Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Zaynab Matitu Vulu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ZAYNABU M. VULU (K.n.y. MHE. ANNA R. LUPEMBE) aliuliza:- Wanawake wengi wa vijijini hawakopesheki kwa sababu benki haziwafikii huko vijijini lakini pia hawana mafunzo maalum ya kuwasaidia ujuzi wa namna ya kufikia huduma hiyo ya kukopeshwa. (a) Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka huduma ya benki kwenye vijiji ili wanawake wa huko waweze kupata mikopo? (b) Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwapa akina mama hao mafunzo maalum yatakayowasaidia katika kujipanga kukopa?

Supplementary Question 1

MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza ni kutaka kujua Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia akina mama walioanzisha VICOBA kwa kuongezewa mtaji wao? Pia Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha taasisi binafsi zinazotoa mikopo kuacha kunyanyasa akina mama wanapochelewa kulipa mikopo yao kwa kuwanyang‟anya vifaa vyao vya matumizi na vinavyowaendeshea maisha? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni lini Serikali itashawishi mabenki kutupelekea benki kwenye Wilaya ya Mafia na Jimbo la Utete? Kwa sababu Makao Makuu ya Wilaya ya Rufiji ni Utete lakini mpaka leo hapo Utete hakuna huduma inabidi waende Kibiti kufuata huduma. Ahsante.

Name

Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Answer

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili japo yameonekana kama manne ya Mheshimiwa Zaynabu Vulu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza ni akina mama kuongezwa mtaji kwa kuwa wameanzisha VICOBA. Kwanza kabisa naomba niwapongeze akina mama wote nchini kwa kuonesha ujasiri wao katika kuungana katika vikundi na kuanzisha VICOBA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi kwamba Serikali imeweka mazingira mazuri na tayari taasisi za kifedha au benki za jamii zinaanzishwa hivyo nawashauri akina mama hawa na mimi nitashirikiana nao kama mama kuhakikisha kwamba tunaanzisha taasisi au benki yetu ya kijamii ya wanawake sehemu yoyote ile. Naomba nitoe nafasi hiyo, tushirikiane kwa pamoja Wabunge wanawake ili tuweze kuungana na akina mama hawa kuanzisha benki ya wanawake ya kijamii sehemu yoyote ile ndani ya nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya pili ya swali hili la kwanza ilikuwa ni taasisi za kifedha zinazokopesha ziache kuwanyanyasa akina mama. Napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba kama nilivyojibu wiki moja iliyopita Serikali inaanzisha rasimu ya sera kwa ajili ya taasisi hizi ndogo za fedha ili sasa kuweza kuzikagua na kuziwekea sheria na taratibu ya kuweza kufanya kazi na kuacha kuwanyanyasa akina mama. Sera hii itakapokuwa tayari, nina uhakika kabisa taasisi hizi zitaacha kuwanyanyasa akina mama. Pia naomba niwashajihishe taasisi zote hizi zinazotoa mikopo kwa akina mama ziache utaratibu huu wa kuwanyanyasa akina mama. Tufuate taratibu zote za utoaji wa mikopo kama vile kuangalia uwezo wa mlipaji anayekopa kabla hujamkopesha kuliko kumkopesha tu kwa kuonekana wako kwenye kikundi halafu baadaye unakuja kuwanyanyasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, nilisema ameuliza maswali mawili lakini yanaonekana kama manne, kwa hiyo, kulikuwa na sub-questions. Napenda kulijibu swali hili, kwamba ni lini Serikali itaweza kuzishawishi benki kupeleka matawi yao Mafia na Rufiji?
Namuomba Mheshimiwa Zaynabu Vulu tushirikiane tuone ni jinsi gani ya kuongea na benki zetu na hasa benki yetu ya NMB na CRDB, nina uhakika wakienda ku-access mazingira ya Mafia wataenda kufungua tawi lao sehemu hii. Naomba tukae na Mheshimiwa Zaynabu Vulu tuone ni jinsi gani ya kushughulikia suala hili.