na wanyama, wanyama ni wengi sana. Maana yake tukiwekeza kwenye hizi cables wakati wanapanda Mlima Kilimanjaro lakini chini yake watakuwa wana-enjoy sana kuona wanyama wakiwa chini wanapoendelea. Kwa hiyo, kwa sababu sisi tulishachora mpaka michoro ya hoteli na hizo cables, namwomba Waziri atembelee Wilaya ya Siha ili aweze kuona. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Siha vilevile ukiangalia tuna mlima unaitwa Donyomorwak ambao ni sehemu ya kuhiji Wamasai Tanzania nzima. Pale kuna heka zaidi ya 3,500 ambayo sasa hivi wameshikiria Polisi CCP. Kwa kushirikiana na polisi na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Idara ya Mambo ya Kale tunaweza pale tukatunza ule utamaduni wa Kimasai tukafanya cultural tourism kwenye ule mlima. Kila baada ya miaka saba Wamasai East Africa wanakutana pale. Tutaweka kwa ajili ya kutunza zile, tukatoa kama heka 500, heka 500 zile zikasaidia kupunguza makazi na shida za wananchi na zile heka zinazobaki tukawekeza ikasaidia Wizara ya Mambo ya Ndani kwa pato lakini ikasaidia maliasili pamoja na vitu vingine. Kwa hiyo, mimi nasema hiyo tukifanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pale Kilimanjaro tuna Uwanja wa Memorial lakini tuna CCP wana eneo kubwa sana; tunaweza tukajenga uwanja wa kimataifa wa mpira pale, Manchester United wakaja kucheza pale lakini wakafanya utalii wa kupanda mlima. Kwa hiyo ndiyo maana leo nikakwambia natumia Kigwanomics ili unisikilize uunganishe hivyo vitu ili twende pamoja tukatengeneze fursa, maana watu wengi wamekuwa wakizungumza yaliyokuwepo na yaboreshweje, twendeni tukaanzishe mapya ambayo yanaweza kutusaidia kuongeza fursa kwenye utalii wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini dada yangu Mheshimiwa Sware ameongea vizuri kuhusu viwanda vya mazao ya miti. Mimi nafikiri ameongelea vizuri viwanda vya mazao ya miti, tuna nchi nyingi sana ambazo zimeingia vitani sasa hivi zinajengwa upya; lakini tukiwekeza vizuri kwenye mazao ya miti na kutafuta masoko nje na kuboresha hivi viwanda vya miti, tutatengeneza sana fursa mpya kwa watu wetu na kutafuta masoko nje na kwa sababu leo tunazungumzia utakuta wanaajiri watu wengi sana, saw-dust nyingi kuna watu wanakuja kuchukua bure tu kwenye maeneo yetu ambayo kuna hivi viwanda vidogo vidogo vya mazao ya miti. Tunaweza tukawekeza pale na tukaleta teknolojia na tukauza mambo mengi sana, nagongea tu vizuri alichokisema Dkt. Sware.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kusema tena, rafiki yangu Mheshimiwa Ruge amezungumzia kitu pale na akataka kulinganisha sayansi kubwa inayoendelea Stiegler’s Gorge na Song of Lawino. Pale Stiegler’s inaendelea sayansi kubwa sana ya ikolojia pamoja na nishati, huwezi kulinganisha kabisa na Song of Lawino. Kinachogomba kwenye taifa letu hapa si suala la kupata tu nishati, kinachogomba kwenye taifa letu ni kupata nishati ambayo ni bei rahisi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huwezi ukalinganisha gharama ya thermo energy (umeme wa jotoardhi) na umeme ambao tutazalisha pale ambapo pamekuwepo. Hapa kwetu viwanda vinashindwa kuja kwa sababu gharama ya umeme ni kubwa, hilo ndilo swali kuu ambalo watu wote tunatakiwa kujibu ndiyo maana mtaelewa kwa nini tukakimbia kule, tumekimbia kule kwa sababu kambi ilikuwa imeshauzwa na imenunuliwa na watu kutoka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niseme hivi George Hartman ni nani anyway? Tanzania tunasema tunaenda kuwekeza kwenye umeme, umeme rahisi utakao-bust viwanda ndani ya Tanzania hii halafu anatokea mtu anaitwa George Hartman anakuja mtu amevaa suti nzuri amependeza kwa pesa za kodi ya Watanzania, anapinga vitu ambavyo vitaboresha kodi ya Watanzania, anakuja kuzungumza mambo ya Hartman hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tunasema watu wamechanganyikiwa, tukisema tunaenda kwenye kamati; tunataka tuende hiyo kamati mpelekeni kwenye hiyo kamati achunguzwe na tuanze sasa kujua wasaliti wa taifa hili. Hatutaki mtu ukiwa Mbunge hapa, ukija hapa Bungeni kama unazungumzia masuala ya kitaifa na yale ya msingi usituletee idea za watu wenye interest na vita vya kiuchumi kwa ajili ya taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi hili Taifa litakwenda kulindwa, mambo ya Hartman, huyu Hartman ndugu yake huko miaka 1800 aliwahi kuandika kitabu kuhusu Stiegler’s Gorge, akasema this is the cornerstone of development ya hiyo nchi yake wakati huo East Africa yaani huyo huyo babu yake alisema wakiwekeza Stiegler’s Gorge itakuwa cornerstone ya maendeleo ya Taifa lao wakati ule kutokea East Africa.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo unatokea na ki- proposal cha mtoto sijui anaitwa Hartman thesis yake ya chuo kikuu unakuja kutuambia hapa Bungeni tukae tukusikilize, haiwezekani. Sisi tunachosema Tanzania iende kujengwa, tunataka vijana wazuri madaktari wenye akili nzuri kama Kigwangala, tunataka waende kuchapa kazi tukija hapa wakifanya kazi nzuri tunawaambia tumefanya kazi nzuri, wakikosea tunawaelekeza vizuri kwa sababu lengo ni kujenga Taifa hili. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi leo siongei sana, nilikuwa nataka kusema hao, nimeshaongea na madalali wa siasa, asante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Wanataaluma wa Kemia wa Mwaka 2016
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Kwa sababu nime-move schedule of amendment naomba nijikite zaidi katika utekelezaji wa sheria yenyewe ambayo tunaenda kuiunda.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuunda hii sheria na tukaipata ni hatua moja, lakini vilevile tunaweza tukaenda kwenye hatua nyingine ya kuhakikisha tuna infrastructure ambazo zitawasaidia wataalam kutekeleza sheria yenyewe. Ukiangalia kwenye maabara yetu ya Mkemia Mkuu tunazungumzia kuweka vifaa vya kisasa na infrastructure, lakini ukienda Mbeya utawakuta wako kwenye chumba ndani ya Regional Hospital, Arusha kuna umaliziaji wa jengo, kweli kuna jengo zuri lakini inahitajika limaliziwe, lakini pia inatakiwa tuzigeuze zile center zetu ambazo ziko huko mikoani badala ya kuwa ni sehemu ya kukusanya tu sample iwe pia ni sehemu ambayo wanaweza wakafanya kazi yenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutekeleza yote hayo unaweza ukaweka infrastructure, ukienda Muhimbili Mloganzila utaona wametenga eneo zuri kwa ajili ya pharmaceutical industry ambapo tukizingatia hilo tutapata sehemu ambapo tutajenga kiwanda cha dawa na kitatusaidia kufundisha wataalam wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tukishaweka hizo structure zote kuna suala linalokuja kwamba, je, kweli tuna brain ambazo zinaweza kufikiri katika hiyo level ambapo tunazungumzia masuala ya DNA? Kwa hiyo, ni lazima kama Taifa tufikirie tunatengenezaje kizazi ambacho kina uwezo wa kufikiri kama waliogundua DNA. Pia tuwe na uwezo wa kufikiria kama wale waliogundua vifaa ambavyo tunavitumia. Kwa sababu hata mfagizi wa maabara akikaa kwa muda mrefu na wataalam suala la kupima anaweza akajifunza na akapima na akatoa majibu sahihi, lakini la msingi, je, tuna brain kubwa za kuweza kufikiri katika hali ya utupu yaani kufika mahali pa kuona hayo mambo makubwa sasa (intelligent quotient).
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzetu kwenye maabara kama hizi kama Marekani sasa hivi wanasema kwa miaka 10 ijayo wanatengeneza namna fulani ambapo baba na mama wanaweza wakakutana wakatumia genetic engineering technology waka-boost intelligence quotient ya watoto na sisi Wabunge utakuta tunaenda huko Marekani ili tuzae watoto wenye uwezo mkubwa wa kufikiri.
Vilevile wanasema wanafanya research kwa kutumia hii hii genetic engineering kuhakikisha kwamba wana uwezo wa kuwa na technology ya ku-boost adult intelligent quotient ambayo hiyo ikitokea nitashauri Wabunge twende na sisi ili itu-boost tufike mahali kwenye mambo ya Kitaifa tuwe kitu kimoja. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kwa sababu na mimi baadaye nita-move schedule of amendment, leo sisi UKIMWI tunaona ni janga na kweli ni janga lakini is a business opportunity. Tungekuwa na brain kubwa tunaweza tukakaa chini tukajifungia kwenye maabara kama hizi wakati Marekani wanatafuta dawa na sisi tunatafuta dawa. Tukipata sisi na tukaweza kupata hakimiliki ya hiyo technology na kutumia Usalama wa Taifa na jeshi letu kuficha hiyo siri tunaweza na sisi tukauza hiyo technology na ikawa ni moja ya chanzo cha mapato katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzetu Wazungu wameendelea na wamefika walipo siyo kwa sababu wana rasilimali nyingi, ni kwa sababu wana siri za kimaumbile ambazo ndizo wanazitumia kutuburuza kama wanavyotaka. Leo tunaongea hapa Bungeni wanaweza wakawa na uwezo wa kujua tunachokifanya, lakini vyote vinapatikana kwenye maabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nasema tunakwenda kutunga sheria hapa na nime-move schedule of amemdment baadaye nitakuja kwenye hilo lakini nachokisema ni kwamba kuwa na sheria, maabara nzuri na kila kitu ni jambo moja, lakini la msingi zaidi do you have brains? Naambiwa hapa nenda kwenye muswada, nikienda kwenye muswada kidogo, nisingependa sana niende kwenye muswada kwa sababu nita-move schedules of amendment, hii Ofisi ya Mkemia Mkuu iweze kupata funding kama linavyopata Bunge ambazo haziingiliwi. Ofisi hii iwe na power kubwa ya kufanya research, research kubwa kama hizi zinatakiwa watu waliotulia akili lakini tutayarishe watoto wetu toka wakiwa tumboni (nutrition).
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana Musukuma alivyosema hapa kuhusu suala la mahindi na kilimo nilimuelewa sana na alivyokuwa anasema tulime bangi nilimuelewa sana, kwa sababu leo kama watu wetu wanalima mazao mengi ya chakula wanakosa soko na wanazuiliwa kuuza nje maana yake wakulima wetu watakata tamaa ya kulima na kiwango cha lishe kitashuka kwenye Taifa letu. Impact yake kubwa ni kwamba lishe ya watoto wetu itashuka na udumavu utaongezeka. Udumavu ukiongezeka tunapozungumzia kwenda kuwa na kizazi chenye uwezo wa kufikiri katika level ya higher mind hatuwezi kukipata kwa sababu udumavu umezidi katika nchi yetu. Ndiyo maana nasema kwamba pamoja na hayo yote ambayo tunayafanya hapa na tuta-move schedules of amendments, let us think of making a generation yenye brain kubwa inayoweza kufikiri kwa kiwango kikubwa. Kwa sababu kuwa daktari ni kitu kimoja lakini kuwa na uwezo wa kufikiri katika hali ya utupu ni kitu kingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzetu wana uwezo wa kutoka kwenye huu ubongo wa kawaida wanaenda kwenye siri za kimaumbile wanarudi wanaleta vitu vilivyo kwenye siri ya kimaumbile kwenye ubongo wa kawaida wanaviandika vinakuwa teknolojia wanatuuzia. Wakati mwingine wanaleta solutions za tiba kwa sababu wametayarishwa toka wakiwa wadogo tumboni kwa mama zao kwa lishe kubwa na vitu vingine na tunatapata generation inayoweza kufanya vizuri. La sivyo, tutaunda maabara mwisho wa siku tutakuwa na watu ambao kazi yao ni kukusanya sample, kupima, wazungu wanakuja wanachukua sample zetu wanatazama kwa kutumia high mind wanagundua vitu, wanatugeuza soko la teknolojia, soko la vifaa tiba, soko la kila kitu kwa sababu uwezo wa kufikiri katika hali ya juu hatuna. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nizungumzie kwa namna hiyo na naamini Profesa ananielewa vizuri ninapozungumzia kufikiri katika hali ya juu. Naomba niseme suala hilo ni la msingi sana, Waziri nakujua ni msikivu naomba iandike na tufikirie tutaunganishaje Wizara zote. Ulaya wamefika hapa walipo kwa sababu wanasema kuna mtu mmoja anaitwa Pilato alikuwa anatembea kwa kuangalia jua lakini alichokifanya baadaye akaanzisha Chuo Kikuu cha Hesabu na hesabu ina tabia ya kujaza misuli ya ubongo kama unavyobeba chuma na ndiyo hapo akagundua teknolojia, watu wakasoma pale wakaacha falsafa wakaanza kugundua na ndipo Ulaya ikaenda juu. Leo Tanzania unaambiwa hesabu huwa ni somo la kawaida ambalo watoto wanafeli. Ukishasema hesabu na sayansi ni kawaida watoto kufeli Taifa hilo limekufa kiroho na kiakili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunatakiwa turudi huko tufikiri tunapataje hawa watoto. Wakati mwingine tunampa Mheshimiwa Ndalichako watoto ambao wamedumaa hata wawachape kwa umeme hawataelewa. Kuanzia leo turudi kwenye kufikiria tunawatengenezaje watoto ili baadaye tupate Bunge ambalo halibishani, linatumia muda mwingi kufikiri mambo ya kitaifa na kawaida ya akili kubwa inapofika mambo ya msingi ukweli ni mmoja wanakwenda wakitofautiana mwisho wa siku wanakutana pale juu wanakubaliana, ndiyo sifa za akili kubwa. Hizo ndizo akili tunazozitaka na tuzitayarishe leo ili miaka 20 ijayo tuwe na Taifa na Bunge zuri ambalo linazungumza masuala mazito ya kitaifa. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Madaktari, Madaktari wa Meno na Wataalam wa Afya Shirikishi wa Mwaka 2016
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze tu kwa kumwambia Dada yangu Mheshimiwa Waziri Ummy Mwalimu kwamba hongera sana kwa kukubali marekebisho mengi ambayo tulikuwa tumependekeza kama Kambi ya Upinzani na wadau mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kusisitiza kwamba shida katika hii nchi siyo kutokuwepo na sheria, miongozo na vitu vingine, shida katika nchi hii ukienda kwenye afya ni kutokupatikana kwa dawa, kutokuwepo kwa vifaa tiba, lakini kuwepo na tofauti kubwa sana ya upatikanaji wa dawa kwenye vituo binafsi na vituo vya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kikubwa kinachotusikitisha sisi wengine ni kwamba unapokwenda kwenye kituo cha mtu binafsi ni vigumu sana kukutana na tatizo la upatikanaji wa dawa, lakini ukienda kwenye vituo vya Serikali, asilimia 70 ya dawa ambazo utazihitaji utazikosa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli uliokuwepo kwamba dawa ambazo ziko kwenye mwongozo wa Serikali, ile catalogue ya MSD inayoonesha kwamba essential medicines ni hizi hapa ni dawa ambazo kimsingi zinahitaji ziangaliwe upya ili ziweze kukabiliana na changamoto za sasa.

Kwa hiyo, kwa kiasi kikubwa hata kama zile dawa ambazo zimeandikwa kwenye utaratibu na ziko kwenye kitabu cha MSD ambazo ndizo Serikali inatakiwa ipeleke kwenye vituo vyetu hata zikiwepo kwa asilimia 90, ni kweli tu kwamba madaktari wanapokutana na changamoto za ugonjwa kule vituoni, wanapoamua kuandika hizo dawa, wanakuta zilizoko ndani ya Serikali dawa hizo hazifai, zilizoko nje ambazo hazijaingizwa kwenye catalogue ile ya Serikali ya MSD ndiyo zinazofaa. Maana yake hilo linaongeza zaidi tatizo la upatikanaji wa dawa kwa upande wa vituo vya afya Serikali, ambapo wakienda kwenye vituo vya binafsi dawa hizo zinapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni changamoto tu tujiulize kwamba, kama kweli Serikali ndiyo ina nguvu zaidi na ndiyo ina network kubwa ya kutafuta dawa na vitu vingine katika viwanda mbalimbali duniani, swali la msingi ambalo tunapenda siku zote tujiulize ni kwa nini vituo na watu binafsi wanakuwa na dawa zile ambazo Serikali hata ufanye nini huwezi kukutana nazo. Ni kitu ambacho Mheshimiwa Waziri utusaidie kulitafakari vizuri sana kama ulivyotafakari muswada huu na kukubali maoni ya wadau mbalimbali pamoja na maoni ya Kambi ya Upinzani na tutafute suluhisho la kudumu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata leo ukienda kwenye hospitali za Mkoa za Serikali, ukichukua hospitali yenye level hiyo ya kanisa au ya private utakuta ukiangalia tu mapato yao kwa bima utakuta Serikali inapata kidogo kuliko inavyopata mapato ya bima hivi vyombo binafsi. Wakati mwingine tunaangalia kwa hizi CDH na DDH, unakuja kukuta gharama za malipo ya bima imekaribia sawa na Serikali lakini wale wanafanya kazi nzuri kuliko Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa tunakuja kwenye kusema kuna umuhimu sana, utakuja kugundua kuna umuhimu sana shida yetu kama Serikali vifaatiba hatuna, hatuna vitendea kazi. Wagonjwa wengi wanaondoka kwa sababu vifaatiba hatuna. Tukiwekeza kwenye teknolojia ya afya vya kutosha, kwanza moja Serikali inaona gharama kununua vifaatiba vile vya gharama kwa ajili ya kusaidia Watanzania, nataka kuwaambia asilimia kubwa ya Watanzania wanaopelekwa nje kwenda kutibiwa wengi hawafuati kwenda kutafuta brain kule, wanaenda kwa sababu hamna vifaatiba vya kuweza kutambua tatizo walilonalo hapa nchini ndicho wanachokifanya.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo Serikali ikijiwekeza kwenye kununua vifaatiba na kuweka, asilimia zaidi ya 99 ya wagonjwa watakaokuwa wanaenda nje hawataenda tena kwa sababu uchunguzi wao na kutambua ugonjwa na matatizo yanayowasumbua inawezekana kufanyika hapa Tanzania. Hata kama tukiwa hatuna wataalam wa ugonjwa husika ndani ya Tanzania ni rahisi kumlipia daktari kutoka Marekani au kutoka India ndege kuja Tanzania kutumia vifaatiba vilivyoko Tanzania kumtibu mgonjwa na akarudi kwenda India kuliko kukusanya wagonjwa na kuwapeleka India au Marekani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ukijaribu kuangalia gharama ambayo tunatumia kwenda nje na gharama ambayo tungenunua vifaatiba tukawa salama na tukahakikisha kila mtu anapata fursa ya kutibiwa, ukiangalia ni gharama kubwa zaidi kupeleka watu nje kuliko kununua vifaa husika. Mheshimiwa Waziri naomba unisikilize kwenye eneo hili sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua kwamba huduma ya afya ni gharama sana na ni ngumu sana kwa Serikali kugharamia kwa namna hii ambayo tunaifanya sasa, tumeanzisha bima aina mbalimbali, sijui kuna NHIF, CHF na bima nyingine lakini hazitakaa zitatue tatizo la afya katika nchi hii. Ni lazima tufikirie namna ya kuboresha bima yetu na kila Mtanzania apate bima ya afya kama hii ambayo Wabunge tunapata, walimu na wafanyakazi wengine wanapata. Tunafanyaje? Ni rahisi sana kwa sababu kama tutakuwa na uadilifu wa kutosha tukaingiza hicho kipengele kwa calculation zisizosababisha mfumuko wa bei na uharibifu wa uchumi tukaingiza kwenye VAT na kila Mtanzania wanaonunua kwa siku, wanaouza kwa siku na wanaougua, wanaouza na kununua ni wengi kuliko wanaougua. Tukiendesha kwa namna hiyo, kwa namna nyingine Serikali itajiondoa kwenye uendeshaji wa kila siku wa huduma za afya, Serikali itajikita kwenye miundombinu mikubwa kwa ajili ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tutakuwa na bima ya afya kwa kila Mtanzania na watu wote maana yake bima itakuwa na nguvu na kodi itapelekwa vizuri bila kuvurugwa ikapelekwa bima. Tutakuwa na Shirika la Bima lenye nguvu sana. Tunapokuwa na Shirika la Bima lenye nguvu sana Waganga Wafawidhi wa hospitali za Serikali wataweza kuendesha hospitali zetu kwa mambo ya kila siku kutumia mapato ya ndani yanayotokana na bima. Serikali itaendelea kujenga majengo na miundombinu na vifaa vikubwa na miundombinu hiyo ukiiweka mara moja umeshaweka na hata gharama ya uendeshaji wa afya katika nchi utakuwa umepugua sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ni aibu sana Askofu akawa na hospitali inayofanya kazi vizuri na kwa ufanisi na upatikanaji wa dawa vizuri na kuwepo na vifaatiba vya kutosha kuliko Serikali yetu ya Tanzania. Mbinu ambazo Askofu anazitumia, hata kama anapata misaada nje, Serikali ina meza ya majadiliano ya kutafuta misaada zaidi kuliko kanisa. Kwa hiyo, ni wakati muafaka wa kuunganisha nguvu na kufikiria ni namna gani tunapatia muarobaini upatikanaji wa huduma za afya katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kusema kwamba ili tuboreshe afya, leo nataka kukuhakikishia ikitokea ugonjwa ambao haujulikani tukaita madaktari wote wa Afrika kuna uwezekano mkubwa nao wakaishia kuugua huo
ugonjwa. Ni mpaka ashuke mzungu kutoka Ulaya anakuja anatuambia ugonjwa huu ni nini. Maana yake ni kwamba tunaendelea kusisitiza kwamba ili tuboreshe afya na tuwe na uhakika wa afya na maendeleo endelevu katika hii nchi, uwekezaji katika utafiti, afya na sekta zingine ni muhimu sana. Hatuwezi tukazungumzia leo nchi hii ni salama na ina Jeshi la Ulinzi la kutosha linaloweza kulinda wakati tunategemea teknolojia kutoka kwa wenzetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia ulinzi na usalama tunazungumzia ulinzi na usalama kuanzia biological weapon na vitu vingine na vyote hivyo ni sayansi. Tuwekeze katika sayansi, tukiwekeza tutalijenga Taifa letu. Ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2018
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kusoma kulingana na maandiko Matakatifu sifa za mtu maskini. Sifa za mtu maskini akili yake inaona matatizo tu na haioni fursa, uwezekano wala kufanikiwa, lakini hujaa masononeko na lawama siku zote huzungumza ugumu wa maisha hiyo ni Mithali 23:7 na ile ya kwanza ni Marko 9:23. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuchangia kwa kwenda kwenye ile Sehemu ya Nne, Sura ya 203 kwenye zao ambalo limezungumziwa, lakini nizungumzie kwanza historia, ukiangalia huku nyuma kwenye zao la korosho kabla ya bodi ambayo inapigiwa kelele sasa haijaanzishwa wakati huo zao la korosho asilimia 40 ilikuwa inabanguliwa ndani ya Tanzania, lakini wakati ule kulikuwa na viwanda vinne vya kubangua korosho ndani ya Tanzania. Pamoja na matatizo yake yote ilikuja hiki ambacho nacho kilikuwa na nia nzuri na kikafanyika lakini kwa muda wake ule wote vile viwanda vinne vyote vilikufa lakini vilevile sasa India ndio inatajwa kuwa ndio nchi ya kwanza kwa kuuza korosho duniani.

Mheshimiwa Spika, lakini asilimia 83 ya korosho yote ambayo inauza ni inatoka Tanzania, Marekani inauza tano, nafikiri Uarabuni huko nne, Kenya mbili, maana yake ni nini lakini ukiangalia sasa asilimia 90…

T A A R I F A . . .

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nakushukuru umenisaidia na sitamjibu nilikuwa na jibu dogo lakini sitamjibu.

Mheshimiwa Spika, lakini hali ilivyo kwa sasa maana yake asilimia 95 ya korosho inaenda nje na maana yake huko nyuma tulikuwa tunabangua wenyewe asilimia 40. Hata hivyo, twende kwanza kwenye bei ya korosho maana yake kwa taarifa tunazozipata tunaambiwa ni Sh.3,800 tuseme ni Sh.4000, lakini ukibangua wanauza kwa kilo dola 35. Maana yake korosho ambazo hazijabanguliwa kilo mbili zinatoa kilo moja maana yake wao wanauza kilo moja iliyobanguliwa kwa Sh.39,000.

Mheshimiwa Spika, maana yake nini fedha zinazotuletea mgogoro hapa na mvutano ni asilimia ndogo ya Sh.4000, maana yake tunapoteza zaidi ya Sh.35,000. Kwa hiyo, ukiangalia Bodi iliyoko sasa, hatukai kabisa kwamba wamefanya kazi nzuri sana ya kuhakikisha mikoa mingine imepata korosho na mashamba mengine makubwa yameanzishwa na idadi ya tani ya korosho zimezalishwa.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, ukiangalia kwa maana ya biashara per se na faida tunakoelekea kwenye sera ya viwanda na kama kweli tunataka tufike mahali na sisi tumiliki uchumi wa nchi yetu maana yake ni kwamba sisi tumegeuka ni shamba la watu wengine kufanya biashara ya korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndio maana nasema ni lazima tuunge Muswada huu mkono kwa sababu unaenda kuiondoa Tanzania kuwa shamba la korosho na kuwa wazalishaji wa korosho na kuuza na sisi korosho duniani ili tuweze kupata mapato halali. Niwaambie kwamba kuna watu nashindwa kuelewa, hata tukifikiria kwa mfano Daraja la Mkapa limejengwa sio na pesa ya korosho, limejengwa na pesa ya Mlima Kilimanjaro, ya Ngorongoro na pesa ya madini huko Mwanza.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo watu tunataka utusaidie, tufike mahali tunapoingia kwenye mijadala kwenye Bunge hili, tuhakikishe kitu cha kwanza kinachokuwa kwenye kichwa cha mtu kuunga na kuhakikisha unapomaliza kuzungumza na kukaa chini unaliacha Taifa letu likiwa pamoja na tukifikiri pamoja kwa ajili ya kuijenga nchi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niseme kwamba Muswada huu tunauunga mkono na tunaunga thabiti kabisa na tunasema mawazo ya kusema tunaiendeleza korosho ni mawazo mazuri, lakini sheria iliyobadilika sasa haiendi kumnyang’anya mkulima wa korosho haki yake ya kupata pato lake. Sheria hii inaenda kuondoa watu wa kati ambao tukitafuta wawekezaji wa kuwekeza viwanda ndani ya Watanzania wanapigwa vita mpaka wanakimbia.

Mheshimiwa Spika, sasa hii sheria itaenda kuwalinda kitakachotokea hapa yatatokea viwanda kwa ajili ya korosho ndani ya Tanzania. Pia tutaanza kupata mapato ya kutosha na hela nyingi zitapatikana zaidi kwa ajili ya kwenda kumsaidia mkulima wa korosho na kusaidia ukuaji wa korosho kwenye maeneo mengine katika Taifa hili lakini vilevile kusaidia mazao mengine ya mkakati kwa ajili ya Taifa letu la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hicho ndicho kikubwa, hata hivyo, nashauri tutafakari zaidi pamoja na tunazungumzia hili zao la korosho, lakini tunazungumzia mazao mengine. Nitoe mfano mmoja wa zao la parachichi au matunda. Ukiangalia utaambiwa mara nyingi sehemu nyingi ambao wanalima matunda hayo tukichukulia mfano Wilaya yangu ya Siha wanalima parachichi unaambiwa wamepewa EPZ.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia EPZ waliyopewa unauliza kwa sababu wanafanya process nauliza definition ya process ni nini? Naambiwa sasa kwa maparachichi utakuta mtu anachukua parachichi anafanya sorting, anachagua kubwa na dogo linalofaa, halafu anafanya serialization, halafu anapaki, tayari amepewa exemption, anaambiwa aende, afanye process.

Mheshimiwa Spika, hapa nilitegemea kwamba, kama ni kufanya process ina maana angezalisha kile ambacho kinatokana na mazao ya parachichi ili kama tunakosa kodi kwingine, basi tuhakikishe tunapata kwa kuwaajiri watu wetu na mambo mengine ambayo yatatokea. lakini bahati mbaya anaenda an afanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tumeangalia korosho tumeangalia na mazao mengine, twendeni tuingie ndani kwa sababu inawezekana definition niliyopewa na mtumishi mmoja wa Wizara ya viwanda inawezekana definition ya halali. Tuangalie hizi definition tunazofundishwa kwenye semina, wakati mwingine zimeficha vita vya kiuchumi ndani yake ili kuendelea kutunyonya ili kuhakikisha kwamba pamoja na kwamba sasa tunataka kuwa Taifa linalojitegemea watu wanakuja kwa kutumia hizi semina, kutumia uwezeshaji, tunapewa definition ambayo unajiuza mwenyewe bila kujijua na ukijiita mtalaam. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile kwa sababu sasa tunaenda kuunda sheria hii, naomba mtu yoyote atakayepewa leseni basi apewe sheria na utaratibu kabisa na kusimamiwa ndani ya miaka mtatu awe amewekeza kiwanda kwa ajili ya kubangua korosho na asipofanya hivyo basi anyang’anywe leseni na apewe mtu mwingine.

Mheshimiwa Spika, tuache wasiwasi wa kufikiri kwamba tutakosa wawekezaji na watu wa kuweza kununua korosho. Watu wengi wanahitaji kununua korosho, kinachotakiwa ni kuzingatia maneno ya Biblia ya kujiamini na kuamini kwamba tunaweza na wote kwa pamoja Bunge hili tuanze kuungana, tuamini kwamba Shida yetu ni Tanzania, shida yetu sio vyama vyetu tunafika tunaendaje Ikulu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa muda mwingi tunaiua nchi yetu sisi wakati tukigombea madaraka tukifikiria ni namna gani natoka, ni namna gani chama changu kitakuwa. Hapa tunachokisimamia ni Taifa letu la Tanzania twendeni tutulize akili, hili Bunge sasa ligeuke ni tanuru la tafakuru kwa ajili ya Watanzania.

Mheshimiwa Spika, tulipoletwa kutoka majimbo yetu hatukuletwa kuja kujenga vyama vyetu huku ndani, tumeletwa kuja kumsaidia Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwenye dhamira yake ya kufanya ukombozi wa pili wa Mtanzania kiuchumi kwa sababu tulichokuwa tunakitafuta hatukutafuta uhuru wa bendera, tulihitaji uhuru wa bendera lakini rasilimali za Taifa hili tuanze kuzimiliki sasa sisi wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa vita hiyo imeanza, twendeni tuungane kwa pamoja, kila mtu aende kwenye tafakuri, aondoe hisia zake, uanze kuwa na mdomo mkubwa kuliko ubongo, tufanye kazi sasa ili tuweze kwenda mbele.