Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Willy Qulwi Qambalo (49 total)

MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Naibu Spika, Naitwa Willy Qambalo Mbunge wa Jimbo la Karatu.
Kwa kuwa, matatizo ya maji yaliyoko Busekelo yanafanana kabisa na matatizo ya maji yanayoukumba Mji wa Karatu na vijiji vinavyouzunguka. Na kwa kuwa Mji wa Karatu unakua sana kutokana na shughuli za utalii zinazoendelea katika maeneo ya jirani. Je, ni lini Serikali itamaliza kabisa matatizo ya maji katika Mji wa Karatu na vijiji vinavyozunguka?
NAIBU WAZIRI (TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu yangu huyu tukiri kwanza Busokelo haifanani na Karatu kwa sababu kule Busokelo kuna mamba, na naamini Karatu hakuna mamba. Lakini kubwa zaidi ni jinsi gani kama Serikali itajielekeza kuhakikisha Mji wa Karatu unapata maji kwanza nikiri kwamba miongoni mwa Miji ambayo Tanzania tunaitegemea katika suala zima la uchumi ni Mji wa Karatu, kwa sababu ni center kubwa sana ya utalii katika nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme kwamba Serikali kupitia Wizara ya maji katika programu ya pili tunayoenda nayo ambayo imeanza hii Januari, tumeweka kipaumbele katika Mji Mikakati yote ambayo kwanza ina vivutio vya Kitalii, lakini ni source kubwa sana ya uchumi wa nchi yetu kuipa kipaumbele katika suala zima la huduma ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiri wazi kwamba katika suala zima la utalii kama nilivyosema awali, Karatu ni Mji tunaoutegemea sana. Kwa hiyo suala hili tunalilchukua kwa ujumla wake, Wizara ya Maji halikadhalika Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, tutahakikisha jinsi gani tutaipa kipaumbele. Ile miradi ambayo imeanza Singida haijakamilika vizuri, au ni jinsi gani tutumie vyanzo vingine ili mradi tupate maji katika Mji wa Karatu, wananchi wa Karatu waweze kupata manufaa katika nchi yao.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2002 mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro ilifanya uhakiki wa mipaka yake na ndipo hapo ilipochukua maeneo ya wananchi katika Vijiji vya Endamaga na Lostete na tangu mwaka huo hadi wa leo kuna migogoro ambayo haiishi ni lini maeneo hayo ya wananchi sasa yatarudishwa kwao?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, jambo moja ambalo napenda labda lieleweke vizuri hakuna mahali ambapo Serikali inatwaa ardhi bila kufuata utaratibu. Utaratibu wa Serikali kutwaa ardhi kwa ajili ya maslahi ya Taifa uko wazi, kwa upande wa hifadhi utaratibu huu ni shirikishi na unaanzia kwenye ngazi ya Vijiji vinavyohusika, Halmashauri zinazohusika, vikao vya Mkoa mpaka kufikia vikao vya maamuzi vya Kitaifa ndipo ardhi itatwaliwa kwa ajili ya matumizi kwa maslahi ya Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo pale ambapo kumetokea sababu yeyote ile ya kutokea kwa mgogoro labda kutoelewana au tafsiri tofauti ya sheria, tafsiri ya GN au matumizi yanayokiuka yale makubaliano ya awali. Hizo ni kasoro ambazo Serikali imekiri na ndiyo maana nimesema awali kwamba tunakwenda kupitia upya.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeshajibu swali kama hili hapo nyuma na ninataka kusisitiza tena kwamba, tunakwenda kupitia mgogoro mmoja baada ya mwingine kuangalia ukweli wa mgogoro huo na ufumbuzi wake utapatikana kwa kushirikisha taasisi zote zitakazohusika ndani ya Serikali.
MHE. WILLY Q. QAMBALO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali madogo ya nyongeza pamoja na majibu yenye matumaini ya Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kisima hiki cha Karatu Mjini kimeombewa umeme sasa ni mwaka mmoja na nusu lakini bado haujaunganishwa na nikiangalia fedha zinazoongelewa kukamilisha kazi ile ni shilingi milioni 33, naona hizi ni fedha kidogo sana kwa Serikali hii ya Awamu ya Tano Serikali ya Hapa Kazi Tu.
Mheshimiwa Waziri kwa nini Serikali isitafute fedha hizi shilingi milioni 33 ili kisima hiki kiweze kukamilika ili wananachi wapate huduma hii muhimu?
Swali la pili, Awamu ya Tatu ya REA inasubiriwa kwa hamu sana katika nchi yetu kwa sababu ni awamu ya kuiwasha karibu Tanzania yote. Hivi sasa tuko mwezi wa tatu ndani ya awamu hiyo; je, ni lini utekekezaji au ujenzi wa miundombinu ya umeme katika maeneo yetu utaanza ili wananchi wetu waweze kujiandaa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Mji wa Karatu Mjini kweli ulikuwa upelekewe umeme tangu awamu iliyopita lakini Serikali kulingana na kutoa vipaumbele imetoa shilingi bilioni 33.81 kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge, nimhakikishie tu kwamba hizo fedha zitatosha na isipotosha Serikali bado itatafakari namna ya kuongeza pesa kwa ajili ya kukamilisha mradi huo. Kwa sasa nina uhakika hizo fedha zinatosha na mji wa Karatu Mjini utapata umeme wa uhakika na visima vya maji vyote vitapata umeme kwa kutumia mitambo ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Qambalo tumekuwa tukishirikiana sana hata kwenye awamu ya Bunge lililopita. Vijiji alivyotaja ambavyo ni vijiji 21 ambavyo havijapata umeme, nimhakikishie Mheshimiwa Qambalo tumekupelekea umeme vijiji 27 bado vijiji 21 na kati ya vijiji 21 ambavyo bado vimebaki navitambua sana na nimeshafika eneo lile. Kijiji chako cha Endamarariek kitapata umeme, Kambi Faru vitapata umeme hata kule Mbuga Nyukundu itapata umeme kule Rhotia Mbulu kwenye kijiji chako Mheshimiwa Mbunge kitapata umeme pamoja na Mikocheni na Changarawe vyote vitapata umeme.
Kwa hiyo namhakikishia Mheshimiwa Mbunge vijiji vyake vyote ambavyo nimevitaja na ambavyo sijavitaja pia vitapata umeme na kwamba REA Awamu ya Tatu inaanza kuingia sasa site kuanzia mwezi wa Novemba na mwezi wa Disemba. Hivi sasa wakandarasi wameshapatikana wasimamizi wa kazi wameshapatikana, kazi iliyobaki sasa ni kuanza kutekeleza kwenye kipindi cha mwezi Novemba hadi Disemba. Nimhakikishie vijiji vyake vyote 27 hata kijiji chako Mheshimiwa kile Kijiji cha Kilimamoja kitapata umeme na Kilimatembo bado kitapata umeme. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Willy Qambalo pamoja na majibu yote hayo sijayaona makofi au umepiga ni mimi nilikuwa sioni. Tunaendelea Waheshimiwa Mheshimiwa Musukuma Joseph Kasheku Mbunge wa Geita, swali lake litaulizwa kwa niaba na Mheshimiwa Lolesia Bukwimba.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Matatizo ya ardhi ambayo haijapata kuendelezwa yaliyopo katika eneo la Mbozi yanafanana kabisa na matatizo ambayo tunayo kwenye Wilaya yetu ya Karatu. Katika Kijiji cha Mang‟ola Juu kuna mwekezaji, Tembotembo ambaye amemilikishwa eka zaidi ya 3,000 lakini ameweza kuendeleza chini ya asilimia 25. Katika kijiji hichohicho pia kuna mwekezaji anaitwa Acacia naye ameendeleza eneo alilopewa kwa chini ya asilimia 10.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mashamba hayo sasa yamebadilika kuwa hifadhi na mapori bubu ya kuhifadhia wanyama wa porini ambao ni hatarishi kwa wananchi wanaolizunguka. Je, ni lini Serikali itatoa mashamba hayo na kuwarudishia wananchi hao ili waweze kuyatumia? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, masharti ya kutwaa mashamba kwa hekta zisizopungua 500 mmiliki wa shamba hilo anapewa miaka miwili tu anatakiwa awe ameliendeleza shamba hilo na asipofanya hivyo yuko halali kabisa kunyang‟anywa kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi, Namba 4 ya Mwaka 1999, kifungu cha 45 na cha 47, anayo haki ya kunyang‟anywa ardhi ile. Wale ambao ardhi yao wamekabidhiwa zaidi ya hekta 500, kama hajaiendeleza kwa asilimia 80 ndani ya miaka mitano ardhi ile inaweza kutwaliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ushauri kwa Mheshimiwa Mbunge wa Karatu, kwa sababu mamlaka haya, nani anayeanzisha kazi hii, kazi hii inaanzishwa na Afisa Mteule wa Ardhi pale halmashauri, waanzishe tu halafu watuletee, tena wafanye mapema na mimi bado nakaimu huu Uwaziri wa Ardhi ili tuweze kuyashughulikia mapema matatizo haya.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza. Mheshimiwa Mwenyekiti, ni fursa kubwa kwa Halmashauri hasa kama ile ya Karatu yenye vivutio vingi vya kitalii na hizi hoteli za kitalii hasa katika kipindi hiki ambacho Halmashauri zetu nyingi zinachechemea katika eneo la mapato ya ndani. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri, huoni sasa umefika wakati wa kubadilisha sheria hiyo ili kodi hiyo ya hotel levy ikusanywe na Halmashauri zetu ili iweze kuchangia katika eneo lile la mapato ya ndani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika swali la msingi uliulizwa suala la Serikali inamkakati gani, lakini majibu bado yamerudi kwa Halmashauri ya Karatu kujitangaza pamoja na kwamba kuna kipengele kidogo cha Serikali kusaidia. Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri zetu nyingi hazina mapato ya kutosha ya ndani, je, Mheshimiwa Waziri tunachouliza, ni mkakati wa Serikali wa kutangaza hoteli zile za kisasa ili wale wageni badala ya kulala hata Nairobi waje Karatu ili waondokee pale kwenda Ngorongoro na Manyara? Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, nadhani yote ni mchakato huu wote mpana kwa sisi Waheshimiwa Wabunge kama tukiona kuna haja ya kubadilisha sheria basi nadhani katika mawazo ya pamoja tutafanya hilo kwa pamoja kwa lengo la Halmashauri zetu, lakini hilo ni takwa la kisheria, kwa hiyo, ni sisi wenyewe kufanya maamuzi katika hilo na mchakato huo ukianza inawezekana kila mtu kutakuwa na michango mbalimbali kama ya wadau nini kifanyike. Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili la utangazaji, ni kweli nimezungumza kwamba website ya Karatu lakini kuna mipango mbalimbali ya Serikali na mpango mkubwa sasa hivi hata ukipitia shirika letu la ndege katika suala zima ambalo wenzetu wa Maliasili na Utalii mara nyingi sana wameamua katika shirika letu la ndege liwe miongoni mwa mojawapo kutangaza vivutio mbalimbali vya kitalii. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika mpango wa kutangaza vitu mbalimbali vya kitalii hapa kama Serikali ina mipango mipana sana kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii na hilo naomba niseme kwa suala la Karatu tutalipa kama special preference kwa ajili eneo lile lina hoteli nyingi zaidi lakini ni eneo la kimkakati mtu akifika pale anapata faraja anakuwa na sehemu nzuri ya kulala, hana mashaka ya aina yoyote. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi naamini Serikali yetu kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii itaongeza upana wake wa utangazaji wa vivutio vyetu vya utalii, lengo kubwa tuweze kukuza uchumi wa nchi yetu kwa sababu tunategemea kwamba kwa fursa tulizonazo za vyanzo vya kitalii tukitangaza vizuri tutakwenda mbele zaidi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge naomba niungane na hoja yako, kama Serikali tutafanya mpango mpana kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri katika nchi yetu.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Mamlama ya Maji ya Mji wa Karatu (KARUWASA) ina zaidi ya umri wa miaka mitatu, lakini uendeshaji wake umekuwa ukisuasua kwa sababu mamlaka hiyo bado haina
bodi ya usimamizi; majina ya wajumbe waliopendekezwa kwenye bodi hiyo yalishapita kwenye ngazi ya Baraza la Madiwani zaidi ya miezi sita. Ni lini bodi hiyo itaundwa ili isaidie uendeshaji wa mamlaka hiyo? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, tuna hizi mamlaka za bodi katika miji midogo zinaundwa chini ya TAMISEMI na ile miji ya mikoa na miradi ya kitaifa zinaundwa chini ya Wizara ya Maji. Sasa naomba nilichukue kwamba suala hili tuliangalie ni kwa nini mpaka leo bodi haijaundwa. Labda kutakuwa na tatizo, sasa siwezi kuwa na jibu sasahivi, nitakwenda kulifanyia kazi na nitamjulisha Mheshimiwa Mbunge ni wapi tumefikia kuhusu kuunda Bodi ile ya Maji katika Mji wa Karatu.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mamlaka ya Maji ya Mji wa Karatu (KARUWASA) ina kisima kimoja na kisima hicho kimeharibika na ni miezi miwili wananchi hawana huduma ya maji; na Mamlaka hiyo iko katika kundi la Mamlaka Daraja la C ambalo zinapata ruzuku kutoka Serikalini:-
Je, ni lini Serikali itapeleka fedha ili kuokoa kisima hicho ili wananchi waendelee kupata huduma hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitembelea Karatu na nilikuta kweli kisima hicho kilikuwa kimepata shida ya pampu. Akiba ya fedha niliyoikuta kwenye Mamlaka ya Karatu ilikuwa shilingi milioni tano na tulitoa maelekezo kwamba ashirikiane na Mamlaka ya Arusha ili waweze kum-support kupata pampu nyingine. Sasa Mheshimiwa Mbunge kwa sababu imekuwa ni muda kidogo, naomba tuwasiliane baadaye, nitafanya mawasiliano na Mamlaka ya Arusha kuona wamefikia wapi ili kurudisha ile huduma pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tulikubaliana, viko visima vitatu ambavyo tayari vimeshachimbwa na Serikali, tuhakikishe kwamba, kwenye bajeti tunayoitoa tuwekee miundombinu na kuweka pampu ili kuhakikisha wananchi wa Karatu wanapata maji safi na salama.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Mradi wa maji wa kijiji cha Getamok katika Wilaya ya Karatu uliojengwa kwa zaidi ya gharama ya shilingi milioni 600 chini ya Programu ya Kwanza ya WSDP hivi sasa haufanyi kazi kwa sababu ya kujengwa chini ya kiwango. Mabomba yaliyofungwa kwenye mradi huo yanapasuka kila kukicha na hata matenki yanavuja. Halmashauri ya Wilaya imejaribu kurejesha huduma kwa kutumia vyanzo vyake lakini imeshindikana kwa sababu fedha nyingi zinahitajika.
Je, Serikali itawasaidiaje wananchi wa kijiji hicho kupata huduma hiyo ya maji safi na salama na pia wale waliofanya ujenzi huo chini ya kiwango Serikali itawachukulia hatua gani?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ipo miradi mingi katika nchi yetu ambayo imepata shida hiyo kwamba kiwango cha utendaji kilikuwa chini aidha mabomba yaliyonunuliwa hayakuwa yamenunuliwa katika viwango vinavyotakiwa. Kwa sasa tunatakiwa ku-review ili tuweze kununua mabomba ambayo ni bora sambamba na kuchukulia hatua wale ambao wamehusika kutufikisha hapo tulipo. Sheria na taratibu tunazo, tutumie Halmashauri na kama utaona kwamba mambo hayaendi, naomba tuwasiliane. Kupitia kwenye Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji, Wizara ya Maji na Umwagiliaji tutaingilia.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, uko utaratibu kama si sheria au kanuni katika nchi hii, kwamba mifugo ya wananchi au wananchi wenyewe wakiingia kwenye hifadhi kuna tozo inawakuta. Je, Mheshimiwa Waziri haoni ili kuondokana na hili tatizo la wanyama kutoka nje umefika wakati sasa wanyama wakitoka nje kwenye maeneo ya wananchi, tozo hiyo hiyo ambayo wananchi wanatozwa wakiingia kwenye hifadhi nayo itozwe? Nakushukuru. (Makofi)
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, wanyamapori si binadamu na wanyamapori hawana akili za kibinadamu, ni wanyama wa porini. Kwa hiyo, tujitahidi sana kuwalinda kwa kuwaeleza askari wanyamapori pale wanapotokea na mimi nasema kwa kweli ni furaha kubwa kwamba kwa mara ya kwanza sasa tembo wameongezeka kutokana na hali mbaya ya ujangili iliyokuwepo hapa nchini na sasa wanaonekana, wanakuja mpaka kwenye maeneo ya watu. Rai yangu kwa kweli tushirikiane ili tuwataarifu askari wanyamapori pale wanyama hao wanapotokea na sisi tunachukua hatua haraka iwezekanavyo kila tukio la namna hii linapotokea.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nasikitika kwa majibu ya Naibu Waziri kwa kusema kwamba mbegu hizi sio ghali. Mbegu hizi ni ghali. Mkulima anapotaka kupanda walau eka moja tu ambayo hata haiwezei kutosha chakula chake cha mwaka inabidi atumie zaidi ya shilingi 60,000 sasa kama shilingi 60,000 kwa eka sio ghali sijui Waziri ametumia kipimo gani!
Mheshimiwa Spika, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Asilimia kubwa ya mbegu hizi pia zinatoka nje ya nchi na zinazalishwa katika mazingira tofauti na ya wakulima wetu jambo ambalo pia zinapoingizwa nchini inaongeza gharama hizi kwa mfano mbegu aina ya seedco, mbegu aina ya hybrid. Sasa miaka ya nyuma tulikuwa na Shirika letu la TANSEED lilikuwa linasaidia sana wakulima kupata mbegu hizi.
Je, Serikali ina mpango gani wa kufufua Shirika la TANSEED au mashirika mengine ya aina hiyo ili mbegu hizi ziweze kuzalishwa hapa nyumbani katika mazingira ya wakulima wetu hatimae bei pia iweze kupungua.
Swali la pili, asilimia 60 hadi 80 ya mahindi yote yanayolimwa nchini yanatumika kwenye kaya zetu. Asilimia 20 tu inaingia kwenye eneo la biashara, lakini changamoto ambayo wananchi wetu wanakutana nayo ni suala la uhifadhi wa mazao haya kwa kipindi chote cha mwaka. Mifuko ya kuhifadhia mahindi aina ya PICS (Purdue Improved Crop Storage) pamoja na hata zile dawa za shamba shumba, hizo bei kwa kweli zko ghali kiasi kwamba wakulima wanashindwa kuzinunua na mazao yao yanaharibika.
Je, Serikali iko tayari sasa kuingiza pembejeo hizo za uhifadhi wa nafaka ili zipunguze bei, wananchi wazipate kwa bei rahisi wakati zikiwa kwenye ruzuku. Nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimuombe sana jirani yangu asisikitike kwa sababu nitajisikia vibaya sana, Karatu ni jirani na Ngorongoro kwa hiyo ningependa sana afurahi.
Mheshimiwa Spika, vilevile nimweleze kwamba akifanya mahesabu sawasawa kwa kweli mbegu bora siyo ghali, kwa sababu mfuko wa kilo kumi wa mbegu ya mahindi aina ya OPV ni shilingi 40,000 wakati bei ya chotara ni shilingi 30,000.
Sasa katika mfuko wa kilo kumi unaweza ukatumia kwenye heka moja ambayo unaweza ukapata gunia mpaka 30 na gunia moja Karatu inauzwa shilingi 50,000 maana yake gunia moja tu ukipata kwa mwaka unaweza ukahudumia heka moja na ukapata magunia mengine mengi. Kwa hiyo, ni suala la hamasa wananchi kuelewa umuhimu wa kutumia mbegu bora.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo niendelee kujibu maswali yake kwamba ni kweli kama alivyosema kwamba bado tunaagiza asilimia kubwa ya mbegu zetu kutoka nje, lakini kwa sasa Wizara na Serikali imejikita katika kuondoa tatizo hili ASA ambayo ndiyo Kampuni yetu ya Taifa ya Kuzalisha Mbegu, wameelekezwa sasa watumie mashamba yao mengi waliyonayo katika maeneo mbalimbali kwa mfano Mbozi, Bugaga, Msamba na Kilingali, Dabaga, Ngaramtoni ili kuongeza uzalishaji wa mbegu bora. Vilevile Serikali imeondoa vizingiti vilivyokuwa kwenye Sheria ya Mbegu ili kampuni binafsi ziweze sasa kwa urahisi zaidi kuzalisha mbegu ambazo zimetafitiwa na taasisi zetu za utafiti. Kwa hiyo, tunategemea tunavyozidi kwenda hiyo changamoto ya kutojitosheleza kwa mbegu itapungua na katika wa mkakati mpango wetu wa kilimo wa pili wa SDP II kuna mkakati mkubwa sana wa kuongeza uzalishaji wa mbegu.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ni kuhusiana na uhifadhi wa chakula, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa Wizara imejikita katika kuongeza uwezo wetu wa kuhifadhi chakula kwa sasa tuna uwezo wa kuhifadhi nafaka ya tani 250,000 lakini tayari tumesaini mkataba na makampuni mawili ili kujenga maghala saba katika maeneo mbalimbali, ikiwepo ghala itakayojengwa Babati ili tuweze kuongeza uwezo wetu na hatimaye kufikia tani 500,000. Tunaamini katika miaka miwili ijayo tutakuwa na uwezo wa kuhifadhi nafaka tani 500,000 na hivyo wakulima wake wa Karatu wakitaka wanaweza wakahifadhi kwa mpango maalum ambao utawekwa na NFRA katika ghala na kihenge kitakachojengwa Babati.
Mheshimiwa Spika, vilevile nimhakikishie kwamba mifuko ile ya kuhifadhi nafaka ambayo haingiliwi na wadudu kama mifuko ya PICS kwa sasa inapatikana kwa bei nzuri sana. A to Z wanazalisha mifuko ile kwa bei ya jumla ya wastani wa shilingi 2,700 kwa mfuko kwa hiyo kwa mkulima ambaye anahitaji mifuko mingi kwa kweli shilingi 2,700 kwa kuhifadhi mazao yale kwa muda mrefu bado ni bei ambayo inahimilika lakini vilevile Serikali inafikiria kuendelea kupunguza gharama za kikodi katika uzalishaji wa mifuko hiyo ili kwa mfano hiyo mifuko ya PICS iweze kupatikana kwa bei nzuri zaidi.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, mbaazi inayolimwa Tanzania bado ina uwezo wa kuingia katika soko lililoko India kutokana na viwango vya ubora ambayo inayo. Nashukuru kwamba Serikali imesema imeandaa makubaliano na mkataba umesainiwa wa kuwasaidia wananchi wetu waendelee kupata bei nzuri.
Je, Serikali iko tayari sasa kusukuma majadiliano hayo ili wananchi wetu waweze kunufaika kuanzia msimu wa kilimo ambao unaendelea sasa hivi baada ya kuvuna?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa biashara ya kuuza mbaazi nje ndiyo hiyo ambayo sasa haitabiliki. Je, Wizara hii iko tayari sasa kuanza mazungumzo na Wizara ya Viwanda na Biashara ili kupata viwanda vya kusindika zao hilo tuweze kuuza nje bidhaa iliyosindikwa ili kuongeza thamani na pia kutoa ajira kwa watu wetu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kufuatilia mkataba na Serikali ya India ili utekelezaji wake uweze kuanza kazi mapema iwezekanavyo ili wakulima wetu waendelee kunufaika bila kuchelewa.
Kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tunalisukuma, lakini wanaochelewesha kwa sasa siyo sisi ni upande wa India, wao wanaangalia mazingira ya hapa kwetu kwa sababu wameongea na nchi zingine za Kenya na Msumbiji, kimsingi wanajaribu kuangalia options mbalimbali, lakini sisi tutaendelea kuongea nao ili kufanikisha huo mkataba ili uanze mapema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu viwanda, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba ni kweli kabisa kati ya mikakati tuliyonayo ya kuweza kutafuta soko zuri la mbaazi na mazao mengine ya jamii ya mikunde ni kuwa na viwanda vya kuchakata hapa ndani ili tuweze kushindana katika soko la Kimataifa. India yenyewe ambayo ndiyo mnunuzi wa asilimia 27 ya mbaazi na mazao ya mikunde duniani wanauza katika nchi zingine baada ya kuchakata. Kwa hiyo, nasi tukiwa na viwanda itatusaidia sana tuweze kupata masoko mengine ikiwepo na masoko mazuri kama ya Marekani na Ulaya. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari hiyo ni moja kati ya mikakati ambayo tunafikiria kama Serikali.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na umuhimu wa watumishi katika kada hii ya Maafisa Ugani kama kweli tunataka kuleta mapinduzi ya kilimo kwenye nchi yetu. Jambo ambalo tunaliona sasa hivi ni kwamba kutokana na kutokuajiriwa kwa Watendaji wa Vijiji na Watendaji wa Kata wa kutosha, baadhi ya watumishi katika kada hii ya kilimo sasa ndiyo wamekaimishwa zile ofisi za Kata kwa maana ya kuwa Watendaji wa Vijiji na Watendaji wa Kata.
Je, ni lini Serikali itaajiri watumishi katika kada hiyo ya utendaji ili watumishi hawa muhimu wa eneo la kilimo warudi kufanya kazi ya kilimo na wananchi? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli pale mahali ambapo Maafisa Watendaji wa Kata hawapo, Maafisa Ugani wamekaimishwa nafasi hizo, hii imetokana na upungufu wa kutotosheleza Watendaji wa Kata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilieleze Bunge lako Tukufu, kazi moja wapo ya Afisa Mtendaji wa Kata ni kusukuma maendeleo ndani ya kata, watu waliofanya vizuri sana katika shughuli hii ni Walimu, Maafisa Kilimo, Mabibi Maendeleo, kwa hiyo pale ambapo Afisa Kilimo anakaimishwa Kata siyo makosa, ni nafasi nzuri ya kumuangalia keshokutwa huenda akawekwa moja kwa moja. Jambo la msingi hapa ni kwamba Wizara yangu inakubali kwamba kuna haja ya kulifanyia kazi suala hili kuhakikisha kwamba Kata zetu zote na vijiji vyetu vinakuwa na Maafisa Watendaji wa kudumu. (Makofi)
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ni sera ya Serikali kuwa na hospitali katika ngazi ya Wilaya ili kutoa huduma ya afya kwa wananchi wetu. Wilaya ya Karatu ina umri wa zaidi ya miaka 20 na haina Hospitali ya Wilaya. Ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Karatu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi naomba niziase Halmashauri zote, ni wajibu wetu wa kuhakikisha kwanza tunaanza kwa kutenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa hospitali za afya, lakini kama hiyo haitoshi, kwa kushirikisha wananchi ni vizuri tukaanza halafu Serikali ikaleta nguvu yake. Ahsante. (Makofi)
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Mradi wa maji wa Kijiji cha Getamog Wilayani Karatu, uliojengwa katika ule mpango wa Benki ya Dunia ambao uligharimu takribani shilingi milioni 600 haufanyi kazi kwa sababu umejengwa chini ya kiwango. Nimshukuru Waziri wa Maji kwa kutuma wataalam wake ili kubaini tatizo hilo, ili mradi huo uweze kurekebishwa.
Je, ni lini Serikali sasa itapeleka fedha ili wananchi wa Kijiji cha Getamog waendelee kupata huduma hiyo muhimu? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli nilipata hiyo taarifa na nikamuagiza Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Arusha, ambaye ameenda kule kuangalia uchunguzi namna gani mradi ulijengwa chini ya kiwango. Taarifa hiyo ikishapatikana, Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie kwamba Serikali itafanya maandalizi ya kuweka mkandarasi wa kuboresha ule mradi na fedha itatolewa baada ya kuleta hati za malipo.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, Wilaya ya Karatu ina zaidi ya umri wa miaka 20 na haina hospitali ya wilaya. Hivi sasa uongozi wa wilaya unakamilisha taratibu za kupata eneo kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo. Je, Serikali iko tayari sasa kuanza kutenga fedha katika bajeti inayokuja ili kuanza ujenzi wa hospitali hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwamba Serikali iko tayari kuanza kutenga, nia na azma ya Serikali ni kuhakikisha kwamba ujenzi wa Hospitali za Wilaya unafanyika katika Wilaya 64 zote ambazo hatuna hospitali za Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama ambavyo yeye mwenyewe amesema katika swali lake, ndiyo wameanza kutenga eneo kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya. Naomba tuongeze kasi ya kutenga hilo eneo, lakini pia kutokana na Halmashauri yenyewe kwa sababu ni hitaji letu, tuanze kutenga pesa na Serikali ije kumalizia.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Tunayo sera katika nchi hii inayotoa kipaumbele kwa ujenzi wa kiwango cha lami kwa barabara zinazounganisha mikoa. Barabara hii tunayoongelea inaunganisha Mkoa wa Arusha na Simiyu. Kutokana na jiografia ya maeneo hayo, barabara hii ni muhimu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri katika jibu lake anasema barabara hii itajengwa fedha zitakapopatikana. Sasa naomba swali, kutokana na sababu hizo za kisera na kijiografia, je, utafutaji wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii umefikia hatua gani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kutokana na mvua nyingi zilizonyesha katika maeneo ya barabara hii na hata ile inayounga Mji wa Karatu na Mbulu, zimeharibika sana na usafiri umekuwa wa shida na maeneo mengine barabara zimekatika. Kwa kuwa mvua sasa zinaelekea mwisho, ukarabati na ujenzi wa barabara hii utaanza lini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu katika swali langu la msingi, suala la upembuzi yakinifu na usanifu wa kina haujakamilika, ndiyo kazi inayoendelea. Hatuwezi kuanza kutafuta fedha kabla hatujajua tunahitaji fedha kiasi gani katika ujenzi wa barabara hii. Tunaposema mara baada ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kukamilika ni wazi hatua inayofuata ni ya kujenga kwa kiwango cha lami na hapo ndiyo fedha tunaziongelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili itakumbukwa kwamba nilipojibu swali la nyongeza wiki iliyopita, nilitoa maelekezo kwa TANROADS pamoja na Mameneja wote wa Mikoa Tanzania nzima, kwamba sasa mvua zimekatika sehemu nyingi, tuelekeze nguvu katika kurudisha mawasiliano kwa barabara zile ambazo ziliathiriwa sana na mvua na kuleta changamoto ya mawasiliano. Hii ni pamoja na hii barabara anayoongelea Mheshimiwa Qambalo.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona. Matatizo ya maji yaliyoko Bukoba Vijijini yanafanana na matatizo tuliyonayo kule Karatu. Kata ya Rotia na Kata ya Mang’ola zina upungufu mkubwa wa maji kutokana na miundombinu iliyokuwepo kuwa ya muda mrefu na hivyo kushindwa kupeleka huduma ya maji stahiki. Je, ni lini sasa Serikali itatenga fedha ili kuboresha huduma ya maji katika Kata hizo mbili. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) : Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo yeye mwenyewe amekiri maeneo ya Karatu ni miongoni mwa maeneo ambayo tangu zamani kumekuwa na uwekezaji kwenye miradi ya maji na ndiyo maana miradi hiyo aliyoitaja amesema kwamba miradi ile ina uchakavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwenye awamu ya pili ya utekelezaji wa program ya maji tumeweka kipaumbele kikubwa kwanza kukarabati miradi iliyokuwepo ikiwemo hiyo ya Kata ya Rotya na Kata na Mang’ola ambayo kuna miundombinu ya maji ya muda mrefu. Kwa hiyo kipaumbele ni kukarabati kwanza hiyo kabla hatujaanza miradi mipya.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Wilaya ya Karatu ilikuwa na Mahakama za Mwanzo nne lakini hivi sasa imebaki Mahakama moja tu iliyoko Karatu Mjini ndio inayofanya kazi, Mahakama zingine za Mwanzo zimesimama kutokana na upungufu wa Mahakimu wa ngazi hiyo. Je, ni lini Serikali itapeleka Mahakimu wa Ngazi ya Mahakama za Mwanzo ili huduma hiyo muhimu ipatikane kwenye ngazi za Tarafa kule chini? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU:
Mheshimiwa Spika, tumepokea ombi lake na natumaini mwaka wa fedha unaokuja tutayafanyia kazi maombi yake ili na wakazi wa Karatu waweze kupata fursa ya kupata watumishi wa kuwahudumia katika Idara hii ya Mahakama.
MHE. WILLY Q. QAMBALO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Tatizo la mabwawa kupasuka lililopo Tabora Kaskazini linafanana kabisa na matatizo tuliyonayo kule Karatu. Bwawa la Bashay lililopo nje kidogo ya Mji wa Karatu lilikuwa chanzo muhimu sana cha maji kwa wakazi wa Kata ya Qurus hadi pale lilipopasuka wakati wa zile mvua za el- nino. Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati bwawa hilo ili wananchi wa Gongali, Bashay na Qurus waweze kupata huduma hiyo muhimu ya maji?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS – TAMISEMI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema Mipango yote ya Serikali lazima ianze katika Halmashauri zetu, tufanye needs assessment, tubainishe na tuweke katika mipango ya Serikali. Hata hivyo, imeonekana kwamba katika maeneo mengi mabwawa haya mengi sana yanapasuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwasihi hasa Waheshimiwa Wabunge tunaposimama katika maeneo yetu, japo kuwa si wataalam sana katika maeneo hayo lakini tuna haki ile miradi wakati inajengwa tuisimamie kwa karibu kwa sababu wakati mwingine wakandarasi wanapojenga ile embarkment haishindiliwi vizuri na hatimaye lile tuta linapasuka au spillway ya kupitisha utoro wa maji haiwi vizuri na mwisho wa siku maji yanafurika na bwawa linapasuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa ndugu yangu Mbunge wa Karatu jambo hili tumesema kwamba kama Serikali tumelisikia, lakini naomba nielekeze kama nilivyotoa maelekezo katika maeneo mengine, kule Halmashauri ya Karatu tuweke kipaumbele cha kufanya ukarabati wa bwawa hili ambalo linasaidia wananchi ili hatimaye tutenge fedha katika bajeti ile ili tuweze kurekebisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, naomba niseme kwamba tumelisikia, tumelipokea na kama Serikali tunajua kuna wananchi wetu huko wanapata shida kwa sababu bwawa limepasuka.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Wakazi wa Kata ya Rotia hususani vijiji vya Rotia, Rotia, Kainam, Kilimatembo, Chemchem na Kilimamoja wanapatwa na shida kubwa ya upungufu wa maji kutokana na chanzo chao pekee cha Mto Marera kukauka hasa wakati wa kiangazi kutokana na ama miundombinu chakavu, au maji kupungua sana. Je, ni lini Serikali itachimba visima katika vijiji hivyo ili waondokane na tatizo hilo la maji? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Qambalo, eneo hilo nalifahamu ni eneo kame sana kipindi cha kiangazi na pale mahali pana Airport, kwa hiyo tuwasiliane na Halmashauri ili tuone tufanyaje, ili kufanya study inayotakiwa, tuchimbe visima wananchi wa sehemu hiyo waweze kupata huduma ya maji kupitia kwenye bajeti yake ambayo tumemtengea, kwenye mwaka wa fedha 2017/2018. (Makofi)
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kambi ya Simba Wilayani Karatu umekamilika kwa ufanisi mkubwa na kituo hicho sasa kiko tayari kuanza kutoa huduma. Hata hivyo, kituo hicho hakina gari la wagonjwa na ukizingatia Wilaya ya Karatu haina hospitali ya wilaya, je, ni lini Serikali italeta gari kwa ajili ya huduma ya wagonjwa kwenye kituo hicho?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tunashukuru kwa kazi nzuri ambayo mwenyewe ana-recognise kwamba kituo cha afya kimekamilika na kiko kwenye hali nzuri. Hatua inayofuata anaomba upatikanaji wa gari la ambulance ili kuweza kusaidia huduma ya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba uhitaji wa gari kwa ajili ya wagonjwa ni mkubwa sana. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwa kadri nafasi zitakavyopatikana, tulipata magari 50 na tumeweza kuyagawa, tukipata gari nyingine naamini na wao watakuwa miongoni mwa maeneo ambayo yatapata fursa ya kupata magari.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Niulize maswali mawili madogo ya nyongeza; kama ambavyo Serikali imekiri katika majibu yake juu ya umuhimu wa zoezi hili la kupanga, kupima na hatimaye kumilikisha ardhi kisheria, lakini nakumbuka katika hotuba ya Waziri ya mwaka 2016/2017 aliliambia Bunge hili kwamba ni 15% tu ya ardhi ya nchi hii ndiyo imefanyiwa upangaji, upimaji na umilikishaji na nyingi ya hizo utazikuta ziko maeneo ya mjini.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuliachia zoezi hili muhimu sana kama ambavyo Serikali imekiri kwa halmashauri zetu za wilaya na vijiji ni zoezi ambalo lina gharama kubwa na halmashauri nyingi hazitaweza kabisa. Je, kama Serikali inatambua umuhimu wa zoezi hili, kwa nini Serikali Kuu sasa isiingilie kati ikazisaidia mamlaka hizo za wilaya na vijiji kuhakikisha ardhi yote ya nchi hii inapimwa, inapangwa na pia kumilikishwa kisheria? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Sheria ya Ardhi ya Vijiji ya Mwaka 1999 kifungu cha saba (7) kinamtaka Kamishna wa Ardhi kutoa cheti cha ardhi ya kijiji kwa vile vijiji ambavyo mipaka yake imetambulika na imekubalika lakini viko vijiji ambavyo vina sifa hiyo na havijapata hati hiyo. Nini kauli ya Serikali kwa Makamishna na Maafisa wa Ardhi wa Wilaya ili vijiji vipate hati hiyo muhimu sana?
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali Kuu imekuwa inasaidia zoezi la upangaji, upimaji na hata kuandaa matumizi bora ya ardhi katika vijiji na master plan. Hata hivyo, kimsingi kwa mujibu wa sheria, zoezi hili lazima lisimamiwe na ni jukumu la halmashauri husika na vijiji. Ni kweli, kazi ya vijiji kupanga matumizi bora ya ardhi unaweza ukasema ni gharama, lakini viko vijiji ambavyo vimesimamia na vimepanga matumizi bora ya ardhi katika vijiji vyao na maisha yanaendelea vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, gharama za upangaji wa matumizi bora katika kijiji kimoja haizidi shilingi milioni 22. Sasa kama wananchi wote wataona ni busara kutoa shilingi milioni 22 ili kila mmoja mwananchi wa kijiji kile awe na uhakika wa ardhi yake, wafanye hivyo, kwa sababu si gharama kwa sababu unapanga na kupima mara moja katika maisha yenu yote. Kwa hiyo, bado nahamasisha kwamba pamoja na Serikali Kuu kuendelea kusaidia, lakini jukumu hili lazima liwe ni jukumu la msingi, kwa mujibu wa sheria, la mamlaka za vijiji na wilaya husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa, kama nilivyosema, Serikali inaandaa mpango wa jumla wa kupanga na kupima nchi nzima. Mpango huu tutaueleza vizuri kwenye budget speech nitakayosoma mwaka huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili, ni kweli kwamba ni jukumu la Kamishna kutoa cheti cha vijiji. Sasa kama ana taarifa juu ya vijiji ambavyo anahitaji na ambavyo havina vyeti vya vijiji, tuwasiliane ili tujue kwa nini imetokea hivyo tuweze kurekebisha tuwapatie hivyo vyeti.
Waheshimiwa Wabunge, tunaendelea, Mheshimiwa Njalu Daudi Silanga, Mbunge wa Itilima sasa aulize swali lake.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Katika msimu huu wa kilimo…
Mhesimiwa Mwenyekiti, nakushukuru katika msimu huu wa kilimo tumeshuhudia wakulima wa zao la mahindi mazao yao yameshambuliwa na viwavi jeshi aina ya fall army worms na viwavi jeshi hao bado ni tatizo. Nini mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kwamba viwavi jeshi hao wanatokomezwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tumejipanga na sasa hivi ninapozungumza Shirika la WFP wameshatoa dola 250,000 na Serikali pia imeweza kutoa pesa kwa ajili ya kuhakikisha kwamba viwavi jeshi vinatokomezwa katika msimu huu wa kilimo, nashukuru.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mradi wa Maji wa Kijiji cha Getamok, Namahaha na sasa Endonyoet katika Wilaya ya Karatu iliojengwa chini ya Mpango wa WSDP I haufanyi kazi kwa sababu ya kujengwa chini ya kiwango. Serikali ilituma wataalam wake kukagua tatizo hilo ili kubaini kiwango ambacho kingehitajika kufufua miradi hiyo. Je, ni lini sasa Serikali itatoa fedha ili kurudisha huduma hiyo muhimu kwa wananchi?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Qambalo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tumeunda Tume maalum ya wataalam watakaohusisha sekta mbalimbali za Serikali. Tutachukua pamoja na hiyo ripoti ambayo anasema kwamba Serikali ilituma timu tuiangalie ili tukishabaini sasa ule upungufu tutatoa fedha na kukarabati mradi husika.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Spika, Mabaraza haya ya Ardhi hasa yale ya ngazi ya Kata yanafanya kazi kubwa sana kwa sababu yako karibu na wananchi lakini mabaraza haya yamekuwa na changamoto kubwa hususani eneo la maslahi yao kwa maana ya posho za usafiri na posho za vikao pamoja na vitendea kazi. Nini kauli ya Serikali juu ya kuhakikisha Mabaraza yale ya Kata yanawezeshwa ili yafanye kazi zao kwa ufanisi mkubwa? Mheshimiwa Spika, ahsante.
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Karatu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli katika muundo huu wa Mabaraza tunaanza na Mabaraza hayo ya Kata na kwa muundo wake Wajumbe wengi wa Baraza lile ni wenyeji wa maeneo yale. Kazi hii kwa kweli ni ya kujitolea kwa sababu inarahisisha na inaondoa kero ya watu wao, hatuna mtumishi wa kudumu kwenye Baraza la Kata.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunatarajia wananchi wajue hilo na ikiwezekana Halmashauri za Vijiji vinavyozunguka Kata ile wafanye utaratibu wa kuchangia uendeshaji wa lile Baraza la Kata, kwa sababu Baraza lile la Kata linatakiwa kusimamia na kusuluhisha migogoro kadhaa inayokuwepo katika maeneo yanayozunguka pale kwenye Kata. Baada ya hapo rufaa huwa zinaenda kwenye Baraza la Wilaya, kutoka kwenye Baraza la Wilaya rufaa zinakwenda Mahakama Kuu.
Mheshimiwa Spika, nataka nimuarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba hatuna posho kwenye Mabaraza ya Kata. Tunataraji kwamba viongozi wanaopendekezwa na wenzao kufanya kazi ile ni wale ambao wana uwezo na wana uwezo wa kujitolea.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ni zaidi ya miaka miwili na nusu imepita tangu upembuzi yakinifu wa barabara ya Karatu- Mbulu- Haydom ufanyike. Je, ni lini sasa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hiyo utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nafurahi kwamba Mheshimiwa Mbunge amekiri kwamba upembuzi yakinifu ulikwishafanyika na usanifu wa kina umekwishafanyika. Kwa hiyo, hatua zinazofuata Mheshimiwa Mbunge ni kwamba tunatafuta pesa kwa ajili ya kulijenga eneo hilo kwa awamu, na hivi karibuni zitakapopatikana utaona wakandarasi wanaingia pale barabarani kwa ajili ya kuanza kutekeleza mradi huo.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na ahadi ya muda mrefu ya Mawaziri wa Wizara hii kutembelea chanzo cha maji cha Mto Qangded kule Karatu ambacho kinatumiwa na wananchi katika kilimo cha umwagiliaji zaidi ya vijiji sita. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri, yuko tayari sasa kutimiza ahadi yake ya kutembelea eneo hilo ili kutatua changamoto ambazo wakulima wa eneo hilo wanakumbana nazo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nilihakikishie Bunge lako niliahidi kwenda kutembelea Jimbo la Karatu lakini kutokana na changamoto sikuweza kufanikisha ahadi ile. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kabla ya Bunge la Novemba tutatimiza ahadi ile kwa kuhakikisha tunatembelea miradi katika jimbo lake.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Miradi ya maji katika Vijiji vya Getamok, Endonyawed, Kansai, Matala na Fusmai katika Wilaya ya Karatu ambayo ni zaidi ya asilimia 50 ya ile miradi kumi katika kila Wilaya haifanyi kazi kwa sababu ya kujengwa chini ya kiwango. Tatizo kubwa ni kama ilivyoelezwa katika swali la msingi mabomba yanavuja. Mheshimiwa Waziri yuko tayari sasa kuja Karatu ili ajionee mwenyewe jinsi wananchi na Serikali walivyohujumiwa lakini pia akae na Halmashauri ili kuona ni namna gani miradi hiyo inafufuliwa? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kama nilivyosema maeneo mengi hasa ya vijijini miradi mingi iliyotekelezwa ilitekelezwa chini ya viwango. Wameweka mabomba ambayo yako chini ya viwango, wameweka valve ambazo ziko chini ya viwango. Sisi tunahakikisha kwamba sasa tatizo hili linamalizika na pale ambapo mkandarasi ameweka vifaa ambavyo viko chini ya viwango anatakiwa aviondoe na afanye kazi hiyo na aweke vifaa ambavyo vina viwango vinavyokubalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekubaliana na Mheshimiwa Mbunge tutakwenda tutaona tatizo hilo na tutalitatua kwani nia ya Serikali naendelea kusema tena ni kuhakikisha kwamba tunawapelekea wananchi maji safi na salama.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bonde la Eyasi Wilayani Karatu ni maarufu sana kwa kilimo cha umwagiliaji, hasa wa zao la vitunguu maji wakitumia miundombinu ya kiasili ambayo inasababisha maji mengi kupotea njiani kabla hayajawafikia wakulima walioko chini. Je, ni lini Serikali itatenga fedha za kutosha ili kuboresha miundombinu hiyo ya umwagiliaji? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari Serikali imekamilisha mpango kabambe kupitia skimu zote za umwagiliaji na tutaleta teknolojia ambayo itatumia maji kidogo na kwenye bonde lile nimeshafika, na juzi mvua zilinyesha mchanga ukafukia yale macho lakini wananchi wakajitolea, ninayo taarifa na wakati wowote nitakwenda huko ili tuhakikishe kwamba tunaboresha ile skimu ambayo ni muhimu sana kwa wananchi wa eneo la Eyasi. (Makofi)
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya mipaka kati ya Vijiji vya Kata ya Buger na TANAPA, pia Vijiji vya Lositete, Upper kitete, Silahamo na Endamagang na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imekuwa migogoro ya muda mrefu ambayo haipati utatuzi.
Je, Mheshimiwa Waziri uko tayari baada ya Bunge hili kuja Karatu ili kuongoza majadiliano ya kumaliza mgogoro huo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba katika lile eneo kuna baadhi ya migogoro ambayo imejitokeza na imekuwepo kwa muda mrefu, ninaomba niseme tu kwamba niko tayari pale ambapo tutapanga ratiba vizuri mimi na wewe tuende tukaangalie, tukawasikilize wananchi ili tuone ni namna gani tunaweza kutatua hiyo migogoro iliyopo.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Katika msimu wa kilimo wa mwaka jana na hata mwaka juzi, mazao ya mbaazi na kilimo yalipata anguko kubwa kwenye masoko. Hivi sasa msimu wa mavuno wa mazao hayo umeanza katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Je, Serikali ina habari yoyote njema kwa wakulima kuhusu masoko ya mazao ya mbaazi na mahindi? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo mara ya mwisho nilijibu suala la soko la mbaazi, kwanza tumekuwa tukitegemea sana soko hilo kutoka nchi za nje hasa India lakini nao wakawa wamelima kiasi kwamba hawakuweza kununua mbaazi kutoka kwetu. Kupitia TanTrade tumewaagiza kuendelea kufuatilia masoko kwa ajili ya mbaazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huu kwa kutambua umuhimu wa zao hili la mbaazi na umuhimu wake katika afya naendelea kusisitiza kwamba Watanzania tupende pia kutumia mbaazi kwa sababu ni chakula bora na kina lishe nzuri. (Makofi)
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kituo cha Afya Endabash katika Tarafa ya Endabash inahudumia kata nne, lakini kituo hicho kina upungufu mkubwa ikiwemo jengo la mama na mtoto, maabara na mortuary. Ni lini Serikali itatoa fedha ili miundombinu hiyo iliyobaki ikamilike ili kituo hicho kitoe huduma stahiki?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninafahamu Endabash ni sehemu yenye changamoto kubwa. Tukijua wazi kwamba Wilaya yetu ya Karatu ni center kubwa ya watalii, ndiyo maana katika mipango mikakati yetu kwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI tunataka kuangalia tuone ni jinsi gani tutafanya tu upgrade kituo kimoja. Mimi naamini kwamba kwa sababu ya ajenda kubwa ya utalii, jukumu langu kubwa ni kuhakikisha unajipanga vizuri na watu wako, ikifika kabla ya mwezi Disemba kituo hicho kiwe kimekamilika kwa ajili ya kuwatumikiwa wananchi wa eneo hilo.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali madogo ya nyongeza. Pamoja na kuwa na doria za pamoja kati ya halmashauri na hifadhi hizo na pamoja na kuwa na hivyo vituo vilivyotajwa bado kasi ya wanyama waharibifu na wakali kutoka ndani ya hifadhi na kwenda nje kwenye makazi ya wananchi, imeendelea kuwa kubwa mno.
Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa ambayo tunayo kwenye Halmashauri zetu ni Halmashauri hazina usafiri kwa ajili ya kuwafukuza wanyama hao, Halmashauri hazina silaha stahiki kwa ajili ya wanyama hao, lakini pia, bajeti ndogo ambazo Halmashauri tunazo, pia, uchache wa watumishi wa sekta hiyo ya wanyamapori.
Mheshimiwa Spika, hapa imesemwa kuna magari mawili yamenunuliwa kwa ajili hiyo. Magari hayo mawili naamini yako Ngorongoro hayako Karatu huku ambako tatizo lilipo. Sasa Mheshimiwa Waziri anaweza akaongea na watu wake wa Ngorongoro ili angalau gari moja liwekwe Halmashauri, wale Maofisa wa Halmashauri pindi tatizo linapotokea waweze kwenda kushughulika?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, fedha hizi za kifuta jasho au kifuta machozi, pamoja na kwamba, ni ndogo sana lakini pia, zinachelewa sana kuwafikia...
Mheshimiwa Spika, swali; kwa nini fedha hizi zisilipwe kwenye hifadhi husika badala ya mlolongo ambao sasa hivi zinalipwa kutoka Wizarani? Mheshimiwa Spika, ninakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa kumekuwa na changamoto hizi za kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu katika maeneo mengi. Changamoto ziko katika upande wa usafiri, watumishi, pamoja na vifaa vile vinavyotakiwa kutumika katika kupambana na hao wanyamapori.
Mheshimiwa Spika, sasa niombe kusema tu kwamba, kama nilivyosema kwenye swali la msingi, magari mawili yameshanunuliwa na tayari kweli yako pale. jitihada ambazo tutafanya ni kulingana na jinsi ambavyo amependekeza Mheshimiwa Mbunge, kuhakikisha angalau gari moja linakuwepo katika maeneo yale kusudi pale linapotokea tukio basi gari hilo liweze kusaidia katika juhudi hizo za kupambana na wanyama wakali.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili, kuhusiana na fedha za kifuta jasho na kifuta machozi kwamba, ziwe zinatolewa na hifadhi inayohusika, ni suala ambalo labda tutaliangalia wakati tunapitia upya hizi sheria ambazo tutaona kama kweli, inafaa. Kwa hivi sasa ilivyo tuna mfuko maalum ambao unatumika kwa ajili ya kifuta jasho na kifuta machozi.
Mheshimiwa Spika, huu mfuko bado unakabiliwa na changamoto ya kuwa na fedha za kutosha. Kwa hiyo, katika pendekezo analolileta nafikiri tutaliangalia, tutaona kama linafaa, tunaweza tukalichukua. (Makofi)
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Katika mwaka wa fedha unaokuja, Serikali imetenga fedha za kujenga Hospitali za Wilaya kwenye maeneo 67, lakini pia ni wazi zipo Wilaya nyingi ambazo bado hazina Hospitali ya Wilaya ikiwemo Wilaya yangu ya Karatu. Ni lini sasa wananchi wa Karatu wategemee kujengewa Hospitali ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimekuwa nikijibu hapa, kuanza na Hospitali za Wilaya 67 tafsiri yake ni kwamba zikikamilika hizo tutakwenda kujenga nyingine. Ni azma ya Serikali inayoongozwa na CCM kuhakikisha kwamba Wilaya zote ambazo hazina Hospitali za Wilaya baada ya kumaliza hizi 67 tutakwenda hatua nyingine ya kwenda kuzijengea.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Mbunge avute subira, bajeti ndiyo imepita, tumwombe Mwenyezi Mungu makusanyo yetu yaende vizuri, tukimaliza 67 tutakwenda hatua ya pili.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ujenzi wa barabara ya Oldian Junction – Mang’ola – Matala - Kolandoto umeshakamilika miaka miwili iliyopita na barabara hiyo ni muhimu sana kwa sababu inaunganisha Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Simiyu. Je, ni lini sasa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hiyo utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Qambalo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli ukiotokea upande wa Lalago ukivuka Sibiti kwa kushoto kule iko barabara hii ambayo itakuwa inakwenda Karatu ambayo michoro na usanifu wake umeshakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii ina interest kubwa sana kwa sababu kuna uzalishaji mkubwa, historia muhimu na pia kuna utalii mkubwa katika maeneo haya. Kwa hiyo, kwa sababu hatua hii imeshakamilika, tuko kwenye hatua ya kutafuta fedha, wakati wowote tukipata fedha ujenzi utaendelea. Ahsante sana.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu yasiyoridhisha kabisa ya Mheshimiwa Waziri ninayo maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, upimaji na uhifadhi wa chanzo cha maji cha Qang’dend si tu ni takwa la kisera na kisheria bali pia ilikuwa ni agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Majaliwa alipotembelea bonde la Eyasi mwishoni mwa mwaka 2016. Ni jambo la kushangaza kwa muda huo wote hadi sasa hatua hiyo ya uhifadhi haijafanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu ni kwamba, je, Mheshimiwa Waziri, yuko tayari sasa baada ya Bunge hili kwenda kutembelea vyanzo hivyo katika Bonde la Eyasi ili ashuhudie mwenyewe kwamba majibu aliyopewa si sahihi na achukue hatua stahiki kwa hawa ambao wametoa majibu hayo?
Mheshimiwa Naibu Spika, swai la pili; kutokana na mvua nyingi zilizonyesha mwaka huu, chanzo hicho kimeharibika na kuathirika sana kutokana na mchanga kujazwa kwenye macho ya chemchem kiasi kwamba wananchi wenyewe wa Bonde la Eyasi wamejichangisha Sh.21,000,000 na Halmashauri ya Wilaya ya Karatu kutokana na mapato yake ya ndani imechan gia Sh.35,000,000 ili kuokoa vyanzo hivyo; lakini bado zinahitajika fedha zaidi ili kunusuru vyanzo hivyo. Je, Mheshimiwa Waziri, Wizara yake iko tayari sasa kuweka mkono ili kuunga mkono jitihada za wananchi hao? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru, lakini nipende kumjibu Mheshimiwa Mbunge; moja, ukirejea katika majibu ya swali lake la msingi tumeweka alama lakini baadhi ya alama hazionekani. Hata hivyo, kama Naibu Waziri wa Maji nataka nimhakikishie kwamba nipo tayari kufika katika Bonde la Eyasi na kujiridhisha katika haya majibu yametolewa ikitokea kwamba kuna udanganyifu kwa haya majibu, sichelei kusema watapata tabu waliondika haya majibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali lake la pili, ni kuhusu suala zima la sisi kama Wizara kumuunga mkono. Waziri wangu amenipangia kufanya ziara katika mikoa mine, mojawapo ni Mkoa wa Arusha. Nataka nimhakikishie nikifika katika eneo lile Mang’ola nitahakikisha namna gani tunaweza tukashauriana katika kuongeza nguvu zetu ili mwisho wa siku umwagiliaji katika chemchem ile uendelee na wananchi wake waendelee kuzalisha. Ahsante sana.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kata za Rhotia na Mbulumbulu Wilayani Karatu ni maarufu sana kwa uzalishaji wa mazao ya chakula. Hata hivyo barabara za kuelekea kwenye kata hizo zinazounganisha Makao Makuu ya Wilaya ya Karatu zina hali mbaya sana kwa kukosa matangenezo ya mara kwa mara lakini pia kutokana na mvua zilizonyesha mwaka huu; je, ni nini kauli za Serikali kwa Meneja wa TARURA Mkoa ili barabara hizo ziweze kutengenezwa ili wananchi waweze kufika kwenye masoko?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimpongeze kaka yangu Mbunge wa Karatu. Kubwa zaidi ni kwamba maelekezo yetu si kwa Meneja wa TARURA wa Mkoa wa Arusha peke yake, isipokuwa ni maelekezo yetu kwa Mameneja wa TARURA wote katika mikoa yote 26, kwamba wafanye needs assessment ya barabara zetu zote zilizoharibika. Lengo letu kubwa ni kwamba kile kichache tutakachokuwa nacho kwa ajili ya ukarabati tuweze kurekebisha maeneo hayo. Kwa hiyo ni maelekezo yangu kwa meneja wa TARURA wa Mkoa wa Arusha na hali kadhalika Mkoa wa Babati, Wilaya ya Karatu wafanye hivyo haraka iwezekanavyo watupe taarifa.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kusisitiza kwamba Awamu ya Tatu ya REA ni awamu ya kuwasha Tanzania nzima na kwamba umeme utakapokwenda vijijini hakuna hata kaya itarukwa. Ni ukweli kwamba usambazaji huu unapofanyika vipo vitongoji au vijiji coverage inakuwa ni ndogo sana. Mfano Kijiji cha Gwangali kule Karatu, kati ya vitongoji vitano, ni vitongoji viwili tu ndiyo umeme umevifikia. Nini kauli ya Serikali juu ya wakandarasi hawa ambao hawazingatii maelekezo ya Serikali?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Karatu, ambaye ameuliza nini kauli ya Serikali?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu jana kupitia hotuba ya bajeti yetu ya Wizara ya Nishati, tumesema kinagaubaga kwamba mkakati wa Serikali ni kuhakikisha vijiji na vitongoji vinafikiwa na huduma ya umeme. Kwa hiyo, tumetoa rai kwa wakandarasi. Kwa mujibu wa hotuba yetu, tumesema kutokana na mpango huo na ndiyo maana kuna vijiji vya nyongeza 1,541 ambavyo tunavifanyia uhakiki. Kwa hiyo, naomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge, nia ya Serikali ni kufikisha umeme kadri inavyowezekana. (Makofi)
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Wilaya ya Karatu ina zaidi ya umri wa miaka 20 na haina hospitali ya wilaya badala yake wananchi wamekuwa wakipata huduma hiyo katika vituo vya afya binafsi na hata vile vya chini. Tayari kama Halmashauri tumeshatenga eneo la kutosha la kujenga Hospitali ya Wilaya. Je, ni lini Serikali sasa itatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la kaka yangu, Mheshimiwa Mbunge wa Karatu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya ujenzi wa vile Vituo vya Afya 350 ambavyo tunaendelea navyo kama tunavyofahamu mpango wa Serikali katika mwaka huu wa fedha tunajenga hospitali mpya 67. Hata hivyo, mwaka huu wa fedha tena 2019/2020 bajeti tunayoenda nayo tutachukua maelekezo jinsi gani tufanye zile wilaya ambazo hazina hospitali za wilaya twende tukamalize tatizo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu Mkoa wa Arusha tulielekeza nguvu kazi kule maeneo ya Ngorongoro na
Longido hata hivyo katika bajeti ya mwaka huu ambao tunaenda kuipanga, si muda mrefu Aprili, 2019 tuka-take consideration ya maeneo hayo. Lengo ni kwamba wananchi wote wapate huduma kama inavyokusudiwa.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Ni sera ya Serikali kuwa na hospitali katika kila wilaya. Wilaya ya Karatu haina Hospitali ya Wilaya na hivi karibuni Halmashauri imetenga eneo la kutosha kwa ajili ya kujenga hospitali hiyo na wananchi kwa kutumia mapato yao ya ndani pamoja na wadau mfano Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro wameanza kujenga…

NAIBU SPIKA: Uliza swali lako Mheshimiwa Qulwi.

MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali sasa iko tayari kutoa fedha ili kukamilisha ujenzi wa hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ni kweli kwamba sasa hivi Serikali ipo kwenye hatua ya kujenga Hospitali za Wilaya mbalimbali nchini na hatua ya kwanza tulianza na hospitali 67 na awamu ya pili inaendelea. Tunawapongeza wananchi wa Karatu kwa kuendelea kuchangia huduma hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri tukamilishe kwanza hizi zilizopo baada ya hapo tutachangia na kumalizia Hospitali ya Mheshimiwa wa Karatu pia na maeneo mengine nchini. Hatua ya kwanza majengo yamekamilika tunapeleka vifaa tiba na kuna hatua ya pili ya wataalam mbalimbali. Tukianza kutoa huduma katika vituo hivyo nafikiri tutaenda na eneo letu la Karatu. Ahsante.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Miradi ya maji katika Vijiji vya Matala, Kansay, Buger, Endonyawet na Getamock Wilayani Karatu chini ya mpango wa WSDP imejengwa chini ya kiwango na hivyo haifanyi kazi, karibu shilingi bilioni nne zimetumika na haziwanufaishi wananchi. Tulimwomba Mheshimiwa Waziri mara nyingi aje Karatu ili aje atatue tatizo hilo…

MWENYEKITI: Uliza swali sasa.

MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba awaambie wananchi wa vijiji hivyo ni lini atakwenda ili kutatua changamoto za miradi hiyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Mbunge, binafsi nilishapata taarifa za Karatu na nimefika, lakini kubwa kuna miradi ambayo imefanyiwa ubadhirifu. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge sisi kama Viongozi wa Wizara tumesha-note na tumekubaliana tutakwenda katika maeneo yale yote na wale walioshiriki katika ubadhirifu ule, lazima fedha watazitapika na hatua kubwa kali tutazichukua.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mji wa Karatu ni Mji wa Kitalii na hauna soko la uhakika. Hivi sasa wananchi wa Karatu kwa kutumia mapato yao ya ndani wameanza kujenga soko lenye hadhi ya Mji huo: Je, Serikali iko tayari sasa kuunga mkono jitihada za wananchi hao ili soko hilo likamilike?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Katika Mkoa wa Manyara tayari tuna mradi wa kimkakati katika Wilaya ya Hanang’. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, fedha zipo, Serikali ipo tayari kutoa ushirikiano. Cha muhimu, Halmashauri husika ikae na kutoa andiko, likija hapa kwenye tathmini hili jambo litafanyika. Sisi tunakusudia kuweka masoko, stendi na majengo mbalimbali ya kimkakati ili baada ya kuwekeza katika maeneo hayo, Halmashauri zetu zipate mapato ya kutosha ili kuweze kuendeleza na kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wananchi wetu.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Hali ya upatikanaji wa maji katika kijiji hicho ni mbaya sana, ukiongea habari ya vituo vitatu kwa wananchi zaidi 5,000 ni chini kabisa ya kiwango ambacho kinaruhusiwa. Sasa nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, Mheshimiwa Waziri anajua Halmashauri ya Wilaya ya Karatu ina idadi ndogo ya watumishi katika sekta ya maji na kazi za kitaalam alizozielekeza kwa idadi ya wataalam tulionao haitaweza kukamilika. Je, yuko tayari sasa kuongeza nguvu ya uhandisi na wataalam wa survey ili kazi hiyo aliyoelekeza ifanyike kwa muda unaotakiwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, vyombo vya watumia maji, mfano, Bodi za Maji, Mamlaka Jumuiya za Watumia Maji na Kamati za Maji zinatambulika kisheria na vimetoa huduma za usimamizi na uendelezaji wa miradi ya maji. Hivi karibuni Serikali imesimamisha uchaguzi wa chombo cha maji kinachoitwa KAVIWASU pale Karatu ambacho kimetoa huduma hiyo kwa zaidi ya miaka 20. Je, ni halali Serikali kuingilia mchakato wa kupata viongozi wa wananchi ili waweze kusimamia chombo chao? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake zuri, lakini kubwa sisi kama Wizara ya Maji tunatambua changamoto kubwa sana ya maji Karatu na ndio maana tuna mradi mkubwa sana wa TOM zaidi ya milioni 650 ambao tunautekeleza. Kikubwa tunatambua utekelezaji wa miradi ya maji unategemeana na watumishi wa kutosha wenye weledi na wenye uwezo na sisi kama Wizara ya Maji ndio maana tukaja na Wakala wa Maji. Nataka nimhakikishie uanzishwaji wa wakala ule tutahakikisha tunaweka wataalam wetu wa kutosha na katika eneo lake ili mwisho wa siku wananchi wa Karatu waweze kupata maji safi, salama na yenye kutosheleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu chombo cha watumiaji maji, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge hilo nimelipokea hebu tulifuatilie kwa ukaribu ili tuweze kulitolea ufafanuzi wa haraka. Ahsante sana.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pia kumekuwa na mpango wa kujenga reli itakayopita Kaskazini mwa nchi itakayounganisha Miji ya Tanga, Moshi, Arusha hadi Musoma. Je, mpango huo umefikia hatua gani? Ahsante.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali moja dogo la Mheshimiwa Mbunge Qambalo lakini kikubwa nimwombe leo tunawasilisha bajeti, asiwahishe shughuli, taarifa zote atazipata kwenye kitabu cha bajeti.
MHE. WILLY Q. QAMBALO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, mkandarasi Nipol group anayefanya usambazaji wa umeme katika Mkoa wa Rushu hususani Wilaya ya Karatu kazi yake ya usambazaji ni ndogo sana, hivi sasa pamoja na kwamba muda wake wa ukandarasi unakaribia kuisha lakini bado vijiji vingi vya Kata za Bugeri, Kansai Endamarieki havijafikiwa na umeme. Nini kauli ya Serikali juu ya mkandari huyo ambaye anasuasua?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kazi za ujenzi wa mradi wa REA Awamu ya III mzunguko wa kwanza zinaendelea na mkandarasi Nipol anafahamu kabisa hivi karibuni tulifanya kikao cha wakandarasi wote na kwamba tumewaambia kwamba ifikapo tarehe 30 Juni, 2020 mradi utakuwa umekamilika na watakabidhi vijiji vyote vitakuwa vimejengewa miundombinu ya umeme na kazi ya kuwasambazia wateja itaendelea.

Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Mbunge baada ya kipindi cha maswali na majibu tuonane ili tuweze kuzungumza zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimthibitishie tu usimamizi umeimarishwa na ni muagize mkandarasi Nipol kwa niaba ya Waziri wa Nishati kwamba azingatie dead line iko pale pale na aitaongezwa muda wowote kwa wakandarasi wote nchini lazima wakamilishe tarehe 30 Juni, 2020 ili uunganishaji pamoja na miundombinu. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na maelekezo yaliyotolewa kwa Halmashauri kutenga fedha kwa ajili kuyawezesha Mabaraza haya, lakini ni ukweli usiopingika kwamba Halmashauri nyingi bado hazijaona umuhimu wa kutenga fedha ili Mabaraza haya yafanye kazi zao kwa weledi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza; kwa kuwa suala kutoa maamuzi kwenye masuala ya ardhi ni suala muhimu sana: Kwa nini Serikali isichukue sasa jukumu hili kama ambavyo imechukua jukumu la kuyawezesha yale Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya ili haki iweze kutendeka vizuri? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Wajumbe wa Mabaraza haya wanapoteuliwa, wanapewa semina ya masaa kadhaa, baadaye wanaapishwa, lakini semina ya masaa kadhaa kwa mtazamo wangu haitoshi kwa watu wanaofanya kazi muhimu ya kutoa maamuzi kama haya: Kwa nini Serikali isije na mpango mahsusi wa mafunzo kwa Wajumbe hawa ili waweze kufanya kazi yao kwa weledi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Ni kweli kwamba mabaraza haya yanasimamiwa na Halmashauri na Mheshimiwa Mbunge anasema Serikali ichukue jukumu hili la kusimamia Mabaraza ya Kata. Katika mgawanyo wa kazi kwa maana ya Ugatuzi wa Madaraka (D by D) tumegawana kwamba Halmashauri itasimamia Mabaraza ya Kata ya Ardhi halafu na Serikali Kuu itaanzia ngazi ya Wilaya kwenda kule juu na Mheshimiwa Mbunge ni Diwani katika Halmashauri yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba, Mabaraza haya hata baada ya kuwa yameteuliwa, usimamizi wake na uangalizi unasimamiwa na Halmashauri chini ya ulezi wa Mwanasheria wa Halmashauri zetu. Kwa hiyo kama kuna upungufu katika eneo hili ni muhimu kama Mheshimiwa Mbunge anavyosema tuchukue hatua na kuelekeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe maelekezo hapa kwa Wakurugenzi wote na Waheshimiwa Wabunge mtusaidie. Kwenye Bajeti ambayo inatengwa pale, mpaka wameelekezwa vikao vingapi wakae katika maeneo hayo ili kuhakikisha kwamba haki inatendeka. Kwenye Bajeti ambayo inaendelea sasa tupitie: Je, kipengele hiki kimewekwa katika Bajeti yetu? Kama kuna tatizo, Bajeti ikifika hapa tuwasiliane ili tuweze kufanya marekebisho hayo. Wakurugenzi wana wajibu huo wa kusimamia, kutenga fedha na kuwezesha.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili Mheshimiwa Mbunge anataka kujua kwamba mafunzo yanatolewa kwa muda mfupi sana, lakini suala la mafunzo ni jambo endelevu. Kama kuna upungufu katika eneo lile Mwanasheria na Viongozi wa Halmashauri; na kama wanashindwa wataomba usaidizi katika ngazi ya Taifa, wanaweza kufanya mafunzo kadri inavyohitajika kutoka muda hadi muda mwingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, hayo ndiyo maelekezo ya Serikali, naomba wazingatie. Kama kuna upungufu tuwasiliane tuweze kuchukua hatua kwa maana ya case by case. Ahsante.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Mji wa Karatu ni Mji wa Kitalii na ni mji ambao unakua kwa kasi sana, lakini bahati mbaya mji huo hadi wa sasa hauna soko la uhakika, Halmashauri kwa kutumia mapato yake ya ndani imeanza ujenzi wa soko la kisasa, je, Serikali lini itaunga mkono jitihada hizo za Halmashauri ya Karatu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba nijibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Qambalo Mbunge wa Karatu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi ni kwamba Halmashauri zote hizi Wakurugenzi wameelekezwa, wameitwa Dodoma Wakurugenzi wote nchi nzima, Waweka Hazina, Maafisa Mipango wakapewa utaratibu, Serikali inachofanya kama soko lenu mnadhani kwamba linakidhi viwango walete kama nilivyosema andiko ili fedha zitolewe waweze kufanya kazi, wanakopeshwa fedha, wanawekeza, wanasimamia wenyewe, wanaanza kurejesha kidogo kidogo. Hiyo ni fedha ambayo ina uhakika tofauti na kuahidiwa bilioni kumi halafu haiji au unapata bilioni moja. Fedha za Miradi ya Kimkakati zipo, walete andiko tupitie, wapate fedha wasimamie na Mheshimiwa Mbunge awepo ili wapate fedha ya uhakika na soko lisimame wapeleke huduma na kupata mapato mema ya kujenga Halmashauri yao.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Miradi ya maji mitano iliyojengwa chini ya mpango wa WSDP katika Wilaya ya Karatu, Kijiji cha Buger, Kansay, Getamok bado haifanyi kazi kwa ajili ya kujengwa chini ya kiwango:-

Ni lini Serikali itawawajibisha Wakandarasi hao ili wananchi wapate huduma stahiki?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwa ufupi sana, hatuna sababu tena ya kumwona Rais wetu anasononeka au Waheshimiwa Wabunge wanasononeka, mmeshatupa rungu. Ninachotaka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge, baada ya Bunge nitafika Karatu kwa wale wote waliohujumu miradi ya maji, tutawachukulia hatua na kama fedha, watazitapika. Ahsante.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, pamoja na majibu hayo ya Serikali ninayo maswali mawili ya nyongeza. Changamoto kubwa ya upatikanaji wa hatimiliki za ardhi ni pamoja na gharama kubwa zinazohusu upimaji wa maeneo. Jambo ambalo wananchi wengi wanalishindwa hasa pale ambapo upimaji unatakiwa ufanyike kwa kundi kadhaa kubwa la wananchi ili yapimwe kwa pamoja. Kwa nini Serikali isipunguze gharama hizo ili wananchi waweze kupata fursa ya kumiliki ardhi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Waziri wa Ardhi Mheshimiwa Lukuvi alipokuwa Karatu tarehe 07 Machi, mwaka huu aliagiza kufutwa kwa hatimiliki ya ekari 20 katika Kitongoji cha Ngorongoro, Ayalabe, Kata ya Ganako ambayo ilitolewa kinyemela kwa mtu binafsi. Hadi leo ni takribani miezi minne eneo hilo bado halijarudishwa kwa umma;

Je, nini kauli ya Wizara kwa Kamishna wa Ardhi Kanda ya Kaskazini ili kutekeleza agizo hilo la Waziri ambalo wananchi walilishangilia sana? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza amezungumzia kwamba gharama za upimaji ni kubwa na hivyo wananchi wengi wanashindwa kulipa na wakati mwingine wanakuwa wako kundi kubwa wanaopimiwa. Naomba tu nimkumbushe Mheshimiwa Mbunge ya kwamba gharama za upimaji zimepunguzwa sana katika kipindi hiki cha miaka mitatu na huu mwaka wa nne tumeanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukikumbuka wakati tunaanza mwaka 2015/2016, gharama za upimaji zilikuwa juu sana zilikuwa wanachaji kwa ekari moja shilingi 300,000. Premium ilikuwa asilimia 15, ikapunguzwa ikawa asilimia 7.5 mwaka wa fedha uliofuatia. Kama hiyo haitoshi mwaka wa fedha uliofuatia 2017/2018 ikapunguzwa ikawa asilimia 2.5 na sasa hivi imepunguzwa ikawa asilimia moja. Maana yake ni kwamba zinakwenda zinapungua kutegemeana pia na uhitaji kama walivyosema.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tukumbuke hapa katikati tumekuwa na zoezi kubwa la urasimishaji ambalo limechangia katika kupima maeneo mengi sana. Wakati wanaanza gharama zilikuwa kubwa, zilikuwa kwenye kama 250,000 mpaka 300,000 lakini kwa sasa kuna watu wanapimiwa kiwanja kwa shilingi 60,000; kuna watu wanapimiwa kwa 150,000; kuna watu wanapimiwa kwa 90,000, mifano tunayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda Halmashauri ya Chemba nadhani wako kwenye 90,000; ukienda kwenye Halmashauri ya Mkinga wako kwenye 90,000; kwa hiyo zinakwenda zinashuka pia kutegemeana na uhitaji wa watu, kadri unavyokuwa na volume kubwa ya kazi na bei inapungua. Maeneo mengi sasa hivi yamepimwa kwa njia ya urasimishaji lakini katika kaya zinazopimwa kwa taratibu za kawaida gharama bado siyo kubwa kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amelalamikia.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili amezungumzia kufutwa kwa hatimiliki katika eneo la shamba moja katika Eneo Lake. Naomba niseme Mheshimiwa Waziri kutamka kwamba hati hiyo ifutwe ni jambo moja, lakini jambo la pili ni process pia kuhakikisha inafutwa na umiliki wake unaanza tena upya kwa namna itakavyokuwa. Unapofuta zile hatimiliki haina maana kwamba basi hapo hapo wanaanza kugawiwa, kuna utaratibu ambao lazima Mheshimiwa Rais aidhinishe na ikiidhinishwa inarudi kwa halmashauri husika na kuwekewa mpango maalum kwa ajili ya matumizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, haufutwi tu ukaletwa kwa wananchi moja kwa moja, unakuwa pia na maelekezo ya namna ya kupanga matumizi kutegemeana na mahitaji yalipo. Kwa hiyo, naomba nikuhakikishie tu kwamba ahadi iliyotolewa na Mheshimiwa Waziri iko pale pale na muda utakapokamilika basi tutawaletea utaratibu wa matumizi mtakayokuwa mmejiandalia.