Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Mary Michael Nagu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Hanang'

Primary Question

MHE. DKT. MARY M. NAGU aliuliza:- Serikali ilitoa fedha kiasi cha shilingi milioni 400 za awamu ya kwanza kwa ajili ya skimu ya umwagiliaji katika Kijiji cha Endagaw na mradi huo kwa ujumla unagharimu shilingi milioni 800:- Je, ni lini Serikali itamalizia kiasi cha fedha kilichobaki ili kukamilisha mradi huo?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa maji ya kijito cha Endagaw yamekuwa mengi kuliko utaalamu ulivyoona na kwa hivyo mfereji mmoja unaweza ukafanya ukuta uliojengwa kubomoka.
Je, Waziri anaweza kuwahakikishia watu wa Endagaw na wa Hanang kwamba huu upande wa pili utajengewa mfereji mara moja?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, palipokuwa na kijito cha Endagaw kulikuwa na wananchi ambao walikuwa na shughuli zao na makazi yao na wakaondolewa kwa ajili ya skimu hiyo.
Je, Serikali inaweza kutusaidia kuwapa fidia wale watu ambao wameondoka pale kwa ajili ya mradi huu? Namuomba Mheshimiwa Waziri aweze kutembelea eneo hilo na kuona umuhimu wa maswali haya mawili ya nyongeza niliyoyauliza, ahsante.

Name

Eng. Gerson Hosea Lwenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze kwa kuibua swali hili. Tunasema kwamba ili tuweze kupata chakula cha kutosha lazima tuende kwenye kilimo cha umwagiliaji. Sasa hivi Taifa letu tumeshaanzisha Tume ya Umwagiliaji itakayosimamia eneo hili. Mpaka sasa Taifa linalima hekta 461 tu tunataka katika miaka mitano ijayo tufikishe hekta milioni moja. Sasa kwa kuanzia na hiki Kijiji cha Endagaw ambapo tayari tumeahidi kuendelea kujenga skimu ile, hizo laki nne tutazipeleka lakini tutaboresha kwa namna ambavyo anashawishi Mheshimiwa Mbunge ili wananchi wale waweze kupata faida ya kilimo cha umwagiliaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili nitakwenda kuangalia katika kuwahamasisha wale wananchi tutaona namna gani ya kuwafidia. Jambo moja zuri ni kwamba fidia nzuri ni ile kuwajengea skimu ambayo wataweza kuendelea kulima kuliko wakipewa fedha lakini wasiendelee kulima. Kwa hiyo, tutaangalia namna bora ya kuwafidia kwa kujenga skimu ili walime kilimo cha umwagiliaji.