Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Augustine Vuma Holle (9 total)

MHE. AUGUSTINO V. HOLLE aliuliza:-
Kwa muda mrefu Mkoa wa Kigoma umesubiri kuunganishwa kwenye Grid ya Taifa ya Umeme:-
Je, ni lini Serikali itaunganisha Mkoa huo kwenye Grid ya Taifa ya Umeme?
NAIBU WAZIRI NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati napenda kujibu swali la Mheshimiwa Augustino Vuma Holle, Mbunge wa Jimbo la Kasulu Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TANESCO mwezi Desemba, 2017 ilikamilisha upembuzi yakinifu kwa ajili ya kujenga njia ya kusafirisha umeme ili kuunganisha Mkoa wa Kigoma na Grid ya Taifa kutokea Tabora. Mradi unahusisha ujenzi wa njia ya umeme ya msongo kilovoti 132 kutoka Tabora hadi Kidahwe Mkoani Kigoma kupitia Urambo na Nguruka umbali wa kilomita 370. Kazi za mradi zinahusisha ujenzi wa vituo vya kupozea umeme vya 132/33 KV katika Miji ya Urambo na Nguruka. Gharama ya kazi hizo inakadiriwa kufikia Dola za Marekani 81,000,000 na ujenzi wa mradi unatarajia kuanza mwezi Machi, 2019 na kukamilika mwezi Juni, 2020.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa upande mwingine inatekeleza ujenzi wa mradi wa kusafisha umeme…
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa upande mwingine inatekeleza ujenzi wa mradi wa kusafisha umeme wa North West Grid KV 400 Mbeya – Tunduma – Sumbawanga – Mpanda – Kigoma – Nyakanazi wenye urefu wa kilometa 1372. Mradi huu utawezesha kuyaunganisha maeneo ya Magharibi na Kaskazini Magharibi mwa Tanzania katika Grid ya Taifa na kuondoa matumizi ya mitambo ya mafuta katika maeneo hayo. Kwa sasa mikataba ya makubaliano ya fedha imesainiwa kati ya Tanzania na Benki ya Dunia pamoja na Benki ya Maendeleo ya Afrika na mradi utagharimu Dola za Kimarekani 455,000,000.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia imeanza utekelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme wa MW 45 kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Malagarasi. Ujenzi wa mradi huo utaenda sambamba ujenzi wa wa njia ya kusafirisha umeme wa mgongo wa KV 132 yenye urefu wa kilometa 53 kutoka Malagarasi hadi Kidahwe Kigoma unatarajiwa kujengwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020 na kukamilika 2020/2021.
MHE. STANSLAUS S. MABULA (K.n.y. MHE. AUGUSTINE V. HOLLE) aliuliza:-

Migogoro ya wafugaji na wakulima nchini imekuwa ya kudumu na hivyo kusababisha vifo kwa watu na uharibifu wa mali:-

Je, Serikali haioni ni wakati muafaka kuja na Sera ya kupunguza idadi ya mifugo nchini ili kuwa na ufugaji wenye tija?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Augustine Vuma Holle, Mbunge wa Kasulu Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi inatekeleza mpango wa kutoa elimu kwa wafugaji kuhusu ufugaji bora na uzalishaji wa malisho kupitia mashamba darasa ili kufuga kwa tija pamoja na kuendeleza malisho katika maeneo yaliyotengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu inayotolewa itawezesha uboreshaji wa kosaafu za mifugo, udhibiti wa magonjwa, matumizi sahihi ya madawa na viuatilifu, uelewa wa sheria, kanuni na miongozo ya sekta ya mifugo ili kuepukana na migogoro ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.

Aidha, elimu inalenga kuwaongezea wafugaji maarifa kwa kuwapatia teknolojia mpya ili kuhamasisha ufugaji wa kisasa na kibiashara nchini. Pia elimu hiyo itasaidia kuongeza uzalishaji wa malighafi zitokanazo na mifugo zenye viwango bora ili kukidhi mahitaji ya viwanda vya vyama, maziwa na ngozi vinavyoendelea kujengwa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ina mpango wa kufanya mapitio ya sera ya Taifa ya mifugo ya mwaka 2006 ili iweze kuendana na mabadiliko ya mazingira ya sasa.
MHE. AUG USTINE V. HOLLE aliuliza:-

Je, ni lini ujenzi wa barabara ya Kasulu Mjini hadi Kibondo utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Augustine Vuma Holle, Mbunge wa Kasulu Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara ya Kasulu Mjini - Kibondo kilometa 149 ni sehemu ya barabara ya Nyakanazi - Kasulu kilometa 236 kuelekea hadi Kigoma na pia kutokea Kasulu kuelekea Manyovu/mpakani mwa Tanzania na Burundi kilometa 68.25.

Mheshimiwa Spika, Serikali tayari imechukua hatua kadhaa za kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami ambapo kwa kupitia Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) zimepatikana fedha kwa ajili ya ujenzi wa kiwango cha lami kwa sehemu ya Kabingo – Kasulu – Manyovu kilometa 260.6.

Mheshimiwa Spika, kwa hivi sasa maandalizi ya kusaini mikataba ya ujenzi yanaendelea na kazi za ujenzi zinatarajiwa kuanza mwezi Machi, 2020.
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE aliuliza:-

World Vision wamejenga Chuo cha Ufundi katika Kata ya Nyamidaho na kukikabidhi kwa Halmashauri ya Kasulu DC:-

Je, kwa nini Serikali isimalizie ujenzi wa miundombinu midogomidogo na hatimaye kukifanya kuwa Chuo cha Ufundi cha Serikali?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Augustine Vuma Holle, Mbunge wa Kasulu Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa nchi kuwekeza katika elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali imedhamiria kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, kupitia uchumi wa viwanda ambavyo vinaedelea kujengwa kwa kasi kubwa. Kwa sasa Serikali inaendelea na mpango wa kujenga Vyuo vya Ufundi Stadi ikiwa na lengo la kutimiza azma ya kuwa na Chuo cha Ufundi katika kila Mkoa na kila Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetoa jumla ya shilingi milioni 530 kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi wa miundombinu wa ya Chuo cha Ufundi Stadi cha Nyamidaho. Ujenzi umefikia asilimia 80, hatua inayofuata ni kuunganisha umeme, kumalizia ujenzi wa vyoo na kumalizia kazi za nje. Kazi hizi zitakamilika mwishoni mwa mwezi Oktoba, 2019. Aidha, michakato ya manunuzi ya samani na mitambo ya kufundishia na kujifunzia imekwishaanza ili kuhakikisha kuwa chuo hicho kinaanza kutoa mafunzo ifikapo Januari, 2020.
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE aliuliza:-

Kata ya Buhoro Wilaya Kasulu ina shida kubwa ya maji:-

Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwapa mradi wa visima vikubwa viwili kwenye kijiji cha Shunga ili kuwasaidia akina mama wanaoteseka?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Augustine Vuma Holle Mbunge wa Kasulu Vijiji kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mpango wa utekelezaji wa miradi ya maji kwa mwaka 2019/2020, Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu imekiweka kijiji cha Shunga miongoni mwa vijiji vitakavyofanyiwa usanifu wa miradi wa maji. Aidha, mradi mkubwa wa maji kutoka chanzo chake kilichopo eneo la Jeshi la Mutabila kinalenga kuwapatia maji wananchi wa kijiji cha Shunga. Lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wake wote wanapatiwa huduma hii muhimu ya maji safi na salama.
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE Aliuliza: -

Je, ni lini Mkoa wa Kigoma utaunganishwa na umeme wa Gridi ya Taifa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Augustine Vuma Holle, Mbunge wa Kasulu Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Kigoma unapata umeme kupitia mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia mafuta ya diesel ambayo ni gharama kubwa kwa TANESCO na Serikali kwa ujumla. Katika hatua ya haraka, Serikali inatekeleza mradi wa kuunganisha Mkoa wa Kigoma katika Gridi ya Taifa kutoka Tabora.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu utahusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kilovoti 132 kutoka Tabora hadi Kigoma kupitia Urambo na Nguruka umbali wa kilomita 395, pamoja na ujenzi wa vituo vya kupozea umeme wa msongo wa kilovoti 132 kwenda 33 vya Urambo, Nguruka na Kidahwe Mkoani Kigoma. Gharama za mradi huu ni shilingi bilioni 142.7 na mradi ulianza ujenzi mwezi Juni, 2020 na unatarajia kukamilika mwezi Juni, 2022.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hatua nyingine Serikali inaendelea na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa njia kuu za kusafirisha umeme, msongo wa kilovoti 400 yenye urefu wa kilomita 280 ya kutoka Nyakanazi Mkoa Kagera hadi Kidahwe Mkoani Kigoma. Mradi huu unahusisha ujenzi wa vituo viwili vya kupoza umeme msongo wa kilovoti 400 kuja 220 kwenda 132 mpaka 33 na 400/132/33 vya Nyakanazi vyenye transfoma mbili zenye ukubwa wa MVA 120.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa mradi huu pia ulianza mwezi Januari mwaka 2020 na utakamilika mwezi Juni, 2022. Gharama ya mradi ni dola za Kimarekani milioni 187 chini ya ufadhili wa Serikali ya Tanzania, Benki ya Maendeleo ya AfDB pamoja na Benki ya Maendeleo ya Korea.
MHE. VUMA A. HOLLE Aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kutatua mgogoro wa ardhi kati ya Kijiji cha Mgombe na Kambi ya Jeshi Mtabila?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijajibu swali, kwa ruhusa yako naomba nimshukuru Mungu kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha kusimama hapa mbele ya Bunge lako. Vile vile namshukuru sana Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na Amirijeshi Mkuu wa Majeshi yetu kwa kuniamini na kuniteua kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nawashukuru sana wananchi wa Jimbo la Ushetu, wapiga kura wangu kwa kuniamini na kunipitisha bila kupingwa na kwa kura nyingi ambazo walizitoa kwa Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakupongeza wewe pamoja na Spika kwa ushindi mkubwa na kuaminiwa na Bunge hili. Vile vile nawapongeza Wabunge wote kwa kuchaguliwa na wananchi kuwa Wabunge wa Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa napenda kujibu swali la Mheshimiwa August Vuma Holle, Mbunge wa Kasulu Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Kambi ya Jeshi ya Mtabila – 825/KJ ipo Wilayani Kasulu, Mkoani Kigoma. Eneo husika lina ukubwa wa ekari 12,206.05 ambalo awali lilitumiwa kama Kambi ya wakimbizi. Aidha, mwaka 2012 eneo hili lilikabidhiwa kwa Jeshi na kuwa Kiteule na mwaka 2014 kiliundwa Kikosi cha Jeshi Mtabila.

Mheshimiwa Naibu Spika, mgogoro wa ardhi ulianza baada ya wananchi wa Vijiji vya Mgombe na Katonga kuvamia eneo hilo kwa shughuli za kilimo na hatimaye kuweka makazi. Kwa sasa wananchi waliokuwa wamevamia eneo hilo wameondolewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imeanza kuutatua mgogoro uliopo kwa kufanya vikao na uongozi wa Wilaya. Tarehe 11 na 12 Januari, 2021 Viongozi wa Kikosi cha Jeshi Mtabila walikutana na Uongozi wa Wilaya ya Kasulu na kuamua kuihamisha barabara inayokuwa inapita katikati ya kambi kuelekea Kijiji cha Shunga hadi Nchi ya Burundi ipite mpakani mwa eneo la Kambi. Pia, TANROADS wameweka alama za barabara tarehe 13 Januari, 2021 ikiwa ni hatua ya kuitambua barabara hiyo na kuiendeleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu itatuma timu ya wataalam kukutana na uongozi wa Mkoa, Wilaya na Vijiji husika kwa lengo la kutatua mgogoro huo. Nawaomba wananchi wawe na subira wakati Serikali inalifanyia kazi suala hili na kulipatia ufumbuzi. Aidha, Wizara inawasihi Viongozi wa ngazi zote kuwaelimisha na kuwasisitiza wananchi katika maeneo yao kutovamia maeneo ya Jeshi. (Makofi)
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA K.n.y. MHE. AUGUSTINE V. HOLLE aliuliza:-

Kumekuwa na mgogoro wa ardhi wa muda mrefu baina ya Kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu na Kata ya Makere:-

Je, ni lini Serikali itatatua mgogoro huo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Augustine Vuma Holle, Mbunge wa Kasulu Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu ilianzishwa mwaka 1996 kwa ajili ya kupokea wakimbizi kutoka nchi ya DRC. Wakati wa uanzishwaji wa kambi hiyo hakukuwa na mgogoro wa ardhi kwa sababu lilikuwa ni eneo lisilotumika. Aidha, pamoja na eneo la kambi, Serikali ilitenga eneo lingine la kambi kwa ajili ya wakimbizi iwapo eneo la awali litazidiwa.

Mheshimiwa Spika, kadiri ya muda ulivyoenda, wananchi walianza kuvamia eneo la akiba kwa lengo la kuwatumia wakimbizi kama vibarua katika shughuli za kilimo katika eneo hilo. Kwa kuzingatia maelezo hayo, ni wazi kuwa hakuna mgogoro wa ardhi baina ya Kambi ya Nyarugusu na Kata ya Makere, bali ni suala la uelewa ambapo wananchi wanaendelea kuelimishwa juu ya matumizi sahihi ya eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na jitihada za kumaliza tatizo la wakimbizi nchini kwa kuwarejesha wakimbizi makwao kwa kushirikiana na Jumuiya za Kimataifa na nchi wanazotoka wakimbizi hao. Baada ya wakimbizi hao kuondoka maeneo yote ya kambi za wakimbizi yatarejeshwa Serikalini ili mamlaka zinazohusika ziweze kuyapangia matumizi stahiki.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE K.n.y. MHE. VUMA A. HOLLE aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Barabara ya Kasulu - Uvinza kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Augustino Vuma Holle, Mbunge wa Kasulu Vijijini kama ifuatavyo;

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanza ujenzi wa barabara ya Kasulu – Uvinza yenye urefu wa kilometa 65.9 kwa kiwango cha lami ambapo kilometa 8.9 kutoka Kasulu njiapanda ya Kanyani ni sehemu ya mradi wa barabara ya Kidakhawe – Kasulu yenye urefu wa kilometa 63 ambayo ujenzi wake kwa kiwango la lami umekamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, wakati Serikali inaendelea kutafuta fedha za ujenzi wa sehemu ya njia panda ya Kanyani hadi Uvinza, Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) inaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali kila mwaka ili iweze kupitika majira yote ya mwaka. Katika mwaka wa fedha wa 2020/2021 barabara hii imetengewa jumla ya shilingi milioni 1,887.9 kwa ajili ya matengenezo mbalimbali. Ahsante.