Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Priscus Jacob Tarimo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Moshi Mjini

Primary Question

MHE. PRISCUS J. TARIMO aliuliza:- Je, ni nini mpango wa Serikali wa kukamilisha Mradi wa Jengo la Mama na Mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi ambao umeanza tangu mwaka 2008/2009 bila kukamilika?

Supplementary Question 1

MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali hii ni ya Rufaa ya Mkoa na ukisoma vitabu vya bajeti kwenye mwaka uliokwisha ilikuwa inahudumia wagonjwa karibu 75,000; mwaka huu ambao tunaumalizia wameongezeka wamefikia 96,000 na ni ongezeko la karibu asilimia 13. Lakini pia vitu vya kawaida kabisa kama nyuzi za kushona, kama giving set, vitu vya kawaida kabisa kwa ajili ya huduma ya akinamama havipatikani na ni Hospitali ya Rufaa.

Je, Serikali inatoa commitment gani kuhakikisha vitu hivi vya kawaida kabisa vinapatikana wakati tunasubiri ukamilishaji wa jengo hilo la mama na mtoto?

Name

Dr. Godwin Oloyce Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Siha

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge Priscus Tarimo kwa jinsi ambavyo anafuatilia kwa umakini sio tu hospitali yetu ya Mawenzi, lakini na Hospitali ya Kanda ya Rufaa ya KCMC hasa kwenye maeneo ya miundombinu, lakini kwenye kuwatetea na kufuatilia maslahi ya watumishi wa hospitali zetu hizi zote mbili.

Swali lake ni kwamba ni lini Serikali itahakikisha kwamba vifaa vinapatikana, ametaja nyuzi na vitu vingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo huko nyuma mmesikia Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan mwezi wa pili alitoa shilingi bilioni 43 kwa ajili ya vifaa tiba na dawa, lakini mwezi wan ne alitoa shilingi bilioni 80 kwa hiyo, ukijumlisha ni kama shilingi bilioni 123 zimetolewa kwa ajili ya eneo hilo la huduma ya tiba. Kikubwa ni kwamba ndani ya mwezi mmoja vifaa hivyo vitakuwa vimefika kwa sababu vimenunuliwa viwandani na hilo tatizo litakwenda kuisha na hospitali yetu itakuwa na vifaa vyote ambavyo vinahitajika. (Makofi)

Name

Flatei Gregory Massay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Vijijini

Primary Question

MHE. PRISCUS J. TARIMO aliuliza:- Je, ni nini mpango wa Serikali wa kukamilisha Mradi wa Jengo la Mama na Mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi ambao umeanza tangu mwaka 2008/2009 bila kukamilika?

Supplementary Question 2

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali nyingi za Halmashauri zimebaki bila kumalizika na kwa bahati mbaya Serikali imekuwa na tabia ya kupeleka fedha na mwisho wa bajeti inazichukua. Jimbo la Mbulu Vijijini hospitali imefikia asilimia 95 kumalizika.

Je, ni lini Serikali itarudisha shilingi milioni 300 ilizozichukua ili hospitali ile iweze kumalizika?

Name

Dr. Godwin Oloyce Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Siha

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tatizo ambalo amelizungumzia Mheshimiwa Mbunge Massay limetokea kwenye Wilaya nyingi hapa nchini, hata ikiweko Wilaya yetu ya Siha.

Mimi ninachoweza kumwambia Mheshimiwa Mbunge tukimaliza hapa, hebu tutoke mimi na wewe twende Hazina tuangalie ni nini kimetokea na waweze kusuluhisha hilo tatizo liweze kufanyiwa kazi na fedha hizo zipatikane kazi hiyo imalizike ambayo ni asilimia tano imebaki ili hiyo hospitali ianze.

Name

George Ranwell Mwenisongole

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbozi

Primary Question

MHE. PRISCUS J. TARIMO aliuliza:- Je, ni nini mpango wa Serikali wa kukamilisha Mradi wa Jengo la Mama na Mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi ambao umeanza tangu mwaka 2008/2009 bila kukamilika?

Supplementary Question 3

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa hii nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Mbozi lenye wakazi 300,000 halina hospitali, linategemea vituo viwili vya afya kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wake, lakini katika hivyo vituo viwili vya afya cha Itaka na Isansa havina vyumba vya kulaza wagonjwa, havina wodi za kulaza wagonjwa. Sasa pamoja na kwamba tuna madaktari wazuri wa kufanya upasuaji mkubwa katika hivyo vituo vya afya wananchi wanakosa huduma kwa sababu hawana vyumba vya kulaza wagonjwa.

Sasa nini mkakati wa Serikali wa kujenga wodi za kulaza wagonjwa kwenye hivyo vituo vya afya viwili vya Itaka na Isansa ambavyo vinategemewa katika Jimbo la Mbozi? Ahsante. (Makofi)

Name

Dr. Godwin Oloyce Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Siha

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kwa Mheshimiwa Mbunge ni kweli kwenye Hospitali yake ya Wilaya ya Mbozi kwanza miundombinu ni michache, lakini sasa hivi ndio inatumika kama Hospitali ya Mkoa na sasa tumeshamalizia majengo ya Hospitali yao ya Mkoa. Kwa hiyo, mzigo ulioko kwenye Hospitali ya Wilaya ya Mbozi ambao ilikuwa inaubeba kama Hospitali ya Mkoa sasa utahamia kwenye hospitali ya mkoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ni kweli kwamba ili kuboresha huduma na kupunguza adha ya wananchi kufuata huduma mbali ni vizuri vituo vya afya viweze kusimamiwa. Kwa hiyo, mimi nafikiri Mheshimiwa Mbunge ni tukitoka hapa Bungeni tukae mimi na wewe, ili uweze kuleta vituo vya afya ambavyo umevifikiri tuangalie kama tayari tumeviingiza kwenye bajeti, kama hatujaingiza tutaweza kuingiza kupitia Global Fund ili viweze kufanyiwa utekelezaji.

Name

Prof. Patrick Alois Ndakidemi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Moshi Vijijini

Primary Question

MHE. PRISCUS J. TARIMO aliuliza:- Je, ni nini mpango wa Serikali wa kukamilisha Mradi wa Jengo la Mama na Mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi ambao umeanza tangu mwaka 2008/2009 bila kukamilika?

Supplementary Question 4

MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii na mimi narejea kwenye lile swali la msingi la Hospitali ya Mawenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Hospitali ya Mawenzi ilipandishwa hadhi ikawa Hospitali ya Rufaa na kule Moshi hakuna Hospitali ya Wilaya. Ni lini Serikali itatujengea Hospitali ya Wilaya ili iweze kuhudumia watu wa Jimbo la Moshi Vijijini, Jimbo la Vunjo na Manispaa ya Moshi? (Makofi)

Name

Dr. Godwin Oloyce Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Siha

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Mwenyekiti, nijibu swali la Mheshimiwa ndugu yetu, Profesa Mbunge wa Moshi Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Wilaya ya Moshi Vijijini haina hospitali ya wilaya na ndio maana hata baadhi ya ambulance kwa ombi la Mbunge ambazo zilikuwepo pale Mawenzi zimetolewa zikapelekwa kwenye vituo vya Moshi Vijijini ili kusaidia wananchi kutokana na hiyo adha ambayo anaisema.

Mimi nafikiri Mheshimiwa Mbunge kuna umuhimu wa kukaa sasa na kuangalia jiografia ya Moshi Vijijini kwa sababu ukiiangalia jiografia yake kwanza ni milimani, lakini imezunguka Mji wa Moshi Mjini; muangalie sehemu nzuri kijiografia ambayo inafaa halafu hatua stahiki zianze kufuata sasa kuanzia kwenye Halmashauri yenu kuja Mkoani - RCC, ili iweze kufika TAMISEMI na mwisho wa siku kazi hiyo iweze kufanyika.