Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Primary Question

MHE. ELIAS J. KWANDIKWA aliuliza:- Serikali imekuwa ikitumia waajiriwa wa muda (vibarua) ambao hawana ujuzi, uadilifu wala taaluma ya uhifadhi:- (a) Je, ni vibarua wangapi walitumiwa katika Hifadhi ya Kigosi kwa kipindi cha miaka mitano (2010-2015)? (b) Je, Serikali ilikuwa imetenga kiasi gani cha fedha na ni kiasi gani kililipwa kwa vibarua hao?

Supplementary Question 1

MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize maswali madogo ya nyongeza. Nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri. Kwa kuwa Askari wa Wanyamapori ni wachache na kwa kuwa hifadhi zimekuwa zikiwatumia Askari wa Wanyamapori wa kujitolea kwa kufanya doria na kwa kuwa askari hawa wanapofanya kazi kama maeneo ya Kigosi kwenye mipaka ya Jimboni kwangu wamekuwa na utaratibu wa kufanya doria na kujilipa. Haoni sasa wakati umefika Serikali ichukue hatua kukomesha tatizo hili ili kuondoa migogoro kwa wafugaji? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Sheria ya Uhifadhi inatoa fursa ya wananchi kushiriki katika uhifadhi kwa kutumia vikundi vya kijamii pamoja na vikundi ambavyo vipo vijijini. Je, Serikali iko tayari kuweka msukumo wa aina yake ili kuhakikisha kwamba vikundi vya jamii ikiwepo sungusungu wanahusika katika uhifadhi ili kupunguza migogoro?

Name

Prof. Jumanne Abdallah Maghembe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Answer

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Askari wa Wanyamapori ni wachache lakini pia malipo yao na mishahara yao ni midogo sana. Kuanzia mwaka 2016/2017, Serikali italigeuza jeshi au askari hawa wa wanyamapori kuwa jeshi usu au paramilitary force ili kushughulikia ujuzi na uwezo wao, lakini pia kuangalia kwa undani mafao na mishahara yao ili wawe walinzi thabiti katika kulinda maliasili zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli pia kwamba vikundi vya wananchi hata vikundi vya sungusungu vinaweza kulisaidia sana Jeshi la Wanayamapori katika kulinda na kuhifadhi maliasili zetu. Serikali imechukua wazo hili zuri na tutalifanyia kazi ili tuone ni jinsi gani vikundi hivi vinaweza kusaidiana na askari katika kuhifadhi mali zetu.